Naomi Simulizi |+1 205 767 8163 |naomisimulizi@gmail.com NILIPOTEA! - SEHEMU YA 10. - Naomi Simulizi

NILIPOTEA! - SEHEMU YA 10.

 

W

akati anashuka, akawasogelea kibabu kilichomuogopesha Tunda,  lakini  akaona  vile  Sadiki  alivyomsalimia kwa heshima,  akabaki palepale mlongoni  anashangaa. .  “Kwa kujulikana tu unakanyaga  huku kwetu, leo imejaa baraka  kila mahali mpaka wake zangu  walikuwa wakiulizana ni nani leo  anayetutembelea! Karibu mama.”  Yule babu akainama kidogo kwa  heshima mbele ya Tunda. Tunda  akakunja uso, akamtizama Sadiki.  “Ani, huyu ndio babu Chonde.”  “Shikamoo Babu.” Tunda  akasalimia. Wakakaribishwa  ndani. Heshima aliyokuwa akipewa  Tunda, hata yeye akashangaa.  Walipewa ugali, nyama ya kuku na  mchicha.  Wakapewa  nafasi.  Waliachwa wao wawili ili wale. 

“Sijawahi kula ugali na nyama ya  kuku vitamu hivi!” Sadiki  akacheka wakati Tunda akiendelea  kula kama anayelishwa. Alikula  mpaka akamaliza. “Sasa nasikia  usingizi.” “Wewe jipumzishe hapohapo kwenye mkeka. Ngoja  nikamtafute Babu.” Hakujua  kilichoendelea  mpaka  alipoamshwa ilikuwa usiku. Giza.  Sadiki akamwambia waondoke  kurudi Dar.  “Mbona miguu inamichanga  kama wa baharini au ziwani!?”  Tunda aliamka akiwa hana viatu,  michanga miguuni na mapajani kama ameloa kidogo.  “Twende, tutazungumza kwenye  gari.” Tunda akasimama. Alikuwa  palepale alipokuwa amelala baada  ya chakula. Kwenye mkeka kama  sebuleni. Akaangalia kulia na  kushoto, akajikuta yupo yeye na  Sadiki tu.

“Twende Ani.”  “Hatuagi!?” Tunda akauliza.  “Babu yupo na wazee wenzake  sasa hivi, wanafanya ibada.  Tutarudi wakati mwingine.”  Akamsaidia kusimama.  Alipoingia tu kwenye gari, akalala  tena usingizi kama wa mtu  aliyefanya kazi nzito sana.  Hakushtuka mpaka tena Sadiki  alipomwambia wamefika hotelini.  “Tumefika  Dar!?”  Tunda hakuamini.  “Umelala  sana.  Twende ukapumzike ndani.”  Tunda akashuka. “Acha nioge  kwanza kabla sijalala.” “Kabla  hujaoga, njoo kwanza hapa  kitandani.” Tunda akashangaa  anamtaka kimapenzi hata kabla hawajaoga! “Wachafu hivi!”  “Hivyo hivyo nakutaka Ani. Njoo  kimapenzi  changu.” Tunda akacheka, akavua  nguo kwa haraka na kumkimbilia  Sadiki. 

Akajiona anauchu naye kama  hawakuwepo hapo kitandani usiku  uliopita. “Nina hamu na wewe!”  Tunda akajikuta akilalamika.  “Naomba na leo tulale wote.”  Tunda akaendelea kubembeleza.  “Sawa. Lakini haya maisha ya  hotelini ni yakubadilisha kabisa.  Tukinunua tu kitanda, tunahamia  kwetu. Mimi na wewe.” Hapo  Tunda  hakujibu,  akaendelea  kumng’ang’ania tu.  “Tukitoka Arabuni  ndio  tunahamia kwetu. Si ndio mama?”  Sadiki akaweka msisitizo. Tunda  akacheka tu. Akawa kama  amepagawa  hapo  kitandani.  Nguvu mpya na shauku kwa  Sadiki ikaongezeka. Akatumia  ujuzi mwingi hapo akitaka Sadiki  afurahi.  Alipochoka  Sadiki ndipo akamwambia wakaoge,  ndio  walale. Bila kubisha, akaongoza  bafuni kuoga, na kurudi kulala.  

Tunda Mpya.

