Naomi Simulizi |+1 205 767 8163 |naomisimulizi@gmail.com NILIPOTEA! - SEHEMU YA 7. - Naomi Simulizi

NILIPOTEA! - SEHEMU YA 7.

  

Wakiwa kitandani mama na baba yao kina Sera, mama akaanza njama zake kwa kuanza kumdanganya mumewe. Akaanza kumwambia juu ya mipango mizuri anayofikiria juu ya Tunda mpaka akamshangaza na mumewe. “Mbona umebadilika gafla!?” “Hata nifanye nini Tunda ni damu yangu. Nimeona heri tumsaidie tu. Nitamsomesha, hata kama ni mafunzo ya muda mfupi kisha nimtafutie kazi.” Baba yake Sera akacheka. “Ingekuwa hatujatoka kwa walokole, ningesema  umelewa!” Mama Sera akacheka sana.

“Au yale maji mwenzangu uliyokuwa ukinywa ilikuwa konyagi?” Mama yake Sera akaendelea kucheka. “Pale napo kazi ipo! Nyumba imepooza, haina hata wine! Khaa! Balaa gani hili?” “Hawamalizi kuomba! Mimi niliamukufunga macho kukubali yaishe.” Walizidi kucheka kwa sauti. “Lakini yule mama ni mtanzania kabisaa, imekuaje awe na mtoto mzungu!?” “Huwajui walokole wewe! Wanahangaika hukooo, wakishindwa maisha,  ndio wanarudi kwa Mungu wanajidai wameokoka. Wanafiki tu.” Mama Sera na mumewe waliendelea kukashifu na kucheka sana, mpaka walipolala. 

Jumapili ambayo Net aliomba kufika jioni ili azungumze na Tunda.

Waliamka siku inayofuata ilikuwa siku ya jumapili. Familia hiyo hawakuwa wakiacha kwenda kanisani. Kwa hiyo Tunda na Nyange walikuwa wakiamka alfajiri kama kawaida yao kuwaandalia kifungua kinywa, na kunyoosha nguo zao ili wawahi misa ya kwanza ya lugha ya kingereza. Tunda alijitahidi kuandaa meza vizuri sana, ili kuepuka ugomvi wa asubuhi asubuhi.

Lakini ghafla hali ya hewa ikatibuka. Shangazi yake  alianza kwa kuulizia mkufu wake wa dhahabu aliokuwa amenunuliwa na watoto wake siku ya mother’s day. Ikaanza kazi ya kusakwa huo mkufu. “Kwani uliweka wapi?” Mumewe akahoji huku akiendelea kusaidia kutafuta.  “Jana wakati naenda kwenye shuguli ya Net nyumbani kwao, niliuacha hapa mezani! Tena nilitaka kuvaa dhahabu, lakini  nikaona nivae tu silver. Yaani nilinyanyua kabisa nikitaka  kuuvaa, tena niliweka mpaka shingoni, nikarudisha hapa mezani  na kuamua kuvaa silver. Tena  moyo ulisita kabisa! Najuta kupuuzia hisia zangu!” Shangazi akalalamika kwa majuto.

“Basi  muulize Tunda na mwenzie  tuliowaacha hapa ndani.” Ndicho alichokuwa akisubiria. Mumewe alipoweka tu kituo, akatoka na kuwaita wote.  Watoto wake wote walisema  waliuona huo mkufu mara ya  mwisho mezani kwa mama yao.  Ndipo baba mwenye nyumba na  yeye akapandwa na hasira . “Sasa  sikilizeni mabinti. Nautaka huo  mkufu wa mke wangu sasa hivi  kabla sijawang’oa meno. Sitaki mchezo.” Tunda na Nyange  walibaki  wametoa  macho.

 “Mmesikia?” “Mimi sijaingia tena  chumbani kwenu baba. Ni vile  asubuhi tu wakati nasafisha.  Sijarudi huko tena.” Nyangeta  akajitetea, lakini Tunda alibaki  kimya kama hakuwepo pale kimawazo. “Na wewe Tunda?” Kama  aliyeshtuliwa kutoka usingizini. “Abee!” “Mkufu wa shangazi yako  uko wapi?” Kabla hajajibu shangazi yake akamnasa kofi kubwa  sana la usoni. Tunda alipepesuka  akarudi nyuma. “Aaaaahh!”  Tunda  alisikika akigugumia maumivu huku ameshikilia uso kama unaotaka kuanguka! 

