Naomi Simulizi |+1 205 767 8163 |naomisimulizi@gmail.com MAPENZI & PESA! - SEHEMU YA 5. - Naomi Simulizi

MAPENZI & PESA! - SEHEMU YA 5.

 Mc akachukua kipaza sauti, kutuliza watu na kuwaambia shuguli ndio inaanza rasmi. Walikuwepo watu wamaana watupu. Malon akaingia ndani. Mc akamwita jukwaani ili kukaribisha wageni, na yeye akasema mtu sahihi wakukaribisha wageni ni Naya. Akaenda kwa hofu kule kwenye chumba alichokuwepo Naya na warembo wengine. Alipoingia tu, kukazuka ukimywa wa gafla. Malon akajua tayari kumeshaharibika. “Vipi?” Naya akauliza huku akiendelea na shuguli. “Inabidi uje uongee neno la ufunguzi na kukaribisha wageni.”
“Si wewe ukaribishe tu? Bado nina kazi kidogo.” “Wewe ndio mwenye shuguli nzima Naya! Unajua nini kitaendelea leo, na nini kitafuata siku za mbeleni. Yote hayo wanatakiwa wasikie kutoka kwako mwenyewe.” Naya akavuta pumzi kwa nguvu huku akiendelea. “Basi nipe dakika mbili zaidi. Nitakuja.” “Sawa, nimemwambia Mc, akaribishe wimbo mwingine.” “Basi nakuja. Sitakawia.” Malon akatoka.

Naya alikunywa maji aliyokuwa ameletewa na Chezo, akatoka kwa haraka. Alikuwa amependeza sana. Vazi alilokuwa amevaa usiku huo, alibuni yeye mwenyewe. Akashonewa palepale na mafundi wao. Alipendeza sana. Akatoka, watu wote wakasimama na kumpigia makofi wakati Mc akimkaribisha. Naya akawa anapunga mkono na kucheka. Akageuka pembeni akamuona Malon, akamkonyeza ili aje. Malon akapanda jukwaani kwa haraka. Naya akamshika mkono. Aliletewa kipaza sauti. “Baba Naya!” Akaanza Naya, baba yake akampungia mkono akicheka. Alikuwa amekaa kiti cha mbele kabisa na mama yake pamoja na kaka zake. Akampungia mkono na mama yake.  

“Nimshukuru kwanza Mungu. Amekuwa mwema sana kwangu. Nikianza kueleza yale Mungu aliyotufanyia mimi na familia yangu, hauwezi kukosa jina la Malon, ambaye Mungu ametenda mengi kupitia Malon.” Watu wakapiga makofi. “Niwashukuru na wazazi wangu. Baba kwa kunitia moyo kufanya hiki ambacho nitaeleza kwa kifupi ninachofanya, na mama ambaye yupo nyuma yangu kila wakati kuhakikisha silemei upande mmoja. Yeye ashasema, anataka mwisho wa yote, nimkabidhi cheti cha chuo, ndio ugomvi wetu utaisha.” Watu wakacheka. Wadogo zake wakacheka zaidi. “Kaka zangu wanajua moto ambao huwa ananiwashia ndio maana wanacheka sana.” Naya akaongeza nakufanya wacheke tena.

“Japokuwa huwa ananifanya nikasirike kila anaposisitiza hivyo, akidai vyeti na kila matokea hata ya vijimitihani vidogo sana ninavyofanya chuoni, lakini mama yangu amenifanya nigundue uwezo mkubwa nilio nao. Kufanya yote kwa wakati mmoja. Nakiri sio rahisi, lakini inanilazimu. Kwa kuwa mama anadai vyeti, na..” Wakacheka kidogo. “Na Malon naye akawa anaamini uwezo nilionao.” Naya akamgeukia Malon.

“Nakushukuru sana Malon. Amesimama na mawazo yangu, mpaka baba ambaye ndio rafiki yangu wa kwanza na msiri wangu huwa tunamshangaa Malon. Nilimweleza tu kile ninachokipenda. Akataka kukiona kwa picha, basi akaanza kuweka mipango mizito iliyonishangaza hata mimi. Alikuwa akimwaga pesa kwa wazo na michoro niliyokuwa nimemuonyesha, mpaka leo nimeweza kuwaletea kitu kipya, kizuri, cha thamani, mbele zenu. Vazi nililovaa mimi na Malon hapa, ni moja ya ubunifu wangu, Mungu alionijalia.” Watu wakapiga sana makofi. Baba yake akasimama kabisa akipiga makofi, ndipo ukumbi mzima ukasimama tena. “Asante baba, asanteni wote.” Naya alisikika.

Baada ya kutulia, akaendelea. “Usiku wa leo, ninao warembo wazuri sana waliokubali kunibebea kazi zangu na kuzileta mbele yenu. Wote tunajifunza. Naomba muwapokee kwa upendo na muwatie moyo. Tusiwazomee hata wakikosea. Mwanzo ni mgumu.” Naya akacheka kidogo. “Na wenyewe ndio mara yao ya kwanza. Tafadhali tuwatie moyo ili tuweze kuona kile walichobeba. Asanteni sana, na niwashukuruni kwa kuja.” Naya akamaliza, akarudisha kipaza sauti kwa Mc, yeye akarudi kule kwenye chumba cha warembo wake,  watu wakiendelea kushangilia. Malon mwenyewe alishangaa na kuvutiwa jinsi Naya alivyozungumza kwa kujiamini.

Maonyesho yakaanza. Wale wasichana wakapita na yale mavazi kwa ustadi, watu wakiwashangilia bila upendeleo kama walivyofundishwa. Kufika na mwisho ambapo Loi ndiye aliyekuwa akifunga kwa vazi la mwisho, akaanguka alipokuwa akigeuka. Ilibidi kwenda kubebwa na kurudishwa ndani. Mc akaomba mwanamziki aliyekuwepo kutumbuiza wakati wanaangalia hali ya Loi. Naya, Malon na baba yake Naya walifuata mpaka kwenye kile chumba kujua Loi anaendeleaje. Hapakuwa na kuumia. Ni mshtuko tu.

Naya alitoka kutuliza wageni na kutangaza kuwa Loi yupo salama. Akanadi nguo zilizokuwepo pale ukumbini, na huku akitaka wamuungishe hata kama mtu atanunua kwa ajili ya mkewe, watoto na marafiki. Naya aliuza karibia nguo zote. Mwishowe akashukuru na kugawa mawasiliano yake kwa anayetaka mavazi kama yale na pengine hapakuwa na saizi yake, aliwahakikishia wageni wake kuwa wanaweza kuwatengenezea endapo watatoa  oda. Wakamaliza na kufunga, ndipo wale warembo wote wakapita kwa mara ya mwisho. Ni kweli ilikuwa nzuri, hata Naya mwenyewe alifurahia.

Wageni wote wakaondoka. Naya akabaki na warembo wake pamoja na Malon. Aliwashukuru sana na kuwaambia Malon atamalizana nao kwenye swala la malipo. Ila atawatafuta tena wakati mwingine kama wanaweza kufanya tena kazi waliyoifanya usiku ule. Walimshukuru Naya, Naya akawapa mkono kila mmoja wao. “Kabla sijawaacha na Malon, naomba nitoke naye kidogo. Atarudi muda sio mrefu.” Naya akatoka, Malon akamfuata nyuma akiwa na wasiwasi sana.

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~ 

“Chezo yuko wapi?” “Aliondoka.” Naya akakunja uso, akafikiria kidogo akaona ayaache tu ya Chezo. “Side ameniambia pesa iliyopatikana.” “Na mimi amenimbia.” “Umefurahi?” Naya akamuuliza. Malon akacheka. “Asante sana Malon, nakushukuru. Naona mwitikio ulikuwa mkubwa, watu wamenunua nguo kwa silimia 85. Hata mimi nimefurahi. Ila naomba nikuombe kitu.” “Nini?” “Nimechoka, mpaka nahisi kuanguka.” “Njaa.” Malon akaongeza. “Na usingizi pia. Tokea kwenye mitihani nilikuwa silali vizuri. Naomba nikuachie hao warembo, umalizane nao. Nimemuomba baba anisubiri nirudi nao nyumbani nijifungie pale kwenye kile chumba changu hata siku tatu, labda nitaweza hata kufikiria. Sasa hivi nipo hoi.” “Nilifikiri tunarudi wote Morogoro!” Naya akamtizama kwa upole, akacheka taratibu tu. “Nenda kamalizane na hao warembo. Acha mimi nikapumzike. Usiku mwema.” “Ila umefanya kazi nzuri Naya. Hongera.” “Wewe ndio unatakiwa kujipongeza kwa uwekezaji sahihi. Umeweka pesa ulipojua itarudi.” Naya aliongea tu hivyo akaondoka na kumuacha Malon amepigwa na butwaa.

Hakuongea chochote juu ya Loi, wala kuuliza kama Chezo. Alimuachia wale warembo kama kumpa ruhusa afanye chochote anachotaka nao. Malon aliumia sana. Kwa kujua Naya anajua tabia zake, na bado kutangazia yupo huru nao usiku huo yeye anaondoka pale kurudi kujifungia nyumbani kwao, haukuwa ujumbe mzuri kwa Malon. Alijua Naya anamfikishia ujumbe mzito, kama asiyejali tena. 

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~ 

Malon alimfuata Side, akamwambia awalipe wale warembo pesa yao yote. Kisha awarudishe hotelini, na kuwaambia usiku huo ndio mwisho kulala pale. Side dereva wa Malon alikuwa amewakodishia hiace, daladala, akafanya kama alichoambiwa na Malon. Wakati wale warembo wanatoka kuelekea ilipo ile daladala, nusu yao walikuwa wakitokea Morogoro, hawakujua Malon alipotokea, alimdaka Loi, akamkaba shingo akamsukuma kwa nguvu mpaka ukutani huku bado amemkaba. Alimnyanyua mpaka juu akiwa bado amemkaba kwa mkono mmoja, akaanza kumpiga vibao.  

Side alikimbia na kwenda kumvuta Malon, Loi chini. Malon alimgeukia Side akampa ngumi moja, Side akakwepa, na kumsukuma Malon. Akamuwahi Loi pale sakafuni. Warembo wote wakasimama na kugeuka. Malon akawa anarudi kwa kasi, Loi akataka kukimbia. “Usithubutu kukimbia, ndio atakumaliza. Wewe simama nyuma yangu.” Side alimsihi Loi aliyeanza kulia. “Umemwambia nini Naya?” “Mungu wangu mimi ni shahidi Malo, sijamwambia kitu.” Loi alikuwa akiongea nyuma ya Side huku akilia kwa hofu na kujishika shingo iliyokuwa imekabwa. “Nitakua Loi! Umemwambia nini Naya?” Malon akauliza huku akijaribu kumzunguka Side amfikie Loi, na Side naye akawa anazunguka na Loi nyuma yake.

“Ni Zelda na wenzake ndio walikuwa wakiongea, hawakujua kama Naya yupo aka..” “We Loi usitutaje.” “Nitakupasua mdomo Zelda wewe! Na unanijua vizuri huwa sijui kumtisha mtu. Nyamaza kabla sijakusogelea na kukutoa meno.” Zelda akanyamaza. Ndipo Loi akaeleza kila kitu. “Zelda ndio amesema, sio mimi Malo.” Loi alikuwa akisikika akilia kwa hofu. “Haya, wote kaingieni kwenye daladala, mrudi hotelini. Kazi yenu hapa imeisha. Haya Loi kimbia kwenda kwenye daladala.” Side akawatoa pale  huku akimtizama Malon kama akimzuia asiwasogelee wale warembo. “Huwezi kumpiga mtoto wakike Malon!” “Side usinichanganye!” Malon akamuonya. “Unaweza kunifanya utakalo, lakini sio hawa watoto wa kike, Malon! Unataka ukafie jela?” Malon akapiga ngumi ukutani, akaondoka pale. 

