Naomi Simulizi |+1 205 767 8163 |naomisimulizi@gmail.com NILIPOTEA! - sehemu ya 43. - Naomi Simulizi

NILIPOTEA! - sehemu ya 43.

 Maya naye!

S

iku hiyo ya kwenda kuonja chakula, asubuhi Net alipoondoka tu, hata dakika haikuisha, ni kama Maya alikuwa akimsubiria kaka yake hapo nje ya mlango, atoke ili na yeye aingie hapo kwa Tunda. Tunda akamshangaa anaingia akiwa kama hakulala
vizuri. Akajitupa hapo kitandani na kujifunika na mto kichwani. Tunda akamgeukia. Akashangaa kimya. Si kawaida ya Maya. “Leo huogi?” Tunda akamuanza. Kimya. Wakatulia kidogo, Tunda akamtoa ule mto kichwani na kumtoa nywele usoni.

“Nataka kuiona sura yako. Ujue unaweza ukawa unafanana na Cote!” Akamuona anacheka, akajilaza juu ya mto. “Umeota ndoto gani?” “Siwezi kuota kama sijalala!” Tunda akamtizama vizuri. “Unawaza nini?” “Kuna kitu kinaniumiza Tunda, na siwezi ku..” Akamuona machozi yanamtoka. “Huwezi kufanya nini?” “Maisha niliyoishi zamani! Niliharibu sana. Sasa hivi siaminiki.” Akalalamika kwa uchungu sana.

“Mimi sio kama wewe Tunda. Mimi nilikuwa nikitangaza nimebadilika, nikikaa hata siku 10 haziishi, naokotwa nimelewa sehemu na nimefanyiwa mambo mabaya.” “Kwani ulikuwa hujui?” Ikabidi Tunda aulize. “Huwezi amini Tunda. Hata mwanzo wa hayo madawa ulikuwa ni ushawishi tu. Nilipokataa, ni kama wakanilazimishia tulipokuwa club. Sasa kwa kuwa walikuwa marafiki, sikujali. Ila nikapenda. Nikaanza kutumia.” Tunda akaendelea kumsikiliza.

“Lakini kila nilipokuwa nikijitahidi kuacha baada ya hapo ikawa kama kunaushawishi wa lazima kutoka kwa baadhi ya marafiki zangu fulani kutaka niendelee. Na wakafikia umbali wakinitishia nikiacha kutumia nao, wananitenga kwenye kundi na kunidhalilisha mitandaoni.” “Maya!” Tunda akashangaa. “Kweli Tunda. Sasa ukumbuke hapo nilishakuwa mtumiaji. Ilikuwa hauhitajiki ushawishi mkubwa sana kunirudisha kwenye madawa. Halafu nilikuwa peke yangu, Tunda. Net hakuwepo. Sina watu wengine isipokuwa hao marafiki zangu. Papa na Nana ni wale watu wanaofuatana kila mahali. Huwezi kuwatenganisha kama Nana anakuwepo nyumbani. Ila mara nyingi Nana anakuwa busy na majukumu yake.”

“Utakuja kumuona. Sasa hivi yupo hapa kwa sababu ulikuja mgonjwa, na umetoka kwenye matatizo hakutaka ujisikie ni kama anakukimbia. Lakini safari na majukumu ya Nana hayaishi. Mikutano ndani na nje ya nchi ipo mingi na mfululizo na yeye ni kiongozi kila mahali kwa hiyo lazima kuhudhuria. Hawezi kuwa anatuma wawakilishi kila mara!”

“Nilikuwa nakuwa peke yangu humu ndani, Tunda. Kama nilivyokwambia Net alikuwa Tanzania. Na wakati yupo hapa pia alikuwa mtu wa mipango. Huwezi kumkuta amekaa tu. Yaani tulikuwa tunamgombania na Vic, kupata naye muda. Mwishoe Vic akawa anashinda, mimi naachwa peke yangu.” Tunda akaumia sana.

“Papa naye yupo kama Net. Tena afadhali ya Net anakuwepo nyumbani mapema kidogo sababu yako. Sasa kama Nana anakuwa hayupo nchini, basi ujue Papa alikuwa akirudi hapa hata saa tano usiku. Anashinda kazini tu. Alikuwa mtu wakufanya sana kazi. Ikabidi na mimi nijifunze maisha yangu. Ndipo nikatengeneza kundi la watu niliokuwa naweza kuwapata kila ninapo wahitaji. Kuanzia asubuhi nikiwapigia tu simu nikiwaambia tukutane mahali, hawana shida. Nikiwa na kitu kinaniumiza, wao ndio watu wakunifariji.”

“Kwa hiyo hata waliponishawishi niingie kwenye madawa, nilipokataa, wakanilazimisha, sikuweza kuwabishia. Kwanza waliniwekea kwenye kinywaji tu. Wakanirudisha hapa nyumbani nikiwa nimelewa sana. Nilipokuja kuwauliza kesho yake, wakasema ni cocaine, waliniwekea makusudi ili nifurahie kwa kuwa nilienda kwao nikiwa mnyonge.” “Maya!” Tunda akazidi kushangaa.

“Kweli tena Tunda. Wakanishauri nijaribu tena nione nitakavyojisikia. Nikakataa. Ndio wakaniambia kama nakataa faraja ya kweli, basi nisirudi tena kuwalilia shida. Kufupisha stori, ndipo nikaanza. Madawa yakawa kimbilio lakuondoa unyonge na kuniweka karibu na marafiki.” “Pole sana Maya.” Tunda akaumia sana. Akahisi hakuna aliyetulia na kujua upande wa Maya wa stori.

“Hapa ndani hapafai kama upo peke yako tu. Panachosha. Panakuwa papweke sana. Muda wote unajikuta na Carter tu na Ms Emily! Na Ms Emily akiondoka, unabaki na Carter usiku kucha. Unamfuata Carter kila mahali mpaka unachoka. Huwezi kuishi hivyo. Na mimi nilikuwa ndio nimepevuka. Nikawa nawafuata na ninaogopa wasiniache. Na nafikiri na wao walijua kua nawategemea, wakatumia upweke wangu vizuri sana.” “Usilie sasa.” Tunda akamgusa kama kumbembeleza.

“Nilikuwa nateseka Tunda! Acha tu. Wanachukua pesa zangu. Wanataka mimi ndio ni wanunulie kila wakati. Nikiwaambia sina hela, wakati mwingine wananifukuza.” “Jamani Maya!” “Kweli Tunda. Basi unarudi nyumbani unatulia mpaka ukipata tena pesa ndio nawatafuta. Nikaendelea kuharibikiwa, hakuna anayejua wala kujali. Mpaka waje wanione kwenye mitandao au wafuatwe na polisi hapa kuwa labda nimekwama mahali, ndipo utawaona wote wanaacha shuguli zao na kunijali. Hata kama Nana anakuwa mbali vipi. Akisikia tu nipo kwenye shida anarudi siku hiyohiyo. Lakini sio kujali siku yangu inaendaje nikiwa sipo matatizoni.” Maya akaendelea kulia taratibu.

“Niliyaharibu maisha yangu sana Tunda. Sina sifa nzuri popote na kwa yeyote. Hata sasa hivi nikiongea kitu kwa mtu, siaminiki. Wananiona mimi muongo tu. Ukiwasogelea karibu wale watu wamaana au vijana wa maana, wanakukwepa au wazazi wao wanakufukuza waziwazi wanaona unataka kuwaharibia maisha vijana wao.” Tunda aliumia sana.

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

Akaona Maya hakuwa na tofauti yeyote ile na yeye. Sema yeye alizaliwa kwenye pesa, Tunda kwenye dhiki. Lakini ni kama walifanana kabisa. Kujikuza wenyewe kwenye nyumba zilizojaa watu wazima na akili zao! Upweke ukawafanya wote waangukie pabaya.

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

“Lakini Tunda, mimi nafikiri ni kama Vic anahusika.” “Kwa nini? Futa machozi uniambie ukiwa umetulia.” Maya akajaribu kutulia akaendelea. “Sina ushahidi, lakini kila nikifikiria, ni kama wale watu waliokuwa wananizunguka, ni kama walikuwa wanatumwa Tunda. Kunisukumia kwa makusudi kwenye madawa. Na kila nilipokuwa nikitaka kutoka, walikuwa wanahakikisha narudi. Tena kwa pressure kubwa kama ambao walikuwa wanasubiriwa kutoa matokeo fulani.” “Pole sana Maya. Pole.”

“Kijana wa mwisho niliyekuwa naye, alikuja kwangu kama ana uwezo mzuri tu. Akaniambia mambo mengi sana. Nikamleta mpaka hapa nyumbani kwa Papa na Nana. Ikawa sasa zamu yake yakunipeleka kwao au kwa wazazi wake. Nikaona ni kama ananizungusha kwa hili na lile.” Akaendelea.

“Mimi najijua kuwa nina akili sana. Hilo nalijua. Hata zakufikiria huwa najua ninazo.” Tunda akacheka. “Kweli Tunda. Sema sikuwahi kujipa nafasi. Lakini huwa nikidanganywa huwa najua. Naweza nikaamua kujifanya mjinga tu, lakini huwa najua kama ninadanganywa. Na ninaweza kumsoma mtu na kumjua kwa kumsoma tu usoni. Na tukipata hata dakika 5 za mazungumzo, ndio kabisaa. Hujifichi kwangu.” Akaendelea.

“Akanizungusha sana, mwishoe akaniambia atanipeleka nyumbani kwake nimpe muda.” “Sababu gani alikupa kubwa ya kutokukupeleka kwa wazazi?” Tunda akauliza. “Alisema hayupo kwenye maelewano mazuri na wazazi wake. Eti akasema huo ulikuwa ni mwaka wa 4, hawaja wasiliana.” Tunda akatulia na yeye akaonyesha kutoridhika. “Siku ya kwanza nafika nyumbani kwake, nikashangaa. Hapakuwa pakiendana na nyumba ya mwanaume anayeishi peke yake! Pazuri sana, na pamepangiliwa vizuri kama mtu aliyekuwa ameajiri designer apapangilie. Halafu hapakuwa na dalili kama alishawahi hata kulala usiku uliopita! Kila kitu kipya kabisa. Nikajaribu kumuuliza maswali kadhaa, nikajua anadanganya ila sikujua ni kwa nini.”

“Nikajiambia pengine anafanya hivyo ili kunivutia kwa kuwa anajua mimi ni Cote. Nikawa najaribu kumfanya atulie ili awe kama yeye. Nafikiri akaja kunipenda. Sasa nahisi Vic anakuja hapa.” Maya akakaa vizuri.

