Naomi Simulizi |+1 205 767 8163 |naomisimulizi@gmail.com MAPENZI & PESA! – SEHEMU YA 9. - Naomi Simulizi

MAPENZI & PESA! – SEHEMU YA 9.

Baada ya miezi miwili, Naya akapata pesa yote. Akaenda ofisini kwa wale wanasheria.  Akamtafuta Joshi. Akamkabidhi hundi ya malipo yaliyokuwa yamebaki, ndipo akaenda ofisini kwa Mati kumkabidhi pesa yake ya mfukoni ambayo itamsaidia kwenye kuharakisha mambo. Akagonga ofisini kwa Mati. Alikuwa akizungumza kwenye simu, akampa ishara ya kumkaribisha ndani. Naya akaingia, akavuta kiti mbele ya meza ya Mati, akakaa.

Baada ya mazungumzo ya kwenye simu, Mati akakata simu na kumgeukia Naya kama asiyeamini. “Nilijua umeamua kuendelea na maisha yako!” “Hapana. Nilikuwa nikihangaikia pesa.” “Ulifanikiwa kuuza nyumba.” “Hapana.” Naya akamuelezea juu ya hali ya ile nyumba jinsi alivyoikuta na kushindwa kuiuza Morogoro. “Lakini nimepata pesa yote yakumuwekea dhamana, kumalizia garama za hapa kwenu na za dharula. Za kiofisi na dhamana, hundi yake nimeshamkabidhi Joshi, na amenipa risiti tayari. Hii hapa. Na za dharula, nakukabidhi wewe mwenyewe. Hizi zipo kwa pesa taslimu. Naomba uende hata kesho!” Mati alibaki akimshangaa Naya.

“Wewe mtoto mpambanaji! Malon alikutoa wapi?” Naya akacheka. “Najua umekutana na habari mbaya tupu za Malon. Lakini wote wamesahau kukwambia kuwa Malon ni mwema. Huwa hawezi kumuona mtu anashida, akaacha kumsaidia. Mimi mwenyewe nimenufaika sana na Malon. Hata hizo habari unazosikia kuwa nimesoma sana, sijui ni binti mzuri, ni kwa sababu ya Malon. Nimesomeshwa na Malon. Si kwa kushindwa kwa wazazi wangu, ila kwa upendo wake. Amenilipia gharama zote, tokea nipo kidato cha nne mwishoni mpaka namaliza chuo.” Naya akaendelea.

“Na amekuwa akinisaidia nisipotee. Alisimama kama kinga yangu kwenye huu ulimwengu, kunilinda na kila hatari, kwa jinsi alivyoweza yeye. Alikuwa mkali sana kwangu kila anaponiona nataka kupotea. Nipo hapa jinsi unavyoniona, ni kwa ajili ya Malon. Malon yupo jela, kwa ajili ya kumfikiria Side. Aliniacha mimi na mali zake zote, akimfikiria mke na watoto wa Side. Hawakumkamata Malon, ila Malon alikwenda kuchukua nafasi ya Side polisi, akidai yeye kuwajibika na kila kosa analoshutumiwa Side.”

“Wote unaowasikia wakimsema vibaya Malon, hata huyo anayelalamika alichukuliwa mchumba wa kukaribia kumuoa, baada ya hapo pia aliendelea kunufaika sana na Malon akijidai ni rafiki yake wakaribu. Hata huyo mwanamke mwenyewe amenufaika sana na Malon. Hakuna aliyewahi kubakwa na Malon! Ndio maana hana kesi ya kubaka. Kama sio wenyewe kumtongoza Malon kwa sababu ya kutaka pesa zake, na kwa kuwa wanajua Malon ni mtoaji, basi kwa tamaa zake Malon ndio amelala nao. Tatizo ni pale wanaponogewa wao, nakutaka muendelezo na Malon.” Mati akacheka sana.

“Wakinogewa!” “Kweli kaka Mati. Si kwa mchezo tu atakaompa huyo mwanamke, hata pesa. Yeye Malon kufanya mapenzi na wanawake, ilikuwa ni starehe tu kama starehe nyingine zozote. Waulize wote kama kuna hata mmoja alitongozwa na kuambiwa ataolewa. Hamna kaka. Lengo lake kwa wasichana wakati wote ilikuwa ni kulala nao tu, na alikuwa akiliweka hilo wazi tokea mwanzo, ila wao walitaka zaidi ya kile Malon alichokuwa anaweza kuwapa. Malon sio au hakuwa mtu wa kukaa chini na kutunza mahusiano na yeyote. Na sababu kubwa  ni kwa kuwa ni muwazi wa kupita kiasi. Hajui ni neno gani alifiche asimwambie mtu. Akiamua hapana yake kwa sababu fulani kichwani mwake, atamwambia huyo mtu vile alivyofikiria yeye kichwani bila kuchuja au kutafuta hekima yakusema hiyo hapana.” Naya akaendelea kumtambulisha Malon kwa Mati mwanasheria wake.

“Halafu ni jeuri, mkorofi asiyeweza hata kujisaidia. Ndio maana hapatani hata na baba yake mzazi, au baadhi ya ndugu zake japo aliwasaidia sana. Na ndio maana inakuwa rahisi kusahau wema wake kwa ukorofi wake.” “Mbona nilisikia kwako alikuwa kama mjinga?” “Anasema yeye mwenyewe hakuwa anajua ni kwa nini.” Wote wakacheka.

          “Nisaidie kumtoa tu, Mati kaka yangu. Najua unapambana na ugumu mkubwa, lakini nafunga na kukuombea ufanikiwe. Samahani kwa kukupa kesi ngumu.” “Hamna shida. Tatizo lilikuwa ni pesa. Kama pesa yote imepatikana, nitakwenda kesho asubuhi sana.” “Nashukuru Mati. Naomba ukae na hizi funguo na hii bahasha. Inabarua ya Malon. Siku yeyote utakayofanikiwa kumtoa, umkabidhi.” “Ni ya wapi?” “Ukimkabidhi vyote, ataelewa. Acha mimi niwahi. Nipo na gari ya watu, natakiwa kuirudisha mapema.” Naya akaondoka, akamuacha Mati haamini ile hundi kama inayo kweli ile pesa, au itapelekwa benki, ikataliwe kwa kuwa hakuna pesa.

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

Ilikuwa siku ya alhamisi wakati Naya anapeleka pesa yote kwa mwanasheria. Hakujua kilichoendelea. Akarudi kumchukua mtoto wa Ino. Akawahi kurudi nyumbani kwao kujiandaa na kazi ya usiku. Mpaka anarudi nyumbani, hakuwa amepata ujumbe wowote kutoka kwa Mati. Akaona ampe muda zaidi. Siku ya ijumaa ilikuwa vilevile. Kumchukua mtoto wa Ino na kumrudisha. Usiku alikuwa akienda kufanya tena kazi.

