Naomi Simulizi |+1 205 767 8163 |naomisimulizi@gmail.com Nilipotea! – Sehemu ya 29 - Naomi Simulizi

Nilipotea! – Sehemu ya 29

 

I

likuwa jumatatu ambayo Net alikuwa na kazi nyingi, lakini akabakia kwenye gari ameduaa. Ni kweli Net hakuwa raia wa nchini Tanzania. Ilimlazimu kupata kibali cha kazi kila wakati ili kumruhusu kuishi nchini Tanzania. Japokuwa mama yake alikuwa ni mtanzania, lakini Net alishindwa kuchukua uraia wa Tanzania pia sababu ya mali zinazomsubiri nchini Canada. Tanzania hairuhusu uraia wa nchi mbili. Inamaana kama angechukua uraia wa Tanzania, angekana uraia wa Canada. Nyumba na mali za babu yake, vingepotea bure. Kampuni ya Cote LTD ambayo ndio ya mama yake hapa nchini, ndiyo iliyokuwa ikimuombea kibali cha kazi kila kinapoisha na kuonyesha inayo uwezo wa kumuweka nchini.

Gabriel kama mtu wa karibu yake sana, alikuwa akilifahamu hilo na mengi kwenye maisha ya Net. Gab alimfahamu Net ndani na nje. Siri zote za Net, za Canada na hapa nchini Tanzania, Gab alikuwa akizifahamu kwa kushirikishwa na Net mwenyewe. “Ni nini Gabriel atafanya!?” Wasi wasi ukamwingia Net. Gabriel alimtisha kana kwamba walikuwa maadui sana. Kumbe marafiki watokea watoto. Pasipo hata kufikiria, Tunda ameingia katikati yao. Kila mmoja anamdai Tunda ni wake.

Na mama yake kama mmiliki wa hiyo kampuni, ndiye aliyekuwa akihusika katika kumuombea kibali kwenye wizara za uhamiaji hapo nchini. Tuseme mama yake ndiye anayemuweka nchini. “Umbali gani mama anataka kwenda ili kunitenga na Tunda?” Nalo likawa swali lakumuumiza zaidi Net. Aliumia sana kujua bado anaendeleza vikao vya siri dhidi ya Tunda.

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

Hiyo jumatatu ikawa chungu kwa Net. Alihakikisha anafanya kazi alizotakiwa kuzifanya jumatatu hiyo, akili ikiwa imevurugika hivyo hivyo. Hajui lakufanya, na ndio alikuwa anamiahadi na Tunda jioni yake. Ndio kisa cha Tunda kumuona ametulia sana siku ile jioni wakati akimuhamishia mama yake na wadogo zake hotelini.

Kwa Tunda ambaye ndio mchumba, mambo yake mwenyewe hayajatulia. Wazazi wake wote wawili wanapitia vipindi vigumu, tofauti tofauti. Na yeye kama mchumba kulazimika kuwa katikati ya hiyo hali ili kumtia moyo Tunda. Nyumbani kwa mama yake kumewaka moto. Ofisini nako mama yupo na hawezi tena kujifanya mambo yapo sawa wakati amejua mipango ya siri ambayo mama yake anafanya dhidi yake na Tunda. Gabriel naye ametuma vitisho dhidi yake, Mama cote na amesema kanisani harudi tena. Alibaki asijue chakufanya.

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

Net akabaki akiwaza. Je, aondoke kurudi nchini kwao Canada, na asirudi tena Tanzania, au afanyaje!? Akazidi kujiuliza ni nini afanye. Hakumtafuta mama yake ili kuuliza vikao vya siri anavyoendesha kutengeneza timu ya kumuangamiza Tunda au kumtafuta ili amfikishie ujumbe wa onyo au vitisho vya Gabriel. Akitaka asithubutu kumgusa Tunda. Akajiambia anahitaji kwanza kufikiria.

Hata nyumbani kwa mama yake, alipo Maya na bibi yake siku hiyo ya jumatatu hakwenda. Aliwapigia simu, na kuzungumza nao tu. Aliwaambia siku hiyo hatafika, kwa kuwa yupo na majukumu muhimu sana. Bibi yake akamtania kidogo, wakakata simu akabaki akiwaza mpaka muda wakwenda kuaga rafiki zake waliokuwa wakirudi nchini Canada. Alipata nao muda mfupi, wakapelekwa uwanja wa ndege, yeye akarudi kufanya shuguli zake.

Tunda alimsaidia jioni yake, vile alivyomwambia akazane kupambana tu, yeye anataka ndoa. Angalau ilizidi kumuhakikishia bado anaye Tunda. Angekuwa amechagua kukimbia tena, kwa hali ilivyo, pengine safari hii Net asingemkimbiza tena. Pengine safari hii na yeye angekubaliana naye! 

Jumanne!

S

iku hiyo ya jumanne, Tunda alimuamsha Net. Akampa ratiba yake ya siku nzima, akamringishia pete yake. Net alikuwa akicheka tu. Alionekana atakuwa busy siku nzima. Na Net naye kwa kuwa hakuwa amemuona bibi yake siku iliyopita, akamwambia Tunda itabidi jioni hiyo aende kumuona bibi yake na Maya. Tunda alielewa kabisa. Hata hivyo na yeye jioni ya siku hiyo alitaka kwenda kumuona mama yake na wadogo zake huko hotelini. Wakaagana na maneno mazuri, kila mtu akaanza kujitayarisha kwa kuanza siku.

Net aliingia ofisini kama kawaida yake bila kuchelewa. Mama yake bila kujua, akamfuta ofisini kwake, baada ya kufika hapo. “Hey Son!” Ritha akamchangamkia kama asiye na hila. “Shikamoo mama. Naona tenda ya Visiga umeipata. Nikuanza kujipanga kwa haraka ili kusiharibike jambo. Nimeshakutumia kila kitu. Ni wewe tu kukamilisha mipango.” Net alikuwa amebadilika usoni, alishindwa hata kumtizama mama yake.

“Nataka kuandaa chakula cha jioni kabla bibi yako hajaondoka. Nafikiri itakuwa vizuri na Tunda naye awepo.” “Hakuna sababu ya Tunda kuwepo. Wewe endelea tu na mipango yako.” Kidogo mama Cote akatulia. Akaingia ndani na kufunga mlango. “Wewe unataka niwe karibu na Tunda, namkaribisha nyumbani kwangu, unakataa! Sasa unataka nifanye nini?” “Naomba hilo swali nilijibu jioni nitakapokuja, ‘nyumbani kwako’ kumuona bibi na Maya.” Net alinyanyua kabisa vidole wakati anaweka msisitizo wa neno ‘nyumbani kwako’, kama mama yake alivyosema “nyumbani kwangu”. Mama Cote akacheka, nakutoka huku akisema kwa sauti. “Hakuna kuchanganya mambo ya familia na kazi!” Kisha akafunga mlango.

