Naomi Simulizi |+1 205 767 8163 |naomisimulizi@gmail.com MAPENZI & PESA! - SEHEMU YA 6. - Naomi Simulizi

MAPENZI & PESA! - SEHEMU YA 6.

 Fimbo Ya Mbali Haiuwi Nyoka.

A

subuhi asubuhi Naya akagonga chumbani kwa wazazi wake. “Vipi mama?” “Naenda kumfuata Malon, baba.” Mama yake kimya. “Nampenda Malon.” Naya akarudia huku akifuta machozi. “Unataka nikusindikize?”  Akatingisha kichwa kukubali. “Nitaanzia nyumbani kwao. Baadaye ndio itakuwa kanisani, halafu ndio ukumbini.” “Malon alileta kadi. Tulimuahidi kufika.” “Mtakuja?” Naya akauliza kwa upole. “Wewe unataka tuje?” “Naombeni mje baba. Malon aliiandaa siku ya leo, akijua nitakuwepo. Nilimkatalia sababu ya...” Naya akasita. “Tutakuja mama. Usiwe na wasiwasi.” “Naomba nisindikize kituoni. Naogopa.” “Haya. Nisubiri hapo nje.” “Nitakuona baadaye mama.” “Haya mama. Uwe na safari njema. Tulia kabisa ili ukafanye vizuri kilichokupeleka. Sawa?” “Kwani nimeharibu sana?” “Najua huwezi kushindwa kutengeneza.” Naya akafurahia hilo, akatoka kumpisha baba yake avae.

Walifika kituoni, walikaa na baba yake wakisubiria mabasi ya Morogoro. “Nampenda sana Malon, baba.” “Najua.” “Lakini sikumdanganya.” “Kuwa unatafuta mtu wakati ulishampata?” Naya akamtizama baba yake akainama. “Tena mtu ambaye alikuwa akiwachonganisha!” “Ozi alikuwa akiniambia ukweli juu ya Malon!” “Ukweli huo ulikusaidia nini?” Kimya. “Hujua nia yake?” “Mimi nilijua ni kwa kuwa ananiwazia mema.” “Naya mama! Mimi najua una akili zaidi ya hivyo unavyozungumza.” “Kwa kuwa tayari nilishakuwa na wasiwasi na Malon, ndio maana niliamini kila alichoniambia.” “Na hilo ndilo lilikuwa anguko lako Naya. Wewe hukushangaa alikuwa akikwambia mambo mengi mabaya ya Malon! Alishawahi kukwambia neno hata moja jema?” Kimya.

“Hakuna mtu mkamilifu Naya. Hata mimi nina mapungufu kwa mama yako. Anavumilia tu.” “Sio makubwa kama ya Malon, baba.” “Unajuaje?” Naya kimya. “Nampenda sana Malon.” Akarudia kwa upole. Baba yake akabaki akimtizama. Basi likaja. Naya akamuaga baba yake, akakimbilia basi.

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

Alifika Morogoro saa mbili asubuhi. Akachukua taksi mpaka nyumbani kwa kina Malon, kwa wazazi wake. Kila mtu alishtuka kumuona Naya. Naya akabaki anacheka kwa hofu, asijue wanajua nini. “Karibu mama.” Aliwakuta wote wameamka. Nyumba imejaa hekaheka, wanajiandaa kwa shuguli nzima. Wakaanza kuitana kuwa Naya amerudi. “Acheni umbea nyinyi!” Naya aliwaambia watoto wa dada yake mkubwa Malon. “Njoo nikwambie Naya.” Wakamvuta pembeni. “Mwenzio Malon jana katukanwa na bibi kama hana akili nzuri.” “Na mama pia.” Mdogo mtu akadakia.

“Walikuwa wanamsema nini!?” Naya akauliza kwa mshangao. “Umalaya utamua, na hatakaa akapata mwanamke kama wewe. Hata akitembea uchi akajiuza na kuwalipa wanawake zake wote pesa zake mpaka suruali zake zote, eti hawezi kupata mwanamke kama wewe.” “Tena mama akamwambia ndio maana umemkataa, sababu hajui kufunga zipu ya suruali yake.” “Shhh! Mama akikusikia, atakubamiza mpaka ukome.”  Wakaangalia kulia na kushoto, hakuna mtu.

Wakaendelea. “Basi ndio babu akamwambia asione wao wanasheherehekea miaka 50 ya ndoa, kama wao sio binadamu. Au sio malijali. Eti na wao mama zao waliwatahiri.” “Haa!” Naya akashangaa kwa kuachama mdomo kwa mshtuko. “Jana walimbadilikia hapa. Aliondoka usiku bila kula. Nusura babu akatae sherehe aliyowaandalia. Alimwambia yeye ni mchafu sana.” “Kwani nyinyi nani aliwaambia nimemuacha Malon jamani.” “Unataka kumtetea?” Wakamuuliza Naya na kuendelea bila kusubiri jibu, maana walikuwa wakipokezana maneno kwa haraka wamalize kabla mama  yao hajawasikia.

“Anko Chezo alikuja hapa, akasimulia kila kitu, ndio bibi akampigia simu mama, na sisi tukaja naye kusikiliza. Si ndio wakampigia simu na kumwita! Akaja. Ilikuwa kama saa moja usiku. Walimtukana anko, mpaka usiku wa saa tano. Anko akaondoka hapa, kimya kimya. Wakabaki wanaulizana, Malon mkorofi imekuaje leo kanywea!” “Hakujibu neno hata moja!” “Lakini ndio hivyo, ndio maana watu wote tumeshangaa umekuja!” Akatokea mama yao.

“Nitawapiga nyinyi! Mnamwambia nini Naya?” “Sisi tunamsalimia na kumuulizia maswala ya chuo cha Mzumbe.” Mama yao akawaangalia kwa zamu kama asio wasadiki. Walikuwa ni wasichana mapacha. “Waongo nyinyi.” “Kweli mama. Anko Malo amesema kile chuo kizuri, hata tukikosa udhamini, atatulipia.” “Anko wenu bangi yule.” Mama yao akamgeukia Naya. “Shikamoo mama wawili.” “Marahaba. Malon ndiye aliyekulazimisha uje?” Naya akacheka tu. “Mbabe yule, mimi namjua.” “Wala hafahamu kama nipo hapa.” Ikabidi amtetee. “Kweli!?” “Kweli tena. Nimekuja tu kuwasaidia, kabla ya ibada.” “Afadhali umtengeneze mama nywele vizuri, ili avae kofia yake, sijui lemba! Hata sielewi mimi! Nimehangaika naye jana usiku, nikashindwa. Ndio maana na mimi umeona nipo hapa asubuhi hii. Twende nikakuonyeshe.” Naya akaelekea chumbani na dada yake mkubwa Malon.

“Hiki ni kilemba mama wawili!” Naya alikishika kile kitambaa. Wakaanza kucheka. “Najulia wapi!” “Mama yeye anataka kiwe vipi?” “Anayo picha yake mwenyewe. Aliyemuuzia hilo lemba, amempa na picha. Ngoja nikafuate. Lakini wewe unaweza kutengeneza?” “Umesahau ndio kazi yangu hii?” Naya akauliza huku akicheka. “Haya mama, ukumbi ni wako. Ngoja nichukue maandazi, niondoke, nirudi kwangu nikajiandae. Nakuitia mama huku huku chumbani.” “Sawa.” Naya akaanza kutengeneza kile kitambaa. Akaletewa picha. Akampima kichwa mama yake Malon, akaanza kukitengeneza.

