Naomi Simulizi |+1 205 767 8163 |naomisimulizi@gmail.com Mapenzi&Pesa! – sehemu ya 7. - Naomi Simulizi

Mapenzi&Pesa! – sehemu ya 7.

Akiwa njiani kurudi nyumbani kwao Kiluvya, akijua kwa hakika amefika mwisho na Malon,  Naya akaanza kuwaza hili na lile na kitu chakufanya. Bado hakuwa na cheti cha kuombea kazi, lakini alijua nilazima kufanya kitu kujiongezea kipato. Njia nzima alikuwa akiandika hiki, nakufuta. Biashara hii, anafuta. Mpaka anafika kwao alishakuwa ameandika biashara tatu, na zote zilihitaji sehemu nzuri, na mtaji. Mawazo yakamrudisha kule kwenye nguo. Akajua ni pesa ya Malon itakuwa inaozea pale kiwandani. Akajuta na kuumia sana.

Alifika nyumbani kwao akiwa ameshawapigia simu watu kadhaa kuwa yale maonyesho yaendelee. Lakini alimkatalia Ozi asiwepo. Akasaidia shuguli za pale nyumbani kwao. 

Akamuomba baba yake jioni amsindikize kule kiwandani kwake, na anaporudi kutoka kupeleka maziwa huko mahotelini, amuombee maboski. Kama kawaida yake, akamkubalia mwanae bila maswali.

Jioni ya siku hiyo hiyo wakaenda kule kiwandani picha ya ndege, wakamsaidia kuhifadhi vile vitu vizuri. Hasa mashine. Ndugu hao walimsaidia Naya kurudisha kila kitu kwenye maboski ili visiharibike, nakuweka vizuri stoo. Wakasafisha. Akaanza kutoa chuma za kuning’iniza nguo. Ni kweli Naya alikuwa na kipaji cha ubunifu wa mavazi. Nguo zake zilikuwa nzuri. Walimsaidia kuzipanga vizuri ndipo wakaondoka hapo.

Siku inayofuata tena, wakarudi na vifaa alivyotaka Zayoni kumuwezesha kupiga picha. Japokuwa alikuwa mdogo lakini alikuwa mpiga picha mzuri sana. Alijua ni mwanga gani atumie na wapi aweke kitu fulani na akipige picha. Katika safari zake za Uchina yeye na Malon, Naya alimnunulia kamera nzuri sana ambayo alikuwa akiitumia. Akapiga picha hayo mavazi, lakini Zayoni mwenyewe hakuridhika japo wote walipenda picha hizo. “Tungekuwa na mtu anayezivaa, ndio zingependeza zaidi.” Zayoni akatoa hilo wazo. “Basi kesho nikatengeneze nywele vizuri na kucha, mimi mwenyewe nije nizivae, unipige picha.” Wazo la Naya likapita.

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

     Siku tatu mbeleni, Naya na kaka zake walirudi tena pale. Naya alivaa nguo mbali mbali, kaka zake wakimsaidia kupiga picha. Bale yeye ndiye aliyekuwa wakuziingiza mtandaoni vizuri, na kuzipanga. Bale mtundu wa komputa, naye akawa msaada. Malon alishampa zawadi ya komputa na yeye, basi na hapo ikawa msaada. Baada ya juma moja, website ya Naya na Malon ikawa imependeza na inavutia. 

Pesa!

M

alon hakuwa amemtafuta Naya hata kwa salamu. Naya akampigia simu. “Sijui ni muda mzuri sasa hivi?” “Ndio nimerudi sasa hivi nyumbani, naangalia mpira.” “Basi naomba unipigie baadaye ukimaliza.” Naya aliongea kwa upole. “Hamna shida. Tunaweza kuzungumza tu. Nitarekodi.” Naya akaridhia kuendelea. “Unayo laptop yako hapo?” “Kama unataka nifungue sasa hivi, inabidi nikaifuate chumbani.” “Nataka nikuonyeshe kitu.” “Basi subiri kidogo.” Akasimama Malon, nakurudi chumbuni kwake kutafuta laptop.

“Nimepata. Unataka nifungue wapi?” “Fungua kwenye ile website yetu.” “Mimi na wewe!?” Malon akauliza kwa kushangaa kikejeli. Na Naya alijua. “Ndiyo Malon.” Kimya kwa muda. “Waw!”  Akamsikia akihamasika. “Nimekukubali Naya!” Naya akacheka. “Sasa kuna tamasha dogo tu nimeandaa. Angalia chini kabisa. Nimeweka tangazo hapo chini. Nia nikutaka tumalize hizo nguo ili pesa yako isipotee bure.” “Subiri kwanza Naya. Kwanza nani amekufanyia kazi zote hizi?!” Naya akacheka. “Picha ni Kiziwanda. Ametumia ile kamera tuliyomnunulia China wakati ule. Halafu Bale ndio amenipangia kwa website. Mwanamitindo wako ni...” “Naya.” Akamalizia Malon na kuendelea. “Japokuwa hukuonyesha sura yote, lakini hilo umbile hapo pichani nimeweza kulitambua. Kazi yako nzuri mama. Nakupongeza sana.” Naya akacheka.

“Sasa turudi kwenye pesa.” “Nakusikiliza mama.” Malon akasikika kutoa ushirikiano mzuri sana uliomuongezea ujasiri Naya. “Nimepiga mahesabu ya garama zote zitakazohitajika kukamilisha hayo maonyesho. Kama Mungu akitusaidia tukauza kila kitu, faida itakuwepo ila chache. Nimefikiria tufanye mida ya jioni, ambapo watalipia vinywaji vyao wenyewe. Isiwe bure. Halafu yupo mama anatengeneza shanga pale mwenge, nimemuomba aniuzie shanga za miguuni, shingoni, hereni na mkononi kwa bei ya jumla. Ukiangalia kwenye picha niliyokuwa nimevaa kigauni cheupe cha ufukweni, nimezivaa hapo. Hizo ni sample tu. Tukikubaliana mimi na wewe, nitampelekea aina ya shanga ninazotaka anitengenezee kuendana na hizo nguo, kisha na zenyewe tuuze siku hiyo hiyo kuongeza pesa. Kuwa tuwauzie nguo na accesories zake. Unaonaje?”  Akamsikia Malon anavuta pumzi.

“Am so proud of you Naya. Najivunia sana. Hakika umenifurahisha.” Naya akacheka. “Asante Malon. Nimesahau kukwambia, na sandozi za kiume na za kike pia zitakuwepo. Kiziwanda amempiga picha Bale, kwenye sendozi, ila mamiguu yake mabaya, nimemkatalia asiziweke kwenye website, tutakutana nazo tu kwenye maonyesho.” Malon akaanza kucheka. “Yaani wewe na Bale!” “Nasubiri kwa hamu sana liondoke humu, ila limegoma. Na sijui lini linaondoka humu ndani wakati anaweza kabisa akaishi chuoni kama mimi! Anang’ang’ania hapa ndani amegoma kuondoka.” Malon akazidi kucheka.

“Nipo kwenye mkakati wakumshawishi mama amfukuze humu ndani. Akakae huko huko chuoni, ajifunze maisha.” “Umefikia wapi sasa?” “Mmmh! Mama na Bale si walewale tu! Sijafika popote. Ananiambia eti mimi ndio natakiwa niondoke, wakati baba ndio ananitengenezea chumba vizuri! Baba amewaambia hapa mimi ndio nimefika, wala siondoki na wote amewaambia hii nyumba ni yangu.” Malon akazidi kucheka.

“Achana na Bale. Kwa hiyo ndio hivyo Malon.” “Maandalizi yakoje?” “Nimefika pazuri. Sasa hivi natafuta wasichana wawili tu. Sitaki wengi. Ili niweze kuwatumia vizuri, na kuwe na utulivu. Sitaki fujo za wasichana kugombana. Nataka utulivu. Watu ambao sitawaweka pamoja kwa muda mrefu. Wanakuja kufanya mazoezi, na kujaribu nguo, basi wanaondoka. Nitawawekea mazingira ya kazi, na kuheshimiana. Wasichana wakawaida tu, ambao nitawafundisha mimi mwenyewe kama hawa mafundi. Natafuta wanao jiheshimu, sio vitoto vidogo.” Malon kimya.

