Naomi Simulizi |+1 205 767 8163 |naomisimulizi@gmail.com Nilipotea! – Sehemu ya 48. - Naomi Simulizi

Nilipotea! – Sehemu ya 48.


B

ibi Cote asingeruhusu kuondoka Tunda na mtoto wake, alijua ni kweli familia itasambaratika na kinachozungumzwa mitandaoni kitatimia. Kuwa ukoo wa Cote ndio umekufa na Mzee Cote mwenyewe. Na asingethubutu kumpa ushindi Ritha. Safari hii alitaka kumrudi Ritha vilivyo. “Nisikilize Tunda. Mwisho wa Ritha upo karibu sana. Usiogope.” Bibi Cote akajaribu kumtuliza. Tunda akabakia akiwaza.

          “Kwani hukumbuki chochote?” Maya akamuuliza. “Hapan..” Tunda akanyamaza kidogo. “Umekumbuka nini?” Maya akaendelea kumuhoji. “Sina uhakika sasa kama ni ndoto, au kama ni hospitali ile nyingine au la. Lakini nakumbuka kuamka na kumuomba nesi aliyekuwepo karibu na kijana mmoja hivi, waniletee mtoto nimnyonyeshe. Yule kijana, alikuwa mdogo kwa yule nesi, akamwambia watakuwa wamenipunguzia dozi, waniongeze. Nikaendelea kuwadai mtoto, nikiwa bado nina usingizi mzito hata siwezi kuamka vizuri. Ni kama yule nesi akaongeza kitu kwenye ile dripu, nikapotelea usingizini.” Tunda akazidi kuingiwa hofu.

“Labda nirudi kwanza nyumbani Tanzania mpaka watakapo kamatwa wote.” Tunda akamwangalia bibi Cote. “Kukimbia ni kuwatangazia kushindwa na watakufuata popote uendako. Lazima kusimama imara. Huwezi kumkimbia adui Tunda. Lazima umtizame usoni na kupambana naye.” “Lakini hii ni mara ya pili Nana! Ritha anafanikiwa kunikamata hata katikati ya ulinzi mkali! Anaakili sana. Naomba tusimpe nafasi ya tatu. Naombeni mniruhusu niondoke kwa muda.” Tunda aliendelea kuwasihi.

“Nilikuahidi na nimetimiza Tunda. Naomba unipe nafasi yakuweka kikomo kwenye hili. Ukiondoka tu utakuwa umenivunja nguvu kabisa. Nitashindwa kupambana naye.” Bibi Cote akamsihi kwa kumbembeleza. Hata yeye alijua anahaki yakuogopa.  “Sio ndio utakuwa huru kwa kuwa nitakuwa mbali?” Tunda akauliza huku akilia. “Siwezi kuwa na amani ukiwa mbali na mimi. Nitakuwa sijui nani anakuzunguka wewe na Cote huko! Wala nitakuwa sijui wewe na mtoto mnaendeleaje! Siwezi kufikiria tukiwa tumetawanyika. Nahitaji kuwaona wote sehemu moja ili tuweze kufanya kitu kimoja kwa pamoja ndipo tutaweza.” Bibi Cote akasisitiza.

“Halafu nikwambie ukweli tu Tunda. Akili na mipango ya hata Vic ndivyo ilivyo. Alikuwa akitumia marafiki zangu wa karibu sana ili kuniangamiza na ndio maana wakati wote amekuwa akifanikiwa. Na amefanya kwako hivyohivyo. Amekuja kwako kwa makusudi na kuhakikisha anakutenga na watu wote ambao wameonyesha wapo upande wako.” Maya akaona na yeye aongee.

“Upendo na mapokezi uliyoyapata kutoka kwenye familia yetu, hakuna mtu aliyewahi kupokea kwa kiwango chako. Sisi wote tumefuatilia mazungumzo yako na Vic.” Tunda akashangaa. “Mlifuatilia wapi?” “Yule msichana aliyekuwa naye, Renee. Alichukua video kuanzia mwanzo wanaingia mpaka mwisho. Kama ukifikiria kwa makini, na ukakumbuka kila neno, alianza kwa kukugombanisha na kila mtu ambaye ulimsifia siku ya tafrija ya kukaribishwa kwako hapa nchini au kwenye familia yetu.” Tunda akawa kama anavuta kumbukumbu.

“Wewe kumbuka tu. Alianza kwa Nana, akaja kwangu, na wafanyakazi wote wa pale ndani ambao uliwataja siku ile kuwa walikupokea na wanaishi vizuri na wewe.” Tunda akatulia. “Usifikiri alifanya kwa bahati mbaya kukwambia kama alilala pale nyumbani na mimi  pamoja na Carter tulijua! Anajua ukaribu wangu na wewe, pamoja na Carter au wafanyakazi wote wa pale ndani. Na anajua wewe utafikiria kama Carter anajua, inamaana na Ms Emily anajua pengine hata Gino. Kwa hiyo utatuchukia wote. Utajiona upo peke yako na wale watu wote pale wanaokuonyesha upendo, ni wanafiki. Akakusudia uwachukie kabisa.” Maya akaendelea kwa makini.

Hakuna aliyemuona Maya huyu. Alijawa hekima na mtulivu. Alishamiri kwenye hiyo dhoruba bila shida. Yeye ndio akaonekana jasiri kuliko wote. Alijawa hekima, kama sio yeye Maya waliyekuwa wakimdharau tu. “Hotuba ya siku ukikaribishwa nyumbani na yote tuliyoongea kwa upendo, yanazungumziwa mpaka leo kwenye mitandao.” Maya akaendelea. “Na ili kuhakikisha kama yeye alivyoshindwa kufikishwa kanisani na Net, alihakikisha anamchafua kabisa Net, kama alivyokuwa akinifanyia mimi. Kwa kusambaza video na picha za ngono mtandaoni ili watu wote wawe kinyume na Net, hata wewe ushindwe kabisa hata kumtizama Net. Na mshindwe kufunga ndoa.” “Hata mimi alikiri kwangu.” Net akaongeza.

“Vic ni kichaa anayesaidiwa mipango yake na watu wenye akili. Anajua anachokifanya.” “Ukisema ni kichaa unamaanisha ni kichaa kweli?” Tunda akauliza. “Namaanisha ni kichaa kweli. Anatatizo la akili kabisa. Wazazi wake walificha. Akawa anatibiwa mbali na Norfolk. Ndio huko huko kwenye matibabu akakutana na kichaa mwenzie Jake ambaye akampa jina la Andy. Akamlipa ili aje kwangu aniangamize.”

“Ni kweli Vic anampenda sana Net, na hawezi kuruhusu mtu yeyote kusimama kati yake na Net. Amekiri ndio maana alikuwa akihangaika kuniangamiza hata mimi kwa kuwa tokea tupo wadogo, nilikuwa namtaka Net, wakati na yeye alitaka muda naye. Unakumbuka Net?” Maya akamuuliza. “Ndivyo alivyoniambia na mimi jana.” Net akathibitisha kwa unyonge. “Mimi nilikuwa nikiwasikiliza kila kitu wakati amenifungia chumbani.” “Vic ni mwendawazimu.” “Hapana Tunda. Nikichaa kabisa. Nafikiri ndio maana hata wazazi wake wameshindwa kumwajiri hata kwenye kampuni yao. Sisi tunasema hataki kufanya kazi, kumbe hana uwezo.” Akaongeza bibi Cote.

“Kabisa Nana. Mama yake alikiri yeye mwenyewe wakati polisi walipotuvamia ndani. Kuwa siku hiyo alikuwa na mambo mengi, akasahau kunywa dawa, lakini hana uwezo wa kudhuru mtu.” “Lakini Net, nao ni waongo. Akiwa amekunywa dawa na akiwa hajanywa dawa, Vic ni hatarishi. Kumbukeni mabaya yote aliyokuwa akinitendea! Halafu usiku uleule alikiri kwangu mimi na Jake kuwa ametoka kuua na alimpiga Jake risasi mbele yangu!” Maya akaongeza na kuzidi kumshangaza na kumuogopesha Tunda.

“Kwa hakika, Vic hawezi kuwasumbua tena. Labda mtu amuite mwenyewe na ajifungie naye mwenyewe.” Bibi Cote akaongeza. Net akajua anaambiwa yeye tu maana Vic yupo jela na hawezi kuachiliwa siku za karibuni. “Aliniwekea madawa kwenye juisi Nana! Sikujua hata nini kilitokea usiku ule. Yaani na mimi ndio nilisikia kama wewe Nana.” Bibi Cote hata hakumjibu wala kumwangalia Net.

“Na kwa vile alivyochukuliwa na CSIS, watampa kifungo cha hukohuko hospitalini. Hatatoka leo wala kesho.” Akaongeza bibi Cote bila hata kumjibu Net. Net akajua bado amemkasirikia. Akanyamaza na kurudi kukaa kwenye kochi akainama. “Kwa hiyo Tunda, tafadhali usifikirie kwenda popote, ila kurudi nyumbani na kulea mtoto wako bila wasiwasi.” “Tena wakikuona umetulia ndio utazidi kuwatoa nguvu.” Maya akaongeza kwa bibi yake. Tunda akabaki kimya.

