Naomi Simulizi |+1 205 767 8163 |naomisimulizi@gmail.com NILIPOTEA! - sehemu ya 40. - Naomi Simulizi

NILIPOTEA! - sehemu ya 40.

 “Nilipanga nije kukutambulisha rasmi kwa Vic. Anajua kama nilikuoa, na ninakupenda sana. Nilimwambia nimekuchagua wewe, wala sina mpango wa kuja kumuoa yeye tena. Sikumficha kabisa.” “Njoo hapa Net.” Tunda akapiga piga pale kwenye kochi alipokuwa amekaa.

Net akasogea kwa kujihami. “Naomba utulie. Tafadhali. Sijali mambo ya Vic mimi. Kwanza hata simjui!” “Sasa mbona umebadilika?” “Nimechoka Net! Unajua tulikuwa shopping zaidi ya masaa 4! Nimechoka tu wala si sababu ya huyo Vic. Ila hivyo ulivyopanic, ndio umenitia wasiwasi, itabidi tukae tuzungumze vizuri.” “Ham..” “Hapana Net. Sio sasa hivi. Mimi nimechoka. Halafu natamani kusikia habari za mtoto wangu tu, sio habari zako na Vic.” Net akatulia. Akajisogeza vizuri.

“Usiseme habari zangu na Vic! Hatuna habari zetu. Mimi nina habari zangu na Tunda wangu tu.” Tunda akamwangalia kama kumsuta. Net akacheka kwa aibu. Maana alikuwa ameshapaniki mpaka akabadilika na rangi. Akajichekesha hapo, Tunda akimwangalia, akaanza kumuonyesha picha za mtoto walizoona hospitalini kana kwamba Tunda hakuwepo. Pakatulia.

Maisha ya Tunda kwenye hilo hekalu, Nchini Canada.

    Maisha yake yakaanza hapo nchini Canada kwenye hilo jumba kama la maonyesho au kihistoria. Kila picha, kila ukuta au sehemu ilikuwa na maelezo yakutosha ya kihistoria. Akawa na kazi ya kuzunguka na kuangalia picha na sehemu husika. Ndani tu, kabla hajaanza kuzunguka nje.

Akaanza kutumia madawa aliyokuwa ameandikiwa hospitalini, na virutubisho. Walishauriwa wasisafiri kwenda popote au kutokatoka hovyo kwenda popote ili kuhakikisha hapati maambukizi yoyote yale ya ugonjwa wowote hata mafua. Ili arudishe kinga mwilini kwa haraka kabla ya muda wa kujifungua.

Walishauriwa kwa mwezi mmoja mzima, apate mapumziko kama mgonjwa mahututi. Kula na kulala tu. Ili kuhakikisha anaongezeka uzito wake uliokuwa ukishandana na ukuaji wa mtoto wake. Wapo watu wembamba kama Tunda wa safari hii aliyetoka jela, lakini wao huwa wakakamavu, shupavu na afya njema. Yaani ndio miili yao ilivyo, lakini Tunda alikuwa amedhoofu. Kwa kumwangalia na Tumbo kubwa alilokuwa amebeba ni kama alikuwa amelemewa.

Akapewa na dawa za kuzuia kutapika, na kujenga huo mwili wake na watoto. Hivyo virutubisho alivyokuwa amenunuliwa na bibi Cote, vilikuwa vya asili vilivyokuwa vimetengenezwa nchini hapo. Net alihakikisha anavitumia bila kuzembea.

Na bibi Cote pia akahakikisha hawapati wageni ndani ya ile nyumba ili kwanza Tunda apumzike kabisa, na kusiletwe magonjwa yeyote kwa huyo Tunda. Na kweli kazi ya Tunda ikawa kula na kulala.

Kwa muda wa siku 15 tu tokea aanze hivyo virutubisho na dawa, hata Tunda mwenyewe alihisi tofauti kwenye mwili wake. Ile hali yakuchoka sana ikaisha. Baridi ikapungua mwilini. Maumivu ya viungo pia yakapungua.

Angalau ile hali ya usingizi mwingi ikaanza kupungua. Akawa mtu wakupata mapumziko ya masaa mawili tu mchana, tena wakati mwingine alijilazimisha kulala mchana ili kuchelewa kulala usiku apate muda na Net. Lakini hakuwa akisikia usingizi hovyo. Ni kama usingizi wa usiku ulimtosha.

          Ndipo akaweza sasa kuzunguka vizuri kwenye hilo jumba akiangalia kila kitu kwa kutulia na kuanza kuzoea mazingira ya mle ndani. Net ndiye aliyekuwa akirudi yeye mwenyewe nyumbani siku anazotakiwa kwenda kliniki. Hakutaka mtu amsogelee mkewe, kwa kuhofia magonjwa.

Anamchukua mkewe, anampeleka kliniki. Tena huko kliniki akifika, wala hatakaa nje na watu wengine kusubiri. Alichukua masaa ambayo akifika na mkewe, wanahudumiwa wao bila kusubiri. Tena alihakikisha anafanya kliniki kwa huyo mama wa kizungu, ambaye ni daktari wa muda mrefu sana wa wakina mama kwenye kliniki yake ambayo ni ya kulipia. Sio ya wenye uwezo wa kawaida.

Tunda akimalizana na huyo daktari, anamrudisha nyumbani moja kwa moja bila kumpitisha kwenye maeneo ya watu wengi, kuepusha magonjwa, kisha Net anarudi tena kazini. Tunda alikuja kugundua ni kweli Net anahitajika kazini. Kule kuwepo Tanzania na yeye, nakuacha kazi huku, ni mapenzi tu.

Kampuni ya Cote!

Siku moja walipotoka kliniki, Net alimuuliza kama angependa kwenda kutembea ofisini kwao akapaone. Tunda akafurahia hilo wazo. Wakaenda. Ilikuwa ofisi kubwa sana.

Ofisini kwa Maya.

Akaanzia ofisini kwa Maya. Alimkuta Maya cha utundu ametulia kama sio yeye! Tunda akaingia nakuanza kucheka. “Kumbe ukiwa kazini unakuwa mtoto mzuri hivi?” “Hivi wewe unawajua mabosi zangu?” Tunda akacheka. Maya akasimama na kumkumbatia.

“Mabosi wenyewe hata chakula cha mchana hawali, wala hawatoki mchana kwenda shopping! Kila saa simu ile pale ya mezani inapigwa, kuhakikisha nimetulia hapo mezani. Na Nana anataka kazi zangu azipitie yeye mwenyewe kwanza, kabla hazijafika ofisi kubwa!” Akamkonyeza akimuonyeshea Net.

“Lazima nitulie.” Tunda akaendelea kucheka, Net alikuwa akimsikiliza tu huku macho yapo kwenye file, alilokuwa amelikuta hapo juu mezani kwa Maya. Kimya akiperuzi kama hamsikii mdogo wake.

Wakazungumzia mambo ya mtoto. Tunda akampa habari kuwa mtoto yupo vizuri na yeye yupo salama. “Na ofisi yako nzuri sana. Safi kama wewe mwenyewe.” Maya akacheka kwa furaha. “Asante Tunda.” “Ngoja mimi nikuache uendelee na kazi.” Net na Tunda wakatoka.

“Kabla hatujaenda kwa Nana, acha nikuonyeshe upande wa pili ambapo kuna ofisi za wafanyakazi wengine. Huku juu ni ofisi za utawala. Kwa chini ndipo wafanyakazi wengine.” Tunda akafuata nyuma. Akaonyeshwa upande wa chini ambapo kulikuwa na ofisi ndogo ndogo tu zilizotengenezwa kwa kugawiwa vizuri sana ndani ya ukumbi mkubwa sana, ndani ya hilo hilo jengo lao.

Ofisi hizi za wafanyakazi wa kawaida zilitengenezwa kama vyumba au vioksi ambavyo juu vilikuwa wazi kabisa bila milango. Ila walitenganishwa na viukuta vifupi kupita vichwa vyao. Na kuweza kumpa kila mmoja faragha ya kile anachofanya.

Tunda akawaangalia akiwa amesimama juu. Aliweza kuwaona wote vizuri tu. Yeye na Net walikuwa wamesimama sehemu ya juu kidogo ya huo ukumbi mkubwa uliogawiwa hizo ofisi ndogo ndogo za wafanyakazi wote. Kila mmoja wao alionekana yupo kazini ameinamia kompyuta yake. Ni kweli palivutia kwa macho. Tunda akavuta pumzi.

Kwa Bibi Cote.

Ndipo sasa akarudishwa juu, ndani zilipo hizo ofisi za utawala. Wakaelekea ofisini kwa huyo bibi. Hapo ndipo Tunda akaelewa kweli yule bibi ni mtu wa maana. Hiyo ofisi yake tu, ilijaa vitu vya maana vitupu. Kulipoa na kulipendeza kuanzia kiti alichokalia yeye mwenyewe mpaka meza na kapeti.

Watu aliokuwa akiwaongoza, au waliokuwa chini yake, ungejua anafanya kazi za maana. Alionyeshwa wasichana wawili ambao aliambiwa ni sekretari wake huyo bibi tu kutokana na majukumu mengine yanayomkabili mbali na ile kazi pale.

Wakati wote bibi huyo alikuwa kwenye kiatu cha juu. Kwa ule umri wake, usingemtegemea kama anaweza kukitembelea. Nadhifu sana na alijua kujitengeneza vizuri. Akili yake ilionekana ipo makini wakati wote. Na alijibeba kitawala.

Akasimama pale Tunda na Net walipoingia. Akavua miwani yake, na kuiweka juu ya meza. Ofisi yake ilinukia pafyumu anayotumia yeye mwenyewe. Kusafi. “Huku sio salama kwa Tunda, bwana! Kwa nini umemleta?” “Daktari amesema ni sawa. Kwa sasa anaweza kutoka kidogo.” “Ila sio kupeana mikono! Umekumbuka hand sanitizer?”  Akauliza bibi Cote akionyesha wasiwasi kidogo na kujali. “Ninayo kwenye pochi.” “Afadhali.” Akaonekana kuridhika.

“Cote anaendeleaje?” Akauliza tena. “Uzito umeongezeka na urefu zaidi. Kweli dokta anasema atakuwa mrefu kama Papa.” Bibi yake akacheka. “Na Tunda?” Akamgeukia Tunda. “Kila kitu kipo sawa kabisa. Amefurahia kuongezeka kwangu. Anasema japokuwa sijafikia uzito ninaotakiwa, lakini ameridhishwa na mabadiliko aliyoyaona. Amesema naweza kuanza kutembea kidogo.” “Hizo ni habari njema. Kazana kula, na usisahau dawa.” Tunda akamuona ameridhika.

“Nakwenda naye ofisini kwangu. Nitakaa naye mpaka tukiwa tunatoka.” Net akamwambia bibi yake wakati anamsogelea. Akambusu. “Okay. Akichoka umrudishe nyumbani.” “Atakuwa sawa tu. Si ndio Tunda?” Tunda akacheka na kutingisha kichwa kukubali. Net akamshika mkono, akambusu, wakatoka pale.

Alipita akimtambulisha kwa wafanyakazi waliokuwa wakikutana nao hapo njiani, ndipo akaenda ofisini kwake. Nje alikuwa na sekretari mwanamke mtu mzima kama wa miaka 60 hivi.  Alionekana kumfahamu vizuri sana Net. “Alikuwa na meza yake hapo ndani kwenye ofisi ya babu yake, akifanya kazi zake za shule pembeni ya babu yake. Ngumu kuamini kama na yeye anakaribia kupata mtoto!” Akamwambia maneno machache Tunda kumuonyesha anamfahamu huyo Net tangia anazaliwa mpaka hapo alipo. Akamuonyesha na picha zake na Net alipokuwa mtoto mdogo tu, wakacheka kidogo, ndipo wakaingia ofisini kwa Net.

Alikuta picha yake na yeye mwenyewe Net, walipigwa na Maya. Net alikuwa amepiga magoti akibusu tumbo lake. Tunda akacheka wakati anaiangalia. Ilitoka vizuri sana. Hakujua kama aliitengeneza. “Nzuri!” Akasifia. “Thanks.” Net akajibu huku akikaa. “Mbona wewe ofisi yako kubwa kuliko wote!?” “Na majukumu ni makubwa. Ofisi yangu ilikuwa ni pale alipo Maya. Hii ilikuwa ofisi ya babu kama ulivyomsikia akikusimulia Ms Linda. Nimechukua majukumu yake yote.”

“Natakiwa kukupa hongera. Si ndiyo?” “Siwezi kulalamika. Bibi kukupa jukumu lolote, ujue amekuamini. Kwa hiyo nilifurahi. Japo imenibidi kuongeza nidhamu na umakini. Nana amefanya kwenye hii kampuni akiwa mdogo kidogo kwa Maya, akisaidiana na Papa. Anasema umakini na kutozembea ndio kitu pekee kilichoweza kuwaweka sokoni mpaka sasa.” Akaendelea.

          “Usimuone vile, haondoki pale ofisini kwake kila siku, mpaka amepitia kazi za kila mtu humu ndani. Hakuna kinachoendelea humu ndani, kwa yeyote, asijue.” Tunda akaendelea kuzunguka mle ndani ofisini kwa Net.

Alishika hiki, akaangalia kile. Picha tofauti tofauti. Akaona picha za Net na babu yake. Kisha picha nyingine alikuwa baba yao, Net mwenyewe, Maya akiwa mdogo sana kama anayejifunza kukaa, mama yao, babu na bibi yao. Ilionekana ni ya zamani sana kama kipindi cha Chrismas kutoka na yale mapambo kwenye ile picha na nguo walizokuwa wamevaa. Akaangalia hiyo picha kwa muda. Wote walikuwa pamoja.

Kisha akaiweka chini na kuendelea kuangalia hiki na kufungua kile. Akazunguka mle ofisini, kisha akarudi kukaa. Kimya. Kwa kuwa Net alishapotelea kwenye kazi zake. Akatulia bila hata kuuliza swali. Baada ya kama nusu saa ndipo Net akanyanyua uso kumtizama. Tunda akacheka.

