Naomi Simulizi |+1 205 767 8163 |naomisimulizi@gmail.com NILIPOTEA! - sehemu ya 41. - Naomi Simulizi

NILIPOTEA! - sehemu ya 41.

 

B

ibi Cote akaendelea. “Ritha aliletwa hapa nchini na mume wake, japo anatangazia watu ni baba yake ndiye aliyemletea.” “Mume wake, yaani unamaanisha baba yake Net?” Tunda akauliza akitegemea jibu la ndiyo. “Hapana. Ritha aliolewa akiwa kwao. Akaletwa hapa nchini na mume wake aliyekuwa mwanafunzi.” Tunda akashangaa mpaka akageuka kabisa.

“Sasa aina ya Visa ambayo alikuwa amepewa mume wake, ilikuwa huwezi kubadilisha. Kwa kuwa mumewe aliletwa na serekali ya Tanzania. Aje achukue ujuzi fulani, kisha arudi kwao akatumikie serikali yake. Kwa hiyo palikuwa hakuna jinsi yakubadilisha aina hiyo ya Viza ili kuwawezesha kuishi hapa, ila kurudi nchini kwao, wakabadilishie Viza hiyo huko ndipo kama wanataka kurudi, warudi na ndipo wangeweza kufanya kazi huku.”

“Waliishi hapa kwa muda wa miaka 3. Wakitafuta jinsi yakuishi hapa moja kwa moja. Lakini wakashindwa kabisa. Ninavyosikia, japo Ritha alikataa kukiri, Ritha akamshauri mumewe waachane. Ili Ritha atafute mwanaume ambaye ni raia wa hapa, aolewe. Akishatengeneza mazingira mazuri. Akafanikiwa kuwa raia, amwache huyo raia kisha arudi kwa mumewe.” Tunda akashangaa sana.

“Basi. Wakaachana kisheria kabisa. Kwa kuwa tayari Ritha alikua ameingia kwenye system za hapa kama mke wa huyo jamaa. Kwa hiyo wakapeana talaka kabisa kwa mwanasheria.” Yule bibi akatulia kidogo.

Kisha akaendelea. “Ndio katika mawindo yake, nafikiri ndipo akampata CJ. Mtoto wangu wapekee! Bila kujua, CJ akiwa amempenda sana Ritha akatangaza ndoa kwa haraka. Nashuku na ujanja/mipango ya Ritha pia ilichangia kumfanya CJ atangaze ndoa kwa haraka. Baba yake akamsihi sana Junior, apate muda wakumchunguza Ritha, lakini yeye akafikiri sisi hatumpendi Ritha sababu ni mweusi. Baba yake akaona tusimpoteze kwa mwanamke mgeni. Ikaandaliwa harusi. Sasa tukamuuliza CJ, mbona ndugu zake Ritha hawaji? Ni kama akasema Ritha ni mtoto yatima au alikuwa na matatizo ya kifamilia. Ndugu ni kama walimtelekeza. Sababu zinazofana na hizo. Basi. Ikafungwa harusi, wakaenda mapumzikoni, akarudi na ujauzito wa Net. Hapakuwa na shida.”

“Mwaka huo ukaisha wakiwa na mtoto mmoja. Net. Net alipofikisha miaka 3 tukaanza kupata fununu kuwa mume wa Ritha alifika polisi, akidai mke wake. Cote akashtuka sana. Yeye mwenyewe ikabidi kwenda polisi kufuatilia.” Tunda akabaki akishangaa.

“Hapakuwa na mashitaka yeyote yaliyoandikishwa. Tukanyamaza kwa muda. Lakini kile kitu kikawa kinamsumbua sana Cote. Siku moja wakati tupo mezani tunakula, Cote akamuuliza Ritha swali la moja kwa moja kama alishawahi kuolewa. Ritha hakutoa jibu la moja kwa moja. Akatuzungusha kwa majibu yenye hekima. Ritha anaakili sana.  Anaakili ya kufikiria kwa haraka na anajua kutunga hoja. Basi. Hiyo siku ikaisha.”

“Baada ya miezi miwili akaaga anakwenda kusalimia wazazi Tanzania. Kila mtu akashangaa, mpaka mumewe. Kwa nini imekuwa ghafla wakati ni kama alisema hana ndugu au niyatima? Hapo napo akatoa majibu ambayo yakamfanya aruhusiwe. Junior alipotaka waongozane na mtoto, akaweka kipingamizi kabisa. Akasema aende yeye, akaandae mazingira, kisha safari nyingine waongozane.”

“Hapo alikuwa ameshamaliza shahada yake ya kwanza. Uzuri alikuwa na akili nzuri za darasani na alijua kutumia fulsa vizuri. Alipoolewa tu, akanza shule. Na tumbo lake, alikuwa akienda shule. Huyo Net ni kama nilimlea mimi mwenyewe tokea anazaliwa. Mama yake hakutaka kusubiri. Kwa hiyo alikuwa anamwacha Net tokea mchanga kabisa. Anaacha na maziwa. Basi mimi na wafanyakazi ndio tukamkuza huyo Net. Yeye anaondoka asubuhi kurudi ni jioni.”

“Basi. Baada ya kama mwezi, akarudi nyumbani na mpango wakusoma shahada ya pili. Hatujakaa sawa, akarudi shule. Pesa ipo na usafiri upo, hakukuwa na shida. Lakini safari hii akatafuta na kazi kitu kilicho tushangaza! Kazi ya nini wakati hapa pana pesa? Nikajaribu kumsihi ili atulie, iwe ni shule na mtoto. Akasema kwao kuna matatizo, anataka kusaidia. Nikazungumza na Cote, tukaanza kumlipa. Pesa yake binafsi ambayo haihusiani na mumewe, wala haulizwi maswali.”

“Basi, maisha yakaendelea. Yupo busy na maisha yake na sisi tukimsaidia kumlea Net. Tukaja kusikia baadaye kuwa alikuja kumrudisha yule mume wake wa kwanza kutoka Tanzania. Akampangia sehemu yakuishi.” “Nana!” Tunda akshtuka sana. Kweli. Subiri usikie yote.” Tunda akakaa sawa akajua mambo ni mazito. “Basi, Net alipofikisha miaka 5, kwenye hekaheka hiyo ya shule ya mama yake na ratiba zake, Ritha akashika mimba ya Maya. Lakini akalalamika sana kuwa kwa wakati ule hakuwa tayari kuwa na mtoto, sababu masomo ni magumu na lazima amalize. Alipoonyesha nia yakutaka kutoa mtoto, CJ akamsihi sana asitoe mtoto wake. Akamwambia amzalie tu huyo mtoto, yeye atalea mwenyewe.” “Nana!” Tunda akazidi kushangaa.

“Usimuone Ritha vile. Anamsimamo, na hana aibu wala hofu kwa yeyote. Zikaanza fujo, kulalamika juu ya hiyo mimba. Mara alalamikie hiki au kile. Ilimradi tu hataki huyo mtoto. Mwishoe CJ akamwambia akimtoa mtoto wake, ataenda kumshitaki.” “Yaani walifikia hapo!?” Tunda akashangaa sana na kuuliza.

“Oooh yeah! Anamipango yake ambayo mimba imeingilia. Ikawa ile mimba ni tatizo sasa. Wakasumbuana wee, akakubali kumzaa huyo Maya. Alipojifungua tu, ikawa ndio amepona matatizo yake. Sidhani hata kama alimnyonyesha Maya. Ratiba zake zikawa ngumu kweli! Mara akahamia hosteli kabisa ili awe sawa kimasomo. Akasema kipindi hicho cha miezi 9 ya ujauzito kimemrudisha nyuma kimasomo. Na kelele za mtoto pia, hataweza kumaliza chuo na yeye amebakisha mwaka mmoja, kwa hiyo akaondoka nyumbani.” “Subiri kwanza Nana! Inamaana akamuacha mtoto mchanga!?” Tunda akauliza kwa kuumia sana.

“Why not? Si CJ alimwambia anachotaka ni mtoto tu, atalea mwenyewe? Sasa ni kama kazi yake imeisha. Ameshambebea mtoto na kumzaa salama, maisha yake yanaendelea!” Tunda akabaki ameduaa. “Ikabidi sasa CJ apunguze kazi. Akahama ofisini, kazi zake baadhi akawa akifanyia nyumbani. Akawa nyumbani muda wote akilea watoto wake kama mama. Hakutaka amwache zaidi Maya ambaye alikuwa ndio amezaliwa tu, mikononi kwa wafanyakazi tu.”

“Tukamtafutia nanny wakumsaidia. Tukapata mwanamke mtu mzima kidogo zaidi ya yule tuliyekuletea wewe ukamkataa.” Tunda akacheka kidogo bila kutaka kujibu. “Alikuwa mama mzuri sana. Lakini na yeye alifariki kama miaka 14 iliyopita. Alimpenda Maya kama mtoto wake. Sasa yeye ndiye aliyekuwa akisaidiana na CJ kuwalea Maya na Net, na sisi tukisaidia pia, lakini mwanzoni sisi ilikuwa sio sana, kwa kuwa CJ alijaa kwenye maisha ya wanae, hakubakisha pengo mpaka alipoanza kuugua.” Akamuona ametulia kama anafikiria.