Wakati amezama anaendelea kutengeneza kile kilemba, akashangaa Malon amesimama mlangoni. “Vipi?” “Umelala Morogoro nini?” “Hapana. Nimekuja muda mfupi uliopita.” Naya akajibu. “Pole na safari na asante kwa kuja.” Naya akatabasamu na kuinama. “Nimeshamtuma Side akawachukue baba na mama.” “Asante Malon. Japo usingehangaika. Wangepanda tu basi.” “Nilishawaambia Side atawafuata. Nafikiri mmepishana naye tu njiani. Aliondoka na yeye mapema. Nilitaka wapate muda wakufahamiana na wazazi kabla ya kanisani.” “Asante.” Naya akashukuru, nakuendelea na kazi.

“Utaenda hivyo kanisani?” “Nimekuja na nguo. Nikimaliza hapa, nitaoga, kisha nibadili.” Malon akatulia kidogo. “Ingekuwa zamani, ningekwambia twende wote nyumbani. Ukaoge, ndio tuje hapa, halafu twende kanisani. Lakini najua sasa hivi mambo yamebadilika.” Naya akanyamaza, akaendelea na kazi. Malon naye akatulia. Walikuwa chumbani, wao wawili tu. Naya akaendelea kukitengeneza kile kitambaa, mpaka akamaliza. Akamwita mama yake Malon nakutaka akae palepale mbele ya kioo. Akamvalisha na kumalizia kukibana vizuri. “Unaonaje?” Naya akamuuliza. “Kama Malkia wa Najeria!”  Akajisifia mama yake Malon. Naya akacheka.

“Basi naondoka na Malon. Nikishajitayarisha kabisa, na wewe uvae kila kitu, ubakize kilemba tu. Nakuja kukumalizia nywele na hicho kilemba.” “Asante mama. Ila usichelewe tu. Maana ukichelewa, utanikuta nacho kanisani nimekibeba kama pochi.” Naya akacheka. “Hatutachelewa kurudi.” Malon alikuwa amenyamaza kimya muda wote ameinamia simu yake. Naya akajua ni kweli alitukanwa na mama yake usiku uliopita. Bado wamekasirikiana. Maana hawakuwa wakiongea. Mama yake alipoingia tu pale chumbani, Malon akatoa simu yake mfukoni akainama. 

Naya & Malon tena.

K

wa haraka, wakatoka pale. Njiani kimya mpaka nyumbani kwa Malon. Naya akaelekea chumbani kwa Malon, akajua Malon atamfuata tu. Na kweli akaingia. Akamkuta Naya anamalizia kuvua nguo. Akamgeukia. “Naomba nisamehe Malon. Najua nimekuumiza. Lakini sikuwa na nia ya kukudanganya juu ya Ozi. Unajua ningekwambia tu.” “Ndiye unayefikiria akuoe?” Malon akamsogelea mpaka pale alipokuwa amesimama mtupu. Naya akajisogeza karibu. “Nisamehe Malon.” Malon alibaki akimwangalia.

“Nikuulize kitu Naya?” Naya akatingisha kichwa. “Ni kweli ukinibusu unapata shida?” “Naomba nijaribu tena.” “Hapana Naya. Sitaki kukukera. Kama kweli unanisikia kinyaa, huna sababu yakufanya hivyo.” Naya akaumia sana. Akajua kweli Malon amebadilika. Malon wakupenda kuvua chupi hovyo, leo amemsimamia uchi mbele yake, anakataa! Naya akafikiria kidogo kisha akaamua kuelekea bafuni. Akaoga, alipotoka, alimkuta Malon ameshaanza kuvaa. Anatengeneza tai yake. Hakuamini. “Usifikiri nimevaa bila kuoga. Nilioga kabla sijakufuata nyumbani.” Naya akacheka. “Mbona unajishuku?” “Hata. Najisalimisha tu.” Naya na yeye akavaa. Hakuamini kuona wanatoka chumbani kwa Malon bila kuguswa! Hilo lilimnyima raha Naya.

Walirudi nyumbani kwao, walikuta wazazi wa Naya na kaka zake sehemu yakulia chakula, na wazazi wake Malon na baadhi ya wajukuu. Kila mtu alikuwa amependeza. Naya na Malon wakaingia, na wao wakiwa wamependeza sana. Baada ya mazungumzo kidogo na Naya kumtengeneza nywele mama Malon, wakaenda kanisani. Ibada ilikuwa inaanza saa 4 na nusu. Malon alikuwa mkimya sana siku hiyo.

Walifika kanisani, Chezo na yeye akaingia na wazazi wake. Hakuamini kumuona Naya pale. Malon alisalimia kwa kumpa mkono tu, akatulia. Naya alishangazwa na ukimya wa Malon tokea nyumbani kwao. Alikuwa ametulia sana. Chezo na Naya walikuwa wakizungumza, Malon kimya kama hakuwepo pale. “Ulinikimbia Chezo. Tena bila kuniaga wakati tulihangaika wote mpaka mwisho!” “Daah! Samahani sana Naya. Siku nyingine nitaaga.” “Wala sitakupa nafasi ya pili Chezo. Wewe unaonekana maji yakizidi unga huwa unakimbia. Mwenzio Malon alibaki na mimi mpaka mwisho.” Hilo likaingia kwenye mioyo yao wote, kila mmoja likafanya kazi kivyake, Naya asijue.

“Yaani ni mimi tu ndio sipewi nafasi ya pili!?” Chezo akauliza akiwa amebadilika kidogo. “Kila mtu na bahati yake Chezo. Usilalie bahati ya mwenzio mlango wazi.” Naya aliongea akicheka, lakini yale maneno yaliwaingia wote. Chezo na Malon walikuwa wamegombana tokea siku ile kwenye tamasha la mavazi. Chezo hakumtafuta tena Malon, ila kumtangazia vibaya sana akimchafua kwa watu. Kuwa tabia zake za umalaya, zimemshinda Naya, ndio maana Naya amemkimbia. Mtu hatari kwa kina dada za watu. Yote hayo Malon aliyasikia, hakutaka kumtafuta Chezo. Chezo hakuishia mtaani tu, akaenda kumsemea mpaka kwa wazazi wake. Hakuna aliyejua kama Naya, angetokezea siku hiyo. Malon kimya, mikono mfukoni kama kawaida yake, macho kwengine kama hawasikii.

Naya alikuwa akiongea bila kujua kama wamekasirikiana, alidhania ni utani tu. Akamgeukia Malon, akaona tai imekaa pembeni, akaanza kumtengeneza. “Umependeza Malon!” Naya aliongea kwa sauti ya chini, Malo akacheka taratibu. “Asante. Hata wewe umependeza sana Naya.” Chezo alipoona vile, bila kuaga,  akaondoka. Naya akakunja uso kama ambaye hajaelewa. Akamtizama na Malon. “Vipi Chezo!?” “Nikuulize wewe!” “Mimi tena!?” Naya akauliza kwa kushangaa. “Wewe ndiye uliyekuwa ukimlevya kwa sifa hata mbele za watu. Leo unamkashifu tena!” “No way! Haiwezekani. Yaani huu utani hapa ndio ameufanyia kweli! Anayake tu.” Naya akapuuza.

