Naomi Simulizi |+1 205 767 8163 |naomisimulizi@gmail.com MAPENZI&PESA! – SEHEMU YA 23. - Naomi Simulizi

MAPENZI&PESA! – SEHEMU YA 23.

 Kazi Tena.

Saa 11 alfajiri, Joshua akawa ameshawasili nyumbani kwa kina Naya, Kiluvya. Naya naye alishakuwa tayari, akatoka bila hata  Joshua kuingia ndani ya geti. Safari yakurudi mjini, ikaanza. “Vipi tumbo lakini?” “Nakunywa zile dawa, limetulia kabisa. Ulilala salama?” Joshua akacheka. “Unacheka nini sasa?” “Jana umekoroma Naya.” Naya alicheka mpaka akajificha. “Ilikuwa kwa sauti?” Joshua akazidi kucheka. “Sasa na wewe kwa nini hukukata simu bwana!” “Nipitwe!” Naya akazidi kucheka kwa aibu. “Bwana Joshua! Ungekata!” Joshua akamwangalia na kuzidi kucheka.

“Sio vizuri bwana!” “Usijali.” “Mimi najali.” “Basi acha nikutetee. Ulikuwa umechoka. Unaumwa, na ukalia sana na kutapika. Ndio ukalala, nakupata utulivu mzuri ndio maana ukawa unakoroma.” “Umeona eeh!” Joshua akazidi kucheka. “Sasa na wewe ulilala saa ngapi?” “Nilichelewa sana kulala. Kuna kazi nilitaka niikamilishe ili uipitie kwanza ili wakati mnakaa leo na Jamal, ujue ni nini chakuzungumza naye.” Naya akashangaa mpaka akamgeukia. “Fungua dashboard hapo mbele, utoe karatasi. Zipo mbili tu.” Naya akafungua akianza kuhisi kutetemeka mikono. Akamwangalia tena na kumeza mate akijaribu kufungua. “Asante Joshua. Asante sana.” Joshua akajua amebabaika. “Sijafanya kitu cha ajabu wala sijakufanyia kazi yako, usizoee.” Naya akacheka kidogo na kuzitoa hizo karatasi. Mwanga wa hiyo droo ya gari ukazimulika, zilichapwa vizuri. Zilionekana safi.

“Ni yaleyale mawazo yako, nimeyaweka kitaalamu zaidi. Nitataka leo mkae na Jamal, lakini kabla ya hapo, nataka  utizame kile nilichoandika mimi, na ulinganishe na mawazo yako, vile unavyofikiria wewe. Kama kuna kitu unataka kurekebisha, rekebisha mapema na chapisha upya kabla hujakutana na Jamal ili mtakapokutana, mkamilishe na Jamal, jioni nataka hitimisho iwe imenifikia.” “Nakushukuru sana Joshua.” “Nilikwambia usizoee?” Naya akacheka kwa hofu kidogo. “Ni kwa kuwa ulikuwa mgonjwa, umekosa kazini jana, leo umetaka kurudi kazini na ndio siku nataka kufunga hilo zoezi. Sitaki upitwe wakati ulitoa wazo zuri sana.” “Nakushukuru sana kwa nafasi unayoniamini nayo Joshua. Asante.” “Karibu.” Wakatulia kidogo.

“Nikwambie kitu Joshua?” “Karibu?” “Siku ile ya kikao kuna mawazo nilitaka kutoa.” “Nilisikia.” “Nani alikwambia?” “Mbali na ile rikodi aliyonipa Jema, yule msaidizi wa CEO alinitafuta tena kuniambia juu ya hilo.” Naya akaingiwa hofu. “Yule baba! Anasemaje!?” “Anataka kujua ni nini ulikuwa ukizungumzia na tunafanya nini kuhakikisha tunakubakisha kwenye kampuni yetu.” “Joshua!” “Nilikwambia maji yametibuliwa. Changamka. Huu ndio wakati wako wa kung’aa. Acha woga, ongeza ujasiri ili watu wakuone Naya kama Naya, sio Naya nyuma ya Joshua. Unanielewa?” “Ndiyo.” “Ukiitwa popote, hakikisha unaacha historia kali, mpaka waje wakuite tena maana sasa hivi wewe bado upo ngazi ya chini sana. Lakini kwa hiki ulichofanya juzi, kinaweza kukupandisha juu kwa haraka kama utaendelea hivyohivyo. Jifunze kwa makini na hakikisha kila kitu unapatia. Tena unapatia haswa.” Naya akajituliza kupokea hekima za Kumu.

“Ondoa woga, fanyia mazoezi kila unachotaka kuzungumza mbele ya watu ili uwe fasaha, uongee kiutaalamu. Sio kurudiarudia jambo moja mara nyingi. Unachosha watu wakubwa wenye nyadhifa zao, ambao wanakusikiliza. Pia itakusaidia kupangilia mawazo yako. Sio unachanganya pointi. Sijui kama unanielewa?” “Nakuelewa.” “Basi ni hivyo tu vyakuongeza kwenye haiba yako ya uchapakazi na kwenye hiki kitengo.” “Nimesikia kufanya kazi karibu na wewe ni ngumu sana.” Joshua akakunja uso kidogo na kutulia.

“Wanasema eti unataka mtu...” “Asiye mzubaifu kwa kuwa sina muda wakurudia jambo mara mbili. Nataka mtu mwenye uwezo mkubwa wa kufikiria, kujituma mwenyewe bila kumfuatilia nyuma na roho ya uthubutu bila mipaka. Ndio maana mimi vikao vya kitengo kizima sifanyi kila siku au niseme mara kwa mara. Sina muda wakuanza kujibu maswali ya hakuna sukari, sijui maziwa ya chai!” Naya akacheka kwa hofu.

“Ndio maana nimechagua watu wachache ambao nikizungumza mara moja, wanaelewa na kutenda. Halafu wao nao ili wasipotee kwenye kujibu hoja za chai, na wenyewe wanawaachia kina Jamal. Kwa hiyo ndio maana unaona nafanya kazi kwa mwendo kasi. Sijui kusubiri. Hilo nalo ndilo tatizo langu. Nikishapima jambo na kujiwekea mikakati yake, huna jinsi ya kunibadilisha. Siwezi mtu mzembe mwenye visingizio. Kwanza...” “Huna muda wakupoteza.” Naya akamalizia kama aliyekuwa akimnukuu mtu. “Nani anakupa habari zangu Naya!?” Joshua akauliza akicheka kidogo. “Nimekufahamu na sifa zako nyingi hata kabla sijakuona Joshua Kumu, mungu wa Coca.” Joshua akacheka na kutulia.

“Nitajitahidi Joshua.” “Na mimi nitakuwa nyuma yako kukutia moyo.” Naya hakutegemea. Akamwangalia. “Najivunia sana wewe Naya. Sana. Huna sifa mbaya pale kazini. Ni nzuri tupu! Na ninajua utafika mbali sana.” “Asante.” Naya akatulia, akawa hajui azungumze nini tena. Joshua alishabadilika pale akawa bosi wake. Akatulia kabisa wakaendelea kuendesha.

“Joshua?” Naya akamuita tena taratibu. “Nikuulize?” “Karibu.” “Katika swala la mshahara, niliambiwa wakati wa ajira, unaweza kuzungumza. Sisi wametuanzia chini sana kwakweli. Natamani kuongezwa. Sasa nitaje kiasi gani? Nahofia nisije nikataja kubwa na kuharibu.” “Huwezi kuharibu kwa kuwa tunakuhitaji. Watakachofanya nikukuomba upunguze tu. Na kwa hakika sijui mishahara yenu japo najua wangu unaimbwa na kila mahali!” Naya akacheka kidogo na kuinama kama anayefikiria. “Sasa inakuaje wewe unalipwa pesa yote hiyo!?” Akauliza kwa hofu kidogo. “Ndio thamani niliyoweka kwenye kazi ninayowafanyia.” Joshua akajibu kwa kujiamini haswa.

“Wewe ndiye unayewauzia huduma. Wakitaka wananunua, wakishindwa unapeleka biashara yako kwa wengine. Si ndivyo biashara ilivyo?” “Ni kweli.” “Usipojiweka thamani wewe mwenyewe, basi ujue wengine watakuthaminisha kwa vile wanavyotaka wao. Lakini ukijijua wewe ni nani, na ubora wa huduma yako, basi, unajiuza kwa urahisi sana.” “Ni kweli. Lakini nilisikia na Pepsi walitaka kukununua mwaka jana, kwa pesa zaidi ila ukakataa. Ni kwa nini?” Joshua akacheka sana. “Kweli unazo habari zangu!” “Niambie kwa nini?”

“Moyo ulisita Naya. Nimefika hatua ya maisha, si pesa tena inaniongoza, ila kibali kutoka kwa Mungu. Hata uniambie utanipa mabilioni ya pesa, kama Mungu hayupo kwenye hilo jambo na hiyo pesa, hutanisogeza hata kidogo, kwa kuwa najua mwisho wake wa huko nitakapokwenda bila Mungu, nikuharibikiwa vibaya sana. Heshima Mungu aliyonipa pale, hailinganishwi na pesa.” “Kumbe unajua!?” “Oooh yeah!” Joshua akakubali kwa haraka sana.

“Ninazungumza na watu hao! Hata nikikwambia unaweza ukashangaa.” “Nimesikia ukizungumza, hao makaburu wanaandika.” Joshua akacheka kidogo. “Sasa hao ni wa chini ya hao ninaokwambia. Nikiwa nakwenda kwenye vikao Afrika ya kusini, hakika mimi mwenyewe huwa naingiwa hofu. Nakuwa sina jinsi zaidi ya kujifungia kwenye chumba walichonitayarishia, nakupiga magoti kunyenyekea mbele ya Mungu. Si kawaida Naya! Ila ni Mungu tu, wala si mimi hata kidogo. Hakika ni Mungu.” Joshua akaendelea kumtukuza Mungu wake Naya akimsikiliza. Akasikika ni kama mtu anayeogopa kuchukua sifa ya mtu mwingine. Kujihami kwa hali ya juu, akisema si yeye ila Mungu.

Walifika ofisini alfajiri hiyo kama waliotokea nyumba moja. “Nakuacha ukafanye kazi.” “Kwa hiyo ndio sitakuona tena mpaka jioni?!” Joshua akacheka. “Nakupa muda wakujiandaa. Kaandae utakachokionyesha kwa Jamal. Na hakikisha kinakuwa kina saini yako sio ya yoyote.” Naya akatulia kidogo. Joshua akajua hajaelewa. “Kazi yako yoyote ile, lazima mtu yeyote akiitizama, hata kama haupo pale, ajue ni yako. Hata kuzungumza pia. Ndio maana ulipotoa wazo lako au ulipokuwa ukizungumza, Njama alikuwa akisisitizia watu wakusikilize kwa makini, watagundua kuwa ni mimi nazungumza kupitia kinywa chako. Ni kwa kuwa wameshajua jinsi ninavyozungumza. Ni siri nakupa na wewe. Hakikisha kazi zako zinabeba jina lako. Ziwe za kipekee ndipo utakua kwa haraka.” Naya akaanza kubabaika.

