Naomi Simulizi |+1 205 767 8163 |naomisimulizi@gmail.com Nilipotea! – Sehemu ya 52. - Naomi Simulizi

Nilipotea! – Sehemu ya 52.

Usiku  huo wakati kina Cote wamelala wakionekana kushindwa kwa hali ya juu. Harusi kubwa ambayo ilikuwa imetangazwa na watu wa maana walikuwa wameshaalikwa, kushindwa kufanyika na kubakiwa na hofu tupu, wakijiwinda kwa hali na mali, maisha ya Ritha yaliendelea kwa furaha zote. Kwa mara nyingine tena, akaibuka mshindi. Hana hatia. Hana alipoguswa na sheria. Aliowahusisha kwenye njama zake wapo chumba cha maiti na wengine kifungoni. Hapo ni mpaka kina Cote waliokuwa wakizungukwa na askari masaa 24 na kushindwa kwenda kila watakapo, waligeuka wafungwa wa Ritha. Kilikuwa ni kama kifungo tu cha nje, ila kiukweli hawakuwa na tofauti na Vic na Bethy waliokuwepo jela bila kuhukumiwa. Hata wao kina Cote walilijua hilo, kuwa Ritha amefanikiwa kuwapa kifungo cha nje.

Wakati kina Cote wakiwa wanazungukwa na ulinzi mkali na wa waziwazi, ikawa hivyo hivyo na kwa Ritha ila asijue. Kwake ilikuwa tofauti. Bado polisi na askari wa CSIS walikuwa mbele ya jengo hilo kubwa alilokuwa amepangisha apartment ila usingeweza kuwatambua kama ni askari. Walionekana kama raia tu. Lakini wakimfuatilia Ritha kwa karibu sana. Kila alipotoka, alifuatwa nyuma bila yeye kujua.

Gari yake yenyewe ilishachomekwa kitu ambacho kilionyesha kwenye mitandao ya CSIS, kila alipo na anapokwenda. Lengo kubwa ni kujua kama atatoka kwenda kukutana na Jeff, ili wawakamate wakiwa pamoja. Askari wa hao walishamuona Jeff amefika kwenye mji anaoishi Ritha mapema tu siku hiyo ya jumamosi. Wakaendelea kumfuatilia na kujua ni nini anafanya mjini hapo bila kumpoteza hata dakika moja.

Alikwenda mpaka kwenye jengo hilo analoishi Ritha. Akagundua kuna ugumu wakuingia humo. Huwezi kuingia tu mpaka mtu wa ndani unayekwenda kwake, akufungulie. Akaona wengine wanafika hapo, wanabonyeza namba ya apartment ya mwenyeji, wanazungumza kwa spika, kisha mtu wa ndani kama anamkubali ndipo anamfungulia akiwa hukohuko kwenye apartment yake.

Na kulikuwa na askari pia. Kwa hiyo usingeweza tu kupita na mgeni yeyote, kwani askari alikuwepo hapo kuhakikisha umekaribishwa na mtu wa ndani. Jeff akajaribu kuingia hapo na wengine, karibu siku nzima, akashindwa. Namba ya apartment anapoishi Ritha alishaijua, lakini shida ikawa kufunguliwa na kuingia ndani.

Siku ya Ritha ilianza na kuendelea kama kawaida. Kwa upande wake akiwa na furaha kuwa jumamosi hiyo ilikuwa harusi ya mwanae na Tunda, amefanikiwa kuivunja tena kwa kishindo kikubwa tu. Akawatikisa kina Cote na afisa usalama hapo nchini vyakutosha tu. Na yeye alikuwa miongoni mwa mamilioni ya watu waliokuwa wakifuatilia kwenye vyombo vya habari tokea Tunda anaanguka mbele ya Vic mpaka kutekwa.

Walimuona Ritha akielekea kufanyiwa manicure na pedicure, kisha akafanyiwa masaji ya lisaa. Baada ya hapo akarudi nyumbani.  Baada ya muda wakutosha tu, wakamuona anatoka tena akiwa amependeza sana.  Wakaendelea kumfuatilia wakaona amekwenda kupata chakula cha jioni sehemu nzuri sana tena ya pesa nyingi, kama anaye sheherekea jambo. Kwa muonekano wake, usingejua ni Ritha, mtanzania. Alijawa ujasiri, akajibeba kishujaa, hata tembea yake ungejua ni mshindi.

Baada ya chakula hicho alichokula kwenye hoteli hiyo ya kifahari sana hapo mjini, wakamuona anarudi nyumbani kwake. Ritha alipishana na kuhudumiwa na watu tofauti tofauti asijue kama ni askari waliovaa nguo za kiraia. Hata askari wa jengo lao aliyeingia mida ya jioni hiyo na kusalimiana naye wakati anarudi kwa chakula cha jioni, pia alikuwa ni afisa wa CSIS aliwekwa hapo makusudi kwa muda kama mlinzi wa hilo jengo kwa kumfuatilia yeye Ritha.

Mfagizi aliyekuwa akisafisha gorofa yao ya juu kabisa na kwenda kumgongea kumuomba takataka mchana aliporudi tu kutoka kutengeneza mwili wake, pia alikuwa ni afisa wa CSIS. Jengo zima lilizungukwa na afisa wa CSIS kuanzia ndani mpaka nje, wakifanya kazi tofauti tofauti, wengine kama ombaomba tu wa mtaani, ilimradi kuhakikisha hakuna linaloharibika na wote wanakamatwa wakiwa hai.

Baada ya juhudi za kuingia kwa Ritha kugonga mwamba, Jeff aliondoka, wakamuona amerudi tena, safari hii akiwa amevalia nguo za kiaskari kabisa, kama polisi. Ilishakuwa imetimu saa tatu usiku.  Askari wa kawaida tu wa hilo jengo, aliyekuwepo hapo ambaye alikuwa ni afisa wa CSIS, akamsalimia kawaida tu, Jeff akaitika na kumdanganya yeye ni polisi wa mji wa karibu na pale. Bila shida yule afisa wa CSIS aliyejidai ni askari au mlinzi pale, akamtania kidogo, Jeff akabonyeza namba ya Ritha, Ritha akasikika kwenye spika.

“Nikusaidie nini?” Ritha akamuuliza. Jeff akajitambulisha kama yeye ni polisi, anataka kumuhoji maswali machache kutokana na tukio la kina Cote. Ritha kwa kujiamini sana, akamkatalia na kumwambia azungumze palepale, anamsikia ameshachoshwa na maswali ya kijinga.

Aliposhindwa kuingia, yule askari wa CSIS akamtania kidogo, kuwa watu huwa wanakimbia polisi bila sababu. Jeff akamuomba kama anaweza kumruhusu aingie. “Lakini usije kunitaja.” Yule afisa akajidai kama anamuonya Jeff. “Kwanza hata sikufahamu wala sijakuona.” Wakacheka kidogo, akamfungulia mlango mkubwa wakumwingiza ndani. Akamfungulia tena mpaka lift yakumpandisha anakoishi Ritha, Jeff akamshukuru sana,  na kuingia ndani ya lift.