“Hakutegemea au hakuna aliyetegemea kuja kukuona tena Moro. Chezo amenichafua kupita kiasi. Wewe si unasema kwa wanawake nikitembea ni kama nipo uchi? Basi na kwa wanaume hivyo hivyo. Chezo amenichafua kupita nitakayokueleza. Lakini tuyaache hayo.” “Samahani Malon.” Malon akacheka kwa huzuni, akanyamaza. “Nikuulize kitu Malon?” Malon akamtizama. “Baada ya haya yote, unafikiri utakuja kunisamehe au ndio basi tena?” “Nilifikiri ndicho unachotaka Naya!” “Nakupenda Malon.” “Ndivyo ulivyoniambia hata wakati ukiniacha. Na hata baada ya kumkubalia Ozi, jumanne, jumatano uliniambia hivyohivyo.” Naya akaishiwa maneno. Akanyamaza.

“Na Ozi pia ulimwambia hivyo hivyo?” Ghafla Naya ndio akawa mkosaji zaidi. “Lakini mimi sijafanya naye mapenzi!” “Kwa kuwa nilikuwahi. Nisingekuja siku ile, unajua nini kingetokea kati yako na Ozi ambaye alifanya kila jinsi uniache na umkubali yeye?” “Nisingefanya kitu Malon. Ilikuwa twende kazini, halafu anirudishe nyumbani. Basi.” “Sasa hivi ukiwa umesimama na mimi hapa, ndio unasema hivyo. Hujui nini kingetokea, Naya! Hujui alikuwa na mipango gani na wewe usiku ule. Ozi amehangaika sana mpaka amefanikiwa kukupata.” Malon akaendelea.

“Amehangaika sana huku Morogoro. Sijui alikuwa akipewa habari zangu na nani, lakini alikuwa akipata habari zangu. Japo zilikuwa za zamani, lakini zilikuwa sahihi. Akahakikisha anaziingiza moyoni mwako taratibu mpaka ukafanikiwa kusema hapana kwangu, ndiyo kwake.” Naya akainama, kama anayefikiria.

“Naona watu wanaanza kuingia kanisani, twende.” Malon akamshtua. “Naweza kuondoka Malon. Sio lazima nikawepo hapa.” “Naomba nikuachie wewe huo uhuru Naya. Kuwa huru kufanya unachotaka.” Naya hakuamini. “Malon!” “Sijui chakufanya Naya. Sijui chakukwambia tena. Nahisi nimeongea moyo wangu wote, na wewe umeongea yote kwangu. Sijui natakiwa kufanya nini tena.” “Uwepo wangu hapa unakuumiza?” “Hata kidogo. Kumbuka mimi ndiye niliyekuomba uje.” “Lakini ilikuwa ni kabla hujanichukia  Malon. Wakati ule ulikuwa ukinipenda na kunihitaji.” “Kama kwako sio shida sana au sikufedheheshi zaidi, naomba ubaki katika hili. Ila kama utajisikia nakutia sana aibu, basi. Nitaelewa.” “Nitabaki, nataka kubaki.” Naya akajibu kwa upole. “Asante.” Wakaingia kanisani.

Walikaa pamoja, lakini kila mtu alikuwa akiwaza lake. Muda wote Naya alikuwa ameinama tu akichezea simu yake kwa kuigeuza taratibu kulia na kushoto. Malon akiangalia kinachoendelea mbele, lakini akili haikuwa pale. Walishangilia na kupiga vigelegele, lakini wao walibaki kimya. Ibada iliisha, watu wakaanza kutoka kanisani.  Naya akamgeukia Malon. “Side ataturudisha au inabidi kuwahi mabasi kabla hatujachelewa?” “Ulikuwa unafikiria kuondoka saa ngapi?” Malon akamuuliza. “Inategemea na usafiri. Kama ni kwa basi, basi nilitaka kumwambia baba tusichelewe kuondoka. Kama Side atatupa lifti, tunaweza kukaa mpaka mwisho wa sherehe.” “Nitamwambia awarudishe.” “Asante. Basi nakwenda kukakaa na baba.” Naya akanyanyuka nakuondoka bila kusubiria jibu.

Baba yake alipomuona tu, akajua mambo hayakwenda vizuri. “Umependeza mama mzazi!” Naya akacheka kidogo nakujiangalia. “Asante.” “Mwenzio yuko wapi?” “Malon?” Naya akauliza. Alipoona baba yake anamtizama, akajirudi. “Sasa hivi atakuwa anashuguli nyingi. Yeye ndio amewaandalia wazazi wake hii shuguli nzima. Atakuwa na mambo mengi. Hata hivyo amesema Side ataturudisha. Kwa hiyo tunaweza kukaa mpaka mwisho tu.” Naya alikuwa akizungumza na baba yake huku akiangalia simu yake kama anayekwepa macho ya baba yake.

“Sasa huendi kumsaidia mwenzio?” Mama yake akamuuliza. Naya akatingisha kichwa kukataa. Nakujisogeza karibu zaidi na baba yake. “Lazima ukue Naya. Hapo unapojificha kwa baba yako, lazima utoke na kufanya mambo kama mtu mzima. Umekosa Naya, na baba yako hatakusaidia. Toka hapo, nenda kwa mwenzio. Unaona pale aliposimama peke yako na wewe umesimama hapa unajificha! Utaendelea hivyo mpaka lini?” “Nimemuumiza sana Malon, mama.” “Kama umejua umefanya hivyo, unakusudia kufanya nini? Yule kijana alijitoa sana kwako Naya. Lazima ukatengeneze wewe mwenyewe. Sisemi umrudiane, lakini usimuache hivyo. Hata wenzake watajua ulikuwa ukimtumia tu.” Naya akajifuta machozi, akatulia kidogo, kisha akaondoka.

Alimkuta Malon amesimama peke yake, mikono mfukoni. “Nakupenda Malon.” Malon akatoa tabasamu. “Naomba unisamehe. Nisamehe kwa maneno machafu niliyokwambia nikiwa na hasira, nisamehe kwa kuondoka Morogoro bila kukuaga. Nisamehe kwa kutokwambia juu ya Ozi.” Malon akavuta pumzi akabaki ametulia akimwangalia. “Usinichukie.” “Unajua siwezi kukuchukia Naya.” “Umenisamehe?” Malon akacheka taratibu. “Mimi na wewe tumekuwa wahanga wa mchezo mchafu ambao nahisi kuna mtu ananichezea makusudi kuniumiza. Kwa kuwa anajua nakupenda, amekutumia wewe makusudi kuniumiza mimi. Na akahakikisha amefikia moyo wako, mpaka akaupata.” “Kwa hiyo na wewe amekupata?” Malon akabaki kimya. “Eti Malon?” “Umeniumiza Naya. Sana.”

