Naomi Simulizi |+1 205 767 8163 |naomisimulizi@gmail.com Nilipotea! – Sehemu ya 51. - Naomi Simulizi

Nilipotea! – Sehemu ya 51.

 “Naomba usubiri Maya.” Akamsikia Malcom, akageuka. “Naomba nikurudishe mimi mwenyewe. Tafadhali.” “It’s okay, Malcom. Wewe kuwa na wakati mzuri na Ethan. Mimi nitapata usafiri tu bila shida.” “Nafahamu hilo. Lakini kwa kuwa mimi ndiye niliyekuchukua naomba nikurudishe. Tafadhali Maya.” “Ni sawa. Ila tu sikutaka kukusumbua.” Maya akajibu akionekana ametulia tu.

“Tunakwenda na Ethan?” Maya akauliza huku akimchungulia Ethan kule alikojificha kwa baba yake. “Naweza kumchukua Ethan.” Akadakia Roy. “Mmmh! Unafikirije Ethan? Bado unataka nikuonyeshe super power nyingine?” Ethan akacheka kidogo huku akitingisha kichwa. “See! We still have unfinished business.” Maya akafurahia kwa Ethan kukubali. “Wakati dad ananirudisha nyumbani, njiani mimi na wewe tunaonyeshana super power nyingine. Nahisi kama unazo nyingine nyingi!”  Ethan akatingisha kichwa kukubali. “Yess!” Maya akaonyesha kufurahia.

“Basi mimi naondoka. Tutawasiliana.” Roy akaaga. “Thanks Man! Mwambie grandma Pauline, Ethan atakuwa amefika kabla ya chakula cha mchana.” Malcom akamwambia Roy, akionyesha uchungu kwenye maneno yake. “Okay.” Akajibu Roy. “You are the best uncle in the entire wide world. And I love you so much.”  Ethan aliongea kwa upendo huku akijifuta machozi. Roy akamsogelea Ethan akambusu. “Na kwa taarifa yako tu, mimi najua ila baba yako ndio halijui hilo.” Roy akajibu huku akimtekenya, Ethan akaanza kucheka. “Kwa hiyo, unatakiwa uwe unamwambia dad kila wakati. Kuwa anko Roy, is the best.” Roy akambusu tena na tena. “Okay. Nitamwambia dad.” Ethan akajibu huku akicheka. Angalau Malcom akaanza kutulia.

          “Njoo nikwambie kitu.” Roy akamchukua kutoka kwenye mikono ya baba yake. “Unajua kwa nini nilikuja kukuchukua asubuhi na hapa?” “Kwa sababu mimi ni mtoto mzuri.” Mpaka Maya akacheka. “Kabisa. Sijawahi ona, mtoto mzuri hapa duniani kama wewe Ethan. Muulize dad wako. Tumezunguka nchi nyingi tu. Eti dad? Umeshaona mtu kama Ethan?” “Nope.” Akakataa Malcom huku akitingisha kichwa kabisa.

“Umeona sasa? Ndio maana mimi, dad, grandma Pauline, grandpa, uncle Neo, antie Kyle, tunakupenda sana na tunakung’ang’ania. Wote wanataka kukuona leo nyumbani. Grandpa amesema leo hakuna mtu atacheza hockey bila Ethan kuwepo. Eti amesema ni heri dad akose, ila wewe uwepo. Can you imagine?” Ethan akatingisha kichwa kukataa akicheka sana. 

“Hata mimi sikuamini hilo. Lakini unajua ni kwa sababu wewe ni mtoto mzuri sanaaaa!” Roy akambusu kwa kumtekenya na mdomo. Ethan akazidi kucheka. “Hatuwezi kuishi bila wewe Ethan. Si ndio dad?” “Kabisa.” Malcom akajibu akisikika angalau ametulia. “Now. Kamuonyeshe Miss Cote super power zooote ulizo nazo.” “Okay uncle.” Ethan akambusu Roy, akamshusha. Roy akaondoka.

Njiani vilisikika vicheko vya Ethan na Maya tu. Ethan alikuwa akicheka sana kila Maya anavyotingisha sikio. Walikuwa wamekaa naye kiti cha nyuma. Mpaka Malcom akaanza kucheka. “Nilijua tu unayo super power nyingine.” “Ipi?” Ethan akauliza huku akicheka sana. “Yakucheka mpaka kumfanya mtu mwenye huzuni afurahi.” “Kweli?” “Kabisa. Niangalie mimi. Unakumbuka mwanzoni nilikuaje?” “Unashangaa!” “Haiwezekani Ethan! Ulinisoma?” “Nimekwambia hiyo ndio super power yangu.” “No kidding!” Maya akashangaa sana.

“Lakini ona sasa hivi!” “Bado upo kama huelewi?” Ethan akawa kama anamuuliza na kumshangaza zaidi Maya. “Kweli upo too smart for your age.” Wakacheka. “Unataka nikwambie siri?” Ethan akamuuliza Maya. “Yeah.” “Kwenye sikio silly! Dad asisikie.” Maya akampa sikio huku akicheka. “Mama yangu huwa anakasirika zaidi akimuona dad na msichana mwingine, zaidi akiwa mrembo kama wewe.” Moyo wa Maya ukapasuka. Maya akamwangalia usoni akabaki ameduaa.

Ethan akatingisha kichwa kama anayemthibitishia anachoongea. “Kweli?”  Maya akamuuliza kwa kunong’ona kwa mshangao. “Nilimsoma hivyo.” “Oooh!” Maya akawa hajui chakusema tena. “Kwa hiyo?” Ethan akamuuliza Maya akiwa bado amepigwa na butwaa, akimtafakari huyo mtoto mwenye akili na uelewa wa namna hiyo, ameyaona hayo mangapi. “Kuhusu nini?” Maya akauliza akiwa hajui Ethan anauliza nini!

“Unafikiri nitakuja kukuona tena?” Akauliza Ethan, safari hii sio sikioni. Maya akabaki kimya, hajui ajibu nini. “Au na wewe umekasirika utakaa mbali na sisi? Anko Roy hajawahi kutukatia tamaa. Wakati wote amekuwa akihakikisha nakuwa na dad.” Maya alijisikia vibaya sana. Yeye binafsi alishaamua kujiachia. Alitaka akishuka hapo, ndio iwe ndio basi kabisa na Malcom. Hakutaka hiyo fujo kwenye maisha yake. Aliumia kumuona Zoe akimtumia Ethan kama mchezo tu. Akamkumbuka mama yake alivyokuwa akiwatumia na wao kujipatia pesa za Cote, akapandwa na hasira. Akaona ni heri aachane nao kabisa, ili asije ishi hayo maisha tena kwa kuyatizama kwa mtoto mwingine akifanyiwa hivyo na mama mzazi.

Maya akabaki kimya, hajui amjibu nini huyo mtoto. “Nilijua tu kuwa huna mpango wa kuja kutuona tena. Lakini unajua nini?” “Nini?” Maya akamuuliza akionyesha kuishiwa nguvu. Mtoto huyo hakuwa mdogo kama anavyoonekana. “Mimi naelewa. Ni ngumu.” Maya akaishiwa maneno. Akabaki kimya. Na Malcom naye kimya. Akaendesha mpaka getini, safari hii akashangaa geti linafunguliwa bila kubonyeza kengele. Maya alijua ni kwa nini lakini sio Malcom.

“Mbona geti linafunguka lenyewe?” “Kwa sababu yupo mtu ameshawaambia ndani kuwa tunakaribia hapa.” Malcom akawa hajaelewa. “Waoooooo!” Ethan akasikika akishangaa. “Naweza kusimama dad?” Malcom akamruhusu. Akajifungua mkanda, akasimama. “Unaishi kwenye castle kama mtoto wa mfalme!?” Ethan alimfanya Maya aanze kucheka. “Waoooo! Kwa hiyo mama hakukosea. Wewe ni tajiri!” Ethan akamgeukia Maya kwa kushangaa sana. Maya akazidi kucheka.

