Naomi Simulizi |+1 205 767 8163 |naomisimulizi@gmail.com Nilipotea! – Sehemu ya 50. - Naomi Simulizi

Nilipotea! – Sehemu ya 50.

Usiku Kwa Ritha.

U

siku  huo wakati kina Cote wamelala wakiwa wanazungukwa na ulinzi mkali, ikawa na kwa Ritha pia hivyohivyo. Polisi na CSIS walikuwa mbele ya nyumba aliyokuwa akiishi Ritha wakiwa wamevaa kama raia wa kawaida tu. Lengo ilikuwa ni ili kujua kama atatoka kwenda kukutana na Jeff, mwanaume wa Malinda, aliyehusika kumteka nyara Tunda. Na kusadikika kuhusika na mauaji ya Malinda pamoja  na mdogo wake, ili kujipatia pesa zote watakazolipwa na Ritha, yeye mwenyewe

Na kule mbele ya Motel aliyokuwa amejificha Jeff pia kulikuwa na polisi wanamwangalia kuona ni nini atafanya. Nia ni kumkamata akiwa na Ritha, kwa ushahidi. Kwa kuwa Ritha yeye alikuwa makini sana. Hawakuwa na ushahidi mkamilifu kuwa anahusika ila ukiri tu wa Vic. Ila  kwa Jeff, yeye walishapata ushahidi kuwa ni yeye muuaji kwani aliacha alama za vidole sehemu moja tu, ambayo inaonekana  alijisahau kuifuta. Kwenye dripu waliyokuwa wamemuwekea Tunda. Walikuta alama zake yeye za vidole,  na Malinda. Ni kama alimsaidia kunyanyua hiyo chupa ambayo ilichukuliwa na kwenda kupimwa, ndipo ikakutwa na alama zao wao wawili. Kuwa wao wiwili waliishika ile chupa ya maji waliyokuwa wamemuwekea Tunda.

Mpaka hapo hawakuwa wamekuta risasi iliyohusika kumuua Malinda na mdogo wake ila miili yao tu. Na Jeff alionekana alifanya juhudi za makusudi kusafisha kwa kutoa alama zake za vidole kila mahali kwenye ile nyumba.

Huku kwa Ritha alilala akiwa hajui hata kinachoendelea. Habari za kukamatwa kwa Vic zilifichwa kabisa na kuhakikisha hazivuji. Mbali na wazazi wa Vic ambao walifurahia kutotangazwa hizo habari, hakuna hata aliyejua kama usiku huo Vic na Jake wapo chini ya ulinzi wa CSIS, na wamelala ndani kama wafungwa.

Jeff alisubiria simu ya Ritha akiwa na simu yao waliyokuwa akitumia Ritha na Malinda, bila kuona mafanikio. Akasubiri na kusubiri, akaanza kukosa uvumilivu. Siku nzima hakumsikia Ritha, na huo usiku pia. Akajua Ritha anataka kuwachezea mchezo mchafu. Walishafanya hatua ya kwanza waliyokuwa wamekubaliana kumteka nyara Tunda. Hayo malipo alifanya kiasi tu, bado hakumaliza. Alisema mpaka amuone Tunda yupo chini yao, na kama Malinda akikubali wamuue, anampa pesa yote.

Yeye Jeff hakuona sababu ya mtoto, alitaka wammalize Tunda, walipwe, maisha yaendelee. Lakini Malinda alitaka mtoto. Alitaka wamfungie Tunda mpaka awazalie mtoto ndipo amwache kwa Ritha. Ndio maana alimgeukia Vic kumdai pesa ya matunzo. Vic alipokataa, na Malinda bado akang’ang’ania kumtunza Tunda hivyohivyo mpaka apone ndipo wampandikizie mtoto, hapo ndipo pakatokea kutokuelewana kati yake na mpenzi wake Jeff.

Jeff akaona Malinda anataka kupoteza muda na Tunda ambaye atakuwa mzigo na kuzidi kuwagharimu wakati pesa kutoka kwa Ritha inawasubiri! Na Ritha aliwaambia ni afadhali wamalizane mapema na Tunda, wakamtupe au kumfukia mahali, lasivyo watakamatwa tu.

          Jeff aliposhindwa kumshawishi Malinda, na mdogo wake akawa upande wa dada yake akitaka dada yake apate anachokita. Yaani mtoto, ndipo Jeff alipowaua wote wawili ili akutane na Ritha, arudi kumuonyesha Tunda kama ushahidi, wamuue, alipwe pesa yote yeye mwenyewe.

Alipotoka baada yakufanya mauaji hayo, na kusafisha. Akaamua kumpigia sasa Ritha simu na kumwambia kwa wakati huo yeye ndio kiongozi. Akapiga simu ya Ritha ikawa haipatikaniki tena. Kumbe alichofanya Ritha, baada tu ya kutembelewa na afisa wa CSIS wakamuulizia Tunda kwake, akachukua ile simu aliyokuwa akiwasiliana na kina Malinda, ilikuwa ni ‘Burner phone’ tu. Simu ambayo haijasajiliwa popote, sio rahisi hata wataalamu wa simu kuifuatilia na kumpata. Akaichukua hiyo simu na kuitumbikiza kabisa chooni ili kuua ushahidi.

Baada yakujaribu kupiga simu ya Ritha mara kadhaa na kumkosa, Jeff alitoka pale akiwa na njaa usiku ule kwenda kununua chakula, kurudi kwa mbali ndipo akaona helicopter na taa za polisi kwa mbali kwenye lile eneo walilokuwa wamemficha Tunda. Akajua tayari watu wa usalama wameshajua eneo alilofichwa Tunda na wamefika.

Hakutaka kukamatwa. Hapohapo akageuza na kukimbilia kujificha kwenye hiyo motel. Napo akajisahau akanunua sigara mchana baada yakujifungia kwenye hiyo motel kuanzia usiku ule. Ndipo maafisa wa CSIS wakachunguza kutoka ilipotumika kadi yake Jeff kama kuna nyumba za wageni karibu na hapo alipoonekana amenunua sigara, ndipo wakampata hapo amejificha kwenye hiyo motel.

Wakati director wa CSIS anazungumza na bibi Cote kumpa maendeleo walipofikia, bibi Cote akamsihi wasimkamate kabisa mpaka waweze kumuunganisha na Ritha. “Tafadhali Mike, naomba unielewe. Najua Ritha ni mjanja sana na ana akili kwenye mipango yake. Hamuwezi mkamkamata kwa ujumbe, au kwa kufuatilia kadi zake za benki au hata mazungumzo ya zamani aliyozungumza na hao wahusika.” Bibi Cote akasisitiza.

“Ni heri tuchukue muda mrefu, lakini tuhakikishe safari hii tunamkamata. Naomba Jeff aendelee kuachwa ili tuone anahusika vipi na Ritha. Pesa anazitoa wapi! Atajifungia hapo lakini tunajua ataishiwa tu, au atakosa uvumilivu na kufanya kosa, na hapo ndipo tutajua ni wapi atakapokwenda kupata hizo pesa au mahusiano yake na Ritha.”  Hilo wazo la bibi Cote likawa zuri.

