Naomi Simulizi |+1 205 767 8163 |naomisimulizi@gmail.com MAPENZI & PESA! – SEHEMU YA 14. - Naomi Simulizi

MAPENZI & PESA! – SEHEMU YA 14.

Alipofika nyumbani akabaki akishangaa. Nyumba ilikuwa safi sana. Mazingira ya nje yalikuwa masafi sana kama enzi za uhai wa mama yao, baba yao akiwa anasafisha mara kwa mara kumridhisha mkewe, kumuonyesha wanapoishi sio pabaya. Alijitahidi kuweka mazingira safi wakati wote. Sasa tokea mkewe aanze kuugua, hakurudi kusafisha tena mpaka siku hiyo. Akasimama pale akishangaa. Zayoni akatoka. “Baba amesafisha nyumba.” “Yuko wapi?” “Ametoka, amesema hatachelewa kurudi.” “Umekula?” “Nilikuwa nasoma. Nina shida Naya.” Naya akamsogelea. “Unataka nini?” “Hela.” “Ya nini?” Naya akamuuliza.

 “Kuna vitu vidogovidogo nikinunua, naweza kwenda kuuza shule. Tukapata pesa.” Naya akacheka. “Kweli Naya.” “Wazo zuri sana lakini sidhani kama ni wakati sahihi. Bado muda mfupi sana umalize shule. Ukimaliza mitihani, ndio anza biashara. Lakini naomba isiwe sasa hivi.” “Sasa nikimaliza shule nitamuuzia nani?” “Ukikosa wateja, utafanya biashara ingine.” “Biashara gani?” Naya akafikiria.

“Na mimi nataka kusaidia Naya!” “Naelewa. Unakumbuka ujuzi ulionao wa kupiga picha?” “Kamera iliharibika!” “Tutanunua nzuri na ya kisasa ili uanze tena. Lakini safari hii tutajitangaza. Ili ufanye kazi nzuri. Naweza hata kuwa nakusindikiza kama ukipata kazi kubwa. Nitakuwa nikikusindikiza. Halafu kuna sehemu nzuri tukipata, tunaweza kupakodisha, ukapatengeneza vizuri, ukawa unawapiga watu picha.” Akamuona anacheka.

“Unaakili yakufikiria Naya wewe! Kila ukiongea unatoa wazo zuri.” Naya akacheka. “Ndio urudishe akili shuleni. Jikaze, umalize shule, ndio tuanze kutengeneza pesa.” “Sawa.” Wakamuona baba yao anarudi. “Bale amesema leo hatarudi. Anamtihani kesho.” “Na mimi ameniambia. Shikamoo baba.” Naya akamsogelea huku akicheka. “Unanicheka?” “Umenyoa, ukapendeza. Nimefurahi.” Baba yake akacheka na kumsogelea Zayoni. “Vipi shule?” “Naendelea. Umependeza.” Zayoni naye akasifia.

“Sasa kwa kuwa wote mpo hapa, nataka niwaambie nimepata kibarua kwa Malon. Ni Mbeya.” “Unarudi lini?” Zayoni akauliza kwa wasiwasi. “Sijajua.” “Mimi naona ni wazo zuri baba. Huwezi jua ni nini utakutana nacho huko. Na juu ya Zayoni, nitajitahidi kuwa nawahi kurudi nyumbani. Ili asiwe peke yake.” “Ulisema unasafiri Naya. Nitabaki na nani wakati Bale amesema atakuwa busy na shule ili amalize huu muhula vizuri? Natamani mama angekuwepo jamani!” “Hapana Zayoni. Naomba huko tusirudi. Sasa hivi sisi ndio tumebaki hapa. Lazima tujipange na tujue tutaishije. Umenisikia?” Zayoni akajifuta machozi.

“Nisikilize Zayoni. Hatuwezi kuendelea hivi tulivyo. Lazima kuenzi kile mama alichokuwa akitaka. Sisi tusome sana, na baba atafute pesa. Sasa hatuwezi kuacha sasa hivi. Itakuwa ni kama kutomuenzi. Lazima tujipange upya. Mama hayupo na hatarudi tena, na hakuna wakuchukua nafasi yake kwetu. Hilo lazima tulikubali. Ila tusaidiane. Mimi nimezungumza sana leo na bosi wangu. Nimemwambia mazingira niliyonayo nyumbani na kuwa wewe unakaribia mitihani yakumaliza shule ya msingi na Bale hatakuwepo nyumbani. Unahitaji mtu nyumbani. Ameniruhusu niwe nawahi kutoka. Saa 9 na nusu amesema naweza kutoka na muda huo kutakuwa hakuna foleni. Kwa hiyo utajikuta nyumbani peke yako kwa muda mfupi sana. Tunahitaji pesa na tunahitajiana. Umeelewa?” Zayoni akatingisha kichwa kukubali. “Na sitasafiri mpaka niwe ninauhakika baba yupo nyumbani au Bale. Kwa hiyo usiogope.” Zayoni akatulia.

“Au nisubiri mpaka Zayoni amalize mitihani?” “Hapana baba. Ulinifundisha linalowezekana leo, lisingoje kesho. Unajuaje kama hapo baadaye kama hatakuhitaji tena?” Kimya. “Tutakuwa sawa baba. Naomba chukua hatua ya imani. Nenda. Ukishindwa kwenda sasa hivi kwa sababu hii, ujue kesho litaibuka jingine. Hutawahi kuondoka humu ndani na hutaweza kuchukua hatua yeyote kwa sababu utajiona upo peke yako na unahitajika kwetu kwa hili au lile. Lakini naomba ukubali kuwa na sisi tupo kukusaidia.” Wakazungumza na kujipanga. 

Siku Inayofuata

Naya & Malon Tena.

W

akati wapo madukani wakinunua vitu vya baba yake Naya, Malon akajaribu tena. “Naruhusiwa kuja kumchukua Zayoni kesho jioni.” Naya akamgeukia na kusimama akimtizama. “Kwa nini!?” “Kupata naye tu muda. Kuzungumza naye kabla ya safari.” “Kwa nini!?” “Naya mama! Kwani vipi?” “Huyu mtoto amefiwa na mtu muhimu sana kwake Malon. Na mimi huwa nakujua. Unaweza kuanzisha kitu kingine kwenye maisha yake, ukamuacha, tukaanza msiba mwingine. Baada yakuona mama anafukiwa kule makaburini, aliingiwa na mshtuko mkali sana. Aliumwa muda mrefu sana, akiwa hawezi hata kutoka kitandani. Tumemjenga kwa shida sana. Nakuogopa Malon. Hakika nakuogopa.” Naya akafikiria kidogo akamwangalia Malon.

“Unayo jinsi yako kwenye mioyo ya watu. Nzuri sana. Unajua kupenya kwenye moyo na akili ya mtu bila shida na  kumfanya mtu akajisikia ndio wewe pekee anakuhitaji duniani. Lakini huwa hudumu Malon. Unaondoka katikati ya hiyo hali na kuacha mtu anakuhitaji. Mimi sio wa kwanza. Ulipokuwa jela, nilikutana na hivyo vilio kwa wengi mpaka kwa wazazi wako. Hujui kujifunga kwenye mahusiano Malo. Hujui kusimama na mtu kwa muda mrefu. Ukianza na Zayoni, ukamuumiza, inaweza kumuharibu kabisa. Na mama wakumjenga hayupo. Mimi nilikuwa nikiweza kusimama, sababu ya baba. Nilikuwa na kimbilio. Yeye hatakuwa na kimbilio. Yaani sasa hivi ndio namfahamu yule mtoto. Maisha yake yalikuwa ni yeye na mama tu. Hata baba kumbe hamfahamu kabisa Zayoni. Ndio tunajifunza tabia zake na kumwelewa ili tuweze kumsaidia. Sasa hivi ndio naelewa kilio cha mama kwa Zayoni. Alijua angepata shida akimuacha.” Naya alibadilika akawa makini sana kwa Malon.

