Naomi Simulizi |+1 205 767 8163 |naomisimulizi@gmail.com Nilipotea! – Sehemu ya 11 - Naomi Simulizi

Nilipotea! – Sehemu ya 11

 

T

unda alifungua macho kama  aliyezinduka kutoka usingizini.  Bahati yao nzuri  wote  walikuwa  wamefunga mkanda. Akajiangalia na  kujaribu kupumua mara kadhaa, hakupata maumivu yeyote. Akaanza  kuangalia alipo. Bado nje kulikuwa  giza. Akajaribu kuvuta kumbukumbu  yuko wapi na anafanya nini kwa  wakati huo! Kelele za nje zikipiga  kelele juu ya ile ajali, zikamrudishia  kumbukumbu na kumfanya ashtuke  sana. Akakumbuka kuona kile  kilichotokea mbele yao na Sadiki.  “Sadiki!” Akaita kwa sauti ya juu  iliyojaa hofu huku akijaribu  kuchungulia chini kutoka kule juu  alipokuwa akining’inia. Gari ilikuwa  imelala kwa ubavu. Upande wa dereva,  Sadiki, chini, upande wa abiria, yeye  alikuwa juu. Ameshikiliwa na mkanda wa gari.

 Akamuona Sadiki bado  amekaa vile vile kwenye kiti chake,  amefunga mkanda. Lakini kichwa kipo  kifuani kama kilichoshikiliwa na ngozi  tu iliyokuwa chingoni ikavutwa mpaka  karibu na tumbo.  Tunda alishtuka sana na kuaanza  kupiga kelele kwa hofu. Uzuri uso  ulikuwa umegeukia kwengine, lakini  aliona kichwa kikiwa kimening’inia na  kushikiliwa na ngozi ndefu. Inamaana  mifupa ya shingo ilikatika kabisa kwa  ndani! Tunda aliendelea kupiga kelele  huku akirusha miguu. “Wapo hai!  Wapo hai!” Akasikia sauti kutoka nje,  na mtu akirukia kwenye gari.  “Nisaidieni jamani. Niokoe!” Tunda  aliendelea kupiga kelele kwa hofu.

“Tulia usijitingishe. Gari imekaa  vibaya. Unaweza kuniangusha na mimi  au na wewe kujidhuru zaidi.” Ilikuwa sauti  kutoka nje. Tunda akajaribu kutulia  huku anaficha uso asimuone Sadiki.  Yule mtu akafungua mlango kwa shida  huku akijitahidi asije tumbukia mle  ndani ya gari. Bado Tunda alikuwa  ameshikiliwa na mkanda. “Jaribu  kufungua mkanda kwa mkono mmoja,  mkono mwingine nipe mimi ili usije  kutoka kwenye kiti.” Yule mtu alikuwa  amelala, huku anamchungulia Tunda  ndani na kumpa hayo maelekezo.

Mpo wa ngapi huko ndani?Wawili, lakini naona mwenzangu  shingo imekatika kabisa. Kichwa  kinaninginia. Naomba nitoe  tafadhali. Tunda aliendelea kulia kwa  sauti ya juu na ya kupaniki. “Sasa  usipaniki na wewe unaweza kuanguka,  ukatua kwenye chuma kikakutoboa.  Fuata maelekezo ukiwa umetulia tu, utatoka tu salama.”  Yule  kijana alizungumza naye kwa kutulia.  Unahisi umebanywa popote? Sitaki  nikuvute, nikakuumiza.” Akasikika mwenye uelewa ana anachofanya. Hapana  kaka yangu. Naomba nitoe tafadhali.  Nivute tu. Tunda aliongea kwa hofu  huku akiendelea kulia, asiamini kama  ule ndio mwisho wa Sadiki.

Alimvuta. Tunda akatoka akiwa  ameshikilia pochi yake kubwa  aliyokuwa ameipakata muda wote,  yenye vitu vyake vyote. Lakini  hakuwa na viatu. Alikuwa amevaa  sendozi ambazo alizivua wakati  anapiga mateke ndani ya hilo gari.  Alipotolewa  tu  pale,  kama  aliyechanganyikiwa akaanza kukimbia  katikati ya watu walioanza kujaa pale.  Wakashangaa kidogo, akili zikarudi  kwenye gari ambako walijua yupo mtu    mwingine na pengine kuna vitu vya  thamani ndani. Wengine wakaanza  kuingia mtaroni lilipokuwepo limenasa  hilo gari ili kujaribu kuiba vitu ndani  ya hiyo gari ya Sadiki.