“Nimekuomba msamaha Malon. Mbona mimi nimekusamehe zaidi ya mara moja, wewe unashindwa kunisamehe mara moja tu!” “Naya!” “Kweli Malon. Kumbuka mangapi mimi nimekusamehe. Tena nikakurudia kwa upendo. Sasa kwa nini wewe unashindwa kunisamehe katika hili? Labda uwe ulikuwa ukinitafutia sababu?” “Naya! Wewe huoni ulivyoniumiza?” “Kwani wewe umeniumiza mara ngapi Malon?” Malon akabaki kimya. “Basi Malon. Mimi nimefanya kwa nafasi yangu. Nimeomba msamaha. Sijui natakiwa kufanya nini?” “Umeniambia unaona aibu na kinyaa kuwa na mimi Naya. Unafikiri tutaishije tena?” “Sijui Malon. Lakini nimerudi kwako, nimekwambia nipo tayari kukusubiria, mpaka ...” “Hujaniambia hivyo Naya. Hayo ndio unayaongea sasa hivi, hapa kanisani. Hujui nikiasi gani nilikuwa natamani kukusikia ukiniambia hivyo.” Malon akasogea karibu zaidi.

“Hata ungeniambia hutaki nikuguse mpaka uone mabadiliko, ingekuwa afadhali! Lakini umenikataa moja kwa moja Naya! Nilikuomba univumilie, kuna jambo nalifanyia kazi, nitabadilika. Ulikataa Naya. Tena vibaya sana.” “Nilikuwa nimekasirika Malon. Uliniudhi kwenye swala la Loi.” Malon akanyamaza. “Nikwambie kitu Malon. Leo sio siku yetu sisi. Ni ya baba na mama. Hawa watu wamekaa miaka 50 ya ndoa. Sisi kama tumeshindwa ya kwetu, basi naomba leo tuweke tofauti zetu pembeni, tukamilishe hili. Tuungane nao, angalau tukubali kuwa mahusiano kweli ni magumu. Lakini wapo binadamu kama sisi, wanaweza kuvumilia.” Malon akacheka. “Sawa.” “Ndio twende sasa tukacheze ngoma za kwenu.” Naya akamvuta mkono wakaenda sehemu waliyokuwa wamekusanyika watu, wakicheza ngoma. Wakaanza kupiga makofi na wao. Ile hali ya hasira ikapungua. Wakajisahau, vikajaa vicheko.

Walifika ukumbini, Naya akiwa na Malon kwenye gari yake. Wao walitangulia kwanza kuhakikisha kila kitu kipo sawa. Ndio baadaye wageni wakaanza kufika. Wazazi wake, Bale na Zayoni walikuwa wakiendeshwa na Side. Dada yake mkubwa Malon, na mumewe, ndio walikuwa wakiwaendesha wazazi wao. “Umeandaa vizuri, hongera Malon!” Malon akacheka. “Nashukuru. Unajua nilijua jana ungekuja, nikuombe tubaki wote, ili jioni tuje kusimamia hapa. Lakini mwenzangu ukaondoka kimya kimya. Nikatafuta sababu yakuja kwenu ili niombe turudi wote, nikaishia kuumia tu.” “Mpaka sasa hivi umeumia?” “Naya?” “Sasa jambo gani haliishi Malon?” “Linaishaje wakati najua upo na Ozi, ambaye hata sijui ni nani alikuwa akimtumia kupata habari zangu?” “Wewe achana na Ozi. Ozi atabakia mambo ya kazi tu.” “Wala hivyo hainifariji.” “Malon! Unataka nifanyaje? Nimekwambia nitamwambia basi maswala ya mapenzi, tubakize maswala ya pesa tu. Kuna shindano nataka anisaidie kuandaa. Dogo tu, ili nimalizie zile nguo. Pengine kutengeneza nyingine.” “Kwa hiyo Ozi ndio anachukua nafasi yangu mimi!?”  Malon akashangaa sana.

“Maswala ya mavazi, ilikuwa ni biashara yangu mimi na wewe. Mpaka tumetengeneza mahali na kununua mashine.” “Hakuna kitakachoharibika. Ninaendelea hivyo hivyo. Mimi na wewe uzalishaji, halafu mimi na Ozi utangazaji.” “Kwa kuwa unawasiwasi kuwa nitaendelea kulala na wana mitindo wako?” Naya akababaika kidogo. “Naya! Kweli unamchukua Ozi, kwa kuhofia hicho?” “Ni kwa nia nzuri. Kukutoa kwenye vishawishi Malon.” “Kwa kuwa mimi sina uwezo wa kupata wasichana mpaka wewe uwe umewatafuta?” “Acha kukasirika Malon.” “Na hayo yote unapanga na Ozi, sio mimi?” “Hapana. Nimeamua mwenyewe.” “Kwa hiyo sasa hivi hatuwezi kukaa mimi na wewe tukapanga mambo yetu?” “Nimekuomba leo tuweke tofauti zetu pembeni Malon. Zote. Kesho jumatatu, tuzungumze. Na naomba turekebishe, ili tuanze vizuri.” Malon kimya, akiwa ameshakasirika.

“Malon?” “Sidhani kama inamaana tena.” “Mimi kwangu inamaana. Kesho nitarudi Moro, kwa ajili yako. Tukae chini tuzungumze.” Hapo Malon akaridhika. “Sawa?” “Sawa.” Sherehe ikaanza. Ni kweli Malon alimwaga pesa kwenye hiyo sherehe. Watu walikuwa wengi. Walikula na kunywa, ikafika wakati wakutoa wosia. Baba yake ndio alisimama kwa kuwa mama yake alikuwa amelewa sana. Na alikuwa akilewa, hawezi kusimama. “Pale akisimama tu, anaanguka.” Malon akamnong’oneza Naya, wakacheka. “Baba yeye hanywi?” “Alikuwa akinywa, kidogo sana, na akaacha zamani sana. Mkewe ndio anapenda pombe.” Naya akacheka kimya kimya. 

Hekima ya Mzee Saduki, baba yake Malon!

W

akarudisha macho na masikio kwa baba yake Malon ambaye alisimama kuzungumza. “Tunashukuru wote kwa kufika hapa.” Alianza mzee Saduki kwa kutoa shukurani kwa kila mtu. Akaja kwa wajukuu zake wote kwa kuwataja majina. Akataka wafike pale mbele. Akataja watoto wake wote watano na kuwataka wafike pale mbele na wenza wao pia. Malon akainama kwa muda. Yeye alikuwa mtoto wa kiume na wanne kuzaliwa. Alianza kuzaliwa kaka yake, wakafuata dada zake wa wiwili, akaja Malon na wa mwisho ni mdogo wao mwingine wa kike. Kaka yake alishaoa, na dada zake hao wakubwa wawili, walishaolewa. Alibaki Malon na mdogo wake wakike ambaye bado alikuwa akisoma ila mtulivu sana. Akiwepo sehemu, huwezi hata kuhisi uwepo wake. Mkimya sana. Na familia nzima waliinuliwa kiuchumi na huyohuyo Malon.

