Naomi Simulizi |+1 205 767 8163 |naomisimulizi@gmail.com MAPENZI&PESA! – SEHEMU YA 18. - Naomi Simulizi

MAPENZI&PESA! – SEHEMU YA 18.

                                                                        Jumatano

Shauku ya kwenda kazini ikaongezeka kwa sababu ya Joshua. Saa moja na dakika 55 asubuhi akiwa mezani kwake, akasikia sauti ya Joshua koridoni akisalimiwa na watu. Naya akajua ameshawasili. Moyo ukajawa furaha. Tayari wenzake Naya wote walishawasili hapo ofisini kwao wakimsikiliza Jamal akitoa maagizo kwa vitisho vingi tu.  Joshua akafika na kusimama pembeni. “Karibu Kiongozi.” “Acha na mimi nisikilize.” Jamal akaanza kubabaika, Naya akainama baada ya macho yake kugongana na Joshua. Jema akamfuata. “Shhh Jema! Tupo kikaoni.” Jema akakunja uso na kumtizama Jamal kisha kurudisha macho kwenye tablet aliyokuwa ameshika mkononi akisoma ratiba ya huyo bosi wake ya siku nzima.

Joshua alijua anachofanya, akatulia tu akimsikiliza Jamal bila yakumwangalia yeye. Jema akamwangalia akimshangaa. “Sio hapa Joshua! Ni...” “Shhh! Come on Jema! Quiet.” Akamtaka anyamaze kwa sauti ya ukali kidogo. Jema akamwangalia na kurudisha macho akimsikiliza na yeye Jamal akawa kama haelewi. Kila mtu akawa kwenye tabia njema, Jamal hakuzungumza sana, akamkaribisha Joshua. “Jamani. Na mimi nilitaka kusikia tu. Napita.” Jamal akajichekesha kidogo na kufunga kikao. “Kikao kinaanza baada ya dakika 5, Joshua!”  Jema akaongea kwa msisitizo. “Nakuja.” Akajibu na kusogea kwenye meza ya Naya.

Naya akacheka kwa aibu. “Uliamka salama?”  Naya akamuuliza kwa kujali.  “Nililala kama mtoto mchanga, nimekuja kuripoti kwamba, naanza kazi.” Naya akacheka akikumbuka mazungumzo yao ya usiku uliopita. Hakuna aliyeelewa, ila wao wawili walielewa. “Haya, wahi kwenye kikao, usichelewe.” Naya akamnong’oneza. “Nashukuru!”  Joshua akajibu kwa heshima, na kuondoka kwa haraka Jema alikuwa akimsubiria pale alipomuacha macho kwenye tablet iliyo na ratiba ya Joshua ya siku hiyo nzima. “Simu ya kwanza nimemwambia Fina aitume hapa kama bado utakuwa hujafika ofisini. Ila kikaoni tumebakisha dakika 3.” Naya akasikia akipokea maelezo huku wakiondoka pale. Naya akajisikia vizuri. Ila akarudisha macho kwenye kompyuta bila yakutizama watu aliojua fika wanamtizama kwa wakati huo Joshua ameondoka. 

Njama!

K

wenye mida ya kama saa nne hivi Naya akashitukia Njama amemsimamia mezani kwake. Kidogo Naya akaingiwa na hofu, maana hawakuishia pazuri na Njama. Alimjua kama ni mmoja wa wasaidizi wakaribu sana na Joshua, na wote wawili Njama na Jema wakiongozwa na huyo kiongozi wao Joshua walijulikana kwa maringo. Ila Njama aliongeza na jeuri ya madaraka. Alipomtongoza Naya akijua kwa hakika Naya angembabaikia na kumkubali kwa haraka, tena akiwa mgeni kabisa na wenzie waliyeanza naye kazi kwa wakati mmoja, walishaanzisha mahusiano, Naya alimkatalia bila kumumunya maneno, wala kutaka kuzungushana.

            Njama alianza kwa ubabe kidogo akimtaka watoke naye kwa chakula cha mchana, Naya hakuweka sura ya kike ila ya kazi, akamwambia hatatoka, ana mambo ya kufanya. Njama akajaribisha tena kumwambia amtoe mida ya jioni baada ya kazi, Naya akamwambia ‘Hapana, asante kwa ofa lakini nisingependelea’. Naya alimjibu akimtizama machoni kumuashiria hampi jibu la mtoto wa kike kumzungusha kwanza ndipo amkubalie baadaye. Akamuonyesha hana shida kwa wakati ule wala baadaye.

Ilimuuma sana Njama hasa jinsi alivyojiona, wadhifa wake na vile alivyo halafu kuja kukataliwa na mtu kama Naya, tena mgeni tu pale kwenye kampuni! Alijua wazi wenzie Naya, wangemtamani na kumkubalia kwa haraka ili kuja kupata ajira za kudumu kwa haraka. Ni yeye Njama, mtu wa karibu sana na Joshua, kiongozi wa bosi wao Jamal! Ikamshangaza sana Njama. “Anaweza vipi kunikataa mtu kama mimi!”  Akawaza bila kuamini. Halafu Naya aliyeanza kazi kwenye kampuni hiyo hakuwa wala wa viwango kama enzi akiwa na Malon! Hakuwa hata na mvuto wowote ule. Hakuweka urembo wowote usoni, kichwani hata masikioni hakuwa akivaa hereni, uso wa  maombolezo, kuondokewa na mama yake. Akaendelea hivyo mpaka aliposhauriwa na Malon arudishe urembo wa nywele, ndipo akaanza kujitengeneza tena.

Naya akarudisha mvuto wa hali yake, na umbile alilojaliwa, sura nzuri, rangi tulivu ya mwili wake, vikachanganya wengi. Ndipo Njama sasa akaamua kumwambia waziwazi kabisa kuwa anataka mahusiano naye. Na hapo napo Naya hakumzungusha, alimpa jibu la moja kwa moja. “Hapana Njama. Sitafuti kuwa na mahusiano kwa sasa.” Alimjibu hivyo na kuondoka ofisini kwake akiwa ametumwa na Jamal ofisini kwake kumpelekea mafaili aliyokuwa akiyafanyia kazi yeye mwenyewe Naya. Kile kitendo kilimuuma sana Njama, akahisi atakuja kudhalilika sana pindi watu wakija kujua amekataliwa na Naya, asijue Naya hakumwambia mtu.

Sasa kuja kuona baada ya muda mfupi sana Naya yupo na Joshua bosi wake, ikamuuma zaidi. Akahesabu Naya anamdharau yeye kwa kuwa hana cheo kama cha Joshua. Asijue Joshua mwenzie alitokea wakati muafaka kwa Naya ambaye alishajivua kwenye mahusiano yaliyokuwa yamemfunga ya kimapenzi. Yeye Njama alitokea wakati Malon ndio amerudi tena kwenye maisha ya Naya aliyekuwa na majonzi ya kupotelewa na mama. Hilo ni moja. Pili alikuwa amechanganywa na Malon huyu aliyerudi na mwanamke wa safari hii ambaye anajielewa, sio kama wanawake zake aliokuwa akiwatoa tu nguo bila thamani, Rita. Mwanamke msomi, ametulia, hana shida ya pesa ya Malon ila mahusiano ya kweli.

Na Malon huyu akarudi akionekana amemfanyia Rita kama yeye tu Naya. Anafahamika mpaka nyumbani kwa kina Rita, kama nyumbani kwa kina Naya! Anamfahamu Nolan kama Bale tu. Halafu wamesafiri kwenda mapumzikoni/ kwenye safari za kibiashara za Malon kama vile alivyokuwa akienda naye Dubai. Kwa Naya yakawa mapumziko, ila kwa Malon biashara na mapumziko. Hilo likamtingisha Naya vilivyo na kumnyima raha zaidi. Kwamba kwa mwanamke huyu naye amekwenda naye umbali mwingine zaidi kama kwake! Mbaya zaidi hakuwa amemtambulisha kwa Rita au hata kuonyesha anamfahamu!

Akawa kwenye kipindi cha kusubiria pengine Malon hata atamtafuta baada ya kurudi safari, lakini kimya. Akasema pengine baada ya kukutana kwenye kesi na kuwapa pole ya kumpoteza mama, pengine atamtafuta tena lakini kikawa kipindi cha kusubiri tu. Kila wakati macho kwenye simu, akirudi nyumbani akawa akitegemea kusiki pengine alipita hapo, lakini kimya.

 Naya akabaki akisubiri na kusubiri bila kutaka kujichanganya na mwanaume yeyote yule ili Malon atakapomrudia asimkute na mahusino yeyote yale wakashindwa kurudiana. Na ndio kipindi hicho nacho Njama eti ndio akajiweka wazi kwa Naya. Naya alimkatalia bila kufikiria mara mbili akijua Malon wake amerudi tena. Watarudiana. Lakini napo kama kawaida ya Malon hakutokea mpaka Naya alipomfuata yeye mwenyewe na zawadi. Njama akakosa, Malon akakosa ndipo akajitokeza Joshua.

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

“Sasa Naya!” Naya akageuka vizuri wakati akifungua huo mfuko aliokuja nao. “Habari yako Njama?”  Naya akajaribu kumsalimia lakini Njama hakujibu ile salamu, akafungua mfuko aliokuwa amekuja nao. “Hii ni bluetooth. Nafikiri una smartphone yenye uwezo wa kuunganisha bluetooth. Si ndivyo?” “Ndiyo.” Naya akaitika akiivuta simu yake. “Nimesha zichaji zote mbili. Hii ina uwezo mkubwa sana. Unaweza kuitumia si chini ya masaa 12 bila kuishiwa chaji. Lakini hii ya pili, ni masaa 6 tu. Kwa hiyo wakati hii ukiwa umeiweka kwenye umeme, unaweza kutumia hii. Nafikiri ukisoma maelezo yake hapa, utaweza kujiunganishia mwenyewe kwenye simu yako.” “Ndiyo, nashukuru.” Naya akamshukuru lakini akajua japokuwa hajamwambia kama inatoka kwa Joshua, alijua ametumwa ndio maana amekuja pale kama na hasira fulani hivi na kushindwa hata kuitika salamu yake. Ofisi nzima kimya.

“Kwa hiyo si unaelewa badala ya kuweka simu masikioni, unapachika hizo bluetooth masikioni, unasikia kama kawaida? Au huelewi lolote juu ya bluetooth?” Akamuuliza kwa sauti ya juu tu kama kumdhalilisha. Naya akamwangalia machoni akijua ni wivu tu ndio unaomsumbua. “Nafahamu.” Naya akajibu kwa kifupi tu akimtizama lakini akiwa ameshangazwa sana na  Joshua! Katikati ya mambo yake mengi hapo kazini na bado ameweza kumfikiria kumnunulia bluetooth! Akakumbuka pengine ni vile walivyozungumza muda mrefu usiku uliopita mpaka akaishiwa chaji kwenye simu yake!

 Akavuta zile bluetooth, akacheka asijue Njama anamwangalia. “Sijui kuna swali lolote kabla sijaondoka?” “Hamna swali. Nimeelewa. Asante na nitamshukuru Joshua mimi mwenyewe.” Naya akafanya makusudi kumwambia hivyo tena macho yakiwa kwenye zile bluetooth zilizoonekana ni za hali ya juu sana, Njama akaondoka pale bila ya kuaga.