Akarudi nyumbani kwa daladala baada ya kumrudisha mtoto wa Ino nyumbani kwao na kuacha gari ya watu safi. Akabadilisha nguo, akajitengeneza siku hiyo ya ijumaa, akatoka tena kwenda Sheratoni hoteli. Siku hiyo walikuwa na kazi huko. Aliaga nyumbani kwao akiwa na haraka na wasiwasi wakuchelewa. Akaondoka. Walikuwa wakifanya maonyesho ya vinywaji vya Henken siku hiyo. Lakini hakumwambia baba yake. Alijua ataumia sana akijua anafanya matangazo ya pombe. Aliaga kuwa anakwenda kuhudumia kwenye sherehe tu, asijue kazi nyingi anazopata binti yake ni kwenye kutangaza pombe. Umbile la Naya, alikuwa mrefu, kaumbile kake kalipendeza hata kwenye matangazo. Alishapata kazi ya tangazo moja la video linalotangaza Safari bia. Ikamwingizia pesa nzuri, akaongeza kwenye makusanyo yake.

Alifanya kazi usiku huo bila kukaa chini. Alikuwa amevaa viatu vya juu, akitangaza kinywaji hicho kwa wateja wote waliohudhuria. Ilikuwa wiki hiyohiyo wakafanye tena tangazo la video kwa watakao chaguliwa kwa kutangaza vizuri usiku huo. Na Naya alikuwa kwenye nafasi kubwa yakuchaguliwa kwenye tangazo la video kesho yake kwa sababu kwanza ya umbile, pili alivyokuwa akijituma. Hiyo kazi ya matangazo alipata wakati akifanya kwa kina Ozi. Kwa hiyo ilikuwa ni yake mwenyewe. Alikuwa akilipwa yeye mwenyewe. Na Mungu alimsaidia, kila anapokuwa kwenye kazi, anapata kazi ingine. Lakini alikuwa akichelewa sana kurudi nyumbani. Mchana ungemkuta nyumbani, lakini sio usiku. Na wakati mwingine alikwenda kufanya kwa kina Ozi. Ila kazi hiyo ya usiku huo, na Ozi naye alipata kazi. Kwa upande wa wanaume, na Ozi naye alipata hiyo kazi ya kutangaza hicho kinywaji. Kwa hiyo waliingia kazini na Ozi.

                          Hakuna Marefu Yasiyo na Ncha.

O

zi akamsubiria, mpaka akamaliza ili waondoke pamoja. “Nimechoka Ozi, namshukuru Mungu kesho jumamosi asubuhi, sina kazi, napumzika.” “Ila ujue na kesho mambo ni hayahaya au nazaidi maana wahudhuriaji  asilimia 99 watakuwa wanywaji kwa hiyo utegemee walevi watakao tusumbua zaidi.” “Nitalala kesho siku nzima ili nikija huku jioni niwe na nguvu sio kama leo.” Naya alijibu huku wanatoka pale ukumbini. Macho yakagongana na Malon, asiamini! “Malon!” Naya akaita kupata uhakika. “Ni mimi, Naya wangu.” Naya alitupa viatu alivyokuwa amevishikilia, akamkimbilia  na kumrukia, Malon akamdaka na kumbemba. Alilia Naya, kila mtu akabaki akiwatizama. Alilia sana.

Bado Malon alikuwa amemkumbatia na yeye akawa amemkumbatia kwa nguvu sana. “Pole Naya. Pole sana.” Naya akadaka midomo ya Malon, nakuanza kumbusu pale pale. Alimbusu tena na tena, Malon akiwa bado amemkumbatia. Ozi akabaki haamini kama kweli yule ni Malon aliyehakikishiwa hatakuwepo mtaani tena, na yeye kujipa moyo akimchukulia Naya taratibu akijua mwishoni Naya atakuwa wake tu, kwa kuwa kipingamizi Malon hayupo!

Bado Malon alikuwa amemkumbatia na yeye akawa amemkumbatia kwa nguvu sana. “Pole Naya. Pole sana.” Naya akadaka midomo ya Malon, nakuanza kumbusu pale pale. Alimbusu tena na tena, Malon akiwa bado amemkumbatia. Ozi akabaki haamini kama kweli yule ni Malon aliyehakikishiwa hatakuwepo mtaani tena, na yeye kujipa moyo akimchukulia Naya taratibu akijua mwishoni Naya atakuwa wake tu, kwa kuwa kipingamizi Malon hayupo!

Naya alikuwa na furaha yakupitiliza asiamini yupo mikononi mwa Malon hata asihisi uwepo wa Ozi, akajivuta mbele kidogo na kumwangalia Malon kama asiyeamini. “Umejuaje kama nipo hapa?” “Mati alinipa funguo za Kunduchi. Nikajua utakuwa kule. Nikakuta kuna joto, giza kila mahali, nikajua hauishi pale. Baada ya kuoga, nikaamua kukufuata nyumbani Kiluvya. Ndio Bale akaniambia una kazi hapa.” Naya akafuta machozi. Akamkumbatia tena kwa nguvu. “Nimekusikia unalalamika umechoka.” Naya akacheka taratibu akiwa bado amemkumbatia. “Uchovu wote umeisha! Umetoka saa ngapi?” “Wamenitoa jioni ya leo. Mati amenisaidia usafiri wa kwenda kushukuru nyumbani kama ulivyosema kwenye barua yako. Sikukaa sana, wala sikutaka kumchelewesha Mati, nikamuomba tena lifti yakuja huku Dar.” Muda wote huo wanazungumza, Ozi anawatizama kwa pembeni.

“Siamini Malo! Nilikuwa na hamu na wewe!” Malon akaanza kumbusu. Akambusu tena na tena akiwa amemkumbatia. “Asante sana Naya, na samahani.” “Twende tukapumzike.” Naya akajitoa mikononi, akamshika mkono Malon. Akamtizama asiamini. “Ozi!” Naya akamgeukia. “Nakushukuru.” Ozi akacheka. “Usiku mwema Naya.” “Asante na wewe.” Ozi akajua ndio safari yakumsindikiza, imeishia hapo. Mwenye mali amerudi.       

Ozi alipoondoka kabisa, akamgeukia Molon aliyekuwa bado amemshika mkono. Akamuona kabisa jinsi alivyobadilika usoni. Akajua ni sababu tu ya Ozi, hakutaka kuligusia hilo. “Pole Malon. Pole sana.” “Asante.” Wakaangaliana. Naya akajiegemeza kwenye mkono huku wakitembea, wakitoka nje kabisa sehemu ya kuegesha magari. “Unarudije nyumbani usiku huu!?” Malon akauliza. “Natumia gari ya baba. Nikiwa nakazi za usiku, mimi ndiye ninayepeleka maziwa na mayai hotelini. Inanibidi kuwahi. Nikishashusha vitu, ndipo nawaomba sehemu yakujisafisha na kubadili nguo. Nikishajitengeneza, ndio nakimbilia kazini.” Naya aliongea huku akicheka. “Unaakili yakufikiria sana, Naya!” Naya akacheka. Malon hakuwahi kuacha kumpongeza kwa kila anachofanya.

“Twende nikurudishe nyumbani, ukapumzike.” Malon akashtuka kidogo. “Nilijua leo tutakuwa wote!” “Natamani Malon. Nina hamu na wewe ya kupita unavyofikiri, lakini nalipa gharama. Ingia kwenye gari, nitakwambia kitu.” Malon akaingia, Naya akaondoa gari. “Ulipoondoka, kila mtu alikuwa kinyume na mimi, isipokuwa baba tu. Sio kwamba baba alikuwa anakubaliana na ninachokifanya, lakini hakuniacha peke yangu. Nimemtia aibu baba yangu Malon, kuliko utakavyohisi.” “Mama ameniambia kwa sehemu.”

