Naya Mbele Ya mshitaki wake, nauongozi wa kampuni.
Walifika
na kuambiwa wakae nje, mpaka watakapoitwa. Akaanza kuitwa Naya. “Kila la kheri
Naya. Naomba usinichome tu.” “Siwezi Jamal, bosi wangu.” Naya akabeba vitu
vyake vyote akaingia navyo ndani. Hofu ikaanza kumuingia baada ya uhalisia. Sura
za viongozi wa ngazi za juu kwenye hiyo kampuni ndio alizozikuta hapo kwenye
hicho kikao kinachomuhusu yeye kilichoitishwa ndani ya siku moja na
Njama, ambapo isivyo kawaida ni ngumu sana kufikia aina hiyo ya viongozi kwa
urahisi. Inamaana kuna ratiba zilizovunjwa ili wawepo hapo! Ndipo akaelewa sasa
kile Jamal alichokuwa akimwambia Joshua, kuwa jambo limekua kubwa zaidi ya
walivyodhania. Na viongozi wote wa kitengo chake cha masoko, yaani waliopo
chini ya Joshua walikuwepo kasoro Joshua mwenyewe ambaye aliwakilishwa na Jema.
Kila alipozungusha macho kuangalia waliokaa mle ndani ya hicho kikao
kinachomuhusu yeye, ndivyo kadiri alivyoelewa kuwa kweli Njama amefanya mambo
kuwa makubwa.
“Karibu
Naya.” Kiongozi wa nidhamu ndiye aliyemkaribisha. Alikuwa mwanamke ambaye aliogopewa
sana hapo kwenye hiyo kampuni. Mkali na mbabe hata kwa kumtizama tu alibeba
utisho wa kinidhamu. Alijulikana kwa jina la Mama Masinga. “Unaweza kukaa tu.”
Akaongeza. Naya akakaa. “Unajua ni kwa nini upo hapa?” Akaanza Mama Masinga.
“Kwa harakaharaka naweza kudhania ni kutokana na barua niliyoambiwa niiandike.”
Naya akajibu. “Inaonekana haikuwa na maelezo yakutosheleza.” Naya akatulia
akisikiliza. Wote wakamtizama. Naya akajiweka sawa. “Nasikiliza.” “Umesikia
kitu nilichokwambia?” Yule mama akauliza kwa ukali kidogo. Jema akabaki
akimtizama Naya. “Kwamba maelezo hayakutosheleza?” “Ndiyo. Una lipi la kuongeza
kabla hatujafanya maamuzi.” Ikawa kama wanamtisha.
Naya
akaweka kijalida chake pale mbele ya meza na kukifungua wote wakimtizama.
“Labda kabla sijazungumzia dakika 9 ambazo nimechukua leo nikatoka bila kumuaga
Jamal ambaye ndiye kiongozi wangu, mbali na masaa 708 ambayo nimekuwa
nikiyatumia hapa kwenye hii kampuni kuzalisha, huku nikiwa nimelipwa masaa 644
tu mpaka sasa bila kulalamika popote, ila kufanya kazi bila kuchoka nikifikiria
jinsi ya kuboresha kile mlichoniitia hapa kwenye hii kampuni, naomba nichukue
muda mfupi tu kuzungumzia Hili. Naona ni wakati mwafaka kwa kuwa karibu
viongozi wa vitengo vyote mpo hapa.” Naya akaanza kwa lugha ya kingereza kile
cha kawaida kabisa, kwa kuwa walimpokea kwa lugha ya kingereza, akajua ndio
anatakiwa kuzungumza lugha hiyo. Mpaka hapo akawashangaza wote na kuwafanya
watulie.
Muda
aliotumia kama matron kwenye shule ya watoto wanaozungumza kingereza kitupu
mpaka wafanyakazi walitakiwa kuzungumzia lugha hiyo tu, siku hiyo ilimfaa.
“Mimi ni mbunifu wa mavazi.” Akaendelea Naya taratibu tu. “Wakati nipo chuoni
mwaka wa tatu, katikati ya ubusy wa chuo, pia niliweza kubuni mavazi 29,
tofautitofauti kwa size mbalimbali. Nilikusanya watu pale
Plaza, nikauza zile nguo kwa asilimi 85 kwa siku moja tu pamoja na
vitu vingine kama sendozi ambazo nilinunua na kuzibuni kuendana na nguo
nilizotengeneza. Ninachotaka kusema si kuwaambia juu ya uwezo wangu wakufanya
kazi nyingi kwa wakati mmoja, au kuwaambia kipaji nilichonacho, hapana. Nataka
kuzungumzia juu ya soko.” Naya akaendelea wote kimya.
“Zile
nguo zilirudisha faiza zaidi ya mara mbili ya gharama za uzalishaji. Hapo
namaanisha ufundi, vitambaa, umeme mpaka wale warembo waliovaa yale mavazi,
nililipa na kuweza kuzalisha hiyo faida. Kivipi! Ndicho ninachotaka kuzungumzia
japo najua mngependa kusikia juu ya dakika 9 nilizopoteza leo,” “Mbali na masaa
708 uliyokwisha tumia na kulipwa 644 tu?” Akamalizia Jema. “Asante.” Naya akamshukuru
Jema na kuendelea.
“Katika
yote niliyofanya wakati nikibuni mavazi, niliwaambia viongozi wangu na ndio
kitu nilitakiwa kufanya na Njama leo, lakini kwa dakika 9 tu nilizopoteza,
nasikitika nimekosa hiyo nafasi. Lakini kama nilivyosema wakati ule kwenye
swala za bidhaa za hapa, ningepata nafasi nyingine ningeweka msisitizo kuwa,
kama tunataka tuuze zaidi, na kuweka mabadiliko, tumfikie huyu mtu wa mwisho
kabisa, mtumiaji. Siongei kwa nadharia tu, ndivyo nilivyofanya mimi, na ikalipa
sana. Na sisemi sicho kinachofanyika hata sasa, ndicho kinachofanyika lakini
yapo mambo ambayo ningepata nafasi ya kusema leo ningeyasema, kama siyo nafasi
niliyopoteza kwenye dakika 9 za leo,...” “Mbali na masaa 708 uliyokwisha tumia,
na kulipwa 644 tu?” Afisa mwajiri mkuu akaongeza, wote wakacheka.
“Kuweka
sawa hilo, huwa naingia hapa kazini saa 11:15 asubuhi na nikichelewa sana ni
11:30.” Naya akaongeza. “Muda huyo ninapofika kazini, siji kwa sababu ya
mtandao wa bure. Nimekuwa nikifanya uchunguzi. Ningekuwa na nafasi ya kuzungumzia
hili, pengine leo ningezungumza na Njama, lakini nimepoteza hiyo nafas...” “Kwa
kupoteza dakika 9.” “Asante kwa kukumbuka hilo.” “Mbona ni kama mnafanyia mzaha
kitu cha msingi na mnakubali awapoteze malengo?” Njama akalalamika.
“Niliambiwa
nizungumze Njama. Tafadhali naomba nimalizie.” Akajibu Naya. “Tulipokuwa Mbeya
kikazi, kuna mambo niliyaona juu ya bidhaa zetu. Kama Jamal angeruhusiwa
kuingia angekumbuka hili. Tulifanya Survey. Sijui kama zilifanyiwa
kazi kiofisi, lakini katika kuwahi kwangu kila siku asubuhi, mimi binafsi, kwa
kuamua kwangu, nilifanikiwa kuweka pamoja na kutengenezea kama maelezo,
nikalinganisha na mazungumzo niliyozungumza na wenyeji wa pale.” “Naomba na
mimi Naya hiyo ripoti uliyotengeneza kutokana na Survey mliyofanya
Mbeya, nimpelekee Kumu, mkuu wa kitengo.” Jema akasimama kabisa. “Hapa ninayo
nakala moja tu, naomba nije kukutumia baadaye nikishazungumza na Jamal,
au kama ni sawa, naomba Jamal akaribishwe wakati nikizungumza. Akiidhinisha,
nitaituma mara nitakapofika kwenye meza. Tafadhali Jema, ili isiwe namruka yeye
aliyekuwa amenituma hiyo kazi.” Watu wote wakakubaliana. Jamal akaitwa.
Aliingia
akiwa amekunja uso. “Kwema?” “Nilikuwa nikizungumzia ile survey uliyotaka
tufanye ulipotutuma Mbeya.” Naya akamjibu kwa kiswahili kama alivyoingia na
kuzungumza kiswahili. Jamal akaonyesha hakumbuki kabisa. “Niliifanyia kazi kama
ulivyonituma, ndio naizungumzia.” Jamal akakaa kwa wasiwasi. “Katika watu 98
ambao nilifanikiwa kupitia karatasi zilizotumika kwa survey, kwa
kuwa zilikuwa karatasi 100, tukahakikisha tunapata hao watu 100, lakini kwa
bahati mbaya mpaka sasa tunazo 98 tu. Wote. Nikisema wote, namaanisha
watu 98 wote walisifia ubora wa bidhaa zinazotengenezwa na kiwanda chetu. Ila
wote walilalamikia vitu viwili.” “Nini?” Ghafla wote wakawa na shauku ya kutaka
kujua. Jamal kimya.
