Naomi Simulizi |+1 205 767 8163 |naomisimulizi@gmail.com Mapenzi & pesa – sehemu ya 12. - Naomi Simulizi

Mapenzi & pesa – sehemu ya 12.

Maisha yakabadilika hapo nyumbani kwao. Kila wakati mama yao alilalamika kuwa yeye hasikilizwi. Anaongea ujinga. Wanamdharau. Akiingia akitoka, analo jambo la kulalamika. Naya akatulia jikoni, mapishi yake mabaya yakaendelea. Hakuacha kusemwa mchana na usiku. Kwa hili na lile kwa mafumbo. Mwezi wa kwanza ukaisha, wa pili na watatu, akahisi atachanganyikiwa mle ndani. Akaanza sasa kutafuta kazi wakisaidiana kutuma maombi ya
kazi yeye na Bale. Bila mafanikio. Naya alichoka, akaanza kukumbuka maneno ya Joshi kuwa mambo aliyosomea hayana ajira. Akaamua kutafuta kazi yeyote sasa ilimradi tu kupunguza maneno ya mama yake aliyejikuta anabakia naye humo ndani muda mwingi. Mpaka mwaka unaisha, Naya akawa hajapata kazi ila kutuma maombi
ya kazi kila mahali. Shahada yake ya masoko ikaishia nyumbani tu.

Mama Naya.

K

atikati ya kutoelewana huko ndani ya hiyo familia, bila kutarajia mama yao akaanza kuugua. Mapafu kujaa maji wakaambiwa ni  nimonia. Akaanza matibabu. Kwenda kufyonzwa maji huku akitumia dawa za nimonia. Anapona kidogo, yanajaa tena. Matibabu yakamfanya adhoofu sana na kazi akaacha akawa mtu wakukaa tu nyumbani. Na hapo ndipo mahusiano yakaribu sana na Naya yakaanza. Naya ndiye akawa wakumuhudumia mama yake mpaka kumuogesha na kumvalisha kwani alikuwa amedhoofu sana. Maisha ya Naya yakawa alipo mama yake. Nyumbani na hospitalini. Walikuja kugundua kuwa ana kansa ya mapafu wakiwa wamechelewa sana ndani ameoza kabisa. Akaanza matibabu ya kansa lakini mwili ulishindwa kuhimili matibabu, mama Naya akafariki. Lilikuwa ni pigo kubwa sana kwa familia hiyo zaidi baba Naya aliyeona mkewe amefariki akiwa bado na shauku kubwa ya maendeleo kiuchumi. Na Zayoni mziwanda aliyekuwa karibu sana na mama yao. 

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~ 

Baada ya mazishi tu Naya akarudi tena kutafuta kazi. Alihangaika mwaka huo wa pili, mwishowe akabahatika kwenye moja ya shule za msingi za kimataifa. Akapata hapo kazi kama msimamizi msaidizi wa malezi ya watoto. Hawakuwa wakimlipa pesa nyingi, lakini ilimsaidia kupoteza mawazo. Kelele za watoto, pilika pilika za asubuhi mpaka jioni, zikamsaidia. Hakuhama hapo nyumbani kwao. Na Bale naye alichukua chumba chuoni, maisha yakawa kotekote inategemeana na msimu wa masomo. Na yeye alikuwa mwaka wa mwisho chuoni.

Siku hiyo akiwa ofisini kwao yeye na mama mlezi mkuu, aliingia mwanamke mwenye mtoto hapo hapo shuleni, akaomba fomu za kujaza kuongeza mtu mwingine ambaye ataruhusiwa kuja kuchukua mtoto wake akisema yeye ameongezekewa na majukumu atakuwa akichelewa kutoka kazini. Kwa hiyo mtoto wake aongezwe kwenye darasa la jioni, na pia ameongezeka mtu mwingine wakuja kumchukua. Mama Mlezi au Matron, akampa fomu. Akawa anajaza. “Ni ndugu?”  Akauliza Matron. Yule mama akacheka kidogo. “Sijui Mungu atakapotuongoza. Anaweza kuja kuwa baba yake kabisa.” Alijibu yule mwanamke, akionyesha bado anadai kabisa kwa umri na ndipo Naya akajua hajaolewa.

Akajaza mpaka akamaliza, akaacha hapo ile fomu akaelekea ofisi ya muhasibu kulipia baadhi ya gharama. Naya akavuta ile fomu aliyojaza ili kuanza kuandaa sehemu ya huyo mtoto kulingana na umri wake. Kwa maana kama ni mdogo sana, alitakiwa wakishatoka shule, wakati wenzao wanarudi nyumbani, wanaobaki walale kwa lisaa limoja na nusu. Wakimka wale, halafu michezo.

“Anapesa huyu dada! Anaitwa Rita.” Akasifia yule Matron na kuonyesha kumfahamu vizuri. “Anaonekana jinsi alivyo nadhifu.” Naya akajibu huku akiendelea kusoma na kuandika. Akageuza sehemu ya aliyoongezwa mtu, jina ni Malon Saduki. Akabaki ameduaa. “Malo!” Naya akajikuta akiropoka. Matron akamgeukia. “Kwema?”  Naya akapotezea. Akamaliza kila kitu.

Muda wa kurudi nyumbani ukafika akiwa amemkumbuka Malon. “Lakini atakuwa amepata mwanamke mzuri.” Naya akawaza kwa kusononeka.  “Msomi, mwenye kazi nzuri inayomlipa. Maana kumsomesha mtoto pale sio mchezo.” Akaendelea kuwaza Naya. Akajicheka nafsini mwake. Akamkumbuka Joshi. Akamfikiria, akarudi kwa mpenzi wa kwanza, Ino ambaye tayari wana mtoto wa pili wa kiume. Akaguna na kuzidi kujidharau.

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

Baada ya majuma kama mawili hivi kupita, wakiwa wafanyakazi wengine wameshaondoka shuleni hapo, yeye na wafanyakazi wengine wanao hudumia watoto ndio walikuwa wamebaki na watoto hao. Jioni ilikuwa mwisho saa 12, wazazi walitakiwa kuja kuchukua watoto wao. Ethan alishazoeleka kuwa anakuja kuchukuliwa wa mwisho. Na kila aliyechukuliwa, ilibidi mzazi aweke saini baada ya Naya kuthibitisha anaruhusiwa kuchukua mtoto.

Akaja Malon akionekana alikuwa kwenye haraka ya kuwahi hapo. Alishutuka sana kumuona Naya. “Naya!” “Nipo Malon.” Naya akacheka. “Najua umekuja kumchukua Ethan. Mama yake alipiga simu kuniomba niendelee kukaa naye mpaka utakapofika.” “Unafahamiana na mama yake!?” Naya akacheka. Naya huyu alikuwa na tabasamu usoni, nywele alikata tokea msiba wa mama yake, mnyonge kweli. “Unafanya kazi hapa!?” Malon akauliza wakati Naya anatafuta jina lake kwenye tablet ndogo aliyokuwa ameshika. “Ndiyo. Nafanya kama Matron msaidizi. Mara nyingi yeye Matron mwenyewe huwa anaondoka saa 12 kasoro. Sasa mimi ndio nabaki na wakina Ethan.” “Wachelewaji?” Malon akauliza, wakacheka.

“Hamna neno lakini. Mama yake ni mtu mzuri sana na Ethan mwenyewe sio msumbufu. Tulikuwa hapo ndani ananifundisha kukunja vidole.” Malon akamtizama Ethan kisha akarudisha macho kwa Naya kama asiyeamini. Naya akacheka. “Ngoja nikakuchukulie kiblangeti chake. Mama yake ameomba nikupe ili akakifue.” Malon akambemba Ethan. Naya akaenda kumchukulia blangeti na kumkabidhi. Malon akasaini, nakuondoka.