“Unajua ndani ya hiyo castle kuna nini?” Maya akamuuliza huku akicheka. “Naamini kuna kila kitu.” Ethan akamjibu Maya, nakumfanya azidi kucheka. “Sio kila kitu ila kuna warm pool! Bwawa linalotoa maji yenye vuguvugu.” “Watu wanaogelea!?” Akashangaa kwa kuhamasika. “Yeah. Na ujajua hata wewe unaweza kuogelea?” “Utanikaribisha kwenu!?” “Kabisa. Siku utakapokuwa tayari, umwambie dad, tutapanga. Halafu unakuja kuogelea.” “Yesss! Na mimi nitaingia kwenye castle.” Akafurahia Ethan.

Malcom akasimamisha gari karibu kabisa ya ngazi.  Akaenda kumfungulia mlango, Maya akashuka. Maya akamuona vile alivyoishiwa ujasiri. “Samahani sana Maya.” Maya akacheka. “Sina jinsi yakukuahidi kwa kuwa ulichoona leo, ni sehemu kubwa ya maisha yangu. Na ninauhakika itarudia tena na tena.” “Tatizo ni nini!?” “Hakuna anayejua Maya.” Maya akanyamaza kama anayefikiria.

“Maya?” “Kwa hiyo huwa mna..” Maya akasita. Lakini Malcom alishamuelewa. Maya akajifuta machozi. Malcom akainama akijua ndio anaachwa. “Maisha yangu yamekuwa magumu Malcom. Sijawahi kutulia na kuwa na mtu wangu mwenyewe, kwenye maisha yangu. Na wewe unajua. Siwezi..” “Naelewa. Naelewa kabisa Maya.” Malcom akajibu akisikika amekata tamaa kabisa.

“Natamani ingekuwa tofauti Maya. Natamani kama ningejua hii hali itakuja kuisha lini, lakini sina jibu. Zoe anaishi na mtoto wangu na kwa sasa ndiye amepewa dhamana na mahakama. Anafanya kile anachokitaka kwangu na mtoto.” “Kwa nini usikae naye chini ukajua ni nini anataka?” Maya akajaribu kushauri. “Huwa hatuwezi kufika popote na Zoe. Hata nijitahidi vipi, huwa naishia kulala jela au Roy ndio anakuja kunitoa kabla sijalala huko jela. Inategemea.” Maya akakunja uso.

“Mnaweza mkakubaliana mzungumze. Akakwambia umfuate nyumbani. Akiniambia jambo nikikataa, anapiga simu polisi. Wakija, anawaambia nimewafanyia fujo yeye na mtoto. Kuna wakati nilipewa restrain order. Nilikuwa siwezi kumuona mtoto wangu. Karibia miezi sita.” “Malcom!” Maya akashangaa sana. “Kweli tena. Ndio ikabidi baba yake Roy aende akazungumze naye, akanipa masharti, ndio nikaanza tena kumuona mtoto wangu. Mshahara wote unaishia kwa Zoe.” “Wazazi wako wako wapi?” Maya akauliza.

“Mwanzoni mimi na mama tulikuwa tukiishi kwa bibi. Lakini baadaye mama alikuja kuolewa, anaishi Califonia. Nikabaki kwa bibi. Akanilea vizuri tu mpaka chuo. Alikuja kufariki wakati nipo mwaka wa mwisho chuoni.” “Unamaanisha mama yako yupo nchini Marekani!?” “Ndiyo. Anamaisha yake mazuri tu na familia yake ya watoto wengine wawili. Aliolewa na mwanasheria akampa maisha mazuri sana. Kwa kifupi mimi nilishatoka kwenye maisha yake muda mrefu sana. Hata mawasiliano ni mara moja kwa mwaka, tena yanakuwa ni kama tunalazimishia tu.” “Malcom!”  Maya akashangaa sana.

“Kawaida tu. Lakini ninachotaka kukwambia Zoe hajaanza leo na usifikiri ameniharibia kwako tu. Nina rekodi mbaya sana. Usishangae hata usiku wa leo nitakapotoka naye, nikaishia kulala jela nisirudi nyumbani.” “Malcom, lazima kuna njia yakufanya.” Maya akaumia sana. “Njia ipi na yeye anaye mtoto wangu, Maya? Nisipofanya anachotaka yeye, Ethan ndio anaumia. Na mimi nipo tayari kulipa garama yeyote kwa ajili ya Ethan. Sitaki aje aishie kama mimi. Nimekua bila wazazi na wote wapo wanaendelea na maisha yao. Nimejiapia kwa garama yeyote ile, Ethan atakuwa akitambua nipo na nina muhitaji. Sitamtelekeza. Japo inanigarimu sana, lakini sina jinsi. Hapa nilipo siwezi kupandishwa cheo na siwezi kwenda popote kwenye maisha, sababu ya kuharibiwa na Zoe. Ni kama amenishika miguu. Mpaka lini, sijui!” Maya akatulia kidogo, kisha akamwangalia.

“Umeshakuwa na mahusiano na Vic?” Maya akauliza taratibu na kwa wasiwasi akihofia jibu la ndiyo. “Naomba uniamini Maya, mimi sio muhuni.” “Nataka kujua kama ulishawahi kuwa na mahusiano na Vic.” “Ya kimapenzi hapana. Ila nilimfanya awe karibu yangu tu ili kupata habari fulani kutoka kwake. Lakini hakuna chochote kilichotokea na ndipo nilipofahamiana na kina Gina, na wengineo. Lakini sikulala hata na mmoja wao.” Maya akashangaa sana.

“Kumbe hao watu wote unawajua!?” “Tunafahamiana vizuri tu. Hukumbuki Vic aliponiona siku ile alipokuwa amekushikia risasi pale kwa Jake, alizungumza na mimi kwa kunitaja kabisa jina?” “Nilikuwa nimeingiwa hofu hata sikuwa nikifikiria kitu zaidi ya kifo.” Maya akaongea huku akivuta kumbukumbu.

“Alizungumza na mimi vizuri kwa kuwa tulikuwa tukifahamiana kabisa. Lakini sivyo atakavyokwambia Zoe. Hawezi kuniona na msichana yeyote yule. Na hata hilo aliniadhibu nalo. Nikajaribu kumueleza kuwa ni kazi tu. Lakini bado ikawa shida. Akaenda kumtafuta Vic, akataka kumfanyia fujo. Wewe unamjua Vic.” Maya akaanza kupata picha. 

“Vic akampiga lakini akaenda kunishitaki mimi mahakamani kuwa mwanamke wangu amempiga.” “Malcom!” “Muulize Roy. Nina rikodi mbaya, ni hivyo nafanya kazi vizuri ndio maana mabosi wangu wananivumilia. Lakini najua itakuja kufika mwisho, watachoka itabidi kufukuzwa kazi.” Maya akanyamaza, huruma ikaanza kumuingia, asijue chakufanya.

“Ni sawa nikurudishe ndani au unafikiri itakuwa mbaya wakimuona mtoto wangu?” “Hapana Malcom! Simuonei aibu Ethan wala simuoni kama ni tatizo. Twendeni tu.” Akafungua mlango. “Unataka uingie kwenye castle?” Akamuuliza Ethan. “Naweza kuingia dad? Please!” “Kama Miss Cote amekukaribisha, ni sawa.” “Yesss!” Akaruka Ethan kutoka kwenye gari. Wakaanza kupandisha ngazi kuelekea ndani.

Wakafunguliwa mlango. “Good morning Sir!” Ethan akamsalimia Carter kwa heshima sana. “Well behave, Son! Well, good morning to you too.” Ethan akampa mkono. Maya akacheka. “Huyo anaitwa Mr Carter. Ni mtu mzuri sana anapenda watoto. Ni kama papa wangu wa pili. Amenilea tokea nazaliwa. Alikuwa akinipa maziwa usiku.” “Na cookies!?” Akauliza Ethan. “Usiku alikuwa anakataa. Ila asubuhi alikuwa akinipa.” Wakacheka. Carter akajisikia vizuri kwa heshima aliyopewa na Maya yakutambulishwa kama babu. Maya akambusu shavuni. Carter akacheka. “Well, nice to meet you Mr Carter.” “Like wise Ethan.” Carter akajibu na tabasamu. Malcom alikuwa akimwangalia tu mwanae.

