Naomi Simulizi |+1 205 767 8163 |naomisimulizi@gmail.com MAPENZI&PESA! – SEHEMU YA 25. - Naomi Simulizi

MAPENZI&PESA! – SEHEMU YA 25.

 Joshua akaangalia siku ule ujumbe ulipotumwa, ilikuwa ujumbe wa juzi yake. Hapakuwa na jina la mtumaji ila namba tu. Joshua alishajua ni Njama. Alipomwangalia Naya, Naya akainama na kurudi kugeukia kompyuta yake. “Nikuulize Naya?”  Naya akamgeukia. “Ni kwa kiasi gani umeyaamini haya?” Naya akapandisha mabega taratibu kama anayesema hajui. “Itanisaidia kujua Naya! Lasivyo hata nikijieleza kwako, hutaniamini.” “Mimi sijui Joshua! Lakini nataka ujue kuishi na Malon kwa muda mrefu sana, nakumvumilia kwa miaka yote tokea tunaanzana naye, kumeniathiriri sana. Najuta kuvumilia maana kwake jumbe kama hizo hazikuwahi kuwa jumbe za uongo. Na sijui watu walikuwa wakipata wapi namba yangu! Sijawahi kupata ujumbe wa Malon, ukawa ni wa uongo. Na yeye alikuwa akishindwa hata kukataa. Ninachoogopa ni historia kujirudia kwangu. Sipo hata tayari kujua ukweli Joshua! Naogopa hata kusikia maelezo yako.” Naya akaongea taratibu.

“Nina majeraha na madonda moyoni mwangu, kiasi ya kwamba natamani ibakie hivyohivyo.” “Ndio maana muda wote huo hukuniambia?! Maana nimeona ni ujumbe wa tokea juzi!” “Kabisa Joshua. Sipo tayari kusikia chochote kuhusiana na hilo. Ndio maana huyo mtuma ujumbe alipoona nimesoma huo ujumbe, akajaribu kunipigia, lakini sikutaka kupokea na nimemblock kila mahali. Sitaki kusikia tena.” “Sasa utafanyaje? Maana chaguzi ya kuachana, haipo mezani.” Naya akanyamaza.

“Sitakuacha Naya.” Naya akamwangalia na kurudi kufanya kazi yake. “Sijawahi kulala na Jema, na Mungu wangu nishahidi Naya.” Naya akatulia akijua pengine kuna maelezo, lakini hapakuwa. Akajua kuna jambo. Akaendelea na kazi. Pakatulia. “Sasa hivi Jema ananiheshimu sana. Na ameelewa hapatakuja kutokea mahusiano kati yetu. Nilimuhakikishia, na nikahakikisha analielewa hilo. Amerudisha heshima ya kazi kwa asilimia zote na akijua mimi ni kiongozi wake. Ananiheshimu na wala sitakaa nikakusaliti kwa ajili ya Jema.” Naya akabaki kimya akiendelea na kazi. Kwa kuwa kompyuta ilikuwa ikimwangalia Joshua pale alipokaa nyuma yake, akaona anarekebisha ile ripoti.

“Naya?” Akamwita. “Nataka kutoa mambo ya idara nyingine, ibakie kuwa ripoti ya idara yetu tu, kisha nione itakavyokuwa. Nitamuomba Jamal ripoti yake. Niipitie, na kulinganisha na hii nitakayoitengeneza.” “Iwe ni baada ya yeye kuwa na yake tayari.” Naya akamgeukia. “Jamal ana maneno mengi vitendo vyake nivichache na vimejaa sababu. Ukimpa ripoti yako tu, ujue ndio hiyohiyo atakayonipa mimi. Hakikisha anayo ripoti yake mkononi.” “Mbona alishachukua ile ya jana?” “Ulimpa?!” “Ulipomkatalia pale kikaoni, akaniomba nije nimtumie kopi.” Joshua akatingisha kichwa kama anayekataa. “Nilimkatalia makusudi ili yeye ndio aandaye hiyo ripoti. Hicho unachokifanya wewe, ujue ndicho atakachofanya na yeye, kisha kuikabidhisha nakuonekana kama ni yake! Hutapata matokeo ya tofauti.” Naya akatulia kidogo akifikiria, mwishoe akarudi kuendelea na kazi yake.

Pakatulia, Naya akiwa amempa mgongo. Hakujua hata kama anafanya kazi zake au la, yeye akaendelea na anachokifanya. “Jana alinipa kazi ya kuwa nikiwagawia na kuwasimamia hapa kazi.” Naya akawa kama amekumbuka. “Ulionaje?” “Niliweza Joshua. Nikaweka kajiutaratibu.” Akageuka na tabasamu usoni. “Unataka nikuonyeshe?” Akamuuliza akicheka. “Nionyeshe.” “Basi mwenzio nilijifunza kule nilikokuwa nikifanya kazi na wale wasichana. Warembo wa mjini. Wabishi na wajuaji. Sikuwa nataka kelele nao, kwa kuwa yule mama aliniamini na kazi yake, sikutaka kumuharibia. Nikabuni njia ambayo nikaitumia na kwa hawa wajuaji wa hapa. Niliowakuta na wageni wenzangu.” Joshua akacheka.

Naya akamtumia kitu kwenye kompyuta yake. “Angalia.” Akafungua kwa haraka, kwanza alishakuwa ameingiwa na hofu na alichosoma kwenye simu ya Naya. Na ikawa kama Naya amemuhamishia yeye tatizo. Moyo wake ukapoa, akamuacha Joshua anahangaika moyoni. “Unaakili Naya!” Wakacheka. “Sasa hapo niambie, nani anabishana na mimi?” Joshua akacheka. “Hawawezi.” “Basi hapakuwa na kelele, ila kununa, na mpaka wanatoka jioni, wakawa wote wamemaliza kazi zote nilizowapa.” Joshua akafurahi sana.

“Mimi naona hiki kitengo wewe utakiweza Naya.” Naya akacheka. “Mbunifu katika kila kitu!” Ikawa kama anampongeza. “Asante. Hapa nishajua nini chakufanya leo. Bila kelele, ila kazi tu.” “Niliona ujumbe kutoka kwa Jamal, akiwapelekea watu wa IT akikuombea access kubwa! Sikujua ni kwa nini! Nilipitia tu kwa haraka nilikuwa na mambo mengi. Kumbe ndio hivi!” “Jana jioni waliniongezea. Usinione hivi!” Joshua akacheka akimwangalia.

“Unaonekana unafurahia unachokifanya Naya!” “Sana. Japo mwanzoni wakati namaliza chuo, sikujua kama nitahangaika ajira. Nilijua tungeendeleza kampuni yetu ya mavazi, nikajua tungefanikiwa sana kwenye huo upande na kuanzisha biashara nyingine. Ila nilikuja kukutana na uhalisia wa maisha! Nikahangaika sana mtaani. Na kwa sasa hiki ninachokifanya ni kama kinategemewa na familia nzima, ndio maana najituma zaidi. Maisha yameniongezea nidhamu.”

“Ila na wewe pia unacho kipaji. Halafu Naya, bado unayo nafasi yakuja kufanya kitu unachokipenda baadaye.” Akavuta pumzi kwa nguvu, nakucheka taratibu. “Sijui Joshua! Naona itachukua muda! Wakati ule Mungu alininyanyulia watu wawili wa nguvu, wakawa wakikimbia na mimi kwenye nilichokuwa nakifanya, nahisi ndio maana ilikuwa rahisi.” “Ni Malon na nani?” “Na Chezo. Rafiki kipenzi wa Malo.” Naya akawa kama anakumbuka kitu.

Joshua akamuona anacheka, kisha akageukia kompyuta yake. “Ni nini?” “Hamna kitu. Nilimkumbuka Chezo.” Joshua akajua na hapo ipo stori. “Na yeye alikuwa kama Malon?” “Hapana. Yeye ulevi wake ilikuwa pombe. Sio mtu wa wanawake. Hata tabia ya wanawake ya Malon ilikuwa ikimuumiza sana na kunionea huruma. Ila aliajiriwa, na pombe haikumfanya kuwa mzembe. Ni mtu anayejiheshimu kwa kweli. Na angalau yeye nilimuona anaweza kumwambia kitu Malo, na Malo akasikiliza. Wakati ule wa Malo, mkorofi.” “Sasa hivi Malon sio mkorofi?” Naya akacheka akifikiria.

