Naomi Simulizi |+1 205 767 8163 |naomisimulizi@gmail.com NILIPOTEA! - sehemu ya 42. - Naomi Simulizi

NILIPOTEA! - sehemu ya 42.


“No nono no no noo Tunda. Tafadhali naomba utulie. Na ujue haitakaa itokee nakuacha wewe au nakusaliti. Kwa sababu nakupenda wewe. Mara ya kwanza tu kukuona, moyo wangu ulifungamanishwa na wewe. Nikakupenda. Nilihamia Tanzania kwa ajili yako Tunda. Naomba uniamini. Hata Papa na Nana wanajua hiyo sio sababu pekee iliyonifanya nimuache Vic. Nilijua hakuna maisha kati yetu. Kwa kufurahia tu utotoni ilikuwa sawa. Lakini nilimuacha hata kabla sijakuona wewe. Mungu ni shahidi. Alivyonisaliti, nilimwambia nimemsamehe lakini hatutakaa tukarudi kuwa wapenzi ila marafiki.” “Na urafiki pia sitaki!” Net akaanza kucheka.

“Usicheke bwana Net! Tabia gani hiyo ya wanawake zako wananiingilia mpaka chumbani?” “Hilo ni kosa kubwa sana. Nimemuonya asiwahi kurudia tena. Na ameelewa na kuomba msamaha. Haitakaa ikatokea tena. Wewe ndio mke wangu mimi.” Tunda akasimama. “Mbona unaondoka sasa?” “Naomba niache Net. Ulificha habari zake, leo ndio unataka kuendelea kunikera kwa kuendelea kumzungumzia hapa chumbani kwetu!” “Acha kukasirika Tunda! Hapakuwa na habari yeyote ya kukwambia mpenzi wangu. Huoni nilikwambia habari za Chloe sio yeye? Kwa kuwa sio muhimu.” Tunda akamwangalia kidogo, akaondoka.

“Acha kunifanyia hivyo bwana Tunda!” Net akasimama akawa anamfuata nyuma wakielekea kwenye upande wa closet ya Tunda. “Mwenzio nilikuwa kazini lakini nakuwaza wewe.” “Usinidanganye Net.” “Kweli mpenzi wangu. Ujue nilikuwa nawaza nini?” “Nini?” Tunda akauliza huku akiendelea kwenda.

“Nilikuwa najiambia nitarudi kwa mke wangu, anipe pole ya kazi ya week nzima. Anibake, nikaoge ndio twende kwenye tafrija.” Ilibidi Tunda acheke tu. “Ulivyokazania kubakwa! Toka siku ile usemi ni huo tu!” “Usinikasirikie bwana Tunda! Mimi na wewe kitu kimoja.” “Waonye hao unaowaita marafiki zako wasiwe wanaingia huku ndani.” “Kwanza ameniambia umemfukuza. Ndivyo Vic anavyotakiwa. Mtu ambaye hamuogopi. Kama hivyo atakuheshimu sana. Lasivyo angekusumbua sana Vic. Mimi namjua jinsi alivyo mkorofi. Umefanya vizuri.” Tunda hakujibu akaingia kwenye closet upande wake Net akamfuata.

“Nimekusifia vyote hivyo Tunda hata kunijibu!” “Kwanza ujue bado nina hasira. Niache.” “Si ndio nikutulize ili ukitoka hapa uwe umetulia? Sio watu wanatambulishwa mke wa Net, unakuwa umenuna kama umelazimishwa bwana, wakati unanipenda!” Net akamsogelea mgongoni akambusu shingoni huku akimtoa taulo. Akiwa vile vile nyuma yake akawa anampapasa juu mpaka chini huku akimnyonya kuzunguka shingo. Alipomuona ametulia, akamlaza mkewe palepale kwenye kapeti. Akaanza kumchezea mpaka akamridhisha mara ya kwanza, akamgeuza, akapata bao moja na yeye.

Wakatulia pale kwenye kapeti wakiwa wamelala. Net akamgeukia. “Nakupenda Tunda. Wala haupo hapa kwa bahati mbaya. Sema umekuwa ni kama puzzle ambayo sasa ime fit kwenye mapengo mengi tu. Umekuwa ni jibu ya maombi ya bibi. Na rafiki wa Maya.” Tunda akaanza kucheka. “Maya anaakili za kitoto nyinyi!” Net akatingisha kichwa kama anayemsikitikia mdogo wake.

“Kwani ulishawahi kumpiga? Mbona anakuogopa sana?” “Ujinga alioufanya zamani ndio unamsuta. Sijawahi hata kumpiga mimi.” Tunda akacheka kama anayemtafakari.  “Hivi unajua wakitoka na Nana kazini kanakimbilia hapa kitandani. Katalala hapa na habari nyingiii. Akisikia unasalimiana tu na Carter, kanaruka kukimbilia kwa Nana.” “Najua pia kama huwa anaogea huku kama sipo.” Tunda akacheka sana.

“Umejuaje wakati ameniomba nisiwahi kukwambia!?” “Najua. Lakini naona nimuache tu. Amepoteza marafiki wote. Sasa hivi yuko peke yake ndio maana anashawishika kurudi kuwatafuta, wakati hawamshauri vizuri. Anapenda sana kuongea. Sasa akimuona Nana yupo busy na mimi kama unavyonijua. Nina mambo mengi kila wakati, anaishia shopping na kushawishika kwenda club. Kwa wewe kuwa naye hapa nakumsikiliza ujinga wake huku ukimshauri, umefanyika msaada kwa wote. Haya, kwangu ndio kabisa.” Akambusu Tumboni.

“Umekuwa mke ambaye hata sikukutarajia Tunda. Tumefika tu hapa, nikaanza kukuacha nyumbani mimi nikahamisha akili kazini kuziba mapengo ya siku nilizokuwa Tanzania. Natoka asubuhi mpaka jioni sana. Lakini hujawahi kulalamika hata siku moja zaidi ya kunitia moyo!” Tunda akacheka kidogo.

“Nashukuru kwa hilo. Lakini ujue mambo yatabadilika. Zipo siku za jumamosi tutakuwepo wote nyumbani na nitakuwa najitahidi kuchukua likizo tusaidiane mtoto. Sitakuachia mwenyewe.” “Nashukuru kunifikiria. Lakini nataka ujue kabisa Net, tena bila unafiki. Niafadhali masaa machache ninayoyapata na wewe, kuliko mengi na wanaume wengine.” Net alifurahi sana. “Hilo limenifurahisha mno. Asante.” Wakaanza kupeana mabusu mengine, mchezo ukaendelea palepale sakafuni mpaka akamaliza roundi ya pili. Ndipo wakaenda kuoga na kutoka.

Tafrija  ya kumkaribisha Tunda kwenye jamii.

N

et alikuwa amemshika kiunoni wakati wanatoka. Wakamkuta Nana ni kama anawasubiria. “Are you okay?” Akamuuliza Tunda kwa wasiwasi kidogo. “She is not Nana! What do you think?” Hawakujua Maya alipotokea, akaingilia kwa kujibu yeye swali aliloulizwa Tunda, wote wakamgeukia yeye. Tunda akacheka. Kalikuwa kamependeza sana. “Si ni kweli Tunda, eeh?”  Kakachochea wakati akiwasogelea, Tunda akacheka tena. “Mimi nipo sawa Nana. Ila njaa inauma tu!” “Naona wageni wamefika, wapo wanatusubiri sisi. Twende ukawasalimie ndio tule.” “Na mimi nitapata muda wakuongea?” Maya akauliza. “Hapana Maya. Wewe utafanya fujo wakati Nana anataka amani.” Net akajibu badala ya bibi yao.

“Nini kinakupelekea kufikiria nitafanya fujo!?” Maya akajidai kumuuliza kaka yake kama anaye shangaa sana na kuona anasingiziwa. Wote wakamgeukia kama kumsuta. Akaanza kucheka yeye mwenyewe. “Watu wanabadilika jamani!” “Kama umebadilika anza kwa kufuta video uliyomchukua Vic.” Maya akacheka sana. “Hivi unajua nilikuwa nataka tu alie? Wala sijamchukua video. Siku hizi nimekua. Sina mambo ya kitoto.” Akapita katikati yao kuelekea ukumbini.

Nana, Net na Tunda wakamfuata huku wakicheka. “You look stunning, Maya!” kaka yake akamsifia kuwa amependeza sana. “So as Tunda, your wife.” Akajibu kwa kujivuna Maya. Wakacheka. Walipofika mlangoni kama aliyejua chakufanya, akampisha bibi yake apite. Akaanza kuingia bibi Cote pale ukumbini. Watu waliokuwa wamekaa sehemu iliyotayarishwa kwa tafrija, wakasimama na kuanza kupiga makofi wakati bibi Cote anaelekea sehemu maalumu ya kuzungumzia. 

Ni kama waliokuwa wanapeana nafasi ya kuingia hapo ukumbini. Si kwa kufuatana sana, lakini pia si kwa kuachana sana. Akafuata Maya, akaja Net na mkewe akiwa amemshika mkewe kwa mkono mmoja nyuma ya kiuno. Makofi yaliongezeka na picha zikaendelea kupigwa kwa wingi zaidi. Wote waliingia wakipunga mkono kwa wageni wao na tabasamu usoni.

Bado baadhi ya watu walikuwa nyuma ya ukumbi huo wamesimama wakiendelea na cocktail. Familia hiyo iliposimama pale mbele sehemu maalumu ya kuzungumza. Ukumbi mzima ukatulia kimya na kugeukia mbele kabisa kwenye jukwaa hilo fupi tu ambalo lilitengenezwa vizuri sana na Tunda mwenyewe alikuwepo.

Tunda aliweza kuona watu wamaana watupu humo ndani. Wazee kwa vijana walionekana na heshima zao. Akamsikia bibi Cote akitamka jina la Mayor, akisalimiana naye kwa sauti ya chini kidogo iliyoweza kusikika na kumpungia yeye mkono, kipekee. Akashangaa kuwa mpaka Mayor wa hapo ameweza kuhudhuria! Tunda akabaki akishangaa pale nyuma ya bibi Cote, na Net akiwa kama anampapasa nyuma ya mgongo, kumtuliza.

“Are you okay?” Net aliinama sikioni kwake akamuuliza kwa kunong’ona. Tunda akavuta pumzi kwa nguvu, akatingisha kichwa kwa wasiwasi. Net akacheka kidogo kama kumtuliza, akambusu kwenye kipanda uso kisha akamnong’oneza tena. “Usiogope.” “Okay.” Tunda akajibu na kujaribu kutulia.

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

Ukumbi mzima ulikuwa umetulia wakati bibi Cote alipoanza kuzungumza. Ni picha tu ndizo zilizokuwa zikipigwa hapo na video kuchukuliwa. Mapigo ya moyo ya Tunda yalikuwa yakienda kasi na kujaribu kukumbuka aliyofundishwa na Maya na bibi Cote wala sio Net. Net yeye alitaka asihangaike kwa lolote. Atulie tu. Ila bibi Cote alimuandaa vizuri ili asiende kushitukizwa pale mbele ya watu. Alimuandaa kwa maswali. Alimwambia kwa sababu ni mke wa Net, na ameolewa kwenye huo ukoo, watu wengi wangetamani kumfahamu na hata wengine kutaka kumuabisha tu kwa maswali ya kufedhehesha.

