Naomi Simulizi |+1 205 767 8163 |naomisimulizi@gmail.com Nilipotea! - SEHEMU YA 33. - Naomi Simulizi

Nilipotea! - SEHEMU YA 33.

 

W

asiwasi ulianza kumpata mama Penny baada ya week ya pili kuanza bila kumsikia Tunda. Mumewe alimtuliza na kumwambia walihitaji huo muda. Wawaache tu. “Tunda sio mtu wa kukaa zaidi ya week bila kunitafuta! Mimi namjua yule. Maswali yake huwa hayaishi.” “Basi ujue safari hii kapata wakumuuliza.” Mama Penny akacheka. “Na kweli.” Wakataniana hili na lile. Wakaacha.

Mama yake na wadogo zake walishahamia kwenye nyumba ndogo aliyokuwa amelipiwa na Tunda. Na kwa kuwa nyumba ya Net ilikuwa imejaa, Tunda akaamua kumpa mama yake vitu vyake vyote vya ndani, kasoro nguo zake na vitu vyake vingine, alivihamishia kwa mama Penny. Hata gari yake aliiacha nyumbani kwa mama Penny. Kuwa wakitoka kwenye fungate ndipo aende akachukue vitu vyake vyote ahamie nyumbani kwa Net, ambapo ndio ilikuwa nyumba yake. Alishaachia nyumba aliyokuwa akiishi.

Vita ya wenyewe kwa wenyewe. Kwa Bethy na Gabriel.

Ni miluzi ya Gabriel tu ndio iliyokuwa ikisikika ndani ya nyumba yake mchana na usiku. Furaha ilimjaa, usingemsikia akibishana na Bethy tena mpaka Bethy akawa anashangaa. Akianzisha kelele, Gabriel anaongeza sauti ya tv, au anatoka nje kabisa. Bethy akimjia kwa heri, basi Gab atamjibu kwa ufupi na kuondoka kabisa pale kama anayemkwepa. Usingemkuta nyumbani kama watoto wake hawapo. Bethy akawa haelewi mwisho wa ile hali ni nini asijue linalomkabili.

Baada ya majuma mawili tokea Net aondoke, na ukimya ukiwa ndani ya nyumba yao, Bethy akiwa ofisini kwake, akaambiwa ana mgeni. Akiwa hamfahamu mgeni mwenyewe, akamwambia sekretari wake amruhusu aingie ndani. Yule mtu alijitambulisha kama ni mwanasheria aliyetumwa na Gabriel, anatakiwa asaini makaratasi ya talaka.

Nusura Bethy aanguke. Alichofanya nikuchukua zile karatasi zote, pochi na funguo zake za gari akatoka ofisini kwake na kumuacha yule mwanasheria amekaa pale pale, yeye akaenda mpaka ofisini kwa mumewe.

Alimkuta Gabriel na wageni watatu ofisini kwake, akaingia bila hata hodi. Akamtupia Gabriel zile karatasi usoni mbele ya wageni wake. “Naona umepata ujumbe wako.” Gabriel alimkejeli huku akijaribu kukwepa zile karatasi, na cheko la kejeli juu kwa mkewe. “Kama unafikiria kuniacha mimi ili umuoe malaya wako, ujue yupo jela. Anakabiliwa na makosa ambayo hawezi kupewa dhamana.” Palepale uso wa Gabriel ukabadilika. Akasimama.

“Unasemaje Bethy!?” Bethy akaanza kumcheka. “Wewe huoni mjini kulivyo na amani? Kila mwenye ndoa yake ametulia kwake na familia yake! Sababu malaya wa jiji yupo selo. Na hatoki kwa dhamana wala hongo. Ndio ujue waliokutangulia mjini wamekutangulia. Sasa vimba, upasuke. Hata ukiniacha mimi, ujue na wewe umekosa.” Bethy akatoka huku anamcheka mumewe. Hasira na mshtuko vilimfanya aropoke kitu alichokuwa ameonywa sana na Ritha.

Gabriel kwa Ritha.

H

apo hapo akawaaga wale wageni nakutaka watoke ofisini mwake. Akampigia simu mama Cote. “Ni nini kinaendelea kwa Tunda?” “Sijui. Kwani vipi!?” Ritha akajibu kwa kujiamini. “Nisikilize mama Cote. Usithubutu kunichezea akili. Hakika nakuonya. Kama unanichezea au ulinigeuka, hakika utajuta. Nilihakikisha unanielewa kabla hatujaanza mchakato…” “Tulia kwanza Gabriel. Kwani kuna nini?” Ritha akajifanya hafahamu chochote. “Bethy ameniambia kila kitu.” Gabriel akaamua kumtega.

“Sio mimi ninayehusika Gabriel. Ni mkeo. Kama amenisingizia mimi, basi ujue nimuongo. Yeye ndiye aliyetaka kumshitaki Tunda. Ndiye aliyewasiliana na mfanyakazi wa kampuni ya simu na kumuomba amtolee mawasiliano ya Tunda ya miaka mitatu mpaka minne iliyopita. Jumbe na malipo yote aliyokuwa akipokea kwa biashara ya ngono aliyokuwa anafanya. Ame..” “Nakupa nafasi ya mwisho mama Cote. Una uhakika kabisa hauusiki na kumuweka Tunda ndani? Sitakusamehe na utalipa kwa kunizunguka. Na nitahakikisha unalipa kwa machungu. Sikudanganyi.” Gabriel alikuwa akitetemeka kwa hasira, hakutaka maneno mengi, akamkatisha Ritha kumtaka ukweli. Kimya. “Mama Cote?” Gabriel akaita, mara akasikia simu imekatwa.

Gabriel alitoka pale kama aliyechanganyikiwa akaenda mpaka kituo cha polisi Kawe. Hakumkuta mkuu wa kituo ambaye ni rafiki yake. Akajaribu kuulizia pale ili kujua alipowekwa Tunda. Hakupata majibu yakumridhisha. Akaamua kumpigia simu mkuu wa kituo, akamwambia atakuwepo hapo ofisini baada ya kama masaa mawili. Huo muda ulikuwa mrefu sana kwa Gabriel, akatoka tena pale mpaka ofisini kwa mama Cote. Hakumkuta. Sekretary wake akamwambia kuwa alitoka, bila kumuaga. Alipojaribu kumpigia, simu zake zote tatu zilikuwa zimefungwa.

Gabriel kwa Bethy

Gabriel akatoka pale ofisini kwa Ritha mpaka ofisini kwa mkewe. “Nimeambiwa wewe ndio umemshitaki Tunda.” “Nisikilize Gab. Kama mmezungukana na mama Cote, mimi hayanihusu. Sijui makubaliano yake na wewe, ila najua yangu na yeye. Tulipeana majukumu kama alivyofanya na wewe. Kwa kuwa mimi nafahamiana na mtu wa kampuni ya simu, nimepata ushahidi nilioutaka, na yeye  ametafuta shahidi wa kukiri kufanyiwa biashara ya ngono na Tunda. Sasa sijui.” “Nani?” Gab akauliza.

“Wewe unawazimu nini Gabriel!? Ni kwambie ili iweje!?” Bethy akamshangaa sana. “Wewe shida yako ilikuwa mfanikishe na mama Cote, Net atoke nchini na asirudi tena. Mmetengeneza kesi yenu, mmefanikiwa. Mimi shida yangu ilikuwa kumuweka Tunda mbali na familia yangu. Anakuwa wapi, mimi sikujali ilimradi iwe mbali.” Gabriel alitulia kabisa akimsikiliza mkewe. Alimjua jinsi alivyo mropokaji anapokuwa na hasira. Kwa hiyo akajua atayasema yote.

