Naomi Simulizi |+1 205 767 8163 |naomisimulizi@gmail.com NILIPOTEA! - SEHEMU YA 36. - Naomi Simulizi

NILIPOTEA! - SEHEMU YA 36.

Tunda amaliza kifungo chake.

S

iku ya mwisho, alisikia jina lake likitajwa. Wafungwa wengine walikuwa wakitangaziwa tarehe zao za kurudi mahakamani, wengine kuambiwa ndio wamemaliza muda wao, ndipo na Tunda akawa amesikia jina lake. Alifuata taratibu zote zakuruhusiwa kutoka hapo jela. Wakati anataka kutoka, askari wa mapokezi akamwambia siku iliyopita ilikuwa jumapili. Akamwambia alipata mgeni ambaye alimwachia mzigo wake mapokezi kwa afande aliyekuwa zamu, akamwambia akiwa anatoka apewe. Tunda hakuamini.

Akakabidhiwa mkoba ambao ulifanana kabisa na wake aliokuwa ameuacha pamoja na vitu vyake vingine nyumbani kwa mama Penny. Akaupokea na kusogea pembeni. Alipoushika tu hata kabla hajafungua na kujua kuna nini ndani, ile harufu yake akajua ni mkoba wake. Ulinukia pafyumu yake. Akastaajabu! Ni mkoba aliopenda kusafiria safari za siku chache. Mkoba mzuri sana. Akafungua ndani kujua ni nini amemletea. Akakuta amemletea nguo yakuvaa wakati anatoka, chupi, sidiria na sendozi za chini kabisa. Akajikuta machozi yakimtoka.

Gari lake na vitu vyake vyote alimuachia mama Penny. Akajifuta machozi. Kwa kuwa alikuwa amebadilika umbile, alijua wazi hata hilo gauni aliloletewa hapo, lisinge muenea. Askari aliyehusika kumsainisha kabla yakutoka, ndiye aliyemtafutia gauni la mfungwa mwingine, ndilo ilibidi kulivaa ili kuweza kutoka pale gerezani.

Hakutaka hata kurudi tena ndani. Hapo hapo pembeni ya mapokezi, akatoa kandambili mbaya alizokuwa nazo mguuni, akavaa zile alizokuwa ameletewa na mama Penny. Vitu vyake vingine kama kadi na barua alizokuwa akiletewa na Net, na baba yake, akatumbukiza kwenye huo mkoba.

Akatoka kwa kujivuta taratibu mpaka nje. Akaanza kuangalia kulia na kushoto. Akashangaa kumuona Net, Mama Penny na mumewe, wanamsubiria pale nje. Tunda akabaki amesimama kama aliyeduwaa na mkoba wake mkononi. Nywele alikuwa amekata zipo chini kama mwanafunzi wa shule ya msingi.

Tunda huyu alitoka na mimba kubwa tu. Iliyoweza kuonekanika kwa wazi kabisa, sababu ya kukonda sana. Net alibaki amekodoa macho. Akawatizama kwa zamu, wote walikuwa wamepigwa na butwaa. Ilikuwa mchana, jua ni kali.

Akavuta pumzi na kuwasogelea palepale walipokuwa wakimtizama kama walioona kitu ambacho hawakukitegemea. Akafika mpaka pale walipokuwa wamesimama. “Pole kwa matatizo Tunda. Pole sana.” Mchungaji yeye akajikaza. Tunda alitoa tabasamu lakichovu. Akamgeukia mama Penny. Akamuona anatokwa na machozi. Akamgeukia Net bado alikuwa ameduwaa.

“Nimechoka, nataka nikalale.” Tunda aliongea hivyo huku akimtizama mama Penny. “Twende nyumbani.” Mama Penny akajibu huku akifuta machozi. “Pole Tunda.” Mchungaji akarudia tena kutoa pole kama asiyejua ni nini aongee tena. “Asante.” Tunda akajibu na tabasamu. Hakika alionekana amechoka. Midomo ilimkauka, amekonda kama kijiti kasoro hapo tumboni.

Akamsogelea Net. “Nashukuru kwa kuja.” “Unaendeleaje?”  Net akauliza. “Vizuri. Ni uchovu tu. Nataka nikalale.” Net akabaki akimtizama. Tunda akainama kwa muda kama wasiojua chakuongea tena. Amshike mkono au amkumbatie! Aombe msamaha kwanza! Net akabaki ametulia tu.

Kwa kuwa alilijua gari la mchungaji, akalisogelea na kuwaacha wao bado wamesimama. Akasikia likitoa mlio kama limeshafunguliwa. Akafungua mlango wa nyuma, akapanda na kukaa hapo na mkoba wake. Ndipo akaona mama Penny na mumewe nao wanapanda. Net akaingia kwenye gari ingine ambayo hakuwa akiifahamu. Tunda alikuwa amechoka, hakuwa na uwezo hata wakujiuliza maswali. Akajiegemeza kwenye kiti, akalala. Kwa kuwa na kina mama Penny walikuwa wakiishi hapo hapo Tabata, hawakuchukua muda mrefu. Tunda akaamshwa kuwa wamefika.

“Nguo zangu bado zipo kule kule stoo?” Akamuuliza mama Penny wakati anashuka. Net naye akawa anaingia getini. “Ndiyo. Unataka nikutolee nini?” “Acha tu nikachambue. Nione kama nitapata chakuvaa. Nioge ndio nikalale.” Ilikuwa siku ya shule. Alimkuta msichana wa kazi. Akamsalimia Tunda wakati anaingia. Tunda alimuona vile anavyomsalimia kwa kumshangaa huku akimuhurumia. Tunda akacheka. “Sasa unashangaa nini na wewe?” Akamuuliza yule msichana wa kazi. “Mwenzio nakuhurumia!” Tunda akacheka na kupitiliza sehemu aliyojua kuna vitu vyake.

Wakati anachagua nguo zake, kutoka kwenye masanduku yake, mama Penny akaingia kule stoo. “Naomba nisaidie sanduku dogo kidogo.” Bila swali akaenda upande wa pili. Akahamisha vitu vilivyokuwepo kwenye sanduku fulani, akampa. Tunda akaanza kuweka vitu humo. “Gari yangu ina mafuta?” “Inayo. Tulikuwa tukiiwasha mara kwa mara. Kwa hiyo ipo sawa.” Akajibu mama Penny. Tunda akaweka vitu anavyovitaka. Akamgeukia mama Penny aliyekuwa ameduwaa akimshangaa.

“Nataka nioge.” “Ingia hapo chumbani kwa kina Penny. Nakuletea taulo sasa hivi. Ukioga, ule kabla hujalala.” Tunda akatoka bila kujibu. Alitoka akiburuza sanduku lake mpaka chumbani kwa kina Penny. Aliona kila mtu amepigwa na bumbuwazi kama wasiojua chakufanya.

Akaoga kwa muda mrefu sana huko bafuni. Alijisugua tena na tena akifurahia uhuru  aliolipia garama. “Sidaiwi tena na mtu.” Tunda aliendelea kufikiria wakati akiendelea kujikausha. Machozi ya hapa na pale yalikuwa yakimtoka. Lakini hakutaka kulia mbele za watu.

Akatoka pale bafuni, akavaa nguo zake. Kigauni kilichokuwa kimechanua chini. Kikamkaa vizuri tu. Angalau akawa na nafuu. Alichana nywele zake, akatoka. Moja kwa moja akaenda jikoni. “Umepika nini?” Akamuuliza yule msichana wa kazi. “Mlo wako unaolambaga vidole. Si unasikia harufu ya Pilau? Sasa nikakuongezea rosti la kuku, lazima utalamba sufuria leo.” Tunda akampa tabasamu lakini akabaki amesimama pale kama anayefikiria.

“Njoo ukae hapa sebleni, atakuletea.” Mama Penny aliongea akiwa sebuleni. Tunda akawasogelea pale walipokuwa wamekaa. Mchungaji, Net na mama Penny.

“Naomba niwashukuru sana kwa kuwa mkija kunitembelea na kuja kunichukua leo. Asanteni.” Kimya. “Nimechoka sana. Nimekuwa nikiugua ugua sana nilipokuwa huko. Hapa natamani kulala tu. Nilale bila kuamshwa wala kelele. Angalau nimalize huu usingizi nilio nao. Natamani utulivu wa aina yake.” Kimya. Mama Penny alijua nyumba yake haiishi wageni na kuna kelele muda wote, na hilo Tunda anajua. Akajua ndio wanaagwa.

“Nashukuru kwa chakula, lakini sijisikii kabisa kula pilau. Naomba nikatafute chakula kingine huko njiani wakati naenda kupumzika. Huu usingizi utakapoisha, na akili ikirudi vizuri, nitawatafuta. Lakini kwa sasa, akili naona hata haifanyi kazi. Nilikuwa navaa huku nasinzia.” Kimya.

“Mama Penny naomba pochi yangu.” Akimaanisha na kadi zake za benki. Mama Penny akasimama kuingia chumbani kwake, akatoka. “Naamini kuna pesa humu.” “Zipo. Nilitumia mwanzoni tu, tena kidogo. Lakini naona Net alimaliza madeni yote ya mwanasheria. Mengine tutazungumza ukisha pumzika.” “Nakushukuru dada yangu. Asante.” Net alikuwa amebaki kimya akiwa ameinamisha kichwa chake.

“Net! Naomba nikuage hapo nje.” Net alinyanyua kichwa akageuka. Tunda alikuwa amemsimamia nyuma yake. Akasimama, Tunda akaenda kuchukua mzigo wake. Vile vitu alivyokuwa amevaa wakati anatoka jela, alikwenda kuvitupa. Akarudi jikoni. “Mimi sijisikii kula pilau.” Akamwambia msichana wa kazi wa mama Penny. “Nashukuru lakini. Ila sitakula pilau.” Wote walimuelewa kuwa ni ile hali ya ujauzito. Akatoka jikoni, akakuta Net alishatoka na ule mzigo wake, amesimama nje ya gari yake Tunda.

Baada ya miezi 6,

Net & Tunda Tena.

T

unda akamsogelea karibu. “Naomba nikuage nikapumzike. Nitakutafuta uchovu ukiisha.” “Lini?” “Sijui Net.” “Naomba basi nikusindikize.” “Nashukuru, lakini hapana. Nataka nikapumzike Net. Sitaki chochote kitokee kwenye hizi siku nitakazopumzika. Nimechoka. Sina nguvu ya kujitetea kwa yeyote yule. Acha nikakusanye tena nguvu yakupambana na haya maisha. Sasa hivi likitokea jambo lolote litakalonihitaji kufikiria, sitaweza.” “Mimi nitakuwa na wewe Tunda.” “Hapana Net. Mara ya mwisho tulikuwa wote, mimi niliishia jela.” Net akaumia sana.

“Tafadhali naomba nikapumzike. Nimechoka sana. Nikiendelea kusimama hapa, nitalemewa hata nitashindwa kuendesha. Ila naomba nikushukuru kwa kuja kunitembelea jela na kumsaidia baba. Asante sana.” “Asante kushukuru. Basi acha nikuendeshe mpaka huko unakotaka kwenda.” “Hapana Net. Nataka kuwa peke yangu kwa muda. Sitaki mtu yeyote ajue nilipo ili nisifuatwe na yeyote kwa lolote. Iwe jema au zuri. Naomba matatizo yangu yanifuate baada ya haya mapumziko mafupi ninayotaka kujipa. Tafadhali Net.” “Sawa. Basi naomba nikupe namba yangu ya simu ili uje unitafute.” “Sawa.” Tunda akafungua pochi yake.

          Wazi alionekana anatetemeka. Net hakujua kama ni njaa, au ugonjwa. “Mara ya mwisho kula ilikuwa lini?” “Asubuhi. Nilikunywa uji. Njaa ilikuwa ikiniuma sana.” Akamtolea kalamu na kijitabu kidogo ndani ya pochi yake. “Naomba uandike hapa.” Net akaandika.

“Unafikiri utakuja kunitafuta tena?” Net akauliza kinyonge. Tunda alikuwa anajisugua Tumbo. “Nitakutafuta Net. Najua inabidi tuzungumze. Nakuahidi nitakutafuta. Acha nikapumzike.” Net alimuhurumia Tunda, akatamani ingekuwa tofauti.

“Ulikuwa ukisoma barua zangu na kadi?” “Hapana.” Tunda akajibu bila kudanganya. “Lakini ninazo. Nimetunza. Nitakuja kusoma.” Net akabaki akimtizama. “Sijatupa hata moja, Net. Ninazo zote. Lakini sikuwa tayari kusoma.” “Pole sana.” Tunda akatoa tabasamu la uchovu. “Nikienda kulala, nitapoa.” Net akaonekana anatamani kama aondoke naye, lakini Tunda alishajieleza. Kulazimisha ni kutokuwa mstaarabu. Maana ni kweli chochote chaweza tokea.

Alibisha mwanzoni, Tunda akaishia kuwekwa jela. Akaona safari hii awe mpole tu, amsikilize. “Naomba usisahau kula.” Akaongeza Net. “Nitafanya hivyo. Maana nikianza kuumwa na njaa, nasikia mpaka kichwa kinauma! Lazima nile.” Tunda akampita, akafungua gari yake. Ilikuwa safi. Akajua waliisafisha makusudi wakijua anatoka siku hiyo. Net akamwingizia mzigo wake nyuma ya gari, akafunga.

“Nakusubiri Tunda.” “Naomba usisubiri Net. Nikipata nafasi, nitakutafuta.” Net akakunja uso. “Mbona kama uliniambia utanitafuta?” “Sijui ni lini. Hali yangu kama unavyoniona. Nina uchovu na usingizi wa miezi. Nahitaji kuwa sawa kiafya na kiakili. Sijui hayo yote yanakamilika lini!” “Tunda please! Nimekuomba msamaha! Ni vile hukusoma barua zangu.” “Sina lawama na wewe Net. Naomba uniamini na wala usijilaumu. Nilikuwa jela kwa makosa yangu.” “Lakini mimi nimesababisha?” Tunda akakunja uso.

“Kivipi tena!?” “Mimi ndiye niliyekupeleka kanisani. Isingekuwa mimi usingekuwa jela.” Tunda akashangaa sana. “Kumbe ndio maana ulikuwa ukija jela sababu yakujilaumu!?” “Hapana Tunda. Sio sababu hiyo.” “Naomba uniamini hivyo ulivyoongea, wala mimi sijawahi kufikiria huko Net. Na ndio maana sikutaka kuonana na yeyote wala kusoma ujumbe wa yeyote ili kutumikia kifungo changu nikiwa na mtazamo wangu tu. Mimi nimeamini Mungu ameruhusu yaliyonipata, yanipate. Kama angetaka kuzuia, hakuna ambaye angenifunga Net. Sasa ni kwa nini, mimi sijui! Tafadhali acha kujilaumu kabisa. Naomba nikalale, nitakutafuta wakati mwingine.”

