Naomi Simulizi |+1 205 767 8163 |naomisimulizi@gmail.com Nilipotea! - Sehemu ya 5. - Naomi Simulizi

Nilipotea! - Sehemu ya 5.

 Tunda alijibembeleza kwa shida pale kitandani, asiamini kama yale maumivu makali anatoka kwenye mwili huohuo uliokuwa ukibembelezwa kwa masaji na  kuwekwa kwenye sauna jijini Arusha. Na ni usiku uliopita tu alikuwa amelala kitandani kwake nyumbani kwa baba Tom akipulizwa na kiyoyozi, akiwa amejawa kiburi na ahadi tele kutoka kwa baba huyo ambaye hakuwahi kutosheka naye. Kila alipomaliza aliomba aanze upya. Leo yupo peke yake wodini hapo, akigugumia maumivu makali sana, bila baba Tom aliyempa ujauzito huo. 

 Taarifa chungu za kutelekezwa rasmi na hata aliyempa mimba ziliendelea  kupita kichwani mwake pale kitandani alipokua akigugumia maumivu, huku  akisikia kutokwa kwa damu mfululizo. Hofu ya kifo pale alipokuwa amelala, na aibu ya kuangaliwa vibaya na kila muuguzi pale, ilikuwa ikimsumbua Tunda. Alijua atakufa kifo cha maumivu makali sana pale kitandani.  Mwili huo uliokuwa umeshazoea AC kila mahali, si kwenye nyumba aliyokuwa akiishi tu, hata kwenye mahoteli aliyokuwakipelekwa kutumiwa mwili huo na baba Tom na kwenye magari yake pia, ulikuwa ukitokwa jasho kama anayenyeshewa mvua, asijue ni jasho la maumivu au joto kali wodini hapo.  

    Hakuweza kugeuka ila kugugumia maumivu makali sana. Alijitahidi kukunja miguu kama anayepunguza maumivu, bila mafanikio. Hakuweza kurudi kulala tena. Alijibembeleza bila  mafanikio. Akajifunika shuka kwa  muda huku akijibembeleza.  Hofu ikamwingia na kujiambia ni  kama  anajifunika  sanda yeye  mwenyewe,  akajifunua  haraka.  Alipigwa na butwaa kukuta baba yake mzazi, amesimama pembeni ya kitanda chake.  Tunda alishtuksana, akajifunika shuka tena harakaharaka kwa hofu na aibu. Alianza kulia kwa kwikwi akiwa amejifunika vilevile. 

    “Unasikia maumivu?” Baba yake akamuuliza. Tunda akatingisha kichwa kukubali. “Ngoja nikamwite nesi, tuone watakupa dawa gani.” Tunda hakujifunua akamsikia baba yake akiondokaIlikuwa imeshapita miaka 5 tokea wawili hao, baba na mwana, waonane. Alimuacha Tunda akiwa darasa la 4.  Kabinti kadogo, leo anakutana na Tunda aliyetolewa mimba! Tunda hakuwa tayari kuiona sura ya baba yake, asijue amesikia nini juu yake. Akatulia ndani ya shuka, akiendelea kulia, kwa uchungu.  

     Baba yake alitumwa kwenda kununua dawa ya maumivu, akaenda kwa haraka na kurudi kwa yule nesi. Akamchoma sindano ya kuzuia maumivu, akabaki amejifunika mpaka muda wakuona wagonjwa ulipoisha jioni hiyo, akamsikia baba yake akimuaga. “Nitakuona kesho asubuhi. Nimekuletea chakula hapo ule na  unywe hiyo juisi itakusaidia kuongeza damu. Kuna hivyo vifaa vingine wamenielekeza hao manesi, wamesema vitakusaidia kujisitiri.” Tunda alishindwa hata kutoka kwenye shuka kumuaga baba yake. Akabaki kimya.  Akamsikibaba yake akiondoka.  

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

     Baada ya maumivu kupungua, akatoka pale kitandani ili angalau akajisafishe. Alikuta baba yake amemletea pedi kubwa na nzito. Na nguo za ndani chache. Hilo likampa aghueni.  Akaenda kuoga na kubadili, akarudi tena kulala. Safari hii alilala mpaka asubuhi. Akajikuta amejichafua tena. Akaamua kwenda kuoga. Ni kweli alikuwa akitokwa na damu nyingi sana, kiasi cha kumtia hofu. Tunda  hakujua mwisho wa ile damu ni nini! Alijua wamemtoa mimba kwa nguvu, swali lililomsumbua binti huyo ambaye haelewi mambo, ni kama kuna kitu  wameharibu  humo  ndani kinachosababisha damu kutoka kwa wingi hivyo au ndio huyo mtoto wake  tu ameharibiwa na kutoka kwa muundo wa damu! 

 Hofu ilikuwa ikimsumbua. Mbaya zaidi hakuwa na mtu wakumuuliza wala kuomba ushauri. Manesi aliokutana nao asubuhi hiyo walikuwa wageni. Na jinsi walivyomtizama, akajua wazi na wenyewe wamepewa taarifa zake. Akaamua anyamaze tu.   

Alirudi kujilaza pale kitandani, bila kujua chakufanya huku akijiambia wakati wowote ule, anaweza kufa kwa kuishiwa damu. Ni kweli alijawa hofu na uchungu wa kuuliwa mtoto wake tumboni. Alianza kuwaza vile kiumbe hai kilivyoweza kuuwawa kikatili bila huruma. Waliwezaje jamani!” Tunda aliwaza huku akitetemeka mpaka miguu, machozi yakitoka. Chuki kwangu, mpaka kuua kiumbe kisicho na hatia! Heri angenifukuza tu ila asimwadhibu kiumbe kisicho na hatia! Huyu mtoto hakuchagua mimba yake utungwe wapi kama mimi kwa Manda!” Tunda aliendelea kuwaza huku akilia kwa uchungu sana, peke yake pale kitandani.   