Alimwambia hatastaajabu kusikia maisha yake ya Tanzania yakitajwa pale. Watu wakimuuliza maswali ya maisha yake aliyoishi. Akamfariji na kumwambia, asionyeshe kushituka wala kufedheheka. Ayajibu kwa tahadhari. Anayetaka kumtia aibu kwa swali la aibu, alijibu kwa kulifanyia na yeye dhihaka.  Kwa hiyo Tunda alikuwa amesimama pale akiwa anajua kinachomkabili mbeleni, kwani aliambiwa na yeye atapata nafasi ya kusalimia na kuwakaribisha tena pale nyumbani kwao, yeye kama mama Cote.

Bibi Cote alimtaka aonyeshe sio mgeni na wala hana hofu. Aonyeshe amezoea na ni kama mwenye amri na ile sehemu. Alianza na Vic. Haikuwa bahati mbaya. Ni shule ya bibi Cote. Hata alipoambiwa na Maya vile alivyomjibu Vic, bibi Cote alifurahia sana. Akajikuta akisema, “That’s my girl!” Akashangilia kwa ushindi kuona Tunda ameweza kufanya kile alichomfundisha.

Hatuba kutoka kwa Bibi Cote

 kwa wageni wao.

M

ara baada ya kutulia, bibi Cote alianza kwa stori fupi iliyowafanya wageni wote wacheke  sana. Alianza hivi, “Kulikuwa na babu kizee chenye umri wa miaka karibia 90. Kilikwenda kwa daktari wake si kwa kuwa alikuwa mgonjwa, ila kutizama tu afya yake. Daktari akamuuliza, ‘vipi unaendeleaje?’ Yule kizee akajibu kwa kujivuna sana akionekana mwenye furaha na majigambo. ‘Nina mke wa miaka 18, na sasa hivi ni mjamzito. Unafikiri nitakuwa ninaendeleaje!?’

Bibi Cote akaendelea. “Yule daktari akamwambia, ‘Nina habari moja nataka kukwambia.’ Kizee kikajiweka sawa kusikiliza. ‘Kulikuwa na muwindaji mmoja. Siku moja wakati anakwenda kuwinda, badala yakuchukua risasi, akabeba mwamvuli. Alipofika porini, akatokewa na simba. Akafungua mwamvuli wake kwa haraka sana, akajifunika. Chakushangaza, akaona yule simba ameanguka mbele yake akiwa ameshakufa. Unafikiri nini?’ Daktari akamuuliza yule Kizee.”

“Yule kizee kwa jazba kabisa, akamjibu, ‘Mjinga kabisa. Si atakuwa yule simba ameuwawa na mtu mwingine aliyekuwa na risasi! Mwamvuli hauwezi ukaua simba!’ Yule daktari akasema, ‘Na mimi nilifikiri hivyo hivyo tokea mara ya kwanza ukinisimulia habari yako.’  Bibi Cote akamalizia kichekesho chake. Wageni wote pale ndani wakaanza kucheka sana, ndipo bibi Cote alipoendelea na salamu kwa wageni wake bila hata kutoa ufafanuzi wa kile kichekesho cha mafumbo, lakini walionekana wengi kuelewa.

Kuna ambao aliwatambua kwa kuwataja kabisa majina na vyeo vyao. Kama huyo Mayor. Kisha wanapunga mkono kila wakitajwa na bibi huyo na watu kupiga makofi. Sio makofi ya fujo, kwa ustarabu tu. Kisha akawashukuru wageni wote kwa kufika kwao, ndipo akaeleza lengo kubwa la kuwaita pale.

“Najua kilikuwa ni kitendawili kwa watu wengi sana. Si wa nje tu, hata sisi watu wa familia. Cote alifariki akiwa na shauku ya kuiona siku ya leo. Ambapo tutapata jibu la fumbo kubwa la nani mke wa Net.” Watu wakapiga makofi. Picha zikazidi kupigwa. “Sasa sisi tuliokuwepo hapa, Mungu ametupa neema kubwa yakushuhudia kitendawili hiki kikijibiwa. Leo kwa heshima kubwa sana mbele za Mungu na kwenu, napenda kuchukua nafasi hii kuwatambulisha kwenu Mama Cote, mke wa Nathaniel, mwenyewe.” Watu wakapiga sana makofi, Tunda akapunga mkono tu na tabasamu zuri usoni. Asiamini kama ile heshima kubwa vile anapewa yeye!

“Wamepitia mengi sana mpaka kuwaona wawili hawa wamesimama hapa mbele yenu. Tena wakiwa wameshakuwa na jukumu la uzazi.” Watu wakapiga tena makofi kidogo tu, wakatulia, bibi Cote akaendelea.  “Nina uhakika ni kule tu ambako Mungu alimpitisha Tunda, ndio maana leo ameweza kusimama hapa pembeni ya Net.” Bibi Cote akaongeza na kuendelea.

“Net alipohamia kuishi nchini Tanzania akisema anakwenda kutafuta ‘true Love’, kwa kuwa nilikuwa na historia ya baadhi ya watu wa kule na niliwafahamu, binafsi niliingiwa na hofu. Najua moyo wa Net, nikajua mwisho wake atakuja kuumizwa tu. Anayo mengi yakusimulia, lakini nakumbuka hofu yangu. Nikazungumza na Cote akiwa bado hajazidiwa sana. Akaniambia anamwamini Net. Anaamini vile alivyomkuza na kile alichomjengea ndani yake. Akaniambia nisiwe na wasiwasi, atakuwa sawa tu.” Watu wakapiga makofi.

“Ni miaka zaidi ya 4 sasa hivi imepita, kabla ya kifo cha babu yake, Net akarudi na jina Tunda tu. Lakini ikawa ni Tunda! Tunda! Na hapakuwa na habari zake zaidi. Alitafutwa Tunda, maana alimuona tu, akampenda, ila hakuwa amemwambia au wamepata muda wa kuzungumza. Net alishindwa kabisa kutulia. Nikapatwa na wasiwasi juu ya huyo Tunda ambaye kwanza hatukuwa tukimfahamu.” Bibi Cote akaendelea.

“Nikiwa namwamini Cote, na vile ninavyomfahamu Net, Tunda nilimuona mara ya kwanza akiwa anachumbiwa na Net, kanisani. Kwamba nilitoa baraka zangu kwa Tunda ambaye sikuwa nikimfahamu kabisa ila kukubali maamuzi ya Net. Na kile alichoniambia Cote kuwa, yule atakayeletwa na Net, ndiye anayestahili kuwa mama Cote.” Watu wakapiga makofi ya kushangilia.

“Na kweli, nilimkubali Tunda kwa kile alichokisema Net, kabla na baada ya kumchumbia. Nilipata habari nyingi sana juu ya Tunda. Binafsi nilitishika, lakini vile alivyokuwa Net, jinsi alivyomtizama Tunda na kumshika, ikaniongezea shauku ya kutaka kumfahamu huyo Tunda ambaye Net anamuona tofauti na wengine!” Watu wakacheka kidogo.

“Net aliniandalia kikao na Tunda, nikapata naye muda mfupi sana ambao naamini kwa vile mnavyonifahamu mimi.” Tunda akashangaa ukumbi mzima unacheka. “Come on people! Cut me a slake!” Bibi Cote akalalamika na wageni wakazidi kucheka. Na yeye akacheka na kuinama huku akicheka zaidi. “Anyway, wengi mnanijua huwa siwezi kufumbia macho ujinga. Kitu kama ni cheusi, nitasema ni cheusi sio kimefifia rangi.” Watu wakazidi kucheka. “Huyo ndio mimi. Hata mimi wakati mwingine natamani ingekuwa tofauti lakini imeshindikana kabisa.” Watu wakazidi kucheka.

Anyways!” Akataka watulie ili aendelee. “Nilipozungumza tu na Tunda, kwa kumuhoji swali dogo tu, nikasema halleluja!” Bibi Cote akapiga makofi ya shangwe pale pale mbele ya watu. “Nikasema Mungu amekubali kunipumzisha.” Watu wakapiga makofi ya shangwe zaidi. “Tunda amekuwa puzzle iliyofit kwa kila mtu kwenye familia yetu.” Maya akaanza kupiga makofi na kushangilia, mpaka Tunda akacheka. “Kweli.” Akadakia Maya pale pale akiwa hana hata kipaza sauti. Bibi yake akacheka huku akimtizama.

Akampisha kidogo, Maya akasogelea kipaza sauti. “Nimepata dada, rafiki wakunishauri bila wivu. By the way, ananisikiliza bila kuchoka sio kama Net.” Maya akamalizia hivyo na kujivuta pembeni kama kumpisha bibi yake, nakufanya watu wote wacheke. Net akatingisha kichwa huku anacheka taratibu. Tunda akaendelea kucheka. “Yaani Maya! Umeshindwa kabisa kunyamaza?” Tunda akamvuta kidogo. “Si uliwasikia walininyima kuongea?” Pale mbele wote wakacheka. Bibi Cote, Net, Tunda na Maya mwenyewe.

Wakacheka kidogo wakatulia. Bibi Cote akaendelea. “Amekuwa rafiki wa karibu wa Gino, Emily na Carter.” Tunda akashangaa Carter, Emily na Gino wanapiga makofi mwisho kabisa kwenye kona. Hata hakuwa amewaona. Akacheka Tunda huku akiwatizama. Wageni wengine wakaongeza kupiga makofi.

“Anawajali na kuwaheshimu kama watu wa muhimu sana kwake. Na hayo nayasikia kutoka kwao wenyewe. Ms Emily alikuwa akisema, wanajisikia vizuri akiwa nao. Amejawa heshima kwao, na anawapenda. Tofauti ambavyo walitarajia kutoka kwa mke wa Net!”  Watu wakapiga makofi.

“Kwangu Tunda amekuwa ni mtoto wa kike ambaye nilikuwa nikimtafuta kwa muda mrefu sana. Ameshindwa kabisa kuniita Ms Cote kama wengine. Ananiita Nana, kitu ambacho sikumwambia Tunda mwenyewe, ila kinanifurahisha sana.” Akamgeukia Tunda, wakacheka. Net akambusu mkewe. “Nafikiri imechukua muda mfupi sana kunizoea na kunipenda, pamoja na kunijali. Ananisikiliza, na anafurahia kuwa na mimi. Hilo sio la kufundishwa, au kujitahidi, unaweza kuliona usoni mwake.” Watu wakapiga makofi.

“Akinisikia tu nimetoka kazini. Maana siku hizi huwa nawahi kutoka kazini kabla ya mume wake. Popote nilipo, atanifuata kutaka kujua kama nipo sawa. Siku yangu ilikuwaje! Ilimradi awe tu karibu na mimi. Amevunja ule ukuta wa ukwe, amejifanya mtoto kwangu. Najisikia vizuri.” Watu wakapiga tena makofi. “Ni miezi miwili imefika tokea awepo hapa. Mumewe amekuwa na kazi nyingi mpaka akanitia wasiwasi, ikabidi kuzungumza na Net. Net akaniambia nisiwe na wasiwasi, Tunda mwenyewe anamuhurumia kwa majukumu yake, anaelewa na anamtia moyo kwa anachokifanya.” Watu wakapiga makofi zaidi.

