“Nimefurahi
kama unakwenda kujinunulia vi...” “Hapana. Nanunuliwa na mpenzi wangu Joshua.” Joshua
akacheka akisikika amelifurahia hilo. “Ukirudi lazima utanisahau.
Naya wa zamani anarudi, lakini huyu atakuwa wa tofauti.” “Siwezi. Wewe nakujua
kwa mapigo yangu ya moyo.” Naya akajisikia vizuri sana. “Jamani
Joshua!” “Hakika. Hata ukonde sana au unenepe sana. Ukate nywele au uwe nazo
nyingi, ukiwepo sehemu, moyo wangu utatambua uwepo wako Naya.” Naya
akacheka taratibu akifikiria. “Nakupenda Naya.” Naya
akaanza kulia akijifikiria alikopita na kumbe upo upendo mkubwa hivyo! Akaumia
kugundua alivumilia maumivu bila sababu.
“Niambie
tena.” Joshua akacheka kidogo na kurudia. “Nakupenda
sana Naya.” “Na mimi nakupenda Joshua. Rudi tuwe wote.” “Nitarudi
mpenzi. Niombee huku mambo yaende vizuri.” “Nakuombea
Joshua. Na utafanikiwa sanaaa.” Joshua akacheka. “From
your mouth to God’s ears.” Naya akacheka taratibu. “Naomba
nikuage kwa sasa, nitakupigia nikiwa naelekea hotelini. Na nikikupigia naomba
uniambie ni nini kimekuudhi.” “Usiwe na wasiwasi, mimi nipo sawa.” “Sawa,
lakini pia nitataka kujua. Kuwa mwangalifu huko madukani.” “Na wewe kuwa
mwangalifu ukijua nakusubiria.” “Hilo litaniongezea sababu ya kuendelea
kupambana. Nashukuru Naya wangu.” Naya akacheka
taratibu akifikiria mazungumzo hayo wanafanya na Joshua akiwa njiani, inamaana
Jema anawasikia. Akajisikia vizuri kwamba Joshua hana shida kuzungumza naye
mapenzi akiwa na Jema! Hofu ikapungu kabisa. Wakaagana, Naya akasikia kutulia
kabisa, mpaka hasira zikaisha.
~~~~~~~~~~~~~~~~
Bale
aliendelea kumfuata Naya kwa nyuma kila anapokwenda. Naya alijua kuwa anamfuata
lakini hakutaka hata kumwangalia. Kila alipoingia na yeye alimfuata kwa nyuma.
Naya akajinunulia vitu vyake alivyokuwa akitamani bila kuhofia fedha.
Akamnunulia na Zayoni, pamoja na baba yao, ndipo akahitimisha manunuzi yake kwa
siku hiyo. Akampigia simu baba yake kutaka kujua alipo. Akamwambia atakua
akimsubiria kituoni, nyumbani kwao. Akalifurahia hilo. Akapanda daladala, na
Bale naye akapanda daladala hiyohiyo kurudi kwao bila ya kumuongelesha Naya
mpaka kituoni nyumbani kwao Kiluvya.
Walimkuta
baba yao kituoni. Akampokea Naya mizigo mpaka nyumbani bila kumsemesha Bale,
ila kuzungumza wao wawili. “Mfuko huo wako na huu wa Zayoni.” “Mbona manunuzi
makubwa na mwisho wa mwezi bado, mama! Tutafika kweli?” “Joshua amenipa pesa
kabla hajaondoka. Nikaenda kujinunulia vitu nilivyokuwa nikitamani ila kuhofia
pesa.” Baba yake akafungua ule mfuko. “Asante Naya. Na mimi umeninunulia nguo
za matajiri?” “Sio zote. Shati moja tu la kanisani ndio la pesa nyingi. Vingine
nimenunua kwenye maduka ya kawaida. Lasivyo tungeishiwa.” “Lakini pia
nakushukuru Naya. Asante.” “Na mimi?” Bale alikuwa kama amepuuzwa na wote.
Kimya.
“Zawadi
ya Bale iko wapi?” Akauliza Zayon. “Ndio nani?” Naya akauliza huku akimsaidia
baba yake kutoa zawadi zake. “Zawadi za Bale?” “Kama huna taarifa, huyo sio
ndugu yangu tena. Na sitaki uje unitajie jina lake tena, lasivyo na wewe
utakuwa sio ndugu yangu. Nitakuwa sikuletei zawadi.” Zayoni akajua safari hii
sio utani. “Kwani amefanya nini?” “Anataka kuniuza kwa Malon, ili Malon ampende
awe anampa pesa.” “Naya! Unanitukana.” “Huo ndio ukweli Bale. Na wewe ni mtu mbaya
sana. Hakika sitaki kukusikia.” “Nilitaka kukusaidia Naya.” “Muongo mkubwa
wewe. Unanisaidia mimi au wewe mwenyewe?” “Na mimi nilimuuliza
hivyohivyo. Na ninakuonya Bale. Haraka hizo za maisha na kushindwa kuweka utu
mbele, zitakuponza!” Baba yake akaingilia.