“Unataka kumuona Nana wangu?” “Na yeye ni mzuri kama grandma Pauline.” “Nafikiri hivyo.” Akatoka bibi Cote. “Woooo!” Akashangaa sana Ethan wakati anatokea Bibi Cote. Akainamisha kichwa kwa heshima mkono mmoja nyuma ya mgongo, mwingine akakunja kwenye tumbo kama anaye msalimia malkia. “Ma’am!” Kakasalimia ka Ethan kwa heshima sana. “Someone has all his manners!” Akasifia bibi Cote akimshangaa yule mtoto. 

“How are you?” “Very well ma’am!” Ethan akajibu kwa heshima sana. “And you are?” Bibi Cote akamuuliza jina lake kistaarabu. “Ethan Malcom Marshal. Son of Malcom, ma’am!”  Alijitambulisha kwa heshima sana akashangaza kila mtu pale. Bibi Cote alitoa tabasamu la kuvutiwa. “Well, I am Ms Cote. Nice to meet you Ethan.” “Pleasure is all mine!” Mpaka Maya akamgeukia Malcom huku ameshangaa. Malcom akacheka.

“Ethan, huyo ndio Nana wangu.” “You didn’t tell me your Nana is a Queen!” Wote wakacheka. “You look magnificent, maam!” “Well, thank you Ethan.” Akashukuru bibi Cote na tabasamu usoni. Na kweli Ethan hakuwa amekosea. Bibi huyo hapo alikuwa kwenye kiatu cha juu na mavazi mazuri sana ya thamani. Lipstick imetulia mdomoni. Nywele imetengenezwa vizuri  na alumasi yakueleweka masikioni na shingoni, mida hiyo mapema tu, kama malkia kwelikweli ndani ya jumba la kifamle.

“Unataka Mr Carter atuzungushe kidogo ndani ya castle? Yeye anaijua hii castle vizuri kuliko hata mimi.” Maya akamuuliza. “Nitafurahi. Nitaenda kumwambia grandma Pauline kuwa leo nimebahatika kuingia kwenye castle na nimemuona Queen Cote and princess Maya!” Wakacheka, na kuondoka pale wakimzungusha. Carter akiwa naye mbele akimuonyesha na kumueleza kila picha na maana ya kila kitu.

Alionekana ni mtoto aliyefundishwa vizuri, mtulivu. Na kweli hakuwa akiendana na umri wake. “Hongera sana Malcom! Sasa hivi nahisi nakuelewa kwa lolote unalofanya kwa ajili yake. Anastahili huyu mtoto.” “Asante Maya. Na samahani sana.” “Huhitaji kuendelea kuomba msamaha Malcom. Nimekuwa na wakati mzuri kuliko nilivyotarajia.” “Kweli?” “Ooh yeah! Unafikiri ni nini kitakuwa kimeniudhi? Tena baada ya kupata muda na Ethan! Mimi mwenyewe sijawahi kuona mtoto kama Ethan!” Malcom akanyamaza huku akitoa tabasamu la kinyonge.

“Kwanza niambie, huyu mtoto unamleaje wewe Malcom!? Anamaadili mazuri sana!” Waliendelea kuzungumza wao wakiwa nyuma, Ethan akitembea mbele yao na mikono ameikutanisha nyuma akimsikiliza Carter kwa makini sana. “Huyo mtoto anakuzwa na mimi, Roy ndio zaidi kwa kuwa anaweza kuwa kati yangu na Zoe. Na ameshazoea matusi ya Zoe. Akikwambia Ethan kuwa Roy hajatukatia tamaa, ujue ni kweli. Huwa anamtusi Roy, mimi mwenyewe huwa najiweka kwenye nafasi ya Roy, najua wazi nisingeweza. Lakini Roy hakati tamaa. Na kwa kuwa yeye hajawahi kumshitaki mahakamani, basi Roy huwa anakwenda nyumbani kwa Zoe muda na wakati wowote kumtizama  Ethan. Akimkuta ametulia, anaweza akaondoka na Ethan hata kwa masaa mawili au matatu katikati ya juma, na kumrudisha. Akimkuta siku hiyo akili haijatulia, basi ujue atamtukana na hatakubali hata amuone Ethan.”

“Haya, na nyumbani kwao kina Roy, anapendwa sana Ethan. Ndugu zake wote kina Roy, wanamuona Ethan kama mtoto wao kabisa. Halafu baba yake Roy alikuwa mwanajeshi. Kwa hiyo naye anamlea kijeshi. Huwezi kumkuta anazungumza naye au anamfanya ajione ni mtoto. Hizo heshima zote ni kazi ya baba yake Roy. Ndiye anayemfundisha na kutumia muda mwingi na Ethan kwa kuwa amestaafu. Yupo tu nyumbani. Wakati mwingine tunaweza kumchukua, tukaitwa kazini kwa gafla, basi ujue atakuwa na grandma Paulina na mumewe mpaka tutoke kazini. Kwa hiyo anatumia muda mwingi sana na hao wazee. Na ukirudi kumwangalia, utakuta anafanya kazi na huyo mzee. Anamfundisha mambo mengi sana ambayo hata mimi mwenyewe sikubahatika kwenye makuzi yangu.” “Kwa kweli amezungukwa na watu sahihi.” Malcom akamwangalia na kunyamaza.

“Ni mtoto mzuri sana Malcom.” “Lakini hakutakiwa kuishi maisha anayoishi, Maya! Zoe ni mkali kwake bila sababu. Anaweza akakosana na mimi, akaamua kummalizia yeye. Ilimradi tu.” “Dad! umemuona Cote the first and Second?” Ethan akamwita baba yake na kumuonyesha. Akaanza kumuelezea. “Huyu ni Cote wa kwanza, huyu ni wa pili, huyu ni wa tatu, huyu ni wa nne, huyu hapa mdogo kabisa, ndiye Cote the fifth. Nimeambiwa hawa wawili. Cote the 4th na 5th, wapo humu humu ndani.” “Oooh yeah?” Malcom akawa kama anashangaa. “Yeah dad! Hawa wawili wapo.” Yaani Net na mtoto wake ndio wapo kwa wakati huo. Ethan akaongea kionekana amefurahia. Maya akacheka.

Akamgeukia Carter. “Samahani Sir!” Carter akasimama. Ikabidi na kina Maya wasimame. “Nina miahadi na grandma Pauline. Ameniandalia chakula cha mchana. Unafikiri itakuwa sawa kama tukiishia hapa kwa leo, halafu ikitokea ninarudi siku nyingine, tutaendelea kuanzia hapa?” Maya akashangaa na kumgeukia Malcom.Yaani na kuhamasika kote huko, bado alikumbuka miahadi! “Absolutely, Ethan. Nitafurahi kupata nafasi ya kukutembeza tena.” “Asante.” Akampa mkono Carter na kumgeukia baba yake. Maya akacheka taratibu na kwa makini akijua akili ya huyo mtoto si ya kuchezea.

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

Malcom na mtoto wake walipoondoka, Maya akaenda kumtafuta Tunda, akaambiwa amerudi kulala. Ikabidi kwenda ofisini kwa bibi yake. Hapo hapo nyumbani. Wote wawili, yeye na Net wana ofisi zao na hapo nyumbani pia. Alimkuta bibi yake ameinamia meza, akionekana anakazi inayomfanya afikirie. Alipoingia na kumuona hivyo, akaenda kujilaza kwenye kochi la wageni. Kimya. Baada ya kama dakika 6 hivi, bibi Cote akavua miwani na kumwangalia. Akamkuta akimwangalia lakini kama akiwaza. 

“Zoe alikufanyia vurugu yeyote?” Maya akashangaa sana. “Nana! Umejuaje!?” “Nimekwambia sasa hivi sitatoa macho yangu kwako.” Maya akakaa.

Akamsimulia mwanzo mpaka mwisho. “Nitafanyaje Nana?” “Wewe unataka nini?” Maya akainama. “Pata muda wakufikiria, halafu uniambie. Tutajua chakufanya kuanzia hapo. Lakini ni kweli Malcom anamtoto mzuri sana. Haendani na umri wake hata kidogo.” Bibi Cote akasifia. Maya akanyamaza kama anayefikiria zaidi.