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~ 

Naya alikuwa amechoka, alifika nyumbani kwao nakujitupa kitandani kama mfu. Alilala usiku kucha wala hakuweza kufikiria. Kesho yake alitoka akala kiporo cha jana yake alichokuta kwenye friji, akarudi tena kulala. Jioni yake akasikia simu yake inaita kwenye pochi. Akakasirika kutozima. Akatoka kitandani akaifuata. “Malon!” Naya akapokea. “Vipi?” “Umeniamsha bwana!” “Pole, nilikuwa nakucheki tu.” “Nilikwambia nataka kupumzika siku tatu mfululizo.” “Ndio hata salamu Naya!?” “Nilijua sasa hivi upo busy unavua tu chupi! Na hivi nilikuachia warembo wote wale, nilijua kutakuwa hakuna kulala mpaka uwamalize na kuwarudia rudia, nikajiambia kuja kukupata tena ni baada ya miezi. Niliamua kukuacha ufurahie matunda ya kazi yako, pesa uliyoingiza na warembo wako.” Akasikia kimya, kuangalia simu akagundua Malon anasikiliza, mwisho akakata. Naya akacheka, na yeye akazima simu yake kabisa. Akarudi kulala. 

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

Naya alilala siku tatu mfululizo bila kufanya chochote zaidi ya kula na kupumzika, na kweli mwili ukajisikia vizuri. Akaanza kufikiria kitu chakufanya na Malon. Aje kutafuta kazi na kuachana kabisa na Malon au aendeleze biashara mpya aliyoanza na Malon! Hakujua chakufanya. Alikuwa imebaki miezi michache sana amalize chuo. Siku ya tatu jioni baba yake akaingia chumbani kwake na kumkuta amejilaza tu kitandani, hajalala.

“Vipi?” “Kaa hapa nikuulize swali.” Baba yake akavuta stuli akakaa.  “Nifanye nini?” “Juu ya nini?” Naya akajua ni kweli ameuliza swali la jumla sana kana kwamba baba  yake anajua kinachoendelea.

“Nimebakisha miezi michache sana nimalize chuo. Na umeona jinsi yale maonyesho yalivyokwenda.” Baba yake alikuwa  kimya akimsikiliza. “Endelea nakusikiliza.” “Watu wengi wamependa nguo zangu baba. Naogopa nikiacha mpaka nimalize chuo, nitakuwa nimepoteza wateja. Nifanyaje?”  “Shule lazima iishe, si ndiyo?” Naya akatingisha kichwa kukubali. “Umenionyesha mitindo mingi sana ambayo umeshaiandaa. Miezi hii mitano iliyobaki, mwombe Malon akusaidie kusimamia. Watengeneze nguo na kuzitangaza. Huhitaji kutengeneza mitindo mingine sasa hivi mpaka shule itakapoisha. Weka akili chuoni.”  Naya akanyamaza.

“Mbona kama kuna kitu hapo? Eti Naya?” “Malon ameniudhi baba. Siwezi kukwambia ni kwa nini ameniudhi lakini..” Naya akasita. “Labda niulize. Amekuudhi kama mpenzi au kama mfanyabiashara?” “Mpenzi.” Naya akajibu kwa upole. “Basi lazima biashara iendelee Naya. Huwezi kuruhusu kitu chochote kisimame kwenye ndoto zako. Kama unashindwa kusamehe upande huo, basi endelea naye kama mfanya biashara mwenzio. Yeye ananufaika, na wewe unanufaika. Mfike mahali mzungumze. Nini unategemea kwenye ile biashara, na wewe ujue ni nini anategemea.” “Wakati anawekeza alikuwa akiwekeza akijua atanioa. Lakini baba, Malon hawezi kuwa mume wangu.” Baba yake akashtuka sana.

Alijua ni kiasi gani Naya anavyompenda Malon na Malon hivyo hivyo. “Malon anajua hilo?” “Atakuwa anajua. Au tuseme sasa hivi anajua.” “Basi nashauri mpate muda wa kuzungumzia upande wa biashara ili mjue mnaendelea vipi? Usiruhusu hasira zikukoseshe vitu vya thamani. Ulifanya vizuri sana. Mimi mwenyewe nilikuwa siamini kama ni Naya wangu amesimama pale mbele.” Naya akaanza kucheka. “Kweli Naya!. Ulifanya kama umekuwa kwenye hilo soko kwa miaka  mingi sana. Umeongea kwa kujiamini, kazi yako nzuri na wasichana uliowapa wawakilishe zile nguo pia walifanya vizuri. Ungejiona pale jukwaani, ungejua nini naongelea. Usikubali kuacha. Jikaze shule iishe, kisha pambana sana na kila kikwazo ili wewe ndio ubakie umesimama. Umesikia mama?” Naya akatingisha kichwa kukubali.

“Kila biashara au jambo lina changamoto zake. Unaweza kupata changamoto kutoka ndani au nje.  Ona wewe. Umefanya vizuri kwenye bidhaa na kujitangaza, changamoto zimetoka ndani. Lazima kupambana. Lasivyo hutaweza kukaa sokoni. Fikiria na  uchukue hatua tena kwa haraka kabla hujaharibikiwa.” “Nimeelewa baba. Asante.” “Toka hapo kitandani uje kula. Mama yako ameniambia hujala tokea chai ya asubuhi. Njoo utafute kitu chakula.”  Baba yake akasimama na kutoka. Naya akamfuata baba yake nyuma akiwa amechangamka kidogo sio kama alivyokuwa amemkuta . 

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

Usiku wakati anataka kulala, akamtumia ujumbe  Malon. ‘Naomba unipigie ukipata  muda tafadhali.’ Akatuma huo ujumbe kitu kisicho cha kawaida kwao. Naya kwa Malon, hasubiri ruhusa. Alikuwa akipiga muda na wakati wowote ule. Bila kupotea dakika hapohapo Malon akampigia. “Yameanza lini kuniomba nikipata muda nikupigie?” “Naomba  tukutane kule kazini. Muda na siku utakayokuwa na nafasi.  Lakini nakuomba iwe juma hili, jumapili narudi chuo.” “Si mmefunga?” “Kwetu sisi mwaka wa tatu si ndio tumerudi tu chuoni.  Na bado miezi michache tumalize. Wenzangu wapo chuoni. Mimi nilitaka tu kupumzika kwa hata siku tano tu. Nilikuwa nimechoka.” “Hata kesho naweza kuja kukuchukua hapo nyumbani ili twende wote.” “Nashukuru sana. Lakini hakuna sababu ya kuja mpaka huku. Naomba tukutane tu kazini.” “Naya!” “Nitakuona kesho. Usiku mwema.” “Naya!” Naya akakata simu. 

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~ 

Kesho yake Naya alijitengeneza vizuri, akatoka mida ya saa nne kuelekea Picha ya ndege, sehemu kwenye kiwanda chao. Walikuwa wamewapa mapumziko ya juma nzima wafanyakazi wote kwa kazi kubwa waliyoifanya. Alimkuta Malon ofisini kwake. Akaingia moja kwa moja. 

“Pole na safari.” Naya akaanza. “Nimeshapoa. Nilifika hapa kama kwenye saa mbili.” Naya akatulia kidogo. “Vipi?” “Nataka nirudi shule na nitulie kabisa mpaka nimalize kabisa chuo. Najua umewekeza sana hapa. Lakini kwa kazi kubwa tuliyoifanya majuzi, kwa asilimia kubwa naamini imerudisha pesa kwa asilimia fulani.  Michoro niliyokuachia hapa, kama utaweza kuendelea kuwasimamia  hawa wafanyakazi kama ulivyokuwa ukifanya, nina uhakika watazalisha vitu vizuri na itakulipa tu.” “Wewe ndio unaacha moja kwa moja?” “Nitakutafuta nikimaliza chuo kama bado kutakuwa na nafasi yangu.” Malon akakunja uso.

“Naya! Najua nimekuumiza, lakini usisahau kama hiki kitu kipo hapa kwa ajili yako wewe. Mimi sina mpango wa kuuza nguo.”  “Na mimi nilifikiri hivyo.” “Sasa ni nini kimebadili hiyo!?” “Nilisikia kuwa ni umewekeza tu. Na mimi nimwajiriwa kama hao mafundi na wale warembo waliotangaza yale mavazi.” “Naya! Unawezaje kufikiria hivyo?” “Hata  hivyo hatukuwa na makubaliano yeyote yale Malon. Nilikupa tu wazo, ukakubali kulifanyia kazi tukijua tunazalisha kitu chetu.” “Sasa ni kitu gani kimebadilika?” Naya akakunja uso kama anayemshangaa Malon.

“Malon! Unajua mimi sio mjinga?”  “Nafahamu  Naya.” “Nilikupa uchague. Tena kwa kurudia rudia na machozi juu. Umejichagua wewe badala yangu Malon. Umechagua maisha yako na tamaa zako za mwili, ukaamua kuniacha mimi unayejua nakupenda na nina kusubiri wewe tu. Mbaya zaidi, unarudi kulala na mimi bila kunihurumia! Unalala na wanawake hovyo, halafu unarudi kwangu bila hofu! Kinachoniumiza zaidi unafanya uchafu wako na watu wakaribu yangu. Bila kunifikiria! Unanichafua na  kunidhalilisha vibaya sana.” Naya akajiweka   vizuri.

“Sikwambii kwa hasira Malon, ila ni kweli wewe ni dhaifu sana. Huwezi kuja kuwa mume wangu.  Unaudhaifu au kilema kibaya sana ambacho nimegundua huna uwezo wakujisaidia. You are very weak Malon. Huwa nasikia wanaume wa aina yako, lakini nahisi wewe umezidi Malon. Unazidiwa nguvu na mkono tu. Mkono wako unanguvu kuliko fikra zako. Linapofika swala la kufungua zipu yako au kuvua nguo ya mwanamke, huwezi kufikiria  wala huwezi kujisaidia.  Huna uwezo wakutawala mikono yako tu! Sasa unawezaji kuzungumzia kuwa mume au baba wa watoto!?” Malon kimya.

“Unataka kujenga familia ya namna gani Malon? Wewe mwanaume uliyeshindwa hata kutawala hisia zako, unakuwa mtumwa wa ngono! Kweli leo bila hofu unanitaka niendelee na mimi kuwepo kama wanawake unao wachezea tu mtaani kwa pesa chache unazo wahonga!? Unanidharau kwa kiasi gani Malon!?”  Kimya.

“Unajua kwa nini nampenda Chezo?” “Sikujua kama unampenda Chezo, Naya!” “Nampenda kwa kumuheshimu sio kumvulia nguo kama wewe unavyofanya kwa wanawake zako.” Kimya.

“Chezo ni mpenda pombe. Ndio udhaifu wake. Jua likiwa kali, kiu yake ni ya bia sio maji. Lakini huwa hathubutu kunywa bia hata moja mchana, au niseme siku za kazi mchana akijua ana kazi. Anaweza kutawala kiu yake mpaka jioni anapojua anakunywa na hana majukumu. Siku tatu zile tulizokuwa tukihangaika naye hapa Dar kuandaa tamasha, Chezo hakunywa kabisa japo alikuwa akilalamikia kiu ya bia. Nikamuhurumia kwa kazi kubwa aliyokuwa akifanya. Nikamwambia kuwa naweza kumsindikiza baa akanywa kidogo. Hivi unajua Chezo alikataa?  Akasema atasubiri mpaka kazi iishe! Kwa siku zote tatu tupo pale, Chezo hakunywa Malon. Aliweza kutawala kiu yake. Kwa hiyo usifikiri kama ni wewe mwenyewe tu huwa unakuwa na kiu, Malon. Kila mtu anakuwa na kiu, ila wengine walijaliwa uwezo wa kutawala kiu zako, wewe huna huo uwezo. Upo dhaifu.” Naya  akaendelea.