“Nipe kazi yeyote.” Net akafikiria kidogo. Akanyanyua simu. “Hey Nana!” Moyo wa Tunda ukapasuka. “Ni sawa Tunda akija hapo kwako ukamuonyesha kitu unachokifanya sasa hivi?” Akamuona Net anacheka na kukata simu. “Haya nenda kwa Nana. Amesema anakazi anataka umsaidie.” “Net! Mimi nilitaka wewe bwana!” Net akasimama, akaenda pale alipokuwa amekaa akaanza kumbusu. Akambusu taratibu tu. Kisha akamtengeneza vizuri.

“Hapa nina mambo ninafanya, yanahitaji umakini kidogo.” “Ni nini?” “Wewe nenda kwa Nana, atakwambia ninachokifanya, maana kila nikimaliza, lazima apitie kujiridhisha. Nenda na uache kumuogopa. Itakusaidia kuanza kuzoeana. Kazi zote anazozifanya yeye, ujue siku moja zitakuwa zako. Kwa hiyo nenda kaige na uzoefu wa miaka ya karibia 70 sasa.” Hapo Tunda akaridhika. Akamsaidia kusimama, akatoka bila kusindikizwa, Net akarudi kuendelea na kazi zake.

Mazungumzo ya kwanza ya Tunda & Bibi Cote wakiwa peke yao.

    Alimkuta bibi Cote akimsubiria. “Ofisi yangu ni ofisi ya ukaguzi. Unaweza kusema nafanya auditing kitaalamu. Ahitajiki msomi kuwepo hapa nilipokaa, ila mtu makini, na anayejua kazi kwa kufanya. Sijui kama umenielewa?” Tunda akakaa. “Nakusikiliza.” “Wasomi tunao wahitaji humu ndani ni wachache sana, kama Logan, ambaye ni mwanasheria wa kampuni, na watu wengine. Hata kazi anayofanya Maya ya masoko, inahitajika mtu makini tu. Kujua wapi kuna uhitaji, na kufuatilia bila kukubali jibu la hapana au subiri. Kwa kuwa ukikubali jibu la subiri la siku moja tu, utaua kampuni.” Bibi Cote akaendelea.

“Kwa hiyo ninapokaa hapa, nafuatilia kazi za Maya. Kujua kwa siku hiyo ametupatia masoko mangapi. Yale tuliyo nayo anayatunzaje ili tusipoteze wateja. Napigia simu wateja tulio nao kwa sasa ili kufuatilia kama madereva walifikisha mizigo kwa wakati na salama.” Akaendelea.

“Napitia kila matumizi ya humu ndani. Kuanzia mshahara mkubwa mpaka wa vibarua. Kupitia majukumu ya kila mtu humu ndani. Kujua nani anabaki, nani ahamishwe na nani haitajiki tena. Pesa zinakwenda wapi na kwa nini ziende huko. Mteja yupi ni wa kumuacha na yupi wakumbana atupe kazi nyingi zaidi.” Tunda akakunja uso.

“Mbona sasa wewe ni kama unakazi nyingi kuliko wote?” Bibi Cote akacheka. “Kwa mfano Maya. Pale alipo amepewa mwezi mmoja wakutafuta angalau wateja wapya wawili watakao taka huduma yetu. Bila hivyo Net amemwambia atamuhamisha kitengo, mbali na hapa, kwa mshahara mdogo, kwa kuwa atakuwa haingizii kampuni faida. Anakuwa anaendelea na wateja alio wakuta tu.” Tunda akaanza kucheka.

“Ndio maana halali! Usiku anachelewa kulala, na asubuhi anawahi kuamka!” Tunda akaanza kuelewa. “Na hatoki mchana muda wa kula, kwenda kununua vitu visivyo vya maana. Bila hivyo tulijua hataweka akili kazini na atajua wote tunacheza tu hapa.” Tunda akaendelea kucheka akimfikiria Maya.

“Hata muda wachakula siku hizi haulizii tena. Isingekuwa hivyo, sasa hivi ungemkuta amelala pale kwenye lile kochi pale mbele yangu, analalamikia hili au lile, anataka tuwahi kutoka tukatengeneze kucha.” Tunda akaendelea kucheka.

“Jumamosi hii ameniambia twende kwenye kucha.” “Mkubalie tu. Amefanya kazi sana mpaka tunamuhurumia.” “Lakini si anajua hata asipopata wateja, Net hawezi kumfukuza?” Bibi Cote akacheka sana. “Kumbe humjui mumeo hata kidogo!” Akacheka tena, akakaa vizuri kwenye kiti chake kilichofanana na Net, lakini chake kilikuwa na rangi za zambarau kama vitu vingi vilivyojazwa ofisini kwake. Hata kapeti ya juu ndogo ya manyoya kuzunguka meza yake na kiti alichokalia ilikuwa zambarau nzuri sana. Alionekana anapenda rangi hiyo yakitajiri.

“Net!?” Tunda akauliza kwa kushangaa kidogo. “Wewe unafikiri ni kwa nini babu yake alitaka akalie kile kiti pale?” Tunda akaangalia alipokuwa Net. Ofisi zao, bibi yake na yeye, zilitenganisha na vioo tu. Lakini ni kama Net alimpa mgongo bibi yake. Ni kama meza yake ilikaa pembeni kidogo. Akamuona ameinama akiandika kwa makini vilevile.

“Vile unavyomuona Net, ndivyo alivyokuwa babu yake. Baba yake Net, CJ, alikuwa kama mimi. Soft kidogo. Huruma na anasikiliza hata matatizo ya wafanyakazi na kusamehe. Lakini sio wao. Wao wanataka kazi ifanyike. Wafanyakazi wote wanamjua Net. Akikupa jukumu, anataka ulifanye. Yaani aone matokeo.” Tunda akamgeukia tena Net kama asiyeamini.

“Kutofanya, kwa sababu yeyote ile. Namaanisha sababu yeyote ile, inamaana huwezi kufanya kazi kwenye hii kampuni. Na hajui kutoa onyo la kwanza na la pili. Anakwambia wafanyakazi wote humu ndani ni kama mwili mmoja. Hakuna wa muhimu na asiye na muhimu. Ukishindwa kufanya jukumu lako hata moja, inamaana umekwamisha kazi za watu wote, na hilo haliwezi kuvumiliwa. Hakika anakutoa. Ni Maya tu ndio anaahadi yakupunguziwa mshahara na kuhamishwa kitengo.” Tunda akamgeukia tena Net. Alikuwa vilevile ameinama.

“Vile unavyomuona pale, hatanyanyuka mpaka akamilishe anachokifanya. Anamaadili mazuri sana ya kazi aliyofundiswa na babu yake. Ile ofisi alikuwa akiikaa tokea anatoka shule, mtoto mdogo, anaingia pale kufanya kazi zake za shule. Jumatatu mpaka ijumaa. Na wakati mwingine siku za jumamosi alikuwa akija na babu yake hapa kazini. Labda awe na kitu anachofundishwa jioni. Yaani masomo ya ziada. Ndipo akitoka shule, atarudishwa nyumbani kufundishwa. Lakini wakati wote utamkuta na babu yake.” Akamuona anafikiria kidogo, kisha akaendelea.

“Kitendo cha kuamua kwenda kuishi Tanzania, tena babu yake akijua hatapona, kilimuuma sana babu yake. Maana alimlea akijua atachukua majukumu yake. Lakini pia aliamua kumuamini kwa kila uamuzi anayoamua Net.” “Nini kilimpelekea kuchagua Tanzania?” Tunda akauliza taratibu.

Bibi Cote akacheka kidogo. “Hakukwambia?” Tunda akatulia kidogo kama anayefikiria. “Alipokuwa anamalizia chuo huku, hakuwa ameamua kama ataishi Tanzania akimsaidia mama yake au la. Lakini kwa jinsi alivyokuzwa, wote tulijua atamaliza chuo na kuanza kazi hapa.” Akaendelea bibi Cote.

“Alikwenda likizo kwa mama yake, mama yake akaanza kumpanga ili akamfanyie yeye kazi. Akawa yupo njia panda. Akawa mtu wa kwenda na kurudi tu bila uamuzi wa kuishi Tanzania moja kwa moja mpaka akamuona Tunda.” Tunda akashituka sana. Hakutegemea.

“Hapo ndipo kila kitu kikabadilika kwenye maisha yake. Kila kitu akataka kisubiri, atafute ‘true love’. Babu yake akamwambia hata hapa anaweza kumpata, lakini tayari akawa ameingia Tunda kwenye picha.” Bibi Cote akacheka kidogo kama anayevuta kumbukumbu. “Kila tukimuuliza Tunda ni nani? Yeye mwenyewe hamfahamu, lakini ikawa ni vurugu. Yupo huku, akili zipo Tanzania.”  Tunda hakuwa anaamini, akamgeukia tena Net. Bado alikuwa ameinamia kompyuta yake, lakini safari hii alinyanyua kichwa kidogo kama anayefikiria.

“Alipomaliza tu chuo, akarudi tena Tanzania. Akamtafuta Tunda kama mwezi, akamkosa. Lakini mwezi huo mmoja alikuwa akimsaidia kazi mama yake. Mama yake akautumia huo mwezi vizuri sana kubadili akili ya Net, baada yakuona jinsi anavyochapa kazi na akili aliyonayo kwenye kuwekeza.”

“Sijui alimwambia nini, akafanikiwa kuingia kwenye akili yake, akageuza kabisa akili ya Net, akajiona analo jukumu kubwa sana lakumtunza au kumsaidia mama yake. Kuishi huku na mama yake kuwepo kule peke yake ni kama kumtelekeza.” Bibi Cote akaendelea, Tunda akimsikiliza.

“Alirudi huku siku moja tukijua ndio anaanza majukumu ya huku, akaomba kikao cha mimi pamoja na babu yake. Akazungumza mambo mengi, akijitetea maamuzi yakuamua kuishi akimsaidia mama yake nchini Tanzania huku akisema anamtafuta Tunda aliyeambiwa alifukuzwa huko alikokuwa akiishi kwa ndugu. Ni kama Mungu anamtuma kitu kwa Tunda.”

“Hapo hakuwa amesema moja kwa moja anakutafuta sababu ya mapenzi. Hata yeye hakuwa akijua ni kwa nini anataka kukuona. Babu yake aliumia sana na kumlaumu sana Ritha. Lakini hakutaka kumwambia Ritha mwenyewe. Kwa kuwa Ritha ni kama aliwatelekeza watoto wake hapo, tena wakiwa wadogo, sisi, au niseme mimi niliwalea kama watoto wangu.” Tunda akakunja uso.

“Lakini Net aliniambia kuwa mama yake alianzisha biashara iliyokuwa ikimuhitaji sana huko Tanzania, nyinyi ndio mkamuomba muwalee wao. Net na Maya.” Bibi Cote akatabasamu huku akifiria kidogo.

“Jumamosi sitakuja kazini. Nimemwambia Net naanza kupunguza masaa ya kazi. Ikiwemo siku ya jumamosi, nitakuwa nakuja ikilazimu. Lakini msimu huu hauna kazi nyingi sana, hata nyumbani naweza kufanya kazi zangu hizo siku za jumamosi. Tena ikilazimu. Nitakwambia kitu ambacho si Net tu, hata Maya mwenyewe hafahamu.” Tunda akatulia kidogo kisha akajibu sawa.

Alimuonyesha kazi anazofanya hapo. Akamzungusha kwenye kila ofisi kwa kutumia kompyuta yake palepale ofisini kwake. Nani anafanya nini wakati huo. Siku hiyo kama ametimiza jukumu lake, na kama hakutimiza, ni kwa nini na akamwambia inamaana Net anajua kama huyo mtu hajatimiza, na ni kwa makubaliano.

Muda wakutoka ukafika. Wafanyakazi wakaanza kutoka, Maya akafika ofisini kwa bibi yake akajitupa kwenye kochi kama aliyelemewa haswa, bibi yake akamkonyeza Tunda, Tunda akacheka na kumgeukia Maya pale alipolala.

“Hey baby girl!” Bibi yake akamuanza wa upendo. “I just wanna go home.” Akalalamika huku amefunga macho akimwambia anataka kwenda nyumbani. Mpaka hapo, wafanyakazi wote walikuwa wameshaondoka, wamebaki wao tu wanafamilia.

“Umemaliza?” “Hapana Nana! Naomba uzungumze na Net. Anafanya maisha yangu yanakuwa magumu! Kila kitu ananikosoa. Hakuna kitu nafanya sahihi!” “Kwa hiyo unakuwa umefanya sahihi lakini anakusingizia?” “Come on Nana!” Maya akakaa.

“Mimi nauliza tu!”  “Ni vitu vidogo vidogo havina hata maana, Nana! Anavikuza. Anataka kila kitu kiwe vile anavyotaka yeye!” “Sidhani ni kama anavyotaka yeye, nafikiri ni kama inavyotakiwa.” “Nilijua hutakosa sababu yakumtetea. I just wanna go home.” Maya akaendelea kulalamika. Siku hiyo walikwenda kazini na bibi yake hakuendesha gari yake.

“Maisha yangu yamebadilika! Kila mtu alikuwa akinijua kwa kuvaa vizuri. Lakini sasa hivi navaa kawaida! Hamna muda wa shopping! Hakuna muda wakwenda salon kama zamani! Hebu angalieni kucha zangu jamani! Zipo hivi zaidi ya …” “Ni jumamosi mbili tu zimepita Maya.” Bibi yake akajaribu kumkumbusha.

“Sasa wewe unafikiri ni kawaida!? Nani anakaa na kucha za aina moja zaidi ya majuma mawili? Siendi club! Na unajua nini?”  Akaangalia kule alipokuwa amekaa kaka yake. Akapunguza sauti, akamsogelea bibi yake pale mezani.

