Naomi Simulizi |+1 205 767 8163 |naomisimulizi@gmail.com Nilipotea! – Sehemu ya 53. - Naomi Simulizi

Nilipotea! – Sehemu ya 53.

Maya alifika kituo cha polisi akakimbia mpaka mapokezi, “Naitwa Maya Cote, nataka kumuona Malcom Marshall. Mlimkamata jana usiku.” Akaanza Maya. Kabla hajajibiwa,  akamuona Roy. Akamsogelea. “Malcom yuko wapi?” “Ya safari hii ni mbaya Maya. Zoe amemzushia uongo ambao hata dhamana hawezi kutolewa.” “Kwani ameua!?” Akauliza Maya kwa hasira na sauti ya juu huku akirudi pale mapokezi ambapo wapo polisi. “Maya Cote!”  Akasikia sauti ya bibi yake ikiita nyuma yake. Akageuka. “Neno jingine lisitoke kinywani mwako.” Akamuona bibi yake na Logan, alifurahi Maya akamkimbilia na kumkumbatia. “Asante Nana. Asante kwa kuja.” Bibi yake akambusu. 

Logan akawapita na kusogelea mapokezi. Tayari ikajulikana bibi Cote yupo pale. Mlinzi wake hakuwa mbali. Alisimama nyuma kabisa. Kimya. Logan akasalimia. “Naitwa Logan, mwanasheria wa Malcom Marshall.” Mkuu wa kituo akatoka. Bibi Cote kimya. Ila ule uwepo wake tu pale, ulishajaa kila mahali. Yule mkuu wa kituo akamsogelea bibi Cote aliyekuwa amesimama na Maya. Mlinzi nyuma. Bibi Cote akampa mkono kiustarabu tu. Kimya.

“Malcom yupo chini ya ulinzi kwa tuhuma za ubakaji.” Wakamsikia polisi wa mapokezi akimwambia Logan. “Mmeshathibitisha hilo?” Akauliza Logan taratibu. “Ndio tupo kwenye uchunguzi.” “Basi, mpaka mtakapothibitisha, naomba niondoke naye.” Logan akaweka msisitizo akijua bibi Cote anasikiliza. Mkuu wa kituo akasogelea pale mapokezi. “Tupo kwenye uchunguzi kwa kuwa simu ilipigwa na Zoe, mama watoto wake. Mpaka polisi kufika eneo la tukio, Malcom alikuwa ameshaondoka. Amekamatwa njiani tu. Kumtoa sasa hivi bila kukamilisha uchunguzi, itakuwa...” “Naomba usubiri kwanza.” Logan akamwingilia.

“Unataka kumshikilia mpaka mmalize uchunguzi!?” Logan akauliza kwa kushangaa. “Hivi mnajua Malcom ni mfanyakazi ambaye jumatatu anatakiwa awepo ofisini? Ana mtoto ambaye anamlipia pesa za matunzo. Atakapofukuzwa kazi kwa mashitaka ambayo bado hamjathibitisha kama ni kweli, halafu ikajulikana kuwa ni uongo, mnajua nitarudi tena hapa ya madai ya kiasi gani?” Logan akamuuliza. Kimya. “Wakati mnatafakari hayo, naomba kuzungumza na mteja wangu kwanza.” Akaomba Logan akijiamini. Akaruhusiwa.

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

Wakati Logan anazungumza na Malcom kwenye chumba alichoelekezwa, Maya akiwa anasubiri na bibi yake, Net naye akaingia hapo kituo cha polisi. “Samahani Maya, nilichukua muda mrefu kidogo.” “Sio kwamba ulichelewa, mimi ndio niliondoka muda mfupi tu uliposhuka.” Net hakuwa ameelewa. “Pale ulipoondoka tu na nikakwambia nitasubiri, nikaona kwenye Facebook ya Zoe, emeandika mkasa mzima wake na Malcom kuwa alimbaka kwa nguvu na kutoroka, ndio polisi wamemkamata na kumfunga. Nilipaniki Net. Nikashindwa kusubiri.” Net akamsogelea na kumkumbatia.

Akamgeukia bibi yake. “Asante kwa kuwa hapa na samahani.” “It’s okay.” Bibi yake akarudisha tabasamu la kumtuliza. “Vipi, Logan anasemaje?” “Nimapema sana. Tumpe muda.” Bibi Cote akajibu. Net akambusu Maya kichwani. Wakatulia wakimsubiria Logan. Baada ya mazungumzo ya muda kidogo kati ya Logan na Malcom, Logan akaomba vipimo kadhaa afanyiwe Malcom siku hiyohiyo kabla hata yakwenda nyumbani. Akaomba afanyiwe pale kwenye maabara ya palepale polisi, kabla hata ya kutoka pale. Akiwaambia itawasaidia hata wao kwenye kukusanya ushahidi wao.

Yaani kupimwa Malcom ili kuona kama watakuta DNA ya Zoe mwilini kwa Malcom. Kwa kuwa bado hakuwa ameoga wala kunawa, na Zoe alikuwa na mikwaruzo aliyosema amepatiwa na Malcom kabla na wakati wakumbaka. Logan akaomba Malcom apimwe chini ya kucha zake kama zitakuwa na ngozi ya Zoe. Akapimwa na sehemu zake za siri kama kweli alimwiingilia Zoe.

Akafanyiwa vipimo hapo, kisha bibi Cote akaomba askari mwingine aongozane nao kama shahidi kuwa wanatoka hapo na kuelekea kwenye hospitali ya kulipia moja kwa moja kwa vipimo zaidi. Alitaka huyo askari awe kama shahidi kuwa Malcom hakupitia popote. Tokea walipomkamata hakuoga na wala hakujisafisha. Yote hiyo ni kwa ajili yakupata ushahidi zaidi na wakutosha. Bibi Cote alitaka ushahidi wa kila pande ili safari hii wamkamate Zoe kama amedanganya, na kumdhibiti kabisa.  

Alipofanyiwa vipimo alivyoshauri Logan palepale kwenye maabara ya polisi, ndipo akaruhusiwa kwa dhamana ya pesa nyingi sana. Roy akashangaa bila swali au kupepesa macho, Logan akatoa hundi na kuandika kile kiwango chote cha pesa, na kuwakabidhi ile hundi askari husika. Akaambiwa Malcom anatakiwa asisafiri mpaka uchunguzi na kesi iishe.

Baada yakukamilisha taratibu zote za pale kituo cha polisi, Malcom akasindikizwa na askari polisi kwenye gari ya polisi mpaka kwenye hospitali aliyowaambia Logan. Familia hiyo ya Cote na mwanasheria wao nao walifuata nyuma pamoja na Roy aliyekuwa akifuata nyuma nyuma tena kimya kimya naye alikuwa akiendesha gari yake mpaka kwenye hospitali hiyo ya kulipia.

Walifika hapo, Logan akaongozana na yule askari na Malcom mpaka kwa daktari. Baada ya kushauriana na daktari, Malcom akaandikiwa tena vipimo vingine. Ni kama alianza upya kabisa kutokana na ushauri wa huyo daktari. Wakaongozana tena na yule askari mpaka maabara ili Malcom afanyiwe vipimo kwa upya ambavyo sasa vingekuwa ni vya Logan atakavyovitumia mahakamani siku ya kesi  pamoja na ushahidi wa huyo daktari mwenyewe afike na aeleze kile alichoona kwenye vipimo hivyo. 

