Naomi Simulizi |+1 205 767 8163 |naomisimulizi@gmail.com NILIPOTEA! – SEHEMU YA 6. - Naomi Simulizi

NILIPOTEA! – SEHEMU YA 6.


Siku hiyo ya jumamosi kwa familia hiyo waliyo karibisha watu kwa jili ya nyama choma, Sara hakuwa na raha siku nzima. Hakujua baada ya 
ule mkasa wa chumvi kama Net atarudi tena pale nyumbani kwao! Kila aliyegonga kengele langoni kwao alijua ni Net. “Kwa nini na wewe hukumuomba namba zake za simu?” Samatha alimuuliza dada yake. “Tena wewe ndio unyamaze kabisa. Umeniharibia kweli siku ile!” Sera alimjibu mdogo wake kwa hasira akilalamika. “Ni mimi au Tunda!? Mimi ningejuaje kama hakuna chumvi? Alitutega makusudi ili kutuharibiaKwanza sijui kwa nini baba yake haji kulichukua!” “Nilimsikia mama akimwambia dad, alifukuzwa kazi kwa kosa la wizi. Hivi yupo nje kwa dhamana. Kina mama na ndugu zake walichanga ndio akatolewa. Kesi yake bado iko mahakamani. Ndio maana haji hapa! Nilimsikia dad akimpiga mama marufuku, eti hataki mjomba akanyagtena hapa mpaka ithibitishwe kweli kama hakuiba.” 

“Na kweli, na hivi hapa kunavyozagaa vitu vya thamani, hakawii kukwapua kitu akaondoka nacho.” Sera na Samatha wakachekaTunda aliumia sana. Alikimbilia chooni nakuanza kulia sana. Alijua ndio sababu hamuoni baba yake. Alikaa huko chooni mpaka aliposikia akiitwa na shangazi yake akaongeze bia nyingine kule wanapochomea nyama. Tunda aliosha uso wake na kujaribu kutulia. Akaenda kwenye friji iliyokuwa imewekwa pombe, akajaza kwenye sinia na kuzunguka nyuma ya hiyo nyumba ambako walikuwepo baba Sera, baadhi ya ndugu za upande wa baba Sera na marafiki zao, walikuwa wakichoma nyama. 

Alianza kugawa vinywaji huku akirudishwa ndani mara kadhaa kubadili hiki, au kuongeza kile. Nyange yeye alikuwa akisaidia kupeleka vyakula alivyokuwa akipika ndani. Ilikuwa vyakula vidogovidogo vyakulia hiyo nyama choma. Kulijaa vicheko vya kilevi, shangazi yake naye alikaa upande waliokuwepo wanawake. Walikuwa wakicheka huku wakigonga mikono karibu siku nzima. 

Ilipofika jioni ndipo Net alipoingia. Sera aliruka kama swala na kumsogelea karibu amkumbatie, lakini Net alimvunja morali. Alitanguliza kumpa mkono. “Karibu sana. Nilijua hutakuja tena!” “Nilikuwa na kazi karibu siku nzima. Nyama zimeisha nini?” Net akajibu na kuongeza swali akitabasamu. “Nilikuahidi nitakuwekea. Twende tuzunguke nyuma ya nyumba ukasalimie kwanza ndipo uje kula.” Sera alitoka kwa kupitia mlango wa jikoni akiongozana na Net. “Habari za sahizi?” Net akasalimia, Nyange alijibu lakini Tunda hakutaka hata kugeuka. Alibaki ameinamia sinki akiosha vyombo.

