Jumatatu.
N |
Net
na Tunda walitoka pale wakiwa wamejawa cheko. Hawakuwa wakiamini kile
kinachotaka kuwatokea. Kutoka kusubiri siku 21 ndipo waoane mpaka kuweza
kufunga ndoa yao ndani ya week! Mungu awape nini! Wakampigia simu mama Penny
wakamweleza kila kitu na kumtaka asimwambie mtu yeyote. Tunda alimwambia
anamfuata ili wakatafute nguo zao na kina Penny watakao simamia, halafu Net
atamtafuta mchungaji wapange mipango yao, lakini ijumaa harusi. Vilijaa vicheko
tu.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
“Vipi
sasa mama Cote?” Tunda akamuuliza Net. “Huyo nitamtaarifu siku yenyewe ya
harusi, nikiwa nimehakikisha wewe upo sehemu ya tukio, na mfungishaji yupo.”
“Net!” “Kweli Tunda. Nashindwa kabisa kumuamini mama kwa sasa, hasa katika
hili. Lolote laweza kutokea.” “Bibi yako?” “Nana nitamwambia. Na hivi anataka
niondoke naye jumamosi, itakuwa sababu nzuri sana. Atajua nipo kwenye honeymoon
na mke wangu.” Tunda akacheka, asiamini kama ijumaa atakuwa mke wa Net.
“Siamini
Net!” “Mimi mwenyewe siamini! Naona siku zinachelewa. Nawahi kuchukua passport
yangu, nikatoe copy, nipige picha nimpelekee leo leo. Naomba na wewe
usinicheleweshe Tunda.” “Mimi naona twende tukapige picha, ukae nazo tu.
Ukienda kumpelekea hivyo vitu, umpelekee kila kitu kwa pamoja.” Wakakubaliana.
Maandalizi
ya Harusi ya
Net
& Tunda.
H |
iyo week ikajaa hekaheka kweli
kwa Net, Tunda, mama Penny na familia yake ili kuweza kukamilisha kila kitu kwa
wakati. Mama Penny yeye alikuwa atafute wapambaji, mtu wa vyakula na vinywaji
pamoja na keki. Tunda alikuwa na kazi zake za kupamba juma hilo, ambazo
alishawakubalia watu, asingeweza kuahirisha tena. Katikati ya juma alimwambia
mama Penny atapamba mwenyewe, ila jumamosi ndio kazi zote akamuhamishia mama
Penny akijua yeye atakuwa kwenye fungate.
Ikawa
tena kuna shuguli nyingine yakutafuta nguo ya harusi itakayompendeza yeye
kwanza kama bibi harusi, na wasimamizi wake, ndani ya siku hizo hizo chache. Na
juma hilo hilo tena alitakiwa kuhama pale alipokuwa akiishi, kuhamisha baadhi
ya vitu vyake kwa mama Penny. Kukajaa heka heka, hata safari ya kwenda kwa
shangazi yake ya kuwaringishia Net, na kujua yaliyojiri baada ya kuwatumia
picha za fumanizi la mjomba wake ikasaulika.
Mama
Cote akashangaa haulizwi chochote. Net anafika kazini asubuhi kama kawaida,
mchana anatoka kwa lisaa au zaidi, kisha anarudi kazini kama kawaida. Salamu
kama kawaida. Hakuna tofauti hata hapakuwa na hasira usoni kwa Net. Ritha
alikumbuka maneno makali na kashfa aliyomtupia Net. Akakumbuka ugomvi aliouacha
kati yake na Bethy, lakini hakuuliza chochote! Na kitendo cha Tunda kufika
kwenye miahadi yao na mama Penny, wazi mama yake alijua Net anajua. ‘Lakini ni nini kinaendelea?’ Mama Cote
akaendelea kujiuliza.
Alitegemea
Maya kugeuka kisirani mara baada ya kusikiliza akimgombesha kaka yake, lakini
akashangaa na yeye ametulia tu. Bibi Cote naye kama vile alivyokuwa akishangaa
siku ya ugomvi, kuashiria hakuwa anaelewa maneno yale makali yaliyokuwa
yakimtoka Ritha kwa kijana wao, basi akaendelea kujidai kama haelewi chochote
na kama amepuuza. Hakuulizia lolote. Akaendelea kuzunguka kwenye sehemu
wanazouza vitu vya asili yeye na Maya, wakinunua zawadi. Wakati mwingine Net
aliwatoa. Basi pakatulia.
Jumatano.
Bibi
Cote kwa Tunda.
N |
et alikuwa amemwambia Tunda kuwa
bibi yake anataka kuzungumza naye. Siku nzima Tunda hakuwa na raha. Tumbo
lilikuwa likimuuma, alishindwa hata kutulia kwa wasiwasi. Alikuwa na kazi ya
kupamba ukumbi wa tamasha. Alipamba zaidi ya alivyolipwa kwa wasiwasi. Net
alimwambia atamfikisha huyo bibi nyumbani kwake mida ya saa 12 jioni ili awahi
kurudi kumchukua kwa kwenda kulala. Tunda aliwahi kurudi nyumbani kwake, ili
kupika chakula chakumkaribisha huyo bibi. Mama Penny alikuwa kwenye simu muda
wote akimtuliza.
