Aina ya mahusiano ya kimapenzi aliyokuwa nayo yalimfanya kujikuta akiishi
kwa kukwepa watu zaidi wasichana waliodhani ni maringo wasijue kinachomkabili
mrembo huyo aliyejaliwa na urefu wa kike uliomfanya avutie kwenye kila aina ya
mavazi anayoweka mwilini. Usingemkuta Naya akisalimia wala kumtizama mtu. Hakujulikana
ni wapi analala. Chuoni au nje ya chuo kwa mpenzi wake. Wanachuo karibu wote
walishamfahamu na wengine kumjua mmiliki wa gari iliyokuwa ikimshusha Naya hapo
chuoni. Alikuwa kijana wa hapohapo jijini Morogoro. Alijulikana kwa pesa, hata
aina hiyo ya gari iliyokuwa ikimfuata na kumrudiaha Naya ilitangaza utajiri wa
Malon. Ilikuwa nzuri na ya thamani sana. Kubwa, SUV ya silver iliyovimba vizuri
na kuzungushiwa vioo vyeusi. Akishuka Naya ndani ya hiyo gari, ungesema ni
mwanamtindo maarufu kutoka nchini Marekani, Los Angelas.
Kila mtu alikuwa akitamani kumuona anaposhuka garini akiwa anarudi
chuoni. Mwendo wake akiwa anatokea kwenye hiyo gari kuelekea chumbani kwake au
darasani kuhudhuria vipindi, ungependa kuwepo na kumtizama.
Hakuwa akikosa kipindi hata kimoja kitu kilichowashangaza wengi.
Nidhamu ya shule ilikuwepo kwa hali ya juu. Alichukua chumba na wasichana
wengine wawili hapohapo chuoni Mzumbe na kukitumia mara chache sana, zaidi kuweka
madaftari yake na baadhi ya vitu vyake vichache. Kilikuwa chumba cha watu
watatu tu na yeye akiwemo humo.
Wenzake walio bahatika kuwa na Naya chumba kimoja, wao walisema
huwa anawasalimia. Na endapo ni zamu yake ya usafi, alikuwa na mtu ambaye
alimlipa kumfanyia usafi, msichana aliyekuwa akitokea mtaani na kuja hapo
kwenye hosteli zao. Basi atafanya majukumu ya Naya yote, ndipo anaondoka na
yeye.
Usingemkuta akibishana au kugombana na mtu. Kwanza hakuwa na huo
muda. Mambo yake aliyafanya kwa utulivu na hakuwa na muda na mtu yeyote
isipokuwa salamu tu au jambo lihusulo masomo awapo darasani na wenzie, basi.
Akawa hivyo tokea anafika hapo mwaka wa kwanza. Naya akawa gumzo kwenye chuo
hicho cha Mzumbe. Alikuwa akisomea mambo ya masoko. Markerting. Watu waliokuwa
wakitaniwa ni wauza sura. Basi hilo jina likaendana kabisa na Naya.
Bila kufungua mdomo, alilipa kumtizama. Na ungetaka kumsogelea
kununua chochote anachotaka kukuuzia. Lakini napo ilikuwa shida kuisikia sauti
yake. Hakujibu swali wala kuuliza swali darasani. Atatulia kwenye kiti chake
kuanzia anaingia mpaka anatoka labda wapangiwe kazi yakufanya kama kundi
nakutakiwa kuiwakilisha mbele ya wenzao darasani, hapo atatoa ushirikiano wote
na akitoa mchango wake ndipo utajua si mjinga kwenye masomo, anao uelewa mkubwa
sana kwa kilichowapeleka hapo chuoni.
Muhula wa kwanza alikuwa anachumba, lakini kila siku jioni alikuwa
anakuja kuchukuliwa na kurudishwa asubuhi. Hakuwa akichukua mkopo wa serikali.
Alijilipia ada yeye mwenyewe. Japokuwa Malon mpenzi wake alishajulikana hapo
chuoni hata kwa wasio wazawa wa huo mji kasoro bahari, Morogoro, lakini wengine
walijua lazima Naya mwenyewe pia atakuwa mtoto wa milionea mmoja mkubwa sana huko
jijini Dar. Hakuonekana kama msichana aliyezikuta pesa kwa Malon. Alionekana kama
aliyezaliwa kwenye pesa, na kukulia kwenye pesa ndipo akakutana na huyo mwenye
pesa, Malon. Ikawa kukisia kwingi na kubashiri kwa hali ya juu. Lakini hakuna
aliyejua ukweli juu ya Naya kwa kuwa hakutengeneza rafiki hata mmoja hapo
chuoni.
Muhula huo wa kwanza kwa mwaka wa kwanza ukaendelea kila mtu
akitamani ukaribu naye na kumfahamu kwa karibu. Lakini akajitahidi kujitenga haswa.
Wakatafuta kujua maendeleo yake darasani. Ikabidi kumfuatilia hata kujua alama
anazopata kama zinaendana na muonekano wake. Lakini wakaja gundua ni msichana
aliyekuwa akifanya kawaida. Hakuwa akipata alama za juu sana, lakini pia hakuwa
akifeli.