“Pole Nana.” Tunda akamtoa kwenye mawazo ili aendelee kupata udaku wa uzunguni. “CJ alipenda sana watoto wake! Hakutaka yeyote alemewe na watoto wake au mtu aone watoto wake ni mzigo. Alikaa hapa nyumbani akimlea Maya kama mama aliyejifungua.” “Mmmh!” Tunda akajikuta anaguna. “Mimi ninavyomsubiri mwanangu kwa hamu! Naona nitakuwa simuweki chini.” Bibi Cote akacheka. “Hutaki mtu amguse?” “Kidogo tu Nana, halafu mnirudishie mwanangu. Sio tena na nyinyi mumng’ang’anie kama hivi Maya anavyompigia mahesabu!” “Na amesema anatunza likizo zake mpaka Cote azaliwe.” “Ndicho anacho nitangazia kila siku.” Wakacheka.

“Ehe Nana!” “Basi, pakatulia. Junior yupo busy na watoto wake kuanzia asubuhi mpaka usiku, mama yao shule. Hakuna aliyewaingilia. Mimi na Cote tukawa kimya. Net alipoanza shule, yeye mwenyewe akawa dereva wa Net. Asubuhi anampeleka mtoto wake shule, mchana anamrudisha kwa ajili ya ratiba za Net za jioni hapo nyumbani. Net alijengewa ratiba tokea mtoto. Babu yake na baba yake walihakikisha tokea mtoto anajielewa yeye ni nani. Na tukabahatisha akawa msikivu kweli. Net hakusumbua kabisa.”

          “Maisha yakaendelea, lakini Ritha na mumewe wakawa ni kama hawaishi pamoja. Baadaye tukamwambia CJ, sio sawa hivyo wanavyoishi. Lazima mkewe arudi, au yeye amfuate ili wakaishi pamoja kama familia. Watoto wasikue bila mama. Sijui wakaelewana vipi, tukaona CJ anahamisha mizigo yake na mkewe na watoto. Wakahamia kwenye apartment. Kile kitu kikatuuma sana. CJ ni mwanangu wa pekee Tunda. Leo anaacha nyumba nzuri, anakwenda kuishi kwenye apartment ya vyumba vidogo vitatu! Hata sijui aliyejenga ni nani, nani anaishi karibu naye! Hapana. Moyo ukakosa raha kabisa.”

“Ndio baba yake akamwambia lazima anunue nyumba kwa ajili yake na watoto. Yale sio mazingira salama kwake na watoto. Akampa na pesa, Junior akanunua nyumba nzuri tu. Nikamtafutia wataalamu wakaenda kupatengeneza vizuri, wakajaza vifaa vya kisasa, ndio wakahamia hapo na familia yake. Hapo nikaweza hata kulala usiku nikijua mwanangu na yeye amelala pazuri.” Tunda akamcheka kidogo.

“Nilikuwa siwezi kulala. Usiku kucha natembea pale ndani. Namwambia Cote siwezi kulala humu ndani wakati mwanangu analala pabaya! Hapana. Hapo nilishindwa. Kwanza ndio ilikuwa mara ya kwanza anaondoka nyumbani tokea anazaliwa. Shule zote mpaka chuo, mwanangu alikuwa akisoma na kurudi nyumbani kwa mama yake. Ilikuwa wakati wowote ninapomtaka, namuweka mikononi! Wakati mwingine nilikuwa natoka kazini, namtoroka Cote namfuata mpaka shule angalau kumuona tu na kumbusu, wakati tumeachana asubuhi!” “Nana! Unamfuata shuleni wakati asubuhi mliachana?” Tunda akauliza.

“Na jioni nitamuona tukirudi nyumbani!” Akajibu na kumfanya Tunda acheke huku akimwangalia yule mama aliyeonekana mjasiri kama simba kumbe ana soft sport kubwa ya namna hiyo! “Sasa eti leo anaondoka pale ndani na watoto wawili! Anakwenda kujibana sehemu wanayoishi watu zaidi ya 1000, tena siwajui! Nilikuwa sipati usingizi.” Tunda akaendelea kucheka taratibu.

“Mlikuwa karibu naye eeh?” “Hivi unavyomuona Maya, ndivyo alivyokuwa CJ kwangu. Wakati wote atataka kuniona. Hakuona aibu hata alivyokuwa mkubwa, mbele ya wenzake eti na mimi nambusu na kumkumbatia muda mrefu hadharani! Hakuona aibu. Kwanza alipenda.” Tunda akacheka.

“Alinifuata popote na nikiwa na yeyote yule kuomba ni mbusu tu. Nilikuwa najisikia vizuri sana. Net yupo kama babu yake. Sio mtoto wa kudekeza au hana muda wakuwekwa mikononi muda mrefu. Akili yake imejaa mipango ambayo lazima aitimize kwa wakati, kama babu yake. Na alikuwa hivyo tokea mtoto. Utafikiri yeye ndio alizaliwa na mimi na Cote na si CJ. Ila CJ wangu? Oooh Tunda, hakuwahi kukua kwangu mpaka namzika.” “Pole Nana.” Akacheka kwa unyonge kama anayevuta kumbukumbu.

“Kilikuwa kipindi kigumu sana kwangu alipoondoka na watoto? Hata kula yangu ilikuwa shida. CJ mwenyewe alikuwa na kazi yakunituliza, lakini nilikuwa nakaribia kuchanganyikiwa, mpaka walipohamia kwenye nyumba niliyoridhika kuwa inamstahili.”  Akatulia tena kidogo. “Anyways, Maya alipofikisha miaka 3, akamwanzisha day care na yeye CJ akarudi kazini sasa. Tukawa wote. Ofisi ile uliyomkuta Maya, ambayo alikuwa Net, ndiyo ilikuwa ofisi ya baba yao.”

“Baba yake CJ alipomshauri amshauri Ritha afanye kazi kwenye kampuni yetu, hapakuwa na jibu la maana. Ila Ritha akawa kama anatukwepa hivi. Maswala ya watoto ikawa ni CJ. Kazi kidogo na watoto. Wakati mwingine Maya akawa anarudi pale nyumbani tunakuwa naye pamoja na yule nanny wake akitusaidia kumlea. Wakati mwingine yeye na kaka yake walikuwa wakiletwa hapa ijumaa, baba yao anakuja kuondoka nao siku ya jumapili ambayo ilikuwa lazima siku za jumapili tukutane kama familia na kuwa pamoja mpaka jioni. Na hapo ndipo CJ alipokuwa akiondoka na watoto wake, au kama Maya akigoma kuondoka jumapili basi asubuhi ya jumatatu mimi na Cote wakati tunakwenda kazini, basi tunawashusha wote shule, ikawa inategemea na CJ mwenyewe au Maya.”

“Taratibu kadiri walivyokuwa wakikua, Net na Maya wakazoelea pale nyumbani. Wakawa muda wakurudi kwao ukifika, wanagoma kuondoka, wanataka kubaki hapa na sisi. Tena kwa kulia haswa. Ikabidi CJ awe anawaacha. Hapo na mimi ndio ikabidi kupunguza kazi nikaanza kuwalea ili CJ asiwe na wasiwasi na watoto wake.” “Mama yao?” Yule bibi akakunja uso kama anayefikiria.

“Ni ngumu sana kumuelewa Ritha. Sijui nikwambie nini! Alikuwa yupo kama hayupo. Hapakuwa na ugomvi. Wala huwezi kusema kulikuwa na matatizo ya ndoa. Ila ni mwanamke ambaye niseme alipenda kujitegemea na asiingiliwe hata kwa maswali. Alifanya kile anachokipenda yeye.”

“Maya alipofikisha miaka 7, Net 12 karibu 13, baba yao akaanza kupata matatizo ya figo. Akaugua, akifanyiwa matibabu ya hali ya juu. Tulihangaika kwa kila namna, ili tu apone. Nilitumia pesa Tunda! Sina jinsi yakueleza. Uhai ungekuwa unanunuliwa, hakika wa CJ ningeununua kwa pesa yeyote ile.” “Pole Nana.” Tunda akamuhurumia. “Asante. Sasa hapo ndipo jukumu la watoto likawa sasa kwangu na Cote ili kumsaidia Junior ajiuguze. Wakati mwingine matibabu yalikuwa yakimfanya dhaifu sana. Hakuwa hata akiweza kujisaidia yeye mwenyewe. Tukamtafutia nesi ambaye akawa akimuuguza hukohuko nyumbani kwao. Anafika hapo asubuhi, anaondoka jioni akiwa amemuacha kitandani.”

“Sasa katika mahangaiko hayo yote yakuuguza na kulea, tukaja kupata fununu juu ya mumewe Ritha sasa. Kuwa anatutafuta ili azungumze na sisi. Cote akampigia simu Ritha, akamwita nyumbani. Akamuomba amueleze ukweli. Kama kawaida ya Ritha, mpaka Cote anamruhusu, hakuwa ametoa jibu la maana.” “Mmmh!” Tunda akashangaa kidogo. Akatamani aulize ila akaona aendelee kusikiliza.

“CJ alifika kipindi hajiwezi kabisa. Kila kitu ni wakufanyiwa. Nikamwambia Cote, ni aidha mimi nihame humu ndani, au CJ arudi.” “Saasa uende wapi?” “Nikaishi na mwanangu Tunda! Nilikuwa siwezi hata kuhema vizuri, eti nipo pale nyumbani, najua kuna mwanamke mwingine ananilelea mtoto wangu! Nilimwambia Cote nitakufa hata kabla ya CJ. Nikamwambia aniletee mtoto wangu niuguze mwenyewe” Akajifuta machozi.

“Pole Nana.” “Yaani nimemaliza tu kuongea hivyo, Cote akaondoka bila kujibu. Baada ya muda, naona gari ya wagonjwa inaniletea mwanangu na mizigo yake. Nililia Tunda, sikuamini.” Tunda alimuhurumia yule bibi. Hapo ndipo akaona roho ya umama ndani yake.

