Kesho yake Chezo aliamua kumfuata Malon nyumbani kwake. Bado Chezo hakuwa ameoa, baba yake ndio alikuwa mfanya biashara kama Malon. Malon alifanya biashara tokea anakataa shule, mwenzie Chezo akiendelea na shule. Wakati
Chezo alimkuta Malon ametulia tofauti na alivyomzoea. “Kwema
Malo!” “Aaah, nipo tu.” “Leo hujatoka kabisa?” “Nimeona leo nipumzike tu
nyumbani. Vipi wewe?” “Ndio tumetoka kanisani, nikaona nije kukuangalia. Jana
tuliachana ukiwa haupo sawa.” “Kawaida tu. Nafikiri uchovu.” Chezo akasimama na
kwenda jikoni akajua bado hayupo tayari kuzungumzia ya Naya.
Akarudi anatafuna apple alilopata jikoni kwa Malon. “Vipi Naya?”
Chezo akaona asiendelee kuzunguka. “Alisema hayupo tayari kwa mahusiano. Au ni
kama yupo na mahusiano mengine yanayofahamika kwao.” “Kwa hiyo?” “Amekataa
kabisa. Na kwa vile nilivyomsoma, sio mbambaishaji. Ila daah!” Malon akasita. “Vipi?”
“Nimejuta kupata naye muda jana.” “Kwa nini tena?” “Nahisi kama nimejichanganya
zaidi! Hata sielewi.” “Kwamba?” “Nampenda yule mtoto, Chezo. Hakika nimempenda
na ninamtaka haswa. Sijui nafanyaje. Na sikukosea. Anaonekana kweli ametulia.”
Chezo akatulia. “Namtaka yule mtoto Chezo. Nahisi kama nitachanganyikiwa!”
Chezo hakuwahi kumuona Malon kwenye ile hali.
“Labda kwa kuwa yeye amekukatalia Malon, ndio maana unazidi
kumfikiria. Jipe muda tu. Sidhani kama...” “Hapana Chezo. Kwake imekuwa
tofauti. Mimi unanijua linapofika swala la wanawake. Nawajua kwa kuwaangalia.
Kama ingekuwa ni kumvua chupi tu, nisingehangaika. Kwani ana kitu gani cha
ajabu na wanawake wote niliokwisha kulala nao?” “Sasa ni nini kinachokuumiza
kicha Malon!?” “Namtaka yeye, Naya. Mimi sijui kwa nini, ila namtaka Naya.”
Chezo alikuwa akimtizama Malon, asiamini. Sio Malon aliyemfahamu. Wakatulia.
“Labda umpe muda.” “Mpaka lini Chezo?” “Tulia kwanza Malon. Si umezungumza naye jana tu?” “Lakini amekataa. Amenielekeza mpaka kwa kina Lulu na wenzake. Kwamba nikawatongoze wale hawatanikataa, yeye amekataa.” “Ndio nakwambia mpe muda. Tulia kidogo ili na yeye afikirie. Si umempa namba yako?” “Nakwambia amenikataa, mbona kama hujanielewa!? Hapakuwa na mazingira ya kumpa tena namba yangu.” “Basi mpe hata mwezi, tutarudi kwa kina Tuli tena ili kumfikia Naya. Na hivi jana tuliwanywesha na kuwaachia pesa, watatupokea tu.” Malon akatulia akaona si wazo baya. Atulie.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
Majuma mawili yakapita, Malon akamuomba Chezo ampigie simu Tuli,
aulizie hali tu na kujua kama watakuwa wanafanya kazi weekend hiyo. Chezo
akashangaa sana hakutegemea kama bado Malon anamkumbuka Naya. “Haiwezekani
Malon! Bado unaye tu yule mtoto!?” “Tafadhali piga simu.” Chezo akajua hali si
njema, akapiga simu. Tuli alimwambia weekend hiyo aliitwa Naya tu kazini, kwa
kuwa ni tafrija ndogo tu, bosi wao alitaka mtu mmoja, akamchukua Naya. Na Tuli
hakuwa akijua ni wapi. Chezo akarudisha ujumbe.
“Muulize kama wanaweza kufanya kazi nje ya Dar. Waje huku
Morogoro. Au nipe nizungumze naye.” Chezo akamkabidhi simu, Malon akapiga simu,
Tuli akapokea. “Habari Tuli? Mimi Malon.”
“Mambo Malo!” “Safi tu. Nilitaka kujua kama huwa mnafanya kazi nje ya Dar?”
“Labda uzungumze na bosi.” “Kwani nyinyi hamuwezi mkajipanga mkaja wenyewe
mkafanya kazi wenyewe bila kupitia bosi wenu? Maana nina tafrija ambayo nataka
nyinyi muhudumie. Na nitawalipa mimi mwenyewe na nitawatumia usafiri.” Chezo
akashangaa sana, lakini Tuli akafurahi sana kuona watalipwa pesa yote wao
wenyewe bila kukatwa na bosi wake, na watapewa na usafiri! Akamkubalia Malon.
“Basi ngoja niwapange
wenzangu.” “Lakini nilazima Naya awepo.” Tuli akanyamaza. “Tuli?” “Mimi nilikwambia juu ya Naya, Malon. Siwezi kuahidi kama
atakuwepo. Sitaki uje unione mimi muongo. Kwa nini usimfuate hapa uzungumze
naye mwenyewe?” “Wewe mwambie umepata kazi ya pesa nyingi. Nina uhakika
atakubali.” “Mmmh! Sijui kaka yangu. Lakini Naya huwa ananionaga mimi namna
fulani hivi.” “Namna gani?” “Kama haniamini na sio mtu anayeweza kunisikiliza
kama dada Wahija. Ni kama ananiona mimi mcharuko. Sijui kama unanielewa? Huwezi
ukamkuta anazungumza na mimi maswala mengine zaidi ya kazi.” “Sasa hiyo si ndio
kazi? Zungumza naye, mimi nitakulipa kama akija.” Akajaribu kuongeza nguvu ya
hongo ili tu Tuli akubali kumshawishi Naya.
“Nitajaribu kaka yangu, lakini
naomba nisikuahidi. Ulitaka tuje lini? Maana weekend hii anakazi.” Tuli
aliendelea akionekana kukosa ujasiri. “Ile
inayofuata je?” “Sina uhakika. Maana kama ni kazi huwa tunaitwa wakati mwingine
hata siku mbili kabla, na Naya huwa hawezi kuacha kwenda kwa yule mama. Lakini
kama ni mwanamke naweza kukuletea msichana mzuri tu.” “Acha upuuzi. Nani
amekwambia huku nilipo hakuna wasichana wazuri? Nimekwambia namtaka Naya. Kw..” Chezo
akampokonya simu alipoona anaanza kugomba.
“Tuli! Tuli!” “Samahani
nilikuwa..” “Hapana, hamna shida. Mimi ni Chezo. Nashukuru kwa kupokea simu.
Kikubwa ni mje na Naya. Ukifanikisha hilo, itakuwa vizuri sana.” “Sawa.
Nitajaribu. Lakini kama nilivyomwambia mwenzio, Naya anaweza asikubali akadhani
nataka kuja kumuuza. Mimi namjua Naya, kaka yangu.” “Mimi naomba uniahidi utajaribu.”
“Sawa.” “Basi nakurushia pesa ya muda wa maongezi kwa ajili yako tu.” Tuli akacheka kidogo. “Asante kaka yangu. Basi usisahau na pesa ya soda tafadhali. Jua
kali!” Tuli akachangamkia. “Nakututumia
na ya soda basi. Ili upate nguvu ya kumpanga Naya.” Wakaagana.
“Vipi Malon!?” “Kuhusu nini?” Malon akauliza kwa jeuri akijua wazi
ni nini Chezo anamuulizia. “Unamjia juu demu wa watu wakati yeye ndio anaweza
kutusaidia? Au humtaki tena Naya?” “Kwani wewe hujasikia mazungumzo yetu tokea
mwanzo?” Malon akauliza kwa jeuri na kuondoka.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
Siki ilipofika, mapema tu Malon akamtuma dereva wake Dar kwenda
kuwafuata kina Tula. Dereva alipofika, akampigia simu Tula atoke. Girls star
wote walikuwa wamejitengeneza vizuri. Tula akaona mpigie simu Chezo kabla
hawajapanda gari. “Vipi, dereva hajafika?” Chezo akauliza. “Nipo naye hapa,
lakini nimeona kabla hatujaanza safari, nikwambie kabisa. Naya hatakuja.” “Kwa
nini tena!?” “Kwanza alianza kugoma kuwa kazi za mikoani hawezi kuchukua.
Nikambembeleza na kumtajia ile pesa mliyosema mtatulipa, kidogo akakubali. Jana
alinipigia simu kuwa amepata dharula anakwenda kwao, hatarudi mpaka jumatatu
asubuhi. Hivi tunavyozungumza hayupo hapa hosteli. Sasa kama safari ilikuwa ya
Naya, basi naona itashindikana. Lakini kama mnataka huduma nyingine, sisi
tupo.” Chezo akaishiwa nguvu. “Nimealika watu wengi, nitahitaji
msaada wenu. Siwezi kuahirisha. Mpo wangapi?” “Wanne, au unataka zaidi?” “Naona
nyinyi mtatosha. Anzeni tu safari.”
Chezo akakata simu, lakini akaamua asimwambie Malon. Akajua akijua
tu, itakuwa fujo na anaweza hata kuahirisha shuguli nzima hapo nyumbani kwake, wakati
yeye ashatangaza kwa marafiki wote kuwa siku hiyo ni mkesha nyumbani kwa Malon!
Watu wasile wala kunywa, kwa Malon kutakuwa na kusaza. Akajua itakuwa aibu
kwake. Akona anyamazie tu.
Mapema sana akapeleka nyama nyumbani kwa Malon na kumwambia kijana
wake aiweke viungo mpaka jioni marafiki zao watakapofika hapo kama yeye
hatakuwepo, basi awatolee ili waanze kuchoma. Uzuri hakuwa amemkuta Malon
mwenyewe.
Kina Tula walifika hapo ilishakuwa jioni ya saa 11. Malon alikuwa
chumbani kwake akihangaika kubadili t-shert kama mtoto wa kike. Alivaa hii na
kuvua mpaka akaona anajidhalilisha yeye mwenyewe mbele ya kioo. Akajipulizia
pafyumu kidogo, ili angalau anukie kama itatokea anamsogelea Naya. Akafungua
vifungo vyote vya hiyo t-shert iliyokuwa imembana vizuri sana, akajitizama.
Akaona hapana. Akafunga vyote. Akajikosoa. Akafunga tena vyote na kubakisha
kimoja tu cha juu. Akajikubali ndipo akatoka.
Aliwakuta kina Tuli wakionyeshwa jikoni, vinywaji vilipo, sahani
na glasi. Chezo alishawaambia wanaweza kuvaa chochote wanachotaka sio lazima
sare. Hakika warembo walipendeza. Malon akaangaza macho, akatoka nje na kuingia
ndani mara kadhaa, mwishoe akamwita Chezo. “Mbona Naya simuoni!?” “Nilikuja
mchana kuleta nyama, sikukukuta.” “Naya amekuja au hajaja? Acha ngonjera Chezo!”
“Alipatwa dharula jana. Ameshindwa kuja.” “Sasa kwa nini hujaniambia tokea
jana?” “Yaani mimi Tuli ndio ameniambia mida hii dereva alipokwenda kuwafuata.
Sikutaka kuahirisha kwa kuwa niliona tuna wageni tayari. Au unataka tuwaage
watu waondoke?” “Hapana. Hamna haja yakufanya hivyo. Nyinyi endeleeni tu. Ila
naomba niitie Tuli.” Kwa wasiwasi kidogo, Chezo akaenda kumwita Tuli.
Wakarudi naye. “Nipe simu
yako.” Malon akamkazia macho Tuli mpaka akaingiwa hofu. Akaenda alipokuwa
wameacha mikoba yake akarudi pale alipokuwepo amesimama Malon na Chezo. “Hii
hapa.” Malon akaipokea. Alikwenda moja kwa moja kwenye contacts, akachukua
namba ya Naya, na kumrudishia simu yake. Hakutoa hata asante. Wakamuona
anachukua funguo za gari nakutoka. Chezo akatingisha kichwa.
“Wewe endelea tu, lakini usimwambie Naya chochote. Namjua Malo,
hawezi kukutaja.” “Sasa anakwenda wapi?” “Sijui. Wewe endelea tu na kazi, usiwe
na wasiwasi.” “Kwani hapa ndio nyumbani kwako Chezo?” Tula akauliza kwa sauti
ya kike. Chezo akafikiria kidogo, akataka kumdanganya, lakini akaona ampotezee.
“Kwani vipi?” “Nauliza tu. Pazuri.” Chezo akaondoka.
Baada kama ya lisaa na madakika kadhaa, akampigia simu Malon. “Uko wapi Malon?” “Nakwenda
Dar mara moja. Nitarudi, sitakawia.” Chezo akatulia kidogo, akijua wazi
wapi anakwenda. “Umempigia
simu lakini? Nashauri umpigie ili ujue kama yupo kwenye nafasi ya kukuona.”
“Sawa.” Chezo akashangaa amekubali ushauri wake kirahisi sana.
Malon kwa Naya Tena.
M |
alon akampigia
simu Naya. Iliita mara moja tu, akapokea. “Haloo!” “Naya!” Kimya. “Mimi Malon.” Kimya. “Naomba usinikatie simu, Naya.
Tafadhali.” “Siwezi kufanya hivyo. Nilikuwa usingizini nikahisi naota.”