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

Jioni Net alifika nyumbani kwa mama yake, akamkuta bibi yake na Maya wapo sebuleni. Akambusu bibi yake, akakaa. “Are you okay?” Bibi yake akamuuliza akitaka kujua kama yupo sawa kwa ule muonekano wake. “Nimechoka tu. Maya amekutoa leo kukuzungusha mjini?” Net aliuliza huku akimtazama Maya pia. “Nimempeleka. Amepata vikapu vya mkeka vizuri kwa ajili ya rafiki zake na vinyago vingi. Ameweka oda maalumu kwa ajili yake na rafiki zake. Wamemwambia kesho jioni vitakuwa tayari.” “Hapo sawa.” Net akaridhika.

“Utatusindikiza kurudi nyumbani?” Maya alipatambua nyumbani kwa bibi yake kama nyumbani kwao. Hakuwahi kuona maisha ya pale kwa mama yake kama yanamuhusu yeye. “Ndio nimemchumbia tu Tunda! Siwezi kuondoka na kumuacha.” “Tunaweza kuongozana naye. Si ni sawa Nana?” Maya akamuuliza bibi yake. “Hivi karibuni atakuwa Cote. Sioni sababu yakutofika nyumbani.”  Bibi Cote akajibu wakati mama yao anaingia. “Nini!?” Mama Cote akauliza kwa mshtuko kidogo. “Nana amesema kwa kuwa hivi karibuni Tunda atakuwa Cote, haoni sababu ya kutokufika nyumbani.” Maya akajibu na cheko usoni. Mama Cote alishtuka mpaka akaonekana usoni.

Bibi Cote akakunja uso kidogo. “Kuna tatizo lolote?” Yule bibi akauliza huku akiwatizama Net na mama yake kwa zamu. Net naye akabaki akimtizama mama yake. Maya akajiweka sawa. “What did you do this time?” Maya akamuuliza mama yake na mikono kafunga kifuani akitaka kujua amemfanya nini tena kingine!

 “Hakuna tatizo lolote. Lakini nilifikiri ingekuwa vizuri afike kule akiwa ameshaolewa kabisa.” Wote wakabaki wamemkodolea macho. Kama waliouliza kwa nini. Akaona awawahi kuwachanganya. “Kwanza ni moja ya mila na desturi za kitanzania. Mwanamke haruhusiwi kufika ukweni kabla ya kuolewa rasmi.” Akadhani ameshinda.

“Lakini sivyo ulivyofanya wewe! Nilikufahamu wewe hata kabla hujaolewa CJ!” Net alitamani kushangilia. “Ulikuwa ukifika nyumbani mara kwa mara hata kabla yakuolewa! Au umesahau?” Bibi yao akaendelea kudadisi. CJ ni baba yao kina Net. Walikuwa wakimfupisha jina lake la Cote Junior.

“Kwanza ni kwa kuwa nilikuwa nje ya hapa nyumbani. Kwa hiyo hakuna mtu aliyekuwa akifahamu. Haikuwa na madhara.” “Si ndivyo atakavyofanya hata kwa Tunda? Nje ya hapa. Tofauti ipo wapi hapo?” Maya akadakia kwa kuuliza na yeye swali. “Lakini jamii itajua kama anaondoka kuja kwenu kabla hata hajaolewa.” Wote wakabaki wakimwangalia kama wanao msuta. “But anyways, tunaweza kulizungumzia na kupanga zaidi siku mtakayotaka aje huko.” Kila mtu kimya. Net akabadili channel kwenye tv, kuonyesha hana mpango wakuendeleza yale mazungumzo.

          Chakula cha jioni kilipangwa mezani, kila mtu alikula kimya kimya. Bibi Cote akajua kuna kinachoendelea. “So?” Akavunja ukimya. Kila mtu akamtizama yeye. “Who is coming with me?” Akataka kujua ni nani yupo njia moja na yeye kurudi Canada. “Mimi najua wote mlalo jibu.” Maya akajibu kwa haraka. “What about you Son?” Akataka kujua juu ya Net. “Ni sawa nikikujibu kesho?” Net akamuuliza bibi yake. Akakubali.

Walimaliza kula, Net akamsindikiza bibi yake mpaka kitandani. Wakaomba pamoja, wakati Net anataka kusimama, bibi yake akamshika mkono. Alikuwa amekaa pembeni ya kitanda, alipokuwa amelala bibi yake. “Nakupenda. Unajua hilo?” Net akacheka. Nakumbusu tena. “Mimi nipo sawa Nana. Usiwe na wasiwasi.” “Una uhakika?” Net akainama kama anayefikiria. Bibi yake kimya akimtizama.

Net akanyanyua uso, akamvuta bibi yake mkono na kuubusu. “Labda niseme, is gona be fine.” “Are you sure?” Bibi yake akaendelea kutaka uhakika. “Naamini hivyo Nana. Kila kitu kitakuwa sawa. Wewe pumzika tu. Nitakuonaaa…” Net akafikiria kidogo. “Nitajitahidi iwe kesho. Nahitaji kuongea na Tunda kwanza.” “Naelewa.” Net akambusu tena bibi yake kwenye kipanda uso, kisha akatoka. 

Usiku wa Jumanne. Mama Cote na Net.

N

et alimkuta mama yake amekaa sebuleni. Akajua anamsubiri tu yeye. Akaenda kukaa pembeni yake. “Nina ujumbe wako kutoka kwa Gabriel.” Mama yake akashtuka sana. “Ametuonya sana juu ya Tunda. Zaidi wewe kuwa usithubutu kumtendea kitu chochote Tunda. Ni nini atafanya endapo utamdhuru Tunda, nafikiri utajua madhara yake pale utakapo kiuka. Amenitaarifu rasmi kuwa, amekataa kujiingiza katika njama zako za kumuangamiza Tunda.” “Mimi sitaki kumuangamiza Tunda.” Net akamtizama kwa kumsuta.

“Naomba nikushauri kwa mara ya mwisho mama. Nilishakwambia na ninarudia. Umeanzisha vita vikali sana, na vibaya dhidi ya Tunda. Unafanya vikao na kukusanya watu wawe upande wako ili kumuangamiza mtu aliyetafutwa kwa damu ya thamani sana.” “Unajuaje kama…” “Naomba nimalize mama. Nivumilie tu. Kwa kuwa sitarudia kukaa tena chini, kulizungumzia hili na wewe. Nitakuachia uwe huru kufanya unachotaka kukifanya.” “Hakuna baya ninalotaka kufanya.” Mama Cote akabisha.

