Kwa
Malon.
M |
alon alikaa pale akiwaza. Akapanga na kupangua. Naya ni msichana
anayempenda. Hajutii kuondoka kwake, kwani ndilo lilikuwa lengo lake. Alitoka
jela akiwa amefilisika haswa. Na alijua amefilisiwa tokea alipokuwa jela kwani
maafande walikuwa wakimwambia makusudi kuwa watu wamekusudia kumfilisi. Hakujua
ataishije. Hakutaka Naya aangamie naye. Alitoka jela akifikiria maisha yake na
deni kubwa alilokuwa nalo kwa Naya. “Hakuna
jinsi naweza kumlipa Naya, isipokuwa na yeye kumuweka huru mbali na mimi. Hiyo
ndio zawadi pekee ambayo naweza kumpa Naya.” Malon aliwaza akiwa njiani
kurudi Dar akitokea jela baada ya wosia mzito pia kutoka kwa Mati. Akakubali
kuwa, kuendelea kuwa na Naya kwenye mahusiano ni kutomtendea haki.
Alipomuona usiku ule alipokuwa na Ozi,
akabadili mawazo, akaamua aendelee naye, atajitahi mbele ya safari. Lakini
akakutana na Naya wa zamani. Amerudisha msimamo wake. Sio wa michezo tena
kukubali kukimbilia kitandani. Anajielewa
na baba yake amerudi kwenye picha. Amesimama na binti yake. Malon asiyejua
kusimama kwenye mahusiano yakueleweka. Asiyeelewa kujifunga kwenye chochote kwa
yeyote, akabadili tena msimamo. Akaona anatakiwa kujitoa tena kwa binti kama
Naya.
‘Naya anataka ndoa!’ Malon akakumbuka
alichoombwa na Naya siku hiyo nyumbani kwao. “Nikimuoa nitamlisha nini mimi Naya? Sijasoma, sina chochote! Siwezi
kuishi nyumbani nikilishwa na Naya.” Hali ya uanaume ikainuka ndani ya
Malon. Sasa kuja kusikia yupo Joshi. Tena anayemfanya acheke mpaka atokwe na
machozi! “Huyu ndiye atakayemfaa Naya
wangu. Angalau atamfariji.” Aliwaza Malon wakiwa njiani kupeleka maziwa
huku akiendelea kumsikiliza Naya anavyocheka kwenye simu na Joshi. Malon
akaadhimia kumuacha mikononi kwa Joshi. “Namwachaje kabla sijamuumiza tena?” Ni swali lililoanza kumuumiza. “Kwa kuwa ameshasikia mengi mabaya juu
yangu, na ananijua mimi ni mkorofi heri ni mtafutie sababu ya maana, anichukie
na aende kwa mwanaume mwingine, aendelee na maisha yake.” Wakiwa kwenye
gari yeye na Naya wakielekea Kunduchi, Malon aliendelea kuwaza kitu chakufanya.
Ndipo akaona atumie kigezo cha Joshi
na Ozi. Huku akimsukumizia kwa Joshi na kumkumbusha kuwa hana uwezo wa kumfanya
awe na furaha kama vile Joshi anavyo mfurahisha. Akaibua ugomvi, na hasira kwa
Naya mpaka Naya akakolea. Akaongea mengi kama kawaida yake, Malon akimsikiliza
tu, mpaka akaondoka na kumtaka asirudi tena kwao. “Ni heri aondoke akijua sina shukurani, kuliko kuja kuteseka naye
kwenye maisha. Kwanza itamsaidia kunichukia kabisa na kuendelea na mwanaume
mwingine. Ni kweli simstahili Naya. Sina uwezo wa kuja kuwa mume au baba wa
watoto. Naanzia wapi?” Malon aliendelea kuwaza akiwa peke yake kwenye ile
nyumba ambayo haina hata chakula. Kwa
kuwa alikula nyumbani kwa kina Naya, alilala hapo hapo kwenye kochi, akiangalia
tv akikubaliana na maamuzi aliyoyafanya kumuacha Naya.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
A |
subuhi siku ya jumatatu aliamka na
kwenda kukimbia baharini baada ya kulala na siku ya jumapili siku nzima. Malon
ni mtu wa mazoezi. Hata alipokuwa mahabusu, alichofanya ni mazoezi. Alikimbia
muda mrefu mpaka alipochoka, akaamua kurudi nyumbani. Njaa ilishaanza kumuuma.
Hana chakula ndani ila pesa kidogo aliyopewa na Naya siku ya ijumaa alipotoka
mahabusu. Akayatizama yale mahoteli yaliyokuwa yamejipanga ufukweni. Akajiambia
akiingia tu pale kula na kunywa, anaweza kukosa nauli yakutoka nyumbani kwake kama
atataka kutoka. Akaamua kujikaza. Arudi tu nyumbani kwake, akaoge, anywe maji. Aendelee
kufikiria chakufanya.
