Naomi Simulizi |+1 205 767 8163 |naomisimulizi@gmail.com Nilipotea! – Sehemu ya 28 - Naomi Simulizi

Nilipotea! – Sehemu ya 28

 

M

ara mama yake akaingia. “Shikamoo mama.” “Funga mlango Tunda. Watu ni wabaya.” Yule mama akakaa chini kwenye kitanda, akamvuta Aneti na kumkumbatia. “Nadai pesa yangu hawataki kunilipa. Nimetembea sana leo. Nimechoka. Aneti yupo kwenye matibabu ila madawa yenyewe ni aghali halafu anatakiwa ale chakula kingi kabla hajanywa dawa. Sasa chakula kinasumbua. Na mimi siwezi kumpa mwanangu dawa bila chakula. Nitakuwa ni kama namuua! Lakini wameniambia atapona tu.” Akaendelea.

“Kesho ni siku yangu ya kulipia umeme hapa, pesa leo sijapata hata ya kukopa. Na wameniambia nisipowapa pesa leo, watanifukuza kwenye hiki chumba mimi na wanangu. Ndugu wa baba Tom ni wakorofi sana. Kiwanja kile cha Tegeta mwisho, nimekiuza, lakini hawajanipa pesa yangu wakati nimewapa hati zote! Wananizungusha tu.”  Net na Tunda wakabaki kimya. Mama huyo hakuwa na kituo. Aliongea kwa kuunganisha.

“Wazazi wa yule binti aliyekuwa akifanya kazi hapa, akabakwa na baba Tom nao wananidai fidia. Unajua yule mtoto amekuwa kama tahira? Inaonekana baba Tom alimziba pumzi vibaya sana na kwa muda mrefu, kwa hiyo hewa ikaacha kufika kwenye ubongo kwa muda mrefu, ndiyo iliyomuathiri. Wazazi wake wananisumbua kweli! Wanataka niwatumie pesa kila wakati ili waweze kumtunza mtoto.” Yule mama akaendelea kuongea kama mwendawazimu. Aliongea mambo mengi sana kwa wakati mmoja.

          “Mama!” Tunda akamwita. “Abee!” Alitaka atulie kidogo ili amwangalie kwakuwa alikuwa akiongea huku akimbembeleza Anet kwa kumsugua mgongoni bila kupumzika, huku akimuuliza kila wakati kama anamaumivu. “Hivi na wewe alikubaka?” Akamuuliza Tunda. Tunda alimuhurumia sana mama yake. Alikaukwa midomo. Nywele hazikuendana na mwanamke aliyemuacha wakati ule. Chumba alichokuwa anakaa na wanae kilikuwa kisafi sana kama kawaida ya mama yake. Mama yake Tunda alikuwa msafi sana.

“Mmekula?” Tunda akauliza bila kutaka kumjibu mama yake. “Hatujala Tunda. Njaa inauma kweli. Unataka kututoa nini?” Tom akauliza na kumfanya Tunda atabasamu. Net hakuwa ameongea kitu chochote tangia aingie humo ndani. Alikuwa kimya kabisa akisikiliza na kushika mkono wa Tunda kama kumtuliza.

“Mnataka nikawaletee chakula humu humu ndani au mnataka twende wote?” “Naomba tutoke kidogo mama. Tumekaa sana humu ndani. Tafadhali mama yangu. Tupo na Tunda hakuna atakaye tudhuru.” Tom alimbembeleza mama yake. Kabla mama yake hajajibu kitu, wakasikia hodi mlangoni.

“Tunataka pesa ya umeme. Leo ndio tulikwambia mwisho. Unatukimbia kila siku, na ahadi haziishi! Huwezi kuendelea kuishi bure, eti sisi ndio tuwe tunakulipia! Haiwezekani” “Nakuja sasa hivi, nina wageni.” Yule mama akajibu lakini alionekana na wasiwasi mwingi sana usoni. “Muongo! Kwani wageni wanakuzuia nini kutoka na kutoa pesa? Tupe pesa bwana.” Tunda aliumia sana kuona jinsi mama yake anavyo dhalilishwa pale tena mbele ya Net!

Tunda akatoka. “Kwani mnamdai kiasi gani?” Tunda alipotajiwa hicho kiasi cha pesa ndipo alipochoka kabisa. Akatoa hiyo pesa kwenye pochi akamkabidhi yule mama, ambaye ndiye dada yake mkubwa Baba Tom.

Tunda akaamua kumwita Net nje. “Na nyinyi mnatukimbia nini?” Tom alichungulia mlangoni na kuuliza. “Hapana Tom. Narudi baada ya muda mfupi tu. Nataka tuongee kidogo.” “Nakuamini Tunda.” Tom aliongea kwa upole kama kumsihi Tunda asije kuondoka moja kwa moja. “Nitarudi Tom.” Tom akarudi ndani na kufunga mlango.

