Naomi Simulizi |+1 205 767 8163 |naomisimulizi@gmail.com MAPENZI & PESA – SEHEMU YA 16. - Naomi Simulizi

MAPENZI & PESA – SEHEMU YA 16.

 

Kweli walisimama sehemu ambayo Jamal alionekana ndiko alipotaka awepo kwa wakati huo. Wote wakaonekana ni sehemu wanayoifahamu. “Hapa mzee Sajo umenimaliza. Mimi nipate choma, mama watoto vitunguu.” Wakacheka wakishuka garini. “Twende tukapate kifungua kinywa kabla ya....” “Ugali wa Kitonga.” Akamalizia Jamal. “Hapo mzee Sajo utakuwa umenikamilishia safari, swafi.” Wakatoka wakicheka. Naya naye akafuata nyuma. Joshua akasimama alipomuona anatembea nyuma yao. “Vipi?” “Nataka kwenda..” Joshua akacheka aliposita, ila akawa amemuelewa. Akamuonyeshea kwa kidole vilipo vyoo. “Usikimbie sasa. Uje ndani tule.” “Nitarudi.” “Ungependa kula nini nikuagizie na wewe?” “Mimi sio mchaguzi. Chochote tu.” “Unauhakika?” “Kabisa. Ila chai iwe ya maziwa tafadhali.” “Hapo umerahisisha.” Naya akaelekea msalani, Joshua akaelekea ndani ya huo mgahawa mkubwa hata  mabasi yalikuwa yakisimama hapo.

Naya alibabaika alipoingia pale baada ya kutumia choo, na kukuta wamekaa tayari wanaendelea kula. Hakujua akae au achukue chakula chake akale meza ya pembeni! “Kaa tule.” Joshua alipomuona amesogea pale akasimama kwa haraka na kumvutia kiti, akakaa na kusogeza karibu ya meza. “Hiyo nyama choma ndiyo inayomchanganya Jamal, ndio maana tupo hapa, na wewe nimekuagizia. Jaribu kama utapenda. Usipopenda tutaagiza kitu kingine.” “Nashukuru. Asante.” Wakaendelea kula, bila mazungumzo mengi, kila mtu alionekana kufurahia chakula chake.

Walipomaliza wote wakarudi garini kwa pamoja. “Asante. Nilipenda chakula.” Wakamsikia Naya akimshukuru Joshua kwa sauti ya chini iliyojaa hofu na heshima. “Karibu Naya.” Joshua akajibu na tabasamu lililomtia haya Naya. Akajibaraguza na kuangalia pembeni.

Safari ya kurudi Dar ikaendelea, Joshua akaonekana hawezi kuachia kitu alichokuwa akikisoma kwenye laptop yake. Simu nyingi zilizoingia kwake, Naya aliweza kutambua ni za kiofisi tu kwa jinsi aliyokuwa akijibu. Akajituliza kimya lakini akagundua hatakuwepo ofisini kwa siku kadhaa kuanzia siku ya jumatatu watakporudi ofisini. Akamsikia akitoa maelekezo ni nani atakuwa na majibu sahihi kwa kipindi hicho asipokuwepo. Na Naya aliweza kuwajua hao watu waliokuwa wakitajwa. Wote ni wa idarani kwao. Heshima ikazidi kuongezeka na kujiona hastahili kuwa hapo na hao watu wakubwa hivyo.

“Naona safari ya shule inafika mwisho?” Jamal akamgeukia Joshua. “Aisee ipo ukingoni. Acha iishe kwa heshima.” “Itoshe sasa Kiongozi!” Joshua akacheka sana. “Basi?” “Daah! Unatutia ubaya kaka. Acha, na wewe uanzishe familia sasa.” “Kama nilikwambia shule ndio ilikuwa ikizuia familia, basi ujue ilikuwa sababu tu.” Mpaka mzee Sajo akacheka. “Kipingamizi sio shule?” “Hapana mzee wangu.” Joshua akajibu macho kwenye laptop yake. “Basi nakuombea kheri.” “Hilo nahitaji mzee wangu.” Akajibu Joshua na kuendelea na anachofanya.

Baada ya muda akamwangalia Naya. Akamkuta anaangalia tu nje, yupo kimya. “Upo Naya?” Naya akamgeukia. “Nipo.” Akajibu taratibu na tabasamu la heshima. “Sawa. Kama kila kitu mpaka sasa kipo sawa, basi sawa. Nacheki tu.” “Nipo sawa. Asante.” Akamwangalia na kurudisha macho kwenye laptop yake. “Naya mama, unaishi wapi pale Dar?” Mzee Sajo akauliza. “Naishi karibu sana na Kibaha, kabla ya kufika Kibamba ukielekea mjini, panaitwa Kiluvya.” “Oooh Kiluvya!” Akajibu mzee Sajo akisikika kupafahamu. “Subiri kwanza wewe mtoto!” Jamal akashangaa mpaka akamgeukia kabisa Naya.

“Sasa Unafanyaje kuwahi kazini!? Maana kwa swala la kuwahi, Naya nakupongeza. Naona ni wewe peke yako ndio unataka kuvunja rekodi ya yule muhindi wa IT.” Mzee Sajo akacheka. “Nilipata habari zake pale getini.” “Mwanzoni alipoanza kazi tu akaingia matatizoni na walinzi pale getini. Eti mgeni siku ya kwanza, unaanza kazi, hata hufahamiki, unaingia kazini hata majogoo yenyewe hayajaamka bwana!” “Kumbe ndivyo alivyoanza?!” “Kumbe! Halafu sasa mbishi. Aisee jamaa mbishi yule! Akakutana na wale wanaume pale getini, bangi tupu. Acha wamuweke mpaka panapambazuka, tena wakamfanyia kusudi, eti saa tatu ndio wakapiga simu kule ofisi za IT kuuliza kama wanamfahamu!” “Nilisikia walimfanyia makusudi.” “Sasa je! Yeye si alijidai mkorofi, na wao wakamuonyesha umuhimu wa ofisi yao.” Wakazidi kucheka.

“Wakasumbuana naye siku za mwanzoni wakimwambia eti ni mapema sana.” “Kusudi tu?” Mzee Sajo akauliza kishabiki. “Kusudi tu ili kumtia adabu. Ndio ikabidi uongozi uingilie kati ili kumsaidia maana alisema yeye eti kichwa chake kinafanya kazi vizuri na kwa ufanisi asubuhi.” “Asubuhi kabla ya jogoo?” Mzee Sajo akazidi kuuliza akicheka. “Wewe acha tu. Lakini yule jamaa mbishi! Daah! Hakuna aliyempatia mwenzie. Usimuone hana nyama!” Mzee Sajo akazidi kucheka.