Baba yake akaingia na chupa ya uji, akamkuta akilia sana. Alisimama pale kwa muda, asijue aseme nini! Hata yeye alikuwa kwenye mshtuko. Tunda alikuwa amelazwa katikati ya wodi ya kina mama. “Mbona hukula chakula nilichokuletea jana?” Tunda akabaki kimya tu akilia. Maumivu bado ni makali?” Tunda akatingisha kichwa kukubali. Baba yake akaenda tena kumwita nesi. “Tafadhali naomba mkamwangalie binti yangu. Bado maumivu ni  makali.” “Ni kawaida. Itachukua muda.” Nesi alijibu. “Naomba basi apewe tena dawa yakupunguza maumivu.” Tunda alimsikia baba yake akimsihi yule nesi. “Si ulishanunua dawa?” “Ndiyo.” Baba yake akajibu.” “Basi atahudumiwa zamu yake ikifika. Wote humu ndani ni wagonjwa. Zamu yake ikifika, atapewa dawa.” Yule nesi, mama mtumzima kidogo, alisikika kwa kiburi. Baba yake Tunda akaondoka na kurudi kitandani kwa Tunda. Akasimama pale huku akimtizama binti yake akilia.   

Yule nesi hakukawia sana kama alivyosikika kwa kiburi, akaja kumchoma tena sindano. “Lakini hii haitakuwa tiba endelevu. Itabidi aendelee kunywa dawa za kawaida za maumivu. Baada ya muda atakuwa tu sawa.” “Nashukuru sana.” Baba yake akashukuru bila maneno mengi. Kidogo, akamuona Tunda anatulia, akajua maumivu yanapungua, ndipo akaondoka akiwa amemuachia ile chupa ya uji na kumwambia atarudi kumuona baadaye. Akatoka. Tunda akalala.   

Alilala mpaka mida ya saa nne na nusu asubuhi wakati madaktari wanapita round, akashtuka kutoka usingizini.  Hapakuwa na sababu ya kuendelea  kuwekwa pale, akaruhusiwa siku hiyo  asijue anakwenda wapi. Akabaki akiwaza pale kitandani asipate jibu. Lakini alitakiwa atoke pale wodini apishe wagonjwa wengine watumie kile kitanda. Akarudi tena kujisafi, akabadili na  kujiweka sawa, akatoka pale wodini, akiwa na nguo alizokuwa amevaa alipokuja pale hospitalini. Alitoka asijue ni wapi anaelekea mara baada  ya kutoka kwenye geti la hospitali. Hakuwa na chochote mkononi zaidi ya vitu alivyokuwa ameletewa na baba yake. Alivyovikuta kwa mama yake, ni  kweli aliacha. Hata simu aliyokuwa amepewa na baba Tom, alinyang’anywa. Kwani alipozinduka kutoka usingizini hakujikuta na chochote. Hata kimkoba alichokuwa nacho pia mama yake aliondoka nacho.  

Wakati anatembea taratibu kutoka hapo wodini akitafuta njia yakumtoa getini, akashangaa kumuona baba yake amekaa chini kama anayemsubiria mtu. Akashtuka kidogoAkasimama baada ya kumuona Tunda. “Vipi? Unajisikiaje?” Baba yake akamuuliza. “Nimeruhusiwa.”  “Nimeongea na shangazi yako atakuja kukuchukua. Twende hapo nje ya geti tukamsubirie.” “Ananipeleka wapi!?”  Tunda akauliza kwa wasiwasi. Hakujua hata kama anashangazi. 

“Imebidi nimuombe ukaishi naye kwa muda wakati najipanga. Umenitia aibu ya miaka Tunda! Na ninakuomba ukatulie huko kwa shangazi yako. Huna pakwenda mwanangu, upande wa mama yako hawataki kukuona  tena.”  Tunda hakujibkituAlinyamaza tu, asijue baba yake aliambiwa nini! Na kwa jinsi baba yake alivyoongea hapo, akajua hata kama ataongea baada ya mama yake kumjaza maneno, akajua haitasaidia tena.  

‘Amemtiaibu!’  Nani wakumsikiliza na kumwamini! Akaona anyamaze tu. Maadamu yeye ndiye aliyeshikwa na mfupa, basi, akajua kila mtu anamjua yeye ndio mwizi. Akanyamaza tu. Wakatoka mpaka nje ya geti.  Wakatafuta sehemu ya kukaa. Wakakaa pale nje ya geti wakimsubiri huyo shangazi mpaka ilipofika jioni. Hakuna aliyemuongelesha mwenzake. Kila mtu alikuwa akiwaza lake. Kwa asili baba yake alikuwa mkimya sana.  Hata hivyo ni watu ambao hawakuwa na mahusiano. Wanazungumza nini!  

Mida ya saa 11 jioni waliona gari nzuri, benzi safi ya kijivu imesimama. Tairi zilikuwa zina marembo ya  chuma. Zilikuwa zikiwaka, utafikiri  zimetoka kupigwa msasa. Tunda alimuona baba yake anasimama na  kusogelea ile gari. Akajua ndiye shangazaliyekuwa akisubiriwa. Shangazi yake aliegesha gari kisha akashuka. Kiatu cha juu, na gauni zuri alilofunga mkanda katikati. Wazi lilionekana ni gauni ya pesa inayoeleweka. Tunda alimwangalia jinsi alivyoshuka na vitu alivyoweka mwilini mwake. Vichache na vya thamani. Alionekana ni msomi na anayejielewa. 

Kaumbile kazuri kama msichana mdogo tu. Alijipaka rangi nzuri ya mdomo,  iliyoendana na weusi wa mwili wake,  kama kaka yake au huyo Tunda  mwenyewe. “Umeshaongea na mwanao?” Ndio likawa swali la kwanza alilomsikia yule shangazi mtu akimuuliza baba yake bila hata salamu. “Sitaki umalaya kwa binti zangu. Sitaki aanze kuwafundisha mambo ya ajabu. Na sitaki akae karibu na mum…”  “Nisikilize dada. Nimeomba msaada wa muda tu. Naomba usianze kututukana mimi na mtoto wangu. Tunda amekosa, lakini isiwe sababu ya kumnyanyasa mwanangu.” “Basi kaishi naye.” Shangazi mtu akamjibu kaka yake bila aibu wala kung’ata maneno. 