Wakati ndugu zake wakisimama kwenda mbele, Naya akamshika mkono Malon. “Unataka twende wote?”  Akamuuliza kwa upendo. Walikuwa wamesimama mwisho kabisa ya ukumbi. Malon akamwangalia na kumuuliza. “Sitakuaibisha?” “Sijali.” Malon akatulia kidogo kisha akamshika mkono Naya, wakaenda mpaka mbele. Ulizuka ukimya wa ghafla. Naya alijua. Akapenyeza mkono wake kule alipoingiza Malon mkono wake wakushoto mfukoni.  Malon akamgeukia, akatoa tabasamu la kuridhika, akautoa mkono kule mfukoni, akamshika Naya vizuri. Akamsikia akipumua kwa nguvu kama aliyepata nafuu, na kuminya tena mkono wa Naya vizuri, wakatulia.

“Hakuna kitu kigumu, kama kuishi na mtu ambaye umekutana naye ukumbwani. Mimi niliyefikisha miaka 50 ya ndoa, ninao ushahidi. Ni ngumu, lakini faida zake ni kubwa, kuliko kuwa peke yako. Bibilia inaposema wawili ni bora kuliko mmoja, na mmoja anapoanguka mwingine anakuwepo kumsaidia kusimama, hapo ipo siri kubwa sana.” Mzee Saduki akaendelea.

“Kumbe kupo kuanguka.” Akatulia kidogo kisha akaendelea. “Halafu kumbe kuna wajibu kwa yule aliyebaki amesimama! Sio kwamba ajisifu kuwa yupo sana salama, hapana. Anao wajibu wakumsaidia yule aliyeanguka kusimama tena. Sijui kama mnanisikiliza? Sio sifa kwa aliyebaki amesimama. Kuwa yeye ni shupavu. Ni kushindwa kwake pia, kama mwenzie akibaki chini. Hakuna ushindi wa mmoja kama mmeshaamua kuwa wawili. Kushindwa kwa mmoja ndio kushindwa kwa wote. Mnakuwa mko timu.” Mzee Saduki akaendelea.

“Kizazi hiki chenu kina kasumba ya ‘ku upgrade’. Sio ‘ku upgrade’ ulichonacho, hapana. Eti ukipata simu mpya aina ya iphone X, unatupa ile simu ya zamani uliyokuwa nayo ya Iphone 8.” Watu wakaanza kucheka. “Naamini mmenielewa. Hamtunzi vya zamani. Na hata kama bado iphone 8 ipo salama, mnabadilisha kwenda Iphone X kwa sababu ya ukubwa tu wa hiyo simu, au wembamba wake. Hicho tu. Kinaondoa uthamani wa ile iphone 8. Na mbaya zaidi, na viwanda navyo vinazidi kutengeneza simu mpya kila leo! Na kila leo zinaundwa kwa miundo mbali mbali. Unajiuliza, utabadili mpaka lini?” Mzee Saduki akatulia.

“Ipo siku huyu kijana wangu mkubwa aliniambia na wenyewe wanakuwa wajanja. Wanaweka expiring date. Yaani utashangaa muda fulani ukifika, simu yenyewe haifanyi tena kazi. Nikalinganisha na ndoa, au mahusiano. Walio kwenye ndoa wenzangu watanisaidia. Kipo kipindi kinafika, mapenzi yanakuwa yanaisha. Hisia zinabadilika. Sasa hapo inatakiwa hekima. Kuendesha ndoa kwa hekima sio hisia. Ndio maana mnaona sisi tunasherehekea miaka 50 ya ndoa. Sio kwamba mimi nilikuwa mwema sana, au mama yenu! Kupo kuvumiliana. Tena sana. Na kubebana pale unapoona mwenzio hataweza kufika. Niwatie moyo na kuwasisitiza kushika kwa makini sana ulicho nacho mkononi. Ni cha thamani sana kuliko kule macho yako yanapokupeleka na kukushawishi. Rekebisha, upgrade ulicho nacho. Utaona ule utulivu wake.” Mzee Saduki akamaliza, kila mtu akasimama kwenda kumpa mkono. Mc akatangaza ndio uwe muda wa zawadi kabisa.

Malon na Naya wakarudi kule walipokuwa wamesimama. Safari hii wakatafuta sehemu ya kukaa. Wakatulia kila mmoja akitafakari lake. Sherehe ziliendelea, wao wametulia tu. Naya akamgusa. “Naona sisi tuondoke. Huko kunakoendelea, kutawachosha kina baba ambao hawanywi pombe.” Malon akacheka. “Na kweli. Niliwasahau wao. Nimezungukwa na walevi, mpaka nimesahau kama kuna watu huwa hawanywi pombe.” Naya akacheka, nakusimama. Malon akatoa simu kumtafuta Side. “Nipo nyuma yenu hapa.” Malon akageuka.

Side akamsogelea. “Najua imeshakuwa usiku, lakini naomba uwarudishe Dar.” “Hawalali?” Malon akasita kidogo. “Sidhani kama watakubali.” “Zungumza na Naya. Tunaweza kuwaweka hotelini, kesho mapema tu baada ya kifungua kinywa, nikawarudisha Dar.” “Ingekuwa wazo zuri.” “Subiri kwanza nizungumze na Naya.” Malon akaenda alipokuwepo Naya na wazazi wake. Akawapa hilo wazo. Wakaangaliana wote kwa zamu. “Itawasaidia kupumzika usiku wa leo. Kesho Side atawarudisha mapema tu. Lakini kama hamtaona ni sawa, anaweza kuwarudisha sasa hivi.” “Tafadhali baba. Maana tumeacha nyumba peke yake na mifugo, hatujajiandaa. Kijana huyo anayetusaidia niwakusimamia kweli na yeye halali hapo! Acha tu twende. Tutakuja wakati mwingine tukiwa tumejiandaa vizuri.” Akasihi mama Naya kwa heshima tu. “Sawa. Hamna shida.” Malon akaondoka kurudi kwa Side.

Naya akamfuata. Alimkuta amesimama na Side. “Naomba nibaki ili tuzungumze.” Naya aliongea akimtizama Malon. Malon akababaika kidogo, akatulia. “Unauhakika Naya?” “Ndiyo.” Malon akabaki akimtizama. “Lakini kama unaratiba zako, sitaki kukuingilia.” “Hapana Naya! Sina ratiba. Siku hizi muda mwingi nakuwepo tu nyumbani.” “Kwa hiyo nimuage baba?” “Nitashukuru Naya.” Naya akageuka kurudi walipokuwa wazazi wake. Akakuta na wenyewe wameshasimama, wanatoka. “Vipi?” Baba yake akamuuliza. Akamshika mkono akamvuta mpaka nje ya ukumbi, mama yake na wadogo zake wakawa wanakuja taratibu.

“Vipi mama?” “Sikupata muda na Malon, baba. Naomba nibaki ili tupate muda wa mazungumzo.” “Utarudi lini?” “Kesho tu. Sidhani kama nitakaa sana hapa. Malon alikuwa akifikiria tufufue ile biashara mapema. Ni kama ameingiwa na hofu ya mimi kurudi kufanya kazi kule kwa kina Ozi.” “Kwani wewe ulitaka kurudi?” “Nilikwambia nilikuwa nafanya kazi na Ozi, baba! Nilikuwa nimepanga naye mipango ya kufanya onyesho moja ili kumalizia zile nguo na kupata wateja wapya.” “Ulimwambia Malon?” Naya akanyamaza. Alipomuona ameinama, akajua hakumwambia. “Naomba kuwa mwangalifu Naya. Kujenga mahusiano ni ngumu kuliko kubomoa. Malon amehangaika sana na wewe, tena bila kuchoka. Usije kulisahau hilo.” Naya akanyamaza. Mama yake na kaka zake wakatoka. Side akasogeza gari. Naya akawaaga, wakaondoka.