“Naomba usinisahau Tunda. Jua nakusubiri.” “Naomba usinisubiri Net. Tafadhali. Endelea tu na maisha yako.” “Mimi huwa sijui kuahidi na kubadilika Tunda. Sijui ndio mnafanyaje! Unamuapia mtu hiki, kesho unafuta kabisa kiapo chako! Mimi siwezi. Sikujaliwa huo moyo au huo uwezo. Ninapokuahidi jambo, nakuwa nalisimamia.” Tunda akainama. Akajua anakumbushia kiapo chao cha ndoa. “Lakini si tulisha achana?!” Tunda akajiuliza. Net akaondoka pale dirishani kwenye mlango wa dereva, Tunda akaondoa gari bila kuongeza neno.

Baada yakutoka jela.

A

litafuta hoteli ambayo hata mama Penny hakuwa akiifahamu. Alikwenda mikocheni B. Ilikuwa ni hoteli aliyolala na mteja wake wa kwanza kabisa, Sadiki. Natangia Sadiki afariki, na kurudi kuchukua mizigo yake pale, hakurudi tena. Ndio siku hiyo akarudi. Alipenda ule utulivu wa pale.

Wakati akisubiria funguo zake za chumba, akaomba kuongea na mtu wa jikoni. Akamuagiza chupa nzima ya chai ya rangi na mkate mkavu. “Basi?!” Yule muhudumu akauliza kwa kushangaa. “Hivyo tu. Niletee bila kuchelewa. Ila chai isiwe na kiungo chochote ila sukari tu. Iwe ya moto. Na mkate usipake chochote. Usichelewe tafadhali.” Yule muhudumu akarudi jikoni.

Wakati Tunda anafungua mlango wa chumbani kwake, chakula nacho kikaja. Akashangaa. “Kweli umefanya haraka!” “Tayari nilikuwa na maji ya moto. Nilichofanya nikuweka tu majani na sukari. Mikate ipo.” Tunda akacheka. “Basi na asubuhi ufanye hivyo hivyo.” Akafungua mlango. Yule muhudumu akamwingizia chakula chake ndani. Alikaa chini kabisa sakafuni, akaanza kula. Alikula ule mkate karibia robo tatu na vikombe viwili vya hiyo chai ya rangi. Kisha akatoa nguo zote, akajitupa kitandani.

Alishawapigia simu mapokezi kuwa wasimpigie simu, wasiruhusu mtu chumbani kwake. Iwe usafi au kuna swali lolote. Akataka wamuache kabisa, yeye ndio atakuwa akiwapigia. Alilala kuanzia muda amejitupa hapo kitandani mpaka usiku. Akala tena ule mkate uliobakiza na chai bado ilikuwa moto. Akarudi kulala.

Siku inayofuata akaamka na homa kali. Akapuuza akijua ni uchovu tu. Akaenda kununua dawa zakupunguza maumivu akaanza kuzinywa. Asubuhi mchana na jioni. Siku ya tatu homa ikazidi kuwa juu.

Akaamua kwenda hospitali ya karibu na pale Mikocheni, TMJ. Muda wake wakumuona daktari ulipofika akaingia. Alimueleza hali anayojisikia. Akaandikiwa vipimo. Akapimwa akakutwa na UTI. Akarudi chumba cha daktari, kutokana na ujauzito wake, akaandikiwa dawa ambazo alitakiwa kutumia siku 7.

Akarudi hotelini akiwa na zile dawa. Akamkumbuka Net. Akaamua kuwasha moja ya simu zake, akamtumia ujumbe. ‘Net! Nimetoka hospitalini. Afya imekorofisha tena kidogo. Lakini sio tatizo kubwa sana. Nimepewa dawa zakutumia siku 7. Naweza kuwa nalala tu, nikashindwa kuwasiliana, msiwe na wasiwasi mjue ni dawa. Asante.’ Akamtumia ujumbe huohuo mama Penny, akazima simu.

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

Alijiuguza hapo hotelini akinywa dawa, kulala na kula. Na chakula chake ni kilekile. Chai ya rangi na mkate mkavu. Akibadili ni kipande cha limao kidogo, kwenye chai. Basi. Akaendelea kumeza dawa bila kukosa mpaka akamaliza. Ni kweli aliona kuna utofauti kwenye mwili wake. Tayari zilikuwa zimeisha siku 10 tokea atoke jela.

Akapumzika tena siku mbili mbele, siku ya tatu yake akaamka akiwa na nguvu. Akaamua kwenda kutengeneza nywele. Kama kawaida ya Tunda, kujipenda. Alitumia siku nzima kutengeneza nywele na kucha. Angalau alirudi hotelini akiwa Tunda wa zamani. Kasoro kukonda na ujauzito.

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

Alipokuwa akitengenezwa huko saluni, hamu ya mkate na chai ya rangi ikampata. Alikuwa anatamani atoke, akale kwanza ndipo arudi wammalizie, lakini akaona avumilie tu. Kitu chakwanza alichofanya baada ya kurudi hotelini ni kuelekea jikoni. Akaomba wampe chakula chake kwa haraka.

Na kweli, bila kuchelewa wakampa. Walishamzoea na walijua lazima ale hivyo hivyo asubuhi na jioni. Akarudi na chakula chake chumbani. Akaanza kula kama mwenye njaa ya mwaka mzima. Aliposhiba akaenda kujilaza kitandani. Akaamua kumpigia simu mama Penny. 

“Vipi wewe!? Mbona unanitia wasiwasi?” “Sasa hivi naendelea vizuri. Nimekupigia kukuomba kazi. Kama una sehemu zakupamba kesho, naomba nikufuate, nitengeneze pesa kidogo.” Mama Penny akatulia kidogo.

“Mama Penny?” “Sawa. Lakini umejaribu kumtafuta Net? Mwenzio anawasiwasi Tunda. Yule kijana atachanganyikiwa!” “Mbona nilimwambia naendelea vizuri asiwe na wasiwasi?” “Hapana Tunda. Naomba uzungumze naye. Yupo kama mwehu!” “Basi nitampigia.” Akamuelekeza ni wapi pakwenda kesho yake asubuhi kufanya kazi, wakaagana.

Akategesha alarm ya kumuamsha asubuhi ili asichelewe. Ile amemaliza tu kutegesha alarm, Tunda alikuja kuamshwa na kelele za alarm kuwa imeshakuwa asubuhi. Hakuamini akahisi alikosea kutegesha saa. Akaangalia muda, akakuta pameshakuchwa. Alilala vile vile na nguo zake alizokuwa ametoka nazo saluni. Pale pale alipokuwa amejiegemeza kitandani.

Alitamani kama asiende alipokuwa amekubaliana na mama Penny, lakini akaona asiahirishe. Aliingia kuoga, akabadili nguo. Akatoka kwenda mapokezi kuomba wambadilishie mashuka. Tunda kwa asili alikuwa msafi sana kama mama yake. Kitendo cha kulala kwenye kitanda alichokuwa amevaa nguo alizokaa nazo saluni, akawa ameshakichukia chumba chake. Akatoka kwenda kufanya kazi.

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

Alifika ilikuwa imeshatimu saa mbili. Ndio na mama Penny na vijana wake nao walikuwa wameingia. Hawakupishana sana. Vijana wakashusha mizigo, kazi ikaanza. Alijua hata wale vijana wanamshangaa. Lakini hakujali. “Umependeza Tunda!” Mama Penny akamsifia. Akatoa tu tabasamu bila kujibu kitu. Akaendelea na kazi.

Hazikupita hata dakika 20, Net naye akaingia hapo ukumbini. Alipomuona tu, akastuka sana. Akasimama wima. Akaweka kila kitu chini, walikuwa wanapamba jukwaa la maharusi, yeye na mama Penny wakati wale vijana wawili wakitengeneza nguzo. Akashuka pale jukwaani akamfuata.

“Za asubuhi?” Tunda akaanza. “Nzuri. Vipi na nyinyi?” Akimaanisha yeye na mtoto. “Tunaendelea vizuri. Nilimaliza dawa. Naona na homa imeshuka.” “Ilikuwa ni nini?” Net akauliza taratibu, kwa kujali.

Infection ya mkojo. UTI. Iliniletea homa kali, ndipo nikaenda hospitalini.” Net akaonekana kuumia. Akatamani aongee kitu, Tunda akamuona anasita. “Pole sana.” Mwishoe akaona atoe tu pole. “Asante. Jana nilitaka kukupigia, lakini nikapitiwa na usingizi. Nimeamka asubuhi hii nakuja kazini. Lakini nilipanga kukupigia leo.” “Hamna neno. Nimefurahi kama unaendelea vizuri. Umeangalia na afya ya mtoto?” Tunda akavuta pumzi kwa nguvu.

Akajiangalia tumbo na kujishika. “Sijaanza kliniki bado. Nilitoka nikiwa naumwa. Nikaona nitibiwe mimi kwanza.” “Pole sana Tunda.” “Asante. Lakini sasa hivi nipo sawa. Hata mtoto mwenyewe yupo sawa.” Akafikiria kidogo. “Nafikiri.” “Mbona umesita?” Tunda akatoa tabasamu kidogo. “Kwa kuwa sina uhakika. Ila alikuwa akicheza muda sio mrefu. Nafikiri yupo sawa.” “Naomba na mimi nimsalimie.” Tunda akawa hajaelewa. “Ni sawa?” Tunda akatingisha kichwa kukubali akiwa hajui salamu hiyo kwa mtoto tumboni inakuaje!

Net akapiga goti akashika tumbo la Tunda. “Hey baby! Ni mimi dad.” Akabusu tumbo la Tunda huku akilipapasa taratibu. “I love you so much. Nasikitika tumechelewa kufahamiana, lakini amini kuwa nakupenda sana. Wewe ni baraka iliyokuja kwenye maisha yetu tukiwa tunakuhitaji sana.” Kadiri alivyokuwa akimpapasa, taratibu yule mtoto akaanza kuzunguka na Tunda akaanza kupata faraja ya ajabu sana moyoni.

Akajikuta machozi yakimtoka. “Nimemsikia anageuka! Si ni kweli?” Net akanyanyua kichwa na kumtizama Tunda akiwa amehamasika usoni na cheko la furaha juu. Tunda akatingisha kichwa kukubali huku na yeye anacheka na kufuta machozi. Net akambusu tumbo.

Okay! Take it easy! Take it easy!” Net akamuongelesha mtoto wake huku akimbusu nakufurahia vile yule mtoto anavyocheza mpaka Tunda akamshangaa. Ametoka jela na mimba, hata hajamwambia kama ni yake, Net akajimilikisha! Ilimgusa sana Tunda. Kwake ilikuwa na maana kubwa.

Net akawa anajaribu kumtuliza mtoto wake tumboni huku akicheka na wengine wakijiiba kuangalia. “Usimsumbue mama. Kwa sasa, take it easy. Naamini tutapata tena muda wakati mwingine wakucheza. Nakupenda sanaaaa. Tutaongea tena hivi karibuni. Promise.” Akambusu tena na tena huyo mtoto aliyekuwepo ndani ya tumbo la Tunda kisha akasimama.

“Asante Tunda. Nilikuwa nasubiri huu wakati kwa hamu sana. Nakushukuru sana.” Tunda alijisikia vibaya. Hakujua kama hata yeye anajipunja. Tunda akatoa tabasamu tu huku akijikausha machozi. “Naona umerudi kazini kwa kasi zote!” “Nataka hela!” Tunda akajibu huku akicheka taratibu, na kuendelea kujifuta machozi.

“Twende na mimi nikasaidie, hata kusogeza maua.” “Huendi kazini?” “Hapana. Nilichukua likizo. Nipo likizo kwa jili yako Tunda.” Tunda akainama kama anayefikiria mbele ya Net. Akanyanyua uso, akakuta Net ametulia akimtizama. “Nitakutafuta Net.” “Bado nakusubiri.” Tunda akatoa tabasamu, akionekana hata yeye amefarijika. “Turudi kazini basi, tutafute pesa.” Net alizungumza huku akimshika mkono kurudi alipo mama Penny.

“Za asubuhi mama Penny?” “Nzuri tu. Naona umeamkia asubuhi asubuhi kwa mwanao?” Net akacheka. “Naona na yeye alikuwa na hamu na baba yake. Amenisalimia bwana!” Net alikuwa amebadilika gafla. Wazi alionekana amefurahi.

Mama Penny akacheka. “Naona umefurahi!” “Sana. Siku yangu imeanza na baraka.” Tunda alikuwa akiwasikiliza tu huku akicheka taratibu. Hata yeye alifurahia kupapaswa kwa upendo kwa kiasi kile. “Na mimi naomba kusaidia. Ni sawa?” Mama Penny akacheka. “Utajichosha Net. Wewe pumzika tu.” “Ndio nimeamka. Acha Tunda awe ananituma nimsogezee vitu.” Wote walijua anataka tu kuwa karibu na Tunda. Mama Penny akawaacha pale, yeye akasogea sehemu nyingine akaendelea kupamba.

“Niambie nikusaidie nini. Vyote vyakunyanyua ni kazi yangu mimi. Wewe nitume tu.” Mama Penny alimsikia Net akimwambia Tunda. “Asante.” Tunda akashukuru na tabasamu. Wakaangaliana kidogo na Net, kazi ikaanza tena.

Walisaidiana hapo. Ukumbi ulikuwa mkubwa sana na wa pesa nyingi. Kwa hiyo mama Penny hakutaka kuharibu. Mida ya saa nne asubuhi, mmoja wa mwanakamati, alifika hapo. Akaangalia na kutoa maelezo zaidi. Wakazungumza na mama Penny, Tunda na Net wakiendelea na kazi. Walitaka maua fresh kwa ukumbi mzima. Watu wamaua walikuwa wameshafika hapo mida ya saa tatu, wakazungumza na mama Penny, wakaendelea kuyapamba. Na yule mwanakamati alirudi hapo kuhakikisha kama hayo maua yamefika. Hakuna kitu kinaharibika.

