T |
unda alicheka sana vile Net
alivyomtizama, akajua ameropoka akamuuliza swali kubadili mazungumzo. “Sasa
nyinyi mkamshaurije huyo Gabriel na mkewe?” “Waliitwa na wachungaji na wazee
wakanisa. Wakasikilizwa na kupewa ushauri. Lakini Gab akasisitiza anachotaka ni
talaka, akuoe wewe.” “Sio mimi. Amuoe Nancy ambaye alishaondoka.” Tunda
alijaribu kumrekebisha Net huku akiendelea kucheka.
“Mimi
naona nikuchukue tu twende wote ndio akili yangu itatulia. Nikikuacha hapa
naweza kuchanganyikiwa huko bure! Kwa jinsi unavyomfahamu Gabriel na yeye
anavyo kulilia! Mimi naona twende tu.” Tunda alizidi kucheka. “Anamfahamu
Nancy. Hamjui Tunda hata kidogo. Net wangu ndiye anayemjua Tunda mwenyewe.”
“Wewe ni poze tu!” “Mimi na wewe Net?” “Bado kabisa Tunda. Naona mpaka nikuoe.”
Tunda alizidi kucheka.
“Sasa
kuna jambo la mwisho linalonisumbua. Maana sasa hivi inabidi nikwambie kila
kitu ili ujue.” Tunda akatulia.
“Si na
mimi sasa hivi unanifahamu kama Gabriel?” Tunda akaanza kucheka tena. “Ujue
uache kujifananisha na Gabriel wewe Net! Yule sio na wala hatakaa akawa
mpinzani wako hata siku moja.” “Kweli Tunda?” “Kabisa. Wewe wala usimsikilize
Gab. Na wala usimuwekee mazingira yakumuonyesha unawasiwasi au mpo wapinzani.
Yeye anamjua Nancy, wewe unammiliki Tunda.” Net akacheka.
“Haya
Tunda.” “Kweli Net. Mimi sikupambi. Hakuna jinsi ikatokea nikarudiana na
Gabriel tena. Yale ni maisha ninayojutia kuyaishi. Wala sifurahii hapa na
kutamani kurudi. Yote niliyafanya kwake ili kufikia pesa yake. Sasa wewe
unafikiri bila kuwa vile, angefikia kuniachia kadi za benki na cheki?” Net
alibaki akimtizama. “Ilikuwa lazima niwe kinyume kabisa na alivyo Bethy ili
kufanikisha malengo yangu. Nancy alikuwa tapeli wa mapenzi. Acha hata kufikiria
hilo, ni kama unanirudisha huko. Naomba sisi tuendelee na yetu Net.” Tunda
akamtuliza.
“Unajua
tukisita sita na kuwasikiliza wanachoongea juu yetu, tutajikuta tunakwama
kwenye njia mbili na hatutaweza kwenda mbele. Tunaishi nyuma, na utashindwa
kunisaidia kama ulivyoniahidi kunisaidia kuishi maisha haya. Tutajikuta
tunaishi nyuma na sasa. Mbele hatuendelei. Tafadhali usiyumbishwe Net. Wewe
ndio nguzo yangu. Ukianza kuangalia nyuma na kusikiliza watu kama Gab, ujue
utanipoteza na mimi. Tafadhali Net, tulia.” Net akavuta nguvu kwa nguvu na
kukaa wima.
Tunda
akasimama na kwenda kumbusu shavuni. “Nakupenda Net.” Akamnong’oneza sikioni.
Net akacheka akionekana ametulia. Akamshika vizuri, akambusu mdomoni kwa muda
tu. Net akiwa amekaa, Tunda amemuinamia. Akambusu tena na tena. Tunda
akafurahia. Maana alilipata busu kama hilo mara ya mwisho ilikuwa jumapili.
“Nakupenda Tunda.” “Nashukuru Net. Nikwawambie siri yangu ndipo tuendelee na
mipango yetu?” Tunda akarudi kukaa.
“Niambie.”
“Nimekuwa na Gab na wanaume wengine wengi tu. Lakini katika yote niliyofanya,
nilitunza busu langu.” Net akashangaa kidogo. “Kwamba ulikuwa hubusu midomo
au!?” “Hata mmoja.” Net akakunja uso. “Hata Gabriel!?” Net akauliza kama
asiyeamini. “Hata yeye.” “Sadiki!?”
Akaendelea kuhoji kwa mshangao zaidi. Tunda akatingisha kichwa kukataa.
“Kwa nini!?” Tunda akacheka kidogo.
“Nilijua
watu wote wananitumia tu. Hakuna anayenipenda mimi kama mimi Tunda. Na mimi
nilijua nawaibia. Nikaogopa kwenye huo wizi, nisije nika fall in love, au
niseme nikapenda halafu nikaja kukimbiwa. Namaanisha ni kitu nilichokuwa
nimejiwekea makusudi ili kujikumbusha kila wakati ni nini nafanya ili
nisipitilize na kuumia kihisia na kiafya. Sijui unanielewa?” Tunda akamuuliza
Net.
“Gabriel
ni mmoja wa walio jaribu sana kunishawishi katika hilo lakini hapo nilichora
mstari hata kwake Gab. Nilikataa kabisa. Nilitaka siku nitakapo kubali kumbusu
mtu mdomoni, iwe nimefika mwisho wa kila kitu. Iwe ni ishara kuwa nimejiachia
kwake kwa asilimia zote. Yaani kwa mara ya kwanza niwe nimejifunga kwa huyo mtu
ambaye atanikubali mimi Tunda. Ni wewe Net. Nimekubali kujifunga kwako kwa ile
garama kubwa ambayo umelipa kwangu. Sina jinsi nitakuwa na furaha na mtu
mwingine isipokuwa wewe. Kwako sijifichi. Kwa hiyo naomba uwe na uhakika na
mapenzi yangu. Nakuahidi nitatulia kwako tu.” Ilimgusa sana Net.
“Nashukuru
Tunda.” “Hii nimekwambia makusudi pengine itakusaidia kwa upande mmoja na yale
yanayokukabili sasa hivi kwa Gab. Tafadhali usije wahi kujifananisha naye.
Tupange mipango yetu au upange mipango yetu bila kutishwa na yeyote juu yangu.
Nakupenda nikiwa nahitaji mapenzi tu kwako, sio pesa zako Net. Nakuhitaji wewe
Net.” “Hilo najua Tunda. Ila uliloniambia ni kweli limeniongezea ujasiri.”
Tunda akacheka.
“Basi
tuendelee na mipango yetu.” “Nyumba niliyonayo nimeshakusimulia. Nimejenga kwa
pesa yangu, lakini kwa kuwa mimi sio mzawa, imenibidi kuiweka chini ya jina la
kampuni ya mama. Hati inaonyesha ni ya kampuni ya mama na ninayo. Sasa naomba
nikuuzie ili ikitokea mama anataka kuninyang’anya niwe nimeshauza nyumba
yangu.” “Hapana Net! Sio kwa jina langu mimi. Unataka mama yako aje aniue!?
Hapana Net.” Tunda alikataa kabisa.
“Nisikilize
Tunda. Tanzania ni nyumbani, lazima kurudi. Tukirudi tutaishi wapi? Nataka
ibakie kwa jina lako ili tuwe na kwetu hata hapa.” “Uwiii Net! Unataka
kuniingiza matatizoni wewe!” “Sina jinsi. Sina mtu ninayemuamini ambaye najua
hatakuja kunibadilikia baadaye. Watu wanabadilika Tunda. Na mimi shida yangu
sio pesa, ni ile nyumba. Nilishaona watoto wangu wakicheza mle ndani.