“Baba!
Nataka kusaidia. Unafikiri mimi ndio napenda kwenda maporini?” “Nakuuliza swali
kama analokuuliza Naya. Unayetaka kumsaidia hapa ni nani mwenye shida? Nani
ameomba msaada wako?” “Sio lazima niombwe baba! Nimeona uhitaji ndio na mimi
nimeona naweza kufanya kitu ili kubadilisha maisha ya hapa.” “Kwa hiyo unataka
maisha kama ya Malon?” Baba yake akamuuliza. “Kwamba umemuona amefanikiwa sana,
ndio unataka kuambatana naye, uwe kama yeye?” “Kwa upande wa biashara ni kweli
Malon amefanikiwa baba. Hata wewe ulimsifia. Siku chache nimekuwa naye,
amenionyesha alipo, yule mtu amefanikiwa baba! Na hana roho mbaya. Ameniahidi
kunisaidia mpaka nisimame.” “Sawa Bale. Ila nakuonywa. Kuwa mwangalifu.
Usije kusimama alipo Malon.” “Kwani kuna tatizo gani kusimama alipo!?” Bale
akawa hajaelewa.
“Mwache
baba. Ila naomba umuonye asiwe ananiingiza mimi kwenye harakati zake
zakujigeuza kuwa kama Malon. Na mkumbushe tu, baada ya yote hayo anaweza
kujikuta na pesa, lakini peke yake.” Bale akacheka kidogo. “Nikifanikiwa mimi,
ujue na nyinyi mmefanikiwa.” “Mimi sina shida Bale. Tafadhali katika hangaika
zako usinihesabu mimi. Na katika heshima niliyojipatia kwa Malon, nikumuonyesha
wakati wote mimi namuheshimu na kumpenda yeye kama Malon na wala si mali zake
kama wewe ambaye upo radhi unione nateseka, ilimradi niwe naye ili unufaike.”
“Sijasema hivyo Naya!” “Lakini ndivyo unavyofanya. Unaonyesha mpaka kwa vitendo
kuwa moyo wako wote unamtaka tu Malon, na kufungia moyo watu wengine wote.”
“Unamaanisha
Joshua?” “Ndiyo Joshua. Sijawahi hata kukuomba umpende, lakini unaonyesha
kabisa umemfungia moyo wako, na umekataa hata kujaribu kumfahamu japokuwa
anaonekana ananipenda mimi.” Naya akawa mkali kabisa. “Macho yako na moyo wako
vyote vipo kwenye pesa ya Malon na kukutoa utu. Na upo huru kuniona nateseka
ili ufikie pesa ya Malon!” “Sio kweli Naya. Mimi nakujali, sitaki uumizwe tena.
Naona ni heri Malon ambaye tunamfahamu, na kama ameahidi kubadilika, inamaana
nirahisi kuwa na Malon kuliko Joshua. Kumbuka zimwi likujualo, halikuli
likakwisha.” Baba yake akashangaa sana.
“Subiri
kwanza baba. Wewe unamfahamu Malon kwa kumuona amekaa na wewe hapa na mnakutana
naye kwa sekunde chache! Mimi namfahamu Malon kwa kuishi naye. Ana mwanzo,
mwisho hana. Na...” “Subiri kwanza Naya. Yaani wewe Bale ndio umegeuka kuwa
mwamuzi wa mwisho wa maisha ya mwenzio!” “Mimi namsaidia baba. Asijekuwa
anafungwa macho na vitu fulanifulani na kumsahau Malon ambaye amekuwa naye
tokea zamani. Naya mwenyewe alisema Malon amemsaidia mambo mengi sana.
Anawezaje kumtelekeza Malon aliyejishusha na kuahidi mabadiliko kwa ajili ya
mwanaume aliyekuja juzi tu?” Bale akamuuliza dada yake akimshangaa kabisa.
“Sisi
tutakuwa watu wa namna gani ambao tunajua kujinufaisha tu na watu,
tukifanikiwa, tunawaacha na kuanza na wengine?” “Haa! Ndivyo unavyofikiria
kinachotokea kati yangu na Malon? Ndivyo alivyokudanganya?” “Mahusiano yanakuwa
na changamoto Naya. Sio kukimbia.” Bale akawa na msimamo na yeye. “Kama wakati
wote ulikuwa ukimsamehe Malon. Kinachokushinda kumsamehe sasa hivi ni nini kama
si Joshua tu?” Naya akamshangaa sana.