Ilipofika saa saba mchana, Tunda alikuwa amechoka. Mgongo unamuuma. Net akamuona anaanza kujinyoosha mara kwa mara huku akikunja uso. Akamsogelea. “Simama, halafu shika hiyo nguzo na mikono miwili.” Tunda akamwangalia kidogo, kisha akafanya kama alivyoambiwa. Net akaanza kumsugua mgongoni na kumminya kiuno. “Kwa hapo chini kidogo ndio nasikia maumivu zaidi.” Net alikuwa amesimama nyuma yake. Akatumia vidole vyake gumba viwili kuminya sehemu aliyoambiwa na Tunda. Ilikuwa katikati ya kiuno. Alifanya hivyo kwa muda, Tunda akiwa ametulia tu.

“Asante.” Tunda akasimama wima. “Unajisikia nafuu?” “Afadhali.” “Nashauri usiende kwenye kazi ya pili, ili upumzike Tunda.” Tunda akabaki akifikiria. “Unahitaji kupumzika, angalau mwili urudie hali yake. Umerudi kuwa mrembo lakini bado unaonekana umechoka.” “Nahitaji pesa Net. Nahitaji kufanya kazi. Nikijiendekeza hivi, maisha yatanishinda nitabaki nikihangaika.” “Lakini afya yako ni muhimu Tunda. Naomba urudishe kwanza nguvu, halafu utafanya kazi kwa kadiri ya uwezo wako. Sasa hivi ukumbuke unaishi kwa ajili yako na mtoto.” Tunda akanyamaza. Akageuka nakuendelea na kazi.

Walimaliza saa 8 mchana. Mama Penny na vijana wake walishakuwa tayari kuhamia ukumbi mwingine ambao walisema hauhitaji kazi kubwa. “Naomba Tunda akapumzike. Itoshe kwa leo.” Net aliongea huku akimtizama Tunda na mama Penny. “Mimi naona ni wazo zuri. Umetoka kifungoni, unaumwa, ukazidiwa, umejiuguza mwenyewe. Hatujui ulikuwa ukila vitu vyakujenga mwili au la! Hata hujapata nguvu vizuri, unaanza kazi! Na mtoto huyo, unahitaji kumpumzika Tunda. Mimba sio mchezo.” “Siwezi kukaa hivi hivi. Lazima nitengeneze pesa. Nitaishije?” “Afya yako na mtoto ni muhimu Tunda!” Tunda akanyamaza.

Mama Penny akabaki akimtizama kama kuweka msisitizo. “Nimeelewa dada.” “Na uanze kliniki. Lazima kujua mtoto anahali gani. Uzito wake na wako ambao hauridhishi kwa kukuangalia tu! Bado unaonekana umechoka. Huko unapoelekea utalemewa! Usifanye mchezo. Hakikisha wanakupima damu na uanze kunywa dawa za kuongeza damu na zile za kina mama wajawazito.Umenielewa Tunda?” Mama Penny akaendelea kuweka msisitizo.

“Nitafanya hivyo jumatatu. Kesho jumapili nitapumzika tu.” “Sawa. Uje nyumbani kwa chakula cha usiku kesho.” “Labda unipikie zile ndizi za mchuzi.” Mama Penny akacheka. “Haya. Nitapika. Uje.” Mama Penny akaondoka na vijana wake, nakuwaacha Net na Tunda.

Net na Tunda Tena.

Net akamgeukia Tunda kama anayemtaka muongozo. “Naomba nikapumzike. Nikutafute baadaye nikiamka.” “Naomba usinifukuze Tunda. Tafadhali.” “Sikufukuzi. Nakwenda kulala, nikiamka, nitakutafuta.” Net akabaki akimwangalia. “Nakuahidi nitakutafuta Net. Acha nikalale kwanza, nimechoka.”

“Unaishi wapi?” “Hotelini.” “Wapi?” “Mikocheni B. Nipatulivu, hakuna kelele kabisa.” “Naomba twende wote. Sitakusumbua. Nataka kuwepo tu. Tafadhali Tunda. Naomba na mimi kupata muda na mtoto.” “Sio kwamba sitaki usumbufu tu.” “Ni nini?” Net akamuuliza.

“Nilitaka muda wakufikiria.” “Nakuahidi sitakusumbua. Naomba unifikirie na mimi Tunda!” “Basi twende.” “Na chakula?” “Mimi huwa naagiza pale pale.” “Sasa leo unahamu ya kula nini?” Tunda akacheka huku akifikiria. “Labda nijaribu kuku wa makange.” “Basi twende Back point.” Wakaongozana.

Walifika, wakakaa. Net alikaa mbele yake akabaki akimtizama. Tunda akainama huku akichora meza kama anayefikiria. “Pole Tunda.” “Nimeshapoa. Asante.” Wakanyamaza mpaka muhudumu akafika kuwaulizia kinywaji. Wakaomba mtu wa jikoni. Kila mmoja akaagiza chakula. Wakatulia.

“Bado unanipenda au nimekuudhi kabisa?” Net akamuuliza taratibu tu. “Hujaniudhi Net. Kwa nini unafikiria hivyo?” “Sijui Tunda! Nataka tu kujua.” Tunda akanyamaza.

Chakula kililetwa, wakala kimya kimya. Tunda alikula kidogo tu, huku Net akimtizama anavyokula. Akawa ni kama hajapata mdomoni kwake kitu ambacho alitarajia. Akavuta sahani mbele kidogo, akanywa maji kidogo, akatulia huku akikitizama kile chakula.

“Ndio umeshashiba hivyo!?” “Nitaongeza kitu kingine. Kwa chakula hiki inatosha. Nataka nikalale.” “Naweza kukuagizia kitu chochote nikakuletea. Unaweza kutangulia ukaoge. Nitakufuata.” “Nashukuru. Lakini kuhusu chakula, nitaagiza palepale. Usiniletee kitu. Acha niondoke sasa hivi. Ni kweli nimechoka.” Akamuachia funguo ya pili ya chumba, akampa namba ya chumba, akaondoka.

Kwa mara nyingine tena, Net&Tunda hotelini.

K

wa asili Tunda alithamini sana usingizi, na alipenda kulala. Alishamwambia Net, ndio muda pekee anaweza kuwepo duniani na asihisi taabu yeyote na wala asikumbuke machungu yake. Ni muda ambao alihesabu Mungu huwa anampa pumziko la masaa machache. Kwa hiyo linapofika swala la kulala huwa hajikosei. Iwe mchana au usiku, atavaa nguo ambayo anajua haitamkera akilala na anapenda alale pasafi.

Aliingia hotelini, kwenye chumba chake. Akapiga simu mapokezi na kuagiza chai ya rangi na mkate. Akamwambia akileta aingize na kuweka mezani. Akaingia kuoga. Bado akili za kuwa gerezani alikokuwa akibanwa zilikuwa zikimsumbua. Kila alipooga na kumaliza, alitaka arudie tena kujihakikishia yupo sehemu safi. Alioga tena na tena, ndipo akatoka.

Alijikausha nakuanza kujipaka lotion. Kwa kuwa Net alishajua aina ya vitu anavyopaka mwilini, hata alipokuwa jela ndio vitu alikuwa akimpelekea. Aliiangalia ile lotion, akapotelea mawazoni akiwa amekaa palepale kwenye kochi na taulo lake bichi.

Mawazo yalimrudisha jela. Akakumbuka yale maisha. Akavuta pumzi kwa nguvu na kujirudisha nyuma. “Nimelipa deni yangu!” Alijisemea kwa sauti huku akiendelea kuwaza. Mwishowe akaamua kula chakula chake. Chai yake na mkate vilivyokuwa vimeletwa.

Wakati Net anaingia na mtoto wake alikuwa akicheza. “Vipi?” “Nimepumzika tu, nimeshashiba, namsikilizia mtoto anavyocheza.” “Naomba kumshika.” Safari hii Tunda hakuwa amevaa nguo. Net aliweka vitu mezani, akamsogelea. “Labda nivae kwanza.” Net akabaki akimwangalia. “Ndio nimetoka kuoga Net!” “Sasa mpaka uvae, umalize si na yeye atakuwa amemaliza kucheza?” “Basi nipande kitandani nijifunike shuka. Taulo bichi!” Hakusubiri ajibiwe. Akatoa lile taulo, akapanda kitandani, akajifunika shuka. Net akaenda kupiga magoti pembeni yake.

“Muone anavyozunguka!” Wote wakacheka. “Sijui anafanya nini huko ndani!? Unaumia?” “Hapana.” Net akambusu na kuanza kumpapasa. Alizungusha mikono kuzunguka tumbo lote. Juu mpaka chini, Tunda akiwa amejilaza chali, ameegemea mto. Yeye mwenyewe Tunda alifurahia. Net alianza kuzungumza na mtoto wake taratibu kama wapo ana kwa ana.

“Unavyoongea naye! Utafikiri anakusikia au anaelewa!” Tunda akamshangaa. “Wataalamu wanasema anaelewa na kusikia.” Net alijibu huku akicheka. “Unaonekana umefurahi Net! Ukimshika mpaka unabadilika!” “Unakumbuka tulivyokuwa kwenye honeymoon yetu nilikwambia nataka mtoto?” “Nakumbuka. Halafu mimi sikujua kama naweza kushika mimba!” Net akambusu tena na tena.

“Naomba tumshukuru Mungu pamoja Tunda. Sijui tunakokwenda, lakini ninachojua hata hapa tulipo sasa hivi ni Mungu ndio ametusaidia.” “Lakini naomba na mimi nikushukuru Net. Unaweza usielewe, lakini nilikuwa nikifurahia sana ulivyokuwa ukija kunitembelea.” “Sasa kwa nini hukutaka kuniona Tunda!?” “Nisingeweza Net. Ingeniumiza zaidi na nisingeweza kuendelea kuishi mle ndani. Nia yangu ilikuwa nimalizie kifungo changu nitoke, mengine nije kuyajulia huku nje.” Mikono ya Net ilikuwa bado ikipita tumboni kwa Tunda taratibu.

“Mwezi ule wa mwisho ambao hukuja, niliumia Net, nikashindwa hata kulala!” “Kweli!?” Net akashangaa sana. “Kweli. Nikajua umenisahau.” “Nianzie wapi? Nilijua ungetoka baada ya siku sita. Halafu sikujua itakuaje ukitoka. Kama ndio utataka kuniona au ndio utanifukuza moja kwa moja. Kwa hiyo ikabidi nimwombe Nana nifanye kazi mpaka overtime, ili ukitoka niwe na wewe. Nikusubiri tuwekane sawa. Nikishajua hatima yetu, ndio nirudi..” Tunda hakuwa ameelewa.

“Kwani siku hizi hufanyi tena kazi na mama yako ni bibi yako!?” Tunda akauliza kwa mshangao. “Siishi hapa nchini Tunda. Hata nilipokuwa nikija kukutembelea, nilikuwa nikitokea nyumbani, Canada.” Tunda alikaa kwa mshtuko. “Net!!” “Kweli. Nilikuwa nafika siku ya ijumaa. Nakufuata wewe siku ya jumamosi na jumapili. Jumatatu narudi Canada kuwahi kazi.” Tunda alishangaa machozi yanamtoka. “Haiwezekani Net!” Net akacheka tu na kukaa pembeni yake. Kitandani.

“Pole na samahani Net. Sikujua kama ulikuwa ukitoka mbali hivyo kuja kuniona! Mimi nilijua mlisameheana na mama yako, ukarudi kazini, maisha yakaendelea.” “Inawezekanaje Tunda, wakati tuliambiwa sisi ni mwili mmoja!?” “Lakini ile ndoa iliisha Net!”  “Uliniapia nini Tunda?” Kimya.

“Mimi nakumbuka uliniapia mbele za Mungu, Nana, Maya na watu wengine kuwa ni mpaka kifo kitakapo tutenganisha, sio mpaka usaini tena sehemu nyingine. Au sikuwa nimekuelewa?” Net akauliza taratibu tu.

“Mimi bado nakithamini kile kiapo changu. Binafsi bado najua mpaka kifo, ndio kinaweza kututenganisha. Huwezi kuumia wewe, mimi nikawa salama. Au mama hawezi akakuumiza wewe, halafu mimi nisiumie. Hata Nana anaheshimu sana kiapo chako Tunda. Alirudi hapa nchini, akachukua picha zetu za harusi, video na pete zako za ndoa na uchumba ambazo mama alikupokonya.” Net akaendelea.

“Nana aliporudi kunisaidia kuweka mambo sawa, akanichukulia kila kitu, akaniletea kule nyumbani.” Tunda hakuwa ameelewa. “Mimi nilikuacha na mama yako Net!” Ndipo Net ikabidi amuelezee kuanzia walipoachana mpaka walipokuwa wamekaa hapo.

Tunda alishangaa sana. “Sijamtafuta tena. Nimeona nimpe nafasi. Najilaumu sana Tunda.” “Kwa nini!?” “Mama hakuwa mnafiki juu ya mahusiano yetu. Tokea mwanzo kabisa, alikiri wazi hakutaki kwenye maisha yetu kama mkwe. Lakini ni kama nilimlazimishia. Nakumbuka tokea mwanzo nilimwambia nampa nafasi mpaka atakapokutafuta, lakini sikufanya hivyo.”

“Niliruhusu ajue maisha uliyoishi nyuma kitu ambacho haikuwa lazima. Na mbaya zaidi, mambo yalivyokuwa mabaya, sikumshirikisha nana. Najua kwa upande mwingine, nana analaumu, lakini hataki kuniambia kwa kuwa anajua haitasaidia tena. Na pia najua anaelewa nilikuwa nikimlinda mama na yeye ili wasifike hapa walipo. Mimi mwenyewe nilikosea sana.” Tunda hakujibu, akajirudisha nyuma, akajilaza.

“Sasa, sasa hivi ukiwa hapa nchini unaishi wapi?” Tunda akauliza. “Hotelini.” Tunda akazidi kushangaa. “Sasa kwa nini usikae kwenye ile nyumba!?” “Sikutaka ije ikae hivi hivi tu wakati mimi sipo hapa nchini, na sikujua hatima yetu. Yule mwanasheria ambaye alinisaidia mambo yako na baba, anaonekana ni mwaminifu. Aliniunganisha na ndugu yake. Wanafanya kazi ya kuuza, kukodisha na wananunua nyumba. Nafikiri ni kama biashara ya familia. Kwa hiyo niliwaomba wawe wanakodisha. Lakini sio ile ya mtu kuishi hapo kwa muda mrefu! Hapana. Labda watalii au watu wanao tafuta sehemu ya kuishi kwa muda mfupi. Iwe chumba kimoja, au nyumba nzima. Inakuwa kama sehemu ya mapumziko tu. Si unajua watu wengine wanasafiri kama familia, wanaepuka gharama za hotelini?” Tunda kimya.