“Jamani tuweni  wastaarabu. Tuokoe maisha.” Mmoja  wao aliongea. Mmeshasikia aliyebaki  huko amekufa. Kufa kufaana kaka.Watu wakaanza kufungua milango  kujaribu kutafuta vitu vya ndani na  wengine walijaribu hata kung’oa vioo  na vifaa vingine vya hilo gari, ilimradi  tu kujinufaisha na hiyo ajali.  Hawakuishia hapo, wakaanza kupekua  maiti ya Sadiki mwenyewe kuona  kama anavitu mfukoni. 

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

Tunda alikimbia kama  aliyechanganyikiwa. Alivuka barabara  akipishana na magari asubuhi  hiyo,  bila  kujielewa.  Alikimbia akilia, mwishoe akaenda  kusimama mataa ya Shekilango akiwa  anahema. Alisimama pale akiwaza  huku akilia. “Sadiki!” Hakuwa  akiamini kama mwili wa Sadiki aliouacha kwenye gari ndiye Sadiki  yule waliyekuwa wakiongea na  kucheka muda mfupi sana uliopita.  Tunda hakupoteza muda. Akavuka  barabara kama anaelekea Sinza,  alitembea  huku  akilia  mpaka  akakutana na taksii imepaki nje ya baa,  alfajiri hiyo. Akamsogelea yule  dereva, akamsalimia huku amejawa  machozi, akaomba imrudishe kwenye ile hoteli waliyokuwa wakiishi na  Sadiki.

Njia nzima alikuwa akiendelea  kulia. Alilia Tunda nakushindwa  kujisaidia. Hofu ilimtawala, asiamini  ni nini kinamtokea. Pale hotelini  walikuwa wameacha baadhi ya vitu  vyao. Sio vingi, lakini kwa kuwa yeye  alijua jioni wangerudi, pengine  wangelala au kila mmoja angekwenda  kwake, hakubeba mzigo mkubwa zaidi  ya hiyo pochi aliyokuwa ameshikilia  hapo.  Dereva alimshtua kumwambia wamefika,  Aliponyanyua uso kuangalia nje ni kweli walikuwa wamesimama mbele ya geti  la ile hoteli. Akamlipa, na kushuka  taratibu kama anayeogopa kitu.  Alielekea moja kwa moja kwenye  chumba chao bila kupita mapokezi. 

Akafungua mlango nakuwasha taa kwa  hofu. Akajikuta yupo peke yake.  Akakusanya vitu vyote vya Sadiki  visivyo na thamani. Akafunga kwenye  mfuko na kwenda kuvitupa asubuhi  hiyohiyo. Pesa zote na vitu vyake  akatia ndani ya kibegi chake. Akaenda kulipia hicho chumba mapokezi, akaondoka  bila kusema chochote, akarudi  nyumbani kwake. 

Tunda alifika nyumbani kwake  nakuanza kulia msiba wa yeye peke  yake. Hana wakumwambia, hana  wakulia naye. Inamaana starehe ndio  mwisho! Sadiki alikuwa ni rafiki wa  pekee kwa miaka hiyo miwili. Wawili  hao waliishi kwa kuelewana katika  starehe na ushirikina. Tunda hakuwa  na kazi, ila kutapanya pesa ya Sadiki.  Anakwenda wapi tena! Ataishije jijini hapo!  Nyumba hiyo alikuwa amelipia kodi  ya miezi mitatu kama walivyokuwa  wamekubaliana na mwenye nyumba.  Kodi ni ya miezi mitatu mitatu. Tena  kwa dola. Ina kila kitu, tena vitu vya  thamani tupu. Alijaza kuanzia mlango  wa mbele mpaka nyuma.

Na Tunda  aliweka ulinzi wakueleweka kwenye  hicho kijumba ili kwamba akisafiri,  akute mali zake salama.  Alikuwa na kijana aliyekuwa akifika  hapo kufanya usafi kwenye hiyo  nyumba. Kufua na kupiga pasi.  Chumba kimoja alikigaramia,  akakibadilisha  na  kukifanya cha viatu, pochi  na nguo zake ambazo  Tunda alimuelekeza huyo  kijana jinsi yakupangilia kwa  ustadi. Tunda hakuwa akipoteza muda  humo ndani endapo akitaka kuvaa kitu  fulani. Nguo zilipangiliwa kwa rangi,  aina, na za wakati gani. Ukiingia humo  ndani ya hicho chumba tu, utafikiri  duka la  wanawake kwenye nchi za walioendelea. Kulipangwa vizuri sana.  Nyumba safi kila mahali na kila  wakati.