Jeff alipoingia tu kwenye lift, afisa wa CSIS wakaanza kumiminika hapo ndani ya jengo kama nyuki. “Show time! Show time!” Kila mmoja akahamasika, wakijua muda waliokuwa wakiusubiria kwa hamu umefika.

Jeff alipanda mpaka gorofa la mwisho kabisa ambako alikuwa akiishi Ritha kwa kutumia lift huku askari wengine wakipanda kwa kukimbia, wakitumia ngazi.  Alipotoka tu kwenye lift, Jeff akakutana na yule mfagizi wa jengo akiwa na vifaa vyake vya usafi, akijidai kufuta vumbi na kupangusa vioo. Akamsalimia asijue na yeye ni afisa wa CSIS pia.

Akafika mlangoni kwa Ritha, akagonga na kujificha pembeni ili akichungulia kwenye tundu la mlango, asimuone. “Ni nani?” Ritha akauliza. “Housekeeping!” Jeff akadanganya kuwa ni mtu wa usafi. “Sina takataka walisha...” Ritha akawa anamjibu huku anafungua mlango. Hapo hapo Jeff akamsukumia ndani na kufunga mlango.

Alimvuta mpaka sebuleni na kumuweka kwenye kochi. “Kaa vizuri, tuzungumze. Sipo hapa kukudhuru.” Akaanza Jeff na kuendelea. “Labda nianze kwa kujitambulisha kwa kuwa ulikuwa ukikutana na Malinda tu. Naitwa Jeff. Ndiye niliyekuwa mtekelezaji wa kile ulichokuwa ukipanga na Malinda.” “Mimi sijui unazungumza nini?” Ritha akakataa. Jeff akatoa kofia.

“Labda nianze upya.” Jeff akatoa kofia, nakukaa mbele yake. “Mimi naitwa Jeff. Sio polisi kama unavyoniona. Hii ni sare tu ili kuweza kuingia humu. Na hii ni risasi niliyotumia kwa Malinda na mdogo wake. Nasisitiza, sio lazima nikaitumia kwako labda unilazimishe. Sijui kama unanielewa?” Jeff akauliza. Hofu ikamwingia Ritha. Maafisa wa usalama walikuwa wakiwasikiliza tu.

“Nipo hapa kupata haki yangu. Sipo kukudhuru.” Jeff akaweka msisitizo. “Kwa hiyo wewe ndiye uliyewaua kina Malinda?” Ritha akauliza. “Narudia. Sipo hapa kukudhuru wewe. Wao ilinilazimu kuwaua ili kufupisha malumbano na safari yakupata pesa yangu. Kwa hiyo, kama ulivyokubaliana na Malinda. Ulimlipa pesa kiasi kama kianzio cha kazi uliyompa kumtorosha Mrs Cote, halafu zingine uliahidi kulipa tutakapo kamilisha kazi nzima.” Jeff aliongea taratibu tu.

“Sasa kama wewe unajua malipo yote ni mpaka kazi itakapo kamilika, yuko wapi huyo Mrs Cote?” Akajikaza kuuliza Ritha. Alikuwa akitetemeka kwa hofu. “Kazi ilikuwa nikumteka nyara Mrs Cote. Tulimtoa pale bila shida. Kazi yetu ilikamilika, ila wewe hukutokea. Ninachotaka ni pesa yote ya kazi kama tulivyokubaliana.” Akaendelea Jeff taratibu tu.

“Mimi sikujui. Ndio nakuona hapa leo. Sijawahi kupanga chochote na wewe. Naomba uondoke.” Ritha akasimama. Jeff alimrukia, akamshika kwa haraka kabla hajafika mlangoni. Akampiga kichwa cha nguvu kichwani, Ritha akaanguka sakafuni. Akampiga mateke ya mfululizo mbavuni. Kisha akamvuta kutoka pale sakafuni alipokuwa akivuja damu, mpaka kwenye kiti cha sehemu yakulia chakula. Ritha alikuwa akilia, damu za puani na kwenye kipanda uso alipochanwa baada ya kupigwa kichwa, zikaendelea kuchirizika usoni, asiamini kama ni damu na si machozi na kamasi. Hofu ikazidi kumuingia akijua kilichompata Malinda na mdogo wake, ndicho kimemfikia na yeye.

Jeff akampiga tena begani na kitako cha bastola. “Tafadhali usitoe sauti. Nitakuumiza zaidi.” CSIS wa mpaka ofisini walikuwa wakifuatilia mazungumzo yao yote. Walimsikia Ritha akilia kwa maumivu makali, na baadhi ya maafisa walikuwa hapo nje ya mlango tayari, lakini amri kutoka makao makuu ilikuwa wasiingie mpaka wapate ukiri wa uhakika kutoka kwa Ritha, ndipo wataruhusiwa kuingia.

Mpaka hapo Ritha hakuwa bado amekiri chochote. Kwa hiyo hawakuwa wamepata amri yakuingia, hata kwa kilio na kitisho cha namna gani, wale maafisa wasingeweza kuingia mpaka kwa amri. Ritha akawa anajitahidi kupunguza sauti kwa hofu ya kipigo kingine, lakini aliendelea kugugumia maumivu, akabaki akifuta machozi na damu.

“Nimekwambia sipo hapa kukudhuru. Ninarudia tena, nimekuja kwa amani kudai haki yangu. Tafadhali usitake nikuumize zaidi. Kama nimemuua Malinda mpenzi wangu na mdogo wake, watu ninaowafahamu unafikiri nitakufanya nini wewe?” Akampiga tena kwa nguvu begani. “Ni kweli hukuzungumza na mimi. Lakini kama utakumbuka Malinda alikwambia tupo watatu anataka malipo ya watu watatu. Kazi yakumteka nyara Mrs Cote haikuwa ya mtu mmoja! Na wewe unajua. Nimewatoa kina Malinda, ili kufupisha mambo. Nipe pesa yangu, niondoke na ninakuahidi hutakaa unione tena.” Akaendelea Jeff huku Ritha akilia taratibu kwa kugugumia.

“Ritha? Naomba pesa yangu. Na kama huna hiyo dola elfu 85 yote iliyobaki kwa taslimu, nihamishie kwenye akaunti ambayo hakuna mtu atajua, kama alivyokuahidi Malinda. Tulishaiandaa hiyo akaunti. Mdogo wake aliitengeneza kwa umakaninifu sana, hata watu wa usalama hawatajua. Naomba pesa yangu.” Akasisitiza Jeff akimpiga piga mgongoni.

“Kwanza hiyo pesa uliyoitaja siyo niliyokubaliana na Malinda. Tulikubaliana elfu 20 tu kwa kazi nzima. Ndio maana nilimpa elfu 5, nikamwambia akinipa Tunda, namalizia 15.” Jeff akaanza kucheka. “Kama unafikiri utanizidi ujanja katika hili, fikiria mara mbili. Mimi si mjinga wakuweza kumuua Malinda kwa sababu ya elfu 15 tu! Nataka pesa yangu na ninaitaka sasa hivi. Unaweka wapi kompyuta yako unihamishie pesa yangu au lete simu yako unihamishie pesa yangu sasa hivi.” Ritha akasimama.