“Mzima?” “Mzima.” “Mbona unalala sasa hivi?” “Nilikuwa na kazi nyingi karibu
siku nzima leo. Namsaidia mama maswala ya kuku. Alianguka jana, ametengua mguu.
Aliangukia bandani. Akamwaga maji, kwa hiyo kukawa kumelowa. Nilikuja jana.
Tukawa naye, leo nikaamka na hiyo kazi ya kubadilisha maranda ya kuku bandani.
Nimekuwa busy, hata sijala, nikajitupa kitandani ndio na wewe umenipigia.”
“Pole.” “Asante.” Naya akakaa.
“Vipi
mama?” “Wamemwambia aning’inize tu mguu. Atakuwa sawa. Vipi na wewe?” “Safi tu.
Nakuja Dar. Nipo njiani. Naomba kukuona.” Naya akatulia kidogo. “Naya!” “Leo?” “Nipo njiani.”
“Nipo nyumbani Malo!” “Nafahamu. Natamani kukuona tu Naya.” Malon
aliongea kinyonge.
“Labda
ukimaliza shuguli zako ndipo unitafute. Nijaribu kuaga hapa kuwa naenda
dukani.” “Nikwambie kitu Naya?” “Nakusikiliza.” “Ninakuja Dar kwa ajili yako.” Naya akashangaa
sana. “Kwa
ajili yangu mimi!?” “Ndiyo Naya. Nimekuwa nikikufikiria. Natamani tu kukuona.” Naya akatulia.
“Tafadhali
Naya.” “Sipo vizuri Malo. Nimekuwa na kazi siku nzima, sitizamiki.” “Mimi
sijali Naya. Ilimradi tu nikuone.” Ikamgusa sana Naya. “Sisi tunaishi mbele ya Kibaha
kutokea Morogoro, panaitwa Kiluvya kabla ya Kibamba.” Akaongea Naya
kwa upole. “Basi nikifika hapo nitakupigia. Nakuahidi sitakuweka sana.
Nashukuru kwa kukubali nikuone.” Naya akacheka kidogo. “Karibu.” Wakaagana,
Naya akabaki akiitazama ile simu huku amekunja uso, haamini.
Alitoka hapo chumbani. Akaenda kumuangalia mama yake sebuleni,
akakuta wapo nje na baba yake wanaongea. “Umekula?” “Nilikuwa nimelala.” Naya
akajibu huku anakaa. “Pole. Naona umefanya kazi kubwa kweli. Lile banda
lilihitaji kusafishwa haswa kama vile ulivyofanya.” Ikawa kama baba yake anamsifia. “Ulikumbuka
kunyunyuza dawa?” Mama yake akauliza. “Niliweka.” Naya akajibu. “Ungekula. Bale
amepika chakula cha mchana na usiku.” “Nataka kuondoka nirudi hosteli. Nitarudi
tena kesho. Nilisahau kubeba vitabu vyangu. Nina mtihani jumatatu. Lazima
nijisomee. Jana usiku sijasoma, na leo siwezi kupitisha.” Naya akadanganya.
“Sawa.” Baba yake akakubali bila shida. “Utakuja kesho saa ngapi?”
Mama yake akauliza. “Mkitoka kanisani.” “Wewe siku hizi ibada ndio basi?” Mama
yake akamuuliza, Naya akanyamaza. “Naya?” Mama yake akaendelea kumuuliza.
“Nitakwenda lakini sio kesho.” Akasimama. “Mmewasiliana na Ino?” “Hapana mama.”
Naya akajibu kwa ukali kidogo. Mama yake akamwangalia. “Sijawasiliana naye na
wala sina mpango wakumtafuta. Ananiongezea matatizo tu kwenye maisha yangu.
Najua nyinyi mnampenda, lakini mimi simpendi. Hawezi kuja kuwa mume wangu. Ni
mnyanyasaji sana Ino. Hana utu.” Naya akaingia ndani kwenda kuoga.
Alitoka bafuni na kukuta missed call ya Malo. Akampigia. “Nipo kituoni tayari.”
“Nilikuwa naoga. Naomba nisubiri kidogo.” “Hamna shida. Nitasubiri tu.” “Pole.”
“Usijali kabisa.” Wakaagana tena, akakata.
Naya hakuahangaika kabisa. Alikuwa bado na uchovu wa kusafisha
banda la kuku. Akavaa gauni refu tu mpaka chini kabisa, halafu kata mikono.
Jeusi rangi moja tu, lilimfanya avutie zaidi kwa ngozi ya mwili wake ambayo
wengi walisema anapaka manjano ili kumfanya aonekane na rangi hiyo ya njano
kidogo usoni. Lakini ikawa sasa ni mwili mzima, halafu haikuwa nyeupe sana. Ni
kama rangi yake ya mwili ikaelekea kwenye weusi. Akawa na rangi ya maji ya
kunde nzuri sana kama mama yake ambaye naye hakujaliwa chunusi. Basi japokuwa
alikuwa ni wakufanya kazi nyingi, nzito, lakini alijaliwa ngozi safi, hakuna
makovu.
Akavaa na sendozi za chini tu. Akachana nywele zake kawaida.
Hakubana. Akaachia tu nywele yake ya kiswahili isiyokuwa hata na dawa.
Kipilipili kilichoonekana hakisumbui kuchana. Ila hakuweka hata kibanio kama
mara ya kwanza alipokutana na Malon alipoongeza kibanio cha mkia mzuri wa
mawimbi na kulambisha hiyo nywele Jelly na kulala vizuri. Kwa hiyo hiyo nywele
ya asili ikawa imejaa tu kichwani ila hakusahau hereni. Zikaongeza muonekano wa
aina yake kwenye sura hiyo ya mchongoko, nyembamba tu na shingo ndefu kuonyesha
hata yeye mwenyewe ni mrefu.
Akatoka na kuwaaga wazazi wake. “Kesho unarudi hapa saa ngapi?” “Hata asubuhi. Nitarudi na vitabu vyangu. Naweza kutokea hapa jumatatu na kwenda shule kama utakuwa unanihitaji.” Naya alimjibu mama yake huku akimwangalia kama kuna nyongeza. “Haya. Kuwa mwangalifu.” “Usiku mwema.” Akaaga na kutoka.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
Kweli alifika kituoni, akakuta gari ya Malon mbele kidogo ya
kituo. Akaenda, akachungulia dirishani upande wa abiria, akakuta amejiegemeza
kichwa kwenye kiti, anaangalia juu. Akagonga, Malon akamfungulia mlango.
Akaingia. “Pole na safari.” “Asante. Pole na wewe na kazi.” Naya akacheka
kidogo. “Nimeshapoa. Nililala. Najisikia vizuri.” Wakatulia kidogo, Malon
akimtizama. Naya akacheka na kuinama. “Nimefurahi umenikubalia nikuone, Naya.”
Naya akamtizama kama mwenye swali. “Uliniambia umekuja huku kwa ajili yangu!?”
“Huniamini?” “Hapana. Sijaelewa. Maana Tuli aliniambia mmewaitia kazi.
Mnatafrija leo.” Malo akanyamaza kidogo.
“Unatakiwa kurudi nyumbani baada ya muda gani?” “Nimeaga kuwa nitaenda
kulala hosteli kisha nirudi kesho.” Malon akafurahi sana. “Kuna kitu unataka
hosteli sasa hivi?” “Hapana, kwa nini?” “Nilitaka twende mahali tukae tu. Ni
sawa?” “Halafu utanirudisha hosteli?” “Ndiyo.” Malon akajibu. “Sawa. Ulitaka
twende wapi?” “Sijajua bado. Tufikirie wakati tunaondoka hapa.” Malon akatoa
gari.
“Nimekwambia nimeshukuru kwa kukubali nikuone?” Naya akacheka tu,
nakubaki kimya. “Vipi lakini?” “Nipo napambana na shule na kazi.” “Ulienda
kufanya kazi kwa Ino?” Naya akakunja uso. “Ulijuaje kama Ino ana kazi?”
“Nilikusikia ukizungumza na baba yako kwenye simu.” Naya akajaribu kukumbuka.
Akacheka kidogo. “Hapana, sikwenda. Yule mama mwenye ile kampuni tunayomfanyia
kazi za waitress naona tumetokea kuelewana. Huwa ananiita mara kwa mara. Wakati
mwingine hata ijumaa, jumamosi, na jumapili. Nakuwa busy, lakini inanisaidia
kutengeneza pesa. Hata leo alitaka niende kazini, lakini nilimwambia mama
anaumwa.” “Kwa hiyo kama isingekuwa hiyo kazi, ungeenda kwa Ino?” “Umeanza
Malo!” “Nataka kujua Naya.”
“Kwa nini!?” “Kwa sababu nakupenda, Naya.” Naya hakutegemea jibu
la namna ile. Tena la moja kwa moja! Akanyamaza. “Kweli Naya. Nakupenda.” “Kwa
nini mimi na wakati umeacha warembo kama kina Tuli huko kwenu Morogoro?” “Sio
kwenu. Wapo nyumbani kwangu. Chezo, rafiki yangu amealika watu nyumbani kwangu,
makusudi ili tuombe huduma yenu. Ili wewe uje.” Naya akatoa macho.
“Malon!” “Kweli Naya. Nimetuma dereva mchana kuja kuwachukua.
Nashangaa wamefika wewe haupo. Nikaambiwa umetoa udhuru. Nikaona sina sababu ya
kukaa kwenye shuguli ambayo lengo haikuwa kusherehekea tu, ni wewe! Nikachukua
funguo na kuondoka kukufuata huku.” Naya akashangaa sana.
“Pole na samahani Malo. Sikuwa na taarifa. Mimi nilijua ni kazi
tu.” Akatulia kidogo. “Lakini Malon, unakumbuka nilikwambiamimi sipo tayari kwa
mahusiano?” “Nakumbuka.” Naya akabaki akimtizama. “Unamfahamu yule rafiki yake
Tuli?” “Mweupe sana hivi, na anamatako makubwa?” Naya akaanza kucheka. Alicheka
na kucheka sana. “Kumbe unawafahamu?” “Nawafahamu sana tu. Si anaitwa Lulu yule
uliniambia nimfuate yeye?” “Jina lakujipa hilo. Lakini ndio yeye.”
“Amefanyaje?” “Anakupenda sana yule msichana. Kwa nini usimkubalie?” “Kwani
unafikiri kama ningekuwa na shida ya kulala na yeyeyote yule ingekuwa shida?
Hata Morogoro wapo weupe wenye matako makubwa, kuliko Lulu.” Naya akajifunika
uso huku akicheka sana.
“Ila kama wewe mwenyewe haupo sawa hivyo ulivyo, tunaweza kununua
chakula, tukakaa kwenye gari tu tukala kama siku ile.” Naya akamtizama Malon
tena. “Wewe umependeza sana.” “Kwa kuwa nilijiandaa kuja kuonana na wewe.” Naya
akaanza kucheka tena. “Kwa hiyo hapo umevunja kabati?” “Sio mchezo. Nimebadili
zaidi ya mara tano, nikijua upo njiani unakuja.” Naya akamtizama, asimwamini.
“Nikuulize swali Malo?” “Uliza tu.” “Unamchumba?” “Hapana.
Sijawahi hata kumpa mwanamke mimba. Kwa hiyo sina mchumba, wala msichana, wala
mtoto. Wewe ndio mtu wa kwanza kukutaka mahusiano. Na usinielewe vinginevyo
kuwa sijawahi kulala na wasichana. Ninalala nao sana tu, lakini sina mahusiano
yakufuatana nyuma.” “Kwa nini?” Malo akafikiria kidogo.
“Unajua mimi sijasoma. Niliishia kidato cha nne tu, nikawa mtaani.
Si unaona hii rangi yangu ilivyo.” Naya akamtizama kwa makini. “Halafu uwe huna pesa, uwe mzurulaji tu.
Hakuna msichana unayemtongoza akakukubali. Labda umwambie unamuomba ulale naye,
kisha umlipe. Napo mpaka umsimamishe akubali, nayo ni shuguli ingine. Tuache
hapo. Kwa hiyo nikakaa mtaani, nikijulikana kama mtoto mtukutu. Malo mlala hoi,
hajasoma. Hakuna mwanamke alikuwa ananitaka.”
“Chezo nilikuwa naye. Yeye amezaliwa kwenye pesa. Wakati anaenda
kidato cha tano na cha nne, akaniombea kazi kwa baba yake. Nikawa mtu wakutumwa
tumwa tu. Kazi za nyumbani, ofisini, basi. Nikafanya hivyo kwa muda huku na
mimi nikijifunza anachokifanya yule mzee mpaka akafanikiwa vile. Maana ni kweli
baba yake Chezo amefanikiwa. Nikaiga, na mimi nikatoka kimaisha.”
“Lakini ukumbuke mimi ni Malo yule yule waliyekuwa wakimkimbia na
kunikataa zamani. Sasa wakinitaka sasa hivi si ni kwa ajili ya pesa tu?
Hainisumbui kuhonga. Lakini kama ulivyosema ndivyo ninavyofanya. Kwa kuwa najua
wananitumia na mimi nakuwa mwangalifu. Siendi kichwa kichwa. Sijui umenielewa?”
“Nimekusikia.” Malo akamtizama. Wakanyamaza.
Hakujua anapokwenda, lakini aliendesha mpaka sehemu. Ulikuwa
mgahawa mzuri tu. “Sasa unataka tukakae pale pale tule, au tuje kula ndani ya
gari?” “Kwanza ujue naogopa. Sitaki mtu anayenifahamu mimi na wazazi wangu,
anikute nimekaa sehemu kama ile, watampigia simu baba na mama. Naomba nisubirie
hapa hapa kwenye gari kama hutajali.” “Hamna shida kabisa. Ngoja nikatoe oda,
nimwambie muhudumu atuletee, halafu twende sehemu tukae.” “Sawa.” Malon
akashuka. Naya akashangaa harudi.