“Basi nilijisajili pia na Air bnb, ndipo ninapopata wateja pia, na hao ndugu ndio wananisaidia. Kwa hiyo ukiingia online, unatafuta sehemu ya kushukia Tanzania, utakutana na nyumba ya Tunda Cote. Unalipia, unakutana na Emma yule kijana wangu pale nyumbani. Anasaidia kuwasafishia kwa siku mtakazokuwa mkiishi pale. Basi.” Tunda akabaki namshangao. Mambo mengi yalikuwa yakipita kichwani. Hajui aulize lipi, aache lipi tena.

“Naomba nilale kwanza.” “Unajisikiaje lakini?” Net akauliza kwa upendo huku akimpapasa. “Kuchoka tu.” “Jumatatu itabidi twende hospitalini. Waangalie huo mwili kujua kama unauwezo wakubeba huyo mtoto. Ili kilichopungua, kiongezwe kwa haraka. Kama ni damu, au madini yeyote yale, uanze kutumia dawa na kula vyakula vizuri.”

“Nitatoka hapa hotelini nikaanze maisha yakujipikia. Niwe napika vyakula vya maana. Haya maisha ya hapa ni gharama sana, na nilifanya kwa muda tu ili nipumzike. Naamini nikianza kula vizuri, nitarudisha mwili.” Net akanyamaza.

“Unataka na wewe kupumzika?” “Ni mpaka na mimi nioge, ndio nitajisikia vizuri kulala. Pale ukumbini kulikuwa na joto kali. Siwezi kulala vizuri.” “Kwa hiyo unaondoka kurudi hotelini kwako?” “Sio sasa hivi. Mpaka ukiamka, na kula tena labda ndio nitaondoka. Sasa hivi nitakuwa nikifanya kazi zangu pale kwenye kochi.” Tunda akanyamaza. Net akambusu tena pale tumboni nakuanza kumpapasa taratibu.

“Lala tu. Mimi nitakuwepo ukiamka.” “Wakati mwingine huwa napitiwa na usingizi na lala mpaka asubuhi. Kama jana nilipanga nikupigie, nikapitiwa hapa na viatu miguuni.” Net akacheka kidogo na kumbusu tena tumbo.

“Wewe muda wako wakuondoka ukifika, funga tu mlango. Usiwe na wasiwasi. Nikiamka hata kama ni usiku sana, nitamalizia mkate wangu na chai, nakurudi kulala.” “Ni sawa ikifika saa 3 nikuamshe ili ule? Kuna chakula kingine nimekuletea, ujaribu.” “Nitapata shida kurudi kulala. Acha tu nilale.” “Sitaondoka mpaka uwe umepata usingizi tena. Nitakubembeleza mimi mwenyewe mpaka ulale.” Tunda akacheka taratibu.

Net alimtizama kama amkumbatie na kumbusu, akakwepesha macho, kisha akayafunga. Akamsikia Net akimpapasa na kumbusu tena na tena. Hiyo furaha yake ilimchukua ikampa usingizi mzito.

   ~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

Aliamka saa mbili usiku, bado Net alikuwa akifanya kazi zake kwenye laptop.  “Vipi?” “Nahisi nilikunywa chai nyingi. Nasikia kwenda chooni.” Tunda alitoka na shuka kuelekea chooni. Bado hakuwa amevaa nguo yeyote ndani. Baada ya muda akatoka chooni, akamfuata Net pale kwenye kochi.

“Ndio unafanya nini?” “Kile nilichokuwa nikimfanyia mama, ndio namfanyia nana. Namtafutia wateja. Lakini sio kama zamani nilivyokwambia namfanyia kwa nchi kadhaa. Sasa hivi nimechukua kitengo kizima. Ninaendesha mimi mwenyewe matawi yote, kwenye nchi zote.” “Hongera Net. Ni vilevile usafirishaji?” “Yeah. Usafirishaji.” Tunda akajua kuwepo pale kwa Net, anamkwamisha mambo mengi.

“Net!” Tunda akaita kwa sauti yake ya chini kama anayefikiria kitu. Net akafunga laptop yake akajiweka sawa. “Kwa kuwa sasa hivi nimetoka jela, unaweza kurudi tu ukaendelea na kazi.” “Nikuache wewe na mtoto!” “Utakuwa ukija kututembelea unapopata nafasi.” Net akakunja uso.

“Ndio yanakuwa ni maisha gani hayo?” Tunda akabaki akifikiria. “Kama tunabaki hapa, tubaki wote. Kama nikuondoka, tunaondoka wote watatu.” Tunda akabaki ameinama akifikiria.

“Unajua nimeanza kukuombea kibali chakuweza kuishi Canada?” Tunda akashangaa sana. Akakunja uso. “Unakumbuka kile cheti chetu cha ndoa, nilikwambia lazima kiwe kinatambulika kote? Sasa baada ya kukamilisha kila kitu, na kikawa sawa. Nikaanza kutuma maombi. Unakumbuka ninayo hata hati yako yakusafiria?” “Hata sikumbuki!” Tunda alijibu huku akionekana akifikiria.

“Nilibakiwa nayo tokea wakati ule. Niliifungia ofisini, nana alipoenda ofisini kwa mama, nilimtuma anijie nayo. Naona imefika pazuri. Lakini Tunda, upo huru kuishi popote unapotaka wewe. Mimi ndio nitabadilika na matakwa yako. Nitajua chakufanya baada ya kuamua wewe.” Tunda kimya.

“Ukiamua kuishi Tanzania, ni sawa. Ukiamua kuishi na mimi Canada, nitakushukuru sana, kwa kuwa nana ni kama anatamani niwepo kule ili aniachie ile kazi apumzike. Anataka kustaafu.” Wakati ule ilikuwa ngumu kufikiria kuondoka na Net sababu ya biashara yake ilikuwa imechanganya. Wateja kila kona mpaka anakataa kazi. Sasa sasahivi Tunda ni mjamzito. Alishapita mtandaoni kama mvunja ndoa ya marehemu Gabriel na Bethy. Wengi walishamsema. Gabriel alimtetea na wengine, lakini tayari jina lake lilishaingia doa. Alibaki ameinama akifikiria maisha yake hapo nchini.

“Nikuagizie chakula gani au nikupashie nilichokuwa nimekuletea?” Net alimstua kutoka mawazoni. “Mimi chakula ninacho. Nilibakiza. Na wewe?” Net akafikiria kidogo. “Naweza kwenda kula hotelini kwangu au nikanunua kitu kidogo tu njiani. Bado najihisi kushiba.” “Unataka kuondoka saa ngapi?” Tunda akamuuliza kama anayetamani abaki. “Utakaponiruhusu.” Tunda akacheka na kuinama. Net akamsogelea, akambusu kichwani.

“Natamani kukukumbatia. Nikupe pole ukiwa mikononi mwangu, Tunda. Unafikiri naweza kufanya hivyo?” Tunda akajifuta machozi, akatingisha kichwa kukubali na tabasamu usoni.

Net akajiegemeza vizuri kwenye kochi. “Njoo hapa.” Akimuonyeshea kifuani. “Nikavae nguo kwanza?” “Haina haja. Njoo. Japokuwa nina hamu na wewe sana, lakini sitafanya kitu bila idhini yako.” Tunda akajisogeza mpaka pale kifuani. Akajilaza upande ili kulipa tumbo lake nafasi. Net akaingiza mikono ndani ya lile shuka, akamfunika ili asimwache uchi, akamkumbatia vilevile uchi ndani ya shuka.

Tunda alivuta pumzi mara kadhaa, akatulia. “Asante Net.” “Pole na matatizo, na samahani sana.” “Usiendelee kuomba msamaha Net. Nimefurahi nimeweza kulipa deni langu. Mwenzio najiambia kila wakati kuwa sidaiwi tena. Najisikia uhuru zaidi. Ilikuwa ngumu lakini namshukuru Mungu ameniwezesha kupita.” Net alikuwa akimpapasa ubavuni. Juu mpaka chini. Taratibu huku akimsikiliza. Kichwa ameegemeza kichwani kwake.

“Umebadili perfyumu?” “Inakukera?” Tunda akatingisha kichwa kukubali. Net akacheka. “Haya mama. Lakini sijabadili. Ni ileile.” “Mbona sasa hivi harufu yake mbaya!?” “Huyo anayesikia hiyo harufu sasa hivi sio wewe, ni mtoto. Wewe ulikuwa ukiipenda mpaka unavaa mashati yangu.” Tunda akaanza kucheka, akakaa. “Kama ndio inaninyima kukumbatia, itabidi nikaitupe!” Tunda akazidi kucheka. Akavuta shuka nakusimama.

“Nilishaanza kunogewa.” Tunda akacheka sana. “Njaa inauma, dad!” “Ngoja nikachukue chakula. Pengine nikirudi naweza kupewa taulo nikaoge, ili niweze kukumbatia zaidi.” Tunda alizidi kucheka. “Net!” “Ninahamu ya kufa mtu.” “Wewe uliniahidi ukiwa hapa, hutanisumbua.” “Na ahadi yangu inabaki palepale. Sitakusumbua hata kidogo. Nitakuwa dad mzuri. Nikihurumiwa, sawa. Nikifukuzwa, usiku naenda kulala peke yangu kule, namuacha mtoto wangu na mke wangu wanalala peke yao huku. Asubuhi tena narudi, mpaka nihurumiwe.” Tunda akazidi kucheka.

“Siamini Net!” “Hata mtoto atakuwa anatushangaa wazazi sisi ni wanamna gani! Eti wazazi wanalala hotelini, tena mbalimbali!” “Nilijua tumeachana Net.” “Hivi wewe ndoa unafikiri nikuandika tu? Sio mchezo Tunda. Ni agano la kimungu. Halivunjiki kwa kuandika kwenye makaratasi au haliingiwi kwa kuandika kwenye makaratasi. Ingekuwa ni hivyo mbona ingekuwa rahisi sana! Au labda ni mimi tu na vile nilivyolelewa kwetu! Mimi nimekuwa kwenye mazingira ya kutokuwa na talaka. Nana amekaa kwenye ndoa ya zaidi ya miaka 50 mpaka papa akafariki. Nimefunzwa kuheshimu ndoa.” Tunda akacheka taratibu huku akifikiria.

Net alitoka kwenda kupasha chakula alichokuwa amemletea Tunda tokea mchana, akidhani angependa. Tunda akashangaa anarudi na sanduku. “Kwani ulikwenda wapi?” “Kupasha moto chakula, na kuchukua moja ya mzigo wangu kwenye gari. Sitaki kukosa bahati kwa kisingizio cha kutokuwa na nguo, sijui taulo, hapana!” Tunda akaanza kucheka tena.

“Net wewe ni mtundu bwana! Sasa gari umepata wapi? Mbona hili silijui!” “Nimekodi. Ujue ulipotoka jela ukapotelea hapa, nilikuwa nampigia mama Penny simu kila baada ya masaa matatu kumuuliza kama mwenzangu umemtafuta! Sasa ulipozungumza naye jana ukamuomba kazi, akanipigia na kuniambia pia uliahidi kunipigia. Acha nikeshe nikisubiri. Kimya. Asubuhi nikaona nifanye marefu kuwa mafupi. Nikakusanya vitu vyangu vyote pale hotelini, nikaweka kwenye gari. Nikajiambia nitakufuata hapo kazini. Nikubembeleze mpaka ukubali nikufuate unapoishi. Nikajiambia nikishafunguliwa tu mlango!” Tunda alikuwa akicheka sana.

“Basi nitafute sababu za kulala. Nikishindwa kabisa, niondoke tena na mizigo yangu, nikatafute tena hoteli. Kesho tena asubuhi, nianze upyaa.” Tunda akazidi kucheka. “Kwa hiyo hapa unavyoniona, nipo kamili.” “Net!” “Niruhusu tu nitumie bafu lako, nitoe hii pafyumu wakati wewe unakula.” “Haya nenda.” Tunda akamruhusu huku akicheka.

“Mvumilivu hula mbivu. Unaweza kuta nikitoka kuoga, nikakubaliwa kukumbatia tena. Huwezi jua!” Tunda alizidi kucheka. “Tena ngoja nioge kwa kutumia sabuni yako kabisa. Na vile hali yangu ilivyo mbaya, napaka na lotion yako kabisa. Vitu vyangu vyote naenda kuvitupa, ili nisiharibu.” Tunda akazidi kucheka. Net akaelekea bafuni huku akipiga mluzi.

Tunda alijawa furaha na faraja ya ajabu. Akajua usiku huo atalala akiwa amekumbatiwa na kupewa penzi la nguvu. Hakutumia muda mrefu huko bafuni akatoka. “Net! Mbona kama umekimbia tu huko bafuni?” “Ninuse kama utasikia harufu ya ile pafyumu. Sasa hivi nanukia kama wewe. Labda uwe unanitafutia sababu tu.” Tunda akacheka sana, Net akamsogelea pale. Alitoa taulo mbele yake, akabaki amesimama. Tunda akavuta pumzi kwa nguvu huku ameng’ata midomo ya chini, akacheka.

“Nina hamu na wewe Net!” Net akainama, nakuanza kumbusu tumboni juu ya shuka. Akazidi kumbusu huku akimtoa lile shuka palepale kwenye kochi. Taratibu huku akimbusu na kumpapasa, akambeba kutoka pale kwenye kochi akamuweka kitandani. Wote wakiwa kama walivyozaliwa. Net akapanda kitandani na kuendeleza mabusu ya mwilini kabla hajafika midomoni.

“Maziwa yanauma?” Akamuuliza taratibu. “Sio sana.” “Basi nitakuwa mwangalifu. Ninahamu na wewe Tunda! Mama alitukatili.” “Nakupenda na ninakushukuru kwa kuwa mwaminifu, kunisubiri na kutonikatia tamaa. Ungeweza kuondoka bila kugeuka nyuma.” “Halafu nikose haya yote!?” Tunda alianza kucheka tena taratibu.

Net akamwinamia, kilichokuwa kikisikika ni kunung’unika kwa Tunda. Net alishindwa romance ya muda mrefu. Hata yeye hali ilikuwa mbaya, taratibu kwa hisia zote, alimnyanyua miguu, akiwa amelala vilevile chali, Net akaanza mapenzi huku na yeye akigugumia. Tunda alimsikia akisugua meno huku amefunga macho kama anayesikilizia. Alikuwa amemshikilia hips zake kwa nguvu, huku akijaribu kumwinua taratibu.