 “Sasa hiyo ilikuwa ni kwenu tu. Bado kwenye mabenki, kwa marafiki zako, wasichana tuliokuwa tukikutana nao kwenye mihangaiko yakutafuta pesa, nikiwa na baba! Maneno machafu huko polisi! Kila mahali baba alipokuwa akinisindikiza, tulikumbana na kashfa mbaya sana. Nikaamua niwe namuacha, lakini baba aliacha shuguli zake, akawa akinifuata nyuma kama namlipa!”

“Mbali na yote hayo, katika hayo mahangaiko, sijui ni kuchoka au vipi, nilijikuta nikimwambia tuliishi wote kuanzia kidato cha tano. Natamani ungeona macho yake na uso wa kumsaliti.” “Bado wao walikuwa wakijua ulikuwa ukiishi hosteli!?” “Ndivyo nilivyowawekea mazingira ya kuamini naishi hosteli. Baba na mama wasingeruhusu hata iweje niishi na wewe bila ndoa. Baba aliumia sana. Japokuwa alinitetea kwa mama, lakini aliumia sana. Hakusema, kama unavyomjua baba. Lakini aliumia sana, ni kama alinilaumu kwa kumdanganya. Lakini Malon, baba alinisamehe bila kuomba msamaha, nikamdanganya nikamwambia tulikuwa na mpango kamili wakuja kuona ili tu kumtuliza. Najua alijua ni uongo kwa sifa alizokuwa akisikia juu yako, lakini Malon, baba amerudi kusimama na mimi.”

“Hii kazi ninayofanya ya usiku, baba na mama hawaifurahii hata kidogo. Lakini baba ameniambia ananiruhusu, kwa kuwa ananiamini. Kwangu hilo sio neno tu. Naona amenipa dhamana kubwa mno. Kwa jinsi alivyohangaika na mimi wakati haupo, sina jinsi ya kulipa fadhila kwake, ila kuwa mwaminifu. Nilikuwa nikilia usiku, siwezi kulala. Anakuja, anakaa na mimi. Nikiwa kwenye kufunga, anafunga na mimi, na anahakikisha tunapata muda wa kukuombea pamoja. Amesimama na mimi, kuliko nilivyostahili. Najiona ninajukumu, na ninawajibika sana kwake. Naona ninawajibu wa kuwa kile anachotamani kukiona kwangu. Ni ngumu mno, lakini najitahidi Malon. Naona ni garama ndogo yakulipa kwa yale aliyonitendea baba. Lakini sio kwamba sikutamani, au sina hamu na wewe, nina hamu na wewe sana. Lakini nilazima baba anione nimerudi kulala kitandani kwangu usiku huu, akijua wewe upo, na kesho pia niweze kumtizama machoni kwa amani.” Malon kimya.

Hawakuongea tena mpaka walipofika Kunduchi nyumbani kwa Malon. “Uliwasha AC sasa?” “Kulikuwa kuna hewa nzito, fukuto, nikawasha.” “Umekula?” “Nilikuta mama anamalizia kupika. Nilikuwa na njaa, Bale aliponikaribisha, sikujivunga. Nikala. Kwa hiyo nipo sawa. Wewe nenda kapumzike, kesho nitakuja nyumbani mchana.” “Sawa. Nakupenda sana Malon.” “Najua Naya. Asante.” “Naomba nikubusu ndio nikalale vizuri.” Malon akacheka. Akashuka kwenye gari, akaenda upande aliokuwa amekaa Naya kama dereva. Akafungua mlango, akamgeuza. Alimkumbatia tena kwa nguvu, ndipo akaanza kumbusu.

Walikaa hapo wakipeana mabusu kwa muda mrefu. Naya alipoona anazidiwa, akaamua kuondoka. Lakini wakati amemkumbatia ili wote watulie kwanza kabla hajaondoka, maana hata Malon hali ilishaonekana mbaya haswa, Naya ndio alikuwa akihangaika mwilini mwake na kumuamsha tamaa vilivyo. Wakaamua kutulia kwanza huku wamekumbatiana tu bila kuendelea kupapasana, Malon alimsikia akiweka kitu mfukoni kwake. Akajua anamuwekea pesa. Akajisikia vibaya sana lakini hakuwa na jinsi. Alitoka jela hana pesa kabisa na hakujua hali itakuweje huko benki kwenye masalio yake. Naya akaondoka kurudi kwao.

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

Hata mama yake hakuamini aliposikia gari linaegeshwa nje kisha mlango kugongwa. Kila mtu alimka kutoka kuangalia. Wakajua labda wamegombana. Naya aliingia na kicheko. “Nimemuona Malon, baba.” “Yuko wapi?” “Alinifuata kazini, nilimkuta nje ya ukumbi akinisubiri. Hatujaongea sana. Wote tumechoka. Nimemrudisha kwake Kunduchi, amesema kesho atakuja hapa mchana.” Naya aliweza kuona furaha usoni kwa baba yake. “Asanteni sana kwa kuwa na mimi wakati wa matatizo. Bale asante sana. Mama, nakushukuru kwa kila kitu. Na dogo, asante kwa kunifulia na kusaidia kazi za humu ndani. Wewe baba, sijui niseme nini!” Naya akaanza kulia.

          “Samahani kwa kukufedhehesha baba yangu. Asante kwa kuwa na mimi. Nahisi ningekuwa peke yangu, ningechanganyikiwa, na wala nisingeweza kumtoa Malon. Ulisimama na mimi japo ulikuwa hukubalini na maamuzi yangu. Asante baba yangu.” Baba yake akacheka. “Naya aking’ang’ania jambo huyu!” Bale akaongeza. “Katuzungusha vichwa wanaume wote humu ndani tukabaki tunamfuata tu yeye nyuma!” Naya akacheka. “Muone kinavyocheka!” “Nimefurahi sana kumuona Malo, mama. Nampenda Malo.” “Mhh!” Mama yao akaguna, nakurudi chumbani. Naya alijua wazi mama yake hamtaki tena Malon. Anatamani atamke waziwazi, lakini ni kama aliyejionya. Kila mtu akaenda kulala.

 Jumamosi.

     Kwa umbali aliokwenda baba yake, bado Naya akaona anawajibika kuwa mkweli kwa baba yake. Asubuhi akaamka na kumfuata bandani kwa ng’ombe. Baba yake kwa kumtizama tu, akajua ana jambo. “Nikusaidie nini?” Naya akauliza. “Anza kupima maziwa na kuweka kwenye ndoo yake.” Naya akaanza kupima maziwa. “Nimepata tangazo la kwenye tv.” Naya akaendelea. “Wanalipa pesa nyingi baba.” Baba yake alijua kuna kitu kinachofuata. “Na itakuwa ndio mwanzo wa kufanya kazi nao.” Akanyanyua kichwa na kumtizama. “Mbona ni kama nasikia kuna ‘lakini’ hapo kwenye hayo mazungumzo yako, halafu unazunguka tu.” “Ni Henhen.” Baba yake akabaki akimtizama.