Net na Tunda wakarudi kwenye gari. Tunda akaanza kulia kwa uchungu sana mara baada ya kupanda kwenye gari. Alikumbuka mateso aliyopitia akiwa mtoto kama Anet, akimuhudumia baba Tom. Hasira juu ya uzembe kwa mama yake ilimpanda kuona wote wanateseka akiwemo humo humo ndani. “Anashindwa wapi!?” Tunda alijiuliza akiwa amejiinamia pale kwenye gari.

“Kwa kipi mno anachohangaikia na kutelekeza familia kwa kiasi hicho!?” Kwa hali aliyomkuta nayo mama yake inamaana hata mahangaiko yake ni bure! Amemkuta hana kitu, ila kudaiwa. Kwa mateso anayosababishia binti zake, basi heri angekuwa na mamilion ya pesa benki. Pesa hana, umama unamshinda na mume ndio huyo ameshindwa hata kujua mabaya yake! Ni kama alikwenda kujitonesha madonda tu pale.

“Sasa mwenzangu wewe ndio unategemewa halafu unalia!?” “Nitafanyaje Net?” “Wewe unataka nini?” “Kuwasaidia.” “Kuwasaidiaje?” Tunda akafuta machozi na kubaki akifikiria kidogo.

“Yale mazingira pale yatamfanya mama azidi kuchanganyikiwa.” “Kwani ile si nyumba aliyojenga na mumewe?” “Hapana Net. Mama alimkuta yule baba alisha jijenga. Ndio maana hata ndugu zake wana nguvu ya kumfukuza pale.” “Lakini si amezaa naye!? Anahaki na ile nyumba!” “Sasa vile unavyomuona mama, anaakili ya kufikiria? Yale mazingira pale yanazidi kumchanganya. Naona nimtoe pale ndani kwa muda mpaka akili yake itulie. Au unasemaje?” “Nakusikiliza wewe Tunda, utakavyoamua ni sawa.”

“Naomba univumilie Net. Najua nina mambo mengi! Mara nikupeleke jela kwa baba yangu, mara nimekuleta hapa tena kuna matatizo!” “Mimi nakuhurumia wewe Tunda. Naona kama mambo yamekuzidia!” “Naamini yote yatakuwa sawa. Usinikimbie tu.” “Siwezi. Mimi nipo sawa kabisa. Wewe fanya kile unachoona kitasaidia.” “Asante, lakini..” Tunda akasita kidogo.

“Nini?” “Usinifikirie mimi ni mbinafsi. Lakini sijawahi kuwa na mahusiano na mama yangu hata kidogo. Tukionana mimi na yeye ni habari mbaya tu. Ndio maana swali lake kwangu sio kama mama anayetaka kujua ninaendeleaje! Kama nimzima! Nina furaha!  Yeye kwa miaka yote tuliyopotezana akiwa ameniacha hospitalini amenitoa mimba ameniuliza, ‘hata wewe alikubaka?’ Hajauliza chochote kingine au kama ambaye hana uhakika na upande wangu na baba Tom!” Net kimya. Na yeye aliliona hilo akaamua kumezea.

“Maisha yangu yamekuwa yakutangatanga Net. Kazi yangu ni ngumu. Pale nyumbani kwangu ndio kimbilio langu pekee ninapoweza kupumzika. Mbali na kelele nyingi za jiji na huko kichwani mwangu, nikirudi pale kwangu ndio naweza kupumzisha huu mwili na kuweza hata kuamka siku inayofuata nakuendelea. Sina kimbilio.”

“Kwa mahusiano yetu na mama, na hivi alivyo, siwezi kupata utulivu kama nitampeleka pale kwangu. Wote tutaishia kuchanganyikiwa, hakuna atakayeweza kumsaidia mwenzake. Naona nimtafutie sehemu ya kuishi kwa muda hata wa siku tatu tu. Kama hoteli. Nimtafutie ambako haitakuwa garama sana. Lakini wawe wanawahudumia kwa siku tatu au tano. Wawe wanaletewa chakula, walale, Aneti amalize matibabu, ndipo nimkutanishe na mwanasheria akiwa ametulia ili ajue atamsaidiaje.”

“Nikiona itachukua muda mrefu wa yeye kurudishiwa mali zake, basi nitampangishia chumba chakuishi yeye na wanae. Lakini sio kuishi naye nyumba moja. Unafikiri nitakuwa nimefanya vibaya?” “Sawa kabisa. Nafikiri wapo kwenye hatua yakupokea aina yeyote ya msaada watakao letewa.” Net akaafiki kiingwana bila kuonyesha anapendelea yeyote, ili isije kumgeuka baadaye.

