Naomi Simulizi |+1 205 767 8163 |naomisimulizi@gmail.com NILIPOTEA! - SEHEMU YA 34. - Naomi Simulizi

NILIPOTEA! - SEHEMU YA 34.

                                             Kwa Net.

S

iku ya tano, Net aliweza kuanza kupata nafuu hata kufungua macho. Daktari aliyekuwa akimuhudumia swali lake la kwanza alimuuliza jina lake. “Net.” Akajibu akijaribu kuangalia alipo. “Unajua upo wapi?” Net akajaribu kuvuta kumbukumbu. Akabaki kimya kwa muda. Akili ikamrudia. “Tunda!” Akahamaki. “Hapana. Upo hospitalini.” Yule dakttari mwanamke akajaribu kumsahihisha akidhani anaweweseka.

“Hapana. Naitwa Nathaniel Cote.” Kila mtu akashtuka sasa na kujaribu kumtizama vizuri. Hawakutegemea kama Nathaniel Cote wanaomjua wao, awepo hospitalini kwa muda wote huo bila ndugu au hata kama amepotea, basi isiwepo ni habari inayojulikana kila mahali!

“Oooh my God! Ni Nathaniel Cote!” Nesi aliyekuwa kwenye chumba hicho pamoja na wauguzi wengine akaongea kwa sauti wote wakamgeukia yeye. Kilikuwa kikundi cha madaktari waliofudhu na ambao wapo mafunzoni, wote walikuwa hapo chumbani kwa Net, wanazungukia wagonjwa mida hiyo ya asubuhi kwa mafunzo pia kwa madaktari waliopo mafunzoni pia.

“Ni nani!?” Mmoja akamuuliza yule nesi aliyehamaki. Kama anayetaka kuuliza kuwa inatakiwa kumfahamu! Na yule nesi naye akawa kama anawashangaa ni kwa jinsi gani wanashindwa kumfahamu Nathaniel Cote. “Cote, Nathaniel Cote!?” Yule nesi naye akawauliza huku akiwatolea macho kushangaa. “Ooooh! Cote.” Mwingine naye akawa kama amekumbuka. Ukaanza mnong’ono pale wao kwa wao wakielezeana juu ya familia hiyo ya Cote, nakumsahau hata mgonjwa mwenyewe.

Cote walikuwa maarufu sana kwenye huo mji. Kampuni ya Cote hapo nchini Canada, ilikuwa ni kampuni kubwa sana ya usafirishaji. Ilikuwa ikisambaza mizigo ndani na nje ya nchi ya Canada. Walikuwa wakiingiza mamilioni ya pesa kwa mwaka. Bado umaarufu wa bibi yake ambao ulijulikana kimataifa. Kwa hiyo walifahamika sana.

Net akawa anahangaika kuongea, wao wanaelezana juu ya Cote. Akatoa kile kitu alichokuwa amefunikwa nacho mdomoni na puani kwa ajili ya kupata oxygen zaidi. Akavuta na mipira iliyokuwa imebandikwa kifuani na kidoleni vyote akang’oa. Kelele zilizoanza kusikika kwenye mashine, zikawarudisha mawazo kwa mgonjwa. Wote wakamgeukia kwa mshtuko wakidhani mashine zinawajulisha amezidiwa au kuna tatizo, kumbe Net alichomoa.

Alipoona wanamwangalia ndipo Net akawauliza, “Sasa hivi ni saa ngapi?”  Akitaka kujua kwa muda ule bibi yake yuko wapi! Nyumbani au kazini. Alipotajiwa muda, akaomba apigiwe simu bibi yake ofisini. Hapo hapo simu ikapigwa. Akapokea sekretari wa bibi yake akawaambia bibi huyo alisafiri safari ya kikazi lakini anarudi nchini hapo siku hiyo jioni. Ndipo akapewa taarifa za kuwepo Net hospitalini hapo.

Akapewa azungumze naye Net mwenyewe. Kwa mshtuko asitarajie kumsikia Net hospitalini, akapokea. “Nana yuko wapi?” Net akamuuliza hivyo ndipo akaamini ni Net. Akamweleza kuwa bibi yao ni kweli yupo safarini ila anarudi siku hiyo na dereva anajiandaa kwenda kuwapokea yeye na Maya uwanja wa ndege. Net akamuomba yule sekretari amwambie dereva anapomtoa bibi yake uwanja wa ndege, ampeleke pale hospitalini. “Do you need anything, Net?” Mdada huyo wa kiCanada, akiwa kwenye mshtuko akamuuliza Net, ambaye alishawahi kufanya naye kazi pia kama anahitaji kitu chochote kwa wakati ule. “No thanks, Claire.” Net akakata simu na kumrudishia simu yule muuguzi.

Mambo yakabadilika sasa. Hata aina ya matibabu yakabadilika. Habari zikaenea pale hospitalini kote, kuwa yule mgonjwa aliyekuwa amepoteza fahamu, yupo kama kwenye koma, aliyeokotwa kwenye baridi ni Nathaniel Cote. Uangalifu ukaongezeka. Akaanza kuangaliwa kwa jicho la pili wakijua ni habari kubwa. Lolote likitokea kwa kijana huyo itajulikana kila mahali ni uzembe wa hospitali hiyo.

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

Akiwa amepotelea usingizini kabisa. Akasikia mtu akimbusu kwa kurudia rudia. Harufu ya bibi yake ikaanza kuenea pale. Bila kufungua macho Net akaanza kulia. Alilia kwa muda. Maya akamnyanyua mkono na kubusu kiganja chake. “Dokta amesema unaendelea vizuri. Pole baby boy.” “Nipo kwenye matatizo makubwa sana Nana, kuliko hivi unavyoniona hapa.” Bibi yake alikua kwenye mshangao. Net alitakiwa awe kwenye fungate na Tunda, nchini Tanzania. Anashangaa kumkuta Net, aliyemuacha nchini Tanzania, yupo nchini Canada tena hospitalini!

“Nini kinaendelea!?” Wakajikuta Maya na bibi yake wakiuliza kwa pamoja. “Mama!” Net aliwaeleza kuanzia mwanzo, mpaka kufika hapo. “She went too far this time. I will never forgive her for this.” Alisikika bibi Cote akiwa amekasirishwa na umbali aliokwenda Ritha safari hiyo kwenye hilo.

“Angefanya chochote kile, au angenifanyia mimi kitu chochote kile, lakini asingekuingilia kwenye maamuzi yako yakuoa! Hata babu yako alikupa baraka zake kwa Tunda!” “Mimi niliwaambia yule mwanamke ni shetani mkasem…” “Usiseme hivyo Maya.” Akamkatisha kwa kumkataza mjukuu wake.

“Sasa wewe bibi unamtetea nini? Hujasikia alichokifanya?” “Haijalishi amefanya nini, lakini huruhusiwi kumsema vibaya mama yako.” “Kwa nini wewe unaruhusiwa kumse…” “Mimi sio mama yangu. Alikuwa mkwe wangu. Na nilimuheshimu kwa kuwa amenipa nyinyi lakini katika hili, atapambana na hasira zangu. Lakini kwa sasa hivi, naomba wote tutulie, mpaka Net apone. Ndipo tuanze kufikiria kitu chakufanya bila kujibu chochote kwenye vyombo vya habari. Nimeweka ulinzi hapo nje, haruhusiwi mtu yeyote kuingia kama sio muuguzi wa hapa. Na nimeomba muuguzi yeyote wa hapa, asiingie humu ndani na simu. Sitaki picha za Net akiwa hospitalini zizagae mitandaoni na wewe Maya usipost chochote mtandaoni. Tulia tu Net.” Bibi Cote alitoa muongozo.

“Amemfunga mke wangu, Nana! Nawezaje kutulia?” “Unakumbuka ni nini alikwambia babu yako kwa kurudia rudia mpaka akiwa hospitalini?” Akamuuliza Net. “Nikiingia kwenye matatizo, kabla sijachukua hatua, au kupanic, natakiwa kufikiria.” “Okay. So, relax. Huu ndio uwe muda wakujipanga. Ametengeneza kesi yake vizuri sana. Lazima na sisi tujue jinsi yakufanya.” Bibi yake akaendelea kumtuliza huku akimbusu.

“Lakini namuhurumia sana Tunda, Nana! Mimi ndiye nimemuingiza katika shida yote hii. Mimi ndiye nilimtia moyo na kumwambia ni sawa kuongea chochote pale kanisani. Kitu ambacho nikifikiria sasa hivi, sioni kama kulikuwa na ulazima huo, Nana!” Net akaanza kujutia.

“Nisikilize Net. Wakati Tunda anatubu pale kanisani mbele ya wachungaji na wale wote, alikuwa akitubu kwa Mungu. Wote mlisimama pale kama wawakilishi wa Mungu. Balozi wa nchi ya Canada, anapokuwa Tanzania, hakuna anayemtambua yeye kwa jina lake, ila kama Canada. Yupo pale akiwakilisha Canada. Na ndio maana unapoingia kwenye ubalozi wowote ule, hata kama ipo nchi ya ugenini, unakuwa umekanyaga ile nchi. Inamaana, kama ni ubalozi wa Canada nchini Tanzania, ukiingia ndani ya geti la ubalozi wa Canada haupo tena nchini Tanzania, unakuwa upo nchini Canada. Wanapokosea wafanyakazi wa ubalozi wa Canada wakiwa nchini Tanzania, wanahukumiwa kwa sheria ya Canada, sio Tanzania. Unanielewa?” Bibi Cote akamuuliza Net aliyekuwa akilia kwa kuugua.

Net akatingisha kichwa. “Kwa hiyo ndivyo ilivyo kwa Kanisa. Wanawakilisha ufamle wa mbingu na wale ni watenda kazi wa ufalme wa Mungu. Ndio maana wanaitwa, watumishi wa Mungu. Tunda alikiri kwa Mungu kupitia wao. Hakukosea hata kidogo. Na ndio maana Mungu alimsamehe Tunda. Waliyoyakosea wale watumishi wa Mungu, Mungu atashugulika nao. Waache kabisa. Watahukumiwa kwa sheria za Mungu.” Yule bibi akaendelea taratibu tu.

“Ila ni kweli namuhurumia mama yako, na wale wote wanao mzunguka na kumsaidia kumuangamiza Tunda. Tunda ni jukumu la Mungu kwa asilimia 100, kuliko hata unavyoweza kufikiria wewe Net. Tufanye kwa upande wetu, lakini nakuhakikishia, Mungu atampigania Tunda. Usiogope, na tusiache kumuombea kokote alipo, Mungu akumbuke msamaha aliompa, na akajidhihirishe.” Net alivuta pumzi kwa nguvu. Akafunga macho nakupitiwa na usingizi asijue Tunda anahukumiwa na makosa mengine zaidi ambayo ni yeye ameyasababisha.

