Naomi Simulizi |+1 205 767 8163 |naomisimulizi@gmail.com MAPENZI&pESA! – SEHEMU YA 20. - Naomi Simulizi

MAPENZI&pESA! – SEHEMU YA 20.

Naya akaenda kukaa pembeni ya baba yake. “Joshua ananipenda sana, baba.” Baba yake akacheka. “Halafu ananihitaji. Anasema mimi ndiye nitakuwa ndugu yake wa kwanza.” Akamuona anacheka. “Na mimi nampenda.” “Ndicho nataka kusikia. Uzuri anamjua Mungu.” “Ni mnyenyekevu sana kwangu. Anajishusha, utafikiri sio Joshua Kumu!” “Mbona ni kama kuna kingine hapo?” Baba yake alimjua Naya. Akajua kuna kitu anataka kusema ila anashindwa. 

“Ni nini?” Baba yake akasisitiza. “Joshua anakosa amani kuona nikiwa na vitu vya Malon.” Akamuona baba yake ametulia ghafla. Akajua ameelewa. “Sina jinsi baba.” “Utafanyaje kufika kazini?” “Mimi sijali ila nawahurumia nyinyi usafiri wa hapa nyumbani!” “Ukisema hujali, utafanya nini?” “Hiyo ni gharama ndogo sana kulipa kwa ajili ya kuwa na mtu kama Joshua, baba yangu.” Baba yake akamwangalia na kunyamaza.

“Hata hivyo naona si sawa, baba. Siwezi nikawa mtu wa kukataa baadhi ya vitu vya Malon, vingine napokea. Naamini Mungu atanipa kwa njia nyingine. Naomba niunge mkono katika hili.” “Sawa mama. Mimi nipo kwenye kukusindikiza kituoni kila siku asubuhi.” Naya akacheka sana. “Tunarudia enzi zetu. Tutakuwa sawa baba yangu.” “Sawa mama. Bora hivi kuliko vile vyakulia kila siku!” Naya akacheka sana na kurudi chumbani kwake. Akampigia simu Joshua. “Nakusindikiza mpaka nyumbani kwako.” “Nashukuru, maana nishaanza kuwa na hamu na wewe.” Wakaanza tena kuzungumza. 

Jumapili.

Naya na familia yake walikwenda kanisani kuabudu kama kawaida yao. Wote wanne. Walipotoka hapo wakaenda sehemu kula. Joshua akampigia simu Naya. “Tulishatoka kanisani, ndio tumefika hapa tunataka kula.” “Naweza kuja na mimi au huu ni muda wa familia tu?” “Na wewe ni familia Joshua. Njoo. Lakini ujue sio zile sehemu za kisu na uma. Huku ni kula nje, tena vumbini.” “Sijali. Ilimradi niwe na wewe.” Naya akafurahi sana. Akamuelekeza, Joshua akamwambia atakuwepo hapo baada ya muda mfupi tu.

“Joshua anakuja. Si ni sawa?” “Mwache aje atulipie. Tena ngoja niongezee kinywaji na nyama.” “Sio vizuri Bale! Huko ni kumtumia vibaya. Ridhika.” “Asante baba yangu.” Naya akafurahi sana kumsikia baba yake akizungumza hivyo. Bale akanyamaza kama ambaye hajaridhika.

Ndani ya nusu saa Joshua akawa amefika hapo. “Nilipitia nyumbani kubadili.” Wakamsikia akizungumza na Naya aliyekwenda kumpokea sehemu ya kuegesha magari. “Umependeza Naya!” “Asante. Hata wewe umependeza. Ila nilitamani kukuona jinsi unavyovaa kanisani.” Joshua akacheka kama anayefikiria. “Sio tofauti sana na ofisini. Kanisani huwa pia napenda kuvaa kikanisani, nikapendeza.” “Hata hapa umependeza.” “Asante lakini sio hivi. Sivai suti wala kufunga tai, lakini navaa shati na suruali. Sijui kama umepata picha mwanamitindo wangu?” “Nimeelewa. Tumekaa upande ule kule mwishoni kabisa, twende moja kwa moja.” “Nimefurahi tutakuwa wote mchana huu.” “Kweli Joshua!?” “Siwezi kukudanganya Naya. Shule ilikuwa ikinichukulia muda mwingi, sasa sasahivi imeisha, najikuta tu nimekaa.” Wakawafikia.

“Shikamoo mzee wangu, na samahani sijui nimeingilia?” “Usijali kabisa. Huu ni muda wa familia. Acha tule pamoja tumshukuru Mungu kwa wakati kama huu.” “Nashukuruni sana. Vipi Bale?” “Safi kabisa. Karibu vumbini?” Joshua akacheka. “Nashukuru sana. Zayoni upo?” “Shikamoo.” Akamsalimia kwa kumpa mkono. Naya akamletea kiti na kumuwekea hapo pembeni yake, akakaa. Wakaanza kuzungumza wote. “Kwani wewe kanisani huwa unakwenda wapi?” Bale akamuuliza. “Kinondoni.” Akamuelekeza. Baba yake akawa akiwafahamu wachungaji wa hapo. Zikaanza stori nyingi tu wakicheka na kutaniana, Joshua akaipenda familia yao. Walionekana ni watu wa kawaida tu, lakini wameshikana sana. Wana umoja na kusikilizana. Walikaa hapo mpaka giza lilipoingia, wakaagana.

Naya alipopanda tu kwenye gari, simu kwa Joshua. Wakaanza tena kuzungumza mpaka wakafika nyumbani bado Naya yupo kwenye simu. Wakaangalia taarifa ya habari pomoja, bado Joshua akabaki kwenye simu masikioni kwa Naya akitumia bluetooth zake. Zikaanza habari za kiuchumi, zilipokuja za michezo, Naya akahama hapo sebuleni maana Joshua akaanza kulinganisha habari za uchumi za nchi mbalimbali alizopata huko mitandaoni na kumshangaza Naya. Wakamuona anahamia chumbani, ndio wakajua hawatamuona tena mpaka kesho yake. 

Jumatatu.

Alishawaambia Bale na Zayoni kuwa anarudisha gari ya Malon. Wakamsaidia kuisafisha vizuri lakini Bale alionekana kutofurahia hilo kabisa, ila kwa kuwa Naya ndiye aliyekuwa na kauli ya mwisho juu ya hiyo gari ikabidi ayaache tu, lakini ukweli alikereka nakuanza kumuona Joshua watofauti. Asubuhi kama kawaida yake Naya akadamka na kuwahi kutoka nyumbani. Moja kwa moja mpaka Kunduchi nyumbani kwa Malon. Alifika getini, akamkabidhi funguo mlinzi na kumwambia hiyo ni gari ya Malon, akiamka amkabidhi na funguo. Ujumbe akawa ameuacha ndani ya gari. Bila ya kupoteza muda Naya akawahi tena barabarani kutafuta daladala ya kumpeleka kazini. Akafanikiwa kupata usafiri, na kujikuta amefika kazini saa 12:15. Akafarijika kwa kuwa bado alikuwa mtu wa kwanza hapo kwenye kitengo chao. Akasafisha ofisi kwa kuyapanga maboksi yaliyokuwa yamezagaa hapo. Pakawa pasafi angalau pakaonekana kama ofisi nyingine. Akakaa mezani kwake nakuanza kuangalia viporo vya kazi.

Saa mbili kasoro Joshua akawa amewasili mezani kwake. Naya akatabasamu na kugeuka. “Upo sawa?” Joshua akamuuliza baada ya kumwangalia vizuri usoni. “Nipo sawa tu, sema siku imeanza na shughuli nyingi, ila nipo sawa. Vipi na wewe?” “Safi tu. Unataka nikuonyeshe kitu?” Naya akacheka na kusimama kumfuata alipokuwa ameegemea meza macho kwenye simu, wengine wakiwaangalia. “Hii hapa ni ya screen server yangu. Hii hapa ni ya lock, hii...” “Sasa mbona haraka Joshua, hata sijajiangalia vizuri!” “Acha kukariri picha Naya!” Naya akacheka sana.