Nilishaona jinsi tunavyoishi mle ndani. Sitaki siku moja mama aje aiuze kwa
hasira au waje wamfilisi na kuichukua nyumba yangu.” “Unahisi wanaweza kuja
kumfilisi?” Tunda akauliza.
“Mama
ameruhusu hasira zimtawale hataki kufikiria. Ile kampuni anasahau kuwa
namsaidia kuiendesha kwa asilimia kubwa sana. Nina uhakika itachukua muda mfupi
sana kuharibikiwa baada ya kunifukuza mimi kama alivyokufanyia wewe Arusha.
Nimeona hapa kuna watu wachache sana wachapakazi, wanaojituma na waaminifu.
Kumpata mtu wa hivyo kwenye kampuni yako! Akakufanyia kazi nzuri, sio kitu
rahisi. Unaweza kumpata mchapakazi, lakini baadaye anaingiwa tamaa, anaanza
kuiba. Mama hilo analisahau wakati limeshamtokea.” Net akaendelea.
“Na kwa
maneno aliyozungumza jana, najua atatekeleza nia yake kwa haraka.” “Nia gani?”
Tunda akaendelea kuuliza kutaka kujua kila kitu. “Aliongea kwa kuropoka sababu
ya hasira kuwa, anaweza kunipokonya kibali cha mimi kuishi hapa nchini.” “Hivi
anao huo uwezo!?” “Kabisa. Kumbuka kisheria yeye ndiye anayeonyesha ananiweka
hapa nchini. Kwamba ni mwajiri wake. Ni kiasi cha kunifukuza kazi kwa maandishi
na kuniripoti kuwa amenifukuza kazi, basi. Itanilazimu kuondoka ili niwe mbali
na wewe.” Tunda akanyamaza.
“Ndio
ujue changamoto zinazotukabili na wewe usaidie sio kulinda nafsi yako.”
“Ninavyojitahidi kujiweka mbali na hizo mali ambazo mama yako anazonihubiria
kila akiiona sura yangu!” “Kwa hiyo na wewe unataka tuwe na ndoa kama ya
Gabriel na Bethy?” “Hapana Net.” “Sasa mbona hutaki hata nikusaidie hata
shilingi wakati umeshasikia ninazo pesa.” Tunda akaanza kucheka.
“Kumbe
kweli unazo pesa?” “Sasa wewe unafikiri kwa nini mama anahangaika hivyo?” Tunda
alizidi kucheka. “Lakini wakati wote wewe umekuwa kunionyesha kwa vitendo vile
unavyofanya kazi kwa bidii Net. Sijawahi kukutana na wewe popote kama haupo
kikazi. Mimi nikajua ndivyo unavyoingiza pesa yako. Kwa jasho lako.”
“Nisikilize Tunda. Ni kweli nimekuzwa kwenye mazingira ya kitajiri sana. Lakini
kila pesa ninayomiliki, babu alihakikisha tokea napata akili yangu, naifanyia
kazi.” Tunda akatulia.
“Hajawahi
kunipa pesa kama kunipa tu. Hata nilipokuwa na shida, alinipa kazi ndipo
ananilipa. Nakiri wakati mdogo alikuwa ananipa kazi zisizoendana na malipo,
lakini nimekuja kuelewa alikuwa akinifundisha. Nimekuja kukua hivyo hivyo.
Hakuna pesa kwenye akaunti yangu ambayo sio jasho langu. Kufanya kazi kwa bidii
ndicho ninachojua tokea mtoto. Na mimi sio kama Maya. Ukimwangalia Maya na
mimi, unaweza kufikiri tumelelewa na watu wawili tofauti. Lakini ni watu hao
hao.”
“Maya
alikuwa akipewa pesa ya matumizi kila week, na akitaka nyingine anapewa bila
kuulizwa swali. Lakini sio mimi. Kwanza babu alinikuza kutoomba pesa ila kazi
ili kupata pesa. Kwa kifupi ninazo pesa kwa kufanya kazi. Nikiwa hapa Tanzania,
namfanyia mama kwenye kampuni yake. Nikiwa Canada, nafanya kazi kwenye kampuni
ya Cote ya Canada, na huko pia nalipwa.” “Basi ndio maana naona kama wewe
unaweza kufanya kazi kwa bidii ukapata pesa, basi na mimi nifanye.” Net
akacheka.
“Sasa
wewe sio mimi. Mimi mwenzio pesa yangu ni yangu tu. Haiombwi na ndugu yeyote
labda niamue kumnunulia mtu zawadi. Nina uhakika nina kazi nyingi
zinazoniingizia pesa nyingi kuliko wewe. Nikikaa pale ofisini, nakuwa nafanya
kazi mbili au tatu kwa wakati mmoja na zote ninalipwa.” “Kivipi?” Tunda
akauliza.
“Kampuni
ya Cote hapa nchini ni ya mama. Cote ya Canada ni ya bibi na babu. Imesambaa
nchi na miji mingi sana. Babu alihakikisha nafundishwa lugha tano muhimu tokea
mtoto. Nina uwezo wakuziongea hizo lugha, na hii ya kiswahili, kama mzawa.”
“Net!” Tunda akashangaa. Net akacheka.
“Nilifundishwa
Tunda.” “Lakini na wewe unayo akili.” “Nikipaji. Babu alikuwa anasema hivyo.
Unajua kuna watu wanakipaji cha lugha tu. Uwezo wakuongea lugha nyingi bila
shida. Na pia kufundishwa. Sasa turudi kwenye swali lako.” Tunda akacheka.
“Babu
naye alikuwa akizungumza lugha nyingi sana. Yule hata ukimtupa kwenye kijiji
chochocte hapa Tanzania, angeweza kuongea kilugha chao.” Tunda akacheka. “Na
wewe unajua kilugha gani?” Net akacheka. “Nimekupita mbali sana kwenye kilugha
Tunda. Nikianza hapa! Utaona aibu unaweza kufikiri wewe ndio mgeni, mimi
mzawa.” “No way! Kilugha gani unazungumza Net?” Tunda akabisha kwa
mshangao. Maana aliuliza akijua wazi Net hajui kilugha chochote kutoka kabila
lolote Tanzania.
“Wewe si
unakijua kipogolo?” Tunda akaanza kucheka. “Net unanitania!” “Kama unabisha, ongea neno la kipogolo kisha nitakwambia
maana.” Tunda hakuamini. “Net! Kwanza kwa nini Kipogolo?” “Kwa ajili yako.”
Tunda akakunja uso kama ambaye hajaelewa. “Unakumbuka uliniambia ulikuja mjini
ulikuwa hujui kuzungumza kiswahili ila kipogolo tu?” “Net!” Net akacheka sana.
“Sasa
huwa nina mtindo wa kuchangamsha akili. Just for fun. Kujichangamsha tu. Hilo
neno la ‘kipogolo’ likanisumbua sana. Nikaona
isiwe shida. Sekretari wa mama ni mtu wa huko huko. Nikaanza kumwambia
anifundishe. Na nikamuomba aniandikie maana ya maneno 100 kwa kipogolo.
Nikamwandikia hayo maneno 100 kwa
kingereza na kiswahili, na kumuomba aandike hayo maneno kwa kipogolo.