“Unakwenda wapi?” “Kufuata simu ili nikuhamishie hiyo pesa yako! Unafikiri nitahamishaje sasa?” “Nakuonya Ritha, usifanye chochote kile, nitakuumiza. Chukua simu kwa ajili yakunihamishia pesa tu.” Ritha akaondoka pale sehemu yakulia chakula, akichechemea na kutema damu akielekea sebuleni alipoacha simu yake.

Jeff alibaki palepale akimtizama kwa makini sana. Aliiacha kwenye kochi. Wakati anaichukua, akabonyeza kwa makini 911, kuita polisi. Kama wasiwasi ukamwingia Jeff akasogea pale kwa haraka. Wakati Ritha anabonyeza tu sehemu yakupiga, Jeff akawa ameshafika. Jeff akaona. Akaiwahi kabla hata haijapokelewa na watu wa 911. Akaizima kwa haraka, wakati amezama kwenye simu, Ritha akawahi urembo wa meza ndogo ya hapohapo mezani, akaunyakua na kumpiga nao Jeff, akakwepesha kichwa chake kwa haraka, akakinga kwa mkono nakumpiga teke Ritha. Alipoanguka akampiga risasi ikampata ya mkono. Hapo hapo askari wa CSIS wakavamia ule mlango, ukaanguka pembeni ya Ritha.

Maana amri ilikuwa ni kuwakamata wote wawili wakiwa hai. Zaidi Ritha akiwa ameshakiri. Na kwa kuwa alishakubali mpaka na kiasi alichokuwa amekubaliana na Malinda, ikabaki uokoaji tu. Waliingia wengine wakamuwahi Jeff. Wakamfunga pingu na kuichukua ile risasi kama ushahidi. Maana ndiyo aliyokiri kuwa ndiyo aliyotumia kumuulia nayo Malinda na mdogo wake, ikachukuliwa kwenda kupimwa.

 Ritha aliokotwa pale sakafuni akilia kama mtoto huku akivuja damu. Watu wa huduma ya kwanza nao walikuwa tayari. Wakamchukua na kumkimbiza hospitalini baada yakumpa huduma ya kwanza.

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

Wakati bibi Cote anapitiwa na usingizi, simu ya Mike ikaingia. Akawasha taa ndogo ya mezani, akapokea. “Unahabari njema?” “Ritha amekamatwa. Yupo chumba cha upasuaji.” “Hapana Mike, nilikwambia namtaka akiwa hai!” Akalalamika bibi Cote. “Hawezi kufa. Ni risasi ya mkononi tu. Usiwe na wasiwasi.” Hapo kidogo roho ikamtulia bibi Cote. “Na akitoka tu chumba cha upasuaji, nimewaambia wamuhamishe huku, usiku huuhuu.” Bibi Cote akafunga macho, akasikia machozi yanamtoka.

“Asante sana Mike. Najua unajua namaanisha.” “Najua.” Mike akajibu huku akicheka. “Tafadhali watakapomfikisha tu huku, niwe wa kwanza kujua ili nimuone mimi kwanza.” “Sawa kabisa. Hamna tatizo.” Wakaagana, bibi Cote akainamisha kichwa chini asiamini kama amefanikiwa kumtia nguvuni Ritha, mwanamke aliyemwendesha kichwa na kumuumiza roho yake kwa miaka mingi sana, tokea yupo na CJ mtoto wake wa pekee, akitamani amlipize kisasi, lakini akafanikiwa kumzidi mahesabu kila wakati na kushindwa. Ritha alikuwa kama samaki aliye hai baharini, mikononi kwa bibi Cote. Alimteleza kila alipodhani amemkamata.

Usingizi ulishindwa kurudi kwa bibi Cote, akabaki akimfikiria Ritha huku akisubiria simu yakutaarifiwa kuwa Ritha amerudishwa Norfolks, kwenye himaya yake. Mji anaotawala kwa pesa yake na mamlaka. Uwanja wa nyumbani. Bibi Cote akabaki akimpigia mahesabu.

Ushindi wa Bibi Cote.

I

likuwa saa 12 asubuhi bibi Cote alipopokelewa na Mike, kiongozi mkubwa sana, ngazi ya juu kabisa ya CSIS nchini Canada. Moja kwa moja wakaelekea chumba alicholazwa Ritha. Alimkuta na pingu mkononi, amelala.  Wakamuona bibi Cote amefunga macho na kuvuta pumzi kwa nguvu kama aliyetua mzigo mzito sana, uliokuwa umemlemea kwa muda mrefu. Akatulia kwa muda akiwa amefunga macho, na wao pia wakanyamaza kama kumpa nafasi.

Baada ya muda bibi huyo akafungua macho. “Naomba muda naye.” Mike akakunja uso. “Unauhakika?” “Unafikiri atanifanya nini huyu?” Bibi Cote akauliza kwa kejeli na kumgeukia Ritha, akamuona amefungua macho anamwangalia. Mike akatoka na walinzi wote. Mpaka mlinzi wa bibi Cote naye alimtaka asubiri nje. Aliporidhika kuwa wamebaki wao wawili pale chumbani, akacheka kwa kejeli huku akimtizama Ritha alivyoumizwa kichwani. Akashusha macho mpaka kwenye mikono alipokuwa amefungwa pingu kote. Hata mkono uliokuwa umepigwa risasi pia ulikuwa na pingu, ukaegeshwa kwenye chuma ya kitanda. Na huo ulinzi hapo nje, bibi Cote akacheka na kurudi kumtizama usoni.

“Hivi ulivyo sasa hivi, ndivyo nilitamani sana kukuona ukiwa hivi kwa muda mrefu sana.” Akaanza bibi Cote. “Ni kwa muda tu. Unajua mimi nina akili ya kukuzidi wewe. Hapa nitatoka tu.” Akajibu Ritha kwa jeuri. “Nashauri utoe hilo tumaini Ritha. Anza kuzoea hayo maisha.” Akaendelea bibi Cote akiwa ameshaanza kubadilika kwa hasira.

“Unakumbuka mara ya mwisho kuzungumza na wewe, Ritha?” “Ulipokuwa ukijaribu kunitisha, kama wafanyakazi wako?” Ritha akamuuliza na yeye kwa kumkejeli akionekana wazi yupo kwenye maumivu makali. “Kama ulifikiri nilikuwa nikikutisha tu, jua safari hii nitakupitisha kwa vitendo. Nitahakikisha hutakaa ukaonja uhuru wako tena. Pingu zitakuwa sehemu ya maisha yako mpaka kifo chako. Nitahakikisha kila siku kuanzia jana, unajisikia uchungu aliopitia CJ, mtoto wangu wa pekee uliyemchagua kumtapeli ili ujinufaishe hapa duniani.”

“Hakika utalipa Ritha. Utalipa kwa uchungu kama unazaa. Na nitahakikisha ni kila siku, unakumbushwa kwa uchungu. Nitahakikisha unaumia sana ili na wewe kwa sehemu uonje kule ulikompitisha Maya ambaye amekuwa bila wewe kuwa mama kwake ila tapeli, ukijinufaisha kwa mali za Cote kwa kuwatumia wao kama kitega uchumi. Utakaa matesoni, ukikumbuka Tunda ndiye mama Cote, wewe hutambuliki popote.” “Hata ufanye nini, mimi ndiye niliyewazaa Net na Maya.” Ritha akamjibu tena akitaka kumuumiza zaidi.

