Naomi Simulizi |+1 205 767 8163 |naomisimulizi@gmail.com Nilipotea! – Sehemu ya 44. - Naomi Simulizi

Nilipotea! – Sehemu ya 44.

 

M

ara bibi yake na Maya wakawa wanarudi wakikimbia pamoja na mlinzi. “On your fit, NOW. This is not the time to freeze, son!” Bibi yake aliongea huku akiingia kwenye gari akimtaka Net asimame pale alipokuwa amekaa. “Come on! Get in the car. We have to run. Tunda needs us.” Bibi yake akaweka msisitizo kwa Net wawahi hospitalini akimwambia afanye haraka kwakuwa Tunda anawahitaji kwa wakati huo. Net akasimama na kuingia ndani ya gari.

     Yule bibi akaanza kupiga simu mara tu alipofunga mkanda wa gari. Ya kwanza kwa mkunga aliyemzalisha Ritha watoto wote wawili. Net na Maya na ndiye aliyekuwa akimtibu Tunda tokea anatua nchini. Bibi huyo ni rafiki wa bibi Cote wa muda mrefu. Na ni daktari bingwa wa wakina mama. Alishastaafu na kurudi kufanya kazi kwenye hospitali yake binafsi.

     “Tunda amekimbizwa hospitalini. Hali sio nzuri. Tafadhali naomba nikukute huko. Sitaki ashikwe na watu wasio mfahamu na wasiojua historia yake. Najua muda huu kuna foleni, nimetuma rubani akufuate. Tafadhali akukute tayari.” Akakata simu baada yakupata jibu aliloonekana ameridhika nalo. 

Wakamuona anapiga simu nyingine. Net alikuwa ameinama tu. “Nataka ukawatoe polisi, Carter na Ms Emily. Cale na Jeff wanaweza kusaidia polisi, lakini namtaka Carter na Ms Emily watoke haraka. Carter anatakiwa kunywa dawa saa 12 jioni. Asipozinywa hizo dawa, moyo utasumbua. Na sitaki simu za watoto wa Ms Emily hasa jioni ya leo. Naelekea hospitalini.” Akakata simu. Kwa maelezo hayo tu, Logan alitakiwa awe ameelewa kila kitu na kutekeleza bila kuuliza maswali mengi. 

Akapiga tena simu nyingine. “Unakumbuka mara ya mwisho kuzungumza na wewe juu ya mtoto wenu?” Maya akajua anazungumza na mama yake Vic. “Nilikuonya Barbara, na nilikwambia Vic anahitaji msaada wa haraka ambao nyinyi wazazi wake mnaonekana mmeshindwa kumpa. Sasa, kama unampenda Vic, ndani ya masaa mawili hakikisha wewe mwenyewe, unamfikisha kituo cha polisi. Baada ya hayo masaa mawili nikiambiwa hayupo kituo cha polisi, nitajua umeshindwa tena, ndipo hapo sasa itabidi mimi niingilie kati. Na nina uhakika hutataka kuniona mimi nikiingilia kati.”  “Amefanya..” Mama yake Vic akataka kuuliza, lakini bibi Cote akamkatisha. “Umebakisha lisaa limoja na dakika 56. Usipoteze muda.”  Bibi Cote akakata simu. 

Kwa kuwa Tunda alikimbizwa hospitali ya serikali ya karibu, ilichukua kama dakika 20 kufika pale. Walishushwa mlango wa mbele na helcopter iliyokwenda kumchukua daktari wa kina Cote ndio ilikuwa inatua juu ya jengo hilo. “Huyo ni Dr. Ross. Naamini atakuwa hajachelewa.” Bibi Cote alizungumza hivyo akiwa anashuka kwa haraka akikimbilia ndani. Dereva wake alimshusha mbele kabisa kwenye mlango wa kuingilia ndani ya jengo hilo la hospitali. 

Wakati wanaingia ndani ni kama uongozi wa hapo hospitalini ulikuwa ukimsubiria bibi Cote kwa kuwa habari zilishafikishwa kuwa Tunda anakimbizwa hapo akiwa hana fahamu na ni mama mjamzito wa mimba kubwa. Si kwa Tunda, ni utaratibu wa wagonjwa wote ili kuhakikisha kuwa wanapomfikisha mgonjwa mwenye hali ya mahututi, awe anasubiriwa na wahusika sahihi. Sasa ikaongezeka kuwa ni Mrs Cote na mlinzi alishapiga simu yakuomba uongozi wa hospitali kutua ndege hiyo ndogo itakayomleta daktari wa Cote. Umakinifu ukaongezeka na habari zikawa zimefika kwa uongozi wote na madaktari bingwa wa hapo kuwa Mrs Cote analetwa hapo. 

Kina Cote waliingia wakakuta uongozi wa hospitali unawasubiria ndani ya mlango, wakiwa pamoja na polisi. “Mrs Cote anaendeleaje?” Hilo ndilo lilikuwa swali la kwanza kabla hajajibu salamu. Wakawatoa pale mbele ya watu wengine wakawa kama wanaingia ndani huku wakijaribu kuwapa taarifa za walipofikia na Tunda, hata kabla hawajafika mbali, akawasogelea daktari akikimbia. Alionekana anatokea chumba ambacho sio mbali sana na pale. “Lazima mtoto atolewe sasa hivi.” Bila salamu akaenda moja kwa moja kwenye pointi akimtizama bibi Cote na Net.

         “Huyu ni daktari wa watoto.” Wakamtambulisha. “Hewa kwa mtoto inaanza kushuka. Tunda ameshindwa kupokea hewa yaku...” Kabla hajamaliza, mlango wa lifti iliyokuwa inatokea juu kabisa ya hilo jengo, ukafunguliwa. Wote wakageuka. Akatoka Dr Ross akionekana ni kama na yeye alikuwa na haraka sana. “Thank God!” Alisikika bibi Cote mara baada yakumuona Dr Ross pale.

“Zungumza nao ili uelewe ni nini kinachoendelea.” Bibi Cote alimwambia Dr Ross aliyekuwa akifuatilia afya ya Tunda na mtoto wake kila week. Akasogea karibu akaanza kuuliza maswali ya kitaalamu huku akipewa majibu ya kidaktari hata dakika 5 hazikuisha akawa ameelewa kila kitu. Walizungumza kwa lugha za kidaktari wakitajiana majina magumu wao kwa wao. Akamgeukia Net. “Lazima mtoto atolewe sasa hivi na kama nilivyokuwa nimewaambia wewe na Tunda, mtoto wenu ameshakomaa na..” “Okay.” Net akakubali kwa haraka bila kutaka maelezo mengi.

“Lakini lazima nimuone mke wangu kabla hamjamfanyiwa chochote.” Net akasisitiza. “Unaweza kuwa naye kwenye hatua za mwanzoni kwenye chumba cha upasuaji, ila wakianza kumshugulikia yeye na mtoto, itabidi....” Mara wakasikia kelele za mashine chumba alichopo Tunda. Manesi wengine wakazidi kukimbilia humo ndani. Baada ya kama dakika tano wakaona Tunda anatolewa kwenye hicho chumba huku anakimbizwa na wauguzi pamoja mashine zilizokuwa zikipiga kelele mfululizo. Walimuona muuguzi mmoja juu ya kitanda alicholazwa Tunda, amepiga magoti juu ya Tunda akijaribu kumfanya aheme kwa kumminya kifua chake kwa nguvu, tena mfululizo.

Kelele zilizokuwa zikipigwa ili lift ifunguliwe na watu wapishe njia, ilizidi kuwaogopesha wote. Tunda alikuwa akikimbizwa chumba cha upasuaji akisindikizwa na hekaheka za madaktari na manesi wengi. Alionekana akiwa amefunga macho ametulia kabisa pale kitandani japo walikuwa wakimminya kwa juhudi zote. Baada ya lift kufunguka, waliingia wote na kitanda cha Tunda, Net naye kama mchale, akakimbia na kuingia ndani. Kufumba na kufumbua, wakajikuta wamebaki Maya, bibi yao pamoja na mlinzi nyuma yao. Wauguzi wote waliondoka hata wale waliokuwa wakizungumza nao pale walikimbilia kwenye ile lifti pamoja na Dr. Ross. Pakatulia kimya, macho yao wote yakiwa yametua kwenye mlango wa ile lifti iliyowabeba wote.

Wakajikuta kila mtu akiwaza lake. Kuanzia kile kilichokuwa kikiendelea pale, hali ya Tunda walivyomuona nyumbani na pale. Maya akaanza kulia taratibu. “Kama Tunda akifa, nahisi na mimi nitakufa Nana.” Bibi yake akamsogelea na kumkumbatia. “Usiogope Maya.” “No Nana. Hujui mahusiano yangu na Tunda. Ameniahidi atakuwa na mimi kila wakati. Ananisikiliza. Tunda ana muda na mimi, Nana. Ndio mtu pekee nimempata ambaye yupo karibu na mimi na kujali kwa undani. Kila mtu hajui ni kwa nini nilikuwa nikitumia madawa, lakini Tunda ametoa muda wake na kuzungumza na mimi.” Bibi Cote akashangaa sana. 

Kwa kuwa mengi yalikuwa yakiendelea kwa wakati mmoja, bibi Cote akaona hilo alinyamazie kwa wakati huo. “Nisikilize sweatheart. Tunda yupo chini ya uangalizi mzuri sana. Macho na akili za kila daktari aliyekuwepo chumbani kwa Tunda vipo kwa Tunda na mtoto. Na kwa kuwa wanajua ni Cote, watahakikisha Tunda anapona na anarudi kwetu salama.” “I do love and need Tunda in my life, Nana!” Maya aliendelea kuweka msisitizo wa vile anavyompenda na kumuhitaji Tunda maishani. “We all do baby. We all do.” Akajaribu kumtuliza kwa kumuhakikishia kuwa hata wao wanampenda na kumuhitaji Tunda. Mmoja wa nesi akawasogelea na kuwashauri wakae sehemu ya kusubiria wagonjwa waliokuwepo chumba cha upasuaji. Akawaongoza njia, wakaenda kukaa. 

 Cote junior cote the 5th!

B

aada ya kama dakika 40 hivi akawafuata yule daktari wa watoto aliyekuja mwanzoni. Lakini safari hii alikuwa na tabasamu la faraja usoni, akawaambia waongozane wakamuone mtoto. Kidogo ikawa faraja. “Haya sio mazingira niliyopanga ayakute Cote. Sio hivyo kabisa!” Alilalamika bibi Cote.

“Hivi ndivyo anavyopenda Vic. Hawezi kuruhusu kitu kizuri kitokee kwenye maisha ya watu kama yeye hajahusika na kupewa sifa. Amehakikisha ameniharibia mimi, watu wakanipuuza, sasa hivi ameamua kummaliza na Tunda! Pengine watu safari hii watamjua hila zake.” Maya aliongea huku akilia. Wakielekea wanapowekwa watoto waliotoka kuzaliwa.

Bibi yake aliumia sana alivyozungumza vile Maya. Tokea hilo tukio litokee, Maya amekuwa akiongea mambo ya kumuumiza sana huyo bibi nakumfanya ashindwe kuongeza. Maya amekiri Tunda ndiye mtu pekee ambaye ametoa muda wake kumsikiliza hata kujua ni kwa nini au ilikuaje akatumia madawa ya kulevya. Tunda ni mgeni kwao kabisa na ameweza kuwa na Maya kwa karibu kwa kiasi hicho! Si yeye tu bibi Cote, wote waliomzunguka Maya waliishia kumtoa kwenye mikasa bila kutafuta chanzo. Na hata aliposema ni Vic ndiye anayehusika, hakuna aliyejali.