Alitembea
taratibu pembeni ya hayo mahoteli huku akikumbukia enzi zake anapesa ya kufanya
chochote. Ni miezi karibu mitatu tu iliyopita, Malon huyu alikuwa na uwezo wa
kuchukua chumba kwenye mahoteli hayo, akaenda kulala na mwanamke yeyote
anayemtaka, nakutoka baada ya muda mfupi wakutimiza haja yake, huku akimuachia
huyo mwanamke hicho chumba. “Nimelipia mpaka kesho. Unaweza tu kuendelea
kukitumia hiki chumba.” Ndio zilikuwa kauli zake kwa wanawake anaokwenda
kuwatumia kwenye majumba hayo. Anaondoka akiwa amelipa mapesa mengi, kwa
starehe ambayo haikuwa ikichukua hata masaa mengi. Na akitoka hapo, anarudi
zake kwa Naya. Anatulia.
Leo anapita
hapo nje, hana hata pesa ya kununulia soda! Malon akajicheka nafsini kwake.
Akamkumbuka Side na Futi. Wao hakutaka kuwalaumu sana. Alijua alikowapitisha. “Nani asingetaka kuokoa nafsi yake?”
Akawatetea nafsi mwake huku akikumbuka jinsi walivyokimbia na mapesa yake, na
magari yake. Wamemuacha Malon hana usafiri! Malon akaendelea kutembea taratibu
akiwaza mpaka akatokea barabarani akirudi kwake.
Akakuta mtu
anabandika tangazo dogo tu. “Tunauza na kununua nyumba.” Malon
akamsogelea. Akamsalimia. “Wewe ni dalali?” “Hapana. Mtu wa masoko kwenye
kampuni yetu. Tunatafuta nyumba kwenye haya maeneo.” “Mimi ninayo nyumba.
Nakodisha. Ina vyumba vitatu. Kila kitu ndani kimekamilika. Jiko lina kila
kitu, sebule ina mpaka tv na vyumbani kuna vitanda pia, upande wa uwani geti
linaingilia baharini kabisa. Ukinitafutia wateja, kama watalii, au watu ambao
wanatafuta sehemu ya kwenda kupumzika kwa muda. Nitakuwa nikikulipa asilimia
fulani ya hayo malipo.” Yule baba akashawishika.
“Lakini hiyo
sio kazi ya kampuni yetu. Kampuni yetu ni kununua na kuuza nyumba.” “Mimi
siuzi. Nakodisha. Na nimekupa dili. Ukipata mteja, mlete kwangu.” “Nionyeshe
basi nyumba yenyewe na unipe namba za simu yako.” Wakaongozana na Malon, Malon
akiwa anafikiria jinsi ya mawasiliano kwani hakuwa hata na simu. Alipokwenda kujisalimisha
polisi, alivuliwa kila kitu na kukabidhi kila kitu kwa afande aliyemkuta
mapokezi. Lakini wakati wakutoka aliambiwa hakuacha kitu chochote pale. Mpaka waleti
yake hakupewa na ilikuwa na kadi zake zote za benki ambako na kwenyewe alikuta
wamemmaliza kabisa. Hakuna afande aliyekubali kupokea au kukabidhiwa vitu na
Malon siku alipoingia hapo rumande. Siku anatoka hapo polisi walimkatalia
kabisa. Malon hakujali, alijua wanamfanyia kusudi tu.
Akabaki akiwaza watawasiliana vipi na huyo
anayemuomba amkodishie nyumba! Wakaendelea kutembea kuelekea kwake. Alipofika
getini mlinzi akamwambia Naya ametoka hapo muda sio mrefu, ameacha bahasha.
Malon akapokea hiyo bahasha. Ilikuwa kubwa na ilionekana na kitu kizito ndani.
Wakamuona
anakunja uso wa mshangao huku akifungua. Akakuta ile simu ya Naya. Ilikuwa
imezimwa na bahasha ndogo ndani. Akafungua. Akakuta pesa na kikaratasi. ‘Hiyo ni simu
niliyokuwa nimenunua kutokana na pesa nilizokuwa nimekusanya. Ni ya kawaida tu.
Sio smartphone, lakini ilinisaidia kwa mawasiliano. Naamini na wewe itakusaidia
kwa kipindi hiki ambacho unajiweka sawa. Samahani jana niliondoka, nikasahau
kukuachia pesa. Sina hela nyingi Malon. Lakini naamini hizi zitakusogeza kwa
mizunguko ya hapa na pale mpaka utakapojiweka sawa. Nimekupikia maandazi jana nilipotoka
kanisani. Ndio kitu pekee nilijua naweza kupika na ukaweza kula.’ Malon
akacheka kidogo baada yakukumbuka mapishi ya Naya, akaendelea kusoma.
‘Nimekuletea maziwa na mayai trei mbili pia. Vyote nimemuachia huyo mlinzi. Sio vingi, lakini naamini vitakusogeza. Nakutakia mwanzo mwema Malon. Mungu atakusaidia tu, usikate tamaa. Mwanzo unaweza ukawa mgumu, lakini nakuamini una akili nzuri. Wewe ni zaidi ya vyeti vya shule ambavyo ungekaa darasi na kupewa na walimu. Nizaidi ya magari waliyokuchukulia. Zaidi ya hata ile nyumba waliyokuchukulia kule Morogoro. Kwa sababu vyote wewe ndio ulifanya vikawepo. Havikuwahi kuwepo mpaka wewe ulipofikiria na kufanya viwepo. Naamini ukitulia na kufikiria, na kutumia njia sahihi, utafanikiwa tu. Nimeishi na wewe, nimeona utendaji wako kazi. Najua ni nini nazungumzia. Unao uwezo mkubwa sana Malon. Nitakuwa nikikuombea popote ulipo, na chochote utakachofanya, Mungu akufanikishe. Ni hayo tu ndio nilipanga kukwambia ukitoka jela. Nasikitika hatukuweza kupata muda wa maongezi, ila namshukuru Mungu ameweza kukutoa ukiwa salama. Mungu awe nawe Malon. Halafu nilisahau kukwambia kuwa nililipa ulinzi wa hapo mpaka mwisho wa mwezi huu.Naya.