Maafisa wawili wa CSIS, wakike na wakiume, wakachukua chumba pembeni ya chumba alichochukua Jeff, kama wapenzi tu ili wasimshtue Jeff. Salamu za kawaida kila wakikutana naye nje ya mlango na kujaribu kumzungumzisha mambo ya kawaida tu kama hali ya hewa na kadhalika.  Walipomuona akitoka kwenda kununua chakula na sigara tena, wakaingia chumbani kwake na kutegesha kamera. Ili kuweza kumuona na kumsikia kwa kila atakachozungumza na kila ambaye angezungumza naye.

Hapakuwa na kutulia kwa hao maafisa wawili. Walipeana zamu kulala, kwenda chooni mpaka hata kutoka kwenda kununua chakula. Macho yalikuwa kwenye screen wakimwangalia Jeff kwa kila anachofanya. Mvuta bangi huyo Jeff alishakata tamaa yakumsubiria Ritha kwa muda wote huo. Akaona amfuate tu anapoishi. Jeff alikuwa na number ya simu ambayo haikuwa hewani. Ikawa kazi kujua nyumba yenyewe anayoishi.

Wale maafisa wakaona na kujua shida ni sehemu anayoishi Ritha. Wakacheza na mtandao mpaka wakamdokeza jina kamili analotumia Ritha kwenye kazi mpya. Akaweza kujua ni wapi Ritha anafanya kazi.

Kutoka alipokuwa amejificha Jeff  mpaka alipo Ritha, ilikuwa mbali. Lakini Jeff akaamua kuendesha tu ilimradi kumfikia Ritha apate haki yake.

Malcon kwa Maya.

A

subuhi ya saa 12 Maya akapokea ujumbe kutoka kwa Malcom. ‘Naomba tupate kifungua kinywa pamoja.’ Bibi yake akamuona anacheka. Akamuonyesha ule ujumbe. “Utamjibu nini sasa?” “Nataka kwenda, Nana.” “Basi mjibu.” Maya akambusu bibi yake kwa furaha akijua amempa ruhusa. ‘Ningefurahia. Unataka tukutane wapi na saa ngapi?’ Maya akajibu. ‘Mimi ndio nakutoa. Nitakuja kumuomba Ms Cote au kaka yako. Wakiniruhusu tunakwenda kwa kifungua kinywa. Itakuwa saa mbili na nusu. Itakuwa sawa?’ Maya hakuamini.

“Angalia heshima anayonipa Nana!” Bibi Cote akasoma na kucheka. “Labda huyu atakuwa ndiye Nana!” “Naomba mpe muda Maya. Najua moyo wako. Naomba mpe muda wakumfahamu ndipo mfungulie moyo wako kabisa. Sitaki kuja kukuona unaumia tena.” Bibi Cote akamtahadharisha. “Ila kwa mwanzoni tu, anaonyesha dalili nzuri. Ananiheshimu huku akinijua ni mimi Maya ambaye nimepoteza heshima kwenye jamii!” “Hiyo ni kweli.” Bibi yake akakubaliana naye.

‘I would love that.’ Maya akamjibu Malcom kuwa angelipenda hilo wazo lake. ‘Okay. Nitakuona baada ya muda mfupi.’ ‘Okay.’ Wakamaliza hapo, Maya akatoka kitandani kwa bibi yake akikimbilia chumbani kwake kwenda kujitayarisha.

Saa mbili na dakika 20 Malcom alikuwa getini akigonga kengele akiomba afunguliwe. Baada yakujitambulisha, Carter akaruhusu afunguliwe. Maya, Tunda na bibi Cote walikuwa dirishani wakimchungulia. Alishuka nakuanza kujitengeneza. Akajitengeneza cola ya shati. Akasimama kwenye kioo cha dirisha cha gari, akaanza kuchomekea shati tena na tena. Tunda akaanza kucheka. “Atakuwa anaoogopa!” Wakamuona anachomoa shati. Akajiangalia tena kwenye kioo cha dirisha cha gari, akachomekea tena. Akarudi ndani ya gari. Wakamchungulia wakamuona anachana tena nywele. Wote wakacheka.

“Anaonekana anahali mbaya sana.” “Sidhani kama ataingia.” Wakacheka. Akatoka tena. Wakamuona anaangalia saa yake ya mkononi. Akazunguka kwenye mlango wa abiria. Akajaribu kufungua na kufunga akiwa anajidai kama anamfungulia mtu. Akasimama mbele na nyuma ya mlango mpaka akaridhika. Akajiangalia tena, akajiweka sawa, kisha wakamuona anatoa maua mawili. Wakashangaa. “He is a gentleman!” Bibi Cote akasifia.

Akajipanga tena. Wakamuona anajiweka sawa, akaanza kusogea kwenye ngazi. Wakati yupo ngazi ya tatu tu, akajikwaa na kuanguka vibaya sana, wakamuona yupo ngazi ya chini kabisa, amelalia maua yote. Kila mtu akashika mdomo. Wakamuona ananyanyuka haraka haraka. Akaangalia kushoto na kulia. Akaokota yale maua. “No No No nooo!” Maua yakawa yameharibika kabisa. Shati la rangi ya bahari alilokuwa amevaa na jinsi nzuri sana ya blue iliyoiva, na vyote vilionekana kama vipya, vikawa vimechafuka, zaidi shati. “Nooooo!” Malcom akazidi kusikitika kila alipojiangalia.

Wakamuona anakusanya yale maua na kuyatupia nyuma kabisa kwenye gari yake. Ndani ya buti. Wakamuona anatoa t-shert nyingine nyeupe. Akavua ile shati aliyokuwa amevaa nzuri imempendeza lakini ikachafuka sababu ya kuanguka, akavaa hiyo tshirt aliyoitoa garini huku akiangalia kulia na kushoto kama kuna mtu anamuona. Kisha akaanza kujifuta ile suruali. Akaangalia muda, akakuta amechelewa kwa dakika mbili. Akafunga gari kwa haraka, akaanza kukimbilia ndani. Alipofika katikati ya ngazi akatulia. Wakamuona anajaribu kuvuta pumzi kwa nguvu na kuzishusha taratibu kama anayetafuta kujituliza.

Wakaanza kucheka wote. Mara wakasikia kengele. Carter akaenda kufungua. Ile anaingia tu, akakutana na Net alikuwa akipita karibu na hapo mlangoni alipoingia yeye. Net akakunja uso. Akamsalimia. “Vipi, mbona asubuhi asubuhi! Kila kitu kipo sawa!?” “Kipo sawa kabisa. Nilitaka kuomba kumtoa Maya kwa kifungua kinywa.” “Hivyo ulivyo hata nywele hujachana!” Net akamuuliza kwa kumshangaa.

“Nilichana. Sema zimevurugika muda si mrefu hapo nje, wakati navaa.” “Ulikuja hapa uchi!?” Net akaendelea kumchemsha. “No no noooo, Sir. Not at all. Nilikuja nikiwa nimevaa kabisa, ila ikabidi kubadilisha.” Malcom alisikika akibabaika haswa. Kule walikokuwepo Maya, bibi Cote na Tunda walizidi kucheka taratibu wakisikiliza.