“Siku moja nikiwa nyumbani kwake, simu ikaita. Akaonekana kupaniki kidogo, akaomba kwenda kuzungumza nayo nje. Nikamwambia hamna shida. Lakini tayari nilishaingiwa na mashaka kwa jinsi alivyo paniki. Nikajiambia nilazima nijiibe nisikilize. Hapo mapenzi yalikuwa yamekolea! Wakati wote yule kijana alitaka aniweke mikononi. Si kwa kufanya mapenzi, ila tu kunishika. Tunakaa hata masaa, amenikumbatia tu.” Machozi yakaanza kumtoka tena Maya.

“Sikuwahi kupendwa vile Tunda. Sikuwahi kujisikia salama vile. Upweke wote uliondoka. Wengi walinichezea. Na mimi nilijua kuwa nacheza tu. Lakini yeye, alinipenda. Mapenzi yetu yalianza kukua taratibu mpaka nafikiri hata yeye akajua mimi ni mtu wake. Akaanza kufungua moyo wake kwa ukweli. Akawa akifufurahia kweli akiniona tofauti na zamani. Mimi mwenyewe niliona mabadiliko.” “Mbona humtaji jina?” “Alinidanganya Tunda. Najuaje kama hata jina alilonipa ni lake kweli?” Akajifuta machozi.

“Usilie sasa ili unisimulie ni kipi kinakufanya uhisi kama ni Vic.” Maya akajifuta machozi. “Alitoka nje kwenda kuzungumza na simu. Nikajificha kusikiliza. Kitu kikubwa nilichomsikia akiongea na huyo mtu ambaye ni kama alikuwa akimpa maagizo na yeye kuitiki ni, ‘Hapana, sitaweza kumfanyia hivyo, anaonekana ni mtu mzuri sana. Na amebadilika. Haonyeshi kama ni mtu hatarishi, ambaye hata wewe atakuingilia.’ Kama anayekataa kunifanyia kitu ambacho walikubaliana na huyo mtu.” “Maya!” Tunda akashangaa sana.

“Kweli tena Tunda. Baada ya hapo akaonekana kupoooza sana. Ukumbuke hapo hata madawa hatukuwa tukitumia. Nikajaribu kumuuliza ni nini? Akashindwa kabisa kuniambia, ila ni kama akaniaga kuwa anaondoka, anaweza asirudi tena. Akawa ni kama mtu aliyejawa na hukumu. Nafikiri ni kwa vile nilivyokuwa nimemueleza maisha machafu niliyoishi nyuma na kumwambia nimeamua kubadilika kabisa. Sitakaa nikarudia hata pombe. Sasa nafikiri dhamira ilikuwa ikimsuta kuja kunirudisha kule.” “Pengine!” Tunda akaafiki.

“Kosa nililofanya, nikumlilia. Nilikuwa nasikia kuchanganyikiwa, ile kuhisi kama atakuja kuondoka aniache tena! Narudi kwa nani! Naishije bila yeye! Tulikuja kuwa tukipatana sana. Aliishi na mimi akijua ni nini anifanyie na kwa wakati gani. Hatukuwa tukibishana. Yaani alikuwa akinipenda na kunidekeza. Simu kila wakati kitu ambacho nahisi aliambiwa kuwa mimi ni mpweke, nahitaji mtu maishani.”

“Sasa nahisi aliingia kwenye mahusiano ya wizi akiwa amefundishwa ni nini anifanyie kwa vile huyo mtu alivyokuwa akinifahamu. Nakwambia alikuwa mtu sahihi. Hakosei kwa lolote. Kwa hiyo ikatusaidia kujenga penzi la kweli kwa haraka, yeye mwenyewe akanasa vibaya sana.” “Na wewe Maya unapendeka.” Maya akacheka kwa unyonge.

“Turudi kwenye kutaka kuondoka kwake.” “Ehe!” “Basi. Nilikuwa sipo tayari kumpoteza. Hapo ukumbuke nilikuwa nimeacha madawa, na pombe. Sina rafiki. Wale rafiki wote wa zamani nilishachana nao. Na wao kama ajabu hivi, wakaacha kabisa kunitafuta. Na mimi nikashukuru Mungu. Nikawa napata muda na Andy wangu.” Tunda akacheka baada ya Maya kuropoka.

Maya akagundua ameropoka jina, akacheka kwa unyonge akainama kwa muda kisha akaendelea. “Na kipindi hicho ndio Papa naye alikuwa amezidiwa. Akili za Nana zipo kwa Papa tu. Net yupo Tanzania. Kwa hiyo yeye ndio alikuwa amebaki kimbilio langu. Papa akizidiwa, basi yeye anakuwepo kunibembeleza na kuwa na mimi.”

“Nikamlilia sana na kumsihi sana asiondoke tufanye kila namna tuwe wote. Nikamwambia kama inamlazimu kuondoka, basi tuondoke wote. Asiniache. Aondoke na mimi tukaanze naye maisha. Nikashangaa analia. Alilia Andy! Mpaka nikashangaa. Aliniambia wazi kabisa, hajawahi kupata upendo mkubwa wa kiasi kile, na anaumia sana. Nikamuuliza unaumia nini! Sasa mimi mawazo yakawa kuwa anaumia kwa kutengana! Nikamwambia kama shida ni pesa, mimi nitamsaidia mpaka atakapopata kazi ya maana.” “Kwani hakuwa na kazi?” Tunda akauliza.

“Ndio kilichokuwa kikinishangaza Tunda. Alikuwa anaishi pazuri. Gari nzuri. Kuvaa vizuri, lakini hana kazi yakueleweka. Ukimuuliza unafanya kazi gani au biashara gani, hana jibu la maana. Mara aniambie anauza hisa online. Na kweli, biashara ya hisa huwa ina pesa kama ukiipatia. Lakini Tunda, ilikuwa hata ukimuuliza tena juu ya hiyo biashara napo akawa hana majibu ya kueleweka. Ni kama mtu aliyeambiwa aniambie tu hivyo ili kuniridhisha au kunitoa wasiwasi wa kwa nini yupo tu siku nzima. Maana alikuwa na muda wakutosha sana na mimi tofauti na mafanikio yake.” “Unamaanisha nini?”  Akauliza Tunda.

“Wote tunajua utajiri una gharama Tunda. Wewe si unamuona Net? Japokuwa anakupenda na angetamani kuwa hapa na wewe, hawezi. Kazi zinamfunga sana. Na ndio maana wakati wote anashukuru kwa kumvumilia. Sijui kama unanielewa?” “Hapo nakuelewa.” Tunda akakubali. “Huwezi kuwa na pesa nyingi kama huzitafuti kwa bidii! Labda uwe unapewa kama Vic anavyotunzwa na wazazi wake tu.” “Kwani hafanyi kazi?” “Hana anachofanya. Ila amesoma. Ukimuona na kumsikiliza, ana mipango mingi mizuri, lakini hajui kuitekeleza.”

“Anajitangazia kuwa anafanya kazi kwenye kampuni ya wazazi wake, lakini kutwa yupo mtaani na mitandaoni akijinadi kwa hili na lile. Kila kitu kwake ni tukio la mtandaoni. Maisha yake yote yapo mtandaoni. Kuanzia asubuhi mpaka usiku. Na watu wanamfuatilia kwa sababu ya vitu vizuri anavyovionyesha. Nitakuja kukuonyesha.” “Wala sitaki. Sina huo muda mimi.”  Hilo likamgusa sana Maya.

“Na mimi nitakuiga Tunda.” Wakacheka. “Sasa ndio turudi kwa Andy, akaonyesha utajiri mkubwa, lakini yupo tu. Nafikiri ndio maana akaja au akapewa sasa hilo wazo la kunidanganya kuwa anaingiza pesa popote alipo, na muda wowote. Na si unajua ni biashara ambayo ukielewa huhitaji kuwa mtandaoni kila wakati! Ukishauza asubuhi au usiku, basi. Nikujua wakati gani ni mwafaka wakuingia sokoni, ukiuza pesa yako inaingia bila shida. Lakini haya ninayokwambia hata yeye mwenyewe hakuwa akiyajua kwa undani hivi kama mimi ambaye hata hiyo biashara sifanyi.” “Wewe umejuaje?” Maya akacheka.

“Unafikiri kwa nini kina Cote wamedumu na utajiri kwa miaka mingi? Ni moja ya kitega uchumi cha kina Cote. Mumeo ndio bingwa wa hiyo. Alitoa kwa babu. Na wazazi wake Vic pia walirithi kutoka kwa wazazi wao ambao walikuwa marafiki wakaribu sana wa Papa na Nana. Ndio maana nahisi alikuwa ni mtu wa Vic. Aliyemtafuta maalumu kwa kazi moja tu ya kuniangamiza.” “Jamani!” “Kwa kuwa nilitulia sana Tunda. Sana. Na yeye akaja kama kijana mtulivu na wamaana. Mzuri. Ungetamani anioe tu. Kwa hiyo moja kwa moja mimi ndio ningekuwa mrithi wa Nana, kitu ambacho Vic asingekubali kabisa.”

Anyway, nikaanza kumuona anabadilika. Hana raha. Kama anayetaka kuniambia kitu lakini hawezi. Ndipo akaanza ulevi sasa kama ambaye yupo na jambo zito linalomfunga. Pombe ikawa ndio silaha ya kunikwepa. Hata mchana unamkuta amelewa. Ukumbuke hapo mimi nilikuwa sitakiwi kuonja hata wine. Kileo chochote kile siruhusiwi hata kukiweka mdomoni.”

“Mambo yakabadilika. Ukimtafuta, unamkuta club amelewa na hataki kuondoka. Kumbuka nilikuwa nampenda Tunda. Sikuwa naweza kumuacha kwenye ile hali pale. Akionekana ana jambo linalomuumiza, wakati mimi ndio alikuwa faraja yangu! Nikawa nakaa naye huku nikimsihi nimrudishe nyumbani asiendeshe akiwa amelewa. Mwanzoni nikafanikiwa kuwa nikimrudisha akiwa amelewa, mimi sinywi. Namrudisha mpaka kwake. Nikihakikisha amelala, ndio na mimi naondoka.”

“Kukutana kwetu sasa kukageuka. Sio tena nyumbani kwake kwenye makochi tukikumbatiana. Andy akaanza maisha yakuwa club. Usiku kucha na hataki kuongea. Ukimuuliza anakwambia kila kitu kitakuwa sawa tu. Lakini hapakuwa na mabadiliko. Haikuchukua muda na mimi nikaanza kunywa kidogo wakati nikimsubiria yeye turudi nyumbani. Nikaanza tena pombe, napo haikuchukua muda, nikarudia madawa kabisa.” “Sas..” Tunda akataka kuuliza.

“Subiri kwanza Tunda. Wewe jiulize tu. Tulikuwa mimi na yule kijana tu. Nani alikuwa na uwezo wa kuingia chumbani kwake, bafuni, kutufuata kwenye gari na kutupiga picha na kutuchukua video?” “Lakini kweli! Labda rafiki zake?” Tunda akatoa wazo.

