Siku
ikaanza kwa wote wawili busy ofisini kwao. Kila mmoja akawa wa kwanza ofisini
kwake. Bosi huyo akawepo ofisini kabla hata ya Fina, sekretari wake. Naya
anachapa kazi mezani kwake, Joshua anachapa kazi ofisini kwake tena wala sio
kwenye simu zao wakiwa instagram au facebook, hapana. Kazi zakuzalisha
kwenye hiyo kampuni, mida hiyo alfajiri wakati wenzao bado wamelala majumbani
mwao! Huwezi kushindana nao hata kwa majungu! Naya akaendelea kufanya kazi kwa
bidii zote, na Joshua akipanga kazi kuhakikisha pengo la Njama halionekaniki.
Watu wanaingia kazini mida hiyo ya asubuhi Joshua alishapanga kila kitu,
nani awepo wapi na afanye nini.
“Kumu
ameitisha kikao saa mbili na dakika ishirini na saba.” Aliingia Jamal akihema
kwa nguvu kama aliyekuwa akikimbia. “Tafadhadhali sana jamani, ifikapo saa
mbili na dakika 25, nawaombeni jamani, wote muwe mmeshakaa kwenye viti
pale chumba cha mkutano. Ikifika na dakika 26, kwa sababu zako binafsi kama
utakuwa hujafanikiwa kufika pale, usije tena, sisi tutakuwakilisha. Isijetokea
unaingia muda mmoja na Kumu. Tafadhalini naombeni siku ya leo iishe vizuri
isiwe kama jana. NIMEOMBA. Sasa msitake tuanze kurudishana nyumbani asubuhi hii kabla siku
haijaanza. Swali?” Wote kimya. “Nauliza kama kuna swali ili msiniabishe, Kumu
awe amesimama pale, ndio na wewe unaingia kwa kuchelewa kana kwamba
sijawataarifu. Nauliza kama mmeelewa.” “Mimi nimeelewa Jamal na kuna kitu
naomba ukiangalie kabla ya kikao, pengine utahitaji.” Naya akamwita.
“Ninachohitaji
ni ripoti nzima ya angalau siku 10 tu Naya. Kilichofanyika hapa ofisini. Hicho
tu, mengine naomba yasubiri. Kumu ataniwajibisha leo.” Jamal akasikika kama
ameshapaniki na kumshangaza Naya, akatoka kwa haraka kama anayekimbizwa. “Kwani
kazi yake huyu Jamal hapa ni nini, kama anachanganywa na vitu vidogo hivyo!” Akawaza
Naya akiwa amerudisha macho kwenye kompyuta yake. Akamaliza alichokuwa
akifanya, akakusanya vitu vyake, akawahi chumba cha mkutano, na hapo akawa wa
kwanza. Akatafuta kiti mwisho kabisa, akakaa. Watu wengine wakaanza kuingia.
Naya akabaki akiwa ametulia tu macho kwenye kikabrasha alichokuwa ameingia
nacho. Watu wakaendelea kuzungumza na kucheka.
Ilipofika
na dakika 26 Jema akaingia, wote wakanyamaza. “Naamini kila mtu anaripoti yake
kama nilivyowataarifu kwenye barua pepe niliyowatumia. Msije kunikana
kwa Kumu kwamba hamjapata! Au kuna ambaye hajapata?” “Mimi laptop yangu
aliangusha Njama jana.” Jema akaanza kutingisha kichwa akikataa. “HAPANA Jamal.
Jana nilikwambia kabisa ita mtu wa IT akusaidie kufufu hiyo laptop au akutolee
taarifa zote zilizokuwepo kwenye hiyo laptop yako. Siku nzima ya jana Jamal!
Leo ndio unatoa hizo sababu!?” “Sasa nifanye nini Jema? Tafadhali nisaidie.”
“Wewe unamjua Kumu, hawezi visingizio!” Naya akamuomba mtu wa pembeni yake ampe
Jamal moja ya kabrasha.
“Nini
wewe? Sio muda wake...” “Inatoka kwa Naya.” Jamal akafungua, alishituka
kukutana na ripoti ya siku 20. “Naya!” Akashangaa Jamal, akabaki mdomo wazi,
ametoa macho. “Za asubuhi!” Kumu akaingia na hiyo salamu, akamkabidhi tablet
Jema. “Niunganishie tafadhali.” Jema akaipokea kwa haraka. Joshua alikuwa
amependeza haswa. Suti safi na tai aliyokuwa amepewa na Naya siku iliyopita.
Naya hakuwa amemuona vile. Asubuhi alikuwa amevaa tu shati, koti la suti alikuwa
amening’iniza nyuma ya gari.
Kumu
alikuwa msafi haswa. Rangi ya maji ya kunde iliyong’aa vizuri sana mwilini
mwake. Nywele imekatwa vizuri na kuwekwa dawa. Akachongwa vizuri. Mustachi
ukachongwa na wenyewe vizuri, ukaunganishwa mpaka pembezoni mwa nywele za
kichwani na kuongeza uzuri wa uso. Mwili wake wa kawaida haukuwa mnene wala
mwembamba. Saa tu aliyovaa ilionyesha ipo pesa. Meno meupe na yamejipanga.
Alikuwa anavutia kumtizama. Naya mwenyewe hakuwa akiamini kama ni wake, tena
wake peke yake! Hakuna mwanamke pale kwenye chumba kizima amemuona akiwa uchi!
Hilo likampa ujasiri.
“Tunaanza
na nani?” Kumu akamuuliza Jema. “Ilikuwa Jamal lakini Jamal...” “Ninayo ripoti.
Tena ya siku 20. Hii hapa.” Jamal akaingilia kwa haraka tena akasimama na
kukimbilia pale mbele, Jema akakunja uso akishangaa, Joshua akabaki akiwatizama
Jamal na Jema. Yeye Jema ndiye akaipokea. “Wewe Jamal si umesema...” “Jema!
Umetaka ripoti, ripoti hiyo hapo.” Jamal akamkatisha kama asiyetaka Joshua ajue
kama yeye hakuwa amefanya kazi.
Wakamuona
Joshua anaangalia saa ya mkononi, Jema akaelewa. “Sawa. Naomba basi wewe
uanze.” “Naomba aanze mwingine wakati mimi najiweka sawa.” “Acha kupoteza muda
Jamal! Upo hapa mbele na ripoti ya siku 20, changamka tuokoe muda.” “Si mtu
yeyote yule anaweza kuwakilisha kutoka kwenye idara yetu? Basi Naya njoo
tuwakilishe.” Wote wakashangaa. “Jamal!” “Sasa wewe shida yako nini Jema? Si
kinachotakiwa ni ripoti ya kitengo changu? Ndio nimemchagua msaidizi wangu
azungumze. Yeye ndio macho na miguu yangu huko ninapowatuma kwenye field!”
Joshua kimya akisikiliza.
“Karibu
Naya.” Jamal akamkaribisha kwa haraka bila kusubiri Jema ajibu tena. Naya
akaingiwa na hofu haswa, lakini akakumbuka Joshua alimwambia kila akipewa
nafasi, aitumie ipasavyo. Akasimama. “Lakini sio hivyo Jamal!” “Kwani wewe vipi
Jema?! Mbona unataka kuanzisha jingine wakati kazi uliyotoa imefanyika?”
Wakabishana kwa sauti ya chini pembeni watu wakimwangalia Naya. “Hili juma
limekuwa baya sana kwangu. Na wewe unajua. Unashindwa vipi kunielewa?” Jamal akaendelea
na Jema pembeni kabisa, wakati Naya anazipanga karatasi kutoka pale alipokuwa
ameacha Jamal alipokuwa akiziangalia, alikuwa amezichanganya. Lakini kwa kuwa
Naya ndiye aliyefanya hiyo kazi, alijua ni nini kinaanza.
“Tutaanzia
kuzungumzia safari ile ya Mbeya. Pesa iliyokuwa imekabidhiwa kwenye idara yetu,
matumizi na kazi kwa jumla.” Akaanza Naya huku akiendelea kupanga. Wazi
alionekana anatetemeka kwa mikono kucheza mpaka karatasi zilionekana
zikitetemeka, ila akajikaza akaendelea kuziweka zile karatasi vizuri, Joshua
kimya kabisa, amesimama pembeni akisikiliza na kumwangalia. “Pesa taslimu kwa
safari nzima ilikuwa.” Naya akaitaja. “Tulikwenda watu 12. 10 tulitangulia,
wawili waliungana nasi siku ya mwisho. Walipata malazi ya siku mbili.” Naya akaeleza
vizuri mchanganuo wa bajeti nzima mpaka akamshangaza Jamal kuwa yote hayo
aliyapata wapi asijue uzembe wa wenzake kutofanya kazi, yeye aliyekuwa akifanya
hizo kazi, amefanikiwa kukusanya taarifa zote hizo. Katika kujifunza kwake
kuandaa ripoti bila ya kutumwa, imemsaidia siku hiyo.
Naya
akaendelea kiutalamu. “Watu tuliowafikia kwa jumla na kwa survey tumekadiria
kuwa wanaweza kufikia.” Naya akataja na kueleza aina ya changamoto
walizokumbana nazo walipofika kule na maoni ya watumiaji. “Ukweli bidhaa zetu
wamesifia kwa ubora wake. Hilo hakuna aliyepinga. Ila kikubwa tulichokumbana
nacho kutoka kwa watu tuliozungumza nao, na hizo karatasi 98 tulizofanikiwa
kukusanya za survey ilikuwa bei na ufikiwaji wa bidhaa.
Walilalamikia bei, na upatikanaji wake kirahisi. Wengine walisema inawalazimu
kufuata mjini, hazifiki kwa wingi vijijini mpaka vipindi vya sikukuu.” Naya
akaeleza vizuri, akiwa anaendelea kuzungumza, akasikia hofu imemuisha na
ujasiri umeongezeka.
“Kwa hiyo
wote tuliokwenda kule na kiongozi wetu, tuliona jinsi walivyofurahia ile
punguzo la bei. Na ukweli tulimaliza bidhaa zote. Siku ile ya mwisho tuliwahi
kufunga kwa kuwa tuliishiwa. Tuliuza na zaidi.” Joshua alikuwa akijisikia
vizuri, wakati Naya akijieleza kwa ufasaha mpaka akamaliza ripoti nzima bila hata
kukosea namba na mahesabu kamili.
“Hiyo ni
kwa kifupi. Ila kila kitu kipo humu kwenye kabrasha ya ripoti.” “Nikabidhi
mimi.” Akawahi Jamal. “Nipe mimi.” Joshua akaingilia. “Hii ni ripoti ya kitengo
chenu, umeandaa wewe Jamal, si ndiyo?” Lilikuwa swali la mtego lililombambaisha
sana Jamal, Jema akabaki akimsikiliza kwa kumsuta, Naya akabaki kimya
akizirudishia zile karatasi kwa kuzipanga tena maana kila alipokuwa akizungumza
alizipekua zile kurasa na kuweka chini ya zote akiendelea kusoma ya juu. “Okoa
muda Jamal. Ndiyo au hapana?” Joshua akamkatisha. “Nahitaji kopi sababu laptop
yangu Njama aliingusha jana, kama nilivyomwambia Jema, nikasem..” “Peleka kwa
watu wa IT, waambie wakuokolee taarifa zako. Hizo nabaki nazo mimi. Nani
anafuata? Jema?” Wakajua Joshua ndio amefunga huo mjadala, anabaki na kabrasha
la Naya.