“Sijawahi kupata mtu wangu mwenyewe Nana! Natamani kumpata mtu wangu, peke yangu, nianze naye mimi mwenyewe.” “Unaweza ukampata ambaye hana Ethan wala Zoe, lakini asikutazame kama Malcom.” “Hicho ndicho kinachoniumiza kichwa!” Maya akamsogelea. “Natamani kama Malcom angekuwa hana Ethan wala Zoe au Ethan awe wangu.” “Lakini Ethan ni wa Zoe!” Bibi yake akaweka msisitizo. Maya akainamia meza.

“Nafikiri nijipe muda Nana. Naweza kumpata Malcom mwingine. Huyu naona...” “Hutakuwa center of his attention? Kwamba kabla hajakufikiria wewe itabidi aanze kumfikiria kwanza Ethan?” “Sio hivyo Nana!” “Mimi nakujua Maya. Na ninajua hilo ndilo tatizo kubwa.” Maya akajilaza kichwa kwenye meza. “Pata muda wa kufikiria. Uamue vizuri ili usije kujuta baadaye. Na ujue kabisa, kila utakaloamua, nipo nyuma yako.” Maya akabaki amefunga macho.

Kabla hapajapoa..!

B

ibi yake akarudisha kichwa na mawazo kwenye alichokuwa akifanya, Maya akabaki amejilaza. Simu yake ikaanza kuita. Bibi yake akamwangalia na kurudisha macho kwenye kazi yake. “Menson!” Akaanza Maya. Bibi yake akamuona anacheka kidogo huku akisikiliza. “Sijui Menson! Ningefurahi kuhudhuria, lakini...” Akasita na kumwangalia bibi yake. “Subiri kwanza. Nitakupigia.” Akakata na kumwangalia bibi yake. “Nana!” Akamuita kama kutaka ahamishie mawazo kwake. Akamwangalia. “Kuna kijana anaitwa Menson, anamdogo wake anaitwa Mat. Menson alikuwa kwenye madawa. Nilikutana naye wakati tupo rehab, hii safari ya mwisho. Akawa rafiki yangu sana.” Maya akaendelea.

“Mimi nilitoka kabla yake, nikawa naendelea kumfuatilia kuhakikisha anamaliza muda wake vizuri na anatoka. Baadaye akaniambia alitoka, akakuta mdogo wake ameishiwa kabisa, sababu yakumlipia pale rehab.” “Na ile rehab ni gharama sana.” Bibi Cote akaongeza. “Sana. Ila wanatoa huduma nzuri. Ndio mdogo wake akahakikisha anamgaramia kaka yake mpaka akatoka. Alitoka hapo maisha yakawa kwao magumu na mdogo wake akawa amepoteza kazi.”

“Kufupisha stori, niliwasaidia kuwalipia kodi ya nyumba, ilikuwa wafukuzwe, na garama nyingine mpaka mdogo wake akapata kazi na Menson naye nikamsaidia kazi ya kuosha vyombo kwenye mgahawa wa mtu ambaye nilikuwa nikifahamiana naye mimi. Sasa baada ya Mat kufanya kazi huko, wanaonekana walimpenda na ananidhamu ya kazi, wakampandisha cheo, kwa kifupi maisha yake yakarudi kuwa mazuri akaamua kumuoa mchumba wake ambaye walikuwa naye muda mrefu tu.”

“Sasa walinialika leo kwenye harusi yao, lakini niliwaambia sitaweza kwa kuwa unakumbuka leo ndio ilikuwa iwe harusi ya Net?” Bibi yake akanyamaza kama aliyekumbushwa kitu. “Amenipigia hapa kuniomba niende, kwa kuwa harusi yetu haikufanikiwa. Unafikiri ni sawa?” “Ooh Year! Why not? Maisha yetu yanatakiwa yaendelee kama kawaida.” Bibi yake akamkubalia bila shida. Hakuona tatizo lolote.

“Kweli Nana?” “Kabisa. Usiogope, nenda kafurahie na wenzako, nitahakikisha unarudi nyumbani salama.” Maya akaelewa. “Asante Nana.” Akasimama kwenda kumbusu. “Lakini umenifurahisha Maya. Sikujua kama ulikuwa ukisaidia watu!” “Sio pesa nyingi sana, ila wao walikuwa wakiona pesa nyingi mpaka nilikuwa nikishangaa.” “Hakuna msaada mdogo kwa muhitaji. Ule moyo wa kuwa nao tu wakati wa shida, nafikiri hilo ndilo la muhimu. Am so proud of you baby girl.” Akambusu. Maya akacheka na kuondoka pale kutafuta chakuvaa kwenye harusi.

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

Ilikuwa mida ya 11:45 jioni wakati dereva anamshusha Maya kwenye ukumbi waliofanyia hiyo harusi ya Mat. Alimkuta Menson akimsubiria nje. Kwanza yeye ndiye aliyemfungulia mlango wa gari. Walipoonana tu wakaanza kucheka. Maya hakuwa akijifanya Miss Cote mbele ya Menson. Aliishi naye rehab akiwa teja. Akihangaika na matibabu. Kuugua kipindi anatolewa madawa mwilini, Menson alikuwepo. Na ikawa hivyohivyo kwa Menson. Aliugua Maya akimuona. Wakawa watu wakutiana moyo.

Maya alikuwa akitokea rehab na kwenda mahakamani, Menson ndiye alikuwa mtu wa karibu yake akimfuatilia kutaka kujua kilichoendelea kiundani huko mahakamani, mbali na taarifa za mitandaoni. Kwani kesi ya Maya wengi waliirusha mitandaoni kutokana na hisia zao juu ya binti huyo. Kwanza sababu ya utajiri wa kwao au umaarufu wa kwao na tabia zake mbaya walizozoea. Wengi walimfuatilia mitandaoni. Kila alipokuwa akitoka mahakamani, Menson alikuwa akimsubiria kujua kilichoendelea huko kwa hakika na kumtia moyo endapo akirudi akiwa amenyongea. Wawili hao wakawa karibu sana.

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

“Mat amesema lazima tupate wimbo mmoja.” “Come on Menson, look at me!” Akamuonyesha Menson vile alivyopendeza. Menson akacheka sana. “Unatunza status?” “Ulijuaje!?” Wakacheka huku wakiingia. Menson amekumbatia mkono wa Maya, akamvuta karibu ubavuni, Maya akajiegemeza kidogo wakawa wanaingia huku wakicheka. Mat na mkewe walipowaona tu wakasimama pale high table, Mat akaanza kucheza style yao ambayo huwa wanacheza wao watatu wakamuingiza na aliyekuwa mchumba wa Mat, ambaye sasa ni mke, ndiye huyo bibi harusi.

Mke wa Mat, Myla alipoona Mat anacheza, na yeye akaanza kucheza. Maya akazidi kucheka. “Maya amesema leo anatunza status!” Menson akamsemea kwa Mat na mkewe. “Come on Maya! Leo ni harusi yetu.” “Kwa sababu sikuja kanisani, nalipiza kwa dance.” Wakaanza kushangilia watatu hao. Menson akaomba Dj awapigie wimbo wao. Hakuna aliyeelewa na haikuwa kwenye ratiba. Wote wanne wakaingia katikati.

Myla akakunja shela yake, wakajipanga nakuanza kucheza. Walicheza huku wakicheka sana, kila mtu akiwatizama wao wanne. Kwanza walifanya wakati tu Maya akiingia na Menson. Ni Maya Cote! Mtoto wa kitajiri, mzuri sana, mwenye kashfa mitandaoni mchana kutwa. Anajulikana na kila mtu, lakini wachache walibahatika kumuona uso kwa uso. Tajiri na mtu maarufu kama Maya akiingia popote, kila mtu anajua. Sasa ameingia kwenye harusi ya watu hao wa kawaida sana, akapokelewa na kucheza.

Wanne hao walicheza ni kama walikuwa wameandaa show yao yakuonyesha watu kumbe hata hawakupanga! Walicheza kwa kupatana vizuri huku wakicheka. Kuna kipindi walitengeneza mduara wa karibu sana na kugonga. Wengi walijiuliza vijana hao wawili, walimfahamuje mtu kama Maya ambaye waliweza kumfanyia utani na kucheza kama vile!