“Na mimi ningedhani hivyo Tunda. Andy hakuwa mzawa wa Norfolk. Alikuwa mgeni kabisa. Watu walikuwa hawamfahamu. Mimi aliniambia amehamia hapa makusudi kuanza maisha mapya. Hakuwa na rafiki na aliniambia hakuwa akimfahamu mtu yeyote kwenye huu mji ila mimi tu. Na aligoma kabisa kutengeneza marafiki.” “Maya!” Tunda akazidi kushangaa.

“Nikikwambia alikuwa na muda na mimi, niamini alikuwa na muda na mimi. Sikuwahi hata kumuona akisalimiana na mtu. Akili na mawazo yake yalikuwa kwangu tu. Unafikiri kwa nini nilichanganyikiwa aliponiambia anaondoka au kwa nini nilimleta yeye kwa Papa na si wanaume wengine?” Maya akauliza huku machozi yakimtoka.

“Kwa kuwa aliniaminisha mimi ndio mtu wa pekee na kitu cha thamani kilichotokea kwenye maisha yake bila hata ya yeye mwenyewe kutarajia! Andy alinionyesha mapenzi Tunda, sitakaa nikasahau. Ndio maana nikimfikiria sasa hivi ndio naona kuna kitu hakikuwa sawa. Kwa kuwa alianza kiusanii kabisa, lakini akaja kukolea haswa.” Akajifuta machozi.

“Tulipokuwa tumefika na Andy, ni ilikuwa heri umfanyie yeye kitu ila si mimi. Alikuwa tayari kunifanyia kila kitu ili tu kunifurahisha. Na si ya kutumwa. Ungemuona akifanya kutoka moyoni. Wengi waliokuwa wakinifanyia uchafu na kunichukua video na kunipiga picha walifanya  kwa sababu maalumu. Wengine ilikuwa kama ulinzi wa kuniweka kwao. Ili nisiwaache. Niendelee kuwa nao tu. Na wengine pesa. Kwa hiyo ikitokea kama mimi siwapi pesa wanazotaka, wanaziuza zile picha au video zangu za ngono magazetini au kwa watu kama Vic. Na walikuwa wakiziuza kwa pesa nyingi sana.” “Maya!”

“Kweli Tunda! Nani asiyependa kununu gazeti lenye habari nzito za kina Cote? Kwanza walikuwa wakizitafuta picha zangu za ngono ili kuuza magazeti yao.  Na kwa upande wa mahusiano, ilikuwa nikiwaacha, wakiomba niwarudie, nikikataa hapo ndipo walikuwa wananitoa mitandaoni wakinichafua kama kunikomoa” “Pole Maya.” Tunda akamuhurumia.

“Lakini yeye Andy ilikuwa tofauti. Siku ya kwanza nimelewa Club, alihangaika sana kunitoa pale bila watu kuniona na kunipiga picha. Alimuomba baunsa wa pale wanitoe mlango wa nyuma. Na akamlipa pesa nyingi tu kuhakikisha sionekaniki na mtu. Akanibeba mpaka kwake. Maana aliniacha mezani akaenda kucheza draft. Akapata mtu wakushindana naye, mimi huku nyuma nikaanza kunywa. Kuja kurudi kuniangalia, ndio akanikuta nimelewa. Aliumia sana.”

“Kesho yake akaniomba msamaha wakunirudisha club, na akaniapia hatutarudi tena club. Na akaniambia atabadilika, na atanisaidia niache pombe. Tulirudia maisha ya kukaa ndani tu. Sasa kwa shida yote ile aliyofanya, kwa nini anichafue tena!?” “Kweli hapo kuna utata!” Hata Tunda akaafikiana naye. “Halafu Tunda, turudi kwenye maisha yake na ile nyumba. Unakumbuka nilikwambia siku ya kwanza tulifika vitu vingi kwenye ile nyumba niligundua ni vipya!” “Nakumbuka.” Tunda akaitika.

“Halafu Tunda, nyumba aliyokuwa akiishi mtu kwa muda mrefu au kama ni yake, inajulikana tu. Kuna milango alikuwa hawezi hata kufungua. Hilo moja. Halafu mtu tajiri, au aliyezaliwa kwenye utajiri, kuna vitu ambavyo anajua tu. Yaani hawezi kubabaika. Ule ustaarabu unakuwa sio wakujifunza, amezaliwa kwenye hayo maisha anajua. Lakini yule kijana alikuwa mshamba kabisa. Vitu vingine mpaka nilikuwa nikimshangaa vile ambavyo asivyo na uelewa navyo au anavyobabaishwa navyo!” “Inakuwa ni kama mtu aliyehamishiwa sehemu au kwenye maisha mageni kabisa kwake?”  Tunda akamuuliza akiwa kama amepata picha ya nini anachomaanisha Maya. “Hapo umenielewa Tunda. Inakuwa ni kama alilipwa kuishi yale maisha. Wakati mwingine alikuwa mpaka anachanganywa na aina ya saa mpya ambayo anakuwa amevaa yeye mwenyewe akiniambia amejinunulia!” Tunda akacheka.

“Sikudanganyi Tunda!” “Labda alikuwa analetewa na huyo Vic.” “Sasa hapo ndio umekuja kwenye kile ninachotaka kukuhakikishia kuwa ni Vic tu. Yule kijana alikuwa akivaa kutokana na pesa ya Vic, ambayo ni kiwango cha juu sana. Hapo Vic alifanya bila kufikiria. Kwa kuwa Vic ni wa viwango vya juu sana. Hajui vitu vyenye thamani ya chini na kwa kuwa hana akili ya kufikiria kabisa. Vic ni mjinga haswa. Sasa ndio maana alishindwa hata kutafuta vitu angalau vya daraja la pili tu, akashindwa kufikiria hapo. Akawa anamnunulia vitu vya thamani sana na kumpa akidhani na yeye Andy atafikiria kama yeye, kumbe Andy hajawahi hata kufikiria kuvaa saa za mapesa yote hayo. Ndio maana alikuwa yeye mwenyewe Andy anashituka. Kwa kuwa hajazoea.” Tunda akazidi kucheka.

“Sasa nahisi aliponipenda, pale mwanzo kabisa nilipomsikia akiongea na simu, nahisi alikuwa akimkatalia Vic asinifanyie mambo mabaya. Ndio Vic akamshawishi labda kwa kumtisha.” Maya akafikiria kidogo. “Unajua kuna kitu kimoja kikubwa sana ambacho Vic amenipita nacho, Tunda?” “Nini?” “Kwa kina Vic, Vic ni kama mboni ya jicho. Akili na mawazo ya wazazi wake Vic, vipo kwa Vic wakati wote. Anajaliwa, na kulindwa sana na wazazi wake. Mtu kama huyo hawezi kuangamia kirahisi. Hata katika ujinga wake, mama yake anamuunga mkono na kumsaidia ili afanikiwe. Wakati mimi ni kinyume.” Akaanza kulia tena.

“Usilie Maya wangu. Sasa hivi mimi nipo.” “Lakini imeniharibia Tunda. Imeniharibia sana. Siaminiki!” “Upande gani? Mbona sasa hivi unakazi nzuri! Nana amekuamini!” “Kumbuka mimi ni Cote, Tunda. Sijawahi kuwa na shida na pesa. Sasa hivi nafanya kazi ili tu kuonyesha uma ninaweza na kuwaaminisha nimebadilika. Lakini sina shida mimi, Tunda. Naweza nikaishi maisha yangu yote bila kufanya kazi na nikawa sawa tu.” Maya akaendelea.

“Papa alipofariki, japokuwa Net ni mrithi wa Cote, binafsi nina share zangu. Naweza nikaamuru pesa iwe inaingia tu kila week kwenye akaunti yangu, nisifanye kazi na nikaishi vizuri tu.” “Na madeni yako?” Maya akacheka na kuanza kulia tena. “Nakaribia kumaliza Tunda. Naomba usinikumbushe! Nilikuwa nadaiwa mamilioni ya pesa.” “Haya nyamaza basi tuzungumze.” Kakanyamaza.

“Sasa kama Net na Nana wanakuamini, unataka nani akuamini?” “Nikikwambia utamwambia Net. Halafu Net anaweza kuchanganyikiwa kabisa.” Tunda akakunja uso na kukaa. “Ni nani?” Maya akamwangalia kwa muda. “Mmmmhh! Nooooooo! No no nooo.” Akakataa mpaka akasimama kabisa. Tunda akaanza kucheka. “Ni nani?” “Sikwambii ila ujue historia yangu ya zamani inaniharibia sana Tunda. Siaminiki.” Tunda akafikiria kwa haraka.

“Nisikilize Maya. Mungu amekupa nafasi ya pili, itumie vizuri.” “Mimi ni tofauti na wewe Tunda. Nilishapewa nafazi zaidi ya 5, na zote nikaziharibu vibaya sana. Nani ataamini sasa hivi nitabadilika? Wanajua mimi ni bomu tu, ambalo wakati wowote naweza kulipuka.”

“Nisikilize Maya. Acha kulia na urudi hapa ukae.” Akarudi kukaa. “Wape watu muda na sababu ya kukuamini. Na wewe kusudia kutorudi huko tena.” “Nimekusudia Tunda, lakini naogopa. Sijui litakalonipata tena.” Akaanza kulia tena. “Nilipomaliza chuo, nilikusudia kubadilika. Huwezi amini, mimi Maya, nilitulia mpaka nikafikia kipindi cha kutaka kuolewa niwe mke wa mtu.” Tunda akaanza kucheka. “Usinicheke bwana!”  Kakaendelea kulia.

“Mimi sijui kwa nini! Nakuamini Maya. Naamini ukipata mwanaume mtulivu na akakupenda kwa dhati vile ulivyo, unaweza kabisa kuwa mke mzuri na ukaweza kumfanya mwanaume kuwa na utulivu.” “Kweli Tunda?” “Kabisa. Unaweza. Umejawa upendo na ni mkarimu sana. Na mimi nipo na wewe Maya. Siwezi kuruhusu Vic akarudia michezo yake, kama anahusika. Na siwezi kukuacha mpweke.” Akamuona anacheka huku anafuta machozi.

“Usilie. Ukumbuke mimi nipo na wewe katika kila jambo. Ni vile sasa hivi bado ni mdhaifu tu na ninamuhofia Cote. Sitaki chochote kitokee. Lakini nikijifungua salama, nimemwambia hata Net. Tutakuwa na sisi na siku yetu yakutoka.”  “Kweli Tunda?” “Kabisa! Hee! Wewe si mfungwa, na ninaamini kuna njia nyingi tu na sehemu nyingi tu unaweza kufurahia mbali na club na hao marafiki wanaotaka kukutumia tu. Wajinga kabisa.” Tunda akachukia kabisa. Alikumbushwa na yeye vile watu walivyokuwa wakimtumia kwa manufaa yao.