“Kweli
kabisa Naya. Na nakushauri ujiulize. Ukishindwa na kwa Joshua,
unakimbilia wapi?” “Kwa hiyo wewe ulitaka niendelee kumvumilia Malon mpaka
lini!?” Naya akamuuliza akiwa na mshangao mkubwa sana. “Ameokoka. Ungempa tena
nafasi! Watu wanabadilika Naya.” “Nimekuwa na Malon huyuhuyu unayemtetea wewe
akiwa ameokoka na akiwa hajaokoka! Sijaona mabadiliko yeyote yale! Maswala ya
Rita si yametokea akiwa ameokoka?” “Naelewa Naya. Lakini ukumbuke Malon
hajalelewa kama sisi. Hana maadili kama yetu. Kwa yeye kutaka kuwa karibu na
sisi, ilitakiwa tumsaidie na kumuelekeza njia iliyo sahihi sio kumtupa mbali
kipindi ambacho wote sisi kama wakristo tunajua kuna kukua kwenye wokovu!” Bale
akawabadilikia.
“Nyinyi
mlitegemea nini kwa mtu kama Malon ambaye alikuwa mtaani muda wote akisumbuliwa
na mapepo! Hajawahi kufundishwa na yeyote yule. Nani amfundishe kama sisi
tukimsukumilia mbali?” Naya alishangaa sana. “Kumbe ndio maana umemng’ang’ania
hivyo!?” “Sisi si ni wakristo? Kwa nini tunashindwa kuishi ukristo? Tunashindwa
kusamehe!? Bibilia imeandika tunatakiwa kusamehe 70 mara 7.” “Baba, naomba mimi
nikaoge, nasubiria simu ya Joshua.” “Sawa Bale. Lakini nakuonya uwe mwangalifu.
Angalia usije ukaanguka vibaya sana.” Baba yake akamtahadharisha. “Mimi sifanyi
kitu kinyume na bibilia inavyoagiza. Malon alikuwa akitujali sana humu ndani.
Kwa haja zetu binafsi! Leo tunamtupa! Sidhani kama ni sawa. Najua mnaweza
mkanichukia, lakini huo ndio ukristo.” Naya akaondoka bila ya kumjibu.
“Kwani
baba amemfukuza Malon tena?” Wakamsikia Zayon akimuuliza Bale. “Aaah!
Hajamfukuza ila naona si sawa.” “Labda hujaelewa Bale. Baba hajamfukuza Malon.
Hata juzi yeye ndiye aliyemkaribisha ndani na kumwambia asikae nje peke yake,
aingie ndani. Maana mimi ndiye niliyemfungulia geti. Alipojua wewe na Naya
hampo akasema atakaa tu nje, ndio baba akatoka kuzungumza naye, akamkaribisha
mpaka ndani. Akaja kukaa hapa akampa mpaka chai na chakula kidogo, kilichokuwa
kimebaki. Akakaa hapa mpaka wewe ulipokuja ndio baadaye akaja Naya na Joshua.
Baba hajamkataa Malon, ila Naya hataki kumrudia kama mpenzi wake. Unakumbuka
alipokuwa anaumwa hakwenda kazini, Naya mwenyewe alikwambia wewe uendelee tu na
Malon, ila yeye ndio hataki kujihusisha naye?” “Sasa si kwa sababu ya Joshua!”
“Wewe Bale humtaki Joshua?” Wakamsikia Zayon akimuuliza taratibu tu, ila
hakujibiwa. Bale akatoka hapo ndani kabisa. Akabakia Zayoni asiyependa ugomvi
peke yake hapo sebuleni. Kimya.
~~~~~~~~~~~~~~~~
Pakawa
kimya jioni hiyo. Hakuna aliyezungumza na mwenzie. Hapakuwa na Joshua wala
Malon usiku huo ila ndugu hao tu, ila Bale akijisikia mshindi kuwa amewashinda
familia yake kwa hoja za kiMungu. Amewapa ukweli mtupu uliowafunga midomo. Baba
yao hakuzungumza naye kabisa, akabaki Bale akijindaa kwa safari ya kesho yake.
Aliingia na kutoka chumbani kwake na miluzi. Akiazima hiki na kile kutoka kwa
baba yake vile alivyotumia akiwa Mbeya na Malon. Baba yake alimpa bila tatizo,
mwishoe akamtolea mpaka begi. “Hapo umenisaidia zaidi.” Akaongeza Bale akiwa
amejawa furaha, kama kazawadiwa benki nzima na huyo Malon. Naya alibaki
chumbani kwake akiendele kujifunza laptop yake mpya aliyonunuliwa.
Joshua Tena.
Joshua
akampigia. “Pole mpenzi wangu.” Joshua akacheka kidogo. “Asante.
Ila namshukuru Mungu mambo yamekwenda vizuri. Na nakushukuru na wewe kwa
maombi.” “Nimefurahi kama umefanikiwa. Ndio unarudi hotelini?” “Ndio narudi.
Njaa inauma! Na kesho nina vikao nahitaji kujiandaa. Hapa natamani kuiona sura
yako tu.” “Pole ila ukifika hotelini kula kwanza.” “Na kuiona sura yako?” Naya
akacheka. “Ukirudi utaniona. Ujue nakusubiri.” Wakaendelea
kuzungumza wapenzi hao wawili taratibu wakibembelezana.