Joshua
akaangalia saa, akaona wote kimya. “Jema!?” Akaita kwa ukali kidogo.
“Kama hakuna anayejitolea, basi nitakuwa nikiwaita. Product Manager.”
Jema akaita. Felix kiongozi wao akasimama. Alizungumza kwa ufupi sana juu ya
bidhaa zao. “Kama mlivyosikia kutoka kwa Advertising department,”
Akimaanisha kitengo cha kina Naya, cha matangazo. “Ubora upo vizuri ila bei.”
Joshua akakunja uso. “Hivi taarifa ya ripoti hii ninayotaka watu wote wasikie
hapa, Jema aliwatumia lini? Mbona inakuwa kama hakuna maandalizi?!” Joshua
akauliza kwa ukali kidogo. Felix alikuwa mtu mzima wa kutosha kwa Joshua. “Ni
jana tu!” Wakajitetea. “Lakini mwisho wa mwezi unakaribia jamani! Inamaana kila
kitengo kingekuwa kina ripoti yake tayari, na pengine ingekuwa haijakamilika
kwa siku chache tu!” Jema akalalamika.
“Naomba
niulize hivi. Kati ya Public Relations Manager and Markerting
reseach Manager, nani yupo tayari kati yenu ili tuokoe muda?” Joshua
akauliza akiwatizama hao viongozi wa hivyo vitengo. Pakazuka ukimya kidogo.
“Umeshaunganisha tablet yangu?” Joshua akamuuliza Jema akionekana amebadilika
na hana muda wakupoteza zaidi. “Tayari.” Jema akajibu akionekana na
wasiwasi tayari. “Labda niseme hivi.” “Kama nikujitetea, sina huo muda,
tafadhali Mwita.” Joshua akamkatisha mapema kabisa akionekana ameshakasirika.
“Nimeitisha kikao ili wote tuwe ukurasa mmoja kwenye kazi. Sio matatizo binasfi
tunayopambana nayo. Kila mmoja akianza lake hapa, ninauhakika hatutatoka leo
humu ndani.” Joshua akawa mkali kabisa. “Nimeelewa kiongozi.” Akajibu Mwita, na
kunyamaza.
Mara
tablet ya Joshua ikaonekana kwenye ukuta mkubwa ambao wanatumia kama screen yao
kwenye hicho chumba cha mkutano. Picha yake na Naya wakiwa kwenye boti,
ikaonekana pale mbele. Joshua akiwa ameiweka kama screensaver yake. Naya
akainama. Wote kimya wakiingalia ile picha, Joshua ameinamia tablet yake
akitafuta jambo bila kuangalia screen iliyoonyesha picha yao. Ukweli
walipendeza sana yeye na Naya. Wote kimya macho kwenye picha.
Joshua
akapekua kidogo na kurusha baadhi ya taarifa kwenye hiyo screen ikafunika hiyo
picha yao, na ndipo na yeye akaangalia. “Hii ni taarifa kwa ufupi juu ya survey iliyofanyika
mkoni Mbeya, tena sehemu moja tu, sokoni. Niliiomba kibinafsi ili kupata picha
ya kile kinachoendelea kwa watumiaji. Naya.” Akaanza Joshua. “Ndiye aliyeandaa
hii ripoti. Aliindaa bila kutumwa na yeyote, ila kundi zima walilokwenda
safari, walitumwa na kiongozi wao kusambaza hivyo vipeperushi kama mara
nyingine zote tunavyofanyaga kuwapatia watumiaji ili kujua maoni yao, lakini
sijawahi kuona ripoti nzuri kama hii ambayo Naya mwenyewe katika kujifunza
kwake, aliiandaa, na imenifikia mimi.” Wote kimya wakiingalia pale kwenye
screen.
“Nirudi
kwenye ripoti ya kitengo chao ambayo ametoka kuisoma.” Hata hiyo walijua ni
Naya tu ndiye ameitengeneza kwani hata Jamal alipopewa ile ripoti, wote waliona
na Jamal mwenyewe alishindwa hata kuitetea na kumtaka Naya ndiye aisome kama
mwakilishi wa idara. Joshua aliizungumzia ile ripoti kwa kifupi ila kwa
utaalamu sana akifafanua mengi yanayoendelea kwa kila kitengo kupitia ripoti
hiyohiyo ya kitengo cha masoko, upande wa matangazo. Advertsment
department.
“Tunaposambaza
hivi vipeperushi kwa watumiaji, kuna kuwa na sababu.” Joshua akaweka
msisitizo. “Kwa mara ya kwanza nimeona hili wazo kufanyiwa kazi na
kutengenezewa aina hii ya ripoti.” Kumu akaendelea. “Kwa sehemu, sio jumla. Kwa
sehemu hawa watumiaji wa mkoni Mbeya, ni kama wamewakilisha mawazo ya watumiaji
wengine. Sasa basi..” Kumu akaendelea, wengine wakipiga picha ile ripoti ambayo
kila ukurasa kwa chini iliandikwa jina la Naya. Na Joshua alifanya makusudi.
Akaieleza vizuri mpaka wote wakabaki wameduaa wasiamini kama ni kazi ya Naya,
mtu mgeni kabisa pale.
“Mbali na
viongozi wa vitengo. Yupo mtu binafsi ana kitu chake pekee anachofikiria
kinaweza kusaidia kitengo kizima?” Joshua akatoa hiyo nafasi ambayo hutoa
mara kwa mara kwa watu wote. “Usiogope. Wote tunategemeana. Naya
alijitengenezea hii ripoti, kwa ajili yake tu akitaka kujifunza yeye mwenyewe.
Hakujua kama leo itakuja kusomwa hapa na kuwa msaada katika kila kitengo.” “Ni
kweli. Hata mimi nimechukua kwa nafasi yangu.” Mwita akajikuta anakubaliana
naye kwa sauti huku akiandika.
“Tunang’aa
kama kitengo kizima, lakini kibinafsi pia. Unachochote unachoona kitanufaisha
kampuni, kiandikie vizuri. Weka jina lako ili tutambue mchango wako moja kwa
moja kabla ya idara yenu.” Joshua akaendelea. “Sasa je, yupo mwingine mwenye
nyongeza kabla sijafunga kwa leo, ili kesho muda kama huu turudi hapa na viongozi
wote wa idara wakiwa na ripoti zao ndipo nizungumze nilichotaka kuzungumza
leo?” Kimya.
Mmoja
kwenye idara ya Research akanyoosha mkono. “Karibu Faith.” Joshua
akamkaribisha. “Sisi tunatatizo...” “Hapana Faith. Sicho nilichouliza.
Inawezekana ni muhimu, lakini hiki kikao sio cha kueleza matatizo yetu. Kazi
tu. Nataka kusikia matokeo. Katika ugumu wote. Matatizo yote tunayokumbana
nayo, nani ameweza kutoa kitu au suluhu? Ndicho ninachotaka kusikia muda huu.”
Faith akarudi kukaa, wote kimya. Joshua akawaangalia kwa zamu. Kimya.
“Hiki
kilichotokea leo, kukutana bila matayarisho, naomba kisirudie tena.”
Joshua hapo akatulia kidogo kutaka kuweka msisitizo akiangalia viongozi wa
idara mmoja baada ya mwingine kisha akaendelea. “Tutarudi hapa tena kesho ila
saa mbili kamili.” Joshua akatulia tena kidogo, kisha akaendelea. “Hii ni kwa
viongozi wote wa idara. Ukiona huna ripoti ila sababu, tafadhali wewe na
watu wako, wa idara yako nzima, msihudhurie kikao cha kesho ila kabla ya siku
ya kazi kuisha nitataka kujua kwa maandishi, sababu ya watu wa idara yako na
wewe mwenyewe kutotokea kikaoni.” Joshua akazima tablet yake wakajua ndio
anatoka. “Tafadhali Kumu.” Joshua akanyanyua kichwa kumtizama.
Alikuwa
ni kiongozi wa idara ya Markerting reseach . Joshua
akasimama wima akamtizama. “Tafadhali sana Kiongozi. Nisaidie ukurasa wa tatu
unaozungumzia maswala ya survey iliyofanyika huko mkoani
Mbeya. Natoa tu kopi narudisha.” Alikuwa ni dada, alionekana umri unakaribiana
na yeye Joshua. Jona Chege, alijulikana kwa maringo akitaka watu watambue yupo
juu, mbabe na mkorofi. Watu wa chini yake hakuna aliyempenda kwa unyanyasaji na
ukali. Akamsogezea Jema file zima watu wote wakiwatizama, akatoka na tablet
yake, ndipo kila mtu akahema kwa nguvu kama waliopata aghueni. Naya na yeye
akasimama ili atoke, Jamal akamuwahi kwa haraka. “Naya mama, nisitiri mjini
hapa. Nitumie ile ripoti kama unayo.” Naya akatulia kidogo. “Si unayo kopi
yake? Usiniambie kama hukuwa na kopi Naya! Utaniii..” Akamkimbilia Jema,
akampokonya lile faili zima alilokuwa nalo na huo ukurasa wa tatu kutoka
mkononi kwa Jona, ambaye ni kama wanalingana kwa cheo.
“Wewe
Jamal vipi?!” “Nitawapa nikimalizana nalo.” “Mbona hukumwambia hivyo Joshua?”
“Jema leo wewe vipi?! Mbona kama upo kinyume yangu?” Jamal akamlalamikia Jema,
na Jona akimshangaa Jamal. “Mimi nimepewa na Kumu mwenyewe! Kwa nini
unipokonye? Mwambie Naya akupe kopi! Wewe vipi?” Wakaanza kubishana, Naya
akamsogelea Jamal. “Hii kazi ninayo kwenye kompyuta Jamal!” Naya akamwambia kwa
sauti ya chini tu kwa utulivu, Jona na Jema wakamgeukia Naya.
“Sasa
mbona hukuniambia Naya, unaniacha naonekana kama mjinga!?” “Unakumbuka
nilikuita asubuhi kabla ya kikao nikakwambia nataka kukuonyesha kitu,
ukakataa?” Jamal akapoa kabisa. Akanyamaza. Jona akamcheka. “Aibu zako Jamal.”
Jona akachukua ile karatasi mkononi kwa Jamal na kuondoka nayo. “Nitakuletea
baada ya muda mfupi tu Jema.” “Sawa.” Jema na Jona wakatoka.
Jamal
akamgeukia vizuri Naya. “Kumbe afadhali ningekusikiliza Naya!” “Naweza kwenda
kukutumia sasa hivi, ukafanya mabadiliko unayoyataka. Naona nimechanganya mpaka
mambo ya idara nyingine! Sikuwa najua. Bado najifunza, na ndio maana nilitaka
uangalie kwanza, uchukue kitakachokufaa.” “Basi nisitiri Naya. Nina mambo
yananitinga ya kifamilia na hapa! Mke wangu kaanza kuumwa ghafla, akili
haijatulia. Nitumie kama ilivyo, sasa hivi nakwenda kuifanyia kazi, ili kesho
hata Kumu akitaka turudie, niwe najua chakuzungumza. Kumu hadanganyiki.”
“Sawa.” Naya akakubali bila shida.