Mwisho wa muhula wa kwanza, alipotoka kwenye mtihani wake wa mwisho, hata hakukaa hapo chuoni. Gari lilelile lililokuwa likija kumchukua kila siku chuoni, lilikuwa likimsubiria nje ya hosteli yao. Alitoka kwenye mitihani, akachukua baadhi ya vitu vyake, na kuchukua baadhi ya vitu vyake, nakuondoka hapo chuoni. Baadhi ya watu walimsikia akizungumza kwenye simu akisema, “Sio jumamosi hii. Ni ile ingine ndio tutakwenda.” Kimya kwa muda. “Siku 8 tu ndio Dubai.” Alisikika tu hivyo wakati anatoka hapo kwenye chumba chao, akiondoka bila yakumuaga mtu.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
Dereva alimsaidia kuingiza mizigo yote ndani. Kuanzia masanduku
makubwa mpaka madogo, yalikuwa ya thamani sana. Walioshuhudia akiingia,
walisimama kukodoa macho. Hakugusa
chochote kwani wakati wote alikuwa na kucha ndefu na nadhifu. Pengine alihofia
kuvunja kucha zake! Lakini dereva taksii alimsaidia kumshushia vitu vyake vyote
na kumwingizia mpaka ndani chumbani kwao, Naya akimwelekeza.
Maisha ya muhula wa pili yakaanza watu wakishangaa harudi tena nyumbani
wala haji kuchukuliwa jioni. Mpaka siku ya ijumaa gari lilelile lilirudi tena
hapo chuoni. Walimuona Naya ametoka. Badala yakupanda, walimuona amesimama
upande wa dereva. Akaonekana akizungumza kidogo na dereva, kisha Naya
akaondoka. Lile gari lilisimama hapo kama nusu saa mbeleni, baadaye likaondoka
bila Naya.
Naya alikaa hapo chuoni mpaka jumapili tena asubuhi. Gari ileile
ikasimama pale pale. Safari hii akashuka kaka mtanashati haswa. Watu wakaanza
kuitana. Kwa mara ya kwanza kushuka mtu. Kijana mzuri na alioonekana hata mambo
yake ni mazuri. Misuli iliyovuta macho ya wadada zaidi na kuzidi kuitana mpaka
madirishani. “Ndiye atakuwa huyo Malon
bwana wake Naya!” “Mimi namjua Malon, ndiye huyo.” Mwingine akaongeza kishabiki.
“Anakuja. Tuondokeni.” “Kwa nini? Tusubirini tuone.” Mwingine akawakataza
wenzie waliokuwa wamesimama nje ya hosteli nyingine.
“Habari zenu?” Akasalimia yule kijana aliyeshuka kwenye gari.
“Salama tu. Karibu.” “Namuulizia Naya. Sijui mnamfahamu?” “Chumba chao ni jengo
lile pale nyuma ya ulipoegesha gari yako. Chumba cha pili kulia ukiingia tu.”
“Asante.” Akaondoka na kuacha manukano mazuri pale. “Ooooh! Atakuwa bwana ake.
Ndio maana Naya ananyodo!” Wakaanza kumteta wakati Malon akiondoka kuelekea
alipoelekezwa.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
Hodi ilisikika kwenye chumba cha kina Naya na wenzake. Wote
walikuwa wamejilaza kitandani mida hiyo. Naya ndio alikuwa amelala kabisa.
Mmoja wao akasimama kwenda kufungua mlango. “Karibu.” “Asante. Namuulizia
Naya.” “Yule pale amelala.” Malon akapitiliza na kwenda kusimama kwenye kitanda
alichokuwa amelala Naya. Ilikuwa double decker. Naya alichukua kitanda cha juu.
Hayo matandiko tu, ungependa kugusa. Mazuri ya Chuichui safi lakini rangi ya
dhahabu ilipendeza na kuvutia haswa. Silk nzuri Ungependa kutizama. Hata
foronya za mito ilikuwa silk ya dhahabu yenye chui chui pia.
“Naya!” Aliita Malon akiwa amesimama pembeni ya kitanda alichokuwa
amelala Naya. “Malo!” Akashtuka Naya alipomuona mgeni wake. “Vipi?” Malon
akauliza. “Nilikuwa nimelala.” “Mzima lakini?” “Mzima. Nilikuwa nasoma,
nikapitiwa na usingizi.” “Naomba twende.” “Hapana Malo.” Naya akakataa
taratibu.
“Unataka nikwambie nini ujue nimekosa na kujutia?” “Leo ni
jumapili Malo. Kesho nina vipindi kuanzia asubuhi. Siwezi kuondoka leo.”
“Nitakurudisha usiku. Mimi mwenyewe.” Kimya. “Naya!” Kimya. “Si unajua leo
sitaondoka hapa bila wewe?” “Naomba muda Malo.” Wenzake Naya wakasikia akijibu.
“Mpaka lini? Nimekuacha muda wote huo, bado unataka muda! Naomba
twende tukazungumze.” “Nitakuja ijumaa.” “Hapana. Nataka twende sasa hivi.”
Malon akasikika akiamrisha, sio kuomba tena. Naya akakunja uso kwa kumshangaa
kidogo. Alipoona sura ya Malon inazidi kubadilika, akaanza kukusanya vitu vyake
taratibu. Akashuka hapo kitandani. Wazi ni kama amelazimika. Akafungia vitu
vyake vyote kwenye upande wake wa kabati au loka, akatoka bila kuaga. Malo
akamfuata nyuma kimya kimya.