“Nitafanyaje Joshua? Sina uzoefu!” “Hivyo nilivyokuandikia ni mfano wa Joshua wa miaka ya zamani. Nikajiongeza mpaka kufikia hapa. Lakini hivyo nilivyokuandikia hapo, ndicho au ndio jinsi ilivyonitoa. Ni msingi wangu. Sasa na wewe angalia jinsi yakupangilia mawazo yako. Nina uhakika hapa kazini hakuna anayetumia namna hiyo hata kidogo. Ukiiga, na kujiongeza kidogo tu, utabaki kuwa yako daima. Kila utakapokuwa ukiongea au kuandika hivyo, watajua ni Naya tu. Unanielewa?” “Naomba nikaanze halafu nikutumie uangalie kabla ya kukutana na Jamal.” “Hapana Naya. Hapo ndio nitakuwa nikikufanyia kazi. Na ndipo wazo la kutoa woga linapokuja. Fanya kuanzia hapo. Nitakachokiona baada ya hapo nitajua ndio kazi yako na umejiongeza mwenyewe na utaendelea kadiri siku zinapozidi kwenda.” Naya akapoa ni kama akawa amekumbushwa nafasi yake na ya Joshua.

“Usinikasirikie.” “Hapana Joshua. Nakushukuru sana kwa kunijenga. Nakuahidi sitakuangusha.” Joshua akafurahia hilo. “That’s the spirit. Huo ndio moyo ninaotaka. Nilijua ungekasirika!” Akaongea kwa kujivuna. “Hata kidogo. Nahitaji kujengwa kama mtu mzima si kuendelea kulelewa kama mtoto mdogo. Na kusukumwa kama hivyo. Nimejificha vyakutosha.” Joshua akajua somo limemuingia. “Uwe na siku njema. Ufanikiwe katika ufanyalo.” “Amina Naya. Nitakuona baadaye, kila la kheri.” Naya akashuka garini kama akimbie kwa hamasa.

Moja kwa moja kwenye meza yake akawasha kompyuta yake, macho kwenye zile karatasi akisoma na kushangaa. “Hata ningepewa mwaka mzima, nisingepata wazo la kuandika kwa namna hii!” Naya akaendelea kusoma vile ilivyoandikwa kwa mtiririko wa ajabu! “Ni kweli Joshua anakipaji cha pekee!” Naya akaendelea kushangazwa na ule mpangilio wa kazi.

Ili ile kazi ikae kichwani, akaanza kuichapa kwa upya. Neno kwa neno huku akijaribu kuondoa maneno magumu ambayo yanasikika kabisa ni ya Joshua, akaweka maneno yaliyobeba lugha nyepesi. Ilikuwa kama ripoti kwa lugha ya kingereza ila alichotaka kisikike kwenye tangazo, akaweka kwa lugha ya kiswahili. Naya aliipanga na kutengeneza vizuri. “Hawatanikamata na kujua Joshua amenitayarishia kweli!” Hofu ikamwingia Naya. Lakini akakumbuka Joshua kumwambia kuwa ni kazi ambayo pale haifahamiki. Akaendelea kuandika na kujaribu kuikariri vizuri. Akajaribu hata kuzungumza kwa sauti bila kusoma. Akarudia tena na tena mpaka akaona muda wa watu kuingia ofisini unakaribia.

Akaamua kuangalia kama kuna kazi hazikumalizika siku ambayo hakuwepo kazini, akagundua ni nyingi. Naya akashangazwa sana. “Inamaana Jamal hakupita humu ndani kwamba hajaona!” Naya akashangaa sana ila aliwajua wenzie. Ilimradi wawepo pale ndani, basi. Sio kufanya kazi, ila stori na macho kwenye simu muda wote. Akaanza kufanya kazi kwa haraka.

 Wafanyakazi wengine wakaanza kuingia na kumshangaa Naya. “Si tuliambiwa unaumwa!” “Nimepona.” Naya akajibu kwa ufupi akiendelea kufanya kazi mpaka saa mbili kamili Jamal alipoingia nakushangaa Naya yupo kwenye kiti chake akifanya kazi. “Mama Kumu!” Jamal akaita akimshangaa, Naya akajikuta akiitika na kugeuka bila kufikiria. Kumbe nyuma ya Jamal sehemu ya kuingilia alikuwa amesimama Joshua mwenyewe. Naya alishituka, Joshua akacheka taratibu akimtizama. Kama kawaida yake, mikono mfukoni. Jamal akageuka alipoona macho ya Naya yameduaa nyuma yake.  Akageuka. “Kumbe kiongozi upo nyuma yangu? Namshangaa Naya! Si alitakiwa kupumzika siku mbili!?” “Hana muda...” “Wakupoteza.” Akamalizia Jamal, wakacheka.

Joshua akawasogelea. “Nimepata ujumbe wako, ndio nataka tukakamilishe na Naya baada yakutoka kwa HR. Au kuna mabadiliko?” “Mimi nimekuja kumtakia kila la kheri na kumkaribisha rasmi kundini.” “Hatujafika bado kwa HR! Akikataa?” Jamal akauliza. “Ndio maana nimekuja kutongoza. Nabembeleza ili akifika huko asikatae. Wewe vipi Jamal? Nipishe.” “Samahani Kiongozi.” Jamal akanyanyua mikono juu akicheka na kuondoka. Naya akacheka kwa aibu. “Njoo.” Akamwita kwa kumkonyeza na sauti ya chini. Joshua akazunguka kule alipokaa.

“Nisamehe nimeitika kwa jina la mama Kumu, sikuwa nimefikiria. Jamal alinishitukiza.” Akamnong’oneza sikioni, Joshua akacheka. “Kumbe ndivyo wanavyokuita?” “Hapana! Yaani leo ndio mara ya kwanza.” Joshua akacheka. “Kumbe! Saafi sana mama Kumu.” Naya akampiga kidogo. “Nimefurahi uliitika. Usingeitika ndio ningesikitika.” “Kweli?!” “Kumbe! Inamaana ungekuwa umenikana.” Akashitukia Joshua anamvuta karibu, akamshika vizuri. Mkono mmoja kiunoni na mwingine shingoni, kisha akampa busu kwenye mdomo, palepale mbele ya watu, tena wafanyakazi ambao wapo chini yake! Ilikuwa ndio mara ya kwanza. Naya hakutegemea. Japokuwa alishituka sana, ila kadiri alipomshikilia vizuri na kuendelea kumbusu, Naya akatulia na kurudisha busu taratibu. Hakutegemea kufurahia busu la mtu mwingine mbali na Malo. Alijisikia vizuri mpaka akajisogeza vizuri.

Joshua alijawa maadili sana. Hakutarajia kupata busu kutoka kwake hata kwa kujisahau. Hakuonyesha dalili hata yakuja kumgusa siku za karibuni. Ni kama huo upande wa mapenzi hakutaka uwe wazi kabisa. Naya alishangaa ila akafurahia. Akajikuta amejisahau na yeye akamshika bila kujua ni wapi. Haikuwa muda mrefu sana, akamuachia, Naya akainama kwa aibu. Akamnong’oneza. “Nakupenda Naya.” Naya akacheka na kumwangalia. “Nimefurahi!” Joshua akacheka taratibu. “Usizoee.” Akamnong’oneza. “Siku njema.” “Na wewe Joshua. Nimefurahi.” Naya akasisitiza akicheka. Joshua akaondoka akicheka na kumuacha Naya mwenye maswali. Watu wote walibaki wameinama. Alipotoka tu Joshua, wote wakamwangalia Naya. Naya akarudi kukaa na kurudisha macho kwenye kompyuta yake.

“Upo tayari?” “Naomba dakika 5 tu, Jamal, bosi wangu. Kuna kazi ya jana namalizia.” “Daah! Nakushukuru Naya. Jana nilibanwa kupita maelezo nikashindwa kupitia hapo.” “Dakika 5 tu. Nakuja bosi wangu. Acha tupaache hapa vizuri.” “Lakini usichelewe tafadhali. Hii kazi inatakiwa leo jioni iwe imeshakamilika. Na Kumu akisema jioni, anataka iwe ni masaa machache kabla hapajaitwa jioni. Kama usemi wake unaopenda kuusema mwenyewe Kumu.” “Early is on time, On time is late, Late is an exceptable.” Kibasa aliyekuwa ametulia kwenye meza yake, mfanyakazi wa hapo wa muda mrefu kidogo, aliyejulikana kama msaidizi wa Jamal kwenye hicho kitengo chao kabla Naya hajaingia kwenye picha nakufanya majukumu mengi bila kutumwa wala kutambulika, akamalizia usemi wa Kumu anaoupenda kuusema sana, aliotaka kusema Jamal kwa Naya. Hawakujua kama wengine wanawasikiliza. Wakamgeukia na Jamal akaongeza. “Umesikia?” Naya akacheka. “Nimesikia bosi wangu.” “Basi changamka mama.” “Sitakuchelewesha.” Jamal akatoka Naya akarudisha macho kwenye kompyuta. Akili ilishachanganywa na Joshua. “Anajua ku ku...” Naya akacheka mawazoni na kujishika midomo kisha akaendelea na kazi baada ya kukumbuka anasubiriwa. 

Shari Yaleta Kheri.

Siku hiyo Naya akaingia ofisi ya mwajiri kuajiriwa rasmi. Alijawa wasiwasi alimtaka Jamal awe naye kwenye kila hatua. Jamal akamtajia pesa ambayo aombe kwa mshahara. Hilo likawa msaada. Akajaza karatasi zote za ajira kwa haraka, Jamal akitaniana na wafanyakazi wa kile kitengo mpaka akamaliza ndipo akatoka naye kwenda kufanya kazi.

Kwanza akashangazwa na vile Naya alivyopangilia ile kazi. “Wewe mtoto!” Jamal akamfanya Naya acheke. “Mbaya au nzuri?” “Mpaka najisikia kutupa kazi yangu!” Naya akacheka sana. “Nakuachia kitengo Naya.” “Wale watu wako sitawaweza Jamal. Mimi siwezi kelele nyingi, nitaishia kufanya kazi zote peke yangu kisha nitakuchelewesha.” “Wala usijali. Natoa ile fujo yote pale, natafuta wengine wachache. Nishamwandikia Joshua. Nasubiri akitulia na kuidhinisha, ijumaa hii napunguza watu pale na kutoa onyo.” “Jamal!” “Nimechoka Naya. Umeona kazi ulizokuta pale? Inamaana bila mimi kupiga kelele, hawafanyi kazi. Usipokuwepo wewe, inamaana kazi kazitafanyika. Wale ni watu wazima, si watoto. Kama hawana shida na kazi, basi wapishe watu wenye shida.” Naya akanyamaza. Walikuwa chumba cha mkutano, wao wawili tu.

Njama Tena.

Njama akaingia. Jamal akamtizama na kuendelea na kazi. “Sijaelewa?” Akaanza Njama. “Yaani huyu mtoto kaja juzi tu, anachukua nafasi yangu?” “Acha kutupotezea muda Njama. Kama unatatizo, nenda kasemelee tena kama mtoto.” “Hakika mtaniona mbaya.” “Sio wewe uliyekataa kufanya kazi na Naya?” “Si hakuwepo?” “Na mimi je?” Jamal akamuuliza. “Sio wewe uliambiwa na Kumu unipe kazi yako ili...” “Ili uniibie?” “Basi kwa taarifa yako tu, nipo hapa na Naya, amenikabidhi kazi yake. Nzuri kuliko yangu na hakuweka hata jina lake. Hakuna kuibiana Njama. Tunafanya kazi kama timu moja. Na hiyo ilikuwa hivyo tokea zamani mpaka wewe ulipoleta ujinga wako wa kitoto.” “Kwa hiyo ndio...” “Tupishe Njama. Kama unamatatizo yako, peleka mbele ya safari.” Akamgeukia Naya. “Endelea na kazi.” Naya akainama.

