Naomi Simulizi |+1 205 767 8163 |naomisimulizi@gmail.com Nilipotea! – Sehemu ya 46. - Naomi Simulizi

Nilipotea! – Sehemu ya 46.

 Kwa Ritha.

N

i kweli yale mazungumzo yalikuwa yakisikilizwa na kufuatiliwa na wakubwa wa CSIS. Pale pale Vic alipotaja jina Ritha kuwa anahusika kuweka njama za Vic awe na Net, tayari maafisa wawili waliokuwepo kwenye mji aliokuwepo Ritha, walitumwa kwenda nyumbani kwa Ritha. Kama kawaida ya Ritha. Hakufanya kosa. Walimkuta usiku huo wa saa tatu sebuleni kwake, anafuatilia tukio lakutekwa nyara Tunda kwenye vyombo vya habari.

Afisa wale wakagonga kama kawaida tu. Ritha akafungua. “Niwasaidie nini?” Ritha akawauliza na tabasamu la kejeli usoni. “Tunamaswali tunataka kukuuliza.” “Karibuni.” Akawakaribisha mpaka ndani. “Niwapatie kinywaji gani?” “Hapana asante.” Wote wakajibu na kukaa. Ritha akawatizama kwa macho makavu kama anayewaambia anawasikiliza.

“Mrs Cote amepotea.” “Kwa hiyo?” Ritha akauliza kwa haraka. “Tunataka kujua alipo.” “Kama usalama wa taifa wameshindwa kujua alipo tokea asubuhi. Tena wao wakiwa na vifaa vyote maalumu. Mnafikirije Mimi raia wa kawaida nitajua alipo!?” Ritha akawashangaa kwa kuwabeza.

“Victoria Cloutier amesema wewe unahusika na kutekwa kwa Mrs Cote.” Wakamtega kujua kama wanafahamiana na Vic. “Huyo ni nani na kwa nini mpaka sasa hivi sipo chini ya ulinzi!?” Akili ya Ritha ikachemka kwa haraka sana. Akajua anategwa. Akajitoa mapema sana. Akawauliza bila hata kuonyesha hofu wala hata kuonyesha kama alishwahi hata kuzungumza na Vic.

“Mnakuja nyumbani kwangu kwa maneno ya uongo tena mnayatoa kwa mtu ambaye hata simfahamu! Mnataka na mimi niwashitaki?” “Inamaana wewe humfahamu kabisa Miss Victoria Cloutier?” Mwingine akauliza. “Ilitakiwa nimfahamu!?” Ritha akauliza akionyesha kuwashangaa sana. “Tunaruhusiwa kuzunguka humu ndani?” “Mkija na warranty nitawaruhusu kuzunguka. Sasa kwa kuwa hamna warranty na mmekuja na tuhuma za ajabu, nawaomba muondoke sasa hivi kabla na mimi sijaita polisi hapa kwa msaada.” Ritha akasimama na kuwafungulia mlango. Ikabidi wale watu wa usalama waondoke tu.

Wakawapigia simu kina Malcom na kuwaambia kilichotokea kati yao na Ritha. Hata wao walijua hawezi kukiri chochote. Ila walimfanyia ujanja tu. Pale aliposimama kwenda kuwafungulia mlango na kuwaacha pale sebuleni, mmoja alibandika kitu kidogo ambacho wangeweza kumsikia wakiwa nje, kama atawasiliana na yeyote ndani.  Wale maafisa wawili wakaambiwa wasiende mbali na hapo kwa Ritha ili kama atapiga simu kuwasiliana na yeyote yule wamsikie na kama atatoka, basi wamfuatilie kujua anapokwenda. Tumaini likabaki kwa wale watatu mle ndani. Vic, Jake na Maya.

Malcom kwa Maya.

H

ofu ikawa imeshamwingia Malcom tokea Vic alipoingia kupitia mlango wa nyuma na Maya kusema anayo bastola. Kwa mlango wa nyuma hawakuwa na kamera. Waliweka chumbani na pale sebuleni tu ambapo waliweza kuona mpaka sehemu iliyokuwa na meza ya kompyuta. Ni kweli Malcom alitumwa na viongozi wake kwa Maya. Lakini ni kwa kuwa walimuona amekuwa dhaifu kwa Maya na Maya naye akaonyesha kama amelainishwa na Malcom zaidi ya Roy. Ni kweli walikuwa nje ya kioo wakifuatilia mahojiano yao na Maya kule kituo cha polisi.