“Kwa nini unafanya ubabe wakati umekosa, Malo?” Naya aliuliza mara
baada yakuingia tu kwenye gari.” “Utakumbushia kosa moja mpaka lini? Jambo moja
haliishi daima!?” “Kwa hiyo wewe unafikiria ni jambo dogo?” “Sasa ulitaka
nifanyaje? Nilishakwambia nilipaniki ndio maana nikakupiga kibao. Nimekwambnia
nimekosa, ni nini usichoweza kusamehe?” Naya akashangaa sana.
“Mbona kosa unalozungumzia ni moja tu, Malo! Kwa nini huzungumzii
usaliti wako?” “Acha mambo ya kitoto Naya! Nimekwambia kabisa yule sio mwanamke
wangu. Imetokea mara moja, basi. Unataka kujiliza mpaka lini! Kwa nini
unashindwa kuwa muelewa?” “Unataka nielewe nini Malo? Nimekufumania kabisa! Upo naye
mnafanya mapenzi! Badala uniombe msamaha, ukanipiga. Ulitaka nifanye nini?” Naya akaanza
kulia.
“Nimekwambia nilipaniki Naya. Sikujua kama ungerudi nyumbani siku
ile.” “Malo! Sasa hiyo ndio inatakiwa inifariji?” “Acha utoto
Naya. Nishakuomba msamaha na nimekwambia yule sio mwanamke wangu. Ilitokea mara
moja tu, na nimekwambia haitatokea tena. Unachotaka kusikia kutoka kwangu ni
nini!? Kwa nini unataka tukae kwenye jambo moja wakati wote? Kwa nini unapenda
kubeba mambo moyoni? Unafikiri au unataka nini kitokee? Niambie Naya.” “Sijui
Malo.” “Lazima ujue na uniambie. Mimi mtindo wa kuzungumzia mambo zaidi
ya mara moja au mbili unajua wazi siwezi. Jambo likitokea naomba tulizungumze
na liishe. Unanielewa Naya?” Kimya.
“NAYA!” Malo akaita kwa ukali mpaka Naya akashtuka na kumtizama .
“Nimeuliza kama umeelewa?” “Nimekusikia.” Naya akajibu kwa upole, kisha
akageukia dirishani, kimya. Malo akaendelea kukanyaga mafuta mpaka nyumbani
kwake alipokuwa akiishi na Naya.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
Malo alikuwa kijana mdogo tu, lakini alikuwa amejijenga haswa.
Maisha yake yalikuwa hapo hapo mjini Morogoro. Mji ulionekana wakushoto au duni
kuishi, lakini sio kwa Malo. Alistawi na kutajirika kwenye huo mji. Biashara
alizokuwa akifanya, Naya hakuwa akizijua, lakini alijua Malo anazo pesa.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
“Kesho nina vipindi asubuhi Malo.” “Nakumbuka. Nilitaka uje
kuchukua zawadi niliyokununulia. Ujue ndio nakuomba msamaha.” Naya akanyamaza,
akapitiliza chumbani. Malo akaja nyuma yake. “Ipo hapo mezani.” Naya akasogelea
meza. Alianza kuhisi ni nini. Ulikuwa mkebe mzuri mezani. Akatizama na kuacha
bila hata kugusa, akaenda kukaa kitandani, kimya.
“Kaa hapo kitandani nikuvalishe mwenyewe.” Malo alifuata ule mkebe
pale mezani, akaenda akamsogelea Naya pale alipokuwa amekaa kitandani. Akapiga
magoti. Naomba mguu. Naya akanyoosha huku akimtizama machoni akiwa ametulia tu.
Akafungua ule mkebe, akatoa cheni ya mguuni, nzito ya dhahabu.
Akamvalisha na kuanza kumbusu kuanzia mguuni kupanda juu taratibu
huku mikono ikimpapasa. Akaendelea kumbusu taratibu mpaka mapajani. Naya
akajilaza. Alimjua Malo akikosa, msamaha wake utaupata kwenye zawadi atakayompa
na mapenzi.
Hata kama Naya anakuwa amekasirika na akili hazipo pale. Huwa
anahangaika kumtuliza kwa kumchezea. Basi hapo atahakikisha Naya anaridhika
kweli kweli. Hata kama yeye atamfikisha mara tatu, atahangaika mpaka ahakikishe
ameridhika ndipo na yeye anaweza hata kuambulia bao moja. Ndio msamaha wake,
lakini sio maneno.
Alimjua jinsi alivyo mbaya wa maneno. Malo alijawa kashifa. Jeuri
na hasira za kupitiliza. Na anapokasirika huwa anapoteza uwezo wa kufikiria
kabisa. Anaweza kufanya jambo, mpaka yeye mwenyewe huwa anajishangaa. Naya
hakuwahi kumuona akivuta bangi, lakini hakushindwa kumfananisha na mvuta bangi.