T

unda akabadilika kabisa. Akawa mtiifu  sana kwa Sadiki. Usingemkuta  akibisha chochote anachoambiwa  na Sadiki. Mapenzi yakaongezeka  wawili hao, hamu ya kuwa pamoja  ikaongezeka.  Tunda  akawa  mwanamke wa hapo hotelini.  Akitoka ni kujinunulia vitu vyake,  saluni, na kurudi hapo akimsubiria  Sadiki.  Alimpenda  na  kumnyenyekea huyo Sadiki,  utafikiri Mungu wake. Hakuna  kitu angeambiwa na Sadiki,  akabisha. Mpole na mnyenyekevu.  Kwanza  usingewakuta  wanabishana. 

          Wakashugulikia  hati  zao  zakusafiria na Visa, Tunda  akajifunika kama mtoto aliyepitia  madrasa, wakaingia Arabuni. Ni  kweli Sadiki alikuwa na pesa.  Walifikia kwenye hoteli nzuri  sana. Walijifungia hapo kama siku  tatu. Wao tu. Hakumuona Sadiki  akipiga hata simu kwa mkewe.  “Umemwambia mama Amini  kuwa tumefika salama?” “Mimi  nilijua unataka muda na mimi!  Sasa unamleta huku mama Amini  wa nini!?” “Kweli mpenzi  wangu.” Tunda akatulia na  kuendelea kufaidi yeye.

 “Tukirudi  lazima  tukatoe  sadaka.” “Sawa.” Tunda  akakubali  huku akimchezea   taratibu kifuani. “Na vitanda  vikifika tu nchini, tunahamia  kwetu.” Tunda akacheka, kisha  kimya. “Au hutaki kuishi na  mimi?” “Nataka Sadiki.” “Lakini  isiwe hotelini.” Akasisitiza. Tunda  akaendelea kumchezea taratibu.  Walizunguka wakitafuta  thamani ya dhani za Tunda bila kuchoka. Na Sadiki naye alikuwa  akinunua kila kitu alichotaka  Tunda bila kupinga. Kwa mamilioni ya pesa ya  kitanzania aliyokuwa amebadili  kwa dola. Tunda akapata kila alichokuwa akitamani. “Umefurahi sasa?” “Sana.” “Mimi nataka ufurahi.” Wakatafuta njia nzuri ya kuvifikisha hivyo vitu mpaka nchini Tanzania. 

Napo hapo pesa yakutosha ikamtoka Sadiki. Walipohakikisha  vitu  vyao  vimepakiwa melini, ndipo wakarudi  nchini Tanzania. Hotelini tena.  Sadiki alikaa hapo hotelini siku  moja, siku inayofuata  akamuaga  Tunda. “Nitarudi kesho jioni.  Ujiandae tutakwenda kutoa  sadaka ndipo turudi kwa babu  Chonde.” “Sawa.” Bila kuuliza ni  wapi wanakwenda kutoa hiyo  sadaka, Tunda akakubali. 

 

Taka Cha Mvunguni, Sharti Ainame.

    Ndiyo yaliyompata Tunda. Mtaka mengi mazuri kwa pamoja, yeye na mpenzi Sadiki, iliwapasa kuinama haswa! Kuyafanya mengi yakutisha ili kuendelea kujinufaisha. Na kweli, kesho yake mida ya saa  nne usiku Sadiki akafika hapo.  Hakutaka mapenzi. Alimwambia  Tunda wakirudi huko ndipo  atamtaka  kimapenzi.  Tunda hakubisha wala  kuuliza.  Akamuona anawasha tu tv  akiangalia kama anayesubiri muda  ufike. Saa tano na nusu usiku  akamwambia watoke, lakini avae  nguo nyeusi tupu. Uzuri walikuwa  wamenunua aina hizo za nguo  walipokuwa  Arabuni.  Kama  baibui lakini kama buu buu.  Magauni mapana, marefu mpaka  chini. Bila maswali mengi  akabadilisha, aliporidhika Sadiki  ndipo wakatoka akiwa amejifunga  na nywele zisionekane. 