Bethy naye akaendelea bila shida akitaka kumuumiza zaidi. “Sasa kwa kuwa na shida ya mama Cote ilikuwa pia kumkomoa Tunda, na arudishe mali zake, basi, tukaunganisha nguvu, na sisi tukapanga mipango yetu, tumefanikiwa. Ushahidi wa kumshitaki Tunda, upo. Tena sio magumashi. Upo ushahidi kabisa na wa uhakika. Tunasubiri siku ya kesi yake mwanasheria awakilishe ushahidi, ahukumiwe makosa yake, afungwe jela atupishe wenye ndoa zetu mjini.” Na kweli Bethy aliongea yote.

Gabriel akatoa simu yake akaanza kumpigia tena simu mama Cote zaidi ya mara mbili hakumpata. Bethy akazidi kumcheka. “Tena kwa taarifa yako tu, huyo malaya wako atahukumiwa kwa haraka sana ili msije kumtoa. Hiyo pesa iliyomwagwa ili kuendesha kesi yake kwa haraka, hakika hatoki. Anza kutulizana kwenye ndoa yako.” “Nishamalizana na wewe Bethy. Wazazi wangu wanajua wewe si mke wangu. Nasubiri kukamilisha tu taratibu kisheria, maisha yangu yaendelee.” Bethy akashtuka sana. Kwamba mpaka wazazi wake Gab wanajua!

Bado Gabriel alikuwa amesimama. Macho kwenye simu. “Namuhurumia mama Cote!” Gabriel aliongea huku akijaribu kumpigia tena. “Hakika atajuta kwa kunigeuka!” “Hebu subiri kwanza wewe Gab. Yaani hasira hiyo ni kwaajili ya kuwekwa ndani malaya yule!” Gabriel akatoa macho kwenye simu na kumtizama mke wake, akacheka kwa kuguna.

“Haupo hata robo ya Tunda.” “Kwa kipi!? Nimesoma kuliko yeye. Nina..” “Kama ndoa inajengwa na shule, mbona wewe mwenye madigirii mengi imekushinda!? Mume mmoja tu na watoto wawili wanakushinda kuwatuliza na kuwafanya walale hata usiku mmoja tu kwa amani! Umejawa kelele! Fujo tupu. Usijifananishe na Tunda hata kidogo. Nakujua wewe na Tunda, ndani na nje. Yeye unamwita malaya, lakini nakuhakikishia Bethy, haupo hata robo yake. Wala usithubutu kujilinganisha naye. Nikujidhalilisha. Kajaribu kwa wasio kufahamu.” Gabriel aliongea taratibu tu bila jazba. Bethy akazidi kucharuka.

“Na usiku wa leo, usirudi nyumbani. Nitamwambia dereva akupelekee mizigo yako kwenye kile kijinyumba chako ulichokuwa ukininyanyasa nacho. Angalau usiku wa leo uishe kwa amani kwangu. Umekuwa adhabu!” “Ujue ukinifukuza mimi naondoka na watoto.” Bethy akamtisha. 

“Ukitaka nenda kawafuate shule hata sasa hivi. Ila ujue kabisa, ukiwatoa kwangu, unawatunza.” Gabriel alijibu bila hata wasiwasi, akarudisha macho kwenye simu.

“Kweli Gab!? Na hayo yote ni sababu ya Tunda, malaya yule!” “Malaya aliyeniheshimu na kunihudumia wakati wewe umeshindwa. Na pili, sitakusamehe kwa kunigeuka. Nisikuone nyumbani Bethy. Kama umeamua kuchukua watoto, niambie sasa hivi na wao wafungashiwe mizigo yao.” Bethy hakuamini.

“Wewe umelogwa Gabriel. Unatelekeza watoto sababu ya upumbavu huo?” “Sitatelekeza wanangu! Wewe vipi Bethy!? Si watakuwa na wewe, mama yao! Una kazi nzuri na uwezo wakuwalea unao. Pili, umenigeuka, sio upumbavu. Kama umeweza kufanya mpango mkubwa hivyo mpaka ukafanikiwa kumuweka Tunda ndani, unafikiri anayefuata ni nani kama sio mimi?” “Siwezi kukufanyia hivyo Gab, wewe ni mume wangu. Nimefanya yote kwa ajili yako. Nataka tubaki kwenye ndoa yetu.” Gafla Bethy akajirudi.

“Hivi unajua unazungumza na mimi sio mtu mwingine?” “Najua.” “Sasa mbona unaongea mambo ambayo hata wewe mwenyewe yanakuwia vigumu kutoka mdomoni mwako! Acha ujinga Bethy. Na ujipange. Umeanzisha jambo ambalo, litakurudi tu. Mwenzio amekimbia hata kwenye simu hapatikaniki. Na kama unafikiri umemkomoa Tunda, ujue nitamtoa tu na wewe utaweka saini kwenye talaka. Nakushitaki kwenye vyombo vya sheria. Na hivi ninavyokwambia nakwenda kutafuta njia yakumtoa Tunda. Hana kosa la jinai linaloshindikana kuwekewa dhamana.” Gabriel akaangalia muda, akatoka.

Bethy akamkimbilia nje. “Huwezi kumtoa Tunda.” Akamshika shati kwa nguvu. “Sijakugusa Bethy, na wewe usiniguse. Acha kunidhalilisha mbele za watu.” “Unaona haya kwa lipi wakati wewe umeamua kuacha familia yako ili ukaishi na malaya anayejiuza hapa mjini!? Mama Cote amekusaidia kukutengenezea kesi nzuri tu ili kumdhibiti na akili yako itulie kwa familia yako na wewe unaenda kumtoa!”  Bethy akaanza kuongea kama amerukwa na akili.

“Wala Tunda hakuwahi kukupenda Gab. Hata yeye alikuja kukutamkia wazi hakukuficha. Alikuomba umuache, sasa hivi ameamua kutulia na maisha yake. Alikwambia wewe ni muhanga kama wahanga wengine aliowatumia kujinufaisha na maisha aliyoishi zamani. Alikuwa akikutumia tu. Kwa nini unashindwa kuelewa hilo wakati alikiri kwako wazi na kukutaka umuache na usimtafute tena?” 

“Kama mnajua hilo ni kwa nini mmemtengenezea kesi ili afungwe!? Nilimuacha Tunda wakati ule akiwa na shida, tena ananililia shida. Akiwa na njaa, nilimtupa, ili nitulie nyumbani na wewe Bethy. Ulibadilika?” “Wewe ndio hukubadilika Gab. Ulimuacha Tunda kwa matendo, lakini akili zako hazikuwa nyumbani.” “Ulitaka nifanye nini kwako ambacho nilishindwa kufanya na wewe ukashindwa kubadilika!?” Gabriel akamuuliza mkewe taratibu tu.

“Akili zako zilikuwa kwa Tunda.” “Ndio shida yako Bethy, na wewe ni muongo. Tangia tukubaliane nimuache Tunda, mbele ya mchungaji, sema ukweli, nilishamtaja hata mara moja kwako?” Kimya. “Wewe ndio unajishuku na kunifuatilia hata kwenye mambo ya msingi! Kila mahali wewe ni wivu na ugomvi. Kila ujumbe unataka kusoma wewe! Unataka kutawala ambako huelewi wala huwezi! Unataka kuwa bosi wa wafanyakazi ambao hufanyi nao kazi! Wewe umeajiriwa na umesoma, umeona wapi huo utaratibu? Huwezi kuwa bosi wa biashara zangu!” Gabriel akaendelea. Taratibu tu.