“Asante. Basi ngoja nikawachukue tuondoke nao.” “Sawa.” Net akakubali bila yakuongeza hata ushauri. Alikuwa mchache sana wa maneno. Ni kama hakujua aongee nini na kwa wakati gani. Jibu lake likawa ‘sawa’, na kuunga mkono kila hoja ya Tunda, tena kwa makini sana. Hata hivyo walizaliwa kwenye tamaduni tofauti kabisa na hali ya uchumi tofauti. Alihofia anaweza kuongeza, na kuharibu. 

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

Kitu ambacho hakuwa akijua Tunda, yupo na mtoto aliyekuzwa na mamilionea. Tena sio wa Tanzania, wa nchini Canada. Net aliyekuwa naye hapo, amebeba umilionea unaompeleka mbio mama yake na kumfanya halali akiwinda na kulinda hiyo pesa isiende sehemu isiyo sahihi. Huyo Net amebeba utajiri, akiwa nchini kwao ni mtu wakuheshimiwa sana. Hilo jina Cote linafahamika na wakuu wa nchini kwao. Ila yeye Tunda hakuwa hata na habari wala kumuhisi. Alimtambua Net huyu wa hapa. Mwenye uwezo wa kawaida na mwenye juhudi na nidhamu ya kazi.

 ~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

“Tunda!” Net akamwita kabla hajafunga mlango wa gari, akiwa ameshashuka garini. “Naomba nilipie gharama hizo za hotelini.” Tunda akabaki amesimama pale akifikiria kwa muda kama anayejishauri. “Acha tu Net. Ninayo hiyo pesa.” “Ndio unataka kumthibitishia mama yangu kuwa unajitenga na pesa zangu?” Kama aliyekuwepo mawazoni kwa Tunda. Tunda akaanza kubabaika.

“Najua una mambo mengi. Na leo tena umetoka kwa mwanasheria. Unahitaji msaada Tunda. Acha kujiumiza sababu ya mama yangu, unaishi na mimi, na utaendelea kuishi na mimi. Mama yangu hajui nina akiba kiasi gani na wala simwambii matumizi yangu. Na kuanzia jana nilipokuchumbia, mambo yangu mimi na wewe yatabakia kwetu tu. Na ukumbuke mimi sikuhongi. Majukumu yako ni ya kwangu pia.”

“Nashukuru Net. Basi nikikwama, nitakwambia.” “Hiyo ni kauli unayoirudia kila wakati ninapotaka kukusaidia, lakini hutekelezi!” Tunda akacheka. “Kwa kuwa bado sijakwama. Kweli tena. Nikikwama nitakwambia. Nisubiri, nikawachukue. Tutakuja sasa hivi.” Tunda akafunga mlango wa gari, akarudi ndani. Walikuwa wakitumia gari moja ya Net.

“Kweli, ‘Kitanda hakizai haramu’.”

Walifurahi sana kuona Tunda amerudi, tena na ahadi ya kuwatoa pale. “Asante Tunda. Hatutakaa sana hapo hotelini. Kuna mahali nadai pesa yangu. Wakinilipa tu, tutaondoka.” “Naomba usianze kuzungumzia kuondoka wakati hata hamjafika. Naomba utulie mama. Mimi sitakutaka uondoke leo wala kesho, ni mpaka mambo yako yakae sawa. Nitakupeleka kwa mwanasheria. Akisema itachukua muda mrefu, basi nitawatafutia sehemu ya kuishi mpaka upate mali zako.” “Kweli?” Yule mama hakuamini.

 “Kweli mama. Naomba wewe utulia, pata muda wakupumzika, ujipange upya.” “Ndicho ninachohitaji. Nimechanganywa kweli! Limeanza tatizo moja likafuata jingine, mchana na usiku sipumziki!” “Pole. Basi twendeni.” Walikusanya vitu vyao, wakatoka.

“Unaondoka mama Tom?” “Kama anaondoka, nachukua mimi chumba chake. Mimi na mwanangu tunabanana na shangazi. Nataka chumba cha mama Tom.” Wakaanza kubishana. Tunda akamshika mkono Aneti. “Twende Tom.” Tom alikuwa amebeba mabegi mawili. Tunda akatangulia akiwa amemshika Aneti. Akafuata Tom, mama yake akafuta nyuma. “Na ukalipe na pale dukani. Usituachie madeni.” Tunda alisikia wakimrushia maneno mama yake. “Na gengeni pia anadaiwa.” Mwengine akadakia. Lakini mama Tom hakujibu.