Waliendesha mpaka makaburi ya  Sinza. Akaegesha gari yake mbali kidogo na  makaburini.  “Tushuke hapa.” Sadiki akiwa  ameshika mfuko mkubwa kidogo wenye baadhi ya vitu aliokuwa  ameacha hapohapo kwenye gari  wakati anaingia kwa Tunda,  akamfungulia  Tunda akashuka garini,  wakaanza kutembea wakielekea  yalipo makaburi, Sadiki akiwa na  ule mfuko.  “Tunaenda wapi Sadiki?” “Hapo  ndani makaburini.” Tunda  akashtuka kidogo. “Usiku huu  makaburini! Mimi naogopa.”  “Usiogope. Tupo wote. Na wala  hatutakaa muda mrefu. Sawa?”  “Nishike mkono basi.” Sadiki  akacheka akamshika mkono vizuri huku akimtuliza kumtoa hofu. Akaangalia kushoto na  kulia kama asiyetaka mtu awaone,  wakaingia ndani eneo la makaburini.

Wakaelekea mwisho kabisa kwenye makaburi  hayo, Sadiki akamwambia hapo panatosha.  “Ndio tunafanya nini huku!?”  “Wewe fuatisha kila kitu  ninachofanya. Ni rahisi tu.”  “Kwani ulishawahi kufanya  hivi?” “Ani kwa maswali!”  “Nataka kujua.” “Sasa unafikiri mafanikio yote hayo yanatoka  wapi? Ni kwa ibada kama hizi. Na  tukifanya pamoja ndio zaidi.”  Tunda kimya huku amejawa hofu  mpaka vinyweleo vikamsimama.  Ibada hiyo ikaanza. Alifuatisha  kila kitu alichokuwa akifanya  Sadiki. Kadiri muda ulivyokuwa  ukienda hapo makaburini, hofu  ikaanza  kumwisha,  akaanza kuzoea hayo mazingira. Baada ya  mambo mengi ya hiyo ibada,  Sadiki akamwambia wamemaliza. 

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

     Maisha hayo yakaendelea kati ya  Sadiki na Tunda. Safari za  Handeni kwa babu Chode zikawa  zakawaida tu. Tunda akawa  amezoea,  akifika  huko  wanaaguliwa. Alishaelewa kuwa babu  Chonde ni mganga wake Sadiki.  Wakawa wakifika huko kwa babu, wakawa watu wakushirikiana bila  ubishi.  Wanafanya uganga pamoja bila  maswali au kubisha.  Akagundua kuna mto ambao huwa  lazima wawe wanakwenda mida  ya usiku, kila wakifika huko  Handeni. Kwa hiyo walikuwa  wakisubiri giza liingie ndipo  wanaenda kwenye huo mto. Babu  Chonde  anawaagua  wakiwa  wamesimama ndani ya huo mto  kama chini ya mwamba kidogo.  Huko  watafukiza  ubani.  Zitaongelewa lugha ambazo hata  yeye Tunda hakuwa akizielewa.  Kutachinjwa ndege, huku Babu  akiwatabiria kuwa wao wawili  watapaa juu sana hata katika  dharuba wao watabaki kuwa juu. Basi watafanya hayo  mambo kisha wanarudi Dar usiku  huohuo.

Na mara zote wakitokea huko kwa babu, kila walipokuwa  wakifika njia panda ya Chalinze,  kuna vitu walitupa hapo usiku huo  wa  giza kali, kisha wanarudi Dar.  Tunda alipouliza ni kwa nini,  Sadiki akamwambia kwa kifupi tu,  kuwa wanaita kila mtu anayefika  jijini Dar, kama wanatafuta  nyumba ya wageni, basi wakalale  kwenye hoteli yao.  Kuna mtu alifilisika jijini. Maeneo  hayohayo ya Sinza ambako  Sadiki alikuwa na baa, lakini  Sinza Mori. Alikuwa amechukua  mkopo ili kuendesha hoteli hiyo,  aliposhindwa kuiendesha hiyo  hoteli na kushindwa kulipa benki,  ikapigwa mnada kwa bei ya chini,  kwa kuwa Sadiki alikuwa na pesa,  akanunua gorofa hilo. Akabadili  jina,  akapakarabati  zaidi.  Akamkabidhi Babu apashugulikie kwa kuvuta wateja. Babu aliporidhika kuwa amemaliza kazi kwenye hilo jengo ndipo Sadiki akapafungua rasmi.