Moyoni alikuwa akilia sana. Baba yake ndio mtu pekee aliyemtegemea, akidhani labda siku moja angemtoa kwenye yale mateso, lakini ndiye huyo amesikia yupo matatizoni. Aliwaza mwisho wa maisha yake ni upi, bila jibu. Ilikuwa ni siku yenye kazi nyingi kwani walipata wageni wengi, na walevi. Alitumwa hiki, akipeleka anaambiwa sio hicho, ilimradi tu wao walikuwa wakifurahiaYeye, Nyange pamoja na kijana wa kazi, mara nyingi chakula chao kilikuwa hakibadiliki sana. Ugali na mtindi {Maziwa ya mgando.} Familia ile walikuwa na ng’ombe wengi sana wakisasa huko mitaa ya Goba ambapo ndipo lilipokuwepo shamba lao kubwa sana. Walikuwa wakisambaza maziwa kwenye mahoteli mengi pale mjini. Kwa hiyo maziwa ya mtindi yalikuwa  hayakauki pale kwao. Hata kupikwe nini, kilikuwa ni chakula cha watoto wa mle ndani na wazazi wao, na wageni kama siku hiyo wakipata wageni, lakini Tunda na wafanyakazi wao chakula chao ilikuwa ugali na mtindi siku zoteNa kwa kuwa walikuwa na kazi nyingi sana, siku hiyo hawakupata hata muda wakusonga ugali wao.

Wageni walikuwa wakipishana, na kila walipopika kama ni chips, au ndizi za kukaanga baada ya muda waliambiwa waongeze. Tunda alikuwa akiosha vyombo karibia siku nzima bila kupumzika, akitoka kwenye sinki anakwenda kutumwa, au kuongeza kutengeneza kachumbari.

Sera alirudi na Net kukaa ndani sebuleni. “Huwa haunywi pombe?” “Sitaki hata kuiweka mdomono.” “Kwa nini!?” Sera akauliza kwa kumshangaa kidogo. “Ni historia ndefu. Kwani wewe huwa unakunywa pombe?” Naye Net akamrudishia swali. “Huwa nakunywa Wine. Lakini  mara moja moja.” Sera alijibu huku akicheka. Waliendelea kuongea. Mara Sera akamwita Tunda. “Tuletee zile nyama.” Tunda alirudi haraka jikoni  kuleta nyama zilizokuwa zimewekwa maalumu kwa ajili ya Net. 

“Mbona nyingi hivyo!? Naomba nikapunguze jikoni.” Net akataka kusimama na ile sahani aliyokuwa ameleta Tunda. “Hapana Net, tutakula wote.” “Labda iwe hivyo.” Tunda alikuwa ameshasogeza stuli karibu yao, ndipo akaweka ile sahani kubwa iliyojaa nyama. “Ungependelea kinywaji gani?” Sera akamuuliza kwa upendo. “Maji tafadhali.” Sera alimgeukia Tunda. “Kalete maji na soda ya Sprite.” “Sprite zimeisha.” Tunda akajibu kwa heshima zote. “Si ukafuate dukani!” Sera aliongea kishari kidogo huku akijitahidi kuweka sura ya kiustaarabu mbele ya Net. “Naomba hela, ili nikafuate.” Tunda aliomba kwa upole sana kama asiyetaka kuingia matatizoni au kuharibu. 

"Kwa nini mimi nisimpelekmara moja huko dukani, ili tununue nyingi?” Net aliingilia. “Hamna haja.  Huwa anaendaga na baiskeli. Au  twende wote basi.” Sawa. Net na Sera wakasimama.  “Halafu unakumbuka ulichokuwa ukitaka kumwambia Net?” Sera akamgeukia Tunda kabla hajapotelea  jikoni. Kwa sekunde kadhaa Tunda hakuwa ameelewa. “Chumvi wewe, acha kutoa mimacho hiyo!” Samatha  aliyekuwa anapita aliingilia, ndipo Tunda akakumbuka maneno aliyokuwa  ameambiwa aje amwambie Net. 