“Naomba niangalie Tunda, ili niridhike kuwa upo hapa na mimi.” Net alimuongelesha taratibu alipofungua macho yake akakuta na Tunda amefunga ya kwake. Akamuomba huku akiendelea kuingia na kutoka kwa hisia zote bila kuacha. Tunda akatoa tabasamu na kufungua macho. Net aliendeleza mchezo huku wakiangaliana kwa penzi zito, hakuchukua muda mrefu Net akafanikiwa.

Tunda akacheka. “Nilikuwa najilipa safari zakuja huku, halafu hutaki kuniona.” “Net!” Tunda akamsukuma kidogo. Akajilaza pembeni yake, akalala hapohapo wakati Tunda akimwangalia. Akacheka, akajua alikuwa amechoshwa na mawazo pia. Akambusu, na kumfunika. Akarudi mezani kula mkate wake na chai. Wala hakugusa chakula alichokuwa ameletewa na Net. Alipomaliza akarudi kujilaza pembeni ya Net.

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

Aliamshwa na mikono ya Net ikitembea tumboni. Akacheka. “Umeamka saa ngapi!?” “Muda mrefu, unajua sasa hivi ni saa ngapi?” Tunda akafikiria kidogo. “Lakini leo si jumapili?” “Ndiyo.” “Nataka kupumzika.” “Unasali?” Net akamuona amenyamaza. “Tunda?” “Nitaanza kwenda kanisani week ijayo.” “Hapana Tunda. Unajua sivyo ninavyomaanisha.” Tunda akanyamaza. “Nasali lakini sio kama zamani.” “Kwa nini?” “Sijui Net. Ni kama nimechanganyikiwa, sielewi tena. Naona mambo mengi niliyoyaelewa na yanayoendelea kwangu ni kama…” Tunda akajifuta machozi.

“Nafikiri nahitaji muda tena. Kile nilichoelewa tokea mwanzo kuhusu Kanisa, wokovu na Mungu imekuwa tofauti Net. Watu wenyewe wa kanisani wamenitenda au wananitenda kama watu niliowaacha tu huko duniani. Simaanishi kanisani kwa mama yako tu, lakini hata pale kwa kina mama Penny. Wamenitendea vibaya tofauti na ulivyoniambia mwanzo, Net.” “Pole Tunda.”

“Nimefika sehemu sijui bora vipi! Kule nilikokuwa mwanzo, peke yangu na maisha yakiendelea, au kuwa kanisani ambako watu wananihukumu!” Net alibaki akimsikiliza, akamfuta machozi na kumbusu.

“Nahitaji muda. Nahitaji kufikiria. Nahitaji kujijenga upya. Kwa jinsi gani, hata mimi sijui.” “Pole.” Tunda akacheka. “Bwana acha kusema pole kila wakati.” “Namaanisha. Mimi nilijua haya yatakupata lakini si kwa umbali wa kuwekwa gerezani.” “Halafu mbaya zaidi ni watu wa kanisani Net! Naona watu wa nje wanaelewa na wana utu kuliko hata walioko kanisani! Ipo tofauti kubwa sana ya watu niliowakuta kule jela na wale niliowaacha kanisani.” Tunda akajifuta machozi.

“Nikuulize kitu Tunda?” Tunda akatingisha kichwa kukubali. “Kwa sasa hivi, mtu akikuuliza mimi ni nani kwako, utanitambulishaje?” Tunda akanyamaza kidogo, akamwangalia, kisha akabaki kimya akifikiria. Akamsikia mtoto anacheza. “Naona ameamka, anataka chakula.” Akajishika tumbo, Net akamtizama machoni, akarudi tumboni akaanza kumpapasa Tunda taratibu huku akizungumza na yule mtoto tumboni.

Akambusu mara kadhaa akaendelea kumpapasa. Tunda mwenye alisikia raha. Akabaki amejiegemeza kitandani huku akimtizama vile Net anavyochezea tumbo lake. “Siku chache zilizopita.” Net akaanza huku akionekana bado anaongea na mtoto wake tumboni. “Tena kabla ya Mungu hajatuonyesha vile anavyotuthamini kwa kutupa wewe. Dady wako nilipewa ahadi ya mpaka kifo. Niliambiwa nitapendwa, nitalindwa. Katika uzima na maradhi. Shida na raha, mpaka kifo kitutenganishe.” Tunda akaanza kucheka. “Net wewe! Ndio unanisemea sasa kwa mtoto!?” Net akambusu tena.

“Naomba unisikilize Net.” Net akarudi kwenye mto huku mikono ipo tumboni. “Nakupenda sana Net. Sijapata mtu akanithamini hivi. Kwa kashfa zote nilizonazo, nimetoka jela nikiwa mjamzito, umeamini kabla na baada ya kwenda jela, nimekuwa mwaminifu kwako. Bila hata kuuliza, umeamini mtoto ni wako wakati tulitengana miezi 6. Kwa hilo limeniongezea imani kubwa sana kwako.”

“Kingine, hukunitelekeza japo uwezo ulikuwa nao na sababu pia. Lakini ulimtuma bibi yako kuja kukusaidia kukutengenezea njia pia ili uweze kurudi kwangu. Umekuja kunitembelea jela bila kuchoka, na sasa hivi upo hapa na mimi. Kwa hilo, nitakuenzi daima. Umehangaika kunitetea na kunitafutia mwanasheria. Akafuta makosa yote uliyonisababishia.” Net akacheka.

“Samahani sana Tunda. Mimi sikujua kama mama anaweza kufika umbali huo bwana!” “Subiri kwanza. Wakili uliyenitafutia akahangaika kutaka nisiwekwe jela hata kwa kosa ambalo nilifanya. Mimi mwenyewe nilikataa, kwa kuwa niliona nimepewa muda mfupi, sikutaka kuanza tena kufufua kesi nikaendelea kuwepo jela.”

“Tena hata wale askari waliniambia nitulie kwanza ndani kwa kuwa sijui ni nani bado anahasira na mimi. Naweza kutoka, wakanidhuru. Halafu kitendo cha kesi yangu kutajwa mara ya kwanza na siku hiyo hiyo kupewa hukumu bila kusogezwa mbele, mimi binafsi nikajua ni Mungu amenitetea kwa namna yake. Sikutaka kufanya mambo yakawa marefu wakati nilishajijua mimi ni mjamzito.” “Sasa kwa nini hukuniambia?” Net akauliza.

“Kama ni swala la ujauzito, nilijua ungepaniki Net. Tena ungezidi kuchanganyikiwa kama ungejua nipo na mwanao jela! Usingeweza hata kufanya kazi.” “Ulijuaje!?” Tunda akacheka. “Nilikuona siku natoka jela vile ulivyokufa ganzi na hivi ninavyokuona ukimshika huyu mtoto jinsi unavyobadilika! Sasa niambie hiyo hali ungeipata wakati unajua nimehukumiwa kifungo cha mwaka, halafu nipo mjamzito na huwezi hata kumgusa mwanao!” “Nahisi ningechanganyikiwa wala si uongo.” Tunda akacheka.

“Ndio maana sikutaka kukuona wala kukudanganya juu ya afya yangu. Miezi ile mitatu ya mwanzo, nilikuwa natapika kupita nitakavyokueleza. Kila harufu kule jela ilikuwa mbaya. Nilikonda kama kijiti. Hakuna chakula kilichokuwa kinapita.” “Hata sasa hivi umekonda sana.” Tunda akacheka.

“Baada ya kipindi chakutapika kuisha, nikaanza kula kidogo kidogo ndio nikaugua tena. Mara nipone hiki, nije kile. Ngozi yenyewe ikawa imeharibika mpaka ulipoanza kuniletea sabuni na lotion nilizokuwa nikitumia. Ndio ngozi ikaanza kurudia hali yake. Kwa hiyo nikajua ukiniona wakati ule, au baba angeniona, angeumia na kukwambia wewe. Isingekusaidia Net. Ungeumia wakati hukuwa na uwezo wa kunisaidia tena.”

“Ulifanya kwa nafasi yako ndio maana nipo hapa leo. Yale makosa yasingefutwa, nina uhakika ningekuwa jela mpaka sasa. Kwa hiyo umenielewa na hasira zimeisha?” “Nimeelewa Tunda. Na pole sana.” “Kwa hiyo sasa hivi utafanya mapenzi na mimi mpaka niridhike?” Net akacheka sana.

“Jana uliniacha hivi hivi wakati sio kawaida yako!” “Uliniudhi Tunda. Mimi nakufuata, halafu hutaki kuniona!?” “Lakini sasa hivi umenielewa?” “Inabidi kukuelewa tu Tunda. Wewe ndiye uliyekuwepo ndani. Ulifanya kile ambacho ulijua kitasaidia. Japo najua ungeniona, tukazungumza kama hivi, tungepanga kitu chakufanya pamoja. Tafadhali matatizo yasitutenge, bali yatusogeze pamoja.” “Sasa mbona hata sijajibu swali lako?” “La kuwa kama mimi ni nani kwako?” “Ndiyo.” Net akacheka tena.

“Sifa zote hizo ulizonimwagia!  Utapata wapi mwanaume kama mimi? Eti mwanangu? Nani atampenda mama yako kama mimi!?” Tunda alikuwa akicheka tu na kumfurahisha Net kumuona angalau anaweza kumfanya acheke. “Unavyojiamini!” “Sana. Mimi mwenyewe huwa mpaka nakuonea wivu jinsi ninavyokupenda.” Tunda aliendelea kucheka.

“Kingine Net. Sasa hivi nakusikiliza wewe katika kila kitu. Mwenzio ni kama nimepoteza ramani kabisa. Ni kama natakiwa nianze moja na mimi ndio kama unavyoniona. Bado sina nguvu, halafu hata nikija kurudisha nguvu, labda ndio nitatakiwa kujifungua, itabidi kuwa na muda na mtoto. Sijui Net.” “Basi kama wewe umepoteza ramani, naomba ufuate ya kwangu Tunda. Tutakuwa salama, na ninauhakika hutajuta.” “Nakusikiliza.” Net akajiweka vizuri.

“Nitakwambia kwa kifupi tu bila ahadi nyingi, halafu mengine iwe ni kwa kadiri Mungu atakavyo tubariki.” Tunda akajiweka sawa. “Naomba tukaishi Canada. Ili tuwe msaada kwa nana. Anatamani kupumzika, lakini hawezi. Ukishajifungua, na mtoto akawa yupo sawa kuwa nyumbani, tutafanya kazi pamoja.” Tunda akashtuka kidogo.

“Acha uoga. Unakumbuka tulivyokuwa Arusha jinsi tulivyofanya kazi vizuri?” Tunda akatabasamu. “Sasa ni kama vile vile tu, lakini safari hii utafanya zaidi, ukijua ni urithi wa watoto wetu pia. Ni kampuni ya muda mrefu sana. Tokea baba yake babu. Akamrithisha babu, babu alitaka baba aiendeleze, ndio akafariki, na mama akasema anataka kurudi huku. Ikabidi na mimi nimfuate, kitu kilichomuumiza sana babu. Ndio bibi ameniambia majuzi. Kuwa walitaka kustaafu ili niiendeleze, lakini nilipochagua kurudi kuishi huku Tanzania, na kukataa kumuoa Chloe msichana wa kule, wakajua bibi akifa, na ndio ile kampuni imekufa.” Net akaendelea.

“Kwa hiyo ukikubali tukaishi kule, utakuwa umenifanyia kitu kikubwa sana na..” “Tutaenda Net. Wala huna haja yakunibembeleza.” “Kweli!?” “Si unakumbuka hata kabla ya kwenda jela huo ndio ulikuwa mpango wetu?” “Nilijua umebadili mawazo.” “Hapana Net. Nataka kuwa na wewe tu, nipendwe kizungu.” Net alicheka mpaka machozi.

“Tunda wewe ni mtundu!” “Sikutanii mwenzio. Mambo kama haya ningeyapata wapi! Kushikwa shikwa hivi, unaongea na mtoto ambaye mimi hata sikujua kama watu wanaongeaga na watoto! Acha kunitania na wala sijivungi.” Net alizidi kucheka.

“Sasa nirekebishie basi kama mimi nilivyokurekebishia jana usiku. Huwezi jua, naweza kupata nguvu yakwenda kanisani.” “Si umesema unataka muda?” “Najua utanisaidia Net. Nimeumizwa sana.” “Na mimi najua ni maumivu tu. Unachohitaji ni muda tu Tunda. Ila amini nguvu za Mungu na uwezo wake. Nilikwambia, haya yote utapitia. Sasa wewe umetoka salama, unatakiwa kuwa msaada kwa wengine. Si unakumbuka?” “Nakumbuka.” “Basi. Naomba ujipe muda, samehe, na kuwa msaada kwa wengine. Ila ujue unaye mtu ambaye atakupenda daima.” “Yesu?” Tunda akuliza, Net akaanza kumbusu. “Yesu kupitia mimi.” Tunda akaendelea kucheka.

“Bado unanidai fungate Tunda.” “Nilijua ndio basi.” “Hapana. Mama alinikatili. Unakumbuka siku kabla ya kukamatwa uliniomba na mimi unihudumie?” “Usahau!?” “Nilijuta mpaka jana nilipopata bao na kulala.” Tunda alicheka sana.

“Nilikuwa natamani siku zirudi, angalau hata kwa lisaa tu. Nikufurahie zaidi.” “Mungu ametupa nafasi nyingine.” “Lakini sio hapa. Leo tukitoka kanisani na kwenda kwa mama Penny kula ndizi, nakutoa hapa nchini haraka sana. Safari hii sitaki kuingiliwa.” Tunda alizidi kucheka.

“Tunaenda wapi?” Tunda akauliza akiwa amejawa furaha ya namna yake. “Yaani hata wewe sitakwambia. Nachukua passport yako, naanza kushugulikia safari.” “Lakini lazima kumuona dokta kwa ajili ya kuangalia afya ya mtoto.” “Ni kweli, na pia tujue jinsia, sio naongea na mtoto ambaye hata sijui ni nani!” Tunda alibaki akimtizama, haamini.

