Naomi Simulizi |+1 205 767 8163 |naomisimulizi@gmail.com NILIPOTEA! - SEHEMU YA 9. - Naomi Simulizi

NILIPOTEA! - SEHEMU YA 9.

S

adiki akamtaka Tunda akae  chini. “Njoo hapa, ukae sasa  nianze kukueleza kuanzia mwanzo mpaka mwisho. Ndio  utaamini mimi na wewe  tumekusudiwa kuwa pamoja.”  Tunda akaguna na kucheka kama  asiyesadiki. Kwa kuwa kulikuwa  na pesa, akakaa. “Haya niambie  Sadiki, baba Amini!” Sadiki  akacheka. Tunda aliiona furaha ya  ajabu kwake. Sadiki aliyekutana  naye jana siye huyu wa leo. Leo  anaonekana anamtaka Tunda hata  kwa magoti!

“Kulikoni!” Tunda  akajiuliza. “Jana nilipotoka tu hapa.” Sadiki  akaanza. “Nikapata simu ya mdeni  wangu. Si unajua pesa  ilivyongumu?” Tunda akabaki  kimya akimtizama. Sadiki  akacheka. “Basi. Nikikwambia ni  mdeni, ni mdeni msumbufu kweli  kweli. Nimemdai mpaka kwa  mganga.” “Mganga!!” Tunda  akashangaa. “Ni pesa nyingi kwelikweli. Si umeona hilo begi?  Nimehangaika kupita kiasi. Ndio  babu Chonde akaniambia anaona  ipo nyota yangu itanijia. Na  ikinijia,  mambo yatafunguka.    Madeni  yangu  yatalipwa, na biashara zangu  zitafunguka.” Tunda akabaki  akimsikiliza kwa kumshangaa. 

  “Sasa nishahangaika na watu  wengi tu. Wala wewe sio msichana  wa kwanza kukukubalia. Maana  babu Chonde alisema nyota yangu  na mke wangu imefifia, tunahitaji  nyota  mpya..”  “Mimi  unanichanganya wewe Sadiki!  Unaongea mambo mengi na  mageni kwangu,  sikuelewi!”  “Tatizo una haraka Ani.” “Kwa  maneno hayo mengiii, kwa hiyo  kwa kifupi unaamini mimi ndio  hiyo Nyota?” “Kabisa. Jana  Nimetoka tu hapa kwako, mdeni  wangu. Ambaye hata sikumtafuta.  Na shida yote hii ya pesa,  kaniletea pesa yangu yote kwenye  ile baa yangu ya Sinza. Kwanza nilikuwa hata siamini wakati  anataka tukutane. Nilishakaribia  kukata tamaa. Na mimi nilikuwa  na haraka yakuwahi nyumbani  nipeleke ile zawadi uliyonipa,  lakini nikajipa moyo kumsubiri tu.”

 “Nimesubiria pale baa mpaka 7  usiku, ndio akanijia na hizi pesa.  Haya, asubuhi hii mfanyakazi  wangu  ambaye  nilikuwa  namwamini sana, anachapa kazi,  alichukuliwa kwenye baa ya  jirani, lakini ameniomba, tena kwa  magoti akitaka arudi kazini. Tena kwa mshahara  uleule niliokuwa nikimlipa mwanzoni,  wakati  kule  walimuongezea! Sasa kama wewe  sio hiyo Nyota ni nini?” Tunda  akasimama na kuondoka pale.

 “Njoo  Ani  wangu.”  “Unanichanganya tu mimi!” “Na  kwambia  mambo  yetu  yamebadilika.” Tunda akasimama na kugeuka kabla hajaingia bafuni. “Mambo  hayo, yamekubadilikia wewe na  mkeo.” “Nimekwambia na wewe  upo. Si ndio maana nimekuletea  wewe kwanza pesa yote? Nusu  zako na mimi na..” “Nyingine  zako na mkeo?” Tunda akauliza  kwa kejeli. Sadiki akacheka.  Tunda akaingia bafuni na kufunga  mlango.  “Njoo tupange mipango yetu  sasa!” Tunda akaoga na kutoka  akiwa amejifunga taulo. Alimkuta  Sadiki amesimama nje ya mlango  wa bafuni akimsubiria akampita.