Akabaki amesimama pale nje kama amepigwa na butwaa. Malon akamsogelea. “Umechoka?” “Lakini hatuwezi kuondoka mpaka tumalize.” Akajibu Naya kwa hekima. “Ni kweli. Kuna watu natakiwa niwalipe. Kama DJ ananidai nusu, na wengineo. Lakini naweza kukurudisha nyumbani ukalale, mimi nirudi kumalizia.” “Hamna sababu yakufanya hivyo. Kama sitazuia chochote, naweza kubaki tu.” “Hamna utakachozuia Naya! Nimekwambia nimebadilika kwa asilimia kubwa sana. Siwezi kufanya mambo ya ajabu.” Naya akatingisha kichwa kukubali. Wakarudi ndani. 

Naya & Malon tena.

B

aada ya kukamilisha kila kitu, na karibia watu wote waalikwa kuondoka pale ukumbini, Naya na Malon na wenyewe wakaondoka. “Nakushukuru kwa kubaki Naya.” Naya akamwangalia na kunyamaza. “Umechoka sana?” “Nina uchovu wa mambo mengi. Mitihani, leo, mawazo. Hata sielewi! Nahisi kuchoka kweli.” “Pole. Basi leo ulale, kesho ndio tuzungumze.” “Nimemuahidi baba kuwa kesho nitarudi nyumbani.” “Hamna shida. Hata jioni nitakurudisha.” Wakaingia nyumbani kwa Malon.

“Mimi naweza kulala kwenye kochi Malon.” “Huna sababu yakufanya hivyo. Au unaogopa naweza kukufanyia kitu kibaya?” “Hapana. Niliona umebadilika Malon.” Malon akakunja uso. “Kama ni kwa sababu ya asubuhi ulipokuwa hapa, ni kwa kuwa sikujua umesimama wapi Naya! Mara ya mwisho uliniambia unapata hata shida kunibusu! Sasa naanzia wapi tena? Ndio maana nikaona nikuache tu. Na ninakuahidi, sitakugusa hata tukilala wote. Tafadhali usilale kwenye kochi. Naamini mimi sio mchafu wa kushindwa hata kukubali miili yetu igusane!” “Hapana Malon.” Naya alishindwa hata kubisha.

     “Basi nenda kaoge, uje ulale. Sitakusumbua.” Naya hakuongeza neno. Akaingia chumbani kwa Malon tena, akavua nguo, akaelekea bafuni kuoga. Wakati anatoka, akamkuta Malon anasafisha meno. “Sijui kama bado mswaki wangu upo?” “Hakuna mwanamke mwingine aliyeingia kulala humu ndani Naya! Kwa hiyo vitu vyako viko vile vile.” “Sikumaanisha hivyo Malon!” “Wala usinielewe vibaya. Nimekwambia kwa nia nzuri tu.” Naya hakujibu. Akasogelea sinki, Malon akaingia bafuni kuoga, alipotoka, alimkuta Naya amekaa kitandani, kama anamsubiria.

“Vipi! Nilijua utakuwa umeshalala.” “Ndio maana umechelewa bafuni ili kunikwepa?” Naya akauliza na kuendelea. “Sikutaka kukunyima raha kwenye nyumba yako Malon. Nia yangu ni kukuomba radhi kwa yote niliyokutendea. Hasa maneno niliyokuwa nikikutamkia kwa hasira. Samahani sana. Natubu kutoka moyoni, naomba unisamehe. Sijui nini kiliniingia na kuniharibu akili yangu. Nika..” “Ozi.” Malon akaingilia na kumfanya Naya ashindwe kuendelea.

“Nakupa jibu ya nini kimeingilia kwenye akili yako, ni Ozi. Endelea.” Naya akatulia kwa muda, akainama kama anayefikiria. “Nakusikiliza Naya.” “Naona kwa swala la mahusiano kati yetu limeisha, naomba tuzungumzie kazi.” Naya akajifuta machozi, akajiweka sawa. Malon akakaa. “Najua na hili nimekosea, lakini itabidi nikwambie tu ukweli, ili kama tunaendelea, tuendelee ukiwa umejua ukweli nisiwe nimedanganya tena au kufanya jambo usilolijua. Na kama itashindikana, kuanzia kesho nianze kutafuta kazi ya kuniingizia pesa.” “Kwa kina Ozi?” Naya hakujibu hilo. Akatulia kidogo na kuendelea.

“Nilimpigia simu mzee Nyenzo, nikamuulizia mzigo uliobaki pale kiwandani na kama wanaendelea kuzalisha. Nilipopata jibu, nikamuomba Ozi, anisaidie kuandaa maonyesho mengine palepale Dar. Ili kumaliza zile nguo, nakupata wateja wengine.” “Kwamba uliamua kuendelea na Ozi, mimi uniache hata kwenye mambo ya biashara!?” Malon akashtuka sana. “Labda niulize hivi Naya. Nilipokupigia simu siku moja kabla ya mitihani yako kuanza, ukanikatalia kila kitu. Lakini mwisho nikakuomba tuwe wote kwenye biashara, ukakubali. Pale ulikuwa umeshamtafuta Ozi au bado?” Naya alishindwa kujibu, akabaki ameinama. Anajifuta machozi.

“Hilo swali nilazima ulijibu Naya. Lasivyo sit..” Malon akanyamaza. Naya akamwangalia. “Ulikuwa umekwisha muomba au ilikuwa bado? Kwamba ulinikubalia mimi, halafu ukaja baadaye kunigeuka?” Kimya. “Lazima unijibu Naya.” Naya akasimama, nakuanza kuvaa. Akakusanya vitu vyake kwenye moja ya begi dogo ambalo aliliacha hapo kwa Malon. Walikuwa wakitumia kwa kusafiria na Malon, kwenye safari zao ndogo ndogo. Akaingia bafuni kuosha uso, akatoka.

“Unakwenda wapi?” “Narudi nyumbani.” “Unajua sasa hivi ni saa 7 usiku?” “Nitakuwa sawa tu. Kwaheri Malon. Naomba unisamehe sana. Nisamehe najua nimekuumiza.” “Hapana Naya, ni umenigeuka.” Naya akanyamaza kidogo. “Naomba unisamehe. Ila nakuahidi sitarudia tena kufanya kazi na Ozi. Nitatafuta kitu kingine chakufanya.” Naya akatulia kidogo. “Baba alinifundisha kuwa, uaminifu hujengwa. Najua ni ngumu kuja kufanya kazi pamoja na tukaendelea vizuri kwa hapa tulipofikia. Nitatafuta kitu kingine chakufanya mpaka baadaye.” Naya akachukua mzigo wake, Malon akamvuta.