“Samahani sana, siku ile niliweka chumvi nyingi kwenye chakula cha Samatha, lakini Nyange hakuwa  ameona, ndio maana alikuja kusema chumvi imeisha wakati chumvi  ilikuwepo, nilikuwa nimeificha.” Net  akabaki akisikiliza na mshangao kidogo usoni. Maana Tunda alikuwa ni kama anajishitaki, lakini kama aliyekuwa amewekewa maneno mdomoni. Net hakutegemea kukutana tena na mazungumzo ya chumvi ya siku ile. “Ana mtindo kuficha vitu huyu! Yaani mnaweza  kuwa mnatafuta kitu siku nzima kumbe yeye amekificha mahali. Ndio tabia  yake.” Tunda aliposikia Sera ameweka kituo tu na Net hajajibu kitu, akaondoka kwa haraka kuhofia lisije zuka jingine yeye akawa sababu. 

Alisikia wakitoka na kurudi bila hata kujisogeza hapo sebuleni. Na Sera naye hakumtaka tena yeye ndio awahudumie, akamtumia Nyange, Tunda akabakiwa na kazi za jikoni na nje mpaka wageni walipoondoka na wao, Tunda na wafanyakazi hao wawili ndio wakabakiwa na kazi ya kusafisha. 

Walianza kusafisha ile nyumba ndani na nje, kwani sheria ya pale ndani, hakuna kuonekana kitu kisichotakiwa sehemu yeyote, muda wowote na kwa sababu yeyote ile. Kila wakati vitu vilikuwa sehemu yake, tena kwa mpangilio. Iwe ndani au nje. Lazima kuwe kusafi wakati wote. Na Shangazi yake alikuwa akihakikisha hilo linafanyika bila kuzembea. Hawakuachiwa nyama hata kidogo. Alisikia shangazi yake akilazimishia wageni wao kubeba nyama hizo wakati wanapokuwwanaondoka. Wasiondoke mikono mitupu!  Sera aliingia jikoni na ile sahani iliyokuwa na nyama za Net. Niwekee hizi nyama, nitazila asubuhi na chai.

Nyangeti alipokea ile sahani. “Jamani  asanteni sana kwa chakula. Nimeshiba sana.” Net na yeye alichungulia pale jikoni na kutoa hizo shukurani zake. “Karibu tena.” Nyange yeye akajibu,  lakini kama alivyojionya, Tunda hata hakugeuka. “Tunda!” Net aksmwita na kumshtua sana Tunda. Akageuka. “Abee!” Nimesema asante kwa chakula. Naona nyama zilikuwa za upendeleo.” Net aliongeza huku akitabasamu. “Hizo nyama ni mimi nimekuwekea Net, na aliyekuwa akichoma ni dad akisaidiana na uncle, dad yake Joe. Ndizi amepika huyo mfanyakazi wa ndani. Yeye ameleta tu. Wala asijishauwe hapo!” Sera akadakia kwa jazba. Tunda alitoka pale jikoni kwa haraka sana, akaenda nje bila ya kujibu kitu.

Walimaliza usafi, Tunda akiwa anaumwa mwili mzima kwa kuzunguka siku hiyo. Hakutaka hata kula ugali aliokuwa amesonga Nyange baada yakumaliza kazi zote. Aliwaacha jikoni yeye na kijana wa kazi wakila. Yeye akaingia kuoga, kisha akajitupa kitandani. Alisikia mlango ukifunguliwa kwa nguvu. Samatha na Sera wakaingia na kuwasha taa. “Ulichokuwa ukijishaua mbele ya Net, ni nini?” Tunda hakutaka kujibu wala kuongea nao, akageukiukutani,  akanyamaza

Lilikuwa kosa ambalo Samatha ambaye ndiye alikuwa mkorofi zaidi hakutakkulivumilia. “Unaletdharau nyumbani kwetu, wewe Malaya!?” Samatha alivuta kile chandarua kwa nguvu na kutupa shuka alilokuwa amejifunika Tunda, sakafuni. Akaingia bafuni kwao akatoka na ndoo ya maji, akammwagia yote Tunda pale kitandani. “Ndio uamke sasa uanze kudeki. Mbwa wewe. Na tukuone tena unajishauwa kwa wageni wetu.” Walitoka nakumuacha Tunda amekaa pale kitandani akichuruzika maji. Alikuwa amelowa yeye na matandiko yake. Kwa jinsi alivyokuwa amechoka, Tunda alitamani alie, lakini hakuwa na  hiyo nguvu. Akabaki ameduaa. 