“Sasa nisikilize  Sadiki.”  Sadiki  akamsogelea kwa haraka. “Si  ungenikaribisha tu bafuni  kama jana, tukaoga wote?”  “Ulivyokuwa  ukiniharakisha  nirudi hapa!” “Mambo hayaishi  Ani?” “Sasa nisikilize Sadiki.  Hutazaa na mimi, hilo moja.”  “Hata  katoto  kamoja  kakuunganisha  undugu,  Ani  wangu?” Sadiki akabembeleza.  “Hapana. Na unisikilize vizuri  kwa makini.” “Mashariti bado  yanaendelea!?” “Hakuna mapenzi  ya mabusu ya mdomoni au bila  kondom.” “Hee! Kondom si jana  tu sababu tulikuwa hatufahamini?  Lakini sasa hivi tunaingia kwenye  maagano yakudum..” “Na nani!?” Tunda akamuuliza kwa kumshangaa kabisa.

Mimi sio mkeo. Wala sitakaa kuwa  mke wa pili. Kondom ni kwa ajili  ya usalama wangu.” “Mimi  nimetulia Ani?” Tunda akakunja  uso.  “Umepafahamuje hapa wewe  mume wa mtu!? Halafu hata  sijatumia nguvu nyingi  kukutongoza, ukanileta hapa moja  kwa moja na kulala na mimi!”  “Ngoja nikurekebishe Ani. Wewe  kukuruhusu kulala na mimi sio  kwa ajili yako.” Tunda  akapandisha nyusi juu na kukunja  mikono kifuani. “Kuniruhusu!?”  Tunda akauliza kwa kushangaa. 

“Sawa nilivutiwa na wewe, lakini  ukumbuke na mimi nilikuwa nipo  kwenye mawindo yangu. Nilikuja  hapa makusudi ili kutafuta na  mimi bahati yangu. Na ndio  maana nilianza kwa kushauri  Kondom. Kumbuka Kondom  ilikuwa wazo langu. Sasa, sasa  hivi nishajua wewe ni mtu wangu  wa kudumu, nakubali tukapime,  tuendelee na maisha yetu.” “Na  wakati wewe unajaribu hiyo  bahati yako yakutafuta hiyo  ‘nyota’ yako na mkeo, kwa kila  mwanamke unayekutana naye  barabarani, unajuaje kama na  mkeo alikuwa hatafuti hiyo  ‘nyota’?” Sadiki kimya kwa muda  kama anayefikiria. 

“Hawezi.” Akamkania mkewe. “Kitakacho mshinda na yeye ni nini? Kwani mliambiwa kati yenu nyinyi wawili na mkewe, wewe peke yako ndio mleta hiyo ‘Nyota’  yenu ya ajabu!?” “Mama Amini  hawezi.” Sadiki akasikika mwenye wivu kabisa. “Acha habari za ajabu!  Kinachomshinda na yeye ni nini?  Mbona wewe umeweza? Wewe  unalala huku na hao wanawake  zako na yeye analala na vijana  huko.  Tatizo  liko  wapi?”  Akamuona anakasirika na kumshangaza kabisa Tnda.

“Kwa  hiyo wewe ndio unajiona unayo  haki ya kulala na watoto wadogo,  mkeo hana!? Nimeona vijana  wanao mfanyia kazi pale Mwenge,  na wewe umesema ile ni sehemu  moja tu. Wapo vijana wengine  anaoshinda nao kuanzia asubuhi mpaka mnakutana huo usiku mwingi. Sasa unajua kinachoendelea siku nzima kwenye hiyo hangaika yake?”  “Naomba tuyaache hayo.”  Akamuona amebadilika kabisa. 

“Sasa sikiliza masharti yangu,  ukishindwa, mlango ule pale,  ondoka. Huwezi kuja kuniua wewe  na mkeo kwa imani zenu ambazo  kwanza hata sizielewi! Wewe  kama unataka kunufaika na mimi,  na mimi ninufaike kwa masharti  yangu.” Sadiki akashtuka kidogo.  “Nakwambia mapema ili tusianze  kusumbuana baadaye. Mama  Amini sijui Sadiki ndio mkeo  mpaka kifo. Mimi tumekutana  jana, na ninajua ipo siku  utaniacha tu.” “Kwa kuwa wewe  mwenyewe hutaki kutulia na mimi.”