“Malon alikuwa mkorofi mno. Sio wakujificha. Wala usingeuliza. Mungu amembadilisha Malo, au anambadilisha. Alikuwa hajui kunyamaza hivyo! Na hana mipaka. Anyway, nilikumbuka kuna kipindi Chezo alinitongoza. Sasa nikajua alikuwa amelewa sana siku hiyo, kumbe alimaanisha. Aliniona jinsi nilivyoshituka, akaja kuniomba msamaha.” “Ulimwambia Malon?” “Nisingethubutu. Walikuwa ni wale marafiki wa kama ndugu, tokea watoto. Nikajua ni pombe tu. Nikaachana nalo hilo, ila tukaja kusikia baadaye alikuwa amewaambia wenzie na yeye alinipenda na kuchukia vile Malon alivyokuwa akinifanyia. Akataka kunitoa kwa Malon. Mbali na hivyo, alikuwa mtu mzuri sana. Alinisaidia sana.” “Pengine ni kwakuwa alikuwa akikutaka kimapenzi.” “Pengine.” Wala Naya hakubisha, akarudi kuendelea na Kazi.

“Huko ninakokwenda si unajua wapo nyuma lisaa tu na hapa?” Naya akawa amemuelewa ila akanyamaza. “Naya?” “Nimekusikia Joshua.” “Naomba leo usiku tuzungumze. Jana sikulala vizuri. Nimeshaanza kuzoea kuwa na wewe masikioni. Inanisaidia kulala vizuri.” “Si umesema huwa mnakuwa na kazi nyingi sana mkiwa huko? Utajuaje kama utakuwa na muda wakupiga simu kama huku?” Naya akauliza taratibu. “Kwa kuwa najua huwa nikirudi hotelini nakuwa sina chakufanya zaidi ya kujiandaa na mikutano ya siku inayofuata. Na mara nyingi nakuwa na Jema, akinipa ripoti ya siku hiyo, ijayo na anakuwa akijiandaa. Ila baada ya muda fulani huwa namruhusu kwenda kulala kwa ajili ya siku inayofuata, maana ni kweli anakuwa na kazi nyingi.” Naya akatulia. Akajua na hapo kuna ujumbe anatakiwa kuelewa.

“Sawa.” “Sawa nini?” Joshua akamuuliza. “Hata sielewi Joshua!” “Ukiwa na mimi, sio kukimbia, utaelewa. Usikusudie kutopokea simu yangu. Nikirudi hotelini tu, nitakupigia ili tuwe wote.” “Umesema unakuwa na Jema mpaka usiku, Joshua!” Joshua akajua ameelewa. “Ataondoka na kutuacha sisi mpaka ulale wewe, ndio na mimi nilale.” Naya akacheka na kumgeukia. “Unacheka nini sasa?” “Kwamba na mimi nitakuwepo wakati ukiwa naye chumbani kwako?” “Naona safari hii isiwe chumbani. Nimeona tunatafarisiwa vibaya. Tutaanza kutumia kumbi za hoteli.” Naya akatulia.

“Unajua mimi huwa kwenye haya mahoteli, nakodishiwa full suite. Chumba chenye kila kitu ndani mpaka sebule. Kwa hiyo huwa tukirudi hotelini, kikao chetu binafsi huwa nahamishia chumbani kwangu. Tukimaliza kazi, ndipo nalala. Hata siku hiyo anayokusimulia Njama, ni kweli Jema alipitiwa na usingizi hapohapo chumbani kwangu. Mimi nilikuja kumgundua amelala, baada ya kama lisaa mbeleni. Sikutaka hata kumgusa, nikamfunika hapohapo kwenye kochi. Maana yeye alikaa kwenye kochi, mimi upande wa mezani. Nikamuacha hapo na kuendelea na kazi zangu na kulala.” Naya akawaza ni kwa nini Njama hakuwepo. Ikawa kama kama Joshua amesoma mawazo yake.

“Tena siku hiyo Njama aliniudhi sana. Sikutaka kuzungumza naye, nikaamua kumuacha ila ni kweli nilimpunguzia safari. Nikawa nikimuacha awe anabakia hapa akisimamia mambo mengine.” “Alifanya nini?” Naya akauliza. “Tulikuwa na kazi nyingi sana siku hiyo. Ni kweli huwa wananitumia sana nikifika huko. Sipumziki Naya. Huwa wananitaka nifanye mambo mengi, na moja kwa moja na wao kina Jema, wanakuwa wapo busy. Sasa siku hiyo anayokwambia, hatukuwa tumekula karibu siku nzima. Tuliporudishwa tu hotelini, nikawaambia tule kwanza tupumzike kidogo, kisha tukutane wote chumbani kwangu. Tufunge kazi ya siku hiyo na kujipanga kwa kesho yake.”

“Tulimuacha Njama sehemu ya kula, kumbe akahamia baa. Njama ni mnywaji. Jema hanywi. Sisi tukarudi vyumbani. Muda ulipofika wakukutana tena, nikashangaa ni Jema tu ndiye amefika, Njama hayupo. Tukamsubiria zaidi ya lisaa, nikamwambia Jema ampigie. Akampigia sana, ikawa anamkatia simu. Jema akamfuata chumbani kwake, hakumkuta. Ikabidi amfute kule tulipomuacha, akamkuta amelewa akaanza kulalamika kuwa tunatumikishwa kupita tunavyolipwa. Akalalamika mengi, Jema akamuacha.”

“Jema akarudi kuniambia hayupo kwenye hali yakufanya kazi. Amelewa sana. Anaongea mambo mengi ni bora kumuacha tu. Hapo alikuwa na kazi ambazo tunazihitaji ili kufanikisha siku inayofuata. Jema akamtumia ujumbe kumuomba alete laptop yake. Alikuja amelewa, hajitambui. Nikamwambia hawezi kufanya lolote akiwa na hali ile. Akapumzike tu. Ndipo akarudi kulala, sisi tukaendelea na kazi. Jema akalala chumbani kwangu, kwenye kochi mpaka asubuhi alipoamka. Sasa mimi sijui walizungumza nini baada ya hapo. Ila nataka kukuhakikishia Naya, hakuna kinachoendelea kati yangu na Jema. Kwanza najua ananiogopa sana.” Joshua akaendelea.

“Alinijaribu nilipofika tu hapa. Maana nilimkuta hapa. Nilipoelewa nia yake kwangu, nikamuonywa kwa wazi kabisa bila mafumbo. Jema alielewa, akaomba msamaha. Na ukweli, sijui kwa upande mwingine, lakini najua anajiheshimu. Si msichana muhuni kwa kuwa kila nikisafiri naye, namuona ametulia haangaiki na wanaume wa huko na hata hapa sijawahi msikia anamwanaume ila kazi tu. Nafahamiana na mchumba wake. Najua wanakaribia kufunga ndoa. Hayo mengine ni ya Njama tu.” Naya akavuta pumzi kwa nguvu.

“Nakaribia kumalizia ripoti yangu. Unataka nikimaliza uione?” Joshua akacheka akimwangalia. Ila alimuona ametulia hata usoni. Akajua amemuamini. “Nikiwa nakwambia nakupenda, Naya. Huwa inaleta maana yeyote ile?” Akamuuliza. “Mimi sikumbuki kama uliniambia unanipenda. Lini!?” Joshua akacheka sana. “Naya?” “Utakuwa umenifananisha, ila mimi sikumbuki kama uliniambia hivyo.” Joshua akacheka sana akitingisha kichwa. “Nakupenda Naya.” “Mimi mwenyewe nakupenda.” Joshua akacheka. “Muone! Wewe unataka kuniacha kwa maneno ya kizushi tu bwana! Ukoje Naya?” “Nilikwambia kuishi na Malon kumenithiri Joshua. Nivumilie tu kama ulivyoahidi.” “Ukiwa unapatwa na mashaka, tafadhali niambie.” “Hii week uliniambia upo leba.” Joshua akacheka sana.