Nikayaweza hayo 100 mpaka na jinsi ya kuweka ulimi. Nikaongeza mengine 100.
Kisha nikaanza kutengeneza sentensi. Yeye mwenyewe hakuamini. Akabaki kutoa
macho kama wewe.” Tunda akashangaa sana.
“Kweli
sikufahamu Net.” Net akacheka tena. “Turudi swali lako la mwanzoni, kisha
tuendelee na mambo yetu. Kwa hiyo. Kama nilivyokwambia, hiyo kampuni ya Cote
huko Canada, inayo matawi mengi tu, nchi mbali mbali. Sasa huwa nafanya kazi
kwenye upande wa mawasiliano na masoko. Nikiwa nimekaa hapa, nakuwa pia
mfanyakazi wao. Nawasiliana kwenye hizo nchi Papa au tuseme Nana anazokuwa
ananichagulie nifanye mwenzi huo. Matawi yake. Nafanya kazi nao kwa simu, na
kompyuta. Namtafutia na bibi masoko kama hivi mama. Namtumia hizo kazi,
nalipwa.” Tunda akabaki ametoa macho.
“Kwa
hiyo ndio hivyo ninavyoingiza pesa. Usijifananishe na mimi. Kubali nikusaidie
kila unapohitaji msaada. Umenielewa?” “Sasa hivi nimekuelewa Net. Lakini acha
nifanye kidogo. Na mimi nijione naweza kufanya kitu hapa duniani. Wewe
umenifundisha. Mungu amenipa uwezo, naona nitumike kidogo. Nakuahidi nikikwama
kabisa nitakwambia.” Net akacheka.
“Kweli
Net. Niamini bado sijakwama. Najua unasema ni msemo ninaokwambia kila wakati.
Lakini ni kweli sijakwama. Kila kitu kinachonikabili. Wazazi na mimi mwenyewe,
vipo ndani ya uwezo wangu. Na ninataka kujiona ni mimi ndiye nimefanya.”
“Nimekuelewa Tunda. Ila na mimi naomba niongezeke kwenye orodha ya wanaotaka
msaada wako. Fikiria jinsi yakunisaidia mimi na wanangu, wewe kama mama wa
familia.” Tunda akacheka sana.
“Haya
Nethaniel Cote, baba watoto wangu, at your service.” Net akacheka sana. “Nyumba
unauza kwa kiasi gani? Mwenzio sina hela ya kununua nyumba sasa hivi. Kodi tu
yenyewe inanitoa jasho!” “Wala usijali. Hiyo pesa itakuwa ya makaratasi tu.
Hunipi pesa yeyote ile. Ninachofanya ni kukumilikisha wewe. Kutoka Cote Ltd
kuwa Tunda.” “Natamani ingekuwa Tunda Cote tayari!” Net alicheka sana.
“Ndio
twende Canada tukafunge ndoa.” “Kwa nini tusifunge hapa ndio twende?” “Hapa
kuna sheria nyingi Tunda. Mpaka itangazwe na kusiwe na vipingamizi.” “Na tayari
tuna vipingamizi tena vya msingi sana!” Tunda akaongeza. “Umeona eeh! Naona
sasa unaelewa ninakopitia.” Net na Tunda walizungumza wakiweka mipango yao.
Mpaka wakafikia mwafaka.
Kwa mara
ya kwanza walitoka pale wakiwa wapo ukurasa mmoja. Kama watu wenye mipango inayo fanana. Wanania
mamoja kama wanaotaka kujenga familia yao kiukweli. Na kwa mara ya kwanza, Net
alijifungua kwa Tunda, Tunda akamfahamu japo kwa kiasi. Akaweza kumfariji na
kama kawaida ya Tunda, Mungu alimpa na yeye lugha ya ushawishi na alikuwa na
uwezo wa kufikiria kwa haraka. Ndivyo alivyoweza kuwatapeli kina Gabriel, Kinny,
Mbawala na wengine wengi. Sasa akampanga na Net. Akatoka pale kama Nathaniel
Cote wa zamani sio anayetishwa na mama yake na Gabriel.
Mipango Kabambe Yaanza.
Tunda Kwa Mama yake.
T |
unda alitoka pale akiwa
ameshakubali kuwa maisha yake sio Tanzania tena, kwa hiyo akaanza kujiandaa
kuacha familia yake vizuri. Na Net hivyo hivyo ila walikubaliana wasiwaambie
watu kwanza. Tunda alirudi hotelini kwa mama yake akamwambia aende naye akamuonyeshe
kitu. Alitoka hapo na wadogo zake, mpaka ofisini kwake. Mama yake alishangaa
maendeleo ya mwanae. “Hongera Tunda.” “Asante mama. Unapenda niwe nakuchukua
kwenda kupamba? Nitakulipa.” Mama yake akacheka.
“Kweli.”
“Nitashukuru Tunda. Sina pesa kabisa. Nitaanza hata kukusaidia kusafisha.”
Wakacheka.
“Mimi
mwenyewe nilifundishwa hivyo hivyo. Utaweza tu na utafurahia. Lakini inabidi
kutafuta pakuishi mama. Yule mwanasheria ambaye nimekwambia nitakupeleka kwake
amesema mambo ya kesi huwa yanachukua muda. Lazima kina Tom warudi shule. Na
pale nilipowakuta, mlipokuwa mkiishi na baba yao, sio mazingira mazuri kwao
kuendelea na masomo.” “Naelewa Tunda. Lakini hata sijui nafanyaje! Unajua kazi
nilifukuzwa?” “Kwa nini!?” Akasita
kumwambia ukweli Tunda.
Tunda
akaona asilazimishie kujua yasiyo muhusu, yeye afanye anachoweza. “Sababu ya
wizi.” Tom akadakia, wote wakamgeukia Tom. Tunda akakunja uso na kumgeukia mama
yake. “Na wewe walikusingizia!?” Akahisi wazazi wake wote wamepata tatizo
linalofanana. “Mambo yalikuwa magumu sana. Nilianza kuchukua madawa, na
kuwauzia watu. Hasa ya usingizi. Wakanitega na kunikamata. Hivi ninavyokwambia
nimefukuzwa kwa barua kutoka wizarani. Niliponea kufungwa. Nimejiharibia,
hakuna ninakoweza kuajirika tena kwa kazi hii ya uuguzi.” “Pole.”
“Mambo
yalikuwa magumu sana. Lakini najua sikutakiwa kuiba.” Tunda hakuwahi kumuona
mama yake akiwa mnyenyekevu vile. Alijirudi kama sio yeye. “Basi biashara
itakusaidia.” Wakazungumza hapo na mama yake, akimuonyesha anachofanya.
Kwa Net.
N |
et yeye akaondoka pale akiwa
amejawa furaha na ujasiri. Mambo yalikuwa yanakwenda vizuri kwa upande wake na
Tunda. Wapo ukurasa mmoja. Walishakubaliana waendelee na mipango yao,
wasiwajali mama Cote na Gabriel.
Kimya
kimya bila kumshirikisha yoyote akaanza kushugulikia karatasi ambazo alijua
Tunda angehitaji kuombea Visa ya Canada. Na kutafuta ushauri wa kisheria jinsi
anavyoweza kumkabidhisha Tunda ile nyumba kisheria na kuhakikisha hakuna mtu
anayeweza kumnyang’anya tena. Ibakie kwa jina la Tunda tu. Siku hiyo hakurudi
ofisini. Akawa na hekaheka nyingi karibia siku nzima.