Walipopanda tu kwenye gari baada ya Net kuweka mizigo ndani ya gari, Tunda akamgeukia mama yake. “Ni wapi huko unakodaiwa?” “Kwa mwarabu na pale gengeni kwa mpemba. Lakini twende tu Tunda.” “Hapana mama. Isiwe ni kama unakimbia madeni. Tulipe tu.” “Ukianza kulipa hapa, hatutakaa tukaondoka dada Tunda. Kila jirani anatudai. Mimi naomba twende tu. Njaa zinauma. Mama arudi kwa wakati wake.” Tom aliongeza nakumfanya Tunda amgeukie Net.

“Nakusikiliza wewe Tunda.” “Basi tutarudi tena kesho.” Tunda akajibu. “Na hospitalini?” Net akauliza. Tunda akakumbuka jumanne ndio baba yake anapelekwa hospitalini. Akataka kuvizia kama anaweza hata kumkuta hospitalini akajua mambo yanakwendaje. “Nitafanyaje Net? Sitaki hii aibu iendelee.” “Yaliyobaki sio dharula au mambo ya haraka. Lakini kama ulivyosikia, wananjaa. Nafikiri cha muhimu nikuwapeleka kula, na wakalale. Hata jumatano mnaweza kurudi.” Net akatoa wazo, alilokubali Tunda. Net akaondoa gari.

“Unasikia baridi?” Tunda akamsikia mama yake akimuuliza Aneti kwa upendo. Walikuwa wamekaa kiti cha nyuma, Tunda amekaa mbele, Net ndio dereva. “Naomba punguza baridi Net. Mtoto anasikia baridi.” Net akapunguza. “Tom!  Ulimpa dawa za maumivu?” Tunda akauliza. “Mama alisema nisimpe kabla ya kula. Ndio tulikuwa tunasubiria mama aje na chakula, ndio tumpe na dawa.” Tom akajibu. “Naona na homa ipo juu!” Mama yake akaongeza. “Pole Aneti. Utapona. Umesikia eeh?” “Asante.” Akaitika Aneti.

“Kwa mida hii nafikiri kitu cha haraka kupata ni chips. Mtapenda chips?” Tunda akauliza. “Tulivyo na njaa! Halafu unasema chips, natamani kuruka ruka.” Tom akajibu nakumfanya Tunda acheke. “Tom!” “Wezako tulikuwa tunashinda na chai ya rangi na mkate mkavu. Sio mchezo.” Tom akaongeza. “Basi tutashuka wote uchague nini atapenda Aneti na mama.” Net akatafuta sehemu wanayouza chips, akasimama pembeni kidogo. Tunda na Tom wakashuka.

Baada kama ya dakika 20 wakarudi na chakula na soda. Tunda akampa Aneti. “Kunywa hii Fanta kwanza, tukifika hotelini ndio mtaanza kula.” Wakaelewa kuwa hawatakiwi kula ndani ya gari. “Asante.” Mama yake na Aneti wote wakashukuru kwa pamoja. Net akaondoa tena gari.

“Tunakwenda wapi?” Net akamgeukia Tunda. “Ndio nilikuwa nikifikiria hapa. Pole mpenzi wangu. Najua umechoka.” “Hamna neno. Wewe ndio nakuhurumia.” Tunda akafikiria. Mama yake na familia yake walikuwa wakiishi mbele ya uwanja wa ndege, Kitunda. Net aliendelea kukanyaga mafuta. Walishapita Tazara, akaingia Buguruni. Alipomuona amenyamaza, akaendelea kutafuta Ubungo.

“Kuna hoteli naifahamu ipo Sinza. Twende mpaka Sinza madukani. Tukifika pale chukua barabara kama tunaelekea Tandale, nitakuonyesha.” Net akamgeukia Tunda kama anayemuuliza umepajuaje. Tunda akainama. Net akaendelea kukanyaga mafuta.

Walipofika hapo hotelini, Tunda alishuka yeye mwenyewe kwanza. Akaenda kuchukua chumba na kulipia, ndipo akaenda kuwafuata kwenye gari. “Twendeni.” Akamgeukia Net. “Nisubiri, sitakawia.” “Sawa.” Tunda aliwasindikiza mpaka chumbani kwao. Kilikuwa ni chumba chenye vitanda viwili. “Naona muanze kula wakati naenda kununua dawa za Aneti.” “Nakushukuru sana Tunda. Ngoja nikupe kikaratasi cha dawa.” Mama yake alikuwa akitetemeka mikono. Tunda akahisi ni njaa. “Asubuhi mpige simu wawaletee kifungua kinywa.” Tunda aliongeza, wakati mama yake akitafuta kikaratasi.

