huko kwa Malon!
Malon alirudi Morogoro, moja kwa moja kituo cha polisi. Hata
polisi wenyewe hawakuamini walipomuona Malon anaingia kituoni. Kila mtu
aliyemkuta pale kituoni alinyamaza wakimtizama Malon aliyekuwa akifahamika kama
chumvi kwenye mji huo mdogo wa Morogoro. Polisi walibaki na butwaa, kwani
habari za kutafutwa Malon, zilizagaa kila mahali. Inamaana hakusikia kama
anatafutwa au!? Ndio swali lililopita kwenye kichwa cha kila mmoja wao pale
kituoni.
“Nimepata taarifa kuwa natafutwa, na dereva aliyekuwa akiendesha
gari yangu amekamatwa.” Malon alianza hivyo. “Una makosa mengi sana, Malon.”
Mmoja wa askari akadakia. “Basi, kwa kuwa ni mimi ndiye ninayetafutwa, nimekuja
kujibu shutuma zangu,
naomba mumuachie Side. Hausiki na chochote kile. Gari ni
yangu, na mimi ndiye huwa ninamtuma sehemu mbali mbali kwa kutumia gari yangu.”
“Kwa hiyo unakubali kosa?” Mmoja wao akauliza. “Kosa gani?” Malon akauliza na yeye.
“Shutuma zako.” “Zipi?” Malon akauliza tena, kwa utulivu tu.
“Maana ninachozungumza hapa ni kile alichokamatiwa Side. Nadhani hamkuwa na
tatizo na Side, ila mimi. Mmemkamata Side, kwa kuwa alikuwa kwenye gari yangu.
Sasa ndio nasisitiza kuwa, Side ni mjumbe tu. Mimi ndiye mtumaji. Nipo hapa
kuchukua nafasi yangu na shutuma zozote. Naomba mumtoe Side.” Malon akashangaa
hakuna hata kipingamizi, wala hakutakiwa alipe pesa yeyote ile kumdhamini Side.
Kama waliookota alumasi, wakamfunga pingu yeye, wakamtoa Side. Malon akawekwa
jela.
Kwa kushindwa kusomewa shitaka hata moja, Malon akajua hawajamkamata Side na mzigo wa bangi. Na kwa kuwa walikataliwa kuzungumza, Side akaondoka huku akimwambia Malon atarudi tena hapo kituoni kesho yake, Malon akaingizwa lupango, akiwa ametulia tu. Ila anafikiria kilio cha Naya. Hakujua ni wangapi wapo nyuma ya huo mpango. Hajua watafanya nini na yeye, kwa kuwa alijua nia yao ni kumkomoa, sasa watakwenda umbali gani kumkomoa! Watamuweka hapo mpaka lini na kwa shutuma gani? Malon akaona atulie kwanza. Maombi yake ni kuwa Naya, aelewe, asirudi Morogoro.
Kwa Naya!
Agonga Mwamba hata kwa wazazi wake Malon.
A |
lisubri simu
ya Malon usiku kucha. Na kwa bahati mbaya, Side naye akawa hapatikaniki kwa
simu. Alfajiri, akaamkia chumbani kwa baba yake. “Naenda Morogoro.” “Naomba
utulie Naya.” “Siwezi baba. Labda unipeleke. Kama hutaweza, mimi nakwenda
mwenyewe. Siwezi kumuacha Malon peke yake.” “Sasa umeshajua alipo?” “Siwapati
kwa simu! Na sina namba za wazazi wake. Naona niende tu kwao.” Ikabidi baba
yake ajiandae, waondoke na Naya.
Walifika Morogoro mida ya saa 4 asubuhi. Moja kwa moja mpaka kwa
wazazi wake Malon. Waliwakuta wametulia kama hakuna kinachoendelea. Kwanza
wakawashangaa wao. “Swala la Malon kuwa jela, ni kama mtu kwenda kanisani au
msikitini.” Aliongea baba yake nakumshangaza Naya. “Nani atamtoa sasa!?” Naya
akauliza kwa kushangaa. “Wavuta bangi wenzake wa huko huko mtaani.” “Safari hii
ni tofauti Mzee Saduki. Marafiki zake Malon wamemgeuka.” Naya akajaribu
kutetea.
“Mama wewe ni mgeni kwa Malon. Sisi tunamjua huyo, tokea analetwa hapa
duniani. Na mama yake alishamkalisha kwenye kochi hilo alilokaa baba yako.
Akamuonya mtindo wa kutembea hovyo na wanawake za wenzake. Tena akamwambia wazi
kabisa, hakuna vita mbaya, kama ya mapenzi. Huwa vita vyake haviishi kwa mshale
wala bunduki. Kama kawaida ya Malon, hakuna aliyemsikiliza. Akatoka pale
mlangoni, bila kujibu wala kuruhusiwa. Kila leo yupo jela! Kwa makosa
yanayopishana majina tu. Mama yake ambaye angalau huwa anamsikiliza,
ashazungumza na Malon, zaidi ya umri wako wewe Naya mwanangu. Akimsihi abadili
maisha yake. Pale alipo hana shule, hana chochote. Kwa mara ya kwanza tokea
azaliwe, wewe ndio kitu cha maana tulichokiona anacho huyo Malon, mbali na
magari pamoja na hizo nyumba mbili alizo nazo.” Yule baba akaendelea.
“Tuliposikia amepata msichana, akatulia hapa kati, tukamwita hapa,
tukampongeza. Mama yake akamsihi kama ampigie magoti vile! Akamuomba atulie
sasa. Aoe. Akasema Naya anasoma, akimaliza chuo ndipo mtaoana. Hee! Hatujakaa
sawa, tunasikia na wewe umemuacha, sababu ya umalaya. Mama yake akamwita hapa
siku moja kabla ya ile sherehe yetu. Maana mama yake ndiye mtu ambaye angalau
akimwambia kaa chini, anakaa. Mimi hanisikii kabisa yule mtoto, kama hana
masikio! Akaja dada yake, shemeji yake, mimi na mama yake. Tukamkalisha kikao
hapahapa. Hakuna ambalo tulimbakisha Malon. Tulizungumza naye kwa undani, kwa
wazi, mpaka mama yake akalia. Mama yake akamuomba abadili maisha anayoishi.
Tukazungumza naye hapa, akaondoka. Akaendelea na maisha yake yaleyale. Mtoto
kama huyo, unamfanyaje? Unamtoa jela ili aje aishi huku mtaani aendelee
kuchafua watu?” Baba yake akauliza. Naya kimya.
“Baba Naya!” Mzee Saduki akamgeukia baba yake Naya. “Mimi nina
mabinti watatu kama Naya. Nazungumza na wewe kama mzazi mwenzangu. Malon sio
mwanaume wa kuoa, wala kutulia. Umesomesha binti yako, shukuru Mungu, muweke
mbali na Malon. Malon ni mtoto wangu nimemzaa. Damu yangu kabisa, lakini
ninachokwambia, sio kijana wakuoa. Vilio kama hivyo vya mwanao hapa Morogoro,
vimetapakaa mji mzima. Malon analiza watoto wa watu, ni hivyo Mungu ametusaidia
kuwa ni yeye peke yake ndio kondoo aliyepotea. Ndugu zake wanamaadili. Hakuna
mtoto wa kike asiyemjua na kulizwa na Malon hapa Morogoro. Huu ni ushauri wangu
tu. Uuchukue au uukatae, itakuwa juu yako, na hakika mtanikumbuka.” Baba yake
Naya kimya akisikiliza, Naya akilia.
“Mchukue huyo binti yako, sasa hivi, panda basi, rudi Dar.
Achaneni na Malon. Mimi ni baba yake, najua ni nini ninachozungumza. ACHANENI
NA MALON. Hakuna jela inayoweza kumfunga, hakuna nyumba inayoweza kumuweka, na
hapajawahi kutokea mwanamke aliyewahi kumtuliza Malon. Sasa kabla binti yako hajaharibikiwa,
kimbia. Nikisema kimbia, namaanisha kimbia, na mfunge milango, msuruhusu
majanga ya Malon nyumbani kwenu. Maana Malon, hana janga moja. Ni hayo tu.”
Akamgeukia Naya. “Naya, nakuhusia binti
yangu, achana na Malon. Nimesikia sifa zako, nitaumia sana, kuja kusikia na
wewe umeingia kwenye mkumbo wa wanaolizwa na Malon. Kimbia mama. Ndio itakuwa
salama yako.” Yule mzee akamaliza. Naya na baba yake wakaondoka.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
Na kweli, baba yake Naya alihakikisha wanapanda basi kurudi Dar.
