Naomi Simulizi |+1 205 767 8163 |naomisimulizi@gmail.com MAPENZI&PESA! – SEHEMU YA 22. - Naomi Simulizi

MAPENZI&PESA! – SEHEMU YA 22.

 Mapenzi.

Naya akatoa simu kwenye pochi yake akampigia Malon. Iliita mara mbili tu akapokea. Naya akaweka speaker. “Pole, nimekuamsha?” “Hapana. Nilikuwa nasoma bibilia, niombe.” Malon akajibu. “Mbona sauti yako ipo kama haupo sawa?” Akauliza kwa kujali kama anayemfahamu sana Naya, hata kwa sauti tu. “Tumbo linaniuma. Halafu unajua sikuwahi kujua ni dawa gani zile ulizokuwa ukinipa na soda ya Sprite mpaka linatulia!” “Pole Naya. Pole sana.” “Asante.” Joshua kimya akisikiliza. “Malon?” Naya akamwita sababu ya ukimya. “Kuja kwangu jana kulikuumiza?” Malon akauliza kwa kujutia. “Ndiyo Malo.” “Samahani Naya. Sikutaka kukuudhi ila kukusaidia tu. Sikutaka makosa yangu yakufanye uendelee kupata shida Naya. Unastahili usafiri mzuri wa kuzunguka hapa mjini. Hii gari niliona ingekufaa sababu ya ulaji wake wa mafuta na matengenezo yake yapo chini. Isingekugharimu hata kama mimi mwenyewe nisingekuwepo kukusaidia, bado ungeimudu tu.” Malon aliongea kwa kujali.

“Unisamehe mama. Nisamehe sana. Sikukusudia kukuudhi.” Naya akajifuta machozi. “Jana hatukupata muda wa kutosha kuzungumza. Lakini pia sababu ya kurudisha gari, ni kwa kuwa nimepata mwanaume mwingine.” Kimya. “Sio sawa kuingia kwenye mahusiano mengine nikiwa na mali zako. Si sawa?” “Ni Joshua?” Naya akashituka sana mpaka akamwangalia Joshua. “Naya? Si yule jamaa mlikuwa mmekaa naye Mbeya kwa muda mrefu tu mkizungumza?” “Ndiyo. Anaitwa Joshua Kumu.” Wakatulia kidogo. “Anakupenda na kukujali?” “Ndiyo, Malon.” “Anakuthamini wewe kama Naya mbali na muonekano wako wa nje?” Malon akauliza tena, Naya akaanza kulia.

“Ni maombi yangu uishie pazuri mama. Wewe ni mtu mzuri sana. Unastahili mwanaume atakayekupenda kwa dhati na kuenzi huo moyo wako.” “Joshua ananipenda. Na yeye anampenda sana Mungu.” Akamsikia akivuta pumzi kwa nguvu. “Dawa niliyokuwa nikikupa ni yakutuliza tu maumivu.” Akamtajia jina lake. “Sema nilizungumza na nesi fulani akasema hajui kuna nini kinatokea. Lakini hiyo dawa ukimeza na soda ya Sprite, inakata maumivu na kichefuchefu na yeye alifundishwa tu mtaani ikawa msaada. Unakumbuka ndiyo niliyokuwa nikikupa?” “Sikuwa najua kwa jina hilo.” “Halafu unakumbuka mwanzoni nilikuwa nikikuwekea taulo la moto hapa chini ikawa inakusaidia mpaka tukanunua heatpad?” “Sijui niliipoteza wapi! Nahisi niliiacha kwenye ile nyumba ya Morogoro.” “Nitakutafutia ingine.” Akamuona Joshua anatingisha kichwa akikataa kabisa.

“Ila kwa sasa chukua taulo, weka maji liwe na unyevunyevu. Liweke kwenye microwave, lipate moto au tumbukiza kwenye maji ya moto kisha kamua kabisa, ndipo uweke chini ya kitovu kabisa. Acha kwa muda utajisikia vizuri.” “Asante sana. Ila huna haja yakunitafutia hiyo heatingpad. Nitamuomba Joshua akaitafute pamoja na dawa. Umenisaidia vyakutosha Malon. Naona ni  wakati na mimi niendelee pale tulipoishia. Ukiendelea kunifanyia mambo, haitakuwa sawa. Unakumbuka wakati ukiniacha kwa yule Joshua mwingine? Joshi.” Malon akanyamaza. “Uliniambia hutaki kunichanganya kwa kuwa unakuwa ni kama unaingilia mahusiano yetu. Ukaondoka na hukurudi tena na wewe ukaenda kuanzisha mahusiano na Rita. Unakumbuka?” Malon kimya.

“Basi naomba na safari hii iwe hivyohivyo Malon. Endelea kuniombea na mimi nitakuwa nikikuombea. Ila ujue Mungu amenirudishia furaha ile niliyokuwa nimepoteza. Kuna utulivu tena moyoni mwangu.” “Kwa hiyo unadhani Joshua ndiye mwanaume atakayekutoa kwa baba Naya?” Naya akakumbuka maneno aliyomwambia. “Niombee Malon. Kwa kheri.” “Naruhusiwa hata kupiga simu kukujulia hali?” Naya akamwangalia Joshua, akamuona ameinama kimya tu. Akajifuta machozi na kuhema kwa nguvu kama anayejaribu kujituliza.

“Sitaki tupotezane Naya. Tumetoka mbali mno mimi na wewe. Ni salamu tu.” “Hapana Malon. Itakuwa namfanyia Joshua kile nilichokuwa nikikikataa wewe usinifanyie mimi. Joshua ametulia sana, Malon. Sitaki kuanza kumchanganya tena kwa wewe kuwepo katikati yetu. Nataka nitulie, niangalie kama naweza kujenga na kupata kile nilichokuwa nikikililia wakati wote. Nisipofanya hivyo, nahisi nitajichelewesha. Niombee, na amini Mungu atatenda.” 

“Kwa hiyo hutaki hata salamu yangu Naya!?” “Haijawahi kutokea hivyo Malon. Huwa ukiondoka unaondoka moja kwa moja. Kwa nini tuanze sasa? Sitaki maumivu na kilio nilichokuwa nacho kwako, kimpate na Joshua. Haitakuwa sawa kwake. Tafadhali naomba uliheshimu hilo kwa kuwa sitabadilisha namba ya simu kwa ajili yako Malon. Naamini utaendelea kuwa Malon kama wa zamani. Ukiondoka, umeondoka. Kwa kheri.” “Kabla hujakata simu, naomba nikuombe kitu Naya?” Malon akaongea kwa kubembeleza.

“Ni nini tena Malon?” “Siku utakayojisikia kunisamehe kutoka moyoni, tafadhali nijulishe hata kwa ujumbe.” “Nimekusamehe Malon.” “Hapana Naya. Mimi nakujua, na ninajua kama si mimi, usingehangaika kwa wanaume wengine. Najua hata huyo Joshua asingekuwepo kwenye maisha yako. Najua nimekusababishia mengi maishani. Uliniambia kunipenda mimi ilikuwa ni adhabu kwako. Na ninaelewa na nimekubali. Naomba hiyo siku. Sijali hata kama ni miaka 20 kuanzia sasa, kama Mungu akinipa uhai. Na mimi sitabadili namba yangu ya simu kwa ajili hiyo, kwa hiyo tafadhali nijulishe. Kwangu itakuwa na maana kubwa sana.” Naya akalia sana.

“Ni hilo tu Naya.” “Mungu amekusamehe Malo.” “Najua kama Mungu amenisamehe, Naya. Lakini italeta maana kubwa sana kwenye maisha yangu yaliyobaki hapa duniani kama na wewe ukija kunisamehe hata na la Rita hili lililotokea hivi karibuni, kushindwa kuwa faraja ulipompoteza mama, na hata madhara niliyoyasababisha sasa hivi na mengine mengi tu. Wakati utakapopata hiyo neema yakunisamehe mimi kushindwa kusimama kwenye nafasi yangu, tafadhali nijulishe Naya. Ujue ni deni ambalo unalo kwangu. Kila la kheri.” “Asante.” Wakakata simu.

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

Naya akajifuta machozi na kumtizama Joshua. “Ni sawa?”  Joshua akavuta pumzi kwa nguvu na kusimama kutoka pale alipokuwa ameegemea. “Nakwenda kukutafutia hizo dawa, nikuletee.” “Nataka unijibu Joshua kama umeridhika.” “Nimeridhika na ninakushukuru. Naomba unisamehe Naya. Nakupenda, nataka nafasi ya peke yangu kwako bila muingiliano na yeyote yule, ili kama nikishindwa, nijue nimeshindwa mimi mwenyewe sio sababu ya mtu mwingine.” “Kwa hiyo sasa hivi umeridhika upo peke yako?” “Kabisa. Ila hiyo siku ya kulipa hilo deni la kumwambia umemsamehe, na mimi nataka kujua. Kwa hiyo ujue upo na madeni mawili.” Naya akachoka zaidi.

“Nitarudi sasa hivi. Acha nikakutafutie dawa. Halafu heating pad nitamtuma mtu akaangalie maduka yakifunguliwa.” Kitu kikampanda Naya, akasimama kukimbilia chooni  na kumpita Joshua kwa haraka mpaka choo cha upande wa kike. Joshua akamsikia akitapika sana huko ndani chooni.

Ikabidi tu Joshua aingie kumsaidia. Akamshika mbavuni, akatapika mpaka akamaliza. “Nashauri urudi nyumbani ukapumzike.” Naya akabaki kimya akijisafisha huku machozi yakimtoka. Joshua akataka kumshika ili amuweke kitu sawa, Naya akamkwepa kabisa kama anayekataa asimguse. Akashangaa. “Ni nini!?” “Tafadhali usiniguse.” “Kwa nini!?” “Siwezi hata kupumua. Nahitaji nafasi.” “Unamaanisha nini Naya!?” “Niache kabisa. Nahitaji kupumua.” “Naya!” “Tafadhali Joshua. Niache kabisa. Nenda tu ofisini kwako. Mimi narudi nyumbani.” “Kwa hiyo hutaki hata nikurudishe?” “Hapana. Nahitaji muda wa peke yangu.” Naya akatoka hapo Joshua asiamini.

Akarudi ofisini kwake akamuandikia email Jamal akimtaarifu yupo kazini, lakini anaumwa na kutapika sana. Hajisikii vizuri. Anaondoka. Wakati akiandika, Joshua akamfuata hapo. Hata hakumtizama. Akamtumia huo ujumbe Jamal, akachukua pochi yake na kutoka akimpita Joshua. Bado ilikuwa mapema sana. Hakuna mtu kwenye hilo jengo la masoko. Naya akatoka akitembea.

“Naya?” Naya akageuka na uso uliojaa machozi haswa. “Sasa hivi bado kuna giza nje. Huwezi kwenda peke yako.” “Sasa hivi sijali chochote kile Joshua. Sijali.” Naya akaondoka, lakini Joshua akawa akimfuata nyuma akamsikia akilia ila akashangaa hata baba yake hampigii simu. Joshua akamkimbilia mpaka akamfikia. “Nimpigie simu baba Naya?” “Nahitaji muda wa peke yangu Joshua. Tafadhali niache.” Hapo kidogo Joshua akaridhika. Kusikia hata baba Naya kwa wakati ule haitajiki, akatulia wakitembea kuelekea kituoni Mwenge. Kimya. 