“Najua Net anayo mengi zaidi, lakini kwa machache haya, namshukuru sana Mungu kutuletea Tunda kwenye maisha yetu. Nyumba imekuwa na amani na utulivu kama yeye mwenyewe Tunda alivyo. Mtulivu sana. Naomba tutengeneze mazingira yakumfanya Tunda ajisikie nyumani. Na aweze kuishi hapa vizuri na sisi. Kwa sababu ndiye mama Cote, na wala hatapokelewa mama Cote mwingine.” Maya akaanza kushangilia yeye mwenyewe, ikabidi tu na wageni waalikwa wacheke na kupiga makofi. 

Maya Naye atoa yake kwa Ufupi.

B

ibi yake akamkaribisha Net. Net akasogea huku akicheka na kumtizama Maya. “Unataka kuongea nini Maya?” Net akamuuliza huku akicheka. Maya akasogea kwa haraka kwenye kipaza sauti bila yakumjibu kaka yake kama asiyetaka abadili mawazo. Net akampisha huku wakicheka. “Mimi nataka kusema nampenda sana Tunda. She is sweet, nice, loving, calm na anapenda wengine pia wapate na wafanikiwe. Kikubwa..” Watu walishaanza kupiga makofi.

“Kingine kikubwa.” Maya akataka watulie amalize kwa haraka kabla kaka yake hajachukua kipaza sauti. “Napenda, japo sijamwambia yeye mwenyewe Tunda. Ila napenda jinsi anavyo mjali na kumuhudumia Net. Utapenda kumuona vile anavyomuhudumia Net, anapotoka kazini!” Watu wakapiga makofi.

“Net anakuwa wakwanza kwenda kazini na mara zote huwa tunamwacha ofisini. Tunda atahakikisha asubuhi anakuwa na mumewe mezani. Na usiku akisikia tu mume wake amerudi, hata kama tupo sehemu na Nana, ananyanyuka kwenda kumpokea.  Atazungumza naye kidogo. Atampa hata juisi. Sio kwa kumuagiza Ms. Emily ndio afanye! No. Anakwenda yeye mwenyewe kuchukua, anamletea. Ndipo Net anaendelea na kitu kingine na vitu vidogo vidogo vya Net, na chakula cha usiku pia, anaandaa meza yeye mwenyewe, sio wafanyakazi.” Watu wakapiga makofi.

“Kwangu au kwetu ni ngeni. Hatukutegemea kuona hivyo kwa mke wa Net. Tulijua tutaletewa Diva. Lakini Tunda amekuwa tofauti! Hataki kutumikiwa. Na ukimfanyia kitu chochote hata kidogo tu, hata kina Ms Emily wanasema. Hatakuonyesha kama unastahili kumtumikia. Amejawa shukurani sana.” Wakapiga tena makofi.

“Anampenda Net kama yeye Net, sio kama Nathaniel Cote.” Wakapiga tena makofi.  “Binafsi kwa muda mfupi nimeishi naye hapa, amenibadilisha sana jinsi ninavyoishi na kujihudumia. Nimependa jinsi anavyofanya mambo yake. Na mimi namuiga bila kumwambia.” Watu wakapiga makofi nakucheka.  Tunda akacheka. “Yaani Maya!” Tunda akasikika taratibu. “Kingine, amehusika kwenye kunirudisha shule. Alizungumza na mimi kipindi hicho hata kabla Net hajamchumbia, mpaka nikaona umuhimu wa kujikana kwa miaka mitatu ili kuweza kupata shahada hii ya masoko.” Watu wakapiga makofi.

“Na amenitia moyo na shauku yakujifunza lugha zaidi kama Net. Kwa ajili yake nimeanza kujifunza kifaransa. Nina zaidi ya mwezi sasa. Najifunza na anakubali kunisikiliza ninapojifunza kuongea.” Net akatingisha kichwa.  “I love her so much. Amekuwa dada ambaye na mimi kama Nana alivyosema, nilimtamani kwa muda mrefu. Lakini Net ametuletea. Asante Net.” Akamkumbatia kaka yake na kumbusu. Akaenda kumbusu na Tunda. “Na mimi nakupenda Maya.” Maya akacheka kwa deko. “Najua sana kama unanipenda.” Akajibu kwa kujivuna kidogo huku akisogea pembeni namkufanya mpaka bibi yao acheke.

Hatuba ya Nathaniel Cote

N

et akarudi kwenye kipaza sauti. “Nana amezungumza mengi na muhimu sana. Ni kweli haikuwa rahisi kusimama hapa na Tunda kama inavyoonekana. Tumepitia mengi magumu sana. Nimshukuru Mungu kwa kutupigania kwa kibinafsi mimi na Tunda.” Watu wakapiga makofi. “Shukurani za kipekee kwa my loving, my sweetheart, Nana.” Net akarudi nyuma kidogo akambusu bibi yake na kumkumbatia kwa muda. Wakamuona anafuta machozi. Akarudi na kutulia kidogo. Wakamuona akiendelea kufuta machozi. Tunda akasogea pale alipokuwa amesimama akamshika mkono kama kumtuliza. Net akamwangalia, Tunda akampa tabasamu. “Thanks.” Akashukuru na kuendelea.

“Kwa mzazi mwingine yeyote, ninauhakika. Kuletewa mtu kama Tunda kwenye ukoo, ingesumbua sana. Kungekuwa na maswali mengi. Pengine kunipinga kama wengi wa watu walivyonichafua mitandaoni juu ya uwamuzi wa mimi kuwa na Tunda.” Kimya. “Lakini nilipomfuata Nana, na kumwambia nimefikia maamuzi ya kumuoa Tunda, Nana aliahirisha mkutano uliokuwa ufanyike Germany, akamtuma mwakilishi wake, akaandaa safari kurudi na mimi nchini Tanzania, kuchumbia.” Watu wakapiga makofi.

“Nana alikwenda Tanzania, akitumia ndege yake, ulinzi ambao wote tunajua uligharimu sana, ili tu kuwa na mimi kwa mwanamke ambaye alishamchunguza, akaambiwa habari zake, bila swali lolote ila kunikabidhi pete yake ya thamani sana aliyokuwa amevalishwa na Papa. Akitaka nikamvalishe Tunda.” Watu wakapiga makofi yakushangilia, bibi Cote alikuwa akitingisha kichwa kukubali.

“Hakuishia hapo. Hata kipindi nilipokuwa huku, na mke wangu alipokuwa amefungwa. Japokuwa watu walimkashifu Nana kwa wazi kabisa. Kumwandika vibaya sana magazetini na mitandaoni kuwa anaua ukoo wa Cote, bado Nana alisimama na sisi. Akinitia moyo kuwa ni majaribu yetu mimi na Tunda, Mungu atatusaidia tu. Na kweli, alisimama na sisi bila kukata tamaa wala kunung’unika.” Tunda hakuwa akijua, akajikuta anamwangalia yule bibi na machozi yakimtoka. Hakujua kama walimchafua hivyo kwa ajili yake.

“Kutoka ndani ya moyo wangu, namshukuru sana Nana kwa kuniamini. Amesimama na mimi pamoja na Tunda, kuhakikisha, leo naweza kulala kitanda kimoja na mke wangu! Haikuwa rahisi hata kidogo. Asante nana.” Watu wakashangilia. Tunda naye akamshukuru bibi Cote.

“Pia napenda kumshukuru sana Maya kwa upendo wake kwa mke wangu. Ni kweli anampenda mke wangu bila unafiki. Na ninauhakika yeye ndio amefanya maisha ya Tunda pia kuwa rahisi sana hapa ndani. Asante Maya.” Akamsogelea na kumkumbatia, akambusu. “You are welcome.” Akajibu Maya.

“Kwa Gino, Ms. Emily ambaye kwetu ni kama Nana au mama, na kwa Carter. Asanteni sana kwa upendo wenu kwa mke wangu. Gino asante kwa chakula kizuri kwa Tunda.” Gino akapunga mkono, watu wakapiga makofi. “Thanks Man!” Akaongeza Net na kuendelea.  “Ms. Emily, asante kwa kutengeneza mazingira rafiki kwa mke wangu. By the way she likes you.” Ms. Emily akacheka wakati akipunga mkono. “Kwa Carter! Ambaye nimekuwa akiniona. Amekuwa kama Papa wa pili kwangu. Asante kwa kumwangalia mke wangu na kuhakikisha yupo salama na furaha wakati wote.” Tunda akacheka na Carter akawakonyeza.

“Wakati namuomba Tunda aje kuishi na mimi huku, hakuwa akimjua Nathaniel Cote ambaye nyinyi mnamfahamu nyinyi. Alikubali kuja huku akiwa anatamani tuishi naye Tanzania. Lakini aliniambia hivi, ‘natamani tuishi Tanzania Net. Ndio na mimi kwa mara ya kwanza nafanikiwa kimaisha. Nimeweza kutengeneza pesa kwa jasho langu na familia yangu inanitegemea. Lakini najua, sitakuwa na amani kuishi mbali na wewe’.” Watu wakashangilia kwa kupiga makofi kwa muda mrefu kidogo.

“Wakati huo Tunda anazungumza na Net, wa kitanzania. Ninayeishi maisha ya kawaida kabisa. Nilikataa watu wasimwambie Tunda ukweli wa Nathaniel huyu aliyesimama hapa mbele yenu. Ila mimi kama mimi. Tunda alinichagua mimi kama Net, kitu nilichokuwa nikikitamani sana.” Watu wakapiga makofi tena. “Tulipokuwa tukijiandaa kuja huku, akiwa bado ananifahamu kama Net niliyetaka amfahamu kwa wakati ule, aliniomba kuwa, ni afadhali akose kila kitu, lakini asiwahi kunikosa mimi kama Net.” Watu walishangilia sana.

“Haikuwa kama hivyo. Nilifika huku na majukumu mengi mno. Nikaanza kujisuta moyoni, nakujiuliza nitafanyaje sasa na huyu mke aliyeniomba asinikose?” Watu wakacheka kidogo. “Ni rahisi kutoa udhuru siku ya kwanza na ya pili au hata juma la kwanza. Lakini sio mwezi mzima! Kutoka asubuhi kurudi wakati mwingine usiku! Jumatatu mpaka jumamosi ambapo bado hakuwa na nguvu!”

“Nikaanza kujisuta mwenyewe moyoni. Lakini Tunda ndio amegeuka kuwa faraja na kunitia moyo katika ninalofanya. Ametulia nyumbani akinisubiria kwa maandalizi ya kuniandalia yeye mwenyewe chakula mezani, kama alivyosema Maya.” Watu wakapiga tena makofi. “Tena akiwa amejawa moyo wakunihurumia na majukumu mazito! Amechukua majukumu ya Gino ya usiku yakunisubiria mimi ili aniandalie chakula. Na asubuhi kama napata kifungua kinywa, lazima ataamka awe na mimi mezani. Atakula kitu kidogo tu, angalau kuwa na mimi pale mezani.” Watu wakapiga tena makofi.

“Ameniambia kitu ambacho kimeninyanyua na kunifanya nisijutie kumsubiri. Kwa hakika, mimi mwenyewe najua Tunda ni mke ambaye Mungu amenipa zawadi ambayo najua kwa wengi hawawezi kukubaliana na mimi. Ni Tunda pekee ndiye anayeweza kuvaa viatu vya mke wa Net.” Wakapiga makofi sana.

“Sio kwa miezi miwili aliyoishi hapa ndani tu. Ni kwa miaka yote niliyomfahamu Tunda. Nafikiri wakati Mungu alipokuwa akimtengeneza Tunda, alikuwa akinifikiria mimi.” Tunda akainama. “Kitu gani kingine alikwambia?” Mayor alitupia swali nakuamsha kicheko kwa wote. Net alikuwa ameinama kumbusu Tunda kichwani akacheka.