“Kwa hiyo unaniweka kwenye kila kitu?” Naya akauliza kwa deko ila kwa kunong’ona. “Hii uliyocheka vizuri, ndio screen server ya kila kitu mpaka laptop na ipad zangu zote.” “Sasa acha mimi nikuonyeshe yangu. Na usiige Joshua!” Joshua akacheka sana. “Wewe nionyeshe.” “Mbona kama nakuhisi vibaya bwana!” “Acha woga. Mimi nishachagua zangu, sibadilishi mpaka nipate picha pinzani. Ziwe zimezidi sana hizi.” “Basi ona sasa simu yangu ilivyopendeza.” Yeye Naya aliweka picha yao wote wawili Joshua alitegesha kamera walipokuwa kwenye boti. Ilitoka vizuri sana.

 “Hapa kweli umenitamanisha.” “Nilikuonya Joshua!” “Hata hivyo sibadilishi.” “Leo tutaonana tena au ndio basi tena mpaka kesho?” Joshua akafikiria. “Ratiba ya leo bado sijaipenda. Acha tuwasiliane baadaye.” Njama akamfuata mpaka pale. “Kikao na jamaa wa uzalishaji ni mbili kamili, Joshua. Nimeona wakielekea kwenye chumba cha mkutano tayari.” “Nipo nyuma yako.” Akajibu Joshua.

 “Sasa Naya, namalizia ratiba za asubuhi, kwenye saa tano kamili nitarudi tujipange vizuri.” “Sasa tena sio uanze kumtumia Naya, wakati na mimi namtegemea hapa. Hapo tena tutakosana Njama, na tutavurugana kabisa.” Jamal akaingia na kumjibu Njama. Joshua akaondoka bila ya kuongeza baada ya kumkonyeza Naya. “Sasa wewe ulitegemea ile kazi nakamilisha vipi!?” Njama akauliza kwa kushangaa kidogo. “Sikuoni mbele yangu Njama.” Wakamsikia Joshua akiongea akisikika ameshafika mbali, Njama akatoka akikimbia. “Uje tuzungumze vizuri Njama. Maana nikiwa na vimeo hamvitaki. Nikipata jembe, mnachukua nyinyi, mnabaki mkinilaumu tu.” Naya akatulia kimya hakutaka kuingilia.

“Nani kahamisha haya maboksi hapa!?” “Ni mimi Jamal. Nimekosea? Kama nimekosea, naweza kuyarudisha, ila nimeyapanga vizuri na nimeyaandika ili isisumbue wakati wa kutafuta vilivyomo ndani.” “Hakika hawakutoi humu ndani Naya. Nitapambana nao mpaka kwa CEO. Hii kazi niliwapa kina Zena, tena nikamwambia Kibasa asimamie ikamilike. Tena tokea hamjaanza nyinyi kazi. Ikawa maneno na visingizio kwamba humu ndani hakuna sehemu ya kuyaweka. Bisha Zena.” Zena na Kibasa kimya. “Sasa mbona Naya amepata? Ona kulivyokaa vizuri! Walinitia shughuli mpaka kutaka nigombane na uongozi wakitaka tupewe stoo nyingine, eti tuna vitu vingi. Mbona vimetosha sasa?” Jamal akaanza kugomba tena na kuwasema wengine kwa sauti ya juu kama kawaida yake. Naya kimya macho kwenye kompyuta yake. 

Malon

Malon alipoamka akiwa anatoka, akakutana na funguo za gari getini. Akaambiwa gari ipo nje, ina ujumbe ndani. Malon akaumia sana. Akaenda kuchukua huo ujumbe. ‘Malon, naamini upo mzima na Mungu anaendelea kukubariki. Nashukuru kwa kunifikiria usafiri, lakini naomba nirudishe tu. Sitaweza kuwa na mali yako nikiwa nimekukosa wewe Malon. Kilio changu na haja yangu ilikuwa wewe tokea nakufahamu, sio mali. Maadamu nimeshindwa kukupata wewe, vingine najihisi ninakuwa kama watu wengine ambao huwa wanakutumia tu. Kila la kheri. Mungu akubariki. Naya.’ Hiyo siku ikawa imeshaharibika kwa Malon. Akafikiria na kuamua kumfuata Naya ofisini kwake.

Ilikuwa saa nne na nusu wakati Naya alipopata simu kuwa anamgeni getini. Akashangaa sana. Hakuwa hata na wazo na Malon. Akatoka kwa haraka kuelekea getini. Akamkuta Malon. Akatulia kwa muda akimshangaa. “Naomba tuzungumze Naya.” “Nipo kazini Malon.” “Nafahamu. Sitakuchukulia muda mrefu.” Naya akafikiria na kuona amsikilize. Akaamua atoke pale getini mbele ya walinzi, wakazungumze nje kabisa ya geti. Akaandikisha jina lake na muda anaotoka, akatoka. Wakaongozana mpaka wakajikuta wamebakia wao wawili tu.

“Huu ni muda wa kazi Malon! Hapa bado mimi ni mgeni hata sijaajiriwa bado. Naomba tusichukue muda mrefu.” “Samahani, nahisi nilipaniki kuona umerudisha gari! Kwani umesahau kama nilikwambia lile gari ni lako? Ni lako Naya, tafadhali usiteseke wakati gari ipo. Sitakaa nikaiulizia hata mara moja. Nimekuahidi hivyo na nitasimamia hilo. Hata kama mengine nilishindwa, hilo nakuahidi sitabadilika.” “Cha kwanza ile gari ni yako Malon. Hata jina ni lako.” “Kwa sababu mimi ndiye niliyelinunua siku ile Naya. Hukuwepo, sikuwa na kitambulisho chako, ningefanyaje mama?” Naya akaanza kulia. Malon akataka kumshika, Naya akarudi nyuma.

“Tafadhali usikubali kujitesa sababu ya makosa yangu Naya. Acha mimi nilipe gharama, lakini si wewe.” “Mimi sikuwahi kutaka mali kutoka kwako Malon. Ila wewe. Maadamu wewe nimekukosa, vingine vyote sina haja navyo. Sina shida na mali Malon. Ndio maana niliuza kila kitu ili niwe na wewe, lakini ulinikataa. Naomba usiniguse Malon.” “Basi naomba usilie. Tafadhali Naya. Nimeshakuliza vyakutosha mpenzi wangu. Naomba usilie tena.” Naya akajifuta machozi. “Kwa heri Malon.” “Nina hamu na wewe Naya! Nakaribia kurukwa na akili.” Malon akaongea kwa upole akilalamika. “Utakuwa sawa Malon. Tulia ufikirie ni nini kinakuchanganya. Lakini nina uhakika sio mimi kabisa kwa kuwa ulikuwa na mimi kwa miaka zaidi ya mitano, ukinikataa kwa manyanyaso makubwa sana. Mimi si sababu ya kuchanganyikiwa kwako. Kila la kheri.” Naya akataka kuondoka.

“Naya?” Akamwita, Naya akageuka. “Nifanye nini ili uweze kunisamehe?” “Nimekusamehe Malon.” “Naomba unisamehe na unipe nafasi nyingine, nakuahidi hii ni ya mwisho na nitafanya tofauti.” “Sina nafasi nyingine yamajaribio Malon. Mimi si mwanamke Mungu anataka niwepo kwenye maisha yako. Tumejaribu mara kadhaa imeshindikana. Yupo mwanamke mzuri tu Mungu amemuandaa kwa ajili yako, lakini si mimi Naya.” “Mimi nakutaka wewe Naya.” “Umeyajua hayo lini Malon? Ni lini umejua hilo au si kutaka kuniumiza tu?” Naya akamuuliza kwa ukali kidogo.