Ijumaa.
K |
ila mmoja alikuwa kwenye
mikakati yake kwa nafasi yake. Net na Tunda kivyao, kukamilisha yao ambayo ni
wao tu wawili walikuwa wakiyajua. Na Ritha naye akawa kwenye mikakati yake,
akiwatumia wanandoa hao. Gabriel na mkewe. Ritha kama kawaida yake.
Alishawasoma wote wawili. Gab na Bethy. Akajua udhaifu wa wanandoa hao.
Akawapigia mahesabu. Akawapanga vizuri akabadili utaratibu. Akaamua awe
anakutana na wana ndoa hao tofauti tofauti na kila mmoja alifanya nao
makubaliano tofauti tofauti. Akiwa na Bethy lengo ni kumuangamiza kabisa Tunda,
lakini anapokuwa na Gabriel lengo linakuwa ni kumtenganisha Net na Tunda. Kote,
yeye ndiye alinufaika bila wengine kujua.
Net
alijitahidi kumkamilishia Tunda vitu vyote ambavyo walitakiwa kuwa navyo ili
kuhakikisha Tunda anapata Visa ya Canada. Ilikuwa ni siku ya ijumaa ambapo
walikutana jioni nyumbani kwa Tunda ili kuanza kutuma maombi hayo ya Visa kwenye
ubalozi wa Canada. Simu ya Tunda iliyokuwa karibu na Net, ikaanza kuita. Net
akaichukua ili kumpa. Akashtuka kuona namba ya mama yake. “Nini?” Tunda
akauliza baada yakumuona Net ameshtuka. Net yeye ndiye aliyekuwa akijaza kwenye
laptop yake, kumuombea Tunda Visa, online. “Mama huyu!” Tunda akakunja
uso.“Amepata wapi namba yangu!?” Tunda akauliza. “Pokea tumsikilize.” Net
akashauri.
Tunda
akapokea na kubonyeza kwenye speaker ili na Net asikie. “Upo sehemu tunayoweza kuzungumza?” “Ndiyo. Shikamoo.” “Upo peke yako?”
Mama Cote akauliza. “Ndiyo sababu uliyonipigia simu?” Tunda
akamuhoji akimtaka asimpotezee muda. “Hapana. Naona ni
kama tumeanza vibaya Tunda. Nataka amani na wewe. Net ni mtoto wangu najua na
wewe utakuwa kwenye familia. Lazima tuwe pamoja na tupatane.” Tunda
alibaki kimya akimsikiliza. “Upo Tunda?” “Nipo na
ninakusikiliza.” “Ndio nilikuwa nataka nikukaribishe kwa chakula cha mchana,
pale Paz city. Tupate muda wa kuzungumza.” Net akakunja uso.
“Lini na saa ngapi?” “Kesho, saa saba mchana.” “Kesho ndio siku
yangu kubwa ya kazi. Kuanzia asubuhi mpaka usiku.” Tunda
akajibu. “Jumapili je?” Mama Cote akauliza. “Nakuwa kanisani.” “Ukitoka kanisani, je?” “Nitazungumza na
Net, kisha nitakujulisha.” “Sio kila jambo letu tunalofanya mimi na wewe, Net
ajue! Kuna mambo ya wanawake yanayotuhusu sisi tu. Wala Net haihitaji kujua.”
Mama Cote alizungumza kirafiki. “Naomba nikujibu
baadaye kama nitaweza kwa siku hiyo ya
jumapili au tufanye wakati mwingine. Asante na usiku mwema.” Tunda
akakata.
“Kuna
jambo linaendelea Tunda. Kuna mtego tu. Kama kweli mama angekuwa na nia ya
kutaka amani na wewe, kwanza asingeficha kukutana kwenu, na angekualika
nyumbani kwake alipo Nana. Mara ya mwisho alikuwa akigomba na Nana alijua kuna
tatizo. Na anajua kabisa vile Nana anavyonipenda na kuniheshimu. Hajawahi hata
kunipazia sauti mbele yake. Kama angetaka kulisawazisha hilo, angeanzia alipo
Nana ambako ameharibu.”
“Kwa
kuwa Nana alishtuka sana, alipotoka na kumkuta mama akinifokea, mimi nimetulia
tu. Alitaka kujua tatizo ni nini, lakini sikutaka kuharibu zaidi, ila najua
Maya atakuwa ameshaanza kuhisi. Alishangaa siku ile ya kukuvalisha pete vile
ulivyoondoka bila kuaga na kutokurudi tena pale wakati bado yeye Nana yupo.
Tena akiwa amekuonyesha amekukubali!” Tunda akajua aliharibu kuondoka bila
kuaga. Ila akaona anyamaze tu, Net aendelee.
“Na Nana
aliposema wakati namrudisha Canada na wewe twende wote, mama alikataa mbele
yetu wote bila kufikiria kitu kilichoamsha maswali kwa Nana na Maya, wakimuhoji
ni kwa nini hataki wewe ufike nyumbani, Canada! Akatoa sababu ambazo hata bibi
alijua anadanganya maana alimuuliza maswali ambayo hakuwa na utetezi mzuri.
Liko jambo Tunda. Na sijui ni nini anataka?” Net alibadilika mpaka sura.
“Nitafanyaje
Net? Naogopa. Akija kunidhuru je?” “Na mimi hilo ndilo linalonitia wasiwasi.
Mama amefika pabaya. Na sasa hivi atafanya chochote ili kushinda. Mbaya zaidi,
sidhani kama atafurahia matunda ya anachopanda sasa hivi. Huwa namjua kuwa
anahasira sana. Sasa najiuliza hiyo hasira ikimwisha, akajikuta katikati ya huo
uharibifu, sijui atajitoaje!? Hakika sijui! Mimi nimemuonya sana. Na mbaya
zaidi ameingia kwenye ndoa ya Gabriel, anawachanganya wale watu, nahisi mwisho
wake hautakuwa mzuri.” Net aliendelea kulalamika.
“Turudi
kwangu Net. Nifanyaje?” “Nenda. Lakini usiende peke yako. Muombe mama Penny
akusindikize. Ila usimwambie mama kama utakwenda na mama Penny. Ashtukie tu
unafika pale na mama Penny. Na mimi nitakuwa karibu. Kwa lolote watakalopanga
kukufanyia, niwepo karibu.” “Hapo sawa.” Wakakubaliana.
Tunda
akampigia simu mama Penny. Akamuelezea kwa kifupi, na hofu yake na Net juu ya
kikao hicho, mama Penny akakubali kumsindikiza. Akamtumia ujumbe mama Cote kuwa
itakuwa jioni ya saa 9 sio saa saba mchana. Mama Cote akakubali. Net na Tunda
wakatuma yale maombi ya Tunda kwenye ubalozi wa Canada, wakabaki wakipanga
mipango yao.
Jumapili!
N |
et alikwenda kumchukua Tunda
nyumbani kwake wakaenda naye ibadani, kanisani kwa kina mama Penny. Walikaa
pamoja. Baada ya ibada wao walikwenda kukaa kwenye gari wakimsubiria mama Penny
amalize mambo yake pale kanisani, waongozane na Tunda. “Nilitamani kwenda kwa
baba leo.” Tunda alianza baada ya muda mfupi kuingia kwenye gari. “Kama ukiwahi
kumaliza, tunaweza kwenda.” Tunda akamtizama Net.