“Sikujua bwana. Mimi namuona akitupita tu pale bila salamu!” “Kikorofi masaa yote. Na akisema hapana, utakesha naye, huna jinsi ya kumbadilisha. Sasa sisi pale masoko tushajua anamuogopa sana Kumu. Basi ukimwambia nimetumwa na Kumu, hata kama ana kazi zake, ana kuhudumia haraka sana.” Mpaka Joshua akacheka.

“Kweli tena. Tena sisi alitufundisha Njama pale idarani. Akasema bila kumwambia umetumwa na Kumu, anakwambia yeye anaratiba yake ya siku nzima, tokea akifika yeye kazini.” “Sasa nyinyi si mnakuwa bado mmelala majumbani kwenu?” Akauliza mzee Sajo kichochezi. “Asante mzee wangu. Kumbe umeelewa sasa tatizo letu! Yaani yeye anapanga ratiba zake wakati wafanyakazi wote wa kampuni, tumelala majumbani kwatu!” Wote wakacheka.

“Sasa eti ndio akuweke kwenye ratiba yake ya kesho kama haijajaa au mtu wake mmoja wa kitengo chake akipungukiwa na kazi, ndio apenyeze kazi yako isiyo ya dharula. Sasa hapo na Njama naye anataka ripoti! Muhindi yule kakugomea na hataki watu wake wapokee ombi lako!” “Yeye ndio kiongozi wao!” “Haswa! Yeye ndio kiongozi wa kitengo. Mbona ukiwa na shida kule IT, jasho linatoka kama Kumu hayupo! Sasa ndio naona Naya anakaribia kuvunja au kufikia rikodi yake ya kuwahi!” Naya akacheka akijua ni sifa nzuri. “Ukiwahi asubuhi sana, kunakuwa hakuna foleni kabisa. Hukai barabarani muda mrefu. Kwa hiyo wakati wote huwa najitahidi kuamka mapema sana.” “Sasa usije zoea kazi ukabadilika Naya. Umeanza vizuri sana, na ubakie hivyohivyo. Na ujue watu wana macho.” Jamal akaweka msisitizo. “Nitajitahidi.” Naya akajibu kwa heshima na kunyamaza. Maongezi yalipoendelea kwa Jamal na dereva, Naya akajirudisha kama alivyokuwa amekaa.

Walipofika Kitonga kila mtu akawa bado ameshiba, wakakubaliana wasogee mpaka Morogoro, napo mzee Sajo aliwaambia anajua sehemu yenye nyama nzuri, atawapeleka. Hilo likakaa sawa. Jamal akanunua vitunguu vya mkewe na vitu vingine baadhi, safari ya kuelekea Moro ikaanza. Kama mwanzo, Joshua aliendelea na yake, Naya kimya. Jamal na mzee Sajo wakiongea na kucheka mpaka Morogoro sehemu ya kula. Naya akakataa kula. “Nashukuru kwa chakula, lakini bado nimeshiba sana. Sitaweza kula tena.” “Basi shuka hata unywe soda tu, usibaki hapa peke yako!” Joshua akaweka msisitizo kwa mzee Sajo aliyemkaribisha chakula . “Nashukuru. Lakini nitakuwa sawa tu. Kama haina shida ya mimi kubakia hapa ndani ya gari, naomba nibaki tu kwenye gari.” Wote wakaangaliana, Jamal akashuka. “Hutaki hata kunyosha miguu?” Akauliza Jamal akiwa nje ya gari. “Labda tu kwenda msalani kisha nitarudi hapa hapa.” “Basi Mzee Sajo atakusubiria hapa mpaka urudi akuachie gari.” Ikawa kama Joshua ametoa maagizo kisha akashuka. “Nashukuru. Sitakawia.” Naya akatoka kwa haraka ili asimuweke hapo mzee Sajo.

Aliporudi hapo, akamkuta Mzee Sajo peke yake, kweli akimsubiria. “Mama hutaki kula pesa ya viongozi wako!? Uzuri wa kuwa nao hao ni kulipiwa. Joshua hakubali mtu alipe ukiwa naye. Atalipa tu. Twende mama.” Naya akacheka. “Asante sana. Lakini nimeshiba mzee wangu. Asante sana.” “Usijivunge mama. Nyama ya hapa ni ya hatari! Hutakaa ukasahau. Au unaogopa? Joshua hajui kudai. Kwanza ana maringo huyo kwa wanawake! Hawezi kurudi kukudai. Wote wanamjua. Mkiachana hapa, ndio basi.” Mzee Sajo akaongea kishabiki akimtaka Naya na yeye asiachie hiyo ofa, asijue hayo mazingira kwa Naya ni maeneo yake sana. Ashakula sana nyama za hapo akiwa na Malon pamoja na marafiki zake kina Chezo. Na wenyewe walipasifia sana. “Asante. Siku nyingine nitalikumbuka hilo.” Ikabidi tu mzee Sajo aondoke.  Akamuacha hapo yeye akakimbilia ndani ili akalipiwe.

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

Naya akabaki hapo. Kumbukumbu za Malon zikamrudia. Akajikuta akilia. Tayari akapatwa hamu na Malon lakini  akajua hataweza kuwa naye. Akajiinamia hapo akalia sana akitamani kama ingekuwa tofauti. Akatamani kama Malon angekuwa na vitu muhimu kwake ambavyo alijua pengine kwa wengine vinaweza visilete maana, lakini kwake vilikuwa muhimu mno. Akatamani kumpa nafasi nyingine, lakini akakumbuka nafasi zote alizokwisha kumpa na bado Malon akaishia kumuumiza. Akalia hapo mwishoe akakumbuka yupo na watu wengine kwenye hiyo safari. Akajitahidi kufuta machozi na kutulia asijue alilia hapo kwa muda mrefu na uso ulishaonyesha.

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

Wakarudi garini wakicheka sana, tena mchekeshaji alikuwa Jamal ambaye sio mchekeshaji. Naya akajitahidi kuangalia nje ya dirisha ili Joshua asimuone. “Nimekuletea nyama. Ukisikia njaa ule, usigope. Na ukishindwa kula hapa, ukale nyumbani.” Joshua akamuwekea pembeni yake. Harufu ikajaa humo garini. “Asante sana. Nashukuru.” Naya akashukuru akiangalia ule mfuko bila yakumtizama Joshua. Mzee Sajo akaondoa gari. Joshua akahisi hayupo sawa. “Naya?” Akamuita makusudi akijua anakwepa kumwangalia na atamwangalia tu sababu amemwita jina lake. “Abee!” Na kweli akamtizama. Ndipo akaona macho mekundu. “Nilikuchukulia na maji. Kunywa.” Naya akaelewa. Akamfungulia kabisa na kumkabidhi. Akayapokea. “Asante. Nashukuru.” Akayanywa akiwa anaangalia dirishani akijaribu kutulia. Hata mzee Sajo aligundua alikuwa akilia kwani alikuwa akimchungulia kupitia kioo cha katikati ya gari.