Daktari mwenyewe alifahamiana vizuri tu na bibi Cote. Alishakubali kutoa ushirikiano wote na hiyo sio mara ya kwanza kumtumia daktari  huyo. Wakati Malcom akifanyiwa vipimo hivyo, wasindikizaji wake walikuwepo hapo wakimsubiri, na safari hii kesi ya Malcom ilishachukua sura mpya, Zoe asijue amecheza na moto.

~~~~~~~~~~~~~~~~~~

Zoe alishazoea kuwazungusha Roy na Malcom. Na wala kufungwa kwa Malcom haikuwa mara ya kwanza. Roy ndiye aliyekuwa akimtoa huko mahabusu kila mara kwa kusingiziwa hili au lile kwa kadiri alivyojisikia Zoe. Kuna kipindi pesa za matunzo ya mtoto alibadilisha njia ya kupokea kwa Malcom. Yeye mwenyewe akasema akaunti yake imesumbua, kwa hiyo awe anampa pesa taslimu. Kwa miezi minne mfululizo wakawa wanapeana tu mkononi.

Baada ya hiyo miezi minne, Malcom na Roy wakiwa ofisini wakashangaa wanafuatwa na barua kuwa Malcom anatakiwa mahakamani kwa kutolipa matunzo ya mtoto kwa muda wa miezi minne. Kesi ilipotajwa, Zoe alikana kabisa kuwa hajapokea pesa kwa miezi minne mfululizo. Malcom aliwekwa jela. Akawa anatoka asubuhi kwenda kazini, nakurudi kulala jela mpaka muda wake aliopangiwa ulipoisha.

Ilimuuma kila aliyemzunguka Malcom, lakini hawakuwa na jinsi ya kumfanya Zoe. Kwanza ni mama watoto wa Malcom na bado alikuwa na dhamana yakuishi na Ethan. Lazima kunyenyekea tu.

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

Sasa safari hii kesi ya Malcom imeshikwa na kina Cote. Wapo hapo bibi Cote akiwa ameshapewa historia nzima ya Malcom na Zoe. Hapo Logan anafanya kazi yake akijua kesi zote alizokuwa ameshashitakiwa nazo Malcom na huyo mzazi mwenzake. Walijua ujanja wa Zoe, na bibi Cote alimwambia Logan aweke kikomo ili kama inatokea Malcom atamuoa Maya, asihamishe hizo kashfa na skendo kwenye familia yake.

Familia hiyo ya Cote ilibaki hapo sehemu ya kusubiria wagonjwa, kimya kila mtu akiwaza lake. Maya hata hakutaka kuuliza habari za mama yake. Net naye akabaki akimtafakari mama yake. Bibi Cote kama kawaida yake, alishajua hilo limeisha, mawazo akahamisha kwengine. Net akamuona anavuta pumzi kwa nguvu na kuzishusha taratibu, akajivuta nyuma kabisa ya kiti, akaegemea na kutulia kabisa.

Net alikuwa amekaa kati kati ya Maya na bibi yake. Maya amejiegemeza ubavuni kwa Net, Net akamzungushia mkono mabegani kwake. Akajisogeza kichwa mpaka akafikia shavu la bibi yake, akambusu. “Nakupenda Nana.” Bibi yake akacheka kidogo. “I know Son. Najua.” Net akajiegemeza kichwa kwa bibi yake kidogo kama anayefikiria kitu, akarudi kutulia. Net huyo alitakiwa jana yake awe amefunga ndoa takatifu, kanisani kabisa wala si bustanini au sehemu nyingine, kanisani kama ilivyo desturi ya familia yao. Bado walishikilia mila na desturi za zamani.

Ilikuwa ifanyike harusi kubwa sana iliyokuwa ikisubiriwa na maelfu ya watu na muda huo alitakiwa awe fungate na mkewe.  Na muda huo pia kwa bibi huyo alitakiwa awepo kanisani kwa ibada ya jumapili kama mkristo wa kawaida, lakini waliishia kituo cha polisi na kuhamia hospitali moja hadi nyingine. Bibi Cote alikuwa akitoa ushirikiano wa ajabu na wa mara ya kwanza kwa Maya. Uwepo wake huyo bibi kwa siku hiyo ya jumapili katika sehemu hizo ulishangaza kila mtu na kuogopesha, lakini kila alipofika, aliwaambia yupo pale kama bibi ya Maya tu na si vinginevyo. Maya alikuwa akilifurahia hilo na kujivunia kuona bibi yake yupo naye kwa wakati huo.

          Kila mmoja alikuwa ametulia pale, wakiendelea kuwaza yao na watu kuwashangaa kwa kujiiba familia hiyo iliyojaa skendo zilizofululiza, na jana yake naye Maya akaongeza yake tena iliyosindikizwa na kejeli ya huyo aliyembusu hadharani kuishia kumbaka mama watoto wake, Zoe. Wengine walisema Malcom alitaka tu pesa ya Maya lakini mapenzi yapo kwa mama watoto wake, Zoe. Wengine walimsema Maya kutokana na kashfa zake za nyuma, kuwa ni mtoto anayesumbua familia. Katikati ya matatizo makubwa ya familia yao, yeye hajali. Anafanya kama zamani alivyokuwa mlevi, akifanya mapenzi bila haya, tena hadharani tu!

Kwa hakika familia hiyo, walipamba mitandao, redio, television  na magazeti ya udaku. Kila mtu akiongea lake kwa zamu. Zaidi wakithaminisha pesa atakayoondoka nayo Tunda mara atakapomtaliki Net kwa kashfa ya ngono iliyozizima na kushangaza kila mtu.

~~~~~~~~~~~~~~~~~~

Wakaona yule askari, Logan na Malcom wanatoka na kuwasogelea. Wote wakasimama. “Naruhusiwa kumshika sasa hivi?” Maya akamuuliza bibi yake baada ya Malcom kuwa anawakaribia. “Kila kitu kimeenda sawa?” Bibi Cote naye akamgeukia Logan. “Kila kitu kimeenda sawa. Nafikiri nina kila kitu ninachokihitaji. Nimemruhusu hata huyu askari aondoke tu. Lakini nimemshauri Malcom kwa kipindi hiki, akae mbali kabisa na Zoe. Naona ameelewa na ameahidi atakaa naye mbali.” Logan akajibu kifasaha.

    Bibi Cote akaonekana ameridhika na hayo maelezo. Hakuongeza neno, akamgeukia Maya na tabasamu. Maya akajua ndio ameruhusiwa. Akamsogelea Malcom aliyekuwa amesimama nyuma kidogo pembeni ya yule askari. Akamkumbatia. “Nanuka Maya!” “Sijali. Unaendeleaje?” “Nilikuwa nipo kwenye hofu kubwa sana. Sijafanya chochote anachosema Zoe. Tafadhali naomba uniamini.”  Maya akambusu. “Nakuamini Malcom na ndio maana nipo hapa.” Malcom akamkumbatia tena kwa nguvu, akavuta pumzi kama aliyepata aghueni.

Maya alibaki ametulia hapo mikononi kwa Malcom hata asijali bibi yake na Net wanasubiri hapo nyuma yao. “That means a lot to me, Maya. Nilijua unaweza kunitilia mashaka.” “Hata kidogo.” Maya akaongea huku akitingisha kichwa kwa kumuhakikishia. Wakacheka kidogo. “Asante kwa kuja.” Akambusu Maya kama mara mbili hivi mfululizo ndipo wakageuka, maana Malcom aliwapa mgongo alipomkumbatia Maya, na alijitahidi kuzungumza naye kwa sauti ya chini.