“Asante Tunda. Nilivyokuwa na hamu na kuku!” Tom aliongea na chakula mdomoni. Tunda akacheka. “Kaoshe mikono Aneti ili uje kula. Mwenzio Tom alishanawa mikono pale tuliponunua chips.” Aneti akaelekea chooni, pale pale ndani ya kile chumba. Bado mama yake hakuwa anakiona kile kikaratasi. “Nilikuwa nacho siku nzima. Sijui nimekiweka wapi!” “Jaribu kutulia mama. Utakiona tu. Fikiria kidogo.” Tom akamshauri mama yake. Ni kweli hakuwa ametulia.

Akasimama. “Angalia kwenye sidiria.” Tom akamshauri tena mama yake. Akaingiza mkono ndani ya sidiria, ni kweli akakipata. “Hiki hapa! Nilikuwa natembea nacho nikijua labda nitapata pesa, ninunue.” Akamkabidhi Tunda. “Nakushukuru sana Tunda. Asante.” “Karibu. Basi kaa chini na wewe ule. Nitarudi nikipata dawa.” Tunda akatoka.

Alimkuta Net ametulia kimya kwenye gari. Akapanda na kufunga mkanda. “Pole Net.” “Mimi nipo sawa kabisa.” “Mbona kama unamawazo?” Net akamtolea tabasamu na kumsogelea pale kwenye kiti Tunda alipokuwa amekaa na kumbusu. Tunda akajua ndio hataki kujibu.

Akambusu kwa muda kidogo, akamwachia. “Usiwe unabeba vitu peke yako Net. Nishirikishe na mimi.” Tunda hakutaka kupotezea. “Sawa. Nitafanya hivyo.” Tunda akacheka. “Sasa naomba mimi unirudishe nyumbani, nikachukue gari yangu ili nikaanze kutafuta dawa za Aneti. Sijui nitazipata wapi! Sitaki kuendelea kukuzungusha.” Net akacheka na kuondoa gari.

“Nafahamu duka la dawa kubwa pale Mwenge, na jingine Mikocheni B, kama tukikosa hapa Sinza kwenye maduka ya madawa.” Tunda akaelewa kuwa ndio ameambiwa atakuwa naye mpaka mwisho. Akakumbuka vile Net alivyomwambia akianza jambo huwa ni mpaka amalize, hata kama ni gumu kwa kiasi gani.

“Nakupenda Net.” Tunda akavunja ukimya kwani kila mmoja alikuwa akiwaza lake. “Asante Tunda. Lakini nipo sawa. Usiwe na wasiwasi.” “Ni nini?” “Ni mambo yakifamilia tu.” “Mimi nahusika?” Tunda akauliza, lakini Net akamtizama na kutabasamu. Ndipo Tunda akajua ni yeye tu ndiye anayesababisha kutokuwa na amani huko nyumbani kwa kina Net.

“Pole Net wangu. Natamani nikwambie tuachane ili kila mtu apumzike, lakini naona nishanogewa.” Net alicheka sana. “Sasa hivi nakutaka kwa nguvu zote.” “Hutaki tena tuachane?” “Hata kidogo. Kwanza hiyo sentensi ishindwe kabisa!” Net alizidi kucheka. “Uje unitoe hii pete kidoleni?” “Hutaki?” “Sikubali! Nakuhurumia, lakini nakuombea Mungu akutie nguvu huko kwenye matatizo ya kifamilia, usiahirishe ndoa.” Net alizidi kucheka.

“Sawa mama Cote.” “Tena ukiniita hivyo ndio kabisa. Endelea kupambana tu mpenzi wangu. Sisi ni washindi zaidi ya kushinda.” Angalau waliendelea kucheka. “Naona mpaka unatumia maandiko.” “Mbele ya ndoa! Hamna namna, lazima bibilia ihusike.” Walizidi kucheka, angalau akamuona Net, ametulia kidogo.

Walipata dawa, wakarudi tena hotelini. Tunda aliwaletea maji ya kunywa, chupa 6, juisi ya Aneti yakumezea dawa. Aliwakuta wamejilaza, Tom ndiye aliyemfungulia mlango dada yake. “Sitakaa sana. Nitarudi kesho jioni kuwaona. Net atakuwa amechoka, inabidi awahi kurudi kwake akapumzike.” “Hongera Tunda. Tom ameniambia ni mchumba wako. Anaonekana muungwana.” Tunda akacheka kidogo. “Asante mama. Namshukuru Mungu. Basi muwe na usiku mwema. Dawa zote za Aneti mpaka amalize dozi nzima zipo hapa, na za kushusha homa. Nitawaona kesho.” Tunda akatoka.