“Wakati namuomba msamaha kwa kutokuwepo hapa nyumbani na yeye kwa muda mrefu, tena sio akiwa amelala tu. Akizunguka kufanya hili na lile akisaidia mambo ya hapa ndani. Nikaanza kuweka ahadi zakubadilika. Nakumbuka tulikuwa tumejilaza kwenye closet yake.” Tunda akamfinya. Net akaruka. Watu wakazidi kucheka.

“Ooooh Net!” Mmoja akashangaa ile kubwa ya kukejeli. Mwingine akadakia “Man! Tulikufundisha nini juu ya kuingia kwenye vyumba vya kuvaa wasichana?” Rafiki zake ndio waliamsha kicheko zaidi pale ukumbini. Tunda aliweza kuwatambua kuwa ni wale waliofika Tanzania kushuhudia akimchumbia. Watu wakazidi kucheka. Net alicheka mpaka akageuka nyuma. “Aibu zako.” Tunda akamnong’oneza.

Anyways.” Net akageuka akitaka kuendelea. Watu wakatulia huku wakicheka taratibu. “Tunda alisema ni heri muda mfupi anaopata na mimi, kuliko muda mrefu ambao angepata na mtu mwingine.” Watu walishangilia sana wakipiga makofi mpaka Tunda mwenyewe akashangaa. Hakutegemea kumsikia Net anaongelea hilo hapo.

“Kingine, aliniambia Tunda.” Watu wakatulia na kurudi kukaa. Tunda mwenyewe akapatwa hamu ya kujua. Akamtizama mumewe. “Kimebaki akilini mwangu na kunitia moyo. Aliniambia hivi, nitamnukuu.” Akamgeukia Tunda, wakacheka.

“Aliniambia hivi, tena akiwa ametulia kama kawaida yake nikiwa nimechelewa kutoka kazini. Najisuta. Akijaribu kunituliza. Akasema, ‘Sijui maisha yatatupeleka wapi, lakini nimekusudia kufanya kila niwezalo ili kusimama, kukusaidia na kukuunga mkono katika kila hatua ya maisha yetu, ili kuwa mwanaume ambaye hata babu yako alikukusudia uwe.’ Huyo ndiye Tunda, niliyekwenda mbali kumtafuta awe mke wangu.” Watu walizidi kupiga makofi mpaka wakasimama. Na Net naye akawapa nafasi yakutosha kupiga makofi. Maana hata safari hii bibi yake alipiga sana makofi.

“Namuomba Mungu atusaidie. Kwa kuwa sisi bado ni vijana. Tunaanzisha familia huku tukiwa tuna majukumu mengi! Basi mzidi kutuombea, ili Mungu atujalie kuwa watu aliotukusudia kwenye jamii yetu.” Hapo napo watu wakapiga makofi.

“Sitawasahau Troy na Lean kwa kuacha shuguli zenu zote kuja Tanzania kunisindikiza kwenye kumchumbia Tunda. Kwangu inamaana kubwa sana. Mlisimama na mimi tokea tupo watoto mpaka Tanzania! Asanteni sana.” Watu wakawapigia makofi Lean na Troy, marafiki hao watatu, waliotambulika kwa muda mrefu sana.

“Lakini bado hatujamaliza safari.” Net akaongeza na kumgeukia bibi yake. Akasogea pembeni kama anayempisha pale kwenye kipaza sauti. Bibi Cote akasogea na tabasamu kama mwenye habari njema.  “Baada ya jumamosi ijayo. Ile nyingine, kabla ya Tunda kujajifungua, tutakuwa na harusi ya kanisani ya Tunda na Net.” Bibi Cote akatangaza, watu wakashangilia sana.

 “Kabla ya kuzaliwa kwa ‘Cote Junior Cote, the fifth’.” Bibi Cote akaongeza na kuamsha shangwe zaidi. Watu wakazidi kushangilia kwa kupiga makofi kiustarabu huku miluzi ya kina Troy pia ikisikika. “It’s a boy!”  Rasmi, haikuwa bahati mbaya, bibi Cote akawa ametangaza jinsia na jina la mtoto anayetarajiwa. Picha zilizidi kupigwa kwa Tunda. Net akambusu mkewe, na kumpapasa tumbo kidogo. Bibi Cote akarudi nyuma na kumpisha tena Net.

          Akarudi kwenye kipaza sauti. “Yes. It’s a boy! Mtoto wetu wa kwanza wa kiume Mungu aliyetuzawadia. Sasa kabla hajaja na kumganga mke wangu, na kuchukua nafasi yangu, nataka nikamlipe fungate aliyokuwa akinidai.” Watu walizidi kushangilia. “Tunajua unachoenda kufanya Net.” Rafiki zake walipayuka na kuamsha vicheko, Net aliinama akicheka huku akitingisha kichwa. Watu wakazidi kucheka.

“Kwa hiyo Troy na Lean, kazi haijaisha.” Akawatuliza Net kwa kuendelea kuongea. “Nitahitaji msimame na mimi mpaka mkinifikisha mbele za Mungu, siku hiyo ya harusi yetu ya pili, ndio mtabakiwa na kazi ya kusimama na mimi kuhakikisha nakuwa mume mzuri kwa Tunda, kama mlivyonisaidia na kusimama na mimi wakati wote.” “Tupo pamoja Net.” Troy na Lean wakajibu na watu wakapiga tena makofi.

“Asanteni sana.” Net akawashukuru rafiki zake. Akamgeukia mkewe. “Karibu Tunda, hawa ndio watu wa Norfolks. Marafiki, majirani na wanajumuia. Jisikie upo nyumbani.” Wakampigia makofi wakati Net anatoka kwenye kipaza sauti na kumpisha Tunda.

Tunda Mbele ya wakuu!

T

unda alisogea kwenye kipaza sauti, Maya akaanza kushangilia. Watu wakaanza kucheka na kupiga makofi. “Maya!” Tunda akaongea kama anamsikitikia. “By the way, analala na kuoga chumbani kwetu akijua Net hayupo.” Tunda aliongea hivyo nakufanya watu wacheke sana. “Mimi nilijua ni siri yetu! Come on now!” Maya alilalamika kwa sauti ya chini iliyosikika na kufanya watu wazidi kucheka. “Huwezi kutosheka na Tunda. Sio kosa langu. Muulizeni Net.” Maya akaongeza nakufanya watu wazidi kucheka, angalau hofu ikapungua kwa Tunda.

Palipotulia, Tunda akataka kuanza, Net akarudi pale mbele kama aliyesahau kitu na kutaka kuzungumza. Tunda akampisha. “Samahanini kidogo. Kwa leo sitaruhusu maswali kwa Tunda. Naomba tumpe muda. Naamini mengine yatajijibu kutokana na tutakavyoishi. Naomba leo iwe kumkaribisha tu. Asanteni sana.” Japokuwa hakuzungumza na bibi yake, lakini hata bibi yake alipiga makofi kuashiria ameafikiana na hilo, kisha akampisha Tunda.

“Nawashukuruni wote kwa kufika hapa. Kwangu sichukulii kitu cha kawaida. Mngeweza kutoa udhuru tu, kwa sababu mmealikwa hapa  kwa ajili yangu mimi ambaye ni mgeni kabisa kwenu. Lakini kuwaona hapa, imeninyenyekeza na kuona upendo wenu kwetu. Asanteni sana.” Wakapiga makofi sana. “We love you Tunda!” Troy akapayuka katikati ya kundi, Net akacheka na wengine. “Asante Troy.” Tunda akashukuru akimtambua moja kwa moja kama kumuonyesha anamkumbuka huku akicheka.

“Mimi sitaongea mengi sana juu yangu, ila shukurani juu ya yale Mungu amenitendea kwenye maisha yangu. Hakuna hata moja ambalo mnaliona na kulisikia kutoka kwa wote waliozungumza ambalo nilidhani ninastahili.” Tunda akatulia. “Nilipokuwa jela, sikutaka kukutana kabisa na Net. Alikuwa akija mara kwa mara akitaka kuniona. Lakini nilishindwa kabisa kumuona.” “Why?” Mmoja ambaye alionekana kama mwandishi wa habari, akauliza akitaka kujua ni kwa nini!

“Nilisema hakuna maswali.” Net akakataa kwa ukali kidogo. Tunda akamgeukia. “It’s okay babe.” Tunda akamwambia kwa upole tu. “Una uhakika?” Net akataka uhakika, asijue mkewe amefundwa vizuri sana na bibi yake pamoja na Maya.  Hapo alipokuwa Tunda japo ilikuwa mara yake ya kwanza tokea kuzaliwa kuzungumza mbele ya umati mkubwa vile, tena uliojaa watu wa maana watupu! Wazungu wa Canada, lakini alikuwa anajua vipi azungumze na asimamaje pale mbele za watu.

Tunda akatingisha kichwa kumkubalia mumewe na tabasamu la kumuonyesha yupo sawa kabisa. Net akaridhia kuwa ajibu hilo swali. Tunda akarudi kwenye kipaza sauti. Akaanza taratibu tu. “Cha kwanza nilikuwa nimekusudia kulipa gharama ya maamuzi mabaya niliyokuwa nimechukua kabla yakumpa Yesu maisha yangu. Hiyo nilikusudia kwa maneno na vitendo. Hata nilipokuwa mahakamani, mshitaki wangu alipojaribu kutengeneza kisa vizuri, niliomba kumsaidia. Niliona anaongea ambacho na yeye anasikia kama wengi wenu. Nilikiri kosa langu na kukubali adhabu yangu.” Watu wakapiga makofi kidogo, Tunda akawakata ili aendelee kuzungumza.

“Nilipokuwa jela, nilijigundua ni mjamzito. Nikaanza kuugua sana. Sikutaka Net anione nikiwa kwenye ile hali. Net alimtaka huyu mtoto hata kabla mimba yake haijatungwa. Nakumbuka siku ananiambia tumtafute  huyu mtoto, Net alinimbia kwa kumtaja jina lake kamili ‘Cote Junior Cote’. Mpaka akaniogopesha!” Watu wakacheka.

“Seriously, who does that!?” Tunda akauliza na kufanya watu wacheke zaidi. “Mimi najua huwa watu wanatafuta mtoto. Mimba ikishatungwa na pengine kujulikana jinsia, ndipo wazazi wanampa jina. Lakini sivyo alivyofanya Net. Alijua anamtaka nani. Akamuomba Cote kwa Mungu.” Tunda akacheka kidogo. “Natamani ningerikodi yale maombi ya Net usiku ule wakati akimuomba Cote kwa Mungu. Yaani aliomba kama vile alikuwa akimuona Cote yupo sehemu, ndipo akamsihi Mungu amlete kwetu, akimwambia Mungu sisi tupo tayari kumpokea Cote. Yaani kwa kumtaja kwa jina, kuwa ndiye anayemtaka aje kwanza. Hakika nilifungua macho wakati anaomba nikamtiza.” Watu wakazidi kucheka.

“Na baada ya hayo maombi, hakutaka kufungua mlango wa mashaka hata kwangu mimi mwenyewe. Akabakia na mazungumzo ya jinsi tutakavyompokea na kumlea Cote, kama kaka ya wengine Mungu atakao tubariki baada ya Cote, tena akisema kama mimi nitataka wengine.” Watu wakapiga makofi huku wakicheka.