Naya alikuwa akilia sana. Baada ya muda, akapitiwa na usingizi. Alimuamsha basi
liliposimama Kiluvya. Naya alimka na kuanza kulia tena. “Nampenda
Malon, baba.” Naya aliongea huku wakitembea kurudi nyumbani. “Na Malon
alikubali kubadili maisha.” “Unajuaje Naya?” “Mimi nimezungumza na Malon,
najua. Huwa hawezi kunidanganya Malon. Ni heri nimkasirikie kwa kuniambia
ukweli, hata tugombane, kuliko kunidanganya. Malon hajui kunidanganya. Sipingi
chochote alichosema baba yake, lakini Malon alifika kwenye kubadilika. Siwezi
kumkatia tamaa.”
“Basi msubiri, atoke jela uone.” “Hawawezi kumtoa jela.
Marafiki zake watamwacha aozee jela. Wanamlipiza kisasi. Na kama ulivyoona
wazazi wake, wameshamchoka.” “Basi tumpe muda tuone. Tukiona kimya, tutajua
chakufanya.” Wakawa wameshafika nyumbani. Naya akaingia chumbani kwake. Alimsikia baba yake akimuelezea mama yake kila
kitu. Akasikia mama yake akiguna. Akajua na pale kwao hatapata msaada kwa
Malon.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
Akamtafuta tena Side, simu yake ikaita bila kupokelewa. Akapiga
tena na tena, kimya. Akaona amtafute Chezo. Chezo akapokea. “Hivi unajua
alipo Malon?” “Unakumbuka ule ushauri wangu wa kucheza kadi zako kwa akili,
ukishazipanga, ukaona zimekaa sawa, chukua chako mapema, kisha ondoka?” Naya kimya. “Basi sasa hivi
ndio muda wakuchukua chako Naya. Malon amefungwa, hatakaa atoke. Jamaa wanahasira
naye, na polisi hivyo hivyo. Alikuwa akitafutwa muda mrefu sana, lakini polisi
wakawa hawajapata ushirikiano wa raia. Sasa, sasa hivi, rafiki zetu wa karibu
kabisa, ndio wanashirikiana na polisi. Polisi wameambiwa habari zote za Malon.
Kwa undani na nje. Tena na wafanyakazi wa Malon ndio wamemuharibia zaidi kwa
kumlipa Malon, sababu ya ukorofi wake. Kila kitu cha Malon, kitachukuliwa. Sasa
ndio nashauri, chukua chako mapemaaaa. Kusanya kila kitu, tunza, kabla kiberiti
hakijawashwa.” “Wewe unajua walipomfunga?” Naya akendelea kuuliza.
“Ninachokwambia ni hivi, Malon sio
wakutoka leo wala kesho.” “Hilo nimelielewa Chezo. Nataka kujua alipofungwa,
basi.” “Nakuonya Naya. Kaa mbali na Malon. Huo ni moto umeshawashwa, usikubali
ukakuteketeza na wewe.” “Malon yuko wapi?” Naya akaendelea kuuliza. “Amefichwa, ili
asije kutoroka, au kutoroshwa.” “Inamaana wewe hufahamu alipo?” “Sifahamu.” Akajibu Chezo,
lakini Naya akajua anamdanganya.
“Unajua alipo Side?” “Ni wewe peke yako umegoma kuelewa Naya.
Nakwambia sasa hivi kila mtu anachukua chake mapema, anaondoka. Hakuna
anayetaka kufa na Malon. Futi alishaondoka na ile gari ingine na pesa za Malon.
Tokea jana hayupo mjini, na amekataa kuwaambia watu ni wapi anakwenda. Side
naye ameniaga kuwa anahamisha familia yake hapa Moro. Mkewe mjamzito, na ana mtoto
mdogo. Malon hana chakupoteza, lakini anasema yeye anavyo vyakupoteza. Akienda
jela, nani atalea wanae na mkewe! Hivi tunavyozungumza, na yeye anakwenda
kuweka mambo yake sawa polisi, anaondoka. Amesema hataki kuondoka halafu polisi
wakamfuata nyuma. Anakwenda kutoa ushahidi wake, aagane vizuri na polisi,
aondoke, akaanze maisha sehemu nyingine, mbali kabisa na Moro.” Chezo akaendelea.
“Na ujue kabisa, Side sio wakumchoka Malon. Ashamtoa Malon jela
zaidi ya nitakavyokwambia, lakini na yeye amefika mwisho. Anaona ataishia
pabaya. Sasa na wewe nakuonya. Mwenzio Side anajishindia lile gari la Malon.
Kasema ndio analoondoka nalo. Sasa na wewe wahi chako. Changamka, usizubae.” Chezo
akakata simu.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
Tumbo la Naya likaanza kuuma kwa mshtuko baada yakusikia kuwa
mpaka Side anamkimbia Malon! Hakuamini. Akaumia sana, na kumuhurumia Malon.
Kwamba amebaki peke yake. Swali likawa, amefichwa wapi? Ndio ukawa mtihani.
Mtoto huyo aliyeamua kuyavulia maji nguo akatoka tena. “Mimi kesho
narudi Morogoro kumtafuta Malon.” Naya akawafuata wazazi wake. “Huwezi kufanya
hivyo Naya. Huyo kijana ataku…” “Naomba mama usiungane na watu wengine kuwa
kinyume na Malon wakati wewe mwenyewe ulisema alinisaidia sana. Mimi kesho
naenda. Naomba baba unisindikize. Lasivyo mimi nakwenda mwenyewe. Wakinikamata
na kuniua, basi. Lakini mjue niliwaaga.” “Sasa Naya mwanangu, na kazi za hapa?”
“Basi wewe baki. Lakini mjue mimi kesho asubuhi, nitarudi Morogoro kwa Malon.”
Naya akaingia chumbani kwake nakuanza kulia.
Bale akatoka chumbani. “Huyo, ni heri umpeleke tu baba. Akili
imeshachanganyikiwa. Mimi nitaamka asubuhi, nisadie kukamua maziwa,
nitayapeleka hayo maziwa huko hotelini na mayai wakati nakwenda shuleni.
Nitazungumza nao, niwaombe tuwe tunawapelekea mara moja kwa siku, ila idadi ile
ile. Niwe nawapelekea kila siku asubuhi kabla ya kwenda shule au wakitaka iwe
jioni baada ya kutoka shule. Mchana mama akirudi, na kama wewe baba utakuwa
hujarudi, mama asimamie ukamuliwaji. Ili maziwa yasishuke. Tutayaweka kwenye
friji, tutachanganya na ya asubuhi, kisha niwe napeleka hiyo asubuhi. Siku
ambazo mimi siendi shule, nitakuwa nikimsindikiza mimi mwenyewe huko Morogoro mpaka
akili yake itulie. Lasivyo atagongwa na gari, tuanze matatizo mengine bure.”
Wakakubaliana na Bale. Kwa mara ya kwanza, Bale akawa upande wa Naya.
W |
alifika
Morogoro mapema ya siku inayofuata, jumatano. Moja kwa moja mpaka kituo kikubwa
cha polisi Morogoro. Naya na baba yake wakajitambulisha kwa majina tu.
“Tunataka kumuwekea dhamana Malon Saduki. Alikuja hapa kituoni siku ya
jumatatu. Dereva wake alikamatwa na gari yake, ndio akaja yeye mwenyewe.
Mkamuweka ndani.” “Hiki ni kituo cha polisi dada, sio jela. Kama alikuwepo hapa
tokea jumatatu, basi ujue hawezi akawa bado yupo hapa. Atakuwa rumande
akisubiria kesi yake itajwe.” “Wapi?” “Wewe unauliza kama nani?” Kimya.
“Ni mume wako?” Polisi akamuuliza Naya lakini Naya alijua wazi
wanamjua ila ni kumkejeli tu. “Hapana.” Naya akajibu. “Mwanasheria wake?”
“Hapana.” “Ni ndugu?” Akaendelea kumuhoji
kwa makusudi ili kumkatisha tamaa. Baba yake kimya, ametulia kwenye benchi
anamsubiria binti yake. “Sasa kama wewe sio ndugu, wala mke, au mwanasheria,
hatuwezi kukwambia kwa sababu za kiusalama.” Naya akajua ni kweli kisheria
hawawezi, ila pia wamekusudia kumbania Malon. Akaondoka na baba yake.
“Sasa hivi tunakwenda wapi tena mama?” Baba yake akamuuliza Naya
kwa upole tu. “Turudi nyumbani wakati natafuta mwanasheria.” “Sawa.” Wakiwa
njiani kurudi nyumani akajaribu kumpigia simu tena Side, simu ikawa imefungwa.