“Kuna nini tena!?” Nyange aliingia nakubaki akishangaa chumba kijivyotapakaa maji. Tunda hakujua hata ajibu niniAkatoka pale kitandani akichuruzika maji na kuanza kudeki usiku ule mpaka alipomaliza. Akaenda kulala kitandani kwa NyangeKesho yake Tunda alitoa godoro nje ili likauke. Aliliacha nje mpaka ilipofika jioni. 

Wakati ametoka kulianua, Sera naye akawa anaiingia na Net. “Nani  anahama tena?” Net aliuliza kwa utani. “Anakojoa kitandani huyo! Kwa hiyo ndio kazi yake ya kuanika godoro asubuhi na kuanua jioni.” Sera akajibu kwa haraka na kumfanya mdogoye,  Samatha aangue kicheko kwa sauti kama mazuri vile. Tunda alipitiliza chumbani kwao bila kujibu kitu. Moyoni alikuwa amefika mwisho, lakini hakuwa napakwenda. Aliwaza jinsi ya kujitoa kwenye ile hali bila jibu.

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

Safari za Net pale nyumbani kwa kina Sera hazikuisha. Sera alijawa furaha sana. Tunda alijitahidi kukaa mbali nao kupita kiasi. Aliacha kufungua mlango kabisa kwa kila mgeni aliyebisha hodi, na kila aliposikia sauti ya Net sebuleni alitoka kabisa ndani ya ile nyumba na kuzunguka nyuma ya hiyo nyumba na kuanza kujitafutia  vijishuguli. Safari za Net zilizidi kuongezeka. Asubuhi na jioni. Alikuja akiwa na sababu tofauti tofauti, mara amesahau simu usiku uliopita, mara kitabu chake asubuhi alipokuja kuchukua simu, mara amemletea Sera  chocolate, mara apple. Ilimradi tu apate sababu ya kuwepo kwenye nyumba hiyo. Uliongezeka ukaribu kati yake na baba yake Sera pia. Net akafahamika hapo ndani na kuheshimika kama alumasi. 

Na hakuwahkuzoelekaKila alipokuja hapo utafikiri Mungu mtu amewasili hapo nyumbani kwao. Alikaribishwa pale ndani rasmi hasa siku za jumapili, wakimtaka awe anakuja kwa chakula cha usiku au mchana, kutegemea muda wake.

Zilikuwa sikianza sifa zake Net, zilikuwa bora kuliko hata za Mungu ambaye huchelewa kujibu maombi au wakati mwingine hutoa jibu la hapana. Hapakuwahi kuwa na kijana bora hapo duniani kama Net. Na baba yao naye akaunga msafara, kumsifia Net. Na kweli Net alionekana ni kijana mtulivu, asiye na makuu.  

 

Mwaliko wa Net nyumbani kwao. Amtaka na Tunda kuhudhuria.

“Ulisema ndio unakwenda kumaliza mwaka wa  mwisho?” Baba yake Sera akauliza. “Ndiyo Mzee. Na ningependa kuwakaribisha nyumbani. Mama huwa anafanya tafrija fupi kila baada ya maombi, wakati ninapokaribia kurudi shuleni.” “Kumbe mama ni mcha Mungu eeh?” Baba yake Sera akauliza tena. “Sana.” Net alijibu huku akicheka. “Huko tusitarajie bia?” Net alicheka sana. “Hapana Mzee.” “Ni maji na juisi tu?” Baba yake Sera aliongeza kwa utani na kumfanya Net azidi kucheka. “Tutakuja.” “Karibuni wote. Hata kina Nyange wanakaribishwa.”  “Hee! Samatha alishtuka sana kisha akaanza kucheka. 