Kulikuwa kumening’inizwa  manukato yaliyokuwa yakijipuliza kila  baada ya dakika kumi. Mishumaa hiyo hiyo ya harufu ya Lavender ilikuwa  imewekwa juu ya meza hata chooni  kwake. Spray za Lavender pia alikuwa  nazo kwa ajili ya kupuliza. Ukifungua  tu mlango kuingia ndani ya hiyo  nyumba, utakaribishwa na harufu  kama sio ya pafyume ya Tunda, basi  manukato  hayo  ya  Lavender  yaliyokuwa yameenea kila mahali.  Hakuwa akinunua vitu hovyo. Na  usingekuta takataka ndani ya nyumba  ya Tunda.

Kila kitu kilionyesha pesa  yakutosha. Na kwa hakika kila kitu kingekuvutia  macho kutazama, kasoro tu, hakuna  mtu aliyekuwa akiingia ndani ya hiyo  nyumba ila Tunda mwenyewe na huyo  kijana wa usafi. Walinzi waliishia nje.  Kila kitu mle ndani kilihitaji pesa ili  kuendelea kuwepo kama kilivyo.  Kuanzia yeye mwenyewe Tunda.  Mwili wake, maisha yake ni pesa  kubwa tu. Kijana anayetunza hiyo  nyumba na vilivyomo humo ndani ya  hiyo nyumba ya kupanga. Kuhakikisha  hakuna vumbi wakati wowote vyote vilihitaji pesa.  Vifaa na aina ya dawa anazoletewa Tunda kwa ajili ya kung’arisha hivyo vitu, ni pesa.  Ulinzi wa hapo nje kuhakikisha yupo  salama wakati wote, nayo ni pesa. Na  pesa yote hiyo ilikuwa ikitoka kwa  Sadiki aliyemuacha kwenye gari akiwa  amekufa. Atafanyaje? Hakujua hata  kilichoendelea kule alipoacha mwili  wa Sadiki. Akaendelea kulia tu peke  yake. 

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

Lakini hawezi kulia daima. Maisha  lazima yaendelee. Kodi ilipwe,  mfanyakazi amlipe na hiyo kampuni  ya ulinzi pia ailipe ili aendelee  kulindwa. Alikuwa na pesa ambazo  alikuwa anapewa na Sadiki. Alikuwa  na akiba yake. Lakini alichokuwa  amejiapia Tunda, ni kutotangatanga  mtaani  tena.  Alipenda  kwake,  akakusudia apatunze na daima awe na  kwake. Anafanyaje! Hilo ndilo likawa  swali lakumuumiza kichwa. Siku  zilizidi kwenda, akitumia akiba yake,  huku akifikiria chakufanya. 

Swala la biashara ndio hakutaka  kufikiria sana. Akajipa vipingamizi  yeye mwenyewe. “Biashara hiyo  naifanyia wapi? Napata wapi wateja  na mimi sifahamiki na yeyote yule!?  Kwanza kuongea sana sipendi.  Kichwa kinaniuma.” Akajiambia  Tunda akiwa peke yake na kuzidi kujikatisha  tamaa. Akaamua kutupilia mbali maswala ya biashara.

Akaanza kufikiria kumtafuta Sadiki  mwingine.  Nitapata  wapi  mwanaume anayejua kuhonga kama  Sadiki?” Tunda akajiuliza nakuzidi  kuombolea. Sadiki alikuwa akitoa pesa  bila maswali. Akimuomba pesa hana  maelezo mengi kwake, yeye anatoa tu.  Akalia bila kufikia mwafaka juu ya hatima yake.  Mwishoe akajua anapoteza tu muda.  Lazima maisha yaendelee. Kwani  Sadiki nilimpataje? Safari moja,  itaanzisha nyingine.” Akajiambia Tunda na kujipa moyo. Akafurahia na  kujipongeza kuwa na kwake.

Hakuna  mtu anayemfahamu kama alikuwa na  Sadiki, hasa ndugu za Sadiki.  Wangenipora kila kitu humu ndani,  au hata kunifukuza. Heri napata  pakufikiria  nikiwa  kitandani  kwangu.” Tunda akajipongeza kwa  hilo. Waliomfahamu yeye na Sadiki,  walijua anaitwa Ani, basi. Hawakujua  anakotokea, au anakoishi.  Kwanza hawakuwa wakionekana  pamoja  hadharani.  Na  endapo  ilipowalazimu kuwa pamoja, kama  wanakwenda kwenye baa zake, kama  hakubaki ndani ya gari, basi alishuka  naye, nakutafuta sehemu ya kukaa,  wakati Sadiki akifanya shuguli zake  kwenye hizo baa zake. Tunda kimya.  Hataongea chochote, na yeyote. Hata  muhudumu  akimsogelea, hatamsemesha kitu. 

