Naomi Simulizi |+1 205 767 8163 |naomisimulizi@gmail.com MAPENZI&PESA! – SEHEMU YA 19 - Naomi Simulizi

MAPENZI&PESA! – SEHEMU YA 19

 Jumamosi Ya Naya na Joshua.

Jumamosi Ya Naya na Joshua.

Jumamosi asubuhi Naya alikwenda kazini kama kawaida. Akajikuta wa kwanza vilevile. Hakukosa kazi. Akaanza bila kutumwa na Jamal. Akafanya kazi mpaka saa mbili kasoro wakaanza kuingia wenzie. Ilipofika saa mbili na dakika tano, wakiwa wafanyakazi wenzie wapo hapo, wakamsikia Jamal na viongozi wenzie wanakuja wakishangilia na kubishana. Ile kelele ikaendelea kuja mpaka wakaingia pale ofisini. Mpaka Njama alikuwepo. “Eti Naya! Naya!” Naya akageuka. “Aliyekaribia jibu lako kati yetu ni nani?” Ikabidi tu Naya acheke. “Sema usiogope ili tujue anayerudi leo shamba akalime  nani, atupishe mjini tufanye kazi ya masoko sisi.” Jamal akasisitiza wote wakisubiria. “Na sio umpendelee Jamal kwa kuwa ni bosi wako.” Naya akazidi kucheka akishindwa kujibu kwa hofu.

“Haya Njama, ondoa kiwingu chako hapo na hiyo timu yako wote, Naya afanye kazi.” Wote wakashitukia Joshua amesimama nyuma kwenye sehemu ya kuingilia hapo. “Ni mambo ya kazi tu.” Akajibu Njama lakini akiondoka. Naya akachungulia katikati ya waliokuwa wamesimama pale mbele ya meza yake, macho yakagongana na Joshua. Akamfanyia ishara kumuita, akimtaka amsogelea kwa haraka. “Kwema lakini Kiongozi?” Jamal akamtupia neno wakati akipita. “Ni asubuhi sana kwa mabishano Jamal! Hudhani hivyo?” “Mimi nilikuwa namshauri Njama, kazi za mjini zimemshinda, arudi shamba tu akalime, aachie meza kwa wanaoweza kuitumia, nashangaa Njama ananigeukia mimi, eti mimi ndio natakiwa kuwahi shamba wakati Naya alisema kabisa, jibu lake limeendana na langu!” Joshua akacheka na kumpita Jamal kwenda kwa Naya.

“Leo unanukia tofauti Joshua!” “Daah! Nimebadili pafyumu kwa ajili yako Naya!” Naya alicheka mpaka akainama. “Kwa nini!?” “Mimi mpaka nikasema ile pafyumu ya mwanzoni pengine hujaipenda wakati mpaka Fina huwa ananisifia na ile pafyumu lakini sijawahi kukusikia hata ukiongelea kama nanukia!” Naya alicheka sana. “Joshua wewe!” “Kweli. Nikaona kwa nini nijitese! Nimeanza kutumia nyingine ili tu uipate harufu nzuri.” “Pole Joshua. Naipenda ile pafyumu pia. Inanukia vizuri, imetulia mpaka kwenye gari unaloendeshwa pia ipo harufu yako. Na nimeipata hiyo harufu hata ofisini kwako jana usiku. Nzuri sana.” “Sasa ipi ndio ipi?” “Zote nzuri.” “Daah! Kumbe nisingehangaika! Yaani hii nimeifuata asubuhi hii ndio maana nimechelewa kuingia kazini.” “Jamani Joshua! Pole.” Naya akashangaa sana asiamini kama Joshua anajali vile anavyomuona. Naya akasimama na kwambia asogee.

Joshua akacheka akijua anataka kumnong’oneza. Na kweli. “Napenda kila kitu chako. Kuanzia utosi mpaka unyayo. Hakuna kitu natamani kibadilishwe kwako, Joshua. Nakupenda hiyo ulivyo. Wewe ni zaidi ya ningeomba Mungu anipe. Upo zaidi ya maombi yangu.” Kisha Naya akambusu shavuni. Joshua akafunga macho na kupumua kwa nguvu. Naya akacheka taratibu. Akafungua macho na kumkuta Naya akimwangalia. “Kwa hiyo sihitaji kujenga misuli?” Joshua akauliza kwa sauti ya chini sana lakini Naya alimsoma midomo yake akaelewa na kushangaa sana.

Ndipo akakumbuka ile ni harufu ya pafyumu ya Malon. Akakumbuka Joshua alimuona Malon vile alivyo, kifua kikubwa, mikono ya misuli, ndio akili zikamjia Naya kuwa anataka kumuiga, ajibadilishe awe kama Malon. Naya akakunja uso akitingisha kichwa kukataa kabisa. “Hapana Joshua! Hata kidogo! Na isiwe kwa ajili nyingine yeyote ila kupenda kwako wewe na unao muda. Mimi nakutaka hivyo ulivyo.” Akamuona kama amepata aghueni.

“Nakupenda Joshua.” “Unafikiri baba Naya na kaka zako watanipokea?” Naya akamcheka na kushindwa kujizuia. “Kweli unanicheka Naya?” “Kumbe ndio hofu yako hiyo?” “Acha basi kucheka Naya!” Wakajisahau kama wapo mbele za watu. Na Joshua ni kiongozi mkubwa sana hapo, na anaheshimika. “Naya?” “Acha nifurahi kwanza.” “Ujue unapoteza muda wa kazi, Naya!” “Mimi mwenzio nimemaliza kazi zote za leo, tokea saa mbili kamili. Hapa namsubiria Jamal anipangie nyingine. Acha nifurahie..” “Hofu yangu?” Akamalizia na kumfanya Naya azidi kucheka. “Sawa bwana!” Joshua akawa anaondoka Naya akazidi kucheka. Mwishoe akamkimbilia koridoni.

“Pale nyumbani, wanachotaka niwe na furaha tu. Kwanza familia yetu ni ya kawaida mno. Hawana makuu. Ila baba ni mkimya mno kama Zayoni mdogo wetu wa mwisho na wamefanana. Mimi na Bale, ni kama tulizaliwa mapacha. Tunafanana mpaka kidole kidogo cha mguu, na tupo kama mama, mpaka urefu na hii rangi yangu ya mwili. Angalau mimi na Bale ndio huwa utakuta tunazungumza na kuleta fujo pale ndani, ila si Zayoni. Zayoni mpole sana na mkimya.” “Na baba Naya?” “Wewe si unajua kusoma watu?” “Sana.” “Basi si baba Naya. Mimi najua mabadiliko yake kwa jinsi atakavyonitizama. Na ni kwakuwa nimekua mikononi mwake. Tena wakati mwingine unaweza usijue kinachoendelea ndani yake mpaka aamue kuzungumza. Mkimya wa kupitiliza.”

“Kulikuwa na Joshua mwingine. Yeye mama alimpenda, akataka niolewe naye.” Naya akamsimulia juu ya Joshi kwa ufupi sana, Joshua akabaki haamini. “Haiwezekani Naya.” “Nikikwambia nimepita Joshua, amini nimepita kwenye safari ya mapenzi. Naona Mungu amemuhurumia baba yangu na kuamua kukuleta kwangu. Baba alikuwa akiniombea sana. Nikikwambia sana, mpaka kufunga na kuomba akimsihi Mungu aingilie kati swala langu la mahusiano, akihofia nisije nikaangukia kwa mwanaume asiye sahihi sababu ya pressure ya mama, nafikiri na Malon pia alichangia. Nakumbuka siku moja nikiomba naye, baba alilia akimsihi Mungu anitetea na kumkatalia shetani kuwa mimi sio kiwanja chake chakuchezea. Au kufanyia mazoezi. Niliumia sana Joshua. Sana.”

“Lakini turudi kwa haiba yake. Katika yote hayo, baba hakumsemesha Joshi mpaka aliponiacha mjini. Wakati mwingine kabisa ile nilikwambia aliniletea makaratasi ya chuo cha huko nje ya nchi, ndipo baba alimwambia maneno machache tu.” “Alimwambia nini?” “Alimwambia siku aliponiacha katikati ya jiji, tena usiku, alifanya kosa kubwa sana. Akamwambia ni heri angempigia simu, aje anifuate baba mwenyewe, kuliko kunitelekeza. Hivyo tu. Basi. Ila vinginevyo baba ni mtu mzuri sana. Usigope hata kidogo. Ila usile, Bale anaandaa chakula cha mchana kwa ajili yetu wote.” “Bora umeniambia.” “Acha mimi nirudi kazini. Nimefurahi umekuja kuniona.” Joshua akacheka na kuondoka. Naya akarudi kuendelea na kazi.

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

Mchana Naya alitoka na kurudi nyumbani moja kwa moja.  Joshua alimwambia na yeye ni lazima arudi nyumbani, ajiandae kwa safari yao kabisa ili wakitoka nyumbani kwao, waende huko alikopanga kumpeleka Naya. Naya alifika nyumbani akakuta nyumba safi, kumepangwa vizuri mpaka meza iliwekwa kama hotelini, wakatoa vyombo vizuri vya mama yao. Na kunanukia harufu nzuri ya chakula. Na kwa kuwa Naya alishamwambia Bale kuwa huyo Joshua anampishi maalumu wa kumpikia, Bale naye akahakikisha anatendea haki huo mlo.

“Nawashukuru sana. Asante Bale. Asante Zayon. Na baba umependeza sana. Wote mmependeza, mpo wasafi.” “Wote tulienda kunyoa nywele.” Zayoni akaongea, Naya akacheka. “Asanteni sana. Joshua atafika hapa baada ya lisaa. Na mimi nataka nijiandae ili akija anikute tayari. Tule, tuondoke.” Bila kusubiri jibu, Naya akakimbilia chumbani kwake. Bafu lilikuwa moja tu nyumba nzima. Wakamuona anatoka kwenda kuoga akikimbia. 

Joshua Ukweni.

Baada ya lisaa wakaona gari nzuri sana inaingia hapo. Naya alikuwa kwenye simu akimuelekeza mpaka akafika. Akatoka kwenda kumpokea. Akashuka akiwa na chupa ya kinywaji mkononi. “Naya wewe ni mtaalamu! Angalia jinsi ilivyopendeza!” “Kweli Joshua au unanitia tu moyo?” “Labda uniambie kama sijapendeza. Lakini mimi nimependa mno. Katika kuvaa, nisingekudanganya Naya. Mimi napenda kuvaa vizuri na huwa najua vitu vizuri.” Naya akacheka. “Na wewe umependeza sana. Isingekuwa ni wewe, kweli ningekusahau.” Naya alicheka sana. Joshua akamsogelea pale karibu na mlangoni maana alianza kuongea tu aliposhuka garini.

“Kweli umetutendea haki. Na nimependa hii linen. Safi sana. Kuanzia leo hii ndio itakuwa kazi yako. Kuhakikisha tunatoka vizuri.” “Kweli Joshua?’ “Kabisa.” Naya akacheka. “Sasa hiyo uliyobeba ni nini?” “Kinywaji tu.” Naya akampokea na kumshuru.

“Karibu nyumbani kwetu. A humble home. Karibu sana.” “Asante kwa ukaribisho.” “Twende nikakutambulishe kwa baba Naya.” Joshua akacheka. Akamshika mkono wakaingia ndani.

“Baba, nimekuletea Joshua.” Joshua akacheka huku akimsogelea kwa heshima. “Sijui kama unanikumbuka?” “Nakukumbuka sana.” Wakapeana mikono. “Shikamoo mzee wangu.” “Marahaba Joshua. Naona mmevaa vyakufanana.” Joshua akacheka. “Kazi ya Naya hii. Mungu amempa kipaji cha ajabu sana. Acha nikuibie siri.” Akaanza Joshua wakiwa bado wamesimama.