“Eti nakufumania, unanipiga! Nakupa chaguzi kati yangu na wanawake zako wa nje, unawachagua wao! Tena na kuniletea karibu yangu kwa makusudi kabisa ukiwa umenifunua kwao kwa kuwaambia mambo ya maendeleo tunayofanya pamoja! Halafu unaniambia kuwa tunafanya mambo kwa ajili yetu. Kweli Malon? Tafadhali acha kujidanganya. Wewe huwezi kuwa mume wa mke mmoja. Hata ubadili dini uwe mwislamu ukaoa wanawake wanne, pia hawatakutosha. Endelea tu na hayo maisha uliyoyachagua na kama kweli unamaanisha kuwa unafanya hii  kwa ajili yangu, nikushukuru tu. Lakini sio kwa ajili yetu. Nijulishe malipo yangu yatakuaje kwa kila kazi nitakayofanya. Nikiona itanilipa, basi nitarudi. Nikiona haitanilipa, nikimaliza shule   nitatafuta kazi sehemu yenye maslai mazuri. Nikifanikiwa na mimi nitafungua kitu kama hiki.” “Hii kitu ni yako Naya.” Malon akaongea kwa utulivu tu.

“Kwa mfano pesa tuliyopata siku ile nimekuandikia chini, nilitaka ukipumzika nije kukuonyesha. Una muda nikuonyeshe garama na matumizi?” Naya akabaki kimya kwa muda. “Najua sasa hivi umenichukia sana Naya.  Tunaweza kuangalia wakati mwingine. Lakini ujue hii ni biashara yako. Ukiondoka hapa, hii kitu nitafunga, nifungue kitu kingine. Mimi nimfanyabishara, ila sio mwizi. Kuendeleza hii biashara bila wewe, itakuwa ni kama kukuibia au kukudhulumu. Sitakufanyia hivyo.” Naya akasimama.

“Kwa hiyo?” Malon akauliza kabla Maya hajatoka. “Nimekwambia nitakuwa chuoni Malon. Siwezi kufanya kitu mpaka nimalize chuo.” “Na kuhusu faida tuliyopata baada yakulipa gharama zote?” “Zitunze tu Malon. Najua  wewe unahitaji hizo pesa zaidi kuliko hata mimi. Unamatumizi mengi sana. Wanawake wengi wa kuwahonga.” “Najua umekasirika Naya, lakini naomba ufikirie na uje unijibu  kitu chakufanya na hizi pesa mpenzi wangu. Ni jasho lako.  Na ni  haki yako.” Naya akataka kufungua mlango, akarudi.

“Tafadhali Malon, usifike tena nyumbani wala usitafute tena wazazi wangu. Nimeshamtaarifu baba kuwa tumeachana moja kwa moja. Tafadhali na ninakusihi Malon. Najua wewe huwa huambiliki, unafanya kile unachojisikia wewe, lakini safari hii, katika hili, nakusihi sana. Muache baba yangu kabisa na familia yangu. Tafadhali. Ulianza na mimi mahusiano, tunamalizana na mimi tu. Usiwatafute.” “Nakuahidi sitawatafuta.” “Sijui hata kama unajua maana ya  hilo neno ulilosema!? Eti Malon?”  Kimya.

“Najua huwa unatatizo la kuongea mambo ambayo humaanishi. Kutoa ahadi za uongo. Hujui  kuishi maisha maadilifu inakuaje. Mimi nimevumilia kwa upande wangu, tafadhali acha kabisa kufika kwetu na kuwatafuta wazazi wangu. Iwe mwisho. Kama tutakuja kuendelea na hii biashara, iwe ni sisi tu. Sio wao. Nitakusaidia kumuomba Chezo awe anakukumbusha hilo, pengine  yeye mwenzangu unaweza kumuelewa na kumsikiliza.”  Malon kimya. “Na mimi hivyo hivyo. Nitakutafuta nikiwa tayari.” “Hivyo sivyo ulivyoniambia mwanzoni Naya. Umesema utakapomaliza mitihani.” Naya akakunja uso kama anayemshangaa.

“Unajua nini Malon, wewe unajua aina ya mchezo unaocheza. Acha mimi nikuache.” Naya akatoka. “Naya!” Malon akamfuata. Naya akageuka. “Ulimalizia ada yote na michango?” Malon akauliza kwa upendo. “Utatugharamia wanawake wangapi Malon? Wangapi unataka kutugharamia na kutulala? Kama hujanielewa katika yote niliyozungumza, basi naomba unielewe hivi, nimejitoa katika msururu wa wanawake zako. Nimejitoa Malon. Kwa kuwa nimeishi na wanaume wanaojua kujiheshimu, najua na mimi Mungu atanijalia wangu siku moja. Atakayenipenda na kuniheshimu.” “Nakuhakikishia Naya, hutaweza kupata mwanaume anayekupenda kama mimi.” “Ndivyo na wenzangu unavyowadanganya hivyo hivyo?” Kimya, Naya akaondoka.

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~ 

Alirudi nyumbani nakujifungia chumbani kwake. Alilia Naya, nakulia bila kunyamaza. Kwa kuwa baba yake alishamwambia kuwa Malon ndiye amemuumiza, akajua sababu ya kilio  hicho ni Malon. Baada ya siku mbili, mama yake alipoona mambo ni hayo hayo, amejifungia chumbani anaendelea kulia hana hata mpango wakutoka, akamfuata  baba yake akiwa bandani. “Hakikisha huyu mtoto anatulia na kurudi shule baba Naya! Nataka cheti mimi.” “Sasa mbona kama unanitupia mimi lawama!?” “Wewe ndiye unayemuendekeza. Umemruhusu kujiingiza kwenye mambo mengi ambayo nilikuonya baba Naya! Imebaki miezi minne tu amalize. Ona hali aliyonayo!” “Atatulia tu. Mimi namjua Naya.” “Mungu akusaidie.” Mama Naya akazidi kutisha.

“Hakika hatutaelewana humu ndani. Na uzuri nilikuonya naye tokea mwanzo. Habari za Malon sijui, kijana ambaye ametokea tu! Nilikuonya.” “Unajuje sasa kama ni Malon na si mambo mengine yakisichana?” “Naya ana mambo gani yakisichana huyo?” “Huwezi jua bwana.” “Atakuwa nani kama sio huyo Maloni? Maana mitihani yake ya mwisho amefanya vizuri. Kazi yake ya mitindo  pia kafanya vizuri kupitiliza! Ni hao hao wanaume wakuokota wenye magari wasio na elimu.” Malon akaanza kutolewa kasoro. “Na nilikuonya baba Naya! Ukanipuuza. Ona kamba ilipomkatikia pabaya!” “Nitazungumza naye. Wewe acha wasiwasi.” Mama Naya akaondoka.

Baba yake akakaa huko kwenye mabanda ya mifugo mpaka usiku. Akarudi ndani kuoga akatoka kula. Aliposikia baba yake anapangiwa chakula, na yeye akatoka. Wote wakashangaa. Akaenda kukaa  pembeni ya baba yake. “Vipi mama yangu mzazi?” Baba yake akamuuliza taratibu. “Naomba kesho unirudishe chuoni.” “Si mpo likizo?” “Wenzangu wapo chuo baba. Acha nijikaze nikamalize.” “Hilo la msingi. Unataka tuondoke saa ngapi?” “Naomba iwe mapema. Ukitoka tu kupeleka maziwa.” “Sawa mama. Umekula lakini?” “Mwezio nilikuwa nimekasirika sana.” Naya akaanza kutokwa na machozi. “Ukikasirika hutaki kumfungulia baba yako mlango?” “Nilitaka kulia kwanza.” Bale akacheka. Naya akachukua kiatu, akamtupia.

“Mwenzio Bale amekurikodi ulivyokuwa ukilia.” Zayoni akadakia. “Anasema ulikuwa unalia sauti ya kwanza na ya tatu.”   Mpaka Naya mwenyewe akaanza kucheka. “Mimi naona unirudishe chuoni usiku huu huu, baba. Sitaki kuendelea kuiona sura ya Bale.” “Nishaweka ndio itakuwa ringtone yangu. Kila ukinipigia wewe ndio mlio huo.” “Na wala sitakaa nikakupigia. Na ujue kabisa, nikimaliza chuo nahama, naenda kuishi kwangu!” Kila mtu akacheka kama asiyeamini. “Chekeni tu. Mtanikumbuka sana nawaambia.” “Tunakujua wewe. Wala hutatupa muda wa kukumbuka. Utarudi tu.”  Bale akabisha. 

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~ 

Naya alirudi chuoni akaamua kutulia na shule ili amalize, lakini hakuna siku hakumkumbuka Malon. Wakati mwingine alikuwa akibaki akiduaa akimkumbuka Malon. Mambo aliyokuwa akimfanyia, mapenzi mazito aliyokuwa akimpa. Swala kama alikuwa anampenda, halikuwa na maswali kwa Naya. Hakika Malon alimpenda. Mbali na udhaifu wa wanawake aliokuwa nao, Malon alikuwa ni mwanaume  wa kuwa  naye.  Alimjali na kujifanya mjinga kwa Naya.

Mwezi wa kwanza uliisha ukiwa kimya kabisa. Japokuwa wote walikuwa hapo hapo Morogoro, hakuna aliyemtafuta mwenzake. Si Chezo, wala Malon. Naya akaona atulie. Siku kadhaa zikaongezeka akakuta ujumbe kutoka kwa Malon. ‘Nataka tu kujua unaendeleaje Naya. Sina nia nyingine. Na wala sitaki kukuudhi.’ Naya akasoma ule ujumbe, akafikiria. Akaamua kuacha  asijibu. Na kweli Malon hakumsumbua tena.

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

Mitihani ya mwisho ikakaribia Naya akiwa busy sana na mitihani, akaitwa kuwa amepata mgeni. Akatoka kwenda kumuona. Alikuwa Side. Naya akamsalimia kwa heshima zote Side dereva wa Malon. Alikuwa kaka mstaarabu sana. “Vipi Side?” “Safi mama. Nimetumwa na Malon.” Naya akacheka. “Amekutuma nini?” “Mizigo yako hapo nyuma.” Naya akafungua mlango wa nyuma ya gari. Akakutana na mazawadi mengi yamefungwa na kadi  kubwa sana. Hakutaka hata kugusa kitu hata kimoja. Akafunga mlango akarudi dirishani kwa Side.

“Nakushukuru sana Side. Lakini hapana. Naomba mrudishie Malon vitu vyake.” “Ungepokea tu Naya.” “Sina shida na hivyo vitu Side. Sina shida kabisa. Malon amezoea kufikia wanawake kwa pesa zake na wenyewe inakuwa rahisi kumkubali kwa hongo anazowapa. Mimi siko hivyo Side. Nampenda sana Malon. Hakuna kitu atanipa nikafurahi kama mapenzi ya kweli. Hivi vitu anataka kunipa, wapo wanaume zaidi ya watano sasa hivi wanataka kunipa tena zaidi ya hivi. Sasa kwa nini nipokee kwa Malon mwanaume asiye na heshima kwangu? Niambie ukweli Side. Kwa nini iwe Malon na sio hao wengine?” “Malon anakupenda sana, Naya.” “Kama kweli angekuwa ananipenda, angehakikisha nakuwa naye. Lakini Malon hanipendi Side. Ila kwa kuwa hajui kukataliwa ndio maana anahangaika.” “Mimi namjua Malon, Naya. Wewe anakupenda.” Naya akamwangalia Side kwa kumsuta, Side akacheka kidogo.

