Naomi Simulizi |+1 205 767 8163 |naomisimulizi@gmail.com NILIPOTEA! - SEHEMU YA 35. - Naomi Simulizi

NILIPOTEA! - SEHEMU YA 35.

 

N

et aliposhindwa kumuona Tunda, akahamisha nguvu kwa mwanasheria ili kumsaidia kumtoa.  Huhusu baba yake, alimwambia anakaribia kufunga kesi yake. Amebakisha kitu kidogo tu kukamilisha ushahidi, ili wafunge hiyo kesi. Kuhusu Tunda aliambiwa wasubiri kesi yake itajwe, ndipo watajua upande wa washitaki wake wamejiandaa vipi na wamtetee vipi kwenye hiyo kesi.

Net alisubiri majuma mengine mawili, akienda mahabusu ya keko bila kuchoka, mwishowe akapatwa dharula iliyomlazimu kurudi nchini Canada. Akaondoka huku akiomba yule wakili kuwasiliana naye chochote kitakachotokea na awe anapokea simu yake.

Kesi ya Tunda.

Z

ilikuwa zimekwisha isha siku 50 tokea Tunda akamatwe na kuwekwa rumande, wakati alipoambiwa anahitajika mahakamani. Alipewa taarifa hizo siku hiyo jioni, akaambiwa kesho yake asubuhi ndio alitakiwa mahakamani. Net alikuwa nchini Canada wakati kesi ya Tunda ikisomwa. Tunda akashangaa anafika pale kesi mbili hazitajwi! Anatajiwa kosa la biashara ya ngono tu. Tunda alikuwa ametulia pale mahakamani akisikiliza kwa makini tu, uso ameinamisha. Wengi walimchukua video na picha.

Kesi yake ikaanza. Mshitaki wake alikuwa akimwakilisha Bethy ambaye alikuwa ameshikiliwa jela kwa kosa la mauji ya mumewe. Yule wakili alitoa ushahidi kama ule uliokuwa umechanwa na mama Cote mbele ya bibi Cote. Sio kuwa mama Cote hakuwa akijua. Alifanya makusudi kutokuwaambia kina bibi Cote kuwa na Bethy anao ushahidi kama uleule. Bethy alitoa copy za mawasiliano yote ya Tunda ya zamani na kumbakizia Ritha za kwake, ambazo ndio zilizochanwa.

Walikuwepo ndugu za Bethy walionekana na jazba. Kesi ikaendelea. Wakabishana kwa hili na lile, mwishowe Tunda akatakiwa asimame kizimbani. Alishangaza kila mmoja pale alipokiri kufanya hilo kosa. Tunda alikiri bila kubisha nakumfunga mdomo wakili wake. Alieleza ndio ilikuwa njia yake yakuishi.

Picha zilizidi kupigwa kila mtu akiendelea kuchukua video kuhakikisha wanapata anachozungumza Tunda. “Hakuna ushahidi mtakaoletewa leo, ukaeleza ukweli wa maisha yangu. Naombeni mnivumilie mimi mwenyewe nieleze ukweli wote, ila kwa kifupi.” Tunda alianza taratibu tu.

 Alieleza historia yake kwa ufupi kuanzia mwanzo mpaka mwisho bila kuficha nakuacha ukimya mkubwa sana mahakamani hapo. Akarudia kukiri kosa nakuomba wamuhurumie ili kumpunguzia muda wakukaa mahakamani, kwa kuwa alishabadilisha maisha yake. Alieleza kabla yakushitakiwa alishaanza kuishi maisha yakujitegemea. Akifanya biashara halali.

“Mungu alinipa nafasi ya pili hapa duniani. Nilipata watu walionisaidia kugundua kipaji changu. Nikaingia kwenye kufanya biashara ya upambaji. Kwa elimu ndogo sana niliyokuwa nayo, niliweza kujiingizia kipato kwa biashara halali. Nilikuwa nimeajiri wafanyakazi wawili ambao nilikuwa nikiwalipa  kila mwisho wa mwezi, na vijana watatu ambao wao pia walikuwa vibarua wangu, nawalipa kwa kazi.”

“Niliweza kulipa kodi katika serikali yangu bila kuiba hata shilingi. Ushahidi wa kuonyesha nawalipa wafanyi kazi wangu na kulipa kodi zao, pia upo. Siibi kodi, au niseme siibii serikali yangu. Maisha yangu yamebadilika. Siishi kwa magendo. Naishi kihalali.”