“Naitwa Tembe na hii ndiyo business kadi yangu.” Akajitambulisha.
“Unaweza kuandika tu Malon. Nitakupigia ili upate mawasiliano yangu. Hapa ndipo
nyumbani. Ukipata mteja, wewe unijulishe.” Wakaagana pale pale getini. Malon
akabeba vile vyakula, akaingia ndani.
Bila kuoga, harakaharaka akapasha moto yale maziwa, mengine
akayaweka kwenye friji. Akala kwanza, akashiba ndipo alipotoka kwenda kusafisha
chumba kidogo cha nje ambacho walikitumia kama stoo. Alikiandaa ili awe anaishi
hapo, ikitokea anapata mteja wakukodisha nyumba kubwa. Kiu ya bangi ikaanza
kumsumbua. Akili ikavurugika kabisa, akaona atoke pale, akazungumze na mlinzi
anayemlindia pale getini. Ili kama anayo hata kidogo, ampe. Akatoka kwa haraka
mpaka pale getini. Akazungumza na mlinzi. Mwanzoni mlinzi akaonekana kuogopa.
Akakataa. Alikuwa kijana tu. Karibu wanalingana na Malon. Malon akamuonyeshea
pesa. Yule mlinzi akajua na yeye nimvutaji. Akampa. Moyo wa Malon ukafurahia
sana.
Akarudi nyuma ya nyumba kule alikokuwa akisafisha. Akatafuta
kivuli kabisa, akaiwasha. Alipotaka tu kuiweka mdomoni, akamkumbuka Naya. “Hii ndiyo
imenikosesha kila kitu!” Malon akawaza. “Isingekuwa wewe, sasa hivi
ningekuwa na Naya na maisha yangu mazuri tu. Umenipokonya kila kitu.” Malon aliiambia ile bangi kwa kuumia sana. Gafla
ile harufu ya bangi ikaanza kumkera sana rohoni. Akasimama na kuizima kabisa.
Kisha akaifukia. Akatoka pale na kwenda kusimama mbali kidogo na pale
alipoifukia. Mpaka yeye mwenyewe akajishangaa.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
S |
iku
zilikwenda, wiki ya kwanza ikaisha, mwezi nao ukakatika, Malon hana kazi,
hawezi kurudi kwao. Akashindwa kuwalipa ile kampuni ya ulinzi. Akabaki yeye
peke yake. Hakusikia chochote kutoka kwa Tembe ambaye alishamtumia mawasiliano
yake. Akajua bado hajapata mteja wa kukodisha nyumba yake. Njaa, upweke
vikaanza kumsumbua Malon aliyezoea watu. Chakufanya ili kumuingizia pesa, hana!
Biashara ilitaka mtaji. Anapata wapi mtaji? Nani wakumkopa na hakuwa na namba za
simu za watu wengi na aliokuwa na namba zao kichwani wengine ni maadui
waliokusudia abakie chini, ndugu wa karibu ndio hao wamemchangia kumtoa jela! Akabaki
akifikiria.
Malon aliondoka kwao akiwa kijana mdogo sana. Akawa mtoto
wakujitegemea. Hata wazo lakurudi kwao halikuwepo. Akakumbuka alipokuwa
kijiweni, alijifunza ufundi wa magari. Alikuwa akitengeneza magari. Akazunguka
kutafuta hata kazi yakutengeneza magari, nayo akakosa. Kupunguza garama za
maisha, akazima kila kitu kwenye nyumba hiyo kubwa, akahamia kwenye nyumba ndogo.
Akawa anatumia hicho chumba kimoja. Anawasha taa za nje tu. Tena usiku. Yeye
mwenyewe akawa mlinzi wa nyumba yake. Usiku analinda nyumba yake, mchana
anazunguka kutafuta kazi. Malon akaanza kulijua jiji la Dar kama Moro. Alikuwa
akitembea kutafuta kazi bila mafanikio.
Hata wale aliokuwa akiwadharau akiona wanafanya kazi za
kishenzi, alitafuta kazi zao, akashindwa kupata. Alikuwa kama ameingiwa mkosi.
Hakuna aliyemwajiri, na hakuwa na uwezo wa kujiajiri. Hata mazoezi kitu
anachokipenda sana akaacha sababu ya njaa. Akawa mtu wakutoka asubuhi, kwenda
kuzunguka kutafuta kazi nakurudi jioni kabla giza halijaingia, kulinda nyumba
yake. Akarudia maisha ya kukaa kijiweni. Akapata vijana waliomkumbusha mwanzo
wa maisha yake akitafuta kutoka kimaisha. Na wenyewe wakafanana na yeye. Akaona
watamfaa kipindi hicho hana chakufanya. Akawa akishazunguka kutafuta kazi akichoka,
anakwenda kukaa nao mpaka jioni. Wakianza kuvuta bangi, anaondoka kabisa hapo.
Jingine tena kwa Malon.