“Side amefanya vibaya sana. Anamtoroka Malon, wakati Malon ndio alikwenda
kujisalimisha ili akamatwe yeye, halafu Side atoke!” Baba yake alimsikia akilalamika wakati
anaendelea kurudia kupiga simu ya Side bila mafanikio. Akamuona ametulia.
Akajua anafikiria.
Joshi.
Akatoa tena simu mfukoni. “Nina shida sana, naomba nisaidie.” “Ni
Naya?” “Ndiyo, Joshi. Mimi Naya.” “Kwema?” Baba yake akaendelea kusikiliza tu. “Si uliniambia
unafanya kazi kwenye ofisi za wanasheria?” “Ndiyo. Lakini kama muhasibu.”
“Naomba unisaidie kunikutanisha na mwanasheria unayemwamini, anisaidie. Nina
shida sana.” Kimya. “Joshi?” Naya akaita. “Nafikiria Naya. Hawa wa hapa, wanashugulikia kesi
nyingi za kibiashara, yaani wanashugulikia kesi za biashara, makampuni makubwa
na kadhalika. Halafu wanagarama sana. Bei zao zipo juu.” “Ninachotaka ni
mwanasheria mzuri. Pesa sio tatizo.” Baba yake akamgeukia kama
anayemshangaa.
“Tafadhali Joshi. Nisaidie ndugu yangu. Wewe nikutanishe na mmoja
unayemfahamu ni mzuri na mwepesi. Mambo mengine niachie mimi mwenyewe.” “Sawa.
Nitakupa jibu jioni. Maana mida hii wengi wanakuwa wanatoka. Na ninayemfikiria
hapa, hayupo.” “Nasubiria basi simu yako.” Wakaagana.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
“Nimesikia mazungumzo yako mama. Umesema pesa sio tatizo. Unapata
wapi pesa?” “Mimi na Malon, tulifungua akaunti yetu ya biashara. Ndiyo akaunti
inayoendesha kile kiwanda. Ameniweka na mimi kama muweka saini. Kuwa na mimi
naweza kutoa pesa. Hata zile pesa zote za maonyesho ya mavazi, japokuwa
tuligombana na Malon, nikamuachia yeye pesa yote, lakini aliniambia aliiweka
huko. Nitakwenda kuangalia.” “Sasa kama wamemkamata, si wanaweza wakawa
wameshikilia akaunti zake zote?” “Inawezekana. Lakini hii tulifungua kwa majina
yetu, au tuseme ya ile kampuni yetu. Mpaka wajue na waishikilie, itachukua
muda.” Baba yake akamtizama.
“Naomba tupitilize mpaka benki, nikatoe pesa yote nihamishie
kwenye akaunti yangu kabla hawajaifikia hiyo akaunti.” “Mimi nina swali mama.
Na uwe makini unaponijibu.” Naya akamwangalia baba yake huku basi likipita Kiluvya
kituoni ambapo walitakiwa kushuka. “Ni kweli umekusudia kutumia pesa ya
biashara kumtoa Malon ambaye huna uhakika wa nini atafanya tena kesho? Huoni
kwamba huo ndio utakuwa mchezo. Unamtoa jela, mnafanya biashara, anakamatwa,
unaenda tena kumtoa jela na pesa yote ya biashara!? Mtajijenga saa ngapi?” Naya
akanyamaza. “Baba yake mwenyewe anasema Malon ni mtu wa kukamatwa kamatwa. Kweli
mama yangu mzazi, umeamua maisha yako yaishie kwa Malon!?” Naya akafikiria
kidogo.
“Nampenda Malon, baba. Hata nikiwa na mamilioni ya pesa bila
Malon, sitafurahia. Hujui ni kiasi gani Malon anavyonipenda na kuniheshimu.
Kila mtu analijua hilo. Malon ni mkorofi sana na anamatatizo yake mengi tu.
Mimi namjua. Lakini kwangu ni tofauti baba yangu. Sitakuja kupata mwanaume
anayenipenda na kunithamini kama Malon. Nimejaribu kanisani. Wewe ni shahidi.
Lakini angalia Malon alivyokuwa akiwapenda na kuwathamini pale nyumbani kuliko
hata Ino! Malon alikuwa akinifikiria mimi na familia yangu kwanza. Wewe
unafikiri kwa nini japokuwa Bale ni mkorofi kwangu, lakini anampenda sana
Malon?” Kimya.
“Kwa kuwa Malon ameonyesha kunipenda na kujali hata ndugu zangu!
Zawadi alizokuwa akinisaidia kuwanunulia kina Bale wakati tupo safarini ni za
mapesa mengi mno.” “Hilo nililihisi.” “Sasa unafikiri ni kwa nini alikuwa
anatumia pesa yote hiyo? Au kila nilipokuwa nikimpa wazo, hakuna jinsi Malon
akapinga. Ilimradi nimeongea mimi, Malon atafanya bila shida, ananisikiliza na
kunithamini kuliko nitakavyokwambia. Nyumba ya Kunduchi sijui ameandika majina
gani, lakini mimi amenipa funguo mpaka leo ninazo. Aliniambia niishi pale muda
na wakati wowote ninaotaka, hata kama yeye hatakuwepo, au nikiwa nimemkasirikia
niende tu pale na walinzi wote wananijua. Nimeishi naye pale kidato cha 5 na 6, akinitumikia kama nini sijui.” Naya
aliropoka, Baba yake akashtuka sana.
“Lakini si nilifaulu?” Naya akajitetea. “Mimi nilijua unaishi
hosteli kama ulivyokuwa ukiniambia Naya!” Naya akainama. “Nampenda Malon, baba.
Sitapata mwanaume anayenipenda nakunijali kama yeye. Nisaidie nimtoe jela,
mengine nitahangaika naye mwenyewe.” Naya akatulia kidogo. “Hakuna kitu nataka
kwa Malon asinipe baba. Hakuna wazo nitampa, asinipongeze. Wamemfunga nikiwa
nimempa wazo la biashara, akalifurahia na kunipongeza. Tulikuwa tunaweka
mikakati yakufanya pamoja hiyo biashara. Niambie baba yangu, napata wapi
mwanaume wa namna hiyo? Hata kama napata pesa yakuwa namtoa yeye tu jela,
sitajali. Ilimradi awe anarudi kwangu.” Baba yake akamtizama, Naya akainama.
“Usiwe na wasiwasi, atanioa.” “Naya, mama yangu wewe!” “Nitaolewa
na Malon, baba. Hivyo hivyo alivyo, atanioa. Na kama ukitaka kuniona ninafuraha
wakati wote, basi uniombee Malon anioe. Ndio nitakuwa na furaha. Nampenda
Malon.” Baba yake akamtizama tena na kunyamaza.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
Naya na baba yake walifika benki. Naya akahamisha ile pesa yote
kwenye akaunti yake, baba yake akimwangalia tu. Alifanya mambo akiwa ametulia
kama aliyekuwa na mipango ya muda mrefu. Alipomaliza, akamuona anatoa simu
wakiwa palepale benki. Akampigia tena Joshi. “Nipo hapa posta mpya na baba
yangu. Tunaweza kuja hapo ofisini kwenu tukasubiria.” “Sijazungumza na yeyote
yule bado, Naya! Labda ungesubiri.” “Naomba tuje tusubirie hapo. Tafadhali Joshi.”
“Sawa. Karibuni.” Ilishakuwa mchana, Naya hazungumzii chakula, bado akili ipo na
mipango ya kumtoa jela Malon.
“Hudhani kama tunahitaji kutulia kidogo, Naya! Mpe muda huyo mtu.
Akiwa tayari atakutafuta.” “Kwamba nikatulie, wakati sijui walipomuweka Malon!
Sijui wanamfanya nini sasa hivi! Sijui anahali gani! Malon anachukiwa baba.
Pale Morogoro kwa sasa hana rafiki hata mmoja. Malon alikuwa akitafutwa na
polisi. Hakuna atakapoangukia, akawa salama. Lazima nimtoe Malon popote alipo,
kwa garama yeyote, tena kwa haraka. Mimi sitaki kutulia, baba.” Naya akaanza
kulia.
“Mimi naweza kufikiria ukiwa na mimi. Naomba usiniache peke yangu.” “Haya twende. Lakini tupitie hata soda, mama. Njaa inauma.” Naya akajifuta machozi, nakuanza kucheka. “Twende nikupeleke ukale, halafu twende tukatafute msaada wa mwanasheria.” Wakatoka pale maeneo ya benki.
Msaada wa Mwanasheria.