“Nahitaji kuwa peke yangu Joshua. Tafadhali niache.” “Sitafanya hivyo Naya. Ni mpaka nijiridhishe upo salama.” Naya akaanza kulia tena. Mara akamuona anakimbilia tena pembeni kutapika. Akaenda kumshika, akatapika mpaka akakaa chini kabisa kwenye majani. Hakuna kilichokuwa kikitoka. Akaanza kulia tena.

Joshua akamnyanyua pale na kurudi naye tena kwenye gari yake walipoiacha ofisini. Walinzi wakiwaangalia wakiingia na kutoka tu. Kimya. Ni Joshua Kumu. Wote nidhamu. Akampandisha garini. “Hutarudi nyumbani ukiwa na hali hiyo, Naya. Nakupeleka hospitalini wakuchome sindano ya kuzuia kutapika, kisha unywe dawa tulizoelekezwa. Hutuwezi kuwa tukimpelekea baba Naya matatizo tu, kila wakati! Tunakuwa wote kama Zayoni! Hapana Naya. Lazima kuonyesha utofauti wako na Zayoni, na kumpa baba nafasi yakufikiria mambo yake mengine.” Kimya. Naya hakujibu. Joshua akatoa gari hapo mpaka kwenye hospitali ya kawaida tu maeneo ya Mwenge.

 Hospitalini.

Akamfungulia mlango pale alipokuwa amejikunja kimya. “Twende.” Akamfungua mkanda, Naya akashuka garini. Akaanza kumtoa michanga na majani kwenye nguo na kumfuta machozi kabla yakuingia. Hakukataa. Akamtengeneza vizuri. “Pole.” Naya akaanza kulia tena, Joshua akamshika mkono taratibu akimuongoza kuingia ndani mpaka mapokezi. Akamueleza aliyemkuta hapo mapokezi na kuongeza. “Anashindwa kuweka kitu chochote mdomoni tokea jana. Mara ya mwisho ametapika, hakuna kitu kimetoka.” “Anaonekana kabisa.” Akaongea nesi aliyekuwa amesimama hapohapo mapokezi akionekana anaandika kitu.

Baada yakutolewa damu, daktari akashauri achome sindano na awekewe maji. Akapewa chumba cha kupumzika, akiambiwa baada ya hapo ataruhusiwa. Naya alikuwa amechoka mpaka mbavu sababu ya kutapika. Alipochomwa tu sindano, akapotelea usingizini akijua Joshua yupo. Akalala.

 Baada yakupitiwa usingizi mzito, akiwa bado usingizini akasikia ni kama Joshua akizungumza, akielezea hali yake. Bila kufungua macho akajaribu kusikiliza, akagundua ni Jamal na Jema wamefika hapo kumuona. Naya akatulia kimya. “Aisee poleni sana.” “Atakuwa tu sawa. Wamempa dawa yakuzuia kutapika, na hayo maji. Wamesema watamruhusu baadaye wakijaribisha chakula nakuona hajatapika.” Joshua akaeleza. Akamsikia Jema akizungumza na Joshua, akampa maelekezo, wakaondoka.

Ndipo Naya akafungua macho akakuta Joshua akimwangalia. “Vipi?” Naya akatulia. Akamshika mkono vizuri kwa upendo kwa kupishanisha vidole kama kawaida yake. Naya akaanza kutokwa na machozi. “Pole.” Akamfuta machozi. “Tumbo bado linauma?” Akatingisha kichwa kukataa. “Umenichukia?” Joshua akamuuliza kwa upendo, Naya akatingisha kichwa kukataa. Akamfuta tena machozi. “Ila nilikuwa sipo tayari!” Naya akaongea kwa kulalamika, Joshua akaelewa. “Najua Naya. Na usifikiri kama ingefika wakati ukajikuta upo tayari. Ilibidi kufanya tu.” Naya akalia sana. Joshua akambembeleza. “Mimi nipo Naya. Naomba unipe nafasi. Naamini tutakuwa sawa tu. Sawa?” Naya akatingisha kichwa kukubali. Hapo Joshua akaridhika.

“Nikwambie kitu Naya?” Naya akajifuta machozi. “Tusingefika kokote, endapo ungebakiwa na daraja linalokuunganisha na Malon. Ungekuwa nusunusu kwangu, ukijua au ukitegemea kuwa...” “Malon yupo tu, nikimtaka yupo.” Akamalizia Naya mwenyewe na kuendelea. “Ilikuwa ikinisaidia kwa sehemu. Nikawa siumizwi tena na mtu mwingine kwa kuwa sikuwa nikiwafungulia moyo wangu wote, nikijua Malo wangu yupo tu sehemu fulani ni mimi tu kumtafuta.” Naya akaendelea taratibu kama anayekiri sasa. “Ikajengeka kama kisiwa cha salama, ndani yangu. Hakuna mwanaume atanifanya kitu, nikaumia kwa kuwa nilikuwa najua bado ninaye Malon.” “Na mimi nilijua Naya. Na samahani nimejuta kuzungumzia hili ukiwa mgonjwa.” “Hakuna siku ungezungumzia hili ikawa salama. Hata hivyo bado nahitaji muda.” “Lakini isiwe mbali na mimi. Nakupenda Naya. Na nipo tayari kukusubiri, ila tukiwa pamoja.” Naya akajisikia vibaya lakini ni kweli Malon amekaa kwenye maisha yake na kuathiri mfumo mzima wa maisha yake kwa muda mrefu sana. Hapakuwa na Naya bila Malon. Akamuhurumia Joshua na kutamani kama angekuja mapema kwenye maisha yake, yeye ndio akawa Malon.

“Nisamehe kukufukuza Joshua. Nilikuwa na hali mbaya! Nilihisi siwezi kuhema tena. Mbavu zilikuwa zimebanwa, siwezi kutulia.” “Nilielewa. Unajisikiaje?” “Mwili umetulia kabisa. Ila natamani kulala.” “Jozee yupo njiani, analeta supu. Unywe ndipo urudi nyumbani ukalale.” “Pole na samahani kukuweka hapa wakati ulitakiwa kazini.” “Usijali. Kila kitu kipo sawa.” Naya akatulia. “Jamal na Jema walikuja kukuona. Wamekuletea na juisi.” “Nashukuru.” Jozee akawa anapiga simu kuulizia walipo. Joshua akatoka kwenda kumpokea, akarudi na chakula bila Jozee. Akatamani kuuliza ila akaona hayamuhusu. “Ametengeneza nini?” “Amesema supu ya mbogamboga ila amesema utaipenda tu.” Naya akakaa ili ale.

Joshua akamuweka vizuri kwenye bakuli na kijiko maalumu kwa kunywea supu, Naya akaanza kunywa. Kijiko tu cha kwanza akapenda. “Ina ladha nzuri ya ndimu.” Akasifia, Joshua akafurahia. “Nimefurahi kama umependa. Vipi kichefuchefu?” “Kimeisha.” “Nimemtuma zile dawa na soda hiyo ya Sprite. Akirudi tutaondoka. Acha nikalipie kabisa hapa.” “Nakushukuru Joshua. Asante.” Baada ya yote, Naya akatolewa hapo akiwa na nafuu kubwa tu.

 ~~~~~~~~~~~~~~~~

“Kwa nini mimi nisirudi tu nyumbani, wewe ukawahi kazini? Bado ni mapema.” Joshua akakunja uso. “Yaani nikuache hapa!?” “Hakuna shida kabisa Joshua. Tena sasahivi daladala zinakuwa wazi tu. Nisogeze tu mpaka kituoni. Nakuhakikishia nitakuwa sawa.” “Mimi huwa sijui kufanya mambo nusunusu Naya. Utanisamehe kama utaniona ni kama nalazimishia mambo fulanifulani. Naomba unielewe na kunizoea. Nikiamua kufanya jambo, na nikajua mkono wa Mungu upo na mimi kwenye hilo jambo, huwa nafanya kwa hakika bila kuzembea. Ndivyo nilivyo.” “Sitaki wote tukwame kwenye jambo moja, Joshua!” “Sihesabu kama nimekwama hapa na wewe, Naya. Usiwe na wasiwasi. Nahesabu nimepata nafasi ya kuwa na wewe kwa kipindi hiki wewe ni mgonjwa. Basi.” “Nashukuru Joshua.” “Usijali kabisa.” Safari ya kurudi Kiluvya nyumbani kwa kina Naya, ikaanza.

Naya alijituliza kitini, akajikunja na kuegemea kiti akiangalia nje. Mkono mmoja akapenyeza kifuani kwenye tisheti ya kazini aliyokuwa amevaa. Akatulia kimya. “Nafurahia muda na wewe Naya.” Naya akamwangalia. “Kama nilivyokuwa nikifurahia tulipokuwa kwenye boti, ndivyo hata pale hospitalini, hapa na popote pale. Ilimradi niwe na wewe.” Naya akavuta pumzi kwa nguvu na kutulia bila ya kujibu. Joshua akaendelea kuendesha, Naya ametulia tu.

Joshua hakuzungumza tena mpaka walipofika nyumbani kwao. Baba yake akatoka akiwa ameshituka. Naya alikuwa amekaa kitini akisubiria kufunguliwa mlango, wakati Joshua ameshuka garini. “Kwema!?” Baba yake Naya akauliza akishuka ngazini akisogelea gari. “Sasa hivi anajisikia vizuri. Nimemrudisha apumzike.” Joshua akamfungulia mlango, baba Naya naye akasogea. “Vipi mama?” “Sasa hivi najisikia vizuri. Joshua alinipeleka hospitali. Wamenichoma sindano ya kuzia kutapika, wakaniwekea maji. Na nimekunywa supu, ameniletea mpishi wa Joshua. Najisikia vizuri, ila usingizi, nataka kulala.” Baba Naya hakuamini alichosikia. Naya amekuwa hospitalini bila yeye! “Amepewa mapumziko ya leo na kesho ili kujiangalia. Kama atahitaji siku zaidi, daktari ameniambia nimpigie, ataongeza ED.” Baba Naya alikuwa na mshangao mpaka akashindwa kuzungumza.

“Karibu ndani Joshua.” Ikabidi Naya amkaribishe. “Karibu Joshua.” Ndipo baba Naya akaongeza kama aliyerudiwa na ufahamu. Naya akawapita hapo na kuingia ndani moja kwa moja. Wakamfuata nyuma Joshua akiwa na dawa pamoja na soda. Naya akapitiliza chumbani kwake, Joshua akamfuata nyuma, baba yake Naya ikabidi asubiri nje. Naya akapanda kitandani. Joshua akimwangalia. “Njoo nishike mkono kama vile ulivyonishika hospitalini. Nikilala ndio uondoke.” Joshua akacheka kidogo, lakini moyoni alifurahia sana. Akaona ni kama amezawadia zawadi ya thamani haswa. Akamfunika vizuri na kukaa pembeni yake. Naya akampa mkono. Akaubusu kwanza ndipo akamshika vizuri kwa kupishanisha vidole, akaupakata huo mkono. “Asante.” Akashukuru na tabasamu lililojaa usingizi. “Karibu.” Akamgusa kidogo usoni kama kumuweka sawa nyusi, Naya akalala hapohapo. Joshua akaangalia saa, ndio ilikuwa ikitimu saa 5 na nusu asubuhi hiyo. Akaona arudi kazini. Akamuweka vizuri na kumfunika. Akatoka.

