Naomi Simulizi |+1 205 767 8163 |naomisimulizi@gmail.com MAPENZI & PESA! - SEHEMU YA 2. - Naomi Simulizi

MAPENZI & PESA! - SEHEMU YA 2.

 Naya akiwa Sekondari.

“Leo tumepata wafanyabiashara watupu! Wamekuja na vijana. Sasa sijui ni watoto wao au ni wafanyabiashara wenzao!” Aliongea Tunu, mmoja wa mwanafunzi na mfanyakazi mwenzake Naya, waliokuwa wakifanya kazi na kampuni ya Madamu Vane, mama aliyewajua wakubwa na wenye nazo nchini na kumuweka mjini kwa kumpa  kazi za kuhudumia sherehe zao. Akitoa huduma nzuri ya wahudumu{Waitress} warembo haswa, kwenye masherehe yao. Ukizungumzia wahudumu warembo wa kuvutia ambao walifurahisha kupokea huduma kutoka kwao, Madamu Vane aliongoza.

Alikuwa akichukua vibinti virembo sana kama warembo wanaogombania taji la kisura wa nchi. Wakiwa kazini ilikuwa nilazima warembo hao wapendeze haswa na kuvutia ndipo unatoa huduma. Hakuna jinsi wangekuhudumia usifurahi. Alikuwa akiwafundisha jinsi ya ugawaji wa vinywaji kwa ustadi. Kuanzia kushika sinia la vinywaji, chupa, glasi na ufunguaji. Jinsi wanavyosimama katikati ya viti kuwahudumia watu na kuzungumza nao! Utafurahia hata wakiwepo mezani. Tabasamu ilikuwa moja ya kazi yao. Lazima kuwepo na tabasamu na lugha laini ukionyesha mteja ni mfalme hata kama ameshalewa.  

Basi, akishapata tenda za mashere makubwa sana hapo jijini, tena mara nyingine hata akipata yenye pesa nyingi mikoani, ziwe za kiserikali au watu binafsi, alituma hao warembo wake kwenda kufanya kazi ya kugawa vinywaji. Alizipata hizo kazi mpaka kwenye Ikulu. Alikuwa ni mzoefu wa muda mrefu na alifahamiana na wake za maraisi, mawaziri hata wa awamu za nyuma na kumsaidia kumuunganisha na wengine kwenye balozi zilizopo nchini. Ukweli Madamu Vane alikuwa na kazi karibia kila juma.

 Basi hapo ndipo watoto hao wa shule walijipatia pesa. Kutoka kwenye malipo ya kazi hiyo na kutoka kwenye ATM watakazojipatia kutoka kwenye kuwahudumia wageni hao, kama wenyewe walivyokuwa wakiwaita, ATM, wanaume wanao watongoza na kuwafanya waishi mjini kwa starehe zaidi.

Na yeye Naya aliunganishwa na mmoja wa mrembo aliyekutana naye alipohamia hapo hosteli na kuvutia wengi. Kwa kuwa Naya alikuwa mrefu na umbile la sita iliyojitengeneza bayana na kuonekana wazi kabisa japo hakuwa mnene, akipendeza na kuvutia katika kila vazi. Wengine wakamshauri aingine kwenye mashindano ya mavazi, wengine wakamshauri agombanie taji la Miss Tanzania. Lakini Naya mtoto wa baba na wa kanisani, asingethubutu hata kutoa hilo wazo nyumbani kwao.

Baba yake aliyekuwa kipenzi chake, alikuwa ameishika dini haswa. Naya amezaliwa kanisani na kulelewa kanisani. Aliijua dhambi ni nini kwa kukua akifundishwa kanisani na nyumbani. Hata gauni juu ya magoti hakuwa akiruhusiwa kuvaa nyumbani kwao, leo uje umwambie baba yake eti Naya apite mbele za watu na kivazi cha ufukweni! Hata kidogo.

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

Ilikuwa siku ya jumamosi. Wahudumu wote walitakiwa kuvaa sare. Magauni meusi na nywele ziwe zimefungwa juu kabisa ili zisiangukie kwenye vinywaji au chakula. Kwa kuwa ilikuwa ni kazi anayoitegemea sana Naya, hakuwa akitaka kuharibu kama wenzie waliokuwa wakivunja masharti hapa na pale. Alivaa gauni lililokuwa limembana juu mpaka chini ya magoti. Nywele aliziweka jeli zote akaziwekea mkia maalumu lakini wa mawimbi. Alivaa hereni zilizokuwa zimemkaa vizuri sana. Zilikuwa ndefu kama cheni zilizokuwa zimening’inia kuanzia masikioni mpaka kwenye mabega. Na kwa kuwa alikuwa na shingo ndefu, ungependa kumtizama. Nazo hizo hereni alizinunua baada ya kulipwa kwa shuguli yake ya kwanza.

Alipolipwa tu mara ya kwanza alipokwenda kuifanya hiyo kazi, akaamua kuwekeza kwenye muonekano, kwa kuwa alikuwa na vitu vya kawaida sana. Pesa yote akajinunulia nguo, viatu vya juu ambavyo vilikuwa vikihitajika kuvaliwa mara zote kila wanapokuwa wanaitwa kazini. Vipodozi, pafyumu na hereni za maana. Maana alipokwenda huko kazini kwa mara ya kwanza, macho yalimtoka baada ya kukutana na hao warembo. Utafikiri wao ndio walikuwa wakihudumiwa! Kumbe wao ndio wahudumu! Walitakiwa kuvaa sare tu, yaani rangi moja ya nguo, lakini alikuta kila mtu amepania kama wanao kwenda kwenye mashindano!

Alibabaika kidogo akidhani ameingizwa kwenye kambi ya warembo wanaotaka kugombania taji la urembo wa dunia. Maana alikutana na warembo weupe na weusi, na wote walijijulia. Usingekutana na mweupe mbaya au mweusi asiye vutia. Moyo ulitulia baada ya rafiki yake kufika hapo akiwa amechelewa kidogo. Angalau akapata mwenyeji aliyeweza kuzungumza naye na kumueleza jinsi wanavyofanya. Kuwa, kikubwa ni kuwekeza kwenye muonekano ili kumvutia hata bosi wao,  Madamu Vane ili kuja kukuita wakati mwingine tena, kukiwa kuna shughuli kama hiyo. Kwa kuwa haikuwa ajira ya kudumu. Kukiwa na kazi, ndipo unapigiwa simu kuombwa ufike sehemu ya tukio. Utapewa na muda wa kuwepo hapo. Sasa akamwambia kama ukionekana mshamba mshamba, au tabia mbaya. Kulewa kabla ya kumaliza kazi na mengineyo, unaweza usije kuitwa tena. Akamwambia ndio maana anaona wote wamependeza ili kutunza ajira.

Ndipo Naya naye ikabidi kupita madukani. Japokuwa Naya alizaliwa na wazazi wakaiwaida sana, wakulalamikia  maisha kila wakati na kwenye kila kitu, lakini Mungu aliweka kipaji cha ajabu sana kwa Naya. Alijua mitindo kupita kiasi. Akiangalia umbile la mtu, anaweza kufikiria ni ana gani ya nguo, na ikitengenezwa vipi kwa aina hiyo ya umbile angependeza zaidi. Hata ukiwa umevaa nguo watu wakakukosoa, Naya atajua ni kwa nini hiyo nguo wewe imekukaa vibaya. Atajua ingerekebishwa vipi ili kukukaa vizuri na kuvutia machoni kwa watu. Na hakuwa akihitaji pesa nyingi sana kubuni kitu kizuri na ndio maana alikuwa akipendeza sana chuoni baada ya kumpata Malon, nakubakia akiigwa kwa kila anachovaa yeye.

Aliposikia siri hiyo ya kutunza ajira na akalipwa malipo ya kwanza kwa kazi ya kwanza waliyokuwa wamekwenda kuhudumia tafrija ya Mabalozi wote waliokuwa wakiwakilisha nchi zao hapo nchini, walialikwa na raisi wa nchi, Naya hakutaka kufanya kosa. Akakusudia kuwekeza kwenye muonekano wake zaidi. Kununua vitu vichache, vya gharama, lakini vitakavyoendana na mwili wake au umbile hilo la urefu. Na kweli Naya alikuwa mrefu wakuvutia. Na alivyojiweka, na rangi yake ya mwili, alikuwa akijibeba kama mwana mitindo kabisa. Vitu vichache, lakini vilimkaa vizuri.

Ndani ya kundi hilo la warembo wengi wahudumu, watano akiwepo Naya wao walitokea kwenye hosteli hiyo waliyokuwa wakiishi wanafunzi wengi wa kike waliokuwa wamekodi kwenye nyumba moja iliyokuwepo maeneo ya Upanga, karibu sana na shule ya Shabani Robert. Lakini walikutana hapo kuishi tu, ila wakisoma kwenye sekondari tofauti tofauti za hapo jijini Dar. Ni wachache sana walitokea shule moja. Wengine walisomea Jangwani, Zanaki, na hapo karibu Shabani Robert. Wapo baadhi waliokuwa wakisoma chuo cha Ustawi wa jamii. Na wenyewe waliishi kwenye hosteli hiyo. Ilikuwa nyumba ya mtu binafsi. Aliibadilisha na kuweka vyumba vidogo na vingine vikubwa vyenye double decker, mpaka tatu kwenye chumba kimoja, akibana ili kupata wanafunzi wengi. Kwa hiyo vipo vyumba vilichukua watu sita, vingine wanafunzi wanne, wawili na cha mtu mmoja mmoja ambavyo hivyo vilikuwa na bei kubwa. Kutokana na uwezo wa wazazi wake, Naya alikuwa akilala chumba cha watu 6. 

Historia ya Naya. 

    Hakutokea kwenye familia ya watu wenye uwezo mkubwa kama wengi wa wanachuo wenzake huko Mzumbe walivyodhania. Hapakuwa na pesa ya ziada ila kula, kuvaa kawaida sana tena nguo kununuliwa ikiwa muhimu sana sio kubadilisha mara kwa mara, na ada zao ni wazazi kuhangaika haswa tena wakati mwingine mpaka kukopa ndipo watoto waende shule.

Karibu maisha yote walikuwa wakiishi kwenye nyumba za kupanga tena wakikodi vyumba viwili, ndani ya nyumba zenye wapangaji wengi. Wazazi wao wakichukua chumba kimoja na wao watoto watatu, Naya akiwa binti wa pekee, dada mkubwa, chumba chao akishirikiana na wadogo zake wakiume wawili. Mama akiwa mwalimu wa shule ya msingi Mkwajuni, wakiishi Mwananyamala. Maisha yao yakaendelea hivyo wakiishi kwenye nyumba za kupanga ila maeneo ya karibu anapofundisha mama yao, mpaka mama huyo alipochukua mkopo huko kazini kwao na baba yake kukopa kila mahali, wakanunu kiwanja karibu na Kibaha, maeneo ya Kiluvya.

Walijinyima sana ili kuweza kujenga. Na kutokana na uwezo kuwa mdogo, huku wakilipia kodi ya vyumba viwili walivyokuwa wamekodisha, walijenga nyumba hiyo taratibu sana. Kwa hakika waliishi maisha ya kujibana kupita kiasi mpaka watoto wao walijua wazazi hawana pesa. Na hata wakiwa katikati ya kundi, ungejua wazazi hao ni wahitaji.

Familia hiyo iliyoendeshwa na mama mwalimu, shule na kufaulu ilikuwa si chaguzi. Ilikuwa lazima kusoma, na kufaulu na ndio maana Naya hakuwa akikosa kipindi chuoni hata mara moja na kushangaza wenzie. Kama hujalazwa hospitalini, na ni siku ya shule, huyo mama Naya, alitaka kukuona darasani. Hapakuwa na ugonjwa wakutokukufanya usiwepo darasani, labda umelazwa hospitalini. Darasani na kanisani ilikuwa LAZIMA, wala hapakuwahi kutokea na mjadala juu ya hayo.