“Tungehalalisha ukawa mke wangu  kihalali hata mama Amini  akakufahamu!” “Hapana, na wala  usifikiri itakuja kutokea. Na kwa  kuwa nakuona umeanza kukasirika,  ondoka. Akili  zikikutulia urudi usikilize masharti  mengine. Ukishindwa, huna haja  yakurudi. Nitakuelewa kabisa.”  Tunda akasimama hapohapo na  kutoa lile taulo na kuanza  kujikausha mbele yake, akijua  wazi anamwangalia. 

“Jaribu kupunguza mashariti ili  kuwe na amani, Ani!” “Amani  itakuwepo ukiyakubali mashariti yangu. Mimi  sikulazimishi. Dogo dogo wako  wengi tu, na umetoka kuniambia mimi sio wa kwanza kupita hapa.  Ushapitisha wengi tu. Endelea,  utapata mwingine asiye na  mashariti.”  “Nimekuchagua  wewe.” “Ndio utulie, usikilize  sasa.” “Kwa nini tusiendelee na  mashariti baadaye?” Akasimama  ili amguse.  “Hapana. Acha bwana Sadiki.  Nisikilize kwanza.” Akasogea  pembeni. “Haya, nasikiliza.”  Akakubali akiwa anavua nguo na  kujitupa kitandani.

“Nitajitafutia  kwangu.  Nitajinunulia  vitu  vyangu. Ukinihitaji tunakutana  mahali.” “Haiwezekani Ani! Ni  jana tu tulipanga tutafute kwetu.”  “Naendelea. Hunimiliki kama  mkeo. Huniiti kama mtoto wako. Unaheshimu ratiba zangu kama  mimi ninavyoheshimu za kwako.  Sikufuati kwa mkeo na watoto  wako, na mimi hivyo hivyo.” Hapo  Sadiki akanywea.  “Wewe  unako pakukimbilia,  nyumbani kwa mkeo na watoto.  Na mimi nataka kwa kukimbilia.  Nyumbani kwangu. Na nikisema  kwangu namaanisha pazuri, sio  kwenye nyumba za vichochoroni  na wapangaji wengi.” “Mimi nina  wivu Ani. Kitendo chakutojua  huko uliko ni wapi na upo na nani,  utanitesa  sana.  Angalau nipafahamu unapoishi tu.”  “Unaonekana utanisumbua sana  Sadiki,  wewe!” 

“Nakuahidi sitakusumbua. Nikitaka kuja,  nitakuomba.” “Hapo mpaka  nijiridhishe na tabia zako. Lakini  mwanzoni,  hapana.”  Sadiki  akabaki kama anafikiria.  “Nakuona unahitaji  muda  wakufikiria. Nenda. Ukiafikiana  na mimi ndio urudi, ukiona  hutaweza, na huwezi mashariti  yangu, wala huna haja ya kurudi.  Nisipokuona  tena,  mimi  nitaondoka hapa, wala hutakaa  ukaniona tena.” Tunda akazidi  kumuwekea ngumu. Akawa mkali.  Gafla akajikuta yeye ndio  ameshika  kwenye  mpini.  Hakutaka kurudia kosa la  kufukuzwa kwenye nyumba kama  alivyokwisha  fanyiwa  tokea mtoto. Alikusudia awe na kwake  mwenyewe. 

“Sawa Ani. Ila naomba na wewe  unifikirie na unihurumie. Ujue  mimi nitatulia na wewe tu.” “Na  mkeo!?” “Sawa. Ila sitahangaika  na mwengine. Mashariti mengine  zaidi ya kimapenzi, legeza  kidogo.” “Naona hujanielewa au  umekataa. Acha mimi niondoke.”  Tunda akajidai anakusanya vitu  vyake.  “Hujaelewa  Ani.  Namaanisha  hapo  baadaye  utakaponisoma na kuridhika.  Ninachoomba hapa ni unipe  nafasi ya kunisoma. Sasa hivi  tuendelee  hivyo  unavyotaka  wewe.” “Nakusoma wewe sawa,  na mkeo huko? Wewe utaamua kutulia  na mimi, sawa. Je, wewe unajua mkeo amefika  umbali gani huko na hao vijana wake?  Wewe utatulia na mimi. Na yeye  anatulia na kijana wake. Haya, na huyo kijana  wake unajua na yeye anatulia na  nani huko mbali na mkeo?”  Akamuona anazidi kuumia.