“Najua nilikosa, na nimeumiza wengi. Sina jinsi yakutetea maafa niliyosababisha kwa maisha niliyoishi zamani. Nakiri nilikosa, naomba mnisamehe. Nipo tayari kutumikia adhabu yangu, lakini naomba mnipunguzie muda ili niweze kusaidia watu wanaopitia kwenye maisha kama niliyoishi mimi zamani.” Tunda akamaliza na kubaki kimya. Wakili wake akamwambia arudi kukaa.

Baada ya kushauriana hukumu ya Tunda ikatolewa ikawa ya mwaka mmoja. Siku 365. Na kwakuwa alishakaa jela siku 50, zikapunguzwa kutoka kwenye huo muda wake wa hukumu zikabaki siku 315. Na kwa kuwa mchana na usiku ni siku mbili, kwa jumla ni kama angekaa jela miezi sita. Ukipunguza siku alizokaa, ni kama alibakisha miezi 5 na siku 7 hivi. Alimwambia wakili wake ameridhika na hataki tena kesi. Akatolewa mahakamani na kuhamishiwa gereza la Segerea kama mfungwa sasa anayetumikia kifungo chake.

Yule mwanasheri aliwasiliana na Net, akamueleza kila kitu kilichotokea mahakamani na hukumu ya Tunda. Net alilia siku tatu mfululizo kama mgonjwa. Siku ya tatu Net akamtafuta tena yule wakili kwani alimkatia simu sababu yakulia. Alimuuliza kama wanaweza kukata rufaa, yule wakili akamwambia hadhani kama itawezekana.

“Kwa nini?”  Net akauliza. “Kwa sababu Tunda ni kama hakutaka utetezi juu ya kesi yake. Hata mimi alinishangaza. Alikiri kosa lake bila kubisha na yeye mwenyewe akaomba apunguziwe. Ni kama alipanga kuendesha kesi yake yeye mwenyewe. Nilijiandaa kumtetea, lakini yeye alifanya tofauti na tulivyokubaliana. Na baada ya pale nilipomwambia nitakata rufaa, aliniambia ameridhika na hukumu yake, hataki tena kesi. Sasa sidhani kama atabadili mawazo.” Net akanyamaza kwa muda.

“Nitajaribu kwenda kuzungumza naye kesho kama atakubali. Ikishindikana basi. Amebakisha kama miezi 5 na siku kadhaa. Atatoka tu.”  Akatulia kidogo. “Ila tu labda nikwambie ukweli. Ndugu wa upande wa Bethy bado walionekana wanahasira sana kwa Tunda. Sikutegemea kuwaona kwa wingi kiasi kile. Ila baada ya utetezi wake mwenyewe Tunda, ni kama kulitulia kidogo.” Yule wakili akaendelea kumueleza Net.

“Tunda alieleza maisha yake kuanzia mtoto anatolewa kwa bibi yake, maisha yake alivyokuwa akibakwa na baba yake wa kambo, nakufukuzwa kwa ndugu akiwa hana ujuzi wowote isipokuwa mapenzi ambayo ilimbidi kutumia ujuzi huo kuishi. Ilichukua muda mrefu sana kutoa hukumu ya Tunda. Wengine walisema asamehewe, wengine walisema hata faini ambayo alitakiwa atozwe asamehewe. Ila kwa jinsi nilivyoona, ni kama bado wanamshikilia kwa ajili ya tukio la Gabriel. Wangeweza hata kumuweka miaka miwili mpaka papoe kabisa kwa usalama. Naona hata kwa huo muda aliopewa, amehurumiwa.” Net akatulia kidogo.

“Unaweza kwenda kuzungumza naye ili kuona kama atakubali kupunguziwa muda?” Net akauliza kama anayemsihi aende tu. “Nitakwenda kisha nitakujulisha. Ila kitu alichosisitiza ni baba yake. Nilimwambia wewe na familia ya mchungaji wote mnafuatilia. Akanyamaza. Hakuzungumza tena.” Wakazungumza kidogo. Wakaagana.