Mbaya zaidi akakutana na Jamal koridoni akiwa anatoka hapo kwa Naya na hasira. “Naona siku hizi mnatutembelea tembelea sana huku kwetu!” “Sasa hivi ndipo kwenye mzinga.” Njama akajibu akiondoka Jamal akicheka kwa uzuri tu, asijue kinachoendelea moyoni kwa Njama. “Nimekusikia Njama.” “Basi ujue nyuki tutarudi tu hata kwa kutumwa. Kazi kwako kusafisha mazingira.” “Mbona nishaanza tokea manyunyu!” Naya alikuwa akiwasikiliza tu. Njama akasikika akifunga mlango kwa nguvu.

~~~~~~~~~~~~~~~~~~

Hapohapo Naya akamtumia ujumbe Joshua. ‘Nashukuru sana kwa bluetooth za hadhi ya juu.’ Joshua alicheka wakati akisoma. ‘Acha utundu Naya. Nipo kikaoni. Nitakupigia.’ Akiwa katikati ya kikao, akiwa anazungumza wakamuona ametoa simu mfukoni. Akasoma ujumbe, wakamuona akitoa tabasamu. Bila shaka, akajibu hapohapo mbele za watu, kisha akaendelea. “Samahanini. Kama nilivyokuwa nikisema....” Jema na Njama wakaangalina. Siku hiyo ikaisha, Naya hakumuona tena Joshua.

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

Kwenye mida ya saa 6:30 jioni, akiwa chumbani kwake akampigia. “Ulisema na wewe ni mvumilivu, si ndiyo?” Naya akacheka. “Pole na kazi na hongera kwa majukumu.” “Nashukuru. Nivumilie tu. Leo ilikuwa mbiombio muda wote mpaka sasa hivi nipo ofisini.” “Ulikula sasa?” “Hata sikupata muda. Nitakula nikifika nyumbani.” “Mwenzio hapa naongelea bluetooth zangu. Sitaki mchezo.” Joshua alicheka sana. “Naya!” “Usinione hivi. Nishaachana na mambo ya kubeba simu kila wakati au kushika kama andazi! Mimi sio mwenzio.” Joshua akazidi kucheka. “Ushakuwa matawi?” “Ya juu mno. Sitaki mchezo mimi . Siku hizi na paa na wale ndege aina ya tai tu. Sio ndege kama mwewe. Huwezi kuniweza hata kidogo.”  Joshua alizidi kucheka.

“Kumbe ni afadhali nilivyokupigia simu sasa hivi! Nilikuwa nimechoka! Nikasema nikupigie, nikusikie, nipate nguvu yakurudia nyumbani.” “Nikwambie ukweli Joshua?” “Nakusikiliza Naya.” “Unanifanya nijione ni wa muhimu sana kwako!” Joshua akacheka kidogo. “Kweli.” “Na ndivyo ulivyo Naya. Najua wewe unaweza usielewe sasa hivi. Ukahisi ninakurupuka, lakini sikurupuki. Wewe siku unaniona kwa mara ya kwanza, kwangu ilikuwa mara ya tatu.” Naya akashangaa sana. “Au umenifananisha Joshua!?” “Hata kidogo. Hivi si nilikwambia huwa nakosea kidogo sana?” Joshua akamuuliza kwa kujiamini tu.

“Uliniambia.” “Basi amini ulikuwa ni wewe Naya. Siwezi kukufananisha.” “Ulinionea wapi!?” Akamsikia Joshua akicheka taratibu. “Ya kwanza ulipokuja kwenye usahili. Mlikuwa mkisubiria nje ya ofisi za mwajiri. Ulikuwa na wasichana wengine, mmefika pale kwa usaili. Nakumbuka mpaka nguo uliyokuwa umevaa.” “Joshua!!” “Hakika. Kwa kuwa nilikuwa ndani nikizungumza na meneja wao pale, na Jamal alikuwepo akipitia CV zenu walizokuwa nazo pale ofisi za mwajiri ili kuanza huo usahili. Nyinyi mlikuwa mkisubiria nje ili usahili uanze, muingie ndani. Nilikuona kwa kupitia kioo ndani ya ofisi ya mkuu wa kitengo chao cha waajiri.” Joshua akacheka.

“Mimi huwa sichanganywi hovyo Naya! Sikujaliwa tamaa za wanawake. Hata  Jema anaweza kuja kukwambia ukija kumzoea. Lakini nilishangaa kwako ilikuwa tofauti.” Naya akatulia kabisa. “Baadaye nikataka kumuulizia Jamal kama ulipita kwenye usaili, lakini Roho wa Mungu akanionya kabisa. Nikaanza kukuombea.” “Joshua!?” Naya akashangaa sana. “Sikudanganyi Naya. Sasa nikamsikia Njama akimchokoza Jamal kama amefanikiwa kupata warembo. Si unajua jina wanalo waita pale?” Naya akacheka.

“Basi akauliza mmepata kuku wageni wangapi? Kama unavyomjua Jamal, akawa hajaridhishwa na wengi wenu mliokuja pale. Akasema angalau mmoja, ila wawili ndio wasindikizaji. Angalau akikwama kabisa, anaweza kuwatafuta hao watatu. Akawa analalamikia wasomi wanaohitimu wa kizazi hiki. Akalalamika weee kama unavyomjua, lakini pia nilishindwa kumuuliza katika huyo mmoja aliyemfurahisha ni nani!” Joshua akaendelea.

“Ndio maana mliona hamkuitwa kazini muda mrefu, maana Jamal akaona kama mtampotezea tu muda, akaomba nizungumze na HR ili wale waliokuwepo waajiriwe kwa haraka na wapewe mafunzo waweze kufanya mpaka kazi alizotaka nyinyi mfanye. Kufupisha habari, nafikiri wale vijana umefanya nao kazi, umeshawajua kwa sehemu. Ndio maana ulikuwa ukimsikia Jamal akigomba kila wakati.” Naya akacheka tu bila kuwasema wenzie. “Katika kusitasita kwake yeye mwenyewe Jamal, mara aseme wapewe ajira, mara akirudi anakuwa amekasirika anataka wafukuzwe ndipo nikamkumbusha nyinyi watatu ambao alisema ni afadhali. Akalalamika zaidi ya siku mbili akisema anahisi atakuwa ni kama anajiongezea tu maradhi. Sikumlazimisha, ila nikamuonya kuwa, lazima mimi nipate matokeo ninayotaka, na sitaweza kumsubiri kwa kuwa malengo yangu yote yanategemeana na watu wa ngazi ya chini kabisa.”

“Nikamwambia nitakapotaka matokeo mazuri, sitaangalia sura, wala wao anao walalamikia, nitamuwajibisha yeye. Nafikiri ndipo akaingiwa hofu, akawapigia nyinyi. Hata sikujua kama na wewe ni mmoja wapo. Sasa mlipoanza kazi tu, niliambiwa natakiwa kuja kuzungumza na nyinyi kama kiongozi wa kitengo. Siku hiyo nikawa na mambo mengi, Jema akafuta hiyo ratiba, akamwambia Jamal atamjulisha lini nitakuwa na nafasi. Hayo nilisikia tu kutoka kwa Fina. Nilimkuta akizungumza na Jamal pale mezani kwake. Jamal aliponiona tu akaondoka kwa haraka, mimi wala sikumsemesha, nikapitiliza ofisini kwangu. Ndio Fina akaja ofisini kwangu kuniambia Jamal alikuwa pale akilalamika kuwa Jema anadharau mipango yake ndio maana inakuwa rahisi kuifuta kwenye ratiba zangu. Mimi hata sikujua kama Jema alibadili hiyo ratiba. Basi, lakini nilikuwa na shauku sana kujua kama ulirudi pale, yaani kama na wewe ni miongoni mwao.” Naya alikuwa ametulia kimya akisikiliza na mshangao mkubwa sana.

“Siku moja nikiwa kwenye gari nazungumza na simu. Tulikuwa ndio tumerudi tu hapa ofisini, nikawaona mnapita nyinyi watatu na Jamal. Nafikiri mlikuwa mkiendelea na kuzungushwa kwenye vitengo vingine ili mvifahamu, sina uhakika. Naya?” “Nipo Joshua!” “Nilishindwa kuzungumza kwa sekunde kadhaa kwenye simu mpaka niliyekuwa nikizungumza naye akahisi simu imekatika. Nilibaki nimeduaa, nikijiuliza kama kweli nimekuona tena! Ila safari hii ulirudi ukiwa umekata nywele, ukawa umepungua zaidi na umenyongea, sio kama nilivyokuona mara ya kwanza.” “Na bado uliweza kunitambua Joshua!? Maana ni kweli najua nilibadilika sana.” “Nakwambia Naya, naangalia kwa macho yangu haya ya binadamu wanayaona watu, na ya rohoni Mungu anaponiongoza. Ipo connection naipata nikiwa nawewe, sijawahi ipata kwa mwingine.” “Jamani Joshua! Mpaka nasikia machozi yanatoka!

“Mimi sio mtu wa kuzungumza baada ya kazi Naya. Nakuwa nimechoka maana kazi yangu ni kama nazungumza siku nzima. Huwa nikirudi nyumbani hata Jema anajua. Sitaki kuzungumza na yeyote. Nataka pawe kimya kabisa ili akili zangu zitulie. Kila kitu kinachonihitaji mimi, Jema na Njama wakijua nimeshashushwa nyumbani, wanahangaika nacho mpaka siku inayofuata. Lasivyo nisingeweza kufanya mambo ninayoyafanya. Nilishawaambia nikiwa nyumbani, ni muda ambao huwa sitaki mwingiliano. Na hilo wamelielewa. Ila sio kwako. Nikizungumza na wewe, nasikia faraja na najikuta natulia.” “Jamani Joshua!” “Sikutanii Naya. Jana nilipokwambia huna haja ya kukata simu hata ukilala, nilibaki na wewe pale, na nitakuonyesha kazi kubwa niliyofanya usiku wa jana.” Akamsikia Naya akilia.

“Usilie sasa.” “Natamani ungeniambia hivyo mapema! Nilikuwa kwenye mateso Joshua wewe! Upweke mkubwa sana.” “Haukuwa wakati wa Mungu Naya. Na mimi nilitaka kukwambia wakati ule, lakini pia Mungu akanionya. Nafikiri haukuwa tayari kwa ajili yangu, na nafikiri Mungu hakutaka nianze kwenye mwingiliano.” Naya akaelewa kuwa ni sababu ya Malon bado alikuwa kwenye picha. “Njia za Mungu sio zetu Naya. Na ugumu mwingine tunakutana nao ni kwa sababu ya kujaribu kuwahi kabla ya wakati wa Mungu.” “Mimi ni muhanga wa hilo.” “Lakini naomba iwe ni shule uliyohitimu, Naya. Usikubali kuteswa sana na shetani. Jisamehe, na utoke hapo. Naahidi kukuombea pia.” “Asante. Endelea kunisimulia.” Joshua akacheka. “Acha nitoke hapa, ili na kina Jema nao wakapumzike.” “Kwani bado hawajaondoka tu mpaka sasa!?” “Sasa wanaondoka vipi na mimi bado nipo?” Joshua akaongea kwa kujivuna kidogo. Naya akacheka. Wakaagana.

Akiwa njiani, akampigia tena simu. “Usinichoke.” “Ungejua jinsi ninavyofurahia! Natamani ningekujua mapema.” Joshua akacheka sana. “Kweli Joshua.” “Haukuwa tayari kwa ajili yangu Naya. Hata ulivyonitizama siku nilipokuja kufanya kikao na nyinyi pamoja na viongozi wote wa kitengo chetu, pia hukuwa tayari. Unakumbuka mimi mwenyewe niliomba tujitambulishe ili tufahamiane?” Naya akatulia kukumbuka. “Tena nilisema tujitambulishe na kusema hata kabla ya pale tulikuwa tukifanya kazi sehemu gani nyingine. Unakumbuka?” “Joshua, yote hayo wewe unakumbuka!?” “Siwezi kusahau kwa kuwa nilikuwa na sababu. Nia yangu nilikuwa nikitaka nikusikie wewe vizuri. Maana pia nilijua haupo tayari na sikupata kibali cha kukufuata.” “Joshua!” Naya akashangaa sana.