Vita ya Mapenzi.

Njama akasogea pale alipokaa Naya na kuvuta karatasi moja aliyokuwa akiisoma na kuandika. Jamal akasimama kama mshale na kumsukuma Njama huku akimpokonya ile karatasi ya Naya mpaka ikachanika. Naya akashangaa ngumi zinaanza kurushwa kati ya Jamal na Njama. Hapohapo akampigia simu Joshua. Katikati ya kikao, Joshua akapokea. “Njama anafanya fujo hapa tulipo na Jamal.” “Mko wapi?” “Chumba cha mkutano.” Joshua alitoka akikimbia bila yakuaga katikati ya mkutano. Kwa kuwa lilikuwa jengo moja, akafika kwa haraka na wafanyakazi waliosikia ile fujo na wenyewe wakakimbilia hapo. Wakakuta wakipigana haswa, wakirushiana ngumi kana kwamba ni wanandondi waliokuwepo ulingoni. Joshua akawaamulia na askari wakawa wamefika.

“Ameanza kumfanyia fujo Naya.” Jamal akamfanya Joshua kushituka sana, akamwangalia Naya. “Amekufanya nini?!” Naya alikuwa kwenye mshituko, akashindwa kujibu. “Nimevuta tu karatasi ndio...” “Subiri kwanza Njama. Naona umevuka mpaka, na hapo sitakuruhusu. Naya ni off limit.” Kumu akaongea kwa hasira. “Si umemchukua mwanamke wangu! Unampa mabusu hadharani kutangaza ushindi wako kwangu!” Naya akazidi kuingiwa hofu akajua maneno yalishaenea wasijue walipigwa picha na hiyo picha ikasambazwa. Kwa muda mfupi tu, kampuni nzima ilishapata picha yao wakiwa wanapeana mabusu. Ila Joshua alishatumiwa na Fina, alishajua akiwa mkutanoni.

Njama akaendelea kulalamika. “Isingekuwa wewe, sasa hivi mimi ndio ningekuwa na Naya. Tulikuwa tumefikia mwafaka na ile safari ya Mbeya ilikuwa niende mimi, lakini wewe ukanipora safari yangu ili ukamchukue mwanamke wangu. Niliambiwa kila kitu. Naya alishanikubali ila wewe ndio umemchanganya.” Jema akaingia akikimbia.  “Acha uongo Njama.”  Naya alijibu midomo ikimcheza kwa hofu, wafanyakazi wengine waliowahi hapo wakiwatizama.

“Hiki kinachotokea ndicho kinachokufanya unikatae Naya. Unataka Joshua akupandishe cheo kwa haraka na unasahau maisha ni zaidi ya hapa!” Njama akazidi kupayuka kwa sauti ya juu iliyozidi kuvuta wafanyakazi wote wa masoko hapo kwenye ukumbi wa mkutano na wengine hata wa nje na kuzidi kumiminika hapo, na kuzidi kumuogopesha Naya.

“Mpumbavu tu wewe. Akutake nani?” Jamal akamkejeli, Njama akataka kumrushia ngumi lakini Jamal akakwepa. Askari wakamshika Njama na kumfunga pingu kwa haraka kama na wao walikuwa wakimsubiria. “Ulichokuwa unakitafuta tokea majuzi, umekipata sasa.” Jema akamtupia neno wakati wanamtoa nje huku Njama akiendelea kupayuka.

“Sijawahi kumkubali. Usimwamini, anadanganya.” Naya akajitetea kwa Joshua huku akitetemeka kwa hofu. “Huna haja yakujitetea Naya.”  Joshua akamsogelea. “Hujaumia popote?” “Jamal aliniambia nisogee mbali.” Joshua akamgeukia Jamal. “Asante aisee.” “Mpuuzi kweli! Amechana kazi zote alizokuwa ametoa Naya na kutupa laptop yangu. Ndio tulikuwa kwenye marekebisho!” “Huna kopi yeyote kwenye kompyuta?” Joshua akamuuliza Naya. “Ninayo nimeacha kwenye ile kompyuta yangu, ofisini.” “Basi kaprint tena kisha mje muendelee.” “Sijui kama hii laptop yangu itafanya kazi tena! Ameitupa kwa nguvu kweli na mimi sikuwa nimetunza kazi yangu sehemu nyingine ila hapa tu.” Jema akaiendea laptop ya Jamal ambayo Njama aliitupa kwa hasira, akamuokotea.

Joshua akavuta pumzi kwa nguvu. “Nenda kalete tena kazi yako Naya, na mimi nitajaribu kuwasha kompyuta yangu nione.” Jamal akamtuma. “Lakini Joshua, nashauri urudi kwenye kikao. Umewaacha wote wapo mtandaoni wakikusubiria wewe. Naya yupo sawa, acha mimi nitasimamia hili zoezi. Tafadhali Kumu.” Jema akashauri kwa kusihi, Joshua akabaki akifikiria. “Tusije haribu kote, Kumu! Tafadhali nenda kamalizie kikao. Nakuahidi hapa patakuwa sawa.” Wafanyakazi wote walibaki wakiangalia kinachoendelea na kusikiliza. “Lazima nizungumze na Naya kwanza, nimtulize mimi mwenyewe. Waambie wanipe dakika 6 tu, nitarudi.” Joshua akatoka kwa haraka bila hata kusubiri jibu la Jema. Jema akatingisha kichwa na kutoka kurudi kwenye kikao akikimbia.

Yeye Joshua alishatoka na kumfuata Naya akamkuta amesimama pembeni ya kompyuta yake kama asiyejua chakufanya. Alikuwa peke yake pale, wengine wote walikimbilia eneo la tukio. “Naya!” Joshua akamuita. “Sikuwahi hata kumuonyesha dalili za kuja kumkubali baadaye. Anadanganya.” “Naomba utulie.” “Na pengine labda tusingekiss! Inaonekana kuna mtu alitupiga picha akasambaza hizo picha mpaka zikamfikia Njama.” “Au ni mtu wa Njama, alitupiga picha makusudi na kumtumia Njama. Na Njama akazisambaza makusudi ili...” “Kutuharibia! Mungu wangu Joshua. Labda...” “Tusikiss tena?” Joshua akamuuliza taratibu tu.

“Au mimi niache kazi hapa nikatafute kwengine.” Joshua akakunja uso. “Kwa ajili ya Njama au mimi na busu nililokupa asubuhi?” “Hapana Joshua. Nimefurahia sana, na nilikwambia, ila sitaki niharibu sifa yako njema.” “Kwa nani!?” “Sijui Joshua! Ila ninachojua nakupenda wewe.” Hilo likamfurahisha Joshua. Akamsogelea. “Nitakubusu kokote, mbele ya yeyote, muda wowote ninaotaka mimi kama wewe hutakuwa na shida.” “Mimi napenda.” Naya akajibu kwa aibu akitabasamu kidogo. Joshua akamvuta karibu yake na kumbusu tena na tena. “Hutaacha kazi uliyoanza rasmi leo. Nilikwambia dhoruba inapopita, lazima sisi kina KUMU.” Akimuonyeshea na yeye Naya, “Ndio tubaki tumesimama.” Naya akacheka.

“Hawajawahi kumuona Kumu kwenye mapenzi. Watazoea tu.” Naya akambusu hapo midomoni akatulia kwa muda, Joshua akimsikilizia, kisha akamwachia na kucheka. “Mimi nakupenda Joshua.” “Asante Naya. Acha nirudi kwenye kikao, na wewe rudi kazini ukiwa umetulia. Au unataka tukae wote?” Naya akashangaa sana. “Hapana Joshua! Nitakuwa sawa. Na samahani kukupigia. Sikujua kama ...” “Muda na wakati wowote unaponihitaji, nipigie.” Naya akacheka taratibu mbele yake. “Nashukuru. Haya nenda.” Kumu akambusu na kutoka kwa haraka akiangalia muda huku akipishana na wafanyakazi wengine wa hapo ofisini waliokuwa wakirudi hapo. Walimpisha kama wanaoogapa hata kugusana naye.

~~~~~~~~~~~~~~~~~~

Baada ya kuhangaika bila mafanikio akijaribu kufufua kompyuta yake ikabidi Jamal achukue kazi ya Naya kama ndio wamefanya wote. Hata hivyo akili ilishachanganyikana. Alikuwa hawezi kufikiria tena baada ya ugomvi alioanzisha Njama. Waliandikisha maelezo kwa askari. Naya peke yake na Jamal hivyohivyo wakieleza jinsi ilivyokuwa, Njama akaonekana ndiye mwenye makosa. Akachukuliwa na yeye maelezo yake yakiwa yanaandikwa kwa makini ili asije kugeuka baadaye.

Kabla ya kutoka kazini kwenye mida ya saa 8 mchana, Jamal akawa ameshawakilisha kazi kwa Joshua kwa njia ya barua pepe na kumkabidhi Fina kabrasha lililokuwa na kazi nzima. Joshua hakuwepo ofisini, Fina alimwambia ametoka. Naya akarudi ofisini mara baada ya kuruhusiwana na  Jamal. Akarudisha akili kazini. Ukweli ilikuwa ngumu kumsema Naya. Hata kabla ya kuanzana na Joshua, Naya alikuwa akichapa kazi na Jamal kumsifia kila wakati akitaka wote waige mfano. Hakuwa na maneno mengi ila kazi kila awapo kazini. Hapo Naya anarudi kwenye meza yake akiwa na ajira kamilifu  na mshahara mzuri. Akawa amewapita hata aliowakuta hapo kwenye hiyo kampuni na wenzake alioanza nao kazi pia. Kimya. Akajua wameongeza heshima sababu ya Kumu pia. Akajichekea moyoni akijua wapo wanaoumia. Hakujali.

~~~~~~~~~~~~~~~~~~

“Nimekuacha na njaa, Naya wangu! Nivumilie mama. Jioni tutakula vizuri.” Akageuka na kumuona Joshua. Akaweka matunda mezani. “Na wewe?” “Sina muda. Nasubiriwa. Wewe kula. Nitakuona baadaye. Si upo sawa?”  Naya akatingisha kichwa kukubali. “Ukimaliza kabla yangu, njoo unisubirie ofisini kwangu.” “Sawa. Na asante kwa matunda.” “Karibu. Baadaye.” Joshua akatoka kwa haraka. Naya akabaki akitizama yale matunda pale. Yaliwekwa vizuri, yakapambwa kwa unadhifu, zabibu zikavutia pale juu ya matunda yote. Akacheka wakati akivuta yale matunda kwenye chombo kizuri sana ila juu iliwekwa mfuniko wa wazi kuonyesha ule umaridadi ndani. Wenzake wote wakabaki wakimwangalia. Kulikuwa na uma pembeni, Naya akatoa, akaanza kula huku akifanya kazi. Hakunyanyuka hapo mpaka jioni akifanya kazi.