“Malo!” “Nipo nakusikiliza mama.” “Nitaomba msaada wa Side na ile gari yako tuliyotumia wakati ule.” “Ile nilikodi maalumu kwa ile shuguli.” “Naomba tukodishe tena. Kwa siku mbili tu. Pale ukumbini nilizungumza nao, wameniambia kama hapatakuwa na shuguli siku moja kabla, wanaweza kuniruhusu nipeleke vitu kabla. Ndio hapo nafikiria tupeleke nguo zote na kuzipanga vizuri pamoja na sendozi na hizo shanga.” Naya akaendelea kumweleza mipango.

“Kwa nini tusikodi na huo ukumbi siku mbili?” “Gharama Malo. Nabania matumizi. Sitaki yawe makubwa kwenye hayo maonyesho.  Sitaki itugarimu kama mwanzoni. Nitakutumia na wewe uone. Utaona nimekata garama za muda wa ukumbi, vinywaji, kuweka warembo hotelini, idadi yao, na garama za usafiri. Kwa kuwa kama ni wawili tu, wanaweza kupanda gari yako au ya Side. Sijui kama unanielewa?” “Huofii nitalala nao tena?” Naya akanyamaza.

“Eti Naya?” “Ilimradi wafanye kazi. Hayo mengine yatakuwa makubaliano yenu Malon. Nimejifunza kutochanganya Mapenzi na Pesa. Vilikaribia kutugarimu sisi wenyewe. Huo upande mwingine wa mapenzi, sitaingilia tena Malon. Najua nimekuumiza kwa maneno machafu, lakini najua sina uwezo wa kukubadilisha, au kubadilisha niliyosema. Nina uwezo wakujibadilisha mimi, na nitakachosema baadaye. Nimeyaacha maisha yako ya mahusiano mikononi mwako. Naomba tusikose na Pesa pia. Unafikiri ni sawa?” Naya akauliza kwa upole.

“Nimeona tangazo. Tarehe na muda. Nitatunza ili mambo yasiingiliane. Kwa sasa unahitaji nini kutoka kwangu?” Naya akafikiria kidogo. “Labda mpaka muda ukikaribia nitakuwa nikikwambia. Sasa hivi ni taarifa tu. Pale nilipofikia, ninachofanya na nitakachofanya. Nitakuwa nikienda pale kiwandani. Nafikiria kumtafuta mzee Nyenzo na dada Ida, ndio warudi kazini kwenye kushona, wanisaidie endapo nitafanikiwa kupata hao wasichana wawili watakao tutangazia nguo. Waje wapimwe, na kutengenezewa nguo.” “Wazo zuri. Ukihitaji chochote kile, usisite kuniambia.” “Nitafanya hivyo Malon. Nakutakia jioni njema.” “Asante na wewe.” Wakaagana. Naya akafurahi kuona ameweza kumrudisha Malon kwenye kazi. 

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

     Naya alirudi kanisani na baba yake. Akawa binti wa kanisani tena. Akakuta Ino ameshachumbia. Majigambo ni yaleyale. Kumsifia mkewe mtarajiwa. Naya kimya. Akatafuta wasichana wawili wa palepale kanisani. Alioona wametulia na wana maumbile mazuri. Akazungumza nao, kwa makubaliano wafike kiwandani kwao, Picha ya ndege siku ya jumatatu. Jioni yake akampigia simu Ida kumuomba arudi kazini, akamwambia alishapata kazi sehemu nyingine. Naya akasikitika kumkosa Ida, kwa kuwa alikuwa ametulia sana na mchapa kazi. Akaona ampigie simu mzee Nyenzo. Naye akamwambia ni mgonjwa, yupo kwenye matibabu. Chakushangaza, wote waliokuwa wakiwafanyia kazi, wakatoa udhuru.” Hapo Naya akawa amekwama.

Akampigia simu Malon. “Vipi tena? Mbona umenyongea?” “Mzee Nyenzo mgonjwa, dada Ida ameshapata kazi sehemu nyingine. Na wengine wamenipa sababu ambazo hata hazieleweki. Nimekwama Malon.” “Hata kidogo. Unakumbuka jinsi tulivyowapata hao?” “Mama alinisaidia Malo!” “Sasa, sasa hivi fanya wewe mwenyewe. Usikate tamaa. Mafundi wapo wengi tu. Wale wameshakuibia ujuzi, pengine wameanzisha kitu kama chako. Sasa ni wewe kutokata tamaa. Tafuta watu wengine. Mimi ningekusaidia, lakini naogopa historia kujirudia.” “Hapana Malon. Sitajali hata kama nitafanya kazi na mkeo. Nimeomba tusichanganye mapenzi na pesa. Akija, nitaliheshimu hilo, ilimradi tu uniambie, ili tufahamiane, basi. Tufanye kazi tukiwa tunafahamiana. Nakuahidi sitakuuliza, nitafanya kazi yangu na yeye nitamtaka afanye kazi kwa usahihi, basi.” Kimya.

“Sasa unaye mtu?” Naya akauliza. “Nitaanza kuangalia.” “Nashukuru. Ila inabidi kukazana kweli. Tangazo la tarehe na muda, nimeshasambaza kwa watu wengi na wote wanaonekana kutoa ushirikiano.” “Mwenzio nilianza kutuma kwa watu muda uleule uliponionyesha hata kabla yakukata simu.” Naya akacheka. “Ndio itabidi tukazane sana. Miezi miwili sio mingi.” “Sawa mama. Nipo nyuma yako.” Naya akacheka na kukata simu akiwa anafurahia jinsi Malon anavyomtia moyo.

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

Akawa ameshapata wana mitindo hao wageni ambao wangevaa mavazi yake, lakini hana mafundi. Kichwa kikaanza kuzunguka. Anapata wapi mafundi wakuacha makazi yao, wahamie kiwandani kwao, wamfanyie kazi zake tu yeye, kwa muda huo mfupi! Akatoka tena chumbani akamueleza baba yake na mama yake. Wakabaki wakifikiria. “Sasa kwa kuwa na mimi ni fundi. Na nimeona mafundi wako wanavyotumia hizo mashine zenu za kisasa, naweza kuanza na hao wawili uliowapata, wakati wewe unahangaika na mafundi wengine.” Naya alifurahi sana. “Asante mama yangu. Maana nilishapaniki. Kesho asubuhi nimewaambia waje pale kiwandani.” “Sasa itabidi twende wote. Mimi nikaanze kuzoea hizo mashine. Wakija nitawapima, nienze taratibu.” “Kazini?” “Kazi ipo tu na wewe! Acha kujiongezea matatizo.” Naya akacheka. Na kumshukuru mama yake.

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

     Kesho yake Naya na mama yake wakapanda daladala kwenda kiwandani, wadogo zake kwenda shule, baba yake akaondoka na gari lao likiwa na maziwa na mayai, kupeleka mahotelini, mjini. Naya na mama yake wakatoa mashine, mama yake akaanza kujifunza, huku Naya akipitia michoro yake. Ilipofika saa nne, Malon akaingia. Naya hakuamini. “Mbona unacheka?” “Nimefurahi kukuona hapa. Sikutegemea!” “Umepata fundi.” Naya akacheka, akageuka nyuma, akamuonyeshea kidole. “Mama!” Malon akamuona mama yake Naya nyuma ya mashine yakushonea. “Sina jinsi. Sijapata fundi, na wale wasichana nimewaambia waje leo. Imebidi aache kwenda kazini leo, aje hapa anisaidie.” Malon akacheka. “Ngoja nikamsalimie.” Akatoka ofisini, na kwenda nyuma upande wa kiwandani. Walitenganishwa na hivyo vyumba vya ofisi ambazo zilikuwa mbele, mlango wa kuingilia. 

Malon akaenda kuzungumza na mama yake Naya. Naya akawaona wanacheka kupitia kwenye kioo. Maana juu ya hizo ofisi, kulijengewe kioo, rahisi kuona mafundi wakiwa wanafanya kazi. Akajua mambo mazuri. Akamuona Malon anarudi. “Kaa hapo chini nikupe dili jingine la ukweli.” Malon akacheka huku anavuta kiti mbele ya meza ya Naya. “Siku ile nilipoondoka kwako kurudi huku kwa basi,” “Bila kuaga?” Malon akaingilia. “Nilikuaga bwana. Sema ulikuwa umekasirika sana usiku ule, ulikuwa hunisikii tena. Anyaways, turudi kwenye pesa, naona swala la Mapenzi mimi nimeharibu, ila kwenye pesa, sina mpango wa kuharibu.” Malon akacheka. “Njia nzima nilikuwa nafikiria kitu chakufanya. Nikapata hili wazo.” Naya akampa simu yake.