“Jana. Yaani jana tu jioni. Ile kampuni imemfahamu Naya ambaye hawakuwahi kumfamu kabla. Sijui kama amewasimulia?” “Siku hizi kumpata Naya nishida! Anakuwa chumbani muda wote.” Naya akacheka na isivyo kawaida wakashangaa anajificha nyuma ya Joshua kwa cheko la furaha na aibu na si kwa baba yake. Wote wakacheka, Joshua alipomchungulia kule nyuma yake. “Kulikuwa na kikao jana.” Joshua akaendelea. “Cha viongozi wa ngazi ya juu wa kitengo chetu cha masoko na watu wengine baadhi nilitaka wawepo kutoka idara ya stoo. Nilijua Naya ameshaondoka kurudi nyumbani. Katikati ya kikao nikapata ujumbe wake ndipo nikajua yupo pale kazini. Nikaomba kumuona. Kufupisha habari akajikuta ameishia kuwa kwenye kile chumba cha mkutano.” “Nikakalia kiti cha Joshua Kumu.” Naya akaongeza wote wakacheka.

“Tulikuwa tumekwama kwenye swala fulani la kikazi. Tulikaa hapo muda wote, hakuna mtu aliweza kutoa jibu nikaridhika na mimi nilitaka kufika alhamisi niwe nimefanikisha jambo fulani. Kama utani tu. Nafikiri ulikuwa wakati wa Mungu kujipatia utukufu kupitia Naya au ulikuwa wakati wa Naya kung’aa. Nikataka na yeye atuambie ni kwa nini tuko pale na tumekwama wapi. Baada ya wote kukwama, nikamuuliza yeye, akiwa tena amekaa pembeni kabisa. Na nilimpa ipad yangu aandike, lakini nikiwa najua itamsaidia kusogeza muda wakati akinisubiria.” Wakamuona Joshua akicheka.

“Naya alijibu ile hoja, mpaka nikahofia pengine wangefikiri nilishazungumza naye, nikampa yale majibu.” Wakacheka wote. “Kweli Joshua. Na mimi niliwaza hivyo hivyo.” “Lakini uzuri uliponiambia upo ofisini, nikashangaa na kumuuliza Jamal, kuwa Naya anafanya nini ofisini mpaka sasa na huwa ngazi za kina Naya hawalipwi overtime! Akanijibu kwa kujigamba tu, kuwa ndio nielewe anaposema safari hii amepata jembe, ndio hivyo. Kwamba Naya ni  jembe ambalo halibakishi jani.” “Acha masihara Joshua! Jamal?” Naya akashi

 “Hakika alisema tena kwa sauti bila kuogopa mbele yetu wote na wale watu wa stoo walikuwepo. Wakadhania anaongea vile kwa sababu nilikuwepo, anakusifia tu. Sasa ulipokuja pale, bila mimi kuweka mipango, na ukajibu vizuri vile, ilikuwa kero kutoka kwa Jamal. Alipiga kelele pale. Nasikia akaendeleza yeye kikao, akisema yale uliyozungumza wewe ni kwa niaba ya kitengo chenu. Acha ajibebee utukufu, ndio maana leo asubuhi walikuja kubishana pale mezani kwako.” Naya akacheka kwa furaha.

“Ninachotaka kusema ni kuwa, una binti mwenye akili sana. Za kufikiria kwa kiwango cha juu sana. Jana mimi nilijivunia kumfahamu Naya.” Wakacheka. “Nashukuru kunikaribisha. Naamini wewe ni Zayoni.” Akampa mkono na kumsalimia. “Na wewe ndiye pacha wa nje wa Naya, Bale.” Wakacheka. “Kweli mmefana sana. Kama mapacha!” “Karibu sana Joshua. Hapa ndio nyumbani kwetu.” Bale akamkaribisha kwa heshima zote. “Nashukuru sana.” Wakapeana mikono. “Naya ameniambia upo hapo chuo kikuu cha Mlimani.” “Namalizia mwaka wa mwisho. Tupo ukingoni kabisa.” “Hongera sana.” “Naya ameniambia na wewe umemaliza shahada yako ya tatu.” Joshua akacheka na kumtizama Naya.

 “Ndiyo, lakini mimi nilianzia chuo kuanzia ngazi ya chini kabisa, certificate.” Wote wakashangaa. “Joshua! Sikujua!” “Ndio maana nakwambia namfahamu Jamal. Alikuwa kiongozi wetu chuoni. Mkali hivyohivyo. Lakini wakati Jamal anafanya advance diploma, mimi ndio nilikuwa nikisoma mwaka mmoja, tena mambo ya stoo tu nikiwa na matokeo yasiyo mazuri ya kidato cha nne. Ndipo nilipokutana na Jamal. Nimepambana mpaka kupata hizo shahada tatu.” “Ndio maana Jamal alikwambia uache kusoma sasa, unawatia ubaya!” Joshua akacheka. “Kumbe unakumbuka?” “Nakumbuka. Wakati tukitokea Mbeya.” “Basi ndio hivyo. Na wewe Zayoni?” “Na mimi najiandaa kumaliza darasa la saba.” “Vipi lakini?” “Ninauhakika nitafaulu tu.” Wote wakacheka. “Saafi sana.” Joshua akampongeza.

“Joshua ameleta na hiki kinywaji.” Naya akaingilia. “Asante sana.” Baba yake akashukuru. “Kuna vitu vingine kwenye gari, labda tutasaidiana na Bale kutoa.” Naya akakunja uso akimshangaa huku akicheka. “Umeleta nini tena?” “Vyakula tu.” “Usinge hangaika Joshua!” “Ni kweli, usinge hangaika.” Akaongeza baba Naya kwa Naya. “Sio usumbufu hata kidogo mzee wangu. Nimefurahi mmenikaribisha. Kwangu huu ni muujiza, nyinyi mnaweza msielewe. Lakini...” Wakamuona amepoa. “Nashukuru mmenifungulia milango ya nyumbani kwenu. Nashukuru sana.” Naya akamshika mkono. “Karibu. Na sisi tumefurahi umekuja.” Joshua akamwangalia na kumrudishia tabasamu. Pakatulia. Naya na Joshua wakiangaliana na wengine wamebaki wamesimama.

“Labda tungekaa mezani. Naya alisema mna safari.” “Ni kweli.” Akajibu Joshua. “Mmependeza sana. Niwapige picha kabla hamjala?” Akaanza Zayoni. “Mimi ni mpiga picha mzuri. Naya anajua.” Wote wakacheka. “Kweli Zayoni ni mpiga picha mzuri.” “Basi acha nikupe simu yangu ili nibakiwe nazo mimi. Ndio nitawatumia.” “Nitatumia na kamera yangu pia. Naya alininunulia.” Zayoni akakimbilia ndani. Akatoka na kuanza kazi ya kuwapiga picha Naya na Joshua. Kwa hakika walipendeza, kisha akamwambia na baba yao aungane nao, pamoja na Bale. Kisha akategesha kamera na yeye akaongezeka.

“Kweli wewe mtaalamu.” Joshua akampongeza. “Basi Naya atakuletea na za kwangu ni kiprinti ili uone.” “Hapo utafanya vizuri. Na ikiwezekana uniwekee kwenye albumu kabisa ili iwe kumbukumbu yetu.” “Sawa. Nitafanya hivyo.” Zayoni akaafikiana naye.

Wakakaa mezani wote watano. Naya akamsaidia kumpakulia. Hilo nalo likamfurahisha sana Joshua. “Asante sana Naya. Nashukuru.” Wakaangaliana wakati Joshua akishukuru. Wakaanza kula. “Kweli Bale unajua kupika vizuri sana.” “Asante. Mama alinifundisha tokea mdogo zaidi ya Zayoni. Nafikiri sababu yakupenda kumfuata kila mahali. Michezo yote nilikuwa nikicheza karibu yake, nafikiri ndio maana nikajua mambo mengi ya jikoni.” “Saafi sana. Hii ni ajira ya mtu kabisa!” Bale akacheka wakaendelea kula.

“Wewe Joshua wazazi wapo wapi?”  Akaanza baba Naya. Joshua akameza kwanza. “Kwa jibu fupi tu, ni kwamba walifariki. Nikiwa mdogo tu.” “Pole sana. Kwa hiyo ulilelewa na ndugu tu?” Joshua akacheka na kuinama kama anayefikiria. Kisha akacheka tena. “Hapana mzee wangu. Mama alipofariki nikiwa ndio nimemaliza kidato cha nne tu, ndugu wa upande wa mama, ambako ndiko nilikokuwa huko nikimuuguza mama mpaka kifo chake, walinitaka niende kwa baba yangu ambaye na yeye alikuwa na familia yake. Nilikuwa mtoto ambaye familia yake hata hawakuwa wakinifahamu kuwa nipo.”

“Kwa hiyo nilikwenda wakati mbaya. Baba naye alikuwa akiugua, walijua asingepona. Uwepo wangu pale kwa wakati ule ukatafarisiwa nipo pale kwa ajili ya mali. Kwa hiyo mkewe baba na watoto wake, hawakutaka kabisa niishi pale. Sidhani hata kama nilimaliza mwezi, na wao wakanifukuza rasmi.” “Pole sana Joshua.” Naya akamuhurumia, akamshika mkono ambao hakuwa akitumia kula. Joshua akamwangalia na kucheka. “Asante.” “Pole sana Joshua.” Na Zayoni pamoja na baba yake wakampa pole.

“Si ungerudi kule kwa ndugu wa mama?”  Akauliza Zayoni akimuhurumia Joshua. “Nilifanya hivyo Zayoni, lakini nako nilikuta milango ilishafungwa. Sikupokelewa. Nilimwambia Naya, kwangu mimi Mungu siye wa kwenye bibilia au Mungu anayekaa kanisani. Hapana. Kwangu Mungu ni baba kama hivyo Zayoni unavyomuona baba Naya. Amenitoa kwenye hatari nyingi sana mtaani. Ikiwemo hatari ya kutaka kubakwa, kuuwawa kabisa kwa kuwa nilikuwa nikiishi mtaani tu. Niliteseka sana mpaka alipoona yeye inatosha, ndipo akaninyanyua na kunipa sehemu ya kuishi.” Wote walipoa wakimwangalia.

“Nilifika mahali, nilibakiwa na Mungu tu. Nazungumza naye kama hivi nyinyi mnavyozungumza hapa ndani. Sikuwa na mtu wala kitu. Pesa aliyonipa baba kwa siri wakati nafukuzwa nyumbani kwake na mkewe na watoto wake, ndizo zilizonisaidia kulipia hicho chuo cha mwaka mmoja. Nikasomea mambo ya stoo ambayo sikupata ajira. Ndipo nikarudi mtaani. Nikisema niliishi mtaani, namaanisha kulala nje kabisa. Huko ndiko nikakutana na mengi, lakini katika rehema za Mungu, nikapata kazi kwa mtu fulani. Kama mesenja tu.”

“Lakini Mungu ameweka ndani yangu kipaji kama cha Naya. Wakati namfanyia kazi yule mzee, nikijua kabisa kitu nilichosomea kitasumbua kazi, nikaanza kujifunza biashara yake. Kwa kuwa nilikuwa mtu wa kutumwa tu, nilikuwa nikiingia kila idara ndani ya ile ofisi. Ikanirahisishia kujua kinachoendelea kwenye ile kampuni. Ilikuwa ndogo tu.” Joshua akanywa kinywaji chake na kuendelea.

“Siku moja wakati nampelekea kahawa ofisini kwake, nikamwambia hivi, nina njia ambayo itamsaidia kubadili historia ya biashara yake. Lakini kwa sharti ya kwamba, anipe pesa ambayo nilishapigia mahesabu ni ada ya shule ya mambo ya masoko. Ila kwa miaka miwili sasa. Maana tayari nilikuwa na certificate. Kwa hiyo nikamtajia hiyo pesa yote. Akahisi kama nimechanganyikiwa. Nikafanya sawa kabisa na kama alichokifanya Naya jana pale kikaoni. Nikamtajia tatizo alilonalo pale kwenye ile kampuni. Nikamwambia ninayo suluhu sahihi kabisa la hilo tatizo la kampuni yake. Sitampa mpaka aiweke hiyo pesa kwenye akaunti yangu ya benki. Nikamuhakikishia sitaitumia mpaka afanikiwe. Na nikamwambia asipofanikiwa, nitarudisha pesa yote kama alivyoiweka.” “Joshua! Alikubali?” “Hakuwa na jinsi Naya. Maana nilimweleza mambo ambayo hata yeye hakuwa akiyajua. Sema na yeye alifariki miaka michache iliyopita, ila alikufa tajiri.” “Ulimsaidia?” Naya akauliza. Joshua akacheka. “Na yeye alinisaidia. Ndio ukawa mwanzo wakurudi tena shule.”