“Ni nini
kilikuudhi?” “Husahau tu! Nilivyojitahidi kuchangamka hivyo!” “Niambie?” “Hamna
kitu, usijali. Utakwenda kula nini?” “Huwezi kunitoa kwenye hilo swali Naya.
Nimekuwa nikilifikiria. Nani amekuudhi? Ni kazini?” “Hapana Joshua. Nipo sawa.”
“Sasa hivi upo sawa. Lakini nataka kujua wakati ule ni nini kilikuudhi?”
“Naomba nisikwambie Joshua!” “Ni nini hicho ambacho ni kikubwa hivyo
kiasi cha kunificha?!” “Naomba wewe uangalie mambo ya huko, mimi
huku.” “Hapana Naya. Huko nikunifanya nijisikie dhaifu sana na unanipokonya
wajibu wangu. Nawajibika kwako kwanza ndipo mengine. Nikishindwa kuwajibika
kwako, Mungu hawezi kuniamini na mengine. Tafadhali niambie ili wakati wangu
huku usiwe mgumu. Au ni mambo yanayohusiana na Malon?” Naya
akatulia.
“Alikufuata
tena kazini?” Joshua akaendelea kuuliza. “Naya?”
“Naomba tuzungumze ukirudi Joshua, japo hakuna lakuzungumza. Kila kitu sasa
hivi kipo sawa.” Joshua akanyamaza. “Joshua?” Naya
akaita. “Joshua?” Akaita tena taratibu, Naya akaangalia simu yake akakuta bado
haijakatwa. “Nipo. Ila kama huoni umuhimu wa kunishirikisha, basi.” “Naona sio
kitu cha msingi.” “Kwa nini mimi nisiwe msemaji juu ya hilo? Kitu kinachokuudhi
wewe kwa nini kwangu kisiwe cha msingi?” “Nilikasirika kwa sababu si kwa Malon
kuja, ila Bale kuja naye. Ndicho kilichoniudhi Joshua. Bale anaamini namkimbia
Malon wakati sasa hivi ndipo anaponihitaji kama mimi nilivyomuhitaji wakati
nina shida.” “Lakini yeye ndiye aliyekukataa!” “Asante Joshua.” Hapo Naya
akaona ameeleweka.
“Nashukuru
kwa kulikumbuka hilo, maana inaonekana ni kama namkimbia sasa hivi kwa ajili
yako, wakati wewe ulinikuta ameniacha! Lakini Bale anaona ni kama namtelekeza
sasa hivi wakati ndio ameamua kumpa Yesu maisha! Kwamba ndio kipindi kizuri
tunatakiwa kuwa naye karibu na kumuelekeza njia iliyo sahihi! Analalamika na
kuona ni kama tunamtupa wakati anatuhitaji.” “Malon ndio amesema anawahitaji?”
“Joshua, mimi namfahamu Malon kwa kuishi naye wala si kusimuliwa. Ana
mwanzo mzuri sana ambao sasa hivi ndiko aliko na Bale. Malon si mtu wa
mahusiano jamani! Anajua kujaa kwenye maisha ya mtu mpaka anakulevya kabisa
kisha anakuacha. Na ukiwa naye, anakuonyesha vile ulivyo muhimu kwake
mpaka akikufanyia jambo unashindwa kumuacha unabaki kumsubiria Malon unayedhani
atakuja kuwepo, kumbe hajawahi kuwepo.” Naya akaendelea.
“Mimi
nilikuwa hapo alipo Bale sasa hivi. Nilitaka kumkasirikia sana leo na
nilishamtamkia maneno mabaya sana, lakini kadiri nilivyozungumza naye, na hoja
alizokuwa akizitoa, hakika amenikumbusha Naya wa wakati ule, nikaona si sawa
kumkasirikia Bale kwa kuwa mimi nilikuwa kwenye hicho kifungo kwa miaka mingi
sana. Sikuwa nikiambilika ila kutoa nafasi zaidi na zaidi mpaka nilipoishiwa
kabisa. Lakini katika yote, nilikuwa na pakurudia. Baba. Baba alikuwa kimbilio
langu. Nikilemewa huko, nilikuwa nikirudi kulia kwake na ananiombea.
Nikajiambia kumkasirikia Bale, nitakuja kumuumiza zaidi pindi atakapogeukwa
na Malon, maana naye hana muda mrefu.” “Na Zayoni naye anasemaje?” Joshua
akauliza.
“Zayoni
hapendi kumuumiza mtu na hapendi ugomvi kama mimi na Bale. Akishaona mtu
amekasirika, anakata kauli kabisa. Anashindwa kuzungumza. Yeye yupo kama baba.”
“Kwa hiyo baba anajua?” “Anajua! Kama kawaida yetu tulianza kugombana ndio baba
akatusikia. Amekasirika sana na kumuonya asijewahi kurudia kuniuza kwa
wanaume. Bale anatulaumu mimi na baba kuwa hatuishi ukristo. Hatutaki kumsaidia
Malon akue kwenye ukristo.” Joshua akavuta pumzi kwa nguvu.