“Ipo
kwenye hii ripoti. Nafikiri Jamal atawakilisha baada ya kupitia na kuridhika,
maana nilitaka kukamilisha kila kitu, ili ninapomkabidhi, asipatwe na maswali.”
“Lakini unaweza kuzungumza kwa kifupi tu.” Msaidizi wa CEO akaonekana na shauku
kubwa zaidi. Naya akamtizama Jamal. Jamal akaonekana kuridhia. “Okay. Naona
bosi wangu ameniamini naweza kusema.” Naya akazungumza akiwa ametulia mpaka
Jema akafurahi maana aliweza kuvuta wote na kuweza kumsikiliza kwa shauku
kubwa, tena si kama mkosaji ila mtu mwenye manufaa makubwa.
“Tatizo
ilikuwa ni bei na upatikanaji wa ile bidhaa kwa urahisi.” Wote
wakatulia. “Najua kwa upande wa bei mliyopanga, nikutokana na uzalishaji wa
hapa ili kupatikanika kwa faida. Usambazaji je?” Naya akauliza. “Na je, endapo
mkipata njia rahisi ya kushusha gharama ya uzalishaji kama nilivyowaambia mimi
nilifanya, nikaweza kuzalisha zaidi ya mara mbili? Ipo njia. Na mbali na hapo
katika hayo masaa..” “708 .” Akadakia Afisa Mwajiri nakufanya wote wacheke
kasoro Jamal ambaye hakuwa anaelewa na Njama mleta kesi. “Ndiyo. Katika hayo
masaa 708 niliyokuwa nikiwahi hapa kazini, nimejaribu kufanya utafiti
nikilinganisha na uzoefu wangu wa masoko wa nini kifanyike ili kufikia mtumiaji
kwa urahisi, nafuu na kwa haraka. Hiyo inaongezwa na ufahamu nilioupata kutoka
kwenye nchi za wenzetu pia.” Naya akawa kama amemaliza.
“Mbona
kama umemaliza tena!?” Wote wakawa wamehamasika wanataka kujua zaidi. “Hapana.
Naomba nimalizie kwa kurudi kwenye zile dakika 9 zilizogharimu kampuni kutopata
mchango wangu leo kupitia kiongozi Njama. Niombe radhi kwanza kwa Jamal
ambaye ndiye naripoti kwake. Nilikosea kutoka bila kumuaga, kwa kuwa nilipata
dharula. Ubaya wa dharula ni mmoja tu, kuwa ni dharula. Samahani sana
Jamal kwa kukufikisha hapa. Jamal ananiheshimu mno na ananiamini. Leo najisikia
kumdhalilisha. Na samahanini sana kuwapotezea muda watu kama nyinyi ambao mna
majukumu mazito na kuwepo hapa kuzungumzia hizo dakika 9 nilizopoteza leo na si
hayo msaa..” “708?” “Hapana, msaa 644 ambayo mmekwisha nilipa.” Naya
akamrekebisha huyo mama ambaye watu walimuogopa sana. Akatulia akiwatizama
kwamba ameshamaliza walichomwitia.
“Tunaweza
kupata kwa ufupi tu suluhu uliyopata kutokana na survey uliyofanya
mkoani Mbeya, uzoefu wa biashara ulionao na uliyoona wakifanya wenzetu huko
nchi za ugenini?” “Ningependa kufanya hivyo, lakini najihisi nitakuwa navuka
mipaka na ninakuwa mtu wa mambo nusunusu kwa kuwa hata wazo la kwanza ambalo
nililichangia siku ya ijumaa, nimepoteza nafasi ya kukamilisha kwa dakika 9
nilizopoteza. Kingine nafikiri nawajibika kwenye idara yangu kwanza kabla ya
watu wengine.” “Unamaanisha mpaka ukazungumze na Joshua? Akupe kitu gani
chakufanya au kusema ndipo uje uzungumze?” Njama akauliza. Watu wote
wakamgeukia Njama.
“Nyinyi
hamumsikii Joshua akiongea hapa kupitia mdomo wake huyu!?” Njama akajitetea,
wote kimya. “Hapo anayezungumza ni Joshua, wala si yeye na ndio maana mnaona
hataki kuongea zaidi mpaka akaulize tena. Joshua anampa mawazo ili tu
mumuajiri.” Naya akafunga mafaili yake, akamtizama Mama Masinga aliyemkaribisha
tokea mwanzo. Wote kimya maana ni kama Njama alitupa shutuma na Naya hakutaka
kujibu.
“Si
mnaona anashindwa hata kukataa! Kwa kuwa anajua ni kweli. Joshua anamwambia nini
chakuja kuzungumza, ndio maana mnamuona ni jeuri.” Njama akaendelea. “Anataka
kuendesha kitengo vile atakavyo kwa kuwa anatembea na Joshua. Kampuni haiwezi
kuendeshwa hivyo kimapenzi.” Njama akaongea tena kwa kingereza vizuri tu,
wakati Naya alimalizia kwa kiswahili baada ya kuingia tu Jamal. “Una chochote
cha kujibu Naya?” “Juu ya nini?” Naya akamuuliza Mama Masinga kwa nidhamu,
akiwa ametulia tu. “Samahani sijasikia swali ninalotakiwa kujibu.”
“Anachozungumzia Njama.” Mama Masinga akawa kama anamkaribisha tena. Ila safari
hii kwa utulivu.
“Ofisini
kwetu nafikiri kuna kamera kama sikosei, au Jamal kiongozi wangu yupo hapa
atawaambia. Nisingeacha kuzalisha nyumbani kwetu, na kuja kupoteza hapa masaa
708 yenye ushahidi na nilichozalisha, kama akili zangu zingekuwa kwenye maneno matupu.
Muulizeni Jamal. Mimi si mtu wa kupoteza muda au kunikuta katikati ya maneno
mengi. Kwa heshima yenu, naomba msitake leo nianze kuzungumzia majungu.
Hizo ni shutuma zake. Mnayo haki yakumsikiliza na kuamua. Lakini mimi huwa masikio
yangu hayaelekei kwenye maneno maneno. Lasivyo nisingefika hapa nilipo
sasa hivi. Mkitaka nizungumzie kile mlichoniamini nacho mpaka kunipa hii kazi,
ningependa na nipo tayari. Lakini si maneno ya uzushi, yakufikirika tu.
Tutajikuta tunapoteza muda mwingi sana hapa, na wote tunakwama kwenye ulalamishi
bila kutimiza kusudi lililotuweka hapa. Kwa heshima kabisa, viongozi wangu,
naomba niishie hapa.” Chumba kizima kimya.
Lakini
baada ya muda wakamsikia Jamal akicheka taratibu. “Unakumbuka nilikufuata
Mkubwa, nikakuomba katika kundi la kwanza na la pili tuliowapa kazi, tumpe
ajira mmoja wao, mkanikatalia mkisaidiwa na Njama kuwa mpaka mjiridhishe?”
Jamal akamuuliza HR, Afisa Mwajiri kiongozi, tena akamuuliza kwa kujiamini
kabisa. Kimya. “Basi kama huwa mnanisikia nikisema jembe langu, ndiyo huyu
Naya. Ndio maana japokuwa walikuwa peke yao, niliwatuma mkoani Mbeya, nikijua
safari hii kazi itafanyika. Nikamwambia hata Njama, kama atabisha, aseme leo,
kuwa, nimetuma jembe langu kule, sina shida. Nitakwenda kufunga tu. Awe
mkweli kama wakati ule huyu mtoto alikuwa ameshaanzana na Kumu.” “BADO.”
Akadakia Jema kwa haraka.
“Basi
ndio mjue hichi ni kichwa bila Joshua.” Akaongeza Jamal kwa kujivuna haswa. “Na
ndio maana Joshua hakutaka kuwepo hapa kwenye hiki kikao yeye kama mkuu wa
kitengo ili kufanya msishindwe kuzungumza. Lakini siku ile ya kikao, Joshua
hata hakuwa akijua kama Naya alikuwepo bado hapa ofisini. Bisha Njama.”
Jema akaongeza. “Mnafiki tu wewe Jema, unataka Joshua akusogeze karibu zaidi.”
“Umekasirika tu Njama na kusahau! Kumbuka mpaka Joshua akauliza kwa kulalamika
kwa Jamal ni kwa nini anamjazia Naya kazi mida ya jioni wakati yeye ndio
anafika hapa kazini wakwanza! Tena akamuita ili aje amsubirie! Sasa alimpa saa
ngapi jibu la kuja kwenye kikao ambacho hata Naya hakuwa muhudhuriaji?”
Wakaanza kubishana wao wenyewe wenye kitengo cha masoko mpaka viongozi wengine
wa idara hiyo ya masoko wakitetea kwamba ni kweli siku ile Naya alipotoa
mchango hakuwa amepangwa na Joshua. Alishitukizwa na kuwashangaza na wao kama
siku hiyo hapo kikaoni. Ndipo Jamal na Jema, wakapata nguvu na kumshambulia
Njama. Naya kimya ametulia tuli.