“Jizi hili mama! Ndiye atakuwa amekuchukulia mkufu  wako. Maana Nyange tumeishi  naye miaka yote hapa, mbona kusiibiwe kitu iwe sasa hivi yeye  akiwepo? Samatha akadakia.  “Nyange kalete mifuko yake  tuangalie ndani.” Shangazi akatoa amri. Nyange alikwenda na kuleta  mifuko ya Tunda. Mfuko wa  kwanza ulipomiminwa tu, ule  mkufu ukaanguka chini mbele ya  macho yao wote. “Haaa!” Kila  mtu akashtuka mpaka Tunda  mwenyewe.

Yule  Mzee  hakupoteza muda. Alichomomkanda kiunoni mwake, nakuanza  kumpiga Tunda kila mahali huku akimpiga mateke kama mbwa na  kumtukana sana. Alimpiga mpaka  jasho lilikuwa likimtoka huku  akimwambia jinsi alivyolaaniwa  na hana bahati kwenye maisha.  Kwa kuwa ndio shangazi yake alikuwa anataka kumpeleka shule lakini ameharibu kwa kumwibia.  

Tunda alikuwa kigaragazwa pale chini kama tambara bovu mpaka Nyange alipoanza kupiga yoe akikimbia nje kama mwehu akiomba msaada kwa majirani,  ndipo yule mzee alipomuachia na kuanza kumkimbizsasa Nyange, kumrudisha ndani. Nyange alimnyanyua pale chini na kumpeleka chumbani kwao. “Na asitoke huko ndani mpaka baba yake atakapokuja kumchukua. Hatuwezi kukaa na jizi humu ndani.”  Shangazi akaweka  msisitizo.

Baba yake alipigiwa simu palepale, huku akitishiwa kuwa akichelewa kidogo tu, atamkuta mwanae kituo cha polisi.  Baada ya muda mfupi sana baba yake Tunda alifika pale. Alielezwa mabaya mengi ya Tunda, na jinsi walivyomvumilia kwa muda mrefu, lakini wamefika mwisho. Yule baba hakusema chochote katika hizo shutuma ila kumuulizia mwanae. “Yuko wapi Tunda mwenyewe?”  “Huko chumbani, amejifungia kwa  aibu.” “Nimewasikia na ninaomba  radhi kwa yote aliyofanya.  Naomba mniitie, tuondoke.”  Aliitwa Nyange, nakuambiwa  akamwite Tunda.

Baada ya muda  Nyange alirudi huku akilia kwa  hofu. “Hawezi hata kunyanyukkitandani.” Baba yake akasimama kwa haraka na wasiwasi. “Kwani nimgonjwa?”  Baba  yake  akauliza  huku  akimtizama  Nyange. Nyange alishindwa  kujibu akakimbilia jikoni.  “Kuna nini dada? Tunda ni  mgonjwa?” “Kwani huwa wezi  wanafanywaje?” Mama Sera  akamuuliza mdogo wake kwa jeuri  sana. Baba yake Tunda akaonelea aende akajionee yeye mwenyewe.  Alishtuka na kurudi nyuma mara baada yakuingia mle ndani na  kumkuta Tunda hatizamiki. Alikuwa amepasuka sehemu ya juu  ya jicho iliyosababisha kuvuja kwa  damu na kulowesha uso mzima  mpaka mto aliokuwa amelalia. Midomo yake ilikuwa imepasuka  juu na chini, kila alipotoa pumzi  nje, damu zilitoka puani.  

“Mungu wangu dada! Unauwa mtoto  wangu sababu ya mkufu!? Mmekosa  utu kiasi cha kuweka mali mbele kuliko binadamu?!” Unatetea tabia chafu kama hiyo kwa kuwa na wewe ni mwizi.” Shemeji yake akadakia.  “Naomba muondoke sasa hivi ndani kwangu, na sitaki kukuona wewe wala  mtoto wako tena mkikanyaga hapa nyumbani kwangu. Nikiiona sura yako  hapa, baada ya dakika tano zijazo,  nakupiga risasi ya mguu. Toa mzoga  wako uondoke.” “Mungu atakulipa shemeji. Ipo siku mtajutia unyama mliofanya kwa mwanangu.” Yohana akambeba mwanae, Tunda na kuondoka naye.  

Hakuna Msiba Usiekuwa na Mwenzie.

 Tunda alishtuka akiwa  wodini na baba yake pembeni. “Sikuiba baba. Wamenisingizia.” Tunda aliongea kwa shida sana. “Nasikia maumivu makali sana.” Tunda aliendelea kutokwa na machozi. “Usiongee. Wamekushona shona sana huko usoni. Pumzika tu.” “Wamenising..” “Nafahamu Tunda. Nyange ameniambia kila kitu. Mungu atalipa mwanangu. Pole sana.” Tunda alipumua taratibu akigugumia maumivu, kisha akalala kwa faraja yakujua safari hii baba yake amemuamini.  