Akajifuta machozi, akaendelea. “Pole Nana.” “Asante. Basi. Nikaacha kila kitu. Akili ikawa kwa CJ na watoto wake tu pale ndani. Nikisaidiwa na manesi pamoja na yule Nanny wa watoto.” “Na Ritha?” Tunda akauliza. “Hapo hata akili ya mwanadamu mwingine ilikuwepo? Sikujali mtu, wala kitu, mimi niliyekuwa namtaka ni mtoto wangu. Nimeletewa, basi. Sasa nafikiri alipojua kama CJ atafariki, akapanga mambo yake vizuri, akarudi kuishi pale ndani. Mimi nilishangaa tu Ritha mwenyewe amerudi pale ndani na mizigo yake na yeye anasaidia kumuuguza CJ. Wala sikumuuliza. Kimya. Mimi nikaendelea na kuuguza na watoto.”

“Baada ya muda, eti CJ akiwa vile vile mgonjwa ananiambia wameamua kuuza ile nyumba. Anaona familia yake irudi kuishi pale. Nikajumlisha kichwani na kutoa, sikujibu kitu. Ila baada ya muda mfupi sana ile nyumba ikauzwa. Sikuuliza kitu. Mimi na Cote tukanyamaza kuleta amani kwa CJ ambaye ni mgonjwa.”

“Tukaendelea kumuuguza bila kuuliza lolote juu ya pesa zilizopatikana baada ya kuuzwa ile nyumba. Hapo tulikuwa tumeshajua kuwa, hatapona mpaka apate figo mpya. Maana ile ya kwake walishindwa kuitibu. Akawekwa kwenye orodha ya wanaosubiri figo kama itapatikana huko hospitalini kuwa kama ikipatikana figo inayoendana na yeye, basi apewe. Akawa anaendelea na matibabu huku akisubiria figo. Akiwa kwenye kusubiri, Mungu akamchukua mtoto mmoja tu aliyekuwa amenipa.” Tunda akamuona amebadilika mpaka rangi.

“Pole Nana.” “He was my sweetheart. Alinipenda kupita nitakavyokueleza. Nakwambia hivi anavyoniganda Maya, ndivyo alivyokuwa baba yake. Alikuwa na moyo wa tofauti! Anyways, baada tu yakuzika, Ritha akaaga.” “Tena!?” Tunda akashangaa sana. “Yeap. Akasema anataka kuondoka kwa kuwa aliyekuwa akimuweka pale ni CJ na CJ ameondoka. Tukamuuliza swala la watoto, akasema wanaweza tu kubaki na sisi. Tukashtuka sana. Watoto wadogo, anataka kuwaacha! Cote akajaribu kumwambia yeye ni kama Junior pale nyumbani. Anaomba abaki angalau mpaka watoto wake wafikishe miaka 18, akasema yeye yupo na kama watoto watataka kumtembelea, waende kwake. Atakuwepo hapa nchini kwa muda.” Tunda akatoa macho.

“Nana wewe! Akaondoka?!” “Nakwambia kama utani. Akachukua vitu vyake vyote, akaondoka.” Bibi Cote akaguna. “Mwezi ukaisha. Kimya. Mwezi wa pili, kimya. Cote akatuma watu wakamtafute wajue alipo. Wakarudi nakutuambia anaishi na mtu. Cote akiwa na hasira sana, akamfuata alipoambiwa anaishi. Ilikuwa apartment tu. Akamkuta yule mwanamme, Ritha hayupo. Cote akajitambulisha. Yule mwanaume ndio akamueleza Cote mwanzo mpaka mwisho na kwamba wapo kwenye kutaka kubariki ndoa yao. Cote akamuuliza kama anajua kama anawatoto. Yule mwanaume akamwambia anajua, na ilikuwa moja ya mipango yao. Cote akaondoka akiwa amemuachia ujumbe kuwa Ritha amtafute ili wazungumzie mirathi. Kumbuka hapo alikuwa na ile pesa ya nyumba waliyokuwa wameuza na mumewe.” “Lakini pesa si zilikuwa za Papa?” Akauliza Tunda.

“Kumbe unafuatilia vizuri!” Bibi Cote akashangaa akili ya Tunda. Akafurahi kuwa hakumpoteza na Tunda yupo makini. “Sasa ukumbuke bado alikuwa analipwa pia na ile pesa ya wakati ule kabla mumewe hajafa. Basi, baada ya wiki moja akaja ofisini. Cote akawa ameshaandaa makaratasi ya adoption. Kwamba anawataka wale watoto, Net na Maya wawe wetu moja kwa moja. Tulijiandaa sana tukijua pengine tutapata shida. Labda atatusumbua.” Akamuona anacheka kwa kusikitika.

“Ikawaje?” “Huwezi amini, Cote alimwambia anataka kumuachia pesa yote, na ataendelea kumlipa kwa makubaliano ya wale watoto, wawe wetu kihalali. Hakutaka kupoteza muda wala kuuliza swali, akasaini kila kitu, akasimama.” “Nana!” Tunda akashangaa sana. “Kabisa. Sasa mimi nikamuwahi. Nikamwambia, nataka wale watoto wamtambue yeye kama mama yao japo sisi ndio tutakao watunza. Nikamuomba awe anakuja kuwatembelea angalau mara moja kwa week. Apate nao muda, sisi wenyewe tutagharamia usafari zake. Kuwa tunamtuma dereva awe anakwenda kumchukua na kumrudisha. Akakubali bila shida. Na kweli, akawa anakuja hata mara mbili kwa week. Anakaa na watoto wake, anaondoka.”

“Baada ya miaka miwili kupita, tukamuona anakuja siku hiyo na nia yakutaka kulala. Cote hakumsemesha, wala mimi sikumuuliza. Akalala siku ya kwanza na ya pili. Akajirudi kama sio yeye Ritha. Siku ya tatu, tukapatwa na wasiwasi. Cote mwenyewe ikabidi aende kule alipokuwa akiishi kujua kulikoni.”

“Moja kwa moja akaenda kwenye lease office. Yaani ofisi ya wanapokodisha hizo apartment kujua kulikoni. Akaambiwa na uongozi kuwa, mwanaume aliyekuwa akiishi naye, alimkimbia na kila kitu. Yaani siku tatu zilizopita, Ritha alirudi kutoka kazini, hakukuta hata kijiko. Na mbaya zaidi, yule mwanaume alimuibia baadhi ya pesa na kama alimwaribia na kazini.” “Nana!” Tunda akazidi kushangaa.

“Yeap. Cote akarudi nyumbani akanieleza. Nikamshauri tumuache tuone mwisho wake. Akakaa hapa kama mwezi. Akiwa ametulia. Mama mwema kwa watoto wake. Hilo likatufurahisha.” “Kwa nini haukutaka kumuuliza!?” Tunda akauliza kwa mshangao. “Unakumbuka Cote alimwambia pale ni kwao kama Junior? Sasa amerudi nyumbani, unamuuliza tena?” Tunda akanyamaza.

“Basi. Maisha yake yakaendelea, baada ya miezi sita, akaaga tena kuwa ameamua kurudi kuishi Tanzania.” “Haiwezekani! Tena!?” “Hapakuwa na jinsi yakumzuia Ritha anapotaka jambo lake. Huwa anataarifu na anakuwa haweki nafasi ya kushauri. Sasa kwa kuwa Cote alitaka asiue undugu, akamuomba atakapofika kwao, atafute kiwanja, tujenge sehemu ambayo hata watoto watakapotaka kwenda, wawe na nyumba. Hilo akalifurahia sana. Alipofika tu huko, baada ya kama mwezi tu, akawa amepata kiwanja. Akili na mawazo ya Cote yakawa huko. Ikajengewa ile nyumba, ndani ya mwaka ikawa imekamilika kila kitu. Cote akaandikishana naye kuwa ile ni nyumba ya Net na Maya, lakini yeye ni msimamizi mpaka wakue au alipe kila pesa aliyowekeza pale. Sawa.”

“Akarudi tena na wazo la biashara. Anataka pesa. Cote akampa kwa makubaliano awe analipa kidogo kidogo kama hivi Net anavyomfanyia dada yake.” Tunda akacheka kidogo. “Si nilikwambia ni roho ya babu yake? Yaani hivi unavyomuona Net, na mume wangu alikuwa hivyo hivyo mpaka tabia. Ila Cote alikuwa mkali sana ambaye hawezi kujificha. Angalau Net anaweza kuficha makucha, ila sio Cote. Pale kazini wanamjua Net. Mkali na hawezi kuvumilii uzembe wa aina yeyote .” Tunda akacheka huku akimfikiria mumewe.

“Basi, ikaonekana ni mkopo ambao lazima alipe. Wakaandikishana mpaka kwa mwanasheria. Akapewa pesa, akaanza biashara. Lakini yote hayo, hatukuwaambia watoto wake. Hata mumewe hatukutaka kumwambia.” “Kwa nini!?”  “Tunda! Alikuwa mtoto wa pekee! Akawa mgonjwa sana. Hatukutaka afe akijua amesalitiwa au anasalitiwa. Kwa hiyo habari zote za mume wa Ritha, tulikubaliana tuzifiche, sisi tusimwambie. Afe kwa amani. Sasa kama yeye mwenyewe alijua akaamua kuzinyamazia, sijui. Ila hakusikia kutoka kwetu.” “Ehe!” Tunda akataka aendelee.