“Nikuombe
tena Naya, siku hizi mbili wakati nikijiweka sawa, nisaidie mambo ya pale
idarani. Kusimamia kila kitu.” “Tafadhali Jamal, labda uwaambie wewe mwenyewe
kama nitawasimamia. Hivihivi haitakuwa sawa.” “Basi acha tukafanye kikao
kifupi.” Jamal akawaambia watu wote wa kitengo chake warudi ofisini kwao wana
kikao.
Naya
kimya, akatangulia na kuanza kufungua kompyuta yake ili amtumie Jamal kazi.
Jamal na wengine wote wakaingia. “Kuanzia leo, Naya atakuwa akiwasimamia na
kuwagawia kazi zote.” Wakanyamaza kimya. “Kuna swali, kipingamizi au wasiwasi
wowote?” “Mimi nilikuwa naulizia kuhusu hatima ya sisi wengine tusiojulikana
hapa kwenye hii kampuni, tunaajiriwa lini?” “Tena wewe ndio usinichanganye
kabisa. Huna unachofanya ila kujizungusha na kusambaza maneno ya hapa.” Jamal
akambadilikia kabisa.
“Tena
nawaambia kabisa, kuanzia sasa, nataka taarifa ya nini mmefanya kila siku. Sio
mnakuja kukaa tu hapa. Naya ameanza na wengine kati yenu, na wengine amewakuta
hapa, lakini amekuwa akifanya kazi na kujituma zaidi! Anayeona hawezi, mlango
huo hapo, ondoka. Acheni kujaa hapa huku hamna mnachokifanya.” Jamal akazidi
kuwa mkali. “Mnakazi ya umbea tu na kusambaza habari za watu!” Wakati Jamal
akiendelea kugomba, ujumbe ukaingia kwa Naya. ‘Am so
proud of you, Naya Kumu.’ Naya akasoma nakujikuta akicheka baada ya
kusoma huo ujumbe wa Joshua akimwambia kuwa anajivunia yeye.
‘Asante.
Leo nimejitahidi? Sikuwa nimejiandaa vizuri.’ Akamuuliza. ‘Ulifanya
vizuri sana na ndipo nilipojua kama ilikuwa kazi yako hata kabla Jema hajaniambia.
Kazana mama. Juhudi zako zinaonekana.’ Naya akajisikia
vizuri. ‘Nahitaji kujifunza kuandaa ripoti kitaalamu zaidi. Hii nimeiandaa
nakuweka mpaka ripoti za idara nyingine! Haijakaa kitaalamu.’ Akaanza
kujikosoa mwenyewe. ‘Ipo vizuri tu, kama ripoti ya kitengo chote cha masoko kwa ufupi.
Ukitulia, jaribu sasa kuitengeneza kwa ajili ya idara yenu tu. Halafu tuipitie
tena kwa pamoja. Kama kuna marekebisho tutayaweka pamoja. Ila umenifurahisha SANA.’
‘Nakushukuru Joshua.’ ‘Karibu.’ Naya akaweka simu chini na kurudisha
mawazo pale Jamal alipokuwa akigomba. Akatulia akisikiliza.
“Sasa
Naya atawasimamia maana naona ndio mwenye kujituma zaidi ya wote na anaelewa
mambo kuliko wote. Mwenye shida na hilo, mlango uko wazi. Ondoka ili
kutupunguzia majungu humu ndani.” Jamal akaweka msisitizo. “Sasa Naya?” Jamal
akamsogelea Naya. “Nimeshakutumia bosi wangu.” “Asante mama. Ukikwama na hichi
kizazi humu ndani, wewe uniambie. Wala usijibishane nao. Kwanza nataka
kupunguza watu humu ndani.” Kidogo akawatisha.
“Sasa
acha nikapambane na watu wa IT, wakishindwa kufufua taarifa zangu na laptop
yangu, nikadai laptop mpyaaa. Tena safari hii nitataka yakisasa. Kufa,
kufaana.” Jamal akataka kutoka ila akarudi. “Naenda kukuombea access kwa watu
wa IT ili uweze kuona kompyuta zao wote hao. Itakurahisishia. Ila kwa sasa,
fanya hivyohivyo. Wakikupa tu access, nitakupigia.” “Sawa bosi.” Naya akajibu.
Wengine kimya.
Juhudi Haimtupi Mtu.
Naya
akainamia kompyuta yake. “Kwa hiyo ndio tunafanyaje, we Naya?” Mmoja akamuuliza
kishari. “Nipeni kama dakika 5 tu. Nitawaambia chakufanya.” Wakaanza kucheka.
“Pumu imepata mkohozi!” Wakamkejeli, Naya kimya akaendelea na alichokuwa
akifanya. Baada ya kama dakika 7 akawageukia wote walikuwa kwenye simu zao.
“Kila mmoja wenu nimemtumia kazi yake kwa leo. Na Jamal pia nimemtumia
nilichowatumia ila kwa email. Itoe kwenye email na kuipakuwa kwenye kompyuta
yako kisha fanyia kazi. Upo huru kufanya au kutofanya. Ila chini kabisa
nimeweka mistari kadhaa inayoonyesha jina lako na kama umemaliza au la.”
“Naya!” Wakaanza kulalamika. “Umewekwa tu leo na unaanza unoko!” “Unataka
kutuharibia?” “Ili iweje sasa?” “Kama kuna sababu ya msingi itakayofanya kazi
isimalizike?” Wote wakamshambulia.
“Wala msinilalamikie au
kupaniki. Siku ndio imeanza. Dharula zipo na ndio maana nimewaachia mistari
chini kabisa, itakayoeleza sababu ya kutomaliza hiyo kazi niliyowapa kwa siku
ya leo, kisha kumtumia Jamal hizo sababu, wala si mimi.” Naya akaongea kwa
kujiamini. Ashaongoza mabinti wa mjini. Warembo na wajuaji wakati akifanya kazi
akiwa shuleni mpaka kwenye kampuni aliyofungua Malon, hao hawakumtisha hata
kidogo. Na wenyewe pia wakamuogopa wakijua ni Kumu wa pili hapo ofisini kwao.
“Na pia
kama hujaridhika, Jamal ametoa nafasi ya kumpelekea malalamiko. Huna haja
yakufanya nilichokutumia. Si lazima, kwa hiyo usipoteze muda kunilalamikia. Ila
kama unaswali, hujaelewa kazi, nipo tayari kukuelekeza.” “Kwamba unajua sana?”
Akamuuliza kwa kumkejeli. “Oooh yeah. Hakuna nisichojua kwenye hii idara. Kwa
hiyo karibu kwa swali lolote lile.” Naya akajibu kwa kujiamini sana. Wote
kimya. “Basi kazi njema.” Akageukia kompyuta yake, akaendelea na kazi. Kimya.
Mapenzi.
Ilipofika
mida ya saa 5 asubuhi akaingia Joshua. “Nilitaka kumtuma mtu.” Naya akageuka
aliposikia sauti ya Joshua. Akacheka na kushika mdomo kwa mshangao uliojaa
furaha ya kutoamini. “Joshua!” Naya akasimama. “Hicho ndicho sikutaka
nikikose.” Naya akacheka akanyoosha mkono kupokea hayo maua. “Uliniambia leo
upo busy, Joshua!” “Umenifurahisha ndio maana, nikaona kila kitu kisubiri
kwanza, nikwambie kwa vitendo, am so proud of you. Umempita mbali
sana hata Joshua Kumu wa wakati ule.” Naya akacheka akimshangaa vile Joshua
alivyofurahia ile ripoti.
“Sasa
mbona hata ripoti yenyewe sio nzuri!?” “Nani amesema!?” Naya akacheka. “Kama
mimi Joshua nimeikubali, jua ni nzuri. Nimeipitia mara mbili na kusambaza kwa
ninao waamini. Vichwa vya uhakika vya masoko kwenye makampuni
mengine hapa mjini, na wenyewe wameikubali na kubisha kama inatoka kwa
mwanafunzi!” “Joshua wewe! Usingeitangaza bwana! Ungeacha labda ya pili!”
“Usinitanie kabisa. Najivunia mwenzio.” Naya akajisikia vizuri sana.
“Asante
kunitia moyo.” “Kabisa. Jua umenifurahisha sana. Sikujua kama unafanyia
kazi kitu kama hiki! Nimefurahia mno. Ni kama umetengeneza ripoti ya kitengo
kizima cha masoko kwa ufupi! Inamaana ungekuwa na taarifa sahihi, ungetoa
ripoti nzuri sana! Itabidi unipe siri ya mafanikio na unionyeshe huko ulikotoa
shule ya hii namna ya kutengeneza hii ripoti.” Naya akacheka sana.
“Kweli ni
ngeni. Nimewatumia vichwa kama vitatu ninavyoviamini kuwa vinajielewa, wenyewe
wamekukubali. Tena wameniambia tukikushindwa tu, wao wanakuiba.” Naya akacheka
sana. “Unataka kuniuza!?” “Si thubutu! Kwanza nimewapiga marufu hata
wasikutafute.” Naya akacheka sana. Kisha akayaangalia maua yake na kuyanusa
kisha akayakumbatia akicheka. “Umeyapenda?” “Sana. Na nimefurahi kukuona na
wewe.” Joshua akacheka.
“Sijapokea
maua muda mrefu mnooo! Mpaka nishasau zawadi za maua!” “Mbona ni zawadi moja tu
ndio imeangaliwa!?” Joshua akalalamika, Naya akacheka. “Hii ndio imevuta
macho.” Naya akafungua mfuko. “Naomba uwe unatumia hiyo laptop.” Naya
akamtizama, akajua ndio anamwambia asitumie tena laptop aliyopewa na Malon. “Asante
Joshua.” Naya akaendelea kuifungua ili kuitoa kwenye boksi lake. Wengine
wakiwasikiliza tu. “Kila kitu mpaka kuweza kupata internet popote vipo hapo.
Ayush, yule kiongozi wa IT amesema ukisoma ni rahisi tu. Ukikwama, amekuwekea
hapo namba yake ya simu. Mpigie yeye mwenyewe moja kwa moja kwenye simu
yake ya mkononi, amesema atapokea kwa haraka tu na
kukuelekeza.” Naya akajua amehangaika kweli kufikisha hiyo laptop
hapo.
“Asante
na pole kwa kunihangaikia Joshua. Nimeipenda.” “Karibu. Na endelea. Chapakazi.
Endelea na ubunifu kama huo. Itakuja kukulipa sana baadaye. Pandisha kiwango.
Jichalenji. Kadiri unapokutana na kitu kigumu, itakufungulia milango ya kujua
mengi. Kama sasa hivi tafuta jinsi ya kutengeneza ripoti ya hapa tu. Kitengo
hiki tu.” “Sawa. Basi nitafanyia kazi.” “That’s my girl.” Akajisifia Kumu na
kuanza kutoka. “Nawahi. Tutakula wote jioni. Chakula chako cha mchana
utaletewa.” Joshua akatoka, Naya akiangalia yale maua na laptop akicheka
asiamini jinsi Joshua anavyomuhangaikia.
Akaamua
kumtumia ujumbe hapohapo. ‘Wanaume wengi wamefanya mengi tena makubwa ya
kusisimua ulimwengu. Lakini wewe. JOSHUA KUMU, umepita woooote.’ Naya
akautuma huo ujumbe. Joshua akaupata nakucheka asiamini hiyo furaha aliyoiamsha
ndani ya Naya, kwa ajili ya maua tu! Tena wala Naya hakuonyesha kuchanganywa na
laptop kama maua. Akacheka na kujipongeza. “100 points. Bem!” Akazidi
kujipongeza akirudi ofisini kwake kuwa kwa alichofanya hapo kwa Naya,
amejipatisha alama kwa asilimia 100!
