Mapenzi & Pesa! – PART 3 - SEHEMU YA 33.
“Sikudanganyi. Umependeza sana, na imekufanya uzidi kuvutia.”
Hapo ndipo akamshangaza zaidi, ila akajikaza akishindwa kumuangalia. “Asante.”
“Na pole kwa maumivu. Ila hivyo ulivyo sasahivi, umependeza. Wala huna haja
yakugusa hizo nywele, ziache hivyohivyo. Ila naomba mafuta ubebe halafu utaenda
kupaka kwenye gari.” Akabembeleza akimshangaza Emelda. Ila akasimama na
kukimbilia chumbani, akakwapua lotion na kutoka nayo. Wakaondoka hapo kwa kasi.
Akampigia simu Ezra akiwa njiani. “Nakuja
Ezra.” “Sawa. Ila taratibu, usipate ajali.” “Nashukuru na samahani.” “Naelewa.
Hamna neno. Utatukuta.” Akahema kwa nguvu akiendelea kukanyaga mafuta.
Safari Ya Jelini, ‘Wake Wa Peke Yake’,
Inaendelea.
Walifika nyumbani kwa kina Jelini wakakuta ndio wanamalizia kula. Mama yao kimya
akiwatizama walipokuwa wakiingia ila mzee ndio akawa kama amevurugwa! Jelini
akawaambia waende mezani moja kwa moja wajichukulie chakula. Junior
akamnong’oneza Emelda. “Nikupakulie?” Akashituka, hakutegemea. “Mimi ndio
nikupakulie kaka!” “Hapana. Wewe ni mgeni wangu hapa. Nakuhudumia mimi
mwenyewe. Vinginevyo twende ukachague kitu unachopenda.” Akaona bora waongozane.
Akamtanguliza.
Kama kawaida yake, Emelda alipopakua chake, akatafuta sehemu
ya kujitenga ili ale akijua lazima Junior atakwenda kukaa na walio wamaana.
Ila Junior alipomaliza kupakua akamfuata, “Twende tukakae pale kwa kina Ezra na
Jelini.” Akaingiwa hofu. Akasita. “Twende. Nipe na hiyo sahani yako nikusaidie
kubeba.” Junior akasisitiza na kunyoosha mkono kabisa kumpokea sahani yake. Akamkabidhi
na kusimama, akamfuata mpaka sehemu waliyokuwa wamekaa kina Ezra.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~
“Mgonjwa naona mambo yako si mabaya!” Jelini akamchokoza
akiwa mwenzie anatetemeka. Kula na kina Ezra! Emelda hajazoea. “Nimepona.”
Akajibu na cheko la wasiwasi. “Na ukapendeza. Umependeza sana.”
Akamfanya aone aibu maana Junior na Ezra wote walimwangalia. “Asante.” “Mwaya
wewe mpole! Kuanzia leo naanza kuwa kama wewe.” Junior na Ezra walicheka.
Wakacheka sana mpaka wengine wakawageukia.
“Nyinyi sio watu wazuri! Sasa mnacheka kwamba siwezi au?
Maana nataka pia niwe naongea kama Emelda!” Mpaka Emelda mwenyewe akacheka.
“Mnacheka nini?” Mama mchungaji akauliza. “Wanao watu
wabaya, mama! Mimi nawaambia kuanzia leo nabadilika. Nakua mtu mpole kama
Emelda na nitakuwa nikiongea taratibu kama yeye. Lakini…” Mpaka
mchungaji akacheka. Kila mtu akabaki kucheka.
“Hakika mimi siamini! Yaani na wewe mama unacheka!?” Akimuuliza
mama Jema. “Huyaweze. Wewe jiachie tu. Huyu binti mpole sana. Mimi namfahamu.
Si yupo upande wa watoto kule kanisani?” Mama Jema akaongeza na kuuliza na
kujijibu. “Alikuwa akiwafundisha kina Jeremy. Mtaratibu sana.” “Sasa mama hapo
wewe unamaanisha nini?” “Wewe huyawezi, jiachie tu.” Wakazidi kucheka,
Jelini akanyanyuka kutoa vyombo eti kwa masikitiko.
“Kweli adui wa mtu, ni wa nyumbani kwake. Mimi siamini!”
Akawa analalamika akikusanya vyombo, wengine wakicheka.” Alipokuwa akitoa sasa
hivyo vyombo alivyokusanya hapo mezani kama kusafisha, Ezra akaenda kumpokea
vile vyombo na kuvirudisha mezani.