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

Yule wakili alikwenda gereza la Segerea. Akaomba kuzungumza na Tunda akiwaambia wazi wamwambie ni wakili wake. Lakini Tunda hakutoka. Alikaa pale akisubiria mpaka akachoka. Na kwa kuwa alikuwa wakili aliruhusiwa bila masharti. Alipoona hatoki akaelewa kuwa amemkatalia. Alitoka pale, akampigia simu Net. Akampa habari zilizozidi kumuumiza. Akamwambia kwa upande wake amemuelewa kama na yeye anataka kwenda kuhakikisha anayomwambia na pengine kumuona Tunda, akampa siku ambazo wafungwa wanaruhusiwa kuonwa na muda.

Kisha akampigia mchungaji na mkewe. Na wao hawakuwepo mahakamani siku ya kesi ya Tunda ilipotajwa. Yule wakili wa Tunda akawaeleza kila kitu na kuwaambia maamuzi ya Tunda mwenyewe. Aliwatajia mwezi na tarehe ambayo anategemea kutolewa. Akawaambia kwa wakati ule atabakiwa na kesi ya baba yake tu, kama alivyoomba Tunda mwenyewe. Akawaambia kwa kuwa sasa Tunda amekuwa mfungwa, jinsi ya kutembelewa kumebadilika. Upo muda na siku maalumu kwa familia tu. Labda waende kama wachungaji au  matumishi wa Mungu. Akawatajia siku na muda. Akaagana nao.

Mama Cote{Ritha}.

H

ukumu ya Tunda ilipotolewa na yeye kukubali kosa lake bila kumpa nafasi wakili wake amtetee au kukaribisha watu wamtetee, ni kama aliwafunga wengi midomo. Pakatulia. Raha ya ugomvi ni kupata mtu wakugombana naye, lakini Tunda hakutaka kubisha. Alipopewa tu nafasi yakujitetea mbele ya wenye jazba, yeye akakubali kosa bila shida tena huku akisema yeye ndio anaoushahidi wote, wengine wanazo habari nusu nusu. Akieleza yeye mwenyewe na kukiri kosa, mwishowe akajitetea yeye mwenyewe.

Mama Cote alipoona kesi ya Tunda imeshatajwa. Pakawa kama pametulia. Ili asiaibike mjini akaharibu zaidi. Akamtumia Logan zile karatasi za kampuni ya Cote. Na kweli Bibi Cote akawa muungwana. Akasaini na kumuachia ile kampuni. Alipoona kila kitu kipo kwa jina lake, akaanza kuuza mali zote za ile kampuni kwenye makampuni ya kigeni yanayotengeneza barabara kama yeye.

Aliuza kwa bei ya hasara, lakini alikusudia kuuza kila kitu ilimradi tu aepukane na ile kampuni. Akafukuza kazi wafanyakazi wake wote. Tena kwa kuwalipa ili wasidaiane baadaye na kushitakiana.

Alijua wazi ingekuwa ngumu kuiendesha bila Net aliyekuwa akifanya biashara za masoko tena kwa kujituma sana. Hata hivyo alijua ameharibu jina lake mjini. Hakuna ambaye angemuamini tena. Wengi walimuona msaliti. Maana Bethy alizungumza ukweli wa kila kitu kilichokuwa kikiendelea kati yake, mumewe na mama Cote au Ritha, kasoro akakosa ushahidi tu.

Tayari akajua amejitengenezea maadui. Lazima aondoke nchini. Ikabaki swala la nyumba yake. Alijua ipo siku patatulia na patakuwa shwari hapo mjini. Hakutaka kuja kuwa kama mgeni au mtu anayeanza maisha nchini kwake. Akakusudia abakishe hiyo nyumba. Akatafuta kampuni ya kukodi nyumba yake bila mafanikio. Akatafuta mtu wakawaida ambaye angeishi hapo, kwa bei nafuu lakini mstaarabu ambaye angeweza kutunza nyumba yake vizuri. Pia akakosa. Akaishia kumuachia ndugu tu aishi hapo bure ila kwa sharti ya kutunza nyumba yake vizuri.

Wakati Tunda na Bethy wapo jela, Gabriel mchangani, mama Cote akahama nchi. Akarudi nchini Canada ambako alikuwa na Permanent residence. Hakuhamia mji wanaoishi kina Cote. Hakutaka kuwatafuta wala kuwaambia wanae alipo. Hata hivyo alijua kwa wakati huo wasingekuwa na hamu yakumuona. Aliondoka nchini na sanduku tu, ila akaunti yake ikiwa na pesa nzuri tu.