“Ukinirudia sasa hivi, nakuhakikishia Naya, hutajuta.” “Hivyo ulivyo sasa hivi, hunifai Malon. Ungekuwa umetoka jela, tukaendelea na kupambana pamoja mpaka sasa hivi! Hapo sawa. Nilikuomba tuanze pamoja, lakini ulinikataa Malon. Kwa nini sasa hivi unarudi?” “Kwa kuwa nakupenda Naya. Hakuna maisha bila wewe.” “Kama kweli unanipenda Malon, tafadhali niache. Acha kunichanganya kama ulivyozoea kunifanyia tokea nakufahamu. Endelea na maisha yako, na mimi niache niendelee na yangu. Kwa heri Malon.” Naya akaondoka bila yakugeuka tena nyuma huku akijifuta machozi. 

Sukari yageuka kuwa Shubiri kwa Naya.

Akarudi ndani akijua wazi uso wake unaonyesha alikuwa akilia. Hakutaka watu wamuone hivyo. Akaingia kwenye choo cha walinzi baada ya kusaini kuwa amerudi ndani. Akashangaa machozi yakianza kumtoka tena asijue ni kwa nini. Akakaa hapo akilia kwa muda. Akaosha uso na kujaribu kutulia, ndipo akatoka hapo chooni kurudi ofisini kwao. Wakati anaingia mlangoni kwenye idara yao akakutana na Njama mlangoni. “Vipi Naya?!” Njama akauliza kwa ukali kidogo na kumshangaza Naya. “Safi tu!” Naya akajibu lakini akiwa kama na yeye anaswali ni nini kinaendelea kwa jinsi alivyouliza Njama.

“Unakumbuka miahadi yetu ya saa tano au umedharau kwa sababu ni mimi nimeongea na si Joshua?” Naya akashituka. Kabla hajajibu Njama akaendelea. “Nilikuja ili tuweke sawa ile kazi kama nilivyokwambia asubuhi, lakini ukanipuuza. Nakuja hapa kukufuata mama bosi,  nikaambiwa unamgeni. Nikajishusha, tena nikiangalia muda ninaopoteza kukusubiria wewe nikiwa nimeacha shuguli za muhimu sana. Au unaona mimi sina mambo mengine yakufanya ila kukufuata tu wewe?” Naya akashangaa ile jazba yote, ila akajishusha.

“Samahani nilitoka kidogo. Ila sasa hivi nipo na sitatoka tena. Tunaweza kuendelea.” “Kwa hiyo sasa hivi wewe ndiye unayeongoza kitengo? Tunafanya mambo vile unavyojisikia wewe?” Naya alishindwa hata kujibu. Ila akaumia sana. Akajua ndio amekosa nafasi yakufanya kazi na mtu kama Njama. Njama ni msaidizi wa Joshua, inamaana kufanya naye ile kazi, ingemsogeza karibu na wakubwa zaidi. “Samahani Njama.” “Hiyo ni dharau.” Njama akaondoka. 

Kwa Baba Naya.

Naya akajua ndio inamaana Joshua ataambiwa. Akazidi kuumia na kuingiwa hofu. Akajua Joshua atamuona ni mbambaishaji. Akajutia wazo la kukubali kusimama na kumsikiliza Malon muda ule. Akatamani kama angemwambia wazungumze wakati mwingine kama kuna jambo la muhimu. Hapakuwa na jinsi tena. Maji yalishamwagika. Akaelekea chooni. Naya alilia sana kwa uchungu. Akampigia simu baba yake na kumuelezea kila kitu akiwa hukohuko chooni.

“Naya mama, kama Mungu amekuandikia chako, ni chako tu. Nilishakwambia, barua yenye jina lako, hakuna malaika anaweza kuitoa mkononi mwa Mungu na kwenda kumkabidhi mtu mwingine. Unaweza ukajichelewesha tu kuipokea, lakini umegundua kosa, rudi pale ambako Mungu amekuweka, atamtuma tena malaika wake, atakuletea tu. Ila hakikisha safari ya pili, huyo malaika hakukosi.” Akamtuliza binti yake, akatulia. Naya akaosha tena uso, akarudi kwenye meza yake kukaa asijue Njama alipata jukwaa. 

Wafanyakazi wenzie.

“Nasikia bwana wako wa mtaani amekuja kukufuata kazini leo?” Naya alishituka sana, akamgeukia Zena. “Unaongea nini wewe!?” “Tumewachungulia na picha tumepiga, usije bisha baadaye. Tumewaoneni wewe na yule mwanaume wako. Tena ili usigonganishe magari, ukaenda kuzungumza naye nje kabisa, wakati ni muda wa kazi! Sasa lilivyokuvujia, Njama naye akawa amekuja, amejua ulikuwa kwa mwanaume wako, nje. Tena muda huu uliotakiwa kufanyakazi.” “Mtakatifu Naya! Maana wewe ndio mchapakazi humu, sisi wote hatufai!” Mwenzake Zena, yaani Prisca aliyemkuta hapo kazini akadakia. Wakaanza kucheka. “Ulitukuta Naya. Ukajidai wewe ndiye mwenyewe, unajitenga. Sasa hapa ni Coca. Tutakuona mwisho wako.”  Wakawa wamemtisha Naya. Naya akawatizama tu bila kuwajibu, akarudi kufanya kazi.

Akajua tayari maneno yataenea. Aliingiwa na hofu, akatamani kutoka kumpigia simu baba yake amwambie tena, lakini miguu ikawa kama imekufa ganzi. Wasiwasi ukamzidi juu ya atakachopelekewa Joshua, na Njama aliyeondoka hapo kwa jazba akiwa amejazwa maneno ya kina Zena wanao muonea wivu nakuona anawapita. Akabaki ametulia hapo kwenye kiti chake, macho kwenye kompyuta hana afanyalo. Akatamani kumtumia ujumbe Joshua, lakini amwambie nini! Akabaki ametulia tu kitini. 

Moyo Wa Mtu, Msitu.

Baada ya kikao cha asubuhi, Joshua alitoka na Jema, wakamuacha Njama. Lakini Joshua alimwacha Njama kwa makubaliano kuwa afanyie kazi wazo alilotoa Naya, tena kwa kumshirikisha Naya mwenyewe. Waweke pamoja hata kwa kurikodi ndipo wawatumie watu wa matangazo ambao pia, wangefanya kazi kwa karibu na Naya ili watoe kitu kilichopendwa kwenye kikao, Joshua asijue kinachoendelea kwa Njama.

Joshua alirudi akiwa amejawa furahi sana baada ya kuingia mkataba mkubwa kwenye moja ya plaza kubwa sana hapo mjini ambao walikubali kufanya kazi nao. Kwamba katika hiyo Plaza nzima, kuanzia nje ambako wangeweka mafriji yao mpaka ndani ambapo kuna migahawa mikubwa na watu wengi wanakwenda kula hapo, zitauzwa bidhaa za kampuni yao tu.

Hata Jema alijua Joshua amefurahi. Ni wazo alilokuwa amelifikiria, na kumtuma Jema amtafute mmiliki wa hiyo Plaza kisha amuunganishe naye, ili wazungumze. Na kweli Jema akafanikisha ndipo wakaenda pamoja na kukubaliana.

Fina sekretari wake alimuona jinsi Joshua alivyoingia akiwa na furaha, akajua mambo yamekwenda vizuri. Ila akamuhurumia akijua moto umewaka. Bila kujua Joshua akagonga na kuingia ofisini kwa Njama bila kusikia kukaribishwa. Ila halikuwa jambo la ajabu. Akaingia akiwa amechangamka ila akashangaa Naya hayupo. “Vipi ile kazi, mara hii mmeshamaliza!?” Akauliza Joshua vizuri tu akiwa amesimama mlangoni ameshikilia kitasa cha mlango hata Fina pale nje anamuona. “Ndio naifanyia kazi.” Njama akajibu.