“Na tafadhali sana, hilo usiwahi kulisahau mpaka unapoingia kaburini. Ulibeba miezi 9, ili mimi na Tunda tunufaike kila mmoja kwa namna yake. Wewe utabakia ni njia tu ambayo ulituletea hao watu wawili, kazi na safari yako imeisha. Nitahakikisha hilo unakumbushwa huko kifungoni kwa uchungu sana.”

“Nitahakikisha wanakufungia jela ya wale wauwaji makatili sana tena wazoefu. Serial killer. Utaishi na wafungwa wale ambao nivichaa wakubwa, tena wanao ogopewa hata na askari wenyewe. Utakwenda kula na kunywa nao kila siku.  Kila utakapofungua macho, nitahakikisha ni wao tu ndio unao waona, ili wakakutese sana.” Bibi Cote akaendelea.

“Na nitahakikisha macho ya askari wote yanakuwa kwako ili hao wafungwa wenzako wasije kukua kabisa, ila mateso tu. Na ili usije kujiua kwa haraka ili uonje hayo mateso kwa muda mrefu sana. Ukakae huko ukijua ninakulipa Ritha. Na kamwe hukuwahi kunishinda ila nilikuwa nikitaka kukuweka mwangani ili kila mtu akubaliane na mimi kuwa huko utakapokuwa baada ya hapa, panakustahili. Na nimefanikiwa vizuri tu. Kila muhusika anafikiri huko ndiko kutakapokustahili kwa kuwa wewe ni mtu wa ajabu sana na hatarishi.” Kidogo akamuona hofu imemuingia. Ritha akanyamaza. Akamtemea mate usoni. Akatoka.

~~~~~~~~~~~~~~~~~~

Alirudi nyumbani mida ya saa moja na robo, karibia na muda wa kifungua kinywa. Akaelekea mezani moja kwa moja. Hakumkuta mtu hata mmoja hapo. Akalifurahia hilo ili ajaribu kutulia baada ya kumuona Ritha. Alikuwa amekasirika sana. Baada ya kama dakika 5 hivi, akamuona Maya. “Mbona uso una wasiwasi?” “Malcom hapokei simu yangu Nana!” “Labda bado amelala Maya. Sasa hivi ni asubuhi sana.” Mara Net na mkewe nao wakasogea hapo sehemu yakulia chakula.

Wakasalimiana, Maya macho kwenye simu. “Ni nini tena?” Net akamuuliza. “Nina wasiwasi na Malcom. Tokea tulipoachana naye jana, sijamsikia tena na wakati aliniahidi angenipigia simu ili kujua kama nilifika salama. Malcom sio muongo.” Akaanza kutokwa na machozi. “Kabla yakuanza kulia, nashauri mpe muda zaidi. Lolote linaweza kuwa linaendelea.” “Na huo ndio wasiwasi wangu. Iweje sasa kama Zoe amemfunga?” Wote wakawa kama wamegutuka.

“Mimi naenda kumtafuta kila kituo cha polisi.” “Tafadhali naomba utulie kwanza Maya. Inaweza pia ikawa sio hivyo. Huyu mtu anajukumu la mtoto pia. Inawezekana kabisa, amejifikiria na kuona anafanya maamuzi ya haraka, yatakayo muathiri mtoto wake.” Net akaendelea kumsihi taratibu tu. “Basi ndio nimpate, aniambie mimi mwenyewe. Siwezi nikabaki nikidhani tu!” “Kwa nini usimpe muda? Mwache kwanza. Mwache akutafute yeye kama alivyokwambia.” Hapo Maya akazidi kulia.

“Uliniahidi utakuwa na mimi Net.” “Na ahadi yangu ipo palepale.” “Hivyo si kuwa na mimi. Hivyo ni mimi kuwa na wewe!” Net akashangaa. Bibi Cote na Tunda kimya wakiwasikiliza. “Ulitaka nifanye nini sasa!?” “Uwe na mimi katika maamuzi yangu.” Maya akajibu huku akiendelea kulia. “Hata nisikushauri!?” “Sio ushauri wa kukaa mbali na Malcom!” Hapo Net akaishiwa nguvu.

“Sijakwambia ukae mbali naye, ila kumpa muda Maya. Please! Huyu mtu anamajukumu.” “Malcom alinichagua mimi jana, Net. Mbele za watu. Malcom sio mtu kigeugeu. Mbona inakuwa ngumu kuamini hilo!” Net kimya. “Kama inakuwa ngumu kwako, basi Net. Ila mimi sitasubiri. Nitakwenda kumtafuta mwenyewe. Hayo unayoniambia, nataka nikayasikie kutoka kwake yeye mwenyewe.” “Sawa Maya. Mimi nitakwenda na wewe popote utakapo. Naomba unyamaze. Tupate kwanza kifungua kinywa ndipo tutoke tukamtafute Malcom mpaka tumpate.” Hapo Maya akatulia.

“Ni sawa?” Net akamuuliza. Maya akatingisha kichwa kukubali huku akijifuta machozi. “Unayo namba ya Roy?” Tunda akamuuliza. “Hapana. Sina.” “Basi tulia Maya. Tuliza akili ili uweze kufikiria vizuri. Kama kweli yupo matatizoni, hivyo unavyoanza, ukiwa na hali hiyo, hutaweza kumsaidia.” Tunda akamtuliza, mpaka akanyamaza. Wakatulia kidogo, bibi yao kimya.

“Ulikwenda wapi Nana?” Net akamuuliza. Bibi yake akashangaa kidogo. “Ulijuaje kama nilitoka?!” “Nana! Am the man of the house.” Net akaongea kwa kujivuna kidogo huku akijisogezea sahani ili ajiwekee chakula. Bibi yao akacheka kidogo. Kimya. Wote wakamwangalia. “What?” Bibi yao akauliza alipoona wote wanamshangaa. “Ulikuwa wapi Nana? Mbona kama unasita!” Net akauliza kwa msisitizo. “Nilikwenda kumuona Ritha.” Pakazuka ukimya. Hata sauti ya kijiko haikusikika.

“Wamemkamata jana usiku...” Akawasimulia kila kitu. Kimya. “Kuna anayetaka kumuona kabla hajapeleka mahabusu?” “Binafsi yangu hapana kwakweli. Sina huo muda wakupoteza.” Maya akajitoa mapema kabisa. “Mimi nataka kwenda.” Wote wakamwangalia Net. “Nina swali nataka nikamuulize. Huwa linanisumbua sana.” Maya akamcheka kaka yake kwa kejeli na kumwambia, “Goodluck with that!” “Kwa nini?” Net akamuuliza.

“Kweli Net unauliza swali kama hilo kwa mtu kama yule!? Unategemea jibu gani kutoka kwa mtu kama yeye ambaye kweli haijawahi kutoka kinywani kwake?” “Labda kujiridhisha tu. Acha mimi niende.” Maya akaaanza kulia tena. “Hakuna mtu ananijali mimi! Mnanipuuza. Ona sasa hivi amekuja yeye, unaamua kuniacha mimi na kumfuata yeye! Mimi naondoka, hata sisubiri tena. Nakwenda kumtafuta Malcom binadamu anayenijali mimi, Maya.” Maya akasimama.