“Na nilijua pia hukutilia maanani wakati najitambulisha maana uliinama tu, ukiangalia simu yako.” “Joshua!” “Kweli Naya. Muda mwingi macho yalikuwa kwenye simu na mimi sikuwa nimezoea hivyo. Huwa nikizungumza ni kweli watu wananisikiliza kwa makini. Wewe hukunitilia maanani kabisa. Ukaonekana upo mbali kabisa na pale, ni kama uliyetaka tumalize, tuondoke pale.” Naya akakumbuka ndio kipindi alikutana na Malon, akahisi pengine angekuja kumtafuta tena. Ni kweli alikuwa akiangalia simu yake kila wakati akitaraji hata ujumbe wa salamu kutoka kwa Malon, lakini hakukosea hata kumtumia ujumbe wa kumwambia alifurahi kumuona. Naya akapoa.

“Basi mimi nakumbuka mpaka leo jinsi ulivyojitambulisha. Ilikuwa kwa kifupi sana.” “Pale Jamal alikuwa ashatutisha vyakutosha kuwa tukileta urembo tu, anatufukuza kazi.” Joshua akacheka. “Alishachoshwa na watu wa kile kiofisi chenu. Lakini turudi kwako Naya. Ulijitambulisha jina lako, kuwa unaitwa Naya. Hukusema hata jina la mzee. Ukataka kukaa, Jamal akakukumbusha useme ulitokea wapi kabla ya hapo. Unakumbuka?” “Joshua wewe!” Naya akashangaa sana.

“Ndio ujue sijakurupuka. Mwenzio nakufahamu. Tena na hapo ukasema kwa kifupi tu bila hata kutaja jina, kuwa ulikuwa ukifanya kazi katika shule, basi. Ukakaa. Ila nikahisi kama Jamal alikustahi! Maana mimi namjua yule, angekusimamisha mara kadhaa. Ndipo nikajua kwa hakika wewe ndiye aliyekuwa amekutaka tokea  mwanzo, na wale wengine ni wasindikizaji kama alivyosema. Na baada ya hapo akawa anasema kule ofisini kwetu bila kuwaambia nyinyi kuwa, isingekuwa wewe, angeshafunga kile kitengo afanye kazi zote mwenyewe huku akianza kuajiri upya. Nilifurahi sana.” “Haiwezekani Joshua! Jamal?” Naya akashangaa sana.

“Ni vile hataki wengine wajue. Lakini Jamal anapenda sana utendaji kazi wako. Kwanza anasema unaonekana  umetulia na unajielewa. Huna papara na husubiri kupangiwa. Anasema ingekuwa mwingine vile unavyowahi kuingia asubuhi, ungekuwa kwenye mitandao tu ukifanya yako, lakini anasema kila wakiingia ofisini, anakuta umesogeza kazi za idara tena bila kutumwa. Anasema hujui kubishana kama wengine, na anasema hujawahi kumlalamikia kwenye lolote. Ni siri nakuibia, ili kukutia moyo. Na ndio maana kila safari anayowapangia pale, anataka na wewe uende.” Naya akashangaa sana.

“Nilisikia kuna safari moja mlipangiwa, na wewe akataka uende, nilisikia tu kuwa umeomba usiende, kwa sababu za kifamilia.” Akakumbuka Malon alimshauri hivyo ili abaki na Zayon wakati anaongozana na baba yao. “Unakumbuka?” “Nakumbuka Joshua. Jamani nilishukuru Mungu sikwenda nao kwenye ile safari maana waliporudi Jamal alikuwa akigomba, mpaka ofisi ilikuwa ikizizima. Mimi nilijua atawafukuza kazi.”  “Hakuna walichofanya na ukumbuke hapo tuliwekeza pesa nyingi ya kitengo, kwenye ile safari. Ilinibidi kufikiria kwa haraka, ili tufanye kitu, ili ile safari isiwe bure. Katika ujinga na uzembe wao, nikautumia kwa haraka, ili nitimize lengo. Na kweli tukafanikiwa kuuza mpaka kufikia lengo.” “Lakini mbona nilisikia kama wamepewa onyo, wakirudia tena ndio wamejifukuzisha kazi.” Joshua akacheka.

“Ni wewe nini?” “Ni Jamal kwa sababu nilimwajibisha na yeye. Na ndio maana unamuona na yeye ameongeza umakini. Tuache hayo turudi kwako. Ile hali niliyokuona nayo ya kunyongea, macho kwenye simu muda wote kama  ambaye unatarajia kitu kisichokuja, na ukawa umekata nywele, nikazidi kukuombea kwamba Mungu akukutanishe na muujiza wako ili upate furaha. Nikawa nikikukumbuka sana lakini ikawa kuonana kwetu ni kama hakupo. Sikuoni popote hata ukipita. Lakini nilijua wakati wa Mungu haukuwa tayari, maana Mungu wangu huwa ana njia zake za kunikutanisha na vilivyo vyangu. Nikawa mpole tu.” Naya akacheka taratibu.

“Sasa niliposikia safari ya Mbeya, Jamal akaniomba niongozane naye kufunga ile kazi. Nikaona ni kama njia yakumpongeza, maana nilikuwa nimemkaba sana Jamal mpaka nikamuhurumia. Nikaona hiyo itamtia moyo lakini pia kwa kuwa nilijua na wewe ungekuwepo, nikaona utakuwa wakati mwafaka! Sikutaka mwingiliano wa Jema wala Njama. Nikawaambia wabaki ofisini, nikataka muda usio na mwingiliano kabisa. Nikiamini ningeweza  kukuona na kupata muda na wewe. Sasa siku ile ya mwisho kule Mbeya, uliporudi pale hotelini na kwenda chumbani kwako moja kwa moja, na mimi nikasema nisile mpaka utakapotoka. Pale nilikuwa nikikuwinda utoke, nije kukaa na wewe.” “Kweli Joshua!?” “Hakika, sina sababu ya kukudanganya.” Naya alizidi kushangazwa sana.

“Sikuwahi hata kufikiria!” “Na nilikaa kwenye kona kabisa na laptop yangu kuashiria sitaki mtu anisogelee, nipo busy. Nikatulia pale mpaka ukaja, ndipo nikarudisha vitu vyangu chumbani kwa haraka na kukufuata kabla hajafika kukaa mtu mwingine kwenye ile meza yako.” Naya akacheka akisikika anavuta kumbukumbua.

“Nikahangaika sana kukutuliza ili angalau usinikimbie, uweze kuzungumza na mimi.” Naya akacheka sana. “Niligopa sana. Sikutegemea eti mtu kama wewe uje ukae na mimi!” “Nilijua. Na vile ulivyokuwa ukinijibu kwa ufupi, nilijua hutakawia kuniaga, ukale chakula chako chumbani, halafu gharama yangu yote ya kukufuata Mbeya, tena kwa gari, ingekuwa bure.” Naya akacheka sana. “Kwa hiyo unasema isingekuwa mimi usingekuja?” Naya akauliza kwa deko. “Naya! Hivi unajua majukumu niliyo nayo lakini?” Naya akacheka sana.

“Sasa ulipotulia na kuweza kuzungumza na mimi, ndio nikaelewa ni kwa nini moyo wangu uliunganishwa na wewe. Mungu alijua hicho kichwa, na hiyo hekima, itanifaa mimi.” “Lakini hata sikuzungumza sana!” “Ulizungumza kile Mungu alitaka nikisikie. Basi.” Naya akacheka taratibu akifikiria.

“Sasa Naya, nimefika nyumbani. Niruhusu nikaoge, ndipo nikupigie. Si ulisema utanivumilia?” “Mimi ndio nafurahia. Tunakuwa wote japo kwa simu.” Joshua akacheka taratibu. “Basi nashukuru. Baada ya muda mfupi tu, nitakupigia ili tuimalize hii siku pamoja.” “Nitakuwa nasubiri simu yako.” “Sawa.” Naya akakata, akabaki akimfikiria Joshua. Ni kama alishafunga kwa Naya na kujihakikishia kwa asilimia zote, kuwa ni wake. Naya alikuwa amejawa furaha, hakuonekana tena kukaa sebuleni. Wakati wote walimsikia chumbani akizungumza kwa sauti ya chini, na kucheka. Angalau vilio vikaanza kupungua humo ndani kwao. Hatimae kwa amara nyingine tena ikatokea sababu ya kumtoa kwapani kwa baba yake muda wote.

Alhamisi.

A

subuhi tena akiwa amewahi kama kawaida yake, akashitukia Joshua anavuta kiti mbele yake. Naya akacheka. “Ulilala salama?” “Kama mtoto mchanga.” Naya akacheka. “Na wewe?” “Tokea nilipokwambia nasinzia, ukaniambia nilale tu, utakata simu ukitaka kulala, sijaamka mpaka alam iliponiamsha asubuhi hii. Nikachukia nikatamani ingekuwa naamkia jumapili, nilale ukiwa umeniombea na unanisubiria.” Joshua akacheka. “Usizoee. Wakati mwingine nakuwa safarini, nchi zinazotofautiana masaa na huku.” “Nitaridhika na kuombewa tu, bila kulala ukiwa masikioni kwangu.” Joshua akatoa tabasamu la kuridhika. “Kama ni hivyo basi zoea.” Naya akacheka sana.

“Kwa hiyo sitakuja kujuta?” “Sio kutokana na mimi. Nikwambie siri yangu nyingine?” Naya akacheka. “Niambie.” “Chochote kilicho changu. Hata soksi. Ilimradi iwe yangu mimi, nikajua ni yangu, ujue nitaitunza na kuienzi.” Naya akajisikia vizuri sana, akainama. “Siri nyingine hiyo. Na ndio maana huwa sina vitu vingi. Vichache, na huwa nahakikisha navitunza vizuri sana na kwa viwango vya juu. Ili Mungu aniamini kwa makubwa zaidi. Ndiyo siri yangu hiyo. Naruhusiwa kuanza siku?” “Asante Joshua. Nimejisikia vizuri.” “Na ndivyo utakavyokuwa kwangu. Mengine utagundua ni ubinadamu tu. Lakini sitakusudia kukuumiza. Na nitafanya juhudi za makusudi ili nisikuumize.” “Asante Joshua.” Joshua akabaki akimwangalia na tabasamu kubwa usoni, Naya akacheka kama hajui aseme nini zaidi.

“Jema atanifuata sasa hivi akiwa na Njama.” Naya akacheka. “Natamani uhamishie ofisi yako hapa kwangu.” Joshua akacheka sana. “Utaweza? Maana mimi ili kazi zangu zifanyike, nilazima watu wangu watatu wanao nizunguka kila ninapokaa kwenye meza yangu, wawepo ndipo siku ya kazi iende vizuri. Sasa utatuweka wapi hapa?” “Nitashindwa kufanya kazi za Jamal.” Joshua akacheka.