“Sikutaka kukuchanganya.” “Sasa ndio ujue ungeniharibia safari nzima kama ningeondoka na kukuacha kwenye hiyo hali. Nilikuwa nimeshavurugukiwa! Hapa nimeshindwa kufanya kazi kabisa.” Naya akamwangalia na kuinama. “Nimefurahi umeniamini Naya.” “Sasa umejuaje kama nimekuamini?” “Najua. Ila nataka ujue sitalala na Jema si kwa sababu yako tu, pia kwa ajili ya Mungu wangu.” “Unakaribia kuharibu bwana!” Joshua akacheka sana. “Naya!” “Wewe ungeacha tu.” “Sasa hudhani hiyo ndio itakuwa sababu nzuri ya kutokukudanganya! Nikilala naye huko, nikarudi nikiwa nimetulia. Yeye hasemi na mimi sisemi, utajuaje?” Naya akanyamaza. “Yaani wewe unamuonea wivu mpaka Mungu!?” Naya akaanza kucheka. “Usinigombanishe na Mungu bwana. Wenyewe tunapata.” Angalau Naya akaonekana ametulia.

Watu wakaanza kuingia. “Umeshazaa sasa?” Naya akamuuliza kwa sauti ya chini. “Mkunga wangu ameniambia nimezaa watoto wazima, tena wana afya njema.” Naya alicheka sana. “Kwamba umezaa mapacha?” “Hata! Ni watatu mama.” Joshua akaongea kwa kujivuna. Naya akacheka. “Mkunga wako nani?” “Roho Mtakatifu. Yeye huwa ndio ananisaidia kwenye kuzaa. Akishapitisha yeye juu ya afya ya kilichozaliwa, hapo huniambii kitu. Ujue lazima masikio ya watu yatawasha tu.” Naya akamwangalia akicheka kama anayemtamania. “Ni hivyo nasafiri. Lakini lazima tungeenda tukasherehekee. Ila nikirudi, kwa mara ya kwanza, nitataka kusherehekea hiki nikiwa na wewe. Mungu wangu amefanya tena.” “Hongera Kumu.” “Asante Naya Kumu. Safari hii Mungu anafanya mambo matatu kwa mpigo! Wuuuu!” Naya akacheka akimtizama.