Alijua  wafanyakazi  wote wanamfahamu mkewe Sadiki kwa hiyo hakutaka kujichanganya, ili kuepuka historia yake kujiridua kama alivyotendwa na mama yake alipomuadhibu kwa ajili ya baba Tom. Alijiapia na  kujiwekea huo usemi, “Ukitaka kula na  kipofu, usimshike mkono.” Hakuiba kwa  kelele wala fujo. Maadamu alikuwa  akipewa mapesa, akawa akimsukumia  Sadiki kwa mkewe pia, ili asije  akapokonywa akiwa anamuhitaji. Hiyo tabia hata Sadiki aliipenda sana.  Aliona Tunda anaheshimu ndoa yake.  Hapakuwa na ugomvi.

 Sehemu walizokuwa huru kuongozana naye ni kwenye club, tena usiku. Watatafuta sehemu yao watakaa. Au wakiwa  wanakwenda mziki. Basi hapo  utawaona pamoja. Au wakiamua  kutoka nje ya jiji. Wakijua hakuna  anayewafahamu, basi hapo utawakuta  hata wakitembea wameshikana mikono  na kucheka kama wapenzi wa kweli.  Lakini si vinginevyo. Katika hilo  Tunda hakuwahi kujisahau. Historia  yake ya nyuma ilimfanya asijisahau.  Akakumbuka alivyoishia hospitalini  akiwa hana mtu na wala hana pakwenda.

 ~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

Tunda akavuta pumzi kwa nguvu  nakujipongeza. Akajiona ameibuka  mshindi.  Akakaa  kutoka  pale  alipokuwa amejilaza. Akaangalia  chumba chake chote. Akafurahi  kujiona yeye ndio mmiliki na hatakaa  akafukuzwa pale, labda ashindwe  kulipa kodi. Akavuta pumzi kwa  nguvu. “Ani amekufa na Sadiki.”  Akajiambia kwa huzuni na kuanza  kulia tena. 

Atafutaye Hachoki.

Kulikuwa na club moja ipo kati ya  Osterbay na Masaki. Alikuwa  akipenda kwenda na Sadiki. Japo  hawakuwa wakinywa pombe, lakini  walipenda kuwepo huko mara kwa  mara sababu ya bendi iliyokuwa  ikitumbuiza hapo nyimbo nzuri za  zilipendwa, Sadiki alipenda sana  kwenda hapo kwa ajili ya hiyo bendi.  Walipenda mandhari yake pia.  Kuliuzwa vinywaji na chakula kwa bei  ya juu kwa hiyo walijiona wapo  salama. Hawakutegemea kukutana na  wasio na shuguli huko. Wakati wote  wanapokuwepo  hapo, walijiona wapo  salama.

Walikuwa  wamejiwekea sehemu yao. Kwenye  kona kabisa, gizani kidogo. Wakifika  hapo, watakaa wakicheka kwa muda  mrefu tu. Watakula huku wakisikiliza  zilipendwa. Basi hapo Tunda ndipo  alipokuwa akimsikia Sadiki akiimba  kwa furaha yote. Tunda alishakutana na wenye pesa zao huko. Akajua huko huko ndiko  kwakuanzia kupata wanaume. Kwa  kuwa alikuwa akijua vitu vya thamani, kwa kumuangalia tu mtu, alijua huyu  anayo pesa au la. Kuanzia saa  aliyovaa mkononi, kiatu au hata tu  shati alilovaa, Tunda aliweza kujua  kama mwanaume atamfaa au la. 

Miezi  miwili  ilikuwa  imeshapita tokea kutokea kwa ajali mbaya iliyosababisha  kifo cha Sadiki, Tunda akiwa  amejifungia tu ndani akiwaza maisha  yake. Ni nini chakufanya ili kuendelea  kujiingizia kipato chakumfanya aishi  mjini vizuri, tena pale pale kwake.  Alikuwa akiendelea kuishi kwa akiba  ya pesa iliyokuwa imesalia kipindi cha  uhai wa Sadiki. Akajua asipokuwa  mwangalifu, ataishiwa kabisa na  kufukuzwa pale anapoishi. Lazima  kuchangamka. Ndipo akili ilipomjia  kwenda kwenye ile Club kuomba kazi  ili apate mwanaume mwingine kama  Sadiki atakayemuweka mjini. 

Kwa mara ya kwanza tokea msiba wa  Sadiki, akatoka kwenda Salon.  Akabadilisha hata aina ya nywele.  Akaweka kucha nyingine nzuri kama  zake.  Akarudi  nyumbani  sasa  kujitengeneza vizuri huku akivuta  muda akitegea kufika pale mida  ambayo  alijua  hata  mmiliki  angemkuta. Hakika alipendeza. Alivaa  vizuri, akajitengeneza kutokana na  rangi yake ya mwili. Aliporidhika na  muonekano wake yeye mwenyewe na  muda ule, ndipo akatoka sasa kuelekea  kwenye hiyo club.