N |
aya na baba
yake walifika kwenye ofisi za mwanasheria baada ya kula. Wakapata bahati
yakumpata mwanasheria aliyekubali kuwasikiliza. “Ninachotaka unisaidie, ni ujue
yuko wapi. Na aweze kuwekewa udhamini, atoke.” “Kwa hiyo kama nimekuelewa
vizuri ni kuwa, hajakamatwa na bangi?” “Hapana. Hata gari yake haikukutwa na
bangi.” “Sasa kwa nini walimkamata?”
“Ndio nakwambia wanamtafutia sababu yakumlipiza kisasi. Ukimpata, yeye wenyewe
atakueleza ili ujue ni jinsi gani yakumsaidia.” Yule mwanasheria akafikiria.
“Unayo pesa yakunitoa Dar kwenda Morogoro?” “Ndiyo.” Yule kaka
akamtizama Naya. “Umesikia swali langu lakini?” “Umeuliza kama ninayo pesa.”
“Ndiyo. Maana mimi sitakufanyia kazi ya kubabaisha. Tutampata. Lakini
inahitajika pesa ya kulipa watu ili kutoa siri kujua alipo, kama polisi
wakishindwa kutusaidia. Halafu najua kwa kuwa hawataki kumtoa, wataweka pesa
nyingi yakumdhamini. Sasa sitaki wote tuonekane wababaishaji. Tunaanza jambo,
halafu tunafika katikati tunakwamwishwa na pesa.” “Kwani unafikiria kiasi
gani?” “Nyingi. Tunaanza na pesa zangu mimi za usafiri, na mfukoni wakati
nashugulikia kujua ukweli wa nini kinachoendelea. Pesa ya kuweka sawa watu
wakuniambia ukweli. Ndani ya polisi, nakuweza kumtoa.” “Hamna shida. Nitajie ni
kiasi gani.” Baba yake alibaki akimshangaa Naya.
Harakati za kumtoa Malon Rumande wakati raia wamekusudia kumtoa mtaani.
B |
aada ya
kukabidhiwa pesa aliyomtajia Naya, akaanza kazi. Ni kweli ilikuwa ikimgharimu
Naya kila siku zilivyozidi kwenda. Na Mati, huyo mwanasheria alikuwa akimpa
taarifa ya kila alipofikia. Ni kweli alikuwa anakutana na ugumu mkubwa. Baada
ya kuhangaika sana, akaweza kujua alipo Malon. Alikuwa amefungwa, na kunyimwa
haki ya kuonwa na yeyote wakati bado hakuwa amehukumiwa. Yule mwanasheria
akaanza kupambana na hilo. Akidai haki ya Malon yakuonana na mwanasheria wake.
Baada ya kupeleka barua hii, kuhangaika vile, ndipo akaruhusiwa.
“Jamaa yako anaonekana anamaadui kila mahali! Mpaka hakimu hamtaki
mtaani!” Mati alimwambia Naya, jioni hiyo akiwa anaelekea kumuona Malon.
Mwezi ulikuwa umeshapita. “Naomba msalimie sana. Mwambie nampenda.” Mati
akachekaa. “Atasikia.” “Nipigie ukiwa naye au ukitoka.” Wakaagana.
Mati alifanikiwa kukutanishwa na Malon. Akamwambia ametumwa na
Naya, ili kumsaidia. Anataka amueleze ukweli bila kuficha kitu. Ndipo Malon ikabidi
kueleza ukweli wote bila kuficha. “Kama nimekusikiliza na kukuelewa vizuri. Ni
kwamba, kwa upande wa hiyo biashara ya bangi, hujawahi kukamatwa hata mara
moja?” “Hata mara moja ila tu kuhisiwa. Hapajawahi kuwa na ushahidi.” “Kuhisiwa
na wafanyakazi wako wamekiri kituo cha polisi, Malon. Wapo mashahidi wawili.
Waliosema wamekufanyia hiyo biashara.” Malon akashtuka sana.
“Haiwezekani!” “Kwa kifupi tu, nataka ujue unao maadui wengi.”
“Hilo nalifahamu wa huhitaji kuniambia. Lakini sio wafanyakazi wangu. Wafanya…”
“Side na Futi?” Malon akatoa macho. “Si ndio hao waliokuwa wakikufanyia kazi?”
Kimya kwa mshtuko. “Wewe usijali. Na mimi ni mzuri kwenye kazi yangu.
Nishafanya uchunguzi wakutosha, wanachotaka ni kukukomoa, na kukutoa mtaani,
ndio maana upo hapa. Wanataka pesa nyingi tu kwa ajili ya kuwekewa dhamana. Kwa
kuwa wewe umekamatwa kama uliyekuwa ukifanya biashara haramu. Na dhamana yake
ipo juu sio sawa na aliyekamatwa akiuza kidogo. Ili kutoka hapa, wanahitaji
pesa nyingi.” Akamtajia mamilion ya pesa zinazohitajika ili tu kutolewa kwa
dhamana. Malon akabaki kimya.
“Unajua sehemu ya kupata hiyo pesa?” “Kwa sasa sina, kwa kuwa pesa nyingi zilikuwa chini ya Side na Futi, kwa ajili ya kufanyia au kuzizungusha kwenye biashara. Nilizokuwa nazo, nimewekeza na Naya. Kwa hiyo, hiyo pesa yote, kwa sasa sina.” “Basi, nitakwenda kuzungumza na Naya, nimwambie. Na sijui atakuwa kwenye nafasi gani! Maana kujua, kukupata na kukaa hapa kama hivi, imemgarimu sana Naya. Lakini nitamfikishia ujumbe. Mkishajipanga, mtanitafuta tena.” Malon akafikiria. “Mwambie auze nyumba yangu ya hapa Morogoro. Anajua ni wapi naweka hati. Na hata kama hatapata mteja, basi akakopee benki.” “Sawa.” Wakaagana.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
Mati alitoka pale akampigia tena Naya. Alimweleza kila kitu. “Lakini mbona
pesa yenyewe ya dhamana ni kubwa hivyo!?” “Nilikwambia ni kama wanamkomoa,
halafu ukumbuke wanamshikilia kama mfanyabiashara haramu. Lazima dhamana yake
iwe juu.” “Nakushukuru.” “Sasa hiyo pesa utakuwa nayo tuendelee?” “Naomba unipe
muda, nitakutafuta tena Mati. Nimeshatumia pesa nyingi sana. Hiyo pesa itabidi
kuuza vitu. Nitajitahidi kukusanya, naamini nitafanikiwa tu.” “Naomba kukupa
ushauri Naya.” Naya akatulia.
“Unaniruhusu?” “Nakusikiliza Mati.” Naya akaitika. “Kuna watu hapa
duniani, wanakuwa salama huko magerezani, kuliko mtaani. Kwa watu wengine, jela
sio kitu kibaya, ni msaada. Wanatoka wakiwa wamejifikiria na huwa wanabadilika
kuwa watu wema katika jamii.” Kimya. “Kwa jinsi nilivyopata habari za Malon,
kutoka kwa polisi, mpaka kwa huyo hakimu, nafikiri Malon yupo sehemu sahihi.
Usijimalize kwa ajili yake Naya. Wewe bado ni mtoto mdogo sana. Some people are
not worth saving, Naya. Wewe bado ni binti mdogo sana, ndio umemaliza tu chuo!
You have bright future a head of you. Naomba utulie kidogo tu, utafakari kabla
hujaendelea sana.” Naya hakujibu.
“Naelewa kuna
kupenda au mapenzi huwa hayachagui, jiulize, at what cost Naya!? Kwa gharama
ipi? Mimi ni kama kaka yako mkubwa sana. Nimeoa, ninafamilia. Nayajua maisha.
Nakushauri ujijenge kwanza wewe mwenyewe kabla hujaangamia kama wengi wa
mabinti wa hapa Morogoro. Ni hilo tu.” “Nashukuru kwa ushauri Mati. Nitakutafuta
nitakapokamilisha hiyo pesa yote.” Naya alijibu tu hivyo, nakukata simu.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
Alilia Naya nakushindwa kujisaidia. Alikumbuka mapenzi ya Malon
kwake. Jinsi alivyompenda na kumuheshimu. Tatizo ni umalaya. Naya alilia kila
akimkumbuka Malon. Jinsi alivyomsadia kulipa ada, kumtunza kuanzia kidato cha 4.
Mapenzi waliyokuwa wakifanya na Malon anapokuwa naye. Jinsi anavyombusu.