“Lakini
ukimsikiliza Bale ni kama anaongea ukweli.” Joshua akaongeza taratibu
kama anayefikiria. “Ukweli mzuri sana na unasikika kiutakatifu kabisa, lakini si
kwa Malon, Joshua. Mimi nisingekuwa mtu wakumtupa Malon kipindi cha shida yake.
Malon hayupo hapa sababu anashida. Hata kidogo. Amerudi kama kawaida yake
anavyoanza jambo. Kurudi, akikuta kuna hitaji basi anaanzisha jambo kwa nguvu
kama hivi kwa Bale. Alirudi kwa kuwa nilimpigia swala la ugonjwa, nikamuomba
jina la dawa, akarudi ndio akakutana na Bale. Amejaa hapa nyumbani kama siku
nyingine zozote anavyokuaga anarudi. Na pia Zayoni amemkumbusha Bale kuwa Malon
hajafukuzwa hapa ndani. Baba alimkaribisha mpaka ndani kabisa, sisi tukiwa hatupo
na alimpa chakula na chai. Hajafukuzwa humu ndani. Lakini ndio
hakuna maswala ya mahusiano kati yetu.” Naya akaendelea.
“Malon hana
shida yakusaidiwa kiroho. Alirudi kwa ajili yangu akiwa na uhakika hata safari
hii nimepata mwanaume wa ajabu kama siku zote ili aanzishe jambo kama kawaida
yake. Sasa amekuta safari hii nimetulia na wewe, halafu unajielewa. Mtu wa
mipango na mimi sina mpango wa kumrudia tena wala kuanzisha michezo yake, ndipo
Bale anaona tumembadilikia Malon kwa kuwa anaona safari hii hatuchezi naye
michezo yake anayopendaga kucheza wakati wote.” “Unamaanisha kurudiana na baba
kukuunga mkono?” Joshua akauliza.
“Si hivyo
tu. Maana nikwambie ukweli tu Joshua. Baba hajanikataza nisirudiane na Malon
ila kunitaka kumuelewa na kuamua kwa hakika. Hata ningesema nimeamua
kumrudia leo Malon, wala baba asingenikatalia kwa sababu hataki kuwa
kwenye nafasi ya kunichagulia kama vile mama. Maana alishaniambia ndoa ni
lazima niwe nimeamua kwa hakika kwa sababu sio yakuingia na kutoka.” “Ambayo ni
kweli.” Joshua akaunga mkono.
“Ndicho
sasa ninachokwambia nilichoka kucheza michezo ya Malon. Anaogopa kujifunga
kwenye mahusiano yeyote yale, zaidi yakiwa yakaribu sana. Hajui na hataki, hata
baba yake anamjua. Akishaanzisha jambo. Akaona linampelekea kwenye kujifunga
kwenye hayo mahusiano, sijui anaingiwa hofu au anajiona hayupo tayari, anajitoa
kwa sababu yeyote ile anayochagua yeye kwa wakati huo. Waliokuwa wanaweza
kumvumilia, tena sio kumvumilia ila kumtumia wakimfuata nyuma kila wakati bila
kuchoka hata Malon akiwa analala na wanawake zao ni wale waliojifanya ni
rafiki kwake ili kujinufaisha naye, kwa kuwa ni kweli Malo ni mtoaji haswa. Si
mchoyo kabisa.” Joshua kimya akisikiliza sifa za Malon tena.
“Ukifanikiwa
kukaa naye meza moja, kama anayo pesa, ujue na wewe hutalala njaa. Hata Chezo
hilo alikuwa akilisema. Kwa mapungufu yake yote, Malon ni mtoaji sana. Kwa hiyo
hata waliokuwa karibu naye wakawa wanalazimishia mahusiano, na yeye alijua wazi
wanamtumia, lakini aliendelea nao ili tu kuwathibitishia kuwa, japokuwa wao
hawakukimbia shule kama yeye, lakini amewapita. Akaishi maisha ya
kuwatawala japo hana shule kama wao, hiyo ikamuongezea kiburi. Haamini kama
anacho kitu cha kutoa kwa mtu ila pesa. Ndio maana akiishiwa tu, anakimbia
watu. Sasa hebu niambie Joshua, maisha yenyewe ndio haya, mambo yanakubadilika,
maisha hayajawahi kuleta uhakika kwa yeyote ila imani tu. Unaweza kuwa nazo leo
kesho huna. Sasa hapo ndio amekuachia pete mkononi, biashara zikayumba,
anakimbia tena. Unabaki na pete kidoleni, umsubirie afanikiwe, umtafute.