“Basi, nakusihi mama yangu, uwe mwangalifu. Usikubali hiyo roho ya uharibifu iliyokuingia ikashinda. Kuna mambo mengine huwa Mungu akiyaruhusu, wewe huwezi kuyazuia. Wapo watu wana…” “Sio Tunda. Na kwakwe siwezi kumruhusu Tunda aka…” “Rithi mali!?” Net akamalizia sentensi ya mama yake kwa kumuuliza swali huku amemkunjia uso kama anayemshangaa. Mama Cote akababaika sana.

“Eti mama?” “Wala sio mali, lakini yeye ndio anaroho hiyo ya uharibifu. Na siwezi kuruhusu akakuharibia maisha.” “Mama please! We are way pass love card. Stop playing with my feelings.” “Yeye Tunda ndiye umemruhusu kucheza na hisia zako.” Net akatingisha kichwa kwa kusikitika. Akainama kwa muda.

“Ni kiasi gani cha pesa unataka kumiliki hapa duniani ambacho unakitafuta kwa nguvu zote, hata kumpinga Mungu?” Net akamuuliza mama yake kwa kuumia sana, kisha akaongeza. “Au ni mali ipi unayoilinda ili Tunda asiifikie? Ni nini mama!?” “Nimehangaika sana kufika hapa nilipo. Siwezi nikamruhusu malaya yule akaja kuchezea tu jasho langu.” Kwa hasira mama Cote akajikuta anaropoka kwa mwanae.

“Afadhali umeweza kuwa muwazi katika hilo kuwa tatizo ni mali.” “Na wewe pia.” “Usinidanganye mama. Kama ingekuwa ni mimi, mpaka sasa ungethamini maamuzi yangu. Ila kwa kuwa wote tunajua tatizo ni mali zako na pesa, kwa nini usifanye taratibu za kisheria? Kwa nini usiweke kwa maandishi kuwa sasa na hata ukifa, hutaki Net wala Tunda na watoto watu wakagusa mali yako wewe? Mbona nirahisi tu na hakuna hata atakayekulaumu kwa hilo kuliko mambo unayotaka kufanya!?” Net alitoa wazo zuri tu. Akidhani mama yake anaweza kuelewa.

“Sasa hivi ndio unaleta jeuri na kujifanya hutaki mali zangu kwa kuwa unazo mali za babu yako?” Net akaumia sana. “Mali gani mama yangu!? Ni mali gani hizo tunazozungumzia wakati bibi yupo hai, amelala hapo ndani na ananguvu zake zote? Anaendesha mambo yake mwenyewe bila shida! Si mgonjwa wala dhaifu wakusema atakufa leo au kesho! Mimi nahangaika kutafuta pesa kwa jasho langu mwenyewe, mama. Kila pesa kwenye akaunti yangu nimeitolea jasho na wewe ni shahidi. Nimekufanyia kazi mchana na usiku, kwa uaminifu bila kuchoka. Nilichochukua na kutegemea kutoka kwako ni mshahara wangu tu. Sio mali ya kurithi.”

“Kama ni juu ya Tunda, anahangaika yule binti. Mchana na usiku yupo kutafuta pesa yake ambayo sasa hivi inategemewa sana na wazazi wake.” Mama Cote akashangaa kidogo. Tunda anayemfahamu hana mahusiano mazuri na wazazi. Alifukuzwa.

“Nakusihi mama yangu, muache Tunda. Muache Tunda, kwa manufaa yako. Unajitafutia matatizo, Mungu hatakuacha. Yule binti anapambana, kuisaka pesa yake sasa hivi. Anafanya kazi kama punda! Na sasa hivi zipo roho za watu wanne, zinamtegemea Tunda kwa asilimia 100. Yapo maisha ya watu 4, wanategemea uhai wa Tunda. Kuanzia kula yao, ishi yao hapa duniani, ni Tunda. Tafadhali mama mwache Tunda.”

“Nakuonya sasa hivi. Kwa umbali wowote uliofika, rudi. Anza upya. Au mwache kabisa. Tunda amekubali kutofika hapa, hataki hata kutumia pesa yangu. Kila ninavyojitahidi kutaka kumsaidia, ameshindwa kupokea msaada wangu. Unanifanya nashindwa kuwa karibu na msichana ninaye mpenda sababu ya mali ambayo hata sina!” Net akaongea kwa unyonge akimsihi mama yake.

“Mali zote zimeandikwa ni za bibi yako akiwa hai, akifa tu, ni zako. Tunda ni mjanja sana. Anakuvuta kimahesabu akitaka umuamini sasa hivi, ujue hajakupendea pesa. Akijua wazi, ukimuoa mali zote zitakuwa zake pia.” Net akatingisha kichwa kwa kusikitika huku akimshangaa mama yake.

“Hakika natamani kama hizo mali zingekuwa zangu ili nikuandikie wewe zote, ili uniache niendelee na maisha yangu kwa amani na utulivu. Unanifanya najuta hata kuzaliwa. Unaninyima raha. Unanitengenezea maadui wa bure bila kunihurumia!” “Gabriel umemgeuza moyo wewe mwenyewe kwa kumpora mwanamke wake. Yeye hajakwambia?” Net alibaki akimtizama mama yake.

“Wala usinitizame vibaya. Wewe mwenyewe ndiye umemkataza kuwa na Tunda, halafu baadaye unakuja kumchumbia Tunda huyohuyo! Hawezi kukubali.” “Ni mara ngapi nilikupa historia yangu na Tunda?” “Sasa nani anayajua hayo ya Tunda ya tokea anaishi kwa shangazi yake!? Eti mambo ya miaka mitano sijui saba iliyopita! Halafu hata Tunda mwenyewe sio kwamba mlikuwa kwenye mahusiano! Ulisema ulitaka kumwambia, lakini mazingira yakawa magumu. Sasa nani anajua ni kweli au si kweli!? Anayejulikana kuwa alikuwa kwenye mahusiano naye ni Gabriel.” Net alizidi kushangaa.

“Tuseme si kweli ninayosema juu ya Tunda. Kwa hiyo wewe unamuunga mkono Gabriel amuache mkewe, aje amuoe Nancy ambaye hayupo?” “Hiyo ni juu yao wenyewe. Sio kila ndoa ilikusudiwa kufungwa, na sio ndoa zote ni mpaka kifo. Gabriel na Bethy hawatakuwa wa kwanza wala wa mwisho.” Net alicheka kwa kusikitika.

          “Hayo yote unayaongea ni kwa ajili ya kutotaka tu Tunda asiwe mke wangu?” “Sikiliza Net, mimi nakujua jinsi unavyokuwa unapotaka jambo lako litokee. Na mimi ninawajibu kama mama kwako. Niache nifanye ya kwangu, na  wewe endelea kunikaidi.”