Malcom na Roy tena!

W

akasikia watu wanabishana nje ya dirisha kwa sauti ya chini. “Subiri kwanza Roy. Tufikirie kwa upya.” “Acha woga Malcom! Sisi tuingie hapo kama maafisa wa CSIS. Tunafuatilia hali ya tuliyemuokoa. Na usianze kumtaja jina lake. Sema Miss Cote.” “Au turudi baadaye? Bibi yake anafahamiana na wakubwa wote pale. Akipiga simu kuulizia kama tupo hapa kiofisi au?” “Sasa wewe usiongee sana. Tukifika hapo tuonyeshe vitambulisho vya kazi na tuwe kikazi.” “Wewe ndio unaongea sana Roy. Jitahidi kuwa mchache wa maneno.” “Sawa twende.” Wakatulia.

“Subiri kwanza Roy. Nahisi kama safari hii tukikamatwa hapa, habari zikafika ofisini, ndio tutarudishwa kwenye benchi kabisa au tukapewa kazi za stoo! Hatutapata kazi za nje tena.” “Kwa muda tu. Hawawezi kututoa kwenye field.” Wakacheka kidogo. “Twende?”  Wakasikia mmoja anamuuliza mwenzake. “Sasa kama kina nani? Hawa watu hawadanganyiki.” Wakasikia ukimya kidogo.

“Kumbuka. Maneno machache. Halafu tuwakumbushe kuwa sisi ndio tuliomuokoa Maya kwenye..” “Sasa hapo unaharibu Malcom. Nimekwambia Miss Cote.” Roy  akamrekebisha. “Yeah. Miss Cote.” “Usisahau Malcom! Tuwaambie sisi ndio tulimuokoa ili asiuawe na Vic.” “No way. Unataka kumuua kwa mshtuko! Usiseme hivyo. Leo iwe smooth.” Wote kule ndani walikuwa wakiwasikiliza. Maya akainama huku akicheka

Come on Malcom! Lazima tuonyeshe umuhimu wetu! Hata hivyo haitakuwa tunadanganya. Ni kweli bila sisi angeuawa.” “Njoo kwanza Roy.” Wakasogea tena. “Kumbuka lengo ni kumuona Maya, sio kumkumbushia machungu.” “Miss Cote.” Wakamsikia Roy akimsahihisha tena. “Yeah Miss Cote.” Malcom akakubali. “Au tuwaambie tunamtaka atoke nje kwa mahojiano?” “Oooh NOO Malcom! Watampigia director hapohapo. Kumbuka Mr Underson ni best ya bibi yake. Hapo ndipo tutafukuzwa kazi bila onyo jingine.” Wakawasikia wakicheka taratibu.

“Au kwa nini tusiseme kwa kuwa sisi ndio tulikuwa tukifanya kazi na Maya jana yakumtafuta Mrs Cote,” “Miss Cote Malcom! Please usijisahau!” “Nikiingia pale nitasema Miss Cote sio Maya. Ni kwako tu.” “Okay.” Roy akakubali. “Sasa tuseme sisi ni maafisa waungwana. Tunataka kujua hali ya Maya.” “Miss Cote.” Roy akamrekebisha tena. “Sawa, Miss Cote. Kwa kuwa jana alipatwa na mshtuko.” “Ripoti ya daktari imesema hajapatwa na mshtuko. Usianzishe kitu kingine Malcom. Tutajiingiza kwenye matatizo.”

“Mimi naona tuondoke tu. Hii kitu imeshakuwa ngumu.” “Usikate tamaa Malcom! Tumehangaika kote huko mpaka kufika hapa! Lazima tuingie.” “Sio kukata tamaa. Naona twende tukajipange tena kwa upya. Halafu tukaanzie kwa bosi tuombe kazi ya kufuatilia chochote kinachohusiana na kina Cote. Halafu ndio tumtafute Maya.” “Miss Cote.” Roy akamkumbusha tena. “Gosh Roy!” Malcom akalalamika. “Fine. Mimi nakukumbusha kuwa kikazi.” “I am.” Roy akaanza kumcheka.

“Huu ni muda wakufikiria Roy sio kubezana.” “Basi nimepata wazo. Tuingie na kuonyesha vitambulisho, halafu tuombe kazi yakujitolea ya kumlinda Miss Cote, mpaka watuhumiwa wote wakamatwe.” “Sasa hivi umeanza kuongea.” Wakawasikia wakigonga. “Tuingie tuseme sisi ndio tulifanya kazi na Maya.” “Miss Cote.” Roy akamsahihisha tena. “Yeah, nakuahidi nikifika kule nitakumbuka. Sitasema Maya.” “Usisahau kuwatizama machoni ili wajue unajiamini.” “Okay. Nitawaambia kutokana na mazingira hatarishi aliyokuwa nayo Maya jana.” “Miss..” “Najua. Acha kuniingilia Roy!” Wakamsikia Malcom amemkatisha kabla hajamsahihisha tena kusema Miss Cote.

Kule ndani walikuwa wanakaribia kucheka. “Tuingie. Tujitambulishe majina na kazi zetu.” “Hudhani kama inabidi kuwaambia kuwa katika darasa letu la CSIS sisi ndio tulikuwa bora?” “Hapo tutawaboa. Matajiri hawana muda mrefu wakusikiliza ujinga Roy. Utaniharibia.” “Kwa nini hufikirii kama tunaweza kupata sifa? Ms Cote akitupenda, akampigia simu director, sisi tutakuwa watu wengine kabisa Malcom.” “Unaanza kupotea lengo Roy! Upo hapa kunisindikiza kwa Maya.” “Kwani hatuwezi kupata vyote?” “Nilishakuonya Roy. Naomba usihame kwenye lengo.” “Sawa.” Wakatulia.

“Kwahiyo tujitambulishe. Tuwaambie sisi ndio tulihakikisha Maya yupo salama. Na kwa kuwa hatujakamata watu wote, sisi tunajitolea kumlinda.” “Na kazini?” “Acha kuweka vipingamizi Roy bwana! Kila mtu sasa hivi macho yapo kwa kina Cote. Kule kazini tutawaambia tunafuatilia ushahidi wa kina Cote. Na kwa kuwa jana tulimsafishia bosi kwa director bado anakumbuka kutulipa fadhila. Au unasemaje.” “Usisahau ni Miss Cote sio Maya.” Wote mle ndani wakatamani sasa waingie ili wawaone na kuwasikiliza.

“Oooh no!” “Nini?” “Usigeuke. Lakini director Underson anakuja! Ametoka kwenye lift, amepokelewa na daktari. Wanaongea pale. Lazima yuko hapa kwa ajili ya kina Cote.Tuondoke, na usigeuke.” “Inama tuondoke kimya kimya?” “Hamna hata haja yakukimbia. Wala hatufahamu. Wewe anza kuondoka kwa kujiamini. Ukianza kujihami hapo ndio utaharibu.” Wakasikia kimya. Wakajua wameondoka.

Bibi Cote akatingisha kichwa. Ikabidi Tunda tu acheke na kumtizama Maya. Kaka yake naye akamwangalia Maya. “Unawafahamu?” Maya akacheka. “Nilikuwa nao jana siku nzima. Wao ndio walinihoji na kweli ndio walioniokoa pale kwa Jake.”

Mlango ukagongwa alikuwa kweli director wa CSIS ambaye ni rafiki wa bibi Cote. Mike Underson. Baba mtumzima sana. Na kweli alionekana ameshiba mamlaka na pesa. “Naona leo kuna matumaini!” Akawatania kutokana na ile hali aliyoikuta pale. Wote walikuwa kwenye hali yakucheka kwa mazungumzo ya Roy na Malcom. Japokuwa hawakuwaona, lakini walishapata habari zao.

“Ninaendelea vizuri. Asanteni kwa kunisaidia jana na kunirudisha kwa mtoto wangu.” Tunda akaongea kwa heshima. “Umeshaambiwa!?” Akauliza kwa mshangao, kwani Tunda hakuonyesha hata kuchanganyikiwa au hali ya hofu. Mazungumzo ya Malcom na Roy wote yaliwatoa kwenye ile hali ya tukio la jana yake. “Nimesimuliwa, lakini sikuwa hata na taarifa kwa kile kilichokuwa kikiendelea. Sikujua ni wakati gani nimetolewa hospitalini na wakati gani nimerudishwa. Hata sikuwa na taarifa kama nipo hospitali nyingine. Ndio maana jana nilikuwa nashangaa kwa nini hawataki kunipa mtoto wangu!” “Pole sana.” Yule director akampa pole.