Watu hao wa usalama wanaoweza kujua ukweli kwa kusikia sauti na kusoma sura, wakagundua Malcom na Maya wamejenga kingine. Ndio maana wakamtuma Malcom na kumtaka lazima yeye ndio akamwingie Maya ili kufupisha na kurahisisha mambo kwa Jake. Njia nzima mpaka pale wanafika kwa Jake, Malcom na Maya walijenga hisia nyingine mbali na kazi, bila kuambiana. Na Malcom hakuwa ameanzia hapo kwenye mahojiano na Maya, siku hiyo ya asubuhi. Hapana. Alipomwambia anamfahamu kwa asilimia 90, ni kweli alikuwa akimfahamu Maya kwa undani zaidi ya hata Maya alivyoweza kumuelewa. Alikuwa ni binti anayemfuatilia kwa muda mrefu tu tokea Malcom na Roy wapo chuoni na Roy alilijua hilo.

Kitendo cha Jake kumtaka kimapenzi Maya usiku huo, Malcom hakuafiki kabisa. Akiwa na viongozi wake ndani ya lile gari wakisikiliza, Malcom akawaambia yeye anaenda kuwazuia wasifanye mapenzi. Viongozi wake wakamwambia haimuhusu. Na Maya sio mtoto mdogo. Asipotaka kufanya mapenzi na Jake, ataomba msaada. Akitaka, atafanya tu.

Malcom akabisha. Akawaambia yeye ndio amemlazimisha Maya kwenda kuzungumza na Jake, kwa hiyo lazima akamtoe matatizoni. Wao wakamwambia mpaka hapo hawajaona kama Maya yupo matatizoni, awaache wapenzi hao wawili. Tena wakamwambia kama atashindwa kuwepo pale, aondoke.

Ikabidi Malcom awe mvumilivu. Japokuwa Maya aliomba wazime video, pia wakakataa. Wakamwambia Malcom kwa hakika Jake anatatizo la akili. Wakizima video halafu huku nyuma akamrudi Maya, binti wa Cote! Watawajibishwa vibaya sana. Na wote wakamgeukia Malcom, na kumwambia hawapo tayari kuingia matatizoni. Yeye kama hawezi kuangalia wapenzi hao wakikumbushia enzi. Tena walimwambia kwa kumkejeli, aondoke.

Kiongozi wake akamwambia lazima kuweka hisia mbali. “Macho na masikio yote ya viongozi wa nchi yapo kwetu. Leo unataka hisia zako kwa Ms Cote zitufukuzishe kazi?” “Sina hisia zozote kwa Maya.” “Miss Cote.” Bosi wao akamsahihisha kumtaka awe kikazi. “Ndiyo ni Miss Cote.” “Kama hisia hazikusumbui, basi tulia tufanye kazi.” Ikabidi Malcom atulie. Roy rafiki yake kipenzi Malcom ambaye walianzana naye urafiki tokea wapo kwenye chuo cha mafunzo ya usalama wa taifa, alikuwepo hapo akisikiliza hayo mazungumzo ya Malcom na bosi wao.

Malcom na Roy walimaliza chuo pamoja na kupangiwa kazi sehemu moja. Kwa hiyo walikuwa marafiki wa muda mrefu na wasioweza kutenganishwa. Kazini walipangiwa kazi sawa na hata kama nikutumwa, basi walitumwa pamoja. Na nje ya ofisi pia ni hivyo hivyo wakawa kama kumbikumbi. Ukitaka kujua Malcom alipo, muulize Roy, na Roy hivyohivyo. Walitokea kuelewana sana. Familia ya Roy ikawa ni kama familia ya Malcom tu.

          “Haitachukua muda mrefu Malcom. Najua wote tumechoka. Mambo yakienda vizuri, leo kila mtu ataenda kulala nyumbani kwake.” Roy akajaribu kumtuliza rafiki yake kwa sauti ya chini kidogo, lakini akijua wazi tatizo sio uchovu ni wivu. Haikuwa hivyo kama walivyofikiri. Mapenzi yalipoanza, Jake alikuwa akifanya mapenzi kwa hisia zote na Maya, tena bila haraka akionyesha akifurahia anachokifanya. Aliita jina la Maya kwa kila alichokifanya huku akifanya mapenzi hayo kwa kufurahia sana tu.