“Angalia tu usije ukaenda umbali ambao ukashindwa kurudi.” “Leo upo hapa, umesimama kama mwanaume wakuweza kubishana na mimi, si kwa kuwa mimi nimeweza kusimama kama mama? Ningekutoa wakati upo tumboni!? Nisingekulea na kukuhangaikia mpaka leo!? Mbona miaka yote hiyo usinihusie juu ya umbali ninaofika na wewe, leo ndio umekuwa mwanaume wakuweza kushindana na mimi!” Mama Cote akambadilikia mwanae.

“Nani amekufanya kuweza kuwepo hapa nchini kama sio mimi?” Net kimya. “Hata huyo Tunda kama isingekuwa mimi, usingemuona. Mimi ndio nimefika umbali mkubwa sana kukufanya uweze kuwepo hapa Tanzania na watu wa usalama wasikusumbue. Nimetoa mahela mengi tu, kukufanya uweze kuishi kwa furaha hapa nchini, leo ndio una uwezo wakuleta jeuri!” Net alibaki kimya akimtizama mama yake kwa kuumia sana.

“Tokea babu yako amefariki, ukajua unamiliki mali za kutosha, unaanza kuniweka pembeni! Sasa Net, nakuonya. Mimi ni mama yako.” “Usiseme kitu ambacho utakuja kujutia mama. Nakushauri unyamaze.” “Mbona hukuniambia ninyamaze wakati watu wa usalama walipokuwa wakikufuatilia miaka 3 iliyopita? Unajua nilizungumza nini mpaka leo umekaa hapa?” Net kimya. Mama Cote aliongea, mpaka Maya akatoka chumbani.

Alipoona Net amenyamaza mama yake anaongea bila kunyamaza, akaenda kumuamsha bibi yake. Bibi Cote akaja pale sebuleni na yeye akakaa kochi la mbele yao. Mama Cote akanyamaza. Akanyanyuka na kuondoka. “Rudi kulala Nana.” “Ni nini kinaendelea Net!?” Bibi yake akahoji. “Kila kitu kinahitaji tu muda. Kutakuwa sawa. Twende ukalale.” Net akasimama, akaenda kumshika mkono, kumsaidia kusimama. Akamsindikiza tena chumbani, akaondoka bila hata kuaga.

Mama Cote kwa Gabriel.

R

itha akiwa na hasira vile vile akampigia simu Gabriel.  Na yeye akapokea. Ilishakuwa usiku haswa. “Unaweza kuzungumza?” “Nakusikiliza mama Cote.” Gabriel akajibu. “Nimepata ujumbe wako kutoka kwa Net. Lakini nataka tuwekane sawa Gab. Mimi siafikiani na kitendo alichokufanyia Net. Mimi najua uchungu wa mtu kuingiliwa kwenye mahusiano ya kimapenzi. Yamenipata hayo. Nipo katika kurekebisha. Sitaki Net ajiingize kwenye hiyo laana.” Mama Cote akajaribu kujitetea.

“Kama ni hivyo ni sawa. Nilijua na wewe unaafikiana na kitendo cha Net kumuoa mwanamke wangu!” Wakati Gabriel anaongea hivyo, kumbe Bethy alikuwa akiwasikiliza. Gabriel alikuwa sebuleni akidhani Bethy amelala ndani. Kumbe alijisogeza mlangoni mara baada yakusikia simu ya mumewe ikiita.

“Sasa unafanya nini kudhibiti hiyo ndoa isifungwe? Maana nakwambia ukweli tu mama Cote, wala sitakuficha, sitaruhusu nizungukwe.” Gabriel alisikika kwa kitisho kidogo. “Inabidi sasa tukutane mimi na wewe, kwa sababu Bethy ameshaanza kuchanganya mipango. Atavuruga kila kitu wote tukwame.” Bethy akatoka kama swala akampokonya mumewe ile simu.

“Huna dhamira mama Cote wewe! Unataka kunizunguka mimi!? Huoni aibu? Unapanga na mimi huku unanirudi kwa mume wangu? Unataka kunivunjia kwangu ili ujenge kwako?” Bethy akauliza kwa kulalamika na hasira.

Gabriel akasimama na yeye kama mshale. Akampokonya Bethy simu. Mama Cote akaanza kusikia fujo na matusi kati Gabriel na mkewe. Akakata simu na kuizima kabisa na kuwaacha wanandoa hao wakitukanana kama maadui wa muda mrefu.

Hawakuishia hapo, Bethy akaanza kumrushia mumewe vitu huku akimtukana. Gabriel anakwepa huku na yeye anarudisha matusi kwa mkewe bila kung’ata maneno mpaka watoto na wafanyakazi wote wakaamka. Walikuwa wakiishi na mtoto wa shangazi yake Gabriel ambaye na yeye  alikuwa akifanya kazi. Alishazoea fujo zao. Kwa kuwa asubuhi alitakiwa kazini na watoto shule, alichofanya ni kwenda kuwachukua watoto wao pale walipokuwa wamesimama wakiangalia wazazi wao wakirushiana maneno makali na vitu, akawarudisha chumbani na kuwasha mziki kwa sauti ili walale wasisikie maneno makali wazazi wao wanoyotupiana. Na yeye akarudi chumbani kwake kulala, wakaacha pale pale sebuleni.

Jumatano! Bethy kwa Ritha.

N

et akiwa ofisini kwake ameshaanza kazi, akashangaa mlango wa ofisini kwake unafunguliwa. “Namtafuta mama yako, Net.” Net akanyanyua uso. “Habari Bethy?” “Mama Cote yuko wapi?” “Umejaribu kumuulizia kwa secretary wake?” Net akauliza na kujirudisha nyuma ya kiti, nakukaa sawia akimtizama. “Sijamkuta.” Net akaangalia saa yake. “Basi watafika baada ya muda mfupi kuanzia sasa. Karibu usubirie.” Bethy alionekana na hasira sana.

“Mama yako anataka kunifanya mimi mjinga. Anatuchanganya mimi na mume wangu ili wote tumfanikishie mambo yake! Kama anatutumia tu. Jana usiku kama kwenye saa tano kwenda saa sita hivi, amempigia simu mume wangu akimwambia wapange mipango yakutofanya wewe usimuoe Tunda, kwa kuwa na yeye hajaafikiana na kitendo chako chakumnyang’anya Gabriel huyo Tunda, wakati alitoka jumatatu kufanya kikao na mimi akiniambia adui wetu wote ni Tunda tutafute mbinu ya kumtoa kwenye maisha yetu!” Net kimya akimtizama Bethy anavyoongea kwa jazba, akiwa bado amesimama.

“Maana mimi nilimkatalia kumtoa Tunda kwako. Nikamwambia kwa kuwa wewe ukiachana na Tunda, inamaana Tunda atarudiana na mume wangu. Halafu mimi ndio niachwe! Nikamkatalia kabisa, nikajitoa. Tena akanikimbilia mwenyewe mpaka kwenye gari kuwa tupange jinsi ya kumtoa Tunda moja kwa moja. Leo anataka kumtoa Tunda kwako ili amrudishe kwa Gabriel! Ataniona mbaya. Hakika sitakubali kabisa.”