Alijua kwa hakika asingepata shida nchini Canada ambako alishaishi huko kwa zaidi ya miaka 15. Alisomea huko huko shahada ya uhandisi kisha akaongeza shahada ya pili ya mambo ya uongozi upande wa biashara akiwa ameolewa na baba yake Net.

Akafanya kazi kwa muda mrefu kwenye makampuni ya huko nchini. Na kwa kuwa alishakuwa na kampuni yake, ujasiri, uwezo wa kutawala na akili yakufikiria, Ritha alijua hatapata shida yeyote akienda kuendeleza maisha huko.

          Alitua nchini Canada, akaamua kuanza maisha yake kwenye mji ambao alijua hatakutana na watanzania wengi. Akatafuta Condo nzuri, ya kisasa akahamia hapo maisha yakaanza. Akapigia simu makampuni ambayo alishafanya nao kazi. Akauza CV yake mpya. Na uzoefu aliokuwa nao, baada ya mwezi, akapata kazi. Tena kwa mshahara mzuri sana.

Akawa ni mtu wakuamka asubuhi, kujitengeneza vizuri. Akili ikiwa imetulia. Hana wasiwasi wa kuharibika kitu kama ilivyokuwa kwenye kampuni yake. Kitengo chake kimoja tu alichokuwa amekabidhiwa, na kwa kuwa pia alikuwa na uwezo mzuri wa kikazi, Ritha maisha yakamwendea shari. Akawa anaishi maisha kama binti mdogo tu. Hana majukumu, wala mawasiliano na yeyote yule. Kazi na yeye mwenyewe. Maisha yakujificha na ubinafsi yakaendelea.

Net!

             Katika kipindi hicho Tunda yupo jela, Net alirudi kuajiriwa kwa bibi yake. Ungemuonea huruma. Japokuwa walikuwa wakiishi nyumba moja, lakini bibi yake alimkuta ofisini na kumuacha ofisini kila siku. Alifanya kazi hivyo, kuanzia jumatatu mpaka jumamosi. Kasoro siku za jumapili. Alikwenda kanisani na familia, na kurudi ofisini. Bibi yake alijua kinachoendelea, akaona ni heri hayo mawazo ayahamishie kazini kuliko kwengineko ambako angeharibikiwa. Aliishi na bibi yake na Maya kwenye nyumba hiyo waliolelewa watoto hao tokea wadogo.

Magazeti yaliandika kurudi kwake nchini bila mwanamke ambaye alichumbia nchini Tanzania. Watu wakahoji na kutaka mazungumzo na familia hiyo angalau kujulikane kulikoni. Lakini bibi Cote alikataa na hakutaka kabisa kuzungumzia hilo kwenye magazeti.

Hawakujua wapi habari zilivuja na kufikia magazeti na mitandao nchini huko, picha za Tunda akiwa mahakamani zikazagaa. Ndipo habari kuwa Tunda alifungwa zikaenea. Ziliandikwa habari zake zote kana kwamba ni magazeti ya nchini Tanzania. Net alijua wazi kuna ambaye ameshapokea pesa ili kuuza habari na picha za Tunda nchini hapo.

Usumbufu ukazidi kuongezeka kwenye familia hiyo wakimtaka bibi Cote aeleze kwa undani kama wakati anamkabidhi Tunda cheo chake nchini Tanzania, kama alijua ni kahaba. Na kwa Net, walitaka kujua pia wakati anamchumbia Tunda kama alijua kama ni kahaba.

Kwa uwezo mkubwa wa familia hiyo ya Cote, kifedha na utawala. Walijua wamemsusa tu Tunda huko nchini. Walijua wasingeshindwa kumtoa jela, kama wangetaka. Wakajua hata wao walichezewa na Tunda kama habari za kuwa Tunda aliwazunguka vijana hao wawili marafiki. Gabriel na Net. Wakajua na wao wanahusika kumfunga Tunda kama kumwadhibu kwa aliyoyafanya kwenye familia hiyo.

Net hakujua walipata wapi kisa cha Gabriel, lakini nacho kikatengenezewa mkasa wa uongo. Kuwa Tunda aliwazunguka wao wawili. Alikuwa na mahusiano na wote wawili na ndiye aliyesababisha kifo cha Gabriel. Hiyo nayo ikawa habari iliyouza sana magazeti na mitandao ya hapo nchini Canada. Picha za marehemu Gabriel siku ya kifo chake pia zikawekwa mitandaoni. Akishutumiwa kuwa Tunda ndiye aliyesababisha.