Ofisi ya Maya ilikuwa upande wa pili wa upande zilipokuwepo ofisi ya Net na bibi yao. Ofisi yake ilikuwa nusu imetengeneza nusu na aluminium nzito, juu ndio kioo. “Kana kwamba haitoshi ile deadline ya mwisho wa mwezi, amesogeza imekuwa week hii. Namaanisha hii tuliyo nayo sasa hivi!” Akamtolea macho bibi yake.

“Hivi unajua zilikuwa zimemebaki siku ngapi hii week iishe kwa usalama nikiwa na furaha?” Maya akaendelea kulalamika.  “Leo ni jumatano, Maya.”  Bibi yake akajaribu kumkumbusha taratibu. “Exactly! Ndivyo ilivyotakiwa iwe kwa watu wote. Na ijumaa jioni niende na marafiki zangu club, jumamosi niende salon. Lakini unajua imebidi ratiba ya juma zima ibadilike Nana! Niwaambie rafiki zangu siwezi kwenda nao club, na jumamosi hatuwezi kutoka. Kwa sababu ‘Mr Boss’.’ Akanyanyua vidole vyake viwili kumkejeli kaka yake.

“Amesema akiingia hapa ofisini jumatatu ijayo, kazi aliyonipa iwe imekamilika! Isipokuwa imekamilika, inamaa…” “Umeshindwa kufanya.”  Bibi yake akamalizia. “There you go Nana! Na unajua kama nimeshindwa mimi kufanya amesema atafanya nini?” “Atampa mtu anayeweza kufanya.” Bibi yake akajibu taratibu tu.

No Nana! ANAAJIRI mtu anayeweza kuifanya. Na amesema hana bajeti yakulipa wafanyakazi wawili kwa jukumu moja. Sasa unajua ni nini kitatokea kwangu?” “Utakuwa na muda wakutosha kufanya shopping zako, kwenda saluni na club na marafiki zako.” Tunda alikuwa anasikia kucheka vile anavyolalamika na bibi yake kumjibu taratibu tu.

No Nana. Nooo! Amesema itabidi nimpishe huyo mtu kwenye ile ofisi. Ili atumie meza yangu, kompyuta yangu, kiti changu, kufanya kazi niliyoshindwa mimi.” “Lakini itakusaidia kupata muda wa kutosha kufanya mambo yako.” Maya akavuta kiti akakaa. “Amesema itabidi amlipe mshahara wangu. Wangu Nana! Hivi unanielewa? Inamaana nitakuwa siingizi tena pesa."

“Inamaana, kila mtu aliyepinga akinikejeli kwamba siwezi kutulia kazini, Vic akiwa mmoja wapo, watasema wapo sahihi. Mimi sio mtu wakutulia nakufanya jambo lakueleweka. Mimi sio smart. Na sitaki kuwapa faida. Zaidi Vic. God I hate the girl!” “Hate is a strong word, Maya.” “Ghhhhhh.” Akanguruma kwa hasira.

Then I DON”T like her. Simpendi yule kiumbe kupita kila kitu hapa duniani. Kama Net akinifukuza kazi hapa, watapata sababu yakunisema. Nitakua gumzo mtandaoni tena! Na siwezi kuwapa sababu.” Akasimama huku ameweka uso wa huzuni.

Tunda alikuwa akimsikiliza huku akicheka taratibu. Hapo alipokuwa alikuwa amependeza sana. Kila kitu alichoweka mwilini mwake, kuanzia juu mpaka chini kilikuwa kizuri na cha thamani. Alipendeza, ungependa kumwangalia. Lakini alilalamika kuwa anaonekana kama msichana mkulima au mfuga ngurue. Kucha zake mbaya. Wakati zilikuwa nzuri tu.

Wakamuona anatuma ujumbe, kisha akarudi kukaa. “Imebidi kumwambia yule dada anayenitengeneza kucha na wa nywele, kuwa sitaweza kwenda jumamosi hii. Maisha yangu yameharibika Nana!” Akaanza kulalamika tena. “Labda uende tu saluni, halafu jumatatu utazungumza na Net.” “WHAT!?” Akashituka Maya kama bibi yake anataka kumponza vibaya sana.

“Wewe si unamjua huwa hanipi nafasi yakuongea? Anachotaka ni kazi yake. Labda…” Akaanza kumchekea bibi yake kama aliyepata wazo. Akajisogeza karibu. “Pengine wewe, my sweet and wounderful Nana, uzungumze naye. Wewe huwa anakusikiliza.” “Oooh! Nimwambie kuwa Maya hataweza kufanya kazi, kwa kuwa anaenda club ijumaa, na jumamosi inabidi akatengenezwe kucha na nywele ili jioni atoke na marafiki zake tena.” “Usiongee kwa kejeli Nana! Nisaidie. Nikifanikiwa weekend hii, nakuahidi, weekend ile nyingine, nitatulia kazini.”

“Sawa kabisa. Hilo wazo zuri. Sasa kwa kuwa tatizo la Net ni kazi ifanyike. Sasa wewe tafuta mtu utakayemlipa kwa weekend hii unapokuwa club. Mlete hapa kesho. Mimi nitampeleka kwa Net. Nitazungumza naye.” Maya akatulia kama anayefikiria.

“Mimi ndio nitamlipa?” “Si atafanya majukumu yako!?” Bibi yake akamuuliza taratibu tu. “Kwa nini usimwambie Net aidhinishe malipo yake?” “Kwani wewe alikwambia nini?” “Can’t remember.” Mpaka Tunda akacheka kwa sauti vile Maya alivyosema hakumbuki alichoambiwa na kaka yake.

“Maya! Si umetoka kusema kuwa amesema hana bajeti ya kuongeza mfanyakazi mwingine?” Bibi yake akamkumbusha. “Oooh yeah!” Akajidai kukumbuka. “Kwa hiyo utazungumza na Net kama nikimtafuta huyo mtu?” “Kabisa. Wewe acha funguo za ofisi hapa na password ya kompyuta yako, pamoja na palipo ya huyo mtu. Nitamkabidhi Net.” Maya akabadilika kabisa. Akapooza.

“Itakuaje awe mzuri hapa kazini kuliko mimi? Hudhani Net anaweza kumpa majukumu yangu moja kwa moja?” “Atakutafutia majukumu mengine ambayo hayatakufunga sana.” “Unawezaje kusema hivyo Nana, jamani!? Sasa hapa upo upande gani?” “Wako Maya! Na itakusaidia kupata majukumu rahisi, na utakuwa huru kufanya mambo yako.”

“Sasa si unajua wazi atanihamishia kwenye ofisi zile za wafanyakazi wote na mshahara atapunguza!?” “Lakini utakuwa na muda wakutosha kufanya mambo yako? Club, saluni na dinner na rafiki zako.” Akaendelea bibi Cote. Taratibu tu.

“Hata yeye alikwambia Maya. Mshahara mkubwa, unakuja na majukumu makubwa. Alikwambia mapema kabisa. Anakupa ofisi, bili ya simu itakuwa juu ya kampuni, na mshahara mzuri lakini anataka kuona matokeo. Alikwambia hatawekeza sehemu ambayo hatapata faida.” Bibi yake akaendelea taratibu tu.

“Alikupa thamani ya kile chumba unachotumia sasa hivi. Matarajio yake. Sasa kama umeshindwa mwambie tu. Atatafuta mtu mwingine ambay…” “No nononooo! Sijashindwa. Na wala usimwambie hivyo. Mimi naweza kufanya kazi zangu zote. Kwanza nimeshakuwa mkubwa. Mambo ya club nimeacha. Halafu saluni naweza kuahirisha nikaenda siku ambayo sina mambo mengi. Sio lazima jumamosi.” Maya akaanza kutoa mipango mipya kama sio yeye. Akakanusha mambo yote. Akaacha kulalamika kabisa. Bibi yake na Tunda wakabaki wakimsikiliza.

Mara akaingia Net. “Nilikuwa namwambia bibi jinsi ulivyoniamini na majukumu mengi na mazito.” Net akamtizama, maana aliingia tu, Maya akamdaka akionyesha wasiwasi kidogo usoni. Kama anayejihami.

“Ila sijalalamika. Nimemwambia Nana, jumamosi wakati wewe unakuja kazini, na mimi nitakuja. Mpaka inafika jumamosi jioni, nitakuwa nimekamilisha kila kitu. Jumatatu ukiingia kazini utakuta kila kitu kipo tayari.” “Good!”  Akajibu kaka yake kwa kifupi tu.

Akamsogelea Tunda, akainama, akambusu midomoni kwa muda kidogo. Akageuza kiti alichokuwa amekalia Tunda pale mbele ya meza ya bibi yake, akamgeuzia upande wake. Akapiga magoti mbele yake. “Vipi?” Akamuuliza. “Safi tu, nilikuwa naonyeshwa kazi.” Tunda akajibu.

          “Nilikuwa pia namwambia Tunda, asione kama maisha ni mapweke sana huku. Kufungiwa ndani tokea anafika. Ningekuwa sina kazi jumamosi, ningemtoa dinner, kwenye hoteli nzuri sana.” Maya akaingilia.

“Pamoja na wale rafiki zako walevi?” Net akamuuliza huku akipapasa tumbo la mkewe na kulibusu. Maya akababaika kidogo. Kaka yake alikuwa amempa mgongo. “Sio wale.” “Unarafiki gani ambaye sio mlevi?” Net akamuuli taratibu tu, kisha akabusu tumbo la mkewe tena.

“Kama sio walevi wa madawa ya kulevya, basi pombe kali na wavuta sigara. Na kama umesahau, Tunda ni mjamzito. Moshi wowote wa sigara na madawa yenu ya kulevya, utamwathiri Cote na mama yake.” Kimya. “Umenielewa Maya?” Net akasimama na kumgeukia Maya. “Siwezi kumpeleka huko!” “Na wala usifikirie. Kama wewe unataka kwenda, nenda. Ila ujue wazi, watakurudisha rehab.” Net akaendelea huku akimwangalia Maya kwa ukali.

“Na safari hii ukirudi tena rehab, ujue umepoteza uaminifu wako wote. Hutakaa kufanya kazi  hapa tena. Itakuwa ni juu yako wewe na Nana. Umenielewa Maya?” Maya alionekana ameshaingiwa hofu yakupitiliza.

“Mbona mimi nimeacha kabisa? Nimekuahidi nitatulia. Ndio maana unaniona mpaka sasa hivi nipo hapa.” “Kwa nini unarudia maisha ya club?” “Sijarudia.” “Maya?” Kaka yake akamuita kwa ukali kama akimuonya, usinidanganye. Maya akababaika sana.

“Nilitaka kwenda tu kusalimia rafiki zangu. Sio club kama zamani.” Maya akajibu kwa hofu huku akimtizama kaka yake. “Sponsor wako alikwambia nini?” Net akamuuliza. Maya akatulia akijidai anafikiria. “Maya?” Net akamuita kama asipoteze muda, amjibu. “Kuhusu nini?” “MAYA?” Net akamuita kwa ukali, akiwa ameshabadilika mpaka Maya akarudi nyuma huku akimtizama bibi yake.

“Alisema nikae mbali na club na kundi zima la marafiki niliokuwa nikitumia nao madawa ya kulevya wakati ule na wakanifanya nirudie tena.” Tunda alishituka kidogo. Hakujua kama Maya alitumia madawa yakulevya.

“Na sasa hivi unataka kufanya nini? Tena unataka umpeleke na mke wangu!” “Sio kwa nia mbaya Net. Am so sorry.” Akaanza kulia. “Sitaki kurudi tena rehab.” “Then stay away from all clubs and your friends. Unaweza kutafuta marafiki wengine, ukatafuta kitu kingine chakufanya na ukafurahia maisha tu. Tafadhali badilika Maya.” “Nimebadilika Net. Nakuahidi nimebadilika. Muulize Nana.” Maya akamsogelea bibi yake akitaka utetezi.

“Mwambie Nana. Nana ndio amekuwa rafiki yangu. Sinywi hata wine. Nakuhakikishia Net. Hata ulipoondoka, nilikuwa naenda saluni na kurudi nyumbani. Mwambie Nana.” Hapo Maya alikuwa akilia kwa hofu. Akiongea huku akimwangalia bibi yake akitaka utetezi kwa Net.

“Unajitahidi Maya. Hata mimi nakupongeza. Sasa jitahidi kuepuka vishawishi. Weka akili zako sehemu sahihi. Hutarudi tena rehab.” Bibi yake akamtia moyo. I love you Net!Mpaka Tunda akamuhurumia. Alionekana Net alimbadilikia. Mahusiano aliyowaacha nayo mara ya mwisho sio haya. Maya alimuogopa sana tofauti na zamani walipoishi pamoja Arusha.

Tunda akamtizama Net kama anayetaka apokee ujumbe fulani. Net akamtizama kidogo Tunda, akamgeukia Maya. “Am so sorry Net.” Maya akaanza. “And I love you so much.” Kakaongea kwa upendo huku akilia kwa hofu kama anayebembelezea undugu.

Net akavuta pumzi kwa nguvu huku akimwangalia. “I love you too Maya. Najua unajua. Nisingekutaka kitu ambacho najua huna uwezo nacho. Nakuhimiza kwa kuwa najua unao uwezo mkubwa sana.  Ndio maana unapokuwa na muda mwingi usio na matumizi, unaanza kufanya maamuzi mabaya. Unafanya kazi nzuri sana. Umetushangaza mimi na Nana. Sikutaka kukwambia kwanza, mpaka baada ya mwisho wa mwezi. Lakini unafanya kazi nzuri.” Net akajirudi kidogo.

“Kuna moja ya mtu ambaye ulikuwa ukimfuatilia. Mteja. Amempigia simu Nana. Amekusifia sana. Kwako alikukatalia. Lakini alikuwa akikuchezea tu akili. Ni wateja wetu wa zamani. Walifilisika. Wakafunga bishara yao. Alikuwa kimwambia Nana, ndio wameanza upya. Wewe ndio umewatafuta. Hakuna hata aliyekutuma. Mimi na Nana, tukahisi ni kuwa ulipitia wateja wa zamani waliokuwa wakiingizia kampuni faida, ukawapigia. Si ndio?” Maya akacheka huku akijifuta machozi.