~~~~~~~~~~~~~~~~

“Naona amelala.” “Pole kwa hekaheka?” “Nashukuru Mungu ametulia. Wamempa matibabu, lakini pia tulifanikiwa kupata dawa alizokuwa akipewa na Malon. Nimeziacha hapo kwenye meza chumbani kwake. Nashauri akiamka hata kama tumbo halitakuwa likiuma, anywe tu ili asirudie ile hali.” “Nitafanya hivyo. Nashukuru sana.” Yule mzee akawa kama na maswali, na Joshua alijua ila hakutaka kuingilia mpaka aulize mwenyewe. Alipomuona amecheka tu akifikiria, Joshua akamuaga. “Acha niwahi kazini mzee wangu. Nitarudi tena jioni.” “Nashukuru sana.” Joshua akatoka. 

Ofisini.

Joshua alirudi kazini akiwa amebeba sura ya kazi tu. Aliingia hapo akijua Jema anayo maagizo yake yote ya siku hiyo ila Njama hakuwa amezungumza naye kabisa. Jema alishangaa hata hakumuulizia, akapitiliza moja kwa moja mpaka ofisini kwake baada ya Fina kumtupia salamu. Wakajua siku ndio imeanza hapo. Fina akaingia ofisini kwake na kuzungumza naye maswala ya kazi, alipomaliza tu. “Namuhitaji Jamal, sasa hivi.” Fina akatoka kwenda kumpigia simu Jamal kumuita. Bila yakupoteza muda Jamal akafika hapo. Jamal alikuwa mkubwa kwa umri ukimlinganisha na Joshua.

“Naya hatakuwepo kazini leo na kesho. ED yake hii hapa. Daktari anataka apumzike kabisa kama nilivyokwambia.” “Poleni sana.” Jamal akapokea hiyo ED. “Nataka kazi ile niliyomkabidhi Njama na Naya, uifanye na jioni niwe nayo hapa mezani. Fikiria mchango wa Naya. Kama unaweza kuweka pamoja na...” Njama akaingia. Jamal akamuona jinsi alivyobadilika. “Kwa nini unaingia ofisini kwangu kama chooni!?” Akamuuliza kwa kumshangaa  na ukali kama ni kitu kigeni wakati Jema na Njama huwa wanaingia hapo bila hodi kila wakati hata kama Joshua anakuwa na mgeni, wao huingia tu nakufanya yao na kutoka. Siku hiyo akambadilikiwa. “Nilitaka kukukabidhi ile...” “Nimekuuliza swali, acha dharau.” “Samahani, sikujua kama una mtu.” Njama huyu alipoa kama siye aliyeanzisha fujo.

“Kwa hiyo kusipokuwa na mtu ndio inakupa ruhusa yakuingia humu utakavyo?” “Samahani.” “Fuata utaratibu tafadhali. Na ninajua wewe ni mzuri sana wa kufuata utaratibu kwa hiyo hilo halitakusumbua. Unanielewa?” “Sawa.”  “Fina yupo nje kwa ajili hiyo au angalia ratiba yangu kwa Jema, upange naye muda ambao anafikiri nina nafasi. Acha kufanya fujo zisizo na sababu.” Mpaka Fina nje akajua mambo yameshambadilikia Njama. Kwamba anatakiwa kuomba miahadi na Joshua! “Samahani sana.” Njama akataka kutoka. “Na Njama.” Njama akageuka. “Hiyo kazi mkabidhi Jamal aipitie.” Mpaka Jamal akashituka.

“Sijaelewa! Yaani unataka kazi yangu mimi aipitie Jamal!?” “Unashida na hilo?” Joshua akamuuliza akimtizama, machoni. “Sijaelewa?” “Kama unafikiri ninao uwezo wa kukuelewesha juu ya sintofahamu yeyote kichwani mwako, pitia ratiba yangu kwa Jema, zungumza naye uone kama nina nafasi ya kuzungumzia hilo ili niyajibu maswali yako. Vinginevyo hiki ni kitengo CHANGU. Mimi. Narudia tena, mimi ndiye ninayepanga timu ya humu ndani. Najua nani nimuweke wapi na acheze vipi ili kufanikisha lengo kuu lililotukutanisha hapa kwenye hii kampuni, tena bila kupoteza muda. Hujaridhika kufanya kazi kama timu iliyopo chini yangu ukifanya kazi na wenzio, nenda kapeleke malalamiko yako popote unakotaka. Tafadhali funga mlango nyuma yako.” Akamgeukia Jamal.

“Ifikapo jioni, kazi iwe imekamilika. Chukua alichokifanya Njama. Pitia, andika kwa upya na weka sawa. Kuna swali?” “Nimeelewa kiongozi. Acha nikaanze sasa hivi.” Joshua akahamisha macho kwenye laptop yake. “Sitampa Jamal kazi yangu. Maana itakuwa ni kama yeye anaandika kitu kipya kutoka kwenye kazi yangu! Halafu itajulikana ni yeye amekamilisha! Hapana.” Jamal alikuwa amefika mlangoni akashangaa sana.

“Wewe vipi Njama!?” “Unataka upate sifa kwa kupitia kazi yangu!?” “Wewe umeandika mawazo yako hapo au ni kile alichozungumza Naya siku ile na kila mtu akakipenda?” Jamal akauliza kwa kumshangaa sana. Joshua kimya. “Msitake kunifanya..” Jema akaingia kwa haraka. “Mimi naomba nikushauri kitu Jamal.” Jema akamkatisha Njama.

“Kila mtu alimsikia Naya siku ile. Na akaongezea kwenye mawazo ya kundi lenu. Huna cha ajabu utakachopata kutoka kwa Njama isipo...” “Na kwa taarifa yako Jema, nimepanga hii kazi vizuri sana. Mtu kama Jamal hawezi...” “Jiangalie Njama!” Jamal akamtahadharisha. “Utanifanya nini?”  Njama akauliza kibabe.

“Jamal, nisikilize mimi tafadhali. Achana na Njama. Nenda kafanye kazi. Kwanza kundi lao siku ile ndilo lilichemsha, na kutoa mchango wakijinga kabisa. Huna kipya utapata kwenye alichoandika huyu, isipokuwa aliyoiga kutoka kwenu na Naya.” “Jema jiangalie wewe!” “Nenda Jamal. Nenda kafanye kazi. Achana naye. Ameingiwa na roho ya uvurugaji, anataka kutuvuruga tu, wakati sisi wote tulikuwa tukifanya kazi kwa kuheshimiana humu ndani na umoja.”

“Unafiki tu. Wakati kumejaa hofu na...” “Twende Jamal. Hakuna wakukusikiliza hapa.” “Una dakika moja yakuondoka ofisini kwangu Njama. Ukiisha huo muda na bado umesimama hapo, utakuja kutolewa. Na ukitolewa hapa, ujue hutakaa ukarudi hapa ndani. Kama unafikiri nakutisha, ujue zimebaki sekunde 40 tu.” Joshua akanyanyua simu. “Niitie askari.” Akamuamuru  Fina.

Fina akatekeleza alichotumwa na bosi wake, kisha akamfuata Njama pale ofisini kwa Joshua. “Kwa nini umeamua kupigana na ukuta Njama?! Umepatwa na nini mdogo wangu?” “Mimi sijakataa kutoka ila nataka ku...” “Umeambiwa nini? Fuata utaratibu!” “Yameanza lini?” “JANA. Na wewe ndiye umeyaanzisha yote haya Njama! Sasa kwa nini hutaki kufuata utaratibu ulioanzisha wewe mwenyewe? Toka kabla hujatolewa!” Njama akatoka akabaki Fina. “Joshua, naomba nipe siku ya leo tu. Nitazungumza naye, atatulia.” “Iwe hivyo Fina. Nataka tufanye kazi, sina muda wa malumbano. Ifikapo jioni awe yupo tayari kufanya kazi kama timu, na sivinginevyo.” “Sawa, Joshua.” Wakaingia askari wakimtafuta Fina.

Akatoka kwa haraka. “Kila kitu kipo sawa. Samahanini kwa usumbufu.” Joshua akamsikia Fina akituliza hao askari. Akawasikia wakitaka kujua ni kwa nini waliitwa hapo, nao wakaweka ulazima. Fina akajua Joshua anasikiliza, hawezi kudanganya. “Yameisha. Mnaweza kuondoka tu.” “Sisi kama watu wa usalama ni lazima kutunza rekodi ya cha chochote kinachotokea humu ndani ya kampuni. Hata kama mnamalizana nyinyi kwa nyinyi, nilazima na sisi tujue. Ili ikija kutokea tena, tunakuwa na kumbukumbu yetu.” Ikamlazimu sasa Fina kueleza kwa ufupi wakaandika kila kitu na kuchukua jina kamili la Njama.

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

Joshua akaendelea na kazi, tena akaanza kufanya kazi ileile aliyompa Jamal ila kwa kiwango kikubwa na kizuri. Baada ya muda Fina akampigia simu kumwambia Jema anataka kumuona. Akajua na yeye amepata ujumbe. “Baada ya kama dakika 5, tafadhali.” Akajibu Joshua na kukata simu. Haikuwa kawaida yao hata kidogo. Jema akajua Joshua amekasirika sana. Akatulia hapo nje akingalia muda. Ilipotimu dakika 5 tu, akagonga na kuingia.

Joshua akanyanyua kichwa na kumtizama. “Nina mambo mawili.” Jema akajikaribisha kwa kuvuta kiti na kukaa mbele yake. Joshua kimya akimtizama. “Wanawake wengi wakiwa kwenye hali kama ya Naya, huwa wanakuaga na hamu na kitu fulani. Inaweza ikawa sio chakula kile chakushiba. Lakini unajikuta labda una hamu ya kitu kitamu. Labda chocolate. Wengine inakuwa ni keki na iwe keki maalumu. Labda vanilla tu, au chokoleti. Haya wengine ubuyu, au ice cream na mengine mengi tofauti tofauti. Kila mmoja anakuwa na hamu ya kitu chake. Wewe unajua Naya anapenda nini?” Joshua akatulia kidogo, lakini akamuona mpaka uso umebadilika, akacheka kidogo.

“Kweli sikuwa najua hilo!” “Basi iwe ndio kazi ya leo. Umdodose ili ukienda jioni, uende na hicho kitu. Na ukijua mapema, naweza nikamtuma mtu akakununulie ili ukienda, uwe nacho.” Hapo akawa amempata Joshua, hata uso ulionyesha amefurahia. “Sawa. Na ninashukuru kwa wazo.” Hapo Joshua akatulia kabisaa. Jema akamfanya atulie hata kuweza kumsikiliza kwenye mambo ya kazi. 