“Tunakwenda Maya. Naomba utulie tafadhali. Nakwenda kuzungumza naye  kidogo tu, kisha tunakwenda popote unapotaka wewe. Tafadhali nifikirie na mimi hata kidogo. Huyu mtu amenitenda ubaya mkubwa sana bila sababu! Kumbuka niliacha maisha hapa nikaenda kumtumikia. Ameniadhibu mimi bila kosa, kama haitoshi amehamia kwa mtoto wangu! Kweli Maya unafikiri sina haki yakumuona mtu kama huyo?” Maya akatulia kidogo.

“Hata kwa dakika moja tu, nataka niione sura yake ajue kile ninachojisikia.” “Unafikiri ameshawahi kujali kile tunachojisikia?” Maya akamuuliza kwa kuumia sana. “Safari hii nitahakikisha anajali Maya. Acha nikamuone na kuzungumza naye kwa mara ya mwisho, kwa kuwa sitakaa nikazungumza naye tena. Tafadhali nivumilie.” “Sawa, lakini mimi sitaingia ndani. Sitaki hata kuiona sura yake tena maishani mwangu kote.” “Sawa. Basi usilie. Hilo halina shida. Utanisubiria kwenye gari. Nenda kaoshe uso.” Wakakubaliana ndugu hao wawili. Maya akaondoka kurudi chumbani kwake kuosha uso na kuchukua pochi.

Net akambusu mkewe na kusimama. “Sasa mbona huli tena na wakati ulikuwa unalalamika umeamka na njaa!?” Tunda akamuuliza. “Hamu ya chakula imeisha yote! Acha tu niende. Nitakuja kula nikirudi.” Akamgeukia bibi yake. Akaenda kumbusu. “Asante kwa kwenda na Maya. Nitajitahidi kuulizia alipo Malcom, nikijua mapema, nitawapigia kuwataarifu alipo ili msisumbuke sana.” “Utakuwa umeturahisishia sana.” Net akaondoka. 

Tunda & Bibi Cote.

T

unda akajikuta amebaki kimya yeye na bibi Cote. “Hiyo hasira na kilio cha Maya sio cha Malcom peke yake. Maya ana mengi yanayoendelea kichwani kwake. Ameumizwa sana na mama yake. Acha Net akamsaidie labda atatulia. Ningekwenda mimi mwenyewe lakini najua itawaogopesha watu zaidi.” Tunda akafikiria kidogo. “Mungu atamsaidia hata haya yatapita tu.” Akaongea Tunda taratibu kama anayefikiria. “Unajua kabla ya haya yote kutokea, alikuwa akiniambia kuwa kuna kitu kimoja tu, ambacho anacho Vic na ndio maana wakati wote alikuwa akimshinda, japo yeye Maya anaakili kumzidi yeye!” Bibi Cote akakunja uso kidogo.

“Kitu gani!?” Akauliza bibi Cote huku na yeye akikitafuta kama asikione. Wao walikuwa matajiri sana kuliko kina Vic, baadhi ya biashara ni wao wamewafundisha wazazi wa mama yake Vic. “Alisema wazazi wa Vic wakati wote wamekuwa upande wa Vic hata katika ujinga wake. Hawakuwahi kumuacha tokea mtoto mpaka sasa na ndio maana katika maovu yake yote, Vic hakuwahi kukamatwa kwa kuwa wazazi wake wamemzunguka na kumfuatilia kwenye kila hatua ya maisha yake.” Bibi Cote aliumia mpaka Tunda akamuona usoni. 

Akainama kwa muda, akanywa juisi aliyokuwa amewekewa na Gino na akakumbuka hata Maya alizungumzia hilo hata na kwake, ila kidogo tu katikati ya mazungumzo yake au maneno yake mengi lakini hakujua kwa uzito huo.

“Na wewe ulitaka kwenda kumuona Ritha?” Akabadili yale mazungumzo. Tunda akashituka sana. “Hapana Nana! Nahisi sitaweza hata kulala usiku. Acha tu Net aende.” Bibi Cote akafikiria kidogo, akamuona anatoa simu. “Nataka kujua alipo Malcom sasa hivi.” Akakata simu na kupiga tena simu kwengine. “Net na Maya wametoka, nataka macho kwao wakati wote mpaka wanarudi hapa kila mmoja in one piece.” Akakata.

“Pole Nana.” Tunda akamuhurumia. Bibi Cote akacheka. “Hivi unapata muda wakulala kweli?” Akacheka. “Sina tofauti na wewe Tunda. Si umeona mwenyewe tokea upewe mtoto wako!” “Kweli Nana! Silali tena usingizi kama zamani!” Wakacheka kidogo. “Basi ndio hivyohivyo. Huwa hawakui, na hata wakionekana nje wamekua na kuondoka nyumbani, bado mawazo yanawafuata huko huko. Hupumziki.” Tunda akafikiria kidogo.

“Sasa ulifanyaje Net alipokuwa Tanzania?” “Mwanzoni alikuwa akilindwa masaa 24. Alipoanza mambo ya kuchumbia, akitaka kupendwa kama yeye.” Tunda akacheka. “Net! Yupo kama babu yake! Akakataa kabisa ulinzi. Nikamwambia hutawaona hao walinzi, akasema hawezi akawa anazunguka au kuonekana na wazungu kila mahali halafu isikushitue. Nikamwambia nimbadilishie waje weusi, pia akakataa. Akasema huko Tanzania kuna amani, hakuna anayemfahamu, hakuna atakaye mdhuru. Yeye anataka Tunda ampende kama yeye.” Tunda akacheka sana.

“Lakini alijuta mlipokuja kukamatwa na Ritha! Wewe ukaishia jela, yeye akafika huku nusu mfu! Alijuta sana. Alikuwa akilizwa na mengi, mimi nilijua nikaona nimuache tu, ajifunze aache ubishi kama babu yake.” Tunda akanyamaza kidogo.

“Mbona kama kuna kitu ambacho unasita kuniambia?” Tunda akacheka na kuhamia pale karibu yake. “Sasa hivi Net anajua maisha yote na kwa undani vile walivyoishi wazazi wake, Nana. Ndio maana unamuona ameumia sana.” Bibi Cote akashituka sana na kushangaa. “Amejuaje!?” “Kumbe kuna sehemu Papa alikuwa akiandika. Sasa hizi siku ambazo hakuwa anakwenda kazini. Tokea mimi nipatwe matatizo, amepata muda wakupitia mafaili yote na diaries zote za Papa, kule ofisini kwake. Amekutana na hayo mambo kwenye kitabu cha kumbukumbu ,Papa alichokuwa akimwandikia yeye Net binafsi. Alikuta jina lake limeandikwa nje, kwa mwandiko wa Papa, Nathaniel Cote. Ndipo alipofungua.” Bibi Cote akabadilika kabisa.

“Hivi unajua kuwa mali zote za Ritha ambazo alizipokea kutoka kwenu, Papa aliandika ni za Net yeye ni kama mwajiriwa au msimamizi tu?” Bibi Cote kimya. “Hata Net hakuwa akijua. Ila inavyoonekana, Ritha anajua, ila akakusudia kunyamazia tu. Zipo karatasi zote alizosaini Ritha na kukubali. Mlizoziona wewe na Logan, hazikuwa na maelezo yakutosha na ilikuwa kwa baadhi ya pesa.” Bibi Cote akakunja uso.