“Sasa nilijua kama akijua nipo jela na mtoto wake, wote. Yaani mimi na yeye Net, tungeshindwa kufanya kazi. Nilijua angechanganyikiwa asijue chakufanya na angenikatisha tamaa yakuweza kutumikia adhabu yangu.” Watu wakapiga makofi. “Hata alipotuma wakili wakuja kunitetea, pia nilikataa kumuona. Niliamini nimetubu kutoka moyoni, na Mungu alinisamehe dhambi zangu zote. Lakini siwezi kukwepa kulipa gharama ya makosa yangu. Nilijua lazima mimi mwenyewe nikubali kulipa.” Watu walishangilia sana mpaka wakasimama tena. Tunda akainama.

Walipotulia akaendelea. “Kingine, nilikuwa nikimpa muda Net ili afikirie zaidi ni nini anataka na kama kweli anajua mtu anayetaka kujihusisha naye. Nilijua ananijua sio kwa kusimuliwa au kusikia mitandaoni. Yeye ndiye mtu pekee anayenifahamu vizuri. Net ananijua kuliko mtu yeyote hapa duniani. Zaidi hata ya mama yangu mzazi. Lakini nilitaka apate muda wakufikiria bila kusongwa. Kumfikiria Tunda kama Tunda ambaye yupo kifungoni. Tena kwa kosa la fedheha! Nilitaka kumpa muda wakutosha bila kumshawishi kwa kuona nimebeba mtoto wake. Sikutaka anichague sababu nimebeba mtoto wake au kwa sababu nitakuwa mama wa mtoto wake! Hapana.” Watu walishangilia sana, wakasimama tena kama kuonyesha heshima kwa kile alicho zungumza.

Tunda akaendelea baada ya kutulia. “Tulikutana wote, mimi na Net, tunatafuta mapenzi ya kweli. Yeye akitaka mtu ampende kama yeye bila kujua historia yake ya maisha. Na mimi nilitaka mtu atakayenipenda kama mimi Tunda, akiwa anaijua historia yangu ya nyuma. Lakini bado anichague mimi kama Tunda.” Watu napo hapo wakapiga makofi.

“Kwa miezi 6. Kila mwezi Net alikuwa akija jela akitaka kuniona bila mafanikio. Hakuchoka wala kukata tamaa mpaka nilipotoka. Nilimkuta Net akinisubiri nje ya gereza.” Tunda akaina na kujifuta machozi. Watu wakapiga makofi. Net akamsogelea. Akampapasa mgongoni na kumbusu akatulia.

“Napo hapo pia sio kwamba nilimkimbilia! Hapana. Nilikimbilia hotelini kwenda kupumzika. Nilitoka nikiwa mgonjwa sana. Sikuwa na nguvu na yeyote na chochote. Nilikwenda hospitalini. Nikarudi hotelini kujiuguza. Sikuwa nikijua kama bado Net ananisubiri. Akiwa hajui nilipo, wala hatuna mawasiliano, Net alinisubiri mpaka tulipokutana tena.” Tunda akatulia kidogo kama anayefikiria kitu.

Kisha akaendelea. “Alichonishangaza mpaka leo. Kwa historia niliyokuwa nayo, halafu nikafungwa jela kwa kosa hilohilo, eti natoka jela nikiwa mjamzito. Nikampotea kwa majuma mawili nimejifungia asipopajua, bado Net aliamini mtoto ni wake bila hata mimi mwenyewe kumwambia kama ni mimba yake!”  Hapo Tunda akalia kidogo. Watu wakapiga makofi tena kwa muda mrefu kidogo kama kumpa nafasi atulie.

“Mazingira aliyonikuta kwa mara nyingine tena baada ya kumpotea nilipotoka jela, ilikuwa ni eneo nililokwenda kufanya kazi. Baada yakupona, nikaamua kurudi kutafuta kazi ili kuweza kumtunza mtoto. Sikujua kama Net atampokea mtoto au kama tutaendelea na mahusiano. Kwanza hata sikujua kama bado yupo nchini Tanzania ananitafuta mimi! Niliamka asubuhi sana kwenda kazini, kumbe yule aliyekuwa amenipa kazi alimtaarifu Net kuwa nimemuomba kazi na nitakuwa kazini muda huo.”

“Net alipofika tu, akaomba amsalimie mtoto. Nikiwa kwenye mshangao, akapiga magoti na kumsalimia mtoto. Akajitambulisha kwa mtoto kama yeye ndio baba yake na akamwambia mtoto kuwa anasikitika hawakuwa pamoja kwa muda wote huo, ila akamuahidi atafanya kila awezalo ili waweze kuwa wakipata muda wa pamoja!” Watu wakashangilia sana.

“Ile imani aliyokuwa nayo kwangu na kwa Mungu akiamini Mungu anaweza kumbadilisha mtu! Na jinsi anavyonipenda Net! Na kunithamini! Kwanza jinsi anavyonitizama tu, najua ananipenda.” Watu wakapiga makofi.

“Umeshawahi kwenda kwenye mgahawa mzuri sana! Ukiwa na njaa. Ukaagiza chakula ulichodhani unakihitaji na kitakuridhisha nafsi yako! Ukala, lakini bado ukahisi kuna kitu hakijakamilika? Sijui kama imeshawahi kuwatokea nyinyi?” Tunda akauliza na kuendelea. “Halafu ukiwa kwenye ile hali ya kutoridhika, anakuja muhudumu aliyekuwa akikuhudumia. Unamueleza kile unachopitia kwa wakati ule baada ya kula kile chakula alichokuletea pengine na kinywaji. Unaweka msisitizo kwake kuwa, japo alileta kitu sahihi, na pengine akakuhudumia vizuri tu, lakini kuna kitu hakija kamilika!” Tunda aliongea kwa hisia zote. Kila mtu alitulia kumsikiliza.

“Pengine muhudumu anaweza kukupa pendekezo lakumalizia na desert. Labda ya cake. Unaomba kuona menu za hizo cake. Unaangalia mwanzo mpaka mwisho. Unachagua velvet cake. Ukidhani itakidhi ile haja yako unayoisikia kwa wakati ule. Inaletwa.” Akatulia kidogo. Ukumbi mzima ulikuwa umetulia kabisa kumsikiliza huyo Tunda ambaye amevikwa heshima ambayo hakutarajia.

“Unapokula ile keki na kuifurahia. Sio kwamba uliiagiza kwa kutaja majina yote ya ingredients zilizochanganywa mpaka ikatokea ile keki! Mtakubaliana na mimi hapana. Nina uhakika hutamwambia muhudumu niletee sukari, iliyochanganywa na maziwa, mayai, vanila, butter na kadhalika.” Watu wakacheka sana.

“Hapana. Utaomba tu velvet cake. Ila mpishi aliyetengeneza ile keki, tokea mwanzo alijua achanganye nini mpaka kitokee kitu kizuri kitakachomfurahisha mlaji kitakachoitwa velvet cake. Ndivyo ilivyokuwa kwa Net, wakati Mungu ananikabidhi mume.” Watu wakashangilia sana.

Tunda akaendelea. “Amekuja na kila kitu ambacho Mungu anajua nahitaji. Wapo waliosema nimempendea pesa.” Watu wakacheka. “Najua ni wengi walisema, wanasema na kufikiri hivyo. Lakini Mungu alijua nahitaji pesa ndio maana akanipa Net. Sitaomba msamaha wala kujitetea kwa hilo.” Watu walicheka sana na kupiga makofi.

“Sitaona haya wala sitajivunga kuwa sijafurahia kukutana na Net huyu ambaye sikujua kama yuko hivi. Nilimwambia Nana, bila kumdanganya. Sijui kama anakumbuka?” Tunda akamgeukia. Nana akasogea. “Ngoja nimsaidie.” Watu wakacheka. Bibi Cote akaanza. “Aliniambia hivi, mara ya kwanza nazungumza naye, wakati nikiwakilisha malalamishi ya wengi, kuwa anampendea Net pesa. Nilimwambia anitajie pesa yoyote anayotaka nitamlipa, ili tu amuache Net kama anampendea Net pesa. Tunda akaniambia mengi lakini akiwa ametulia. Nitafupisha.”

“Aliniambia, ‘Nimeteseka sana na maisha kufika hapa nilipo. Sitakudanganya kukwambia eti nipo tayari kuolewa na mwanaume masikini. Hapana. Isipokuwa Net.’” Watu wakashangilia sana. “Subirini kidogo. Aliendelea akasema ni kwa Net tu, ndiye yupo tayari kumuweka ndani na kumlisha hata kumtunza kama hana pesa. Lakini sio mwanaume mwingine yeyote yule. Na aliniambia wazi ni kwa ule umbali ambao Net amefika naye.” Watu walipiga makofi kwa kushangilia mpaka wakasimama tena huku wakicheka.

Tunda naye alikuwa akicheka vile bibi Cote alivyokuwa akimnukuu kwa kumuigilizia mpaka sauti. “Nana!” Tunda akaendelea kucheka huku akimtizama bibi Cote, asiamini vile alivyompatia sauti yake. Mpaka Net alikuwa akicheka huku wakimtizama bibi Cote, hata yeye asiamini kama ni yeye! Akamaliza kumwigiza Tunda, akaondoka pale mbele, Tunda akarudi huku akicheka. “Siamini Nana!” Bibi Cote na yeye akaanza kucheka.

Anyway, sasa kuja kuona Net yule ndiye huyu! Kwa kweli ninafuraha na wala sitajivunga au kujitetea kwa hilo.” Watu wakaanza kucheka tena. “Nampenda mume wangu. Nimeamua kusimama na yeye kwa kila hatua ya maisha yetu. Jua litoke, mvua inyeshe, nitakuwa na Net kama Net wangu niliyekabidhiwa na Mungu wangu kwa upendo mkubwa sana.” Hapo watu wengi walishangilia sana.

Bibi Cote mwenyewe hakutegemea. Akamsogelea na kumbusu. “Thank you, baby girl.” Bibi Cote akambusu tena. Na Net mwenyewe ikamgusa sana. “Asante Tunda. Nakushukuru.” Net akajikuta akiongea kwa kiswahi pale pale mbele ya watu. Akamkumbatia.  “Nakupenda Net.” “Na mimi nakupenda.” Wakaanza kupeana mabusu palepale, watu wakishangilia.

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

Kwa Tunda kutoa ahadi nzito vile mbele ya umati kwa familia hiyo iliyokuwa ikiwindwa na wao wakihofia kupata mkwe ambaye ataingia pale kwa ajili ya kujinufaisha tu! Aolewe na kuomba talaka ili apewe nusu ya mali iliyotafutwa kwa jasho sana na kina Cote. Ilimgusa sana kila mtu kwenye familia hiyo.

Kuona Tunda ametangaza mpaka kifo! Tena huyo bibi alimuonya Tunda kwa kumsisitizia kuwa, asije akazungumza jambo lolote siku hiyo mbele ya watu kwa kuwa hata baada yamiaka 20 anaweza kuja kukutana na maneno yake. Alimwambia hiyo tafrija itarushwa hewani live. Alimwambia macho ya wengi ulimwenguni, wenye vyeo vyao na mashabiki tu, watakuwa wakifuatilia hiyo tafrija kuanzia mwanzo mpaka mwisho.