Kama
kawaida ya Net, hakuchelewa. Kumi na mbili kamili, anagonga mlango akiwa na
bibi yake na Maya. Net alianza kucheka pale Tunda alipofungua mlango. “Sasa
unacheka nini bwana? Pisha mlangoni wageni waingie.” “Unaonekana una hali mbaya
kweli bibi harusi wangu. Ndoa ipo kweli?” Tunda akacheka na kumsukuma Net pembeni
kidogo, akampa mkono Maya, na kumkumbatia. Maya akaingia ndani, akamsogelea
bibi Net. “Net aliniambia unajua shikamoo.” Tunda alimwambia bibi Cote na
tabasamu la wasiwasi usoni. “Najua.” Akajibu yule bibi wa kizungu kwa kiswahili
na kumshtua sana Tunda. “Sasa ukimsema huyo, ujue anasikia.” Net akaongeza na
kuingia ndani akawaacha Tunda na bibi yake hapo nje wakishangaana.
“Shikamoo.”
Tunda akasalimia. “Marahaba Tunda.” Aliitika vizuri tu, kwa kiswahili chenye
lafudhi ya kigeni kisha akaendelea kuzungumza kwa kingereza. “Nina swali kabla
hatujaingia ndani.” Moyo wa Tunda ulipasuka. “Huyu bibi anataka kuniuliza nini tena!?” Kwa haraka Tunda
akajiuliza huku akimeza mate. “Karibu.” Tunda akajibu kwa upole, na wasiwasi
usoni. Akaangalia mlango kama anayetamani Net atoke ili amsaidie kwenye kujibu
hilo swali.
“Funga
huo mlango vizuri.” Alimwambia Tunda kwa lugha ya kingereza fasaha na chepesi
tu. Tunda akafunga na kurudi pale pale alipokuwa amesimama na bibi Cote. “Hataki Net asikie!?” Tunda alizidi
kupatwa na wasiwasi.
Alikuwa
bibi wa kizungu bila kuchanganya hata kidogo. Alionekana ni mwanamke aliyesoma.
Na kwa kuwa hakuwepo Net wala Maya, hakuweka ile sura yake ya utani. Akavaa
sura ya kimama, yenye jukumu kwa kijana wake. Hakuwa na umbile kubwa. Alikuwa
na mwili wa kiasi unaonekana unafanyiwa juhudi za makusudi, kutunzwa vizuri,
japo usoni alionekana umri umeshakwenda, ila ipo neema yakifedha.
“Why
Net?” Akauliza swali la moja kwa moja, nakumuacha Tunda ametoa macho.
“Umenielewa?” “Ndiyo.” Tunda akajibu kwa upole kama anayetafuta sehemu
yakuanzia kujibu swali hilo fupi tu. “Kwa nini iwe Net?” Akarudia swali lake
tena, bila maneno mengi. Lakini kwa muonekano wa yule bibi, hakuwa mtu
wakudanganyika au kupewa majibu mepesi.
Tunda
akabaki ametulia tu kama anayefikiria, akiwa ameinama. “Ninakuuliza hivyo kwa
makusudi kwa ile garama anayotaka kulipa Net kwa ajili yako. Wewe unaonekana ni
binti mzuri kabisa. Hilo halina swali. Nikiwa na maana kuwa, unaweza kuolewa na
mtu yeyote unayemtaka. Najua kwa sehemu pale alipo kwa sasa Gabriel juu yako,
lakini umeamua kuolewa na Net. Sasa swali langu nataka kujua, ni kwa nini
umemchagua Net, wakati ulishakuwa na mahusiano na Gabriel, na yeye anaonekana
bado anakupenda na anakuhitaji?” Bibi Cote akaendelea taratibu tu akimuelewesha
Tunda ili ampe majibu yatakayomridhisha.
“Kwa
sababu kama ni pesa.” Akatoa kijitabu cha hundi kwenye mkoba aliokuwa amebeba.
Tunda aliweza kujua aina ya ule mkoba. Ni wa Gucci ile ya bei kubwa. “Naweza
kukulipa bila ya yeyote yule kujua. Nitajie tu kiasi unachotaka, nitakupa bila
kukuuliza mara mbili ili umuache Net.” Yule bibi akaendelea, lakini Tunda
akabaki kama amepigwa na bumbuwazi. “Na wala usifikiri huu ni mtego. Sikutegi
ni kutaka kurahisisha mambo tu.” Yule bibi akaongeza.
“Labda hujajua pale alipo Net. Hajawahi kuwa
na tatizo na yeyote mpaka ulipokuja kwenye maisha yake. Alikuwa ni kijana
mwenye furaha na amani na kila mtu mpaka alipotokea Tunda kwenye maisha yake.