Wote wakamgeukia yeye. “Vipi?” Baba yake akamuuliza Samatha, mtoto wake kipenzi. “Nacheka huo ugeni nyumbani kwa kina Net, dady. Mpaka Nyange!? Samatha alimjibu baba yake huku akiendelea kucheka. “Ni maombi na chakula cha usiku tu. Sio vibaya wote tukiungana kumuomba Mungu kwa pamoja.” “Tutakaribia Net. Tena ndio vizuri tufahamiane na mama.” Mama yake Sera akaona avunje mzizi wa fitina, akubali tu yaishe kwa haraka.

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

     Siku hiyo ya kwenda nyumbani kwa kina Net ilipofika, nyumba hiyo ilijaa heka heka. Hakuna nguo Sera aliyoona inamfaa. Alikosa raha, nakulalamika siku nzima. Tunda ndiye aliyekuwa akipiga pasi, nakurudishwa kurudia tena na tena, akiambiwa hajanyoosha vizuri. Alijawa hasira kwa wasiwasi wa kwenda kukutana na mama yake Net.

     Jioni ilipofika, Net aliingia pale ndani. “Nimekuja kuwachukua wageni  wangu.” “Karibu sana Net.” “Asante.” Sera  alimsogelea na kumkumbatia. “Kila mtu yupo tayari?” Net akauliza. “Wote tupo tayari. Baba na mama watakuja na gari yao.” “Sawa.” Samatha na yeye akatoka. “Mimi nipo tayari. Tunaweza kwenda.” “Wengine wako wapi?” Net akauliza. “Nani tena? Baba na mama nilikwambia watakuja na gari yao.” “Nyange na Tunda?” Net akawaulizia hao wawili. Wote walikaa kimya kwa muda

    Samatha akatumia akili za haraka akajibu. “Nyange ana kazi nyingi, hajamaliza.” “Na Tunda?” Net akauliza tena. “Tunda amekataa.” Samatha akajibu tena kwa haraka. “HaiwezekanbwanaNgoja nikazungumze naye mimi mwenyewe.” Wakiwa wamepigwa na butwaa, Net alisimama  na kuelekea jikoni. “Vipi Nyange?” Wakamsikia akisalimia huko jikoni. “Safi tu. Karibu.” Tunda yuko wapi?” Sera na mdogo wake wakamsikia akiuliza tena, wakajua kijana wa kizungu amekusudia. “Atakuwa huko nyuma ya nyumba akisafisha. Nikamwite?” Nyangeta aliuliza kwa heshima kidogo. “Hapana, asante. Ngoja nimfuate mimi mwenyewe. Wewe endelea tu na kazi.” Bila kupoteza hata sekunde  Net akatoka kwa kutumia mlango wa hapohapo jikoni na kuelekea nyuma ya nyumba alipojua wazi ndipo Tunda alipo.   

Net kwa Tunda.

Net  alimkuta Tunda akimwagilia maua. “Habari yako Tunda?” Tunda  alishtuka karibia ya kuanguka. Ilikuwa ni muda mrefu sana hajamuona Net. “Samahani nimekustua.” Tunda alibaki amekodoa macho. “Leo kuna ibada nyumbani kwetu. Nakukaribisha.” Ni kama Tunda hakuwa akimuelewa kitu anachoongea. Ilikuwa kama lugha ya kichina  masikioni mwake. “Ni maombi tu na chakula. Hamna kitu kingine. Naomba tuungane pamoja.” Net akarudia kuweka msisitizo. “Hawezi kukubali huyo. Hivyo hapo anatamani tuondoke haraka aende kwa mabwana zake.” Hawakujua Sera alipotokea, ila akajibu yeye kabla Tunda hajaongea chochote, hata salamu hakujibu.  