“Nilishakwambisababu yakushindwa kumchukua sasa hivi. Yule mwanamke alitaka kumuua huyu mtoto. Unataka nimrudishe tena wakati nimekwambia wazi mama yake alikuja kutuambia wote pale nyumbani  makosa aliyofanya Tunda? Na  amemjaza mke wangu maneno yakijinga sana juu ya Tunda akimshauri asimpokee tena Tunda. Unataka nimpeleke huyu mtoto pale ili  nini kitokee sasa?” Tunda aliendelea  kusikiliza“Lakini Yohana, naomba iwe kwa muda kweli. Mume wangu mwenyewe anawasiwasi sana kumkaribisha huyu pale nyumbani, wakati tuna binti  wanao soma.” “Unajua nini dada? Niachie mwananguNitajua chakufanya naye.” “Mbona hasira sasa wakati nakwambia ukweli!?” Akasikia shangazi yake akiuliza kwa ukali.

“Nahisi mtaenda kumnyanyasa sana binti yangu. Hakuna mtu anayejua maisha ya Tunda kama yeye mwenyewe.” “Kwa hiyo unamtetea!?” “Hata yeye nimemwambia amekosa,  lakini si kumnyanyasaHilo hapana kwakweli. Hata kama tunashida lakini si kwa namna hiyo. Kama unatakkumsaidia sawa, kama huwezi basi bwana. Nitatafuta njia nyingine.” “Twende!” Aligeuka na kurudi kwenye gari yake bila yakumtizama Tunda mara mbili.

Baba yake alitoa kadi ndogo na kumkabithi. “Hizi ndizo namba zangu. Unipigie wakati wowote. Kazana kula ili urudishe nguvu. Nitakuja kukuona jumapili.” Tunda aliipokea na kubaki akilia pale mbele ya baba yake, bila kutaka kuondoka. Alisimama pale akiwa ameinama mbele ya baba yake akilia bila yakuongea kitu. Tunda alilia nakushindwkujizuia“Nitakuja kukuona. Nenda usimcheleweshshangazi yako.”  Tunda alitembea kwa shida mpaka kwenye gari akiwa ameshika mfuko wake. 

Mfuko wenyewe wala haukuwa na kitu cha maana zaidi ya pedi na chupi alizoletewa baba yake. Mfuko wa chupa za uji, alimuachia baba yake. Hakuwa na kitu kingine chochote, hata kitambaa cha kufutia hayo machozi yaliyokuwa yakitoka kama mvua! Bado alikuwa kwenye mshtuko na maumivu ya mwili uliotolewa mtoto ambaye hakuwa hata akijua kama huymtoto alikuwepo humo mwilini mwake. Bado aibu na mshtuko wakukataliwa na kila mtu mpaka na baba Tom aliyemuona msaliti mkubwa sana. Kwani walipokuwa kitandani alimuahidi mambo mengi sana yaliyomtia jeuri hata yakutukanana na  mama yake.  

Zaidi wasiwasi wakupelekwa sehemu ambayo tayari anajua hatakiwi, yeye ni hatari kwa wote zaidi kwa watoto wa huyo shangazi ambaye ndiye wanakutana naye kwa mara ya kwanza. Historia inajirudia tena.  

 

Tunda kwa Shangazi yake.

Njia nzima Tunda alikuwa akipewa maonyo makali sana. “Nina mabinti wawili wanaopenda sana shule. Nakuomba sana, usiwaingize kwenye michezo yako.” Aliendelea kuongea naye kwa kurudia rudia mpaka walipofika. Geti lilifunguliwa. Kutoka getini mpaka kwenye nyumba yenyewe kulitandazwa vitofali vizuri vyenye rangi tofauti tofauti zilizopangiliwa kwa ustadi. Maua yalikuwa yamejaa kuzungua ua nzima na yalichanua vizuri sana. Gari ikaegeshwa kwenye sehemu maalumu yakuwekea magari pembeni ya nyumba hiyo, akaambiwa ashuke ili kuingia ndani.  

Alikaribishwa kwa machya mshangao, na kupelekwa kwenye chumba cha msichana wa kazi.  Ilikuwa nyumba nzuri sana, ya kiasi. Kulinukia kuanzia unaingia mlangoni. Patulivu, utafikiri hawaishi watu. Hewa safi iliyochujwndiyo iliyokuwepo ndani ya hiyo nyumba.  Aliingia kwenye hicho chumba alichoelekezwa, baada ya muda mfupi tu msichana wa kazi akaingia hapo. Alimtambua kwa jinsi alivyokuwa amevaa kama mfanyakazi wa hoteli. “Karibu sana TundaNaitwa Nyange.” Tunda alishtuka kidogo kusikia akilitaja jina lake kama ambaye na yeye alishapewa habari zake kabla. Akajua na hapo habari zake zilisha tangulizwa hapo kabla ya yeye mwenyewe kufika. “Naomba unionyeshe bafuni, nikaoge.” Akamuonyesha. Ilikuwa ni hapohapo chumbani

Tunda akaingia kuoga. Alipotoka Nyange akamwambia shangazi yake  alimletea vitenge viwili, khanga mbili, mataulo mawili makubwa na mafuta yakupaka mwilini. Akamuonyesha sehemu ya kuegesha mfuko wake. Japokuwa kulikuwa na maakabati yaliyojengewa ukutani, lakini akamwambia hayo makabati hayatumiki. Aweke hivyo vitu kwenye mifuko yake. Asiguse makabati. Tunda akaweka vitu vyote ndani ya mfuko wake akauegesha kwenye kona pembeni ya vitu vya Nyange, maisha yakaanza pale. Tunda alijiuguza yeye mwenyewe mpaka akapona kabisa. Ilikuwa ni nyumba ambayo kila mmoja alikuwa busy na mambo yake. Walitoka asubuhi na kurudi jioni. Tunda alianza kuzoea mazingira ya hapo kwa shangazi yake ambapo kulikuwa na kanuni nyingi na zilikuwa lazima  kufuatwa vile zilivyo bila kukosea.  