Sasa bomu jingine la Vic limewalipukia na wao usoni. Tena zikiwa zimebaki siku 4 tu harusi kufungwa, muda mfupi sana ili mtoto wao azaliwe. Vyote hivyo Vic amevibadilisha kwa muda mfupi sana, tena kwa kuwagarimu wao, garama kubwa sana. Ya pesa na uhai.

“Anaendeleaje Tunda?” Akauliza bibi Cote angalau kujitoa kwenye kilio cha Maya. “Bado wanamshugulikia. Lakini amejifungua mtoto mzima kabisa. Tulifikiri angehitaji kuwekwa kwenye mashine kwa muda mrefu, lakini anaonekana ameshakomaa kabisa. Anahitaji uangalizi wa masaa 24 tu ili kujiridhisha kama yupo salama.” Aliongea yule daktari wa watoto akionekana ametulia.

Aliwafikisha kwenye hicho chumba, lakini waliambiwa wanamwangalia kwenye kioo tu, sio kuingia ndani. “Ni kweli ni mkubwa! Ni Cote kweli kweli!” Alisikika bibi Cote kwa sauti ya kuhamasika, wakamuona anafuta machozi. Maya naye akaanza kulia kwa furaha baada yakumuona yule mtoto. “He is so cute and tall! Hafanani na Net wala Tunda!” Wakacheka huku wakilia.

“Net amemuona?” Akauliza bibi Cote. “Ndiyo, alimuona kulekule chumba cha upasuaji. Ndiye aliyesema tuje kuwaita mumuone.” Bibi Cote akarudisha macho kwa mtoto. “Hivi sivyo nilivyotaka kukutana na Cote kwa mara ya kwanza!” Akalalamika tena bibi Cote kwa sauti ya chini iliyoweza kusikika. “Kwa nini hatuwezi kumshika!?” Akauliza kwa kusikitika Maya. “Umeona pale alipowekwa na mashine pembeni yake?” Wote wakamwangalia yule daktari na kurudisha macho kwa Cote. “Japokuwa anaonekana amekomaa kwa nje, lakini bado tunataka kuwa na uhakika hakuna kinachobadilika angalau kwa masaa 24 na kujiridhisha kabisa kuwa kila kitu ndani na nje kinafanya kazi sawa.” Wakatulia kidogo wakimwangalia.

“Rudi chumba cha upasuaji, waambie zimepita dakika 50 sasa, hakuna aliyetoka kutupa taarifa za Tunda. Nahitaji kujua kinachoendelea.” Akamwambia yule daktari wa watoto. Akaondoka na kuwaacha pale wamesimama wakimtizama mtoto.

Maya alipiga picha baadhi na kumchukua video huku akiongea maneno mazuri kwa Cote, akampiga picha na bibi yake na kumuomba aongee chochote. “Namshukuru Mungu upo salama na nimefurahi unafanana kabisa na Cote wangu.” Maya akacheka, bibi Cote akajifuta machozi. “Mungu anajua ni kiasi gani nakupenda na nilivyokuwa nikikusubiri nikushike kwenye mikono yangu na kupata bahati ya kukubusu tena na tena. Wewe ni zawadi ya pekee na ya ajabu Mungu aliyotupa. Nakuombea afya njema na ulinzi wa kimungu kwenye maisha yako yote ya hapa duniani. Ukafanikiwe katika kila utakalochukua hatua na kulifanya. Zaidi ya Cote mwenyewe.” Maya akaridhika. Wakajichukua video pamoja. Akazima camera ya simu na kurudisha mkobani.

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

Baada ya muda akarudi yule daktari wa watoto na daktari mwingine. “Tunda anaendeleaje?” Akawahi kuuliza bibi Cote. “Anaendelea vizuri. Upasuaji ulienda vizuri. Hakuna kilichoharibika.” “Ameweza kuzinduka?” Akauliza tena bibi Cote. “Mwanzoni alipoingia mume wake. Alifungua macho lakini hakuzungumza. Walimchoma sindano ya usingizi kwa ajili ya upasuaji, wanamalizia kumshona watamuamsha kabla hajatolewa. Dokta Ross amesisitiza nikwambie usiwe na wasiwasi. She is gona make it.” Wakamuona bibi Cote anapumua kwa nguvu kama aliyepata aghueni. “Asanteni sana.” Akashukuru bibi Cote, yule daktari akaondoka.

Simu ya Logan ikaingia. Bibi Cote akajivuta pembeni. Maya alimuona vile anavyobadilika kila muda unavyozidi kwenda bila yakujibu chochote. Maya akajua mambo si mazuri. “Nimesema ni lazima Carter atoke leo. Anatumia dawa kila baada ya masaa 6. Lazima arudi nyumbani leo. Unanielewa Logan?”  Akamsikia bibi Cote akitoa amri. “Na watoto wa Emily hawawezi kuelewa kama mama yao leo asiporudi nyumbani. Kwa kifupi, fanya kila linalowezekana, kufupisha mambo yote. Na unitaarifu kujua wamefikia wapi?” Akamuona bibi yake amekata simu kisha amesimama vilevile. Maya akajua anajaribu kutulia.

Mara wakamuona Net anakuja. Wote wakakumbatiana.“Tunda anaendeleaje?” “Wanamalizia ili wamtoe. Kila kitu kimeenda salama. Daktari wake amejitahidi asipoteze damu nyingi. Wameniomba nitoke, wamalizie.” “Afadhali.” Bibi yake akasikika kuridhika. “Tumemuona Cote.” Maya akaongeza. Wakamuona Net anafuta machozi. Akasogea pale dirishani. “Anafanana sana na Papa!” Wakacheka.

Baada ya Tunda kujifungua.

T

unda alirudishwa chumbani kwake akiwa bado na madawa ya usingizi na amechoka.  Wakamuweka sawa,  na kumwekea mashine za kuendelea kuangalia mapigo ya moyo na mengineyo. Waliporidhika, manesi na madaktari wengine wakatoka. Alibaki dokta Ross ili kuzungumza na familia. Bibi Cote, Net na Maya wakaingia hapo chumbani. Tunda aliwaangalia bibi Cote na Maya, akashindwa hata kumtizama Net. Akafunga macho kabisa. Wakaona machozi yakimtoka.

“Kila kitu kilienda sawa. Anahitaji mapumziko makubwa. Mrs Cote yupo dhaifu na bado pressure yake hairidhishi. Imerudi kuwa kama nilivyomuona mwanzoni kabisa, wakati kulikuwa na maendeleo! Nashauri apate muda wakutosha wa mapumziko, na  sisi tutaendelea kumfuatilia. Naamini akipata mapumziko yakutosha baada ya siku tatu, angalau tunaweza kufikiria kumruhusu arudi nyumbani.” Bibi Cote akamshika mkono. “Nakushukuru sana. Asante kwa kuja kwa haraka na kuweza kumsaidia Tunda. Asante sana.” Akashukuru bibi Cote. “Chochote kwa ajili yako Ms Cote.” Akajibu yule daktari wa wakina mama.

Akazungumza kidogo na wao wakapa muda wa kuuliza maswali, akatoka kama kuwapisha. Kimya. Tunda hakufungua macho tena. Bibi Cote akasogea pale kitandani akamnyanyua mkono na kuubusu kisha akabaki ameukumbatia. “Pole sana Tunda. Pole sweetheart.”  Akarudia rudia yule bibi lakini Tunda aliendelea kutokwa na machozi. Simu ya bibi Cote ikaita. Akajua lazima  atakuwa tu ni Logan ambaye ndiye aliyetaka kumsikia kwa wakati huo. “Nitarudi baada ya muda mfupi sana.” Akaaga na kutoka.

“Pole Tunda.” Aliongea Maya kwa kiswahili kabisa, lakini hata Tunda hakufungua macho. Tunda huyu alijawa kusalitiwa na maumivu makali sana. Ya upasuaji na maneno ya Vic yaliyomkumbusha mengi. Alibaki akitokwa na machozi bila hata kutaka kufungua macho kabisa. Net alipomsogelea ili kumfuta machozi, akahisi harufu yake, bila kufungua macho akajua ni yeye, taratibu tu bila fujo nyingi wala kufungua macho akakwepesha uso upande mwingine kama anayemwambia usiniguse.

Wanandoa hawa walikuwa na kutoelewana tokea siku iliyopita Net alipogomba sana na kushindwa kutulia hata Tunda alipomtuliza wakiwa wanachagua chakula. Akaja akaongeza kugongelea msumari Vic. Walisimama hapo, Net na Maya wameshageuka wasaliti wake kabisa. Alitamani waondoke, wampishe hapo kwenye hicho chumba. Net akaelewa kuwa hataki amguse. Lakini hakuanzia hapo. Ni tokea jana yake waliporudi nyumbani, Tunda alikimbilia chumbani na kujifungia. Net akajua kuna mengi aliyobeba hapo Tunda. Ila wasijue ni nini Vic aliongea.

Maya aliona alichofanya Tunda, na bado aliendelea kulia. Asijue kama na yeye asogee au amwache. “Utapona tu Tunda.” Akaongeza Maya kwa upole, kisha akamtizama kaka yake. “Labda tumuache apumzike mpaka kesho.” Akamshauri kaka yake kwa sauti ya chini. Nesi akaingia na sindano kwenye tray. Akamkuta akilia. Akamsogelea.

“Upo sawa Tunda? Au maumivu ni makali sana?” Yule nesi alimuuliza kwa upole. Wakamuona Tunda akitingisha kichwa kukataa huku akilia kwa uchungu sana. “Lakini pia lazima nikupe dawa ya maumivu ili kuhakikisha maumivu hayarudi tena.” Wakamuona anatingisha kichwa kukubali. “Naomba nisikilize Mrs Cote. Afya yako sio nzuri. Unahitajika kupumzika kabisa. Daktari amekuandikia dawa za usingizi kabisa. Ninazo hapa pia. Nitakuchoma ili ulale kabisa. Naomba utulie.” Wakamuona anavuta pumzi kwa nguvu lakini machozi yakiendelea kumtoka.

Yule nesi akamfuta machozi na kumchoma sindano kwa kupitia sindano iliyokuwa imepitishiwa ndipu inayoingia mkononi mwake. “Nitazima taa zote kasoro ile ndogo pembeni ili kumfanya atulie kabisa. Hata hivyo dawa niliyomuwekea, itamfanya alale kabisa. Nashauri hata nyinyi mumpishe, na ikiwezekana hata hao polisi hapo nje muwaombe waje wazungumze nae baada hata ya masaa 24, ili kumfanya atulie kabisa.” “Asante.” Akashukuru Net, yule nesi akaondoka.

Net akarudi pale na kuinama. “Nakupenda Tunda. Nakupenda sana mke wangu. Naomba usije kulisahau hilo.” Akaongeza kilio. Akambusu kichwani. “Nitarudi tena kesho asubuhi, pengine dawa zitakuwa zimeisha na tutaweza hata kuongea. Cote anaendelea vizuri. Naamini kesho wataweza kumleta huku.” Tunda hakufungua macho. Net akamfuta machozi. Safari hii hakukataa. Akabaki akimwangalia kwa muda, wakamuona anavuta pumzi taratibu, wakajua dawa zimeshamchukua. Nesi aliwaambia wakitoka atarudi ndipo atazima taa. Net akamfunika vizuri, akabaki akimtizama.