Mama yake alimwambia hatamshitaki kwa yale mawili ila la ngono lipo nje ya uwezo wake, anaachia sheria ya Tanzania, kwa sababu amesaini karatasi za talaka na amekubali kuachana na Net, kumbe uongo. Net alipoondoka, Tunda akafikishwa kituoni na kushitakiwa kwa makosa yote, vilevile. Hapo alipolala Net, anajua kosa linalomkabili Tunda ni moja tu, kumbe amemuacha kwenye matatizo makubwa sana.

Hiyo ilikuwa siku yake ya tano tokea atoke nchini Tanzania, na Tunda akiwa jela. Alilazwa hapo akiwa kwenye matibabu makali huku akimfikiria Tunda. Mengi yalikuwa yakiendelea kichwani. Kumuhurumia Tunda ambaye ni kama alipokonywa tonge mdomoni. Katikati ya penzi zito la fungate. Wakiwa ndio wanaamka siku ya pili tu! Hawakuwa hata nusu ya hayo mapumziko yao waliyokuwa wakiyasubiri wote kwa hamu. Ni kama aliyeazimwa tu huyo Tunda, kabla hajamfaidi, akapokonywa!

Mbaya zaidi, Tunda analiliwa na Gabriel wanayefahamiana na kushibana vilivyo. Hata kama Tunda alikuwa kwenye biashara, lazima kulikuwa na hisia. Ziwe za mapenzi au za urafiki tu, hawa watu wawili wote wakiwa kwenye shida, wakakutananishwa, Net alihofia hapatachukua muda mrefu kuweka penzi la uhakika si kama lake lenye vipingamizi vingi na vigumu.

Ilikuwa lazima atoke pale hospitalini na kuhakikisha yeye ndio anayemtoa Tunda jela wala si Gabriel. Alijawa hofu na wasiwasi uliokuwa hauwezi kuvumilika. Alishaonja penzi la Tunda, akataka kujenga mzinga kabisa. Na hivi ndoa yenyewe aliambiwa haipo tena, basi anatofauti gani na Gabriel ambaye alishakuwa na mahusino ya muda mrefu na mazuri yasiyo na kipingamizi na Tunda?

Akiwa pale kitandani hospitalini, Net aliendelea kukumbuka mazungumzo yake na Tunda juu ya Gabriel. Hayakuwa mahusiano ya kawaida. Kwa hakika walishibana vilivyo na walikuwa na wakati mzuri. Gabriel alijifunua kwa uwazi kwa Tunda si kama yeye ambaye hata Tunda hakuwa akimfahamu kwa undani. “Ni kweli siwezi kujilinganisha na Gabriel hata kidogo. Mwenzangu amenipita mbali sana.” Akazidi kujikatisha tamaa.

“Gabriel akifanikiwa tu kumtoa Tunda jela, mimi ndio basi tena. Nitabaki kuandika historia yakuwa na ndoa ya masaa tu.” Net alizidi kukosa raha nakutamani kutoka pale hospitalini kwa haraka.

Lakini alisisitizwa kuwa mvumilivu mpaka amalize matibabu ili asije kupata matatizo yakudumu na bibi yake aliendelea kumsisitiza awe mtulivu, ajipange vizuri ili kusiwe na kushindwa tena. Net alikuwa akipewa matibabu ya hali ya juu, na uangalizi wa namna yake, mpaka akapona. Bibi yao ndiye aliyekuwa akimuhudumia bila kuchoka akiwa na Maya.

Alilazwa hapo kwa siku 9. Bibi yake akihakikisha hapotezi mwanaume mwingine kwenye hiyo familia. Akifuatilia kwa karibu, hatua kwa hatu, ili Cote huyo aliyebaki hapa duniani apone. Net ndiye kijana wa pekee aliyebaki. Hakutaka kosa litokee. Abaki yeye na Maya tu! Hapana. Net alishika hatima ya ukoo huo wa kitajiri wa Cote. Bila Net, ukoo huo inamaana utakufa na kupotea. Ni kosa ambalo hakutaka mtu yeyote alisababishe. Iwe kwa uzembe au bahati mbaya. Alihakikisha mjukuu wake anahudumiwa na wataalamu tu. Na alihakikisha anamkumbusha Mungu kila siku kuwa, ahakikishe Net anatoka pale kitandani.

Na kweli Mungu alimsaidia, Net alimaliza matibabu yake yote aliyopangiwa. Na akapona kabisa. Ndipo akaruhusiwa kurudi nyumbani. Bibi Cote hakutaka Net atoke akiwa na matibabu yeyote endelevu nyumbani. Aliongea na madaktari wote waliokuwa wakimtibu hapo kuwa, lazima Net atoke pale mzima kabisa.

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

Siku inayofuata baada ya kutolewa hospitalini, Net alimka akiwa amechelewa kidogo. Akaambiwa bibi yake alishakwenda kazini. Bila kuchelewa na yeye akajitayarisha na kumfuata bibi yake kazini. Lengo ilikuwa ni kwenda kuzungumza na mwanasheria wa kampuni yao.

Bibi yake akashangaa kumuona Net pale. Hakutegemea. Aliingia moja kwa moja ofisini kwa bibi yake. “Nilifikiri leo utapumzika!” Aliongea bibi yake wakati anatoka kwenye kiti chake na kwenda kumkumbatia Net. “Siwezi kutulia Nana, wakati mke wangu yupo jela!” “Naelewa. Acha tumwite Logan tuzungumze naye, tuone atatushauri nini.” Net akakaa mbele ya meza ya bibi yake.

Bibi yake akarudi kukaa kisha akabonyeza simu kwa sekretari. “I need to see Logan, right away.” Akaamuru bibi huyo akimtaka huyo sekretari amwitie huyo mwanasheria ambaye na yeye yupo hapo hapo kwenye hilo hilo jengo lao.

Yule kijana alifika bila kuchelewa. Kikao kikaanza. Alikuwa Net, bibi Cote na yule mwanasheria, Logan. Walikaa ofisini kwa bibi Cote. Net akamuelezea kila kitu yule mwanasheria bila kuficha huku yule mwanasheria akiandika anachozungumzia Net. Aliuliza baadhi ya maswali, mpaka akajiridhisha na habari nzima. Kuanzia ya ajira ya Net kwa mama yake mpaka hiyo ndoa.

“Tunafanyaje?” Bibi Cote akamuuliza Logan. “Cha kwanza.” Alianza Logan. “Net anaonekana bado anamaslahi makubwa sana nchini Tanzania.” “My wife/mke wangu!” Akadakia Net. “Sawa kabisa. Ili kuweza kuwa huru kuingia na kutoka hapo nchini, nilazima kutengeneza nyuma. Kule alipoharibu Ms. Ritha.” Akaendelea Logan. “Kwa kufanyaje?”  Akauliza tena bibi Cote.

“Kuhakikisha, kila kitu kipo kwa maandishi. Nikimaanisha hivi, kuanzia mkataba wa kazi. Lini aliajiriwa na lini alifukuzwa kazi. Tokea anaanza kazi, ni jinsi gani alikuwa akilipwa mshahara. Majukumu yake na mipaka yake. Ananafasi ipi kwenye ile kampuni. Yote hayo yalitakiwa yawe kwa maandishi tokea mwanzo, lakini kwa sasa ni kama itakuwa ngumu.” Kila mmoja akabaki akifikiria.

“Sidhani kama ni ngumu.” Alivunja ukimya bibi Cote. “Wakati Ritha anaanzisha ile kampuni kule Tanzania, aliisajili kama ni tawi la Cote la huku, na babu yako ni kama mdhamini wake. Nikimaanisha ni kama alimfungulia yeye ile kampuni. Kwenye memorandum ya ile kampuni ya Cote, Tanzania, babu yako alionekana ni mmiliki mwenza kwenye ile kampuni. Sasa kwa kuwa babu yako ameniacha mimi kama mrithi, na wewe of course, unazo haki nyingi sana kwenye ile kampuni ya Tanzania, na hata mimi naweza nikatengeneza ushahidi.” Net akatia wasiwasi. Alijua janja ya mama yake.

“Unafikiri babu yako angeruhusu ukapoteze maisha yako kule kama anajua hajaweka mambo sawa? Asingekubali! Pengine alifikiria mbali na kuhofia kitu kama hiki kutokea.” “Labda alibadilisha Nana! Huwezi jua!” Net alitia mashaka.

“Kwa idhini ya nani!? Hawezi kubadili mambo kiholela.” “Nana!”  Bado Net hakusadiki. Alijua janja ya mama yake kwa kuishi naye na kumbadilikia waziwazi akigeuza maneno na nyaraka za muhimu waziwazi ili kujinufaisha na yake.

“Najua umeingiwa hofu Net, lakini mimi ninauhakika na ninachozungumza. Mpe muda Logan. Atayarishe na kutafuta kila kitu anachojua kitahitajika nchini Tanzania, halafu mimi mwenyewe na Logan tutarudi nchini Tanzania kuzungumza na Ritha.” Logan yule mwanasheria akashtuka kidogo. “Na mimi nakwenda!” “Ndiyo. Au kuna tatizo?” Bibi Cote akauliza kibabe kidogo. “No ma’am.” Akajibu kinyenyekevu.

“Good! Go back to work.” Akimtaka arudi kuanza kazi hiyo. “Tayarisha kila kitu unachofikiria tutakihitaji tukiwa kule. Tafuta na file la kampuni ya Cote Tanzania. Soma kwa makini ujue nini chakujibu na kukusaidia. Ukiwa tayari, nijulishe tupange safari. Tunakwenda Tanzania. Nenda kaanze kazi.” Logan akasimama ili atoke. “And Logan!” Kabla hajatoka mlangoni, bibi Cote akamwita. “Yes Ma’am!” Akageuka Logan. “God’s speed!” Logan akaelewa kwa haraka sana. Bibi huyo anataka akamilishe kila kitu kwa haraka. “Yes ma’am.” Akaitika kwa heshima, Logan akatoka nakufunga mlango.

“Nana!” Net akaita kwa upole akionekana anamawazo. Bibi yake akamwangalia. “Samahani nakusumbua. Lakini nahitaji msaada wako. Sina jinsi.” “Hata kidogo Net. Mimi nakufahamu.” “Nachukia kukurudisha safarini tena. Zaidi Tanzania ambako umetoka hivi karibuni na inakugharimu sana. Pia najua unamajukumu mengi. Lakini nampenda Tunda. Natamani nikae hapa, nisahau kila kitu. Lakini siwezi. Nilimuahidi ni mpaka kifo.” Bibi yake akacheka.

Akasimama na kurudi pale alipokuwa amekaa Net, akambusu kichwani na kumkumbatia. “Usiwe na wasiwasi. Kila kitu kitakuwa sawa. Lakini nafikiri na wewe unahitaji kwenda kutafuta Certificate of No Impediment. Nitataka kuondoka nayo.” Bado alikuwa amemkumbatia mjukuu wake.“Nakwenda sasa hivi.”  Na yeye akambusu bibi yake, akamkumbatia kwa nguvu akiwa amekaa, bibi yake amemuinamia pale kitini. Akamsikia akivuta pumzi mara kadhaa, akasima na kutoka.