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
Jioni
Naya alimfuata mpaka ofisini kwake bila hata kumuita. Joshua akamuona
alivyoingia na furaha usoni. “Ni maua tu!” Akajiuliza. Huku
akimtizama. Alikuwa akizungumza na mtu kwenye simu. “Fina aliniambia naweza tu
kuingia. Nimekutana naye mlangoni akitoka.” Akanong’ona akiwa amesimama
mlangoni kama anayejishauri atoke nje kumpisha amalizie mazungumzo ya kwenye
simu. Joshua akamuashiria aingie akae. Naya akafunga mlango na maua yake
mkononi na pochi begani. Akakaa kwenye kiti macho kwenye maua. Joshua
akizungumza kwenye simu. Aina ya majibizano, na lugha, akagundua ni ya kikazi
tu. Akatulia.
Alipokata
tu simu, Naya akaanza kwa furaha hata asijue mwenzie hayupo sawa. “Unajua
sijapokea maua tokea kwenye mahafali yangu ya kidato cha nne?” Ikabidi tu
Joshua acheke. “Kweli tena! Unajua ni nani alinipa?” “Sijui Naya.” “Baba. Basi
tokea hapo, sijawahi kupata maua hata mara moja!” “Sikujua kama ni mpenzi wa
maua hivyo!” “Sana Joshua. Lakini sikuwahi kupewa. Napenda sana maua. Yaani
haya, nitayatunza utakuja kuyaona hata baada ya miaka mitatu kuanzia sasa.”
Joshua akashangaa.
“Naya! Si
yataharibika?” “Ooh nooo! Hata kidogo. Najua jinsi yakufanya yasiharibike.
Nikikwambia napenda maua, jua napenda haswa. Yale aliyonipa baba, yalipotea tu
wakati nikihamia hostel. Nafikiri tuliyaacha kwenye ile gari iliyosaidia
kunihamisha. Najua jinsi yakuyakausha na kuyatunza. Yanakaa muda mrefu sana.”
“Naya! Umefurahi kupitiliza!” “Sana Joshua. Mno. Nakushukuru. Umeifanya
siku yangu kuwa nzuri mno!” “Na ile laptop!? Umepata hata muda wakuiangalia
lakini?” Naya akacheka macho kwenye maua yake.
“Ukitaka
hii zawadi ikamilike, ungenitafutia na vessal.” Joshua akatingisha kichwa kama
anayesikitika. “Sawa mama. Twende tukatafutie sehemu yakuweka hayo maua. Lakini
na mimi huwa napend..” “Acha kuiga Kumu! Leo ni siku yangu mimi.” Joshua
akanyanyua mikono juu kama aliyekubali kushindwa, akachukua funguo za gari
yake, akaanza kutoka akicheka. Naya akamfuata.
“Haya
maua ya leo, watakuja kuyaona mpaka watoto wangu.” “Naya!” “Kweli Joshua.
Nitayatunza na haya hayatapotea.” Akamsikia anaanza kuimba na kuzidi kumshangaza
Joshua. “Haya maua leo yamefanikiwa kutoa wimbo ndani ya Naya!” Joshua
akawaza na kutulia kumsikiliza akiimba kwa sauti ya chini huku akiyanusa na
kuyapanga vizuri hapo mkononi, asiamini kama amefurahi kwa kiasi hicho. “Sema
harufu inaweza ikapotea. Lakini uzuri unabakia palepale.” Akaendelea Naya hata
walipokuwa ndani ya gari. “You are the best.” Joshua akacheka sana. “Leo
napendwa!” “Sana.” “Sifa zote hizo zangu?” “Nilikuwa hata sijaanza.” Joshua
akacheka sana. “Naona leo hata ningeomba kuoa ningekubaliwa.” Joshua akamtania.
“Ungeoa bila mahari.” Joshua akazidi kucheka.
Akaona
asimwambie chochote ili asimuharibie siku yake. Akampitisha dukani, akamnunulia
chupa nzuri sana yenye mdomo mpana, ya glass, nzuri sana, na nzito. Ukweli pesa
ilimtoka na hapo Joshua, lakini alifurahia sana vile Naya alivyoyathamini hayo
maua. Akamkabidhi hapo alipokuwa amemuacha garini. “Sasa hapa, ndio umezidi
kupatia. Hiki chungu cha kioo, kitatunza haya maua kwa muda mrefu sana, japo
kimezidi ukubwa.” Joshua akacheka na kuondoa gari. Naya akazidi kuongea hapo
garini. Akasimulia mengi tena bila hata kuulizwa, Joshua akicheka tu.
Walipokaribia
nyumbani kwao Naya akaanza kuimba tena. Wakaingia ndani getini, wakakuta gari
ya Malon. Naya hakuonekana kujali kabisa japo Joshua hakupenda ikamuongezea
wasiwasi. Hakusubiri hata afunguliwe mlango. Akashuka akikimbilia ndani. “Njoo
Joshua.” Hakumsubiria, akaingia ndani. Alimkuta Malon na Bale mezani, Zayoni
sehemu ya makochi kwenye tv.
“Baba
Naya?” Akaita Naya bila hata salamu kwa yeyote yule akiwa ameficha maua yake
nyuma mtu asiyaone. Joshua akamsikia akimwita baba yake kwa sauti. “Baba yuko
wapi?” “Acha kelele Naya bwana! Baba ameingia ndani muda si mrefu.” Baba yake
akatoka wakati Bale akimkatisha Naya. “Kwema mama?” “Unakumbuka yale maua
ulinipa wakati ule namaliza kidato cha nne?” “Ukayatunza kwa muda mrefu sana?” “Ewaa.”
“Nayakumbuka.” “Sasa mwenzio leo nimepewa mengine. Ona na chungu chake
chakuwekea, chakioo.” Baba yake akacheka.
Joshua
akaingia. “Amenipa Joshua. Pongezi ya kuandaa ripoti bila yakutumwa na mtu.”
“Na nzuri sana.” Joshua akaongeza. “Shikamoo mzee wangu.” Akaunganisha Joshua
akicheka. “Marahaba. Karibu Joshua.” “Asante.” Akageukia wengine na
kuwasalimia. “Baba Naya, kaa nikuimbie wimbo amenifundisha Joshua.” Joshua
akacheka huku akitaka na yeye kusikia huo wimbo. Baba yake akaenda sehemu ya
kukaa. “Unataka kusumbua tu Naya na lisauti lako baya!” “Usimjibu maana
ukimjibu tu utaanza kulia na kushindwa kuimba.” Baba yake akamtahadharisha.
“Kwanza wala sijamsikia, halafu mimi nakuimbia wewe baba yangu na Joshua.” “Na
mimi nataka kukusikiliza Naya.” Zayoni akaongeza. “Basi punguza sauti ya tv ili
mnisikilize vizuri.” Bale akaanza kucheka.
“Bale!”
“Sasa kwani mimi nimefanyaje, baba!?” “Ukimliza tu usiku huu aliokuja na furaha
hivi, ujue leo utakuwa mlinzi.” “Hata hivyo tunahitaji mlinzi baba na yeye hana
kazi. Mimi naunga mkono hoja. Anakaa tu bure ndio maana anafikiria jinsi ya
kunili...” “Wewe ungeanza tu kuimba Naya. Unasauti nzuri sana.” Bale akazidi
kumchokoza “Sitaki. Kama ndio hivyo nakaa na siimbi tena.” Naya akakaa.
“Haya
Bale.” Baba yake akamtaka atoke. “Jamani baba! Kumsifia pia ni kosa!? Au labda
amesahau....” Akataka kumalizia ila akanyamaza. “Nakumbuka sana wimbo wenyewe.”
Akasimama. “Joshua kaa hapa, halafu niwekee ule wimbo bila maneno.” Bale akawa
anacheka taratibu. “Wala sitakusikiliza. Namwimbia baba.” Wengine wakawa
wanacheka taratibu Malon akageuka vizuri akimtizama. Joshua akauweka. Ukaanza.
Naya akaanza taratibu nakumshangaza Joshua. Hakuwa anakosea biti anafuatisha tu.
“Sasa safari ya pili ndio nakwenda juu. Jiandae baba.” “Wewe ungeimba tu.”
“Kwani wewe ndio baba? Wewe ndio baba? Na siimbi tena. Twende zetu
Joshua.” “Haya Bale toka.” “Mimi nimefanyaje jamani baba?! Nilikuwa namtia moyo
tu!” “Hata hivyo sitaki kuimba tena mbele yako. Labda ulipie hela.” Bale
alicheka kwa sauti mpaka wengine wakaanza kucheka. Naya akaenda kujaza chungu
chake maji na kuyaweka maua yake.
“Njoo
Naya uimbe, nitakulipa.” Bale akamwita akicheka. “Huna pesa yakunilipa wewe.”
“Ninayo Naya. Njoo umalizie.” “Sitaki. Nitakuja kumwimbia baba, tukiwa
wawili tu. Tena kwa sauti zote mpaka afurahie. Ila ukiwa wewe haupo. Twende
zetu Joshua.” “Sasa mbona unamtoa mwenzio bila kula?” Baba yake akamshitua ndio
akili zikamrudia Naya. “Halafu Joshua wangu hajala siku nzima! Pole mpenzi
wangu, nilikusahau. Sasa mbona hukunikumbusha?” “Uliniambia unaharaka yakuwahi
nyumbani Naya. Lakini nilikwambia tukitoka kazini ndio tungekwenda kula.”
“Nilisahau swala la kukimbilia nyumbani, kukutana na li Bale. Pole. Acha nikuangalizie
chakula.” “Hapana. Nisindikize, tukazungumze kidogo.” Naya akajisikia vibaya.
“Samahani Joshua.” “Usijali kabisa. Mimi nitakuwa sawa. Twende.” Akaaga,
nakutoka akiwa amemshika mkono Joshua.
“Natamani
kukusikia ukiimba Naya.” Naya akacheka sana. “Basi niwekee tena ule wimbo. Si
utanisaidia?” “Kabisa.” Wakakaa hapo nje kwenye ngazi. Joshua akawasha tena
kutoka kwenye simu yake. Naya akaanza tena. Joshua akamsaidia hapo mwanzoni kwa
sauti ya kawaida tu, ila vikaendana haswa. Ndani wakiwasililiza. “Naanza mimi.”
Joshua akatingisha kichwa kukubali akicheka kwa furaha. Naya akaanza. “Great is
your Mercy towards me, Your love and kindness towards me, Your tender mercy, I
see, Day after day. Forever faithful towards me, and You’re always providing
for me. Great is your Mercy towards me, Great is your grace.” Joshua
akajikuta anapiga makofi kwa furaha, na yeye akampokea kwa sauti nzuri sana,
lakini si juu kama alivyomwimbia baharini. Alipomaliza tu, Naya naye akampokea,
ila safari hii akamfanya mpaka Joshua akasimama akishangilia. Zayoni akatoka.
“Naya!”