“Side, ujue mimi ni mtoto wa pekee wa kike nyumbani kwetu? Ndio dada. Baba yangu ananipenda kuliko nitakavyokwambia. Hivi leo tu alikuwa hapa kuniangalia, wakati simu zipo angeweza kunipigia tu ikatosha kuliko kuja mpaka huku Morogoro na wewe kwetu unapafahamu. Kwa mwezi huu amekuja huku zaidi ya mara 5. Anataka tu kuniona na kuhakikisha mimi ni mzima. Leo napokea zawadi za Malon. Mwanaue malaya hivi, kweli Side? Akiniua na maradhi? Niambie ukweli tu Side, mimi ningekuwa ni dada yako kabisa, tumezaliwa na mama mmoja, hata kama Malon ananipa nini, ungenishauri nirudi kwake?” Hapo Side mwenyewe akakwama. Kimya.

“Niambie ukweli Side. Niuze uhai wangu kwa mamilioni ya pesa ya Malon? Mimi nimeishi na wewe na Chezo. Wewe ni kijana mzuri tu. Unayo pesa ya kutosha kuwa na wanawake wengi tu Side, mbona umeoa na umetulia na mkeo mpaka kina Chezo wanakutania hujui mapaja ya wanawake wengine ila mkeo tu? Wanakuita malaika kwa maadili uliyo nayo. Kwani hupati vishawishi?” “Napata.” “Sasa! Mbona umetulia? Kwa kuwa unampenda mkeo. Na mimi nimemuona mke wako Side. Wala hana nyota usoni. Wakawaida tu kama mimi, lakini mbona wanawake wakikushawishi unatulia? Ninayo mifano ya watu kama wewe. Wengi tu. Na mimi natamani mtu atakayenichagua kama wewe ulivyomchagua mkeo.” Naya akaendelea.

“Unamkumbuka Tunu?” Side akacheka. “Si umekumbuka mwenyewe? Alikuwa akikusimulia pale hosteli alivyotaka kukushawishi na kukubembeleza baada ya kuwaleta Morogoro na baada ya pale! Tunu ni mzuri sana tu, mbona hukulala naye? Wala mkeo asingejua. Sasa kwa nini unataka mimi ndio niangukie pabaya?” “Nimekuelewa Naya, dada yangu. Mimi sikujua kama wewe ni wa hivi. Nishazoea nikitumwa huwa siulizwi. Napokelewa mizigo, mambo yanaisha. Ila nimekuelewa dada. Acha mimi niwahi kurudi. Nakuombea kheri.” “Asante.” Naya akataka kuondoka. Side akamwita. Naya akarudi.

“Naomba nisaidie ujumbe wa mwisho wakumrudishia Malon. Tafadhali Naya. Wewe unamjua Malon.” Naya akacheka. “Wewe kamwambie kama nilivyokwambia. Kuwa mimi sijawahi kuwa na shida na vitu vyake isipokuwa yeye mwenyewe. Na sijawahi kumuomba kitu chochote isipokuwa yeye mwenyewe. Kwa kuwa ameshindwa kunipa mapenzi yake, basi.” “Ujumbe umefika. Nashukuru.” Naya akaondoka.

 Baba Naya, Mzumbe Tena.

S

iku moja kabla ya mitihani, baba yake Naya akarudi tena pale chuoni. Naya alifurahi sana. “Nimechoka baba!” “Pole. Naona umejikaza kweli. Unakaribia mwisho mama. Endelea kujikaza.” “Nimefurahi umekuja kunitia moyo. Twende tukale.” Naya akamshika baba yake mkono akimuelekeza kwenye vibanda vya chakula. “Mbona huna raha?” “Nimekwambia nimechoka, baba.” “Naya!” Naya alijua hawezi kujificha kwa baba yake, ikabidi ajisalimishe tu. 

“Namkumbuka Malon! Nina hamu naye.” Naya akaanza kulia. “Umemtafuta?” “Hapana.” “Kwa kuwa amekuudhi?” “Kwa kuwa sioni mwisho wangu na Malon, japo nampenda sana. Sijui nitafanyaje? Nampenda Malon. Wakati mwingine natamani hata kusikia sauti yake tu.” “Kwani anamapungufu makubwa sana ambayo hayawezi kurekebishika?” Naya akatingisha kichwa kukubali.

“Basi jipe muda na muombe Mungu. Hata katika hili atakujibu tu. Tena yeye akikujibu, utapata  na amani. Kabla yakuondoka, tutapata muda wakuomba pamoja. Naamini Mungu atakutia nguvu tu. Unahitaji kutuliza mawazo umalize hiyo mitihani yote.” Naya akajiegemeza kwenye mkono wa baba yake wakaendelea kutembea.

Walifika sehemu ya kula, baba yake akaanza kumpa habari za nyumbani. Kidogo akatulia na kuanza kucheka. Wakakaa muda kidogo na kutafuta sehemu ya peke yao, wakaanza kumuomba Mungu pamoja. Zaidi baba yake ndiye aliyekuwa muombaji. Alishika mikono ya binti yake,  nakuanza kumuombea. Alimuombea amani na utulivu. Akamsihi Roho wa Mungu awe anamkumbusha akiwa kwenye mtihani. Akamuombe utulivu. Akavunja roho za kupaniki. Akambariki binti yake huyo na kumalizia kumuombea ulinzi.

Naya alifurahi sana. Baba yake akataka kuondoka, lakini akamzuia.“Usiondoke kwanza baba. Tukae tena kidogo. Tukae tu.” Baba yake akacheka na kurudi kukaa. NayaAkakaa pembeni yake. Naya akajiegemeza hapo pembeni ya bega. Akatulia kwa muda.

 “Sasa hivi unaweza kwenda.” Baba yake akacheka nakusimama. “Nirudi lini?” “Jumamosi ijayo njoo na mama na kina Bale. Wanichokoze kidogo, ndio nipate nguvu yakumaliza week hiyo ya mwisho ya mtihani.” Baba yake akacheka tena. “Mwenzio ameweka kweli kile kilio chako kama ringtone yake.” “Kanitumia kwa makusudi ili kunikera. Yaani Bale! Na wala sikumjibu.” “Lakini anajua kama umepata.” Naya akafyonza. “Sijui yukoje Bale jamani! Hasikii raha mpaka anikere au ..” “Akulize.” Baba yake akamalizia wakacheka. Akamsindikiza baba yake mpaka kituoni, akaondoka. 

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

Alikwenda kujisomea na wenzake kwa mara ya mwisho, wakakubaliana kwenda kupumzika tayari kwa mitihani itakayoanza kesho yake. Naya alirudi chumbani kwao, akaoga na kupanda kitandani kwake. Kama kawaida kilikuwa kitanda cha juu. Akaona simu ya Malon inaingia. Akataka kupuuza, lakini alikuwa na hamu naye sana. Akafurahia ile simu. Akajua itamuongezea nguvu ya kweli. “Malon!” Naya akaita kwa upole. “Asante kupokea simu yangu Naya.” Naya akacheka taratibu. “Pole na mitihani.” “Asante.” Naya akajibu kifupi tu, wakatulia kwa muda. “Naya!” “Nipo.” “Nikwambie kitu, lakini usikate simu na si lazima ukaamini. Lakini nataka tu ujue.” Naya akatulia.

“Upo?” “Nipo Malon.” “Nakupenda sana Naya. Hata kama kutakuwa kuna kukosea, lakini nataka ujue najitahidi sana na umenibadilisha kwa asilimia kubwa sana. Sikuwa hivi Naya. Nilikuwa mbaya kuliko hivi. Lakini tokea uwe kwenye maisha yangu, najitahidi sana. Nakiri nimeathirika na maisha niliyoishi muda mrefu sana mtaani na kukataa kulelewa na wazazi. Na kujikuza mwenyewe mtaani huku nikiwa na wazazi kama wako tu. Nimeathirika sana. Lakini nakuhakikishia najitahidi. Wewe ni mtu wa mwisho ambaye natamani kukuumiza. Nakupenda Naya. Na ninajua nimeshakuahidi sana. Na ninaogopa kukuahidi tena, nisije nikakosea tena. Ila nataka ujue najitahidi kubadilika.” Akamsikia Naya anavuta pumzi kwa nguvu.

“Namaliza mitihani baada ya week mbili. Nimemuomba baba aje kunichukua na gari yake ili kuweza kupakia vitu vyote. Unafikiri ni sawa nipite naye hapo nyumbani kwako nichukue vitu vyangu?” Malon akawa kama amemwagiwa maji. Naya akaona kimya, akaangalia simu yake. Akakuta haijakatwa. “Malon?” “Nipo Naya.” “Umenisikia?” “Nimekusikia, na wewe umenisikia?” “Ndiyo.” Kimya. 

“Najitahidi Naya.” “Nimekusikia Malon. Labda nikupe pongezi.” “Unajua hiyo sio kitu ninachozungumzia Naya.” “Siwezi Malon. Napatwa kinyaa mno. Mimi mwenyewe nashangaa jinsi unavyofanya! Unawezaje!? Unamudu vipi kufurahia kuingilia kila mwanamke, Malon!?” Kimya. “Kwa kweli siwezi Malon. Wewe endelea hivyo na kama umekusudia kubadilika, basi endelea tu na Mungu akusaidie. Lakini huwezi kunichanganya na wanawake zako Malon! Kwa nini iwe hivyo!? Yaani ni kwa nini niendelee kujidhalilishe kwa kiasi hicho?” “Labda mapenzi ya kweli. Mimi sijawahi kuwa kwenye mahusiano Naya, lakini nimeona watu wanaopendana wakibebana na kuvumiliana. Nimekuahidi kubadilika. Kwa nini usinipe nafasi?” “Mpaka lini Malon? Utakuja kuniua na maradhi kwa kisingizio cha kuvumilia. Utamuacha baba yangu akiteseka bure.” Naya mtoto wa baba.

“Siwezi kukuua Naya.” “Unauhakika gani? Hata kama utaniambia unatumia kinga. Ile ni mipira Malon, ikikupasukia huko? Halafu kile kitendo tu chakujua umetoka kulala na wanawake wengine, kinaniuma sana Malon. Heri ningekuwa nimesafiri ndio nijiliwaze kuwa ulizidiwa. Lakini nipo! Unaniacha ndani na kwenda kulala nje! Kitakachokutuliza ni nini wewe Malon kama sio kifo!? Halafu angalau ungekuwa na mwanamke mmoja. Unazunguka kwa wanawake zako, Morogoro nzima wanakujua. Ukitembea utafikiri unatembea uchi!? Hapana Malon, hayo maisha wewe ndio unayaweza. Binafsi nimechoka kujidhalilisha. Wewe niambie kama ni sawa nije na baba. Kama unaona sio sawa, basi. Hata hivyo ni nguo tu. Naweza kununua nyingine.” “Hapana. Karibuni kabisa. Muda na wakati wowote unakaribishwa Naya. Karibu.” “Asante.” Kimya.

“Naya!” “Nipo Malon.” “Naomba hata kama nimeshindwa kwenye mambo mengine, basi hata urafiki wa kawaida tu.” Kimya. “Na mimi niwepo tu Naya. Kama watu wengine wanaoweza kukupigia simu. Kukukaribisha kwenye shuguli zao ukaenda. Yaani mahusiano ya kawaida tu. Unafikiri itawezekana?” Kimya. “Sitaki tugeuke kuwa maadui. Najua tunaweza kufanya mengi kwa pamoja. Unakumbuka jinsi tulivyofanya vizuri kwenye upande wa mavazi?” “Nakumbuka.” “Basi naomba udhaifu wangu usitunyime kila kitu. Au kwa upande huo pia mimi nipo dhaifu sana kuliko Chezo?” Naya akajua maneno yale, yalimuumiza sana.