Katikati
ya huo mzozo, Naya akaruhusiwa kuondoka. Akasimama na kumsogelea Jamal.
“Zimebakia dakika chache tutoke, sijisikii vizuri, naomba nikapumzike.
Kisha utanijulisha mwafaka.” Akamnong’oneza Jamal. “Pole sana. Wewe nenda
kapumzike, nitakujulisha.” “Asante.” Akageukia wengine. “Asanteni sana na
samahanini kwa usumbufu wote niliosababisha.” “Hakuna tatizo Naya. Wewe endelea
na kazi. Tunachotaka ni uchapakazi na inaonekana Jamal anakutegemea sana.
Tutajipanga vizuri ili kuweka mazingira mazuri ya wewe kufanya kazi.” Akajibu Afisa
Mwajiri wao mkuu. “Asante sana.” Ukweli kichwa kilikuwa kikimuuma sana Naya,
halafu katikati ya kikao tumbo nalo likaanza kumuuma. Na akakumbuka hana
usafiri ni kwenda kuwahi daladala. Hata hakugeuka nyuma, akatoka kuwahi
daladala kabla fujo za watoka kazini hazijaanza.
Kwa Naya.
Kichwa kilikuwa kikimuuma kwa kulia siku hiyo na sababu ya hofu,
Naya akaanzwa na siku zake akiwa njiani. Akampigia simu baba yake. “Naumwa
sana, mimi sijui kama nitafika nyumbani.” Baba yake akajua tayari hilo juma
limeshaharibika. “Unataka
nikufuate wapi?” “Nipo
kwenye daladala, nimesimama. Tumbo linauma, kichwa kinagonga karibu kupasuka.
Mimi naumwa baba, sijui kama nitakuona tena!” Naya
akaendelea kulia taratibu kwa sauti ya chini watu wengine kwenye daladala
wasimsikie. “Utanikuta kituoni nikikusubiri. Nakuombea ufike
salama. Tulia kabisa. Maana unajua ukilia na kichwa kitazidi kuuma.” “Nasikia na
kutapika. Nimezidiwa.” “Pole mama.
Pole sana mama mzazi.” “Heri nikukute tu kituoni lasivyo sitaweza kufika
nyumbani.” “Nimeshaanza kutafuta
viatu ili nisogee kituoni.” Hapo Naya
akaridhika. Ndipo akakata simu na kurudisha mfukoni.
Kikaoni.
Huku nyuma kikaoni kukaendelea kutupiana maneno. Jamal anatetea
kazi yake huku Naya naye anatetewa na yeye Jamal, Jema pamoja na viongozi
wengine walioweza kubishana zaidi waliokuwepo kikao cha kwanza Naya alipotoa
wazo. Halafu sasa Naya mwenyewe akawa ameacha jina tofauti na walivyotegemea.
Naya waliyemuhoji anajiamini na anajua kazi yake. Kubishana kukaendelea,
ikageuka ugomvi sasa. Ugomvi nao ukaendelea, ikawa tena lawama.
Mwishoe ikabidi msaidizi wa CEO aulize wanaweza vipi kupitisha
hata mwezi bila kumuajiri mtu kama Naya! Ambaye anaonekana atasaidia kampuni!
“Hana lolote huyo, ni Joshua tu ndiye anayezungumza.” Njama akapinga. “Sasa
kuna shida gani ya kutumia Joshua Kumu wawili, tena kwa wakati
mmoja, kwa kazi tofautitofauti, halafu kwa bei nafuu!?” Akauliza
yule msaidizi wa CEO na kufunga wote mdomo.
Maana Jamal na Jema walikuwa wakitetea ni akili ya Naya mwenyewe,
Njama anapinga ndipo akauliza tatizo lipo wapi na kunyamazisha wote. “Maana
hebu tufikirie kwa pamoja tukiwa tu tumetulia. Je, Joshua ameshindwa kufanya
kazi yake?” Akauliza. Wote kimya. Hakuna anayeweza kumgusa Joshua Kumu kwa
utisho alioweka hapo kwenye hiyo kampuni. “Kwa ukimya huo inamaana jibu ni hapana.
Au sivyo Njama?” Wote wakamgeukia yeye. “Sema sasa Njama. Unatatizo na Joshua?”
Jema akamuuliza kwa kumsuta. “Mimi sijasema ninatatizo na...” “Kwa maana
nyingine jibu ni hapana.” “Kwa nini unanikata?” “Ushatupotezea muda mwingi sana
Njama. Siku ya leo umeiharibu vibaya sana kwa kutokuwa mwanaume wakuweza
kupokea jibu la ‘hapana’.” Hapo pakalipuka ugomvi mwingine.
“Mimi sijawahi kumtaka Naya, ila Naya mwenyewe ndiye aliyenitongoza
nikamkataa.” Hapo napo Jamal na Jema wakambadilikia kwa kelele kubwa mno. Watu
wazima hao na majukumu yao wakageuka kama wasio na kazi, wasutanaji. “Naya
aliona mimi sina mpango naye ndio akajisogeza kwa Joshua. Lengo lake...”
Wakaanza kumcheka, ghafla yeye Njama ndio akageuka kichekesho pale.
“Binafsi naomba kukutahadharisha kabla sijaondoka, Njama.”
Mama Masinga akafanya wote watulie. “Huko unako kwenda, kama hujachelewa,
nashauri rudi kwa haraka.” “Sikukwambia mimi Njama? Nilikuonya wewe.” Jema
akaingilia. “Unafanya mchezo wa hatari sana ambao unaanza kukugharimu. Sijui
kama unanielewa Njama?” “Mbona kama umeshaamua kuwa upande wa ....” “Upi Njama?”
Mama Masinga akauliza kwa ukali kabisa.
“Wote mnanijua mimi sina ninayemuogopa hapa, ila kusema kweli. Na
ndicho ninachokwambia. Unashika maeneo na watu hatari sana, itakugharimu
wewe mwenyewe. Unanielewa Njama?” Akauliza kwa ukali zaidi. “Sikutishi, ila
nakutaarifu tu. Wote tumeajiriwa hapa. Lakini wapo ambao wameshika hii kampuni.
Ajira zao zipo kwa wino usiofutika kwa urahisi, wengine tumeandikwa kwa penseli
tu. Kufutika kwetu ni rahisi sana. Hawa waajiriwa wa aina ya kwanza hawa, bila
wao mambo hayaendi hapa. Na kampuni inalipa gharama kubwa sana
kuhakikisha kila siku ya asubuhi, wanajulikana kama ni wafanyakazi wa hii
kampuni. Halafu hawa wezangu na mimi hawa ambao ajira zetu zipo kwa maandishi
ya penseli, hata tusipokuwepo hapa, hakuna anayejali au kuona utofauti. Sijui
kama unanielewa?” Yule mama akauliza kwa ukali zaidi. Jamal na Jema wakaanza
kucheka taratibu.
“Gharama ya kuwepo kwao kwenye hii kampuni haiangalii mtu
yeyote, ila wao tu. Na wapo watu wanawekwa maalumu, kwa ajili yao tu. Wanaweza
kuwa hata watano ila lengo ni mtu mmoja tu. Unanisikiliza Njama?” Kimya.
“Ukitoka wewe hapa, ukaenda kutafuta kazi sehemu nyingine, bado watapiga simu
kuulizia ulikuwa mtu wa namna gani hapa kazini. Unataka kuharibu maisha yako
kwa dakika 9 tu ambazo ninauhakika hata wewe huwa unafanya kama alichokifanya
huyu binti! Leo unafanya haya yote kwa mtu unayejua kabisa ni muhimu sana kwa
Jamal!” Akamshangaa kwa hasira kabisa.
“Acha Njama. Kama hujaharibu bado kiti unachotakiwa kukalia kesho
ukirudi kazini, nashauri tengeneza. Unanielewa Njama?” Aliuliza lakini kila mtu
alijua anachomaanisha. “Nafasi yako ilitengenezwa Njama! Usisahau hilo.” Afisa Mwajiri
mkuu akaingilia. “Binafsi niliipinga kabisa hiyo nafasi yako, sikuona
sababu, lakini Joshua aliing’ang’ania mpaka ikakubaliwa kwa
sababu yeye ndiye aliyeitaka na kutaka wewe uwepo ili wewe usimamie
utendaji, Jema mawasiliano upande huo wa masoko.” Huyo Afisa Mwajiri ikabidi
aweke wazi kabisa, wote kimya. Mama Masinga akasikitika kwa sauti. “Hivi
unaelewa unapoambiwa unacheza mchezo hatari, Njama?” Akamuuliza. Njama kimya.
“Hawa vijana hawakumbuku wanakotoka! Ila ukumbuke nimekuonya Njama.” Mama Masinga
akakusanya vitu vyake.