“Nimekuelewa Naya. Na mimi sitafanya hilo kosa la kumuunganisha na mimi. Nimekuelewa tokea jana. Ni kweli mimi ni mtu mbaya sana lakini nataka kumuunganisha kule nilikopata msaada mimi, nilipokuwa kwenye hali kama yake.” “Hujawahi kuwa, alipo Zayoni! Usijifananishe naye.” “Naya! Mimi ndio nakwambia.” Naya akamwangalia kwa kumsuta akaona aachane naye tu ila amuulize kinachomuhusu. “Ni wapi huko unakotaka kumuunganisha apate msaada?” “Kanisani. Lipo kundi la vijana ambao huwa nawasadia wasije pita nilikopita mimi. Huwa tunapata muda wa mazungumzo na michezo mbalimbali zaidi mpira wa miguu. Tumetengeneza timu ya kanisa. Kwa sasa nawadhamini mimi mwenyewe. Ni vijana wazuri sana, kwa kuwa karibu nao. Wanapata mafunzo mazuri.” Hapo Naya akatulia.

“Najua mimi sio wakuaminika, ila yupo ambaye ananisaidia Naya. Najijua mimi ni dhaifu sana, na wewe ni shahidi mama. Sikuwa hivi. Yesu ananibadilisha kwa hatua. Yapo mengi mabaya sana Naya. Tafadhali tambua kazi ya msalaba kwangu, angalau katika hilo nipe pongezi.” Naya akajirudi kidogo. “Ni kwa kuwa umeshaniumiza sana Malo. Ila ni kweli umebadilika.” “Sasa! Na mimi najua Naya. Najua kabisa nilikuwa mbaya, na ninajua nahitaji msaada. Wala sikatai.” “Hongera.” “Asante. Kwa hiyo niruhusu nije kumchukua Zayoni. Tena kwa kuwa unawasiwasi na mimi, nitamkabidhisha kwa mtu mwingine ambaye yeye ndio anakuwa na hao vijana muda wote. Kwanza kesho ni ijumaa. Hata akichelewa kurudi haitakuwa na neno.” “Na nyinyi mnaondoka jumamosi saa ngapi?” “Mapema tu.” “Sawa.” Naya akaafiki kwa upande wa baba yake lakini si kwa Zayon. Moyo ulishagoma kumrudisha Malon kwa ndugu zake kama zamani.

“Na kuhusu Zayoni naona hiyo itamsaidia kumchangamsha, lakini naomba usinielewe vibaya Malon. Utatusaidia kututambulisha kwa huyo mtu tu, kisha mimi na Bale tutaendelea. Tafadhali naomba unielewe. Siwezi kumuacha Zayon mikononi mwa mtu mwingine yeyote isipokuwa mimi au Bale, mbali na baba. Nilimwapia mama, na nitalisimamia hilo. Hapo sitatoa hata mwanya wa kukujaribisha Malon.” Malon akapoa, akajua ni kweli Naya amebadilika.

“Sasa lengo si lilikuwa ni kusaidia? Mbona kama umebadilika tena!?” Naya akauliza akishangaa kidogo na kijiukali. “Nimeelewa Naya.” “Hapo sina utani. Tafadhali mchukue kesho, kamtambulishe, sisi tutaendelea tu.” Naya akaweka msisitizo. Wakazunguka, Naya akapata kila kitu cha baba yake, lakini Malon ndiye aliyelipia kila kitu kwa kulazimisha sana mpaka wakatia aibu mbele ya wauzaji kwa kubishana.

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

Wakiwa kwenye gari Malon akaanza tena. “Naya! Nikuulize swali?” “Niulize tu.” “Unaamini kama nakupenda?” “Daah! Hakika kila kitu kimepotea akilini mwangu na mawazoni mwangu juu yako Malo. Kilichobaki kwa hakika ni uthibitisho kuwa, huaminiki. Hilo tu ndilo nimebakiwa nalo.” “Hivi Naya, si unakumbuka kule nilikotoka na historia  ya maisha yangu? Tokea mdogo tu, nilifanya kile bangi kinaniongoza. Nilikimbia malezi ya wazazi, mimi sio kama Bale au wewe! Hakuna mwanadamu ameweza kusimama na mimi katika upumbavu wangu isipokuwa ananufaika na mimi kwa namna moja au nyingine. Nilipokuwa mdogo, walinitoa jela ili niendelee kuwauzia bangi mtaani. Nilipokuwa na pesa, walinitoa wakijua nikiwa mtaani wataendelea kunufaika wao na familia zao. Ndio maana walipojua sitatoka tena, wakanikimbia na mali zangu. Maana kwa uhakika, najua kama wangejua nitatoka jela, hakuna ambaye angethubutu kutoroka na mali zangu.” “Kwamba na mimi unanihesabu kama hao watu unaowazungumzia Malon!?” Naya akauliza kwa ukali akishangaa sana.

“Aisee acha kuniumiza Malon! Katika yote na matendo yote, bado unanihesabu mimi kama watu wengine waliowahi kukupendea pesa!?” “Sio wewe, Naya. Naomba usikasirike.” “Nilitaka kukushangaa maana ni kama unataka kujitetea wakati mimi unanifahamu na hata nilikwambia Malon. Tena ukiwa na wasiwasi wa elimu yako! Unakumbuka nilikwambia usiwe na wasiwasi, kwa kuwa umenisomesha mimi, kutakapokuwa na uhitaji ya elimu mimi nitakuwepo, mengine tuje tufanye pamoja! Nikakupa mawazo mengi sana ya nini tuje kufanya pamoja, ukaja kunigeuka! Leo unasema watu wote wanaokuzunguka wanakupendea pesa!? Ni kwa kuwa hukuwahi kuniona mimi kama Naya, Malon. Japokuwa nilikuwa nikikulilia sana, ulinipuuza, na macho yako yaliendelea kuangalia waliokuwa wakikutumia, ndio maana japokuwa nilizungumza na wewe kwa kurudia rudia, hukuwahi kunisikia mimi, ila wengine wote. Tafadhali naomba tuache tu haya mazungumzo. Sitaki nirudi nyumbani nikiwa nimekasirika.” Malon akanyamaza kimya kabisa.

Malon akaendelea kuendesha. Kimya kwa muda, kisha akaanza tena. “Lile gari nimenunua kwa pesa nyingi mama. Kulikataa mikononi mwangu nikiwa nimekununulia wewe, na siwezi kulirudisha, nabaki nalo pale nyumbani, halina matumizi naona si sawa. Ili kukuthibitishia sitakuja kubadilika na kukupokonya, naomba ulichukue lile gari na nitakupa hata kadi zake. Ujue ni lako kabisa, na wala sitakuja kukuuliza tena.” Naya kimya.

“Ungekuwa na uwezo wa kuniuzia kila kitu nilipokuwa jela. Lakini sasa hivi nina nyumba, sababu yako Naya. Biashara niliyonayo ni mtaji wa pesa uliyokuwa umehangaika kuniwekea dhamana. Tafadhali chukua lile gari. Huna haja hata yakuhesabu kama nimekupa, bali kama moja ya haki yako. Ni jasho lako Naya. Ulifanya kazi za kujifedhehesha kwa ajili ya kukusanya ile pesa. Niliondoka bila kukuachia kitu. Sasa nakupa hii gari si kama nakuhonga. Ni yako Naya. Yako kabisa wala haiitaji mjadala au kuja kuzungumzia baadaye. Ulihangaika, ni pesa yako ambayo imekujia hivyo kwa njia ya gari. Usikubali hasira ikakupotezea haki yako.” Hapo Naya akashawishika ila akatulia tu.