Kwa Net kumepamba Moto. ipango mikali dhidi yao yaendelea.

W

akati Tunda anahangaika na wazazi wake, Net naye alikuwa akipitia changamoto zake. Jumatatu baada ya Tunda kuvalishwa pete, mama Cote hakutaka hata kupoe. Akamwita tena Bethy na mumewe Gabriel, ambao hakuwepo kwenye kuchumbiwa kwa Tunda. Kila mmoja wake alimpa Net sababu ya kutokuweza kuhudhuria kwao kwenye shuguli nzima. Kuanzia kanisani mpaka jioni kwenye tafrija. Mke na mume wote walisema wasingeweza kufika. Net hakujali. Aliyetaka awepo ni Tunda, basi.

Gabriel na mkewe walifika kwenye hoteli hiyo kwa muda tofauti tofauti na wote walionekana ni kama hawapo kwenye mawasiliano. Alianza kufika Bethy. Alimkuta mama Cote akiwasubiri. Akasalimia, nakukaa. Baada ya kama dakika 10 hivi, ndipo Gabriel naye akafika. “Samahani nimechelewa kwa kuwa nilikuwa na miahadi na mtu ambaye nisingeweza kumuahirisha. Na baada ya dakika 45 kuanzia sasa, natakiwa kuwa sehemu nyingine.” Gabriel alizungumza hivyo na kukaa bila salamu.

Kaka huyo mtanashati mwenye mafanikio hapo mjini, na yeye Mungu alimjalia uzuri wa kiume, ungependa kumtizama. Mkewe hakujibu. Akageukia pembeni. Akajua wapo na ugomvi. Mama Cote hakujali. Bora yake yamwendee sawa.

“Pole na majukumu, Gab.” Mama Cote akajibu hivyo, mkewe kimya. “Asante na wewe.” Gabriel akajibu. “Nashukuru lakini bado tatizo lipo pale pale. Jana Tunda amevalishwa pete ya uchumba. Na Net anaonekana anataka harusi ya haraka. Tunda amefanikiwa kumwingia yule bibi. Naona amemtangaza kabisa kama ndiye mrithi.” Akalalamika mama Cote.

“Kabla hujaendelea sana mama Cote, mimi binafsi naomba nijitoe. Sioni kama ni tatizo langu. Bethy alinilazimisha siku ile kukutana na Tunda, akisema ni lazima ili kuhakikisha kama ni kweli sijawasiliana tena na Tunda. Nikakubali kudhalilika mbele zenu. Nasikia mmetumia fedheha yangu, kuyanadi mapenzi ya Tunda kwa Net kanisani, ambaye kwangu amekuwa msaliti.” Kila mtu akashtuka.

Mkewe akamkazia macho. “Ndiyo. Net alinionya mimi nisiwe na Tunda, halafu akamchukua yeye! Aka…” “Subiri kwanza Gab! Yaani leo bila hofu unasema hapa umenyang’anywa mwanamke wako mbele yangu na ukiwa kwenye ndoa!?” “Ndoa gani Bethy? Ndoa ipi? Unataka kumdanganya mama Cote ili iweje? Ndoa ilishaisha na kwa Tunda mimi sikukosea kuwa naye. Hata mchungaji nilimwambia kuwa nataka kumuoa Tunda. Na Net pia nilimwambia. Akatumia ujanja wake, akamchukua mwanamke wangu.” Mama Cote alibaki ametoa macho.

“Wewe ni mshenzi Gab.” “Wewe ndiye mshenzi. Ulimuahidi nini Net na mchungaji na unafanya nini sasa hivi!? Hujabadilika hata kidogo. Kiburi vilevile. Nyumba haikaliki na sina pakukimbilia kwa kuwa Net amechukua faraja yangu.” Bethy alichukua kinywaji alichokuwa akinywa mama Cote, akamwagia Gabriel.

“Acha fujo zakijinga Bethy.” Gab akasimama huku akijikung’uta. “Naombeni mtulie Gab na Bethy. Tulieni.” “Sasa kama ulifikiri utamuoa Tunda, andika maumivu. Mimi ndiye nitahakikisha Net anamuoa Tunda. Na nitakuona kama utapasuka. Wewe si unajidai unamlilia Tunda!? Sasa nitakukomesha.” Bethy akachukua pochi yake nakuondoka kuelekea kwenye gari yake. Mama Cote akasimama na kumkimbilia Bethy kwa haraka.