Pakatulia, Naya akapitiwa na usigizi. Joshua akachukua maji aliyokuwa amebakiza mkononi taratibu asimuamshe. Akayafunga na kurudisha chupa sehemu yake. Akamtizama vile alivyokuwa amelala, akajikuta anavuta pumzi kwa nguvu akimtizama. Pakatulia kabisa na Jamal naye akalala kwa shibe. Joshua akarudi kwenye kazi zake, mzee Sajo akawasha mziki sauti ya chini, safari ikaendelea mpaka walipofika Kibaha.

“Nafikiri inabidi kumuamsha Naya, tujue tunamshusha wapi.” Naya na Jamal wote wakaamka. “Tunapita Kibaha, unataka tukushushe wapi?” Naya akajiweka vizuri na kuangalia nje. “Sio mbali sana na hapa. Nitakwambia mzee Sajo, asante.” Akaongea Naya akijiweka sawa.

“Naombeni niwashukuru.” Akaanza Naya na sauti ya kutetemeka kidogo. Joshua akabaki akimwangalia. Akainama na kuendelea kuzungumza. “Asanteni kwa kila kitu. Nimekuwa na safari nzuri sana. Asanteni.” “Karibu.” Wote wakaitika. “Utakaposhushwa haitakuwa mbali na nyumbani?” Joshua akauliza kwa kujali. “Sio mbali sana na baba atakuwa akinisubiria hapo kituoni na usafiri.” “Kama ni hivyo ni sawa.” “Muwe na safari njema. Mungu awasaidie na nyinyi mfike salama.” Naya akaongeza. “Asante Naya.” Wote wakaitika akamwangalia Joshua, akacheka kidogo bila yakuzungumza kitu. Naya naye akarudisha tabasamu na kugeukia dirishani asije pitishwa kituo.

Walifika kituoni, mzee Sajo akashuka kumtolea mizigo, akashangaa na Joshua naye anashuka. “Mzee asije akafikiria ulikuwa ukisafiri na wahuni tu. Acha tumsalimie.” Jamal aliposikia hivyo na yeye akashuka. “Kweli bwana.” Na kweli walimkuta baba Naya amesimama nje ya gari ya Naya aliyopewa na Malon akasogea. “Pole mama na safari.” “Asante kuniombea. Tumesafiri salama, tumekuwa na safari nzuri.” Naya akamwambia baba yake akimkabidhi mizigo. “Shikamoo mzee.” Akaanza Joshua, akaja Jamal. “Hawa ni viongozi wangu, baba. Tupo nao kitengo kimoja. Ila wao ni wajuu zaidi. Sana.” Wakacheka. “Hongereni sana. Na asanteni kunifikishia binti yangu salama.” “Karibu sana.” “Ila Naya alitukatalia kutupa ukaribisho wetu uliomwambia atupe.” Wote wakacheka. “Walisikia.” Naya akamwambia baba yake akicheka. “Naya hataki wageni.” Jamal akaongeza. “Muoga tu. Lakini mzuri sana kwa wageni huyo.” Wakacheka Joshua akimwangalia. “Basi kama na ukarimu wa wageni pia upo, acha tujiandae tuje wakati mwingine tukiwa hatujachoka, ili kuweza kupokea ukarimu vizuri.” “Kabisa. Mkaribie nyumbani, msiishie tu barabarani.” Wakaagana, wakasubiri mpaka wanaondoka, ndipo Naya na baba yake wakaingia garini.

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

Baba yake akamwangalia. “Malon alikuja kule hotelini.” Akaanza Naya, baba yake kimya. Akamuona anaanza kulia. “Unajua ni nini unataka Naya, ila unaogopa tu kukubali.” “Sijui baba!” “Unajua na ndio maana unalia. Na unalia kwa hofu tu ukiwa hujui itakuaje. Na hutatoka hapo mpaka uchukue hatua usonge mbele. Lasivyo tutajikuta tunakaa hapo kwa muda mrefu sana. Mimi na wewe hatusogea hapo.” Baba yake akaondoa gari. “Yale uliyotuambia sisi, juu ya ukawaida mpya, inakuhusu na wewe pia. Usipotoka hapo na kupokea huo ukawaida mpya, utajikuta na wewe unajichelewesha. Lazima utoke kwenye hilo pazia ulilokubali kujifunika wewe mwenyewe ukijiambia hakuna maisha ya furaha bila Malon. Mungu hakukuweka hapa duniani kwa ajili ya Malon, Naya. Narudia hili kwako kila mara. Nakuombea Mungu akufungue hapo, na uelewe.” Naya akazidi kulia.

“Nampenda Malon baba. Nampenda sana. Natamani angekuwa wa tofauti kidogo!” “Sio awe watofauti! Malon hayuko kama hivyo unavyomtaka wewe. Sasa lazima uchague mambo mawili. Kuwa naye hivyo alivyo au ukubali sio wako, umuachie mwenye naye. Halafu uamini wako atakayekupa unachotaka, yupo.” “Yuko wapi sasa, baba? Au umesahau historia yangu na kina Joshi pamoja na Ino?” “Hao watatu ndio kipimo chako cha mwisho?” “Unakumbuka nilijaribu hata na kwa Ozi?” Baba yake akamwangalia kwa kumsuta. “Sawa Ozi sikuwa naye ila unafikiri nitapata wapi mwanaume atakayenipenda na kunipa ninachotaka? Ukute mama alikuwa sahihi. Ni mimi ndio nina matatizo. Labda nivumilie tu!” “Ujue utavumilia hivyohivyo mpaka kifo kiwatenganishe.” “Usiniogopeshe baba bwana!” Baba yake akafika nyumbani na kuegesha gari nje, akamgeukia.

“Nisikilize Naya. Kilio cha mama yako akitaka maendeleo usifikiri alinibadilikia. Mama yako alikuwa hivyohivyo tokea sijamchumbia. Na wakati wote sisi tulijua atakuja kuolewa na mwanaume tajiri sana. Hakuwa mnafiki. Mzungumzaji kama hivyo wewe akiongea mawazo yake, wote sisi vijana tulimjua enzi zile ndio wokovu umeingia tu. Tukajikuta ndio vijana wa wakati ule, kanisani. Alisema hataolewa na mwanaume masikini, au mvivu eti kwa kuwa tu ameokoka. Vijana wakawa wakimuogopa na yeye hakuwa na shida juu ya hilo maana aliliweka wazi na wote tukamuelewa hivyo. Mimi nilivyofanikiwa, nikamrudia, akakubali nimuoe akitegemea tutafika mbali zaidi ya vile tulivyoanza au alivyonikuta maana na yeye ni mpenda maendeleo akaweka mipango ya kujipanua zaidi yeye mwenyewe akisema atanisaidia hata kifedha tusonge mbele zaidi. Mimi nikazane na biashara niliyokuwa nikifanya, na yeye ajira aliyokuwa nayo. Ninachotaka kukwambia ni kuwa, shauku yake ya utajiri haikubadilika ila tu, mimi ndio mambo yangu kifedha yalibadilika na ndipo manung’uniko yakaanza mpaka kifo chake.” Naya akapoa.