“Hukuamini ulichovaa kutoka nyumbani kwako!? Unakuwa mtu usiye amini mawazo yako na uamuzi wako wa kwanza! Itakuaje utoke hapa na Maya, ufike huko ugundue ulifanya kosa?” “Hapana, kuhusu..” “Nisikilize nani tena?” Net akamsogelea. “Malcom, Sir.” Malcom akajitambulisha huku akimeza mate kwa wasiwasi. Alishakuwa mwekundu. “Yes, Malcom. Maya sio binti wa kuchezea na wamajaribio kama ulivyokuwa ukimuona kwenye mitandao. Sasa hivi macho yangu yapo wazi nikiangalia kila mtu anayemsogelea Maya. Unanisikia?” “Yes Sir.” Malcom akaitika.

“Kama upo hapa kujaribisha, uondoke.” “Hapana. Mimi sijaribishi. Mimi namfahamu Maya kwa miaka mingi sana na sijawahi kumdharau hata mara moja. Wakati wote namuheshimu na ninamtetea. Hata Roy anajua. Sipo hapa kujaribu.” Malcom akajikaza na kujieleza kwa ujasiri. “Nampenda sana Maya.” Akajikuta akiropoka. Net akamkazia macho. “Umesema?” “Nampenda Maya.” Akaongea kwa utulivu, safari hii akaweka na hisia. “Na sipo hapa kujaribu. Na wala sitaki kumuona anaumizwa tena. Ndio maana nipo hapa. Kama ukinipa nafasi hiyo Sir, mimi nitahakikisha Maya anakuwa na furaha. Na ule moyo wake wa ukarimu na kuamini watu, nitauenzi. Sitamchezea kama watu wengine walilolijua hilo na kumtumia vibaya.” Malcom akaendelea kutetea hoja yake.

“Sipo hapa kujaribu au kuchunguza. Nipo hapa kwa mtu ninayemfahamu kwa muda mrefu, tena nina uhakika au ujasiri wakusema ninamfahamu zaidi ya kila mtu au yeye mwenyewe. Kwa kuwa nimemfuatilia kwa muda mrefu sana. Nampenda Maya.” Kule alipo Maya akaanza kutokwa na machozi ya furaha. Ilimgusa kila mtu. Hapo hata Net akafungwa mdomo katika hilo.

“Unatokwa jasho na hujachana nywele. Huwezi kutoka na msichana kwa mara ya kwanza wewe mwenyewe ukiwa hujatulia. Carter atakuonyesha ilipo maliwato. Ujisafishe kidogo, ndipo uitiwe Maya.” “Asante sana. Nashukuru sana.” Karibia Malcom apige magoti. Net akaondoka. Akamsikia akihema kwa nguvu na kuinama ameshika magoti kama asianguke. Net akacheka moyoni, hakugeuka. Akaondoka asijue bibi yake na kina Maya walikuwa wakiwasikiliza wakati akimchemsha Malcom.

Malcom alipelekwa kwenye maliwato ya wageni hapo karibu na sebuleni. Akaanza kuchanganyikiwa humo ndani. Kulikuwa na kila kitu. Akaanza kujisafisha akatamani kama aoge kabisa. Ila akajua atachelewa zaidi. Akatumia taulo dogo kujisafisha. Aliporidhika ndipo akavaa tena ile t-shert yake. Akaamua kuchomekea. Akajiweka sawa. Nakutoka.

“Upo tayari?” Ilibidi Carter amuulize maana alitoka nakuanza kushangaa hapo. “Yes. Naomba uniitie Maya. Au unafikiri nizungumze na bibi yake kwanza?” “Una maua?” Carter naye akaanza kumchanganya. “Nilikuwa nayo kabisa na Mungu wangu ni shahidi. Lakini..”  Akasita Malcom. “Sina.” Akaongea kwa upole Malcom. “Lakini nampenda sana Maya. Sitaki kuharibu mwanzoni.” Carter akampa tabasamu.

“Nina uhakika atafurahia moyo ulio muwazi kuliko maua.” “Unafikiri hivyo?” Malcom akauliza kwa wasiwasi huku akimsogelea Carter. “Najua hivyo. Upo tayari.” Malcom akatingisha kichwa kukubali. Carter akashangaa. “Come on Son! Man up!” Akajiweka sawa. Akasimama kwa kujiamini. “Upo tayari?” Carter akamuuliza tena. “Yes Sir.” Akajibu kwa kujiamini. Carter akamtengeneza vizuri kola ya ile t-shirt.

“Halafu usiongee sana kwa Ms Cote, labda iwe lazima sana. Maneno machache tu, tena yamuhimu.” Akamshauri huku akimpiga piga mabegani. “Nitakumbuka hilo.” Akakubali kwa haraka sana. Akameza mate, Carter akaondoka. Baada ya muda akaona bibi Cote na Maya wanakuja. Malcom akabaki ameduaa kwa Maya. Maya alivaa vizuri na akapendeza sana. Maya akacheka, ndipo Malcom akagutuka.

Akasalimia mikono ameweka kwa heshima huku akimtizama bibi Cote na Maya. “Umependeza sana.” Akanong’ona huku akimwangalia Maya. Maya akacheka. “Asante.” Maya akajibu na cheko la taratibu. Malcom alibaki akimtizama.

Akakumbuka bibi Cote anamtizama. “Maam!”  Akaanza Malcom. Bibi Cote akabaki akimtizama na yeye. “Naomba nitoke na Maya kwa kifungua kinywa. Nitamrudisha salama.” “Salama na mwenye furaha kama hivi alivyo hapa.” Bibi Cote akajibu kwa msisitizo. “Nitahakikisha hivyo, Maam!” Malcom akakubali kwa haraka sana. “Okay. Mimi sitawachelewesha zaidi.” Malcom akakumbuka amechelewa. “Samahani sana kwa kuchelewa. Nilifika kwa wakati lakini...” Carter akasafisha koo kidogo kama kumkumbusha. Akatulia. Akakumbuka asiongee sana. “Samahani kwa kuchelewa.” Akajirudi. Lakini wote walijua hajachelewa. Kwani walimuona muda wote tangia anaingia hapo kwenye ua wao.

“It’s okay, Mal.” Maya akamtuliza. Akajisogeza taratibu kwa Maya. “Nilikuletea maua lakini niliyaharibu.” Akaongea kwa upole na sauti ya chini. “It’s okay. Nimefurahi kukuona.” Maya akajaribu kumtuliza. Akanyoosha mkono, Maya akamshika, wakatoka. “Umependeza sana Maya!” Wakamsikia akimsifia tena wakati wanatoka. Maya akacheka. Akamfungulia mlango kama vile walivyomuona akijaribisha kabla ya kuingia ndani. Maya alipokaa, akafunga mlango. Akaenda upande wa dereva akawasha gari.

 {Atafuataye, Hachoki}. 

Kwa Mara ya Kwanza Malcom Afanikiwa Kumtoa Maya.

“Kabla hatujaondoka hapa, naomba nikutahadharishe kitu.” Maya akaanza. “Unatoka na mimi.” Malcom akawa hajaelewa. Akabaki akimsikiliza. “Inamaana haitakuwa siri, Malcom. Kila mahali utakapotokea na mimi, watakuandika mitandaoni na magazetini. Haiwezi ikawa siri, labda tupate kifungua kinywa hapahapa nyumbani.” Malcom akatulia kidogo.

“Najua ni nini nafanya Maya.” “Nina uhakika hujafikiria kwa upande huu. Watakuchunguza kuanzia siku ya kwanza utakayoonekana na mimi. Yale yako ya sirini ambayo hukutaka watu wayajue, watayajua kwa undani, hadharani. Watakudhihaki kwa kuwa upo na Maya Cote.” Maya akaanza kutokwa na machozi.