“Sasa kwa kuwa mlianza na yeye hayo mazungumzo, nafikiri ni vizuri mkaendelea na yeye mwenyewe. Mpigie simu kumtaarifu kuwa upo hapa unataka kumuona.” Bethy akashangaa sana. Hakutegemea kama Net angejibu hivyo tena taratibu tu bila hata kuonyesha hasira.

“Simu yake haipo hewani tokea jana usiku nilivyompokonya Gab simu wakati anazungumza naye na kumwambia nimetambua hila yake.” Bethy alijibu akionyesha kuishiwa nguvu kabisa. “Basi msubiri tu. Lazima atakuja hapa. Na kama unaharaka, naweza kukupa kalamu na karatasi ukamuachia ujumbe.” Bethy akakaa. “Mimi naona nimsubirie tu.” “Karibu.” Net akageukia kompyuta yake, akaendelea na shuguli zake. Kimya.

 Baada ya nusu saa akamsikia secretary wa mama yake ameingia. Net akampigia simu. “Yupo mgeni wa mama hapa. Amefika mapema. Naomba umpatie huduma.” Bethy akajua ndio anafukuzwa ofisini kwa Net. Bila kusubiri kutolewa, akasimama na kutoka mwenyewe bila kuaga.

Baada ya dakika tano akasikia sauti ya mama yake, akajua ameshaingia. Palizuka ukimya wa gafla, kisha akasikia Bethy akianza kupayuka. Net alishindwa hata kufanya kazi kwa kelele. Siku hiyo ndipo walipomjua Bethy mwenywe. Sio Bethy msomi wa kileo anayezunguka na kiatu cha juu maofisini na kuongea kingereza muda wote kama anayejifunza kiswahili. Wala siye yule wa kanisani, anayeongoza kwa sifa njema na mfano bora wa kuigwa. Aliwabadilikia, akawa kama tembo aliyejeruhiwa.

Aliongea bila kumeza mate. Kila mama Cote alipotaka kumtuliza, Bethy alimjia juu vibaya sana. “Huwezi kunichezea mchezo wa kitoto mimi! Unaning’ata huku unanipuliza! Nimekutambua na kukukamata.” “Sio kweli Bethy. Punguza hasira.” “Basi chukua simu yangu na ukanushe kwa Gabriel yote uliyomwambia jana usiku. Sasa hivi.” Net akasikia kimya.

“Si umeona mwenyewe?” “Hatuwezi kufanya mambo kwa hasira Bethy. Twende ofisini kwangu tukazungumze na kupanga, tukiwa tumetulia.” Net akachukua funguo zake za gari, akatoka. “Shikamoo mama.” Bila kusubiria kujibiwa, akapita katikati yao na kuondoka pale ofisini.

Net kwa Tunda.

N

et hakupiga hata simu, Tunda akashtukia anakaa mbele ya kiti chake. Akaanza kucheka. “Utauwa watoto kwa njaa, dady! Saa mbili na nusu hii upo kwa mpenzi!” “Nina hamu na wewe.” Tunda akacheka sana. “Kwa mapenzi hayo, naona nikutoe kwa kifungua kinywa.” “Afadhali. Twende.” Net akasimama haraka, Tunda akachukua funguo na pochi yake wakatoka.

“Si tunatumia gari yangu?” “Mimi ndio nimekwambia nakutoa Net. Mbona hivyo!?” “Kwa hiyo naendeshwa?” “Nabembelezea ndoa mwenzio.” Net alicheka sana huku akitoka. “Kweli ndoa unaitaka.” “Si kidogo!” Tunda akajibu na kisauti chake cha upole. Wakapanda kwenye gari ya Tunda, mwenyewe akiwa dereva.

“Sasa ikitokea inanilazimu mimi kurudi nchini Canada, utafanyaje? Utakuwa tayari kunifuata?” Tunda akamtizama Net, wakati anafunga mkanda wake, kisha akanyamaza nakuondoa gari. Hakujibu na tabasamu lilimuisha kabisa usoni. Net naye akanyamaza kama kumpa nafasi yakufikiria. Tunda aliendesha mpaka kwenye mgahawa aliotaka wakape kifungua kinywa. Akagesha gari. “Twende ndani tukapate kifungua kinywa.” “Asante. Maana asubuhi hii ingeweza kupita bila kula.” Net akashukuru wakati akishuka.

Akazunguka kule alipokuwepo Tunda. Akambusu kidogo tu. “Umependeza sana Tunda. Upo nadhifu.” Tunda akacheka kidogo akiwa amebadilika kidogo usoni, na Net alimuona. “Asante.” Akashukuru kwa hizo sifa. Net akamshika mkono wakaingia ndani. Hawakuwa wamekwenda mbali sana na ilipo ofisi ya Tunda.

          “Unaondoka Net?” Tunda akauliza kwa kupooza mara baada ya kukaa chini. “Mimi ndiye niliyekuuliza wa kwanza, Tunda. Itakuaje kama naondoka, utakuwa tayari kuondoka na mimi?” Net naye akauliza. “Wewe unajua maisha yangu mpaka sasa Net. Nimehangaika sana kufika hapa nilipo. Na sasa hivi ndio kabisaa. Nategemewa na wazazi wangu na wadogo zangu. Nawaachaje?” Net akainama hakujibu. Ndipo Tunda akajua yale hayakuwa mazungumzo tu. Muhudumu alifika akawauliza wanachotaka, wakaagiza, nakuondoka.

“Kwa nini tusifikirie kuishi hapa Net, mpenzi wangu? Tafadhali naomba hapa ndio iwe kipaumbe kwetu. Ndio kwa mara ya kwanza na mimi napata wazazi wangu. Yule wakili wa baba, anasema kati ya miezi mitatu mpaka sita baba anaweza  kutoka. Haya, ijumaa nataka kumpeleka mama kwa mwanasheria, ili wazungumze. Nina mambo ambayo yote yananihitaji Net. Nikiondoka sasa hivi nitakuwa nakimbia.” Net kimya akabaki akimsikiliza. Alimuona ameshakuwa mwekundu.

“Naomba tushauriane Net. Usikae kimya.” “Nakusikiliza Tunda.” “Ndio hivyo. Nimekuomba tufikirie kuishi hapa tafadhali.” “Na mimi nimekuuliza kama ikinilazimu kuondoka, itakuaje?” Tunda akafikiria kwa haraka. “Kwa nini ikulazimu kuondoka?” Tunda akauliza swali. “Unajua mimi sio raia wa Tanzania.” Tunda akakunja uso. “Nilizaliwa Canada, na baba ni mtu wa huko. Ukiniona nipo hapa, nipo kwa kibali maalumu.” “Kibali gani?” “Mama alikuwa akinitafutia kibali cha kazi.” Ni kama Tunda akapata majibu yote.