“Najua unapenda kukimbia kila kukiwa na tatizo. Lakini sio usiku huu ambao baba yako anajua upo kwangu. Lala hapo kitandani, asubuhi ndio uondoke. Mimi nitalala kwenye kochi.” Naya akarudi ndani, Malon akatoka nje. Kwa uchovu wa muda mrefu, alilala akiwa anajifuta machozi. 

Maji yamemwagika, nakushindwa kuzoleka.

Alikuja kuamka saa tano mchana. Malon hakuwepo pale ndani ila alikuwa ameacha kifungua kinywa mezani. Naya alikiangalia kile chakula. Akarudi kusafisha tu kinywa na uso. Akakusanya vitu vyake vyote. Kuanzia chooni, mpaka chumbani kwa Malon. Akaviweka kwenye mabegi na kuvifungia kwenye chumba ambacho Malon alikuwa hakitumii. Kwa kuwa alilala akiwa amevaa, hakubadilisha chochote, akatoka na na begi dogo tu. Mlinzi getini alimuuliza kama akamtafutie usafiri, lakini akakataa. Akatoka akitembea taratibu akielekea kituo cha mabasi.

Huku akitembea Naya alifikiria hili na lile bila kupata jibu. “Naya!” Akageuka, akaona gari ya Malon ambayo anaendesha Side. “Naya!” Side akarudia tena. Akampungia mkono. Alikuwa upande wa pili wa barabara. Side akamfanyia ishara kuwa amfuate. Akasubiri magari yapite, akavuka barabara. “Mbona upo barabarani peke yako?” Naya akainama alipokuwa amesimama dirishani kwa Side. Side akabaki akimwangalia. “Unakwenda wapi?” “Narudi nyumbani.” Naya akafuta machozi. “Umemuaga Malon?” Naya akatingisha kichwa kukataa, lakini akakumbuka. “Usiku nilimwambia asubuhi nikiamka nitarudi nyumbani. Sasa nilipoamka, sikumkuta.” “Yupo kazini. Ungemsubiri umuage.” “Haina maana tena Side. Acha tu niondoke.” “Basi nikurudishe.” “Labda unipeleke mpaka kituo cha mabasi. Lakini nataka kupata muda mrefu njiani ili kupanga mambo yangu.” “Sawa. Basi ingia kwenye gari.” Naya akapanda. 

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

     Side alifanya kazi na Malon kwa muda mrefu sana. Alimjua Malon. “Katika tafakari zako, naomba uongeze na hili.” Naya akamwangalia Side. “Mimi namfahamu Malon tokea mdogo tu. Ni mtoto wa hapa Moro. Amekuwa nikiwa namfahamu vizuri sana. Yeye na Chezo. Nimeshakuwa kijiweni na Malon kwa muda mrefu sana tu. Nikikwambia namfahamu Malon, sio kama bosi wangu, kama mdogo wangu. Namfahamu sana kuliko hata mama yake mzazi, kwa kuwa nilishakaa naye sana mtaani. Najua ongea yake, najua udhaifu wake, najua siri ya mafanikio yake. Namfahamu sana. Na ndio maana japokuwa ni mkorofi sana, kwangu anayo mipaka. Hata kama amekasirika vipi, akafanya fujo zake, lakini kwangu anayo mipaka ambayo hata iweje, hawezi kuvuka. Kila mtu anajua. Ndio maana ananiamini hata na hili gari na mambo mengine mengi ya undani sana.”  Side akaendelea.

 “Malon yupo makini sana kwenye mambo yake, pengine ndio siri ya mafanikio yake.” Side akaendelea, huku akiendesha kuelekea kituo cha mabasi. “Alipoacha shule, wazazi wake waliumia sana. Kwa kuwa ndugu zake wote walikuwa watoto waliotulia kasoro yeye tu Malon. Ilikuwa ni kama anatafuta kitu zaidi ya kile alichokuwa akipewa au alicho nacho. Mama yake alikuja mpaka pale kijiweni akiniomba nimsaidie kuzungumza na Mlaon, arudi shule amalize hata chuo kama mwenzake Chezo. Kwa kuwa namfahamu Malon, mimi nikazungumza sana na mama yake. Nilimueleza vile Malon alivyo na ndoto zake, nikamwambia kwa vile alivyo Malon, na alipofikia, sio mtoto wakumuweka tena chini nakumfundisha historia za kina Mandela, au sayansi za kina Newton.” Naya akacheka.

“Kweli. Nikazungumza sana na mama yake. Mama yake akaelewa, nakuanza kuwa karibu naye ili tu asimpoteze, lakini sio baba yake. Baba yake wamepatana na Malon miaka michache iliyopita, kwa kuwa yule Mzee alikuwa akipambana sana ili watoto wake wasome. Malon akawa kama mtoto muasi. Na tatizo la Malon, hajui kupunguza ukali wa maneno. Ndio kwa mara ya kwanza, naona kwako. Hapana ya Malon, ni hapana ya uwazi na huwa ana jinsi yake akiitamka, anahakikisha inamwingia mtu na anaelewa ili asimbughudhi tena. Na ndicho kilichomfarakanisha na baba yake.” Side akaendelea.

“Tokea mtoto, anajua anachokitaka. Mbaya zaidi, huwa anataka vitu vikubwa visivyoendana kabisa na uhalisia.” Naya kimya akisikiliza. “Wakati hana kitu, tupo tu kijiweni, alikuwa akituambia hivi, yeye atakuja kuwa mfanyabiashara mzuri sana. Atamiliki nyumba nzuri, na awe na magari mazuri. Tulikuwa tukimcheka kwa kuwa alikuwa ni Malon, mtoto wa mtu wa kawaida sana! Baba yake dereva tu tena gari za hospitali! Tunajua nyumba wanayoishi, tunayajua maisha yao. Rafiki yake Chezo ni kweli alizaliwa kwenye pesa, lakini sio Malon. Kwa hiyo tukawa tukimpuuza tu.” Naya akaendelea kusikiliza.

“Akaanza ujanja ujanja wa mtaani. Aibe hapa, auze hiki ilimradi tu. Wakati mwingine alikuwa anakamatwa na polisi, mimi naenda kumtoa polisi bila hata wazazi wake kujua. Ukorofi wake upo vilevile. Hajui kujishusha, hajui kushukuru. Unamtoa jela kwa pesa yako, ukifika mtaani ukimkorofisha, anakurushia ngumi. Lakini anao upande mwingine ambao, huwezi kutulia kama ukisikia yupo matatizoni. Siku moja akakamatwa na polisi, wakamuweka ndani. Ilikuwa kosa kubwa ambalo wangemfunga miaka mingi. Nikaenda kuzungumza na mapolisi, wakawa wanataka hongo kubwa. Nikamwambia Malon. Malon akaniambia hiyo pesa anayo. Akanielekeza sehemu anayoficha pesa zake. Kwamba niende, nikachukue hiyo pesa, nihonge, atolewe na kesi zake zote zifutwe. Sikuamini nilipoenda nikakuta hizo pesa. Kufipusha stori, alipotoka, akiwa ametulia, nikamuuliza kwa nini anaendelea kufanya anachokifanya wakati tayari anapesa nyingi hivyo! Maana tulikuwa naye kijiweni kama kawaida, kumbe mwenzetu anazo pesa!”