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

Baada ya kukamilisha kila kitu anachohitaji Logan, nakujua kitamsaidia kwenye kesi ya Net, bila kupoteza muda, wakapanga safari ya kurudi nchini Tanzania zikiwa zimeshapita siku 16 tokea Net aondoke nchini.

Bibi Cote nchini Tanzania TENA.

B

ibi Cote alitua nchini Tanzania akiwa amejiandaa vilivyo akizungukwa na walinzi wake wawili ambao anazunguka nao kila mahali hapa ulimwenguni na huyo Logan mwanasheria anayejua kazi yake. Alikuja kibabe, aliyejawa na mamlaka, akikusudia kumkabili Ritha vilivyo. Alikusudia hakuna atakayesimama mbele ya Net tena, ila yeye mwenyewe Net. Alivaa sura yake ya uongozi, utajiri wala si kibibi tena. Alikuwa amevaa ule wajihi wake uliozoeleka kuonekana kwenye majukwaa ya kimataifa, akitetea kile anachokiamini. Sasa ndiye huyu aliyetua hapo nchini. Akitetea hatima ya ukoo huo wa Cote. Hakika alijipanga.

Ilikuwa ni safari ya pesa nyingi, lakini alikusudia kutengeneza jina la mjukuu wake, na akakusudia mpaka anaondoka nchini Tanzania, awe amesafisha jina la mjukuu wake. Na Net awe huru kuingia na kutoka nchini Tanzania kwa utajiri wao, bila kuficha uzaliwa wake wa nchini Canada, na iwe bila msaada wa Ritha tena.

Walifika usiku, asubuhi ya siku inayofuata, mwanasheria wa bibi Cote, Logan, akapiga simu ofisini kwa mama Cote. Akaambiwa mama Cote hayupo na wala hana nafasi yakumuona mtu yeyote kwa wakati huo. Hilo halikumtisha bibi Cote.

Akajitayarisha, akamwambia Logan waende ofisini kwake bila miahadi. Ni kweli walifika pale, hawakumkuta. Akamuuliza yule sekretari wake alipo Ritha na anatarajia kuwepo hapo siku gani, akasita. Baada ya bibi Cote kujitambulisha, ndipo akapewa sasa habari zakushtua.

Aliambiwa mama Cote aliondoka hapo ofisini, hajulikani alipo. “Kuna tatizo lolote?” Akauliza bibi Cote. “Alikuwa akimkimbia Gabriel. Nilimsikia akiwa anazungumza naye hapa. Kuna mipango aliifanya dhidi ya msichana fulani hivi ili..” “Unamaanisha Tunda?” Yule bibi akauliza na kumshangaza kidogo yule dada ambaye hakuwa hata na taarifa kama Net alifunga ndoa na Tunda. Ritha alihakikisha ni kosa ambalo hatafanya hata kwa kuropoka kama hiyo ndoa ilifungwa.

“Endelea.” “Basi Gabriel alionekana kukasirishwa na kitendo cha mama Cote na Bethy mkewe Gabriel kumfunga Tunda. Ndio mama Cote akakimbia maana Gabriel alimwambia anakuja kumfuata hapa. Tokea siku hiyo hajarudi tena, na sidhani kama atarudi. Maana anatafutwa na polisi. Hivi hapa nimefurahi mmekuja ili mniambie chakufanya na hii ofisi, endapo hatarudi tena.”

“Kwa nini anatafutwa na polisi?” Bibi Cote akaendelea kuuliza. “Gabriel alipoondoka hapa majuzi na kumkosa mama Cote, akamfuata mkewe ambaye alishirikiana na mama Cote kumuweka Tunda ndani. Hayo yote niliyaona kwenye video iliyokuwa inasambazwa kwenye mitandao.” “Eehe, nini kilitokea.” “Tena kama ungekuwa unajua Kiswahili, ningekuonyesha hiyo video. Imeenea sana!” “Mtumie Logan, Logan atamtumia Net. Net atatuambia.”

“Net anaendeleaje? Aliondoka bila kutuaga wakati..” “Anaendelea vizuri. Unaweza kutuma hiyo video sasa hivi?” Bibi Cote alimkatisha kwa ukali kidogo. Yule sekretari akajua hakuna utani wala kupoteza muda hapo. Logan akampa business card yake nakumuomba amtumie kwenye email, kwani hawakuwa na simu yakutumia pale nchini.

Bibi Cote na Logan wakaaga nakutoka baada yakuandika namba ya simu ya hoteli waliyofikia na chumba cha bibi Cote. Walimwambia Ritha akirudi tu, ampigie simu. Akamwambia anaelekea polisi, akipiga hotelini na kuwakosa, aache ujumbe.

Bila kupoteza muda yule msichana sekretari wa mama Cote akamtumia Logan ile video, na Logan naye bila kuiangalia akamtumia Net. Kwani walikuwa na hekaheka wakikimbizana na muda hapo nchini na bibi Cote alionekana hataki kupoteza hata dakika moja. Alikuwa akitoa maelekezo mfululizo na Logan akiandika bila kukosea ili asiwe anauliza uliza kama mjinga.

Alikuwa na walinzi wake na Logan hapo kwenye gari wakati akizunguka hapo mjini. Walitoka hapo kwenye ofisi za Ritha, wakielekea polisi. Walipofika kituo cha polisi ndipo walipoelezwa kwa mapana kitu kinachoendelea. Waliambiwa ni tukio la siku mbili zilizopita. Bado watu wapo kwenye mshtuko, hata Tunda waliyetaka kumtolea dhamana, waliambiwa kwa usalama wake, hawezi kutolewa. Waliambia kwa wakati huo kila mtu anataka kumuona Tunda. Kumtoa, ni kuhatarisha maisha yake. Na mama Cote ameanza kutafutwa kuanzia siku hiyo. Bibi Cote akauliza ni jinsi gani anaweza kusaidia, akaambiwa aachie vyombo vya usalama.

Yule bibi hakuridhika. Akaomba kuzungumza na mkuu wa kituo. Kwa ulinzi unaomzunguka pale, vijana wakakamavu waliovaa suti nyeusi, weupe, wanaoonekana wapo kazini, moja kwa moja akapelekwa ofisi ya mkuu wa hicho kituo. Yule bibi hakutaka kupoteza muda. Akajitambulisha na kuuliza kama hapo nchini anaweza kupata wapelelezi, atakao walipa. Ili wamtafutie mama Cote kwa haraka na garama zake.

Baada ya mazungumzo ya hapa na pale, yule mkuu wa polisi aliwapa namba za simu za watu ambao wanaweza kuwasaidia japo sio chini yake ila ni watu wa usalama. Bibi Cote akashukuru na kuondoka ofisini kwake.

Walitoka hapo nakurudi hotelini akiwa kwenye mshituko wa kifo cha Gabriel na mama yake. Akajua jambo hilo ni zito zaidi. Alifahamu hiyo familia kwa karibu sana. Mama yake Gabriel alikuwa kama Ritha tu nyumbani kwao. Walifika na kuhudumiwa nyumbani kwa bibi Cote kama watu wa hiyo familia.

Alishaishi na Gabriel kwa miezi kadhaa nyumbani kwake kipindi wazazi wake waliporudi kuanza maisha tena, nchini Tanzania. Walimuacha hapo nyumbani kwake, ndipo wakarudi kumchukua. Na kila Gabriel anapokuwa nchini Canada, lazima afike kwake kumsalimia na kulala hapo kwa siku kadhaa. Aliumia sana.

Kitu cha kwanza alipofika tu hotelini akampigia simu Net. Bibi huyo alikuwa na simu ambayo aliitumia nchi au mahali popote ulimwenguni. Walizungumza zaidi ya lisaa. Net aliumia sana kwa kifo cha Gabriel na mama yake, zaidi alihuzunika kwa bibi yake kushindwa kumtoa Tunda kwa dhamana. Ndilo lilikuwa ombi la Net, akamtoe Tunda polisi.

“Wamesema kwa ajili ya usalama wake, Net. Na ukifikiria ni sawa. Wapo sahihi. Nimezungumza na mkuu wa kituo kwa muda mrefu sana. Ni kama kwa sasa na yeye anahusika na hicho kifo, mpaka upelelezi ukamilike. Tayari kwa namna moja au nyingine, anakabiliwa na kosa la jinai. Japo hakuhusika moja kwa moja, lakini jina lake limetajwa.” Net alibaki kimya. “Son!” Bibi yake akaita.

“Sijui nifanye nini Nana! Natamani kurudi mwenyewe.” “Niambie kile ungefanya hapa ili mimi nikufanyie Net.” “Sijui! Sasa utafanyaje juu ya mama?” Net akauliza akisikika sauti ya kulia. “Ndio kitu nilitaka kukwambia. Nimepata namba za private investigator. Nimeambiwa hao watanisaidia kumtafuta na kumpata. Nataka wewe ndio uwapigie uzungumze nao, sababu ya hawa niliozungumza nao, tumetumia muda mrefu sana kuelewa, sababu ya lugha.” “Pole Nana. Na asante.” “Utanishukuru tukishaweka sawa haya mambo.” Akamtajia ile namba.

Bila kupoteza muda, Net akawapigia simu wale watu. Akawaambia wanamtafuta mama Cote. Na wapo tayari kulipia. Wakaomba picha. Lakini Net akawasihi sana wasisambaze picha za mama yake mtandaoni. Akawatumia picha moja tu. Akawaelekeza alipo bibi yake, nakuomba anayezungumza kingereza fasaha ndio aende, ili waelewana.

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

Kesho yake vijana watatu walimfuata bibi Cote pale hotelini kwa mazungumzo. Lakini Net alikuwa ndiye anayezungumza nao kwenye simu huku akimweleza bibi yake. Bibi Cote alitoa maagizo kuwa atafutwe,  akishapatikana, wasitaarifu vyombo vya usalama, wampeleke pale hotelini kwa siri bila kuonekana na yeyote, na wasimwambie wapi anakwenda mpaka yeye mwenyewe aje akutane nao. Aliwalipa pesa kiasi, wakakubaliana siku watakayomleta mama Cote, watamalizana. Wakaagana na kutoka.

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

Alitamani kwenda nyumbani kwa kina Gabriel, yaani kwa wazazi wake kwa ajili ya kuwapa pole, lakini Net alimkataza kabisa. Alijua familia nzima itakuwa imewachukia wao. Kitendo cha Gabriel kumchukia yeye na kumuona adui au msaliti wake, alijua wazi mama yake alilijua hilo, kwa hiyo hata baba yake alijua kinachoendelea kati yao.