Ngumu kumlalamikia kuwa ameajiriwa kabla yao kwa kuwa ni kweli alikuwa akichapa kazi bila ya kutumwa wala kulalamika. Akikaa hapo, hatanyanyuka wala kuzungumza na watu hovyo akizungumzia habari nje ya kazi. Mtulivu, usingemkuta akibishana kwa lolote. Jamal alimpenda tokea hata hajaanzana na Joshua. Wivu uliwasumbua lakini ilikuwa ngumu kusema amependelewa.

~~~~~~~~~~~~~~~~~~

Jioni wenzake walitoka wakiwa kama wamemziria kazi. Alijua, lakini hakujali hata kidogo. Akazifanya bila hata kujali au hata kumwambia Jamal. Jamal alitingwa na kitu kingine, hakurudi tena hapo ofisini kwao. Naya akaendelea na kazi akiwa amejawa morari akijua yeye ni mwajiririwa halisi pale, mshahara upo juu, na kikubwa zaidi akajua anakubalika. Joshua yupo upande wake! ‘Nivumilie tafadhali. Naomba tena nusu saa. Unaweza kuja kunisubiria ofisini kwangu.’ ‘Hamna shida. Wewe endelea tu, usijali. Nitakuwa hapa ofisini kwetu, na mimi nikimalizia kazi.’ ‘Ndio maana nakupenda.’ Naya akacheka na kuendelea na kazi.

~~~~~~~~~~~~~~~~~~

Akiwa amepotelea kwenye kazi akasikia. “Utajuta kunifahamu!” Naya akageuka na kucheka. “Hata kidogo. Nimepata muda wa kufanya kazi zaidi. Njoo nikuonyeshe kitu.” Joshua akamsogelea. “Nataka kukuonyesha wewe na unishauri kabla ya Jamal.” Joshua akaenda kusimama nyuma yake ili aangalie. “Inabidi kutafuta laptop yako.” “Ninayo. Malo alininunulia tokea nipo chuo, ila sikujua kama naweza kuitumia hata kwa mambo ya kazini!” “Haina shida.” “Haya. Unakumbuka ile safari ya Mbeya?” “Ile uliwaambia kwenye kikao kuwa ulifanyia kazi survey?” Naya akamgeukia vizuri kwa mshangao.

“Jema aliniambia hata Jamal alionyesha ni kama hakujua ni nini unazungumzia au ni kama alisahau. Ninachotaka kukwambia ni kuwa, hii tabia hii, itakufikisha mbali sana. Kuzingatia au kuwekea maanani vitu kama hivi. Ni mimi huwa nawatuma ili nipate maoni ya watu. Kumfikia mtumiaji moja kwa moja. Ila nataka kukwambia ukweli Naya, sijawahi kupata majibu ya kueleweka kama hivyo wewe.” “Labda uangalie kwanza ili nisikuvunje moyo Joshua!” Akamtahadharisha. “Sijali itaonekana vipi, lakini ile tu kutenga muda na kufanyia kazi, kwangu inanirahisishia sana kujua wapi nifanye nini. Kwa hiyo umenifurahisha.” Naya akacheka na kumfungulia ile kazi kwa ujasiri.

Akamuona Joshua anacheka mara alipoiangalia tu. “Nimeiga ufanyaji kazi wako. Kama vile ile uliyonipa asubuhi.” “Daah! Unaakili sana Naya! Umepangilia vizuri sana. Sasa hii usiite tena kazi yangu. Hii ni yako. Na usijibadilishe ila kujiongeza ukiendelea kutokea hapa.” “Kwa hiyo umependa?” “Sio tu kupenda, umenisaidia sana na hichi ninachotaka kukizindua. Naomba nijitumie, ili nitumie kwenye kikao cha wote kesho asubuhi.” “Hamna shida kabisa.” Naya akafurahia sana kuona Joshua amemkubali kazi yake.

“Naruhusiwa kufanya marekesbisho kidogo?” Joshua akauliza kwa heshima. “Sio makubwa. Ni lugha kidogo tu.” “Nakushukuru Joshua. Najua umechoka.” Naya akampisha pale kwenye kiti. “Kaa yeye.” Akaanza kuisoma hiyo kazi kwa makini na kuifanyia marekebisho kidogo huku akirudia kusoma tena na tena mpaka akamuona ameridhika. Akaandika jina la Naya mwisho kabisa ya ile kazi kisha Naya akamuona akajitumia. “Nakushukuru Joshua.” “Karibu japo naona umeshakuwa mtaalamu!” Akampongeza. “Nina mwalimu mzuri je!” Joshua akacheka akisimama. “Inatosha kwa leo. Tuondoke hapa.” “Bado kitu kimoja.” Naya akarudi kukaa.

“Unakumbuka kusikia kuna suluhisho nililifikiria?” “Nakumbuka. Na ninakuomba kitu kimoja. Usimuonyeshe mtu yeyote hata Jamal, mpaka nitakapo kwambia. Itoe kabisa kwenye komputa ya hapa kazini, jitumie kwenye email yako ambayo sio ya hapa. Kisha futa ili ikabakie kwenye hiyo kompyuta ya nyumbani tu. Nina sababu yangu. Nitakwamwambia tukifika kwenye gari.” “Sawa.” Naya akafanya kama alivyoelekezwa, akafunga kompyuta, kisha wakatoka.

~~~~~~~~~~~~~~~~~~

Wakiwa kwenye gari Naya akamuomba Joshua ampitishie madukani mara moja. “Hujachoka tu?!” “Ni kitu nimejiambia ni lazima nifanye leo.” Joshua akampeleka mpaka Mlimani City kwenye mall. “Sasa wewe usiingie. Nisubirie kwenye gari.” “Ndio nini Naya!?” “Joshua! Nataka niende mwenyewe.” “Basi tuingie wote, mimi nitakuwa nikisubiria nje ya kila duka utakalokuwa ukiingia.” Naya akafikiria kidogo kisha akakubali, wakashuka wote.

Na kweli Joshua akasubiria nje. Lakini kwa aina ya duka aliloingia Naya, akajua ameenda kumnunulia na yeye zawadi, asijue ni nini. Lilikuwa duka la kiume, tena la bei. Na kwakuwa alishamwambia havai vitu vya hadhi ya chini, Joshua akajua itamgharimu, ila akamuacha tu. Akatulia nje kama mlinzi. Baada ya muda Naya akatoka na mifuko miwili. Joshua akacheka.  “Nikupokee?” “Hujachungulia nikiwa ndani?” “Mimi ni mwaminifu Naya.” “Sawa. Basi twende.” Wakarudi garini. 

Mapenzi.

Walipofika tu garini Naya akaanza. “Hizi ni zawadi zako. Zipo mbili. Moja ya kuwa mpenzi mzuri. Unayenipenda na kunitanguliza mimi katika kila jambo. Nimeona, na ninataka kukwambia nathamini sana hiyo.” Naya akaanza kulia, Joshua hakutegemea. “Usilie sasa.” “Hakika unanipenda Joshua. Katika kila fujo upo na mimi kama Naya, unanijali vile ninavyojisikia, kitu ambacho sijawahi pata kwa mwanaume yeyote hapa duniani! Unajali hisia zangu kwanza. Nakushukuru na usije kubalika.” Joshua akacheka sana. “Yaani hizi shukurani zimejaa na vitisho!” “Mimi sikutanii bwana. Uendelee kunijali hivyohivyo hata tukiwa wazee au na watoto, mimi nibakie wakwanza.” Joshua alicheka sana mpaka akapiga makofi. Naya akajifuta machozi.

“Na hii ya pili ni ya kuwa mfano wangu wa kuigwa. Unaniongoza vizuri.” “Kweli Naya!?” “Kabisa Joshua. Kwa muda mfupi tumekuwa wote hata nyumbani wanaona mabadiliko. Nakua kimawazo. Na kazini pia unanijenga. Isingekuwa wewe, mimi leo ningeacha kazi.” Joshua akakunja uso. “Kweli Joshua. Mimi sehemu za fujo siziwezi.” “Hata siku moja, mwanadamu asikuondoe sehemu Mungu aliyokuweka.” “Unaelewa sasa kile ninachozungumzia? Hayo maadili mimi sikuwahi kuyafanyia kazi. Ndio maana nakushukuru na ndio maana hata nyumbani wananishangaa. Hii leo tu, kama usingekuwa wewe haupo na mimi, baba angekuwa kwenye simu siku nzima nikimlilia. Lakini najihisi nampumzisha. Hata yeye ataweza kufanya mambo yake sio kunifuata nyuma kila wakati na matatizo yangu.” “Yetu. Sasa hivi kila kilicho chako ni chetu.” “Nakushukuru Joshua.” Akamkabidhi ule mfuko.

“Kabla sijafungua na kuangalia kilichopo ndani nataka ujue nimefurahi sana kukusikia ukiona uzee wako na mimi. Au watoto wako, mimi ndio nikiwa baba yao.” “Sasa wewe ulifikiri nani atakuwa baba yao?!” “Sijui Naya! Wewe ni mzuri sana na bado mdogo. Upo na nafasi yakuendelea kuchagua.” “Hapana Joshua. Naomba Mungu hilo eneo niwe nimefunga na wewe.” “Kweli unaomba au ni usemi tu?” “Hakika naomba Joshua. Tena nakuombea wewe ndio uwe wa mwisho. Hili zoezi la mapenzi linachanganya Joshua! Na uzuri wowote unao uona kwangu, sijawahi kuthaminiwa hivi kama wewe unavyonithamini. Hebu niambie Joshua, wewe utajisikiaje, tunakuwa kwenye mahusiano, halafu unasikia nakuwa na wanaume wengine, nalala nao tu hovyo halafu narudi kwako kila wakati nakuomba msamaha na kukwambia lakini nakupenda, ila naendelea tu kulala nje hovyo?” “Vibaya.” Joshua akajibu.

“Hapana Joshua. Vibaya haijaweza hata kueleza hiyo hisia yake. Ni mbaya! Hakika niamini mimi ni hisia ambayo hutaki mtu apitie. Unajiona hutoshi. Huwezi. Upo na kasoro. Huwezi kumtosheleza  ndio maana anakwenda kutafuta kwa wengine. Inaathiri utu kuliko nitakavyokwambia. Kila anayekutizama unajua anakudharau, zaidi marafiki wa karibu wanao wafahamu nyinyi wote wawili na wanayajua maisha machafu ya mwenzio! Huna ujasiri hata mbele yao! Lakini kwako nalala nikijua nikiamka kesho, bado Joshua yupo na hakutakuwa na sifa mbaya. Imeniongezea ujasiri na imekuwa kama dawa inayoanza kunitibu taratibu.” “Mimi sitakubadilikia Naya. Kwanza nitamkosa Mungu wangu na mimi sina mpango wa kukosana na Mungu wangu. Nayajua maisha bila Mungu. Huko sirudi. Wewe niombee tu niishi maisha marefu.” “Nitazidi kukuombea.” Joshua akafungua huo mfuko akicheka.

“Akatoa tai nzuri sana. Naya alipomuona anacheka baada ya kuishika, akajua ameipenda. “Nakushukuru sana. Ni nzuri.” “Nimefurahi kama nimepatia.” “Sana. Itaendana na mavazi ninayovaa ofisini.” Akaongeza akiangalia ndani. Akamuona anacheka. “Kila ukinywa chai au kawahawa, uwe unamkumbuka Naya.” Joshua akacheka sana baada ya kusoma. ‘My Heart Is Whenever You are’  Ndio maneno yaliyokuwa yameandikwa hapo juu ya hicho kikombe. “Kwa hiyo moyo wako upo popote nilipo?”  Joshua akauliza akicheka. “Ndio ramsi. Najifunga kwako tu Joshua.” “Daah! Mungu anipe nini Joshua Kumu!? Asante sana Naya. Na ninakuahidi sitakuumiza.” Akafungua mlango. Naya akashangaa anatoka.

Akaenda kufungua mlango pale alipokuwa amekaa, akaanza kumbusu ila kwa heshima bila kuvuka mipaka. “Naomba tukasherehekee kumpongeza Joshua, kupata mwanamke wake peke yake.” Naya akacheka. “Hivi tulivyo!?” “Hivyohivyo.” “Na hizi nguo za kazini!?” “Ndio siku Mungu wangu amenitendea muujiza wangu. Nifanyaje?” Naya akacheka. “Shuka twende.” Naya akashuka garini. “Lakini acha nimpigie simu baba nimtaarifu nitachelewa kidogo.” “Sawa.” Naya akazungumza na baba yake kwa kifupi tu, wakatafuta mahali pakula hapohapo kwenye moja ya migahawa ya Mlimani City.

Wakaka na kuagiza. Ukweli haikuwa siku ramsi, siku ya kazi tu, lakini walipata wakati mzuri sana. Mtulivu. Wao wenyewe, japokuwa walizungukwa na watu wengine, lakini kila mmoja wao akili ilikuwa kwa mwenziwe. Joshua akakuza maneno ya Naya kana kwamba ameapiwa kanisani mbele ya kadamnasi! Naya alimuona vile alivyofurahia na kuonyesha kwake ni jambo kubwa sana. Walimaliza kula ndipo wakaondoka kurudi nyumbani.