Zile hazikuwa habari njema hata kidogo kwa mama Cote. Bethy hawezi kwenda kinyume naye. Alitaka watu wengi upande wake ili kuhakikisha anashinda kuwatenganisha Net na Tunda. Kitendo cha Bethy kuapa atamsaidia Tunda kuolewa na Net, asingeruhusu. “Bethy! Bethy!” “Hapana mama Cote. Kwa nini unataka kuvunja kwangu ili yako yakuendee sawa? Atakapoachika Tunda, inamaana atakuwa huru. Unafikiri itakuaje kama sio kuolewa na Gab!?” Hapo Bethy akawa ametumia akili.

Mama Cote akatumia akili za haraka sana kumrudisha kwenye mstari. “Tulia nikwambie Bethy. Lazima wote tutumie akili. Na tumjue adui yetu na kumtoa kabisa. Maana hakuna uhakika kama Tunda akiolewa na Net, ndio hatarudiana na Gabriel.” Kidogo Bethy akatulia.

“Yule binti ni Malaya, na ananguvu za giza zakuweza kumwingia mtu au kugeuza watu wawe upande wake. Huwezi amini jinsi mama mkwe wangu jinsi anavyomsifia! Amekuwa ni kama amemfahamu huyo Tunda kwa miaka mingi! Maya naye ndio kabisa. Anatoa shukurani zake kwa Tunda kumfanya arudi shule na kupata shahada yake ya kwanza! Anasema bila Tunda, asingekuwa vile alivyo wakati mimi nimehangaika sana na wale watoto! Sio kitu cha kawaida. Lazima wote tusimame pamoja, tumtoe kabisa Tunda kwenye maisha yetu wote. Tusipoangalia anaweza akapata vyote. Net na Gabriel. Hebu tulia na kumfikiria Gabriel. Kwa nini gafla aone ndoa yake haifai, wakati matatizo yenu hayakuanza leo?” Mama Cote akazidi kumvutia Bethy.

“Maana ni kweli. Gab hakuwahi kuwa mlalamishi. Mambo mengi alikuwa akisema tuombe! Gabriel alikuwa mtu wakufunga na kuomba kila wakati. Tena yeye ndiye alikuwa mstari wa mbele hata kutotaka watoto watuone tunapishana maneno. Ugomvi wote alitaka uishie chumbani.” Bethy akaendelea.

“Hata nilipokuwa nikimpandishia mbele ya watoto au wafanyakazi pale nyumbani, alikuwa ananyamaza, na kuelekea chumbani. Sasa hivi amekuwa kama mwehu! Anatoa mambo ya ndani kabisa hadharani! Zile sio akili zake kabisa. Amegeuzwa.” Angalau hapo mama Cote akampata, japo alikuwa akimshangaa moyoni. Kwa nini asifikirie labda mwenzie amechoka! Hata mama Cote aliwaza, akaamua kwenda naye hivyohivyo kutumia ujinga wake kwa manufaa yake.

“Sasa tutafanyaje!?” Bethy akamuuliza mama Cote. “Net anamsimamo sana. Nilazima kumfungua macho juu ya Tunda. Aelewe kuwa Tunda ni mshirikina na lazima atakuja kumgeuka tu.” “Sasa uthibitisho tunaupata wapi?” “Ndio tuanze kuhangaika.” “Kumbuka tumebaki wawili tu na wote tunamajukumu mazito.” Bethy akaanza kuona ugumu wa hiyo Vita anayotaka kuianzisha mama Cote dhidi ya Tunda.

“Watu wapo Bethy. Wala usijali. Wewe tulia kabisa, nitakupa mipango yote. Usiharakishe kumfikisha Tunda kanisani, aolewe na Net.” Wakacheka. “Mwenzangu niliingiwa na hofu! Siwezi kumruhusu Tunda anichukulie mume. Hata kama tunaburuzana, hivyo hivyo. Akiniacha sasa hivi Gabriel, si nitafia mtaani?” “Hawezi. Na hata kama akikuacha, lazima mali mgawane nusu kwa nusu. Si mmezaa naye bwana? Na watoto bado wadogo, utatakiwa wewe ndio uwatunze.” Mama Cote akamuona Bethy anababaika wala asifurahie. Akahisi kuna jambo limejificha hapo.

Kwani vipi?” “Ngoja niwahi mama Cote. Nimeacha wateja ofisini kwangu ili nikuwahi. Sasa maadamu sasa hivi tumefikia muafaka. Na adui yetu ni mmoja, Tunda, turekebishe mambo mapema.” Bethy akajichekesha na kuingia kwenye gari bila kutaka kujibu swali la mama Cote. Lakini mama Cote akajua lipo jambo juu ya hiyo ndoa.

Gabriel kwa Net!