Hakuna kilichoendelea kwenye maisha ya Gabriel, mama yake asijue. Hata akiumwa kichwa, mama yake alijua. Na kama mama yake alijua, basi na baba yake pia. Na kwa mkasa ule, lazima baba aeleze ndugu wote tokea mwanzo mpaka kumfika mauti kijana wao. Kwa hiyo Net alijua kwenda kwa bibi yake huko msibani, wakati Gabriel alikufa akiwa anamtaja mama Cote kuwa ni adui yake, na akajua habari zake za kumpokonya mwanamke zitakuwa zikijulikana huko. Akamsisitiza bibi yake akae mbali kabisa. Atulie hapo hotelini akisubiria kupatikanika kwa mkwewe basi.

 Ritha mbele ya Bibi Cote.

W

atu husema pesa huongea popote. Kwa pesa aliyolipa kwa haraka bila maswali na ahadi ya kulipwa nyingine, siku ya tatu usiku wakati Net na Maya wakizungumza na bibi yao kwa kutumia skype, walisikia mlango ukigongwa. Logan alikuwa amekaa kwenye makochi akiendelea kujibu email na kuwasiliana na ofisi za Cote zilizoko nchini Canada na ndogo iliyopo nchini Marekani, akamtizama bibi Cote. “Are you gonna open the door?” Bibi Cote ni kama alimtuma afungue mlango.

Logan akaweka laptop aliyokuwa akiitumia, akasimama. Net na Maya wakawa kimya upande wa pili. Logan aliuliza ni kina nani kabla ya kufungua mlango. Mtu wa nje akajibu, lakini Logan hakuelewa. Ikabidi Net awapigie simu wale wapelelezi waliowalipa. Ndipo wakajitambulisha kwa Net kuwa ni wao wapo mlangoni ndipo Net akamwambia Logan afungue. Na wakati huo huo Logan akawa amewapigia simu walinzi wa bibi Cote chumba cha pili, wote wakafika hapo.

Wakashangaa wanaingia wakiwa wamemfunga pingu mama Cote. Kimya. Alionekana ameingiwa na hofu ya kupita kiasi. Bibi Cote akakaa sawa. Ritha alishtuka karibu kuanguka baada yakumuona mkwewe pale. Wakaangaliana kwa sekunde kadhaa, kisha akawageukia wajukuu zake na kuwaaga. “Nataka kusikiliza Nana!” Maya akasikika. “No Maya.” Net akamkataza mdogo wake. “Fine.” Maya akaondoka, Net akazima ile komputa hata yeye hakutaka kusikiliza.

“Sikuwa nimekusudia mabaya. Nilitaka kumuokoa Net.” Ritha alianza kujitete huku akitetemeka midomo. “Save it Ritha! Just STOP.” Bibi Cote akafoka. Alishakuwa mwekundu na mama Cote alijua amekasirika. “Logan, mwambie ni nini tunachotaka kutoka kwake.” Wakiwa wamesimama mbele ya bibi Cote, wale vijana na Ritha mwenyewe, Logan akafungua laptop yake akaanza kusoma.

“Tuanze kikazi. Nahitaji barua yenye tarehe ya kweli ya kuajiriwa kwa Net. Na barua au karatasi zinazoonyesha majukumu yake Net aliyokuwa akifanya, na mshahara aliokuwa akilipwa, na ielezwe njia sahihi alizokuwa akitumia kupokea mshahara wake. Nitahitaji pia vibali vyote vya uhamiaji vinavyoonyesha tarehe alizoruhusiwa kuwepo nchini. Mwisho kwa upande wa ajira yake, nitahitaji barua yakuachishwa kwake kazi. Vyote hivyo viwe na muhuri wa kampuni na saini yako.” Logan akamaliza na kumtizama Ritha na bibi Cote.

“Umemuelewa Logan au ungependa arudie?” Bibi Cote akamuuliza Ritha kibabe. “Ninavyo vyote ofisini kwangu, nimefungia kwenye safe.” Akajibu Ritha. “Good. Kwa hiyo tukienda sasa hivi, Logan atapata kila kitu anacho kihitaji?” “Ndiyo.” Ritha alikuwa mnyenyekevu kama sio yeye.

“Okay. Hilo tumemaliza. Kinachofuata, Logan muonyeshe makubaliano aliyokuwa ameingia na Mr. Cote wakati anafungua hii kampuni ya huku.” Logan akatoa karatasi kadhaa, nakuanza kumsomea. Yalikuwa makubaliano ya kuwa, anapokea pesa zote kutoka kwa Mzee huyo kwa makubaliano kuwa, asilimia 75 ya hisa za kampuni hiyo ni za huyo Mzee na mkewe. Watakapokufa, Nethaniel Cote ndiye mwenye hizo hisa, na ikitokea chochote kile, kama Ritha anakufa yeye, au anashindwa kuendesha hiyo kampuni, na wakajikuta wanaingia hasara, mali zote za kampuni ziuzwe, na kukabidhiwa yeye huyo Mzee Cote na mkewe, na kama wao hawapo, apewe Net. Logan alisoma kisomi na kifasaha mpaka akamaliza.

“Umeelewa Ritha?” Bibi Cote akamuuliza. “Ndiyo.” Akajibu Ritha. “Je, unakumbuka kusaini hayo makubaliano wakati unachukua pesa kwetu?” Bibi Cote akauliza tena. “Ndiyo lakini hiyo ni miaka mingi sana iliyopita.” “Kwa hiyo!?” Bibi Cote akauliza. “Mambo mengi yamebadilika.” “Nini?” Kimya.

“Ritha?” Bibi Cote akamwita kwa ukali kama asiyetaka kupotezewa muda. “Huwezi kunipokonya mali nilizozihangaikia muda wote huo! Hata kama ni pesa yenu, nimeifanyia kazi, na nimeizalisha zaidi.” “Sijakudai chochote mpaka sasa.  Na bado sijakuhesabia pesa tulizokuwa tukikuongezea kila mwaka na jasho au juhudi ya Net kwenye hii kampuni ya huku.” Kimya.

Ritha akakumbuka pesa aliyokuwa akipokea kila mwisho wa mwaka kutoka kwa wakwe zake ili kumsaidia kwenye biashara. Akaona atulie. “Sasa nataka unisikilize vizuri Ritha. Na ninataka unisikilize kwa makini, kwa kuwa usipokubaliana katika hata moja katika haya, utaona upande wangu mwingine, ambao nina uhakika hutaufurahia. Umekwenda mbali sana, na sitakuruhusu. Hasa inapofika upande wa Net, ambaye amejitoa sana kwako! Ameacha maisha mazuri, ili aje awe na wewe huku! Umewezaje hata kuthubutu kumfanyia uliyomfanyia!?” “Nilikuwa namlinda mtoto wangu.” Ritha akajibu kibabe na kuendelea.

“Wewe unawapa kila kitu wanachohitaji au wanachokutamkia bila kufikiria madhara yake baadaye. Ilimradi wakulilie tu, hufikirii, unatekeleza. Unawalea watoto wangu vibaya, na hufikirii madhara yao ya baadaye. Mimi ni mama yao. Naijua Tanzania na watu wake. Najua ni nini watoto wangu wanastahili na nini hawastahili. Sasa hivi Net anaumia kwa ajili ya Tunda, lakini najua baadaye atanishukuru tu.” Hapo Ritha akajikaza na kuongea.

“Niambie ni nini unachomuepusha Net kwa Tunda? Niambie tu Ritha. Na usinitajie juu ya maisha aliyoishi zamani. Kwa sababu mimi na wewe tunajua tatizo hapa si Tunda na maisha aliyoishi zamani.” Bibi Cote akamuuliza huku amemkazia macho.

“Tunda anampendea Net pesa tu.” “Sasa tatizo liko wapi!?” Yule bibi akamuuliza kwa mshangao. “Watu wote tunapenda watu kwa sababu tofauti tofauti. Kama inatokea Tunda anampendea Net pesa, na anamfanya anakuwa na furaha, tatizo liko wapi Ritha? Kwa nini umeshindwa kumpa nafasi Net na Tunda? Ni nini inakuwa ngumu kwako? Kama Tunda atatapanya pesa ya Net, wewe inakuhusu nini?” Bibi Cote aliongea bila wasiwasi akimshangaa Ritha.

“Net amejitenga na mali zako. Na wote sisi anatutangazia kuwa yeye ni mfanyakazi kwako na ndivyo anavyoishi. Akiwa hapa au kule nyumbani. Hakuna pesa ambayo Net anaipata kwa kupewa tu, kila pesa inayoingia mfukoni kwake, ameifanyia kazi. Na wote sisi tunajua Net sio mjinga. Angeweza kuoa msichana yeyote yule, lakini amemchagua Tunda.”

“Hata mimi ningependa au hata babu yake alipenda kama angemuoa Chloe, lakini Net alishindwa kabisa. Babu yake alitamani kumuona Net anaoa kabla ya kifo chake, lakini Net alishindwa. Wakati wote na sisi wote alituambia anampenda Tunda. Ningekuwa na sababu zote zakumlazimisha ili aoe na babu yake amuone, lakini mimi na babu yake tuliheshimu maamuzi yake kama tulivyoheshimu maamuzi ya baba yake kukuleta wewe mgeni kabisa kwenye maisha yetu. Sikuwahi hata kufikiria kama naweza kuwa na mtu mweusi kwenye familia yangu! Lakini mbona tulikupokea Ritha?” Bibi Cote alikuwa mwekundu na kuongea kwa hasira.

“Kulikuwa na mabinti wazuri tu. Waliotokea kwenye familia zakitajiri kule kule Canada. Lakini ulipoletwa wewe, japokuwa tulishtuka sana, ilitubidi kukupokea tu. Hatukuwa na jinsi, kwa kuwa ulikuwa chaguo la CJ. Niambie ni wapi tulipokutendea ubaya wowote au kukuonyesha hustahili kuwa na baba yake Net, CJ?” Kimya.

“Ritha? Sema ukweli. Ni wapi tulipokuonyesha kuwa wewe hukustahili kuwa mkwe wetu?” Kimya. “Au wewe ulifikiri ulikuwa wa maana sana kuliko Tunda!?” Yule bibi akamjia juu zaidi. “Tulikupokea na kukuendelea kukuvumilia mpaka kifo cha Cote bado tulikuvumilia. Kwa mabaya yako yote. Tena ya ajabu kupita kiasi, hatukuwahi hata kuropoka mbele ya watoto wako kwa chochote! Ulifikiri mimi ni mjinga?” Kimya.

“Nakushangaa sana Ritha! Narudia tena. Uliwezaje kumfanyia hivyo Net? Ni uchungu upi huo ulionao kwa Net, mtoto uliyemtelekeza mikononi mwangu tokea unaishi nchini Canada!? Nani anayejua uthamani wa Net kati yangu mimi na wewe? Ulitelekeza watoto wako, ulifikiri mimi ni mjinga kutowaambia ukweli wakabaki upande wako?” Yule bibi alipata jukwaa. Hakumbakiza Ritha.