Wakaendelea kumsalimia. “Acha nikajiandae Naya. Nina vikao vitatu mbeleni kabla sijaondoka leo.” “Sawa. Uzidi kufanikiwa Joshua.” “Na wewe zaidi.” Akarudisha kiti kwenye meza alipochukua, nakurudi pale mezani kwa Naya kuchukua laptop yake. “Usiache kunitumia hiyo kazi. Kabla ya kikao.” “Kweli?!” Naya akashangaa kidogo. “Nina maana yangu. Nitumie tu.” “Sawa bosi wangu.” Joshua akacheka nakutoka akitembea mwendo wake watu waliokuwa wakimwiga jinsi anavyotembea. Naya akamsindikiza kwa macho na tabasamu kubwa usoni, wenzie wakimwangalia.

~~~~~~~~~~~~~~~~

“Yaani nahisi Kumu atanihamisha kitengo LEO!”  Jamal akaingia akilalamika. Naya akageuka kumwangalia. “Hali mbaya Naya! IT wameshindwa kunipa kompyuta nyingine. Nimekwama. Hapa nina dakika 10 kabla yakuingia mkutanoni, niweke ile ripoti yako sawa.” Naya akamshangaa sana moyoni. Jana yake alimwachia kitengo kizima kwa madai yeye anakwenda kuandaa ripoti. Asubuhi hiyo bado analalamikia bado ripoti! Naya akaanza kumuelewa Joshua. Akajua ndio maana Jamal ni mkali sana. Anataka watu wafanye kazi kumrahisishia yeye. Akabaki akimtizama.

“Au sijui nimtumie ujumbe sasa hivi nimwambie IT wameshindwa kunipa nyenzo!” Akawa anajiuliza mbele ya meza ya Naya. “Ila ujue sisi wote kwenye hiki kitengo, hatutakuwepo mkutanoni.” Naya akamkumbusha. “Lakini kosa sio langu!” Akajitetea. “Ndipo aliposema tusipohudhuria, itabidi kutoa maelezo ni kwa nini kitengo chetu hakikuwepo kikaoni!” “Na leo anakwenda hukohuko kwa wenye viwanda. Akiulizwa cha kupunguza gharama kwenye kampuni, naona na mimi nitakuwa mmoja wao. Lakini kosa sio langu!” Naya akabaki kimya akimwangalia.

“Lakini vipi hapa?” “Hapa pako vizuri, nishamtumia kila mtu kitu chakufanya leo. Nashukuru hao watu wa IT waliniongezea access.” “Jana nilishinda ofisini kwao. Nikawasisitiza. Afadhali kama wamefanya.” Naya akajiuliza moyoni huo muda anaopoteza hapo kuzungumza naye, si angefanya kazi. “Nina wazo bosi wangu.” “Unayo ripoti nyingine!?” “Sio hilo. Kwa kuwa watu wa IT wanakuzungusha, kwa nini usichukue hii kompyuta yangu, mimi nikatumia laptop? Ninayo laptop mpya, nataka kuhamishia kazi zote hapo.” “Nikifanya hivyo ujue sitapata mpya.” Naya akamshangaa na kubaki amemkodolea macho, mwishoe akaamua kurudi kufanya kazi zake.

“Ile ya jana hukutengeneza tena hata kidogo?” Jamal akauliza kwa wasiwasi kidogo akijibaraguza na cheko. Naya akamgeukia tena. “Joshua alinipa kazi ya pembeni. Akitaka nijifunze zaidi. Nikaitengeneza, leo asubuhi ameniulizia, nimemtumia.” “Mungu wangu! Hapo atanibana.” Akawa kama amekwama, lakini akapata tena wazo jingine. “Nipe tu nikaibadili kidogo.” Bila kubisha akiwa ameshaandaliwa na Joshua, akamtumia. “Tayari nimekutumia.” Jamal akatoka hapo mbio bila hata kushukuru, Naya akabaki akimfikiria. 

Kikaoni.

Kabla ya dakika 6 za muda wa kikao kuanza, kitengo chote walikuwa wameshafika mkutanoni. Naya akagundua vitengo vyote wapo hapo na viongozi wao. Akajua ripoti zimeshaandaliwa. Wakabaki wakitaniana mpaka Jema alipoingia. Naya akaangalia muda, zilibaki dakika 4 tu. Wakatulia kidogo wakimtizama Jema akijaribu kuunganisha vitu, mara Kumu mwenyewe akaingia. Moyo wa Naya ukajawa furaha, moja kwa moja Joshua akamwangalia, Naya akainama na tabasamu usoni. Wote wakaliona hilo, wakaanza kukonyezana.

Akasalimia. “Faith, tatizo lako lilitatuliwa?” Akauliza Joshua, macho kwenye saa ya mkononi. Faith akasimama kama mshale. “Hapana bosi wangu. Nimegonga mwamba.” Joshua akamwangalia na kumtizama kiongozi wake. “Jona, unajua anachozungumzia?” Joshua akamuuliza kiongozi wao wa idara yao ya Research macho kwenye tablet yake. Kimya.

Joshua akatoa macho kwenye tablet akamwangalia Jona. “Hivi nimeuliza swali kwa sauti au nimeliwaza tu?” “Nimekusikia. Ndio najaribu kufikiria anachoongelea hapa ni nini nakushindwa kukizungumza kule idarani!” Joshua akasimama wima. Tayari mikono akaweka mfukoni. Ungependa kumtizama. “Kwa maana nyingine, mlipotoka hapa jana, hukutaka kujua ni nini alitaka kuuliza hapa!?” Joshua akauliza taratibu tu. “Nilikuwa na mambo ya ripoti, Kumu! Siku ya jana ilikaa vibaya sana. Pengine leo ndio tutazungumza kwenye idara yetu.” “Basi tunaomba kusikia hiyo ripoti.” “Kwa hiyo mimi ndio niwe wa kwanza!?” Jona akauliza kwa wasiwasi, Joshua akamtizama kidogo na kumgeukia Faith. “Baada ya hapa, nitakuwa na dakika mbili, tunaweza kuzungumza, Faith.” Joshua akaonekana kujali. “Nashukuru sana bosi wangu.” Faith akaonekana kulifurahia hilo, akakaa na cheko usoni kila mtu akimtizama.

“Naomba changamka Jona. Hatuna muda mrefu hapa.” Jema akaweka msisitizo. Joshua akaangalia saa. Huyo dada akasimama na kusogea hapo mbele. Ukweli alikuwa nadhifu na uzuri wa kuvutia. Ni kama aliyekuwa amevaa makusudi kwa hilo tukio. Kiheshima, vizuri na kila kitu kilionekana ni cha thamani. Akasoma ripoti yao vizuri sana tena kwa lugha ya kingereza kilichokaa sawa. Kwa hakika alikuwa amependeza na anaonekana anaelewa anachozungumza. Akajieleza vizuri mpaka akamaliza. “Safi sana.” Joshua akawa amesifia. “Imekaa vizuri sana.” Akampongeza, na Jona akapumua kwa sauti mpaka wengine wakacheka. “Najua mlikuwa mkimtumia Njama hizo ripoti, kwa sasa naomba mnitumie mimi moja kwa moja.” “Sawa.” Jona akakubali akionekana kufurahia.

“Kuna swali lolote kwake kabla hajarudi kukaa?” Wote kimya. Jona akarudi kukaa. “Mimi jana nilikuwa wakwanza, leo nakuwa wamwisho.” Akasikika Jamal. Joshua akamtizama na kumgeukia Jema. “Naomba tuokoe muda, tafadhali.” Jema akaweka msisitizo. Viongozi wengine na wao wakafanya kama alivyofanya dada Chege, ambaye ni Jona, Joshua akaonekana kuzifurahia. Akabakia Jamal akasimama. “Kama nilivyosema jana. Bado watu wa IT hawajanifanikishia tatizo langu. Wanalalamikia...” “Acha maneno mengi Jamal bwana! Wewe soma ulichonacho, na kama huna pia tuambie.” Jema akawa mkali kidogo.

“Nina ripoti yangu kabisa.” “Soma sasa!” “Jema naye!” Jamal akaanza. Kabla hajafika katikati ya kuisoma hiyo ripoti, Joshua alishajua ni ripoti ileile ya Naya, ila amebadilisha kidogo sana. Na akaiongea kwa ujasiri sana, kitaalamu, mpaka akamaliza. “Kuna mwenye swali?” Yeye mwenyewe akauliza nakufanya watu wacheke, kasoro Joshua akarudisha macho kwenye tablet yake. “Naona hakuna mwenye swali Jamal, unataka porojo tu, nenda kakae.” Jema akamfukuza, watu wakacheka kidogo na kutulia baada ya kukutana na picha yake na Naya kwenye screen. Wakajua tablet ya Joshua ndio imeunganishwa hapo kwenye screen. Watu wakatulia kuangalia picha. Naya alikuwa amekaa kwenye boti, nyuma yake yeye Joshua akiwa amesimama. Akawa amemlalia begani macho yakitazama shingo. Akawa amejilaza vizuri hapo kwa Joshua, Na Joshua akawa ni kama akimwangalia pale alipojilaza begani kwake. Ilipendeza sana.

“Kiongozi hiyo picha ipo vizuri sana! Unaweza kuuza kabisa, ikaongeza kipato cha familia.” Felix akamtania Joshua, watu wote wakacheka. “Mimi mwenyewe nitanunua wa kwanza kuunga mkono biashara.” Akadakia Mwita. Wote walionekana watu wazima kwa Joshua. Joshua akacheka akiwa ameinama, kisha akanyanyua macho kumwangalia Naya. “Eti, tuanze biashara ya kuuza picha?”  Akamuuliza Naya, Naya akacheka tu na kuinama. Wote wakacheka, Joshua akarudisha macho kwenye tablet yake, kisha akasimama akiwa amerudisha sura ya kazi.

“Cha kwanza, naomba niwapongeze wote. Kama ambavyo nasema. Kitengo chetu ni cha muhimu na ndicho kinachofanya hii kampuni iendelee mpaka leo.” Wakajipigia sana makofi. “Ni kweli na ndio maana napigania maslahi yenu wote, nikijua hii kampuni inamuhitaji kila mmoja wetu.” Joshua akawapongeza na kurudia zile ripoti kwa ufupi. “Ndio maana, kwa heshima yenu. Nimeona kabla sijazungumza na yeyote yule kwenye hii kampuni, niwashirikishe nyinyi kwanza, kitu kipya tunachokitoa.” Naya akashangaa wanapiga miluzi na kushangilia sana.

“Sasa mbona hata hajasema ni nini!?” Akajiuliza Naya akiwatizama wanavyoshangilia huku wakipiga meza, mwishoe wakaanza kupiga meza wakiita jina la Kumu kama wapo bungeni. Wakagonga meza kwa pamoja huku wakisema, “Kumu! Kumu! Kumu!” Naya akashangaa sana, akabaki ameinama akicheka. Wote walionekana wamefurahia sana.

“Naomba nimalizie. Na ninasisitiza, sio mimi bila nyinyi.” Wakapiga tena makofi. Akatupa picha tatu kwenye screen. Ukumbi wote kimya. “Hivi ni vifaa vya kuuzia. Tunataka hata wauzaji wa karanga, waweze kuuza bidhaa zetu.” Wote kimya. “Hiki ni kifaa kwa muuzaji anayetembeza bidhaa zake. Tumemuwekea sehemu maalumu yakuweza kubeba bidhaa alizokuwa akiuza mwanzo, makusudi ili asione tumemwingilia. Ila tutampunja sehemu ya kuweka bidhaa zake za awali, kwenye hiki kifaa chetu tutakachompa kama inavyoonekana pichani, ili sehemu kubwa itakayobaki, abebe bidhaa zetu zaidi. Na hili sinia ni maalumu, litakuwa na matundu yake na chini kitu cha kushikilia ni kwa ajili ya kuwekea chupa/bidhaa zetu ziwe salama, zisiwe zikianguka hata akiwa anakimbilia wateja wake.” Watu walishangilia sana.

Naya alibaki ametoa macho. Ilitengenezwa muundo mzuri, picha yenyewe ilivutia kuitizama. “Kila kijana atakayetaka kuuza bidhaa zetu, tutamkabidhi hii, pamoja na tisheti 3, mkoba maalumu wa kuhifadhia pesa, pamoja na kofia. Ila kwa sharti la kutouza bidhaa nyingine yeyote inayofanana na yetu isipokuwa zetu tu.” Watu wakazidi kushagilia.

“Na hii picha ya pili ni kwa wale wauzaji wenye vibanda vidogo tu barabarani. Wanaochoma mishikaki na mahindi, au hata mihogo. Ataweka hapa kwenye coolerbox, anauza bidhaa zetu, naye tutampa bidhaa kama huyu mtembezaji endapo atataka kuajiri na mtu wakumtembezea, pamoja na mwamvuli mkubwa kwa ajili ya jua. Na wote hawa, tutawauzia kwa bei ya jumla ili wajitengenezee faida.” Watu wakashangilia sana. “Hii ni awamu ya kwanza, kufikia watumiaji moja kwa moja. Lakini kutakuwa na shindano.” Hapo wote wakatulia.

“Katika hawa wauzaji wa aina mbili, 10 watakao uza bidhaa zetu kwa asilimia kubwa ya kiwango tutakachoweka, ndani ya mwezi mmoja, watajishindia pesa tasilimu, na tutawapa mafunzo maalumu ya uuzaji, kisha kuwafungulia sehemu maalumu ya kuuzia, ili waendeleze biashara yetu. Na hiyo itakuwa kwa mikoa yote, mpaka vijijini. Jamal jiandae na idara yako. Nataka timu ya watu watakaochapa kazi, sio sababu.” Watu wakashangilia sana.

“Zipo sehemu ambazo hazina maduka, au kuna maduka lakini wanauza vitu vingi inakuwa shida kwa mnunuaji kupata bidhaa yetu kwa haraka. Hiyo nitakuja kutoa suluhu nitakaporudi kutoka safari. Inahitaji pesa nyingi, lazima nikaanzie juu.” “Inyeshe.” Wakaanza tena kushangilia, Joshua akicheka. “Kabisa. Nataka hii nchi nzima, isambae bidhaa yetu kwa wingi mno mpaka iwe kama alivyosema Naya. Mpaka watoto, wagonjwa, wasioona kabisa na kuitambua bidhaa yetu kwa macho, wote waimbe bidhaa zetu, na pia wafikiwe na bidhaa zetu.” Watu wakazidi kushangilia.

“Ndani ya miezi miwili tu, nataka hivi vifaa viwe vimezagaa mtaani.” Watu wakazidi kushangilia wakijua ndio ishakamilika. Kumu akisema jambo, hakuna anayepinga. Akajua hata watu wa fedha watapitisha tu. Akisimama Kumu, ni kama amesimama mmiliki wa hiyo kampuni. Walimuheshimu mno. “Tukaendelee kuchapa kazi, tukijua hakuna kati yetu mwenye mchango mdogo. Kila mmoja wetu anahitajika.” Kumu akafunga kikao. “Faith, bado unazo dakika mbili. Unataka bado kuzungumza?” “Ningeshukuru.” “Basi twende.” Joshua akatoka kwa haraka, Faith naye akamfuata akimkimbilia. Alipotoka tu watu wakaanza kushangilia tena na kufurahia Bonus kubwa ya mwisho wa mwaka. Huwa mauzo yakiwa makubwa sana kama hivyo anavyopambana Kumu, anahakikisha watu wa kitengo chake wanalipwa pesa ya ziada mwishoni mwa mwaka.

“mungu wa Coca, kaongea tena. Neema mwishoni mwa mwaka.” Wakazidi kucheka. “Hicho kichwa kingine aisee! Daah!” “Na lazima itajibu tu. Acha nikaongeze mkopo, najua nitalipa tu.” Wote wakacheka na kuzidi kushangilia. Kila mtu akazungumza lake. Naya akajikusanya na kutoka kimya kimya akiacha watu bado wakishangilia, lakini hata yeye alishangazwa na Kumu. Muundo wa hicho kifaa, jinsi itakavyomrahisishia muuzaji kukibeba muda mrefu bila kuchoka, usalama wake! Akajikuta akicheka huku akirudi ofisini kwao. Alichora vizuri sana na akaelezea kwa ufasaha!