“Lakini mimi naona ni afadhali hivyo kuliko ungejua kinachoendelea.” Akaongeza bibi Cote. “Unafikiri hivyo Nana?” “Kabisa Tunda. Hebu fikiria ile hofu yakujua wamekuteka!” “Na pengine ungeongea na kuibua kitu kingine, wakakudhuru! Au wakahofia kuwa umewaona sura zao, wakahofia kuja kuwataja baadaye. Pia wasingekuacha hai.” Yule director akaongeza. Tunda akabaki akifikiria.

Anyway, nilikuja kuangalia mnaendeleaje na kuwahakikishia kila jicho na sikio la maafisa wa usalama lipo kwenye kesi yenu. Hakuna kitakacho endelea mpaka tumkamate yule aliyewaua kina Malinda na...” “Malinda alikufa!?” Akashituka sana bibi Cote. “Yeah! Kumbe sikukwambia?” “Hapana. Lini?” “Hakutoka chumba cha upasuaji. Alishapoteza damu nyingi sana kabla yakufikishwa hospitalini na ile risasi alipigwa kusudi kuuwawa. Karibu kabisa na moyo. Hakuna jinsi angepona.” Bibi Cote akaishiwa nguvu. Alitegemea Malinda ndio aje awe msaada, kwa kuja kumtaja Ritha na kutoa ushahidi hata kidogo, kama upo.

“Wala usiwe na wasiwasi. Kifo cha Malinda hakijabadilisha chochote. Tupo pazuri tu.”  Mike akamtuliza bibi Cote. “Kwani mmeshamjua ni nani aliyewaua Malinda na mdogo wake?” “Kabisa. Na tunajua tatizo ni pesa. Watakuwa walikuwa wakisubiria pesa kutoka kwa mtu. Tunahisi ndio maana aliua wenzake, ili amtumie Mrs Cote kama kitega uchumi kwa huyo anayewatuma kumteka. Ili pesa zote ziingie kwake. Tunajua alipo na tunamtega ili kuona anakutana na nani ili tuwakamate wote. Msiwe na wasiwasi kabisa.”

Akamgeukia Tunda.“Umesikia Mrs Cote? Usiogope hata kidogo. Kesi yako inafuatiliwa na wataalamu. Na tunamshukuru Miss Cote kwa kuturahisishia. Ndani ya masaa 24, tuliweza kukurudisha kwa familia yako. Ni ushindi mkubwa na imewanyenyekeza wengi. Hata kama kuna aliyefikiria kuja kurudia, nina uhakika hawatafanya hivyo tena.” Tunda akatingisha kichwa kukubali.

          Akamgeukia Maya. “Kibinafsi na kama kiongozi wa CSIS naomba kukupongeza na kukushukuru. Umefanya kitendo cha kijasiri sana. Na umekipa sifa chombo cha usalama, CSIS. Ndani ya masaa 24, tumeweza kufanya mambo makubwa sana. Ikiwepo kukamata watu wa yale madawa hatarishi. Tumeweza kumuhoji Vic mmpaka tumejua alikokuwa akiyatoa na aliyemua, na wapi aliacha mwili wake.” “Wapi na ni nani?” Maya akauliza kwa haraka.

“Mmoja wa kijana aliyekuwa akimtumia kumtafutia hayo madawa. Alimuua ili asije kumtaja. Alimwita kule eneo la bandarini, akampiga risasi na kumficha huko kwenye moja ya boti ambazo ni mbovu. Inaonekana ndiko walikokuwa wakikutania huko wakati wakipeana hayo madawa.” “Mungu wangu!” Wote wakahamaki.

“Haya, tumemkamata Jake. Tumempata Mrs Cote, tumeweza kupata maiti ya Malinda na mdogo wake ambazo zilikuwa zimeachwa kule chini kwenye nyumba ya wazazi wao. Na kwa uchunguzi wa alama za vidole tulizopata kwenye ile nyumba waliyokuwa wamemficha Mrs Cote, ndio tumejua muuaji ni nani, na ndio huyo anafuatiliwa ili kuweza kumkamata na aliyewaagiza. Kwa hiyo hayo yooote, ni kwa sababu yako wewe Miss Cote na ujasiri wako.” Akamsogelea na kumpa mkono.

          “Na mimi naomba nikushukuru sana Mike. Na uniombee msamaha kwa Nancy kwa kukutoa nyumbani kuanzia asubuhi ya jana mkiwa mmelala mpaka kukurudisha usiku kama ule!” Bibi Cote akashukuru. Mike akacheka. “Na yeye ametuma salamu. Atakuja kukuona nyumbani mkitulia.” “Ni kweli nashukuru kutoka moyoni Mike. Mmekuwa msaada mkubwa sana kwa familia yangu. Umeona yule mtoto pale?” Mike akacheka  na kumsogelea Cote kwenye kitanda chake. Alikuwa amelala.

“Usiku wa jana amerudi kunyonya kwa mama yake sababu ya watu ambao hawajalala wala kupumzika siku nzima ya jana, kuhakikisha Tunda anarudi nyumbani. Naomba uwashukuru kwa niaba ya familia yangu. Asante, asante sanaaa.” Bibi Cote alisikika kama hajatosheka kutoa shukurani zake kwa chombo hicho cha usalama. “Utatushukuru vizuri tutakapomaliza hili. Acha nirudi ofisini nijue kinachoendelea. Ila naomba ushirikiano kwa maafisa watakaotumwa kuzungumza na Mrs Cote.” “Bila shida.” Mike akawapa mkono na kutoka na bibi Cote. Kukawa kimya.

“Nikupashie hiyo supu moto?” Akavunja ukimya Net. Tunda akaangalia ile supu na kunyamaza kimya. Akabaki amejiinamia. Net akasimama na kuchukua ile bakuli. Akagairi kupasha moto. Akamwaga na kuweka supu nyingine. Tunda akaanza kunywa tena.

    Bibi Cote akarudi. “Hao maafisa wapo nje. Upo tayari kuzungumza nao?” “Naomba amalize kunywa hiyo supu kwanza. Tutawaruhusu.” Akajibu Net. Kimya. Tunda akaendelea kula mpaka akamaliza ndipo wakaruhusiwa wale maafisa wawili.

Mahojiano ya Tunda na Maafisa wa CSIS.

“Unaendeleaje?” “Vizuri tu.” Tunda akajibu. “Hatutachukua muda mrefu. Tutakuuliza maswali machache tu. Na kama ukiona haupo tayari kujibu, basi.” “Nitajitahidi.” Akajibu Tunda. “Tutaanzia siku ya kwanza kabla hujaletwa hospitalini. Unakumbuka kitu chochote?” Tunda akavuta pumzi. Akajaribu kukumbuka.

“Nilikwenda kwa matembezi, niliporudi ndipo Vic na rafiki yake, walipoingia nakuomba kuzungumza na mimi. Katikati ya mazungumzo ndipo nilipopoteza fahamu.” “Walikufanyia kitu chochote chakukufanyia vurugu?”  Akamuhoji. “Hapana. Sikumbuki hata kama walinigusa. Nakumbuka walikaa upande wa pili wa ile sebule. Na hapakuwa na fujo. Alitumia tu maneno.” Mmoja alikuwa akiandika.

“Kuna kitu chochote unakumbuka kabla yakurudi nyumbani ukiwa matembezini?” Mmoja akauliza. Tunda akabaki akivuta kumbukumbu. “Chochote kile ambacho labda kilikufanya kufikiria. Mtu au tukio? Labda mtu aliyekuwa akikufuata au kukuangalia kila wakati?” Mwenzake akaongeza kama kumsaidia Tunda.

Tunda akafikiria. “Nilijua mlinzi yupo karibu yangu, kwa hiyo hata sikuwa na wasiwasi wakuangalia nilipo na nani ananifuata. Kwa kuwa wakati mwingine huwa nakuwa na walinzi hata wawili na mara nyingine wapili huwa anabadilishwa badilishwa. Kwa hiyo ni ngumu kujua nani ni mlinzi nani siye. Kwa kifupi huwa sinataarifa na nani yupo karibu yangu.” Akajibu Tunda.

“Je, baada ya kufikishwa hospitalini, unakumbuka chochote?” “Ilikuwa ni hali ya kupoteza fahamu na kurudi. Ila nilipofikishwa chumba cha upasuaji, daktari wangu aliyekuwa akinihudumia tokea nipo mjamzito. Aliniambia nipo hospitalini, kwenye chumba cha upasuaji. Wanataka kunisaidia kumtoa mtoto. Watanichoma sindano ya usingizi. Hapo hapo nililala, wakaja kuniamsha tena na kuniambia nilipata mtoto mzima, wakiume na wananirudisha chumbani kwa mapumziko.” Tunda akanyamaza.