Jelini akacheka. “Nasafisha ili niweke dessert! Naona
mchungaji kama amechoka, anadalili za kuondoka wakati mimi sijamaliza kumlisha.
Nataka ale full-corse.” Akaongea kwa kunong’ona asijue wameshaanza
kuchukuliwa video.
Akashangaa Ezra anapiga goti na kutoa pete. Jelini alifurahi
huyo na kuanza kurukaruka. “Jelini bwana! Sasa wewe umejua ni nini?” Junior
akamfanya atulie. “Muone! Umeshaingiwa na hofu!” “Mimi nilijua anataka…” Ezra
akamdaka mikono yote miwili. “Utulie sasa. Usikilize.” Junior akafanya wote
wacheke. Akacheka na kutulia.
Ndipo Ezra akaendelea akiwa magotini. “Nakupenda hivyo
ulivyo Jelini?” Akacheka. “Hivihivi na maneno mengi?” Akamuuliza, wote
wakacheka. “Hivyohivyo ulivyo, sitaki ubadilike.” “Kama hivyo, nakubali. Halafu
mimi nakupenda Ezra! Wala sijivungi.” Watu walicheka wengine mpaka
machozi. Ezra mwenyewe alicheka akiwa amepiga bado magoti akionyesha wazi hakuwa
amemaliza alichotaka kumwambia, lakini biharusi alishakubali
kabla hata hajaombwa!
“Wewe mvalishe tu yaishe. Naona hakuna ustarabu mwingine
tena.” Junior akamwambia Ezra. “Sasa kwani nilitakiwa kufanya nini na wewe
Junior?” “Havina hata maana tena. Wewe vaa pete, tuanze mipango ya harusi.”
Akacheka hana mbavu huku kanyoosha mkono tayari avalishwe pete, hataki mengi
mwenyewe.
“Nimefurahi Ezra! Sasa mbona hata nilikuwa sijui!” “Kuna
kitu kinaitwa surprise Jelini!” Junior akamjibu huku Ezra akimvalisha,
yeye hana mbavu mpaka akamaliza. Akambusu huo mkono na kumuachia.
Jelini akaiangalia ile pete akawa tena kama haamini.
“Mwenzenu naolewa na Ezra!” Akaongea akijiangalia kidole huku akicheka, gafla
akaanza kulia. “Tena? Sasa unalia nini?” “Mimi
siamini bwana! Sasa kama ni ndoto?” Kila mtu anacheka. Ezra akamsogelea
na kumshika mikono yote miwili. “Nakupenda Jelini wangu. Hata ukiamka kwenye
hiyo ndoto, ujue mimi bado nipo. Na ni wako.” “Kweli?
Na hutabadilika?” Akamuuliza kwa sauti ya chini akilia.
“Sithubutu. Nakuhitaji Jelini. Umeleta furaha na faraja
kwenye maisha yangu, siwezi kukupoteza. Una upendo wa kweli kwangu na kila mtu
anayenizunguka. Na ahadi ya kubaki peke yako kwangu itabakia hivyohivyo mpaka
kifo changu. Utabakia wewe kuwa dharula yangu ya kwanza daima.”Akalia
huyo! Akamkumbatia. Vigelegele kwa mama mchungaji.
Mpenda mikono akatulia hapo akajisahau kama yupo mbele za
watu. “Njoo nione pete.” Mpaka Jema alipomuita maana walimjua. Akajitoa hapo
kwa Ezra na kwenda akijifuta machozi. “Na mimi
nimepata wangu wa peke yangu.” Mama yake akabaki akimtizama. “Nzuri
sana. Hongereni.” Akaenda kumuonyesha na mama yake. “Mwenzio
naolewa na Ezra.” “Hongera mama yangu mzazi.” Akaanza kucheka kwa furaha.
Kisha akamgeukia Junior. “Ujue Junior mimi sikuelewi kabisa?
Mbona sikusikii sasa!” “Nachukua video Jelini! Nitafanya mangapi?” “Sasa si
uchukue video huku useme hongera!” “Haya mama. Hongera sana
Jelini.” “Naolewa na Ezra mwenzio.” “Na mimi naona. Umependa pete?” “SANA. Sisi tunapenda vitu
vizuri. Ila hii ni sana. Halafu nimevalishwa na Ezra!” Pakawa na furaha
ya namna yake. Huyo Jelini kila mtu akahakikisha anaona pete yake kidoleni.