Baada kama ya nusu saa akarudi na chakula. “Watu walikuwa wengi.
Nilijua nikiondoka, hawatanikumbuka tena.” “Asante.” Naya akapokea. “Lakini
mbona huna rangi mbaya Malo!” Malon alicheka sana huku anaondoa gari. “Kwa kuwa
nipo ndani ya hili gari. Nimetoka kuoga, nikajipaka mafuta, na sikushinda
juani. Ungekutana na Malon wa wakati ule, ungeelewa ninachozungumzia.” Naya
akanyamaza.
“Utakuja lini kunitembelea Morogoro?” “Sijui Malon.” “Naya kwa
jibu la Sijui! Unalipenda!” Naya akacheka kidogo. “Sitaki kukupa ahadi za
uongo.” “Wala sitakupa mwanya wakunidanganya. Siku utakayonitajia, nakuja
kukufuata mimi mwenyewe.” Naya akacheka sana. “Kama leo?” “Ulinichanganya Naya.
Sijawahi kusumbuliwa na mwanamke kwa muda mrefu sana. Mpaka nimeshasahau jinsi
wanavyotongoza!” Naya akazidi kucheka.
“Sijakusumbua bwana. Mimi nimejitahidi kuwa mkweli kwako.” “Kwa
nini hunipendi Naya?” “Sijakwambia sikupendi Malo. Ila nimekwambia sipo tayari
kwa mahusiano.” “Kwa hiyo unanipenda ila haupo tayari kwa mahusiano?” “Sijui
Malon.” “Usinipe jibu la sijui Naya. Tafadhali.” “Kwa kuwa kweli sijui Malon!”
“Mtu kama unampenda, unampenda tu. Kama humpendi unajua. Nataka kujua vile
unavyojisikia juu yangu.” “Labda unipe muda nifikirie.” “Hapo afadhali.
Nilitaka kukusikia ukiniambia kama utanifikiria.” Naya akanyamaza.
“Malon!” Naya akajirudisha nyuma ili kumtizama Malon pembeni yake.
“Nimekuwa nikikufikiria pia.” Malon alifurahi sana. Akacheka. “Umenifikiriaje?”
“Sijui.” “Acha bwana Naya!” Naya akacheka. “Niambie ukweli.” “Nilikumbuka muda
na mazungumzo tuliyokuwa nayo siku ile. Nikajuta kuondoka kwa haraka.
Nilitamani tungeendelea kuzungumza tu.” “Basi leo usifanye haraka kuniaga.
Tukae wote mpaka uchoke.” “Utarudi saa ngapi Morogoro!?” “Utakaponiruhusu.”
Naya akacheka kwa aibu na kujirudisha mbele kwenye chakula chake. Wakaendelea
kula mpaka wakamaliza.
“Asante kwa chakula na asante kwa kuja kuniona.” “Kweli?” “Kweli
Malon. Huoni mpaka nimeondoka nyumbani? Sikuwa na mpango wakuondoka nyumbani
leo. Hata kazi nilikwambia nimekataa. Ila uliponiambia umekuja huku kwa ajili
yangu, nimefurahi sana, japo sikuwa nimeamini.” “Sasa hivi umeamini?” “Sijui.”
“Naya!” Akacheka kidogo. “Nafikiri nimeamini kidogo, japo nina maswali na hofu
Malo.” “Maswali ni kitu chakawaida. Ila hofu ya nini?” “Sijui.” “Naya! Acha
kusema hujui katika kila kitu. Niambie wasiwasi wako ulipo. Labda naweza
kukusaidia.” Naya akanyamaza.
“Niambie Naya.” Malo akaongea kwa kubembeleza. “Bado sijajua ni
kwa nini mimi Malo! Wewe unayo pesa. Wasichana wazuri wengi wanakutaka.
Amebakia Lulu ambaye unamjua, ni kwa kuwa wamekubaliana abakie yeye tu kwako.”
“Usiniambie?” “Acha utani na kucheka Malo bwana!” “Sikujua. Ehe!” “Wote wale
wasichana walikuwa wakisimuliana siku ile ya tafrija kule jikoni. Wakajikuta
wote wanamsifia kijana mmoja, ambaye nilikuja kujua baadaye kuwa ni wewe. Wengi
walivutiwa na umbile lako, halafu sijui ni nani aliwaambia pesa pia ipo. Kwa
kifupi wanakupenda japo pia wanakuogopa.” “Hilo najua. Nimemuona Lulu
ananiogopa japo alimuomba Chezo namba yangu.” “Ulimpa?” Naya akauliza na
kumfanya Malo acheke sana.
“Sasa mama wivu wa nini wakati wewe hunitaki?” “Bwana Malon!”
“Sikumpa.” “Kweli?” “Mbona huniamini Naya? Sikumpa. Hivi unakumbuka nilikwambia
Lulu yupo nyumbani kwangu sasa hivi na mimi nipo hapa na wewe?” Naya akanyamaza
na kuinama. “Nakupenda wewe Naya. Nakupenda.” “Kwa nini Malo?!” Naya akauliza
kwa upendo. “Nakupenda jinsi ulivyo. Umetulia. Nakutaka wewe kwenye maisha
yangu. Nahisi ukiwa na mimi, nitatulia.” “Kwani sasa hivi hujatulia?” Malo
hakujibu hilo, akanyamaza. Naya naye akanyamaza.
Walikaa pale kwa muda Malo akaanza kumchora mkono ule uliokuwa
karibu yake. Kuanzia begani mpaka kwenye kiwiko. “Unasikia baridi? Naona vipele
vya baridi vimeanza!” “Kidogo.” “Nikukumbatie?” Naya akaona aibu, akacheka na
kuinama. “Nitakuwa sawa tu.” Malon akacheka taratibu. “Hivi, nimekushukuru kwa
kukubali nije kukuona?” Naya akacheka na kunyanyua uso kumtizama. “Zaidi ya
mara mbili.” Malon akabaki akimtizama. “Na mimi nimefurahi umekuja kuniona.”
“Ungenitafuta?” Naya akatingisha kichwa kukataa.
“Kwa nini?” “Sijui.” “Nimekuomba usiwe unanipa jibu la sijui, Naya!
Nataka kujua unachofikiria.” “Nilikwambia kuwa walikubaliana wote wakuache,
wamwachie Lulu tu. Sasa ningeanzia wapi kukutafuta wakati nilijua wewe ni wa
Lulu? Na alikuwa anasema leo kama mtaonana, angekwambia. Na nikajua kwa jinsi
alivyo Lulu, angekwambia, usingekataa.” “Kwani Lulu yukoje?” Naya akatulia
kidogo.
“Eti Naya? Lulu yeye yukoje?” “Kwanza hilo jina amejipa na kupewa
pia. Wengi wanamsifia kuwa ni mzuri sana. Ni mali hadimu. Ndio maana anajiita
Lulu.” “Aaha! Kwani hana mwanaume?” “Si naona watu wanakuwa nao wawili au watatu?”
“Kwa hiyo na mimi ilikuwa nikapangwe mstari!?” “Labda angeacha wengine kwa
ajili yako.” Malo akanyamaza kama anafikiria.
“Kwa hiyo isingekuwa Lulu, ungenitafuta?” “Sijui Malo.” “Naya!”
“Basi niseme ingetegemea.” “Na nini?” “Sijui. Labda na wewe mwenyewe. Niliamua
kujipa muda. Pengine ningepata jibu mbele ya safari.” “Mimi nilipewa ushauri wa
kujipa muda nifikirie ndipo nikutafute. Nikiwa najua yupo Ino, lakini
nilishindwa kuendelea kusubiri.” Naya akacheka kidogo na kuinama.
Malo akageuka upande ule aliokuwa amegeukia Naya, akamvuta karibu
yake, akampitishia mkono wa kulia juu ya mabega. Akamuona Naya mwenyewe
anajisogeza karibu yake zaidi. Akajua amependa. Akajiegemeza pembeni ya kifua
chake. “Naomba uje kunitembelea Morogoro.” Malon aliongea taratibu akiwa
amemkumbatia. “Nakuahidi wakati mzuri. Hutajutia.” Naya akacheka taratibu. “Eti
Naya?” “Labda nikimaliza mitihani hii.” Mkono ule wakushoto akaupitisha kwa
mbele, akafikia mkono wa Naya uliokuwa pembeni, akaendelea kuupapasa. Naya
alitoshea kwenye ile mikono bila shida. Wakatulia, Naya akifurahia joto la
kifuani.
“Lini mnamaliza mitihani yenu?” “Tutaanza mwezi ujao karibu na
mwisho, halafu ndio likizo ya mwezi wa sita inaanza, tukirudi tunajiandaa na
mitihani ya mwisho ya kumaliza kidato cha nne.” “Daah! Mbali. Lakini
nitakusubiri tu.” Naya akacheka taratibu na kunyamaza. “Lakini si unajua
Morogoro sio mbali?” “Nafahamu.” “Basi ukibadili mawazo kabla ya kumaliza
mitihani, naomba unipigie, nije kukufuata. Sawa?” Naya akamwangalia. “Nitakuja
kukuchukua mapema, na kukurudisha siku hiyo hiyo kama utataka.” “Tutawasiliana basi.” Naya akajibu kisha
wakatulia, Malon akiendelea kumpapasa. “Naona leo nitalala vizuri.” “Kwa nini
Malon?” “Nimefurahi sana.” Naya akacheka taratibu nakunyamaza.
“Ulikamilisha swala la ada?” “Tulimaliza, japo kwa shida hivyo
hivyo. Mama ameuza kuku, tumepata pesa kiasi. Akanipa, nikachanganya na zile
nilizoenda kuchukua kanisani, pamoja na nilizolipwa kwenye kazi ya jumamosi
iliyopita. Nimemaliza ada na michango ya shule. Nimebakiwa na deni la kanisani.
Nalo nimepunguza kidogo. Sikutaka kumpa sababu Ino.” “Kwani Ino anahusikaje!?” Naya akaguna.
“Ino ndio msimamizi wa pesa na matumizi yote pale kanisani. Kwa
hiyo kama hivi baba anavyokopa pale kanisani, usifikiri ni siri. Ino pia
anakuwa ameidhinisha kuwa apewe. Ndio maana unamuona anajeuri yakumwambia baba
nikafanye kazi anakotaka yeye. Inamaana ni kumwambia baba ana uwezo
wakutokukopa kopa hovyo, kama mimi nitafanya kazi. Yaani kwa jinsi ninavyomjua
Ino, anaona tunakopa kwa kuwa niwazembe, hatufikiriii vizuri. Au hatuna mipango
inayoeleweka kwenye maisha ndio maana tunakopa hovyo. Unafikiri ni kwa nini
nahangaika kufanya kazi?” “Eeeh!” “Namsaidia baba. Hajashindwa kunisomesha,
lakini najua wazi anahangaika sana.”
“Kwani baba yeye anafanya wapi kazi?” “Mfanyabiashara tu. Si ndio
maana mama hapendi mimi niolewe na mfanyabiashara! Anasema nitakuja kuishia
kuwa kama yeye!” “Yeye ameishiaje?” “Si kama hivyo sasa hivi wanakopakopa!
Lakini haikuwa hivyo tokea mwanzo. Hakuwa na pesa nyingi, lakini hatukuwahi
kukopa sana kama hivi sasa. Mambo yamezidi kuwa magumi, uchumi ulipobadilika,
na kuweka juhudi za kuhamia kwenye nyumba yetu. Sisi tulizaliwa kwenye nyumba
ya kupanga tu. Sasa nafikiri wakaona umri unakwenda, wanapoteza pesa kwenye
nyumba za watu, ndio wakaamua tuhamie kwetu.”
“Sasa bado mama anadaiwa huko kwenye mabenki. Anakatwa mshahara.
Baba ndio mfugaji. Ni kama wote tunategemea huo ufugaji. Kuna mwezi mambo
yanakuwa mazuri, miezi mingine mifugo inaugua ndio hasara hata kupunguza deni
kanisani ni shida. Sasa naona deni linalowatia presha ni hilo la kanisani.
Maana tunadaiwa tena kwa kukumbushwa kumbushwa mara kwa mara. Sasa hapo ndipo
mama anazidi kuchanganywa na Ino. Anatudai, na kutoa njia zake za kibinafsi za
upatikanaji wa pesa. Acha tu. Naomba tusimuongelee tena Ino. Tumuache tu kama
hivyo Mungu alivyomjalia.” Malon akanyamaza.
“Kwanza kwa nini umeniuliza?” “Nilitaka
kujua tu. Naona unafanya sana kazi na
bado unajukumu la shule.” “Nitafanyaje Malo? Lazima vyote viende kwa
pamoja. Ila najitahidi nisilemee upande mmoja. Nahakikisha hata kama napata
kazi za pesa nyingi, basi nisinogewe. Nikifikisha lengo, narudisha akili
darasani.” “Hongera Naya. Unajitahidi!” “Namshukuru Mungu kwa kweli. Naona
ananifungulia milango. Siwezi kulalamika.”
“Kwenye kazi zako huko hujapata
wafadhili?” Malon akachokoza. “Hawawezi kukosekanika. Lakini si unajua hakuna
kitu cha bure, Malo? Utapewa misaada yenye masharti magumu, mwishowe unajikuta
unakuwa na uwezo wakulipa ada, lakini uwezo wa kusoma tena hamna. Najiona ni
heri hivi ninavyohangaika peke yangu, nakuwa huru na kuamua chochote.