“Unaona sasa? Hiyo akili bila madawa ya kulevya, inafanya kazi vizuri sana.” “Net!” “Yes Maya. Mbali na wale marafiki zako, na ulevi, wewe ni msichana mwenye akili sana. Una uwezo mkubwa wakufikiria na kufanya mambo. Umepata nafasi nyingine, na naomba iwe ya mwisho. Usirudie tena.” “Sitarudia. Kwa hiyo wamekuwa wateja wapya?” Net na bibi yao wakacheka.

“Wanaanza biashara, na sisi ndio tutakuwa tukiwasambazia bidhaa zao sehemu zote. Na hiyo ni wewe umefanya. Hata Nana amekiri kuwa aliwasahau. Lakini wewe umewasaka mpaka umewapata. Nikafurahi sana. Sasa nashangaa unataka kurudia tena kule ilikotugharimu kukutoa! Mbaya zaidi na mke wangu! No Maya.” “Am so sorry Net. Nakuahidi sitarudia tena. Nakuahidi. Nisamehe.” Net akamsogelea akambusu kisha akamkumbatia.

“Jumamosi tutakuja wote kazini.” Maya aliongea akiwa amekumbatiwa na kaka yake. Net akacheka. “Na uhitaji kukaa hapa kazini muda mrefu kama mimi. Jumamosi unaweza kujipangia masaa machache kama alivyokuwa akifanya Nana, kisha unaendelea na mambo yako. Shopping au saluni.” Maya akacheka.

“Basi kama ni hivyo sihitaji kuahirisha saluni. Nitawaambia nitakwenda mchana.” Bibi yake akacheka, “Hutafuti tena mtu..” “Shhhhh! Nana!?” Maya alishituka sana akaruka pale alipokuwa amekumbatiwa na kaka yake akaenda kumnyamazisha bibi yake. Hakutaka Net asikie.

“Nimebadilika. Sasa hivi ni Maya Cote. Cote huwa tunafanya kazi kwa bidii, na tunaishi kwa kufikiria.” Wote wakacheka. “Twende Tunda.” Net akamshika mkono mkewe, wakaondoka.

Net ampa Tunda historia ya Maya hapo nchini.

    Wakati wapo njiani ikabidi Tunda kuuliza. “Kwani Maya alishatumia madawa za kulevya?” “Pale alipo, hawezi kuajiriwa popote. Yupo kwenye mitandao yote ya sheria kuwa ni binti mlevi, mwizi, kahaba na kila sifa mbaya unayoweza kufikiria. Hata wakati ule alipokuja Tanzania, ukakutana naye mara ya kwanza, tukaishi naye Arusha, mama ndiye aliyelazimisha aletwe kule kwa muda. Alikuwa ametoka tu rehab, na ni kama alikuwa na hatari ya kurudia tena madawa ya kulevya.” Tunda akashangaa sana.

“Unakumbuka alimaliza tu high school akawa hataki kwenda chuo?” “Uliniambia.” “Basi kazi yake ilikuwa hiyo. Wanaume na madawa ya kulevya. Gari anayoendesha sasa hivi, ni yake. Tumekataa kumnunulia gari nyingine, kwa kuwa gari ya kwanza aliyokuwa amepewa na babu na Nana kama zawadi ya birthday yake alipofikisha miaka 16, alipata nayo ajali mbaya sana.” Tunda akamgeukia Net aliyekuwa akiendesha.

“Alikuwa yeye na boyfriend wake. Wote wamelewa. Nikikwambia ni gari ya thamani, niamini ilikuwa ni ya thamani SANA. Walimnunulia kwa pesa taslimu. Wakaigonga vibaya sana. Yeye alipata michubuko tu, mwenzake alilazwa karibia mwezi. Ilikuwa mbaya sana. Maana walinasa kama chini ya daraja. Waokoaji walipata shida sana kuwatoa. Ulikuwa uokoaji zaidi ya masaa 12. Kila chombo cha habari hapa nchini kiliwatangaza wao. Walikuwa wakionyeshwa jinsi wanavyohangaika kuwatoa kwenye gari bila madhara.” Net akaendelea.

“Manesi, madaktari, polisi, watu wa zima moto, walikaa hapo eneo la ajali kuanzia huo usiku wamejulikana wamepata hiyo ajali, wakiwahudumia, mpaka kesho yake jioni, ndipo wakafanikiwa kuwatoa hapo kwenye gari.”

“Ilibidi huyo mwenzake aanzishiwe matibabu hapo hapo kwenye eneo la ajali wakiwa bado wamenasa ndani ya hilo gari, chini ya hilo daraja. Alipasuka vibaya sana, ikabidi kushonwa na kuongezewa damu hapohapo wakati juhudi za kuwatoa zikiendelea. Sidhani kama alikuja kutembea tena yule kijana.” “Net!” Tunda akashangaa sana.

“Ilikuwa mbaya sana Tunda. Mbaya zaidi ni mtoto anayetoka kwenye familia ya Cote. Hakuna mtu aliacha kututangaza. Papa na Nana walikaa hapo eneo la tukio muda wote wakisubiria atolewe. Akatoka hapo anamikwaruzo tu. Nafikiri na alivunjika mkono.”

“Kwa ile kashfa, ndio akakubali kurudi rehab. Alipotoka hapo, akatulia kidogo, mama akasema apelekwe tena Tanzania. Ndio wakati ule ukakutana naye wewe, akiwa ametulia kidogo. Ukamshauri arudi shule, ndio akarudi huku. Akasoma miaka 3, akamaliza shahada yake vizuri tu.”

“Hatujakaa sawa, akapata mwanaume mwingine aliyekuwa akitumia madawa ya kulevya, akamrudisha tena huko huko.” “Net!” Tunda akashangaa. “Maya amesumbua sana. Anajulikana kila mahali. Kila mtu anamfahamu kuwa ni binti asiye na maadili na haaminiki.” “Ikawaje tena?” Tunda akauliza. “Ipi sasa? Hii ya baada ya shahada au kabla?”

“Mhhh! Hata sijui niulize ipi. Maana alinisimulia juu ya kadi aliyokuibia, ndio maana humuamini na kadi yako.” “Alinitenda vibaya! Niliumia kupita kiasi. Na mbaya zaidi mimi mwenzie pesa yangu huwa napata kwa kufanya kazi sana.” Net akaendelea.

“Kuna kipindi mpaka nilikuwa nikiendesha trucks za babu. Kupeleka mizigo mbali ili kukusanya pesa. Wakati ule hawaajiri watu ofisini, ila madereva tu. Na mimi nilikuwa bado nipo chuo. Kwa hiyo kila ninapokuwa likizo, nikija kuomba kazi kwa papa, unakuta hana nafasi ya ofisini. Lakini upande wa madereva, maana huko ndio mara nyingi kunakuwa na upungufu wa madereva. Kwa hiyo babu alikuwa akiniambia kama nataka kazi, basi niendeshe lori kusambaza mizigo.” Net akacheka.

“Ni ngumu sana hasa kipindi cha baridi. Wakati mwingine unakuwa unalala kwenye barafu usiku kucha. Labda gari imeharibika au unasubiria mzigo sehemu ili urudi nao huku. Hapo nafanya kwa juhudi huku nikijenga kule Tanzania. Na sikutaka msaada hata wa tofali moja. Nilipokwenda kumpeleka papa kwenye ile nyumba, alilia Tunda. Hakuamini!”

“Ninachotaka kukwambia ni kuwa, japokuwa tulizaliwa kwenye pesa, lakini papa alinifundisha kupata pesa kwa jasho langu. Sasa hangaika yote hiyo, Maya akapotea. Baada ya siku ya 5, ndio tukaanza kupatwa na wasiwasi. Kwa sababu huwa akipotea ni siku 3, ya 4 anarudi.” “Subiri kwanza Net. Kuwa hiyo ndio ilikuwa tabia yake?” Tunda akauliza.

“Hiyo ya kupotea?”  Net akauliza. “Eeeh!” “Kabisa. Akishakusanya pesa. Maana huwa alikuwa akipewa pesa kila baada ya majuma mawili. Anakusanya pesa, anapotea na wanaume zake. Zikiisha, anarudi. Na usifikiri anaenda kupotea sehemu za kimasikini? Anaenda kujifungia kwenye mahoteli ya maana. Wanakula unga huko, akiishiwa yeye na huyo mwanaume wake wa wakati huo, anarudi.” Tunda akashangaa sana.

    “Sasa tukashangaa siku ya 5 inaisha, harudi. Babu na bibi wakasema kuna kitu hakipo sawa. Babu akasema kila mtu aangalie kadi zake. Nikakuta kadi yangu ya akiba haipo. Nikakumbuka nilimtuma akamnunulie Nana zawadi, hakurudisha. Nikaangalia kwenye salio. Tunda nililia kama mtoto mdogo.”

“Ndio ikabidi babu atume watu wakamtafute usiku huo huo. Sijui alipata mwanaume tapeli wa kiasi gani! Akamsaidia kuhamisha dola laki moja, kutoka kwenye akaunti yangu, akajiwekea kwenye akaunti yake.” “Mungu wangu Net!” Tunda alishituka sana.

“Acha Tunda. Ni akiba niliyokuwa nikiweka tokea nina miaka 14, nilipoanza kazi ofisini kwa Papa. Ananipa kazi, ananilipa. Haya, nikiendesha malori yake, akawa ananilipa pia. Sasa ukumbuke nilikuwa sina matumizi. Nakula na kulala bure. Gari yangu ya kwanza pia Papa alininunulia. Kwa hiyo kila pesa niliyokuwa nikipata, natunza. Labda matumizi kidogo sana.”

“Basi. Akamnunulia gari huyo mwanaume. Gari ya dolla elfu 45. Akamlipia kutoka kwenye hiyo pesa yangu. Ndio wakaanza starehe. Baada ya siku mbili mbele, yaani ya 7. Ndio waliotumwa kumtafuta, wakampata kwa kuangalia ni wapi mara ya mwisho kadi yake imetumika, maana hapo ikabidi Papa afunge kabisa ile akaunti yangu, akaniambia nifungue nyingine, kwa kuwa yule mwanaume wa Maya wameshaijua.” “Walimfunga?” Tunda akauliza.

“Hakuwa na kosa la kushitakiwa. Pesa zilitoka kwenye akaunti ya Nethaniel Cote, kwenda kwa Maya Cote. Haya, gari amenunuliwa zawadi na mpenzi wake. Na lipo kwa jina lake yeye huyo kijana. Anakosa gani la kumshitaki? Mbaya zaidi, walikutwa wapo hotelini wote wapo high. Wamekula madawa, hawajitambui. Ukiita polisi, inamaana unamtia matatizoni huyo Maya.” “Mungu wangu!” Tunda akaendelea kushangaa.

“Akarudishwa nyumbani. Hapo kila mtu anajihami na pochi yake. Papa na Nana wanafunga chumba chao wakiondoka. Mimi ndio alikuwa akiniogopa, hataki hata nimsogelee. Alikuwa anamfuata Papa mpaka chooni! Sababu ya madawa, akaanza kuuza vitu vyake.” “Jamani!” Tunda akasikitika.

“Wanaume wakawa wanampenda. Kazuri, halafu katoto ka Cote. Kule kuwa naye tu, ni kujipatia sifa mitandaoni. Moja, pili wananufaika. Hakajui uchoyo. Mtu akimlilia shida tu, anasaidia.”

“Fujo zikaanza. Wanamg’ang’ania. Hakuna anayekubali kuachwa na Maya. Mwanaume huyu akijua ameachwa yupo na mwanaume mwingine, hakubali. Picha zake za ngono zikaanza kuzagaa mitandaoni. Wanamtaka. Akikataa kurudiana nao, wanamchafua kwa picha au video wanazokuwa wamemchukua kipindi amelewa hajitambui.” “Net!” Tunda akaumia sana.

“We acha tu. Basi nayo ikawa fujo. Kila kukicha, Maya yupo mitandaoni akifanya mapenzi na mwanaume huyu au yule. Mara wakiwa club au kwenye gari, ilimradi ni fujo tupu.” “Maskini Maya!” Tunda akajikuta akimuhurumia.

“Ilikuwa mbaya sana. Na yeye hapo hawezi kutulia tena, sababu ya madawa. Akifungiwa mlango, anatoroka. Papa na Nana wanapokuwa wakienda kazini, wanakuwa wakimuacha ndani, wanamwambia Carter asimruhusu atoke. Carter anakuja kuwapigia simu kuwaambia hayupo, na hajui saa ngapi ameruka dirisha.” “Kwenye lile jumba anaruka dirisha!?” Tunda akashangaa maana hiyo nyumba ina madirisha marefu sana kutoka chini.

“Madawa! Hapo hajali jinsi atakavyoumia. Ilimradi atoke tu akapate madawa. Akahangaika hivyo ndio mpaka akapata ajali, akakubali kwenda rehab. Akatoka akiwa ametulia, ndio akaja Tanzania. Kipindi kile mkakutana naye kwa mara ya kwanza.” Tunda alibaki na mshangao.

“Sasa alipomaliza chuo, safari hii ya pili. Akampata huyo jamaa niliyekwambia naye akamrudisha kulekule. Walianza vizuri. Tukajua wataoana. Maana alikuwa ametulia kweli Maya. Ila kazi akawa hapati sababu ya sifa mbaya. Hakutaka kufanya kazi na Nana. Alijua kanuni ya pale ni kazi tu. Hakuna kucheza. Akahangaika kutafuta kazi bila mafanikio.” “Sasa kwa nini hamkumsaidia na jina hilo la Cote?” Tunda akauliza.