Joshua akaendelea. “Naya, sikuwahi kusoma kama kipindi kile. Hapo nikijua shule ndiye atakuwa mkombozi. Hakuna somo au mtihani ambao sikupata zote.” Wote wakacheka. “100?”  Zayon akauliza akicheka. “Kabisa. Nikisema kupata zote, namaanisha zote na si kwakukisia! Ni kwa kujua haswa. Na ndio kwa mara ya kwanza nikaweza kurudi kulala kitandani, baada ya karibia mwaka mzima wakuhangaika mtaani. Yaani kurudi kulala kwenye vitanda vya hosteli.” “Hostel!?” Naya akamshangaa. “Acha Naya. Nimelala mpaka msikitini mimi. Kanisani kwenye viti, tena kwa kujificha ili nisifukuzwe, maana sikuwa na jinsi.” Daah!” Bale akashangaa.

“Basi kuanzia hapo nilipomaliza hiyo miaka miwili, huyohuyo mzee akanisaidia kuniunganisha na kijana wake, alikuwa akifanya kazi benki. Na mimi nikapata hapo kazi kama Benk Teller tu. Wale wagawa na wapokea pesa. Lakini kile nilichokuwa nikijisikia ni kama hivi anavyosema Zayoni, nilijua kwa hakika mimi ni nani.” Zayoni akacheka.

“Nilijua kwa hakika pale napita tu. Si sehemu yangu. Na nikajua mimi ndio nina hatima ya lini natakiwa nitoke pale. Mnajua SWIFT?” Wote wakaangaliana. “Ni njia yakuhamisha pesa kimataifa. Sasa hivi nafikiri mabenki mengi sana wanayo. Sasa ile ni mimi ndiye mwanzilishi.” Wote wakamshangaa sana. “Hakika. Sijisifii, lakini ndiyo ilinitoa pale na kunisogeza kwenye kitengo cha masoko. Nilikaa pale nikipokea tu pesa huku nikihesabu kwa siku benki inapoteza kiasi gani cha pesa kwa wateja wanaokuja kuulizia hiyo huduma ya kutuma pesa nje ya nchi na kuambiwa hakuna, kisha wanaondoka na ile pesa. Nikaipigia mahesabu huku nikimuomba sana Mungu kwa kufunga na kuomba anipe kibali maana niliambiwa na mama, amenirithisha roho ya kukataliwa kama yeye. Sijui kama hicho kitu nyinyi mmeshakisikia.” Baba yake Naya akawa anajua anachozungumzia.

“Basi nahisi na mimi nilikuwa nayo hiyo roho. Nilifukuzwa na hata watu wanaopokea kila mtu! Ikabidi kupambana magotini nikimsihi Mungu anitetea. Nilipokamilisha uchunguzi juu ya SWIFT, nikaomba kikao na meneja masoko mkuu wa pale pamoja na wasaidizi wake.” “Kwa nini sasa?” “Sikutaka tuje kuwa wawili tu, halafu aje anigeuke baadaye aseme ni wazo lake. Sijui kama unanielewa?” “Unaakili wewe!” Wakacheka.

“Nilishawajua binadamu. Na mimi nilijua hiyo ndio tiketi yangu yakutokea ambayo Mungu amenipa, nilijua nikichezea tu, sitatoka. Wakiwa hawajui ni  nini nataka, ila tu kuwaambia jambo zito. Kiongozi wangu wa tawi akanilazimisha sana nimwambie lakini nilikataa kabisa. Nikaitwa makao makuu. Nikakuta mpaka wazungu wapo hapo. Bwana wakati wa Mungu ukifika, umefika tu. Halafu huyu Mungu, jamani haitaji jopo la watu kumsaidia kukamilisha ajenda yake.” Joshua akacheka na kutingisha kichwa. Akatulia kidogo. Wote kimya.

“Hapo nilikuwa nimeshafanyia mazoezi jinsi ya kuzungumza. Ilikuwa kila nikirudi nyumbani kutoka kazini, nafanya majaribio kuwa nimesimama mbele za watu wengi, nazungumza.” “Joshua!?” “Hakika Naya. Vile unavyoona naweza kuzungumza mbele ya watu kwa ujasiri, nikujifunza. Nilijifunza kuzungumza kingereza mimi mwenyewe kwa kuwa nilisomea shule za kawaida kabisa. Na kidato cha nne nilimalizia shule ya kijijini nikiwa nimerudi kumuuguza mama. Sikupenda vile walivyokuwa wakimuhudumia mama yangu. Nikaamua kurudi nyumbani kwao, nisomee pale ili tu kumsaidia.”

“Maana mama aliposhindwa kulipa kodi na mambo mengine mjini, akiwa mgonjwa akaamua arudi kwa wazazi kijijini, mimi akaniombea niishi kwa rafiki yake mjini ili nimalize shule. Nilipokuwa likizo nikaenda kumuona, sikupenda hali niliyomkuta nayo. Alikuwa mgonjwa halafu na masimango mengi mno. Nikaamua kubaki naye ili kumuuguza ndipo nilipomalizia shule huko. Kwahiyo kingereza unachosikia nakizungumza Naya, ningekijua wapi kama si Mungu kunifundisha?” “Aisee!” Naya akashangaa.

“Nilikuwa nakula mara chache sana sababu yakufunga na kuomba. Halafu nikirudi tu najifungia chumbani naanza kufanya mazoezi ya kuzungumza. Naweza nikarudia hoja niliyoandika hata mara ishirini kwa siku moja, nikiiongea kwa kichwa bila kusoma. Hivyohivyo huku nikijiambia siku Mungu atakaponifungulia tu mlango wakaniita kwenye kikao na kunisikiliza, hawataweza kukataa. Na kweli. Niliingia pale nikiwa sijala siku tatu. Nimefunga. Nilijawa ujasiri ambao haukuwahi kuondoka. Nilizungumza mpaka wote wakasimama nakunipigia makofi kama vile walivyokufanyia wewe jana. Kuanzia hapo maisha yangu yakabadilika. Kutoka ofisi moja kwenda nyingine nikinunuliwa kwa pesa nyingi. Ila nikajiambia siwezi kuishi maisha yakuomba omba kibali tu kwa Mungu, yaani kubahatisha bahatisha tu. Lazima nijiongezee thamani mimi mwenyewe. Kwa hiyo nikawa nasoma huku nafanya kazi, mpaka leo.” Wote wakabaki wamepoa. Joshua akacheka.

“Mimi ninaposema Mungu yupo, kwangu si msemo. Ni kwa kuwa nimemthibitisha, na nikajua kweli Mungu yupo. Yupo. Na ukimtaka atembee, anatembea. Kuna neno nilimwambia Naya, na ndilo najikumbusha kila siku kutoka kwenye bibilia kitabu cha 1 wakorintho 2 mlango wa 9.” “Hakuna jicho limepata kuona, wala sikio limepata kusikia, wala hayajawahi kuingia moyoni yale Mungu amewaandalia wale wampendao?” Baba Naya akaongea hilo andiko kwa kichwa kama lilivyoandikwa kwenye bibilia, tena kwa ufasaha sana mpaka Joshua akafurahi sana.

“Halafu Isaya 64:4 imemalizia ‘kwa wale wamngojeao’. Hakuna jinsi ukanitoa kwenye kumsubiria Bwana. Ilimradi nikijua yeye ndiye ameniambia nisubiri, hakika nitasubiri. Nilimwambia Naya, ndio maana wakati mwingine watu huniona kama nachelewa kwenye mambo fulani fulani, lakini huwezi kunitoa kwenye kusubiri, endapo Mungu ameniambia nisubiri.” Wakacheka.

“Nilimwambia Naya, nilipomuona mara ya kwanza, nusura nimkimbilie nimsalimie. Alikuwa amekuja pale kwenye usahili tu.” Wote wakacheka. Joshua akajua Naya alishawasimulia. “Naya amewasimulia eeh?” “Ndiyo.” Wote wakakubali. “Ilikuwa nusura nimkimbilie, lakini Roho akanionya kabisa na kunitaka nimuache. Nikiwa sijui kama atakuja kufanya kazi pale, lakini kulikuwa na tumaini kubwa sana moyoni mwangu. Ikatokea hivyo kama mara tatu. Nilipobahatika kukaa naye Mbeya, Malon naye akaja.” “Ni Zayoni huyo ndiye aliyemwambia kama nipo Mbeya.” Wote wakacheka. “Ulisema umenisamehe Naya!” Zayoni akamkumbusha dada yake. “Hapana Naya. Ulikuwa ni wakati wa Mungu.” Joshua akaingilia na kunywa kinywaji.

“Nikiwa nimekata tamaa. Maana Malon alituingilia, Naya akarudi chumbani kitu ambacho nilikuwa nikizuia kisitokee angalau mpaka niweze kuzungumza na Naya vizuri. Lakini Naya akawa ameondoka. Ametuacha mimi na Malon pale mgahawani. Sijui tena chakufanya!” “Pale nilikimbilia chumbani kumpigia simu baba ili nilie ndipo nilale.” “Naya!?” “Kweli. Ndiye anayenisikiliza nikilia. Sasa nifanyaje?” Joshua akacheka kidogo na kunyamaza kwa muda kama anayefikiria. “Huyo Naya ndivyo alivyo Joshua. Utamzoea tu. Kwanza ndio maana tulikuwa na hamu ya kukuona, mtu unayemfanya ajifungie chumbani muda wote akizungumza na asitoke hapa kwa baba! Wote tulitaka kukuona tukujue wewe ni mtu wa namna gani.” Joshua akalifurahia sana hilo. Akamwangalia Naya na kucheka. Naya akacheka na kuinama.

“Nikiwa nimekata tamaa ya kumuona tena, lakini akawa alishaniambia jambo zito mno. Mungu akatumia hilo aliloniambia. Akaliongezea uzito, ikawa kama amekamilisha kusudi zima la mimi kumfuata Mbeya. Kwa upande fulani nikaridhika kwamba angalau nimeweza kuzungumza naye, nikamjua moyo wake, lakini nikawa nikimlalamikia Mungu kuwa mbona hakunitengenezea mazingira tukapata muda mrefu kidogo?” Wakacheka.

“Sasa Jamal, kiongozi wake aliponifuata chumbani kumuombea mtu mmoja nafasi! Kwanza nikashangaa. Jamal atake kusafiri na mmoja wa watu waliopo chini yake! Tena nikacheka tu nikamuuliza ni nani huyo aliyebahatika kuombewa lifti na Jamal? Aliposema Naya, tena akawa akinielekeza akidhani simfahamu Naya. Nilimshangaa Mungu mpaka nikashindwa kuongea. Jamal alipoondoka, nilipiga magoti na kumwambia hivi Mungu, ‘wewe ni Mungu, badala yako hakuna mwingine, na wala hatawahi kutokea mwingine.’ hivyo tu tena kwa hofu kubwa sana. Nikasema lile andiko la Zaburi 37:23” “Hatua za mwenye haki huongozwa na Bwana?” Baba Naya akalisema  tena hilo andiko kwa muundo wa swali. Wote wakacheka.

“Sawasawa mzee wangu. Hapo ndipo Mungu akaniachia uwanja. Mpaka leo nimekaa hapa! Hakika ni Mungu. Hakuna jinsi ukaniambia vinginevyo nikaelewa, isipokuwa ni Mungu. Mimi Joshua, leo amenikalisha hapa! Nakula chakula na watu kama nyinyi! Wenye familia bora! Nipo hapa na binti kama Naya!” Wakamuona anatingisha kichwa na kucheka. “Hakika ni Mungu. Nilimwambia Naya, nimpaka apite nilipopita mimi ndipo atanielewa. Ndugu zangu, huyo ni Mungu tu. Na narudia kuwashukuru sana.” Wote wakaelewa vile Naya alivyosema anajua kujishusha.  Mpaka hapo akawa ameshauvuta na moyo wa baba Naya.