Ndipo kila kitu cha Net kimebadilika. Sasa hivi hayupo kwenye maelewano na mama
yake sababu yako. Sasa kama wewe upo kwa ajili ya pesa tu, naweza kukulipa pesa
yeyote unayotaka ili tu, tuachane kwa amani na Net aendelee na maisha yake.”
Yule bibi akamkazia macho Tunda.
“Hata
mimi natamani ingekuwa ni pesa tu, pengine hata kwangu ingekuwa rahisi.” Tunda
akaanza taratibu huku akimtizama bibi Cote. “Kwa sababu ya Net, hata mimi
maisha yangu yamebadilika. Sivyo kama nilivyokuwa zamani. Kabla sijaamua
kutulia kwa Mungu, hata baada ya kutulia kwa Mungu, Net amebadili maisha yangu.
Ile amani na utulivu niliyokuwa nayo siku chache kabla Net hajaja na kuniambia
alikuwa ananipenda anataka anioe, imeisha kabisa. Niliweza kurudisha heshima
kwenye jamii, na watu wakamtizama Tunda ambaye ametulia kanisani, lakini sasa
hivi nalipa garama kubwa sana ambayo hailipiki kwa pesa, kwa kuwa kwenye
mahusiano tu na Net.” Tunda akaendelea.
“Nimejitengenezea
maadui ambao sikuwa hata nikifikiria kama wanaweza kuwa adui. Mbaya zaidi
wanatokea kanisani ambako mimi kumenisaidia kunipa heshima. Na sikuwa
nimejiandaa wala sikuwa nimetegemea.” Tunda akacheka kidogo, kisha akaendelea.
“Nilikuwa
nikimwambia mtu fulani aliyekuwa akinilalamikia ni kwa nini sikuwa nimemwambia
kabla kama yupo mtu kama Net kwenye maisha yangu, nimekuja kumshtukiza tu baada
ya Net kutokea! Nikamjibu kuwa hata mimi sikujua kama Net yupo, japo alikuwepo.
Nakwambia kweli Ms Cote, siku chache zilizopita, kama ungeniambia kama Net
anaweza kunipenda na kutaka niwe mke wake, nisingekubali wala kudhania.”
“Hakika
sikuwahi kumfikiria japo nilishaishi naye kwa kipindi fulani, Arusha. Tena
tulikuwa karibu sana tu, lakini hata sikujua kama anazo hisia zozote za
kimapenzi kwangu na wala mawazo yangu hayakuwahi kumfikiria Net kuja kunipenda
niwe mke wake. Hata kama dunia nzima tungebaki mimi na Net tu, pia nisingeweza
hata kudhania kama Net, anayenifahamu Tunda mimi angeweza kunichagua na
kunitaka niwe mke wake. Bado siamini.” Tunda akaendelea.
“Kipindi
Net ananifuata kunitaka nije niwe mke wake, nilikuwa nina kijana ambaye alitaka
kunioa kama hivi Net. Yeye naweza kusema anauwezo, sio kama Net ninayesikia
kutoka kwa mama yake kuwa anapesa. Naweza kusema yule kijana alikuwa na pesa,
zakuzishuhudia. Za Net nazisikia tu kutoka kwenu. Hatuongelei pesa za Net
tukiwa naye. Hapa naishi kwa jasho langu. Anyways, turudi kwenye jambo la
muhimu. Yule kijana alikuwa akiitwa Julius. Na sio kwamba ni yeye tu aliyetaka
kunioa, ila yeye ndiye anayefanana na Gabriel ambaye nimeshawahi kuchezea pesa
yake, lakini nilishindwa kusema ndiyo kwao, hata Gabriel kwa sasa nimemwambia
hapana, kwa kuwa hawamfahamu Tunda hata kidogo. Ni Net tu ndiye anayenifahamu.
Angalia kiganja chako cha mkono.” Tunda alimwambia bibi Cote.
Yule
bibi akaangalia. “Huo mkono unapokuwa mchafu si unauosha?” Tunda akamuuliza
bibi Cote, kimya. “Unapokuwa mkavu si unaupaka mafuta?” Tunda akamuuliza tena.
“Kwani huo mkono huwa unaongea na wewe mpaka unaufanyia hayo yote?” Kimya.
“Jibu ni hapana. Uwe umechafuka kwa bahati mbaya au makusudi, huwa unauosha.
Uwe mkavu wakati wa baridi au joto. Usiku au mchana, huwa unajua na kuupaka
mafuta zaidi ya mara moja na huwa huchoki wala hakuna mahali unakolalamikia
jinsi unavyouhangaikia huo mkono na kutamani ukatwe.” Tunda akaendelea.
“Hivyo
ndivyo Tunda huyu aliyesimama na wewe hapa, ndivyo nilivyo mkono kwa Net.
Ananifahamu, ananisafisha na hajawahi kuchoka kuyasaka yale mazuri yaliyopo
ndani yangu na kuyatoa nje yale ambayo hakuna mwanadamu ambaye amewahi kuyaona,
hata mama yangu mzazi alishindwa, ila Net ameweza. Kwa kunisifia, na kunihimiza
niyaishi. Sijawahi kuwa mchafu kwa Net kiasi chakushindwa kunisafisha.” Tunda
akaanza kutokwa na machozi.