Naya alifaulu kidato cha kwanza kwenda sekondari ya Jangwani kutoka shule ya msingi aliyokuwa akifundisha mama yake hapo Mkwajuni. Alikuwa shule ya kutwa. Wakati wanahamia Kiluvya kwenye nyumba waliyojenga wazazi, Naya akiwa ndio anaingia kidato cha tatu, ndipo ikawalazimu kumtafutia hosteli ili iwe rahisi kwake, kuliko usafiri wa kila siku asubuhi kutokea Kiluvya mpaka kituoni Fire ambapo ni karibu na shule.

Alipohamia hapo hosteli, na kuvutia wengi kwa urembo wake ndipo Hawa rafiki ya Tunu aliyewakuta wakiwa wanafanya kazi tayari kwa Madamu Vane, akampa dili ya kazi hiyo ya waitress. Akamshawishi kuwa atafaa sana. Kwa umbile lake lazima bosi wake atampokea tu. Anachohitajika ni marekebisho machache tu. Kwa ugumu wa maisha aliokuwa akipitia kipindi hicho, na kumuona baba yake akidhalilika sana akikopa kila mahali, Naya hakuhitaji ushawishi mkubwa. Ikawa kama Mungu amefungua mlango na yeye kujipatia kipato na kusaidia kiuchumi. Naya akamtafuta Madamu Vane. Ikawa bahati yake nzuri kwenye kipindi hicho, kwa kuwa wasichana wake wawili aliokuwa akiwategemea kwa kazi, waliacha kazi ghafla baada ya kupata wanaume wenye pesa, akamchukua Naya huku akimsihi ajifunze kazi kwa haraka na ajitahidi kupendeza.

Kabla hata ya familia yake kuhamia Kiluvya, tayari ufugaji ulikuwa umeshaanza. Walipohamia hapo ndipo biashara yakufuga kwa wazazi wake ikawa imechanganya hasa ili kuongeza kipato na kulipa madeni waliyokuwa wakidaiwa kila kona sababu ya kumaliza nyumba hiyo haraka ili wahamie. Ni kweli walikuwa wakidaiwa. Hata mama yake alikuwa akienda kazini kama kulipa madeni tu. Mshahara wake ulikuwa mdogo sana.

Kilipopita kipindi kigumu cha uchumi wa Tanzania, baba Naya aliyekuwa akifanya biashara ndogo ndogo aliishiwa kabisa, akafunga biashara zote akabaki akimtegemea mkewe. Sasa walipohamia kwenye nyumba yao huko shamba, ndipo akahamisha mawazo na nguvu zote kwenye biashara ya ufugaji wa ng’ombe na kuku wa kisasa na kienyeji. Na hapo ndio walipotegemea kipato cha familia. Ng’ombe akifa, au akiugua, basi ni tatizo la familia nzima. Inamaana kiwango cha maziwa kitapungua, kipato kitapungua. Waliuza na mayai pia hapo nyumbani kwao.  Hawakuwahi kulala njaa, lakini hawakuwahi kusaza hata mlo mmoja.

Mungu hapo nyumbani kwao alitajwa kuanzia asubuhi wakiamka, redio zote zinawashwa kwenye station za dini, mpaka usiku wakienda kulala wakiwa wanamalizia kwa ibada ya pamoja. Kanisani ilikuwa ni lazima. Naya hakuwa anakumbuka ni lini alikosa kwenda kanisani siku za jumapili anapokuwa nyumbani.

Naya alifanana sana na mama yake, huwezi kuuliza. Mtoto huyo wa kike wa pekee tena wakwanza, ilikuwa ni kama mama yake amejizaa mwenyewe. Walifanana sana na mama yake. Alifuatwa na hao wadogo  zake wa kiume, wawili. Bale ambaye naye alikuwa kama pacha wa nje wa Naya. Na yeye alifanana sana na mama yake. Wote walikuwa warefu, ungeweza kusema ni Masai. Ndipo wa mwisho akazaliwa wakiume tena. Zayoni, ambaye yeye alifanana sana na baba yake, mpaka haiba ya ukimya sana kama baba Naya, tofauti ya Bale na Naya. Wao ndio walikuwa na kelele, wakigombana mchana na usiku. Wakibishana kwa hili na lile, ilimradi tu. Na walikuwa hivyo wakishandana tokea watoto. Zaidi wawapo nyumbani, hata wapangaji waliwajua Naya na Bale, kwa kubishana. 

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~ 

M

uda wakuanza kugawa vinywaji ukafika. Wakawa wameshagawiwa meza za kuhudumia. Ilikuwa ni tafrija ya namna yake. Kulikuwa kumejaa matajiri watupu walioshika uchumi wa nchini, kwa biashara. Na ulinzi pia ulikuwa mkubwa. Ukweli ni Naya tu ndiye hakuwa akifika pale na lengo la wanaume. Japokuwa malipo yake yalikuwa hayamtoshi kujikimu lakini alifundishwa kuridhika na kila anachokifanyia kazi. Baba yake alikuwa akilipia ada, yeye anasaka michango ya shule ikiwemo chakula na malazi. Japokuwa hakuwa na muda mrefu sana hapo kazini kama wenzake, lakini Madamu Vane alimpenda sana Naya. Akamsoma kwa haraka, akaona ni binti wa kuaminika. Na hana tamaa ya wanaume. Akajua ni mtu atakaa naye kwa muda mrefu, akamuweka karibu sana.

Kila shughuli anayopata Madamu Vane, Naya naye aliitwa akafanye kazi. Alibahatika kufanya kazi mpaka Ikulu na kwenye tafrija mbali mbali za kisiasa. Aliyokuwa akiyaona na kuwaona kwenye luninga, Naya akabahatika kushuhudia kwa macho. Lakini hakuwa akiondoka na namba ya mwanaume yeyote yule hata atongozwe na nani, mwenye jina kubwa nchi! Naya hakujisumbua. Ikawa kazi tu, basi. Akikupa tabasamu anapokuhudumia, ujue litaishia hapohapo mezani anapokuhudumia, usijisumbue kuomba mwendelezo. Wenzake wakaanza kujua hiyo tabia yake. Wakamshangaa sana, kwani walikuwa wakimwambia ni kama waliokuwa na kiu sana, halafu wanapewa maji, yeye anajivunga! Hakuna aliyemuelewa.

Wote walitaka pesa. Na wanao wahudumia walikuwa nazo, na wapo tayari kuzimwaga,  sasa kwa nini usijichukulie mmoja ukaendelea kumuhudumia pembeni kibinafsi na kuendelea kunufaika? Watoto hao wa mjini, wahudumu, wakawa na kazi ya kuambizana ni nani amemuwahi yupi ili wasije kuchukuliana mabwana. Wanatoka nje wakiwa na vinywaji kwenye trei. Wanagawa. Wakirudi upande wa kaunta au jikoni kuongeza vinywaji, basi wanaambizana yupi ni wa nani, ili kuepuka kugongana baadaye, au ukaondoka bila mtu.

Naya alikuwa akiwasikia wanavyobishana wakimgombania huyu au yule, yeye kimya. Anasubiri kazi iishe, achukue malipo yake, aombe lifti arudi zake hosteli. Nyumbani alikuwa akienda kila anapoweza. Japokuwa ilikuwa ni hapo hapo jijini, lakini Naya alimshukuru Mungu kupata mwanya wakuishi mbali na nyumbani. Kwa mara ya kwanza akawa huru, hakuna wakumbana. 

Mwanzo wa Yote!

N

aya akiwa amewekeza akili zake kwenye kazi tu, akihudumia kwa tabasamu kama moja ya masharti ya kazi yao. Mteja ni mfamle. Na kwa kuwa wateja wao walikuwa watu wa hadhi, basi kujinyenyekeza ilikuwa lazima. Wakati shuguli ikiendelea, akiwa anatoka upande aliokuwa akihudumia akirudi kuongeza vinywaji, kijana mmoja mtanashati akamsimamisha. “Najua wametoa maelekezo ya sehemu ilipo msalani. Nilikuwa nimetoka nje kwa ajili ya kuzungumza na simu. Unaweza ukawa unafahamu ni wapi?” Naya akajaribu kumuelekeza, akamwambia bado hajaelewa. “Labda nikupeleke.” Naya akaona amsaidie tu. “Chooni!?” Akauliza yule kaka akijifanya kama ameshtuka kidogo kumbe ndio lilikuwa lengo lake. “Si ndio msalani na si ndiko unakotaka kwenda!?” Naya akauliza taratibu akionyesha kuingiwa na hofu kidogo.

“Au naweza kukuitia mlinzi akakupeleka.” “Twende bwana. Nakutania.” Naya akarudisha tabasamu kidogo na kuongoza njia mpaka nje ya ule ukumbi mdogo, lakini mzuri sana. “Naitwa Malon. Ila wengi wamezoea kuniita Malo.” Akajitambulisha kwake huku wakiwa wanatafuta mlango wa choo. “Naya!” Mwenzake akamfuata akimtaka arudi ukumbini, kuwa anaitwa na kiongozi wao. “Samahani. Natakiwa kurudi ndani. Ila vyoo vipo kona hiyo inayofuata. Umeshafika.” “Nashukuru Naya.” Naya akarudisha tabasamu la heshima, akili ikiwa ilisharudi kazini. Akageuka na kurudi ndani. Siku hiyo kazi ikaenda vizuri. Hapakuwa na shida. Walikaa hapo mpaka saa nane usiku ndipo wakamaliza kazi. Walipata wateja wengi walevi. 

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

     Kesho yake Naya alilala  karibu siku nzima. Kwanza alifanya kazi ya masaa zaidi ya 8, tena akiwa na mchuchumio, na ilimlazimu kuwa akitabasamu kila wakati. Kila anapotembea ni lazima awe anatembea na hivyo viatu virefu. Alilala kama mfu. Aliamka asubuhi akiwa hoi. Akapata kifungua kinywa na wenzake, sehemu kulikokuwa na tv ya hosteli, kisha akarudi chumbani kwao. Hiyo ilikuwa siku ya jumapili. Akiwa na kazi huwa anakwenda nyumbani kwao mchana na kurudi jioni, lakini siku hiyo akakusudia asiende. Akamtumia ujumbe baba yake kumjulisha malipo ya pili ya ada, yanatakiwa shuleni. Muda umefika, kisha akazima kabisa simu nakurudi kulala.

Aliamka jioni kukiwa na shamra shamra nje. Akawauliza anaolala nao hapo chumbani kwao. “Kuna nini, mbona kelele!?” Kwenye chumba hicho walilala na wanafunzi wa ustawi wa jamii. Kina dada wenye akili zilizokomaa kuliko wao watoto wa sekondari. Na ni yeye tu kwenye chumba hicho ndiye aliyekuwa akifanya kazi kwa Madamu Vane pamoja na wasichana watatu hapo hosteli. Pengine kwa kuwa wao walionekana warembo zaidi na maumbile ya kuvutia.

“Utawaweza hao watoto?” “Kina nani?” Naya akamuuliza Wahija, aliyemjibu. “Kwani unafikiri nazungumzia kina nani?” Naya akacheka, akawa ameshawafahamu. Wanafanya kazi pamoja, tabia zao sawasawa. Starehe na kukamua yeyote mwenye pesa ndio kazi yao kubwa hapo mjini. “Sasa safari hii wanashangilia nini?” Naya akaendelea kuhoji.  “Kuna waliopata wanaume jana huko mlikokuwa kazini, ndio wanakuja kuwachukua ili wawatoe kwa chakula cha usiku.” Naya akacheka na kujirudisha vizuri kitandani. “Wewe huendi?” “Mie huyu? Akuu. Nitaenda kununua chips ikifika saa mbili, nirudi nilale. Hapa miguu haina kazi! Inauma.” Naya akajibu. 