“Naya wewe upo kama mama yako. Hicho kinachokusumbua wewe, hakitatulia mpaka ukipate au mpaka kifo. Tabia hiyo yakung’ang’ania mambo umetoa kwa mama yako, mwanangu, sio kwangu. Ni kiu inayokusumbua, na hautakaa ukawa na furaha hata kama ni Malon atakuoa mpaka utakapo pata hicho ambacho wengine hawawezi kukielewa.” Naya kimya. “Sasa tofauti yako na mama yako ni hii. Mimi nakujua wewe, ukishindwa kukipata huko kwenye ndoa, utarudi tena hapa nyumbani, tuanze tena upya.” “Kwani wewe hutanipokea?!” “Ndoa sio zakuingia na kujaribu Naya. Tulia, fikiria ili kuamua kuchukua maamuzi sahihi. Huna haraka.” “Wenzangu wote wameolewa baba! Wote niliokuwa nikiwafahamu wameolewa mpaka yule mdogo wake Joshi naye alishaolewa na ana mtoto tayari! Mimi bado tu nahangaika!” Naya akalalamika.

“Ni kwa kuwa umeamua kuhangaika. Umejifunga bila sababu.” “Wala sijajifunga.” “Kwa hiyo unataka kuniambia hupati hata salamu huko nje?” Naya akacheka huku akijifuta machozi. “Wananisalimia sema wanakuwa ni wale wanaume wa ajabu ajabu?” “Sema sio kama Malon.” “Ndio sio kama Malon.” “Umeona sasa?” “Sio kihivyo baba!” “Ni kivipi? Maana nakujua Naya. Unamtafuta Malon ambaye unaye kwenye kichwa chako hata Malon mwenyewe hana uwezo wa kuwa Malon huyo unayemtaka wewe.” “Mimi sio kwamba nataka vitu vigumu baba! Nataka mwanaume atakayenijali na kunipenda kwa dhati na kusimama na mimi wakati wote. Sio mara leo yupo, mambo yakienda asivyopenda yeye, ananiacha tena! Panakuwa hakuna mahusiano ya kueleweka! Hivyo tu baba yangu. Mapungufu mengine najua tutarekebishana na kuvumiliana.” “Sasa kama unajua hayo yote kinachokuliza nini?” Naya akatulia.

“Toka hapo Naya! Fungua macho. Na kwa kuwa unaomba, utakutana na mwanaume Mungu aliyekupangia. Anaweza asiwe na vigezo vyote, lakini hata wewe utajua ni wako. Umejifunga sana kiasi ya kwamba unahisi hutaweza kufanikiwa tena. Na ninahisi una kipimo kibovu sana cha mapenzi, Naya mwanangu.” “Unafikiri hivyo baba?” “Kabisa. Fungua moyo wako. Ruhusu kupendwa upya bila kufananisha, utakuja kunikumbuka. Mungu amekuandalia upendo mzuri sana. Mimi nakuombea, ninajua hilo. Mungu hawezi kukuacha kwa kuwa na wewe ni binti mzuri. Umetulia, atakupa wa kufanana na wewe. Hata kama ni huyohuyo Malon, basi atakuja kufanana na wewe. Acha kumtilia mashaka Mungu.” Naya akatulia.

“Kwa hiyo nisiwe na wasiwasi na itakuaje?” “Wote tumeona ‘itakuaje’ huwa haitupeleki popote ila hofu tu ya kuchukua hatua. Hizo itakuaje zote mwachie Mungu azitawale. Atatenda tu. Ukijua na Mungu naye anakuwazia mema.” “Asante baba. Nilipofika pale Morogoro kumbukumbu za maisha ya zamani ikanijia, uchungu wa ajabu ukanijaa, nikashindwa kujizuia.” “Kuanzia leo na kuendelea, mambo ya zamani yakikujia, jiambie ile ilikuwa shule ambayo ulijiingiza mwenyewe kwa kutonitii, ukashindwa kutulia.” “Baba!” “Kweli. Ulikuwa na haraka ya nini na wewe hata shule hukuwa umemaliza? Ukaenda kuanzisha mahusiano ambayo ulishaona ndoa, wakati mwenzio hakuona hivyo.” Naya akainama.

 “Ila sasa, usikae hapo. Jua hiyo shule Mungu ameigeuza kuwa njema kwako. Umefundishika. Hakikisha unaishi kama uliyeelewa lasiyo utarudia hapo tena na tena mpaka Mungu akuone umeelewa. Sikutanii.” “Nimeelewa baba.” “Basi ishi kama uliyeelewa. Acha kulia tena. Furahia ukijua angalau hukuachwa na gonjwa au watoto waliokataliwa na baba yao, endelea. Basi.” Naya akavuta pumzi na kutulia kabisa. 

Jumatatu.

K

ama kawaida yake, Naya alifika wakwanza ofisini kwao. Akawasha yeye taa. Akakaa kwenye meza yake na kuanza kuangalia viporo vya kazi ambavyo wenzake walipewa na hawakumaliza. Akaanza kufanya kazi akijaribu kuweka mambo sawa kabla Jamal hajafika hapo na kuanza kugomba. Mara simu ya hapo mezani ikaanza kuita. Akashangaa sana. Ilikuwa saa 11:30 asubuhi. Akasimama na kuifuata mezani kwa Kibasa ambapo huwa inakuwepo hapo wakati wote. Akaipokea akijua ni getini ambapo aliwakuta walinzi waliokwisha mzoea kufika mapema sana.

“Halo!” “Subiri.” Akasikia sauti ya mlinzi getini, kisha akasikia. “Haloow!” Naya alishituka sana kusikia sauti ya Joshua nusu atupe simu. Akajikuta anasimama. “Halo?” Akasikia tena. “Halow. Shikamoo.” Akajikuta akisalimia bila kufikiria. Joshua alikuwa kijana tu. “Habari za asubuhi Naya?” “Nzuri ila mimi ni Naya. Jamal bado hajafika.” Akamsikia Joshua akicheka. “Acha woga bwana Naya!” “Hapana sijaogopa.” “Basi anza kwa kurudi kukaa.” Naya akashangaa amejuaje kama amesimama! Akaanza kuangaza macho akihisi pengine yupo  mahali akimwangalia kumbe mlio wa kusukuma kiti kwa nguvu akisugua sakafu wakati amesimama bila kutarajia, ulisikika.