“Binafsi sioni kesi yakuendelea kupoteza muda hapa. Kama unatatizo
jingine, utafuate njia kama ulizofuata leo. Tutakuja tena kukusikiliza. Ni haki
yako.” Akamgeukia Afisa Mwajiri. “Kama na nyinyi hamjachelewa, nafikiri
mnahitaji mtu kama Naya kwenye ofisi hiyo ambayo Jamal amekuwa akilia wakati
wote hapati watu wa kueleweka. Yule binti anajielewa. Wakimkamata
kampuni nyingine, mjue sisi tumekula hasara.” Yule Mama Masinga akaondoka.
Ikaanza mipango juu ya Naya.
Kwa Joshua.
Tayari
ilikuwa saa 12 jioni wakati Jema anarudi ofisini na kumkabidhi Joshua rekodi
nzima ya kile kikao. “Naya yupo na hali gani?” Hilo likawa swali la kwanza hata
kabla hajafungua hiyo rikodi kusikiliza. “Alitoka pale, nilimsikia akimuomba
Jamal ruhusa aondoke, hajisikii vizuri.” “Kwa hiyo muda wote huo
hakuwepo kwenye kikao?!” “Aliondoka, lakini Joshua!” Joshua alishasimama.
“Nini?” “Yule mtoto ni kichwa kilichokamilika! Halafu kumbe anajua kuzungumza
lugha ya kingereza vizuri bwana!” Joshua akamtizama na kuanza kumpigia simu
Naya. Ikaita bila hata kupokelewa. “Habari imegeuka, sasa hivi wanataka kumuajiri.”
Joshua akamtizama na kurudisha macho kwenye simu. “Naomba tuzungumze kesho
Jema. Natoka.” “Kila kitu nimerikodi. Utasikiliza kwa wakati wako.” Joshua akatoka
kama anayewahi.
Muda
wote alikuwa akimsubiria Naya atoke kikaoni amrudishe nyumbani akijua baba yake
amejua kuwa yeye ndiye amemwambia arudishe gari kwa Malon. Alishaagiza gari
yake iletwe kutoka nyumbani, akijua Naya akitoka kwenye kikao, atarudisha yeye
mwenyewe nyumbani kwao asijue Naya alishatoka. Joshua akajaribu kumpigia tena
lakini pia haikupokelewa. Akaingia garini na kutoka kuelekea nyumbani kwa kina
Naya ili kumwangalia huku akihukumiwa moyoni na kushindwa hata kusikiliza
rikodi aliyopewa na Jema.
Kiluvya.
Alifika
kwa kina Naya giza lilishaingia kabisa. Zayoni ndiye aliyemfungulia geti.
Akafunga na kumfuata. “Karibu.” Joshua naye ndio alikuwa akishuka garini.
“Tumeanza kufunga geti muda wote kwa kuwa Naya hana tena gari.” Akaanza Zayoni.
“Ulikaa sana getini?” “Hapana Zayoni. Nimepiga honi mara mbili tu.” “Basi
sikukusikia mara ya kwanza. Baba ndio alinituma nitoke niangalie ili
tusimuamshe Naya.” “Naya ameshalala?” “Amerudi akilia anasema anaumwa. Alikuwa
akitapika kwa muda mrefu tokea atoke kazini, lakini ametulia. Naya akiwepo baba
hazidiwi. Baba asingekuwepo huwa anazidiwa sana. Atapona. Baba alikuwa naye
chumbani kwake, anasema na kichwa pia kinamuuma sana. Ila amelala sasa hivi.”
“Poleni sana.”
“Ila
kwa kuwa baba yupo, atakuwa sawa tu. Hata nilipompigia simu Bale kumwambia Naya
amerudi nyubani analia, akaniuliza kama baba yupo. Nilipomwambia baba alikwenda
kumpokea kituoni, akasema nisiwe na wasiwasi, kwa kuwa baba yupo, atapona tu.”
Zayoni mkimya lakini mzungumzaji haswa akiamua.
“Ujue
Naya akiwa anaumwa, ukitaka apone haraka, sio dawa. Hata mama alikuwa anajua.
Akiumwa yeye, baba awepo. Hapo hata ukimpa dawa zinafanya kazi. Ila kama baba
hayupo, hata ukimpa dawa zinakuwa hazimsaidii. Anazidiwa kabisa mpaka
mnampeleka hospitalini. Baba akija tu, akikaa naye kidogo, anapona. Kwa hiyo
atapona.” “Naamini hivyo.” Joshua akajibu maana hata ndani hakuwa
amekaribishwa, Zayoni alikuwa akizungumza tu hapo. “Naya..” Kabla hajaongea
jingine baba yake akatoka. “Kwa nini humkaribishi mgeni ndani?” “Nilikuwa
namwambia Naya anaumwa.” “Hayo unamwambia akiwa ameshaingia ndani, Zayoni!”
“Hamna shida kabisa mzee wangu. Shikamoo.” Joshua akasogea mpaka pale mlangoni.
“Marahaba.
Karibu ndani.” Wote wakaingia ndani. “Sikujua kama Naya alishaondoka! Nilikuwa
nikimsubiri nimrudishe nyumbani!” Joshua akawa kama anajitetea. “Ameniambia
imebidi arudi alianza kuumwa katikati ya kikao walichokuwa wamemwita huko
kazini kwenu. Lakini atakuwa sawa tu.” “Au tumpeleke hospitalini?” “Hapana.
Atakuwa sawa tu. Amelala muda si mrefu, baada ya kumeza tena dawa. Za mara ya
kwanza alitapika, naona hizi za pili zimekaa tumboni.” “Au ni malaria?”
“Hapana. Ana miezi yake huwa anakuwa hivyo. Atakuwa sawa tu. Anahitaji
kupumzika tu. Nafikiri pia amelia sana leo. Kesho atakuja tu kazini.” Joshua
akabaki ametulia lakini akawa ameelewa kinachomsumbua Naya mbali na kichwa.
“Ni
sawa nikienda kumuona?” “Acha Zayoni akuonyeshe chumbani kwake.” Zayoni
akaongoza njia, Joshua akafuata mpaka alipoonyeshwa mlangoni, Joshua akaingia,
Zayoni akaondoka. Akaenda mpaka pale kitandani. Akakuta amewekewa taulo
kichwani. Akajua ni baba yake tu. Akabaki akimwangalia. Mwishoe akaamua kukaa
pembeni ya kitanda. Akamtoa kitambaa na kumshika kichwa. Kikawa baridi tu.
Akamkausha usoni vizuri akamvuta tena shuka kumfunika. Akamvuta mkono wake
uliokuwepo karibu. Akaubusu kama mara mbili, Naya akageuka. Uzuri akageuka
upande aliokuwa amekaa. Akaupakata ule mkono na kupishanisha vidole akabaki
ametulia.
Joshua
alijawa hukumu kujua Naya alifika kwao na daladala, tena akiwa anaumwa, na baba
yake ndiye aliyekwenda kumpokea! Akajisikia vibaya, akatamani hata angezungumza
na Naya mwenyewe, lakini akaambiwa Naya alikuwa akitapika, kichwa kilikuwa
kikimuuma, ndio amelala. Hawezi kumuamsha. Akabaki amekaa pale amemshikilia mkono,
Naya amelala hana habari. “Njama ameniharibia siku yangu nzima ya leo!” Akalaumu
mawazoni na kuchukia kabisa. Akaona huo ndio muda muafaka wakusikilizakiliza
kilichokuwa kikiendelea kikaoni.
Akaunganisha
ile rikodi na bluetooth yake sikioni, akaanza kusikiliza kwa kupitia bluetooth
ili asimwamshe. Akaendelea kusikiliza huku akimwangalia Naya na kucheka
taratibu bila kujijua kwa furaha ya ushindi. Akajisifu kila alipokuwa
akimsikiliza Naya. Akarudia kipengele cha Naya tena wakati akizungumza huku
akizidi kujawa furaha. “That’s my girl!” Akashabikia
nafsi mwake. Alipomsikia Njama ametupa shutuma na kusikiliza jibu la Naya, akazidi
kufurahia. “That’s what am talking about!” Akamsifia huku
akimwangalia. “Kweli Mungu umenipa wa kufanana na mimi. Mfupa kutoka kwenye
mfupa wangu na nyama kutoka kwenye nyama zangu.” Akapata nafasi ya
kumshukuru Mungu wake huku akimwangalia Naya kwa kumpenda zaidi.
Akasikiliza
ile rikodi mpaka mwisho kabisa na majibu ya wote waliokuwepo kwenye kikao.
Akajua Njama ameshindwa, na bado hajapoteza heshima hata kwa viongozi wenzake
wa ngazi za juu. Bado wanamtambua kama yeye ni kiungo muhimu sana kwenye hiyo
kampuni. “Well!” Akaanza tena Joshua kuzungumza na Mungu
wake. “Umenguruma tena
Baba yangu. Nashukuru hata kwa hili jema jingine unalokusudia litendeke kwenye
hili pia. Asante Mungu wangu kwa kuwa hata sasa bado unatembea na mimi. Na bado
unaendelea kudhihirisha uwezo wako mbele za wanadamu. Nipo tayari kupokea na
uniongoze kule utakap...” Wakati anaendelea kuomba akasikia
Naya amevuta mkono wake, ikabidi kufungua macho. Akamuona kama anayeugulia
maumivu usingizini.