Kulikuwa na tamthilia waliyokuwa wakiifuatilia wote hapo hosteli. Basi ikifika mida yake, kila aliye mtaani au chumbani, ataanza kusogea karibu na tv ili wajue kulikoni, kisha kuja kusimuliana week nzima. Na Naya alikuwa mpenzi kweli. Taarifa ya habari ilikuwa ikiisha tu, tamthilia inaanza. Akapitiwa na usingizi, akaja kuamka saa moja na nusu. Akaruka kutoka kitandani kwake juu, akavaa harakaharaka, wala hakujitengeneza. Hosteli nzima ilikuwa kimya. Naya akajua amebaki peke yake humo ndani kila mtu amekwenda kutafuta chakula ili waje kuwahi hicho kipindi.

Wakati anatoka chumbani kwao, mwisho kabisa, mlango wa mbele akawa anaingia mtu. Akafunga mlango wa chumbani kwake na kusogea sebuleni ambako kulikuwa katikati ya vyumba. Naya ni kama akawa anajaribu kufikiria amemuona wapi! Kadiri alivyomsogelea ndivyo alivyokumbuka kuwa ni mmoja wa wateja wao. Swali likawa ni kwenye shuguli ipi! Akaamua amkaribishe tu.  

“Hujambo Naya?” Akamtaja kabisa na jina. Naya akamsogelea karibu. Akakumbuka alivyoambiwa na Wahija, kuwa kuna wenzake usiku uliopita walipata wanaume na wanakuja kutolewa kwa chakula cha usiku. “Naona utakuwa umewachelewa hawa warembo, kidogo tu. Wametoka sasa hivi kwenda kwa chakula cha usiku.” “Sasa mbona wewe hukwenda?” “Nilikuwa nimelala. Ndio naamka sasa hivi. Nakwenda kununua chips hapo nje getini nije kula humu ndani. Karibu ukae tu. Baada ya nusu saa watakuwepo hapa kuja kuangalia tamthilia.” “Basi kwa kuwa na mimi sijala, na nina njaa, acha tuongozane na mimi ninunue chips.” “Pakawaida sana huko ninapoenda mimi kula. Hapakufai wewe na hadhi yako.” “Ukiwa na njaa, unakula popote.” Bila kufikiria akiwa na haraka ya kuwahi kurudi, akaitika sawa.

Walifika pale, wakiwa wameongozana lakini ni kama Naya alikuwa yupo peke yake tu. Akili haikuwepo kwa yule mgeni. Na kwa kuwa walikuwa wakienda kwenye kibanda wanachouza chips karibu tu ya hiyo hosteli yao, haikuchukua hata dakika tano kufika. “Mwidini!” Naya akaita. “Inakaribia saa mbili. Nirekebishie niondoke.” “Foleni kubwa Naya!” “Mimi na wewe Mwidini? Umeanza lini kunibania? Njaa inauma. Sijala mwenzio tokea asubuhi nilivyopata chai na andazi.” “Hukosi sababu Naya!” “Tutakatana kwenye mahari. Usijali, mimi wako Mwidini. Nirekebishie hapa na mimi nitakubembelezea kwa baba Naya, akupunguzie mahari.” Naya akamfanya Mwidini acheke na kutingisha kichwa.

“Maneno hayo kabla hamjatoka hapa. Mkishasoma, hamtukumbuki.” “Tatizo lako wewe Mwidini unaamini kila mtu! Mimi mkeo. Anza kupunguza mahari.” “Sawa Naya. Kama kawaida?” “Vile vile. Naenda kukaa pale. Wewe utaniletea kimtindo.” Muda huo Naya anazungumza na Mwidini mwenye hicho kibanda, akimbembeleza kwa sauti ya chini wateja wengine wasisikie, huku akiwa hana hata wazo kuwa kuna mtu aliongozana naye  na alimwambia na yeye ana njaa.

Alijivuta taratibu mpaka kwenye meza ya mwisho kabisa. Akawasha simu yake. Zikaanza kuingia jumbe. Ukaingia ujumbe wa baba yake pia, uliomchosha na kumnyima raha kabisa. Akavuta pumzi mara kadhaa, akaweka simu mezani akaanza kuzungushia simu yake kidole taratibu huku akifikiria. Alibadilika mpaka usoni. Naya aliyekuja na haraka ya kuwahi tamthilia akawa ametulia hapo mezani kama hana haraka tena. Ameinama  na kuendelea kuchezea simu yake, wazi mawazo yalionekana yalishahama.

“Tunaweza kuagiza soda wakati tunasubiri.” Naya akanyanyua uso kumtizama anayemuongelesha. Akamuona yule yule kijana amekaa kiti cha mbele yake. “Mimi nipo sawa tu. Unataka nikuitie Isa?” “Isa?” Akauliza. “Yule kijana pale, anaweza kukuletea kinywaji chochote unachotaka.” Naya akanyanyua mkono. Isa akaja kwa haraka. “Shemejiii!!” Akamtania Naya. “Hivi mnavyonichelewesha, naanza kumfikiria mara mbilimbili huyo kaka yenu. Hapa sijaolewa mnaniua kwa njaa. Nikiolewa je?” “Tatizo lako Naya, wewe haraka! Kila siku unakuja ukiwa unataka kuondoka hapohapo!” “Sasa kama mnamapenzi na mimi mnayejua chakula changu ni kile kile kila siku, si mngekuwa mnaniandalia kabisa? Kila siku lazima nije niwabembeleze wee!” “Jumapili leo Naya.” “Kwa hiyo?” Naya akauliza. “Hutabiriki.” Naya akatulia kidogo. “Hapo sawa. Umenishinda. Sasa tuone kesho utakuwa na kisingizio gani.” “Kesho ukija, na kukabidhiwa chakula.” “Ukifanya hivyo mbona kaka yenu ataoa bila mahari!” “Bure!?” Akauliza Isa. “Bureeee! Ashindwe tu yeye mwenyewe.” Isa akacheka sana.

“Haya Shemeji. Subiri turekebishe mambo.” “Hayo ndio maneno.” Isa akaondoka, Naya akarudisha macho kwenye simu yake. Mara simu ya Naya ikaita,  akakata na kutuma ujumbe. Akaonekana kubadilika tena usoni na kukosa furaha. Kisha akavuta tena pumzi. Akajiweka sawa. Wazi alishahama tena pale kimawazo. Baada ya muda mfupi Isa akamletea chakula. Naya akamlipa kisha na kumuongezea kama tip. “Sasa Shem, na ya soda hapohapo. Unywe.” “Nashukuru shemeji wa mimi. Na hivi najua tutagawana na vya kaka! Sina shida.” Naya akacheka, akasimama na kuondoka. 

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

Alikwenda nyuma ya hiyo hosteli ili apate utulivu wakuzungumza na mama yake aliyekuwa amemtafuta kwa kumpigia, akamkatia na kumtumia ujumbe kuwa atampigia baada ya muda mfupi. Yupo sehemu ambayo ina kelele, hawatasikilizana. “Mama!” “Nipo.” Akaitika mama  yake. “Mbona leo hujaja nyumbani?” “Nilimwambia baba nitakuwa na kazi jana usiku. Tumetoka karibia saa 8 usiku, mpaka kufika hapa hosteli kuoga na kupumzika, ilikuwa imeshakuwa asubuhi. Nimelala siku nzima.” “Kwa hiyo hata kanisani hukwenda?” Naya akanyamaza.

“Ni kwa faida yako Naya.” “Naelewa mama. Lakini ningefanyaje na nilikuwa nahitaji hii kazi? Nina michango shuleni na hapa nadaiwa pesa ya hosteli.” Naya akajibu kwa kuumia kidogo. “Na sisi tunafanya kwa kadiri ya uwezo wetu Naya. Hakuna pesa, maziwa yameshuka sana, ng’omba waligua ndio maana. Haya na tokea kuku wapate ule ugonjwa, ni kama wameacha kutaga. Mwezi huu hatujapata kitu. Tungekusaidia.” “Naelewa mama na ninawashukuru.” Naya akajibu kinyonge. Na simu ikakatika. Alijua wazazi wake jinsi ambavyo wanavyohangaika kujishugulisha, lakini kila leo kunatokea jambo la kuwakwamisha. 

Mpaka simu ya mama yake inakatika, Naya machozi yapo shavuni. Alijua baba yake atapambana mpaka apate hiyo pesa anayodaiwa shuleni. Lakini alijua wazi itamlazimu akakope tena kwa watu walewale waliokuwa wakimkosea heshima. Walimkopesha kwa masimango mengi na kejeli juu! Tena mara nyingi kila walipomdai inakuwa kama wimbo! Kila mtu atajua huyo mzee anadaiwa tena.

Alikaa pale nje kwa muda akiwaza hili na lile zaidi kumfikiria baba yake, mwishoe akaamua kuingia ndani. Ulishafika muda wa tamthilia. Akaingia ndani na kukuta makochi yote yamejaa. Kumetulia, kila mtu macho kwenye luninga, kuangalia na kusikiliza kwa makini. Hakuna hata aliyechukua muda mrefu kumtizama wakati anaingia. Akajisogeza taratibu mpaka kwenye kochi ambalo lipo pembezoni, akakaa chini kabisa sakafuni akakunja miguu taratibu tena kwa tahadhari, asisumbue wenzie.

Ujumbe ukaingia kwa sauti ya juu. Naya akakimbilia simu yake aliyokuwa ameweka chini ya mfuka wa chips, akatoa sauti ndio akasoma ujumbe. Pesa imeisha kwenye simu.’ Ilikuwa namba ya baba yake, lakini akajua aliyeandika ujumbe ni mama yake. Poleni kwa matatizo mama. Nimeelewa kabisa. Na mimi nahangaika. Nikifanikiwa nitawajulisha. Nawaombea mfanikiwe.’ Naya akajibu hivyo huo ujumbe. Hapakuwa na ujumbe mwingine. Mara kwa mara Naya alirudisha macho kwenye simu yake kuona kama mama yake amejibu huku tamthilia ikiendelea, alipoona kimya kwa muda, akakata tamaa. Akajua na baba yake pia atakuwa ameishiwa pesa kwenye simu yake. Akaiweka chini ile simu taratibu, nakujirudisha kichwa kwenye kochi kama kuegemea. Alijaribu kurudisha mawazo pale kwenye tamthilia, lakini akagundua tamthilia yenyewe ilishakwenda mbali. Ameshapitwa na mengi. Akaona aachane na siku hiyo, atafuatilia marudio.

Taratibu tena kama anayetembea kwa kunyata, akamsogelea mmoja wa anayekaa naye chumbani, akamnong’oneza kitu, kisha akapotelea chumbani. Akala taratibu juu ya kitanda chake huku akifikiria itakuaje. Akili zikawa zimeshavurugika hakuna aliloweza kuwaza tena. Muda wakulipa ada sio tu kuwa ulifika, ni kwamba ulishapita na bado hajaweza kupata ada ya shule ila alilipia tayari hapo hosteli. Akafikiria bila jibu mwishoe akaamua alale tu, kwa ajili ya kesho yake shule.

 ~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

Wiki nyingine ya shule ikaanza ambayo alijua itamgharimu pesa ya daladala na kununua chakula chake. Kwa kuwa alilipwa, akajiwekea bajeti. Juma likaanza taratibu kukiwa na tatizo ambalo bado hakuna suluhu. Nusu ada ambayo hakuwa amemaliza na michango baadhi ya shule. Na ilikuwa lazima kulipia ili kuweza kufanya mitihani yake ya mwisho ya kidato cha nne. Swali ni watapataje hiyo pesa na walishakopa wote wanaowafahamu wana uwezo, tena kwa kurudia rudia bila yakulipa!