“Na baada ya hapo?” “Niliporudi chumbani nakumbuka kuwaona Nana, Maya na Net. Waliondoka baada ya kutakiwa waniache nipumzike. Niliamka katikati ya usiku. Nikaomba mtoto wangu. Wakaniletea. Nilimnyonyesha. Wakamchukua na kumrudisha kwenye nursery.” “Unakumbuka muda?” Wakamuuliza. Akafikiria kama anayevuta kumbukumbu. “Ile ilikuwa saa sita hivi. Nakumbuka yule nesi alisema muda, wakati akinilazimisha kunipima pressure na kunipa dawa. Nilipomkatalia na kumwambia mpaka aniletee mtoto wangu kwanza, aliniambia muda ule ilikuwa ni saa sita, nilitakiwa kupewa dawa.” “Safi sana.” Wakaandika.

“Nini kilitokea baada ya hapo?” “Kwenye saa 10 alfajiri. Niliamka tena. Nikawaomba tena waniletee mtoto ajaribu kunyonya tena kwa kuwa maziwa hayakuwa yakitoka mengi. Wakanisafisha na kidonda kabisa. Wakanibadilisha, ndipo wakanipa mtoto. Nilimnyonyesha nafikiri kama dakika 15 hivi, nikaanza kusinzia mtoto naye akiwa amelala, ndipo wakamchukua mtoto, na mimi nikarudi kulala ndio mpaka hapa.” “Kuna kumbukumbu nyingine?” Akauliza taratibu tu.

“Mmmmh! Nilipoteza masaa kadhaa mpaka muda mfupi uliopita ndipo nikaelezwa nilitekwa nyara. Lakini sikumbuki chochote. Ni kama nilipolala wakati ule, nikaja kuamshwa kwa nguvu sana na madaktari hapa. Wakinitaka nijitahidi hata nifungue macho. Kumbe ndio muda walikuwa wananirudisha hapa. Sikuwa nikijua.” Wakaandika.

“Hukumbuki chochote hata kama inafanana na ndoto?” “Ndio nilikuwa nikiwaambia hawa. Sina uhakika.” “Tuambie tu. Hata kama ni kitu kidogo.” Tunda akavuta pumzi kwa nguvu, akajisogezea mto. Maya naye akamsaidia, akajilaza vizuri. Maya akambusu. “Nakupenda Tunda.” “Asante Maya. Nashukuru.” Akamshika mkono na kuwageukia wale polisi.

“Kuna muda ni kama nilitoka usingizini. Lakini bado nilikuwa na usingizi. Nikafungua macho kwa shida. Nikamuona mwanamke aliyevaa nguo za kinesi. Kama tu wale waliokuwa wakinihudumia na kuniletea mtoto. Nikamuomba akaniletee mtoto wangu. Sasa nakumbuka kusikia sauti ya kiume iliyonifanya nigeuke, kwa kuwa hakuwa akisikika kama Net.” “Alisema nini?” Akamuhoji tena.

“Naweza nisipatie sana kwa kuwa nilikuwa na usingizi, hata macho hayakuwa yakifunguka vizuri. Ila alimwambia yule nesi kwa kumlaumu kwamba amenipa dawa kidogo. Sio dozi iliyokamilika ndio maana nimeamka. Alitakiwa kuwa makini. Sasa kwa kuwa mawazo yangu yalikuwa kwa mtoto. Nikimtaka akaniletee mtoto wangu, nikarudisha macho kwa yule nesi ili kumuomba akaniletee mtoto. Nikamuona anachoma sindano kwenye ile sindano iliyokuwa imeunganishiwa dripu. Hapo hapo nikalala. Sikuamka tena mpaka hapa.” “Tukikuonyesha picha, unaweza kuwatambua?” Tunda akajifunika uso kwa mkono mmoja.

“Upo sawa, Tunda?” Net akauliza. Tunda akatoa mkono. “Sikumbuki kuwaangalia usoni. Nilikuwa ninausingizi mzito sana. Hata sijui kama ni kweli au ilikuwa ndoto!” “Ungependa kujaribu kama unaweza kuwatambua?” Wakamuuliza kiuungwana. “Sidhani. Kwa sababu nina uhakika hata wakirudi tena leo hapa, sitawafahamu. Sikumbuki chochote. Lakini kwa kuwaridhisha, acha tu niangalie.” Wakamtolea picha za wanaume na wanawake wengi kwenye tablet.

Tunda aliangalia kwa kutulia. Kuanzia mwanzo mpaka mwisho. “Samahanini jamani. Sikumbuki kabisa!” “Na hizi?” Wakamfungulia sehemu nyingine. Akaangalia tena mpaka mwisho. “Hakika sikumbuki kuona hizi sura zote hapa. Samahanini sana.” “Usijali kabisa. Hata hapo umekuwa msaada.” Tunda hakuwa ameelewa.

“Kivipi wakati hakuna nilichofanya?” “Kutokana na damu uliyochukuliwa jana kabla ya matibabu, kuna aina fulani ya kemikali zilikutwa humo ambazo zinatokana na madawa ambayo yanauzwa na mtu ambaye amekiri kuwauzia baadhi ya watu. Kuwafanya walewe. Na kufanya mambo fulani ambayo hufuta kabisa zile kumbukumbu siku inayofuata au pale hayo madawa yanapoisha. Huyo mtu ameshakamatwa. Na baadhi ya madawa yamekamatwa nyumbani kwake.” “Mmejua ni kina nani alikuwa akiwauzia?” Akauliza Maya.

“Wapo wateja wake ambao huwauzia, na bado tunaendelea na uchunguzi mpaka utakapo kamilika.” “Ni Vic?” Maya akauliza tena moja kwa moja akijua wanaficha. “Bado tupo kwenye uchunguzi. Utakapokamilika, tutawajulisha.” Walishindwa kumtaja mtu hata mmoja. Wakamshukuru Tunda na kina Cote, wakaondoka.

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

“Rudi nyumbani ukaoge ulale kidogo.” Maya alimsogelea kaka yake pale alipokuwa ameinama kwenye kochi. “Jana niliondoka, huku nyuma wakamteka nyara mke wangu. Nataka nikitoka hapa, nitoke nao wote.” Maya akambusu kichwani. “Pole Net.” Net akamwangalia tu. “Unaonekana umechoka sana. Basi jilaze kidogo hapo kwenye kochi. Mimi nipo hapa kumsaidia Tunda.” Maya akasimama. Akamtolea kaka yake mto na shuka. Akamfunika. Akazima taa ya pembeni yake ya kwenye meza. Akambusu kaka yake shavuni. Hapo hapo Net akapotelea usingizini. Tunda na bibi Cote kimya kama hawapo pale.

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

Net alilala pale kwenye kochi kama na yeye amepewa dawa za usingizi. Akili ilikuwa imepitishwa kwenye mikasa mizito, kisha akatengwa na watu wawili muhimu sana kwake. Kwa mara ya kwanza Net anakuwa kwenye matatizo nakushindwa kusaidia na wala hakuna anayemtambua! Na kwa mara ya kwanza kwenye maisha yake ndio anapatwa na kashfa mbaya sana na ikasababisha madhara kwa mkewe. Vic alimchafua haswa hakuwa hata na hamu na simu yake wala kushika kompyuta. Redio ndio kabisa, hakuta iwashwe popote alipo.

Video yake ya ngono ilisambazwa na watu walishare kila mahali. Ilipata watizamaji kuliko hata habari nzito za nchi. Kila alipopita na kuzungumza hata na manesi wa hapo, alijihisi yupo uchi. Ile kufunga macho akijua angalau mkewe na mtoto wapo pale salama, ikamsaidia.

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

Upade mzima alipokuwa amelazwa Tunda, ilikuwa haina mgonjwa mwingine ila yeye tu. Hakuna aliyeruhusiwa kwenye huo upande wa gorofa hilo bila kitambulisho. Manesi pia waliingia hapo wachache na walichunguzwa kila walipokuwa wakiingia na kutoka. Hakuna aliyeruhusiwa kumpa dawa Tunda, bila daktari na mlinzi wa Tunda kuwepo hapo. Tunda alishakataa dawa yakumfanya kulala. Alikataa kabisa.

Na tokea aelezwe kuwa alitekwa akiwa usingizini, hakuweza kulala tena. Alibaki amekaa hapo kitandani, hata hakufunga macho. Wakati wote macho kwa mtoto wake. Alikuja nesi kutaka kumchukua mtoto wake akamuogoshe, nusura Tunda avunje mguu. “Nooooo.” “Nakwenda kumuogesha.” Yule nesi akajibu kwa upole na tabasamu ili kumfanya Tunda atulie. “Hapana. Hapana na HAPANA.” Tunda akasimama. Ikabidi bibi Cote asimame na yeye.

“Wanaenda kumuogesha na kumbadilisha. Huyu ni nesi wa hapa. Ni salama.” “Hapana Nana. Naomba usimguse. Tafadhali mwache tu.” Tunda akawa ameshaingiwa hofu. Akasogea mpaka kwenye kitanda cha mtoto wake. Machozi yakaendelea kumwagika. “Basi twende wote Tunda. Twende naye.” Maya akamtuliza. “Naona sipo tayari aogeshwe, Maya. Kwanza amelala. Kwa nini aogeshwe sasa hivi? Naomba mumuache mwanangu apumzike.” Bibi Cote akamsogelea.