“Niombee Mungu nijifungue salama na Cote akue salama. Tutapanga. Na tutakuwa tunakwenda sehemu nzuri, sahihi ili tu kufurahia. Na ninakuahidi kukulinda. Usiogope kuanguka tena. Ila ujifunze kuomba kama kaka yako. Net anaomba ile ya kupiga magoti. Wewe unakuwa na muda wa kumuomba Mungu?” “Hata kidogo. Nikiamka tu nakimbilia kuangalia saa kujua kama Net amenipisha hapa, na mimi nije.”  Tunda akaanza kucheka.

Akazungumza naye kwa kumfariji mpaka akaweza kwenda kazini akiwa amechangamka, japo hakuwa amemwambia ni nini kinamsumbua! Na Tunda akapata shauku yakutaka kujua “Ni nani anayesumbua kichwa cha Maya, akimtaka amwamini lakini ameshindwa!” Tunda akabakiwa na hilo swali baada ya kuunganisha malalamiko yote ya Maya, akajua kuna mtu ameanza kumsumbua kichwa.

“Alirudia vipi madawa!” Hilo nalo likaibuka kichwani kwa Tunda. Maya aliishia kumwambia Andy alimuahidi hawatarudi tena Club na wala kunywa pombe. “Nini kilitokea tena? Ni kweli Andy alionyesha kumlinda Maya. Nani alikuwa na uwezo wa kuingia ndani kwa Andy na kuwapiga picha wakiwa wamelewa? Ni kweli Vic anakihitaji hiki cheo cha bibi Cote! Kama alikwenda umbali wote huo wa kumuharibia Maya kiasi hicho, mimi je?” Tunda akabakiwa na hayo maswali akiyatafakari baada ya Maya kuondoka. Akaamua kuyapa muda yaje yajijibu au akipata tena muda kama wa siku hiyo na Maya basi amuulize ambayo yatakuwa hayajajibika.

Mkasa wa Kwenye Kutafuta Chakula Cha Harusi.

M

aya alikwenda kazini asubuhi kama kawaida na bibi yao na Net ambaye alishaondoka mapema sana alfajiri ya siku hiyo. Carter alishaandaa usafiri wa kumpeleka Tunda kwenye hayo mahoteli ambako ilikuwa wakutane na Gino pia hukohuko ili amsaidie kuonja hivyo vyakula kisha amsaidie kufanya maamuzi.

Tunda alipofika kwenye hoteli ya kwanza, akakuta mpaka Net anamsubiria. Akafurahi sana kuwaona pale. Akaanza kucheka. “Sikutegemea kuwakuta hapa na nyinyi!” Akimaanisha bibi Cote na Net. Akamkumbatia Maya. Maya akamtania kidogo, akamsogelea bibi Cote, akamtania kidogo, ndipo akamsogelea Net, akambusu.  “Nimeona tu nije. Vipi wewe na Cote?” “Tupo sawa. Nilikuwa na watu wa nguo nyumbani, karibu siku nzima. Anasema itabidi kuwa makini na vipimo vya nguo. Ameangalia ukuaji wake kwa kila week, anasema ni mtoto anayekuwa haraka. Inabidi aongeze umakini kwenye hilo gauni. Tunaweza kufika siku yenyewe, gauni likawa halitoshi. Mwanao amekazana kukua kama uyoga!” Wote wakacheka. Net akapiga magoti na kumbusu tumbo.

“Asante Nana kwa kuja. Nimefurahi!” Tunda akamshukuru bibi Cote na sura iliyojaa furaha tele. Bibi Cote akacheka. “Unafikiri kuna ambaye angejali chakula ambacho ungechagua?” Tunda akacheka. “Lakini kwa sasa mimi sio mtu mzuri wa kutoa uamuzi mzuri juu ya chakula. Bado kuna vyakula kama samaki siwezi kuvila kabisa. Sikutaka kuwanywesha wote uji wa ulezi.” Wote wakacheka. Bado Net alikuwa amepiga goti moja huku akimpapasa Tunda. “Mimi ningekunywa tu.” Maya akadakia, wote wakacheka.

Net akasimama na kuangalia saa. “Gino yuko wapi?” “Amenipigia simu wakati tupo njiani. Ameniambia atachelewa dakika kama 5 zaidi.” Akamuona Net amekunja uso, akaangalia tena saa. “Kama 5 au dakika 5? Hatuwezi kumsubiria yeye. Tuna..” Tunda akamshika mkono taratibu maana alishaanza kugomba kwa sauti. Net akamwangalia na kutulia kidogo.

“Hatuwezi kumsubiria, Tunda!” “Naomba tumpe hizo dakika 5.” Net akaangalia saa. “Pole na kazi.” Ikabidi amtoe akili na macho pale kwenye saa. “Asante Tunda. Lakini Gino anatakiwa awe akisema sawa kwa jambo awe amezingatia muda. Kama anashindwa au anakuwa na majukumu mengine, anasema tuweke muda mwingine. Inakuwa ni kama sisi hatuna kitu cha muhimu chakufanya, yeye ndio anakuwa na majukumu muhimu zaidi yetu! Tunaacha shuguli, wote tupo hapa. Kumsubiri yeye!” Net aliongea kwa ukali.

Akatoka muhudumu wa hapo, akawasogelea  kina Cote pale walipokuwa wamesimama akiwa na tabasamu la heshima. “Bado mnasubiriana?” Akauliza kiustarabu sana. “Call Gino. Now!” Akamgeukia kijana aliyekuwa amesimama pembeni kama mlinzi/bodyguard. Mbali kidogo na wao. Net akampa hiyo amri akiwa amekasirika kabisa.

“Naomba niangalie Net.” Tunda akamuita kwa upole. Net akamgeukia. “Naomba tufanye hivi, kwa kuwa Gino aliniomba, nikamruhusu. Na kwa kuwa sisi tumeshafika hapa, nashauri twende tukaanze sisi kuonja hicho chakula. Nitawaambia wamuwekee Gino chakwake. Kisha twende kwenye hoteli ya pili. Tutafanya hivyo hivyo. Kesho nitawapigia simu kutoa maamuzi ya chakula kipi tutataka kwenye harusi yetu baada ya sisi wote kuonja na kuchagua. Ni sawa?” Tunda akatoa ushauri akiwa ametulia na sauti iliyotulia ili kutuliza ile hali ya wasiwasi pale.

“Lakini hii ni zaidi ya dakika tano sasa!” Tunda akamshika mkono kama kumtaka atulie. “Pole na samahani mpenzi wangu. Naona sisi tuanze ili asiwacheleweshe zaidi. Kwani unarudi kazini?” “Hapana. Tunarudi wote nyumbani.” Tunda akamgeukia bibi Cote. “Samahani Nana.” “Gino anajua hakupaswa kuchelewa hata kwako. Anafanya hivi, akijua ni wewe tu na Maya, sidhani kama anajua kama Net na mimi tutakuwepo hapa.” Bibi Cote akaongeza. “Pole Nana na samahani.” Tunda akaendelea kuomba msamaha ili kutulie.

“Naona tufuate ushauri wako tu. Hatuwezi sisi ndio tukawa tukimsubiri Gino hapa! Wote tutaonekana hovyo.” Walishangaa Maya amenyamaza kimya hata hajaongeza neno. “Sawa Nana. Twendeni.” Tunda akamwambia yule muhudumu, wapo tayari, akaongoza njia. Tunda na Net wakamfuata nyuma. Net akamvuta karibu, akamuwekea mkono begani akambusu. “Umekuwa na siku ngumu?” Tunda akauliza kwa upendo tu. Net akafikiria kidogo.

Akaanza tena kama ambaye alikatishwa kutoa dukuduku lake. “Sipendi watu wasio heshimu muda, Tunda. Na kila anayefanya kazi na mimi analijua hilo. Kama alivyosema Nana, Gino hakutegemea sisi kuwepo. Ndio maana nimekasirika. Lakini sio kazini. Kazini pako sawa.” Net akaendelea kugomba, Tunda akanyamaza kabisa, hakujibu tena kitu. Wakaendelea kuelekea kule walipoelekezwa kuingia ili waletewe hicho chakula.

Lakini tayari mudi ya Tunda na yeye ikawa imeshabadilika. Akajikuta hatamani kabisa kuwepo pale tena. Akabadilika mpaka usoni. Walipelekwa kwenye hicho chumba walichoandaliwa vizuri sana. Kwa kuwa walikuwa ni kina Cote, kila kitu kikawa tofauti na huduma pia. Ulinzi ukawekwa mpaka jikoni. Chakula kikaonjwa na kusimamiwa wakati kinapelekwa mezani walipokuwepo.

Tunda na Maya wakawa kimya. Tunda akaendelea kupapasa tumbo lake taratibu akiwa amejiinamia. Maya macho kwenye simu yake. Wakabaki Net na bibi yake wamekaa kimya wakiangaliana. Pakatulia kwa muda.  Wakaingia wahudumu na kuanza kuwahudumia. Tunda kimya. Zilishapita dakika 15. Akamuona Net anaangalia tena saa yake ya mkononi, lakini akanyamaza. Na yeye akanyamaza. Aliyetumuita kumpigia Gino alishajibu kuwa Gino hakupokea simu.

Wakati wanakula Gino akaingia pale kwenye kile chumba kama aliyekuwa anakimbia. Alishituka, akakaribia kama kurudi alikotoka. Wote wakanyanyua uso kumtizama. Gino alibaki amesimama palepale mlangoni asijue aseme nini. Tunda akarudisha uso wake kwenye sahani, kimya. Maya akamtizama kaka yake na bibi yake, na yeye akainamia sahani yake.

“Nilijua habari ya kuja hapa, nikiwa nimeshakubali kazi ya watu. Lakini Mrs. Cote aliponiomba nije hapa ili nimsaidie kufanya maamuzi, nilimweleza kila kitu. Kuwa nitakuwa na kazi kwa muda huo. Ila nikamwambia ninaweza kuja kwa kuchelewa kidogo kama itakuwa sawa. Akakubali kwa makubaliano ya hata nikichelewa ni sawa, ila tu nije nijaribu chakula, halafu tutaamua pamoja hata kesho. Sikujua kama...” Gino akasita.  Maana alianza kujieleza bila hata kuulizwa. “Samahanini sana.” Mwishoe Gino akaona aombe tu msamaha. Kimya. Net na bibi yake wakainamia sahani zao na wao kuendelea kula bila hata kumjibu.

Gino akabaki amesimama akiwa ameshakuwa mwekundu haswa kwa hofu. “Njoo ukae hapa.” Ikabidi Maya amkaribishe tu, maana aliachwa akiwa amesimama. Gino akavuta kiti na kukaa kwa tahadhari na hofu pembeni ya Tunda. Kwa hiyo akawa katikati ya Tunda na Maya. “Samahani sana Tunda.” Akamnong’oneza Tunda, lakini walisikia. Tunda akanyanyua kichwa akamtizama kwa tabasamu. “Ulimaliza kazi yako lakini?” Akamuuliza taratibu tu. “Yeah. Thanks.” Gino akajibu, muhudumu akaanza kumuhudumia na yeye.