~~~~~~~~~~~~~~~
Wakati wanakula keki, Emelda akamuuliza Junior. “Wifi Hope
yuko wapi?” “Hapa hayupo.” Akamjibu hivyo akijua wazi silo jibu alitakiwa
kutoa. Emelda akanyamaza.
Wakasherehekea hilo, wakaagana wakiwa wamekubaliana
kinachofuata ni mahari lakini uchumba lazima kutangazwa siku ya jumapili
kanisani, na tafrija fupi kwa mchungaji. Sio jambo geni, hata Junior alifanyiwa
hivyo.
Mchungaji akafanya
maombi, akaomba Jelini na Ezra wapige magoti kisha watu wote wawazunguke,
wakawawekea mikono. Wote wakawaombea. Mchungaji akatamka baraka kwao mpaka
watoto wa watoto wao. Jelini alifurahi sana.
Ndipo wakawasindikiza nje. Kabla hajapanda kwenye gari,
akamgeukia Ezra na Junior. “Mkitoka hapa, safari iwe ya nyumbani. Sitalala,
nawasubiria.” Ezra na Junior wakaangaliana. “Nikimaanisha msichelewe.”
“Tumeelewa baba. Tunakuja sasahivi.” Mzee akaondoka. Ila vile alivyowatizama,
walijua kinachoendelea.
Junior akaondoka na Emelda kama kuwapa nafasi hao wawili
hapo kwenye gari la Ezra. Wakakiss kwa muda tu wakisherehekea uchumba
wao, ndipo Ezra akaondoka kuwahi nyumbani, akiwa amemuacha Jelini na familia
yake wakiwa wamefurahi.
~~~~~~~~~~~~~~~
Zaidi mama Jema.
Alifurahia kwa heshima ya kufuatwa na mchungaji na mkewe siku ya
jumatano na kuombwa rasmi kuposwa binti yake. Hilo lilimgusa sana. Ndipo
akaonyesha na zawadi walizokuwa wamempa. Jelini hakuwa akiamini jinsi mama yake
alivyomficha. “Basi mimi sikuwa hata najua kama wana huo mpango leo!”
“Mchungaji alikuwa akisema unajiandalia uchumba wako mwenyewe. Wema wako
umelipa.” Wakabaki kucheka.
“Wewe si ulisema hutaki wa kanisani wewe?” Jema
akimkumbushia siku yake ya kuchumbiwa yeye, jinsi alivyomuomba asimuombee apate
mume mlokole. “Huko duniani wa peke yangu nimekosa dada yangu.”
“Naona mpaka umefunga!” Wakazidi kumcheka. “Nampenda Ezra! Mtaratibu sana. Na
naona wamefurahi kweli yeye na Junior nilivyokubali kuwa nao kwenye maombi leo.
Ezra alikuwa ananiambia pale kanisani, eti imemfurahisha sana mchungaji na
mkewe. Kwao ni watu wa maombi sana.”
“Sasa sio uishie
leo.” “Siwezi Jema. Sasahivi naongeza juhudi kwenye mambo ya kanisani, ili niwe
nao. Ni watu wazuri sana.” “Na kuanzia sasa ndio fungu lako hilo
ulilochagua na kulikubali. Huna jinsi. Taratibu tu, utakuwa kama wao. Na naona
wenyewe wanakupenda.” Mama Jema akaongeza. “Katika hilo namshukuru Mungu.
Wazazi wao wana upendo sana. Hawana neno.” Ikawa faraja kwao.
Kwa Wazazi.
Walipofika nyumbani Junior hakuingia ndani akabaki garini
akimsubiria Ezra mpaka alipofika ndipo akashuka. “Emelda yuko wapi?”
“Nimemwambia aende chumbani kwake moja kwa moja.” Wakasimama hapo kwa muda.
Kimya, kisha wakajikuta wanaongoza njia kuingia ndani. Wakakuta wanasubiriwa.
Ule ukimya ukaashiria si shwari.
“Tumepanga kesho ndio nihitimishe rasmi na Hope.”
Akaanza Junior hata kabla hajakaa vizuri na mzee hajaongea. “Ezra ameshaandaa
mazingira mazuri. Nitakwenda kuzungumza naye, ili tuachane kwa ustarabu japo
natamani iwe kwa amani pia.” Kimya mzee akimtizama.