Ukweli Sadiki aliwekeza kwenye hiyo hoteli. Alikuwa ameweka na vivutio vingi kwa wateja. Na kweli walikuwa wanajaza hilo  jumba kwa wageni wa kutwa na  kulala.  Hiyo ikamtia moyo Sadiki huku  akimuhamasisha  na  Tunda.  Waliona mafanikio ya ushirikina wanaofanya kwa kupitiae  biashara za Sadiki zilizokuwa zikishamiri haswa. Tunda akatoa  ushirikiano wote. Mara moja kwa  mwezi  walifanya ibada makaburini  makaburini. Wakizika  umaskini, mikosi,  kulogwa, na mengine mengi  Tunda aliyokuwa akimsikia Sadiki  akiyatamka wakiwa wanafanya  ibada hizo hapo makaburini. Na  kwa Babu Chonde hawakuacha  kwenda kufanya ibada za  kufufuliwa bahati na kutakaswa  nyota zaidi.

Siku nyingine maisha  yanaendelea jijini kama kawaida.  Kuponda raha. Sadiki na Tunda,  wala  usingewadhania  kuwa  wanafanya ibada makaburini.  Hayo maisha akayazoea Tunda.  Ikawa kitu cha kawaida kwake.  Hofu ikaisha.  Tunda akawa na pesa. Akitokea  mahali, utajiuliza mara mbili.  Kuanzia juu mpaka chini,  alivaa vitu vya madesigner  wenye majina makubwa  duniani. Viatu vingi  alipenda vya Jessica  Simpson.  Alisema  ndivyo  vizuri  vinavyomkaa  mguuni  kwake na  vinaenda na umbile la nyayo zake. Basi ikawa kazi ya  kuvisaka kwa pesa nyingi,  ilimradi miguuni amvae Jessica. 

Na wakati wote utamkuta Tunda  kwenye kiatu cha juu, hata kama  ni sendozi. Pochi yake ukiitazama  kwa macho, ungejua kuna pesa  kubwa iliachwa kwenye hilo duka.  Wakati wote ungekuta na kucha  safi. Kuanzia za miguu mpaka  mikononi. Tunda akawa wa dhahabu  halisi na silver za hali ya juu.  Akitokea mahali, ungependa  kumtizama binti huyo mwenye  rangi nyeusi haswa. Mtaratibu,  ongea na tizama yake, hana  haraka. 

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

Mwaka wa kwanza na miezi  yakutosha ukapita, Tunda na  Sadiki wakiishi hotelini, wakiwa  wamejaa mafanikio ya namna yao.  Mapenzi kwa Tunda yakazidi.  Hakuna jinsi ungemtenganisha na  Tunda, Sadiki akaweza. Baada ya  hiyo  nyumba  waliyokuwa  wakiilipia kujaa vitu alivyotaka  yeye mwenyewe Tunda, Sadiki  akiwa amegharamia mapesa mengi  kuvitoa nchini Arabuni ambapo  wangeweza kupata nchini hapo  kwa bei nzuri, Tunda akakosa sasa  sababu ya kuendelea kuishi tena  hotelini. 

  Kontena kutoka Arabuni ilishusha  chumba  cha  kama  alivyotaka yeye Tunda   alivyochagua  walipokuwa nchini Arabuni.  Kuanzia mapazia, kitanda,  makabati  makubwa na  dressing  tables.  Viti vya  hapo  chumbani na vioo vyake. Na  sebule ikawa hivyo hivyo.  Hawakukosea hata mapambo.  Walimletea kama alivyochagua  kule, na vikawa vimefungwa  na  vilifika  vizuri,  vikiwa  hakuna  kilichoharibika.  Akamtaka wahamie kwenye hiyo  nyumba ambayo Tunda hakuta  kabisa kuhamia na Sadiki.

Tunda  alikuwa akimtii katika kila kitu,  kasoro katika hilo na baadhi ya  vitu fulani alivyokuwa amevikataa  tokea  mwanzo  kitu  kilichomshangaza sana Sadiki  aliyekuwa amehakikishiwa na  babu  kuwa  amekwisha  kumtengeneza Tunda. Tunda  akawa akienda peke yake  nyumbani  kwake.  Sadiki  akimtaka, wanakutana hotelini.  Hilo likazidi kumkera Sadiki  aliyehisi kwenye hilo, uganga wa  babu umeshindwa. 