Najipangia mambo yangu nitakavyo. Najipanga na ninajua wapi nimelemea, wapi
niongeze nguvu.” Malon akazidi kumpenda Naya. Akamvuta karibu yake zaidi.
Wakatulia.
Malon akambusu kichwani upande
aliojiegemeza. Lilikuwa busu moja lakini alilolivuta kwa muda, kama
anayesikilizia, huku amemminya kwa nguvu. Mpaka Naya mwenyewe alilisikia
rohoni. “Asante.” Naya alimgeukia, akashukuru taratibu na tabasamu. Akabaki
anamtizama. Naya akacheka na kuinama.
“Naomba unirudishe hosteli,
nikapumzike.” “Sawa. Unafikiri tutakuja kupata muda mwingine kama huu?”
“Naamini hivyo Malo. Japo sijui kwa hakika itakuwa lini. Siku za shule
najitahidi kuweka akili shuleni, ili weekend jioni nifanye kazi. Jumamosi
asubuhi nakuwa najisomea na wenzangu.” “Nikuulize
swali? Uwe huru kujibu au kutojibu. Sio lazima, ila nilitaka tu kujua. Kwa kazi
kama hizi anazokuita huyu mama, kwa masaa yote yale, anakuwa anawalipa kiasi
gani?” “Wasichana wengi pale wanamlalamikia yule mama kuwa ni mnyonyaji. Lakini
wengi wanapenda kufanya ile kazi kwa kuwa wanapata bahati yakuonana na watu
kama nyinyi. Kwa hiyo kwa kukujibu tu kwa jumla, sio pesa nyingi hata kidogo.
Ila mara nyingi tunafaidika kwenye tip. Kwa hiyo inategemea unawahudumia vipi
wateja na ni watu gani.” Malo akamvuta pembeni kidogo, akamtizama.
“Kwa hiyo siku ile tulipokuwepo sisi,
uliondoka na tip kiasi gani?” Naya alicheka sana. “Usicheke Naya! Wewe mwenyewe
umetoka kuniambia hakuna msaada wa bure.” “Tip sio msaada Malon! Ni shukurani
baada ya huduma nzuri.” “Haya ulipewa shukurani ya kiasi gani?” Naya akazidi
kucheka. “Siku ile haikuwa nyingi kama nilivyofanya majuzi.” “Naya! Wewe mtoto
unataka kuninyima tena usingizi.” Naya alizidi kucheka. “Ni kazi.” “Walikupa
tip kiasi gani?” “Uliniambia sio lazima nijibu.” “Naona kama ulazima unaanza
kuwepo!” “Usijali. Hakuna kinachofuatia baada ya hizo tip.” “Unaweza kuniahidi
kuwa hapatakuja kutokea kitu baada ya hizo tip?” Naya akatulia kidogo.
Akamwangalia Malon, bado alikuwa
akimtizama. “Naya!” “Hakuna kitu kitakuja kutokea Malon. Mimi ni mwaminifu. Na
nitakuwa mwaminifu kwako.” Bila kujijua, Naya akajikuta anatoa kiapo kwa Malon.
Akashangaa anapata busu la mdomoni. Akatabasamu. Malon aliposikia asante,
akamvuta kiunoni akamshika shingoni, akaanza kunyonya midomo yake. Hakutumia
muda mrefu sana. Akamuachia, Naya akainama.
“Naomba unisindikize mahali kwanza, ndio nikurudishe hosteli. Hatutakawia.”
“Sawa.” Wakasimama, Malon akamshika mkono, wakaongozana mpaka kwenye gari.
Safari hii akamfungulia mlango.
Akapanda, kisha akamfungia mlango. Naya hakuamini. Alibaki akilamba midomo
yake. Alifurahia sana lile busu. Hapakuwa na maongezi, akamuona anasimama
sehemu yenye ATM. Akashuka, kisha akarudi. “Hizi zitakusaidia kwenye mahitaji
yako.” “Asante Malo. Nakushukuru.” “Karibu.” Wakatoka pale, wakarudi mpaka
hosteli. Naya hakuwa akiamini. Pesa na busu la Malo!
Akasimamisha gari nje ya hiyo hosteli
yao. Ujasiri wakumtizama machoni ukapungua, na maneno mengi ya Naya,
yakapungua. “Asante kwa kila kitu. Na uwe na safari njema ukiwa unarudi.”
“Asante. Naamini tutaonana tena hivi karibuni.” Naya akatingisha kichwa
kukubali. Malo akacheka. Akamuona anashuka. Akajua anaenda kumfungulia mlango.
Akatulia pale pale kwenye kiti.
Akamfungulia mlango. Naya akashuka.
Wakawa wamesimama palepale mlangoni. Naya akacheka kidogo na kuinama.
“Nitakupigia kujua kama ulifika salama. Ni sawa?” “Nitafurahi kukusikia tena.”
Kama waliokuwa wakitaka kurudia busu, lakini wakasita. Naya akajisogeza na
kumbusu shavuni. “Usiku mwema.” Malon akamvuta karibu yake, akapitisha mikono yote
miwili chini ya masikio, karibu sana na shingo, akaanza kumbusu tena. Alimbusu
tena na tena. Naya alitamani asimalize. Alimbusu vizuri, mpaka akajisikia
upendo wa kweli. Akamuachia kidogo, akampa mabusu mawili ya juu juu.
“Tutawasiliana.” Naya akatingisha kichwa na kuondoka palepale, akamuacha Malo
akimsindikiza kwa macho.
Aliingia tu ndani, akamtumia ujumbe. ‘Nimefurahia busu langu la
kwanza maishani. Asante kwa kuja kuniona. Asante kwa pesa. Asante kwa chakula,
asante kwa kila kitu.” Simu ya Malon ikatoa mlio wa
ujumbe ikiwa mfukoni. Akataka kupuuza, lakini akajiambia inaweza kuwa ni Naya.
Akaitoa mfukoni. Kweli ilikuwa ikitoka kwa Naya. Akasoma ule ujumbe huku
akiendesha. Hakuamini. Akasoma tena na tena. “Inamaana huyu mtoto alikuwa hajawahi hata kupata busu!” Malon akashangaa sana. Akaanza kulamba midomo
yake, nakutamani arudi. Akaanza kujiuliza kama alilitende haki lile busu.
Akajuta.
“Ningejua kama ni mara yake
ya kwanza, ningetendea haki lile busu. Sidhani kama lilikuwa...” Malon
akazidi kuwaza akijilaumu kwa furaha. Akajikuta anacheka na kujipongeza
kuchukua maamuzi ya kuja kumfuata. Gari liliposimama kwenye mataa, akaamua
kujibu. ‘Asante kwa kunipa nafasi hiyo ya kwanza. Nitaienzi daima.’ Akamrudishia
hayo majibu. Naya alipopata ule ujumbe, alishindwa kulala. Uzuri, hakumkuta mtu
chumbani kwao. Alikuwa akicheka peke yake huku akirudia ule ujumbe tena na tena
na kujishika midomo yake.
Akiwa amepitiwa na usingizi, akashtuliwa na mlio wa simu.
Akaipokea kwa haraka. “Nimekuamsha tena?” “Nilikuwa nasinzia tu, lakini nilikuwa
nikisubiria simu yako kujua kama ulifika salama. Umefikia wapi?” “Nimefika
nyumbani salama. Nashukuru kwa kukubali tuonane Naya. Asante.” “Asante
kushukuru Malon. Na mimi asante kwa kurudi kuja kuniona.” “Karibu.” Wakatulia
kidogo.
“Eti nimeshakuwa na hamu na wewe!” Naya akacheka tu bila kujibu. “Umesema utakuja baada ya mwezi!?” “Ndio tutakuwa tumemaliza mitihani, na mimi akili zitakuwa zimetulia. Na hivi umenipa pesa, itanisaidia kutulia nijiandae vizuri. Asante.” “Kidogo hivyo!?” “Sio kidogo. Kwa kuwa nishapunguza deni kanisani, hizi nazifanya zakupunguza deni la hapa hosteli na za kwangu za matumizi.” “Hosteli huwa mnalipa kiasi gani?” Naya akamtajia. “Okay. Basi pumzika. Nitakupigia tena kesho.” “Usiku mwema Malon.” “Na wewe Naya.” Wakakata simu.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
Chezo akashangaa kusikia geti
limefunguliwa lakini hamuoni Malon. Baada ya muda alipoona kimya akidhani ni
Malon, kwa kuwa hakuwa ameingia ndani, akachungulia dirishani. Akaona gari ya Malon
imegeeshwa. Akajua amerudi lakini akashangaa ni kwa nini haingii ndani wakati
pale ndio kama kulikuwa kunapambazuka na aliacha wanachoma nyama! Na Malon kwa
nyama, utafikiri hawezi kuishi bila nyama choma. Linapokuja swala la nyama hakuwa
akijua kujivunga.
Ikabidi Chezo atoke. Akamkuta anamwagilia ukoka na maua huku akipiga
miluzi. Chezo akaanza kucheka. “Kuna nyama ndani.” Chezo akamsogelea karibu.
“Sitaki kuchafua kinywa changu.” Chezo alicheka sana huku akipiga makofi.
“Gafla kaka! Nyama imekuwa uchafu!” “Inategemea na kile kilichoingia mara ya
mwisho mdomoni.” Malon akajibu na kuendelea kupiga mluzi tabasamu kubwa usoni.
“Usiniambie umebana mpaka umepewa ulimi!” “Sio kidogo kaka.
Nimejitahidi mpaka nikashika na kiuno. Nimekamua kaka, mpaka nikaona
nitapitiliza, nikamuacha. Mtamu! Hujawahi onja hapa duniani. Akiwa mkononi,
unaweza ukadhani umekumbatia mamilioni ya dola za kimarekani, au zaidi.”
“Alumasi?” “Daah! Alumasi nimeshika Chezo, haifikii raha ya Naya, mkononi.”
Chezo alicheka sana, nakuendelea kupiga makofi.
“Chezo!” Malo akaita. “Niambie kaka.” “Pale nimesalimu amri. Mungu
kanikamata pabaya! Hata mimi sijui imekuaje!” “Umekamatika kaka?” “Kama kondoo!
Hata akiniambia niiname, mimi nitambeba tu.” Chezo alizidi kucheka. “Juzi
ulisemaje tena kuhusu kunyonya?” Chezo akamchokoza. “Sio kwa Naya. Yule nikifanikiwa
kumuweka kitandani, hakika nitamnyonya mpaka kidole kidogo cha mguuni.” Chezo
alicheka kwa sauti huku anapiga makofi mfululizo.
“Mimi nakumbuka uliapa na kusema kunyonya haramu kwako. Huthubutu.”
“Nakwambia si Naya. Siku akija humu ndani, sitaki hata simu. Nawaambia walinzi,
mtu asipite pale getini. Nibaki naye tu humu ndani. Peke yetu.” “Lini hiyo?”
“Daah! Yule anatakiwa taratibu. Mtoto wa kanisani yule. Sio kama haya
makurubembe yangu unavutia popote.” “Naya wa mrija?” Chezo akazidi kumchokoza.
“Tena mrija mwembamba kaka! Yule! Nitabeba mpaka kifo.” “Utaweza Malo wewe,
mzee wa sketi!” Chezo alimjua Malo kwa kupenda wanawake.
“Napenda kufunua tu sketi
kama burudani kaka. Fahari ya macho. Najipitia tu kama wengine. Lakini Naya!”
“Eeeh!” “Naya natunza mwenyewe. Nakula mimi mwenyewe. Namiliki mimi mwenyewe. Mwanaume
atakayepita kwa Naya, kifo ndio adhabu yake.” “Sio kumtahiri?” “Namtahiri
kwanza bila ganzi, halafu ndio namtoa hapa duniani kwa kifo.” Chezo alizidi
kucheka.
“Sasa naomba sherehe iishe Chezo. Nataka kulala. Ondokeni na
wanawake zenu wote.” “Hutaki tukuachie hata mmoja.” “Sitaki shombo leo. Acha
nifurahie busu la Naya.” “Lulu anakuulizia.” “Tena huyo mtoe kabisa.
Asiniharibie kwa Naya huko hostelini kwao bure. Wanaongea sana huko hosteli.
Sitaki hata kumsogelea asije kwenda kutangaza, Naya akaniacha. Mwambie Side
awarudishe sasa hivi.” “Naona wawili wamepata watu hapa hapa.” “Basi wewe mpe
Tula pesa yao. Mwambie usafiri upo kwa anayetaka kurudi Dar. Lakini hapa kwangu
asibaki hata mtu mmoja.” “Sawa.” “Na umwambie Fido, achangamshe mkono. Nataka nije
kulala.” “Tutamsaidia kusafisha kidogo, kabla hatujaondoka.” “Sawa.” Chezo
akaondoka akamuacha Malon akiendelea
kupiga miluzi huku akimwagilia maua yake, kazi aliyokuwa anawapa walinzi wake,
usiku huo akajikuta anafanya mwenyewe.
Tula na Lulu, waliokuwa wakiwamendea Chezo na Malon, waliambulia patupu walirudishwa na dereva mpaka hostelini kwao. Kwa kuwa walikuwa wamelewa, walilala tu. Hawa na msichana mwingine, anayeitwa Naiki, ambaye walimchukua, kufidia pengo la Naya alipokataa kwenda huko Morogoro kwa kazi waliyoitiwa na Chezo, wao walipata wanaume pale pale, wakaenda kulala nao. Kesho yake asubuhi wakarudi Dar kwa basi.