Joshua akakunja uso kidogo. “Kwani vipi? Si unataka kazi ifanyike?” Isivyo kawaida, Njama akamuuliza kwa kumfoka kidogo Joshua, Joshua akatulia akimtizama Njama ambaye alipotoka kwa Naya, akaingia hapo kwa Fina, Joshua na Jema wakiwa hawapo, akaongea mengi sana mabaya, ndipo akaingia ofisini kwake.

“Ndio nafanya kazi. Au ghafla unaona mimi sina uwezo wa kufanya kazi kama hii, ila Naya?” Joshua akaachia kitasa, akasimama wima, mikono akakunja kifuani akamkazia macho Njama. Jema aliposikia akashituka sana na kumwangalia Fina kwa mshangao. Fina akamwandikia kwenye kikaratasi ‘MOTO’. Jema akakunja uso. “Maana hili ni wazo la kawaida tu ambalo kila mtu analijua. Na yeye Naya alizungumza pale akitumia mawazo ya watu tu. Nashangaa vipi ghafla ije kuwa jambo la mpaka ashirikishwe yeye na wakati kwanza si mwajiriwa hapa, na wala hawezi kuajiriwa.” Jema akasogea karibu kujua kulikoni. Akampita Joshua pale mlangoni akaingia ndani kabisa ofisini kwa Njama.

“Kuna nini Njama, mbona kama unawaka kupita kiasi?” “Huyu mtoto anakiburi sana. Kaongea jambo moja mbele yetu, sijui kaambiwa na nani kuwa ashapata ajira hapa, eti mimi namwambia kabisa, saa tano nitamfuata ili tufanye kazi, halafu anaondoka ofisini muda wa kazi, tena bila hata kiongozi wake kujua alipo! Mimi nakwenda pale, namuulizia, wenzie wananiambia kafuatwa na mwanaume wake, wametoka. Saa nne na nusu asubuhi, muda wa kazi!” Njama akaendelea kwa jazba, Joshua kimya akisikiliza.

“Nikamfuata Jamal kumuuliza kama muda ule wa kazi kama Naya amemuaga, maana nilimwambia tena mbele ya Jamal kuwa ningemfuata tufanye kazi, Jamal ananiambia hajamuaga, ametoka tu. Nikapiga simu getini, naambiwa amesaini kabisa, ametoka! Anatoka vipi mida ile ya kazi, nikiwa nimemwambia kuna kazi ya kufanya, anakwenda kukaa nje anazungumza na mwanaume wake kwa kujiamini  kama si dharau kwangu ni nini? Lazima nitamuwajibisha.” Njama akaweka mkwara mzito.

 “Mimi nashauri utulie kwanza Njama. Naona umepaniki sana.”  Jema akamtuliza. Joshua kimya. “Sijapaniki! Naongea ukweli. Huo ni utovu wa nidhamu na nimemwambia sitaweza kufanya naye kazi.”  “Kumbe alisharudi na mkaonana?” Joshua akauliza taratibu tu. “Amekuja kurudi baadaye sana muda wa kikao ulishaisha!” Njama akasimama kabisa kama ambaye hakutaka ababaishwe na Joshua.

“Hiyo ni dharau kwangu kwa kuwa anajua sasa hivi na wewe...” “Njama! Nashauri utulie. Tafadhali tulia Njama. Maneno huwa yakitoka hayarudi hata ukiomba msamaha. Tafadhali tulia Njama.” “Na wewe Jema unaona alichofanya ni kizuri au kutaka kujipendekeza tu? Na nimemwambia Jamal anipe majibu ya kueleweka juu yake Naya. Lasivyo na yeye nitamuwajibisha. Inamaana hafanyi kazi zake vizuri. Hajui kuongoza idara. Anakuwepo vipi tu pale na watu wa chini yake wanaingia na kutoka tu ofisini kama wanavyotaka! Hatuwezi kuendesha kampuni kwa namna hiyo.” “Kweli Njama!?” Jema akashangaa sana. “Kweli nini?” Njama akamuuliza kwa ukali sana.

“Umeingiwa nini kaka? Kwani Naya ndio amekuwa wa kwanza kupata mgeni hapa kwenye hii kampuni!” Jema akashangaa sana. “Mbona kama huelewi hoja yangu Jema au unajipendekeza tu kwa jamaa hapa? Anatokaje nje kabisa ya kampuni, muda wa kazi, eti sababu ya kutembelewa na mwanamme wake!? Hii kampuni ikiendeshwa kwa kuendekeza mapenzi si itatufia mikononi mwetu?”  Joshua akacheka kidogo akimtizama Njama kisha akaondoka.

“Fina, naomba vitabu wanavyosaini wafanyakazi wote vilivyopo getini, sasa hivi, ofisini kwangu. Nataka mpaka vya miezi miwili nyuma.” Wakamsikia Joshua akiongea na Fina. Jema akamshangaa sana Njama. “Ni nini Njama? Mbona unawasha moto ambao huna uwezo wa kuja kuzima!?” “Hakuna wakunitisha mimi. Nayajua majukumu yangu, ndio ninayoyasimamia. Kama mtu atanifikiria vibaya kwa kuwajibika kwangu, basi. Hakuna mwajiri wangu hapa. Wote tumeajiriwa. Mtu hawezi kunibabaisha. Kila mtu anashida zake, na tunatakiwa kuwajibika. Kama mnataka mapenzi ndio yaongoze hii kampuni, waambieni wamiliki.” Njama alipaza sauti kama anayetaka Joshua amsikie. Jema alikuwa akimshangaa Njama, kama ameona mzimu.

“Unashangaa nini kama huelewi? Au jamaa ashakutisha sana mpaka unashindwa kufikiria?” “Labda nikuulize Njama, ni hilihili unalozungumzia hapa au kuna jingine nyuma ya hili?” Jema akamuuliza kwa upole tu. “Maana kama ni kweli ni hili, nashauri leo ukapumzike nyumbani, uje kesho ukiwa umetulia. Unaharibu.” “Kwa lipi na kwa nani?” Njama akauliza kwa kujiamini.

“Hivi huyu Naya, siye sifa zake zinaimbwa hapa na Jamal tokea walipoanza kazi kuwa anafanya kazi zaidi ya alivyopangiwa?” “Si anajipendekeza tu Jamal ili jamaa hapa amuone yupo upande wake.”  “Tulia Njama wewe! Vita unayoanzisha hiyo ni hatari mno! Huyu Jamal anamtegemea sana Naya kwenye ile ofisi. Na alianza kutaka Naya apewe ajira tokea muda mrefu tu akisema anazo sifa zote.  Ukakataa Njama.” “Kwa kuwa hata hakuwa ametimiza muda wa probetion!? Ulitaka niidhinishe ajira kwa mtu ambaye hata hatumjui! Sasa umeona jinsi tabia zake zilivyo baada ya kuitwa kwenye kikao kimoja tu?” Jema akafunga mlango.