 

Tunda na baba yake.

Baba yake hakuja siku ya jumapili kama alivyomuahidi, akaja jumapili inayofuata, Tunda akiwa na nafuu kubwa tu. Hata ile damu ilikuwa imekata. Kidogo alionekana hofu imepungua. Akatoka naye nje ya ile nyumba ili waweze kuzungumza kwa uhuru. Walisimama nje ya geti, pembeni ya ukuta. “Unataka kurudi shule?” Tunda  alikataa katakata. “Kwa nini?” “Sina ninachoelewa darasani.” “Kwa nini usijaribu tena?” “Hapana. Sitaki kukupotezea pesa yako bure. Sina akili iliyotulia yakuweza kukaa darasani nikafundishwa nikaelewa chochote.” “Utakuwa ukifanya nini sasa?” “Sijui. Hivi unajua hapa nilipo nina elimu ya  darasa la pili? Ile niliyopata nikiwa kijijini wakati naishi kwa bibi na babu.”  Tunda akaendelea. 

“Baada ya kutolewa kwa bibi, nikiwa darasa la pili nikaletwa kwako mpaka sasa, akili yangu haijawahi kutulia tena. Nimisukosuko ya kila namna, iliyobadilika sura tu, lakini mimi ndiye ninayelaumiwa.” Tunda alianza kutokwa na machozi. “Unafikiri kwa elimu hiyo nafanya kazi wapi na kwa nani? Au kama ni shule naanzia wapi kwa umri huu?” Baba yake aliumia sana. Alishindwa chakujibu akabaki kimya kwa muda, kisha akamuaga nakuondoka.

 

Maisha ya Tunda nyumbani kwa Shangazi yake.

                 Hakuishi hapo kwa shangazi yake kwa muda mfupi kama alivyoahidi baba yake. Ni kama alikwamia hapo, na baba yake hakuwa na pakumpeleka  tena. Tunda akaendelea kuishi hapo. Mwaka wa kwanza ukaisha, wapili nao ukatimia akiwa ndani ya nyumba hiyo  huku akionekana ni tatizo kubwa lisiloweza kuvumilika.  Hawakuacha kumtangazia anatakiwa  kuondoka hapo. Hawakumzoea, na  walihakikisha wanaweka mazingira yakutozoeleka hapo. Yalikuwa  ni  maisha  yaliyojaa  manyanyaso ya hali ya juu. Walimnyanyasa Tunda ndani ya nyumba ile mpaka Tunda alijisahau kabisa kama yeye ni binadamu.  

    Walimuaminisha kuwa yeye ni mjinga, malaya na hafai kwenye jamii. Binti aliyekataliwa na kila mtu sababu ya umalaya. Walimuonyesha ni msichana wa kukimbiwa na kutengwa kwa mabaya aliomfanyia mama yake mzazi. Walimfanya aamini hana kimbilio, pale alipo ndio mwisho wa maisha yake yote hapa duniani. Hakuruhusiwa kutoka mle ndani, wala hakupewa matumizi yeyote yale. Msichana wa kazi ndiye aliyemsaidia matumizi madogo madogo. Alikuwa kama mtumwa wakudharauliwa sana pale ndani, kuliko hata huyo msichana wa kazi. Wakamfanya kama mnyama asiye hata na thamani.

    Binti yao mkubwa wa pale ndani, Sera alikuwa chuo kikuu mwaka wa pili na mdogo wake Samatha ndio alikuwa akisubiri kwenda chuo kikuu akiwa amefaulu kwa alama za juu sana. Walikuwa ni mabinti waliokuwa wamelelewa kwenye mazingira ya uwezo wa kifedha na kisomi ya hali ya juu. Wazazi wao wenyewe walikuwa  ni wasomi haswa. Kwa ufupi hawakuwa wakijua maisha bila elimu  ndio inakuaje hapa duniani! Walitumikiwa mle ndani ya nyumba  yao, kazi yao kubwa ilikuwa masomo tu. Na kweli walifanya vizuri sana shuleni na walikuwa watulivu sio watoto wenye mambo ya wanaume. Hata mazungumzo yao yalikuwa yakujielewa. 

    Ukifika humo ndani utafikiri umetua nchi za Ulaya. Lugha ya kingereza na vijidesturvya  waingereza vilitawala. Walijitahidi kumuonyesha Tunda wao ni watu wa madaraja mawili tofauti kabisa, na wala hastahili kuwa nao karibu. Usingewahi kuwakuta hao mabinti wa shangazi yake pamoja na Tunda, sehemu yeyote ile labda wawe wamemwita awafanyie kitu. Alimuona mume wa shangazi yake  akitoka kila siku asubuhi akiwa mevaa nadhifu sana, hakujua anafanya kazi wapi. Ilikuwa lazima awe kwenye tai. Kama hakuwa na suti, basi alitoka akiwa ameshika koti mkononi. Hakuwa na muda na Tunda hata kidogo. Kwa kumtizama tu, alijawa utisho wa elimu na pesa. Nadhifu wakati wote, hata ukimkuta sebuleni huwezi kumkuta amekaa kihasara. Na shangazi yake hivyo hivyo. Kiatu cha juu wakati wote akiwa anatoka hapo ndani. Huwezi kumkuta  amefunga khanga au kitenge. Hata akiwa hapo nyumbani na hao binti  zake, utawakuta nadhifu. Kuanzia  nywele mpaka kucha za mguu. Wote  walikuwa wasafi haswa. 