“Nataka kuishi kwa amani baba. Na niwe na mwanamke
anayenipenda na kunijali. Hope anaweza kuwa mke mzuri tu, lakini kwa mwanaume
mwingine, si kwangu. Nikiishia kumuoa yeye, maisha yangu hayatakuwa na
furaha. Na naona si sawa kwangu na kwake. Tumejitahidi kwa muda mrefu, au
niseme nimefumbia hiyo hali kwa muda mrefu, lakini naona sipo tayari
kuendelea kuishi hivyo. Sina sababu.” Kimya.
“Ni hilo tu nimeona
nikwambie mzee wangu na mama najua utaelewa. Najua unataka niishi kwa furaha.”
Junior akamalizia, mzee akamtizama mkewe. “Umeshindwa wapi na hawa vijana wako,
mama?” Wote walitegemea kutupiwa mama yao hiyo lawama.
“Mbona kama nimesikia kuna mipango ya kueleweka tu! Au
sijaelewa?” Wote walishangazwa na mama yao jinsi alivyochukulia hilo jambo.
Junior akajiweka sawa sasa. “Mama Junior!? Hivi wewe umefikiria pale kanisani?”
“Mimi nafikiria mwanangu kwanza. Hayo mambo mengine ni baadaye. Wewe
mwenyewe ulinionya hata mimi nisiwahi kuingilia chaguzi zao kwenye maswala ya
mke.” “Lakini huyu amechumbia na kanisa zima linajua! Tutasema nini?”
“Sasa imeshindikana! Tufanyaje?” Akajibu mama bila wasiwasi.
“Kweli mama?!” Mumewe akashangaa sana. “Kwani ile ni ndoa? Si ndio maana kuna
kuwa na uchumba ili wasomane! Umemsikia hapa amesema amemsoma, Hope si kwamba
hafai, lakini si mke wake yeye! Sasa ulitaka mwanangu ndio aoe mke wa
mtu!” Mama huyo akaongea kwa mshangao kabisa.
“Hapana! Furaha ya mwanangu kwanza ndio mengine baadaye!
Kweli mimi nianze kufikiria hisia za watu wengine halafu mwanangu ndio akateseke!
Hapana baba Junior. Mbona wao walilifurahia swala la mwanangu kuachwa?
Wakambariki yule binti na watoto wake wakizungu, wakashangilia pale na uchumba
ulikuwa karibu kabisa na ndoa! Hawakujali mwanangu. Wakamuacha Ezra anasononeka
peke yake!” Mama Mchungaji akaendelea.
“Kwanza wakati wote umekua ukisifia akili za Junior. Kwa
nini katika hili uone hajafikiria?” Mzee akanyanyuka. “Kuna jambo jingine.”
Ezra alishituka, asiamini. “Kwa nini usisubirie kwanza Junior!?” Akamtizama
Ezra, akafikiria kidogo ila akashindwa. “Siwezi tena Ezra. Acha tumalize hili
jambo.” Akasimama kama baba yake.
“Naomba ukae baba. Na nakuomba katika hili usimame na mimi
kama baba na si mchungaji. Sasahivi nakuhitaji wewe kama baba yangu.
Unajua kwenye huduma sisi wote hapa na kila mtu humu ndani tunasimama na wewe
baba yangu. Iwe mchana au usiku tuko na wewe tukitumika pamoja. Leo nakuhitaji
usimame na mimi kama baba.” Mzee akakabwa, akarudi kukaa.
Na yeye akarudi kukaa. Akamtizama Ezra, naye akabaki
akimtizama. “Ni jambo la kushitua kidogo, ila kabla hamjasema hapana
na kukataa, tafadhalini naomba mpate muda wakufikiria, tunaweza
kuzungumza zaidi kesho. Naomba msiwe na haraka mkataka kunijibu sasahivi.
Mnaweza toa jibu ambalo hamjafikiria. Naomba ufikirie kwanza baba.” Mzee
kimya akimtizama.
Akatulia kidogo kama ambaye anatafuta pakuanzia, Ezra
akimtizama pembeni yake. “Nampenda na nataka kumuomba Emelda awe
mke wangu.” Palizuka ukimya hapo. Kama ambaye hakuna anayehema. Mpaka mama yake
akaishiwa maneno.