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

  Mwanzoni Sadiki  alimlalamikia  babu Chonde  ugumu anaopambana nao kwa  Tunda. Babu alitaka awe  anakwenda naye kuaguliwa, lakini  haikuwahi kuwezekana. Tunda  hakuwa  akitaka  kabisa  kuongozana naye sehemu yeyote  na alikuwa mbishi kwa kila jambo.  Alimwambia akitaka mambo  yaende anavyotaka yeye basi  akazane  kumshawishi mpaka afanikiwe  kumpeleka Tunda kule  kwake.  Siku Tunda amekubali kwenda na  Sadiki Handeni, akala chakula na  kulala zaidi ya masaa 8, mengi  yaliendelea akiwa usingizini.  Haikuwa shibe iliyomfanya alale.  Chakula chake kiliwekwa dawa,  ndipo akalala na kufanyiwa  mengi. Alipoamka, alikuwa ni  kama amepokonywa hiari yake,  akawa mtumwa wa Sadiki.  Hakuna aliloambiwa na Sadiki,  akabisha tena isipokuwa baadhi ya  hayo masharti. Alibadilika akawa  mtumwa wake. Ila mapenzi ya  Sadiki  kwa  Tunda  ndiyo  yaliyomfanya kumtunza vizuri.  Hakuwahi kumnyanyasa japo  Tunda hakuwa anajielewa. 

 ~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

“Mbona bado kuna ugumu napambana nao?”  Sadiki alimlalamikia babu kwenye  simu. “Nini tena?” “Swala la ndoa, mtoto  na kuishi naye nyumba moja! Ni mwaka wa  pili huu, tunakutana hotelini tu! Ameshindwa  kabisa kunikaribisha kwenye nyumba ambayo  hata mimi nimeshiriki kununua vitu! Na  maanisha kwa kuchagua kabisa!” Sadiki  aliendelea kulalamika. “Nilikwambia  kama upo tayari, tumfunge kabisa ufahamu  wake, ukakataa. Hiyo nafasi ndogo uliyoacha,  ndiyo inampa mamlaka. Huyo binti ana  nyota kali sana Sadiki.” “Sasa nitafanya  nini?” “Nakuachia wewe mwenyewe. Lakini  ukitaka nimtengeneze, uniletee kwa siku 7 tu.  Niachie kabisa. Mpaka unakuja kumchua  huyu, hakuna utakalomwambia akabisha tena.  Na ukifanikiwa kumuweka ndani huyo kama  mkeo, hakuna atakayeweza kukushika tena.  Utakuwa habari nyingine mjini.” Hilo  likamuhamasisha Sadiki. 

Kummiliki kabisa Tunda! Awe  mkewe kabisa na amazalie watoto,  ni jambo alikuwa akilitamani sana.  Lakini hakutaka amfanye mjinga kabisa! Napo ikawa ngumu.  Alipenda  vile  wanavyoweza  kutoka, kusafiri na kuzungumza  na Tunda mambo yao. Akajua  Babu  akimtengeneza  zaidi,  anaweza kuwa mjinga, akakosa  hata rafiki na mapenzi yakaisha. 

Sadiki  akaona amjaribishe  kwanza,  kabla  hajampeleka kwa babu kwa siku  hizo saba amtengeneze.  Akampigia tena simu Tunda. “Ani  mama, upo wapi?” “Nipo tu nyumbani.  Unataka nije?” “Kwa nini mimi nisije  huko?” Tunda kimya. “Eti Ani, mama  watoto!?” “Tulikubaliana tusizae Sadiki.”  “Hata kamoja kakuunganisha undugu!?”  Tunda akaanza kucheka. Sadiki  hakushangaa. Huwa anacheka  hivyo hivyo bila jibu la hapana au  ndiyo.  “Nina hamu na wewe Sadiki! Leo  utakuja tulale?” Sadiki akajua  ndio amebadilisha hoja, hataki. “Nitakuja. Lakini  inabidi tufikirie jinsi yakuhalalisha Ani.  Mama Amini ameanza kulalamika.  Sionekaniki nyumbani. Lakini akijua  yupo mwenzake, atatulia. Naona swala la  ndoa sio baya. Ndoa zina baraka zake  mama. Halafu utajuana na mwenzio.  Mtapanga mambo pamoja. Itakuwa  rahisi.” Tunda akanyamaza.  “Ani!?” Sadiki akaita. “Nakusikiliza.”  “Umeamua nini sasa?” “Labda tuache  kulala pamoja usiku, tuwe tunakutana  mida ya asubuhi au mchana. Usiku uwe na mama  Amini. Na safari za hapa na pale  tupunguze. Hizo ndizo zitakuwa zikimtia  wasiwasi. Na swala lakuongeza mtoto  mwingine, naona ubakie na hao hao sita  wa mama Amini. Usiongeze mtoto  mwingine.” Sadiki akakata simu,  na kumpigia simu babu  kumtaarifu kukubaliana na wazo  lake.