Ilipofika ijumaa akapata ujumbe akiwa shuleni kuwa wanaofanya ile kazi ya waitress wanatakiwa wakutane kwenye baa moja iliyokuwepo Masaki, mtumaji alikuwa Tula. Mmoja wa wasichana wa Girls Star. Akafikiria, akaamua kumpigia simu yule rafiki aliyemuunganisha nao, ambaye naye pia ni rafiki ya Tula, Lulu na Tunu. Hawa ambao ndio hao wanajiita Girls Star. Akamwambia na yeye amepata ujumbe na atakwenda. “Kwenye wengi kuna mengi Naya. Mimi nakwenda. Huwezi kujua tunaweza kupata dili za kikubwa.” “Basi na mimi nitakuja. Nivaeje?” “Pendeza lakini usivae zile sare. Umesikia? Ni kukutana tu sisi kama sisi, sio kazi. Pendeza.” “Sawa, nimeelewa.” Wakaagana.

 Jumamosi!

N

aya aliamka na kwenda kujisomea na wenzake kama kawaida. Hiyo ilikuwa ni baada ya kufua nguo zake. Mchana akarudi hosteli akakuta walewale wasichana anaofanya nao kazi, Girls Star, wanapilika pilika. Kelele, wajuaji ndio wao, wanajiandaa kwa kutoka. Ukweli walikuwa ni wadada wa mjini na wanajua kupendeza. Ujuaji ni kweli wanajua mambo mengi. Huwezi kumlinganisha na Naya mtoto wa kanisani. Pesa inatumiwa kwa mahesabu. Wao wakitoka kazini, ujue kitanunuliwa kiatu kipya, au pochi au gauni la maana. Na hapo wanakuwa wamepata na bwana wa maana. Sasa safari hii wakawa wamekuja na neno la , ‘ATM za Moro’. Wakigonga wanasema, ‘zinatoa kama hazina akili nzuri’. Kila mtu akajua kuwa hao Girls Star kama walivyozoea kujiita wenyewe, wamepata wanaume wa Morogoro.

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

“Kwani wewe mdogo wangu huko unapoenda na wenzio hao wanaume hawakuoni?” Naya akaanza kucheka. “Dada Wahija wewe!” “Kweli tena. Maana nakuona mwenzangu unalia shida kila siku wakati wenzio wana neema!” “Wale hawaendi kufanya kazi moja da Wahija! Wanapelekwa na mengi.” Mwingine akadakia. “Basi Naya mdogo wangu na wewe pelekwa japo na mawili tu, loh!” Naya alizidi kucheka. “Maana una kazi yakutufanya kioo kila ukienda! Tunakusifia wee, hata soda huleti! Kila ukirudi, ‘Da Wahija nipo hoi! Anayenipenda aniletee maji ya kuoga’. Basi kazi yetu sisi inabaki hiyo tu, matunda hatuyaoni.” “Kama ni soda tu, usijali dada yangu. Wewe kazana kuchota maji.” “Basi maneno yake ndio hayo! Yakitapeli tapeli!” Naya akazidi kucheka huku akijiandaa.

Mlango ukafunguliwa bila hodi. “Sasa Naya?” “Ndio namalizia kujiandaa.” Naya akajibu taratibu. “Changamka upate lifti!” “We Tula hebu njoo.” “Da Wahija sikuwa nimekuona dada yangu, mbona ningekusalimia tu! Shikamoo dada yangu.” Tula akajihami kwa haraka na kutoka haraka kama anayemkimbia Wahija. “Naya uwahi, tunakusubiri, usafiri upo njiani.” Walimsikia akiongea huku anakimbia huko nje.  Naya akajiweka sawa. Wahija ndiye aliyekuwa akimsaidia kumpaka wanja wakati wote. Akaanza kumtengeneza macho. “Usinikoleze sana da Wahija bwana!” “Umeanza Naya. Kama unaweza si ujipake mwenyewe?” “Basi dada yangu. Kiasi. Nisije nikatokea huko, nikawa mimi kituko!” “Na ulivyojibana hivyo! Kila mtu atakuwa anakumezea mate.” Naya akazidi kucheka.  

“Na urudi japo na zawadi Naya mdogo wangu, sio unarudi na matatizo tu kila siku! Kuchoka, kusumbuliwa kazini, hujalipwa vizuri wakati kazi ilikuwa kubwa, hatutaki! Njoo na hata paja la kuku.” “Dada Wahija naye! Paja tu!? Mimi nilijua unataka kuku mzima?” Wote waliokuwa wakiwasikiliza pale chumbani wakacheka. “Muone! Maneno mengi, hata mguu wa kuku huleti! Tulia nisikuharibu.”

Zikaanza hodi anauliziwa Naya. “Mbona leo ni kama hamuwezi kuondoka humu bila Naya!?” Wahija akawashtukia. “Maana siku nyingine mnafanya kumwitia mlangoni na maneno yenu ya kashfa. ‘We Naya tunakuacha sisi’. Lakini leo naona mnambembeleza mdogo wangu! Mnaenda kumuuza?” Wakaangaliana wale Girls Star, wakatoka na kumtia wasiwasi Wahija.

“Mmmh!” Akaguna Wahija. “Nini dada?” “Hawa watoto mimi nawajua. Wanachokung’ang’ania leo ni nini!? Walikwambia mnaenda wapi tena?” “Nilikuonyesha ujumbe da Wahija! Ukasema niende nikajichanganye. Umenitia shuguli yakujitayarisha, halafu sasa hivi unataka nibaki tena! Sibaki. Lazima niende.” “Wewe nenda lakini akili kichwani. Hawakawii kukuuza hawa.” Naya akacheka. Akasimama mbele ya kioo. “Au nimejibana sana dada? Niambie ukweli.” “Kujibana umejibana, ila umependeza. Si umesikia biashara matangazo?” Naya akacheka na kutoka. “Ulete zawadi, sio tunakuwa na kazi ya kukupamba tu na kukusifia!” “Nitakuletea dada yangu.” Naya akaondoka.

Alikwenda chumbani kwao, hakuwakuta. Akaamua kutoka akiwa na wasiwasi kuwa ameachwa. Alipotoka akakutana na gari nzuri sana imesimama nje ya geti. Akaanza kujiuliza kama wapo humo ndani! Akasita kusogea, akabaki amesimama anajifikiria. Tula akashusha kioo ndani ya hiyo gari, na kumwita kiustarabu kama sio Tula. Naya akajivuta mpaka kwenye gari akawa anajiuliza akae wapi! “Kaa mbele.” Naya akamtizama Tula kwa mshangao. Gari ilikuwa giza ndani na hata vioo vyake vilikuwa havionyeshi ndani. Hakujua nani ni dereva, nani amekaa nyuma na mbele. “Mimi nataka kukaa nyuma Tula. Kwa nini wewe usikae mbele?” “Naya naye?” Tula akashuka kwa kulalamika, Naya akacheka. Wakapishana. Tula akakaa mbele, Naya nyuma.

 Aliwakuta wale wasichana wa Girls Star wamekaa pale alipokuwa ameingia, wakawa watatu. Tula mbele na dereva. Ukimya mzito. Naya akajua amewaudhi kwa kuwachelewesha kama kawaida yake siku zote kuchelewa wanapokuwa wakitoka. Sema safari hii hawakuwa wanachangia taksii. Ilikuwa gari ya maana. Akajua ndio mmoja wa hao wanaume wa Moro.

Wanapokuwa wanaenda kwenye kazi yao, kwa kuwa wanakuwa wamependeza, huwa wanachukua Uber au taksii. Wanachangia ndio wanakwenda. Sasa safari hii ilikuwa gari nzuri, safi. “Samahanini nimechelewa.” Naya akavunja ukimya. “Kama kawaida yako.” Wote wakajibu kwa pamoja mpaka Tula aliyekaa kiti cha mbele. Naya akacheka kwa kusikitika. “Haya bwana. Lakini nimeomba msamaha.” Safari ikaendelea. Kimya kwa Naya aliyeanza kutumia simu yake, Girls Star wakaanza stori. Viwanja gani walishakwenda. Wapi wanapenda. Wapi wanapanga kurudi. Ikawa ni wao tu humo ndani ya gari mpaka wakafika sehemu hiyo waliyoambiwa wanakutana.

Kweli walikuta wenzao na baadhi ya sura ambazo aliweza kuzitambua japo si kwa majina, ila sura. Wakaunganisha meza. Stori na vicheko vikaanza. Vijana hao watanashati, wamezungukwa na warembo wa jiji la Dar. Ni kweli walipendeza. Kulisha tolewa ruksa ya kuagizwa chochote wanachotaka warembo hao. Naya akachekelea moyoni. “Na nilivyo na njaa!” Akanong’ona Naya pembeni ya Hawa, aliyemuunganisha na Madamu Vane. “Si umeona bora umekuja?” Naya akacheka.

Vinywaji vikaletwa. Naya aliagiza soda anayopenda Sprite. Wapo waliogiza pombe. Kwa kuwa walikuwa wengi, hakujua nani amegiza nini. Baada ya muda meza ikajaa vyakula na vinywaji. Naya asiyejua mengi akainamia sahani yake akaanza kula, mara simu yake ikaanza kuita. Alipoangalia, akashtuka mpaka walio karibu yake wakamuona.

Akasimama kwa haraka kama anayekimbilia mbali na pale kwenye kelele. Akaenda kuzungumza na hiyo simu nyuma kabisa ya magari. Hakukaa muda mrefu, akarudi na kuvuta kiti pembeni ya Hawa pale alipokuwa amekaa,  akaanza kumnong’oneza. “Mimi lazima niondoke sasa hivi, Hawa.” “Naya naye!” “Kitu muhimu mpenzi wangu, wala nisingeondoka.” “Unauhakika huwezi kusubiri hata kidogo?” “Dili na muda. Mbona kama unasahau Hawa?” Hawa akacheka. “Basi muombe muhudumu akufungie chakula chako.” “Hayo mawazo. Nitakuwa nakula huko njiani.” “Sasa tena sio utie aibu Naya! Umependeza bwana, sio kuanza kushindana na mifupa barabarani, tutakosa shemeji wa maana!” Naya akacheka sana mpaka akainama.

“Kujitia unanjaa kama upo jangwani!” Hawa akaweka msisitizo maana na mwenyewe alikuwa wa viwango haswa. “Basi usijali, siwezi kukuangusha. Utaniagia hao warembo.” “Pombe zimeshaanza kuingia kichwani hapo, tutakesha.” Naya akacheka na kuondoka na sahani yake ya chakula kuelekea jikoni.

Akamuomba muhudumu amfungie. Wakati anasubiri, akamsogelea mmoja wa wale vijana waliokuwa wote mezani. Yeye ndio alikuwa amekwenda kuwachukua pale hosteli. Naya akampa tabasamu la kiuungwana, akijua na yeye anataka kuagiza kitu, akampisha. “Nimesikia ukiaga. Kwema?” “Kwema kabisa.” Naya akajibu kiustarabu akajisogeza pembeni zaidi akimpisha ili aweze kuzungumza na watu wa jikoni. Yule kijana akacheka kiustarabu huku akimtizama Naya. “Vipi?” Naya akauliza. “Labda niulize kama utarudi.” “Hapa?” “Ndiyo Naya. Nauliza kama utarudi tena.” “Hapana. Kwa leo sitaweza kurudi tena.” Naya akabaki akimtizama kama anamshangaa kidogo.

“Unaelekea wapi?” Naya akabaki amekodoa macho akimshangaa kama anayemuhoji ‘kwa nini uniulize!’. “Kama hutajali lakini.” Bado Naya akabaki anamtizama. “Maana na mimi natoka. Naweza kukusogeza.” “Aaaah! Wala usijali. Mimi nitachukua usafiri hapo nje.” “Na mimi nina usafiri, ndio nakupa wazo la kutumia usafiri wangu.” Naya akacheka. “Nina mizunguka mingi ndio maana naona lifti yako haitanifaa.” “Unataka kuanzia wapi? Naweza kuwa dereva wako leo.” Naya akacheka tena kama anayesita. “Na malipo ni nini?” “Sio kila kitu ni sababu ya kulipwa, Naya. Wakati mwingine ni wema tu.” Naya akacheka kama hamsaidiki. “Haya bwana. Nashukuru.” “Shukurani hiyo ni kwamba umekubali niwe dereva wako?” “Nilikwambia nina mizunguko mingi?” “Nakumbuka.” “Sasa huhisi nitakuchosha?” “Hata kidogo.” Naya akatabasamu huku akimwangalia kutaka uhakika.