Dereva wa Uber  aliyefika hapo kumchukua, ilimshusha  hapo club ikiwa imeshafika saa tatu  usiku. Alikuta watu wengi tu. Ilikuwa  siku ya ijumaa. Watu wameshatoka  makazini, wanasheherekea weekend.  Alitembea  taratibu  kupita  watu  waliokuwa wamekaa nje wakisikiliza  bendi iliyokuwa ikitumbuiza taratibu  tu, akaingia mpaka ndani mapokezi.  Alimkuta mrembo aliyempokea kama  aliyemdharau Tunda. Alipomuulizia  mmiliki,  akamjibu  bila  hata  kumtizama. “Yupo ofisini kwake.”  Tunda akatulia kidogo, kisha akaomba  kwenda kumuona. Yule dada akawa kama amepatwa  wivu alipomtizama tena vizuri na kugundua Tunda amekamilika kimuonekano,  jeuri  ikaongezeka.  Akamkatalia kwa kumwambia bosi yupo busy, labda  afike hapo siku za jumatatu asubuhi,  weekend anakuwa busy sana. Hapokei  wageni.

Tunda hakubisha. Akaomba  namba zake za simu, pia akamkatalia.  Tunda hakuongeza neno, akatoka pale na kwenda kutafuta meza upande  mwingine kabisa, sio ule aliozoea  kukaa na marehemu Sadiki.  Baada ya muda mfupi tu, muhudumu  akamsogelea  kumuuliza  anataka  kinywaji gani. Tunda akatabasamu.  Akaagiza maji na kutumia akili ya  haraka sana. “Na wewe upate kinywaji  chochote, halafu mwambie Kinny,  anamgeni wake hapa.” Tunda aliongea  taratibu.  Kinyami  Unamaanisha  Kinyami, bosi mwenyewe?”  Yule  muhudumu akauliza kwa kubabaika  kidogo kwani hilo lilikuwa jina la  kwanza la mmiliki, na aliitwa hivyo na  marafiki zake wa karibu sana. Vijana  wenzake waliokuwa wakifahamiana  tokea zamani. Hata wao wafanyakazi  wenyewe  hawakuwa  wakimwita  hivyo.

“Ndiyo. Nenda kamwambia Fina anakusubiri. Na akichelewa,  nitaondoka, sitamsubiri na siwezi  kurudi tena.” Tunda akaweka msisitizo. Kwa haraka sana yule  muhudumu akaondoka pale.  Baada ya muda mfupi, yule  muhudumu na mmiliki ambaye ni  Kinny mwenyewe, wakafika pale  kwenye meza ya Tunda. Kinny  akababaika kidogo mbele ya Tunda  aliyekuwa akimtizama kwa kujiiba  huku macho yapo kwa muhudumu  aliyekuwa akiweka maji hayo kwa  kubabaika mbele ya bosi wake. Alifuta  ile chupa ya maji mara kadhaa. Kisha  akaweka glasi mbele, pembeni,  kushoto, ilimradi akawa ameshasahau  wapi aweke hiyo glasi kwa kuwa bosi  wake alikuwa akimtizama.

“Acha tu,  mimi nitamimina hayo maji kwenye glasi.” Kinyami au Kinny kama rafiki  zake wa karibu walivyozoea kumuita,  akatoa hiyo amri kwa muhudumu  wake. Akaelewa anatakiwa kupisha  hapo  kwa  haraka.  Karibu.”  Akamkaribisha Tunda, Tunda alitoa tu  tabasamu, akarudisha macho kwa  Kinny, muhudumu akaondoka. 

“Habari Fina? Sijui ni sawa au  amekosea kuniambia?” Akimaanisha  muhudumu wake  aliyekwenda kumwita. “Umepatia.” Tunda  akasimama na kumpa mkono na yeye.  “Karibu sana.” Bado alikuwa ameshika mkono wa Tunda akiuminya.  Laini kama sponji! Tunda akacheka  taratibu huku akimtizama na yale  macho yake. Kinny akajishtukia,  akaachia mkono wa Tunda kwa  haraka. Karibu ukae. Tunda akarudi kukakaa  na yeye akakaa “Mbona umeagiza maji tu wakati  weekend ndiyo inaanza?” Tunda  akacheka kidogo na kujibu taratibu. Maji yanatosha. “Karibu sana. Kwa vile alivyomuona  Kinny amebabaika mbele yake, Tunda  akabadili mawazo yakuomba kazi pale  kwenye ile club. Utizamaji ule na kushindwa kuachia mkono wake kwa  haraka, akajua ameshavutiwa naye na  ameshamthaminisha.