Jake alipomaliza safari ya kwanza na kumtaka Maya kwa ya pili, hapo Malcom uzalendo ukamshinda. Wengine walikuwa wakiangalia, yeye alikuwa ameinamia simu yake huku akisikia miguno ya mapenzi na vile Jake anavyomuita Maya. Wakamuona Malcom anatoka ndani ya ile gari na kutupa headphone za kusikilizia sauti katikati ya mchezo wa pili. Jake alisikika kwa kukera sana kwa wenye wivu.

Jake na Maya walimaliza, na wao wakawa wameangalia kila hatua huku maafisa hao wakifurahia nakushabikia kama watoto wadogo. Alipoingia Vic, Roy akatoka kwa haraka kwenda kumtafuta Malcom. Akamkuta amesimama nje kabisa ya lile gari. “Vic amewafuata.” Malcom akashituka sana. Akakimbilia ndani. “Naingia.” “Nimekwambia hutaingia ndani Malcom, mpaka Maya mwenyewe akuite au tuone hatari.” Bosi wake akaweka msisitizo.

“Na ukiharibu au kuingilia hili tumaini la mwisho la kumpata Mrs Cote, nitahakikisha unalala chumba kimoja huko jela na yule aliyehusika kumteka Mrs Cote. Nitahakikisha na kuripoti na hutakaa kutoka jela.” Bosi wao akamtisha Malcom. Ikabidi Malcom atulie.

 Vic, Jake & Maya.

          “Vic, naomba utulie. Mimi naondoka nakuachia Jake wako.” “Hajawahi kuwa wangu. Na wala simtaki. Nimelala na wewe leo nimegundua najipunja tu.” Vic akampiga risasi ya mguuni. Maya akapiga yowe na kumwita Malcom kwa sauti. “Malcom!” Sababu ya kelele ya Jake aliyekuwa amepigwa risasi ya mguu, hawakuelewa nini Maya anaongea, lakini Maya aliendelea kupiga kelele.

Malcom alipoona kwenye video Maya anapiga kelele kama aliyeingiwa hofu, akakimbia bila kuomba ruhusa tena. Akasukuma mlango wa mbele  nyumbani hapo kwa Jake, akajikuta amesimama mbele yao. Kwa haraka sana Vic naye akamvuta Maya na kumuwekea risasi kichwani. “Ukisogea hata hatua moja, nampasua kicha, Maya.” Vic alikuwa akitetemeka kama aliyepagawa kabisa. “Nisaidie Malcom. Vic ataniua.” Maya alikuwa akilia sana, Jake  sakafuni anavuja damu kichwani na mguuni huku na yeye akilia kama mtoto.

“Nisikilize Vic. Bado huna kosa la mauaji hapa. Usitafute kosa la mauji ukaishia jela hata nafasi uliyonayo ya kuwa na Net ukaipoteza.” Malcom akaongea taratibu. “Net ameniambia anampenda mke wake sio mimi. Sina kitu cha kupoteza tena. Na yote hayo amesababisha huyu Maya.” Akamgonga Maya kichwani kwa nguvu na kitako cha bastola, Maya akazidi kulia kwa hofu na yeye Vic pia alikuwa akilia.

“Niangalie mimi Vic. Niangalie.” “Usinifanye mimi mjinga Malcom. Najua wewe ni polisi.” “Mimi sio polisi. Niangalie na uniambie unafikiri Net atakuwa na nani sasa hivi wakati mke wake ametekwa?” Malcom akajaribu kumtuliza. “Kama huamini, Net yupo njiani, anakuja. Utamsikia yeye mwenyewe. Ndipo utaamini kuwa anakupenda na kukuhitaji wewe. Kwani uliona hata amekuuliza lile swala la kusambaza video yenu ya mapenzi?” Malcom akaendelea kumuliza taratibu akimchota akili.

“Hapana. Kwa kuwa Net amenikasirikia. Net amenikasirikia mimi.” Vic akazidi kulia kwa sauti. “Hapana Vic. Hapana. Niangalie mimi acha kulia. Unakumbuka ulivyosema kuwa Net anakupenda wewe hawezi kuwa na mwanamke mwingine?” Vic akatulia kama anayefikiria. “Nataka kumsikia Net mwenyewe akiniambia sio wewe Malcom.” “Basi naomba utulie. Net anakuja kukwambia yeye mwenyewe. Na ili Net akute mazingira mazuri, nashauri mtoe huyu anayevuja damu hapo. Mtoe nje kabisa, akukute kwenye mazingira mazuri na safi.” Malcom akaendelea kumshauri akiwa ametulia kabisa.