“Basi, Net ndio alikuwa akikubali kwenda kwa mama yake mara kwa mara. Maya alilelewa na baba yake na mimi. Alipokufa baba yake, mimi na babu yake ndio tukawa kama wazazi wake. Kumwambia atuache hapa aende Tanzania, alikuwa akilia sana. Hataki kabisa.” “Labda kwa kuwa hawakuwahi kuwa na mahusiano ya karibu na mama yake!” “Kabisa. Sidhani hata kama alimnyonyesha!” Hicho akakirudia tena huyo bibi kwa uchungu. “Kwa hiyo kwake akawa mgeni, hata walipokuwa wakiishi pale nyumbani na mama yake, alikuwa akinifuata mimi, hataki kuwa na mama yake karibu.”

          “Ila Net alikuwa mkubwa kidogo na kama nilivyokwambia. Net alikomaa akiwa bado mdogo. Walikuwa wakizungumza na Net kama mtu mzima, tokea mtoto. Kwa hiyo alikuwa na akili ya kumtambua mama yake. Ila si Maya. Maya hakuwahi kuwa na mama yake karibu. Nafikiri madawa ya kulevya ndiyo yalimfanya aende kwa mama yake. Tena ilikuwa kama adhabu, kumtoa hapa na kumpeleka kule ili akajifikirie. Kwa hiyo hayo ndio yakawa mahusiano ya Ritha na watoto wake.”

“Sasa kitendo cha Net amekuwa mkubwa, anatakiwa aanze kazi hapa, halafu mama yake anamng’ang’ania kule, kilimuudhi sana Cote.” “Haikuwa sawa.” “Kabisa. Cote aliona anavuna sehemu ambayo hakutaka hata kupanda! Na sisi hatukutaka kuweka fitina kati yao kwakuwa tulijiona tunakuwa wazee, tutaondoka na kuwaacha hapa duniani. Tukajiambia ni afadhali wabakie na mama yao kuliko wapoteza baba na waje watupoteze na sisi. Wajikute wamebaki peke yao bila ndugu na tumeua mahusiano na mama yao! Kwa hiyo ndio hivyo.” Tunda akavuta pumzi kwa nguvu. Akajiegemeza kwenye kiti akafikiria kwa muda.

Kisha akamgeukia bibi Cote. “Ni kweli maamuzi mengi mlifanya sio kwa hisia, maana nirahisi kukasirika nakuchukua hatua kutokana na hasira. Kama mimi yule mama amenitenda vibaya sana. Sijui kama unajua?” “Nafahamu sana.” Bibi Cote akajibu. “Na ilinibidi safari hii niwe mkali sana kwake. Hakuamini. Nilikwenda na Logan nikiwa nimejiandaa kumshitaki na kumfilisi vibaya sana. Nilimwambia akibisha tu, nampokonya mali zote nakupa wewe.” “Nana!?” Tunda akashtuka sana nakujiweka sawa.

“Kabisa Tunda. Sikumwambia hata Net. Lakini nilijiapia kumtenda ipasavyo. Nilikuwa nimekasirika nakaribia kupasuka. Hivi unajua nilimuuguza Net kwa majuma mawili, amebanwa mbavu sababu ya kumsafirisha kama mfungwa!” “Alinisimulia Net.” “Aliniudhi mpaka akanifanya nikumbuke mambo mengi sana. Nikakaribia kumfilisi kabisa. Nilimbemba bila kuchoka, halafu anamgeuka Net hivyo! Nilikasirika sana.” Tunda akafikiria kidogo.

“Sasa hivi unajua alipo?” Tunda akauliza. “Alitumia akili. Nilipokwenda mara ya mwisho nikamsainisha kwa masharti yakumsamehe pesa yote ilimradi asikuingilie wewe na Net. Awaache kabisa na afute kesi zote alizokushutumu. Na masharti mengine ambayo nilimwambia akiyatimiza hayo yote na kujiridhisha, hata akitaka abadilishe jina la kampuni na nyumba, sitamzuuliza.”

“Baada ya mwezi tu, alipotimiza kila sharti nililompa, akatuma karatasi, nikamsainishia kuwa nimemkabidhi kila kitu. Kwa hiyo nyumba na kampuni vyote vikawa kwa jina lake. Nasikia ameuza kila kitu, kasoro ile nyumba. Nasikia amerudi huku.” Tunda akashtuka sana.

“Wala usiogope. Huku hawezi kukufanya chochote. Hana huo uwezo hata kidogo. Na yeye anajua hilo, hatathubutu kukusogelea.” “Unajuaje Nana? Ritha anaakili na uwezo mkubwa wakushawishi watu wawe upande wake. Hukusikia alichowafanya Gabriel na mkewe?” Tunda akauliza kwa wasiwasi. “Kwa sababu mimi nimekwambia, basi usiwe na wasiwasi. Halafu alifanikiwa kwa Gabriel na mkewe kwa kuwa tayari walikuwa na ugomvi. Hawakuwa kitu kimoja ndio maana ilikuwa rahisi kwa Ritha kuwatumia kufanya ubaya wake.”

“Nimeishi na Ritha. Nimeona kazi zake na ujanja wake. Aliweza kumgeuza Net akawa upande wake. Hatukutaka kumtenganisha Net na mama yake kwa kumwambia mabaya ya mama yake. Lakini Mungu alikuja kumfungua macho Net, kwa machozi. Yuko makini sana sasa hivi na amaeshajua linapokuja swala la pesa, mama yake anaweza kufanya chochote.” Bibi Cote akafikiria kidogo.

“Kwa mara ya kwanza, Net alikaa akapata muda wakufikiria na kukumbuka yeye mwenyewe mambo mengi tokea mtoto mpaka mama yake anamfukuza Tanzania, akauliza kama alishawahi kuwapenda na kuwahesabu wao kama watoto wake kabisa?” “Ukamwambia nini?” “Tunda! Hata iweje, Ritha ni mama yao. Siwezi kuwaacha Net na Maya wakiwa na taarifa mbaya za mama yao, tena kutoka kwangu! Kama sisi mabaya ya Ritha yalitufikia hapa, na wao siku moja watakuja kumjua tu mama yao.”

“Huwezi kuingilia mahusiano ya mama na mtoto, hata siku moja. Na wewe nakuonya. Ukitaka Net awe upande wako siku zote, usiwe adui wa mama yake kwa maneno machafu au kupanga na Net mipango ya kuwa kinyume na mama yake. Utaona jinsi vita yako itakavyokuwa rahisi. Net mwenyewe atapigana vita yako, kwa kuwa ameshajua udhaifu wa mama yake, na anajua anakuonea. Hawezi kukubali. Atafanya kila awezalo kukulinda wakati wewe umetulia tu.” Tunda akaridhika.

“Net anakupenda sana. Hawezi kuruhusu chochote kutoka kwa yeyote kikupate. Usiogope kabisa. Na kuhusu Vic, usiwahi kumuonyesha unamuogopa.” Hapo napo Tunda akajiweka sawa.

Juu ya Vic.

B

ibi Cote akaanza kama anafikiria kidogo. “Tabia ya Vic ipo hivi, anapenda kuwa juu ya kila mtu na kila kitu. Na anataka kila mtu alitambue hilo. Atakachofanya cha kwanza ni kukuonyesha yeye ni bora kuliko wewe. Atakuonyesha anamipango mikubwa au alikuwa na mipango mikubwa sana. Asikutishe kwa lolote. Yeye ni mtoto aliyezaliwa akiona mambo yanafanyika. Anaangalia na kujua mambo kwa macho tu sio kuyatenda. Juhudi kubwa inawekwa na wazazi wake, yeye ni mmaliziaji tu. Sijui kama unanielewa?” Tunda akatulia akisikiliza.

“Vic hayajui maisha kwa ujumla wake. Anajua maisha aliyoishi yeye tu. Watu wakimuhangaikia kuanzia wazazi na watu wanaomzunguka. Nikikwambia ni ‘Diva’, ujue ni Diva kweli! Utakuja kumuona. Anaongea kama mtu muelewa sana. Anatoa mipango ya umakinifu sana, lakini hajui na hana uwezo wakutekeleza. Kwa kuwa amezoea kuamuru na vitu, vinakuja. Anaamuru pesa iingie kwenye akaunti yake, bila kujua inatoka wapi, au huyo mtu anafanya nini kuingiza pesa kwenye mifuko yake.”

“Hiyo pia imechangiwa na wazazi wake. Anapotaka juisi kutoka kwa mfanyakazi yeyote yule, hataomba. Ataamuru juisi ifike mbele yake bila kujali juhudi zilizotumika kufanya ile juisi imfikie mkononi. Na wakati wote anaonyesha kwa juhudi zake zote kuwa hakuna mtu anayefikia kiwango chake. Anaamini ni yeye tu, lakini ni kwa kuwa anastawi kwenye juhudi za mtu au watu fulani.”

“Net aliposema hatamuoa, wengi walishangaa sana. Kwa kuwa ni kama wamekua kwenye mazingira yanayoendana. Kwamba wana historia za pesa nyingi. Namaanisha wametoka kwenye utajiri. Halafu Vic ni mzuri kwa viwango vingi alivyowaaminisha watu, lakini hatoi ruksa wala mwanya wa kusikiliza mtu yeyote, hata wazazi wake.” Tunda akaendelea kusikiliza.