“Niangalie Tunda.” Tunda akageuka. “Hakuna atakayefanya kitu kwa Cote bila wewe kutaka. Mwambie ni nini unataka. Basi.” “Sitaki mtoto wangu ashikwe na kila mtu! Diaper anabadilishwa na huyu. Nguo anabadilishwa na yule! Siwafahamu na ..” “Aliyekuwepo asubuhi ametoka.” Yule nesi akaongeza kwa tabasamu. “Mimi nimepona. Nitamuhudumia mtoto wangu mwenyewe, Nana. Tafadhali. Najua kuogesha watoto na kuwavalisha. Sihitaji msaada. Nimefanya hivyo..” Net akatoka usingizini akamkuta Tunda akilia.

“Kuna nini?” Net akauliza taratibu. “Nataka kwenda nyumbani. Sehemu nitakayotulia na mtoto wangu tu. Hapa watu wengi wanapishana kila wakati. Naogopa, situlii mawazo. Kila mtu anamgusa mtoto wangu. Wanapishana hapa kila wakati kunigusa, wakati vipimo vinaonyesha nipo sawa! Sitaki nesi yeyote aingie tena humu ndani, Net. Na ninataka kurudi nyumbani.” “Okay. Tulia. Ngoja nikazungumze na daktari. Turudi nyumbani.” Net akasimama pale.

“Njoo ukae hapa kitandani.” “Mimi sio mgonjwa Net. Wakati umelala hapo wamekuja kuangalia kidonda wamesema kipo sawa na pressure ipo nzuri. Lakini kila baada ya nusu saa wanarudi humu ndani! Siwezi kutulia! Tafadhali nitoeni hapa. Nitachanganyikiwa. Sasa hivi kila anayeingia humu ndani naingiwa hofu. Nataka kurudi nyumbani, Net.” “Sawa. Tutaondoka.” Net akatoka.

Bibi Cote akamwambia yule nesi atoke. Kisha akamwambia mlinzi, asiruhusu mtu mwingine yeyote aingie hapo ndani. Kisha akamfuata Net kule alipokwenda kwa daktari. “Hajalala hata kusinzia tokea wale maafisa waliomuhoji waondoke. Nafikiri ameingiwa hofu. Naomba uturuhusu tu, tuondoke. Kukitokea chochote nitampigia simu daktari wake. Nashukuru sana. Lakini nafikiri mturuhusu tu tuondoke. Itamsaidia kutulia.” Bibi Cote akaweka msisitizo.

“Hiyo inaeleweka kabisa. Kwake sasa hivi hospitalini hapatakuwa sehemu salama tena. Hata hivyo hakuonekani kama kuna tatizo lakuendelea kumlaza hapa. Nafikiri anaweza kurudi nyumbani tu.”  Wakaongozana mpaka chumbani kwa Tunda. Wakamkuta amembeba mtoto wake. “Upo tayari kurudi nyumbani?” “Ndiyo.” Tunda akaitikia kwa haraka. “Ungependa nesi aje kukuonyesha jinsi ya ...” “HAPANA.” Tunda akakataa kwa haraka bila hata kumruhusu yule daktari amalizie.

“Sihitaji kufundishwa chochote kwa mwanangu.” “Je, kwa nyumbani ungetaka nesi awe anakuja kuku..” “Hapana. Sihitaji nesi karibu yangu wala mtoto wangu. Please Nana!” “Hakuna nesi kwenye ile nyumba.” Bibi Cote akatoa kama amri. Tunda akatulia. “Asante Nana. Si tunaweza kuondoka sasa hivi?” Tunda akauliza huku akimbembeleza mtoto aliyekuwa amelala, hana hata habari. “Hapa silali kabisa. Halafu..”  Akasita. “I just want to go home.” “Sawa. Twende ukatoe nguo za hospitalini wakati usafiri wakututoa hapa ukiandaliwa.” Net akamtuliza.

“Mpe Maya mtoto.” Taratibu akamkabidhi Maya mwanae. “Naomba usimpe yeyote kwa chochote. Iwe wewe na Nana tu. Tafadhali Maya. Au twende naye tu?” Akamgeukia Net akiwa amebadili tayari mawazo. “Sitamuweka hata chini Tunda. Nitampakata. Kwanza na mimi nina hamu naye.” Maya akawahi kabla hajapokonywa huyo mtoto. Akambusu mara kadhaa, hapo Tunda akaridhika. Net akamsindikiza bafuni. “She will be fine.” Bibi Cote akanong’ona.

Tunda arudi nyumbani na mtoto wake.

T

unda akashangaa anapanda gari ngeni kabisa kwake na imefungwa kiti maalumu kwa umri wa mtoto wake. Nzuri, safi sana. Dereva alikuwa yuleyule wa Tunda. Net ndiye alikuwa amembeba mtoto wao. Huo ulinzi uliokuwa ukiwazunguka, mpaka Tunda akaingiwa hofu. Waliambiwa wasubiri dakika 20 ili kuweza kusindikizwa. Na kweli walisindikizwa. Ilianza gari ya usalama. Akaja bibi cote na ulinzi wake pamoja na Maya. Ikaja hiyo gari ya mtoto, Tunda na Net. Polisi nyuma yao. Wakaondoka.

Hakuna waliposimama hata kwenye taa, polisi wa pikipiki waliwasaidia kusimamisha magari wapite bila kusimama hata kwa sekunde chache. Walifika nyumbani geti lilifunguliwa kama waliokuwa wakisubiri. Kulikuwa na ulinzi, Tunda akashangaa sana. Net alimfungulia mlango, akakuta Maya bibi Cote, Carter, Ms Emily wamesimama mwanzo kabisa wa  kwenye ngazi wakiwasubiria. Walizungukwa mpaka na askari wa bunduki.

Tunda alishuka na kuzungusha macho kote. Uzio mzima ulikuwa na ulinzi. “Twende ndani ukapumzike.” Net akaongea kwa kujihami. Carter akasogea kumkumbatia, kisha Ms Emily. “Nimefurahi umerudi nyumbani.” Ms Emily alimnong’oneza wakati amemkumbatia. Tunda akatoa tu tabasamu. Net alikuwa amebeba mtoto. Walisimama hapo kidogo kwa picha, kisha wakaingia ndani. Cote alimka palepale nje wakati baba yake akimnyanyua ili apigwe picha na kuchukuliwa video.

“Namuomba nikamnyonyeshe.” Net akamkabidhi, Tunda akaelekea chumbani kwa mtoto, Maya na yeye akafuata nyuma kwa haraka bila hata kusubiri aitwe. “Nikusaidie nini?” “Sitaki msaada Maya. Nataka muda na mtoto wangu.” Tunda akajibu huku akiingia chumbani kwa Cote. Na Maya naye akaingia. “Kwani bado umenikasirikia au umenisamehe? Maana ulipoondoka mwenzio nilikuwa nakulilia!” Maya akaanza. “Unajua nilikuwa nakulilia nini?” “Kuwa umenificha kitu kikubwa na kuniacha mimi nimedhalilika?” “Tunda!?” Maya akashangaa sana.

“Sio hicho. Wewe usimsikilize Vic. Vic anataka kutugombanisha mimi na wewe.” “Kwani ni uongo? Wewe hukujua kama alilala hapa baada ya kufunga ndoa na kaka yako?” “Nilijua Tunda. Lakini..” “Naomba undoke uende kwa kaka yako.” “Come on Tunda! Hata wewe mwenyewe ungekuwepo siku ile Net ameamka pembeni ya Vic ungemuhurumia! Alikuja ofisini kwangu, Net anatetemeka mpaka midomo. Akaniomba msamaha akasema hata hakujua ilikuaje ameamka pembeni ya Vic!” Maya akajaribu kujitetea.

“Yeye kwa nini alimwalika chumbani kwake, kama sio alikuwa anataka?” “Sasa kwa nini wewe, mimi na Nana, tusiungane tukamkasirikia Net? Na mimi mniingize kwenye kundi lako na Nana!” Tunda akamwangalia na kuendelea kunyonyesha.

Maya akajilaza kwenye kapeti mbele ya Tunda. “Ujue hata Nana hataki kuniongelesha kama wewe ambavyo humuongeleshi Net?” Maya akaendelea. “Lakini turudi kwenye pointi yangu Tunda.” “Pointi gani? Ile ya kunililia ukijuta?” “Ndio maana nilikuwa nakulilia Tunda. Wewe unanisikiliza.” “Mbona sasa hukuniambia huyo ambaye hataki kukuamini tena?” Tunda akamuuliza habari waliyozungumza hata kabla hajafuatwa na Vic.