Japokuwa alijua anakuwa na wanawake wengine nje, lakini alithamini sana muda
anaokuwa naye. Malon alikuwa akitulia sana kila Naya anapokuwa karibu. Kila
kitu huwa kinasubiri, kila mtu huwa anajua, na kuelewa kuwa Naya yupo, na Malon
hataki usumbufu kwa muda huo awapo na Naya. Aliweka heshima kwa Naya, kila
awapo karibu na marafiki wa Malon, walimtambua kuwa ni mtu muhimu sana kwa
Malon.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
“Malon amesema niuze nyumba ya Morogoro.” “Utauzaje bila hati?!”
Mama yake akauliza. “Najua anapoficha au kuweka hizo hati. Nitamuomba Bale
anisindikize. Baba wewe pumzika.” “Mnakwenda Morogoro!?” Mama yake akauliza.
“Hapana. Huwa anafungia kwenye Safe ya Kunduchi. Nataka leo nikachukue, kesho
ndio niende Morogoro. Nikajaribu kuiweka sokoni au hata kuiombea mkopo benki.”
“Nitakusindikiza Naya.” Bale akakubali kwa haraka.
Naya akaanza kulia tena. “Utanisindikiza wapi sasa?” “Kesho
sitakwenda kujisomea na wenzangu. Nitakupeleka Morogoro, na tutakwenda wote
Kunduchi sasa hivi. Nisubiri nile, nibadili nguo, twende.” “Asante
Bale.” Naya akasimama huku analia, akarudi chumbani kwake. “Huwezi
ukamwachia Bale. Usipokwenda naye huyo, hatanyamaza mpaka anarudi hapa. Na
hatafikiria chochote. Ni heri umwambie akusubiri, uchukue maziwa, mpeleke, ndio
muende huko Kunduchi.” Mama yake alitoa huo ushauri. Baba yake akaafikiana nao.
Walitoka jioni hiyo, wakamsindikiza baba yao kushusha maziwa na
mayai kwenye hoteli mbili tofauti, ndipo wakaelekea Kunduchi. Pale kwenye
nyumba ya Kunduchi hakuna aliyekuwa akiishi hapo, lakini Malon alikuwa ameweka
kampuni ya ulinzi. Morogoro alikuwa ameweka mtu tu wa kawaida ndiye aliyekuwa
akilinda nyumba yake. Walipokezana kulinda. Mchana mlinzi mmoja na usiku
walikuwa walinzi wawili.
Naya aliwakaribisha pale sebuleni. Ilikuwa nyumba nzuri sana.
Ndogo tu, lakini ilijengwa maeneo karibu kabisa na mahoteli, karibu na
ufukweni. Mmiliki wake alionekana alikuwa na ramani nzuri. Kwani ilipangiliwa
vizuri sana. Ndani na nje. Ilikuwa na vyumba vitatu tu. Hapakuwa na uwanja
mkubwa sana mbele, na nyuma hivyo hivyo. Lakini ilikuwa karibu kabisa na
baharini.
Naya aliingia chumbani kwao. Akatoka na bahasha kubwa. “Umepata?”
“Nimepata. Lakini lazima kulipia ulinzi. Nisubirini niandike kundi ya malipo.
Nizime taa zote na Ac, niache taa za nje tu, ili umeme usiishe.” Baba yake
alibaki akimtizama. “Unataka nikusaidie nini?” Bale akauliza. “Naomba
niangalizie hapo jikoni kama kuna uchafu wowote kwenye ndoo ya takataka hapo
pembeni ya friji na kwenye sinki. Kwa kuwa nazima kila kitu, panaweza kunuka
kama tukiacha uchafu.” “Unazima na friji?” Bale akauliza. “Hapana. Kuna nyama
humo na vyakula vingine. Nikizima vitaharibika. Labda..” Naya akafikiria.
“Naomba niangalizie vitu vilivyopo kwenye Friza. Hiyo nilazima niizime. Huwa
inakula sana umeme.” “Sasa kama ina vitu?” Bale akauliza, Naya akafikiria tena kidogo.
“Hamishia kwenye friji ndogo, unavyofikiria kama utatumia nyumbani, chukua.
Weka kwenye gari, turudi navyo nyumbani.” Naya akaanza kupekua ile bahasha.
Baba yake akamuona anatoa hati moja, ingine akarudisha ndani.
“Hiyo nyingine ni ya wapi?” “Hati ya nyumba hii, kule kiwandani, na documents
za magari yake.” Naya akanyamaza kidogo, akamsikia anaguna. “Magari yenyewe
wameondoka nayo yote. Yaani kila mtu amejimilikisha mali za Malon! Tena baada
ya kumkamatisha mwenyewe polisi! Mungu atawalipa lakini.” Akamuona anaandika
hundi. “Sasa hizo pesa za kulipa hao walinzi, utapata wapi?” “Kwenye ile
akaunti yangu na Malon, nilibakisha pesa kidogo. Sasa kwa kuwa naona watu
wanajichukulia tu, heri niimalize kabisa. Nalipia hapa, na kule kiwandani.”
Wakamsubiria, akaweka mambo yake sawa. Wakaondoka.
Mji Kasoro Bahari, Malon Alizwa vibaya sana.
S |
aa 12
alfajiri, Bale, Naya na baba yao walikuwa wapo kituoni wakisubiria mabasi ya
kwenda Morogoro. Naya akamsogelea baba yake aliyekuwa mbali kimawazo, akamshika
mkono. “Asante baba.” “Kwa kuwa ni wewe Naya, mama yangu mzazi. Lakini hakika
sioni sababu mama. Naona ni kama nashiriki kwenye kukuangamiza tu.” “Nampenda
Malon, baba. Hakuna jinsi nikasikia yupo matatizoni, nikaweza kulala.” Baba
yake akamtizama. “Nimefurahi unakuja na sisi. Asante.” Baba yake akavuta pumzi
kwa nguvu bila kujibu, akajisogeza kwenye huohuo mkono wa baba yake aliokuwa
ameushika, akamuegemea. Bale alikuwa kimya, ameingiza mikono yake mfukoni.
Alifanana na Naya, utafikiri mapacha. Urefu na sura kama mama yao.
Basi lilifika, wakaingia humo ndani, safari ya Morogoro ikaanza
wote wakiwa wamejawa tumaini kuwa hayo
mamilioni ya pesa yanayohitajika kwa ajili ya Malon, yatapatikana kwenye hiyo
nyumba ya Morogoro. Walitua jiji kasoro bahari, wakapanda tena daladala mpaka
kwenye nyumba ya Malon.
Naya akashtuka sana akiwa bado nje. “Nini?” Baba yake akauliza.
“Mbona kama wameng’oa geti! Halafu hakuna hata mlinzi!” “Kwani panalindwa hata
mchana!?” Bale akauliza. “Mchana huwa anakuwa na mlinzi mmoja, usiku ndio
wawili. Ila hapa wanalinda watu tu wakawaida, sio kampuni ya ulinzi kama kule
Dar.” Naya akaongeza mwendo kufikia lilipokuwa geti, kuingia ndani! Macho
yalimtoka Naya, wakamuona machozi yakimtoka huku ameweka mikono mdomoni. Bale
na baba yake walikuwa hawaifahamu hiyo nyumba. Ni yeye peke yake Naya. Wakaongeza mwendo na kumfikia.
“Mbona unalia tena!?” Baba yake akauliza. “Wewe huoni kuwa imebaki
gofu tu!?” “Kwani hii ilikuwa nyumba kabisa?” “Ndipo tulipokuwa tukiishi
tukiwa hapa Morogoro. Ilikuwa nyumba yenye kila kitu, kama vile ya Kunduchi ila
hii kubwa zaidi!” Naya aliendelea kulia. “Mungu wangu!” Wakamuona anaingia ndani. Hapakuwa na mlango
wala dirisha. Kweli lilikuwa gofu. Waling’oa kila kitu. Wakachukua kila kitu
mpaka vyungu vya maua! Bale na baba yake hawakuamini. “Hii kweli ilikuwa nyumba
iliyokamilika!?” Bale akauliza huku na
yeye anazunguka mle ndani.
“Wameiba nguo zetu zote!” Naya alitoka chumbani kwao huku
akielekea jikoni. “Huku nako wameiba mpaka vijiko! Mafriji wamechukua, makabati ya
ukutani wameng’oa!” “Yaani hapa kwa ufupi ni kwamba wamebakisha kuta na paa.” Baba
yake akaongeza. “Nashauri huku usiingie Naya. Wameandika ukutani matusi matupu
na kunanuka sana mikojo.” Bale alikuwa kwenye chumba kingine. Naya akaendelea
kulia.