“Vipi?”
“Nina wasiwasi Net. Naomba chochote kikinipata, usiache kumfuatilia baba yangu
na kuhakikisha anatolewa jela.” “Tunda!” “Kweli Net. Chochote kinaweza kutokea.
Nililala nikiwaza. Mama Cote nimempokonya watu wawili muhimu sana kwenye maisha
yake. Nakumbuka chuki aliyokuwa nayo tulipokuwa Arusha! Ile ilikuwa kwa mchumba
wake tu. Sasa, sasa hivi itakuwa zaidi kwa kuwa nimeingia kwenye familia yake
yote. Maya na bibi pia wanaonekana wapo upande wangu. Hawezi kukubali hivi
hivi.” Net akanyamaza.
“Au
usiende?” Hofu ikawa imeshamwingia Net. “Siwezi kuacha kutokwenda. Ikiwa ni
kweli anataka amani je? Nitakuwa nimekimbia kitu cha msingi sana kwetu.” Net
kimya. “Tunamuhitaji Net. Hatuwezi kumpuuza. Katika lolote lile analotaka
kufanya, nia nikulinda kilicho chake.” Net kimya, alimjua mama yake.
Tunda
naye akanyamaza mpaka mama Penny alipokuja kuwagongea kioo. “Mbona mpo kama mko
msibani!?” Wote wakacheka. “Twende Tunda.” Mama Penny akaelekea kwenye gari
yake. Tunda akambusu shavuni Net na kutaka kuondoka. Net akamuwahi tena kupata
busu la mdomoni. Akambusu kwa muda kidogo, akamuachia midomo lakini akabaki
amemshilia pale pale pembeni ya shingo alipokuwa amemshika wakati akimbusu.
“Nakupenda
Tunda. Na nina kuombea.” Angalau Tunda akatabasamu.“Asante Net. Na mimi
ukumbuke nakupenda.” “Siwezi kusahau Tunda. Asante.” Tunda akampa busu la juu ya midomo, akashuka
kwenye gari ya Net, akaingia kwenye gari ya mama Penny. Wakaondoka, Net akiwafuata nyuma kwa gari yake.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
“Acha
wasiwasi wewe Tunda!” “Sijui mama Penny, moyo wangu umekosa amani kabisa!”
“Sasa mimi si nipo na Net naye amesema hatakuwa mbali?” Tunda akavuta pumzi
mara kadhaa na kuzishusha. Wakatulia hapo garini. Mama Penny akaendesha moja
kwa moja mpaka Paz City. Kwa kuwa ilikuwa siku ya jumapili, hamna magari mengi
barabarani, iliwachukua muda mfupi kufika. Akaegesha gari, wote wawili
wakashuka.
Akajaribu
kumchokoza kidogo, Tunda akaanza kucheka huku wanaingia ndani. Kuingia tu,
akawaona mama Cote na Bethy wamekaa wakimsubiria. Wote walionekana kushtuka.
Kicheko cha Tunda kiliisha gafla baada yakumkuta na Bethy aliyekuwa ameonyeshwa
picha zake na Gabriel na yeye yupo pale. Moja kwa moja akajua lipo jambo. Na
mama Cote naye aliduwaa wazi baada yakumuona mama Penny.
Wakatembea
mpaka kufikia meza. “Karibuni.” Bethy yeye akajikaza kuvunja ukimya maana yeye
Ritha ni kama alibaki ameduaa tu. “Naona umeamua kuleta mtu mwingine!” Ritha
akajikuta anaropoka. “Huyu ni mama
Penny, ni dada yangu. Sidhani kama anashida kuwepo kwenye kikao chetu chakuleta
amani, kama ambavyo na Bethy yupo hapa.” Tunda akamjibu taratibu tu.
“Kumbe
mnafahamiana na Bethy?” Ritha akauliza kwa mshangao. “Ataacha kunifahamu vipi
wakati alikuwa mke mwenzangu?” Bethy akajibu. “Ulikuwa mke mwenza na Nancy,
wala sio Tunda. Na Nancy alishaondoka muda mrefu sana, anayeishi sasa hivi ni
Tunda.” Tunda akajibu bila kubabaika au
kuonyesha hofu. “Akijakurudi Nancy tena itakuaje?” Akauliza Ritha. Tunda
akacheka. “Nilijua tu kama hukuwa na nia ya amani mama Cote. Ila kwa kuwa
nimeshafika mpaka hapa, naomba uniambie ulichoniitia.” “Ni mazungumzo tu ili
kuwekana sawa. Una wasiwasi gani?” “Sina wasiwasi wowote.” Tunda akajibu.
“Basi
niseme haraka.” Ritha akaongeza. Tunda akanyamaza akabaki akimtizama, muhudumu
akafika. “Naona wageni wenu wamefika. Mpo tayari kuagiza vinywaji sasa?”
Muhudumu akauliza na tabasamu akimtizama mama Cote na Bethy. “Naomba red wine.”
Bethy akamwambia muhudumu. “Kama tukipata chupa ya champaign ingetufaa. Isio na
kileo lakini. Tunataka kusherehekea. Lete na glass 3.” “Mimi sitakunywa champ…”
Tunda akataka kukataa, Ritha akamuwahi kwa swali la kejeli. “Hutaki
kusherehekea kumilikishwa nyumba ya Cote?” Kimya.
Tunda
akajua tayari yule mama ameshajua. “Ulifikiri itakuwa siri mpaka lini?” Ritha
akauliza huku akicheka wazi akionekana na maumivu moyoni. “Ulifikiri sitajua
kama umeshaanza kuchukua mali zangu?” Akauliza tena. Tunda na mama Penny kimya.
“Hakuna kitu cha Cote kinaendelea hapa mjini, mimi nisijue. Umefanikiwa kuingia
kwenye akili za Net, kwa akili kubwa sana, kuliko shule aliyosoma yeye! Tena
umehakikisha umefanya mambo yako kisomi sana, hakuna penye swali, wala utata.
Sasa hivi wewe ndio mmiliki halali wa nyumba ya Net, iliyokuwa ipo chini ya
kampuni yangu. Alikwambia hayo yote?” Tunda kimya.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
Akakumbuka siku ya alhamisi Net
alipomfuata ofisini na makaratasi kutoka kwa mwanasheria akimuomba aweke saini
kwenye hizo fomu, ili kukamilisha utaratibu wa kumiliki hiyo nyumba na kutuma
maombi ya kubadili jina lililopo kwenye hati. Kutoka Cote, kuwa Tunda. Net
alimwambia ameshakamilisha kila kitu. Na baada ya yeye kuweka saini tu, ile
nyumba ni yake kihalali, na akampa milioni 3 taslimu, kisha akamuomba yeye
Tunda, amwandikie hundi ya milioni tatu kama malipo ya kununua nyumba kwa kina
Cote.
Akiwa na wasiwasi, bila amani, huku Net
akimsisitiza kuwa ile nyumba ni jasho lake, hawezi kuacha ikapotea bure, Tunda
alisaini. Akaandika na hundi ya milioni 3 tu, inayoonyesha jina la mlipaji kuwa
ni yeye Tunda, akamkabidhi Net. Net aliondoka akimwambia yeye mwenyewe
atamalizia kila kitu.