“Si ndio maana nilikuwa nakulilia sasa? Nikasema wasingekuiba kabla sijakwambia siri yangu!” “Kwa hiyo ungekuwa umeniambia, ndio ingekuwa sawa mimi kutekwa?” “Hata kidogo. Nani sasa angenisikiliza sasa hivi?” Akakaa. “Ndio ujue nyumba hii ilivyo. Sasa hivi kila mtu analake kichwani. Basi ujue mimi nitasahauliwa kabisa. Net ndio atakuwa hata hajui ninaendeleaje tena. Na ilimradi Nana anajua nipo humu ndani, hakuna hata atakayeniuliza kama nimekunywa hata maji!” Tunda akamwangalia.

“Umeniudhi Maya!” “Usinichukie Tunda. Mimi nitakusaidia kumnunia Net. Lakini mimi niwe na wewe. Au hata Net tumsamehe tu. Kwa kuwa hakuwa akijua kama..” “Unaniudhi zaidi Maya!” “Basi. Net ni mbaya sana. Tumchukie kabisa. Hamia chumbani kwangu. Tulale mimi na wewe tu. Tuwe tunaongea usiku kucha!” Ikabidi Tunda acheke.

“Na mtoto?” “Usiku tunahamisha kitanda chake chumbani kwetu.” Tunda akamwangalia na kurudisha macho kwa mwanae. “Kwa hiyo hutataka mfanyakazi wa mtoto?” “Amshike mtoto wangu wakati mimi nafanya nini!?” Maya akanyamaza. Tunda akamwangalia. “Nini sasa?” “Cote anabahati, sio kama mimi na Net. Sidhani hata kama mama yangu alininyonyesha Tunda! Mimi sikulelewa kama Vic. Sikukuzwa na wazazi wangu!” Maya akaongea kwa kunung’unika.

“Lakini Papa na Nana walikupenda sana.” “Lakini hawakuwa wazazi wangu Tunda. Ni tofauti mtoto akilelewa na mama yake. Ona hivyo ulivyomkumbatia mtoto wako! Mimi sidhani kama nilipata hayo mapenzi.” “Sasa wewe hakikisha watoto wako wanapata hayo mapenzi. Hata mimi mama yangu hakunitaka Maya. Alinizaa tu na kwenda kuniacha kwa wazazi wake. Tena afadhali wewe alikuwa akija hata kukuangalia kujua unavyoendelea. Mimi mama yangu hakunipenda kabisa. Kwanza nilizaliwa na hii rangi ambayo hakuwahi kuipenda. Mpaka sasa hanipendi. Lakini..” “Mungu amekupa Net.” Maya akamalizia.

“Nilitaka kusema lakini hainizuii mimi kutompenda mwanangu. Mungu amenipa nafasi ya kurekebisha kile nilichokosa.” “Nikuulize Tunda?” “Uliza tu.” “Wasichana wengi hapa. Hata Vic alikuwa akisema kama ni kuzaa, atazaa mtoto mmoja tu na hata akizaa hatamnyonyesha mtoto ili asiharibu matiti yake, zaidi mwili. Maana wanasema ukinyonyesha unazidi kusikia njaa.” Tunda akacheka sana.

“We Maya!” “Kweli. Sasa wewe huogopi?” “Akuu. Hata kidogo. Kwanza nilishafundishwa jinsi yakunyonyesha ili matiti yasiharibike. Halafu vipo vyakula unaweza kula na usinenepe. Hata hivyo sijali Maya. Zipo faida nyingi kwa mtoto wangu kunyonya kuliko mimi kutilia mashaka huu mwili unaoweza kuharibika hata kwa magonjwa tu.” “Ndio maana nakupenda Tunda.”

“Yaani nishindwe kumnyonyesha mtoto wangu sababu yakuhofia matiti yataharibika! Hata kidogo. Nitamnyonyesha Cote bila kumpa kitu kingine mpaka afikishe miezi 6, ndipo nitamchanganyia na kitu kingine. Akifikisha mwaka, ndipo naweza kufikiria  kumuachisha.” “Mpaka mwaka!” Maya akashangaa sana. “Kabisa.” Wakaendelea kuongea. Huwezi kumkasirikia Maya.

Net kwa bibi yake.

N

et alijikuta ameachwa hapo sebuleni peke yake. Akafikiria akaona ni lazima atengeneze. Akatoka hapo bila yakuaga. Alikwenda kununua maua ya bibi yake na Tunda. Na zawadi kidogo. Akarudi nyumbani. Moja kwa moja akaenda ilipo ofisi ya bibi yake. Akamkuta ameinamia kompyuta yake. Kimya. Net akagonga na maua aliyojua bibi yake anayapenda sana. Tulip. Akawa ameshika tulip bouquet mkononi. Bibi yake akatoa miwani na kuiweka mezani. Akamtizama.

Kwa aina ile ya rangi za hayo maua ya Tulip, bibi Cote akajua ameingia kuomba msamaha. “Nimekuja kuomba msamaha Nana. Samahani sikukwambia kilichotokea siku ile na Vic. Samahani nilimkataza Carter na Maya pia wasikwambie. Najua ningekwambia mapema, tungejua kitu chakufanya. Nilikosea sana. Ninaomba unisamehe.” Bibi yake akavuta pumzi kwa nguvu. Akajiegemeza kwenye kiti.

“Hayo ni maua yangu?” Net alikuwa bado ameyashikilia. “Ni yako Nana.” Akampelekea. “Naweza kukukumbatia? I miss you so much Nana.” “Umenifedhehesha vibaya sana Net.” Bibi yake akalalamika. “Najua Nana. Lakini nakuhitaji sana sasa hivi. Sijui nitafanya nini na mama! Amefika mbali sana. Anataka kumuua Tunda!” “Ritha ni mama yako. Mwache sheria imshugulikie ili usije kujilaumu baadaye.” Net akanyamaza.

“Niangalie Net. Nimetoka kuzungumza na Mike, hawana muda mrefu, watamkamata tu. Labda asiwe yeye anahusika. Naomba tuliza mawazo kwenye familia yako. Hakikisha Tunda hahami chumba.” Net akaenda kumkumbatia na kumbusu bibi yake. Akatulia hapo kwa muda. Akambusu tena na kutoka akiwa ameelewa jukumu alilopewa na bibi yake.

Net kwa Tunda!

A

liingia na kukuta Tunda ameweka mtoto wake kifuani anamsikiliza Maya akiongea akiwa amekaa hapohapo chini mbele ya Tunda. Maya akasimama kwa haraka. “Mimi nilijua unasaidia mambo ya mtoto!” “Nimesaidia kuongea na mama yake huku akinyonyesha. Ameshiba. Tunamuacha alale, akiamka tunamuogesha. Sisi wenyewe sio mfanyakazi!” Maya akaanza. “Unajua kuwa huyu mtoto atalelewa na sisi tu sio wafanya...” Akamwangalia Tunda, akamuona amenyamaza wala hamwangalii Net. “Nimekumbuka, wote tumekununia. Hatukuongeleshi. Bad bad dady!” Maya akamkunjia uso kaka yake kama amemkasirikia. Net akatingisha kichwa na kumfanyia ishara atoke.

“Nitarudi baadaye Tunda. Nikusimulie stori yangu. Mimi na wewe ni marafiki. Usisahau hilo. Nikirudi tunaanzia kwenye urafiki. Tumeshasahau mambo ya.....” Tunda akasimama kwenda kumlaza mtoto. “Umemletea mtoto maua?” Maya akanong’ona wakati akitoka. “Noo! Haya maua ni ya mke wangu.” Maya akamcheka. “Mwenzio nimesamehewa.” Akamnong’oneza Net. “Lakini wewe, sidhani.” “Toka Maya.”  Net akamsukumia nje.

Tunda akabaki akimfunika mtoto wake pale kwenye kitanda. “Unajisikiaje?”  Akaanza Net. Kimya. “Kila kitu unachohitaji cha mtoto kipo?” Kimya. “Yule nesi aliyekuwepo hapa, aliandika orodha ya vitu vyote ambavyo vinahitajika kwa Cote, vikanunuliwa. Nikuangalia tu humuhumu ndani na Ms Emily ata...” “Naenda kuoga na kubadili. Unafikiri unaweza kukaa hapa na mtoto mpaka nirudi?” “Au nikusindikize kule kuoga halafu..” “Net!” Tunda akaita kwa ukali. “Basi mimi naona nibaki na mtoto hapa mpaka utakaporudi kutoka chumbani kwetu. Chumba changu mimi na wewe.” “Na Vic.” Akaongeza Tunda na kutoka. Net akang’ata meno.

Tunda alioga. Na kubadili nguo zake. Akatoka na kibegi kidogo chenye baadhi ya nguo zake. Wakati anaingia pale chumbani kwa mtoto, Net akamuona anaingia na begi akilivuta. “Umetoka kufanyiwa upasuaji Tunda. Naomba usibebe vitu vizito.” Akaenda kumpokea. “Ni sanduku la nini tena?” Tunda hakujibu, akaenda kukaa kwenye kiti chake chakunyonyeshea.