Chumba kimoja kilionekana kuna mtu huwa analala hapo. Walikuta
matandiko chini, na visufuria. “Uwii, Mungu wangu!” Naya
alisikika akilia taratibu huku akizunguka. Baba yake na Bale wakatoka kumfuata
hapo nje alipokuwa amekaa akilia.
Ghafla wakamuona amenyamaza. Akatoa simu, akapiga. “Chezo, ni mimi
Naya.” “Unataka nini kwangu wakati uliniambia mimi sio mtu wa kuaminika?
Mbambaishaji. Na hutakaa ukanitafuta tena wala kuniamini.” “Sikusema hayo yote
Chezo, lakini pia nilikuwa nikikutania tu.” “Unajisahau sana Naya. Ulisahau
mimi ndiye niliyekuwa nikihangaika kukufanikishia shuguli yako yote!? Niliacha
mambo yangu yote huku Moro, nikaja Dar ili niwe na wewe, ufanikiwe. Japo
sikutoa pesa, lakini nilitoa muda wangu na mawazo, wakati Malon akilala na
wafanyakazi wako! Nikahangaika mchana na usiku, ukaja kunitukana mbele za
watu!” “Chezo! Tulikuwa mimi na wewe, pamoja na Malon tu! Halafu nilikuwa
nikikutania! Tafadhali naomba usikasirike. Nakuhitaji sana sasa hivi.” “Ili
unitumie tena, halafu aje afaidi Malon?” Naya akaishiwa nguvu.
“Mimi nimeamua kukaa mbali na nyinyi bwana. Nilikuwa nakufuata mpaka
Mzumbe, pale Malon alipokuwa akikukosea. Malon alikuwa analala na wanawake
wengine, anakupiga, mimi nilikuwa na wewe Naya. Ukaona mimi sina kitu, ukaamua
kubaki na Malon aliyekuwa akilala na kila mtu aliyekuwa akikuzunguka. Ni aibu
mara ngapi amekutia Malon, mimi nikasimama na wewe? Mara ngapi nimekuwa na wewe
Naya? Ukaja kunigeuka! Nimeondoka kwenye shuguli yako, usijue nimekwenda wapi,
hata usinitafute! Nakuja kukutana na wewe, nakusalimia, na wewe unanipa lawama?”
Chezo akaendelea
kutoa ya moyoni.
“Umekuwa na tabia kama za Malon! Mnapenda kutumia tu watu. Hamna
utu. Sasa kila mtu amewajua tabia zenu. Wamewakimbia. Kama na wewe unaakili,
ondoka kwenye huu mji. Masela wakikukamata, watamlipa Malon kisasi, kupitia
mwili wako. Tafadhali usinipigie tena simu wala usinitafute Naya. Nina maisha
yangu. Sitaki uniingize matatizoni. Sasa hivi hata usalama wanaangalia. Yeyote
anayejihusisha na Malon, wanamkamata. Sasa sitaki uniingize matatizoni.
Tulifahamiana kupitia Malon. Malon ameondoka, tafadhali kaa mbali na mimi.
Usijaribu hata kukosea kunipigia.” Chezo akakata simu.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
Naya alibaki amepigwa na butwaa, kama dakika mbili hivi.
Akaitazama simu yake kama asiye amini. Baba yake na Bale walikuwa wamesimama
hapo kimya. Wakamuona anasimama. “Naombeni msinisindikize nyumbani kwa kina
Malon.” Akaongoza njia, wakafuata. Bado ilikuwa mapema tu, asubuhi. Jua kali.
Kwa kina Malon Tena.
Wakapanda tena daladala mpaka nyumbani kwa kina Malon. Walikuta
wamekaa tu, siku hiyo ya jumamosi. Baba yake Naya, alitamani kama asingerudi
tena kwa yule mzee aliyemuonya kwa wazi kabisa. Lakini hakuwa na jinsi. Ni
binti yake wapekee. Alijiambia ni heri apotee au aharibikiwe akiwa anamuona,
kuliko kumuacha peke yake.
Walikaribishwa vizuri tu. Tena mama yake Malon akataka wanywe na
chai. Naya akakataa. “Nina shida yakuzungumza na nyinyi, niombe msaada.” Baba
yake Malon akatulia kabisa, akimsikiliza. Naya akaeleza alipofikia yeye na
mwanasheria na pesa zinazohitajika. Na ushauri wa Malon kuwa auze ile nyumba.
“Naomba mnisaidie chochote mlicho nacho, nitahangaika kuuza hiyo nyumba kwa
kiasi chochote kile, tumuwekee dhamana.” Naya akawaangalia kwa zamu.
“Hata nikiuza suruali zangu zote, siwezi kupata hata robo ya hiyo
pesa. Gari alilotununulia Malon, hilo hapo nje, ndio usafiri pekee tulio nao.
Mama yake ana matatizo ya miguu. Umri umekwenda, hawezi kukimbizana na daladala
tena. Haya, tukisema tuuze hii nyumba aliyo tujengea, wote tutaishia kulala
barabarani. Malon sio mtu ambaye utasema atatoka, aanze maisha ya tofauti na
aliyozoea kuishi. Mimi ninamjua Malon, ni mwanangu. Atarudia yaleyale, kama sio
kesho, basi kesho kutwa atakamatwa tena na polisi. Atafungwa. Hapo tutakuwa
hatuna tena gari yakuuza au hata nyumba yakuishi, na yeye yupo tena jela.” Yule mzee aliongea kwa
utulivu tu.
“Naya mwanangu, narudia tena. Huyu Malon unayemuhangaikia, huko
aliko, wala sio kugeni kwake. Ni maisha aliyochagua. Mbaya zaidi, amekataa
kubadilika. Kukamatwa na kufungwa kwa Malon ndio maisha yake na ndipo pesa yake
inapoishia huko. Kuwekewa dhamana na wenzake, kuhonga mapolisi. Kilichobadilika
tu ni wazazi wa hapa Morogoro wamechoshwa naye, wameungana, nakuomba msaada kwa
vyombo vya usalama vya mpaka Dar-es-Salaam ili tu kumkamata huyo Malon. Ana vilio
vya wazazi wengi sana huyo Malon. Anaharibu watoto wakiume na wa kike. Bangi na
mapenzi. Wazazi wamechoka. Ndio maana wameamua kumchukulia hatua kubwa zaidi. Sasa
hivi kesi ya Malon wamechukua usalama wa taifa, ndio maana unaona hata wenzake
wanakimbia. Huko alikofichwa, sio kwa bahati mbaya. Na hata hicho kiwango
walichoweka, sio bahati mbaya. Wamekusudia asitoke kabisa. Na hata akitoka, awe
amefilisika kabisa.” Naya akatulia kidogo. “Umenielewa mama?” “Nimeelewa.”
“Afadhali. Endelea na maisha yako mama. Wewe bado mdogo.” Mzee Saduki
akasisitiza na kudhani wapo upande mmoja na Naya.
“Kwa hiyo hamna pesa yeyote ambayo mnaweza kunisaidia? Hata kama
nikidogo tu. Sio lazima mkafikia nusu au robo. Chochote mlicho nacho. Naomba
mnisadie au hata kama hamna sasa hivi, naomba mtakapo pata, mnipe. Napokea
chochote.” Yule baba hakuamini. Akabaki akimtizama Naya.
Naya akamgeukia mama yake Malon. “Tafadhali mama yangu. Naomba
uongee na ndugu zake. Chochote kile, mimi napokea. Hata shilingi moja,
itanisaidia. Asanteni, naomba sisi tuondoke.” Naya, baba yake na Bale waliondoka
hapo kimya kimya, hakuna hata aliyeongeza neno.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
“Tunakwenda wapi tena?” Ikabidi baba yake aulize tena. “Nakwenda kuzungumza
na watu wa benki, nione kama watanunua kile kiwanja, sijui nyumba ya Malon au
gofu, hata sijui niiteje! Kwa jinsi ileile ilivyo, nione watanipa kiasi gani.”
Hakuna aliyejibu, wakafuata nyuma. Walifika wanakaribia kufunga benki. Naya
akaingia ofisi za mikopo. Kwa bahati yake mbaya, akakutana na dada ambaye naye
alishalizwa yeye na mdogo wake na huyohuyo Malon. “Nakufahamu sana Naya.