Moja kwa moja chumbani kwa kina Tula. Zikaanza stori. “Nasikia
Malon jana alipotuacha pale, alirudi huku Dar, kumfuata Naya!” Wakaanza stori
za yaliyojiri mji kasoro bahari, Morogoro. Maana jana yake kila mmoja alikuwa
busy na kazi huku wakiwinda wanaume. “Kwani hukumwambia kuwa Naya hamtaki?”
“Chezo kanipa stori za Malon. Kaniambia ana roho ngumu kama chuma. Akitaka
jambo lake, ndio hilo hilo. Akaniambia hajawahi kupenda kama alivyompenda Naya.
Maana tulivyofika tu, Chezo si aliniita kule upande wa jikoni, unaambiwa Malon
akatoka kule juu chumbani kwake, akaanza kumtafuta Naya. Alipomkosa si ndio
akamuuliza Chezo! Chezo kumpa taarifa za Naya, bwana yule kaka alibadilika,
kama sio yeye! Akaniita kwa ukali anataka simu yangu. Bila kuomba, katafuta
namba ya Naya, akaondoka kurudi huku kumtafuta Naya.” “Sasa alimpata huyo
Naya?” Hawa akauliza.
“Atakuwa alimpata. Maana mimi nilifuatwa na Chezo, akaniambia
niachane na Malon kabisa. Sasa hivi yupo kwenye mahusiano na Naya.” Lulu
akajibu. “Heee!” Wote wakashangaa. “Haiwezekani. Naya!” “Ndiyo. Tena Chezo mimi
kanionya kabisa, akaniambia Malon bangi ile bangi mbaya. Nisitake kuingia kwenye
anga zake. Unaambiwa haogopi mtu. Akaniambia niachane na Naya, na wala asisikie
namtaja Malon. Akasema ikitokea Naya anamkataa Malon kwa ajili ya maneno yangu,
eti atanipasua kichwa.” “Anakutisha bwana.” Hawa akadakia.
“Mmmh! Hata hivyo mimi basi bwana. Mwenyewe ameshaonyesha msimamo
wa waziwazi. Hivi unajua alirudi mida ile ya usiku sisi tukiwepo pale pale,
lakini hakutaka kabisa kuingia ndani tulipokuwepo sisi na marafiki zake!”
“Kwanza nasikia hanywi.” Tula akaongeza. “Kwani pale ni kwa Malon au Chezo?”
Hawa akadadisi. “Mimi nilimuuliza Chezo, hakujibu.” “Mimi yule rafiki yao
niliyeenda naye kwake ameniambia pale ni kwa Malon.” Naiki akadakia. “Kweli?”
Lulu hakusadiki. “Mimi nahisi ni kweli, pale ni kwake Malon. Unafikiri kwa nini
rafiki yao anidanganye?” “Basi itakuwa kweli.” Wakakubaliana na Naiki.
“Ila alivyosema kama alivyokwambia Chezo. Maloni bangi kweli
kweli. Mkorofi wakupitiliza. Ila Chezo ndio mtu wake. Wamekua pamoja tangia
watoto. Alipo Chezo, ndipo alipo Malon. Ndio maana japokuwa Malon hanywi,
lakini Chezo anaweza kuita walevi wenzake pale nyumbani kwa Malon, watakunywa
kama vile, na Malon hana neno.” Naiki akaongezea alichosikia juu ya vijana hao.
Wakatulia kwa muda.
“Basi Naya kaupatia!” “Si kidogo. Nyumba nzuri!” “Unakumbuka Side
alivyotuambia wakati anaturudisha?” Lulu akauliza. “Kuwa hata hii gari
iliyotufuata na lile lililoturudisha yote ni ya Malon?” Tula akauliza kama
aliyekumbuka. “Eeh. Wakati tunaondoka Moro, unakumbuka ulimpa wazo lakubeba
abiria hata wawili apate pesa ya mafuta, akakwambia Malon akijua anaweza
kumkata mikono. Ukauliza kwa nini Malon na si Chezo, akakujibu kwa kifupi tu,
mali za Malon.” “Ndiyo nimekumbuka. Lakini pale nilikuwa nishalewa. Alisema
kweli. Kwa hiyo magari yote yake?” “Lile lililokuja kutuchukua sisi huku, na
lile aliloturudisha nalo sababu tuko wawili tu, na alilotoka nalo mwenyewe
Malon, yote nasikia ni yake. Bado mapya!” “Daah! Ningempata mimi yule!” “Mbona
tungekoma!” Tula akamalizia kwa Lulu, wakaanza kucheka.
Malon kwa Bosi wake Naya.
K |
itu cha
kwanza alichokifanya Malon siku ya jumapili alipoamka, nikutafuta namba ya simu
ya bosi wake Naya, Madamu Vane, ambae anamwita kazini mara kwa mara. Akazungumza naye nakumwambia
hataki awe anamwita Naya kazini. “Kwanza unajua kama wale ni watoto wa shule za
sekondari?” “Mimi sijui.” “Basi ndio nakujulisha. Acha kuwapa kazi watoto ili
uwanyonye. Ajiri watu wazima. Inakuwa ni kama unawauza kwa wanaume!” “Wakija
wanadanganya umri ili niwape kazi.” “Sio kweli. Kama ungekuwa hunufaiki na umri
wao, si ungekuwa ukiomba kuangalia vyeti vyao vya kuzaliwa kabla hujawapa
ajira.” Kimya.
“Sasa
ili tusifikishane mbali, usimtafute tena Naya.” “Naya mwenyewe anataka kazi.
Anasema anashida na kazi. Tena nisipomwita, ananipigia.” “Sina muda wakubishana
na wewe. Ila ukumbuke nimekuonya.” “Sasa akinipigia simu huyo Naya, nimwambie
nini?” “Na mimi unataka niwaambie nini polisi, wizara ya elimu, na haki za
watoto?” Kimya. Malon akakata simu.
Naya alimka
na kushangazwa na pesa aliyokuwa ameingia kwenye simu yake zaidi ya mara 4.
Akakaa kwa haraka huku macho yakiwa yamemtoka. Akapangusa macho mara kadhaa,
akarudia kusoma salio. “Oooh My!”
Naya akazidi kushangaa. Hapo hapo akampigia simu. “Malo!” “Vipi?” “Umenitumia
pesa kimakosa!?” “Kwa nini?” “Nimeona umetuma tena pesa, zaidi ya mara 4 wakati
jana ulinipa nyingine!” “Naomba ukalipie deni la kanisani na hapo hosteli. Kama
kuna kitu unadaiwa shuleni, nijulishe. Sawa?” “Nakushukuru sana. Sijui kama
unaelewa Malon?” “Naelewa Naya. Na mimi nilifanya kazi kama hivyo unavyokuwa
ukifanya wewe. Kwa hiyo naelewa sana tu.”
“Basi
najua unaelewa shukurani zangu. Umenisaidia zaidi ya hivi nitakavyo kwambia.
Deni la kanisani lilikuwa likininyima raha sana. Nilichukia kuona baba yangu
anafundishwa maisha na mtoto kama Ino! Eti sababu ya kutaka mkopo! Hakika Mungu
akukumbuke Malon. Asante sana.” “Karibu.” “Naomba nikuage sasa hivi, ili nijiandae kwenda kanisani,
kwa ibada, lakini pia nikalipe deni.” “Utanipigia ukitoka?” “Lazima Malon.
Nitakutafuta tufurahie wote. Asante sana. Sana, Sanaaaa....” Malon
akacheka. “Utachelewa
sasa.” Naya akacheka. “Natamani ungeniona nilivyofurahi!” “Nakusikia.” Wakacheka.
Na kuagana.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
Naya alikwenda kutoa pesa yote aliyokuwa ametumiwa siku hiyo. Akaigawa
na kuweka kwenye mahasha mbili kubwa, kisha akakimbilia kanisani kabla ya ibada
kuanza, hakuwakuta wazazi wake. Na wakati mara zote wazazi wake wanawahi.
Akawapigia simu. Baba yake akamwambia mama yake ameamka mguu ukimuuma sana.
Aliutonesha asubuhi hiyo, aliamka unanafuu, akadhani umepona. Akaanza kuutumia,
umerudi kuvimba. “Basi
nakuja sasa hivi kuwasaidia hapo nyumbani. Nilikuwa hapa kanisani.” “Sasa si
usubiri ibada iishe!” Naya hakuwa hata na nia ya ibada ila kulipa deni.
Akaingia ofisini kwa mchungaji kwa ujasiri wote. Akamkuta na Ino,
pamoja na mama yake. Alitamani kuruka kwa furaha. Kwa ujasiri wote, akamsogelea
mchungaji pale kwenye meza. “Siku ile ulinitajia kiasi mnachomdai baba.
Nimekuja kumalizia deni.” “Lote!?” “Ndiyo. Naona tumalize tu.” Naya akamkabidhi
zile bahasha mbili zikiwa hazijafungwa kabisa. Mchungaji akazitoa zile pesa
nakuanza kuhesabu. Wengine wote kimya.
“Nashukuru sana kwa msaada wenu.” Naya akataka kutoka. “Naya!” Ino
akaita. Naya akageuka. “Tunaweza kuzungumza?” “Naomba iwe wakati mwingine Ino.
Sio sasa.” “Ujue nataka kuoa.” “Kila la kheri. Mungu akufanikishe.” Mama yake
na Mchungaji wakashangaa ujasiri wa Naya. “Hatuwezi kuagana juu juu Naya.
Lazima tuzungumze.” “Ulazima huo unatoka wapi Ino? Au ni katika kuendeleza
tabia zako zakibabe? Wewe umeshasema unataka kuoa, sasa kuna kitu gani
chakulazimishia mazungumzo kati yetu?” Kabla hajajibu, Naya akatoka.
Walishamkera, hakuwa na hamu nao.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
“Nakusikiliza
Naya.” “Tutaongea vizuri wakati mwingine.” “Acha kunifanyia hivyo Naya! Malizia
basi.” “Sitaki kutoa ahadi ambazo nitashindwa kutimiza baadaye.” “Nakuahidi
nitakusaidia kutimiza. Niambie tu.” “Nilifikiria kuja kukuona Morogoro.”
“Naomba usibadili mawazo tafadhali. Nitakuja kukuchukua mimi mwenyewe. Angalau
ufike tu nyumbani kwa mara ya kwanza. Halafu wakati mwingine mimi ndio nitakuwa
nakuja kukuona Dar, mpaka unapokuwa likizo.” “Sawa. Kwa hiyo tupange jumapili?”
“Kwa nini sio ijumaa au jumamosi?” Malo akauliza.
“Ijumaa
nakuwa natoka shule mchana. Sitaweza kuja na kurudi.” “Sio lazima ukarudi siku
hiyo hiyo. Naweza kukurudisha hata kesho yake.” “Malon!” “Nakuahidi nitakuwa na
nidhamu.” Naya akabaki kimya. Akaingiwa na hofu. “Sitafanya chochote bila
ruhusa yako, Naya. Ikilazimu mimi nitakuachia kitanda.” “Halafu wewe utalala
wapi sasa!?” “Nina makochi pia. Hivi sikukwambia?” Naya
akacheka kidogo. “Malon!”
“Kweli. Nina kitanda na makochi.” “Haya bwana.” “Kwa hiyo nijiandae na ugeni wa
ijumaa?” “Ndiyo.” Naya akajibu na cheko la aibu kidogo. Akamsikia Malon akisema, “Yesss!” Naya akacheka.
“Umefurahi
nini sasa?” “Kutembelewa na Naya!” “Lakini kama nikiwa na kazi jumamosi,
itabidi..” “Uahirishe.” “Malon!” “Kweli Naya. Nina hamu na wewe.” “Hata mimi
nimeanza kukumiss.” Malon akafurahi kusikia hivyo. “Basi nakuahidi wakati mzuri. Hutajutia.” Naya
akacheka. “Bye.”
“Bye.” Wakakata.
Juma hilo likawa zito kweli kwa Naya na Malon. Masaa hayaendi.
Lakini kila mtu alijua mambo ya Naya yamebadilika. Alijawa furaha kila wakati.
Ametulia sio mtu wa wasiwasi kila wakati. Hakuulizia maswala ya kazi kabisa.
Akatamani yule mama anayempa kazi, asimtafute ili asimkatalie na kuharibu kazi.
Akashangaa mpaka alhamisi hakuna simu yeyote yakuitwa kazini.
Alifika kwao akamuomba mdogo wake na baba yake wamsaidie kushusha
mizigo. Walipomaliza baba yake akaanza. “Unapata wapi pesa Naya!?” “Kule
ninapofanya kazi, wanakopesha. Nikaona kuliko kudaiwa kanisani wanakokujua
wewe, ni heri nikope wasipokujua. Nimemuomba bosi wangu awe ananikata asilimia
75 ya mshahara wangu mpaka nimalize deni. Nilitaka kutuliza mawazo shuleni. Sio
nasoma huku nawaza maswala ya madeni!” “Mungu atatusaidia. Na hapo tutatoka tu.”
“Naamini hivyo baba.” Naya hakuamini kama uongo wake umepokelewa kirahisi
hivyo.
Kwa kuwa alikuwa na nguo za shule bado, angalau akaaminika kuna
shule inayoendelea. Sio kazi tu. Mdogo wake akaambiwa amtayarishie chakula
haraka. Na yeye alikuwa ametoka shule. Wakala na mdogo wake. Akasaidia kufua
nguo za mama yake na baba yake, akaondoka akiwa amezianika, jioni hiyo, akarudi
hosteli.
Pale hosteli kila mtu alishajua mahusiano mapya ya Naya na Malon.
Na pale chumbani walishazoea kumsikia Naya akizungumza na simu taratibu
kitandani kwake kwa muda mrefu tu. Aliporudi, alikuwa amechoka. Akapanda
kitandani kwake, akampigia Malon.