“Gabriel alishakuwa na mahusiano na Nancy, aliyekuwa akiishi
hapa, akitumia huu mwili wangu kama mpenzi wake. Tunda ambaye alijigeuza Nancy
alimtumikia Gabriel mchana na usiku bila kuchoka, lakini Gabriel alimuacha
Nancy akiwa anamlilia hana pakwenda. Ilikuwa usiku. Mvua ikimnyeshea. Net.
Nathaniel Cote..” Tunda akakwama kwa muda. Akajaribu kutulia.
Akafuta machozi mbele ya yule bibi.
“Usiku
ule, nikiwa nimeachwa peke yangu. Pengine kila mtu angefurahia kupatwa na kile
kilichokuwa kikinipata kwa wakati ule. Wakifurahia nisulubishwe kwa maisha
mabaya niliyokuwa nikiishi wakati ule. Lakini Net hakunihukumu. Alimchukua
Nancy, akijua wazi yupo Tunda ndani ya huyo Nancy, akamhifadhi usiku ule,
akanilisha, akanilipia madeni ya wakati ule, akanipeleka kanisani. Alihakikisha
kila aina ya Nancy, na wengine ndani yangu, wanaondoka ili tu, Tunda aliyemjua
Net, ambaye hata mimi sikujua kama Tunda anaweza kuwa hivi, ila Net. Alihakikisha
anawatoa kina Nancy wote, na kumbakiza Tunda huyu.” Tunda akaendelea.
“Mwanamke
anayemtaka sasa hivi Gabriel, hayupo. Mungu alimtoa na kumbakisha Tunda mbaye
ni Net tu anamfahamu na kumjua, na bado anampenda. Kwa mwanaume yeyote yule
anayekuja sasa hivi, akimtaka Tunda, halafu akaja kujua habari za kina Nancy
ambao walishaishi zamani kwenye mwili wa Tunda, hakuna anayeweza kunitizama
kama Net, Ms Cote. HAKUNA. Nalijua hilo kwa hakika kwani hata Julius alipojua
historia yangu ya nyuma, alishindwa kunitizama kama zamani, ila Net.”
“Nimekula
na kuichezea pesa ya Gabriel kuliko Net. Ila sijawahi kulala usingizi mzuri,
kama ninaoupata sasa hivi ambapo nipo na Net, nikifanya kazi kwa bidii
kujiingizia kipato kwa jasho langu. Na ndio maana kwa sasa hivi ambapo Mungu
amenipa uwezo wakutengeneza pesa mimi mwenyewe, hata sihitaji pesa ya Net. Net
alinisaidia kunitoa kwenye madeni, akanipa akili ya kuzitafuta pesa. Sasa hivi
sina shida na pesa yako, wala pesa ya mama yake, au hata yeye Net mwenyewe. Isipokuwa
Net mwenyewe. Mimi namtaka Net.” Tunda akaendelea taratibu tu kama kawaida
yake.
“Nitakudanganya
nikikwambia eti habari za Net kuwa na pesa nyingi eti sio habari njema kwangu.
Nitakudanganya. Nimeishi kwenye shida, na ni kweli nimejiapia sitaolewa na
mwanaume ambaye hana pesa au akili ya maendeleo, labda awe Net. Net atanioa
hata kama ni masikini ila mapenzi yatanitosha. Nitakuwa radhi hata kumuweka
ndani nimlishe kama mtoto mdogo, lakini sio mwanaume mwingine. Nimeteseka sana
maishani. Sitaki kuja kuanza kupata tena shida nikiwa na umri huu. Hapana.
Sitaki kurudi nyuma labda na Net. Sasa nikisikia kuwa anazo pesa, nafurahia
naona ni kweli Mungu amekusudia kunipumzisha.” Tunda akamuona yule bibi
anatabasamu.
“Net
ameniambia umenitayarishia chakula cha kitanzania. Naona nipo tayari kula.”
Tunda akacheka huku anavuta pumzi kwa nguvu mpaka akainama kwa kushika magoti
yake. Hata yeye hakujua ni wapi aliupata ule ujasiri wakuzungumza na yule bibi.
Tena kwa kingereza kizuri tu. Akamsikia yule bibi anacheka. Akajua anacheka
vile alivyofanya mbele yake bila kutarajia. Tunda akasimama na kumwangalia na
tabasamu la ushindi. “Karibu ndani.” Tunda akamkaribisha na kumfungulia mlango,
wakaingia.
Kwa
muonekano wa bibi yake tu, akajua mambo yalienda vizuri na amempenda Tunda. Hakuna
aliyeondoka. Wote walikaa jioni hiyo hapo kwa Tunda, vicheko vikaanza. Ile sura
ya yule bibi alipokuwa na Tunda nje, sio hii aliyokuwa nayo alipokuwa na Net
pamoja na Maya, hapo ndani. Tunda akaamini ni kweli anawapenda na kuwadekeza
hao watoto.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
Wasiwasi
ulikuwa umemwingia huyo bibi baada yakugundua ugomvi mkubwa uliokuwepo kati ya
Net na mama yake. Japokuwa alimfahamu Ritha, lakini hakutaka kumpuuza. Akaona
na yeye apate muda na Tunda kabla hajaolewa na Net na kuingia kwenye familia
yake. Kwa kuwa yule bibi alikuwa msomi, na kazi zake nyingi anakutana na watu
aina tofauti tofauti.