Machozi
yakaanza kumtoka akiwa usingizini bila kufungua macho. Akageuka upande wa pili
akiwa ameshika tumbo. “Baba!” Akaanza
kwa sauti ya chini. Kisha akaita tena kwa sauti akiwa amegeukia ukutani. “Babaa!” “Naya!” Joshua akamwita taratibu.
Akatulia kama aliyehisi amesikia akiitwa lakini kabla hajaelewa, baba yake
akaingia kama aliyekuwa akisubiria mlangoni. Joshua akasimama kwa haraka kama
mshale utafikiri mtoto aliyevunja kikombe, anamkimbia mama yake asimkute kwenye
tukio, anajihami. “Vipi mama?” “Tumbo
linaniuma mpaka nimetoka usingizini! Nifanyaje baba? Au nimpigie tu nimuulize?” Akalalamika
Naya akiwa amelala akifinya tumbo nakushindwa kugeuka. “Pole Naya.” Joshua
alimfanya Naya kushituka mpaka akakaa.
“Joshua!?” “Pole
sana.” Naya akawa kama haamini. Akamwangalia baba yake, baba yake akamsogelea.
“Pole sana.” “Asante.” Akavuta
mkono wa baba yake akauegemea kwa upendo akatulia. “Kwani mara ya mwisho ulimpa
dawa gani?” Joshua akauliza. “Za maumivu tu za kawaida. Ila kipindi mama yake
alipokuwepo, baada ya Malon ambaye huwa anajua hizo dawa ambazo hata mwenyewe
Naya anasema hazijui, ilikuwa likimuanza, anampeleka kwa rafiki yake kwenye
dispensari fulani pale Mbezi, wanamchoma sindano fulani hivi. Inamsaidia
kutulia. Lakini yule nesi naye aliacha kazi pale, mama anayejua hiyo dawa
aliyokuwa akichomwa hayupo na hataki tumuulize Malon ni dawa gani alizokuwa
akimpa, anasema zilikuwa zikimsaidia sana.” Joshua akamwangalia Naya alivyokuwa
amejiegemeza kwenye mkono wa baba yake amefunga macho akilia maumivu bila
yakutoa sauti ila machozi kumtoka.
“Napo
sio kwamba ndio kila mwezi anakuwa hivi! Hapana. Sio kitu cha kila siku ndio
maana naona hata mimi unaona nimeshindwa kushika hayo matibabu. Naweza kusema
ni tokea kifo cha mama yake. Wakati ule wa msiba aliiugua hivihivi, lakini
tokea apone, hajaugua tena ndio linarudia tena leo! Sasa inakuwa kama linakuja
akipatwa na mshituko mkali, ndio hayo maumivu na mengine yote yanakuja kwa
pamoja.” “Pole sana Naya.” “Asante, lakini
nitakuwa sawa tu.” “Unataka twende hospitalini?” Joshua akamuuliza
kwa upendo. Naya akabaki kama akifikiria kisha akamwangalia baba yake. “Wewe
unataka nini?” Baba yake akamuuliza. “Sitaki kwenda wasije kunipa madawa
ambayo siyo nikawa napoteza tu muda.” “Basi tumpigie Malon, tumuulize
alikuwa akikupa nini, na sisi tukanunue kwa haraka.” Naya akamwangalia vizuri
Joshua kama hajamuelewa.
“Ni
sawa?” “Malon ameniudhi sana leo. Ningefukuzwa
kazi kwa sababu yake na ungekuwa sio wewe ni mtu mwingine mwenye akili za
kijinga, pengine usingetaka hata kuja kuniona tena! Sitaki kumuona kwa sasa.
Acha tu nivumilie. Maana mimi namjua Malon, akijua kuwa naumwa, atajaa hapa na
dawa zake na yeye mwenyewe na hatakubali kuondoka humu ndani.” Akalalamika
Naya.
“Kama hivi anakuwa ametulia kabisa huko. Anasubiri nimtafute.
Nikimtafuta tu, ndipo anakuwa mwingi mpaka amenigharimu sana leo kama vile
hakuwa akijua kama nafanya kazi pale, leo ndio amejua na kunifuata! Heri
nimuache tu nitumie dawa alizonipa baba.” “Basi naomba tujaribu kwenda hospitali
Naya. Mimi nitakuwepo na nitaulizia matibabu wanayotaka kukupa au watakayokupa
na nitahakikisha nayajua ili wakati mwingine tujue ni nini chakukupa.”
Naya
akaanza kulia. “Mimi naona ni kama nakusumbua
tu Joshua! Acha baba anipe dawa zake, nitakuwa sawa.” Joshua
akarudi kukaa. Akamvuta mkono ambao haukuwa umeshikilia mkono wa baba yake na
kuubusu pale mbele ya baba yake. “Nipo hapa kwa ajili yako Naya. Siwezi
kuondoka mpaka nijue upo sawa. Sina ninapokwenda, sina ninakowahi, wewe unajua.
Nisipokuwa masikioni na wewe kupitia simu, unajua nakuwa peke yangu nyumbani.
Hapa nipo sehemu sahihi na muda sahihi. Hunisumbui hata kidogo. Sawa?” Naya
akatingisha kichwa kukubali. “Lakini kama
limeanza kutulia!” Akaonekana kusita tena.
Wakatulia
kidogo, ni kama Joshua akawa anasita kuzungumza chochote mbele ya baba Naya.
Baba Naya akagundua na kukumbuka huyo sio Malon asiyeweza kusubiri anapotaka
kuzungumza jambo lake. Liwe la hasira au heri. Atalizungumza tu. Hajui kujizuia
anaongea chochote, popote mbele ya yeyeote. Joshua yupo makini na maneno yake. Akatoka
kuwapa nafasi.
“Njoo.”
Joshua akamwita kwa upendo, Naya akamsogelea. “Jilaze hapa. Likirudia tena,
tunakwenda hospitalini. Sawa?” Naya akajilaza hapo alipoambiwa na Joshua.
Akamuwekea mto chini ya tumbo, kichwa akajilaza miguu kwa Joshua kama
aliyekipakata, akaanza kumsugua mgongoni. “Nimefurahi
kukuona Joshua.” Joshua akacheka taratibu. “Kwa nini hukuniambia?” “Nilijua unamajukumu mengine. Halafu kulizuka ugomvi mle
ndani ikachukua muda mrefu, nilitoka muda wa kazi unakaribia kuisha kabisa,
nikajua na wewe utakuwa ulishaondoka au upo na majukumu mengine. Tumbo nalo
likaanza kuuma katikati ya kikao, nikajiwa na hali ya kutapika. Nikaona heri
niwahi kurudi kwa baba.” “Pole sana Naya. Lakini mimi nilikuwepo ofisini
kwangu. Nilikuwa nikikusubiri nikurudishe nyumbani. Nisingeweza kuondoka na
kukuacha katikati ya ile kesi.” Ikamgusa sana Naya.
Akageuka
na kumwangalia. Joshua akamfuta machozi. “Nakupenda sana Naya. Sana. Shida yako
ni yangu.” “Sikujua kwa umbali huo Joshua.
Asante pia kwa kuniamini. Niliingiwa hofu habari zilipoenea kuwa Malon alikuja,
na nikaenda kuzungumza naye nje!” Joshua akacheka taratibu na
kumfuta tena machozi. “Huwa sikubali kuchindwa kirahisi hivyo.” Naya akacheka
taratibu. “Hujamjua Malon wewe!” “Na kwa
kuwa na wewe hujanijua vizuri mimi.” Akaongea kwa kujiamini. “Kile chenye jina
langu. Nikajua ni changu kwa hakika na Mungu amekusudia kunipa mimi, huwa
siachii hata kidogo. Nitapambana mchana na usiku, magotini nikimsihi Mungu na
mimi mwenyewe mpaka kinakuwa changu. Hakuna umbali ninaocha kwenda kwenye
changu.” Naya akajisikia vizuri. Akarudi kujilaza vizuri, Joshua akarudi
kumpapasa mgongoni taratibu. Naya akatulia.
“Tumbo
likiwa linauma hivi, huwa unakula nini?” “Siwezi. Nikiweka kitu mdomoni nakuwa
natapika sana. Bora nisile chochote.” “Nahisi ni kama hujajua ni nini
unapenda.” “Malon alishajaribisha vyakula na vinywaji tofautitofauti nikawa
naishia kutapika tu. Lakini ni hali ambayo huwa haidumu kwa muda mrefu. Siku
mbili zikizidi ni tatu tu, natulia kabisa. Ila hizo dawa alizokuwa akinipa
yeye, ni kweli zilikuwa zikinisaidia. Alikuwa akinipa na soda ya Sprite.