Zikaanza sasa kejeli kwa familia hiyo wakiwakejeli kuwa na wao wamewezwa na mweusi. Wengi walisema huo ndio mwisho wa ukoo huo. Kuondoka kwa Mzee Cote mwenyewe, ndio anguko lao. Ameacha familia hiyo kwenye mikono ya bibi huyo ambaye ni dhaifu na ataiteketeza hiyo familia kwa maamuzi yake dhaifu. Vyombo vya habari vikatangaza udhaifu wa bibi huyo kwa wajukuu zake. Kuwa huwapa watakacho bila kufikiria na ndiye amesababisha yote hayo.

Kashifa za waziwazi ziliendelea magazetini huku visa vya ukweli vilivyotengenezewa kashfa, uzalilishwaji vikiendelea magazetini. Bibi Cote alichafuliwa vilivyo. Akabezwa. Net naye hivyo hivyo. Lakini hapakuwa na kukanusha wala jibu kutoka kwa familia hiyo. Kimya.

Mabinti wa kizungu wakajua huo ndio wakati wakujisogeza kwa Net. Wapya na wazamani wakajaribu kumsaka Net kama kumpa pole na kutaka sasa afikirie nyumbani. Arudi kuoa nchini kwao. Walijisogeza mchana na usiku. Maua nyumbani na ofisini kwa Net, pamoja ni viujumbe havikukoma.

Kila binti aliandika lake na kujitongozesha kwa njia yake, ilimradi tu kutaka kufikia moyo wa kijana huyo milionea. Kilichomshangaza Net ni kutokusambaa kwa habari kuwa alifunga ndoa na Tunda. Ni picha zao tu za kuchumbiana ndizo zilizoenea. Lakini hapakuwa hata na fununu kuwa alishaoa. Akajiuliza hili na lile, akaamua anyamaze, bila kumjibu mtu chochote. Wala hakurudisha shukurani ya zawadi na maua. Kimya.

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

Lakini kila mwezi siku zakuona wafungwa, Net alirudi nchini Tanzania kujaribu kumtembelea Tunda gerezani. Alikuwa akitua nchini siku ya ijumaa. Jumamosi muda wakuona wafungwa ukifika saa sita kamili mchana, Net anakuwa amewasili gereza la Segerea. Na baadhi ya mahitaji ambayo anajua Tunda atahitaji huko gerezani. Atajiandikisha kama kawaida. Atakaa akimsubiria Tunda kama wageni wengine wanaosubiria wafungwa wao. Kuanzia saa 6 mchana mpaka saa 11jioni. Hataondoka mpaka anakuwa wa mwisho.

Kesho yake tena siku ya jumapili anarudi tena. Saa 2 asubuhi anakuwa ameshafika hapo. Atakaa mpaka saa 6 mchana. Atatoka na kwenda kukaa nje ya gereza mpaka tena saa 8 mchana hadi saa 10 jioni. Atafanya hivyo hivyo. Atajiandikisha tena. Ataomba aitiwe Tunda. Atakaa hapo mpaka mwisho saa 11 jioni, anaondoka. Jumatatu anageuza kurudi nchini Canada. Mpaka tena siku ya kumtembelea akifika hiyo weekend moja kwa mwezi. Anarudi tena na kufanya hivyo hivyo.

Net akutana tena na Mama Penny na Mumewe Gerezani Segerea.

N

et alifanya hivyo mwezi wa kwanza na wa pili pia. Hakukosa. Na hakuacha kumpelekea vitu ambavyo alijua angehitaji akiwa gerezani. Barua akieleza anachojisikia pia hazikukoma kila anapokwenda kumtembelea, pamoja na kadi nzuri. Wakati mwingine alipeleka na maua. Ilimradi kumtaka Tunda atoke. Alitamani kumuona, lakini Tunda hakutoka.

Mwezi huo wa pili wa Tunda kuwepo gerezani hapo Segerea, akafika jumamosi bila kuchelewa hata dakika moja. Akafanya kama kawaida. Akajiandikisha na kukaa mpaka jioni bila Tunda kutoka kumuona. Akarudi siku ya jumapili kwa mara nyingine tena, saa nane mchana, akakutana na mama Penny na mumewe. Na wao walifika hapo kumuona. Net alikuwa anahali mbaya, mpaka mama Penny aliyekuwa amemkasirikia, ilibidi kuzungumza naye tu.