Siku inayofuata ni mama yake Ethan ndiye aliyekuja kumfuata mtoto. Walizungumza kidogo na Naya kutaka kujua maendeleo yake, akaondoka. Kesho yake ikawa jumatano. Akarudi tena mama yake Ethan. “Najua shule zinakaribia kufungwa. Nilitaka kusafiri na boyfriend wangu. Nataka nimsindikize Brazil. Nafikiria swala la mtoto.” Alijiongelesha mama yake Ethan. Naya kimya akimfikiria Malon ambaye ndiye boyfriend. “Unamfahamu mtu yeyote anayeweza kuwa na mtoto wangu kwa siku chache tu. Nitamlipa vizuri.” Naya akabaki akifikiria. “Mmmh! Labda nikuulizie hapa. Unamaanisha amchukue na kuishi naye?” “Hapana. Usiku lazima Ethan alale kitandani kwake. Akiwa huru anaweza hata kuja kuishi hapo kwa muda. Nitamwachia gari na pesa za matumizi yake na Ethan.” “Basi nitakuulizia. Na malipo itakuwa kiasi gani na ni siku ngapi?” “Sita tu. Nachukua likizo kazini kwa ajili ya hiyo safari ya Brazil.” Akamalizia kwa cheka kidogo.

“Basi nipe muda niulizie. Naamini utafanikiwa tu.” Rita akaondoka na kurudi huku akicheka. Akamkuta na yeye Naya ndio anatoka kama siku yake ya kazi ndio imeisha baada ya Ethan mtoto mchelewaji kuja kuchukuliwa. “Kwani wewe Naya hufahamu kuendesha gari?” “Nafahamu na nina leseni.” “Umeolewa?” Naya akacheka. “Hapana.” “Sasa kwa nini usije kukaa kwetu na Ethan kwa siku hizo chache, nakuahidi kukulipa vizuri tu.” Naya akasita. “Naomba mimi nisikuahidi. Ila nakuahidi kukusaidia kutafuta mtu.” “Naona Ethan amekuzoea!” “Tupo kwenye kipindi kigumu kidogo cha familia. Tulimzika mama hata miezi mitatu haijaisha. Kifo cha mama, hakikumuacha vizuri baba na mdogo wetu wa mwisho. Inaniwia ngumu kuwaacha kwa siku zote hizo.” “Upo huru asubuhi kwenda na Ethan popote unapotaka. Ilimradi tu usiku muwe naye.” “Basi naomba nikujibu kesho. Leo nikazungumze na baba. Kwani mlitaka kuondoka lini?” “Jumapili usiku.” Akajibu mama yake Ethan.

“Mnaishi wapi?” Naya akauliza tena. “Kunduchi.” “Basi kesho nitakuwa nimepata jibu.” “Unisamehe kwa kukushtukiza. Nilitegemea mdogo wangu aje anikalie na mtoto, lakini naye amenipa udhuru.” “Hamna shida. Ethan mwenyewe hana shida. Naamini kama mdogo wangu atakubali kuwepo nyumbani week hiyo inayofuata, basi mimi nitakuwa huru kuja. Hatupendi kumuacha baba na mdogo wetu huyo mdogo peke yao.” “Naelewa kabisa. Na ikishindika pia naomba usijisikie vibaya.” Naya akacheka. Wakaagana, Naya akaondoka.

 ~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

Kwa kuwa ilikuwa ni swala la kuongeza kipato cha familia, Bale aliposhirikishwa na Naya alikubali bila shida kwa makubaliano ya kuwa atakuwa akirudi nyumbani kila siku wakati Naya atakapokuwa kwa kina Ethan. Wakati mwingine mambo yalipokuwa yakimlemea chuoni alikuwa akilala chuoni hata siku mbili au tatu ndipo anarudi nyumbani. Lakini kwa sababu ni kama Naya angekuwa kazini, basi wakakubaliana hivyo.

Kesho yake Rita, yaani mama Ethan alipokuja shuleni kumchukua mtoto wake, Naya akampa jibu alilolifurahia sana. “Unaweza kutusindikiza naye uwanja wa ndege?”  Akamuuliza Naya. “Bila shaka. Ulitaka nije kwenu saa ngapi?” “Mapema kidogo ili nikuonyeshe vitu vya Ethan na uanze kuzoea mazingira kabla yakuondoka.” “Basi nikitoka ibadani tu, kwenye saa nane nitakuja.” “Saa nane utachelewa Naya. Hamna ibada ya mapema kidogo?” “Kwani ulitaka nifike kwako saa ngapi?” “Isizidi saa nne. Hata saa moja asubuhi.” Naya akacheka kidogo huku akitafakari kidogo mwishowe akakubali. “Sawa.” Akamwambia apande daladala, atakapofika kituo alichomtajia, akamwambia atamfuata kituoni ili amfikishe kwake. Hilo likakaa sawa.

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

Siku ya jumapili Naya alisindikizwa na baba yake mpaka Kunduchi kwenye kituo alichoelekezwa na Rita. Alikuwa na kibegi kidogo tu. “Ule baba.” “Wewe si umeniahidi kesho unakuja kuniangalia? Sasa mbona unawasiwasi?” “Leo mchana na usiku?” “Nitakula mama. Wewe katulize mawazo kazini.” Naya akatulia. Hakuwa amemwambia chochote baba yake juu ya Malon.

Rita alifika na Ethan ndani ya gari. Naya alipowaona, akamuaga baba yake, akashuka kukimbilia alipoegesha gari Rita. Akafungua mlango na kuingia. “Nakushukuru Naya. Maana isingekuwa hivyo, safari ningeikosa.” “Hamna shida.” Wakazungumza huku Rita akiondoa gari kurudi kwake. Naya akashangaa wanapita njia anayoifahamu. Akatulia tu. Akashangaa wanaelekea kwa Malon. Nyumbani kwake! Mlinzi akafungua geti, Rita akaingiza gari ndani.

Akamkaribisha ndani Naya, asijue Naya alishaishi ndani ya hiyo nyumba kama mama mwenye nyumba. Swali likawa je, na Malon anaishi humo humo! Wakati anamzungusha, Malon akaingia. Alishtuka sana kumkuta Naya hapo ndani. Naya akatulia tu. “Unakumbuka nilikwambia nilipata mtu wa kukaa na Ethan?”  Akamuuliza Malon huku akimsogelea. “Sijui kama utakuwa ulimuona pale, na yeye anafanya kazi pale shuleni kwa kina Ethan, kama Matron msaidizi. Ndiye nitakayemwachia Ethan na gari. Na amekubali kutusindikiza uwanja wa ndege. Kwa hiyo tutaagana na Ethan uwanjani.” Rita aliendelea kuzungumza na Malon, Naya akisikiliza tu. Malon kimya.

          “Angalau naondoka nikiwa nina amani. Sina wasiwasi.” Rita akaongeza. Alionekana ni dada mtumzima kidogo. Mkubwa hata kwa Malon. Hata zungumza yake alionekana anayo pesa. Akamgeukia Naya. Naomba ujisikie huru. Kama una njaa, jikaribishe tu huko jikoni.” Naya akaelewa anatakiwa awapishe. Akaelekea jikoni na kumuacha bado Malon anamshangao. “Umepata?”  Akamsikia Rita akimuuliza Malon. Akajua alikuwa amemtuma mahali. Akaanza kuosha vyombo alivyovikuta pale jikoni, akasikia wakizungumza kwa mbali akili zikahama pale.

Alisafisha pale ndani mpaka akamaliza ndipo akatoka nakuelekea alipokuwa amekaa Ethan. Akakaa naye. Hakumuona tena Malon mpaka mchana wakati alipokuja kuomba funguo za gari aweke mizigo yake kwenye gari. “Kuna chakula Malo. Utakuja kula?” Rita akauliza huku akimlisha mwanae. “Naona muda umeisha. Nafikiri nivizuri tukawahi foleni.” “Sawa. Ngoja kidogo tunamalizia kulishana, ndipo tutoke.” Akajibu Rita, Malon akatoka bila hata Naya kunyanyua uso. “Nenda kajiandae, mimi nitamalizia kumlisha na kumuandaa Ethan.” Naya akatoa wazo. “Utakuwa umenisaidia kweli!” Naya akamwandaa Ethan, alikuwa mtoto wa miaka mitatu tu. Akatoka chumbani kwa Ethan, akiwa amembeba. “Mbona mnabebana tena!?” Alimkuta Malon sebuleni. “Anasinzia.” “Mlete nikupokee.” Malon akampokea kutoka kwa Naya, akatoka naye nje kwenda kumfunga kwenye gari. Alikuwa ameshaliwasha gari. Rita alifunga nyumba, wakaondoka.