Jumbe za Ozi zikazidi kuingia. “Naona mpenzi wako anatuma tu jumbe huku!” “Wewe funga. Achana na Ozi. Weka macho yako kwenye pesa.” “Sasa kila nikisoma ujumbe unaingia!” “Basi nipe hiyo simu.” Malon akarudisha simu. Naya akamtumia picha kadhaa. “Nimekutumia kwenye simu yako.” Malon akachukua simu yake. “Nilijua mapenzi umeshindwa, kumbe umeshindwa kwangu tu, kwa mwenzangu Ozi, unaendelea kama kawaida!” “Malon, eyes to the prize. Focus.” Naya akaweka msisitizo kwa Malon akitaka azingatie kwa anachomuonyesha. Malon akamtizama na kurudisha macho kwenye simu.

“Naona chupa nzuri tu za sabuni!” “Sasa, ondoa hayo majina hapo, weka jina letu. Malon na Naya. MaNa.” Malon akacheka. Je, unatafuta sabuni safi ya kuoshea vyombo na Choo chako? Itakayokuacha mikono yako laini na nyororo! Itakayobadili harufu nzima ya nyumba yako hata ofisini na viwandani? MaNawanalo jibu lako. Watakuletea popote ulipo, tena kwa bei nafuu. Kwa mahitaji ya ofisini, viwandani, majumbani, MaNa, ni jibu yako. Changamka, upate Sabuni yako, kwa bei yako!” Malon alikuwa akicheka sana. Hapo Naya alikuwa akitumia sauti ya utangazaji.

“Hapo vipi Malon?” “Mimi mwenyewe nishapata hamu na hiyo sabuni.” Malon alikuwa akicheka kwa furaha. “Sasa je! Acha mchezo, Malon. Lazima kuhamisha pesa ya watanzania wote, tuhakikishe zinaingia na mfukoni kwetu. Matangazo ya sabuni yetu ndio tuhakikishe mpaka watoto wa mtaani wanaimba sabuni zetu tu.” “Mama nimekukubali. Naona na shule uliyosomea wala hukuhitaji. Kipaji kipo.” “Sasa na Malon yupo au bado anahasira?” “Mapenzi na Pesa, au pesa kwanza!” “Hiyo fani ya mapenzi tuwaachie wenyewe kina mzee Saduki, sisi tutafute pesa kwanza.” Malon alizidi kucheka.

“Umenifurahisha sana Naya.” “Ndio tuingie kazini Malon. Kila nyumba nilazima itumie sabuni. Sasa ndio lazima na sisi tuhakikishe wanatumia sabuni za MaNa. Na huo ndio mwanzo. Tutatengeneza mpaka sabuni za kufulia na dawa za chooni. Tujitangaze haswa, na tuhakikishe tunatengeneza vitu vizuri.” “Sawa mama. Mimi nipo nyuma yako.” “Ndio maana nakupenda Malon. Unaamini na kukubali mawazo yangu.” “Ozi?” “Achana na Ozi, Malon. Kwanza nahisi ni kama alitumwa huyu Ozi! Amenikazania, ana habari nyingi, haniachi! Ameniharibia kweli! Achana naye.” Naya akafikiria kidogo kama anayeandika kitu.

“Nimemsikitisha sana baba yangu. Lakini basi tu.” “Kwa nini tena?” “Si mambo ya Ozi! Hakutegemea kama naweza kuyumbishwa kijinga vile, mpaka kufikia kudanganya! Lakini Malon, Ozi alikuwa akiongea kwa makusudi akijua ni nini nataka kusikia. Akafanikiwa kupata sikio langu. Akajiwekea mazingira mazuri mpaka nikamwamini! Sikuwa hivi Malon. Sikuwa mtu wakuyumbishwa na matukio. Nilikuwa nina msimamo sana. Sijui ni nini!? Lakini maadamu nimeshamjua, basi. Na mimi najifunza kutokana na makosa yangu.” “Sasa sasa hivi anataka nini?” Malon akamuuliza.

Naya akamtizama na kucheka kwa kuguna. “Tuyaache tu Malon. Nimefurahi mimi na wewe tupo ukurasa mmoja. Hayo mengine nitahangaika nayo taratibu. Najua nitafika tu.” Malon akabaki akimtizama. “Hata hivyo ndio yalikuwa mahusiano yangu ya kwanza, nilikuwa under pressure. Mambo mengi muhimu na mazito yalikuwa yakiendelea kwangu, kwa wakati mmoja. Najifariji kuwa ninajifunza, pengine mahusiano mengine naweza nisiharibu hivi tena.” Naya alikuwa akiongea taratibu kama anayefikiria huku akichora chini.

“Una mpango wa kuwa na mahusiano mara ngapi mpaka utulie?” “Sijui Malon. Mpaka nitakapopata mtu anayenipenda kama wewe, na kukubali kunichukua na madhaifu yangu.” “Hakuna mwanaume atakayekupenda kama mimi Naya.” Naya akamwangalia nakuanza kucheka.  

“Malon kwa kujisifia!” “Sawa. Mimi si nipo. Tutaona. Turudi kwenye Pesa.” Naya akacheka kidogo nakufikiria. “Endelea mama, nakusikiliza.” “Haya, eneo hili ni kubwa. Tunaweza kuweka sehemu nyingine ya mambo ya sabuni. Hatuna haja ya ofisi tena. Hizi zinatosha. Tutafute tu vijana kadhaa, watakaoanza kwa kutusaidia kuzitengeneza. Halafu hizo hizo za mwanzoni, ndio zinunue mashine ya kisasa.” “Kwamba watengeneze kwa mkono!?” “Ndiyo Malon. Inawezekana. Nishauliza, kuna mtu amenielekeza. Yeye anafanya, lakini kwa kiwango cha chini, tena nyumbani kwake tu. Hizo picha ni zake. Ni kaka mstaarabu.” Malon akanyanyua nyusi na kukunja mikono kifuani.

Naya akaanza kucheka. “Focus Malon! Zingatia ninachokwambia.” “Huyo tena ni kaka mwingine!?” “Huyo ni wa biashara Malon. Acha wasiwasi. Amekuwa mwema sana kwangu, akanionyesha. Juzi nilikwenda, nikaona anachofanya. Wala hatutahitaji vitu vingi. Lakini sisi tufanye kwa kiwango cha juu, na kihalali. Ili watu wasije kutushitaki nakusema hatulipi kodi. Tusitafutie watu sababu.” Malon kimya.

“Ni nini tena?” “Kwa hiyo ulikwenda mpaka nyumbani kwake!?” “Malon Saduki! Tafadhali weka akili kwenye pesa. Ni nini lakini?” “Pesa za kujitoa kafara, hizo sizitaki Naya.” “Hapana bwana. Nimekwambia ni kaka mstaarabu. Muhangaikaji, na anajiheshimu sana.” “Wewe ulimfahamu vipi?” “Ni kaka wa mmoja wa msichana mmoja tuliyekuwa naye kwenye kundi la kujisomea chuoni. Nikiwa chuoni hiki kipindi cha mwisho, calculator yangu iliibiwa. Nikataka calculator lakini sikutaka kwenda mjini. Ndio Zera akaniambia nimuagizie kaka yake, alikuwa anakuja siku inayofuata, kuna vitu alikuwa amemuagiza kutoka huku Dar. Tena Zera mwenyewe akampigia, akamuomba na kukubali. Alipoleta, ndio ikabidi kwenda kushukuru na kumlipa. Ndio kuanzia hapo tukafahamiana.” Malon akabaki ametoa macho.

“Sasa ni nini tena Malon!?” “Kwa hiyo Calculator ndio ikazaa mahusiano mpaka yakumtembelea nyumbani kwake?” Naya akafunga macho. “Naya?” “Nisikilize tena Malon. Siku analeta hiyo Calculator tulikuwa na Zera, tunasoma. Alipopiga simu kuwa amefika, Zera akanishauri ni vizuri twende nikaione kwanza kabla yakulipia. Ili kama nitaipenda ndio nichukue, kama sijapenda, nimrudishe nayo. Nikaona wazo zuri. Nikaenda. Nikamkuta ni mtu muungwana sana.” “Ameoa?” Malon akauliza. “Sijui Malon.” “Naya?” “Nafikiri labda hajaoa au anamchumba. Sijauliza haya maswali Malon! Siku nilipofika pale kuchukua calculator kwenye mazungumzo yake na mdogo wake nikamsikia wakizungumzia hayo mambo ya sabuni. Ndio nikamuuliza. Akasema anafanya kama kitu tu cha pembeni, kwa kuwa yeye ni mwajiriwa. Tena mimi mwenyewe ndiye niliyemuomba kwenda kuangalia. Anafanyia kwenye nyumba yake tu, huko alipohamia Salasala, anaenda kuwauzia wafanyakazi wenzake tu. Ndio mimi nikapata wazo tufanye kwa aina yetu.” Kimya.