Mkono mwepesi kupiga hata wafanyakazi wake. Ukimuudhi popote na
mbele ya yeyote, hakuwa akiweza kujisaidia. Kijana mdogo aliyekuwa amefanikiwa
sana, na kuogopewa mno hata na rafiki zake. Usimwibie wala kujaribu kumzunguka
kwenye biashara zake, kudhuru haikuwa shida. Naya alishamshuhudia akimpiga
ngumi za usoni mmoja wa wafanyakazi wake, akashangaa kama ipo roho ya
kibinadamu ndani yake! Alimpiga mfululizo karibu ya kumuua na kumfukuza kama
takataka.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
Malo kijana wa Moro. Alizaliwa hapo Moro mjini, na mama muuguzi aliyekuwa
ngazi ya chini kabisa kwenye hospitali kuu ya serikali na baba akiwa dereva
kwenye magari ya hapo hospitalini, hapohapo jijini Morogoro. Malon kama ndugu
zake wengine walisomesha na wazazi wao hapohapo Morogoro kwenye shule za kata
tu. Kwa kifupi ni mtoto wa Mji kasoro bahari. Hakuna asilolijua kwenye mji huo.
Hakuna asiyemjua. Na kwa kuwa alishakaa sana mtaani baada ya kufeli kidato cha
nne na kukataa kuendelea na masomo, hakuna asilolijua hapo mjini. Kuanzia maovu
mpaka mazuri yanayoendelea mtaani, Malon aliyajua.
Alifahamika hata na watoto wadogo wa mtaani. Ila Hakuna aliyejua siri
ya nafanikio yake ya haraka. Ilikuwa ni kufunga na kufungua, Malo akawa
anamiliki thamani nyingi sana. Wengine walisema ni madawa ya kulevya, lakini hakuna
aliyemkamata nayo.
Ndipo akaangukia kwa Naya aliyempenda kufa. Kila mtu alijua
ukitaka maneno na Malon, msogelee Naya. Alikuwa kama pumzi yake. Alimpenda kupitiliza
kasoro umalaya ndio ilikuwa tatizo la Malon. Alimtunza Naya na kumpa kila
atakalo, lakini tatizo ni mahusino ya hovyo aliyokuwa nayo kwa wanawake mbali
mbali. Rafiki yake wa karibu sana waliyekuwa naye tokea utotoni, Chezo kama
wengi walivyozoea kumwita, alishindwa kujua tatizo la Malon.
“Shida ni nini Malo!? Unataka nini na kwa nani!?” “Swala la nani ni
Naya tu.” “Sasa kwa nini hutulii naye!?” “Nani amekwambia sijatulia na Naya!?”
Hapo anacheka kama mazuri. “Acha kunitazama hivyo Chezo! Kuonja mboga sio
kula, baba! Na hata nipewe vipi na nani, lazima nikamalizie kwa Naya, ndio
naridhika. Hata wewe unajua.” Chezo hubaki akimtizama na kushindwa kumuelewa. “Mbona
wewe hutosheki na bia moja, kaka?” Malo hakuacha kumuuliza hivyo. “Usilinganishe
pombe na wanawake Malo! Unamuumiza sana Naya.” “Naya mwenyewe anajua yeye ndio
mwenyewe, hana mpinzani.” “Muonyeshe kwa vitendo basi!” “Ulitaka nimfanyeje?
Wewe Ni shahidi. Naya anamiliki mpaka roho yangu! Natakiwa kufanya nini tena?!”
Hapo huwezi kumshinda Malon. Na Chezo alimjua. Ukiendelea zaidi, ni ugomvi.
Heri yeye ashinde.
“Naya kwa kupenda kubeba mambo! Ni nini kisichoisha? Mbona mwenzio
siweki mambo moyoni? Nakuhakikishia hao wote hawana maana Naya. Ila wewe tu. Au
hilo unamashaka nalo?” Naya akanyamaza. Alijua Malo anampenda sana, lakini
hakujua ni nini kinachomsumbua. “Mapenzi ninayokumbuka ni yako tu Naya wangu.
Wote wapuuzi. Wala wasikusumbue kichwa chako.” “Sasa kwa nini hutulii Malo?
Utaniua na UKIMWI.” “Hakuna ninayelala naye bila kondomu.” “Kweli Malo!
Unaniambia bila kunifikiria nafsi yangu? Unajua na mimi ni binadamu? Nina hisia!”
Malo akazidi kucheka na kumuumiza Naya zaidi. Akataka kutoka pale kitandani
lakini Malon akamvuta mkono kwa nguvu na kumrudisha palepale kitandani.
“Acha hasira Naya. Ninachojaribu kukwambia nipo makini. Nakulinda
sana mpenzi wangu. Katika kila jambo ninalofanya nakufikiria. Kwamba kabla ya
kufa wewe, ujue na mimi nitakufa.” “Kwa hiyo hata unapokuwa unafanya nao
mapenzi unakuwa ukinifikiria?” “Unapenda kufikiria mbali wewe!” “Acha kucheka
Malo! Utajisikiaje na mimi nikifanya kama unavyofanya wewe?” Kicheko cha Malon kikakata
ghafla na kukaa.
“Na mwanaume gani huyo asiyependa nafsi yake!? Nitamtahiri bila
ganzi.” Naya akamtizama, akasimama. “Rudi Naya.” “Naenda kuoga niondoke.” Malon
akaruka pale alipokuwa amekaa akamfuta kwa haraka. “Nakuonya Naya! Usithubutu.”
“Mbona wewe unafanya? Kitakachonizuia mimi ni nini?” “Nakuonya Naya.
Usishindane na mimi.” “Niache Malo. Acha kunitolea macho na kunishika mkono
wangu kwa nguvu.” Alimuona ameshabadilika kabisa.