“Na ni mjanja sana. Anazungukwa na wasichana wengine wawili. Wapo kama vijakazi wake. Nilishawasikia mimi mwenyewe wakilalamika. Hawakujua kama mimi nipo nawasikiliza. Kuwa Vic ni mjanja na mbabe. Anachukua mawazo yao na kutangaza kama ni yake. Hilo ndilo hata Net alimgundua. Hana kila kitu, lakini analazimishia watu wajue yeye ni kila kitu. Na ndipo ugomvi wake na Maya ulipo. Maya anamdharau kwa wazi kabisa, kitu ambacho kinamuuma sana, na ndio maana na yeye alimtenda kwa makusudi ili kuhakikisha yeye ndio anabaki juu. Hawezi na haruhusu mpinzani kwa namna yeyote ile.”

          “Lakini wewe kuwa naye makini kuanzia mwanzo kabisa. Atakapokuonyesha anamfahamu sana Net, na kutaka kukuonyesha pale kwetu na yeye anauhuru wakufanya anachotaka kwa kuwa alikuwa pale tokea mwanzo, muonyeshe kwa wazi na mapema sana kuwa wewe ndio incharge, yaani wewe ndio kiongozi pale kwa sasa. Unanielewa?” “Nana!! Sijamaliza hata…” “Stop right there.” Bibi Cote akamkata kwa haraka.

“Utakapomfungulia Vic mlango hata kidogo leo, utamkuta chumbani kwako. Hajui mipaka, hajui hapana, hajui wapi atawale na wapi asitawale. Atajaa kwenye ndoa yako, atataka kukufundisha hili na lile, ilimradi watu wote wajue kuwa anakusaidia. Na wewe si kitu. Na akifanikiwa hilo nalo, hatakuacha. Atakufanya kama Maya. Kuanzia mwanzo, lazima umuonyeshe pale ni kwako sasa hivi. Yeye ni mgeni ambaye atafika, utakapomkaribisha wewe na sio Net. Na Net naye umuweke sawa tokea mwanzo.” Akaendelea.

“Ulimwengu huu mnaoishi sasa hivi, utatawaliwa na wenye nguvu, hekima na mipango. Kikipungua hata kimoja, watakutawala na kukurudisha jela kwa haraka sana kama alivyofanya Ritha.” Hapo Tunda akakaa sawa.  “Sasa hivi unaanza kuwa mama. Toka huko uliko, vaa roho ya Simba, King of the Jungle. Hapo ndipo utaweza kuwa salama na kutawala ufalme wako. Lasivyo jumuia inayotuzunguka sasa hivi, watakusumbua sana. Kwanza sababu ya rangi ya ngozi yako, pili historia yako ya nyuma. Make your past as a present precious gift.” Tunda akamgeukia kwa mshangao.

“Hivi unajua maisha yangu ya nyuma!?” “Najua kama ulishaishi kwa ukahaba. Najua. Na ninajua hiyo ndio sababu kubwa ya kuwekwa jela. Nafahamu vizuri tu. Usingeweza kuishi kwenye ile nyumba na sisi bila kukuchunguza vizuri na kukufahamu.” Tunda akapoa, akapoa haswa na aibu. “Nilifanya kosa kwa Ritha, sikutaka kurudia kosa.” Tunda akaishiwa nguvu kabisa. Akageukia pembeni

“Lakini!” Tunda akamgeukia tena. “Ukifanya maisha uliyoishi zamani kuwa siri, kitu cha aibu, watatumia huo udhaifu wako vibaya sana kuliko utakavyofikiria. Ritha alilijua hilo, sitaki kukukumbusha kule alikokupeleka. Mungu alikusaidia umelipa deni lako, sasa hakikisha inakuwa ndio shule na nguvu yako kubwa kwa kila anayekuzunguka. Lasivyo miezi yote sita uliyokaa jela itakuwa bure. Unanielewa?” Tunda akafuta machozi.

“Hayo machozi yaishie kwangu na kwa Net tu. Usiruhusu hata Maya ayaone. Uongelee maisha yako kwa ujasiri. Kule ulikotoka, ulikopitishwa na madhara yake, kisha tumia kwa faida ya wengine na watoto wako. Maana watakuja tu kuambiwa. Hutaki waje wateseke kwa maisha uliyoishi nyuma.”

 Juu ya Taasisi Anayotaka kuachiwa.

T

unda akaongeza umakini ili kuweka kichwani hayo mazito mengi aliyokuwa akimwagiwa na bibi huyo aliyeonyesha kumkubali yeye kama Tunda. Aliona ni shule ambayo hawezi kuzembea hata kidogo. Zaidi kutoka kwa bibi wa aina hiyo! Akajiweka vizuri.  

“Nilikwambia ninaongoza chama cha wasomi na wenye pesa. Wengi wa wale kina mama, wanataka kuongoza kwenye maono ambayo hawajui chanzo chake. Nilikwambia mimi nilikuwa mwanzilishi. Nilianza mimi na Cote. Lakini kulikuwa na sababu. Hakuna mtu anayeweza kumfikiria mwenye njaa, kama haijui njaa. Sijui kama unanielewa Tunda?” Tunda akajiweka sawa.

“Sikuanzisha ile taasisi kwa sababu mimi ni mwanamke! Hapana. Kwa sababu nilishapitia wanakopita wengi wa wale wanawake wanakopitia sasa hivi.” Tunda akakunja uso kama asiyeamini.  “Najua kuishi na baba mlevi anayepiga mke. Najua kuishi na mama aliyepigwa usiku kucha, na asubuhi inamlazimu kuamka, kuwataarisha nyinyi muende shule, tena akiwa na tabasamu usoni ili muende shule na furaha.”

“Najua kwenda shule nikiwa na njaa. Najua kufungiwa ndani kutokwenda shule. Najua kupigwa mpaka kuzimia bila kosa. Najua kutokuwa nacho, na kuwa nacho. Najua wanachopitia wale wanawake, au mtoto wa kike, kwa kuishi. Sio kusoma au kusimuliwa kama Vic na wale wanawake wengine wanaovaa alumasi zakupewa na wanaume zao. Unanielewa Tunda?” Tunda akaongeza umakini na kumtizama yule bibi kwa jicho la pili.

“Ukiniona mimi navaa alumasi, ni kwa kuwa nimeifanyia kazi, nikaitolea jasho na ninaistahili. Iwe ilitoka kwa Cote au nilijinunulia mimi mwenyewe. Vitu vyote ninavyomiliki ni kwa kuwa nilivihangaikia kwa kutokulala. Tukiwa mimi na Cote. Kwa shida sana. Ninapoandika muongozo wa kitu gani kifanyike kwenye ile taasisi kumsaidia mtoto wa kike, sio kwa sababu inanibidi mimi kama kiongozi! Hata kidogo. Naandika kwa kile nilichopitia, na ndio maana imedumu kwa muda mrefu sana na bado ipo.”

“Ninapokwambia nina shida ya billion moja kwa ajili ya ile taasisi. Na lazima niipate mwaka huu, ni lazima nitaipata. Hata kama wote watasema ni kubwa sana, hatuwezi. Mimi najua nilazima niipate. Kwa kuwa kwanza najua madhara ya kutoipata ile pesa. Inamaana yupo mwanamke mmoja na watoto wake, wataendelea kupitia alikopita mama yangu na sisi, mpaka kifo.” Tunda akashituka sana. “Au, inamaana kuna  binti wadogo sana, wataendelea kufanyiwa biashara za ukahaba kwa kuwa ninasikiliza wanaokula vizuri, wanao endesha maisha yao yakifahari kuniambia haiwezekani! Sio mimi na wananifahamu.”

“Nakwambia hivi, mimi ninapokwambia ninahitaji kiasi fulani cha pesa, hakuna atakayesimama mbele yangu akanizuia kutoipata hiyo pesa. Hakuna mlango nitagonga wasifungue. Hata ikinilazimu kukaa nje ya huo mlango mpaka nikutane na muhusika. Hakuna malkia nitashindwa kumfikia na kumuomba hiyo pesa. Kwa kuwa najua uharaka wa hiyo pesa na umuhimu wake. Sitakula wala kunywa, mpaka hiyo pesa yote ipatikane kwa muda ninaopanga mimi. Sio kwa sababu nataka watu wanione au wanisifie, hapana. Ni kwa kuwa najua umuhimu wa ile pesa. Sijui kama unanielewa?” Tunda akavuta pumzi kwa nguvu.

“Sasa hivi nakuelewa Nana.” Bibi Cote akaridhika. “Haiitajiki shahada mbili au tatu za elimu kumsaidia mwanamke mwenye shida! Ila inahitajika kuelewa alipo kwa wakati ule wenye shida, na atakapokuwa kama utamsaidia. Ndio maana unaona mpaka leo nimeshindwa kustaafu au kumuachia mtu majukumu yangu, kwa kuwa sijaona anayeweza. Hakuna anayeweza kuvua viatu, akapiga magoti mbele ya tajiri, kuomba chakula cha mama au mwanamke aliye na matatizo isipokuwa anayejua njaa. Aliyeshiba, atakwambia nikujidhalilisha. Inabidi kuomba appointment.”

“Matajiri hawana muda wakupoteza. Utaomba appointment leo, ukifanikiwa sana kumshawishi mtunza kalenda wake, utapewa tarehe ya mbali sana, tena hiyo ni bahati. Lakini hata kumpata mtunza kalenda wake ni kama umemuona Mungu.” “Sasa wewe unafanyaje?” Tunda akauliza. “Nikishajua unayopesa ninayoitaka. Hata nusu yake. Natafuta wapi unakuwa na kwa wakati gani. Hata kama unalindwa kama raisi, nitakufuata tu. Hiyo fujo itakayotokea getini kwako, lazima utataka niingie ndani. Sitaharibu kitu, ila sitaondoka hapo mpaka nikuone.” Tunda akaanza kucheka.