“Karibu sana Joshua. Ujisikie nyumbani. Naya anatujua. Hapa kwetu hatuna makuu. Hivi tulivyo ndio tumemaliza. Karibu sana.” Joshua akasimama na kumpa mkono baba Naya. “Asante mzee wangu.” “Karibu sana.” Wote walijua kama baba yao amefurahi. “Asante baba.” Wakamsikia Naya akishukuru kwa deko, mtoto huyo wa baba akajua baba yake amempokea. Wote wakacheka

“Basi nisirudi kukaa, naomba Bale unisaidie kama utaweza ili tuwahi kutoka na Naya.” “Bila shida.” Bale akasimama. “Mbona hujamaliza chakula?” Naya akamuuliza taratibu. “Inatosha. Asante sana.” Naya akabaki akisafisha pale mezani Joshua na Bale wakatoka kurudi kwenye gari ya Joshua hata Naya hakuwa akiifahamu. Kwanza hakuwahi kumuona akijiendesha. Ilikuwa gari mpyaa, hata kwa muonekano ilionekana safi. Wakaanza kuingiza vitu ndani mpaka baba yake Naya akasimama. “Naona hammalizi! Nisaidie?” “Tunamalizia mzee wangu. Pumzika tu.” Joshua akakazana hapo ukweni akajaza hapo sehemu ya kuingilia. “Asante Joshua. Tunashukuru.” Naya akatoka na kushukuru. “Karibu.”

Akamsogelea pale mezani na kumnong’oneza. “Si twende sasa? Au kuna kitu unataka nikusaidie ndipo tuondoke?” “Nimemaliza.” Joshua akamshika mkono na kusogea naye pale sebuleni alipokuwa amekaa baba yake Naya. “Nikuombe mzee wangu.” Baba Naya akawaangalia. “Naomba nitoke na Naya. Nitahakikisha anarudi salama.” “Hilo ndilo ombi langu Joshua. Hata mkishindwana huko, wewe nipigie tu simu, nitamfuata mwenyewe.” Naya akacheka taratibu nyuma ya Joshua. “Naamini hatutafika huko mzee wangu. Niombee tu niweze kuwa kile Mungu anatarajia niwe kwa Naya.” “Ninaomba sana tu. Nilianza mapema sana tokea Naya ana mwaka, nafikiri.” “Waw! Kwa hiyo umeona Naya, tupo salama.” Akamgeukia Naya. Naya akacheka.

“Asante sana mzee wangu. Tutaonana baadaye.” Wakatoka Naya akiwapungia mkono na cheko kubwa. Wakachungulia dirishani, wakamuona anamfungulia mlango. “Anamfunga mpaka mkanda!” Zayoni akashangaa. “Atakuona wewe Zayoni!” Wakacheka. “Naya anavyocheka! Sasa pale sijui anacheka nini!?” Bale akajiuliza ila kwa sauti ya chini. Baba yao alibaki amekaa tu. Lakini wazi alionyesha kufurahi. 

Joshua & Naya.

“Tunakwenda wapi kwanza?” “Moja kwa moja kule club nilipokwambia. Kuna vitu vingi vyakufanya, ila naomba kwa wakati huu usiogelee. Tuache hiyo kwa wakati mwingine.” Naya akawa kama amemuelewa ila akajaribu kufikiria. “Au ulitaka sana kuogelea?” “Mwenzio sijui kuogelea Joshua.” “Basi nitakufundisha. Mimi naogelea sana. Sana. Ndio mazoezi pekee ninayofanya, vinginevyo sina muda. Lakini nitakufundisha wakati mwingine sio sasa. Si umesema unatunda la uvumilivu pia?” Naya akacheka. “Hiyo hata si kuvumilia. Ni kitu ambacho hakikuwahi hata kupita akilini mwangu.” Joshua akacheka kidogo na kutulia.

“Mbali  nakuogelea, huwa unapenda kufanya nini?” Naya akamuuliza. “Kuimba.” Naya akacheka. “Huamini?” “Hakika siamini.” “Ngoja nikwambie habari za mama yangu ambazo sikuwa nimewaambia pale.” Naya akakaa sawa. “Mama yangu hakuwa amesoma sana. Aliishia darasa la saba tu, akaenda mjini kutafuta kazi. Akapata kazi hotelini. Hoteli tu ya mkoani. Sio mahoteli ya kisasa. Akawa akifanya kazi hapo na akapewa chumba na mwenye hiyo hoteli. Mama akawa anaishi chumba cha nje. Kwa mujibu wake, hakuwa mtu wa wanaume mpaka akakutana na baba yangu mimi. Anasema hakumwambia kama anafamilia. Wakaanza mahusiano. Kila baba alipokuwa akienda hapo mkoani, akawa anashukia kwa mama, mpaka mama akapata ujauzito na kunizaa. Pale kazini akafukuzwa, baba akampangishia chumba, akawa akitutunza mimi na mama.” Joshua akaendelea.

“Naya, mama yangu mzazi alikuwa akiimba bila kuchoka. Nimekuwa mimi, nikimsikia mama akiimba. Ilikuwa kama ndio maisha yetu ya kuzungumza kwa kuimba, tunapokuwa mimi na mama. Nakumbuka wakati mdogo, alikuwa akiniamsha kwa maneno ya kuimba. Pale tulipokuwa tukiishi wapangaji wenzetu walikuwa wakijua tumeamka ndani kwa mama kuimba.” Naya akacheka. “Alikuwa akinisimulia eti wakati mimi ni mtoto mchanga kabisa, nilikuwa nikilia, eti ananiimbia mpaka nanyamaza. Kwa hiyo mimi naimba tokea mtoto. Hata nyumbani kwangu, walinzi wanajua nimeamka ndani kwa kuimba. Na sipangi.  Najikuta tu. Kwa hiyo mimi ni mwimbaji.” “Utaniimbia?” Joshua akacheka sana.

“Na mimi nataka kukusikia.” “Utanisikia na utazoea. Mziki ni sehemu yangu. Na wewe unapenda kuimba?” “Nilikuwa nikiimba sana kabla sijaanzan...” Akamuona ametulia kwa muda, akamuona ameinama kama anayefikiria kisha akaendelea. “Maisha yangu yalibadilika sana Joshua. Sana. Lakini nilikuwa nikiimba na kina Ino.” “Ino ni nani tena?” Naya akacheka. “Ni kijana tuliyekuwa wote kanisani. Kama amenipita ni kidogo sana. Ana vipaji yule kiumbe, mpaka namshangaa. Hakuna chombo cha mziki pale kanisani hajui kutumia. Tena kutumia kifasaha. Sasa mara nyingi tulikuwa tukiimba naye na Bale pia, mpaka mimi nilipokuja kubadilika au nilipoanza na Malon. Maisha yakachanganyikana! Na wao pale kanisani wakawa wameshanichosha kwa kumdharau baba yangu au niseme wazazi au sisi kwa ujumla. Nikaacha kwenda kabisa. Ila jumapili iliyopita tumerudi tena.” “Ino ameoa?” Naya akacheka sana.

“Niambie.” “Alishaoa na wanakaribia mtoto wa tatu. Usiwe na wivu.” Joshua akacheka na kunyamaza. “Nimalizie habari ya mama Joshua.” Joshua akacheka. “Mama anasema ni kama baba akaanza kupotea kwenye picha. Kadiri siku zilivyozidi kwenda, mawasiliano yakawa magumu. Na ubaya mama hakuwa akifahamu wapi anaishi huku Dar, wala hakuwahi kumtambulisha kwa ndugu yeyote. Mwishoe ikawa kama ametelekezwa kabisa. Akabakia yeye tu akihangaika kunilea peke yake. Nilipofika darasa la 6, mama akasema amepata mwanaume anataka kumuoa. Kumbe yule jamaa alikuwa muathirika. Nafikiri alimdanganya tu mama akamuachia ugonjwa, sikuona ndoa na wala yeye sikujua muendelezo ulivyokuwa.” “Pole sana Joshua.” “Asante.” Joshua akatulia kidogo na kuendelea.

“Basi, mama akaanza matibabu. Akawa akitumia madawa hayo ya waathirika. Akaonekana kuendelea vizuri tu kwa miaka hiyo yote mpaka mimi nikafika kidato cha nne, ndipo akaanza kuugua. Sijui nini kilitokea maana nilisikia wapo wanaoishi miaka mingi  zaidi ya hiyo 5. Akapoteza kazi, na ukumbuke hapo tunaishi nyumba ya kupanga. Tunalipia kila kitu. Ndipo mama akamuomba mpangaji mwenzake anihifadhi mpaka nimalizie kidato cha nne, ndipo nimfuate kwa wazazi wake kijijini. Haikuwa shida sana. Nyumbani ni nyumbani, na kwa mtu mwingine ni tofauti. Ila kwa kuwa ni kwa kitambo, mama akaniambia nivumilie kila shida, nimalize shule. Ikawa nikipata mwanya, nakwenda kumuona mama yangu kule kwa bibi.” Joshua akacheka kwa kusikitika.

“Naya, nyumbani kwa babu na bibi yangu sikuwa mgeni. Tulikuwa tukienda siku za sikukuu, na nakumbuka mama alikuwa akibeba zawadi. Lakini ghafla mama akaonekana ni kama mtoto aliyekuwa hajali nyumbani kwao, eti amerudi akiwa mgonjwa, wakati mzima hakuwa akiwataka wazazi! Nikashangaa sana maana karibu kila mwaka siku za siku kuu, tulikuwa tukirudi kijijini na tunakaa mpaka sikukuu ziishe ndipo tunarudi mjini! Wakaanza kumnyanyasa mama ambaye alikuwa mgonjwa.”

“Kuna siku nilikwenda kumuona, nikamkuta na hali mbaya sana, nilishindwa kuondoka Naya. Nikaona ni bora nibaki nimuuguze mimi mwenyewe. Nikahangaika mpaka nikahamishiwa shule pale kijijini. Ikawa shule na mama. Maisha yakaendelea mpaka mama alipofariki. Hapo nikawa nimeshamaliza shule na matokeo yametoka nina daraja la 4.” “Pole sana Joshua.” “Asante. Nafikiri nilikaa kama miezi miwili tu, wakanishauri nije huku Dar nimtafute baba, anisaidie kusoma. Mungu akawa amesaidia. Nikawa na jina kamili la baba, na wizara ya fedha, ambako mama alinimbia ndiko alikokuwa akifanyia kazi. Nikaja mpaka huku, moja kwa moja ofisini kwake.”

“Nikakutana na mtu ambaye nirafiki yake wa karibu sana, na wanaishi naye Tabata, mtaa mmoja. Aliniambia walinunua naye kiwanja, wakajenga kwa pamoja. Sawa. Akanichukua mpaka kwa mzee. Kufika mzee mwenyewe yupo hoi, kwa ugonjwa wa kisukari. Hata hakunikataa ila akashangaa sana jinsi nilivyokuwa mkubwa. Nikamueleza kuwa mama aliugua, akafariki. Nikakaribishwa pale lakini kumbe familia yake wenyewe wanasubiri urithi, pesa watakayolipwa kazini akifa na mengineyo. Mimi sina habari ila baba alijua.”

“Siku moja akaniita na kuniambia nikafungue akaunti benki, kisha yule rafiki yake atanipa pesa, nikaifiche huko. Nisiitumie mpaka itakaponilazimu sana. Nikamuelewa. Na kweli nikafanya hivyo. Sijui ni pesa ya nini alilipwa huko kazini miezi michache kabla hajafa, mimi nikaitunza ndio hiyo ikanisaidia kuanza shule ya mambo ya stoo. Mengine ni kama nilivyosimulia pale nyumbani.”