Umbembeleze. Kama ukimkuta alifanikiwa na na ameanzisha mahusiano mengine, ndio
usubiri atafute sababu ya kuachana na huyo mtu, umfuate tena,
ndipo akurudie tena. Ndio hiyo michezo mimi nimekataa kucheza,
Joshua. Malon si mtu wa kujifunga kwenye mahusiano. Ingekuwa kutaka kwake, sasa
hivi tungekuwa na yule mtoto wa pili niliyekwambia. Kwamba angeshakuwa amenioa
muda mrefu tu na tulishaanzisha familia. Lakini haikuwahi kutokea, si mtu wa
mahusiano. Hataki kujifunga kabisa, kila siku sisi tunaanza!” Joshua
akatulia akisikiliza.
“Ndio maana
nakwambia hata kwa Bale, nimejutia sana kumsemea maneno mabaya.” “Ulimwambia
nini?” Naya akatulia kidogo. “Naya?” “Nilihisi hajali
hisia zangu. Hafikirii vile nilivyokuwa kipindi nipo na Malon, na utulivu nilio
nao sasahivi nikiwa na wewe! Nikamlaumu kwa mengi na kumkasirikia ni kwa nini
hajakupa wewe nafasi, anamng’ang’ania tu Malon!” “Mimi naungana na wewe Naya.
Mwache kabisa, na wala usimuonyeshe hasira. Ni bora yakamshinde mwenyewe,
kuliko wewe umkatalie, halafu aje akulaumu baadaye. Nimemsikia jinsi alivyo na
matumaini makubwa na Malon. Nashauri muunge mkono kabisa.” “Kivipi?” Naya
akauliza. “Tafuta kutengeneza naye kabla hajaondoka ili apate pakurudia.” Naya
akatulia kidogo kama ambaye hataki kwenda umbali huo.
“Unanisikia
Naya?” “Nakusikiliza Joshua.” “Tena ikiwezekana mpe hata pesa za kujikimu,
asiondoke akiwa hana pesa na mkiwa hamjapata. Unaweza ukakuta wewe ndiye
ulishindwana na Malon, lakini si yeye. Pengine yeye atafanikiwa, hutaki
muharibu mahusiano. Sijui kama unanielewa?” “Nakuelewa Joshua.” Naya
akaitika taratibu. “Lengo ni kutengeneza na wala si kuharibu. Tunataka Bale afanikiwe
sana. Basi muunge mkono. Mengine yaache yatajiweka sawa yenyewe. Sawa?”
“Nashukuru kwa ushauri. Nakupenda Joshua. Nakupenda wewe kama Joshua sio sababu
nataka kukutumia.” “Mimi sioni hivyo Naya. Mimi najua ukweli. Na ninakupenda
sana. Najua yote hayo yanatoka katika sehemu ya upendo tu. Bale anakupenda,
anataka uishie pazuri.” “Nashukuru. Basi acha nikazungumze na baba kisha na
Bale, halafu nitakupigia. Kumbe ni afadhali nimekwambia umeweza kunishauri
vizuri!” Naya akawa anacheka. “Usiwe unanificha mambo!
Tuzungumze tu.” “Sasa hivi nitakuwa sikufichi tena. Nikupigie saa ngapi?” “Sasa
hivi nipo huru mpaka nikiwa nalala. Muda na wakati wowote unipigie. Ukiona
sijapokea ujue naoga, nitarudisha simu yako nikitoka kuoga.” “Sawa.” Naya
akakata na kurudi kwa baba yake.
Kwa Baba Naya.
Alimkuta
amekaa sebuleni ametulia. “Naomba tukazungumze hapo nje, baba.” Baba yake
akatoka naye. Wakaenda kukaa sehemu ambayo kulikuwa na mabanda ya ng’ombe.
“Unakumbuka nilipokuwa na Malon, wewe ulikuwa upande wangu? Vipindi vya vilio
vyangu, ukinibembeleza, kuniombea na kunisubiria nilale?” Baba yake
akamwangalia tu. “Kipindi kile ungeniambia niachane na Malon, pengine
nisingeelewa?” “Uliniambia hutajali hata kama utakuwa ukifanya kazi na pesa
yote unayolipwa uwe unaitumia tu kumtoa yeye jela!” Naya akacheka na kuinama.
Akafikiria kidogo na kuendelea.
“Pale
baba ilikuwa mwishoni mwishoni, lakini tokea tunaanzana na Malon, haikuwahi
kuwa rahisi. Ukiniuliza ni kwa nini niliendelea kuwa naye kwa miaka yote hiyo,
nafikiri na mimi ni miongoni mwa wale waliokuwa wakisubiria kubahatika kwa
Malon. Nikidhani pengine mimi ndiye nitaweza kufanikiwa kuwa wa Malon.
Ninachotaka kusema ni hivi, nilianza kugombana na Bale tokea hatujafika hapa.