“Inabidi
ujifunze, ili na mimi nije nifaidi.” Naya akacheka. “Mbona unacheka?” “Pale
nyumbani hawapendi chakula changu. Heri wanipe kazi nyingine, mdogo wangu
anayenifuata, tena wakiume, ndio apike, lakini sio mimi.” Malon
akazidi kucheka. “Kwa
hiyo hujui kupika, mke wa Malon.” Naya alicheka sana. “Umefurahi nini?” “Unataka
kuja kunioa?” “Kabisa. Nikumiliki kihalali.” “Basi ujue mkeo mapishi sifuri.”
“Tutakula vibichi hivyo hivyo.” Naya akazidi kucheka.
“Kesho
umeniandalia nini?” “Wewe mgeni uje ukiwa umejiandaa kufurahishwa tu.”
“Utanifanya nione masaa hayaendi.” “Mbona hicho ndio kiliochangu tokea
uliponiambia utakuja! Masaa yamenigomea kwenda kabisa” Wakaendelea
kuzungumza mpaka Naya alipolemewa na usingizi. Wakagana.
Ijumaa.
N |
aya alitoka
darasani mida hiyo ya mchana, akarudi hosteli kuoga. Wakati anavaa, Tula akaja
kumwita kuwa Malon yupo sebuleni anamsubiri. “Asante.” Tula akatoka. Akamaliza
kuvaa. Hakujitengeneza sana. Akatoka. Malon alisimama alipomuona Naya.
Akamdaka, nakuanza mabusu palepale. Naya hakukataa. Akajituliza. Akamkumbatia vizuri
na kumvuta karibu na kuendelea kumbusu. Walianza kuitana na kujiiba
kuchungulia. Akaacha kumbusu.
“Nilikuwa na hamu ya kukuona Naya!” Akamnong’oneza akiwa bado
amemkumbatia. “Nimefurahi kukuona Malon. Asante kwa kuja.” Malon akarudia kunyonya
midomo ya mwanadada huyo taratibu tu. “Twende.” Naya akacheka. Akapitisha mkono
kiunoni, wakatoka. Ghafla ule ukimya wa mle ndani ukabadilika wakati wanatoka
mlangoni. Wakasikia watu wakishangilia na kuitana. Naya hakugeuka nyuma,
akafunguliwa mlango, wakaondoka.
“Njaa inakuuma sana au
unaweza kuvumilia mpaka tufike nyumbani?” “Nitavumilia tu.” “Basi anza na
soda.” “Naona mgeni nimeandaliwa kweli!” “Nilivyo furahi! Acha tu.” Naya
akazidi kujisikia vizuri. Waliposimama kwenye taa za Ubungo, Naya akamtolea
risiti tatu. “Nini tena?” “Nakuonyesha furaha yangu. Risiti ya malipo ya ada,
hosteli na kanisani alipewa baba, jana baba alinipa. Hivi unavyoniona,
sidaiwi.” Malon akacheka. “Hongera sana.” Waliendelea kuongea na kucheka mpaka
walipofika Moro, nyumbani kwa Malon. Giza lilishaanza kuingia.
Nyumbani kwa Malon!
“Unataka kuoga kwanza au unakula
kwanza?” “Kwanza nikupongeze kwa nyumba nzuri. Nilisikia sifa zake, kule
hosteli.” “Daah! Wale watoto wanaongea eeh?” Naya akacheka. “Lakini wameongea
kweli. Hongera.” “Asante, na karibu. Jisikie upo nyumbani.” “Asante.” “Kwa hiyo
nini kinaanza?” “Naomba kula kwanza.”
“Twende.”
Akapelekwa jikoni. “Vyakula vyote hivi peke yetu tu au kuna wengine
wanakuja!?” “Mimi na wewe tu. Chakututosha muda wote utakao kuwepo na mimi
hapa. Hakuna kutoka.” Naya akamwangalia Malon, akacheka kidogo. “Nataka nikae
na wewe tu. Hata kama ni masaa matatu tu, lakini yasiyo na mwingiliano wowote ule
hata njaa. Si sawa?” Naya akatingisha kichwa kukubali huku akicheka. “Basi
tule. Wewe pita hapo, chagua chochote unachopenda, pakua. Na mimi nitapakua.
Lakini nataka uanze wewe.” “Asante.” Walikaa hapo wakila na kuzungumza mambo ya
kawaida tu mpaka wakamaliza.
“Nimefurahia chakula. Asante.” “Kama
umependa, nimefurahi.” Malo akabaki akimtizama. Naya akainama. Akamsogelea
pale. Akasimama nyuma yake akaanza kumbusu mgongoni, akaja begani kuja mpaka
sikioni, shingoni. Kisha akamuacha. “Nisubiri nisuuze hivi vyombo tulivyotumia,
tukamalizie matunda na juisi sebuleni.” “Acha nikusaidie.” “Mgeni siku ya
kwanza. Leo wewe mgeni wangu.” Naya akacheka. Akambusu kichwani, akaenda lilipo
sinki. Akaosha hivyo vyombo viwili na vijiko. Akamaliza.
Kisicho
Ridhiki, hakiliki.
Naya naye akawa amemaliza juisi yake. “Tuhamie sebuleni au
chumbani, tukakae huko. Hapa nimeshakinahiwa na harufu ya chakula.” “Sawa.”
Naya alikuwa akiangalia simu yake. “Unategemea simu kutoka kwa yeyote?”
“Nimeshangaa yule mama hajanitafuta weekend hii wakati amewaita kina Tula!
Sijui niliharibu mara ya mwisho! Nimekosa raha.” “Ulitaka kwenda?” “Hapana
Malon. Lakini angalau nikatae. Kutoniita mimi wakati tulifika kwenye ngazi ya
juu ya mahusiano, mpaka watu walianza kujiuliza ni kwa nini mimi wakati mgeni,
gafla kunibadilikia, sio kitu kizuri kwa malengo niliyokuwa nayo kwenye ile
kazi.” “Labda hakuwa na nafasi za watu wengi.” “Hapana Malo. Hata akiwa na
nafasi ya mtu mmoja siku hizi, nakuwa mimi kwanza. Ndio maana hata siku ile
alinipangia meza za mbele kwa wageni wake anaowaheshimu. Nimekosa raha sana na
nimeingiwa na wasiwasi!” Malon akamuhurumia.
“Nikwambie kitu lakini usikasirike?” “Nini?” “Naweza kuwa
nimechangia kutokuitwa kwako.” Naya akakunja uso kama asiyeelewa. “Nilimwambia
asikutafute tena.” Naya alishtuka na kutoa macho. “Kwa nini!?” Ule mshtuko wa
Naya, ukamtia wasiwasi Malon mwenyewe. Akababaika.
“Ilikuaje Malo? Ni nini kilikupelekea ufanye hivyo!?” “Kwanza
nikuombe msamaha Naya. Nahisi ni kama kutaka kukulinda.” “Na nini!?” “Yale
mazingira.” “Yapi Malon!?” “Yale ya vishawishi.” Naya akafunga macho. “Naya! Naomba
usipaniki.” “Hujui ulinichonifanyia Malon. Ile ilikuwa zaidi ya kazi kwangu.
Nilikuwa najifunza vitu vingi sana kwa yule mama. Ili siku moja na mimi nifanye
kitu kama kile! Hiyo ni moja. Mbili, ni maisha yangu Malon. Mimi ni mdogo kwa
umri, lakini nina malengo Malon! Wewe kuwa mwanaume wangu wa kwanza kukukiss
haijawa bahati mbaya. Walishanifuata wenzako wengi kama wewe, wenye ahadi na
maisha mazuri tu. Nimekuchagua wewe Malon. Sijui kwa nini! Lakini nilikuahidi
nitakuwa mwaminifu kwako! Vishawishi havitaanza baada ya kuwa na wewe. Ninavyo
vingi tu. Nategemea ile kazi inisaidie kuishi kwa sasa.”
“Nitakusaidia Naya.” “Hunijui na wala sikujui Malon. Ndio tumeanza
mahusinao. Hujui shida zangu. Hatujui tutadumu kwa muda gani. Hujui kesho yako
ikoje. Tumeanza hata hatujamaliza juma, tayari unakuwa kama Ino ambaye
nimekusimulia shida zake!” Naya alikuwa anasikia kama kuchanganyikiwa.
“Samahani Naya.” “Nahisi nimefanya haraka Malon. Sipo tayari kuwa
kwenye mahusiano yeyote ya kimapenzi kwa sasa.” “Naya! Unaniacha kwa kosa
moja!?” “Hapana. Sio kwa kosa hili. Kwa vile ulivyo Malon. Unataka kunifanyia
kama Ino! Kutawala kila kitu, wakati hamjui nilipo na ninapopitia. Hujui
malengo yangu Malon. Hunifahamu na umeweza kuchukua hatua kubwa kama hiyo
kwenye maisha yangu! Halafu nimekuahidi nitakuwa mwaminifu kwako! Inawezekana
umeshadanganywa sana, lakini Malon, hushangai kwa mimi mtoto niliyezaliwa Dar,
kukulia Dar, katikati ya jiji na kunikuta nafanya kazi kama zile, nazungukwa na
wanaume wengi kama wewe, leo wewe kuwa mtu wangu wa kwanza kukuruhusu unishike
vile na kunibusu?” Malon kimya.
“Kweli bado umeshindwa kuniamini Malon! Ni nini nitakufanyia
baadaye uje uniamini?” “Nilikosea Naya.” Malon akataka kumsogelea. Naya akarudi
nyuma. “Hapana Malon. Hukukosea. Hivyo ndivyo ulivyo. Naomba niondoke.”
“Tafadhali Naya, usiondoke.” Naya hakujibu. Akarudi sebuleni alipoacha mkoba
wake, akauchukua. “Naya!” “Nakuhakikishia Malon, hunihitaji mimi kwenye maisha
yako. Mimi sio msichana unayemuhitaji. Nina mambo mengi na malengo makubwa sana
kwenye maisha yangu. Kwa sasa najihitaji mimi na akili zangu tu. Wala sio
misaada unayonipa na kutaka mimi nifanye unachofikiria ni sawa. Utaua ndoto
zangu kabisa Malon. Nitabakia kujulikana mimi ni mwanamke wa Malon. Basi.” Naya
akatoka.
Malon akamkimbilia. “Naomba usubiri tuzungumze Naya. Tafadhali.”
Naya akasimama. “Kwa kuwa mimi ndiye nimeharibu, naomba nipe nafasi ya
kutengeneza.” “Kwa kufanya nini?” “Nitampigia simu yule mama, nizungumze naye.”
“Sawa, nitashukuru.” Naya akageuka na kuanza kuondoka. “Sasa unaenda wapi
Naya?” “Narudi Dar.” “Sasa hivi!?” “Kabisa Malon. Naenda kwa yule mama sasa
hivi kwenda kuzungumza naye.” “Tafadhali Naya, usinifanyie hivyo!” “Angalia
hapa.” Naya akamsogelea Malon.
Akafungua simu yake sehemu ya Doc. Akaanza kutafuta sehemu
aliyokuwa ameandika mambo fulani. “Soma hapa, na hapa.” Malon akapokea ile
simu. “Hayo ni malengo yanayofanana na yule mama na hayo ni makosa niliyogundua
anafanya kwenye ile biashara. Chini nimeandika vitu gani vya kuboresha, kama
nitafanya biashara kama ile. Mawazo machache ninayompa yule mama, na
kumuongezea faida, yamenisogeza karibu naye japo mimi ni mdogo kwa kiongozi
wake. Najipendekeza kwake zaidi, ili anisogeze karibu na watu anaowaita wamaana!
Ili nikija kuanza kitu changu iwe rahisi nakuwa nimeshatengeneza mtandao wa
watu watakao nisaidia. Kunitengenisha na yule mama, nikufuta kila kitu
nilichoandika hapa.” Naya akachukua simu yake.
“Umenikatili Malon. Hivyo vitu nilivyoandika, sijakurupuka.
Nimeandika nikiwa nimetulia. Unaponiona sina mahusiano na wateja tunao wahudumia
sio kwa sababu sina shida au sina tamaa za mwili. Ni kwa sababu naona ni
afadhali nikose milioni moja sasa hivi, nije kutengeneza milion 10 baadaye.
Sijui kama unanielewa Malon. Kwa kulala na wale watu pale, au watu kama nyinyi
kwa pesa chache hizi mnazotuhonga sasa hivi, nikufuta mahusiano mazuri ya
baadaye.” Naya akamgeukia vizuri.
“Angalia sasa hivi. Kwa kukuruhusu tu unibusu, umenipa pesa, na
kuamua kufuta malengo yangu bila hata kuniuliza! Kwa busu na pesa chache tu ulizonipa.
Lakini ningefunga hisia zangu, nikasimamia msimamo wangu tokea mwanzo
nilipokukatalia, sasa hivi ningekuwa na yule mama. Pengine kuna kitu
kingeongezeka katika malengo yangu ya baadaye. Nimevunja maadili yangu.
Nimeruhusu hisia zangu zinizidie. Nimekukaribisha kwenye maisha yangu,
umeniharibia jambo kubwa sana lililobeba hatima ya maisha yangu.” Naya hakuwa
akiongea akiwa amepaniki.