“Naomba chukua hii simu, angalia jumbe zake Malon. Huyu kaka ni mtu anayejiheshimu. Jumbe zake ni za heshima. Kutia moyo, tena huwa anatuma neno la Mungu kila siku asubuhi.” “Hee!” Malon akashangaa kabisa. “Sio kwangu mimi peke yangu! Nafikiri anatumia watu wote. Ni kama mtumishi wa Mungu. Anasoma neno, na kulichambua kidogo, kisha anaomba. Naomba fungua hapo usikilize Malon. Hana kitu cha ajabu, au hana hata mambo mengi. Naomba usome Malon.” Naya akamuwekea Malon simu mbele yake. Malon akabaki akimtizama.

“Tafadhali usiondoke ukiwa umekasirika Malon au unaswali ambalo hujapata jibu kutoka kwangu.” “Kwa hiyo leo unakubali kujibu maswali yangu?” Naya akameza mate. Akajiweka sawa. “Ndiyo.” Naya alijibu kwa upole. “Siku uliyokuwa umempigia simu Ozi, kuwa unataka kuwa naye kwenye biashara. Ulikuwa umeshazungumza na mimi au bado?” “Sikuwa nimemuomba kuwa naye kwenye biashara. Nikatika mazungumzo ndio...” “Naya?” Malon akamwita akionyesha hataki maelezo mengi. “Ilikuwa baada ya mazungumzo na wewe.” Naya akajibu. “Kwa hiyo uliamua kuniacha mimi moja kwa moja! Kwenye mahusiano na kazi?” Kimya.

“Uliniambia utanijibu Naya.” “Kutokana na kile alichoniambia Ozi, ndio nikaona ni heri nikuache tu uendelee na maisha yako.” “Kwa hiyo ukaamua kuniacha mimi moja kwa moja uendelee na Ozi?” Malon akarudia swali. Naya akameza tena mate. “Naya?” “Lakini si nimejirudi Malon? Nimeomba na msamaha?” “Jibu lake ni ndiyo au hapana?” “Ndiyo.” Malon akacheka kwa kusikitika.

“Kwa hiyo akitokea Ozi mwingine?” Malon akamuuliza. “Sasa ukute tunakuwa tumeanza haya yote uliyosema hapa. Biashara zikaanza, tukapata wateja kama tulivyofanya kwenye mavazi. Halafu akaja kutokea Ozi mwingine. Akakupa habari zangu, si utaninikimbia wewe utafute mtu mwingine?” “Nimekwambia nilikosea Malon. Wakati ule tulikuwa na mahusiano ya kimapenzi. Habari zako na wanawake wengine, zilikuwa zikiniingia sana na kunichanganya. Nimekuomba msamaha na ahadi kuwa sitakufuatilia tena kwenye mahusiano yako yakimapenzi. Na hata wakiniletea habari zako, sitajali tena. Na Ozi naye nimemwambia.” “Umemwambia nini?” Naya akavuta pumzi.

“Naomba katika hili, usinitafutie tena kosa Malon. Nimejiapia nitakuwa mkweli kwako. Naomba niwe muwazi, na wewe usinihukumu kwa lolote.” Malon akabaki akimtizama. “Malon!” “Nakusikiliza.” Mara mlango ukafunguliwa. Naya akapumua kwa nguvu. Walikuwa wale wasichana wa kanisani.

Naya akasimama na kuwasalimia kwa kuwashika mkono.  “Huyu ni Malon. Ndiye mwenye hiki kiwanda.” Wakamsalimia Malon aliyekuwa amekaa. “Twendeni kule alipo mama. Tutazungumza kidogo, wakati anawapima. “Twende Malon.” “Unataka na mimi niwepo?” “Si ndio tunaweka msingi nao! Nataka uwepo ili kama kuna kitu chakuongeza, uongeze.” “Nafikiri wewe unatosha. Nenda nao tu.” “Sawa.” Naya akataka kuchukua simu yake ili aondoke nayo, Malon akaiwahi. Naya akamtizama. “Wewe nenda, utanikuta hapahapa na simu yako.” Naya akajua kazi imeanza. Akaondoka, nakumuachia ile simu.

 Malon ajua ukweli.

M

uda ambao Naya alikuwa na wale wasichana, Malon alipata muda mzuri sana na simu yake. Akaanza kwa Ozi. Akaanza kusoma jumbe zake na Naya. Akaanza kushangaa ile shauku ya kutaka kumpa habari zake Malon. Kwa Naya. Kuna jibu moja tu ambalo Malon alilipenda. Kutoka kwa Naya, akamjibu Ozi. ‘Hakuna jinsi ukamvua nguo Malon, kwa yeyote, hata kwangu, ukadhani unanisaidia na kunisitiri. Malon ndio mimi. Ukimwaibisha Malon, ujue umeniabisha mimi.’ Huo ulikuwa ujumbe wa zamani kidogo. Hata kabla ya sherehe ya miaka 50 ya wazazi wake. Ilimgusa sana Malon. Akavuta pumzi na kuendelea kusoma.

Alishangaa habari alizonazo Naya juu yake. Mambo makubwa sana aliyoambiwa. Tena ya ndani sana. Lakini hakuwahi kumuuliza Malon. Akaanza kuhisi ni kwa nini Naya alichanganyikiwa kwa kiasi kile. Ozi alikuwa akimpa habari zake, nzito, za siri na kweli tupu. “Ameyapata wapi haya mambo huyu Ozi!?” Malon akajiuliza huku akiendelea kusoma. “Nani amempa habari zangu, wakati haya mambo ni ya Morogoro, yeye anaishi Dar!?” Malon akazidi kuchanganyikiwa. Yalikuwa ni mambo mazito ambayo hakutaka hata Naya ayahisi. Alimficha na kumuepusha nayo kwa kila namna. “Mtu akiiba hii simu ya Naya, akapata hizi jumbe, ndio nimekwisha.” Akajisemea Malon wakati akiendelea kusoma.

“Labda ndio maana Naya anataka nifanye biashara hizi, ili nibadili maisha?” Malon akajiuliza. “Lakini ni nani atakuwa anampa habari zangu?” Malon akajiuliza na kujisuta. Mishipa ya kichwa ilisimama, asielewe na kuamini ni nani anamuharibia kwa kiasi hicho. “Nia ni kuniharibia mimi kwa Naya, au kuna anayemtaka Naya wangu, sasa anataka kunigombanisha tu na Naya?” Akaendelea kujiuliza Malon. “Ni nini kinaendelea?” Malon akaendelea kusoma. Mikono ikaanza kutokwa jasho. Akagundua hata ujibuji wa Naya, ni kama hakuwa anaelewa vizuri, na haamini.

Naya akashangaa anamuona Malon anatoka bila hata ya kuaga. Akajua atarudi tu. Hakuwa na wasiwasi. Kumbe Malon aliondoka pale makusudi akiwa na simu ya Naya, ili apate kujua ni nini kinachoendelea. Nani anampa habari Ozi, na kutaka kumaliza jumbe zote. Maana zilikuwa nyingi sana, na Ozi alionekana amekazana kweli kweli. ‘Huyo anayekupa habari za Malon, anakudanganya. Malon ana maadui wengi, kutokana na maendeleo aliyo nayo. Watakupa uthibitisho wowote ule, ili kukuaminisha. Achana na mambo ya Malon, Ozi. Hayakusaidii na hayatabadilisha lolote kwangu.’ Moja ya majibu ya Naya kwa Ozi.

Upo ujumbe mwingine ambao Malon alipoangalia na tarehe, ilionyesha ni kipindi Naya yupo chuoni akimalizia mitihani siku chache kabla ya unyesho la mavazi. Aliamwambia kuwa, ‘Hapa ninapokutumia huu ujumbe, Jamaa yako yupo Antique hotel, anachapa demu.’ Malon alishtuka sana. Kwani ni kweli alikwenda Antique Legacy Hotel siku hiyo ujumbe ulipotumwa. Tena mida hiyo ya jioni ulipotumwa ujumbe. Alikuwa akikutana na mwanamke, lakini haikuwa sababu ya kufanya mapenzi ni mambo yake ya biashara. Malon akajifuta jasho. Akaangalia majibu ya Naya, hakuwa amejibu. Akaanza kufikiria, anayemfahamu na kumfuatilia kwa kiasi hicho ni nani?

‘Bangi anazovuta na kuuza mumeo, ndizo zinazomfanya atembee zipu wazi. Anaua watoto wa watu kwa bangi, na yeye amepata laana ya umalaya. Haridhiki na mmoja! Mjini anaitwa Chovyachovya. Laana hiyo. Sasa anza kutafuta jeneza lako kabisaa. Unalala na kutembea na kifo.’ Ndipo akajua ni wapi Naya amepata hofu ya kufa, na kumwambia Malon kuwa atakuja kumuua na maradhi. “Ozi!”  Akajikuta akimtamka kwa sauti. Alisoma, nakurudia, mpaka ikafika jioni. Alikuwa na hali mbaya. Kichwa kilikuwa kimevurugika, mpaka uso ulionyesha.

Akaenda kununua maji ya baridi. Akaosha uso mara kadhaa. Huku akijiuliza anafanyaje na anarudije kwa Naya, ambaye hakujua kama anamfahamu kwa kiasi hicho! Kila mwanamke aliyekuwa akikutana naye kwa siri, Naya alikuwa akiambiwa na Ozi. Aliolala nao na ambao alikutana nao tu kwa mazungumzo kumbe Naya alikuwa akiambiwa! Lakini hakuwahi kumuuliza. Hofu ilimuingia Malon akabaki hajui chakufanya na kushindwa kumuelewa Naya.

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

Alirudi pale kiwandani, alikuta walinzi tu, akaambiwa wote wameondoka, amebaki Naya ndani. Malon akavuta pumzi mara kadhaa, akaingia. “Nilijua hutarudi tena.” Naya alimpokea hivyo tu. “Kuna kitu nilikwenda kufuatilia. Sikujua kama nitachukua muda mrefu. Mama alishaondoka?” “Amewahi kupika. Naona baba alishaanza kumpigia simu, na Bale. Li Bale linakuwa kama linanyonya! Yaani akiwepo yeye nyumbani anataka na mama awepo! Sijui kama litaoa lile.” Malon akacheka. “Hana mchumba?” “Ampate wapi hutwa lipo nyumbani! Kama halinichokozi, basi anamdanganya mama kwa stori zake za uongo, au yupo kwenye kompyuta.” Malon akazidi kucheka. Akakaa.

“Sasa wewe unaondoka saa ngapi?” “Kuliko kwenda nyumbani, Bale anilize. Heri nikae tu hapa nifanye kazi zangu.” Malon akacheka. “Sasa huwa anakuchokoza nini?” “Hatabiriki Bale. Na haniachi mpaka nilie au baba amfukuze. Anaweza akaja na jambo hilo, lazima ulie Malon. Na anaweza akaamka siku hiyo ananiigilizia ninavyoongea, kulia na kila kitu. Na mbaya zaidi ananirikodi. Siku hiyo anaweza kuamua kuweka kilio changu kama mlio wake wa sauti. Ukimpigia, utasikia sauti yangu nikilia, au nikimwita.” Malon akazidi kucheka. “Namsubiria kwa hamu sana aondoke mle ndani. Ipo siku Mungu atasaidia tu. Na nimemwambia akiondoka mle ndani, mimi nafanya sherehe.” Malon akazidi kucheka.

“Vipi lakini wewe? Ulipitia chakula?” “Sijala. Nilipata masaa machache mazito, nikasahau kula.” “Pole. Wahi ukale.” “Na wewe?” Malon akamuuliza. Naya akacheka. “Wakati mama anampima mmoja wa yule msichana, nikapata wazo. Mtindo ambao sijauweka sawa, ndio nahangaika hapa kuchora. Lakini kila nikichora, macho yangu hayaridhiki.” “Basi hapo ukute hata maji utakuwa hujanywa!” “Ulijuaje?” “Nakujua Naya. Pumzika bwana.” “Acha nivute muda kidogo. Nitegee mama apike, waoshe vyombo kabisa ndio nirudi nyumbani.” Malon akacheka.

“Sasa wewe mke wa namna gani kazi za nyumbani hupendi?” “Basi hapo ndipo Bale anaponiliza kila siku. Eti anamwambia baba asipokee mahari yangu, mimi sijui kupika wala si mke wakuweka ndani. Eti anasema nitarudishwa mchana kweupe, baba abakiwe anadaiwa hiyo mahari.” Malon akacheka.

 Mambo hadharani.

     “Unarudi Morogoro sasa hivi?” “Nafikiria kubadili maisha yangu Naya. Nafikiri nihame Morogoro kabisa.” Naya akastuka sana. Akamgeukia. “Kwa nini!?” Malon akavuta pumzi. “Nimesoma jumbe zako na Ozi.” Naya akabaki kimya. “Zote. Tokea mwanzo mpaka mwisho. Nashukuru Mungu hukuwahi kufuta.” “Ozi mzushi.” “Hapana Naya. Mengi aliyokwambia mle ndani ni kweli.” Naya akatulia. “Asilimia 90 ni kweli. Kweli tupu. Ila imenitia wasiwasi sana. Mambo aliyokwambia wewe, ni ya ndani sana ambayo hata sikutaka uyahisi. Nilikuwa nakuficha, sikutaka ujue. Na nikamshukuru Mungu ambavyo hukuwa na maswali mengi juu yangu. Nikajiambia ni wakati wakurekebisha.” Malon akaendelea.

“Ni kweli kuwa navuta bangi. Na ni kweli pia kuwa ninauza bangi. Bangi ndiyo iliyonipa pesa ya haraka. Kwa kuwa inatumiwa na masikini pamoja na matajiri pia. Vijana wa mtaani, mashuleni, wazee kwa vijana. Nikujua soko lake, kukamata wawili watatu, basi unauza. Soko langu kubwa ni hapa Dar, na Morogoro. Side ndiye anayenisaidia kuleta huku. Morogoro ninaye kijana mwingine, ambaye anasimamiwa na Side.” “Biashara ile ya sukari ya Brazil?” “Zote nafanya ila bangi inafaida zaidi. Nikikwambia bangi ina faida, niamini ipo faida. Kwa kuwa hata uwekezaji wake haugarimu.” Naya akabaki akimtizama.

“Na ni kweli kuwa bangi ndiyo inayonipelekea kufanya mengi mabaya. Kila mtu kuna jinsi bangi inamfanya. Mimi inaamsha hisia za ajabu. Siwezi kujizuia. Mwanzoni nilipokupata wewe, kipindi kile nikatulia, nilijaribu kuacha, lakini nilishindwa kabisa.” “Mbona sijawahi kukuhisi hata kwa harufu?” Malon akacheka. “Sijaanza kuvuta bangi leo Naya. Wote unaowasikia wakiniita bangi ni kwa matendo yangu, lakini sio harufu. Hata mama yangu hajawahi kunikamata na harufu.” Naya akamwangalia na kunyamaza.

“Unakumbuka nilipokwambia naomba muda nitabadilika?” Naya akamwangalia na kutingisha kichwa kukubali. “Ni kwakuwa niliamua kuacha tena, nikashindwa.” “Kwa nini ulishindwa?” “Ndio ulevi wangu, na nimeshakuwa siwezi kuishi bila bangi. Nikarudia tena, lakini kwa kujitahidi kuacha wasichana. Nikajiambia lazima kuchagua, kama ni lazima kuvuta, basi lazima kujitahidi kuacha kulala na wanawake hovyo. Nikajaribu, na ndio maana wakati ule nikakuomba tuishi wote. Kunduchi na Morogoro. Tukawa tukifanya sana mapenzi. Ilikuwa sababu hiyo. Tuache hayo. Ukawa umefungwa na shule, ndio nikalala na Loi. Sikuwa hata namfahamu.”

“Kuna mashindano waliniomba kuyadhamini kule Morogoro. Tena walimtumia Chezo. Mimi nikampa hiyo pesa Chezo ambaye alikuwa akifahamiana na yule mama aliyekuwa akifanya hayo mashindano. Siku yenyewe ya mashindano, Chezo akaniambia twende tukaangalie wao wanavyofanya kama kujifunza wakati tukiandaa maonyesho yako, akasema tunaweza pata chakujifunza, tuige. Nikaona sio wazo baya. Tukaenda. Sasa Loi naye akawa mmoja wa washiriki, na yule mama alipokuja kunishukuru kwenye meza tuliyokuwa tumekaa, akaja na Loi kama mshiriki aliyekuwa amefanya vizuri kwenye onyesho zima na kama mtu anayemtegemea kwenye yale mashindano. Ila Loi hakuondoka pale kwenye meza yetu tuliyokuwa tumekaa na kina Chezo pamoja na jamaa wengine. Akaniganda wee. Kila nilipomkwepa, na kutoka pale ili kumuacha na wengine, akaonyesha nia na mimi ya waziwazi. Ndipo nikalala naye, nakuachana naye.” Naya akainama kwa kuumia.

“Nikasahau kabisa. Sasa wakati wewe unatafuta mtu, ndio ikabidi nizungumze na yule mama niliyemdhamini. Tena yeye ilikuwa anafungua saluni ya kupamba maharusi. Kwa hiyo akawa anaonyesha nywele. Ndipo akanipa mawasiliano yake. Nikiwa hata simjui, nashanga katika miahadi ya kukutana baada yakuzungumza naye kwenye simu, anatokea Loi. Ndio nikamwambia ipo kazi. Lakini ni ya mwanamke wangu. Sitaki afike kwako akwambie kilichotokea kati yetu. Ile ilikuwa bahati mbaya, na haitakaa ikatokea tena. Ndio akaniuliza mbona yule mama alimwambia ni mashindano yangu. Nikamwambia mimi niliwekeza tu pesa, lakini wewe ndio unaendesha kila kitu. Sasa sijui yeye aliongea nini!” Naya kimya.

“Baada ya lile tukio siku ile, nilijilaumu sana. Nikaamua sasa kutafuta msaada kwa wataalamu.” “Msaada wa nini?” “Kuacha bangi. Maana mbali na kuamsha hamu ya mapenzi, huwa inanifanya nakuwa mkatili sana. Siwezi kujizuia. Unakumbuka siku niliyokupiga kibao?” Naya akanyamaza hakujibu. “Nilijishtukia tu nakupiga. Halafu na yule dada sikuwa hata nina mpango wakufanya naye mapenzi. Alinipigia simu kuwa yupo Moro, na anadakika chache, anaweza kunifuata popote. Bila kufikiria, kwa kuwa alikuwa ni dada ninayemuheshimu, nikamkaribisha pale nyumbani. Amefika na ajenda moja tu, ananiambia hajavaa nguo ya ndani, nimsaidie mara moja aondoke. Sijaelewa vizuri akanivulia nguo. Akaniambia hali yake mbaya, amekuja mpaka Moro kwa jili yangu. Tokea siku ile pale hotelini alipotuona tukiwa wote alinitamani. Alishanivua nguo, tukawa tumeshafika kitandani. Kwa hiyo ananiomba nimalizie tu. Hapo anazungumzia hivyo ameshavua kigauni alichokuwa amevaa, akanifungua zipu. Akili ilikuja kurudi, pale wewe unaingia. Nikawa kama nimezinduka kutoka usingizini.”

“Basi, kufupisha stori. Nilikuja hapa Dar.  Nikatafuta daktari kabisa. Nikamueleza mambo yote. Akaniambia nimeshakuwa na addiction, inabidi kuanza matibabu.” “Umeanza?” Naya akauliza kwa upole. “Ndiyo.” Malon akajibu. “Inakusaidia?” Naya akauliza tena. “Taratibu Naya. Sio kitu cha siku moja. Hata siku ile nilipomkuta Ozi nyumbani kwenu, nilikuwa nimetokea kwa huyo daktari. Ndio maana nilikasirika zaidi. Nikaishia kukulaumu wewe.” “Kuwa unafanya hayo yote kwa ajili yangu?” Naya akauliza. “Ndiyo, nafanya kwa ajili yako Naya.” Naya akamuhurumia.

“Naomba usiache Malon. Makosa yangu yasikufanye ukaacha matibabu. Nakiri nilikosa, sitakuficha wala sitakudanganya tena.” “Ila Naya, yupo mtu nyuma ya haya yote. Sijajua ni nani, lakini ni mtu anayenifahamu mimi vizuri, na wewe. Walikusudia kukuingia akilini kwako ili kufikia walipotufikisha. Sasa sijajua kama nia ni kunikomoa mimi, au kututenganisha ili wakupate wewe! Sijui. Lakini najua wapo watu au mtu wa karibu yangu sana anayetoa habari zangu.” Naya akafikiria kidogo.

“Lakini Malon, naomba nikuombe kitu au vitu.” “Nini?” “Acha biashara ya bangi.” “Nitaacha.” “Lini?” “Leo.” Naya akakunja uso. “Usinidanganye Malon.” “Hata kidogo. Leo imekuwa kama kengele ya kunitoa huko. Hao watu wanaotumia habari zangu kuniharibia kwako, sijui wamefika wapi! Inamaana kama bado, basi wanaweza hata kuniharibia mimi polisi. Nina uhakika sio Side.” “Kwa nini?” “Kwa sababu nikiharibikiwa mimi, ndio na yeye. Side ni zaidi ya dereva wangu.” “Hata yeye aliniambia.” Malon akakunja uso. “Ila aliniambia kwa nia nzuri siku ile naondoka kwako, akinihakikishia kuwa unanipenda. Kwa jinsi alivyozungumza na mimi siku ile, sio Side. Side anakupenda sana Malon.” “Hata mimi najua. Ananipenda sana Side, na ananitakia mema. Kitu gani kingine?” Malon akataka Naya aendelee.

“Naomba uendelee na matibabu, lakini pia uombewe. Naomba baba akuombee.” “Nimwambie ukweli wote!?” “Yapo mambo yanatoka kwa dawa za hospitalini, na vitu vingine ni mpaka maombi Malon. Unaweza kukuta una pepo la ukahaba. Bangi ni kisingizio tu. Halafu baba yeye ni muelewa. Na yeye anakuhesabu wewe kama mtoto wake. Huna jambo utakalomwambia baba, likamfanya akukimbie. Halafu ninamuona akitoa mapepo pale kanisani. Wakija watu wenye mapepo, baba huwa anakemea, na wale watu wanawekwa huru ndio maana wakina Ino wanakuwa kama wanamshikilia hivi. Kumng’ata na kumpuliza ili abakie. Mimi nahisi ni kwa ajili ya huo uwezo Mungu aliompa, ndio na wao wanamtumia vibaya kama kulifanya lile kanisa libakie na sura ya kanisa wakati wao hawana hata uwezo wa kuongoza kanisa!” Naya akaongea kwa hasira akaonyesha kukerwa kabisa.

“Tuyaache hayo. Naomba uzungumze naye.” Malon akainama kama anayefikiria. Naya akamuacha afikirie akarudi kuchora. “Naya!” Naya akamgeukia. “Nikiacha biashara ya bangi, ujue ndio nitaishiwa kabisa.” Malon aliongea kwa hofu. “Mungu atatupa kwa njia nyingine Malon. Unakumbuka ulivyotoka kuniambia? Kuwa huwezi kupata pesa kwa kujitoa kafara. Itanisaidia nini mimi kutengeneza pesa, halafu muda mfupi unarukwa na akili. Au unakuja kufa na maradhi?” Kimya. Naya akasimama na kumsogelea pale.

“Naomba niangalie Malon. Naomba kipaumbele iwe wewe kwanza. Mimi na wewe tumefanya jambo moja kubwa. Inawezekana ikawa ndio ishara kutoka kwa Mungu. Anatuonyesha yupo na sisi.” “Nikiishiwa hutanikimbia?” Malon akauliza kwa upole. “Naomba usinijibu kwa haraka Naya. Fikiria kwanza. Mimi nayajua maisha kwa kuyaishi. Nimekaa kijiweni nikidharaulika sana sababu ya kukosa pesa.” “Ni mimi Naya, Malon. Niangalie. Ni lini uliwahi hata kuhisi kuwa nataka pesa zako?” “Lakini pesa ndizo zimetukutanisha, Naya! Isingekuwa kuwa na pesa, nisingeweza hata kuingia kwenye ile tafrija, na kukuona.” “Basi naomba iishie hivyo. Kuwa hiyo pesa ya bangi, iwe imetimiza kusudi lake. Kukukutanisha na mimi, basi. Itoshe hivyo.” “Hutanikimbia Naya? Mbali ya hii pesa, mimi sio kitu Naya. Sijasoma kama wewe. Wakati mwingine juhudi ulizokuwa ukiniona nazo, ni nguvu ya bangi.” Naya akaanza kumbusu.

Akambusu midomo yake kwa muda huku amekaa palepale kwenye kiti. “Umenisomesha mimi, Malon. Kutakapohitajika elimu, mimi nipo. Maarifa na juhudi, ni mimi na wewe. Siwezi kukuacha hata iweje.” “Ukiniacha ujue ndio umeniua Naya.” “Nakuahidi, sitakuacha Malon.” Malon akavuta pumzi.

 Malon ataka kubadili maisha, lakini Kamba yamkatikia pabaya.

B

aada ya kuhakikishiwa penzi, Malon akaona achukue hatua tu. “Naomba nizungumze na Side hapo nje, kwenye gari.” “Hamna neno. Mimi nitakuwepo hapa.” Malon akatoka. Naya akarudi kwenye kiti chake, akaendelea kuchora. Lakini akiwa amejawa mawazo na hofu. Malon alikuwa ameiacha simu yake mezani. Akaichukua, nakumpigia Ozi. “Hatimaye umenikumbuka mrembo!” Naya akacheka. “Nina shida Ozi. Najua wewe utanisaidia.” “Nipo kwa ajili yako Naya.” “Unakumbuka yale mambo uliyokuwa ukiniambia juu ya bangi ya Malon?” “Kuwa anavuta bangi na kuuza?” “Ndiyo!” Naya akakubali.

Malon akaingia, Naya akamfanyia ishara ya anyamaze, kisha akabonyeza speaker ili wasikilize wote. “Sasa washikaji kijiweni wamemtosa kwa polisi. Leo si jumatatu?” “Ndiyo.” “Basi leo ndio siku ya mzigo wa Dar. Kijana wake Side ndio anamletea bangi huku. Unaambiwa jamaa yako anaingiza pesa ya bangi huku anajidai anauza sukari. Polisi walikuwa wanamtafuta muda mrefu, sasa kuna mtu wake wakaribu anayejua ratiba zake na Side, amewapa polisi mchongo mzima.” “Unamjua ni nani?” “Siwezi kukwambia Naya! Unataka kumwambia jamaa nini?” “Kwa yote aliyonifanyia yale!” Naya akajidai yupo upande wake.

“Kwanza ngoja nikwambie ukweli Naya, Malo anamaadui wengi sana. Bangi ndio zimemponza jamaa yako. Ukorofi kwa wenzie, na umalaya. Si nilikwambia wanamwita Chovyachovya?” Naya hakujibu. “We Naya!” “Nipo Ozi.” “Basi unaambiwa alikuwa hana mipaka. Kachovya mpaka kwa demu wa rafiki yake, ndio huyo sasa anamuharibia.” “Lini alifanya hayo?” Naya akauliza. “Muda tu. Sema mambo ya kisasi huwa hayaishi. Sasa rafiki yake akachukia kuona eti sasa hivi kakupata wewe, ndio anatulia, wakati yeye alimuharibia. Mbaya zaidi unaambiwa huyo mwanamke aliyemlala, naye alikuwa mchumba kabisa wa jamaa. Huyo jamaa alishamlipia mpaka mahari! Malon akamgonga. Dada sijui akakolezwa, akaanza kumzingua jamaa, ndio siku moja katika ugomvi, akamtukana jamaa yake  eti yeye sio mwanaume kama Malo. Katika kumbana na kipigo juu, akakiri kuwa Malo alishamgonga. Kuomba msamaha, jamaa kavunja harusi.” “Alimuuliza Malon?” Naya akauliza.

“Jamaa yako mbabe Naya! Nasikia alikubali bila hofu. Sasa utamfanya nini Malon? Pesa ipo mfukoni, bangi kichwani. Masela wanamuogopa. Wewe mbona hushangai kwa nini mimi sikupata shida kupata habari zake? Mchafu huyo mpaka wanawake wa stendi wanamfahamu. Wala hupati shida kupata habari za Malon. Walikufuatilia wewe, kukwambia ukweli. Wakaona jamaa ameweka ukali. Hakuna wa kukusogelea. Sasa mimi nilivyojitokeza na kuwaambia simuogopi, ndio wakawa wananipa habari zake. Alipo na anachokifanya ili kumkomoa, na yeye akose kama alivyokosa mwenzie. Hakuna besti wake Malon aliyekutongoza wewe?” Ozi akauliza nakumfanya Naya ababaike sana. Malon akamtolea macho.

“Ndiyo au hapana? Wewe jibu Naya. Ule ulikuwa mtego. Alitaka akugonge, makusudi kwa ajili ya Malon. Ulipokataa ndio akajidai utani. Uongo?” Naya akanyamaza. “We Naya?” “Sasa ilikuwa nikimkubali ndio iweje?” “Hapo ilitegemea na wewe. Kama ungetaka mara moja sawa, lakini ungetaka uendelee, jamaa alisema yupo radhi. Ni kama na yeye ulimnasa hivi. Akakupenda sana. Lakini aliogopa kuwa muwazi sana, sababu ya Malon. Wanamuogopa sana. Tena alitaka ukikubali, wewe mwenyewe ndio umkatae Malon. Kwa kuwa wanasema wewe Malon hawezi kukufanya kitu. Chochote ukimwambia anakubali. Sasa ponea yake yeye huyo jamaa aliyekutongoza, ilikuwa akuweke sawa, umtose Malon, umkubali yeye. Mpaka jana alikuwa ananiulizia kama umejirudi.” “Unamaanisha nini?” Naya akauliza.

“Si ulikwenda kwenye shuguli ya wazazi wake Malon, wakati mimi nilishawaambia umenikubali! Ndio wakanipigia simu kuniuliza ni nini tena! Mbona niliwadanganya wakati jamaa walishafurahia kuwa wewe umemtosa Malon. Ndio nikawaambia ulikwenda tu kwa kuwa unafahamiana na wazazi wake Malon. Lakini sisi tupo pamoja na biashara tunaendelea mimi na wewe kama walivyonishauri.” “Kumbe wao ndio walikushauri tufanye wote biashara?” Kidogo Ozi akasita.

“We Ozi?” “Ngoja nikwambie Naya. Nilikuwa under pressure. Walikuwa wapo kooni, sihemi.” “Hivi wewe ndio wakudanganywa ili uje kunidanganya Ozi!?” “Lakini tungefanya wote. Ilikuwa ni kumtoa tu jamaa kwenye picha. Kwani ni nini anafanya cha tofauti na tunachokifanya kila wakati na Madamu Vane? Si yaleyale tu. Ila mimi ningefanya kwa heshima sio kutembea na wafanyakazi, Naya! Katika hilo nipe hata Credit. Mambo mengine ni jamaa aliniongezea tu nguvu ili kukushawishi.” “Sasa hivi nakuwa sikuamini Ozi. Lipi lako na lipi umepewa, na umepewa na nani? Kama hutaki kuniambia, nakata simu na usinitafute tena.” “Subiri kwanza Naya. Acha hasira.” “Umenidanganya Ozi!” “Mengi ni mimi mwenyewe.” “Kama lipi?” Naya akaweka ukali.

“Kukupenda ni wazo langu Naya. Hata kabla ya Malon hajaja kwenye picha, mimi nilikupenda, na wewe unajua. Sasa alipokuja Malon, ndio nikaona kama amenipokonya tonge, kwa kuwa kweli Naya sisi tulikuwa tunaendana. Hata kazini walikuwa wanatusifia. Tunaelewana vizuri tu. Sasa alipokuja Malon, ndio nikawasikia kina Tula, Lulu na Tunu wanamzungumzia sana. Na wakasema uliacha kazi kwa kuwa umepata mwanaume mwenye pesa. Ndio nikaanza kumfuatilia kwa kuwauliza kwanza wao. Ndio kina Tula wakanieleza kwa sehemu vile wanavyomjua Malo, wakaniambia habari kamili anazo mwanaume aliyekuwa amelala naye Tunu, waliyekuwa wamekutana kwenye party nyumbani kwa Malon. Akanipa namba yake, nikampigia, ndio akanipa mkasa mzima.” “Muulize jina.” Malon akanong’ona.

“Ndio nani sasa?” “Naya!” “Kama hutaki basi.” Naya akajidai kuzira. “Naomba usinitaje Naya. Huyo jamaa, ni rafiki yake pia Malon ila sasa best yake kabisa ndio amezulumiwa mwanamke na Malon.” “Mbona humtaji sasa?” “Naomba usije nitaja.” “Ozi!” Naya akamwita kwa kugomba. “Ni Dunda.” “Unamaanisha Madunda!?” Naya akauliza kwa kumfahamu kabisa. “Ndiyo. Lakini mtaani  wanamkatisha Dunda. Sasa best yake ndio kachukuliwa mwanamke na Malo, bwana wako.” “Kwa hiyo ndio wanamchomea polisi?” “Nakwambia anawindwa huyo, sema amekuwa mjanja. Kazi zake anawapa watu wamfanyie, ndio maana hakamatwi. Na jamaa walikuwa hawataki kumtosa Side, lakini hamna jinsi. Side hataki kumtaja Malo. Sasa ndio wameamua kumtosa Side ili akamatwe yeye Side. Kisha polisi wambane mpaka amtaje mwenye mali, halafu wamtoe Side, jamaa aozee jela.” Naya akamtizama Malon.

“Sasa bado tunafanya wote yale maonyesho?” Ozi akauliza kishawishi. “Nilikwambia nimerudiana na Malon.” “Acha hizo Naya! Jamaa hana muda mrefu mtaani. Nakwambia ukweli leo Side anakamatwa kama bado. Na wameapa kumbana mpaka amtaje Malon. Utaabika mjini Naya wewe! Jitoe mapema, tufanye dili yetu. Mimi na wewe. Kwanza huwezi kujua, wanaweza kumkamata Malon, wakakufuata na wewe, maana wewe unajulikana kama mwanamke wake kabisa. Watakuweka ndani Naya! Jiweke mbali na Malon. Sasa hivi vyombo vya sheria vinamtizama Malon na kila anachokifanya.” Ozi akaendeleza ushawishi.

“Unakumbuka nilikwambia nini juu ya Malon?” “Kwamba ndio udhaifu wako?” “Kumbe unakumbuka?” “Acha hizo Naya wewe! Una maisha marefu sana mbeleni. Tena mazuri. Malon ashaishi maisha yake yote tena kwa kuchagua kuishi vibaya sana, kwa nini ujitoe muhanga kwa ajili yake? Tena akiwekwa jela huyo, biashara ile ya mavazi inakuwa yako peke yako. Hakuna wakukuuliza, kwa kuwa hata kwao hawafahamu. Utaponea pazuri. Acha kuwa mjinga! Malon hawezi kuja kutulia na wewe hata siku moja. Analaana ya wanawake na hata hivyo jamaa wameungana kumtoa mtaani kabisa, akikamatwa na kuwekwa jela, hatakaa akarudi uraiani.” Ozi hakuchoka kushawishi.

“Nashukuru kwa ushauri Ozi.” “Kwa hiyo?” “Unataka kusikia nini Ozi!? Au unataka kurudisha jibu kwa marafiki wa Malon?” “Acha hizo Naya.” “Nampenda Malon. Na nilikwambia, aibu ya Malo ni yangu. Huna jinsi ukamfedhehesha Malon, mimi nikawa salama. Nilishajiingiza kwake, siwezi kujitoa leo. Acha liwalo na liwe.” “Kweli Naya, wewe!? Umelogwa?” Ozi hakuwa anaelewa.

“Wewe umemaliza chuo juzi tu Naya. Una ahadi nyingi tu mbeleni. Vipaji vingi ambavyo watu wanalilia! Mungu amekupa watu wakusimama na wewe.” “Kama wewe?” “Sasa je? Wapi utapata watu kama sisi? Tena wanaofahamiana na watu watakaokusaidia kufikia ndoto zako! Leo unataka kufa na Malon?” “Kwaheri Ozi. Asante kwa taarifa. Naomba tuzungumze wakati mwingine. Hapa nipo ofisini, nataka kurudi nyumbani.” “Sawa Naya. Utanikumbuka.” Naya akakata simu.

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

Akahema kwa nguvu na kumgeukia Malon. “Wamesha mkamata Side.” Naya akashtuka sana. “Umejuaje!?” Naya akauliza. “Nimempigia Side sijampata. Nikampigia Futi. Futi ameniambia wamemkamata Side, na yeye anatafutwa. Alichofanya nikupoteza mzigo wote, ndio alikuwa akiniomba pesa alizonazo, atoroke Moro.” “Mungu wangu Malon! Utafanyaje?” “Nimemruhusu aondoke na hizo pesa. Lakini nimemwambia asikimbie. Ili asiishi kwa hofu. Na kwa kuwa amepoteza ushahidi, hawata mkamata. Nimemshauri aende kituo cha polisi. Ajifanye kama anakwenda kumuona Side, ajionyeshe tu. Akishatoka hapo, aondoke moja kwa moja. Akaanze kwengine.” “Wakimkamata?” “Hawana ushahidi. Ni maneno kama hivyo ulivyosikia wewe hapo kutoka kwa Ozi. Halafu shida yao ni mimi, wala sio wao. Sasa maadamu wamemkamata Side, hawawezi kumkamata na yeye Futi.”

“Utafanyaje sasa?” “Lazima nirudi Morogoro sasa hivi Naya.” “Malon! Umesikia unatafutwa!?” “Siwezi kumuacha Side jela. Amekamatwa na mzigo wangu, hiyo ni moja. Mbili, Side amekuwa akinitoa jela tokea nipo mtoto. Hata wazazi wangu hawajui maisha yangu kwa undani kama Side. Side ni zaidi ya dereva kwangu, Naya. Ni heri mimi wanifunge, kuliko Side. Halafu ana mke, mjamzito na katoto kadogo. Siwezi nikakubali wale watoto wakue bila baba, Naya. Side anampenda sana mkewe. Mwaminifu, sio kama mimi.” Naya akaanza kulia.

“Naogopa Malon!” “Utakuwa sawa tu Naya.” “Bila wewe? Hapana Malon. Naomba usiende.” “Naya! Siwezi kujificha. Nikijificha, ndio watakutafuta na wewe. Kwa kuwa kila mtu sasa hivi anajua nipo na wewe. Na Ozi atawathibitishia kwa ulichotoka kumwambia kuwa huwezi kuniacha. Nisipoonekana, watajua umenificha. Acha mimi niende. Naamini kila kitu kitakuwa sawa. Kwanza nimtoe Side, mengine nitayajua mbeleni.” Naya alilia sana.

“Nichukue twende wote Malon.” “Sithubutu. Sasa hivi Morogoro itakuwa imechafuka, anatafutwa Malon. Sithubutu kurudi na wewe. Tena hata hapa upafunge mpaka nitakapokwambia pako salama. Chezo alishatangaza kuwa nimepanunua hapa. Wote wanapajua kuwa nilikununulia. Sitaki ujihusishe na chochote kile, kilicho changu.” Naya aliendelea kulia.

“Lazima niondoke Naya.” “Malon!” Naya aliendelea kulia. “Basi nenda na baba.” “Naya! Siwezi kumuingiza baba yako kwenye matatizo! Acha niende. Huwezi jua naweza nisikamatwe.” Akamnyayua pale alipokuwa amekaa. Akamkumbatia kwa nguvu na kuanza kumbusu. Alimbusu tena na tena. “Nakupenda sana Naya. Na asante kuwa upande wangu mpaka mwisho.” “Naomba usiseme mwisho Malon. Tafadhali.” “Huwezi jua Naya.” “Naomba usikate tamaa Malon! Nitakuombea, na Mungu atakusamehe. Na kukusaidia.” “Sawa.” Akambusu tena, nakuondoka kwa haraka.

 ~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

 Baba yake Naya alimpigia simu kujua alipo, akakuta analia huyo mtoto, hawezi kuongea. Alifanikiwa kusema yupo kiwandani, basi. Baba Naya bila kupoteza sekunde akamfuata. Naya alimueleza kila kitu na mazungumzo yao ya mwisho. “Malon alikuwa anataka akutafute umuombee baba. Watamfunga Malon wangu. Nitabaki na nani?” Naya akaendelea kulia, baba yake akabaki kimya akifikiria. “Twende baba.” “Malon amekwambia wazi usiende Morogoro sasa hivi, watakukamata. Naomba tuwe wavumilivu Naya. Subiri.” “Mpaka lini?” “Naomba utulie kwanza. Naomba turudi nyumbani, utulie, tujue chakufanya.” Akamtoa hapo Naya, akamrudisha nyumbani.

 

CONVERSATION

0 Comments:

Post a Comment