“Twende Net. Atakuwa sawa. Tumpe muda wa kupumzika.” Maya akaongea na kaka yake kwa upole. Akamshika mkono. Net akambusu tena Tunda. Wakatoka. Walimkuta bibi yao anazungumza na polisi huku amekuwa mwekundu haswa. Wote wakasogea. “Tafadhali naomba mumuache kwa sasa. Mbali na upasuaji aliofanyiwa, Tunda yupo dhaifu sana. Hata sisi tumeombwa tuondoke ili tumpishe apumzike kabisa.” “Hata hivyo wameshampa dawa za usingizi. Amelala kabisa, hawezi kuzungumza.” Net akaongeza kwa bibi yake.

Polisi wakasema watarudi tena kesho yake kumuhoji, kujua kilichotokea. Wakaondoka. “Hakuna kitu tunachoweza kukifanya sasa hivi, turudini nyumbani. Nimeweka ulinzi hapo nje ya mlango wake, nimesema ni wauguzi tu ndio wanaoruhusiwa kuingia hapo, na nimekataza hata wauguzi wasiingie na simu humo ndani.” “Asante Nana.” Hivyo tu ndivyo alijibu Net akionekana amelemewa hawezi hata kuzungumza.

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

Wakiwa njiani kwa kuwa kila mtu alikuwa kimya. Net macho dirishani, bibi Cote macho dirishani, Maya akaona atoe simu yake. Akakuta mmoja wa rafiki yake amemtumia video na ujumbe.  ‘It’s all over the social media. It went viral Maya! Ni mbaya mno. Renee ameisambaza makusudi anasema ni ushahidi wake yeye kwa vyombo vya usalama. Hakumtendea ubaya wowote Tunda na alimuonya Vic lakini Vic hakusikia. Ndio maana tokea mwanzo alianza kuchukua video.’ Maya akashituka sana.

Akawasha ile video. Waliposikia sauti ya Vic, wote mpaka bibi yake wakamgeukia Maya. “Ni nini tena?”  Akauliza bibi Cote. Maya akawasomea ule ujumbe. Bibi Cote akataka ile sauti iunganishwe na spika za gari ili kuweza kusikia vizuri. Mpaka video inaisha Tunda ameanguka chini, Maya na Net wakaelewa ni kwa nini Tunda alikuwa akilia na kushindwa hata kuwatizama usoni.

Bibi yake akamtizama Net akiwa amebadilika. Mwekundu mpaka anatetemeka midomo. “Haikuwa kama anavyosema, Nana. Tafadhali naomba uniamini.” “Hapo ndipo mtakapojua wakati wote nilipokuwa nikiwaambia juu ya Vic, na mimi sikuwa nikidanganya. Lakini mlishindwa kuniamini. Kwa hili Net, hakuna jinsi ukajitetea na kuaminika.” Maya akaweka msisitizo.

“Vic amedanganya makusudi na kuongeza maneno aliyokuwa akiyasikia mtandaoni ili kumuaminisha Tunda. Tafadhali Nana!” “Nataka unijibu swali moja tu Net. Jibu la ‘ndiyo au hapana’. Unanielewa?” Maya mpambe akasogea kabisa kama vile waonane vizuri usoni. “Nakuahidi nitakuwa mkweli Nana.” “Nataka jibu la ndiyo au hapana. Basi.” Akaweka msisitizo bibi Cote.

“Okay.” Akakubali Net na yeye akionekana ameishaingiwa hofu kubwa kama anayejua swali la bibi yake.  Akajiweka sawa yule bibi. “Vic alilala na wewe baada ya kufunga ndoa na Tunda? Ndiyo au hapana. Basi.” Net akabaki kimya. “Net?” Net akamwangalia bibi yake. “Ndiyo au Hapana?” “Kwa nini hutaki nijieleze Nana?” “Net! Kama kuna maelezo yeyote juu ya hili, mimi na wewe tunajua wazi hukukusudia nijue. Na inaonekana zilifanyika juhudi za makusudi ili mimi nisije hata kuambiwa. Nataka ibakie hivyo. Kwa manufaa ya nani! Wewe unajua ni kwa nini ulificha. Sasa, kabla sijafanya chochote zaidi na kujidhalilisha, au kumdhalilisha Tunda zaidi, nataka jibu kwa ufupi tu. Ndiyo au Hapana?” Akamuona Net anatokwa na machozi huku akimwangalia.

“Son?” Bibi yake akamuita taratibu kwa unyonge kama aliyekwishapata jibu lakini anatamani isiwe vile alivyofikiri. “Ndiyo.” Akakiri Net kwa machozi. Bibi yake alimwangalia kwa sekunde kadhaa. Yale macho tu, Net alijua bibi yake ameumia sana. “Naomba usimamishe gari. Sasa hivi.” Dereva akaegesha gari pembeni, mlinzi wake akashuka na kumfungulia mlango. Akatoka ndani ya gari. Wakamuona ametoka akatembea kidogo, akainama huku ameshika magoti. Mlinzi alisimama hatua chache pale alipokuwa ameinama bibi Cote.

Kwa Tunda.

H

uku nyuma kwa Tunda, alilala mpaka saa sita usiku, akaamka. Nesi aliingia amamkuta ametulia kimya kitandani. Alipotaka kumpima, akakataa. “Ukaniletee mtoto wangu kwanza.” Tunda aliongea taratibu tu akikwepesha mkono. “Mtoto yupo kwenye uangalizi mpaka kesho atakapo ruhusiwa na daktari.” Nesi akamjibu kwa ustaarabu tu. “Basi na muda huo ndio na wewe urudi hapa ndani. Hakikisha si wewe wala muuguzi mwingine anarudi tena humu ndani bila mtoto wangu.” Tunda akamaliza hivyo na kufunga macho. 

“Mrs Cote!” “Naomba uzime na taa ya pale kwenye sinki.” Akamaliza Tunda bila kumwitika yule nesi na hakufungua tena macho wala hakutaka amguse. Akamsikia yule nesi ametoka. Baada kama ya dakika 20 akahisi taa kubwa zimewashwa. “Muone mama! Muone!” Akasikia sauti ya mtu mzima ikiongea kitoto, Tunda akafungua macho kwa haraka, akajua ameletewa mtoto wake. 

Alikuwa mtoto wa kizungu kabisa. Wakamsogezea karibu. “Unauhakika huyu ni Cote!?” Tunda akauliza huku akilia. “Ndiye. Jitambulishe kwa mama.” Yule nesi akamwambia Cote huku akimfunika vizuri. Wakampandishia kitanda juu kidogo akawa kama amekaa kidogo ila uzito ukawa mgongoni. Nesi aliporidhika amekaa vizuri, Tunda akampokea kama asiye amini. Akasoma jina mkononi. ‘Cote Junior Cote’. Akambusu na kumkumbatia. “Naomba muda na mtoto wangu.” “Uliniambia nikikuletea mtoto utakubali nikupime. Naomba niangalie pressure kwanza.” Yule nesi wa pili aliongea na tabasamu la kubembeleza. “Asante sana. Nakushukuru.” Tunda akampa mkono. 

“Naona pressure sio mbaya. Ukija kupumzika na kuamka tena, utajisikia vizuri zaidi.” “Hata sasa najisikia vizuri.” Akajibu Tunda, macho kwa mtoto wake. “Naweza kumnyonyesha?” Wakaangaliana wale wauguzi wawili pale kwenye chumba cha Tunda. “Nimesubiri kumnyonyesha huyu mtoto kabla hata hajazaliwa! Naomba msiniwekee kipingamizi.” Tunda akawasihi. “Alikuwa kwenye uangalizi mpaka wa mapafu. Naomba nimpigie simu daktari wake niulize kwanza.” “Kwani ni mgonjwa?” Tunda akauliza taratibu tu akimtizama Cote aliyekuwa amelala. 

“Mpaka sasa kila kitu kinaonyesha yupo sawa kabisa. Ila naomba niulize kwanza.” Yule nesi ambaye alionyesha ni wa upande wa watoto, akamueleza vizuri tu Tunda, mpaka akaridhika. “Sawa.” Tunda akakubali. Yule nesi akatoka kwenda kuwasiliana na daktari wa watoto. Baada ya muda akarudi na kuambiwa anaweza kumnyonyesha tu. Wakamuweka sawa, Tunda akawaomba wamsaidie kumuamsha. Alifurahi sana alipofungua macho. “Anamacho yenye rangi kama ya Net!” Tunda aliongea huku akimshika vizuri baada ya nesi wake kufanikiwa kumuamsha. 

Wakampisha. Japokuwa hakuwa akitoa chochote, lakini Tunda akafurahia kule kuona mtoto wake akivuta chuchu zake. Hakuwa akiamini kama ni yeye ananyonyesha! Cote alivuta hizo chuchu akaishia kulala tu, hakupata kitu. Lakini hiyo furaha aliyopata Tunda kwa kunyonyesha, hakuwa na jinsi yakueleza. Akamuweka kifuani, akamkumbatia kwa upendo, akajirudisha kulala. Nesi aliingia. Akamchukua mtoto kwa makubaliano akiamka tena, ataletewa tena mtoto.  Ilikuwa usiku huo lazima Cote arudishwe alipokuwa amehifadhiwa kwa uangalizi zaidi. Bila hata dawa, Tunda akarudi kulala tena. Lakini wakampa dawa ya pressure. 

Aliamshwa saa 10 ya asubuhi. Safari hii aliletewa mtoto aliyekuwa akilia njaa. Tunda alifurahi sana. “Labda akivuta akiwa na njaa yatatoka!” Akampokea huku akilia. Alipomuweka tu kifuani, akatulia na kuanza kuvuta. Tunda na wale manesi wakacheka. Akavuta kwa nguvu, akaanza kusikia chuchu zikisisimka. Akawaambia wale manesi. Wakamwambia haitachukua muda mrefu, ubongo utapata taarifa kuwa kuna chakula kinahitajika, yataanza kutoka. 

Tunda aliendelea kunyonyesha huku akimtizama huyo mtoto kwa furaha yote. Alishasahau hekaheka za Vic na msaliti Net. Akili zikawepo hapo kwa mwanae. Baada ya kama nusu saa wakamchukua mtoto, Tunda akasafishwa na kupewa dawa, akarudi kulala. 

Tunda atoweka kwenye mazingira ya kutatanisha.

U

siku wa kwa kina Cote ulikuwa mzito sana. Saa 12 alfajiri, Net akawa amesharudi kwenye chumba alichokuwa amelazwa mkewe hapo hospitalini. Hakumkuta yeye wala kitanda. Hicho kikamfariji akijua hakuna baya lililompata usiku. Kama ingekuwa ni kifo, basi angekuta kitanda tu na wangeshakuwa wamepigiwa simu. Akahisi labda amechukuliwa kwa vipimo fulani. Akakaa hapo kidogo akitafakari kitu cha kumwambia Tunda kutokana na kile alichoona Vic amemwambia. Akakaa kama dakika tano zaidi, akaona atoke akamuulize mlinzi aliyempita hapo nje bila hata salamu, aliyekuwa ameachwa siku iliyopita ili kumlinda Tunda .

“Amekuja kuchukuliwa kama dakika 20 zilizopita. Amekwenda kufanyiwa MRI ili kujua kama alivyoanguka jana kama kuna sehemu aliumia.” Mlinzi akatoa hayo maelezo kwa Net. Net akaafikiana naye akiona inaleta maana. Akarudi ndani kwenye chumba alichokuwa amelazwa mkewe, akakaa. 

Baada ya nusu saa Maya na bibi yake wakaingia hapo. “Tunda yuko wapi?” “Mlinzi ameniambia wamekwenda kumfanyia MRI ili kujua kama ameumia popote ndani.” “No. Nilisema Tunda asi asi... No.” Akatoka bibi Cote kwa haraka.