Malon ndiye aliyekuwa dereva, Rita amekaa mbele, Naya amekaa nyuma na mtoto. Alikuwa amefungwa kwenye kiti chake. Naya aliegemea dirishani, kimya akiwaza. Mara kadhaa Malon alimtizama kwa kupitia kioo, akakuta amekaa vile vile. “Eti Naya, umekumbuka kubeba leseni yako?” Rita akamtoa mawazoni kwa hilo swali. Akageuka. “Ndiyo.” Naya akajibu kwa heshima, akajirudisha kujiegemeza. “Sitaki tukuache halafu huku nyuma ukapata shida na polisi.” “Nilikumbuka. Ninayo hapa.” “Basi jitahidi kuwa tu mwangalifu. Pale kuna walinzi masaa yote, usiogope. Ila nisingependa watu waingie ndani. Kama una wageni, naomba iwe nje, usiwaingize ndani.” “Sawa.” Naya akakubali bila shida.

 Rita akaendelea. “Unakaribishwa kulala kwenye kochi lolote. Mashuka nimekutolea, nimeyaacha pale kwenye meza.” “Kwa nini asilale chumbani!?” Malon akauliza kwa kushangaa. “Vyumba vyenyewe si unajua vipo viwili tu. Kile kingine nilikigeuza ofisi. Na huwa chumbani kwa Ethan sipendi mtu atumie kile kitanda cha pembeni. Nataka kibaki kiwe chakulala naye mimi mwenye mchana, ikitokea nalala naye mchana.” Kimya kikazuka. “Au kwani wewe Naya unashida yakulala kwenye makochi? Maana yale makochi ni mazuri tu. Yapo kama kitanda.” “Hamna shida. Nitakuwa sawa tu.” Kimya mpaka wanafika uwanja wa ndege.

Ethan alikuwa amelala. “Labda umrudishe tu nyumbani akalale. Siku ya leo mtulie tu nyumbani. Kama una mizunguko yako ifanye kesho. Au itakuwa mbaya?” Rita akauliza na tabasamu. Malon alikuwa akishusha mizigo nyuma. “Hata hivyo sina mizunguko yeyote ile. Nafikiri nitakuwepo tu nyumbani, usiwe na wasiwasi.” “Afadhali. Na anko wake atapita usiku kuwaangalia. Anakunywa kidogo, lakini anajiheshimu. Hatakufanyia kitu kibaya, usiogope ukisikia harufu ya pombe.” “Atalala hapo hapo?” Ikabidi Naya kuuliza. “Hapana. Atapita tu kuwaangalia.” Naya akatulia kidogo. “Usiogope. Anajiheshimu. Nakutahadharisha kwa harufu tu. Usijemfungulia, ukasikia harufu ya pombe, ukaogopa.” “Sawa.” Malon akawa ameshatoa mizigo, akawasogelea.

“Kama una swali lolote, niulize, na mimi nitakupigia kila wakati kujua kinachoendelea. Maelezo yote ni vilevile, naomba usibadili kitu.” “Nimeelewa.” Naya akajibu kwa heshima. “Kama hutakuwa na mizunguko mingi, na kwakuwa baharini ni palepale karibu na nyumbani, haya mafuta kwenye gari yatakutosha mpaka na kuja kutupokea siku tunarudi.” Naya akachungulia geji ya mafuta. Ilikuwa nusu. Akamuelewa alikuwa akimwambia asitumie gari yake kwa mizunguko yake binafsi. Tofauti na walivyokubaliana mwanzoni wakati akimuomba. Alimwambia anaweza hata kuwa anakwenda kwao.

“Au unaona hayatoshi?” Akauliza Rita na tabasamu la kiungwana usoni. Malon akanyanyua uso kuwatizama. “Hata yasipotosha, mimi nitaongeza kwa pesa yangu. Usiwe na wasiwasi.” Naya akajibu taratibu tu. “Sawa basi. Nakushukuru sanaaa Naya. Mungu akubariki.” “Amina. Muwe na safari njema.” Wote wakaitikia amina. Naya akaondoka pale.

 Kwa Rita & Malon.

“Anaonekana ni binti aliyetulia. Sijui kwa nini haolewi mpaka sasa!?” Akaanza mazungumzo Rita kwa Malon mara baada ya Naya kuondoka. Malon kimya. Akanyanyua mizigo kuelekea sehemu yakuingia abiria. “Au unafikiri nimemfanyia vibaya, kumwambia alale kwenye kochi?” Rita akajishuku. “Nafikiri alijibu yupo sawa.” “Sawa, lakini wewe unaonaje? Maana ni kama ulishtuka kidogo.” Malon kimya. “Maana huyu binti ni mgeni kwangu Malo. Sizijui tabia zake. Na yeye anaonekana anashida ya pesa, kweli leo nimuachie chumba changu kilichojaa vitu vyangu vya thamani vile?” Malon akamgeukia.

“Alikwambia anashida au kwa muonekano tu?” “Sio muonekana. Muonekano anaonekana bado yupo anaomboleza. Hiyo inaeleweka kabisa, lakini tabia zake ukitoa hayo majonzi! Nitamjuaje mimi kwa hakika?” Malon akakunja uso huku wakitembea. “Majonzi!?” Malon akauliza. “Si amefiwa na mama yake! Ndio anasema hata miezi mitatu haijaisha tokea wazike. Na sidhani hata kama wanawalipa pesa nyingi pale shuleni. Sasa kwa shida ya pesa, halafu umuachie chumba wazi, huko si kumwingiza majaribuni bila sababu! Kwa hiyo nimefunga vyumba vyote, nimebakisha chumba cha Ethan na nguo zake za kawaida sana. Ila viatu na nguo nilizonunua kwa bei mbaya, nimefungia chumbani kwangu. Hata kama atashawishika, vitu atakavyoiba, sitaingia hasara.” Malon aliumia sana. Alipoa, kama alimwagiwa maji ya baridi.

“Halafu nimesahau kumwambia swala la usafi. Asipaache pachafu. Sijui nimpigie?” “Nafikiri yeye ni mtumzima, anajua kitu chakufanya Rita. Mwache. Ukirudi kama hujaridhika kwa kile atakachokufanyia, basi usimpe tena kazi.” “Asije akaacha milango wazi, AC ikawa inaisha bure. Halafu sitaki aaa.” Akaona ampigie tu Naya simu. “Sijui nilikwambia kama hiyo nyumba ina AC?” Akamuuliza. Naya akatulia kidogo. “Naya?” “Nipo, nasikiliza.” “Ndio nilitaka kukusisitiza usiache milango wazi, AC ikapotea tu bure ndani kukawa na joto. Ethan hapatani na joto kabisa. Anaotwa vipele. Usizime wakati wowote ule.” “Sawa. Nimeelewa.” Naya akajibu kwa heshima.

“Na usafi. Nakuomba uwe unambadilisha mara kwa mara. Akijimwagia tu maji, jitahidi kubadilisha ili asikohoe. Usije kumlaza kitandani kwake kabla hujamuosha na kumbadilisha nguo. Si unajua akilala na nguo alizoshinda nazo anaweza kuugua kwa kuvuta vumbi akiwa usingizini?” “Ndiyo.” Naya akaitikia. “Basi tutazidi kuwasiliana. Nakushukuru sana Naya mdogo wangu.” “Karibu.” Naya akajibu na kukata. “Anaonekana ni binti mtiifu.” Rita akasifia wakati anarudisha simu kwenye pochi. Malon kimya.

     Wakaingia ndani baada yakuonyesha hati zao zakusafiria, wakaweka mizigo, wakapanda juu kabisa sehemu ya kusubiria. “Nolan atachanganyikiwa kukutana na Naya. Anavyopenda vimwana yule!” Malon akashtuka kidogo. “Rita! Yule ni binti wa watu. Kama unajua Nolan hataweza kujiheshimu, kwa nini unataka aende?” Rita akacheka. “Hawezi kufanya kitu asichokipenda. Atamtongoza tu. Na anavyojua kubembeleza, mpaka amkubali. Huwa hajui jibu la hapana, labda asimpende huyo Naya.” Malon akanyamaza kama anayetafakari. “Acha hofu. Nolan hawezi kumbaka. Akimpenda atamtongoza tu. Na anavyojua kuhonga, Naya mwenyewe ataingia kwenye anga zake. Ngoja nimpigie nijue walipofika. Asije kuwa amekata kona zake kuonyesha mashoga zake ufahari na gari langu.” “Kama unashindwa kumwamini na gari yako, kwa nini umemwachia mtoto wako?” “Si ndio maana na Nolan yupo! Huwezi kuamini mwanadamu kila wakati!” Simu za kumtaka kujua alipo na anafanya nini ziliendelea kwa Naya, mpaka wanaondoka hapo nchini. 

Kwa Naya.

Naya alitoka pale uwanja wa ndege na kurudi nyumbani kwa Rita kumlaza Ethan. Akaanza kusafisha nyumba na kupanga vizuri akiokota toys za Ethan na usafi mwingine mpaka mabafu yake mpaka alipomaliza. Alikaa hapo mpaka saa kumi na mbili jioni, Ethan hakuwa ameamka, akasikia hodi. Akajua tu ni huyo Nolan. Akaenda kufungulia. “Hujambo Naya?” Moja kwa moja na kumtaja jina kumuonyesha anajua kinachoendelea. “Sijambo. Karibu Nolan.” Na yeye akamuonyesha anamfahamu. Nolan akaingia. Hakuwa akinuka pombe. “Vipi, za hapa?” “Nzuri tu.” “Kuna shida yeyote?” “Hapana.” Naya akajibu. “Kuna kitu chochote unahitaji?” Nolan akaendelea kuuliza huku anakaa. “Hapana.” Naya akajibu na kukaa.

“Sasa mimi sijisikii vizuri. Nipo kwenye matibabu. Sitakaa sana. Rita amesema amekupa namba yangu. Ukiwa na shida, nipigie muda wowote.” “Sawa, na pole.” “Asante.” Akajibu Nolan. “Kuna chakula dada Rita alipika mchana. Nikuwekee?” Nolan akamtizama Naya kama ambaye hakumsikia vizuri. “Ni viazi na nyama ya kuku.” “Kuna limao?” Akauliza Nolan. “Labda niangalie kwenye friji.” “Basi ukiniwekea na hicho chakula, hapo utakuwa umenisaidia. Nitakula hapa, nikifika nyumbani ni kumeza dawa na kulala.” Naya akampashia moto, akamuwekea na limao. Akampelekea. Alikula vizuri tu. Akamshukuru Naya, akaaga na kuondoka. Na yeye alionekana kijana anayejielewa. Alifanana na Rita, ungejua ni ndugu tu.

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

Kesho yake Rita akampigia simu kumwambia walifika salama. Akatoa maelekezo kama kawaida yake. Akazungumza na mtoto wake, wakaagana. Naya hakutoka siku hiyo. Alibaki tu pale na huyo mtoto. Ilipofika mchana Nolan akampigia. “Nitakuja na chakula cha usiku. Huna haja yakupika.” “Sawa.” Ilipofika jioni wakati Naya anapika chakula cha Ethan, Nolan akaingia akiwa na nguo za kawaida tu. “Unaendeleaje?” Naya akamuuliza. “Nimelala siku nzima leo. Hata kazini sikwenda.” “Pole. Ni nini kinakusumbua?” “Malaria. Naona mbu wa baa, wamenigeuka.” Naya akacheka. Karibu. Mimi nipo jikoni na Ethan. “Nilikwambia usipike.” “Ni chakula cha Ethan.” “Kwani mtoto wakishua hali chips? Njoo Ethan.” Akamwita. “Maana huyu mtoto kama mboni ya jicho la Rita!” Ethan akaenda kwa anko wake. Akampakata. “Niambie Ethan, mtoto wa mama.” Naya akaamua kurudi jikoni. Hiyo siku ikaisha hivyo.

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

Safari za Nolan zikawa za kila siku jioni. Akitoka kazini, anakwenda hapo nyumbani kwa dada yake. Atakula na Naya wataongea na kucheka kidogo kisha anaondoka kwenda kulala nyumbani kwake. Hakuwahi kuja hapo akiwa amelewa hata mara moja. Mcheshi, na alionekana kupenda watoto. Alifika hapo na kucheza na Ethan. Naya alikuwa akizungumza tu na baba yake kwa simu. Hakuwahi kutoka hapo.

“Sasa jumamosi lazima twendeni tukachezee maji ya baharini.” Naya akacheka. “Utakuja kumchukua huyu?” “Nataka na wewe twende wote. Hatutakwenda mbali. Hapahapa Kunduchi. Mtarudi kupumzika, halafu usiku ndio tutakwenda kuwapokea Rita na mpenzi wake.” Moyo wa Naya ukapasuka. Akanyamaza kidogo. “Au unampango gani?” “Hakuna. Tutakwenda tu ili na yeye Ethan afurahie. Nimekuwa nikimfungia tu humu ndani.” “Basi mwandalie begi lake, nitakuja kuwafuata mapema tu.” “Sawa.” Naya akakubali.

Ijumaa siku moja kabla ya Rita na Malon kurudi, asubuhi alitoka na Ethan, akarudi kwao. Alikaa na baba yake mpaka mida aliyojua atamuwahi Nolan. Akabadilisha nguo akachukua vivazi vya ufukweni, miwani na kofia. Naya mtoto anayejijulia, akachukua vitu vyakumtoshea. Akarudi nyumbani kwa Rita na Malon. Alikuja tena Nolan, akawaambia anawatoa kwenda kula icecream. Walitoka na gari ya Nolan. Wakaenda kula icecream wakaishia kula na chakula cha jioni. Wakapata wakati mzuri, Nolan akawarudisha nyumbani kwa makubaliano ya kuja kuwachukua kesho yake kama walivyokubaliana. 

Siku ya jumamosi. 

M

ida ya saa nne kasoro, Nolan akawa amewasili hapo. Alibaki amekodoa macho. Naya alikuwa amevaa pensi fupi haswa, nyeupe na kitop kilichomkaa vizuri, kata mikono kama singilendi ya rangi ya maji ya bahari. Kofia nzuri ya mkeka yaduara iliyopitishwa kitambaa cheupe kuzunguka mduara wa juu ikafanana na penzi aliyovaa. Miwani ya jua. Akaweka hereni ndogo tu. Ni kama alinyoa vinyweleo vyote vya miguu. Mapaja mpaka miguu safi. Hakuna kinyweleo hata kimoja. Na rangi yake ile, ungependa kumtizama Naya. Kucha safi. Alikata tu na kusafisha vizuri. Akamvalisha Ethan kidogo kama yeye na kofia.

“Umependeza sana Naya. Kama toto la majuu! Wewe ni mwanamitindo?” Naya akacheka na kukubali. “Ndiyo.” Nolan akamtizama mara mbili mbili. “Unafanyia wapi shuguli zako?” Nolan akazidi kudadisi. “Tuondokeni utanisimulia zaidi kwenye gari.” “Hakuna hata habari ndefu. Ni kitu tu ambacho nakipenda.” “Ulishajaribu kufanya?” “Ndiyo. Lakini kwa mazingira ya hapa, hakilipi kwa haraka. Inabidi kuwa mvumilivu na siunajua na maisha nayo huwa hayasubiri? Pesa inahitajika.” “Mimi ningekuwa mteja wako wa kwanza.” Naya akacheka sana. “Kama hii kofia, nimejitengenezea mwenyewe.” “Nzuri sana. Unaonekana mtaalamu! Umependeza.” Walikuwa na wakati mzuri sana huko beach.  Nolan akawa mstaarabu na mcheshi tu. Na kweli hawakwenda mbali.

Mtoto alipoanza kusinzia, Naya akaona warudi nyumbani. “Nashukuru kwa wakati mzuri Nolan. Nilihitaji haya mapumziko.” “Karibu. Lakini si unajua leo sio lazima ikawa mwisho?” Naya akacheka kama anayefikiria. “Sio lazima kukawa na maandalizi mazito. Nikuamua tu.” “Basi hiyo siku utakayopanga kuja huku tena, uniambie. Ili kama nina nafasi, na mimi nikufuate.” “Sawa. Tutapanga zaidi.” Akashuka, akambeba Ethan kumwingiza ndani. Alikuwa amelala. Naya akachukua vitu kwenye gari, akamfuata nyuma.

“Ulisema usiku tutakwenda wote kuwapokea au wewe ndio utakwenda?” “Rita anamtaka mtoto wake. Anataka akifika uwanjani pale, amkute mwanae ndio akili yake itatulia.” Naya akacheka. “Sasa ni lazima na mimi niwepo? Au naweza kukuachia mtoto mkaenda tu?” Nolan akafikiria kidogo. “Sijui makubaliano yako wewe na Rita. Ila nafikiri ni vizuri ukawepo.” “Sawa.” “Nitakurudi kwenye saa tatu hivi. Mwache huyu alale, usimuamshe, ili mama yake amkute macho.” “Sawa.” Nolan akaondoka.

Naya akajitahidi kuacha nyumba ya watu safi. Akafua mashuka aliyokuwa amelalia. Akayakunja vizuri. Mpaka saa tatu Nolan anawafuata, nyumba ilikuwa ikiridhisha. “Hapa mtaelewana na Rita. Huwa hajui kuishi na watu. Anajipenda yeye na vitu vyake tu. Tokea mdogo yupo hivyo. Anathamini sana vitu vyake, na hapendi kuishi na watu wengi kwenye nyumba yake.” “Baba yake Ethan?” “Walishindwana mapema tu. Rita alipoona umri umekwenda na hakuna muelekeo, akashika mimba. Wala huyo mwanaume hajui kama Rita anamtoto wake. Alimfumania, akajua hawezi kumsamehe, na akajiambia hataki tena kuanza mahusiano. Akamdanganya kama amemsamehe ili tu ashike mimba. Lengo lilipotimia, akaachana naye moja kwa moja na kukimbia nchi kabisa. Walikuwa wakiishi huko ugaibuni.” Naya akashangaa sana.

“Rita anajipenda sana.” Naya akacheka. “Uliniambia.” “Naona hujaelewa.” Naya akacheka. “Ni anajipenda haswa.” “Anaonekana.” “Basi ndivyo alivyo. Huwa hapendi kujisumbua nafsi yake. Matatizo hayataki kabisa. Sijui kuumizana kichwa, hawezi. Lakini naona kwa Malon, amependa. Sasa sijui watafika wapi. Maana naye huwa ana mwanzo, mwisho wake huwezi kuutabiri.” “Ungejua na Malon yupo hivyohivyo!” Naya akawaza nafsini mwake. Wakatulia. Na hapo pia Naya alikuwa amependeza tu, na nywele zake za chini. Malon na Rita walikuwa wakifika nchini na ndege ya saa tano usiku. Walitoka pale mida ya saa nne. Ethan ndio alikuwa ni kama ametoka usingizini tu.

Walifika uwanja wa ndege mapema kidogo, wakatafuta mahali wakakaa, Ethan akikimbia huku na kule. Nolan na Naya wakizungumza mambo ya kawaida tu, wakijaribu kufahamiana. Muda ulipofika, wakasikia tangazo kuwa ndege ya KLM ndio inatua. Ilikuwa saa tano na nusu usiku. Wakasimama kusogelea mlango wa kutokea abiria, Nolan akiwa amembeba Ethan. Mama yake alitoka akiwa amemtangulia Malon. Walionekana wamepata mapumziko mazuri.

“Ethan!” Rita akapiga kelele na kumkimbilia mwanae aliyeanza kumshangilia mama yake. Naya akapokea mizigo kutoka kwa Rita ili kuweza kumbeba mtoto wake. Rita alipompokea tu mtoto wake, Nolan akamgeukia Malon. Akamsalimia, na kumsogelea Naya. “Nikupokee nini?” Naya akajiangalia vile vitu alivyokuwa amebeba. “Chochote tu. Au pia unaweza kuacha. Sio mizigo mizito.” Akampokea karibu yote kasoro pochi.

“Poleni na safari.” Nolan akamgeukia tena Malon aliyekuwa kimya akisukuma kigari cha mabegi. “Asante. Tunamshukuru Mungu tumerudi salama.” Naya kimya, hata hakumgeukia au hata kumsalimia. Wakatembea mpaka kwenye gari ikisikika milio ya mabusu kwa Ethan na mama yake na vicheko vya wawili hao. Wote wakapanda kwenye gari. Nolan dereva. Malon Akaka mbele, Naya na Rita wakakaa nyuma. Ethan katikati kwenye kiti chake.

“Pole na majukumu Naya.” “Asante, japo tumekuwa na wakati mzuri. Nolan alitupa kampani. Hatukuwa wapweke.” “Nimeona picha zenu za beach.” “Haaa! Nolan wewe!” Naya akashangaa huku akicheka. “Rita naye? Nani amekwambia useme?” “Hukuniambia kama ni siri bwana. Lakini mlipendeza sana. Ulikuwa kama toto lililoshushwa kutoka Los Angelas!” Naya akacheka sana. “Nolan hakuniambia kama anakutumia!” “Hamna neno. Nimefurahi kama mmepata wakati mzuri. Naona na Ethan wangu anafuraha. Uzito umeongezeka! Nashukuru sana.” “Na mimi nimefurahi kama umeridhika. Ila naomba leo nikalale nyumbani.” “Umechoka kulala kwenye makochi?” “Hapana. Hiyo sio sababu. Ila kwa kuwa wenyewe mmerudi, sioni sababu yakuendelea kuwepo.” “Usiku huu Naya!?” Nolan akadakia.

“Hivi tunavyozungumza, baba yupo kituoni ananisubiri. Nataka nikifika nikukabidhi nyumba yako, niondoke. Hata hivyo jumatatu natakiwa kazini. Inabidi kesho niwepo nyumbani nijiandae na kazi jumatatu.” “Hapo sawa. Nashukuru Naya. Asante.” “Karibu. Na mimi nashukuru kwa kuniamini na Ethan. Nimepata naye muda mzuri sana.” Wakaendelea mazungumzo mpaka wakafika. Rita alifurahia kukuta nyumba ipo sawa. Naya akampigia simu baba yake, akasogea mpaka getini. Rita akamlipa pesa yake na kumwambia zawadi yake atampa siku ya jumatatu shuleni. Naya akashukuru na kuondoka.

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

“Hapa sio nyumbani kwa Malon!?” Akauliza baba yake mara baada ya kupanda kwenye gari. “Ni kwake. Naona sasa hivi anaishi dada mmoja anaitwa Rita, na mtoto wake Ethan. Ethan huwa anakuja kwenye ile shule ninayofanya kazi. Kwa kuwa ni mdogo, muda mwingi nakuwa naye na yeye yupo kwenye kundi la ‘after school care’. Kwa hiyo huwa nakuwa naye mpaka jioni kabisa mama yake anapokuja kumchukua.” Baba yake akatulia kidogo.

“Mbona kama naona kuna swali ambalo haliulizwi?” Naya akamgeukia baba yake. “Kuna jibu la kutaka kunijibu?” Baba yake na yeye akamuuliza. “Ndiyo, nimemuona Malon. Lakini sijazungumza naye. Ila anaonekana alifanikiwa kwenye biashara zake. Amerudia afya yake nzuri au niseme hali yake ya zamani. Amenunua gari nzuri tu na nyuma ya ile nyumba kulikuwa na kinyumba kidogo kama kichumba kimoja tu, nimeona amepatengeneza vizuri kweli. Amejenga zaidi kikawa kinyumba kidogo tu lakini kilichokamilika na ameongeza sebule na choo kizuri tu humo ndani. Nilichungulia wakati yeye amesafiri.” Baba yake akamwangalia. “Alisafiri na huyo mwenye mtoto?” Naya akanyamaza na kuinama. Baba yake akapata jibu, hakuuliza tena maswali. 

Hata kama usiku ukiwa mnene kwa kiasi gani huwa Panambambazuka...

S

iku ya jumatatu akiwa kazini, anasafisha na kupanga sehemu wanayolala watoto, akapokea simu kutoka kiwanda cha Cocacola. Alishafanyiwa mpaka usahili, lakini wakamwambia watampigia. Alisubiri Naya mpaka akakata tamaa, maana hiyo ilikuwa kabla hata mama yake hajafariki. Aliulizwa kama bado anataka kazi upande wa masoko. Naya akakubali kwa haraka sana. Akaambiwa aende ofisini siku inayofuata kuanza kujaza karatasi za kazi, vipimo na kupewa orientation kabla hajaanza juma lijalo. Naya alifurahi sana.

Kwa kuwa alikuwa akifanya kazi ya watoto pale, asingeweza kuacha tu. Akazungumza na kiongozi wake, akamshauri aandike barua ya kutoa notice ya muda mfupi, ili waachane kwa amani. Ila alimwambia pia madhara ya uachaji kazi kwa namna hiyo ni kukosa mshahara wa mwezi huo. Kwa kuwa bado hakuwa amelipwa, akamwambia inamaana itabidi aachie huo mshahara ili aondoke kwa haraka na bila kharibu hapo kazini. Hilo akaafikiana nalo kwa kuumia kidogo maana ilikuwa anaacha mshahara alioufanyia kazi mwezi mzima na unahitajika sana nyumbani kwao. Lakini akajifariji kuwa kule kufanya kazi kwa Rita akamlipa, ilikuwa ni njia ya Mungu kumpa pesa. Akaanza kupigia mahesabu ile pesa aliyokuwa amepewa na Rita. Akajua hatapata sana shida. Atapata ya kujikimu kipindi hicho anaanza kazi mpya. Akajua atapata pesa ya nauli, na ukiongezeka usafiri wa baba yake, akajua atafikisha mwezi mpaka atakapopokea mshahara wa huko anapokwenda kwenye kiwanda cha Soda.

Akampigia simu baba yake na kumueleza. “Hongera mama.” Naya akaanza kulia. “Nije kukuchukua?” “Labda jioni. Lazima nikae mpaka jioni baba. Ila nimefurahi.” Baba yake akacheka. “Nimesubiri mpaka nikaanza kusahau kama nina shahada ya masoko! Nikasahau hata kama nimesoma baba. Nimekuwa na kazi ya kusafisha watoto na kuwalisha siku nzima mpaka nikaanza kuzoea.” “Na ndio maana Mungu akaona akutoe huko. Alijua unaanza kubweteka, unazika ndoto zote.” “Na kweli baba. Sina tena mipango! Kuna ukimya mkubwa sana ndani yangu. Sio kama zamani. Nimeshajiridhikia na maisha. Nimepoteza sababu.” “Ndio maana Mungu ameona akutoe hapo.” “Uje na Zayoni basi ili tukasherehekee mahali.” “Sidhani kama atakubali. Si unajua bado?” Wakatulia kwa muda, kila mtu akiwaza lake. Zayon aliumwa sana baada ya kifo cha mama yao. Alikuwa anashindwa hata kutoka kitandani. Kwa muda wa mwezi mzima, Bale ndiye alikuwa akimuhudumia hapohapo kitandani mpaka kumuogesha. Hata shule alikuwa akishindwa kwenda.  

“Nitazungumza naye. Atoke kidogo. Amekula?” Naya akauliza. “Bado hajarudi kutoka shule. Ila nitahakikisha anakula.” “Nitampigia simu na Bale nimwambie. Asirudi nyumbani, tukutane naye sehemu hukuhuku mjini.” “Sawa. Ila hata kama wao hawataweza, mimi nitakuja kukuchukua.” “Asante baba.” Wakaagana na kukata simu. 

Katikati ya Mafanikio, hapakosi vikwazo.

K

ama kawaida, Ethan alikuwa mtoto wa mwisho kuja kuchukuliwa na siku hiyo tena. Mama yake alilalamikia foleni za jioni kumtoa huko ofisini kwake mpaka Mbezi Beach ilipokuwepo hiyo shule ya mtoto wake na ndipo alipokuwa akifanya kazi Naya na kumlazimu kuwa akimsubiria mpaka afike hapo kumchukua mwanae na mara zote huwa yeye Naya wa mwisho kutoka kazini akimsubiria huyo mtoto. Lakini Naya hakuwahi kulalamika hata kwa kiongozi wake japo wafanyakazi wote mpaka kiongozi wake walichukia hiyo tabia ya uchelewaji.

Saa moja kasoro usiku ndipo Rita akawasili hapo shuleni. “Nisamehe Naya.” Naya akacheka tu. “Nahisi watanifukuza hapa na mwanangu jamani! Kila siku yeye ndio wa mwisho! Na mlinzi ameniambia unaacha kazi. Ni kweli?” Naya akashangaa sana. “Mlinzi amejuaje?” “Alikuwa ananiambia nimuombe Mungu aletwe msichana mwingine mzuri atakayeweza kunivumilia na mwanangu, wewe unaondoka.” “Na kweli dada Rita. Mida hii wafanyakazi wote wanakuwa wameshaondoka. Kama hapa tumebakia mimi na Ethan tu. Itabidi kutafuta mtu. Lasivyo ni kweli watakufukuza hapa. Uongozi hawataweza kumlipa mtu kwa masaa ya ziada. Na matron anakuvumilia kwa sababu nilimwambia sina neno kubaki na Ethan.” Rita akawa kama anafikiria.

“Tafuta dereva.” Naya akampa wazo. “Watu hawaaminiki Naya! Wakianza kumchezea mtoto wangu?” “Basi endelea kumuomba boyfriend wako na Nolan. Peaneni zamu. Ili muweze kumchukua Ethan kwa wakati.” “Mmmh!” “Nini?” “Sidhani kama kuna muendelezo wa maana na Malon!” Naya akacheka moyoni. Alimjua Malon. Mambo yanapoonekana kushika kasi yakueleweka, huwa anakimbia. Kwa sababu yeyote ile. Alimjua sio muoaji. Hakutaka kuuliza wala kuendeleza hayo mazungumzo yao. “Omba Mungu, atakusaidia kupata mtu wa kukusaidia. Ethan ni mtoto mzuri sana, sitaki aje aonekane mzigo.” Hilo likamfurahisha sana Rita.

“Halafu nilikujia na zawadi yako, jana akaja Thia nyumbani, akaipenda na kuichukua.” Naya akacheka. “Thia yule mdogo wenu?” “Yeye yeye! Anatamaa huyo!” “Basi hiyo ilikusudiwa iwe yake. Naomba mimi nikuage, niwahi. Baba ananisubiri hapo nje tokea saa 12.” “Samahani sana Naya. Kwa hiyo kesho hutakuwepo? Nilitaka kesho nibane muda wa chakula cha mchana, hata kama sitakula ilimradi nikakununulie zawadi yako nikuletee.” “Huna sababu yakufanya hivyo. Vitu hapa mjini vipo tu. Ingekuwa ni kitu umeleta kutoka safari, hapo sawa. Kwenda kuninunulia hapo mjini inakuwa kama deni!” “Sio deni. Najisikia vibaya.” Naya akaona ni unafiki tu. Kama angekuwa na nia asingegawa zawadi yake, hilo ni moja. Pili, jana ilikuwa siku ya jumapili, alikuwepo tu nyumbani. Si angenunu tu hiyo zawadi akaleta siku hiyo kuliko kumtangazia hapo ugumu atakao pambana nao ili kupata hiyo zawadi!

“Usijali kabisa. Kuwa na amani. Hata hivyo kesho sitakuwepo.” Naya akamjibu vizuri tu bila kuonyesha kinyongo. “Basi nitakuachia hapa.” Naya akashangaa kidogo. “Hapana! Hakuna sababu ya kufanya hivyo. Sio deni. Nilifanya kazi kwako, umenilipa haki yangu, huna sababu yakuhangaika tena. Eti mpaka uache kula sababu ya zawadi yangu tu! Sidhani hata kama ina umuhimu huo. Naomba nikuache dada Rita. Usiku mwema.”  Naya akarudi ndani akamuacha amesimama hapo. Alimjua Rita ni mbinafsi sana. Alimlaza kwenye makochi muda wote, asitake kutumia vitanda vyake. Alimuomba amsaidie mtoto akimuahidi atamruhusu kwenda kwao, lakini akaja kumgeuka akihofia gari yake na mafuta aliyoacha nusu tanki ya gari! Akajua anampotezea muda tu na hana shukurani japo amekuwa akikaa hapo na mwanae kila siku akichelewa hapo shuleni. Alipotoka, hakumkuta hapo.

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

Rita akiwa njiani kurudi kwake akampigia simu Malon. “Vipi?” “Sijui nimemuudhi nini Naya!?” Akaanza kwa kulalamika. “Kwa nini tena?” “Amenibadilikia!” “Amekutukana?” Malon akauliza. “Hapana. Ila jinsi alivyonijibu! Kama sio yeye!” “Kwani uko wapi?” “Njiani nipo na Ethan, ndio nimetoka kumchukua.” “Saa hizi saa moja hii!?” “Nilibanwa Malon! Kazi zilikuwa nyingi.” Malon akatulia. “Si unajua sikuwepo kazini week nzima? Sasa nimekuta viporo kibao!” “Unakuwa ukiwalipa sasa hizo za ziada ambazo unachelewa kuchukua mtoto?” “Hee! Mamilioni yote hayo ninayolipia hapo shuleni na bado niwalipe zaidi!” “Unalipia mpaka saa 12 kamili, Rita. Usisahau muda huo wa ziada hao wafanyakazi wanabaki hapo kwa garama zao wenyewe.” “Garama gani wakati wanabaki kwenye jengo la shule ambako sisi wenyewe tunalipia umeme na ulinzi? Kwanza msichana kama huyo Naya anayekuwa anabaki na mtoto wangu hana chochote chakufanya. Anawahi nyumbani kwenda kukaa tu bure. Mimi najenga taifa. Kukaa na mtoto wangu nusu saa au dakika 45 zaidi huoni kama na yeye anachangia kwenye ujenzi wa taifa?” Malon kimya.

“Kwanza nimemlipa pesa nyingi sana kwa kuishi kwangu. Nimemuachia chakula, gari na Nolan amekuwa akimletea chakula hapa nyumbani na kumtoa hiyo siku ya jumamosi! Hajaingia garama yeyote ile. Pesa yote mfukoni.” Rita akaendelea kuongea kana kwamba yeye ndio anamsaidia sana Naya.

“Kwani hiyo hasira yote na vyote unavyomuhesabia Naya, vinatokana na nini Rita? Mbona unakuwa kama alikuja kukuomba kazi wakati wewe ndiye uliyemfuata na kumuomba? Kwani amekutukana?” “Hapana. Lakini naona amekasirika sababu sikumpa ile zawadi niliyomnunulia wakati tupo Brazil.” “Kwa nini tena?” “Alikuja Thia, nikampa yeye. Kwanza tuliona ni kitu cha thamani sana kumpa mfanyakazi ambaye hajui hata thamani yake.” Malon akaumia sana. “Ndio nikamwambia nitamnunulia kesho, naona amezira.” “Nakuuliza, amekutukana au amekujibu vibaya?” “Amesema haoni sababu inakuwa kama deni. Hata hivyo hapa vitu vipo tu, haoni sababu ya mimi kununua.” “Sasa huo si ukweli na ni kama amekupunguzia shuguli?” “Tatizo ni jinsi alivyonijibu Malon. Amenijibu kwa dharau kama asiyetaka ni ni… sijui niseme nini!” Malon akatulia lakini akihofia asije peleka hayo malalamishi kazini kwa Naya na kumuharibia kazi.

“Kwanza anaondoka pale shuleni. Wanasema amepata kazi sehemu nyingine. Naona ni afadhali maana nisingeweza kufanya naye kazi tena. Ningewaambia uongozi anakiburi.”  Malon akashangaa sana. “Kwa kuwa amekataa zawadi tu!?” “Anakiburi Naya. Ana kama kijiunafiki.” “Sio wewe ulikuwa ukimsifia hata jana hapa kuwa amefanya vizuri na ni mnyenyekevu.” “Nafikiri niliongea kwa haraka bila kumchunguza. Au labda ndio yale ya masikini akipata. Labda hiyo kazi aliyopata ndio imemjengea kiburi. Na nitamwambia Nolan asimfuatilie tena. Anaonekana ni kiburi na Nolan alitaka atulie naye.” “Hapana Rita. Nahisi ulikuwa ukimtumia tu. Sasa kwa kuwa unaona huna matumizi naye tena, ndio maana unambadilikia.” Rita akashtuka sana.

“Mbona unaniambia hivyo Malon!?” “Mimi ni mkweli na ni muwazi Rita. Itabidi unizoee tu. Nishakuwa kwenye nafasi aliyokuwepo Naya. Nikakutana na watu walionitumia kwa manyanyaso makali. Najua na kuelewa watu kwa kuwatizama. Naya sio mbaya. Sifa ulizompa juzi japo hukumaanisha, ni za kweli. Amekaa na mtoto wako, hakutumia gari yako vibaya. Ukasifia umekuta amejaza gari yako mafuta. Ameacha nyumba ‘yangu’, safi japo alilala kwenye makochi. Amekufulia na mashuka yako na nguo zote zako na mtoto umekuta safi. Ukafurahia hata hajala vyakula vyako.” “Si kwa kuwa Nolan alikuwa akimletea chakula!” Akajibu Rita bila hata aibu.

“Mtu aliyekaa na mtoto wako siku zote hizo bila shida ila upendo tu, unaona shida kula chakula nyumbani kwako! Kweli Rita? Huyu binti anakaa na mtoto wako pale shuleni mpaka usiku huu, huoni unayo sababu yakumshukuru kuliko kufikiria kumuharibia kwa uongozi, kwa kosa la kukataa zawadi duni uliyopanga kumpa.” “Isingekuwa duni.” “Naomba nikuage Rita. Ila umenishangaza sana.” Malon akakata simu.

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

Naya alikuwa akila na familia yake kama kumshukuru Mungu kwa hiyo kazi aliyopata kwenye kiwanda cha Coca. Ila ilikuwa kimya kimya tu usiku huo. Hapakuwa na utani tena. Alifanikiwa kumshawishi Zayoni na Bale naye akafika pale walipokubaliana wakutane. Wakaagiza chakula wakawa wanakula kimya kimya tu. Mara simu ya Naya ikaanza kuita. Akaitoa kwenye pochi, akasoma jina akaona ni Rita. Akaipuuza. Ikaita tena na tena.

Baba yake akamwangalia. “Huyu ni Rita, baba!” “Kwa nini hutaki kupokea?” “Sioni sababu. Nahisi anasumbuliwa na dhamira tu.” Naya akawasimulia kwa ufupi tu. “Huwezi kujua. Umelala kwake siku 5, kama kuna kitu anataka kukuuliza hakioni?” “Sidhani baba. Nilimkabidhi vitu vyake vyote. Itakuwa ni nini tena usiku huu?” “Jibu utalipata ukipokea hiyo simu.” Naya akanyamaza.

Mara simu ya Nolan nayo ikaingia. Naya akakunja uso. “Huyu ni Nolan, mdogo wake Rita!” “Inawezekana kuna tatizo. Pokea Naya.” Bale akashauri. “Basi itabidi nirudishe simu ya Rita. Nikipokea ya Nolan, kama wapo pamoja, hatajisikia vizuri.” Hapo hapo Naya akampigia simu Rita.

Akapokea akiwa analia sana. “Kuna nini!?” Naya akauliza kwa mshangao. Rita alikuwa akilia sana. “Ethan yupo sawa?” “Nataka uniambie ukweli Naya, eti mimi nakutumia?” Akauliza Rita. “Hayo yanatokana na nini!?” Naya akauliza kwa utulivu tu akishangaa. “Wewe nijibu tu.” Akasisitiza Rita. “Mimi nakuheshimu sana dada Rita. Umenipa kazi, nimekufanyia kazi yako. Umeridhika, tumeachana kwa amani. Naomba kusiwepo na kesi nyingine ambazo hata sielewi! Kama kuna tatizo na kazi niliyofanya, naomba uniambie. Hayo mambo mengine, naomba nisijihusishe nayo. Tafadhali sana.” “Sio kwamba ni kesi. Nahisi naonekana mbaya kwa sababu…” “Rita! Dada Rita! Tafadhali naomba nikuage. Usiku mwema.” Naya akakata simu.

Baada ya muda mfupi hata kabla hajamueleza baba yake, simu ya Nolan ikaingia. “Nolan!” Naya akapokea, akamsikia Rita bado analia sana. “Upo mbali sana?” “Kwani kuna nini!?” “Nafikiri tunahitaji kuweka mambo sawa. Unaweza kuja?” “Usiku huu!?” “Tafadhali Naya.” “Kwani ni nini tena!? Kuna kitu nimeharibu?” “Labda ufike tuzungumze.” “Basi nakuja na baba yangu na kaka zangu. Kesi mimi siziwezi.” “Sawa.” Naya akakata simu. “Naombeni mnisindikize.” “Kuna nini?” “Mimi sielewi kwa hakika. Ila naomba mnipeleke.” Wakaondoka hapo.

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

          Ilikuwa saa tatu usiku wakati Naya na familia yake wanaingia hapo nyumbani kwa Malon. “Hapa si ni nyumbani kwa Malon!?”  Akauliza Bale. Naya akamueleza kwa kifupi kuwa amempangisha huyo dada, lakini ni kama wapo kwenye mahusiano. Bale akanyamaza. Wakakaribishwa na walinzi, wakaingia ndani.

Walikuta ndugu wa Rita. Naya aliweza kumtambua Nolan. Wakakaribishwa. Alikuwepo msichana mwingine, Naya akahisi ni Thia na wazazi wao. Naya akasalimia kwa kuwapa mkono na mshangao usoni. “Kuna nini Nolan?” Naya akauliza kwa wasiwasi. “Samahani Naya. Ni kutaka kuwekana tu sawa.” “Juu ya nini?!” Naya akauliza. Mara mlango ukafunguliwa, akaingia Malon. Wote wakageuka. Naya akamtizama, alionekana ametoka usingizini.

“Ni nini kinaendelea?” Akauliza Malon kwa mshangao. “Kwani wewe nani amekuita hapa? Wewe si unaniona…” “Rita! Chochote kisicho chema kinachoedelea kwenye haya mazingira, mimi kama mmiliki kinanihusu. Walinzi wamekuja kunigongea kuwa kuna tatizo, wewe unalia sana na msichana aliyekuwa akikutunzia mtoto ameletwa hapa na wanaume watatu. Nikajua ni Naya. Sasa nilitaka kujua, kuna nini?” Malon alizungumza bila hata salamu.

“Labda Naya aeleze yeye.” Akadakia Thia. “Nieleze nini!?” Naya akauliza kwa mshangao. “Kisa cha huko shuleni.” Akafafanua Thia. Baba yake Naya, na ndugu zake bado walikuwa wamesimama. “Jamani, ni nini kinaendelea mbona sielewi? Mbona ni kama tuliagana na dada Rita kwa amani kabisa! Ni nini tena chakuzungumzia!?” “Labda yeye Rita aeleze.” Nolan akadakia.

Wote wakamgeukia Rita. “Naya hakuwa hivyo.” Akaanza Rita. “Mimi nimemsaidia kwa kumpa kazi, nimemlipa vizuri, anakuja kunijibu vibaya! Ananidhalilisha mbele ya walinzi!” “Labda kabla hujaendelea sana Rita na kumtenda Mungu dhambi, naomba kujua ni kazi gani uliyo nisaidia?” Naya akauliza taratibu tu. “Nimekukuta ukiwa na shida, nimekupa kazi ya kukaa na mwanangu. Nimekupa mazingira mazuri ya kulala. Siku tano mfululizo! Wenzio kulala kwenye nyumba kama hii wanalipia pesa nyingi sana tu. Kwa siku hizo tano ambazo umelala hapa, tumekulisha bure, na bado nimekulipa pesa zaidi ya mshahara unaolipwa pale kazini kwako. Nimekuthamini nikakuweka karibu na mwanangu, leo kukunyima zawadi niliyompa mdogo wangu ndio inakufanya unidhalilishe kiasi cha kunijibu hovyo! Hivi unajua baba yetu ana hisa nyingi tu kwenye kampuni hiyo ya Cocacola, anaweza kuongea chochote na hiyo ajira inayokupandisha kiburi, ukaiokosa kabisa?” Naya akakunja uso akiwa haelewi kabisa.

“Ni nini unaongea Rita!? Ujue sikuelewi kabisa!? Unaongea mambo ambayo hakika sielewi! Ni kama unaonyesha kuna kutokuelewana kulitokea kati yetu ulipokuja shuleni kumchukua Ethan, au mimi ndio sielewi?” Naya akauliza akiwa haelewi kabisa. “Ndiyo. Vile ulivyonijibu hovyo?” “Juu ya nini Rita, dada yangu? Ni nini nilichozungumza kibaya au wewe ulichozungumza kibaya tukajibishana? Maana tumeagana nikiwa nakushauri tu. Kuanzia swala la kuchelewa kuchukua mtoto, na swala la zawadi uliyosema itakulazimu kuacha kula kesho ili ukaninunulie. Nikakwambia usijisumbue, haina haja isiwe kama deni nikakwambia mimi nipo sawa tu. Tukazungumza pale, tukaagana vizuri tu. Hapakuwa na mlinzi ila mimi na wewe pamoja na mtoto! Hayo majibu mabaya niliyokujibu ni yepi?”

“Na mimi nataka kuyasikia Rita. Maana ulinipigia simu ukimlalamikia Naya. Nikakuuliza amekutukana, wewe mwenyewe ukasema hapana ila jinsi alivyokataa zawadi, ndio hukupenda. Nikakuuliza huhisi ni kama anakupunguzia shuguli ya kwenda kununua hizo zawadi? Hapakuwa na tusi au neno la moja kwa moja wakati tukizungumza Rita. Maneno haya yanatoka wapi!?” Malon akaingilia na kuuliza.

“Mbona kama unamtetea Naya?”  Akauliza Thia kishari. “Amekwambia nini huyo Naya kama sio kutaka kuwachonganisha tu?” Thia akaendelea kumbana Malon mbele za watu akisikika kumtetea dada yake. Naya alibaki kimya maana hata Malon hakuonyesha kumfahamu Naya mbele ya hiyo familia, zaidi huyo mpenzi wake Rita. Tokea mwanzo anakutana naye na kuwa na Rita sehemu moja hapo kwake kabla ya safari, hakuonyesha kabisa kumfahamu Naya kitu kilichomuumiza sana Naya kushindwa kumtambua mbele ya Rita kuanzia mwanzo mpaka mwisho wanarudi kutoka safari!

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

CONVERSATION

0 Comments:

Post a Comment