“Mimi siogopi hata wakisikia. Nishamtumia Jamal email yamkutaka maelezo juu ya Naya, na nimemtumia HR pia. Sitaki mambo kiholela.” Jema akashituka sana. “Njama!” “Kabisa. Tulizungumza nini kikao cha asubuhi? Si tuwajibike? Tena Joshua mwenyewe alisema tuchape kazi. Ndio nachapa kazi sasa. Mbona mnalalamika. Panga linapita kotekote.” Jema akamshangaa sana Njama.  “Mimi nakuonya Njama. Tulia, kaka. Huko kilipo kichwa chako leo, tafadhali kitoe, kirudishe kwenye uhalisia. Sasa hivi unacheza na ajira za watu muhimu sana. Jamal umemkuta hapa kazini, kisha Joshua ni kiongozi wako hata iweje. Na hawa watu wawili unaotaka kushindana nao,  ni watu muhimu sana kwenye hiki kitengo. Nashauri tulia.” “Usinione mimi mjinga. Nafanya mambo yangu kwa umakini sana. Nimejidhatiti. Siwezi kuwa kibaraka wa mtu.” Jema akamtizama, nakufungua mlango akatoka kurudi ofisini kwake akamuacha Njama akifoka haswa. 

Kwa Naya.

Jamal akamfuata. “Naya, naomba uje ofisini kwangu.” Mwili mzima wa Naya ulikuwa ukitetemeka. Akasimama na kumfuata nyuma, wenzake wakaanza kumcheka. Akaingia ndani akakuta wenzie Jamal wapo hapo.  Jamal akakaa. “Niambie ni nini kinaendelea? Mbona sielewi?”  Jamal akaanza. “Asubuhi wakati na wewe upo pale, unakumbuka Njama alisema anakwenda kuweka mambo yake sawa, kisha kwenye saa tano. Tena akasema kama kwenye saa tano hivi, akasema angerudi tufanye kazi!” “Nakumbuka.” Jamal akaongeza. “Basi, nikiwa nafanya kazi ulizonipangia wewe, nikapigiwa simu nina mgeni getini. Samahani Jamal, sikufikiria bosi wangu. Mimi nikatoka bila kuangalia muda wala sikukuaga kwa kuwa nilijua sitachukua muda mrefu. Kwa kuwa sikutaka kuzungumzia pale, ikabidi nitoke naye nje nikazungumze naye. Niliporudi nikakutana na Njama na yeye anatoka.” Kila mtu akakunja uso.

“Mmmh! Wewe Naya, hebu zungumza vizuri. Hakuna ulipojibishana na Njama?” Mwenzie Jamal akauliza. Naya akashangaa kidogo. “Hapana dada yangu. Nilimuomba msamaha na kumwambia nimerudi, tunaweza kuendelea. Lakini nafikiri alishakuwa amekasirika.” “Sasa hiyo yakusema Naya anataka kuendesha hiki kitengo kama anavyotaka yeye ametoa wapi?” “Sijui Jamal kaka yangu. Mimi nilikosea, nipo tayari kuwajibika.” Naya akaongea kwa unyenyekevu ila akitetemeka haswa.

“Huyu Njama ana lake huyu! Kwani Naya ndio wakwanza kutoka hapa muda wa kazi?” Jamal akacheka. “Na ananitafuta. Anatafuta ugali wa wanangu! Kwa hili tu ndio aniandikie barua na kumtumia nakala mpaka Afisa Mwajiri!?” Jamal akauliza akishangaa sana. “Sasa acha nicheze naye. Wewe nenda kaandike barua ya kujieleza kama hivi.” “Wewe Jamal, si ndio anajifunga?! Naya amekiri kutoka muda wa kazi.” Mwingine akadakia.

“Sina jinsi. Maana na yeye ameshapiga simu getini, ameomba nakala ya aliposaini Naya kutoka. Inamaana hatuwezi kukwepa. Wewe Naya kaandike barua. Kazi zako zote nazihamishia kwa kina Kibasa. Najua hazitaisha leo, lakini najua wameshakuchanganya, huwezi kufikiria tena.” “Hapana Jamal. Nitafanya tu. Maadamu bado sijafukuzwa kazi, mimi bado nipo chini yako, nitazifanya tu. Nakuandikia barua sasa hivi, nakutumia. Na samahani sana Jamal. Naomba nisamehe.” “Wewe usijali. Ungekuwa mtu mwingine, hakika ungeondoka sasa hivi Naya. Lakini najua huwa unafanya kazi zaidi ya muda tunaokulipa tena bila kulalamika.” “Halafu si huyuhuyu Naya ulikwenda kumuombea kwa Njama amlipe overtime na amwajiri, akakataa.” “Nenda Naya.” Jamal akamtoa pale kama hakutaka asikie zaidi.

Naya akarudi mezani kwake, ili anaandike hiyo barua. Wenzie wakaanza kumkebehi na kumcheka tena. Muda wa chakula cha mchana ukawa umefika. Wakatoka huku wakicheka na kurusha maneno ya kebehi, ambayo Naya alijua wanamrushia tu yeye. Naya akaandika ile barua kama alivyomueleza Jamal. Wakati anamalizia, Joshua akawa ameingia. Naya akageuka aliposikia hatua zikimkaribia. Akabaki akimwangalia na kushindwa hata kumsalimia. Hakujua amesikia nini tayari! Akabaki akimwangalia. Joshua akasimama mbele yake, mikono mfukoni. “Umeshakamilisha barua uliyotakiwa kuandika?” “Ndiyo. Hii hapa.” Naya akainyanyua na kumkabidhi. Mikono ilikuwa ikitetemeka, karatasi ilikuwa ikicheza haswa. Joshua akaipokea. Akamuona ameisoma ndani ya sekunde chache sana akawa amemaliza.

“Twende.” Akamnyooshea mkono. “Siwezi hata kusimama Joshua!” Naya akaanza kulia. Joshua akazunguka kule alipokuwa amekaa, akamsaidia kusimama. Wakatoka hapo mpaka ofisini kwa Jamal. “Mbali na hii barua, kuna kitu kingine unataka kutoka kwa Naya, sasa hivi?” “Bado Njama hajanipa maelezo mengine. Ametaka iandikwe kwa mkono kabisa, kisha itolewe kopi. Nakala moja iwekwe kwenye faili apelekewe yeye, halafu hiyo ya pili nipeleke kwa Afisa Mwajiri.” Joshua akamkabidhi ile barua, Naya amesimama nyuma yake. “Tafadhali angalia kama kuna kitu kingine kinahitajika kabla sijaondoka na Naya.” Jamal akasoma mwanzo mpaka mwisho. “Nafikiri anachotaka Njama kipo hapa. Kuwa Naya alitoka muda wa kazi. Na Naya ameandika hapa kwa uwazi tu. Acha nitoe kopi kisha niwapelekee, nipate muongozo mwingine. Nitamjulisha Naya.” Joshua akatoka akiwa amemshika mkono Naya. 

Joshua Katika Nafasi yake.

Kila mtu akaona wakitoka hapo kuelekea sehemu ya kuegesha magari, akiwa amemshika mkono Naya akilia taratibu. Kabla ya kumfungulia mlango Naya akamvuta mkono kidogo, Joshua akageuka. “Sisikii kula kitu.” Naya alikuwa akitetemeka sana. Mpaka midomo. “Halafu sidhani kama sasa hivi ni sawa tukionekana pamoja Joshua. Nimeshajiingiza doa, sitaki nikuharibie na wewe.” Joshua akamgeuka vizuri. “Ikiwa mimi ndio nakuharibia?” Naya kawa hajaelewa. “Unajuaje pengine mimi ndiye ninayesababisha uwe matatizoni?” “Hapana Joshua. Nilikosea kutoka muda wa kazi bila kuaga.” “Unafikiri wewe ndio wa kwanza kufanya hivyo? Unafikiri hiki ulichokifanya wewe ni kitu kigeni sana kwamba uongozi hautambui kuna watu wanatoka?” Naya akaendelea kulia.