“Kwa kuwa nimeanza, acha tu nimalizie. Emelda ndiye
anayenitunza hata huko ninakoishi. Nimeondoka hapa, lakini bado ananifikiria na
kunihudumia. Ni, kwa nini sasahivi na si wakati ule hata kabla ya
kumchumbia Hope? Najua mnaweza kujiuliza hivyo.” Kimya wakimtizama. Anajiuliza
mwenyewe, na kuendelea kujijibu.
“Sikuwa nikijua kama nafungia macho upendo mkubwa wa namna
hii. Sasa matatizo yangu na Hope ndiyo yalinifanya nikapata muda wa kutafakari
na kutamani kama ningepata mwanamke anayenijali hata nusu ya Emelda. Nikajaribu
kufikiria usiku kuchwa, nikagundua sitakuja pata mwanamke kama
Emelda. Mbali ya kuniheshimu na kunijali. Ananifikiria, anani…” Akaanza
kuwatajia wazazi wake mambo anayofanyiwa na Emelda kana kwamba hawamjui Emelda.
Kimya wakimtizama.
Akaendelea tu kama anayekamua jipu. “Ndio nikaona
bora nitulie kwa Emelda ambaye kwanza sio kwamba nahitaji kumsoma. Wote
tunamjua. Amejawa upendo, mtaratibu, anajiheshimu, hana kiburi,...” Akaendelea
kutaja sifa zake mpaka Ezra akamshitua. “Nafikiri wanamfahamu Emelda.” “Kabisa.
Ni binti wa hapa nyumbani. Kwa hiyo kwa sababu yeye namfahamu vizuri, akikubali,
ndani ya miezi mitatu, tunafunga ndoa. Ni hilo tu.” Kimya, hao wazazi wamepigwa
na butwaa hata hawasogezi mkono. “Sasahivi nimemaliza.” Akajitahidi akimeza
mate. Kimya.
“Na swala la safari.” Akaongeza Ezra. “Asante Ezra.
Nimemuomba kesho asisafiri. Na naomba asianze likizo yake kesho. Ili nikitoka kuhitimisha
na Hope ndio nizungumze naye sasa. Akikubali ndio nafikiri kutakuwa na
chakuzungumza. Maana hata sasahivi mkikubali au mkikataa bila
mimi kuzungumza na Emelda mwenyewe, haitasaidia. Ni bora tudhibiti hisia
zetu na neno lolote mnalofikiria kuniambia sasahivi mkiwa na mshituko,
mpaka tupate jibu lake Emelda. Hapo nimemaliza. Au kuna nilichosahau?” Akamuuliza
Ezra.
“Naona kwa sasa itoshe, wazee wakapumzike. Tuendelee
ukishazungumza na Emelda hiyo kesho ambayo nafikiri sio wazo baya akawa off,
ili apate muda mtulivu wakujiandaa na mazungumzo.” “Wazo sio baya. Nashukuru
mama kumuomba mama Leti aje asaidie kazi kwa kesho pia. Maana kila kitu
kikienda sawa, tutakuwa na chakula cha usiku cha pamoja pia. Sisi wanne.
Tukiombea safari yetu.” “Inamaana mimi, Junior, Jelini na Emelda.” Ezra
akaongeza. Wawili hao wakabaki kupokezana maneno na mipango, wazazi kimya
wakiwatizama. Pakatulia kwa muda. Kimya.
“Naona kweli tuache wazazi wakapumzike.” “Kabisa. Lakini
kabla hatujaondoka, ili mpumzike, naomba niwashukuru wazazi wangu kwa
kufanikisha hili la usiku wa leo. Naona safari yenu inakaribia kufika mwisho
kwetu. Tukishaweka sawa la Junior, ndani ya miezi mitatu, tunaoa kabisa,
huu ukurasa tunafunga, wote mpumzike.” Kimya. “Na kweli ilifana.”
Akaongeza Junior.” Kimya. Ezra akasimama.
“Twende Junior.” “Naomba nizungumze na Emelda mara moja ili
kuweka sawa mipango ya kesho.” Wote wakamtizama mama yao. Kimya. “Naona
tuondoke tu, utazungumza naye kwa simu ili wazazi wakapumzike. Siku ishakuwa
ndefu.” “Ni kweli. Wazo zuri. Usiku mwema.” Wakaaga. Kimya. Wakaondoka hao
wawili bila yakujibiwa.