~~~~~~~~~~~~~~~~~~

Wakiwa njiani Joshua akaanza kuimba wimbo wake wa ‘Great is your Mercy towards me’. Joshua aliimba mpaka Naya akasisimkwa mwili tena kana kwamba huo wimbo anausikia kwa mara ya kwanza. “Joshua wewe ni mwimbaji sana!” Joshua akaendelea kuimba, kumbe alikuwa na cd yake hapo kwenye gari. Akaiweka, ndipo Naya akawasikiliza vizuri hao waimbaji wa huo wimbo. “Kumbe wakiimba wengi kwa sauti tofauti tofauti inavutia!” “Inakosekana sauti yako tu!” “Wewe unaimba sana Joshua mpaka unaogopesha!” “Usiogope. Naomba shika tu maneno kisha jaribu. Sitajali utakavyosikika. Ila nitapenda tukija kuimba wote.” Naya akacheka akifikiria. “Nakuahidi itavutia zaidi ya hivi unavyonisikia mimi.” “Sawa. Basi nipe muda.” Wakaendelea na safari yao.

“Nikuulize kitu Joshua?” “Karibu.” Naya akatulia kidogo, Joshua akamtupia jicho na kurudisha barabarani alipokuwa akiendesha. “Itakuaje juu ya Njama?” “Kwanza unajua walimpeleka polisi?” “Joshua!” “Kweli. Ni kama wale askari na wenyewe walikuwa na hasira naye. Nilisikia aliwatukana kabla ya leo. Kwa hiyo na wenyewe ni kama wamemkomoa. Amejiharibia sana Njama. Hawezi kuja kuajiriwa kwa urahisi. Maana hata ofisi za mwajiri kwenyewe ameharibu. Nasikia aliwajibu vibaya sana viongozi wake. Sasa hayanihusu mimi, ila ninachojua, hatarudi kuja kufanya tena kazi chini yangu. Kwanza siwezi kuja kumuamini tena.” “Sasa nani atafanya kazi zake?” Naya akaendelea kudodosa.

“Si utalemewa sana!?” “Ile nafasi yake niliitengeneza tu mimi mwenyewe tena kwa kugombana sana na haohao aliowatukana huko ofisi za mwajiri.” “Walimkumbusha siku ya kikao.” “Kwa hiyo haikuwa ramsi. Kwa kuwa niliitengeneza mimi mwenyewe, nimeshajua chakufanya.” “Unamchukua Jamal?” Naya akadodosa zaidi. Akamsikia akisema, “Mmmmhhh...” Huku akifikiria kama ambaye anapingana mawazoni. “Njama alifaa kwenye ile nafasi.” Naya akawa kama amemuelewa.

“Nilitaka mtu mwepesi. Sijui kama unanielewa?” “Nafikiri nakuelewa.” “Yeah. Nilitaka mtu kama Njama, ambaye anaweza kubeba mawazo yangu kwa haraka na kuyafanyia kazi bila visingizio. Mtu akishakuwa ni wa visingizio mara kwa mara, huwa simuwezi.” Naya akajua hatawezana na Jamal. Jamal analalamikia sana kitengo chake. Yaani waliopo chini yake.

“Hichi ulichofanya wewe ndio nakitaka kukiona kwa mtu anayekuwa karibu yangu. Nikimpa wazo, alielewe na kuzalizasha kwa haraka. Na nione matunda kwa haraka bila visingizio. Mfano ni wewe na siku ya leo. Ungekuwa na sababu zote zakutofanya uliyoyafanya leo. Au kutoendeleza ile kazi ya Mbeya kwa sababu kwanza hata kiongozi wako alikuwa hakumbuki! Lakini umeenda umbali mkubwa sana na ndio maana sikutaka umpe wewe hiyo kazi. Itamuongezea yeye sifa, na atakushikilia ili uendelee kufanya kazi zake, yeye akipokea sifa. Sijui kama unanielewa!” Joshua akauliza na kuendelea.

“Tunafanya kazi kama timu. Ndicho ninachotaka. Ila hata wao huwa nawaambia na kuwapa nafasi ya kukua huku wakionekana. Mimi si mtu wakuchukua sifa ya mtu.” “Hilo nimesikia.” “Basi. Huwa nawaambia nilazima tufanye kazi kwa ushirikiano, lakini...” “Shine.” Naya akamalizia, Joshua akaitika na kuendelea. “Kabisa. Ng’aa. Tujue kwamba kitengo cha masoko kinafanya kazi nzuri sana, lakini yupo anayekwenda mstari wa mbele, anachukua muda wakufikiria na kufanya jambo la kufanikisha timu nzima. Na huwa kila mwisho wa mwaka natoa award. Zawadi kwa waliofanya jambo kwenye kundi, tena naalika kabisa wakubwa ili wawatambue kwa sababu na mimi nimekua. Kutoka sehemu moja mpaka hapa. Kazi zangu zilionekana. Sikubahatisha na ninajua tupo pamoja ila kila mmoja amejaliwa na Mungu kwa namna yake. Sina...” “Tamaa na vitu visivyo vyako.” Safari hii Naya akamfanya Joshua acheke.

“Naya!” “Nakwambia mimi nakujua Joshua kabla sijakutana na wewe! Ndio maana hujawahi kufika nyumbani na kunisubiria, wakati wote unanikuta nipo tayari. Maana niliambiwa Kumu anausemi wake wa, ‘early is on time, on time is late, late is an exceptable’ usemi wa Kumu huo.” Joshua akacheka sana. “Wanakunukuu kila mahali mpaka kule uzalishaji wanajua. Kumu akikwambia anataka bidhaa tarehe 15, basi ukitaka umfurahishe, hiyo bidhaa ikamilike kabla ya hiyo tarehe.” Joshua akazidi kucheka.

“Nina shida ya kusubiri. Itabidi unizoee tu. Nikishajua kitu kinawezekana, ni changu, mimi natakiwa nichukue hatua, huna jinsi ya kunibadilisha hapo.” “Niliambiwa kuna wakati ulihamishia ofisi kule uzalishaji, mpaka ikabidi uongozi mzima uingilie kati, walikuwa wakifanya kazi masaa 24, bila kupumzika ili kukukamilishia.” “Na niliuza bidhaa huo mwezi, mpaka walishangaa. Imeingia kwenye historia ya hapa.” Akajisifu. “Hongera Joshua.” “Ni Mungu. Sasa ndio na wewe. Japokuwa upo ngazi ya chini, hakikisha unang’aa na usikubali mtu akachukua sifa yako. Hata kama nikiongozi, kama hii kazi ya leo.” Naya akawa hajaelewa.

“Baada yakusoma hii kazi uliyonionyesha sasa hivi, ndio nimegundua kazi aliyoniletea Jamal haikuwa yake ila ni yako.” Naya akatulia kidogo. “Lakini yeye ameileta kwangu akionyesha mlifanya naye!” “Laptop yake Njama aliiharibu ndio akasema tulete yangu. Imekaa vizuri.” “Jamal anajua kama nikitoa kazi, nataka majina ya wahusika wote. Ameandika jina lake tu bila kukuweka na wewe.” Naya akashangaa sana. “Sasa kwa nini amefanya hivyo?! Wakati hakufanya chochote!?” “Ndio maana nataka uongeze umakini ukijua mwanadamu ni kiumbe hatari sana. Na ni mzuri sana kutumia mwanadamu mwingine kujinufaisha.” Joshua akaendelea.

“Mara nyingi watu hupenda watu wanao nufaika nao. Jamal anakupenda sana na anakutetea kila mahali. Lakini kwa kuwa pia unamfanikishia mambo yake. Amepunguza kelele kwa kuwa anajua wewe upo kufanya kazi za kitengo kizima, yeye akifanya mambo yake. Huzungumzi, hulalamiki, kwa hiyo sifa zote ni zake. Kitendo cha kutoweka jina lako kwenye ile kazi ndio kimenishangaza. Nilimuhisi tu kwa kuwa kazi zake huwa nazijua, hana uwezo wa kuandaa kazi kama vile. Nilipoona tu ile nikaitilia mashaka, kama ni wewe au kweli ni yeye amebadilika. Kwa hiyo ongeza umakini kwenye kazi zako. Na hilo nitalirudia tena kwa wote ili ajue hata nyinyi wageni mnajua. Wasiwatumie tu.” Naya akatulia na wakawa wamefika nyumbani kwao, akashangaa geti lipo wazi. 

                        Malon.

“Kutakuwa na mge...” Naya akasita baada ya Joshua kuingia mpaka ndani na kuona aina ya gari iliyokuwepo hapo nje ya nyumbani kwao. Joshua akamwangalia. “Ni Malon?” Naya akainama kama anayefikiria. Joshua akajua kama ni yeye. “Sina haja yakuingia ndani. Naweza kukushusha tu, nikaondoka ili kukupa muda na mgeni wako. Nimekuahidi kukusubiri Naya, mpaka utakapokuwa tayari. Sitabadilika.” “Sihitaji muda mbali na wewe Joshua.” Joshua akacheka kidogo akionekana hilo limemfurahisha. “Twende wote ndani ili na wewe umsalimie.” “Unauhakika kama upo tayari Naya?” “Nilimaanisha kila neno nililokwambia pale Mlimani City, Joshua. Sitabadilika kwa kuwa unanipa sababu zote zakutobadilika. Twende wote.” Hapo Joshua akashuka kijasiri.