“Huwezi kunizuia na kutaka ujue na kuelewa kila mtu ninaye zungumza naye wakati wewe unajua mimi ni mfanyabiashara! Nafanya biashara na wanawake na wanaume. Mimi sichagui. Popote pesa ya halali ilipo, naifuata. Lakini wewe unashindwa kuniamini, na hutaki kuelewa. Nikiishiwa unashindwa hata kunipa nauli ya daladala au hutaki nitumie hata gari yako! Sasa ulitaka nifanye nini? Nikae nyumbani uendelee kuninyanyasa kuwa sina akili?” Gabriel aliendelea kumuhoji bila jazba.

“Mbona ulitembea na Tunda? Tena sio kutembea naye mara moja! Ni kuwa na mahusiano naye!?” “Nilikujibu wewe na mchungaji. Ni wewe mwenyewe ulinifikisha kwa Tunda, na nilikuonya usimlaumu Tunda. Nilihitaji msaada ambao ulishindwa wewe kunipa, akanipa Tunda. Ulitaka nikubembeleze mpaka lini? Hukuwahi kunithamini nilipokuwa na shida, mpaka sasa nimefanikiwa pia bado hunithamini.”

“Narudia tena. Haupo hata nusu ya Tunda. Na Tunda siye aliyenifanya nikuache wewe, wala hakunitongoza. Mimi mwenyewe nilimtaka Tunda. Sikuwahi kuwa na mahusiano yeyote na yeyote isipokuwa wewe. Niliapa kuwa mwaminifu kwako, lakini wewe ukanitesa ukijua sina pakwenda. Nilimpata Tunda, nikamuomba awe na mimi. Akakubali na kuniheshimu sana. Narudia tena, sijui ilikuwaje kwa wengine, lakini mimi najua kwa upande wangu, ndiye niliyemuhitaji Tunda, na nikatulia kwa kuwa aliweza kunipa kile ulichoshindwa wewe kunipa.” “Alikukubali sababu ya pesa tu. Hakuna lolote, wala si mapenzi.” Bethy akajibu kama kumshushua.

“Kwani mimi nakataa! Nilimuacha, na nilihakikisha ananufaika na pesa yangu, kwa kuwa na mimi nilikuwa nanufaika zaidi na yeye. Tunda alinifanya nitulie nakuweza kufikiria zaidi na nikaweza kutengeneza pesa zaidi. Heshima, utulivu na uwezo wa kunisikiliza kutoka kwa Tunda vilinifanya nitulie hata wakati wewe ulipokuwa ukininyima usingizi tukiwa wote, Tunda alinituliza nyumbani.”

“Na kwa taarifa yako tu, Tunda hakuwahi hata mara moja kunishauri nikuache. Wakati wote alikuwa akinituliza ili mimi na wewe tuweze kulea watoto. Tunda anajua umuhimu wa ndoa. Hakutaka watoto wangu wakue bila wewe au mimi. Wakati wote alinitaka nijaribu kutafuta jinsi yakuweza kuishi na wewe kwa amani na utulivu. Akinishauri hili na lile, pengine kutakuwa na amani.” “Alikushauri nini kama sio uongo?”  Bethy akauliza kwa jazba.

“Ni mengi Bethy. Mengi mno. Tena alikuwa akinifuatilia kama nimekufanyia ili kuleta amani, lakini pia ilishindikana. Tunda hakuwa malaya kwangu. Alikuwa rafiki ambaye sikuwa na sababu yakujificha kwake. Niliongea mbele yake kwa uwazi kabisa na yeye alinishauri akitaka nitulie kwako. Lakini ilishindikana Bethy. Ulinitoa kwa Tunda, tena ukakataa hata nisiwasiliane naye kwa salamu tu! Nikakubali. Nikatulia nyumbani, lakini wewe hukuwahi kubadilika Bethy. Ukawa ni kama umenitoa kwenye heri, nakunitupa kwenye dhiki, ambako ni kwenye nyumba niliyojenga mwenyewe.”

“Ulishindwa ndoa wewe mwenyewe. Huna wakumlaumu. Wewe mwenyewe na roho yako mbaya, ndio ulimrudisha Tunda kwangu. Wewe mwenyewe ili tu kumuumiza Tunda. Hakunitafuta wala sikumtafuta. Ukanipa namba zake za simu, na kutaka nipange naye miahadi tukutane ili kuhakikisha kama Tunda amebadilika kweli. Unakumbuka fujo ulizofanya kunilazimisha nimtafute tena Tunda mpaka nikakubali kumtafuta tena Tunda, tena ukiwa umenisimamia kuhakikisha namtafuta Tunda ili mumchafue kuhakikisha hajabadilika? Unakumbuka Bethy au umesahau?” “Nilitumwa na mama Cote.” Akajaribu kujitetea.

“Kwa fujo zile zakuamsha nyumba nzima, mpaka watoto na kunifuata mpaka kazini kwa kelele nyingi ili nimtafute Tunda!? Ni mama Cote peke yake au alikuwa akikusaidia kukujaza ujinga tu. Ulimrudisha Tunda kwangu, wewe mwenyewe ukisaidiwa na mama Cote bila kufikiria sababu ya hila zenu kwa mtu ambaye hata hakuwa na habari na nyinyi.”

“Na Mungu naye akawapa mlango wa kwanza wakutokea, ili mumuache Tunda. Mkanivalisha spika. Mkasikia mazungumzo yetu yote na Tunda. Akajibu Tunda bila hila. Tena na wewe ukisikia jinsi alivyokuwa akinishauri nitulie nyumbani, nikurudie wewe bila kujua mateso niliyokuwa nikipitia tokea ututengenishe naye. Umesahau hata hilo!? Eti Bethy?” “Ule ulikuwa ni unafiki tu. Hana lolote. Kama yeye anajua sana ndoa, mbona asiolewe sasa, tukamuona ametulia kwenye ndoa yake?” Gabriel akatingisha kichwa kama anayemsikitikia mkewe.

“Sasa nakuonya Bethy, kwa kuwa Mungu mwenyewe aliwapa mlango wakutokea, hamkumsikiliza Mungu mkaendelea kumkaidi kwa kumfuatilia Tunda ambaye alishajitenga na nyinyi na akakiri amebadilika, lakini bado mkaendelea kumfuatilia. Sasa mwambie na mama Cote, mchezo mliomfanyia Tunda, sitauruhusu.” “Tunda yupo jela kwa makosa sahihi. Tulichokifanya sisi ni kutafuta ushahidi tu na kumpeleka kwenye vyombo vya usalama.” Bethy akajibu kwa jeuri.

“Na ushahidi upo wa uhakika. Mwanamke wako hatakaa atoke jela.” “Basi tutashindana mahakamani. Kusanyeni ushahidi wenu wote. Wewe na mama Cote, mwanamke aliyejawa uchu wa mali, yupo tayari hata kumuangamiza mtoto wake sababu ya mali!” “Sio mali, hataki mtoto wake aoe changudoa.” Bethy akatetea.

“Tunda ameokoka, ametubu dhambi zake, amesamehewa. Nyinyi ndio mmemtoa kanisani, na kumpeleka jela. Na Mungu hatawaacha.” “Kama yupo kanisani mbona unamfuata?” “Kwani wewe nilikutoa wapi? Si kanisani? Ndivyo nitakavyofanya kwa Tunda. Utasaini makaratasi ya talaka, namuoa Tunda kama nilivyokuoa wewe, na mimi nipumzike na kutulia na Mungu wangu. Wewe ni shetani utakayeniingiza kuzimu. Na leo ni mara ya mwisho kubishana na wewe Bethy. Tutahamia kwenye vyombo vya sheria, watuhukumu kwa haki. Nimechoka na wewe mwanamke mbaya kuliko shetani! Mwishowe utanifanya kama mlichomfanya Tunda.” Gabriel akaendelea.