~~~~~~~~~~~~~~~~

“Kumu anataka kukuona Jamal.” Jema akamwambia Jamal akisoma ujumbe, wakiwa palepale chumba cha mkutano akiwa anasubiria hao viongozi wamtumie Joshua na yeye hizo ripoti walizosoma. Hakutaka kusubiri ahadi ya kutumiwa baadaye, aliwajua wanaweza wasitume hata baada ya juma. “Nilihisi tu.” Jema akamwangalia. “Naomba nenda Jamal. Leo hana muda kabisa. Ratiba imebana mno. Kila kitu najaribu kubana ili tusichelewe uwanja wa ndege.” “Nakwenda mama.” Jamal akaondoka hapo lakini akajua ni nini Joshua anamwitia.

“Anakusubiri ndani.” Fina akamuwahi hata kabla ya salamu. Jamal akazidi kuingiwa hofu. Akagonga na kuingia baada yakumsikia Kumu akimkaribisha. “Naitika wito Kiongozi.” “Tafadhali fanya kazi.” Jamal akatulia kidogo, hata hakukaribishwa kiti. “Unanielewa Jamal?” “Nimekusikia Kiongozi.” “Nataka kuona mabadiliko kwenye idara yako Jamal. Punguza visingizio, fanya kazi.” Jamal akashindwa hata kujitetea. “Sitaki watu wapya kwenye kile kitengo. Walewale waliopo, nataka uhakikishe wanafanya kazi. Uza vizuri kazi yako kwao. Hakikisha wanaelewa, wawekee mikakati inayoeleweka, wafanye kazi. Hakuna chochote kitakwenda kwenye hii kampuni, isipokuwa idara yako imefanya kazi yake. Hata kama tutabuni vitu vizuri vya namna gani, bila kuvitangaza ili kuwafikia wateja, hakuna kitakachotoka hapa. Na SITAKI wewe, utukwamishe.” Hapo Kumu akaweka msisitizo.

“Sijui kama unanielewa Jamal?” “Nimeelewa.” “Kama kwa sasa kuna jambo linakufunga, tafadhali nijulishe ili nijue chakufanya. Sina hata dakika moja yakupoteza kama hii tunayopoteza mimi na wewe sasa hivi, tukiambiana chakufanya wakati wewe ni mzoefu hapa na unajua umuhimu wa idara yako. Tafadhali naomba kuona mabadiliko Jamal. Na kikao kama hiki naomba kisije wahi rudia tena.” “Sawasawa. Lakini nilifikiria safari hii nibadilishe watu pale ida...” Kabla hajamalizia, akamuona Kumu akitingisha kichwa kukataa.

“Hapana Jamal. Inawezekana unao watu wazuri sana ila hujajua jinsi yakuwatumia. Sitaki mabadiliko ya watu ila utendaji. Asante.” Jamal akajua ndio anaambiwa aondoke maana Kumu alisharudisha macho kwenye alichokuwa akiandika, hakumwangalia tena. “Sawasawa.” Jamal akajibu hivyo na kutoka. Fina akamuona anahema kwa nguvu, hata hakumsemesha. 

Kuagana Kwa Naya Na Kumu.

Baada ya muda Naya akiwa anafanya kazi akasiki, “Nimekuja kuagwa.” Naya akacheka na kugeuka baada yakusikia sauti ya Kumu akiingia. “Nilijua ulishaondoka?” “Bila kuagwa!?” Joshua akauliza akimsogelea. “Ripoti nzuri sana. Hongera. Kuna mambo kidogo tu yakubadilisha, tutazungumza usiku kabla hujalala. Ila nimebakisha dakika 5, kwa ajili yako.” Naya akacheka kwa furaha. “Twende.” “Hii hapa barua yako. Nimekuandikia, usome njiani au ukifika.” Joshua akaipokea akiwa amehamasika. “Wao! Asante.” Akabaki akiitzama, Naya akacheka. “Nimefurahi.” “Nimekuona. Nimefurahi kama umeifurahia.” Akaiweka mfukoni.

“Kumu! Kuna...” “Hapana Jema. Nimekwambia nipe dakika 5 zisizo na mwingiliano. Naomba kila kitu kisubiri, tafadhali.” “Ni makao makuu!” “Zungumza nao.” Joshua akajibu kirahisi tu na kumshangaza Naya. Maana kama ni makao makuu, inamaana ni huko wanakokwenda. 

“Twende Naya.” “Wanataka kuzungumza na wewe Kumu!” “Unazidi kupoteza muda Jema. Maana muda wote huo unaozungumza hapo nakushindwa kunielewa, ujue zile dakika 5 zinabakia vilevile, hazisogei. Kama huna majibu ya kuwapa, waambie nitawapigia nikiwa njiani. Naomba dakika 5, tafadhali.” Akaweka msisitizo akisikika kwa ukali. “Sawa.” Jema akarudi kwenye simu aliyokuwa ameshika mkononi, Naya akamsikia akizungumza vizuri kwa lugha ya kingereza huku akiondoka. “Twende.” Akamnyooshea mkono ili kumshika. Naya akacheka, akamshika mkono wakatoka.

“Umekula sasa?” Ilikuwa imeshafika mchana. “Nilikuwa nakimbia leo, sikuwa na dakika hata moja ya kutulia. Kikao nilichofanya na nyinyi kwenye idara yenu, ilinibidi nikifanye zaidi ya mara mbili tena ili kuwakilisha wazo letu.” Wakawasikia wakizungumza huku wakitoka. “Sitaki kuchelewesha. Imebidi kuwauzia wazo kwa haraka na kwa muda mfupi, ili utengenezwaji uanze na kama kuagizwa viagizwe. Kwa hiyo ilibidi kukaa na watu wa manunuzi pia. Watu wote wa idara yao kuhakikisha wanaelewa ile michoro.” “Umefanikiwa kuwauzia wazo zima?” “Kwa asilimia 100.” Naya akacheka.