“Hapana Malon. Naamini tunaweza kufanya mambo makubwa na mazuri zaidi ya yale. Kwanza wewe ndiye uliyeniamini na kuchukua hatua yakuweka ndoto zangu kwenye uhalisia. Kama sijashukuru vya kutosha, naomba uniamini nimeshukuru. Sitajali nia yako yakufanya hivyo. Ila kwangu umenijenga na kunifanya nijiamini.” “Hapakuwa na nia nyingine Naya, zaidi ya kukuamini na kukupenda. Mimi sio mjinga. Najua mtu anayeongea kitu cha maana na mtu anayeongea ujinga. Na hata kama ungeongea ujinga, kwa kuwa nakupenda, ningefanya ili uje ushindwe mwenyewe.” Naya akacheka kidogo. “Usiku mwema Malon.” “Asante. Mungu akusaidie umalize salama.” “Amina. Na ninakushukuru kwa kujali.” Malon akacheka kidogo, wakaagana. Hapo Naya akalala usingizi mzito, uliojaa furaha yakumsikia Malon. 

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

     Mitihani ilikuwa ikichukua majuma mawili, ila wao watu wa masoko, wauza sura kama walivyozoea kutaniwa pale chuoni, walikuwa wakimaliza juma hilo la pili siku ya jumatano, asubuhi. Wakati wahasibu na wanachuo wengine wa mwaka wa tatu walikuwa wakimaliza ijumaa. Wengine mpaka ijumaa jioni.

Mitihani ikaanza. Kila akitoka kwenye mtihani anampigia simu baba yake nakumueleza ilivyokuwa. Na kila anapokwenda kwenye mtihani, hata kama ni asubuhi, atampigia simu baba yake. Wataomba kidogo kwa pamoja, baba yake atamuombea na kufunga kwa maombi, Naya ndio anakwenda kwenye mitihani. Weekend hiyo ya katikati ya mitihani Naya akabadili mawazo. Akamwambia wasiende tena kumtembelea kama alivyomuomba aende na kina Bale wamchokoze kidogo. Akamwambia baba yake mambo yamekuwa mengi inabidi kutulia na kusoma na  wenzie ili kumalizia vizuri. Kwa hiyo baba yake hakwenda, kwa makubaliano jumamosi asubuhi au ijumaa ndipo atakwenda kumchukua. Inategemea na ukamilishaji wa mambo yake pale chuoni.

Hakuna jinsi baba Naya angeeleza furaha yake kwa binti yake mtu akaelewa. Alikuwa akimpenda huyo mtoto, na Naya alijua. Angefanya chochote kwa huyo mtoto. Alimwita mama mzazi. Na Naya angekosa kila kitu, lakini sio baba yake. Alimpenda baba yake, na kumthamini sana. Hata kama akiwa na tatizo, baba yake ndio faraja yake.

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

Siku ya jumatano baada yakumaliza tu mitihani, kwa mara ya kwanza tokea aanze mitihani ndio akampigia simu mama yake. “Nimemaliza mama.” Mama yake akaanza kucheka. “Hongera na pole.” “Nimechoka sana. Hapa naelekea chumbani kulala.” “Sasa hivi hatudaiani mimi na wewe. Fanya utakalo, ila kuwa mwangalifu tu.” “Najitahidi mama. Niombee.” “Nakuombea. Mungu atakupigania. Unarudi lini?” “Nataka nilale. Nikiamka nianze kurudisha vitabu, na kuanza kutafuta walimu wanisainie. Najua inaweza kuchukua muda. Labda leo na kesho. Nitamwambia baba. Nilitaka aje anichukue ijumaa kama nitamaliza mapema au jumamosi asubuhi. Nataka kurudi nyumbani mama. Nimechoka.” Naya akalalamika.

Mama yake akafurahi kusikia anarudi nyumbani na si kwa Malon. “Utaenda kwa Malon?” “Nitamuomba baba anisindikize nikachukue vitu vyangu vyote.” “Imekuaje tena?” Naya akatulia kidogo. Hakuzoea kuzungumza na mama yake kama baba yake. “Naya?” “Malon hawezi kuwa mume wangu mama. Na sitaki kuendelea kupoteza naye muda.” “Umemwambia?” “Nimemwambia. Naona mazungumzo ya majuzi, ameelewa.” Mama yake alimsikia akiongea kwa unyonge. “Pole mama. Tutakuja kuzungumza zaidi ukija. Na zawadi yako nzuri inakusubiri. Nimekutayarishia.” Naya akacheka. “Ni nini?” “Pongezi yakumaliza chuo.” Akacheka. “Asante mama. Ila sitaki kina Bale waje na baba. Mimi nimechoka, sitaki kelele.” Akasikia kicheko nyuma.  

“Mama! Hakikisha hawaji hao.” “Naya, mimi sikuchokozi dada yangu.” Mdogo wake wa mwisho, Zayoni, aliongea. “Sitaki.” “Nakuahidi nitakaa nyuma kabisa. Nitanyamaza. Nakuja kuwasaidia wewe na baba, kubeba mizigo.” “Muongo. Umeanza lini kuwa mwema kwangu?” “Sio kwa ajili yako wewe Naya. Ni kwa ajili yangu mwenyewe. Nataka kuja kupaona Moro.” Wakacheka. “Kama hivyo sawa. Umekuwa mkweli. Ila simtaki Bale. Bale ananitumia ile sauti yangu yakulia kila siku.” Wengine walicheka, lakini sio baba yao.

“We Bale! Hata kipindi wakati mwenzio yupo kwenye mitihani?” Akamsikia baba yake anamuuliza Bale kwa ukali kidogo. “Ndiyo baba. Alikuwa ananitumia kila siku.” “Hakuwa akijibu baba, mimi nikajua hajapata.” “Hapana Bale. Hukufanya vizuri. Mwenzio alikuwa kwenye mitihani, halafu wewe unampelekea vitu vya huzuni!” Alimsikia baba yake akilaumu kwa ukali kidogo.  “Samahani baba.” “Usimsamehe baba. Adhabu yake iwe kutokuja naye Moro.”  “Tafadhali baba. Na mimi nataka kwenda. Nakuahidi sitafanya fujo wala sitamchokoza Naya.” “Mwambie aniombe mimi msamaha, baba. Tena aseme shikamoo, na aniite dada katika kila neno.” “Haa!” Bale akashangaa. “Kama hutaki basi. Hakuna kuja. Ukija Bale, mimi siondoki hapa chuoni. Mpaka unipe shikamoo, na uniite dada.” Wengine wakaanza kucheka lakini si Bale. Walijua hapo amemkamata. “Kama ndio hivyo basi bwana.” Bale akasalimu amri. “Basi. Na nisikuone sura yako huku.” Naya akakata simu.

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

Aliamshwa na Malon. “Malon.” Alikuwa akimpapasa mgongoni. “Umelala kama mzoga!” Naya akacheka huku anafuta mate. “Naona unalowesha tu mto.” Naya akacheka sana. “Nilikuwa nimechoka bwana! Vipi?” “Kwa kuwa nilijua hutakubali kutoka na mimi, nimekuletea mlo wa pongezi.” Naya akacheka nakujigeuza vizuri. “Ungenijaribu Malon!” “Nakujua Naya.” “Ni kweli nisingekubali. Wala hujakosea. Sasa chakula chenyewe kipo wapi? Njaa inauma. Maana niliingia kwenye mtihani na njaa, nikatoka nina njaa na usingizi. Nikaona nilale kwanza.” “Pole. Ila chakula kipo kwenye gari.” Naya akabaki akimtizama.

“Hutaki hata kukaa kwenye gari yangu!? Mbona ulisema tutakuwa marafiki?” “Na wanawake zako wa hapa je?” “Ushawahi kuniona nakuja Mzumbe kwa ajili ya mwanamke yeyote isipokuwa wewe?” “Hilo ndio natakiwa kulifurahia, na kujiona mimi ndio wa maana kuwazidi wao?” Malon akanyamaza. “Eti Malon?” “Nimeleta chakula tu Naya. Sikuja kukuudhi.” Naya akacheka. “Nashukuru. Ila ningefurahi kama kingenifuata hapa, sio kwenye gari yako ambayo kila mtu anaifahamu kuwa ni yako. Na wanawake zako wote wanapanda humo.” “Sio kweli Naya. Labda kama umeamua kuniadhibu tu. Sina mwanamke ninayembeba kwenye ile gari isipokuwa wewe.” “Kwa hiyo huwa unawakuta hukohuko unapokwenda kuwalala?” Akamuona anatoka bila kujibu. Naya akacheka tu, nakubaki palepale kitandani.

Baada ya dakika 5 Malon akarudi. “Nilijua umeenda kuniletea chakula!” “Acha kuniringia kwa kiasi hicho Naya!” “Mimi nakuringia Malon!?” Naya akauliza kwa mshangao na hasira kidogo. Mwenzake mmoja alikuwepo amelala kitanda cha pembeni. “Kwa kipi nilichonacho cha ajabu ambacho nikuringie nacho, ambacho wanawake zako wameshindwa kukupa? Sina kitu cha thamani na tofauti na wanawake zako wote ulio nao! Hilo umelithibitisha kwa maneno na vitendo. Sina thamani hiyo Malon.” “Ningekuwa nahangaika na wewe kwa kiasi hiki, Naya!” Naya akakaa kwa hasira.

“Unahangaika kwa lipi na tofauti na wanawake zako Malon? Wote unatuhonga. Inatofautiana aina tu na namna ya jinsi unavyotuhonga. Wote unatuvua chupi na kutufanyia unachotufanyia. Ila mimi ndio nimeweka kikomo, kwa kuwa nilichokitaka kwako ni tofauti na wenzangu. Wao wanaendelea kupata wanachotaka mutoka kwako, tena unawapa kwa kadiri ya ulivyojaliwa. Mimi nimekosa kupata ninachotaka kwako, nimeamua kusitisha huo upuuzi.” “Naomba utulie Naya. Unaanza kupandisha hasira.” “Nimebadili na mawazo Malon. Hata nguo ambazo ziko kwako sihitaji tena. Wape wanawake zako.” “Naya! Sikuja kukuudhi.” “Na sitaki chakula chako. Natamani kukufukuza hapa, na kukwambia uondoke, lakini nakosa huo ujasiri. Unao wanawake zako watatu hapa chuoni. Upo huru kwenda kwa yeyote yule. Ila kwa kuwa hapa chumbani bado sijajua kama kuna ambae ushamvua nguo, au una mpango wakumvua kwa sasa, naomba utoke tu hapo uliposimama. Upo huru kuwepo popote hapa chuoni. Hata nje ya huo mlango unaweza kuona wanawake zako wakipita au ukapata mwingine.” Malon alibaki amesimama pale chini, mikono mfukoni. Naya juu ya deka, kitandani kwake.

Wakatulia kwa muda wakiangaliana. Naya akainama. Malon sio mtu wakutukanwa, au wakukejeliwa kwa kiasi hicho. Na Naya anamjua. Angeshaondoka na kufanya fujo zakutosha hapo, lakini ni Naya. Akamuona Naya anafuta machozi, akarudi kujilaza kwenye kitanda chake. Malon akamsogelea pale kitandani, bado alikuwa akilia. “Twende ukale. Nimekuletea kitu kizuri unachopenda. Tena nimepika mwenyewe. Twende.” Naya kimya. “Hata ukikataa sasa hivi Naya, kila mtu anajua wewe ni mwanamke wangu na gari yangu ipo hapo nje, nipo kwako. Hamna chakujificha tena. Au kuna mwanaume umemuhakikishia kuwa umeachana na mimi mnataka muendelee naye, ndio maana unanitukana ili nikasirike niondoka?” Naya akaka kwa mshangao.