“Na mwambie mama Cote, tukimalizana na kesi ya Tunda, naanza kumfungulia na yeye mashitaka. Mwambie nafahamu mabaya yake yote. Sasa naenda kumtoa Tunda jela, ili tumpe mama Cote nafasi. Maana kwa serikali hii, lazima wamfunge tu.” Gabriel alipoona watu wanazidi kukusanyika pale waliposimama huku wakiwachukua video, na mmoja wa askari anayelinda lile jengo anawasogelea, akaamua aondoke. Ili wasije kutoka kwenye mitandao.

“Na kwa taarifa yako Tunda hawezi kutoka kwa dhamana.” Gabriel akamgeukia mkewe. “Kwani Tunda ameua? Amefanya Money laundary? Ameuza madawa ya kulevya? Anakosa gani la jinai linalomzuia asipewe dhamana au ni pesa yenu ndio inaongea? Sasa ndio utajua kuwa hii nchi siku hizi inaendeshwa kwa sheria wala sio pesa. Mwambie mama Cote, jioni ya leo, Tunda analala nyumbani kwake. Akinisamehe, nampeleka kanisani, namuoa kihalali. Upende usipende Bethy. Na mimi nataka kupumzika.”

“Mwanamke maneno mpaka nje ya nyumba! Ugomvi hauishi kila siku unabadilisha visa tu!” “Huwezi kwenda kumtoa Tunda.” Bethy akamzuia kwa hasira kali.“Watch and see!” Gabriel akajibu kwa jeuri, akageuka na kuondoka. Wakati anaondoka mkewe akamvuta kwa nguvu huku akimtukana. Akamchania shati.

Alipoona Gabriel hajibu kitu anaondoka, akamvuta kwa nguvu zake zote. Gabriel akajigonga kwenye nguzo, wakati anataka kutua sakafuni, kisogo kikajipigiza  kwenye ncha ya urembo uliokuwa umejengewa kuzunguka ile nguzo. Gabriel alitua chini sakafuni akiwa amelala chali. Kimya. Walichoona ni damu zikichuruzika chini ya kichwa cha Gabriel. Zilianza kusambaa na kutengeneza dimbwi la damu chini ya kichwa chake huku amefunga macho. Bethy alishtuka sana.

Msiba mzito, Bethy amuua mumewe.

K

ilikuwa kitendo cha muda mfupi sana, alichokifanya Bethy kwa hasira bila kufikiria. Kutoka alipomvuta, kujigonga kichwa kwenye nguzo, mpaka kujipigiza kisogo kwenye ncha ya kona ya urembo wa hiyo nguzo na kuwa pale sakafuni kimya amefunga macho! Kilikuwa kitendo cha muda mfupi sana.

“Jamani kaua!” “HaaH Kaua!” “Kaua!” “Kaua!” “Heee kaua!” Watu wakaanza kupiga kelele na kuzidi kujaza watu pale. Hapo ndipo kila mtu akageuka mtangazaji wa habari. Badala tu ya kuchukua video wakaanza kujichukua na wao, wakieleza tukio zima kila mmoja kwa jinsi yake wakiripoti live kutoka kwenye tukio.

Maaskari waliokuwa wakilinda pale wakakimbilia pale, wakamshika Gabriel pale sakafuni ni kweli hakuwa akihema wala hapakuwa na mapigo ya moyo. Bethy alipoona hivyo, akataka kukimbia. Watu wakamkamata wakaanza kumpiga Bethy kama mwizi huku wakimtukana.

Ikabidi tena wale askari walinzi wa lile jengo ambapo pembeni kulikuwa na benki waingilie kumuokoa Bethy aliyekuwa anagaragazwa sakafuni kwa kipigo kikali. Alishachaniwa nguo zake zote, zikawa zikining’inia mwilini mwake. Hakuwa na tofauti na kuwa uchi kwani wengine walifanya juhudi za makusudi kumtoa hizo nguo kama kumdhalilisha.

Walimchukua Gabriel kwenye gari akakimbizwa hospitalini, mkewe kituo cha polisi Osterbay. Kufikishwa Gabriel mapokezi, wauguzi wakamwangalia, wakawaambia wale waliomleta na askari mmoja wao kuwa alishafariki. Kila mtu akabaki na mshangao.

Alikuwa ni Gabriel! Kijana aliyekuwa amefanikiwa hapo nchini. Akisaidia wenye shida mbali mbali. Sifa kubwa zaidi, alijulikana ni mcha Mungu. Hakuwahi kuwa na kashfa, ndio kwa mara ya kwanza siku ya kifo chake mkewe alitangaza hadharani mahusiano aliyokuwa nayo na Changudoa, na anataka kumuacha yeye na watoto ili awe na huyo malaya, Tunda.

Kila mtu pale mapokezi akataka kujua kilichomsibu kijana huyo. Wakaanza kusimuliana. Mwenye kuongeza lake akaongeza, ukawa mjadala mkubwa sana pale mapokezi. Mmoja wa wauguzi akaona video ya tukio la Gab na mkewe imesharushwa kwenye group lao la whatsapp. Akawaonyesha kuanzia mwanzo akionekana Bethy akimtukana mumewe wakati Gabriel yupo kimya. Akaonekana Gabriel anataka kuondoka, mkewe akamvuta kwa hasira na kumsababishia kifo.

Maneno yakaendelea pale na mwili wa Gabriel mwenyewe ukiwa bado hapo hapo mapokezi. Kila mtu alisema lake kutokana na ile video. Baada ya muda mfupi sana kile kisa kikasambaa kila mahali. Kila mtandao ukaonyesha ile video. Ndipo sasa ikaanza kusambazwa ya kisa chote kuanzia Gabriel anatoka ofisini kwa mkewe mpaka mkewe kumkimbilia nje.

Wanandoa hao wacha Mungu, walioamka asubuhi hiyo kwenye jumba la kifahari, nakutoka hapo nyumbani na magari ya kifahari, siku hiyo iliisha tofauti. Gabriel alipelekwa chumba cha maiti wanakowekwa maiti zote. Waliokufa fukara na yeye tajiri akawekwa nao hapo hapo. Walio kufa kwa kuugua kwa muda mrefu, na yeye aliyekufa bila kutajaria, akiwa na mipango mingi hata ya siku hiyo, wote waliwekwa humo ndani wakisubiri safari yao ya mwisho hapa duniani.

Bethy naye alifikishwa kituo cha polisi akiwa anavuja damu, na maumivu makali mwili mzima kwa kipigo alichokipata kutoka kwa wananchi wenye hasira kali. “Amemuua mumewe kikatili sana!” Mmoja wa maaskari aliyekuwa anamvuta Bethy aliongea huku akimsogeza mapokezi. Wote walio wakuta pale mapokezi wakawageukia wao. “Wapi?” “Karibu na mitaa ya Posta ya zamani. Ni mke wa Gabriel.” “Haiwezekani!” “Amemuua Gabriel!!?” Askari mwingine akauliza kwa mshangao mkubwa sana.

“Amemuua bwana! Ameyatoa maisha ya yule kijana hivi hivi, mbele za watu!” Bethy alizidi kulia asijue kama ni hofu, au maumivu. Alikuwa akitetemeka kama amepigwa na baridi. Na yeye alisukumwa kikatili sana mpaka selo walipokuta watuhumiwa wengine.