“Huku Tunda sio kama kule Tanzania. Ukishakuwa na makosa yanayokupelekea kufungwa tu. Au ukaingia kwenye mkosa ukaingizwa kwenye mitandao ya usalama, umejiharibia kabisa. Kuna kitu kinaitwa background check. Unafanyiwa na mwajiri kabla hujaajiriwa. Ili wajue wanamwajiri mtu wa namna gani.”

“Sasa kwa Maya, ilikuwa hata haiitajiki background check. Alijulikana kuwa ni mwizi, anatumia madawa ya kulevya, haaminiki, na mengine mengi. Sasa ni nani atamwajiri?” Tunda kimya. “Na papa naye hakutaka aweke jina lake popote asije akaharibu huko, akaharibia Cote wote! Wakamuacha tu. Maana Nana alisema kama kweli amekusudia kubadilika, angeomba kazi pale. Kuwakwepa, inamaana hajakusudia kutulia.”

“Wakamwacha ahangaike mwenyewe, huku wakijiambia, akikwama, atarudi kuwaomba wao msaada, na hapo watajua kuwa ametulia. Papa alikuwa akifanya kazi pale, huku akiwafikiria mpaka hawa kina Cote. Alisema ni kampuni ya kizazi hadi kizazi. Hakutaka mtoto mmoja aliyekusudia kutotulia, aje aharibie wenzake. Kwa hiyo wakamwacha tu.” Tunda akashangaa mipango ya hiyo familia.

“Na kweli, baada ya muda, akarudia tena madawa. Akaanza taratibu. Akizidiwa harudi nyumbani. Analala huko huko anasema labda usiku huo atalala kwa huyo mchumba. Haya, akaendelea hivyo hivyo.”

“Subiri kwanza Net, inamaana alikuwa akiruhusiwa kulala kwa mwanaume wake?” “Tunda! Labda hujaelewa juu ya Maya. Ilikuwa ni bora hivyo anajulikana yupo na mwanaume mmoja, kuliko vile alivyokuwa hajulikani yupo na mwanaume gani na wapi!” Tunda akastaajabu sana.

“Huyo jamaa mwenyewe mwanzoni alikuja kumtambulisha kwa kina Papa, akaonekana ni kijana mzuri tu, tena mwenye maadili. Kidogo ikawa afadhali. Kwamba anajulikana yupo na mwanaume mmoja tu. Halafu wakati huo Papa alishaanza kuumwa. Hakuna anayefikiria chochote ila ugonjwa wa Papa. Akawa huru na huyo kijana, Nana anauguza.” “Jamani Maya wangu!” Tunda akamsikitikia.

“Haya, uhuru ukaongezeka. Hana kazi, ila pesa anayo. Nana na Papa walikuwa wakimpa pesa za kujikimu wakati akitafuta kazi. Akazidisha madawa, akaanza kuaga kuwa anasafiri labda siku tatu au nne. Kumbe yupo nyumbani kwa huyo jamaa wanatumia hayo madawa.”

“Sasa mbaya zaidi, safari hii akawa amepata mwanaume ambaye na yeye alikuwa na pesa kidogo. Halafu kama mtu mzima hivi, hana mambo ya kitoto kama vijana wengine kujiweka mitandaoni. Mambo yakawa yanaenda kimya kimya, hakuna anayejua. Maya haishiwi hovyo wala haibi. Akiishiwa yeye pesa, yule kijana ananunua yeye hayo madawa.”

“Wakaendelea hivyo mpaka Papa akaja kuzidiwa, akafa. Mimi na mama tukaja kuzika. Hakuna anayejua kama amerudia tabia zake. Msafi tu. Tulipoondoka sasa. Akabaki Nana akiomboleza, yeye ndio akapata uhuru mkubwa sasa. Hakuna wakumuuliza wala kumgundua. “Ni kama hapakuwa na mtu tena anayemfuatilia. Hata Nana alipokuwa naye nyumbani, hakuwa na muda. Ni kama kifo cha Papa kilimsumbua sana Nana. Ni mpenzi wake waliyekuwa kwenye ndoa ya zaidi ya miaka 65. Tokea Nana ni binti mdogo, anasema walianzana akiwa na miaka 14 tu, mpaka akaja kumuoa na ndio kifo.” “Maskini!” Tunda akamuhurumia bibi Cote.

“Sasa siku moja Nana akaja kugutuka, Maya hayupo! Akili ndio ikamrudia. Akamuuliza Carter. Carter akamwambia alimsikia akimuaga kuwa atasafiri na boyfriend wake kwa siku tatu. Nana akasema akashituka kidogo. Hiyo ilikuwa siku ya 8 tokea aondoke. Ndio Nana akaanza kutuma watu wapeleleze. Kumbe alikuwa jela. Alikamatwa na huyo kijana wanafanya mapenzi kwenye gari, pembeni ya barabara, wamelewa hata hawajitambui.” “Net!” Tunda akashangaa sana.

“Kweli! Huyo polisi aliyewakamata, alimwambia Nana ilikuwa ni heri vile alivyowachukua kuliko angewaachia. Wangepata ajali mbaya sana. Wanasema walikuwa hata hawajitambui. Walipimwa, wakakutwa ni cocaine. Maya akaogopa kupiga simu nyumbani. Akasema yeye yupo tayari kufungwa. Ila Nana na mimi tusiambiwe. Basi. Ndipo hao watu waliokuwa wametumwa na Nana wakaja kumpa hizo taarifa.” “Atakuwa aliogopa!” Tunda akaongeza.

“Kabisa. Na kipindi hicho nilikuwa Tanzania, ikabidi nirudi nianze kufuatilia kesi yake. Logan akamtetea kuwa alilevya. Yeye hakuwa na hayo madawa. Mahakama ikataka dhamana ya dolla milioni moja kwa ajili yake. Kwa kuwa tayari alikuwa na makosa mengi yanayofanana na hayo. Kuanzia ana miaka 17 mpaka hapo.” Tunda hakuwa akiamini.

“Ndio Nana akasema hiyo pesa ilipwe, Maya atolewe. Lakini mimi na Nana tukamfuata akiwa huko huko jela amefungwa, tukampa masharti. Nikamwambia hiyo  pesa itatolewa kwa masharti yafuatayo. Arudi rehab asafishwe kabisa au kutibiwa. Akitoka, atafue kazi itakayomsaidia kulipia gharama zote, ya hiyo rehab na garama za mwanasheria atakayemtetea kwenye kesi yake. Akakubali haraka sana. Maana alisema akihukumiwa kufungwa atakufa jela.”

“Basi. Ndio ikabidi sasa tugharamie gharama zake za rehab na hiyo kesi ambayo ilinguruma Tunda. Hakuna jinsi nikakwambia ukaelewa. Tulichafuliwa kupita kiasi.” “Poleni Net.” “Na hapo ukumbuke Papa ndio amekufa amebaki Nana. Magazeti yakawa yanaandika kuwa ndio mwisho wa kizazi cha Cote.” “Jamani! Kwa nini sasa?” “Hiyo pesa iliyokuwa ikidaiwa ya mahakama Tunda! Nyingi mno. Halafu ilibidi kutafuta mwanasheria wa hali ya juu ili ashinde kesi ya Maya ambayo hapakuwa na uwezekano wa kushinda.” “Net!” Tunda akashangaa.

“Ni Maya. Kumbuka alikuwa ana makosa kama hayo yanayofahamika kila mahali. Wazazi wengine, rafiki tu wakaribu wakawa wanasema ni heri Maya afungwe pengine akitoka atakuwa amebadilika, anaharibu vijana wao. Kuna wazazi walikuwa wakisema Maya alishawatoa vijana wao mashuleni na kuwafundisha madawa ya kulenya.” “Jamani!”

“Ilikuwa mbaya sana. Lakini Mungu akasaidia. Ni kweli pesa ilitoka, lakini Maya akashinda kesi. Alikuwa akitolewa rehab, anapelekwa mahakamani. Mpaka akashinda kesi na kutoka rehab. Ndio pale unamuona anafanya kazi kubwa, malipo madogo.” “Net!” Tunda akashangaa.

“Unafikiri namtania? Ameshamaliza kulipa kampuni gharama zake za rehab. Sasa hivi analipa gharama za mwanasheria. Kesi yake ilichukua karibia mwaka mzima. Ikafutwa. Yote hiyo ilikuwa gharama ya kampuni. Sasa ndio analipia.” “Mmmh!” Tunda akachoka kabisa.

“Pale alipo hakuna sehemu yeyote wanaweza kumuajiri, wala hana ujanja wakutolipa.” “Unanuonaje lakini?” “Anajitahidi. Na tunamfanyia makusudi kumpa kazi nyingi ili atulie. Tunaamini kadiri siku zinavyozidi kwenda. Tukimpa ukweli wa maisha. Anaelewa, na kutulia. Papa alimfanya aishi bila kufikiria. Alikuwa akimpa kila kitu na alikuwa akimkingia kifua. Hakuwahi kukua kwa Papa. Mpaka leo analia msiba wa Papa.” “Maskini Maya wangu!”

“Vile unavyomuona sasa hivi. Hana tofauti na wewe hapa nchini. Anajifunza maisha mapya kabisa ambayo hakuwahi hata kufikiria anaweza kuja kuishi. Zaidi akijua hayupo Papa. Papa alikuwa mkali kwa kila mtu, kasoro Maya. Alikuwa anamfanya kama mtoto wa miaka 5. Sasa kuja kuona ameangukia kwangu! Ni maisha ambayo hakuwahi hata kufikiria kama atakuja kuishi.” Walikuwa wameshafika nyumbani. Wameegesha gari nje wakiendelea kuzungumza.

Jumamosi ya Bibi Cote na Tunda.

Jumamosi hiyo Net aliamka akiwa na ahadi yakuwahi kurudi kutoka kazini. “Wewe utakuwa na Nana?” “Amesema anataka twende wote tukafanye manicure na pedicure.” “Safi. Najua mtapata muda wa mazungumzo pia. Naomba jaribu kumzoea. Ana mambo mengi mazuri ambayo najua ukikaa naye, utanufaika sana.” Tunda akacheka kidogo kama anayefikiria.

“Vipi?” “Namuona anajitahidi kweli kuwa karibu na mimi, lakini naona kuna kama ukuta kati yetu!” “Ndio maana nakuomba ujitahidi. Kuwa huru. Usimuogope.” “Najitahidi Net. Kumbuka ni wewe na mama Penny tu ndio mmekuwa watu wakuwa karibu na mimi. Mnanielewa na kunichukulia vile nilivyo. Mmenibeba zaidi na nilivyowahi kufikiria. Sijui mahusiano ya watu wengine yanakuaje!” “Mbona Maya umemzoea?” Tunda akacheka.

“Wewe unamuona Maya anasubiri kuzoelewa? Akitoka tu kazini, anakuja kujilaza hapa kwenye kitanda pembeni yangu mpaka akusikie nje ndio anakimbia. Ananifuata mpaka chooni! Hasubiri hata nimkaribishe au nimjibu. Atapiga stori zake hapo weee. Mpaka akusikie wewe ndio anakimbia.” Net akacheka.

“Naomba mpe nafasi na Nana.” “Nitajitahidi. Sasa nani atalipia?” “Halafu inabidi twende wote benki jumatatu.” “Kufanya nini?” “Kufungua akaunti yako ya hapa uwe na kadi yako.” Tunda akanyamaza. Net akarudi pale kitandani alipokuwa amelala Tunda. Alikuwa anamalizia kuvaa aende kazini.

Akambusu. “Unawaza nini?” “Hamna kitu.” Tunda akajibu. Net akabusu tena, na tena. Akaanza kumpapasa. “Utachelewa kazini Net!” Net akacheka huku akimbusu shingoni na mikono ikimpapasa. “Huko unakokwenda, mwisho wake nitakubaka!” Net alicheka sana. Akasimama.

“Nataka nikirudi, unibake.” Tunda na yeye akaanza kucheka. “Net!” “Nani hataki kubakwa na mkewe? Tena Tunda! Mimi nibake tu.” Tunda akazidi kucheka. “Nana atalipia. Halafu nimefikiria, naona jumatano wakati tunatoka kliniki ndio twende benki.” “Sawa. Uwe na wakati mzuri kazini.” “Na wewe ukawe na wakati mzuri huko.” Akambusu, nakutoka.

Net alipotoka saa 11:30 asubuhi hiyo, akapitiwa tena na usingizi mpaka kwenye saa tatu na nusu haja ndogo ilipomuamsha tena. Ikabidi tu aamke na kuoga kabisa. Kwenye saa nne hivi akatoka. Moja kwa moja mezani. Akakuta Gino alishamtengenezea uji na vyakula vingine vipo hapo mezani. Lakini Gino mwenyewe hayupo.

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

Jumamosi ilikuwa siku ambayo karibu wote wanachelewa kuamka kasoro Net ambaye kuanzia jumatatu mpaka jumamosi anatoka hapo nyumbani saa 12 kamili au kasoro, alfajiri ili saa 12 na nusu au na robo awe amefika ofisini kwake. Inategemea ametoka nyumbani muda gani.

Wakiagana kwa muda mrefu na mkewe asubuhi hiyo basi ujue Net atakuwepo ofisini kwake saa 12:30. Kama ni mazoezi tu na kupata kifungua kinywa pamoja, wakati mwingine saa 12:15 au 12 kamili atakuwa ameshawasili ofisini.

Maya yeye siku za jumamosi huondoka hapo nyumbani mida ya saa mbili na nusu ili saa tatu kamili awe ameshafika ofisini kwake. Ratiba yake na bibi yake iliendana kasoro siku hizo za jumamosi alizoamua bibi huyo kutoenda kazini.

Mara nyingi siku za jumatatu mpaka jumamosi hawakuwa wakipata kifungua kinywa pamoja, ila jumapili. Kwa kuwa mara nyingi Maya na bibi yake walikwenda kazini muda unaofanana, wao walipata kifungua kinywa pamoja. Saa moja na nusu asubuhi wao wanakuwepo mezani wakati Net na Tunda wanakuwa walishapita hapo mezani mapema sana.