“Ujue Malon wewe umechanganyikiwa!”  Akamrushia ule mto aliokuwa amelalia, Malon akakwepa nakutabasamu. “Hapana Naya. Naona unatafuta kila sababu yakunitoa hapa. Ni nani huyo uliyemuahidi..” “Naomba unyamaze Malon. Nyamaza kabisa. Ni kwa nini wewe hufikirii hata jambo jema, mawazo yako ni machafu tu?” “Jema kama lipi Naya? Au zaidi ya haya ninayokufanyia? Hivi unajua leo ni jumatano, saa 10 jioni, nakwambia nipo hapa na chakula nilichokupikia mimi mwenyewe. Sio nimekununulia, nimepika! Inamaana siku nzima leo sijafanya kazi, nakupikia wewe.” “Na ulivyo na mkono mzito kwenye kupika! Hapo utakua umejaza jiko zima kwa vyombo vichafu!” Malon akacheka na kutingisha kichwa.

“Unaona kejeli zako? Lakini ujue leo sijafanya kazi kwa ajili ya kukupikia wewe tu. Gari imejaa vyakula kama mhagawani!” Naya akaanza kucheka huku anafuta machozi. “Yote hayo nimefanya kwa ajili yako Naya.” “Asante Malon.” Wakatulia. “Twende ukale, ndio uje uendelee kupumzika.” “Nina kazi zakufanya hapa, kabla sijaondoka. Hata hivyo nahisi nimechelewa. Nitaanza kesho.” Akashuka Naya kutoka pale kitandani, Malon akampokea. “Kaoshe uso Naya. Umejaa mate.” Naya akacheka. “Umekosa busu kwa maneno yako ya kejeli.” “Unanidanganya tu Naya. Wala huna mpango wakunibusu. Wewe kaondoe hayo mate usoni, tukale.” Naya akacheka nakutoka.

Baada ya muda akarudi nakumkuta Malon anamsubiria nje ya mlango. “Twende.” Wakatoka tena wanacheka, kama sio wao. Wakaingia kwenye gari ya malon. Akakuta Malon amevipanga vile vyakula, nyuma ya gari yake, vizuri sana. Naya akacheka, nakuchukua sahani na kijiko. “Natamani ungekuwa mtu watofauti Malon.” “Ungepata wapi sasa mtu wa kukujali hivi kama ningekuwa tofauti?” “Ni kweli. Lakini najiuliza kama kwangu unafanya haya, na kwa wenzangu unakuwa unawafanyia nini?” “Kabla hujaongeza neno jingine la kukuudhi wewe mwenyewe zaidi, naomba pakua chakula ule Naya. Hapo unachofanya, nikujipandisha hasira wakati wazi unajua mimi sio mtu wakumfanyia msichana haya, zaidi yako na mama yangu mzazi.” Naya akakunja uso.

“Naomba ule Naya. Tafadhali. Nimepika kwa ajili yako. Leo nimeahirisha kila kitu kwa ajili yako.” “Na wengine huwa unawafanyia nini?” “Naya!” “Kama hunijibu, basi sili. Ondoka na vyakula vyako.” “Naya!” Naya akarusha sahani aliyokuwa ameshika, na kijiko. Akarusha mbali kabisa. Ilikuwa sahani ya udongo. Wakasikia ikipasuka huko ilipokuwa imetupwa. Naya akarudi kumtizama. “Kinachofuata ni hiki chakula. Kwa kuwa ulikipika kwa ajili yangu, nitakimwaga hapa hapa, uondoke na hotpot zako zikiwa tupu ili usirudi na mzigo.” Malon akatingisha kichwa.

“Umekuwa mkorofi Naya!” “Wewe ndio umenisababisha Malon. Niambie kwa wanawake zako wengine huwa unafanyaje?” “Ni kweli unataka kujua au ni hasira tu?” “Nataka kujua.” “Naya, umekasirika. Utakuja kujichukia zaidi. Naomba tuache hayo mambo. Jua nakupenda.” “Hayo ni maneno unayowaambia wanawake zako wengine wote. Mimi nataka uniambie ukweli.” “Sijawahi kujieleza hivi kwa mwanamke Naya! Mbona kama unasahau kama unazungumza na mimi?” Naya akasogea kwenye gari akachukua mboga za majani, Malon akamuwahi ili asimwage. Akampokonya na kurudisha kwenye gari. Akachukua bakuli la matunda.

“Acha fujo Naya.” Akampokonya na kurudisha kwenye gari, akafunga mlango wa nyuma, akamvuta Naya kwa nguvu, akamkumbatia kiunoni. “Nisikilize Naya. Wanawake wote sasa hivi wananipenda, kama sio kwa muonekano nilionao sasa, ndani ya hizi nguo nilizovaa, basi ni pesa. Sina haja yakutongoza, wala kuwaambia maneno mengi kwa kuwa na wao wanataka niwavue nguo ili waone kifua changu, niwashike tu, au niwahonge pesa.” Naya akaanza kulia kwa uchungu. “Bado unataka kujua?” Malon akamuuliza. Naya akajitoa mikononi, akasogea pembeni.

“Umbali niliofika na wewe, sijawahi kufika na mwanamke yeyote hapa duniani. Muulize Chezo ambaye unamuamini na kumpenda. Atakwambia yeye ukweli, labda mwenzangu utamuamini.” Naya akabaki kimya. “Wewe inakuwa tofauti, kwa sababu kabla ya wewe kunipenda, mimi nakupenda sana. Natamani ingekuwa tofauti, nisikufuate tena. Niendelee na maisha yangu kuliko hivi ninavyoteseka, lakini siwezi Naya. Maisha niliyoishi hayakuhitaji kujieleza kwa mtu yeyote. Hilo nilihakikisha nalifuta hata kwa wazazi wangu. Sikutaka mtu anifuatilie wala aniulize jambo mpaka niamue. Ukikaa na mama atakwambia Naya. Hata kwake nazungumza naye kile ninachotaka mimi. Imenifanya kuongeza uhuru hata kwa wanawake. Imechafua tabia yangu. Ikaniweka huru. Hakuna wakunihoji ninapokuwa na yeyote, kwa kuwa hakuna niliyekuwa nimekusudia kumuweka karibu kwenye maisha yangu kama wewe. Najua nitabia chafu, lakini kwa wakati ule ilinisaidia kuishi kwa amani, hakuna ugomvi na msichana yeyote. Wote niliokuwa nikilala nao walikuwa wakiona ni kama wamebahatika. Na mimi ikawa inaniongezea ujasiri na uhuru, mpaka ulipokuja wewe.” Naya kimya akiendelea kulia.

“Kwa kifupi, huwa sitongozi. Kwa kuwa kama mwanzo nilivyokuwa nimekwambia. Wanawake hawakunitaka sababu sikuwa na pesa, na sasa hivi wananitaka sababu nina pesa. Navaa vizuri, nina nyumba, gari na nimejenga huu mwili. Wao ndio wananifuata. Sihitaji kumwambia yeyote kuwa nakupenda, wala sihitaji kumpikia yeyote kwa kuwa najua wananitumia, na mimi nawatumia tu, tofauti na wewe Naya. Pesa yangu haikuwahi kukuzuzua. Unanipenda kwa dhati, ndio maana nakuahidi nitabadilika. Idadi nyingine ya wanawake unaowajua wewe ni wale niliokwisha lala nao kabla yako.” “Sasa kwa nini husemi, kama sio unanidanganya sasa hivi?” Naya akauliza huku akilia.

“Inasaidia nini au itapunguza nini wakati ni kweli nilishalala nao? Na kweli nilikuwa mchafu?” “Ulikuwa au bado ni mchafu?” “Ninapokwambia najitahidi kubadilika, naomba amini kuwa najitahidi Naya. Pengine Chezo anaweza kuwa shahidi wa hili. Nabadilika kwa ajili yako Naya. Tafadhali nipe muda.” “Mimi sina muda huo Malon. Wewe endelea na maisha yako, ila ujue na mimi nimeendelea na yangu.” “Unamaanisha nini?” “Sihitaji kujieleza kwako Malon. Ila ujue haya ni maisha yangu. Nilishakupa nafasi uchague. Ukajichagua wewe, wakati ulijua nakupenda. Nimeamua kujaribu na kwa wengine nione. Labda huko nitabahatika Malon. Umeniumiza sana.” Malon akatulia akiwa amekosa raha kabisa.

Naya akamuona amebadilika. Lakini kwa kuwa alimjua Malon hataki kuhisi kama anaweza kuwa na mwanaume mwingine. Akaamua kumpuuza. Akajifuta machozi vizuri akatulia. “Naomba tule.” “Umevunja sahani moja Naya.” Naya akacheka. “Tutatumia hiyohiyo iliyobaki. Kwanza ukimwi hauambukizwi kwa kuchangia sahani.” Malon akacheka na kutingisha kichwa. “Na kijiko?” Malon akamuuliza. “Kwani una vidonda mdomoni?” Naya akauliza. “Kwa nini usiangalie mwenyewe?” Naya akaanza kucheka. “Mimi nakuamini huna vidonda bwana.” “Huniamini Naya. Nashauri uhakikishe.” Naya akainama huku akicheka. Ni kweli alikuwa na hamu na Malon.

“Itakuwa kiss ya kuagana.” Malon akatabasamu vizuri, mikono mfukoni, Naya akainama. “Utanikumbatia?” Naya akauliza kwa upendo na upole. “Ndiyo.” Malon akajibu huku akisogea. Akamvuta karibu yake, akamkumbatia vizuri. Naya akaanza kulia tena. Akazungusha mikono yake kwa Malon, akaanza kumbusu taratibu. Hata Malon alijua alikuwa na hamu naye. Alimbusu muda mrefu, watu wakipita wakiwaangalia. “Nimekumiss Malon.” Naya alinong’ona. Malon akamtizama. “Samahani Naya.” “Kwa nini umeshindwa kubadilika?” “Nimekuahidi kubadilika Naya. Ungekuwa mtu mwingine, ningeweza kukudanganya tu. Kila kitu ningekudanganya. Lakini nakupenda na sitaki kukudanganya. Nakuahidi, nitafikia sehemu utakayofurahia.” Naya akarudia kumbusu kwa muda mrefu, Malon akiwa amemkumbatia. Baada ya muda akamuachia.

“Asante Malon.” “Karibu.” Wakatulia. “Ukiamua kubadilika, na kuamua kubakiwa na mpenzi mmoja, naomba unitafute mimi. Kama bado nitakuwa sina mtu, tuendelee. Unajua ninavyokupenda Malon.” Naya akajifuta machozi. “Nivumilie Naya.” “Natamani, lakini siwezi Malon. Naomba nikutakie maisha mema. Nitakutafuta nikitulia.” “Na chakula!?” Malon akashangaa Naya anaondoka.

“Naya!”  Malon akamfuata na kumwita. Naya akageuka na kukunja mikono yake kifuani akiwa amenyongea. “Chakula? Nimepika kwa ajili yako.” “Unajua chakula sio kitu nataka kutoka kwako Malon. Unaweka juhudi kwenye vitu ambavyo havina umuhimu kwangu. Naweza kupata chakula kwa yeyote na popote, lakini sio jinsi unavyonishika na kunibusu wewe. Sio jinsi unavyofanya mapenzi na mimi.” “Mimi nipo Naya.” “Inaniwia vigumu Malon. Huwezi amini jinsi ilivyokuwa ikinisumbua wakati nikibusu midomo yako. Nilikuwa nikishindana na picha nyingi sana wawazoni mwangu ili tu kukubusu. Najiuliza ni wapi hiyo midomo inapita au imepita tokea tumeachana, mpaka leo mimi ninaibusu? Umenikumbatia hapo, nikiwa nakuhitaji, lakini najiuliza mikono hiyo imetoka kushika vingapi, wangapi, mpaka kunifikia mimi! Ni vile nilikuwa na hamu na wewe sana Malon.”