Naya akachukua zawadi aliyokuwa amemnunulia baba yake, akashuka nayo pamoja na pochi yake. “Nikusaidie?” “Hapana. Nipo sawa tu.” Wakaongozana wote kimya. Naya akaingia yeye wa kwanza. “Karibu Joshua.” Akamkaribisha akiwa ndani macho nje. Watu wa ndani wote wakawageukia wao. “Shikamoo baba.” Akaanza Naya, na Joshua naye akamsogelea na kumsalimia. “Naona umegeuzwa dereva!” Joshua akacheka. “Hapana mzee wangu. Tukiwa kazini tunakuwa na mambo mengi, hata kuonana ni shida. Huu ni muda wa pekee ndio tunapata humo barabarani.” Akajibu Joshua kwa heshima.

Akamsikia Naya amemsalimia Malon, Joshua akawageukia. “Mimi mzima, mama. Nimekuja kukuona tu. Nilikuwa Mbeya wakati tukizungumza. Nikajua leo ungepumzika!” “Nilitumia zile dawa ulizoniambia, naona zimenisaidia. Nashukuru kujali.” “Karibu na afadhali. Nimeleta na heating pad.” “Nilikwambia usisumbuke Malo!” “Kwamba umeshanunua?” Malon akauliza. “Bado lakini nitanunua.” Joshua kimya akisikiliza. “Sasa kuna sababu gani ya kununua ingine na wakati hii ipo hapa na mimi situmii! Hata kama maumivu yameisha, unakumbuka ilivyokuwa ikikusaidia?” “Nakumbuka.” Naya akajibu kwa hofu kidogo. “Basi itumie tu na kuitunza kwa kipindi utakachohitaji. Unakumbuka kunywa maji yakutosha lakini?” “Malon, huyu ni Joshua.” “Namfahamu Naya. Ulinitambulisha tulipokuwa Mbeya. Au umenisahau?” Akamgeukia Joshua na kumuuliza kiungwana tu.

Baba Naya, Bale na Zayoni kimya wakisikiliza. “Japokuwa siku ile hapakuwa na utambulisho ramsi, lakini bado na kukumbuka.” Akajibu Joshua. “Joshua huyu ni Malon, nafikiri nilikwambia juu yake. Malon, huyu ni Joshua. Mpenzi wangu.” Naya akaingilia na kutoa utambulisho zaidi. Pakazuka ukimya kidogo. Naya akamgeukia baba yake. “Nina habari njema.” Akamshika na Joshua. Baba yake akacheka. “Nini?” “Hapa unaponiona mimi, ni muajiriwa kamili wa Coca, na mshahara mpya.” Baba yake akacheka tena. “Pongezi sana mama yangu mzazi. Na asante sana Joshua najua na wewe unachangia.” “Hata kidogo mzee wangu. Yote ni Naya mwenyewe. Mimi mwenyewe najihisi nimebahatika! Naya anaakili sana. Bado anashangaza watu pale. Kwa hiyo kwa asilimia 100 ni yeye na Mungu wake.” Joshua akamsifia Naya wakiwa bado wamesimama.

“Na hii ni zawadi yako baba yangu. Najua unaniombea sana. Na ulikuwa ukinisindikiza kazini kila siku asubuhi ili niwahi.” “Na kukutengenezea maji ya moto ya kuoga pamoja na...” “Chai.” Bale akaongezea kwa mdogo wake, Zayoni aliyeongeza  wakati Naya akimshukuru baba yake. Wakacheka. “Na mimi zawadi yangu ya kukufulia ipo wapi?” “Na wewe Zayoni umefua siku moja tu tena jana wakati naumwa, leo unataka zawadi! Hapana bwana.” Joshua akabaki kucheka.

“Hata kama ni siku moja tu, lakini si amekusaidia siku ya shida yako! Ulitakiwa kumnunulia mtoto zawadi yake, lasivyo usimfulie tena.” Naya akachukua kandambili mlangoni na kumrushia Bale pale alipokuwa amekaa na Malon, Bale akakwepa akicheka. “Umbea tu na kutaka kunichonganisha na Zayoni. Endelea mwaya kunifulia Zayoni mdogo wangu, ipo siku nita...” Kila mtu akazidi kucheka. “Ona anavyomrubuni mtoto! Hakuna kumfulia tena mpaka zawadi.” “Hayakuhusu Bale.” “Na hivi nimerudi mwenyewe, labda Malon anichukue twende naye.” “Afadhali. Tena ondoka naye sasahivi. Wenyewe tulikuwa na amani! Sijui kwa nini hujafeli huko chuo ukarudia hata miaka mitatu tena!” “Majibu bado mama. Ila dua la kuku halimpati mwewe. Nishamaliza, nipo mtaani na wewe. Mtetezi wa Zayoni nimerudi. Ndio maana mtoto amekonda!” Wakaanza hao wawili kubishana mpaka karibu Naya aanze kulia.

“Haya, Bale nenda. Toka hapo.” “Sasa mimi nimefanyaje baba jamani!?” “Nenda Bale. Unamliza mwenzio wakati amekuja na habari njema hapa!” “Zakutaka kumwonea mtoto tu!” Naya akakaa pembeni ya baba yake akaanza kulia, Joshua akiwaangalia ndugu hao, Malon alishawazoea.

“Mimi naondoka humu ndani kama Bale ndio amehamia hapa rasmi.” Bale akazidi kucheka na kurudi. “Akiondoka Naya, nachukua chumba chake.” Naya akamrushia tena kiatu, Bale akakwepa. “Naenda kukufungashia mizigo yako.” Naya akazidi kulia. “Mimi nakwambia kila siku, usimsikilize huyo anaishia kukuliza, ona sasa.” “Mimi sijui kama nitakuja kuolewa humu ndani jamani!” Naya akalalamika akilia. Wote wakacheka. “Twende zetu Joshua wangu.” “Sasa mwenzio mbona humpi chakula? Bale amepika...” “Sitaki chakula cha Bale. Kinaweza kumkaba Joshua wangu bure!” Bale akasikika akicheka ndani. “Joshua alikisifia sana chakula changu.” Bale akajibu akiwa chumbani. “Alikuwa muungwana tu. Toka hapa. Chakula chako kibaya tu.” “Nimekwambia usimjibu.” Baba yake akamuonya. Bado Joshua alikuwa amesimama hata hakuwa amekaa.

Naya akasimama na kujifuta machozi. “Twende Joshua wangu. Watu wa humu ndani...” “Ni wema sana na ...” “Toka zako Bale.” Naya na yeye akamkatisha, wakamsikia Bale akizidi kucheka. “Nikujie na mizigo yako yote? Ili ukitoka ndio iwe moja kwa moja?” “Baba unamsikia Bale lakini?” “Bale wewe ndio unakaribia kuondoka usiku huu.” Hapo Naya akafurahi. “Au baba umfukuze, japo kwa huu usiku tu wa leo sisi tufurahie ajira yangu?” Wote wakazidi kucheka. “Mimi nanyamaza baba. Atakayeongea tena ndio atoke.” “Nyinyi hamuoni hata aibu mbele za wageni jamani!?” “Namshangaa Naya.” “Mfukuze baba. Alisema mwenyewe atakayezungumza ndio aondoke. Hii nyumba ilikuwa na amani kabla halijamaliza chuo. Limerudi na kuanza fujo! Sijui yukoje Bale! Twende zetu Joshua.” Bale akazidi kucheka.

“Wakataka kutoka, Naya akawa kama amekumbuka. “Malon asante kwa kuja kuniona na vitu ulivyoniletea, lakini hapana.” Naya akarudi mpaka pale alipokuwa amekaa Malon na Bale, kwenye meza ya chakula. “Nakushukuru. Ila nataka nianze kujitegemea na kujifikiria mwenyewe. Umenisaidia vyakutosha. Sasa basi.” “Unakunywa maji lakini? Macho yanaonekana yamechoka na midomo imekukauka.” “We Malo! Hivi unanisikia chochote ninachoniambia?” “Na wewe unanisikia chochote ninachokuuliza?” “Mimi nakusikia ila sitaki kukujibu.” Wakamsikia Bale akicheka huko chumbani. Naya akatulia akiangalia mlango alipokuwa ameenda Bale kisha akaendelea.

“Kwa hiyo hunywi maji ya kutosha na ninajua utakuwa umetapika sana.” “Naya anakunya maji, na hata hapo kwenye gari ameacha maji ya chupa niliyokuwa nimempa. Na alipotapika sana, nilimpeleka hospitalini akawekewa maji yakutosha tu.” Akajibu Joshua. “Kwa hiyo swala la unywaji wake maji usiwe na wasiwasi nalo. Anazingatia.” Pakazuka ukimya kidogo.

“Labda nikuulize Joshua. Kuna tatizo gani kwa Naya kupokea kitu chochote kutoka kwangu hasa akiwa yeye hana hicho kitu?” Naya akashituka mpaka akatoa macho. “Tafadhali naomba usianze na Joshua! Tafadhali sana Malon! Joshua ni mstaarabu sana sio kama...” “Mbona ni swali dogo tu Naya?! Kwa nini unanigombesha?” “Wewe tulipokuwa wote ulikuwa ukikubali nipokee vitu vya wanaume wengine?” Naya akamuuliza.

“Tena ulikuwa mkali hutaki hata nizungumze na mwanaume mwingine kama wewe haupo wakati ulijua mimi sio muhuni! Haki yakumuhoji Joshua wewe unaipata wapi? Naomba muache Joshua.” “Mimi sijauliza kwa ubaya Naya. Maana uliniambia hata gari umenirudishia sababu umeanza mahusiano na Joshua! Nikajua wazi yeye ndiye anayekukataza. Sasa nikajiuliza huyu Joshua anayepokonya usafiri mmoja tu wa familia, anataka nyinyi hapa muishije! Najua wewe anakusaidia usafiri. Na wengine!?” “Naomba Malon uondoke.” “Usinifukuze Naya. Nipo pia hapa kuzungumza biashara na Bale. Na wala sifanyi fujo. Hata kama utaolewa na Joshua, mimi ni kama mtoto wa humu ndani tu. Hapa ni nyumbani, huwezi kunikwepa.” “Bora nisingewahi kurudi hapa ndani.” Joshua akarudi.

“Hapana Naya. Wala usilie. Njoo.” Akamvuta karibu na kumshika mkono. “Sijitetei, lakini najua tunatofautiana kimaadili. Wewe sijui umekuzwa vipi, tunaweza kutofautiana makuzi. Lakini mimi kama mimi, sipendi kusaidiwa majukumu yangu.” “Kusa...” “Tafadhali naomba nimalize.” Malon akataka kumkatisha, Joshua akawa muungwana tu. “Sasa hivi Naya ni wangu na ni jukumu langu pia. Nafikiri mimi ndiye ninayetakiwa kumtunza Naya nikijua bado ni binti ya mtu na anaishi na mzazi wake. Sitavuka mipaka na wala sitamuacha Naya akateseka. Na kwa kifupi tu Malon, sitafanya kwa mashindano na wewe au mtu mwingine yeyote yule, ila ni kwa kuwa nampenda na kumfikiria Naya. Sitaki kumtesa, ila tupo kwenye kujenga msingi wetu mimi na yeye. Kwa kile Mungu atakachotujalia, tutajenga. Sisi wawili, tukimtumainia Mungu bila mkono wa mtu mwingine yeyote yule. Hata kama tunaanzia chini sana, tena kwa kuhangaika, lakini itakuwa ni msingi wangu mimi na Naya. Tutavumilia huku tukimwamini Mungu kwa baraka zaidi.”