Alijua
kwa kukaa na Tunda kwa muda mfupi tu, atamjua kama ni mkweli au la. Na kweli,
kwa muda mfupi sana aliozungumza na Tunda, akajua moyo wake. Si kwa yale tu
maneno, lakini aliweza kusoma mpaka moyo wake. Hiyo nayo ni karama yake ambayo
Mungu alimjalia huyo bibi na kufanikiwa kufanya anachokifanya huko kwao na
ulimwenguni.
Alhamisi.
Tunda
kwa baba yake.
S |
iku ya alhamis Tunda akaamua
kwenda kwa baba yake kabla ya siku ya harusi. Alishatoka hospitalini. Alilazwa
siku tatu tu, akarudishwa gerezani. Ilibidi kuomba kibali maalumu kumuona kwani
haikuwa siku ya kutembelea wafungwa. Alikwenda na mwanasheria wake akamsaidia
kumuombea, alipofanikiwa, yeye akaondoka na kumuacha Tunda akimsubiria baba
yake hapo.
“Unajisikiaje?”
“Nashukuru angalau. Japo bado mwili hauna nguvu. Kuna dawa bado natumia.”
“Pole baba.” “Asante. Nakushukuru sana
Tunda mwanangu. Naona mwanasheria uliyenitafutia anahangaika kweli! Najua
inakugarimu.” “Nahangaika utoke baba. Hata yeye anasema anaona atafanikiwa.
Ameanza upelelezi wa chinichini, anasema ameshapata watu wawili ambao
walimwambia ni mpango walikufanyia pale ofisini ili utolewe. Wanasema
walipokuwa wakitaka upitishe malipo yao kama ni ya uongo, ulikuwa ukiwakatalia
ndio maana walikubambikizia receipt ya uongo, wao wakala pesa, uonekane wewe
ndio uliiba. Sasa anasema anataka kumtega mmoja wao. Amrikodi, ndipo awapelekee
wale wenye kampuni wajue ubaya wa wafanyakazi wao. Na anasema wakikubali kufuta
tu kesi, anafungua ya madai ili ulipwe fidia zote.”
“Ameniambia
na mimi hivyo hivyo. Ila amenisisitiza wakinilipa na kuniomba nirudi kazini,
nisikubali.” Tunda akashangaa kidogo. “Kwa nini tena?” “Anasema hakuna mtu
anafuraia kuingia hasara. Kwa kunilipa mimi fidia, nikuwaingiza wao hasara.
Sasa kuja kurudi tena pale, wanaweza kunitega kokote. Amenishauri nianze
kufikiria kujiajiri.” Baba Chale yaani baba yake Tunda akacheka kidogo kama anayefikiria.
“Nini?”
Tunda akamuuliza. “Anajiamini huyo! Anasema hajawahi kushindwa kesi. Kwa hiyo
anasisitiza niendelee kufikiria biashara yakufanya, pesa inakuja.” Tunda
akacheka kidogo. “Kuwa na imani baba.” “Aaaha!” “Nini? Usikate tamaa.”
“Tusubiri tuone.” Akajibu kama anayefikiria. “Najuta kuacha kazi wizarani
nakuhamia kampuni ya watu binafsi. Najuta mengi tu.” “Pole baba. Naamini kila
kitu kitakuwa sawa. Anza kufikiria chakufanya baada ya kutoka hapa.” Wakatulia
kidogo.
“Naolewa
kesho.” “Net ameniambia. Mbona huna furaha sasa?” Baba yake akamuuliza. “Kwanza
wameshakulipa mahari?” Baba yake akaanza
kucheka. “Au umesamehe mahari?” “Huko kukupenda tu ni mahari tosha. Ningepata
wapi mtu wa kukupenda hivyo? Nimemwambia ahakikishe tu anakuheshimu.” Tunda akajifuta
machozi. “Net ananipenda sana, baba.” “Sasa
tatizo liko wapi!?” Baba yake akamuuliza.
“Kuna
kitu nilikuwa sijakwambia baba na hata Net siku ya kwanza kuja naye hapa
aligusia, lakini najua hukuwa umeelewa vizuri.” “Juu ya nini tena?” Baba yake
akauliza. “Kipindi kile uliponiacha hospitalini
nikiwa mgonjwa, ndio wakakufunga. Nikatoka lakini nikashindwa kuja kukuona, ni
kwa kuwa nilikuwa nakuogopa.” Baba yake akakunja uso.