“Hii ni kwa  faida yako na yangu. Ila ukiona  ngumu, basi. Huwezi kuja kuniua  mimi kizembe hivi!” “Basi mama.  Tutafuata masharti yako.” Tunda  akaweka vitu vyake chini. “Kwa  hiyo mapenzi wakati wote na  kondom, hakuna mabusu ya  mdomoni, na kwangu ni kwangu.”  “Sawa.  Ila  sitajali  kama  utanikaribisha hapo baadaye.”  Tunda hakumjibu. 

 

Maisha Mapya ya Tunda.

Tunda akaanza kujitafutia  nyumba. Sio chumba tena.  Pesa ikawa inaingia nyingi mpaka akawa haelewi. Mara kwa  mara Sadiki alikuja na pesa na  kumuachia. Simu za kubadili  maeneo kwa madalali zikawa  haziishi.  Kila  nyumba  anayoonyeshwa, ikawa haiendani  na uwezo wake. Maisha yakaendelea  palepale hotelini, yeye na Sadiki.  Lakini Sadiki akiondoka, Tunda  anaendelea na maisha zake.  Sadiki alikuwa akifika hapo asubuhi na  jioni. Wanapata muda wa pamoja,  anaondoka kwenda  kwenye shuguli zake, Tunda anaendelea na  ratiba zake. Kujinunulia vitu vya thamani na kutafuta  nyumba nzuri.

Mida ambayo  anajua Sadiki anakwenda pale  hotelini, basi na yeye anarudi  hapo.  Kula,  kulala  na  kujitengeneza ikawa kazi ya  Tunda. Mapenzi ya haja kwa  Sadiki, naye akawa anamwaga tu  pesa.  Tunda  hata  haulizi  zinapotoka anapokea tu na  kutapanya.  Baada ya kama mwezi akapata  nyumba nzuri sana. Ndogo tu ya  vyumba viwili. Kila kitu kilikuwa  humohumo ndani. Kazi ikawa ya  kujaza hiyo nyumba. Wakati  wengine wanalia njaa, pesa  ngumu, Tunda alikuwa anatafuta  matumizi. Akiwa anaishi hotelini,  akaanza kujaza nyumba yake huku  analipia kodi.

Akaanza jikoni.  Tunda aliyekwisha ishi kwenye  majumba mazuri na ya maana,  hakuwa akinunua takataka au vitu  vyakijinga.  Vyombo vyake vya chakula  vyenyewe vilikuwa ni vya maana.  Sahani  ya  Tunda  ilikuwa  ikianguka chini mpaka ivunjike,  sio rahisi. Vijiko sio vya bati.  Chuma  nzuri  yakueleweka.  Alianza kujaza jikoni taratibu.  Akaanza kupata shida na thamani za kisasa.  Alizunguka kila mahali hakuna  kochi wala, meza aliyoona inafaa  kwa hiyo nyumba yake. Ilipofika  swala la kitanda, ndio kabisa.  Alizunguka kwenye maduka ya  matajiri na masikini, hakupata kilichomvutia na kuona kinastahili kuwekwa ndani kwake. 

Siku hiyo akiwa na Sadiki hapo  hotelini  akilalamika  huku  anaangalia simu yake, akaona  picha ya jumba la mfalme wa  Arabuni. “Babe!” Akamwita  Sadiki. “Hii nyumba inavifaa  vyote ninavyotaka mimi.” “Huko  ni Arabuni, Ani!” “Kwa hiyo?  Kwani hapafikiki? Sio lazima viwe  kama hivi, lakini hawa waarabu  wanaonekana  wana  vitu  ninavyovitaka.” “Wewe hijabu  hutaki. Hata juzi nilikwambia  ujaribu kufunga, umekataa.”  “Wewe tafuta tiketi na hiyo hijabu  uone kama sitafunga, tukaenda.”  Wakacheka hapoo, Sadiki akaona ndio wakati wakuweka ombi lake  na yeye. 