“Na anavyopenda kuzurula huyo, kila mtaa ana  mwanaumeMpaka majibaba mazee.” Samatha aliyekuja  nyuma ya dada yake na yeye akaongeza. Tunda aligeuka haraka na kupotea pale bila yakuzungumza chochote. Alikwenda mbali kabisa na pale walipokuwa wamesimama.  Mwisho kabisa wa nyumba hiyo, tena gizani wala hakutaka kurudi ndani mpaka aliposikia  magari yote yameondoka.  

 

Sifa mbaya za Tunda kwa Net!

Wakiwa kwenye gari dada hao wawili wakaanza kumchafua Tunda vilivyo “Tunda ni Malaya, wakupindukia. Usimuone yupo pale, kashindikana kwa wazazi wake wote wawili.” “Tena hatakiwi kuonekana kwenye nyumba ya ndugu yake yeyote yule. Mama yake mwenyewe anapita kila nyumba kuonya watu wasimpokee.” “Hivi mama tu ndio kamuhurumia baba yake, ndio anamsaidia.” Walikuwa  wakipokezana kumchafua Tunda, kwa maneno mabaya bila kuchoka na wala kumpa nafasi Net yakupumua. “Heri ukae naye mbali yule. Atakuvuruga na kukuchafua sana hapa mjini.” Wakahitimisha baada ya kuzungumza mengi hata ya uongo.

“Kwani amefanya nini mpaka mama yake wakumzaa amkatae?” Ikabidi Net aulize. “Sio kumkataa tu. Nakwambia anapita kwa kila ndugu kuonya watu wasimpokee! Pale nyumbani kwenyewe alikuja kutuonya na kututahadharisha juu ya uwepo wa Tunda kwenye maisha ya watu. Lakini  baba yake alibembeleza sana ndio mama akampokea.” Samatha akajibu. “Alifanya nini?” Net akarudia swali  lake. “Yaani mpaka aibu Net!” “Kwa  nini?” “Uchafu aliofanya. Hausemeki.” “Alifanya  nini?” “Mmmhh!” Sera akaguna. 

“Alikuwa na mahusiano na baba yake wa kambo, mpaka akambebea mimba.” Samatha yeye akajibu bila woga. “Kwa hiyo alizaa naye?” Net  akaendelea kuuliza taratibu. “Subutu!  Pale alipo hata kizazi hana. Mama yake alimtega, akaenda  naye hospitalini, akamchoma sindano ya usingizi wakamkwangua kizazi chote mpaka wakatoa hiyo mimba.” Net alishtuka sana. Akawageukia.  “Hiyo habari ni ya kweli au ni kama ile ya kuzidishiwa chumvi kwenye  chakula?” Kidogo wakapoa. “Kweli Net. Wewe unafikiri aibu hiyo mama yake angeibeba vipi? Eti mwanae azae na mume wake!” Sera alijibu kwa utulivu kidogo. 

“Sijakuelewa  Sera! Inamaana unasema ni sawa kumlevya mama mjamzito, halafu ukamuua mtoto wake, tena kiumbe kisicho na hatia!? Kwa kuepuka aibu ya wanadamuKweli?” Wote wakanyamaza. Net alibadilika sura kabisa. Walimuona jinsi masikio yake yalivyobadilika rangi na kuwa  mekundi. Usoni alipooza kabisa.  Walifika nyumbani kwao, lakini wazi alionekana hana furaha. Walifanya ibada hiyo fupi wakimuombea Net na safari yake ya mwisho akiwa anaenda kumalizia mwaka wake wa mwisho, kisha wakapata chakula cha pamoja. Baada ya chakula tu Net aliomba awarudishe kwani alisema anataka kuwahi kulala, kwa kuwa kesho yake alikuwa na siku ndefu sana inayomsubiri. Wazi walijua Net hakufurahia mazungumzo yao ya mwisho.

“Tutaonana kesho?” Sera aliuliza wakati wanaingia getini kwao.  “Sidhani. Tutarudi nyumbani usiku sana.” Sera alinyamaza, huku akiwa na wasiwasi asijue kama huo ndio utakuwa mwisho wao au la. Waliingia mpaka ndani ya geti, Net alishuka kumfungulia Sera mlango, wakaona gari la wazazi wao nyuma yao nao ikiingia getini. Baba  yao aliegesha gari na kuwasogelea.