“Kwa
nini!?” “Nilikuwa nikiishi maisha mabaya sana. Nilijua ungeniona tu, na vile
nilivyokuwa nimefanikiwa, ungeniuliza maswali ambayo ningeshindwa kukujibu, na
mimi sikutaka kukudanganya.” Baba yake kimya. Akainama kama anayefikiria. “Niliishi maisha machafu sana baba. Nilionekana
nimefanikiwa kwa nje, lakini hayakuwa maisha mazuri mpaka Net aliponitoa huko
nakunipeleka kanisani. Huko nako nikapona roho, lakini imekua ndio chanzo cha
matatizo yangu.” Baba yake akawa haelewi.
“Kanisani
tena!?” Akamuuliza. “Ilibidi kutubu dhambi zangu. Nilikuwa na mashetani
ambayo mengine yaliongea uchafu waliokuwa wakinitumia niufanye, mengine
nilikiri mwenyewe. Nilikuwa nimefika mwisho baba. Nilikuwa nimechoka. Nikajua
nimepata sehemu yakutoa matatizo yangu. Lakini hata Net aliniambia pale ni
sehemu sahihi naweza kuongea chochote. Sasa kama nilivyokwambia. Nilikuwa
nimefika mwisho, nataka kupumzika. Na kama unavyojua, uliniacha peke yangu nikiwa
nimefungiwa milango na ndugu wote. Nikajikuta nakiri kila kitu.” “Hukukosea
Tunda. Ulifanya vizuri kukiri kanisani. Si ndio umepata msaada sasa?
Nakupongeza.” Baba yake alijaribu kumsifia.
“Na mimi
ndivyo nilivyofikiria baba. Lakini imekuwa tofauti. Badala yake nimekuwa ni
kama nimetengeneza mwiba wakunichoma. Moja ya wanaume niliokwisha kuwa na
mahusiano nao, alitaka kumuoa mama yake Net.” Baba yake alishtuka mpaka Tunda
akamuona. Tunda akainama. “Net anafahamu hilo!?”
“Anafahamu baba. Na mwingine alikuwa rafiki kipenzi, kama ndugu kwa Net.”
Tunda akaendelea huku anafuta machozi.
“Siku nimeenda kukiri pale kanisani, huyo baba aliyekuwa amuoe
mama yake Net, alikuwepo na mama yake Net alikuwepo. Net hakuwa akijua kama
mama yake alitaka kuolewa na yule mzee. Na mimi nilipaniki nilipomkuta yule
mzee pale ofisini kwa mchungaji. Kwa kuwa nilitaka kuanza maisha mapya, Net
akaniambia amenipeleka pale kwa watu wacha Mungu, nafika pale nakutana na yule
Mzee, nilipaniki sana. Mbele yao, nikapaniki. Nikamwambia Net mbona anataka
kunirudisha kule kule kubaya? Mimi sikujua kama yule mzee ni wa kanisani. Maana
alishawahi kunilipa mara mbili japo kanisani alisema ni mara moja tu. Basi,
ndio uadui umeanza. Mama yake Net hanitaki kabisa.” “Na Net
mwenyewe!?” Baba yake akiwa kwenye mshangao, akauliza.
“Huna
utakachomwambia Net juu yangu, mbali ya kunioa mkaelewana baba. Na hivi
ninavyokwambia sio kwamba alisikia siku nakiri kanisani! Alishanifumania zaidi
ya mara tatu. Hata huyo rafiki yake, anaitwa Gabriel, alishanifumania naye.
Mimi mwenyewe sikuwahi kujua kama Net anaweza kuja kunifikiria mimi kama
mwanamke wakuoa.” Yule baba alivuta pumzi kwa nguvu, akatulia kidogo.
“Utafanyaje?”
Mwishowe akamuuliza. “Sijui baba. Ila ninachojua kesho naolewa naye. Japo ni
kwenye mazingira hatarishi sana. Mama yake anatafuta kila mbinu yakuniangamiza.
Hataki hata kuniona, na ametengeneza watu ambao wanatugeuka. Huyo Gabriel,
amemgeka Net, anamtisha kuwa asinioe kwa kuwa mimi ni mwanamke wake na bado
ananipenda ni kama amempokonya mkewe.” Tunda alimuelezea baba yake kila kitu
bila kumfisha mpaka maswala ya nyumba.
Alimuacha
baba yake haelewi huyo Net anatakaje bado kumuoa binti yake. Tunda aliondoka
akiwa amempa baba yake habari chungu na tamu. Tamu kwa kuwa anajua Net
anampenda kwa dhati. Chungu akiwaza mwisho wake ni nini!? Maana anaingia kwenye
ndoa akiwa na vita na mwanamke mwenye jina kubwa na pesa hapo nchini. Mbaya
zaidi, ni mama yake Net, na ndiye anayemuweka Net mjini
Ijumaa.
Harusi ya Net na Tunda.
S |
iku hiyo Tunda aliamkia saluni
akiwa na mama Penny pamoja na watoto wake. Mama yake alifika hapo saluni
akitokea hotelini akiwa na Aneti. Wote Tunda alitaka watengenezwe. Tunda mpenda
nywele, alishashonewa nywele nzuri sana siku iliyopita kabla ya kwenda kwa baba
yake. Siku hiyo ilikuwa kupambwa tu, na ile nywele kutengenezwa muundo wa
kuweza kubeba shela na maua. Net, mchungaji na Tom walikuwa saluni yao.