“Unataka kunipiga tena?” Naya akamuuliza. “Nipige tu, umalizie
hasira zako.” Malon akamuachia. “Nimekuonya Naya.” “Mbona mimi nakuonya na
huachi? Mara ngapi umelala na wanawake na mimi nikiwa nipo hapa nakusubiria?
Mbaya zaidi unalala nao, halafu unakuja kulala na mimi! Unanichafua tu.” “Wewe
ndio unakuwa unanihisi nimetoka kwa wanawake wengine wakati sio kweli.” “Mara
ngapi nimekufumania Malo? Mara ngapi?” “Kwa nini unapenda kutunza mambo!?
Unataka litokee nini!?” Naya akaondoka na kuingia bafuni akajifungia.
“Naya!” Akamsikia akiita nje ya mlango. “Nitavunja huu mlango Naya
wewe fungua!” “Vunja. Kwani ndio itakuwa mara yako ya kwanza?” Naya akajibu
huku akifungulia maji ili aoge. “Naya!” Malo akaita tena kama anayemtisha
lakini Naya hakumjibu tena. Akamsikia ametulia. Akaendelea kuoga mpaka
akamaliza. Akatoka akiwa amejikausha kabisa, akamkuta akimsubiri nje ya mlango.
Akampita.
“Umeanza mahusiano huko chuo?” “Mimi sio kama wewe Malo.” “Nani
amekwambia nimeanzisha mahusiano? Sina mahusiano na yeyote ila wewe tu.” Naya
akanyamaza akaendea ilipokuwa meza yake ya vipodozi. “Nimekuuliza Naya. Maana
mimi nimekujibu. Sina mahusiano na mwanamke yeyote ila wewe.” “Kwa hiyo unaita
nini kile ninachokuona ukifanya na wanawake wengine?” “Ujue uwe unatumia akili
Naya wewe. Nani umemuona analalia kitanda changu isipokuwa wewe peke yako?”
“Kwa hiyo ukiwa unalala na wanawake zako hapo nje ya hiki chumba ni sawa, mbaya
isiwe hapa kitandani?” “Naya!” “Basi usiwe na wasiwasi, na mimi watakuwa
wakinilala kwenye vitanda vyao sio hapa kwenye kitanda chako.” Malo alipiga
ngumi kwenye ile meza aliyokuwa amesimama Naya akijipaka lotion. Naya alishtuka
mpaka akaruka. Kila kitu kilianguka sakafuni na kuzagaa kila mahali pale
chumbani kulikokuwa kuna sakafu yenye marumaru nyeupe na kapeti chini ya
kitanda.
Akamuona anavaa nguo zake nakutoka. Akajua hapo ndio amekasirika
mpaka mwisho anakaribia kurukwa akili. Naya akahema kwa nguvu. Hakujisumbua
kuokota kitu hata kimoja. Akavaa nguo zake, akampigia moja wa dereva wa Malon,
akafika pale akamchukua usiku huo na kumrudisha chuoni.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
Kwa muda huo alipokuwepo hapo chuoni alikuwa akijisomea maktaba ya
chuo, au chumbani kama wenzake hawapo au wamelala. Hawakuamini vile Naya
alivyokuwa akisoma. Hata usiku alikuwa akiamka kusoma kitu kilichowashangaza. Walijua
ni urembo tu ndio unaoendelea kwenye kichwa chake, kumbe na shule pia!
Ijumaa wakati anatoka kwenye kipindi cha mwisho kabisa akiwa
anaelekea chumbani kwao, akaona gari ya Chezo nje ya hosteli yao. Akashtuka
kidogo. Akaongeza mwendo mpaka pale. Alimkuta Chezo ametulia tu garini.
“Kwema Chezo!?” “Kwema. Ila nimekuja kukuchukua.” “Kwenda wapi!?”
Naya akashangaa. “Malo atachanganyikiwa, Naya.” “Anachanganywa na nini?” “Acha
utani Naya.” “Sikutanii Chezo, kwanza yuko wapi?” “Kwake. Yupo kama mgonjwa.
Nikaona nije tu kukufuata.” Naya akaingia ndani ya gari.
“Naomba tuzungumze Chezo.” “Nini tena?” “Hivi unajua alichokifanya
Malo?” “Hajaniambia kabisa. Ila ameniambia kwa mara ya kwanza umemtamkia upo
huru kufanya mapenzi na mwanaume mwingine kama kumlipiza kisasi wakati
alishakuomba msamaha na amekiri kosa.” Naya akashangaa sana maelezo aliyonayo
Chezo. “Wewe amekwambia amekosa nini?” “Nilimuuliza hivyo, hakujibu.” “Kwa kuwa
anakujua Chezo, ndio maana ameshindwa kukujibu.” “Amefanya nini tena?” Naya
akaguna.
“Nini?” “Unakumbuka nilikuwa likizo, nikamwambia lazima niende
nyumbani, baba ananiulizia?” “Nakumbuka. Si tulikuwa wote baa.” “Sawa sawa.
Sasa baada ya kama siku mbili mbeleni, Malo akanirudisha mpaka karibu kabisa na
nyumbani. Akaniuliza lini nategemea kurudi, nikamwambia inategemea na hali ya
nyumbani, sina uhakika. Nimekaa nyumbani kama baada ya siku kumi nikapanda basi
asubuhi, nikajiambia nikae naye mpaka jioni, nirudi nyumbani. Nilikaa pale
mpaka jioni, Malo hayupo, hapokei simu na hakuwa safari.” “Wewe ulijuaje?”