“Uliuza kila kitu cha mtoto wetu, bila hata kufikiria watoto aliowaacha, ukarudi huku na pesa yote. Ulipoharibikiwa ndipo, ukarudi tena kuomba msaada bila hofu wala aibu ukijua wazi watoto uliowatelekeza tena tangia wapo wadogo sana, nawalea mimi! Niambie ni lini tulikaa chini tukakuhoji ni kwa nini uliuza mali zote za mumeo na kubaki na pesa yote wewe mwenyewe bila kujali watoto wenu au ni kwa nini unatuomba tena msaada wakati uliondoka bila kushauriana na sisi! Tulijifunza kuheshimu maamuzi yako.” Bibi Cote akaendelea.

“Tukiwa tunakuletea watoto waje kukusalimia kwa upendo tu. Ili msipoteze mahusiano, ulipoona Net atakufaa, ukaanza kumgeuza moyo kwa maneno yako ya ujanja ujanja.” Ritha akashtuka kidogo. “Ulifikiri nilikuwa sijui hila zako Ritha? Kumbuka mimi ndiye niliyemlea Net. Akiongea jambo, najua ni yeye au ni mtu mwingine anayeongea kichwani mwake.” Ritha akatulia.

“Ulipoona tumekuza kijana mzuri ambaye atakufaa kwa maendeleo yako ndipo ukaanza kumchota akili taratibu huku ukimdanganya kwa upendo wa kimama ambao haujawahi hata kuwa nao kwa watoto wako Ritha! Ukafanya hivyo mpaka ukafanikiwa kumbadili malengo Net, akaamua kuja kuishi na wewe huku wakati ulijua wazi tulijitahidi kuwekeza kwake ili aje awe mtawala wa Cote. Lakini ukatuzunguka!”

“Ulifikiri hatukujua hila yako!? Ilituumiza sana. Tulijua unakuwa mbinafsi, unashindwa kufikiria maisha yake ya baadaye. Lakini tulinyamaza tu, nakumpa baraka zetu. Ulifikiri sisi ni wajinga?” “Kwani na huku si alikuwa akifanya kazi?” Ritha akajibu kwa kiburi.

“Unaongea nini Ritha wewe? Umelewa? Wamekutoa baa hawa vijana!?” Yule bibi akasimama akitetemeka hasira. Ritha akarudi nyuma kidogo, wale waliomleta wakamsukumia mbele kwa bibi Cote. “Umemfukuza Net hapa nchini ukimpa makosa kama mtu baki tu! Unamuondoa hapa kama mfanyakazi wa kawaida! Unamtupia hati yake yakusafiria na tiketi bila hata sweta! Unajua alizimia uwanja wa ndege, polisi ndio walimpeleka hospitalini?”

“Alilazwa Net kwa siku 9, kwa kumtoa hapa kama mwizi wakati ni mtoto wako, aliyekuwa ameacha kila kitu kwa ajili yako! Unamtoa katikati ya mapumziko akiwa na mkewe, humuogopi Mungu, Ritha?”

“Uliwezaje kumtoa kwenye mapumziko aliyokuwa akiyasubiria miaka yote hiyo na wote tunamjua jinsi Net alivyomwaminifu mbele za Mungu hata kwetu! Ulitaka Mungu akupe kijana wa namna gani?” Ritha kimya.

“Sasa, nataka unisikilize na ujue nataka utekeleze kwa haraka ili niweze kuondoka hapa nchini. Wewe unajua kuwepo kwangu hapa ni kiasi gani napoteza wala sio kuongeza. Na kinachoniudhi zaidi ni wewe Ritha ndiye unayesabisha haya yote ukiwa unajua ukweli wa kila kitu! Huna tofauti na Tunda ulipokuja kwenye maisha yetu. Hukuwa bikra wala tajiri.”

“Hukuwa mkamilifu, na wala hukuwahi kuwa mke mwema kwa CJ, mimi na baba yake tulijua uchafu wako wote, lakini tulinyamaza kwanza kwa kuwa CJ alikuwa mgonjwa pili kwa ajili ya Net na mdogo wake.” Hapo Ritha alipooza sana. Hakujua kama mkwewe alikuwa akijua kwa undani kile kilichokuwa kikiendelea na mumewe.

“Sasa nataka umuache Net, na uheshimu maamuzi yake. Hiyo ni moja. Unanisikia Ritha?” Kimya. “Sikutanii Ritha na sitarudia kuwa na mazungumzo ya namna hii na wewe. Hii ni mara ya kwanza, na hesabu  ni onyo. Na ndio maana upo hapa na wala sio kituo cha polisi ambako waliniambia unatafutwa kwa kusababisha kifo cha Gabriel.”

“Sijamuua Gabriel.” “Hiyo ni juu yako na vyombo vya usalama. Hainihusu, ila mambo ya Net ndiyo yananihusu. Ukishindwa kufanya ninayotaka ufanye sasa hivi, hawa vijana wanakutoa hapa na kukupeleka kituo cha polisi.” “Huwezi kufanya hivyo. Mimi ni mama yake Net na Maya.”

“Lini umelikumbuka hilo?” “Mimi najua hivyo siku zote na ndio maana ...…” “STOP! Just stop. Sisi wote tunajua ukweli juu ya malezi ya hawa watoto. Nimekuachia Net kwa miaka michache tu, umemrudisha kwangu nusu mfu. Kwa hiyo nyamaza na unisikilize.” Ritha akatuli.

“Nataka ufanye yafuatayo, moja, kaa mbali na Net, na usijihusishe na maamuzi yake. Usimtafute mpaka yeye atakapo kutafuta. Mbili, ninataka nyumba ya Net, irudi kuwa ya Tunda.” Ritha alishtuka sana. Akatoa macho. “Haiwezekani!” Akakataa. “Niamini mimi Ritha, utafanya tena kwa maandishi. Na iwe leo. Uandike na kumkabidhi Logan kuwa nyumba ya Net au kama ulivyomwambia Net ni ya kampuni ya Cote, inakuwa ya Tunda kuanzia tarehe aliyoamua Net. Nitataka saini yako na muhuri wa kampuni kwenye hiyo barua. Na uende kwenye ofisi husika za aridhi ukatoe mkono wako kule, uache waendelee kushugulikia kubadilishwa kwa hati.”

“Huna nafasi ya kukataa katika hilo kwa kuwa wote tunajua ile nyumba ni jasho la Net. Alikataa mtu yeyote kumsaidia kuijenga ile nyumba. Hukuweka pesa yeyote ile kwenye ile nyumba. Anavyoamua juu ya ile nyumba, mimi na wewe haituhusu. Unanielewa?” Kimya.

“Tatu, nataka umkabidhi Logan, karatasi zote za talaka ulizomsainisha Tunda na za ndoa ulizochukua. Nne, nataka picha na video zote za harusi ya Tunda na Net. Tano, nataka pete zao za harusi na usithubutu tena kushika pete yangu ya uchumba. Nilimkabidhi Net, amvalishe Tunda. Nina maana yangu. Usiwahi wala kuthubutu tena, kujaribu kunisahihisha. Iwe mwisho.” Ritha kimya.

“Sita na mwisho kabisa, achana na Tunda kabisa. Umenielewa Ritha?” Kimya. “Namaanisha hivi, ushahidi wote ulionao dhidi ya Tunda, nataka umkabidhi Logan na umpigie simu huyo aliyekusaidia kuprint mawasiliano yote ya zamani ya Tunda, umwambie unampa tena kazi ya kufuta kabisa mawasiliano yote yazamani ya Tunda na yasiwahi kuonekana tena hapa duniani.”

“Kama vile dhambi zake zilivyofutwa huko mbinguni, ndivyo utakavyohusika wewe kuhakikisha unanipa hayo mawasiliano uliyokwisha printiwa na kufutwa ili yasiwahi kuja kuonekana tena. Kisha utakwenda kufuta kesi yake polisi.” “Huwezi kuniamrisha kitu chakufanya.” Akajibu Ritha kijeuri.

“Wote tunajua kuwa NINAWEZA. Na ndicho ninachofanya sasa hivi. Na ninataka hayo yote uyafanye usiku huu. Tunatoka wote sasa hivi, ukakamilishe hayo yote. Leo kabla ya kesho. Na ukimaliza hapo, hutaniona tena kwako, na upo huru kubadilisha jina la kampuni kuwa lako. Andaa karatasi unazotaka nisaini, mtumie Logan, akiridhika zipo sawa, nitaidhinisha na kukiri kuwa nimekuruhusu mali zote za Cote, kuhamishwa kwenye kampuni yako. Lasivyo nitahitaji kila dola ya Cote iliyowahi kuingia kwenye mfuko wako. Inamaana nitakufilisi vibaya sana, na utaishia jela. Logan anayo orodha ya kila pesa tuliyowahi kuwekeza kwako. Sasa nataka kujua, ni nini uamuzi wako? Hao vijana wanakupeleka polisi au ofisini kwako utukabidhi vitu vyote nilivyo kutajia?” Kimya.

“Kwa usemi mwingine ninaotaka kukwambia, kwa namna moja au nyingine, nitapata vyote ninavyovitaka kutoka kwako. Iwe kutoka kwako kwa hiari au kwa kutumia vyombo vya sheria. Ila nataka ujue tu, nitakapokushitaki mimi, nakutoa madai yangu, nitaidhinisha mali zako zote mpaka kijiko chako, apewe Tunda. Kitu ambacho hutaki na ndicho kimekufikisha hapo ulipo.” “Twendeni nikawape.” Baada yakusikia hivyo Ritha akakubali kwa haraka sana. “That’s what I thought!” Bibi Cote alisikika kibabe, akimkejeli Ritha.

 

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

Walifika ofisini kwa Ritha usiku huo huo. Walikuwa wale wapelelezi wa kitanzania waliolipwa kumkamata Ritha, walinzi wa bibi Cote, bibi Cote, Logan na Ritha mwenyewe. Moja kwa moja mpaka ofisini kwake, akafungua Safe yake. Akaanza kutoa mikanda ya video na picha. Ikiwa hata hazijakuwa print. “Mkabidhi Logan. Yeye atakwambia ni nini umpe.” Akamgeukia Logan na kumwita. “Logan!” “Yes ma’am!” “Hakikisha una kila kitu kabla yakuondoka hapa.” “Yes maam.” Akajibu Logan kwa heshima. Kisha akamgeukia mama Cote.

“Kwa kuwa tumeanzia kwenye maswala ya ndoa, nataka uhakika kama hizi ndizo picha zote na video?” Logan akamuuliza Ritha. “Ndiyo. Kwani wewe unafikiri nini?” Ritha akamjibu Logan kwa hasira.