“Nikuulize kitu Joshua?” “Karibu.” “Kwa nini kule kwa bibi yako, au upande wa mama yako walikufukuza?” “Waliniambia nirudi mjini nikapiganie haki yangu kama mzaliwa wa yule mzee. Niliporudi tena, nilisimulia uhalisia wa mazingira niliyoyakuta kule kwa baba, na wao wakaniambia hawawezi kunitunza pale. Nikapambane mpaka wanipe na mimi mali. Niliondoka, sikurudi tena Naya. Kwa sababu nilishawaona tokea mama ni mgonjwa. Jinsi walivyokuwa wakinifanyia na mengineyo. Nilivumilia tu kwa sababu mama alikuwa mgonjwa. Sikuweza kuondoka na kumuacha. Kwa kifupi haikuwa mara ya kwanza kunifukuza.” “Pole sana. Hivi uliniambia ni kama ulishakuwa kwenye mahusiano au nimekosea?” Joshua akacheka.

“Nilipokuwa chuoni. Hapo ndio nilikuwa nimefukuzwa upande wa mama na baba, unakumbuka nilikuwa na zile pesa?” “Ndiyo.” “Basi, nafikiri sijui uoga wa maisha, kuhofia nitakuwa peke yangu! Sijui. Ila nikapata msichana pale chuoni. Yeye alikuwa akisoma diploma ya mambo ya uhasibu. Akasema tuishi naye mtaani. Na yeye hakuwa na ndugu hapa mjini.” Akamuona anacheka kwa kusikitika. “Nini?” “Hivi unajua Naya, yule binti, au mwanamke maana sasa hivi ameolewa. Alinisaidia kuimaliza ile pesa yote benki, na kunikimbia mchana hivi!” “Jamani Joshua! Kwa nini?” “Aliniambia hakuwa akiona maisha kati yetu. Amepata mwanaume mwingine.” “Haiwezekani!” “Acha Naya. Yule dada aliniacha Naya. Aliniacha nikiwa nimemueleza hali yangu ya maisha. Nipo peke yangu. Sina ndugu ila yeye. Aliondoka si kwa kujificha. Nikiwa namtizama hivi, na hapo nilikuwa nimelipia chumba kodi ya mwaka, kodi inakaribia kuisha, sina pakwenda! Sikuamini. Akafungasha vitu vyake huku akiniaga, jamaa yake akaja kumchukua na gari, akaondoka bwana.” “Joshua!” Joshua akacheka.

“Acha Naya. Niliingiwa na hofu. Ndipo nikaamini usemi wa mama kuwa pengine ni kweli nina hiyo roho ya kukataliwa, akasema nimeipata kutoka kwake. Nakwambia Naya, unaweza usiamini. Bibi na babu walikuwa wakitunza watoto baki pale nyumbani kwao, sio ndugu kabisa, lakini walinifukuza mimi! Na upande wa baba nao walinifukuza, hawakutaka hata nikae pale kwa maandishi kuwa sitaki mali. Si unajua makanisani wanapokea watu, na kuwasaidia?” Naya akaumia sana. “Basi mimi nilikuwa nikifukuzwa, Naya. Niliijua misikiti inayogawa sadaka siku za ijumaa, na kugawa chakula. Nilijua makanisa yanayofanya mikesha usiku. Nikikwambia nilishaishi msikitini, ni zaidi ya usiku mmoja. Nayajua maisha kwa kuyaishi.”

“Nikikwambia Mungu ni baba yangu, sio kwa sababu nilihubiriwa! Ni kwa kuwa alinihurumia, na kuamua kujitambulisha kwangu kwamba yeye ni ‘Niko, ambaye Niko’. Alinifundisha kumtambua yeye. Siku moja usiku nililia sana. Walinikamata wahuni, wakataka kinibaka. Ni usiku, sina mtetezi, nipo peke yangu sehemu niliyokuwa nimejificha ili nilale. Naya, nililia ule usiku maana walikuwa vijana watatu. Tena wachafu tu. Nikakumbuka vile mama yangu alivyokufa kifo cha mateso kwa lile gonjwa, nikajua watanibaka na kuniachia magonjwa, halafu sina wakuniuguza. Naya, binadamu muone hivihivi. Akikubali kutumiwa na shetani, ni mnyama hatari kuliko simba mwenye njaa.” Naya alishaanza kulia.

“Wale vijana walishanivua nguo kabisa, na wawili wamenishikilia ili mwenzao aanze. Nililia kwa uchungu nikimwita Mungu aniokoe, ndipo nilipomuona Mungu. Hapakuwa na mvua, lakini Naya, radi ilianza kupiga. Ilikuwa sehemu ya fundi viatu. Ameweka kama mifuko ya safleti tu juu. Kufunika mchana jua lisimpige wakati akifanya kazi zake. Sasa mimi ndio nilikuwa nikienda kulala pale usiku na aliniruhusu. Sijui radi ilipotokea Naya, kile kibanda kiliraruliwa na kikawa kama kiliteketezwa kwa moto.” “Joshua!” “Sikudanganyi Naya. Wale vijana walikimbia, na mimi mwenyewe nilikimbia uchi. Sina nguo ya chini.” Naya alilia sana. “Acha Naya. Sijui nini kilitokea usiku ule, ila mimi nachukulia ni Mungu alinitetea. Nililia ule usiku, sitakaa nikasahau.”

“Ndipo nikaanza kujificha misikitini na makanisani sasa na ndipo nikakutana na huyo mzee ambaye alinipa hiyo kazi. Hakuwa hata akijua ninapoishi. Wakati mwingine nilikuwa namwambia aniachie funguo ili nisafishe usiku, kumbe nia ni kulala hapo ofisini kwake, mpaka nikapata pesa ya kupanga, nikapanga na kupata chumba, lakini hamna kitanda wala godoro na niliishi hivyo nikilala juu ya nguo kwa muda mrefu sana tu, mpaka nilipoanza tena chuo.” “Pole sana Joshua. Pole.” “Kwa hiyo ndio yamekuwa maisha yangu. Sikurudia tena kuwa na mahusiano yakaribu na mwanamke kimapenzi ila kazi. Nafikiri nikawa kama nimezira! Sikutaka tena kutafuta ndugu wa pande zote. Nikaona nikae nao mbali kabisa.” “Pole sana Joshua.”

“Naamini Mungu ameanza kunipumzisha Naya. Amenitoa mbali sana. Ila nilikuwa nikijijua mimi ni zaidi ya kile nilicho kwa wakati ule. Kulikuwa na kilio ndani yangu chakutaka zaidi na zaidi kila wakati. Sikuwahi kuridhika.” “Sasa hivi umeridhika?” Naya akauliza. “Ndiyo na hapana. Mungu amenipa kila kitu, bado namlilia familia. Natamani na mimi nije kuwa na familia, Naya. Ila nimejiapia sitafanya kosa kama la baba. Kwenda kuzaa nje. Tokea yule msichana anikimbie, nikajiambia sitagusa mwanamke isipokuwa niliyekabidhiwa na Mungu, nikajua kwamba ni wangu. Na hilo Jema amelielewa kwa wazi kabisa. Akaongeza nidhamu kwangu na kutaarifu wengine.” Naya akainama. Kimya. Mpaka wakafika.

“Naona tumefika muda mzuri.” Akamfungulia mlango wakashuka.  Ukweli Naya na Joshua walipendeza sana. Ikaonekana sehemu nzuri sana wanayofahamiana kwa karibu. Wengi Joshua aliwasalimia kwa furaha na cheko kubwa, wakaonekana ni kweli watu wa hadhi ya Joshua. “Kuna mambo mengi sana yakufanya hapa. Tunaweza tukachukua boti, tukaenda kuzunguka kidogo, au tukakaa huko kwa muda kisha tukarudi.” “Sijawahi kupanda hata pantoni mwenzio.” Joshua akacheka.

“Naya wewe mtundu bwana.” “Kweli Joshua. Sasa nakwenda wapi?” “Basi twende nikakuzungushe baharini.” “Sasa nani anatuendesha?” “Mimi mwenyewe. Nimejifunza kuendesha.” “Kweli you are full of suprises.” Joshua akacheka na kumshika mkono mpaka sehemu. Akaandikisha mambo kadhaa, wakaongozana mpaka huko kwenye boti Naya akishangaa tu.

Akamsaidia kuingia ndani. “Hatuwezi kupinduka?” “Na Mungu naye atakuwa wapi?” Naya akacheka, kidogo akatulia. Joshua akafungua kamba zilizokuwa zikishikilia hiyo boti, akatoa nanga, akaenda sehemu ya kuendesha. “Ni rahisi sana. Njoo karibu yangu uone. Naya akamsogelea, akawasha na kuanza kuondoka taratibu tu sio kwa haraka. Naya akaanza kucheka. “Woga umeisha?” “Nipo na wewe, siogopi tena.” Hilo likamfurahisha Joshua. Akaendesha mpaka mbali kidogo na nchi kavu, kisha akasimamisha hapo boti ila wakiona nchi kavu kwa mbali. Akamwambia wakae tu hapo.

“Nikwambie kitu Joshua?” “Nakusikiliza Naya. Njoo tukae hapa.” Akamsogelea na kukaa sehemu ya juu. Maalumu kwa kukaa. “Niambie.” “Mimi sitakukimbia wala sitakusaliti. Na mimi sina tamaa. Nitakaa na wewe mpaka wewe mwenyewe uje unichoke.” “Hiyo itakuwa kifo Naya.” “Kuna kuchokana Joshua!” “Sio mimi. Najua ninachoongelea. Ndio maana mimi uliponifungulia tu mlango, sijasita. Si umeona?” “Mpaka umenishangaza!” “Nataka watu wajue Joshua huyu akiwa na mtu. Nimevumilia ati Naya! Unafikiri na mimi sitamani kupendwa?” Naya kimya akicheka.

“Tulikuwa tukija huku na wenzangu wakiwa na wapenzi wao, mimi nipo peke yangu. Mpaka unachoka kuwa msindikizaji kila wakati, wakati mwingine nakuja tu peke yangu. Nikikwambia mpweke, ndio hivyo. Nilikuwa nakuja kukaa hapa peke yangu. Ila huwa nakwenda mbali zaidi ya hapa. Nakaa huko nachakula changu, nitaimba na kusoma mpaka nikichoka ndipo narudi nyumbani.” “Ukiwa unajisikia mpweke uwe unanipigia mimi.” “Ndicho ninachofanya. Na hivi umesema si tatizo! Ndio maana napenda niwe na wewe kwenye simu muda wote mpaka wakati wakulala.” Naya akanyamaza.

“Unataka nikuimbie wimbo gani?” “Wowote unaotaka wewe. Ule unaoupenda sanaaa.” Joshua akacheka akifikiria. “Ehe! Unajua wimbo wa ‘Great is your Mercy’?” Naya akatulia akijaribu kuvuta kumbukumbu. “Umeimbwa na Donnie McClurkin.” “Mimi nyingi najua za kiswahili. Za kingereza ni zile za zamani alizokuwa anachagua Ino. Na ni zile za zamani sana. Niimbie huo nione kama naufahamu.” “Una beti mbili tu, lakini unaweza kurudia kwa sauti tofauti tofauti mpaka uridhike. Maneno yake ndio mazuri sana. Yanasema hivi. Great is You mercy towards me, Your love  and kindness towards me, Your tender    mercy I see, Day after day. Forever faithful towards me, And You're always providing for me,  Great is Your mercy towards me, Great is Your grace.

“Nataka uyapate hayo maneno vizuri. Angalia haya meneno hapa.” Akamkabidhi simu yake sehemu yenye huo wimbo. Naya akaanza kutafasiri. “Kuwa, ‘Rehema za Mungu kwako ni kubwa, upendo na wema wake viko kwako, Rehema zake unaziona kila siku’.” Joshua akafurahi sana vile anavyotafasiri. “Sijamaliza.” “Nakusikiliza Naya.” “Unasema, ‘Uwaminifu wake kwako ni wa kudumu’.” “Milele.” “Sawasawa. ‘Kuwa yeye Mungu wakati wote anakubariki.” “Hajawahi kunipungukia.” Akaongeza Joshua kwa hisia zote. Naya akamwangalia na kucheka, kisha akaendelea. “Rehema zake kuu ziko kwako Joshua Kumu.” Basi Joshua akaanza. “Naanza kukutambulisha wimbo.” Naya kimya na cheko.