Kwa Mchungaji!

W

akati mama Penny yupo sebuleni na mumewe, wote wametoka kwenye shuguli zao, msichana wa kazi akawafuata akiwa amestuka sana. “Mama Penny! Mama Penny! Nimesikia jina la anti Tunda kwenye hii video ya huyu dada aliyemuua mumewe.” “Nani kamuua nani na wewe!? Acha kunitia pressure bwana!” “Ona mwenyewe.” Akamkabidhi simu mama Penny. Baba Penny akahamia pale alipokuwa amekaa mkewe.

Alianza kuonyeshwa Bethy akimtukana mumewe. Alimtukana kwa kutaka kumuacha yeye ili amuoe Tunda. Likasikika jina la mama Cote, kumsaidia Bethy kufanya mpango wakumfunga Tunda kwa shutuma zinazomkabili akiwa amefanikiwa kukusanya ushahidi wote, ili yeye Gabriel atulie na familia.

Bethy alionekana kuendelea kutupa shutuma kwa marehemu mumewe, huku akiropoka mfululizo. Mara amtetee Tunda, amshutumu Gabriel. Mara ajitetee yeye, amshutumu mama Cote. Akaonekana na Gabriel na yeye akimtetea Tunda kwa mkewe na kumwambia yeye mwenyewe ndiye aliyevunja ndoa yao asimsingizie Tunda.

Mwishowe alionekana Gabriel akitaka kuondoka baada ya mkewe kumtukana zaidi na kumuonya asiende kumtoa Tunda rumande, Gabriel hakuonekana kujibu tena ila kuondoka ili kuepusha shari zaidi, Bethy akaonekana kuanza kumvuta nguo. Alifanya hivyo kama mara tatu nakufanikiwa kumuangusha. Akaonekana Gabriel akijigonga kwenye nguzo, kona ya urembo mpaka sakafuni akivuja damu nakupoteza maisha. Mwili wa Gabriel ulionekana umelala pale sakafuni, damu zilionekana kutapakaa chini ya kichwa chake.

Mama Penny akarusha ile simu. “Mungu wangu, Tunda!” Alisikika mama Penny akipiga yowe. Mikono kichwani. Ghafla akaanza kulia kama aliyefiwa. “Naomba utulie mama Penny. Hizi habari tumepata nusu, halafu hatujui kama ni Tunda tunayemfahamu.”

“Ni Tunda wetu, baba Penny. Umesahau habari za Gabriel? Alinisimulia Tunda kuwa amemgeuka Net kuwa amemchukulia mwanamke wake ambaye ni yeye. Na Gabriel alikuwa tayari kumuacha mkewe sababu ya Tunda. Nilikwambia hiyo habari niliyokuwa nimeambiwa na Tunda. Tena alikuja hapa amepooza sana. Ukawa unamtania lakini amenyamaza. Nilipomsindikiza kwenye gari yake ndipo akaniambi kuwa wamemgeuka Net. nakunisimulia kila kitu. Umesahau?” “Sasa hivi ndio nakumbuka. Mungu amsaidie yule mtoto. Sijui atakuwa amefungwa wapi!?” Tayari hali ya pale ikageuka majonzi.

“Kweli yule mama ameshindwa kabisa kumsamehe Tunda, mpaka amemfungulia mashitaka jamani!” “Tena akiwa amekwenda kutubu kanisani! Hakika Mungu hatamuacha.” Mchungaji akaongeza akionekana kuumia zaidi. Wasijue mkasa mzima uliompata Net ambaye yu taabani huko nchini kwao, na Tunda huko gerezani. “Sasa na Net yuko wapi?” “Inamaana wamemkamata leo huyo Tunda?” Yakawa maswali juu ya maswali yasiyo na majibu. Wakaanza kupiga simu ya Tunda na Net bila mafanikio.

Mama Penny na mumewe waanza kumsaka Tunda.

K

esho yake asubuhi kitu cha kwanza wakaenda kituo cha polisi cha pale pale Tabata kuulizia kama Tunda anaweza kuwa wapi. Wakawaambia polisi mara ya mwisho Tunda na mumewe walikuwa kwenye fungate. Wakaeleza kwa kifupi kuwa wao ni wachungaji na Tunda ni mshirika wao. Habari zile za mauaji yaliyotokea siku iliyopita walisikia Tunda kutajwa kuwa amefungwa.

“Lakini kwa jinsi ilivyo sasa, kwa kosa lolote wanaweza wakamnyima dhamana, kwa ajili ya usalama wake binafsi. Maana yeye anaonekana ni kama chanzo cha ugomvi.” “Ni wivu tu wa maswala ya mapenzi. Tunda hakuwa na mahusiano na Gabriel.” Wakajaribu kueleza bila kutoa mambo ya Tunda ya zamani.

Mchungaji alijieleza kiungwana sana mpaka wakamuelewa. Mmoja wa wale askari akawasaidia kupiga simu kwa rafiki yake, baada ya muda akapewa jibu kuwa Tunda atakuwa yupo gereza la Keko. Mchungaji na mkewe wakashukuru na kutoka pale kuelekea gereza la Keko.

Gerezani Keko.

Walifika pale, wakaandikisha majina. Wakakuta watu wengine wakizungumza na mahabusu wengine. Na wao wakakaa. Baada ya muda Tunda akatolewa. Alipowaona tu, akaanza kulia. Tunda alilia zaidi ya nusu saa. Alilia. Akalia bila kunyamaza. “Ni nini kilitokea Tunda?” Mchungaji akauliza, lakini Tunda alishindwa kujibu.

“Net yuko wapi?” Akaendelea kuuliza lakini Tunda alikuwa akilia na mkewe naye analia. “Mama Penny naomba nyamaza bwana ili tuweze kuzungumza na Tunda!” Wote wawili waliendelea kulia.

Baada ya muda, wakashangaa Tunda ananyanyuka na kurudi ndani bila kuongea chochote ila kulia tu. Alikuwa akilia kwa kwikwi huku amejifunika uso. Wakabaki pale mama Penny akilia na mumewe ametulia hajui chakusema tena. Walikaa pale wakisubiria labda Tunda angerudi, lakini hakurudi mpaka muda ulipoisha na kutakiwa waondoke. Mchungaji akamnyanyua mkewe, wakaondoka.

Mama yake Gabriel Naye.

Siku hiyo kabla yakuisha tena, kukazuka habari yakuhuzunisha zaidi. Mama yake Gabriel afariki kwa mshtuko. Habari zilieleza kuwa baada ya mama huyo kupata habari kuwa mtoto wake amekufa, hapohapo alianguka na kupoteza fahamu kwa mshtuko.

Alikimbizwa hospitalini. Juhudi za kuokoa maisha yake hazikufanikiwa. Yule mama hakuzinduka mpaka saa kumi alfajiri siku inayofuata, mashine zilipoonyesha amefariki. Familia hiyo ilikuwa na msiba mzito ulioinua simanzi kwa wengi. Mama na mtoto wake! Tena ni Gabriel kipenzi cha wengi!

Gerezani.

Tunda aeleza Yote na kuweka kikomo.

K

esho yake wakarudi tena mahabusu kumuona Tunda. Lakini safari hii walifika na mama yake Tunda. Wakajiandikisha kama jana yake, wakakaa wakisubiri Tunda aitwe, wakijua labda siku ile atakuwa ametulia. Lakini alirudi yuleyule askari aliyekwenda kumwita na barua mkononi.