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

Kila mtu akiwa anaendelea na kazi siku hiyo baada ya chakula cha mchana, Njama akapata simu kuwa anaitwa kwenye ofisi ya usalama hapo kazini. Fina akaingiwa na wasiwasi. Njama akaenda asijue hata kama kulikuwa na hiyo ofisi hapo. Alihojiwa kwa muda mrefu tu huku maelezo yake yakiandikwa. Akaongea mengi na kukanusha askari wakimsiliza tu.

Baada ya kama lisaa tena Fina akapigiwa simu kutoka kitengo cha Parsonel Relations au HR relations ambacho ni kitengo maalumu kwa mambo ya nidhamu kilichopo ndani ya ofisi ya mwajiri, HR kwa kifupi cha Human Resources, tena na Mama Masinga. “Ametoka kidogo, ila nitamtaarifu kuwa unamtafuta.” “Na mwambie aangalie email yake. Hajajibu kama ameipata.” Mama Masinga akakata simu hofu ikamwingia Fina zaidi. Alijua mambo yameshafika mbali.

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

Akili ya Joshua ikawa imehamishiwa kwa Naya. Akawa ana kazi ya kuangalia simu yake kila wakati kuona kama Naya ameamka na kama amemtafuta. Akaamua kuiweka mezani kabisa ili ujumbe utakapoingia tu, asome bila kuchelewa. “Mama Masinga amepiga simu anakutafuta.” Fina akasikika. “Jamaa ashaenda kuniharibia nini?” Akasikia Njama akimuuliza Fina. “Wewe unamjua Joshua. Hana muda wa kijinga kama wewe Njama. Umeingiwa na nini Njama!?” “Nilikuwa nawajibu wale askari, bwana. Walidhani nina silaha. Wameniweka muda kweli!”

“Acha kunizunguka Njama! Ni nini kinakupata wewe!? Kweli unataka kuharibu maisha yako sababu ya mwanamke!?” “Mimi sitaki kudhulimuwa Fina. Sipendi ujinga.” “Sawa Njama! Na mimi nakuwa kama Jema kukuonya. Unashindana pabaya sana.” “Kwani watanifanya nini!? Mimi sio mjinga Fina.” Akapunguza sauti kama asisikike na wengine na kuendelea. “Nishazungumza na mwanasheria anayejua maswala yahaki za wafanyakazi.” Joshua akaona simu yake ya mezani kwake, inawaka taa, kutokea kwa Fina. Akabonyeza bila kuzungumza lakini akasikia sauti ya Njama akizungumza kwa sauti ya chini kidogo. Akatulia, akijua Fina anataka amsikilize na yeye.

 “Nishazungumza na huyo mwanasheria. Nimemweleza kila kitu kuhusu hapa. Nasubiri wajichanganye tu, niwashitaki na ameniambia makampuni mengi huwa hayapendi kesi, wanapenda kumaliza kesi kimyakimya. Utashangaa sana Fina, nitaondoka hapa na mabilioni ya pesa na kukuacha hapa unahangaika na kutengenezea waume za watu chai na kuwapelekea maji kila wakati.” Fina akashangaa sana mpaka akaangalia simu kama Joshua ameweza kusikia.

“Mjini hapa Fina! Jamaa anajidai ndio mungu wa hapa. Na makaburu wanamtetemekea! Sasa itawagarimu. Na watanijua mimi ndio Njama, mtoto wa jiji.” “Yaani fujo zote hizo kumbe ili ufukuzwe kazi halafu ukaanzishe kesi uje ulipwe fidia?!” Joshua akatulia akisikiliza. “Siwezi nikaendelea kuwa mtumwa wa mwanaume mwenzangu! Wote tunakimbia kama wajinga! Akifungua yeye mdomo kampuni nzima inatetemeka mpaka wanawake zetu wanamkimbilia yeye! Sifanyi huo ujinga aisee. Na siondoki kijinga. Hilo ujue. Kila kitu naandika.” Fina akaingiwa hofu akimshangaa sana, asiwe na uhakika kama Joshua amesikia yale yote.

“Nashauri nenda kamuone mama Masinga.” “Naye yule ni walewale tu kama Jema na haya makaburu. Sijui jamaa analoga wapi!? Wakimuona wanakimbia kama wajinga! Kama anadhani uchawi wake unampata kila mtu hapa duniani mpaka makaburu aliyoyafanya majinga basi ajue hapa amegonga mwamba. Akaloge tena.” “Ndio unatakiwa ujue Njama, kama mpaka mtu kama mama Masinga anafanya hivyo ujue ni kwa kuwa amejua siri.” “Sasa wewe muache ajichanganye. Nitawanyoosha hapa, hawatakaa wakanisahau. Faida yote ya huu mwaka, itaishia mfukoni kwangu.” Fina mpaka akaogopa na kunyamaza kabisa, Njama akaondoka akicheka kwa ushindi. 

Naya kwa Joshua.

‘Najisikia vibaya jinsi nilivyokufanyia asubuhi, Joshua. Tafadhali naomba unisamehe na usinielewe vibaya. Sipo kama ulivyoniona asubuhi. Hata mimi sijui nilipatwa na nini! Nisamehe tafadhali. Na naomba usichoke shukurani zangu za kuwa na mimi hospitalini. Nakushukuru sana. Na samahani kwa usumbufu.’ Huo ujumbe ukaingia kwenye simu ya Joshua na kumtoa mawazoni. Akajua Naya ameamka. Hapohapo akapiga. “Vipi sasa hivi unajisikiaje?!” “Najisikia vizuri. Asante kwa kujali. Ulisoma ujumbe wangu wote?” Joshua akacheka taratibu. “Nilikwambia hamna shida Naya.” “Hapana Joshua. Si sawa. Mimi sitaki uje unifanyie hivyo. Ingeniuma sana.” “Ujue haitakaa ikatokea hata siku moja. Kwa sababu sitataka muda wa kuwa peke yangu mbali na wewe Naya na sihitaji kufikiria kama nakuhitaji maishani au la. Najua kwa hakika nakuhitaji. Hata Mungu anajua nakuhitaji .” Naya kajisikia vibaya zaidi.

“Unazidi kuniumiza Joshua!” “Hapana Naya. Sio nia yangu, nakwambia tu ukweli.” Naya akajifuta machozi. “Naomba nisamehe. Hakika nimejisikia ni kama vile Malon alivyokuwa akinifanyia mimi. Wakati wote nilikuwa nikimuonyesha namtaka yeye, na yeye hakuwahi kulithamini hilo! Ikawa mimi ndio nina kazi ya kumfuata nyuma hata alipokosa ilibidi kumfuata na kumtangazia msamaha ili turudi kuwa wote kwenye mahusiano. Sitaki na mimi nikufanyie hivyo Joshua. Najua nimekukosea. Nimemuomba na Mungu msamaha, nimejionya, sitarudia tena. Kabla sijazungumza neno au kukufanyia kitu, nimeomba Mungu anisaidie kunikumbusha. Sitaki kukuumiza Joshua. Mimi nimekuwa kama hivyo wewe. Ikawa nipo na maumivu wakati wote. Ikafanyika kama adhabu! Sitaki na wewe nikupitishe hapo. Hustahili. Ni bora nikishindwa nikwambie mapema, kuliko kukufanya uishi kwenye mateso.” “Tafadhali naomba usishindwe Naya. Hapo ndio nitaumia zaidi. Nakuahidi kukuombea.” Naya akaumia zaidi. Akabaki kimya.

“Nakupenda Naya. Naamini ipo siku na mimi nitakufanya uwe na furaha tu.” Naya akaumia sana. “Unanifanya niwe na furaha Joshua.” Joshua akanyamaza. “Kweli. Ni vile maisha yamenipitisha kwa wanaume waajabu ajabu sana. Wakautia tatizo moyo wangu mpaka nimekuwa kama nimekufa ganzi! Nasubiri tu chochote tena kitokee. Na imekuwa hata na kwako pia. Nakuwa nasitasita.” “Nimeliona hilo. Moyo wako upo mguu mmoja ndani na mwingine nje. Ukijua na mimi ni walewale tu. Kuna mwanzo mzuri ila mabadiliko mabaya mbeleni.” Hapo Joshua akawa amemziba mdomo.

“Lakini Naya, kama umenisikiliza vizuri, mwanzoni kabisa mimi sikuvutiwa na chochote chako cha nje. Mungu aliniunganisha moyo wangu na wako mpaka ikabidi sasa nianze kukuangalia mtu wa nje, kwa sababu ndani nilijua Mungu ameshakuleta kwangu. Ndipo nikabaki kukutizama nje kujua safari hii Mungu amenipa zawadi ya namna gani! Ndio maana naamini, kama hutanikimbia, Mungu atatusaidia tu. Usiogope. Tupo kwenye mpango na makusudi ya Mungu. Atatuponya na kote tulikopita na kujeruhiwa. Atatuwezesha kuchukuliana pia.”

“Natamani ningekutana na wewe muda mrefu Joshua!” “Mungu alijua sikuwa tayari, Naya. Bado alikuwa akiniandaa kuja kuwa mume wako. Huu ndio wakati wa Mungu. Ndio maana nina imani kubwa na huu wakati wa Bwana. Tutakuwa sawa tu. Naamini hatujachelewa.” “Sasa huoni kama Mungu amekupa kitu kisicho kikamilifu?”  Naya akauliza akimuhurumia. 

“Kwa kuwa bado hujaunganishwa na mimi Naya. Wewe ni mfupa kutoka kwangu na nyama zilizotolewa kwangu. Huwezi kukamilika, au hata mimi sikamiliki mpaka wewe.” Naya akashangaa hiyo hekima. “Jamani Joshua! Mpaka nimekuwa na hamu ya kukuona tena!” Joshua akacheka. “Nitakuja kukuona. Unataka nikuletee nini?” “Nakutaka wewe.” Joshua akacheka tena taratibu. “Mimi nitakuja. Lakini niambie unahamu ya nini?”  Naya akatulia kama anayesita kusema kisha akamsikia kama akicheka akiwa mawazoni.

“Hichohicho ulichokicheka ndicho nataka uniambie.” “Chakijinga!” Naya akajibu akicheka. “Ndicho hichohicho nataka kujua.” “Kwanza natamani kula kitu kitamu. Chenye sukari, lakini sio soda.” Joshua akajua Jema alikuwa sahihi. “Kuna chocolate fulani hivi tulikuwa tunazinunua. Sio nyeusi sana, ni kama zinakaribia rangi hizo. Basi tulikuwa tukinunua nyingi, zinakuwa kwenye friza. Siku ninazopatwa hamu nazo, natoa kwenye friza, nakula zikiwa zimeganda kama barafu. Ni leo tu nilikuwa nakumbuka hilo. Basi nilikuwa nikifurahia, japo sikuwa nikila kila wakati. Ni mara mojamoja tu ninapopatwa hamu kama leo, lakini tulihakikisha siishiwi. Zinakuwepo ili kila ninapojisikia kula, nipate. Lakini hiyo nizaidi hata ya mwaka sasa! Sijui leo imekuaje nikakumbuka!” Joshua akacheka taratibu akifikiria.