“Mimi sina neno, twende tu. Labda kama huko unakokwenda hutaki uonekane na mimi.” “Sehemu ya kwanza haina shida, ila ya pili ndio hutakiwi kuonekanika.” Naya alijibu huku akicheka. “Basi nitaishia njiani, sitafika sehemu ya pili.” Akarudishiwa chakula chake kikiwa kimewekwa kwenye boksi maalumu kwa chakula. Akapokea, akashukuru na kurudisha macho yake kwa yule kijana. Macho yakagongana. Akajikuta anacheka. “Mimi nipo tayari.” “Una uhakika!?” Naya akauliza. “Kwa nini unawasiwasi?” “Kwa sababu najua umekuja na watu hapa. Sitaki wafikirie kama mimi nimewaibia mgeni wao. Sijui kama unanielewa?” “Kwamba unaniiba?” Naya akacheka ila yule kijana akabaki akimtizama.

“Bwana mimi najua umenielewa. Sitaki kina Tula wanichukie kwa kukuchukua hapa! Au kuondoka na wewe wakati ni lifti tu!” “Oooh! Kwamba unafikiri mimi ni bwana wa Tula, sasa hutaki akufikirie umemchukulia mwanaume wake?” Naya akakunja uso na tabasamu. “Yeah! Kitu kama hicho ila umeiweka kwa uwazi sana!” Akacheka.

“Basi ngoja nikutoe wasiwasi. Mimi sio mtu wa Tula.” “Na wale warembo wengine pale unamakubaliano nao gani?” Naya akauliza, akabaki akimtizama. “Nataka uhakika tu. Unajua tunaishi pale hosteli pamoja na wote wale tunafanya kazi mara nyingi pamoja. Tupo tofauti, lakini kuna mambo tumejiwekea, hakuna kuvuka mipaka.” “Yaani hamchukuliani mabwana?”   “Wewe ni muwazi mpaka shida!” Naya akaongeza kwa kulalamika. Akacheka. “Lakini si ndio hivyo unavyomaanisha?” Akamuuliza tena. “Ndiyo na  sitaki mimi ndio nionekane mwizi.” “Basi, usiwe na wasiwasi. Mimi sio bwana wa mtu yeyote na wala sina makubaliano na yeyote. Nimekuja na wenzangu kuburudika tu. Nipo huru kukaa au kuondoka muda na wakati wowote.” Naya akamtizama kama anasita.

“Bado hujaridhika tu?” Akamuuliza Naya aliyeonekana bado anawasiwasi. “Lakini si nilazima ukaage?” “Ukikubali nikusindikize, na ukaniahidi utanisubiri, hutanikimbia kama siku ile uliponitoa pale hostelini kwenu na kuniacha kwenye kibanda cha chips, basi, nitarudi kuaga.” Naya akashangaa sana. “Umesahau au ndio umekumbuka?” “Nilikuacha wapi!?” “Subiri kwanza. Tuanze taratibu. Umekubali nikusindikize na unaahidi kunisubiri wakati naaga wenzangu?” Bado Naya alikuwa na mshangao, amebaki akimwangalia. “Naya? Au ulipanga unikimbie au ulifikiri nakutania kuwa nataka niwe dereva wako leo?” “Nimekubali uwe dereva wangu.” Naya akajibu hivyo huku akitaka kucheka. “Nakusikiliza Naya.” “Na nitakusubiri, ukaage.” “Naomba nikukute hapahapa tafadhali.” Naya akacheka na kujibu, “Sawa.” Akaondoka na kumuacha Naya amesimama akicheka taratibu. 

Naya & Malon. 

B

aada ya muda mfupi sana akarudi. “Nilijua ungenitoroka tena.” “Bwana mimi sijawahi kukukimbia!” Akamgeukia kwa macho yakumsuta. Naya akacheka. “Twende.” Wakaongozana mpaka kwenye gari. “Lini nilikukimbia!?” Naya akauliza mara alipopanda kwenye gari na kufunga mkanda. “Unajua Naya, miaka ya zamani, nilikuwa nikidharaulika sana. Namaanisha watu walikuwa wakinipita bila salamu au hata wakizungumza na mimi, walikuwa wakizungumza na mimi kama takataka tu. Nikahangaika sana mpaka nikafanikiwa kurudisha heshima. Watu wakaanza kuniheshimu na kunitafuta kwa hali na mali. Ili tu kuniona au hata kupata bahati ya kuwa karibu na mimi.” Naya akatabasamu.

“Kwa nini nakwambia hivi? Sio kujisifia kwako, ila kwa vile nilivyoshangazwa. Nilikuwa nikimwambia Chezo, ni rafiki yangu. Sikumbuki kwa muda mrefu sana, kupuuzwa au kudharauliwa kama ulivyonifanyia wewe.” Naya akashtuka sana. “Kwa nini unasema hivyo!?”  Naya akajua sio utani tena. “Kwanza niambie sehemu ya kwanza ambayo naruhusiwa kwenda ni wapi.” “Naomba turudi hosteli tafadhali.” Naya akawa amepooza kidogo.

“Nikuulize kitu Naya?” Naya kimya akimtizama. “Nilijitambulisha kwako. Unakumbuka hata jina langu?” Naya akababaika sana. Hakuwa hata akikumbuka ni wapi alijitambulisha. Sasa aseme hakumbuki jina au hakumbuki ni wapi alipojitambulisha! Akababaika kidogo, akatulia kwa kuwa alishasema amemdharau. “Lakini nataka ujue mimi sina dharau.” “Unakumbuka jina langu, Naya?” Akamuuliza taratibu tu. “Hapana.” Naya alijibu kwa upole. “Unakumbuka mara ya kwanza ni wapi uliniona?” Naya akafikiria kwa muda kidogo akijaribu kuvuta kumbukumbu. Akanyanyua kichwa akamtizama. Alikuwa ametulia akiwa anaendesha. Akashindwa kukumbuka kabisa.

“Nafikiri kwenye moja ya tafrija nilizokuwa nikihudumia.” “Lakini hukumbuki hata ni ipi?” “Samahani. Wanakuwa watu wengi na tunakuwa na hekaheka akili hazitulii. Halafu unajua watu tunakuwa tukiwahudumia mara nyingi ni watu wanaokuwa na hadhi fulani hivi. Kwa hiyo hata unapokuwa katikati yao unakuwa na hofu. Inakuwa ngumu kupeleka mawazo mbali na kile wanachotaka ufanye kwa wakati ule. Sijui kama umenielewa?” Naya akajaribu kujitetea.

“Lakini wenzako wote wananikumbuka Naya!” “Mimi ni mgeni. Sio mzoefu kama wao. Wengine wamefanya kazi ile tokea ile kampuni inaanza. Wana uzoefu. Mimi bado najifunza. Kwa hiyo najitahidi ili nisiharibu. Nikiwa pale najitahidi akili iwe kazini tu. Samahani sana kama kuna jinsi nilikufanyia ikaonekana kama nimekudharau.”

“Nilikufuata hosteli kesho yake. Unakumbuka?” Ndio akili zikamjia Naya. Akakumbuka. Akafunga macho nakujirudisha nyuma ya kiti. “Ulinikaribisha na kutaka nikae kwenye makochi niwasubirie kina Tula, wewe unakwenda kutafuta chakula. Hapo hukuwa hata umenisikiliza. Nilikwambia nina njaa naomba tuongozane. Ukasita kidogo huku ukitoa sababu ya sehemu unayokwenda kula ni duni. Nikakwambia sitajali. Tukaongozana. Lakini hukuwa hata ukijua kama nipo nyuma yako au pembeni yako! Ukaenda kujitafutia sehemu ya kukaa baada ya kusalimiana na wahudumu wa pale, ukajiagizia chakula chako, ukatafuta sehemu ya kukaa, ukaenda kukaa.” Naya akaanza kurudisha mawazo taratibu huku akisikiliza shutuma zake.

“Nikajua wazi umenipuuza. Lakini nikajikaza kiume, nikakufuata pale ulipokuwa umekaa. Ukaanza kuwa busy na simu yako. Nikajipendekeza tena kukuonyesha na mimi nipo. Nikashauri tuagize vinywaji wakati ukisubiria chakula chako. Pia ukanipuuza vibaya sana. Ukaletewa chakula chako, ukaondoka bila hata kuniaga! Nikabaki nimepigwa na butwaa nisiamini. Pia nikajikaza tena kiume. Nikajua utakuwa ndani ukiangalia tamthilia uliyosema huwa mnafuatilia pale. Nikarudi ndani. Nikakaa pale zaidi ya dakika 15. Ndipo ukaingia. Nikamshukuru Mungu ulikaa pembeni ya kochi nililokuwa nimekalia. Ukajiegemeza karibu kabisa na magoti yangu. Nikajifariji kuwa pengine umenikumbuka.” Akacheka kwa kujidharau.

“Ukaanza kutumia simu yako. Kusoma jumbe na kujibu. Baada ya muda ukaondoka tena, bila hata kuniaga! Nimekaa juma zima nikiwaza. Chezo akajua wazi lipo tatizo. Aliponiuliza, nikamuelezea kisa kizima. Akasema kwa sababu Tula alimpigia na kumkaribisha huku, lakini alikuwa amemkatalia. Basi ampigie tena simu amkubalie kutoka, ila akuulizie na wewe. Akanishauri turudi tena, nijaribu bahati yangu.” Naya akawa bado anashangaa. Hakuwa hata na habari na yote hayo.

“Nimekuja kuwafuata hosteli, ukawa bado haupo tayari. Wakina Tula wakataka niondoke tukuache utakuja na taksii. Lakini nikawaomba tukusubiri na wakiache kiti cha mbele kwa ajili yako. Ukaja ukiwa hutaki kukaa kiti cha mbele. Tula akakupisha, ukaingia. Uliniona Naya, lakini hata hukunisalimia! Tumefika pale baa, nakuvutia kiti, ukapita kama hujaniona! Ukaenda kukaa na Hawa.”  Naya akazidi kushangaa.

“Nilijua unamvutia kiti Tula! Sikuwa hata nikijua kama ni mimi! Samahani sana.” “Ukakaa na Hawa. Na kunipuuza kabisa. Chezo akanitumia ujumbe labda nikuite pembeni nijitambulishe tena. Nikashangaa umeondoka na kwenda kuzungumza na simu. Ukarudi na kumuaga Hawa tu. Kuwa unaondoka. Yaani mimi nimekusikia kwa kuwa nilikuwa nikikuangalia na kukusikiliza muda wote. Ndio nikajua unaondoka! Ndio ikabidi nijikaze tena, nikufuate.” Naya akawa amepigwa na butwaa.

Akamgeukia. “Naomba kwanza unisamehe. Yaani hapa ndio kama unanifungua macho! Hakika nilikuwa sina hata habari! Nilichojua ni kwamba nyinyi ni watu wa kina Tula. Yaani kina Girls star, wamepata kazi mpya, ndio maana na mimi nikaja ili kula asali. Lakini nilijua wazi nyinyi ni watu wa kina Girls Star kama walivyokuwa wametuambia pale hosteli!” “Tula hakukwambia kuwa nakusubiria nje?” “Mungu ni shahidi kaka yangu. Alichosema, wananisubiria nje, nifanye haraka. Tena nilijua tunapanda taksii kama siku zote. Sasa kuja kukuta hii gari pale, kweli nilibabaika. Sasa Tula aliponiita, nikajua ni gari ya mmoja wa mabwana zao. Nikaogopa kukaa mbele ili tusije kuanza ugomvi baadaye. Lakini sikuwa na hila au kukudharau.” “Hata salamu Naya!” Akamuuliza kwa mshangao.