“Utakuwa gumzo kwa mabaya. Watu watakukumbusha upo na mimi. Watakwambia nitakuharibia maisha yako. Mimi ni bomu ambalo hulipuka wakati wowote. Naa..” “Please stop.” Malcom akamtaka atulie. “Mimi sijui ulikuwa unakuwa na kina nani kwenye maisha yako. Sijui wamekuwa wakikwambia nini! Lakini nipo hapa nikiwa nakufahamu Maya. Nimechagua kuwa hapa kwa kuwa ni nafasi niliyoitamani muda mrefu sana, lakini sikuwahi hata kufikiria kama naweza kubahatika kuwa hapa na wewe.” Malcom aliongea taratibu tu.

“Na kama kuchambuliwa hadharani ndio garama yangu yakulipa ili kuwa na wewe, nipo tayari.” “Wata..” “Naomba niangalie mimi, Maya.” Akamkatisha. Maya akajifuta machozi na kumwangalia. “Tafadhali, naomba kwa mara ya kwanza kwenye maisha yako, angalia karibu. Hapa. Halafu funga masikio, macho na muda wako kwa watu wasiojalisha kwenye maisha yako. Anza taratibu, utajikuta unazoea hayo maisha. Acha waandike watakacho. Acha wakufuatilie. Acha wakuhesabie siku zilizobaki kurudi kwenye madawa.” “Kumbe unajua!?” Maya akashangaa, hakutegemea.

Malcom akamgeukia vizuri. “Naomba uamini nipo hapa nikiwa nakufahamu Maya. Sitaki pesa yako wala umaarufu. Nataka kuwa na wewe kama Maya, basi.” Ilimgusa sana Maya. “Asante Mal. Kwa hiyo wakiniuliza juu yako, nisijibu?” Maya akauliza taratibu tu. “Mpaka iwe muhimu na ukiwa na uhakika. Usikimbilie kujibu mtandaoni. Jipe muda kujiridhisha na kila kitu. Ndipo ujipe muda wa kujibu na unaweza pia usiwajibu. Huwajibiki kwao. Wakati mwingine ukimya au kunyamaza ni jibu kubwa na la hekima.” Maya akavuta pumzi kwa nguvu, akajiegemeza nyuma.

Malcom akabaki akimwangalia vile alivyofunga macho. “Njaa inauma!” Maya akasikika ametulia, akafungua macho na kumtizama Malcom, macho yakagongana, akacheka. “Najua sehemu wanayouza kifungua kinywa kizuri sana. Twende.” Kisha akaondoa gari. Maya akawa kimya akimtafakari Malcom na maneno yake.

Malcom hakuwa tajiri kama wao, lakini alikuwa kijana aliyesoma vizuri na mwenye kazi yakuheshimika kwenye jamii. Japokuwa hakuwa akipata mshahara kama Maya, wala hana hata gari inayoendana na Maya, lakini alijawa hekima na utulivu wa aina yake.

Huyu Maya ashachezewa sana. Akipita popote au akionekana popote, huna haja yakujiuliza mwili wake ndani ukoje, ni kwenda tu mtandaoni na kuangalia kama ni matiti au sehemu yeyote ya ndani ya Maya, utaona tu. Alianikwa vilivyo.

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

Alipotoka tu, Tunda akamsikia bibi Cote akiongea kwenye simu. “Maya ametoka hapa sasa hivi. Hakikisha anarudi nyumbani leo, tena in one peace. I don’t want any surprises.” Akakata simu. Tunda akajua ndio unatumwa ulinzi kumfuatilia Maya na Malcom.

Malcom&Maya Hadharani Pamoja.

M

alcom alimpeleka mpaka kwenye mgahawa wakawaida sana. Lakini waliuza ‘Butter tarts’ nzuri sana. “Najua hapaendani na hadhi yako, lakini hakuna sehemu utapata butter tarts nzuri hapa Norfolks, kama hapa.” Maya akacheka taratibu. “It’s okay.” Malcom akamtizama kama anayejua anajikaza tu kuwepo pale. “Kweli mimi nipo sawa, Mal. Tuingie na kuagiza chochote ulichokuwa unakifikiria.” “Kama ndio hivyo sawa. Nakuahidi hutajuta.” “Okay.” Wakatafuta sehemu ya kuegesha, kitu ambacho Maya hakuzoea. Alishazoea kufika kwenye mlango wa mahoteli makubwa, watu wanakwenda kuchukua gari yake na kutafuta wao sehemu ya kuiweka. Akitoka hapo, gari yake inaletwa palepale mlangoni.

Sasa siku hiyo walikwenda kuegesha gari wenyewe. Gari ya kawaida sana. Maya hakuwahi kupanda gari ya hadhi ya chini kama ile. Malcom akabaki kuwa muungwana. Akamfungulia mlango. Wakaanza kutembea kurudi sehemu ulipo huo mgahawa. Akamfungulia na mlango, Maya akapita akimshukuru. Maya akaanza kuangaza ili kutafuta meza ili akae. “Hapa wanapanga mstari unachukua kahawa yako kama unataka kahawa na kitafunwa. Lakini naweza kukuchukulia.” Malcom akamnong’oneza. “Sikujua!” Wakacheka kidogo.

“Niambie ni nini unataka, nitakuletea.” Maya alizoea chakula kuletwa mpaka mezani. “No. It’s okay. Twende wote.” “Unauhakika? Mimi naweza kwenda kuchukua na kukuletea.” “Nashukuru. Lakini twende wote.” Wakasogea walipokuwa watu na wengine wakishangaa kumuona Maya hapo, tena wakiongozana na Malcom! Ulikuwa mgahawa mdogo tu, lakini ulijaza watu wanaoonekana wanawahi makazini.

“Watu wengi wanapapenda hapa. Lakini kwa kununua vitafunio na kahawa, na kuondoka. Sio kukaa.” “Lakini sisi tutakaa. Si ndiyo?” “Labda kama unataka tuondoke, naweza kubeba.” Malcom akajua pengine yale mazingira yamemshinda. “Hapana. Mimi nipo sawa tu. Tunaweza kukaa, tukala.” “Unauhakika?” “Tafadhali usiwe na wasiwasi na mimi. Nipo sawa kabisa. Unakumbuka maisha niliyoishi ya club?” “Unaongelea zile club zenu za mapesa mengi?” Maya akacheka taratibu.

“Naomba usiwe na wasiwasi. Nimefurahia kuwa hapa na wewe.” “Kweli?” Malcom akauliza na kumshika mkono. Maya akacheka kwa deko huku akitingisha kichwa. “Nimefurahi sana. Sijali tulipo, ilimradi tupo wote. Unaniheshimu Malcom. Kwa hilo linaniongezea ujasiri.” Malcom akatoa tabasamu la kuridhika na kumvuta mkono karibu akauweka kwapani. Maya akajiegemeza kidogo begani. Wakaendelea kusogea na mstari wote kimya. Kama hawajui kama kuna watu hapo wanawatizama.