Akashangaa. Joshua akaimba tena taratibu, Naya akampokea katikati wakamaliza
kwa pamoja. Joshua alifurahi sana. “Naya! Na wewe umeufanya usiku wangu kuwa
mzuri! Kumbe ndio unaimba hivyo!” “Alikuwa akiimba sana pale kanisani. Maisha
yakamchanganya huyo, sijamsikia tena mpaka leo.” Baba yake naye akatoka, Naya
akacheka. “Umenisikia baba?” “Lazima Bale akulipe.” Bale akasikika akicheka
sana.
Akatoka
Bale. “Hapo kweli nitakulipa. Naya wa aina hii alipotea muda mrefu mno, humu
ndani hajasikika zaidi ya miaka! Mimi nilijua umeshasahau kuimba!” Naya
akacheka. “Naya na Bale walikuwa wakiimba sana kanisani. Sana.” “Tukisaidiwa na
mchumba wa Naya.” Bale akaongeza na kumfanya Naya acheke sana. “Yaani Ino!”
Naya akaongeza. “Mara wagombane na Bale. Mazoezi ya kuimba yanasimama.” “Eti
mwanaume mzima ana zira!” Wakacheka sana, Joshua akakumbuka kusimuliwa habari
za Ino, kuwa ni mjuaji sana.
“Sasa
akizira, hapo ujue uimbaji unasimama kwa muda. Bale naye hajui kubembeleza.
Anaanza kumcheka. Sasa mimi tena aliyenigombelezea, inabidi tena hasira ziishe,
nimbembeleze Ino ili aje atupigie kinanda au gitaa. Inategemea siku hiyo
mtaalamu yule ameamua nini!” “Sijaelewa.” Joshua akaingilia.
“Nilikwambia
Ino ni mjuaji?” “Nakumbuka.” “Sasa yeye ni mjuaji anayejua haswa.
Anajua vitu vingi mno. Sijui Mungu alimpendelea vipi jeuri yule!” Wakazidi
kucheka kila wakimkumbuka Ino. “Sasa pia akawa ndio mwalimu wetu wa sauti.
Anataka kila mtu aimbe anavyotaka yeye. Ukikosea tu, anagomba mpaka hamu yakuimba
inaisha. Sasa kaka huyu.” Akamuonyeshea Bale. “Hataki dada yake nigombeshwe
pale. Anamwambia ananitia hofu, mwishoe nitaona kuimba ni kitu kigumu, nikimbie
kuimba.” “Ambayo ni kweli.” Joshua akaongeza. “Sasa uongeaje wa Bale kwa Ino
ndio huo ulikuwa ukimkera Ino, anazira mpaka Bale akamsemelee tena kwa baba
yake, ambaye ndio alikuwa mwenye kanisa, au tena mimi ni mbembeleze.” Wakazidi
kucheka.
“Akija
siku hiyo anazungumza kingereza!” Wakazidi kucheka. “Ino ana fujo yule mtu!”
“Anazungumza kingereza na nani?” Joshua akauliza. “Eti sisi! Wote anaotukuta
pale tuliofika mazoezini.” Naya akazidi kucheka. “Sasa Bale alikuwa ana mkera
kupita kiasi! Eti akizungumza kingereza, anamsaidia kukalimani kila neno huku
akimcheka. Basi Ino alikuwa anakasirika. Akikataa kumfundisha kupiga kinanda,
Bale anaenda kumuita baba yake, anamsemelea.” Wakazidi kucheka. “Sasa ulijua?”
Joshua akamuuliza Bale. “Nilichoka manyanyaso ya Ino! Nilijiambia nilazima
nijue kupiga kinanda na ngoma. Tukasumbuana hivyohivyo mpaka nikajua. Tukawa
tukiimba kila siku kanisani na Naya. Kundi lilikuwa la watatu. Na yeye akiwemo
huyo Ino. Sasa anataka kutupanga mimi na Naya. Labda tuvae nguo za rangi fulani
ili tuimbe naye. Mimi nikawa namkatalia. Namwambia baba yangu hawezi akaingia
gharama ya nguo kila jumapili eti sababu ya kuja kuimba na wewe hapa!” “Basi
akija siku ya jumapili kama hatujavaa rangi hiyo aliyotaka yeye, haimbi na
sisi. Tunabakia mimi na Bale ndio tunaimba. Basi ananuna karibia kupasuka.”
Wakazidi kucheka.
“Ino! Na
habadiliki. Anamisimamo yake migumu kweli!” Baba yao akaongeza. “Halafu baba
yake wala hakuaga hivyo! Alikuwa mstaarabu sana yule mzee.”
Akaongeza Bale. Leo umenifurahisha sana.” “Basi tuimbe ule wimbo wako ulikuwa
ukiupenda Bale.” Bale akacheka na kuanza kuimba hapohapo. “You came
from heaven to eath!” Naya akampokea. Ulikuwa wimbo wa zamani sana, lakini
waliuimba vizuri sana. Bale akaweza kuweka sauti zao sawa, ungependa warudie
watoto hao waliokuzwa kanisani. Waliimba vizuri sana.
“Kumbe
nyinyi ni waimbaji hivyo!” “Wamechukua kwa mama yao. Huyo alikuwa akifundishwa
sauti hapa na mama yake, mpaka akamudu kutumia pumzi yake vizuri kwenye kuimba.
Ndio maana ule wimbo wenu mliokuwa mkiimba hapa mpaka ukatutoa wote hapa nje,
aliweza kupanda juu sana, na kubakia juu akitetemesha sauti bila kukwama! Basi
ni kazi ya mama yake huyo. Alikuwa muimbaji sana.” “Ila Naya amezidi kufanana
na mama bwana!” “Basi wakati mwingine akikaa pale kwenye kochi namuona kama
mama!” Zayoni naye akaongeza. “Ila hata Bale mnafanana sana na Naya. Kama
mapacha!” Akaongeza Joshua. Wakacheka na kutoka kwenye hali ya unyonge
iliyotaka kuwaingia baada ya kumkumbuka mama yao. “Shuleni walikuwa wakituita
mapacha wa nje! Na hivi huyu alirefuka haraka na kunifikia, ndio kabisa.” Naya
akaongeza kukubaliana naye.
Ndio siku
ya kwanza angalau Joshua akapata nafasi ya kuwa karibu na Bale na kumsikia
akizungumza kwa furaha. Joshua alimuogopa kidogo Bale. Alimuona ni kama
hajajifungua kabisa kwake, ila kumtizama tu. “Lazima nikupe pesa ukanywe hata
soda.” “Sitaki soda. Ninazo huko kazini, na sinywi.” “Naya naye! Sasa unataka
nini?” Bale akauliza akiwa amesimama pembeni ya baba yake. “Unamaanisha kweli?
Maana sio nikutajie kitu ninachokitaka, halafu usininunulie!” “Nitakununulia.
Niambie.” “Baba unamsikia Bale lakini?” “Atanunua tu. Si ameahidi mwenyewe?”
“Sasa sio utaje nyumba!” Wakacheka.
“Hakawiii
huyu. Unataka nini?” “Kuna viatu nimeviona kule dukani. Navitaka, vyakuendea
kazini.” “Naya! Sio viwe vya hela nyingi mpaka unimalize kabisa!” “Wewe
umemwambia utamnunulia. Na ununue Bale.” Baba yake akaweka msisitiza. “Asante
baba.” “Naya naye! Kwani kinachokushinda kutaja zawadi za kawaida ni nini?!”
Bale akalalamika. “Mimi sio wakawaida. Muulize baba.” Walicheka sana. Ila Naya
hakucheka. “Kweli wewe si wakawaida Naya! Naya niwatofauti sana!
Anatushangaza wote pale kazini.” Joshua akaongeza akisifia. “Umesikia wewe
Bale? Maana Bale haamini. Mwambie tena bwana!” Wakazidi kucheka.
“Mwenzio
Joshua amenipa maua, na laptop mpyaaa. Kunipongeza.” “Naya! Iko wapi?”
Bale akashangaa sana. “Ipo kazini nimeifungia. Nimeona isichukue furaha yangu
ya maua. Mpaka kesho.” “Naya naye wa ajabu! Yaani maua na laptop unafurahia
maua?” “Basi sikupi laptop ile ya zamani uliyokuwa ukiipenda.” “Naya!?” “Wewe
si umesema mimi ni waajabu? Nampa Zayoni.” “Asante Naya.” Zayon akafurahi sana.
“Hapana Naya. Ile laptop ni ya thamani sana, kama umepata nyingine, mpe Bale
mwemye uhitaji kuliko Zayon.” “Afadhali unisaidie baba! Mimi nimehangaika
laptop sana, mpaka nikawa nakuazima! Nipe mimi Naya. Nitakununulia viatu
unavyotaka. Mwenzio nataka kuja kurudi shule.” Bale akabembeleza.
“Naya
amesema atanipa mimi.” Zayon akalalamika. “Sasa wewe Zayon laptop ya nini kama
sio mambo ya picha tu?” “Ndio hayohayo. Mimi nataka. Naya ameshaninunulia
kamera. Napata shida yakutengeneza picha zangu. Naya alikuwa akiniazima ile.”
“Basi na mimi nitakuwa nakuazima. Na kwa kuwa wewe ni mtunzaji, nitakuachia kwa
muda.” Hapo Zayon akakubali kwa furaha. “Basi ndio unifuate kazini tukanunue
hivyo viatu.” “Iwe kesho Naya. Mimi kesho kutwa naondoka na Malon.” Naya
akapoa.
“Usiondoke
Bale! Tutafute kazi hapahapa. Mungu atatusaidia tutapata.” Naya akaongea
kwa kulalamika akimsihi kaka yake kwa kumuhitaji. “Nataka biashara Naya. Cheti
kikitoka ndio nitatafuta kazi na kurudi tena shule angalau nipate shahada ya
pili, lakini biashara ikiwa inaendelea.” Naya akarudi kukaa. Akanyamaza akiwa
ameinama. “Nakwenda kwa muda. Nikijiweka sawa na kutengeneza njia zakumfikishia
baba mazao huku nyumbani kwa urahisi, narudi.” Naya akanyamaza akiwa ameinama.
Wakatulia hapo kwa muda hakuna aliyeongeza kitu, mwishoe wengine wakarudi ndani
walipokuwa wamemuacha Malon, akabaki Joshua na Naya hapo nje.
Naya & Joshua,
Bado Malon Ndani Ya Picha.
Joshua
akamchungulia pale alipokuwa amejiinamia. “Naomba usiondoke bila kula, Joshua.
Tafadhali sana. Itanisumbua, sitaweza kulala vizuri.” “Nitakuwa sawa
Naya. Nataka tuzungumze.” “Tuzungumze ukiwa unakula. Hujala tokea asubuhi!
Nilikusahau mpenzi wangu. Nisamehe.” Joshua akacheka. “Ila ujue sitarudia
kukusahau tena. Haya maua yamenichanganya Joshua! Sikutegemea. Ni kitu nilikuwa
nikitamani, ila sikutaka kuwa nikiomba. Nilikuwa nikisubiria mtu ndio
anifikirie, aje anipe kama hivi. Nimefurahi mpaka nikakusahau mpenzi wangu. Ila
haitarudia tena.” “Usijali. Hata mimi nimekuona jinsi ulivyofurahia. Ila
chakula utapata wapi Naya? Acha nikifika nyumbani nitatafuta kitu nile.” “Bale
amepika. Nimesikia harufu ya chakula. Na lazima atakuwa amenibakishia. Twende
ukale.” “Subiri kwanza Naya. Pale mezani amekaa Bale na Malon. Sitajisikia
vizuri kula pale. Sitaki nionekane nawaingilia.” “Basi nitakuletea kwenye gari,
maana hapa kuna mbu. Tafadhali Joshua. Kula kidogo ndio uondoke.” “Sawa.