“Kwa hiyo Malon, kama alivyosema Naya, tunashukuru sana kwa misaada yako, lakini, hapana. Ulishapata hiyo nafasi. Na kwa maelezo ya Naya, uliitumia vizuri sana hiyo nafasi bila ubahili. Lakini Mungu amemtoa Naya kwako, amenikabidhi mimi kwa upendo kabisa. Nikiwa simstahili Naya, Mungu amenipa. Najua mengine Mungu atatuwezesha tu. Ameniambia alizungumza na familia juu ya swala la gari, wakaelewa. Ipo siku mimi na Naya tutakuwa msaada kwa familia, lakini sio kwa kukutumia wewe. Ni hilo tu.” Joshua akawafunga wote midomo, Naya akafurahi sana.

“Twende Joshua wangu.” “Usiku mwema wote. Mzee wangu!” Joshua akamgeukia kwa heshima. “Mimi nikitoka, ndio nitakuwa nikitoka moja kwa moja mpaka tena kesho.” “Asante sana Joshua. Nakushukuru kwa hiyo kazi ya kuja kumchukua na kumrudisha huyu. Ni kweli inampunguzia usumbufu.” “Itaisha tu mzee wangu. Nimemuagizia gari yake, itachukua kama majuma matano mbele, lakini itafika tu.” Wote wakashangaa mpaka Naya mwenyewe akashangaa. “Umemuagizia aina gani ya gari!?” Bale akatoka chumbani kwa haraka. “Nafikiri bado ninazo picha zake hapa. Hata Naya mwenyewe sikuwa nimemwambia. Nilitaka iwe suprise.” Joshua akatoa simu yake mfukoni.

Mpaka Naya mwenyewe akasogea karibu kuona picha. “Kweli Joshua!?” “Kweli. Niliiagiza Japan siku ile tu tuliporudi kutoka kuendesha boti. Usiku. Acha nikuonyeshe.” Na Zayon akasogea. Joshua akaperuzi kwenye simu yake, akapata. “Hii hapa.” Akamkabidhi simu Naya. “Mungu wangu Joshua! Hii gari ni kama hiyo ya Malon hapo nje sema..” Naya akabaki ametoa macho. “Uliniambia unapenda aina hizo za magari ila unahofia mafuta.” Naya akamwangalia Joshua kama asiyeamini, Bale akampokonya ile simu. “Hii ni ya kijivu inayong’aa vizuri!” Akasifia Bale. “Tuone.” Baba yake akataka kuona na yeye, Bale akamsogelea baba yao kwa karibu na kumuonyesha. “Ni nzuri sana.” Akasifia.

“Sijui hata niseme nini Joshua! Sikuwa najua!” “Tuombe Mungu ifike salama wasiibe vitu vya ndani. Ni ya kisasa. Inavitu vingi sana, vipya na vya kisasa, tekinologia mpya. Nina uhakika utaifurahia tu.” “Nakukushukuru hata kutufikiria tu. Hivyo itakavyokuja, vyovyote vile, pia nakushukuru sana.” “Karibu.” Naya akabaki akimwangalia kama haamini. Joshua akacheka. “Ila usingeagiza ya aina hiyo! Siitakuwa gharama sana!” “Wewe ndio hustahili vya gharama?” “Si kwa kiasi hiki Joshua! Halafu huku mbali na...” “Acha woga Naya.” Joshua akamtuliza, Malon kimya kwenye meza macho kwenye simu yake. “Na mimi utanifundisha kuendesha?” Zayon akauliza. “Ukifikia umri wa kuendesha nitakufundisha Zayon.” Bado wote walikuwa kwenye mshangao, hapakuwa na utani. Bale akachukua tena ile simu kutoka kwa baba yake, akabaki akingalia lile gari.

“Bale kwa kupenda magari! Mrudishie simu yake arudi kwakwe, akapumzike.” Baba yake akamshitua Bale, akacheka na kumkabidhi simu Joshua. “Isee hiyo gari nzuri sana. Hongereni.” “Asante.” Naya akajibu kwa haraka na cheko akimwangalia Joshua. “Nimefurahi!” Joshua akacheka taratibu kisha akaaga tena, ndipo wakatoka.

“Kwa nini hukuniambia Joshua!?” “Leo nimeropoka tu. Sikutaka nikwambie mpaka ifike. Ila ndio ujue muda wetu wa njiani utapokonywa.” “Kweli bwana. Tutarudi kwenye simu.” “Sio sawa na kuwa pamoja kila asubuhi na jioni.” Wakawasikia Naya na Joshua wakizungumza hapo nje, mwisho sauti zikaanza kusikika kwa mbali, wakajua anamsindikiza garini.

“Nimefurahi ulivyoweza kutulia na kumjibu vizuri Malon! Kweli Mungu amekujalia hekima Joshua. Malon ni mkorofi sana. Ungemjibu vibaya pale, angekubadilikia!” “Kidogo ameniudhi. Alikusudia kuniharibia pale kwenu na ndio maana niliamua tu kusema, nikihofia gari isije kuja, nikaonekana nilinunua sababu ya maneno yake ya leo!” “Pole Joshua wangu. Naomba sisi tuendelee kama ulivyosema pale ndani. Au kama tulivyofanya leo kazini kwa Njama.” Joshua akavuta pumzi kwa nguvu kama anayejaribu kutulia. “Nenda kapumzike. Mimi nikitoka kuoga, nitakupigia kama bado hujalala, tuzungumze kidogo.” “Basi nitakusubiri mpaka unipigie.” “Basi acha nikaoge halafu nikupigie.” Joshua akaondoka, Naya akarudi ndani akiwa ametulia kabisa.

“Umependa zawadi yako?” “Nimebaki nikiingalia tu hii saa.” “Umeipenda?” “Sana. Naona na Bale ameomba niwe namuazima.” Naya akacheka. “Kama umependa, nimefurahi.” “Sasa si utakuwa ukiishiwa pesa yote mama yangu! Usinunue vitu vya gharama hivi!” “Nataka na wewe uonje matajiri wanavyojisikia baba yangu.” “Na mimi nataka kuonja matajiri wanavyojisikia.” Zayoni akaongea kwa kulalamika na kufanya wacheke. “Haya vaa hii saa mpaka unapokwenda kulala ndipo unipe.” Baba yake akampa hiyo saa, Malon akiwa ametulia kimya hapo mezani, Bale akamsogelea kumalizia mipango yao. Naya akapitiliza chumbani bila kuwasemesha tena, ila akajua Malon amekasirika sana.

~~~~~~~~~~~~~~~~~~

Hakuwahi kupenda kupitwa. Na yeye ndiye alijithaminisha kuwa aliwekeza kwa Naya kwa viwango vya juu sana, hakuna mwanaume anaweza kufika hapo. Ndio maana aliingia na kutoka kwenye maisha ya Naya vile anavyojisikia yeye, akijua hakuna mwanaume anaweza kufikia hicho kiwango alichoweka kwa Naya. Sasa anatokea Joshua, mwenye sifa zote za mama Naya, tena nakupitiliza! Anajielewa! Sio mbambaishaji! Anamipango ya kueleweka! Ndio kwa mara ya kwanza anatokea mwanaume kwa Naya, Malon anakosa mwanya. Naya alikuwa akimcheka moyoni kwani alishamwambia hatakuja kupata mwanaume kama yeye.

~~~~~~~~~~~~~~~~~~

Akaelekea kuoga kwa haraka, alipotoka tu bafuni, bluetooth sikioni, wakamsikia akizungumza. “Bado sijafika.” “Pole. Basi acha nikusindikize mpaka nyumbani.” “Nashukuru.” Joshua akajibu, maongezi yakaanza katikati yao, Naya akiwa amejawa furaha yakupitiliza. Gari ya nguvu inakuja! Alijawa furaha sana. Na kitu kingine kikajengeka kwa Joshua. “Joshua ananifikiria sana!” Akawaza Naya na kuanza kumsihi Mungu awasaidie kitu chochote kibaya, kisitokee katikati yao. Wakaagana baada ya masaa kadhaa mbele. Alimsubiri mpaka alipokuwa tayari na yeye kuingia kuoga. Ndipo wakaagana.

Naya akaona haitoshi. Akamtumia na ujumbe. ‘Nakushukuru kwa kuweza kunifikiria na kuniweka mimi mbele ya hata vitu nilivyovikuta ni vya muhimu kwako, Joshua. Asante sana na Mungu azidi kukubariki. Usiku mwema.’ Joshua anatoka bafuni, akakutana na huo jumbe. Akakaa na taulo kiunoni. Akasoma ule ujumbe kwa kurudia. Akajisikia faraja kuona Naya anatambua juhudi zake. ‘Nakupenda Naya. Nilikuwa nikimsihi Mungu atuepushie majaribu. Chochote kisitokee katikati yetu na kututenganisha.’ Naya aliposoma tu, akampigia. “Nilijua umeshalala!” Joshua akashangaa wakati akipokea simu ya Naya. “Nimeanza kusinzia. Kichwa kimechoka sababu ya fujo za leo, ziliniingia akilini. Lakini nimetaka kukwambia na mimi nimeomba hivyohivyo. Mungu atusaidie, chochote kisitokee katikati yetu.” Mazungumzo yakaanza tena kwa wapenzi hao, Joshua kwa ujasiri wote akiwa ameshatambulishwa mpaka kwa Maloni kuwa ni mpenzi, na baba Naya kuendelea kumshukuru mbele ya Malon akiwa hata hajui kama kuna gari imekuja.

Siku Inayofuata.

Alamu ilimuamsha Naya hata asijue Joshua alikata simu saa ngapi, na kama Malon aliondoka muda gani. Akacheka akifikiria kama na usiku huo alikoroma, Joshua akimsikiliza. Akajitayarisha kwa haraka wakati baba yake akimtayarishia kifungua kinywa ambacho huwa kinamsaidia sana. Mara nyingine anashindwa hata kula mchana au kabla ya kuja Joshua kwenye maisha yake, alikuwa akibania pesa. Badala yakula kazini mchana, akipata hicho kifungua kinywa, ni mpaka arudi kula hapo nyumbani. Alijua kwa hakika pesa yake inategemewa sana hapo nyumbani kwao, hakuruhusu matumizi yasiyo lazima hata kidogo.