“Nikuulize swali Net?” “Niulize tu.” “Kibali kimeisha?” Net akatulia kidogo. “Kinakaribia kuisha, na sidhani kama kuna mazingira ya kuja kuombewa tena.” Tunda akaelewa. “Na sasa hivi hapa pamekuwa pagumu sana. Lazima kuwa na kibali, lasivyo unafukuzwa. Miaka mitatu iliyopita niliingia matatizoni, nusura kurudishwa, ndio mama akahangaika nikafanikiwa kubaki. Sasa kwa sasa, sidhani kama hiyo nafasi ipo tena.”

“Ninachojua nakupenda Net. Naomba tupate muda wakufikiria kitu chakufanya. Tuzungumze na wanasheria, tuone watatushauri vipi.” “Swali langu lipo pale pale Tunda. Je, ikinilazimu kurudi kuishi Canada, utafanyaje?” Tunda alitamani kama kuchanganyikiwa.

Ni kama ndio kila kitu kinaanza kujiweka pamoja na kuleta picha inayoeleweka. Tunda anastawi kwenye nchi ya wengi wanaolia pesa ngumu. Amka yake kitandani, ndio ingiza yake pesa bila shida, bila elimu kichwani. Leo Net anataka kumtoa katikati ya mafanikio yake! Ndio jina Tunda limeanza kuvuma kwa kazi nzuri ya upambaji anayofanya. Kwa mara ya kwanza ameweza kuweka heshima kwenye jamii kwa jasho lake. Amemiliki gari na kununua kiwanja japo bado hajaanza hata kujenga. Lakini vipo kwa jina lake. Leo aondoke!

Akanyanyua uso kumtizama Net akakuta anamtizama kama anayemsubiria. “Nitakuwa na wewe Net.” Tunda akajibu kama mtu anayesema ‘nitafanyaje sasa?’. “Unauhakika?” “Nimehangaika sana kujijenga Net. Wewe unajua. Lakini najua sitakuwa na amani kuishi mbali na wewe.” Akaona uso wa Net umebadilika kama alitepata aghueni.

“Nashukuru Tunda. Asante sana.” Akashukuru Net na kumshangaza Tunda. Kumuacha Tunda nchini, ni kama kumtangazia Gabriel ameshindwa na anamwachia Tunda. Ilishamnyima raha. Jibu la Tunda lilikuwa na maana kubwa sana.

“Nakushukuru sana.” Akarudia Net. “Kwa nini Net? Kwani ndio unataka kuondoka?” “Ngoja nikwambie ukweli Tunda. Hali nyumbani sio nzuri. Na mimi hapa Tanzania nina mali kidogo sana. Ile nyumba tu, lakini nayo ipo kwa jina la mama. Ipo chini ya kampuni yake. Mimi siruhusiwi kumiliki chochote hapa. Mama amebadilika vibaya sana. Hakuna jinsi nikakaa naye tena chini nikazungumza naye, tukaelewana.” “Kwa nini?” “Kwa sababu kwa mara ya kwanza, nafanya kitu ambacho yeye hataki mimi nifanye.” Tunda akaelewa kuwa tatizo ni yeye.

“Kwa hiyo umeelewa wakati nilio nao?” “Nakururumia Net. Nikusaidiaje?” “Kuniahidi hata iweje, utahakikisha unakuwa na mimi, kama ulivyosema. Popote pale. Hata iweje, hutabadilika.” Tunda akavuta pumzi kwa nguvu. “Na wazazi wangu?” “Hapa ni nyumbani Tunda. Utakuja muda na wakati wowote watakao kuhitaji. Na baba anakaribishwa hata kuja kututembelea kule. Unakumbuka ulisema ulitaka akitoka, uishi naye kwa muda mpaka awe tayari kujitegemea?” “Ndiyo. Maana atakuwa hana pakwenda. Nataka mimi ndio nimtunze mpaka apate nguvu au arudie hali yake.”

“Basi, nakuahidi nitakusaidia kuhakikisha mambo yote yanakaa sawa. Sitakubali utelekeze wazazi. Mtafutie mama mahali pakuishi ili maisha yake yaendelee na watoto warudi shuleni. Mkabidhishe kwa mama Penny ili amsaidie kumuelekeza kitu chakufanya. Hata kama ni ile biashara yako yakupamba. Anaweza kuendeleza kwa jina lako. Halafu tutaendelea kumfuatilia baba. Mimi mwenyewe nitakuwa nikimfuatilia wakili wake. Ukihitajika kuja, nitakusindikiza. Nije kama mtu wakutembea tu. Lakini tukijua nyumbani kwetu ni Canada.” Tunda akavuta pumzi kama aliyechoka haswa. Lakini Net alipata ujasiri wa gafla. Furaha na tumaini vikaonekana vimerejea tofauti hata na vile alivyokuwa ameingia ofisini kwa Tunda.

“Mbona kama unaongea kama vile unataka tuondoke kesho!?” Tunda akauliza kwa wasiwasi. “Hapana. Week ijayo na Nana.” Tunda aliishiwa nguvu. Ndio kesi ya baba yake ilikuwa imefufuliwa. “Net!” “Sina jinsi Tunda. Ujue nikiondoka week ijayo kumrudisha Nana, sitaruhusiwa kurudi tena hapa nchini.” “Naomba nikufuate Net. Niweke sawa mambo yote ndio nije!” Ule uchangamfu wa gafla wa Net, ukamwisha tena gafla. Net anawindwa na Gabriel. Tena sasa hivi ndio anatangaza bila woga, anamtaka mwanamke wake. Net hakutaka aondoke amwache tena Tunda hapa nchini.

Akamkumbuka Chloe. Mchumba aliyekuwa akitaka kumuoa. Alipomuomba aje naye Tanzania, alikataa na kumwambia yupo radhi kumsubiri huko huko Canada lakini si kuwa naye Tanzania. Mwishowe wakaishia kuachana. Akajua mwisho wake ni kuachwa na Tunda pia. Akabaki kimya.

“Nakuahidi kukufuata Net. Naomba muda tafadhali. Hata hivyo Visa ya Canada si rahisi kupata kama unavyodhani.” Net akakunja uso. “Umejuaje?” Tunda akatulia kidogo. “Tunda?” “Kuna kipindi nilitaka kusafiri na Gab. Hakujua kama ingechukua muda mrefu hivyo. Nilifanya vipimo vyote walivyotaka. Tukatuma maombi yote. Tulisubiri zaidi ya majuma matatu, ikabidi Gab aende tu. Alisema asingeweza kusubiri zaidi. Akaniacha kwa makubaliano kama hiyo Visa ingetoka akiwa bado yupo Canada, nimfuate. Mpaka anarudi, ilikuwa bado. Ilichukua kama majuma 6 hivi.” Net akabaki akimtizama.