Net akafungua lile sanduku alilokuja nalo Tunda. Akakuta baadhi ya nguo zake. “Basi ngoja na mimi nikafungashe nguo zangu, nije.” “Naomba wewe usihamie huku.” “Tunahamia wapi?” Net akauliza. “Naomba uache kelele mtoto amelala na uondoke humu ndani nenda kwenye lichumba lako ambalo unaingiza wanawake zako na kulala nao mpaka asubuhi.” “Tunda naomba uniamini. Sikumkaribisha Vic mle chumbani. Alinifuata nyuma na kuingia na juisi ambayo niliacha kule sebuleni nilipomwambia anisubiri nakwenda kumfuatia vitu vyake chumbani. Nimeingia tu chumbani na yeye akanifuata. Aka..” “Naomba acha kelele Net.” Tunda akamkatisha.

“Hayo maelezo ungetaka kunipa, ungenipa kabla na mimi hujaniingiza kwenye kile chumba. Sasa hivi unaongea hivyo kwa kuwa unaona siri yako imejulikana. Naomba uondoke, unipishe na mtoto wangu. Sitaki maneno mengiii na sitaki uanze kuongea uchafu wako mbele ya mtoto wangu. Huoni aibu kueleza mambo ya mwanamke wako mbele ya mtoto!” “Sio mwanamke wangu Tunda. Mbona hunielewi?” “Ondoka Net. Lasivyo naenda kumuita Nana akutoe humu ndani.” “Tunda!” “Tena toka na maua yako. Usirudi hapa na maelezo yako ya uzinzi.” “Mimi sijazini Tunda. Alinilevya.”

“Kitendo cha kunificha mimi kuwa uliamka pembeni ya mwanamke wako, tena baada ya kunidanganya mbele ya umati wa watu kuwa utakuwa mwaminifu kwangu daima, huo ni uzinzi Net. Naomba uondoke.” Tunda akaendelea.

“Unanirudisha kwenye maisha machafu sana ya zamani Net. Maisha ya kuishi ya kudanganywa! Nakuwa kwenye mahusiano ya watu watatu! Bado na mwanamke wako naye alikuwa na wanaume wengine. Nakuwa kwenye mahusiano ya watu zaidi ya wawili! Kunakuwa na tofauti gani vile nilivyoishi zamani na hiki unachonifanyia sasa hivi?” Net akaishiwa nguvu kabisa.

“Ipo tofauti Tunda.” “Tofauti gani? Unatofauti gani wewe na wanaume wengine wengi waliokuwa wakinitumia na kunidanganya? Kama kweli ungekuwa ukinipenda na kunithamini, usingeacha nadhalilishwa na mwanamke wako!” Tunda akaanza kutokwa na machozi. “Mimi namfukuza chumbani nikijua ni chumbani kwangu na mimi kumbe ndio na yeye ni chumbani kwake! Tena ulipo mhalalishia! Unaniacha natoa viapo hadharani, nikijua nipo mimi na wewe tu, kumbe unavyo viapo na maagano uliyokuwa umewekeana na kuishi na mwanamke wako!” Tunda aliongea kwa kuumia sana huku akilia na ongea yake ni ileile ya taratibu, akapunguza sauti zaidi ili mtoto wake asiamke.

“Kwa ujasiri bila woga, anaingia hapa si kama mgeni, kama mtawala humu ndani! Tena baada ya mimi kumfukuza! Ananiongelesha kama anaongea na takataka, kumbe hiyo jeuri anaitoa kwako wewe mwenyewe Net. Unafikiri nitakaa humu ndani kama kina Ms Emily mimi? Hapana Net. Ulinikuta nikiheshimiwa na mimi nilikuwa na wafanyakazi waliokuwa wakiniheshimu kama hivyo wewe unavyoheshimiwa. Umenitoa nyumbani, unakuja kunidhalilisha huku! Unanitukana mbele ya watu na ndugu zako!” Net akakumbuka kugomba kwake siku yakuonja chakula alipochelewa Gino.

“Ninakusihi utulie. Mimi ndiye nilipanga mambo yote. Kwa kuwa huniamini na kuniheshimu kama mwanamke wako unayeweza kumtunzia siri na kumsitiri hadharani, unatokea tu nakuanza kunitukana na kunidhalilisha mbele za watu! Kama kweli wewe ni mtu mwadilifu kama ulivyonifanyia mimi na kuwa na msimamo mkali kwangu na kama hukupenda kubakwa na Vic, si ungechukua hatua siku ileile?”

“Mbona ulinyamaza na mkaendelea kama kawaida? Unanidanganya mimi eti hukujua kama ulifanya mapenzi naye, kama si kunifanya mimi mtoto mdogo, wewe ufanye mapenzi muda wote huo uamke asubuhi usijue kama ulifanya mapenzi usiku!”

“Ulijua sana tu na kupenda mlichofanya kwa kuwa ni mwanamke wako. Ukafurahia kufanya naye mapenzi. Wala usinidanganye kama ulibakwa. Ni uongo wa kijinga sana. Nenda kadanganye mashabiki wako huko nje. Kamtetee kuwa hana akili ndio maana alifanya aliyofanya. Pengine anatakiwa kuongezewa dawa. Wampe dawa, wamtoe, muendelee. Lakini Net, sio na mimi.”

“Nilishaachana na watu kama wewe kwa garama kubwa sana. Wewe hujui hilo kwa kuwa wakati mimi nahangaika kubadili maisha yangu, ulikuwa ukifurahia na watu kama Ritha na Vic. Huko sitarudi Net. Na kama nikiamua kurudi, nitarudi kwa heshima sio kwa kudhalilishwa.” Net akavuta pumzi kwa nguvu.

“Na ujue wakishakamatwa tu hao watu wako wanaotaka kuniua, naondoka humu ndani. Nitaondoka kwa heshima yangu kabla hujanidhalilisha zaidi. Na wala usiwe na wasiwasi na pesa yako. Sitakuchukulia chochote. Kwa hiyo uwe na amani, utaendelea kuwa na mali zako kama kawaida. Ondoka humu ndani ya hiki chumba Net.” Net akataka kuondoka. “Usisahau maua yako. Beba na uondoke nayo. Usirudi na maua hapa. Nilikwambia tokea tupo Tanzania. Sikufuata maua mimi. Nilikufuata wewe. Kama nimeshindwa kukupata wewe..” Tunda akasimama akilia kuelekea upande wa chooni huko huko ndani bila hata kumalizia.

Gino akawa anagonga na kigari cha chakula. Net akamfungulia. Gino akaingia ndani, akaacha chakula na kutoka. Net naye akatoka na maua yake mkononi.

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

          Kama aliyekuwa akisubiria nje ya mlango, wote walipotoka tu Maya naye akarudi. Tunda alitoka chooni akiwa kimya kabisa. Maya akaona amebadilika, sio kama alivyomuacha. Akajua mambo hayakwenda vizuri na kaka yake. Hakumsemesha. Tunda akachukua chakula, nakuanza kula kimya kimya.

Maya akabaki akimwangalia kwa kujiiba huku macho yapo kwenye simu. Wakati anamaliza tu kula, mtoto akaamka. Akaweka kila kitu chini. Akaenda kumchukua mtoto wake akaenda naye bafuni. Maya akamfuata nyuma. Akamuona anaandaa maji ili amuogeshe mtoto. Akaendelea kumfuata kila anaposogea. “Ulijifunza wapi mambo ya watoto? Jinsi unavyomshika Cote, ni kama mzoefu kabisa!”  “Nilimlea mtoto wa mama tokea mdogo sana. Au tokea anazaliwa. Kwa hiyo najua.” Tunda akajibu.

Alipomaliza kumuogesha, akaenda kukaa naye kwenye kiti. Tunda huyu alikuwa amefanyiwa upasuaji. Lakini hakuwa hata akijifikiria kwa hofu na hasira. Akakaa na mtoto wake kwenye kiti nakuanza kumnyonyesha. Maya akimwangalia. “Nikuulize Tunda?” Maya akamrushia swali. Tunda akamwangalia. “Unafikiri mtoto kama huyo hapo ulipomshika, anahisi kama umebeba uchungu?” Tunda akaanza kulia.

“Najua umeumia sana Tunda. Lakini nikwambie ukweli Tunda, hilo ndilo lilikuwa kusudi la Vic. Kwamba kama yeye amekosa, basi mwingine asimpate Net. Na pia ndio furaha ya mama yetu. Mimi najua kama mama alitutelekeza Tunda. Najua mama hajali kile mimi na Net tunajisikia. Ndio maana yupo radhi kukuangamiza wewe, bila kujali kile Net atajisikia.” Maya aliongea taratibu tu.

“Unajua ni kwa nini nilihangaika mpaka nikakubali kufanywa mapenzi mbele ya wale maafisa wa CSIS?” Tunda akashituka sana. “Maya!” “Sijamwambia mtu yeyote. Lakini sharti la Jake ilikuwa nilazima nifanye naye kwanza mapenzi ndipo akutafute wewe. Nikijua kabisa wale maafisa wananisikiliza na kutuangalia, nilikubali Tunda.” Tunda aliumia sana.