Nakunywa kwa pamoja. Sijui aliambiwa na nani! Lakini ilikuwa ikinituliza sana.”
Joshua akatulia akifikiria.
“Au
baba yeye ndio ampigie?” “Wewe humjui Malon. Mwache tu.” “Kwa nini?” “Hanaga
aibu yule. Wewe unaweza ukaondoka hapa, ukamwacha. Na akamwambia hata baba
akalale yeye atabaki hapa. Wanamjua humu ndani. Anaweza kulala hapahapa ndani,
pale kwenye kiti alichokuwa amekaa baba kama tupo wodini, hospitalini.
Akizidiwa ndipo anaenda kulala na Bale. Masaa machache, anarudi hapa ndani.
Akitaka jambo lake, hajui hapana na hana mipaka. Utashangaa wewe, yeye haelewi
ni nini kinakushangaza.” “Alishafanya hivyo?”
“Mara
mbili alifanya hivyo tena mama akiwa hai na alijua mama hampendi, lakini alibaki
hapa siku mbili tukiuguza hili tumbo tena yeye mwenyewe ndiye alinisababisha
kuumwa. Akawa anakwenda kuoga na kubadili nguo hapo chumbani kwa kina Bale
anarudi kukaa hapa. Nilipoona tumejaa humu ndani, nyumba yenyewe bafu ni moja,
nikaamua niondoke naye tu. Mara ya pili, alilala usiku mmoja hapo chumbani kwa
kina Bale, kesho yake tukaondoka. Na hakusubiri hata kukaribishwa, yeye
mwenyewe akaomba akalale na kina Bale. Hapo usiku ulikuwa umeshaenda, na
akasema alitokea Morogoro. Ikabidi aachwe tu. Kwa hiyo Malon kichwa chake,
anakijua yeye peke yake. Mwache tu. Likinizidia tena, tutaenda hospitalini.”
“Sasa hivi unajisikiaje?” “Limetulia kiasi. Sio sana.” Joshua akaendelea
kumpapasa hapo mgongoni.
Naya
akaanza kusinzia tena, akawa kama amekumbuka kitu. “Joshua!” Akamwita taratibu.
“Vipi?” “Maumivu yamepungua. Nataka kurudi kulala. Nenda na wewe ukapumzike,
tutaonana kesho kazini.” “Wewe usijali.” “Hapana Joshua. Najali. Tafadhali
kapate masaa machache yakupumzika, ili kesho mmoja wetu awe na nguvu. Mimi
nitakuwa sawa tu.” Akamvuta mkono na kuubusu. “Asante kwa kuja kuniona.”
“Karibu. Lakini naomba usinifukuze sasa hivi. Ukilala kabisa, ndio nitaondoka.”
“Kwa hiyo utaendelea kunibembeleza?” Joshua akacheka taratibu. Akainama na
kumbusu shavuni. “Sikujua kama unapenda!” “Najisikia vizuri zaidi kwa sababu ni
wewe unanishika.” Joshua alifurahia sana kusikia hivyo. Akamvuta karibu zaidi,
akamfunika shuka tena, nakuendelea kumpapasa mgongoni, Naya akalala
kabisa.
Joshua na Baba Naya.
Ilipofika saa tano na nusu usiku, Joshua akamlaza kwenye mto
vizuri akamfunika na kutoka hapo chumbani. Akamkuta baba yake amekaa sebuleni.
“Naona amelala muda mrefu, nahisi tumbo litakuwa limetulia pia. Maana amesema
kichwa kimepoa kabisa. Nitarudi tena saa 11 asubuhi.” “Mapema hivyo!” “Nataka
kupata naye muda kabla ya kwenda kazini. Nimeshaanza kuzoea kuanza siku nikiwa
namuona pale ofisini kwao. Naona siku itakuwa nzito sana. Heri tu nianzie hapa
ndio nijue siku nzima itakuaje.” “Sawa. Lakini mimi namjua Naya. Kesho nilazima
aende kazini, pengine akute ujumbe kutoka kwa kiongozi wake kumwambia
amefukuzwa kazi.”
“Hakuna mtu atamfukuza kazi Naya bila idhini yangu. Mimi ndiye
napanga timu ya idara yangu. Najua ni nani anatakiwa awepo na acheze wapi ili
kuweza kufunga kwa urahisi. Na hiki kilichotokea leo mzee wangu, ilikuwa ni kwa
ajili ya utukufu wa Mungu tu. Mungu alitumia mpumbavu mmoja ili kumpa
Naya kile anachostahili.” Joshua akakaa kabisa. Baba Naya asielewe.
“Mimi huwa Mungu wangu akitaka kufanya jambo lake, huwa namjua.
Hata Naya nilimtuliza mchana na kumwambia, huyo ndio Mungu anapotaka kufanya
jambo. Kwanza kabla hajakupa kitu kikubwa, anajaribu tabia yako kuona kama
utaweza kumiliki ile baraka anayotaka kukukabidhi!” Baba Naya akaanza kuvutiwa.
“Ndio maana nilimwambia Naya, nilazima abaki amesimama.” Akamuona Joshua
anacheka.
“Nini? Ameharibu?” Akauliza kwa wasiwasi kidogo. “Hapana baba
yangu. Natamani hata nijichukulie sifa. Lakini hata mimi Naya amenishangaza.
Amethibitishia uongozi wa pale kuwa anao uwezo mkubwa sana wakufanya kazi
‘under pressure’. Sijui kama unanielewa?” Akamuona Joshua anahamasika.
“Katika moja ya maswali ya kwenye usahili kabla hujapata kazi, ni
mwajiri kutaka kujua kama wewe unauwezo wa kufanya kazi na wenzio, na je,
unaweza kufanya kazi kukiwa na mazingira si tulivu pamoja na mengine mengi.
Sasa leo, Naya ameyajibu hayo maswali bila kuulizwa, kana kwamba anafanyiwa
usahili aje achukue nafasi yangu!” Baba Naya akacheka sana.
“Ni vile hana uzoefu tu kwenye hicho kitengo cha masoko, na ndio
anaanza kuijua ile kampuni. Lakini nina uhakika kwa uwezo alio nao, alitakiwa
kuwa hata mtu wangu wa karibu pale ofisini. Nikimaanisha msaidizi wangu mimi.
Lakini kwa kifupi tu, hili la leo ilibidi litokee ili Naya ajulikane, apewe
haki yake pale kama mwajiriwa. Anajituma sana pale bila kulipwa anachostahili,
nafikiri juhudi zake zimefika mbele za Mungu ndipo ameamua kushuka mwenyewe ili
afanye kitu.” Baba Naya akafurahi sana. “Nashukuru kusimama naye. Alikuwa na
wasiwasi sana akihofia kufukuzwa kazi na kukufedhehesha.” “Hata kidogo. Ndio
ameniongezea sifa.” Wakacheka. Akamuona kama anayefikiria aseme jambo. Baba
Naya akatulia kumpa nafasi.
“Najua unaweza kusema ni kama naharakisha mambo, lakini mzee
wangu, Naya ni mfupa kutoka kwenye mfupa wangu na ameumbwa kutoka katika nyama
yangu.” Baba Naya hakutegemea. “Kama kuna ulikosikia kuna msaidizi hapa duniani
aliyeumbwa kwa mwanaume, basi Naya ni msaidizi wangu. Nilikuwa
nikisikiliza rikodi ya mazungumzo yao kwenye kikao alinirikodia mmoja wa
wasaidizi wangu, hata wao wamekiri ni mimi nazungumza kupitia kinywa cha Naya,
wakati si kweli. Naya anazungumza lugha yangu mimi ambayo amenipa Mungu, mpaka
nashangaa! Jinsi anavyozungumza na kufanya, kwa hakika Naya ni wangu mzee
wangu. Mungu ananithibitishia kila leo kuwa subira yangu, imefika
mwisho, ameshaniletea wakufanana na mimi. Ni Naya.” Joshua akaendelea.
“Na kwa kuwa ni Mungu amenipa, nakuahidi nitampenda Naya, kama
nafsi yangu na nitamuheshimu kwa kuwa najua Mungu ananingalia katika kila kitu
anachonipa kwa upendo. Kabla sijamtenda Naya dhambi, ujue nitakuwa nimekosana
sana na Mungu, na hilo siruhusu litokee, kwa kuwa sina kimbilio jingine ila
Mungu wangu. Kwa hiyo kama ulikuwa ukimuombea Naya kama anavyoniambia mwenyewe
huwa unamuombea sana, naomba sasa hivi utuombee mimi na Naya, mzee wangu. Najua
zipo historia nyingi katikati yetu, lakini namuomba Mungu atusaidie kuweza
kujenga msingi wetu, mimi na Naya, kwake Mungu.” “Na hapo ndipo
mtabakia salama. Hata pepo zikipiga, bado mtabakia salama.” “Asante sana
mzee wangu.” Joshua akafurahi sana maana ni kama huyo mzee alishamkubali.