“Eti Naya?” “Malo akitaka jambo lake! Ndio maana unaniuma sana Malo. Kuna vitu ukivitaka huwa unapambana mpaka unapata!” “Najua ni ngumu kusahau mabaya yangu. Turudi kwenye usafiri. Huoni kuwa itakusaidia kuwahi kurudi nyumbani kwa Zayoni, na jumapili kwenda kanisani? Halafu hujahongwa na mtu. Ni kama pesa yako ilikuwa mahali, sasa imerudi. Huoni kama unastahili mama? Acha kuendelea kujitesa kusipokuwa na sababu. Ni jasho lako, na unahitaji. Itakusaidia sana tu.” “Nikweli litasaidia.” Malo akatulia na kuogopa kuongeza neno asije tibua huku akisubiria kujua muendelezo akiwa na tumaini kuwa anaanza kukubali gari.

Alipoona wanaendelea kwenda yupo kimya na wanakaribia kufika Ubungo akimrudisha nyumbani kwao, akaona ajaribu tena. “Kwa hiyo tunaenda kuchukua gari?” Akawa kama amemtoa Naya mawazoni.  Akamwangalia. “Vipi?” “Nipo tu sawa. Kwani umeniongelesha?” Ulipomsikia na sauti imetulia akaongeza. “Nilikuwa nikifikiria tupitie nyumbani ukachukue hilo gari na karatasi zake zote, leo.” Akamuona anavuta pumzi kwa nguvu kama anayejifikiria. “Ukilichukua leo, hutanisikia nikilizungumzia tena.” Malon akaongea kwa tahadhari sana.

“Nilikuwa nikikumbuka vile ulivyoyabadilisha maisha yangu Malon. Ulinionjesha maisha ya usafiri. Nikawa nimeshasahau haso za daladala ambazo sikuwahi kuona ni tatizo mpaka ulipokuja kwenye maisha yangu na ile gari yako na yale maisha ya kunilipia taksii pamoja na kunitumia Side anipeleke nitakako. Nikazoea hayo maisha. Halafu..” Akaamua kunyamaza tu. “Nashukuru kwa usafiri.” Naya akaamua kushukuru akijiambia ni kweli anastahili hilo gari na ni haki yake. “Karibu. Basi twende ukachukue.” Malon hakuongeza neno, akatafuta njia kuelekea nyumbani kwake Kunduchi kimyakimya tu.

Hakuna lililozungumzwa tena mpaka walipofika nyumbani kwa Malon. Mlinzi akafungua geti, Malon akaingia na kumwambia asifunge geti, gari ndogo inatoka. Akavuta gari yake na kuiegesha pembeni ya hiyo gari ndogo. Naya aliona gari ya Rita hapo nje. “Subiri nikakuletee kabrasha lenye hati zake zote.” “Mbona hunikaribishi sasa!?” “Naogopa kuharibu mama. Usije ukaniacha nalo na leo tena. Hapa najiwinda kwa kila neno.” Naya akacheka kidogo. “Karibu mama.” “Nashukuru. Naona wazo lakuniacha hapa ni zuri, ili nisikawie kurudi kwa baba Naya, nikamtia wasiwasi.” Malon akaingia ndani baada ya muda mfupi akatoka na kabrasha.

Naya akatoka garini baada ya kurudi Malon. Akamkabidhi. Naya akacheka kidogo asiamini kama anamiliki usafiri wa uhakika. “Asante.” “Lakini bado lipo kwa jina langu. Nikitoka safari ukitaka naweza kukusaidia kufanya taratibu liwe kwa jina lako.” “Siamini! Asante.” “Nikuombe kitu Naya?” “Nini tena?” “Naomba urudishe nywele kichwani.” Naya akacheka kidogo na kujishika kichwa. “Najua umefiwa, lakini anza kutoa hayo mazingira ya majonzi usoni ili hata Zayoni aone kuna mabadiliko. Tumaini jipya.” “Nitarekebisha. Asante kwa ushauri.”  Wakacheka kidogo, Naya akaondoka.

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

Bale alitoka tu kwenye mitihani yake akarudi nyumbani moja kwa moja. Walikuwa wote nje wakimwangalia na kumsaidia baba yao akijengea senyenge ndani ya michongoma kuzunguka nyumba yote. Wakashangaa Naya anaingia na gari. Wote wakaduwaa wakati anashuka. Akawasogelea, wote walikuwa kimya. “Amenipa Malo lakini ni haki yangu kama jasho langu sio hongo.” Akaanza kwa kujihami akimwangalia baba yake. “Amesema ni katika zile pesa nilizokusanya wakati ule kumtoa jela. Alishindwa kunipa wakati ule ili nianze biashara. Sasa safari hii amenipa gari akisema itanisaidia usafiri wa kwenda kazini, na hapa nyumbani nikibaki na Zayoni. Alitaka kunipa jana alipolinunua, lakini nikamkatalia nikidhani ameanza mambo yake yaleyale. Sikutaka hongo zake. Au vile anavyo...…” “Wakati unajieleza, naomba funguo nizunguke nalo kidogo tu.” Bale akadakia.

“Subiri kwanza Bale bwana, nimwambie baba. Akikataa na kutaka nilirudishe je?” “Mbona usiniulize kabla hujapokea?” Baba yake akamuuliza kwa kumsuta. “Mimi naomba niendeshe kidogo. Hata kama baba akisema ulirudishe, niwe na mimi nimeendesha.” Akampokonya dada yake funguo. “Acha nishushe mizigo ya baba kwanza, bwana Bale!” Akamfuata Bale kwa nyuma kwa haraka.

“Umemnunulia nini?” “Vitu vyake vya huko safarini.” “Sasa na mimi umeninunulia nini?” Bale akauliza. “Miwani ya jua na tsheti zakuvaa chuoni.” “Basi nipe miwani yangu nivae sasa hivi.” “Na giza lote hili! Hapana Bale. Utagonga gari wakati hata sijui kama baba atakubali libaki au atataka lirudi.” “Wewe mlilie tu. Mimi namjua baba. Wewe ukilia tu huwa anakukubalia chochote umuombacho.” “Mwenzenu baba anawasikia.” Zayoni akawashtua. Bale na Naya wakageuka. “Usimfundishe huyo ujinga.” Baba yao akamwambia Bale huku akiendelea kufanya kazi. Bale akacheka, na kuondoka na gari. “Na mimi umeniletea nini Naya?” Zayoni akamfuata dada yake. “Chupi, tisheti, singlendi, soksi na miwani ya jua. Huna shupi Zayoni.” “Kweli. Asante Naya. Unajua mama ndio alikuwa ananibadilishia kila mara?” “Aliniambia. Alisema unapenda sana chupi.” Zayoni akacheka. “Sasa tokea azidiwe, sijabadilisha chupi. Nashukuru sana.” Naya akacheka. 

“Malon anataka aje akuchukue kesho akupeleke kanisani kwao kwenye kundi la vijana. Wanacheza mpira. Ungependa kwenda?” “Sijui Naya.” “Nenda. Itakusaidia kutengeneza marafiki na kukufanya uchangamke. Umekula?” “Nimekula na kusoma. Nimetoka muda sio mrefu kumsaidia baba. Anataka kujenga geti kabla hajaondoka.” Naya akamsogelea baba yake.