“Tukiwa huko, wakati tunasubiria visa yako ya Canada, nitarudi Canada kidogo, sikumbili au tatu halafu…” “Sasa si ni heri mimi nirudi kuishi hata kwa mama Penny wakati nakusubiria?” “Hapa sikuachi. Wanavyokuwinda hivyo! Hapana. Kama hutataka, ni afadhali tubaki wote. Na pia inategemea, kama nana akisema sio lazima kwenda, tutabaki wote mpaka tuondoke wote kabisa.” Tunda akahema kwa nguvu kama aliyepata nafuu.

“Ningekuwa sio kuwa mjamzito, ningeenda kuona anapoishi baba kabla yakuondoka.” “Kwani mnawasiliana?” “Tunawasiliana. Anaonekana ana amani na utulivu, japo biashara hazimuendei vizuri.” “Watoto wake?” “Alipotoka jela, moja kwa moja alikwenda kwa mkewe. Kwenye nyumba yao. Anasema yule mama alimfukuza na kumwambia aondoke kabla hajamwitia mwizi. Sasa baba akasema ilibidi aondoke tu, asije akajiingiza kwenye matatizo mengine, akarudishwa jela.”

“Anasema mama yangu alinitenga naye, lakini kwa kuwa hakuwa na kosa, Mungu amemrudishia mimi. Kwa hiyo hata kina Chale, hatawapoteza.” “Mzee wako mpole sana Tunda. Hana makuu.” “Mpaka nahisi ndio maana wanamuonea. Amezidi jamani! Ungemuona jinsi alivyokuwa akiishi na yule mke wake, mama Chale, mpaka aibu. Utafikiri mjinga!” Tunda aliongea kwa upole.

“Mungu atamsaidia. Yeye aliyemuumba hivyo, anajua ni kwa nini alimpa haiba ya namna hiyo, na atamsaidia. Amejawa shukurani huyo, hana lawama kama hivyo wewe ulivyo. Watu wengi walinilaumu kuwa mimi ndio nimekusababisha ufungwe. Nikaogopa hata kuonana na baba yako. Yule wakili ndio akawa mtu ninayemtumia kunifikishia ujumbe kwake. Siku moja tukakutana pale gerezani. Yaani yeye alijawa shukurani tu mpaka akanishangaza. Tulizungumza kidogo tu, akaniaga kuwa ameamua kurudi kwao, Mara. Basi.” Tunda akanyamaza.

“Mama yako je?” Tunda akavuta pumzi kwa nguvu akakunja uso. “Hatukuwahi kuwa na mahusiano na mama, Net. Unakumbuka mama yupo sasa hvi ni kwa sababu tulimfuata? Hajawahi hata kuja kunitembelea jela. Juzi uliponikuta na mama Penny napamba, aliniambia alimfukuza, lakini baadaye akawahurumia  sababu ya watoto wake. Kina Tom. Ikabidi ampe vile vitu vyangu vyote. Kwa hiyo akawa akipata tenda nyingi, nyingine anampa na yeye. Anasema hakutegemea, lakini anafanya vizuri tu. Hajawahi kulalamikiwa. Ameniambia anaonekana kwa muda mfupi alioanza hiyo biashara, yupo vizuri tu.” “Kwa hiyo anavyo vitu vyako vyote vya biashara?” Net akauliza.

“Mama Penny alimpa. Alisema yeye hakujua kama nitatoka mjamzito. Na pia alimuona ni msafi sana na mtunzaji. Kwamba ningetoka, ningeendeleza biashara yangu. Hata kama nikununua vitu baadhi, nisingehangaika. Lakini huwezi amini Net!”  Tunda alikuwa kiongea kwa unyonge. “Nini?” Net akauliza.

Tunda akacheka kwa kuguna. “Mama Penny anasema week iliyopita nilipokuwa nimejifungia hapa hotelini baada ya kutoka jela, akaamua kupitia website yangu. Akakuta imefungwa. Akampigia simu mama. Akamuuliza kulikoni mbona haoni website yangu tena! Mama akamwambia aliamua kubadili au kufunga kabisa jina la kampuni yangu. Sasa hivi kampuni ipo kwa jina lake. Kwa kuitwa Tunda, wateja wanamkimbia sababu ya kashifa zinazonikabili. Net aliumia sana. Hakutaka hata kuweka neno.

Akamtoa Tunda pale kwenye mto, akamuweka kifuani. “Nataka tukabariki ndoa yetu kanisani Tunda.” Net akabadili kabisa yale mazungumzo. “Wapi?” Tunda akauliza, Net akiendelea kumfuta machozi. “Tukifika nyumbani. Kwenye kanisa tutakalowakuzia watoto wetu.” Tunda akaanza kujisikia faraja baada ya kukumbuka ubaya wa mama yake. Akamkumbatia Net vizuri na kujiweka kichwa chake kifuani huku akijaribu kutulia.

“Nakupenda Tunda.” “Sasa mbona hatu..…” Wakasikia hodi mlangoni kabla Tunda hajamalizia swali lake. Lakini Net alikuwa ameshaelewa analalamikia nini na ni kweli alikuwa akimzungusha pale kitandani. Kila Tunda alipotaka mapenzi, Net alimzungusha kwa hili na lile. 

“Hiyo ndio sababu.” Alitoka kitandani huku akicheka. Tunda hakuwa akielewa. “Ni nani huyo?” “Vaa nguo, mama Penny huyo.” Tunda akakurupuka. Alilala uchi. “Mbona hukuniambia bwana!? Kafungue mlango sasa.” Tunda alikuwa akicheka huku akikimbilia bafuni.

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

Net alivaa sweat pants harakaharaka na t-shert nyeupe aliyotoa kwenye sanduku lake, akarudisha nywele vizuri, akafungua mlango. “Karibu.” “Nimewaamsha nini?” “Hapana. Tulishaamka. Nilikuwa namuongelesha ili asiagize tena mikate.” Wakacheka, mama Penny akaingia na chupa ya uji, na hotpot kubwa, akaweka mezani.

“Yupo bafuni, atatoka sasa hivi.” “Mimi mwenyewe sitakaa sana, nawahi kwenye ibada. Mtakuja?” “Sijui.” Net alijibu kwa sauti ya chini kama kunong’ona huku akipandisha mabega. Mama Penny akavuta pumzi kama anayefikiria kidogo kisha akauliza.

“Anaendeleaje?” Mama Penny akauliza na yeye kwa sauti ya chini. “Anahitaji tu muda. Atakuwa sawa.” “Na kula vizuri. Amechoka sana. Sio sawa kwake na kwa mtoto. Anahitaji kumuona na dokta, tena kwa haraka.” Mama Penny alisisitiza. “Lazima kesho tutaenda.” Tunda akatoka.

“Karibu dada yangu.” “Nimekuletea chakula kinachoeleweka. Hiyo afya yako haiendani na mikate mikavu unayokula siku nzima.” Tunda akamgeukia Net kama anayemsuta. “Sio mimi. Ni mama Penny mwenyewe ndiye aliyenituma kuulizia wana vitafunio gani hapa. Wakaniambia huwa unakula mikate mikavu na chai nyingi ya rangi.” Tunda akaanza kucheka, akaenda kukaa kwenye kochi.

“Kwa hiyo umeniletea nini dada yangu?” “Usifanye mchezo Tunda. Mwili huo ni dhaifu kubeba mtoto. Huo sio mwili wako, umekonda kwa maradhi. Mkifanya mchezo mtapoteza huyo mtoto!” “Usiniogopeshe bwana!” “Nakwambia ukweli. Acha kula mikate mikavu na chai ya rangi! Haviwezi kukujenga huo mwili na mtoto wenu. Lazima kubadilika jinsi unavyojitunza. Makazi magumu sio kwako wewe ambaye umepitia shoruba. Umebakiza miezi mitatu ujifungue, tulia.” Tunda akainama akifikiria.

“Unanisikia Tunda?” “Net amesema atatutunza mimi na mtoto, nipumzike kwanza mpaka nitakapo jifungua. Na kesho tutaenda kufanya vipimo vyetu wote. Mimi na mtoto kabla yakusafiri.” “Mnakwenda wapi!?” “Kumalizia fungate, na mambo mengine tutakuja kuzungumza na nyinyi nyumbani.” “Sawa. Basi mimi natangulia kanisani. Si mnakuja?” Swali hili aliuliza huku akimtizama Tunda. Tunda akamgeukia Net, wote wakabaki wakimwangalia yeye.

“Mimi bado nahitaji muda.” Tunda akajibu taratibu. “Wa nini?” Mama Penny akamuuliza. “Eti Tunda? Muda mbali na Mungu?” Kimya. Tunda akainama. “Hapo ndipo utapotea kabisa Tunda. Unanisikia?” Tunda akabaki ameinama. “Ni heri uangukie msalabani kuliko nje. Unayoyaona ndani ya Kanisa sasa hivi, ni afadhali hivyo kuliko utoke. Usifikiri jaribu lako limepita. Kushindwa kwako ni kukimbia baada ya yote yaliyokupata.” Mama Penny akaendelea.

“Wengi wanabaki hivyo hivyo kwa kuwa wakijaribiwa, hawasimami. Wanataka kukimbia kama wewe. Umefanya sehemu ya kwanza kwa uaminifu na juhudi zote. Usirudi nyuma. Huo mtihani lazima kumaliza. La sivyo utajaribiwa tena na tena na utakuwa wewe ni mtu wakuanza upya kila siku. Unanisikia Tunda?” Tunda akajifuta machozi huku ameinama.

“Na Mungu hatakuacha mpaka umefaulu mitihani yake. Sasa ni wewe mwenyewe na juhudi zako. Unaamua kuahirisha leo, au la. Na ujue utarudia tu hiyo mitihani unayokimbia leo. Sasa nijuu yako wewe. Upo tayari kuanza upya au kuendelea?” Tunda akapandisha mabega kukataa. “Basi ndio nikuone kanisani baadaye, na kwenye bible study jumatano na maombi alhamisi.” Mama Penny akaweka kila kitu chini.

“Na hizo ni nguo nimekununulia jana. Acha kuvaa nguo za ajabu. Uje kanisani ukiwa umependeza.” Tunda akaanza kucheka huku anafuta machozi. “Yaani mama Penny, jamani!” “Wewe unataka kujiliza hapo mpaka lini? Umeanguka, umesimama, tena umesimama vizuri sana. Kung’uta vumbi, endelea na safari.” Akamaliza hivyo na kutoka.

        Mama Penny!” Tunda akabaki akimtafakari dada yake wa hiari. “Lakini amekwambia ukweli.” “Nahitaji muda, Net.” “Mpaka lini!? Kujifungia hapa na kuwa mbali na watu ndio kujipa sababu yakuzidi kujitenga na watu na kuona mabaya zaidi. Kula tutoke humu ndani. Na uzuri unatoka na mumeo akiwa pembeni yako! Huoni huo ni ushindi?” Tunda akacheka taratibu.

“Kwa hiyo ulijua kama atakuja?” “Aliniambia atakupitishia chakula asubuhi ndio maana sikutaka kuanza mapenzi, halafu aje atukatishe katikati.” Tunda akacheka.

“Kula.” “Nawaza ingekuwaje bila wewe na mama Penny! Unajua maisha yangu yote nimekuwa peke yangu! Nikikutana na changamoto ni mimi mwenyewe nachukua hatua na kile ninachofikiria kinafaa kwenye akili zangu zilizojaa kusalitiwa, manyanyaso, kutumiwa bila kujaliwa, kutothaminiwa na mengi mabaya. Sasa unaweza kufikiria maamuzi yote yatakayotoka kwenye fikra kama hizo!”

“Afadhali sasa hivi na mimi nipo.” “Hilo linanifanya nimshukuru Mungu, Net. Asante.” Net akainama pale alipokua amekaa. Akaanza kumbusu. Tunda alikuwa na robe tu, aliyojifunga baada kukimbilia bafuni. Ndani hakuwa amevaa kitu.

Net aliivua, nakumtoa pale kwenye kochi akiwa mtupu nakumuweka kitandani. Alihakikisha anamkata kiu yote ya tokea wanaachana. Anampa pole ya namna yake, na kumridhisha. Tunda alikuwa akifurahia kila alichokuwa akifanyiwa na mumewe pale kitandani. Hakutaka amalize. “Tutashindwa kwenda kanisani Tunda. Njoo ule twende.” “Natamani kulala tu.” “Najua. Twende, tukirudi nitakufanya ulale, sitakusumbua.” “Nataka unisumbue.” Net akacheka na kumbusu.

Kwa mara nyingine tena, Tunda na mumewe Kanisani.

                Walipofika kanisani wakaegesha gari na kubaki wakizungumza ndani ya gari. Mara wakawaona Penny na mdogo wake wanachungulia dirishani. “Anti! Anti!” Penny alisikika akiwa na furaha sana. Tunda akashuka garini. “Nilikuwa na hamu na wewe anti!” Penny akaanza. “Hata mimi Penny. Hujambo?” “Mwenzio mama amemwambia Penny akikuuliza yale maswali yake tu, anamkata ulimi wake wote.” Mdogo wake akaingilia. Tunda akaanza kucheka.

“Maswali gani?” Tunda akamuuliza Penny mwenyewe. “Si ndio ameniambia atanikata ulimi sasa! Huu hapa wote.” Penny akatoa ulimi wake wote. “Amemwambia atamkata kuanzia kwenye koo.”  Pendo, akaweka msisitizo.

Tunda akazidi kucheka. “Kweli. Ila ameniambia utakuwa na mtoto. Nikamuuliza kwa hiyo mtoto wako atakuwa wakizungu kama dad wake?” “Maana Penny yeye ananywele za kipilipili kama za dad.” Pendo akaingilia nakumfanya Tunda na Net wacheke.

“Nywele za Penny hazichaniki.” “Zinachanika ila dada ndio hajui kuchana.” Penny akabisha. “Anajua sana, mbona zangu zinachanika?” Pendo na yeye akambishia dada yake.

“Hajui.” “Anajua.” Wakabishana Tunda na Net wakiwasikiliza. “Kwa hiyo mtoto wako atakuwa mzungu?” Penny akaendelea. “Dad wake mzungu na yeye atakuwa mtoto wakizungu. Mama amesema atakuwa hasumbui kuchana nywele kama wewe.” “Mama anachana kwa nguvu ndio maana!” Penny akakunja uso akilalamika.

“Anti, kwa hiyo kweli atakuwa mzungu?” “Sijui, Pendo.” Tunda akamjibu huku akicheka. “Ningekuwa mimi ningetaka mtoto wakizungu na macho ya rangi ya bahari kama ya dad wake.” Net akazidi kucheka. “Yaani watoto hawa! Mama yenu yuko wapi?” “Yupo kanisani. Amemwambia Penny aje asalimie tu. Asiulize yale maswali yake mengine, ila kuhusu mtoto amemruhusu.” Tunda akacheka tena.