“Mimi ni msichana. Najua mambo ya wasichana linapokuja swala la kuchukuliana wanaume! Sio ugomvi unaotaka kushuhudia. Halafu kwa kuwa walishawatangaza kwamba mnakuja kwa ajili yao, nikajua mpo au upo pale kwa ajili yao.” “Na siku ile ya chips je?” “Niamini sikukufanyia makusudi. Nafikiri ulinikuta nikiwa katikati ya mazungumza yaliyokuwa yameshanichanganya akili. Halafu nilipokuona pale, nilikumbuka sura kama nilikuona mahali. Na vile ulivyokuwa umependeza, nikajua ni kwenye moja ya shuguli za matajiri. Nikaunganisha na kauli za kina Girls star, nikajua nilazima upo pale tu kwa ajili yao.” “Kauli gani?” “Naomba nisikwambie ni mambo ya pale hosteli tu. Lakini sikudhania hata kama ulikuwa pale kwa ajili yangu!” Akafikiria kidogo nakushindwa kuamini.

“Daah! Naomba unisamehe. Sijui hata ilikuwaje siku ile nikakuacha! Nafikiri nilijua uliamua kubaki uwasubirie kina Tula! Wala sikujua kama..” Naya akasika kama anayejaribu kuvuta kumbukumbu. Wakawa wameshafika pale hosteli.  “Naomba unisamehe sana. Ila niamini sikukusudia kukudharau. Kuna sehemu ambayo nataka kuwahi kabla ya saa tatu na nusu. Lazima nikabadili nguo kisha niende. Ni sawa nikikutafuta wakati mwingine?” “Unanitafutaje wakati hata jina langu hulifahamu, Naya?” “Kama ungekubali nikutafute, ningekuomba namba yako ya simu na jina lako.” Akaonekana ameridhika.

“Nakuahidi kukutafuta. Safari hii nitakutafuta mimi.” “Naitwa Malon, au..” “Malo.” Naya akamalizia kama aliyekumbuka. Malo akacheka. “Sasa hivi nimekumbuka hilo jina. Na nilikumbuka kukupeleka sehemu vyoo vilipokuwepo siku ile.” “Umekumbuka eeh!” Naya akacheka. “Pole na samahani sana. Huwa tunafanya kazi kwenye mazingira ambayo sio tulivu kwetu au labda ni mimi tu!” “Nilikuona.” Naya akacheka.  

“Naomba nikuage kwa sasa, nikutafute wakati mwingine ili nisichelewe.” “Huko ambako sitakiwa mimi kufika?” Malo akauliza kwa uchokozi. Naya akacheka. “Ndiyo.” Malo akabaki akimtizama. “Ni kanisani Malo.” “Na mimi pia ni mkristo Naya.” “Naomba tusiuongozane.” “Kwani mimi siruhusiwi kufika kanisani?” “Unaruhusiwa. Lakini mimi siendi kanisani kama kusali. Naenda kwenye nyumba ya mchungaji pale pale kanisani. Kuna mzigo naenda kufuata. Sasa nikitokezea na wewe, nitaibua maswali mengi na mzigo wenyewe naweza nisipate wakati nilikuwa au tulikuwa tukiusubiria sana.” “Wewe na nani?” Naya akainama. “Wazazi wangu.” Akajibu kwa unyonge.

“Sio lazima tukaingia wote. Naweza kukushusha nje au mbali kidogo ukaingia peke yako, ukitoka nitakurudisha hapa.” “Haitakuwa usiku sana kwako?” “Hata kidogo. Nipo sawa tu. Twende nikusindikize.” “Nakushukuru sana. Na samahani.” “Nenda kabadili nguo kwanza. Naamini tutapata muda wa mazungumzo.” Naya akashuka kwa haraka kurudi chumbani kwao akamuona anakimbia mpaka akamshangaza Malon.

Alifika na kumpa Wahija kile chakula alichokuwa amebeba. “Hapa sawa. Sasa mbona mbio mbio?” “Naenda nyumbani kwa mchungaji. Natakiwa kufika hapo kabla ya saa tatu na nusu.” Alichofanya Naya ni kutoa nguo  aliyokuwa amevaa iliyokuwa imembana haswa. Akarushia kitandani na kutoa gauni jingine refu mpaka chini na mikono mpaka karibu na viwiko. Akapunguza vipodozi usoni na kubana nywele nyuma tu, akatoka kwa haraka.

Akaingia ndani ya gari na kufunga mlango. Naya alikuwa amebadilika kabisa. Alikuwa msichana wa heshima zaidi. “Nakushukuru sana. Naona itanisaidia kuwahi. Muda umekwenda kweli! Nahofia kumchelewa.” “Si umesema yupo nyumbani kwake?” “Lakini wamemwambia baba iwe kabla ya saa tatu na nusu. Ikizidi hapo wanafunga milango, wanalala.” Malon akanyamaza.

Walifika Kimara, Naya akamuelekeza lilipo kanisa lao. Malo akajitahidi kuongeza mwendo. Ilishakuwa ni saa tatu na dakika 25. Akasimamisha gari kituoni. “Ngoja nikimbie.” “Sio mbali na hapa?” “Nikikimbia nitafika kabla ya muda au tatu na nusu kamili.” Akashuka kwa haraka, akamuona anakimbia haswa kama anayekimbizwa, Malo asielewe.

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~ 

Alifika kwenye mlango mkubwa ndio ilikuwa inatimia saa tatu na nusu. Naya alikuwa akihema kwa kukimbia. Akaanza kugonga huku akihema kwa kasi. Akafunguliwa na mama mchungaji. “Nilimwambia kabisa baba yako uje kabla ya saa tatu na nusu.” “Samahani.” “Ingia. Mchungaji anakusubiria ndani.” “Asante.” Naya akashukuru kinyenyekevu sana. Akaingia. Alimkuta mchungaji sebuleni. Yakaanza mazungumzo. Ukaanza wosia. Akakumbushwa madeni ya baba yake yote. Akaelezwa vile wazazi wake walivyoanza kukopa hapo tokea zamani na ulipaji wake umekuwa wa shida lakini wamevumiliwa. Akaelezwa jinsi wazazi wake wanavyohangaika kwa hiyo lazima hiyo pesa awe nayo muangalifu. Wosia wa muda mrefu ukaendelea ndio akapewa hiyo pesa. Hakujibu kitu zaidi yakusema asante na kunyanyuka. Alikuwa ameshakasirika karibu ya kulia.

Hakupenda vile alivyorudia rudia kutaja madeni ya wazazi wake. Aliona ni kama kumdhalilisha baba yake. Na kwa kuwa walikuwa wakikopa kwao, akawa kama kumdhalilisha wala sio kumuhusia. Naya alichukia kabisa ile hali, lakini hakuwa na jinsi. 

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

Alitoka pale na kurudi alikokuwa amemuacha Malon. Akapanda kwenye gari. Uso aliorudi nao, Malon akajua mambo hayakwenda vizuri, japo alikuwa na bahasha mkononi. Akatulia kwa muda huku akishindana na machozi yake, kisha akajikaza kushukuru. “Asante kunisindikiza.” “Karibu.” Malo akatulia kidogo, Naya akainama huku akizungusha ile bahasha mkononi.

Malo alimtizama kwa muda, akaamua kuvunja ukimya. “Unajua pale sikuwa nimemaliza chakula changu?” “Pole Malon. Unataka nikusindikize ukatafute chakula? Safari hii sitakuacha.” Wakacheka. “Nitashukuru. Kuna mahali unataka twende?” Naya akafikiria kidogo. “Huwa unakula chips vumbi?” “Sana tu.” Malo akajibu. Naya akamtizama kama asiyeamini, kaka aliyependeza vile! “Huamini?” Naya akacheka. “Umechoka?” Naya akauliza kwa kujali. “Hata kidogo. Wewe twende kokote unakotaka.” “Basi twende Fire.” “Sawa mama.” Kidogo Naya akachangamka.

Walifika Fire, Naya akamuelekeza sehemu yakuegesha. “Naomba mimi nikununulie chakula kama kukuomba msamaha wa kukutelekeza siku ile. Niambie unachotaka kula, nitakwenda kukununulia, nikuletee hapa hapa.” “Kwa nini tusiende kula palepale? Naona kuna viti.” “Una uhakika? Maana kuna kelele na mbu.” “Basi twende wote tununue halafu tuje kula kwenye gari.” “Sawa.” Wakashuka.

Kila mtu aliagiza anachotaka. Malo akawahi kulipia yeye. Alinunua soda za kopo wakachukua chakula wakarudi garini. “Asante kwa chakula.” “Asante kushukuru. Nikuulize swali Naya?” Naya akaweka soda yake chini akamgeukia huku akitingisha kichwa kukubali.  “Unamchumba au boyfriend?” Naya alishtuka kidogo. Baada ya kuuma meno na kubabaika vyakutosha ikabidi kujibu maana Malo alionekana kutaka jibu. “Sijui niseme ndio au hapana!” Malo akakunja uso. “Nilikuwa naye. Au sijui ninaye! Lakini ni kama hatuko kwenye maelewano!” “Mmekubaliana nini?” Malo akauliza wakati anafungua chakula chake.

Naya akanyamaza kama hajui chakusema. “Naya?” “Mimi sijui Malo! Nimeshindwa kumuelewaga yule mtu. Nimeona niache tu.” “Umeachaje?” Naya akanyamaza. “Namaanisha mmefikia mwafaka gani?” “Hakujawahi kutokea mwafaka kati yetu. Wakati wote huwa tunaishia yeye akiwa ameshinda.” “Naona kama sipati jibu sahihi Naya!” “Kwa kuwa hata mimi sina jibu sahihi.” Malo akamtizama.

“Labda niulize, upo uwezekano mkarudiana?” “Sijui Malo.” “Kwani tatizo ni nini?” “Sijui niseme ni hatuendani! Hakuna kitu tunaweza kuzungumza na kuelewana! Ana wivu wakupitiliza na anapenda kutawala kila kitu changu mpaka muda na mawazo yangu!” “Labda kwa kuwa anakupenda.” “Yale sio mapenzi Malo. Mtu ukipendwa unajua. Ni mtu anayependa kutawala tu. ‘Control freak’. Sijui unanielewa?” Malon akabaki kimya akiendelea kula na kumsikiliza.

“Na kwa kuwa amesoma, ndio shida kabisa. Yaani sijui. Nimeamua nipumzike.” “Mpaka lini?” “Sijui Malon. Hata sielewi. Nina mambo mengi sana sasa hivi, na yeye hawezi kuongezeka kwenye matatizo yangu. Nimeshindwa. Labda miaka ya baadaye sana. Na wala sidhani. Ananiongezea matatizo badala ya kupunguza.” “Mlijaribu kuzungumza?” Naya akacheka.

“Mungu atujalie siku moja tuje kukutana naye na wewe ukiwepo. Ni shida!” “Kwa nini?” Malo akaendelea kudodosa taratibu. “Nakwambia ni control freak. Anataka kutawala kila kitu. Anajua kila kitu. Hamuwezi mkakaa chini mkazungumza, ila umsikilize yeye tu. Yaani hajajaliwa kusikiliza. Ukianza sentensi, yeye anamalizia. Na kuongeza anachokitaka yeye. Anaweza akapanga mipango ya pamoja, bila kujali mfuko wangu. Labda atataka mkutane sehemu. Muda anaotaka yeye. Na upendeze. Na ujue ukifika huko, baadhi ya gharama inakuwa juu yako. Halafu mkali. Hajui kubembeleza.” Malo akacheka.