Nikataka kumkasirikia sana. Lakini baba, alipo Bale kwa Malon, mimi nimekuwa
naye kwa zaidi ya miaka 5. Hivyohivyo nikimtetea kwa watu wengi tu, kama hivyo
Bale, na wewe nishahidi jinsi nilivyokuwa nikimtetea mpaka kumtafutia
mwanasheria kwa pesa nyingi tu. Ana jinsi fulani yakumpumbaza mtu, unashindwa
kujitoa kwake mpaka Mungu aingilie kati. Naomba tumuelewe Bale, na naomba mimi
niwe kama wewe ulivyokuwa kwangu. Nimsubirie pale atakapohitaji msaada, niwepo
kumsaidia. Na mimi namjua Malon, hana muda mrefu, atamgeuka tu Bale. Sitaki
Bale apotee kwa muda mrefu kama mimi.” Baba yake akawa amemuelewa.
“Sawa.”
“Nakushukuru kwa uelewa.” “Umenishangaza!” Naya akacheka. “Nikwambie ukweli?”
“Niambie.” “Njiani niligombana sana na Bale pamoja na Malon. Joshua alipiga,
akanikuta nalia huku nikienda madukani. Leo amenipa pesa nyingi sana. Sasa
nikakataa kumwambia ni kwa nini nalia, muda huu aliponipigia, akataka kujua.
Akaweka msisitizo mpaka nikamuona ameumia akidhani namficha kwa ubaya.
Nilipomsimulia na kumwambia najilaumu kwa kumchukia Bale, na yeye akaniunga
mkono. Amesema tumuunge mkono tu. Tusimtenge, wala kumkasirikia kwa kuwa nia
yake si mbaya. Ameniomba hata nimpe pesa ya kujikimu na kumuwekea mazingira ya
kuwa chochote kikiwa kibaya huko, awe huru kurudi kwetu, hatutamuhukumu. Kwa
kuwa hatuna nia ya kubomoa chochote ila kujenga. Tena amesema inaweza ikawa
ilikuwa ngumu kwangu kwa Malon, lakini ikawa rahisi kwa Bale. Na Bale
akafanikiwa sana. Kwa hiyo tusimvunje moyo.” Baba Naya akashangaa sana ila
akanyamaza kama kawaida yake. “Acha nikazungumze naye kabla hajaondoka kesho.”
“Sawa.” Naya akarudi ndani na kumuacha baba yake hapo nje.
Naya Kwa Bale.
Akamkuta
Bale chumbani kwao. “Bale!” Bale akamwangalia. “Naomba tusigombane kwa ajili ya
Malon. Najua wote tunampenda Malon na hatutaki kumuumiza. Upo sahihi. Malon
alitusaidia sana. Inawezekana kwenye swala la mapenzi ilikuwa ngumu, au hakuwa
tayari, lakini akawa mzuri kwenye mahusiano mengine.” Bale akawa kama haamini.
“Unisamehe kwa maneno ya ukali niliyokuwa nimekwambia. Sitaki tugombane. Mimi
bado ni dada yako.” Bale akacheka. “Mimi ni dada yako tu.” “Sawa Naya.
Nikifanikiwa utafurahi. Nachukia hii hali hapa ndani! Kama kuna jinsi
yakufanya, kwa nini nisifanye?” “Nimezungumza na baba, nafikiri na yeye
amekubaliana na hilo. Nia yako nzuri. Nakuombea ufanikiwe.” Bale akafurahi sana
asijue dada yake anampa ruhusa ya kwenda kujaribu akishindwa apate pakurudia.
“Asante
Naya. Na tukiwa pamoja hivi, nitafanikiwa tu. Ila ujue nia si kutaka kukuuza.”
Naya akacheka na kukaa. “Acha nikusaidie kufungasha.” Wakaanza stori, ndipo
Zayon akaingia na yeye nakuanza kufurahia vitu vipya alivyonunuliwa na Naya.
Watatu hao wakacheka na kutaniana. Naya akampa pesa Bale. “Ukiwa na uhitaji
usiache kuniambia.” “Nakushukuru sana Naya.” Wakapata wakati mzuri sana usiku
huo, na wakaomba kwa pamoja na baba yao. Kila mtu akarudi chumbani kwake
kupumzika.
Jumamosi Ya Safari Ya Bale Na Malon.
Kama
kawaida yake Naya aliondoka asubuhi na mapema kuwahi ofisini akisindikizwa na
baba yake kituoni. Alimwambia siku hiyo japokuwa anawahi kutoka, lakini
atakwenda kutengenezwa nywele. Alishanunua vazi la jumapili kanisani, Naya
akawa na hamu ya kuweka nywele mpya. Akajiwekea mikakatati ya siku hiyo. Akiwa
kituoni na baba yake, Joshua akampigia simu. “Joshua!
Mbona mapema sana?” “Nakusindikiza kazini.” Naya akacheka kwa
furaha. “Usingehangaika! Nipo na baba kituoni amenisindikiza.” “Basi mimi
nitakusindikiza mpaka kazini.” “Jamani Joshua wangu! Usingehangaika bwana!
Ungelala tu.” Baba Naya akawa anawasikiliza tu, kimya akisubiria binti
yake apate gari, aondoke ndipo na yeye arudi nyumbani. “Nililala
salama, na wewe?” Akamsikia Naya akimuuliza. Gari ikaja, Naya akamuaga baba
yake na kumshukuru, daladala ilipoondoka, ndipo baba Naya naye akaondoka.