“Hapana Njama. Lazima aanze nao kwanza.” “Acha kulazimishia vitu visivyo na maana Jema! Ulazima unatoka wapi?” Wakawasikia Jema na Njama wanakuja wakibishana. Naya na Joshua wakaangaliana. Naya akacheka. “Uwe na siku njema. Ufanikishe kila kitu.” “Amina. Na wewe hivyohivyo.” “Kwanza mimi nilishamtumia tokea saa moja kasoro.” Akaongeza Jema wakiwa wameshafika pale. Joshua akasimama na kupita katikati yao, na wao wakageuza bila hata kupoteza sekunde. Wakawa wakitembea nyuma yake. “Nilizungumza na wewe jana wakati tukiagana, tukakubaliana vizuri tu na kupanga. Wanategemea simu saa moja na nusu na wewe unalijua hilo tokea jana. Hiki unachotaka kufanya sasa hivi ni fujo, Jema!” “Muulize kama hana....” Naya akaanza kufikiria jinsi atakavyokuwa busy siku hiyo. Walisikika wakibishana wawili hao huku wakielekea ofisini kwao, Joshua akisalimiana na wafanyakazi wengine hapo njiani.

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

Mida ya karibia chakula cha mchana, Joshua akampigia simu. “Mlo uliotamani jana usiku wakati nakula, unaletewa sasa hivi. Nilimwambia akupikie kisha akuletee, uone kilivyo kizuri. Nimpishi mzuri sana. Naamini na wewe utapenda.” “Sasa na wewe umeshakula?” “Nilimwagiza smoothie tu. Leo ratiba hairuhusu. Atakuletea na matunda. Mlo mwema.” “Asante kujali Joshua. Sikutegemea!” Joshua akacheka. “Karibu. Baadaye.” Wakaagana na kukata, Naya akabaki akimtafakari Joshua.

Mara simu ya Fina, sekretari wa Joshua akimtaka Naya, ikaingia hapo osifini kwao. Safari hii Naya akasimama na kufuata simu yeye mwenyewe. “Hujambo Naya?” “Mzima kabisa, dada yangu.” “Sasa Joshua ametoka, ila chakula kimeletwa hapa. Nataka kujua unakuja kula huku au kiletwe huko?” “Huku tafadhali dada yangu. Asante.” Akamsikia akicheka. “Basi kinakuja.” “Asante.” Naya akakata simu na kuvuta pumzi kwa nguvu.

Baada ya kama dakika 5 hivi akaingia kijana kama umri wa Joshua tu, akamuulizia Naya akiwa na begi maalumu la kubebea chakula kisipoe. Naya akasimama. “Mimi ndio Naya. Karibu.” Akamsogelea. “Mzigo wako huu.” Akaweka ule mfuko pale mezani. “Asante sana, nashukuru.” Akaondoka, Naya akabaki na cheko bila ya kumtizama mtu. Akachukua simu yake na ule mfuko akaenda sehemu ambayo hula chakula. Wafanyakazi wenzake kimya. Naya hakujali, alijua kinachoendelea mioyoni mwao. Hawakuwa wageni kwake, hakujishughulisha nao hata kidogo.

Simu ya Joshua ikaingia wakati akila. “Nahisi nitajing’ata ulimi!” Joshua akacheka sana. “Taratibu Naya!” “Si kwa utamu huu! Kumbe ndio unakula vizuri hivi!?” Joshua akasikika akicheka sana. “Anajua sana kupika. Ni ndugu wa mmoja wa wale vijana niliokwambia niliwasomesha. Huyo ni mdogo wake. Aliwahi kuja kumtembelea kaka yake pale nyumbani kipindi nikiishi naye, akatupikia, kuanzia siku hiyo nikamchukua mimi. Nilimpeleka tu kuongeza ustadi tu, lakini upishi ni karama yake. Anapika sana.” “Mimi nahisi ningepasuka kwa kunenepa.” Joshua akazidi kucheka .

“Unafanya nini sasa hivi?” “Ndio napata mapumziko yale ya dakika 5, ndipo niendelee na siku. Nimerudi ofisini muda si mrefu.” “Joshua?” Naya akamuita kwa upole. “Nakusikiliza Naya.” “Asante kunijali na kunifikiria. Sikutegemea kama ungefikiria kunifanyia yote haya. Asante.” “Karibu. Na nimefurahi kama umefurahia chakula. Natamani na mimi ningekuwepo hapo tupate mlo wa pamoja. Lakini ratiba yangu hairuhusu.” “Pole. Ipo siku tutapata muda wa pamoja. Mungu atajalia.” “Jumamosi. Hiyo naisubiria kwa vitendo nikihakikisha hakuna kitu kinaingilia siku hiyo, na Mungu asaidie.” Naya akacheka taratibu.

“Tena nimekuletea nguo. Zipo kwenye gari.” “Umeona mambo hayo? Asante sana. Njama atakuja kuchukua kwa ajili yakumpa dereva apeleke dry cleaner.” Naya akacheka akimfikiria Joshua. “Tutazungumza baadaye. Dakika 5 zinaisha. Acha nikasafishe kinywa.” “Sawa. Nakuombea ufanikiwe. Ila ujue unanifanya nakuwa na furaha.” “Karibu, na hiyo ndio ninataka kusikia.” “Asante.” “Byee.” Naya akaendelea kula. 

Joshua kwa Naya.

Joshua akawa kama mtu wa kubuni kitu cha kumfurahisha Naya kila siku awapo ofisini na ni kama alimuonyesha hamfichi kwa yeyote na anataka watu wamjue ni wake. Aliweka umiliki mzuri kwa Naya, ambao haukuwa mzigo. Alimuonyesha kumthamini sana na kumuhitaji. Alijishusha kwake akimuonyesha huwa anamfikiria kwa maneno na vitendo. Alilizwa kutotambuliwa na Malon kwa Rita, sasa hivi Joshua anamuweka mwangani, ashindwe tu yeye mwenyewe. Naya alijawa furaha. Machungu yote yakafutwa ndani ya juma moja tu.

Kwa muda huo mfupi habari zao zikaenea kama moshi mkali, usiofichika hapo kwenye hiyo kampuni. Akajulikana kwenye kampuni nzima. Kila mtu akataka kumuona huyo msichana aliyemchanganya Joshua kiasi cha kujibu jumbe katikati ya vikao! Akaunyanyua uthamani wa Naya kutoka mfanyakazi mgeni kabisa ambao bado walikuwa wakisubiri ajira ya kudumu ndani ya hiyo kampuni, mpaka kuwa mashuhuri.

Naye Naya akaongeza umakini sana ili asiharibu na kumwaribia sifa Joshua. Hakuna kazi Jamal alitaka ifanywe pale kwenye ofisi yao Naya asiichangamkie, tena kwa umakini mno ili asiharibu. Kuwahi kazini kukabaki paleple. Alikuwa wa kwanza ofisini na alitulia, usingemkuta akizurula hovyo au kwenye simu kila wakati nakushindwa kufanya kazi. Wengine walisema pengine ndio maana Joshua alimpenda. Gafla kila kitu mwilini kwa Naya kikaanza kuonekana kizuri. Watu wakaanza kusifia umbile, rangi ya mwili, muundo wa nywele anazoweka kichwani. Nywele fupi. Kila kitu cha Naya kikaanza kuvutia sababu ya kuwa karibu na Joshua.

IJUMAA.

S

iku hiyo ya ijumaa nayo mida ya kabla ya kazi kuanza, Joshua akatokea tena mezani kwa Naya. Alimtegemea Joshua kwa kuwa ndio muda alioweza kukutana naye wakiwa ofisini japo kwa kifupu. “Pole, jana simu iliishiwa chaji mapema wakati wa taarifa ya habari. Na huwa inachukua muda mrefu kuingia chaji, nikapitiwa usingizi wakati nikiisubiria. Nimekuja kuamka saa 6 usiku. Nikajua utakuwa umeshalala. Nimekosa kuagwa ili nilale unono.” Joshua akacheka sana maana Naya aliongea kwa kulalamika. “Nilijua tu simu imekata. Pole. Kwa hiyo hukurudi kulala tena?” “Nilirudi kulala kama kwenye saa 9, na saa 10 na robo huwa ndio naamka ili saa 10:45 niondoke nyumbani. Nikachukia!” “Naomba kuiona simu yako.” “Ila siyo mbovu. Usijali. Nilikosea tu muda wa kuichaji na...” “Naya! Nimeomba kuona simu.” Naya akacheka na kuitoa mfukoni.

Akamkabidhi. “Nilikuaga na simu nzuri sana. Tulinunua Dubai. Nikaja kuiuza.” “Kwa nini unauza simu!?” Naya akasita kidogo, ila akaona amwambie tu maana Joshua akamwangalia akijua kuna kitu hapo. “Nilikuwa kwenye kukusanya pesa ili kumuwekea dhamana Malon, wamtoe jela.” Joshua akashangaa kidogo. “Subiri kwanza Naya. Kwa nini uuze vitu kumtoa jela na kwa nini walimfunga?” “Malon alikuwa akiuza bangi. Na...” Naya akamsimulia kwa kifupi, Joshua akabaki akimwangalia. Akamsimulia mpaka akamaliza na kumshangaza sana. “Naya wewe una moyo mkuu!” “Ila sikuwa nikijua kama ndio biashara inayomwingizia sana pesa. Nilijua hiyo biashara ya sukari ndiyo inayompa pesa. Halafu mpaka nikamuuliza. Unajua sikuwahi kumuhisi hata mara moja kwa harufu! Mpaka nikahisi wanamsingizia nilipokuwa nikisikia anavuta bangi! Ila alikuja kukiri mwenyewe kuwa ni kweli na ndio ilikuwa ikimpelekea kulala na wanawake hovyo. Anyway lakini hiyo simu sio mbaya.” “Na pia sio nzuri.” “Joshua wewe!” Wote wakacheka.

“Unataka nikudanganye? Wewe huoni hata jina lake halieleweki!” “Bwana linaeleweka. Nione yako.” “Nilikwambia huwa nakuwa na vitu vichache na vizuri?” Naya akacheka sana. “Acha basi mimi nikusifie Joshua!” “Wanadamu wanachelewesha Naya. Acha tu niisifie kabla sijakuja kukuonyesha.” “Iko wapi sasa?” “Ningekuwa nayo sasa hivi hapa, tusingeweza kuzungumza. Nimeiacha ofisini makusudi ili nipate muda mfupi na wewe. Nikuone japo kwa muda mfupi nipate nguvu yakufanya kazi.” “Nimefurahi kuja kuniona. Ila ujue Naya huyu unayemuona hapa, kesho unaweza usimtambue.” Joshua alicheka sana mpaka kupiga makofi.

“Jinsi utakavyokuwa umependeza?” “Sitaki utani. Naenda kuketishwa na wakuu mimi!” Joshua akazidi kucheka. “Umepania?” Joshua akauliza akicheka. “Vizuri sana. Nakwambia hutanitambua.” “Nilikwambia siwezi kukuchanganya Naya. Ni lini utaelewa huwa nina vitu vichache sana na huwa navijua?” Naya akacheka kwa furaha. “Uwe na nywele, usiwe na nywele, nitakutambua tu. Unenepe, ukonde, mimi nitakutambua tu. Kabla haya macho yangu ya nje hayajakuona, ya ndani yanakuwa yameshapata taarifa zako. Kwa hiyo hata uweje, upo hapa.” Akamuonyeshea moyoni, ilimgusa Naya mpaka akainama, akaona machozi yakimtoka. “Naomba uniage kwa furaha Naya! Mwenzio nimekuja kuchukua nguvu yakuanza siku.” Naya akabaki ameinama tu akifikiria. Akakumbuka maombi ya baba yake juu yake. Akashindwa kujizuia, akainamia meza kabisa.

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