“Usicheke Malo!” “Wewe unataka kubembelezwa?” “Hata kidogo jamani! Sasa wakati wote anataka mambo yaende unavyotaka yeye! Na yasipokwenda hivyo, hasira na kugomba juu! Nimechoka.” “Akiomba mrudiane?” Naya akacheka sana. “Hathubutu! Jeuri huyo. Kwanza anahisi mimi ndio nitamrudia na kumbembeleza.” “Kwa hiyo utamrudia?” Malon akaendelea kudadisi taratibu huku akila. “Malo una maswali kama polisi! Tuachane na Ino, hatuwezi kumaliza habari zake.” “Kwa nini?” “Ni wale watu waliojaliwa vipaji zaidi ya kimoja. Na ni miongoni mwa wale watu walijaliwa akili nyingi. Hapa ninapokwambia ni kijana tu, lakini ameajiriwa, amepewa mpaka gari. Analipwa mamilioni ya pesa. Hapo kanisani anatumia vyombo vya mziki zaidi ya kimoja. Nikisema kutumia, namaanisha kifasaha. Baba yake alifariki miaka mitatu iliyopita, ndiye aliyekuwa mwanzilishi wa hilo kanisa. Kwa hiyo lipo chini yake na mama yake. Ni kiongozi wa kila kitu hapo kanisani. Anajua kila kitu. Anaabudiwa na kila mtu, kwa kuwa ni kijana mwenye maadili ya kimungu. Namaanisha ni kijana aliyetulia kanisani, msomi, au tuseme anaakili sana, vipaji vingi, anapesa na nikijana ambaye hana muonekano mbaya. Mwanaume ambaye uthamani wake unaongezwa na hizo sifa nilizokutajia. Kwa hiyo kila jicho linamtizama yeye, na yeye anajua.” Naya akacheka.

“Akaanza na mimi. Utongozaji wake ni kama anakusaidia. Akawaambia wazazi wangu. Baba na mama, mama ikawa ni kama amezawadiwa ulimwengu. Kuwa nikimaliza shule, anioe, kwa hiyo nitulie. Tukaanza. Mama yake akijua mimi ndio mkwe, kwa hiyo na ukaribu ukaongezeka kwa wazazi wangu. Lakini Malo, mimi nimeshindwa.” “Umewaambia wazazi?” “Nilimwambia mama. Lakini mama anataka niwe mvumilivu. Anasema kila mtu anakasoro zake na mambo mengi akimtetea. Nikimwambia matatizo ya Ino, anasema mimi ndio nina matatizo, natakiwa kuwa mvumilivu, na natakiwa nikue. Kwa kifupi hakuna anayenielewa nawezaje kukataa bahati ya kuwa na Ino!” “Ikawaje, uliendelea kumvumilia?” Malon akaendelea kudodosa.

“Aaah! Shida tu. Kwanza hakwepeki kwa kuwa tumekuwa kwenye mazingira ya pamoja, hapo kanisani. Yaani wote sisi ni watoto wa hapo kanisani. Lakini nilipolemewa, ikabidi tu kumwambia mama. Muda tu, nilimwambia mama. Mama akaendelea kunihimiza nimvumilie. Nilipoonyesha msimamo wangu wa wazi kuwa simtaki na nikamwambia hata yeye mwenyewe, naona ni kama akaona nataka kumdhalilisha. Akaanza kunizulia vitu vya uongo uongo hapo kanisani ili nionekane mimi ndio nina tatizo, kwa hiyo yeye sasa ndio hawezi kuwa na mimi. Watu wakaanza kuniangalia kwa jicho la pili.” “Alisema nini?”  

“Ujinga tu. Akiongelea uhuru nilio nao sasa hivi wa kuishi hosteli bila uangalizi wa wazazi. Hana kitu kibaya anachoweza kunisingizia nimekifanya moja kwa moja, lakini anasema vitu vya ajabu. Ninavyofikiri alitumia akili baada ya kumwambia simtaki tena. Kwa sababu ya kiburi chake, alishindwa kujirudi kwangu na kuomba msamaha, ndipo akaanza kutangaza mimi nina matatizo, huku kwa siri akitaka tuendelee. Sasa hapo alifanya hivyo ili ikitokea nakataa kabisa, basi yeye ndio awe wakuonekana ameniacha sio mimi. Huku nikijua wazi ananihitaji niwepo kwenye maisha yake ila kiburi ndio kinamsumbua. Sasa anamtumia mama yake kumshawishi mama anilazimishe, mimi nisimwache, nije kuolewa naye.”  

“Sasa mama amekwambia nini tena?” “Ndio nimemkatalia. Mama anahisi Ino atakuwa mume mzuri kwa kuwa ni msomi, ametulia na anapesa bila kujali tabia zake ngumu. Mama hataki nije kuishi maisha ya dhiki au kuomba omba pesa na kukopa kama wao. Na anasema mwanaume aliyesoma ni tofauti na ambaye hajasoma. Anaamini mwanaume aliyesoma na anataaluma fulani, hawezi kufilisika au hatalala njaa. Lakini anasema biashara huwa zinakufa. Kwa kifupi kwa mama, Ino ni mume sahihi. Lakini mimi ninamwambia mama kuwa Ino sio mume wangu. Hata kama anataka niolewe na msomi, lakini sio Ino. Maana katika umri huu mdogo, hatujaona wala hajanichumbia, ananipa matatizo kama mimi ni mke wake!” “Kwani mlianza mahusiano lini?” Naya akafikiria kidogo.

“Kama nilivyokwambia, ni kama tulikulia kwenye hilo kanisa lao. Yaani baba yangu alikuwa mshirika hapo kwa miaka mingi sana. Kwa hiyo mimi na Ino tulikuwa pamoja. Niseme kwenye mazingira hayohayo ya kanisani. Kadiri tulivyokuwa tukiendelea kukua ndivyo tulivyokuwa karibu. Zaidi mimi. Kwahiyo tokea nakua ndiye mwanaume niliyekuwa naye karibu kwa kuwa muda mwingi alikuwa kanisani. Ni kijana aliyetulia kwa kweli. Namaanisha hana tamaa za wanawake. Aliniambiaga tokea zamani atanioa. Na sikuwahi kumuona wala haijawahi kusikika kuwa na msichana mwingine hata alipokuwa chuoni.” “Unajuaje?” Malon akauliza.

“Mtu muhuni anajulikana tu, Malon. Na njia ya muongo huwa ni fupi. Japokuwa alikuwa akisoma, lakini maisha yake mengi yalikuwa hapo kanisani ambako zamani kabla hawajajenga, ndio ilikuwa nyumbani kwao pia. Baba yake alikuja kujenga sehemu nyingine, pale wakaachia kanisa. Kwa hiyo ni mtu wa muda mrefu kwenye maisha yangu. Kila shule aliyosoma alikuwa akiwa anaishi nyumbani kwao. Muda mwingi anakuwa kanisani. Wasichana wengi walikuwa wakipita kwenye lile kanisa, na vijana wengi walikuwepo, wengine walipata kashfa, lakini sio Ino. Haikuwahi kutokea kashfa hata mara moja. Ni kijana mwenye maadili kweli kweli. Yaani ukimuona ni kama mkoloni. Hana masihara, kidogo kwangu ndio alikuwa angalau kuna mambo utamuona anafanya tofauti kwa wengine. Kwanza anaogopeka. Sio mtu wakumzoea kwa haraka.” “Labda utakuja kumzoea.” Malo akaendelea kumtaka Naya undani.  

Naya akaguna. “Hapana Malo. Picha ya mwanaume ninayemtaka awe kwenye maisha yangu, Ino siye. Anazo baadhi ya sifa, lakini anamapungufu makubwa sana ambayo yatanishinda au yatanifanya nisiwe na furaha daima.” “Unataka mwanaume wa namna gani?” Malon akaendelea kuuliza. Naya akacheka.

“Malon!” “Nataka kujua.” “Unamaswali sana! Na umenifanya niongee mambo mengi wakati hata sikufahamu!” “Si ndio mwanzo wa kufahamiana?” “Mmmh! Hapana.” “Unamaanisha nini ukisema ‘Hapana’?” “Namaanisha sipo tayari kuongeza mahusiano na mtu yeyote sasa hivi. Yawe mahusiano ya urafiki wa kawaida au mapenzi. Sina nafasi. Nilio nao kwenye maisha, wananitosha. Kwanza Ino ni kama ameniharibia mahusiano na wazazi wangu. Swala la kumkataa Ino, imekuwa tatizo. Ukaribu na mama umepungua. Anaona napiga teke bahati na wanafikiri sijatulia. Akija kuongezeka mtu mwingine sasa hivi, itaonekana ndio sababu. Naona nitulie kwanza. Nihangaike na shule, labda ikiisha, nikawa na changu, nikisema nimepata mtu mwingine, watampokea. Lakini kwa sasa hivi itakuwa ngumu. Nitazidi kuharibu mahusiano na wazazi wangu watadhani huyo mtu ndio sababu ya mimi kumkataa Ino. Nataka nimalize hiku kidato cha nne akili ikiwa imetulia.” Malo akamtizama.

“Nini?” “Kwa hiyo hata mimi nikikuomba mahusiano, hutakubali?” “Hata kidogo. Wewe kama unataka mwanamke, mfuate Lulu yule rafiki yake Tula. Lulu anakupenda.” “Anapenda pesa zangu sio mimi.” “Sasa si ni yale yale tu! Wewe unakuwa umepata mwanamke na yeye atapata pesa yako? Au na wewe unakuwa kama Ino?” Malon akamtizama na kunywa soda kidogo.

“Kuwa kama Ino ndio nakuaje?” “Unataka kila mtu ajitegemee! Kwamba pesa yako inabaki kuwa yako tu na hata ukiitoa nilazima ijulikane na kila mtu kama umetoa! Ni mahusiano tu, bila kusaidiana kwenye maisha.” Malo akanyamaza. “Mimi nataka kurudi hosteli. Naweza kupanda daladala hapo kituoni.” Malo akamtizama. Naya akacheka kidogo. “Asante kwa chakula, na kunisindikiza au kuwa dereva wangu. Naamini nitakuona tena.” “Naweza kukurudisha tu hosteli. Sina haraka ya kwenda popote.” “Nitashukuru.” Malon akatoka kwenda kutupa mifuko ya chakula na makopo ya soda.

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

 Naya akaamua kuwapigia simu wazazi wake kuwashukuru kwa pesa. “Pole baba, nimekuamsha?” “Bado sijalala. Nasinzia tu. Hujambo?” “Sijambo, shikamoo.” “Marahaba. Utakuja kanisani kesho?” Naya akanyamaza. Malon akarudi ndani ya gari. “Naya?” Baba yake akaita.   “Sijui baba. Ninashuguli kidogo. Bado natafuta pesa za michango shuleni. Lakini nilitaka kukushukuru kwa pesa alizonipa mchungaji.” “Nimekopa hizo pesa. Nimeoomba waniongezee kwenye deni la nyuma.” “Ameniambia na kunitajia pesa yote anayodai. Kuna kazi nimeahidiwa sehemu, naweza kulipwa pesa nyingi kidogo. Nikilipa michango ninayodaiwa shuleni, zikibaki nitapunguza deni la kanisani.” Naya aliendelea kuzungumza na baba yake taratibu wakati Malo anaendesha kurudi hosteli. 

“Sasa utakuwa ukisoma au unafanya kazi?” Baba yake akauliza. “Nitafanya vyote baba.” “Naomba weka akili shuleni Naya. Mwishowe tutabakiwa na madeni bila vyeti.” “Napangilia muda kwa makini. Na uliona ripoti iliyopita, wewe mwenyewe ulifurahia.” “Sawa. Na Ino alikuwa hapa jioni hii.” “Alinitumia ujumbe.” Naya akajibu kwa kifupi tu.  “Anaonekana anaweza kukusaidia kazi ndogo ndogo zitakazo kuingizia pesa.” “Nitamtafuta.” “Unaniambia kweli au unanitoa tu barabarani?” Baba yake alimgundua. Naya kimya. “Naya?” “Nilikwambia kuna sehemu nasubiria majibu ya kazi, baba. Acha niwasubirie ili kama namtafuta Ino kwa kazi iwe natulia na kazi moja. Unamjua Ino. Akinipa kazi, nikashindwa kufanya, itakuwa tena tatizo jingine. Na mimi sasa hivi siwezi kufanya kazi mbili. Nitashindwa shule wakati ndio mwaka wa mwisho huu.” “Hapo umeongea sahihi. Basi nakuombea ufanikiwe.” “Asante baba. Muwe na usiku mwema.” Wakakata simu.