“Alisaini kwa makubaliano kuwa pesa zote, mali zote mpaka nyumba aliyouza Ritha ambayo mlimnunulia CJ, ilikuwa ni yako na Papa, mrithi ni Net. Wala  haikuwa ya CJ kama ulivyodhani. Nafikiri Papa alishajua ujanja wa Ritha, akaamua kuwa naye makini. Na hakutumia mwanasheria huyo wenu Logan, ameandika copies zote sahihi zipo kwa mwanasheria wenu mwingine wa mambo ya mirathi. Net amemtaja kwa jina moja tu la Leon.” Bibi Cote akajiweka sawa.

“Papa ameandika kuwa siku akifa tu yeye, kila kwenye jina lake yeye Papa, watu wasome Nathaniel Cote au kila anapotakiwa kusimama yeye Papa, asimame Nathaniel Cote. Kusiwahi hata kuwepo na kuhisiwa na utofauti, popote. Kasoro tu sura yake ndio iwe haipo. Ila Papa amemwambia Net, anajua ataishi kwa kupitia yeye, kwa kuwa anauhakika na alichokifanya akiwa hai.” “Hiyo najua na nina uhakika. Alijihamisha kwa Net, kwa asilimia 100.” Bibi Cote akathibitisha na kufuta machozi.

          “Basi ndio hivyo. Kwa kifupi, mali zote alizouza Ritha ni za Net. Sasa Net ameamua kuchukua kila centi iliyoingia kwenye mfuko wa Ritha.” “Tunda!” Bibi Cote akashituka sana. “Hivi moja ya sababu  ambayo anakwenda kumuona Ritha leo, ni kumuonyesha aliposaini baada ya makubaliano na Papa. Na kumwambia atamfilisi mpaka centi ya mwisho ili hiyo pesa yake yeye Nathaniel Cote, ambayo aliishika kwa dhamana tu, asiendelee kuitumia kudhuru watu.” “Nyumba ya Tanzania?” Bibi Cote akauliza.

“Amesema atafanya kama alivyofanya ile yake kule Tanzania. Atahamishia kwa jina langu. Na vyote ameniambia anaenda kumwambia siku atakayoiona sura yake. Ndio maana mimi nimeona leo nisiende.” Bibi Cote akavuta pumzi. 

“Usiku hajalala, Nana! Kuna muda niliamka usiku nikamkuta akilia bafuni. Nikasema nimuache. Kwenye saa 9 usiku tena, nikamkuta bado yupo macho. Ndio nikambembeleza, akalala.”

“Pengine anahofia utamuacha!” “Hapana Nana. Hilo tulishalimaliza.” “Mbona bado umehama chumba?” Tunda akacheka. “Siwezi kulala chumba mbali na mwanangu Nana! Sitalala. Nahisi kama wanaweza kuja kumuiba nikiwa usingizini!” Wakacheka. “Hawawezi. Unaulinzi mkali sana hapa.” Tunda akabaki kama anayefikiria. 

Kisha akamuhakikishia. “Anyway. Hilo tulishalimaliza. Yameisha na nimemwambia tutafunga ndoa kama alivyotaka tokea mwanzoni.” “Kweli Tunda!?” Bibi Cote hakuamini. “Nana! Nitapata wapi mimi mwanaume atakayenipenda kama Net?” Bibi Cote akafikiria kidogo. 

Kisha akaona aseme tu. “Mimi nilipoona wanaanza kutangaza kiwango cha mali utakachopata baada ya kuachana na Net, na kuwa hata mtoto atakuwa wako sababu Net amezini, nikajua watakuchanganya.” “We Nana! Nipate mali nimkose Net!? Halafu hizo mali zitanisaidia nini mimi? Sijawahi kupata utulivu wa akili na moyo maishani mpaka alipokuja Net kama Net kwenye maisha yangu.”

“Labda aje anikatae mwenyewe. Lakini hivihivi, nitatafuta sababu yakusamehe tu ili niwe naye mpaka kufa.” Bibi Cote alicheka sana. “Bila kuombwa msamaha?” “We Nana, asiponiomba je?” Tunda akamfanya bibi Cote azidi kucheka. “Nimekwambia nitatafuta sababu yakusamehe tu Nana, ili nikae na Net wangu. Hapa nimemwambia kwa kunikosea, nataka watoto mapacha, tena haraka.” Bibi Cote akatoa macho.

“Tunda! Hujachoka?” “Hata kidogo. Ndio tiketi yangu hiyo mwenzio yakuweka ugumu wakutoachana.” Angalau bibi Cote alicheka asubuhi hiyo baada ya juma hilo lililokuwa limejaa hekaheka.

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

Simu ya bibi Cote ikaita. Akamuona amepokea kwa haraka. Akasikiliza kwa muda bila kujibu akamuona bibi Cote amefunga macho kwa sekunde kadhaa. “Mtaarifu Logan, mwambie anipigie na majibu ya nini chakufanya. Isichukue muda mrefu.” Akakata simu. “Ni nini Nana?” Akavuta pumzi kwa nguvu. “Maya atachanganyikiwa.” “Kwa nini tena?” Akavuta tena pumzi kwa nguvu. “Malcom alikamatwa na polisi jana usiku akiwa njiani kuelekea kwake, ameshikiliwa na polisi.” Tunda akashituka sana.

“Kwa nini?!” “Zoe alipiga simu polisi na kuwaambia Malcom ametoka kwake akiwa amembaka. Ameonyesha majeraha aliyomjeruhi wakati akimbaka.” “Nana! Unafikiri ni kweli?”  “Tutajua. Lakini...” Akasita. Akaonekana kama anafikiria. “Nikuulize Nana?” Bibi Cote akamwangalia. “Katika vipindi kama hivi vya matatizo makubwa mfululizo. Tena ambayo yote yanakuhitaji, unafanyaje?”  Akamuona amecheka kidogo na kubaki akifikiria.

“Maana mimi  kwa tukio moja tu, nilitaka kukimbia kabisa.” Tunda akamfanya bibi Cote acheke tena kidogo. “Muonekano wa nje usikudanganye Tunda.” “Hapana Nana.  Nimekutizama tokea Tanzania na nilipokuja hapa! Unawezaje!?”  Akajiweka sawa. “Unakumbuka nilikwambia wakati wote katika kila maamuzi unayochukua  chukua ukiwafikiria mpaka watoto wa huyo Cote. Unakumbuka?” Tunda akavuta pumzi kwa nguvu, nakunyamaza.

“Umetoka kusema utafanya kila njia kubaki na Net. Hiyo ni hatua ya kwanza na ya msingi. Unachotakiwa kufanya sasa, kila jambo zito na gumu linapokuja mbele yenu, ukumbuke hilo, ndipo hisia zifuate. Kingine, najua mimi nikichanganyikiwa hata kidogo tu sasa hivi, si hasara kwa Net na Maya peke yao, hata Cote ataathirika. Kwa hiyo tunarudi palepale. Lazima kuwafikiria mpaka watoto wa Cote. Na lazima kufikiria kwa haraka na kuchukua hatua ya haraka bila kupoteza hata sekunde. Na wakati wote huwa nahakikisha nipo hatua moja mbele ya kila kitu.”