“Ni bia ya Henken.” Akarudia Naya. “Wanasema nina urefu mzuri, halafu walipenda lile tangazo nililolifanya la benki. Sema hawa wanalipa pesa nyingi zadi.” “Kwa hiyo sasa hivi unatafuta pesa kwa njia yeyote ile?” Kimya. “Umbali gani upo tayari kwenda ili kupata hizo pesa?” “Nitangazo tu baba!” “Unatangaza kitu usichokijua?” Kimya. “Au umeanza kunywa?” “Hapana baba jamani!” “Kwa nini wewe hunywi?” “Pombe!” Naya akashangaa. “Mbona unashangaa wakati unataka kwenda kuwauzia wenzako? Wewe hutaki kunywa, kwa kuhofia mdhara yake, leo unaenda kuwapa wenzio pombe! Ukishapata hizo pesa unataka kufanyia nini?” Kimya. “Na utakuwa na tofauti gani na biashara ya bangi aliyokuwa akifanya Malon?” “Basi baba, nitaendelea na matangazo mengine.” Baba yake akaendelea na shuguli zake bila hata kuongeza jingine na Naya naye akanyamaza. 

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

     Mida ya mchana wakati wapo tu nyumbani, Malon akagonga mlango. Malon huyu wa safari hii hana gari anatembea tu na kutumia daladala. Mdogo wao mdogo akamfungulia. “Karibu Malon.” Akaingia ndani. Akamsalimia mama yake Naya. Wazi alionekana kutomfurahia kabisa. Hata Malon alijua mambo yameharibika na hapo. “Naya yuko huko nyuma anaosha gari na baba yake.” Mama Naya alimwambia mara tu baada ya kuitikia salamu wala hakuonyesha kutaka habari nyingine. “Naweza kwenda?” “Nenda tu.” Malon akatoka.

“Baba Naya!” Naya aliigiza sauti ya mama yake. Baba yake akageuka akiwa kwenye banda la ng’ombe, Naya anaosha gari pembeni. Baba yake akaanza kucheka. “Sijui mnatumiaje hii gari na wanao  bwana! Inanuka maziwa kama tupo zizini!” Naya akaendelea kumwigilizia mama yake nakumfanya baba yake aendelee kucheka. “Umempatia kweli!” Wakacheka. “Haya baba Naya, gari yako hiyooo, safi. Mama Naya hana chakulalamika tena. Sasa hivi unaweza kumpeleka kokote utakako.” “Asante mama yangu mzazi. Sasa nani anapeleka maziwa?” “Mwambie Bale, baba. Na yeye siku hizi anajua pia kuendesha.” Naya akapunguza sauti. “Tena mlazimishe.” “Kwa hiyo wewe utapika?” Baba yake akamuuliza nakumfanya Naya ajirudi. “Mimi naona nipeleke tu maziwa.” Wote wakacheka.

Malon alikuwa amesimama nyuma yake akimsikiliza na kucheka. Akamuona baba yake anaangalia nyuma yake akiendelea kucheka. Naya akageuka. Akamuona Malon. “Malon!” Naya akashtuka, akamkimbilia na kumkumbatia. Hakumbusu. “Karibu.” “Asante.” Bado walikuwa wamkumbatiana. “Leo unaonekana umelala vizuri, usingizi umeisha. Sio kama jana.” “Nimeamka muda sio mrefu.” “Tokea jana!?” “Nilikuwa nimechoka Naya, zaidi mawazo.” “Pole. Umekula sasa?” “Nilikuta mayai kwenye friji, nikayapika. Nimekula mayai na soda.” “Sasa twende ukale ugali, maharage na nyama ya kukaanga. Bale amepika. Ni vitamu hivyo! Si unajua maharage yaliyo lala?” Malo akaanza kucheka. “Matamu, usiombe kulamba mwiko!” Usemi wa Naya. “Nimsalimie kwanza baba na kumshukuru.” “Twende kwa baba Naya.” Wakaongozana, Naya akiwa amemshika mkono.

Malon akasalimia. “Karibu.” “Asante.” Mikono michafu hii, nilikuwa nasafisha vyombo vya kuku, Naya maneno mengi kanifanya nisahau kuosha mikono, nimesimama namsikiliza tu yeye.” Malon akacheka. “Karibu sana, na pole kwa matatizo.” “Naomba nikushukuru kwa dhati na nikuombe radhi kwa kule ulikopitia na Naya, ili kunisaidia nitoke. Samahani sana na ninakushukuru.” “Lakini Malon, wewe ni kijana. Tena bado ni mdogo sana. Badili maisha yako. Badili kabisa. Itakuwa ngumu, lakini utaishi kwa amani.” Naya akainama.

“Nitabadilika baba yangu. Sasa hivi naahidi kubadilika.” “Unahitaji kupumzika Malon. Kwa jinsi nilivyosikia, unahitaji kubadilika ili upumzike.” Malon akanyamaza. “Naamini tutapata muda wa mazungumzo zaidi. Nenda kale.” “Twende Malon.” Naya akamwita kwa upole. Wakaondoka pale.

“Nakupenda Malon.” “Na mimi nakupenda sana Naya. Inawezekana nimeishi maisha mabaya sana, nikashindwa kukuonyesha jinsi ninavyokupenda. Au inawezekana nimefanya maamuzi mabaya mengi maishani, lakini Naya, sikukosea kuhangaika mpaka ukanikubali. Katika yote, naona wewe ni maamuzi pekee na ya maana niliyofanya hapa duniani.” Naya akacheka. “Sasa si unioe tu Malon!” Malon akamtizama Naya asiamini. “Naya!” “Kweli Malon. Unanipenda na mimi nakupenda. Sasa kwa nini hunioi tu.” “Nakulisha nini Naya? Nakuweka wapi? Hata wazazi wako hawawezi kukubali.” “Wewe unataka kunioa?” Naya akamuuliza taratibu tu. “Tunaweza kwenda sehemu tukazungumza?” Malon akauliza na yeye bila ya kujibu swali la Naya. “Tutoke wote wakati napeleka maziwa mjini. Lakini twende ukale kwanza.” Wakaingia ndani. 

“Mimi ndio napeleka maziwa.” Bale akaanza. “Mimi nimeshawahi.” Naya akamkatalia. “Umewahi wapi wakati sasa hivi ndio tupo hapa wote?” “Kamuulize baba.” “Ili akutetee? Leo mimi ndio napeleka maziwa.” Bale na Naya wakaanza kubishana. Malon na wengineo wapo kimya wanawasikiliza. “Nimewahi mbele yako na wengine wamesikia, mimi napeleka maziwa.” “Mimi nishamwambia baba ndio napeleka maziwa. Kama unabisha, kamuulize baba.” “Wewe unakimbia kupika.” “Ndiyo.” Naya hakubisha, mpaka mama yake akacheka na kutingisha kichwa kama nayesikitika. “Basi leo ujue unapika.” “Mimi ndio napeleka maziwa.” Wakaendelea kubishana, mpaka baba yao akaingia.

“Hamuoni hata aibu nyinyi!?” Baba yao akawauliza kwa kuwashangaa sana. Wote wakasimama kwa kushindana na kumkimbilia baba yao. “Eti baba nani anapeleka maziwa leo?” Naya akauliza. “Mimi nimewahi baba. Kila mtu amenisikia.” Bale akawahi kabla baba yake hajajibu. “Naya ndiye anayepeleka maziwa. Alishawahi tokea nje.” “Nilijua tu utamtetea Naya! Mama sasa mbona wewe husemi!?” Bale akamgeukia mama yake akilalamika. “Leo ni jumamosi. Nataka kula chakula kizuri, ndio maana nimenyamaza, nikijua atakayeshinda ni Naya tu. Aende, wewe ubaki upike.” Mpaka Malon akacheka. “Hata kama umenitukana mama, lakini nakushukuru sana, leo kuwa upande wangu.” Naya hakujali.

Bale akaondoka, Naya akaanza kucheka. “Ucheke hivyo hivyo hata ukiachika kwa kutojua kupika.” Bale akafunga mlango wa chumbani kwake. “Ni nyinyi tu watu wa nyumba hii hamfurahii chakula changu. Watu wengine wote wanapenda chakula changu.” Kila mtu akaanza kucheka. “Siamini baba kama mpaka wewe unanicheka!” “Mimi nimefurahi na yangu mama. Kwani ukipika humu ndani ni nani anayekula?” “Wewe peke yako.” Wakazidi kucheka. “Bwana chakula cha Naya, ni heri ukalale na njaa, au unywe maziwa basi.” Zayoni akaongeza nakufanya wazidi kucheka.

“Hamna shida. Bora huwa naivisha.” Wakazidi kucheka. “Acheni dhambi jamani! Kwani huwa hakiivi?”  Wote wakazidi kucheka. Bale akatoka chumbani. “Kikiiva, basi ujue hakina ladha. Na kinaweza kikawa na ladha ya chumvi kali, mpaka hamuwezi hata kumeza, halafu pia kinaweza kisiwe kimeiva, au kwa ile chumvi, mkaishia kumwaga, msijue hata kama kiliiva.”

“Muongo Bale! Muone kwanza. Sasa ipo siku nitapika humu ndani, mpaka mnikumbuke.” “Sasa si iwe leo?” Bale akauliza. “Hapana. Tafadhali sana.”  Mama yake akapinga kwa haraka sana.  “Mama!” Naya akashangaa sana, watu wakazidi kucheka. “Wewe tushangaze tu siku nyingine mwanangu. Leo tuache tu.” Wakazidi kucheka. “Siamini mama, na wakati huwa unanisifia!” “Mama huwa anakutia tu moyo. Lakini mmmh!”  Zayoni akaongeza. “Kula mwaya, twende zetu Malon. Usiwasikilize. Mimi ni mwanamke wakuoa sana.” “Huyo mahari yake haitaliwa humu ndani. Nishamtahadharisha baba. Atakuja kudaiwa kabla hata mwaka haujaisha.” Bale aliongeza, Malon akazidi kucheka. “Wivu, tu.”  Wakaendelea kucheka pale, mpaka kijana anayekamua maziwa alipokuja na kuwaambia maziwa yapo tayari. Malon na Naya wakatoka.

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

Walipokuwa wanatoka tu pale, Malon akiwa dereva, simu ya Naya ikaanza kuita. Malon akamuona anacheka kabla ya kupokea. “Joshi!” “Niambie mama.” “Nipo tu. Za mapumziko?” “Namshukuru Mungu. Jana umenichunia simu yangu.” Naya akaanza kucheka. “Unanicheka?” “Nilikwambia jinsi ijumaa zangu zinavyokuwa. Nimekuja kukuta missed call yako leo asubuhi nilipoamka baada ya uchovu wa ijumaa.” “Ungenirudishia simu yangu Naya.” “Basi nikuombe radhi.” “Umesamehewa.” Wakacheka.

“Leo nilihudhuria kanisani kwenye kwaya na yale mambo yetu yalikuwepo.” Naya aliendelea kucheka na kuuliza. “Na leo umefanya vyote? Kujihudhurisha mbele ya kiti cha enzi.” “Mimi tena! Ungeniona usingenitambua.” “Joshi?” “Kali mno.” Naya akazidi kucheka. “Pambio letu?” Naya akauliza huku akicheka sana. “Huwezi kulikosa. Na hilo ndilo lililonitoa jasho.” Naya alizidi kukaukiwa kwa kucheka. “Najua kesho lazima mtalikuta kanisani. Kwani jumapili iliyopita lilikosekana?” Joshi akauliza kama anayethibitisha tu, ila anajua jibu na kumfanya Naya azidi kucheka. “Na kweli tuliliimba.” Naya alijibu huku akicheka. “Yaani jumapili iliyopita nilikuwa naimba huku nakukumbuka nacheka, mpaka baba akaniuliza.” “Ukamwambiaje sasa?” Joshi akauliza. “Nikawasimulia wakati tunatoka kanisani. Kila mtu alikuwa anacheka. Mama anasema wewe mtundu.” “Nikikutana na Mama Naya nitawambia mimi sio mtundu, ila ni katika zile taratibu zetu za ibada.” Naya na Joshi waliendelea kucheka. Naya asijue walipo. Malon dereva.

          Kwa kuwa Malon alishajua ni wapi wanakwenda, hakuuliza. Aliendelea kuendesha, Naya akicheka mpaka machozi huku akiulizana na kujibishana na Joshi. “Hapana, wewe Joshi ni mkimya wa kuonekana tu. Lakini una maneno sana.” “Lakini si kweli au nadanganya?” Naya akazidi kucheka. “Halafu ukiwa kwenye tukio, unatulia kimya kama haupo pale, kumbe unasoma tu! Na nitamwambia Mati.” “Hawezi kukuamini.” Joshi na yeye alijibu huku akicheka. “Na kweli. Sasa unajua nitafanyaje?” Naya akauliza huku akicheka. “Nitafanyaje?” “Sio wewe, mimi. Lazima nije kukurikodi halafu nimsikilizishe Mati.” “Pia hatakuamini. Atahisi umetengeneza tu.” Naya akazidi kucheka. “Tumefika Naya. Sijui nashusha wapi maziwa.” Malon akamshtua. “Joshi, baadaye. Uwe na jioni njema.” “Na wewe naya.” Wakaagana na kukata simu, Naya akiwa amejawa tabasamu usoni. Alipomgeukia Malon, akamkuta ametulia kimya, anamsubiria yeye.

“Samahani. Joshi ni mtundu sana. Haishi vituko.” Malon alitulia tu bila yakujibu. “Twende ndani. Tunapita mlango huo wa nyuma. Au unaweza kusubiri tu kwenye gari, nitashusha maziwa mimi mwenyewe.” “Wewe ongoza njia, mimi nibebe.” Wakashuka. Siku hiyo walikuwa wakipeleka maziwa kwenye hoteli moja tu. Hawakuwa wakisambaza mayai wala nyama ya kuku. Naya akaandika sehemu, wakatoka.

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

“Unataka twende sehemu tukakae kidogo kabla ya kuagana?” Naya akamuuliza kwa upendo, Malon akanyamaza kidogo. “Upo sawa mpenzi wangu? Mbona umekosa raha?” “Hapana, nilikuwa nikifikiria ni sehemu gani nzuri tunaweza kwenda kukaa tukapata muda wa mazungumzo.” Naya akatulia na yeye. Malon akamtizama. “Nakupa muda wakufikiria.” “Wewe huna pendekezo?” “Popote. Mimi sitajali.” “Lakini unakumbuka Malon huyu amefilisika? Sina pesa yakukupeleka popote.” “Kama ungekuwa na pesa, ungetaka kunipeleka wapi?” Naya akauliza kwa upendo tu, kwani alishamuona amekasirika. Akajua ni ile simu aliyokuwa akizungumza nayo.

“Eti Malon?” “Sijui. Popote ambako wewe ungependa.” “Mimi nataka kuwa na wewe, Malon. Sitajali ni wapi tutakuwa, ilimradi tuwe wote.” Malon akatulia kidogo. “Labda twende Kunduchi.” “Sawa.” Malon akaondoa gari. Ukimya wakati wakielekea Kunduchi. Naya huyu aliyekuwa akicheka na Joshi, siye huyu akiwa na Malon. Ukimya mpaka wakafika nyumbani kwa Malon. 

Hakuna Msiba Usio na Mwenzie.

Matarajio ya Malon hayakuwa hivi. Akiwa ameshikiliwa na polisi, alikuwa akipata habari zote ya kinachoendelea mtaani. Polisi waliokuwa wakiingia zamu, walikuwa wakimwambia kwa kumuumiza tu. Vile rafiki zake walivyokimbia na kila kitu chake. Baadaye akapewa maendeleo ya ile nyumba yake. Kwa hiyo alijua amepoteza kila kitu, lakini anaye Naya. Alijua atatoka akiwa amepoteza kila kitu, lakini atamkuta Naya wake nyumbani, amliwaze. Lakini Naya huyu amekuja na msimamo mwingine. Hakuna tena mchezo wa hovyo wa mapenzi, anafikiria maisha ya mbeleni.

“Njoo ukae hapa, Malon. Halafu niambie unachofikiria mpenzi wangu.” Naya akamwita kwa upendo. “Njoo.” Malon akabaki amesimama. “Ni nini tena Malon?” “Najihisi labda nakunyima raha Naya. Sidhani kama mimi naweza kukufanya ukacheka kama Joshi. Sikumbuki kuwa na wewe nikakuona au nikafanikiwa kukuchekesha kwa kiasi hicho!” Naya akaona atulie kwanza amsikilize. “Sidhani kama mimi ninaweza kukufanya ukawa na furaha kwa kiasi hicho.” Akaendelea Malon, Naya akimsikiliza. “Njia nzima, kutoka Kiluvya mpaka Posta, upo naye kwenye simu akikuchekesha tu! Hukujua ulipo wala upo na nani! Ni kama ulikuwa naye tu pale garini. Sidhani kama mimi ni mtu sahihi unanihitaji kwenye maisha yako.” Naya kimya, akainama kama anayefikiria kitu.

“Sitaki nije kuwa sababu ya  wewe kuwa mnyonge, kukosa furaha na kadhalika. Kwa mfano kukuzuia kufanya mambo ambayo unaona kwako ni muhimu.” Naya akamtizama. “Tulizungumza juu ya kutofanya kazi na Ozi. Ukijua ni adui yangu, wewe ukaenda kufanya naye kazi, na naona anakusindikiza mpaka kwenye gari na kukufariji ukiwa umechoka. Mwanaume anayekutaka kwa hali na mali, ameniweka mimi jela, huku nyuma ndio anageuka kuchukua nafasi ya mbele kabisa! Kwangu sio sawa Naya, inaniuma kuona unashirikiana na watu walioniweka jela. Sasa hilo sio tatizo lako, ni langu mimi na siwezi kukuzuia uwe na mahusiano na nani na umuache nani.” Naya akabaki akimtizama.

Kimya. “Nakusikiliza Malon.” “Ndio nimemaliza Naya. Naona ni heri mimi nikae pembeni, nikuache uendelee.” “Sijaelewa. Kwamba unataka tuachane, nisikutafute tena kwa sababu nimecheka na Joshi, na umenikuta na Ozi!?” “Najua umenielewa Naya.” “Unajua Malon, binafsi nimefanya kwa sehemu yangu. Nimefanya haswa. Tokea tumeanzana na wewe, nimefanya kwa nafasi yangu. Mpaka leo nimekaa hapa, nimefanya kwa sehemu yangu. Hata nikiangalia nyuma, sina nilichobakiza kwako. Au hata ningerudishwa nyuma, sina kitu ningefanya tofauti kwako. Nikikwambia nimefanya kwa sehemu yangu, elewa nimefanya Malon. Mchana na usiku kama mwehu. Mitaani na maofisini. Majumbani na kila nilipoweza, nilifanya kwa ajili yako. Tena nikiwa peke yangu, bila ushauri wa kuniambia nifanye nini, zaidi ya kila mtu kunitaka nigeuke, nikukimbie. Siwezi kukufanya unipende, siwezi kukufanya uwe kile ambacho huna na wala hutaki kujifunza uwe.” Naya akaendelea taratibu tu.

“Tokea tunaanzana, umekuwa na mahusiano ya wanawake wengine wengi, mbali na mimi. Kila nilipokuwa nikikufumania, ombi langu lilikuwa moja tu kwako, naomba unichague mimi, badala ya unayofanya. Nikakupa mpaka mwisho wangu. Nikakwambia, ukirudia tena ndio uthibitisho kuwa umechagua wanawake wengine na maisha yako, umenikataa mimi. Malon, ulienda kulala na Loi, na  bado ukaniletea anifanyie kazi. Nikaingia aibu mbele ya watu. Nalo nikalisamehe. Siku  ninakuahidi kuwa nitasimama na wewe, kamwe sitakuacha, tukiwa ndio tumejua nani yupo kinyume na wewe, ndio ukafungwa jela.” Naya akaendelea.

“Nikaanza kuhangaika kama mwehu. Matokeo yangu yametoka, nimefaulu, wote nyumbani wanafurahia matokeo yangu, lakini sikuwa na muda wakukaa chini na kufurahia, akili na mawazo yangu, ni kutafuta pesa ili nikutoe jela. Malon, nimefanya kazi zakujidhalilisha, ili nipate pesa. Nilichukua kazi ya kuwa dereva wa mtoto wa Ino, ambaye ananidharau kupita kiasi, ili tu nipate pesa. Ozi ambaye nilimkataa, ilibidi kujirudi kwa heshima zote, ili tu, wanipe kazi, na nikawapa wazo la bure la biashara, ambalo sasa hivi linamwingizia pesa nzuri tu dada yake, Madamu Vane, ili tu, wanipokee, niweze kufanya kazi kwao, na hapo hapo niuze zile nguo tulizokuwa tumebakisha kiwandani.”

“Kila mtu, mpaka baba yako mzazi, aliniambia ule ndio wakati wakuondoka na kuanza maisha yangu, kwa kuwa Malon, hujawahi na huwezi kuwa na mahusiano na yeyote. Akaniambia hata mahusiano na wazazi wako yalikushinda, nisikusubiri, kwa kuwa huna kitu chakunipa. Niliuza kila kitu changu. Mpaka simu ya mkononi uliyokuwa umeninunulia. Nikanunua hii ya kawaida tu. Napiga na kupokea simu na jumbe za kawaida, basi. Nimepata ile pesa niliyokusanya kwa kuuza mali zote mpaka dhahabu ulizokuwa ukinipa, na kufanya kazi asubuhi na mchana, kwa Ino na mkewe, kama dereva wa mtoto wao, na masimango ya gari, na usiku kwenye mahoteli nikifanya kazi bila kuchoka, kwa ajili yako Malon. Nimekwenda umbali mkubwa sana, hata kwenda kinyume na maadili ya kwetu, kutangaza vileo, ili tu, nipate pesa, nikutoe jela.”

“Nilipobakisha milioni 2, na muda unazidi kwenda, nikarudi tena kwa Ozi. Nikamkopa hiyo pesa, kwa makubaliano, kila kazi ninayofanya, wasinilipe, achukue ile pesa. Ili tu, kuharakisha kukutoa jela Malon. Nimefanya kazi kwao, kwa muda bila kupata hata shilingi moja, ili tu kulipa deni ya pesa niliyochukua kwa Ozi.” Malon akazidi kuumia.

“Mpaka majuma mawili yaliyopita, ndipo nimepata kazi ya matangazo. Na yeye akapata kwenye kampuni hiyo hiyo, tupo naye huko. Hapo ndipo nikaanza kulipwa pesa nzuri, nikaweza kumalizia deni la Ozi.”

“Ilinibidi kurudi kwa Joshi, ili anisaidie kumpata Mwanasheria kutoka kwenye ofisi anayofanya kazi. Mungu bariki akanikutanisha na Mati ambaye amekuwa kama kaka. Nilikwambia tokea mwanzo, Joshi ni mcha Mungu. Mwadilifu wakutosingizia. Vichekesho vyake, maneno yake mengi, ni mambo ya kanisani. Hata ofisini kwao wanamjua hivyo. Sitaweza kuomba msamaha, wakufurahia maongezi yangu na Joshi. Sitakuomba msamaha wa kucheka, kwa kuwa hata Mungu anajua, nahitaji kucheka Malon. Nimelia mno. Nimelia mchana na usiku nikikulilia wewe Malon.”

“Nimefunga, bila kula wala kunywa, nikimsihi Mungu akulinde kule ulipokuwa na anipe nguvu yakuweza kukusaidia. Sitaomba msamaha kwa kufurahia juhudi zangu. Iwe umeridhika na nilichokufanyia au la, lakini nikiangalia nyuma, binafsi najipongeza. Najiambia naweza kufanya chochote kile endapo nikiamua, hata kama mazingira yakisema hapana au watu wote wakinipinga. Najiambia mimi Naya, nikisimama na kuamua kufanya jambo naweza kufanya chochote, hata kama ni kigumu vipi, nitafanikiwa tu.” Malon kimya.

“Ila pengine, natakiwa kukuomba msamaha kwa kutokuwa na kiasi cha mazungumzo kwenye gari. Nilipitiliza mazungumzo na Joshi, napo nahisi ni kwa kujisikia vibaya kushindwa kupokea simu zake jana, wakati yeye alikuwa akipokea simu zangu hata usiku, wakati ninaomba msaada wa kunisaidia nikutoe jela.”

“Nasikitika nimeuza kila kitu chako, isipokuwa hii nyumba yako Malon. Ni kwa kuwa sikuwa na jinsi. Nilifanya nilichoweza kwa wakati ule nilipokuwa nimechanganyikiwa na sijui chakufanya. Nasikitika nimeomba msaada kwa adui zako Malon. Lakini ni kwa kuwa nilifika mahali, nilimshika kila niliyejua anaweza kunisaidia. Mungu akageuza hata mioyo ya adui zako, wakafanyika msaada. Nasikitika kushindwa kufuata maonyo yako juu ya wanaume wanaonitongoza, lakini nafikiri ni kwa kule kujiamini kwangu na msaada wa Mungu ambao amenijalia mpaka leo hii nazungumza na wewe, ni wewe peke yako ndiye mwanaume pekee niliyeweza kukaa uchi mbele yako na kufanya mapenzi. Mpaka sasa hivi ninazungumza na wewe, midomo yangu, haijui busu la midomo ya mwanaume mwingine isipokuwa wewe tu. Mikono yangu, haijawahi kumkumbatia mwanaume mwingine kimapenzi, au hata kawaida, mbali ya wewe na baba yangu mzazi.”

“Sasa naomba nikusaidie hivi Malon. Nimeamini na kuelewa kuwa, huwezi kunipa kitu ambacho huna. Nakiri kuwa nimekuwa mbinafsi na kushindwa kukufikiria. Nilidhani vile ninavyoweza kufanya mimi, ni rahisi sana, kuwa kila mtu anaweza kufanya. Kumbe ni kwa neema na rehema za Mungu. Si rahisi ki hivyo. Japokuwa nimekupenda sana. Nimekuwa mwaminifu kwako hata pale ambapo hukustahili uaminifu wangu na upendo wangu, leo umenihakikishia yale aliyosema baba yako na watu wengine. Huwezi kunipa ninachotaka, na wala nisisubiri tena. Nashukuru Mungu umenitamkia wewe mwenyewe. Nilikataa kusikiliza kila mtu, kwa kuwa nilikuwa na tumaini kutoka kwako. Nilijua ukitoka, tutaendelea mimi na wewe. Leo unanitamkia huwezi kuendelea na mimi kwa sababu nimecheka na Joshi, na kwa sababu umenikuta natoka kazini nikiwa nimechoka, na Ozi! Najua hizo ni sababu tu Malon. Ukweli halisi unajua wewe mwenyewe moyoni mwako.”

“Sijakasirika Malon. Na wala sitalia tena. Nimekulilia vyakutosha! Nimekusubiri vyakutosha Malon. Hujawahi na wala hutakuja kuwa wangu. Hunidai, sikudai. Kila kitu ulichowahi kunipa, mali zako, elimu na ujuzi wote ulionipa, nimetumia kukusanya pesa za kukutoa jela. Kwa pesa yote niliyokusanya tangia ufungwe, sijamnunulia baba yangu hata shati, zote nimekulipia wewe. Nimeuza dhahabu zote, ulizoninunulia. Simu, viatu, nguo nilizokuwa nazo huku Dar vyote niliuza, maana zile za Morogoro ziliibiwa pamoja na milango na madirisha. Kiwanda niliuza. Mashine, nguo nilizokuwa nimetengeneza kwa pesa yako, niliuza.”

“Ada uliyokuwa unanilipia shuleni, na kuniweka hapa mjini nikafanikiwa kufahamiana na watu zaidi, pia nimetumia kupata pesa. Ujuzi ulionipa wa kuendesha gari na leseni uliyonitafutia, nimetumia kupata kazi ya manyanyaso na dharau ya kumuendesha mtoto wa Ino. Vyooote nilifanya kwa juhudi zangu zote, nikakusanya pesa yote, nikampa Mati. Akulipie dhamana. Hiyo sina risiti yake ila ninazo risiti za kulipia kampuni yao kwa ajili ya huduma za kisheria walizokupa mpaka ukatolewa jela. Ila sitakupa, ukitaka kuhakikisha kama pesa yako iliingia hapo, nenda kwenye ofisi zao, Joshi ni muhasibu, atakupa kopi. Hakika Malon, hunidai, na mimi sikudai. Pesa yako yote na mali zako zote, vimekusaidia kukuweka huru. Tumia uhuru wako utakavyo Malon. Nakuombea kila la kheri.”

Naya akataka kutoka, akarudi. “Tafadhali, usirudi tena nyumbani kwetu. Utamuumiza zaidi baba yangu niliyekuwa nikihangaika naye mchana na usiku, tukifunga na kuomba kwa ajili yako. Nimemzungusha asubuhi na usiku kwenda nakurudi Morogoro, nikihangaika naye kwenye maofisi ya watu nikisaka pesa kwa ajili yako. Alikuwepo siku naonywa na baba yako juu ya hili unalolifanya kwangu sasa hivi. Na baba akanikumbusha kuwa yeye Mzee Saduki ni baba yako, hana sababu ya kukusingizia. Mimi nikambishia, nikamwambia Malon kwangu ni tofauti. Msichana mwingine wa benki. Ulilala naye yeye na mdogo wake, akanionya kuwa, nisifikiri mimi ni watofauti kwako. Yaliyowapata wao, na mimi yatanitokea. Na hapo baba alikuwepo.”

“Inawezekana kwako isiwe na maana, kwa kuwa ndio maisha yako hayo umezoea kuishi. Lakini nakuomba Malon, acha mimi mwenyewe nitatafuta hekima yakuzungumza na baba yangu ili asijisikie vibaya. Maana kuna siku aliniambia, ‘naumia kukusindikiza. Ni kama najiona, nakupeleka kwenye kujiangamiza’. Naomba usifike kwetu, ili niweze kuwajenga familia yangu, waelewe vile nitakavyowajenga mimi bila kuwaumiza juu yakuvunjika mahusiano yetu ambayo mimi nilijua yapo. Nakutakia kila la kheri Malon. Mungu wangu akubariki.” Naya akachukua funguo zake za gari, na pochi, akatoka na kumuacha Malon amesimama.

 Kwa Naya!

S

wali ni kuwa atamwambia nini baba yake juu ya Malon! Akarudi nyumbani nakuanza kushusha vyombo vya maziwa. Ile purukushani nje, mama yake akamgeukia baba yake. “Naona huko nje ndio kunapambazuka. Naomba ukapatulize, huu usiku wa leo watu tulale, kesho tuende kanisani tukiwa tuna akili safi.” Bila yakuongeza neno, baba Naya akatoka. Alimkuta Naya ameloa kila mahali kwa kuosha madumu ya maziwa tu. Akabaki amesimama anamtizama mwishoe akaona amsaidie. “Naona sabuni yote imeisha na yenyewe yatakuwa yametakata.” “Bado yanaharufu ya maziwa.” Naya alijibu huku akiendelea kuosha. “Labda kwa sababu ni ya kubebea maziwa.” Baba yake akaongeza kama kujaribu kumkumbusha. Naya akaendelea kuosha. 

Baba yake akatafuta sehemu akakaa, huku akimwangalia. Naya aliosha kwa kurudia rudia. Akamaliza, akaingia kwenye mabanda ya kuku. Akaanza kuosha vyombo vya maji wakati huwa vinaoshwa asubuhi. Giza lilikuwa limeshaingia. Baba yake akabaki akimtizama. Aliosha na kuosha. Akarudia tena na tena. “Kesho tunakwenda kanisani?” Akamtupia swali. “Nakwenda.” Naya akajibu huku akiendelea kuosha. “Na jumatatu asubuhi si unakwenda kazini kama kawaida?” “Naacha kazi kwa Ino.” Naya akajibu kwa ukali. “Hutaki tena pesa?” “Sina sababu ya kujiabisha tena. Kwanza nilifanya sababu ya Malon. Sasa Malon ameshatoka, naona nibakiwe na kazi ya jioni tu. Asubuhi nitakuwa nakusaidia kazi za huku mabandani.” “Umemwambia Ino?” Kimya. Naya akaendelea kuosha.

“Naya?” “Nitamwambia kesho kanisani.” “Basi ni lazima jumatatu uende kazini. Ukamchukue mtoto, umpeleke shule na kumrudisha. Mpaka wapate mtu mwingine. Huwezi ukawa unatumia watu hovyo.” “Si nilimuomba mwenyewe kazi?” “Sawa sawa. Sasa utaiacha kwa utaratibu mzuri. Huwezi ukakurupuka tu eti kesho jumapili unawaambia kwa kuwa Malon ametoka jela, sina tena shida na pesa yenu, mtajijua wenyewe na mtoto wenu hiyo jumatatu.” Naya akasimama na kumwangalia baba yake.

“Wewe ni zaidi ya pesa ya siku moja. Hujakuzwa kutumia watu. Eti ukiwa na shida ndio unatafuta watu, shida zako zikiisha, unaacha kazi! Tena unaacha kiholela tu! You are better than that Naya. Na huishi hapa duniani kwa kumtumikia Malon. Mungu alishakutumia kumtoa Malon kutoka jela, inawezekana kazi yako kwa Malon ndio ilitakiwa iishie hapo. Basi. Sasa weka akili yako sehemu nyingine.” Yakaanza kumwingia. Akaacha kila kitu akaenda kukaa pembeni ya baba yake.

“Maisha yako hayajawahi kuwa ni kwa ajili ya Malon tu. Pengine ile ilikuwa ni njia kubwa na ya pekee Mungu alitaka kukufungua macho! Alimtuma Malon kwako ili kukuonyesha kuwa unaweza kufanya mambo makubwa sana. Ndani ya miezi miwili, wengine wakilia shida. Nchi hiii hii. Wewe umesimama peke yako. Wengine wote tukikupinga, ukakusanya mapesa yote yale! Mamilioni ya pesa! Leo unakuja kuniongezea bili ya maji na kushindwa kujitambua!” Naya akaanza kucheka. Akamuegemea baba yake.

“Una uwezo mkubwa sana Naya. Acha kujishusha na kukubali kupotea kijinga. Kama umeanguka, simama kwa haraka. Jikung’ute na uendelee. Simaanishi upuuze maumivu, lakini usikae hapo muda mrefu, unatupa kila kitu eti kwa sababu umeumia! Hapana. Tena uzuri ni kuwa hakuna geni linalokutokea sasa hivi, ambalo hukutarajia. Ulijua inaweza kukutokea hata wewe.” Baba yake akaongea kwa wazi kabisa. Naya akajua amejua kama ameachwa tayari kama wengine waliosikia walikuwa wakiachwa na Malon. Akajisikia vibaya nakushindwa hata kuongeza. Akainama. Kimya.

 “Umekula?” Naya akapandisha mabega kukataa. “Sasa kabla hujaua kuku kwa kiu, warudishie maji yao ndani. Tena uweke na ile vitamini. Halafu twende ukale, ukalale. Kesho asubuhi tunawahi kanisani. Huko ndiko ukamwambie Ino, unampaka week moja, atafute dereva wa mtoto wake, wewe unaacha kazi. Halafu ukirudi hapa, uniambie badala ya kazi ya Ino, utakuwa ukifanya nini chakukuingizia pesa.” “Si nitakuwa nikikusaidia huku!” “Hapana Naya. Unajua wazi kuwa huku nikujificha. Hapa hamna kazi yakufanya. Naomba usiku wa leo uanze kufikiria, kesho unipe jibu.” Naya akanyamaza.

CONVERSATION

0 Comments:

Post a Comment