“Sikujua kama upo nchini!” “Nilifika juzi, ijumaa. Huwa sikai. Nakuja tu hapa kwa Tunda na kuondoka.” “Umefanikiwa kumuona hata mara moja?” Mama Penny akamuuliza akimuhurumia. “Hapana.” Net akajibu kwa ufupi tu. “Pole Net. Nafikiri ameamua kutumikia muda wake.” Net hakujibu. Akatulia tu.

“Lakini baba yake alitoka majuma matatu yaliyopita. Alitoka mgonjwa, tumehakikisha ametibiwa. Naona anaendelea vizuri. Ameanza na biashara ya Uber wakati anasubiri kulipwa fidia.” “Mnaishi naye?” Net akauliza. “Alishahama. Alitafuta chumba Buguruni. Alitaka sehemu yake ambayo angalau hata watoto wake wakitaka kumuona, awe huru.” Net akanyamaza.

“Tunayo namba yake ya simu. Kama unataka, tunaweza kukupa.” Net akamtizama mama Penny, akainama kama anayefikiria. “Sidhani kama mimi ni mtu anayetamani kunisikia sasa hivi. Maadamu ametoka, basi. Acha nimpe nafasi.”

“Lakini yule Mzee anakusifia sana, Net. Hana shida na wewe. Wakati wote anatoa shukurani kwako. Jinsi ulivyomlipa yule mwanasheria na kumuhimiza ahakikishe anatoka. Anasema yule wakili alikuwa akimwambia vile unavyowahangaikia yeye na mwanae, bila kuchoka. Kumpigia simu wakili kufuatilia maendeleo yake na hiyo pesa uliyompa wakili ampe ili anunue gari ya biashara. Hasahau.” “Anasema anakushukuru kwa kuwa amepata pakuanzia.” Mchungaji akaongeza.

“Ndivyo Tunda angefanya mwenyewe kama angekuwepo. Alitaka kumpa pesa ya mtaji baba yake. Kwa hiyo nilichofanya mimi ni kile Tunda angefanya, sio mimi. Wazo la Uber alinipa yule wakili nilipomuuliza ni biashara gani anayofikiria mtu kama baba yake Tunda angeweza kufanya baada ya kutoka jela, ndipo akasema hiyo Uber kwa sasa mpaka atakapojiweka sawa na kupata pesa yake.” Net akaendelea taratibu.

“Anabiashara yake nyingine alituambia mimi na Tunda angefanya endapo atalipwa fidia bila matatizo. Kwa hiyo hamna kitu cha ajabu nimefanya. Ni kile ambacho angefanya Tunda. Sasa kwa kuwa mimi ndiye niliyemsababisha Tunda awepo jela, sikutaka pesa ndogo aliyoibakisha kwenye akiba zake, atoke, halafu ajikute hana kitu kabisa.” Wakamuhurumia Net. Nakujuta kwa nini walimlaumu kwa ukali kiasi kile.

“Bado nashauri umtafute baba yake uzungumze naye.” Mchungaji akasisitiza. “Nitamtafuta, lakini sio kwa sasa. Acha nimpe muda zaidi. Nimesababisha matatizo ambayo hata sijui nikimuona nitamwambia nini! Alitegemea akitoka, akutane na Tunda. Lakini yeye anatoka, halafu anakuja kujua mimi ndiye nimehusika kumfunga binti yake! Sidhani kama mimi ni mtu sahihi wakuonana naye. Nitamtafuta. Lakini sio sasa hivi.” Net aliongea kwa majuto, huku akisugua mikono yake taratibu akiwa amejiinamia.

Walikaa pale mpaka saa 11 jioni. Hakuna aliyemuongelesha tena mwenzake. Kila mmoja wao alikumbuka mazungumzo ya mwisho waliyokuwa nayo na Net alipowafuata nyumbani kwao. Net akabaki kimya tu akiangalia kila anayetoka na kuingia upande ule wa wafungwa, mwishowe muda ukaisha. Net akawaaga kuwa kesho yake anarudi kwao Canada. Akaondoka. Hawakujua anapolala wala usafiri anapata wapi. Ila walipotaka kumsadia lifti aliwaambia anao usafiri. Akaondoka.