Alikuwa amevunjwa mbavu na damu  ilikuwa ikivuja kwa ndani. Mkono wake wakushoto pia ulikuwa  umevunjika  kabisa  mpaka  ulitengana na kuonekana mfupa  kwa nje kuwa imetengana. Na bega hilohilo la kushoto, lilitenguliwa. Matibabu yakaanza baada  yakufanyiwa x-ray. Akatobolewa  na kuwekewa vyuma vilivyotokeza  nje kama mshikaki. Waliambiwa  sio wakutoka pale siku za karibuni. Hilo likawa sio jambo baya.

Zikawa habari njema zaidi kwa baba yake ambaye hakujua atampeleka wapi binti huyo aliyekuwa anakaribia miaka 20Akaanza matibabu. Baba yake peke yake ndiye aliyekuwa akimuuguza bila kuchoka asubuhi na jioni alirudi pale hospitalini kumuona mwanae. Alimletea  vyakula vyakawaida. Wakati mwingine uji, wakati mwingine Tunda alijua kabisa amemletea chakula alichonunua kwa mama Lishe. Lakini hakuacha kufika hapo. Alileta juice za kuongeza damu na kumsisitiza awe anakunywa. Na kabla hajaondoka jioni, alihakikisha angalau anamnywesha hiyo juisi, ndipo anamuacha mpaka kesho yake anapomletea uji. Napo pia alikuwa akiwahi sana. Anahakikisha  anamsaidia kumpigisha mswaki, anamsaidia kunywa uji. Akiona  ameshiba vizuri, anamuongezea  tena juisi ya kuongeza damu, ndipo anamuachia nyingine pembeni na kumsihi awe anakunywa kila wakati. “Itakusaidia kuongeza damu.” Alisisitiza baba yake.

Wakati mwingine alimletea juisi za majani ambayo alisema ameambiwa na watu inaongeza damu kwa haraka. Rosella. Au matembele. Ikawa basi tu,  anamuona vile baba yake  anavyohangaika kumuuguza na hakuwahi kuzungumzia habari za ujauzito aliokuwa amepata wakati anaishi na mama yake, ila tu kumuuguza kwa juhudi zake zote.

Siku zilikwenda, madaktari  akiridhishwa na upataji wake nafuu. Swali la akitoka hapo atakwenda wapi, sio kuwa lilimsumbua Tunda peke yake, hata baba yake pia. Anampeleka wapi  binti huyo! Elimu yake ni ya darasa la pili. Ndugu aliyebaki ni yeye tu. Hata Tunda mwenyewe alizidi kukosa raha kila alipoambiwa anaendelea vizuri. Akakumbuka kuwa kwa ndugu wote amezuiliwa kwenda kuishi. Hana ujuzi wowote ule, na baba  yake hakuonekana kama anazo pesa zakumtafutia chumba kama alivyokuwa ameahidiwa na baba Tom.

Ilimbidi baba yake azungumze na uongozi wa hospitali kuomba Tunda aendelee kuwepo hapo mpaka atakapopona kabisa. Alieleza hali yake na maisha ya  Tunda kwa ujumla, ndipo akaruhusiwa kuendelea kuugulia pale akiwa anapewa chakula cha bure bila kutakiwa kuondoka, kwa sababu kwa taratibu za kihospitali alitakiwa akishawekewa vile vyuma, baada ya juma moja, arudi nyumbani. Ila kurudi hospitalini hapo kwa siku maalumu atakazokuwa amepangiwa  na daktari kuwa akifika kuonana na wataalamu na baadaye kufanyiwa lazoezi. Lakini ndipo uongozi ukamruhusu kubakia hospitalini hapo.

Ndipo maishya Tunda yakaendelea hapo hospitalini akiuguzwa kwa utulivu, huku akifikiria pakwenda baada yakutoka hapo. Hakuwahi kumsahau baba Tom na ahadi zake nzuri alizokuwa akimpa kila akimtumia. Ni kweli hakutegemea kama angemtelekeza na kutomtafuta hata kujua anaendeleaje! Akazidi kuumia kujikuta yeye ndiye aliyebaki akilaumiwa wala si baba Tom.  “Mama ameweza kumsamehe mumewe, lakini sio mimi! Tunda alizidi kuumia.