Akiwa amemshika Maya, hapohapo akamsogelea bibi Cote akiwa na Logan. “Nashukuruni kwa kila kitu. Zaidi kuwa hapa na Maya. Najua sio rahisi. Ni aibu na fedheha.” Malcom akaanza mbele ya bibi Cote, Net, Logan na Roy aliyekuwa pembeni kidogo akimtizama Malcom bila kummaliza.

“Mungu wangu ni shahidi, sijambaka Zoe. Kama hawatabadilisha matokeo, vipimo vitaonyesha. Sijambaka. Mimi mwenyewe nilishangaa waliponisimamisha polisi njiani na kuniambia nipo chini ya ulinzi kwa kosa la ubakaji na kumjeruhi Zoe.” Malcom akaendelea taratibu. “Nilishangaa kwa kuwa mbali ya kumshika mkono wakati wa kuingia ukumbini, tena kwa kunilazimisha, na kucheza naye mziki, sikumgusa tena Zoe. Nilipotoka pale ukumbini na Maya na nikahakikisha amepanda gari, Zoe alitoka na kutaka nimrudishe nyumbani akiwa amekasirika sana. Sikutaka kuzungumza naye chochote njiani wakati namrudisha kwa wakati ule, kwa kuwa ninamjua Zoe.” Bibi Cote akakunja uso kidogo.

“Zoe anahasira na anapenda kupigana. Kwa hiyo nilijua nikiongea chochote na mimi ndiye niliyekuwa nikiendesha, nilijua anaweza kuanzisha ugomvi tukiwa njiani, tukaishia kupata ajali mbaya kama sio kifo.” Malcom akaendelea. “Na yeye akanyamaza mpaka nilipomfikisha kwake, kabla hajashuka aliniambia hivi, ‘utalipa kwa yote uliyonitendea. Na safari hii nitahakikisha hutatoka jela hata kwa dhamana.’ Sikumjibu. Akashuka.”

“Wakati nataka kuondoka, akapiga jiwe gari kwa nguvu. Ikabidi nisimame. Niliposimamisha tu gari, akaja upande wangu akaanza kugonga kioo kwa nguvu, nikashusha kioo nikifikiria pengine aliniambia kitu halafu sikusikia. Nikashangaa anaanza kunipiga makofi. Nilichofanya nilikwepa na kuondoa gari nikijua anataka ugomvi tu. Na hata hapo naapa hata sikumrudishia. Kwanza huwa simrudishii.” “Kwani huwa anapenda kupigana!?”  Akauliza Maya kwa mshangao.

“Zoe?”  Akauliza Roy kwa mshangao, wote wakamgeukia. “Yaani hata siku ile pale mgahawani, ilinibidi kuwahi kuja, nikijua angewafanyia fujo.” “Na pia nivile na wewe ulikuwa umetulia na ukaonekana mstaarabu zaidi yake, ndio maana alikosa sababu ya kuanzisha fujo.” Malcom akamkata Roy.

“Kwani Malcom hakukwambia kama Vic alishampiga Zoe?” Bibi Cote na Net wakamgeukia tena Roy na kutoa macho. “Vic yupi?”  Akauliza bibi Cote. “Vic huyuhuyu Vic aliyekuwa akimdhuru Maya. Zoe alitaka kumfanyia fujo, Vic akampiga sana tu.” Roy akaendelea. “Walichofanya wazazi wa Vic na mwanasheria wao, baada ya Vic kumpiga sana Zoe, wao ndio wakawahi polisi. Yaani wao wakawa kama ndio wamemshitaki Zoe. Zoe akaomba msamaha, wakafuta kesi. Kwa hiyo Zoe anapenda sana kesi na ugomvi.” Kimya.

“Nenda ukapumzike Malcom. Tutawasiliana.” Maya akamuongelesha kwa upendo. Malcom akambusu kichwani kwa upendo na kumvuta karibu. Safari hii karibu kabisa ya ubavu wake, mbele ya Net na bibi Cote huku akimwangalia. “Malcom!” Roy akamshitua kwa kumwita kidogo. Malcom akamwangalia Roy, akamkonyeza. “Nashukuruni sana kwa kuja.” Akarudia Malcom kuwashukuru kina Cote kama aliyekosa chakusema.

“Nitawapa muendelezo.” Akaaga Logan baada yakuona hakuna chamaana tena. “Unisalimie Maria na watoto.” “Asante sana.”  Logan akamjibu bibi Cote kwa heshima na kuondoka. Maya akajua bibi yake na Net wapo pale kwa ajili yake, na hawawezi kuondoka bila yeye ikabidi na yeye aagae. “Tutawasiliana Malcom. Nenda ukapumzike.” “Nikiamka nitakupigia.” Maya akambusu Malcom. “Asanteni sana.” Ikabidi na Roy naye aage kwa kushukuru. Net na bibi Cote wakageuka kidogo. “Asanteni.” Akarudia. “Anytime. Naamini safari hii Logan atalimaliza hili.” Net akaongea kwa kujiamini, akiwahakikishia.

“Ethan yuko wapi?” Akauliza bibi Cote. Malcom akamgeukia Roy. “Alikuja kumchukua usiku uleule.” Hapo hapo Malcom akabadilika sura, mpaka macho yakawa mekundu. “Kama alivyosema Net. Naamini safari hii Logan atamaliza kila kitu. Jitahidi kufuata kile alichokushauri. Ukiwa na swali, mpigie Logan, atakushauri vizuri.” Malcom akajifuta machozi. “Pole Malcom.” Maya akamsugua mgongoni kama kujaribu kumfariji.

“Sasa kuhusu mtoto?” Maya akamuuliza bibi yake kama ndio hakimu au mfanyakazi wa ustawi wa jamii. “Jumatatu Logan atafuatilia. Naamini mpaka jioni atakuwa na jibu lakueleweka.” Angalau Malcom akaridhika na wengine. Ni bibi Cote ameongea. Wakaagana, Maya akaondoka na bibi yake pamoja na Net. Roy akaondoka na Malcom.

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

Waliporudi nyumbani wakaambiwa Tunda amelala, Bibi Cote akamuita Net ofisini kwake. Maya akaenda moja kwa moja chumbani kwake. Net alimweleza bibi yake yote yaliyoendelea kati yake na mama yake. Lakini akamuona ametulia kama amekosa raha. “Asikuogopeshe. Ritha ni mjanja na anaakili, lakini safari hii amekamatwa na hatakaa akatoka. Naomba fikiria juu ya familia yako sio aliyokwambia Ritha.” Net akafikiria kidogo.

“Lakini Nana, sidhani kama huyu mtu yupo na akili timamu na sidhani hata kama anadhamira! Kwa upande fulani nimejuta kwenda, Nana. Nimepata majibu ambayo ni heri nisingeyajua. Natamani kama ningefanya kama Maya.” Bibi Cote kimya. “Hana majuto na chochote kile!” Net akaendelea kama anayevuta kumbukumbu. “Hajutii kutotulea! Hajutii kuharibu mahusiano na sisi! Hajutii kutaka kumuangamiza Tunda! Ni kama hana dhamira kabisa!” Net alilalamika.

“Kitu kilichomshitua tu, ni pale nilipomwambia nitamfilisi. Basi! Ni kama..” “Niangalie Net.” Net akajifuta machozi. “Mungu amekupa dhamana ya mambo mengi. Amekuamini na mke mzuri, mdogo ambaye unajua ni wapi amepita na wapi ameathirika. Pesa. Na sasa ni baba.” Bibi Cote akasimama na kumsogelea. 