“Kwa kuwa mimi nitakusindikiza  kwenye safari yako, huoni na  wewe unatakiwa kunisindikiza  kwenye safari yangu?” Tunda  akamtizama. “Nasafiri peke yangu  tu, Ani! Nakuwa kama sina mtu  wangu?” “Tatizo la hizo safari  zako hazieleweki! Nikikuuliza  unaenda wapi na kufanya nini,  hunipi majibu ya maana. Ila  ukirudi unarudi na pesa.” “Kwa  nini sasa tusiende wote safari hii  ili ukajionee mwenyewe?” Tunda akacheka. 

“Kwa babu Cha, nani tena!?”  “Babu Chonde. Au mwite tu Babu.  Na sio mbali. Ni hapo Tanga tu,  Handeni. Tena amekuwa  akikuulizia sana. Anatamani  kukuona.”  “Kwani  ananijua mimi!?”  “Si  ndiye  aliyekutabiria  na  imekuwa  kweli?” Tunda akazidi kucheka kama mazuri asielewe upana wake. “Kweli Ani. Huoni pesa  inayoingia? Unafikiri ni bure?” “Unaipata wapi sasa?” “Wewe unachangia. Sasa kabla ya safari  ya Arabuni, twende tukachukue  baraka  zake.  Nipe  muda  wakutengeneza pesa, twende  Arabuni tukiwa tumejiandaa  vizuri. Tafadhali Ani. usinikatalie.” Tunda akamtizama.  Akataka kumkatalia tena, lakini  akajirudi. 

Sadiki amekuwa akijitoa sana  kwake. Akajigeuza kuwa kama  mtumwa  kwa  Tunda.  Mnyenyekevu. Anamtumikia bila  kuchoka. Mchana na usiku. Kwa  miezi hiyo 7 waliyoishi wote hapo  hotelini, alikuwa akilipia na  kumletea pesa bila kumuuliza  matumizi.  Lakini kila  mahali,  alipotaka amsindikize, Tunda  alimkatalia. Ni kama hakutaka  wawe wanaongozana naye popote.  Sadiki alishasafiri zaidi ya mara 5.  Akimwambia anakwenda Tanga,  anaomba amsindikize, Tunda  alikuwa akimkatalia.

Kuna siku  alimfuata na kumuomba kama  atakubali  sadaka ya shukurani kwa pesa  wanazopata nakutumia bila kuuliza zinatoka wapi wala kuulizwa matumizi yake, akimtaka  amsindikize  kutoa hiyo sadaka, Tunda akamkatalia  kwa jeuri kabisa, ila siku hiyo akaona ajirudi. 

“Nakupenda Ani. Mimi ni wako.  Nimekuonyesha na kwa vitendo  mpenzi. Sina haya na wewe. Sikutengi na chochote kilicho  changu. Bado kwa muda wote huu  tumeishi pamoja umeshindwa kunipokea tu mama?” Tunda  akamuhurumia. “Sawa tutakwenda wote.” Tunda akajibu  kwa upole. Tunda huyu hata ukimuona mahali hutamtambua.  Tunda wa viwango zaidi ya  alivyokuwa kwa baba Tom.  Kwanza sasa hivi amekua binti  mkubwa. Pesa ipo, anapendwa na kudekezwa vilivyo na Sadiki.

 “Nakushukuru mama. Asante sana  Ani. Na utaona tutakavyofanikiwa  zaidi. Tena babu Chonde alikuwa  akiniambia siku tukifanikiwa  kusimama pamoja, tutakuwa  watofauti. Baraka zitaongezeka.”  Tunda akacheka kama asiyesadiki.  “Tatizo huniamini Ani!” “Nishakukubalia Sadiki. Wewe  twende popote utakapo.” “Na  mimi nakuhakikishia hutajuta. Si  unafikiri hizi ni pesa nyingi? Basi  nyingi zaidi zinakuja.” Tunda  akacheka tu. Maana hapo alipo  alikuwa na pesa, sasa akiambiwa  nyingi zinakuja zaidi!  Tunda akabaki na maswali mengi akivutiwa moyoni. “Kwamba ndio nimeaga umasikini kabisa!” Tunda hakuwa akiamini. Ikabaki fumbo ambalo aliona aache mwanya wakuja kujibiwa.