Utanikuta garini.” “Sawa.” Naya akaingia ndani, Joshua akarudi garini.
“Hongera
mama. Ni ripoti ya nini hiyo?” Baba yake akampokea. “Asante baba yangu. Lakini
acha nimtayarishie chakula Joshua. Nimejisikia vibaya, nimemsahau wakati yeye
alimtuma mpishi wake mchana, anipikie na kuniletea chakula kazini! Hapo yeye
hajala tokea asubuhi.” “Sasa kwa nini usile naye? Au huyo mpishi alipika
kidogo?” Zayoni akauliza. “Hivi unavyomuona amekaa hapa, sio hivyo anapokuwa
kazini. Yupo mbiombio kila wakati. Vikao vya ndani na nje ya ofisi siku nzima, hana
muda. Alipanga tukitoka kazini ndio twende tukae sehemu tule pamoja, ila
nikajisahau, nikamwambia anirudishe kwa baba Naya haraka, nije nimuonyeshe
maua. Ukweli nimejisikia vibaya sana.” Naya akamalizia akiwa anaelekea jikoni.
Kukawa kimya, lakini kila mtu alikuwa akimsikiliza.
Akamuwekea
chakula alichokuwa amepika Bale na kukipasha moto. Huyo Bale akipika hata ugali
tu na maharage, hutoona haya kumpa mgeni. Alijaliwa kipaji cha kupika haswa.
Usiku huo alitengeneza tambi za chumvi, nyama ya kuku alikata vipande vidogo na
kuchanganya na njegere. Kwa kutizama tu ilivutia. Akavipanga kwenye sinia,
akatoka jikoni. “Funika bwana Naya!” Bale akamuwahi. “Nilijisahau sababu ya
haraka.” “Subiri.” Bale akanyanyuka na kwenda kumtafutia kitu cha kufunika.
Akajikuta amesimama pembeni ya Malon, ameinamia simu yake.
Akajifikiria,
akaona amsalimie. “Unaendelea vizuri Malo?” Akamuuliza kwa upole. Malon
akamwangalia. “Nipo sawa tu. Na wewe?” “Mimi naendelea vizuri.” Bale akarudi na
kumsaidia kufunika kile chakula. “Asante.” “Siku nyingine ndio ukumbuke. Sio
unatoka na chakula kinapigwa na upepo mpaka unakifikisha huko kimejaa wadudu!”
“Naye Bale! Sasa si nimekwambia nimejisahau sababu ya haraka?” “Sasa unaanza
kubishana badala ya kupeleka chakula!” Baba yake akamshitua. “Si Bale huyo!”
“Mimi nimekushika mguu?” “Naomba usijibu, toka Naya.” “Ananiudhi Bale mimi
jamani!” Naya akasikika akilalamika huku anatoka. “Taratibu usimwage sasa.”
Baba yake akamtahadharisha. “Maneno mengi mpaka akifika huko sahani tupu,
amemwaga chakula chote!” “Wewe unataka arudi.” Baba yake akaongea, wakacheka.
“Nimekusikia sana ila sina muda na wewe.” Naya akasikika akijibu huko nje.
Joshua
akafungua mlango ili kupokea chakula. “Nitakuwa mama mzuri. Usiwe na wasiwasi.
Nikishiba, nitakuwa nikikumbuka familia.” Joshua alicheka sana. “Sasa mbona
chakwako sikioni?” “Josee alileta chakula kingi! Nikala nusu mchana. Jioni
wakati nakusafishia vyombo, nikamalizia.” “Usingekuwa unasumbuka kuosha!”
“Usijali. Huwa nasuuza tu, kuondoa harufu ili visije nuka. Huwa anaweka vyakula
vyake kwa usafi sana, mpaka naogopa kuchafua ile bag ya chakula!” Joshua
akacheka tu. Naya akazunguka na kupanda garini. “Chakula ni kizuri sana.” “Bale
anajua kupika sana. Na anapenda. Sio kitu chakulazimishwa. Anabuni mapishi
yake, huwezi kuiga.” Joshua akaendelea kula.
Pesa/Kazi.
“Kuna
safari nimekuwa nikiahirisha, sasa inanilazimu kwenda.” Naya akatulia kidogo.
“Yule uliyenikuta nikizungumza naye kwenye simu ni Hugo.” Naya akatulia. Joshua
akajua hajaelewa. “Hugo Gutsche mwenyewe.” Joshua akaweka msisitizo Naya
akabaki ametulia. “Humfahamu Philip Hugo Gutsche? Mwenyekiti au mmoja wa
mmiliki wa kiwanda chetu?” “Joshua Kumu!? Pale ndio ulikuwa ukizungumza naye
huyo baba mwenyewe!?” Joshua akacheka alipomuona Naya amehamaki vile. “Sasa
mbona ulikuwa umetulia vile hata huogopi?” “Nimeshamzoea. Jumbe zake nyingi
huwa anapenda kunifikishia yeye mwenyewe, sio mtu mwingine.” Naya akajiweka
sawa.
“Joshua
wewe si mwenzangu!” Joshua akacheka sana. “Ndio maana pale kazini wanakuogopa
sana Joshua!” “Sio kwa ajili hiyo bwana! Mimi ni mchapakazi ndio maana na Mr
Gutsche ananiheshimu.” “Nitakumiss Joshua! Unakwenda kwa siku ngapi?” Joshua
akameza chakula kilichokuwepo mdomoni. “Nimemwambia nina kikao lazima nikifanye
kesho asubuhi. Kwa hiyo tutaondoka na ndege ya mchana.” Naya akakutulia kidogo
ila akaona aulize kupata uhakika. “Umesema tuta!? Unakwenda na nani?” “Jema.”
Moyo wa Naya ulishituka, kisha akapoa mwili mzima. “Historia inajirudia
tena.” Akawaza Naya na kuinama akichezea mikono yake.
“Huwa
haichukui muda mrefu. Mambo yakienda sawa na kufanya vikao vyote kwa haraka,
baada ya siku 4 au 5 tunakuwa tunarudi.” “Kwa hiyo muda wote huo mnakuwa na
Jema hotelini?” Joshua akashituka hilo swali na kutulia kidogo akitafakari.
Haikuwahi kuwa tatizo wala halikuwahi kuwa wazo la kulifikiria kichwani mwake.
“Mara
nyingi sana huwa nasafiri na Jema. Ndiye mtu anayepanga kila kitu changu cha ofisini.
Zaidi kwenye vikao kama hivi.” “Kwa hiyo jibu ni ndiyo?” Naya akarudi
kwenye swali lake tena. “Ndiyo Naya. Wanatutafutia hoteli moja. Lakini Jema
ananiheshimu sana. Hajawah..” Akasita kidogo. “Anaujua msimamo wangu.”
Akarekebisha usemi wake. Naya akamwangalia. “Hata hivyo anaye mchumba wake,
nafikiri watakuja kuona. Ila sijui. Ninachojua hakuna mazingira ya mambo ya nje
ya kazi.” Naya kimya. “Kwanza sitampa hata sababu yakufikiria hayo. Anajua wewe
upo na mimi.” Naya akacheka taratibu na kusugua mikono yake.
“Tafadhali
naomba uniamini Naya. Mimi si mtu wa kigeugeu.” “Nakuombea Joshua.” Naya
akajibu taratibu na kutulia. “Nakuahidi nitakuwa mwaminifu kwako Naya. Sio kwa
Jema tu, hata kwa wanawake wengine. Nimejiapia hivyo. Kwanza sitaki kumkosa
Mungu wangu. Endelea kuniombea tu, nirudi salama.” “Nakuombea Joshua.” Naya
akatulia, lakini Joshua akamuona amebadilika kabisa ile furaha yote ikaisha.
“Swala
la usafiri ungependa nikuachie gari au nikutumie dereva?” Naya akakunja uso
akiwa ameinama. “Usafiri wa kukupeleka na kukurudisha kazini, na jumapili
kanisani.” “Hapana Joshua. Huna sababu ya kufanya hivyo. Hapa mtaani huwa
kunakuwa na wezi. Wakijua kuna gari hapa, na hatuna ulinzi, watakuja kuiba
vifaa vyake. Baba alitoa ulinzi baada yakurudisha gari ya Malo. Hatuna mlinzi. Halafu
swala la kuja kufuatwa asubuhi na kurudishwa jioni na dereva, baba hawezi
kukubali.” “Ni mtu ninayemfahamu.” “Hapana Joshua. Mimi namfahamu baba. Hata
ukimwakikishia vipi hawezi kukubali.” Naya akaendelea.
“Anasema
wanadamu wana mtindo wakubadilika, hasa tamaa yeyote ile ikiwapata. Huwa
wanakwenda umbali mkubwa sana, na hubadilika mpaka unashindwa kuamini kama ni
mwanadamu au mnyama. Wewe mwenyewe alitaka kukuona kwanza na nikazungumza naye
sana juu yako ndipo akakubali. Hawezi kunikubalia kwa mtu baki. Anaona ni heri
awe ananipeleka mwenyewe kituoni, anione nimepanda kwenye daladala, na
kunisubiria jioni pale kituoni, kuliko anichukue mtu baki.” Naya akageuka.
“Yupo
baba mmoja anaishi upande wa juu, kabla kuingia hapa, unaendelea na hiyo
barabara hapo mbele mpaka kwake. Anafanya kazi posta. Ana mke na watoto wake.
Wadogo kwetu. Mkewe alimwambia baba kuwa mumewe anaweza kuwa akinisogeza mpaka
Ubungo, baba akakataa kabisa. Anapita hapo barabarani kila siku asubuhi, lakini
baba alikataa asinipe lifti. Nitakuwa sawa tu. Usijali.” Joshua
akapoa kabisa. Akajua mambo yatamuharibikia. Naya anarudia maisha yakupanda
daladala baada ya kumtaka arudishe gari! Anaondoka na kumuacha Malon hapo
kwao! “Heri hata haya mahusiano yangekuwa yamekomaa! Ndio machanga hivi
na ninatakiwa kuondoka?” Akawaza Joshua.
“Umeridhika
na chakula?” Naya akavunja ukimya. “Asante. Nimeshiba kabisa.” “Basi acha
nikuage. Ili nikirudisha vyombo, nikaoge kabisa, nipumzike.” Joshua
akamwangalia. Naya akacheka na kuinama. “Sitakusaliti Naya.” “Nakuombea
Joshua.” Akajibu Naya taratibu. “Nenda ukapumzike Joshua. Usiku mwema.”
Akashuka garini na kuzunguka upande aliokuwa amekaa Joshua ili kuchukua vyombo.
Kuishi na Malon kulimwathiri sana Naya. Imani kuwa mwanamke na mwanaume
wanaweza kuwa pamoja sehemu, haswa mwanamke akiwa anamtaka huyo mwanaume! Naya
akajua historia inajirudia. Na ujumbe aliokuwa ametumiwa! Akazidi kukosa
raha.