“Kwani nimekuudhi?” Baba yake akamwangalia na kuendelea. “Nimekununulia kila kitu cha safari.” “Asante. Hata sikujua kama natakiwa vitu vya safari.” Naya akasogea. “Mbona unatokwa jasho hivyo?” “Kazi ya tokea niliporudi asubuhi kutoka kukusindikiza kituoni. Jana nilichimba mashimo na msingi kuzunguka uzio wote huu, kwa ajili yakujengea msingi. Leo nikatafuta vijana wawili. Wamenisaidia kumwaga zege, ndio namalizia hapa mwisho. Niweke msingi. Pakauke, nisimamishe geti.” “Pesa umepata wapi?” “Zile za gari. Wamenilipa, nimechanganya na akiba yangu.” “Hongera, pamependeza.” “Mimi nataka usalama wenu. Sitaki niondoke, waje waanze kuwaingilia usiku. Nataka kumuomba Malon nimfuate huko Mbeya siku ya jumapili. Angalau jumamosi nisimamishe geti. Hizi nguzo zitakuwa zimekauka.” “Sawa. Na kuhusu gari?” Naya akachomekea.

“Kuhusu nini?” “Malo amenipa gari baba.” “Si ukakubali? Sasa sasa hivi unaniuliza nini?” Naya akaanza kucheka taratibu. “Siku nyingine nitakuuliza.” Baba yake akamwangalia. “Kweli tena.” “Siku zote unauliza kabla hujapokea vitu vya watu. Wala leo hukukosea. Ulifanya kusudi ukijua wazi jibu langu.” “Mimi sijui jibu lako baba.” “Unajua sana na ndio maana jana ulilikataa, na hukuniambia. Ukaenda kubembelezwa huko, ukakumbuka shida ya leo asubuhi karibu uchelewe kazini, ukaenda kulifuata, nakuja nalo hapa. Halafu unanidanganya kwa kuniuliza!” “Lakini litatusaidia baba.” Naya akajisogeza karibu.

“Nimefikiria nikajiona nakuwa mpumbavu bila sababu! Ni haki yangu baba yangu. Umeona jinsi nilivyokuwa nikihangaika kukusanya ile pesa. Malon mwenyewe ukimsikiliza yupo vilevile si wakubadilika leo yule wala kesho. Sasa nikajiambia ni kama napigana na upepo. Nikijifanya kuzira, nikujitesa mimi mwenyewe. Nikaona ni heri nijifute jasho mwenyewe. Sina sababu yakujitesa. Nimehangaika sana na yule kiumbe. Hata kama vingine vimeshindikana, acha nipate kiinua mgongo. Hata hivyo nani atakuja kunipa gari?” Baba yake akamtizama tu.

“Hii gari ni yangu kabisa baba. Amenihakikishia wala hatakuja kuniuliza juu ya hili gari na tumefunga mjadala. Mpaka kadi zake zote za gari amenipa. Kwa hiyo acha litusaidie baba yangu. Tuliteseka naye sana.” Naya akaendelea kumshawishi baba yake akamuona amenyamaza tu akiendelea na kazi. Akatulia kidogo akiwa na wasiwasi wakuambiwa alirudishe. Hata yeye alijua baba yake anamuhofia sana Malon kwa tabia yake ya kutotabirika. “Nenda kale.” “Nataka kukusaidia.” “Kale kwanza, ndio uje uniambie vizuri juu ya habari za gari.” Naya akacheka kwa furaha. Akaondoka na Zayoni akijua ndio amemkubalia abakiwe nalo. “Umeoga?” Akamsikia akimuuliza mdogo wake. “Bado.” “Usilale bila kuoga Zayoni.” “Mbona sasa hunipi zawadi zangu?” “Nimeweka kwenye hilo begi la baba. Twende ndani nitakupa.” 

Malon na Zayoni.

S

iku hiyo ya ijumaa Malon alifika nyumbani kwa kina Naya, akamkuta baba yake na mafundi. Busy anatokwa jasho. “Natengeneza ulinzi wa mama mzazi. Wasije kuniibia wakati sipo.” Malon akacheka. “Hongera. Naona umezungushia pote.” “Bado geti. Sio zuri sana, lakini angalau nitaondoka nikiwa na amani yupo ndani sio hivi yupo nje! Tena nilitaka kukuomba nikufuate. Ili kesho nijengee. Nikiliona limesimama hapa, ndio hata nikiondoka kichwa kitafanya kazi huko. Hivi hivi, siwezi baba.” Malon akabaki kama anayefikiria.

“Na kwa kuwa sasa hivi anausafiri ndio imesaidia kabisa. Nimemwambia Bale awe anakuja kulala nao hapa. Asiwaache peke yao. Dada yake akienda kazini asubuhi, amshushe chuoni, jioni arudi naye.” “Wazo zuri. Au tutafute mlinzi?” “Unafikiri sijafikiria hilo? Nimezunguka tokea tumezungumza, wanataka pesa nyingi. Na kwa sababu wananifahamu uwezo wangu, wanaona hakuna chakulinda hapa, kiasi chakuja kuwalipa baadaye. Nikaona heri nijenge tu. Wasije kuniibia binti yangu bure.” Baba yake Naya alikuwa akiongea huku akiendelea na kazi.

“Kuna watu nafahamiana nao, nilishawafanyia kazi kipindi fulani.” “Kazi ya ulinzi?” “Ndiyo. Nafikiri wanaweza kuwa na watu wanawafahamu maeneo ya huku. Tukienda wote, wanaweza wasikusumbue.” “Hilo nitashukuru. Japo kwa muda tu baba. Nitalipia huo ulinzi mimi mwenyewe. Niondoke nikijua yupo mtu ananilindia mama yangu.” “Sawa. Lakini leo nilitaka tutoke na Zayoni. Mazungumzo tu na kumtambulisha kwenye kikundi cha vijana pale kanisani. Wengine wanalingana au anaweza kupata watu wa umri wake. Pale kanisani kwetu wamewekeza sana kwa vijana.” “Ameniambia Naya. Na kaka yake ameona ni wazo zuri, atakuwa naye huko baada ya wewe kumtambulisha.” Malon akajua ndio kwa hakika haaminiki tena pale. Akawa mpole tu.

“Alisita mwanzoni ila naona baadaye akakubali. Muda si mrefu atarudi hapa. Kifo cha mama yake kimemuharibu sana akili. Aliugua sana. Hakuwa akiweza hata kutoka kitandani kwa muda mrefu sana!” “Poleni sana.” “Ila mimi nilishamuonya mama yake hata kabla hajaanza kuugua. Alimlea vibaya sana Zayoni. Itamchukua muda kuwa sawa. Hana marafiki. Hajui kucheza mchezo wa aina yeyote ule. Hata mpira wa miguu hawezi. Kutwa alikuwa mgongoni kwa mama yake. Anamenya vitunguu au nyanya akitaka awepo alipo mama yake!” Malon akacheka.

“Enzi za uhai wa mama yake alipokuwa shuleni, ilikuwa hivyohivyo. Wakati wote kama hayupo darasani basi ujue yupo ofisini kwa walimu pembeni ya mama yake. Hana anayemjua wala kumfahamu isipokuwa mama yake tu. Sasa hivi inamuia ngumu hajui maisha yanakuaje hapa duniani bila mama yake. Sio tu kama mama, ndiye aliyekuwa rafiki yake na msiri wake haswa. Kwenda na kurudi naye kutoka shule. Wao wawili kila mahali. Kwa hiyo ukimsogeza huko, itamsaidia.” “Nimefurahi kama nimepata baraka zenu. Na ninaamini itasaidia tu.” Malon akasaidia kazi mpaka Zayoni akarudi kutoka shule.