“Okay. Naomba na nyaraka zote za ndoa yao.” Logan akaendelea akiwa ametulia bila jazba. Ritha akatoa, na kuzitupa mezani. Logan akaziokota na kuanza kuzisoma huku akiangalia kwenye laptop yake kama anayehakikisha kitu, kisha akamtizama mama Cote. “Hujanipa za  Net’s wife.” “Tunda sio mke wa Net, hawakuwa wamekamilisha mambo mengi sana na ndoa yao sio halali. Usi..” “Ritha! Ritha!” Akaita bibi Cote. Ritha akamgeukia.

“Hayakuhusu kabisa. Mpe kile anachokitaka Logan. Now Ritha.” Akaamuru bibi Cote. Ritha akarudi kwenye safe tena. Kumbe alifanya makusudi kutompa, akidhani Logan ni mbambaishaji, hatajua. Akatoa hizo nyaraka zilizokuwa na picha za Tunda, safari hii akazitupa sakafuni kabisa. Logan akaziokota bila kinyongo. Akasoma huku akihakiki kwenye laptop yake. Kisha akaziweka pamoja na kuweka kwenye faili lililokuwepo kwenye mkoba wake.

“Umeridhika?” Bibi Cote akamuuliza Logan. Logan akaendelea kusoma. “Naomba mawasiliano yazamani ya Tunda.” Logan akamtizama Ritha. “Nimelipia pesa nyingi sana kupata haya mawasiliano. Kwa hiyo…” “Acha kumzungusha Logan. Wewe mpe kila anachokihitaji.” Mama Cote akafikiria kidogo, akarudi kwenye safe yake, akatoa bahasha iliyokuwa na karatasi. Akaanza kuchana pale pale mbele yao. “Hizi ni pesa zangu.” Aliendelea kuongea huku akichana kwa hasira, kisha akatupa pale sakafuni wote wakimtizama.

“Umemaliza?” Akamuuliza bibi Cote kwa kumkejeli. Ritha akapiga tena teke vile vipande vya karatasi alivyokuwa amevichana. “Sasa hivi ndio nimemaliza.” Akamjibu bibi Cote huku akimtizama kwa jeuri. “Logan! Okota hivyo vipande na uhakiki kama kweli ni yenyewe, halafu kama ni yenyewe, weka kwenye bahasha.” Logan akaanza kuokota vile vipande vya karatasi vilivyokuwa vimezagaa pale sakafuni. Alizunguka pale ofisini akiokota mpaka akamaliza. Nakurudi kukaa.

“Ili kumaliza kabisa upande huo wa Net’s wife…” “Kwani huwezi kutamka Tunda!?” Bibi Cote akamuuliza Logan kwa ukali kidogo. Logan akakohoa kidogo. “Okay. Ili kumaliza kabisa upande wa Tu-n-da, naomba kwanza namba ya simu ya huyo aliyekusaidia kupata mawasiliano yake, halafu kabla hujapiga, naomba Net ambaye anaelewa lugha ya Kiswahili awepo hewani akisikiliza mazungumzo yenu unapomuomba kufuta mawasiliano yote ya mke wake ya zamani ili anisaidie kuhakiki kuwa unachozungumza na hao wahusika ni sawa na ili Net anisaidie kuwafuatilia baada ya mazungumzo yako ili kuhakikisha ni kweli walifuta kila kitu.” “Hiyo ipo sahihi kabisa Logan. Good job!” Hapo Logan akamfurahisha bibi Cote. Akakubaliana na lile wazo. Akampongeza na kumgeukia Ritha

Now Ritha!” Akamuamuru. Ritha akabaki amesimama. “Unanipa au umegoma?”“Sikumbuki namba zao.” “Usinichezee Ritha!” “Nimekwambia sikumbuki.” “Basi twende kwa Bethy ambaye mmesaidiana naye kutengeneza huo ushahidi.” “Bethy yupo polisi!” Ritha akajibu. “Kumbe unafikiri nitakupeleka wapi kama sitapata kile ninachokihitaji!?” Bibi Cote akamshangaa kwa wazi.

“Najua unajua wazi unatafutwa na polisi. Upo hapa, sijakufikisha polisi kwa kuwa najua utanisaidia kumuweka huru Net. Sitakubali visa vyako, viharibu maisha ya Net. Atakuwa huru kuishi atakapo, kwa msaada wako wewe uliyemuharibia. Sasa kwa kuwa wewe umeshindwa kumsaidia kuwepo hapa nchini, Tunda atamsaidia. Kwa garama yeyote ile. Net atapata anachokitaka. Kwa hiyo Ritha, nakuonywa, USINIJARIBU.” “Kama ndio hivyo, mimi nitazungumza na Net mwenyewe.” Ritha akataka kujirudi.

“Nilikupa hiyo nafasi, ukashindwa vibaya sana. Ulikuja kumtisha Net mbele yangu. Nikanyamaza nikijua ni hasira tu, utajirudi. Lakini unaonekana huna hasira, umekusudia kumuharibia maisha yake. Na kwa kuwa mimi nipo, sitakuruhusu tena Ritha. Kuanzia sasa kila kitu kwa wale watoto utakifanya kupitia mimi na ninakuonya, USINIJARIBU.”

“Sasa kwa mara ya mwisho, mkabidhi Logan mawasalino ya watu wanaohusika na mambo ya mtandao na uwapigie baada ya Net kuwa hewani.”  Akachukua kikaratasi na kuandika ile namba. Akaacha pale pale mezani. Logan akasimama na kwenda kukichukua.

Akampigia simu Net, akamueleza kitu anachotaka afanye, Net akakubali lakini akaomba azungumze na bibi yake kwanza. “Namfahamu mama. Anaweza kutuzunguka wote tukiwa tunamtizama na kumsikiliza. Naomba umwambie amwambie huyo muhusika, apokee simu yangu kwanza kabla hajazungumza naye chochote, atuweke kwenye conference call wote ili niweze kusikiliza mazungumzo yote. Na umwambie mama baada ya kukata tu simu sasa hivi, amwambie huyo mtu, mimi ndiye nitaendelea naye, sio yeye mama tena.” Nalo hilo wazo likawa jema.

“Lakini pia nana?” Net akaita. “Hakikisha pia wakati anampigia sasa hivi ili kumwambia apokee simu yangu, aweke kwenye sauti ili na mimi huku nisikie kuanzia mwanzo akimwambia apokee simu yangu kabla sijakata na kumpigia yeye huyo muhusika ili asije akaongeza neno lolote lile la kiswahi la kutuzunguka kwa huyo muhusika ambalo nyinyi hamtafahamu.” Net akaongeza akijua janja ya mama yake, anaweza katika kufikisha tu huo ujumbe mfupi wakati Net hayupo kewani, akamkonyeza yule mtu kwa neno la kiswahili, ikawa kuzungumza na Net tena akiwepo ikawa kazi bure.

Bibi Cote akamgeukia Ritha. Akamwambia afanye kama alivyosema Net. Akataka kubisha, lakini ikabidi tu afanye. Ritha akatoa simu yake, akapiga namba, akasubiria. Ikiwa inaita kwa sauti tu na Net akisikia. “Mimi ni mama Cote.” Akajitambulisha. “Bado ninayo namba yako mama. Unataka kutupa deal nyingine? Wewe mama yetu, safari hii tutakufanyia kwa bei nzuri.” Net alimsikia yule kijana akizungumza na mama yake kwa utani kidogo. “Safari hii nataka kitu cha tofauti. Na..” Ritha akasita kidogo. Akawatizama bibi Cote, Logan, walinzi wa bibi Cote. Mmoja alikuwa pale ndani, mwingine nje akilinda. Akawatizama na wale walioenda kumtoa mafichoni. Akatulia kidogo.

“Nana?” Akasikika Net akiita. “Why is she quet!?” Akauliza Net na kumwambia bibi yake bado hajampa maelekezo yule mtu upande wa pili yakupokea simu yake, asimruhusu kuongea chochote tena. Bibi Cote akamkazia macho. “Usinitanie Ritha!” Bibi Cote akamuonya. “Kabla hatujaendelea, kuna namba inakupigia sasa hivi, naomba upokee na utuweke kwenye conferenze call ndipo tuzungumze pamoja nikwambie chakufanya. Kisha kuanzia hapo utaendelea na yeye. Mimi sihusiki tena.” Ritha akaona aendelee tu.

“Mbona unanitisha tena?” “Usiogope. Hakuna tatizo, ni ulaji mwingine. Tena safari hii watajie pesa kubwa. Hawa wanapesa.”  Ritha akataka kumkomoa bibi Cote. “Haya. Mwambieni huyo Net ampigie sasa hivi, anawasubiri.” Ritha akaongea kishari. Bibi Cote akamuuliza Net, ni nini ameongea kwanza. Net akamwambia vile alivyomshauri yule mtu awatoze pesa nyingi zaidi. Bibi Cote akacheka kwa kusikitika. Akamwambia Net apige, awepo kwenye hayo mazungumzo. Net akakata huku kwa bibi yake, akampigia yule mtu aliyetoa mawasiliano ya zamani ya Tunda.

Walipokuwa wote watatu na bibi Cote kusikia sauti ya Net upande wa pili ndipo alipomruhusu Ritha kuendelea kuzungumza na yule kijana. Simu alikuwa ameweka mezani. Bibi Cote alimkatalia hata kuigusa tena simu yake mpaka baada ya hayo mazungumzo yao watatu na Net akiwepo.

Walimsikia Net akijitambulisha kwa yule muhusika. Ndipo mama yake akaendelea. “Unakumbuka yale mawasiliano ya yule mala..” “Nilikuonya usimtukane mke wangu.” Net alisikika tena. “Jina lake ni Tunda. Huwezi kutamka, niache mimi niendelee mwenyewe katika hili. Kata simu.” Net akasikika akiwa amekasirika sio kubembeleza tena. Bibi yake akasimama. Akamuuliza Net kama kila kitu kipo sawa.

“Sitaki amtukane mke wangu, Nana. Amwite jina lake. Akishindwa kuzungumza aache.” Akajibu Net kuonekana amekasirika. “Safari hii nataka ufute kabisa yale mawasiliano uliyotupritia mimi na Bethy. Isiwahi kuja kuonekana tena, popote.” Akaendelea Ritha bila kumjibu mwanae upande wa pili au yule bibi aliyekuwa amemsimamia pale kwa hasira.

“Kwa nini tena mama yangu? Au…” “Wewe usiulize maswali mengi, watajie garama yake, basi.” Akamtajia garama yote. “Ukipewa hiyo pesa, ni lini utakamilisha hiyo kazi?”  Wakamsikia Net akiuliza. “Haitachukua muda mrefu.” Yule mtu akajibu tena, safari hii Net akaweza kuitambua ile sauti. Akashtuka sana. “Fred!” Net akaita kwa mshangao. Kimya.

Fred ni rafiki wa Net na Gabriel pia. Ndiye aliyemsaidia kumwambia Net, alipokuwa amekimbilia Tunda, Kigamboni baada ya kufuatwa na Ritha ofisini kwake akamtukana sana. Tunda akakimbia asijulikane alipo, Fred ndiye aliyemsaidia Net kumwambia Tunda yupo Kigamboni. Akashangaa ndiye anayetumiwa na mama yake.