Lakini hakumshangaa sana mama yake. Alijulikana hata na ndugu zake pamoja na wazazi wake kuwa ana roho mbaya na ni mbinafsi wakupitiliza. Tokea anakuwa pale kijijini kwa bibi yake, alikuwa akisikia aliyedhani wakimsema ni dada yake anayemfuata, kumbe mama! Baba yake akaendelea kumuuguza bila kuchoka. Hakukosa kila siku asubuhi na jioni pia. 

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

 Akiwa bado hapohapo hospitalini, siku hiyo asubuhi Tunda alimuona baba yake akiingia na chupa ya uji lakini hakuwa na furaha kabisa ila wasiwasi mwingi usoni mpaka akamshtua Tuna. “Kuna nini?” Tunda akamuuliza. “Nilipata matatizo kazini. Wakanikamata  na kunifunga. Hapa nipo nje kwa dhamana. Lakini leo ndio siku ya hukumu.” “Lakini si utashinda hiyo kesi?” Tunda  aliuliza akionyesha na yeye ameingiwa hofu. “Sijui mwanangu! Lakini nikihukumiwa jela..” Yule baba akasita. “Nitafanyaje baba?!” Tunda naye akazidi kumchanganya baba yake. Nitahudumiwa na nani? Nikitoka hapa nitaenda wapi mimi!? Naomba wasikufunge.” “Usiponiona mpaka jioni usifikiri  nimekukimbia, ujue nimefungwa Tunda. Na lazima niondoke sasa hivi niwahi  mahakamani..” Tunda akazidi kulia.

Hata kama hutakaa ukaniona tena maishani, nataka ujue wewe  sio mtoto wa bahati mbaya. Mama  yako alinikimbia akiwa na ujauzito  wako, kwa sababu zake mwenyewe.  Akaenda  kumdanganya  mwanaume mwingine kuwa ile  mimba ni yake. Ulipozaliwa na  rangi hiyo na yule jamaa yake  alikuwa akijua wazi mahusiano yangu na mama yako, ila walikuwa  wakiiba tu, ndipo akamuacha  mama yako na mama yako  akaamua kwenda kukuacha kwa  wazazi wake. Siku ya kwanza  kuniona ndio na mimi ilikuwa mara  yangu ya kwanza hata kujua kama  mimba yako ilitungwa.” Hofu  iliyokuwa imemuingia Tunda,  hakuweza hata kuongea ila kulia  tu.

“Na wakati ule tunaishi wote,  unakumbuka uliondoka nikiwa  safarini? Nilimpigia simu mama  yako maana niliambiwa na mke  wangu ulitoroka nyumbani. Mama  yako akasema nisiwahi kumpigia  simu kamwe kukuulizia kwa  unyama niliokufanyia mimi na mke  wangu. Tena alinitishia na  kuniambia alikupiga picha zote  wakati  unamajeraha  tuliyokusababishia wakati tukiishi  wote. Kwa hiyo ikitokea tu  nakutafuta tena, hatasita kuniripoti  polisi. Nikaamua kunyamaza,  mpaka tena siku ile alipokuja  nyumbani kwangu tena na kuanza  kuongea kama mwehu kuwa  hakutaki  tena  kwa  kuwa  unamahusiano na mumewe, na  ulitaka kuzaa naye pia. Aliniambia  upo hospitalini amekutoa ile  mimba hataki nikupokee tena.”  Baba yake aliendelea kuongea  kinyonge.  

“Nilitamani urudi nyumbani,  lakini ndoa yangu ilishaanza kuwa  kwenye misukosuko sana.  Nilisimamishwa kazi, nikawekwa  kwenye uchunguzi. Yule mama  ndiye anatunza familia kwa sasa. Niseme ndiye anayenilisha. Nilijua  wazi asingekubali atulishe mimi na  wewe. Nilimomba dada akae na  wewe nikijua kibiashara ambacho  nilikuwa nimekianza kukifanya,  kingenilipa kidogo, ili nikutafutie  angalau chumba uanze maisha,  lakini nimesumbuka mpaka hivi leo  sijafanikiwa. Kwa hiyo Tunda,  sijawahi kukuona wewe ni mzigo,  mwanangu. Ni hivyo maisha yangu  yamekuwa kama nina laana, lakini  ningekutunza mama.” Tunda  alikuwa akilia sana.

“Lazima niondoke sasa hivi,  lasivyo nisipotokea mahakamani  nitaonekana nimekimbia kesi, au nimetoroka. Kila la kheri  mwanangu. Chukua hii bahasha  ina pesa kidogo, angalau utapata  pakuanzia ukitoka hapa. Baba  yake aliondoka na kumuacha  Tunda akiwa amechanganyikiwa  kabisa.  