Kilipoletwa chakula cha aina ya baharini, Tunda akaomba yeye asipewe. Akamnong’oneza Net. “Nitarudi baada ya muda mfupi.” “Okay. Unataka nikusindikize?” “Hapana. Nitakuwa sawa tu, asante.” Tunda akatoka akaenda kukaa chooni kwa muda. Alijaribu kutulia lakini akajikuta kitu kimemkaba kooni, anashindwa hata kutulia. Hakujua kama ni hasira au nini! Alitamani kama kuondoka kabisa pale, lakini akakukumbuka yeye ndio mwenye hiyo shuguli nzima ya kuchagua vyakula. Hawezi kuzira.

Gafla akahisi uchovu mwili mzima, anatamani kama alale pale. Hamu ya kila kitu ikamuisha. Ule mukari wa sherehe ukakata gafla, akaanza kuona anajisumbua tu. Harusi tena ya nini! Akakumbuka walishafunga ndoa Tanzania. Sasa usumbufu wote huo ni wa nini! Akaanza kujiuliza Tunda. Alikaa hapo chooni, mwishoe akaamua kutoka asije akachelewa na yeye.

Akatoka kwa kujivuta wazi alionekana ule uchangamfu aliokuja nao umepotea kabisa. Akawa anajivuta taratibu kutoka, akamkuta Net akimfuata. “Are you okay!?” “Yeah. Nipo sawa.” Akajibu Tunda na kumuonyesha warudi wakamalize. Akampita kidogo. “Subiri kwanza Tunda.” Tunda akageuka. “Mbona unaondoka wakati nimekufuata wewe!?” “Sikujua kama umenifuata mimi. Nilijua na wewe unaelekea restroom. Na pia nilikuwa naharakisha, sikutaka kuendelea kuwachelewesha zaidi, ndio maana nilikuwa nikiwahi kurudi ndani nikihisi mtakuwa mmeshamaliza vyakula vya baharini. Sitaki kujichefua.” Tunda akajibu taratibu tu.

“Umependa mlo wa kwanza?” Net akauliza. “Siyo mbaya.” Akajibu na kutulia. Kimya wakabaki wakiangaliana. “Nisawa nikirudi kule? Nataka nimalize hili zoezi la chakula, nikapumzike. Najihisi nimechoka sana.” “Pole, Carter aliniambia ulikuwa na wageni karibu siku nzima na fundi wa gauni naye akachukua muda mrefu. Ndio maana niliona tuwahi ukapumzike.” Tunda kimya. “Basi twende.” Tunda akageuka kuondoka bila kuongeza neno wala tabasamu. Ule uchangamfu ulimwisha kabisa usoni. Sio kama alivyokuja na tabasamu na cheko juu. Net akamfuata nyuma, wakarudi kule walipokuwa wakila wengine.

Walimaliza pale, wakaamua kwenda hoteli ya pili. “Umekuja na usafiri Gino?” Tunda akamuuliza taratibu wakati wanatoka pale. Gino akababaika kidogo. “Tunaweza kuongozana tu.” Tunda akamkaribisha kwenye gari iliyomleta yeye. “Asante.” Moja kwa moja Gino akakubali kwa kushukuru. Ndipo akajua hakuwa na usafiri. Bibi cote alikuwa na ulinzi wake na gari aliyokuwa akiendeshwa, alishaondoka na Maya.

“Nilifikiri tutaongozana!”  Akaongea Net kwa kulalamika kidogo ila kwa lugha ya kiswahili. “Nilikuja na dereva. Unafikiri nimruhusu arudi nyumbani?” Tunda akauliza kiustarabu tu. “Utakavyoamua wewe. Lakini mimi nipo hapa kwa ajili yako. Na tukimaliza tunarudi wote nyumbani.” “Basi ngoja nimruhusu arudi nyumbani.” Tunda akataka kuondoka kumfuata dereva nje alipokuwa akimsubiri.  

 “Atampeleka Gino na kumshusha anapotaka. Leo usiku hapatapikwa nyumbani. Si Gino amekwambia?” “Ndiyo.” Wakatoka nje ya hiyo hoteli. Gari ya Net ikaletwa na muhudumu wa pale wa Valet, na dereva wa Tunda akasogeza gari baada yakumuona Tunda. Net akamfungulia Tunda mlango kwenye gari yake, akapanda, yeye akaenda kuzungumza na dereva huku Gino akimfuata nyuma.

Baada ya kuweka mambo sawa, akamuona Net anarudi. Alishavuta kiti nyuma na kujilaza kabisa. Akatulia, Net akaondoa gari. Kimya kwa muda. “Kesho ndio siku ya keki, si ndiyo?” Net ni kama akapata chakuvunja ukimya. “Ndiyo.” Tunda akajibu taratibu tu, tena kwa ufupi. Pakatulia. Tunda akajivuta zaidi kama anayemtaka asimuongeleshe zaidi. Net naye akanyamaza.

Walifika hoteli ya pili, walimkuta Gino alishafika. Hata hawakujua walifanyaje kufika kwa haraka vile. Kijana alikuja kuchukua gari ya Net mara tu walipofika karibu kabisa kwenye mlango hotelini. Net akaenda kumfungulia Tunda mlango. Akatoka kama amelazimishwa. Hata hakumwangalia Net, akamsogelea Gino. “Vipi kile chakula cha kwanza?” Tunda akamuuliza mara alipomfikia Gino wakati anamfungulia mlango wa kioo wa pili wakuingia ndani. “Kawaida. Tusubiri na cha hapa tuone.” Gino akajibu. Akasubiri Net aingie ndipo na yeye akafuata nyuma. Walimkuta bibi Cote na Maya walishafika.

Net akaangalia muda, waliwahi kama dakika 3. Muhudumu akawasogelea pale walipokuwa wamesimama. Wakasalimiana. “Sisi tupo tayari wakati wowote mtakapokuwa tayari. Maana Mrs Cote alitupa window ya nusu saa zaidi, lakini sisi tupo tayari hata sasa. Na kama mnahitaji kusubiriana, tunaweza kuwaonyesha sehemu ya kukaa.” Akawaambia yule muhudumu na tabasamu lililojaa heshima usoni. Net akamgeukia Tunda kama anayemuomba muongozo Tunda. “Nafikiri tupo tayari.” Tunda akajibu taratibu tu. Wakaelekezwa sehemu ya kwenda.

Safari hii kukawa kimya. Hakuna kutembea wakiwa wamekumbatiana tena wala mabusu. Tunda alijiweka pembeni kabisa, akishukuru Mungu jinsi yule dada alivyoongea vile kuwa alishawataarifu kuna uwezekano wa kuchelewa nusu saa. Kwa hiyo watoe nafasi ya hiyo nusu saa. Na wala Gino hakupitisha nusu saa.

Vilisikika visu na uma tu hapo ndani na muhudumu akiongea kila wanapowabadilishia chakula. Walikula mpaka ilipofika vyakula vya baharini, Tunda yeye akakataa asiwekewe, nakubaki amekaa palepale. Safari hii hakutoka. Wengine walikula hicho chakula. Wakaletewa na dessert tofauti tofauti wakiwa wamezipamba kiustadi ili kuvutia familia hiyo ya Cote. Wakala.

“Unaonaje Gino?” Akauliza bibi Cote baada ya kuomba muhudumu awapishe wabakie wao tu. Gino akatulia kwa muda kama anafikiria. “Labda kwa kuwa mimi ni mpishi, naomba niwe wa mwisho kutoa maoni yangu. Mrs Cote wewe umekionaje?” Akamrushia mpira Tunda. Wote wakamgeukia Tunda. “Bado sidhani kama mimi ni mtu sahihi wakutoa maamuzi ya chakula. Hapa nilipo nakaribia kutapika.” “Labla sababu ya samaki.” “Nafikiri. Wewe Nana umeonaje?” Tunda akamrudishia mpira bibi Cote.

Akafikiria kwa muda. “Sijui! Ni kama kuna kitu hakijakaa sawa! Lakini bado sijaweza kujua ni nini!” “Excactly!” Akadakia Gino. “Kuna kitu kinapungua.” Akaongeza Gino. “Ni nini Gino?” Akauliza Maya. “Ladha yake.” Akajibu Gino. “Labda tujue ni nini ili tuombe chenye nafuu kirekebishwe, vingine vitolewe kabisa. Nimependa upangwaji wa hawa.” Akaongea bibi Cote.

“Ila sio juisi. Juisi sijapenda hata moja.” Akaongeza Tunda. “Hata dessert sio nzuri.” Akaongeza Maya. “Kuku na samaki viko so so so...” Akashindwa jinsi yakueleza, bibi Cote. “Plain?” Akadakia Net kama aliyeuliza hivi na hana na yeye uhakika. “Yeah. Kuna viungo havijatimia. Vipo so plain! Yaani hakuna ladha inayoeleweka!” Bibi Cote akakubaliana na Net. “Basi naomba mnipe tena nafasi nyingine yakujaribu kutafuta watu wengine. Nimejifunza kutokana na kosa la leo. Safari hii nitakuwa makini na muda. Nitahakikisha nakubaliana nao muda ambao wote mtaweza kufika kwa wakati. Sio kama leo ambavyo nililazimishia ili Gino awepo.” Tunda aliongea kwa upole na unyenyekevu kisha akaendelea.

“Naomba mnisamehe kwa leo. Nilipanga kuwa flexible na muda sababu nilijua ni mimi tu na Gino. Hata Maya sikuwa na uhakika kama angekuja. Alinipigia simu kwenye saa nne asubuhi, akaniambia leo anakazi nyingi. Kwa hiyo sikujua kama hata yeye angefika. Kwa hiyo sikuwa na wasiwasi kwa kuwa nilishawaomba wapishi wote kuongeza muda zaidi. Yaani kutupa window ya kama nusu saa, nikiwaambia mtu ambaye nataka anishauri, yaani Gino, angeweza kuchelewa. Wakasema ni sawa. Ndio maana mimi sikuwa na wasiwasi tena. Kwa hiyo sio kosa la Gino. Tulikubaliana hivyo.” Tunda aliongea taratibu akionekana kuishiwa nguvu kabisa. Alikuwa kama mshitakiwa mbele ya hakimu.

“Mimi sikujua kama mlikubaliana hivyo!” Net akajaribu kujirudi, lakini akawa ameshachelewa. Alishamkera Tunda kuingilia kitu ambacho hata hakuuliza wakati yeye mwenyewe alimwambia amemuachia apange! Tunda alijaribu kumuomba msamaha mpaka na kumshika mkono ili tu atulie, lakini akaendelea kugomba! Alishamkera Tunda, hakuwa na hamu tena. Tunda akanyamaza tu.