“Ninachotaka kukwambia ni kuwa, huwa inachukua muda mrefu.” Tunda akaona aendelee tu. “Inaonekana mlikuwa kwenye mahusino na Gabriel, sio kwamba ni mteja tu!” “Naomba usianze Net!” “Nini Tunda?” “Kipindi kile Gabriel alikuwa kwenye matatizo makubwa sana ya ndoa na mkewe. Ilibidi mimi kuwa karibu naye zaidi, au niseme nilitumia udhaifu wa mkewe, ili kuweza kumvuta Gabriel. Na ni kweli nilifanikiwa.”

“Na kwa kuwa Gabriel alikuwa akinipa pesa nyingi, nilipunguza wateja wengi sana ili kuwa naye kila anaponihitaji. Yeye pekee ndiye mteja ambaye hakuwa akisubiri. Muda na mahali popote alipotaka niende, nilienda bila kuchelewa. Mara nyingi alikuwa hawezi kulala mpaka tuzungumze. Ndio maana siku ile aliponifukuza, sikuamini. Gabriel alionyesha mapenzi makubwa sana kwangu na katika wote, Gab aliniheshimu. Japo sikujua kama alitaka kumuacha mke wake sababu yangu.” “Hakukwambia?” Net akauliza. Lakini alishakuwa anamamiumivu ya kupitiliza. Akaanza kuelewa ni kwa nini Gabriel alikuwa akimng’ang’ania Tunda.

“Hapana Net. Huo mpango wa kumuacha mkewe nilimkataza. Na nikawa nikimtia moyo abaki kwenye hiyo ndoa kwa ajili ya watoto. Japo ni kweli nilihisi wasingeweza kudumu. Bethy..” Tunda akasita. “Anyways. Sikujua kama anataka kumuacha mkewe kwa ajili yangu. Mimi nilijua ni kwa sababu ya matatizo waliyo nayo. Ugomvi ulikuwa ni kila wanapokuwa pamoja, nyumbani. Kwa hiyo simu za usiku kutoka kwa Gabriel nilikuwa nikizitegemea mara kwa mara.” Tunda hakujua ni kwa jinsi gani anamuumiza Net.

“Kwa hiyo wewe ukawa kama ndio usingizi wake?” Net akauliza akisikika amejawa wivu haswa, nakumfanya Tunda atulie kidogo. Net akabaki akimtizama. “Sijui Net. Lakini yeye ndivyo alivyokuwa akipenda kusema hivyo. Amekwambia hivyo na wewe?” Tunda akauliza kwa upole. Net akamwangalia tu.

“Net, mpenzi wangu, hayo ni maisha nimeishi nyuma. Gabriel aliishi na Nancy ambaye alishatolewa. Anayeishi hapa ni Tunda uliyempenda kabla kina Nancy, Mary, Anna, Ani sijui na wengineo hawajaanza kuishi. Tunda huyu wa sasa anakupenda wewe Net, na nitahakikisha unanioa. Nitakung’ang’ania tu mpaka unioe.” Tunda alitaka Net acheke. Lakini akabaki ameinama.

Akamkanyaga. “Bwana acha mawazo ya mbali wakati mkeo nipo hapa!” Net akatabasamu kinyonge. “Nahisi kama nimekwama Tunda.” “Kwani bibi yeye ndiye anayetaka kuondoka mapema?” “Kwanza ujue sio mapema. Huwa hakaagi hapa zaidi ya siku 10 sababu ya afya yake, shuguli zake kule na hali ya hewa ya hapa. Halafu sina mazingira mazuri yakumuweka hapa. Pameshaanza kuchafuka na bibi ni mtu wa maneno mengi, lakini ya amani. Sio ugomvi. Hajui kugombana. Hata Papa alikuwa akisema kwa kila mtu kuwa, ndio ilikuwa siri ya kudumu kwa ndoa yao.” Akaendelea Net.

“Unajua walikuwa na ndoa ya miaka zaidi ya 50?” “Sikuwa nikifahamu.” Tunda akajibu. “Basi walikuwa na ndoa ya muda mrefu sana. Na walikuwa wakipendana sana. Papa alikuwa mkali sana na mtu wa misimamo na kanuni. Wafanyakazi walikuwa wakimuogopa sana. Lakini Nana aliweza kuishi naye vizuri na kushangaza kila mtu anayemfahamu papa. Alikuwa na uwezo mkubwa sana wakumtuliza. Hata awe amekasirika vipi, lakini Nana alikuwa akiweza kugeuza hasira za papa kuwa kicheko mpaka papa anajikuta ametulia.”

“Walifanya kazi na Nana miaka yote wakisaidiana mpaka papa anaugua sana, ndio na Nana naye ikabidi akae nyumbani akimuuguza. Pale alipo ana kampuni kubwa sana ambayo bado anaendesha. Hakuna kinachofanyika huko bila yeye kuidhinisha na kuweka saini. Pale unapomuona yupo hapa ni kama yupo nusu ofisini. Lazima kila siku afanye kazi kwa simu na kompyuta kuendesha kazi kule.” Tunda akatulia kidogo.

“Tutafanyaje sasa?” Tunda akauliza akionekana wazi hayupo tayari na jibu la Net.  “Hata Nana anataka twende wote Tunda. Na Maya pia.” Tunda akashangaa kidogo. “Sasa kwa nini hukuniambia muda wote huo?” “Sikujua kama nitakuwa kwenye wakati huu Tunda. Mambo yanazidi kuwa magumu.” “Ni nini?” Net akaona heri amwambie Tunda ukweli kuanzia mwanzo wa hivyo visa vinavyoendelea mpaka asubuhi hiyo Bethy amefika ofisini kwao, ndio maana akamfuata ofisini kwake, na kumuacha Tunda ametoa macho.

“Net!” “Kweli. Ndio hivyo. Gabriel anatangaza vita na mimi kwa kuwa anadai nimempokonya mwanamke wake. Mama anahofia mali na Bethy anamtaka mume wake.” “Bethy anataka mali tu wala si Gab! Maana nilishamsikia akitukana kwenye simu tulipokuwa n..” Tunda akaona anyamaze baada yakuona ameropoka.