“Ila
kesho asubuhi unisubirie. Nitakufuata.” “Nashukuru.” “Na nakuomba nikuombe kitu
Naya.” Naya akamwangalia. “Hivyo viatu unavyohitaji vya kazini, naomba mimi
ndio ninunue.” Naya akacheka kwa wasiwasi kidogo. “Sio kwamba sina pesa Joshua.
Zile ulizonipa bado ninazo. Unakumbuka kiasi cha pesa ulichonirushia lakini?”
“Tafadhali naomba kununua mimi hivyo viatu.” “Nataka kuvaa na viatu
atakavyoninunulia Bale, Joshua. Naona kama nitajisikia vizuri. Acha aninunulie
tu. Kwanza akija kesho kunifuata kazini ndio itakuwa vizuri nirudi naye
nyumbani. Usijali.” Akampokea vyombo. “Usiku mwema Joshua.” “Mbona unaniaga
kama hatutazungumza tena?” “Naomba leo niwahi kulala. Sijisikii
vizuri.” Naya akaongea bila kumtizama.
“Huna
haja yakuzungumza. Ila nataka tu kujua upo na mimi kwenye simu. Nisijisikie
mpweke. Ni sawa au nitakuwa nikikusumbua?” “Hapana. Sio usumbufu. Basi nikioga,
nitakupigia.” “Nitashukuru. Ila usisahau kuwa nakupenda Naya. Na ninakuhitaji
wewe.” Naya akacheka huku akiangalia vile vyombo. Maneno mazuri alishayasikia
sana. Aliambiwa na Malon mchana na usiku, ila vitendo ndio vilishindwa
kulingana na maneno. “Usiku mwema Joshua.” Akaaga na kuondoka na kumuacha
Joshua kwenye wakati mgumu. Ni safari ya kikazi! Sio starehe! Na
Jema ameshajua kuwa hiyo safari ipo. Anafanyaje!
Akabaki
pale kwa muda, akaamua kurudi kuzungumza na baba yake Naya. Akagonga na kuingia
wote wakamgeukia. “Samahani mzee wangu.” “Bila shaka. Karibu.” Joshua akaenda
kukaa kochi la karibu yake. “Samahani lakini.” “Karibu.” Joshua akajivuta mbele
kidogo. Wote kimya, wakitaka kusikia. “Nina safari ya kikazi ya siku
zisizopungua 5. Naondoka na ndege ya kesho mchana. Asubuhi nitakuja kumchukua
Naya, ili twende kazini. Jioni hatakuwa na usafiri, na siku hizo 4 mbeleni.
Nimemuomba nimuachie hii gari.” “Hapa hakuna mlinzi Joshua. Nilitoa ulinzi.
Wezi watakuja kuiba vioo mpaka matairi.” Joshua akacheka kidogo kwa wasiwasi.
“Ameniambia
Naya. Lakini yupo kijana huwa namtumia kwa kazi za udereva. Kwa gari hii hii
maana kama sio Naya, mimi huwa natumia gari ya ofisini na dereva wa ofisini.
Kwa hiyo hii gari inakuwepo tu nyumbani mpaka nikiwa na shuguli binafsi, na
ndiyo anayotumia huyo dereva. Naweza kumwambia akawa anakuja kumchukua Naya
asubuhi na kumrudisha jioni.” “Nakushukuru sana Joshua kwa huo msaada. Lakini hapana.”
Hakutaka hata kuuma maneno. “Huyu atakuwa sawa tu. Huwa nampeleka mwenyewe
kituoni, na kumsubiria jioni anapotoka kazini. Hana tatizo. Wewe nenda kafanye
kazi kwa utulivu kabisa. Huyu Naya niachie tu mimi. Atakuwa sawa.” Joshua
akatulia kwa muda akifikiria.
“Unakwenda
wapi?” Zayoni akauliza. “Makao makuu ya hii kampuni yetu. Johannesburg, Randburg, huko Afrika ya kusini.”
Akamjibu akiwa amepoa. “Kumbe wewe unaendeshwa na dereva kabisa?” Kila mtu
akacheka, kasoro Malon. “Ndiyo Zayoni.” Joshua akajibu. “Baba hataki mtu
asiyemjua yeye vizuri, amuendeshe Naya. Kila mtu anajua. Naya hajakwambia?”
Zayoni akaendelea na maswali yake taratibu tu. “Aliniambia.” “Basi baba
hakubali. Ni heri hata...” “Haya Zayoni, ni muda wakuoga, na wewe ukalale.”
Bale akaingilia. Zayoni akasimama bila yakubisha, na kuondoka akiwa
ameshaingiwa hofu. Akajua ameongea kitu ambacho hakutakiwa kuzungumza. Joshua
akabaki amekaa tu pale.
“Twende nikusindikize Joshua.” Naya akatoka jikoni. “Asante.
Usiku mwema.” Akaaga lakini nakushukuru moyoni kuona Naya amemtoa pale. “Asante
Joshua. Uwe na safari njema leo, na hiyo kesho ukisafiri. Usiwe na wasiwasi juu
ya Naya. Atakuwa sawa tu.” “Nashukuru sana mzee wangu.” Kabla hajatoka, maana
alimpisha Naya, baba Naya akamwita.
“Joshua!” “Naam!” Joshua akaitika kwa heshima na kugeuka.
“Nakushukuru sana kwa heshima unayompa Naya. Hujichukulii tu mamlaka kwake.
Hilo nakupongeza.” Kidogo hapo Joshua akapata ujasiri. “Nakushukuru mzee
wangu.” “Kabisa. Unampa heshima kubwa sana! Ila kuna mambo nimejiwekea, sitaki
kuja kujuta au niseme kujuta tena. Nahisi gharama ya kuja kulipia huo uzembe au
mwanya mdogo ninaokuwa nikiuachia inakuwa kubwa sana, kwa kuepuka kuwajibika
kidogo tu. Hapana. Naomba univumilie tu.” “Nimekuelewa kabisa mzee wangu. Na
ninashukuru. Asante.” “Usiku mwema.” “Asante na wewe.” Baba Naya akafikisha
ujumbe mpaka kwa Malon. Joshua akatoka na yeye baba Naya akarudi chumbani
kwake. Kukapoa, kimya.
“Mimi nitakuwa sawa Joshua. Wala usiwe na wasiwasi juu ya
swala la usafiri. Hakika nitakuwa sawa. Rudi nyumbani ukapumzike.” Wakamsikia
Naya akimtuliza huko nje. “Nilifikiria hata niwe nakuchukulia taksi, lakini
nikagundua taksii ndio sio salama kabisa.” Naya akacheka kidogo. “Usiwe na
wasiwasi. Nitakuwa sawa kabisa. Nenda kapumzike. Leo umekuwa na siku ndefu.”
“Asante. Nitakuona kesho.” Joshua akaondoka.
~~~~~~~~~~~~~~~~~
Naya
akarudi ndani kuoga, na kurudi chumbani kwake akijishauri kama apige simu au
aache tu kwa usiku huo. Hofu ilimjaa kila alipokuwa akirudia ujumbe alioupuuza
aliokuwa ametumiwa na Njama jana yake. Akaurudia tena na tena. Mwishoe akaona
amtumie ujumbe baba yake. ‘Naomba uje tuombe pamoja. Nashindwa kulala.’ Baba
yake alikuwa chumbani kwake. Aliposoma ujumbe, akatoka. Bale akashangaa
anaelekea chumbani kwa Naya bila hata kuzungumza nao. Malon akaona aage tu.
Alishapata ujumbe wake kwa kupitia pongezi alizopewa Joshua, akamuaga Bale na
kuondoka.
“Mbona
umejawa wasiwasi tena, ile furaha yote uliyokuja nayo leo imepotea!” Baba yake
akamuuliza. Naya akazima simu kabisa na kuiweka chini. “Njoo ukae hapa na mimi
kidogo. Uniombee, halafu unisubirie nilale.” Akajua hataki kuzungumzia linalo
mkera. Akavuta kiti na kumshika mkono binti yake. “Kabla ya kuanza kuomba.
Unataka nikuombee nini?” “Kila kitu.” Naya akajibu. Baba yake akamwangalia na
kuanza kumuombea kwa jumla tu, zaidi faraja. Akamaliza. “Ukae hapohapo
usiondoke.” Baba yake akavuta kiti kwa nyuma na kutulia. Akamuona anawasha tena
simu. ‘Nipo na baba. Nashindwa kukupigia simu. Naomba tuzungumze kesho.
Usiku mwema Joshua. Na maandalizi mema ya safari.’ Akatuma
huo ujumbe na kuiweka simu chini bila kusubiria jibu akiwa amezima sauti
kabisa. Akaingia ndani ya chandarua na kulala, baba yake kimya kama kawaida
yake. Naya akalala kwa haraka tu, akijua baba yake yupo pembeni yake.
Asubuhi ya Safari ya Joshua na Jema.
Alilala
bila Joshua masikioni mpaka alarm ilipomuamsha. Akachukua simu yake ili kuzima,
akakuta ujumbe aliorudisha Joshua usiku uliopita. ‘Nakupenda
Naya. Na sitachoka kukwambia jinsi ninavyokupenda na kukuhitaji maishani.’ Naya
akatulia kwa muda. Akakumbuka maneno hayohayo aliyokuwa akiambiwa na Malon,
kisha kutoka na kwenda kulala na wanawake wengine. Akaweka simu pembeni na
kuanza kujitayarisha kwa haraka asijue jinsi anavyomtesa Joshua ambaye bado
hakujua ni nini chakufanya.
Alipomaliza,
akakuta baba yake alishamwandalia kifungua kinywa. “Siwezi kula baba. Tumbo
limejaa gesi.” “Huo ni wasiwasi Naya. Ni nini?” “Sijui baba yangu. Ila
ninachojua kwa hakika, kumvumilia Malon kwa muda mrefu sana kwenye mahusiano,
kumeniathiri mno baba yangu.” Akafikiria kidogo na kunyamaza. Baba yake
akaangalia muda. “Mwenzio atakuwa amefika.” “Jioni unisubirie kituoni.” “Sio
hapa. Njoo mpaka Kibaha. Leo kuna mambo nataka niyamalize. Nitakuwa huko mpaka
usiku.” “Nitakupigia.” Baba yake akamsindikiza mpaka nje ila hakutoka getini
baada yakuona gari ya Joshua hapo.
Naya
akaingia garini. “Ulilala salama?” Joshua akamuuliza mara alipoingia. “Ndiyo.
Na wewe?” Naya akamuuliza akifunga mkanda. “Sikulala vizuri Naya.” Naya akawa
amemuelewa. Akanyamaza. “Niambie ni nini kinakusumbua? Au ni nini nimekosa?”
“Hujakosea Joshua. Huna ulipokosea. Ila kama nilivyomwambia baba, kuishi kwa
muda mrefu na Malon, nikimvumilia kwa mengi, kumeniathiri Joshua. Kumeniathiri
sana, ndio sasa hivi natambua hilo. Ila huna tatizo.” “Labda niulize hivi, unawasiwasi
na mimi kusafiri na Jema?” Naya akatulia kwa muda hajui ajibu nini.
“Kama ni
Jema, tafadhali usiwe na wasiwasi Naya. Siwezi kukusaliti hata iweje. Kwanza
naanzia wapi? Akili zangu na mawazo vipo kwako Naya. Natafuta nini kingine?