“Nashukuru sana. Naomba mimi nitoke, ili niweze kurudi. Na naomba
mwambie Naya hata kama ataamua kwenda kazini, anisubiri nitakuja kumchukua,
sitachelewa.” “Sawa.” Wakasimama. Joshua akafungua mlango kisha akageuka.
Akamkuta baba Naya akimwangalia. “Nikuulize jambo?” “Karibu.” “Unadhani mimi
naweza kumfaa Naya?” Akauliza swali la moja kwa moja. “Mimi sijui, ila Mungu.
Na kwa kuwa Mungu anajua, na nilikwambia namuombea Naya tokea akiwa na mwaka
mmoja, aje aolewe na mume wake. Si mume wa mwingine. Mume ambaye
Mungu amemuandaa kwa ajili yake Naya. Sijawahi kuacha kuliombea hilo. Hata
ulipokuwa hapo chumbani kwake pia nilimkumbusha Mungu juu ya mume wa Naya. Kwa
hiyo naamini Naya ataolewa na mume wake Mungu aliyemwandalia.” Akajibu
kwa ufasaha kabisa na kumuacha Joshua ametulia. Kimya. Kisha akamuona anacheka
kidogo.
Akaaga. “Usiku mwema mzee wangu na samahani kukuweka macho mpaka
mida hii.” “Usijali kabisa. Hata hivyo bado. Nitakwenda kukaa naye tena kidogo
ndipo nikalale.” “Sawa. Na ikitokea unataka kwenda hospitalini, nipigie ili
nirudi twende.” “Huku ni mbali sana na huko mnakoishi nyinyi. Nina namba za
simu za watu wenye biashara za usafiri. Usiwe na wasiwasi.” “Ila tafadhali
naomba unijulishe kabla hujampigia mtu yeyote simu au niseme kabla hamjaenda
hospitalini.” “Sawa.” Akakubali lakini si kama aliyeridhia, Joshua akajua.
“Tafadhali mzee wangu.” Akasihi. “Nitafanya hivyo Joshua. Ila tuamini atakuwa
sawa tu.” “Amina.” Wakaagana tena na kutoka.
Jumanne.
Saa
11 asubuhi Joshua akawa ameshawasili nyumbani kwa kina Naya, akamkuta Naya
akimsubiria. Naya alisimama wakati akiingia. Baba yake ndiye aliyekwenda
kufungua geti na kumkaribisha. “Usingehangaika Joshua! Baba huwa ananisindikiza
mpaka kituoni, nachukua daladala. Huku kwetu mbali!” “Kwanza umeamkaje?
Maumivu?” “Naendelea vizuri. Nataka kwenda kazini.” “Kwa nini leo usipumzike?”
“Sitaki kuwapa sababu. Halafu hata hivyo najisikia vizuri. Twende tu tuwahi
foleni.” Wakamuaga baba Naya na kuondoka. “Nilifurahi ulivyokuja jana.”
“Kweli?” “Kweli Joshua. Nililala vizuri.” Baba Naya akawasikia wakizungumza
wakati wanatoka.
Akamfungulia
mlango, akapanda ndipo akafunga na kuelekea upande wa dereva. Wakaondoka. “Bado
hujaweza kuweka kitu tumboni?” “Sio leo. Nikijaribu tu, nitarudia kutapika siku
nzima. Acha leo ipite, labda kesho.” “Kweli hutakula kitu chochote!?” “Sitaweza
Joshua. Nitashindwa kazi.” Joshua akatulia lakini kama ambaye hajaridhika.
“Nitakuwa sawa tu Joshua. Ni mshituko. Ndivyo ninavyokuwa nikipatwa mshituko.
Inanisababishia hii hali na kupata siku zangu tarehe ambazo sizo.” “Lakini
nimesikiliza mazungumzo yenu kwenye kikako! Naya wewe unaakili sana.” “Kweli
Joshua?!” “Hakika umenishangaza. Umekwenda umbali ambao hata sikukutegemea!
Ulisikika ukiwa umetulia sana.” “Pale nilitulia kwa sababu nilijua upo upande
wangu. Lakini kabla ya pale niliingiwa hofu sana. Sikujua utanielewa vipi juu
ya ujio wa Malon pale kazini na watu wakawa wameshatengeneza picha mbaya!
Nikajua utakasirika. Nikaingiwa hofu ya ajabu.” Joshua akatulia kidogo kama
anayetafakari kitu.
“Ni
kweli nilishtuka Naya. Sikutegemea kuja kumsikia tena Malon akikufuata kazini
na wewe kutoka naye nje kabisa kama uliyetaka naye faragha! Ikanishitua sana.”
“Pole Joshua.” “Lakini pia sikuwa nikijua kama umerudisha gari! Imenifanya
nijisikie vibaya.” “Kwa nini tena!?” “Aaah!” Hakutaka kuzungumza
sana, akanyamaza. “Ndio maana umekuja kunichukua leo?” “Hilo, na pia sitaki
upate shida Naya. Wewe ni wangu. Nijukumu langu. Napaswa kukufikiria. Itakuwa
haina maana mimi nazunguka na gari, halafu wewe unahangaika usafiri!” Naya
akanyamaza. Wakaendelea kwenda wote kimya.
“Nikuulize
swali Joshua?” Naya akavunja ukimya. “Karibu.” “Itakuaje hatima yangu pale?
Unafikiri wataniwajibisha?” “Hujanisikia nilivyokwambia ulizungumza vizuri
sana!” “Sasa ndio itakuaje?” “Kwanza watakutaka kukuajiri. Nina uhakika leo
Jamal atakuletea karatasi za ajira, na mshahara mpya. Ni vile tu huna uzoefu
kwenye hii kazi. Lakini ungewadai mshahara mkubwa na bado wangekupa. Ila najua
kutakuwa na mabadiliko mazuri tu. Jamal anakupenda na kukuheshimu sana.” Naya
akatulia kidogo akitafakari.
“Ni
nini?” “Na wewe utafanyaje juu ya Njama?” Akamuona anacheka taratibu. “Najua
kila mtu anajiuliza na kusubiri kuona itakuaje.” “Utafanyaje?” Joshua akatulia.
Naya akamuona akivuta pumzi kwa nguvu. Akatulia kidogo kisha akaanza.
“Nimemuomba Mungu na kumsihi anipe uwezo, kwanza kumuonyesha ameshika eneo
nyeti sana la maisha yangu. Akielewa hilo, kisha kuhakikisha anaelewa
haruhusiwi kurudia tena.” “Kazi yako?” Naya akauliza akiwa hajaelewa ni wapi
hapo Njama ameshika, anatakiwa onyo kali hivyo kutoka kwa bosi wake!
“Kazi
yangu hakuna mtu anayeweza kuitishia, kwa sababu hata mimi najua sina mpinzani
na wananihitaji sana pale.” Naya akakunja uso. “Sasa nini?” “Amekugusa wewe.
Tena si kama mfanyakazi wa pale, kama mpenzi wangu mimi. Hilo ni kosa ambalo
kwa hakika litamgharimu sana.” Naya akafurahia moyoni kusikia hivyo. “Isingekuwa
ni Mungu, sasa hivi tusingekuwa hapa Naya. Alikusudia kuharibu mahusiano yangu.
Amesababisha umepatwa na mshituko. Ameharibu mpango wangu wa jana. Na...”
“Mpango gani tena wa jana!?” “Nilikuwa nikikusubiri utoke kwenye kikao, ili
tutoke kwa chakula cha usiku ndipo nikurudishe nyumbani! Nilitaka tupate muda
na wewe. Lakini Njama ameniharibia!” Akaongea kwa kulalamika.
“Jamani
Joshua! Sikujua! Ungeniambia.” “Haukuwa kwenye hali yakusikia hilo kwa wakati
ule.” “Ni kweli. Kichwa kilijawa mambo mengi nikijipanga nini chakuzungumza. Na
nini kingine?” “Unafikiri baba amejisikiaje kuona unarudi nyumbani ukiwa
unaumwa, tena peke yako?” Naya akatulia. “Lazima aliumia ila hakusema tu.
Ameniharibia sifa kwa baba.” “Lakini usijali Joshua.” “Oooh! Lazima nijali
Naya. Nyumbani kwenu hawanifahamu mimi. Wote wapo kwenye kuniangalia kwa karibu
sana wakinilinganisha na Malon au wanaume wengine. Kitendo chakujua tunafanya
wote kazi na umeondoka pale mimi sina habari! Unafikiria nini?” Naya akafikiria
kidogo.
“Lakini
baba anakuona wewe umekuwa, kuliko wengine wote, Joshua.” “Sasa kama nimekua na
ninashindwa kutimiza wajibu wangu, nitakuwa na tofauti gani na kubwa jinga?”