~~~~~~~~~~~~~~~
Alipofika tu kwenye
gari akakumbuka vile Emelda alivyokuwa amependeza. Akafurahia moyoni, ila
akakumbuka kumwambia ngozi ya kichwa inauma kwa kuvutwa akiwa anasukwa.
Akaona aanze kumtafutia dawa ya maumivu usiku huo. Ezra akampigia. “Mbona sikuoni nyuma yangu?!” “Natafuta dawa ya kupunguza
maumivu kwa Emelda. Wamemvuta sana wakati wakumsuka. Wewe tangulia kulala.”
“Kwamba unapango wa kurudi tena nyumbani!?” “Siwezi kulala bila ya kumpelekea
dawa. Najua si muhimu, lakini nataka kumhakikishia kuwa nimebadilika na
sasahivi namsikia.” Ezra akatulia.
“Ujue
ameniambia ni kweli aliniaga siku ya jumapili?” “Ikawaje?” Akamsimulia
jinsi alivyoambiwa na Emelda. “Daah!” “Nimejisikia
vibaya! Mpaka nimebaki nikijiuliza nimekuwa nikimfanyia hivyo mara ngapi!”
Ezra akabaki akimfikiria huyo binti. “Sasa sijui kwa
kuwa na yeye ni mkimya sana na sauti yake ni ndogo pengine ananikuta nakuwa na
mambo mengi, kwa hiyo naishia kumuitikia hata kitu ambacho sijaelewa!” “Hapana.
Tukiri tu kuwa tumekuwa tukimpuuza. Hakuna jinsi ya kujitetea katika
lolote lile, Junior. Na nakuunga mkono kwa hichi unachotaka kufanya,
japo sijui unarudije nyumbani!” “Sina jinsi, itabidi tu nirudi. Nitajua
chakufanya nikifika pale mlangoni.” “Nijulishe kama utafanikiwa.” “Sawa.”
Wakaagana, kazi ya kutafuta dawa ya kupunguza maumivu ya ngozi ya kichwa
ikaendelea.
~~~~~~~~~~~~~~~
Kila duka aliloingia
usiku huo akieleza tatizo lake linalohitaji dawa, walibaki wakimshangaa.
Mwishoe akaenda duka kubwa la madawa Mikocheni, akapata muhudumu aliyesomea
mambo ya madawa. Akamuhisi ndiye mmiliki mwenyewe. Maana alimkarimu vilivyo na
kumpa muda wa kutosha kumsikiliza na kumshauri. Akampa dawa ya kupulizia ya
kupunguza maumivu. Akamwambia pengine itasaidia. ‘Pain relif spray’.
Akalipia na safari ya kurudi kwao ikaanza.
~~~~~~~~~~~~~~~
Akampigia simu
Emelda. “Umeshalala?” “Bado.” Akajibu. “Nakuletea dawa ya kupunguza maumivu ya kichwa kwa ajili ya
kusukwa. Kwa hiyo usilale, nisubiri.” Alishituka Emelda hakutegemea
kabisa. Kwanza hakujua hata kama amemsikia au hata kutilia maanani alichokuwa akisema.
Hakuzoea kabisa. “Utanifungulia mlango?” “Naogopa kaka!
Unajua baba ndiye anayefungua milango usiku.” “Basi acha nimpigie simu
anifungulie.” “Au tufanye tu kesho kaka. Usisumbuke.” Akaongea kwa hofu.
Mpaka aamshwe mzee kwa ajili ya msuko wake! Haikuwa imekaa yakueleweka. “Hapana. Sisumbuki,
nataka ulale vizuri. Na usiogope. Umesikia?” Akatulia. “Nakuja. Usilale, unisubiri.” “Nitakusubiri kaka. Asante.”
~~~~~~~~~~~~~~~
Alifika kwao
akaingiza gari mpaka ndani. Junior mtoto wa nyumbani na walinzi wanamfahamu.
Akampigia simu baba yake. Ilishapita lisaa tokea atoke hapo. “Samahani sana baba yangu. Kuna dawa nataka kumpa Emelda.”
“Ambazo haziwezi kusubiria kesho?” “Haziwezi. Nimeshafika, nipo hapa mlangoni
kwako. Naomba nifungulie.” Simu ikakatwa, akajua anakwenda kufunguliwa.