 “Nitamleta kwa hizo siku saba.  Tafadhali usimfanye akawa kama tahira.  Atakosa maana. Sitaki aje kuwa mtu  wakumsaidia tena. Ninachotaka ni awe chini ya himaya yangu tu. Afanye kile ninchotaka mimi. Kuishi naye, ndoa na watoto. Basi. Ila awe anajielewa. Tafadhali sana  babu Chonde.” “Usijali. Wewe mlete kwa  huo muda tuliokubaliana. Ukija  kumchukua utaona mwenyewe. Tena tunaweza kufunga ndoa huku huku.”  “Hapana. Nataka wajuane na mwenzie.  Iwe ndoa inayotambulika na kila mtu.  Nampenda sana Ani. Nataka watu wajue  ni mke wangu, na aheshimike hivyo. Kwa  hiyo nataka harusi kubwa.” “Sawa.”  Babu akakubali bila shida, Sadiki  asijue hila nyingine ya babu.

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

 Ni kweli babu Chonde alikuwa  mganga wa Sadiki wa muda  mrefu. Hata mke wake mkubwa  walikuwa wakifahamiana. Lakini  alipompeleka Tunda na Sadiki  kuanza kufungukiwa mambo yake,  tamaa ikamuanza babu Chonde. Kwanza na yeye alitafuta jinsi ya  kunufaika na huyo Tunda ambaye  walijiambia anabahati ya pekee.  Pili, kule kuchanganyikiwa kwa  Sadiki, akimtaka asimuharibu  Tunda ili awe na akili zake, babu  Chonde akajua kuna analonufaika  nalo zaidi Tunda akiwa kwenye  akili zake. Na Sadiki naye  hakuacha kumsifia Tunda kwa  babu. Akimwambia ni bora kuliko  mke mkubwa. 

Tamaa ikamuanza babu. Kila  Sadiki alipokuwa akienda na  Tunda, alitamani na yeye apate  bahati japo yakulala na Tunda.  Anafanyaje? Ndipo akazua hizo  siku 7 za kumuagua Tunda peke  yake, Sadiki akiwa hayupo, ili  aweze kufanya analotaka kwa  Tunda akiwa ameteka ufahamu  wake. Iwe kwa kumlaza au  kumteka ufahamu kwa kujibadili  yeye kama Sadiki na Tunda kulala  naye kwa hiari yake akijua ni  Sadiki ili babu naye afaidi ya  Sadiki. Babu akaandaa mazingira  hata kwa wakeze, kwa siku hizo 7  atakazokuwa na Tunda, ikabakia  kusubiria Tunda aletwe. 

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

Sadiki aliaga kwa mkewe kuwa  anasafiri kikazi, akahamia hotelini  kwa Tunda ambaye alijua  watatengana kwa siku 7. Kula,  kulala ni hapo hapo hotelini. Kazi  ilikuwa ni mapenzi tu. Walikaa  siku mbili hapo ndani, ila mida ya  usiku walikuwa wakitoka kwenda  kwenye kumbi za starehe. Wote  wakiwa  wamependeza,  usingeweza kusema Sadiki ni baba  wa watoto 6, kwa mkewe.  Ujana  ukarudi,  Sadiki  anayekimbizana na Tunda kila  mahali kwa starehe, akabadilika  haswa.

Hata uvaaji alibadilika,  akarudi kuwa kijana angalau  aendane na Tunda. Na Tunda  ndiye aliyehakikisha anabadilika  na kupendeza. Kila alipokuwa  akijinunua nguo, alimnunulia na  yeye.  Akambadilisha  kabisa  Sadiki. Badala ya kuvaa masharti  ya vitambaa vya ajabu, Tunda  akaanza kumnunulia nguo za  kisasa na viatu vinavyoendana na  suruali alizokuwa akimnunulia.  Sio raba alizomkuta akivaa. 

Usiku wakuamkia siku ya tatu  akamwambia Tunda kuwa  wanakwenda kwa babu. Lakini  hakumwambia kama anakwenda  kumuacha kwa siku zote hizo  saba. Kwani Babu alimwambia  Sadiki, atamfanyia dawa Tunda,  wala hataelewe kama Sadiki  hayupo naye, au hata asijue kama  amekaa huko kwa siku zote hizo  7. Alimwahidi  siku  atakayokwenda  kumchukua,  atajua ndio siku hiyo hiyo  waliyokuwa wamekwenda. 