“Umesharudi kukaa?”  Naya akarudi kukaa taratibu.  “Ewaa!” “Jamal hajafika. Na Kibasa ambaye huwa anachukua maagizo yake pia bado hajafika.” “Nafahamu Naya. Nimepiga nikijua nitakukuta sasa hivi ofisini.” Naya akatulia kidogo mapigo ya moyo yakienda kasi. “Ulikuwa na mapumziko mazuri, na uchovu wa safari uliisha?” “Ndiyo. Nashukuru kwa lifti pamoja na chakula. Na yale maji pia.” Joshua akacheka. “Karibu. Nilikwambia nilifurahia mazungumzo yetu tulipokuwa Mbeya?” “Uliniambia siku ile. Ndiyo.” “Basi nilimaanisha.” “Sasa mbona hata hatukuzungumza kitu hata cha maana!?” “Kwako haikuwa na maana ila kwangu umenifungua sana. Kuna mahali nilikuwa nimekwama. Mwingine anaweza kupaona padogo, lakini nilibaki hapo nikiwa nimekwama kwa muda mrefu sana na kushindwa kutoka.” “Pole.” Naya akasikika kujali.

“Lakini kuna kitu ulikizungumza, kimenisaidia sana. Unaweza usikumbuke, lakini ulikuwa ni ujumbe wangu. Nafikiri Mungu alinihurumia, akakutumia uzungumze na mimi ili nitoke hapo.” “Kweli Joshua!?” “Hakika Naya. Najua unaweza usiamini. Lakini ni kweli kila mwanadamu anao udhaifu wake. Hata kama ni padogo sana, lakini akiguswa hapo, anaweza akashindwa kutoka kwa muda mrefu sana. Inakuwa ni kama ndege ambaye amebanwa kwenye tundu, bovu kabisa. Lakini hajui.” “Pole na hongera.” “Asante. Nilijua utakuwa ofisini, nikaona nikuwahi kabla siku haijawa na shughuli nyingi pamoja na kelele za hapo, halafu nipige ukashindwa kunisikia.” “Ningekusikia tu Joshua.” Naya akaongea vizuri, Joshua akacheka taratibu.

“Basi nashukuru. Inamaana wakati mwingine hata mchana naweza kupiga?”  Naya akababaika sana mpaka akashindwa kutoa jibu la kukubali au kukataa. Joshua akacheka. “Basi Naya. Sitaki kukupa wakati mgumu.” Naya akanyamaza. “Upo sawa lakini?” “Sijui Joshua! Na mimi nasubiria Mungu anitoe sehemu nilipo anipeleke mbele zaidi.” “Unauhakika upo tayari?” “Huo ndio wasiwasi wangu. Nahisi nimeingiwa hofu. Sitaki kuwa tayari.” “Basi usiharakishe. Taratibu tu na maombi, utasogea. Inaweza kuchukua muda, lakini nina uhakika utasogea tu.” Naya akajisikia machozi yakitoka.

“Na kingine Naya, ‘It always gets better’. Uchungu wake haukai kwa muda mrefu sana. Kadiri siku zinavyosogea, utashangaa jinsi unavyopata nafuu.” “Sijui Joshua. Kwangu haipo hivyo.” Naya akalalamika akilia. “Mungu si mwanadamu hata aseme uongo, Naya. Jipe tu muda. Utashangaa jinsi utakapojiachia kwa hakika mikononi mwake, vile atakavyokusaidia. Sikwambii kama utasahau, lakini utashangaa ile kumbukumbu Mungu anavyoibadilisha. Kutoka kuwa kilio mpaka fundisho. Usiogope.” Akamkumbusha maneno ya baba yake. “Usiharakishe. Tulia kabisa. Kwanza huna haraka. Jipe muda wakutulia kabisa. Utashangaa.” Naya akajisikia vizuri, akajisahau hata kama anazungumza na Joshua bosi wake. Maana Joshua alizungumza naye kama anayefahamu anapopitia, asijue Joshua ameshaunganisha matukio, anapicha ya kinachoendelea, japo si kwa undani.

“Nikutakie siku njema Naya. Usisahau nilikushukuru.” Naya akacheka taratibu. “Japokuwa sijui ni kwa vipi nimekusaidia, lakini karibu. Na asante na wewe kwa ushauri ulionipa. Niseme na faraja.” “Karibu. Nitakuona wakati mwingine.” “Leo hautakuja kazini?” “Nimechukua likizo fupi ili nimalizie mambo ya chuo. Nimekuwa na mwezi wa hekaheka sana hapo kazini, sijamaliza research zangu. Nataka huu muda nitakaokuwepo likizo, nikamilishe mambo ya shule kabisa. Niachane na shule nirudishe akili kazini.” “Nitakuombea ufanikiwe.” “Hizo ni ahadi tu Naya!” “Kweli nitakuombea, sikudanganyi.” “Nahisi ni mpaka nikikusikia mwenyewe ndio nitajisikia vizuri.” Naya akacheka kwa wasiwasi kidogo.

“Unanafasi sasa hivi, nikuombee?” Akauliza akisikika na hofu kama aliyekumbuka anazungumza na nani. “Kabisa. Hapa nishafunga mpaka na laptop ili kushiriki maombi.” Naya akacheka asiamini kama hata Joshua huwa anaomba! Alionekana ni kijana makini sana akiwa ofisini. Kama asiye na muda na chochote ila kazi tu. Alizungukwa na kusikilizwa na watu wa maana watupu! Usingedhania hata kama anapata muda na Mungu au anatoa kipaumbele kwenye mambo mengine mbali na kazi. Akamtafakari hata asiamini kama hata anao muda wakusikiliza akiombewa.

“Haya, ufunge na macho. Ungekuwa karibu ningekushika mikono kama baba anavyonifanyia.” Joshua akacheka. “Nakushika mikono kwa imani. Nikiamini ipo siku utaniombea tena tukiwa pamoja na nitakushika mikono kabisa uniombee.” “Hapo sawa.” Naya akamuombea vizuri akimbariki na kumsihi Mungu ashike ufahamu wake na ampe utulivu ili aweze kufikiria vizuri. Akamuombea na kumaliza. “Amen.” Ameen. Daah, nahisi hivi vitabu vyote vinavyoniangalia hapa, nishavielewa sana.” Naya akacheka. “Bila hata kusoma!?” “Nakwambia kwa hayo maombi tu, nahisi najua kila kitu ni kuandika tu.” Naya akacheka sana.