Chezo akauliza.
“Kumbuka nilikuwa naye Dubai? Baada yakupokea mzigo wake kutoka
Brazil na kuusambaza pale, tukarudi naye Dar. Tukakaa Dar kama siku mbili ndio
tukarudi huku Moro. Aliniambia ratiba zake zote. Akataka kukutana na mwanamke
fulani hivi. Akaniambia ni mambo ya biashara kwa kuwa alitaka yule mwanamke
sijui nikwambie msichana aje pale hotelini. Yule dada akaja, alitukuta tunakula
chakula cha usiku sehemu ya mgahawani. Wakazungumza kidogo, kisha wakahama
meza.”
“Mimi sikujali kwa kuwa nilijua ni mambo ya biashara. Wakazungumza
baada ya muda wakarudi pale mezani wakiwa wanacheka. Malo mimi namfahamu Chezo.
Namfahamu vizuri tu. Jinsi alivyokuwa akimtizama yule dada kabla na baada,
nikajua tayari lipo jambo.” “Umeanza Naya.” “Subiri Chezo. Yule dada akaropoka,
‘tutaonana basi hiyo jumamosi’. Nikashtuka, nikamtizama Malo. Malo akapotezea.
Yule dada akaondoka. Nikamuuliza Malo, mnaonana wapi hiyo jumamosi? Kama
unavyomjua Malo, akaanza kucheka, akasema kama hivi ulivyosema wewe. ‘Umeanza
Naya. Huyu dada mtumzima nataka nini? Ni mambo ya biashara tu.’ Akanijibu
hivyo, nikanyamaza.”
“Si ndio tukarudi Moro, tukawa wote! Mimi sikuondoka kwa haraka
kama nilivyomwambia Malo kuwa tukirudi tu Moro sitakaa itanibidi kurudi
nyumbani. Inamaana na ile jumamosi yule dada aliyosema angekutana na Malo, mimi
nilikuwepo na Malo, nafikiri wakashindwa kuonana. Nikaja kuondoka baada siku
ile kuwaaga pale baa. Sasa turudi niliporudi na kumkosa pale nyumbani nikijua
hana safari. Nikamuuliza Side. Tena kwa kumpigia. Nikamuuliza Malo yuko wapi?
Akasema yeye alijua yupo na mimi Dar. Maana
alimuaga anakwenda Dar. Basi, mimi nikarudi Dar. Nikatulia. Alikuja
kunitafuta kesho yake, kwa uongo kuwa alikuwa amepoteza simu, hakujua wapi
alikuwa ameiacha.” Chezo mwenyewe akacheka.
“Umeona eeh! Hata wewe unajua ni uongo. Malo hawezi kupoteza
simu.” “Kupoteza simu kwa Malo ni kama amepoteza pumzi.” Chezo akaongeza. “Sawa
sawa. Sasa mimi nikajua tayari. Ila sikujua ni nani. Nikamtega bila yeye kujua, nikamwambia huko
unakoegesha gari mchana kutwa, wanamuona. Wewe unamjua Malo nikimfumania
anavyokuwa mwema. Akaongea mengi wee, mimi namsikiliza tu. Mwishoe nikaona
nikate simu.”
“Nikatulia kama siku 4 hivi, nikarudi tena kwake. Huwezi amini Chezo, nilimkuta Malo
na yuleyule dada aliyetufuata kule hotelini Dar, sebuleni. Sebuleni Chezo, bila
aibu Malo anafanya mapenzi na yule mwanamke. Dada mtu mzima kama yule dada yake
mkubwa.” “Haiwezekani Naya!” Chezo alishtuka sana. “Mungu wangu nishahidi.
Nisingeweza kumsingizia Malo. Nikajiambia ni dharau ya namna gani hiyo kuleta
mwanamke ndani!”
“Nilishtuka sana. Nikamuuliza kwa nini anafanya vile? Hivi unajua
Malo alinipiga kibao?” “No way!! Haiwezekani Naya.” “Muulize. Alinipiga mbele
ya yule dada, tena wakiwa uchi vilevile. Mimi nikaondoka, nikarudi nyumbani.
Hakika niliumia Chezo.” “Pole Naya. Sasa naelewa ni kwa nini ameshindwa
kuniambia.” Chezo akaumia sana.
“Basi. Zikaanza simu na jumbe zakuomba msamaha. Kwamba alipaniki.
Hakukusudia kunipiga. Ikawa msamaha ni wakunipiga, sio kumfumania. Sikumjibu. Nikaamua
kunyamaza tu. Chuo kilipofungua sikumtafuta, nikapitiliza kutoka nyumbani mpaka
huku Mzumbe. Sijui alijuaje kama chuo kimefunguliwa, siku hiyo nimelala,
nikamshtukia amenisimamia pembeni ya kitanda, anataka niondoke naye.”
“Mwanzo nikamkatalia. Lakini kama unavyomjua Malo, akabadilika
akataka kuanza kufanya fujo. Nikaona yaishe, nisijiharibie na hapa chuoni.