Joshua akaanza kuimba tu kama kawaida. “Na kwenda ya pili Naya.” “Nakusikiliza.” Alipourudia ule wimbo kuuimba kwa mara ya pili, Naya hakuamini. Ya tatu, mwili mzima ulisisimka. Naya akabaki ametoa macho. Joshua aliimba kwa sauti ya ajabu, nzuri na kwa hisia zote. Akipanda juu sana, akawa katikati na kupiga sauti nzito ya kiume. Naya akabaki ametoa macho.

Joshua akamalizia kwa kutulia, Naya akabaki amepigwa na butwaa. Joshua akamcheka. “Mbona hukuniambia kama unajua kuimba!?” “Nilikwambia Naya.” “Hapana. Hukuniambia kama UNAJUA, kuimba!” Joshua alicheka sana. “Basi mimi sitakaa nikakuimbia! Mimi nilifikiri unasema ule uimbaji wa kawaida, kumbe mpaka kutetemesha sauti!” Joshua akazidi kucheka. “Joshua! Hakika you are full of suprises! Umejawa maajabu mengi! Sikuwahi hata kufikiria kama unajua kuimba hivyo!” “Nimekuleta huku ili umfahamu Joshua huyu ambaye akifika mbele za Mungu, anajishusha chini kabisa, ili yeye azidi. Huwa nakaa huku peke yangu, naimba mpaka nasikia uwepo wa Mungu kama yupo hapa. Wakati mwingine nakaa huku mpaka walinzi wanakuja kuniangalia kama nipo salama, wananikuta nikiomba.”

“Joshua wewe unampenda Mungu!” “Naya, elewa sina mtu mwingine maishani ila yeye Mungu.” “Mbona na mimi hunihesabu?” Naya akaongea kwa kulalamika. “Nimekwambia sitakuacha Joshua. Na sitaki Joshua mwingine, hata muonekano, namtaka huyu Joshua aliyesimama mbele yangu. Mimi nipo Joshua.” “Hujui inanifariji kiasi gani kusikia hivyo. Na kwa kuwa sijazoea, tafadhali usichoke kunikumbusha. Nahitaji kusikia mara kwa mara mpaka huyu mtu wa nje, huyu Joshua, aelewe kuwa sipo peke yangu tena.” Naya akacheka kidogo na kutulia.

Joshua akarudi kukaa. “Na wewe niimbie.” Naya akacheka sana. “Heri ningeanza mimi. Hivi nishakusikia wewe, acha tu mimi nikuonyeshe mitindo ya nguo.” Joshua akacheka sana. “Hutaki tena?” Joshua akamuuliza akicheka sana. “Nitaharibu uwepo mzima uliovuta kwa kuimba kwako. Nipe muda akili irudi vizuri, nitulie nafsini kwangu, ndipo naweza hata kukumbuka kuimba. Nimekuwa na miaka ya uchungu Joshua! Hakuna jinsi nikakueleza ukaelewa. Maisha yalinipokonya kabisa hali fulani niliyokuwa nayo mwanzoni. Ule ujasiri wa ndani, utulivu na kujiamini, nilivipoteza vyote, nikabaki kuona kama natembea uchi na kila mtu ananitizama na kunidharau!” “Kwa nini?!” “Hapakuwa na sehemu, au wanawake zaidi ya kumi sehemu moja na mimi, Malon awe hajalala nao japo wawili kwa uchache, au wote tumejikuta tumeshalala naye. Ilikuwa ikiniuma Joshua, kupita nitakavyokueleza, halafu mimi ndio nikawa najulikana ni mwanamke wake!”

“Pole Naya.” “Lakini ungeniona kwa nje! Ungejua mimi ni mwanamke wa Malon. Nilikuwa navaa, Joshua! Chuoni watu walikuwa wakisubiri nitoke siku hiyo, waone nimevaa nini. Na nilikuwa sijikosei. Malon alikuwa akinipa pesa. Tulikuwa tukienda Dubai tulikuwa tukirudi na masanduku kama tunafanya biashara! Kumbe nguo na viatu vyangu tu. Nilikuwa nikienda shule, kidato cha tano na sita, na SUV gari. Safi. Kwa hiyo kwa nje hivi, nilionekana bora mno, lakini hiyo shida niliyokuwa nikijisikia ndani, hamna mtu akaelewa. Kilio kila siku kumuomba Malon atulie. Hofu ya pengine atakuja kuniua kwa maradhi ilikuwa imenijaa sana.” “Kwa nini uliendelea kuwa naye Naya?” Naya akajicheka.

“Hakuna mtu alikuwa anaelewa Joshua. Hata watu wake wakaribu walikuwa hawanielewi, wananishangaa. Lakini Malon ndio alikuwa mwanaume wangu wa kwanza. Malon akiwa na mimi, hashiki simu. Na watu walijua hata marafiki na wafanyakazi wake kuwa Naya yupo. Ni kama kila kitu kinasimama ila mimi. Alikuwa na jinsi fulani kwangu, siwezi kueleza. Kabla sijalia shida, Malon ametatua. Kwanza hakuwa akitaka niwe na shida hata kuumwa tumbo kwenye siku zangu tu. Alikuwa anakuja huku Dar, ananiuguza mpaka napona. Usiku unaweza kuamka ukamkuta bado anakusugua kiuno, ili maumivu ya hedhi yasirudi nilale. Alikuwa akithamini mawazo yangu, mpaka nilikuwa nikishangaa.” Naya akacheka.

“Hivyo watu ambavyo wanakusikiliza wewe ukiongea hivyo, mimi nilipata hiyo kwa Malon. Ananiami mpaka alinipa nguvu yakufikiria zaidi na zaidi. Hii mitindo ninayotaka kukuonyesha hii, Malon aliiweka kwenye uhalisia. Kutoka kuwa michoro, mpaka kuitisha tamasha! Acha nikuonyeshe.” Akamfungulia website yake ya mitindo. “Naya hii ni kazi yako!?” “Nilijaza watu pale Plaza, nguo zilinunuliwa kwa silimia 85. Alinunua kiwanja, tukajenga kiwanda. Tukanunua mashine za kisasa, nikaajiri watu, wakatengeneza hayo mavazi, huku nikisoma, Malon akinisaidia bila kuchoka. Lakini na vyenyewe vikakosa ladha kwenye onyesho la kwanza tu, warembo wote hawa niliokuwa nimeletewa wanisaidie kutangaza mavazi, mmoja alitoka kulala na Malon, na wengine walikuwa wa zamani. Wakaanza kusimuliana wasijue mimi nipo.”

“Haiwezekani Naya!” “Acha Joshua. Nilikuwa nikilia mchana, na usiku. Baba ndiye anakazi ya kunibembeleza. Malon! Acha jamani. Akanitoa kwenye amani niliyokuwa nayo kabla hajanikuta nikiwa sina kitu, tunahangaika na baba pesa hata ya ada hatuna! Akajaa kwenye maisha yangu, akaleta na mapesa, lakini Joshua! Ilikuwa ni furaha na uchungu kila wakati. Vyote vikawepo kwa wakati mmoja.”

“Nimempoteza Naya wa ndani. Hii ndiyo week ya kwanza, baada ya miaka mingi sana, nalala nimetulia kwa sababu najua ni wewe upo masikioni kwangu, halafu sina hofu ya alipo Malon, na yupo na nani. Hivi jumatatu nataka niwahi kutoka, nikabadilishe jina lake kwenye lile gari, mambo yaishe.” Joshua akakunja uso. “Sijaelewa.” “Ile gari ninayotumia au tunayotumia nyumbani, alinipa Malon ikiwa mpya. Hata miezi miwili sidhani kama imetimia tangia anipe.” Joshua akatulia kabisa. “Alikuja akakuta nahangaika usafiri, ndipo akaninunulia hiyo gari.” Naya akamuona Joshua amebadilika kabisa  akainamia michoro ya Naya, akaendelea kuperuzi. Kimya.

“Lakini amenipa mpaka kadi zake zote. Ameniambia hatakaa akaniulizia juu ya hilo gari na hata nilipomkatalia asinioe, nikamrudishia pete yake, akaondoka bila hata kuulizia gari. Amenipa kabisa. Ni langu, alininunulia mimi. Kwanza ni kama jasho langu tu kutokana na ile pesa aliyorudishiwa baada ya kutoka jela, niliyomuwekea mimi dhamana.” Ikawa kama Naya anajitetea tena. “Kwa nini aliandika jina lake na si lako?” Naya akapoa kidogo kama anayefikiria, Joshua akarudisha macho kitabuni. “Lakini amesema nipo huru kubadili iwe jina langu. Na jumatatu nakwenda kubadili jina.” “Lakini itabakia palepale, kuwa ni kumbukumbu ya gari uliyopewa na Malon. Si ndiyo?” Naya akanyamaza, Joshua akarudisha macho kitabuni na kuendelea kuangalia mpaka mwisho. Akarudia tena.

Akamuomba na simu yake aangalie tena picha mtandaoni. “Katika hili, Malon alikuwa sahihi. Unakipaji kikubwa sana.” “Huna haja ya kumnukuu, Joshua!” “Nafikiri ndivyo ulivyomtambulisha kuwa yeye ndiye ameweka haya mawazo kwenye uhalisia. Sasa kama yeye ndio mwanzilishi, wengine si tunarudia tu?” Naya akajua anaanza kusumbuliwa na wivu. Akanyanyuka pale na kusimama akasogea mwisho kabisa wa boti, akainama kama anayejaribu kushika maji.

“Hii ni kazi, ambayo nikiingalia mimi, ni kubwa kama ile kampuni yetu. Ambayo ikiwekezwa na kichwa kama chako, inamaana utahitaji kina Jema, Njama, Jamal na kila unayemuona pale.” Naya akacheka na kugeuka. “Sikutanii. Kile unachokifanya pale sasa hivi, na vile nilivyokusikia, na kuona jinsi ulivyofanya hizi nguo zetu! Pale ulipo sasa hivi, sio hata robo ya hichi ninachokiona hapa.” Joshua akaongea huku akiendelea kuangalia.

“Unajua ninazo nguo kama hizi lakini suruali na shati ila ni vya rangi ya maziwa. Off white. Sikuwahi hata kuwaza kama mtu anaweza akaongeza kitu kwenye nguo kama hizi! Lakini jinsi ulivyounganisha hivi vitambaa na kutoa hizi nguo kama hivi, unakipaji kikubwa sana. Sana Naya. Najua inaweza isilete maana kwa kuwa narudia kwa wenzangu walio tangulia. Lakini upo vizuri Naya.” Naya akainama bila ya kujibu. “Mimi najua vitu vizuri, na si muongo. Hii kazi ni nzuri.” “Asante.” Naya akashukuru bila yakumtizama. Akageuka baharini akaangalia kidogo akamgeukia Joshua akamkuta bado macho yapo kwenye michoro.

“Mimi nataka kurudi nyumbani kwetu.” Naya akaongea kwa upole.  “Umeshachoka?” “Nataka kurudi kwa baba Naya.” Naya akajibu macho chini. Joshua akatulia akimwangalia, Naya hakumwangalia. “Asante umenileta huku.” Naya akaangalia kuzunguka baharini. “Ndio kwa mara ya kwanza leo nimepanda boti. Na tumepata muda wa kuzungumza, naona mimi nirudi tu nyumbani.” “Nilifikiri tungekaa muda mrefu kidogo!” “Wewe bado unataka kukaa hapa na mimi?” Naya akauliza taratibu tu. “Ndiyo, Naya. Naona kama unanikimbia!” “Sitaki kukuudhi Joshua. Sitaki kuongezeka katika watu watakaokunyima raha au watakao ongeza shida kwako na si furaha. Binafsi najua niliishi maisha ambayo itabidi kuyalipia gharama tu. Sitaki na wewe nikuchoshe au kukuumiza na historia ya maisha yangu ya  nyuma. Ndio maana naona bora niondoke tu ili nisikuumize.” “Ukiniacha ndio utaniumiza Naya.” Joshua akaongea kwa upole akimtizama.