Akamwambia Maya kwa kifaransa kuwa atulie asiwe na wasiwasi. “Unaongea nini wewe? Unanichanganya!” Vic akawa hajaelewa. “Hapana. Usichanganyikiwe. Niangalie mimi. Tulia, jiandae kumpokea Net. Sawa?” Vic akajikuna kichwa na ule mkono uliokuwa umeshika bastola, kama anayejaribu kufikiria lakini anashindwa. Bado mkono mwingine alikuwa amemshikilia Maya kwa nguvu zote kama asimponyoke. Akatoa ile kofia na kuitupa chini.

“Sasa unataka nifanye nini na huyu? Si heri nimuue tu ili asije akasema kwa polisi?” Vic akauliza juu ya Jake kwa Malcom ambaye alikuwa haonyeshi kama ni mtu wa usalama. Alikuwa amevaa nguo za raia. Ila safi na akapendeza. “Kama nilivyokwambia Vic, bado unanafasi kubwa sana ya kuwa mke wa Net. Utakapomua huyo, utakuwa na kesi ya mauaji. Watakufunga kifungo cha maisha au kukunyonga. Utakuwa umepoteza kabisa bahati ya kuwa na mwanaume unaye mpenda. Acha mimi nitoke naye hapa, ili kukupa muda wakutulia mpaka Net atakapokuja.” “Lakini siwezi kumruhusu Maya.” Vic akajibu huku akifuta machozi.

“Sawa. Mtoe huyo Jake anayevuja damu ili asije kukufia hapo na kukuletea matatizo. Na huyo Maya, nashauri uchukue tape, mfunge mikono na miguu, umuweke chumbani. Mfungie ili Net akukute peke yako ukiwa umetulia.” Hilo akaliafiki Vic kwa haraka. “Kwa hiyo naweza kumtoa Jake sasa hivi?” “Fanya haraka ili nisafishe kabisa hizi damu. Sitaki Net apakute hapa pachafu.” “Wazo zuri.” Malcom alikwenda kumbeba Jake pale sakafuni na kumtoa nje. Tayari kulishajaa magari ya wagonjwa, ambulance na polisi pale kwenye hilo eneo, kila mtu roho mkononi. Mtoto wa Cote yupo ndani ameshikiwa bastola! Kila mtu hofu. Wanamwambia nini bibi Cote! Amepoteza mkwe na mjukuu! Afisa wa usalama wakazidi kumiminika hapo. Jake akapokelewa na watu wa huduma ya kwanza kwa haraka.

Kwa kina Cote.

B

ado bibi Cote na Net walikuwa sebuleni na maafisa wa CSIS wakisubiria simu yeyote kutoka kwa mtekaji au mtu mwenye fununu. Simu ya kutoka kwa director wa CSIS ikaita. Bibi Cote akapokea kwa haraka. “Kwanza nataka usipaniki, Emily. Nisikilize kwa makini na utekeleze kwa haraka. Mr Cote yuko wapi?” Bibi Cote akageuka kumwangalia Net. “Yupo hapa. Ni nini kinaendelea?” “Weka kwenye spika. Wote mnisikilize kwa ufupi, nitajibu maswali yenu baadaye.” Bibi Cote au Emily kama alivyomtambua kwa jina la kwanza, akatulia. Net akasogea.

“Hapa tunapozungumza, ipo dalili yakumpata Mrs Cote kwa kupitia Maya.” Bibi Cote na Net wakaangaliana. Kwa masaa hayo matatu, hata hawakujua Maya alipo. Walijua yupo na mtoto ndani. Yule kiongozi akawaeleza kwa kifupi kinachoendelea. Na kumtaka Net aondoke na helcopter ya CSIS ambayo ipo umbali wa dakika tano kufika hapo nyumbani kumchukua yeye ili kwenda kuzungumza na Vic, amtulize kwa kumwambia kile anachojua Vic anataka kusikia, ili amuokoe mdogo wake.