“Naya, nimeahidi kurekebisha.” “Nitashukuru sana. Lakini sitaweza
kuendelea na wewe Malon. Tafadhali tafuta mwanamke mwingine. Hunihitaji mimi
kabisa. Nina mambo mengi mno yanayoendelea sasa hivi. Nina shida ambazo
haziwezi kutatuliwa kwa misaada unayoahidi kunipa.” “Umekasirika Naya, naomba
utulie.” “Sijakasirika, lakini naona sipo tayari kwa mahusiano Malon. Hata
hivyo nafikiri sikufikiria vizuri na sijui kwa nini! Sijui nimeingiwa na nini
hata mimi sijielewi! Ndio nipo mwaka wa mwisho, nimalize O level, halafu
naanzisha mapenzi! Sidhani kama ni wakati mwafaka huu. Tafadhali endelea na
maisha yako, Malon. Sipo tayari. Samahani sana kwa kukupotezea muda wako.
Naomba niondoke.” “Basi naomba nikurudishe.” “Hapana. Huna sababu yakufanya
hivyo.” “Basi naomba nikupe dereva wangu, kama mimi umenichukia kwa kiasi
hicho.” Naya kimya.
Ni kweli hakutaka kutumia masaa mengine pamoja na Malon kwenye gari akimrudisha Dar. Malon akatoa simu yake. Akapiga na kumuita Side. Alimtaka afike hapo mara moja bila kuchelewa. “Side atakupeleka kokote unakotaka kwenda. Hatakuacha mpaka umruhusu. Unaweza kumtumia pia kukupeleka kwa huyo mama.” “Asante.” Naya akashukuru. “Naomba ukasubirie ndani basi.” “Hapana Malon. Naomba nikasubirie nje ya geti. Nitakuwa sawa tu.” Naya alitoka bila kugeuka.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
S |
ide alifika
hapo bila kuchelewa. Akamchukua Naya, wakaondoka. Side alijua amembeba Naya.
Alijua habari za Naya zaidi ya Naya anavyofikiria. “Tunaelekea Dar?” Akauliza
kiustarabu sana. “Ndiyo.” Naya alijibu kwa kifupi tu, macho kwenye simu yake
akimtumia ujumbe Madamu Vane akiomba radhi na kumuomba arudi kazini. Bila
kuchelewa akamjibu kwa uwazi kabisa, akimkatalia. Side alimuona Naya ameinama
akilia kwa uchungu sana. Alishindwa hata kumtuliza. Alilia Naya. Akalia na
kulia huku ameinama kwenye hicho kiti cha mbele alichokuwa amekaa.
“Tafadhali
naomba umpokee tena Naya. Mimi mwenyewe nitakutafutia kazi na nitakulipa.” “Hii
ni biashara. Nikiharibu kwa makosa yakijinga kama hayo naweza kufungwa jela.
Sasa pesa utakayonilipa itanisaidia nini nikiwa jela? Nina majukumu ya watoto.
Nina binti kama Naya. Nikiwa jela nani atawatunza watoto wangu? Ile simu
uliyonipigia na onyo ulilonipa ni vile niliogopa kukupigia tena simu na
kukushukuru, kwa kuwa ulikuwa na hasira. Umeniepusha na mengi.” Malon
akaishiwa nguvu kabisa, akawa kama amefungwa mdomo. “Naomba nikuage. Nipo kazini.” Yule mama
akakata simu. Alimuacha Malon kwenye majuto, asiamini kama amemuharibia Naya
kwa kiasi hicho.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
“Naomba unishushe Kiluvya, tafadhali. Sitafika mjini.” Baada ya
kutulia, Naya aliweza kuzungumza na Side. “Bila shaka.” Side akajibu huku akiendelea
kuendesha. Naya akapitiwa na usingizi akiwa anafikiria nini chakufanya tena.
Aliamshwa na Side kuwa wamefika kwenye kituo alichokuwa amemwambia Kiluvya.
“Nakushukuru.” “Unataka nikushushe hapa hapa kituoni?” “Inatosha, asante.”
“Naweza kukufikisha kabisa.” “Nakushukuru kaka yangu. Asante.” Naya akashuka na
kumuacha Side pale pale kituoni.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
Naya kipenzi cha baba yake, alimjua kwa kumtizama. “Mbona leo
usiku hivi?” Naya kimya. “Umekula?” Baba yake akaendelea kuuliza. Akatingisha
kichwa kukubali. Akaona machozi yanatoka. “Nisindikize bandani. Nimesikia
ng’ombe wanalia.” Akafungua mlango, wakatoka tena nje na Naya. Wakazunguka
nyuma ya nyumba, wakaelekea kwenye banda la ng’ombe. Hapakuwa na mlio wowote wa
ng’ombe. Naya alijua baba yake anamtaka atulie.
“Nimepoteza kazi baba.” “Kwa nini?” Naya akaanza kulia tena.
“Umri
mdogo. Amesema mpaka nitimize miaka 18.” “Lakini mwaka huu ndio unatimiza
miaka 18!” “Amesema hatanipokea mpaka nitimize. Na hapo ujue inategemea
kama atakuwa na nafasi ya kazi. Nitafanyaje baba?” “Nilikwambia Naya, Mungu
anaona kila mapito. Najua ulikuwa na malengo makubwa na hii kazi, lakini
inawezekana Mungu ana malengo makubwa zaidi na unavyofikiria. Jipe muda.” “Sasa
wakati najipa muda, unafikiri nitaishije sasa?” “Sijui. Ndio unatakiwa kuanza
kufikiria Naya. Bado anakudai pesa ulizokopa kwa ajili ya kulipa madeni?” Naya
akakumbuka uongo aliomdanganya baba yake.
“Ndio imeisha hivyo. Nitalipaje nikiwa sina kazi!” “Basi naomba
utulie. Fikiria. Mimi nakuona unaakili sana Naya. Zaidi ya unavyofikiria. Na
mambo yako hayo ya ubunifu wa mavazi, unaweza kufikiria jambo zuri tu.” “Nitapata
wapi pesa?” Naya akamuuliza tena baba yake.
“Kuku wapo hapa. Mayai ya kienyeji yapo. Umeshafanya kazi,
umekutana na watu wengi ambao itakuwa rahisi kwako kufunguliwa milango kwao
kuliko mimi mgeni kwao ambao hata hawanifahamu. Tumia haya mayai kupata pesa.
Wapelekee hata maofisini na majumbani kwao.” Naya akaanza kucheka. “Muone.” “Nilikuwa
nimekasirika.” “Nilijua tu. Sasa hao watu wote Mungu aliokuwa amekukutanisha
nao, haikuwa kwa bahati mbaya. Anza kuwatumia kujinufaisha na utajiri wao.” “Ndio maana
nakupenda baba yangu. Ujue tumefanana akili za biashara?” Baba yake
akacheka.
“Halafu mbona sisikii ng’ombe anayelia hapa.” “Alikuwa akilia
mmoja. Muda tu. Nikaja, nikakuta amejifunga kamba shingoni. Amejizungusha,
ikawa imemkaba. Nikamtoa. Sasa hivi nilikutoa wewe uje ulie hapa mpaka umalize,
ndipo ukalale.” Naya akacheka. “Ujue nimelia kama lisaa?” “Nakujua. Na ninajua
ukichoka kulia, ndio unakuja nyumbani.” Naya alicheka sana. “Kumbe unanijua?”
“Najua sana.” Naya akacheka.
“Kesho nitakwenda kununua trei za mayai Kariakoo. Huku nawasiliana
na watu nione kama watahitaji mayai. Nitafanya kesho, jumapili narudi hosteli.”
“Kanisani?” “Nikwambie ukweli baba?” “Nakusikiliza.” “Mimi pale siwezi kurudi
tena.” “Kwa nini? Au sababu ya deni?” “Walikudai vibaya sana baba, wakati wewe
ni mshirika wao wa muda mrefu, tena mwaminifu! Unajitoa pale kwa uaminifu tena
bila kutaka kulipwa. Wakati ule kabla mambo hayajakuharibikia ulikuwa ukitoa
michango mbali mbali, leo naona kama wanakugeuka!” “Ujana mwingi. Baba yake Ino
alikuwa mtu mzuri sana asiyeangalia kipato. Ameacha kanisa kwa vijana wale wanao
endesha mambo kisheria, sio kiroho. Kama uliahidi kulipa deni tarehe fulani,
basi watataka hiyo tarehe pesa yao ilipwe.” Naya akaguna.
“Mimi nimeshindwa baba. Hawana utu. Halafu pia Ino amenifika kooni
baba. Siwezi kukaa naye sehemu moja. Ananikera, halafu..” “Hana nidhamu.” Baba
yake akamlizia. “Kumbe unajua! Sasa kwa nini humwambii mama?” “Anasema hataki
uishie kama yeye.” “Sasa itanisaidia nini kuishi kwenye nyumba nzuri lakini
sina raha baba?” “Mimi pia nilimwambia hivyo. Lakini naona mwenzangu amempenda
sana Ino. Sasa sijui.” “Mimi simtaki na nimemwambia kabisa simtaki. Kwanza
ameniambia anaoa.” “Muongo.” Naya akashtuka.
“Baba! Mbona ameniambia.” “Anamuoa nani yule. Maneno mengi tu.
Nilimsikia mama yake akimwambia mama yako. Si alikwambia mkiwa ofisini kwa
mchungaji ulipoenda kulipa deni?” “Umejuaje!?” “Nakwambia mama yake alimfuata
hapa mama yako. Akalalamika kuwa ulimvunjia heshima Ino. Lakini hana mwanamke
yeyote. Alikwambia vile ili kukutisha tu. Lakini nakubaliana na wewe Naya, Ino
atakusumbua sana. Anaujuji mwingi.” Naya akafurahi sana kuona baba yake yupo
upande wake. Wakati wote alikuwa anakuwa kimya linapokuja swala lake na Ino.
“Asante baba.” “Wewe nenda kalale, kesho uanze siku ukiwa umetulia.” Naya
akarudi ndani chumbani kwake. Wadogo zake wakiume walikuwa wakilala chumba
chao, yeye peke yake, na chumba cha wazazi wake, nyumba ikawa imekamilika.
Vyumba vitatu tu.
Usiku huo alichofanya nikuhamisha namba zote anazotaka yeye,
kwenye namba hiyo mpya. Uzuri namba zake alikuwa akizitunza kwenye simu sio
line. Akaanza kuandika majina ya watu wakuwasiliana nao kesho yake. Akawapanga
vizuri. Ndipo akalala.
Mlango Mmoja ukifungwa.....
A |
lichofanya
chakwanza ni kumtafuta tena yule yule Madamu Vane akamwambia bado anashida na
kazi, kwa kuwa anahitaji sana pesa. Akamwambia kwa wakati huo anafanya biashara
ya kuuza kuku na mayai. Kienyeji, akampa bei na ya kuku wa kisasa. Akaandika
bei zote vizuri. Akamuomba amtafutie wateja, na akamsihi asiwape kina Tula
namba yake. Akamtumia ule ujumbe. Akaandika ujumbe kwa watu wengine aliokuwa
akiwafahamu na alio wahudumia kwenye shuguli. Akiwaambia anauza kwa jumla na
rejareja. Kwamba anaweza hata kuwapelekea majumbani. Naya alituma huo ujumbe
kwa watu wengi tofauti fofauti.
Wakati anaendelea kujibu maswali ya watu aliowatumia ujumbe, simu
ya Madamu Vane ikaingia. Akamuelezea mazungumzo yake na Malon. Naya akamuomba
msamaha. “Nilitaka kujichanganya tu mama yangu. Lakini basi. Nimeelewa. Na
yeye ameomba msamaha. Naomba umsamehe. Nia yake ilikuwa nzuri, hakujua kama
wewe ni mama unayejiheshimu. Alijua unatuuza.” Naya akampamba wee, mpaka
yule mama akatulia. “Sasa hayo mayai unayo mengi kwa kiasi gani?” “Ya kisasa ninayo
mengi.” “Kuna mtu anahoteli mjini. Nimezungumza naye, ndiye ameniuliza hivyo.
Una uwezo wakumpeleka trei ngapi kwa siku?” “Naomba nipige mahesabu, kisha
nikujibu kwa hakika.” “Unaakili Naya! Ndio maana mimi nakupenda na nilikuweka
karibu.” Naya
akacheka. “Ila mimi nataka trei mbili za mayai ya kuku
wa kienyeji, kila week.” “Sawa mama yangu. Asante kuniungisha. Nikuletee na
wewe leo?” “Wewe tu.” Naya akacheka. “Basi nakuletea leo, na nitakupigia tena ili kukupa idadi ya
trei ninazoweza kupeleka.” “Sawa.” Wakaagana,
Naya akatoka anakimbia.
“Babaa!” “Acha kelele Naya. Mama kalala.” Mdogo wake mdogo, Bale
alimjibu akiwa jikoni. “Baba yuko wapi?” “Aliamka alfajiri kwenda Kariakoo.
Alisema anaenda kununua trei za mayai.” Naya akafurahi sana. “Mama ameamkaje?”
“Mguu ulikuwa ukimuuma. Zayoni amempelekea uji na dawa, amesema anarudi
kulala.” Naya akaona aende akamsalimie mama yake chumbani kwao. Aliamka na
mambo ya biashara.
Alimkuta amejilaza tu kitandani. “Kelele za nini asubuhi asubuhi?”
Naya akacheka. “Shikamoo mama.” “Uso huo wafuraha. Kuna habari gani njema?”
“Nimepata wateja wa mayai.” “Wewe utakua na akili ya biashara kama baba yako!
Haya umewapatia wapi hao wateja? Maana yanaharibika tu huko ndani!” “Kule
nilikokuwa nikifanya kazi. Nimemuomba bosi wangu anitafutie wateja. Sasa amenipatia
kwa rafiki yake mwenye hoteli mjini. Ndio anauliza nina uwezo wa kupeleka trei
ngapi!” “Yapo mengi tu.” “Bwana mama! Sema idadi tutengeneze pesa.” Mama yake
akacheka. “Hivi ujue hujanijulia hali Naya mwanangu!” “Pole mama. Lakini unajua
tukipata pesa hata mguu utapona!” Wakacheka. “Unajisikiaje?” Naya akajiweka
kitandani kwa mama yake wakaanza kuongea.