“Kwani ulitaka kuuliza maswali gani?” Tunda akamgeukia tena Penny na kumuuliza. “Mwenzio nitakatwa ulimi na mama. Ila nitakwambia kitu.” “Nakusemea Penny! Mama amesema nikusikilize kila neno. Ukisema tu, nikamwambie.” “Sijasema bado. Nimemwambia nitamwambia kile kitu kingine.” “Hata kile mama amesema usiseme.” Wakaendelea kubishana ndugu hao wawili, Tunda na Net wakiwaangalia huku wakicheka. Penny akakunja uso na mikono.

“Wala sio raha tena!” Penny akanung’unika. “Kwani ni nini?” “Pendo mmbea. Nikikwambia tu kama niliwasikia kina mama Vero wanakusema kuwa umefungwa jela hutakaa utoke tena, atamwambia mama, halafu nitakatwa ulimi.” “Hee! Pennyy! Pennyyyy! Umesema! Naenda kumwambia mama.” “Sijasema hata nusu yake. Niliwasikia kila kitu. Kwani anti nimekwambia?” Tayari Penny akawa ameingiwa hofu. Kama aliyeropoka.

“Hujaniambia Penny! Usiogope.” “Umesikia na umbea wako? Sasa mimi anti amenitetea. Shauri yako!” “Naenda kumwambia mama.” Pendo akaondoka akikimbia. Penny akaanza kulia huku akimfuata mdogo wake akisema hajasema. Net na Tunda wakabaki wakicheka.

“Mama yake ndio kiboko yake. Sasa ngoja Pendo akamsemee. Atapooza leo, mpaka walimu wake wamshangae huko Sunday school. Ujanja wote utamwisha kwa hofu yakuchapwa huko nyumbani.” Tunda na Net walizidi kucheka. Wakaamua kuingia kanisani.

Kuanzia nje mpaka ndani, kila mtu alikuwa akimshangaa Tunda na Net. Walijua, lakini hawakujali. Penny alishawapa kwa kifupi kilichokuwa kikiendelea. Mama Penny akawasogelea huku amemshika Penny mkono. “Hajasema bwana. Muache.” Tunda akajaribu kumtetea. “Huyu leo nakaa naye pale mbele kama shemasi. Hasikii Penny.” Mama yake aliongea huku akimwangalia Penny.

“Sio mimi ni kina mama Vero ndio wanadhambi ya kusengenya.” Penny aliwafanya wacheke mpaka mama yake. Kila mtu akawageukia pale kanisani wakimsikiliza Penny akiongea huku akilia.

Mbaya zaidi na mama Vero na mumewe walikuwepo. “Yeye ndio wakumkata ulimi mama, sio mimi.” “Penny wewe mtoto utalia Penny! Nyamaza.” “Mimi sijamwambia kitu anti. Pendo muongo.”

“Amemwambia vile alivyowasikia kina mama Vero wakimsema anti Tunda, mama. Muulize anti mwenyewe.”  “Lakini sijamwambia kila kitu. Si ndio anti, eeh? Yale mambo waliyokuwa wakionyeshana kwenye simu kwani nimekwambia?” “Penny! Penny! Mdomo huo wewe utakuponza mwanangu!”

“Pendo ananisingizia mama. Muulize anti. Sijasema. Hata vile walivyosema mzungu wake amemkimbia sijamwambia anti. Muulize.” Penny alitaka utetezi wa Tunda huku akilia kwa hofu na kuzidi kuharibu zaidi.

“Sasa wewe mama Penny ndio utamfanya ayaseme yote hapa. Unamjua Penny. Hawezi kunyamaza mwenzio. Bora umuache kabla hajayasema yote hapahapa.” Tunda alikuwa akicheka mpaka machozi.

Mbona yeye amemwambia anti achague mtoto awe wakizungu na macho ya rangi ya bahari kama dad wake, na nywele za kizungu kama dad wake zisiwe kama zangu za kipilipili hazichaniki kama za dad wangu! Mimi sijamsemea?” Kila mtu alikuwa akicheka.

“Si nimekwambia mama Penny wewe? Mimi naona umuachie tu, kesi tukamalize nyumbani.” “Hata mimi naona.” Mama Penny akakubaliana na Tunda tu. Maana Penny alizidi kutoa maneno. Mpaka Net alikuwa akicheka.

“Mama Vero ndio ananiponza mama. Sio mimi. Mimi nilimtetea anti. Hata walivyosema hataolewa na Mzungu, mimi nikasema...” “Penny wewe mtoto!” “Sikusema vibaya mama. Mungu wangu shahidi. Mimi sisemi uongo kama shetani. Nilimwambia mbona alishamuoa!?”

“Penny nakuonya wewe mtoto nyamaza!”  Net alikuwa akimwangalia Penny, nakuzidi kucheka. Alimsikiliza vile anavyojitetea na kuzidi kuharibu.

“Basi mama. Mimi siongei tena. Sisemi yote aliyoyasema mama Vero, tena alikuwa na..” “Penny!” Mama yake akamwita kwa ukali, akanyamaza.

“Haya poteeni haraka. Na niwakute mmekaa kimya darasani kwenu.” “Yaani hata maswali tusijibu!?” Penny akauliza huku akifuta machozi. “Penny utalia zaidi wewe mtoto!” “Mimi sitajibu mama. Hata mwalimu akinichagua, sijibu. Mimi mtoto mzuri.” Pendo akajitetea kwa haraka huku akiondoka taratibu kwa tahadhari.

“Tena na wewe unyamaze Pendo. Aliyekwambia ukaulizie maswala ya watoto wa kizungu ni nani?” “Na Penny pia amemwambia anti achague mtoto wa kizungu, mama. Sio mimi peke yangu.” Kila mtu alizidi kucheka.

“Haya poteeni haraka.” “Mimi siongei tena mama. Kwa hiyo hata nyumbani usiniulize tena. Yaishie tu hapahapa kanisani.” “Penny utalia wewe mtoto wewe!” “Basi mama Penny!” Penny alimfanya mpaka mama yake acheke. Akaondoka.

Mchungaji aliingia nakukuta kanisa zima wakicheka. “Kuna nini?” Akauliza. “Wala hutaki kujua! Jiachie tu.” Mama Penny akajibu, nakufanya kila mtu azidi kucheka.

“Huyu Penny ni wakutoa sadaka kabisa. Awe anaishi hapahapa kanisani na mlinzi.” “Kafanyaje tena mwanangu!?” Mchungaji akauliza.

 “Ningekuwa naye zile enzi za Mtume Eli akimlea Samweli kule hekaluni, na Penny ningempeleka akasaidie hata kusogeza kuni za kuteteteza sadaka. Angalau aishi huko huko asirudi tena nyumbani. Labda na yeye Mungu angemwita jamani kama Samweli!” Watu wakazidi kucheka. “Mtoto huyu!” Mchungaji akaanza kucheka. Alimjua Penny, akajua ameacha jambo hapo.

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

Ibada ikaanza, muda wakutoa ushuhuda mchungaji alikaribisha watu. Net akanyoosha mkono. Akaenda. “Napenda kumshukuru Mungu kwa ajili ya mema yake kwangu na familia yangu. Haikuwa rahisi si kwa Tunda mke wangu tu, hata kwangu na mtoto wetu. Haikuwa rahisi hata kidogo. Mengi yamesikika, lakini ni mimi na Tunda ndio tunaojua ukweli. Sipo hapa kusafisha jina la Tunda, mke wangu kwa kuwa nimejua ni ngumu kubadili fikra za binadamu ila nipo hapa kumshukuru Mungu.” Net akaendelea.

“Katika kipindi hicho kigumu cha miezi sita, Mungu amemuwezesha mke wangu kubeba mtoto wetu kwenye mazingira magumu mno. Kusimangwa na maneno yakusingiziwa ambayo watu walimshutumu nayo bila huruma. Amelipa deni ambayo Mungu alimfutia msalabani. Lakini bado yupo hapa na sisi akiamini kanisani ni sehemu sahihi anayotakiwa kuwepo na nyinyi watakatifu wa Mungu. Ni kwa Neema na Rehema za Mungu kwa Tunda kuwa hapa.”

“Huwa nafikiria na kutafakari kule Tunda alikotoka, anakopitishwa sasa hivi, nashindwa kujiweka kwenye viatu vyake. Ni yeye tu mke wangu ndiye anayeweza kuvivaa viatu hivyo. Na mimi pia nimechangia kupita alikopitishwa. Lakini Tunda yupo kama baba yake. Hajui kulaumu. Hajui kunyoshea watu vidole. Amekubali mapito yake, namuombea Mungu azidi kumtia nguvu. Namshukuru Mungu kwa kunipa Tunda. Na sasa ametuamini na maisha ya mtoto ambaye tunamtarajia miezi michache ijayo.”

“Kwa niaba yangu na familia yangu, naomba pia niwashukuru mama Penny na mume wake. Kwa Tunda wamefanyika zaidi ya wachungaji. Wamembeba mke wangu bila aibu wala kuchoka. Kwa asilimia kubwa sana, wamechangia yeye kuwa hapa leo. Sina chakusema zaidi, ila nawaombea Mungu awabariki sana.”

“Kabla sijaendelea na shukurani za mwisho, tumekubaliana na mke wangu, kutoa sadaka ya shukurani. Naomba mtuvumilie.” Net akaendelea. “Tungeweza kusubiri wakati mwingine, lakini tumeona hapana. Mkono wa Mungu umekuwa juu yetu kwa namna ya tofauti na ya ajabu. Ametulinda. Amepigana vita kwa niaba yetu. Ametenda mambo makubwa zaidi ya tulivyoomba na kufikiri. Acha leo tutoe sadaka yakutambua uwepo wake kwenye maisha yetu.”  Watu wakapiga makofi.

“Mwisho katika yote, nakipekee, namshukuru mke wangu. Am so proud of you babe! ‘Binti za watu wengi wamefanya vizuri, lakini wewe Tunda, mke wangu, umewapita wote’.” Net akampongeza mkewe kwa kupitia andiko la kutoka kwenye bibilia. {Mithal 31:29}. Tunda alikuwa ameinama. Akanyanyua uso akamtizama. “Thanks Net.” Alijibu kwa kunong’ona, na tabasamu lenye chozi juu. Hata kina mama Penny walijisikia vizuri. Tunda akasimama na kwenda kumsindikiza Net kwenye kutoa sadaka ya shukurani. Waliweka pesa kwenye bahasha. Wakamaliza, watu wakapiga makofi wakati Net na mkewe wanaenda kukaa.

Waliosutwa wakasutika. Waliofungwa mdomo wakafungwa na Net. Maana neno mke wangu alihakikisha analitamka bayana kama anayesisitizia ndoa yake kwa Tunda, na ni kama kusema hakukosea kumuoa Tunda. Alijawa na shukurani kwa mkewe na Mungu wao.

Net&Tunda Kwa Mchungaji Tena.

Baada ya ibada, Net na Tunda walielekea nyumbani kwa mama Penny lakini baada ya kupitia dukani kama kawaida ya Net. Akanunua vinywaji na dessert ya keki ndipo akaelekea nyumbani kwa mchungaji. Njia nzima walikuwa wakicheka kila wakimkumbuka Penny.

Walifika wakamkuta Penny amekaa kwenye kochi kimya ametulia wala hatingishiki. Tunda akaanza kucheka. “Subirini chakula kitakuwa tayari sasa hivi. Njaa inauma?” Walimsikia mama Penny jikoni. “Net aliniwekea ule uji wakati tupo njiani. Ndio nimemalizia hapo nje na kuingia ndani.” Akajibu Tunda na kwenda kukaa pembeni yake Penny.

“Penny!”  Tunda akamwita taratibu huku akimgusa lakini Penny hakuitika. Akabaki amefunga mdomo kwa nguvu huku akimtizama. “Mbona huongei bwana!?” Tunda akamuuliza akicheka. Pendo akawahi yeye kujibu. “Mwenzio ameambiwa na mama, akifungua tu huo mdomo wake, iwe kunywa maji au chakula. Lasivyo anaenda kumtoa sadaka kwenye kanisa la watu wanaokunywa damu za watu ili wainywe damu yake yote.” Tunda alicheka na kucheka bila kunyamaza mpaka mchungaji na yeye akaingia kutoka kanisani.

“Mbona Tunda anakufa kucheka? Wewe Penny umemwambia nini?” Penny akatingisha kichwa kukataa, Tunda akazidi kucheka. “Mbona huongei wewe!? Umeng’oa jino?” Mpaka Net akacheka.

“Mwanao ameambiwa na mama, akifungua tu huo mdomo wake, anaenda kumtoa sadaka kwenye yale makanisa ya wanao kunywa damu za watu.” Pendo akajibu kishabiki.

“Wanakula na nyama za watu pia. Tena za watoto ndio wanazipenda sana. Si niliwasomea kwenye bibilia kuna wakati watu walipoasi, walikuwa wakitoa sadaka za watu kwa miungu yao na kuwateketeza kwa kuwachoma moto kama sadaka?” Mchungaji akaongeza. Pendo akazidi kucheka, Penny akaanza kulia huku amefunga mdomo.

“Leo lazima wakamchome Penny. Hawezi kunyamaza huyo.” Pendo akazidi kumcheka dada yake. “Mwache bwana Penny wangu! Si umenyamaza?” Tunda akamuuliza. Penny akatingisha kichwa kukubali huku akilia. “Na akifungua tu mdomo wake huyo, anaondoka hapa leo. Halali humu ndani.” Mama Penny alitoka jikoni na sahani. Penny akazidi kujivuta mwisho kabisa wa kochi. Akakunja miguu, akainamisha mdomo kwenye magoti huku akimwangalia mama yake. Tunda akazidi kucheka.

Mama yake akapanga chakula huku wakicheka hili na lile, wakamuona Penny ananyoosha kidole. “Penny! Penny wewe mtoto wewe! Kuna linalokutafuta.” Wakaanza kucheka tena. “Mwanao huyo hawezi kunyamaza. Na mazungumzo yote haya yanayoendelea, asiongee chochote! Sijui!” Baba yake akaongeza. “Basi dada aende akamfungashie mizigo yake. Maana akifungua tu mdomo wake, anaondoka humu ndani.” Penny akashusha mkono taratibu huku akilia. Pendo akazidi kucheka. Wakampelekea chakula palepale alipokuwa amekaa. Wao wakahamia mezani.