“Nilikwambia nini jana?” “Kila anapokwenda Tunda niwepo. Ila muuguzi aliyemchukua amesema ni kipimo ambacho huko anapokwenda ni wafanyakazi tu ndio wanaruhusiwa kuingia.” “No. No. Noooooo!” Bibi Cote akakataa kwa hasira sana. “Nahitaji kuzungumza na kiongozi aliyekuwepo zamu jana.” Akaanza bibi Cote kwa sauti. Ile kelele yake ikasikika na manesi waliokuwepo chumba cha pili wakatoka na mapokezi ndogo ya hiyo gorofa aliyolazwa Tunda pia wakasogea.

“Jana nilizungumza na uongozi wa hospitali na kumuacha huyu mlinzi kuwa amfuate Mrs Cote popote atakapotakiwa kwenda, tena kama nimuhimu. Kwa nini Mrs Cote anafanyiwa MRI bila mlinzi wake?” Tayari bibi Cote alikuwa akiwaka mpaka daktari wa zamu akaja. “Ni muda gani umepita tokea apelekwe?” Yule bibi akaunganisha swali kwa mlinzi. “Dakika 52 mpaka sasa.” Akajibu yule mlinzi. Walipogeuka kuwangalia daktari na wale manesi, walishakimbilia chumbani kwa Tunda. Wakafuata nyuma.

“Mrs Cote hana kipimo cha MRI!” Akaongea dokta wa zamu akiwa anasoma kwenye tablet yake. Wakaangaliana. “Piga simu MRI kuuliza.” Wote wakarudi mapokezi kwa haraka. Kupigwa simu MRI, Tunda hakuwepo. Baada ya dakika 10, hospitali ilishafurika polisi na ikawa imefungwa, hakuna kutoka wala kuingia. Anatafutwa Tunda.

Bibi Cote akataka apelekwe yeye mwenyewe kwenye chumba kinachohifadhiwa kamera za hospitali yote. Akaongozana na mapolisi, Net, Maya na mlinzi wa bibi Cote nyuma wakimfuata huyo bibi aliyekuwa akitembea kama anakimbia. Mlinzi aliyekuwa ameachwa nje ya mlango wa Tunda naye alikuwepo. Akaeleza muda kamili Tunda alipokuja kuchukuliwa. Muhusika wa zile kamera akarudi nyuma mpaka kwenye muda ule aliosema mlinzi kuwa Tunda alikuja kuchukuliwa. Na kweli. Wakamuona muuguzi akimtoa Tunda akiwa kwenye kitanda chake vilevile akionekana amelala. Akamsukuma mpaka kwenye elevetor. Lift.

Akaonekana ni kama anayejua anachokifanya na kuifahamu vizuri ile hospitali na zilipo kamera zote. Hakugeukia kamera hata moja. Kwa hiyo hawakuona sura yake ila mgongo tu. Wakahamia kwenye kamera ya ndani ya lift. Wakamuona anatoa simu mfukoni, kama amempigia mtu simu, wanazungumza lakini ndani ya lift walikuwa wakirikodi bila kuchukua sauti, kwa hiyo hawakusikia mazungumzo. Wasiwasi ukaanza kuwaingia.

Tunda hakuonekana hata kutingishika. Ni kama aliyekuwa kwenye usingizi mzito sana. Wakamuona ameshuka naye mpaka gorofa ya tatu, akamtoa sehemu ya kuegesha magari. Wakahamia kwenye kamera ya sehemu ya kuegeshea magari. Wakaona kijana mmoja anatoka kwenye gari ndefu tu na yenyewe kama ya wagonjwa, ila nyuma imefunikwa kabisa. Hamna hata madirisha. Wakasaidiana kumbeba Tunda, wakamwingiza nyuma ya hiyo gari na yule nesi naye akapanda kulekule alipolazwa Tunda. Yule kijana alionekana amevaa soksi usoni, akafunga mlango wa nyuma, akapanda upande wa dereva na kuondoa gari kwa kasi.

Net alitoka hapo anakimbia mpaka sehemu ya kuegeshea magari, akakuta kitanda kile alichokuwa amelalia Tunda kimeegeshwa palepale pembeni, lakini Tunda hayupo. Hapo hapo bibi Cote akatoa simu. “Samahani kwa usumbufu. Lakini ninashida ambayo haiwezi kusubiri hata sekunde.” Akaanza bibi Cote. Chumba kizima kikawa kimya. Akasikiliza kidogo kisha wakamsikia akijibu. “Asante. Lakini hii ni kwa masikio yako na macho yako tu, mpaka nitakapokuruhusu uzungumze na mwingine.” Upande wa pili akajibu.

Kisha akaendelea. “Mrs Cote amechukuliwa hapa hospitalini na watu nisiowafahamu au bila ruhusa.” Akamgeukia yule muhusika aliyekuwa akiwaonyesha kwenye Kamera.   “Naomba mtajie muda wa hiyo gari ilipoacha viwanja vya hospitalini na aina ya gari yenyewe, ili anisaidie kufuatilia kwenye satellite. Sasa hivi tafadhali. Nakuweka kwenye speaker.”  Akamtajia aina ya gari na muda. Huyo aliyepigiwa simu akauliza maswali machache sana akaomba awarushie na wao kile anachokiona. Hilo likawa jema. “Nipo hapa na  polisi pamoja na uongozi wa hospitali.” Akaweka angalizo bibi Cote kwa mtu aliyempigia simu ambaye hakumtaja jina.

Baada ya sekunde chache wakashangaa wamerushiwa picha kamili na wao wakaanza kuona anachokiona yule mtu wa bibi Cote. Ile gari ilionekana imetoka pale hospitalini. Wakaifuatilia kwa kuiangalia. Ilikuwa ikienda kwa mwendo kasi. Na kwa kuwa walitoka alfajiri sana, bado nje kulikuwa na giza na hapakuwa na magari mengi. Ni kama dereva alijua ni wapi apite na nini chakufanya. Alivutwa kwa karibu, bado alikuwa amevaa soksi usoni. Na watu wa nyuma kwenye hilo gari hawakuonekana kabisa ila yeye tu dereva aliyekaa mbele. 

Wakaona anapeleka gari kwenye barabara yenye magari mengi kidogo. Akaendesha mpaka barabara hiyo inapopita kwenye tunnel. Kama chini au ndani ya daraja iliyozibwa kote isipokuwa mbele na nyuma. Haikuwa tunnel ndefu lakini akapita hapo. Akavuta kamera kuona alipotokea. Hawakuona gari. “Mbona sioni tena hiyo Van/gari!?” Akauliza bibi Cote kwa wasiwasi. “Huyo dereva aliyemchukua Mrs Cote ametumia akili sana!” Akaongea yule mtu kule kwenye simu.  “Sielewi!” Akaongeza bibi cote. 

“Amepita chini ya daraja makusudi ili kutupoteza. Lazima kuna mtu wa  tatu au wapo zaidi ya wawili ambao wanashirikiana.” Polisi mmoja wa palepale ndani ya kile chumba akaongeza. Wote wakamgeukia. “Ambaye atawasaidia kubadilisha gari. Alijua hiki kinachofanyika sasa hivi kitatokea. Mtafuatilia gari kwa satellite. Kwa kiyo ameliacha  hilo gari ndani ya hiyo tunnel.” Maya akaanza kulia. 

Hapo hapo ikapigwa simu ya polisi ambao wapo doria karibu na hiyo tunnel, waende kuangalia. Kisha askari wawili na wenyewe wakatoka kwa haraka wakikimbia kufuata hiyo tunnel. Baada ya dakika 5 tu, simu ikapigwa na polisi waliokuwa doria ambao walishawasili pale chini kwenye tunnel. Walitaarifu kulikuta hilo Van/gari nyeupe  hapo lakini hapakuwa na mtu yeyote ndani. 

Bibi Cote akafunga macho kwa muda. Wakamuona anapiga simu nyingine. Iliita mara moja tu. “Wamemuiba mke wa Net  hapa hospitalini asubuhi hii. Tafadhali nisaidie.” Akasikiliza kidogo.  “Ndiyo.” Wakamsikia akijibu lakini akiwa ameishiwa nguvu kabisa. Akamkabidhi mmoja wa kiongozi wa polisi ile simu. Bila kujua anazungumza na nani, lakini akiwa amejiandaa kuwa lazima ni kiongozi  mkubwa tu kwa kuwa ni bibi Cote, akaanza kwa heshima. Yule mtu alionekana kujitambulisha na kuomba taarifa kwa ufupi. Alikuwa mkuu wa CSIS. {Canadian Security Intelligence Service}. 

Wote, bibi Cote, Maya, Net pamoja na mlinzi aliyekuwepo akimlinda Tunda wakatakiwa kwenda kituo cha polisi kwa mahojiano. 

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

Lile tukio likachukua sura mpya na nzito. Mpaka Net akawa kwenye matatizo kutokana na ile video na kile kilichozungumzwa na Vic kwa Tunda. Walipofika tu kituo cha polisi waliambiwa Tunda anatafutwa na watu wenye uzoefu sana. Anatafutwa kuanzia kwenye satellite mpaka kwenye lile gari lililohusika kumtorosha Tunda, tayari wapo watu wataalamu kwenye eneo la tukio. Wakifanya uchunguzi ndani na nje ya hilo gari kuona kama wanaweza kupata fingerprints/alama za vidole au hata nywele itakayokuwa imeachwa humo ndani ili ikapimwe ijulikane waliomchukua Tunda ni kina nani. Ila wakaomba ushirikianano wao.

Kwa haraka sana bibi Cote akaitika bila shida. Wakaingizwa kwenye chumba kikubwa sana cha mkutano chenye tv. Wakashangaa kuona na kina Carter, Ms Emily na walinzi wote waliokuwepo jana na siku hiyo wanaingizwa pale. Akafika mkuu wa kituo na kiongozi wa CSIS. Bibi Cote akasimama na kusalimiana nao kwa kuwa aliwafahamu vizuri tu. Wakaongea kidogo, kisha akaanza yule kiongozi wa CSIS.

“Ninaomba mtoe ushirikiano wenu wa asilimia 100, ili kuweza kusaidia vyombo vya usalama kumpata kwa haraka Mrs Cote. Hakuna aliyekamatwa wala kuhisiwa anahusika mpaka sasa. Jambo lolote lile mnaloona litasaidia hata kidogo tu, tafadhali usiache kuwaambia polisi watakao husika kwenye kuwahoji baada ya hapa.” Akaendelea yule mkuu wa CSIS.

“Tutawawekea video ambayo ni muhimu sana kuiangalia na kuisikiliza kwa makini ili kuweza kujibu maswali mtakayoulizwa baadaye kutokana na video hii.” Wakakubali bila shida, lakini kila mmoja akiwa na wasiwasi. Mara akaingia Vic na Renee, wakisindikizwa na polisi lakini hawana pingu. Walikaa pembeni kabisa. Wakaongezeka polisi mle ndani ya kile chumba chote na taa ikawashwa vizuri, kukawa na mwanga wa kutosha.

“Ili kuharakisha mambo na wote tuwahi kwenye shuguli zetu, tafadhali usiongee chochote kama hujaulizwa. Na kila mmoja atapata muda wa kuongea anachotaka, pale atakapopewa nafasi.” Akasisitiza mkuu wa polisi. Kimya. Wakashangaa inawekwa video aliyochukua Renee ya mazungumzo ya Vic na Tunda mpaka mwisho. Bibi Cote alibaki kimya. Maya akilia na Net ndio hakuwa akitizamika. Mwekundu, anapenga kamasi kila wakati na macho yalikuwa yamevimba haswa.