Baada ya muda mlango
ukafunguliwa. “Ni usiku sana sasahivi Junior, nahitaji kupumzika.” “Sitakaa
sana.” “Tafadhali usikae kabisa. Mkabidhi na uondoke.” “Sawa.” Akampita hapo
mlangoni akiwa hajasogea kabisa kumuashiria anamsubiria.
Akagonga mara moja
tu, kama aliyekuwa amesimama mlangoni akafungua akiwa na wasiwasi. “Pole kwa
usumbufu.” “Usijali. Ni ya kupuliza. Kwahiyo jipulizie kwenye ngozi ya kichwa,
itafanya ngozi kuachia na kutulia. Vingine humo ndani ya mfuko mwingine ni
vyako. Tutaongea zaidi kwenye simu au unalala sasahivi?” “Nitasubiri mpaka
tuongee. Uwe nasafari njema ukiwa unarudi nyumbani.” “Asante. Nitakupigia muda
si mrefu.” “Sawa.” Akatoka kwa haraka, akamkuta baba yake palepale alipokuwa
amemuacha.
“Nashukuru baba.
Usiku mwema.” “Asante na wewe. Na uwe makini huko barabarani.” “Nitajitahidi.”
Akatoka, mzee akafunga mlango, huku nyuma Emelda anafurahia kama arukeruke.
Mfuko mmoja ulikuwa na hiyo dawa, na mwingine chocolate nzuri sana.
Zikaonekana za kiwango cha juu haswa. Akabaki akijichekesha hata asipulize
dawa. Simu ikamtoa kwenye furaha.
~~~~~~~~~~~~~~~
“Kaka?”
“Umepuliza dawa?”
Ndio akakumbuka. “Bado.” “Nataka uipulizie nijue kama
itasaidia au tutafute nyingine.” “Itasaidia tu. Asante. Nimefurahi! Sikujua
hata kama ulinisikia!” “Nipo kwenye kupunguza kelele zote zilizokuwa
zikinifanya nishindwe kutulia na kukusikia. Narekebisha ili niweze kukusikia
wewe Emelda. Nivumilie kidogo tu. Kila kitu kitakuwa sawa.” Alivyokuwa
akimbembeleza, ikamfanya atulie kabisa.
“Nashukuru
kukubali kubaki na kuwa na mimi kwa kina Jelini. Uliumia?” “Safari hii sijaumia
sana, kwa kuwa tulikuwa wote kaka. Na angalau ulijua kama nipo pale.” Junior akamuhurumia.
“Samahani kama huwa inaonekana ni kama nakupuuza
Emelda. Sikudharau.” “Ila huwa unashindwa kabisa kuniona kaka, au hata
kunisikia. Wakati mwingine hata nikikusalimia unakuwa mbali, huitiki.” “Naomba
unisamehe. Nakuahidi nitabadilika. Na nimeanza kuchukua hatua kwenye mapungufu
yangu.” Akatulia.
“Kesho
naomba uje nyumbani. Nimeshakuombea ruhusa kwa wazazi. Au unaratiba ingine?”
“Hapana kaka. Nitakuja. Ulitaka iwe saa ngapi?” “Nitatuma mtu aje akuchukue saa
nne na nusu asubuhi. Mpaka mfike nyumbani, nitakuwa nimesharudi, nakusubiria
wewe tu. Ulitaka kula nini ukifika?” Akashangaa kidogo ila akajibu. “Utakachotaka nipike, nitapika na mimi nitakula.” “Kesho mimi
ndio nakuandalia chakula.” Akamsikia akicheka.
“Nitakuandalia
chakula kizuri. Na usiku tutakuwa na Ezra pamoja na mchumba wake.” “Kwamba na
mimi nitakuwepo!?” “Ndiyo. Tupate nao chakula cha usiku.” “Sitaweza kukaa huko
muda wote huo. Natakiwa kurudi kusaidia kazi. Mama Leti huwa anawahi kuondoka,
na baba ni lazima apate chai ya saa 10.” “Nimezungumza na mama. Hamna shida.
Kesho ni mapumziko yako. Nitakurudisha nyumbani usiku.” Akafurahia moyoni
ila na wasiwasi ukizidi kumnyemelea. Wifi Hope! Maana hanaga utani. Akatulia na
kuaga. “Usiku mwema kaka.” “Na wewe. Nitakuona kesho.”
“Asante.” Wakakata simu.