Aliweka msisitizo kwa Tunda kuwa ni tafrija ambayo itakuwepo kwenye vyombo vya habari vingi sana ndani na nje ya nchini. Zaidi alimtahadharisha kwa kumwambia kila litakalozungumzwa hapo, litajadiliwa kwa muda mrefu sana mitandaoni, magazetini na hata maredioni. Kwa hiyo akamwambia kila neno hapo ni kumbu kumbu ambayo itatunzwa hata kuja kuonyeshwa mkwe wa huyo mtoto aliyembeba hapo tumboni. Kwa hiyo asiropoke, wala kuongea neno ambalo hamaanishi.

Kwa kitendo cha kutamka hapo hadharani, bibi Cote alijua ni ahadi ya ukweli. Si kwa mumewe tu. Hata kwake na kwa familia nzima. Kuwa yupo pale na wao, na hana mpango wa kuondoka. Iliwagusa sana.

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

“Mwisho kabisa.” Watu wakatulia na kuendelea kumsikiliza. “Nilipokuwa nakuja huku, baba yangu alikuwa na wasiwasi sana na wenyeji wangu. Kama watanipokea kwa jinsi nilivyo. Lakini nimejikuta nimepata familia ambayo hata sikuwahi kuwa nayo. Sijawahi kuishi kwenye familia kama hii.” Wakapiga makofi wakijua kitakacho fuata ni sifa kwa familia hiyo maana ulikuwa usiku wakuongea mazuri tu. “Na ninaposema familia ni kila mmoja niliyemkuta ndani ya hii nyumba. Wamegusa maisha yangu kipekee sana. Naomba nianze kwa kumshukuru Gino, ambaye amefanya maisha yangu kuwa rahisi kwa kunisaidia kula ninachopenda kama nyumbani. Asante Gino.” Wakapiga makofi.

“By the way, sijawahi kuona mpishi anayeweza kupika vizuri, tena chakula cha asili. Kwa kutajiwa tu. Tena akaweza kukitoa mpaka ladha ya asili, iliyo sahihi kama Gino! Hongera sana Gino. You are the best.” Gino akapunga mkono. Watu wote mpaka familia ya Cote, wakaongeza kumpigia makofi.

Kwa Gino ilikuwa kitu kikubwa sana. Inamaana usiku huo jina lake na sifa zake zilivuma na kusikika na wengi sana. Wenye nacho na wasio nacho wanaofuatilia hilo tukio na watakaoendelea kufuatilia hilo tukio. Akafurahia sana.

“Ms. Emily!” Tunda akaendelea. “Amekuwa rafiki wa karibu. Ananifundisha mengi ya hapa ndani na kuniandaa kuja kuwa mama mzuri na mke bora kwa mwanaume kama Net ambaye amekua akimuona tokea mdogo mpaka sasa. Anaupendo mkubwa sana kwangu. Asante Ms. Emily.” Wakapiga makofi. Ms Emily akapunga mkono.

“Babu Carter.” Carter akacheka. “By the way babu is swahili word for grandpa. Kwa hiyo nimempa Carter jina la babu.” Wakapiga makofi. “Asante kwa kila kitu. Kunipokea na kuhakikisha nipo sawa kila wakati. Namaanisha kila wakati. Hata nikizidisha muda wa kulala, kwake ataingiwa na wasiwasi. Nisipokula vizuri au kwa wakati wake yeye, kwake hatalifurahia. Anataka kuniona nina furaha na nipo salama wakati wote.”  Watu wakacheka. “Thanks Carter.” Net naye akaongeza.

“Nana! Akamgeukia. Wewe nikushukuru kwa kunipokea jinsi nilivyo na kuniweka karibu yako na kuniamini na kila kitu.” Wakapiga sana makofi. “Umekuwa kama Net kwangu. Kutoa ndani yangu yale ambayo hata sikujua kama yapo! Unanijali sana na umeniweka karibu yako kama mtoto wako kabisa! Asante sana.” “Karibu Tunda.” Akajibu bibi Cote wakati watu wakipiga makofi.

“Maya!” Tunda mwenyewe akaanza kucheka. Wengine nao wakacheka mpaka Maya. “Namuhesabu kama mdogo ambaye alizaliwa akafichwa ndio tumekutana. Alinipenda siku ya kwanza tu aliponiona nikiwa hata sijaanza mahusiano na Net. Mpaka leo, amekuwa..” Tunda akacheka tena. “Huwa Net akiondoka tu, nahesabu dakika ambazo ataingia chumbani kwetu. Hana asubuhi wala usiku, uchangamfu wake upo vilevile. Ananifuata mpaka chooni!” Watu wakacheka.

“Ni mtu ambaye unatamani atoke kazini arudi nyumbani au asubuhi asiende kazini bila kukupitia kukuaga.” “See Net! Tunda mwenyewe ndiye anayetaka nije chumbani kwenu kila wakati!” Wakacheka. “Anyways, najihesabu kubarikiwa kuwa na wewe Maya. Nakupenda sana na ninakuombea kila siku ili hiyo furaha idumu siku zote. Asanteni sana. Na karibuni.” Watu wakapiga makofi na kusimama wakati Tunda anatoka kwenye kipaza sauti.

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

Bibi Cote akasogea pale mbele kwenye kipaza sauti. “My My My!”  Akasema bibi Cote kama anayestaajabu, watu wakazidi kupiga makofi bado wakiwa wamesimama. “Seriously! Si mmemsikia wenyewe? Natamani ningekuwa hata nimewekeza hata wazo ili leo nijisifie, lakini !” Watu wakaanza kucheka.

Anyways, huyo ndio mke wa Nathaniel Cote. Na sisi tuliletewa kama hivyo nyinyi. Tukamkubali na kumpa nafasi. Namaanisha wote waliokubali kumpa nafasi kwenye hii nyumba, sasa hivi tunamfurahia. She is special!” Wakapiga makofi.

Ukanyoshwa mkono kutoka katikati ya wageni wao. “Najua swali lako.” Akasema hivyo bibi Cote na kuamsha kicheko. Mwenye pesa akiongea chochote, kila mtu anacheka tu. 

“Jibu ni NDIYO. Kile mlichokisikia nikikitamka nchini Tanzania, ni kweli. Nahisi, narudia tena, nafikiri, hata kama Net asingemleta Tunda kama mkewe, na nikakutana na Tunda, bado naamini ndiye angekuwa mtu badala yangu.” Watu walishangilia sana.

Tunda akaona watu wakimchukua video na picha zaidi. “Zipo sababu au sifa nyingi sana nilizokuwa nikizitafuta kwa mtu atakayefanya majukumu yangu, Tunda anazo hizo sifa kwa asilimia 90, japo yeye mwenyewe hakuwa akijua kama yeye ni mtu sahihi.” Watu wakapiga sana makofi na kusimama tena.

“Nitakuja kueleza hilo wakati mwingine, kama Mungu akitupa uzima. Lakini leo nitazungumza kwa kifupi tu kukuthibitishia kuwa sikukosea kwa Tunda.” Watu wakarudi kukaa ili kusikiliza. “Alikuja akiwa dhaifu. Daktari akashauri apumzike kabisa na kumtenga na watu ili kuepusha maamumbukizi yeyote kwake nakumfanya aumwe. Daktari alisema hakuna mwanya hata mdogo wa Tunda kuumwa chochote kile. Hata mafua! Lazima wote tumlinde.” Akaendelea.

“Aliendelea na matibabu mpaka daktari akaridhika kuwa anaweza kutoka sasa, ndipo nikampeleka kule kwenye kituo. Alipokwenda mara ya kwanza, akataka turudi naye tena. Nikamrudisha tena bila yakumuuliza ni kwa nini ametaka nimrudishe.  Huwa tunamuacha hapa wakati tunakwenda kazini. Siku hiyo nikiwa kazini, nikapata taarifa kuwa yupo yeye mwenyewe kwenye kile kituo, bila hata mimi kuniambia. Nikapata hamu yakujua ni kwa nini yupo pale! Kipi kilimrudisha mara ya pili na hiyo ya tatu akiwa peke yake! Nikaamua kumuacha kabisa, ila nikawaambia apewe ushirikiano kwa chochote kile.” Ukumbi wote kimya.

“Kuna mama na binti zake walikuwa wageni kabisa pale kituoni. Binti mkubwa alishindwa kabisa kutulia pale na alikuwa akimsumbua sana mama yake na wafanyakazi wa pale. Kumbe Tunda aliwaona mara ya kwanza kabisa nilipompeleka. Mimi hata sikujua kama kile kitu kilimgusa Tunda. Maana tulifika pale kiongozi wao akawa anatuelezea kwa kutulalamikia juu ya huyo binti kwenye familia hiyo ngeni. Tukazungumza na kuondoka bila Tunda kuongea chochote.”

“Kumbe Tunda akaamua kumfuatilia yule binti. Akaanza na yule binti taratibu tu. Kimya kimya. Mpaka akaweza kufikia moyo wa yule binti. Nimeambiwa amebadilika kabisa. Alianza kwa kuomba msamaha wafanyakazi wote wa pale kituoni. Ametulia na ameanza kusaidiwa na wataalamu wa afya.” Watu wote wakasimama na kupiga makofi.

“Huwa naamini sana hisia zangu.” Yule bibi akajisifia. Watu wakacheka. “Let me have it!” Akaongeza nakufanya watu wazidi kucheka. “Sikumtuma Tunda. Nilichofanya siku ya kwanza nikumtambulisha kwa wafanyakazi niliowakuta pale siku ile, na ile kuwaambia wampe ushirikiano ambao hata hakuhitaji, basi. Lakini Tunda alirudi yeye mwenyewe. Akiwa amepanga yeye mwenyewe na Carter kumtafutia usafiri wa kumpeleka pale, basi. Alirudi kule bila kutaka mitandao ijue kama wengi wetu.” Watu wakacheka sana.

“Wala hakujitangaza popote. Akarudi nyumbani na maisha yake yakaendelea kimya kimya kama yeye mwenyewe alivyo mtulivu. Hata mimi hakuniambia.” Watu wakapiga makofi. “Na mimi wakati wote tangu nilipoanza hii taasisi nilikuwa nikiomba Mungu anipe watu wa jinsi hii.” Wakapiga tena makofi. Net alikuwa amemuwekea mkewe mkono na kumbusu mara kwa mara. Tunda mwenyewe alishangaa.

“Kwa hiyo Ndiyo. Na ninazidi kumshukuru Mungu kwa kuniongoza kwa mtu sahihi. Kadiri ninavyoutazama jinsi moyo wake ulivyo na wale watu aliowakuta pale. Na kwa kadiri Mungu atakaponijalia uwezo, nitahamisha yote yaliyomo hapa na hapa.” Akajishika kichwa na moyoni. “Nitahamishia kwake na kumsihi Mungu aendelee kumsaidia. Na nyinyi naomba mumpe nafasi na tumsaidie. Na nina hisi, Tunda atakuja kufanya bora zaidi yangu.” Haya yeye mwenyewe bibi Cote alicheka alipomalizia hivyo, watu wakapiga makofi na kusimama tena. “Asante Nana.” Net akashukuru. Bibi yake akamgeukia na kucheka kidogo.

“Bado Tunda anajukumu la umama, mke, tena mke wa Nathaniel Cote! Atahitaji kila msaada ambao tunaweza kumpa. Na kwa kuwa nimeona jinsi walivyoweza kusimama hawa wawili. Maya na Tunda. Na vile Tunda anavyomshika vizuri Maya, naamini kila kitu kitakuwa sawa, tena Net na mimi mwenyewe tukiwa nyuma yao! Ninauhakika hakuna kitakachoharibika.” Hilo nalo likawa tangazo jipya na la kushitua kila mtu.