“Na haikuwa kitu kidogo cha muda mfupi! Jake alihakikisha ananitumia haswa. Unafikiri ni kwa nini yule director wao alinishukuru vile? Anajua kilichonipata, ila hawezi kumwambia Nana.” Tunda akaumia sana. “Usingekubali Maya!” “Leo usingekuwepo hapa Tunda. Huwezi kujua wangekufanya nini huko walipokuteka. Tena kama sasa hivi ambavyo wamembana mama! Yule nesi, Malinda walimpiga risasi wakitaka kummaliza kabisa kama walivyomuua kaka yake wakiwa hukohuko walipokuficha na wewe. Unafikiri huyo mtu aliyebaki na kuwauwa wale angekufanya nini na wewe kama sio kukuua kwa kuwa huna faida tena kwake? Ungegeuka kuwa mzigo ambao asingeweza kukuhudumia tena.”

“Kumbuka aliwaua wale wenzake mpaka mwanamke wake, polisi wanahisi ni kwa kuwa alitaka mama amlipe yeye pesa yote na kufuta ushahidi. Kumbuka nia ya mama pia ilikuwa uuwawe. Sasa unafikiri mpaka sasa ungekuwa hai?” Maya akamuuliza taratibu tu.

“Hakuna anayetupenda mimi na Net kama sisi. Hata mama yetu mzazi amekuwa akitutumia tu ili kujinufaisha. Hakuna anayejali furaha yetu kama sisi. Ndio maana mimi nikakimbilia madawa ya kulevya, Net akakimbilia Afrika. Unafikiri ni kwa nini?” Maya akajifuta machozi.

“Wote tulikuwa tukihangaika kutafuta kujaza pengo ambalo halikuwahi kujazwa tokea baba yetu afariki. Tulikuwa tukitafuta mapenzi ambayo tunajua yapo, lakini sisi hatukubahatika tena baada ya baba kufariki, Tunda. Baba alitupa mapenzi mazito sana, halafu akatuacha tukiwa bado tunamuhitaji. Akatuacha tukitafuta kujaza hilo pengo. Pesa kwetu imekuwa kama laana. Imetuweka mbali na uhalisia. Tumezungukwa na watu wanaotaka kunufaika na pesa ya Cote tu.”

“Vic hakuwahi kumpenda Net kama Net. Ila marupurupu yanayotokana na Net kama  Cote. Nina uhakika, Vic angekutana na Net uliyekutana naye wewe Afrika, asingemng’ang’ania kama hivi.”

    “Mimi nililelewa na dad, wakati mama alikuwepo! Dad alipofariki, nililelewa na Papa na Nana, bila mama, wakati mama alikuwepo! Ninachokuomba Tunda, usimuunge mkono mama katika kuendelea kutuumiza. Hujui nikiasi gani Net alivyofurahi ulipokubali kuja kuishi huku na yeye, tena baada ya mama kukufunga. Alipiga simu huku akilia kwa furaha. Kuwa umemchagua yeye, zaidi ya majaribu yote shetani aliyowatupia!”

“Na ninakuomba usikubali Vic akuingie akilini mwako kama alivyowaingia familia yangu kipindi akiniangamiza mimi. Ni ngumu sana Tunda. Huwezi kuelewa mpaka uwe umepita hapo.” Maya akaendelea taratibu tu. “Mimi najua anakopita Net, kwa kuwa Vic alinipitisha hapo. Na ni mjanja sana katika mipango yake. Anaakili katika maovu yake. Haachi mwanya wa mtu kusimama na wewe anapokutenda jambo.”

“Nilikuwa nikilia mimi Tunda, sina msaada. Yaani hiki anachopitia Net, ndio nilikuwa nikipitia mimi, halafu sina mtu wakumueleza au kunisikiliza akanielewa. Maana ni kweli nakuwa nilienda club kunywa kama kawaida. Kesho unakuta video zimesambaa mitandaoni. Unajitetea nini kwa watu? Unasema nini na wakati unakuwa ni kweli ulienda baa! Kweli unatumia madawa ya kulevya. Lakini hata hukumbuki kumruhusu mwanaume akuguse. Lakini video zinaonyesha unafanya mapenzi."

"Wakati mwingine kwenye gari yangu mwenyewe nje club au hata kwenye mahoteli. Huonekaniki wakati huo kama unabakwa! Inaonekana unatoa tu ushirikiano. Halafu sasa Tunda, sio mara moja. Ni matukio yakujirudia. Kila mtu humu ndani alikuwa hanielewi. Ananilaumu mimi. Lakini sikujua jinsi ya kufanya, kwa kuwa kumbe hata marafiki zangu wale wakaribu sana, walikuwa wakitumiwa na Vic.” “Kivipi?” Tunda akauliza kwa mshangao kidogo

“Alisema Vic mwenyewe, kuwa kina Gina. Wale marafiki niliokuwa nikikwambia walikuwa wakinifukuza kama nisipokunywa au kutumia madawa. Nikawa nawakimbilia, kumbe walikuwa wakitumwa na Vic.” “Jamani Maya!” Tunda aliumia sana. “Kweli Tunda. Ndio maana ilikuwa rahisi sana kwangu kuharibikiwa. Vic alikuwa na akili na anafanya mambo yake kwa makini sana. Tena akitumia watu wa karibu yangu. Akiamua jambo lake Vic, anahakikisha anafanikiwa. Na hakurupuki. Anapanga hata miezi 6 kabla.” Maya akaanza kulia tena.

“Tafadhali usimsikilize Vic. Usituache sababu ya Vic. Net na mimi tunakuhitaji sana kuliko utakavyofikiria. Hatujawahi kupendwa hivi Tunda. Tunatumikiwa sana na watu wanatuchekea, lakini kwa sababu ya pesa.” Maya akajifuta machozi. “Ulisema wewe hauna tofauti na sisi. Lakini nikwambie ukweli Tunda, huyo Cote, hatakuwa na tofauti yeyote ile na mimi, wewe pamoja na Net. Mama atampitisha huyo mtoto kule alikotupitisha sisi wote watatu. Atamnyima Cote mapenzi ya kweli.”

“Cote naye atakuwa kama sisi akihangaika. Net anakupenda sana Tunda, naomba usisahau hilo na kukubali watu wawaibie huu wakati mliokuwa mkiusubiria kwa hamu sana. Wote wewe na Net mlikuwa mkimsubiria huyu mtoto. Ona sasa hivi upo hapa peke yako, Net na yeye yupo kwengine akiendelea kusononeka! Usikubali Tunda. Wewe umebeba hatima ya kina Cote. Wewe ndio unaweza kuvunja upweke wa watoto wako na sisi. Mimi nakuacha, uamue mwenyewe. Ila ujue popote utakapokwenda, mimi nitakufuata tu.” Tunda akacheka huku akifuta machozi.

Maya akasimama. “Njoo kwanza unikumbatie hapa.” Maya akacheka na kumsogelea Tunda pale alipokuwa amekaa na mtoto wake. Akambusu na kumkumbatia kwa tahadhari yeye na mtoto. “Nakupenda Tunda.” “Lini umekuwa mkubwa kiasi hicho na kuwa na hekima hivyo!?” Maya akacheka wote machozi yalikuwa yakiwatoka. “Muweke mtoto kwenye kitanda chake na wewe ulale kidogo. Bado hujapona Tunda!” “Acha nimshike tena kidogo ndipo nimuweke chini. Bado ninahamu naye.” “Kesho zamu yangu.” Wakacheka Maya akatoka.

~~~~~~~~~~~~~~~

Tunda akamuweka mtoto wake kifuani, akampapasa kidogo, akapitiwa na yeye na usingizi palepale kwenye kiti akiwa amemuegemeza mwanae kifuani. Tokea asubuhi mpaka jioni hiyo hakuwa amelala kwa hofu. Na chumba hicho walizuia mtu yeyote asiingie ili kumfanya atulie.

Akiwa usingizini, Net alirudi hapo ndani akamkuta Tunda na mwanae wote wamelala. Akajaribu kumtoa mtoto mkononi taratibu. Tunda alishituka mpaka akapiga kelele.

~~~~~~~~~~~~~~~

Bado Ritha yupo mtaani, amewasha moto mwingine tena. Wengi wameteketea. Tunda ameharibiwa akili kwa hofu. Yu mgonjwa katikati ya utajiri mkubwa, anahangaika kulea peke yake sababi ya utisho wa Ritha. 

Je na ndoa ya Net nayo itapona? Maya aliyekuwa kidharaulika na watu wote ndiye ameibuka mwenye hekima na mkombozi wa hiyo familia wala si Net mrithi wa mamilioni ya pesa. 

Nini kitaendelea? Ritha atamudu kuwazidi akili hata hao maafisa wa CSIS nchini Canada?

Endelea kufuatilia...


CONVERSATION

0 Comments:

Post a Comment