Akasalimia. “Nenda ukaoge, ubadili hizo nguo, ule, ndio uondoke.” Baba yake alimpa maagizo. “Kuna sehemu nataka nikupeleke ukale ndio twende kanisani. Muda bado.”  Malon akaingilia. Zayoni akatulia kidogo kama anayesita. Baba yake akasimama. “Nini?” “Naya atakuja?” “Utamkuta Naya hapa nyumbani. Bale alishakwambia ukajichanganye Zayoni. Utakuwa sawa.” Akabaki amesimama huku ameinama. “Vipi?” “Sitaki kwenda baba.” Akaanza kulia. Baba yake alitegemea hilo. Akabaki akimwangalia. “Nisikilize Zayoni. Sio lazima kabisa, lakini ninauhakika utafurahia. Naomba ujaribu tu. Tukifika, halafu usipopenda, nitakurudisha nyumbani. Sawa?”

 “Sitaki waanze kunicheka sijui kucheza!” “Usiwe na wasiwasi. Wale vijana wamefundishwa kucheza palepale kanisani. Wengi walikuwa hawajui kitu. Hata mimi nimewasaidia, na wewe tutakusaidia. Na sio lazima ukifika leo leo ucheze! Hapana. Unaweza tu kuwa muangaliaji mpaka ukazoea. Leo utakuwa na mimi, ijumaa ijayo utakuwa na Naya. Usiogope.” “Hutaniacha hapo peke yangu na wao tu?” “Hata kidogo. Nitakuwepo na wewe mpaka nikurudishe hapa nyumbani.” “Umesema hutaniacha nao peke yetu na si lazima nicheze?” “Ndiyo.” Malon akamkubalia. Ndio akakubali kwenda kuoga.

Alitoka amevaa vitu alivyonunuliwa na Naya siku iliyopita, akawa msafi. “Unataka tupitie kunyoa nywele kwanza?” Malon akamuuliza wakiwa wanaondoka. “Mama alikuwa akinipeleka kunyoa, au anamlipa yule kijana aninyoe palepale nyumbani.” “Basi naweza kukupitisha mahali ukanyolewa ndio tukaenda kula. Au njaa inauma sana?” “Hapana. Nikanyoe kwanza ili niwe msafi.” Akanyamza. 

“Vipi shuleni?” Malon akajaribu kumuuliza. “Naendelea kwenda. Lakini sasa hivi naenda peke yangu. Unajua nilikuwa nasoma shule anayofundisha mama?” “Ndiyo.” “Tokea naanza darasa la kwanza mpaka alipoanza kuumwa tulikuwa tunaenda naye shule. Mara nyingine alikuwa mgonjwa, lakini alikuwa anakwenda ili tuwe naye.” “Sasa sasa hivi unafanyaje?” “Ni ngumu! Lakini Naya ameniambia kila nikimkumbuka niwe nafanya kitu chakumuenzi.” “Kwa hiyo sasa hivi unafanya nini?” Malon aliendelea kumdadisi taratibu. 

“Najitahidi nikifika shule niwe na kitu chakufanya wakati wote ili muda uende haraka nitoke pale. Natamani nimalize haraka niondoke pale. Pananikumbusha sana mama.” “Pole sana Zayoni. Umejaribu kutengeneza marafiki?”  Akanyamaza kwa muda akamuona anakunja uso na kujibu. “Mimi sijui michezo Malo. Watataka twende tukacheze, wakati mimi sijui kucheza, halafu sipendi kuchelewa kurudi nyumbani. Bale hakuwa akichelewa kurudi nyumbani. Sitaki mimi niwe watofauti.” “Unafanya vizuri. Na upo sahihi.” Wakaendelea kuendesha.

“Sasa umefikiria nini chakufanya ukimaliza shule?” “Naya ameniahidi kuninunulia tena kamera. Unakumbuka ulininunulia kamera?” “Nakumbuka.” Malo akajibu. “Iliharibika. Lakini Naya ameniambia ataninunulia nyingine, halafu atanitafutia sehemu niwe napiga picha hata za maharusi.” “Yaani kuwe kama studio?” Zayoni akacheka. “Ndivyo alivyosema Naya.” “Naya anaakili sana.” “Hata mimi nilimwambia hivyo hivyo. Lakini unajua nimeshangaa?” “Kwa nini?” “Unavyoniamini! Eti anitafutie studio mimi! Halafu anasema kama wakiniita hata kwenye maharusi au shuguli za watu, atakuwa ananisindikiza.” “Safi sana. Ni kwa kuwa ameona kazi zako. Hata mimi niliona picha ulizokuwa ukipiga wakati ule. Unakumbuka wakati ule anafanya mambo ya mavazi, ukapiga picha na kuziweka kwenye website?” Akacheka. “Zile picha zilikuwa nzuri sana. Hicho nikipaji. Naungana mkono na wazo la Naya.” “Kweli!?” “Kabisa. Na ninauhakika watu watafurahia kazi yako.” Akamuona anaanza kutulia. Akamuacha.

“Unampenda Naya?” Malon akashtuka kidogo, na kumwangalia. “Nampenda sana.” Akanyamaza kwa muda. Malon akamwangalia, akamuona ametulia. “Nikuulize kitu kingine Malon?” “Niulize tu?” “Umemchukia mama yetu kwa kukufukuza?” “Wewe unajua kwa nini alinifukuza?” “Ili aolewe na Joshi?” “Hapana. Mama alitaka Naya aolewe na mwanaume mzuri ambaye ataweza kumtunza vizuri Naya kitu kinachonifanya nimpende zaidi mama na kumuheshimu.” “Kwa nini?” “Kwa sababu ni mama mzuri. Hakuna mama anayependa mtoto wake aje kupata shida. Kwa wakati ule, mimi sikuwa mtu sahihi kwa Naya. Nilikuwa nimefanya makosa mengi sana ambayo kwa maneno pekee, ilikuwa ngumu kuaminika. Ndio maana mama alikuwa na wasiwasi na mimi. Alitaka mwanaume mzuri aliyetulia kwa Naya.” Zayoni akatulia.

“Kwa hiyo sijawahi kumchukia mama. Ila nitamuiga. Na mimi niwe nalinda watoto wangu.” “Lakini Bale alisema Joshi hakuwahi kumpenda Naya.” “Kwa nini?” “Sijui sana kama Bale. Lakini ninachohisi hakuwa akimjali kama wewe. Siku moja Joshi alikuja kumchukua Naya nyumbani, akamuacha mjini. Baba na Bale walichukia sana. Joshi hakuwa kama hivyo wewe unampa gari Naya. Joshi alikuwa mchoyo sana na hamjali hata kidogo Naya.” Akatulia tena kidogo akamwangalia.

“Vipi?” “Hivi unajua kama Naya huwa anakulilia sana?” Malon akapoa. Hakuwahi kukaa na huyo mtoto, hakujua kama nimzungumzaji na anaangalia mambo kwa makini hivyo. “Unakumbuka siku ile ulikuja kwenye mahafali yake kule Mzumbe?” “Nakumbuka.” “Basi siku ile alilia sana. Njia nzima alikuwa anakulilia wewe, tulishindwa hata kula. Tulifika mpaka hotelini, akawa analia tu. Ndio baba akasema tumrudishe nyumbani. Nikamuuliza kesho yake kwa nini alikuwa analia sana wakati ulimletea zawadi nzuri, akasema anahamu na wewe. Nikamwambia baba twende mjini tukakutafute, baba akasema tuache tu, ila tumuombee. Kwani ulikwenda wapi?” Akauliza kwa upole.