Mara akasikia sauti ya baba yake. Akaruka mbio kutoka pale
kitandani. “Baba! Baba!” “Naya kwa kelele! Usipokuwepo humu ndani kunakuwa
kimya.” Bale mdogo wake anayemfuata, akalalamika akiwa jikoni. “Nimefanyaje? Si
nimemwita tu baba?” “Kwa nini usimfuate nje, kuliko kupiga kelele humu ndani? Nilishakwambia
acha kelele, mama kalala!” “Wala hajalala kwa taarifa yako. Tulikuwa naye
chumbani.” “Umeshamuamsha!” “Nimekuta hajalala kwa taarifa yako.” “Atalalaje ni
kisauti chako hicho chakelele.” “Usinipotezee muda. Wewe ndio unakelele.”
“Aliyekuwa..” “Mmeanza, Naya na Bale. Ni nini mnabishana tena?” Baba yake
akaingia. “Si Bale huyo!” “Bale gani, wakati ni wewe?” Bale akajibu. “Haya
naomba mnyamaze, muache kelele.” Baba yao akawanyamazisha. Bale alikuwa kidato
cha pili, wakati Naya cha 4, walikuwa hawaishi kubishana.
Naya akamvuta baba yake. “Umefurahi nini?” “Lile wazo lako la jana
usiku limejibu baba yangu. Sasa swala ni mayai. Tunayo yakutosha?” Naya
akamuelezea baba yake alichofanya, Bale akimsikiliza. “Akitulia huwa akili zake
zinafanya kazi huyo!” “Niache Bale.” “We Naya! Hebu rudisha akili hapa. Sasa
mjibu mwambie, tunaweza kwa sasa, kupeleka trei...” Baba Naya akafikiria kidogo
kisha akamtajia idadi ya mayai wanayoweza kupeleka. “Na mayai ya kienyeji?
Maana nayo nimepata wateja. Ngoja nikalete simu nikupe idadi wanayotaka.” Naya
akarudi ndani kwa haraka. Na mama yake akatoka akichechemea.
“Nimewasikia huko chumbani. Naona unamfundisha biashara mwanao.”
Baba Naya akacheka. “Lakini naona mwenzangu amechangamka!” “Akikufuatisha,
atafanikiwa.” Gafla baba Naya akaanza kupewa sifa na mkewe. Akacheka. Naya
akatoka akiongea na Madamu Vane. “Nakushuru sanaa, mama yangu. Kwa tenda
hiyo uliyotutafutia. Leo nakuletea lita moja ya maziwa, na mayai ya bureee.” Wakacheka na
kuagana.
“Haya tupe habari.” Baba yake Naya akamtaka asimulie. “Huyu mama
ndiye aliyekuwa bosi wangu. Ameniunganisha na huyo mwenye hoteli. Nimezungumza
naye hapo chumbani, lakini ameongea kwa haraka tu. Anasema kuna watu walikuwa
wakimpeleka mayai. Lakini wameanza kusuasua kwa sababu Mzee mwenye hiyo
biashara ya kumpelekea mayai, amekuwa akiugua kwa muda mrefu. Amewaachia
wafanyakazi tu. Hawampelekei mayai yakutosha na wakati mwingine hawapeleki
kabisa. Sasa anataka uhakika kama sisi tutakuwa tukimpelekea. Nikamuhakikishia.
Anasema kama tunayo hayo mayai, tumpelekee sasa hivi.” Wakaanza kushangilia.
“Subirini kwanza. Ila amepunguza bei kwa kuwa anasema anachukua
mengi. Na hata kama tunayo zaidi tumpelekee tu.” “Hamna shida. Ni bora hivyo
kuliko hivyo yanavyo haribika hapa ndani. Twende ukanisaidie kuyapanga vizuri,
tupeleke.” “Baba alivyochangamkia!” “Malaika ndio ametibua maji hivyo. Ukichelewa,
ujue mwengine atatumbukia apone yeye, wewe uendelee na matatizo. Nayafunga sasa
hivi kwenye pikipiki yangu, nampelekea sasa hivi. Nipe tu namba yake.” Naya na
baba yake wakachangamkia kazi. Baba yake akatoka na trei 14 za mayai.
Huo ndio ukawa mwanzo wa kufufuka kwa wazazi wake. Biashara hiyo
ya mayai, ikazaa na uhitaji wa maziwa kwenye hoteli hiyohiyo. Kwa hiyo baba
Naya akawa akipeleka mayai, maziwa na akishinja kuku pia alikuwa akimpelekea
huyo mwenye hoteli. Ufugaji ukakolea hapo, pesa ikawa inaingia, Naya akatulia
shuleni.
Kwa kuwa kibarua kiliota majani, Naya akawa anatulia tu shuleni,
anategemea kutunzwa na wazazi wake. Akisikia mtu anataka mayai, basi anampigia
simu baba yake. Kazi yake ikawa kutafuta masoko. Baba yake akaongeza jihudi
yakuzunguka kwa wafugaji. Ananunua kwa jumla, tena kwa bei ya chini sana,
anaenda kuuza kwenye masoko anayokuwa anatafutiwa na mwanae. Mambo yakawa
mazuri. Utulivu ukawepo hata nyumbani kwao.
Baada ya kama mwezi hivi akiwa amejilaza kitandani kwake, kina
Wahija na wengine pia wamejilaza tu wanaongea hili na lile. Wakipeana stori za
mitaani na wakitoa uchovu wa shule wa juma zima, wakasikia Girls star
wanashangilia nje. “Wameshapata bwana hao watoto!” Wahija akasema. Naya
akacheka. Wahija akaita kwa sauti, akimtaka Tula aende. Tula akaingia akiwa
amechangamka kweli.
“Haya, kelele za nini?” “Sio mimi da Wahija.” “Ni nani wakati
nimekusikia wewe na wenzio?” “Ni Lulu.” Tula akajibu huku anacheka. “Bwana si
usimulie? Acha kunifanya nikuulize ulize.” Tula akaangalia nje ya mlango kama
wenzie wanamuona. Akaingia na kufunga mlango.
“Naya yupo?” Tula akauliza. “Hayupo, yupo kwao.” Wahija
akamdanganya. “Basi, sisi tulisikia Naya kaachana na Malon. Sijui ilikuwa vipi,
wewe unamjua Naya kwa maringo! Sasa Malon anapesa sana. Lulu alikuwa anamtaka
sana Malon. Sasa Chezo, niliyekuwa namtaka mimi akamuonya Lulu kipindi kile
asimfuatilie tena Malon, yupo na Naya. Sasa tulipoona Naya hayupo tena na
Malon, Lulu akaniomba nimtafute Chezo, amuunganishie kwa Malon. Sasa mimi
jumamosi ile nilimtafuta Chezo, jumapili tukawa naye siku nzima. Nikampa
yakikubwa mpaka nikamuona ametulia.” “Wewe mtoto ulienda mpaka Moro!?” Wahija
akamshangaa.
“Hapana da Wahija! Wale vijana wanapesa. Alichukua chumba kwenye
hoteli ya maana hapahapa mjini. Akaja na akanipa pesa ya maana. Basi turudi
kwenye ya Lulu sasa. Mimi nilipoona nimefanikiwa kumkoleza Chezo mpaka akakolea
ndio nikamwambia Lulu anampenda sana Malon. Na yupo tayari kutulia naye. Chezo
akasema ataenda kuzungumza na Malon, lakini linapokuja swala la wanawake, Malon
anakuwa na misimamo yake.” Tula akakaa kwenye kitanda cha Wahija.
“Sasa Chezo ameniambia Malon anampenda sana Naya. Unaambiwa karibu
kuchanganyikiwa!” Tula akapunguza sauti. “Usije kunitaja da Wahija. Hata Naya
usimwambie.” “We bwana unawasiwasi gani?” “Mwenzio Chezo kaniapisha. Kasikia
hapa maneno yanasambaa sana. Ameniambia akija kusikia Malon mwenyewe, hakawii
kuja kunivunja mbavu.” “Wewe nisimulie. Mimi nampata wapi huyo Malon
wakumsimulia na msikitini haji?” Tula akacheka sana.
“Da Wahija kwa maneno!” “Bwana wewe sema.” “Basi, unaambiwa siku
ile Malon alipokuja kumchukua Naya, akamfikisha mpaka nyumbani kwake. Unaambiwa
Malon alikuwa amejiandaa. Marafiki zake wote walikuwa wanajua siku hiyo
mwanamke wa Malon atakuwepo mjini, hakuna kumtafuta Malon. Wanasema ndio
ilikuwa mara yake ya kwanza kwa Malon kuwa na mwanamke, japo nasikia ni malaya,
ila hakuwahi kuwa na mwanamke. Sasa hawajui ilikuaje, Malon hajawaambia wenzie,
lakini si Naya akaondoka hata hajalala!” Wahija akaka kwa mshtuko.
“Acha masihara!” “Kweli tena. Unaambiwa Malon alikaribia
kuchanganyikiwa. Naya aliondoka nyumbani kwake usiku, akamuacha yule kaka
amepiga magoti anamsihi asiondoke. Lakini unaambiwa Naya akaondoka. Halafu
haijaishia hapo. Si Naya kabadili namba?” “Ndiyo.” Wahija akajibu kishabiki.
“Basi nasikia ni kwa ajili ya Malon. Kamkataa yule kaka. Naya kwa maringo!
Sijui anataka nini! Basi sisi tukaona tumchangamkie Malon. Maana akipona Lulu,
na sisi si tumepona?” “Ehe!” Wahija akataka aendelee.
“Mbona nilifanya sarakasi siku ile kwa Chezo! Siku nzima mtoto
nipo ulingoni kumuweka sawa Chezo, akamuunganishie Lulu. Basi ikawa kimya mpaka
sasa hivi Malon amemtumia pesa Lulu na ujumbe kuwa, akatafute gauni zuri la
heshima, kesho anakuja kumchukua, kuna harusi hapa Dar, anataka kwenda naye.
Amemwambia asiende kazini, atakuwa naye kesho.” Moyo wa Naya ulipasuka kwa
mshtuko.
Alitetemeka pale kitandani asijue ni kwa nini wakati yeye mwenyewe
ndiye aliyemuelekeza Malo kwa Lulu. Ilikuwa kama amemwagiwa maji ya baridi
sana, mwili ukafa ganzi. Akaumia sana moyoni. “Lulu kauchinja dada yangu! Sio
mwenzetu tena! Chezo aliniambia yule kaka anapesa sana. Hiyo pesa ya gauni tu
aliyomtumia Lulu, imetutoa mate. Na Lulu amesema hiyo kesho atamng’ang’ania
mpaka amlale. Na amesema akilogwa tu amtoe nguo, hatakaa akamsahau.” Tula
akaongea hapo kishabiki, akieleza mikakati ya Lulu mpaka akachoka. “Haya kampe
hongera zake.” Tuli akatoka akicheka. Chumba kile kikawa kimya. Hakuna
aliyeongeza neno.
Ni kweli Lulu alikuwa amejawa na furaha. Alikuwa akiimba kwa sauti
bila kuchoka. Kesho yake siku ya jumamosi ni kweli akaenda kutafuta nguo ya
maana na kiatu. Jioni wakasikia wakishangilia. Kuwa Malon yupo nje,
anamsubiria. Naya alinyamaza kimya bila kuweka neno. Lakini aliumia sana,
asijue kwa nini. Girls star walimkuwa wakimshangilia Lulu, mpaka Wahija naye
akatoka kwenda kumtizama. Alirudi akicheka.
“Bwana Lulu kapendeza yule mtoto! Na kweli amevaa nguo ya maana.”
Wahija akasifia, Naya kimya. “Sasa Naya mdogo wangu, kwa nini ulimkataa Malon?”
“Mimi naomba nisikujibu dada Wahija. Tafadhali dada yangu.” “Nipe tu sababu kwa
juu juu bila undani.” “Da Wahija!” “Sasa ubaya upo wapi Naya mdogo wangu?”
Wahija akazidi kumbembeleza. “Nimejiona mimi sipo tayari kwenye mahusiano. Ni
hilo tu.” “Kwamba wewe mdogo!?” “Sio udogo tu. Ndio mwaka wangu wa mwisho wa O level,
siwezi kuanzisha jambo ambalo...” Naya akasita.
“Wewe hukumtaka tu huyu bwana. Lakini huna udogo wakushindwa kuwa
kwenye mahusiano bwana! Tena kwa mwanaume anayekupenda hivyo! Kamuulize mama
yako au bibi yako aliolewa na miaka mingapi kama sio 14 au 13.” Naya akanyamaza
nakuendelea kusoma. Hakuna hata kilichokuwa kikiingia muda huo. Amekosa
mwanaume na kazi pia! Aliumia sana.
Kitendo chakutorudi Lulu usiku huo mpaka kesho yake mchana,
kilimuumiza sana Naya. Kuwa amelala na Malon. Aliumia sana. Lakini hakuwa na
pakusemea. Anamlaumu nani? Hakujua kama anampenda Malon kiasi kile. Akajiambia
labda ni wivu tu. Akatulia. Lulu alirudi akiwa amejawa kelele. Kila mtu alijua
amelala na Malon usiku huo. Aliongea bila kuficha huku akimsifia vile
alivyomtenda.
Usikose Mwendelezo kujua kilichoendelea kati ya Malon na Lulu
aliyempania mpaka amefanikiwa......
0 Comments:
Post a Comment