S |
iku moja akiwa
amekaa tu kijiweni na vijana wa jijini Dar, maana Morogoro hakurudi tena.
Hapakuwa mbali sana na nyumbani kwake. Akapita kijana mmoja amevaa shati jeupe,
suruali nyeusi, amefunga tai. Mchana, jua linawaka. Ameshika bibilia,
anashuhudia. Wakaanza kumcheka pale kijiweni. “Sasa wewe huwezi kusema neno la
Mungu mpaka ufunge tai na joto lote hili!?” Mmoja akamkejeli. “Basi hata kanisa
lako likupe gari!” Wakaendelea kumtania, lakini kwa heshima kidogo kwa kuwa
alionekana ni mstaarabu. Hakuna aliyemtukana. Malon akamwambia akae kidogo ili
angalau afute jasho. Wakacheka. Malon akampa na maji ya kunywa aliyokuwa
ameshika mkononi. Tena na yeye Malon alikuwa amepewa tu. “Ni ya bomba lakini!”
Malon akamtahadharisha. Yule kijana akanywa kidogo, mengine akaoshea uso, akakaa
pembeni ya Malon aliyempa maji na bado hakuwa amemkejeli.
“Nikuulize kitu?” Malon akaanza. “Karibu.” Yule kijana akamgeukia
Malon. “Kuna mtu aliniambia mimi nina mapepo. Hebu niambie. Yaliingiaje na
yanatokaje? Na je, nitajuaje kama ni kweli ninayo na nifanyeje ili yasiwahi
kunirudia kama yapo?” Wale vijana pale wote wakamgeukia yule kijana huku
wakicheka. “Mimi mwenyewe mama yangu wakunizaa ananiambia nina mapepo!”
Wakaanza kutaniana vijana hao huku wakicheka, mpaka yule kijana akaanza
kuzungumza nao maana ni kama Malon aliweka tena msisitizo wa maswali yake
akitaka watulie wamsikilize akijibu. Aliongea nao kwa kimapana na mifano ya
waziwazi. Wapi shetani hupenda kukaa, nini kazi zake. Zawadi zake na madhara ya
kupokea zawadi zake. Jinsi ambavyo anapenda kutumikisha watu ambao ni wana wa
Mungu.
“Shetani hana zawadi ya bure.” Akaendelea Gwamwa, kama
alivyojitambulisha kwao. “Kazi yake shetani anapokuja kwenye maisha ya watu, kwenye
bibilia kitabu cha Yohana 10:10 inasema ni kuiba, kuu, na kuangamiza. Atakuibia amani
yako, mahusiano yako na watu wako wakaribu sana. Atahakikisha anakutenga na
kukuacha peke yako sehemu ambayo ataweza kukufikia ili kukuangamiza kabisa. Atahakikisha
anaangamizia furaha yako ya kweli na kukupa furaha ya vitu fulani fulani
ambavyo furaha zake ni lazima ikugharimu sana kuipata, na pia huwa ni za muda
tu.” Tarimu akaendelea.
“Inakuwa inakulazimu ufanye mambo fulani ili kuipata hiyo furaha.
Atahakikisha anakupokonya uhuru wako kabisa. Hata kama utakuwa ukitembea nje na
kuongea mambo mengi tu kiujasiri, lakini moyoni mwako utajua wazi huna ule
uhuru wa nafsi. Yapo mambo atakufunga nayo tu. Atahakikisha unakuwa mtumwa wa
hayo mambo aliyokuonyesha kama vile huwezi kuishi bila hayo mambo. Anahakikisha
unaishi ukitumikia hilo jambo tu. Hiyo kiu tu. Hiyo tamaa ambayo unakuwa
ulishamruhusu aitumie kwako.” Akaendelea Tarimu kwa lugha rahisi sana. Wote
kimya kama alioanza kuwagusa.
“Halafu hataishia hapo, kabla hajakuua kabisa kwa kukuangamiza
wewe mwenyewe baada yakuua nafsi yako, kama nilivyowaambia mwanzo kuwa anahakikisha
anaua hata mahusiano yako na watu unao wapenda sana au wanao kupenda sana. Hufika
umbali mkubwa sana wa wakufanya ukachukiwa na kutengwa kabisa na jamii. Si kwamba
inatokea hivyo kwa bahati mbaya. Ni katika mikakati yake juu yako. Kwa yale
atakayokutumikisha uyatende, yanakuwa chukizo kwa wakupendao au uwapendao kiasi
ya kwamba hakuna jinsi wakakuvumilia. Niweke msisitizo hapa.” Tarimu akajiweka
sawa.
“Niliwaambia anakutumikisha ufanye maovu yakutengwa?” Akawaona
wote kimya. “Lengo lake la kwanza la kuiba, kuua linakuwa sasa
limefanikiwa. Bado lile la tatu kuangamiza. Ameshakuibia marafiki,
familia. Ameshaua nafsi yako. Umekufa katika haki mbele ya Mungu na
jamii. Huna uwezo wakufanya tena mema. Ameua uhuru wako. Ameua kila kitu. Sasa
ndipo lile jambo la tatu la kuangamiza ndipo linafuata. Atakutumia wewe vile
atakavyo kwa kuwa ameshafanikiwa kukuweka kwenye upande wake. Umatekwa sasa.
Hakuna anayekufikia tena kukurejesha, maana umechokwa, umeshindikana, kila mtu
amekukatia tamaa. Huna nafsi iliyo hai. Huna ufahamu. Umekufa. Unayoyasikia na
kuyatenda ni maovu tu.”
“Basi ndipo anaanza kuangamiza. Sio wewe tu, hata walio karibu na
wewe. Atakutumia vile yeye atakavyo. Unakuwa ndio mtumwa wake yeye, akikutuma
ufanye mambo ambayo hata baadaye ukishayafanya, ukikaa chini, unajishangaa kama
ni wewe kweli umeweza kufanya hivyo au kumfanyia mtu jambo kubwa na baya la
kiasi hicho! Lakini napo hata ukijutia, unakuwa huna jinsi yakubadilisha kwa
kuwa umeshaharibu sana na huna huo uwezo. Ameshakufunga kupita kiasi hujui ni
wapi pakuanza kujifungua ili kurekebisha msururu wa mambo mabaya aliyokusababisha
kuyatenda pale alipokuachia kiu ya kufanya hilo jambo unaloshindwa kulala bila
kulifanya, na kwa watu wanao kuzunguka maana umeshafanya kwa kurudia rudia
mpaka wanajitenga na wewe na hawakuamini tena.” Hapo kila mmoja akabaki
akijifikiria nafsi yake. Tarimu akaona wametulia. Mzaha tena hakuna.
“Lakini lipo tumaini kwenye andiko hilohilo la Yohana 10:10
linaloongelea kusudi la shetani kwa wana wa Mungu.” Tarimu akafungua ile
bibilia aliyokuwa ameshika. Akasoma. “Yesu akamalizia hivi, lakini mimi nimekuja
ili wawe na uzima, tena wawe nao tele.” Akawatizama. “Mimi ni shahidi wa
mambo haya ninayowaambia. Nilikuwa teja kabisa wa pale kituo cha Fire.
Nilishamwibia kila ninayemfahamu ndani na nje ya familia yangu. Hakuna
aliyekuwa tayari kunifungulia mlango. Nilifika hatua, nauza mwili wangu ili tu,
kupata pesa yakununua unga.” Wakamkazia macho na kujiweka sawa maana hakuwa
kiendana kabisa na anayo zungumza juu yake.
“Niliteseka karibia ya kufa kwa maradhi au niseme magonjwa ya
zinaa. Nilikuwa nikikaa sehemu, huwezi kupumua, jinsi nilivyokuwa nikinuka! Maisha
haya ya kijiweni yalikuwa ni yangu na sikuwa na jinsi nyingine yakuishi ila hii
kama nyinyi hivihivi. Hapakuwa na lugha safi na fasaha inaweza kutoka kinywani
mwangu isipokuwa matusi tupu. Kufupisha habari yangu. Yesu ameniokoa.
Amenisamehe dhambi, amenitakasa na kuniponya maradhi yote. Tena mimi mwenyewe
nilikwenda kwenye mkutano palepale jangwani. Lengo lilikuwa nikutafuta hata mtu
nimwibie, nipate pesa ya kula. Lakini nikakutana na mahubiri, yakutangaziwa
kuwa huru. Yule muhubiri aliongea kama aliyekuwa akizungumza na mimi. Mimi
sikuwa mkristo wala sikuwa namjua Yesu. Kwa vile nilivyokuwa nimechoka,
nikakubali kuombewa niwe huru.” Akacheka.
“Nilipata nguvu ya ajabu ambayo sikujua ni nini kinaendelea kwa
wakati ule. Walinisimulia kuwa nilitupwa mbali na pale jukwaani nilipokuwa
nimesogea ili nisikilize anachozungumza. Nikalipuka mapepo, nusura nikimbie
barabarani nikagongwe na gari ili nife. Walinikamata, nikaombewa na kuwekwa
huru. Sijawahi kwenda kutibiwa chochote hata ulevi au ugonjwa wa zinaa
niliokuwa nao kwa wakati ule. Lakini huyu Yesu siku ile aliniponya. Nikisema
kuponywa, ni yote. Kijana mmoja, aliyekuwa akihudumu pale, alinichukua na
kunipeleka kwake. Nikaoga kwa mara ya kwanza baada ya miaka mingi sana, nikala
chakula kizuri na kulala kitandani. Hiyo ni baada ya miaka mingi sana yakulala
nje tu nikitumiwa na ibilisi atakavyo.” Wakabaki wamekodoa macho.
“Ni kweli kanisa halinipi gari, kwa kuwa nafanya hivi mimi
mwenyewe kwenye siku ambazo siendi kazini. Nazunguka tu sehemu kama hizi zinazofanana
na sehemu ambazo na mimi nilikuwa nikiishi nakuteswa na ibilizi. Lakini mimi sikuwa
kama nyinyi hivi, eti na jioni mnapo pakwenda! Mimi nilikuwa nikikaa na kuishi
sehemu kama hizi. Ndio maana nazunguka kujaribu kuzungumza na vijana kama
nyinyi. Japokuwa nikiwaangalia nyinyi nawaona mpo bora sana kuliko vile
nilivyokuwa mimi kipindi kile, mimi nilifikishwa pabaya zaidi, naomba Mungu
asiwafikishe huko.” Akatulia kidogo kisha akaendelea.
“Nafunga tai sio kwa sababu nyingine yeyote, ni kwa sababu naweza tu. Nilishatamani sana kuwa msafi kama hawa watu waliosoma, wanaokwenda kwenye maofisi makubwa. Basi, siku ambazo na mimi huwa siendi kazini, navaa shati nakufunga tai.” Wakacheka. “Kwani unafanya kazi wapi?” Mmoja akauliza. “Nafanya kazi kwenye kampuni moja ya ulinzi. Ni mlinzi. Tunalinda kwenye mabenki, sonara, majumba ya watu wenye pesa. Inategemea unapangiwa wapi.” Malon akawa amevutiwa sana na yule kijana. Wakauliza maswali mengi sana. Yeye Malon akataka zaidi. Akamuomba aongozane naye mpaka nyumbani kwake. Tarimu akakubali wakaondoka hapo.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
“Katika walioibiwa mahusiano, basi mimi ni mmoja wao. Shetani
ameniibia msichana mzuri sana. Kwa jinsi nilipokuwa nimefikia, nisingekuwa mtu
sahihi kwake. Tamaa ya bangi ilikuwa ikinitesa. Na kila nilipokuwa nikivuta,
ilikuwa ni lazima kulala na wanawake. Nimemuumiza sana Naya.” Akampa historia
yake Naya, Malon huyu, alikuwa mchovu. Akieleza kuwa yeye alimsomesha Naya,
usingeamini.
Tarimu akazungumza naye tena. Akampitisha kwenye mafundisho mengi.
“Kwani wewe unaweza kuniombea?” Malon akauliza. Taribu akacheka. “Kabisa.
Nataka uweke imani yako kwa Yesu, Malon. Haujafika umbali niliofika mimi. Na
bado Mungu aliniokoa! Hata wewe anaweza kukusaidia.” Tarimu akaanza maombi. Ni
kweli Malon alikuwa na mapepo. Akashangaa hakutumia hata muda mrefu, mapepo kwa
Malon yakatoka. Akawekwa huru. Alimuongoza sala ya toba. Akamwachia ile bibilia
yake.
“Huyu atakuwa mwalimu wako wa pekee na mkubwa sana. Huwezi amini
nguvu iliyokuwepo kwenye hiki kijitabu tu. Ukiwekeza muda wako hapo. Hata
kidogo tu. Soma utakuja kunishuhudia siku moja.” “Nitaelewa kweli?” “Yaani wewe
soma. Soma tu. Utashangaa ule uwelewa wako unavyobadilika. Ipo nguvu ya ajabu
sana kwenye hicho kijitabu. Kina nguvu ya kufungua ufahamu na kumuweka mtu yeyote
wa namna yeyote, huru. Hata kama fahamu zako zimefungwa kwa upana wa namna
gani, basi hiki kitakuweka huru. Kesho nitaingia kazini asubuhi. Na kesho
kutwa. Ila baada ya siku mbili, nitakuja hapahapa kukutembelea.” Malon akabaki
akipekua ile bibilia. Tarimu akamuachia pesa kidogo, akatoka.
Malon hakulala siku hiyo. Alibaki akisoma ile bibilia. Kulikuwa kuna furaha fulani ndani yake. Lakini hofu ya kurudia yale maisha ya zamani yaliyopokonya furaha na utu wake ikaanza tena na kutaka kuanza kumpokonya hata furaha mpya aliyopokea. Shetani akimnong’oneza jinsi atakavyoshindwa. Akamkumbusha vile alivyokuwa akijitahidi na kunuia kuacha lakini akawa akishindwa. Akawa akimkumbusha tena na tena vile ambavyo haitakuwa tofauti hata safari hii. Lakini Malon akaendelea kusoma tu ile bibilia na kukutana na majibu mengi sana humo ndani yaliyoanza kumpunguzia hofu.
Siku ya Mahafali Ya Naya.
N |
aya na
familia yake waliwasili mjini Morogoro mapema tu, wakaelekea Mzumbe chuoni alipohitimu
Naya miezi mitano na siku kadhaa zilizopita. Hakuwa amealika watu wa nje ya
familia yao isipokuwa Joshi ambaye familia nzima walimtarajia kuwepo hapo
mapema tu kwani walishaanzisha mahusiano zaidi ya salamu na Naya. Joshi
alishawatembelea kanisani kwao mara kadhaa. Kwa haiba yake ya utulivu na kwa
kuwa alikuwa mcha Mungu na elimu aliyokuwa nayo, mama yake Naya alimpenda sana Joshi.
Hakuacha kumtaja hapo nyumbani kwao na kumzungumzia mara kwa mara ili tu, Naya
amfikirie kwa ndoa. Alishamkaribisha hapo nyumbani kwao mara kadhaa. Joshi
alishakwenda na kuwepo nyumbani kwa kina Naya, Kiluvya akipata mapokezi mazito
kutoka kwa mama Naya ambayo hata Malon hakuwahi kuyapata. Lakini baba yake
alimjua Naya. Jinsi alivyokuwepo na Joshi, sivyo alivyokuwepo na Malon. Ni
kweli Naya alibadilika kwa kiasi fulani. Joshi hakufanikiwa kumchekesha tena
kama siku ile. Alikuwa akicheka, lakini sio kama zamani. Aliongeza utulivu hata
kwa baba yake alikuwa mkimya sana.
Siku hiyo ya mahafali yake alikuwa amejitengeneza vizuri,
akapendeza kwenye joho lake. Mahafali yakaanza. Wakatakiwa kujipanga kwenye
viti vyao. Naya akakaa pale, akawa ameinama. Kwa kuwa baba yake alikuwa hawezi
kuweka macho yake kwengine kama yupo Naya, muda wote alikuwa akimtizama
alivyoinama. Walipotakiwa kusimama akasimama, walipotakiwa kukaa alikaa.
Wakaitwa majina mmoja mmoja kupokea vyeti, akaenda. Mama yake alikuwa
amechangamka kuliko hata Naya mwenyewe. Zayoni ndiye aliyekuwa akipiga picha.
“Mwanao picha zote ameinama.” Akamnong’oneza baba yake. “Ona!” Akaanza kumuonyesha picha alizompiga dada yake.
Na zote alikuwa ameinama. “Kasoro hii moja tu aliyokuwa akienda kupokea cheti.” Akaendelea kumuonyesha. “Tutamwambia
anyanyue kichwa baadaye.” “Sasa mbona hafurahii wakati amefaulu vizuri? Kwani
wewe ndio umemlazimisha kuja kwenye mahafali yake?” Baba yake akampa jicho
hilo, akajua ndio anyamaze. Akajirudisha kwenye kiti chake akatulia.
Wakati wanakaribia kumaliza, Joshi akaja. “Nimepitwa nini?” Akaongea kwa sauti ya chini, akiuliza familia
hiyo iliyokuwa imekaa pamoja. “Wanamalizia tu. Vipi?” “Shikamoo mama.
Nilitingwa kazini, hivi nimelazimishia tu kuja.” “Pole.” Wakaendelea kuzungumza
kwa sauti ya chini. Wakatulia wakati wanamalizia. Ikaisha, Naya akawasogelea. “Joshi!”
Akashangaa kumkuta Joshi pale.
“Nimechelewa kazini. Tulikuwa na mambo mengi, lakini nikalazimishia tu.”
“Asante kwa kuja.” “Hongera mama.” Baba yake akampongeza. Naya akacheka kicheko
cha kawaida sana. “Asante baba.” Mama yake naye akampongeza. “Njoo ni kukumbatie
mwanangu. Hongera sana mama.” Naya akacheka, akamsogelea mama yake,
akamkumbatia wakati mdogo wake anapiga picha.
Wakapiga picha nyingine ya pamoja. Wakati wamesimama, wakamuona
Naya amegeukia upande mwingine ameduaa. Wote wakageukia ule upande. Wakamuona
Malon amesimama kwa mbali anawatizama. Alipoona wote wamemuona, akapunga mkono.
Naya akabaki ameduaa kama wenzake. Malon alikuwa amebadilika sana kama sio yeye!
Amekonda na kweli amekuwa mweusi haswa kama alivyomwambia Naya kipindi
wanaanzana na Naya hakumsadiki kuwa huwa akiishiwa hubadilika mpaka rangi ya
mwili wake!
Akapunga tena mkono, akawasogelea pale huku akimtizama Naya.
“Hongera.” Aliongea taratibu, Naya akainama. Ndipo akasalimia kila mtu kwa
kumshika mkono. Malon huyu alikuwa na hali mbaya ya muonekano kuliko hata
alivyotoka jela. “Umekuja kwenye graduation ya nani?” Baba yake Naya akauliza. “Nilikuja kumpongeza
tu Naya. Sikutaka kusumbua.” Naya akamwangalia akiwa amekunja uso kama haamini.
“Kumbe ulikuwa hapa muda mrefu!?” Akauliza
tena baba yake, wengine wakiwa wanashangaa tu. Malon alibadilika, akawa mtulivu
sana. “Ndiyo, nilifika mapema.” Malon akajibu, Bale alikuwa kimya akimtizama
kwa mshangao haswa.
“Basi naomba niwaage. Ili niwaache muendelee kusherehekea.” “Huna
haja yakuondoka Malon. Tumekuja na soda kidogo, na keki. Ungesubiri tule.”
“Nashukuru baba. Lakini naingia kazini usiku. Inabidi niwahi tu. Maadamu
nimehudhuria shuguli nzima ya muhimu ya mwanzoni, huko kwengine mfurahie kwa
niaba yangu.” Naya akamtizama tena kama asiyeamini.
Muda wote huo alipowasogelea tu Malon, mama Naya alikuwa kimya kabisa
hakuongeza chochote kwa yeyote akabaki kimya tu wazi akionyesha kuingiliwa
lakini pia akawa kama akimkumbusha Naya na baba yake juu ya alichozungumza
kuhusu Malon. Ukweli mama Naya hakuwahi kumkubali Malon tokea alipojua tu ni
mfanyabishara asiye na elimu. Kilio cha mama huyo ni Naya aolewe na mwanaume
aliyesoma. Hata kama hana pesa kama huyo Joshi mwenye elimu tu ila hana pesa
kama alizokuwa nazo Malon, lakini yeye alimpenda kwa haraka sana pale alipojua
amesoma, na ni muhasibu kwenye kampuni ya wanasheria.
Alishamwambia Naya kuwa hatakaa akalala njaa kama ambavyo angeolewa
na mfanyabiashara kama yeye, yaani vile alivyoolewa na baba Naya. Wakati wote
alisema biashara huwa na mtindo wa kufa na mtu kufilisika, lakini mwenye shule
kichwani, hata akifukuzwa kazi, anaweza pata kwengine. Au mwenye shule anaweza
kuajiriwa na kuwa na biashara pia. Lakini si biashara bila elimu. Sasa siku
hiyo pointi yake ikathibitishwa pale alipotokea Malon aliyekuwa anayopesa haswa,
lakini amechoka vile, akatamani kimuingie Naya vizuri na kuelewa alichokuwa
akizungumzia.
“Huu ni mzigo wako Naya. Hongera sana. Am so proud of you.”
Akaongea Malon kwa tabasamu, akimkabidhi Naya mfuko mzuri maalumu kwa zawadi.
Naya akapokea na kushukuru. “Asante kwa
kuja.” Malon akacheka kidogo. “Muwe na wakati mzuri.” Malon akaaga na kuondoka.
Naya akaanza kulia. Alijifuta machozi tena na tena. Akainama akiwa ameshika
mfuko aliokuwa amekabidhiwa na Malon. Ukimya ukatanda kwa muda. Ni kama
walimuona mzimu wa Malon. Kila mtu alibaki akiwaza lake. Naya akampa baba yake
ule mfuko, na yeye akaaga. “Nitarudi baada ya muda mfupi.” Naya
akaondoka.
Baada ya muda, Naya alirudi akiwa ameosha uso na ametulia kabisa.
Wakakata keki, wakanywa na soda, wakaamua kuondoka pale wakatafute chakula
sehemu nyingine. Joshi alikuwa amekuja na gari yake. Bale akapanda gari ya Joshi,
wakaondoka mjini Morogoro. Naya alikuwa ametulia kwenye gari. Akavuta ule mfuko
aliokuwa amekabidhiwa na Malon. Akakuta
kadi ya kumpongeza. Akasoma maneno yake, chini akakuta Malon ameandika jina
lake. Akakuta na barua ndani akaifunua.
‘Naya, inawezekana sijakupongeza vyakutosha. Hongera sana kwa kuwa
makini na mzuri kwenye kufikiria. Wewe ni zaidi ya hicho cheti walichokupa leo.
Unao uwezo mkubwa sana ndani yako. Nimeishi na wewe, nimekuona. Hujawahi
kujaribu jambo ukashindwa. Shule yako na mambo mengi unayofanya hujawahi
kushindwa, wewe ni shahidi wa hayo yote.’ Naya akakumbuka ni kama maneno
aliyomwandikia na yeye.
‘Nakushukuru kwa kujali kwako. Na msimamo ulioonyesha kwenye maisha.
Wewe ni mdogo kwangu, lakini nimejifunza mengi mno kutoka kwako. Umekuwa sababu
ya kubadilika kwangu. Najua unaweza ukashangaa vile nilivyo sasa. Lakini Naya,
ninayo amani ya ajabu. Yesu amenisamehe na kunitakasa. Huwezi amini niliweza
kuacha bangi bila hata matibabu. Nimewekwa huru. Kwa kichache nilichonacho,
nalala kwa amani. Maisha yangu yamebadilika Naya.” “Haaa!” Wakamsikia
Naya akishangaa kwa sauti ya juu huku akilia. Wote wakamgeukia kasoro baba yake
aliyekuwa akiendesha, akamtizama kwa kupitia kioo.
‘Naomba iwe hiyo ndio zawadi yako kwa leo Naya. Furahia pamoja na
mimi. Mungu amenibadilisha. Yale yaliyokuwa magumu kuyafanya, Mungu
ananiwezesha. Najua ndio yalikuwa maombi yako, Mungu amefanya. Natamani
ningekuwa na pesa nikakununulia kitu kizuri sana, lakini kwa sasa mambo
hayajakaa sawa. Naomba upokee kidogo nilichokuletea.’ Naya akajifuta
tena machozi. Na kuinama. Ili kutafuta hiyo zawadi. Akakuta sheni nzuri ya
dhahabu. Ilikuwa nyembamba tu. Wazi ilionyesha ni ya bei ndogo. Naya akaina
nakuanza kulia tena. Alilia huku ameshika ile cheni mkononi. Mdogo wake kimya,
pembeni yake.
Baada ya muda, akaendelea kusoma. ‘Nilipata kazi ya ulinzi. Ndio hapo nipo kwa sasa huku nikitafuta mteja wakupangisha ile nyumba. Nakusanya pesa ili nije kurudi Dubai. Nafikiria nirudie ile bishara ya sukari, bado naamini italipa tu. Namuomba Mungu anifanikishe katika hilo, ili angalau mambo yawe marahisi zaidi kwa upande wa kifedha. Ni hayo tu. Nimeona nikushirikishe pale nilipo kwa sasa. Nakutakia kila la kheri. Nakuombea mchana na usiku, ufanikiwe. Malon!’
Naya akainama nakuendelea kulia taratibu. Kilichosikika ni mlio wa
kuvuta kamasi tu. Alilia Naya, nakushindwa kujisaidia. Walifika jijini Dar.
Kwenye hoteli nzuri ambayo walichagua kwa ajili yake ili wapate mlo wa pamoja
kama familia na huyo Joshua, kama kumpongeza Naya kwa kuhitimu, lakini walifika
pale Naya akilia nakushindwa hata kutoka garini.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
0 Comments:
Post a Comment