    Lugha yao  kingereza wakati wote, ukaaji wao  migongo imenyooka wakati wote. Sio  kukaa kihasara hasara.  Chakula kililiwa kwa masaa maalumu.  Kila kitu kilikuwa kwa mpangilio, hapakuwa na uholela olela hapo ndani.  Msichana wa kazi alitambua nafasi yake na kujipanga itapasavyo. Usingemkuta amejichanganya na wao sebuleni hata mara moja. Ukimkuta hapo katikati yao, basi ujue yupo kwa sababu maalumu, akitoa huduma fulani, basi. Na akimaliza anachofanya anawapisha wenye nyumba bila kuchangia lolote hata kama analijua, labda awe ameulizwa. Na wakati wote alitakiwa kuwa kwenye sare za kazi.  

    Shangazi yake hakuwa akitaka uchafu. Ukiwa jikoni basi nilazima kuvaa kofia, kufunika kichwa nywele zisije angukia kwenye vyakula au vinywaji. Na kuvaa aproni safi. Meza iliandaliwa kiustadi, sio kutupia sahani na vijiko. Usingekuta mabakuli yakuoshea mikono hapo mezani. Kulikuwa na sinki ya kuoshea mikono hapohapo kwenye chumba cha kulia chakula na sabuni maalumu yakuoshea mikono, na taulo dogo likiwa limening’inia pembeni ya hilo sinki. Na taulo hilo lilikuwa likibadilishwa kwenye kila mlo. La asubuhi sio la mchana au usiku. Mara tatu kwa siku, mataulo hayo yakukaushia mikono yalikuwa lazima yabadilishwe.  

Kila kitu hapo mezani kilikuwa kikipangwa kwa  mtindo ambao ilibidi na Tunda kufundishwa. Sio vijiko vinawekwa tu. Kulikuwa na upande maalumwa kuweka vijiko, glasi  za juisi, na napkins.  Na ilikuwa lazima vipangwe hivyo ndipo  wakaribishwe  mezani. Msichana wa kazi aliyaelewa majukumu yake, hapakuwa na kukumbushana au kuitana hovyohovyo. Usingesikia mtu anapayuka eti kuitana hovyohovyo humo ndani. Hapana. Kila kitu kwa wakati na  mpangilio mzuri na msichana wa kazi alilijua hilo. Ukisikia unaitwa, inamaana hujatimiza jukumu lako. Kwa hiyo sio kitu kizuri. Au ni dharula tu. 

Kuna nguo zilifuliwa na mashine ya humo  ndani,  nyingine  Tunda  alifundishwa ni zakuandaa na kumpa  dereva kwa ajili ya kupeleka dry  cleaner. Kila chumba kilipangiliwa.  Wakishafua, Tunda na msichana wa  kazi, waliingia vyumbani mwao  nakuanza kupangilia nguo kifasaha.  Vitanda vilikuwa vikitandikwa na  vyumba kusafishwa kila siku kana  kwamba ni hotelini. Wakifutia taulo  mara moja, basi wakiondoka, Tunda au  msichana wa kazi wakati wakusafisha,  walikusanya mataulo yote na kwenda  kufuliwa. Ila mashuka yalikuwa  yakibadilishwa siku ya jumanne,  alhamisi na jumamosi. Vyumba vyote.  Kila kitu kilifanywa kwa siku yake na  saa yake. Hapakuwa na mvurugano. Tunda akaendelea, akaunga tela  kutumika humo ndani.   

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

     Wote walikuwa kwenye furaha siku hiyo walipokuwa wakienda uwanja wa ndege kumpokea kaka yao Joe, mtoto wa baba yao mkubwa aliyekuwa ametoka masomoni nchini Canada, anarudi nyumbani kwa likizo ndefu. Walipendana sana na kaka yao huyo  na kila wakati aliwaletea zawadi mbali mbali mabinti hao wawili.  Kama kawaida Tunda aliachwa nyumbani pamoja na msichana wa kazi. Ilipofika usiku sana, walirudi  wakiwa wamejaa vicheko. Tunda  alisikia wakipanga mipango ya kumkaribisha huyo kaka yao siku ya jumapili. Hakutegemea kuwaona wakirudi bila huyo mgeni, kwa shamrashamra walizokuwa nazo wakati wakienda uwanja wa ndege. 

    Kumbe Joe mwenyewe alikuwa akiishi na wazazi wake Mbezi Beach ambako  walifanya na tafrija fupi mara baada ya kumpokea kijana wao“Mimi nahisi amenipenda bwana!”  Tunda alimsikia Sera na mdogo wake wakiongea. “Kwani anasoma na Joe darasa moja?” “Hapana, Joe  ameniambia yeye yuko mwaka wa mwisho.” “Acha utani Sera!” Sera alikuwa mwenye furaha sana. Aliendelea kucheka mfululizo. “Nimemuomba Joe aje naye jumapili.” Umeuchinja dada yangu, kijana wakizungu!” “Akija nataka nimbane mpaka aingie kwenye anga zangu. Nitapata wapi mwanaume kama yule?” Sera akasikika.

    “Unajuaje labda ana mtu wake?” “Hapo sasa!” “Kwa nini hujamuuliza Joe?” “Joe mwenyewe hamfahamvizuri. Anasema wamekutana naye tu chuoni siku za  mwisho. Alimsikia tu akipita huku  anazungumza kwa simu kwa lugha ya kiswahili  huko chuoni. Ndio akamsimamisha na kumuuliza kama anatokea nchini Tanzania. Wakazungumzkidogondio akamwambia na yeye akimaliza mitihani anakuja huku Tanzania. Ndio akatangulia kuja huku Tanzania mara baada ya mitihani yake kuisha akamuacha Joe anamalizia mitihani yake. Pale uwanja wa ndege alikuja ili wafahamiane zaidi kwa huku Tanzania.” Alieleza Sera. 