“It’s okay Tunda. Nafikiri sisi tuliingilia, na tulitakiwa kuuliza kwanza.” Bibi Cote na yeye akaongeza. “Basi wakati mwingine nitajitahidi kufanya au kumshirikisha kwa karibu sana Maya ambaye anauelewa mzuri wa haya mambo ili awe ananishauri kisha kuwajulisha kile ambacho tutakubaliana na wahusika wa kila idara kabla hata ya siku yenyewe ya tukio. Kama ni kuonja au kuangalia tu. Ili mfahamu kinachoendelea hata kama hamtaweza kuhudhuria.” Kimya.

“Kwa mfano kesho, muda wa kuonja keki ni saa nane kamili mchana. Nimeshakubaliana nao, na nitampa Maya, namba yao ya simu. Na yeye kuhakikisha huo muda, na Gino aliniambia kesho atafika kwa wakati. Kwa hiyo kesho ni saa 8 mchana, ni uhakika bila kuchelewa.” Akamalizia Tunda kwa upole kama aliyekubali kujivua majukumu ambayo walimpa na kumthibitishia ameshindwa kuyafanya.

Hakuna ambaye hakumuona jinsi alivyobadilika. Maya naye alishabadilika tokea sehemu ya kwanza kaka yake alivyoanza kugomba. Wawili hao, Net na bibi yake wakajisuta nafsini kwao kwa zamu. Pakawa pametulia kama kila mtu akiwaza lake.

“Mimi naomba niwahi kurudi nyumbani. Sijisikii vizuri.” Akavunja ukimya Tunda. Tunda anayetoka hapo siye waliyemuona muda mfupi aliyewapokea kwa shangwe huku akiwaambia kwa wazi, amefurahi kuwaona. Alikuwa amejawa na furaha na nguvu. Huyu Tunda anayewaaga sasa hivi alikuwa amechoka gafla na hakuna tena tabasamu.

Net akasimama ili kumvutia kiti. Ile kusimama tu, akasikia kama chakula kinakaribia kutokea mdomoni na puani. Akatoka pale kwa haraka na kukimbilia chooni. Akaanza kutapika. Kwa mara ya kwanza tokea atue nchini hapo na mimba hiyo ambayo imeshatimiza week 36, Tunda akaanza kutapika. Akatapika tena na tena mpaka akapiga magoti hapo chooni. Akatapika mpaka akasikia nafuu.

Alipotoka chooni akamkuta bibi Cote na Maya wamesimama nje ya choo alichokuwepo. “Are you okay au tuite ambulance ikukimbize hospitalini?” Wakamuuliza wakionyesha wasiwasi. “Hapana. Nitakuwa sawa tu. Nilikuwa nikitapika hivi hivi wakati nilipokuwa Tanzania. Naona hii hali imenirudia. Nitakuwa sawa. Naona mimi nirudi tu nyumbani. Nahitaji kupumzika.” Net naye akaingia kwenye choo hicho cha kike.

“Vipi?” Akauliza Net. “Nipo sawa. Naomba nirudi nyumbani nikapumzike.” “Nilifikiri yule daktari alikupa dawa ya kuzuia kuta..” Kabla hajamaliza, Tunda akakimbilia tena chooni na kuanza kutapika tena. Net akamfuata chooni na kumshika mbavu kwa nguvu. Tunda akatapika tena na tena, mpaka akabakisha mate machungu. Akabaki akihangaika kutoa hayo mate mpaka na machozi. Mlio wa mateso akiteseka wakati akitapika, ulisikika na kutia wasiwasi wote waliokuwepo pale chooni.

Mwishoe wakatoka chooni. “Pole.” Maya akamuhurumia. Wazi alionekana ameingiwa na wasiwasi. “Asante. Lakini nipo sawa.” Tunda akasogea kwenye sinki kwenda kusafisha mdomo na uso. “Unauhakika au twende hospitalini?” “Sidhani kama kunatatizo. Nitakuwa sawa. Lakini nataka kurudi nyumbani.” Tunda akaweka msisitizo. Wakatoka hapo kurudi nyumbani.

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

Net alipofika tu karibu na mlango ili ashuke akamfungulie mlango, Tunda akajifungulia mwenyewe mlango na kutoka kwa haraka na kuanza kutapika tena. Carter akatoka kwa haraka akamsogelea Tunda pale alipokuwa ameinama akitapika. “Hey sweetheart?” Carter akamgusa mgongoni kwa kujali. Tunda akatapika mpaka akamaliza. “Nipo sawa.” Tunda akamjibu Carter huku akisimama maana alikuwa amepiga magoti. Net naye akasogea. “Nikupe nini?” Akauliza Carter. “Nipo sawa babu Carter. Usiwe na wasiwasi.” Tunda akampita Net, nakuingia ndani moja kwa moja chumbani kwao, chooni na kufunga mlango kwa ndani.

Net aliingia akikimbia mpaka chumbani kwao. Akamsikia akitapika chooni. Alipojaribu kufungua mlango, ukawa umefungwa. Akajua ndio hatakiwi ndani maana huo mlango haukuwahi kufungwa tangia Tunda anafika hapo. Akabaki akijaribu kusukuma kwa nguvu kidogo. Tunda akamaliza na kukaa hapohapo chini pembeni ya choo. Akamsikia akilia taratibu. Net akabaki amesimama nje. “Pole Tunda.” Hakujibu. Baada kama ya dakika 5 hivi, akaanza tena kutapika.

Safari hii hakukusikika kama anatoa tena kitu. Akahangaika hapo akitapika, mwishoe kimya. Akamsikia amekaa chini tena. “Naweza kukusaidia.” Akaongea Net kwa upole. Kimya kwa muda, akaona mlango unafunguliwa.

Tunda akatoa nguo zake hapo, akaingia bafuni kuoga huku akilia taratibu. Hakutumia muda mrefu bafuni, akatoka. Akavuta taulo lake, akaenda kujifungia ndani ya chumba chake chakuvalia. Akabadili nguo humo ndani, akatulia kidogo. Ndipo akatoka, moja kwa moja kitandani. Akajisogeza mwisho kabisa, kama asiyetaka hata ajali ya kuguswa. Akajifunika vizuri mpaka kichwani, kimya. Mungu akamsaidia, hapohapo akapitiwa na usingizi mzito kama aliyetoka kulima juani kwa muda mrefu, akapata kivuli, akalala. Alilala Tunda, wala asijue alipo na kinachoendelea ulimwenguni. Na kwa kuwa hakuwa na chakufanya mpaka saa nane mchana siku inayofuata. Alishajipangia kulala tu.

Asubuhi ya Kwenda kuonja Keki.

Tunda alipofungua macho, akamuona Net amekaa pembeni kabisa ya hicho chumba kwenye meza yake anayowekea kompyuta. Kwa kuwa wakati mwingine huwa anafanya kazi zake hapohapo nyumbani mpaka usiku sana. Kama hatafanya kazi zake hapo chumbani, basi kwenye ofisi yake ya hapohapo nyumbani.

Tunda alitulia kimya bila hata kujisogeza. Akamwangalia kwa muda kama anaye tafakari kitu. Net alionekana amezama kwenye anachofanya. Tunda akageuza macho kwenye saa ya ukutani. Ilishakuwa saa tano asubuhi. Akabaki kimya palepale kitandani bila hata kujigeuza. Kwa utulivu ule, Net akajua bado amelala akatuliza na yeye akili zake kwenye kitu anachofanya. Kwa asili Tunda alikuwa mtulivu sana. Kukaa kimya, kusingemsumbua. Akatulia kimya kwa dakika nyingi tu.

Ghafla Net akageuka kumtizama, macho yakagongana. “Nilijua bado umelala!” Akasimama kumsogelea pale kitandani, alipokaribia kitanda tu, na yeye Tunda akatoka hapo kitandani, akaelekea kilipo choo na sehemu ya kuogea. Net akamfuata nyuma. Tunda aliingia chooni moja kwa moja akafunga tena mlango. Alikaa humo kwa muda kidogo. Akatoka. Akamkuta Net anamsubiria nje ya choo.

“Umeamkaje?” “Najisikia vizuri. Hali ya kichefuchefu imeisha.” Akajibu huku akielekea kwenye sinki la kuoshea kinywa bila hata kumtizama usoni. “Gino amekutengenezea uji na ndizi tayari. Unataka nikuletee huku?” “Hapana. Nitakwenda kula mezani kama bado nitakuwa na muda. Lasivyo nitakuja kula nikirudi kutoka kwenye keki.” “Naona kama labda mambo ya kuonja chakula uache tu!” “Kama ndivyo hivyo mlivyoamua, ni sawa. Hamna shida.” Tunda akajibu kwa upole, lakini Net akahisi anaharibu zaidi.

“Sio kwamba ndivyo tulivyoamua. Wewe unaonaje?” “Kuhusu nini?” Tunda akauliza. “Kuhusu kuonja hivyo vyakula. Kwa sababu..” “Net, mimi nipo sawa na kila maamuzi mnayoamua. Nipo sawa. Na wazi sisi wote tunajua sipo kwenye nafasi ya kuchagua au kufanya chochote kigeni kwenu. Naona uamuzi mlio amua wa mimi kutoendelea ni mzuri.”

“Sio kwa kutokukuamini Tunda! Ni kwa sababu ya hali hiyo ya kutapika. Hatukutaka vyakula vingi tofauti tofauti vikutese kama jana! Lakini si vinginevyo.” “Sawa.” Ikabidi tu Tunda ahitimishe. Maana alishapata jibu kuwa ni jambo walilozungumza na bibi yake. Lakini ikawa kama imemuuma kwa namna nyingine. Akajua hawakufurahia kilichotokea jana yake. Hakuzungumza tena. Akasafisha meno na kuoga hapohapo bafuni ndipo akatoka kwenda kuvaa kwenye chumba chake. Safari hii akamuona Net naye amenyamaza.

Alitoka hapo kwenye chumba chake cha nguo na viatu kama mtu aliyevaa kutoka hapo ndani. Alijifunika vizuri, akavaa sweta zito kidogo na viatu vyepesi kidogo kama buti fupi za baridi lakini ndani vilikuwa kama vimetengenezwa maalumu kuleta joto. Net akabaki akimtizama. “Natoka kwenda kutembea. Nitarudi baadaye.” “Naweza kuja?” Akauliza Net kwa tahadhari. “Muda wa kwenda kuonja keki umekaribia. Na mimi nataka nitembee bila kujiwekea kipingamizi cha muda. Sitaki kukuchelewesha tena kama jana. Wewe endelea na ratiba zako tu. Mimi nahitaji kusafisha kifua na kichwa.” Tunda akajibu hivyo nakutoka.