Wimbo wao ulipoisha, ndipo Maya alipowasalimia na kuwapongeza Mat na Myla huku akiwabusu shavuni na kuwakumbatia kwa furaha. “Finally!” Hatimaye! Wote wakajikuta wakiongea kwa pamoja na kucheka. Kwamba wawili wale wameoana. Baaada ya kusubiriana kwa muda mrefu sana,  hatimaye wameoana.

“Samahanini sana. Tumefurahia peke yetu.” Akaongea Mat. “Huu wimbo na aina hii ya uchezaji ni wa Maya. Alipokuwa akija pale tulipokuwa tukiishi akitukuta mimi na Menson tumekaa kizembe na mawazo. Wakati nimepoteza kazi. Mimi na Menson hatujui chakufanya, tumekata tamaa.” Mat akatulia kidogo. “By the way, they were realy broke.” Myla akafanya watu wacheke pale aliposema Mat na shemeji yake kuwa ni kweli walikuwa wameishiwa.  Kidogo Mat akacheka na kuendelea.

“Ni kweli tulikuwa tumeishiwa. Na wote hatukuwa na kazi. Basi Maya alikuwa akija labda kutuletea chakula au kuja kutuona tu, alikuwa anaweka huu wimbo. Mwanzoni alikuwa akicheza peke yake huku tukimwangalia. Mnamjua Maya!” Menson na Myla wao walicheka, kwa kuwa walimfahamu Maya kwa karibu. Si wengine. 

“Akaendelea kucheza yeye peke yake sisi tukimwangalia tu. Ukweli hatukuwa na hamu yakucheza kwa kile kipindi tulikuwa tukipitia. Na hatukuwa na sababu. Mwishoe akanishawishi mimi, mpaka akanifundisha kucheza kama yeye. Tukaja kumfundisha na Menson ndipo akaja Myla. Kwa hiyo kila alipokuwa akija, wote tulikuwa tukicheza ndipo anaondoka. Ilitusaidia sana kupunguza ile hali ya wasiwasi kwetu. Ndio maana leo tuliona tucheze tena.” Wakacheka.

“Nawapenda nyinyi watu!” Akaongea Maya akiwa ameshikiliwa kiunoni na Menson. Ungejua tu hao watu ni marafiki. “Kitu kimoja alituambia Maya.” Myla akataka na yeye kuzungumza. “Mnajua umasikini huwa unakuja na kutokuelewana! Tulifika kipindi mimi na Mat tulitaka kuachana kabisa. Maya alinifuata mimi kazini kwangu.” Wakamuona Myla anaanza kulia na kushindwa kuzungumza kwa muda.

Mumewe akamsugua mgongoni kama kumtuliza. “Nilikuwa sijamuona Mat kama siku tano hivi, ni kama tulijua ndio itakuwa mwisho wetu. Nikashangaa Maya anakuja kazini kwangu. Akaniambia, pesa haiwezi kununua tulicho nacho mimi na Mat.” Myla akajifuta machozi. “Akaniambia akijitolea mfano kuwa, yeye anazo pesa, lakini hana tulicho nacho mimi na Mat, na hata angetaka, hawezi kununua. Na akasema kama ingekuwa inauzwa popote, kwa garama yeyote ile, yeye na wengine wengi wenye uwezo wangenunu.” Watu wakapiga makofi.

Wakajikuta wao watatu. Maya, Myla na Mat wakifuta machozi. “Alinipa mifano mingi, akiniambia nyumba haijengwi na pesa tu, japo ni muhimu, lakini hujengwa na kile tulichonacho mimi na Mat. Akanisihi sana nisikubali kuua tulicho nacho hata kwa garama ya umaskini.” Watu wakapiga tena makofi. “Nakumbuka Maya alipoondoka tu, nikamtafuta Mat, nakumuomba anioe.” Watu wakacheka sana.

“Hata Mat alishangaa.” Myla akaongeza huku akicheka na kufuta machozi. “Lakini kufupisha stori, Maya ni rafiki tuliyeletewa na Menson, amekuwa rafiki wa karibu sana na sisi wote watatu. Anavyosema Mat, ni kweli. Alikuwa akija, lazima tucheze huo wimbo ndipo aondoke. Alikuwa karibu sana na kina Mat, akiwasaidia kifedha na faraja, mpaka Mat na Manson wakapata kazi.” 

“Ndio maana tumefurahi sana kumuona hapa. Ilikuwa asihudhurie harusi yetu kwa kuwa iliingiliana na ratiba zake. Lakini Mungu amemfanikisha na ameweza kuja kushuhudia kile tulichofanikisha.” Mat akaongezea kwa mkewe. “Karibu sana Maya na tumefurahi umekuja.” Akamalizia Menson huku akimtizama Maya aliyekuwa amemshikilia kwa karibu sana wakati Mat na mkewe wakizungumza baada ya kucheza. Maya akawakumbatia tena na kuwabusu wote watatu.

Wakaenda kwenye meza aliyokuwa wamekaa wazazi wa Myla na ndugu zake, wakamtambulisha tena Maya. Maya akawasalimia kwa heshima akiwa karibu sana na Menson. Wote wanne walikuwa wakihama meza moja kwenda ya pili kwa ndugu wa Myla wakisalimia. Menson na Mat hawakuwa na ndugu yeyote siku hiyo. Ndipo Maya akaongezeka. Kwa hiyo Maya ndio akaenda kukaa na Menson kwenye meza  aliyokuwa amekaa Menson tokea mwanzo. Wakaendelea kuzungumza huku wakicheka.

Wawili hao hawakuhitaji kutafuta mazungumzo maalumu yakuongea. Waliongea chochote na kucheka sana. Haikuwa harusi ya watu wengi wala si yakitajiri, lakini akili na mawazo ya Maya yalikuwa kwa Menson, hakuhangaika kuangalia kulia wala kushoto, wakaendelea kunywa na kula.  Na kwa kuwa wote walitoka kwenye ulevi, meza yao ilikuwa ya soda, maji na juisi tu. Hawakuwa wakinywa hata wine.

Muda wa mziki wa taratibu ukafika ambapo maharusi walianza wao kwanza. Akaja Myla na baba yake. Walicheza vizuri sana. Na kweli Myla alipendeza. Wakati Maya anaangalia vile Myla anavyocheza na baba yake katikati ya  ukumbi, baba yake akimzungusha binti yake kwenye ukumbi huo. Waalikwa wakiwafuata kwa macho, na Maya vilevile, Maya akajikuta macho yamegongana na Malcom aliyekuwa amekaa upande wa pili.

Kwanza akahisi ni kama amemfananisha. Akainama kwa muda. Kisha akanyanyua macho na kumtizama tena. Alikuwa Malcom kweli! Akamtizama na watu waliokuwa wamekaa naye meza moja, akamuona na Zoe yupo. Akajua ni kweli ni yeye. Akarudisha macho kwa maharusi. Malcom alikuwa akimwangalia Maya muda wote tokea anaingia. Lakini Maya hakuwa amemuona. Akakumbuka Zoe alimwambia ili awape mtoto, nilazima Malcom atoke naye. Akajua  wapo pale pamoja.

Maya akawatizama tena. Akakuta bado Malcom akimwangalia. Alikuwa amependeza sana. Msafi na suti aliyokuwa amevaa kama alivyoamrishwa na Zoe, nyeusi. Ni kweli alipendeza. Maya akajua ndio maana Zoe alimtaka baba watoto wake avae hivyo. “Umependeza sana.” Akasoma midomo ya Malcom. Maya akarudisha tabasamu. “Asante.” Akashukuru nakuongeza. “Na wewe umependeza.” Maya akamsifia na yeye. Wote wakacheka.

Akili na mawazo ya Malcom na Maya yakahama kabisa pale harusini wakabaki wakiangaliana wao kwa kurudia rudia. Walikaa upande ulitizamana. Kila walipokwepesha macho, wakajikuta wanaangaliana tena. Menson akagundua hata uso wa Maya umebadilika. “Ni nini kinaendelea?” Menson akamuuliza. “Hamna kitu.” Maya akakataa huku akicheka. “Haiwezekani Maya! Mimi nakufahamu. Hukuwa hivyo muda mfupi uliopita. You are blushing!” “No am not!” Akabisha Maya huku akicheka kwa aibu. Wakaanza kunong’ona wawili hao pale mezani, Maya akicheka na kukataa kumwambia juu ya Malcom.