Lakini akajua ni Malon ndiye aliyekuwa akimnunulia hizo. “Kuna jina maalumu za hiyo chocolate unataka?” “Sasa sijui kama nilipendea jina au aina! Japo Malon aliji...” Akanyamaza. “Ni sawa tu. Niambie.” “Samahani Joshua.” “Hatuwezi kuepuka hilo. Ehe?” Joshua akataka aendelee. “Alikuwa akinunua aina hiyohiyo moja. Brand name hiyohiyo.” “Zinapatikana hapa nchini?” “Nilikwenda na Malo, mara moja tu. Akaninunulia. Nikazipenda sana, kwa hiyo yeye ndio akabakiwa na kazi yakuzinunua aina hizohizo na kuziweka kwa wingi kwenye friza, ili niwe nazipata kila wakati ninaohitaji. Sikufuatilia tena ununuaji wake kujua ni wapi aliendelea kuzipata.” Naya akamuelekeza mpaka sehemu waliyonunua kwa mara ya kwanza na kumtajia jina lake.

“Basi nitakwenda kuziangalia.” “Lakini usisumbuke Joshua. Sio kwamba ni kitu ambacho sitaweza kuishi bila hicho. Ni hamu inayonijia mara chache sana.” “Usijali. Umekula vizuri lakini?” “Nilikunywa tena ile supu niliyoletewa na Jozee hospitalini.” “Na hukutapika?” “Hata kidogo. Najisikia mzima kabisa. Nilikuwa nimekaa tu hapa kitandani na baba Naya. Ametoka hapa muda si mrefu. Nilimuita nilipoamka na kukukosa wewe, nikajua ulishakwenda kazini. Ikabidi nimuite baba Naya, nikae naye.” Joshua akacheka.

“Pole.” “Ndiye mnyonge wangu. Ameshanizoea. Eti haamini kama kweli nilikuwa hospitalini, mpaka nikawekewa maji, bila kukutaka umpigie aje!” Joshua akacheka. “Mpaka ikabidi nimuonyeshe nilipochomwa sindano. Eti anasema ni muujiza.” Wakacheka hao wawili, Joshua akamsimulia alichoambiwa na Zayoni. “Wala hakukudanganya. Huwa siponagi bila baba. Leo yeye mwenyewe ameona ni muujiza! Mama mwenyewe alishajua. Hata nikiumia tu, atampigia baba simu na kumtaka arudi nyumbani. Lasivyo nalia, na sitanyamaza mpaka baba aje. Hapo matibabu yeyote ukinipa ndio yatafanya kazi. Na ninahisi ni imani tu.” Wakaendelea kucheka.

Wakati Joshua alipokuwa akizungumza na Naya, hapo hapo akamtumia ujumbe mama Masinga kwenye simu yake ya mkononi. ‘Kuwa makini sana na huyo kijana. Anayoyatenda kumbe ni makusudi tu. Anakusanya ushahidi ili kuweza kushitaki kampuni kwa ajili ya mabilioni ya fidia.’ Mama Masinga alishituka baada ya kusoma ule ujumbe. Lakini akajibu. ‘Hakika nakushukuru Kumu. Leo ningeharibu.’ Joshua hakujibu tena. Akaendelea kumsikiliza Naya.

Njama Kwa Mama Masinga.

Njama alifika kwa mama Masinga, hata yeye alikubaliana na Joshua. Alijawa jeuri. Majibu mabaya kama aliyekuwa akimtafutia sababu. “Kwanza nataka kujua ni kwa nini nipo hapa, muda huu wa kazi. Sikusikii unachongea, unanipotezea tu muda.” Mama Masinga hakumjibu. Akanyanyua simu na kumuita Afisa Mkuu mwajiri na kumuomba afike hapo ofisini kwake mara moja. Alishazungumza naye kile alichoambiwa na Joshua kabla ya Njama hajafika hapo. Bila kupoteza muda, akafika hapo.

“Hakuna tatizo. Ila naona tunashindwa kuelewana na Njama. Nilitaka mtu wa tatu.” “Labda kabla sijaendelea, naomba haya mambo yaende kiofisi kama Njama mwenyewe anavyopendelea.” Akaitwa sekretari, akaambiwa aje na rikodi. Njama akashangaa. Akaambiwa akae hapo aandike na arikodi yale mazungumzo. “Labda nikuulize Njama. Unajua ni kwa nini umeitwa na Personel Manager? Sio mama Masinga kama yeye, hapana. Yeye kama anayehusika na mambo yetu wafanyakazi hapa kwenye hii kampuni?” Afisa Mkuu wa ajira kwenye kampuni hiyo Tanzania nzima akamuuliza kwa heshima tu. “Ameongea mambo ambayo hayaeleweki. Hayana mashiko ni kama majungu tu.” Akajibu Njama bila heshima. Yule mama akacheka tu lakini sekretari alishituka mpaka akashindwa kuandika.

“Basi naomba mimi niliweke hili swala wazi.” Akaendelea. “Afisa wa mambo ya usalama hapa kwenye hii kampuni, amekuja akishitaki kwanza fujo ulizofanya ofisini kwa Joshua na matusi mengi uliyozungumza getini ukitukana uongozi wa hapa.” “Upo ushahidi au hayo ni majungu tu?” “Nilikuwa nikizungumza mimi bwana Njama. Naomba nimalize.” Pakatulia. “Sasa kwa kuwa mama Masinga ndiye anayehusika na hayo mambo nikamuomba yeye ndio azungumze na wewe kujua kama lipo tatizo. Kama ataweza kulitatua, basi afanye hivyo au achukue malalamiko yako apeleke mahali husika.” “Kwanza ninahisi kudhulumiwa na sidhani kama mtaweza kunisaidia.” Akaanza Njama.

“Siwezi kufanyiwa mambo ya dharau. Mimi nazijua haki zangu.” “Ni katika upande upi?” Mama Masinga akauliza. “Jamaa yenu ananiambia eti mimi nikabidhi kazi niliyofanya mimi mwenyewe, kwa mtu kama Jamal!” “Unamaanisha nini ukisema mtu kama Jamal?” “Mdogo kwangu kwa majukumu!” “Labda kabla hujaendelea Njama, labda nikusaidie jambo moja mimi kama Afisa Mwajiri. Hukuwahi kubadilishiwa cheo, ila majukumu. Narudia tena Njama, ulipo sasa hivi ni nafasi aliyoiunda Joshua, akakutaka wewe uwepo ili kumrahisishia kazi ya vikao na kila mtu asubuhi. Akakutaka wewe uwepo pale, mtu mmoja tu, utakayeelewa kwa upesi anachotaka kifanyike, kisha wewe sasa, uweze kufikia wenzako pale kitengoni. Sijui kama umenielewa? Maana kama hilo linasumbua, na umekosa imani na sisi, tafuta mwanasheria wa nje ambaye atakusaidia kukuelewesha.” “Hilo halina mashaka. Nikishindwa kupata haki zangu hapa, nitazitafuta popote.” “Hilo ni wazo zuri.”

“Kama nimekuelewa vizuri Njama, leo umegoma kufanya kile ulichotumwa na mkuu wa kitengo chako! Si ndiyo?” Mama Masinga akauliza kutaka uhakika. “Si kugoma, ila kutokukubaliana naye.” “Na ndipo ukaanzisha fujo ofisini kwake?” “Jamaa ni mjinga kabisa. Ndivyo alivyokuja kujiliza kwenu!?” “Acha matusi Njama. Na hapa upo si kwa sababu ya Joshua, ila watu wa usalama. Tumekuita kwa heshima kabisa, kutaka kujua tatizo lipo wapi? Kama unashindwa kufanya kazi na wenzio kwa sababu ya kuona wapo chini yako sana, nalo hilo nataka kujua.” “Huo ni uzushi.”

“Sio wewe uliyekuja ukiwa na malalamiko juu ya Naya uliyetumwa kufanya naye kazi, lakini ulisema umeshindwa kwa sababu alichelewa kwa dakika 9?” “Naya ali..” “Na leo unafanya fujo zote hizo kwa sababu umeambiwa umshirikishe Jamal kazi uliyofanya?” Njama akababaika ila akajitetea. “Kwani Joshua huwa anatoa kazi zake kabla hajakamilisha?” “Maelezo uliyotoa getini ulisema ulikuwepo ofisini kwa Joshua kumkabidhi kazi aliyokuwa amekupa. Ila tatizo lilitokea pale alipokwambia umpe Jamal! Je, hayo nayo ni uzushi unataka kurudi tena ofisi za Usalama kubadilisha?” “Mimi sijui wamekwambia nini, lakini ninachotaka kusema, hamuwezi kunionea. Nazijua haki zangu.” Hicho kikao kiliendelea bila kufikia mwafaka. 

Joshua kwa Naya.

Alipomaliza mambo yake pale ofisini kwa siku hiyo, Joshua akampigia simu Fina kumtaka amletee chocolate ambazo alishaagiza na kutaka baadhi ziwekwe kwenye friza. Fina akaleta zote bila kuchelewa. Joshua akamshukuru bila hata kuzungumzia maswala ya Njama. Akashangaa sana. “Nakushukuru Fina. You are the best.” Alishazoea hiyo sifa. Akacheka. Akatamani kama Joshua angeanzisha hayo mazungumzo, lakini alionekana na haraka yakuwahi kutoka. Fina akatoka bila nyongeza. Joshua alimwambia dereva hatahitaji usafiri jioni hiyo, akatoka na gari yake mbio akiwahi Kiluvya nyumbani kwa kina Naya akiwa na matunda pamoja na galoni ya maziwa, juisi, kreti ya soda aina ya Sprite. Na vyote hivyo aliagiza mara baada ya kuzungumza na Naya. Hahutaka kwenda ukweni mikono mitupu.

Naya alijikuta moyo ukifurahia geti lilipokuwa likifunguliwa na Zayoni, akajua ni Joshua tu. Hawakuwa na mgeni wa kuwatembelea usiku huo, tena na gari! Akajua huyo ni lazima ni Joshua. Akatoka na yeye. Gari ya Joshua ikawa ikiingia, Naya akajikuta akipunga mkono na giza hilo. Joshua alimuona, akacheka. Akafungua kioo na kutoa mkono kumpungia na yeye huku akisogeza gari karibu zaidi. Naya akacheka. Kwa kumuona Naya nje, tena mida ile, Joshua akajua anasubiriwa kwa hamu. Akashuka garini akiwa amejawa tabasamu, Naya akamfuata.

“Nimefurahi umekuja Joshua.” “Na mimi nimefurahi kuja.” “Kweli? Sio usumbufu kwako kuja mpaka mbali kote huku!?” “Kama isingekuwa kuja huku, inamaana ningekuwa nyumbani peke yangu. Ni bora hivi kuja kukuona wewe.” Naya akacheka kwa furaha. Akamshika mkono.  Zayoni akawasogelea kutoka getini. Akamsalimia Joshua. “Upo msafi! Halafu unanukia kama zile nguo za Naya nilizomsaidia kufua leo.” Naya na Joshua wakacheka. “Nilikwambia pafyumu yako inanukia vizuri na inakaa kwenye nguo muda mrefu.” “Asante Zayoni. Habari za kushinda?” “Nzuri. Leo nilikuwa nikimsaidia baba kazi kwenye fremu yake mpya. Naya amekwambia kama tunataka kufungua duka la mazao kule Kibaha?” “Bado.” Joshua akajibu huku akimwangalia Naya.