Gino alikuwa akifika hapo alfajiri ya saa 11, ili kuhakikisha Net anapata kifungua kinywa kabla ya kwenda kazini. Zaidi smoothie ambayo humtengenezea mara baada ya mazoezi. Ndipo anakwenda kuoga na kuja kupata kifungua kinywa rasmi.

Mara nyingi akitoka hapo kwa mara ya pili baada ya mazoezi na kunywa smoothie, wakati anapata sasa kifungua kinywa rasmi, anakuwa na mkewe. Tunda atakaa naye hapo wakati anapata kifungua kinywa na yeye anakula kwa mara ya kwanza. Anarudi kulala, akiamka kwenye saa nne tena, lazima anywe uji.

Kasoro siku za jumamosi ambapo Net huwa hapati kifungua kinywa kikubwa. Akinywa tu smoothie baada ya mazoezi, basi. Anakwenda kazini, na kurudi nyumbani mchana kwa ajili ya mlo mkubwa. Jumamosi alifanya kazi nusu siku.

Mara nyingi vitu wanavyokula asubuhi huwa havibadiliki sana. Ni kama Gino alishawajulia kila mmoja anachokula mida ya asubuhi na jioni alikuwa na ratiba ya nini kipikwe kwa wote. Kwa hiyo ilikuwa ukifika mezani, Gino anatoka jikoni nakuja kukuhudumia kwa kile unachohitaji.

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

Wakati anakaa ili ale, Ms Emily akamsogelea pale mezani. “Ms Cote yupo kwenye chumba chakusomea. Amesema ukiwa tayari umfuate huko.” Tunda akaangalia saa, akajua kwa muda ule atakuwa alishaamka na kupata kifungua kinywa na Maya alishaondoka kwenda kazini.

“Asante. Wewe umeshakula?” Tunda akamuuliza Ms Emily kabla hajaondoka. Akababaika kidogo na tabasamu la kinyenyekevu usoni. Kwa kuwa haikuwa kwenye ratiba kuwa anatakiwa kula akiwa pale kazini na wala hakuna mtu wakuwauliza wafanyakazi kama wamekula.

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

Ulikuwa utaratibu mgeni kwao ambao Tunda alianzisha. Akibaki nao pale nyumbani mara baada ya Gino naye kuondoka asubuhi akiwa ameshamtayarishia na yeye chakula chake, Tunda alitaka na wao wale. Tena wale sio kwa kujificha. Wawe huru, wachukue muda wa mapumziko wa kula. Wote wawili, Ms Emily na Carter.

Tena wakati mwingine aliwashangaza alipokuwa akiwaita wale pamoja mezani au kuwafuata kula nao jikoni huku akiwaongelesha hili na lile.

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

“Kaa ule kwanza. Mimi nitakunywa tu uji. Hivyo vitu vingine alivyoandaa Gino ni vingi sana. Jipakulie ule, umwambie na Carter atafute muda apate kifungua kinywa. Mimi nitamfuata Nana hukohuko alipo.” Ms Emily akatoa tabasamu la shukurani. “Asante Tunda.” Tunda akacheka.

Alijua tu atakuwa hajala sababu bibi Cote siku hiyo alikuwepo nyumbani. Alishawajua wanamuogopa sana, na wanaongeza nidhamu wakiwepo wao. Lakini yeye alitaka kuondoa huo mpaka kati yao. Tunda akajinyanyua pale na tumbo lake na kikombe kikubwa cha uji mkonono, akaelekea alipoambiwa bibi Cote yupo. Alimuacha Ms. Emily akila.

Yeye hakuwa akifuata sheria kama wao. Kila kitu kufanyika sehemu sahihi kwa wakati sahihi. Akaendelea kujivuta huku akinywa uji wake taratibu. Akijua wazi alitakiwa kulia chakula mezani, hata huo uji asiingie nao chumba cha kusomea. Tunda hakujali.

Alimkuta yule bibi akisoma kitabu. “Unasoma nini?” Tunda akamuuliza wakati anaingia. Bibi Cote akacheka kidogo na kukigeuza kile kitabu. “Morning devotional.” Akajibu kisha akavua miwani na kumtizama. “Mbona unakikombe cha uji mkononi?” “Nimeambiwa uko huku. Nikaona nije kukaa na wewe. Sitaki kukaa peke yangu.” Yule bibi akacheka kidogo.

“Lakini wewe ni mkimya sana Tunda!” “Sio sana. Hivi unavyoniona, ndivyo baba yangu alivyo. Halafu pia nilikuwa, nikiwa sijazungukwa na watu au mtu ambaye alikuwa karibu yangu. Nilikuzwa kwenye mazingira ambayo hayakuwa rafiki kabisa. Kunyamaza ndio ilikuwa afadhali yangu. Nafikiri ndio sababu. Net ndiye mtu wa kwanza kukaa chini na kutoa muda wake na kuweza kunisikiliza. Nafikiri ndiye binadamu pekee anayenifahami zaidi kuliko hata wazazi wangu au mtu mwingine yeyote. Kwa hiyo ndio maana nipo hivi. Endelea tu kosoma. Mimi sitakusumbua. Nilitaka tu kukaa sehemu ambayo kuna mtu.” “Nilishamaliza. Nilikuwa natafakari tu.” Tunda akakaa.

“Unajisikiaje?” “Vizuri. Naona sasa hivi ndio nafurahia zaidi ujauzito wangu. Sijui daktari alinipa nini! Sina kichefu chefu tena! Sijatapika muda mrefu!” “Afadhali.” Tunda akanywa tena uji wake.

Kisha akamuuliza. “Maya alishaondoka? Leo hajapita chumbani kwetu.” “Mapema sana. Yeye ndio ameniamsha. Alikuja kuvalia chumbani kwangu.” Tunda akaanza kucheka. “Maya! Ni waina yake! Lakini katika yote, huwa namshukuru Mungu kutupa Maya. Ananipenda sana na hataki nimtizame kama amekuwa. Anataka abaki vilevile Maya mtoto!”  Akaongeza bibi Cote, wakacheka.

“Ila ana upendo sana!” Akamuona bibi Cote anacheka. “Nini?” Tunda akamuuliza baada ya kumuona amecheka. “Akupende yeye. Asipokupenda Maya, hutatamani kukaa sehemu alipo. Wewe utakuja kumuona akikutana na watu asio wapenda yeye. Hutaamini kama ni Maya huyu.” Tunda akacheka kama anayefikiria.

“Kama Vic?” Tunda akatupa swali. Akamuona bibi Cote ameshituka kidogo. Kisha akajibaraguza. Hamu yakupata habari za Vic ikamjia akajiweka sawa akimtizama ili ampe kwa ufupi habari za Vic.

Ikabidi bibi Cote acheke na kuona amzungumzie tu Vic. “Ukitaka kumuudhi Maya. Au kumbadilisha mudi yake, mtaje Vic, au mlete Vic humu ndani. Anakuwa kama anapatwa na wazimu.” “Kwa nini? Walishawahi kuwa marafiki?”  Tunda akauliza tena.

“Kwa kiasi fulani japo hawakuwa karibu sana. Ila mambo ya Maya yalipobadilika. Alipoanza tabia zake mbaya, anaamini Vic ndiye anayemsambazia habari mbaya kwa watu ili kila mtu amuone sio binti wa kuaminika.” Tunda akakunja uso kidogo.

“Kwani wanalingana? Au kwa nini Vic afanye hivyo?” Tunda akauliza tena taratibu. Bibi cote akafikiria na kucheka kidogo. “Haya ninayokwambia, hujasikia kutoka kwangu.” Tunda akacheka. “Sawa.” Tunda akakubali ili apate umbea wa uzunguni.

“Vic ni umri wa Net. Na yeye ni mjukuu wa familia moja ambayo walikuwa marafiki zetu sana. Lakini wao wazee wao, yaani bibi na babu ambao ndio walikuwa rafiki zetu wa karibu sana, walishafariki. Bibi yake Vic, alikuwa best friend wangu wa muda mrefu sana.” Akaendelea. “Vic ni mtoto wa pekee, anaishi na wazazi wake, ambao nao walizaliwa sisi tukiwaona. Ni kama watoto wetu. Vic na Net walikuwa pamoja. Kadiri walivyokuwa wakikua, Vic alitambulika kama mpenzi au mwanamke atakayeolewa na Net.” Kiroho kikaanza kumdunda Tunda.

“Wakaendelea hivyo wakisoma na kufanya kila kitu pamoja. Lakini wakaanza kutofautiana. Vic akageuka kuwa ‘DIVA’.” Bibi Cote aliongea hapo kwa kejeli kidogo akinyanyua na vidole viwili juu aliposema Diva.

“Ukweli ni binti mzuri sana. Na yeye anajua hilo. Kutokana na uwezo wa nyumbani kwao, hata makuzi aliyolelewa, ni kama mtoto wa mfamle. Ikawa tofauti kwa Net. Babu yake Net alimkuza Net katika kutumika, sio kutumikiwa.” Yule bibi akatulia. “Wakaanza kujiona tofauti, japo Vic anampenda sana Net. Nikisema sana, yupo kama mwehu kwa Net. Anampenda kupita nitakavyokueleza hapa, ukaelewa. Asikuhisi wala kukuona unamtizama Net kwa vile asivyopenda yeye, atakufuata tu na kukuonya ukae mbali na Net. Linapofika swala la Net, anakuwa kama amechanganyikiwa na hawezi kujisaidia.” Tunda akatulia tu akisikiliza.

“Wakaendelea hivyo mpaka wakamaliza high school. Vic akijitangazia yeye ndio atakuwa mke wa Net, wakati huku nyumbani Net alikuwa akisema, haoni maisha kati yake na Vic. Ni watu wawili tofauti. Papa yake Net akamwambia nilazima amwambie Vic ili ajue. Vic anajua kuganda! Kupita kiasi. Swala au jambo la kuwa mbali na Net, halipo kwenye msamiati wake. Hajawahi kulielewa wala kulikubali.”

“Kingine, anapenda kutawala kila mtu na kila kitu. Sasa akakutana na Maya. Na yeye Maya kadiri alivyokuwa anakua anataka ajaliwe na kila mtu na atambuliwe na kila mtu. Yakaanza mashindano kati ya Vic na Maya. Maya akisema anataka muda na kaka yake, basi Vic asiingilie. Muda wa Net ambao anakua hana kazi ni siku za jumamosi jioni na jumapili. Ndio muda huohuo Maya anapanga na kaka yake mipango yao yakuwa pamoja. Na Vic naye anataka aonekane na Net mtaani.” Tunda akamuona anacheka na kutingisha kichwa.

“Nini?” “Ilikuwa fujo hapa! Wakianza kugombana, mpaka Papa yao aingilie kati. Maya anamsemea Vic hili na Vic naye anamsemea Maya hili. Hapo Net amekaa anawasikiliza. Wote wamekutana ni wazuri. Wanakosoana sasa kwa hili na lile. Haya, Vic anaondoka. Mshindi Maya. Mnapumzika kidogo. Mara linaibuka jingine. Maya anakuja kulalamika labda alikuwa sehemu, gari yake ameegesha nje, ametoka amekuta imewekwa pancha, akashindwa kuondoka, Vic amemfanyia kivyo. Akiulizwa kwa nini anahisi ni Vic, basi atasema Vic alipita hilo eneo itakuwa ni yeye tu.”

“Haya mara mko tu hapa nyumbani mnamuona Vic anakuja akilia, labda gari yake imevunjwa kioo makusudi au imechanwa tairi na Maya. Na ni zile gari za pesa nyingi sana. Kitu kidogo tu kwenye hiyo gari ni gharama kweli! Haya, ukimtafuta Maya, unamkuta huko nyuma anaogelea. Ukimuuliza Vic, anakwambia Maya ni muongo, alipoharibu gari yake ndipo akakimbilia nyumbani. Ikawa fujo hapa, visasi haviishi.” Bibi Cote akakumbuka kitu kingine akacheka sana.

Tunda naye akacheka. “Siku nyingine tena.” Yule bibi akazidi kucheka. “Ooh my goodness, Maya! She is something else!” “Alifanya nini tena?” Yule bibi alicheka. Akacheka tena.

“Kuna sehemu Vic alikuwa akipenda sana akifika hapa, anakaa hapo halafu anaanza kutuma wafanyakazi wa humu ndani wamtumikie kwa hili na lile.” “Subiri kwanza Nana, kwani yeye huwa anakuja hapa wakati wowote!?” Tunda akauliza.

“Nakwambia amekua sisi tukimuona. Hapa nyumbani ni kama kwao tu. Amekua pamoja na Net tokea hawajaanza shule. Walikuwa wanne. Na wale vijana wawili waliokuja Tanzania. Humu ndani wanaingia mchana na usiku. Walikuwa wakisomea humu ndani na wazazi walipapenda hapa sababu ya maadili ya Net. Na vile babu yake alivyoweza kumudu kumtawala Net na Net kufuata kila kitu anachoambiwa. Ile iliwavutia wazazi wengi sana.”

“Kwa hiyo mtoto yeyote akijulikana yupo kwa Cote, kukawa hamna shida. Na hapa kukawa na mafunzo mengi. Kwa hiyo kila wakija, walikuwa wakijifunza na Net. Walikuwa wakifundishwa lugha mbali mbali, michezo, kutumia vifaa vya mziki. Kwa hiyo hapa ikawa sehemu wanayopenda kuja mpaka leo. Sema kumetulia sababu tuliwaambia upo na unahitaji utulivu. Wakuache kwanza mpaka tutakapowaalika tena rasmi.” Tunda akajisikia vizuri.