Kulikuwa na hekaheka wakitaka kumaliza mapema, ili harusi ifungwe mapema kabla
ya giza kuingia. Bibi Cote alikuwa akiondoka kesho yake, yeye na Maya kurudi
nchini Canada.
Mama
Penny na baadhi ya vijana wa pale kanisani, walishapamba nje ya nyumba ya Net,
ambako kwa wakati huo kisheria ilikuwa nyumbani kwa Tunda. Hawakutaka kufunga
hiyo ndoa kokote ila hapo. Mama Penny alikuwa ameshamsaidia Net kutafuta
wapishi wazuri na waliahidi kuja na vinywaji. Na akawataka wafike hapo mapema
tu. Wakakubaliana na mama Penny. Net alishamkabidhi mama Penny pesa yote bila
maswali. Akabaki mama Penny kufanya mipango yote. Yeye peke yake akipiga simu huku
na kule. Mpaka inafika ijumaa, mama Penny akiwa saluni bado alikuwa kwenye simu
akihakikisha jambo haliharibiki. Alitulia mida ya saa 9 mchana wakiwa bado wapo
saluni, alipopata simu kuwa watu wa chakula, vinywaji, Dj na keki wameshafika
nyumbani kwa Tunda na Net.
Hapo
mama Penny akawa amebakisha kumpelekea Net mke tu. Na Net naye akawa ametulia
kuona kila kitu kinaenda sawa mpaka muda huo. Na yule mwanasheria
aliwahakikishia kila kitu kitakuwa sawa, wakalipia garama zote za mtu wakufika
pale kufungisha hiyo ndoa yao. Na kweli na yeye akafika kwa wakati.
Kama
kawaida Tunda hakujikosea. Alivaa shela nyeupee, kama asiyemjua mwanaume.
Akatengenezwa vizuri, na ile rangi yake ya weusi, usingechoka kupiga
vigelegele. Japokuwa walikuwa wachache lakini palitengenezwa kupendezea
wachache hao. Hakutaka kuhusisha watu wa kanisani kabisa. Wao walikuwa
wachungaji, halafu ndoa inafanyika nyumbani na ni ya serikali! Wanawaambiaje
watu? Hata hivyo walifanya kwa kuwa ni Tunda. Na alishamwingia mama Penny mpaka
rohoni.
Mama
Penny alimuona Tunda kama mdogo wake wakuzaliwa na rafiki haswa. Penny hakuacha
kujisifia. Furaha yake ilitimia pale alipoambiwa ataanza kuingia yeye na mdogo
wake pamoja na Aneti. “Wataniona mimi kabla ya aunt Tunda.” Hakuacha kujisifia.
Net, Tom
na Mchungaji walishafika hapo kutokea saluni. Bibi Cote na Maya walikuwepo hapo
nyumbani kwa Net mapema tu. Wakati Tunda anakaribia na hapo nyumbani ndipo Net
akampigia simu mama yake kumtaka afike nyumbani kwake. Akiwa na mshangao kwani
hawakuwa wakizungumza mbali ya salamu. Akakubali kufika. Lakini akitaka kujua
kuna nini na kama ni mazungumzo kwa nini wasizungumzie tu ofisini, Net
akamwambia anamuomba afike nyumbani kwake, hatamuweka muda mrefu.
Gari
hiyo ya Limousine iliyokuwa imembeba bibi harusi na wasimamizi wake pamoja na
mama yake Tunda, iliwasili nyumbani hapo saa 10 kamili jioni. Net alimpigia
simu mama Penny akimuomba wasubiri kwenye gari mpaka atakapowaambia washuke.
Mama Penny akashangaa ni kwa nini wasubiri nje!
Mama
Cote alifika nyumbani kwa Net bila kuchelewa. Akashangaa kukuta shamrashamra na
nyimbo za taratibu zikipigwa na pameandaliwa kama kwenye sherehe. Net akamfuata
pale alipoegesha gari. “Ni nini kinaendelea?” “Tunaweza kuzungumza pale kwenye
meza aliyokaa bibi?” “No.” Yule mama alikataa bila kupepesa macho. “Niambie ni
nini kinaendelea Net?” “Leo, namuoa Tunda.” Mama Cote alibaki akimtizama mwanae
kwa sekunde kadhaa bila kujibu kitu.
“Nampenda
Tunda, mama. Na nilikwambia lazima nimuoe.” “Kwa shida zote nilizopata na wewe
Net, leo, sasa hivi ndio unaniambia unaoa!? Unaniambia kama
mpitaji tu? Unanitoa ofisini kuja kwenye harusi yako!?” Net alimuona vile mama
yake alivyobadilika. Alipandisha hasira mpaka midomo ilikuwa inacheza.
Ritha amtangazia Vita iliyo ramsi Mwanae, Siku ya harusi yake.