“Nilikuwa nahangaika kutafuta kazi.” “Naya anaakili sana. Ungetafuta kazi ukiwa naye ili akushauri. Usingemuacha. Au uliogopa atakusema huna pesa?” “Hapana Zayoni, Naya ni mvumilivu sana kwangu. Hajawahi kunichukia nikiwa sina kitu. Lakini sikutaka kumtesa kuwa naye bila pesa.” Akafikiria kidogo, akauliza tena. “Kwani hivi wanawake wao hawawezi kuwalisha wanaume na kuwatunza nyumbani?” Malon akajua anauliza pia akikumbuka malalamiko ya mama yao kwa baba yao. “Wanaweza Zayoni. Lakini Mungu alimuumba mwanaume kuwa mtafutaji. Kuna ile hali yakutamani baba ndio atunze familia.” Hapo akanyamaza kabisa.

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

Naya naye alitoka kazini, na kwenda saluni. Akashonewa wiving ya kawaida tu lakini wakaikata chini kabisa ila kwa ustadi mzuri. Upande wa juu, katikati ilikuwa na mawimbi ya rangi ya dhahabu inayowaka kiasi. Halafu kuzunguka kichwa hiyo nywele ikawa nyeusi iliyochongwa vizuri sana, ikawa imelala kwa ustadi. Akapendeza haswa. Angalau Naya wa zamani akaanza kuonekana tena. Akampigia simu Malon kabla hajatoka hapo saluni. “Vipi Kiziwanda?” “Naona amechangamka. Yupo anacheza mpira. Lakini sio kwenye timu. Pembeni tu na kijana mmoja, yeye ni mtaalamu sana. Ila mtaratibu. Nimeona ataendana naye. Nimemuomba amchukulie taratibu sana na amsikilize zaidi. Hapa macho yako kwake. Naona anacheka mara kwa mara.” Naya akacheka. “Afadhali akirudi awe amechoka, alale. Alikula?” “Aliniambia anahamu na kitimoto. Nimempeleka, amekula vizuri tu.” “Sasa unataka nimfuate sasa hivi?” “Acha nimuulize au zungumza naye wewe mwenyewe umsikie.” Malon akampelekea simu Zayoni.

Akazungumza na Naya. Akamsikia akimwambia, “Nitarudi na Malon.” Wakajua anapata wakati mzuri. Akarudisha simu kwa Malon, akaendelea kucheza. “Naona anafurahia. Muache tu kwa leo nitamrudisha.” “Sawa. Basi tutakutana nyumbani.” “Ulitaka nije na nini?” Naya akafikiria. “Sidhani kama kuna kitu kinahitajika. Tupo tu sawa.” “Naona itabidi nimsubiri baba. Kuna mambo anataka kukamilisha kabla hajaondoka.” “Hapana Malo. Asikukwamishe. Nenda tu, atakuja na basi.” “Tofauti ya siku moja, sidhani kama nitaokoa kitu. Acha nimsubiri tu.” “Sawa.” Wakazungumza kidogo, wakaagana. 

Malon na Baba yake Naya. 

J

umapili saa 11 asubuhi, Malon alikuwa akiegesha gari nyumbani kwa kina Naya kwenda kumpitia baba yake Naya. Wakapata muda wakuomba, Naya akatoka nje na Malon. “Naomba umwangalie. Tafadhali Malo.” “Usiwe na wasiwasi Naya! Atakuwa sawa.” “Nitakuwa nawaombea. Mungu awafanikishe.” “Amina mama.” “Nakushukuru Malo. Asante/ kwa kila kitu. Baadaye tutaenda kanisani kwenu. Zayoni anataka kurudi kule.” Malon akalifurahia hilo. “Mtakuwa na Bale?” “Lazima. Tutakuwa wote. Nimefurahi tutakuwa na usafiri.” Malon akacheka.

“Nitakuona tukirudi Naya. Naomba asije akatokea tena Joshi mwingine mimi nikiwa huko.” Naya akacheka kama anayefikiria. “Tuzidi kuombeana.” Malo akashangaa kidogo. “Acha majibu ya jumla Naya bwana! Na hivyo ulivyopendeza! Mpaka nimejuta. Heri ningekushauri ujitengeneze nikiwa nimerudi.” Naya akacheka tu lakini Malo akagundua kuna utofauti.

“Vipi mama? Au kuna Joshi mwingine tayari?” “Tuzidi kuombeana Malon. Tunakuwa tunaweka mipango mingi ambayo haijawahi kutimia tokea tunafahamiana, ndio maana nasema tuombeane tu. Naomba safari hii kusiwe na ahadi tena. Wakati wewe maisha yako yakiendelea, mimi huwa hizo ahadi zinanifunga na kuniumiza vibaya sana. Ndio maana safari hii nimeshauri kwa mara ya kwanza, hebu tumuachie Mungu aingilie kati na kutuongoza.” Hilo likampoozesha Malon kabisa. Alijua ni kawaida ya hasira za Naya, kuzungumza mengi, angepoa tu. Lakini safari hii akaonekana kuna tofauti.

Naya akacheka kidogo akimtizama. “Safari njema.” “Subiri kwanza Naya! Naomba usiondoke.” Naya akageuka wakati anataka kurudi ndani. “Nataka kumsaidia baba kumalizia kufunga mizigo yake.” “Nataka kujua tumekubaliana nini mpaka sasa?” “Sijui Malo.” “Hilo sio jibu Naya. Na nimeomba usiwe unaniambia sijui. Natamani kujua nafasi yangu kwa sasa.”  “Kwa hakika sijui Malo. Sijui tena. Ndio maana nakwambia tumuachie Mungu.” “Nimekuelewa tunamuachia Mungu. Lakini angalau nijue ni unanipa muda wa kunichunguza mpaka uridhike. Ila usikubali watu wengine. Tubaki hivi hivi.” Naya akarudi pale alipokuwa amesimama Malon.

“Hivi hicho unachozungumza sasa hivi, sicho nilichokuwa nikikifanya tokea tupo kwenye mahusiano, Malo?!” Naya akauliza taratibu tu. “Ulishawahi hata kuhisi nimekuwa nikiwa na mahusiano mengine nikiwa na wewe?” Kimya. “Nafikiri katika hilo ulitakiwa kunisifu Malo! Wakati wote mimi nimekuwa mtu ninayejua nini nataka. Labda hayo ujiambie wewe mwenyewe. Ila ukiniambia mimi sidhani kama utakuwa unanitendea haki. Na kwa kuwa sitaki kukudanganya, ndio maana nimekwambia tumuachie Mungu. Ninayo sababu yakusema hivyo ndio maana.” “Ipi?” Malon akauliza. “Kubwa na ya kwanza nilishakwambia. Na...” Baba yake Naya akatoka nakumkatisha Naya.

“Nilikuwa nakuja kumalizia sanduku, baba.” “Naona kila kitu kilikuwa ndani. Nimeshafunga mama. Asante.” Baba yake alishawapita na kuelekea nyuma ya gari akiwa na mizigo yake. “Unipigie simu kila wakati nijue mmefikia wapi?” Naya akaendelea kuzungumza na baba yake, Malon kimya. “Nitafanya hivyo. Na upunguze woga.” Baba yake akajibu kule nyuma ya gari. “Wewe nipigie tu baba. Usiache. Ndio nitatulia lasivyo..” “Sawa mama. Nitapiga kila baada ya lisaa kama ulivyosema.” Naya akacheka na kutaka kumfuata baba yake, ila Malon akamuwahi na kumdaka mkono na kumshikisha hela mkononi. Naya akashangaa kidogo. “Tutawasiliana.” Akaongea kwa sauti ya kusihi. Naya akazitizama zile pesa, na kuzirudisha kwenye mfuko wake wa shati kwa haraka sana bila hata Malon kutarajia.