‘Mama Penny na mchungaji, nawashukuru sana kuwa na mimi kwa miaka yote hiyo. Mlinipa familia ambayo sikuwahi kuwa nayo. Nakushukuru mama Penny, kufanyika dada ambaye sikuwahi kuwa naye wala kudhani nastahili kuwa na dada wa aina yako. Lakini nawaomba kwa sasa msinifuate tena hapa. Msije hapa. Haya ni mapito yangu binafsi, ambayo siwezi kuruhusu na nyinyi kuingia doa.’

‘Sasa hivi ninasakwa na watu wengi ili tu kumfahamu Tunda waliyemsikia kwenye ugomvi wa marehemu Gabriel na mkewe. Sitaki nyinyi niliowakuta na sifa nzuri, tena mnamajukumu ya roho nyingi za watu wanao wahitaji, kupotea au kuangamia na mimi mtu mmoja tu! Hapana. Tafadhali naomba msifike tena hapa, ila mniombee tu.’ Tunda akaendelea kuandika.

‘Siku ile baada ya kuagana pale kwenye harusi yangu na Net, tulikwenda Resort, kama alivyowaambia Net. Siku ya jumapili asubuhi, tuligongewa na askari polisi, walituamuru tutoke pale twende kituo cha polisi. Tulipokuwa tukipakizwa kwenye gari la hao polisi, nje ya ile resort, alikuja mama Cote. Alitusomea mashitaka yetu. Naomba niwaeleze makosa ya kwangu tu. Na ninafanya hivi kwenu kwa ule umbali mliofika na mimi kwenye maisha yangu.’ Mchungaji aliendelea kusoma kwa sauti ya kusikika kwa wao watatu tu.

‘Nimeshitakiwa kwa makosa matatu. La kwanza ni kumuoa Net. Mama Cote amenishitaki akidai ni moja ya njia ninazotumia kumrubuni Net ili kumvuta upande wangu, kwa sababu ambazo alizitaja. Ameita au amenishitaki kwa kosa la kuendeleza biashara ya ngono. Kwa bahati mbaya sana, yule mwanasheria tuliyemuamini kutukamilishia makaratasi yetu, ili kukamilisha taratibu zote kabla ya ndoa, aidha kwa kutokujua au kwa makusudi, hakukamilisha taratibu kama ilivyotakiwa.’

‘Kwa kifupi, mama Cote alituambia ndoa yetu haitambuliki kisheria hapa nchini, kwa hiyo nayo ni ushahidi kuwa mimi nimetengeneza uongo, ili kuolewa na Net, ambaye siye raia wa nchini Tanzania. Anao ushahidi mwingi tu, na kwa kuwa anaonekana ameweza kumfikia yule mwanasheria tuliyemlipa atusaidie maswala yote ya ndoa, amesema huyo mwanasheria atatoa ushahidi, utakaonishitaki mimi kuwa ni kama nilikiuka sheria ya ndoa za kimataifa, nakudanganya ili kuweza kuolewa na Net, kujirahisishia njia yakutumia au kumiliki mali ya kampuni yake. Kwa vipi au ni ushahidi gani watatoa siku hiyo ya mahakamani, sielewi. Ila wanaonekana wamejipanga vizuri.’ Mchungaji akaendelea kusoma.

“Kosa la pili ambalo ni kweli nililifanya kwa hiari yangu nikitaka kumsaidia Net, ni juu ya ile nyumba yake ambayo ilikuwa kwa jina la kampuni ya yule mama. Nakumbuka mama Penny na mchungaji mlituonya sana, lakini Net alituambia ni jasho lake asingependa lipotee. Mimi nikakubali kununua kwa pesa ambazo alinipa Net mwenyewe.’

          ‘Mama Cote anadai ile nyumba ni yake. Hata hati ya nyumba ambayo Net alikuwa tayari ameshajaza fomu huko wizara za aridhi, kubadilisha jina iwe kwa jina langu, ilikuwa kwa jina la kampuni ya yule mama. Na mbaya zaidi anao ushahidi wa makaratasi yote ambayo Net alijaza habari zangu zote akiwa ananiuliza maswali huku anajaza hizo karatasi za kununua nyumba, na kubadili hati ya nyumba. Na mwishoni mimi niliweka saini kote. Net kama mfanyakazi tu wa ile kampuni, kisheria haruhusiwi kuniuzia mali ya kampuni bila idhini ya mmiliki wa kampuni ambaye ni mama Cote.

‘Sasa mama Cote amenishitaki kwa kosa la kutumia rushwa ya ngono, kumrubuni mfanyakazi wake wakigeni, asiyejua sheria za aridhi hapa nchini. Si mume tena, kwakuwa ameshatusainisha talaka, hiyo nayo ni habari ingine. Anataka kuhakikisha hiyo ndoa haitambuliki wala haina ushahidi popote kule, hataki ijulikane hata kama ilisha wahi kutokea. Ametupokonya kila kitu mpaka pete za ndoa.’

‘Turudi kwenye kosa la nyumba. Kwa hiyo amenishitaki kwa kutoa rushwa ya ngono au kuuza ngono ili kupewa nyumba ya kampuni yake. Ukiangalia ni atashinda tu. Maana ni wapi nyumba inauzwa kwa milioni tatu!? Hakuna inapoonyesha kama Net ndio mmiliki. Na kisheria, Net haruhusiwi kumiliki mali yeyote hapa nchini kwa kuwa sio mzawa. Basi, kweli makosa ni yangu.’ “Mungu wangu huyu mama!” Alisikika mama Penny aliyekuwa akilia.

“Sijui kwa nini hili jambo lilikuwa likinisumbua sana! Hata baada ya Net kulazimishia siku ile, unakumbuka usiku wake nilikuamsha na kukwambia hili jambo ni la kuombea?” “Nakumbuka baba Penny! Lakini Tunda alifanya kwa mapenzi, kumridhisha Net.” Mama Penny akajibu akimtetea Tunda.

“Hebu tumalizeni kwanza hii barua, ndipo tujadili.” Akamalizia mama Tom, au mama yake Tunda. Wakaamua kuendelea. Mchungaji anasoma, mama Penny na Mama Tom wanasikiliza.

‘Kosa la tatu au la mwisho kwa hapa, ni biashara hiyo ya ngono sasa. Mama Cote kwa kushirikiana na Bethy, wanaonekana wamelipa mtu aliyeweza kuingia kwenye simu zangu za zamani. Ameweza kuprinti au kutoa mawasiliano yangu yooote yazamani. Malipo niliyokuwa nikipokea kwa kutumia mtandao na jumbe zangu zote kama ushahidi wa kunishitaki juu ya biashara ya ngono.’  “Huyu mama amemkosea Mungu kwa hakika! Ametumia ukiri wa madhabahuni kwa Mungu kumuangamiza Tunda! Hakika Mungu hatawaacha.” Alisikika mama Penny.

‘Kwa kumalizia kisa kizima, alituambia ili mambo yaishe, nilazima kusaini karatasi za talaka. Na niandike kuwa naachana na Net, nikiwa sitaki kitu chochote kutoka kwake. Na karatasi nyingine aliyokuwa ameonyesha kuwa ile nyumba inarudi kwake au kampuni yake yeye mama Cote. Ilinibidi mimi kufanya kama alivyotaka. Tulikuwa kwenye hali mbaya, sina jinsi nikasimulia mtu akaelewa. Tulitolewa kwenye usingizi. Tukatolewa pale chumbani na pingu huku tukisindikizwa na askari wanne!’ “Mama anadhambi huyu!” Alisikika mama Penny tena huku akifuta machozi.