Ile video ikaisha. Watu wote kimya. “Utakaposikia jina lako likitajwa, tafadhali ongozana na polisi mpaka chumba cha mahojiano. Huko utapata nafasi ya kuuliza chochote, na ninarudia tena. Mpaka sasa hatuna muhalifu. Ila nyinyi mpo hapa kwa kuwa ni watu wa mwisho mliokuwa karibu na Mrs Cote, tunahitaji ushirikiano wenu.” Kimya. Wakaitwa walinzi wote waliohusika kumlinda Tunda siku iliyopita na mpaka anatoroshwa pale hospitalini. Wakahojiwa kila mmoja kwenye chumba chake huku wakichukuliwa video.

Bibi Cote.

I

kafika zamu ya bibi Cote. Akaongozana na polisi mpaka chumba maalumu cha mahojiano. Wakajitambulisha kwake kwa majina yao wote, bibi Cote akiwatizama tu, akaanza kuulizwa maswali. “Uliona na kusikiliza mazungumzo ya Mrs Cote na Vic?” “Ndiyo.” Akajibu  bibi Cote kwa ufupi tu akiwa ametulia ila sio jasiri vile.

“Uliyajua mahusiano  kati  ya  Net  na Vic?” Bibi Cote akakunja uso kidogo. “Wakiwa   bado vijana wadogo. Ndiyo.” “Baada ya hapo?” “Net alikaa muda mrefu tu bila kuwa na msichana yeyote. Ndipo akataka kumuoa Chloe, lakini alisema moyo wake uko kwa Tunda. Ndipo akaachana na Chloe na kurudi nchini Tanzania kumtafuta Tunda.” Akajibu Bibi Cote. “Wewe ulishawahi kukutanishwa na Chloe na mkapata naye muda wa mazungumzo?” “Ndiyo.” “Ulimuonaje?” Bibi Cote akafikiria kidogo. “Okay!” Akajibu bibi Cote huku akifikiria.

“Just Okay?” Yule anayemuhoji hakuwa ameridhika na hilo jibu ikabidi aulize tena. “Kumbuka alitakiwa kuwa mkwe kwangu sio  mke wangu au mume. Mtu sahihi kwangu alikuwa Cote na ndiye aliyenioa. Sasa nani anaolewa na Nathaniel au anamuoa Maya ni juu yao wao.” Bibi  Cote akatumia akili za haraka.

“Lakini si Vic?” Akamuuliza kwa kumtega. “Unamaanisha nini?” Na yeye bibi Cote akauliza akijua anategwa. “Kwenye ile video, Vic alimwambia Tunda wewe ndiye mtu pekee unayesimama kati yake na Net.” “Unakumbuka kumsikia Vic akisema mimi nimesema hivyo?” Bibi Cote akauliza kwa makini akimtizama machoni. “Hapana.” Akajibu yule anayemuhoji bibi Cote.

“Lakini anaonekana Vic anauhakika juu ya hilo.” Akadakia mwenzake na yule anayemuhoji. “Kwa hiyo hapa mnataka nizungumzie juu ya hisia za Vic?” Akawauliza bibi Cote akiwatizama kwa zamu. Kimya. “Kama hakuna swali la nyongeza, naomba nikasaidie kutafutwa kwa Mrs Cote.” “Hiyo kesi sasa hivi ipo chini ya CSIS. Sisi sasa hivi ndio tunafuatilia. Na hiki unachokifanya sasa hivi ni hatua moja wapo yakupatikana kwa haraka Mrs Cote.” “Kwa kuzungumzia hisia za Vic!?” Akauliza bibi Cote.

“Kwa kusaidia kujua motive au lengo. Aliyemchukua alikuwa na nia gani!” “Labda kwa ufupi tu, tuanze kwa  kusema ni kwa sababu ni Cote. Pengine wanataka umaarufu au pesa. Kwa hiyo muda na wakati wowote mtu anaweza kupiga simu akitaka alipwe pesa ili wamrudishe. Mmeshalifikiria hilo?” Akaongeza bibi Cote. “Simu zenu zote zipo chini ya mitambo ya CSIS. Atakayepiga, aliyepiga, anayewasiliana tokea jana, wote mnachunguzwa. Hilo usiwe na wasiwasi nalo.” Bibi Cote akavuta pumzi na kujirudisha nyuma.

Net!

K

wa Net mambo yalimgeukia vibaya sana. Mpaka akafika mahali akasema hatajibu tena kitu mpaka Logan awepo. Walianza taratibu tu. “Mahusiano yako na Chloe yalikuaje?” “Mazuri tu mpaka nilipomuomba tuhamie naye nchini Tanzania na kukataa ndipo mambo yalipoanza kubadilika.” “Kivipi?” “Chloe alitaka nimuoe kisha nimuache pale nyumbani, halafu mimi niende popote ninapotaka. Wakati mimi nilitaka mwanamke ambaye nitakuwa naye popote.” Akajibu Net.

“Ndipo ukamuacha?” “Ndiyo.” “Alilichukuliaje swala la kumuacha?” Net akatulia kidogo kama anayefikiria. “Mr Cote?” “Alilia sana. Lakini nilimwambia ninampenda mwanamke mwingine, ambaye ni Tunda.” “Oooh! Kwa hiyo ulimwambia unamuacha sababu ya Tunda na si kwa kukataa kwake kwenda nchini Tanzania?” Hapo Net akajua ameshajichanganya. Akatulia kidogo.

“Mr Cote?” Wakamuhoji tena. “Tunda alikuwepo kabla ya Chloe. Lakini Tunda akanipotea ndio maana nikaamua kumuoa Chloe kabla ya papa kufariki ili angalau ashuhudie nikiwa nimeanzisha familia kabla hajafariki.” Akajibu Net. “Je, Chloe alijua kama unamtumia kwenye kutimiza ndoto zako kwa babu yako?” Net akakunja uso. “Sikuwa nikimtumia mimi Chloe!” “Ndivyo ulivyosema Mr Cote. Au tukuonyeshe ulichozungumza muda mfupi uliopita?” “Najua ni nini niliongea.” Akajibu kwa jeuri Net.

“Je, Chloe alijua kuwa unamuacha kwa ajili ya Tunda?” Net akatulia. “Mr Cote?” Net akanyanyua uso kuwatizama. “Chloe alijua kama unamuacha kwa sababu ya Tunda?” “Huu muda tunaopoteza hapa, si tungeutumia kumtafuta mke wangu?” Akagomba Net. “Hivi hapa ndio tunamtafuta Mrs Cote. Maana aliyemchukua anaonekana anajua wazi ni nini anafanya. Kwa kuwafahamu nyinyi vizuri sana na Mrs Cote, pengine kwa kupitia nyinyi wenyewe. Sasa kwa kujibu maswali hapa, ndipo tutajua ni wapi pakumpata Mrs Cote. Sijui kama umeelewa?” Kimya.

“Narudia swali. Je, Chloe alijua kama unamuacha kwa ajili ya Tunda?” “Ndiyo.” Akajibu Net akiwa ameshabadilika kabisa. “Kwa hiyo ulimtamkia wazi kuwa unamuacha kwa ajili ya Tunda.” “Ndiyo.” Net akajibu huku ameinama kama ambaye anazidi kuumizwa. “Mpo kwenye mahusiano na Vic kwa muda gani?” Yule muuliza maswali wa kwanza akauliza. “Sipo kwenye mahusiano na Vic, mimi ni mume wa Tunda.” Wote wakamwangalia na kalamu mkononi akiwa amekaa mbele yao.

“Labda tuweke msisitizo. Tunahitaji ukweli.” “Na mimi najibu ukweli. Sipo kwenye mahusiano na Vic.” “Tunao ushahidi aliotupa jana Vic, ukionyesha mkinywa chumbani kwako na mkifanya mapenzi.” Net akatingisha kichwa kwa kuumia sana.

“Ilikuwa hivi.” Net akaanza. “Nilijua mke wangu angetoka jela na tungerudi naye kuishi huku. Katika kutengeneza chumba changu, au watu waliokuwa wakitengeneza chumba changu ili kuchukua sura yangu na mke wangu tu, niliwaambia watoe picha zote ambazo walikuwepo watu wengine akiwepo Vic.” Akaendelea Net.

“Niliwapigia simu Troy na Lean. Wakaja nyumbani nikawakabidhi kumbukumbu za picha zetu tulizokuwa tumepiga sisi wanne, yaani na Vic akiwemo. Nikawaambia itabidi nimtafute na Vic nimkabidhi. Waliondoka na baadhi ya picha, tukikubaliana zinazobaki nije kumkabidhi Vic.” Net akaendelea. “Nilitoka kazini. Ilikuwa mida ya jioni tu. Nikampigia simu Vic kumuomba apite kesho yake pale nyumbani achukue zile picha. Vic akaniambia yupo karibu na pale, anaweza kufika jioni hiyo. Sikuona tatizo.”

“Lakini haikuwa hivyo. Haikuchukua muda mfupi kama alivyosema Vic kuwa yupo karibu na pale. Alifika nyumbani kama baada ya masaa mawili. Alinikuta nimekaa mimi na mdogo wangu Maya. Tulikuwa tumemaliza kula, tunakunywa tu. Maya akaniaga, akaelekea chumbani kwake kwenda kulala. Maana ilishakuwa muda wa kwenda kulala. Ms Emily alishaondoka kwenda nyumbani kwake. Mara nyingi Ms Emily huondoka muda unaofanana na Gino, ambaye ni mpishi wetu. Carter ambaye miaka yote huwa anaishi hapo, na yeye muda wake wa kazi ukishaisha, anahamia upande ulipo sehemu anayoishi. Ndani ya nyumba hiyo hiyo.”

“Vic akaagiza kinywaji. Carter alipoleta, akaaga moja kwa moja kuwa anakwenda kulala. Akatuacha mimi na Vic. Kwa kuwa na mimi nilitaka kulala ili niwahi kazini siku inayofuata, nikamwambia Vic anisubiri, niende chumbani nikamletee picha zake. Akauliza kwa nini natoa picha zake kwenye chumba changu? Nikamwelezea kuwa mke wangu anatoka jela. Tunaanza upya. Nikamwambia ninaanza kumbukumbu mpya na mke wangu. Sitaki kuje kuwe na maswali au picha zao sehemu nitakayokuwa nikilala na mke wangu.”

“Kama Vic alivyo. Akalalamika huku akiniuliza maswali mengi juu yangu na Tunda, nikajaribu kumjibu, mwishoe kwa hasira, nikamwambia mimi siwajibiki kwake kwa lolote. Nikaondoka nikaenda chumbani kumchukulia vitu vyake. Ile nimeingia tu chumbani, Vic naye akanifuata na ile juisi yangu niliyokuwa nikinywa. Akaniomba msamaha na kuniambia ni kweli alitakiwa kuheshimu swala la kuoa kwangu. Na mambo mengine mengi. Alikuwa ameshanikabidhi kinywaji changu tokea alipoingia. Kwa hiyo wakati anaongea, mimi nikaendelea kunywa.” “Ilikuwa ni kinywaji gani?” Akauliza anayemuhoji.

“Juisi tu. Haina kileo. Ni matunda tu. Huwa anatengeneza mpishi wetu pale nyumbani. Na utaipata hapo nyumbani kwetu tu.” “Okay, endelea.” Akamtaka Net aendelee. “Vic ni mzungumzaji. Ni wale watu wenye uwezo mkubwa wakuelezea jambo hata dogo na kulipa kisa kikubwa tu. Wakati akiendelea kuzungumza, nikajisikia kama kizunguzungu. Nikamwambia. Akaniambia labda ni uchovu tu, nijaribu kukaa.” Wakamuona Net akitingisha kichwa kwa masikitiko.