Malon akamwangalia kwa mshangao. “Sasa hivi nina kazi ninayo pesa ya kujikimu.” “Nafahamu Naya!” “Basi jua nipo sawa tu. Asante.” Naya akaondoka pale na kuzunguka nyuma ya gari ambako baba yake alipokuwepo akipandisha mizigo. 

“Uwe na safari njema baba.” “Asante mama. Ngoja nifunge hapa uniombee.” “Uvae sweta lile la rangi nyeusi usiku, halafu lile la kijani kidogo na majivu, iwe mida ya mchana. Malo amesema kuna baridi.” “Sawa.” “Tisheti za mikono mirefu nimeweka juu, mikono mifupi chini. Na singilendi zipo. Usivae tisheti bila singilendi, itasaidia kulinda kifua na baridi. Kuwe na kitu kinachoshika kabisa mwili kabla ya nguo za juu.” “Sawa.” Baba yake akafunga mlango wa nyuma kabisa.

“Sababu ya baridi usisahau mafuta ya mdomo ili isipasuke ukaotwa vidonda. Moja nimekuwekea kwenye mfuko wa suruali, nyingine kwenye begi lako. Mablangeti nime..” “Naya mama, nitakuwa salama. Na kwa kuwa nitakuwa nikikupigia simu, naona uwe unanipa hayo maelezo. Lasivyo hatutaondoka leo.” “Naona kama hutilii maanani baba!” Naya akalalamika.

“Tokea jana unanipa maelekezo, huamini kama nimeelewa?” “Sijui bwana! Wewe uwe muangalifu huko. Halafu maelezo mengine nitakuwa nakupa kila siku au kutokana na wakati. Kama ni asubuhi, unanipigia kabla hamjaanza kazi ili kukwamba nini chakuvaa.” “Sawa.” “Kula na kunywa maji yakutosha ni muhimu. Kulala…” “Mimi nina wazo mama. Ili bosi wangu asijute kunichukua, labda nipande ndani ya gari, unipigie simu, halafu tuendelee kupeana maelekezo. Hii kazi isije ikaisha kabla hata sijaanza. ” Naya akacheka. 

“Hata hivyo nimemaliza. Ni msisitizo tu juu ya kupata usingizi wakutosha na..” “Naya, baba atakuwa sawa. Acha kuwa na wasiwasi.” Ikabidi Malon aingilie. “Najua. Ila nilitaka kumsisitizia tu.” “Atakuwa sawa.” Naya akacheka. “Unipigie.” “Sawa mama. Nitapiga, nikisikia kuumwa tu, nirudi nyumbani kwa haraka. Hata kama ni mafua tu, nisipuuze, nirudi. Baridi ikinizidia, pia nirudi nyumbani kwa haraka. Mazingira nisipoyapenda, nirudi nyumbani kwa haraka. Si ndio hivyo au kuna nililosahau?” Naya akazidi kucheka.

“Kumbe jana usiku ulikuwa ukinisikiliza?” Malon akacheka. “Sana tu. Na ninakumbuka. Kwa hiyo usiwe na wasiwasi. Naomba turuhusu sisi twende.”  Naya akacheka na kurudi upande aliokuwepo Malon. “Na mimi nina maagizo yangu?” Naya akacheka sana. “Muwe na safari njema. Nawaombea. Naomba muangalie sana..” “Baba?” Malon akamalizia kwa kumuuliza swali. Naya akacheka nakuondoka. Wote wakacheka.

Baba yake akaingia na kufunga mlango wa gari. “Usisahau mkanda baba.” Naya akapiga kelele akiwa nje. “Ndio nafunga mama.” Naya akawapungia mkono kuwaaga, lakini akakumbuka hajamuombea baba yake. Akamfanyia ishara Malon asubiri. “Hapa hatutaondoka leo.” Baba yake akanong’ona. Malon akacheka. Akakimbilia alipokuwa amekaa baba yake. Akafungua mlango kabisa. Zayon naye akawa ameamka. “Mbona kelele Naya?” “Nimesahau kumuombea baba. Njoo na wewe tuombe pamoja.” “Kweli mama.” Naya akamshika mkono baba yake na Zayon pia. Wakawa wameshikana mikono wao watatu Malon akiwatizama kwa kujiiba. Naya akaomba vizuri tu, akamaliza. “Amen.” “Amina mama.” Malon na baba yake Naya wakaitikia kwa pamoja hiyo ‘Amina mama’. Wakaangaliana kidogo, wakarudisha macho kwa Naya akacheka. “Sasa hivi mnaweza kwenda. Kuweni waangalifu barabarani.” “Nitafanya hivyo.” “Nitakupigia baba ili kukuaga vizuri. Nilipitiwa na usingizi.” “Hilo wazo zuri Zayon. Unipigie na baadaye muende kanisani.” “Sawa.” Naya akafunga mlango wa gari, akasogea pembeni. Malon na baba yake wakaondoka Naya akipunga mkono, Zayon ametulia tu pembeni. 

 Kwa Kina Naya.

M

aisha ya bila wazazi pale nyumbani kwao ndio yakaanza rasmi mara tu waliporudi ndani. Tena bila Bale ambaye alikuwa chuoni. Naya akasikia kuumia sana. Nyumba hiyo iliyokuwa imejaa vurugu ikabaki papweke. Wote walijikuta wamerudi kukaa hapo kwenye makochi kimya. Yeye na Zayon kila mmoja akiwaza lake. Naya akaanza kujutia kumshauri baba yake aondoke. Akachukia kukubali ushauri wa Malon, kumchukua baba yao, lakini akajirudi akikumbuka shida ya pesa na ile hali ya kuomboleza aliyokuwa nayo baba yao. “Maisha yamebadilika Naya!” Akaongea kwa kulalamika Zayon. “Ni kweli. Mambo hayatakuwa kama zamani Zayoni. Kuna ukawaida mpya Mungu atatupa, itabidi kuja kuuzoea tu.” “Baba naye atakuwa akiishi huko huko?” “Kwa muda tu. Ili kumfanya achangamke. Ila najua hata yeye hataweza kuwa mbali na sisi. Atarudi na kutafuta kitu chakufanya hapa mjini.” Zayoni akanyamaza, Naya naye akapotelea mawazoni.

Siku hiyo ya jumapili wote walienda kanisani kwa kina Malon, kwa ajili ya Zayoni akutane na vijana wenzake. Hata Bale alifika pale akitokea chuoni. Akawaona wameshuka garini wamepoa. Akaelewa tu kwa kuwa alitoka kuzungumza na baba yake akamwambia amewaacha nyumbani peke yao, na yeye arudi nyumbani. Bale akamuahidi baba yake siku hiyo atakuwa nao na akimaliza mitihani atarudi nyumbani. “Dogo umependeza! Naona unakula pamba za ukweli!”  Bale akamsifia mdogo wake, angalau Zayon akacheka. “Hizi ni nguo mpya na viatu, ameninunulia Naya.” “Saafi!” Wakasalimiana na Naya na kuingia kanisani vijana hao wasio na vingi ila wao tu.