Wakati baba yake akimuombea akiwa anamlilia Malon, yale maombi hayakuleta maana kabisa. Alikuwa amejawa uchungu wakupitiliza. Hakujua kama anaweza pata mwanaume kama Malon. Na Malon mwenyewe alishamuhakikishia hivyo kuwa hatapata mwanaume atakayempenda na kumjali kama yeye. Na kweli ikawa hivyo. Kila aliyejaribisha naye, hakufikia viwango vya Malon. Hofu ya kuendelea kwenye maisha na mwanaume mwingine ikamwingia, akabakia akimsubiria Malon kila wakati.

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

 Joshua akasimama na kwenda kuegemea meza upande wa nyuma na kumvuta amuegemee miguuni. Naya akajua watakutwa pale. Akatulia kidogo na kusimama. “Uwe na siku njema. Acha mimi nikaoshe uso.” “Twende wote.” “Chooni!?” “Nitasubiria nje. Usijali. Hata hivyo hamna watu.” Wakatoka hapo, na kweli akamsubiria nje ya choo, ila mlangoni kabisa. Wafanyakazi wengine wakaanza kuingia wakimshangaa kwa nini amesimama mlangoni, tena choo cha kike!

Naya akatoka akamkuta hapo nje. Akamshika mkono kwa upendo kwa kupishanisha vidole akiutizama. Kisha akatingisha kidogo Joshua akimtizama. “Asante Joshua.” Joshua akacheka. “Kesho tutakuwa na wakati mzuri.” Akavuta ile mikono yao, akabusu wa Naya. Akamuona Naya amecheka. “Asante.” “Karibu.” Akamwangalia vizuri kwa kumthamini. “Za asubuhi?” Jema akawasogelea. “Baada ya dakika 4 kuanzia sasa, nimemwambia Fina atume simu kwenye hii simu ya mkononi. Tayari wote wapo hewani wanakusubiria.” Naya akamwangalia Joshua. “Uwe na siku njema.” “Aisee wanakusubiri.” Njama naye akaja akikimbia. “Na wewe Joshua. Ufanikiwe.” “Amina. Na wewe.” Akamwachia mkono na kupita katikati yao. Naya akagundua ndivyo anavyowafanyia, wakaanza kukimbia wakimfuata nyuma. “Acha kupaniki Njama!” Akamsikia Joshua. “Wote wapo hewani!” “Jema ameniambia baada ya dakika 4, kwa hiyo inamaana  nimebakiwa na dakika ......” Akaitizama saa yake ya mkononi. Naya akaondoka pale kurudi mezani kwake. 

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

Mchana Joshua, Jema na Njama wakaja hapo wote watatu wakizungumza kwa zamu na Joshua akiwa mbele yao. Kila mmoja na tablet yake mkononi. Naya akashangaa wote wanafanya nini pale! “Upo busy sana?” Joshua akamuuliza. “Nimeshamtumia Jamal kazi aliyonipa. Nilikuwa nasubiria kama atanitumia nyingine.”  Bado Njama alikuwa akiongea bila hata kunyamaza. Mpaka Naya akashangaa kama Joshua anasikilia. “Basi, twende ukasubirie wakati tunakula.” Akamnyooshea mkono ili amshike. Naya akachukua simu yake na kusimama. Akamshika mkono. Wakawapisha, Jema na yeye akaendelea kuzungumza, Joshua ametulia tu akiwa anatembea amemshika mkono Naya wanatoka hapo. Naya akamwangalia na kukunja uso. “Nawasikiliza kila kitu wanachoongea na wanajua ndio maana hawanyamazi mpaka wamalize. Usijali.” Naya akacheka taratibu kama aliyesoma mawazo yake. Hakuzungumza kitu ili asiwaingilie.

“Iwe hivyo ulivyosema, Jema. Usiongeze neno. Na waambie tunategemea jibu kwa haraka. Ifikapo jumatatu hawajajibu, tunapeleka biashara yetu kwenye mall nyingine. Nashukuru sana.” “Sawa.” Akashangaa Jema anaondoka bila ya kuaga. “Sio siku ya alhamisi, Njama. Hatuwezi kufanikisha kwa wakati. Weka jumatatu. Ili mpaka jumanne tuwe  tumeshakusanya kila kitu, jumatano uhakiki tu. Alhamisi tunafunga kazi ya juma.” Akaona Njama amesimama, haondoki. “Hakuna mjadala kwenye hilo Njama.” Joshua akaongea bila kusimama wala kugeuka nyuma. “Tumekata siku tatu nzima!?” Joshua akasimama na kugeuka. Ikabidi na Naya naye asimame maana alimwachia mkono na kuweka mikono mfukoni.

“Ni nani anayelalamika?” Akamsikia akiuliza kwa ukali kidogo. “Ni wewe niliyekwambia hakuna mjadala au wao kwa kuwa wameshindwa kufanya kwa wakati niliokwambia sasa hivi?” Naya akaingiwa hofu. “Hapana. Nilikuwa nikiwafikiria. Maana kutoka alhamisi mpaka kurudi jumatatu ni kama papana sana!” “Ni kwa kuwa nimepima nimeona hizo siku tatu ulizokuwa umeziweka tokea mwanzo ni kupoteza tu muda na kuvuta jambo dogo kwa muda mrefu bila sababu. Waambie wote leo ni ijumaa. Siku ya kesho wanakuja kazini na jumatatu wote watakuwepo kwenye meza zao. Siku nzima. Watumie hizo siku ipasavyo.” Akaangalia tena saa yake ya mkononi.

“Halafu hata hivyo mpaka sasa hivi hapa, ni nusu siku. Yamebaki masaa mengi tu kumaliza siku ya kazi. Wapo tu kwenye simu zao, hakuna soko jipya! Au wewe unataarifa ambazo hujanipa?” “Hapana. Hakuna mpya.”  “Basi usikatae kazi. Anayeshindwa mwambie aniandikie mimi barua kabisa, yakunitaarifu ameshindwa. Niikute ofisini kwangu jumanne asubuhi. Sijui kama tunaelewana Njama?” “Sawasawa. Naona huo mchanganua mzuri. Tuanze mapema leo. Nitaitisha kikao...” Joshua akageuka na kuanza kundoka. Naya naye akafuata. “Leo baada ya chakula tu cha mchana.” Njama akamalizia bila kupata jibu kutoka kwa kiongozi wake, na yeye safari yake ikaishia pale, Naya akajikuta amebaki yeye na Joshua wakitembea.

“Tunakwenda wapi?” “Kula kwa utulivu. Maana wote wawili wanakazi ambazo zina wahitaji kuchangamka, hutawasikia wakinifuata tena leo mpaka nitoke jioni. Kwanza watakuwa wananikwepa mpaka kila mmoja akamilishe chake. Kwa hiyo twende tukale.” “Tusiende mbali Joshua. Mwenzio hata sijaajiriwa bado.” Joshua akamcheka. “Wewe si unataka kukaa na wakuu!” “Basi nitafukuzwa kazi.” Joshua akazidi kumcheka. “Kwani hujaajiriwa mpaka leo!” “Acha kunicheka bwana!” Joshua akazidi kucheka. “Jamal anawachelewesha makusudi ili mkimtibua iwe rahisi kuwafukuza. Sasa hicho nilichompa Njama sasa hivi, najua ataenda kuwachemsha kina Jamal, mjiandae. Kama unafikiri Jamal ni mkali, utamuona leo akiwa anakazi yenye deadline yangu ya jumatatu.” “Usinitishe bwana!” Joshua akazidi kumcheka.

Wakakuta gari haijafungwa. Akamfungulia mlango, Naya akapanda baada ya kushukuru. Akakuta ndani kuna vyakula. Akacheka. Na yeye Joshua akapanda upande mwingine. Akamtolea lunchbox yake na yeye akachukua yake. “Njama ndiye alikwenda kununua baada ya kutoka kununu simu yako.” Naya akamwangalia kwa mshangao. “Nataka kukusikia mpaka mimi ndio nikate simu Naya. Hii simu yako ambayo siielewi naona itakuwa ikinikatili kila siku.” Naya alicheka sana. “Ujue unadharau hii simu wakati watu wanalilia!” “Acha waililie, lakini mimi nataka mawasiliano na wewe yakueleweka.” Naya akacheka kidogo kama anayefikiria kisha akamwangalia.

“Asante sana Joshua.” “Nataka uniambie ulichofikiria sasa hivi hapa.” Naya akaguna. “Nafikiria jinsi nilivyoteseka Joshua! Nilikuwa kama mgonjwa! Ungeniambia kama leo, mida hii ya mchana ningekuwa nafuraha hivi, ninacheka! Hakika nisingeamini. Kweli Mungu kwake siku moja inamtosha kubadilisha mengi sana. Sikutegemea!” Naya akafungua chakula chake na kukifunga, akacheka kwa kuguna. “Baba alikuwa akinifuata kitandani kwangu nikilia. Sina tumaini. Nimeumia. Nimejawa aibu na fedheha hata kwa baba mwenyewe. Basi anaingia na kunishika mikono na kuanza kuniombea. Mambo aliyokuwa akimsihi Mungu juu yangu nilikuwa siamini Joshua, lakini akaniomba niamini tu pamoja naye.” “Kwa nini aibu na fedheha.” Joshua akauliza.

“Baba alikuwepo wakati nikimuhangaikia Malon, Joshua! Aibu niliyomuingiza baba yangu wakati nikikusanya pesa!” Naya akamsimulia kilichoendelea kipindi hicho. “Niliuza kila kitu changu mpaka viatu vyangu vya thamani kwa wanafunzi niliokuwa nikifanya nao kazi za ushering, ili tu nimtoe Malon jela. Nikijua ni mwanaume atakayekuja kuwa mume wangu!” Naya akatulia. “Hakika sikutegemea kuja kuachwa na Malon na kumkuta eti na mahusiano mengine! Hakika sikutegemea!”

“Aliponiacha tena, ni kama nilikuja kupona. Lakini kuja kumkuta tena na Rita, na wapo tu hapa mjini akishindwa hata kunitafuta, niliumwa Joshua, lakini sikuwa na jinsi yakumueleza mtu akanielewa. Siwezi tena kukaa chini nikalia. Sina mama. Familia inanitegemea, na nina kazi. Halafu eti anarudi na pete! Nilihisi ni kunidharau kupita kiasi. Nilimwambia ni heri nizeekee pale kwa baba Naya, kuliko kuongozana naye popote pale.” “Pole Naya. Pole sana. Na mimi ninahistoria mbaya hivyohivyo, kasoro mimi sikuwa hata na mtu wakuniombea. Niliachwa peke yangu, mpaka Mungu alipojitokeza na kuni adopt, mimi kama mtoto wake.” Joshua naye akacheka.

“Vurugu za mapenzi, mimi nazijua Naya. Nazijua kwa kuishi.” “Hivi kwa nini inakuwa ngumu hivyo jamani!? Haiwezi ikawa tu rahisi watu wakafurahia!” “Inawezekana Naya. Inawezekana kabisa. Nahisi nikukusudia na kuamua kwa makusudi kufanya iwe rahisi.” Wakatulia na kuanza kula kila mmoja akiwaza lake.

 “Umetoa kitu kipya?” Naya akauliza. “Ni msingi wa ile kubwa niliyokwambia inakaribiwa kuzaliwa. Naweka mazingira mazuri ili mtoto akizaliwa, nikiweka sokoni, ijibu kwa haraka.” “Hongera Joshua.” “Hizo pongezi nitazipokea vizuri siku ya jumatano nitakapoweza kuona kila kitu kipo pamoja. Acha Njama awachemshe kwanza, najua lazima jumanne nitakuwa na kila kitu. Jumatano nitakusanya kila kitu kiwe pamoja. Alhamisi nataka iwe hewani. Hapahapa ndani kwanza, ikiwezekana weekend ijayo iwe kwenye tv.” Naya akamwangalia kwa kumpongeza.