Akasahau
hata kumuuliza iliendaje. Alhamisi jioni yake hakumuona Net, alimtoa bibi yake
na Maya kwa chakula cha jioni. Ijumaa walikutana wakiwa na lengo lakutuma
maombi ya Visa. Kila mtu akili ikazama huko kwenye kuhakikisha hawakosei kutuma
hayo maombi. Tunda akimsaidia kumpa Net baadhi ya taarifa zinazomuhusu yeye
tokea anazaliwa, Net anazijaza kwenye kwenye hizo fomu za maombi, mtandaoni.
Ndipo simu ya mama Cote ikaingia kumtaka wakutane. Mambo yakavurugana. Net
akaondoka kwenda kulala kwa makubaliano ataenda kumsaidia mpenzi wake kupamba
siku inayofuata jumamosi.
Tunda
aliamka siku ya jumamosi akiwa na mawazo ya kazi na hofu yakukutana na Ritha
hiyo siku ya jumapili. Alianzia hotelini alikokuwepo mama yake na wadogo zake.
Akamchukua mama yake. Ilikuwa saa 11 asubuhi ya siku hiyo ya jumamosi wakati
Tunda alipowasili ukumbini na mama yake ili waanze kupamba. Net hakuchelewa, na
vijana wa kazi nao hawakuchelewa. Wakaanza kazi. Kufika saa tano asubuhi,
wakawa wamemaliza ukumbi wa kwanza, kwenda wa pili.
Kwa
kuwa kazi zilikuwa mbili tu jumamosi hiyo, wakaambiana wapumzike kidogo, wakutane
saa 6 na nusu kwenye ukumbi mwingine. Mama yake aliondoka kwenda kukutana na
dalali, Tunda na Net wakaelekea ukumbi mwingine. Tunda alirudi nyumbani saa
mbili usiku akiwa hoi, hata wazo la kuuliza juu mipango ya Net na nyumba yake
hakuwa nalo ila wasiwasi wa kukutana na mama Cote kesho yake ndio uliokuwa
umebaki.
Makubaliano
na mama yake ilikuwa ni atafute chumba hata kimoja, aishi hapo kwa muda wakati
anafuatilia mambo ya mali zake na mumewe. Tunda alimuahidi kumlipia kodi ya
mwaka mzima, wakati anatafuta kitu chakumwingizia kipato na wadogo zake warudi
shule. Aneti alishaanza kupata nafuu kubwa tu. Hapo ndipo mama Cote ndio
anamkumbusha maswala ya hiyo nyumba ambayo hata hawakuwa wameongea itakuje
baada ya nyumba hiyo kuwa yake kihalali.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
“Kwa
hiyo nyumba ishakuwa yako kihalali sasa! Bado tu hati, ni nini kinafuata Tunda?
Hebu tuambie.” Ritha akamtoa Tunda mawazoni.
“Hilo swali ni la msingi sana. Lakini hata sijafikiria kinachofuata.”
Tunda alijibu ukweli wa mambo, lakini wao wakachukulia wanabezwa. “Labda
kuhamisha kampuni yako mama Cote iwe kwa jina lake.” Bethy akaongenza kwa
kejeli. “Hapana. Mnafanya biashara ambazo sina nia wala mpango wa kuzifanya.
Kwa hiyo katika hilo usiwe na wasiwasi. Mimi nipo na Net, wala nyinyi msiwe na
wasiwasi na vyenu.” Tunda akajibu akiwa ametulia tu.
“Ni
kweli. Una haja gani yakufanya kazi wakati pesa yote ninayoitolea jasho na
niliyoitolea jasho inaingia mfukoni mwako?” Ritha akaongeza. “Mama Penny,
naomba twende dada yangu. Naona kikao kimeisha.” Tunda akasukuma kiti nyuma,
akasimama. “Huyo ndio mlinzi wako?” Bethy akauliza kwa kejeli. “Kama ulivyo
wewe kwa mama Cote.” Akajibu Tunda, wakaondoka.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
Alipoingia
tu kwenye gari, mama Penny akampigia simu Net na mumewe akawaomba warudi
kanisani wakazungumze. Hakuna aliyekataa. Tunda akamuona mama Penny
amebadilika. Lakini hakutaka kumuuliza. Akanyamaza tu, alijua ataongea tu. Mama
Penny hawezi kuweka jambo moyoni. Akaamua ampe muda ayapange maneno yake mpaka
atakapokuwa tayari kuongea ambapo pengine itakuwa kwenye hicho kikao.
Wakaendesha kimya kimya mpaka kanisani.
Wakamkuta
na mchungaji naye ndio anashuka kwenye gari yake. “Njaa inaniuma mama! ”
Mchungaji akamlalamikia mkewe. “Wote hatujala baba Penny. Pole. Lakini hili ni
la muhimu. Umewarudisha kina Penny?” “Ndio nimeingia tu ndani na wewe ukapiga
kunitaka nirudi hapa, kwema?” “Twende tukazungumzie ofisini.” Net naye akafika,
wote wakaingia ofisini.
“Ni nini
kinaendelea Tunda na Net!?” Mama Penny akauliza. “Labda ufafanue zaidi mama
Penny.” Net akaongea kiungwana. “Tuanzie swala la nyumba. Ni nyumba gani
anayolalamikia mama yako?” Net akaeleza kwa kifupi mwanzo mpaka mwisho na
kumuacha mama Penny na mumewe wametoa macho.
“Nia ni
nzuri Net, lakini huoni kama unamwingiza mwenzio matatizoni?” Mchungaji
akauliza. Net kimya. Mchungaji akaendelea. “Kwa historia ya Tunda, na hiki
ulichokifanya wewe, watu wote watajua nia ya Tunda kwako ni kweli ni mali.”
“Sina jinsi baba Penny. Sina namna nyingine. Tunda atakuwa mke wangu. Hiyo
nyumba ikiwa chini ya Tunda, nitakuwa sijapoteza.” Net akaendelea kutetea
lakini akaona kila mtu kimya. Wazi usoni walionyesha kutoridhika. Tunda alibaki
ameinama tu.
“Jamani,
hiyo nyumba ni jasho langu. Nimetengeneza kwa jasho langu mimi bila msaada hata
shilingi kutoka kwa mtu yeyote yule na Mungu wangu ni shahidi. Sio nyumba ya
ajabu sana, lakini ni yangu. Nimeijenga mchana na usiku, kwa kujinyima. Kwa
maombi mpaka nikamaliza. Siwezi kuruhusu hasira ya mama ikafanya ipotee bure.”
Net akaendelea kuweka utetezi wake.
“Babu
mwenyewe kabla ya kufariki alitaka kunisaidia kwa kuwekeza pesa, lakini
nilikataa. Ile nyumba nimejenga nikiwa mwanafunzi, huku nikiwafanyia kazi babu
na Nana. Niliwaambia msaada ninaotaka kutoka kwao, ni kazi. Wakaniajiri kwenye
kampuni yao. Nilikuwa nikifanya kazi huku nasoma, ili tu nijenge kitu changu
kisichokuwa na mkono wa mtu. Sikatai kuwa mama ndiye alihusika kunitafutia
kiwanja.”
“Sijui
alifanyaje kukipata, ila pia nilikilipia mimi mwenyewe kwa pesa niliyoipata kwa
kufanya kazi. Kuanzia msingi mpaka vigae, ni pesa yangu. Hakika siwezi kuruhusu
ikapotea bure. Babu alishawahi kuja kabla hata hajaanza kuugua na kuiona.