“Asante Nana. Kweli nilihitaji kupumzika. Nashukuru kujali.” Nana akacheka kidogo. “Karibu. Sasa turudi kwa Maya na Vic.” “Ehe!” “Siku hiyo akamsikia Carter anazungumza naye getini akitaka afunguliwe geti ili aingie. Maya akakimbilia kwenye kile kama kibembea pale ukiingia mlango mkubwa, kuelekea sebuleni. Akalegeza nuts mbili kwa haraka. Sasa Vic alipokuja akampita Carter mlangoni bila salamu wala heshima kama kawaida yake Vic. Na yeye Carter alimuona Maya akiharibu ile bembea lakini hakumwambia Vic makusudi. Akajua kitakachompata.” Tunda akaanza kucheka na yeye kama mazuri.

“Sasa si Vic alimpita pale mlangoni bila salamu wala heshima, na yeye Carter akanyamaza kimya. Kama kawaida yake Vic, akamuita Ms. Emily amletee juisi ya nanasi. Ndio juisi anayopenda sana kila akija humu ndani. Gino huwa anachanganya na vitu vingine, inakuwa nzuri sana, hutawahi kunywa popote aina ile ya juisi anayotengeneza Gino. Na hajawahi kumwambia mtu huwa anatengeneza vipi. Ni siri yake.”

“Hata mimi huwa naipenda.” “Basi, ile utaipata humu ndani tu. Sasa kila Vic alipokuwa akiingia humu ndani , anamuita Emily amletee glasi moja, kabla hata hajakaa akiwa anamsubiria Net, waende kule nyuma wakacheze tenesi. Emily aliposikia jina lake likiitwa na Vic, bila kupoteza muda, akammiminia glasi ya juisi. Akampelekea.” Yule bibi akacheka tena na tena.

“Sasa alipoletewa juisi, ile anakaa chini kwenye lile bembea huku amemtuma Carter akamuite Net, si akaanguka! Wakaanza kucheka kwa pamoja. Carter, Maya na Emily.”  “Jamani! Sasa kwa nini Carter asimwambie?” “Wakati na wao shida yao ni aanguke!” Wote wakacheka.

“Carter anampenda sana Maya. Sana. Na hamkosei sababu yakumtetea. Anamtetea kwa kila kitu. Basi, ile juisi si unajua inakuwa kama nyekundu hivi?” “Nahisi Gino anachanganya na Berries.” “Hata sisi tunahisi hivyo hivyo. Sasa Net anasogea pale, na Vic ndio anaanguka, miguu juu, glasi kushoto, juisi yote imemuishia mwilini. Jamani Vic alilia!”

“Maya acha aanze kucheka! Halafu kumbe alikuwa anamchukua video. Akamtumia hapohapo video yake huku mwenzie akilia. Sasa Net anashangaa Vic analia, halafu Carter, Emily na Maya wanacheka sana. Kumbe wote walijua mtego anaotegewa Vic.” “Sasa nyinyi mlikuwa wapi?” Tunda akauliza.

“Chumbani! Ndio tulikuwa tumetoka kazini. Wote. Kasoro Maya ndio alikuwa hapa. Ndio ilikuwa siku yao, Net na Vic yakucheza tenesi. Ndio alikuwa amekuja wakacheze. Vic akamuonyesha ile video Net, huku akilia kuwa Maya amemfanyia makusudi.”

“Maya alipoona hivyo, akakimbilia chumbani kwetu. Mgongoni kwa Papa. Net akaingia amekasirika. Ndio akaelezea vile alivyoambiwa na Vic. Maya akasema Vic nimuongo, yeye alikuwa anajichukua video, akaacha simu yake kwenye meza ya karibu na lile bembea, bila kuzima kamera. Kwa hiyo ndio ikachukua lile tukio la kuanguka kwa Vic. Kama hatumwamini, aitwe Carter.” Tunda alikuwa akicheka sana.

“Sasa Carter alivokuja?” Tunda akauliza huku akicheka. “Carter kuja, akasema lile bembea lilikuwa na matatizo. Ameshapigia simu mafundi waje walitengeneze. Akaulizwa kwa nini hakumwambia Vic, akasema Vic aliingia na maagizo ya haraka. Akimtaka yeye Carter akamuite Net kwa haraka, na Emily akalete juisi haraka. Sababu ya haraka, akasahau kumwambia. Hapo Maya akawa amepona. Ameshikilia kiuno cha Papa, hataki hata babu yake asogee hatua moja. Anaongea na Net huku amejificha nyuma ya babu yake.” Tunda alicheka mpaka machozi.

“Maya!” “Ila wewe alikupenda tokea siku ya kwanza anakuona. Hakuacha kukusifia. Na kukupenda kukaongezeka pale mama yao alipoonyesha hakupendi.” “Kwa nini tena!?” “Ili tu kumkera mama yake zaidi. Ukitaka kumsikia anakuwa mkali Maya kwa mama yake, basi awe kinyume na maamuzi ya Net kuwa na wewe. Hapo anakuwa mkali bila woga. Sasa turudi kwa Maya na Vic.” “Ehe!” Tunda akataka waendelee.

“Mimi ni kiongozi wa foundation moja hivi ya wanawake tuliianzisha hapa nchini. Sasa lazima kuwe na mrithi wangu. Iwe mtoto wa kike au mkwe.  Sasa Vic akatangaza kuwa Maya hawezi kuchukua hicho cheo, au kukalia kiti changu. Kwa sababu kile kiti kinakaliwa na wanawake smart, kama yeye mke wa Net, sio Maya.” “Kwa nini isiwe mama Cote? Yaani mama yao kina Maya?” Yule bibi akafikiria kidogo.

“Nitakwambia habari za Ritha. Ila kwa kifupi tu, ni kama Ritha alitoka mapema sana kwenye picha, alipotaka kurudi baada ya kujua alichokimbia ni kitu kikubwa sana, amejipunja, nilikuwa nimeshamfungia milango yote. Nikahakikisha namwachia mlango mmoja tu wakurudi kwetu, watoto wake. Lakini napo..”  Akasita kidogo.

Anyway, tuendelee kwa Maya na Vic kwanza. Vic akawa anatafuta makosa na udhaifu wowote ule wa Maya, na kutangaza hadharani ili watu wajue kuwa Maya hawezi kuja kukalia kiti changu. Au kama kushawishi uma kuwa Maya hana uwezo wa kubeba madaraka ya kile kiti. Akawa anamfuatilia sana Maya. Maya alipoangukia kwenye madawa ya kulevya, ndipo Vic akapata jukwaa. Kila siku ni habari za Maya mitandaoni. Maya hajui anazipataje. Anahisi pia baadhi ya wanaume alikuwa akiwalipa yeye ili wampe madawa. Akishalewa, basi wamfanyie uchafu, wachukue video.” “Haiwezekani!” Tunda akashtuka sana.

“Sijui Tunda! Ila jinsi Maya anavyonieleza, anasema alipoamua kubadilika, wakati anamaliza chuo, huyo kijana akaanza kumfuatilia. Anasema akivuta kumbukumbu ni kama nikijana ambaye alishakuwa na taarifa zake. Anajua ni nini anataka na kwa wakati gani. Na akawa yeye ndio anamuhudumia Maya. Haihitaji pesa ya Maya kama wanaume wengine. Ndio maana ilituchukua muda mrefu kuja kugundua kama Maya amerudia madawa. Maana alikuwa akienda kumfungia huko, anampa madawa tu na kumfanyia mambo mabaya bila Maya mwenyewe kujua. Sasa kwa mtu kama Maya ambaye alishakuwa mtumiaji, haitaji nguvu nyingi kumrudisha nyuma.” Tunda aliumia sana.

“Kwa sababu ni kweli Maya alitulia sana. Akabadilika. Kwa hiyo yule mwanaume akamjia na nia yakumuoa kabisa. Akawa anamuonyesha vile ambavyo watakuwa na maisha mazuri. Watoto wao. Na watakavyoendesha maisha yao bila shida kwa kuwa na yeye anao uwezo.” “Jamani! Kwani nyinyi hamkumuona huyo kijana?” Tunda akauliza kwa uchungu.

“Tulimfahamu. Alimleta mpaka hapa kwa babu yake. Tena babu yake alikuwa ameshaanza kuumwa. Lakini kwa ajili yake, alitoka siku hiyo chumbani, tukapata naye chakula cha jioni na huyo kijana. Ukweli alionekana ni kijana aliyetulia. Anaongea mambo sahihi kama aliyejifunza ni kitu gani tunataka kusikia kutoka kwake. Na ukumbuke hapo Maya alikuwa ndio ametulia. Anamalizia chuo, aanze kazi. Kila mtu alijua Maya amebadilika, amekuwa binti mkubwa sasa na yeye alishahojiwa kwenye vyombo vya habari, akakiri ulikuwa ni utoto, na marafiki wabaya ndio walimuingiza kwenye madawa ya kulevya. Ameamua sasa kutulia. Kwa hiyo moja kwa moja, yeye ndio angekuja kuchukua cheo changu au angekalia kiti changu.” Tunda akaumia sana.

“Kwani Nana, hicho kiti chako kina faida gani?”  Ikabidi tu Tunda aulize. “Oooh honey! Usitake nianze kutaja.” Yule bibi akakaa sawa. “Kwanza ujue ni foundation yenye mamilioni ya pesa. Kuwa president, au raisi wa hiyo foundation, ni unajulikana na watu wakubwa wa nchi nzima. Nianzie tu hapa Canada. Inamaana hakuna mlango unaotaka ufunguliwe, usifunguliwe. Si unakumbuka Viza yako?”  Akamuuliza Tunda.

“Nakumbuka! Mimi mpaka nikashangaa!” “Basi, ndio nguvu ya hicho kiti na jina la Cote, of course!” Wakacheka maana yule bibi aliongea kwa kujivuna kidogo wakati anasema Cote. “Basi ndio hivyo. Kina nguvu kubwa sana na kinajulikana, kwa kuwa tunagusa maisha ya mtoto wa kike moja kwa moja au mwanamke kwa jumla. Tunasaidia wale watoto wanao bakwa majumbani. Waliopitia kwenye biashara za kulazimshwa kwenye ukahaba. Nikisema kusaidia, naamisha kuanzia kuwatoa kwenye hayo mazingira, kusomesha, na kuhakikisha wanakuwa na ujuzi wa kujitegemea wao wenyewe.”

“Haya, kwa upande wa wanawake, tunawafikia wajane walioachwa kwenye mazingira magumu. Wanawake walioachika na kubaki bila msaada. Sisi ndio tunawasaidia kuwapa kila aina ya msaada unaohitajika kwa wakati huo. Iwe msaada wa matibabu, kisheria, chakula mpaka malazi. Na tukikupitisha kuwa unahitaji msaada wetu, inamaana maisha yako hayatakuwa kama yalivyokuwa. Tutahakikisha unasimama kwa miguu yako, tena unasimama vizuri. Hatuanzi jambo na kuliacha katikati. Labda mlengwa mwenyewe ashindwe. Hapo hatuna jinsi.” Hapo Tunda akawa amefunguliwa macho. Akakumbuka maneno ya Ritha.

“Sasa taasisi kama hiyo, kila mtu anataka kuwekeza. Wanasiasa wanapotaka kuingia madarakani, basi wataweka pesa zao hapo. Kuonyesha jamii kuwa anajali wanawake. Makanisa pia wanawekeza kwenye hiyo taasisi yetu pia. Matajiri wenye nia nzuri na wanaotaka kujitangaza kwa jamii, pia wanaweka pesa zao hapo.”

“Bado mimi mwenyewe huwa kila mwaka nafanya tafrija yakuchangisha pesa. Hapo napo huwa makampuni mengi huwa wanachangia sana.” “Nani mwanzilishi? Najua mpo na wenzio. Lakini lilikuwa wazo la nani?”  Akauliza Tunda.

“Nilianzisha mimi baada ya Mungu kutufungulia milango ya pesa, mimi na mume wangu. Cote aliamua kuniunga mkono kwa kuwa ni kitu nilimwambia lazima nije nikifanye Mungu akija kunifanikisha. Tulinunua eneo kubwa sana. Hapa ni padogo. Tukaanza kujenga. Mimi na Cote tu. Mwanzoni hakutaka kuomba msaada. Akasema lazima kisimame kwanza, ili watu wote wajue na kuelewa kama ni kitu changu, na watoto wangu ili wasije kunibadilikia baadaye.” Akamuona ametulia. Akaina kama anayefikiria.

“Cote alinipenda, kuliko nitakavyokwambia. Alifanya chochote kwa ajili yangu na kunipa chochote ninachotaka. Mpaka nilikuwa nikiogopa kulalamika mbele yake. Alikuwa akinisikia tu naongelea kitu kuwa nakipenda, ujue kama sio siku hiyohiyo basi ujue baada ya muda mfupi sana, kitakuwa changu. Atafanya kazi mchana na usiku kuhakikisha nakipata hicho kitu mpaka nilikuwa namuhurumia. Tena tokea tupo watoto.” “Pole Nana.” Tunda akamuhurumia.

“Asante. Lakini nitammisi sana Cote! Sana. Tulianzana nikiwa mdogo mno. Yeye ndio alikuwa kimbilio langu. Kila nilipokuwa na uchungu, nilikuwa nakimbilia nyumbani kwao, hata kama anakuwa anafanya kazi na baba yake, anaacha ananichukua, atanipeleka mahali, atakaa na mimi mpaka natulia.”

“Na kwa kuwa baba yake alitaka awe kama hivi Net, alikuwa akimfundisha sana kazi. Wakati wote ungemkuta Cote yupo nyumbani kwao na kazi. Basi akawa akiniita nifanye nao kazi. Ili tu niwe naye karibu. Na ndivyo ilivyokuwa mpaka yule mzee akaja akafariki, na Cote naye. Lakini tulifanya kazi sisi watatu kwa miaka mingi sana.” “Na mama yake?” Tunda akauliza.

“Mama yake alifariki wakati Cote yupo na miaka 12. Na yule mzee hakuja kuoa tena! Hata tulipokuja kufanikiwa sana na yeye alibaki hivyo hivyo. Alishindwa kupata mwanamke anayefanana na mama yake Cote. Tukawa tukiishi hapa watatu tu mpaka tukampata CJ, baba yake Net.”