‘Basi, baada yakufanya yote aliyoyataka, tukijua tupo huru, mimi nilitolewa kwenye gari moja na polisi nakuhamishiwa kwenye gari nyingine. Net akiwa analia sana, nilimsikia akimuuliza mama yake, kwa nini wananichukua tena wakati nilifanya kila alichotaka! Nilichosikia yule mama akijibu, alisema kuwa, yeye alikuwa pale kwa ajili ya mali zake, amezipata. Maswala ya biashara haramu ya ngono, ni mimi kupambana na sheria ya Tanzania. Hausiki tena. Basi, niliondoka pale, nakumuacha Net na mama yake. Mimi nikapelekwa kituo cha polisi Kawe.”

 

‘Lakini chakushangaza,  nilipofikishwa kituoni, nilisomewa mashitaka yote kama yalivyo, halikuachwa hata moja.

1.      Kumrubuni raia wa kigeni, kwa kumuwezesha kuishi hapa Tanzania, kwa kumwingiza kwenye   ndoa feki ili kujinufaisha na mali zake na za mama yake.

2.      Wizi. Hapa habari ikabadilishwa tena. Ikaonekana niliiba hiyo hati ya nyumba kutoka kwa kijana wake. Na kuibadili hiyo hati ya nyumba kutoka kwa kampuni ya Cote, iwe kwa jina langu mimi. Na mwisho kabisa,

3.      Biashara ya ngono.

Kwa hiyo ndiyo hayo makosa matatu yanayonikabili kwa sasa.’

“Kama ulivyosema mama Penny. Huyu mama anacheza pabaya sana. Hajui vita yake haikuwa juu yake na Tunda, bali na Mungu. Mungu atamchapa mama Cote, mpaka atajua kuwa Mungu anamuadhibu. Yeye mama anayejua nguvu ya msamaha, kusamehewa dhambi, na kutakaswa, leo anatumia siri za madhabahuni kumuhukumu Tunda! Hakika Mungu hatamuacha.” Alisikika mchungaji akiongea kwa kuumia sana. “Mimi ndio sielewi kabisa. Itabidi tukitoka hapa mkanielezee kila kitu.” Alikuwa mama Tom. Mchungaji akaendelea kusoma kwa sauti ya juu kiasi.

‘Jamani, hayo makosa yote, nilifanya. Iwe kwa kutokujua au kujua, niliyafanya. Wameyatengenezea mkasa mkubwa sana, ambao waliniambia siwezi kupewa dhamana. Nimekaa hapa muda wote huo, nikimlilia Mungu mliyeniambia amenisamehe, basi anitetee hata mbele za watu. Nimetubu kwa machozi, nimekosa. Nimepoteza kila kitu. Nipo hapa peke yangu, lakini najua Mungu hataniacha. Sijui kilichoendelea kwa Net na mama yake. Ila kwa kifupi, Net si mume wangu tena. Yule mama alihakikisha nasaini talaka, na kujitenga na mali zao na kunipokonya pete zote mpaka ya uchumba.’ “Jamani Tunda wangu!” Alisikika tena mama Penny.

‘Najua mngetamani kunisaidia. Lakini sidhani kama mtaweza. Naomba msaada wa maombi tu. Ili hiyo siku nitakapoitwa mahakamani, basi, yeye mwenyewe Mungu, akajidhihirishe huko. Mimi sijui hata pakuanzia kujitetea, kwa kuwa nilikosa. Kuna ushauri walinipa hawa askari wa hapa, kwa sasa nitulie tu hapa ndani. Kifo cha Gabriel kimeshtua watu wengi sana. Mimi wamenionyesha wao wenyewe, wakanishauri vizuri tu. Kuwa kwa sasa, hapa nilipo nisehemu sahihi hata kwa usalama wangu.’

‘Japo ni kama wananipa moyo kuwa, Gabriel alifanyika mtetezi wangu. Kabla ya kifo chake, kwenye ile video, anaonekana alikufa akinitetea. Lakini, wameniambia, Bethy anao ndugu na wazazi. Siwezi kujua wao watachukuliaje hilo. Bethy anaonekana amesababisha kifo cha mumewe, akiwa anamzuia asinitoe mimi huku jela. Haya, na hiki kifo cha mama yake Gabriel naye! Imekua balaa juu ya balaa na ilionekana sababu au chanzo ni mimi. Bethy akipigania ndoa yake. Wapo ambao watakuwa na hasira na mimi tu. Ni heri nitulie hapa kwanza. Sina jinsi ila kutulia. Maana hilo nalo limekuwa tatizo la nne. Ni kama nimesabisha kifo cha Gabriel ambacho kimepelekea kifo cha mama yake pia.’ Kilisikika kilio cha mama Penny.

Baba Penny akaendelea. ‘Tafadhali nawasihi sana, najua mnao na watawajia kina Tunda wengi sana kwenye maisha yenu, msiharibu huduma yenu kwa ajili yangu. Kama mnamwamini Mungu, naombeni mkae mbali na hapa, mpisheni Mungu afanye kwa namna yake. Sitaki chochote au ushiriki wenu kwangu na Net, ujulikane kwenye vyombo vya sheria au hata mitandaoni. Ninachomshukuru Mungu, ni kama nilimsikia mama Cote akisema aliwahi video zote na picha zote za harusi. Anavyo yeye. Kwa hiyo naamini mtakuwa salama kwa muda, mpaka mambo yakae sawa. Na ukweli utambulike.’ “Tunda anasahau yeye kwetu sio mshirika tu. Ni ndugu sasa.” Aliongeza baba Penny akiwa na majonzi.

“Hata hivyo, ni mchungaji gani anayechunga kondoo asichafuke? Sisi tunachunga wenye dhambi. Ndio wito aliotuitia Mungu. Kuwasogeza wenye dhambi karibu na Mungu. Hatuna chakujificha kwa yeyote.” Aliongeza mchungaji. Mama Tom akabaki akiwashangaa wanavyotaka kujiingiza kwenye lawama!

‘Mama Penny, najua nimeacha gari yangu kwako na vitu vyangu vyote nyumbani kwenu. Nakusihi sana, uendelee kufuatilia kesi ya baba yangu. Lipo tumaini la kutoka kwake jela. Nilibakisha malipo kidogo kwa yule wakili wake. Naomba uwasiliane na huyo wakili, tumia pesa yangu umlipe hicho kiasi atakachokwambia. Mwambie kisibadilike kitu. Hakikisha baba anatoka jela. Tafadhali dada yangu. Sitaki baba yangu aje afie jela.’

‘Siku ya kumtizama, naomba ukamwangalie ujue anaendeleaje. Walimtoa hospitalini, sijui atakuwa amepona au bado, nilimuacha bado mwili hauna nguvu. Naomba umfuatilie mpaka atoke. Akitoka, naomba umtunze kidogo mpaka apate nguvu. Najua nakupa mzigo mzito, lakini nakusihi dada yangu, nisaidie. Hana pakwenda. Nilipanga akitoka, apumzike kidogo, arudishe nguvu na mawazo, ndipo umpe mtaji. Zungumza naye ili kujua nini anataka kufanya. Mtolee pesa kwenye akaunti yangu ya akiba, mpe, mtafutie chumba, mlipie kodi hata ya miezi sita tu, aanze maisha. Naamini hata mwezi ujao, atatoka jela kama si mapema na hapo.’ Mama Tom akawa amechanganyikiwa zaidi.