    “Kumbe! Basi hakuna kumlazia damu. Msisitize Joe aje naye.” “Kesho nampigia Joe kumsisitiza. Niliona wakibadilishana namba za simu.”  “Sasa huyo Joe ametuletea nini?”  Kanipa begi, akaniambia kila kitu nilichomuagizia na zawadi zako, vyote  vipo ndani ya hilo begi. Nilipomuona  yule kaka, nikapagawa. Nikashindwa  hata  kuangalia zawadi zenyewe.”  “Na wewe unajua kupagawa vibaya! Akikukataa sasa huyo kaka mwenyewe?” “Anaitwa Net.” “Mmmh! Ushamjua mpaka jina!?” “Sio mchezo dada. Tena akaniambia ‘i’ ni silent. Akasema rafiki zake wote hata kwao wanamwita Net.” “Haya Mama Neit.” Sera na mdogo wake waliendelea kucheka huku wakigonga pale jikoni wakati Tunda anamalizia kusafisha akalale. Zilimwagwa sifa za huyo Neit. Kuanzia macho, urefu, nywele, ongea yake. Walimsifia huku wakipokezana na checho juu.   

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

     Jumapili haikuwa mbali. Kweli Joe aliwasili hapo akiwa na wazazi wake. Baba yake Joe na baba yao kina Sera au mume wa shangazi yake Tunda, walikuwa ndugu kabisa wa tumbo moja. Kaka mkubwa na mdogo. Joe au Joseph alionekana mwingi wa majivuno. Aliongea kingereza cha madoido mengii. Alivaa vitu vya gharama vyakueleweka. Aliingia jikoni na kina Sera,  hakumsalimia Tunda wala Nyange. Waliendelea kuongea wenyewe wakicheka. 

     “Yuko wapi Net?” Sera akauliza. “Leo anamambo mengi. Nitakuja naye jumatano, usijali.” “Jumatano nina vipindi mpaka jioni.” Nitakusubiri Kaz, mbona wasiwasi!?” Walizoea kuitana ‘Kaz’ wakimaanisha Cousin. {Binamu.} “Haya basi. Anaonekana anajielewa!” “Mimi simfahamu vizuri. Kwa hiyo nguvu yako tu.” Waliendelea kuongea pale jikoni kwa lugha ya kingereza huku wakicheka sana wakijifanya maridadi kumbe ni lugha ambayo hata Tunda aliweza kuizungumza na yeye kifasaha tu, utafikiri alizaliwa na yeye hukohuko nchini uingereza. Akabaki akiwasikiliza tu. 

    Mpaka anaondoka Joe na wazazi wake, hakuwa hata amemtizama Tunda usoni zaidi yakumtuma mara kadhaa akalete soda, na kumrudisha akilalamika soda aliyoletewa si aina ile, na alipoletewa aliyoitaka tena, alisema si baridi sana huku akiendelea kuongea na kina Sera, bila kumtizama Tunda aliyekuwa akimpa maagizo, akimzungusha kama tiara. “Kalete Sprite sinywi tena Coke.” AlipoletewSprite baada yakuagiza Coca Cola na kubadili mawazo, akamtuma tena. “Kalete baridi kiasi, hii baridi sana.”  Tunda alikwenda na kurudi bila hata yakupewa asante. Haikumsumbua hata kidogo, alishazoea kutumika pale nyumbani kwa shangazi yake kama punda, huku akirushiwa maneno ya kashfa.  

 

Net ndani ya Picha.

Jumatano nayo haikuwa mbali. Ilipofika jioni Tunda akiwa jikoni akasikikengele kuashiria kuna mgeni mlangoniAlienda kufungua mlango, alikuwa Joe na kijana mwingine. Tunda alijua wazi atakuwa ndio Net, aliyekuwa akitajwa mle ndani kama alumasi. Kama kawaida yake Joe alipita ndani bila hata salamu, huku akimsukuma Tunda kidogo pale alipokuwa amesimama mlangoni akisubiri waingie ndani afunge mlango. “Karibu sana Net. Hapa ndio kwa  anko wangu. Kaz zangu wameniambia  wote wapo njiani wanakuja.” Tunda alibaki ameduwaa pale mlangoni. 

Kweli Net alikuwa kama mzungu. Alikuwa na weupe uliokolea sana.  Nywele nyeusi zilizonyolewa vizuri,  lakini pia zilionekana ni za kizungu.  Alikuwa na macho ya rangi ya maji ya bahari, kama aliyevaa ‘eye contact’ za kike. Tunda alianza kumuelewa Sera, kwa nini amechanganyikiwa kwa kiasi kile. “Habari?” Kabla yakupita hapo mlangoni Net akamsalimia Tunda kwa Kiswahili fasaha kisicho endana na muonekano wake wakizungu. “Nzuri tu. Karibu ndani.” Tunda alimkaribisha ndani, kwani bado Net alikuwa amesimama mlangoni kama anayesubiri ukaribisho wa mwenyeji wao. “Asante.” Net alipita akamfuata Joe sebuleni. 

Tunda  akafunga mlango kisha akarudi jikoni. “Mbona hamna utambulisho?” Net akasikika akiuliza.  “Nimekwambia wenyewe wanakuja  wapo njiani.” “Na yule aliyetufungulia mlango?” Tunda aliwasikia wakiwa wanaongea sebuleni. “Atakuwa Beki tatu tu. Si unaelewa?” Kabla Net hajajibu Tunda akamsikia Joe akiendelea kama asiyetaka wapoteze muda hapo kwenye aina hiyo ya mazungumzo. “Achana naye, hana mpango.” Joe aliongea kuonyesha kumdharau Tunda. Akaendelea kueleza hili na kujisifu kwa lile. 