          “Anyways, hiyo ni habari ya wakati mwingine. Sasa baada ya kusajili hiyo taasisi na kuandika katiba mpya ndipo sasa tukaanza kuitangaza. Hapo nilikuwa tayari nimeshaanza kusaidia baadhi ya mabinti waliokuwa wamefungiwa mahali, wakitumiwa na watu kwa biashara ya ngono. Wao hawanufaiki kwa chochote, ila hao watu waliokuwa wakiwaingiza nchini kwa siri. Tena walikuwa mabinti wakutokea nchi mbali mbali ulimwenguni zaidi Mexico.”

“Sasa kile kitendo cha mimi kutetea binti wakutoka nchi mbali mbali ulimwenguni tena wageni kabisa hapa nchini, waliokuwa wakija kutafuta maisha na kuangukia kwenye hiyo mikono ya hao watu wabaya, waliokuwa wakiwaingiza kwenye biashara haramu ya ngono! Ilivuma kwa haraka sana na hiyo taasisi kujulikana.”

“Maana walikuwa wakifanya hivi. Ili kuwafunga na kuwamiliki hao wasichana wadogo, waliohakikisha ni warembo sana, wanaokuwa wanawaingiza hapa nchini kwa siri au kuwatafuta kwa kuzingatia umri na urembo, wakishajithibitishia labda sio wazawa wa hapa nchini au binti ambaye hana familia ya kueleweka ili asije kutafutwa na kuishia kuwaharibia biashara yao. Wanahakikisha ni binti walio na shida ya maisha au wamekuja hapa nchini kutafuta.”

“Basi, wakishampata binti wa namna hiyo, mwenye hivyo vigezo, cha kwanza kabisa, kumpa madawa ya kulevya.” “Nana!” Tunda akashangaa kwa kuumia. “Ni wajanja sana. Mmoja wa hao mabinti ambaye alikuwa kama kiongozi wao, alisema kila binti ambaye alikuwa akiingia kwenye hiyo nyumba ambayo wanawapa hifadhi wote, siku ya kwanza kabisa wakiwaingiza hao mabinti kwenye hiyo nyumba yao, wanawachoma sindano ambayo inaanza kuwapa kiu ya madawa. Na wanafanya hivyo makusudi.”

“Kisha wanamuacha huyo binti anateseka kama siku mbili hivi, halafu wanampa madawa ya kulevya sasa. Anajisikia vizuri siku ya kwanza na ya pili. Kisha wanamnyima tena. Ujue hapo wameshafanikiwa kumfanya mtumwa wao kwa madawa.” “Jamani!” Tunda akahuzunika.

“Ukumbuke huyu binti hapo alipo hana pakwenda. Wamempa malazi kwenye nyumba yao. Wakishajiridhisha kuwa hawezi kuishi tena bila madawa, ndipo wanamwingiza kazini sasa. Wanampa mavazi yathamani sana ambayo anavaa wakati wanaenda kumuuza usiku huo ili watengeneze pesa nyingi. Huku wakiwatisha nakuwaambia wasipoenda kutumika huko vizuri na mteja akawasifia, hawatawapa madawa ya siku hiyo.” “Jamani!” Tunda akazidi kuumia. Angalau yeye alitumiwa na pesa iliingia kwake. Hakuna aliyemlazimisha. Alijua ugumu wa hiyo biashara. Akaumia zaidi.

“Basi, ikawa ikiwalazimu kwenda kutumika, wanarudi kufungiwa kwa malipo ya madawa ya kulevya. Wakiwapatia wateja, wanawavalisha vizuri, nakuwapeleka kama ni kwenye mahoteli makubwa, au kwenye masherehe ya vijana, au majumba ya watu. Wanatumiwa huko kutokana na malipo ya hao watu, kisha wanarudishwa tena ndani wao ndio wanalipwa.”

“Sasa mimi niliposikia, nikafanyia uchunguzi, nikaenda kuvamia hiyo sehemu na polisi. Tuliwakuta na hali mbaya, halafu wengi wao wapo nchini kinyume cha sheria. Mimi nikawaambia wale polisi nitawachukua wote kwa kuwa ninayo sehemu ya kuwatunza na ninao uwezo wa kuwatibu mpaka wapone.”

“Wao wakataka kuwarudisha kwenye nchi zao. Mimi nikapinga sana. Nikawaambia kwanza mimi ndio niliwagundua hao mabinti, wakati serikali ilifumbia macho, pili nikawaambia kibinadamu tu, wale ni watoto wa watu. Walikuja nchini kutafuta maisha, hawawezi kuwarudisha kwa mama zao wakiwa na hali ile.”

“Nilipambana kufa na kupona. Na hapo nilikuwa nina jeuri kwa kuwa nilikuwa na sehemu ya kuwahifadhi na pesa. Nikawaambia serikali waniachie mimi hao mabinti, sihitaji chochote kutoka kwao. Nikawaambia nitawatibu na kuwarudisha shule. Wakikosea ndipo wawarudishe. Sasa ikawa ni habari kubwa sana iliyoenea karibu ulimwenguni kote. Nchi walizotoka wale mabinti wakawa wakiniunga mkono, na nikapata uungwaji mkono na wanawake wakubwa sana ulimwenguni.”

“Ikageuka jambo la kisiasa sasa. Chombo cha kupigania haki za binadamu kikaingilia kati. Na mimi huwa sijui jibu la hapana.” Tunda akacheka. Akakumbuka Maya na Net walimwambia hivyo. “Waliniambia!” Tunda aliongea huku akicheka. “Hao waliokwambia wala hawakukosea. Nikitaka jambo langu! Huwa jibu la hapana haliwezi kukubaliwa akili mwangu. Nitapambana kufa na kupona.” Tunda akacheka huku akimwangalia.

“Basi, kwenye hiyo harakati nikiwa nahangaika na hao mabinti, vyombo vya habari havikuacha kunitafuta nakujua nilipofikia. Na ndipo watu sasa wakaanza kujitokeza kwenye kutaka kusaidia kwa namna yeyote ile. Wengine pesa, wengine taasisi za vitengo vya kusaidia watu kutoka kwenye madawa ya kulevya. Wanasheria! Ikawa misaada ya kila namna inaingia kila kona. Nje na ndani ya nchi ili tu kuniunga mkono.”

“Ndio mpaka sasa ipo hiyo sehemu. Nimehakikisha panabaki kuwa pazuri. Kuna majengo ya kisasa. Utakuja kupaona.” Tunda akawa amejibiwa maswali mengi sana. Heshima kwa huyo bibi ikaongezeka na maswali juu yake kwa hiyo familia yakaongezeka pia.

Akajikuta amepotelea mawazoni mbele ya huyo bibi, akijumlisha na kuongeza kutokana na kashfa za Ritha juu yake ya kwa nini ameolewa na kukubaliwa na huyo bibi! Akakumbuka mengi aliyosema Ritha kwa kumkashifu zaidi siku ya tafrija ya kuchumbiwa kwake na Net nchini Tanzania na huyo bibi kumtangaza kama ndiye mrithi wake. Hapo yakaanza kuleta maana. Ukweli ulikuwa mkubwa, japo aliongea akiwa na hasira kwake.

          Akangundua yule bibi alikuwa ametulia tu akimtizama. “Ni majengo ya nini?” Tunda akauliza na kuficha kile kilichokuwa kikiendelea mawazoni. “Yakuishi watu kwa muda wakati wanatafuta pakwenda. Unakuta ni mama mjane labda anawatoto, amewajia na kuwalilia shida. Sasa na matapeli ni wengi. Kabla yakumpa msaada, lazima kumchunguza. Lakini ukumbuke wakati huo yupo na watoto, hana pakuishi. Lazima umpe hifadhi yeye na watoto wake. Na mkijiridhisha mkaamua kumsaidia. Huwa tunapenda wajipatie ujuzi fulani, ili tunapowasaidia kuwapa makazi, baada ya muda fulani, waweze kujitegemea wenyewe, wasirudi kuwa tegemezi tena.” Tunda akarudishwa mawazoni. Akakumbuka maisha yake.

“Ni kitu kizuri na ni pakubwa sana. Tutakuja kwenda siku moja ili ukapaone. Uangalie mambo jinsi yanavyoendeshwa. Labda utaelewa ni kwa nini Vic anapataka.” Bibi Cote akamtoa mawazoni, Tunda akacheka  na kuinama kama anayefikiria tena. Safari hii akakumbuka vile Net alivyomwambia watafanya mambo kama hayo. Asimame, ili aje asaidie wanawake waliopita kwenye maisha kama yake. Akaanza kuunganisha hili na lile. Akajua labda ndio alikuwa akimtayarisha. Akanyanyua uso, akamtizama yule bibi. Macho yakagongana. Yule bibi akacheka.

“Nashuku. Narudia tena, NASHUKU, Vic alitaka kumuharibu Maya makusudi ili ashindwe kuchukua yale majukumu. Kwa kuwa ndio kipindi nilikuwa nimetangaza nataka kupumzika. Hapo nilikuwa bado sijamaliza kuomboleza. Nilimuuguza Cote kwa muda mrefu sana. Lakini bado sikuwa tayari aniache.”

“Kifo chake kikawa ni kama kifo cha gafla kwangu wakati madaktari walishaniambia muda uliokuwa umebaki. Niliumia sana. Nikawa nikijua pengine Maya atanisaidia kuendesha kule. Na yeye akarudia ulevi. Haya, Net naye akawa sio mtu wakuoa. Kwa Vic ikashindikana, Chloe naye akashindwa. Nilipoona vile, nikaona nikae tu kwanza mwenyewe.” Tunda akafikiria kidogo. Kisha akaamua kuuliza.   

“Vic alijua kama Net ameanza mahusiano na Chloe?” “Ndiyo. Net alihakikisha anafahamu ili aliheshimu hilo na aelewe kuwa hatakaa amuoe.” “Vic alilichukuliaje?” Bibi Cote akafikiria kidogo.

“Nisikilize Tunda. Net si myumbishwaji. Kitendo cha kukuchagua wewe tu, ujue tayari unao ulinzi mkubwa sana, ambao cha kwanza, Vic lazima atakuangalia kwa hofu. Net anaheshimika sana kwenye jamii na anajulikana kwa maamuzi mazuri. Kwa kukuoa tu wewe na sio wao, tayari wamekuogopa na wanakutizama kwa jicho la tofauti sana.” Tunda akainama.

“Na mimi nipo hapa. Vic ananiogopa sana kwa kuwa ananijua huwa sipendi ujinga. Kwa wewe kuishi hapa ndani, kwenye hii nyumba iliyokuwa ndoto ya mabinti wengi, halafu na mimi nipo hapa, pia hicho kinawaogopesha zaidi. Ndio maana unaona pametulia kabisa.” “Uliniambia uliwaambia kwamba nipo nahitaji kupumzika. Labda ndio maana wametulia.” “Wangesumbua sana mitandaoni.” “Mitandaoni!” Tunda akawa hajaelewa.

“Hivi umemsahau Maya?” Tunda akacheka. “Anakazi ya kukutangaza huko mtandaoni, kama kuwasuta tu au kuwaumiza roho. Kila mtu atakuwa anawaza lake lakini hawathubutu kusema sababu umeolewa na Net, na wanajua unaishi hapa. Lazima wanakuogopa sana. Nilitaka upate nguvu, niandae tafrija fupi ili niwaalike, wakutambue kabla Cote, hajazaliwa.” Tunda akavuta pumzi kwa nguvu.

“Utakuwa sawa tu. Usiogope. Umepata mume mzuri sana. Atasimama na wewe katika kila hatua yamaisha yako. Usigope kabisa. Nenda kajitayarishe tutoke kabla Net hajarudi na kutukuta hapa.” Tunda akacheka huku akisimama.

Historia ya Ritha.

W

akiwa njiani bibi Cote akaanza. “Usinielewe vibaya, lakini nataka kukwambia jambo ambalo hatukuwahi kuwaambia watoto wa Ritha.” Tunda akamgeukia. Walikaa kiti cha nyuma kwenye gari hiyo safi, nzuri, nyeusi kwa nje, lakini kila kitu ndani kilikuwa cheupe na kinavutia.

Kwanza ilikuwa Bullet proof. Hata mtu akipiga risasi, haiingii ndani. Ni gari aina ya ‘Luxury Mercedes Benz’.  Ndio ilikuwa gari ya huyo bibi. Ilitangaza utajiri mtupu. Ilikuwa mara ya kwanza kwa Tunda kupanda hiyo gari. Akabaki akishangaa vile yule dereva alivyobadilisha vitu kadhaa mlangoni na dirishani mara baada ya wao kupanda na kufunga milango. Bibi Cote alifunguliwa mlango, ndipo akapanda.

Akaona vioo vya madirisha ni kama vilipanda na kushuka vingine. Kukarekebishiwa hiki na kile ndipo dereva ambaye pia ndio mlinzi wa huyo bibi, akaondoa gari. Ndipo hapo huyo bibi akamtoa kwenye kushangaa. Akajiweka sawa ili kumsikiliza hapo nyuma walipokuwa wamekaa pamoja.

 “Nia yangu, nataka kukwambia mambo ya msingi ambayo nikija kukuacha, au hata sasa hivi, usiwe na maswali. Na pia nataka ujue kuwa, kuwa mama Cote, kunakuja na majukumu mengi, na kila uamuzi unaochukua, chukua ukiwa unawafikiria wajukuu wa huyo Cote hapo tumboni. Iwe ni zaidi ya hisia zako za wakati huo.” Tunda akashtuka kidogo.

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

Mambo ya uzunguni yanazidi kupamba moto, na Tunda akiona wameweka imani kubwa sana kwake kana kwamba hawamjui hata kwa kusikia tu! Ritha naye amefanya nini? Usikose muendelezo wa uzunguni...

CONVERSATION

0 Comments:

Post a Comment