“Sasa hivi ni wakati wa wewe kusimama kwa nafasi yako kufanya kwa juhudi zako zote, huku ukiangalia nyuma na kurekebisha kule ambako sisi wote. Kuanzia baba yako, mama yako, Papa, hata mimi, kule kote tulikokosea. Rekebisha na msaidie Tunda kuwa mke mzuri na mama anayetamani kuwa. Msaidie Maya aishie kwenye mikono ya mwanaume mzuri. Kama hivi leo ambavyo umefanya. Najua ni ngumu, lakini kile kiasi cha kujishusha. Kuacha mke wako akiwa mgonjwa na mtoto mdogo, kuwepo pale na yeye. That’s a lot, Son!” Akambusu.

“Am so proud of you.” “Asante Nana.” “Hakikisha huishii hapo. Ni ngumu, kunagarama yakulipa, lakini nakujua utaweza tu.” Net akamtizama bibi yake.

“Mbona kama unakitu hujui ukiweke vipi? Ni juu ya Malcom?” Bibi yake akamuuliza huku akimcheka. “Nahitaji muda Nana!” “Nimekuona jinsi unavyomtizama. Tafadhali mpe nafasi.” Net akasimama. “Sijui Nana!” “Niambie ni nini kinachokufanya umfungie moyo?” Net akafikiria. 

“Amejawa matatizo mazito kila kona ya maisha yake! Tunaanza mahusiano na kurekebisha matatizo yake wakati na sisi tuna mambo mengi sana! Maya mwenyewe hana muda mrefu tokea atoke rehab. Anajiingiza tena kwenye matatizo mengine! Anakuwa ni mtu ambaye anamikasa mizito kila wakati!” Net akaendelea kulalamika.

“Huyu mtu alishakuwa na ndoa ya kanisani. Kwa nini alioa na kwa nini aliacha?” “Watu wanakosea Net.” Bibi yake akajaribu kutetea. “Na huo ndio wasiwasi wangu Nana. Ndoa sio kitu cha kukurupuka. Msichana kama Zoe ni kama Vic tu. Hawana tofauti na hawajifichi. Alifanyaje maamuzi ya kumuoa na kupata naye mtoto? Ananitia mashaka kwenye maamuzi yake na uchukuaji wake hatua pia kwenye mambo, haonekani kama ni kijana anayeelewa ni nini anataka kwenye maisha! Sijui kama unanielewa?” Net alikuwa akiongea huku amesimama.

“Maya amepitia kwenye ukuaji uliomuathiri. Sitaki aje aishie kwenye ndoa itakayo muathiri pia. Sijui kama unanielewa Nana?” “Njoo hapa.” Akanyoosha mkono, Net akamsogelea. Akamshika mikono yote miwili. “Sipo kipofu katika hili. Nilishaulizia tabia zake. Na uzuri wote ule, hana mwanamke yeyote na wala hakuanzisha mahusiano yeyote yale baada ya kuachana na Zoe. Ni kijana ambaye anajitunza na ni mtu wa familia. Katika ugumu wote huo, hajatelekeza mtoto wake. Nimeambiwa walitaka kumuhamisha hapa Norfolk apelekwe Toronto kwa ahadi ya mshahara mkubwa tu, lakini alikataa sababu ya mtoto wake.” Bibi yake akaendelea.

“Ungedhani ndio angekubali ili awe mbali na Zoe, awe anatuma tu pesa za matumizi, lakini alishangaza viongozi wake pale alipokataa kwa sababu yakuwa karibu na mtoto wake. Tukio la jana limezidi kidogo tu, lakini nimeambiwa hayo ndiyo yamekuwa maisha ya Malcom. Jela na mahamani. Zoe anamuendesha vile atakavyo. Lakini amebaki. Kwa sehemu kubwa sana, kwa sasa hana sifa za kuwa mtumishi wa CSIS. Alishapoteza vigezo hivyo tokea amuoe Zoe, lakini nimeambiwa hao vijana wawili wanawashikilia kwa karibu sana. Na inabidi kufumbia macho matatizo ya Malcom, sababu ya utendaji kazi wao yeye na Roy.”

“Walichokifanya kwa Maya. Kuanzia kupeleleza mpaka kumuokoa, wanasema sio tukio geni kwenye chombo cha CSIS. Wanawatumia sana, na ni wazuri sana kazini. Ninachotaka kusema ni hivi. Ni kweli Malcom hana kitu upande wa sifa na pesa, sababu ya kashfa zake na Zoe. Anakatwa pesa kubwa sana kwa ajili ya talaka ambayo aliiomba yeye mwenyewe Malcom.” “Kwamba pale alipo anamtunza Zoe pia!?” Net akashangaa kidogo. “Yeap! Ameambiwa mpaka Zoe atakapoweza kujitegemea, na yeye Zoe nasikia anafanya makusudi. Hatafuti kazi kwa kuwa anajua mshahara wa Malcom upo. Na hilo Logan atashugulikia.” Bibi Cote akaongeza.

“Ila ni kweli Malcom anampenda Maya, ile yakutojifanya.” “Hilo halina ubishi.” “Basi msaidie kufikia viwango unavyotamani kuona mume wa Maya yupo.” Net akaweka mikono kichwani, akageuka. “Sina muda wa kufix au kurekebisha maisha ya watu Nana! Nina mambo mengi. Nina...” Akanyamaza kama aliyekumbuka kitu. Akamgeukia bibi yake na uso uliojaa cheko la kujisuta. “Nitafurahi ‘kujikana na kumsaidia. Najua itakuwa ngumu, lakini najua nitaweza’.” Akarudia maneno aliyoambiwa mwanzoni na bibi yake, ila akarudia kwa kejeli. Bibi Cote akaanza kucheka.

“Ukitulia, na akili zako zinatulia. Usiruhusu Ritha akakuchanganya wewe Net! Wewe umekuwa Cote kwa sababu.” “Nimekubali Nana. Ni hasira tu za mama. Lakini najua Malcom anampenda Maya. Na hilo ndilo ninalotamani kuliona kwa Maya. Anapendwa kwa dhati ili atulie. Maya ana moyo mzuri sana. Anastahili mtu ambaye atamuenzi.” “Sasa hivi umeanza kuongea.” Wakacheka.

“Na sasa hivi lazima uwe naye makini sana.” Bibi Cote akamtahadharisha. “Nimemuona. Ameweza mpaka kunigombesha!” Wakacheka kwa sauti ya chini na kuendelea kuteta. Angalau hasira za Net alizopandisha alipokwenda kukutana na mama yake zikaisha. Wakapanga mipango mingi tu, safari hii wakiwa na amani kuwa Ritha na Jeff wamekamatwa.

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

Juma hilo likaanza na hekaheka. Logan na kesi ya Malcom akifuatilia kila kona. Juu ya mtoto wa Malcom ambaye Zoe anamtumia kama fimbo huku mahakama kumpa yeye dhamana kubwa kuliko baba yake. Akaendelea kufuatilia malipo makubwa anayokatwa Malcom kwa ajili ya Zoe ambaye anakataa kutafuta kazi. Na uthibitisho kuwa Zoe amedanganya hakubakwa.