Natamani mngeona furaha iliyokuwepo usoni mwake baada yakuiona ile nyumba.
Alijivunia sana na ikawa ni kitu anachojisifia kwa wenzake mpaka anakufa.”
“Babu
alikuwa na mtoto mmoja tu, ambaye ni baba yangu. Baba naye akafariki na
kuniacha mimi nikilelewa na babu. Babu naye alizaliwa peke yake. Mimi na Maya
ndio ukoo kwa babu. Alinilea mimi na Maya kama watoto sio wajukuu. Chochote
nilichofanya, kilimgusa babu moja kwa moja. Ile kuona nimebadili udogo kuwa
jengo vile, kwake ni kitu amekisema mpaka anaingia kaburini anasimulia mpaka
madaktari na manesi waliokuwa wakimtibu, tena kwa kurudia rudia.”
“Alikuwa
akiwaambia kuwa, ‘Net amejenga nyumba kutoka kwenye msingi. Amebadili vumbi
kuwa jengo, msitu kuwa mahali pamakazi.’ Ndio usemi babu yangu alisema na
kujivunia mpaka kifo chake. Leo niache mtu baki tu aje aishi kwenye ile nyumba!
Hapana jamani. Ni garama ambayo nimemuomba Tunda anisaidie kulipa ili hiyo
nyumba ibaki kuwa yetu na watoto wetu.” Hata Tunda hakujua kwa mapana kiasi
hicho.
Yeye
Tunda alijua ni nyumba tu ambayo inamuhangaisha mtoto huyo wa kizungu.
Alishatamani kumwambia wajenge kwenye kiwanja chake nyumba kama ile, lakini
kumbe nyumba yenyewe ina historia nzito sana kwa Net. “That’s my legacy!
Tafadhali naomba mnielewe.” Net alimalizia hivyo akiweka msisitizo, nakuwaacha
wote wanavuta pumzi kwa nguvu.
“Mimi
narudia pale pale Net. Nia ni nzuri. Lakini unamwingiza au tuseme unahalalisha
vita inayoendelea kwa Tunda.” “Ningefanyaje baba Penny? Rafiki au familia ya
pekee mbali na mama yangu ninayoifahamu na ambao nipo karibu nao ni ya Gabriel
ambaye kama tulivyowaambia, ndio wako kinyume nasi kwa sasa. Nikisema niende
kwa wazazi wake Gabriel ndio nitakuwa naharibu kabisa. Gabriel ni zaidi ya
alumasi kwa mama yake. Hakuna mtu mkamilifu hapa duniani kama Gabriel kwa mama
yake.”
“Ni vile
tu yule mama si mtu wa mbele mbele kwenye mambo, najua hili ambalo Gabriel
analalamika nalo, atakuwa anajua kabisa, na kunilaumu. Kwa kuwa ninauhakika ni
sisi tu ndio tulikuwa hatujui kama Gabriel anamatatizo ya ndoa, lakini si yule
mama. Anamjua mwanae kwa kumtizama tu. Furaha ya Gabriel ndio ya yule mama.
Hajui kusema hapana kwa Gabriel, mpaka baba yake alikuwa akihofia atamuharibu.
Kwa kifupi nilikuwa sina wa kumkimbilia ila Tunda.” Kimya.
“Tunda
amesema unamrudisha bibi yako Canada. Ukumbuke utamuacha hapa peke yake. Na kwa
baya lolote litakalompata Tunda, ujue limeathiri watu wanne wanao mtegemea kwa
karibu sana Tunda.” “Naelewa mama Penny. Nimeshaongea na bibi, amekubali arudi
tu na Maya. Sisi tumfuate tutakapokuwa tayari. Japo alitoa ushauri mgumu
kidogo. Najua kwa desturi ya hapa ni ngumu. Sikumjibu ndio au hapana,
nilinyamaza kwa kuwa nilijua haiwezekani.” “Ni nini?” Tunda akauliza. Net
akabaki kama anafikiria.
“Net?”
Tunda akauliza tena kwa upole. Akamshika mkono. “Ni ushauri gani bibi amekupa?”
“Nilimweleza kwa kifupi, kwa kuwa yeye pia anajua ni kwa nini nipo hapa na
ninaishi hapa kwa kibali cha kazi. Akashauri kwa kuwa mambo ya kanisani
yanaweza kuchukua muda mrefu kabla ya ndoa, akatoa ushauri nimuoe Tunda
mahakamani, tukitulia ndio tufanye kanisani. Lakini nika..” “Sawa.” Tunda
akakubali kwa haraka bila hata Net kumaliza. Net hakutegemea.
Wote
wakamgeukia Tunda. “Tunda!” Mchungaji na mkewe wakajikuta wakimshangaa kwa
pamoja. Tunda akamgeukia Net vizuri. “Nisikilize Net. Kama itakusaidia kwenye
mambo yako yakuwa hapa Tanzania bila shida na maswala mengine kama hiyo nyumba.
Angalau ikijulikana ipo kwa jina langu, na mimi ni mkeo, itapunguza maswali na
makali ya hilo jambo. Tufanye tu hivyo.” Kimya.
“Kwani
ndoa ni nini?” Tunda akamgeukia mchungaji na mkewe. “Binafsi nina amani. Ndoa
ni makubaliano ya mume na mke. Kama mimi na wewe tumekubaliana, sidhani kama
kuna shida.” Net akaongeza akionekana kulifurahia hilo. Mama Penny na mumewe
wakaangaliana.
“Kweli
safari hii tumejaribiwa pabaya!” Baba Penny alisikika Tunda akacheka. “Mimi
naombeni mfikirie baba Penny. Hii ndoa yetu mtatangaza lakini wote tunajua
mtagonga tu mwamba, hamtafika popote. Mimi na Net wote tuna vipingamizi ambavyo
hatuwezi kukwepa. Watawapinga kwenye kila tangazo na kila eneo. Na wote
watakuwa na sababu zakueleweka.” “Nakushukuru Tunda.” Net akamgeukia na kumbusu.
Furaha ikawajaa gafla.
“Naomba
msubiri kwanza.” Mama Penny akawakatiza. “Hivi wewe Tunda unajua harusi za
mahakamani?” Akamuuliza Tunda. “Kwanza ujue ni ndoa halali tu, hakuna watu
zaidi yenu na mashahidi. Huwezi kutokea pale na mashela kama maharusi wengine
na kelele za vigelegele. Ni kimya kimya!” “Lakini Net si atakuwepo?” Tunda
akauliza.
“Tunda!
Naomba ufikirie.” “Baba Penny, najua maisha niliyoishi, najua nilipo na
ninapokwenda. Hakuna mwanaume atakuja kunipenda na kuniheshimu ila Net.
Sitakubali apande ndege, hata kwa ahadi ya kurudi, bila kunioa. Iwe kanisani,
iwe mahakamani. Sijali. Na kama Net mwenyewe anaona nisawa, nataka ndoa.”
Ilikuwa faraja kubwa sana kwa Net.
“Binafsi
itanirahisishia mambo mengi sana. Hata ukaaji wangu hapa nchini, hautakuwa wa
shida kama hivi sasa ambavyo nahangaika kuombewa vibali vya kazi kila wakati,
na zaidi sasa hivi inavyojulikana nafanya kazi chini ya kampuni ya mama, ambaye
ndio ananitishia . Najua ni garama kubwa analipa Tunda, lakini sina jinsi.”