Walifika mbele ya muhudumu, hata muhudumu akashangaa. “Nimekufananisha au kweli ni wewe!?” Maya akacheka kidogo. “Umenifananisha na nani?” “Maya Cote!” Maya akacheka kidogo. “Ni mimi.” “Wao. Ni mzuri zaidi in personal kuliko kwenye picha.” Akacheka zaidi. “Asante. Mimi nitakula kile atakachokula Malcom.” Akaongea huku akimtizama Malcom. Malcom akamtizama Maya na kurudisha macho kwa yule dada ambaye bado alikuwa akimshangaa Maya.

Malcom akakohoa kidogo kama kumshtua. “Yuko wapi Roy?” Yule mrembo akamuuliza Malcom. “Leo nimeamua kupunguza kelele humu ndani.” Wakacheka na kutaniana kidogo ndipo wakaagiza vyakula vya wote wawili, wakasogea pembeni wakisubiria namba yao itajwe wachukue chakula chao.

“Inamaana wewe hapa unafahamiana na watu wote na umeshakula kila kitu?” “Yule msichana ni mtoto wa huyu mwenye mgahawa. Mimi na Roy nilazima tupite hapa karibu kila siku kununu vitafunio kama si kukaa na kuanza kula hapahapa.” “Lakini huyu msichana ni mzuri!” Malcom akacheka. “Hatuji hapa sababu yake, Maya! Baba yake ni mcheshi zaidi. Na Roy anawapenda sana wazazi wake. Akija ni lazima awachokoze.” Maya akatabasamu na kunyamaza.

Akamvuta tena mkono na kuushika. “Na ndiyo. Nimeshakula hapa karibu kila kitu. Ila napenda ‘butter tarts’ zao zaidi. Nzuri.” Maya akamwangalia na kumtolea tabasamu. Kisha akarudisha macho kwenye ubao mkubwa wa menu uliokuwa umetundikwa mbele yao.

Baada ya muda ikatajwa namba yao, Malcom akaenda kuchukua chakula chao ndipo wakaenda kutafuta meza iliyokuwa pembeni kabisa kwenye ukuta wa kioo. Kwa hiyo walikuwa wakiona wapita njia, nje. Maya akaonja hizo butter tarts zilizokuwa zikisifiwa. Malcom akabaki akimwangalia ili asome sura yake aone kama atapenda. Akamuona anatafuna huku akisikilizia utamu wake, akameza na kucheka. “Ni kweli ni nzuri.” “Nilijua tu utapenda.” Wakacheka na kuendelea kula.

“Unafikiri siku nyingine unaweza kurudi hapa?”  Maya akacheka kama anayefikiria huku akiangaza kulia na kushoto. “Labda niwe na wewe. Lakini si peke yangu.” “Kwa nini? Nilifikiri umependa hizi butter!” Maya akacheka kidogo. “Yule aliyetuhudumia jana kwa chakula cha usiku pale nyumbani, anaitwa Gino. Anakipaji cha ajabu sana. Unaona hii butter tarts?” “Ehe!” “Nikiichukua hii na kumpelekea Gino, nikamwambia naitaka hii kwa kifungua kinywa kesho asubuhi, atatengeneza kitu kama hiki au kinachofanana na hiki, ila kizuri zaidi.” Malcom akashangaa.

“Haiwezekani Maya!” “Kabisa. Ndio maana sisi tukitoka kwenda kula, sio sababu ya chakula, ni kwa sababu ya matembezi tu. Ila tunaye mpishi mzuri sana. Lakini hiyo sio sababu yakutorudi hapa.” Maya akanywa kahawa kidogo. “Ni nini?” “Kwa wakati huu, zaidi sifa yangu. Baada ya kutulia sasa hivi na kusikia watu wazima na vijana waliotulia kama wewe wanazungumza vipi juu yangu. Au wananitazamaje, imenitoa ujasiri kabisa Malcom.” Malcom akatulia kidogo akimtizama.

“Unajua zamani nilizungukwa na watoto au vijana wadogo au tuseme watu ambao wote hatukuwa tukiitizama jamii kwa macho haya niliyonayo sasa hivi. Nilikuwa nikiishi katika ulimwengu tofauti na huu ulimwengu ninao ishi sasa hivi.” “Ulimwengu wa sasa ukoje?” Akauliza taratibu Malcom. “Ulimwengu wa kuwajibika katika kila eneo la maisha yangu. Kwa maneno na vitendo. Nililelewa na Papa akiwa ananipa kila kitu. Kazi yangu ilikuwa ni matumizi tu. Sikujali ni nani anayehusika au kuumia kwa kuwepo kwenye maisha yangu.”

“Sasa, sasa hivi nimetulia ndipo naangalia madhara niliyoacha kwenye familia za watu!” Maya akajifuta machozi. “Wapo wakina mama wanao nilaumu kwa vijana wao. Wanasema mimi nilikuwa nikiwapa watoto wao unga.” “Kivipi?” “Sijui Malcom! Lakini ndivyo wanavyoniambia. Sasa sijui nilipokuwa nikinunua na wao walikuwa wakitumia ya kwangu! Mimi sijui.” Maya akajifuta machozi.

“Haya, wapo vijana kama wewe.” “Ndio wakoje hao?” “Wanao jiheshimu. Walio tulia. Waliokwenda shule na kutulia na kazi zao. Wananikimbia Malcom. Hawataki niwe karibu nao kabisa.” Malcom akakunja uso. “Subiri kwanza Maya. Hilo la vijana wanao kukwepa, umejua kutokana na watu wangapi uliozungumza nao?” Malcom akauliza taratibu tu. “Kwa sababu usije kuchukua mawazo ya watu wawili au mmoja, ukayaweka moyoni kuwa ni mawazo ya watu wote.” Maya akabaki kama anafikiria.

“Maya?” “Unakumbuka nilikwambia kuna kitu nilitaka kumwambia Tunda kabla hajatekwa? Ulipokuja nyumbani wakati unaondoka, ukaniuliza kama nilimwambia. Nikakwambia bado. Unakumbuka?” “Nakumbuka.” Malcom akaitika. “Basi jana niliporudi ndani baada ya kukusindikiza, nilipata muda na Nana, Tunda pamoja na Net. Nikazungumza nao. Unataka na wewe nikwambie?” Maya akauliza kwa upendo.

“Ningependa kujua na mimi.” Malcom naye akajibu kwa kujali. “Kuna mtu. Nilimuomba tukutane sehemu kwa chakula cha mchana.” “Kama date?” Malcom akauliza kwa wivu kidogo. “Hapana. Nilitaka tuzungumzie maswala ya harusi. Ni kipindi namsaidia Tunda na maandalizi yake ya harusi. Sasa yeye anautaalamu na mambo fulani. Nikataka tupange naye, tukishakubaliana ndipo nimshirikishe Tunda.” Maya akanyamaza kidogo.

“Nini kilitokea?” Malcom akauliza baada ya kumuona Maya amenyamaza kama anayeshindana na machozi. “Pale ndipo alipowakilisha mawazo ya wengi na watu wanavyonifikiria.” Malcom akakunja uso kidogo. “Aliniambia maneno mabaya sana. Kwa kifupi hakutaka hata kuwa karibu na mimi au hata kuonekana na mimi hadharani ili kwanza nisimuharibie sifa na baadaye nisije nikamuharibu.” “Kivipi!?” Malcom akauliza tena.