Menson akaona amtege. Akajifanya kama amemwamini na mawazo hayapo tena kwake. Akamuona anarudisha macho upande wa pili  walipokuwa  wamekaa wao. Akamuona mpaka uso wa Maya unabadilika na kuwa na furaha zaidi. Menson akaanza kuchunguza anamwangalia nani upande ule! Akakuta Malcom akimtizama na yeye Maya, wala macho hayapo kwa bibi harusi na baba yake.

“Oooh!” Maya akashituka na kumgeukia Menson. “Nini?” “Sasa hivi najua.” Maya akaanza kucheka. “Huwezi Maya.” “Kwani mimi nimesema nini Menson!” “Nimeona sura yako Maya.” Maya akacheka tena na kuinama. “Huwezi hata kuruhusu moyo wako kumfikiria Malcom.” “Kwa nini?” Maya akauliza taratibu. “Alikuwa mume wa Zoe, Zoe ni mtoto wa mjomba wake Myla. Wana mtoto mmoja anaitwa Ethan. Sitaki kukuona unaumia tena Maya. Achana na Malcom, Zoe hawezi  kuruhusu uwe karibu naye.” “Kwa nini na wakati wameachana!?” Maya akauliza kwa kushangaa.

“Zoe hawezi kuona mwanamke mwingine anamsogelea Malcom kimapenzi akakubali. Na anaamini ipo siku watarudiana tu. Anawaambia hivyo kila mtu na kuwahakikishia lazima aje arudiane na Malcom. Kwanza Zoe ni mwendawazimu. Humuwezi.” Maya akainama kama anayefikiria. “Maya?” “Nahisi nampenda Malcom.” “Come on Maya!” “Kweli Menson. Leo asubuhi nilikuwa naye kwenye kifungua kinywa. Zoe akaja akitaka kufanya fujo. Alikuwa na Ethan.” “Kwa hiyo kumbe unawafahamu?!” Menson akashangaa. “Zoe na Ethan ndio nimekutana nao leo. Ila Roy na Malcom walishakaribia mpaka nyumbani kwa chakula cha usiku.” Menson akamgeukia Maya vizuri. Maya akacheka.

“Hayo yote yanaendelea mimi nikiwa wapi!?” “Hayana muda mrefu Menson. Na  sharti la Zoe kumtoa Ethan awepo kwa kina Roy leo, ilikuwa nilazima Malcom awepo hapa na yeye.” “Na kweli Zoe anamtumia mtoto wao kama fimbo kwa Malcom.” Maya akanyamaza.

“Nikushauri kitu Maya? Japo nahisi nimechelewa.” Maya akamwangalia. “Kama kunauwezekano na haujafika mbali, achana na Malcom.” “Nahisi nimechelewa Menson. Hata mimi nilijiambia hivyohivyo kuwa sitaweza fujo za Zoe na kashfa nyingine mtandaoni.” Maya akamwangalia tena Malcom. “Lakini..” Maya akasita na kunyamaza. Wakasikia watu wanapiga makofi. Wakajua Myla amemaliza kucheza na baba yake. Wao walizama kwenye mazungumzo.