“Basi nimefurahi kama umepata nguvu.” “Kumbe na uombaji pia upo ndani yako!” Naya akacheka tu. “Asante sana kwa maombi na kuchukua muda wako na kuzungumza na mimi.” Joshua akazungumza kiungwana sana. “Asante kushukuru. Na asante kwa kupiga.” “Karibu.” Wakatulia kidogo, Naya akacheka kidogo. “Kwaheri Joshua.” “Kazi njema.” Wakakata simu. Naya akabaki akiiangalia ile simu asiamini kama ametoka kuzungumza na Joshua mida hiyo alfajiri vile! Akashangaa ule upande mwingine aliomfahamu nao. “Anaonekana anamtumaini na Mungu pia, si akili zake tu!” Naya akabaki akimtafakari Joshua. Alikata simu bila hata yakuomba namba, wala hakutaka kulazimishia kumpigia tena simu. Naya akataka kujilaumu kutomruhusu ampigie tena simu lakini akakumbuka vile alivyomshauri. Akajisikia kutulia. “Amesema sina haraka.” Akabaki akimfikiria Joshua siku nzima, nakucheka mwenyewe.

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

Hilo juma likaenda bila kumsikia Malon hata kwa ujumbe au simu. Kukawa kimya, lakini Naya akashangaa hatilii wasiwasi ila kufurahia kuwa ameelewa somo, ameamua kuachana naye. Mpaka jumamosi ambapo hufanya kazi nusu siku pia hakumsikia hata Joshua. Hakupiga tena simu na kweli hakutokea pale ofisini lakini Naya hakuacha kumfikiria kwa hili na lile, akijicheka. “Siku nyingine akipiga simu, sitamsalimia. Napaniki nini sasa!?” Naya akawaza akiwa anatoka ofisini akielekea saluni kubadili nywele na kwakuwa hawakuwa wakifuga tena, kazi za shoruba hazikuwepo tena pale nyumbani kwao akaamua kutengeneza kucha kabisa. Alisha mpigia simu baba yake kumtaarifu kuwa atapitia saluni, kwa hiyo atachelewa kurudi nyumbani.

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

Giza lilishaingia wakati anatoka saluni kurudi nyumbani kwao Kiluvya. Njiani akampigia simu baba yake kumtaarifu ndio yupo njiani anarudi. Akamchokoza baba yake kidogo, wakaagana. Naya akakanyaga mafuta kwa furaha vile alivyopendeza na yupo ndani ya usafiri wake! Hapiganii tena daladala wala kukaa muda mrefu kituoni! Akawa anafurahia njia nzima mpaka karibu na nyumbani kwao akapunguza sauti ya redio. Akakuta geti ipo wazi. Akajua baba yake amemfungulia akijua yupo njiani. Akacheka. Wakati akiingia akaona gari ya Malon imesimama. Akacheka. Ni kama alimtegemea kwa asilimia fulani. Akatoa zawadi alizowanunulia hapo wakati yupo hapo saluni, akaingia ndani. Akawakuta wote wamekaa sebuleni wakiangalia luninga ila kimya tu.

“Sasa mbona unaniangalia tu, hunisifii?” “Nani amekwambia umependeza?” Bale akamjibu nakufanya wote wacheke. “Mimi wala nisingecheka! Kwani eti baba mimi sijapendeza?” “Anakuchokoza tu Bale. Umependeza sana.” “Wivu tu.” Akamgeukia Malon. “Karibu Malon. Sijui nikupe pole ya safari?” “Asante.” Naya akamwangalia kidogo na kupita ndani chumbani kwake na kuweka vitu vyake, Zayoni akamfuata kwa haraka. “Umeninunulia?” Wakamsikia Zayoni akimuuliza dada yake. “Siwezi kusahau Zayoni. Upo kwenye gari nimesau tu kushusha. Nimepata na tisheti nzuri za kata mikono. Usiwe unavua shati ukicheza.” Wakamsikia Zayon akicheka. “Asante Naya. Wewe ni dada mzuri.” “Kamwambie basi na Bale!” Kila mtu pale sebuleni akacheka. Wakatoka.

“Kwani mmetusikia?” Wakabaki wakicheka. “Zayoni ameniambia mimi ni dada mzuri kuliko li Bale lilivyo. Ni likaka libaya.” “Hajasema hivyo! Wote tumemsikia mtoto. Acha dhambi wewe.” “Basi Zayoni mwambie Bale.” “Naya ni dada mzuri.” Zayoni akarudia. “Ungemalizia tu Zayoni!” “Acha kumrubuni mtoto kwa mpira wewe. Utacheza naye sasa?” “Aliyekwambia mimi siwezi kandanda ni nani?” Bale alicheka sana mpaka kero. “Baba unamuona Bale lakini?” “Huyo anataka kukuliza tu, usimsikilize. Umependeza sana, usikubali kulizwa sasa hivi.” “Kwanza wala simsikii anavyonicheka.” “Kucheza rede tu wewe ulikuwa ukishindwa! Pale mtaani wote walikuwa wanajua hujui kucheza, hawakuchagui.” “Si kwa sababu nilikuwa naumwa na pumu siwezi kukimbia? Wewe vipi?” Naya akajitetea akisikika ameshaanza kukereka. “Visingizio hivyo! Wewe miguu hiyo imepinda, hujui mchezo wowote ule.” Naya akachukua kiatu kimoja kilichokuwa mlangoni, akamrushia, Bale akakwepa akicheka.

“Nilikwambia usimsikilize. Wewe unamjibu. Atakuliza sasa hivi huyo.” Naya akaenda kukaa pembeni ya baba yake, Malon akicheka taratibu. “Naya umependeza.” Bale akamsanifu. “Sitaki.” “Nimekwambia usimjibu. Shauri yako Naya. Utakwenda kulala ukilia sasa hivi. Nia yake akuone unalia huyo.” Baba yake akamtahadharisha zaidi. “Sijui likoje li Bale.” Bale akazidi kucheka akirudi kukaa. Naya akanyamaza kimya hakumjibu tena.

Naya akamgeukia baba yake. “Umekula baba yangu?” “Kitambo kweli! Bale katengeneza chakula kizuri sana.” “Anajua kupika tu, lakini hajui chochote kile!” Bale akaanza kucheka tena. “Nikuletee chakula Naya?” “Asante Zayoni mtoto mzuri. Lakini nimekula chips muda si mrefu. Nimeshiba. Wewe umekula?” “Sana. Amepika tambi nzuri na nyama akakata ndogondogo akaunga vizuri na nazi. Imekuwa tamu kweli!” Naya akamwangalia Bale. “Unasemaje Naya sista wangu?” “Achana na mimi.” Zayoni na Bale wakacheka kwa pamoja. 

Malon Akumbuka Shuka kumekuchwa.