“Nana!” Tunda akamshangaa huku akicheka. “Wananifahamu sehemu nyingi sana. Na kwa kuwa pesa yao naifanyia kitu chamaana, sasa hivi hakuna mlango ninaotaka ufunguliwe, ukashindwa kufunguliwa. Nishatolewa kwenye magazeti nimepiga magoti huku na kule nikiomba msaada kwa machozi.”

“Historia yangu ya mateso ya utotoni imegeuka kuwa baraka. Sikuona haya kusema mateso yangu na kueleza umuhimu wa kumsaidia mtoto wa kike. Utakwenda kupaona, utajua ni kwa nini nasema hivyo. Ni anayejua njaa tu, ndiye anayeweza kumkumbuka aliye na njaa. Sio elimu nzuri au ujuaji wa kula na kisu na uma! Sisemi kuwa navyo ni vibaya, lakini hivyo sio vigezo pekee vinavyohitajika.” Hapo angalau Tunda akatulia.

“Ritha alikuwa na shahada tatu nzuri na zakuheshimika kwenye jamii. Lakini kwa kuwa alishindwa hata kutunza watoto aliozaa yeye mwenyewe, na mwanaume mmoja tu. Nilihakikisha anaelewa yeye sio mrithi wangu na wala hatakuwa mtawala hapa. Kwa kitendo chakupokea pesa kwa kuuza watoto wake, kiliniuma kama nawazaa wale watoto mimi mwenyewe labor.” Hapo hata Tunda akakubaliana naye.

“Huwezi ukanikuta mimi nazungumza kwa muda mrefu na Vic. Hata mara moja, na yeye amenijua hivyo. Kwa kuwa najua moyo wake. Najua kiwango alichopo au anachojiweka, mimi sipo na wala sitaki kuwa huko. Heshima ninayompa Ms Emily leo, ndiyo ninayompa Logan mwanasheria wangu, ila naweka mipaka tu. Ni kwakuwa nilishawahi kuwa kama Ms Emily au hata mama yangu alitamani kuwa kama Ms Emily lakini hakubahatika.”

“Nafasi au kazi anayofanya Emily mfanyakazi wangu wa ndani, inatamaniwa na wengi sana, na hawajabahatika. Emily amesomesha watoto wake wote na kusaidia wazazi wake wakiwa wagonjwa mpaka akawazika kwa kazi yake hiihii ya nyumbani kwangu. Sasa unawezaje kusema ni mtu duni? Unawezaje kumdharau mtu kama huyo ambaye akiamka asubuhi, watu zaidi ya watano wanasema asante Mungu? Ni kwa kuwa mtu hafahamu na hajui. Ila wewe umeweza.” Tunda akashituka kidogo.

“Nafahamu kila kitu kinachoendelea mle ndani.” Bibi Cote akacheka. “Hakuna kitu kinaendelea pale ndani, nisijue. Najua mahusiano yako na Emily, Gino na Carter. Najua huwa unamsaidia Emily kazi ili awahi kuondoka kurudi nyumbani kwake. Najua kama unasaidia jikoni na unapenda kumchokoza Gino.” Tunda akacheka.

“Gino anaakili za kitoto na anapenda kujifunza Kiswahili.” “Kwa kuwa na wewe umemuonyesha unamthamini. Inawezekana wala hakuwa na lengo lakujifunza Kiswahili. Lakini ule uthamani unaouweka kwake, na kumwambia awahi kuondoka, mara tu akimaliza kunitayarishia mimi na Maya, asikusubirie wewe mpaka ukiamka. Utajihudumia na kumalizia pale jikoni mara ukiamka, usifikiri ni kitu kidogo!” “Eeeh!” Tunda hakuwa akielewa anachomfanyia Gino. Yeye aliona kawaida tu.

“Kwanza ujue kazi yake ya asubuhi inatakiwa kuisha pale anapokuhudumia wewe na kuacha meza na jiko safi. Sasa kwa kumwambia asikusubiri, inamsaidia kuwahi kwenda kufanya kazi kwenye hoteli nyingine.” Tunda akashangaa kidogo. “Anapika huko chakula cha mchana, ndipo jioni anarudi tena pale kutupikia sisi. Na vile unavyomwambia akipika aondoke tu, wewe mwenyewe utaandaa meza, ameniambia imemsaidia kuongeza kazi ya tatu. Usifikiri ni kitu kidogo!” Tunda akabaki kimya akifikiria.

“Umekaa hapa mwezi mmoja unakwenda wa pili tu, lakini umegusa maisha ya watu. Gino anasomesha dada zake huko nchini kwao. Kwa kumsaidia hivyo, kunamuongezea kipato.” Tunda akajisikia vizuri. “Haya, kitendo cha kuhakikisha Emily na Carter wanakula na kushiba, kwanza hawakutegemea.” “Nana wewe! Nani anakwambia bwana?” Bibi cote akacheka.

“Nakwambia hakuna kitu kinaendelea mle ndani mimi nisijue. Mahusiano niliyonayo na wale wafanyakazi si ya kikazi tu na si ya siku moja! Maya alizaliwa Carter na Emily wakiwepo. Wale ni kama watoto wao. Nafikiri Carter alikuwepo hata kabla ya Net kuzaliwa. Yeah. Alikuwepo. Ila Emily ndiye alikuja Net akiwa ameshazaliwa na Maya akiwa analelewa na huyo mama niliyekwambia alifariki, Emily akiendelea kufanya anachofanya sasa hivi. Kwa hiyo wamefanyika watu wa pale. Pale ni nyumbani pia. Lakini hapakuwepo mtu wa kuwafikiria hivyo kama wewe unavyowafanyia.” Tunda akabaki akifikiria.

“Nilipoomba kuzungumza na wewe Tanzania. Haikuwa kwa ajili ya Net.” Bibi Cote akaendelea na kumfanya Tunda arudishe mawazo pale. “Ilikuwa ni kwa ajili yangu mwenyewe kwa kuwa hata ungejibu vinginevyo ambavyo nisingependezwa navyo na bado Net angesema anataka kukuoa wewe, ungeolewa tu.” Tunda akacheka kidogo.

“Lakini mimi mwenyewe niliridhishwa na wewe. Nikajiambia wewe ndiye ninayekutaka hapa. Swali likawa unakujaje huku nakuacha watu wanaokutegemea kule? Maana Net alikataa kabisa kukuonyesha mali zinazomzunguka huku. Na hata kwa kichache alichokuonyesha anacho, ulikataa kukitumia.” Tunda akashangaa kidogo. “Alijuaje?”  Akajiuliza.

“Mara nyingi tulipokuwa Tanzania kila tulipokuwa tukitolewa na Net, nilikuwa nikimuuliza mbona hauji naye, alikuwa akiniambia unafanya kazi mpaka usiku sana, unatafuta pesa yakumtoa baba yako jela au unatafuta pesa yakujilipia kodi. Wewe mwenyewe! Kwa jasho lako! Kwa maisha uliyoishi, ulikuwa na sababu zote zakuwa tegemezi, lakini ulipambana, ukijua umuhimu wakusaidia mtu mwingine. Sasa huyo ndiye mtu ninayemtaka mimi.” Tunda akajisikia vizuri.

“Na ndio maana nilikuja mimi mwenyewe Tanzania huhakikisha Ritha hakugusi tena. Na nilipoambiwa umekubali kulipa gharama ya makosa yako, kwa kukaa jela! Oooh my!” Yule bibi akacheka nakutingisha kichwa. “Nilipiga magoti pembeni ya ofisi yangu, nikamshukuru Mungu kukuleta kwenye maisha yangu. Lakini sikumwambia Net, kwa kuwa yeye alikuwa anakazi ya kulia tu.” Tunda akacheka huku akijifuta machozi.

“Mimi nikaendelea kufurahia moyoni. Nikajua Mungu anataka kunipumzisha.” Tunda akakumbuka mambo mengi na mipango ambayo Net alikuwa akimwambia afanye naye baadaye, akajua ndio hayo anayozungumzia huyo bibi sasa hivi. Net aliongea kwa mafumbo lakini hapo ikawa kama huyo bibi anajibu mafumbo yote.

“Lakini naogopa sana Nana. Unafikiri nitaweza kweli? Sijasoma kabisa. Halafu mwenzio kushika hata hii mimba ni muujiza mkubwa sana. Sijui kama unajua?” Akamuona kama anafikiria kidogo, kisha Tunda akaendelea baada ya kutulia.

“Nitakuja kukusimulia wakati mwingine. Ila kwa huu muujiza wa Mungu kunibariki na hii mimba tu, nimemuomba Net anipe muda wakulea kwanza. Nitamsaidia majukumu mengine baadaye. Lakini sasa hivi aniache nilee watoto wangu kwanza. Nakwambia hivi ili ujue sina mpango wakurudi shule sasa hivi. Nitafanyaje?” Bibi Cote akacheka kidogo.  “Ndio maana mimi nipo na wewe sasa hivi. Usiwe na wasiwasi. Umechagua kitu kizuri. Tulia kwanza na watoto ambao Mungu atakubariki. Na sisi tutakusaidia tu, usiogope. Na nimeshakwambia huhitaji shule kukuwezesha kufanya ninachofanya. Ila umakini na mipango. Pesa ya Cote na ile taasisi ndio itakusaidia kukupatia wasomi. Sijui kama unanielewa?” Tunda akajiweka sawa.

“Angalia wapi na nani unamuhitaji, unaajiri. Mimi sikusomea sheria. Lakini ninaye Logan. Sijui kupika hata kidogo, lakini napenda kula vizuri, ndio maana ninaye Gino.” Tunda akacheka. “Ni kweli hujui kupika Nana!?” “Hata kidogo. Na wote wananijua. Tulipoona na Cote ndiye aliyekuwa akipika. Na ndio kitu wananitania mpaka leo. Sijui kupika na wala sipendi hata kupita jikoni.” Tunda alicheka sana.