“Kama mimi nakufurahia hivi na kujivunia, mama yako ingekuaje?” Akamuona ametulia kisha akacheka kidogo na kutulia kabisa. “Malizia chakula.” Ikawa kama Naya anamrudisha pale. “Kweli.” Akaangalia saa na kuanza kula tena. “Nilikwambia kesho nitakueleza habari za mama yangu?” “Ninahamu yakusikia.” “Basi kesho nitakutambulisha kwake. Utamfahamu japo hutabahatika kumuona, ila utapata picha ni mtu wa namna gani.” “Sawa.” Naya akaangalia muda, akaona muda wa chakula umeisha.

“Acha niwahi Joshua. Sipendi kuchelewa popote. Napenda Jamal akiingia pale ofisini anikute nikimsubiri yeye. Asante kwa chakula.” “Ndio maana Jamal anakusifia! Unanidhamu ya kazi, Naya. Na unaonekana na wewe unapenda vitu vyako hata kama kwa wengine havina thamani.” “Nafurahia kazi yangu Joshua. Kwanza nilihangaika sana kupata kazi mpaka nilikata tamaa. Huu ni muujiza ambao siwezi kuchezea. Naona wengine wakilalamikia mshahara na mazingira ya kazi, mimi bado nipo kwenye kutoamini hata kama nimeipata!” “Utafanikiwa sana. Kazana. Na iwe hivyo kwenye kila kitu.” Naya akawa amemuelewa. Lakini bado moyo haukuwa umefunguka kwake kabisa.

Alijua ni nini Joshua anatamani kumsikia akisema, lakini alijawa hofu ya uthubutu na pia kuhofia pengine Joshua atamuhisi anamdanganya. Akaona anyamaze tu. “Umehamia wapi huko, ukaniacha mimi hapa?” Naya akacheka na kumwangalia Joshua. “Upo makini Joshua! Unakuwa kama unayasoma mawazo yangu!” “Nilikwambia ndio moja ya jukumu langu. Kusoma nini jamii inataka, na kutoa kitu sahihi ili mimi ndio nibakie sokoni. Sasa siwezi kukushindwa wewe mmoja, Naya.” Naya alicheka sana. Akakumbuka kwa hilo juma moja tu, mpaka hapo, alishamteka mpaka fahamu zake. Kila alipotaka kumkumbuka Malon, akajikuta Joshua amejaza furaha kweli. “Mimi nawahi kazini.” “Si tutazungumza baadaye?” “Kabisa.” Naya akakusanya uchafu, nakutoka kwa haraka. Alijua watu wanajua alikuwa hapo garini.

Alipoingia tu ofisini, Jamal akamfuata. “Nisogezee hiki kimeo, leo kisilale. Tafadhali Naya. Ukiona kazi kubwa, niambie nifanye mwenyewe. Leo siwezi kuondoka hapa bila kukamilisha hii. Na nasikia baadaye tuna kikao na Njama.” “Hamna shida. Acha nianze sasa hivi.” Naya akapokea mafaili yote kutoka kwa Jamal, akatulia hapo mezani akaanza kazi. Ilikuwa kazi kubwa na alijua alipewa asubuhi ya siku hiyo mmoja ya mwenzie waliyeanza naye kazi lakini akamlalamikia Jamal mchana kuwa kompyuta yake ilimgomea. Ndio alikuwa akihangaika nayo tangia asubuhi. Jamal alikasirika, akaanza kugomba kwa nini hakusema mapema. Ndio kazi anapewa Naya. Na akaipokea bila shida na kuanza kufanyia kazi.

Jamal alishaondoka hapo. Wengine wakaanza kutoka Naya hakuwa amemaliza kazi. Na kwa kuwa Jamal alimwambia asipomaliza yeye, itabidi aje amalizie baada ya kikao, hakutaka iwe hivyo. Alishakusudia kujipendekeza kwa Jamal. Kwa hiyo alikuwa akifanya kila kazi anayopewa, tena kwa ufasaha. Akafanya mpaka ikafika saa 10 na nusu, wenzie wote wakawa wametoka, amebaki yeye peke yake hapo ofisini. Mawazo juu ya Joshua yakamjia. Vile alivyojifunua mbele ya kila mtu kuonyesha Naya ni wake. Akatulia akimfikiria.

‘Kuna kitu natamani kukwambia Joshua. Lakini moyo unasita. Nahofia pengine unaweza usisadiki au ukafikiria vinginevyo. Lakini ipo siku nitakwambia tu. Nitataka ujue. Inaweza isiwe leo, au kesho. Lakini ipo siku nitataka ujue.’ Akamtumia huo ujumbe tena kwa kutumia simu yake mpya aliyopewa mchana wa siku hiyo, alishabadilisha kutoka ya zamani kwenda hiyo mpya. ‘Sijawahi kukuhisi ni muongo hata mara moja. Ningependa kujua.’ ‘Kama unaniamini, umenipa moyo. Kesho tukionana nitakwambia. Nataka nikwambie tukiwa wote, si kwa simu wala ujumbe.’ Naya akatuma tena huo ujumbe.

‘Umeshafika mbali? Naweza kukufuata japo bado nina kazi ofisini.’ Naya akasoma na kujibu. ‘Bado nipo ofisini ndio nataka kutoka. Kuna kazi alinipa Jamal, nilitaka kuimaliza kabla ya kesho. Naweza kukufuata. Sitachukua muda mrefu.’ Hakupata jibu. Akajua ametingwa. Naya akafunga mafaili yote na kufunga kompyuta. Wakati anatoka ili akaweke yale mafaili mezani kwa Jamal, atoke ofisini, akasikia simu yake ikiita. “Joshua!” “Njoo chumba namba 5.” Akashituka sana. Alijua ndipo wanakofanyia kikao kina Jamal. “Sikujua kama na wewe upo kikaoni Joshua! Naogopa.” “Njoo nakusubiria mlangoni.” Naya aliingiwa na hofu kubwa sana ila ikabidi kwenda. Ilikuwa jengo hilohilo ila mwishoni kabisa.

Mwili ulikuwa ukitetemeka mpaka akaanza kusikia baridi. Akatembea kuelekea huko na kweli kwa mbali akamuona Joshua amesimama katikati ya mlango kama ambaye yupo ndani na nje. Naya akaongeza mwendo mpaka akamfikia. “Naomba unisubiri. Tutatoka wote. Ni sawa?” “Sawa. Ila naomba nikusubirie hapa nje.” “Hiki ni kikao cha watu wa kitengo chako. Ingia nimekuwekea kiti.” Naya alijua ndani wanamsikia. “Joshua!” Akanong’ona. “Jamal alishakwambia huwa hatuli watu. Umesahau?” Naya akatingisha kichwa kukubali kwa hofu. Joshua akamshika mkono na kuingia naye ndani mpaka kwenye kiti alichojua ni cha Joshua mwenyewe maana Jema na Njama walikuwa pembeni ya hicho kiti. Jema upande wa kulia, Njama upande wa kushoto. Ilikuwa kama wakijadiliana kitu kwa makundi, Joshua akisubiria jibu.

“Kwa manufaa ya Naya. Nauliza tena swali. Asije fikiri tunapiga tu kelele humu ndani.” Joshua akaanza. “Jema?” Ni kama akataka Jema ndiye arudie. “Nani mwenye bidhaa zetu kwa wingi sasa hivi huko sokoni? Kwa nini? Na nini kifanyike?” Jema akarudia swali. Wote wakamwangalia Naya. Naya akamwangalia Joshua. “Ukitaka kuchangia. Karibu.” Naya akatoa tabasamu kama anayefikiria. “Na mimi naomba muda wakufikiria.” Naya akajibu kwa kujiamini, wengine wakiwatizama.

“Ukitaka sehemu ya kuandika.” Joshua akasogea na kumfungulia ipad yake. “Andika hapa.” Akashangaa Naya hakatai. Akaivuta ile Ipad na kuvuta kiti nyuma kabisa mpaka pale aliposimama Joshua. Kiti kilikuwa na matairi. “Mbona unakimbia meza?” “Pale uliponiweka, naogopa, kutanifanya nishindwe kufikiria.” Joshua akacheka kwa furaha. Akamuona Naya anaanza kuandika huku akifikiria.

Makundi yalikuwa matatu. Kundi la kwanza likanyoosha mkono na kusema, ‘Kwa wakati ule wenye bidhaa zao kwa wingi ni watu wa mahotelini. Kwa sababu wanao wateja wa uhakika na uwezo wa kununu bidhaa zao.’ Kundi la pili wakasema, ‘wanaouza kwa jumla ndio wanazo bidhaa zao kwa wingi kwakuwa wanapelekewa mpaka madukani na wanapewa kwa bei ya jumla, ipo chini.’ Kundi la tatu wakasema, ‘Wanayo watu wenye maduka ya kawaida, wao ndio wenye bidhaa zao kwa wingi kwa kuwa wanawateja wa uhakika kila siku, kila wakati, tofauti na mahotelini na maduka ya jumla.’ Joshua akaonekana kama hajapata kitu alichokuwa akikitafuta. “Sijapata vizuri. Halafu kuna kipengele kimoja ni kama sijakisikia kutoka kwenu wote.” Joshua akaongea akisogea katikati, na uso wakutoridhika.

“Jamani kwenye ofisi yangu kuna mwakilishi. Acha na yeye azungumze.” Alikuwa Jamal. Naya akaanza kutetemeka. Wote wakamgeukia. Akasimama. “Natetemeka.” Akanong’ona akimwambia Joshua. “Upo sawa kabisa. Ongea mawazo yako.” Joshua akamgeukia na yeye akitaka kumsikia. “Labda nianze kwa kusema sikutegemea kama ningekuwa hapa. Kwa hiyo ni kama nimeshitukizwa, sijajiandaa. Lakini nina mchango kidogo tu.” “Karibu.” Joshua akamkaribisha asiamini kama Naya ndio mwepesi vile! Shauku ikaongezeka. Kisha Joshua akamsogelea na kusimama mbele yake ili amwangalie tu yeye. Wakamsikia akimwambia kwa utulivu. “Jaribu kuvuta pumzi kwa nguvu na kuachia taratibu ili kukutuliza. Na fukuza hisia za hofu kabisa.  Ona kama upo na watu wanaohitaji msaada, na wewe unayo suluhu. Itakupunguzia hofu na kukuongezea ujasiri. Sawa?” Watu wote kimya wakiwasikiliza. Wengine vichwa chini maana Joshua huyu, anabembeleza, siye Joshua wanayemfahamu anayetaka majibu yakueleweka.

“Nimetulia.” Joshua akacheka. “Karibu.” Akasogea pale mbele yake, wengine nao wakamuona. “Okay. Mimi sitakuwa mbali sana na wengine. Kundi la kwanza lilisema wenye maduka ya jumla, wengine mahoteli makubwa, halafu kundi la bosi wangu Jamal walisema maduka ya rejareja. Naomba niweke hapo msisitizo lakini tofauti kidogo.” Naya akaanza lakini macho yalikuwa kwenye ipad muda mwingi kisha kwa Joshua tu. Hakutaka kuwatizama wengine.

Akaendelea. “Nafikiri tukisema kwa hao watu watatu, ni kweli lakini mimi nafikiri wenye bidhaa yetu au anayetakiwa awe nayo ni third part. Huyu mnywaji ambaye haihitaji friji wala duka kuhifadhi bidhaa yetu. Yeye akiipata ni kuitumia moja kwa moja. Uwekezaji wetu kwake upo chini, sana. Kuizalisha, utunzwaji kwenye chupa au kopo na kumfikia. Yeye ndiye anayetakiwa kuwa na bidhaa yetu. Na yeye ndiye tunatakiwa kuwekeza kwake.” Wakaanza kumpigia makofi. Naya akacheka maana Joshua alishaanza kutingisha kichwa kukubali.