“Ndipo akaeleza kuwa, anayo malengo. Wakati mwingine alikuwa akipewa kazi na baba yake Chezo, wakati mwingine utundu wake mtaani. Mimi nikawa najua pesa anafanyia starehe, kumbe mwenzetu anatunza. Ndipo akanionyesha anapokuwa anaandika malengo yake. Nilimtizama Malo, nikajua atafika mbali. Na anakuwa ameshaona anapotaka kufika. Haya aliyonayo sasa hivi, aliyaona tokea yupo kijiweni. Alipoanza kufanikiwa, akaniweka mimi kuwa mtu wake wa karibu sana. Mimi sio dereva wa Malon kama wengi mnavyodhani. Nina kazi zake namfanyia. Lakini siku moja nilipokuwa namshauri aoe, ili aachane na mambo ya wanawake, akaniambia mkewe bado hajaja. Akija mkewe, wala sitamuuliza. Nitajua tu.” Side akacheka.

“Nikamuuliza mkeo yukoje? Maana Malon namfahamu kwa swala la wanawake. Ni kweli wapo wengi sana. Na ni kweli alikuwa mchafu zaidi ya utakavyoambiwa. Sasa nikawa namuuliza, ataoa mwanamke wa namna gani wakati wote anao? Nikamwambia si achague tu hapo mmoja, ahalalishe? Akasema katika wote alio nao, hayupo mkewe. Nikamwambia nitajie sifa za mkeo. Alipozitaja, nilicheka sana. Sana. Nikamwambia huo upande hawezi kuvuka. Hawezi kukubaliwa na mwanamke wa namna hiyo.” “Mwanamke wa aina gani?” Naya akauliza, Side akacheka.

“Sifa zote za Naya, alizozikuta kwake mwanzoni kabisa, ndizo sifa za mke wa Malon.” Naya akainama. “Nilijua hawezi kupata mwanamke wa namna hiyo kwa kuwa, Malon haendi kanisani. Labda kuwe na tukio kama vile jana. Sijawahi kumuona hata akisali. Kwa kifupi ni kijana asiyemcha Mungu wala hana mahusiano na Mungu, lakini alikuwa akitaka mwanamke mcha Mungu. Haya, akataka mwanamke aliyetulia. Awe wake peke yake. Malon hajatulia, wala hafiki sehemu tulivu za wanawake waliotulia. Nikamwambia mwanamke aliyetulia utampata wapi? Tena awe wake peke yake!? Kwa kuwa navijua viwanja anavyofika Malon, hawezi kupata mke wa peke yake. Najua wanawake wanaomzunguka. Wala hatongozi, anatongozwa kwa vile alivyo sasa. Nilimcheka sana tu, lakini yeye akaniambia huyo mwanamke yupo.”

 “Chezo akaja kumwambia aina hiyo ya mwanamke, hawezi kumudu tabia zake. Kuna kitu Malon akajibu, kikanifanya nifikirie. Akamjibu hivi Chezo, ndio maana anatafuta mwanamke mcha Mungu ambaye anajua atamuombea mchana na usiku. Ndio maana anatafuta mwanamke wake peke yake ambaye atamuonyesha mapenzi ya ukweli. Yeye tu. Ambaye penzi pekee ndilo litamfanya avumilie. Mwanamke ambaye atamsitiri, siku ya aibu yake. Yale aliyosema baba yake jana kwenye sherehe yao, ndio usia wa yule Mzee kwa kila kijana. Anabadili maneno tu. Kila mtu aliyeishi hapa Morogoro kwenye haya maeneo yetu, anamfahamu baba yake Malon, mzee Saduki. Ni mzee aliyeshiba busara na hekima. Mtulivu mno. Mtu wa maadili kuliko hata mama yao. Kwa hiyo Malon, alijua atapata mwanamke kama wewe.” “Nimemuumiza sana Malon. Hatuwezi kuja kuendelea tena. Ndio basi.” Naya aliongea huku akilia.

“Pengine ni kwa muda tu. Tena ni kwa kuwa hamjajua tatizo lenu lilipo. Wote wawili mlidhani itakuwa rahisi tu. Wakati Malon anafikiria mke kama wewe, hakuhesabu gharama na hakuangalia mapito mtakayopita mpaka kufikia alichokuwa anataka. Na wewe hivyo hivyo. Uliingia kwenye mahusiano na Malon ukiwa mtoto. Tena mtoto haswa. Ulikuwa na picha fulani ya mahusiano ambayo ni ngumu kupata na kutunza.” Naya akabaki akifikiria ni nini alibakisha kumfanyia Malon ili atulie. “Ulimkubali Malon ukimjua, lakini ukashindwa kuhesabu garama ya kumtunza na kumfanya awe wako.” “Nimefanya kila kitu Chezo. Malon hatulii!” “Ulifikiri mtu kama Malon anatulizwa na mapenzi ya kitandani peke yake?”  Naya akainama.

“Wewe unajua wanawake wangapi ashakwisha kulala nao Malon?” “Wengi.” Naya akajibu kwa upole. “Na niwazuri haswa. Unao onyeshwa sasa hivi, ni kwaajili yakutaka kuumizwa tu. Mimi nawafahamu wanawake waliokwisha lala na Malon. Usijisikie vibaya, lakini nikikuonyesha, wewe mwenyewe unaweza kushangaa ni kwa nini anakung’ang’ania wewe. Na kwa nini anakwenda huko kwao, nakurudi kwako!”  Side akacheka.

“Malon anakupenda bwana! Malon sio mtu wakubembeleza au kuongea na mtu kwa unyenyekevu kama hivyo! Mimi na Chezo hatuamini kama ni Malon! Najiuliza amejifunza wapi, na anawezaje kuwa kondoo, wakati ni chui pori! Malon hajui kunyenyekea Naya! Hajui kubembeleza hata mama yake mzazi! Mkorofi wakupindukia. Anajulikana kwa ukatili. Katili la kuua. Anayo roho yake ya tofauti, lakini sio kwako na wenzake ndio wamegundua huo udhaifu na ndio wanautumia kumuumiza.” Naya akakunja uso huku ameinama.

Walishafika kituo cha mabasi, Side akawa ameegesha tu gari wakizungumza. Simu ya Side ikaanza kuita. “Malon huyu.” Side akapokea. “Uko wapi?” Naya akamsikia Malon akiuliza. “Stendi ya mabasi. Namshusha Naya. Nilimkuta njiani, nikampa lifti.” Kimya. “Unanitaka nirudi sasa hivi?” “Kwa nini humpeleki mpaka nyumbani kwao?” “Amekataa. Anataka kupanda basi.” Kimya. “Unanihitaji?” “Ukimalizana naye, nipigie.” “Sawa.” Malon akakata simu.

Naya akabaki ameinama. Wakatulia kwa muda. “Nakushukuru Side. Uwe na wakati mzuri. Naamini Malon atampata mwanamke mwingine mwenye sifa nzuri zaidi. Naomba ukiwa na safari ya Dar, na kama huna mizigo mingi kwenye gari, nichukulie vitu vyangu nimefungia kwenye kile chumba cha mwisho, karibu na jikoni.” “Sawa.” Naya akashuka garini.


CONVERSATION

0 Comments:

Post a Comment