Tushakusikia na kukuona na huyo Malon. Wala wewe usifikiri ni tofauti na
wengine. Malon ni tapeli wa mapenzi na pesa. Hapa benki hakopesheki.” “Sitaki
kukopa. Nataka kuona kama benki inaweza kununua.” “Nini?” Yule dada akauliza
kwa kejeli. “Lile gofu lake? Wala sio siri, kila mtu amepita pale kuchukua
anachotaka. Habari ya kuwa Malon, tatizo la mji ameondolewa mtaani, kila mtu
analijua. Na kwa taarifa yako ni furaha na kujibiwa kwa maombi ya kila mmoja wetu
hapa Morogoro. Hakuna atakayenunua ile nyumba ya laana. Ile imejengwa kwa vilio
vya wengi. Pesa ya laana ya bangi. Anageuza watoto wa watu vichaa ili
ajinufaishe yeye.” “Nahisi sio wote wanaoona ni laana.” Akajibu Naya.
“Uliza hapa ndani au nenda hata kwa meneja wa tawi uone kama
atakusaidia kununua hiyo nyumba ya laana ya Malon.” “Kwa hiyo kilichokuwa laana
pale ni kuta tu. Vingine vyote sio laana? Maana mmechukua mpaka chupi zetu.
Sijakuta hata vijiko!” “Naya! Naya!” Bale akamwita. “Simama hapo, twende.” Naya
akafyonza. “Wanamsema Malon sasa hivi wakati alikuwa akiwalala na kuwapa
pesa, mbona wakati anawahonga wasikatae waseme ni za laana?” Bale akaenda
kumshika mkono, akamnyanyua pale kitini kwa nguvu. “Unatukana, na baba
anakusikia Naya. Twende.” Naya akaendelea kulia, nakutoka hapo bila yakujibiwa
na mtu yeyote pale ofisini. Baba yake akafuata nyuma kimya kimya.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
Wakiwa njiani kurudi Dar, wakamuona anatoa tena simu yake. “Sasa
hivi unampigia nani?” “Kuna mama ambaye alizipenda sana zile mashine
tulizonunua na Malon. Yeye anatengeneza magauni ya harusi.” “Kwa hiyo!?”
“Nataka kumuuzia.” Baba yake alishtuka sana. Akampokonya simu. Naya akashangaa
sana. “Baba!” “Tafadhali, tulia kwanza Naya. Vuta pumzi kwa nguvu. Mara tatu
tu. Tafadhali Naya. Ukiuza zile mashine ndio utakuwa umeua ndoto zako zote,
mama yangu. Tafadhali tulia ufikirie. Mwisho wa yote unataka kukamilisha nini?”
Naya akanyamaza. “Naya mama?” “Umeniambia nifikirie baba na umenipokonya simu
yangu!” “Tafadhali sana. Jipe muda wakufikiria kabla hujachukua hatua nyingine.
Tukifika nyumbani, ukipumzika. Nitakurudishia simu yako.” Naya akavuta pumzi
kwa nguvu, akajirudisha nyuma ya kiti vizuri. Akalala.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
Hakuomba simu yake wala hakuwa akilia. Usiku huo akasaidia kazi
pale nyumbani, wakakaa pale sebuleni kila mtu akapumua. Hapakuwa na kilio usiku
huo. Naya akaonekana amekuwa mtulivu, tofauti na walivyotarajia. Akala vizuri,
akawa ametulia tu. “Kesho tunakwenda wote kanisani?” Baba yake akamuuliza taratibu. “Ndiyo.” Naya
akakubali. Kila mtu hakuamini.
Na kweli, asubuhi akawa yeye wa kwanza kuamka. Akasaidia kuandaa
kifungua kinywa, wote wakala, ndio wakaondoka na hiyo gari ya familia, kuelekea
kanisani. Njiani alikuwa ametulia tu, mpaka wakafika kanisani. Walipofika, baba
yake akampa simu yake. Naya akacheka taratibu wakati anaipokea. “Sio uanze
kupiga simu zako sasa hivi. Tulia ibadani.” Baba yake akatoa onyo. Wakiwa wamesimama
palepale, wakaona Ino anaingia getini, na gari yake nzuri sana.
Ukweli mama yake Naya alikuwa akiumia kila alipokuwa akimuona
mkewe Ino, mtoto ambaye walishajaliwa. Maisha matulivu yaliyokuwa yakionekana dhahiri
kwa familia hiyo ya Ino, alimuhurumia mwanae, nakubaki akijiuliza ni wapi
walikosea kwa mtoto huyo ambaye walifikiri walifanya kila kitu mzazi
alihitajika kufanya kwa binti yake, lakini akaishia kwa Malon!
Ino, na mkewe wakiwa na katoto kao ka kike, wakawasogelea.
Walikuwa wasafi, kwa kuwatizama tu, walionekana wanamafanikio. Msichana
aliyemuoa, hakuwa ametokea kwenye kanisa hilo. Walishakuwa na ndoa ya miaka miwili.
Ino alioa wakati Naya yupo mwaka wa kwanza chuoni Mzumbe. Naya alionekana wazi
amechoka usoni. Wakasalimia. “Mzima Naya? Unaonekana umechoka!” Kama kwaida yake
Ino, bila kuficha hisia zake akaanza mara walipowafikia. “Nahangaika kazi Ino.
Naomba nisaidie kazi yeyote ile.” “Sasa si vyeti bado havijatoka? Utaajiriwa
vipi?” “Ndio maana nimekwambia kazi yeyote ile!” Maongezi hayo wanazungumza
wakiwa wamesimama hapo nje ya kanisa, watu wote wakiwasikiliza.
“Ungekuwa unajua kuendesha gari, tungekupa kazi ya kumpeleka mtoto
wetu daycare na kumrudisha. Dereva wake ameacha kazi. Na kama unavyojua, mke
wangu anafanya kazi world benki. Anatoka alfajiri sana. Kwa kuwa ofisi zao
zipo…” “Najua kuendesha gari na ninayo leseni pia.” Naya akamkatisha wakati
akiendelea kujigamba hapo, wote wakamgeukia. “Mtanilipa kiasi gani, na saa
ngapi mnataka niwe nimefika nyumbani kwenu kumchukua mtoto na kumpeleka huko shule?”
“Actually ni some sort of daycare, not shule!” Ino akamsahihisha kwa majigambo.
“Popote mnapotaka nimpeleke mtoto wenu, mimi nitampeleka.” Kwa aina ya uongeaji
wa Ino, mama yake alijua Naya angekataa.
Ino akamgeukia mkewe. “Eti darling!” Akamuuliza mkewe. Yeye ndiye
aliyekuwa amebeba mtoto wao huyo wa kike wa mwaka na miezi michache. Kilikuwa
kitoto kizuri, afya nzuri. Wamemvalisha vizuri na kumbana nywele vizuri sana.
“Labda tuzungumze halafu tutampigia simu.” Mkewe akajibu. “Kwa nini? Vitu
vingine nivyakutolea maamuzi hapo hapo. Wewe unajua unaondoka nyumbani saa
ngapi na kurudi saa ngapi! Swala ni unataka awepo hapo ukiwepo wewe au haina
haja. Yaani kama unataka kumuona kabla hajamchukua Princess au la. As simple as
that! Hatuwezi kufikiria jambo dogo kama hilo, wakati tuna mambo mengi sana
yakufikiri.” Naya akajichekea nafsini kwake na kujiambia, “Huyo ndio Ino, bwana!” Akamgeukia mkewe kujua atakachojibu.
“Ni kweli. Labda awepo nyumbani saa moja na nusu. Atakuwa Princess
yupo tayari. Na saa kumi jioni utatakiwa uwe umeshafika tena shule, kumchukua
na kumrudisha nyumbani.” “Sawa, mama Princess. Natakiwa kuanza lini?” “Kesho.”
Akadakia Ino. “Na gari linatakiwa kuwepo wapi wakati Princess yupo hapo kwenye
daycare?” “Alipo Princess ndipo linapotakiwa kuwepo gari yake.” Akajibu Ino kwa
kiburi kidogo. “Sawa sawa bosi. Kesho saa moja na nusu, nitakuwepo getini
kwenu. Au hamna geti?” Naya akauliza kwa uchokozi kidogo. “Lazima kuwe na geti!
Ni nyumba gani haina geti?” Akauliza Ino
kwa dharau akishangaa kabisa. “Ya kwetu haina geti.” Bale akamjibu kwa haraka, Zayoni
akaanza kucheka. Na Naya naye akacheka. Ino akaondoka, mkewe akafuata nyuma.
“Bale nyinyi!” Mama yao akataka
wanyamaze. “Mpuuzi sana Ino! Anajidai kama anaishi nchi gani sijui! Yeye
anapitia wapi kufika hapa kanisani? Inamaana
anakutana na nyumba zenye mageti tupu?” Wakazidi kucheka wote. “Ni kweli utaenda kuwa
dereva wao?” Baba yake akauliza. “Nitaenda. Na kwa jinsi anavyopenda sifa,
najua atanilipa vizuri tu ili kunionyesha anazo pesa na nimechezea bahati.”
“Alivyo bahili yule, wala usiweke tumaini kubwa.” “Nitatafuta na kitu kingine
chakufanya nikishamshusha mtoto wao.” “Umejifunza lini kuendesha?” Mama yake
akamuuliza. “Malon mwenyewe alinifundisha. Nilikuwa nikitumia moja ya gari yake
wakati nipo kidato cha 5 na sita.” “Acha masihara Naya! Yaani ulikuwa ukienda
shuleni kwa gari!?” Akashangaa sana
Bale.
“Alikuwa akinipeleka, au kama ikitokea anataka kulala zaidi siku
hiyo, hataki kuamka asubihi sana mida yangu ya kuwahi shule, nilikuwa nikiondoka
na gari yake.” “Subiri kwanza Naya. Kumbe ulikuwa ukiishi naye!?” Akauliza mama
yake kwa mshangao sana. Naya akagundua ameropoka akainama, bila kujibu. Bale
akakohoa huku akimtizama baba yao. Mama yao akashtuka sana. “Usiniambie baba
Naya kama wewe ulikuwa ukijua.” “Mimi mwenyewe nimejua jana! Ametuambia jana.
Na mimi nilijua alikuwa akiishi hosteli.” “Sasa kwa nini na wewe hukuniambia?”
“Ingesaidia nini?” Baba yake akauliza.
“Naombeni twendeni ibadani. Hayo mambo tuyaache kama yalivyo.” “Na
huko Morogoro pia ulikuwa ukiishi naye kama mumeo?” Mama yake akauliza kwa
ukali. Naya akajisogeza nyuma ya baba yake. “Naombeni twendeni ibadani. Mambo
mengine utazungumza na Naya, tukiwa nyumbani. Tena kama utaona kuna umuhimu.”
“Ujue baba Naya huyu mtoto unamuharibu wewe!” “Punguza sauti mama. Naya
amesoma. Amekuletea vyeti vyote ulivyotaka.” Bale akaingilia. “Sio vyote. Bado
cha Chuo.” “Basi kinakuja mama yangu. Sasa hivi tutulie, tukamuabudu Mungu.”
“Na mimi natamani kujifunza kuendesha gari.” Akadakia Zayoni. “Hata mimi.” Bale
akaongeza. “Nitawafundisha.” Akaitikia Naya akiwa nyuma ya baba yake. Mama yao
akaondoka pale kwa hasira. Wakamfuata nyuma.
Baada YAKUSHINDWA KUWA MKE, NAYA AWA MFANYAKAZI WA INO.
A |
subuhi ya
siku ya jumatatu kila mtu alimka na shuguli zake. Mama yake akaenda kazini,
kina Bale shuleni, baba yake akampa lifti Naya mpaka nyumbani kwa Ino, yeye
akiwa anapeleka maziwa na mayai mjini. Aliwahi kidogo, kwa kuwa alimfahamu Ino,
hakutaka shida. Naya akaamua kukaa nje ya nyumba yao, asubirie muda.
Wakati anasubiria, akamtafuta Ozi kwa ujumbe. ‘Ukiamka nipigie.’ Hapo hapo Ozi akapiga. “Niambie mrembo.” “Bado nataka tuuze zile nguo.” Ozi akaanza kucheka. “Unacheka nini sasa?” Naya akamuuliza. “Unavyoringa Naya! Mara useme unamtaka Malon. Malon akifungwa jela, unarudi kwangu!” “Malon ni mpenzi wangu. Wewe nakutaka tufanye wote biashara. Kama unaona huwezi, basi.” “Bado Malon ni mpenzi wako tu!?” “Kwani umesikia amekufa?” “Habari nilizonazo za Malon, hazina tumaini ya kuonekana kwake kwenye uso wa dunia hivi karibuni. Nimesikia amechimbiwa.” “Utafanya kazi na mimi au la?” “Tena dada anatafuta watu wa kazi. Nikutaje tuone kama anaweza kukuajiri? Wewe huwa anakupenda sana. Atakuajiri.” “Basi zungumza naye.” “Lini unaweza kuanza?” “Hata leo.” “Basi nitakujulisha. Ngoja nizungumze naye kwanza. Halafu nitakupigia. Ameanzisha vimiradi vingi. Lazima atakuhitaji tu.” “Nitashukuru Ozi.” Wakaagana.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
Alimkuta Ino akimsubiria na masharti mengi. Juu ya gari na mwanae. “Tafadhali sana kuwa makini na gari ya Princess na Princess mwenyewe. Hairuhusiwi kula chochote ndani gari yake. Wala kudondosha kitu. Ibakie safi ndani na nje. Kuwa mwangalifu sana humo barabarani na hakikisha umemfunga mkanda Princess wakati wote. Acha gari hapohapo daycare kila unapomshusha. Hakikisha…” Aliendelea Ino, Naya akimtizama tu. “Hivi unanisikiliza lakini?” “Unanipotezea muda Ino. Hayo mambo unarudia rudia, wakati mmesema mtoto anatakiwa kuwepo shuleni saa mbili kamili.” “Nataka umakini, na..” “Ino, hivi ujue unazungumza na mimi Naya? Najua ni nini unataka. Wewe nipe hizo funguo za gari, tuondoke.” Ino akamkabidhi funguo. “Tafadhali kuwa makini Naya.” “Sawa bosi Ino.” Naya akajibu.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
Akamshusha mtoto wao shuleni kwao. Uzuri ilikuwa ni upnde huo huo
wa Mbezi walikokuwa wakiishi Ino, ila karibu na Kibamba. Akatafuta sehemu
nzuri, akaegesha gari ya watu kama alivyoambiwa, akamtafuta mtu aliyejua
atanunu zile mashine. Akampigia simu mwanamke ambaye anashona nguo za harusi.
Yule mama akakubali kuchukua zile mashine zote kwa haraka sana. Baada ya
kubembelezana bei, akakubali kwenda kuzifuata hizo mashine palepale kiwandani.
Swala la usafiri nalo akawa ameua ndege wawili kwa jiwe moja.
Kesho yake yule mama ndio alimwambia atakwenda kuzifuata hizo
mashine. Bado pesa ilihitajika. Naya akafikiria kuuza kile kiwanda pia. Aliwaza
siku nzima nini chakufanya ili kupata pesa yakumtoa Malon rumande. Mwishowe
akakubali kuuza kile kiwanda na kiwanja chake.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
Baada ya mwezi mmoja akiwa anahangaika kuuza vitu ili kufikisha
ile pesa, akapata simu kutoka kwa mama yake Malon. “Umefikia
wapi?” “Bado nahangaika mama yangu. Lakini nimefika pazuri. Naamini
nitafanikiwa mama yangu. Mnaendeleaje huko?” “Na mimi nilikuwa nahangaika kuuza mikufu yangu. Sijapata pesa
nyingi, lakini naona zitakusogeza.” “Nakushukuru sana mama yangu. Mungu
akubariki.” Ikawa Naya ndiye anajiona anawajibila kwa Malon kuliko hata mama
yake wakumzaa. “Nikushukuru wewe Naya. Najua kila mtu amemkatia tamaa Malon, lakini
nakushukuru kuchukua nafasi yangu.”
“Malon ni mwanangu. Hata nifanyeje, au aweje, nilibeba mwenyewe.
Ningetamani Mungu angenipa kiumbe kingine, lakini amekuja Malon. Sijachagua,
mama! Na mimi nilipewa hivyo hivyo. Naomba usije ukamuelewa vibaya baba yake. Amehangaika
sana na Malon, tokea huyo mtoto anaanza kutamka neno la kwanza. Hatujawahi
kupumzika na Malon, mpaka leo.” “Naelewa mama yangu. Naomba nikushukuru kwa
kuniunga mkono.” “Pole mama. Mungu akutie nguvu. Nitakurushia hizo pesa.”
“Asante mama yangu.” Wakaagana.
Baada ya juma moja, na baba yake Malon naye akamtumia Naya pesa.
Akaja na kaka yake Malon. Yeye ndio aliongea, mpaka Naya akamwambia basi. “Nitahangaika
kwa njia nyingine. Asante.” “Usione kama nakusimangia! Malon ni tatizo. Hapa
imebidi kuhangaika kukopa ndio nimepata hicho kijipesa.” “Asante.” Naya akakata
simu.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
Nini kitaendelea? Baada ya kila mtu kuwa kinyuma na Malon, Naya
atafanikiwa kumtoa Malon? Usipitwe..
0 Comments:
Post a Comment