“Lakini hili busu tulilopeana sasa hivi, limenihakikishia hatuwezi kuja kuwa pamoja tena. Siwezi Malon. Mimi mwenyewe najichukia. Natamani niwe kama wanawake zako ambao hawana shida kuchanganywa, lakini sina jinsi yakujibadilisha Malon. Sijui kwa nini nimeubwa hivi au nipo hivi. Mpaka nahisi ni kwa kuwa nafsi yangu inajua yupo mtu mmoja, sehemu fulani, kwa ajili yangu. Wala sio wewe. Acha nijipe muda Malon. Labda nitapona na kuweza kuendelea na maisha yangu. Pengine nitarudia ile amani uliyonikuta nayo.” Naya akajifuta machozi.

Akaendelea. “Unajua Malon, sikuwa na pesa, lakini nilikuwa na amani sana. Nilikuwa nikiweza kulala usingizi mpaka asubuhi. Lakini sasa hivi ni uchovu kama vile ulivyonikuta, ndio unanisaidia kulala. Unanifanya nakosa amani. Nakuwaza wewe wakati wote, hata kwenye mitihani nilikuwa nikikuwaza Malon. Najiuliza kwa wakati huo uko wapi, na nani na ukimfanyia nini! Nakumbuka unayonifanyia tukiwa wote, nakuona ndivyo unavyowafanyia wanawake zako. Nakosa raha. Sina furaha Malon. Umechukua ile furaha yote uliyokuwa umeiongeza mwanzoni kabisa wakati tunaanzana. Ulinikuta nina furaha. Ukaijaziliza mpaka kufurika. Ukaweka uthamani wangu mbele za watu, kisha ukaanza kurarua moyo wangu bila huruma Malon!”

“Ukatembea na watu wakaribu yangu. Nasikia yale yale unayonifanyia mimi, ndio unayowafanyia na wao. Mbaya zaidi ukijua ni watu wa karibu yangu! Umenidhalilisha vyakutosha Malon. Ulifika umbali wakunipiga kwa kosa lakukufumania! Acha nijiuguze Malon. Pengine nitapona na Mungu atanikutanisha na huyo mtu wangu.” Naya akataka kuondoka.

Malon akamuwahi tena. “Unakumbuka jumapili hii ndio ile jumapili ya wazazi wanatoa shukurani kanisani kwa ajili ya  miaka 50 ya ndoa?” “Endeleeni tu, Malon. Mimi sitaweza kufika.” “Tafadhali Naya. Naomba nifichie aibu yangu. Niliwaomba iwe jumapili hii ili na wewe uwepo.” “Kwa nini tuendelee kudanganya wazazi Malon? Heri tuwaache wajue kuwa tumeshindwa kuwa pamoja.” “Tafadhali Naya.” “Hapana Malon. Naomba niache niendelee na maisha yangu. Inatosha. Wewe unayo pesa na wanawake wanakutaka kwa kukugombania. Tafadhali tafuta wakuendeleza naye hichi unachokifanya kwangu.” Naya akainama akiwa ameshika magoti. Akalia sana mbele ya Malon. “Natamani ungekuwa umenichagua mimi kama niliyokuomba Malo.” Akaongea hivyo akilia na kuondoka, akamuacha Malon amesimama palepale. 

Naya aondoka mkoani Morogoro bila yakuaga.

            Baba yake alikuja kumchukua siku ya jumamosi asubuhi. Kwa kumsikia tu kwenye simu siku ya alhamisi usiku, baba yake hakutaka kuja na yeyote yule. Naya alikuwa amepooza sana wakati akiongea na baba yake kwenye simu. Akajua kuna linaloendelea. Akaona asimuudhi zaidi kwa kuja na wadogo zake. Aliwakatalia wote, akafika Morogoro na gari yao. Ya kawaida tu, ndiyo hiyo hiyo alikuwa akifanyia biashara jijini. Akamsadia Naya kupandisha kila kitu chake kwenye gari. “Vimeisha baba. Turudi nyumbani.” “Ni kama uliniambia kuna mizigo yako kwa Malon!” “Hatutapitia huko. Turudi tu nyumbani.” Bila maswali mengi, Mzee akaondoa gari kurudi Dar. Njiani Naya alikuwa ametulia sana.

“Vipi mama? Mipango yako ikoje?” “Jana nimezungumza na Madamu Vane. Ameniambia niende leo jioni nikazungumze naye. Anaona tunaweza kufanya naye kazi.” Baba yake akamtizama. “Nitakuwa mwangalifu baba. Na nitafanya kazi ninayojua itanilipa. Usiwe na wasiwasi.” “Na Malon?” “Nampenda Malon, baba, ila kwa kuwa siwezi kuwa na mahusiano naye ya kimapenzi tena, siwezi kuja kurudi kufanya naye biashara.” “Naya! Lazima ujue kutofautisha mambo. Yule kijana amewekeza pesa nyingi sana kwenye kitu ulichomwaminisha wewe mwenyewe! Sasa unajuaje huko unakokwenda nako hutaishia tu njiani na yeye akikuudhi?” Naya akanyamaza.

“Huwezi ukawa unaanzisha mambo makubwa, halafu unaruhusu kuendesha mambo yako kwa hisia! Utakuwa mtu wakuanza kila leo. Labda nikuulize tu, kwa sasa hivi unataka nini?” “Pesa baba.” “Hiyo pesa unayotaka, hutajali ni wapi inapotokea?” “Isiwe tu haramu. Ila ningetamani itokane na kitu ninachopenda kufanya.” “Unajua ni nini unapenda kufanya?” “Najua na wewe unajua baba.” Naya akajibu. “Kwa hiyo tatizo ni Malon?” “Ndiyo. Ananiuma huyo Malon, baba! Sijui nifanyaje?” “Basi jipe muda wakati hujui chakufanya na Malon. Ila usimwambie kuwa hutaendelea na kile alichowekeza. Utakuwa unatupa bahati yako wewe mwenyewe wala si Malon. Utamkosa Malon na pesa pia.”

“Kwani huamini naweza kufanya peke yangu nikafanikiwa?” “Kwa mwanzo upi? Maana kila kitu ni cha Malon. Na mnaonekana upande wa kazi, mnafanya vizuri sana.” “Ni kweli.” “Sasa? Hata ukipata mtu ambaye atakufanyia kazi kwa kumlipa, huwezi kupata mwaminifu, mchapakazi, anayekuamini kama Malon. Lazima ifike mahali uweze kuweka tofauti zenu pembeni, muendelee. Sawa?” “Nitajitahidi baba.” Hapo akatulia. Wakaanza kuongea. Mpaka wanafika nyumbani, Naya anafuraha.

Alikaa hapo akisaidia kazi za nyumbani na kupanga chumba chake, mpaka jioni alipoaga anatoka. “Utarudije?”  Baba yake akamuuliza. “Kuna mtu atanifuata, na ndiye atakayenirudisha. Ni ndugu yake Madamu Vane.” Baba yake akamtizama, Naya akacheka. “Sasa ni nini baba?” “Naomba kuwa mwangalifu Naya.” “Ni kijana wa muda mrefu tu baba. Alikuwepo hata kabla ya Malon. Nilikuwa nikifanya naye kazi. Yaani kupokea maagizo kutoka kwa Madamu Vane, kupitia yeye. Ametulia sana. Katika wasichana wote aliokuwa akitusimamia, hajawahi kuwa na mahusiano na hata mmoja wetu. Ndio maana alikuwa karibu yangu.” “Anaitwa nani?” “Nimekwambia usiwe na wasiwasi baba.” “Naya?” “Anaitwa Ozi. Na kama una wasiwasi, nitamwambia aje mpaka hapa akusalimie kabla ya kuondoka. Maana nilimwambia anisubirie kule barabarani.” “Tafadhali naomba afike hapa. Haya mambo yakuchukuliwa kichochoroni, hapana Naya.” “Sawa baba.” Naya akacheka na kurudi ndani kujiandaa. 

Naya & Ozi.

Ozi alipiga simu kuwa amefika kituoni. “Baba anataka kukuona Ozi. Naomba ufike mpaka nyumbani, umsalimie. Ndio atakuwa na amani.” “Unauhakika?” “Yeye mwenyewe baba ndio anataka kukuona kwanza, ndio atakuwa na amani nikiondoka na wewe.” “Sawa. Basi nakuja.” Naya akakata simu na kumalizia kujitengeneza.

Akasikia gari nje, akajua ni Ozi, akatoka kwa haraka kabla hajapokelewa na kina Bale. “Gari yake wala sio nzuri kama ya Malon!” “Naomba nyamaza Bale. Tafadhali usinitie aibu.” Naya akanong’ona. “Kwani hamjui Malon?” “Baba! Baba!” Naya akaanza kuita kwa sauti kabla hajafungua mlango kumkaribisha Ozi. Baba yake akatoka. “Naomba mfukuze Bale. Anataka kuniharibia kwa mgeni wangu.” “Sasa mimi naharibu nini jamani!? Mimi nimemuuliza kama huyu mgeni anamfahamu Malon, ndio anataka kulia, anakuita wewe!” Baba yake akamgeukia Naya.

“Kwani hafahamu kama yupo Malon?” Baba yake akauliza nakumfanya Bale afurahie sana. “Shhhh! Baba na wewe umekuaje? Huyu kaka ndio natoka naye mara ya kwanza.” “Lakini sivyo ulivyoniambia Naya. Umeniaga unakwenda kazini.” “Jamani baba! Si nimekwambia kabisa ni ndugu wa yule mama! Huwa nafanya naye kazi.” “Kwa hiyo unachanganya mapenzi na pesa?” Bale akaongeza kichochezi. Ozi akagonga mlango.

“Baba mimi sikudanganyi, na wala sijawahi kukudanganya. Naomba tumpokee mgeni, nitakueleza kila kitu nikirudi. Naomba usihamie upande wa Bale. Nitakufa humu ndani. Wewe bakia kuwa mtetezi wangu mimi tu?” “Hata kama ukiwa unamdanganya baba, yeye anatakiwa anyamaze tu!?” Naya akamsogelea Bale kwa hasira nakuanza kumsukumia chumbani kwake. Akamsukuma kwa nguvu na kufunga mlango. Baba yake akawa ameshamfungulia mlango Ozi, Bale na mdogo wake wakatoka huku wakicheka.

“Mimi sijui kama hii nyuma nitakuja kuolewa tena!” Naya akakaa kwa hasira huku akitaka kulia. Bale na mdogo wake wakazidi kucheka na kumsogelea Ozi. “Sisi ni kaka zake Naya.” “Usiwasalimie Ozi mwaya, na wala usiwasikilize hao. Msalimie tu baba, tuondoke zetu.” Mama yake akatoka. “Haya, Bale na mwenzio tokeni nje. Sasa hivi.” “Ozi karibu sana. Kama ulivyosikia sisi tumefukuzwa nje, ili mtoto wa baba asilie.” “Ona mama jamani! Ni maneno gani hayo yakumwambia Ozi?” Naya akazidi kulalamika. “Wewe usimsikilize Bale. Alikuwa anakusubiria urudi awe anakuliza kila siku. Sasa naona unatimiza azma yake.” “Na wala silii.” “Mbona nayaona machozi?” “Bale toka wewe!” “Sawa mama. Bye Naya.” “Sitaki. Sijui ukoje! Urefu tu lakini huna akili.” Bale alizidi kucheka huku akitoka.

Kisha akarudi kwa haraka. “Bwana leo patamu hapa! Gari ya Moro ileee, inakuja. Mzee mwenyewe anakuja.” Naya akasimama kwa haraka, akachungulia dirishani, alikuwa Malon. Bale akazidi kucheka. “Leo patakuwa patamu hapa! Mimi niliuliza, ukaenda kumwita baba. Sasa mimi nakaa kimya, nisikilize.” Bado Ozi alikuwa amesimama kimya tu.