“Hongera Joshua.” “Umeafikiana nalo?” “Sana! Lakini umenishangaza! Sikujua kama ni mchoraji hivyo!” “Unapokuwa na mimi kwenye simu usiku, nakuwa nachora huku nipo na wewe. Huwa napenda mawazo yangu yatoke yakiwa yamekamilika. Cha kwanza inanisaidia usalama wake. Najua hakuna atakayeiba hapo katikati kabla sijakamilisha, na pili inanipa muda wa kutafakari zaidi. Ningeweza kutafuta mchoraji, lakini huwa nafanya mwenyewe. Hata hivyo Mungu alinipa kipaji cha uchoraji. Sifanyii nacho mambo mengi, ila naona kinanisaidia hapa kazini.” “Hongera.” Wakaelekea ofisini kwake. “Hujambo Naya?” Fina akamsalimia. “Mimi mzima. Pole na majukumu.” “Asante. Karibu pande hizi.” Naya akacheka Joshua alishaingia ofisini. “Asante.” Akaingia na yeye ofisini kwa Kumu.

Akamdaka na kufunga mlango. Yakaanza mabusu ya nguvu. Alimkumbatia kwa nguvu mpaka Naya akashangaa. Hakuwahi kumkumbatia hivyo. Akajituliza hapo, akifurahia harufu na ladha nzuri ya midomo ya Kumu. Kama aliyepulizia kinywani kitu maalumu kwa ajili ya hilo busu! Na hakuwa amembusu muda kidogo. Naya akafurahia kushikwa na Joshua. Asiamini hatimaye anashikwa na mwanaume mwenye uhakika hashiki wanawake wengine hivyo. Hamu ya mapenzi ikampata, akatamani mengi hapo, lakini akajiambia apokee atakachopewa. Akaendelea kwa muda mrefu tu, Naya naye akarudisha taratibu kisha akamwachia.

Tumepita hatua ya kama tunaachana au tunakuwa pamoja. Si ndiyo?” Joshua akamuuliza taratibu wakiwa bado wamesimama. “Ndiyo.” Naya akajibu akiwa anatamani arudie busu. “Ujue mimi nitasimamia hilo neno Naya! Maswala ya jambo linapotokea unafikiria kuachana, naomba ubadilike. Fikiria ni jinsi gani tunaweza kutengeneza tulichonacho sio kuvunja. Tafadhali sana Naya. Mwenzio nakuhitaji sana maishani! Wewe unaye baba ambaye unaweza kumkimbilia, ukalala bila kunitafuta! Tafadhali uwe unanifikiria na mimi ambaye sina hata mtu mwingine wakumpigia simu usiku ila wewe!” Naya akajisikia vibaya.

“Samahani Joshua. Nilipaniki.” “Naomba usisahau kuwa nakuhitaji sana. Sina ndugu, nawewe ulinihidi utakuwa na mimi. Naomba na wewe usinibadilikie. Tafuta jinsi yakuniweka karibu sio kunitoa kwenye maisha yako. Utaniumiza mno, Naya. Tafadhali nifikirie kila kunapotokea tatizo.” “Nitabadilika Joshua. Naahidi nitabadilika.” Akarudi kumbusu tena, na tena.

“Kingine. Majibu ya kila shutuma zangu, tafadhali pata majibu kutoka kwangu mimi mwenyewe. Najua umeishi na Malon muda mrefu, lakini tafadhali usinilinganishe na Malon. Mimi sio yeye, na hivi nilivyokushika wewe, utabakia kuwa wewe tu. Tulisema ni mpaka lini?” Naya akacheka na kujibu. “Mpaka kifo.” “Basi naomba ulikumbuke hilo na naomba uwe unanisikia ninapokwambia nakupenda. Najua umezoea kusikia hivyo huku ukitendwa mpaka ikapoteza maana. Lakini Joshua Kumu anapokwambia anakupenda, anamaanisha amemaliza kila kitu, na maisha yake ameyaweka kwako.” “Jamani Joshua! Kweli?” “Kweli Naya! Safari ya leo ingekuwa ngumu sana kama tungechana kama jana. Tafadhali naomba nafasi yakusogezwa karibu sio kunifikiria kuniacha. Nakupenda Naya, na nimeamua kuwa na wewe. Mimi nitakupenda kwa dhati.” “Nashukuru Joshua.” Naya akajilaza kifuani kidogo.

“Nikuulize kitu Joshua?” “Karibu.” Naya akamwangalia. “Kwa hiyo nijihesabu nimeshapata mtu wangu wa kudumu?” “Mimi mwenzio nimemaliza Naya. Nipo na wewe kwa asilimia zote. Sitafuti wala kuangalia tena. Mungu amenipa wewe, nimekupokea hivyo ulivyo, najua mengine Mungu atatusaidia tu.” Naya akacheka. “Nimefurahi Joshua. Nimekuwa nikihangaika kutafuta mtu wangu mpaka nilikuwa nakaribia kukata tamaa!” “Mungu alikuleta hapa kwa ajili yangu, Naya. Najua unazo ndoto zako. Na mimi nitahakikisha lazima uje uziishi, ila ujue kuna mambo Mungu aliyashikilia kwako, ili ujikute unaishia kwenye hii kazi, anikutanishe na wewe.” “Hapana Joshua, ni ili anikutanishe na wewe. Mimi ndio nilikuwa nakuhitaji sana Joshua. Mpaka ikafika kipindi nikahisi namuomba Mungu kitu ambacho labda ni kigumu sana! Hakuna mtu wa aina yako! Hivi unavyoniona nababaika, univumilie. Najifunza kuishi na muujiza wangu.” Joshua akacheka na kurudia busu jingine la muda wa kutosha akiwa amemkumbatia Naya vilivyo mpaka simu ya mezani ilipoanza kuita.

Akaendelea kidogo kumbusu, kisha akamwachia. “Huyo atakuwa Jema. Mizigo yote amepeleka kwenye gari. Inabidi tuondoke.” “Samahani kukuchelewesha. Ila nimefurahi, natamani tungekuwa na muda zaidi Joshua.” “Na mimi natamani hivyo. Lakini nipe muda tena kidogo. Nitarekebisha hii hali.” Naya akawa hajamuelewa. “Nimefurahi tumepata huu muda Naya. Nimefurahi umeniaga vizuri. Nimefaidi midomo yako mitamu!” Naya akacheka na kujificha uso. “Wewe ndio ulikuwa na ladha nzuri mdomoni. Nilitamani tusimalize!” Joshua akainama tena na kumbusu, wakasikia hodi mlangoni. Joshua akavuta pumzi kwa nguvu na kumuachia Naya.

“Bakisha muda wa usiku kwa ajili yangu Naya. Naomba pokea simu zangu kila ninapokupigia.” “Nitafanya hivyo. Uwe na safari njema. Subiri nikuombee.” Naya akamshika mikono. Akamuombea kwa ufupi tu, akamaliza. “Hapo ndio umemaliza kabisaaa. Naamini nitakuwa na wakati mzuri zaidi.” Naya akacheka. “Ni sawa nikikusindikiza mpaka kwenye gari au haitakuwa sawa?” “Ndio ningependa zaidi.” “Basi twende ili tusimuharibie ratiba Jema.” Wakatoka na kumkuta Jema mlangoni.

Jema aliwapisha, Kumu akatoka akiwa amemshika Naya mkono. “Naomba iwe safari ya kwenye gari Kumu. Sina dakika nyingine iliyobaki.” Wakamsikia  Jema akizungumza nyuma yao. Joshua hakujibu akaendelea kutembea. Jema akawapita. Alikuwa amependeza haswa. Na kiatu chake cha juu kama kawaida yake. Naya aliweza kupata harufu nzuri  kutoka kwake. “Unataka nikuletee nini?” “Kwani huwa kuna nini huko? Hata sijawahi kufika huko. Mimi nilikuwa nikinunua vitu vingi kutoka Dubai. Hata pafyumu zangu zote nilikuwa nikitoa huko.” “Basi nitakuangalizia kama wana aina nzuri za pafyumu. Nitumie majina.” “Naomba usihangaike huko Joshua. Fikiria kurudi huku ili tuwe wote.” “Unataka nisimame tena nikubusu wakati unajua sina muda uliobaki? Acha kunogewa Naya!” Naya alicheka sana na kumpiga kidogo ngumi.