“Nimeangalia muda uliotoka na kurudi kutoka kwenye chati uliyo saini pale getini, hukumaliza hata dakika 10 tokea utoke na urudi.” Naya akashangaa kidogo. “Ninazo rikodi zote ofisini kwangu. Hujafanya jambo la ajabu Naya, na si kigeni kabisa. Hujatoroka kwamba ulionekana nje ukiwa hujaandikisha popote. Tena uliitwa na walinzi kutokea ofisini kwako ukifanya kazi. Ila hukumuaga mkuu wa idara.” “Nilipaniki kusikia nina mgeni. Sikuwa hata nikitegemea kuwa na mgeni hapa! Sikujua kama ni Malon amekuja.” “Ingia ndani ya gari tuzungumze.” Akamfungulia mlango, Joshua akawasha gari na kurudi kukaa nyuma ya gari pamoja na Naya.

“Kwanza naomba utulie Naya.” “Naogopa sana siwezi kujisaidia.” Naya akazidi kulia, akiendelea kufuta machozi kwa mikono bila kumaliza. “Niangalie mimi.” “Mwili unatetemeka sana Joshua. Labda nimuite baba.” “Huwezi kuwa ukifanya hivyo Naya. Hii ni kazi ambayo watu wengi wanakuamini. Umekosea padogo tu, ndipo Njama amepata sababu. Baba hawezi kukusaidia hapa ila wewe mwenyewe.” “Labda hata nizungumze naye kidogo tu, akili inaweza kutulia nikaweza hata kufikiria. Sijawahi kuogopa hivi Joshua. Naomba nimpigie tu baba ili nitulie.” Naya alijawa kwikwi kwa hofu.

“Kila baraka inakuja na kuwajibika Naya. Usifikiri mimi nimefika hapa nilipo kwa urahisi tu! Kwamba eti niliomba, halafu kila kitu kikatokea! Na kwa taarifa yako tu, hii si yako peke yako. Ibilisi amepata huo mlango ili kunifikia mimi aharibu mimba niliyokwambia inakaribia kuzaliwa.” Naya akatulia kidogo kwa alichoongea Joshua. “Hakuna mtu amepata mwanya kwangu, hata mara moja isipokuwa sasa hivi. Shetani amenitafuta katika mengi mno. Sasa hivi ndipo anataka kunivuruga kupitia wewe.” “Samahani Joshua.” “Huna haja yakuomba msamaha. Hili ni jaribu langu mimi, nakuhakikishia Naya, tutashinda na tutatoka tukiwa tunang’aa. Simama, utauona mkono wa Mungu.” Naya akamshangaa sana Joshua.

“Mbona sasa hata huulizi habari za Malon!?” “Nilikwambia kila kilicho changu Mungu ananiletea mwenyewe. Sikukutafuta mimi. Mungu alikuleta kwangu, najua wewe ni wangu Naya. Sina hofu. Tabia yangu inapimwa sasa hivi nikiwa kwenye mahusiano. Si na Mungu tu, hata watu wengine. Na kwa taarifa yako tu, sasa hivi kampuni nzima, macho na masikio yao yapo kwangu wala si kwako. Kila mtu anataka kujua nitafanya nini.” Naya akaumia sana. 

“Sikukusudia Joshua. Asubuhi nilikwenda mpaka nyumbani kwa Malon. Sikutaka kuonana naye, nikamuachia ujumbe kwenye gari na funguo nikaacha getini kwa mlinzi. Ujumbe niliomwachia kwenye gari, nilijua ungemtosha kumuelewesha Malon kuwa nimemrudishia gari yake, na sihitaji tena. Wakati tupo wote asubuhi, Njama aliongea vile kuwa kama kwenye saa tano, atakuja tufanye kazi.” “Subiri kwanza Naya. Ni wakati ule ndipo Njama alipokwambia na si kwamba pengine alikupigia simu na kukwambia umsubirie anakuja saa tano kamili, kuweka miahadi kamili?” 

“Hapana Joshua. Lakini pia hilo lisingekuwa lazima. Unajua sijawahi hata kutoka tokea nianze kazi! Sijawahi hata kuomba ruhusa kutoka kabla ya muda wa kazi! Tena nilipanga leo ndipo nimuombe Jamal, niwahi kutoka, tena ni kwa kuwa najiona nafanya kazi zaidi ya masaa niliyopangiwa, nilitaka niwahi kutoka ili nikabadili jina la gari. Lakini tulipokubaliana na familia nilirudishe tu gari, nikaona niwahi zaidi asubuhi, nilipeleke Kunduchi kabla ya kazi, ili nisiombe ruhusa. Kwa hiyo nilijua muda wowote atakao kuja Njama, tungeweza kufanya naye kazi.” Naya akaendelea.

“Nilipopigiwa simu kama kwenye saa...” “Ulionyesha umetoka getini saa 4:30 asubuhi na kurudi saa 4:39.” Mpaka Naya akashangaa, maana alikuwa akiandika tu muda pale getini bila kujua kama kungekuwa na kesi. “Nilikwambia nilichukua vitabu vyote vya getini na mahudhurio yenu wote pale ofisini kwenu, kwa miezi miwili.” Mpaka machozi yakakauka. “Utafanyaje Joshua?” “Hakuna aliyewahi kuniona nikiwa na mwanamke.” Joshua akazungumza kwa kujiamini mpaka akamtia moyo Naya.

“Samahani Joshua. Sikutaka kukuletea matatizo, tena mapema hivi! Mimi nilijua tutazungumza kwa muda mfupi tu. Tena palepale getini, nirudi ndani. Lakini aliposema anataka tuzungumze, na kulikuwa na watu wengine pale getini, nikajua maneno yatasambaa, na mimi namjua Malon anapotaka jambo lake. Huwa anatabia yakulazimishia. Nikatoka naye, tena wala hakufanya fujo. Nikamueleza tu kuwa nilirudisha gari kwa kuwa lilikuwa lake na kwa kuwa sasa hivi hatupo pamoja, na sina mpango wa kumrudia tena, ni heri nimrudishie. Tena Malon akawa tu muungwana wala hakuleta fujo zake, akanieleza lile gari alilinunua kwa ajili yangu. Ilimlazimu kuweka jina lake kwa kuwa mimi sikuwepo wakati akilinunua, ikamlazimu kutumia kitambulisho chake. Akanishauri nisikatae usafiri, niende nikabadilishe jina. Nitoe kabisa jina lake niweke langu na ahadi yakunisaidia hata barua ya maelezo kuwa alinipa mimi ili nisisumbuke kwenye vyombo vya usalama wakati nabadili jina. Nikamkatalia na kurudi ndani.” Joshua kimya akisikiliza.

“Nilipoingia getini nikatumia vile vyoo vya pale karibu na getini, ndipo nikarudi ofisini, mlangoni nikakutana na Njama ndio anatoka. Akawa mkali. Ila nikamuomba msamaha, nikamwambia nilipatwa dharula, ila nimerudi, tunaweza kuendelea. Ndipo akasema mimi nimemdharau, nataka kuendesha idara nitakavyo mimi na mengine mengi. Basi mimi nikarudi ndani ndipo Jamal akaniita na yeye akaniuliza kulikoni. Nikawaeleza. Wote wakashangaa wakidhani kuna kitu naficha. Mimi nikawaambia ndivyo ilivyokuwa, hivyo tu. Wote wakawa hawaelewi.” “Ni kweli haieleweki!” “Ndio Jamal akaniambia natakiwa kuandika barua, tena Njama anataka niandike kwa mkono, kisha nimpelekee yeye.” Joshua akacheka na kufikiria kidogo.

“Samahani sana Joshua.” “Kwa hiyo ulirudisha gari?” “Sitaki kukunyima raha Joshua. Mali sitaki ziwe tatizo kwetu, hata baba nilimwambia. Sitaki mali zinitenge na wewe.” “Sasa baba si atakuwa amenichukia?” “Baba yangu ana imani sana Joshua. Wakati wote huwa ananiambia barua yenye jina langu, malaika hawezi kukosea akampa mtu mwingine. Inaweza kuchelewa tu, lakini itanifikia. Ameniambia nisiwe na wasiwasi, atakuwa akinipeleka kituoni kama zamani na kunisubiria mpaka niondoke kituoni na kuja kunipokea jioni.” Joshua akajisikia vibaya sana. Akagundua amesababisha usumbufu mkubwa. Akatulia.