“Tunapajenga. Namsaidia baba kupaka rangi, halafu kupajengea vizuri. Naya amesema akipona atakuwa akiungana na sisi zaidi siku ya jumamosi. Si unajua siku za jumamosi huwa anafanya kazi nusu siku?” “Nafahamu Zayoni.” “Basi atakuwa akija kutusaidia mimi na baba.” “Unafanya vizuri kumsaidia baba, Zayoni. Na mimi nikipata nafasi nitakuja.” “Wewe utachafuka.” Mpaka Naya akacheka. “Kweli Naya. Mwambie jinsi kulivyo kuchafu!” “Ni kijijumba kilichokuwa kimetelekezwa sehemu. Ndio baba amekodisha hapo anapakarabati. Kweli ni pachafu, bado hata hapajachukua sura yeyote ile. Tutakukaribisha pakitengemaa.” “Mimi sitaki kuwa mgeni ramsi. Nataka na mimi niwe katika wakaribishaji.” “Basi tutakwenda wote siku ya jumamosi.” Zayoni akafurahia na kukimbilia ndani kumwambia baba yake. Akawaacha wakicheka hapo pembeni ya gari.

“Njoo hapa.” Akamvutia kwenye gari yake na kumuegemeza. “Funga macho na uwe mwaminifu.” Naya akaanza kucheka. “Naya!” “Nafunga na sitachungulia.” “Sawa.” Joshua akajaribu kupitisha mkono mbele ya macho, akagundua kweli amefunga. “Haya. Subiri.” Naya akaendelea kucheka akiwa amefunga macho. Akamsikia akifungua mlango wa gari, baada ya muda mfupi akamsikia akifunga tena. “Bado umefunga?” “Kabisa.” Naya akajibu akicheka. “Kumbe wewe mzuri wa suprise?” “Sana. Ushindwe tu wewe.” Joshua akacheka sana.

“Sawa. Sasa bila kufungua macho, fungua mdomo.” Naya akawa ameshaelewa. Akacheka sana. Kisha akafungua mdomo, Joshua akamuwekea chocolate mdomoni ilikuwa baridi haswa. Naya alisikia kuburudika mpaka kwenye nafsi. “Fungua sasa macho!” “Acha kwanza nile hata mbili! Kama naota niwe nimefaidi ndotoni.” Joshua akacheka, akacheka sana. “Acha utundu Naya! Niangalie bwana nijue kama umependa.” “Sana Joshua. Sikutegemea kuzipata leo. Nilizikumbuka tu, nikajionya na kujiambia nayo hiyo enzi yake imepita. Asante Joshua.” “Karibu. Kama umefurahia na mimi nimefurahi. Nimekununulia nyingi na zimeganda.” “Nimeona. Naomba na wewe uonje Joshua. Ni nzuri sana.” Joshua akacheka na kumuwekea nyingine mdomoni na yeye akaonja moja, kweli akapenda.

“Ni nzuri.” “Sasa utakuwa ukielewa ni kwa nini tulikuwa tukizipenda. Nzuri sana. Halafu nyingine alikuwa aki...” Naya akashituka mpaka usoni. Akamshika mkono. “Twende ukamsalimie baba Naya.” Akabadili mazungumzo akiwa anamvuta kidogo. Joshua akajivuta nyuma na kukunja mikono. “Maliza ulichokuwa ukitaka kuniambia.” “Ni nzuri sana.”  Joshua akakunja uso. “Nilitaka kukwambia hata Malon alikuwa akizipenda.” “Naomba usinidanganye Naya. Naogopa sana kudanganywa, ni heri usiniambie kuliko kunidanganya.” “Kweli hata Malo alikuwa akizipenda. Sidanganyi.” “Lakini sicho ulichotaka kuniambia.” “Hapana.” Naya akajisalimisha. Joshua akatulia akimwangalia.

“Karibu ndani.” Naya akapoa kabisa mpaka usoni. “Nakupenda Naya.” Naya akaingiwa hofu. “Naomba usinikatie tamaa Joshua.” “Kweli? Maana sitaki kukupotezea muda au kujaa kwenye maisha yako halafu ikaja kuwa ni kero tu.” “Mbona kama umeanza kunikatia tamaa Joshua! Uliniambia Mungu ame, ame...” Naya akashindwa hata kumalizia. Akanyamaza. “Wewe unaniamini?” “Nakuamini sio tapeli.” “Hapana Naya. Unaamini kama ni mtu ambaye naweza kuzungumza na wewe na kukusikiliza na bado ukabaki salama?” “Sijui Joshua! Sijui ni kwa kiasi gani naweza kuwa wazi kwako.” “Unafikiri lini au kipi kitakufanya uwe wazi kwangu?” “Muda na kufahamiana zaidi. Kukujua kama unao uwezo wakunifahamu hata kwa undani na bado ukanipenda na usinihukumu. Kumbuka nilikwambia niliishia na Malo kama mke kabisa, yaani kuishi naye nyumba moja!”

 “Unakumbuka na mimi nilikwambia niliishia na Benadina nyumba moja?” “Hata jina hukuwa umenitajia Joshua! Halafu hiyo ilikuwa zamani sana kwako. Mimi ndio nimetoka kwenye mahusiano!” “Ni kweli umetoka?” Joshua akauliza tena. “Nimetoka Joshua. Au umesahau nilivyozungumza na Malon mbele yako, leo asubuhi?” “Sasa ni kwanini unashindwa kuniamini kama umeamua kuwa na mimi?” “Nani amekwambia itakuwa rahisi Joshua?” Naya akauliza swali mpaka akamshangaza Joshua.

“Nimeishi na kujengwa na Malon kwa miaka zaidi ya 5, nikawa hivi nilivyo. Alimuondoa yule Naya wa zamani na kumtengeneza huyu Naya aliyesimama hapa mbele yako. Nimejawa kutoamini na kutomiliki. Nakuwa na mtu kama sipo naye hujui nini kitatokea kesho au hata baada ya nusu saa! Na imekuwa hivyo kwenye historia yangu yote na wanaume kasoro kwa baba tu. Ndiye mfano wa mwanaume ambaye najua anayo maadili na anaweza kumvumilia mtu. Akasimama na huyo mtu katika kila nyakati, kwa kumuona vile alivyoishi na mama. Wewe tuna siku chache tu pamoja. Nawezaje kujenga imani kubwa na kujifunua kwako kwa kiasi hicho cha kukwambia kila kitu?” Joshua akatulia.

“Nilikwambia kwa asili mimi sina marafiki. Wala sijawahi kuwa na marafiki kwa hofu ya kuja kugeukana kama nilivyokuwa nikiona kwa wengine. Nikajijengea tabia yakutunza mambo yangu mimi mwenyewe. Hata Malon alipokuwa akiniumiza nilikuwa nikiyabeba mwenyewe. Sina wakumwambia. Hata mama yangu mzazi hakuwa akijua kama naishi na Malon kama mume. Nisingethubutu mimi mtoto wa kanisani kuja kulilia kusalitiwa mapenzi kwenye familia kama yetu, wakati stori za baba na mama ni kwamba walisubiriana mpaka walipoingia kwenye ndoa.”

“Haya, walionizunguka wenyewe walikuwa wakitembea na Malon na wakimsubiria kwa hamu. Wakipokezana huyo Malon kama mpira! Nikafungiwa uwanja wa kuzungumza na yeyote, ila kupambana mwenyewe. Ni tabia iliyojengeka miaka na miaka. Nahitaji muda, na kukujua uliposimama na mimi. Nijenge imani kwako na kujua kama naweza kuzungumza kwako lolote na bado nikabaki salama, Joshua!” Kimya.

“Unakumbuka nilipokuuliza huoni kama Mungu amekupa mtu asiyefaa?” Kimya. “Unakumbuka jibu lako? Maana mimi najua nilipo Joshua. Moyo wangu umejeruhiwa vibaya kweli. Niliishi maisha ya fedheha kwa muda mrefu sana nikikubali kudhalilika sana ili niwe na Malo. Mpaka rafiki zake na wazazi wake wenyewe Malon, walikuwa wakinishangaa. Na nilikwambia tokea Mbeya. Nilijua ni nini chakufanya, lakini nilijawa hofu hata kukubaliana na taarifa ya nini chakufanya. Lakini wewe mwenyewe, tena leo tu, ulinituliza Joshua. Ukaniambia sitakamilika bila wewe!” Joshua akavuta pumzi kwa nguvu na kutulia kabisa.

“Haitakuwa rahisi Joshua.” “Lakini ulisema inaweza ikawa rahisi! Wewe mwenyewe ulisema Naya. Unakumbuka tulivyotoka kwa mara ya kwanza tukaenda kuendesha boti?” “Nakumbuka Joshua.” “Basi nirahisishie Naya!” “Ukibahatika kunioa mimi Joshua, utabaki ukimshukuru Mungu kila siku.” Joshua alicheka, akacheka sana.

“Naya!” “Kweli tena. Ujue utapata mwanamke wakusimama na wewe katika kila hali. Halafu mimi nitakuwa faraja yako. Sitakukimbia wala kuiba penzi la nje. Utakuwa na uhakika wa maombi ya watu wawili. Yaani kule mbinguni wewe unakuwa unatajwatajwa tu. Pakipoa kidogo tu, baba Naya anawakumbusha. Haya, bado na Naya mwenyewe! Huwezi ukabakiwa hivyo ulivyo.” Joshua alicheka sana tena kwa sauti. “Wewe hayo masomo uliyosomea yamekuharibu Naya.” “Biashara matangazo Joshua.” Joshua hakuwa akiamini. Alibaki kucheka.

“Wewe usikasirike Joshua. Maadamu mimi mwenyewe nimekuahidi nitakuwa na wewe, ujue mimi ni wako tu. Hayo mengine nisaidie kunirekebisha taratibu.” “Hutakasirika?” “Nitajitahidi.” Joshua akatingisha kichwa kama anayesikitika akimwangalia na tabasamu. “Niambie kitu gani kingine.” “Niambie ulichotaka kuniambia ukasita.” “Niamini mimi, hutaki kujua Joshua. Ila kwa kuanza tu kutaka kukwambia, ujue moyo wangu unaanza kufunguka kwako. Nipe muda.” “Ni juu ya nini? Maana kama ni Malon, usiwe na wasiwasi.” Akamuona anamwangalia kisha akaanza kutingisha kichwa taratibu akikataa kama anayepingana na wazo la kwamwambia.

“Ni nini hicho?” “Joshua wewe! Nikikwambia kitu hutakiwi kujua, basi amini hivyo na uache.” “Basi ndio udhaifu wangu huo mwingine na wewe unatakiwa kuuvumilia.” “Joshua, tafadhali tuzungumze jambo jingine kama habari za kazini.” “Nzuri kabisa. Lakini bado nataka kujua.”