Baada ya ibada, Zayoni akaonekana alipata wakati mzuri. Bale na Naya ikabidi wafikirie swala la kuhamia hapo kwenye hilo kanisa kwa ajili ya Zayoni. Alisimulia mengi wakiwa kwenye gari akimtaka Naya awe anampeleka zaidi hapo. “Wanakuwa na mechi siku za ijumaa na jumamosi.” “Basi kazi zitanishinda.” Naya akajibu, Zayoni akacheka. “Siku za jumamosi mimi nitakuwa nakuleta, ila ijumaa itategemea.” “Asante Bale.” Walienda mahali kula. Naya akiwa mlipaji. Walianza kucheka wakitaniana hili na lile. Angalau ile hali ya majonzi ikapungua siku hiyo. 

Safarini.

S

afari ya Dar kwenda Mbeya ilikuwa ndefu vyakutosha. “Nataka kumuoa Naya.” Malon akavunja ukimya, baba Naya akamtizama na kumuuliza swali. “Unafikiri upo tayari?” Malon akatulia kidogo akijua hilo swali lina agenda nyingi sana nyuma yake. “Sijui natakiwa kufanya nini kabla ya kumuoa? Labda unisaidie. Lakini sitaki kuendelea kusubiri. Hatuna sababu, wakati najua tunapendana. Nahisi mengine Mungu atatusaidia mbele ya safari.” Malo akaendelea. “Najua haikuwa sawa, lakini niliishi na Naya zaidi ya miaka mitatu, kama mke wangu, vizuri sana. Sidhani kama nitapata mwanamke mwingine atakayeweza kuishi na mimi kama Naya?” “Unamaanisha kukuvumilia?” Baba Naya akauliza. Malon akatulia kidogo akijua kwa kuwa Naya anazungumza mengi na baba yake, na yale mabadiliko aliyoyaona kwa Naya, akaona awe mtulivu kidogo. Afikiri kabla ya kujibu.

“Umekuwa mtu wakuingia na kutoka kwenye maisha ya Naya vile utakavyo wewe. Unamuacha akiwa mtu wa kulia na sononeko kila wakati! Ni nini kimebadilika?” “Nimeokoka. Mungu atanisaidia.” Malo akajitetea. “Ni juzi tu umetoka safari na mwanamke ambaye sio mkeo, Malon! Mmekaa huko karibu juma zima! Leo unasema unataka kumuoa Naya!? Ni nini unataka maishani Malo? Huoni kama utamsumbua sana Naya?” “Kwanza wakati namkubalia Rita kwenda naye, nilijua Naya alishachumbiwa. Juu ya hiyo safari ni mipango au ni ombi alilokuwa ameniomba kwa muda mrefu baada ya kufahamiana tu. Aliniomba siku nikija kwenda Brazil, na yeye angetamani twende naye apafahamu. Wakati huo alikuwa mgeni tu pale kwangu. Hata hatukuwa tukifahamiana sana. Sikuona sababu ya kumkatalia.” Malon akaendelea.

“Na nilipofika kule, Mungu wangu ni shahidi, sijamgusa. Na si kwa sababu ya Naya, ni kwa usalama wangu mimi mwenyewe. Najua madhara ya maisha niliyoishi zamani. Huko nimekusudia kutorudi, kwa gharama ya kujikana mwenyewe. Na Rita akimaliza mkataba wake, itakuwa basi. Nitaikarabati nyumba yangu, nihamie mwenyewe nikimsubiria Naya.” Baba Naya akamtizama vile alivyo jihakikishia. “Sitarudia maisha ya zamani. Na sitaki tuendelee kusubiri niwe mkamilifu sana. Naona tunazidi kujichelewesha.” Baba Naya hakuongeza neno.

“Sasa hivi nipo na wala sitamuacha tena. Na ni kweli nilirudi kwa ajili yake. Nilikuwa nimekufuata siku ile nikwambie. Ndio nikaishia mikononi kwa mama.” “Alikuja kujuta. Akitaka kukiri, lakini nilimkatalia nikiwa sijamuelewa ni nini anataka kufanya. Lakini alijua amefanya kosa.” “Nia ilikuwa nzuri. Naelewa kabisa. Lakini nampenda Naya. Nina uhakika mimi naweza kuwa naye na kumfanya akawa na furaha. Na yeye najua bado ananipenda.”  Alivyomalizia hivyo, baba yake Naya akamtizama. Vile alivyomtizama Malo hakufurahia hata kidogo. Ni kama aliyemuuliza ‘una uhakika?’ Malon akaingiwa na wasiwasi.

Akaona amchokonoe zaidi ili aongee neno. “Nampenda Naya. Safari hii ukiniruhusu mzee wangu, na kunipa baraka zako, nikirudi tu nataka kumchumbia, taratibu za harusi zianze. Hapa ni wewe tu. Mimi na Naya tupo tayari.” “Umezungumza na Naya mwenyewe?”  “Namjua Naya. Yupo tayari. Naomba tu na wewe unisaidie kumtia moyo, tukamilishe hili.” Baba Naya akanyamaza kabisa. Hakuongeza neno jingine hata Malon alipoendelea. Akaona anyamaze asije akaharibu. Safari ikaendelea.

                                                    Mbeya.

Zilipita siku 10 ngumu na za haso haswa kwa Malon na baba Naya, wakiwa mkoani Mbeya ila vijijini kwa wakulima kabisa, mashambani wakikusanya mazao mpaka Malani akakamilisha kiasi alichokusudia na ndipo walipohamisha hayo mazao sasa kwenye eneo lililomshangaza sana baba Naya. Kwa hakika Malon alijijenga huko vijijini. Aliweka eneo maalumu kukusanyia mazao na kuweka vitu vya kisasa. Kazi ya kusafisha mazao na kuyaandaa kwa kusafirishwa ikaanza hapo kwenye ngome ya Malon. Walikuwa wakifanya kazi mchana na usiku wakisaidiana bila kuchoka. Malon alikuwa akichoka, lakini akashangaa nguvu aliyonayo yule baba Naya.

Alikuwa akifanya kazi mchana na usiku bila kuchoka au kutumwa. Tokea alivyojua ni nini anatakiwa afanye, hakuwa akisubiri atumwe. Alfajiri alimkuta ameshatoka ameanza kazi akiweka mazao vizuri ndani ya magunia, na kuyapanga. Alikuwa wa kwanza kuamka, na wa mwisho kulala. Wakati wote Naya alikuwa kwenye simu na baba yake lakini Malon akagundua kwake ni kama analazimishia mawasiliano. Naya anayemfahamu yeye, asingekuwa akisubiri Malon ampigie endapo anajua alipo na wapo kwenye mahusiano fulani. Lakini ikawa ni shida.

Wakati mwingine akajaribu kumtega asimtafute asubuhi. Basi hatamsikia Naya hata kutuma ujumbe, ila kumuona baba yake akisoma jumbe na kujibu au kupokea simu mara kwa mara akawa anajua ni Naya tu. Lakini akashangaa napo hakuna hata salamu anazopewa na baba yake kutoka kwa Naya. Malon akajua mambo yamebadilika. Akahisi pengine amepata mwanaume mwingine. “Lakini mbona hapakuwa na dalili ya mwanaume mwingine! Namfahamu Naya. Kama kungekuwa na mwanaume mwingine, angesema tu.” Akabaki akiwaza Malon na kujaribu kuvuta kumbukumbu tokea amuone Naya shuleni kwa mtoto wa Rita mpaka wanaagana. Akajiuliza hayo mabadiliko ni ya nini!? Siku zikazidi kwenda, mambo ni yaleyale.

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

CONVERSATION

0 Comments:

Post a Comment