 “Utakunywa nini?”  Joe alimuuliza mgeni wake. “Hata maji.” Net akajibu. Baada ya sekunde chache Tunda akasikia mlango ukifunguliwa. Joe akapitiliza moja kwa moja kwenye friji ya hapo jikoni bila kuuliza akatoka na chupa ya maji nakurudi nayo sebuleni. Akamsikia Net akishukuru. Stori zikaendelea. 

Baada ya muda wakina Sera wakiongozanna mama yao wakaingia. Viliibuka vicheko, utani. Walikaa palepale sebuleni wakiongea na kucheka. Tunda alimsikia shangazi yake akimwita Nyange, akimtaka aandae chakula mapema kidogo sababu ya ugeni. Nyange naye alimuomba Tunda akaandae meza wakati yeye anamalizia kupakua. Walitakiwa wawahi kama nusu saa kabla ya muda wa kupangwa chakula. Tunda alitoka na kwenda sehemu ya kulia chakula, akaanza kupanga glasi, sahani, vijiko na napkins. Kama kawaida yao kila chakula lazima waandaliwe na juisi ambayo Tunda alishatengeneza. 

Nyange aliweka chakula mezani na kwenda kuwakaribisha wote mezani. Wakahamia wote mezani. Wakapakua, kila mmoja akaendelea na sahani yake. “Vipi, mbona huli Net?” Joe akamuuliza. “Nilifikiri tunasubiriana!”  “Hapa familia ndio imekamilika kaka.” Joe alijibu huku akicheka. “Na siku za jumatano dady huwa anachelewa kurudi nyumbani.” Sera akaongeza kwa binamu yake. “Karibu Net. Ujisikie upo nyumbani.”  Aliongeza  shangazi akitaka Net aendelee tu. Net alicheka kidogo kisha akajibu kistaarabu. “Unajua nishazoea hapa kwa mama, muda wakula huwa wote tunakuwa mezani, mpaka mpishi.” Kilizuka kimya kidogo. 

“Vipi? Naharibu nini? Maana namuona mama ndivyo anavyofanyna msichana wake. Nikajua ndio desturi za kitanzania. Au sivyo?” Net akauliza natabasamu. “Hapana. Ila hawa huwa wanapenda kula wamwisho.” Sera akajibu. “Hawa!?” Net akauliza tena kwa mshangao kidogo na tabasamu lakupoozea. “Hao wapishi unao wazungumzia.” “Ooh!” Net aliitikia tu hivyo na kuinamia sahani yake. Ukimya uliendelea kwa muda, ndipo Shangazi alipoanza maswali kutaka kumfahamu Net zaidi. 

Tunda aliitwa kwenda kuongeza juisi. “Chakula cha leo hakina chumvi kabisa, sijui mmepikaje!?” Samathalianza kulalamika. “Na huwa sipendi chakula cha kuongezea chumvi mezani.” Akaendelea kulalamika. “Kichukue ukiongezee chumvi kidogo halafu kiweke kwenye microwave kipate moto kama dakika mbili ili chumvi iyeyuke, ndio uniletee.” Samatha akaamrisha. Tunda aliweka chini lile jagi ya juisi iliyobaki baada ya kuwaongezea kila mtu kwenye glasi yake na kuchukua sahani ya Samatha. “Sio sasa ndio ukaweke chumvi nyingi mpaka kimshinde kula!” Shangazi yake akamtahadharisha Tunda kabla hajaondoka na ile sahani yenye chakula. Tunda akaitika na kuondoka na kile chakula na kurudi nacho jikoni. 

Baada ya dakika kama tatu hivi, akakirudishkile chakulaAkamuwekea pale mezani, mbele yake na kurudi jikoni. Baada ya muda kidogo tu, akasikia. “We Tunda! Ndio umefanya nini sasa!? Na umefanya kusudi. Nilikwambia mama, Tunda anafanyaga kusudi. Hebu onja hiyo chumvi jamani! Chakula hakiliki kabisa!” “Yaani mtoto mjeuri huyu! Hasaidiki! Hebu njoo wewe Tunda.” Shangazi mtu akaingilia. Samatha alisukuma ile sahani kwa hasira akasimama. 

“Usiende kulala bila kula baby. Subiri akupashie moto kingine.” “Si shida yake hataki nile? Mwache akile yeye sasa hicho chakula.”  Samatha akaondoka. Tunda alibaki kimya kama aliyeduaa. “Umefurahsasa?” Shangazi yake akamgeukia Tunda kwa hasira sana na kumuuliza hivyo. “Umefurahnakuuliza? Haya sasa, kula wewe, yeye akalale na njaa. Roho mbaya tu!” Tunda alichukua kile chakula na kurudi nacho jikoniAkaitwa msichana wa kazi, Nyange. 

Akaenda pale kwenye chumba cha chakula, akasimama karibu na mama  mwenye nyumba wake. “Hebu mtengenezee Samatha hata mayai na  sausage umpelekee huko chumbani  kwake na maziwa. Sitaki alale bila kula.” “Chumvi imeisha mama. Hata Tunda alikosa yakuongeza kwenye chakula cha Samatha, amepasha tu moto. Nimemwambia aje akuombe pesa, nimtume kaka akimbie dukani  akanunue tuje kumuongezea Samatha, akasema anaogopa kukuomba pesa wakati unakula. Labda unipe mimi pesa nikimbie nikafuate chumvi mara  moja nije nimpikie hayo mayai kabla hajalala.” Wote walinyamaza kimya kama waliosutwa. Kwani Samatha alimsingizia tu Tunda, chakula hakikuwa hata na chumvi.  “Kachukue pesa kwenye pochi yangu haraka. Na nilishasema sipendi  kununuliwe vitu rejareja. Andikeni vitu vyote vilivyoisha, vikanunuliwe kwa  jumla. Sio kuzunguka na kitu kimoja  kimoja huko mtaani.” Shangazi  alivunja ukimya na kubadili mazungumzo.  