“Nitafanyaje Joshua?” “Nisikilize Naya. Mama akiwa mjamzito kabla hajapata furaha ya kunyonyesha si anapita kwenye uchungu mkali sana?” “Ndiyo.” “Dhahabu ili ing’ae si lazima ipitishwe kwenye moto?” “Ndiyo.” “Unajua ili matofali yawe imara sana, yale yakuchomwa, si unajua lazima yawekwe kwenye moto?” “Sikujua.” “Mimi nimekulia kwenye hayo mazingira ya matofali ya kuchomwa. Lazima yapangwe, ndipo chini yake uwekwe moto mkali sana. Yakishakaa kwenye moto mkali sana kwa muda mrefu, ndipo yanatolewa yakiwa yameshakuwa imara. Sasa hata katika hili, lipo kubwa litazaliwa.” “Joshua!?” Naya akashangaa sana.

“Usikimbie, wala usikate tamaa. Hayo machozi yawe kwangu tu. Mbele za watu usiwahi kulia. Sasa hivi, muda huu, tabia yako inapimwa. Usiniulize na nani. Sijui kama ni Mungu au Mungu anataka kumthibitishia nani! Mimi sijui. Lakini huwa namjua Mungu anapotaka kufanya jambo lake.” Joshua akaongea kwa hisia.

“Hawezi kuweka msingi juu ya msingi wa mwanadamu. Sijui kama unaelewa?” Naya akabaki kimya. “Huyu Mungu ninayemjua mimi. Anapotaka kufanya yake! Yale yakufanya masikio ya wanadamu yawashe, anamtindo wa kutingisha misingi. Na anapotingisha huwa hajali kipi hakijakaa sawa. Hata wewe mwenyewe kama hujakaa sawa, unakwenda na maji. Nilichojifunza, tena kwa msaada wa Roho mtakatifu, nikuhakikisha Mungu anapotingisha kila msingi ili kujenga upya, mimi nabaki nimesimama. Sasa hata katika hili, lazima uhakikishe wewe unasimama. Hawezi kuweka divai mpya kwenye chombo kilicho chakaa! Huyo si Mungu ninayemjua mimi, bwana!” Tayari ujasiri ukaanza kuongezeka kwa Naya.

“Lakini nasikia amefikisha jina langu mpaka kwa HR, Afisa mwajiri!” “Ungejulikana vipi kwa Afisa Mwajiri, bila hili?” Naya akaanza kucheka. “Mungu hutumia hata wapumbavu kukufanikishia mambo yako. Acha pangurume. Acha Simba wa kabila la Yuda angurume hapa mpaka wajue Mungu wetu yupo. Atanguruma hapa Coca, mpaka watachanganyikiwa, lakini hakikisha unabaki wewe umesimama. Kila mtu atajua yupo Naya hapa. Mungu akisharidhika pako sawa, ndipo atatuliza bahari.” Naya akaanza kufurahia. “Acha kushangilia. Sio rahisi Naya! Njama amejipanga kwelikweli. Ameomba kikao cha dharula na viongozi wa ngazi za juu. Lakini najua shida yake ni mimi wala si wewe.” “Joshua! Huogopi?” “Hivi unafikiri wangekuwa wakininunua kwa mamilioni ya pesa kama nababaishwa na ujinga kama huu? Nimethibitishwa mimi, Naya! Na nikaonekana nimesimama.” Naya akacheka sana.

“Joshua!” “Naya, nimetoka kwingi! Nimekutana na watu zaidi ya Njama ambao nilichukua nafasi zao, tena wakiwa wamekaa kwenye hivi vitengo kwa muda mrefu sana. Eti mimi natokea tu na wazo, tena nikiwa mdogo tu, nachukua nafasi zao, unafikiri ilikuwa rahisi tu?” “Lakini kweli?” “Sasa. Wewe umetukuta tunasugua vichwa juzi, ukatoa wazo lililopendwa na kila mtu, leo Njama anaambiwa na kiongozi wake hawezi kuifanya kazi ya Naya bila Naya mwenyewe, unafikiri atafurahia tu? Lazima patibuke. Sasa pakitibuka halafu wewe ukakimbia, ujue ndio hayo anayokwambia baba yako, barua yako inachelewa. Mimi sina baba waziri wa uchumi wala mkurugenzi sehemu fulani. Bila kusimama pale Mungu anapotaka niwepo kwa wakati wake ili malaika aliyemtuma anikute na kunikabidhi barua yangu, nisingefika hapa Naya! Huwezi kunitoa sehemu ninayojua Mungu anataka niwepo. Hata mafuriko yaje. Nitashika sehemu moja, nitaogelea ilimradi kuhakikisha baada ya wote kuondoka, malaika anikute MIMI nimesimama palepale na kunikabidhi barua yangu. Ndio maana unaniona nipo hivi, umri huu, na nimekumbatia baraka zangu zote.” Naya akacheka akimtafakari Joshua na yeye mwenyewe.

“Ubinadamu ulitaka kunizidia kidogo tu leo, Njama aliponipandishia mbele ya kina Jema.” “Haiwezekani Joshua!” “Ilikuwa mbaya sana. Tena hapo anatangaza ulitoka kwenda kuzungumza na mwanaume wako! Nikatamani kuzungumza jambo fulani, lakini nikakumbuka kutozungumza nikiwa na hasira na Jema akawa anamwambia Njama kuwa huwa maneno yakitamkwa hayarudi, hata ukiomba msamaha. Japokuwa alikuwa akimwambia Njama, lakini ikaniingia mimi mwenyewe. Nikanyamaza kabisa na kuondoka pale, ndipo Mungu akanipa akili ya nini chakufanya kwa haraka na kukumbuka wakati wote kabla sijatoa kitu kikubwa, huwa kuna jambo linatokea. Nikajua wakati wa kujifungua umefika, shetani anataka kuniangusha kupitia wewe. Nikacheka sana nafsi mwangu. Nikamwambia shetani, nimekukamata. Huniwezi.”

“Sasa utafanyaje Joshua?” “Wajibu wangu wa kwanza ni wewe Naya. Wewe ukitulia na mimi nitatulia na kuweza hata kumsikiliza Mungu kwa muongozo. Ila ukianza na kumuita baba Naya!” “Basi Joshua. Nakusikiliza wewe.” “Basi tulia uone wokovu wa Bwana. Si rahisi kama inavyosikika, lakini nimekwambia nini?” “Nihakikishe katika yote, nibaki mimi ndio nimesimama.” “Safi sana. Sasa huu mchana wa leo, tunatembeza mfungo, ili kuweza kumsikia Mungu vizuri. Shibe itatufanya tushindwe kusikia vizuri. Masikio ya rohoni yanataka utulivu.” Naya akambusu shavuni.

“Asante Joshua. Niliingiwa hofu nilikuwa sijui itakuaje! Kwanza kwako baada yakusikia Malon amekuja mpaka hapa, na nilitoka bila kuaga!” “Ulikosa Naya. Ulitakiwa kumuaga Jamal. Na ujue umemuharibia na Jamal. Ataonekana anazembea.” “Nimekosa Joshua. Hata Jamal nimemuomba msamaha. Akaniambia nishukuru kwa sababu ni mimi na huwa namsaidia sana kwenye mengi. Amesema ingekuwa mwingine angeshanifukuza muda mrefu sana.” “Unaona mbegu ya uadilifu imeshaanza kutoa mazao? Haikukulipa wakati uleule, lakini wakati unaohitaji imejibu.” Naya akatulia akifikiria.