“Kama utang’ang’ania hivyo. Nashauri ukamsalimie baba kwa kuwa ameshajua umekuja hapa ndipo utoke hapa. Tukae hapo kwenye ngazi nikwambie. Maana...” “Unahisi nitakimbia?” Naya akatulia tu akimwangalia. Joshua akachukua mizigo kutoka kwenye gari na kumpita Naya akielekea ndani. “Acha nikupokee.” Joshua akamsubiria, akampa baadhi, mingine akabeba mwenyewe. Wakaingia ndani.

“Naona unaongeleshwa tu hapo nje na kila mtu humu ndani, huna wakukukaribisha ndani!” Wakacheka. “Hamna shida mzee wangu. Shikamoo.” Wakapeana mkono na kusalimiana. “Naona Bale anarekebisha chakula huko jikoni.” “Basi acha nisubirie na Naya hapo nje. Maana niliambiwa mapishi hayataki mikono mingi.” Wakacheka. “Mimi ndivyo nilivyoambiwa. Ningesaidia.” Wakataniana kidogo ndipo wakatoka na Naya ila Bale hata hakusogea hapo kumsalimia Joshua japo walikuwa wakimuona hapo jikoni. Naya aliumia, lakini akanyamaza tu. Akajua bado anahasira na Joshua sababu ya gari Naya alilorudisha kwa Malon.

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

“Naomba kesho nirudi kazini.” Akaanza Naya mara baada ya kukaa tu nje. Walikaa kwenye ngazi. “Una ED ya siku mbili! Unatakiwa kupumzika, Naya.” “Unaona hivyo vichwa vyote humo ndani?” Joshua akanyamaza. “Vinategemea kazi moja tu kwa sasa. Hiyo ya Coca. Leo Bale ametoka chuo katikati ya juma la mitihani, ili kuja kuniangalia mimi kama dada yake, lakini pia anahofia nisije poteza hii kazi.” “Haitakaa ikatokea.” “Basi naomba kesho nirudi Joshua. Tafadhali.” “Haina shida kabisa. Ila nilitaka tu upumzike.” “Sio kwa sasa, tafadhali. Najua ipo siku tutakuja kupumzika, lakini sasa hivi tupo kwenye kupambana ili kujikwamua kiuchumi.” “Ndio maana hata mmerudia kufanya kazi na Malon?” Joshua akaunganisha swali lililopo moyoni akikumbuka mazungumzo yao ya mwisho, Naya mwenyewe alisema hawatafanya naye biashara.

“Ndiyo na hapana.” Naya akatulia kidogo na kuanza kusugua mikono taratibu huku akifikiria. “Malon alikuwa akinifanyia mambo mengi mazuri sana Joshua. Sana. Yaliyokuwa yakinifanya nakuwa kama mwendawazimu kwa kuwa nilikuwa ninajua ndivyo anavyowafanyia watu wengine.” “Unamaanisha wanawake wengine?” Naya akatulia kidogo. “Kama mambo ya chocolate?” Naya akamwangalia na kucheka kwa kujidharau. “Ila alisema hafiki umbali huo na wanawake wengine. Anakuwa anawaonea kinyaa. Kwanza umejuaje kama...” “Wewe umeniambia.” Naya akakunja uso kwa woga kidogo. “Sijasema Joshua! Wewe ndio...”  Akasita na kubaki akimtizama.

Anyway, mbali na mapenzi, Malon alikuwa akinifanya situlii. Nilijawa hofu na fedheha ya usaliti kila wakati, kila mahali. Si kwenye mahoteli au baa, lazima utakutana na wanawake asilimia kubwa tu, alishalala nao, zaidi pale Morogoro. Chuoni, shuleni au hosteli nilizokuwa nikiwepo, sikuwahi kujikuta nipo peke yangu. Sikuwahi kutulia. Kumpenda Malo ikawa kama adhabu kwangu. Chungu na tamu. Kumuacha siwezi kwa vile anavyonifanya nijisikie kwa muda ninaokuwa naye, tofauti na wewe.” Hapo Joshua akakaa vizuri kumsikiliza.

“Hatujafika umbali mrefu na wewe Joshua. Sikufahamu au hunifahamu kwa undani, lakini nimejawa amani ya ajabu. Ile tu kuwa na mimi inanituliza. Sifa zako nimezisikia pale kazini kwa vijana na wazee, mpaka nasikia fahari wewe kunichagua mimi! Nafurahia kuwepo kazini. Nafurahia kulala ukiwa masikioni kwangu kwa kuwa najua kesho utabaki kuwa Joshua yuleyule niliyekuacha usiku. Unajiheshimu Joshua, kitu kinachonipa heshima na mimi sio kama nilivyokuwa nikidhalilika! Uthamani wangu umeongezeka kwa mimi kujulikana nimechaguliwa na wewe!” Joshua akacheka kidogo.

“Halafu mbali na yote, wewe ni mtu mzuri Joshua. Mzuri sana.  Kwa muda mfupi niliokuwa na wewe, tukapita hali zote hata kukukera mpaka mwisho, lakini nimekuona jinsi ulivyo na stamina ya kuhimili mshindo, upo kama baba yangu.” Joshua akakunja uso kidogo. “Hiyo ni habari nyingine lakini baba yangu ni mvumilivu mno Joshua. Kifo cha mama kimemuumiza baba si kupoteza mke, ila kukosa nafasi yakumdhihirishia kuwa anaweza kumpa anachokitaka.” “Kivipi?” Naya akacheka kidogo.

“Nadhani kwa namna fulani umeshaelewa sisi ni watu wa namna gani. Kwa aina ya mazingira yetu tu. Na si kwamba tumeamua kuwa hivi. Kuishi kwenye nyumba kama hii au kutumia thamani za aina hizo unazoziona hapo ndani kwetu, au hatujui vitu vizuri! Hapana. Ni uwezo tu. Mama amekufa akiwa analipia mikopo ya pesa alizokopa kujenga hii nyumba. Kwa biashara ya kusambaza mayai na maziwa pamoja na kuku tulifanya kipindi fulani, vilisaidia kulipa madeni mengi sana tuliyokuwa tukidaiwa mpaka kanisani na humo kwenye maduka, pamoja na Malon pia alisaidia sana tu. Kwa hiyo tumekuwa tukiishi maisha fulani hivi, yakudunduliza. Kwa kifupi, hali ya uchumi ya humu ndani haijawahi kukaa sawa. Na ikikaa sawa, ni kazi yakulipa madeni na ada za shule.” Joshua kimya.

“Kwa muda mrefu baba alikuwa akijaribu kutafuta kitu chakufanya kujikwamua kiuchumi. Tokea mama yupo hai na kushindwa. Sijawahi kumuona amehamasika na biashara kama hiyo ya mazao. Ubaya au uzuri sisi familia yetu tuna umoja. Tukiambizana jambo tukakubaliana, kila mmoja anasimamia hilo. Niliwapokonya gari na kulirudisha kwa Malon, nikijua itakuwa shida kwetu wote, lakini walikubali wote. Baba alikusudia kuiacha hiyo biashara ya mazao kwa ajili yangu na Malon! Nimeona si sawa Joshua. Nitakuwa mtu dhaifu sana na sitaendelea, kama nitakuwa nikimkwepa Malon kwa namna hiyo. Baba ni mtu mzima. Ananipenda na kunilinda. Sidhani kama atafanya kitu anachojua kina madhara kwangu.”

“Nilizungumza naye na Bale. Nikawaambia mimi sitakuwa na tatizo wakianzisha hiyo biashara na Malon kama watataka. Nikawaambia Mungu amenilipa kwa njia ya ajabu sana. Amenipa wewe. Kuendelea kumkimbia Malon, ni kutangaza bado ananguvu kwangu. Sitamkimbia tena. Wala sitaogopa kuja kumuona tena popote na wala sitaumia kwa lolote. Nimejiambia lazima nikubali kutoka hapo kwa kuwa Mungu amenitoa. Kwa hiyo ndio Bale amejinyima pesa kutoka kwenye pesa anazolipwa chuo, na mimi nimewaongezea yeye na baba, wataanzisha hiyo biashara.”

“Bale anakaribia kumaliza chuo, amemwambia baba watasaidiana. Ikitokea anatakiwa kusafiri kwenda kusaka mazao hata mashambani, amesema atafanya, sio lazima kuanza au kuendelea na Malon. Wakimaanisha ikilazimu, wataanza naye kisha waendelee peke yao. Lakini Joshua, mbali na tabia hizo za wanawake na udhaifu mwingine wa Malon ni mzuri sana wa biashara na ana roho nzuri sana. Kisha wakatokea kuelewana sana na Bale. Sitaki kumfunga sababu ya maisha niliyoishi mimi. Nimemwacha awe huru kabisa. Atakachoamua kufanya na Malon, iwe juu yake. Kwa hiyo ndio hivyo.” Joshua akavuta pumzi kwa nguvu sana, akatulia.

“Naomba nivumilie tu Joshua. Sina jinsi.” Joshua akamshika mkono. “Niahidi hutaniacha katikati ya safari yetu sababu ya Malon.” “Nawezaje Joshua!?” “Nyinyi mnahistoria ndefu na nzito Naya!” “Tafadhali tutengeneze ya kwetu ambayo haina maumivu. Yakuaminiana. Tutaweza Joshua. Nakuahidi ni rahisi kuliko vinginevyo.” “Sawa. Nakuamini Naya.” “Hiyo itanipa ujasiri sana. Itanisaidia. Nakuahidi sitakusaliti Joshua. Sio mimi na wala Malon hawezi kunibadili mawazo, nikakusaliti.” “Sawa.” Wakatulia, Naya akamuegemea begani.

“Unajua wewe ndio sababu ya kuwa hivi?” “Vipi?” Joshua akamchungulia akimuuliza. “Hivi nilivyo sasa hivi. Nimepata uhakika kuwa nipo salama kwa kuwa wewe upo na mimi.” Joshua akampitishia mikono mabegani na kumkumbatia vizuri. Naya akajivuta karibu. “Malon alikuwepo, lakini sikuwa na amani hivi Joshua, wewe ni shahidi. Uliona hata siku ile uliposema tulikuwa na kikao na wewe kwa mara ya kwanza kule kazini. Sasa ujue ile hali ya wasiwasi uliyoniona nayo haikuwa hata nusu ya vile ninavyokuwa nikiwa na Malon. Sidanganyi kama sikuwa nampenda. Sana. Lakini ilikuwa ni maumivu ambayo sina jinsi yakueleza. Sasa hivi nalala nikijiambia sio jukumu langu tena. Hainihusu. Siwajibiki kwake tena. Hayupo kwenye maisha yangu. Moyo umetulia nikijua Joshua wangu yupo.” Wakatulia kwa muda.

“Kesho huna haja yakunifuata huku Joshua. Nitawahi kuamka, baba atanisindikiza mpaka kituoni. Nitapata usafiri bila shida. Usije huku.” “Ni kama mimi uniambie nipande daladala kwenda kazini.” “Hapana. Sitaki uhangaike kuja mbali kote huku!” “Kwani wewe unajua ninapoishi?” Naya akatulia. Akakumbuka hata hajawahi kumuuliza anaishi wapi. “Ukweli sikumbuki kama ulishaniambia.” “Kwa nini hukuuliza?” “Mimi naona kuna mambo mengine ni mpaka mtu aamue kusema mwenyewe!” “Kwa hiyo na mimi unanihesabu kama mtu mwingine tu?” “Hapana Joshua. Mimi nilipotaka ufike kwetu, nilikwambia na kukuelekeza mpaka hapa. Ila kabla ya hapo sikuwa tayari ufike kwetu. Unakumbuka tulipokuwa tukitoka Mbeya?” Joshua akatulia.