“Sasa safari ni lini Net?” Baba yao akauliza. “Bado kama siku tatu.” “Naamini tutaonana tena. Si ndivyo?” “Lazima nitakuja kuwaaga. Lakini..” Net akasita akamgeukia mama yao. “Nini? Zungumza tu Net.” Mama yao akamsogelea baada yakuona Net  amesita. “Naweza kuja kesho jioni kuongea na Tunda?” Walishtuka sana. Lakini mama mtu alijikaza. “Haina shida kabisa. Hapa ni nyumbani Net.  Unakaribishwwakati wowote.” “Asante sana mama. Basi tutaonana kesho.” Sera aliumia sana. “Nilifikiri kesho utakuwa na kazi nyingi sana!” Sera aliongea kinyonge akimlalamikia  Net. “Tutasafiri na Mama, lakini  tutarudi na ndege ya jioni. Kwa hiyo kama kwenye saa mbili naweza kuwa  hapa. Au nitakuwa nimechelewa sana?” “Hamna shida Net. Hapa ndani tunachelewa sana kulala. Karibu wakati wowote.” Mama yao alijibu na tabasamu kubwa usoni.  “Asante sana.” Net alishukuru na kuondoka.

Alimuacha Samatha na Sera  kwenye mshangao mkubwa, wakahisi  na mama yao anawasaliti. “Naomba  utangulie ndani  baba Sera, tunamazungumzo kidogo.” Mzee  akangia ndani na kumuacha mkewe na binti zake pale nje akijua nimazungumzo yao tu. “Hebu niambieni kilichojiri. Mbona sielewi tena! Kwa nini anataka kuongea na Tunda?” Walimuelezemama yao kila kitu, nakumuacha mama yao akiwaza. “Nilijua kabisa  huyu mtoto ni mkosi. Sijui kwa nini  nilimkubali!” “Sasa nitafanyaje mama?” “Usiwe na wasiwasi Sera. Huyu ni shetani niliyemfungulia mlango mimi mwenyewe na nitamtoa mimi mwenyewe.” “Lini sasa wakati Net anakuja kesho usiku kuongea naye? Tunda ni Malaya sana mama. Huwezi jua kwa kipindi hicho kifupi anaweza kumshawishi vipi Net!” Aibu, wivu na wasiwasi vilimjaa Sera mpaka usoni alionyesha.

  “Nimekwambia usijali.” Yule mama  aliwaambia kitu atakachomfanyia Tunda. Wale watoto wakafurahi sana.  “That’s why we love you mummy!” Walicheka na kugonga. “Net ndio mkwe wangu, wala usijali. Mbona atatangaza ndoa tu!” Sera alifurahi sana.  Wakaingia ndani, na kukuta Nyange na  Tunda wapo chumbani kwao. Hawakutaka kugonga. Kila mmoja aliingia chumbani  kwake kulala wakiwa wameridhika na  mipango yao kwa Tunda.  

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

~Ni nini Net anataka kuzungumza na Tunda, ambaye ameshapewa sifa zake mbaya?  

~ Je, atafanikiwa kupata muda naye?  

Shangazi ameweka mipango kabambe kuhakikisha Tunda anayemwita shetani hafanikiwi kuzungumza na Net.  Je, ni nini hicho kikubwa anataka kufanya, kiasi cha kuwatuliza wanae na kufanya walale usingizi wa matumaini yakufanikiwa kutokukutana kwa Net & Tunda?

Usikose kujua kitakachojiri kwa Tunda na Net  kijana mzuri aliyekubaliwa mpaka na wazazi  wa Sera?  Je, Sera atafanikiwa kwa Net?  Nini kitampata tena Tunda ambaye na baba yake yu matatizoni?  

Endelea kufuatilia.... 

CONVERSATION

0 Comments:

Post a Comment