Alijua Maya na bibi yake watakuwa kazini. Kwa muda ule hata Net alitakiwa awepo kazini. Kuwepo pale inamaana yupo kwa ajili yake kitu ambacho Tunda hakutaka. Hakutaka kabisa kuwa pale na Net. Bado ile hasira ya jana ilikuwepo na akamtibua zaidi kwenye kumvua madara ya kuonja keki! Tunda akaona atoke hapo.

Ms Emily akamuona akitoka chumbani. “Uji wako upo tayari.” “Nitakunywa nikirudi Emily, asante.” Yule mama akabaki akimtizama. “Upo sawa Tunda?”  Akamuuliza kwa upendo, Tunda akatingisha kichwa kukubali. Akajiona machozi yanaanza kutoka, akajifuta na kutoka hapo ndani akitembea kwa miguu tu.

Akiwa hana kitu tumboni. Kutapika kote siku iliyopita bila hata kunywa maji, hasira zikamfanya atembee parefu tu akiwaza hili na lile. Alijua lazima kuna mtu anamfuata kumlinda. Hakujali wala kugeuka nyuma, akaenda kukaa sehemu ya peke yake. Kwanza ilikuwa ni siku ya kazi, mida ile alijua watu wapo kazini, kwa hiyo akapata utulivu wakutosha. Pia hakutoka na simu, akatulia. Alikaa hapo kwa muda mrefu tu, zaidi ya masaa mawili. Baridi ikamtoa kwenye mawazo, akaona arudi tu nyumbani.

Mazito Mengine Kwa Tunda.

T

unda alianza kurudi nyumbani taratibu akijivuta. Hakujua kama alikwenda umbali mrefu vile! Sababu ya njaa akaanza kujisikia hata tumbo linamlemea. Akaanza kushindwa hata kunyanyua miguu. Akawa anaivuta taratibu. Akaangalia alipo na anapokwenda, akajua hatafika. Akasimama kabisa na kuanza kuangaza akitafuta mlinzi ambaye alijua yupo tu akimlinda. Akashangaa hata dakika tano hazijapita, dereva anakuja na gari. Akashukuru kuolewa na milionea. Japokuwa alimkera, lakini katika hilo akafurahia. Akajiambia atafia pazuri.

Bila maswali, likasimama pembeni yake, dereva akamfungulia mlango wa nyuma, akapanda. Hata yule dereva alijua wazi ni mlinzi pia. Akajiegemeza kitini, akavuta pumzi kwa nguvu akafunga macho huku akimpapasa mtoto wake. Tumbo lilikuwa ni kubwa haswa. Ghafla hali yakujiona amebeba mtoto mkubwa zaidi ikamjia, wakati alishakuwa akiambiwa na daktari, lakini hakuwa akiliona hilo. Siku hiyo ni kama ukweli ndio ulianza  kumwingia na kulemewa ghafla.

Akafikishwa mpaka mlangoni, akamkuta Carter pale nje chini ya ngazi kama aliyekuwa akimsubiria. Akamfungulia mlango na kumshika mkono wakati anashuka. “Nimechoka!” Tunda akamlalamikia Carter. “Unaonekana mpaka usoni kama upo dhaifu. Twende ukale ndipo ukalale.” Akamshika mkono wakati anapanda ngazi. 

 Vic Amvaa Tunda.

 Ile wanaingia tu ndani hawakujua hata Vic na msichana mwengine walitokea wapi, na wao wakaingia mpaka ndani kabisa wakati Carter akimsaidia Tunda kuvua sweta alilokuwa amevaa. “Nataka kuzungumza na wewe Tunda.” Wote wakageuka  kwa mshangao. Wakaingia ndani kabisa na kufunga mlango.  “Nataka tu kukuweka sawa.” Akaongeza Vic, mwenzie akiwa amesimama nyuma, pembeni kidogo ya Vic akimtizama Tunda na Vic kwa mbele. Carter akatoa lile sweta la Tunda kimya bila yakujibu.

     “Haitachukua muda mrefu.” Vic akaendelea kuweka msisitizo.  “Kwa kuwa umenikatalia kuzunguka humu ndani kwenye nyumba niliyokulia mimi, ukasema niwe naishia sebuleni, basi na sasa hivi nakwenda kukusubiria sebuleni. Utakapokuwa tayari, utanikuta sebuleni.” Bila kusubiri jibu, Vic akapitiliza sebuleni na mwenzie akamfuata. Tunda akavuta pumzi kwa nguvu. Bila yakujibu, akawafuata nyuma taratibu kwenda kuwasikiliza.

     Alipoingia tu Vic akaanza. “Nataka ujue hili, kabla hujafunga ndoa na Net. Siku ile nilikuja kuzungumza na wewe kiustarabu, naona hujazoea ustaarabu ukaanza ukorofi.” Tunda akakaa.  “Najua umekaa jela, na umeishi maisha yasiyofanana na haya, kwa hiyo hujui ni kitu gani cha kuongea na jinsi gani ya kukaribisha wageni kwenye nyumba kama hii.” Akaendelea Vic, Tunda akimwangalia tu.

     “Hata hivyo mimi sio mgeni hapa kama nilivyokwambia. Nilishaishi hapa tokea mtoto mpaka kipindi upo jela, mimi nililala na Net hapahapa. Kwenye chumba kile kile ulichonifukuza. Usiku mpaka asubuhi. Kama huamini muulize hata Carter anayejifanya kukupenda wewe na huyo Maya anayejifanya anakupenda na kukusifia. Hao wawili wote walikuwepo kasoro bibi yao alikuwa amesafiri.” Moyo wa Tunda ukapasuka kama kumeanguka chuma, mpaka usoni akaonyesha ameshituka. Vic akamuona akapata ujasiri zaidi.

  “Umeona sasa walivyo wanafiki? Kumbe hawakukwambia!?” Vic akauliza kwa kejeli. “Ndio ujue ubaya wao. Wanajifanya kukupenda na kukukaribisha kumbe na mimi wananifanyia hivyo hivyo!” Akaendelea Vic. “Ila mimi sikutaka kukuficha kama Net, Maya na Carter wanachokufanyia. Mimi sio mnafiki. Na sijui kufanya mambo ya kujificha. Ndio hicho nilitaka kukwambia siku ile nilipokufuata pale chumbani, naona ukanidharau! Wakati mimi nilikuja tu kwa wema ili kukiri kwako kilichotokea kati yangu na Net wakati upo jela, ili ukiingia kwenye hii ndoa uwe unajua ukweli wote.” Vic akaendelea.

     “Kwanza nataka ujue kuwa ni ukweli unaofahamika kila mahali na kila mtu kuwa Net ananipenda sana mimi. Ila tatizo ni bibi yake na mimi sijui ni kwa nini bibi yake ananichukia wakati alikuwa rafiki kipenzi cha bibi yangu! Yeye ndiye anayemfanya Net ashindwe kuwa na mwanamke anayempenda ambaye ni mimi.” Vic akaendelea.

Sura ya Net siku Maya akimwambia atamtag Vic picha za Cote huko Facebook, ikamjia. Akakumbuka kule kupaniki kwa Net baada ya Maya kumtaja jina lake mbele yake. Akawa kama amekumbushwa kitu, akashtuka sana na kuingiwa hofu ya ajabu. “Siku aliyonikaribisha hapa Net mpaka tukalala naye, wakati wewe upo jela na bibi yake akiwa safarini, tulizungumza mengi sana. Moja ya tuliyozungumza ni Net alitaka turudiane. Wewe na Chloe mlipita tu kwenye maisha yake, lakini moyo wa Net upo kwangu” Vic akaendelea kwa ujasiri wote.

     “Tulifikia huo muafaka ukiwa umebakisha mwezi mmoja utoke na ndio maana hakuja kukuona  mwezi huo. Alisubiri utoke jela ili akakwambie. Ndio akaja nchini kwenu siku ulipotoka jela ili akwambie ndio akakukuta na mtoto wake. Hapo ndipo ikabidi akuchukue tu kwa kuwa...” ‘....na Mungu atakutafutia msaidizi na wewe kwenye ndoa yako.’ Maneno ya mama yake yakarudia akilini mwake kwa gafla.

     Giza zito likapita usoni kwa Tunda. Mambo mengi, laana za mama yake na maneno mazito mpaka ya Ritha vilikuwa vikishindana kupita kichwani kwake kwa wakati mmoja, wakati Vic akiendelea kuongea pale.

     “Tena kama huamini kama mwaka huuhuu na mimi nililala palepale kitandani kwa Net, na tukakubaliana turudiane, angalia hizi picha. Mimi huwa sidanganyi. Nataka kukusaidia usijiingize kwenye kitu usichomudu au hata kukielewa.” Vic alitoa simu yake na kuanza kumuonyesha, akiwa amekaa palepale bila hata kumsogelea Tunda. Akakumbuka stori zote juu ya Maya. Vic hupenda ushahidi wa picha na video kuthibitishia uma kuwa jambo lilitokea. Hicho kipengele huwa hasahau.

     Alibaki akiwa amekaa palepale, vilevile lakini hali ya kusalitiwa ikamwingia na kumnyong’onyesha kabisa. Akaumia sana kuona watu wote wanajua kama Vic alikuwepo hapo ndani akilala na Net kwenye chumba hichohicho kama mpenzi, tena baada ya kumuoa yeye, wasimwambie ila kumchekea tu!  Akakumbuka hotuba nzito aliyotoa juu yake kwa Net mbele ya umati mkubwa wa watu walio hudhuria siku ya kukaribishwa kwake kwenye hiyo jamii ya Norfolk. Akajisikia kudhalilishwa na kufedheheshwa na kila mtu ndani ya ile nyumba.

     “Hata hicho cheo cha bibi Cote umepewa kwa kuwa tayari umebeba mtoto wao. Asingeruhusu mwanamke mwingine aje atawale wakati huyo Cote ametoka kwako! Cote atatawala vipi na mwanamke mwingine? Yaani kama hivi Net anavyotawala sasa hivi, halafu bibi Cote awe ni mwanamke mwingine wa babu yake sio bibi yake aliyemzaa baba yake! Hata wewe mwenyewe huoni kama haileti maana?”

     “Hii familia huwa haipendi mchanganyo ndio maana imebidi tu kukupa wewe mtu ambaye kwanza hujasoma, huna sifa nzuri kwenye jamii na huelewi chochote kinachohusiana na jamii ya huku.” Vic aliendelea kuongea na Tunda akihakikisha anamuelewa kifasaha kabisa bila kumpoteza kwenye kile alichokusudia amsikie. Vic akafanikiwa kuingia kwenye moyo wa Tunda na kuamini yupo pale akihudumiwa kwa heshima sababu ya huyo mtoto aliyebeba. Akajishika tumbo akijipapasa kama anayetafuta pumzi.