“Alisema huwa nina mtindo wa kuanza na vijana vizuri, wakiwa vijana wazuri tu na malengo makubwa ya maisha. Kisha nawaharibia maisha na kuwageuza mateja. Wanashindwa kuendelea na shule au hata kazi.” “Ouch!” Malcom akafanya kama aliyeumia. Maya akacheka huku akifuta machozi.

“Alitumia maneno mabaya sana akiwakilisha kile ninafanya na vile nilivyo. Kuwa ni kama bomu. Ukilishika ni dogo na halionekani kama halina madhara, lakini mwishoe nalipuka vibaya sana na kuathiri wengi. Kwa kifupi alikataa kukutana na mimi.” “Unajua Maya, kuna watu wanauwezo mkubwa sana wakuumiza watu, zaidi kwa maneno. Simjui ni nani na hao vijana anao walalamikia ni kina nani lakini hata mimi kuna kipindi nilitoka chini ya uangalizi wa wazazi nikatupwa kwenye ulimwengu huuhuu wanaoishi wengine na kuishia kufanya maamuzi mabaya.” Malcom akaendelea.

“Yapo makosa nilifanya kama mwanadamu, na sina mtu wakumlaumu kwayo. Siwezi nikageuka nyuma na kumnyooshea mtu kidole kwamba amenisababisha kutenda niliyotenda. Sijui kama unanielewa?” Malcom akaendelea. “Nimelelewa na mama kiasi na sehemu kubwa ni bibi. Wakati nikiishi nao au wakati nikiishi na bibi, hatukuwa matajiri, lakini alijitahidi kuwekeza kwangu kiasi ya kwamba nilitoka nyumbani nikijua mema na mabaya. Niliyoyafanya, nilijua ni nini nafanya. Sina mtu wakumlaumu.”

“Mzazi unayemsikia anamlaumu mtoto wa mwengine kwa ajili ya mtoto wake, huyo anatatizo tu.” Maya akatabasamu. “Kweli. Unawezaje kumlaumu mtoto mwingine kwa ajili ya kuharibika kwa mtoto wako? Inamaana hukumwandaa mtoto wako kukutana na watu wa namna hiyo.” Malcom akajiweka sawa.

“Wote tunatupwa kwenye ulimwengu uliojaa wema na ubaya. Ni jukumu langu mimi kama baba, kumuandaa kijana wangu kukabiliana na kila hali ndipo niwe huru kumruhusu kutoka nyumbani.” Malcom akaendelea. Taratibu tu. “Huwezi kumruhusu mtoto asiye na maadili hata madogo tu nyumbani, kwenda kukutana na marafiki ambao hata huwafahamu! Nyumbani tu anashindwa kufanya maamuzi sahihi, unamwamini vipi akiwa club? Ataweza vipi kushinda vishawishi vya huko!” Maya akainama.

“Huko ni kujifariji katika kushindwa kwao. Kila mtu anatakiwa kuwajibika kwa maamuzi yake mabaya. Wewe unagarama ya kulipa kwa maisha uliyoishi zamani, lakini sio kwa vijana waliokuwa wakitaka kutumia na wewe madawa! Huo ni uongo na wanatafuta kukubebesha mzigo kwa kushindwa kwao.” “Sasa wewe ungefanyaje?” Maya akauliza. 

“Kama hivyo wewe. Kukubali kuwa ulikosa na kufanya maamuzi mabaya yaliyokupelekea kuishi kama vile. Nilisoma post yako moja, na nilisikia mahojiano yako wakati ulipotoka rehab. Ukaomba msamaha hata kwa mabinti wadogo waliokua na ambao bado wanakuangalia wewe kama msichana kwenye jamii. Unakumbuka?” Malcom akamuuliza Maya, akatingisha kichwa.

“Ulisihi mabinti vizuri sana. Ukawafundisha na kuwaambia yale sio maisha mazuri kwa mtu yeyote kuyaishi na wanatakiwa kutumia kila fulsa Mungu anayowapa, hata ikiwa ndogo ya namna gani, kufanya kwa bidii, na kusaidia wengine. Na mengine mengi. Basi. Endelea na maisha kama mtu mwingine ila safari hii ukiwa makini zaidi, ili usirudi ulipoanguka.” Maya akanyamaza.

“Huwezi kuruhusu watu wenye roho mbaya wakuumize Maya. Lini na wewe utaishi kile ulichowaambia mabinti wengine waishi kama utajifungia ndani?” “Sijui Malcom!” “Hapana. Sasa hivi ndio unatakiwa uishi na kugusa maisha ya watu bila woga. Tena sasa hivi ni rahisi ukiwa unajua kuwa ulikuwa ukifanyiwa makusudi na watu ili kukuweka kwenye hiyo hali. Basi, chagua watu sahihi wa kukuzunguka na hakikisha unakuwa mahali sahihi. Fanya kile unachoweza. Huna haja yakujibu kila shutuma. Acha muda ujibu shutuma, zaidi za kijinga.” Maya akaanza kujisikia vizuri. 

Jingine Tena kwa Maya!

W

akati wapo katikati ya mazungumzo na ndio wanaanza tu vicheko hata hawajui ni nani yupo pale akiwaangalia. Ni kama walikuwa kwenye ulimwengu wao peke yao. Hawajali watu wengine. Maya akashangaa kitoto cha kiume kimesogea pale mezani. “Hey!” Maya akamsalimia kwa upendo na tabasamu. Mara akasogea mdada mwingine, mrembo tu. “Nilikwambia usiwe unakimbia!” “Acha kumgombeza mtoto!” Maya akashangaa Malcom anamjibu huyo mrembo kwa hasira. Akahisi ndiye mama watoto wake. “Ulitaka nimwambieje!? Kama kila kitu ninachozungumza naye ni kosa, mbona sijaona leo sura yako wewe unayejidai ni baba mzuri? Leo ilikuwa siku yako ya kuja kumchukua, mbona hukuja?” “Nilimtuma Roy aje amchukue!” Malcom akajibu.

“Kwani Roy ndiye baba yake?” “Tokea lini imekuwa tatizo kwa Roy kumchukua Ethan?” Yule dada akavuta kiti palepale kwenye meza yao akakaa. “Utalala na wasichana matajiri wangapi ili kuweza kufanya kazi yako?” “Tafadhali usianze Zoe. Tafadhali sana.” “Hapana. Mimi nataka tu kujua. Utalala nao wangapi?” Maya akaona awapishe.

“Ni sawa kusogea na Ethan pale pembeni ili kuwapa nafasi? Sitakwenda naye mbali. Tutakuwa hapo nje tu.” “Unafikiri wewe ni tofauti na kina Vic, Gina, Renee, Emily na wengineo alio lala nao huyu?” Zoe mama mtoto wa Malcom akamuuliza Maya kwa kumkejeli. Maya akamwangalia Malcom. “Tafadhali acha kumchanganya Maya, kwa shutuma zako ambazo huna hata..” “Kama unafikiri mimi natupa shutuma tu, nenda kazungumze na warembo wenzako wakitajiri, uone kama wote hawajamuona huyu akiwa uchi, kwa kisingizio cha kazi.”