Tafadhali naomba usiwe na wasiwasi. Mimi sio mtu wa tamaa!” Naya akacheka kwa
wasiwasi kidogo kama akijaribu kujituliza huku akikumbuka ujumbe wa Njama
unaomfanya azidi kujawa hofu.
Akajishangaa
kuona mikono yake inaanza kutetemeka. Akaikalia akijaribu kutulia. “Bale
atakuja kunichukua nikitoka kazini. Tutaenda naye kununua viatu.” Akaona
abadili mazungumzo. “Nakuhurumia swala la usafiri, sijui chakufanya! Hakika kwa
mara ya kwanza nimechukia safari za kikazi.” “Naomba usichukie Joshua.”
“Naachaje Naya? Jana usiku umeshindwa hata kuzungumza na mimi kwenye simu?”
“Nilikuwa na baba. Tuliomba pamoja, akanisubiria mpaka nikalala, ndipo
akaondoka. Nilikutumia ujumbe. Hukupata?” “Nilipata, na nikakujibu. Niliona
umesoma ujumbe wangu asubuhi, lakini hukunijibu Naya?” “Nilikuwa najitayarisha
halafu nikawa na baba.” Naya akajitetea.
“Tafadhali
naomba nafasi ya kukusikia wasiwasi wako. Tafadhali sana. Kama mimi ambavyo
huwa nakuomba uniombee hata kwenye simu nikiwa ninauhitaji, na mimi naomba hiyo
nafasi unayompa baba Naya. Sihitaji kuchukua nafasi yake, ila angalau
unishirikishe tu. Jambo linapokuwia gumu, na mimi naomba kujua, tusimame pamoja
huko kugumu.” “Sawa.” Naya akakubali kwa haraka na kutulia, lakini bado Joshua
akamuona hayupo sawa.
“Mimi
sina tamaa za wanawake Naya.” “Ni kweli. Hata mimi. Halafu mara nyingine na
Malon walikuwa wakimfuata wanawake. Wao wenyewe walikuwa wakimtaka alale nao.
Halafu Malo alikuwa hajui kukataa. Basi alikuwa akilala nao lakini
anasema ananipenda mimi. Kila mtu alikuwa akimwambia mimi ndio mwanamke wake.
Na kila mtu alikuwa akijua, lakini bado wanawake walikuwa wakimtaka alale nao.”
Joshua akamsikia akiongea kama mtu aliyeshikwa na baridi kali. Akapunguza AC ya
gari.
“Wanampenda
vile mwili wake ulivyo. Na pesa anazokuwa anawapa. Kwa hiyo wanawake wakawa
wanajua yupo na mimi, huku bado wanamtongoza, na yeye akawa hajui kukataa.
Kuna siku nilimfumania kwenye nyumba tuliyokuwa tukiishi naye Morogoro,
akanipiga kibao. Lakini akaniomba msamaha. Akasea aliingiwa na mshituko. Na
huyo dada alikuwa mkubwa kwa Malo, na alikuwa akinifahamu mimi kuwa nipo na
Malo, lakini bado alimfuata Malo nyumbani baada ya kujua mimi nimerudi huku
nyumbani akamfuata ili Malo amlale.” Naya akajikuta akizungumza tu.
“Pole
Naya, lakini...” “Najua wakati mwingine ni kama naonekana kama ninakuwa na
wasiwasi tu. Hata rafiki yake wa karibu Malo alikuwa akisema nipunguze
wasiwasi. Lakini katika hisia zangu mara zote nilikuwa sikosei. Nakuwa napatia.
Ila sisemei kwako wewe! Namzungumzia Malon.” Naya alizungumza mengi. Akasimulia
mengi na mengine akawa anarudia japo alishamsimulia huyo Joshua. Aliongea bila
kumpa nafasi, mpaka wakafika kazini.
“Mimi
nahisi nimewahi sana kuinga tena kwenye mahusiano. Nilitakiwa baada ya Malon,
nitulie kwanza. Kama kuna kupona nipone ili niwe tayari kwenye mahusiano
mengine. Hivi nilivyo, sitaweza.” Hapo Joshua akashituka. Akaegesha gari
na kumgeukia. “Unasemaje Naya!?” “Naombe muda Joshua.” “Nilikwambia
nitakusubiri Naya.” “Hapana. Naomba nitulie kabisa. Nitakapokuwa tayari kama
utakuwa hujapata mtu mwingine, nitakwambia.” “Ni nini Naya?” “Siwezi
Joshua. Nahisi kuchanganyikiwa. Sitarudi kwenye hayo maisha ya wasiwasi tena. Sitaweza.” Naya
akaanza kulia. “Naogopa mno. Sina nafasi ya kuumizwa tena. Naomba unielewe tu.
Nitashindwa hata kufanya kazi. Nimejawa hofu isiyo na sababu.” “Nashukuru
kama umetambua hilo. Umejawa hofu isiyo na sababu Naya!”
“Siwezi
kujisaidia Joshua.” “Nisikilize Naya. Nilikwambia na nitaendelea kukwambia.
Sijui uliishije na Malon, lakini hiki tulichonacho mimi na wewe, nakiheshimu
sana. Kinaweza kisiwe kimekomaa, lakini mwenzio nimeshaingia agano na
nimejifunga kwako. Nilikwambia huwa sijui kuanza jambo na kuishia katikati.
Hapo utanisamehe. Ulishanikubalia. Ukaniambia unanipenda, mimi nitasimamia
hapo, wala sitarudi nyuma. Mashaka yanaweza kuja, lakini isiwe sababu ya
kutengana! Sitakuacha Naya. Kama unachanganyikiwa, jua upo na mimi, na
nitasimama na wewe. Changanyikiwa ukiwa na mimi sio mbali na mimi. Unanielewa?”
Naya akatingisha kichwa akikubali.
“Basi
naomba utulie.” “Sawa.” Akakubali kwa haraka na kuanza kujifuta
machozi. “Acha nikaoshe uso, nianze kazi. Kuna kitu nataka kumaliza kabla
ya mkutano ulioitisha.” Naya akafungua mkanda. “Nakupenda Naya. Najua umeshazoea
kusikia hayo maneno, lakini naomba tulia na kuyatafakari hayo.” “Sawa. Nashukuru
kwa usafiri Joshua. Najua unatoka mbali kunifuata mpaka kule. Asante.” “Karibu,
lakini ujue wewe ni jukumu langu.” Naya akacheka taratibu lakini Joshua alijua
bado kuna kitu kimemfunga. Bado alijawa hofu asielewe ni kwa nini! “Asante.”
Akashukuru na kushuka.
Sumu Ya Chini Kwa Chini.
Baada ya
kama ya dakika 15 akiwa anafanya kazi zake, Joshua akaingia na laptop yake
mkononi. “Vipi?” Naya akamuuliza. “Nimekuja kufanya kazi hapa karibu na wewe.”
Akavuta kiti mbele ya meza ya Naya. Akaweka laptop yake Naya akabaki
akimwangalia. “Uliweza kuwasha laptop yako mpya?” “Bado.” Joshua akamwangalia.
“Naweza nikawa sijaweza kukufahamu kwa undani Naya, lakini nahisi kuna kitu
kinaendelea ambacho hutaki kuniambia.” Naya akatulia.
“Ni
nini?!” “Sijui Joshua!” “Hapana. Unajua na ndicho kinachokusumbua. Ila ninaumia
kuona bado unashindwa kuniamini Naya!” Hapo Naya akaumia kidogo. “Niambie ni
kitu gani bado kinashindwa kukufanya unashindwa kuniamini japo nimejifungua
kwako kwa asilimia 100! Ninakupa sababu gani hiyo? Au hujawahi kunipenda?”
“Hapana Joshua. Nakupenda na ndio maana naogopa. You are soo good to be true.”
Joshua akakunja uso na kutulia.
“Kwamba
unanitilia mashaka?” “Hapana. Hivyo ulivyo na kila kitu unachonifanyia, ndivyo
nilivyokuwa nikimlilia Mungu anipe. Umekuja ulivyo na zaidi mpaka naogopa Joshua!
Afadhali vile alivyokuwa Malon, nilishazoea umalaya wake, lakini naogopa
chochote kisijetokea kwako ukiwa na mimi, nitashindwa kuja kumuamini mwanaume
yeyote tena. Ndio maana naona ni heri...” “Uwe mbali na mimi ili chochote
kikitokea, usionekane ulikuwa na mimi wakati nafanya uzinifu?” Akamalizia
Joshua akimtizama.
“Hivi
unajua nina miaka mingapi sijalala na mwanamke?” Naya kimya. “Sina tatizo la
nguvu za kiume wala sina tatizo la wanawake kwa sasa. Na ninajijua sio mbaya.”
Naya akatulia. “Mwanzoni nilikuwa silali na wanawake kwa kuwa walikuwa
wakinikimbia. Sasa hivi silali na wanawake si kwa sababu ya shida ya wanawake,
au sina hamu ya kulala na mwanamke!” Naya akainama. “Ni kwa kuwa ....” Kabla
hajamaliza akashangaa Naya anamkabidhi simu yenye ujumbe. Akajua anataka asome.
Akatulia na kuvuta simu ya Naya.
‘Usifikiri
Jema anakutetea wewe. Anatetea ajira ya hawara yake. Anajua Joshua akiwa juu na
yeye atabaki kuwa juu. Jema anafaidika kwa mafanikio ya Joshua ndio maana
hataki chochote kitokee kwa Joshua hapo kazini, anahangaika kuficha ukweli.
Lakini huwa wakitoka hapo, wakiwa nje kikazi, wanalalana kama kawaida.
Nilishuhudia kwenye safari moja tulienda na jamaa South.’ Joshua
akakaa sawa na kuendelea kusoma.
‘Tulikuwa
wote watatu. Tumekodishiwa vyumba kwenye gorofa moja ndani ya hiyo hoteli. Kila
mtu chake. Asubuhi, nilimuona Jema anatoka chumbani kwa jamaa anarudi chumbani
kwake, tena akiwa hovyo kweli! Nikamuuliza, hakukataa ila kuniambia
hayanihusu.’ Naya akamuona Joshua anakunja uso.
‘Baada tu
ya kuwafumania, wakajua nimeshawajua, ndipo nilipoanza kuona mabadiliko.
Nikaanza kuachwa kwenye safari nyingi za kikazi. Wakawa wanakwenda wao wawili
tu. Jamaa anakula Jema nje ya nchi, wanaficha watu hapo kwa kuwa Jema
anajulikana anaye mchumba tena anakaribia kuolewa. Na hilo pia halikuwahi
kumzuia Jema. Alimwambia Jamaa, akimuhakikishia penzi, anamuacha mchumba wake
waliyekuwa wameanzana naye tokea sekondari. Unachezewa Naya. Unanikataa mimi
kwa ajili ya Jamaa ambaye anavifichovificho huyo! Na usifikiri kuolewa kwa Jema
ndio kutawatengenisha. Joshua na Jema ni watu wa muda mrefu sana hao, wanajua
kuzicheza karata zao vizuri tu. Wewe na wa Jema wote mnachezewa tu.’ Ujumbe
ukaishia hapo.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
Ø Historia
inajirudia kwa Naya?
Ø JE, Tabia za Joshua ni kama Malon?
Kamba
yakatika pabaya haswaa!!
Ø
Faida kwa nani??
Usikose muendelezo.
0 Comments:
Post a Comment