“Nilikuja kustuka asubuhi. Nipo kitandani kwangu na Vic na wote tupo uchi! Nilipaniki mpaka na yeye akaogopa maana nilifungua macho nikamkuta pembeni yangu akinitizama. Nilipiga kelele na kuruka kitandani. Kwanza nilikuwa nimechelewa kazini. Na si kawaida yangu yakupitiliza muda. Kuangalia saa ilikuwa siku ya kazi na ni saa nne asubuhi. Ile kelele ikamfanya Carter aje agonge chumbani kwangu.”

“Nikamuuliza ni kwa nini hakuniamsha au hata kuja kuangalia kwa nini nimelala muda wote huo siku ya kazi! Akasema aligonga pale chumbani, lakini Vic akamwambia nimeomba muda wa kupumzika! Ndio ikabidi Carter aondoke bila kuzungumza na mimi mpaka hapo nilipomwita tena. Palepale mbele ya Carter nikamuuliza Vic, ni kwa nini aliongea vile. Akasema usiku nilimwambia kuwa nimechoka sana. Kwa hiyo akafikiri nahitaji muda wakupumzika kwa kuwa nimekuwa na mambo mengi. Carter akaondoka.”

“Nikamuuliza na yeye kwa nini yupo pale? Akasema aliniona asiniache kwenye ile hali.” “Hali gani?” Akauliza mmoja wa afisa aliyekuwa akimuhoji Net maswali. “Na mimi nikamuuliza hivyo hivyo. Akajibu hali niliyokuwa nayo ya uchovu na upweke. Akaanza kuongea mambo mengi. Mimi nikamwambia achukue zile picha na aondoke asiwahi kurudi kuja kulala tena pale. Nikamwambia mimi nimeoa na sitakuwa tayari kumsaliti mke wangu. Nikamsisitiza kuwa nampenda mke wangu.”

“Vic aliondoka. Sikumsikia tena mpaka siku aliporudi tena chumbani kwangu na mke wangu, akamkuta mke wangu amelala. Nilimgombesha sana Vic na kumuonya asiwahi tena kurudia kuja kuingia chumbani kwetu na nikamwambia asirudi tena pale nyumbani mpaka atakapo karibishwa kwa kuwa mambo yamebadilika, mimi ni mume wa Tunda na pale ni nyumbani kwa mke wangu pia. Akaondoka akilia huku akinikumbusha tulipotoka na mambo mengine. Lakini mimi nikamwambia hiyo ni zamani nikiwa sijaoa.”

“Juzi nipo kwenye kuonja keki ya harusi yangu na mke wangu, ndipo tukapata taarifa yupo nyumbani kwetu. Ikabidi kukimbia kwenda kujua amefuata nini?” “Video inaonyesha alimwambia Mrs Cote kuwa anamazungumzo na yeye. Kwa amani tu. Kwa nini unafikiri Carter aliingiwa na wasiwasi na kumtafuta bibi yako kwa haraka?” Afisa mwingine akarusha swali kwa Net.

“Carter anamfahamu Vic. Huwa hana jema na hakubali kushindwa. Anajua wazi kitendo cha Vic kutofika pale nyumbani mpaka akaribishwe na hakuwa amekaribishwa kwa muda mrefu, Carter alikiri kwangu jana kuwa alijua Vic atakwenda kumkorofisha mke wangu tu, ambaye hakuwa akijisikia vizuri. Ndio maana alimtaarifu Nana kwa haraka.” “Kwa nini sio wewe? Hudhani ni kwa kuwa anajua upo kwenye mahusiano na wote wawili kwa hiyo unaweza kutotilia uzito! Ukapuuza umuhimu wa kuingilia kati?” “Hata Carter anajua sipo kwenye mahusiano na Vic, na anajua nampenda mke wangu!” Net akajibu kwa kushangaa.

“Sasa kwa nini hakukutafuta wewe mwenye mke, amtafute bibi yako?” Yule afisa akasisitiza swali lake. “Narudia tena. Carter anamfahamu Vic tokea yupo mdogo. Jambo la haraka linalohitajika kufikia akili ya Vic na akatulia na kumsikiliza mtu, nilazima Nana ahusishwe. Ni mtu ambaye anaweza kumfanya Vic akatulia bila hata Nana hajafungua mdomo. Ule uwepo wake tu, unatosha kwa Vic.” “Unafikiri ni kwa nini?” “Siwezi kuzungumzia hisia za Vic jamani! Naomba nikamtafute mke wangu.” Net akasimama.

“Kabla hujaondoka. Tunaomba uangalie hizi picha na video.” Wakamgeuzia laptop. Akajiona yeye na Vic wakifanya mapenzi chumbani kwake. Net akakaa akiwa ameishiwa nguvu. “Mimi sijui Vic amefanya nini, lakini mimi sikumbuki hata kufanya mapenzi na Vic miaka ya karibuni. Ni zamani sana kufanya mapenzi na Vic, hata kabla ya Chloe. Na sitajibu swali jingine lolote mpaka awepo mwanasheria wangu.”

“Mimi nafikiri hivi Mr Cote.” Akadakia mmoja wa wale maafisa wawili waliokuwa wakimuhoji maswali, kabla Net hajanyanyuka tena. Alikuwa ni afisa mwanamke. Alionekana yupo makini sana. “Unafikiri nini?” Akauliza Net akiwa amekunja uso. “Nafikiri hivi. Baada ya kupata mtoto aliyekufanya umchukue Tunda kutoka Afrika. Huoni umuhimu wake tena. Na kwa kuwa umebahatika kupata mtoto tayari tena akiwa salama, umeamua kumtowesha kabisa Tunda. Sio kwa talaka ili asije kuchukua mali zako.” Net akashangaa sana.

“Unawezaje kusema hivyo!?” Net akashangaa sana. “Kwa yote uliyozungumza hapa, ukijaribu kukana mahusiano yako na Vic, mpaka tukakuonyesha ushahishi wako ukifanya naye mapenzi. Tena miezi michache tu iliyopita. Tena bila kushurutishwa! Ukionekana unafurahia kabisa unachokifanya na Vic kwa hisia zote! Wazi inathibitisha alichozungumza Vic ni kweli. Kuwa, kilichokufanya umchukue Tunda ni mtoto tu. Kwamba, ulikwenda kuachana naye baada ya haya mapenzi mazito hapa.” Akamuonyeshea ile video yake na Vic kwa kidole akigusa ile laptop, Net akafunga ile laptop kwa nguvu.

“Sasa mimi nakuhakikishia Mr Cote. Nitakukamata tu. Nitatafuta ushahidi wangu wote juu ya hila yako na hao uliowatuma kumtorosha Tunda, na nitakufunga. Hata kama mtatumia akili ya namna gani kumficha Tunda. Mimi nitawakamata!” Yule afisa ambaye alikuwa mwanamke akasimama kwa hasira na kwa kujiamini mbele ya Net. “Na usikae mbali wala usisafiri mpaka uchunguzi utakapo kamilika. Umenielewa?” Akamgeukia Net. Walikuwa watatu tu kwenye hicho chumba cha mahojiano. Wao maafisa wawili. Wakike na kiume, pamoja na huyo Net waliyemchemsha kupita kiasi.

“Mr Cote! Huruhusiwi kutoka nje ya nchi mpaka uchunguzi utakapo kamilika. Na ujue utakuwa ukifuatiliwa. Usifanye watu ni wajinga. Mtu mmoja tu Tunda, hawezi akawa anafatwa katikati ya ulinzi mkali kiasi hicho. Halafu achemshwe mpaka aanguke na kupoteza fahamu na ulinzi ukiwa upo hapohapo, wanamtizama tu Vic kama sio wote wanajua mahusiano yako na Vic!”  Akaendelea yule dada huku akiwa amesimama.

“Halafu eti leo amelazwa hospitalini, anatoroshwa kirahisi kabisa katikati ya ulinzi mkali kiasi hicho! Halafu eti mtu anayemtorosha anajua wapi zipo kamera, na jinsi yakuzikwepa asionekanike! Wapi apite na nini chakufanya kirahisi tu! Akamudu kuondoka na mgonjwa asiye na fahamu, na kitanda kizima, asiulizwe wala kuzuiwa na yeyote yule, mbele ya mlinzi aliyepewa maagizo asiruhusu Tunda atolewe pale! Kama hana baraka za mtu wa ndani ni nini?” Bila kuongeza neno Net akasimama na kumpita yule afisa pale, akatoka kabisa pale ndani ya kile chumba kimyakimya.  

Kwa Maya.

M

aya alichukuliwa na yeye mpaka kwenye chumba cha mahojiano. Akakutana na maafisa wawili vijana. Walijitambulisha kwa majina yao kamili lakini akili za Maya haikuwa kwenye kumfahamu yeyote kwa wakati ule, akabaki akiwatizama na macho mekundu kwa kulia. “Mahusiano yako  na Vic yakoje?” Afisa mmoja akaanza kwa hilo swali na kumshangaza sana Maya. Akabaki ametoa macho kama anayemuuliza “WHAT!”

“Miss Cote?” Akamuita kama kumstua. “Mlisema kujibu maswali hapa si lazima, si ndiyo?” Akauliza Maya. “Ndiyo.” Akachukua pochi yake akasimama. “Nilisikia ukisema Tunda ni dada ambaye hukuwahi kufikiria kama unaweza kuja kuwa naye. Unampenda, anakupenda na kukujali. Si ndiyo?” Afisa mwingine akamuwahi. Maya akageuka alishafika mlangoni. “Kama unataka arudi, lazima utusaidie. Na kwa kadiri tunavyochelewa ndivyo itakavyokuwa ngumu kumpata.” Akaongeza yule afisa. Taratibu tu.

“Sasa kama unalijua hilo, kwa nini bado umekaa hapo ukitaka kuzungumzia habari za mtu kama Vic!?”  Maya akauliza. “Kwa nini si Vic?” Akamuuliza kwa haraka. Maya akageuka vizuri. “Ukiangalia kwenye mitandao yenu ya kipolisi, jina Maya Cote ni baya sana. Lakini ni sababu ya Vic. Hakuna aliyetaka kuniuliza na kunisikiliza isipokuwa Tunda, juzi.” Maya akaanza kutokwa na machozi. “Kama Vic ndiye aliyemchukua Tunda, nawahakikishia kabisa, hamtampata Tunda kwa kumuhoji mtu yeyote hata yeye mwenyewe Vic. Kwa kuwa ni mzuri sana katika uovu wake.” Maya akarudi na kukaa na kujifuta machozi.

“Aliniingiza mimi kwenye madawa ya kulevya. Akahakikisha sitoki. Na nilipotoka, akahakikisha ananirudisha. Vic anatumia madawa ambayo akikulevya au akiwapa watu wake wakuleweshe, kesho yake yale madawa yanapoisha mwilini, hukumbuki ulichofanya. Ukiwa kwenye hiyo hali, atahakikisha anakupiga picha wakati unafanyiwa uchafu na kukuchukua video kama ushahidi wake kuwa ulifanya kwa hiari.” Maya akaendelea.

“Hakuna aliyeniamini mimi, wala kuchukua muda wake kuchunguza vyanzo vyote vya uchafu wote juu yangu mnaouona mtandaoni, isipokuwa Tunda ambaye wamemuiba. Sasa nafikiri sasa hivi Net ataamini na kuonja kule Vic alikokuwa akinipitisha mimi.” “Kwa nini unasema hivyo?” Akamuuliza tena.