“Ni sawa nikitoka na mtoto?” Maya akasisitiza swali lake. “Sikuamini, na wala sikujui zaidi ya kukuona kwenye mitandao ukiwa uchi na umelewa.”  Zoe akamkatalia mtoto wake kwa kumkashifu. “Tatizo lako ni nini Zoe!?” Maya akatoa tabasamu akainama kidogo. Akachukua pochi yake. Akaifungua palepale mbele ya Zoe. Akamwaga kila kitu pale mezani. “Hamna madawa humo ndani. Kwa hiyo kuwa na amani kuwa ninachotaka ni kutoka tu na Ethan hapa, wakati mkizungumza. Sio kumpa madawa. Na sitakuwa mbali na hapa. Ni hapo nje sehemu ambayo mtakuwa mkizungumza huku mkimuona Ethan. Unafikiri ni sawa?” Maya akawa ametulia hata Malcom hakutegemea.

“Hapana.” Akajibu Zoe kibabe. “Hata hivyo leo ni siku yangu na Ethan. Na kwa kuwa naona umeamua kuja kunitukana hapa mbele za watu, basi naomba Maya atoke na mtoto wangu, asisikie jinsi unavyozidi kunitukana na kunidhalilisha.” Malcom na yeye akaongea kwa msisitizo. “Asante Maya. Nitawafuata hapo nje baada ya muda mfupi sana.” Maya akamwangalia Ethan. “Unataka twende nje nikufundishe kitu?” Ethan kimya. “Nina uhakika hukijui. Twende, dad atakuja sasa hivi.” “Nenda na Maya, Ethan. Nitakuja sasa hivi.” “Okay.” Yule mtoto akakubali kutoka na Maya baada yakupata ruhusa kutoka kwa baba yake.

Maya akaanza kuokota vitu vyake pale mezani akirudisha kwenye pochi ili atoke na mtoto. “Na kwa taarifa yako tu, usifikiri wewe ni bora kuliko wanawake wengine wote ambao anawapitia huyu Malcom. Kazi yake ni kulala na warembo wenye majina kwenye jamii, ili kuwapeleleza. Usifikiri ni mapenzi.” Zoe akamwambia Maya, lakini wazi alionekana ameishiwa nguvu. Maya akacheka tu. Akamaliza kuweka kila kitu kwenye pochi akamgeukia Ethan aliyekuwa amesimama kimya akisikiliza wazazi wake. “Twende Ethan.” Akamshika mkono, wakatoka.

“Una miaka mingapi Ethan?” Akamuanza kwa kuwa alimuona Ethan ameinama. “Minne.” Akajibu akionekana amenyong’onyea, akajua pengine alikuja na mama yake akiwa anamgombeza huko njiani au kuna lililotokea huko ndio maana akapooza hivyo. “Wao! Kumbe wewe ni kaka mkubwa hivyo!” Ethan kimya. “Umekula?” Akatingisha kichwa kukubali.

“Niangalie halafu nikuonyeshe kitu.” Ethan akamwangalia. “Umeniona sasa hivi?” Akatingisha kichwa kukubali. “Niangalie sasa hivi uniambie tofauti ni nini?” Ethan akamwangalia kwa makini.

Maya akainama ili amfikie. “Nini?” “Nyusi hii ipo chini hii juu.” Maya akacheka. “Na hivi?” Ethan akamwangalia. “Unafanyaje hivyo!?” Ethan akamuuliza huku akianza kucheka. “Mimi nina super power ya sikio. Naweza kutingisha masikio.” “Umepata wapi huo uwezo?” Ethan akauliza. “Nimezaliwa nao. Jaribu na wewe.” Ethan akajaribu na kuishia kujicheka. “Unatingisha kichwa bwana, unatakiwa kuchezesha sikio tu.” Ethana akazidi kucheka akitingisha kichwa huku akimwambia Maya ameweza. “God, you are so Cute!” “Hata dad ananiambia hivyohivyo na anasema am too smart for my age.” Maya alicheka sana.

“Unafikiri ni nini kilimpelekea kusema hivyo?” “Naweza kumsoma mtu kwa kumwangalia tu.” “Haiwezekani Ethan!” “Na mimi ndio super power yangu.” Maya akacheka sana. Ethan alionekana mtoto mdogo lakini kweli anaakili. “Haya, nisome mimi uniambie.” Ethan akacheka sana. “You are so nice na sweet.” Ethan aliongea hivyo kuwa Maya ni mwema sana huku akicheka na kumshangaza sana Maya. “Ethan!” “Kweli. Wewe ndivyo ulivyo.” Maya akabaki ameduaa. Akaanza kumfikiria yule mtoto na wazazi wake. Mama yake anaongea kila kitu mbele ya yule mtoto mwenye akili vile!

“Nafikiri umeshakutanishwa na Ethan.” “Anko Roy!” Ethan akamkimbilia, Maya akageuka. Roy akambeba na kumkumbatia kwa upendo na kumbusu. “Samahani kwa alichokwambia mama. Lakini ujue mimi nakupenda.” Ethan akamwambia Roy. “It’s okay Ethan. Unafikiri nimekasirika?” Roy akamuuliza huku amembeba. “Sijui!” Akajibu Ethan. “Hata kidogo. Leo ni lazima tukacheze hockey.” “Halafu tunaenda kwa grandma Pauline kula cookies na hot coco?”  Ethan akauliza. “Kabisa!” Akamjibu. “Yesss!”  Akashangilia  kitoto. Maya akacheka.

Roy akamsogelea. “Upo sawa?” “Ethan alikuwa akinishangaza vile alivyo smart kwa umri wake!” Alijibu Maya, akijua kabisa Roy anachouliza. “Na ninaondoka na Ethan.” Wote wakageuka. Malcom na Zoe wakawa wanatoka ndani. Wakawasikia tena. “Sisi tuna mipango na Ethan leo. Huwezi kumchukua.” Akajibu Malcom. “Unataka ukamzungushe mtoto na mwanamke wako ambaye hata jamii haimkubali!” “Niliposema sisi, namaanisha mimi na Roy. Huyo mtoto anasubiriwa nyumbani kwa kina Roy. Jioni mimi, Roy, mdogo wake Roy na baba yake Roy tunakwenda kucheza hockey. Baba yake Roy ameshaweka reservation kwenye huo uwanja. Na ndio maana Roy alikuja kumchukua ili ampeleke kwa grandma Pauline kwanza, amekuwa akimuulizia sana Ethan.” Akaongea Malcom kwa utaratibu kama anayeepusha shari.

“Kwa hiyo unaenda kumtupa kwa mama yake Roy!?” Akashangaa kwa ukali sana Zoe. “Tafadhali punguza sauti Zoe. Unamuogopesha Ethan bila sababu! Kwa nini unashindwa kuzungumza kawaida tu. Hatugombani.” “Nani amekwambia tunagombana?” Zoe akamjia juu. “Namuomba mtoto wangu Roy.” Akamsogelea Roy. “Come on Zoe! Ni siku ya leo tu! Mama anataka kumuona Ethan halafu jioni ndipo twende naye hockey. Kwa nini leo unakataa wakati jana usiku ulikuwa ukipiga kelele aje achukuliwe leo asubuhi na mapema kwa kuwa unamambo yako yakufanya?” “Ratiba imebadilika. Leo na mimi nataka muda na Ethan.” “Upo naye jumatatu mpaka ijumaa. Leo tu!?” Roy akauliza kwa kumshangaa sana Zoe huku amembeba Ethan.