     Vic aliendelea kuongea, lakini Tunda alishaondoka pale muda mrefu. Mawazo yalimtoa pale na kumrudisha Tanzania. Akakumbuka alianza kwa mchezo mchezo na Ritha. Akampuuza. Mbele ya Net mwenyewe, alimkamata na kumuweka jela. Net akawa uraiani maisha yakiendelea na Vic wakati yeye yupo jela! Hofu ya historia kujirudia kwake, safari hii kutoka kwa Vic aliyesimuliwa makubwa na mazito anayoweza kufanya kwa kila anayejaribu kusimama mbele yake, ikamwingia. Akaanza kuhangaika pale kochini.

     Maiti ya Gabriel akiwa amelalia damu yake nayo ikapita. Kifo cha mama yake Gabriel kikamjia. Bethy yupo jela. Naye hatakaa akatoka. Yote hayo ni Net! “Atanifanya nini mimi huku ugenini, na sina mtu upande wangu? Safari hii nitaishia wapi?”  Hapohapo akaanguka mbele ya Vic na rafiki yake. Akapotea kabisa hapa ulimwenguni asijue kinachoendelea tena. 

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

Kumbe vile Tunda alipowafuata tu pale sebuleni, Carter alishamtumia ujumbe bibi Cote. ‘Vic amemfuata Tunda. Sijui ameingiaje getini, tumemshtukia yupo ndani akisisitiza ana kitu cha muhimu chakuzungumza na Mrs Cote. Wapo sebuleni wakizungumza. Nina hisia mbaya sana juu ya hili Ms Cote! Hali ya Tunda sio nzuri. Yupo dhaifu mno. Imebidi mlinzi wake aite usafiri kumrudisha nyumbani. Nimemshika mkono kumsaidia kupanda ngazi, sidhani kama yupo na nguvu ya kumkabili Vic kwa sasa.’ Carter akatuma huo ujumbe. 

Bibi Cote, Maya na Net ndio walikuwa wamekaa wameletewa tu keki ndipo ujumbe ukaingia kwenye simu yake ya dharula. Hiyo simu alijua hakuna anayeitumia mpaka iwe dharula. Huwa haisubiri na wakati wote inakuwa na mlio. Akakunja uso na kuamua kusoma. Hata Net akashtuka baada yakusikia simu hiyo ikitoa mlio. Inamaana ipo dharula. “Is everything okay, Nana?” Net akauliza na Maya akanyanyua uso kumtizama. “Ujumbe kutoka kwa Carter!” Akajibu wakati anaanza kusoma. 

“I need my car ready, like yesterday!” Akasikika bibi Cote akiongea kwa sauti. Huwa akiongea hivyo inamaana anatoka hapo na akifika nje, mlinzi awe alishakimbia kwa dereva na kumwambia awashe gari, yaani akiwa anatoka nje, gari imewashwa, na mlango uko wazi, yeye anaingia bila kupoteza hata sekunde moja, gari liondolewe hapo.

     “Kuna nini Nana?” Net akamuliza wakati bibi yake ameshanyanyuka na mkoba wake tayari begani anatoka. “Vic yupo nyumbani amemfuata Tunda kwa madai ya kuwa na mazungumzo naye maalumu. Sasa nataka safari hii nimpe muda wangu pia.” Bibi huyo alimaliza hivyo na kupotea hapo mbele ya macho yao. Maya aliyekuwa ameongozana naye hapo akitumia gari yake, akajua ndio anaachwa. Akaruka na pochi yake akakimbia mpaka akampita bibi yake kutoka pale, kweli akakuta gari imesimama nje ya mlango wa hiyo hoteli. Na mlango wake ulikuwa umeshafunguliwa upo wazi.

     Maya akakimbilia upande wa pili akapanda kwa haraka na kufunga mkanda. Bibi Cote akaingia, mlango ukafungwa na mlinzi wake. “Nyumbani kwangu, sasa hivi!” Yule bibi aliongea hivyo kwa kifupi tu, dereva akaondoa gari maana na mlinzi alikuwa ameshapanda.

Kwa Tunda.

H

uku nyuma alipoanguka tu Tunda, kwa kuwa aliangukia Tumbo rafiki wa Vic akashtuka sana na kuanza kupiga kelele. Carter na Ms Emily wakakimbilia pale sebuleni walipokuwa wamekaa. Hapohapo Carter akapiga 911 bila hata kumgusa Tunda aliyekuwa amelalia tumbo. Kufumba na kufungua, nyumba ya Cote ikajaa magari ya wagonjwa zaidi ya matano. Police nao pia wakajaa. Kwa kuwa Carter alisema ni hatari, Tunda ni mjamzito na ameangukia tumbo akimshika haoni mapigo ya moyo.

     Kina Vic walipoona hivyo, wakatoka taratibu kwa mlango wa nyuma, wakakimbia. Tayari nyumba hiyo ilishajaa watu wa huduma ya kwanza kutoka zima moto na mahospitali ya karibu kila mmoja akimtaka Tunda aamke kwanza ndipo wamkimbize hospitalini.  Lilikuwa likisikika jina la Tunda tu humo ndani wakijaribu kumuamsha. Tunda huyu amezimia akiwa amedhoofu kwa njaa, na msongo wa mawazo. Walitumia muda wakutosha wakijaribu kumuamsha lakini hakuitika hata mara moja wala hakufungua macho.

     Kiwango cha Oxygen na chenyewe kikaonekana kinaanza kushuka mwilini. Kwamba Tunda hakuwa akipata hewa yakutosha mwilini. Ikawaingia hofu, ikabidi kuingizwa kwenye gari ya wagonjwa kwa haraka ili kujaribu kuokoa maisha ya mtoto kama itashindikana Tunda. Tayari tukio likawa limebadilika pale. Carter, Ms Emily, dereva aliyemleta Tunda kutoka matembezini na mlinzi wa Tunda, wakawekwa pingu. Polisi wakazidi kumiminika. Ni kwa Cote!

     Wakati gari ya bibi Cote inaingia getini, hata dereva hakujua anapitishaje gari pale kufikia mlango. Wakabaki wanapiga honi kwamba watu wawapishe. Maya akaona wanamchelewesha. Akafungua mlango akakimbia bila ya viatu. Akafuata bibi yake na mlinzi nyuma wakikimbia kufikia nyumba ambayo ilikuwa imejaa polisi na magari yao yakiwa yanawaka taa za bluu. Magari ya wagonjwa na yenyewe yalikuwa yameshawasha taa. Moja likaanza kutoa mlio. Mwashirio wakutaka ipishwe ikiwa inaondoka na Tunda.

     Maya na bibi yake wanafika pale, ndio Tunda anapandishwa kwenye hiyo gari ya wagonjwa huku akikandamizwa kifua kama kumfanya aheme. Akaingizwa kwenye gari ya wagonjwa, polisi wakatengeneza njia kwa kuomba magari mengine yaliyokuwa yamejaa hapo kwenye ua, yapishe, ili ile gari ya wagonjwa iliyombeba Tunda ipite.  Baadhi ya polisi wa pikipiki nao wakaongeza nguvu wakawa wanaongoza njia kwa kutengenezea hilo gari njia.

Walitoka hapo kwa mwendo kasi huku wakiwa wamewasha ving’ora kuashiria wapishwe na yeyote barabarani na pikipiki za polisi nazo ziliandamana na hiyo gari ya wagonjwa kama msafara. Wakiendelea kusafisha njia wakielekea hospitalini. Ikawa kelele ya kuongeza wasiwasi.

     Wakati na Net anaingia getini, ndio Tunda anatolewa hapo getini kwa hiyo kelele. Na yeye akaamuriwa na polisi akae pembeni apishe njia. Akiwa hajui kinachoendelea, nani yupo ndani ya hiyo gari ya wagonjwa! Polisi wawili wa pikipiki waliongoza hiyo gari ya wagonjwa nakuzuia watu na magari yao kabisa mpaka lile gari lilipopita. Net akajifariji akijiambia sio Tunda. Kama ingekuwa Tunda, yeye ndio angekuwa wa kwanza kupata taarifa. Akatulia garini lakini moyo ukiwa umejawa wasiwasi.

      Walipopita akajaribu kuchungulia ndani ya ua. Akashangaa ule umati wa magari ya polisi na zima moto pale ndani kwao. Na magari ya polisi yakazidi kumiminika humo ndani. Gari ya bibi yake aliiona mbele kidogo ya geti. Akashuka kwa haraka kuikimbilia akijua atamkuta bibi yake ndani kujua kulikoni. Akakuta dereva tu. Bibi yake, mlinzi na Maya hawapo. Gari bado ilikuwa ikiwaka.  Akakimbilia upande alipokuwa dereva. 

“Ni nini kinaendelea!?” Net akauliza akionyesha wasiwasi mkubwa usoni huku akiomba Mungu asiwe Tunda. “Ron amenipigia simu sasa hivi na kuniambia nisizime gari wanarudi sasa hivi, tunaelekea hospitalini. Mrs Cote amekimbizwa hospitalini sasa hivi, hali sio nzuri. Wanajaribu kama wanaweza kuwahi kuokoa japo mtoto.” Akamuona Net anapepesuka kama anayetaka kuanguka. Akakaa chini kabisa. Ron ndio mlinzi wa bibi yake, inamaana zile ni taarifa za hakika. 

    Dunia ilisimama kwa muda. Akashindwa kufikiria kabisa, akakaa pale nje ya gari kwenye dirisha la dereva. Na dereva naye hakushuka. Akabaki akimchungulia na kumuuliza kama yupo sawa. Maana amri aliyoambiwa asizime gari, bibi Cote anarudi kukimbilia hospitalini. Asingethubutu kutoka hapo garini, asije kutokutwa ndani ya gari, nyuma ya usukani na kuharibu zaidi. 

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

 

Ni nini kitaendelea? Usipitwe na

muendelezo uliojaa mazito, mapya na ya zamani yaliyokuwa yamewekwa sirini yatawekwa mwangani

     v  Utakutana na Andy, Live! Aliyemrubuni Maya, atarudi kwenye picha. Alitumwa na nani?

v  Vic amekiri hakudanganya. Anao ushahidi wa kulala na Net baada ya kumuoa Tunda. Maya na Carter pia amewataja kama ni shahidi zake. Na bibi Cote ndiye anayesimama kati ya penzi la Net & Vic! Kweli mtoto ndiye anayemketisha Tunda na wakuu?

v  Nani anaumiza kichwa cha Maya, binti mrembo anayetamaniwa na kila mwanamme kwa urembo na pesa?

v  Vic anaonekana kujua mengi na ya undani juu  ya Tunda, nani anamtumia safari hii? Nani anayempa mbini makini za kumuangusha Tunda?

v  Tanzania ilikuwa jela, safari hii nchini Canada mahututi.

v  Nini hatima ya Tunda na mtoto aliyembeba ambaye ameanza kukosa hewa?

 

Yooote yatajibiwa. Usikose.

CONVERSATION

0 Comments:

Post a Comment