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

Net naye akaanza kuhangaika ubalozini tena kuondoa vile vikwazo alivyowawekea kina mama Penny  ili wafike Canada week hiyo. Jumatatu alipothibitishiwa tu kuwa Ritha alipelekwa jela siku ile ya jumapili, ndipo alipowasiliana na ubalozi na kuwapigia simu kina mama Penny. Akimsihi zaidi mama Penny afike yeye kwa haraka, hata kama mchungaji na wengine watachelewa, lakini yeye awahi kwani Tunda anamuhitaji sana.

BadoTunda hakuwa akitaka mtu yeyote amsaidie yeye wala mtoto. Maya ndio akawa msaada wakati bibi Cote na Net wakienda kazini. Na Ms Emily naye akawa msaada kwa sehemu tena Tunda akimuita, mara chache sana. Napo akimsikia tu mtoto wake analia, hata kama anausingizi kiasi gani, anaamka nakutaka apewe mtoto wake. Tunda akawa hapati muda wakutosha kupumzika.

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

Bibi Cote yeye alikuwa akihangaikia kifungo cha Ritha kuhakikisha safari hii hashindi kesi na anafungiwa sehemu yenye ‘maximum security’. Ulinzi mkali sana ambao hawasiliani na yeyote. Na kweli alitolewa hospitalini na maumivu yake vile vile na kupelekwa kifungoni.  

Familia ya Mchungaji na baba yake Tunda, nchini Canada.

I

likuwa siku ya jumatano Tunda alikuwa amelala kulekule chumbani kwa mtoto wake mida hiyo ya mchana, akiwa usingizini akasikia mtu anamuita kwa sauti yataratibu kama mama Penny. Akajua anaota. Maana hata kumpigia simu, Net alimwambia asubiri. Kwa hiyo hawakuwa wamewasiliana kwa muda mrefu kidogo. Tunda akaendelea kulala. “We Tunda!” Tunda akafungua macho. Akabaki akimtizama mama Penny. Akatulia kwa muda akidhani anaota. Wakabaki wakiangaliana kwa muda. “Mama Penny!?” Akaita taratibu. “Vipi? Nimeambiwa unaumwa.” “Kwa hiyo sio ndoto?” Mama Penny akaanza kucheka.

“Nimekuja na timu yangu yote.” Tunda akakaa. “Wako wapi!?” “Sebuleni. Wako na Maya pamoja na Net. Nimeingia hapa nimekukuta umelala sana. Nikakuacha, hapa nimerudi kukuangalia tena kujua kama umeamka.” Tunda alishaanza kulia. “Naumwa mwenzio.” Mama Penny akakaa pale kitandani, Tunda akamsogelea na kumkumbatia. Akaendelea kulia. “Nini?” “Sijui hofu! Kidonda cha operation kinaendelea vizuri. Ila nimejawa hofu, sina raha dada.” “Pole mama. Pole sana. Net ametusimulia kila kitu tulipofika tu hapa. Lakini Tunda, tumekuombea sana mdogo wangu. Mungu yupo na wewe. Usigope kabisa. Sasa hivi lea mwanao kwa furaha.” Akajaribu kumtuliza, maneno mengi ya mama Penny, nyumba hiyo isiyozoea kelele, kwa mara ya kwanza wakamsikia Tunda anacheka kwa sauti. Mpaka Carter akashangaa.

Tunda alikuwa akicheka kama sio yeye aliyekuwa anamuhofu kila mtu! Tokea arudi hapo ndani na mtoto wake, hata uchangamfu mdogo aliokuwa nao, ulimuisha kabisaa. Siku hiyo akatokea Tunda mwingine tena. Kicheko kikajaa hapo chumbani kwa mwanae.  “Ninavyocheka kwa sauti! Mpaka Cote ataamka!” “Mbona nishaanza kazi ya ulezi! Mwanao hayupo hapo kitandani kwake. Nilivyoambiwa tu ukimsikia akilia  unaamka, nikaomba aende akakae na babu yake hapo sebuleni na kina Penny wamshangae mtoto wa kizungu, ili ulale kidogo.” Tunda akacheka sana.

“Na nimzungu haswa dada! Hafanani hata na Net! Hajachanganya hata!” “Maya ametuambia amefanana na babu yao.” “Hata Nana amesema hivyohivyo.” Mara kina Penny wakaingia. “Sasa sio mumvamie. Mwenzenu anamshono wa upasuaji.” Mama yao akawazuia. “Tumemuona mtoto wa kizungu! Alikuwa amelazwa kwenye kitanda cha kizungu, sasa hivi dady yupo naye!” Penny akaanza bila hata salamu. Tunda akazidi kucheka.

“Anti Tunda unaishi kwenye jumba la kifalme!” Pendo naye akadakia. Tunda akazidi kucheka. “Yaani nyinyi viumbe nilikuwa na hamu na nyinyi! Halafu Net hakuniambia kama mtakuja!” Net akaingia na tabasamu la ushindi. Tunda akatoka pale kitandani na kumfuata pale mlangoni na kumbusu. “You are the best husband in the entire wide world.” Tunda akambusu tena. “I know.” Net akajibu kwa kujigamba kuwa yeye anajua kama yeye ni mume bora ulimwenguni kote. Tunda akampiga ngumi ya bega.

“Kweli sitanii. Hii ni surprise ambayo sikuwa hata naifikiria. Asante Net.” “Nilijua tu utafurahi.” “Umemuona Penny lakini?” Net akamtizama Penny na kuanza kucheka. “Tumekutana tu pale uwanja wa ndege, akaniuliza kama bado nakumbuka kiswahili.” Wote wakacheka. “Halafu akauliza kama mtoto ni wa kizungu.” Tunda akazidi kucheka. “Yaani Penny nyinyi! Sasa umemuona?” “Nimemuona na mama ameniosha mikono nikamshika nywele. Ni za kizungu!” Tunda akazidi kucheka na kushangaa.

“Basi nimelala sana! Hata sikuwasikia wakati mnafanya yote hayo.” “Maya alituambia ndio umelala tu. Tukaona tukuache tuondoke na mtoto. Maana maswali yalianza hapahapa! Pendo naye akataka kujua kama macho ni ya rangi ya bahari!” Wakazidi kucheka. “Nikaona tutoke naye tu huyo mtoto, akaamkie hukohuko mbele ya safari, tuyaone na hayo macho.” Tunda akabadilika kabisa. Furaha ilimjaa, utafikiri ndio anaingia kwenye hilo jumba lenye kila kitu, kumbe amepata watu anaofahamiana nao, na anauhakika kuwa wanampenda kwa dhati. Hata wazo la mtoto kama yupo salama au la, halikupita tena kichwani mwake. Yeye kicheko tu. Akatoka kwenda kumsalimia baba yake na mchungaji.

Ilikuwa ni furaha iliyojaa kilio kwa Tunda. Hakuamini kama kwa mara nyingine tena, yupo nyumba moja na baba yake. Baada ya salamu mchungaji akataka waombe wote kwa pamoja. Wakamuombea Tunda na mtoto, na kukemea roho ya hofu ili Tunda ajawe amani yakulea mtoto wake. Angalau nyumba hiyo siku hiyo watu waliomba, wakaongezewa na vicheko. 

Kina Cote na mahakamani.

K

ina Cote wakawa na kesi mbili kwa wakati mmoja. Ya Malcom na ya Ritha ambayo ilinguruma haswa, na kupamba vyombo vya habari. Mama anayedhuru watoto wakuwazaa mwenyewe na watoto wanaomshitaki mama yao! Halafu ni kina Cote sasa! Jeff alitoa ushahidi wake wote bila kuficha jambo hata moja. Akaeleza sehemu ya kwanza ambayo walikutana Malinda na Ritha kumkabidhi pesa ya kwanza. Net akamsikia bibi yake amesema “Yess!”