Malon akaegesha gari yake pembeni ya gari ya Ozi. Bale akaanza kucheka na kutoka nje vizuri kumpokea Malon. “Karibu sana Malon na pole kwa safari.” “Asante. Vipi wewe?” “Nipo mkuu. Karibu sana. Naya naye amerudi leo.” Wote walikuwa ndani, wanawasikiliza. Naya mapigo ya moyo yakienda mbio, Ozi anamwangalia. “Afadhali. Nimemletea baadhi ya vitu vyake, nilijua angehitaji.”  “Karibu sana. Acha nikusaidie kabisa mpaka ndani.” Bale alisikika akishabikia. “Kwanza tukushukuru kwa yule fundi wa cable. Naona sasa hivi tunaangalia mpira bila shida.” Bale alisikika. “Ni jamaa yangu. Tunaelewana sana. Namtumia sana kwa kuwa ni mwaminifu. Ni yeye pia ndio alitusaidia kwenye ile nyumba ya Kunduchi.” Wakaingia na mizigo ndani.

Malon akabaki ameduaa kidogo. Mama na baba yake Naya walikuwepo sebuleni, Naya amesimamana kama Ozi  ambaye hata hakukaribishwa kiti. “Shikamooni baba na mama.” Malon aliwashika mkono baada yakuweka vitu chini. “Vipi Ozi? Kumbe unafika mpaka huku?” Akauliza Malon huku amemgeukia Naya. Naya akanyamaza. “Kumbe mnafahamiana?” Akualiza baba yake Naya. “Ndiyo, na nilishamuonya akae mbali na Naya. Na aache kumtumia jumbe hata zakumtakia Naya usiku mwema.” Bale akaanza kucheka. “Bale, naomba ingiza mizigo ndani na uondoke.” “Sawa baba.” Bale akaitikia, na kweli akaondoka.

“Naomba kabla hujaanza fujo, tuzungumze hapo nje Malon.” “Lakini Ozi akiwa ameondoka. Tafadhali Naya. Nisaidie, na hapa nyumbani nisiharibu.” “Sasa kwa nini ukasirike Malon, wakati hujui ni kwa nini Ozi yupo hapa?” “Nilikwambia ni afadhali mtu mwingine yeyote, lakini sio Ozi. Kwa kumuona hapa leo, wakati alhamisi tulikuwa wote, na ukaniambia yale uliyoniambia, naanza kuhisi yeye ndio sababu. Ozi amekuwa ni mpinzani wangu tokea zamani. Yeye ndiye amekuwa akitafuta habari zangu mpaka za Morogoro, anakuletea wewe. Nilipokuta jumbe zake kwenye simu yako, akikwambia habari za Aisha, tena wa Morogoro, nikataka kumfuata, lakini uliniambia yaishe, utazungumza naye na hutawasiliana naye tena. Leo naona umemleta mpaka kwa wazazi!” “Baba ndiye amesema afike nyumbani asalime, sio aishie barabarani.” Malon akamgeukia Ozi.

“Unampeleka wapi Naya?” “Kazini.” “Kazi gani?” Malon akauliza. “Sio lazima kazi zote uwe unazijua wewe Malon. Kwani yeye anajua kazi zako zote?” “Nisikilize Ozi. Kwa heshima ya wazazi wa Naya, nitajie kazi unayompeleka sasa hivi Naya. Kisha nihakikishe sasa hivi kwa kumpigia dada yako simu, ili kujua kweli kama hiyo kazi ipo. Lasivyo nitakuumiza. Nitakupiga kama mtoto mdogo. Nitakupiga kwa maneno ya uongo uliyokuwa...” “Sijawahi kumdanganya Naya juu yako. Nimempa habari za kweli na wasichana wote nilizungumza nao kwa uthibitisho na niliwarikodi, nikamtumia Naya.” “Mambo ya zamani hayo!” “Sio yote yazamani Malon. Mengine ni uliyokuwa ukiyafanya hata ulipokuwa na Naya.” Malon akafunga macho na kutingisha kichwa.

“Watu wanakuogopa Malon. Lakini mimi sikuogopi. Wewe mtoto wa mjini na mimi..” “Naomba nyamaza Ozi. Tafadhali usiendelee kuongea kitu chochote tena. Mimi namjua Malon.” “Atanifanya nini?” “Naomba nyamaza Ozi. Mambo ya Malon, niachie mimi mwenyewe. Kwanza siwezi kuruhusu ukamdhalilisha hapa.” “Naya!” Ozi akashangaa sana. “Wewe unafikiri nitakuruhusu mdhalilishe Malon mbele yangu tena mbele ya wazazi wangu! Hapana! Nashukuru kwa kuniambia ukweli juu yake, inatosha. Naomba mengine niachie mimi na yeye. Nyamaza kabisa.” Naya akaingilia kati, hapo akambadilikia Ozi.

“Malon, hii kazi ni ya kweli, nimezungumza na yule mama. Ni kweli kazi ipo. Naomba uamini ni kweli kazi ipo.” Malon akatulia. “Malon!” Naya akamwita. “Naomba tukazungumze nje.” “Naomba Ozi aondeke Naya.” “Namtegemea kwa usafiri.” “Hapana Naya. Mimi nakufahamu wewe. Sio mtu wakutaka usafiri wa mtu. Niambie ukweli.” “Ndio nilitaka tuzungumze pembeni.” “Ni nini, kwa nini hutaki yeye asikie?” “Umesema nikusaidie usianze fujo Malon. Mimi nakujua.” “Wewe sema.” “Niahidi hutafanya fujo.” “Baba na mama wapo hapa, siwezi.” Naya akamtizama. “Hapana Malon. Mimi nakujua. Twende chumbani kwangu, nifunge mlango, nishike funguo. Ndio nikwambie.” Malon akaongoza njia mpaka chumbani kwa Malon. Aliwaacha pale wazazi wake na Ozi.

“Ongea Naya.” Malon akasisitiza wakiwa chumbani. “Jumanne alinipigia simu. Ndio nikamkubali.” “Nini!?” Malon akahamaki. “Subiri kwanza Malon. Kwa masharti ya kumchunguza kwanza. Hata wewe nilikwambia kuwa nitatafuta mtu, nikipata mwaminifu, atanioa.” “Uaminifu wa Ozi ni upi!?” Naya akatulia. “Mtu aliyekuwa akikuletea habari za uchonganishi, ili uniache mimi uwe naye yeye!” “Haikuwa hivyo tokea mwanzo. Ozi alikuwa rafiki na wewe nilikwambia.” “Nimuongo na mnafiki. Alikuwa akikutaka tokea upo na mimi na ndio maana alitumia uchonganishi, ili uniache, aanze kukuganda yeye.”  

“Lakini anaonekana ametulia!” “Hayo umeyajua lini? Eti Naya? Sio wewe jumatano tu uliniambia unatafuta mtu. Leo jumamosi, nakukuta hapa, unatoka na Ozi! Tena unayesema ulimkubali jumanne! Nilikuomba hata kama umenikasirikia, basi nifichie aibu yangu, kesho twende wote kanisani, uungane na familia yangu, kwa muda tu wakati wazazi wanatoa sadaka ya shukurani. Ulinikatalia kwa kisingizio kuwa mimi ni mbaya, umenichoka, kumbe sababu ni huyu Ozi! Umenidanganya Naya. Kwa mara ya kwanza, umeniumiza sana. Najijua mimi sio mwaminifu, na wanawake wote niliokwisha kuwa nao, nawatofautisha na wewe kwa uaminifu wao na wako. Nilikupenda kwa kuwa nilijua wewe ni mwaminifu kwangu.” “Sikukudanganya Malon.” “Umenidanganya Naya. Naomba usiendelee kuniumiza.” Naya akaanza kulia.

“Inawezekana mimi nikawa mbaya sana. Nikakubali lawama zote, ili tu nisije kukudanganya Naya. Lakini wewe umeweza kuniangalia machoni, ukanidanganya, ukiwa umeshamkubalia Ozi!” Malon akacheka kwa kusikitika. “Unajua nini Naya, nilikuwa nikihangaika, nakutana na watu waajabu. Hata mimi nilishajikatia tamaa, lakini tokea nakuwa na wewe, nilikuwa nahangaika, navumilia watu wa ajabu ajabu nikijua yupo mtu mmoja, sahihi, mkweli. Nilikuwa nikimwambia hata Chezo, mimi ni giza, na Mungu ananijua hivyo, ndio maana akaamua kuniletea wewe nuru. Hata niende wapi, nilikuwa nikirudi kwako, najiona nimekamilika. Kuna pumziko nilikuwa nikipata, kila nikikufikiria wewe Naya. Kuna vitu vigumu nilikuwa napambana navyo, na wala usifikiri unavijua, hujui hata nusu yake, onayonilaumia, ni matokeo ya hayo magumu ninayokwambia. Nahangaika kubadilika kwa ajili yako Naya. Na wewe nilikwambia. Sikuwa hivi anavyokwambia Ozi.”

“Ozi anakupa habari za kile nilichoruhusu watu wakifahamu. Wewe ndiye uliyeanza kunitoa huko Naya. Ndio maana nilikuwa nikikuomba univumilie. Sio kwenye maswala ya wanawake, lakini umenikataa katakata, unamkubali Ozi! Yaani leo unaona ni heri kuwa na Ozi, mpuuzi wa mwisho huyo. Mchonganishi, mfitini, ndiye unamkubali! Ndiye unamuona wa muhimu na bora kuliko mimi!” Naya alikaa chini nakujifunika na mto huku akilia.

“Umeniumiza Naya. Sana. Umebadili kila kitu kwenye maisha yangu. Umeniingiza hofu kwa kupokonya ile shauku yakutaka kotoka kule nilikokuwa. Nahisi nimeshapoteza tena maana ya kila kitu. Na kwa kuwa nakupenda sana, nakuacha kama ulivyoniomba. Inawezekana tabia zangu mbaya, ndizo zinaanza kukubadilisha moyo wako. Acha nikuache Naya. Endelea na maisha yako. Pengine Mungu atakupa huyo mtu bora kuliko mimi Malon.” Malon akatoka, nakuacha Naya akilia.   

“Samahanini sana wazazi wangu. Mniwie radhi, pale nilipokosea. Nahisi kama nimevunja heshima.” “Hamna neno.” Akajibu baba yake Naya. “Nilileta baadhi ya vitu vya Naya. Nitamtuma dereva ili kuleta vingine vilivyobakia kwangu. Muwe na jioni njema.” Malon akatoka akiwa na sura iliyobadilika, sio kama Malon aliyejawa kiburi na majivuno.

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

Kilisikika kilio cha Naya, taratibu. Wakabaki baba na mama yake Naya, wakimtizama Ozi. Ozi akakohoa kidogo, akajiweka sawa. Kimya. “Sidhani kama Naya ataweza kufanya kazi usiku wa leo.” Akavunja ukimya Ozi. Kimya. Wazazi wa Naya wakimtizama. Yale macho hakuyapenda Ozi. Yalizidi kumtia hofu. Zaidi ukimya wao. Bale akaingia.  “Mimi tokea unaegesha gari yako pale, nilijua wewe ni tatizo. Wala humfai Naya. Kama kweli ungekuwa unampenda Naya, usingemuumiza.” “Malon ndiye aliyekuwa akimuumiza, mimi nilikuwa nikimfungua macho.” “Unapomsikia akilia hapo sasa hivi, unasikia kilio cha furaha kuwa umemsaidia kuachana na Malon?” Bale akamuuliza taratibu tu ila kwa ukali kidogo.

“Nashauri wewe uondoke hapa, na wala usiwahi kukanyaga huo mlango. Hatutaki umbea humu ndani. Haya, nenda. Na kamwambie dada yako, Naya hataki kufanya tena kazi na wewe.” Ozi akatoka kimya kimya.  Naya alilia kidogo, wakasikia kimya. Wakajua amelala. Baada ya muda, baba yake akaingia chumbani kwake. Akamkuta kweli amelala. Akamfunika vizuri. Akatoka.

CONVERSATION

0 Comments:

Post a Comment