“Fred!?” Net akaita tena. “Unazungumza na Net. Mimi sitaki kesi na wewe. Nitakulipa pesa yako ila naomba unihakikishie utafuta kweli hayo mawasiliano ya zamani ya Tunda.” “Kwanza naomba uniamini Net, sikufanya kwa nia mbaya. Hii ni kazi yangu ya pembeni. Kama kuna jambo baya lolote lililotokea kwa hili, naomba tusameheane.”

“Shida yangu ni hayo mawasiliano yasije kuonekana tena. Unafikiri unaweza kunisaidia?” “Bila shaka. Tena nipo kwenye kompyuta sasa hivi. Ukinipa dakika 10 tu, nitakuwa nimekamilisha.” “Nashukuru. Basi nitakupigia baada ya dakika 10.” Wakaagana. Net akampigia simu tena bibi yake. Akamweleza walipofikia na Fred. Bibi yake na Logan wakaridhika. Wakaagana na Net ili wao wamalizane na Ritha.

Net alipokata tu, bibi Cote akamgeukia Logan. “Umemaliza kila kitu kuhusu Tunda?” “Bado kufuta tu kesi.”“Hiyo sitaweza. Ni kama mnataka kunifunga mimi ili yeye atolewe! Hapana. Hata kama mmenichukia kiasi gani, hamuwezi kunifanyia hivyo. Mimi bado ni mama yake Net na Maya. Hata ufanye nini, huwezi kubadili hilo. Huwezi kunifanya niende polisi, wakati unajua wazi wananitafuta!” Hapo Ritha akawajia juu na yeye.

“Sasa utajificha mpaka lini? Kwa nini usiende ili kusafisha jina lako?” “Sio sasa hivi. Lazima niweke mambo yangu sawa ndipo nitaenda, lakini sio sasa hivi. Nikienda sasa hivi sijui kama watanikamata au wataamini maneno yangu. Na wakinikamata ujue ndio mali zangu zote zitapotea. Hapana. Nahitaji muda. Niambieni nifanye chochote, lakini sio kurudi polisi.”

Bibi Cote akamgeukia Logan. Logan akajua ndio anaulizwa. Akaendela. “Anaweza asifike polisi kufuta kesi, lakini pia asitokee siku ya kesi ya Tunda kutajwa, au asijihusishe tena na kesi ya Tunda ili endapo kunafanyika uchunguzi, au kama kunafanyika utetezi wowote, namaanisha kama tukiamua kumtafutia Tunda wakili wakumwakilisha, asipate shida. Kusiwe na ushahidi wowote wakupinga. Na kusiwe na shahidi wakupinga.” “Hapo ndipo tunarudi kwenye swala la kukaa mbali kabisa na Tunda. Umeelewa Ritha?” Kimya.

“Ritha?”  Bibi Cote akaita kwa ukali. “Hata hivyo sina muda huo tena. Na sijali tena. Nimejaribu kuwasaidia naona hamtaki. Kitakachowapata na huyo Tunda, itakuwa juu yenu.” Ritha akaongeza. “Kuthibitisha hilo na kuhakikisha husahau. Karatasi zako za kubadili jina la kampuni na kuonyesha wewe ndio mmiliki wa hii kampuni peke yako, sitazisaini mpaka nihakikishe huweki pingamizi kwenye kesi ya Tunda.” “Hiyo sio sawa. Kama hiyo kesi ikichukua miaka 10?”  Akauliza Ritha.

“Kwenye ile video ya Gabriel na Bethy, alisikika Bethy akisema ulihonga ili Tunda ahukumiwe haraka. Sasa nashauri uongeze hongo ili kesi yake itajwe, kisha ijifute, ndipo nikusainie karatasi ya umiliki. Lasivyo ujue kwa kadiri Tunda anavyosubiria jela, ndivyo na wewe utakavyosubiri na ninaweza kuchoka nikaamua kubadili mawazo.” “Utafanyaje!?” Akauliza Ritha kwa mshangao.

“Utajua pale nitakapokuwa nimebadili mawazo.” Kisha akamgeukia Logan. “Logan!” Akimaanisha Logan aendelee. Logan akaendelea. “Tumemaliza upande wa Tunda. Turudi kwa upande wa barua za kikazi za Net, nitakazohitaji kutoka kwako.” Akarudia kumtajia zile barua zote. “If I may!” Logan akamgeukia bibi Cote kumuomba atoe ushauri. Bibi Cote akamruhusu.

“Kwa kuwa mengi yanaendelea. Naomba atumie barua ambazo mimi nimeandaa mwenyewe. Asome vizuri tu, na kama akiridhika, aweke saini yake na muhuri kwenye hizi nilizoandaa mimi.” “Kwa nini!?” Akauliza Ritha kwa mshangao. Logan akamgeukia bibi Cote. “Naomba iwe hivyo kwa sababu za kiusalama. Hizi nilizoandaa mimi nimeandaa kiutaalamu, haziwezi kuja kubadilika baadaye.”  Logan mwenyewe alikuwa ameshaziandika, ni mama Cote tu kujaza tarehe na kusaini.

“Nafikiri umemuelewa Logan. Mtolee asome, kisha akurudishie. Uzipitie tena Logan. Ukiridhika, akupe wewe mwenyewe muhuri, uweke unapotaka.” Akaongeza bibi Cote.

Ritha akakaa na kuanza kusoma zote ili asije kuwa na yeye ametegwa. Aliporidhika, bila shida akaweka saini. Akatoa muhuri na kumkabidhi zile karatasi zote na muhuri. Logan akazipitia huku akiweka muhuri kwenye sehemu alizotaka yeye. Aliporidhika na kila kitu. Wakamuona anakusanya karatasi zote na kuzipanga vizuri kwenye mkoba wake.

Kisha akatoa bahasha iliyokuwa na pesa, akamkabidhi mmoja wa wale vijana waliokuwa wamemkamata Ritha. Wakapokea. Bibi Cote akawashukuru, na kuondoka zao. Wakawaacha walinzi waliokuja na bibi Cote nchini. Mmoja ndani na Logan na bibi huyo, mwingine nje.

“Inaonekana umefanya kwa sehemu.” Bibi Cote akaongea hivyo wakati anasimama kuashiria amemaliza pale. “Kwa sehemu wakati nimekamilisha kila kitu!” Akashangaa Ritha. “Umebakisha pakubwa ambapo panakushinda. Kaa mbali na Tunda. Nisisikie umetokea mahakamani siku kesi yake ikitajwa. Nisiwahi kusikia umejihusisha na chochote kinachomuhusu Tunda. Hakikisha hati ya nyumba ya Tunda..” “Ni ya Net.” Akakanusha Ritha akionekana ameumia sana.

“Usirudie kunikatisha ninapoongea Ritha.” Kimya. “Kama nilivyosema. Hakikisha unatoa mkono wako kwenye hati ya nyumba ya Tunda huko wizara ya aridhi. Namaanisha, wewe Ritha, uhakikishe hiyo hati inakamilika na  inamfikia Logan kwa haraka ikiwa na jina kamili la Tunda, wala si kampuni ya Cote.” Kimya.

“Na siku nyingine ninaporudi hapa nchini kwa ajili ya upuuzi mwingine wowote utakao fanya, mazungumzo yetu yatakuwa tofauti na haitakuwa hapa. Na ujue wazi, safari hii ni nyumba imeenda kwa Tunda. Safari nyingine kila kitu ambacho unadhani ni chako kwa jasho letu, vitakuwa vya Tunda. Usinijaribu.” Akatoka yule bibi, akafuata Logan, akaja yule mlinzi. Wakamuacha Ritha pale ofisini kwake.

Net arudi nchini Tanzania kwa ajili ya Tunda.

B

aada ya kushugulikia na  yeye vitu ambavyo alijua vingehitajika nchini Tanzania, Net alirudi nchini ukiwa umeshapita mwezi na siku kadhaa tokea aondoke nchini katikati ya fungate. Alirudi akiwa amejiandaa na kila kitu ambacho alijua kitahitajika kumtoa Tunda matatizoni. Logan alimkabidhi yeye kila kitu alichokuwa amekipata kutoka kwa mama yake. Net alitua nchini akapewa Visa kama mgeni tu anayekuja kutembea nchini Tanzania. Aligongewa Visa ya siku 90. Akajua kwa muda huo kabla hajaaribu Visa yake, atakuwa amemsaidia Tunda.

Alichofanya, nikumtafuta wakili yuleyule aliyekuwa akifahamiana na Tunda, aliyekuwa akishugulikia kesi ya baba yake. Alimweleza kisa kizima, akamshauri vizuri tu. Net akarudi kwenye ofisi za usajili wa ndoa, akakutana na kijana muungwana tu mapokezi. Net hakuonyesha uso wa tahadhari au wasiwasi. Alimweleza alifunga ndoa na Tunda, lakini hakuwa na uhakika sana na nyaraka walizosaidiwa kuzikusanya na mwanasheria wao.

Yule muhusika bila hila akalitafuta faili lao, akaliona. Na kweli halikuwa na baadhi ya nyaraka muhimu. Bila shida, akapokea nyaraka alizokuwa nazo Net. Yeye mwenyewe akaanza kumpa pongezi Net kukamilisha faili lake na madhara ya kutokuwa na nyaraka zote. Akamwambia kwa kufanya vile, amekamilisha faili lake na Tunda, na ndoa yao inafahamika kimataifa. Wakapeana mikono, Net akatoka pale asiamini kuwa ndio amefanikisha kirahisi vile bila hongo wala shida yeyote.

Alikwenda tena ofisi za aridhi kufuatilia hati ya nyumba. Alikuta inashugulikiwa. Akajua mama yake alitoa mkono wake hapo. Akaambiwa baada ya majuma mawili itakuwa tayari. Hilo nalo likawa limekaa sawa. Likabakia swala la kosa la uchangudoa tu ambalo yule wakili alimwambia kama Bethy na mama yake hawakuwa wameficha ushahidi mwingine, ni kesi ambayo watashinda bila shida.

Net kwa kina mama Penny Tena.

N

et akaamua kwenda kuwaona kina mama Penny na mchungaji ili kuwaeleza kinachoendelea na pengine watakuwa na chakuzungumza. Alikwenda nyumbani kwao ilikuwa mida ya jioni. Na mchungaji alikuwepo. Hakuna aliyemchangamkia. Net aliliona hilo, lakini akajikaza.

“Mlifanikiwa kwenda kumtembelea gerezani?” Akauliza Net. “Tunda hataki kuonana na yeyote yule, Net. Tutakupa barua alizotuandikia siku ya pili tulipokwenda kumuona. Kwa maana siku ya kwanza alikubali kutoka. Alilia tu, mwishowe akaondoka. Siku ya pili tulipokwenda na kuomba aitwe, yule askari magereza akatoka na hiyo barua. Tuliporudi baada ya siku mbili, hakutoka na wala hakutuma ujumbe.” Akaongea mama Penny.