Akaona kuomba  kazi, nikuanzia chini sana. Uthamani  wa Tunda ukapanda kwa haraka,  ujasiri ndani yake ukapanda. Akanywa maji  kidogo.  Vile tu alivyoishika ile glasi, kucha yake  kidoleni, cheni iliyoning’inia hapo  mkononi, hata Kinny alijua anaongea  na mdada wa hali ya juu.  “Najua hatuna miahadi yeyote ile,  lakini nilitaka tuzungumze biashara.” Tunda akaanza taratibu huku akili yake ikiendelea kuchemka  kwa haraka akifikiria nini chakumwambia Kinny aliyekuwa akimsikiliza kwa makini. “Sitakuibia  muda  wako  mwingi.”  Tunda  akaendelea taratibu. Hamna neno.  Hata hivyo sina kitu chakunifunga na kunifanya  nisiwepo hapa na wewe. Una habari  gani njema?” Tunda akatoa tabasamu huku akifikiria akatazama upande  waliokuwa  wakitumbuiza.  Walipokuwa wamesimama waimbaji.  Kinny naye akageuka.

Kulikuwa na  baadhi ya watu ambao walionekana  pombe  zilishaingia  kichwani,  walisogea kucheza karibu na ile bendi.  Mmoja alifanya vituko, Tunda na  Kinny wakajikuta wakicheka kwa  pamoja. Kinny asijue cheko ile ya  Tunda ni yakuzuga tu. Yupo kwenye  kufikiria  kwa  kina,  nini  chakumwambia na kilete maana.  Akakumbuka kwenye baa ya Sadiki, ni  nini alikuwa akinunua chamuhimu na  nini hata hapo kinatumika sana. 

Akanywa maji na kumtizama Kinny.  “Unanunua  wapi  bia  zako?” Akamuuliza taratibu tu. Kinny akawa  kama anafikiria. “Mmmh! Huwa  wananiletea hapahapa kutoka  kiwandani. Vipi? Una dili nzuri nini?” “Wanakuuzia kwa bei gani? Tunda  akauliza tena. Alipomtajia, Tunda  akakunja uso. Vipi? “Mimi naweza  kukupatia kwa bei ya chini zaidi, na  ukitaka, wanaweza kukuletea pia.”  Kinny akacheka huku akimtizama. “Wapi huko kwenye neema, Fina?  “Wewe sema kama utataka. “Ila  isiwe magendo tu. Sitaki matatizo  baadaye. Kinny akatahadharisha. “Hakuna magendo. Watu haohao  wanaokuletea wewe hapa kama  wafanyakazi wa kicho kiwanda, ndio  haohao watakao kuletea ila kwa bei poa. Wanatoa hapohapo kiwandani,  tena kwa halali. Ila wao kama  wafanyakazi huwa wanauziwa kwa bei  ya chini sana, na kwa kuwa huwa  wakati mwingine ni kama wanapewa bure, basi wanakuwa na mzigo kwenye  maduka yao, wanauza kwa bei nzuri.  Kwa risiti kabisa. Wala sio wizi.”  Tunda akaongea kwa uhakika kabisa  kumuaminisha. Kinny akatabasamu. 

“Na wewe unapata kiasi gani kwenye  hiyo? Tunda akacheka kidogo. “Wewe usijali. Tunajuana na wao.” “Kwa  hiyo tukimalizana hapa na wewe,  tukaachana leo, ndio sitakuona tena?  Akauliza Kinny na tabasamu la uchu  usoni. Tunda akajua tayari, akaona  amzungushe kidogo. Usiwe na  wasiwasi. Sio wababaishaji hata  kidogo. Wakishajua ratiba yenu ni lini  mtahitaji mzigo, hata wewe huna haja  ya kuonana nao. Inakuwa wao na mtu  wako wa stoo tu.” Akajidai akili ipo  kazini.

Mbona umeanza na habari  njema, halafu unamaliza na habari  mbaya?” “Kwa nini tena? Mimi  nilijua utafurahia punguzo la bei! Tunda  akauliza huku akicheka.  “Huko kutokuonana, ndio habari  mbaya.” Tunda akacheka sana. Mimi  nilijua wewe upo busy, hupendi  usumbufu. Unaonana na watu muhimu  tu.” “Wewe umeshakuwa mtu muhimu  kwangu, Fina. Ningependa tuje kuonana tena. Huwezi jua ni nini  kitazaliwa baada ya hapa. Tunda  akacheka  na  kuinama  kama  anayefikiria.