Tabia yao yakufanya dawa kwa  babu,  matambiko  ya  kila  wanapoelekezwa na babu. Kafara  na sadaka walizokuwa wakitumwa  watoe na huyo babu, Tunda  alishazoea. Wala hakuwa akibisha  tena.  Alipomwambia  wanakwenda  Handeni,  kesho yake  wala  hakuuliza maswali mengi, asijue  anasubiriwa kuwa kitoweo cha  babu kwa siku 7. Na kwenda  kuharibiwa akili ili akirudi awe  kama mjinga kabisa kwa Sadiki.  “Tunaondoka ngapi?”  Akauliza Tunda bila wasiwasi.  “Mapema sana. Nataka tugeuze  mapema, ikiwezekana chakula cha  usiku tuje kukila hapa hapa Dar.”  “Sawa.” Tunda akakubali.

 Ila  akaona usiku huo ukawa wa  tofauti. Sadiki hakutaka watoke,  na wakati wote walitaka wawepo  hapo kitandani kama wanao agana.  “Kwani kesho umeamua kurudi  kwa mama Amini? Unataka  ukalale kwake?” Ikabidi Tunda  aulize. “Ni vile hutaki tu na  unafanya mambo kuwa magumu.  Mngefahamiana ingekuwa rahisi  sana. Na ratiba zingeeleweka  kuwa nipo wapi na ninafanya  nini.” Hapo Tunda akanyamaza na  kulala kabisa. 

 Janga jingine kwa Tunda.

A

subuhi ya saa 10, Sadiki  alimuamsha ajiandae. Akiwa bafuni, Sadiki akamfuata,  akaomba penzi. “Nilifikiri unataka  tuwahi!” “Safari ina mambo  mengi mama. Acha tuondoke  tukiwa tumeridhishana.” Tunda  akacheka.  Wakatumia  muda  wakutosha tu hapo bafuni, ndipo  wakatoka na kujiandaa kwa safari.  Walitoka hapo bado giza nje.  Kwa kuwa wote walikuwa  wamechangamka tu, zikaanza  stori. Sadiki akatoa gari hapo  hotelini, Mikocheni B taratibu tu  wakiwa wametulia na mipango ya  kawaida.

Tunda alijawa na furaha, asijue kinachomsubiri mbeleni,  wala Sadiki akiwa hana hata  habari na hila ya babu.  Walipofika mataa ya Ubungo,  wakiwa wanakata kona kulia ili  kuliacha jiji la Dar, kuelekea  Kibaha, mbeleni kwenye mataa  ikiwa imewaka taa nyekundu.  Kuzuia magari ya upande wao  kuelekea Buguruni. Kwa kuwa  yeye alikuwa anakata kulia,  hakusubiri taa ya kijani. Alipofika  pale akakanyaga mafuta zaidi  kukata kona. Lori la kokoto  lililokuwa linatokea Manzese  kwenda upande uleule na wao  waliokuwa wakielekea kama  Kibaha, ikiwa imeruhusiwa na taa za kijani, dereva  alikwisha ziona tokea mbali akawa  anakanyaga mafuta kwa nguvu  kuziwahi kabla taa hazijabadilika,  aliigonga hiyo gari ya Sadiki  iliyokuwa imeingia tu barabarani,  ile gari ilirushwa kama kitenesi  kwa kuwa zote zilikuwa kwenye  mwendo kasi. 

Gari aliyokuwa anaendesha Sadiki  ikawa kama inapaa mpaka ikatua  ndani ya mtaro mkubwa upande  wa pili. Kilikuwa kitendo cha  sekunde chache, chakustua na  kuogopesha sana. Dereva wa Lori  alishuhudia akaona vile gari  ilivyokuwa ikirushwa. Alisimama  mbele kidogo, lakini gari  ilipoingia tu mtaroni, kimya kwa sekunde kadhaa yule  dereva akakanyaga mafuta na  kuondoka pale bila kutaka kujua  kulikoni ili asikamatwe kama ameua.

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

Tunda amepata ajali mbaya sana  akiwa na mume wa mtu, akiwa  anakwenda kwa mganga wa kienyeji.  Mengi yalipangwa juu yake. Lakini  safari imeishia mtaroni. Nini  kimempata Tunda safari hii?  Endelea kufuatilia.

CONVERSATION

1 Comments: