Naomi Simulizi |+1 205 767 8163 |naomisimulizi@gmail.com Mapenzi & pesa – sehemu ya 13 - Naomi Simulizi

Mapenzi & pesa – sehemu ya 13

Muulize dada yako kama mimi nimezungumza na Naya. Ila mimi huwa ni muwazi na linapokuja swala la Naya, huwa nakosa uvumilivu.” Kimya kikatanda wote wakamgeukia vizuri Malon aliyekuwa amebanwa na Thia. “Mnakumbuka nilipofika nyumbani kwenu kwa mara ya kwanza, mlinikaribisha kwa ajili ya chakula cha usiku mimi na Rita, mama ukaniuliza kama nilishawahi kuoa?” Kimya. “Mnakumbuka habari au kisa nilichowapa juu ya msichana niliyejaribu kutaka kumuoa. Mpaka nikanunua pete ya uchumba, nikaenda nyumbani kwao ili nikazungumze na baba yake kwanza, niombe baraka za kumuoa nikaishia mikononi mwa mama yake. Aliyenifukuza na kuniomba nisiwahi kurudi kwao, kwa kuwa simstahili mtoto wake?” Kimya. Mpaka wakina Naya wakashangaa.

“Unakumbuka hata Brazil nilikueleza umbali wa huyo msichana aliokwenda na mimi kwenye maisha? Kwamba hata uhuru nilionao ni kwa ajili yake, nashindwa kuoa au kujiingiza kwenye mapenzi kwa hofu yakutoweza kutulia kwenye mahusiano kwa ajili yake?” Kimya. “Sikuwa nimekutajia jina. Ila ujue tu, hata sisi wote sasa hivi, tupo hapa kwenye hii nyumba kwa sababu ya Naya.” Wote wakatoa macho, zaidi Rita.

“Usifikiri Naya ni mgeni wa hii nyumba Rita. Au usidhani ni mjinga kama unavyomuona anafanya kwako. Niliishi na Naya hapa ndani kama mke wangu kwa zaidi ya miaka mitatu. Tukilindwa na kutumikiwa kama hivyo wanavyokutumikia wewe tena na zaidi kwa kuwa Naya alikuwa jukumu langu sikuwahi kutaka hata kuhisi anashida. Maamuzi yangu mabaya ya maisha zamani, ndiyo yametufikisha hapa tulipo. Nilipoteza kila kitu. Naya akauza kila kitu ili kunitoa jela, kasoro hii nyumba aliniachia ili nipate pakuja kuishi. Namfahamu Naya ndani na nje. Hata ukizungumza sentensi nitajua hiyo ni ya Naya au la. Lakini Rita, unamsingizia Naya, na sitakuruhusu umchafue kwa sababu zako binafsi.”

“Alichokifanya tokea unamfuata kumuomba akusaidie kukaa na mtoto wako, ni kukuheshimu japo ulimnyanyasa kwa kumwangalia tu na kumuhisi. Naya hana shida na sehemu ya kulala. Ni vile humfahamu. Hana shida na pesa uliyompa kiasi cha kutoa utu wake. Ni vile humfahamu, hiyo zawadi uliyomletea Naya, si kitu cha kukuvunjia heshima. Hana uroho wa mali hata kidogo. Na ndio maana alikujazia gari yako mafuta japo hukutaka atumie na wewe ulimuachia gari nusu tanki. Unaweza ukamuona ni fukara kama unavyomsema, lakini Mungu alimjalia utajiri wa nafsi. Sitakuruhusu umseme vibaya Naya kwa kumchafua. Na ninakuonya Rita, usiguse kazi yake ya Cocacola. Amekufanyia kazi yako vizuri, mliachana kwa amani, mwache na yeye aendelee na maisha yake.” Naya na familia yake walibaki wameduaa, kimya.

“Samahani sana Mzee wangu. Niombe radhi kwa usumbufu. Naombeni nyinyi mkapumzike tu. Haya mambo mengine, yatamalizwa tu hapa.” Malon alimgeukia baba yake Naya. “Asante.” Akajibu baba Naya akimtizama Naya. Naya akatoa pesa kwenye pochi akaweka pale mezani. “Hii ni pesa yako Rita. Naomba iwe nilikaa tu na Ethan kwa kujitolea, isiwe kama ni kazi. Naona itakusaidia kutulia. Huwezi na wala huna uwezo wa kunisaidia Rita dada yangu. Nina mahitaji mengi ambayo hayatimiziki kwa malipo kama haya wala kwa hiyo kazi unayonitisha nayo ya Cocacola.” “Usikasirike Naya. Hili ni jasho lako. Chukua hiyo pesa, usiache.” Nolan akamsihi.

“Hapana Nolan. Nimeumia sana. Nikichukua hiyo pesa, ni kujifedhehesha sana. Acha tu. Pengine itasaidia hata kulipia bili ya maji niliyooga na umeme niliotumia.” Akamgeukia baba yake. “Twendeni baba.” Naya akatangulia baba yake akafuata na kaka zake. Malon akamfuata nyuma.

“Naya!” Malon akaita, Naya akageuka. Baba yake na ndugu zake pia wakageuka na kusimama wote. “Naombeni msinielewe vibaya. Cha kwanza, sikujua kama Rita atamuomba Naya kumfanyia kazi. Naya ananijua. Nisingekubali. Nilimkuta humu ndani akiwa ameshamkubalia Rita, na ndio siku tunakwenda safari. Na pili, sikujua kama kuna kikao kama hiki. Nisingeruhusu Naya kuja kudhalilika hapa. Mnisamehe sana.” “Hamna neno Malon.” Akajibu Naya. Malon akabaki akimwangalia. “Kweli kabisa. Sisi hatuna neno na mtu. Hata Rita sijamchukia, ila tu nimeelewa moyo wake, basi. Naomba muwe na amani. Usiku mwema.” Naya akasisitiza.

 “Poleni kwa kumpoteza mama. Sikuwa najua. Rita ndiye aliyeniambia tukiwa safarini. Poleni sana.” “Asante.” Wote wakaitika, Malon akaona ni kama bado wapo na ule uchungu wa kufiwa na hapakuwa na nyongeza kati yao. Malon aliondoka akiwa na ahadi yakuleta mabadiliko makubwa, ndio wanakutana naye hapo na sababu ya kufukuzwa na marehemu mama Naya. “Usiku mwema Malon. Kesho Zayoni anatakiwa kwenda shule na anahitajika usingi wakutosha, acha sisi tuwahi.” “Ni kweli.” Naya na familia yake wakaondoka. Malon alibaki amesimama akiwaangalia.

Naya.

W

aliondoka hapo nyumbani kwa Malon kila mmoja akiwa na butwaa, hakuna aliyemuongelesha mwenzie njia nzima, kimya. “Wewe ulijua kama mama alimfukuza Malon nyumbani?” Naya akavunja ukimya kwa kumuuliza baba yake wakiwa wanakaribia kufika nyumbani kwao. Baba yake akanyamaza tu bila yakujibu. “Kwa hiyo ulijua?” Naya akasisitiza swali lake alipoona kimya. “Nia ya mama yako ilikuwa nzuri Naya.” “Kwa hiyo ulifahamu?” “Aliniambia wakati amezidiwa sana. Lakini nikahisi anaongea tu sababu ya maumivu. Kipindi kile alikuwa akikiri na kutubu mambo mengi.” “Kwa nini hukuniambia wakati wewe unajua jinsi nilivyokuwa nimeumia kutokurudi kwa Malon? Nilikuwa nakushirikisha kila kitu baba. Lakini..” “Naya mama, sasa hivi ukinilaumu utakuwa unanionea mwanangu. Wakati ule nilikuwa kwenye wakati mgumu mama. Nilikuwa nimejawa hofu. Chakula chenyewe nilikuwa sili kwa kufunga ili Mungu anihurumie amponye mke wangu. Akili ya kufikiri ilikuwa haipo. Unakumbuka wewe na Bale ndio mlikuwa mnaongoza mambo yote mpaka kwenye msiba?” Naya kimya.

“Nisamehe mama yangu. Halafu sijui sikuwa nimemuelewa vizuri! Nikahisi ni vile alivyokuwa akimpinga tokea mwanzo, nikahisi ndio anaomba msamaha. Sikujua kama kipindi kile kama Malon alipotoka Dubai alirudi nyumbani. Mimi mwenyewe nilikuwa nimemchukia Malon. Nilijua alipokwenda ile safari ya Dubai akafanikiwa, akakusahau. Nilimchukia sana, wala sikuwa nikitaka kumsikia tena. Ndio maana nilipokuona na wewe umepata amani kuwa naye mbali, nikaona tuyaache hayo mambo kama yalivyo. Hata mama yako nilimuomba asije akaanzisha habari za Malon tena.” “Kwani alitaka kuniambia nini?” Naya akauliza huku akifuta machozi.

“Nafikiri alitaka kukwambia kuwa Malon hakukukimbia. Nafikiri kukiri mambo yote. Sina uhakika mama yangu. Sasa kwa kuwa maelezo yake yalichanganyikana na kilio cha maumivu, sikuelewa vizuri. Hivi leo wakati Malon alipokuwa akisimulia pale, ndipo nimeelewa alichokuwa akiongea mama yako siku ile. Mimi nilimkatiza mama yako kwa kumuomba kuwa, akuache kabisa wala asimtaje tena Malon kwako kwa kuwa sasa hivi umeshakubali kuwa Malon hatakaa akawa kwenye maisha yako. Nikamwambia kwa wakati ule ukiwa unamuuguza, akikutajia tena Malon itakuwa ni kukuchanganya. Heri akuache akili iwe pale kwenye kumuuguza.” Naya akanyamaza.

“Umenisamehe mama?” Baba yake akamuuliza kwa upendo. “Hata mama pia. Najua nia yake ilikuwa nzuri. Mama alitamani kuniona naishi maisha mazuri kitu ambacho hata mimi ningekitamani kwa watoto wangu. Sina lawama kwa mtu baba. Ila natamani kama angekuja kuniona naolewa kama ningepata mwanaume aliyeridhika naye. Kipindi hiki cha mwisho alikuwa kama ananiandaa. Sasa sijui kwa ajili ya nyumba yake au yangu!” “Vyote.” Baba yake akajibu. “Nahisi kweli. Alikuwa anahangaika kuniona naelewa na kuishi vile alivyotaka. Wakati mwingine alikuwa anaamka na maumivu, anakaa na mimi jikoni, kuhakikisha natoa wali ulioiva.” Wote wakacheka.

“Na mama alihakikisha mpaka unaweza kupika Naya! Umebadilika!” Bale akaongeza “Nahisi pia na akili zikakua gafla. Alihakikisha naelewa mambo ya pale ndani. Kuanzia mambo ya Zayoni kibinafsi mpaka baba. Alitaka akiondoka mambo mengi yasibadilike. Akaniwekea roho ya umama kwa ajili ya Zayoni.” Wote wakatulia. Wakamsikia Zayoni analia kwa uchungu sana. Bale aliyekuwa amekaa naye pale nyuma akaanza kumtuliza.

HATIMAYE.

B

aada ya kukata tamaa, hatimaye Naya akaanza kazi kwenye kiwanda hicho cha Soda, upande wa masoko kama shahada aliyosomea. Akapangiwa kitengo cha matangazo ndani ya idara hiyo ya masoko. Kazi ikaanza kukiwa na shida ya usafiri kila anapokwenda kazini na kurudi. Alianza kazi hapo akiwa hana pesa kabisa ila kutumia akiba ya baba yake kumfanya aweze kuwepo kazini. Pesa hiyohiyo ya baba yake alitumia  kwa nauli na chakula cha mchana mara moja moja sana. Wakati mwingine alishindwa hata kula mchana hapo kazini. Alibakia na njaa, akisubiria kwenda kula nyumbani akitoka hapo kazini ili kubania pesa ibakie ya nauli tu. Hakujutia kuacha pesa ya Rita.

Kampuni ilikuwa kubwa na vishawishi vingi vya kuvutia kujipatia pesa kwa haraka, kwani walikuta walionza kazi hapo na walio ajiriwa kabisa wanayo pesa haswa. Ukweli walikuwa wakilipwa vizuri haswa kwa waajiriwa kabisa. Walikuwa na marupurupu mengi sio kama wao walioanza kazi tu na hawakuwa wamepewa ajira ya kudumu. Vishawishi vikawa vingi kwa wao wageni pale kwenye kampuni, lakini Naya alijikaza. Na kwa kuwa waliajiriwa wasichana watatu kwa wakati mmoja. Wakapitishwa kila kitengo ili kufahamu hiyo kampuni, wenzake hawakuchukua muda mrefu wakapata wanaume ambao walikuwa wafanyakazi wa hapo muda mrefu tu, lakini si Naya. Naya akajikana nafsi yake.

Akajitenga na vishawishi hata kukaribishwa chakula hakuwa akitaka. Akiwa hana hela kabisa, na hawezi kutoka kwenda kula mida ya mchana hapo kazini, alibakia peke yake ofisini wakati wenzake wakienda kula yeye anafanya kazi. Swala la ofa hapo kwenye hiyo kampuni lilikuwa jambo la kawaida kabisa lakini Naya hakutaka kulizoea. Baada ya muda mfupi sana wakaanza kumtambua hapo kazini kama ni msichana mwenye tabia za ajabu. Hapendi kujichanganya na mshamba. Na ule muonekano wake! Nywele fupi tu, hakuna kipodozi wala hereni. Uso wa majonzi, kukataa kila ofa na kuchapa sana kazi, wakamuona mshamba wa kupitiliza. Yeye akaendelea na yake.

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

 Siku moja Naya alirudi nyumbani akashangaa kukuta baba yake anahesabu pesa. Alipoingia tu akamkabidhi pesa zote. “Za nini!?” “Matumizi ya humu ndani na yako pamoja na kaka zako. Nimetoa hicho kilio chote huko nje.” Naya akabaki ameduaa, hajaelewa. Bale akatoka chumbani. “Unashangaa nini sasa na wewe? Baba kauza ng’ombe wote mpaka ndama.” Naya akatoa macho. Baba yake akasimama na kuingia chumbani kwake. Naya akatoka kwenda kuhakikisha. Akakuta hakuna hata ndama! Naya akabaki ameduaa pale mabandani.

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

Mwezi wa kwanza alipopokea mshahara wake wa kwanza, akakumbuka nadhiri yake aliyokuwa ameweka mbele za Mungu akajiambia lazima kuitimiza. Binti huyo alifundishwa na baba yake kutoweka nadhiri mbele za Mungu. Akimfundisha kutoweza kununua baraka za Mungu. Lakini akamwambia endapo ikatokea ameweka nadhiri, nilazima aitimize. Sasa katika hangaika yake ya muda mrefu bila kazi, Naya akiwa amechoka, alimwambia Mungu endapo akimkumbuka na kumpa kazi, na akilipwa mshahara wake wa kwanza, atatoa sadaka ya shukurani asilimia 10 ya huo mshahara, atamnunulia zawadi Malon. Kama shukurani yakumsomesha. Na zawadi kwa wazazi pia. Sasa mama amekufa, amebaki Malon na baba yake na hiyo sadaka ya shukurani. Ikabidi kuitimiza tu.

Akaenda kumnunulia Malon saa nzuri ya mkononi na kadi ya shukurani. Akaiandika upande wa juu. “Malon, nachukua nafasi hii ya kipekee kukushukuru kwa kusimama na mimi tokea kidato cha nne mpaka namaliza chuo. Asante kwa kusimama na mimi kwa hali na mali. Asante kunisomesha na kunitunza. Umechangia kunifikisha hapa nilipo. Nakuombea na wewe Mungu akuinulie watu wa kusimama na wewe, kukushika mkono na kukufikisha sehemu ya juu zaidi. Nakuombea ufanikiwe, Malo. Asante.” Akaifunga vizuri akiwa chumbani kwake usiku huo akiwa anafunga hiyo zawadi ya Malon, huku akifikiria ni nini chakumnunulia baba yake ambaye amezira maisha. 

Naya Kwa Malon Tena.

S

iku inayofuata alitoka kazini na kuamua kwenda kuipeleka ile zawadi ya Malon nyumbani kwake. Alifika getini, hata hakutaka kuingia ndani. Akamuomba mlinzi atoke nje ya geti, akamkabidhi. “Naomba uhakikishe huu mzigo unamfikia Malon Saduki yeye mwenyewe.” “Huingii?” Mlinzi akauliza. “Hapana. Asante. Jioni njema.” Naya akaondoka taratibu akirudi barabarani kutafuta daladala yakumrudisha nyumbani kwao Kiluvya. Bado giza lilikuwa halijaingia, na kulikuwa na umbali kidogo kutoka nyumbani kwa Malon mpaka barabarani kwenye daladala. Upande huo kulikuwa na mahoteli, taksii zilikuwa zikiingia upande huo kupeleka wateja kwenye hayo mahoteli. Lakini Naya alikusudia kupanda daladala, hakuwa na hela ya ziada ya kupanda taksii ila kujikimu tu. Akawa anatembea tu taratibu kuelekea barabarani.

          “Naya!”  Akasikia mtu akimwita. Akageuka kwa haraka. “Malon!”  Akamuona Malon kando ya pili ya barabara, ndani ya gari yake. Akatoa tabasamu na kumpungia mkono. Malon akacheka na kurudisha kupungia mkono, akabaki amesimama wakiangaliana. Malon ndani ya gari upande mwingine, Naya akimtizama. Akampa ishara ya kumwita. Naya akakunja uso kidogo. Akajinyoshea kidole kama anayeuliza, ‘Mimi!?’  Akageuka kulia na kushoto. Akajikuta yupo peke yake upande ule. Akajinyoshea tena kidole akimtazama Malon kama asiyeamini kama Malon anamwita. Safari hii akauliza kwa ishara, akitaka uhakika kama anayeitwa ni yeye. Malon akacheka kidogo na kutingisha kichwa kuwa ni yeye, na aende.

Akavuka barabara huku akiangalia magari yanayopita. Akaenda upande wa dirishani. “Mbona hukuingia ndani, mama?” “Sikutaka kusumbua. Hata hivyo nimetoka kazini tu, ndio nikaja hapa. Nawahi nyumbani.” Malon akamwangalia kidogo. “Mzima lakini?” “Mzima.” Naya akajibu na tabasamu kidogo. “Unaendeleaje Naya?” “Namshukuru Mungu naendelea. Nilitaka kukushukuru Malon. Niliweka nadhiri mbele za Mungu kuwa nikilipwa mshahara wa kwanza nikununulie zawadi wewe. Uonje matunda ya jasho lako.” Wakacheka. “Pamoja na mama na baba. Sasa kwa kuwa mama yeye amefariki, nitamjengea kaburi, ila baba ndio sijui nitafanyaje?” “Kwa nni tena?” “Aaah! Sijui Malon. Amebadilika kweli, mpaka nina hamu naye!” Akamuona Naya ameinama kama anayefikiria.

“Pole.” “Nimepoteza mama na baba. Lakini uchungu nilio nao ni kama yeye baba ndio amekufa! Amebadilika, amepoteza hamu ya kila kitu. Kumtoa tu hata kitandani ni kazi kweli! Na kama mimi sipo ndio kabisa. Hapa Bale atakuwa anasubiri nikamlazimishe kula. Hajapokea simu zangu tokea asubuhi.” “Kwa nini?” “Basi tu. Hataki kutoka kitandani. Imebidi kumpigia simu Zayoni aende akamwangalie chumbani kwake, akasema amemkuta amejilaza tu kitandani anaangalia dari. Amekuwa kama amepoteza dira na hamu ya kufanya mambo! Anasema alikuwa akifanya kila kitu kwa ajili ya mama. Ili kumfanya aishi vizuri. Lakini anaumia kuona mama amekufa kabla hajampa alichokuwa akikitaka au hajatimiza ndoto za mama. Amebadilika sana baba. Siye yule uliyekuwa ukimfahamu.” “Poleni sana Naya.” “Nashukuru. Anyway, acha mimi niwahi kurudi nyumbani kupika.” Malon akacheka.

Naya naye akacheka. “Siku hizi napika mwenzio. Muda mwingi Bale hayupo pale nyumbani.” “Anakuwa wapi?” “Alichukua chumba chuoni. Wakati mwingine anakuwa chuoni au anarudi usiku. Na akirudi anataka kusoma. Kwa hiyo mimi ndio nimekuwa mama. Kufua, kupika na usafi.” “Unaivisha lakini?” Naya akacheka sana. “Mama alihakikisha anahamisha ujuzi wake wote kwangu kabla hajaondoka. Siku hizi mpaka Bale anasifia chakula changu.” “Hongera mama.”  “Asante. Na asante sana Malo. Asante sanaaa. Naamini unanielewa. Asante kwa kunisomesha, asante kwa kunitunza. Asante kwa kuniamini. Asante kwa kila kitu. Nakushukuru kwa dhati. Sijasahau hali uliyonikuta nayo siku ya kwanza nikienda kuchukua pesa ya mkopo iliyokuwa imejaa masimango, kanisani. Nakumbuka uliponitoa kwenye ile hali na kuhakikisha sidaiwi tena na ninasoma kwa utulivu. Asante.” Naya akashukuru kwa dhati kutokea moyoni.

“Unafurahia kazi yako?” Malon akauliza. “Sana. Nafanya kitu nilichosomea. Mazingira mazuri, nahusishwa kwenye mipango na kiongozi wangu wa idara. Ananiamini sana pale idarani. Haya, tuna safari ya kikazi ya week moja. Kutangaza bidhaa mpya nje ya hapa Dar. Na mimi amenichagua nimuwakilishe kwenye hilo kundi tunalokwenda. Kuhakikisha majukumu yanayotupeleka yote yanafanywa kwa usahihi. Nimefurahi kuona japokuwa mimi bado ni mgeni, ananiamini na anatambua ufanyaji kazi wangu. Kwa kweli siwezi kulalamika. Ila tu naona imekuja wakati mbaya.” “Hapana Naya. Huu ndio wakati sahihi. Mungu alikuwekea maalumu kwa ajili ya wakati huu.” “Unafikiri hivyo Malo?” “Kabisa. Huu ndio wakati sahihi.” Naya akainama tena akiwa anamchungulia kwenye gari.

“Umeona nimevaa saa yangu?” Naya akamtizama mkononi na kucheka. “Umeipenda?” “Sana. Asante kushukuru, mama. Naona katika wote niliowahi kuwasaidia, wewe tu ndio unakumbuka.” Naya akacheka taratibu. “Watakuwa wanakumbuka ila mambo ni mengi wanashindwa kukwambia.” Malon akaguna na kucheka kama anayejikejeli. “Kweli Malo. Umesaidia wengi. Umesomesha wengi sana. Mimi nawakilisha hao wengi. Tunakushukuru.” “Asante kushukuru.” Naya akainama, Malon alikuwa akimwangalia.

“Unadhoofu Naya! Unakula lakini?” “Nahisi mawazo tu. Ila nakula sana tu na ninapata muda mwingi wakupumzika. Siku hizi hatufugi kitu chochote. Kwa hiyo tukimaliza kazi za pale ndani, ni kukaa tu.” “Baba aliuza kila kitu?!” “Mifugo yote, kila mnyama pale kwetu kasoro sisi tu.” Wakacheka. “Nakuwa na hamu naye sana. Yaani nakuwa na hamu naye wakati yupo hapo hapo!” Naya akalalamika. “Tuliambiana na Bale tumpe muda wakuomboleza, lakini naona wala hapati nafuu ndio anazidi kunyong’onyea. Hivi naandaa mazingira ya kumuomba tusafiri naye. Kwa kuwa wananilipia chumba hotelini, nataka nimuombe tusafiri naye. Nimuombe anisindikize. Angalau atoke pale nyumbani labda itamsaidia.” Malon akazima gari akashuka. Naya alimpisha pale mlangoni.

“Njoo.” Naya akamwangalia, nakusita kumsogelea. Alijua anataka kumkumbatia. Akainama. “Sijawahi kulala na Rita. Bado nimeokoka Naya.” Naya akamwangalia na kukunja uso. “Hakuna kilichotokea hata safarini. Na unanijua mimi huwa sikudanganyi. Ni heri niseme ukweli niingie matatizoni kwako, kuliko kukudanganya.” Naya akabaki tu kimya. 

“Katika mazungumzo yetu siku moja nilimwambia nakwenda Brazil kuwaona watu ambao wananiletea sukari. Maana ile biashara ni kweli imekua. Mungu alinisaidia na kunipa wazo la kuzungusha, nazungusha nchi mbili. Turudi kwa Rita. Akasema na yeye angependa kuona Brazil, akataka tuongozane. Sikuwa na sababu ya kukataa. Ila mimi nilipanga nikifika kule, pia nitembelee mpaka wakulima. Ili tu kujua na kuona mashamba yao. Na nikawa nimezungumza na huyo anayeniuzia hiyo sukari, aniandalie safari. Uzuri ni baba au babu mtumzima sana. Yeye ndio mmiliki wa hayo mashamba pia. Ana nyumba pia huko mashambani. Akanikubalia. Tena Mungu alifanya kitu ambacho nikashangaa. Hata sikulipia garama za hoteli. Akatukaribisha kwake siku tuliyofika. Nikisema kwake, namaanisha nyumbani kwake kwa familia yake. Ni Mzee aliyefanikiwa, lakini anaisha maisha ya kijamaa sana. Ana mke wake hapo mjini. Siku inayofuata, tukamuacha Rita hapo mjini, mimi na yeye tukaelekea huko kwenye mashamba yake.”  Akamuona Malo anacheka.

“Nipazuri Naya. Nilitamani uwepo. Nilikupigia picha nyingi, utapaona. Pazuri sana. Jinsi anavyofanya kazi, lile eneo lenyewe! Pazuri mno. Nilipata wakati mzuri ambao hata sikutegemea. Nikajiambia lazima nije kukupeleka.” Naya akacheka. “Sasa kwa nini hukwenda na Rita?” “Cha kwanza niliona sio sawa kwake. Alikuwa yupo mapumzikoni. Ametumia pesa yake kusafiri. Sikutaka kumpeleka sehemu nisiyoijua, tena mashambani, wakati pale tulipewa sehemu nzuri sana. Huyo Mzee ananyumba nzuri Naya! Ungefurahia. Halafu mkewe ni mkarimu japo hajui sana kuzungumza kingereza. Ila mkarimu. Nikaona ni heri Rita abaki naye azunguke na kupaona Brazil. Halafu pia sikutaka kujijaribu. Rita alikuwa na matarajio fulani kwenye ile safari. Sikutaka kujishawishi. Nikaona maneno na vitendo viende pamoja. Nafikiri ndio maana alirudi akiwa na hasira kidogo.”

“Anyway, lakini nilitaka kukuhakikishia bado nimesimama kwa Mungu, sijabadilika. Nakiri nipo hapa kwa msaada wake Mungu. Nilifikishwa chini, chini sana. Sio akili yangu iliyonifikisha hapa. Ni Mungu mwenyewe. Sina jeuri yakutoka kwake, kwa kuwa nimepitishwa mahali nikajiona mimi si kitu. Sina kimbilio au wakumtegemea kwa hakika ila yeye tu.” Malo akajicheka.

“Nilipoteza kila kitu na kila mtu Naya. Wewe ni shahidi. Kila kitu! Mungu amekuja kuniokoa, sio nikiwa nimekaa. Amenitoa chini, kijiweni, nikiwa nimeishiwa na nina mapepo. Niligonga mwamba. Nikauzunguka huu mji kwa miguu, sio hata daladala nikiwa sina kitu. Kitendo chakunirudisha ndani ya gari na kitandani wakati nilikuwa nakesha macho na bunduki mkononi usiku kucha nikilinda majumba ya watu, kutoka katika kulindwa, nikapokonywa kila kitu, hakika sitarudi nyuma, Naya. Nimelipiwa garama kubwa sana kuwa hivi nilivyo hapa sasa hivi. Uhuru wangu umekugarimu wewe na Mungu wangu. Narudije kirahisi kule nilikotoka? Tena nikiwa nimefikishwa na tamaa za wanawake tu? Maana rafiki wote walinigeuka sababu ya umalaya. Kulala na wanawake zao, mpaka wake zao! Sasa nirudi tena huko!? Hapana mama. Naona huku kwa Yesu nipo salama zaidi. Nimekusudia kutulia tu na nikimuomba Mungu aniwezeshe.” Naya akacheka taratibu kama anayefikiria.

Kisha akaona awe muungwana t. “Hongera.” “Asante.” Wakatulia kidogo kila mtu akifikiria lake. “Unafikiri baba atakubali nikimwambia twende naye Mbeya kule ninakokusanya mchele na kokoa kwa wakulima?” Naya akabaki kimya kama ambaye anafikiria kitu. “Au itakuwa vibaya?” “Amebadilika sana baba. Sio yule uliyekuwa ukimfahamu, mchapakazi. Amepoteza ladha ya kila kitu. Alikuwa ananiambia haoni tena sababu kwa kuwa alikuwa akihangaika zaidi kwa ajili ya mama. Anaumia kuona mama amekufa akiwa hajampa maisha mazuri.” “Lakini mbona mlikuwa mkiishi maisha mazuri tokea mwanzo, Naya?” Naya akafikiria.

“Kuna jinsi mama alikuwa akilalamika, Malo. Hata kitendo cha kunikatalia mimi nisiolewe na wewe, alikuwa akisema hataki nije kuishia kama yeye. Akimaanisha na yeye aliishia na mwanaume wa aina kama yako. Sasa yale maneno yalikuwa yakimuingia na kumuuma sana baba ndio maana ulikuwa ukimuona anapambana muda wote ili kutafuta pesa, kumridhisha mama angalau amsikie hata mara moja halalamikii maisha yake. Sasa kila baba alivyokuwa akijitahidi, nafikiri mama hakuwahi kuridhika au kumuonyesha amefanya vizuri, wakati baba alikuwa akifanya zaidi ya uwezo wake. Nafikiri unakumbuka wakati wote au mara nyingi ulikuwa ukitukuta na baba bandani?” “Nakumbuka.” Malon akajibu.

“Basi kumbe vile baba alikuwa anapambana ili kumridhisha tu mama. Sasa mama alipoanza kuugua mfululizo, hofu ikamwingia baba. Akaanza kufunga akimsihi Mungu asimchukue mama kabla hajarudia hali yake ya kiuchumi ya zamani wakati tu wameona, baba akiwa na pesa. Nafikiri, sina uhakika, nikutaka kumuhakikishia mama kuwa hata biashara huwa zinalipa. Sasa sijui alikuwa akifanya kwa ajili yangu pia ili kumfungua mama na kuniacha niwe huru, ili niolewe na yeyote ninayemtaka, sijui! Lakini Malo, ungemuonea huruma baba jinsi alivyokuwa akiomba. Ila mimi nilimwambia Bale, baba ameingiwa na hofu. Ni kama alijua, au nafikiri walimwambia hospitalini kuwa mama hawezi kupona.” “Kwani aliugua sana?” Malon akauliza.

“Yaani Malon, alianza kama utani tu! Tunakuja kugundua kama ana kansa, imeshamla mapafu yote, yupo stage 4. Na hiyo ni ndani ya mwaka mmoja. Alianza vichomi. Akapuuza, na kupunguza kazi. Baba akaja kumlazimisha kwenda hospitalini. Wakasema ni nimonia. Akaanza dawa. Akatulia kidogo tu, vichomi vikarudi. Kupigwa xray, akaambiwa mapafu yana maji mengi inabidi kufyozwa. Akafyozwa mara mbili. Wakasema yupo sawa. Sijui akapata vipi infection, hatujui. Kuja kugutuka, ziwa la kushoto linatoa usaha. Ndio wakaamua kumfanyia upasuaji. Wanasema walipompasua huko ndani wakakuta ameharibika kuliko vipimo vilivyoonyesha. Hata kutoka chumba cha upasuji walisema ni muujiza. Akakaa hospitalini kama mwezi, kidonda kinazidi kuoza. Wakaendelea na matibabu, ndio akafariki.”

 “Kipindi hicho mama mgonjwa, ungemuhurumia baba. Alikuwa hali, anafunga wakati wote. Mchana na usiku mama akiwa hospitalini, utamkuta chumbani au sebuleni amepiga magoti analia, akimsihi Mungu amtendee muujiza. Nahisi hata imani yake imetingishwa kidogo. Kanisani tunakwenda kwa shida sana.” “Poleni sana Naya.” “Asante. Acha mimi niende Malo. Giza limeingia.” “Naomba nikusogeze Naya.” “Sio usumbufu kwako?” “Nilikuwa nimekaa tu najisomea wakati mlinzi ananigongea na kunipa zawadi yangu.” Naya akawa kama amesita. 

“Ingia kwenye gari twende.” “Kweli? Maana ni kama ulikuwa umepumzika. Sitaki ujio wangu uwe usumbufu na ndio maana uliona niliacha mzigo getini. Mimi nitafika tu nyumbani. Usijali.” “Hamna neno. Twende tu. Hata hivyo kuna mahali nataka kwenda. Kwa hiyo twende tu. Nitaunganisha na safari yangu baada ya kukushusha.” “Hapo sawa. Asante. Nashukuru.” “Karibu.” Akazunguka upande wa pili, akamfungulia mlango. Naya akapanda. Wakaondoka.

“Naona mambo yako safi Malon! Umenunua gari aina ile ile!” “Nilikuwa nalipenda sana lile gari. Nilijiambia Mungu akirudisha tu pesa mikononi mwangu, lazima ninunue tena aina ile gari. Ndio nikaona ninunue la silver.” Naya akacheka huku akiangaza macho humo ndani ya gari.

“Hongera. Naona umerudia na hali yako.” “Ni Mungu mama. Na maneno yako yalinitia nguvu. Unajua ninayo ile barua uliyoniachia siku ile na simu, pamoja na maandazi?” Naya alicheka sana. “Kweli!?” “Kweli ninavyo mpaka leo. Tena nimeipiga na picha. Naisoma kila wakati ninapoona nakata tamaa au nikikutana na kitu kigumu. Naisoma, najikumbusha mimi ni nani, naendelea.” Naya akacheka kidogo.

“Lakini hata mimi umenisaidia Malo. Uliniamini kupita mtu yeyote yule. Imenijengea imani kwenye maamuzi yangu na ndoto zangu. Hata kama hazijatimia, najiambia ni za msingi, ipo siku zitakuja kutimia tu. Natunza, nikijiambia ipo siku zitatimia.” “Mama, aliniambia mlitoka na Joshi kwenda kutambulishwa ukweni.” Naya akacheka. Akajua na hilo lilimfanya Malo kukasirika zaidi ya maneno ya mama yake. “Ni kweli tulitoka Malo. Alikuja kuniomba msamaha mbele ya mama, kama kusudi tu. Tena mara zote mbili, akitaka twende naye mara ya kwanza kwenye shuguli ya kiofisi mara ya pili nyumbani kwa dada yake, mdogo wake yule tuliyekuwa tukisoma naye, alikuwa akilipiwa mahari. Anyaway, lakini mimi sikuwa nataka kwenda Malo.” “Kwa nini?” Malo akauliza.

“Nilijua hakuna maisha kati yangu na Joshi. Kuna jinsi Joshi alikuwa akinidharau, nilikuwa nikiisikia mpaka rohoni! Hata hiyo siku tuliyoenda kwenye shuguli ya ofisini kwao, nilipendeza Malo, mpaka mwenyewe nilijua.” Malo akacheka. “Kama kawaida yako?” “Haswa! Na kila mtu akanisifia, kasoro yeye. Njia nzima ananisema jinsi nilivyovaa.” “Anasemaje sasa? Hakupenda nguo?” “Analalamika kuwa ni kama nili over dress. Yaani nimevaa kama niliyekamia nikaonekanae huko. Nimefika ukumbini, amenuna, hata haongei na mimi na wala hakunikaribisha hata kinywaji!” “Haiwezekani Naya!” “Kweli Malo. Mpaka kaka Mati nafikiri akajua. Akaja kunitoa pale, tukacheza wote. Nilikuwa nimevaa ile set yote ya dhahabu uliyokuwa umeninunulia. Kumbe anasema alishaviona ukiwa umevishika, kimoja kimoja ukimwambia ni zawadi ya mtu, ila unachangisha pesa ili ukamilishe. Akasema ni kama akapata bahati ya kukutana na wewe ukiwa umeshika kila kimoja wapo kwa wakati tofauti tofauti.” Malon akajaribu kukumbuka.

Naya akamuona anacheka. “Halafu kweli bwana. Sasa ikawaje?” “Ndio akanibana nimwambie ukweli nilipotoa. Ndio nikamwambia ukweli kuwa nimepewa na Malo. Akaniuliza kwa wakati ule nipo na nani? Wewe au Joshi. Na kama Joshi anajua kama wewe unanipa vitu? Mimi nikamjibu kwa kifupi tu, lakini nikajua kaka Mati ni mtu mzima, msomi, tena sheria, nikajua atapata majibu.” “Ulimjibu nini sasa?” Naya akanyamaza kama anafikiria. Akamuona anafuta machozi kwa haraka. Akatulia.

“Wakati ule unakumbuka uliniacha kwa upendo sana! Nikiwa natumaini utarudi Malo. Uliniacha kukiwa natumaini kubwa.” “Nilirudi Naya. Mungu wangu nishahidi nilirudi. Tena nilirudi na pete, mama. Nilikuacha na Joshi ambaye nilimuona hana uwezo wa kukutunza. Nikajiambia hakustahili hata kidogo. Siku nimerudi kwenu, ilikuwa nizungumze na baba yako, niombe baraka zake, nikijua baba akikubali tu, nimekupata na wewe. Lakini Naya, mama! Ilikuwa ni kama nimeenda kuchapwa makofi ya usoni. Nilimkuta mama anafua pale nje. Oooh! Ilikuwa mbaya sana. Nilijua mama hakuwa akinikubali, lakini si kwa kiasi kile. Alijifunua kwa mapana, bila jazba, wala matusi. Kwa hekima kubwa, akimlinda binti yake. Akanisihi sana nikuache na nisikuchanganye. Akasema mmefikia pazuri sana na Joshi, anaomba nisiingilie. Nakuwa ni kama nakuvuruga.” Naya akaumia sana.

“Natamani ungeniambia Malo!” “Nilikuwa nimeumia sana Naya! Niliumia sana. Nikaona haina sababu kwa kuwa hata muda huo mimi nakufuata na pete kumbe naambiwa mwenzangu ulikwenda ukweni kutambulishwa! Nilikaa siku tatu sipati usingizi.”  “Katika yote, najua mama alikuwa na nia nzuri. Alifanya kwa upendo akinitakia mema, japokuwa baba anasema ni kama alikuja kukiri akitaka kuomba msamaha, lakini baba hakuwa amemuelewa vizuri. Alikufa akiwa kwenye maumivu makali sana. Muda mwingi alikuwa akilia. Wakati mwingine tulikuwa tunahisi ni kama anachanganyikiwa. Anaongea mambo ambayo hayaeleweki. Sasa alipomwambia baba, alikuwa akilia maumivu pia, huku akitaka aje azungumze na mimi. Sasa hapo baba akamkatalia, kwa kuwa ndio ni kama na mimi nikawa nimeshakubaliana na wazo lakutokuja kuwa na wewe tena. Maana nilikuwa na hali mbaya Malon! Karibu kuchanganyikiwa kwa maumivu ya kuniacha kikatili vile.” “Nilirudi Naya.” Malon akawa kama anajitetea.

“Baba alihangaika sana kunirudisha kwenye hali ya kawaida hata kuweza kurudi kukaa hivi na kuweza kuwaza jambo la kawaida. Nikawa kama mgonjwa huku mama naye amenichukia kumkataa Joshi! Kwa hakika nilikuwa na hali mbaya sana. Lakini baba alisimama na mimi mpaka nilikuwa nikimuhurumia! Alikuwa akiniombea bila kuchoka huku akinijenga kwa maneno na kunikumbusha safari niliyopita na wewe, niitumie kama fundisho kwenye maisha. Chochote kilicho kizuri, nikibebe na kukitumia. Kilicho kibaya, nihesabu kama ni shule niliyopitishwa, na lazima nikubali kuhitimu ili nisije rudi tena hapo. Ikaendelea hivyo mpaka nikaafikiana na ile hali kuwa ndio umeondoka, hutarudi tena. Nikatulia. Sasa mama aliposema anataka kuja kuniomba tena msamaha juu yako, baba akaona atanichanganya zaidi. Halafu hakuwa amejua kama alikufukuza. Wote tulijua hukurudi.” “Nilirudi Naya. Nilirudi na pete!” “Mama hakusema, japo alijua nilikuwa nakusubiri sana.”  Wakatulia kidogo.

“Anyways, kile kitendo cha kucheza na Mati, nafikiri kikamuudhi zaidi Joshi, na yeye akataka kujua ni wapi nilipata zile cheni na hereni baada yakumuona kaka mati amezishika tukiwa tunacheza nafikiri hapo ndipo alipoziona na kuibua maswali. Akasema tuondoke. Hapo njaa inauma, ukumbi mzima unanukia harufu ya chakula kizuri. Joshi amekasirika, anasema tutoke anawahi kwenda kulala.” “Anawazimu!?” “Sijui. Haya tukatoka akiwa ametangulia. Tumefika nje, akanivuta kwa hasira anataka kujua ukweli. Nilikasirika Malo, nikajiambia ananidharau kupita kiasi. Nilichofanya nikuvua viatu mbele yake, nikaondoka kwenda kutafuta daladala kunirudisha nyumbani.” “Naya! hakukufuata?”

“Hapana Malo. Na wala hakutaka kujua kama nilifika nyumbani salama. Baba na Bale walichukia sana, mimi sikujua. Mama akamtetea.” “Haiwezekani!” “Kweli. Mama shida yake ilikuwa niolewe na msomi, kwa garama yeyote ile. Basi. Hiyo siku ikaisha, eti akaja kutokea baadaye ananiomba tena twende naye kesho yake siku ya jumamosi huko kwenye kulipiwa mahari, ili akanitambulishe kwa ndugu zake! Hapo amenifuata nyumbani mbele ya mama. Acha mama afurahi. Akakubali hapo hapo. Sasa vile alivyojirudi, nikajua ni kaka Mati tu. Sio Joshi. Nikasita kwenda.” “Lakini ulikwenda Naya.” “Mama alikuwa anamtuhumu baba. Anamwambia yeye ndiye ananifanya mimi nisimkubali Joshi. Nyumba ilikosa amani Malo! Baba akawa ndio analaumiwa.” “Kwa nini sasa?” “Mambo mengi. Aliona jinsi baba alivyosimama na mimi kipindi kile wewe umefungwa. Halafu baba usimuone kimya vile, yupo so observant. Makini mno. Kwa kukuangalia tu, anajua kama mtu ananipenda au la. Ndio maana alikupenda sana wewe. Alijua unanipenda. Sasa huo upendo kwako, hajawahi kuonyesha kwa kijana yeyeyote yule aliyeonyesha nia ya kutaka kunioa. Ndio mama akawa analaumu.” Naya akatulia.

“Sasa ikawaje?” “Nilipoona lawama zinazidi kwa baba, hata Bale akaniambia niende tu ili kuwe na amani mle ndani. Haya. Tukaenda hiyo siku ya jumamosi ambayo wewe ulikuja, ukanikosa. Lakini Malo, mtu ambaye hamuendani, wala haiitaji malaika ashuke akwambie. Na hata ukilazimishia, utakuja kuona madhara zaidi baadaye. Nikamwangalia Joshi na mimi. Jinsi alivyo kwangu na mbele ya watu wengine, ni watu wawili tofauti! Kwangu anakuwa mkatili, hanijali, sio kama anavyojionyesha mbele za watu. Kwenye jamii yao, anaheshimika sana. Sifa zake ziko kwa kila ndugu, lakini sivyo ninavyomfahamu mimi Joshi. Nikajiambia akija kuwa mume wangu, akinitesa, sitakuwa na kimbilio. Nitaonekana mimi nina tatizo. Ndugu zake walionekana watu wa kawaida tu. Hawana neno, ila wanamatarajio makubwa sana kwa Joshi na huyo mke mtarajiwa.” 

“Nikajiangalia vile jinsi mimi nilivyo, nilikotoka na mipango yangu, nikajiambia sina sababu yakujidanganya. Akanichukulia taksii kunirudisha nyumbani, aka…” “Subiri kwanza Naya. Hakukurudisha mwenyewe?” “Hapana Malo. Alisema amepata dharula, kuna sehemu anatakiwa kwenda, tutawasiliana baadaye. Akanipandisha kwenye taksii, akamlipa mwenye taksi, nikaondoka.” “Naya!” “Lakini sikujali Malo. Akili zangu zilikuwa kwako tu. Nasubiria simu yako, huku nikijiambia Malo wangu akirudi hiki na kile kitatokea.” “Pole mama.” Naya akajicheka kwa kujidharau.

“Ila usiku huo akapiga simu kuhakikisha kama nimefika salama. Hilo akawa muungwana. Lakini alishanikinahi, niliporudi tu, nikamtoa baba pale ndani. Tukajidai tunaenda kuwapa kuku maji, kumbe tunaenda kuteta. Nikamuelezea baba kila kitu. Sasa eti kesho yake tupo kanisani, ananijia na makaratasi ya scholarship za nchi gani sijui! Za huko Ulaya, eti anataka nikasome! Sasa kasumba yake ile yakulazimishia mambo na kunidharau. Akaanza kuponda masomo niliyosomea, akajidai ananisaidia. Acha Bale amjie juu mbele ya kila mtu.” “Naya!” “Weee! Usimuone Bale mpole kwako. Mkali yule. Alimgombesha na kumshushua palepale. Mimi nilikuwa nimeshamkabidhi makaratasi yote baba tokea mwanzo.” “Kama nakuona ukakimbilia mgongoni.” Naya akacheka sana bila kujibu hilo.

“Mama aliyachukua kutoka kwa baba, akasoma na kuanza kuhamasika. Baba naona akaona ni ujinga ule. Hapo hapo akayachukua yale makaratasi kutoka kwa mama, baba akamrudishia makaratasi yake yote na kumwambia siku aliyoniacha katikati ya mji, akiwa amenitoa nyumbani, alifanya kosa kubwa sana. Na mimi hapohapo nikapata mwanya. Nikamwambia sitaki kwenda kusoma popote na simtaki tena na yeye. Akaondoka na karatasi zake asiamini jeuri yule.” “Mama alisemaje?” “Mbona hatukaa ibadani siku ile? Kwanza Bale alimgombesha na mama. Halafu akaondoka bila kuingia kanisani. Haya, mimi na baba tukasema tuingie kanisani, Zayoni akaja kututoa kanisani, kuwa mama anasema turudi nyumbani. Mbona tulikoma!” “Kwa nini?” Naya akacheka.

“Yaani mama! Alilalamika zaidi ya miezi miwili.” “Anasemaje?” “Ametukasirikia mimi, baba na Bale kipenzi chake. Hatumsikilizi, tunamdharau yeye. Basi mtu akawa Zayoni tu. Ndio kipenzi cha mama na ndio mwema. Anazungumza na Zayoni tu ambaye anamsikiliza. Halafu ikageuka kuwa msaada bwana.” “Kwa nini?” “Akaanza kunifundisha kazi kwa hasira. Akanitoa kwenye kazi za nje kule kwa baba. Akasema zile kazi ndizo zinanifanya nisijitambue kuwa mimi ni mwanamke, nakwepa majukumu kama mwanamke. Nikaanza kazi za ndani kwa nguvu. Chakula nikipika kama hajapenda yeye, anamwaga hata saa nne usiku narudi jikoni naanza kupika upya. Mpaka nikaweza.” Malon alikuwa anacheka sana kila akikumbuka Naya na jikoni. 

“Lakini amekusaidia.” “Sana. Mbona nashukuru. Tulikuja kupatana alipoanza kuumwa. Mimi ndio nikawa mtu wake wakaribu sasa. Ananiachia maagizo ya mtoto wake Zayoni. Ananisihi kwa hili na lile juu ya Zayoni. Mama amekufa akimlilia Zayoni!” “Daah!” “Alikuwa akilia anamwacha mtoto wake bado mdogo.” “Lakini Zayoni ni mkubwa!” “Sio kwa mama. Hajawahi kukua yule. Nakwambia mama anakufa, anaacha wosia juu ya Zayoni. Kipindi cha mwisho na yeye alikuwa akimuomba Mungu amuongezee miaka kwa ajili ya Zayoni. Angalau amsogeze. Lakini ndio hivyo.” Naya akanyamaza. “Pole sana mama. Pole.” Wakatulia kidogo.

“Umefikiriaje juu ya wazo langu?” “Lipi?” “Juu ya kuongozana na baba. Naona kama itamsaidia akitoka kwenye yale mazingira. Na pengine akiondoka ujaribu kubadilisha chumbani kwao hata kidogo.” Naya akamwangalia. “Anaweza kukasirika, lakini itamsaidia. Zungumza na Bale, uone na yeye atasemaje?” Naya akanyamaza. “Naya?” “Nafikiria jinsi ulivyo Malon!” “Nini tena?” “Huwa unarudi na mipango mizuri, halafu unaniacha katikati.” “Nilirudi Naya. Nilirudi mama.” Naya akanyamaza.

 “Naomba hilo ulikubali. Najua umeshazoea kuwa na Malon mkosaji. Ambaye huwa anakosa au kuharibu. Lakini sio mimi sasa hivi Naya. Nimebadilika. Na nimevuna malipo kwa niliyoyafanya. Tena nimevuna kwa garama ya kukuacha wewe kwa mwanaume mwingine. Hilo lilinilaza macho Naya. Ilikuwa bora walivyokimbia na mali zangu, kuliko kujua upo na mwanaume mwingine ambaye hakufai, na unaweza kuolewa naye hivyohivyo kwa mimi kushindwa kusimama kwenye nafasi yangu. Na hilo ndilo lilikuwa likiniuma sana. Niliporudi na kukuta Joshi anakunyanyasa, hajui wala kuelewa thamani yako, nikajua ninayo nafasi. Nilirudi Naya.” Naya kimya akiwaza akionyesha wazi hajaridhika, akabaki kimya macho nje ya gari amejishika shavu.

“Naya?” Malon akauliza wakiwa wameshafika karibu na kwao. “Unanisikiliza?” “Nimekusikia.” “Unaniamini kama nilirudi?” “Nimejua kama ulirudi.” “Kwa ajili yako Naya. Wala si kwa sababu nyingine. Naomba hilo ulikubali na uamini.” “Nitazungumza na Bale. Naona wazo ni zuri. Itamsaidia.” Malon akaingia mpaka njia yakuelekea nyumbani kwa kina Naya, kisha akaegesha gari pembeni. Akashuka ndani ya gari akaenda upande wake. Naya hakujua ni nini anafanya.

Akafungua mlango. Kabla hajamgusa, Naya akajifungua mkanda wa gari na kushuka garini tena akimpita kama asiyetaka amguse kabisa. “Nilirudi Naya. Nilirudi mama. Nilirudi kwa ajili yako. Naomba hilo liingie kichwani mwako.” Naya akaanza kulia kwa uchungu sana. Alilia kama ndio ameambiwa mama yake amekufa. Malon akamvuta karibu akataka kumkumbatia lakini isivyo kawaida mpaka Malon akashangaa Naya akajisogeza pembeni kabisa hakutaka ambusu. “Nilirudi Naya. Ila sikukutafuta tena kwa sababu mama yako aliniomba. Alinisihi sana nikuache. Akiniambia upo kwenye wakati mzuri na Joshi. Na ningejua kama mama ni mgonjwa, ningekuja kukusaidia kumuuguza, nisingekuacha peke yako. Lakini sasa hivi nipo. Nataka kusaidia.” Naya akajaribu kutulia, Malon akajua ameridhika kumbe Naya hakutaka kurudi kwao akiwa na majonzi.

Walitulia vile kwa muda Naya akiwa anajaribu kutulia. Akajituliza mpaka akatulia mwenyewe. “Nakaribishwa nyumbani? Naweza kukusogeza mpaka nyumbani.” Malon akauliza alipoona Naya ametulia. “Mazingira siyo mazuri. Huwezi jua tukienda sasa hivi tutakutana na nini. Acha tu mimi niwahi.” “Basi naweza kuja kesho mkiwa nyinyi wote hampo ili kuweza kupata muda naye. Najua itamsaidia. Anatakiwa aondoe mawazo yake pale kwa muda. Na akikubali tu, ndio itakuwa mwanzo wake mzuri wa kufanya maisha yake yaendelee bila mama.”  Naya hakujibu, akabaki kimya kama anayeshindwa hata kumkaribisha nyumbani kwao tena. “Usiku mwema Malon.” Bila yakusubiri jibu Naya akaondoka. 

Alifika nyumbani akamkuta Bale na mdogo wake mezani wanasoma. “Baba yuko wapi?” “Amesema anawahi kulala leo.” Bale akajibu. “Amekula?” “Amekula.” Naya akapitiliza chumbani kwa baba yake. “Baba!” “Ingia.” Akaingia.  Naya akaenda kupiga magoti pembeni ya kitanda cha baba yake. Akanyamaza bila hata kuwasha taa. Baba yake alipoona kimya akawasha taa akiwa hapohapo kitandani. Akamuona Naya analia. “Ni nini tena?” “Nina hamu na wewe baba! Maisha yangu yamebadilika. Hunisubiri tena! Huzungumzi na mimi! Hujui linaloendelea kwenye maisha yangu! Nakuwa kama nimefiwa na wazazi wote?” “Najua kila kinachoendelea kwenye maisha yako.” “Wewe unajua kama juzi nimelipwa mshahara?” Baba yake akacheka akiwa amelala palepale amelala.

“Nimelipwa mshahara wangu wa kwanza, mwenzio.” “Hongera mama.” “Lakini nipo mkiwa. Unamaliza lini kuomboleza?” Baba yake akanyamaza. “Zayoni anakuwa amempoteza mama na wewe! Mwanzoni nilielewa, lakini siku zinazidi kwenda, hatumalizi msiba!? Hivi unajua hata mimi na Bale tumefiwa? Bale hajapata hata muda wakuomboleza! Anahangaika mambo ya shule na wewe. Anawasiwasi sana na wewe. Tumekuwa kama tumepoteza wazazi wote, tupo peke yetu.” Naya akaendelea kulia. Bale na Zayoni wakaingia. Wakakaa hapo kitandani.

“Mimi baba natamani hata nikisoma, niwe kama wewe.” Bale akaanza. “Umekuwa mtu wa familia. Nimekuwa nikikuona jinsi unavyohangaika na sisi. Hiyo imenisaidia sana kuepuka makundi mabaya na kunifanya nikae nyumbani muda mwingi, kwa sababu nimekuwa nikikuangalia wewe. Kazi na mambo ya hapa nyumbani. Sikuoni kama mtu uliyeshindwa maisha. Najivunia sana wewe. Hata kama nilikuwa karibu sana na mama, lakini nilikuwa nikikuangalia kwa karibu sana.” Akaongea Bale. “Mimi ninahamu na mama. Uchungu hauishi!” Zayoni akaanza kulia.

“Mimi najua pengo la mama itachukua muda kuzibika, kwa kuwa tulijizoesha kuwa humu ndani sisi tu watano. Na muda mwingi tumekuwa tukizunguka pamoja. Itatuchukua muda kuzoea. Lakini kama tukikubali hii hali mapema, itatusaidia kuendelea vile mama alivyotaka. Wote tunajua mama alitaka tusome sana. Lakini Zayoni, unaanza kufeli wakati ulikuwa unakuwa wakwanza darasani kila wakati! Mama alikuwa anakusifia sana. Naomba umuenzi mama kwa kuwa kile alichokitarajia. Kila ukimkumbuka, naomba ufanye kitu unachojua hata angekuwepo, angekifurahia.” Naya akaongea jambo lililomtuliza Zayoni.

“Mimi naomba nikuombe kitu baba.” Bale akapokea. “Najua unauchungu wakutofika pale mama ulipotamani akuone umefika. Pole. Lakini naomba unisaidie na mimi nifike hapo. Nisaidie baba yangu. Bado tuna Zayoni, bado maisha yetu hata sisi tuliobaki hayajakaa vizuri. Bado tunahitaji pesa zaidi na kuishi vizuri zaidi. Naomba usikate tamaa. Tuendelee. Na kama ni kukazana, basi tukazane zaidi. Nimebakisha muda mfupi sana chuo kiishe, naamini kama nikituliza akili chuoni, nitafanya vizuri.” Bale akaongea kwa hekima na taratibu. “Nimewasikia.” Baba yao akajibu. Wakaa naye hapo kidogo, kila mmoja akatoka hapo kasoro Zayoni aliyepitiwa na usingizi hapohapo.

Naya akamvutia Bale chumbani kwake. “Njoo nikwambie kitu.” Akanong’ona. Bale akaingia wakafunga mlango. “Bado unampenda Malo?” Naya akamuuliza, Bale akakunja uso. “Aliyekwambia mimi nampenda Malon ni nani?” “Toka hapa. Kwani mimi sikujui?” Bale akacheka. “Amefanyaje tena?” Naya akamsimulia mpango wote. “Daah! Hiyo itakuwa afadhali. Itamchangamsha baba. Au ndio maana leo umeongea vile?” “Nilikuwa natengeneza njia ili kesho Malo asipate shida.” “Angalau atapata pakuanzia. Najua amekubali, lakini swala la wapi aanzie najua ndio utakuwa mtihani.” Wakatulia kidogo.

“Baba akiondoka, atabaki hapa Zayoni. Na mimi nina mambo mengi kupita kiasi huko chuoni. Nakuwa hapa lakini wenzangu wanasoma Naya. Najiona nipo nyuma.” “Usijali. Kwa kuwa tumezungumza nao wote wawili, tutegemee mabadiliko. Baba akiondoka, nitajitahidi kuwa nawahi kurudi nyumbani ili Zayoni asijikute peke yake. Wewe rudi chuo, au hosteli mpaka huu muhula uishe.” “Hapo utanisaidia Naya. Na uwe unarudi nyumbani sio unachelewa sasa kama leo.” “Leo nilikuwa na Malo.” “Umeanza Naya!” “Siwezi kumuacha mtoto peke yake. Nilikuwa huru kuchelewa sababu nilijua wewe upo nyumbani. Kuna jambo nilitaka kuliweka naye sawa. Lakini sitarudia tena kuchelewa. Nakuahidi.” “Hapo sawa.” Wakazungumza kidogo, Bale akatoka. 

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~ 

Naya akampigia simu Malo, kumwambia kila kitu. “Hapo umefanya vizuri.” Ikawa kama Naya akakumbuka anafanya maamuzi kwa haraka tena bila kufikiria. Akajirudi. “Lakini Malo, nafikiria kama baba akiondoka, na mimi nikitakiwa kusafiri kikazi, nani atabaki na Zayoni? Ndio anakaribia mitihani yake ya darasa la saba.” “Kuna gharama yakulipa mama. Lazima ubadilike na wewe ujue unayo majukumu ya kifamilia. Safari kama hizo kama ni kwa ajili ya pesa ya ziada tu, itabidi zikupite.” “Malo!” Naya akaongea kwa kusikitika.

“Huna jinsi Naya. Jinsi mlivyomlea Zayoni, ni tofauti. Hawezi kujikuta hapo peke yake. Ataanza msiba upya. Itachukua muda kujijenga kuwa mama hayupo na amekua. Ila kwa sasa, naomba uridhike na mshahara tu. Mungu atatupa kwa njia nyingine. Jaribu kuzungumza na bosi wako umueleze mazingira ya nyumbani kwa sasa. Muombe muda. Mtakapotulia, utakuwa huru kuendelea na kazi.” Naya akaelewa. “Naona itanibidi kufanya hivyo. Nashukuru kwa ushauri. Asante.” “Karibu mama. Nikuache ulale, ili kesho usichelewe kazini.” “Sawa. Usiku mwema.” “Na wewe.” Wakaagana na kukata simu. 

Malon kwa baba yake Naya.

I

likuwa mida ya saa 4 asubuhi wakati Malon akiegesha gari nyumbani kwao kina Naya. Alimkuta baba Naya akisafisha nje. Anakata majani na michongoma iliyokuwa imeota sana na kuchanua kama maua. Akawa anaitengenezea vizuri. Alisimama kidogo ili kumsalimia, akarudi kukata michongoma huku akizungumza naye kidogo. Malon akachukua reki, akawa anakusanya yale majani na michongoma anavyokata baba Naya. “Naona kunachukua sura mpya.” Malon akasifia. “Nilipaacha muda mrefu, naona kumegeuka chaka. Heri nipasafishe kabla simba hawajahamia hapa.” Wakacheka kidogo.

“Biashara zako zinaendaje?” “Kwa kweli namshukuru Mungu. Siwezi kulalamika kabisa.” “Nimekuona jinsi ulivyobadilika!” Malon akacheka. “Na kanisani bado unakwenda?” “Nakwenda. Bado nimeokoka.” Baba yake Naya akasimama na kumwangalia. “Sidanganyi.” Malon akajitetea. “Kwa nini upo hapa Malon wakati nimesikia upo na yule dada anayeishi nyumbani kwako?” “Rita yupo pale kama mpangaji. Na Mungu wangu ni shahidi. Na yeye anajua yupo Naya.” “Sasa kwa nini ulienda mpaka nyumbani kwa wazazi wake, ukatambulishwa kwa ndugu zake kama hivi hapa kwa kina Naya, na ulisafiri naye?” “Alitaka kwenda kupaona Brazil, sikuona sababu ya kumkatalia kuongozana. Ila Mungu wangu ni shahidi, hakuna lililotokea kati yetu.” “Sio kweli Malon.” Baba yake Naya akabisha na kumshtua sana Malon.

Akashuka kutoka kwenye ngazi aliyokuwa akiitumia kufikia juu ya michongoma. Akamsogelea Malon. “Mimi nitakwambia kwa kuwa naijua historia yako Malon. Usipoangalia, kile ulichoishi duniani, utakiishi na kanisani pia ila tu ukikitetea au ukikipa sura ya utauwa.” Baba Naya akaendelea.

“Ninapokataa usemi wa kuwa hakuna kilichotekea kati yenu, ndivyo hivyo hivyo ulikuwa ukifanya na mabinti wengine kabla hujasema umeokoka. Kwako hakukuwahi kuleta maana kuwa na binti kwa muda kisha kumuacha tu. Historia yako tokea zamani mpaka hapa nikikusikiliza, unaonekana ni hivyohivyo. ‘Hakuna kilichotokea’, kama unavyosema lakini si kwa unao waacha. Rita ameondoka nchini akiaga anakwenda kupumzika na wewe kama mpenzi, huko Brazil. Ameacha mtoto wake kwa Naya, wewe ukiwepo na ukielewa kabisa lengo la Rita. Sijui kilichoendelea huko, ila kwa kukusikiliza hapa ni kama ulimkatili vibaya sana kwa kutotimiza azma yake ambayo najua kwa hakika, wewe uliijua, Malon.” “Sio moja kwa moja mzee wangu.” Baba Naya akatingisha kichwa kukataa.

“Hapo utajichelewesha sana Malon kwa kuwa kwa upande mmoja unajua ukweli ila umekusudia kutokubali tatizo lako na hutaki kubadilisha hapo. Hata mtu mjinga kabisa anaweza kujiuliza hili na kupata jibu kwa haraka tu. Kwani huyu Rita si alikuwa akiishi huko nchi za nje? Hapafahamu Brazili?” Malon kimya. “Kwani alikuwa na shida ya nauli kufika huko kwamba alitegemea msaada wako kufika huko?” Baba Naya akauliza swali jingine lililomziba mdomo Malon. “Mimi na wewe wote tunayo majibu yake, kama Naya amenieleza sahihi juu ya Rita! Kwa maana nyingine kwa hakika alikwenda huko Brazili kwa kuwa uliweka mazingira ya kuwa naye huko. Ama  si kweli Malon?” Baba huyo akambadilikia Malon.

“Inamaana na yeye Rita sasa hivi anapita kama wanawake wote ambao wameshapitishwa kwenye maisha yako, Malon, akiwepo Naya mmoja wao. Kasoro Rita anapitishwa na wewe wewe Malon ukiwa kanisani. Ila kilio chake ninahakika kipo kama wanawake wote unaowaacha vibaya sana.” Baba Naya akaendelea.

“Kama kwa Naya. Umekuwa mtu wakutoka na kuingia kwenye maisha yake vile utakavyo, kwa sababu unazochagua wewe, bila kuhesabu madhara yake.” “Najua madhara yake kwa kuwa na mimi huwa sibaki salama. Nampenda sana Naya na nateseka kuishi bila Naya. Mara ya kwanza niliamua kumuacha Naya, kwa kuwa nilitoka jela, nikamkuta akiwa na Joshi na amejawa furaha sana. Nikajiangalia hali yangu, na nilivyo, nikajua kuwepo kwenye maisha ya Naya, nikuendelea kumtesa. Nikaamua kumuachia Joshi. Niliporudi tena, nikakuta bado yupo na Joshi, lakini akimnyanyasa sana. Ndipo nikaona ni heri nirudi tu mwenyewe, tutapambana na maisha tukiwa pamoja na Naya, kwa kuwa huwa tunaelewana kwa kila kitu.” Malo akaendelea kwa makini sana asije akaharibu.

  “Mungu wangu ni shahidi, nilirudi nikiwa na nia yakumchumbia Naya. Lakini nilitaka kuzungumza na wewe kwanza. Kukwambia nimebadilika, na nimeamua kumuoa Naya. Nilitaka kukuahidi nitamtunza Naya kwa kadiri Mungu atakavyonijalia, lakini nikaishia mikononi mwa mama. Mama Naya aliniomba kwa kunisihi huku akinieleza alipo Naya na Joshi. Kuwa Naya ameenda kutambulishwa ukweni, na wanafuraha na wana amani. Hakuishia hapo, akanionya kabisa nisimtafute na wala nisiwahi kumpa mawazo ya biashara. Itakuwa nikuingilia mahusiano yao na kumchanganya Naya. Akataka nimuache Naya aendelee na maisha yake na Joshi. Ilibidi niondoke Mzee wangu, na kutii. Maana aliniambia maneno mengi na mabaya sana ila sitaweza kuyarudia. Ila sio kwamba najisifia, lakini hakuna mwanaume atakayeweza kumpenda Naya na kumthamini yeye kama Naya pamoja na kumuenzi kama mimi.” Baba yake Naya akamwangalia na kurudi kuendelea na kazi zake.

“Ila sina haraka. Nampa muda anichunguze yeye mwenyewe. Naya huwa ananijua vizuri, na mimi huwa simdanganyi. Kwa hiyo nimetulia, nampa nafasi mpaka yeye mwenyewe aseme. Hilo kama la Rita nimelifanya bila kufikiria, naahidi nitaongeza umakini kuanzia sasa nikimsubiria Naya aridhike na mimi. Na mimi sitasumbua tena.” Baba yake Naya akamtupia jicho tena na kuendelea na kazi. Kimya.

“Kwa sasa unafanya biashara gani?”  Akauliza Malon kwa tahadhari kidogo akijua na kwa baba Naya hapako sawa kwake ila akakusudia kupambana tu. “Vipi, unataka kuniajiri nini?”  Akauliza kwenye swali. “Kama ungependa. Huwa nakwenda Mbeya kukusanya mchele na kokoa. Nakuwa peke yangu. Ila nikipata msaidizi mwenye uelewa, itanisaidia kutumia muda mfupi  huko mashambani.” Kimya, akaona aendelee kupambana. “Kokoa huwa nasafirisha nje ya nchi, mchele ni hapahapa nchini. Nilianza kama utani tu. Sikujua kama ingelipa. Lakini utashangaa hiyo pesa inayopatikana kwa huo mchele!” “Watoto wangu wananihitaji sasa hivi.” Akajibu baba Naya akisikika mawazoni. “Sina watoto, lakini nafikiri wangehitaji uwepo wako na uwezo wako pia.” Akamuona ametulia tu, akiendelea na kazi. Kwa kuwa Naya alimwambia na anamjua sio mzungumzaji akaona na yeye atulie kidogo. Pakazuka ukimya, kazi ikaendelea.

“Na kweli sasa hivi nimeishiwa.” Kama aliyekuwa akiwaza kwa sauti, baba Naya akasikika. “Gari hiyo imeharibika, sina hata pesa yakutengenezea! Mtoto wangu anahangaika usafiri wakumpeleka kazini. Nimemsindikiza asubuhi hii kupanda daladala, wanamsukuma, sukuma, ameishia kusimama tu.” Akajua huyo mtoto anayemlalamikia ni Naya tu. Alijua jinsi anavyompenda Naya. “Kuna watu nafahamiana nao, ni mafundi wa gari. Nilifanya nao kazi. Naweza kuwaomba wakaja kulichukua ili waliangalie.” “Aaah! Hata hivyo ni kwa kuwa nina shida tu. Hiyo gari niyakuuza na kununua yakawaida. Naya alinisaidia kuinunua hiyo kwa sababu ya kipindi kile nafuga. Hata hivyo, nimekusikia. Acha nizungumze kwanza na Naya. Maana yeye ndiye anayepanga siku hizi mambo ya humu ndani. Tuone tunajipangaje kama mimi nikiondoka.” “Sawa kabisa.” Malon akakubali akijua jibu tayari.

“Kama nikuondoka, tunaondoka lini? Kwa kuwa nikweli tunahitaji pesa.” Akaongea baba Naya kama aliyerudishiwa ufahamu wake na kukumbuka wajibu wake kama baba wa familia. “Mimi lazima jumamosi niondoke. Ukiwa tayari tutaongozana. Lakini kama bado, unaweza kunifuata na basi muda na wakati wowote utakapokuwa tayari.” “Basi nitakujibu kesho. Acha leo nizungumze na mama yangu mzazi kwanza.” Akimaanisha Naya. “Na kuhusu gari, tunaweza kulitengeneza tu. Ukauza likiwa zima.” “Kwa sasa sina pesa na sitaki kuanzisha huo mjadala kwa Naya. Atatumia pesa yake yote kwa kutengeneza gari ambayo haitakuwa na faida. Acha tu tuhangaike kwa muda.” “Naomba basi mimi nilitengeneze.” Baba yake Naya akasimama na kumwangalia. 

“Naya aliniambia huwa hujui jibu la hapana.” Malo akacheka kama anayekubaliana naye. “Kwa hiyo hapa utalazimisha mpaka ukalitengeneze?” “Naona ni jambo la msingi.” “Sawa.” Malon akacheka. “Basi acha nipige simu waje kulichukua.” Baba yake Naya akacheka na kutingisha kichwa. “Nashukuru.” Akaona ashukuru tu. “Tusubiri wakaliangalie. Tukiona limeharibika sana, nitawaambia wauze vifaa vyake wakuletee pesa. Linaonekana limechoka sana. Sidhani kama kwa kuliuza hivyo zima kama lilivyo sasa kama utapata pesa nyingi.” “Na hiyo ndiyo ilikuwa hofu yangu. Nililinunua kwa mtu kwa bei nafuu akiwa ameshalitumia sana. Ila limenisaidia vyakutosha.” Malon akawapigia simu mafundi, akaomba waje walichukue.

Akiwa pale pale akisaidia kazi, wale mafundi wakaja. Wakazungumza naye, mwishoe mzee akaamua aliuze tu. Wakalichukua kwa makubaliano ya kumlipa baada ya siku mbili mbeleni. Malon naye akaondoka pale nyumbani kwao akiridhika kwamba kazi iliyompeleka pale ameimaliza na angalau amepata nafasi ya kujitetea na kwa baba Naya pia. Hata kama hakuwa amemuweka sawa, akajua muda utawabadili wote mawazo. Kwa asili Malon alijua kumfanya mtu akampenda, kama akiamua yeye. Hachoki, na anaweka juhudi haswa na kuweza kumuonyesha mtu yupo naye mpaka huyo mtu akabweteka akijua anaye mtu wakuwa naye kwenye jambo. Akajiaminishia kwa familia hiyo ambayo ilimpenda sana, kwamba hata safari hii aliyorudi tena itakuwa rahisi sana kwani kipingamizi mama, alishaondoka. Akaendelea kujiwekea mikakati.

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

‘Nipigie simu wakati unakaribia kutoka. Nitakuja kukuchukua.’ Ujumbe ukaingia kwa Naya, kutoka kwa Malon. Naya akafikiria, akaamua kumtumia ujumbe. ‘Usisumbuke Malon. Leo nitawahi kutoka, nafikiri sitasumbuka usafiri. Na endepo nikichelewa, baba amesema atanisubiri kituoni.’ ‘Naweza kupiga?’ Naya aliposoma ule ujumbe, akampigia yeye. “Ni nini Naya, mama?” “Naona nisikusumbue. Kwetu mbali Malo. Na wewe najua umechoka, sitaki kukusumbua.” “Umemaliza?” Naya akacheka kidogo akisikika aliyegoma. “Kuna jambo nataka kukwambia. Nilikuwa na baba leo.” Hicho kikamvutia Naya kutaka kujua ni wapi walifikia kabla yakurudi nyumbani. “Sawa nikiwa nakaribia kutoka nitakupigia. Vipi siku yako?” Naya akauliza kiuungwana. “Mpaka sasa sio mbaya. Nipo sehemu kuna kitu nafanya, nipigie wakati unakaribia kutoka ili nisogee.” “Nashukuru.” “Karibu.” Wakakata.

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

Jioni Malon alifika hapo na gari ya tofauti. Kadogo tu aina ya Vitz. Naya akacheka wakati anamsogelea. “Umepata wapi hii gari?” “Mbaya?” “Hapana. Sio mbaya. Ila sijawahi kukuona ukiendesha gari ndogo hivi tokea nakufahamu!” Malon akacheka. “Unayo leseni yako?” “Unataka leo nikuendeshe bosi?” Malon akacheka na kumfungulia mlango wa dereva na yeye akaenda upande wake. Naya akawasha gari. “Tunaelekea wapi?” “Kwangu kwanza.” Naya akaondoa gari.

“Uzuri wa hiyo gari, haitumii mafuta sana. Rahisi kuitengeneza.” Naya akawa anamsikiliza huku akiendesha. “Hii ukiitumia kwa matumizi yako ya kila siku asubuhi na jioni  kwa kazini, na mizunguko ya pale nyumbani, haitamaliza pesa ya mtaji wa biashara.” Naya akamgeukia. Akakunja uso kama ambaye hamuelewi, akaendelea kuendesha. “Umenisikia?” “Nimesikia lakini sijaelewa Malo!” “Nimenunua hili gari, likusaidie usafiri.” Naya akatulia kidogo. “Baba anaonekana anaweza kwenda na mimi Mbeya. Na yeye ndiye anayekusindikiza kituoni. Anasema leo aliona jinsi unavyohangaika na usafiri. Ameshinda siku nzima anasononeka!” “Nilipanga nikipata pesa nitengeneze ile gari yake.” “Ile gari imechoka Naya. Yazamani. Nimempelekea fundi leo. Wameitizama, gharama ya kutengeneza mpaka iweze kuwa barabarai ni kubwa sana.” “Kwa hiyo haitafaa tena?” “Haiwezi. Itawalia pesa zaidi. Lakini wakiichukua wao, wanaweza kuiuza vifaa vyake, wakapata pesa.” Naya akatulia.

“Ni nini Naya?” “Naona unamajukumu mengi! Na mimi sitaki kuingia huko. Halafu hili ni gari Malo. Nikiiharibu kwa sababu yeyote ile?” “Kwa nini usifikirie urahisi utakaopata kukufikisha kazini na kwenye mizunguko yako kwanza? Kwa nini unafikiria shida wakati wote? Tukiwa hatuna uwezo, inaeleweka mama. Sasa sasa hivi uwezo upo, bado tuhangaike tu!” Naya akabaki kimya. “Kama hutaki kuchukua, basi mimi nitakuwa nikija kukuchukua asubuhi na kukurudisha nyumbani.” Naya akacheka kidogo kwa kusikitika kisha akaguna.

 “Ni nini Naya?” “Nimeshindwa kukutabiri Malo! Hakika nimeshindwa na kukuelewa. Nilidhani nakufahamu sana. Ukajenga tabia iliyonifanya nikufahamu kama unayenijali sana kuliko mtu yeyote yule, lakini inapokuja kwenye uhalisia unageuka tena, unakuwa ni kama usiyejali kabisa. Unaweza ukawa katili, mpaka najiuliza unawezaje! Hakika nashindwa kukuelewa!” Kabla hajajibu Naya akaendelea.

“Sijawahi kuogopeshwa na uwepo wa mtu kwenye maisha yangu kama wewe Malo.” “Haiwezekani Naya!” “Hakika Malon. Umeyabadili sana maisha yangu na moyo wangu. Imefikia kiasi kwamba nikiwa na wewe, sifurahii tena ila kuogopa.” “Kwa nini!?” Malon hakutegemea hata kidogo. “Kwa kuwa unakuwa mtu wa msimu! Unakuwa hivi, unapotea. Ukirudi unanikuta kwenye hali isiyofaa. Unanipa matumaini makubwa sana. Nakufungulia moyo wote na akili. Nikishazama kabisa kwako, nikiwa nimejawa tumaini na furaha ya ajabu, ndipo unapotea! Nabakia nateseka sana. Na wewe huwa hujui kugeuka nyuma hata kuangalia naendeleaje pale uliponiacha. Unaendelea na maisha yako mpaka nije kukutafuta tena.” Naya akamgeukia kidogo.

“Sasa kama hivi sasa hivi, kwanza tupo hapa pamoja kwa sababu jana nilikufuata nyumbani kwako kukupa zawadi ukiwa upo tu hapa mjini, umekaa tu nyumbani kwako, ndipo umerudi na mipango mizito na mizuri sana kama kawaida yako. Sijui hii itakuwa ni leo tu! Sijui kama kesho utakuwepo! Sijui hii gari kama itakuwepo na itakuwepo kwa siku ngapi! Naogopa hata kwenda nayo nyumbani. Nisije nikawapa tumaini kama ile biashara uliyoniambia tutafanya. Nikamzungusha baba yangu mjini tukisaka vifaaa. Tukatafuta mpaka fremu na mkataba tukaingia. Ukaja kuniacha kwa ukali sana, ukinisukumia kwa Joshi. Nimeingiwa hofu na wewe Malo.”

“Mama alinifukuza Naya!” “Kumbuka unazungumza na mimi Malo. Sio mtu mgeni kwako. Mimi nakujua. Kama ungenitaka kwa hakika, hakuna mtu wala kitu kingekuzuia. Linapokuja jambo unalolitaka wewe, huwa wewe sio mtu wa kukubali ‘hapana’. Hata kama ungeambiwa nimetambulishwa kwa wakwe na mahari nililipiwa, basi ungenipigania tu. Hujawahi kunipigania Malon. Hata mara moja. Sitaki kukuhesabia, lakini mimi nilikupigania Malo. Kwa moyo, nafsi na juhudi zangu zote. Bila aibu, bila kuchoka. Nilijua ni wewe nakuhitaji. Mvua ilinyesha, jua lilitoka, huku nikitukanwa juu yako. Lakini nilijua ni wewe nakutaka.” Naya akaendelea taratibu tu bila jazba.

“Ulijua vile baba yako naye alivyonifukuza kwenu, akimwambia baba yangu asiniruhusu kuwa na wewe kwa kuwa nitaharibikiwa kama wengine. Lakini Malo, nilikuchagua wewe. Ila wewe ulitoka jela, ukanisukumia mikononi kwa wanaume wengine. Ni mapenzi gani hayo?” “Nilikuwa sina kitu Naya. Nimetoka kila mtu akiniambia sikustahili. Shukurani pekee kwako nikukuacha. Ningefanyaje?” “Wewe sio wakuniuliza ungefanyaje Malon, linapofika jambo unalolitaka! Halafu mbona mimi waliniambia mengi hivyo hivyo tena ya aibu yakupitiliza! Sikuwasikiliza Malo, nilibaki na wewe tu.” Malo kimya.

“Halafu kwa hiyo kama ulivyosema mahusiano yetu yanakuwa yanajengwa kwenye pesa tu! Ukiishiwa tena? Unataka tuje kuwa na ndoa kama ya wazazi wangu wakihesabiana mambo ya mali? Ukiwa na pesa unarudi, ukifilisika unaondoka! Hayo yanakuwa mahusiano gani Malon?” Kimya. “Tokea mwanzo nimekuwa nikikuomba unichague mimi Malo. Mvua inyeshe, jua litoke, uwe umenichagua mimi, hilo lingenipa faraja. Lakini Malo, hujawahi kunichagua. Unakuwa na sababu nzuri sana na zakueleweka kila wakati unapoamua kuniacha na kunirudia mimi. Ningefurahi ungesimama na mimi katika shida yako, halafu sasa hivi tukafurahi pamoja.” Naya akaendelea.

“Lakini huku ni kunidhalilisha Malo. Najihisi unaniona ni kama nipo dhaifu sana, siwezi kuwa na wewe katika maisha yako. Nakuwa ni mtu unayeweza kunitoa unapojisikia wewe, na kuniongeza unapotaka wewe. Nakuwa sina uhakika na wewe Malo. Sijui lini utaamua nini na utaniacha kwenye wakati gani! Hunifikirii mimi kama Naya!” “Hakuna mtu namfikiria kama wewe Naya.” “Ni unaponiona au kukutana kama hivi sasa hivi. Narudia tena Malo, na huo  ndio ukweli. Tupo hapa sasa hivi, safari hii, wakati huu ni kwa sababu mimi nilirudi kwako kukuletea zawadi ya saa, ya kukushukuru. Inamaana nisingerudi jana kukuletea zawadi, na kukupa mwanya wa kunirudisha nyumbani, tukazungumza machache ukajua kinachoendelea kwetu, ukapata sababu ya kurudi nyumbani kuzungumza na baba, ukajua sononeko lake juu yangu, inamaana usingejua nina shida ya usafiki wakati wa kwenda na kurudi kazini, na wala hili gari usingenunua, Malo. Maisha yako na Rita yalikuwa yakiendelea vizuri sana, bila shida.”

          “Rita hajawahi kuwa mwanamke wangu.” “Acha kumfanyia Rita kama ulivyotufanyia sisi wote Malon! Unatenda dhambi.” Naya akaongea kwa kuumia sana kama baba yake tu alichomwambia Malon asubuhi hiyohiyo. “Kwa maelezo yako wewe mwenyewe mbele yetu wote, unasema ulikwenda mpaka nyumbani kwa wale wazazi wao kutambulishwa na kwa ndugu zake. Najua wewe si mjinga Malon useme hukuwa ukifanya hilo kwa kutofahamu! Kwa nini mtu kama Rita akupeleke nyumbani kwao na ndugu wakutambue kama mpenzi wa Rita? Unakuja kuchukua mtoto wa Rita shuleni wewe kama nani kama hamkuwa kwenye mahusinao? Umemtoa hapa mpaka Brazil!” “Nilikueleza jinsi ilivyokuwa Naya. Rita alitaka kupaona Brazil, sikuona sababu ya kumkatalia.” Akajibu hoja moja tu.

 “Mimi ningefanya hivyo, ingekuwa sawa kwako? Ulikasirika ulipokuja nyumbani na kuambiwa nilitoka na Joshi kwenda kwao. Kinachokufanya ufikiri ni sawa kwa wewe kwenda Brazil na Rita, huku ukijua kabisa anakutaka kimapenzi, amekupeleka mpaka kwao ukakubali kwenda kutambulishwa, amekuamini mpaka na mtoto wake, ndugu zake wote wanakufahamu wewe na yeye mpo kwenye mahusino!? Ni nini unaendelea kufanya Malon? Mpaka lini na kwa umbali gani utaendelea kuumiza watu? Wewe unaweza usielewe madhara unayoacha kwa watu Malon, kwa sababu kama sasa hivi ushamalizana na Rita, umerudi hapa. Lakini mimi naweza kuhisi alipo Rita sasa hivi na kule alikokwisha kukutambulisha. Ni aibu na fedheha Malo, wewe hujawahi kuishi hapo. Maana kama sasa hivi unayo sababu nzuri tu inayokupa amani kumuacha bila kujali eti kuwa ulishindwa kumkatalia! Utashindwa kumkatalia kwa mangapi na wangapi Malo?” Kimya.

“Hivi sivyo ulivyokuwa ukiwafanyia wasichana wote uliokuwa ukilala nao kipindi tupo wote?” “Naya!” “Unakataa nini Malo? Unabisha nini wakati nimekukumbusha kabisa kuwa unazungumza na mimi! Tuache wengine wote, turudi kwa Loi. Ulinipa sababu gani kama sio kama hii inayofanana na Rita? Alikung’ang’ania au kukuomba ukashindwa kukataa. Si ni hivihivi Malo? Kanusha kama si kweli?” Malon kimya akainama.

“Najua tupo kwenye wakati mgumu wa maisha pale nyumbani. Naamini ni kwa muda tu. Mungu atatusaidia. Acha nizoee maisha yetu, pengine yatakuja kubadilika baadaye. Kuliko haya maisha yanayoendeshwa kwa hisia, Malo! Ukijisikia kunihurumia, unanitendea jambo kubwa, zuri lakunisisimua. Hisia zako kwangu zikiisha, unaniacha nateseka sana.” Naya akafikiria kidogo. “Hapana Malo. Umenichezea hisia zangu vyakutosha. Kwa sasa ulitakiwa wewe unielewe mimi ni mtu wa namna gani, sio kama hao wasichana wako wazuri, wasomi wanaokutaka kipindi ukiwa kwenye magari ya thamani! Hapana Malon. Inatosha.” Wakati huo Naya anazungumza naye, alishageuza njia zamani sana kuelekea nyumbani kwao wala sio Kunduchi nyumbani kwa Malon.

“Nakushukuru kwa msaada wa usafiri, lakini tokea tunaanzana Malo, ombi langu kwako lilikuwa moja tu. Nikikuomba mpaka kwa machozi mpaka Side nilimtuma kwako, nikikuomba unichague mimi na hujawahi kunichagua Malo.” “Nakupenda Naya. Na nimekuchagua wewe. Nilirudi kwa ajili yako.” “Sivyo ulivyoniambia siku nakupigia simu na kukuta upo nchini nikiwa nakusubiri. Sivyo ulivyofanya kwa vitendo vyako baada ya ile simu. Hata hukuniachia shilingi moja uliyojua nilihusika kuikusanya kwa jasho langu mpaka kuifikisha kwenye kuwekewa dhamana na kurudi mikononi mwako. Ulinikuta na shida sana, na ukaniacha na shida vilevile usiniache hata na pesa kidogo tu! Haya, ukaendelea na maisha yako na Rita bila shida yeyote. Na kwa jinsi ninavyokujua Malon, Mungu anisamehe kama ni sivyo?” Naya akacheka na kutingisha kichwa.

“Nini?” “Kwa mahusiano niliyoyasikia kwa Nolan, pamoja na Rita mwenyewe kabla hujajua mimi ninayekufahamu nipo na mtoto wa Rita, inaonekana na kusikia ulikuwa pazuri tu na Rita, mpaka mimi nilipoingia kwenye picha ndipo hapo nikatibua mapumziko yenu huko Brazili, lakini inaonekana mlikuwa na mipango mizuri sana. Kwa kumuangalia tu Rita si mpumbavu au mjinga kudandia safari ambayo hakuwa na uhakika nayo. Kulikuwa na ahadi nzuri tu, na ndio maana akaenda umbali mkubwa sana hata kuacha mtoto anayempenda vile kwa mtu kama mimi mgeni kabisa. Unajua sana unalolifanya Malo, acha kuepuka ukweli.” Kimya. “Anyway, nashukuru kwa usafiri Malo, lakini asante. Tunza tu mali zako na uzitumie kwa furaha. Unastahili. Ni jasho lako, huwa unahangaika peke yako.” Naya akaegesha karibu na kituo cha kuelekea nyumbani kwao. 

Akamgeukia Malon. “Tafadhali usije kunichukua asubuhi. Nitapanda tu daladala. Mimi bado nipo palepale uliponiacha. Acha na mimi nihangaike kama wewe. Ila nashukuru kwa ajira ya baba. Nitazungumza naye na kumtia moyo, ili muongozane. Naona itamsaidia kumrudisha kwenye hali ya kufikiria.” Malo akabaki ametulia.

“Nikuulize kitu Malo?” “Niulize tu.” “Nafikiria zawadi ya kumnunulia. Hivi huko mnakokwenda, mashambani, mazingira yakoje? Atahitajika nini?” Malon akavuta pumzi kwa nguvu akijaribu kutulia. “Kama viatu. Aina gani ya viatu, nguo na mashuka vinahitajika ili niweze kumuandalia begi lake. Mnalala wapi? Vitu kama hivyo.” Malon akacheka.

“Cha kwanza ujue ni mashambani. Vijijini kabisa. Wakati mwingine mimi huwa nalala kwenye gari tu. Wakati mwingine unaweza kupata familia ikakualika nyumbani kwao.” “Malo! Hamna hoteli?” Malon akacheka sana. “Nilikwambia huwa nakwenda vijijini kabisa, mama. Kwa wakulima. Lazima nisimamie hiyo kokoa katika kila hatua, ili nisikusanyiwe na mbaya. Kwa sababu hebu fikiria, nitumie pesa yote kuisafirisha mpaka huko, halafu waje waniambie mzigo haufai! Si unaona nitakuwa nimeingia hasara  sana?” “Kweli.” Naya akabaki akimfikiria baba yake. Malon akacheka. “Unamuhurumia baba?” “Ulijuaje? Natamani kuahirisha, asiende.” Malon akabaki akimwangalia.

“Au uende naye wakati mwingine. Safari hii muache tu. Tutafikiria kitu kingine chakufanya.” Malon alimtizama asimmalize. “Nitatafuta biashara nyingine au hata nimpe pesa afanye kitu kingine.” “Mbona mimi nafanya Naya?” “Wewe ni kijana Malo. Baba mtumzima. Akienda huko na kuanza matatizo? Ndiye mtu pekee tuliyebaki naye maishani. Heri tuwe na vichache ila tuwe pamoja, kuliko vingi akiwa yeye hayupo. Tutakuwa sawa tu. Naona wewe uendelee Malo.” “Acha kuogopa Naya. Huko nako wako watu wazima na wazee zaidi ya baba yako wanaishi na wananifanyia mimi kazi.” “Mmmh! Hayo ni mazingira yao Malo. Baba kwa umri alio nao kuanza kitu kipya! Hapana Malo. Mungu hawezi kutuacha tukalala njaa. Huu mshahara wangu utatosha kwa sasa. Acha tu tubaki naye.” 

“Naya! Umeingiwa hofu mama. Naomba mpe baba nafasi yakufanya kitu na kuona matunda yake. Sasa hivi hapa nchini mambo yamebana. Lakini sio nchi nyingine. Kule tunapokwenda atakutana na watu wazima kama yeye na zaidi yake, ataona jinsi wanavyohangaika bila kuchoka na kutokata tamaa. Siku nyingine za jioni wanakuwa na starehe zao. Na ngoma za kwao. Kwa kichache walicho nacho, wanayo furaha. Wanashida nyingi sana, lakini maisha yanaendelea. Wanakuja siku nzima wananikusanyia kokoa. Wananiuzia mazao yao. Wacheshi wachangamfu. Ndicho kitu baba anachohitaji kukiona sasa. Kwa vitendo sio maneno. Kitu kipya na kigeni kitakachochukua mawazo yake. Watu wanaopitia changamoto ngumu na bado wanapambana. Hiyo itamsaidia na kumsogeza karibu zaidi na Mungu.” Malo akaendelea.

“Ukifikiri kuwa wewe unashida, ukienda kule utaelewa. Watu wanashida Naya. Shida haswa. Imenifanya kuwa mnyenyekevu na kujiona nina bahati kubwa hata hapa nilipo. Utakuja kuona baba atakaporudi.” Naya akabaki akifikiria. “Atakuwa sawa, usiogope.” “Naomba unisaidie kumwangalia Malo. Ukiona anashindwa, mtafutie sababu yakurudi. Tafadhali Malo. Ndio nguzo pekee niliyobakiwa nayo.” “Nitafanya hivyo mama. Usigope. Na kuhusu nini chakubeba, naweza kukuandikia kwa ujumbe, nikakutumia. Ukipenda, naweza kukusindikiza ukanunue.” “Nitashukuru sana ili nisinunue vitu visivyo.” Naya akafikiria kidogo. 

     “Nashukuru kwa usafiri. Mungu akubariki.” “Naomba ulichukue hili gari Naya. Litakusaidia wewe na kina Zayoni.” Naya akafikiria tena kidogo. “Asante Malo. Lakini hapana. Nitakuwa sina amani nalo. Nitakuwa nikiliendasha kwa hofu, sina amani. Silistahili hili gari Malo. Naomba usianzishe kitu kingine ambacho unajua wazi kitakuja kuniumiza tena.” “Nakuahidi sitakuumiza tena Naya. Najifunza kutokana na makosa.” “Hapana Malo. Tutakuwa sawa tu. Kwanza nahisi wote tupo kama baba. Hakuna anayelalamika sasa hivi. Kila mtu yupo sawa na haya maisha. Nahisi malalamiko ya mama yalimuingia baba kichwani ndio yanamtesa. Baba sio mtu wakulalamikia mimi kupanda daladala. Bado anatembea na hukumu ya kushindwa maisha. Lakini daladala sio kitu kibaya. Ni rahisi, hupotezi pesa, na nikijitahidi kuwahi kuamka zaidi, napata nafasi ya kukaa. Kwa hiyo nipo sawa Malo. Asante. Nasubiria orodha ya vitu vyakumnunulia.” 

 “Kwa hiyo hiyo kesho nije kukuchukua kazini au ungependa tukutane wapi?” “Naweza kukufuata unapojua yapo hayo maduka.” Malon akacheka na kutingisha kichwa kama anayesikitika. “Nini sasa? Nimekosea nini tena?” “Naishi Kunduchi. Unafanya kazi CocaCola, njiani na kwangu. Yaani nikupite pale, niende madukani, halafu wewe unapanda kwenye daladala kunifuata nilipo! Ni nini unataka kitokee Naya au kunionyesha?” “Nakupunguzia shuguli Malo.” “Sawa. Ni saa ngapi unafikiri utakuwa na nafasi.” “Jioni nitakuwa nimechelewa sana?” “Hapana. Tunaweza kufanya jioni baada ya kazi. Sio vitu vingi na vinapatikanika sehemu za karibu.” “Sawa. Nitakuona kesho Malon.” “Naomba uchukue hili gari Naya. Tafadhali mama.” “Hapana Malo. Asante.” Naya akashuka, na kuondoka.

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

CONVERSATION

1 Comments:

  1. Habari zenu. Ilikuwa ngumu sana kwangu wakati mpenzi wangu aliniacha kwa mwanamke mwingine. Niliharibiwa kihisia, nilivunjika moyo na sikujua la kufanya ili kumrudisha. Nilihangaika kwa miezi mingi na niliendelea kutafuta msaada kutoka kila mahali hadi nilipopata kujua kuhusu DR DAWN. Niliwasiliana naye na kumweleza shida zangu. Alikuwa tayari kunisaidia na kunisisitiza nifuate taratibu ili aweze kurejesha penzi kati yangu na mtu wangu na pia kuhakikisha tunarudiana wote wawili. Nilipata mahitaji yote na ilifanya kazi hiyo. Baada ya saa 48, nilipata ujumbe kutoka kwa mpenzi wangu akiniuliza tarehe. Sasa tuko pamoja tena na shukrani zote kwa DR DAWN. Anaweza kukusaidia kumrudisha mpenzi wako,
    Anaweza kukusaidia na uchawi wa ujauzito,

    Anaweza kukusaidia kuponya aina yoyote ya ugonjwa.

    ikiwa uko tayari kuamini na kubaki na matumaini. Watumie barua pepe tu kupitia: dawnacuna314@gmail.com
    WhatsApp: +2349046229159

    ReplyDelete