“Hukufanya vizuri Mike!” Bibi Cote akamlaumu yule director kwa ngazi ya chini sana yakufahamiana wao kama marafiki wakawaida tu, si kama kiongozi mkubwa sana wa ngazi ya juu hapo nchini. “Kwanza ni Maya mwenyewe ndiye aliyekuwa akimtafuta Mrs Cote. Amekutwa na mmoja wa afisa wangu akiwa analia nje ya club akiwa anatafuta habari kutoka kwa marafiki wa Vic. Tulichofanya sisi ni kuongeza nguvu na kumlinda. Kwa jinsi alivyokuwa, jibu la kumkataza isingekuwa sahihi ila kumuongoza kwenye njia njema.” Hakumpa ukweli kamili ili kufupisha habari.

“Hapa tunapozungumza, Jake au Andy...” “Yule aliyekuwa mchumba wa Maya!?” Bibi Cote akamkatisha kwa kuuliza swali. “Ndiyo. Kwa ufupi tu ni Jake sio Andy kama mnavyomfahamu. Na alitumwa na Vic kwenye maisha ya Maya ili kumuangamiza. Wote wawili wamekiri na tunao ushahidi.” Kiongozi huyo aliendelea, asijue zile habari ni kama kumpiga kofi la usoni bibi huyo.

“Na hapa tunapozungumza, Jake ametoa ushirikiano mzuri sana kwa Maya, amesema anayo njia yakufuatilia gari lililomchukua Mrs Cote. Ila amepigwa risasi na Vic, ndio wapo kwenye kumsaidia tuone kama anaweza kusaidia.” Mara wakasikia mlio wa helcopter nje. “Naona helcopter imefika. Na mimi nakwenda Mike.” “Kwa nini usisubiri, Emily? Itakuwa rahisi kumlinda Maya na Nathiel. Acha akili za maafisa wote ziwe sehemu moja, kumuokoa Maya na Net atakapoingia ndani kwa Vic mwenye risasi. Yule binti ni kichaa kabisa. Unatakiwa umakini wa hali ya juu sana sasa hivi kwake. Ukienda kule itabidi wagawane wengine wakulinde na wewe, Emily. Naomba usubiri.” Mike na yeye akamsihi kama rafiki kabisa kwa kumtaja jina lake la kwanza, bibi Cote.

“She is my baby, Mike. Yupo kwenye hiyo hali sababu ya mimi kuzembea kwenye maisha yake. Mimi ndiye nimemfikisha Maya hapo. Ningemtilia maanani tokea mwanzoni kabisa, pengine ningeweza kumdhibiti Vic. Siwezi kumuacha Maya sasa hivi. Nakwenda.” Bibi Cote akakataa ushauri. Lakini walishamjua ni mtu asiyejua jibu la hapana. “Lakini lazima uelewe kuwa hutaruhusiwa kuingia ndani. Ili Vic asimdhuru Maya, lazima Net awepo peke yake na aonekane ametulia na amwaminishe chochote anachojua Vic anataka kusikia kwa wakati huu.”  “Tengeneza mazingira ya mimi kuwepo huko Mike.” Bibi Cote akakata simu. Afisa mmoja aliingia akikimbia. Bila mengi, Net na bibi Cote wakatoka na wao wakikimbia.

 ~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

 Bado hakuna fununu zozote juu ya alipo Tunda.

Maya amekwenda umbali mkubwa sana ili  kumpata Tunda. Na amekusudia kumpata kwa gharama yeyote ile, arudi kwenye maisha yake.

Je, watafanikiwa kumpata kwa wakati na akiwa bado hai hawajamdhuru?

Je, kujitoa kwa Maya kutalipa?

Baada ya kutulizwa na Maya kwa penzi la muda mrefu tu, kupigwa risasi na Vic, Je, kichaa huyo Jake ambaye ndio kama tumaini la mwisho, kweli ataweza kuwa msaada au ndio sadaka ya Maya imepotea Bure?

Ritha ameongezwa kwenye picha lakini ameweza kuwazidi akili kwa kukwepa maswali ya mtego waliodhani wangemkamata nayo. kama kawaida yake kutumia akili za haraka kwenye kila jambo. Amekataa kabisa kuwa hausiki kwenye kumteka Tunda na amefukuza afisa usalama.

Je, anamjua muhusika ALIYEMTEKA TUNDA?

Je, Net atafanikiwa kumtuliza Vic na kumuokoa dada yake?

 Nani ameuawa na Vic?

Usikose  muendelezo

CONVERSATION

0 Comments:

Post a Comment