Maana Ritha alitumia hoja ileile kuwa siku ile alikiri kwa kuwa Jeff alimshikia risasi na alishampiga. Kwa hiyo alikana kuwa hamfahamu Jeff wala Malinda, ila alikiri kwa kuwa alikuwa anatishwa na Jeff. Pale pale mahakamani, wakati kesi inaendelea. Jeff akitoa ushahidi wake kuwa walitumwa na Ritha, bibi Cote akaandika kiujumbe kwenye kikaratasi kumwambia Logan aombe kwa hakimu apewe muda wakuleta ushahidi mwingine.

Logan aliposoma tu ule ujumbe, akafanya kama alivyoambiwa na bibi Cote. Akamuomba hakimu. Kesi yao ikaairishwa. Wakapewa tarehe ya kurudi mahakamani wakiwa na huo ushahidi mwingine.

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

Wakati kina Cote wanahangaika kutafuta ushahidi wa kumfunga Ritha, Logan naye akahamia kwenye kesi ya Malcom. Hiyo haikusumbua. Malcom alikuwa afisa usalama pia. Wenzake walimbemba vizuri sana. Na kwa kuwa Logan alishaanza vizuri, haikusumbua hata kidogo kumshinda Zoe.

Siku walipoitwa mahakamani. Kesi ikawa nyepesi sana. Polisi waliomkamata Malcom siku ile usiku na kumsindikiza kwenye vipimo pia wakawa mashahidi wa Malcom. Logan akawakilisha ushahidi wake wote, Zoe akaishia kuwa mkosaji. Malcom hakutaka kumshitaki. Yeye akasema anataka haki yake na ya mtoto wake, tu. Akapewa siku sawa za kuwa na mtoto wake. Matumizi kwa Zoe yakafutwa kwa kuwa mahakama ilimwamuru kwa kipindi hicho ambacho wanagawana au ku share custody ya mtoto, siku ambazo mtoto yupo na Malcom, yeye aende kazini.

Na palepale mahakamani, Malcom akaomba kuongea. Akasema mtoto wake anaakili sana. Haoni kama ni sawa awe anakaa tu nyumbani, anataka kumuanzisha shule na yeye mwenyewe ndio atalipia. Mahakama ikakubali.

Hatimaye Maya naye!

W

akati wanatoka mahakamani siku hiyo ya mwisho ya hukumu kati ya Malcom na Zoe, Malcom akiwa amesindikizwa  na familia yote ya Roy na baadhi ya wafanyakazi wenzake. Maya naye akiwa amesindikizwa na bibi yake pamoja na Net na mkewe, Tunda. Na ndivyo walivyokuwa wakifanya kila siku, siku ya kesi ya Malcom. Wote watatu yaani mpaka Tunda, kumsindikiza Maya, ili Maya asiwe peke yake mahakamani. Na kweli ilimsaidia sana Maya. Akachukua sura mpya mitandaoni. Hakuwa kituko tena. Kwani safari hii familia yake, mpaka bibi Cote, alisimama naye kila mahali. Badala ya kashfa kwa Malcom na Maya, ikawa sifa sasa.

Sasa wakiwa nje ya mahakama siku hiyo wakipongezana na kufurahia ushindi wa Malcom, familia ya Roy kama ndugu wa karibu wa Malcom na Ethan, ikishukuru familia ya Cote, Malcom akapiga goti mbele ya Maya. Pakazuka ukimya mkubwa sana kwani kila mtu alijua ni nini Malcom anakaribia kufanya. Hata vyombo vya habari, wapiga picha na watangazaji waliokuwa wamewapa kina Cote kipaumbele wakiwapiga wao picha, nakutaka bibi Cote au hata Net, azungumze chochote, wakawageuzia kamera, macho na masikio yao kwa Malcom na Maya.

“Umesimama na mimi, na kuniamini kipindi ambacho nilihitaji sana. Hapakuwa na mazingira yakuaminika tokea siku ya kwanza tunakutana Maya. Lakini nimeona mapenzi ya kweli kutoka kwako. Nimeona vile unavyokuwa na mimi na Ethan. Umejawa upendo na heshima kwangu, Maya. Unawapenda na kuwaheshimu wazazi wangu.” Akimaanisha wazazi wa Roy. Grandma Pauline naye alikuwa hapo na mumewe, akakubali kwa kutingisha kichwa huku akifuta machozi. “Kweli wewe ni mwema Maya. Tunakupenda.” Akaongeza Grandma Pauline, watu wakacheka kidogo. Bado Malcom alikuwa amepiga magoti mbele ya Maya, amemshika mikono yake yote miwili.

“Nataka uishi na mimi pamoja na Ethan. Tutengeneze familia ambayo hata mimi sikubahatika kuwa nayo. Itakayojengwa na mapenzi tu.” Maya alibaki anacheka kwa furaha akijifuta machozi. “Marry him already!” Akasikika Roy, watu wote waliokuwa wamewazunguka wakacheka. “Marry me, Maya!” Akasisitiza tena Malcom akiomba ndoa kwa mrembo huyo. “With one condition.” Akajibu Maya. Kila mtu akatulia wakitaka kujua hilo sharti la Maya. Ni picha tu ndizo zilizokuwa zikisikika mlio wake. Wakavuta watu pale nje ya mahakama. Wakasogea kushuhudia.

“Anything.” Malcom akawa tayari kwa lolote. Maya akacheka huku aking’ata meno akimfikiria. “Ni nini?” Akauliza Malcom kwa shauku akiwa bado amepiga magoti, akitaka kujua hicho kitu anachotaka Maya. “Kama tutaishi na Nana!” Watu wote wakacheka tena, mpaka bibi Cote. Malcom akatoa kimkoba cha pete mfukoni bila kujibu, Maya akashangaa. “Ndio umekubali!?” “Oooh yeah! Popote nitaishi na wewe Maya, hata kama ni chini ya mti ilimradi tu niwe na wewe.” Watu wakapiga makofi nakufurahia jibu la Malcom ambalo lilijaa hekima si lakilimbukeni. 

Malcom akamvalisha ile pete, akasimama kupata busu sasa. Malcom alilitendea haki hilo busu, ungependa kuona jinsi alivyomshikilia kimwana huyo. Picha zilipigwa kila kona. Ni kweli kwa kuwaangalia tu, ungejua wanapendana.

Malcom akaomba msamaha kwa kina Cote. “Samahanini sana. Najua huu sio wakati mwafaka wa kumchumbia Maya, lakini nisingeweza kusubiri. Najua nimefanya makosa mengi kwenye maamuzi yangu, lakini si katika hili na kumpenda Maya.” “Hakuna muda muafaka kwenye mapenzi Malcom. Na wakati wote mapenzi hayatakiwi kusubiri. Nawapongeza sana, na karibu kwenye familia.” Net akajibu yeye wa kwanza na kumpa mkono, wakakumbatiana. Ilimfurahisha sana bibi Cote, na kumgusa Maya. Ilikuwa na maana kubwa sana kwao. Ni Net amemkaribisha Malcom kwenye familia! Tena kwa kumkumbatia! Hata Malcom alijisikia vizuri.