Naya akanyamaza. “Njama ameniumiza sana. Na sijui nia yake ni nini! Hicho
ndicho kinanitia wasiwasi.” “Labda wivu tu.” “Umbali aliokwenda mpaka kumpata
msaidizi wa CEO, ndani ya siku moja mpaka kuweza kupata nao kikao, akinishutumu
bila woga! Hapana Naya. Nimemuomba Mungu aingilie kati lakini nitahakikisha
anaelewa mambo yamebadilika. Na nitamuonyesha yeye ni hatari kwangu. Hakika
ataelewa na nitahakikisha anajutia alichofanya, na hatakaa akarudia kwa
mwingine tena.” “Asante kuwa upande wangu Joshua. Nashukuru.” “Nawajibika kwako
Naya. Nisipokupenda wewe kama nafsi yangu, inamaana huna sababu ya wewe kuwepo
kwenye maisha yangu!” Ilimgusa sana Naya na kujichukia kupoteza muda na Malon.
Ofisini.
Joshua
ni miongoni mwa viongozi wa chache sana kwenye hiyo kampuni ambao wana nafasi
maalmu ya kuegesha magari yao. Alifunguliwa geti na kwenda kuegesha sehemu
yenye jina lenye cheo chake. Akamfungulia mlango akamshika mkono, Naya
akamuegemea wakitembea. “Joshua?” Joshua akamungalia wakitembea. “Asante kwa
kuja kunichukua nyumbani. Nashukuru.” “Lakini natamani kama ungekula kitu!”
Naya akanyamaza. “Naomba niagize uletewe hata supu tu.” “Itanitibua, na
kuharibu siku nzima.” “Usiogope, mimi nitakuwa na wewe. Leo sitatoka, nitakuwa
hapahapa. Ukianza tu kutapika, mimi mwenyewe nitakuwepo.” “Hapo sawa. Lakini
huoni kama itakuvuruga kazini!” “Ndio Joshua mpya huyo.” “Utajuta kuwa na
mimi!” “Mungu anajua nipo tayari kwa ajili yako Naya.” Naya
akamwangalia na kurudi kumuegemea akimshika mkono vizuri tena kwa kupishanisha
vidole. Wakatembea mpaka ofisini kwake Naya.
Joshua
akamvutia kiti na kuegemea meza. Naya akakaa na kujiegemeza kichwa pembeni ya
kiuno cheke kidogo akatulia akiwa ameegemea upande mwingine. Joshua akamuwekea
mkono mgongoni. Akatulia si kukimbilia kufungua kompyuta na kutafuta kazi kama
kawaida yake. “Leo ungetakiwa kupumzika Naya.” “Najua Joshua. Lakini jana
niliharibu. Hapa navuna nilichopanda mimi mwenyewe.” “Unajisikiaje lakini?”
“Tukae wote kidogo kabla hujaondoka. Ni sawa?” “Sawa.” Naya akaweka mkono pale
alipoegemea kwa Joshua kama ametengeneza mto kwa mkono, akajilaza vizuri.
Joshua akarudisha mkono mgongoni akawa kama anamsugua mgongoni wakatulia.
“Naya?”
Joshua akamuita. “Najua ni mapema kukuuliza hili, lakini nataka kujua kama
Malon anajua kama mimi nipo?” Naya akashituka nafsini kwake, lakini akabaki
ametulia tu. “Au unafikiri ni mapema sana?” Joshua akauliza tena. “Alituona
kule Mbeya.” Naya akajibu. “Mimi kama mfanyakazi mwenzio.” Naya akatulia
akifikiria na kukaa vizuri. “Ulitaka nimwambie nini juu yako?” “Wewe uliweza
hata kunitaja kwake?” “Hapakuwa na hayo mazingira ya hata kukutaja kwake hiyo
jana alipokuja, Joshua. Halafu sijui nakutambulishaje kwake!” Joshua akabaki
akimwangalia. “Kama ulivyosema, ni mapema hata kusema lolote. Ua nilitakiwa
nikutambulishaje?” “Kama isingekuwa mapema, ungenitambulisha kwake?” “Kabisa
Joshua.” “Siku ya kwanza tu kuwa na wewe, nilijua yupo Malon.” Ikawa kama
analalamika. Naya akamuelewa.
“Joshua,
naomba amini sikufichi kwa Malon na sina sababu ya kukuficha kwake. Lakini
hatupo kwenye wakati mzuri wa kuzungumza na Malon, kama hivi ninavyozungumza na
wewe. Wewe unanifanya natulia, ndio maana nikaweza kuzungumza. Lakini si kwake.
Kwanza naona ni kama kumfaidisha bila sababu.” “Mimi nataka anitambue kama nipo
na wewe sasa hivi.” “Sawa Joshua. Yakitokea hayo mazingira, nitamwambia.”
Joshua akaonekana kutoridhika.
“Ameniumiza
sana Malon, na hatupo kwenye wakati mzuri wa mawasiliano. Siwezi kumpigia tu
simu na kumwambia wewe upo!” “Basi mimi nimpigie nimuombe dawa, na pia
uniruhusu nijitambulishe ili ajue hawezi kurudi tena kwako hata iweje na
haruhusiwi hata kukugusa tena kwa kuwa mimi mwenyewe sasa hivi nipo.
Kwamba hata kama anakuja kukuona leo au kesho kwa swala la ugonjwa, awe na
heshima akijua sasa hivi mimi nipo na aache kukufuata tena akitaka kukuhudumia
wewe. Haruhusiwi.” Naya akachoka kabisa.
“Malon
hawezi kurudi tena. Ni mpaka mimi nimtafute.” “Chakwanza watu wanabadilika.
Huwezi jua baada ya kumrudishia gari atafanya nini tena. Chapili, hatujengi
uadui au hutakiwi kumuogopa hata kumuulizia dawa kwa kuhofia anaweza kurudi
tena! Akijua mimi nipo, hawezi kurudi kama alivyokuwa akirudi kwako zamani
akijua huna mtu.” “Hakuna kipindi Malon amerudi kwangu kusiwepo na mtu
mwingine!” “Asante sana. Sasa hiyo ndio pointi yangu. Mimi sitaki huo
mchezo wake.” Mpaka Naya akafunga macho.
“Nataka
akija kukutana na wewe, kwa mazingira yeyote yale, ajue mimi mwenyewe
nipo. Nasitaki michezo isiyo na maana kwako. Iwe mwiko kukuhonga. Awe na
nidhamu ofisini na nyumbani pia. Hawezi akawa mtu wa kutokea bila miahadi.”
Naya akamwangalia Joshua na kushindwa chakuongea.
“Labda
kama uwe huna uhakika na sisi.” “Nakupenda Joshua.” “Hiyo haitoshi
kwa sababu wewe unajua wakati mwingine mapenzi tu huwa hayatoshi. Inatakiwa
commitment ya hali ya juu. Hata ukiamka asubuhi ukagundua hujisikii kunipenda,
au nimekuudhi kwa namna yeyote ile, lakini uwe unajua Joshua ni wangu mpaka
kifo. Jua litoke, mvue inyeshe, tumejifunga kwenye mahusiano yetu. Sasa pengine
uwe hutaki hiyo.” “Nata Joshua. Nilikwambia nitatulia na wewe na sitakusaliti.”
“Basi naomba namba ya Malon.” “Unafikiri ni lazima iwe leo?” “Ulitaka iwe lini?
Maana mimi sina ninachosubiria kwako. Nishakuthibitisha wewe ni wangu. Nakutaka
wewe Naya. Nimemaliza. Sasa pengine ndio uniambie wewe, kama bado kuna
unachosubiria kwangu!” “Nakupenda Joshua.” “Hilo nimekusikia Naya. Lakini
ninachokipata hapa ni kuwa haupo tayari kunitambulisha kwa Malon,
si ndiyo?” “Kwa kuwa sioni sababu?!” Joshua akakunja uso.
“Naya,
wewe ni smart mno. Naamini umenisikia na kuelewa hoja yangu ila hutaki
kunitambulisha kwa Malon, kitu kinachoanza kunitia wasiwasi.” “Usiwe na
wasiwasi na Malon, Joshua! Malon si mpinzani wako na wala hatakuwa.” “Sivyo
unavyofanya hapa. Hayo ni maneno yanayosikika vizuri sana. Lakini vitendo
vinapingana. Jana ulikuwa na sababu tosha yakunitaja kwake kama na mimi
nimechangia kurudisha hilo gari. Kwamba upo kwenye mahusiano mengine, huwezi
kushikilia mahusiano yaliyopita. Hivyo ndivyo mimi ningefanya. Pengine labda
uwe huna mpango wa kudumisha tulicho nacho, unataka iwe kitu cha muda tu kama
kina Josh na Ino ila Malon akiwa ndiye mmiliki mkuu. Na unatazamia
pengine siku moja atakuwa unachokitaka awe, na kukufanya uwe na furaha. Kwamba
unaamini ni yeye tu ndiye anayeweza kukufanya uwe na furaha.” Naya akajua Malon
ameshamtisha Joshua. Ameweka picha kubwa sana ya Malon kiasi cha kumtisha.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
Naya atafanyaje? Mapenzi!!??
Na Pesa je! PESA ambayo ndiyo Ajira yake inayotegemewa nyumbani kwao?? Bado ni
Malon tu.
Usikose Muendelezo.
0 Comments:
Post a Comment