Eti Fina? “Basi leo ni  mimi ndio nimekutafuta kwa shida  yangu. Na wewe nakupa ruksa  kunitafuta kwa wakati wako.” Kinny akacheka kwa kuridhia. “Maswala ya biashara mimi na wewe tumeshamalizana. Agiza chakula hapa, kula wakati  unanisubiria nitakuitia mtu  anayehusika na manunuzi ya vinywaji.  Panga naye kila kitu. Muelewane.  Nisubirie mimi nivute muda kidogo,  wakati nasalimiana na wateja wangu.  Halafu  nitakuja  kukuangalia  tutapanga kutokea hapo. Au una  haraka?” Hapana. Nitakusubiri Kinny.” Hiyo sauti ikamfanya Kinny  alambe midogo.  Tunda akacheka sana. Kinny wewe ni  mtundu sana. “Kwa nini tena? Na  yeye akacheka huku anasimama. “Nitarudi kukuangalia. Usije nikimbia tu. Utanikuta hapahapa. Usisahau  kuniitia mtu wa manunuzi.” “Ona  sasa! Sauti hiyo imenifanya mpaka  nimesahau.  Acha  basi  Fina!  Unanishika miguu! Tunda alizidi  kucheka, Kinny akaondoka huku na  yeye akicheka.

Alionekana ni mcheshi.  Alikuwa akipita kwenye meza baadhi  akisalimia. Tunda alimuona jinsi  anavyocheka kwa sauti huku akigonga  mikono na baadhi ya wateja.  Tunda alikuwa kazini na mahesabu makali. Akaendelea kumtizama kila  anayezungumza  naye.  Kuanzia  mkononi mpaka miguuni. Taratibu.  Akagundua anasalimiana na watu  ambao na yeye anania nao. “Huyu  mbaguzi huyu! Mbona anasalimiana na  wenye pesa tu?” Tunda aliwaza huku  akimsindikiza kwa macho.  Baada ya muda akamuona anaingia  ndani.

Tunda akaendelea kuwaza  akiwa peke yake pale mezani.  Akapanga hili na kufikiria lile.  Akamsogelea kijana aliyejitambulisha  kuwa anahusika na vinywaji. Tunda  akamwambia  akae  wazungumze.  Akaanza kumuuliza maswali kwa  makini. “Huwa mnachukua bia mara ngapi kwa juma na kwa kiasi gani?”  Yule kijana aliendelea kujibu kwa  makini. Tunda hakuonekana mshamba  au hajielewi. Alijibeba kimaana.  Unaweza kufikiria ni msomi mwenye  mipango mizito sana. Aliendelea  kumuuliza yule kijana maswali  yaliyomfanya afikirie kidogo, huku  akimtizama na kumsikiliza kisha  anaandika  kwenye  simu  yake.  Mwishowe akachukua namba yake ya  simu na kumwambia kesho atampigia. Yule kijana akashukuru, na kuondoka. 

Baada ya kama dakika 45, Kinny  akarudi. “Umechoka?” “Kelele nyingi  sana hapa kwako. Huwa sipendi sana  kelele, hasa zikiwa za muda mrefu na  mimi nikiwa kama hivi peke yangu.  Nahisi ni kama wapo wote masikioni  kwangu. Naomba nikuage, tutakutana  wakati mwingine.” Akajilalamisha kwa deko. “Basi acha  nikusindikize kwenye gari yako.” “Natumia taksii tu. “Basi naomba  bahati  ya  kukusogeza  mpaka  nyumbani.  Tunda  akacheka.  Nisogeze mpaka Mlimani City tu. “Mzee mkali nini? Tunda akacheka  huku akisimama, hakujibu hilo.  Wakatoka pale. 

Tunda aliwaza jinsi yakumuanza  Kinny kama alivyomuanza Sadiki  kwenye gari. Kinny alionekana sio  limbukeni. Mtoto wa mjini, anayejua  wanawake. Hakutofautiana sana na  Sadiki aliyembadilisha zaidi, hasa  kimavazi,  lakini  Kinny  yeye  alionekana bado kijana mdogo kidogo  halafu mjanja. Wakapanda kwenye  gari ya Kinny, akaondoa gari.  Wakajitahidi kuzungumza mambo ya  kawaida wakiwa njiani. Tunda alikuwa  amekaa  pale  huku  akimpigia  mahesabu.

Alikuwa makini sana na  kila anachojibu au kuchangia ili  asiropoke na kujichanganya baadaye.  Akawa  mchache  wa  maneno, msikilizaji mkubwa.  “Unaonekana wewe ni mtulivu sana  Fina?” “Kelele nyingi huwa  zinanichosha akili. Tunda akajibu  taratibu na tabasamu usoni. Kinny  akamtizama na kutoa tabasamu  lililoficha maneno. Tunda akacheka. “Wewe ni mtundu Kinny.” “Jamani!  Siruhusiwi kutamani? Labda uniambie  ni mali ya mtu. Tunda akacheka  cheko zuri bila kuongeza neno.  Akageukia dirishani.