“Nilikwambia acha kumng’ang’ania Ethan. Ni mtoto wa Malcom sio wako. Kinachokushinda na wewe kuzaa mtoto wako ni nini? Zaa na wewe mtoto wako umpelekee mama yako!” Akamnyang’anganya Ethan kwa nguvu. “Hiyo ni roho mbaya sana Zoe! Usifikiri unayemuumiza hapo ni Roy, unamwadhibu mtoto bila sababu! Kwa nini unafanya hivyo?” Malcom akamsogelea akiongea kwa kuumia na kwa tahadhari kama wanao muogopa. Maya akashangaa.

Ethan akaanza kulia. “Nataka kwenda kwa grandma Pauline. Nataka kuwa na dad na anko Roy, mami!” Akamuweka chini na kuanza kumvuta. Akashangaa Roy na Malcom wamenyamaza wanamwangalia tu. “Usilie Ethan, tutapanga wakati mwingine. Sawa Ethan?” Roy akajaribu kumtuliza, Malcom akabaki kama bubu. “Come on buddy!” Roy akaendelea kuwafuata kwa nyuma akimbembeleza Ethan. Huku Ethan akivutwa mkono na mama yake wakielekea sehemu yakuegesha magari. “Nipe tano?” Ethan aliendelea kulia tu. 

Roy akakimbilia mbele ya Zoe. “Naomba nisikilize Zoe. Niambie chochote unachotaka nitakupa. Ilimradi leo utuachie Ethan.” Zoe akasimama. “Chochote?” Zoe akauliza kama anayefikiria. “Chochote.” Roy akamuhakikishia. “Mmmh! Akafikiria.” Akamgeukia Malcom aliyekuwa amesimama kimya nyuma yao palepale walipomuacha amesimama kama aliyeonywa asisogee hata hatua moja. Malcom alikuwa mwekundu kama anayetamani kulia.

“Nataka jioni ya leo Malcom anisindikize kwenye harusi ya binamu yangu, kama..” “No way Zoe! Hapana.” Hapo Malcom akakataa. Zoe akamgeukia Roy. “Kuwa mtu unayefikiria Zoe! Nimekwambia usiku wa leo ndio tunakwenda kucheza hockey sisi wanaume. Sasa..” “Nawezaje kumuacha tena Ethan acheze na watu wengine halafu mimi mwenyewe nisiwepo?! Maana lengo ni na mimi niwe na mtoto wangu!” Akaingilia Malcom na kumkata Roy.

“Nitamuhitaji aje anichukue na ile gari yako wewe Roy, sio ule uchafu wake. Hakikisha yupo kwenye suti nyeusi. Saa kumi na moja kamili, awe amefika mlangoni kwangu ili saa 11:30 jioni tuwe kwenye harusi. Hatutakwenda kanisani. Ila kwenye sherehe tu.” Akaendelea kuongea Zoe kama hajamsikia Roy wala Malcom. “Hapana Roy.” Malcom akakataa. Ethan akazidi kulia. Roy akamtizama Ethan, akarudisha macho kwa Zoe. “Unataka avae suti nyeusi, na viatu gani?” Roy akamuuliza Zoe.

“Come on Roy!” Malcom akamlalamikia Roy. “Hakikisha unamuweka kwenye tabia yake njema. Na mwambie sihitaji mlinzi, ila mpenzi. Kwa hiyo unaelewa ninachomaanisha.” Akamkonyeza Roy na tabasamu usoni. “Mabusu na kukumbatiwa kila ninapohitaji.” “No way Zoe and Roy! Siwezi kumbusu na kum..” “Deal.” Roy akamkubalia Zoe kwa haraka kama asiyemsikia Malcom.

“Na usinitanie Roy. Ukimchukua Ethan sasa hivi, Malcom aje kwangu jioni. Akija Malcom kama yule!” Zoe akamnyooshea kidole Malcom pale aliposimama. “Ujue jumatatu yupo mbele ya hakimu. Na ujue ndio utakuwa mwisho..” “Acha kututisha Zoe. Nimekwambia Malcom atakuja kukuchukua jioni. Nipe Ethan.” Akamuachia mkono Ethan. Ethan akaenda kumbusu mkono Roy, kisha akamkimbilia baba yake. Malcom akambeba mtoto wake huku akifuta machozi.  “Na...” “No Zoe. Inatosha. Huwezi kuendelea kutoa vitisho wala matakwa mengine. Wewe ondoka.” “Fine.”  Akataka kuondoka Zoe, akamgeuka Malcom na tabasamu la ushindi.

“Sina pesa ya kwenda saluni kutengeneza nywele na kucha.” “Kwa hiyo?” Akamuuliza Malcom kwa hasira huku amembeba kwa kumkumbatia mtoto wake. “Ndio unipe! Tunatokaje nikiwa sijapendeza!?” “Unafikiri mimi naitoa wapi hiyo pesa?” “Unamlala mtoto wa Cote, unakosaje pesa? Kwani wewe hakuhongi kama wenzako?” Maya alikuwa ni kama mwili umeishiwa nguvu, umepigwa na ganzi kama kilichompata Tunda mbele ya Vic na Renee.

“Unataka kiasi gani?” Akadakia Roy. “Ngoja nifikirie. Mmmh! Kucha dola 85, nywele dola 120 naaa..” “Nakupa dola 200, Zoe. Uondoke na usiongeze kitu kingine. Tafadhali.” Zoe akaanza kucheka. “Shida sana kuwa karibu na wanaume maskini kama nyinyi wawili! Dola 200 tu! Labda Miss Cote atabadilisha maisha yenu.” Zoe akavuta zile pesa kutoka mkononi kwa Roy, akaondoka huku akicheka. Wakabakishwa pale wote kimya. Wameduaa Maya akikumbuka maonyo ya bibi yake juu ya kutofungua moyo kwa haraka kwa Malcom. Akajicheka taratibu.

Hali ya Malcom ilikuwa imebadilika kabisa. Akabaki amemuinamia mtoto wake aliyekuwa bado amembeba, akaendelea kumsugua mgongoni. “Mimi naweza kuita dereva akaja kunichukua kunirudisha nyumbani.” Maya akavunja ukimya. Kimya. Akamsogelea Ethan pale alipokuwa amebebwa na baba yake, akamgusa taratibu mgongoni. Akageuka huku amejawa machozi. “Uwe na wakati mzuri kwa grandma Pauline, na kwenye hockey.” Akatingisha kichwa kukubali. Maya akampa tabasamu na kumfuta machozi.

“Bye Malcom.” Maya akamuaga kwa upole. Malcom alikuwa mwekundu mpaka masikio. Alibaki akimwangalia Maya. “Asante kwa kifungua kinywa.” Akaongeza Maya na tabasamu la kiuungwana lakini akisikika ndio anaaga moja kwa moja. Kimya. Maya akamgusa begani, na kuondoka.

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

Mambo yanazidi kuchanganya. Ni kweli Maya analipa gharama ya maisha machafu aliyoishi zamani na kusubutu kumtoa tonge mdomoni. Malcom aliyekuwa na vigezo vyote, akamgusa moyo wake vilivyo! Naye ndio huyoooo!

Jeff yupo njiani kumfuata Ritha kudai haki yake. Kama amemudu kumuua mpenzi wake kwa ajili ya pesa, kwa Ritha je? Usipitwe na muendelezo...

CONVERSATION

0 Comments:

Post a Comment