Mc akaruhusu watu wengine waingie na kucheza. Wakamuona Zoe na Malcom nao wanasimama kwenda kucheza. Ilikuwa karibu na mwisho.  Maya akamvuta Menson.  Akainama. “Mimi naomba niondoke.” Menson akamwangalia kidogo. Maya alikuwa amebadilika usoni. Ile furaha iliisha gafla, akapooza. “Nina zawadi hii ya Mat, nataka kumkabidhi kabla sijaondoka.” Ilikuwa bahasha.  “Sikupata muda wa kuzunguka madukani kuwanunulia zawadi. Kumekuwa na mambo mengi.” “Pole kwa matatizo Maya.” Maya akatoa tu tabasamu, kwa sababu ni kweli bado walikuwa kwenye mataatizo.

~~~~~~~~~~~~~~~~~~

Waliohusika kumteka wifi yake walitangazwa kuwa wawili wameuwawa na hawajui walikuwa wahusika wangapi. Kwa hiyo inamaana  bado walikuwa hatarini. Na harusi ya kaka yake ndio ilikuwa imevuma, ilikuwa ifanyike siku hiyo, haikufanyika. Picha za kaka yake akifanya ngono bado zilikuwa zimeenea mtandaoni. Kashfa ya Vic kumvamia Tunda nyumbani bado ilikuwa habari moto kabisa maredioni. Mambo ya juma hilohilo!

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

Wakasimama kumsogelea Mat aliyekuwa akicheza na mkewe. Maya akamuwekea ile bahasha kwenye mfuko wa suti. “Nilishindwa kwenda madukani.” “Naelewa kabisa Maya. Hata hukutakiwa kuleta zawadi. Kufika kwako hapa ni zawadi tosha.” Maya akambusu Mat. “You are sweet, Mat.” Wakacheka. Lakini Maya huyu alishabadilika, sio kama alivyoingia. Wivu ulishamuingia kumuona Malcom amemkumbatia Zoe.

Akambusu na Myla. “Muwe na wakati mzuri mapumzikoni.” “Unaondoka?” “Tuna mtoto mchanga, nataka nimuwahi kabla hapajawa usiku sana.” “Naelewa. Asante kwa kuja.”   Akambusu Myla shavuni tena. Akamgeukia Menson. Akamuona Malcom akiendelea kucheza na Zoe mziki huo wa taratibu, mbali kidogo na pale walipokuwa wamesimama. Akasikia kuumia. Walishikana kama wapenzi haswa.

Akiwa ameshangaa na Menson akimwangalia tu, macho yakagongana na Malcom, Maya akakwepesha yake na kurudisha kwa Menson.  Kweli Maya alibadilika. “Mimi nipo tayari kuondoka. Naomba unisindikize mpaka nje.” Maya akaongea kwa kunyong’onyea, Menson akajua kinachoendelea kwa Maya. “Huwezi kuondoka hivyo. Tucheze kidogo.” Kabla Maya hajajibu, Menson akamvuta karibu. Akamshika vizuri, na wao wakaanza kucheza mziki huo wa taratibu.

Wakati wanacheza mziki huo wa taratibu, Maya amejiegemeza kwa Menson, akasikia mtu anamgusa begani. Akageuka. “Malcom!” Maya akashituka, hakutegemea. “Naomba tucheze wote.” “Na..?” Maya akasita. “Wewe niangalie mimi tu.” Malcom akamwambia kwa utulivua. Maya akashangaa kidogo kama anayejishauri mbele ya Menson na Malcom aliyekuwa amebaki amenyoosha mkono akitaka Maya amshike.

Mwishoe Maya akajitoa kwa Menson, akanyoosha mkono wake mpaka akaufikia ule mkono wa Malcom. Malcom akamvuta karibu haswa. Akamkumbatia. Maya akajisahau, akapitisha mikono yote juu ya shingo ya Malcom, akamkumbatia kwa huba. Si kama vile alivyokuwa na Menson. Aliweka mkono kwenye bega tu wakaendelea kucheza. Hapa kwa Malcom alimkumbatia na kujilaza karibu kabisa ya shingo. Malcom aliweza kuzipata sawia pumzi zake shingoni kwake na yeye akajilaza kichwa chake juu yake.

Wakazunguka kidogo. Maya akatoa uso shingoni kwa Malcom.  “Itakuaje sasa juu ya Zoe? Si atakasirika sana!” Maya akauliza taratibu wakati bado wanacheza na wamekumbatiana. “Sio kwa hiki, ila kwa ambacho nakaribia kukifanya.” Maya akawa hajaelewa. “Nini?” Maya akamuuliza huku wakiangaliana machoni na kuendelea kucheza taratibu. “Nataka kukubusu Maya.” “Hapa hapa!?” Maya akaingiwa na wasiwasi. “Sasa hivi.” “Na Ethan?” Maya akauliza akijua nilazima Zoe atamuadhibu.

“Sijui Maya! Ila ninachojua nakupenda wewe na sasa hivi nataka kukubusu wewe. Naruhusiwa?” “Ningefurahi Malcom.” Hapohapo Malcom akamsogeza karibu kabisa, mkono wa kushoto akaupitisha chini ya kichwa cha Maya, akawa ni kama amekilaza kichwa chake kwenye kona ya kiwiko cha mkono wake huo wa kushoto, mkono wa kulia akamshika shingo chini kidogo ya sikio, na kuanza kupata busu. Pale pale mbele ya umati.

Vile alivyoshikwa Maya, ungejua anapendwa. Alijaa mikononi kwa Malcom akavutwa kwa karibu na kukumbatiwa kama mtoto mdogo anayeepushwa na baridi au anayenyonyeshwa kwa mapenzi mazito na mama yake. Maya alitulia hapo, akaendelea kusikilizia lile busu bila kujali kashfa itakayomkabili baada ya kumaliza hapo. Na yeye Malcom hakujali anamtizamaje Zoe baada ya hapo. Alijiambia atajua yote baada ya hapo. Alimbusu kwa hisia zote, huku mziki wa taratibu ukiendelea kupigwa na wengine wakiendelea kucheza taratibu huku wakishuhudia kimwana huyo akipewa busu na Malcom aliyekuja na Zoe.

Halikuwa busu la sekunde chache. Malcom alihakikisha busu lake la kwanza kwa Maya, linabeba historia na hata kama ataadhibiwa baada ya hapo, iwe kwa haki. Akamtendea haki Maya, akamshika vizuri, kwa heshima, akaendelea kupata busu la mrembo huyo. Malcom anamaliza lile busu, wakakuta ukumbi mzima unawashangaa wao kwani mziki ulishaisha muda tu. Maya akarudisha macho kwa Malcom. Bila kupoteza sekunde, akamshika mkono na kutoka naye pale ukumbini.

Walikuta dereva wa Cote ameshasogeza gari mlangoni. Akasogea mtu na kufungua mlango. Maya akajua ndio mlinzi aliyekuwa hapo akimlinda. Hata hakuwa amemuona. Akaingia bila hata kumuaga Malcom, dereva akaondoa gari.

Wakati yupo njiani akasikia simu inaita kwenye spika ya gari, dereva akapokea. Akajibu kwa kifupi tu, “Nipo naye hapa. Ndio tunarudi nyumbani.” Simu ikakatwa,  Maya akajua ni bibi yake na habari zilishamfikia. Hakujali. Akajiegemeza vizuri, akashika midomo yake, akailamba na kucheka, kisha akaanza kupitisha kidole kwenye midomo yake taratibu huku akikumbuka vile alivyoshikwa na Malcom. Jinsi alivyombusu. Harufu nzuri ya midomo aliyokuwa akiipata wakati Malcom akimbusu. Maya akaendelea kuvuta kumbukumbu za furaha.

Geti lilifunguka mara tu walipokaribia wala hawakusimama getini. Akafunguliwa mlango walipofika akashuka. Ilikuwa ni mwendo kama wa nusu saa huko alipokwenda kwenye harusi na nyumbani kwao.

Alifunguliwa mlango na Carter. Kwa mtazamo tu ule wa Carter akajua anasubiriwa ndani. Maya akasimama pale mbele ya Carter kama anayesita kuingia ndani. “Nampenda Malcom.” Akamwambia Carter kama anayetaka kulia. Carter akambusu kichwani. Maya akaelekea sebuleni alijua kwa kutoongea Carter, bibi yake anamsubiria sebuleni. Hakumkuta tu bibi yake. Alimkuta na Net pamoja na Tunda. Akabaki amesimama.

“Kweli Maya!?” Net akamuuliza kwa ukali kidogo kama anayemshangaa. “Yaani katika siku zote. Na yote yanayoendelea katika familia,  na wewe ndio umeamua kuongeza jingine!” Net akaongea kwa kushangaa kidogo. “Nampenda Malcom, Net.  Nimeamua kuwa naye. Mengine  nitajua baadaye.” Maya akaanza kulia. “Nimekataa mama kuendelea kututesa Net. Maisha yetu hayawezi kuendelea kusimama kwa ajili yake.” Maya akaendelea kulia.

“Hatuwezi kukosa kila kitu kwa ajili yake. Ona wewe. Ulitakiwa uwe umeona leo. Lakini amekufanya hujao na hujui ni lini utaoa tena. Kama isingekuwa Mungu, sasa hivi tusingekuwa na Tunda hapa. Mama anataka kutupokonya kila kitu, Net. Mimi sikubali kuendelea kufanywa mtumwa wake.” Maya akaendelea kujitetea.

“Nampenda Malcom. Sijakosea. Na nimeamua kuwa naye leo kwa kuwa sijui kama kesho nitakuwa hapa au mama atatuma mtu aje anichukue na mimi! Siwezi kuendelea kusubiri Net. Kama wewe na Tunda mnaendelea kumsubiri yeye, hiyo ni juu yenu. Lakini mimi sisubiri.” Hasira zikazidi kumpanda Maya.

“Aliniacha hapa mdogo sana bila kunilea au hata kujali nakuaje!  Jana Tunda anamlilia mtoto wake pale hospitalini mpaka mimi roho ikaniuma! Kwa nini na sisi mama hakutulilia? Tunda amefanyiwa operation, hataki mtu amguse mtoto wake, anahangaika naye yeye mwenyewe! Kwa nini sisi mama hakutaka hata kuwa karibu na sisi, Net?” Maya akazidi kulia kwa hasira. 