“Unanidharau mimi Net!? Unapanga
mipango yako na bibi yako mimi nakuwa kama mtu wa kando tu?” “Naomba utulie
mama. Hii mipango nimepanga mimi mwenyewe. Bibi hausiki.” “Na yeye bibi yako
umetoka kumpigia simu sasa hivi?” Mama yake akauliza akionekana amekasirika
kupita kiasi.
“Mama!”
Net alitaka kumshika, mama Cote akarudi nyuma. “Niambie ukweli Net. Na yeye
bibi yako ndio anajua leo kama unamuoa Tunda, mwanamke malaya huyo, aliyetembea
na kama baba yako na kaka yako pia!?” “Anajua mama. Maya alikusikia ukiwa
unagomba siku ile. Tuliposhindwa kumjibu ni nini tunaongea, akaja kumuuliza
Maya kesho yake, ndipo Maya akamwambia kile alichokusikia ukisema. Akaja
kuniuliza kama ni kweli juu ya Tunda. Ni kamwambia ni kweli.” “Kwa hiyo yeye
anaona ni sawa umuoe malaya yule!?” Mama Cote akauliza.
“Kwanza
nakusihi mama yangu, usimtukane Tunda. Masaa machache sana, anakuwa mke wangu,
yaani mwili mmoja na mimi. Pili, Nana anaamini kwenye kukosa na kusamehewa
dhambi. Nakuomba..” “Kwa hiki ulichonifanyia leo, ni kunikana hadharani mbele
za watu. Umemchagua Tunda, dhidi yangu. Umemthamini bibi yako anayekupa mali
zao, umenidharau mimi mama yako niliyekubeba tumboni miezi 9, na
kukunyonyesha.” “Mama!” Net akaishiwa nguvu.
“Sasa
kuanzia leo, utakapofanyika mwili mmoja na Tunda tu, sahau kabisa kama mimi ni
mama yako. Nisikuone nyumbani kwangu wala ofisini.” “Mama Please!” Net
alishakuwa mwekundu akatamani kulia. “Sikutanii Net. Ukimuoa tu Tunda. Leo au
kesho, ujue wazi wewe sio mtoto wangu tena. Usiwahi kuja kuniita mama tena
maishani. Hata ukisikia mimi nimekufa leo, usije kwenye mazishi yangu. Usisogee
kwenye chochote nilichokitafuta kwa jasho langu. Wewe sio mwajiriwa wangu.”
Ritha alikuwa akitetemeka kwa hasira. Akaendelea.
“Yaani
kwa kifupi nataka ujue, tokea siku ulipouza mali ya kampuni yangu kwa Tunda,
yaani hii nyumba, ulijifukuzisha kazi, na ujue wazi, umefanya kosa kisheria.”
“Hii nyumba ni yangu mama. Nipo huru kufanya ninachotaka.” Net alimshangaa mama
yake.
“Ilikuwa
kwa jina gani?” Mama yake akamuuliza huku amemtolea macho. “Cote LTD kwa
kuwa..” “Exactly! Ilikuwa chini yangu. Mali yangu kisheria, wewe ni mfanyakazi
wangu. Umeuza mali ya kampuni kwa mwanamke wako. Wewe ni mwizi. Nimekuleta
nchini kama mfanyakazi, umeniibia. Ujue ninapoondoka hapa, nakwenda kukushitaki
kwa watu wa usalama na uhamiaji. Kitakachokupata, ndipo utajua mimi ni nani! Na
ukumbuke nilikuonya. Usinijaribu. Kama unadhani nakutania, muoe huyo malaya.”
“Mama! Nimejenga hii nyumba kwa
pesa yangu, ni jasho langu!” Bibi Cote akasogea. “Kuna nini?” Bibi Cote
akauliza. “Na umwambie bibi yako, kuanzia leo, asinitafute tena, na jina lenu
namwachia Tunda. Nitabadilisha jina la kampuni yangu nirudishe la baba yangu.
Mwambie mtoto wake hakuniokota. Alinikuta Canada sababu baba yangu alinilipia
pesa yakuishi huko. Mizigo yake yote itamfuata hapa kwenye hii nyumba
mliyoniibia. Na umwambie Maya, ana siku ya leo tu kuchagua. Awe mtoto wangu, au
anikane kama wewe utakavyonikana leo, endapo utamuoa Tunda. Uamuzi ni wako.
Tunda au mimi.” Mama Cote akamalizia kwa lugha ya kiswahili, akapanda gari
yake, akaondoka.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
Net maji yamezidi
unga. Anamwaga ili asonge ugali? Usikose mwendelezo. Vita yake ndio inaanza
rasmi endapo anamuoa Tunda. Usikose muendelezo kujua kama ameamua kusuka au kunyoa!
Kama Tunda alivyompokonya ndoa yake kwa kutembea na mwanaume wake, ndivyo
anavyotaka kumpokonya na yeye ndoa. Yupo garini, ameshapambwa, anasubiri
harusi. Je, ndoa ipo? Usipitwe.
0 Comments:
Post a Comment