“Sijui chakufanya Joshua! Ni kweli Malon ametengeneza historia kwenye maisha yangu, lakini sasa hivi hayupo. Sina uwezo wakubadili nyuma, nipo katika kutengeneza mbele. Pengine nahitaji muda zaidi. Nitulie, nijijenge tena. Labda nitakuwa mtu wa kufaa.” “Uliniambia ni kama unanipenda. Ile hisia imeisha?” Naya akainama. “Eti Naya?” “Nakupenda wewe Joshua. Lakini najiona sipo sawa. Sitaki kukuumiza.” “Ukiniacha sasa hivi, ndio utaniumiza zaidi.” “Basi niambie kitu chakufanya Joshua. Usinyamaze kama hujafurahia jambo! Kama kuna kurekebisha turekebishe. Nikishindwa nitakwambia.” “Na mimi sitakwambia jambo  ninalojua hutaweza kufanya.” Naya akaenda kukaa pembeni yake.

“Sikwambii habari za Malon kukuumiza Joshua. Na kama nimezungumza vibaya, naomba unisamehe. Sitazungumza tena habari za Malon. Ni sawa?” Joshua akamwangalia na kutoa tabasamu lakini bado akamuona hayupo sawa. “Niambie Joshua.” “Ulikaribia kuniacha Naya!” Naya akaumia sana. “Nilitaka utulie kwanza Joshua. Unajua nisingeweza kukaa mbali na wewe.” Ikawa Naya anajirudi akibembeleza. “Ningejuaje Naya?” “Kwa sababu mimi ndiye nakwambia. Sitakuacha ila nilitaka tu angalau kutulie, nije nianze upya. Samahani. Ila bado nafikiri ni heri tu nirudi nyumbani. Kwa leo itoshe Joshua.” Akamuona amenyong’onyea.

“Nakupenda Joshua. Nilikuahidi sitakuacha mpaka wewe mwenyewe utakapoamua iwe basi.” Joshua akamwangalia na kucheka kidogo, macho yalishakuwa mekundu. “Kama upo tayari kurudi nyumbani, nitakurudisha.” “Unafikiri tutakuja kuonana tena kama hivi?” Naya akamuuliza kwa upendo. Joshua akavuta pumzi kwa nguvu na kuzishusha taratibu. “Binafsi ningetamani kuwa na wewe wakati wote.” “Basi tubaki tena kidogo.” “Sawa. Nashukuru.” Naya akaonana na Joshua wa tofauti kabisa ambaye hafahamika na watu wengine. Joshua huyu ni watofauti na wanaume wote ambao amekuwa nao. Akabaki kimya akimtafakari.

 Wakatulia hapo, Joshua akarudisha macho kwenye ile michoro. “Haichoshi!” Akarudia Joshua. “Acha nikuonyeshe ya kitabuni. Fungua hizo kurasa za mwanzo, kisha chagua moja nikuonyeshe nguo iliyokamilika kutoka mtandaoni.” Joshua akacheka akaanza kuchagua, Naya anamuonyesha. “Picha hizi ni za Zayoni, hizi nilikuja kuongeza baadaye kutoka kwa mpiga picha aliyepiga siku ya shindano.” “Hakika ni nzuri sana!” Akasifia na kumwangalia. “Kuna usemi unasema ‘beauty with brain’. Ulishawahi kusikia?” Naya akaanza kucheka akitingisha kichwa kukataa. “Naya wewe ni mzuri sana. Sana. Na kichwa chako kinafanya kazi sana.” Naya akajificha mgongoni kwake akicheka. “Kweli. Upo mzuri na umebeba uwezo mkubwa sana ndani yako.” Naya akacheka akiwa amejificha nyuma yake.

Akamchungulia kule alikokuwa amejificha. “Sema basi asante.” “Asante. Ila ujue nimefurahi kusikia kutoka kwa mtu kama wewe.” Joshua akacheka kidogo akimtizama kule alikojificha. “Mtu kama mimi nikoje?” “Umesoma. Unauelewa mkubwa wa mambo, sio muongo, halafu unajua mavazi kwa kuyavaa.” Joshua akacheka nakutulia. “Mbona kama kuna kitu kimekushikilia kimekufanya umekosa raha Joshua? Au ukapumzike?” Joshua akacheka. “Natafuta jinsi ya kukwambia juu ya gari ya Malon ambalo unalo, lakini nashindwa nizungumze vipi!” Naya akashituka sana.

“Ile gari ni yangu Joshua!” “Ni ya Malon, aliyokupa kama vile ile pete aliyokuletea, ukaikataa. Ni kama unachagua nini cha kuchukua kutoka kwake, na nini uache.” “Joshua, tafadhali usichukulie hivyo! Halafu ile gari sio kwamba ni mimi tu natumia. Inatumiwa na kutegemewa na kila mtu pale nyumbani!” “Wakijua ni msaada wa Malon.” Naya akachoka kabisa. “Yaani unakuwa upo na mimi, lakini ukitunzwa na Malon!” “Malon hayupo Joshua!” “Ila gari yake ipo, tena ikiwasaidia nyinyi wote.” “Joshua! Tafadhali usiende mbali. Mimi nitakwenda kubadili jina jumatatu.” “Lakini bado itabakia ni gari aliyokupa Malon!” Naya akabaki hajui chakufanya. Ukweli ile gari ilikuwa ikitegemewa sana nyumbani kwao, na Joshua ni kama alitaka hiyo gari irudishwe. Anafanyaje Naya anayeishi Kiluvya, anatakiwa kuja kazini siku 6 kwa juma! Akabaki kama amemwagiwa maji.

“Kabla hujaondoka, twende nikuzungushe kidogo nikuonyeshe kuzunguka hii bahari. Pazuri sana. Siku nyingine nitakupeleka kisiwani.” Joshua akasimama na kuondoa boti. Naya na yeye akamfuta baada ya muda kidogo, akaenda akasimama pembeni yake wakati akiendesha. “Mimi nilijua leo tutapata wakati mzuri!” Akalalamika Naya pembeni yake. “Nilifikiri unafurahia?” “Mimi nakutaka wewe Joshua. Sio haya unayonionyesha. Nataka mimi na wewe tuwe kitu kimoja.” Joshua akasimamisha boti na kumgeukia. Akamshika mikono yote miwili.

“Kitu kimoja, inamaana mimi na wewe tu, si ndiyo?” “Ndiyo. Sisi tuelewane. Mimi sitaki vitu Joshua. Lasivyo sasa hivi bado ningekuwa na Malon. Malon anapesa, lakini hakuwahi kunichagua mimi. Ndio maana nilikwambia ubora wa mtu kwa mtu, unatofautiana na mtazamo wa mtu.” “Basi tuanze kwa kujenga msingi wetu mimi na wewe, kuanzia chini.” “Sawa.” “Hapana Naya. Nataka ukubali ukiwa umeelewa na umekusudia. Nimesema, tuanze kujenga msingi wetu, mimi na wewe tu. Ambao hauna muingiliano wa Malon, wala kukimbilia kwa baba, mambo yanapokuwa magumu.” Hapo pakawa pagumu. “Labda maswala ya baba tungeyaacha tu.” “Sasa utajengaje huku, wakati mwenzangu unapo pakukimbilia? Mimi sina familia yakusema eti mambo yakiwa magumu nikimbie.” “Nikimbilie mimi.” Ikabidi tu Joshua acheke.

“Mimi nimkimbilie baba Naya, wewe nikimbilie mimi.” Joshua akacheka mpaka akaenda kukaa. “Naya!” “Wewe achana na baba Naya. Ila tujenge msingi wetu bila Malon. Ukitaka nisimtaje tena, hutamsikia tena. Nini kingine unataka.” “Niambie ukweli Naya. Kwa mfano mimi ningekuwa ndio kama wewe. Halafu wewe kama mimi. Kila siku unaniona na kitu alichoniachia mwanamke wangu. Tena ndio kama msaada mkubwa sana mpaka familia inatambua huo msaada! Ungejisikiaje?” Naya akatulia.

“Kama kweli unanipenda Naya. Na umekusudia kuwa na mimi, tafakari hilo.” Naya akapoa kabisa. “Inamaana naonekana na mimi ni kama nipo kwenye huo msaada wa Malon! Kwamba na mimi ananisaidia kukutunza! Unakataaje vingine halafu vingine vyenye manufaa kwako unang’ang’ania?” “Basi Joshua. Kwa kuwa tumezungumza sasa hivi, tafadhali nipe muda na mimi nifikirie na kujipanga. Maana kama nilivyokwambia, ni usafiri unaotegemewa na kila mtu pale nyumbani. Si sawa kufanya maamuzi bila kuwashirikisha. Tafadhali nivumilie katika hili. Uliniambia wewe ni mvumilivu sana.” “Naya!” “Wewe mwenyewe uliniambia.” “Acha bwana kutumia maneno yangu mwenyewe kunifunga.” “Mungu amenileta kwako niwe nakukumbusha Joshua.” Joshua akaanza kucheka.

“Twende ukanizururishe majini, kisha unirudishe kwa baba Naya. Mengine niachie mimi nitarekebisha tu au sema jingine.” Akasimama. “Ni hilo tu. Na asante hata kwa kusema utafikiria.”  “Basi ungenifundisha kuendesha boti ili hata nikirudi nyumbani niwe na chakuringishia!” Joshua akaanza kucheka. “Naya wewe ni mtundu!” Akaanza kumuelekeza na kumuachia afanye. Naya alikuwa akicheka sana tena kwa sauti. Baada ya muda ile hali ya uzito ikaisha, wakawa wanacheka sana. Wakazunguka mpaka wakaona giza litawakuta huko na mafuta kuwaishia, wakaanza kurudi ila wakiwa wamejawa sana furaha na wakiwa wamepiga picha nyingi tu.

“Naomba tule pamoja ndipo urudi nyumbani.” Joshua akaongea kwa kubembeleza. “Sawa.” Naya akakubali bila shida. “Ila kumeanza kuwa na baridi. Tukae ndani.” Wote walikuwa wamevaa pensi. Na nje kulishaanza kupokea upepo mkali wa baharini. Wakatafuta sehemu na kukaa ndani. Joshua akawa akimwangalia. “Sasa unafikiria nini?” “Nimefurahi tumeweza kuwa wote mpaka sasa hivi.” Naya akacheka na kutulia. Muhudumu akaja kuwahumumia kila mtu akaagiza chake, wakatulia.

 “Siku nyingine kama leo. Siku za jumamosi, huwa unafanya nini?” “Kama nakuwa sijaja hapa, nakuwepo tu nyumbani nikifanya shuguli zangu tu. Na pia mimi si mtu wa marafiki sana ila ninao watu wawili hao, huwa wananivutia sana. Nikiwa na muda huwa nawatafuta japo niwe nao karibu.” Naya akacheka. “Wakoje hao?!” “Ni wanandoa. Wenyewe wanasimulia walipita kwenye mengi, lakini Naya!” “Nini?” “Hakika namsihi Mungu aje anipe ndoa si chini ya ile. Wale watu wanapendana na wanaendana. Wamezaa watoto wazuri, utatamani kuwa nao karibu. Na wenyewe ni wanachama wa hii club. Huwa wanakuja hapa na watoto wao, na mimi nilitambulishwa kwao na kaka aliyemlea huyo mke mtu. Nikafanya juhudi zote niwe nao karibu. Na pia wamefanikiwa sana kiuchumi.” Naya akacheka.

“Mimi nikikwambia najisogeza kwa mtu, jua huyo mtu ana kitu cha ziada. Sina marafiki wengi, au niseme sina marafiki kabisa. Ila huyo kaka mtu ambaye nimemfahamu kupitia maswala ya kazi, na ndio akanitambulisha kwa mdogo wake kama mtoto wake, ndipo nikakutana nao hao kina Magesa. Ila vinginevyo nakuwepo tu nyumbani, kama si kazini.” “Naona kweli kuna mambo mengi tunafanana.” “Kwa nini?” “Hata mimi si mtu wa marafiki sana. Sina tatizo na watu, lakini najikuta sina muda na watu. Sijui kama unanielewa? Hata kabla ya Malon kuja na kunichanganya hapo katikati na kunitia hofu ya marafiki sababu ya tabia zake, lakini pia mimi ni mtu wa nyumbani. Na nyumbani ni pale alipo baba Naya. Basi.” Joshua akacheka.