W

alipotulia tu Malon akaanza. “Nilikuwa nikikusubiri wewe Naya ili niombe radhi kwa wote. Sio kwamba nilidharau kupotelewa kwenu na mama ndio maana sikuja kutoa pole. Na mimi nilikuwa kwenye mshituko, sijui nini kilinifunga sikuja kwa haraka! Pengine nilikuwa nikijaribu kupokea zile taarifa! Sijui. Maana mama niliyemuacha mimi hakuwa hata akikohoa! Alikuwa mzima kabisa. Sasa kuja kusikia hayupo tena! Kwa kweli ilinishitua sana.” “Hata sisi bado tupo kwenye mshituko, Malon. Imekuwa ni kama upepo wa kimbunga ulipita hapa, ukapuliza kwa muda mfupi na kuondoka naye. Hakuna aliyetarajia kati yetu na wala hakuna aliyetegemea kama siku ya leo anaweza asiwepo hapa! Kwa kweli hapakuwa na hilo wazo. Tulikuwa na mipango ya mpaka siku ya mahafali yake huyu Zayoni na Bale. Alijiandaa kwa mengi kweli, akijua Zayoni ndiye atakayemuacha pale shuleni. Lakini ndio hivyo. Ilikuwa ni siri kubwa sana. Na sisi tunaishi tukiipokea kila siku inavyokuja.” Akaongea baba Naya. “Aisee poleni sana.” Malon akamalizia wote wakaitika. “Asante.”.

“Kingine najua wote mnajua jinsi Naya alivyohangaika juu yangu. Lakini naahidi kubadilika na kutulia na Naya. Nimekubali makosa, na ninaahidi kujirekebisha. Nimekuja na pete kabisa. Hii hapa.” Malon akaitoa, “Nataka leoleo nimvalishe, kisha taratibu nyingine zianze. Halafu nilipanga pia nikamvalishe kabisa na kanisani mbele ya mchungaji atuombee.” Wakamsikia Naya akicheka. “Hebu tuione hiyo pete yenyewe.” Naya akanyoosha mkono, Malon akamkabidhi. Naya akaiangalia kwa muda mrefu. Akaitizama kwa kuigeuza geuza, kila mtu akimtizama kuona kama ataivaa.

“Ni nzuri sana. Hongera Malon.” Akawa anamrudishia. “Nimeitengeneza kwa ajili yako Naya!”  “Hii pete sio yangu Malon. Yupo ambaye Mungu amemkusudia aje aivae, lakini sio mimi.” Pakazuka ukimya pale sebuleni, Malon hakutegemea. “Naomba uipokee Malon. Hakika haitakaa ikaingia kidoleni mwangu. Wewe siye mwanaume utakayenitoa hapa kwa baba Naya. Hata kidogo. Japokuwa nakupenda sana Malo, na ninaumia sana kukukosa, lakini sithubutu kutoka hapa kwa baba Naya, nakuongozana na wewe popote pale, hata uniambie ni Ulaya, pia sitaki. Ni bora nibakie tu hapa kwa baba Naya.” Naya akaongea taratibu tu bila jazba.

“Siku nilipokupigia simu, ukaniacha bila huruma, ukinisukumia kwa Joshi, na hukugeuka nyuma kuniangalia kujua hata ninaendeleaje! Nikaja kukukuta na Rita, ukashindwa hata kunitambua, ule ndio ulikuwa mwisho wetu mimi na wewe Malon. Katika yooote uliyokwisha wahi kunitenda, hapo nimeshindwa kabisa kukusamehe na nimekuthibitisha wewe hukukusudiwa kuwa mume wangu. Kama Mungu wangu aishivyo, hakika sitakurudia Malon. Acha Mungu atanipa wa kufanana na mimi, na hata asiponipa pia basi. Nitazeekea hapahapa nyumbani kwa baba Naya.” Akasimama na kwenda kuiweka ile pete kwenye mfuko wake wa shati.