Baada ya pale hapakuwa na  mazungumzo kabisa pale mezani mpaka Net aliposhukuru. “Jamani nashukuru sana kwa chakula.” “Karibu Net.” Sera alijibu. “Nyange! Nyange!” Tunda alimsikia shangazi yake akiita tena. “Hajarudi bado.” “Njoo basi wewe utoe vyombo hapa mezani.” Shangazi akaamrisha. Wote walinyanyuka pale mezani kurudi sebuleni kasoro Net, akabaki wa mwisho akimalizia juisi yake. Tunda alifika hapo mezani na kuanza kukusanya vyombo vichafu pale mezani.  “Mimi nitabebmabakuli.” Tunda alishtuka sana na kumwangalia Net kwa hofu kubwa,  akajua atamtia matatizoni tu. “Acha tu, nitamalizia.” “Wala usijali.” Net alijibu na kusimama huku akikusanya yale mabakuli yaliyokuwa yamebaki na vyakula

Sera aliposikia yale mazungumzo, akarudi pale mezani kwa haraka. “Ungeacha tu Net. Atamalizia huyo.” “Hamna shida. Nimeshiba sana. Nataka hiki chakula kilichopo tumboni kianze kusagika kabla yakwenda kulala.” Net alijibu huku akicheka.  Alimsaidia Tunda kurudisha vile vyombo vyote jikoni, Tunda akabakiwa na kazi ya kusafisha meza na kufagia chini. 

Net aliporudi tu sebuleni akaaga. “Mbona mapema kaka?” Joe akauliza. “Zitaanza simu za kuulizwa nilipo sasa hivi, ndio maana naona nipunguze huo usumbufu.” “Kumbe umeoa?” Joe  akaendelea kudadisi. “Ooh Noooo! Hahaha.” Net akacheka kidogo. “Sijao. Ni mwenye mtoto huyo! Na mama akianza kuongea kwenye simu huwa hamalizi mpaka anione sura yangu mbele yake ndipo anaridhika. Huwa hajui kukata simu.” Wote walicheka kidogo. 

“Nitawaona wakati mwingine jamani. Mama asante sana kwa kunikaribisha nyumbani.” “Karibu Net. Uje wakati wowote, sio lazima Joe awe anakuleta.” Aliongeza Shangazi. “Tena jumamosi hii tuna nyama choma. Karibuni.” “Anti mimi sitakosa. Nitakuja na Mzee mapema tu.” Joe alijibu kwa kuchangamka. “Mimi naomba nisitoe ahadi jamani. Sijui siku hiyo nitapewa kazi gani.” Net akajibu kiuungwana. 

“Wakati wowote utakapomaliza shuguli zako, wewe njoo tu Net. Nitakuwekea nyama.” Sera akadakia kwa haraka. “Kama ni hivyo basi nitakuja hata kwa kuchelewa. Maana mimi na nyama, ni marafiki wakaribu sana.” Wote walicheka, Joe na Net waliaga wakaondoka kwa pamoja. “Mbona huna raha tena wakati amesema atarudi.” Tunda alimsikia shangazi yake akiuliza hapo sebuleni walipokuwa wamebaki. Akajua anayeulizwa ni Sera. 

“Samatha ameniharibia kila kitu mama! Halafu na wewe ulishindwa nini kujizuia pale mbele ya mgeni? Umejisahau, unagomba mbele yake! Wote ametuonhovyo!”  Akasikia Sera akilalamika. “Na wewe Tunda! Hebu njoo hapa.” Tunda alishtuka sana kusikia ameitwa na shangazi yake tena kwa ukali. “Abee!” “Umetuabisha sana! Kwa nini hukutuambia kama hakuna chumvi? Ona aibu uliyotutia! Umefurahi sasa?” Tunda akabaki kimya hajui ajibu niniShangazi yake akasimama na kumpa makofi mawili ya nguvu, bahati nzuri yaliishia mgongoni. “Roho mbaya  kama shetani! Unamtaka wewe yule mwanaume?” “Ulimuona jinsi alivyokuwa akimimina juisi, mama? Taratibu ili Net amuone.” “Si nilimalaya hili! Sasa kwa taarifa yako humpati huyu mwanaume. Kama uliweza kulala na mume wa mama yako, huyu uandike maumivu. Lione jinsi lilivyo! Nitakufukuza mimi. Sijui likoje! Toka hapa.” Tunda alitaka kuondoka lakini Sera akamuwahi tena. “Na jumamosi akija umwambie ni kweli uliweka chumvi nyingi, Nyange, hakukuona wakati unaweka. Umesikia wewe Tunda?” Sera aliongea kwa ukali sana. “Sawa.” “Na ole wako usimwambie, utanikoma.” Shangazi aliongeza.

  ~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

     Mambo yanazidi kuendelea. Umri unakimbia nsiku zinasonga.Tunda huyu ni binti wa miaka 19 sasa. Yupo kwa shangazi kama mtumwa mwenye sifa mbaya sana. Anakaribia kutia doa tena kwenye mahusiano anayoyataka Sera, binti mkubwa wa

shangazi. Net amefika hapo kama rafiki wa Joe, lakini Serametokea kumpenda sana. Na ameapa kuwa naykwa gharama yeyote ile. Mama yake anaonekana kuunga mkono. Bado Net hajaeleweka sana kama yeye ni mtu wnamna gani ili kuendana naye. Imekuwa ngumu kusomeka, lakini tayari tatizo ameshakuwa ni Tunda. Wanataka kumdhibiti mapema kwa Net ambaye amemsaidia kutovyombo mezani na kutaka wawepo na wao kwenye chakula hapo mezani.

Mambo ndio kwanzaaa yameanza kwenye simulizi hii. Tunda akidhani maisha yake yamefika mwisho pale kwa shangazi yake, lakini ipo safari ndefu sana mbeleni. Kipi kitaendelea na pale kwa shangazi, na  Net ameongezeka?

Endelea kufuatilia

 

                                   Sehemu ya 6

CONVERSATION

0 Comments:

Post a Comment