“Ndio maana huingii jikoni?” “Sina nitakachokifanya huko, halafu pia ni sehemu inayonikumbusha kifo cha mama yangu.” “Pole Nana.” Akamuona anafikiria. Muda mrefu tu dereva alikuwa ameshawafikisha salon, ameegesha gari. Kimya. Wao wanaendelea kuzungumza. “Twende tuingie ndani. Tuwahi kurudi nyumbani. Jumamosi jioni na jumapili ni muda na familia. Karibu sana Net anatoka kazini.” Tunda akafikiria kidogo.

“Natamani tuendelee kuzungumza Nana! Ujue mimi sikupata malezi kabisa. Yaani sasa hivi ni Net na mama Penny ndio wananisaidia. Na ndio maana lazima nizungumze na mama Penny kila siku. Ananielekeza mambo mengi. Nakuwa ni kama naishi naye nyumba moja.” Bibi Cote akacheka.

“Wewe usiogope. Sidhani kama Mungu atanichukua karibuni, ni mpaka akuone wewe upo tayari. Tutapata muda mzuri tu wakuelekezana. Sasa hivi fikiria jinsi ya kupendeza kwenye sherehe ya ukaribisho wako. Na siku hiyo ndipo nitatangaza siku ya baby shower.” Tunda akacheka. “Sawa.” Wakashuka na kuingia saluni.

 Party ya kukaribishwa Rasmi Tunda Norfolk, Ontario, Canada.

Norfolk ilikuwa ni kama kijiji kilichokuwa kipo ufukweni. Zilikuwa familia za watu walioishi hapo muda mrefu. Wakazi wa hapo walijuana kwa vizazi na vizazi. Nyumba ya kina Net ilikuwa mwisho kabisa wa huo mji, na mipaka yao imeingia mpaka ndani ya hilo ziwa Erie. Walikuwa na boti za kisasa zimeegeshwa kwenye ziwa hilo upande wa nyuma ya nyumba yao.

Moja ya kumbukumbu alizonazo Net, ni kwenda na babu yake kuvua samaki siku za jumamosi au siku awapo likizo. Mzee Cote alikuwa akimchukua Net na kwenda naye kuvua samaki. Ni kitu alikuwa akipenda sana Net tokea mdogo na enzi za uhai wa baba yake pia alipokuwa mdogo. Alikuwa akimsimulia Tunda vile wakati mwingine, wao watatu walivyokuwa wakitoka pale na boti na kwenda kuvua samaki na kukaa huko mpaka jioni. Alijifunza kuvua samaki akiwa bado mdogo tu. Ndio kitu alichokuwa akipenda kufanya na baba yake pamoja na babu yake.

Familia hiyo ya Cote pia ilikuwa na eneo lao la biashara kwenye bandari ndogo ya ziwa hilo. Ambapo walikuwa wakisafirisha watalii kwenye ziwa hilo lililobeba historia nyingi. Watalii walipokwenda kutembelea mji huo, walipenda kutalii kwenye ziwa hilo ambapo kina Cote pia waliwekeza boti za kisasa zakutosha. Na vyote hivyo viliachwa chini ya uangalizi wa Net.

Baada yakuonyeshwa utajiri wote ule, Tunda akaelewa ni kwa nini Net alifurahia alipojua Tunda ana mimba ya mtoto wa kiume. Alimwambia Tunda, kwao hawakuwa na uzao mkubwa. Baba yake alizaliwa peke yake. Kwa babu yake walizaliwa wanaume wawili tu. Cote ambaye ndio babu yake Net na kaka mtu ambaye naye alifariki zamani sana alipokuwa vitani. Na wao wakazaliwa na Ritha. Wawili tu. Net na Maya. Kwa hiyo akamwambia hata kama Tunda ataishia hapo, lakini angalau anauhakika wa mrithi wake.

Ni kweli walikuwa na eneo kubwa sana kuzunguka hiyo nyumba ya kihistoria. Kuanzia getini mpaka kwenye hiyo nyumba, ilijipanga miti mingi sana kutengeneza barabara ya kuzunguka uwanja wa mbele wa hiyo nyumba. Napo hapo mbele kulikuwa na bwawa zuri lililokuwa likimiminika maji kwa muundo tofauti fofauti kutokana bomba la katikati linavyozunguka. Majani na maua kuzunguka eneo zima, vilikuwa nadhifu sana. Ungependa kuangalia au kukaa hapo. Kulipangiliwa vizuri sana.

Kasoro Tunda alifika hapo kilikuwa ni kipindi cha baridi kuanza. Na kikawa kibaya zaidi kwake yeye muoga wa baridi. Alipenda kusimama madirishani, akichungulia nje. Labda awe na Net azunguke naye kidogo kisha warudi ndani. Tunda hakuwa akiamini kama na yeye anaishi humo ndani. Macho na nafsi yake havikuwahi kushiba thamani za humo ndani.

Ilikuwa ni familia iliyojulikana kwa utajiri mkubwa na harakati za huyo bibi mgombania haki za wanawake. Kila mtu alijua mke wa Net ndio atakula mema ya nchi na pengine ndiye atakalia kiti cha bibi Cote. Kwa hiyo kila mtu alikuwa akimsubiria huyo mke wa Net kwa hamu sana. Maya alishadharaulika kwenye jamii sababu ya tabia zake za madawa ya kulevya na wanaume waliokuwa wakifuja pesa ya Cote kupitia yeye Maya. Hata huko kutulia kwa safari hii, walishaambizana ni kwa muda tu. Wengi walimtarajia kuja kumuona tena mtaani na madawa ya kulevya.

Tunda alishatafuta nywele yakuvaa siku hiyo. Aliagiza human hair ya Indian Remmy. Ilikuwa ni ya pesa yakutosha. Akatafuta saluni za watu weusi kwenye mji wa jirani, akaenda kutengenezwa mbali kidogo na hapo kwa kuwa eneo hilo wengi walijaa weupe. Nguo zake Maya ndio aliyeenda naye kutafuta.

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

Ilikuwa siku ya jumamosi jioni ndipo bibi Cote alipotaka watu wafike nyumbani kwake. Kulikuwa na ukumbi mkubwa na wathamani sana kwenye jumba hilo. Kama kawaida walikuja watu wakupamba. Tunda alikwenda kuangalia ujuzi wa hapo pia. Akatoa maelekezo namarekebisho, mpaka akaridhika, akatoka kurudi chumbani kupumzika wakati anasubiria muda wa tafrija na Net arudi kutoka kazini.

Mkasa wa Kwanza wa Tunda &Vic.

T

unda alingia na kujilaza kitandani, akapitiwa na usingizi. Alishituliwa na binti mrembo sana. Tunda akashituka na kukaa. “Wewe ni nani unayeingia chumbani kwangu bila ruhusa!?” Tunda akamuuliza kwa mshangao. “Vic!” Tunda akakunja uso kwa hasira. Kwanza alimuamsha kutoka usingizini. Pili ameingia chumbani kwake bila hodi! “Wewe ndiye mfanyakazi mpya niliyeletewa?” Tunda alimfanyia makusudi, akijua wazi ni Vic aliyeambiwa habari zake. “OooHoo! Noowo!” Vic akashituka sana akijiangalia juu mpaka chini.

“Mimi ni Vic! Vic!” Tunda akakunja uso. “Natakiwa kukufahamu!?” Tunda akamuuliza kama anayeonyesha kupotezewa muda. “Mimi ndiye nilikuwa mpenzi wa Net.” Vic akajibu kwa jeuri. “Oooh kumbe jina lako jingine ni Vic? Sikujua!” “Kwani wewe unafahamu jina gani!?” “Chloe.” Tunda akamjibu huku akimtizama.

“Mimi sio Chloe! Inamaana hakuna mtu aliyekwambia kama kuna Vic? Chloe hana hadhi kama yangu! Ni watofauti kabisa. Mimi nimekuwa na Net tokea..” “Subiri kwanza. Nyamaza kabisa. Huwa sipendi watu wanaongea sana. Sipendi kelele.” “Unamaanisha nini?” “Nimekwambia unyamaze. Unaongea sana. Just hush and listen.” “Kwa nini nikusikilize wewe?”  Vic akauliza kwa dharau huku akimtizama Tunda juu mpaka chini.

“Swali zuri sana. Cha kwanza, umesimama ndani ya chumba changu na mume wangu. Umeingia bila kubisha hodi. Hiyo ni dharau kubwa sana ambayo leo iwe mwanzo na mwisho.” “Nilikuwa nikikilalia mimi hicho kitanda.” “Mbona umeshindwa kuendelea kukilalia mpaka leo?” Tunda akamkazia macho. Vic akababaika.

“Umeshindwa, na huna hadhi hiyo ndio maana mimi nipo hapa. Sasa nakuonya. Leo iwe mwisho kuingia kwenye hiki chumba. Usithubutu kurudia tena.” “Utanifanya nini nikirudia?” “Leo ndio itakuwa mwisho wako wakuingia kwenye hii nyumba na pale getini. Kama unabisha, toka pale kwenye huu mlango, kisha rudi tena hapa ndani. Nitakuonyesha mimi ndio Tunda Cote, mke wa Nathaniel Cote. Nijaribu tu kwa hilo, nitakuonyesha. Na ninakuahidi, sijui nani tena!..” “Jina langu ni Vic. Kila mtu ananifahamu.” “Kasoro mimi. Na hakuna aliyenitajia wewe kwa kuwa hawakuoni kama ni wa muhimu humu ndani. Haya, toka kabla hujatolewa hapa na askari.” Kimya.