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

Naya akatulia na Malon akanyamaza akiendelea kuendesha mpaka wakafika hosteli. Hapakuwa na mazungumzo mengine tena kati yao mpaka walipofika. “Nakushukuru sana Malo. Mungu akubariki.” Malo akamgeukia na kutoa tabasamu. “Karibu na amina Naya. Nimefurahi kwa muda mfupi tuliopata pamoja. Japo nimesikitika kunikataa.” Naya akacheka na kuinama kama anayefikiria. “Angalau niambie utanifikiria Naya. Usinikatae moja kwa moja.” Naya akamwangalia tena. Malon alikuwa akivutia, hata Naya alivutiwa naye.

“Mbona wapo wasichana wengi tu, Malo? Lile kundi la Girls Star wote wanawapenda na walikuwa wakiwasubiria kwa hamu sana. Kwa nini usimchague mmoja wao pale. Nina uhakika hutakuwa na shida.” “Nataka mtu aliyetulia kama wewe. Nataka mtu wangu peke yangu. Huko unakonisukumia siko Naya, na wewe unajua. Hakuna hata mmoja wao pale anayeonyesha yupo tayari kutulia kwenye mahusiano.” “Malo! Unajuaje kama nimetulia!? Halafu usiwakatie tamaa. Inawezekana wanahangaika kwa kuwa hawajapata kitu wanachokitaka.” Naya akamgeukia.

 “Inawezekana kila mwanaume wanaopata wanawafikiria kama wewe, Malo. Kuwa wanataka pesa tu. Sio wasichana wote wanataka pesa kwa wanaume. Pesa sio kila kitu kwenye mahusiano. Sasa unaweza kuta wanawapa pesa tu, halafu hawawapi kile wanachokitaka.” “Kama nini?” Malon akauliza. “Kupendwa. Kuthaminiwa, ndio kujaliwa. Na ulinzi. Kila mtu anahitaji kujiona salama kwenye mikono ya mtu fulani. Na pesa haiwezi kutimiza yote. Nashauri jaribu, utafanikiwa tu.” “Lakini sio kwako?” Naya akacheka kidogo huku akifikiria. Akamuona anatingisha kichwa akikataa.

“Hapana Malo. Sio na mimi. As much as convicing you are, lakini hapana.” “Unamaanisha nini kuwa nipo convicing.” Naya akacheka. “Namaanisha unashawishi sana. Sio kwa maneno yako, ila hali yako. Jinsi ulivyo wewe mwenyewe na maisha yanayokuzunguka.” “Ndio nikoje?” “Upo vizuri Malo. Najua na wewe unajua. Mtu yeyote au msichana yeyote yule angetamani kuwa na wewe.” “Lakini sio wewe?” “Hapana. Sio mimi na zaidi kwa wakati huu.” Malo akabaki anamtizama. Naya akacheka. “Naomba nikutakie kila la kheri na usiku mwema. Naamini nitakuja kukuona wakati mwingine.” Naya akashuka bila kusubiri laziada.

  Naya akakumbuka hicho kipengele, akacheka peke yake akiwa bado amekaa peke yake hapo kwenye mti, chuoni Mzumbe.

 Kwa Malo Usiku aliokataliwa na Naya! 

K

itu ambacho hakuwa akijua Naya, ni wakati mgumu aliokuwa amempa Malon usiku ule. Malon hakuamini masikio yake. Kiburi cha pesa anayoitafuta kwa udi na uvumba ili kutetemekewa na watu, leo msichana kama Naya anamkataa tena bila kung’ata maneno! Hakuamini. Alibaki pale nje ya ile hosteli kwa muda, akiwaza. Alikuwa kwenye mshtuko mkubwa sana. Naya alionekana ana shida, na yeye anajua watu wanampenda iwe kwa umbile la kiume alilonalo, au pesa. Lakini Malon alijua kwa hakika kwa pale alipofika, aliyonayo yote, hakuna msichana angeweza kusema hapana kwake, isipokuwa ndio Naya!

Alikuwa mfanya mazoezi tokea mlalahoi wa kijiweni mpaka wakati huo amefanikiwa. Walikuwa na kundi lao, wakifanya mazoezi ya kunyanyua vyuma. Malon alijenga misuli aliyokuwa akifanya juhudi za makusudi kuonekana kwa aina ya mavazi ya ujana aliyokuwa akivaa. Vijishati vya kubana kifua na cheni kifuani inayongaa na kufanya lazima utake kuiangalia ndipo utakutana na hicho kifua kilichozungukwa na misuli ya kiume. Alivutia kutizama. Alivaa nadhifu, na maisha ya mazoezi hakuwahi kuacha. Lakini Naya amemkataa!

Mbaya zaidi, hakuwahi kupenda. Ndio mara yake ya kwanza kutaka mwanamke. Kwa asili alikuwa malaya wa kiume. Hakuwa na shida kulala na yeyote aliye mrembo. Alipenda wanawake wazuri. Na kila alipoona sketi aliyovutiwa nayo, lazima ataivua tu. Hata kwa kulipia. Hakuwahi kuwa na mahusiano yakudumu. Alikuwa player tu, mchezea wanawake vile atakavyo. 

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

Lakini kwa Naya ilikuwa tofauti mpaka mwenyewe akashangaa. Mara ya kwanza tu alipomuona pale ukumbini akatulia sana mpaka Chezo akamcheka. “Unaondoka na yupi leo?” Chezo alimtania. Malon akacheka. “Maana leo umeletewa mezani tena buffet ya nguvu! Unajipakulia tu.” Chezo aliendelea kunong’ona wakati tafrija ilikiendelea maana alimjua rafiki yake linapofika swala la ngono, hapuuzii.

“Ushaniona mimi somba somba sana Chezo! Nimekua.” Chezo alicheka sana. Naya hakuwa akihudumia upande wao. Alipewa meza za mbele kabisa, lakini kushoto. Kila aliposubiri labda atakuja upande wao, hakuona dalili bila kujua kuwa wasichana wote wanao wahudumia, wamepangwa. Lulu na wenzie ndio walikuwa wakihudumia meza za nyuma walipokuwepo wao kina Malon.  Girls star, ambao walikuwa wakiwahudumia meza ya kina Chezo na Malon, ambapo Chezo yeye alifika hapo na baba yake ambaye ndiye mmiliki, na Malon kama mmiliki wa kampuni yake.

Chezo alipoona kina Lulu wanahangaika na Malon, na Malon hana habari nao wakati yeye ndio huchangamkia wanawake kwa haraka, akahisi kuna jambo. Akampa Lulu business card yake, ili wawaache. “Vipi Mwana!?” Malo akacheka tu. “Leo mbona kama sio wewe vile!” “Nahisi leo nimepata mke. Sitaki tena wakuchezea.” Chezo alitingisha kichwa, akijua kuna aliyemtoa mate, rafikiye. “Yupi?” Malo akamuelekeza mpaka wote wakajikuta macho yapo kwa Naya. Chezo akamgeukia Malo kwa mshtuko. “Unanitania!?” “Nishawahi kukwambia maswala ya mke?” “Hata mara moja!” “Basi yule ndio mwenyewe.” “Mbona kama kuku mgeni, kamba nyingi sana!!” “Ndio maana nakwambia ni mke wangu. Hawa watoto wote naweza kuwavutia hata chooni nikakata kiu. Na wewe ukitaka kuunganisha pia hawatakataa. Si umeona walivyochanganyikiwa hapa? Lakini yule ukimuacha nyumbani, ukirudi utamkuta.” Chezo akatulia na kumkazia macho Naya.

“Lakini tokea mwanzo, haji upande huu!” Malon aliendelea kunong’ona na Chezo. “Hakika siondoki bila namba yake ya simu, au nijue anaishi wapi na jina.” “Utafanyaje?” “Tumuulize kwa hawa mademu wanao tuhudumia.” Chezo akamkonyeza mmoja wao kama anayetaka huduma. Haraka Tula akaja. “Unamuona yule msichana pale?” “Nani? Naya!” “Kumbe anaitwa Naya?” Akamtizama na Malon, wakacheka. “Naomba niitie.” “Bosi yupo. Yaani anapita pita kila wakati na yeye amepangiwa meza za mbele. Kuja huku hataweza ni kama kumtia matatizoni.” Chezo akamtizama Malon. 

“Unaweza kunisaidia namba yake ya simu.” Malon akaingilia. Tula akasita kidogo. “Naya hapendi tugawe namba yake hasa kwa wateja kama nyinyi tunao wahudumia.” Wakabaki wamekodoa macho. “Sio kwamba nawanyima. Mimi nitaondoka, halafu mwiteni mtu mwingine, mwambieni moja kwa moja, kuwa mnataka namba ya simu ya Naya, halafu msikie jibu lake. Wote tunamjua. Hataki mtu agawe namba yake.” Tula akaendelea.

 “Mwanzoni kuna msichana, yule pale ameinama anahudumia meza ya pili kutoka hapa tulipo.” Tula akawaonyoshea kidole kwa tahadhari. “Basi yule, aligawa namba ya Naya, alikasirika mpaka Naya akataka kuacha kazi. Lakini huyu mwenye kampuni, Madamu Vane anampenda sana Naya, mgeni lakini anachapa sana kazi. Akasema kuliko Naya aondoke, ni heri amfukuze yule dada. Ndio akaomba msamaha kwa Naya, Naya akamuombea msamaha kwa bosi, akarudishwa kazini. Ndio ikawa fundisho kwa wote. Ingekuwa mtu mwingine ningekupa kaka yangu. Wala nisingekunyima.” “Nimeelewa, asante.” Malo akashukuru, na kusimama palepale.

Naya alikuwa ndio ametoka kuongeza vinywaji kwenye moja ya meza alizokuwa akihudumia, ndipo akakutana na Malon akimuomba amuelekeze sehemu vilipo vyoo. Alipomuona anaondoka bila hata kumtizama mara ya pili, ndipo safari za hosteli zikaanza. 

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~ 

Malon aliondoka pale kwenye hosteli za kina Naya, nakurudi kule alipokuwa wamewaacha kina Lulu, Tula, Chezo na wengineo. Chezo alipomuona tu, akajua mambo hayakwenda vizuri. Akavuta kiti na kurudi kukaa. Kimya. Kwa kina Chezo na rafiki zao ndio ilikuwa kama kunapambazuka. Pombe zilikuwa zikinywewa hapo. Kelele. Kina dada hao walijawa vicheko vya kilevi kupita kiasi.

“Vipi?” “Poa tu.” Malon akamjibu Chezo akionyesha hataki kuendelea na mazungumzo. Kwa kuwa alimfahamu Malon tokea watoto, akaona amuache. Mbaya zaidi walikuwa wametumia usafiri mmoja, gari ya Malon. Walikuja wanne kutokea Morogoro, wakakutana na rafiki zao wa hapo Dar. Pakawa pamechangamka haswa. Alitamani kuondoka mapema, lakini Chezo alionekana ndio alikuwa anaanza starehe.

Masaa yalizidi kwenda, wenzake wakinywa, yeye alikuwa ametulia tu. Malon hakuwa akinywa pombe, ulevi wake ni wanawake tu. Ilikuwa ni bora ale vizuri. Akipata nyama choma anayopenda, hatakuwa na shida kuwa nao wakinywa pombe zao mpaka wachoke na stori zikiendelea. Chezo alipomuana ametulia hata hachangii, akawakonyeza wenzake kama wajiandae waage warembo hao, warudi Morogoro.

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

Ilikuaje? Endelea kufuatilia....

CONVERSATION

0 Comments:

Post a Comment