“Umekula na wewe Malon, au nikupashie moto ule kidogo?” Naya akabadili mazungumzo kabisa. Wakashangaa safari hii halii tena. Malon kimya ameinama. “Malo, ungependa kula kidogo?” “Hapana, asante.”  Naya akarudi kukaa pembeni ya baba yake, kimya. Wote macho kwenye luninga. Baada ya muda Malon akasimama. “Usiku mwema.” “Na wewe Malon. Taratibu huko barabarani. Mungu azidi kukufanikisha.” “Asante mzee wangu.” Malon akatoka, baba Naya naye akatoka kwenda kufunga geti bila yakuongeza neno. Naya naye kimya hata hakusogea pale mpaka baba yake aliporudi, akajiegemeza pembeni ya kiti chake.

~~~~~~~~~~~~~~~~~~

“Umetengeneza na kucha?” Baba yake akamuuliza kwa upendo. “Nimebandika. Hizo ni za bandia.” “Sasa kwa nini huachi za kwako zikakua, mama?” “Nashika shika sana maji, zinakatika. Kwani hizi hazijapendeza?” “Zimependeza, ila najua zako zingependeza zaidi. Una vidole vizuri na kucha kama za mama yako.” Naya akacheka. “Basi zikitoka hizi, siweki tena. Naanza kufuga zangu.” “Hayo ndio maneno.” Wakaendelea kuzungumza mambo mengine mpaka wakaenda kulala. Malon hakuzungumziwa tena.

Naya alishangaa analala usingizi mzito tofauti na alivyotarajia. Akahisi ni kama ametua mzigo uliokuwa mzito, na asijue kama ulikuwa umemlemea muda wote. Ile hali ya kuwa huru ikamwingia. Kwamba hana wasiwasi tena na alipo Malon, anafanya nini, na na nani! Akashukuru ameachana naye akiwa na pesa, asije akasema alimuacha akiwa masikini. Akalala akijiambia hana deni kwa mtu. Amerudia maisha yake kabla hata hajampata Malon. Hakuwa na pesa, ila utulivu mkubwa moyoni na pengine atakuja kufanikiwa kurudisha heshima kwenye jamii. Kujulikana ni wa Malon, wakati Malon mwenyewe akilala na kila mwanamke! Akaifurahia sana ile hali ya utulivu na uhuru. Akalala. 

MAISHA BAADA YA SHILINGI KUPINDUKA.

K

ila mtu kwenye familia yake alijua kitendo cha kukataa pete ya Malon si kidogo kwa Naya. Wakatamani kumuona pale uhalisia utakapomwingia vizuri kuwa Malon ndio hatarudi tena hasa wakijua garama aliyolipa kwa huyo mwanaume. Siku inayofuata asubuhi wakiwa wanajiandaa kwenda kanisani, hawakumuona akitoka chumbani kwake. Bale na Zayon walishakuwa tayari wapo mezani wakipata kifungua kinywa tayari kwenda kanisani. Baba yao akatoka chumbani. “Naya yuko wapi? Mmemuona ametoka huko chumbani kwake?” Bale na Zayon wakaangaliana bila kutoa jibu, baba yake akaenda chumbani kwa Naya kugonga. “Ingia baba.” Akaingia.

Alimkuta tu amejilaza kitandani. “Njoo ukae hapa.” Akamuonyeshea pembeni yake, kitandani. Akaenda kukaa. “Umependeza baba! Umekuwa msafi.” “Huendi kanisani leo?” Naya akabaki kama anayefikiria chakueleza mtu akamuelewa. Hakutaka kurudi kanisani kwa kina Malon tena, ila akajua Zayon amependa kundi la vijana wa kule. Na pia hawakutaka kurudi tena kanisani kwao kwa zamani kwa aibu ya kujikuta kila siku hana hata mchumba ni kama anaanza upya kila siku. Hakuna maendeleo. Mabinti wengi waliozaliwa wakati mmoja na kukua wote pale kanisani na vijana, wengi walishaanzisha familia kasoro yeye. Naya akaona uzito kurudi pale.

 “Naya?” “Pengine leo nyinyi muende tu.” “Hicho kinachokuzuia leo kutokwenda kanisani, ujue na jumapili ijayo itakuwa hivyohivyo. Tafadhali toka huko unakoona uzito kutoka, anza kutembea Naya, mama! Mimi nakuombea, naomba na wewe chukua hatua ya imani.” Naya akaanza kulia. Akachukua mkono wa baba yake akajifunika usoni. “Nani alikudanganya itakuwa rahisi?” “Na kwa nini haiwi rahisi baba?” “Kwa kuwa vitu vyote vya thamani havipatikaniki kirahisi mama. Na wakati mwingine ni sisi wenyewe tunajikoroga na kuweka ugumu. Ila Mungu yupo na wewe Naya. Tafadhali jipe moyo, tuendelee. Na silazima tukarudi kanisani kwa kina Malon.” “Na Zayon?” “Huo mpira wa miguu unaweza kuchezwa hata hapo nje. Tayari umeshamnunulia mpira na viatu. Hata Bale atakuwa akicheza naye au wewe.” Naya akaanza kucheka.

“Sasa hapo baba una mdanganya huyo.” Bale na Zayon wakaingia wakicheka. Naya akamrushia mto. Bale akaudaka akicheka. “Hayakuhusu Bale. Mwaya Zayon tutacheza wote.” “Labda akufundishe kwanza.” “Unaona Bale anavyo nidharau baba?” “Nilikwambia usimsikilize. Haya jiandae twende kanisani kabla hatujakosa ibada zote.” “Tutakwenda wapi sasa?” “Turudini kanisani kwetu.” “Naona aibu baba!” “Mimi ndio wakuona aibu Naya. Wala si wewe. Mungu angekuwa ni wale washirika pale, hapo sawa. Hata mimi ningeliacha kwenda pale muda mrefu sana kwa dhihaka wanazonifanyia mpaka wakawa wakimchanganya mke wangu kwa maneno yao ya fedheha. Lakini wale ni binadamu mama. Tutakutana nao kila mahali. Huwezi kuwakwepa. Twendeni tu. Nia ni tukamuabudu Mungu wetu. Wala usiwatizame wao.” Hapo Naya akatulia.

“Kwanza wanao tuchekaga sisi na kutudharau hata sijawahi kuona ubora wao! Akili zao zipo kwenye mali tu.” Bale akaongeza. “Na Bale wewe ndio unawaweza pale.” Kidogo wakaanza kucheka wakitaniana. Ndipo Naya akapata nguvu za kujiandaa, wakatoka wote wakiwa wasafi na Naya amependeza. Ungejua angalau yapo mabadiliko. Hawakuwahi kurudi hapo na hilo gari jipya alilopewa Naya na Malon. Nao huo ukawa mjadala wakizungumza njiani na kucheka. Bale ndiye aliyekuwa akiwaendesha.

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

Siku hiyo Naya akawa mtulivu sana. Walipokuwa kanisani akamuona mke wa Ino akihangaika na mtoto wao Princess, tena peke yake wakati Ino akiendesha mambo hapo kanisani na tumbo lake kubwa tu la ujauzito. Naya akamuhurumia. Ndugu zake wakamuona akinyanyuka na kumfuata. “Naweza kukusaidia Princess.” Akamchukua kutoka kwa mama yake, akatoka naye huyo mtoto. Mama yake akamfuta nyuma akiwa amembeba mdogo. “Kwani anaumwa?” “Alianguka jana usiku. Tukampeleka hospitalini, akaonekana kila kitu kipo sawa. Sasa sasahivi analia, baba yake anadhani aliumia sana jana ila hatukupata wataalamu wazuri.” Naya alimjua Ino.  “Kwa hiyo usiku mlikuwa hospitalini, asubuhi mkawahi hapa tokea vipindi vya asubuhi?” “Si unajua Ino ni lazima awepo?” “Mimi nahisi huyu mrembo ana usingizi tu. Acha nimbembeleze, wewe nenda kakae na huyo kaka ili atulie.” Naya akamwangalia yule mtoto wao wakiume na kurudisha macho kwa dada mkubwa, Princess.

“Eti dada mzuri? Una usingizi?” Naya akamuuliza kwa upendo huku akimbembeleza. “Sasa unajua dawa yake huo usingizi?” Akaendelea kumuuliza akimbembeleza. “Funga macho.” Naya akaendelea kuzungumza naye kwa upendo huku akimbembeleza. Na kwa kuwa huyo mtoto alikuwa akimfahamu Naya, dereva wake wakumpeleka shule, basi hakuwa na shida hapo mabegani kwake. Akaanza kusinzia, mpaka akalala. Akamrudisha ndani kwa mama yake. Akamuwekea kwenye kigari chake. Mambo ya Ino wa viwango! “Ulikuwa usingizi tu.” Naya akamnong’oneza mkewe Ino, wakati akimuweka sawa hapo kwenye hicho kigari kikionekana kwa hakika ni kizuri na cha kisasa. “Asante sana, Naya. Nilikuwa nakaribia kurukwa akili.” Naya akacheka na kurudi kukaa.

Ibada ilikuwa nzuri tu, wakatoka. Washirika wengine wakaendelea kutoa pole kwa kumpoteza mama yao. Mwishoe wakaondoka nakurudi nyumbani. Walikaa hapo sebuleni tu, lakini Naya alikuwa mtulivu sana. Kimya. Hata hakupokea uchokozi wa Bale. Jioni wakatoka wote kwenda kucheza mpira. Naya alikaa tu akiwatizama Bale, baba yao wakicheza na Zayoni. Muda mwingi alikuwa amejiinamia tu. Baba yake alitegemea isingekuwa rahisi. Hayo mahusiano yao ilikuwa ni kama mzigo ulioonekana kama una utamu na uchungu mwingi ndani yake.

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

Ø    Safari ya Malon na Naya ndio imeishia hapo!?

Ø    Malon asiyejua kujirudi mpaka atafutwe akijua Naya yupo tu sehemu ni wake, safari hii Naya ameweka hitimisho, mwisho wa Naya anayetamani kuolewa lakini hakuna mahusiano yaliyofaa, utakuwa upi?

Usikose mwendelezo....

 

CONVERSATION

0 Comments:

Post a Comment