G

abriel alitoka pale na hasira. Akampigia simu Net. “Nilifikiri wewe ni rafiki yangu, kumbe mtu wakunizunguka!” Net akashtuka kidogo. “Kwema Gab!?” “Kwako ndio kwema, sababu unaye mwanamke wangu ambaye anakuliwaza. Unashida gani!? Tatizo lipo wapi! Umeniacha kwangu kunawaka moto. Faraja pekee niliyokuwa nayo umejidai kutumia jina la Mungu kumchukua mwanamke wangu!” Net kimya.

“Ulipiga mahesabu ya haraka, ukakimbilia kwa wachungaji kwenda kunishitaki, ukitumia kigezo kuwa nina ndoa takatifu, ili wakusaidie kumtoa Tunda upande wangu, halafu wewe ndio akuone mwema sana kuliko mimi, halafu akutake wewe, mimi anihesabu msaliti.” Gabriel alisikika akiongea kwa machungu sana.

“Niliwaeleza wazi bila kuwaficha juu ya mwanzo wangu mimi na Bethy mpaka sasa. Matatizo ninayopitia kwenye ndoa yangu kila siku. Mkakazana kufunika, mkitumia maneno ya kwenye bibilia. Huku mkinikumbusha kuwa Tunda hakuwahi kunipenda, alikuwa akinitumia mimi kama wanaume wengine anavyowatumia. Nikae naye mbali. Mbona wewe sasa unamuoa!?” Net kimya.

“Nakuuliza Net. Kama Tunda ni mbaya, kwa nini wewe unamuoa?” “Kwanza mimi siye niliyefikisha mambo yako kwa mchungaji. Ni mkeo. Mimi niliitwa tu kueleza kama nafahamu hayo mahusiano na kama ulinishirikisha kama unataka kumuacha Bethy umuoe Tunda. Ndipo nikaeleza upande wangu kwa kile ninachokifahamu juu yako na maisha ya Tunda. Pili.” Net akaendelea.

“Sikuwahi kukwambia kama Tunda ni mbaya, Gab. Nilikueleza kwa kifupi maisha yaliyompelekea Tunda hata kukutafuta wewe. Alikuwa na shida na pesa yako sio wewe kama Gabriel. Hata mlipomtega ili kuona kama atakurudia tena, alikwambia kwa wazi kabisa Gab. Hukuwahi kuwa na mahusiano na Tunda ila Nancy ambaye sasa hivi hayupo.” Net akajaribu kujitetea.

“Nani alikwambia nilikuwa na tatizo juu ya hilo? Ni afadhali ya Tunda sijui Nancy ambaye alikuwa anakula pesa yangu, lakini ananiheshimu na kunipa pumziko, kuliko Bethy ambaye anavuna ambako wala hajapanda! Ukanitibulia mapenzi ya kweli, kwa wivu wako, ukiona ninafaidi, ili na wewe unufaike ukisaidiwa na wachungaji! Leo wanakupa baraka kwa mwanamke asiye wako! Na wao uwafikishie salamu zangu maana huko sitarudi tena.” Hapo Net hakuwa ameelewa.

Maana anajua Bethy na Gabriel walianza zamani sana. Tokea Gabriel anarudi nchini,  mwanamke wa maana aliyemtambulisha kwao ni Bethy, na akaja kumuoa baada ya muda mfupi. Mara kadhaa alishakwenda na Bethy nchini Canada kuwatembelea kina Cote, akiwa tayari mkewe.

“Cha pili, mimi sikumtega Tunda.” Gab akaendelea. “Siwezi kujidhalilisha mwenyewe. Mimi sio mjinga. Ni mama yako ambaye mpaka leo, tena sasa hivi hapa ametoka kutuitisha kikao, akitaka tuendelee kumuunga mkono kumuangamiza Tunda. Nimejitoa kwa kujiweka wazi kabisa,  kuwa hata mwanzoni nilikubali sababu ya kelele za Bethy. Lakini sitarudia huo ujinga kwa mwanamke ninayempenda.” Gab akaendelea, asijue jinsi alivyomshtua Net juu ya hicho kikao cha siri mama yake alichoitisha.

“Na umwambie mama yako kabisa Net, chochote kibaya atakachomfanyia Tunda, atapambana na mimi. Wapange mipango yao kukuangamiza wewe ili usimuoe Tunda, lakini sio Tunda. Na wewe nakuhakikishia kabisa Net, utaiona hii nchi chungu. Wewe si unajidai mjanja? Sasa nakwambia huwezi kufunga goli kwenye uwanja wa ugenini. Mtu kwao. Hata kama unamamilioni ya mapesa, nitakuonyesha mimi ni Mtanzania wa kuzaliwa sio kuombewa vibali vyakufanya kazi.” Gabriel akakata simu kwa vitisho hivyo.

          ~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

CONVERSATION

0 Comments:

Post a Comment