“Kwa mfano katika hili la Malcom, kabla sijafanya chochote na kuharibu au kuaibika, nimemtaka Logan anipe ushauri wa kisheria juu ya hili. Sitatoa mguu wangu hapa. Wala sitampigia simu yeyote, bila kujua nataka kuongea nini na nani. Sijui kama unanielewa?” Tunda akabaki kimya. 

“Kupaniki kwangu ni jambo la mwisho sana na huwa siruhusu kupaniki katika maisha yangu. Kwa kuwa sijajaliwa hiyo nafasi kama wengine. Nafasi yangu kwenye jamii na familia, hainiruhusu kupaniki, ila kutafuta suluhu katika kila jambo. Na ndio maana huwa sishindwi.”

“Imenisaidia kufanya akili yangu kuwa na uwezo wa kufikiria kwa haraka sana. Mfano. Nilipokuja hospitalini siku uliyotekwa nyara, nilimkuta Net anakusubiri, wewe haupo. Akaniambia umekwenda kufanyiwa vipimo hata yeye hakukukuta. Hapohapo nikajua kuna kitu hakipo sawa.” “Nana!” Tunda akashangaa kidogo.

“Hata wao hawakuwa wakiamini na kuelewa. Walishangaa  ninachukua hatua kama kuna moto mkali sana unaowaka nakutaka kuteketeza jengo wakati mazingira yalikuwa matulivu, hakuna chakushitua, kwa kuwa Tunda yupo kwenye vipimo! Lakini tangia naingia pale hospitalini, mpaka kujua haupo kwenye vipimo. Umetoroshwa na watu wawili, wamekutoa pale kwenye mazingira ya hospitalini na gari fulani. Kuifuatilia hiyo gari mpaka ilipoishia chini ya tunel au daraja,  haikuchukua hata dakika 20. Sijui kama umenielewa?”

“Mpaka wale polisi walishangaa. Nilijua nini chakufanya na wakati gani. Nani nimpigie kwa haraka ili anipe majibu ya haraka. Na ni hapohapo mbele ya polisi, mpaka wao wenyewe wakabaki wamepigwa na butwaa. Lakini sio kwa sababu ya akili kuwazidi  wao au pesa yangu tu, lakini ni kwa sababu yakujizoesha kufikiria kwa haraka bila kutoa nafasi ya kupaniki. Lakini sio kwamba huwa siingiwi hofu? Hapan..”  Simu ya bibi Cote ikaita.

Akapokea akamuona ameshituka sana. “No No nooo! Usingemuacha akashuka kwenye gari.” Akakata simu. Akamuona anapiga simu nyingine. “Maya yuko wapi?” Tunda akabaki akimtizama. “Nashukuru sana. Hata iweje, asiwe mbali na wewe hata kwa hatua tano. Unanielewa? Nakuja sasa hivi, tutakutana huko huko.” Akakata. “Nahitaji gari yangu iwe tayari sasa hivi.” “Yes ma’am.” Carter akajibu.

“Ni nini tena Nana?” “Nafikiri Maya amepata taarifa za Malcom kutoka vyombo vya  habari au kwenye mitandao yao hiyo! Dereva aliyekuwa nao anasema walikuwa wakimsubiria Net nje ya hospitali, akamsikia Maya anapiga simu kuulizia alipofungwa Malcom, inaonekana alipojua, akatoka ndani ya gari na kuanza kukimbia. Bahati nzuri mlinzi niliyemtuma kuwafuatilia alimuwahi akamwambia apande kwenye gari yake. Hapa walipo wanaelekea kituo cha polisi. Inabidi niende Tunda. Hali aliyonayo Maya, kama mimi mwenyewe nisipoenda pale, watamfunga na yeye. Anahasira na mama yake, ataenda kumalizia polisi huko kituoni. Acha niwahi.” Hapo hapo akanyanyuka.

Tunda akamsikia akipiga simu nyingine.  “Nikukute na majibu yote kituo cha polisi cha Norfolk sasa hivi.” Tunda akajua huyo ni Logan tu. Akamsikia kama anayekimbia, baada ya dakika 2, kimya. Akajua ameachwa peke yake humo ndani na wafanyakazi. Tunda akavuta pumzi na kujivuta nyuma ya kiti. Akabaki kimya ameduaa. 

Net kwa mama yake.

N

et alifika pale akamkuta mama yake amelala vizuri, kama aliye kwenye usingizi mzito. Nesi aliyekuwepo pale akataka kuwapisha. “Hapana. Moja ya sifa zake huyu, ni mzuri sana wakubadilisha maneno. Tafadhali kama huna kazi nyingi, naomba uwepo hapa ili nizungumze naye. Haitachukua muda mrefu. Na acha mlango wazi. Tafadhali sana.” “Sawa.” Yule nesi akakubali kwa heshima. Alipogeuka akamkuta mama yake amefungua macho.

“Unakumbuka mara ya mwisho nilipozungumza na wewe tulipokuwa nchini Tanzania?” Net akamuuliza mama yake, akiwa ametulia tu tena kwa lugha ya kingereza. “Nilikwambia angalia usifike umbali ambao ukashindwa kurudi. Usiruhusu hiyo roho iliyokuingia ikakufikisha mbali, lakini nisijue kuwa ndivyo ulivyo tokea kabla hujakutana na baba.” Ritha akacheka kwa kejeli.

“Naona bibi yako amekazana kweli! Safari hii ameamua aniangamize mimi na watoto wangu. Amekusudia kukuharibu kichwa chako ili tu kuniumiza. Haya, endelea kuongea ili nijue amekwambia nini?” Net akazidi kuumia. “Wala Nana hajaniambia baya lolote kuhusu wewe! Na ni kama amejionya juu ya hilo. Hajawahi hata kuropoka kukutaja kwa ubaya mbele yetu. Nafikiri ni kwa kuwa anatupenda sana, hataki kuona tunaendelea kuumizwa na wewe. Na wala hafahamu ni nini nataka kuzungumza na wewe.” Net akaendelea.

“Ni mimi mwenyewe nimechunguza mpaka nimejua ukweli wote. Nikisema wote namaanisha nimegundua ambayo hata Nana hakuwa akiyajua. Au ambayo hata wewe hukuwa ukijua kama Papa anayajua.” Ritha akakunja uso. “Sipo hapa kurudia maovu yako. Kwa kuwa najua unayajua maovu yako yote. Ila najua kwako sio maovu ni maisha uliyoyachagua kuyaishi zamani sana hata kabla mimi na Maya hatujazaliwa na wala hata kabla hujakutana na baba.” Bado Ritha alikuwa akimtizama mwanae kwa makini tu, kutaka kujua ni nini amejua!

“Wewe kwa asili ni muovu na wala huwezi kutenganishwa na uovu kwa kuwa wewe ni MUOVU.” “Acha kunipotezea muda Net. Nenda kwenye pointi, maana sina muda mrefu wa kijinga wakukusikiliza. Kama bibi yako amekudanganya kuwa wamenikamata safari hii, nitakaa hapa muda mrefu, ujue amekudanganya. Hapa kwenye hizi pingu sina muda mrefu. Tumia huu wakati vizuri.” Ritha akaongea kwa kugomba na kujiamini.