“Mimi sitaki busu. Nataka usihangaike huko!” “Kwa hiyo nikisimama hapa na kutaka busu, utakataa?” “Nitakufikiria.” Joshua alicheka sana mpaka kwa sauti ya juu huku wakitoka. “Yamekuwa hayo Naya!?” “Kumbe! Wewe unafikiri unapata mabusu kwa urahisi tu?” Joshua akazidi kucheka akimwangalia asiamini. “Lakini si nilichokipata pale ndani ofisini wakati ukining’angania.” Naya akacheka sana kwa aibu. “Mimi huyu?” “Wewe Naya.” “Utakuwa hukuwa umeelewa.” Joshua akazidi kucheka mpaka wakafika garini. Ilikuwa imeshawashwa dereva yupo ndani na Jema amekaa mbele tayari na mkanda. Akamgeukia Naya. Akambusu tena kidogo. “Safari njema?” “Asante. Na wewe kazi njema. Tutaongea.” Naya akasubiri akapanda kwenye gari, akampungia mkono, dereva akaondoa gari, ndipo Naya akaanza safari yakurudi ofisini kwake taratibu na cheko usoni.

~~~~~~~~~~~~~~~~

Alipofika ofisini na kuangalia simu yake aliyokuwa amefungia kwenye droo, akagundua Joshua alimtumia pesa. Akabaki ameduaa. Ikawa ni kama amemlipa mshahara wake wa mwezi mara mbili yake. Naya alibaki akikiangalia kiwango kile cha pesa, akaanza kusikia mikono inatokwa jasho asiamini. Akaangalia muda, akagundua ni masaa mawili yaliyopita, halafu hata Joshua hakumwambia walipokuwa naye ofisini kwake. Akatamani kumpigia simu, akakumbuka kuna simu alisema atapiga akiwa njiani. Akamtumia ujumbe. ‘Nashukuru sana kwa pesa, Joshua. Ndio nimeziona! Zitakuwa msaada mkubwa sana. Mungu azidi kukubarki, usipungukiwe daima.’ Hapohapo akarudisha ujumbe mfupi tu. ‘Amina. Tutaongea.’ Naya akajua amebanwa, asijue ujumbe huo anajibiwa huku akizungumza na simu ya muhimu sana. Jumbe za Naya hazikuwa zikisubiri majibu. Wakati wowote, muda wowote, ujumbe wa Naya ukiingia tu, lazima ajibu. Ila ujibuji wake ndio huwa anajua yupo busy kwa kiasi gani.

Muda wa chakula cha mchana ulipofika, akaletewa tena chakula. Mpaka Naya akabaki akicheka. “Nakushukuru sana. Sasa vyombo utavipataje?” “Wakati nikileta chakula kesho, nitachukua vya leo. Kuna kitu maalumu unataka kula kesho?” “Jumamosi huwa tunakula tu nyumbani. Usihangaike.” “Hujawahi kula chapati niliyopika mimi.” Naya akacheka. “Kesho nitakuletea chapati, nyama ya foili, na mchuzi wa maharage. Nitakuwekea vizuri, ukale nyumbani.” Naya akacheka kwa shukurani. “Nakushukuru sana, Josee. Asante.” “Kesho.” Akaondoka. Huwa Joshua anataka chakula kiwe kinamfikia Naya mwenyewe moja kwa moja si kukiacha getini au kumkabidhi mtu mwingine.

“Kama ni kingi, naomba kidogo Naya. Njaa inauma na nimeishiwa kabisa, wangu.” Kijana mmoja ambaye alimkuta hapo akaomba kinyenyekevu. “Huwa anaweka kingi. Kalete sahani nikuwekee. Ila sijajua hata amenipikia nini!” Tayari hadhi ya Naya ikawa imeshabadilika. Naya aliyekuwa akishinda na njaa kazini, sasa hivi anaye mpishi wa kumletea chakula! Joshua alijua kumuenzi kwa namna ya juu mno. Aliingia hapo kazini asubuhi hiyo akiwa amenyongea, lakini Joshua akaondoka hapo nakumuacha na furaha.

~~~~~~~~~~~~~~~~

Akapata simu kuwa anamgeni. Akaangalia muda, akagundua muda wakutoka kazini aliomwambia Bale ndio huo. Bado kulikuwa na baadhi ya watu ofisini na nje kuna mwanga. Naya alishazoea kutoka wa mwisho hapo ofisini. Ila akaona asimuweke Bale, atoke tu. Kuna dada hapohapo kwenye kitengo chao cha masoko, alitangaza kuuza wigi za nywele halisi kutoka Brazil. Naya akazipenda ila hakuwa na pesa. Kwa kuwa alitumiwa pesa yakutosha na Joshua, akaamua kununua hiyo nywele bila kujali gharama. “Nataka kubadilika kidogo.” Akakusudia kumrudisha Naya wa zamani mwilini mwake. Naya mwenye nywele ndefu. Hapo akiwa na nywele fupi tu alivutia, sasa akiweka ndefu ndio utafikiri Mungu alimpendelea huko tumboni wakati akifinyangwa! Na kwa kuwa alijijulia, Naya akajua akija kurudi hapo siku ya jumatatu, watamsahau.

Akaelekea ofisini kwa huyo dada upande wa Research. Ndani ya hilo jengo, lakini upande mwingine. Akamkuta amejiinamia mezani kwake. “Samahani, Zera. Bado unazo nywele?” “Ninazo mpenzi. Unataka ngapi?” Naya akacheka. “Naomba niangalie tena picha, ili nichague.” “Na nitakushauri pia.” Akahamasika na kutoa simu. “Hii ukiweka kichwani, ina baby hair nyingi na imejaa. Usiogope bei, nitakupunguzia. Utakuwa kama toto la kimanga! Na uzuri huo! Watakusahau.” Naya akacheka akiendelea kuangalia picha nyingine. “Naona kweli hii nzuri. Naomba basi uniletee kesho tafadhali.” “Malipo lini?” Naya akakunja uso kidogo kama hajaelewa.

 “Nakopesha mpaka siku ya mshahara. Ila kama huna mwisho wa mwezi huu basi tutaelewana.” “Mimi naona nikulipe tu utakaponiletea hiyo nywele.” Zera akafurahi sana. “Ndio raha yakufanya kazi na wenye nazo. Huwa nakuwa na hereni pia. Hereni zangu za ukweli, na huwa hazichuji wala kuumiza masikio.” “Basi naomba kuziona pia.” “Mambo yote kesho. Na nilivyoishiwa! Kesho nakuletea mzigo wote. Nitakuita kwenye gari uchague.” “Asante Zera.” Naya akatoka. “Mwanamke wa Kumu huyo, unafikiri atakopa?” Naya akasikia wakianza kumsengenya ndani. Wote wakacheka. “Na kweli. Nilijisahau. Kesho najaa. Sitaki kukopwa.” “Sasa usianze kujishaua Zera!” Naya akaendelea kutembea kutoka huo upande kwenda nje. Wala hakujali. Alishazoea. 

Bale na Naya Juu ya Malon.

Naya alitoka nje getini akitegemea kumkuta Bale akimsubiria, badala yake akakuta gari ya Malon. Akajua Bale amekuja naye. Naya alikasirika sana. Akaamua aondoke tu. Akaanza kuondoka na kuwapita wakiwa ndani ya gari, Bale akashuka kwa haraka akimkimbilia. “We Naya vipi!?” “Umeniumiza sana Bale! Sijui ni kwa sababu ya shida tulizo nazo, au vipi! Sijui! Lakini umeniumiza na sikutegemea.” Naya akaanza kulia. “Shida zote ulizoniona nikizipata kupitia huyo Malon, bado leo unamshikilia na kutaka aniharibie kwa Joshua!” “Malon amebadilika Naya.” Naya akashangaa sana.

“Kwa hiyo?! Unategemea nini Bale!? Unafikiri ni nini kitatokea?” Naya akazidi kulia. “Mimi sio muhuni Bale na sina tamaa, muulize Malo. Alikuwa na wanawake wengie tu, lakini sikuwahi kumsaliti. Ndivyo nitakavyofanya kwa Joshua. Hata kama wewe humpendi, lakini Joshua ananipenda na ananiheshimu. Nabakia na Joshua wangu. Sina shida ya usafiri wa Malon wala msaada wake. Wewe endelea kutumia vitu vyake, akutajirishe. Ila mimi sitaki tena uninunulie viatu. Wewe sio ndugu mzuri Bale. Unaweka pesa mbele kuliko mimi.” “Kweli Naya ndio unaongea hivyo!?” Naya akaondoka bila kugeuka nyuma.