“Kwani Yohana alifungwa na yeye!?” Akauliza mama Tom, wote wakamgeukia. “Mimi sikuwa nawasiliana naye kabisa. Hata habari zake sikuwa nazo tena. Alishanikera yeye na yule mkewe mwenye roho kama ya shetani! Mkewe alimpiga Tunda karibu ya kumuua, na yeye Yohana alikuwa akiishi humo humo ndani! Nikamuona ni mpuuzi anayetawaliwa na mkewe, sikutaka hata kumsikia tena.” Akajitete mama Tom, nakumuudhi zaidi mama Penny.

“Sasa anatofauti gani na wewe uliyemuacha Tunda akibakwa kila siku na mumeo, na wewe ulikuwa ukiishi humohumo ndani? Huogopi kusema! Kwanza wewe ndiye uliyemsababishia Tunda matatizo yote haya. Mama gani unashindwa kujua kama mtoto wako wa kike anabakwa! Upuuzi gani huo!?” “Majukumu mama Penny.” Akajaribu kujitetea nakuharibu zaidi.

“Acha kujitetea ujinga! Umenunua ulimwengu sasa hivi? Mbona wenzako tunafanya kazi na tunalea? Watoto wako wakike wote wawili walikuwa wanabakwa na mumeo humohumo ndani halafu unajitetea ujinga! Msichana wako wa kazi karibia auwawe kwa kubakwa na mwanaume huyohuyo na wewe upo nyumba hiyo hiyo halafu sasa hivi unaongea nini? Nitakupiga mimi sasa hivi hapa.” Mama Penny alikuwa amekasirika anatetemeka karibu amrukie.

“Mama Penny naomba utulie.” Mumewe akamtuliza. “Huyu ndio chanzo cha yote haya! Amemsababishia Tunda matatizo ambayo hawezi kumsaidia. Wewe mtoto wa kwanza umejua alikuwa akibakwa. Halafu..” “Sikuwa najua mama Penny. Naomba usinilaumu. Mimi nilichojua ni kuwa Tunda alianzisha mahusiano na...” “Nitakupiga mama Tom acha kujitetea ujinga wewe!”

“Wewe mtoto wako wa kike unaishi naye humo humo ndani, hujui chochote kwenye maisha yake, mpaka unakuja kumgundua mjamzito! Kana kwamba haitoshi, umempeleka hospitalini kwa nguvu, wewe na manesi wenzako sijui daktari mkamchoma sindano. Unapata habari kutoka kwake akiwa na madawa ya usingizi! Ulivyo mshezi wewe, ukamtoa mimba mtoto wako wakumzaa wewe mwenyewe kwenye starehe zako. Ukamtelekeza hospitalini anavuja damu, halafu wewe ukaanza kupita kwenye majumba ya watu unamuharibia mwanao sifa!” Kimya.

“Ulifikiria au ulitegemea aende wapi kama sio kufanya biashara ya elimu ya ngono aliyomfundisha mumeo tangia yupo mtoto mdogo? Ameanza kumbaka Tunda tokea hajavunja ungo mpaka amevunja ungo, anamlala binti yako na wewe upo palepale, mshenzi wewe. Halafu bila huruma ukamtupa!”

“Usimfukuze mumeo, ukamfukuza mtoto mdogo! Kana kwamba haitoshi, mwanaume huyohuyo ukamuachia mtoto wa watu uliyemtoa kijiji. Kambaka mpaka kutaka kumuua. Mpumbavu wewe, mshenzi usie na akili, unamrudisha yule mtoto kijijini kwao kashageuzwa tahira na mumeo, ukaona mkabidhi mumeo mtoto mwingine wa kike awe anamchezea wakati wewe unazungusha kiuno kutafuta pesa.”

“Kamchezea mtoto mpaka kampa gonorea, mtoto ananuka ndio mama unashtuka, mshenzi wewe. Huna aibu umekuja hapa kumsanifu Tunda! Na unaonekana kama sio kufukuzwa na ndugu za mume, usinge..” “Mama Penny! Mama Penny! Naomba tulia kidogo. Tulia mama. Huko unakokwenda utashindwa kurudi. Tafadhali tulia.” Mumewe akamsihi.

“Nimemuomba Tunda msamaha. Na ameniambia amenisamehe.” “Basi msubiri huyohuyo Tunda atoke jela ili akusaidie. Nisiione sura yako nyumbani kwangu. Nishakuelekeza kupamba, Tunda ameshakutafutia chumba. Amekupa vitu vyake vyote vya ndani na pesa ya mtaji, nenda kaanze maisha. Na usipobadilika na yule mwanao wa kiume watamlawiti wakati unahangaika kutafuta pesa.” Mama Penny akaendelea.

“Na kama ulivyosikia, Tunda yupo Tanzania. Haondoki tena, ipo siku atatoka tu jela. Nakuja kuchukua vitu vyake vyote vyabiashara, namtunzia. Akitoka, anaendelea na biashara yake. Ushamuharibia maisha yake, sitaki aje atoke jela aanze maisha upya. Na ile ofisi pia sio yako. Kwa kuwa amelipia kodi ya mwaka, naenda kumtafuta mteja mwingine, napakodisha, pesa namuwekea benki. Yaani unapotoka hapa, ujue upo kivyako. Nisiione sura yako tena. Haya kwenda.” Mama Penny alijisahau yupo gerezani. Watu wote wanawasikiliza.

“Unajidai ulimuomba Tunda msamaha baada ya Tunda kufanikiwa na kuwafuata yeye mwenyewe! Mbona wakati anashida hukumtafuta umuombe msamaha? Alihangaika kufanya kazi usiku kucha na mchana, akitafuta pesa kukutunza wewe uliyeharibu maisha yake! Baba ambaye hata hakuwa akimfahamu ndiye aliyemsaidia, tena wewe ukiwa unamkataza baba yake na wanao mzunguka wasimsaidie Tunda, leo unamtukana baba yake! Mjinga kabisa. Sasa nikuone karibu na vitu vya Tunda. Na mimi nitakufungulia mashitaka wewe kwa kumtoa mimba Tunda. Uliua kiumbe cha Mungu. Toka kabla sijaanzisha kesi nyingine mimi.” Askari magereza akawasogelea. Walianza taratibu, lakini baadaye mama Penny akashindwa kujizuia. Wakatolewa wote nje.

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

Mambo yanazidi kuwa mambo. Jambo juu ya jambo.

Njama zakumuangamiza Tunda zimeishia tofauti. Lengo ilikuwa awapishe mtaani. Lakini imeisha tofauti. Kaburi walilomchimbia Tunda nani analia sasa hivi?

      Msiba mzito kwa kina Gabriel.

      Bethy ameishia mikononi mwa polisi kwa kosa la kumuua mumewe kikatili.

      Kifo cha Gabriel kimesababisha kifo cha mama yake.

      Mama Cote amekimbia. Hapatikaniki.

      Tunda yupo jela kwa makosa matatu yenye ushahidi.

      Hakuna anayejua kama Net yupo mahututi hospitalini. Na hata wauguzi wameshindwa kumtambua.

      Ndoa iliyofungwa kama kwa siri hivi na mchungaji akiwa msitari wa mbele pamoja na familia yake, haitambuliki kisheria. Mama Cote anao ushahidi akitaka kufuta kabisa hiyo ndoa isijulikane wala kutambulika kisheria. Itakuaje kwa watu wakijua ushiriki wa mchungaji kwenye aina hiyo ya ndoa yenye tuhuma nzito?

      Safari hii Tunda anatoka vipi? Net? Mama Cote je? Kanisa wanalochunga baba Penny na mkewe! Bibi Cote naye? Endelea kusoma...

CONVERSATION

0 Comments:

Post a Comment