“Ametuacha tumelelewa na watu baki bila kujali mimi nitakuwa vipi! Nimekua peke yangu kwenye hili jumba wakati nyinyi wote mpo na yeye akiwepo! Nimecheza na Carter mpaka nimekuwa mkubwa na kuweza kutoka kwenda kutafuta watu wa kuwa na mimi huko nje. Matokeo yake wote mmeyajua!”

“Leo Malcom anaonyesha kunihitaji. Ameonyesha hadharani amenichagua mimi mwenye sifa mbaya. Mbele ya Zoe aliyenitusi vibaya sana asubuhi ya leo mbele yao. Amenichagua mbali na mtoto wake! Hakufanya kwa bahati mbaya! Malcom ametangaza kunichagua mimi kwanza akijua wazi anajiingiza matatizoni. Anajiabisha, lakini amenichagua mimi. Halafu eti mimi leo niachie bahati kama hiyo, sababu yakutunza sifa ipi ambayo bado tunataka kung’ang’ania hapa?” Maya alikuwa akiongea na yeye kwa hasira na ukali.

“Sisi tunateseka na kujinyima wakati mama yeye anafurahia lengo lake limetimia kwetu. Ameshajinufaisha na pesa za Cote kutuuza sisi kama bidhaa. Haya, na kwako wewe Net sasa hivi amefanikisha kutokuoa kwako. Ukute sasa hivi hata amefungua champagne anajipongeza kwa kazi nzuri aliyofanya. Anakunywa na kufurahia kinachokutokea wewe na Cote. Hajali furaha yetu Net. Ameanza na sisi, sasa hivi ameingia hata kwa CJ huyo mtoto wako. Hajawahi kuacha na ataendelea tu. Tunasubiri mpaka lini?”

“Mimi nimekataa kuwa kama wewe. Nataka kuwa nafuraha Net. Hata kama ni ya muda mfupi, sijali. Naombeni mniache nifurahie kwa kuwa hatujui anampango gani ya kesho. Wakati wote mwenzenu nimekuwa nikitafuta kuhitajiwa na kupendwa, na ndio maana niliishia kwa watu wabaya. Na Malcom anaonekana ananipenda mimi. Halafu mnataka nikatae!?” Maya aliwafunga wote mdomo wakabaki kimya. Akashangaa Net anamsogelea na kumkumbatia. “Nampenda Malcom, Net. Na yeye ananipenda sana. Leo amenichagua hadharani!” “Okay.” Maya akashituka sana. Akajitoa pale mikononi.

“Umesema okay!?” Akamuuliza kaka yake na uso uliojaa machozi. “Si umesema unampenda?” “Nampenda sana. Siwezi kupata mtu anayeniangalia kama Malcom, tena baada ya uchafu wote huo! Na mimi nimepata mtu anayeniangalia kama hivyo wewe unavyomwangalia Tunda, Net.” “Okay.” Net akaitika hivyo tena bila maneno mengi.

Maya akafurahi sana, akatoka pale kwa Net na kumsogelea bibi yake akamuona anatabasamu. “He kissed me!” Akamwambia bibi yake vile Malcom alivyombusu huku akifuta machozi. “Hilo busu limeshaenea kila mahali.” “Sijali Nana. Nampenda Malcom.” “Am happy for you sweetheart.” Tunda alikuwa akicheka taratibu. Akamkumbatia bibi yake palepale alipokuwa amekaa kwenye kiti chake.

Wakatulia kwa muda. Maya akasimama. “Samahani Net.” “Hapana. Upo sahihi Maya. Kama inawezekana, inatakiwa maisha yetu yaendelee tu. Umeongea ukweli. Kama umebahatika ulichokuwa ukikitafuta. Usisubiri. Nitakuwa na wewe na mimi nitakuunga mkono.” Maya akarudi kwa kaka yake akakumbatia. “Asante Net. You are the best brother in the whole wide world.” Wakacheka.

Hapo ndipo Maya akapata jukwaa la kuwasimulia kwa mbembwe kuanzia alipokuwa akicheza na Menson mpaka alipokuja Malcom. “Kwani wewe ulijua kama atakuwepo?” Tunda akauliza. “Hata sikuwa na taarifa. Ila asubuhi  wakati tulipokuwa tunapata kifungua kinywa,...” Maya akasimulia kila kitu juu ya Zoe, Ethan, Malcom na Roy. Wakabaki wanashangaa.

“Sasa kwa nini?!” “Menson ameniambia anamtumia mtoto wao kama fimbo kwa Malcom na pia kama njia ya warudiane. Najua kesho lazima Malcom atakuwa matatizoni tu.” Maya akaongea kwa  kumuhurumia Malcom. “Na yeye anajua. Nilimuuliza hata kabla hajanipa busu.” Wakamuona anacheka na kushika midomo. Wote wakacheka. “Maya!” “Ni mzuri huyo, Tunda. Kwani wewe hukumwangalia vizuri?” “Nimemuona.” Tunda akajibu huku akicheka. “Sasa je!” Maya akajisifia. “Basi nilipomkumbusha juu ya Ethan na kile atakachofanyiwa na Zoe, kwa kuniomba nicheze naye, unajua aliniambia nini?” Bibi yake akacheka.

“Nitamwambia Tunda baadaye, sasa hivi Net yupo. Naona aibu.” “Video yako kuanzia  unaanza kucheza na Menson, unapewa mabusu na Malcom mpaka unatolewa ukumbini ukiwa umeshikwa mkono na huyohuyo Malcom, huyo kaka yako ameiona. Ni vile maneno yalikuwa hayasikiki, ila pia mlionekana mnaongea kabla ya busu.” Maya akajifunika na mto usoni huku akicheka.

“Malcom ananipenda mimi.” Maya aliongea huku amejifunika mto usoni. Wote wakacheka. “Ni kweli anaonekana anakupenda. Kitendo cha kukubusu pale. Wakati ule ambao hata wazazi wa Zoe pia walikuwepo, aliamua haswa.” Maya akashituka mpaka akatupa mto. “Nana!” Maya akashangaa. “Kwani wewe hukujua kama Myla na Zoe ni ndugu?” “Hapana Nana! Nimekuja kujua leo pale ukumbini. Na sikujua kama wazazi wa Zoe wapo! Mimi nilitambulishwa kwa wazazi wa Myla tu. Wewe habari zao umezijuaje?” “Nimekwambia macho na masikio yangu vyote vipo kwako sasa hivi. Na nilikuahidi kwa kila uamuzi utakaochukua nitakuwa na wewe.”

“Sasa mbona umeacha Net akanigombesha?” Maya aliongea kwa kulalamika. “Yeye ananafasi yake kama kaka na mimi kama Nana. Haviingiliani.” Maya akacheka huku akimsogelea bibi yake. “Sasa itakuaje?” Akamuuliza bibi yake. “Kwa kuwa sasa hivi umeamua. Na naona umekubaliana na kaka yako. Tunaanza juu ya Malcom na Ethan kwanza. Tutahakikisha Malcom anapata mwanasheria mzuri ambaye atamtetea na kupata haki ya kuwa na mtoto wake.” “Yes.” Maya akafurahi sana.

“Ili isijeonekana kama wewe umeua mahusiano kati yake na mtoto wake. Tumsubiri kesho atakapoenda kumshitaki, ili sasa tuweke utetezi mzuri. Safari hii Malcom atashauriwa asikimbilie kujitetea, ila mwanasheria kudai haki ya Malcom kwa mtoto wake. Apangiwe siku za kuwa na mtoto wake ambazo zitasimamiwa na mahakama.” Bibi Cote akaendelea.

“Akipewa masaa 24, lazima yawe 24 na Malcom ayatumie atakavyo bila Zoe kuingilia.” Maya akaenda kumbusu bibi yake. “Asante Nana. You are the best.” “I know.” Bibi Cote akajivunia akisema anajua kama yeye ni bora, nakufanya wote wacheke.

Wakaweka mikakati ambayo mingi ilishindwa kufika mwisho, kwa kuwa wote hawakujua hatima yao ipoje! Ritha anafikiri na kupanga nini! Huo ukabaki mtihani uliomuumiza zaidi bibi Cote, kuona Ritha, mwanamke mweusi, anaweza kuwazidi wazungu hao na heshima zao, ujuzi wao, amemudu kuwazidi mahesabu kwa kiasi hicho! Amefanikiwa kusimamisha harusi ya Net! Vizuri na kirahisi tu. Vic aliyemtumia kijanja, na yeye ameishia jela kama Bethy. Yeye hajaguswa!

Alimteka nyara Tunda, katikati ya ulinzi alioweka yeye mwenyewe bibi Cote! Kwake ilikuwa ni kumfedhehesha kwa hali ya juu. Ni kama alimuhakikishia, anaweza kufika popote anapotaka. Na yeye bibi Cote si kitu kwake, amemzidi mahesabu. Napo hapo akaishia kufa Malinda na mdogo wake, kama vile Gabriel. Yeye yu hai, maisha yake yanaendelea swafi mtaani akiwa na kazi nzuri tu.

Mpaka siku hiyo ya jumamosi wanakwenda kulala, siku ambayo ilitakiwa Net awe ameshaoa yupo fungate na mkewe, wameishia hapo na majonzi, hawakuwa na ushahidi wauhakika wa kumkamata yeye Ritha. Kwamba Ritha anayo akili kumzidi yeye bibi Cote anayevuma mitandaoni na kusikika na mipango mizito, lakini inamaana Ritha amemzidi mbali sana. Anajua kujipanga vizuri katika njama zake kuliko yeye bibi Cote katika mipango yake ya kifahari.

Ilikuwa ikimuuma sana bibi Cote kila alipokuwa akimfikiria Ritha ambaye maisha yake yalikuwa yakiendelea kama kawaida. Kwa uhuru wote, wakati wao wamefungiwa ndani, hawawezi hata kwenda kazini kwa hofu. Hawajui nani ni mbaya wao. Nani anatumiwa na Ritha! Wakabaki wao na pesa zao ndio kuwa wafungwa ndani ya hekalu lao, na askari wakiwalinda nje.

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

 Usikose Muendelezo wa Simulizi hii ili kujua kilichoendelea kwa familia hiyo ya Cote inayozungukwa na mikasa mizito kila kukicha na yote inabidi bibi Cote aitafutie ufumbuzi.

Ø  Malcom naye yuko ataponaje usiku huo baada ya alichokifanya kwa mama watoto wake?

Ø  Je safari hii Maya atafanikiwa kupata alichokuwa akikitafuta maishani?

Ø  Hatima ya Tunda & Net!

Ø  Hatima ya Ritha nayo ni ipi!?

 

 

USIPITWE vyooote vipo mbeleni.


CONVERSATION

0 Comments:

Post a Comment