“Mimi nipo tayari Net. Naombeni baraka zenu mama Penny na mchungaji. Tafadhali
sana. Nawahitaji sasa hivi kuliko mtakavyofikiria.” “Mmmh! Kazi ipo!” Alisikika
mama Penny. Tunda na Net wakabaki wakiwaangalia kwa zamu.
“Labda
ni hivyo pia ambavyo hata bado hatujaitangaza kanisani. Lasivyo watu
wasingeelewa. Kutoa harusi kanisani kupeleka mahakamani!” “Sio hivyo tu baba
Penny, na sisi ndio wasimamizi!” Akaongeza mama Penny. “Tutabariki kanisani
mambo yakitulia. Hata Nana amesema hivyo. Nana mwenyewe alikuwa anategemea
harusi kubwa ya kanisani, lakini hatuna jinsi. Amesema tutafanya tena nyingine.
Nawaomba mtusaidie mama Penny. Tafadhali.” “Lini?” Akauliza mchungaji.
Net
akamgeukia Tunda. “Wewe ulitaka iwe lini?” Tunda akamuuliza Net. “Utajali
tukifanya kabla ya bibi kuondoka?” “Inamaana iwe week hii inayoanza kesho!?”
Tunda akauliza kwa kushtuka kidogo. “Unafikiri itawezekana?” Net akauliza tena,
Tunda akamgeukia mama Penny. Mama Penny akavuta pumzi kwa nguvu. Akarudi
kumtizama Net. Akajiweka tena sawa kama anayefikiria.
“Maswala
ya mahari! Unaelewa mambo ya mahari Net?” Mchungaji akamuuliza Net. “Sidhani
kama nilazima.” Akawahi kujibu Tunda. “Hapana Tunda. Baba yupo hai. Lazima
kumuuliza yeye.” “Sawa. Nitakwenda kuzungumza naye mimi mwenyewe na kumwambia
nia yangu yakutaka tufunge ndoa kwa haraka. Akitoka, atashuhudia harusi yetu ya
kanisani.” “Hapo sawa.” Mchungaji akaridhika.
“Sasa
mtatusimamia au kwa kuwa ni ya mahakamani hamtaki tena.” Mama Penny
wakaangaliana na mumewe. “Msibadili mawazo bwana!” Tunda akabembeleza. “Ni
hivyo nakupenda tu Tunda, lakini…” Tunda akaanza kucheka. “Unacheka nini wakati
mnatuingiza matatizoni?” “Heri niwe na wewe matatizoni mama Penny, naona
nitashinda kuliko niwe peke yangu.” Mchungaji na Net wakacheka. “Unaakili mbovu
wewe!” “Kweli tena mama Penny. Sasa unafikiri nitafanyaje?” “Haya, nendeni
mkapange mambo yenu mkiwa mmetulia, halafu kesho mtatujulisha.” Net na Tunda
wakashukuru, nakutoka.
Wakiwa
njiani Net akampigia simu mmoja wa mwanasheria ambaye wanamtumia sana kwenye
mambo ya kampuni yao kumuomba muongozo. Yule mwanasheria akampa namba ya simu
ya mtu ambaye alijua anaweza kumsaidia kumpa taratibu zote. Alipompigia tu
simu, akapokea bila kuchelewa. Moja kwa
moja Net akamweleza nia yao yakutaka kuoana. Akamwambia kuwa yeye hakuwa mzawa,
lakini alitaka kufunga ndoa ambayo itatambulika kimataifa.
Akamwambia
inawezekana kabisa, lakini kwa kuwa yeye hakuwa raia wa Tanzania, ili kufunga
ndoa nchini anatakia kwanza kuwa na ‘Certificate of No
impediment’ , kutoka nchini kwao. Ili kuonyesha kuwa hujawahi kuoa
kabla. Na iambatanishwe na cheti chake cha kuzaliwa. Aliendelea kuwaeleza pia
lazima kwenda kwenye ofisi za Msajili wa ndoa ili kujaza fomu ambazo utalipia
pesa. Kisha ndipo waombe cheti cha ndoa maalumu kinachoweza kufahamika
kimataifa ambacho watalipia pesa zaidi kwa kuwa watajaza fomu tofauti na zile
za kuombea cheti cha kawaida cha ndoa.
Aliwaambia watakapofika pale waombe fomu
zinazojulikana kama RGM 111, kwa ajili ya ‘International Certificate of Marriege’. Kwa hiyo
akamwambia lazima akienda kwenye ofisi hizo za msajili wa ndoa, awe na copy ya
passport yake, na hiyo Certificate of No Imediment, atakayokuwa ameipata kutoka nchini kwao, na
picha mbili za passport size. Kisha unasubiri siku 21 ili kama kuna mtu
anakipingamizi chochote aweze kufika na kuweza kuwasiliana na ofisi hizo.
Tunda na
Net wakaangaliana. Maana Net aliweka kwenye speaker kwa hiyo Tunda alikuwa
akisikiliza. “Mmmh!” Tunda akaguna. “Hakuna jinsi
yakufupisha hayo mambo yote?” Net akauliza. “Upo
uwezekano wakufupisha hizo siku 21.” Net na Tunda wakajiweka sawa
kusikiliza. “Mnaweza kuomba kwenye hizo hizo ofisi,
lakini itabidi kulipia zaidi.” “Hamna shida.”
Net alijibu kwa haraka sana.
“Okay. Basi mtakapofika pale, muombe ‘Special Marriage License’. Mtakapomaliza kujaza hizo fomu na kulipia
garama zake, mtapewa cheti chenu, kisha mnaweza kufunga hiyo ndoa popote
mnapotaka ambapo Msajili wa ndoa akawafuata mtakapo lakini itabidi kugaramia
zaidi. Mtalipia na usafiri wake pia. Na kama mtataka mfungie pale pale, mnaweza
kuulizia kwa siku yenu mtakayokuwa mmepanga kama wanaweza kuwafungisha. Lakini
mjue itakuwa siku na muda wa kazi.” Yule mwanasheria akaendelea.
“Siku yakufungishwa hiyo ndoa nilazima kuwepo na mashahidi
wasiopungua wawili. Haijalishi kama ni wa zawa au sio wazawa wa nchi. Lakini ni
lazima kuwepo na hao mashahidi. Baada ya kufunga ndoa, ndipo mtakapo ka bidhiwa
vyeti viwili vya ndoa.” Yule mwanasheria akawa amemaliza.
“Sasa na
hiyo ‘Certificate of No impediment’ utaipata wapi Net? Hayo sio mambo ya
leo wala kesho. Hiyo kitu ishakuwa ngumu.” “Naomba tusikate tamaa mapema
Tunda.” Bado yule wakili alikuwa akiwasikiliza.
“Lakini kila kitu kinawezekana.” Wakamsikia yule
mwanasheria akionea. Wote wakatulia. “Mnanisikiliza?”
“Tupo.” Net akaitika. “Njooni kesho ofisini,
tutazungumza zaidi. Naweza kuwasaidia hata ijumaa mkafunga ndoa.” Hiyo
ikawa habari njema sana kwao. Wakaagana kwa makubaliano wakutane kesho yake.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
Mipango kabambe, inayosukwa kisomi na kwa makini inaendelea. Mpango
upi utafanikiwa? Endelea kufuatilia.
0 Comments:
Post a Comment