Maya! Kila mtu akashangaa. Kamera zikamgeukia Maya. Akaanza kupigwa picha kwa upya na kuchukuliwa video Maya akiwa ameduaa. Hakutegemea. “Asante Nana. Asante sana.” Akajikuta akilia kwa mshituko palepale mbele ya watu wote waliokuwa wamemgeukia yeye. Ilimgusa sana Maya, mpaka akasahau jinsi alivyokuwa amependeza na vipodozi alivyoviweka usoni kwa ustadi. Alishindwa hata kujificha. Akabaki ameduaa machozi yakichirizika na kuharibu vipodozi vyake usoni ambavyo navyo vilikuwa vikichirizika. Kuanzia wanja mpaka foundation.  Tunda akamsogelea. Akamshika na Net akamkumbatia. Ile ilikuwa inamaana kubwa sana kwa Maya. Kwamba bibi yake ametangaza kumsamehe na kuridhika na mabadiliko yake.

Ni bibi Cote. Kioo cha jamii. Asiyekurupuka wala kufanya kosa katika mipango yake. Ametangaza ramsi kuwa taasisi yake anaiacha chini ya Tunda na yeye Maya kama msaidizi wake! Hakuna aliyetegemea. Maya! Binti aliyeharibu na kuchafua vilivyo kwenye hiyo jamii! Leo bibi Cote anamkabidhi majukumu mazito vile! Alifurahi sana Maya na wala bibi yake hakuwa amemwambia. Inamaana watu waliokuwa wakimcheka, wameaibika. Zaidi Vic. Amerudisha heshima kwenye jamii!

“Tunda aliniambia kabla hatujaingia hapa, njaa inauma.” Bibi Cote akabadili ile hali pale, angalau watu wakacheka. “Najua Gino na timu yake wametuandalia vyakutosha. Karibuni tuendelee kula na kunywa huku tukishukuru Mungu kwa yale anayotubariki zaidi ya tulivyoomba. Karibuni na Mungu awabariki.” Akawa amemaliza huyo bibi. Alikuwa amependeza sana na muda wote huo alikuwa kwenye kiatu cha juu.

Ndipo wakashuka sasa kusalimia watu kwa kuwashika mkono. Tunda akamshika mkono Maya, wakatoka pale ukumbini kwa kupitia mlango wa mbele. Akaenda naye chumbani kwake ili atulie, na kujitengeneza upya.

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

Walirudi Maya akiwa ametulia kabisa na cheko juu. Net alipomuona tu mkewe mlangoni akiingia na Maya, akawaaga aliokuwa akizungumza nao, akamfuata. “Twende nikakutambulishe kwa karibu kwa Mayor.” “Njaa inauma Net!” “Hatutachukua muda mrefu. Watu wachache tu, kisha tunaenda kula. Nitahakikisha unakula wewe wa kwanza.” Wakaendelea kunong’ona huku wakirudi kwenye kundi la watu. Picha zikaendelea kupigwa na kuchukuliwa video katika kila kitu anachofanya Net, na mkewe.

Alikwenda kumtambulisha kwa Mayor wa huo mji wao. Akawatania kidogo na kumkaribisha Tunda rasmi akimsifu mumewe aliyemfahamu kwa muda mrefu sana kwamba anamfahamu Net tokea mtoto mdogo sana. Wakataniana kidogo kisomi ndipo wakaendelea kusalimia wengine huku akiwa karibu na Tunda. Kila aliposogea, alisogea naye akiwa amemshika kiunoni kwa nyuma.

Kila alipotambulishwa na yeye akafanya kama alivyofundishwa na Maya jinsi yakusalimia. Jinsi ya kushika mikono, na jinsi ya kutabasamu. Ujasiri uliongezeka vile alivyokuwa amejazwa sifa usiku huo na vile alivyokuwa amependeza kuanzia juu mpaka chini. Bibi Cote alimtolea mkufu wake, akamkabidhi kama zawadi. Maya alimwambia ule mkufu ni wa alumasi na nigharama sana.

Alitembea na kusogea kama Maya alivyokuwa amemfundisha, mpaka Net akashangaa. Yeye Net alitaka Tunda awe vile alivyo. Hakuhangaika hata kumuelekeza chochote. Lakini Maya alikuwa na kazi yakumuelekeza na kumpa muongozo wa nini chakufanya hata jinsi ya kuzungumza mbele ya ule umati. Asimamaje, atizamaje umati wote na jinsi ya kutabasamu, ilikuwa kazi ya Maya na bibi Cote kidogo kwa pembeni akimsikiliza Maya anavyomfundisha Tunda.

Ila Bibi Cote yeye alimsisitiza kuwa asiogope, kwa kuwa hakuna kitakachobadilika. Yeye ni mama Cote tu. Aidha wapende, wasimpende, hakuna kitakachobadilika. Akamuongezea ujasiri na kumtaadharisha juu ya atakachozungumza hapo kuwa makini nacho. Hiyo tafrija ikaenda vizuri tu. Watu wakala na kunywa mpaka kusaza. Wakaondoka.

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

Wakabaki wao wenyewe watu wa familia wakitathimini mambo yalivyokwenda. Tunda akapata nafasi yakumshukuru bibi Cote kipekee kwa heshima aliyompa. Na jinsi alivyomwamini. “Sikujua kuwa walikwambia habari za Lorin!” Tunda akashangaa. “Kwanza ujue hakuna jambo linafanyika bila mimi kuambiwa.” Tunda akakumbuka hilo, wakacheka. “Halafu yule binti alisumbua sana pale kwenye ile taasisi. Kuna waliotaka tumfukuze yule mama na watoto wake sababu ya yule binti. Wengine wakashauri nimtoe yule binti pale. Lakini nikawakatalia. Hivi nilikuwa nasubiri nimalize mambo fulani, niende nikazungumze naye mimi mwenyewe nimwambie nampa nafasi ya mwisho, lasivyo nitampeleka jela ya watoto kama kiongozi wa pale alivyoshauri.”

“Sasa kuja kuambiwa Lorin ameomba msamaha na ameomba aanze kufuata taratibu ya kwanza kabisa. Kuanzia afya yake mpaka kurudi shule! Nikashangaa sana. Ndipo wakaniambia walikuona ukizungumza naye. Ulimfuata pale zaidi ya mara mbili akawa ametulia kabisa na hatoroki tena pale.” “Ulizungumza naye nini?” Maya akauliza. Tunda akacheka kidogo akawa kama anafikiria.

“Sijui nini kilimgusa zaidi! Ila nafikiri ni Mungu tu. Maana nilianza kumuwekea mazingira yakuniamini. Nikazungumza naye taratibu kama vile Net alivyofanya kwangu. Kuweka mazingira rafiki kwanza.” Tunda akaendelea taratibu tu. “Mwanzoni alikuwa mbishi na anahasira sana. Nafikiri sababu ya hayo mazingira aliyopitia na mama yake pamoja na wadogo zake. Taratibu nikamuwekea mazingira ya kuniamini. Nikamsimulia na mimi kule nilikopita mpaka nikampata Net. Akiwa tu ni msaada wala si mpenzi. Nikamwambia kama nisingekubali msaada wa Net, ningebakia vilevile.”

“Nikamwambia hapo anajiadhibu kwa makosa ya baba yake. Nikamwambia hastahili kubeba hasira kwa mabaya aliyofanya baba yake na mengineyo. Tukazungumza sana mpaka nikamuona analia na kufunguka. Ndio maana nilikuwa nikirudi mara kwa mara ili tu kuzungumza naye. Alishakosana na watu wa pale karibu wote. Pakawa na ukuta kati yao.” “Aliwasumbua sana. Tena kwa kuwatusi vibaya sana.” Akaongeza bibi Cote.

“Aliniambia mwenyewe. Na nikamwambia ili aweze kusaidiwa pale, nilazima aanze kwa kuwaomba wote msamaha. Ndipo watamwangalia kwa jicho jingine. Ajishushe, achukue msaada wake, atoke na yeye akawe msaada kwa wengine.” “Nimesikia amechangamka! Anamsaidia hata mama yake kuogesha wadogo zake.” Wakacheka.

Net akambusu. “Unakumbuka nilikwambia utakuwa msaada kwa wengi?” Tunda akacheka huku akitingisha kichwa. “Naona umeanza mwenyewe bila kusubiri nikusaidie.” Tunda akacheka. “Najua una mambo mengi Net. Na kwa kuwa Nana na Maya wapo, na Nana ameniambia muda na wakati wowote nikiwa na swali asipokuwepo naweza kumpigia.” “Kabisa Tunda. Ukikwama popote. Hata kufanya chochote, ukakwamishwa kwa chochote. Nipigie.” Akavuta kumbukumbu kidogo.

“Lakini kwa jinsi ilivyoenda leo, sidhani kama kuna utakapokwenda usipewe huduma ambayo wangenipa mimi.” “Kweli Nana!?” “Kabisa. Nana akiongea jambo ndio mwisho, na wote wanajua.” Maya akaingilia. Wakamuona anaanza kucheka. “Yess!” Wakamsikia akishangilia kwa furaha. Wakajua amekumbuka kitu chakumfurahisha. Wote wakacheka. “Sasa hivi nakuwa mtu mzima. Sifanyi tena mambo ya kitoto.” Akaanza kujiwekea mikakati yake. Wote wakacheka.

“Naacha kupost vitu vya kijinga huko mitandaoni. Nakuwa kama Tunda. Mtulivu!” Wakacheka sana kama hawamsadiki. “Si mtaniona! Sibishani tena na Vic. Matendo tu. Kwanza nishajua nipo juu yake sana. Halafu sasa hivi mimi nina majukumu mazito sio kama yeye kujipendezesha na kuzunguka kwenye magari ya kifahari kutoa mipango tu bila utelekezaji!”  “Hapo utakuwa kweli umebadilika. Na watajua tu.” Waliendelea kuzungumza hapo wakijipanga. Mpaka muda wa kwenda kulala, wakatawanyika.

Maandalizi ya Harusi ya Pili ya kanisani Tunda & Net.

T

unda ndiye aliyeachiwa jukumu zima la mambo ya harusi. Achague kile anachokitaka yeye. Kuanzia rangi, mapambo, chakula, keki, kila kitu kisha amwachie Stacy, ambaye ni mtu maalumu anayeshugulikia hiyo harusi. Ndipo yeye sasa Stacy amalizie kila kitu baada ya Tunda kuchagua anachokitaka. Kuhakikisha kila kitu kinafika ukumbini kwa wakati.

Net alimwambia kwa mila na desturi za huko nchini kwao, upande wa bibi harusi ndio wanagharamia harusi nzima. Yaani wazazi wa bibi harusi. Na bibi harusi ndiye anayechagua kila kitu cha harusini. Upande wa bwana harusi wanakuwa kama waalikwa tu. Kwa hiyo akamwambia anampa heshima yakufanya anachotaka kwenye hiyo harusi. Achague atakacho yeye.

Makampuni ya maana yalikuwa yakipishana hapo kwa Cote, kumuonyesha Tunda vitu mbali mbali ili kupata hiyo kazi yakufanikisha harusi yao ambayo walijua ni kuuza kazi zao kwa asilimia kubwa sana. Harusi ya Nathaniel Cote! Kila mtu alitaka apewe yeye kazi.