Tukarudi naye nyumbani kwake, nikakuta ameninunulia cheni nzuri sana ya mguu,
eti ndio ananiambia ananiomba msamaha wakunipiga, sio kumfumania! Na maneno
yake yaleyale anayowaambieni na nyinyi kuwa mimi ndio mpenzi wake huku wote
tukimshuhudia akilala na kila mwanamke.”
“Nikamuuliza kwa nini anafanya hivyo kama kweli ananipenda? Ndio
akasema mimi ndio mwanamke wake na ndio maana analala na wanawake wengine nje
ya kitanda chetu. Ndio nikamwambia basi na mimi nitalala na wanaume wengine nje
ya kile kitanda. Acha apagawe. Kapiga ngumi dressing table. Akaangusha kila
kitu sakafuni aka..” “Ndio maana ameniambia ameumia tu, ila hajaniambia
ameumiaje!” “Mbona sikuona kama alitokwa na damu!?” “Ametegua kidole cha kati.
Amefungwa mabendeji. Kama POP.” “Mimi sijui Chezo. Nimechoka. Malo ataniua kwa
magonjwa.”
“Hawezi. Hilo nimemuuliza.
Amenihakikishia anatumia kinga, hapo hajisahau.” “Sasa hilo ndio litatakiwa
liwe sawa? Ananidhalilisha kupita kiasi! Hakuna tunapokwenda sehemu hata kwenye
migahawa asiwe amelala na hao wanawake mtakao kutana nao hapo. Wawe wahudumu au
mmiliki wa hilo eneo kama ni mwanamke. Basi jua Malo alisha lala nao. Analala
na kila mwanmke! Nimechoka Chezo. Niambie ni kwa nini niendelee naye?”
“Malo anakupenda Naya. Mimi sijui anakuwa aningiwa na tamaa gani,
lakini anakupenda sana. Yupo kama mgonjwa.” “Sidhani kama ni kwa ajili yangu
Chezo. Itakuwa ni hicho kidole alichokitegua.” Chezo akacheka. “Kweli Chezo.
Anachotaka kwangu ni nini ambacho hakipati kwa wengine?” “Mimi nashauri
ukazungumze naye. Unamjua Malo. Amenyamaza, hatujui anawaza nini. Akija
kuibuka, anaweza kuja kukufanyia fujo huku. Nashauri ukamtulize Naya.” “Mpaka
lini Chezo!?” “Akili kichwani. Wewe si ndio umeanza chuo? Mtumikie kafiri upate
mtaji wako.” Naya akabaki kimya.
Akakumbuka ada anayolipiwa na mapesa anayompa. Akaona Chezo yupo
sahihi. Malo alikuwa kama mvuta bangi. Kichaa kikimpanda, hakawii kuja kumtoa
katikati ya darasa. Hata hivyo bado alikuwa akiiihitaji pesa yake. Bado Chezo
alikuwa akimtizama anavyofikiria. Naya akamgeukia. “Nisubiri nikaweke haya
madaftari, nitarudi sasa hivi twende wote.” “Hayo ndio mambo. Mjini watu
wanaishi kwa akili Naya. Panga karata zako vizuri. Ukipata chako ndio unaota
mbawa. Sasa unataka kuota mbawa wakati kujajua hata kuelea angani!?” Naya
akacheka na kutoka kurudi chumbani kwake. Akachukua vitu baadhi akatoka na
kuondoka na Chezo.
Njia nzima Chezo alikuwa akimpa mikakati. Nini chakufanya huku akimuonya asije kumwambia Malo. “Fungua akaunti yako ya pembeni ambayo yeye haifahamu. Rushia humo pesa.” “Wewe unamjua Malo. Anafahamiana na kila mtu! Watu wa benki wakimwambia?” “Basi weka kwenye akaunti ya mama yako. Jiwekee akiba. Kuna leo na kesho, Naya. Huwezi jua.” Naya akanyamaza.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
Ni kama hakuamini alipomuona Naya. Akapitiliza bafuni bila
yakumsemesha. Akaoga na kurudi kitandani. Akamvuta mkono. “Unauma?” “Mpaka
niutoneshe. Lakini hivyo walivyonifunga sasa hii inasaidia.” Malo akajibu.
“Pole.” Akajiweka sawa. “Umepata mwanaume mwingine?” Malon akamuuliza. “Mimi
siwezi kufanya au kuishi kama wewe Malo.” “Kwa nini unapenda kurudia mambo!?”
“Hivi unajua hata mwezi haujaisha na hivi unajua hiyo sio mara yako ya kwanza,
Malo!? Kilichobadilika ni kumleta mwanamke humu ndani kitu ambacho hukuwa
ukifanya tangia tumeanzana! Ulikuwa ukikutana nao huko huko. Ukaniahidi
umebadilika, haitarudia tena. Matokeo yake umeleta mwanamke kama dada yako humu
ndani!” “Nimeomba msamaha Naya.” Naya akakunja uso.
“Au unataka nifanye nini?” “Malo! Kwa hiyo ndio inatakiwa iishe na
maisha yaendelee mpaka nikufumanie tena?” “Kwa nini unafikiria nitarudia tena?”