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

Siku zilizidi kwenda akiwa pale  hospitalini bila baba yake kutokea, akazidi kuamini ni kweli baba yake amefungwa. Kosa alilojiapikutofanya nikukubali kuondoka pale kwa haraka, mpaka atakapopona kabisa. Na kwa kuwa hakuna mtu mwingine aliyetokea hapo hata kumjulia hali, uongozi wa hospitali ukamkubalia kuendelea kukaa pale. Akaanza kula chakula cha pale hospitalini, na kwa kuwa alikaa pale muda mrefu kidogo, manesi wengine walianza kumfahamu. Walimletea vitu vidogo vidogo vyakula.

Kwake yale yalikuwa mapumziko makubwa sana. Alipata muda  mtulivu wakula na kushiba, huku akiwaza kitu cha kufanya akitoka pale. Mbali na lugha ya kingereza aliyoweza kuiongea kifasaha, hakuwa na elimu yeyote ile. Kifaransa hakuwa mzuri sana, lakini aliweza kuongea japo chakuombea maji. Alijaliwa  mwandiko mzuri sana. Ndio hatua  ya mwisho aliyofanya kwa makini alipokuwa shuleni wakati akili  zake zimetulia akiwa kwa bibi yake. Darasa la kwanza na la Pili. Aliishia kwenye kujifunza kuumba herufi na kusoma, ndipo akapelekwa mjini na mikasa yake ya maisha ikafuata. 

“Nani ataniajiri sababu ya mwandiko?” Tunda aliendelea kuwaza akiwa pale hospitalini akiendelea kupona  na madaktari wakimpa habari  walizodhani ni njema kwake. Kuwa karibuni sana, watamruhusu. “Lazima kujua kitu chakufanya  mara baada ya kutoka hapa.” Tunda aliendelea kuwaza wakati wanamtoa vyuma vya mkono baada ya mifupa yote kuunga vizuri.   

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

         Siku hiyo akiwa ameamka hata yeye akijua wazi amepona, aliruhusiwa wakati madaktari wanapita kuwaona wagonjwa mida hiyo ya asubuhi. Tunda alikuwa amepona kabisa, aliandikiwa dawa za maumivu tu, kwani bado bega lake lilikuwa lina maumivu kiasi. Alitoka pale hospitalini akiwa kama ameshushwa kwenye sayari nyingine. Hajui pakwenda na wala hajui chakufanya. Kwani kwa muda wote aliokuwepo pale  hospitalini akitafakari hayo, hakupata jibu. Alijivuta mpaka kituo cha daladala. Akaanza kufikiria aingie kwenye daladala ya kwenda wapi. Wakati anatafakari, daladala ya Mwenge ikasimama mbele yake. Akiwa na njaa, akaamua apande ndani ya hiyo daladala ya kwenda Mwenge, atajua mbele ya safari. Akapata kiti, akakaa.  

Mwenge nako hapakuwa mbali kwa mida hiyo ambayo hapakuwa na foleni, alisikia konda akitangaza wamefika mwisho, na hakuwa hata amepata jibu la wapi pakwenda. Ikabidi tu kushuka na kuamua kutafuta sehemu ya kula. Alikuwa na pesa kidogo aliyokuwa ameachiwa na baba yake. Akasogea mpaka kwenye vibanda vya chips. Akaagiza chips yai. Alikuwa hajala hicho chakula kwa muda mrefu sana. Tokea akiishi kwa mama yake. Akajicheka akiwa amekaa anasubiria. Kumbukumbu ya vile baba Tom  alivyokuwa akimuhonga aina hiyo ya chakula ikamjia. Alichokuwa akimfanyia ni kubadili tu. Kama sio chips yai na firigisi, basi alimnunulia kuku wakukaanga. Atamfungia kwenye mifuko na kumpelekea nyumbani. Mpaka na yeye akajenga mazoea. Akibakia nyumbani peke yake,  basi ataagiza chips yai. Chuki ikazidi kujengeka kila alipokuwa akimfikiria baba Tom kituoni hapo, peke yake hajui pakwenda.

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

Tunda anatakiwa aanze maisha mapya yakujitegemea akiwa anahesabika ni tatizo la jamii. Ndugu hawamtaki, shule hana, ujuzi aliyonayo ni wa mapenzi tu. Endelea kuwa na Tunda kujua ni nini atafanya huko mtaani baada yakutoka hospitalini!?

 

Usikose Sehemu ya 8  

CONVERSATION

0 Comments:

Post a Comment