Walikaa hapo mezani wote wakila na kucheka. Net ndiye aliyempakulia Tunda chakula kama kawaida yeke. Tunda alikula sahani mbili za ndizi za mchuzi, bila shida. Kwa mara ya kwanza akaonekana amekula chakula chakueleweka. Net akalifurahia hilo. “Nashukuru mama Penny. Naomba nimuwekee kingine hapa kwenye hii sahani. Ili ale tena usiku.” “Wala usijali. Nitamuwekea kwenye bakuli zuri, mtaenda kupasha moto.” “Asante. Naona hizo ndizi zimekubaliwa.” Net akashukuru. Wote wakacheka.

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

“Naomba niwashukuru Mchungaji na mama Penny.” Wote wakamgeukia Tunda. “Asanteni kwa kuja kuniona nilipokuwa jela bila kunikatia tamaa japo niliwafukuza.” “Sasa mbona hukuwa ukitoka kutuona Tunda?” “Nisingeweza kumaliza muda wangu baba Penny. Ingeniwia ngumu sana. Halafu muda mfupi tu nilipoingia mle, nikajigundua ni mjamzito. Nilijua mama Penny akiniona tu, angejua, halafu ingemuumiza zaidi na pengine angemwambia Net, angezidi kuchanganyikiwa.”

“Halafu nikaanza kuugua mfululizo. Kilianza kichefuchefu na kutapika sababu ya mimba. Miezi mitatu ya mwanzo ilipoisha tu, wakiniambia labda nitapata nafuu, zikaanza UTI. Nikadhoofu! Kuna kipindi nilikuwa siwezi hata kusimama. Sikutaka kuhurumiwa. Ingenikatisha tamaa, nikaogopa pengine ningeshindwa hata kutoka.” Kila mtu kimya.

“Ila nilikuwa nikifurahi sana nilipokuwa nikisikia mmekuja kuniona. Nilikuwa nasubiria siku za kutembelewa kwa hamu kweli. Ile kusikia baba Penny, au mama Penny amekuja kuniona, nilikuwa nafajirika nakupata nguvu. Net ndio kabisa.” Tunda akacheka kidogo, nakujifuta machozi.

“Nilikuwa naangalia saa, nasubiri kuja kuitwa kuwa Net amekuja. Wakichelewa kuja kuniambia, nilikuwa nasikia kama kuchanganyikiwa! Uzuri kila mtu alikuwa akimfahamu pale. Basi nikiambiwa yupo pale ananisubiri, nilikuwa nasikia uwepo wake kule nilipo. Ilikuwa ikinifariji sana.” Kimya. Tunda akaendelea.

“Siku moja nilikuwa naumwa. Ndio kipindi hicho siwezi hata kusimama. Hakuna kinachopita mdomoni.” “Walikupeleka hospitali?” Net akauliza.

“Hapana! Waliniambia ni hali ya ujauzito tu, nitakuwa sawa. Basi, nilikaa nikilia, namsubiria Net. Halafu kama Mungu, siku hiyo Net akawa mtu wa kwanza kujiandikisha. Askari akanifuata kule infumary, kijihospitali cha jela, nilipokuwa nimelazwa, akaniambia, ‘Mzungu wako kaamkia gerezani. Amekuwa wa kwanza leo na kabeba maua kibao!’” Wakacheka wote.

Nilifurahi mpaka basi. Ndio nikamwambia asimwambie kama ni mgonjwa. Net akaondoka baada ya muda kuisha, akarudi tena mchana. Akakaa hapo mpaka jioni, akarudi tena kesho yake. Najua mnaweza msielewe, lakini kwangu ilikuwa faraja sana. Nawashukuru.” Kimya kikazuka kwa muda. Kila mmoja akiwaza lake.

“Pole sana Tunda. Pole mama.” Akavunja ukimya mchungaji. “Sasa hivi nimepoa.” Akacheka huku akijiweka sawa. “Lakini lazima kuangalia afya yako Tunda. Bado umedhoofu mama.” “Kesho tutaenda kumuona daktari.” “Na ujitahidi kula. Umesikia Net?” Mama Penny akaingilia. “Nakusikia.” “Huo mwili hauna nguvu yakubeba mtoto mkubwa. Msizembee hata kidogo. Ale virutubisho vingi na kwa haraka ili kushindana na muda uliobaki kujifungua.” Mama Penny akasisitiza.

“Sawa. Na pia nafikiria kuwachukua wote wawili. Pengine kabla hata bado hajajifungua.” “Mnakwenda wapi?” Mchungaji akauliza. “Kwanza mapumzikoni. Kumalizia mapumziko yetu, pili tunarudi nyumbani kwetu sasa. Akatulie kabisa mpaka amalize swala la uzazi ndipo afikirie swala la kazi.” “Inamaana unakwenda naye Canada!?” Mama Penny akashituka sana.

“Kule ndio nyumbani mama Penny. Nilikuwa hapa kwa kuwa nilikuwa nikimsaidia mama na maswala yangu na Tunda. Sasa mama haitaji tena msaada wangu. Halafu hata hivyo naona niwakati muafaka na mimi nijenge familia yangu.” “Mama yako yuko wapi?” “Hata sifahamu.” Net akajibu kwa kifupi tu.

“Sasa hufahamu alipo, halafu unamchukua Tunda hapa! Kama yuko huko huko Canada!?” “Naomba uniambie ni nchi gani Tunda atakuwa salama, ili mimi nimpeleke nikaishi naye huko!” Kimya. “Hapa nyumbani kwao, walitufuata hotelini wakamchukua. Sasa..” “Si kwa kuwa mama yako ndiye aliyesababisha hayo!” Mama Penny akaongea kwa hasira.

“Isingekuwa mama yako yote hayo yasingempata Tunda.” “Nishauri natakiwa kufanya nini mama Penny. Nifanye nini!? Mama Cote ni mama yangu. Nipende nisipende yupo kwenye maisha yangu hilo siwezi kukwepa. Wapi anaishi na nini anafanya, siwezi kuzuia. Tunda ni mke wangu. Siwezi kuishi popote bila Tunda. Sasa natakiwa kufanya nini?” Net alishabadilika rangi. Tunda kimya.

Kuongeza umakini juu ya mama yako kwa Tunda. Na hilo sitalinyamazia Net. Nakuambia ukweli kabisa. Usije kuwa mnaruka moto, mnaenda kukanyaga tanuru. Tumeona nguvu ya mama yako na kile anachoweza kufanya akiamua. Amewasha moto, ameishia kuteketea Gabriel na mkewe ambaye hatakaa akatoka jela. Yeye yupo sehemu ametulia. Sasa kinachonitia hofu ni kuona ile juhudi yake mpaka kufikia kumwaga damu halafu haijatoa matunda aliyotarajia!” Tunda kimya. Akabaki ameinama.

“Sijui kama unanielewa Net? Mimi ni mkweli, na sitawaficha kwa lolote. Gabriel amekufa akiongea machache juu ya mipango yake ya kumuokoa Tunda dhidi ya mama yako na mkewe. Sasa na wewe upo tayari kupambana na adui wa Tunda kama Gabriel?” “Ukinilinganisha na Gabriel unakosea mama Penny.”

“Kivipi? Maana na yeye alikuwa akimpenda Tunda na kumpigania. Niambie tu, ni juhudi gani unafanya au utafanya kumlinda Tunda dhidi ya mama yako? Maana mama ni mama.” “Sina majibu ya kukutosheleza mama Penny. Tokea Tunda yupo jela nilikwambia kile nilichofanya kumsaidia Tunda.”

“Kwa kumtumia bibi yako! Net?” Mama Penny akamshangaa sana. “Hatuombei mabaya, lakini endapo bibi yako akifa leo, ukabakia wewe na mama yako! Akamkabili Tunda kwa staili ileile na uongo atakaochanganya na ukweli fulani kwa vile anavyomfahamu Tunda, utafanyaje? Wewe mkeo anasainishwa talaka mbele yako, umetulia tu!” “Alisema angemuweka jela kama hatasaini.” Net akajaribu kujitetea.

“Sasa ulizuia nini na ni nini kilimpata Tunda na mtoto wenu? Uliishia palepale, Net. Ulishindwa kumlinda Tunda na mtoto wako. Leo tupo hapa, tukizungumzia haya kwa ajili ya maamuzi mabaya uliyochukua, au kushindwa kumlinda Tunda.” Mama Penny alikuwa mkali kwa Net. Alizungumza naye bila kumficha.

“Leo unataka kumtoa tena hapa, unampeleka Canada sijui! Nakuuliza mama yako alipo, hujui! Mipango gani uliyonayo dhidi yake, huna! Kuna mambo yakuombea, na mambo yakusimama wewe kama mume na baba. Ukifanya mchezo, Tunda ataishia jela maisha yake yote. Hakuna mwanadamu ambaye anaweza kutafutwa kasoro, ikakosekana.” Net kimya. Akabadilika, akawa mwekundu. Alishindwa hata kuzungumza tena.

“Labda mimi nikuulize Net. Huko unakotaka kumpeleka Tunda, ni kwako au kwa bibi yako? Na ni kama ni kwa bibi yako, anazo taarifa za ujio wa Tunda? Na je, ameridhia? Nikimaanisha, yeye mwenyewe anafurahia kumpokea Tunda? Kabla hujajibu, naomba kukumbusha Net.” Mchungaji aliingilia, nakuanza kuongea yeye.

“Unakumbuka siku ya harusi yenu? Siku yenyewe kabisa ambapo alikuja mama yako wakati maharusi wapo nje kwenye gari, wanasubiri kuingia? Unakumbuka?” Net kimya. “Mama yako alikuja, akakutisha sana tu. Alilolifanya kwa Tunda, halikuwa geni kwako ila kwa Tunda.” Tunda akamwangalia Net kwa mshangao kisha mchungaji.

“Sina nia yakuwagombanisha, ila nataka kukukumbusha ule ushauri wangu. Nilikwambia, Tunda ni muelewa sana. Ahirisha harusi, nenda kawekane sawa na mama yako, ndipo ujipange upya. Nafikiri unakumbuka majibu yako kwangu. Lakini mlitulia siku mbili tu, Tunda akaishia jela, wewe ukarudishwa Canada na mama yako.” Mchungaji akaendelea.

“Fununu zinasema. Sasa sijui ni kweli au la. Maana zinatoka kwa ndugu wa Bethy. Kuwa mama yako aliwachezea akili Bethy na Gabriel. Ni kama alikuwa akiwazunguka. Akikutana na Gabriel, anapanga hili, na akikutana na Bethy anapanga jingine tofauti na alilolizungumza na mumewe. Amefanya huo mchezo, akijua kote atafanikiwa kufikia lengo moja tu, kumtoa Tunda kwenye maisha yake. Kwa Gabriel alimwambia atakutoa wewe nchini, akutenge na Tunda, ili warudiane. Kwa mkewe, wamfunge Tunda, amtenge na mumewe. Wanandoa wale wote wamekosa, yeye alishinda kwa muda. Lakini katika mipango yake yote, hakutaka kukuumiza wewe hata kidogo, fununu ndio zinasema hivyo.” Mchungaji akaendelea.

“Kinachoendelea sasa hivi, si Tunda tena kusakwa na ndugu wa Bethy na Gabriel, ni mama yako ndiye anayesakwa. Na ninasikia, alichofanya. Tena kwa akili sana. Ameuza mali zake karibia zote hapa nchini, akatoroka.” Tunda na Net wakashituka sana.

“Lakini kila alichouza, au kila mpango aliofanya hapa nchini, alihakikisha hachafui jina lake. Inasemekana kisheria, ameacha mambo yake vizuri sana. Tena kwa kuaga kwenye vyombo vya usalama kuwa anasafiri kikazi au kibishara. Alikaa hapa akiuza mali zake huku akienda polisi akijidai anatoa msaada wowote watakao uhitaji.” Mchungaji akaendelea.

“Kisheria, mama yako ni mtu mzuri sana. Na alihakikisha anaondoka bila lawama, wala deni. Alipokwenda, ndio hapajulikani. Sasa ndio wasiwasi alionao mama Penny.”

“Anapokuuliza mama yako yuko wapi? Au mipango gani uliyonayo dhidi yake, jinsi ya kumkabili, anamaanisha Net. Mama yako anaakili sana katika mambo yake. Lazima ufikirie na kujipanga haswa. Ndipo na maswali yangu sasa ndipo yanapokuja. Unampeleka wapi Tunda? Huko atakuwa ana wenyeji? Sasa je, umeweka sawa mazingira ya huko kwenu? Hapa nyumbani kwao ulishindwa kumtetea. Huko ugenini itakuaje? Jibu la sijui, halitoshi Net. Halitamridhisha mama Penny, na huyo hajui kunyamaza kama mwanae Penny.” Mama Penny akacheka na kumgeukia Penny.

Alipitiwa na usingizi palepale kwenye kochi alipokuwa amekaa. Na mdogo wake alilala pembeni yake. “Kinachomtia wasiwasi mama Penny, au kinachomuumiza ni vile Tunda alivyotupwa. Hata akiwa jela huyo au akapotea, hakuna atakayemdai Tunda wala kumgombania akitaka atolewe.” Tunda akafuta machozi.

“Amefungwa jela, mama yake akachukua kampuni yake, akaigeuza yake. Tena na yeye anafanya vizuri tu! Muulize mama Penny. Anatumia vifaa vya Tunda huyo huyo. Mwanzoni mama Penny alitaka kumpokonya, lakini akawahurumia watoto wake. Akamfundisha kazi kidogo tu. Akaamuachia aendelee kivyake. Alimpa kazi mbili tatu alizokuwa akizipokea mama Penny, hakuchukua hata mwezi, yule mama anakipaji kizuri sana. Tunafikiri ndiko Tunda alikorithi. Mama Penny alikuwa akiniambia jinsi watu wanavyomsifia kama Tunda.”

“Hakuonekana jela, wala hajarudi hapa kutoa shukurani au kujua la kheri wala la shari! Hatujamsikia akimuulizia Tunda, ila akisema anafuta jina la Tunda kwenye kampuni yake, ili isimuharibie kazi. Baba yake naye ndio hivyo. Yule mzee ni muungwana, mpole wa kupitiliza. Hataki maneno kama Tunda. Mkewe kamfukuza, alikuja hapa akaaga, anarudi kwao kufanya biashara. Wewe unamchukua Tunda, unampeleka Canada, wakimfunga huko, ni nani atamtetea?”

CONVERSATION

0 Comments:

Post a Comment