“Finaaa! Hutaki kelele mwenyewe! Basi niambie nitakuona wapi?” “Si  tuko wote hapa?” “Hapa sio patulivu  Fina! Nataka na mimi nipate huo  utulivu.” Tunda akacheka sana. Hata hapa ni patulivu, ni wewe tu.” “Kwamba nina kelele? “Hapana.  Simaanishi hivyo. Namaanisha ni  wewe ndio unapadharau. Lakini pana  utulivu wakutosha kabisa. Ushindwe tu wewe mwenyewe.” “Wewe unaweza  kupata utulivu humu? “Kabisa.  Kinny akamgeukia.  Nini sasa? Mbona kama huniamini?” “Nahisi kama unanisukumia  barabarani, kuninyima kukuona tena,  au kutoonana hiyo sehemu tulivu.  Naona unanibania Fina.” Kinny akajilalamisha.

“Tatizo lako umekariri  Kinny. “Kweli?” “Kweli tena.” Tunda akamuhakikishia. Kinny asiamini na kuendelea kuuliza akicheka tu. “Lakini wewe unahisi hata hapa ni  patulivu? Sana tu. Tunda akazidi kumuaminisha. Kinny akamtizama. Wote wakacheka. “Nakupa ruksa  kunisahihisha.” “Usije ukalia tu.  Kinny akacheka sana mpaka akagonga  usukani.

“Unavyojiamini  Fina!” “Mimi  nimetoa angalizo tu. Mida hii ni ya kazi kwako! Usije ukanililia, wakati unatakiwa  kazini.” “Mimi mtoto wa kiume Fina,  silii kishamba. Tunda akamtizama, akageuka dirishani huku akicheka. “Mbona unanicheka?” “Nimefurahi  tu. “Furaha hiyo ni ya kunicheka  mimi tu. Sasa hapa lazima tumtafute  muongo nani. Naegesha gari mwisho  kabisa. Tubaki mimi na wewe.” Tunda  akamtizama tena.

“Au umeingiwa na  hofu?  Kinny  akauliza  kama  aliyemkamata Tunda. Utashindwa  wewe! Nakuhurumia. “Nimechezwa  mwenzio, tena na kina mama wa  kizanzibari,  kisha  wakanikabidhi  mke.” Kinny akajisifia, nakumfanya  Tunda acheke zaidi. Alicheka Tunda hakutegemea maneno ya Kinny.  Kama utani, Kinny akaegesha gari  mwisho kabisa alipoona hakuna  magari mengine pembeni yao.  Akatulia na kumgeukia Tunda. 

Akamuona Tunda anapitisha mkono  pembeni yake, akalaza kiti chake  taratibu huku akimtizama kwa macho  yake. “Oooohooo!” Kinny akatania  kwa kutoa huo mlio kwamba ameingia  hatarini. Baada ya dakika 2, maneno  yalimwisha  akabaki  akigugumia,  Tunda akiwa amepiga magoti kwenye  kiti chake. Akamwachia akabaki  akimtizama  vile  alivyokuwa  akiweweseka pale kitini. “Nilaze  kabisa?” Kinny akauliza huku  anababaika, asijue ashike wapi. Au  tuhamie nyuma?” Tunda akaanza  kucheka. Akachukua pochi yake. “Acha hizo Fina bwana! “Nilikuonya  usininganganie Kinny. Huu ni muda  wangu wakwenda kulala, na wewe  rudi kazini. “Daah! Akavuta kiti akakaa huku akijifunga zipu ya suruali vizuri. 

“Tafadhali usiondoke Fina.” “Hapana Kinny. Rudi kazini.” “Sio vizuri Fina! Usiniache hivi nusunusu.” Kinny akawa kama  ameshachanganyikiwa. Nimekupa  ruhusa yakunitafuta. Nipigie simu, tupange  vizuri. Wewe mtu na heshima zako,  kwa nini unataka mambo ya kwenye  gari  bwana?  Nipigie.”  Tunda  akachukua kalamu kutoka kwenye  pochi yake. Akamvuta mkono,  akaandika namba yake ya simu bila  jina kwenye kiganja cha Kinny, kisha  akafungua mlango nakutoka hapo  ndani ya gari bila kuaga. 

 ~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

Tunda tena mtaani. Safari hii ni Fina, akitafuta pesa ili kuweza kuishi mjini.

-       Je, Kinny ataweza kuvaa viatu vya Sadiki?

-       Mwisho wao ni upi?

-       Nini kitaendelea kwa Tunda aliyekusudia kufa na kupona ili aweze kuishi mjini, tena kwa kujinafasi?

 

Endelea kuwa na Tunda katika sehemu ya 12.

 

CONVERSATION

1 Comments: