Naomi Simulizi |+1 205 767 8163 |naomisimulizi@gmail.com Mapenzi & pesa – sehemu ya 11 - Naomi Simulizi

Mapenzi & pesa – sehemu ya 11

Kwa Malon.

A

kiwa ndio amefika tu jijini, yupo kwenye chumba chake hicho akibadili nguo kutoka alizokuwa amevaa na kuvaa sare za kazi, akasikia simu yake ikiita. Alikuwa Tembe. “Mpaka nimekusahau Tembe ndugu yangu! Upo mheshimiwa?” “Nipo. Vipi ile nyumba yetu, ilipata mtu?” “Bado kaka. Vipi, umepata mteja nini?” Malon akauliza huku akiendelea kujiandaa kwa haraka asichelewe kazini. “Naona zitakuwa habari njema sana. Yupo dada, amerudi nchini na mtoto mmoja, anatafuta nyumba yenye mazingira kama yako kabla hajaanza kujijenga upya hapa nchini. Anaonekana alikuwa masomoni huko nje ya nchi,


ndio amerudi na huyo mtoto. Si bado vifaa vipo?” “Njoo uitazame kesho kwenye mida ya saa 4 asubuhi.” “Basi nitakuja na bosi wangu. Ndio anahusika na hao wageni. Na nimemwambia umeahidi utamkatia pesa kidogo.” “Tutazungumza tukionana.” Wakawekana sawa katika hilo, Malon akaaga ili kuwahi kazini.

Alikwenda kazini akiwa amejawa tumaini. Ni kweli alifanya kazi hapo kwa takribani miezi miwili. Pesa aliyokuwa akilipwa, alikuwa akikusanya huku akijinyima sana. Hakuwa akilipwa mshahara mkubwa. Ilipokwenda kwenye mahafali ya Naya, akachukua asilimia 85 ya pesa yake aliyolipwa mshahara, akamnunulia yeye hiyo cheni ya dhahabu. Kwa hiyo ni kama alijimaliza kabisa kwenye akiba zake. Alifika kazini akiwa na wenzake wanne. Wao walikuwa wazoefu. Usiku huo walikuwa wakilinda sehemu wanayouza magari. Waligawana wawili wawili, wakapeana zamu yakuzunguka.

Malon alikuwa amepoa sana. Sura ya Naya akiwa ameinama wakati wote pale kwenye mahafali yake haikumtoka. Aliwahi mapema tu pale chuoni Mzumbe. Japokuwa watu walikuwa wengi, lakini alitafuta sehemu ambayo aliweza kuona kila kitu kinachoendelea. Tokea Naya na familia yake wanaingia pale, aliwaona. Macho yake yakaweza kufikia alipokuwa amekaa Naya. Naya aliyemuacha mara ya mwisho siye huyu aliyemuona kwenye yale mahafali. Alikuwa amepoa haswa. Hata Joshi alipoingia, pia alimuona. Alikuwa akiangalia kila kitu, huku akijiuliza kama akasalimie au amkabidhi vile vitu mtu, akampe Naya bila yeye kujitokeza! Akiwa anajiuliza, ndipo Naya akamuona. Na hata alipoaga kuwa anaondoka, pia alikwenda kujificha mbali kuangalia kinachoendelea baada ya pale. Alimuona Naya akilia. Usiku huo walimfurahia Malon hapo kazini. Maana alikuwa akizunguka bila kuchoka.

Wenzake walipeana zamu za kulala, lakini sio Malon. “Naya!” Malon aliwaza na kuvuta pumzi kwa nguvu. “Mungu nisaidie. Fanya muujiza. Nifungulie milango. Nibariki tena.” Malon aliomba huku akizunguka. “Nitendee lililokubwa sana. Mpaka watakaosikia, wakajue upo Mungu mtenda miujiza. Usimsahau Naya wangu. Mfariji, mtunze.” Malon aliomba karibia usiku kucha. Malon huyu mlinzi, hata akisema anamfahamu Naya, watu wasingemwamini. Naya alionekana wajuu sana. Alikuwa amechoka kwa kujinyima chakula, akifunga na kumuomba Mungu amfungulie milango tena, ila afanye biashara halali tu si haramu kama alivyofanya ile ya bangi na kumfanikisha kwa haraka.

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

Asubuhi baada yakutoka kazini akarudi nyumbani kwake. Alijitupa akiwa na usingizi, mpaka simu ya Tembe ilipoita tena. Akashtuka. “Tupo getini.” Malon alikurupuka na nguo zake za kazi vilevile. Akatoka. Alikutana na Tembe na mwanaume mwingine, yeye alikuwa mdogo kidogo kwa Tembe. “Ulisema unanikutanisha na mwenye nyumba, sio mlinzi Tembe. Sina muda wakuzunguka.” Malon alimsikia yule kijana akilalamika kwa kiburi cha pesa. “Aliniambia yeye ndiye mwenye nyumba.” Malon alimsikia Tembe akijibu kama asiye na uhakika. Akawafungulia geti na kuwakaribisha ndani.

Kwa muonekano wake na maneno aliyoanza kuzungumza, Malon akajua hata akimpa mkono, asingekubali salamu ya kupena mikono, akaona awe mpole tu. “Karibuni.” Malon akasimama akiwatizama. “Tunataka kuzungumza na mwenye nyumba.” Akaongea yule kijana. “Ndiye mimi, karibuni. Niwasaidie nini?” “Unazo karatasi zote na upo tayari kuandikisha kisheria? Maana sitaki utapeli. Watu watakao kuja kuishi hapa sio wababaishaji. Sitaki ubabaishaji.” “Hata mimi ningependa iwe hivyo. Ninaye mwanasheria ambaye atatusaidia kuingia kwenye mkataba mzuri tu. Usiwe na wasiwasi. Lakini kabla hatujafika huko, karibuni muangalie ndani. Ili muone kama ndio kitu ambacho mnatarajia.” Malon akatangulia kufungua geti la kwanza lakuingilia ndani. Uzuri alikuwa akiishi hapohapo, kila wakati alikuwa akisafisha. Kwa hiyo nyumba ilikuwa safi sana, japo kulikuwa na joto.

Ni ijumaa tu alikuwa humo ndani akisafisha na kuomba Mungu amkumbuke na amtafutie mteja. Kwa hiyo hata alipofungua milango, alifungua kwa kujiamini. “Kuna AC humu ndani kweli!”  Akauliza yule kijana ambaye ndiye bosi wake Tembe. “Ipo, na inafanya kazi. Nimezima kwa sababu hakuna anayetumia hii nyumba.” Malon mtoto wa mjini, na mfanyabiashara. Lugha ya biashara aliijua, na alikuwa mjanja. Dharau za yule bwana ilikuwa ni asili yake kabla hajafikishwa hapo na maisha pamoja na rehema za Mungu. Akamzungusha mle ndani akizungumza naye, mpaka wanamaliza, yule kijana yeye mwenyewe akajishusha nakuanza kucheka na Malon akitaka mpaka wagonge. Malon akajua amependa nyumba. Lakini alitaka wao walipwe asilimia 15, sio 10 kama walivyozungumza na Tembe.

“Nakulipa pesa ya mwaka Malon! Pesa taslimu!” “Ndivyo nilivyotarajia ndugu yangu. Nikisogea sana, ni asilimia 12, tena hapo ni kwa kuwa siwapi chumba cha nje na mimi mwenyewe ndio nitalipia huduma za kisheria. Sitaki mikataba ya hovyo.” Kwa kuwa Malon alishajua amepapenda pale na vitu vyake ni vya kisasa, hakubabaika. Akajua hata akiondoka, atarudi tu.

Lakini akashangaa anataka wamalizane kisheria ili ampe pesa. Malon akampigia simu Mati, akampa hiyo kazi. Mati akamwambia asubuhi hiyo ana mambo mengi sana. Atakuwepo hapo ofisini jioni, ataandaa kila kitu, kesho yake ndio afike hapo ofisini yeye kwanza na nyaraka za hiyo nyumba. Tembe na bosi wake wakasikia. Wakaafikiana kutafutana baada ya hapo. Wakaondoka na kumuacha Malon akiomba Mungu. Aliufunga ule mkataba katika ulimwengu wa roho huku akiomba chochote kisitokee. Hata dhuluma au kubadilika kwa mawazo. Maana ni kweli waliipenda ile nyumba na wakabaki wakimuuliza Malon ni wapi alinunua vile vifaa vya mle ndani.

Pesa.

M

paka inafika siku ya jumatano jioni, Malon alishakuwa na pesa yake benki na amekabidhi funguo za nyumba. Hakuna jinsi Malon angeeleza furaha yake na shukurani yake kwa Mungu, mtu akamuelewa. Alipopata tu ile pesa kwa kuwa alishafanyia uchunguzi biashara yake ya sukari nchini Dubai, na wateja wake walikuwepo, akataka kwenda na Cocoa. Aliulizia soko huko. Akaambiwa kama atapeleka Cocoa grade A, basi itapokelewa. Hilo likamtia moyo, na akawa ameshatafuta mtu wakutokea Mbeya. Akamwakikishia Cocoa nzuri. Malon akaaga kazini na kuondoka akiwa hana uhakika wa hiyo nafasi ya kazi pindi atakaporudi.

Kitu cha kwanza akaenda benki kukopa pesa. Akaweka dhamana hiyo nyumba, akaongezea na pesa ya kodi, akaenda Mbeya, Kyela mpaka mashambani kwa wakulima. Alikaa huko karibia majuma mawili akikusanya Cocoa nzuri huku akiwasiliana na watu wa Dubai. Kwa kuwa haikuwa mara yake ya kwanza kusafirisha bidhaa hasa mazao nchini huko, ikamuwia rahisi. Alijua ni bandari ipi atumie. Nani wakumsadia kutoa pindi mzigo wake utakapofika huko. Akaweka mambo sawa akiwa bado yupo huko huko Kyela kwa wakulima. Akapenda na mchele. Akakusanya kidogo tu kama kujaribu bahati yake akifika Dubai.

Akakatia ushuru na kulipia kila kitu. Safari hii hakufanya magendo kabisa. Alitaka kila kitu chake kiwe cha halali. Baada ya majuma mawili akawa anarudi Dar na mzigo wa Cocoa na mchele. Akaelekea bandarini yeye mwenyewe na makaratasi yote. Akapakia mzigo wote na kupigia simu watu wa kule. Alikuwa amebakiwa na pesa kidogo. Akaanza kuzunguka maduka ya mchele, akionyesha mchele wa Kyela. Akawaambia anao na anaweza kuwauzia kwa bei ya jumla. Akakusanya oda kwenye maduka kadhaa, akarudi tena Mbeya. Wakati huo anasubiri mzigo wake ufike Dubai, aufuate.

Akakusanya mchele, karudi nao yeye mwenyewe Dar na kusambaza siku hiyo hiyo, kwa kuwa hakuwa na sehemu ya kuhifadhi na dereva wa Lori alishamwambia nilazima washushe mzigo siku hiyo hiyo. Mpaka anamaliza kushusha mzigo, Malon akawa ameingiza pesa nzuri sana. Hakuamini. Alirudi kwenye chumba chake, akabaki akicheka. Wageni wake walishahamia. Kwa hiyo tayari walishaweka ulinzi pale wa masaa 24, ila kwa garama zao wenyewe, sio Malon. Ikawa kama mchezo hivi. Akaona akajaribu kutafuta tena soko la mchele. Tena alijiambia anajaribu tu. Hana chakupoteza sababu anasubiria kwenda Dubai kwenye kazi kubwa.

Siku hiyo nayo alitoka amefunga. Hakula kitu wala kunywa. Alielekea benki kupunguza deni ili riba isiwe kubwa sana, akaanza kuzunguka. Akashangaa anakutana na wauzaji wanaolalamika kuwa watu waliokuwa wakiwaletea mchele wameacha sababu ya ugumu wa maisha. Malon hakuelewa maana yake. Maana alipokuwa akiutoa huo mchele, huko Kyela, ilikuwa mashambani, na ulikuwa mwingi. Na wao walimuuzia kwa bei ya chini, wakisema maisha ni magumu wapate pesa kidogo tu. Hakupoteza hata muda. Kesho yake, akarudi tena Kyela. Akaingia mashambani na vijijini kwenye maghala ya watu. Malon mfanyabiashara, aliyejawa na maombi. Akapata kibali kwa wanakijiji wengi. Alikonunua mwanzoni, wakamtambulisha na kwa wengine. Akakusanya mzigo, baada ya juma moja, akarudi tena mjini na mzigo. Akauza wote, akapata pesa yake. Malon akabaki akijiuliza, ni nini kinamtokea.

Ilikuwa kufumba na kufumbua, Mungu anamtendea jambo la ajabu na kubwa. Tayari akaunti zake zikaanza kuwa na uhai. Angalau kukawa kuna jambo linaendelea kwenye maisha yake. Akarudi chumbani kwake, pembeni ya kitanda, akapiga magoti, akamshukuru Mungu kwa machozi.

 Mapenzi.

I

likuwa siku ya alhamisi. Malon aliamka asubuhi, akaamua kwenda nyumbani kwa kina Naya. Alinunua baadhi ya vitu vyakupeleka. Kwa asili, Malon alikuwa mtoaji. Na linapofika swala la Naya, hajui kubania. Hakuwa na uhakika kama atamkuta mtu hapo nyumbani kwao Kiluvya. Akagonga mlango wa hapo mbele, hakuna aliyeitika japo alisikia redio ikimba ndani. Akaacha hapo mizigo, akazunguka nyuma ya nyumba. Akamkuta Naya, baba yake na kijana wa ng’ombe wakiosha ng’ombe. Baba yake Naya ndiye aliyemuona wa kwanza, akamwambia Naya ageuke. Naya akabaki ameduaa.

Malon aliwasogelea na kuwasalimia. “Mikono michafu hii baba. Ina dawa ya kuua kupe.” Akaongea baba Naya. “Acha niwasadie.” “Usisumbuke kabisa. Utaingia uchafu, utashindwa kabisa kurudi kwako. Hata hivyo tumebakisha kidogo tu. Karibu ndani utusubirie, tutakuja baada ya muda mfupi tu.” Naya kimya. Alikuwa amevaa buti za mvua, amebeba mgongoni galoni kubwa la dawa ya kuoshea ng’ombe, na mkononi ameshikilia bomba ambalo alikuwa akinyunyuzia ile dawa kwa ng’ombe. Malon akamtizama, akakwepesha macho na kuendelea na kazi yake. Malon alikuwa akimtizama akifanya ile kazi bila shida na alionekana ni mzoefu nayo.

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

Naya alimwambia kila kazi anayofanya baba yake, na yeye anaijua kuifanya tokea mtoto. Kwani mara zote alikuwa akienda kucheza pembeni ya baba yake na ndipo alipozijua hizo kazi. Ikatokea hivyo hivyo na kwa Bale. Alipenda kucheza pembeni ya mama yake. Ikawa tofauti. Naya alijua mpaka kubadili tairi la gari. Mzuri sana kwa kazi za mkono, za nje. Sio ndani. Afadhali kaka yake Bale, alijua zote zote, lakini kwa kuwa walikuwa wakigombana na Naya kila wakati, usingewakuta wawili hao sehemu moja. Kwa hiyo wakakua Naya yupo nje na baba yake wakati wote, Bale na Zayoni ndani na mama yake.

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~ 

Malon hakuondoka pale. Akabaki amesimama tu akiwaangalia wanavyofanya ile kazi mpaka wakamaliza. Walitoka hapo kujisuuza na kusuuza vyombo vya ng’ombe. “Leo hukwenda kazini? Au unaingia usiku tena kama siku ile?” Baba yake Naya akauliza wakati yeye na Naya wakiosha miguu. “Ilikuwa kazi ya ulinzi. Niliacha.” Alijibu Malon kwa kifupi tu, Naya akamtizama nakuendelea na kujisafisha. “Ulipata kazi sehemu nyingine?” “Mungu alinifungulia milango ya biashara.” Ile kauli aliyozungumza Malon, ikamfanya baba Naya asimame na kumtizama Malon.

“Umebadilika sana Malon! Sio muonekano wa nje. Hapana. Upo tofauti.” Malon akacheka. “Nilikutana na Yesu, baba. Nilifungwa na nguvu za giza. Niliombewa na kuwekwa huru. Nafikiri mabadiliko haya ni lile pumziko la ndani. Unakumbuka mara ya mwisho kuzungumza na mimi ukaniambia nahitaji mapumziko?” Malon akauliza na kuendelea. “Wakati ule nilikuwa sielewi kabisa. Ila sasa hivi naelewa. Japokuwa huu mwili umechakaa sio kama nilivyokuwa zamani, ila nimepata pumziko la ajabu sana. Ipo amani hata katika kukosa, au kupungukiwa vitu hivi vya nje. Ile hali ya wasiwasi sana imepungua. Sina hofu yakukamatwa na polisi. Sina hofu ya kuingiliwa niibiwe. Nalala usingizi mzuri.” Baba Naya akacheka.

“Juzi nilikwenda Morogoro kwenye ile kesi yangu, hata mimi sikuwa najiamini ile hali ya utulivu Mungu aliyokuwa amenijalia. Sikuwa najua litakalo nikabili. Nani atakuja kutoa ushahidi gani. Lakini niliamka mapema tu, nikaenda mpaka mahakamani. Nazungumzia ile amani na utulivu wakujua sio mimi tena ninayeishi, yupo anayepambana vita yangu. Huwezi amini baba,” “Eeeh!” “Nilikaa pale. Kesi yangu ikatajwa, hakuna shahidi hata mmoja aliyejitokeza, hakuna wakunishitaki. Tumebaki mimi, Mati na hakimu tukiangaliana. Mwishowe hakimu akaniruhusu niondoke, kesi imefutwa. Nilimshukuru sana Mungu kwa kunifutia ile kesi.” “Hongera sana Malon. Hongera sana.” “Nashindwa hata kusema asante baba yangu. Hakika ni Mungu tu.” Wakati Malon akiongea na baba yake, Naya aliyekuwa amesimama nyuma ya baba yake akisikiliza, akaondoka kurudi ndani. Malon na baba yake Naya wakazungumza kidogo, wakarudi na wenyewe ndani.

Walikuta Naya alishaingiza ile mizigo ndani, lakini ameacha sebuleni. Baba yake Naya akaona. “Kumbe ulikuja na mizigo?” “Nauza mchele. Huo ni mchele wa Kyela kabisa. Mzuri sana. Nimewaletea na mafuta ya mawese yale ya wenyewe kabisa.” Wakacheka. “Asante sana.” Malon alikuwa amenunua na vitu vingine, sio ule mchele na mafuta tu. Alileta na unga wa ugali, maharage, sukari, mafuta ya kupikia kwenye dumu kubwa kabisa la lita 20 na chumvi. Akakaa wakati wenyeji wake wameenda kuoga.

Baada ya muda, Naya akatoka. Akaenda kukaa pembeni yake. Malon akamsukuma kidogo kwa bega lake. Naya akamwangalia macho yakiwa yamejaa machozi. “Umekula?” Naya akamuuliza. “Nitakula jioni.” Naya akaelewa amefunga. Akanyamaza. “Umechoka?” Malon akamuuliza. Naya akatingisha kichwa kukataa. “Una kazi gani baadaye?” “Sina. Niliacha kwa Ino. Na zile za matangazo waliingiza mambo ya mapenzi, baba akaniambia niache. Ndio nipo kwenye kutafuta kazi.” Malon akambusu kichwani. Naya akainama. “Naomba unisindikize Morogoro.” Naya akanyanyua kichwa na kumtizama. “Hatutakaa sana. Naenda mahakamani kufuatilia pesa ile uliweka dhamana. Kwa kuwa sikushitakiwa mahakamani, na kesi imefutwa, natakiwa kurudishiwa. Nilienda mara ya kwanza, wakaniambia nirudi leo. Halafu tutaenda kumuona mama, tunarudi.” Baba yake Naya akatoka akawakuta wamekaa.

“Sasa mama, si ungemwandalia mwenzio chai!” “Amefunga.” Naya akajibu moja kwa moja na kujifuta machozi. “Umekubali?” Naya akatingisha kichwa na kumwangalia baba yake. “Nini?” “Nimemuomba anisindikize Morogoro, hatutachelewa kurudi.” “Kwema?”  Baba Naya akauliza huku akikaa. “Nafuatilia malipo ya ile pesa Naya aliniwekea dhamana, na kwenda kuwasalimia wazee kidogo. Juzi nilikwenda, nilikuwa na haraka, sikukaa sana nyumbani. Nilimuacha mama anawasiwasi na afya yangu. Nataka niende nikakae naye hata kidogo tu, kumtuliza.” “Utakuwa umefanya jambo la msingi.” Akaongeza baba Naya. “Niende baba?” Naya akauliza. “Nyinyi nendeni, lakini naomba muwe waangalifu huko.” “Sitampeleka sehemu nyingine mbali na mahakamani na nyumbani. Kisha tutarudi.” “Sawa.” Naya akarudi chumbani kwenda kubadilisha nguo.

Alitoka chumbani kwake, akiwa amebadilika akaonekana amejitengeneza kidogo na hata baba yake aliyaona mabadiliko ya mpaka usoni. Aliweka tabasamu la ukweli, likaonekana lina tumaini. Wakaaga hapo, wakatoka wakitembea tu. Safari hii hapakuwa na gari la kifahari ila kutembea tu kuelekea kituoni ili kutafuta basi la kuwapeleka Moro, wala sio Side tena. 

Malon & Naya tena.

M

alon akamtupia jicho wakiwa wanatembea kuelekea kituoni. Akamuona ametulia sana, akamshika mkono na kumvutia karibu. “Unaendeleaje? Sio kwa ujumla.” Akamuuliza akimaanisha kutaka majibu kwa kina. Naya akatoa tabasamu akifikiria kidogo. Akamuona anajifuta machozi mara kadhaa. Malon akatulia akiwa amemshikilia mkono na kuuminya taratibu, akimsubiria atulie. “Naendelea vizuri kiafya. Ila kazi zinasumbua! Baba alinikataza nisiendelee na zile kazi za usiku. Unakumbuka mara ya mwisho ulinikuta na Ozi?” Malon akaitika. “Ilikuwa tukafanye tangazo la kinywaji, lakini pombe.” Malon akacheka. Alimjua baba yake Naya. “Lakini ilikuwa inilipe vizuri bwana!” “Kama vile nilivyokuwa nikiwauzia watu bangi?” Malon akauliza. Akamkumbusha baba yake naye alimuuliza hivyo hivyo. Akatulia.

“Ehe!” Malon akataka aendelee. “Kabla ya kufanya lile tangazo, ikabidi nimwambie baba. Kwanza nilijuta. Akaonyesha kushangaa sana. Ni kama ambaye hakutegemea hata ile tu mimi kufikiria kufanya hivyo!” Malon akacheka tena. “Basi, nikaacha lile tangazo wakati nilichaguliwa na Ozi akiwemo. Yule meneja wa ile kampuni ambayo alikuwa akitutafutia kazi, akaumia sana. Kwa kuwa alikuwa alipwe pesa nzuri tu, kama endapo mimi na Ozi, tungefanya lile tangazo. Ikabidi afanye msichana mwingine ambaye sio wakutoka kwenye kampuni yake. Basi, ndio baada ya hapo akaanza usumbufu sasa. Mara aseme kuna matangazo mengine yanafanyika nje ya Dar!” “Ulishawahi kwenda naye?” Malon akauliza.

“Nilikwenda Malon. Alinichukua mpaka Dodoma. Akaniambia ndio kuna matangazo. Tumefika kule, naona anafanya mambo yake. Tukafika hotelini akachukua chumba kimoja. Sikumbishia. Nikatoka nje, nikampigia simu baba. Nikamuelezea kila kitu. Baba akaniambia nirudi ndani, nichukue mizigo yangu, nirudi nyumbani muda uleule. Nikafanya hivyo. Nikarudi nyumbani. Baada ya siku tatu akanipigia tena simu, ananitaka kazini. Ndio baba akaniambia nisirudi tena, na kazi za usiku hataki tena. Basi. Ndio nipo naye hapa nyumbani. Nimejaribu kutuma maombi ya kazi kwenye makampuni tofauti tofauti, ndio nasubiri.” Walikuwa wameshafika kituoni.

Malon akamwangalia. “Na Joshi?” Malon akauliza. “Yupo.” “Nilimuona nilipokwenda kuzungumza na Mati. Nilipata mpangaji kwenye ile nyumba. Ndipo nilikopatia pesa za mtaji.” Basi likafika pale, Naya na Malon wakaingia ndani. Hawakupata nafasi za kukaa, wakasimama kwa ahadi ya kupata viti wakifika mbeleni. Hawakujali. Wakasimama, Malon akaanza kumsimulia Naya. Kuanzia siku anakutana na Tarimu, alivyomuombea na kumpa bibilia. Tarimu ndiye aliyemtafutia kazi kwenye kampuni ile ya ulinzi ambako na yeye ndiko anakofanya kazi. Akamuelezea jinsi alivyokutana na Tembe na mpaka akamtafutia mteja.  

Walipofika Kibaha kabisa kwenye kituo cha mabasi, ni kweli wakapata nafasi, wakakaa. Malon akaendelea kumsimulia mpaka siku hiyo alipokwenda pale. “Nakushukuru sana Naya. Asante kwa mema yote uliyonifanyia. Lengo la kukuomba uje na mimi huku, ilikuwa nikushukuru. Ulinitendea mambo ya ajabu mpaka leo unamshangaza mama yangu. Siku natoka jela, mama alizungumza sana na mimi mpaka nikajiona sikustahili Naya. Nilitaka tuachane kwa makusudi ili upate mwanaume atakayekupenda na kukutunza vizuri zaidi yangu.” Naya akainama.

“Siku ile nilifanya makusudi ili uondoke umenichukia ili uendelee na maisha yako. Iwe Joshi au Ozi, sikujali tena. Kwa kuwa nakuamini, nikajiambia utakayemchagua, ni kwa kuwa unajua atakufaa. Ulipoondoka ukiwa umekasirika, nikashukuru Mungu kuwa lengo langu lilifanikiwa. Sasa kuja kukukuta tena kesho yake umeniletea maandazi, sijui mayai na maziwa kwa mlinzi! Na simu unaniambia unaniombea na hivyo vitu vitanisogeza. Hakika uliweka hukumu kubwa sana moyoni mwangu. Nikajuta kukuacha, lakini sikuwa na jinsi. Hofu ya maisha ilikuwa imeniingia. Sijui nini chakufanya. Shule sina, na pesa sikuwa nayo.”

“Nikapatwa na kiu ya bangi. Nikatafuta, mlinzi akanipa. Nikaenda kukaa sehemu ili nivute. Nikakukumbuka. Nikaichukia ile bangi na kuifukia. Nikajiambia ndiyo iliyonisababisha kukuumiza tokea mwanzo, ndio imenifikisha pale mavumbini nilipokuwa nimekaa jua kali, njaa na kiu. Kuanzia siku ile nikaichukia bangi kabisa. Hata nikisikia harufu inaniumiza. Unakumbuka wakati ule nilikwambia nilitafuta msaada wa daktari?” Naya akacheka. “Basi safari hii nimeiacha bangi mimi mwenyewe bila tiba.” “Hongera Malon.” Malon akabaki akimtizama.

“Mati ameniambia mpo kwenye mahusiano na Joshi.” “Ndiyo.” Naya akajibu na kuinama. “Unampenda?” Malon akamuuliza. Naya akanyamaza. “Anakujali?” Malon akamuuliza zaidi. Akamuona anageukia dirishani na kunyamaza. “Ni maombi yangu uwe na furaha Naya. Unastahili.” Naya akainama. “Unanielewa?” Naya akatingisha kichwa kukubali. “Nakuombea sana.” “Asante Malon.” Wakatulia.

“Unakwenda lini Dubai?” “Kesho kutwa. Mzigo umefika. Nataka niwepo wakati unapokelewa na kusambazwa. Nataka niangalie kama naweza kupata soko zaidi.” “La nini sasa?” Naya akauliza. “Vyote. Sukari na Cocoa. Unajua sikujua kama tunayo Cocoa nzuri hivyo hapa nchini! Halafu nyingi. Nimeulizia masoko, yapo mengi tu. Ila kufika huko nchi nyingine ndio kazi. Watu wengi huko nje za nchi wanatumia sana cocoa. Au niseme inayo matumizi mengi sana. Acha niende kwanza Dubai, nitajua chakufanya nikifika huko.” “Hongera Malon. Nilijua utafanikiwa tu.” Malon akacheka.

“Nikuletee nini?” Naya akainama nakuvuta pumzi kwa nguvu. “Naya?” Malon akamwita na kumshika mkono. Akamwangalia. “Nimefurahi umekuja kunioana.” Malon akacheka taratibu huku akimwangalia. “Kazama kula Malon. Mwili umeisha!” “Sidhani kama ni chakula tu. Bado sijatulia. Nina kazi nyingi. Nimekaa huko Kyela, mpaka wamenizoea wanafikiri ni Mnyakyusa mwenzao.” Wakacheka. “Nazunguka mashambani kukusanya mazao, mchana na usiku bila kupumzika masaa mengi. Lakini inalipa, huwezi amini Naya. Hizi safari chache tu nilizokwenda, nimezalisha pesa nzuri!” “Hongera Malon.”  Naya aliendelea kumpongeza.

“Naruhusiwa kukupa zawadi?” Malon akauliza kwa upole. “Au nitazua matatizo kwa Joshi?” Naya akainama bila kujibu. “Nimekununulia hereni nzuri sana za dhahabu. Nilijua utazipenda. Naruhusiwa kukupa?” “Nitashukuru.” Naya akajibu nakujifuta machozi. Akazitoa mfukoni, akamkabidhi mkononi. Naya alishazoea kuvalishwa kila anapoletewa zawadi hizo na Malon. Lakini safari hii alimkabidhi mkononi. “Naomba usilie Naya. Tafadhali. Natamani kukuona unafuraha. Hayo machozi nilishayona sana. Tena wakati ule, mara nyingine niliyoona nikiwa na bangi kichwani. Sasa hivi naomba usilie tena. Sawa?” Naya akatingisha kichwa kukubali. “Vaa basi.” Naya akacheka huku anafuta machozi na hereni zake mkononi. “Asante Malo.” “Karibu.” Naya akatoa alizokuwa amevaa, akavaa hiyo dhahabu.

Wakatulia kidogo. “Nikuulize kitu Naya?” Naya akamwangalia. “Ukipata pesa sasa hivi, unataka kufanya biashara gani?” Naya akabaki akifikiria. “Bado ndoto za ubunifu wa mavazi bado zipo?” Naya akanyamaza kidogo. “Ni nini Naya? Naya niliyekuwa naye ni Naya wa mipango bwana! Usiniangushe.” Naya akatabasamu. “Nahisi kukaa na kumsikiliza sana Joshi kunaanza kuniathiri Malon.” “Kwa nini?!” “Unakumbuka nilikwambia Joshi alianza biashara ya sabauni?” “Nakumbuka, na ukamsifia sana.” Naya akacheka. “Sikumsifia bwana!” “Sijasahau kata sauti yako ya msisitizo.” Naya akaanza kucheka.

“Imekuaje?” Malon akataka aendelee. “Alikopa pesa. Akawekeza kwenye hiyo biashara. Anasema imemuingiza hasara tu. Hamna wateja! Amebaki na bidhaa, hana pakuuza. Amechukia biashara kabisa. Ananisisitiza kuweka mawazo kwenye ajira ndio kitu cha uhakika. Hivi yeye ndiye anayenisaidia kutafuta kazi kwa nguvu zote. Hata maswala la mavazi ameshauri niache kabisa. Anasema nikupoteza pesa na muda. Sasa hivi Tanzania maisha magumu. Watu wanafikiria nini chakula, sasa nikiwekeza pesa kwenye mavazi, nani atanunua hizo nguo?” Malon akashangaa na kukasirika sana moyoni, lakini akaamua kunyamaza tu, mpaka Naya akamshangaa. 

Malon wa zamani angeshatukana na kuongea kwa ukali sana. Lakini Malon huyu akanyamaza kabisa. Hakuongeza neno. “Malon!” “Nakusikiliza Naya.” “Ndio hivyo.” “Kila mtu anamtizamo wake Naya. Siwezi kuingilia maamuzi yako na mwenzio. Nyinyi wawili ndio mnahusika kujenga msingi wenu. Ila unanijua mimi. Huwa nathamini sana mawazo yako, kwa kuwa huwazi kijinga. Sijawahi kuona ukifikiria jambo, na kulitendea kazi, likakwama. Huwa linafanikiwa sana tena kwa asilimia za juu sana. Hapa hapa Tanzania, na mimi na wewe ni mashahidi kwa vile Mungu alivyojidhihirisha kwako. Kwa uchumi huu huu wa Tanzania, nimeona Mungu akikufanikisha.” Naya akajiegemeza pembeni yake. Akatulia na Malon naye akajiweka sawa ili amuegemee vizuri.

“Mnaoana lini?” Akamuuliza. “Anataka kurudi shule. Amesema mpaka amalize CPA ndio atafikiria swala lakuoana.” “Anarudi lini shule?” “Hata sijui Malon!” “Na wewe unataka kurudi shule?” “Sio kwa haraka. Ingekuwa amri yangu, ningeanza kazi au kufanya kitu kwa muda fulani, huku najenga familia kwanza. Sina haraka ya shule, japo najua nikitaka kurudi sitashindwa. Ila natamani kufanyia kazi hii shahada ya kwanza, kwanza. Na hata nikiishia hapa, sitajisikia vibaya.” “Niambie ni nini unataka kufanya kama ungepata pesa na kama Joshi angekubali.” “Hata simwambii tena.” “Tufanye kwamba atakubali kirahisi tu, endapo utamshirikisha. Nini ungependa kufanya?” Naya akanyamaza akiwa bado amemuegemea Malon.

“Naya?” Malon akauliza tena. Akainama na kumchungulia kule alipokuwa amegeukia. Ni kama alikuwa amempa mgongo kidogo. “Biashara.” “Hilo ni jibu la jumla sana Naya. Mimi nakufahamu. Huwa unaandika ndoto zako mpaka na pesa unayohitaji.” “Niliacha uliponiacha Malon. Nilitupa kila kitu.” Malon akambusu kichwani. “Kwanza naomba ujue sikuwa nimekuacha. Nilitaka uwe na furaha.” “Ndio kuniacha kwenyewe huko.” “Kwa nia nzuri lakini.” Naya akanyamaza.

“Sasa nakupa kazi, Naya. Ni juu yako kumshirikisha Joshi au la. Ila ningeshauri umshirikishe baadaye ukiwa umekamilisha ili usikutane na vikwazo mwanzoni.” “Kazi gani?” Naya akamgeukia. “Nataka utulie, ufikirie ni kitu gani unataka kufanya. Usijali swala la pesa na jinsi itakavyorudi. Hayo tutajua mbele ya safari. Nikirudi kutoka safari, uniambie.” “Kwani utanitafuta tena!?” Malon akacheka. “Ndiyo. Au siruhusiwi?” “Unaruhusiwa Malon.” “Haya. Naomba Naya ninayemfahamu arudi kazini. Huko unakojificha, sio wewe. Na wala hutakaa ukawa na furaha. Umenielewa?” Naya akacheka na kutingisha kichwa kukubali.

“Nikwambie kitu ambacho nilitamani?” “Hayo ndio nilitaka kuyasikia.” Naya akacheka tena. “Ningekuwa na pesa, ningefungua fremu au niseme duka au bucha ya nyama. Kubwa lenye yale mafriza makubwa yakulala. Halafu hivi baba anavyouza hao kuku wake, mimi ndio niwe nanunua kwa bei ya jumla kama hivyo anavyowauzia huko mahotelini kwa bei ya hasara. Halafu wale kuku mimi nikiwanunua, nauza kwa muundo tofauti tofauti. Naweza kuuza firigisi tu, au maini tu, miguu, mapaja na kadhalika. Kisha kuku wengine naweza kuwauza nikiwa nimewaweka viungo mbali mbali, nauza wabichi. Sehemu ya pembeni na hapo, naweka viti vichache tu. Namuomba Bale anipe recipe yake fulani hivi ya kuku wakuchoma. Natafuta yale maoveni marefu kama tuliyoyaona kipindi kile tulipoenda Dubai kwa mara ya kwanza, kwenye ile sehemu ukapenda nyama choma yake, tukawa tukirudi pale kula nyama kila tukienda Dubai?” “Napakumbuka sana tu. Si pale The City Grill?” “Ewaa! Kama vile sasa. Na mimi niige. Niwe nikiuza na kuku wakuchoma pia. Wale wazima. Naweka na friji ya juisi anayoitengeneza mama na soda. Nakuwa nauza. Kwa hiyo anayekuwa anakuja kununua kuku wakuchoma, anakutana na ile juisi ya mama na kuku wabichi pia yakupeleka hata nyumbani. Kuku walio na viungo tayari na wasio na viungo. Kisha nitengeneze nyama ya kusaga yakuuza pia.” “Sasa huyo ndiye Naya ninayemfahamu mimi. Anayefikiria kuzalisha jangwani. Mawazo makubwa zaidi ya mfuko wake.” Naya akacheka sana.

“Kweli tena Naya! Sasa hivi wewe ndiye unayeongea. Na kwa kukusikiliza tu, hilo wazo lako ni faida kubwa sana. Hata kama maisha magumu hapa nchini, watu wanakula na kunywa. Biashara ya chakula huwa haifi kirahisi, labda iwe haijawekwa sehemu nzuri au hapajawekezwa vyakutosha. Ukitafuta eneo zuri, ukafanya kama ulivyonieleza, baada ya mwaka mmoja au miwili, utakuwa mbali sana. Hata Joshi mwenyewe atakupongeza.” “Kweli Malon au unanitia tu moyo?” “Sikwambii hivyo ili kukuridhisha tu, Naya! Hiyo biashara ni nzuri sana.” Ujasiri ukaanza kurejea kwa Naya.

“Sasa mtaji Malon?” “Subiri tuone huko mahakamani kama huyo muhasibu atakuwa ametuandalia hiyo hundi yetu. Kama atatulipa, tutaiweka kwenye ile akaunti yetu. Mimi nitaomba kidogo ili niongeze kwenye biashara ya sukari. Unakumbuka nilikwambia kwenye biashara ile ya sukari mtaji ukiwa mkubwa na faida inakuwa kubwa na ya haraka?” “Nakumbuka.” “Basi. Tukishatoa hizo, zitakazobaki wewe wekeza, tena ukiwa huna presha. Taratibu, ukiipa muda. Na maombi Naya. Ipo nguvu kubwa sana kwenye maombi. Weka mipango yako kwenye maombi, ongeza juhudi, lazima Mungu atabariki kazi ya mikono yako.” “Siamini kama naongea na wewe Malon! Umebadilika.” Malon akacheka.

“Lakini Malon, nahisi ndio maana nilikuwa nakukumbuka sana.” “Kumbe ulikuwa ukinikumbuka!?” Malon aliuliza huku akicheka. “Sana Malo. Hakuna siku inapita nisikufikirie. Najiambia angekuwepo Malon hapa, angefanya hivi au angesema hivi. Au angenitia moyo katika hili. Hivi unajijuaga vile unavyokuwa ukiwa na mimi?” Malon akacheka akifikiria. “Nakuaje?” “Kila kitu kinasubiri, anakuwa Naya tu. Wakati mwingine hata simu unazima unapokuwa na mimi. Mawazo na akili zako zinakuwa kwangu tu. Nilimiss sana hiyo Malon. Nikawa mpweke wakati nilikuwa nimezungukwa na watu!” “Pole sana mama. Ila ujue sikutaka uangamie na mimi. Hata baba alinitisha sana. Aliniambia sikustahili hata kidogo. Tena akanishauri nikuache mapema kabla hujaharibikiwa zaidi. Hata Mati alichangia.” “Mati!?” “Mati ametokea kukupenda sana Naya. Amekuheshimu mno. Njia nzima kutokea Morogoro alikuwa akizungumza na mimi bila kuchoka.” “Anakwambiaje sasa!?” Malon akafikiria kidogo.

“Tuache hayo. Tupate muda wakuomba kidogo, ili Mungu atutangulie huko tuendako. Ombea huko mahakamani. Mungu atupe kibali. Kwa sababu mimi kama Malon, hakuna anayeniangalia kwa jicho la heshima. Nilishaharibu sana kwenye huo mji. Lakini Mungu akiwa na sisi, atatustahilisha. Tuombee ugeni wetu pale nyumbani. Japo hatutakaa sana, lakini basi tukafanyike baraka.” Naya hakuamini kama mzungumzaji ni Malon. Wakatulia, kila mtu akiangalia dirishani wakiomba. 

Jiji Kasoro Bahari Tena.

W

alifika Morogoro, kwa kuwa alikuwa na Naya, akachukua taksii. “Sitaki nikurudishe nyumbani umechomwa na jua.” Naya akacheka. Alimjua Malon jinsi anavyomjali. Walifika mahakamani, wakaambiwa wamsubiri muhasimu. Wakatafuta sehemu wakakaa. Naya akampigia simu baba yake kumtaarifu walifika salama. Wapo hapo wakisubiria. Walikaa zaidi ya masaa matatu, ndipo muhasibu akaja na maneno mengi. Lakini mwishowe wakapewa hundi yao. Malon na Naya wakaangaliana, wasiamini.

“Umeona ukiwa na mipango na pesa huwa inakuja?” Malon aliongea wakati wanatoka hapo mahakamani. Naya akacheka. “Kuanzia kesho lazima uanze kuzunguka kutafuta sehemu ya hiyo biashara. Mungu ameshakujibu kuwa pesa sio tatizo.” “Asante Malon.” “Sasa twende kwa mama Saduki. Anione kidogo, nimtulize, nikurudishe nyumbani, mchumba wa Joshi. Sitaki apige simu, akute nakuzungusha Morogoro.” “Joshi yupo busy sana.” Naya aliongea kwa upole. Malon akamtizama na kuamua kubadili mazungumzo. “Sasa kesho unaanzia wapi?” “Na hivi utanisaidia pesa, nitazunguka kesho siku nzima.” “Ingekuwa sawa, ningekusindikiza tukazunguka wote.” “Sasa kwa nini isiwe sawa!?” Naya akawa hajaelewa.

“Maana hapo ningepata na ushauri kutoka kwako. Wewe huwa unajua mambo mengi zaidi Malon. Nikichagua kitu, huwa unakifikiria kwa mapana kuliko mimi. Huwa unaona mpaka kesho yake kabisa. Naweza kuchagua sehemu kwa ukubwa, nikajisahau kwenye eneo.” “Kama haitaleta shida, basi nitakutafuta kuanzia kwenye saa tano hivi. Asubuhi kuna kitu lazima nikamilishe ili kunihakikishia safari yangu ya kesho kutwa.” “Nitashukuru Malon. Asante.” Wakatulia.

“Lakini Malon.” Naya akamwita wakati wapo kwenye taksii tena kuelekea nyumbani kwa kina Malon. “Vipi?” “Hatuwezi kwenda nyumbani mikono mitupu.” “Wanashida na pesa zaidi. Nilizungumza na mama. Akaniambia wanachakula, lakini hawana pesa ya kununua vitu vidogo vidogo. Akataka pesa. Nitawaachia pesa.” “Basi naomba tupitie hata mafuta yakupikia tu. Tusiende mikono mitupu kabisa.” “Nitawaachia pesa Naya! Wametaka pesa.” “Sawa. Lakini mafuta yakupikia huwa hayaharibiki. Hata wakiwa nayo mengi kiasi gani, yatawasaidia tu siku moja. Mimi nitalipia kama zawadi yangu kwa mama Saduki. Shukurani ya kusimama na mimi kipindi nina shida, alikuwa upande wangu japo kila mtu alinipinga, yeye alinitia moyo ndipo wengine wakafuata.” “Dada alinimbia. Nakushukuru Naya.” “Sio mimi sasa! Leo tunamzungumzia mama Saduki.” Wakacheka na kukubaliana wanunue vitu kidogo. Walimuomba dereva taksii apitie kwenye duka la jumla. Wakanunua vitu zaidi ya mafuta ya kupikia, ndipo wakaelekea nyumbani kwa kina Malon. 

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

Mama yake Malon alifurahi sana kumuona Naya. “Yaani hata sasa hivi nikifa, sina wasiwasi. Najua nimemuacha Malon kwenye mikono salama kama ya kwangu au zaidi na ya kwangu.” Naya akacheka na kuinama. “Angejua mwanae alishachelewa!” Malon akamnong’oneza Naya sikioni. Naya akaelewa, lakini mama yake hakujua ni nini Malon amemnong’oneza Naya. Ile kuwaona pale pamoja, akajua wapo pamoja. Baba yake Malon alikuwa ametoka.

Walikuta ugali hapo. Naya yeye ndio alikula wakati Malon akizungumza na mama yake. Akamsikia akimuaga mama yake kuwa atasafiri kibiashara. Mama yake akamuuliza maswali akionyesha wasiwasi. “Nimebadilika mama. Nakuahidi hutasikia nimeingia matatizoni tena. Ni kweli nimepeleka mchele na Cocoa. Mambo ya bangi nimeacha.” “Mungu akusaidie Malon, usirudi tena huko, baba.” “Amina mama. Uzidi kuniombea. Na nikifika huko nitakupigia simu mama yangu.” “Tafadhali upige. Hata usipofanikiwa naomba upige  tu Malon. Usiniache nikiwa na wasiwasi kama hapa majuzi.” “Nimekuahidi sitarudia tena. Nitapiga mama.” “Nakuamini baba.” Naya akamaliza kula na kurudi pale alipokuwa amekaa Malon na mama yake. Wakatulia kidogo na kuaga. “Basi muwe na safari njema mkiwa mnarudi Dar. Naya mama, usitutupe. Uwe unatukumbuka hata kwa simu.” “Nitafanya hivyo mama.” Wakaondoka.

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

Wakiwa njiani wakirudi Dar, hapakuwa na mazungumzo mengi sana. Kila mtu aliwaza lake. Bado Naya alikuwa kwenye mshtuko wa kupata pesa ya mtaji bila kutarajia. Malon akamuona anamvuta mkono, akaushika na kumuegemea. Akamuhurumia, akambusu kichwani, kisha akamchungulia. “Niambie unawaza nini?” “Kulala masikini na kuamka tajiri.” Malon akacheka. “Ushajiona tajiri?” “Kumbe! Kuna watu unakua nao kwenye maisha, inakuwa ni zaidi ya pesa na mali.” “Hilo mimi nalijua na nishahidi.” Wakatulia.

“Malo!” Naya aliita taratibu akiwa amemuegemea. Malon akamchungulia. “Utarudi lini?” “Sijajua Naya. Sijui kama safari yangu itaishia hapo hapo Dubai au la! Sijui itachukua muda gani na itaanzisha nini! Niombee tu.” “Nitakuombea.” “Lakini nataka uendelee Naya. Usiwe mtu wakurudi nyuma bwana! Kama sasa hivi tumeshazungumza, nakupanga, naomba Naya wangu wa zamani arudi. Yule Naya aliyekusanya mamilioni ya pesa mpaka akafanikiwa, ndie huyo huyo namtaka arudi, usimamie hilo wazo lako mpaka ufanikiwe. Umenisikia?” Naya akatingisha kichwa kukubali. “Pambana sana. Mimi najua utafanikiwa.” “Nimefurahi umerudi Malon na umenitafuta. Nashukuru kutafuta muda wa kunisikiliza tena, na kunitia moyo.” Malon akavuta ile mikono yao Naya aliyokuwa ameikumbatia, mpaka kifuani kwake, akabusu mkono wa Naya.

          Naya akafunga macho kama anayeruhusu faraja ipite moyoni mwake. “Nikuombe kitu Malo?” “Nakusikiliza.” “Naomba turudishe mawasiliano. Tuwe tunawasiliana. Hata kama haitakuwa kila siku, lakini niruhusu nikiwa na swali, nikupigie unishauri.” “Bila shaka Naya. Muda na wakati wowote wewe piga. Hata saa sita za usiku, nikiona simu yako nitapokea kwa haraka sana.” “Na wewe utanipigia?” “Ukiniruhusu, na ukanipa muda ambao sitawasumbua wewe na mwenzio, nakuahidi kupiga, japo kukujulia hali.” “Basi naomba na mimi unijulishe utakapofika Dubai. Hata usipofanikiwa, nipigie.” “Muda gani ni mzuri wakupiga?” “Wakati wowote.” “Hapana Naya. Lazima tuwe na nidhamu. Sitapenda nikuingize matatizoni au kumfanya Joshi ajisikie vibaya.” Naya akainama nakuanza kulia. “Basi tufanye hivi, uwe unanitumia ujumbe muda unaokuwa unanafasi ambao unaona tunaweza kuzungumza. Sawa?” Naya akatingisha kichwa akiwa ameinama. Malon akaweka mkono mgongoni kumtuliza.

Walishushwa Kilivya, kituo cha kwenda nyumbani kwa kina Naya. Ilishakuwa saa 12 jioni. “Unafikiri tumechelewa sana?” “Hapana. Usiwe na wasiwasi. Nilishamtumia ujumbe baba kumwambia tupo kwenu. Na wakati tupo njiani nilimtumia ujumbe. Hana neno.” “Nimefurahi umenisindikiza. Kitu cha kwanza nitakachofanya kesho asubuhi kabla ya kukutana ni kwenda kuiweka hii pesa benki. Nikishamaliza shuguli zangu, nitakupigia ili tuzunguke wote.” Malon na Naya walikuwa wakizungumza huku wakitembea kurudi nyumbani kwa kina Naya.

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

Kila mtu alimuona vile Naya alivyorudi tofauti. Baba yake akacheka. “Naona unawaka masikioni!” “Zawadi amenipa Malon.” Naya alimjibu baba yake huku akimsogelea na cheko kubwa usoni. “Umependeza mama mzazi.” Baba yake akamsifia. “Asante Malon kwa zawadi. Nimerudi nimekuta vyakula. Mungu akubariki baba. Naona una moyo wa utoaji kweli!” Akashangaa wengine wanacheka. Hakuwa ameelewa. “Kidogo tu mama. Naomba mimi niwaache. Muwe na usiku mwema.” “Na chakula?” Akauliza baba Naya, Malon akamtizama Naya. “Kama kipo ningeshukuru. Ili nile kabisa, nikifika iwe mambo mengine.” Malon akakaa.

“Kwani sasa hivi unaishi wapi Malon?” “Pale pale Kunduchi nyumbani kwangu. Lakini chumba cha uwani. Mbele nilikodisha. Ila nafikiri nikirudi kutoka safari, nitafute chumba kikubwa kidogo.” “Unakwenda wapi?” “Kuna biashara nilikuwa nikifanya zamani kidogo. Ya sukari. Natoa Brazili napeleka Dubai. Sasa kujibu swali lako, naelekea Dubai. Kuna mizigo nimetanguliza huko. Nimepata taarifa umefika. Nataka niwepo wakati inatolewa bandarini na kupelekwa kwa wateja, ili chochote kisitokee. Baada ya hapo ndipo nitajua pakwenda tena.” “Kwa hiyo utakaa Dubai kwa muda mrefu?” “Nafikiri hivyo. Nitajua nikifika huko.” Malon akajibu mama Naya kwa heshima zote.

“Bado chakula kidogo.” Naya alirudi na hiyo taarifa. “Basi, nitakula wakati mwingine.” Malon akataka kusimama. “Kwa kuwa ulikuwa umefunga, nimekubandikia chai. Uanze kunywa chai kwanza wakati unasubiri chakula.” “Hapo umefanya vizuri, Naya.” Baba yake akampongeza. “Hongera Malon. Nilisikia ulimpa Yesu maisha yako.” Akaongeza mama Naya aliyekuwa akimuhoji maswali. Malon akacheka kidogo. “Ni neema ya ajabu kwakweli. Hata mimi sikutegemea. Nilipokea nikiwa sijui thamani yake.” Malon akaendelea kuzungumza taratibu akiwashuhudia kile Mungu alifanya siku ile kupitia Tarimu. Akawasimulia mapepo aliyokuwa nayo na vile alivyowekwa huru.

Bale akaleta chai. “Muone! Anapenda stori huyu! Hapo amekaa ametulia tuli, amesahau hata kama amebandika chai jikoni!” “Kwani wewe ungeleta kimya kimya tu, ungepungua wapi?” “Bale na Naya, naomba msianze hapa. Sisi tunasikiliza mambo ya maana.” “Si Bale huyo!” “Bale gani, wakati ni wewe? Unaogopa jiko kama nini sijui!” “Siogopi jiko ila sitaki kuwa na wewe huko jikoni.” “Basi natoka nikupishe.” “Sitaki. Nina mgeni.” “Muongo. Hutaki tu kukaa jikoni. Kwani Malon anakuja hapa kila siku? Mbona jana hukuingia jikoni?” Malon akaanza kucheka. Akamkumbuka Naya na kaka yake.

“Haya, Bale, ondoka.” “Ungetufukuza wote baba!” “Ili mkazidi kubishana huko huko jikoni?” Baba yake akauliza. “Ondoka. Baba amekwambia uondoke.” Naya akaweka msisitizo. Bale akaondoka huku anamkazia macho Naya. “Sijui ukoje Bale?” “Wewe ndio sijui ukoje!” “Sasa na wewe Naya unamtafuta mwenyewe. Yeye alikuwa anaondoka, kwa nini unamuanza tena?” Mama yake akaingilia. Malon akazidi kucheka huku akinywa chai yake. Malon alimaliza ile chai, akamuomba Naya akamuongezee. Akarudi na chakula kabisa. Wakala huku wakizungumza, mwishoe Malon akaaga na kuondoka akiwa ameshiba.

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

          Naya akaanza kucheka. “Muone alivyofurahi!” Mama yake akamrushia neno. “Unampenda Malon wewe!” “Kwa kuwa ananijali sana mama. Hapo alipo anajua kama nipo na Joshi. Aliambiwa hukohuko ofisini kwao, lakini bado alikuja kuniona. Ona dhahabu alizo ni nunulia! Yaani Malon, kila akipata pesa, lazima anifikirie mimi kwanza. Huwezi kumlinganisha na ..” “Joshi!”  Kila mtu akadakia wakaanza kucheka. Mara zote Joshi akienda hapo, anakwenda mikono mitupu. Hakuna zawadi hata moja Naya alishaonyesha hapo kwao kwamba imetoka kwa Joshi. Hata siku ya mahafali yake, Malon ambaye alikuwa mlinzi, alipeleka cheni ya dhahabu. Joshi alikwenda mikono mitupu akilalamikia kutingwa na kazi.

“Baba!” Naya akamgeukia baba yake. “Unakumbuka ile biashara ya kuuza kuku niliyokuwa nimekwambia?” “Nakumbuka. Si ndio ile uliniambia ulimwambia Joshi, hata kabla hujamaliza kumueleza, alikwambia uachane nayo?” “Kumbe unakumbuka!?” “Siwezi kusahau.” “Basi Malon aliniuliza. Nikamwambia. Ungekuwepo, ungesema sijaongeza baba. Malon amefurahia na kunipongeza sana.” “Sasa mtaji? Maana wazo lipo sawa, sasa pesa unapata wapi hata kama wazo zuri? Labda ndio maana mwenzio Joshi aliona uache tu.” Mama Naya akatetea kidogo.

“Sasa subiri kwanza mama. Hapo Malon ananiuliza tukiwa njiani tunakwenda Morogoro. Na mimi nikamwambia tatizo ni pesa. Malon akaniambia tatizo sio pesa, tatizo ni wazo sahihi, ndipo pesa zinapokuja. Na kupata faida kwenye wazo sahihi ni sehemu sahihi, juhudi na maombi.” Kila mtu akastaajabu kasoro mama Naya, akatulia tu  akisikiliza.

Naya alikuwa akiongea kwa kujivuna. “Amenipongeza na kuniita nina akili sana. Hapa tunavyozungumza, amelipwa pesa yake yote. Anakwenda kuiweka kwenye akaunti yetu. Ameniambia nianze kesho kutafuta sehemu. Nishajua sehemu yakupata mafriji makubwa. Na atanisaidia kuzunguka kesho kutafuta yale maoveni marefu na sehemu nzuri. Pesa itakuwa benki. Ameniambia nianze.” Wakashangaa sana. “Husemi ukweli Naya!” “Kweli baba. Malon amenitia moyo na kunitaka nianze bila kuchelewa. Ameniambia nitafanikiwa nijipe muda.” “Sasa utamwambia nini Joshi?” Hapo mama Naya akauliza akionyesha wazi kuna mwingiliano ambao asingetaka utokee.

 “Joshi yeye anaonekana ni muoga wa kuthubutu.”  Naya alisema hivyo. “Na mbahili.” Akaongeza Bale nakufanya wacheke kidogo. “Bwana mwanaume muoga wakutoa pesa yule! Sijawahi ona. Anaona shida hata kulipia maji aliyokunywa yeye mwenyewe! Alinizungusha siku ile alipokuja kanisani nikawaambia tunaenda kununua maji nje!” “Kwani siku ile hakulipa?” Mama yake akauliza kwa mshangao. “Alihangaika mama, mpaka nikaona ni heri mimi nilipie maji yote. Kwanza alitaka alipie yake tu. Sasa mwenye duka akamwambia hana chechi. Eti akataka atoke hapo, akatafute chechi kwengine wakati alishayanywa maji! Ikabidi mimi nilipie tu.” Wakashangaa sana.

“Inawezekana kwa sasa anamajukumu mazito! Si alisema anajiandaa kurudi shule?” Mama Naya akatetea. Wote kimya maana walimjua jinsi anavyompenda Joshi. “Basi. Nimeona nianze tu. Ikishakomaa ndipo nimwambie.” Naya akaendelea bila kutaka kuongeza hapo kwa mama yake. “Kwanza hana muda wakufuatilia mambo mengine zaidi ya kazi yake anayolalamikia mchana na usiku.” Akaongeza Naya.

 “Mimi nikupongeze mama yangu mzazi, kwa mawazo mazuri ambayo huwa hujawahi kuacha kuyafikiria hata katikati ya ugumu. Ingekuwa rahisi kujipuuza pale unapokatishwa tamaa. Hongera sana.” Yeye baba Naya kama kawaida yake akasimama na binti yake. “Asante baba. Nimefurahi sana. Si unajua nilivyokuwa natamani kujiajiri?” “Ndio maombi yako siku zote. Naona Mungu amekujibu.” Ujio wa Malon ukawa wa furaha kubwa sana kwa Naya lakini si kwa mama Naya. Naya wa kucheka na maneno mengi akarudi. Yeye akawa ndio mzungumzaji mkubwa usiku huo mpaka wakaenda kulala mama yake akimsikiliza tu.

 

Naya kwa Malon.

‘Ulifika salama?’ Naya akatuma ujumbe. ‘Bado nipo mtaani mama. Sijarudi bado. Unalala sasa hivi?’ Malon akamuuliza kwenye ujumbe aliorudisha. ‘Bado kidogo. Nikilala sasa hivi, inamaana itabidi nivue hereni zangu, wakati bado hamu haijaisha.’ Malon alicheka sana alipokuwa akisoma ule ujumbe. ‘Nitakucheki nikifika nyumbani. Kama utakuwa umelala, basi nitakuona kesho.’ ‘Naomba nisubiri simu yako Malo!’ ‘Basi nitakupigia. Nitajitahidi kuwahi ili nisikuweke sana.’ ‘Usijali.’ ‘Sawa.’ Malon akarudisha hayo majibu.

Baada kama ya lisaa, Malon akapiga simu. “Umeshavua hereni?” “Zimegoma sikioni. Nimeona nilale nazo tu mpaka hiyo siku zitakapokubali kutoka.” Malon akacheka sana. “Asante Malo.” “Nini tena mama?” “Hereni, kuja kupata muda wakunisikiliza. Kwangu inamaana kubwa sana. Nilihitaji hiyo. Na asante kwa kuniamini. Nashindwa kulala kwa mshtuko. Siamini.” “Karibu sana. Ila nataka ulale ili kesho uamke na nguvu. Una kazi kubwa mbeleni. Inakuhitaji zaidi wewe. Sawa?” “Sawa.” “Basi acha tuombe kabla hujalala.” Malon akamuombea kwa kifupi tu. Wakaagana.

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

Kesho yake Naya aliamka mapema akiwa amejawa na furaha sio Naya waliyemzoea akijiweka na shuguli nyingi mpaka jikoni! “Basi leo huko jikoni kutavunjwa kila kitu! Si umwite huko nje?” Mama yake alinong’ona walipokuwa mezani wakinywa chai alfajiri hiyo ili kila mmoja awahi kwenye majukumu yake. “Ili mumwambie mwanangu anakimbia jiko? Mwacheni avunje tu.” Wazazi wake wakacheka, wakasikia tena kijiko kimedondoka. Wakaangaliana na kucheka tena taratibu. “Vipi mama? Kwema huko?” “Sio mimi, baba. Ni Bale.” “Ujue Naya unapata dhambi wewe!?” “Sasa aliyenitingisha hapa mwanzoni nikaangusha sahani ni nani kama sio wewe? Unahangaika huku jikoni hutulii!” “Na hicho kijiko cha sasa hivi?” “Si bahati mbaya na wewe! Nini usichoelewa?” “Umesikia majibu yake mwanao, baba? Hana chakutingishwa wala nini! Mikono yake ndio yote ipo yakushoto.” Kila mtu akacheka.

Akaoga na kuvaa. Akataka kutoka, akarudi. “Nisindikize baba.” “Sasa na wewe utakosa mengi. Mtu amekwambia anasafiri kesho. Leo anataka akusindikize. Na mimi unataka niwepo! Utaolewa kweli wewe!?” “Mkweo Joshi, mwenyewe sijamsikia tokea jana asubuhi.” “Ndiye anayekuoa? Au unamdanganya tu mama yako?” Naya akacheka sana. “Mama anavyompenda Joshi! Anatamani niolewe naye hata kesho! Acha nimuwahi Malo.” “Akiondoka ndio nitakuwa na wewe huko. Tuhangaike mpaka tufanikishe hilo swala la duka la nyama na vingine vyote.” “Ndio maana nakupenda baba yangu.” Naya akatoka huku akicheka kwa furaha. Akajua hivyo alivyojibiwa hapo ndio amesharudisha kuaminiwa na baba yake.

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

Kwa kuwa kuanzia maeneo ya Kibaha mpaka Kibamba kualinza kujengeka sana, Naya akaona asianzie mbali sana. Akaangalia maeneo hayo. Akapanda na basi mpaka Kibaha kabisa, akazunguka maeneo ya wazi, akitafuta sehemu zenye makusanyiko ya watu wengi huku akibania pesa ya kodi ili kuweza kununua vifaa vingine. Alizunguka Naya bila kuchoka huku amehamasika akijua pesa ipo benki. Akatoka hapo na kupanda basi mpaka mjini kabisa, akiacha hilo eneo la upande wa Kibaha.

          Ilipofika saa 6 mchana Malon akampigia. “Uko wapi?” “Nimekaa mahali naandika. Maana nimezunguka sehemu nyingi ninazopenda, kodi zake zipo juu! Sasa nikaona lazima kufikiria kitu kingine zaidi chakufanya kama nikipata hizo fremu ili ziniongezee pesa ya kulipa kodi.” “Kwa hiyo?” “Hapa nimetoka kuongea na dalali mmoja wa hapa Ilala. Ana maneno mengiiiii! Nimemuomba aniache kwanza, anipigie akifanikiwa.” Malon akacheka.

 “Ila amenipa namba ya simu ya dalali mwingine. Amesema kuna fremu kubwa, na nzuri, maeneo kabla ya Ubungo kutokea posta. Anasema ni mpya bado, na hakuna kituo cha daladala. Na bei nzuri, kwa kuwa huyo baba ndio anatafuta wateja. Sasa nimemwambia nitakwenda. Amesema mwenye hizo fremu atakuwepo hapo saa nane mchana. Ndio nimekaa hapa, nawaza. Nafikiria ni lazima hiyo sehemu iuze kitu ambacho kitavuma sana. Ambacho wenye pesa na walionazo za kati, itawalazimu hata kushuka kituo kimoja kabla au baada ya hapo ili tu kufikia hilo duka langu.” Malon akafurahi sana.

“Safi sana. Sasa na mimi nimemaliza huku. Naweza kukufuata hapo ulipo au tuzungumze tu kwa simu.” “Uliniahidi leo tutakuwa wote Malo!” “Sijabadilika. Nataka kujua tu kama naruhusiwa kuja sasa hivi? Maana hii mida ya chakula cha mchana. Mnaweza mkawa mpo sehemu mnataka kula. Sasa sitaki kuingilia.” “Nipo tu hapa nimekaa peke yangu. Njoo, haina shida.” Baada ya kumuelekeza alipo, wakaagana. Naya akaanza kumfikiria Joshi. Hakuwa amemsikia kwa simu zaidi ya neno la Mungu alilokuwa amemtumia asubuhi hiyo. Akabaki ameshikilia peni yake, akifikiria. Alipotea kabisa pale, akabaki akiwaza. Akaamua kumpigia. Ikaita kwa muda mrefu, haikupokelewa. Akaamua kuacha, akabaki ameinama anachora lile karatasi.

Akamsikia mtu anamshika bega. “Malon!” Akasimama. “Unawaza nini?” “Napanga tu mambo. Njoo ukae hapa uone.” Malon akakaa. “Kwanza niambie kama umefanikiwa mambo yako.” “Nimefanikiwa. Nina tiketi, kila kitu. Naondoka kesho. Na hii ni risiti ya benki.” Malon akamtolea na kumkabidhi. “Kumbe pesa inaingia hapo hapo! Mimi sikuwa najua.” Naya akakiangalia kile kikaratasi cha salio, akakiweka chini. “Utanipigia ukifika huko?” “Nimekuahidi kukupigia Naya. Nitafanya hivyo.” “Jitahidi pia usikawie kurudi.” “Ukiona nimekaa huko muda mrefu, ujue mambo yanakwenda vizuri.” Naya akainama, akendelea kuchora. “Lakini tutawasiliana. Utakuwa ukijua kinachoendelea. Usihofu.” Naya akatingisha kichwa kukubali.

“Umeshakula?” “Bado. Nilitaka nimalize kwanza.” “Tule wakati tunapitia ulicho andika.” Wakaita muhudumu, wakatoa oda zao. Naya akaanza kumueleza Malon. “Ningekuwa mjuzi wa kupika kitu fulani, ningepika hapo eneo la biashara, kikawa kama kivutio. Sitaki kuweka tumaini langu kwa mtu mwingine, halafu asipokuja kazini nakuwa nimekwama.” “Lakini mimi sioni sababu yakuongeza kitu kingine Naya. Wazo lako la mwanzoni ni zuri sana. Naomba tulifanyie kazi hilo. Jifunze hiyo ya nyama choma. Ukiweza kutoa kuku wazuri, watu watapitia kama chakula cha majumbani kwao. Yaani mboga ya siku hiyo. Kuwa ipo tu tayari au ukapata wateja ambao watataka tu kukutana hapo na kula hiyo nyama na juisi ile ulisema mama anatengeneza vizuri.” Malon akaendelea.

“Cha msingi, uwekwaji. Tafuta maboksi mazuri, yenye kuonyesha yule kuku aliyeiva vizuri ndani, atauzika tu. Kingine, hata utakavyowahifadhi hao wabichi, itavutia wateja. Na bei. Isiwe kubwa sana yakuogopesha wateja. Kwa kuwa na wewe unanunua kwa bei nafuu, fremu hulipii pesa nyingi, basi, usiuze kwa bei ya tamaa sana. Weka bei itakayowafanya wateja warudi. Tafuta na mashine yakusagia. Uza na nyama ya kusaga ya kuku kama ulivyosema. Nashauri fanya na ya kusaga ya ng’ombe. Hifadhi kwa size tofauti tofauti. Unaweza weka na samaki pia. Anzia hapo, tuone.” Akamuona anacheka.

“Na usisahau Naya, biashara matangazo. Tengeneza vipeperushi. Mwanzoni jitahidi kusimama vituo vya daladala, gawa. Nenda maofisini na sample, waonyeshe watu. Ukipata wateja wa maofisini, hata kama ni wa chache tu, haohao ndio unawakamata, wanakua watu wako wakukutangazia.” Wakaanza kupanga hili na lile, mara simu ya Naya ikaita. Akamuona amebadilika sura. Sio ya furaha. Ikaita akiitizama, kisha akapokea.

“Joshi!” “Mzima?” “Mzima, nilitaka kukujulia hali. Nimeona kimya tokea jana!” “Sasa kwa nini usipige?” Joshi akauliza. “Nilijua labda upo busy, maana tokea jana utume ujumbe asubuhi wa neno la Mungu, sikukusikia tena mpaka asubuhi hii ulipotuma tena ujumbe kama jana wa neno la Mungu. Ndio maana nikaona nikupigie nikusalimie.” “Kumbe ulipiga?” Naya hakutaka kujibu hilo. Alijua anamdanganya tu, ameona missed call ndio maana amepiga.

“Uko wapi?”  Akamuuliza. “Mtaani tu.” Naya akajibu bila maelezo mengi. “Unafanya nini badala ya kutafuta kazi!? Lazima ujitume Naya. Hakuna atakayekufuata nyumbani na kukupa kazi! Au huko mtaani unakozunguka sidhani kama utakutana na watu sahihi wa kukusaidia. Wewe unakuwa unajifungia huko Kiluvya sijui Kibamba nyumbani kwenu tu, kazi haziwezi kukufuata huko. Toka, na ujichanganye na watu wa maana. Zungumza na watu. Sio unasubiri kupigiwa tu. Hata kama unaomba, Mungu hawezi kutuma malaika. Musa aliulizwa una nini mkononi? Sasa wewe ulichonacho ni cheti kizuri, pesa huna, tumia hicho cheti acha kupoteza muda ukifikiria mambo yasiyo…” Malon akaona aondoke pale. Aliumia sana. Akatoka hapo na kuacha Naya anaelimishwa na mpenzi wake.

Malon alikwenda kusimama mbele kidogo. Ilikuwa sehemu ya wazi. Naya akabaki akimwangalia huku akimsikiliza Joshi. Akamuona anatoa simu yake nakuanza kupiga na yeye. Mawazo ya Naya yakatoka pale kwenye ile simu aliyokuwa akizungumza Joshi, akili zikabaki kwa Malon. Akabaki akimtizama huku Joshi bado yupo sikioni akiendelea kuongea. Akapunguza sauti ya simu yake, kisha akairudisha sikioni. Joshi akaendelea. Akatoa mifano ya bibilia na kuelezea kwa kina. Naya akaona aweke mute na kuweka ile simu pale juu meza. Malon alipomuona ameweka simu chini, akajua amemaliza. Akarudi.

Alipokaa tu, akamsikia bado Joshi anaongea. Akakunja uso kama anashangaa. Akamwangalia Naya. “Kaa tu tuendelee. Bado ana mifano kama mitatu yakunieleza ndipo amalize. Sasa sio leo. Huwa akifikia hapo, anachukua muda mrefu sana kunieleza. Tuendelee tu.” Malon akabaki ameduaa. “Malon!? Tuendelee bwana. Hasikii.” “Akikuuliza swali?” “Hata maswali yake huwa nayajua. Usiwe na wasiwasi. Akitoka hapo atamuelezea Ibrahamu. Alivyochukua hatua yakutoka kwenye mji wao na kwenda asikokujua, akifuata maelekezo ya Mungu. Ndio maana akafanikiwa. Utakuja mfano wa Naomi na mkwewe Ruthi. Ruthi alikubali ushauri wa Naomi. Akachukua hatua, akafanikiwa na ndio maana yupo kwenye bibilia mpaka leo. Atakuja Yona. Alikuwa mbishi, hakufuata maelekezo, akamezwa na samaki. Ilimbidi Mungu amfungie jela ambako ni kwenye tumbo la samaki, akamfundisha na kutii akiwa hukohuko tumboni. Nisiwe kama Yona. Sasa hapo huwa anaeleza kwa kirefu sana, sio kama hivi ninavyokwambia mimi kwa kifupi. Hatakaa akamaliza sasa hivi.” Malon akashangaa sana.

“Sasa hatumii pesa nyingi sana!?” “Cha kwanza ujue ndio muhasibu mkuu pale kwenye ile kampuni inayotoza mamilioni ya pesa kutoa huduma zao. Analipwa pesa ya simu na usafiri. Cha pili, anahesabu hiyo ni kama huduma anamtumikia Mungu.” Malon akatulia kidogo kisha akaona aulize tu. “Ni nini anataka ufanye?” “Anasema nazembea kutafuta kazi. Napenda kukaa tu nyumbani. Sitaki kuchukua hatua. Nina visingizio vingi.” Malon akashangaa sana. Naya anayemfahamu yeye sio huyo anayemfahamu Joshi. Akanyamaza, hakuuliza tena swali.

“Kwa mfano Ruthi.” Wakamsikia Joshi anaendelea. Malon akashangaa sana. “Haiwezekani Naya!” “Mimi nilikwambia. Naomba tuendelee tu Malon. Sitaki uondoke uniache katikati.” “Siwezi. Samahani kwanza Naya. Sasa huwa unafanyaje?” “Ndio namsikiliza mpaka amalize. Na hata ukiwa naye umekaa tu hivi, hakosi cha kukosoa. Unakumbuka kipindi kile nacheka sana nasema ana maneno mengi?” “Nakumbuka mpaka ulikuwa ukitokwa na machozi!” “Basi wakati ule alikuwa akiongelea mambo ya kanisani. Akikosoa taratibu fulani na nyimbo fulani za kanisani.” “Anasemaje?” “Havina maana, lakini watu huwa wanafanya bila kufikiria. Sasa mimi nikawa nacheka. Nikifikiri utani. Kumbe ni tabia yake! Ni mkosoaji sana Joshi. Hadhani kama kuna watu wanauwezo wakufikiria kama yeye.”

“Mbona ni kama anafanana na Ino!?” “Basi ndio ujue bahati niliyonayo kwa wanaume. Ndio maana nimeona nitulie tu. Nimchukulie hivyo hivyo. Mama ananiambia hakuna mkamilifu. Na ni kweli. Nitabadili mpaka lini? Ino ameoa, na ana mtoto mzuri kweli wa kike. Namapungufu yake niliyoshindwa mimi, anaye mwanamke mzuri tu, msomi, ana kazi nzuri, anaishi naye. Wana maisha mazuri tu. Huo mfano mama ananipa kila siku. Huna jinsi ukamlalamikia mama juu ya Joshi akaelewa. Anampenda, na anataka nijifunze kuishi naye. Ndio tupo na Joshi wangu. Hamna tofauti yeyote ile na Ino. Lakini tupo tunaendelea.” Malon akanyamaza.

“Tuendelee. Sasa mashine za kusagia nyama sio gharama sana?” “Nitakuangalizia Dubai na kama nitapata nafuu China, nitaagiza. Usijali. Ila nataka usipaniki Naya. Tafadhali sana. Biashara nitofauti na ajira. Unaweza usiingize pesa kwa muda mrefu tu, lakini ukivumilia, na kukazana na kumuomba Mungu, utafanikiwa tu. Sawa?” “Sawa.” “Tulia. Mawazo yako ya mwanzo ni mazuri sana. Naomba tuanze kuyafanyia hayo kwanza kazi kabla hatujaanza kuongeza. Sitaki uwe na vitu vingi kwa wakati mmoja. Utaishia kupaniki, kuchoka, na kujichanganya. Usijue lengo kubwa lilikuwa ni nini.” “Basi nitatulia kwenye nyama, mbichi na kuchoma. Juisi, maji na soda.” “Hapo sawa.” Wakazungumza mambo hayo ya biashara mpaka wakamaliza.

“Bado tuna kama nusu saa. Tusogee?” “Sawa, lakini nikuulize swali Naya?” “Juu ya nini?” Naya akamtizama. “Najua umefanya kazi kwa Ino. Umeona maendeleo yake. Mtoto, nyumba na kila kitu Mungu alichomjalia. Unajutia kumkataa.” “Hata kidogo Malon. Nilipata nafasi yakujua kama naweza kupendwa kwa dhati na kuthaminiwa mimi kama Naya. Mungu kupitia wewe ananionyesha mawazo ninayowaza, mipango ninayoifikiria, nimejua vyote vinatoka kwake Mungu na ni ya msingi hata kama wanao nizunguka wakiona ni ujinga. Nilipata kipindi cha kujifunza kuwa chochote nitakachowekea juhudi, nitafanikiwa. Namshukuru Mungu kwa hiyo miaka michache aliyonipa na wewe, kuliko ya mpaka kifo kinitenganishe na Ino. Nipo na Joshi sasa hivi nikijiambia inawezekana mimi ndio tatizo.” “Hapana Naya. Hata kidogo.” “Usikatae Malon. Kama sio kweli, niambie kwa nini mpaka sasa hivi kwa umri huu bado nahangaika kwenye swala la mahusiano? Sijabahatika kupata mwanaume wa kunihitaji kiasi chakutaka kuniweka nikawa wake maisha!”

“Ni Ino tu ndio alionyesha nia yakutaka kunioa. Napo alitangaza kwa kiburi tu. Nimekuwa ni kama njia tu. Wanaanza kwa kasi, nikishawakubali sijui wanakutana na kasoro gani, dharau inaanza. Ule uthamani wa mwanzo unaisha kabisa. Nabakia kuwa mtu wakuvumilia tu.” Malon akaumia sana, akashindwa hata chakuongeza.

“Twende Malon. Au kunamahali unataka uwahi?” “Hapana. Kwa sasa nimemaliza kila kitu, nasubiri tu safari yangu ya kesho. Tunaweza kwenda. Ulishiba lakini?” “Nimekula mpaka nimesaza. Asubuhi niliamka, nikapika chapati za maji.” Malon akacheka. “Walikula?” “Tena Bale ndio alikula mpaka nikampokonya. Mtu gani hashibi!?”  Malon akacheka sana. “Hivi wewe na Bale huwa mnakaa na kuzungumza jambo na kumaliza?” Naya akacheka huku akifikiria.

Akakumbuka. “Ulipofungwa, alinihurumia kama sio yeye! Huwezi amini Malo.” “Nini?” “Li Bale lilikuwa jema hilo! Kama sio lenyewe. Nikawa namcheka rohoni. Wakawa wanagawana kazi yeye na Kiziwanda. Walikuwa mpaka wananifulia! Nikiwa natoka siku za weekend alikuwa ananisindikiza bila hata kumuomba. Usiku tukawa tunazunguka naye. Hakunichokoza hata mara moja na hajawahi kunitania kuhusu hicho kipindi, mpaka leo.” “Kumbe anakupenda?” “Sana. Sema hatambui kama mimi dada yake wakati nimemzidi mbali tu. Anafikiri kwa sababu tunashindana urefu, ndio basi.” Malon akazidi kucheka.

“Ila kina Bale wanakupenda sana Malon! Sijawahi kuwasikia wakikukosoa hata mara moja!” “Kwani wanamkosoa Joshi?” “Sana. Wakianza kumsema, ni kama Ino. Tena afadhali Joshi wanamuheshimu kidogo kuliko Ino. Ino ndio wanamkejeli mbele yake. Huwezi kumkuta Ino anaongea na Bale hata sekunde tano zikaisha kwa amani. Bale mchokozi wakupitiliza. Anamchokoza waziwazi ili amsikie akijisifu, halafu anamkebehi.” Waliongea wakicheka mpaka kwenye hiyo fremu.

Walipanda daladala mpaka Shekilango. Wakashuka na kutembea kidogo kama wanaelekea Ubungo kituo cha mabasi. Upande unaoangaliana na kicho kituo ila nyuma kidogo. “Sio mbali sana na kituoni.” Malon aliongea baada ya kufika. Walipenda fremu na bei. Mwenye nyumba akawaambia anapokea kodi hata ya miezi mitatu mitatu japo ni mkataba wa mwaka. Hilo Malon akaafikiana nalo. Wakaandikishana na Naya pamoja na Malon. Malon akaomba mwezi mmoja wa kupatengeneza pale. Mwenye nyumba akakubali. Wakamlipa, nakuondoka.

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

“Nimefurahi Malo. Asante.” “Karibu. Sasa unataka kufanya nini?” “Kuna mama mmoja huwa analeta mafriji, majiko na vitu mbalimbali vya umeme ambavyo vilishatumika Ulaya. Nataka nikaangalie kama anayo mafriji ninayoyataka. Ndio nirudi nyumbani.” “Unanunua vilivyotumika tena! Vikikuharibikia?” “Uzuri anakuwa anatoa na warranty. Vitu vyake vizuri. Hata lile friji jingine pale nyumbani, tulinunua kwake. Na halijawahi kusumbua. Nataka nianzie na vitu vyake kwanza. Biashara ikichanganya, ndio ijinunulie vitu.” “Unataka nikusindikize?” “Ningefurahi Malo. Ila naona nimeshakuchosha sana.” Malon akacheka.

“Hujanichosha hata kidogo. Ulivyonifurahisha, natamani kuona maendeleo yake.” Kisha Malon akacheka kidogo kama aliyekumbuka kitu. “Nini?” “Umenikumbusha kuchoka. Nilichoka kipindi nimetoka jela. Nilikuwa nikitembea Naya, kama mwendawazimu. Jua kali, sina hata pesa ya kununua maji.” “Sasa kwa nini hukunitafuta Malo?” “Ulinipiga marufuku hata kufika kwenu.” Naya akajisikia vibaya. “Nakutania bwana. Wewe si unanijua mimi? Katika hilo huwa hunitishi, kwanza sijawahi kukusikiliza. Ningekuja tu.” Naya akaanza kucheka. “Kweli. Ila niliona nikuache na wewe upumzike. Ulishanihangaikia vyakutosha. Halafu bado nilikuwa na tabia zile zile. Sikutaka nije kukuumiza tena. Nikasema kukaa mbali na wewe ndio itakuwa shukurani yangu kwako. Nikuache ufurahie na Joshi.” Naya akanyamaza.

“Nikwambie kitu Naya?” Naya akamwangalia. “Katika vitu ambavyo sijawahi kutilia mashaka ni wewe. Nimeishi na wewe Naya. Huna kasoro. Unao upendo wa dhati. Kwa upande wako, hakika sijaona kosa lolote. Ila sisi wanaume tunaokuja kwako ndio tuna matatizo. Sio wewe hata kidogo.” “Kama lingekuwepo ungeniambia?” “Mimi na wewe kwani huwa tunafichana?” Naya akacheka sana akakumbuka jinsi wanavyo ambizana wote wanapokuwa na hasira.

“Ningekwambia kabisa. Kwa hiyo naomba usiishi kama wewe ndio mwenye tatizo. Naomba utuhesabu hivi, sisi ndio tumechezea bahati. Na ndivyo ninavyojihesabu mimi. Nilipata nafasi yangu ya thamani, nikaichezea. Ni mimi nimepoteza, wala sio wewe. Na hata Joshi ni hivyo hivyo, na Ino pia. Nitabia zetu tu ngumu ndio zinatufanya hivyo. Lakini wewe Naya, ni msichana wa kuwekwa ndani, ukawa mke mzuri sana. Katika kila eneo. Mimi nimeishi na wewe kama mke wangu, najua. Nilikuwa nakimbilia nyumbani nije tuwe wote. Na wewe ni shahidi. Tuliishi vizuri sana. Ila mimi tu.”

“Haya, nina uhakika kwa aina ya familia bora uliyotoka, unamifano mizuri sana ya wazazi, utakuwa mama mzuri sana tu. Naomba usikate tamaa, ukaharibu hiyo sifa. Vitu vizuri vinakuja. Naomba uvumilie. Wakati wako ukifika, uutumie vizuri. Na ninakuomba usifikiri umechelewa. Hapana. Mungu anao mpango mzuri sana juu yako. Fanya kile unachoweza kwa sasa. Jua na mimi nipo. Nakuombea. Sawa?” “Nimefurahi kusikia hivyo Malon.” “Na ndivyo ilivyo, na ni kweli.”

Malon na Naya walizunguka kila sehemu waliyojua kuna friza nzuri kwa biashara bila mafanikio. Mpaka giza likawakuta mtaani. “Naomba ukapumzike Naya. Inatosha kwa leo. Utaendelea kesho.” “Nashukuru kuwa na mimi leo.” “Karibu.” Wakabaki wakiangaliana. Naya akacheka. “Utanisindikiza kituoni?” “Wakikuiba huko njiani wakati baba yako anajua nipo na wewe!” “Kwa hiyo?” “Nakurudisha mpaka nyumbani, ndio na mimi nitakuwa na amani.” “Asante kujali Malo.” Wakaondoka na kurudi nyumbani kwa kina Naya, Kiluvya. 

“Uliniahidi kunipigia Malon. Naomba usinisahau?” “Haijawahi kutokea Naya. Wala huhitaji kunikumbusha. Na hivi umenipa kibali cha kupiga wakati wowote, wala usijali mama. Utanisikia tu.” Hilo akalifurahia Naya. Wakaendelea kutembea kutoka kituoni waliposhushwa kuelekea nyumbani kwa kina Naya. “Naomba nikuombe jambo la mwisho, kabla sijakuacha.” Naya akasimama na kumwangalia. “Tafadhali Naya, usikubali maisha yako yakaendana na matakwa ya mtu mwingine. Au ukakubali kuwa mjinga, bila sababu! Usijisahau kuwa wewe ni smart, Mungu amekujalia uwezo mkubwa sana wakufikiri. Anayeshindwa kukuelewa, inamaana Mungu hakumkusudia, au mpe muda wa kuja kukuelewa baadaye, lakini sio kubadilika kwa ajili ya mtu. Unanielewa?” Naya akatingisha kichwa huku analia.

“Hivi ni kwa nini inakuwa ngumu wakati wote kupata kitu unachotamani Malon?” Naya aliuliza huku akilia taratibu. “Wakati mwingine unajitahidi. Unafunga na kuomba, lakini hupati! Hivi umeshajiuliza ni kwa nini?” “Ngoja mimi nikwambie kitu Naya. Nimejifunza hivi majuzi tu kwenye kuhangaika kwangu. Nilifunga siku nyingi sana nikimuomba Mungu anitafutie mteja pale. Sikupata majibu kwa wakati wangu. Siku natoka Morogoro kwenye mahafali yako, nikiwa sina hata habari, ndipo nikapokea simu. Kwa hiyo wakati mwingine sio vile tunavyoomba sana ndipo tunapata hapohapo. Mungu anajua ni nini tunahitaji, na kwa wakati gani. Naomba uwe mvumilivu katika yale unayotamani. Kwa kuwa umeshamwambia Mungu, tafadhali amini kwa wakati muafaka, atakujibu tu. Sawa?” Naya akatingisha kichwa kukubali.

“Kabla sijakuacha, naomba tuombe pamoja. Nikuache ukiwa na furaha. Njoo.” Naya akasogea. Walikuwa barabarani tu. Giza lilikuwa kubwa, na nyumbani kwa kina Naya palikuwa na umbali kidogo kutokea kituoni, na miti pembeni ya barabara. Akajivuta pembeni kabisa, Naya akamfuata. Malon akamsogeza karibu yake, akamkumbatia na kuanza kuomba.

“Hata sasa, najua unatusikia na unatuona Mungu wangu na Baba yangu. Nakushukuru kwa ajili ya Naya. Natubu kwa niaba yake na yangu. Tumetenda mengi na kukukasirisha mfamle. Turehemu na ututizame kwa upya. Nashukuru kwa mawazo mazuri unayompa Naya. Nakusihi ukamfanikishe. Tenda kwa ajabu mpaka watakaoona na kusikia ulichotenda kwa Naya, masikio yao yakawashe na kustaajabu ukuu wako kwake. Tembea naye katika kipindi hiki. Anakuhitaji kwa karibu na waziwazi. Mfungulie hata ile milango iliyokuwa migumu kufunguka kwa wengine. Mpe kibali kwa watu. Nilindie Naya wangu mpaka nitakaporudi tena. Katika jina la Yesu, nimeomba na kushukuru. Ameni.” Yalikuwa maombi yaliyomfariji sana Naya. “Amen.” Naya akaitika huku akicheka.

“Naomba uniage hivyo hivyo ukiwa unacheka. Sitaki niondoke nikuache ukilia. Itanisaidia kutulia huko ninapokwenda.” Naya akambusu pale alipokuwa amefikia. “Asante Malon.” “Karibu. Sasa hivi twende nyumbani.” Wakarudi mpaka kwao. Alimkuta baba yake amekaa sebuleni. “Mbona sasa umepooza halafu upo peke yako?” “Mama yako yuko jikoni. Bale kaondoka hapa na mdogo wake kupeleka maziwa, hawajarudi mpaka sasa hivi. Amepiga simu kuwa kuna mahali anataka kupitia, atachelewa kidogo. Ndio maana nipo hapa.” “Ungemwambia unamruhusu alale huko huko, asirudi hapa hata mpaka kesho au week ijayo kabisa.” Malon akacheka. “Nani atapika?” Naya akatulia kidogo. “Umeona eeh!” “Basi heri leo asirudi. Angalau tupumzike.” Akatoa simu yake akampigia Bale. “Baba amekuruhusu ulale huko huko, leo usirudi hapa.” “Nipo hapa nakaribia nyumbani. Ndio uandike maumivu.” Naya akakata. “Linapenda nyumbani hili! Sijui likoje! Halikui tu?”  Mpaka mama yake huko jikoni akacheka. Na kweli hawakukawia kufika.

Malon alikula ndio akaaga. “Sasa mbona umepooza tena?” Malon akamuuliza kwa sauti ya chini pale walipokuwa wamekaa. “Nakuombea usafiri salama na urudi salama.” “Amina.” Malon akaitikia. “Nisindikize kidogo. Mpaka hapo nje tu.” Naya akacheka. Malon akaaga, wakamtakia safari njema, Naya akamtoa. “Wakati natengeneza hizo hereni, nilitengeneza na cheni ya mkononi. Nilikuwa nimepungukiwa pesa ndio maana sikuweza kuchukua zote kwa pamoja. Leo asubuhi nimeenda kwa sonara kummalizia pesa yake, ndio nikachukua. Hii hapa.” Akamtolea na kumkabidhi mkononi.

Naya hakuamini. “Malon! Usingehangaika! Herini zinatosha!” “Ingekuwa haijakamilika. Ni muundo mmoja. Tukipata pesa, tutatengeneza na cheni yake nzito. Sasa hivi naomba uwe na hivyo tu.” Naya alibaki akiangalia ile bracelet. “Nenda kapumzike, na mimi niwahi kulala.” “Nakushukuru sana Malon. Asante kunijali.” “Najifunza kwako Naya. Najua sijafika hata nusu yako, lakini nivumilie tu. Taratibu.” Naya akambusu shavuni. “Nitakupigia asubuhi kabla hujaondoka.” “Nitashukuru.” Wakaagana, Naya akaingia ndani, Malon akaondoka.

Akaenda kukaa pembeni ya baba yake. “Umenunuliwa na cheni nyingine tena!?” “Hiyo ni ya mkononi.” Akamkabidhi baba yake. “Sasa mbona umekosa raha?” Bale akamuuliza. “Mimi hata sijui bwana!” Bale akaenda kuichukua ile cheni kutoka kwa baba yake, mama yake akatoka jikoni. “Tuone.” Bale akamkabidhi. “Anasema alitengeneza pamoja na hereni, lakini akaishia kulipia hereni hakuwa na pesa. Ndio amepata pesa ameenda kuchukua na hiyo.” “Mmmh! Malon anakujali sana, Naya!” “Sana Bale. Najua humtaki kusikia kama niliishi naye. Lakini kipindi hicho, alikuwa hataki nipande daladala. Ilikuwa kama amebanwa na kazi Morogoro, ni heri amtume dereva au anitumie pesa ya taksii au Uber. Alinifundisha kuendesha gari ili nisipate shida ya usafiri. Ananijali kuliko nitakavyoeleza. Kabla sijalia shida, Malon ananitimizia. Halafu anaamini sana mawazo yangu.” “Nilikuona ulivyokuwa umebadilika. Nikakuuliza mwenzangu hiyo kazi inayokulipa kiasi cha kuvaa kama mwanamitindo wa nchini Marekani, niambie na mimi niende. Ukasema ooh mama, hutaweza ni ya kuvaa viatu virefu!” Naya akacheka sana.

“Malon huyo! Acheni tu. Nilifika pale chuoni Mzumbe wakati naanza mwaka wa kwanza, watu walikuwa wakiniita mwana mitindo. Walikuwa wanasubiri nitoke chumbani kwangu ili waone nimevaa nini siku hiyo. Yote hiyo ilikuwa pesa ya Malon. Akiniona nimependeza ndio ilikuwa furaha yake. Wakati mwingine tulipokuwa tunakuwa naye Dubai, atanizungusha kwenye maduka ya wanawake ili ninunue nguo na viatu. Tunarudi Tanzania nakuwa na masanduku utafikiri yabiashara! Mpaka rafiki zake walikuwa wakiniuliza nimemfanya nini Malon. Na wakati mwingine walipokuwa wakitaka kitu kigumu kwa Malon, basi wananitafuta mimi, ndio niwaombee.” Mama yake na baba yake walibaki kimya wakisikiliza.

“Ungemuona jinsi anavyohangaika leo! Mpaka nikamuhurumia. Amehakikisha nimepata fremu, na akalipia.” “Naya!” Bale akashangaa sana. “Kweli Bale. Tumetoka hapo, tukaenda kutafuta mafriza, sema hatukufanikiwa, ndio akaona usiku umeingia, akasema niendelee kesho, baba atakuwa na wasiwasi. Ananiombea. Yaani amenishika, akaniombea. Anamsihi Mungu anifanikishe na amlindie Naya wake.” Naya akajifuta machozi. Kisha akaendelea.

“Unakumbuka ile akaunti ulinisindikiza benki nikaenda kuhamisha pesa zote kwenye akaunti yangu, baba?” “Nakumbuka.” Baba yake akajibu. “Basi huko ndiko amekwenda kuweka ile hundi ya pesa aliyolipwa na mahakama. Ameniambia niitumie kuanzisha hiyo biashara huku akiniambia nisiwe na wasiwasi. Hata kama haitajibu kwa haraka, niipe muda.” “Mmmh! Mungu naye! Kwa nini hampi mtu mmoja kila kitu?” Mama yake akaongea kwa kunung’unika. Wote wakamgeukia. “Kwa nini?” Bale akauliza. “Namfikiria huyo Malon na mapenzi yake kwa Naya. Natamani hata angekuwa na shule kidogo kichwani!” Wote wakashangaa.

“Naombeni msinishangae jamani! Biashara huwa zinakufa. Lakini kama umesoma, umesoma tu. Ukikwama hapa, unakimbilia kwengine. Sasa huyu Malon akikwama biashara ndio familia yote imekwama, kwa kuwa hana mbadala!” Naya aliumia sana. Akainama. Baba yake katika hilo hakuwa akiongea, maana na yeye ni muhanga wa hayo maneno. Alishakwama kwenye biashara, wakawa wanaishi kwa mshahara wa mkewe. Na huyo mama alishamwambia hataki Naya aaishie kama yeye. Baba yake alinyamaza kimya.

“Najua Malon hajasoma mama na anamapungufu yake, lakini sidhani kama nitakuja kupata mwanaume atakayenipenda na kunijali kama Malo. Ananipenda kuliko nafsi yake.” “Naelewa kuna mapenzi, lakini hakuna mapenzi na njaa jamani! Tusidanganyane. Ndoa sio cheni za dhahabu. Itafika kipindi inatakiwa maisha yaendelee. Hapo labda wapo watoto. Wanatakiwa wale na waende shule. Pesa hamna. Mnafanyaje? Njaa huwa haichagui kwenye mapenzi. Ikipiga hodi sehemu haichagui. Mkubwa na mdogo itammaliza mpaka kuliwe. Sasa huyo Malon na umri huo bado anaanza maisha tu! Mpaka leo anahangaika hana biashara ya maana anayofanya. Yaani ndio anakwenda kutafuta huko. Akifanikiwa safari hii na kukosa hayo masoko safari nyingine si ndio biashara imekufa tena?” Kimya.

“Sasa wewe na uzuri wako wote huo utakuwa mtu wakuanza kila siku? Hapajulikani hata kipato cha mwaka kikoje! Hamjui kesho yenu inakuaje, hamuwezi hata kuweka malengo! Biashara ikifa ndio anarudi tena kuwa mzigo wako wewe!” Kila mtu kimya. Walimjua mama yao na shule. Hakuna utakalomwambia bila elimu ya darasani mkaelewana. Na hivi tayari alishakuwepo Joshi, na anajulikana yupo na Naya kwenye mahusiano, mama yake alimuona Malon ni kama mvurugaji. Naya alinyanyuka na kwenda chumbani kwake, wengine nao wakatawanyika kimya kimya wakamuacha mama yao pale sebuleni.

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

     Ikabaki kazi ya Naya na baba yake wakitafuta vifaa vyakuanza biashara, kwa bei nafuu. Siku ya tatu Naya akiwa na baba yake, Malon akampigia simu. “Vipi mama?” “Nilikuwa na wasiwasi. Ulifika salama?” Naya akaongea kwa upole. “Nilifika mama. Pole kwa kukutia wasiwasi. Si unakumbuka aina ya simu niliyonayo?” Naya akacheka kidogo. “Pole.” “Basi nilikuwa na kazi yakuhangaika kutafuta jinsi ya kukupata ili tu kukutuliza. Ila sauti yako imepoa! Mzima?” “Mzima. Ila bado nahangaikia kutafuta vifaa vya pale kwenye lile duka. Vitu gharama Malon.” “Nilikuwa nafikiria, kwa kuwa kuna mashine na mimi nataka kuagiza China, kwa nini nisikuagizie na vitu vyako? Nitamtumia yuleyule jamaa wangu wa China, atutafutie kwa bei nzuri na atutumie.” “Wewe unataka mashine ya nini?” Naya akauliza.

“Huku nimekutana na wazo jingine zuri ya jinsi yakutambua grade ya Kahawa na Cocoa. Ipo mashine nzuri tu. Lakini inahitaji pesa kubwa kidogo. Na sitaki kuua biashara, au niseme sitaki kuanzia chini tena. Kuna kitu nakifanya hapa na Brazili, nataka kuzungusha hii pesa kidogo, faida ndio niagize vitu China. Usiwe na wasiwasi tena wala usihangaike. Mimi nitashugulikia kila kitu. Ila itabidi usubiri kama mwezi au zaidi.” “Na pale kwenye ile fremu?” Naya akauliza. “Patasubiri Naya. Ni afadhali uanze vizuri, kuliko kuanza kama mbambaishaji wateja wakakukimbia tokea mwanzo.” “Kweli.” Wakaafikiana.

“Unapata muda wa kula?” Naya akauliza. “Nahangaika mama. Nikipata kifungua kinywa asubuhi, situlii mpaka usiku. Labda hapo baadaye patatulia na nitakuwa na ratiba yakueleweka.” “Pole Malo. Nakuombea ufanikiwe.” “Amina mama. Hilo ndilo la msingi. Tutafanikiwa tu. Mungu yupo upande wetu. Naomba na wewe uamini na ujaribu kutulia. Tafuta kitu chakufanya ukiwa umetulia sio kwa kupaniki. Na hata ukikosa, jua upo mapumzikoni, kitu kizuri kinakuja.” Naya akaridhika.

“Unapaonaje huko?” “Nimeanza kupapenda. Mpaka nashawishika kuhamia huku.” “Malo!” Naya akashangaa. “Kwa baraka zako mama. Sitakimbia.” Naya akacheka kidogo. “Urudi.” “Hata kama nikuhamia, sio kwa sasa. Bado nyumbani kuna malighafi nyingi zinazoweza kuuzika kwingi. Kuna ugumu kidogo tu napambana nao. Nipo kwenye kumsihi Mungu, naamini atatufungulia milango.” “Ni pesa?” “Na hilo pia. Tunahitaji mtaji mkubwa.” “Sasa kwa nini usichukue na hizi? Biashara ya nyama inaweza kusubiri.” Malo akatulia kidogo.

“Ongeza mtaji Malo. Mimi nitasubiri. Ukifanikiwa, ndipo na mimi nitafanya. Sio lazima tukawekeza wote kwa pamoja.” “Lakini pia sio vibaya tukatupia shilingi kila mahali. Huwezi jua wapi patajibu. Anyway, kwa kuwa nimefika tu, acha nione Mungu ataniongoza vipi. Si ulisema unaniombea?” “Nakuombea Malo.” “Basi usiache. Niombee Mungu anipe muongozo mzuri, awe na mimi huku na anifungulie ule mlango nitakao fanikiwa.” “Na urudi nyumbani salama.” Malon akacheka. “Na hilo pia.” Wakazungumza, na kukata simu.

 

Joshi!

J

uma hilo likaisha, Naya akiwa ametulia sasa, akijua Malon ataleta vifaa. Joshi kimya kama kawaida yake. Kumtafuta Naya sio kipaumbele. Na yeye Naya akaacha kumpigia. Jumamosi hiyo akaona ujumbe wake na neno la Mungu. Hakusoma wala hakujisumbua. Akaangalia tu na kuweka simu pembeni. Ilipofika usiku wake, akapiga. Ikaita mara ya kwanza mpaka ikakata. Wote wanamwangalia. Ikaita tena, hakupokea. “Nani huyo ambaye simu zake hazipokelewi?” Mama yake akauliza akihisi ni Joshi tu. Naya akazima simu kabisa na kuondoka pale.

Kesho yake wakati wapo kanisani wakamuona Joshi naye anaingia na gari yake. Walikuwa wamesimama tu nje, ndio na wao wamefika. Naya alipomuona, akajisogeza karibu na baba yake, akatulia. Kila mtu akamuona. Baba yake akamgeukia kule alikojificha nyuma yake kisha akamgeukia Joshi aliyekuwa akiwasogelea. “Nakuona mzee umeingia na kifaa!” Bale akamchokoza. “Kitu kisafiii, kama kimetoka kiwandani!” Bale akaendelea, Joshi akacheka. Akasalimia kila mtu. “Vipi Naya?” “Safi tu.” Naya akajibu akiwa amesimama palepale pembeni ya baba yake kama anayemchungulia kidogo. “Nimejaribu kweli kukupigia simu jana na leo asubuhi.” “Simu nimeiacha nyumbani.” Naya akajibu kwa ufupi tu. Wakatulia ila jibu likapatikana kuwa aliyekuwa hapokelewi simu zake ni Joshi.

“Kwema baba?”  Akaanza mama Naya. “Kwema tu. Nimekuja kuwatembelea, lakini zaidi kumuona Naya.” Naya akakunja uso huku ameinama. Akajivuta taratibu zaidi kwa baba yake. “Karibu sana. Tumefurahi kukuona.” “Asante mama. Alhamisi kuna sherehe kazini, nilitaka Naya aungane na mimi.” Naya kimya. “Afadhali umtoe kidogo. Amekuwa tu ndani na baba yake.” Wote wakamwangalia mama yao ambaye ndio alikuwa akijibu. Na wala hakuishia hapo. Yeye ndio akaendeleza mazungumzo na Joshi mpaka kuingia ndani ibadani. Wakatoka bado mama Naya akawa anamsemesha Joshi kwa uchangamfu sana, kisha wakaagana.

 ~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

Baada ya mama kuweka ubabe na kulazimisha lazima Naya aende huko anakotaka Joshi, ikabidi Naya kumpigia simu na kumwambia Joshi kuwa itabidi amfuate hapo nyumbani. Kwa kurudi kwa Malon, japo hakumwambia anataka kumuoa, ila kila kitu kusema ‘changu, chetu, Mungu atatufanikisha’, kuliibua kutokubabaishwa ndani ya Naya. Hakumtetemekea tena Joshi na alikwenda kwa sababu mama yake alishikia bango hiyo safari kana kwamba ndio siku ya harusi. Hakuna lililozungumzwa kwa amani humo ndani isipokuwa Naya kwenda kwenye hiyo shuguli na Joshi. Akilala na kuamka ni Naya atoke na Joshi.

“Wewe ndiye unayeharibu akili za Naya, baba Naya.” Kibao kilimgeukia na baba yake. “Unamtia moyo kwenye vitu visivyo na maana. Kutwa yupo mgongoni kwako. Huyo Malon akimuoa na kumzalisha, akashindwa kuwatunza, utambeba huyo Naya na watoto wake? Mwanaume mpaka sasa hana linaloeleweka maishani! Anahangaika na maisha mpaka leo! Akifanikiwa ndipo anaonekana. Anafanya maonyesho yake hapo weeee! Akifilisika anapotea. Mungu ametuma rehema, huyu Naya apumzike, bado unatetea upuuzi wa kijana ambaye hana hata maadili! Hajui hata kutulia ni nini!” “Malo ameokoka mama.” Bale akaingilia.

“Ameokoka ndio, wala sikatai. Lakini hana wala hajui maadili. Mpaka aje aanze kujifunza maisha na kuelewa kutulia ni nini, au kijana anatakiwa aweje kwenye jamii, huyo sio wa leo. Kwanza kama atatulia sehemu moja. Maana kukua inatakiwa utulie na ukuzwe. Mara yupo Mbeya vijijini, mara Dubai kwa Waarabu. Hajulikani leo yupo wapi na amelala wapi na nani! Hakuna atakayejua kama bado anamsimamo wa wakovu au alisharudia njia zake chafu! Imani ni ya kujengwa jamani. Sasa unafikiri utamfananisha na vijana kama kina Joshi? Alishakataa kuwa chini ya malezi ya wazazi, hajui kijana anatakiwa awe vipi, anabaki akihangaika tu. Hilo alitakiwa baba yenu alione, na kuzungumza na Naya, lakini…” “Mama! Mama!” Naya akamwita. “Nishampigia simu Joshi, tutatoka hiyo siku ya alhamisi.” “Hiyo ndio akili. Utakuwa mtu wa kuhangaika mpaka lini wewe! Unataka maisha yako yawe kama yangu yalivyoharibika! Hata uki…” “Naomba yaishe mama. Naya ameshakubali kutoka. Naomba yaishe.” Bale akaingilia. Baba yao akatoka bila hata jibu,  Naya naye akafuata nyuma. Akamfuata baba yake. 

 Joshi & Naya.

Naya alikwenda Salon siku hiyo ya alhamisi. Akatengenezwa vizuri. Akavaa vizuri na kupendeza. Akavaa cheni, hereni na bracelet au cheni ya mkononi. Akajiangalia nakuweka vipodozi kadhaa usoni, akajipenda. Akasikia gari nje, akajua ni Joshi ameshafika. Mama yake akawa yeye wa kwanza kumfungulia mlango. Akasikia akisalimia, akatoka. Kila mtu alimshangaa jinsi alivyopendeza. “Umependeza mama.” Baba yake akamsifia. “Asante.” Naya akacheka. Hakuna aliyemsikia Joshi akisifia, ila kumtaka Naya waondoke ili wawahi foleni.

Wakiwa njiani ikabidi Naya aulize kwani aliona vile Joshi alivyojawa wasiwasi usoni kama amechelewa au kuna jambo. Honi za kila mara hazikuisha humo barabarani. “Kwani inafanyikia wapi?” “Ni ofisini kwetu tu ndio maana nashangaa jinsi ulivyovaa na kujitengeneza kama tunakwenda kwenye kumbi kubwa sanaa!” Naya akaumia sana. “Sasa kwa nini hukuniambia nibadilishe pale uliponifuata nyumbani?” “Hivi unajua kama kuna swala la muda hapa duniani? Watu wanakwenda kwa mipango na muda. Huwa hatupeleki mambo kiholela holela.” Naya akanyamaza akiwa amekosa raha. Ikabidi atulie huku akitamani avue hiki au atoe kile.

Wakafika ofisini kwao. Akajifungulia mlango na kutoka haraka akimfuata Joshi nyuma. Akafunga gari yake kwa rimoti bila hata kugeuka nyuma. Naya akaendelea kumfuata kama anayemkimbilia akiwa na wasiwasi. Anajishuku kwa kujishika hiki na kile huku akiongeza mwendo asije kuachwa. Ni kweli Naya alikuwa binti mzuri, jasiri, anajiamini. Lakini si mbele ya Joshi. Kuna jinsi Joshi alikuwa akimfanya ajione si kitu tofauti na Malon. Joshi aliweza kumshusha kwa sekunde, na kujiona sifuri. Ila Malon alikuwa akiweza kumwinua na kujiona ni kila kitu.

Wakaingia kwenye huo ukumbi mdogo tu, Joshi akiwa ametangulia mbele, Naya nyuma. Akatafuta meza wakakaa. Kimya kimya Joshi akiwa kama amekasirika hivi au ameboreka. Naya akatulia. Akawasogelea Mati. “Mbona mpo kama mpo msibani? Simama kwanza Naya mdogo wangu. Naona unavutia kwa mbali.” Naya akatabasamu na kusimama. “Shikamoo.” “Marahaba, Naya. Umependeza sana. Tena Sana. Twende nikakutambulishe kwa mke wangu. Nilishampa habari ya viumbe wachache kama wewe, mliobaki hapa duniani.” Naya akacheka, Mati akanyoosha mkono amshike.

“Vipi Joshi! Upo kwenye maombi nini? Mbona sura hiyo mkuu!?” Mati akamtania. Joshi alikuwa kijana wakuheshimika sana pale ofisini. Alijulikana ni kijana mwenye maadili na mcha Mungu. Mnyenyekevu na mwadilifu. Mati akapokea mkono wa Naya, akashtuka kidogo. “Nini?” Naya akauliza kwa kushangaa. “Hii bracelet niliiona kwenye wallet ya mtu!”  Mati akaongea kama anayefikiria. Naya akajishika shingoni kwa wasiwasi. Mati akahamia shingoni kwa Naya akiwa ameduaa.

“Uliona kwenye wallet ya nani?” Akauliza Naya taratibu. “Mmmh!” Mati akaguna na kuhamia masikioni. “Hii si ni set nzima?” Akauliza Mati, kisha akacheka kidogo. “Nimeshajua vilipotoka.” Akajijibu Mati mwenyewe, na kumvuta mkono Naya. “Naamini kasisi hutajali?”  Akimaanisha Joshi. Walikuwa wakimwita Kasisi hapo ofisini kwao. “Bila shaka.” Joshi akajibu kwa heshima, Naya na Mati wakaondoka.

Alipofika kwa mkewe, akamvutia kiti Naya. “Huyu ndiye Naya.” Mkewe aliyekuwa akinywa kinywaji fulani kwenye glasi akageuka. “Ulivyomchanganya mume wangu! Haishi kukutaja. Hujambo Naya?” Naya akacheka. “Sijambo, shikamoo.” “Marahaba mama. Hongera kwa kumaliza chuo na kuwa mtoto mzuri. Mati anakusifia sana, au umebadilika?” Naya akacheka na kutingisha kichwa huku akikataa. “Sasa nasikia umemuacha Malon, upo na Joshi. Unampenda lakini au?” Mke wa Mati aliendelea kumuuliza taratibu tu huku akinywa. Alionekana ni dada anayejitambua. Mtu mzima kidogo, mrembo tu japo alikuwa na mwili kumpita mumewe. Kwa harufu ile, Naya akajua anakunywa kinywaji kikali.

Mati akabaki akimtizama. “Lakini umebadilika Naya! Umekua mtulivu kuliko ninavyokufahamu. Naya ninayemjua mimi ni machachari. Vipi bwana?” Naya akamtizama Mati na kucheka. “Au Joshi anakupitisha kwenye maombi mengi?” Mati aliendelea kumtania, mpaka mkewe akacheka. “Ila Umependeza na unaonekana ni binti mzuri. Nimefurahi kukufahamu Naya. Ukaribie nyumbani.” “Asante.” Naya akamjibu mkewe huku akimtizama Mati na kucheka. “Twende tukacheze mziki halafu tutete kidogo kabla hujarudi kwa Joshi.” Akamshika mkono. “Narudi mama. Ngoja nikacheze na Naya.” Mati akamuaga mkewe, na kuondoka.

Akamshika vizuri Naya kwa heshima tu, wakaanza kucheza mziki wa taratibu. “Malon yupo wapi?” Mati akauliza swali la moja kwa moja. Naya akacheka kidogo na kuinama. “Najua hivyo vitu vinatoka kwa Malon.” Mati akaendelea. “Amesafiri kwenda Dubai.” “Kwema?” Mati akaendelea kudadisi. “Kwema. Ni mambo yake ya kibiashara tu.” “Kumbe alifanikiwa?” “Kwenye nini!?” “Hakuniaga kama anaondoka, lakini mimi ndio namsaidia kwenye mambo yake ya biashara. Sio kiofisi, lakini huwa akikwama au akitaka ushauri wa kisheria kwenye mambo ya biashara, huwa ananipigia. Hata mkataba wa ile nyumba yake ni mimi nilimsaidia. Ila sikujua kama bado mpo pamoja! Nilipomkuta na hii bracelet peke yake, alikuwa akitoka kwa sonara. Akasema alitoa cheni, lakini haikuwa imekamilika. Hakuwa na pesa. Ndio amemalizia bracelet. Siku nyingine akiwa anashugulikia kibali chake cha kusafirisha mzigo kuutoa hapa nchini, aliniomba tukutane nje ya sonara moja kule posta. Nikamuuliza pale anafanya nini, akanikumbusha ile bracelet, akasema ilikuwa pia haijakamilika kwa kuwa haikuwa na hereni zake. Ndio alikwenda kupunguza pesa hapo kwa sonara. Nikajua amepata mwanamke mwingine. Sikukufikiria kama ni wewe, kwa kuwa wewe najua upo na Joshi!” Naya akashindwa hata ajibu nini.

Mati akamuona kama anafikiria na kukunja uso. “Naya?” “Abee!” Naya akamwangalia. Lakini safari hii hata macho yalikuwa yameshajaa machozi. “Upo na Joshi au Malon?” “Hizi ni zawadi tu kaka Mati. Nipo na Joshi. Hata Malon anajua.” Naya akajibu kwa unyonge. Mati akabaki akimtizama machoni huku wakicheza. “Ni zawadi tu kaka yangu.” Naya akasisitiza. “Siku ya mahafali alikuja mpaka kule Mzumbe, akaniletea hii cheni. Lakini sikuwa najua kama havijakamilika. Kwa kuwa alinikabidhi na kuondoka. Baada ya siku chache, kama majuma mawili hivi, ndipo akaniletea na hii ya mkononi. Siku kumi kabla hajaondoka kwenda Dubai akaleta na hereni zake. Akaniambia sasa ndio imekamilika.” “Joshi anajua?” Mati akadadisi. “Joshi yupo busy sana na kazi zake. Hana muda wa mambo kama haya.” Hilo jibu likatosha kabisa kumfanya Mati aelewe kila kitu. Walicheza mpaka mziki ulipoisha, akamrudisha Naya kwa Joshi.

“Kasisi! Nimekurudishia mrembo wako. Naona jamaa wanameza mate, wasije kumpora mikononi mwangu bure. Sitaki kesi.” Mati aliongea huku akimvutia kiti Naya. Akakaa. “Asante.” “Karibu.” Mati akajibu na kuondoka pale. Kimya. Baada ya muda Mati akarudi tena na kinywaji cha Naya, maana alikuwa amekaa tu hana hata kinywaji. “Asante.” Akashukuru Naya, na tabasamu usoni. Alipoanza tu kunywa, Joshi akamgeukia. “Nataka kuwahi kulala. Naomba umalizie kicho kinywaji sijui pombe, nikurudishe nyumbani, ili nikalale.” Naya akashangaa sana. Hata hawakula wakati harufu ya chakula ilikuwa imeshaenea mle ndani. “Hii ni juisi Joshi! Na hakuna ulazima wa kuimaliza. Tunaweza tu kuondoka.” Naya akajibu kwa upole. Joshi akavuta kiti, akasimama na kutoka pale ukumbini. Ikabidi Naya afuate nyuma tena.

Akamkuta amesimama pembeni ya gari lake kama anayemsubiria. Naya akamsogelea. “Unaumwa?” Naya akauliza tu kwa upendo. “Hivyo vitu umevipata wapi?” “Vitu gani.” “Si hivi!”  Akamvuta mkono kwa nguvu. “Unaniumiza mkono Joshi! Kuna nini!?” Naya akashangaa. “Nakuuliza umepata wapi haya maurembo?” “Amenipa Malon.” Naya akajibu huku anavuta mkono wake ambao Joshi alikuwa ameushikilia kwa nguvu. “Kwa hiyo unahongwa na Malon?” “Unaniumiza Joshi! Tafadhali naomba niachie mkono wangu?” “Nakuuliza unahongwa?” Naya akauvuta mkono wake kwa nguvu nakuanza kulia. “Hii ni zawadi alinipa kwa sababu ya kuhitimu chuo. Hata wazazi wanajua.” Joshi akazunguka upande wa dereva akapanda kwa hasira. Kitu kilimkaba Naya, akashindwa hata kusogea.

Joshi akawasha gari na kumpigia honi wakati yupo palepale akimtizama. Alipoona Naya hazunguki upande wa abiria, amebaki akijiangalia mkono wake aliokuwa amemuumiza, akashusha kioo. “Panda wewe. Unashangaa nini? Kaa hata nyuma kama unashindwa kutembea sababu ya maviatu hayo marefu uliyovaa bila sababu.” Naya hakumjibu. Moyo wake ulikuwa umeumia sana. Akaamua aondoke. “Unakwenda wapi sasa? Ingia mlango huu.” Naya hakujibu. Akainama, akavua viatu vya juu alivyokuwa amevaa, akaondoka pale bila hata ya kugeuka nyuma, akielekea posta mpya kufuata daladala. Joshi naye hakutaka kubembeleza, Naya akamuona anatoa gari yake na kuondoka bila hata kujua ananauli au anarudije nyumbani kwao Kiluvya.

Naya alifika posta, akasubiria hapo daladala. Kwa kuwa ilikuwa siku ya kazi kwa mida ile bado akapata daladala. Akaunganisha daladala mbili mpaka kufika kwao ilikuwa saa 3 usiku. “Joshi yuko wapi!?” Baba yake akauliza wakati anamfungulia mlango. Naya alikuwa akilia kabla hajafika hapo. Baba yake akajua. “Kwa nini umerudi peke yako?” Kimya. Akarusha viatu na kuelekea jikoni. “Wewe unatoka kwenye sherehe, unakuja kula nyumbani!” Bale akamuuliza kama kumsanifu. “Joshi aliniambia anataka kuwahi kuondoka ili awahi kulala. Hatukula.” Ukimya ukazuka. Naya alijibu huku akifunua masufuria ya huko jikoni. Wote bado walikuwa sebuleni, Bale mchokozi alikuwa kwenye meza ya chakula, akifanya mambo yake ya shule kwenye komputa.

“Sasa kama ana usingizi wa kipuuzi hivyo kwa nini alikuja kukufuata? Kwanza kwa nini hakukurudisha?” Bale akahoji kwa hasira kidogo. Raha ya Bale ni yeye ndio amlize Naya, lakini sio vinginevyo. Na tokea wadogo wakiwa wanacheza. Usimguse dada yake huko nje. Ila wakiwa ndani, yeye ndio mchokozi, na hatulii mpaka amuone analia ndio furaha yake. Naya akanyamaza. Akachukua chakula, na kwenda kukaa pale pale mezani. Kimya. “We Naya?” Bale akamuuliza tena. “Nilimuacha  nje sehemu ya kuegesha magari.” “Kwa nini?” Naya akasimulia mwanzo mpaka mwisho. “Anahaki yakuchukia.” Mama yake akadakia na kushangaza kila mtu. Mpaka Bale akabaki ametoa macho.

“Unasema kweli mama!?” Bale akauliza kwa mshangao mkubwa sana. “Ndiyo. Sasa kwa nini apokee hongo kwa mwanaume mwingine?” “Hongo au zawadi hii ya kumaliza chuo? Yeye alikuja kwenye mahafali ya Naya hata kadi ya pongezi hakumletea Naya!” “Si alisema ametoka kazini?” Mama yake akazidi kutetea. “Kwani hizi zawadi zakutoka kwa Malon alizileta lini? Au swala la kuwa Naya anahitimu Mzumbe yeye alikuwa hajui? Zawadi inaandaliwa mama. Na kwa sababu yeyote ile, asingemuacha Naya usiku huu anarudi nyumbani peke yake! Sasa hivi Malon hana usafiri, lakini anamrudisha Naya nyumbani kwa daladala! Anahakikisha Naya yupo ndani ndio anaondoka. Ni nini unatetea mama!?” Bale akauliza kwa hasira. “Kwani wewe hujamsikia jinsi Naya mwenyewe alivyosimulia? Anasema aliondoka pale. Sasa mlitaka yeye Joshi afanye nini?” Mama yao akazidi kutetea. Bale akasimama pale kwa hasira na kuingia chumbani kwao. Hakutaka kuongea tena. 

Siku ya Ijumaa, Mati kwa Joshi.

M

ati akachungulia ofisini kwa Joshi, alipomuona yupo akamsalimia na kuingia. “Vipi Kasisi?”  Joshi akanyanyua kichwa. “Karibu Mkuu.” “Upo busy sana?” “Karibu tu.” Mati akaingia ndani kabisa na kufunga mlango. “Jana mbona mliwahi kuondoka, kwema?” “Nilikuwa sijisikii vizuri nikaona nikapumzike.” Mati akabaki akimwangalia kama bado hajapata ukweli, Joshi akababaika na kuongeza. “Hata hivyo niliona muda umekwenda sana. Halafu nikaona mambo yanavutwaa.” “Saa mbili!” Mati akashangaa kidogo. “Sijui lakini, ila nahisi uliharakisha Joshi. Yule binti alikuwa amejiandaa kwa shuguli. Kumwingiza kwenye shuguli na kumtoa bila hata chakula, sidhani kama ilikuwa uungwana!” Joshi akanyamaza.

“Mimi ni mkubwa kwako, Joshi. Na ninaheshimu kumfahamu Naya kupitia wewe. Ila unanijua jinsi ninavyoweza kumsoma mtu kwa haraka. Mtu akishazungumza na mimi maneno machache tu, najua mengi hata ambayo bado hajazungumza. Nakumbuka kukupongeza mwanzoni kabisa mlipoanza na Naya. Simfahamu kwa undani, lakini kwa kile ninachokijua kwa yule binti, na mapito aliyopita na Malon, ni binti wa kumuenzi sana.” Mati akavuta kiti akakaa mbele ya Joshi.

“Nazungumza na wewe kama nilivyozungumza na Malon. Mwanaume atakayefanikiwa kumuweka ndani Naya, atanufaika kwa mengi.” “Labda muonekano tu.” Akaropoka Joshi. Mati akatulia kidogo. “Namaanisha maisha yanataka zaidi ya muonekano.” Akasisitiza Joshi. “Mimi sijui huwa unazungumza nini na Naya, lakini nafikiri upo na Naya wa tofauti na ninayemfahamu mimi na Malon. Nilikaa zaidi ya lisaa, nikimsikiliza Malon akimzungumzia Naya. Lakini siye Naya niliyekuona naye jana.” Mati akacheka kidogo.

“Naya aliyemzungumzia Malon, Naya niliyemfahamu mimi, ni binti anayeweza kukusanya mamilioni ya pesa, kwa muda mfupi sana. Tena kwa nchi hii hii ambayo mimi na wewe tunasikia watu wakisema na kulalamika uchumi ni mgumu. Naya huyu unayesema ni muonekano tu, siye huyu aliyekuletea mamilioni ya pesa kumtoa Malon jela?” Mati akamuuliza na kuendelea. “Mbali na hizo pesa, Naya alinipa pesa zingine zakuharakisha Malon atolewe jela. Akihangaika kwa jasho lake. Malon anakiri kwangu hajawahi kukutana na binti mwenye akili na uelewa mkubwa wa mambo kama Naya. Anasema anaweza kugeuza kitambaa cha pesa ndogo sana, kikawa kitu cha thamani kubwa sana watu wenye pesa na akili zao, wakanunua kwa kugombania. Anauwezo wa kugeuza kandambili au sendozi ya mmasai, ikawa kitu cha thamani akauza kwa pesa nyingi. Malon anasema akiongea Naya, huwa anaandika au anatekeleza kwa haraka. Na anasema hajawahi kutofanikiwa kwenye mawazo ya Naya.” Joshi kimya.

“Kuna kasumba. Na wengi tunaanguka hapo.” “Kasumba gani?” Joshi akauliza. “Ni wachache sana. Tena narudia ni wanaume wachache haswa, ni kama Malon ndio namuona baada ya miaka mingi sana kuona mwanaume anakuwa na kitu cha thamani mkononi, na kutambua kama ameshika kitu cha thamani na kukienzi. Na wakati mwingine, ni ngumu kuishi na wanawake hawa wenye uelewa mkubwa sana. Ni ngumu. Kwa hiyo badala ya kuwaenzi, upo udhaifu wa kuwadidimiza.” Mati akasimama na kutoka akiwa ameshamchukia sana Joshi.

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

Joshi akabaki pale akifikiria. Akaamua kumpigia simu Naya. Akagundua ni kama haiendi kabisa. Akajua amemblock. Akampigia na simu ya pale ofisini kwao. Ikawa hivyo hivyo. Akajua kwa hakika amemfungia kabisa kila aina ya namba aliyojua Joshi anaweza kumtafuta nayo. Jioni alipotoka kazini akaamua kwenda nyumbani kwao.

Sababu ya foleni, akafika nyumbani kwa kina Naya usiku wa saa mbili. Akakaribshwa vizuri sana na mama Naya. Bale, Zayoni walikuwa mezani, Naya na baba yake wanaangalia mpira, Naya akishangilia kama kocha wa hiyo timu. Ila kwa sauti zaidi ili kumkera Bale ambaye walikuwa upande mmoja. Nyumba nzima waliipenda hiyo timu. Ila ushangiliaji wa Naya ndio uliokuwa ukimkera Bale. “Acha kelele Naya! Ni nini bwana?” Alipoingia Joshi, kila mtu kimya. Mbali na kuitikia salamu, baba yake Naya hakutaka hata kuongeza neno.

Mazungumzo yakawa ya mama Naya na Joshi. Pongezi za hapa na pale zikasikika. “Kesho kuna tafrija nyumbani kwa dada. Mdogo wangu yule aliyemaliza na Naya chuoni analipiwa mahari. Wazazi na ndugu mbalimbali watakuwepo pia. Nilitaka na Naya awepo ili kumtambulisha kwa ndugu. Bahati kama hizo za ndugu kukusanyika pamoja huwa hazitokei mara nyingi.” “Ni kweli baba. Mambo kama hayo huwa ndiyo yanakutanisha watu.” Akajibu mama Naya. Wengine wote kimya. “Basi nitakuja kumchukua kwenye saa nne asubuhi, ili apate muda na familia. Wafahamiane kabla ya shuguli ya jioni.” “Wazo zuri kabisa.” Akajibu mama Naya.

“Mnafanyia wapi?” Akadakia Bale. “Nyumbani kwa dada.” “Hilo nimelisikia. Nataka kujua eneo kabisa ili tujue pakumfuata usiku, utakaposhindwa kumrudisha hapa nyumbani.” Ukimya mzito ukatanda. Joshi akajikaza kiume na kujibu. “Jana ni Naya mwenyewe aliondoka.” “Na wewe ukamuacha mtoto wa kike anarudi nyumbani peke yake! Wangemkamata huko usiku na kumtenda vibaya?” Bale akaendelea kumuhoji. Kimya. “Halafu ulivyo wa tofauti, hata usipige simu kujua kama alifika nyumbani salama au la. Unarudi tena leo kumtaka tena!” “Ilitokea kutoelewana tu.” Joshi akajitetea. “Ndio na mimi nakuuliza ni wapi mnakofanyia hiyo shuguli ili ikitokea kutoelewana tena, tuje tumfuate wenyewe?” “Siwezi kurudia kosa. Hata mimi nimejifunza. Naomba radhi kwa Naya, na kwenu. Ikitokea kutoelewana tena, na Naya akaondoka kama jana, nitamfuata. Hata ikibidi kupanda naye daladala mpaka nimfikishe hapa, nitafanya hivyo ndipo nirudi nikafuate gari yangu.” Hapo akawa amewafunga mdomo. Baba Naya kimya.

Wakati anatoka, akamuomba Naya amsindikize. Naya akatoka naye. Alijishusha mpaka Naya akashangaa. Akaomba msamaha, akajinyenyekeza mpaka Naya hakuamini kama ni Joshi. Akaongea maneno ya upendo na yakiuungwana, mpaka Naya akaona asamehe tu yaishe. “Kwa hiyo nitakuona kesho?” Akauliza Joshi na tabasamu baada ya kusamehewa. “Ulisema saa nne?” “Ndiyo.” “Utanikuta nipo tayari.” Wakaagana, Joshi akaondoka.

 

Naya ukweni, Malon naye arudi nchini.

Apambana na mama Naya, nakumfukuza vibaya sana. 

I

lipotimu kama saa 4 na robo asubuhi, Joshi akawa anaegesha gari nyumbani kwa kina Naya. Akaingia ndani, akamkuta mama yake Naya. Wakazungumza kidogo, Naya akatoka. Baada ya kusalimiana, wakatoka. Baba yake Naya alitoka na kina Bale. Bale alikuwa akishushwa Ubungo, akielekea chuoni Mlimani. Nyumbani alibaki mama Naya tu.

Wakati anafua nje, Malon naye akaingia akitembea tu. Akamsogelea mama Naya. Alijua wazi yule mama hampendi, na alitamani awe anamkuta Naya au angalau baba yake. Akamsogelea kwa tahadhari kidogo. Akamsalimia. “Karibu.” “Asante mama.” “Umerudi lini?” “Nimeingia na ndege ya leo asubuhi, nilikwenda nyumbani kubadilisha tu, nikaja hapa.” “Na hapa napo nipo mimi tu. Naya amekuja kuchukuliwa na mchumba wake, anakwenda kutambulishwa kwa wakwe zake.” Moyo wa Malon ukaumia sana.

“Na sidhani kama watarudi mapema. Maana jana walikuwa wakizungumza hapa kuwa asubuhi hii utakuwa muda wa familia tu. Kuwa pamoja na kufahamiana zaidi. Jioni kuna shuguli. Mdogo wake Joshi analipiwa mahari leo. Ndio wakwe nao wanataka kumuona Naya.” Malon kimya akisikiliza. “Naona Joshi amekazana kweli!” Akaongeza mama Naya na kucheka kidogo. “Anaonekana ni kijana aliyetulia. Mwenye maadili, msomi, anampenda Mungu na Naya. Juzi pia alikuja kumchukua hapa na kwenda naye kwenye pati yao yakiofisi. Naya amejawa furaha na ana amani.” Malon kimya. Wakatulia kidogo.

“Basi nitarudi wakati mwingine.” “Hapana Malon. Huko nikumchanganya Naya. Labda niulize tu, nia yako ni nini kwa Naya kama si kumchanganya tu? Eti Malon?” Yule mama akambadilikia. “Umekuwa mtu wakutoka na kurudi bila taarifa wala kuaga. Umeharibu maisha ya Naya. Sasa hivi unarudi na miradi ambayo haina kichwa wala miguu. Unataka nini kitokee kwa Naya? Kwa nini unataka kumvuruga? Cheni na hereni havijawahi kujenga maisha ya unyumba. Unakuwa mtu wakurudi na kumvuruga, halafu unapotea. Wewe mwenyewe hujajiweka sawa. Si kimaisha tu, hata na Mungu wako! Hujulikani utalishwa na kukua kiroho Mbeya au Dar! Tanzania au Dubai! Hujatulia sehemu moja! Halafu eti leo unataka kumchanganya na Naya kwenye kuchanganyikiwa kwako!” Malon kimya kama amepigwa na kibumbuwazi.

“Hebu kuwa mtu mwenye utu wewe kijana. Au kwa kuwa hujawahi kulelewa unakuwa kama upepo tu!? Hapana, sitakuruhusu uendelee kuharibu maisha ya Naya. Kama unazo pesa, tafadhali nenda ukajijenge wewe kwanza. Tulia kanisani angalau ukue kiroho. Kwa umri huo umechelewa kujengwa na wazazi, lakini sidhani kama na Mungu naye atakushindwa. Tulia sehemu moja. Kubali kulelewa kwenye kanisa moja. Chini ya mchungaji mmoja, pengine utasaidika.” “Nimeelewa mama.” Malon akageuza hapo hapo nje, nakuondoka.

 ~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~ 

Ilipofika jioni, watu wakaanza kurudi hapo nyumbani. Kwenye mida ya saa mbili Naya naye akarudishwa akiwa amepooza sana. Joshi akaingia naye ndani. Akasalimia. Mama Naya akamkaribisha chakula, akasema ndio wametoka kula tu. Hakukaa sana, akasema anawahi kanisani kuandaa ibada ya kesho yake, kanisani kwao. Akaondoka baada yakusifiwa sana na mama Naya. Baba yake akamtizama Naya, akajua mambo hayakwenda vizuri. Hakuna aliyeuliza. Kimya.

Wiki hiyo ikaisha kimya. Naya hakumsikia Malon. Kwanza hakujua hata kama amerudi nchini. Akaanza kukosa raha. Kila wakati macho kwenye simu. Hapakuwa na ujumbe wala simu. Jumapili waliondoka hapo kwenda kanisani akiwa amepooza, akashindwa hata kunywa chai. Waliwahi kidogo kufika kanisani. Wakawa wamesimama tu nje ya gari yao wakisalimiana na watu. Mara wakaona tena gari ya Joshi inaingia. Naya alipoiona tu akakunja uso. Akashuka kwenye gari yake akiwa amehamasika kweli, akawasogelea pale akiwa ameshika karatasi.

“Nimemletea Naya habari njema. Nahisi Mungu wetu amejibu kwa moto.” Akamkabidhi Naya zile karatasi. Naya akaisoma kwa muda kidogo, ilikuwa imechapishwa. Akasoma na kuigeuza huku Joshi akicheka kwa ushindi. Kama ilivyo, Naya akamkabidhi baba yake karatasi zote kisha akasimama nyuma ya baba yake kabisa, akainama. Baba yake akamgeukia akamtizama vile alivyoinama. “Ni nini?” Mama Naya akauliza. “Au labda Naya hujaelewa. Hiyo ni scholarship. Wanakulipia kila kitu. Bahati kama hizo haziji mara mbili hasa kwa aina ya masomo hayo mliyosoma nyinyi.” Akasisitiza Joshi.

“Kwani ni nini!?” Mama Naya akavuta zile karatasi kutoka mikononi kwa mumewe akaanza kusoma. “Masoma hayo aliyosomea Naya hayana ajira baba yangu.” Joshi akamgeukia baba yake Naya. “Wanaitwa wauza sura. Hakuna kazi hapa nchini ndio maana mpaka sasa unaona Naya anahangaika hapati kazi.” Yale maneno yalimkasirisha sana baba yake Naya. “Bahati kama hizi haziji mara mbili. Kwanza aniambie mwenyewe Naya ni wapi ameshawahi kuona scholarship za watu wa masoko! Atahangaika hapa nchini mpaka…” “Nani amekwambia Naya anahangaika?” Akadakia Bale huku anacheka.

“Si anahangaika kutafuta kazi hapati?” “Wapi umemuona Naya anahangaika kutafuta kazi!?” Bale akauliza tena. “Wewe ndiye unayehangaika. Huna habari yeyote unayozungumza na Naya isipokuwa kuajiriwa kwake. Wakati wote unamtia pressure kumuonyesha amechelewa, hajafanya juhudi zakutosha, anatakiwa afanye hivi au vile. Unamtia wasiwasi na kuonyesha hajafanya au hana uwezo wakufikiri.” “Hapana Bale. Anataka kumsaidia Naya.” Mama yake akaingilia. “Anamsaidia kufanya nini? Eti mama? Kipi kinakufanya ufikirie Naya anahitaji msaada wa Joshi?” Bale akawa amekasirika kabisa nakushindwa kujizuia.

“Kabla Joshi hajaja kwenye maisha ya Naya, Naya alikuwa mtu wa mipango ya kueleweka. Wote tumeshuhudia akili ya Naya. Ni zaidi ya kukaa darasani na kufaulu. Naya kabla hajamaliza chuo, alijaza watu pale ubungo Plaza, akafanya mambo makubwa ya kihistoria hapa nchini. Wapo wanamitindo wa ngapi hapa nchini jamani? Tena kwa umri mdogo wa Naya? Wewe mwenyewe mama ulikuwa huamini kama ni Naya amesimama pale mbele siku ile akipigwa picha na waandishi wa habari. Ghafla amekuja Joshi, amemgeuza Naya kama mjinga asiyeweza kufikiri! Kwa kuwa yeye anayo kazi ya uhasibu?” Bale akapata jukwaa.

“Unamgombesha nani sasa hapa?” Mama yake akauliza kibabe. “Mimi sigombi mama, lakini nataka tufikirie na tusipelekeshwe. Kwanza wewe mwenyewe Joshi hata humfahamu Naya, halafu unajichukulia tu mamlaka juu yake.” “Ulitaka amfahamu vipi?” Mama yake akauliza kwa ukali. “Usikasirike mama. Lakini nina uhakika kama Joshi angekuwa anamfahamu Naya hata kidogo tu, asingekuwa anazungumza hata kidogo mbele yake. Watu wanaomjua Naya, akiongea huwa wanasikiliza.” “Ni huyo Malon?” Akauliza mama yake kwa kejeli.

“Huyu Naya anasehemu zake tatu anazosimama akiwa na mwanaume yeyote anayemtaka, akiwa na baba. Nyinyi hamjamsoma Naya na kumfahamu.” Wote wakamgeukia yeye Bale, mpaka Naya mwenyewe. “Kwanza anayo sehemu moja tu anayotupa mambo yake. Pale kwenye ile mikono ya baba. Iwe furaha au huzuni. Akiwa na mwanaume anayemtaka yeye, na anayejua anampenda kwa dhati na kumuheshimu yeye na mawazo yake, atasimama mbele kidogo ya baba. Anakuwa kama ametangulia hivi. Akisimama pembeni yake, ujue unayo nafasi. Hata mama akiongea, anaweza kumsikiliza, akakusikiliza tena. Lakini kwa wanaume kama wewe Joshi, akishafika hitimisho kama hivi leo, kwa mara ya kwanza katika watu wa sampuli yako, anasimama nyuma. Kama pale alivyo kwa baba. Nyuma kabisa. Huna utakalomwambia tena pale Naya, akakusikiliza tena. Hata kwa vitisho vya mama, au hata umwambie unampa gari, hatakusikiliza tena.” Naya akainama na kujivuta nyuma ya baba yake zaidi.

“Kumtoa pale anaposimamaga, inahitaji mwanaume haswa, sio wavitisho wala gari. Ndio anaweza kukutizama tena na akakusikiliza. Na usifikirie wewe ndio mwanaume wa kwanza kumfuata Naya ukiwa na gari. Usijidanganye, na wala hutakuwa wa mwisho. Washakuja wasomi, wenye nyumba na magari mazuri tu, hakuna aliyembambaisha Naya. Naya anayo mapenzi ya baba, anajua kupendwa ni nini. Hizo scholarship zako hazimtishi. Na nikupunguzie tu matatizo, hivi unavyotuona sisi, hatuna shida wala hatuhitaji mkombozi. Usije kwa Naya kama unayetaka kumsaidia. Naya hahitaji msaada wala mtu wa kumkomboa. Kama unataka mke, njoo ukiwa umejipanga kuwa mume, acha kumnyanyasa Naya.” Bale akaondoka kabisa pale kanisani.

Naya akabaki vile vile ameinama pale nyuma ya baba yake. “We Naya?” Mama yake akamwita kwa ukali kidogo. “Mimi sitaki kwenda kusoma popote pale. Hata Joshi mwenyewe simtaki.” Mpaka baba yake akamgeukia. “Utakuja kujuta Naya wewe! Huyo anayekupa kichwa hivyo sio..” “Acha kumtisha mtoto mama Naya!” Baba yake akapokonya zile karatasi, akamkabidhi Joshi mkononi. “Usiku uliomuacha mtoto wangu peke yake, akarudi anatembea peke yake na giza, ulifanya kosa kubwa sana. Ni heri ungenipigia mimi mwenyewe simu, nikamfuata mtoto wangu, kuliko kuja kumfuata nyumbani, na kwenda kumtelekeza katikati ya jiji.” Baba yake aliongea tu hivyo na kuondoka pale. Naya akamfuata kwa haraka. Walipofika tu ndani kanisani Naya na baba yake, wamekaa, Zayoni akaingia. “Mama amesema tuondokeni. Anataka tumrudishe nyumbani.” Bila kujibu kitu, wakanyanyuka.

Naya akajua moto utawaka. Na kweli, walipoingia tu ndani ya gari, akaanza kuongea mama Naya. Aliongea mengi bila kunyamaza wala kutulia. Aliongea kama anataka kutoa laana. Akalaumu. Akampa angalizo Naya, akamtisha mpaka wakafika nyumbani. “Naomba usinitafutie mwanaume mwingine tena na wala usining’ang’anize kuolewa.” Kila mtu akashtuka. “Umeniambia nini Naya?” “Mimi sipo tayari kuolewa mama. Naomba niachwe kwa sasa.” “Basi hata huyo Malon nisimuone hapa nyumbani kwangu.” “Sawa.” Naya akajibu nakushuka garini.

“Unakufuru mama Naya, mke wangu! Kwa yote haya Mungu aliyotupa, jitihada zangu zote. Mchana na usiku nahangaika, bado unamtisha Naya kwa kumwambia ataishia kama wewe! Kana kwamba maisha yako ni mabaya sana! Kweli!?” Baba Naya naye akashuka, na Zayoni naye akashuka. Walimkuta Bale nyumbani. Siku hiyo hapakuwa na ibada, kila mtu akaingia chumbani kwake.

Ilipofika mchana, Naya akasikia anaitwa kwa ukali. “Unalala ukitegemea nani akupikie? Ingia jikoni uandae chakula.” Naya akaingia jikoni. Hakuwa anajua hata anatakiwa kupika nini. “Na itabidi ubadili maisha yako. Kwa kuwa umekataa kuolewa, unaonekana unataka kuendelea kuishi humu ndani na baba yako, itabidi sasa uanze kujifunza kupika. Kuanzia leo, kazi za jikoni ni zako. Na ninaomba uivishe. Hakuna wakukusaidia. Maana muda mfupi tu Bale ataondoka na kuhamia chuoni kabisa, atakuacha hapa. Na mimi nitakuwa kazini. Sasa wewe ambaye huolewi, huna kazi na hutaki kuendelea kusoma tena, huwezi kukaa bure tu. Kule mabandani yupo mtu wakumsaidia baba yako, kunakohitajika mtu ni humu ndani. Anza kujipanga. Kufua, kupika na mambo yote ya humu ndani ni wewe.” Kila mtu akajua ndio adhabu yake. Na wakajua mama yao anafanya makusudi kuwaadhibu wote. Lakini hakuna aliyejibu. Na kweli Naya akaanza majukumu ya ndani muda huohuo, mama Naya hakumtania. 

kukosa Bara na Pwani...

A

kiwa amechoka sana, usiku huo wa jumapili, akiwa amelala kitandani kwake, akaamua kumpigia simu Malon. Kama kujaribisha tu, kujiliwaza. Kwani alijua Malon yupo bado Dubai. Akashangaa simu yake inaita. Akakaa kwa haraka. “Malo!?” Naya akaita kwa mshtuko. “Pole nimekuamsha.” “Hamna neno. Vipi?” “Upo Tanzania!?” Naya akauliza kwa mshangao. “Ndiyo.” Naya akahisi hajaelewa. “Upo Tanzania hii hii!?” “Nipo Naya!” Naya akatulia kidogo kama mwenye maswali. “Umerudi lini?” “Kwani vipi mama, mbona maswali?” Naya akaishiwa nguvu kabisa asiamini kama ni Malon.

“Nilijua ukirudi utanitafuta!” Naya aliongea kwa unyonge akisikika kuishiwa nguvu kabisa. “Nakumbuka mara ya mwisho wakati tupo kwenye mahusiano, kilio chako ilikuwa nitulie na wewe Naya. Hukupenda jinsi nilivyokuwa na wewe, huku nikiwa na wanawake wengine. Sasa na wewe usiwe kama mimi. Au usiige tabia mbaya. Sitaki mimi niwe sababu ya kukuharibu. Unaye mchumba wako, ambaye mpaka unafahamika kwa wazazi wake, nashauri utulie naye. Na mimi kuwepo kwenye maisha yako, sio salama na si sawa hata kwa Joshi. Inakuwa kama nakusababisha kumsaliti mwanaume uliyemkubali kwenye maisha yako. Hata wazo lakufanya mambo bila kumwambia, nimefikiria, nimeona sikukushauri vizuri. Hamtajenga mahusiano mazuri.” Naya alikuwa ametulia tu akisikiliza.

“Si sawa kuwa kwenye mahusiano ya kueleweka ambayo unaingia mpaka kwenye ndoa, huku nikikushauri mambo kinyume na mwenzio. Nafikiri unahitaji kumsikiliza na kujenga mahusiano yenu bila kuingiliwa. Nakiri nilifanya kosa kukupa ushauri mbaya, nimetubu kwa Mungu na ninatubu kwako. Naomba nikupe nafasi ya kujijenga. Nimeshakubali mimi sio wako, na umeshakuwa na mahusiano na mtu mwingine, naona nichukue hatua yakukaa pembeni. Kwa faida yako Naya. Nakutakia kila la kheri. Maisha yenye furaha na amani. Mungu akufanikishe.” Kimya. Naya akavuta pumzi kwa nguvu.

“Naya?” Malon akaita. “Nimekusikia Malon. Asante. Nakuombea Mungu akufanikishe zaidi.” Naya akakata simu. Naya alibaki haamini. Kulikuwa kuachwa ambako hata hakutegemea! Mara ya mwisho waliachana kwenye mapenzi na makubaliano mazuri tena mazito yenye tumaini mpaka kuombewa! Naya hakutegemea hata kidogo! Aliwaza usiku huo, akamkumbuka Malon huyu aliyekuwa amerudi kama mcha Mungu na kurudisha tumaini la ajabu sana kwake. Alikuwa kama aliyeona mzimu akabaki akitetemeka, ametoa macho na kushindwa hata kusogea pale alipokuwa amekaa kwa hamasa ili kumsikiliza Malon. Lakini akaamini kama alivyosema baba yake Malon, Malon sio wamahusiano. Naya akaumia sana moyoni.

 ~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

Itaendelea.....

 


CONVERSATION

0 Comments:

Post a Comment