“Mimi binafsi nimerudi pale zaidi ya mara 10. Baba Penny ametoka huko jumamosi hii iliyopita, lakini hakumuona Tunda. Hataki kuonana na mtu yeyote.” Mama penny akamalizia hapo na kusimama kwenda kufuata barua alizokuwa amewaandikia Tunda.

Alirudi akamkuta Net amejiinamia kwenye kochi. Akamkabidhi. Net akaanza kuzisoma. Muda ukazidi kwenda hamalizi na wala habadili kurasa, yupo kwenye ukurasa ule ule wa kwanza wakati zipo kurasa kama tano! Mpaka akamtia wasiwasi mama Penny. “Vipi?” “Inabidi kutumia akili ili kusoma na kuelewa. Naunganisha maneno. Sijui kusoma kiswahili vizuri.” “Oooh! Lete nikusomee.”

Mama Penny akachukua zile barua na kuanza kumsomea kuanzia mwanzo kwa sauti ili asikie vizuri na kuelewa. Mpaka anafika mwisho, Net alikuwa mwekundu kama nyanya. Na kuna sehemu mama Penny alisoma kilawama kabisa. Kama anaye msisitizia Net kuwa yeye ndiye amesababisha kila kitu.

“Nitakwenda kujaribu kumuona kesho.” “Sawa. Kama itasaidia.” Akaitikia mama Penny. Kimya. Kwa hakika Net alijutia. Akajua kwa asilimia zote yeye ndio amemuingiza Tunda kwenye matatizo na hata mchungaji na mkewe wanamlaumu. Mapokezi aliyopewa hayakuwa kama zamani.

“Nimejitahidi kurekebisha mambo kadhaa.” Net akavunja ukimya. Kimya. “Bibi yangu alirudi, akahakikisha anaweka mambo sawa.” Kimya. “Maswala ya nyumba na ndoa yapo sawa kwa sasa. Kwa hiyo kisheria Tunda ni mke wangu.” “Inasaidia nini yeye sasa hivi yupo jela?” Mchungaji aliyekuwa kimya muda wote kwa mara ya kwanza akamuuliza.

“Eti Net?” Net akabaki kimya. “Unakumbuka siku ya harusi nilikwambia rekebisha mambo ya familia yako kwanza ndipo umuoe Tunda? Unaona ulipomfikisha Tunda lakini?” “Sikukusudia baba Penny.” Net akajaribu kujitetea.

“Wewe ulijua kabisa hatari iliyopo mbele. Ukaamua kumtoa muhanga mwenzio! Umemuingiza kwenye matatizo makubwa, hata hatujui jinsi yakumtoa! Wewe sasa hivi unalala pazuri, mwenzio yupo mahabusu! Halafu unarudi na stori ya nyumba na ndoa!? Itamsaidia nini Tunda?” “Angalau kupunguza hayo makosa mawili.” “Hivi unajua kuwa sasa hivi hawezi kutolewa dhamana sababu ya kifo cha Gabriel?” Kimya.

“Mimi najiuliza kulikuwa na haraka gani Net!? Ni nini ulikuwa ukikimbilia nakushindwa kusubiri?” Kwa kuwa Net alijua wamekasirika. Akaamua asijibu kitu akae tu kimya. Mama Penny akampokea mumewe kulaumu. “Tunda alifika pazuri sana. Lakini wewe na familia yako mmemuharibia kila kitu! Unafikiri kwa kashfa hiyo aliyonayo, hata akija kutolewa jela, nani atampa yeye kazi?”

“Ndugu wa Bethy ndio wamechachamaa, wanataka Tunda ahukumiwe wala si Bethy. Wanasema Tunda ndiye amesababisha kifo cha Gabriel wala sio mtoto wao. Wanasema Tunda ameingilia ndoa yao, yeye ndio amesababisha kutoelewana kati ya Bethy na marehemu Gabriel. Wanasema ndoa yao ilikuwa na amani kabla ya Tunda. Sasa kwa namna hiyo Tunda hawezi kutolewa kwa usalama wake.” Net alibaki kimya.

“Mbaya zaidi, alichotumia akili mama yako. Amekwenda polisi kujisalimisha. Tena akishangaa ni kwa nini Bethy anamtaja yeye. Akajitoa kwenye vyombo vya habari! Tena akitumia akili sana. Hakumtaja kwa ubaya Tunda wala maswala ya Bethy na Gabriel. Alichojieleza ni kuwa Gabriel na Bethy ni kama watoto wake. Walikuwa karibu sana. Alipoulizwa maswala ya mahusiano kati ya Gabriel na Tunda, akatumia maneno ya ujanja ujanja, akajitoa na hakutaka kabisa kuzungumzii maswala hayo. Ila akajiweka katikati kwa kusema kuwa kwenye mahusiano ya ndoa, huwa kuna matatizo. Akajieleza hapo ili asiharibu kwa yeyote yule.” Mama Penny akaendelea kwa jazba.

“Alipoulizwa ni kwa nini hakuwa akionekana wakati anatafutwa. Akajitetea kuwa yeye ni mfanya biashara, alikuwa kwenye safari za kikazi. Hakuwa akijua anatafutwa na wala hana sababu yakujificha. Na amejitetea kuwa hata safari zake za nje ya nchi ataahirisha ili kama atahitajika kwa kusaidia polisi, awepo. Akaji.. ” “Na mimi nilitumiwa hiyo video yake ya utetezi, mama Penny.” Net akamkatisha, maana aliona anamuumiza tu.

“Ninachotaka kukwambia Net, nyinyi maisha yenu yanaendelea kama kawaida. Wakati ya Tunda yamesimama na mmeyaharibu kabisa. Tunda alikuamini wewe tokea mwanzo. Akijua utamuongoza vizuri. Matokeo yake ukijua kabisa maisha machafu aliyoishi, eti unampeleka akakiri mbele za watu ambao hamuwajui uwezo wao wa kiroho!” “Wale walikuwa wazee wakanisa.” Net akajaribu kutetea tena.

“Sasa mbona walikuwa ni wateja wa Tunda? Tena ukishajua kabisa hao wazee wenu wa hilo kanisa lenu sio waaminifu hata kidogo, bado ukamtaka Tunda akiri mambo yake mbele ya watu! Kulikuwa na umuhimu gani wakufanya hivyo? Ilikuwa ili iweje!? Ayaseme mabaya ya zamani mbele ya watu ili iweje Net!?” Kimya.

“Kwanza ni utaratibu gani nyinyi mnautumia kwenye hilo kanisa lenu? Eti watu wanasimama mbele ya watu na kuanza kutaja dhambi zao!” Akashangaa mama Penny. “Halafu watu wenyewe ndio hao kina Gabriel, Bethy, mama yako na hao wazee wakanisa wanaokwenda kwa machangu? Kweli Net!?” Baba Penny akaongeza kwa mshangao.

“Wakati huo nilikuwa sijui kama…” “Subiri kwanza Net. Usiniudhi zaidi. Wewe kabla ya kumpeleka Tunda kutubu mbele ya hao wazee wenu, hukujua kama Gabriel alitembea na Tunda?” “Nilijua mama Penny. Lakini..” “Lakini nini Net? Gabriel ambaye ndiye alikuwa na mfano wa ndoa yakuigwa hapo kanisani kwenu. Na yeye alikuwa kiongozi wenu, ukajua alikuwa akizini. Kwenye kanisa hilo hilo ambalo lilifunika dhambi yake, watu wasijue, ndipo hapo hapo ukampeleka Tunda! Ulijuaje kama mchungaji huyo huyo aliyeweza kuficha dhambi ya Gabriel ili asiumize washirika, hajaficha dhambi ya viongozi wengine uliowapelekea Tunda?” Net akainama.

“Umeharibu maisha ya Tunda, Net. Iwe kwa kutokujua au….” “Alijua baba Penny. Wala usimfiche. Mwambie tu ukweli. Ameharibu maisha ya Tunda kwa haraka zake na kutokufikiria. Mimi ni mkweli Net. Na sijui kumficha mtu. Hapo ulipo huna jinsi yakumsaidia tena Tunda. Umepunguza makosa mawili tu. Je, na la ukahaba? Dhambi aliyokuwa amesamehewa, mmeiweka mwangani!”

“Ushahidi wa hiyo pia bibi alihakikisha unafutwa.” “Unajuaje kwa upande wa Bethy?” “Sijui mama Penny. Sijui. Ila nakiri nilikosea. Naomba na nyinyi mnisamehe.” Net akasimama nakutoka.

Net kwa Tunda.

S

iku inayofuata, Net akaenda kujaribu bahati yake. Alifika mahabusu akajiandikisha kuwa yeye ni mume wa Tunda, akaomba kabisa aambiwe kuwa mumewe amefika kumuona. Akaingia sehemu ya kusubiria, akakaa hapo. Alikaa mpaka muda wakuona mahabusu ukawa unakaribia kuisha.

Akamsogelea mmoja wa askari magereza aliyekuwa akizunguka zunguka pale. “Mimi ni mume wake Tunda. Nimeomba kumuona.” Yule askari akamtizama kwa mshangao kidogo. “Mimi ninachojua ni kuwa Tunda hataki kuonana na yeyote yule. Nina uhakika ujumbe ameupata ila hataki kuonana na wewe. Hajataka kuonana na yeyote yule tokea afike hapa. Wala wewe si wakwanza.” Net akarudi kukaa mpaka muda ukaisha kabisa. Akaondoka.

Kesho yake akarudi tena. Safari hii akarudi na barua. Akajiandikisha, akaomba aitiwe Tunda na apewe hiyo barua. Akaenda sehemu ya kusubiri. Akakaa hapo mpaka muda ukaisha tena. Tunda hakutokea. Siku inayofuata akarudi na kadi. Akafanya kama jana yake. Akakaa hapo mpaka muda ukaisha tena, Tunda hakutokea. Akamuomba mmoja wa askari ampelekee Tunda ile kadi. Akaondoka.

Alifanya hivyo zaidi ya mara 7. Anafika hapo gereza la Keko, anajindikisha jina, nakusubiri bila mafanikio yeyote. Alikuwa akirudia rudia kuomba wale askari warudi kumwita Tunda, lakini hakuwa akipata majibu. Angalau mama Penny na mumewe walipata barua, lakini Net ilikuwa kimya. Hakupata ujumbe wowote ule. Akapumzika siku mbili, akarudia mchezo uleule bila mafanikio.

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

Tunda bado hajahukumiwa. Japokuwa makosa mengine yamefutwa, lakini bado yupo na kosa hilo la biashara ya ukahaba. Bado yupo rumande, na amekusudia kuangamia peke yake. Amekataa kumuhusisha yeyote yule. Nini kitatokea? Usikose muendelezo... 

CONVERSATION

0 Comments:

Post a Comment