Tunda akasogea mlangoni. “Baada ya sekunde 30, nikishamaliza kukupa haya maelekezo, uwe umetoka hapa. Na uende ukakae sehemu husika kama waalikwa wengine. Nisisikie unazunguka humu ndani wala kutoa maagizo yeyote kwa mtu wa humu ndani. Nenda ukapate huduma kama waalikwa wengine. Sio kwa Ms Emily wala Carter.” Tunda akaendelea. “Kama ulilala na kucheza humu ndani, ujue ni wakati huo. Sasa hivi Net ameoa, na anafamilia. Ukishindwa, ondoka kabisa. Maana sio lazima wewe kuwepo kwenye tafrija.” Uzuri lugha nayo ilikuwa si ya kubabaisha kwa Tunda. Akaongea kwa kujiamini mbele ya Vic, kama alivyofundishwa na bibi Cote.

“Haya toka lasivyo baada ya sekunde 30 kuanzia sasa, nitaufunga huu mlango, nitakao wafungulia ni askari tu watakao kutoa hapa na kukupeleka kituo cha polisi kwa kosa la kuvamia chumba na nyumba yangu. Haya toka.” Vic akatoka pale alipokuwa amesimama akaanza kusogelea mlango.

Mara Maya akaingia huku akicheka sana nakumpiga picha Vic. Maya alikuwa akicheka kwa sauti ya kukera! “Nitakutag picha zako facebook. Mungu amekuletea kiboko yako Vic.” Maya aliendelea kumcheka mbele ya uso wake. “Wala simuogopi. Alinikuta humu ndani.” “Wapi!? Wapi!?” Maya akaendelea kucheka. “Aibu zako Vic. Leo umeingia aibu ya miaka! Buuuuu!” Maya akaanza kum buuu.

“Na kwa taarifa yako, hawezi kunifukuza mimi.” “Si amekwambia ubaki hapa ndani baada ya sekunde 30 anaita polisi? Kama kweli wewe jeuri mbona unaongelea hapo nje? Ingia humu ndani ubishane na mimi uone jeuri ya mke wa Nethaniel Cote! Mmiliki wa mali ya Cote. The one and Only. Tunda. Baem!” Akajigongeshea ngumi mikononi mwake.

Yeye aliingia ndani, Vic akawa ametoka nje ya mlango. Tunda amesimama mlangoni anamsikiliza Maya, cha uchokozi. Akaendelea kumzomea kwa sauti huku akimcheka. Ni kama naye Vic alikuwa ameshikwa na kibumbuazi. Kuondoka haondoki amebaki amesimama. Amebadilika rangi akawa mwekunduuu. Alikuwa amependeza sana. Hata Tunda aliona huo uzuri wake.

Wakati Maya akiendelea kumzomea na kumkejeli, mara wakashitukia Net amesimama pale. Maya akanyamaza kwa haraka akakimbilia nyuma ya Tunda. “Ni nini kinaendelea?” Akauliza Net akiwa amekunja uso, anamtizama Vic. Akaanza kulia Vic. “Wamenidhalilisha.” Akaongea Vic kwa kujiliza mbele ya Net. “Yeye ndio amemdhalilisha Tunda.” Akadakia Maya akiwa mgongoni kwa Tunda, tena kishabiki. Ikabidi Net amgeukie yeye.

Akaanza Maya. Pale pale mgongoni kwa Tunda. “Amemdhalilisha vibaya sana Tunda tena kwa sauti ya juu mpaka ikabidi mimi nije kuangalia kulikoni kumbe ni Vic! Cha kwanza na kibaya sana, ameingia chumbani kwenu Tunda akiwa amelala. Mimi mwenyewe na Nana tulikuja tukataka kumsalimia Tunda, Nana akasema tumuache alale kwa kuwa Carter alimpigia simu Nana kuwa Tunda anafanya sana kazi kule ukumbini, Nana ampigie simu amwambie akapumzike. Sasa eti sisi tumemuacha Tunda apumzike, yeye akamuamsha!” Net akakunja uso.

“Maya anadanganya.” Akakanusha Vic. “Sasa kama huniamini mimi, muulize Tunda kama Vic hajamuamsha na kumwambia kwamba hicho kitanda alicholalia yeye Tunda, alikuwa akikilalia na wewe! Muulize Tunda.” Net alishituka mpaka akawa mwekundu. “Umechanganyikiwa wewe Vic!?” Net akamsogelea na kumuuliza kwa ukali. “Na wala hajamwambia hivyo tu.” Maya akaendelea kuchongea kishabiki.

“Amemwambia Tunda mlikuwa mkifanya mapenzi hapo usiku kuc..” “Maya! Maya! Come out. NOW!” Bibi yake akaja na yeye akamuwahi Maya.  Alijua Maya atazidi kuharibu. “Muongo, sijasema hivyo.” Vic akabisha. “Nimekurikodi. Kama unabisha narusha sasa hivi hewani naandika ‘Net alikuwa akikutumia tu lakini….” Bibi Cote akaingia kwa haraka. Akamvuta Maya nje kwa kumshika mkono. Maya akaanza kucheka wakati anatolewa pale.

Tunda akafunga mlango kwa nguvu. Wakabaki wamesimama nje ya mlango Net na Vic. “Unashida gani Vic? Kwa nini unataka kumvuruga Tunda?” “Maya anadanganya Net. Ananisingizia.” “Nani amekwambia unaruhusiwa kuingia chumbani kwangu na mke wangu?” “Nilikuja kumsalimia tu.” “Hapana Vic. Lazima uheshimu hii nyumba. Sio kama zamani. Mimi nimeoa, na ninampenda sana mke wangu. Unanielewa?” Vic akasikika akilia.

“Iwe mwisho kuingia upande huu. Na ninaomba uwe kama wageni wengine. Ufike hapa nyumbani pale unapokaribishwa na uishie sebuleni. Tafadhali sana.” Tunda akaondoka pale alipokuwa amejificha ndani akiwasikiliza, akaelekea bafuni kuoga. Akajiridhisha na hilo onyo. Alitoka na kumkuta Net ameinama pembeni ya kochi ameshindwa hata kukaa.

“Pole na kazi.” Tunda akasalimia. Akanyanyua uso. Ulikuwa mwekundu na mishipa imesimama kichwani. Tunda akamsogelea akiwa amejifunga taulo, akakaa pembeni yake kwenye kochi. “Samahani sana Tunda. Usije kufikiri nilikuwa nikiishi maisha yakihuni zamani. Vic nilikuwa naye pamoja. Hapa ilikuwa kama nyumbani kwao. Wakati mwingine wazazi wake walipokuwa wakisafiri, walikuwa wakimuacha hapa.” “Kama mpenzi wako au kama mtoto wa hapa?” Tunda akauliza.

Net akanyamaza kidogo. Tunda akataka kusimama, akamshika mkono. “Vyote. Wengi walijua yeye ndio angekuwa mke wangu.” “Wewe ulijua kama na yeye ndivyo anavyojua?” “Ndiyo.” “Kwa hiyo ulimpa sababu gani yakubadili mawazo? Maana mlikuwa mkilala naye hapa. Unasema tokea watoto. Iweje ghafla nafasi yake aichukue mtu mwingine?” “Usiseme nafasi yake. Nani aliitamka kama hii ni nafasi yake?” “Wewe kwa kufanya naye mapenzi humu ndani na kumtangaza kwa watu kama ni msichana wako.” “Hiyo ilikuwa zamani sana Tunda! Hata kabla ya Chloe.”

“Net! Ni sababu gani uliyompa?” “Kwanza alinisaliti. Alifanya mapenzi na mtu mwingine.” “Yaani hiyo ndio ikawa sababu ya kuachana!?” Tunda akauliza kwa mshangao. Net akatulia kidogo. “We Net? Inamaana hiyo ndio sababu?” “Sasa ingekuwa nini kingine?” “Usinichezee akili Net. Mimi sio mtoto mdogo.” “Mungu wangu ni shahidi.” Net akawa akijitetea kwa hofu hakutaka kuharibu siku hiyo maalumu kwa historia ya hiyo familia.

“We Net! Wapenzi wanakoseana. Hasira zikiisha wanarudiana. Wewe ulinikuta mara ngapi na wanaume tofauti tofauti ukaishia kunioa? Kama ulinioa ukiwa na hasira na mpenzi wako, hasira ikikuishia ukaamua kurudiana? Naomba usinipotezee muda Net. Nishahangaika kwenye maisha. Sitaki uje uniumize. Na nilishakwambia, nitakosa kila kitu isipokuwa wewe. Sijaja hapa kufuata mali ambazo kwanza hata sikujua kama unazo! Nimekufuata wewe. Sasa hasira zakusalitiwa zikikuisha!?” Tunda akambadilikia Net.

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

Wageni wamaana, wakumbwa wa nchi na mji huo, vyombo vya habari wanakaribia kujaza ukumbi kwa ajili ya utambulisho rasmi Mrs Cote/Tunda ambaye Vic ameshamtibua. Wanandoa hao wapo chumbani, je nini kitaendelea? Usiache kujua mikasa mizito mbeleni. Kama Vic aliweza kumdhuru Maya ili ampishe enzini, atamfanya nini Tunda aliyemfukuza kwa kumdhalilisha vibaya hivyo! Usipitwe....

CONVERSATION

0 Comments:

Post a Comment