“Anachotaka bibi yako nikunilipiza kisasi. Na ninakuhakikishia, hajanipata. Mimi nina akili, usifikiri ni mjinga. Huwezi kunishitaki kwa ukiri nilioongea nikiwa nimeshikiwa risasi! Au nimepigwa risasi!” Akaongea Ritha bila wasiwasi. “Mtu anaongea chochote anapokuwa akitishwa ili kujiokoa. Confession under duress! Jua sheria wewe mtoto, acha kukurupuka nakuja hapa kuongea ujinga! Kwanza ondoka ili nilale. Sidhani hata kama una kitu chakuzungumza na mimi isipokuwa uzushi tu.” Net alishituka sana maana mama yake alikuwa sahihi. Lakini akajikaza.

Ritha alishageuza kichwa upande mwingine. “Jiandae kutafuta mwanasheria atakayetetea huo ujinga unaoendelea kichwani mwako tena atakayekufanyia bure. Maana mimi kwa kutumia kila senti  ambayo unadhani ni yako  nitahakikisha unakaa sehemu ambayo hutaweza kumdhuru mtu mwingine yeyote hapa duniani, hiyo ni hata na wewe mwenyewe, mpaka Mungu mwenyewe atakapoamua kukutoa hapa duniani.” Ritha akashituka sana. Akageuka.

Net akacheka. “Ninapokwambia nimefanya uchunguzi wa kina na ninajua mambo zaidi  ya unayodhani wewe na anayojua Nana, ulifikiri nakutania?” Net akacheka akionekana anahasira yakupitiliza. “Wewe unasainishana na Nana, bila mimi? Mimi ndio mrithi wa CJ na Cote. Mimi ndio mwenye mali. Papa amekufa mwili, lakini anaishi hapa.” Net akajionyeshea kidole yeye.

“Hilo ameandika kwa maandishi, kwa mkono wake yeye mwenyewe Papa. Na ameacha nakala tatu. Kwa wanasheria wawili tofauti tofauti, siwezi kukutajia wewe, na nakala moja ameniachia mimi. Kila mkataba alioingia yeye akiwa hai, amesema yeye ndio atakufa, lakini mikataba yoote aliyoingia yeye, haitawahi kufa kama Nathaniel Cote, ninaishi.” Net akaongea kwa jeuri.

“Sasa ni hivi, mkataba uliongia na Nana,  kupitia Logan, SIUTAMBUI.  Hapa ninapozungumza mimi kama Nathaniel Cote, nimeshatuma Tanzania makaratasi ya kumuuzia Tunda ile nyumba uliyodhani ni yako, kwa shilingi 100 tu.” Akamuona mama yake amebadilika. Net akacheka.

“Umesikia?” Net akamuuliza kwa kejeli. “Sio milioni. Shilingi 100 tu. Ambayo hivi karibuni itakosa thamani. Itakuwa ni kama nimempa bure kabisa. Nimesema kila kitu kilichopo ndani mpaka kijiko ulichotumia muda kwenda kununua kwa pesa yangu, ni cha Tunda. By the way, yupo hai. Nimemuacha anakaribia muda wa kwenda kumnyonyesha mtoto wetu.” Net akamtizama usoni.

“Usiku wa jana, nimeandaa madai yangu yote kwako. Na uthibitisho wote mliokubaliana na Papa. Nitamlipa mwanasheria mkubwa sana, ili kuhakikisha kabla hujafikishwa mahakamani, uwe na uhakika kuwa umefilisika kabisa. Huna hata chumvi unayomiliki kwa jina lako.” Net akamkazia macho.

“Nitahakisha safari hii hutakimbia hukumu yako Ritha. Najua umeshajipanga kwa utetezi, lakini  ujue safari hii utalipa kwa kifo cha  Gabriel. Alikufa akiwa anakutafuta, nimekuja kukutangazia, NIMEKUPATA. Na nitahakikisha unalipa.”

“Hii ni Canada. Hakuna ujanja ujanja wa meneno kugeuzwa geuzwa. Utahukumiwa kwa maneno ya kinywa chako wewe mwenyewe. Na ujue hapo unapolala ni dakika za mwisho. Unakaribia kupelekwa kunapokustahili.” Ritha akakunja uso. “Mimi bado ni mgonjwa!” “Wapo wauguzi watakaoendelea kukuhudumia ukiwa jela. Usiwe na wasiwasi. Baada ya muda mfupi sana gari ya kukupeleka unakostahili itakuja kukuchukua. Utapata muda wakujifikiria na kujipanga vizuri huko jela. Wewe si umesema unayo akili? Nenda sasa ukajipange ukijua huna pesa na upo na pingu mkononi. Na kingine, kuwa na uhakika kuwa, pesa yangu uliyokuwa ukiihangaikia kuizalisha miaka yote, ndiyo itakayosaidia kuhakikisha unakaa ndani mpaka kifo, ili mke wangu alee vizuri na kwa amani akijua hutaweza kumdhuru tena.” Net akaongeza.

“Na nitahakikisha, Cote na wadogo zake, wanapata kutoka kwa mama yao, ambaye ni Tunda kile ulichoshindwa wewe kutupa  mimi na Maya, kwa kuhakikisha unaishi jela maisha yako yote, bila kutoka au hata kuwa na uwezo wa kutumia watu kufanya maovu yako tena, kwa kuwa hutakuwa hata na senti moja kwa jina lako, kuweza kuwalipa watu kama kina Jeff.” Akamtizama na kutaka kuondoka. Akasimama.

“Nilitaka kukuuliza kitu, lakini naona Maya yupo sahihi. Nitapoteza muda tu. Wewe ni muongo, na wala kweli haijawahi kukaa ndani yako. Huna majibu ya maswali yangu.” “Nijaribishe.” Net akageuka akamtizama kwa muda. Akakunja uso, huku akicheka kwa kumkejeli mama yake. “Naaaah!  Nina mambo ya muhimu ya kufanya na mke  wakumuwahi.” “Malaya yule!”  “Yeap! Yale yooote aliyokuwa akiwapa wengine, sasa hivi mimi ndio nayafaidi peke yangu! Nalala nikiwa tajiri. Nina uhakika wa utajiri wa mpaka kifo changu na watoto wangu, halafu napata na penzi safi kutoka kwa Tunda. Na ninakuhakikishia, ni mzuri kitandani.” Akamtusi mama yake huku akicheka. “Deal with it!” Akamuwekea mama yake msisitizo wakati anatoka.

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

Je ni kweli safari hii wamemkamata Ritha? Amashatengeneza hoja ya kweli kisheria. Huwezi kuchukua ukiri wa mtu aliyekuwa akitishwa, kama ushahidi. Mtu akiwa anatishwa anaweza kuzungumza chochote ili kujitetea nafsi yake. Ritha ndio umesimamia huo utetezi wake. Watafanyaje kushinda hilo?

Maya na Malcom nao je?

Usikose sehemu ya mwisho ya  Simulizi hii.

CONVERSATION

0 Comments:

Post a Comment