“Sijamaliza.” Watu wakacheka. “Uwanja ni wako.” “Tangazo tunaloweka kwenye tv, linamgusa mwenye hoteli, mwenye duka la jumla, rejareja na huyu mtumiaji wa mwisho kabisa. Wazo langu na ndicho nilichokuwa nikifikiria. Kama tukikubaliana mtu wa mwisho ambaye anatakiwa kuwa na bidhaa yetu awe ni mtumiaji. Kwamba tukijua watu wenye maduka ya jumla, tukimpa vitu tuseme 1000, itachukua muda mrefu kidogo kuja kuleta pesa moja kwa moja maana na yeye atahangaika mpaka aje auze vyote. Lakini yule mwenye duka la rejareja anamfikia moja kwa moja huyu mtumiaji. Na huyu mtumiaji hata akiwa nazo mbili, moja anatumia palepale na akitaka kubeba  nyingine ataondoka nayo na lazima atakwenda kuitumia siku hiyohiyo bila kusubiri kesho na kuamsha shauku kwa hata wengine watakayemuona nayo.” Watu wote wakatulia kimya.

“Ndio swali langu ikawa hivi, tufanyaje  ili hayo yote yatimie kwa huyu mtumiaji? Awe kila akiwepo sehemu. Mchana au usiku. Akiwa ameshiba au ananjaa. Juani au kivulini. Awe mtoto au mkubwa. Kipofu au anayeona. Mgonjwa au mzima. Masikini au tajiri. Wote watake bidhaa yetu tu kiasi ya kwamba hawawezi bila hiyo, na wakiwa nayo hawawezi kutunza ila kutumia na kesho watafute tena kwa lile kundi la tatu, muuzaji wa rejareja!” Hapo mpaka Joshua akakunja mikono kifuani na kurudi nyuma akajiegemeza, akiwa anamtizama Naya.

Naya akacheka kidogo akimtizama. “Nimekuachia ukumbi.” “Njoo.” Naya akamnong’oneza kwa mdomo, lakini kila mtu alikuwa akiwaangalia. Walikaa pande tofauti za chumba maana Joshua ni kama alisogea pale alipokuwa amesimama naye kumpisha watu wamwangalie yeye, na yeye aweze kumuona vizuri. Alijivuta upande mwingine dirishani. Joshua akamsogelea baada ya kumwita. “Waambie kama kuna mwenye wazo anaweza kuchangia.” Joshua akacheka sana. “Sasa si useme Naya?” “Wewe ndio muendesha kikao bwana Joshua! Mimi naogopa.” “Huwezi ku drop the ball now! Umefika pazuri sana. Naomba uongeze ujasiri zaidi. Unakumbuka ninapokwambia huwa nazaa?” Naya akatingisha kichwa kukubali. “Upo leba sasa hivi. Kazana huyo mtoto atoke. Mimi mwenyewe unanishangaza. Unafanya vizuri sana.” Naya akacheka kwa furaha. Akasogea pembeni  ya Joshua.

“Nimepewa ruhusa kuwauliza. Kama kuna anayetaka kuchangia.” Naya akaongea kwa hofu kidogo. “Kwa ufupi Naya amesema bidhaa yetu ibakie kwa mtumiaji kwa kuwa wao wapo wengi kuliko hayo makundi matatu tuliyotajwa. Tukichukulia tu huu mkoa tu mmoja wa Dar. Asilimia 85, watumie bidhaa zetu kila siku. Wagonjwa, wazima, masikini, vijana, wazeee, watoto, na...” “Mpaka vipofu ambao hawawezi kuona bidhaa zetu. Kwamba ndio ameshushwa leo hapa mjini, ametoka kijijini ambako soda ni mpaka sikukuu. Tunafanyaje hao watu wote wabakiwe na shauku ya bidhaa zetu tu?” Pakazuka ukimya. Joshua akazungusha macho chumba chote na kurudi kwa Naya.

Ikabidi Naya aendelee. “Matangazo. Na si matangazo yale yakuonyesha mtu anatokwa jasho ndio anataka maji au soda zetu! Hapana. Tangazo litakaloimbwa na watoto mtaani. Tangazo ambalo likiwekwa hata kipofu atasisimkwa na kutaka kuweka mdomoni na akiondoka ataweza kumsimulia hata kipofu mwingine. Mgonjwa ambaye hata amezidiwa hataki kula kitu, adai bidhaa zetu. Hata kama mtu amebakiwa na pesa ya nauli tu, basi awe radhi kutembea ilimradi tu aweke bidhaa yetu mdomoni.” Wakaanza kupiga makofi.

“Sijamaliza Joshua.” Watu wakacheka maana Naya aliongea akimtizama Joshua kwa kulalamika. “Naya hupigiwi, unacheza!” Joshua akafanya kila mtu acheke, Naya naye akacheka sana mpaka kujifunika ipad usoni. “Utanifanya nishindwe kumalizia bwana!” “Haya samahani. Endelea kabla huo moto haujazima.” “Basi.” Naya akaanza tena na cheko. “Kuna jinsi yakufanya mtu azungumze lugha yako, au kile unachokitaka akizungumze bila hata yakumwambia arudie. Si mnajua?” Kimya. Naya akawaangalia na kurudisha macho kwa Joshua. “Leo nimekwambia uwanja ni wako. Wewe endelea.” Naya akacheka. “Wimbo na milio.” Kila mtu akapiga makofi ikawa kama wamekumbuka. Ikaanza kelele kila mtu akiunga mkono.

“Ila mimi bado sijamaliza!” Akamlalamikia tena Joshua. Joshua alicheka mpaka akapiga makofi mfululizo. “Naya leo umetuamulia watu wa masoko! Umeona tunacheza tu hapa mjini nini!” Watu wakazidi kucheka. “Sawa mama tupange. Leo nakuachia ukumbi.” “Usindoke sasa. Simama hapahapa.” Watu wakaanza kucheka tena maana alimvuta mkono. “Hapa ni sawa?” “Usisogee sasa.” Joshua akacheka na kutulia.

“Mwimbaji anapoimba wimbo wake. Akaurudia mara kwa mara, haitaji kuwaambia watu rudia kuimba huu wimba. Utashangaa wimbo unaenea mpaka watoto ambao hawajui kuongea vizuri, mtaani, kule uswahilini kabisa, watauimba. Wanaosoma shule za kata pia wataimba wimbo uleule kama wale watoto wanaosoma zile shule za wenye kipato kikubwa.” Wakacheka sana.

“Kweli tena. Utashangaa nguvu iliyopo kwenye wimbo. Mimi nimefanya kazi kwenye shule ya watoto wa walio nazo hapa mjini, na hawazungumzi lugha ya kiswahili, ila utashangaa sana nyimbo wanazoimba! Ni kama watoto wa uswahilini tu.” Watu wakazidi kucheka. “Linapofika swala la wimbo, kila mtu anaimba. Ndipo ninapokuja kwenye swala langu la mwisho la mlio. Tajiri na maskini, wakiume wote wanapiga mluzi.” Mpaka Joshua akacheka sana. “Hata wasomi na wasio soma pia.” Joshua akaongeza. “Sawasawa. Ipo nguvu pia kwenye mlio. Naomba niwasikilizishe mlio mmoja hivi.” Wote kimya. Naya akatoa simu yake.

Akabonyeza vitu kadhaa. Wote kimya kabisa. “Huu mlio nikiusikia mimi, hata kama pale ofisini kumewashwa baridi kali ya namna gani, nakunywa maji.” Naya akaweka. Ilisikika kama kinywaji kinamiminwa. Watu wakashangilia sana. “Nimejiwekea mimi mwenyewe makusudi kunikumbusha kunywa maji, maana mimi ni msahaulifu sana wa kunywa maji. Au huwa nazembea. Sasa fikiria mlio huuhuu, uongezwe sauti. Utoke kwa sauti kubwa yakuvutia! Kisha kusikika na jina ya bidhaa zetu.” Wengi wakasimama na kupiga makofi wakishangilia. Naya akakimbilia nje.

“That’s my girl!” Joshua akaongea kwa kutamba sana. Watu wakazidi kushangilia. Joshua akabaki akitingisha kichwa. “That’s what I am talking about.” Joshua akaongeza na kupiga ngumi kwenye mkono wake mwenyewe. Alijisikia vizuri sana na kushindwa kuficha hisia zake juu ya Naya. Miluzi ikaanza kusikika humo ndani, Joshua akacheka sana. “Njama, nakuachia kikao. Naona Naya ashatumalizia kazi kubwa sana. Hakikisha tunapata picha nzuri ya kinywaji kikimiminwa iwe kwa glasi, mdomoni na kila mahali. Kwengine mmalizie wenyewe.” “Na sauti ya hata umezwaji wake. Hapa kwenye koo.” Naya akachungulia na kuongeza hapo kwa Joshua, akionyesha koo lake. Watu wakacheka sana. Joshua akatoka.

Akamkimbilia na kumbemba juu kabisa. “Naya! Naya! Naya! Naya! Naya!” Eti akawa anamshangilia huku amemnyanyua juu kabisa. Naya alikuwa akicheka sana na ipad imemfunika usoni kwa aibu. Akamshusha na kumuwekea mkono mabegani, wakawa wakitembea. “Duuuuh! Wewe mtoto!!” “Umeniambia mwenyewe niseme.” “Hakika Mungu alikuleta kwenye kile chumba kwa makusudi na muda muafaka! Nilikuwa nishachoka, hakuna majibu yakueleweka!” Naya akajisikia vizuri sana. Akajiegemeza kidogo.

“Uuuuu! Unaona Mungu alivyo wa ajabu? Umeona jinsi ulivyotoa wazo zuri leo?” “Nimefurahi kama hata wewe umekubaliana na mimi Joshua.” “Nikwambie ukweli Naya?” Naya akatingisha kichwa kukubali. “Umefikiria vizuri sana, hakika sikutegemea kama kwa muda mfupi vile ungeweza kufikiria jambo zito vile na kuliweka kwa urahisi vile! Umenifanya nijivunie sana kuwa na wewe.” Naya akacheka huku akifikiria.

“Nikwambi Joshua, hizo zilikuwa moja ya ndoto zangu ambazo sijui niseme zimekufa?” “Tukae kidogo. Au baba atakasirika?” “Anajua nipo kazini. Hamna neno.” Wakawa wanaelekea ofisini kwa Joshua. Ilikuwa mara ya kwanza kwa Naya kwenda huko. “Utaniruhusu nikae kwenye kiti chako?” Joshua alicheka sana. “Nataka upako wako.” “Sasa si uuchukue hapa nilipo?” “Nataka kila mahali. Na mimi nikalie kiti cha Joshua Kumu.” Joshua akazidi kucheka.

“Niambie. Ni ndoto gani hiyo unafikiri imekufa?” “Nilikuwa nimefikiria kufanya biashara ya sabuni. Nikamshirikisha hilo wazo Malon. Mpaka jina nilikuwa nimepata. Nika...” “Jina gani?” “Nilifikiria MaNa. Hiyo sabuni iitwe MaNa. Kwamba ilianguka kutoka jangwani na...” “Naya unaakili yakufikiria wewe! Japokuwa nimeelewa ni kifupisho cha majina yenu, lakini hiyo akili yakufikiria MaNa, na kuinganisha na MaNa, chakula kilichoanguka jangwani na kulisha wana wa Israel WOTE! Inamaana hiyo MaNa, kama sabuni, ingeunganishwa na ahadi za Mungu, ingeanguka mpaka vijijini!” “Naona wewe umenielewa zaidi Joshua. Nilitaka iimbwe mtaani kama ile sabuni ya Komoa ilivyoimbwa na kila mtu, kisha kuhakikisha inamfikia mtumiaji bila shida."