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

Mwezi wa tatu tokea awepo gerezani Net alirudi tena kumuona. Akafanya vilevile. Akakaa sehemu yakusubiria na baadhi ya mahitaji yake. Akasubiria mpaka saa 11 jioni. Akamkabidhi mmoja wa magereza vile vitu vya Tunda, lakini akataka azungumze naye kidogo. “Samahani. Unakuwa unahakikisha Tunda anapata mizigo yake?” “Mara ya kwanza kama unakumbuka, ulinikabidhi mimi. Nilimfikishia. Mara ya pili ulimpa askari mwingine. Nilisikia wakizungumza na mwenzie kuwa alimpelekea.” “Anaendeleaje lakini?” Net akauliza.

“Hapa ni gerezani. Yupo anatumikia kifungo. Kwa hiyo ujue yupo kifungoni.” “Mzima?” Net akauliza tena. Lakini yule askari akasita kidogo. “Anaumwa?” Net akauliza tena akionyesha wasiwasi. “Kwa sasa naona anaendelea vizuri.” “Kwani alikuwa mgonjwa?” Net akaendelea kuuliza. “Kama nilivyokwambia. Yupo jela, anatumikia kosa lake. Kama kuna kitu ambacho najua atahitaji msaada, ningekwambia tu.” Net akabaki akifikiria. Alishabadilika rangi. Akajua kuwa alikuwa mgonjwa.

“Huwa wakiugua wanapewa matibabu mazuri?” Yule askari akabaki amemkodolea macho, Net akapata jibu lake. “Nitarudi tena kesho. Naomba umuombe aje anione.” “Huwa anapata ujumbe wako. Sasa hivi kila mtu anakufahamu hapa. Mpaka wafungwa wanaokuwa wanakuja kutembelewa wanakujua. Hata kama mimi au askari mwingine asingetaka kumwambia, wafungwa wenzake huwa wanamfikishia ujumbe. Kwa hiyo huwa anajua kama umefika.” Net akanyamaza. Yule askari akaondoka.

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

Kesho yake saa mbili kamili ya asubuhi, Net akawa wa kwanza pale. Akaandikisha jina lake, wakati anataka kuondoka ili kwenda kukaa asubiri, askari aliyekuwepo upande wa pili wa dirisha walipokuwa wakiandikisha majina, akampa barua. Haikuwa ndani ya bahasha. “Ni yako.” Net akaipokea. “Asante.” Net akashukuru. Akasogea pembeni, akaifungua ile barua.

Net!

Nashukuru sana kwa kuja kuniona. Nashukuru kwa mahitaji unayokuwa ukiniletea. Yananisaidia sana. Asante. Namshukuru Mungu kwa sasa tunaendelea vizuri. Naomba nikushukuru pia kwa kumsaidia baba. Kumtoa jela na kumpa mtaji.  Mungu akubariki.

Tunda.

Walimuona Net amesimama akifuta machozi. Aliirudia ile barua, akabaki amesimama palepale. Asijue akakae au aondoke. Mwishowe akaenda kukaa pale pale mpaka saa sita mchana. Muda ulipoisha akaondoka. Saa 8 mchana akarudi tena. Hapakuwa na barua wala ujumbe mwingine kutoka kwa Tunda.

Saa 9 akaja baba yake Tunda. Na yeye akafanya kama Net. Akajiandikisha na kwenda sehemu ya kusubiria. Hakuwa amemuona Net. Alikaa pembeni kidogo. Net alipomuona amekaa akasimama na kumfuata. Wakasalimiana. Yule mzee alijawa na shukurani kwa Net, tofauti na alivyotarajia Net mwenyewe.

“Umewahi kuonana na Tunda?” Net akamuuliza. “Hapana. Hata mara moja. Lakini nilipojua hataki kuonana na mimi, nilimletea barua kumueleza kuwa ulinisaidia kunitoa, na yule wakili anazo pesa ulizompa ili anikabidhi na kuhakikisha napata gari ndogo ya biashara. Basi. Hivi hapa nimekuja kujaribu na barua yangu mkononi. Akitoka sawa, asipotoka nataka nimwachie hii barua. Nilitaka kumtaarifu kuwa yule wakili amenisaidia kufuatilia, nimelipwa fidia, ila nafikiria kuhama hapa mjini.” “Kwa nini tena!?” Net akauliza kwa mshangao.