Malon akabaki akiwaangalia. Naya analia, Bale anamkimbiza nyuma. Bale akaona ampigie simu baba yao. “Naomba uzungumze na Naya, baba.” “Unataka nizungumze naye nini?” Baba yake akauliza kwa utulivu tu. “Anashindwa kuwa muelewa.” Baba yake kimya akimsikiliza. “Baba?” “Nakusikiliza.” “Nimemfuata kazini twende kununua viatu, hataki.” “Kwamba ghafla viatu alivyokuwa akivitaka sana jana, sasa hivi havitaki tena!?” “Naona anachanganya mambo ya Malon hapohapo.” “Kwamba Naya ndio anachanganya mambo ya Malon!?” Bale akababaika kidogo. “Mimi niliona nije na Malon ili kumsaidia usafiri.” “Umeanza lini kujihusisha na mambo ya Naya?” Kimya.

“Wewe umezaliwa na kumkuta Naya, nilishawahi kukuomba unisaidie hata siku moja kwenye malezi yake?” “Nilitaka kusaidia tu baba.” Bale akajua ameshaharibu. “Usikubali shida za muda zikakupotezea utu wako Bale. Unanielewa?” “Naelewa baba. Ila nilitaka kusaidia.” “Kumsaidia Naya au wewe mwenyewe?” Baba yake akamuuliza. “Naya, baba! Unawezaje kufikiri hivyo?” “Unauhakika kuwa ni Naya na si wewe mwenye haraka ya maendeleo?” “Baba! Nataka kujishughulisha na mimi! Nilifikiria utanipongeza kwa kuonyesha juhudi na utayari wa kuthubutu!” “Kwa nia na sababu sahihi, ndiyo. Lakini si vinginevyo Bale. Taratibu. Na katika mipango yako yote, tafadhali usimuhusishe Naya wala usimguse. Hakuhusu kabisa. Unanielewa  Bale?” “Nakuelewa baba.” Bale akawa mpole. “Basi ongeza utu. Na Bale?” “Nipo baba.” “Usiwahi kurudia hata kufikiria kuuza binti yangu na usirudi hapa bila Naya, maana ni wewe mwenyewe ulisema unakwenda kumfuata.” Simu ikakatwa.

Bale alibakia kama amegandishwa kwenye friji. Hakutegemea! Akabaki akimtizama Naya aliyekuwa akiendelea kutembea kuelekea kituo kikubwa cha Mwenge. Malon akasogeza gari. “Twende Bale.” “Acha nimfuate Naya, Malon. Asante sana. Tutawasiliana.” Bale akaanza kukimbia, akimkimbilia Naya. Malon akahisi kilichokuwa kikiendelea. Akaongeza mwendo mpaka akamfikia Naya. Akashusha kioo na kwenda kusimamisha gari karibu kabisa na Naya.

“Tafadhali usimlaumu Bale. Nia yake ni nzuri.” “Ipi Malon? Ipi?” Naya akamuuliza kwa hasira. “Kwa miaka yote niliyokuwa na wewe Malon, ulishawahi kunifumania, au kunikuta na mwanaume mwingine?” “Unafika mbali Naya.” “Si mbali. Ni ukweli Malon. Hata siku moja sijawahi kukuingilia kwenye mahusiano yako. Hata yale ya wizi uliyokuwa ukiyaanzisha tulipokuwa wote, nikajua, sijawahi kukufanyia fujo wala kukuingilia Malon. Nilibaki nikiwaheshimu wanawake zako wote mpaka Rita aliyeninyanyasa mbele yako ukanyamaza. Sikuwahi kukuingilia. Nilikuacha ukawa huru huku ukiniumiza. Uliniacha, nikikubembeleza usiniache, Malon.” Bale alishawafikia, akabaki amesimama pembeni.

“Ulinisaliti nikiwa nakusubiria Malo! Nilikupa miaka zaidi ya mitano, nikikubembeleza, kukusihi na kukuvumilia ili tu niwe wako. Maisha yangu yalijaa maumivu makali sana ni kiishi kwa fedheha kwa ajili yako Malon! Uliniacha nikilia mchana na usiku bila kunijali! Hukuwahi kunithamini ila tamaa uliweka mbele. Ulilala na mpaka watu wa karibu yangu bila kunihurumia, lakini sikuwahi kukusaliti ila kukusubiria mpaka uliponiacha rasmi. Wewe mwenyewe Malon uliniacha. Mungu amenihurumia, amenipa Joshua, kweli bila huruma unataka kuniharibia! Kwa kosa gani nililokutendea Malo ila kuwa mwema kwako?” “Nataka kusaidia tu Naya?” “Kwa lipi na kwa nini?” Naya akamuuliza akiwa analia na kwa hasira.

“Unataka kumthibitishia nani, nini?!” Naya akaendelea kumuuliza. “Unamsaidia nani hapa? Nani anataka msaada wako?” “Ni mimi mwenyewe ndiye nilimtafuta Malon, Naya. Sio yeye.” “Sasa kwa nini mnaniingiza mimi kwenye mambo yenu?” Naya akamgeukia Bale. “Wewe ni mtu wa namna gani Bale!? Ulikuwa na mimi Morogoro ukishuhudia nikihangaika kumtoa Malon jela. Ulisikia vile Malon alivyokuwa. Ukajua uchafu wake kwa undani kabisa, kutoka kwa wanawake zake mpaka baba yake mzazi pia alinikataza nisiwe naye. Yote hayo ulijua. Nilifikiri ungekuwa umeelewa kilio ulichokuwa ukikiona kwangu na kujua ni kutokana na yale uliyoyasikia kutoka kwa watu mpaka baba yake mzazi! Lakini umenishangaza na kuniumiza sana Bale. Sijui ni shida, na kuona tunatoka kwa mzazi asiye na pesa!?” “Usiseme hivyo Naya! Unakufuru?”

“Anayekufuru kati yangu mimi na wewe ni nani Bale? Ingekuwa wewe ulikuwa na mwanamke kama Malon, ukaja ukapata mwanamke mwingine, kwa sababu yeyote ile, ungelifurahia kuona namrudisha yule mwanamke wa kwanza aliyekuwa akikutenda mabaya kwenye maisha yako, tena nimrudishe karibu na mwanamke mwingine aliyetulia?” Naya akamuuliza. “Kuwa mkweli Bale. Ungefurahia mimi nikufanyie kama unachonifanyia wewe? Ukijua wazi ndio nimeanzana tu na Joshua. Ametulia yule kaka, mstaarabu. Ananijali kuliko nafsi yake. Eti kila siku anakuja nyumbani anakukuta upo na Malon! Malon amejaa pale ndani na unajua wazi anajua mahusiano niliyokuwa nayo na Malon! Ingekuwa wewe nakufanyia hivyo ungefurahia?” “Basi Naya.” “Hakika basi Bale.” Naya akajifuta machozi.

“Sijawahi kukuomba umpende Joshua wala Malon. Ni uchaguzi wako wewe ni nani umemchagua kuwa rafiki yako. Lakini ningetegemea ungenifikiria hata kidogo! Mimi nakupenda Bale. Wewe na Zayoni ndio watu wangu wa kwanza kuwafikiria. Hakika mimi nisingekufanyia unachonifanyia.” “Samahani Naya.” “Sina shida Bale. Sina shida na chochote chako. Endelea na maisha yako ila achana na mimi kabisa. Wewe sio mtu mzuri.” “Sasa unaenda wapi? Baba amesema lazima turudi wote.” “Nitampigia simu baba, mimi mwenyewe. Achana na mimi, na sitaki kukuona hata unakuwa karibu yangu. Endelea na maisha yako.” Naya akaondoka, na kumuacha Bale amesimama nje ya gari ya Malon. “Naomba mfuate Bale. Giza lisimkute peke yake tafadhali.” “Amekasirika sana. Mwache tu.” “Hapana. Mfuate kwa nyuma, na usimsemeshe. Halafu ukifika nyumbani ukitulia, naomba unipigie.” “Sawa.” Bale akaondoka akikimbia.

~~~~~~~~~~~~~~~~

 

CONVERSATION

0 Comments:

Post a Comment