"Halafu Joshua. Kuongezea katika nilichosema pale kwenye kikao. Najua wewe ndiye umeanzisha zile soda za chupa ndogo kabisa. Niseme nimeambiwa. Ulianzisha vile visoda vidogo kwa bei ndogo ili kila mtu aweze kumudu kununua bidhaa zetu. Si ni kweli?” “Ndio wazo langu la kwanza hapa. Na waliuza, mpaka wakabaki kunipigia simu kunipongeza. Na nikuibie siri tu, vile visoda vidogo, vina faida kubwa kuliko haya machupa makubwa.” “Kweli?” “Kabisa. Na kuna mkakati mwingine nipo kwenye kuusimamia huo, mpaka wanakuja kufunga hiki kiwanda. Au vizazi na vizazi watakuja kuambiwa Joshua Kumu, alipita kwenye hii ofisi na nikaitendea haki.” Naya akacheka sana.

“Mimi mwenyewe najivunia wewe!” Joshua akacheka sana. “Na hivi hukuwahi kuwa na mwanamke hapa! Basi umaana wa Naya umeongezeka mara dufu.” Joshua akazidi kucheka. Akamfungulia mlango Naya akaingia. “Mungu wangu Joshua! Ndio una ofisi nzuri hivi!” “Karibu.” Naya akabaki akishangaa. “Daah! Ndio maana hata ukifikiria mawazo yanakuja masafi. Sio kama sisi kule utafikiri tunafanya kazi stoo!” Joshua alicheka sana. “Kweli. Tuna maboksi ya kila matangazo.” “Uwe unakuja huku kupumzika.” “Mwenzio nimeamini kweli Jamal ananitegemea. Wakishindwa kazi zao, ananiomba nifanye mimi.” “Sasa na yeye asikufanye mtumwa.” “Mwenzio napenda. Anazidi kuniheshimu.” “Nilikwambia Jamal huwa anaheshimu watu wanaostahili kuheshimiwa. Ukiwa hovyo, hawezi kukuheshimu. Kila mtu anamfahamu alivyo mkorofi.” Naya akacheka kidogo na kutulia kama anayefikiri.

Joshua akatulia. Akajua anataka kumwambia kitu alichomwandikia kwenye ujumbe. Akakaa kabisa na kutulia kabisa. Akamuona anaanza kuingiwa hofu kama anayetaka kugairi. “Tafadhali niambie Naya. Usigairi.” “Umejuaje!?” “Niambie.” Joshua akaweka msisitizo akionyesha kama na yeye ameanza kuingiwa hofu na anachotaka kuambiwa. “Niambie chochote kile unachokifikiria.” “Nahofia unaweza kusema sio kweli, pengine nimepatwa tu na tamaa!” “Mimi sio mtu wakutoa hukumu kwa mtu kwa haraka. Usiogope.” “Najua nimekuwa karibu na wewe hata siku saba hazijatimia. Halafu ni kama wewe ndio ulionekana kunifahamu zaidi mimi kuliko...” Naya akasita. Akavuta pumzi kwa nguvu na kuzishusha taratibu kama anayejaribu kutulia kwa hofu.

Akamwangalia Joshua. “Au labda nitakuja kukwambia wakati mwingine.” “Hapana Naya. Tafadhali niambie.” “Ninachotaka kusema, umezivuta hisia zangu kwa namna ya tofauti sana. Haikuwa hivi hata nilipokuwa...” Akasita. Akatulia kwa muda akiwa ameinama, kisha akaendelea. “Nakupenda Joshua.” Akamuona Joshua amefunga macho na kucheka kwa mbali. “Asante Mungu wangu.” Akamsikia akiongea vile akiwa amefunga macho. Naya akashangaa. Akavuta pumzi kwa nguvu na kurudisha kichwa nyuma kabisa akakilaza kwenye kiti alichokuwa amekalia akiangalia juu lakini amefunga macho.

Akatulia kidogo kisha akavuta kiti mpaka pale alipokuwa amesimama Naya, akamshika mikono yake yote miwili. “Huo upendo uliosikia kwangu. Hata kama sasa hivi upo kama mawingu. Kwako haujaleta maana yakueleweka. Huo ukiri tu. Nilikuwa nikiusubiri kwa hamu mno ili nimlilie Mungu wangu, aukuze. Kutoka kwenye mawingi mpaka iwe mvua yakukata ukame ndani ya maisha yangu yote niliyoishi hapa duniani. Hujui ni kiasi gani nilivyokuwa nikimlilia Mungu aniunganishe na mwanamke atakayenipenda mimi kama Joshua sio wadhifa nilio nao sasa hivi.”  “Sasa unaniaminije mimi? Pengine na mimi ni wadhifa wako tu!” Naya akauliza kwa upole.

“Namjua mwanadamu kwa kumsikiliza na kumuona. Kwa kuwa nilikwambia naanza kusikiliza na kuona kwa kupitia macho ya ndani kwanza kabla ya haya ya nje ambayo dunia imeshayaharibu wakati mwingine ni ngumu kutambua kwa macho haya ya kawaida. Nakwambia nilichokuwa nikimuomba Mungu ni huo ukiri tu, kutoka kwako. Nilikuwa nikitamani jinsi unavyomzungumzia Malon! Ilionekana unahisia kubwa sana kwake mpaka nikaanza kupatwa na wasiwasi kama nitaweza kupenya kwenye moyo wako! Hukuwahi hata kuropoka au kunidanganya kama unanipenda Naya. Hata nilipokuwa nikikuwekea mazingira useme jambo tu, japo kunionyesha unaelewa ninachokwambia, hukusema.” Naya akajisikia kuumia kusikia hivyo.

“Wapo wengine nikiwanunulia tu chakula. Hata kama tupo kwenye shuguli za kikazi, tayari wanaanza kumsumbua Jema awaunganishe na mimi kuwa wananipenda. Lakini haikuwa hivyo kwako. Nikawa nikimwambia Mungu, hata uropoke tu, ning’ang’anie hapohapo magotini, lakini ukawa kimya. Nimefurahi sana Naya. Asante. Hata kama bado hujanielewa vizuri, nakuombea Mungu akufungamanishe na moyo wangu.” Naya akajisikia kumpenda zaidi Joshua.

“Unaweza usinielewe Naya, lakini ujue nilikuwa nikikusubiri uje kwenye maisha yangu. Ninashahada tatu. Kazi ambayo nipo kiwango cha juu sana kwenye taaluma yetu. Najua unajua jinsi ninavyolipwa maana kila mtu anaimba mshahara wangu mpaka kero!” Naya akacheka taratibu maana na yeye aliambiwa huo mshahara wa Kumu, ikawa ndio habari ya kwanza kuisikia alipoingia hapo kwenye hiyo kampuni. “Basi ujue ni wewe tu ndiye niliyekuwa nikikisubiri, ndio maana unaniona mwenzio sipotezi muda. Najua wewe ni wangu. Nimethibitisha, ndio maana nilikwambia nakusubiri, nikitaka uelewe kuwa mimi nimeshamaliza. Ni wewe tu.”

“Nilielewa Joshua. Lakini pia ukumbuke sikuwa nakufahamu, halafu nilitoka kwenye mahusiano magumu. Bado nilikuwa na hofu. Lakini jinsi ulivyofanya kwangu, umeonyesha urahisi wa mambo! Mpaka umenishangaza!” “Ni kwakuwa sidhani kama ilikusudiwa na Mungu iwe ngumu Naya. Naona binadamu ndio tunafanya mahusiano kuwa magumu mpaka watu mliowahi kupendana sana, mnageuka kuwa maadui!” “Kumbe na wewe umeona?!” “Haikukusudiwa kuwa hivyo Naya. Tuache upande huo, nataka ujue umenifurahisha sana. Leo nitalala tena kama mtoto mchanga.” Naya akacheka akimtizama vile anayomaanisha.

“Twende nikusindikize kwenye gari yako, ili urudi nyumbani. Tutaendelea kwa simu.” “Sasa na wewe unaondoka saa ngapi?” “Naona tuongozane na mimi nikapumzike. Nilikupa asante wa mchango mzuri uliotoa?” “Si ndio kesho unakwenda kunipongeza?” “Hapana. Kesho namtoa Naya mpenzi wangu, sio mfanyakazi wa kampuni ya Coca. Wasinitanie kabisa.” Naya akacheka sana. “Waache wakupongeze kama kampuni, na mimi nikafurahie na mpenzi wangu.” Akamuona anafikiria kidogo.

“Duuh! Siamini kama na Joshua naye anampenzi. Usije tu kubadilika Naya.” “Si mimi Joshua. Kwa kuwa nimekwambia leo nakupenda wewe, hutanisikia na mwanaume mwingine, labda uniache kama alivyofanya...” Naya akanyamaza. “Sijui kubadika Joshua. Mimi si muhuni. Na sina tamaa. Nikiwa kwako ni kwako mpaka utanihurumia kama wewe ni mwanadamu mwenye utu, halafu ukinitesa, au ukiwa unaniumiza moyo wangu. Wewe ni mtu wa pili kukwambia nakupenda. Nakuomba uwe wa mwisho Joshua. Tafadhali usije nibadilikia.” Naya akaanza kulia.

“Mpaka najiona ninamkosi Joshua. Unakuwa umetulia, lakini hupati mtu anayethamini hilo. Unamridhisha mtu kwa kila namna na bado!” Joshua akamshika tena mikono yote miwili wakiwa wameshafika nje. “Mungu ameniagiza, nikupende wewe kama Kristo alivyolipenda kanisa na kujitoa kwa ajili yake. Nitajitoa kwako Naya, na Mungu anisaidie. Kabla sijafikiria kukuumiza wewe, ujue mimi nitakuwa nimeumia zaidi. Na mimi nilikwambia sikujaliwa tamaa na visivyo vyangu. Ila vilivyo vyangu, utavitambua kama ni vyangu.” Naya akatingisha kichwa kukubali.

“Basi wahi, na mimi nikiingia tu kwenye gari nitakupigia. Usisahau kuweka bluetooth. Usishike simu wakati ukiendesha na tafadhali kuwa makini, Naya.” Tayari giza lilishaingia. “Nitakuwa makini.” Naya akacheka na kumuachia mikono. Akachukua funguo za gari ya Naya mikononi kwake wakati akijifungulia mlango. Akamfungulia yeye mlango, Naya akapanda. Akamfunga mkanda kabisa ndipo akamkabidhi funguo na kumsaidia kufunga mlango. “Asante.” Joshua akacheka taratibu akimtizama. Naya akawasha gari, akampungia mkono, nakuondoka.

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

Joshua Kumu ameingia pichani kwa nguvu zote tena kivingine. Ndani ya juma moja tu, amepata ukiri hadimu wa Naya, na kubadilisha moyo wa Naya vilivyo. Usikose siku ya jumamosi ambayo Joshua alisema alikuwa akiisubiria kwa hamu sana hata kabla hajazungumza na kuanzana na Naya mwenyewe. Huko ndipo amemuahidi Naya atamfahamu Joshua Kumu halisi. Ipi historia yake na yeye? Naya anakwenda kuketishwa na wakuu!

_ Njama ambaye alimtongoza Naya wa kwanza, anaonekana na hasira pamoja na Wivu. Amebakia akitumwa kwa Naya, na huyohuyo Joshua. Wanasema hakuna vita mbaya kama vita ya mapenzi.

Usikose muendelezo.

CONVERSATION

0 Comments:

Post a Comment