“Ni nini?” “Nikwambie kitu Joshua?” “Nakusikiliza.” Joshua akaangalia saa yake ya mkononi. “Nahisi Njama anahasira na mimi kwa sababu nilimkataa yeye, nimekukubali wewe.” Joshua akacheka na kumtolea simu yake akamuonyesha ujumbe. ‘Analia wivu huyo. Naya alimkataa.’ Ulikuwa ujumbe ametumiwa Joshua. Naya akashituka sana. “Nani amekutumia huu ujumbe.” “Mimi hata sikujua kama Njama alishawahi kukutongoza mpaka Fina aliponitumia huu ujumbe baada ya kuniletea mahudhurio yenu. Hapo ndipo nikafunguka macho. Lakini pia, amechukia kutambuliwa wazo lako wala si yeye. Ameona unampita. Sasa wewe usiwe na hofu. Baada ya yoote, mimi na wewe tutoke tumesimama.” “Acha nikuombee Joshua.” Akamshika mkono na kumuombea kwa ufupi tu.

Wakati wanaomba Jamal akagonga kioo. Wakamaliza, Joshua akafungua. “Namuhitaji Naya, Kiongozi. Naona habari imegeuka.” “Nini tena?” “Jamaa anashitaki kuwa wazo alilotoa Naya, wewe ulimpa ili aje aseme pale, aonekane wa maana, apewe ajira ya kudumu. Hapa ameomba kamati ya nidhamu pia ifanye kikao na sisi. HR mkuu akiwepo.” “Mungu wangu!” Naya akashituka sana na kumwangalia Joshua. Joshua akacheka. “Show time.” Joshua akaongea hivyo kwa kujiamini, Jamal na Naya wasielewe. “Kiongozi unaelewa lakini upana wa hili jambo?” “Oooh Sana tu Jamal. Ni kubwa zaidi ya hivyo ulivyosikia.” “Nitafanyaje Joshua?” “Kumbuka kila kitu tulichozungumza. Nenda na Jamal. Kumbuka, it may get worse before it gets better.” Akashuka garini.

Akaenda kumfungulia mlango Naya, akashuka. Jamal akasogea pembeni kidogo. Akawa kama amemkumbatia Naya, akamnong’oneza. “Fanya kila utakachoambiwa, ila fanya kwa ufasaha sana. Ukiitwa mbele ya wakubwa, hakikisha unamuwakilisha Naya vizuri, tena nenda umbali mkubwa ila kwa kifupi na ufasaha sana. Hii ni nafasi ya pekee Mungu anakupa kukutana na wakubwa wa hii kampuni. Inaweza isirudie tena. Ni nafasi ya pekee. Wewe ndio unahatima ya huo mwisho. Hujajiandaa, lakini Mungu atakupigania.” Akambusu karibu sana na sikio Naya akasisimka mwili mzima, akafurahi.

Joshua akamgeukia Jamal. “Jamal hii sura niione hivi hivi jioni baada ya kazi.” Akimuonyeshea Naya anayecheka. “Mbona kama huelewi ukubwa wa hili jambo kaka!” Joshua akacheka. “Kazi yangu ya wakati wa chakula cha mchana, nimeifanya kwa uaminifu, tena vizuri sana Jamal. Nimekurudishia mfanyakazi wako akiwa ametulia, na anauwezo wa kufanya kazi vizuri. Si ndio maana yupo hapa? Kazi.” “Kweli kaka.” “Basi chapakazi, jembe unalo nimekukabidhi, tayari kwa kazi.”  Joshua akandoka kwa ujasiri wote. “Huyo ndio Joshua Kumu bwana!” Jamal akaongea akimtizama anavyopotelea bila shida. “Kichwa chake sijui kina nini huyu Jamaa!” Jamal akaendelea kuongea akimshangaa Joshua ambaye alishaondoka. Naya akajisikia furaha, ujasiri ulishaongezeka.

“Halafu wewe Naya, kwa nini hukuniambia kama Njama alishakutongoza?” Naya akamshangaa Jamal kama anayemwambia haikuwa ikikuhusu. “Mwenzio analia wivu tu.” Naya akajua Fina ashasambaza. “Umemkataa yeye, ukamkubali bosi wake!” “Kweli Jamal unashangaa hilo? Wewe mwenyewe unaona akili yake kwa kile anachokifanya sasa hivi. Atakuwa mwanaume wakuongoza familia gani yule!?” Jamal alicheka sana. “Naona Joshua ameshakuambukiza Naya!?” “Kweli bosi wangu. Ona fujo yote hii anayofanya! Ni nini sasa?” “Kwa hiyo sasa hivi huogopi tena?” Naya akapandisha mabega kukataa macho chini. Jamal akacheka sana. “Mimi ilimradi Joshua wangu yupo sawa, wengine sijali.” Hilo lilimgusa sana Jamal. “Kumbe mpo serious na Jamaa!?” “Sitaki kucheza Jamal! Mimi sio mtoto mdogo.” “Ndio maana nakupenda Naya. Twende tukapige kazi.” Jamal na Naya wakarudi ofisini hata Jamal akaonekana ametulia sasa. 

~~~~~~~~~~~~~~~~~

Alipoingia tu ofisini ujumbe ukaingia kutoka kwa Joshua. ‘Tokea uanze kazi, haya ndiyo masaa uliyofanya kazi. Na kuzalishia kampuni.’  Akamtumia jumla ya masaa yote. ‘Lakini umelipwa kwa masaa haya tu.’ Akamtumia ujumbe mwingine. ‘Ndio mambo yakuzungumza mbele ya Uongozi, kikaoni, sio upuuzi wa dakika 9 ulizotoka. Umenielewa?’ ‘Nashukuru kwa hizi taarifa. Nitazitumia vizuri sana.’ ‘That’s my girl.’ Joshua akamrudishia huo ujumbe. Naya akacheka akijua amemfurahisha. Naya aliyerudi siye waliyemuacha wakimcheka. Naya alirudi jasiri, akarudi kitini na kuanza kuchapa kazi akiwa ametulia.

Baada ya lisaa Jamal akamfuata. “Nusu saa kuanzia sasa unatakiwa kwenye kamati ya nidhamu.” “Mpaka hapo na mimi nitakuwa nimekamilisha kila kitu. Acha nimalizie kabla ya muda kufika. Tunakwenda wote?” “Na mimi natakiwa Naya! Hili jambo limekuwa kubwa na naona linaibua mengine mengi.” Wote wakawa wakiwasikiliza. “Nisamehe bosi wangu. Sikukusudia kukuingiza matatizoni.” “Daah!” “Nisamehe Jamal. Sikujua kama itakugharimu hivi.” “Naamini na hili litapita.” “Hata mimi nina matumaini. Acha nimalizie kwa haraka.” Naya akarudisha akili kwenye kompyuta na kuendelea na kazi, Jamal akaondoka, nakushangaza wenzie waliokuwa wakifurahia anguko lake. Kimya akiendelea kufanya kazi.

“Ndio muda wenyewe Naya. Tusogee.” “Hata hivyo nishamaliza kazi uliyonipa.” Ghafla Jamal na Naya wakawa watu wakuzungumza lugha moja. Naya akatoka hapo na pochi yake na kijalida pamoja na simu yake akamfuata Jamal nyuma. “Niliwaambia nyinyi, atatuacha tu.” Naya na Jamal wakawasikia wakimsema Naya. “Yako wapi? Hekaheka za kudamka, kujidai mfanyakazi bora! Yako wapi?!” Wakaongea kwa kejeli wakimcheka Naya. Jamal akamwangalia Naya, Naya akacheka tu akiendelea kutembea.

~~~~~~~~~~~~~~~~~

Mambo yanazidi kupamba moto. Usipitwe kujua kitakachoendelea kwa Naya.

 

CONVERSATION

0 Comments:

Post a Comment