“Kwa nini nisifikirie hivyo? Niambie ukweli Malo. Kipi kitakuwa kimebadilika
kwako? Mimi ni Naya yuleyule. Sijabadilika. Kile unachokikosa kwangu na
kukufanya unahangaika na wanawake wengine, sikijui mpaka leo! Na tabia yako
hiyo haijawahi kubadilika Malo. Na mimi ni mwanadamu.” “Unamaanisha nini?” Malo
akauliza. Naya akachoka kabisa kuona ni kama haelewi. Akashindwa hata amjibu
nini.
“Nakusikiliza.” “Siku nitakayokufumania tena Malo, ndio itakuwa
mwisho wa kurudi kulala kwenye hiki kitanda. Na ndio itakuwa mwisho wetu.
Nakupenda, lakini nitakuwa nimefika mwisho. Nakuapia Malo, huo ndio utakuwa
mwisho wetu.” Malo akashtuka sana asitegemee. “Naya!?” “Kwani unampango wa
kurudia tena?” Malo kimya. “Wewe si umeahidi hutarudia? Basi hapatakuwa na
shida. Naomba tulale. Nimekuwa na week ndefu yenye mitihani kila siku, nilikuwa
silali.” Naya akageuka pembeni nakujifunika.
“Nilikuwa na hamu na wewe Naya! Umeniacha majuma mawili!” Naya
akamuhurumia, akageuka. “Hukutoka?” “Mungu wangu ni shahidi Naya. Sijatoka
kwenda kwa mwanamke yeyote. Kwanza yule dada ni kama..” Akasita. “Basi. Acha
nibebe makosa yangu mwenyewe. Ila naomba ujue sikutoka na wala sijafanya
chochote. Naomba yaishe tafadhali.” Kwa kuwa alikuwa anaumwa mkono, Naya
akamkalia na kumlalia kifuani.
“Na mimi nina hamu na wewe Malo.” “Naomba usije kulala na mwanaume
mwingine Naya. Tafadhali sana.” “Hapana Malo, wewe naomba utulie. Kila kitu
kina expiring date. Mwisho wa matumizi yake au uhai wake. Hata mwanadamu anayo
expiring date, ndio maana ya kifo. Na mapenzi ni hivyo hivyo. Lazima
kuyapalilia. Na sitaweza kufanya mimi mwenyewe. Siwezi kukuahidi Malo.
Usharudia kunisaliti mara nyingi sana. Tafadhali badilika. Binafsi sina mpango
wala nia na mwanaume mwingine. Nimetulia shuleni. Najua na wewe unayo hiyo
taarifa. Sina mwanaume yeyote yule. Ni wewe na shule tu. Sasa naumia kuona
mwenzangu unahangaika wakati mimi nakuwepo, Malo! Nipo na wewe karibu kila siku
na kila mahali! Unanidhalilisha sana. Sina hata ujasiri kwa rafiki zako. Wote
wanajua uchafu unaofanya na mimi nikiwepo!” “Lakini wanakuheshimu wewe Naya.
Wanakuheshimu kama vile mimi tu au kama mke wangu.”
“Hapana Malo. Wanaheshimu pesa yako. Wala sio sisi kama Malo na
Naya. Wanahisi nakuvumilia kwa yote sababu ya pesa. Hakuna mwanadamu anaweza
kukuvumilia kimapenzi kama mimi Malo. Ushanifanyia makubwa yakutisha na mimi
ndio naishia kujirudi. Watu wanafikiri ni kwa sababu ya pesa kumbe ni kwa
sababu nakupenda Malo. Nakupenda sana. Tafadhali naomba badilika.” Malo akavuta
pumzi kwa nguvu, akamgeuza Naya. Yeye akawa juu. “Nitabadilika Naya.” “Asante.”
Malo akaanza mabusu ya kila mahali. Ilisikika sauti ya Naya akifurahia mapenzi
ya Malon usiku huo. Aliujua mchezo, Naya hakuwa akijivunga pale Malo
anapomshika.
N |
aya hakujua kama ni hofu iliyomuingia Malo au ni kweli ameamua kubadilika! Mapenzi yale ya mwanzoni kabisa wanaanzana kimapenzi, yakarudia. Malon aliyemtongoza kwa kumbembeleza karibu kuchanganyikiwa akarudia enzi zile za mwanzo. Hata Naya alijua anapendwa. Kutoka katika kashfa, kumsaliti hata mbele za watu, Malon akarudi kumtetemekea Naya.
Mara ya kwanza Malon alipomuona Naya.
Siku hiyo Naya akiwa chuoni Mzumbe, akakumbuka siku anakutana na
Malon. Akacheka na kuinama huku akivuta kumbukumbu. Alikuwa amekaa peke yake
ilikuwa bado mapema tu, baada ya vipindi vya asubuhi kuisha hapo chuoni. Wenzake
wanaosoma darasa moja wakila, wakisubiria vipindi vya mchana. Wengine wakiingia
madarasani. Yeye alikuwa amekaa tu, hakutaka kula chakula cha mchana hapo
chuoni. Kumbukumbu zikamrudisha miaka michache nyuma akiwa na wenzake kipindi
anaishi hosteli akiwa shule ya sekondari na warembo wengi tu, ila yeye
kuchaguliwa na Malon na kuacha warembo wengine hawaamini.
Usikose
Sehemu ya 2, iliyobeba historia ya
mwanzo wa Naya na Malon uliobeba uzito mkubwa wa Simulizi hii.
Wow!amazing .Natamani kuona wanaishia vp ila mapenzi matam bwana.
ReplyDelete