Stacy alikuwa na kazi ya kuchagua katika kila idara, makampuni matatu mazuri. Anawekeana nao miahadi kutokana na muda wa Tunda, kisha wanakwenda kujinadi sasa kwa Tunda.

Tunda alikuwa na kazi ya kuangalia kwa makini ili asije chagua kitu akaharibu shuguli nzima ya matajiri hao. Makampuni yalituma wataalamu wao mbali mbali kwenda kumshawishi Tunda ili wachaguliwe wao. Upande wa chakula, alimtaka Gino na Maya wamsindikize kwenda kuonja aina hiyo ya chakula. Yeye Net alisema chochote atakachochagua Tunda hatakuwa na shida.

Stacy alimletea Tunda caterers kama wanne ambao alimwambia Tunda, hao ndio wanasifika kwa chakula kizuri na maandalizi yao ni ya ustadi. Tunda alimuomba kwanza menu yao. Kujua huwa wanatoa vyakula vya namna gani kwanza, hata kabla hajakutana nao. Alimtaka yeye Stacy ndio alete menu ili kupunguza kuonana na watu wengi. Stacy alipoleta menu, akamuomba muda wa kuzipitia akiwa na Gino kwanza ili kuelewa kila chakula na Gino amshauri.

          Walishauriana kujaribu chakula cha caterers wakubwa wawili ambao Tunda alivutiwa na menu zao. Wakapanga muda wa kwenda kuonja baadhi ya vyakula na juisi ili kuweza kufanya maamuzi sahihi. Kwa upande wa kuonja hivyo vyakula, walitakiwa wahudhurie watu watano. Kwa kuwa bibi Cote alionekana katikati ya week anakuwa na ratiba inayobana, basi Tunda akamuomba Maya aungane nao ili kuchagua ladha sahihi ya chakula ambacho anadhani wageni waliozoea kuwaalika, wangefurahia. Maya alikubali, akasema atatokea kazini kuungana nao. Kwa hiyo watakutana eneo husika.

Katikati ya Yote, Kabla ya Harusi.

K

atikati ya hekaheka hiyo ya kukamilisha maandalizi ya harusi kwa wakati, ili iwe nzuri na baada ya hapo na Net naye akatulie kwenye fungate. Busy kazini kuweka mambo sawa, kabla ya siku ya harusi yao ili baada ya harusi apate muda mtulivu na mkewe. Na mkewe naye busy akitaka asiharibu kitu.

Bibi Cote naye kuna ambao mbali na kuwatumia kadi za mwaliko, ilibidi kuzungumza nao kwa simu. Na kutafutwa sehemu maalumu za kushukia wageni hao mamilionea, wanaotoka nje na ndani ya nchi ya Canada kushuhudia Nathaniel Cote akioa.

Vyombo vya habari vilitangaza. Magazeti yaliandika. Mashabiki wao ndio walijaa mitandaoni wakihesabu siku. Kila mtu alitaka kuhudhuria harusi hiyo, lakini mwaliko ulikuwa kwa wachache, ila vipo vyombo vya habari vilitangaza kurusha harusi hiyo ‘Live’, baada ya kuomba na kupewa ruhusa na familia hiyo ya Cote. Ikaanza kazi ya kushindana mitandaoni watu wakikisia gharama nzima ya hiyo harusi. Wengine walipingiana dau hadharani. Wakaja gauni atakalovaa mke wa Net. Yaani Tunda.

Watu walishindana mtandaoni wakibashiri gharama ya gauni tu atakalovaa siku hiyo Tunda. Nani atabahatika kutengeneza gauni hilo au ni designer gani atabahatika nguo yake kuvaliwa na Tunda siku ya harusi yake! Hilo nalo likawa jambo. Mjadala uliopewa muda na mashabiki wengi tu. Hapo bado walikuwa wakiendelea kumthaminisha Tunda kwa vile alivyotokea siku ya kutambulishwa kwake. Bado mijadala ilikuwa ikiendelea mtandaoni. Watu wakichambua neno moja hadi jingine kutoka kwa kila mtu aliyezungumza siku ile. Kuanzia bibi Cote, Net, Tunda hadi Maya. Kila mtu alisema lake. Wenye wivu walizidi kuumia kwa sifa zilizokuwa zimemwagwa kwa Tunda na kuponda hadharani kutokana na ile hotuba.

Penzi la kweli lililotangazwa na kuonyeshwa pale hadharani. Wakaanza kujadili hata jinsi Net na Tunda walivyosimama na kushikana mikono. Yale mabusu! Kila mtu akasema lake. Na kweli ulikuwa mjadala ambao ulijaa kwenye mitandao na magazetini. Ya udaki yaliandika kwa undani. Yale magazeti ya maana, yaliwapongeza nakuongea mazuri. Wakiwatakia kila la kheri kwenye maisha yao. Kukajaa hekaheka kila upande. Shamra shamra wengine wakisubiria siku ya harusi kwa hamu, na wengine wakiona ni kama walidhalilishwa hadharani.

Kwa Upande wa Vic!

V

ic alishajitangazia kuwa yeye ndio angekuwa mke wa Net na mchukua  kiti cha bibi Cote. Leo Tunda aliyemfukuza nyumbani kwake kwa dharau kiasi kile ndiye anajaa magazetini akisifiwa vile! Tunda anaonekana akipewa mabusu hadharani na mwanaume ambaye bado anamuhesabu ni wake! “Net ananistahili mimi. Net ni wangu!” Vic alilia mbele ya wazazi wake. “Tunda amebeba mtoto wa Net na si mimi!” Kila alipokumbuka nakusikia juu ya Tunda na Net, Vic alizidi kulia.

Maya ndio anachukua nafasi aliyoisubiri kwa hamu tokea miaka na miaka! Ikawa tofauti kwa Vic, wazazi wake na wapambe wake waliona yeye Vic ndiye anayestahili kuliko Maya au Tunda. “Mlevi yule ndio anachukua cheo changu! Alikuwa akifanywa mapenzi mpaka kwenye gari, hadharani, kwenye vyoo vya clubs, leo yule bibi ndio anampa nafasi yangu! It’s not fare mom.” Vic alizidi kulia na kusononeka moyoni.

Mbaya zaidi ni kama akatolewa kabisa kwenye picha. Hakutajwa hata kwa upande wa marafiki wa Net. Net hakumtaja kati ya marafiki zake. Alimtaja Troy na Lean tu! Vic amekua pamoja na Net! Amelala chumbani kwa Net tokea yupo binti mdogo tu! Net ndiye aliyekuwa mwanaume wake wa kwanza kufanya naye mapenzi! Na wakawa kwenye mahusiano ya muda mrefu sana. Leo Tunda anamwambia hajawahi hata kumsikia, na Net naye anashindwa hata kumtaja mbele za watu! Hilo likamuuma sana. Ulikuwa ni udhalilishwaji ambao, ilikuwa bora afe, kuliko kuona hiyo harusi ikifungwa.

Na kumdhihirishia hilo, aliambiwa asifike tena pale nyumbani isipokuwa kwa mwaliko maalumu. Akashangaa maandalizi yanaendelea, hakuna hata anayemtafuta hata kwa swali! Inamaana hayupo hata katika kundi la wasimamizi wa harusi! Ni Troy tu na Lean! Vic akaumia sana.

Kwa Upande wa Ritha/ Mama Mzaa Chema.

R

itha naye huko alipokuwepo habari zilimfikia bila chenga. Japokuwa alikuwa mji mwingine, lakini hapohapo nchini Canada, alipata kile kinachomtokea Tunda huko mjini Norfolk. Tunda alijaa kila kona akipambwa na bibi Cote. Hata watoto wake wakuwazaa hawakuropoka hata kwa bahati mbaya kutaja jina lake kwenye tafrija nzima! Yaani ni kama hajawahi kuwepo kwenye maisha yao! Nana akawa kama mama wa wanae! Halafu  Tunda ndiye anasifiwa na kupewa kiti!

“Kwanza hajasoma kama mimi!” Hilo nalo likamuuma sana Ritha. “Wakati mimi nahangaika kuzaa, na kulea, yeye alikuwa akifanya umalaya tu!” Ritha akazidi kuumia nakusahau Tunda ni kama mtoto wa kumzaa kwa umri alionao. Mdogo hata kwa Net. Lakini hilo la umalaya hata yeye Tunda alikiri hadharani na kujisifia kuwa amelipa deni. “Anakula jasho langu! Amechukua familia yangu! Watoto wangu wanashindwa kunikumbuka, anachukua nafasi yangu!” Ritha akazidi kuumia. Akajidharau kuona ameanza jambo na kuishia katikati! Anashindwa na Tunda! “Haiwezekani!” Akasema Ritha kwa kuumia sana.

Mawazo yakamrudisha kwenye sifa alizomwagiwa na wote. Maya, bibi Cote na Net. Kitu kikapanda ndani yake. Hasira zikawaka. “Yaani malaya huyu amenipokonya kila kitu mpaka uhuru wangu!” Ritha akaangalia alipo. Kutoka kwenye jumba la kifahari, ameishia kwenye Condo! Gorofa alilopangisha kijisehemu na wengine wakiishi kwenye jengo hilohilo, juu yake na chini! “Haiwezekani!” Akakumbuka heshima kubwa aliyokuwa amejipatia nchini Tanzania na Kampuni ya Cote aliyomiliki kabla ya kuja kwa Tunda kwenye maisha yake. Vyote ni kama vilipotea. Akaishia kuuza kila kitu na kukimbia nchi! Na hayo yote alihesabu ni sababu ya Tunda.

Ni kweli Ritha hakuwa na shida na pesa. Alikuwa na ajira nzuri tu, lakini mpweke. Hakuna ule utukufu aliokuwa nao wakati anaishi nchini Tanzania kabla Tunda hajaingia kwenye picha. Au kabla hajaamua kuanza vita na Tunda. Akili na mawazo ya Ritha vikagoma kabisa kuona Tunda anafikishwa kanisani na yeye ndio kubaki mama Cote anayetambulika kila mahali. “Mimi ndio mama Cote. Kila mtu alilijua hilo na lazima ibakie hivyo.” Kwa hasira sana, akatamka Ritha na kuanza kuweka mikakati ya jinsi ya kumaliza alichoanza. Akajiona atakuwa mtu wa ajabu sana, kuanza jambo na kutomaliza. Mwanamke mwenye akili ambaye hata Bibi Cote mwenyewe anamkubali, akaanza kujipanga upya kurudi vitani.

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

Watu wawili wanguvu, Vic&Ritha, na mipango yao ambayo haijawahi kushindikana wameamua kusimama kinyume na Tunda. Wote hawakubali kushindwa, na hawajawahi kushindwa. Vic alimmudu vizuri sana na Maya. Ritha alifanya makubwa yanawauma mpaka hapo walipo.

Sasa Je, nini kitamtokea Tunda katikati ya maandalizi mazito yakifahari ya harusi yake na Net?

Ritha alimtoa kwenye fungate akiwa na pingu akishindwa kufanikiwa kusimamisha harusi sababu ya uwepo wa bibi Cote nchini Tz,

Je, safari hii Tunda atafanikiwa kufika kanisani?

au

Majeshi yataungana kukusanya nguvu dhidi ya Cote waliomwahidi Tunda ulinzi?

Endelea kufuatilia visa na mikasa ya kusisimua.

CONVERSATION

0 Comments:

Post a Comment