Bibi Cote naye akapata nafasi ya kuwapongeza palepale. Naye akamkaribisha Malcom na Ethan kwenye familia. Kila mtu akajua jinsi Ethan alivyogusa moyo wa huyo bibi. Alimsifia na kumwambia ni jinsi gani anasubiri kwa hamu kupata naye muda wa pamoja. “Mimi sijui kupika kama grandma Pauline, ila naamini tutakuwa na wakati mzuri tu.” Bibi Cote alimwambia Ethan  nakufanya watu wacheke. Tunda naye akawapongeza kwa kuwakumbatia ndipo kila mtu akapata nafasi yakuwapongeza.

Kwa heshima kubwa sana, familia ya Roy, yaani wazazi wake wakawakaribisha kina Cote nyumbani kwao kwa sherehe ya kuwapongeza Malcom na Maya. “Tunajua huu sio wakati mwafaka kwenu kufanya sherehe, lakini tunawakaribisha kwa chakula cha usiku ili kumshukuru Mungu pamoja.” Akaongea grandma Pauline akimtizama kwa heshima zote bibi Cote. Bibi Cote naye akamtizama Net na Tunda. 

“Na mimi nataka nikale cookies za grandma Pauline.” Tunda akajibu huku akicheka. Wote wakacheka. “Nafikiri kila mtu anataka kula cookies za grandma Pauline. Ethan amekuwa akizisifia sana.” Net akaongeza kwa mkewe. Inamaana wamekubali huo mwaliko. Maya akashukuru sana familia yake. Angalau kina Cote wakawa wameshinda kesi moja ya Malcom na angalau safari za mahakamani zikapungua ikabaki kazi ya kukusanya ushahidi kumaliza kesi ya Ritha. 

Hatima ya Ritha yawa Mbaya zaidi na alivyo fikiri.

N

dani ya muda huo waliopewa na mahakama, bibi Cote akaomba mtu avute picha kutoka kwenye satelite siku na muda aliosema Jeff kuwa Malinda na Ritha walikutana kwa makabidhiano ya pesa. Bahati nzuri Malinda na Ritha walikutana Park. Sehemu ya wazi kabisa. Yule mtu wa bibi Cote, alitoa picha za Malinda na Ritha, kama waliokwenda kupiga picha studio. Akamkabidhi Logan. Wakatafuta ni wapi Ritha alipata kiwango chote cha pesa bila kuonekana amekitoa kwenye akaunti zake za hapo nchini. Ndipo sasa Net kama mmiliki wa Cote, akawasiliana na benki za Tanzania kuomba benki statement zote za kampuni aliyokuwa amefunga mama yake, lakini akaunti za benki hakuwa amefunga.

Ritha alijua hakuna mtu ambaye angeweza kufikiria hilo. Kuwa akaunti za kampuni aliyofunga bado zinafanya kazi! Akasahau mwembe hauzai pera. Net akafikiria na kuomba kupewa benk statement. Ndipo wakajua alichukua hiyo pesa kutoka nchini Tanzania. Wakawa wamemkamata Ritha vizuri sana. Wakawa na ushahidi ambao Ritha hawezi kupinga tena. Kiwango kilekile cha pesa Ritha alichokitoa kwenye dola akaunti ya akaunti ya Cote ya nchini Tanzania ndicho hicho hicho Jeff alisema alimlipa Malinda kama malipo ya awali.

Na ushahidi mwingine ukawa sasa wa hizo picha ambazo zilionekana Ritha na Malinda wamekaa kwenye benchi la Park, kama waliokuwa kwenye mazungumzo kabisa. Na siku ya kesi mtaalamu wa mahakama alipopewa hizo picha kuzitazama, akathibitisha si zakutengenezwa ni picha za ukweli. Siku hiyo ndipo hukumu ya Ritha ikatolewa. Kifungo cha maisha tena kwenye jela yenye maximum security, kama muuaji hatari sana. Kwani hata njama zake za Tanzania, wakati Net alipokuwa akihojiwa mahakamani hapo, alizieleza kwa undani kabisa, mbele ya hakimu na waandishi wa habari.

Alimshitaki mama yake bila kumbakisha huku akisema hana sababu yakumsingizia mama yake ambaye aliacha maisha yake huko nchini Canada na kwenda kumtumikia bila kujua anatumika kwenye mali zake mwenyewe. Na hilo Net alilishitaki kuwa mama yake alijua, lakini alimficha ili kumdhulumu tu. Akimpa mshahara kama mfanyakazi wa kawaida, na baadaye kumsingizia kuwa alikuwa akimwibia.

Bibi Cote alikuwa akishangaa vile Net alivyokuwa amejipanga kwenye kumshitaki mama yake bila hata kuzungumza naye. Net hakumbakisha mama yake. Aliongea mengi huku akiomba vyombo vya usalama vimsaidie yeye na mke wake Tunda, kumfungia Ritha, ili waweze kukuza familia ambayo yeye na Maya waliikosa na ili pia Ritha asiendelee kumwaga damu ya watu wasio na hatia.

Aliposikia mama yake anakwenda kufungiwa kwenye aina ya jela aliyomuahidi siku alipoenda kumtembelea hospitalini akiwa na pingu, Net akafurahia sana moyoni, akamgeukia bibi yake akijua hiyo ni kazi ya bibi yake. Bibi Cote akamkonyeza, wakacheka. Wakati Ritha anataka kutolewa pale mahakamani bibi, Cote akamuita taratibu. Ritha akageuka. “Gotcha!” Akamnongoneza kwa sauti ya chini iliyojaa ushindi kuwa amemkamata. Ritha akageuka bila ya kujibu.

Si Maya wala Tunda waliotaka kufika mahakamani siku za kesi ya Ritha. Maya alisema yeye hataki hata kuiona sura yake. Ila anataka kujua kama yeye yupo huru. Akimaanisha uhuru wake unategemea na kufungwa kwa mama yake. Kwa muujiza na kufahamika kwa bibi Cote, kesi ya Ritha ilichukua miezi mitatu na nusu tu mpaka hukumu yake. Hilo likawa jambo lililowaridhisha wote.

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

Bibi Cote akaona wao kama familia, wanawajibika kwa vyombo vya habari na raia ambao walikuwa wakiwafuatilia kwa karibu sana. Angalau kuzungumza nao na kuwaambia kilichokuwa kikiendelea na kujibu maswali yao. Waandishi wa habari wakakusanyika kwa wingi sana sehemu yakutoa habari katikati ya mji. Bibi Cote, Net, Tunda, Maya na Malcom waliwasili hapo. Mdahalo ukaanza. Bibi Cote akaeleza kwa kifupi kilichokuwa kikiendelea kwenye familia hiyo. Akakiri makosa yake yeye kama mlezi wa Maya na Net. Akatoa nafasi ya maswali matano tu.

Moja wapo likawa kwa Tunda ambaye hakutegemea kabisa. “Watu wengi wamekisia kiasi cha pesa ambayo utapata baada ya kumtaliki mumeo. Kwa hakika ni pesa nyingi sana. Unalichukuliaje hilo?” Mpaka Net akabadilika rangi, lakini wakashangaa Tunda anacheka taratibu. “Pesa bila Net! Labda nipewe pesa na Net wangu.” Akajibu Tunda huku akicheka taratibu. “Huyu atabaki na mimi tu, hana pakwenda.” “Na juu ya kosa lake la kuzini baada ya ndoa?” Wakamuongezea Tunda swali la haraka haraka. “Nani ambaye angepata nafasi yakumlevya mtu kama Nathaniel Cote na asitumie bahati hiyo ipasavyo! Na by the way, ndoa takatifu bado. Namdai ndoa ya kanisani kwa hiyo msiseme baada ya ndoa, mnanifupishia safari. Nahesabu ndoa baada ya kiapo cha kanisani.” Tunda akampiga kidogo Net begani, angalau akabadilisha ile hali ya kashfa pale, wakacheka.  