“Wewe usiwe na wasiwasi Net.” Akabadili mazungumzo kwa haraka Net akabaki akimtizama kwa kumsuta, Tunda mwenyewe akaanza kucheka. “Unanichanganya Tunda. Na hivyo unavyoonekana unamjua Gab kwa undani hivyo! Ndio naona mimi si kitu.” “Hamna bwana Net. Acha kuwa na wasiwasi.” “Lazima niwe nao Tunda. Unaonekana unamfahamu Gabriel kuliko hata mimi.” “Ni kweli. Wala hujakosea. Wewe ni msiri sana Net. Na unaweza kubeba mambo yako mwenyewe. Nakufahamu kupitia mama yako tena akiwa amekasirika. Lakini sio Gabriel. Nafikiri na wewe unaweza kuwa unamfahamu Gab. Hawezi kubeba jambo linalo muumiza.”

“Ni kwako tu Tunda. Mimi nimekuwa na mahusiano ya muda mrefu na Gab, lakini sikujua kama anamatatizo ya ndoa ya kiasi hicho. Kanisani wao ndio wana ndoa yakutolewa mfano. Hakuna aliyekuwa anajua. Mpaka wewe ulipoingia kwenye picha, ndio Gabriel akawa kama amechanganyikiwa kusema mabaya ya mkewe. Lakini hakuna aliyetilia sana maanani, wengi tulijua ni kwa kuwa amechanganywa na penzi la wizi. Anataka tu kutafuta sababu ili amuache mkewe.” “Wale watu wanamatatizo ya kweli Net. Mpaka Gabriel alikuwa anahisi Bethy anaweza kuja kumuua ili achukue yeye mali zake.” Net akakunja uso.

“Yeye si ni mkewe? Sasa cha Gab si ndio cha Bethy?” “Sio kwao, Net. Wale watu mpaka wanasikitisha. Gabriel alinisimulia mwanzo wao. Yeye alipomuoa hakuwa na kitu. Anasema Bethy alimnyanyasa sana. Na kwa kuwa Bethy alitoka kwenye pesa, na alikuwa na kazi nzuri, ndio ilikuwa kabisaa. Hata nyumba yao ya kwanza waliyoenda kuishi baada ya kuoana ilikuwa ya Bethy. Gabriel anasema alioa akitokea kwa wazazi.” “Gabriel mtoto wa mama yule. Huwa hakui.” Wakacheka kidogo. “Anaonyesha. Hata akijikwaa kidogo tu, atalalamika kama amejikata kidole kizima.” Net akamtizama. “Unaniogopesha Tunda!” Tunda alicheka sana.

“Mama yake mwenyewe anampigia simu utafikiri mtoto mdogo, kujua alipo kila wakati.” “Nakusikiliza tu Tunda.” Tunda akazidi kucheka. “Mimi nakuchokoza tu bwana Net! Mimi mkeo. Acha wahangaike tu. Basi ndio Gab anasema Bethy alihakikisha wanasaini prenup mapema sana kabla hata ya ndoa.” “Aaaah! Sasa hivi ndio naelewa. Kwa hiyo ndio maana Bethy anahangaika?”

“Sana. Pale alipo hata hajui mumewe ana kiasi gani benki. Mimi nilikuwa naichezea pesa ya Gab, mpaka basi. Alikuwa ananiachia kadi zake za benki na hundi zilizosainiwa. Ananiambia niwe huru. Sasa nikawa namuuliza mkewe si atagundua? Ndio akanipa hiyo story yao ya maisha. Kuwa tokea mwanzo wanaingia kwenye ndoa, Bethy hakutaka mali zake zishikwe na Gabriel. Na Gabriel anasema Bethy alihakikisha anaelewa na wanaishi hivyo.”

“Ni kweli alikiri kwangu kuwa yeye alikuwa mtoto wa mama. Hawazi mbali. Ilimradi anakula na kuishi vizuri, hakuwa na shida. Sasa alipoingia kwenye ndoa, akawa pia hana hata kazi ya maana. Bethy akawa anamfichia pesa. Wakati mwingine anamnyima usafiri, inabidi mama yake ndio anakwenda kumchukua nyumbani kwao na kumpeleka anakotaka yeye Gab. Wakawa wanaishi pamoja na Bethy lakini hajui anaingiza kiasi gani wala wanaishije.” Tunda akaendelea.

“Si unajua Bethy ana cheo kikubwa huko kazini?” “Sana na yupo very smart. Anaakili sana Bethy.” “Basi ndio hivyo. Wakati huo mumewe hana kitu, Bethy alikuwa akiingiza pesa kweli. Anasafiri mchana na usiku kikazi. Gab anasema tena alikuwa wala haagi kwa kiburi. Wakati mwingine anampigia simu akiwa tayari yupo safarini tena kumpa maelekezo ya kitu gani chakufanya hapo nyumbani. Ila anasema, alichokuwa akihakikisha ni pale nyumbani kunapikwa, kuna umeme na maji wakati wote. Basi. Gabriel akawa anatunzwa na mama yake akiwa kwenye hiyo ndoa, mpaka mama yake akamsema sana Gabriel ndio akabadilika nakuanza kuchangamka.” Tunda akaendelea kumsimulia Net na kumfungua macho zaidi.

“Alinisimulia wakati wanaishi Canada ni kama hakusoma sana au hakumaliza chuo, mambo kama hayo. Akaja kusomea hapa Tanzania. Akapata shida yakupata ajira. Akamuomba Bethy mkopeshe pesa ili aanze biashara, nasikia Bethy alimkatalia.” Net akashangaa.

“Kwa nini!?” “Alimwambia anamuona hana akili za maendeleo, yeye hawazi mbali kwa hiyo anaona atapoteza pesa yake, ni bora aendelee kumlisha tu. Ndio ikabidi tena arudi kwa wazazi wake. Wakamkopesha pesa. Anasema ndio akaanza hiyo biashara yake, sasa Bethy ndio akaanza fujo. Anataka kujua mambo ya Gabriel wakati yeye alikuwa akimficha. Na Gabriel anasema, amejiapia, haitakaa ikatokea akamshirikisha mali zake Bethy, wala hatampa pesa. Amesema anachofanya ni kama yeye. Kuhakikisha wanaishi pazuri, amempokea mzigo wa kulisha familia, ada za watoto na kumpa yeye pesa za matumizi kama mke mwenye kazi inayomuingizia pesa nyingi. Inamaana anampa pale akijisikia.” Net alibaki amechoka.

“Sio alichotuambia na mchungaji. Sisi ametuambia Bethy ni mkorofi, anafujo, mbinafsi sana, hataki kumuona Gabriel anasaidia ndugu zake na anatumia tendo la ndoa kama fimbo yakumchapia. Anafanya naye mapenzi pale anapotaka Bethy, labda awe anampa pesa anayokuwa amemuomba, au akiwa amefurahi yeye ndio anaweza kumkubalia.” “Hata hilo pia aliniambia.” Net akapandisha nyusi moja juu huku akimtizama Tunda.

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

Mambo yanazidi kuchanganya, nini kitaendelea? Usikose muendelezo.

CONVERSATION

0 Comments:

Post a Comment