“Hapa mjini maisha magumu baba. Nisipokuwa makini, vijipesa hivi vidogo nilivyolipwa, vitapotea vyote kabla sijafanya kitu. Naona nirudi tu nyumbani Mara. Nikawekeze kwenye  uvuvi tu. Nikifanikiwa nitakuwa naleta huku samaki na dagaa.” “Mkeo na watoto!?” Baba Chale ambaye ni baba yake Tunda akajicheka.

“Mjini, heshima haiombwi!” Alijibu tu hivyo bila kufafanua zaidi. “Nitamuachia Tunda namba ya simu. Ili akitoka tuwasiliane. Najua amebakisha muda kidogo. Acha mimi nitangulie ili nimuwekee mazingira mazuri yakuchagua. Apate hata pakukimbilia akitoka hapa.” Akamwita askari mmoja aliyepita karibu yake.

“Naomba umkabidhi binti yangu Tunda, hii barua.” Yule askari akaipokea. “Naomba msisitize asome hii barua. Nimuhimu.” Net akashangaa kidogo ule ujumbe. “Kwani kuna uwezekano kuwa hasomi barua tunazomtumia!?”  Net akauliza kwa kushtuka kidogo. Walimtizama tu, bila kujibiwa. Baba yake Tunda akamuaga Net, yeye akaondoka. Net na yeye akakaa hapo mpaka muda ulipoisha, wakaambiwa waondoke. Kama kawaida yake, akawa wa mwisho. Akaondoka.

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

Mwezi wa 4 wa kuwepo kwake hapo gerezani, siku ya jumamosi iliisha bila kusikia anaitwa au anaambiwa Net amefika. Tunda akashangaa kimya. Hakuna aliyemwita jumamosi asubuhi wala jioni. Akashangaa iliisha kimya kimya. Mpaka akahisi maaskari wamechoka kumuita. Akamuuliza mmoja wa wafungwa, kama alimuona Net siku hiyo alipoenda kuonana na ndugu zake, kwa kuwa Net alikuwa mzungu, kila mtu alimfahamu, hafichiki, akamjibu tu, “Leo sijamuona mzungu wako.” Akampita Tunda. Tunda akaumia sana. Akajua kila mtu ameshachoka.

Alitegemea kufurahia kutofuatwa tena, lakini akajikuta akiumia.  Lakini jumapili asubuhi akasikia askari akimwita kuwa anamgeni, tena akamtania vile vile, ‘Mzungu wako’. Tunda akafurahia moyoni, japo hakwenda.

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

Mwezi wa 5 wa kuwa kwake kama mfungwa, na ndio ulikuwa mwezi wa mwisho, Tunda hakupata mgeni yeyote yule. Hata Net hakuonekana tena pale. “Wameshanisahau!” Aliwaza Tunda siku ya jumapili usiku, mwishoni mwa mwezi ambapo watu hutembelewa. Akaumia sana moyoni.

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

Alitakiwa kufungwa miezi 12. Yaani siku 365 ambazo ni siku 182 za magereza. Alishakaa rumande siku 50 kabla ya hukumu yake. Akaanza kuhesabu siku kana kwamba amesahau wakati alikuwa akihesabu kila siku. Kwa miezi hiyo 5 aliyokuwepo hapo gerezani, inamaana alikaa kama siku 152, kwa miezi yenye siku zaidi ya 31 na 28. Ukizidisha mara mbili kuwa mchana na usiku ni siku mbili. Jumla alishakaa kama mfungwa siku 304. Ukijumlisha zile siku za mahabusu 50. Alishakaa hapo siku 354. Akawa amebakiza siku 11 za kawaida, ambazo ni siku kama 6 na masaa kadhaa kwa magereza.

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

Akaanza kuwaza pakwenda baada ya siku hizo 6. Mchungaji na mkewe walikuwa wakijitahidi kuja kama watumishi wa Mungu kwa ajili ya ibada. Japokuwa wao hawakuwa wakija kama Net, lakini angalau walikuwa wakifika hapo angalau mara mbili kwa mwezi. Kwa upande wa dini, angeruhusiwa kuonana nao japo kwa wiki mara moja ili kufanya ibada. Lakini Tunda hakuwahi kuonana nao. Kwa mwezi huo wa tano, alisikia walifika mara moja tu. Hakuwasikia tena. Akazidi kuamini amebaki peke yake.

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

Usikose Muendelezo. Nini kitatokea kwa Tunda akitoka jela? Nani amebaki naye?

CONVERSATION

0 Comments:

Post a Comment