“Ahadi ipo pale pale.” Net akajibu na kumbusu. “Na usichelewe hivyo!” Watu wakacheka tena. Angalau wakasafisha ile hali ya hewa, ujasiri ukarudi kwa Net na kuweza kuongea machache. Yakaongezwa maswali machache kwa Maya na Malcom, wakatangaza tarehe yao ya harusi kina Cote wakaondoka.

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

Kwa heshima ya kaka yake, Maya akasubiri mpaka kaka yake aoe ndipo na yeye aolewe. Maandalizi ya harusi kati ya Net na Tunda yakaanza upya. Tena safari hii na Tunda ambaye amejifungua. Hana kichefu chefu, hana uchovu wala ugonjwa. Jasiri akijiamini na kujua yeye ndio mama Cote haswa! Amri yote ipo kwake! Na Net naye akawa amejifunza kutokana na makosa. Adabu na heshima kwa kila anachofanya Tunda ikaongezeka.

Muda wote huo mama Penny na familia yake bado walikuwepo pale. Mama Penny akisaidia kumlea Cote na kulipwa pesa nzuri tu. Shida ya kurudi Tanzania ambako kanisa lilishakufa na biashara ya upambaji ilishaanza kusumbua ikaanza kuingia akilini. Wanaishi kwenye jumba la kifahari, wamepewa malazi upande wao. Wapo huru. Watoto wakaingizwa kwenye shule za hapohapo wakipelekwa na kurudishwa! Wanakula chakula chakupikiwa na mtaalamu wa mapishi kabisa! Hamu yakurudi Tanzania ikaisha.

Mchungaji akachangamkia maisha. Akamuomba kazi Net. Akamwambia anaweza hata kumpa lori moja akaanza kuendesha. Net akafurahia utayari wake. Akampa kazi upande wa boti zinazozungusha watalii kwenye mto. Wakaanza kujiingizia dola. Mama Penny kwa kumlea Cote, mchungaji kwenye kazi hiyo kwenye boti akizungusha watalii. Wanaishi na kula buree. Watoto wanasomeshwa shule nzuri. Yote hayo Net alifanya kwa ajili ya mkewe, kumfanya ajisikie vizuri. Na mtoto akawa analelewa vizuri. Tunda akawa huru hata kutoka na kufanya vitu vingine sababu ya mama Penny kuweza kummudu mtoto wake.

Kipindi hicho Tunda alimwambia baba yake apumzike tu.  Alimpeleka hospitalini na kufanyiwa vipimo kama yeye. Kisha akamtafutia mtu maalumu wa kumfanyia mazoezi na chakula maalumu chakumjenga mwili. Mzee huyo akawa anafurahia uzazi, huku akisubiri siku ya harusi.

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~ 

M

aandalizi yao yalipokamilika, ndani ya mwezi tu, Net na Tunda nao hatimaye wakafunga ndoa takatifu kanisani, wakiwa wamezungukwa na watu wanao wapenda. Baba yake Tunda ndiye aliyemshika mkono kumkabidhisha Tunda kwa Net pale kanisani.  Kama shauku ya Tunda. Tunda alipendeza sana. Akakata kiu yake. Alivaa gauni ambalo lilisimuliwa mitandaoni bila kikomo. Alikuwa amesimama mbele ya mchungaji mbele kabisa kanisani, lakini shela ilikuwa katikati ya kanisa hilo. Na ilikuwa imejaa vizuri sana.

Bibi Cote alimvalisha taji ya alumasi tupu kichwani. Na ule weusi wa Tunda, alijawa alumasi, usingejua kama ni yule Tunda aliyezaliwa na kutupwa milima ya Ulugulu, mjini Morogoro. Ambaye hata hakuwa akizungumza si kingereza tu, hata kutengeneza sentensi ya kiswahili ilikuwa ni shida!

Siku hiyo ndipo watu waliposhuhudia utajiri wa Cote. Kuanzia muonekano wa Tunda mpaka sherehe yenyewe. Habari zake na picha zake na Net, zilipamba magazeti ya uzunguni, akabakia gumzo.

Mrembo huyo kutoka Africa, tena Tanzania, alikataa talaka yenye pesa nyingi, akisema anamtaka Net. “Kama nitalipwa pesa yote hiyo halafu wakanipa na Net, sitafikiria hata mara mbili. Lakini si pesa bila Net wangu.”  Usemi huo wa Tunda ulifunga wengi midomo, na ukawa wa kusemwa kila mahali.

Maya naye akafunga ndoa nzuri sana na Malcom. Iligaramiwa na kina Cote kama ilivyodesturi yao, mwanamke kugaramia harusi. Maya akamtaka Tunda ndio awe msimamizi wake wa harusi. Na Malcom naye akamtaka Roy ndio awe msimamizi wake. Harusi nzuri, tulivu ikafungwa. Wasimamizi Tunda na Roy.

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

Maisha ya kina Cote yakaendelea bila hata kutamkwa tena mama mzazi wa Maya na Net. Nana akawa ndio Mama. Ila wito wa utumishi ukazidi kumsumbua baba Penny. Kila kitu alikuwa nacho, lakini si utumishi kama alivyokuwa mchungaji. Akakosa raha ya kila kitu. Kila akimtizama Tunda, pale alipo na yale aliyofanikiwa kuyapata sababu ya msaada wao yeye na mkewe, akaona wanajifunga kwenye madogo sana.

“Wapo kina Tunda wangapi huko nyumbani ambao tunaweza kuwasaidia na kuwafikisha kama hapa tulipomfikisha Tunda?” Baba Penny akazungumza na mkewe walipokuwa wenyewe, chumbani kwao, kwenye jumba hilo la kifahari! Alijua wazi ni kama kujipokonya tonge mdomoni kwa aina ya kipato wanachojiingizia, na maisha wanayoishi kwa wakati huo lakini wakakubaliana na mkewe warudi tu kuishi nyumbani.

Ilimuumiza sana Tunda lakini na yeye akakubaliana nao. Asiwe mchoyo na kufungia wengine bahati zao kama yeye alivyonufaika na utumishi wa baba na mama Penny. Wakawaruhusu kwa upendo kurudi Tanzania kwa utumishi. Familia hiyo waliosimama pamoja kwa utumishi wakarudi nchini Tanzania. Mama Penny wakakubaliana na familia ya Cote. Yaani Tunda na Net, kusimamia nyumba za Tunda nchini Tanzania kwa biashara huku wakiwekeza yeye na Tunda kwa kila wazo wanaloshauriana. Mama Penny kichwa inayofanya kazi, akawa mtu wakubuni na kushauriana na Tunda, kisha wanawekeza kwa pamoja. Maisha yakaendelea kuleta maana kwao. Mchungaji alianzidha tena kanisa na kituo kama kinachofanana na cha bibi Cote kusaidia wanawake, Tunda akiwa msimamizi mkuu. Wakiita tawi dogo la Canada. Angalau mchungaji akaweza kutumika katika wito wake vizuri wakisaidia sana wanawake.

*************MWISHO**************

CONVERSATION

0 Comments:

Post a Comment