“Nakujibu swali hili tu, halafu nakwenda kumtafuta Tunda. Mimi mwenyewe bila hata msaada wa Cote.” “Kwa nini?” Akamuuliza tena. “Nimekwambia nitakujibu ‘kwa nini’ ya kwanza tu.” Bado alikuwa akiongea na kumwangalia yule afisa aliyefanikiwa kumrudisha wakati anataka kutoka.

“Okay.” Akajibu kumuonyesha ameridhia. “Siku anayosema Vic kuwa aliitwa kuja kulala pale na Net, mimi nilikuwepo na Net tukizungumza. Akaniambia Vic atafika hapo kuchukua nafikiri picha zake za zamani au vitu ambavyo vilibaki kwa Net kwa muda mrefu. Nisikilize kwa makini.” Maya akajiweka sawa. “Mimi huwa siwezi hata kumtizama Vic kwa sekunde nyingi. Amejawa ushetani usoni kwake, na ameshanitenda bila watu kunisaidia na kuniamini. Amenichafua, na kuniharibia sana.”

Anyways. Alipoingia tu Vic, sikutaka hata kuhisi uwepo wake. Mimi niliwaacha sebuleni, nikaenda kulala. Kesho yake asubuhi wakati mimi nakwenda kazini, nikashangaa kukuta magari yote ya Net na Vic yapo nje!” Maya akatulia kidogo. “Katika watu waadilifu wa kazi na washika muda ambao nimeshawahi kukutana nao, Net ni mmoja wao mbali na Papa pamoja na Nana. Net hajawahi na hajui kuchelewa kukoje. Mbali na mali nyingi alizorithishwa sasa hivi, Net alirithi huu usemi tokea anakua. Unasema hivi, ‘Early is on time. On time is Late. Late is unacceptable.’  Hayo ndio maisha ya Net.” Maya akaendelea.

“Nasisitiza kuwa, Net hajui kuchelewa ndio inakuaje. Na ukitaka kumkasirisha Net, usijali muda. Kila mtu anayefanya kazi na Net, anajua hilo na kuliheshimu. Basi. Mimi nikashituka sana na kuogopa ni nini kimempata Net nakushindwa kuwepo kazini, na imekuaje mtu aliyekuwa akimlilia mkewe masaa machache kabla ya Vic kuja nyumbani, leo alale na Vic mpaka asubuhi!”

“Maana Nana alikuwa yupo safarini. Akampigia simu Net kumuulizia maswala ya Tunda huko jela. Net akaanza kulia kwa Nana kuwa hajasikia chochote. Na  alimtuma tena mwanasheria mwezi huo ambao yeye hakwenda, lakini Tunda alikataa kutoka. Baada ya kuzungumza wote na Nana, baada ya kama nusu saa ndio Vic anakuja kuchukua mizigo yake, eti Net aje alale naye mpaka asubuhi! Wewe inakuingia akilini?” Maya akauliza. Safari hii akawatizama wote kwa zamu.

“Labda alikuwa amezidiwa na Vic akamkumbushia Net mapenzi.” Yule afisa mwengine akajibu. “Net haongozwi na hisia. Wakati wote, Net amekuwa akimtanguliza Mungu. Alikaa muda mrefu tu bila kufanya mapenzi. Tena kwa kujua kutoka hata kwa Chloe aliyekuwa mchumba wake aliyetaka kumuoa. Chloe alikuwa akilalamikia marafiki zake, ndio ikasambaa na kutufikia kuwa Net ameshindwa kufanya naye mapenzi amemwambia mpaka ndoa. Muiteni Chloe mumuulize kama Net ni mtu wa kukimbilia kitandani na wasichana.”

“Labda kwa Vic!” “Ndivyo hata na yeye Vic atakavyowaaminisha na kuwapa ushahidi. Lakini mimi sijali kile utakachoamini. Ila nataka kukwambia hivi, siku ile asubuhi ilibidi nirudi kumuuliza Carter kulikoni. Carter akasema alikwenda kugonga chumbani kwa Net, akatoka Vic akiwa amevaa shati la Net na kumwambia aondoke awapishe, Net amechoka. Nikamwambia Carter kuna kitu hakipo sawa, Net sio mchokaji katikati ya kazi na kushindwa kuwepo kazini kwa wakati.  Mimi nikaondoka.”

“Kwenye saa tano hivi, asubuhi, Net akaja ofisini kwangu na kuanza kuniapia kuwa hakuna kitu kilichotokea kati yake na  Vic anaomba nimuamini. Alionyesha kupaniki sana. Akasema hata kama angekuwa dhaifu kiasi gani, asingethubutu kulala na Vic pale mbele yangu huku nikijua ameoa. Angelala naye popote lakini sio pale na hajui ni nini kilitokea na kupitiwa na usingizi mzito kiasi hicho mpaka kesho yake.” Maya akaendelea.

“Mimi nimetumiwa hiyo video  na Gina. Vic akizungumza na Tunda. Nimejua mambo yafuatayo. Na nitamwambia Tunda nitakapompata. Na nitampata Tunda na nitamwambia ukweli.” Maya akaongea kwa uhakika. “Siwezi nikamruhusu Vic amtoe Tunda kwenye maisha yangu. Hata kidogo! Amechukua kila kitu kwangu, lakini si Tunda.” “Ni mambo gani umejua?” Akamuuliza kwa haraka maana Maya alishaonyesha kukasirika zaidi.

“Kwanza, Vic haruhusu mtu yeyote kuwa na Net.” “Mbona alimwacha Chloe akawa na Net?” “Nani amekwambia alimuacha? Ni mshenzi Vic asiyeweza kujisaidia. Ni vile Chloe hakujua ni vipi Vic anavyomtenga na Net. Na alitumia akili za ujanja, akamfanya mpaka Net ajithibitishie kuwa Chloe si mke wake. Na kwa taarifa yako tu,  Vic anahusika kwa asilimia 100 kwa Chloe kuachwa na Net.” “Ki vipi?”  Akauliza yule afisa aliyemrudisha.

“Sitakujibu hilo sasa hivi, mpaka unisaidie kumpata Tunda. Nisaidie kumpata Tunda, ndio nitajibu maswali yako yote  na nitakueleza ubaya wote wa Vic na vile hata wazazi wake wanavyomsaidia na ndio maana hamuwezi kumkamata Vic kwa hizi njia zenu. Ila kama nilivyokwambia. Nia ya Vic ni kumtoa Tunda pale ndani kwenye ile nyumba ya ndoto zake. Vic tokea anakuwa alikuwa akiota kuja kuishi mle ndani kama mke wa Net. Ndio maana tokea mwanzo kabisa kwenye mazungumzo yake yote kwa Tunda chakwanza kabisa, alihakikisha anamgombanisha na watu wote wa mle ndani ya ile nyumba. Mpaka wafanyakazi waliomuonyesha Tunda upendo, amewachafua kwa Tunda.”

“Pili, amemfanya Tunda ajione yeye hana uwezo wa kuwa mke wa Net, na Net hampendi ila anampenda mtoto aliyebeba. Akamwaminisha hata cheo alichopewa Tunda, hakistahili  kwa sababu ya historia mbaya ya nyuma ya Tunda. Ambayo haipo hata nusu na historia yakutisha ya Vic. Na akamuaminisha ni kwa kuwa hana elimu wakati Tunda anauwezo mkubwa wa kutenda na kufikiria kuliko mpumbavu Vic. Na nitakwambia kwa nini wakati naondoka.”

“Tafadhali!” Yule afisa aliyefanikiwa kumtuliza akajiweka sawa. “Nikikwambia kitu, unaniahidi kunisaidia kumtafuta Tunda?” Maya akamuuliza akitaka uhakika. “Hata hapa nilipo namtafuta.” Akamjibu yule afisa. “Hapana. Usinifanye mimi mtoto mdogo. Mnachofanya hapa ni kupoteza muda na kumtafuta mtu wa kumtupia lawama ili mfunge kesi.  Mimi nataka uwe na mimi kufuatilia kila nitakapokuwa nikipata fununu ya mtu aliyemteka Tunda.” “Wewe utajuaje?” Maya akakunja uso.

“Wewe hujasikia kuwa mimi nilikuwa nikila madawa yakulevya na kufanywa mapenzi mpaka club!?” Maya alimtupia swali la moja kwa moja na kumbambaisha sana yule afisa. “Najua unajua. Kwa hiyo nitaanza na walevi wenzangu.” “Nilijua umeacha!?” “Kumbe unanifuatilia!?” Maya akamuuliza kwa kumsuta. Alikuwa kijana mzuri sana. Alionekana anajua kazi yake, na mzoefu. Na afisa mwenzake pia akamgeukia kama anayemsuta. Akaonekana kuishiwa hoja.

“Kwa hiyo unaahidi kunisaidia au niondoke?” Maya akamuuliza tena. “Kila kitu kitafanyiwa utaratibu wa..” Maya akanyanyuka kwa hasira. “Mbona unaondoka?” Na yeye akasimama. “Mimi na wewe wote tunajua unaongea tu.” “Hapana.” “Ni mara ngapi mimi nimekamatwa nikiwa nimelewa na madawa ya kulevya na niliyekuwa naye pia akiwa amelewa. Mlishawahi kujiuliza nyinyi kama watu wa usalama kwa raia, nani anakuwa anatupiga picha na nani anauzia vijana wadogo kama sisi hayo madawa?” Maya akauliza kwa uchungu sana.

Wale maafisa wote wawili, aliyekaa na aliyesimama, wakabaki wameduaa. “Exactly!” Maya akataka kutoka. “Subiri kwanza Miss Cote.” “Unanipotezea muda. Na kama ulivyosema. Tunavyozidi kuchelewa hapa ndivyo itakavyo kuwa ngumu kuja kumpata Tunda. Na mimi sipo tayari kumpoteza Tunda.” “Nitakusaidia Miss Cote.” “Hapo tunaweza kuzungumza.”  Maya akarudi kukaa. Na yeye akakaa.

“Nakusikiliza.” “Ulisema jina lako ni nani tena?” Maya akauliza. “Roy.” Akadakia afisa aliyekuwa akiwasikiliza. “Hapana. Sio wewe. Ni wewe. Jina lako. Moja tu, la kwanza. Usinitajie majina mengi mpaka la baba yako. Moja tu ili baadaye usianze kunizungusha na taratibu zenu za kiusalama mlizofundishwa shuleni. Utanichelewesha.” Maya aliongea kama asiyetaka kupotezewa muda zaidi. “Malcom!” Akajitambulisha yule afisa aliyefanikiwa kumtuliza. “Okay.” Maya akasikika ameridhika.

 “Kama Vic ndiye anayehusika kumteka Tunda, hamtampata kwa kumuhoji yeyote kati yetu. Kwa kuwa mpaka sasa Vic anamajibu yote sahihi, tena kisheria, kama anayeulizwa mahakamani, kuhusu kila mmoja wetu hapa mpaka walinzi wanaolipwa na Cote. Tena atakuwa alikuwa nayo hayo majibu tokea hajafanya kitu hata kimoja. Namaanisha tokea hata hajamfuata Tunda nyumbani.” Akaanza Maya.

“Ila kwa kuwa nimpumbavu, mjinga wa mwisho kabisa. Na mimi namjua tokea tunamgombania Net, ipo sehemu atakosea tu. Na hapo ndipo tutamkamata. Hana akili ya kufanya jambo kubwa kwa muda mrefu! Hawezi.” “Unazungumza kama ambaye umeshakuwa naye kwenye tukio fulani!” Malcom akaongeza kijanja, sio swali. “Sana tu. Nisikilize kwa makini.” Maya akajiweka sawa. Malcom na Roy wakajiweka vizuri, kalamu mkononi.