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

Sadiki  akapanga  safari.  Akaandaa mazingira yote.  Ndipo akamfuata sasa Tunda. “Naomba usibadili mawazo  Ani. Ulinihidi tutakwenda.” “Sasa  kesho nina miahadi mahali. Kwa  nini tusifanye week ijayo?” “Babu  Chonde anatusibiri! Na ameandaa  kila kitu. Kwanza hatutakaa sana.  Tunaondoka  kesho  alfajiri,  tukimalizana naye tu, tunarudi.  Tafadhali ahirisha hiyo miahadi  ya kesho, sogeza mbele kidogo  tu. Nakuomba Ani wangu.” Sadiki akaongea kwa upole  akijinyenyekeza, ikabidi Tunda  akubali akiwa na maswali mengi kuliko majibu. Lakini kwa jinsi Sadiki alivyo kwake, akaweka imani kwake.   

“Na leo tutalala wote, siondoki.”  Tunda  akacheka.  “Karibu.”  “Nashukuru.” Usiku huo aliokuja  Sadiki,  hakuondoka  kurudi  nyumbani kwa mkewe. Walipata  muda mzuri sana na Tunda. Tunda  naye akawa kama analipa fadhila  kwa wema wake wakupitiliza.  Alimuhudumia na kumuenzi,  mpaka  Sadiki  akafurahia.  Kulikuwa na utulivu wa aina yake  usiku huo. Tunda akapunguza  kiburi akamuhudumia vilivyo bila kelele. Na Sadiki naye akamtendea haki kimapenzi. Tunda mwenyewe alifurahia wakati wao wapamoja. 

Asubuhi ya saa 11 alfajiri, Tunda  na Sadiki wakaondoka jijini Dar,  wakielekea Handeni, Tanga.  Alichojua ni wanakwenda kwa  babu Chonde.  Kutambulishwa, na kukutana na  huyo babu aliyemtabiria. Kwa  kuwa walikuwa na usiku mzuri,  njiani walikuwa na wakati mzuri sana.  Wakiongea na kucheka. Gari ya  Sadiki ilikuwa nzuri sana. Ilitangaza uwezo wa kifedha wa Sadiki vilivyo. Safi na nzuri hata ndani imetulia. Kubwa  na ipo juu. Japokuwa walikuwa  wakiingia ndanindani sana. Vijiji  vya ndanindani huko Handeni  ambako hapakuwa hata na  barabara yakueleweka, lakini  Tunda  hakuwa  akilalamika.  Mitingishiko ilikuwa midogo tu.  Vicheko  vikatawala na Tunda kupata muda wa kumuonyesha Sadiki umaana wake kwake. Akamwaga sifa nzuri jinsi alivyo dume haswa hata kitandani, akampamba kwa mengi, ilimradi tu kumfurahisha Sadiki,  mpaka  walipofika na Sadiki akawa amelewa sifa vilivyo.

 “Pole na safari mama.” Sadiki  aliongea wakati akimfungulia  mlango kwa upendo huku akimfungua na mkanda. Tunda akazidi kucheka. “Asante, pole na wewe. Ninavyopendwa leo, mpaka naingiwa wasiwasi!” Tunda akaongeza nakumfanya Sadiki acheke sana. “Mimi nakupenda siku zote, ni wewe tu ndio umechagua leo kuyaona mapenzi yangu kwako.” Wakaendelea kuongea wawili hao, wakiwa wameegesha gari nje ya nyumba ambayo Tunda akajua ndipo walipokuwa wakisubiriwa. 

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

 Tunda amepelekwa wapi? Sadiki amekuwa  mtumwa haswa kwa Tunda! Anataka nini zaidi kwa Tunda! Wapi zinatoka hizo  pesa asizoulizwa matumizi yake? Ni shukurani ipi hiyo wanatakiwa kutoa na kwa namna gani!? Babu Chonde ni nani kwa Sadiki?  Mangapi watafanya pamoja?

Mengi yatajibiwa mbeleni, Endelea  kusoma. 

CONVERSATION

0 Comments:

Post a Comment