“Naona Bale ameamua kufanya biashara na Malon.” Baba yake akajaribu kutupia neno wakati Naya akila. Naya akatulia bila ya kujibu. Baba yake alijua amesikia “Naya?” “Nimesikia baba.” “Najua umesikia.” Akatulia kidogo kisha akamgeukia baba yake pale alipokuwa amekaa sebuleni. “Unajua ningetamani Malon asiwe anakuja hapa nyumbani. Na wote niliwaambia baba. Lakini kwa sasa hatuna jinsi. Tunafanya kile kinachowezekana. Bale amemaliza chuo na anatafuta kujishughulisha. Kama Malon anaonekana kuwa msaada kwake, hata yeye nilizungumza naye kuwa aendelee naye tu. Lakini si kitu ambacho nafurahia baba yangu. Ila hatuna jinsi. Tunashika pale Mungu anapofungua mlango.” Baba yake akanyamaza, Naya akaendelea kula mpaka alipoona simu yake inaita. Akajua Joshua ameshafika nje na kugeuza gari tayari.

“Nashukuru kwa chakula, baba Naya. Joshua ameshafika.” “Uwe na siku njema.” “Na wewe. Nitakupigia baadaye. Ila pesa ya rangi pamoja na vitasa nimetuma sasa hivi. Utakuta kwenye simu yako.” “Na Bale naye alihitaji pesa kidogo. Sijui kama alikushirikisha!” “Nitampigia. Ila pesa bado ipo. Usiwe na wasiwasi.” Naya akatoka kwa haraka. Yeye ndio alikuwa kama mtunza pesa hapo kwao. Hata baba yake alipotoka Mbeya kikazi, alimpa yeye pesa aliyotengeneza. Akawa kama ndio muendesha bajeti ya familia yao.

~~~~~~~~~~~~~~~~~~

Joshua akamuona jinsi alivyoingia akiwa usoni amepoa. Akajua kuna kitu hakijakaa sawa. “Uliamka salama?” “Nashukuru Mungu niliamka salama.” Akajibu kisha akacheka. “Nilikoroma?” Joshua akacheka na yeye. “Jana hukukoroma. Kwanza nimegundua wewe sio mkoromaji. Juzi ulionekana ulichoka.” Naya akacheka. “Wewe ulilala saa ngapi?” “Kwenye saa nne na nusu. Sikuchelewa sana. Nilikuwa nimechoka. Ila nashukuru nilimaliza vitu vyote nilivyojipangia kufanya jana.” “Afadhali. Kwa hiyo ulilala vizuri?” “Bila hata ndoto mpaka alamu iliponiamsha.” Naya akacheka. “Na mimi hivyohivyo hata sikujua ulikata simu muda gani.” Wakaendelea kuzungumza kidogo lakini kila mtu akiwa na lake.

“Nimesikia Bale anaanza rasmi kufanya biashara na Malon!” Naya akabaki ametulia tu. Joshua akamwangalia. “Ndiyo.” Akajibu tu hivyo kwa ufupi, wakanyamaza kidogo, ila Naya akajua anawajibika kujieleza zaidi. “Hali ya uchumi pale nyumbani ipo chini sana Joshua. Kwa sasa kama nilivyokwambia, wote tunategemea hii kazi yangu. Baba amehangaika sana kutafuta biashara na kufanya biashara zingine, hata kwa kurudia alizokuwa anauzoefu nazo imeshindika na anajikuta anapoteza tu pesa. Bale amemaliza chuo, inamaana hata ile pesa ndogo aliyokuwa akipewa chuoni ya mkopo, haipo tena. Cheti hakijatoka. Hawezi kuanza kuomba kazi popote. Mimi mwenyewe nilikaa muda mrefu nikihangaika kutafuta kazi bila mafanikio. Nimezungumza naye kwa muda mrefu sana juzi ambapo sikwenda kazini, tukafikiria jinsi yakufanya, akaona ni heri akafanye kazi kwa Malon, kama alivyokuwa akifanya baba, lakini na yeye ajitahidi awe anakusanya mazao na kumtumia huku baba, auze, bila kuanza kwa mkopo mkubwa sana.” Naya akajieleza kifasaha.

“Kwa hiyo atakuwa akiishi na Malon?” Joshua akauliza zaidi. “Ndiyo na hapana. Malon atakapokuwa anakuwa huko mashambani, inamaana atakuwa naye. Lakini Malon huwa anasafiri nje ya nchi mara kwa mara. Kwa hiyo atakapokuwa hayupo, inamaana Bale atakuwa akibakia huko akikusanya mazao. Malon alimlipa baba vizuri kwa muda aliokwenda kumfanyia kazi. Sijui kwa Bale wataelewana vipi! Lakini amesema atakuwa huko kwa malengo. Kazi na yeye kuanzisha kitu chake akijifunza kwa Malon. Baba amemsifia sana Malon jinsi anavyoifanya hiyo biashara, ndio Bale anataka na yeye akajifunze kutoka kwake. Akija kupata ajira, basi amuachie baba.” “Sio wazo baya. Mwanzo huwa unakuwa mgumu, na wakati mwingine milango inayokuwa ikifunguliwa na Mungu sio yote inatamanisha kuingia humo, ila inabidi tu.” Naya akanyamaza, hakujibu hilo.

Asubuhi hiyo pakawa patulivu wakiwa wanaelekea kazini, ila wote wawili walijua kwa hakika, hicho si kitu wanachokifurahia, ila hapakuwa na jinsi. Na hapo Joshua alishindwa kuingilia mipango ya familia. Kwanza hata aina hiyo ya biashara hakuwa akijua. Na hakutaka kutoa wazo la kumtafutia kazi Bale, kuhofia kuonekana anashindana na Malon. Akaona anyamaze.

“Ungependa kula nini mchana, ili nimwagize Jozee apike na kukuletea kazini.” Naya alikuwa amepotelea mawazoni. “Na wewe utakula au ni kwa ajili yangu tu?” “Inategemea. Si unajua ratiba zangu zinavyokuwa ngumu?” “Wewe ungependa kula nini?” Joshua akacheka. “Naya! Nimekuuliza wewe.” “Hata sijui! Sasa hivi nimeshiba halafu nina mengi nafikiria. Swala la chakula hata halipo! Kama ni kwa ajili yangu tu, usihangaike tafadhali. Nitakuwa sawa.” “Sio usumbufu. Ndio kazi yake. Namlipa kwa ajili ya hiyo.” “Basi naomba nifikirie.”

“Unawaza nini sasa wakati mambo yako yanajipanga vizuri?” Joshua akamuuliza. “Kazini umejitengenezea sifa nzuri. Mimi nipo na wewe. Nimekuahidi sitabadilika. Ni nini tena kinakunyima raha?” “Natamani mambo yangekuwa tofauti Joshua. Asiwe Malo.” Naya akalalamika. “Ni ukurasa ambao nilitamani niufunge kabisa. Lakini Bale na Zayoni walitokea kuelewana sana na Malon, akawa kama kaka kwao, hata ni ngumu kuingilia. Halafu Bale yeye sio mtu wa marafiki, ila akatokea kumkubali Malo. Kwa kuwa Malo naye ni mtu ambaye akiamua kuwepo kwenye maisha yako, anajali sana na anajua kumfuatiliza mtu mpaka akafanikiwa kwenye moyo wa Bale. Sasa na yeye Malo marafiki zake walimkimbia. Najua Bale atakuwa mtu wake wa karibu sana kitu ambacho sina jinsi ya kukizuia, na mimi namjua Malon. Alichokifanya jana usiku pale, wala sio mwisho wake.” Joshua akakunja uso kidogo.

“Kwamba aina ile ya maswali...” “Na kunifuatilia, hataacha. Malon hajui jibu la hapana, Joshua. Anafanya kile akili yake inamtuma. Mimi sitaki anifuatilie tena nyuma! Sitaki tena. Nafikiria..” Naya akanyamaza. “Nini?” “Natamani kuhama pale, nijitegee mwenyewe, lakini baba na Zayoni wananitegemea! Au wananihitaji sana. Kuondoka kwenye maisha ya Zayoni sasa hivi itakuwa kumchanganya. Baada ya mama kufariki, tulihangaika sana kumfanya awe vile. Hata sijui!” Naya akafikiria tena kidogo. “Nafikiri nitazungumza na Bale, yeye ndio azungumze na Malon. Mambo yao wasinihusishe mimi.” “Unafikiri Bale atakubali?” “Bale anapenda yeye ndio anilize lakini sio mtu mwingine.” Wakacheka.

“Hata kwa mama alikuwa akinitetea sana. Na nimemuona akinitetea kwa wanaume wote niliokwisha kuwa nao karibu, kasoro tu Malon! Nafikiri ni kwa kuwa alijua nilikuwa nikimpenda sana, hakutaka kuingilia. Ila safari hii itabidi nizungumze naye vizuri. Katika mahusiano yao, mimi nisihusishwe, na amwambie Malo ni kaka yao wao sio mimi. Mimi sitaki anifuatilie kabisa.” Hapo Joshua hakuchangia.

“Unajua ratiba yangu umeibadilisha? Lakini ni kama nimeanza kuipenda.” “Kivipi?” Naya akauliza. “Badala ya kufanya kazi zangu binafsi usiku nikiwa nimechoka, mida hii ninayoanza kazi bila simu za Fina na Jema, nafanya mambo yangu pale ofisini akili ikiwa safi! Nahisi nitaiendeleza hii ratiba. Niwe naamka alfajiri kila siku na kufanya mambo yote. Ikifika saa 11 na nusu jioni, nafunga kazi, nakuwa kinyumbani nyumbani tu.” Wakaendelea kuzungumza. Naya akajua ndio amebadilisha mazungumza juu yake na Malon.

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

Watoto wa mtaani wameingia nyumbani kwa baba Naya wanataka KUOA. Hakuna mwenye dalili yakutoka wala kukubali kushindwa. Wote wanajua wanachokitaka. Malon yupo, Joshua naye yupo ndani ya nyumba na ahadi ya kutomkimbia Naya.  

Safari hii Malon amerudi kama mtoto wa familia na mipango ya PESA kwa Bale si kwa Naya tena kama zamani. Na hajui jibu la Hapana na ameahidi kuendelea kuwepo.

·               Je, safari hii nayo atasimamia mipango anayoweka na Bale? Kwa umbali gani, hasa akijua nafasi yake kwa Naya si ya kuchezea tena na milango ni kama imefungwa? Au ataondoka tena kama kawaida yake akitoa sababu makinifu?

·               Joshua naye ameingia pichani akiwa anajua anachokitaka na kuvunja usemi wa Malon kuwa Naya hatapata mwanaume kama yeye! Usemi aliohangaika nao sana baba Naya kuuvunja kwa kufunga na kuomba bila hata Naya mwenyewe kujua kama baba yake anatengua hiyo kauli katika ulimwengu wa roho na kumuweka huru binti yake bila ya kumuingilia maamuzi yake ila kuomba mume sahihi kwa Naya.

o   Sasa amekuja Joshua. Itakuaje? 

o   Je, yeye ndiye?

o   Kwa umbali gani?

o   Au na yeye atatafuta sababu yakuondoka kama Malon anavyofanyaga pale maji yatakapozidi unga?

·               Wote Watoto wa mtaani. Kasoro Joshua hakuvuta bangi ila na yeye pia hajui jibu la Hapana na mpambanaji piaNaya ndiye amebeba hatima ya yote.

o   Nani mume wa Naya?

o   Itakuaje?

Usikose muendelezo kujua itakuaje kwenye mchakamchaka wa Maisha unao changanywa na MAPENZi pamoja na PESA!

CONVERSATION

0 Comments:

Post a Comment