“Hakuna kazi anafanya baba, mimi nisijue. Tokea nina akili zangu ndio imekuwa hivyo. Ni miezi michache tu kabla mama hajazidiwa, ndipo alinirudisha ndani, kufanya kazi kama mtoto wa kike. Napo ilikuwa kama adhabu, lakini baadaye ikageuka kitu kizuri sana na kuniunganisha naye.” “Kwa nini uadhibiwe tena?” Naya akacheka. “Mama alitamani sana niolewe na Joshi.” “Na wewe hukuwa ukimtaka.” “Huwezi kumlinganisha na...” Naya akasita na kumtizama Joshua vizuri. “Alikuwa mbahili kupita kiasi. Halafu kuna jinsi alikuwa akinidharau, ilikuwa ikiingia mpaka rohoni. Halafu alikuwa kama mchana na usiku ukimlinganisha n...”  Akaona anyamaze kabisa.

Joshua akacheka. “Wewe ongea. Ndio njia moja yakufahamiana.” “Inakuumiza sasa.” “Kuendelea kumiliki vitu vyake ndio inaniumiza. Lakini si historia za nyuma. Nakuelewa kabisa wala sina tatizo. Malon ulianza naye ukiwa mtoto sana. Umeishi naye kama wanandoa. Nikimaanisha zile shida wanazopitia wanandoa zote, akiwa ameyatawala maisha yako kabisa. Hapakuwa na mtu mwingine kwa muda wote huo ila yeye tu. Kwa hiyo najua sitaepuka kumsikia au hata na mimi kulinganishwa kama hivyo Joshi ulivyomlinganisha naye. Kwa hiyo endelea tu. Uwe na amani.” Naya akamwangalia na kunyamaza.

Wakaletewa vinywaji wakati wakisubiria chakula. “Unajua mambo yako pale kazini yatabadilika Naya.” “Kwa nini tena!?” “Lile wazo ulilolitoa, nimehakikisha linawekwa sawa na ijulikane ni wewe ndio ulitoa hilo wazo. Utafanya kazi kwa karibu sana na Njama, kuhakikisha kile unachokifikiria kichwani, kinatokea.” Naya akacheka kwa hofu kidogo. “Kwahiyo, hiyo itakuwa project mpya ambayo itabidi ubadili kitu ulichokuwa ukifanya. Na Jamal mwenyewe anashugulikia ajira yako ya kudumu. Yeye mwenyewe ametaka bila mimi kumwambia. Aliniambia lazima wakutunze pale ili usaidie zaidi.”

“Natakiwa nifanyaje? Nisaidie mawazo.” “Cha kwanza, jiamini. Beba wazo lako kama mmiliki haswa kuhakikisha hakuna anayekupora. Ukisimama katikati yao, usijione upo chini yao, jiamini. Simaanishi ufanye kwa kiburi, ila jibebe kwa ujasiri. Ukitakiwa kuzungumza zungumza kwa makini kama ndio nafasi yako ya pekee. Tendea haki, usiwe mropokoji katikati yao. Hata kama watafanya mizaha ofisini, usiwe katikati ya hiyo mizaha. Kama tu hivi unavyofanya sasa, itakutunzia heshima sana.” Hilo Naya akalifurahia.

“Kumbe ni bora nilivyokuuliza! Asante.” “Na endelea kufikiria. Usiishie hapo. Akili ifikirie kila wakati. Kuwa mbunifu wa kidogo unachopewa. Utafika mbali sana.” “Asante Joshua. Lakini nilikuwa nikitamani kazi ambayo sitahitajika kazini mpaka siku za jumamosi ili siku za jumamosi niwe nafanya mambo yangu haya ya mavazi.” “Mwanzoni hutakuwa na jinsi ya kuepuka kulipa gharama, Naya. Hakuna kitu kizuri kinakuja kwa urahisi. Inamaana itabidi kukata muda wako kwenye mambo fulanifulani ili kupata yote, au sasa, kuchukua hatua ya imani ukijiamini na upande wa mavazi, uachie ajira.” “Hii kazi ninayofanya mimi, ndiyo inategemewa kwa asilimia kubwa sana pale nyumbani. Baba hana kazi na biashara nyingi zilimfia. Malon alimpa kazi kule Mbeya. Lakini si kitu ambacho ataendelea kufanya. Kuwepo Mbeya na kutuacha sisi!” “Ni kweli familia itayumba.” Joshua akakubaliana naye.

“Tulikuwa tukifikiria naye awe anachukua mchele kutoka kwa Malon kwa bei ya jumla na kuuza, lakini nafikiri amenihurumia. Amesema kama nimeamua kutoendelea kuwa na Malon, tumuache kabisa. Tutafute njia nyingine ya kuianza hiyo biashara.” “Kwani si mlitaka tu bidhaa? Sioni tatizo.” “Ni bidhaa tu, ndiyo. Ila kwa mkopo ili pesa aliyo nayo na nitakayopata mimi kwenye mshahara, isaidie kukodi sehemu yakuhifadhia huo mchele utakapokuja. Na tulitaka iwe sehemu ya wazi, penye watu wengi. Kibaha, aliona sehemu inayofaa. Lakini tumeona tuache kwanza, tufikirie kufanya biashara tutakayomudu bila kumwingiza tena Malon kwenye maisha yetu.” Joshua akanyamaza.

“Ila nimefurahi kama wazo langu umelithamini Joshua. Maana hiyo ndio fani yako na wewe ndio unajulikana mzaa maono ya ile kampuni. Kwa kuhakikisha na mimi najulikana, imenigusa sana. Asante.” “Karibu. Ni wazo lako. Mungu alikupa wewe wala si mimi. Siwezi kuchukua kisicho changu. Nilikwambia Naya.” Naya akacheka taratibu. “Mimi sina tamaa. Vyangu navijua, na ninajua kuvimiliki.” “Nimeamini.” Naya akajibu akiendelea kucheka taratibu akimfikiria Joshua Kumu huyu ambaye nilaini ndani kuliko yai. Alijawa na kushangaa pamoja na kumuhurumia.

~~~~~~~~~~~~~~~~~

“Joshua?” Naya akaita wakiwa njiani kurudi nyumbani kwao. “Niambie Naya.” “Nashukuru nimekuwa na wakati mzuri. Sana.” “Karibu, hata mimi nimekuwa na wakati mzuri. Nikuulize swali Naya?” “Nakusikiliza.” “Nikipanga tena kutoka, ungependa?” “Popote na wewe, Joshua.” Joshua akacheka akimwangalia. “Kweli. Kama nisingekuwa na wewe leo, ningelala tena nikilia. Lakini umejishusha, umenivumilia mpaka nikapata wakati ambao hata sikutegemea! Wewe ni mnyenyekevu Joshua! Mpaka umenishangaza.” “Kwa kuwa najua Mungu amekuleta kwangu kwa makusudi Naya.” “Nashukuru Joshua. Tafadhali nivumilie tu. Naamini nitakuwa mtu ambaye utakuja kunifurahia.” “Hata sasa nakufurahia Naya. Sijaona tatizo lakuvumilia bado.” “Kweli Joshua?” “Nisingetaka uwe na mimi kwa muda mrefu hivi. Ni kwakuwa nakufurahia.” Naya akaridhika na kutulia.

Joshua akaanza kuimba tena, lakini taratibu tu Naya akimsikiliza na kucheka huku akimsifia hapa na pale mpaka wakafika nyumbani kwao. Wakaingia wakionekana walikuwa na wakati mzuri. Naya alijawa cheko lililoonekana tokea anaingia mlangoni. “Mmeshakula?” Baba yake akawauliza. “Tumekula tayari.” Akajibu Naya. “Najua kuendesha boti, baba.” Naya akajivuna. “Mara hii!?” “Amenifundisha Joshua. Tumekaa baharini muda wote. Joshua amenifundisha.” “Nawahurumia samaki huko baharini!” Bale akafanya wote wacheke mpaka Joshua. “Wivu tu Bale. Muulize Joshua kama sijamshangaza kwa uhodari wangu.” Wakazidi kumcheka. “Umeendesha vizuri sana utafikiri mzoefu!” Joshua akamsifia.

 “Ngoja niwaonyeshe picha labda mtamuamini na Joshua.” “Nilikuchukua video Naya. Acha niwaonyeshe video.” “Kweli!? Hata sikuwa najua!” “Ningekwambia ningekuchanganya.” Joshua akawawekea video wakaanza kuangalia. “Kweli bwana!” Bale akaamini. “Umeniona sasa?” “Hapa nimeamini.” Picha walizojipiga zilikuwa nyingi na nzuri sana. Walipendeza na wote walikuwa wakicheka. “Naya ulivyokuwa ukicheka!” “Sikupata muda kama huu kwa muda mrefu sana. Ni kweli nimekuwa na wakati mzuri.” “Umekumbuka kushukuru?” Baba yake akamuuliza. “Nimemshukuru.” Naya akajibu na kumuangalia Joshua. “Hata mimi nimeshukuru, nimekuwa na wakati mzuri sana na Naya.” Joshua naye akaongeza. Wakaangaliana na kucheka. Wakawaona.

“Labda mngekaa.” Zayoni akafanya wacheke. Wakaenda kukaa upande wa sehemu yakulia chakula. Wakaanza kuonyeshana picha. “Hii nzuri Joshua. Nitumie.” Wakawasikia wakizungumza. “Na mimi hii nimeipenda Naya. Naiweka screen server yangu.” “Joshua wewe!” “Kweli. Au wewe hujaipenda?” “Nimecheka sana bwana! Meno yote nje!” “Ndio nzuri, na ikakufanya uvutie zaidi.” Bale na Zayon wakaangaliana, baba yao akawafanyia ishara wasicheke. Naya na Joshua walikaa pale mpaka Zayoni akaaga kwenda kulala. Joshua akaaga na yeye.

“Acha nimsindikize.” Naya akawahi na kutoka na Joshua nje baada ya kuagana ndani. Wakawasikia wamekaa nje kwenye ngazi, maongezi yakaanza upya tena Naya ndiye anayecheka kama saa tano asubuhi. Bale naye akasubiri mpaka akachoka na kwenda kulala. Saa tano usiku ndipo Naya akaingia ndani, Joshua naye akaondoka baada ya kuhakikisha Naya amefunga mlango. Baba yake bado alikuwa amekaa tu sebuleni akisinzia.

~~~~~~~~~~~~~~~~~~

Haya, Joshua amejiacha wazi kabisa kwa Naya. Lakini anataka kujenga msingi wao wawili tu. Yeye yupo tayari, kazi na wajibu ni kwa Naya ambaye ameshaanza kukiri kumpenda Joshua na linaonekana tumaini kubwa sana. Si kwenye mapenzi tu ambapo amemfanya awe na furaha juma zima na kuitimisha siku hiyo ya jumamosi botini, hata kwenye taaluma pia. Amemnyanyua Naya kutoka chini ambako hakuwa akijulikana na yeyote kwenye kampuni yao, mpaka sasa ni gumzo kwenye kampuni!  Juhudi za Naya zinaonekana kuanza kuzaa matunda pale kazini. Karama yake ya ubunifu inaanza kumketisha na wakuu.

Ø Je, Watafanikiwa?

Ø Je, Umbali gani Naya atakwenda kwa ajili ya kuwa na Joshua tu? Amekiri wazi kama ni mali, basi angezipata kwa Malon. Malon hakuwa mchoyo kwa Naya. Anamtaka mtu wake, sasa kampata Joshua mwenye sharti linalosikika gumu. Gari.

Ø Je, Naya ataweza kulipa gharama?

Ø Familia itachukuliaje hilo?

Ø Changamoto gani watapata kazini? 

Usikose Muendelezo.

 


CONVERSATION

0 Comments:

Post a Comment