          “Kijana wa mwisho aliyenitafutia Vic ili anirudishe kwenye madawa ya kulevya ili nisichukue cheo cha Nana, alianza naye kwangu vizuri tu. Anaitwa Andy.” Maya akaanza. “Lakini kadiri nilipotaka kumfahamu Andy, nikagundua ni wa Vic kwa kuwa hakuwa amemuandaa vyakutosha. Bila Vic kufikiria, kwa kila swali nililokuwa nikumuuliza Andy, Vic akaishia kumpa majibu ya maisha anayoishi baba yake yeye ambayo ni ya hali ya juu sana hayaendani na yeye Andy hata kidogo.”

“Andy akaanza kunitajia biashara anazofanya ambazo ndizo anafanya baba yake Vic. Saa, nguo, pafyumu, viatu na vitu vingi tu vya thamani alivyokuwa akimpa Andy, aje navyo kwangu, yule kijana mwenyewe alikuwa akijishangaa jinsi alivyovaa vitu vya thamani.” Roy akacheka kidogo, Malcom alitoa tabasamu tu.

“Wakati amevaa mwenyewe?” Malcom akauliza. “Ehe! Yaani hapo ndipo nilipojiridhisha kuwa Vic ni mjinga. Anampa majina ya biashara ambazo anatakiwa anidanganye kuwa anafanya, ukimuuliza juu ya hizo biashara, hata yeye mwenyewe Andy alikuwa hazijui hizo biashara!” “Lakini ulihisi tu hukuwa na uhakika kama ni Vic?” “Nitakuja kupata uthibitisho kamili juu ya hilo, na wewe utakuwa shahidi. Nipe muda tu. Lakini japokuwa Andy alikuja kama tapeli kwangu, nikaishi naye vizuri sana, mpaka akashindwa kunitenda vibaya. Nilikuja kumsikia akimwambia Vic kwenye simu kuwa, hataweza kunitendea mimi ubaya, kwa kuwa mimi ni mtu mzuri na sionekani kama naweza kuja kumdhuru.” “Ulijuaje kama anazungumza na Vic?” Malcom akauliza.

“Ndio nimekwambia nitakupa uthibitisho. Kwa kuwa sasa hivi amenichokoza vibaya sana, nitahakikisha anawekwa mwangani.” Akabaki akimtizama. “Najua sasa hivi chochote nitakachoongea na wewe utanipuuza kwa kuwa watu wananichukulia mimi kama mlevi tu.” Maya akaongea kwa unyonge na kulalamika, akainama kama anayefikiria. Wakamuona anajifuta machozi.

“Mimi sitakuchukulia kama mlevi. Nitaheshimu kila kitu utakachoniambia na ninakuahidi nitafanyia uchunguzi.” Maya akamwangalia na kujifuta tena machozi. “Kweli?”  Akamuuliza kwa upole. “Kweli. Nakuahidi hivyo.” Malcom akamthibitishia kwa utulivu tu. Maya akamtizama, wakabaki wakiangaliana kama wanaosomana, Maya akainama kidogo kama aliyeridhika na kile alichoona machoni kwa Malcom.

Roy akakohoa kidogo. “Hiki kilichompata Net. Akaamka akiwa hajui kilichotokea usiku uliopita, ndicho kilitupata siku moja, mwanzoni kabisa mimi na Andy.” Akaendelea Maya baada ya Roy kuwastua kwa kukohoa. “Ile nyumba aliyokuwa akiishi Andy, nilijua wazi amekodiwa na mtu. Hiyo ni habari ya siku nyingine.”

“Siku hiyo tulitoka kwenye movie jioni tu. Tukarudi nyumbani kwa Andy, mimi mwenyewe nikaenda kuchukua juisi iliyokuwa kwenye friji. Tulinunua mimi na Andy. Tukaiweka kwenye friji. Tuliagiza pizza. Ndio tukawa tukila na hiyo juisi.” “Hamkuwa mkinywa pombe?” Akauliza Malcom. “Kumbuka nilikuwa nimetoka rehab. Sikuwa nikinywa kileo chochote kile. Andy alikuja kunipenda sana. Na nilishamsimulia maisha machafu niliyoishi nyuma. Akaniahidi kunilinda.” Maya akainama kama anayefikiria.

“Kwa hiyo hatukuwa tukinywa kabisa.” Maya akaaamua kuendelea tu aache kufikiria. “Lakini tulipokula ile pizza na kuinywa ile juisi siku ile, tukashangaa kuamka asubuhi tukiwa kitandani kama tuliofanya mapenzi usiku. Tuliamka tukiwa uchi kabisa! Tukaulizana na Andy, wote kumbukumbu ziliishia tukiwa tunakula. Kwenda pale sebuleni tulipokuwa tukila, ni pasafi kabisa hata boksi la piza limetupwa! Mimi na Andy tukashangaa. Tukaishia kutaniana labda tulifanya hayo yote tukiwa usingizini.”

“Basi, lakini mimi nikahisi ni ile juisi tu. Nilimwambia Andy nataka kuonja au kuinywa tena ile juisi ili tujiridhishe kuwa ilikuwa sio ile juisi, lakini ukweli nilikuwa na hamu yakulewa tu. Nafikiri kule kunywa kwa mara ya kwanza na kunilevya, kulitibua kiu.” “Ulikunywa?” Akauliza Malcom taratibu tu. “Ndiyo.” Maya alijibu akiwa ameinama. Kwa unyonge na aibu. “Nakumbuka Andy alinikatalia kabisa na kuniambia anakwenda kuimwaga. Mwanzoni Andy alihakikisha sirudii ulevi. Alinilinda kwa kila namna ili nisiingie kwenye matatizo tena. Ukweli mwanzoni alijitahidi.” Maya alimtetea kidogo, akaona aendelee tu maana wale maafisa wote walibaki kimya wakimtizama.

Anyways. Haijalishi tena. Turudi kwa kile nilichokuwa nikiwaambia juu ya ile juisi. Wakati anakwenda kuifuata jikoni kwenye friji ili aimwage, simu yake ikaita. Nakumbuka ni kama akakasirika baada yakuangalia simu yake, akatoka kwenda kuzungumza nje, na mimi nikaikimbilia ile juisi na kwenda kuinywa. Nililewa tena.” Maya akaongea kwa upole.

“Hudhani kwamba ndilo lilikuwa lengo la Andy?”  Akauliza Malcom. “Kwa ile juisi na mwanzoni, hapana. Alinikataza kabisa na alikuwa akienda kuimwaga ndipo hiyo simu ikaingia. Lakini sema Andy anakuja hapa.” Maya akajiweka sawa. “Baada ya ile siku ni kama akaacha au kama aliyeshindwa tena kunizuia kwenye ulevi. Lakini nilipokuja kuamka kesho yake akaumia sana na kunilaumu kwa nini sikumsikiliza wakati alinionya nisinywe tena ile juisi? Akaongea kwa kuumia sana. Niliondoka pale kwa kuwa alikuwa amekasirika na mimi sikuwa nimerudi nyumbani hiyo ilikuwa siku ya 4.”

“Akanipigia simu baada ya kama siku mbili nilipoondoka, akaniomba msamaha wa kukasirika na kuniambia amenitayarishia kitu kizuri zaidi. Nilipokwenda nikakuta amenunua wine kitu ambacho alijua wazi sitakiwi kunywa, ila akanipa akaniambia tufurahie tu, hataruhusu nilewe sana. Ila hakuonekana na furaha kabisa. Kwa kuwa mimi nilikuwa na kiu, nikanywa sana. Sikumbuki kumuona yeye hata kumaliza glasi ya kwanza aliyokuwa amejimiminia. Ila mimi nakumbuka kunywa tena na tena. Safari hii nakumbuka mpaka nikamaliza chupa yote. Siku hiyo nakumbuka kilichonilevya ilikuwa ni ile wine. Na nilifanya makusudi, yaani nilitaka kulewa.”

“Ilipoanza tu pombe, yakaja na madawa. Lakini chakushangaza, hata mwezi haukuisha, zikaanza kutumwa picha zangu nikiwa nimelala chumbani, au sebuleni kwa Andy tukiwa tunafanya mapenzi. Kilichonishangaza ni mpaka picha za siku ile ya kwanza kabisa yulipokunywa juisi na Piza! Sasa jiulize, ni nani aliyekuwa akitupiga hizo picha na kutuchukua video vizuri tu. Sio kwa kuegeshwa kamera. Hapana. Picha na video nzuri kabisa. Zikionyesha kila upande, kama hapakuwa na mtu wa tatu ambaye aliyekuwa na funguo,..” “Na uhuru wa kuingia ndani kwa Andy.” Akamalizia Malcom.

“Hapo umeelewa.” “Labda rafiki wa Andy!” Akaongeza Roy. “Andy hakuwa na rafiki. Alisema alihamia kwenye huu mji akiwa mgeni na mimi ndiye mtu pekee niliyekuwa nikifahamiana naye. Sikuwahi hata kumuona akisalimiana na mtu.” Roy akakunja uso. “Najua huamini. Na wewe sio wa kwanza. Hata Net naona sasa hivi ndio ataelewa kile nilichokuwa nikiwaambia na kunipuuza. Na ipo siku nitathibitisha kuwa ni Vic na ndipo Mungu atamuhukumu kwa sheria.” Mara mlango ukafunguliwa.

“Miss Cote, asante kwa ushirikiano wako. Tutakapokuwa na swali la nyongeza tutakutafuta, ila kwa sasa unaweza kwenda tu.” Aliingia na kuongea baba mmoja mtu mzima kabisa. Ndipo Maya akageuka pembeni akaona dirisha kubwa la kioo. Akajua wapo watu wengine waliokuwa wakiwasikiliza.

Maya akarudisha macho kwa Malcom. Akamuona amebadilika kabisa usoni, akarudisha sura ya kazi. Ile sura ya kumbembeleza wakati anamuhoji maswali ikapotea. Maya akajua alikuwa vile ili tu kumtumia kumtoa maswali. Hakumaanisha chochote. Akainama kama aliyeumia sana. “Ilikuwa kidogo tu nikuamini!” Akamwambia Malcom kwa macho na sauti yakukatishwa tamaa. Maya akachukua pochi yake akatoka bila kuongeza neno jingine. Akawaacha pale wale maafisa wawili. Malcom na Roy pamoja na yule aliyeingia pale kama kiongozi wao.

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

Familia hiyo ya Cote ilionja uchungu ambao hata hawakuwahi kudhania maishani. Tunda alitekwa nyara. Badala ya watu kuwahurumia, wakageuka kuwa wao ndio watuhumiwa. Mitandaoni kukajaa tuhuma zakupita kiasi. Kila mtu ndani ya hiyo familia akituhumiwa kivyake.

Anaibiwaje mgonjwa katikati ya ulinzi mkali kiasi hicho kama sio njama za mtu kutoka ndani! Ni nani mwenye uwezo huo kama sio amesaidiwa na mtu kutoka ndani! Vic yupo sahihi. Kila mtu akawa upande wa Vic. Mtoto ambaye alikuwa akisubiriwa kwa hamu zote, na matayarisho kama kitoto chakifamle, kila mtu akibashiri ujio wa Cote, habari ikawa imegeuka. Yeye hayupo tena kwenye picha. Ila picha za baba yake akifanya ngono mtandaoni na hawara.

    Ilikuwa hali ya kusikitisha iliyojaa wasiwasi kwa familia hiyo ambayo nyumba yao ilijaa watu wa usalama, ndani na nje. Hapakuwa na utulivu, redio call za polisi ndizo kelele zake zilisikika humo ndani kila wakati.

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

Tunda yuko wapi? Usikose muendelezo.

CONVERSATION

0 Comments:

Post a Comment