“Japokuwa baba alisema niwakaribishe, lakini mimi sikuwa tayari mpaka nilipokuwa tayari na wewe. Kwa hiyo nikadhani na kwako ni hivyohivyo. Unisamehe kama nilielewa vinginevyo.” Joshua akanyamaza. “Eti Joshua Kumu, unaishi wapi?” Ilibidi tu Joshua acheke. “Naya wewe! Sawa bwana.” “Niambie Mr. Kumu. Unaishi wapi?” Joshua akamwangalia. “Unataka kweli kujua au kwa kuwa nimeanzisha hili?” “Sasa ukiumwa nani atakuja kukupa maji ya kunywa?” “Hayo ndio umekumbuka sasa hivi?” “Taratibu Joshua. Nilikwambia akili ilikuwa imevurugwa. Kadiri siku zinavyoendelea, ndio natulia nakuweza kufikiria na kurudia hali ya ubinadamu. Mwenzio nilikuwa nalelewa tu.” Joshua akacheka sana.

“Kweli. Malon alikuwa akinifikiria kwa kila kitu. Nafikiri ilikuwa njia yakunitawala vizuri, sijui. Haya, hapa nyumbani nilikuwa nalelewa kwa kila kitu. Kazi zangu zilikuwa na baba nje, mpaka mama alipotaka nianze kufikiria kama mwanamke. Ndipo nikaanza sasa. Kwa hiyo akili bado haijazoea. Sasa hivi ndio nipo kwenye kuanza kumfikiria Zayoni, kama vile mama. Kuanzia anapoamka, mpaka siku anapokwenda kwa mkewe.” Joshua akacheka sana. “Kweli. Ndio wosia wa mama huo. Aliniomba rasmi. Sasa niambie Joshua, si bado nina safari ndefu?” Joshua akamwangalia na kuamua kuendelea.

“Naishi Goba. Nilipata eneo kubwa sana kule. Ndipo nilipojenga na ndipo ninapoishi.” “Hongera sana. Swali jingine, unataka watoto wangapi?” Joshua akakunja uso akicheka. “Hilo swali unamaanisha?” “Kabisa.” Joshua akacheka akifikiria. “Nikuulize na wewe unataka wangapi?” “Joshua Kumu, jibu swali.” Wakacheka. “Familia kama hii ya kwenu sio mbaya. Ila wawili ndio ningependa.” “Jinsia?” “Naya!” “Hivi ndivyo unajaliwa Joshua! Jibu.” Joshua akacheka sana. “Nitajuta!” Naya akacheka. “Nikipata jinsia zote sio mbaya. Ila nitapokea kile Mungu atakachoona ninaweza kukikuza. Na wewe unataka watoto wa ngapi?” “Nilishakuwa na watoto wawili mawazoni na wa kwanza alikuwa wakiume, wapili wa kike.” Joshua akacheka akifikiria.

“Lini?” “Mwenzio nilifikiria, nikimaliza tu chuo, basi nitaolewa. Nitashika mimba kwenye fungate, nitazaa mtoto wa kiume ndani ya mwaka mmoja, huyo kaka akifikisha tu mwaka na nusu, nashika mimba ya dada yake, nimemaliza.” “Kumbe ulikuwa umejiandaa hivyo?!” “Sana Joshua. Nilijua baada ya chuo tu, kazi ya umama na kusaka pesa vitaanza. Sikuwahi kufikiria kama ningerudi kuanza tena kwenye swala la mahusiano.”

“Nikuulize Naya. Maana najua mume uliyemtegemea alikuwa Malon. Kweli ulikuwa tayari kuendelea naye hivyohivyo!?” “Hata baba aliniuliza hilo swali. Lakini Joshua, hakika nilikuwa tayari. Kwenye swala la wanawake ni kama alianza kubadilika na aliniambia anafanyia kazi. Swala la uwezo wa kipesa, sikujali. Nilijua nimesoma, nitapata tu kazi. Na tabia yake yakufungwa jela mara kwa mara, nilikuwa radhi kabisa hata kama ndio yatakuwa maisha yangu yakumtoa jela kila wakati, nisingejali ilimradi tu niwe naye.” Joshua akashangaa sana.

“Na yeye alikuwa akilijua hilo?” “Nategemea awe alikuwa akilijua hilo. Niliishi naye kwa vitendo. Kumthibitishia mchana na usiku namtaka, na mimi ni mwanamke wa tofauti na wote anao wachezea, nikimuomba aje anioe mimi. Ninapokwambia nimekataa pete ya Malon, ni kwa kuwa sina nilichobakisha kwa Malon. Nimegundua hakuwahi kukusudiwa awe wangu, na Mungu aliruhusu nifanye yote ili leo, nisiyumbe tena. Hakika nilifanya yote Joshua. Na nikikwambia sitakusaliti sababu yake hata kama tuna historia, ni kwa kuwa kweli sina sababu yakufanya hivyo. Sina jipya lakumpa Malon, na nimekuja kugundua hata yeye hana sababu ya msingi ya kuwa namimi, ila tu uhakika wa mtu kama mimi kwenye maisha yake. Kwa hiyo wala usiwe na wasiwasi na Malo. Nimekuwa naye akiwa anavuta bangi na havuti. Nimekuwa naye akiwa jela na huru. Nimekuwa naye akiwa mtaani na kanisani. Namjua haswa, zaidi yakumfahamu.” Joshua akatulia kidogo.

“Nikuulize kitu kingine, Naya?” “Chochote kile, niulize.” “Ila usione ni kama nakuharakisha.” “Sitajali hata kama utaharakisha. Najihisi nimejichelewesha vyakutosha, ni wakati wa kuchangamka.” Joshua akacheka kidogo. “Mbona kama unasita?” Joshua akamwangalia na kuamua kuongea tu. “Unakumbuka ile familia ya kina Magesa?” “Ile uliniambia ndio familia pekee  au watu pekee uliopenda kujisogeza kwao?” “Kumbe ulitilia maanani!?” “Kwa nini unasema hivyo!?” “Siku ile nakuambia juu yao, hukuonekana kujali sana.” Naya akataka kujitetea lakini akaona atulie. Akaanza kumuhisi Joshua ni mtu wakujali vitu vidogovidogo, akajiambia inabidi kuongeza umakini kwake, yeye sio Malon.

“Nisamehe Joshua kama huwa naonekana nakuwa sikufuatilishi. Nitaongeza umakini, ila nilikusikia siku ile. Vipi?” “Unafikiri ni sawa nikikutambulisha kwao?” “Ningefurahi na mimi kuwafahamu. Lini?” “Utakapokuwa tayari. Maana huwa mkewe, tena mna majina yanayofanana kidogo, yeye anaitwa Nanaa.” Naya akacheka. “Basi huwa ananisisitiza sana kuoa na kusema nisichelewe, halafu mama yake Geb, anaitwa mama G, huwa ananiambia nisichague sana. Na ameniomba rasmi, nikipata tu mwanamke, kabla ya kumtambulisha kokote kule, nimpeleke kwake kwanza.”

“Wanaishi pamoja!?” “Nakwambia hiyo familia utapenda. Huyo mama G, alizaa mapacha wawili, Grace na huyo Geb mume wa Nanaa. Grace naye anahistoria ndefu, ila ameolewa tena wanaishi Arusha. Geb na mkewe Nanaa, wana watoto watatu na wanaishi na huyo mama G. Geb sio mzungumzaji sana, lakini ile kuwepo tu nyumbani kwao, kuna hali ya tofauti. James ambaye ndiye alimlea Nanaa, alinitambulisha kwao mara moja tu tena kwenye sherehe, ilibidi kumuomba James anipeleke tena kwao, ndipo nikaongeza watu wengine.

 Joshua akamsimulia mengi juu ya Geb, Nana, mama G, James na Grace mpaka Naya akatamani kweli kuwaona. {Historia yao zaidi ipo kwenye simulizi ya ‘Ni  Wangu’ Karibu ujisomee kwenye website ya NaomiSimulizi.com.}

“Joshua! Kweli hao watu wanavutia. Nipeleke na mimi nikapate huo upako wa mahusiano.” Joshua akacheka sana. “Ndicho kikubwa nilichosikia hapo.” “Kwa hiyo kweli upo tayari nikakutambulishe?” “Kabisa Joshua. Mimi ni wako, na sitabadilika.” Joshua alifurahi sana. Alicheka huku akimwangalia Naya. “Sikutanii Joshua. Mungu anipe nini tena ili niridhike na kutulia!? Au hujaelewa nikikwambia hichi ndicho nilichokuwa nikikilia na kukisubiria kwa Malon!” “Akirudi hapo katikati?” “Alisharudi na pete mkononi, wewe ukiwa haupo kwenye maisha yangu, na nilimkataa. Baba huyo hapo ndani ni shahidi. Nimeamua kusonga mbele. Na acha kutishwa na Malon, Joshua bwana!” “Lazima anitishe. Amejaa mdomoni mwako kwa makubwa matupu!” Naya akatulia kidogo kama anayefikiria kisha akamgeukia Joshua.

“Nimeamua kutulia kwako Joshua. Nitambulishe kokote utakapo, sitakukimbia wala kukubadilikia. Nakuhakikishia.” “Nakushukuru Naya. Basi nitaweka mipango mizuri.” “Sawa.” Wakakubaliana na kutulia.

Zayoni akatoka kuwaitaa sababu ya chakula, wakaingia ndani. “Baba ameniambia Naya alikuwa hospitalini. Akawekewa mpaka maji na kupewa dawa bila baba kuwepo!” Bale akaanzisha hayo mazungumzo wakila. Wote wakacheka. “Ni kweli kabisa.” “Naya!?” “Ndiyo Naya.” “Hajakwambia mpigie simu baba, yeye amezidiwa, atakufa bila kumuona ba..” “Sio hivyo Bale. Anasema atakufa bila baba kumuona yeye.” Zayoni akamrekebisha Bale, wote wakacheka. “Nope.” Joshua akakataa huku akicheka. “Hajakwambia baba Naya atapata sana shida yeye akifa!?” Bado Bale hakuwa akiamini akaendelea kuuliza. “Kumbe hali ndio inakuaga mbaya hivyo!?” Joshua akauliza akimcheka Naya. “You have noooo idea!” Bale akamjibu nakufanya wazidi kucheka.

 ~~~~~~~~~~~~~~~~

v    Njama ameahidi kutokubali kushindwa, amejipanga.

v     Na Joshua naye ameapa kuwakilisha onyo kwake, kuhakikisha anaelewa amegusa sehemu ambayo hakutakiwa kugusa.

v    Malon naye ndio ameelewa na kukubali kukaa pembeni kama afanyavyo nyakati zote amuachapo Naya?

Vita ya Mapenzi&Pesa inaendelea.

Kwa umbali gani?

Usikose Muendelezo.

 


CONVERSATION

0 Comments:

Post a Comment