Siku
hiyo ikawa imejaa furaha kwa Naya. Amepatana na Bale, na Joshua yupo upande
wake. Pesa anayo, hana shida. Akaletewa nywele nzuri sana pamoja na hereni na
urembo mwingineo. Naya akalipa pesa yote bila kubabaika. Na kweli mpishi wa
Joshua naye akamletea chapati kama alivyomuahidi pamoja na mboga. Akampigia
simu baba yake kuwa Zayoni aende kufuata chakula ofisini kwao kwa kuwa yeye
atapitia saluni kabla ya kurudi nyumbani.
“Lakini na
Bale bado yupo.” Naya akashangaa sana. “Si alisema walipanga
waondoke saa 12 asubuhi? Malon amebadilisha muda?” Naya
akauliza na wasiwasi kidogo. “Nilivyoambiwa na Zayoni ni
kwamba hakuwa akimpata tena kwa simu.” Naya akaumia
sana. “Sasa yuko wapi?” “Zayoni ameniambia amekwenda kumwangalia nyumbani
kwake.” Wakatulia kidogo. “Nitamtuma Zayoni. Naona
nimuache tu Bale.” “Asante baba.” Naya akakata simu.
~~~~~~~~~~~~~~~~
Ilipofika
mida ya saa 11 na nusu jioni Naya ndio akawa anaingia nyumbani
kwao. “Mbona hukunipigia nikufuate?” “Nilijua ungenipotea tu.” Naya
akaongea kwa kujisifu, baba yake akacheka akimwangalia. “Umependeza mama!
Umependeza sana.” “Si ungenipotea?” “Uzuri huo, naujua.” Naya akacheka sana.
“Enzi zinarudi baba yangu. Bale yuko wapi?” “Hajarudi mpaka sasa.” “Mizigo
yake?” “Ipo hapo nyuma ya kochi. Alikuwa amekaa hapa kwenye kochi asubuhi
nzima. Mimi nilitoka mida ya saa nne, nilimuacha amekaa hapo na Zayoni.” Naya
akaumia sana. “Mmependa chakula?” “Nimemsikia Zayoni akila bila kumaliza.”
Naya akacheka. “Na wewe?” “Mimi nitakula usiku.” Akajua baba yake alikuwa
amefunga.
“Basi
acha nikutengenezee chai. Nimekuletea na sendozi zakuvaa kwenye shughuli zako.”
“Utaishiwa Naya, mama yangu!” “Wala si gharama. Acha nikapike chai.” Naya
akaelekea jikoni na kuandaa chai ya nyumba nzima ili kula na hizo chapati.
Akandaa meza kabisa.
Kwenye
mida ya saa moja kasoro Bale akawa anaingia, macho mekundu haswa. “Pole na mihangaiko
Bale.” Naya akamuwahi. “Asante. Njaa inauma kweli!” “Kuna chapati na mchuzi.”
“Wewe ndio umepika?” “Nimeletewa kazini na mpishi wake Joshua. Ila chai
napika.” “Ningeshangaa jinsi ulivyopendeza na mapishi ya chapati ungeyafanya
saa ngapi!” “Baba alikuwa anaomba ili aje tule. Unaweza kuanza kula kama
umezidiwa.” “Acha nisubirie.” Akakaa sehemu ya kulia chakula, Naya akamuona
jinsi alivyonyongea. Akajua tayari ameshatendwa. Hakutaka kumuuliza.
Akaona amuache tu. Walikula kwa pamoja, Bale hakuzungumzia chochote ila
wakamuona anarudisha begi lake ndani kimyakimya. Naya akarudi chumbani
kuzungumza na Joshua, kila mtu akaenda kulala.
Jumapili.
Kwa kuwa
walikuwa na kitafunwa tayari, Bale hakupata shida kuandaa kifungua kinywa
asubuhi hiyo. Wakamuona Naya anatoka kwa haraka, wakashangaa kuona anafungua
geti, gari ya Joshua inaingia ndani. Wakajua Joshua amerudi nchini, kumbe
dereva aliagizwa alate hilo gari na kurudi kulichukua atakapoambiwa na Naya.
Naya alijawa furaha kutumia gari ya fahari siku hiyo! Akarudi ndani na
kuwaeleza ndugu zake. “Itakuja kuchukuliwa usiku. Joshua anataka tuwe na
usafiri wa kanisani na wakutupeleka sehemu tukapate chakula cha mchana pamoja.”
“Joshua anakupenda, Naya!” Zayoni akaongea kwa kumaanisha. “Sana mpaka huwa
namuhurumia.” Naya akaanza kushangilia. “Leo tunaingia kanisani na usafiri wa
maana, na nataka tupendeze.” Naya akawa amepata moyo wa kwenda kanisani, si kwa
ajili ya Mungu, bali kujionyesha.
Na
kweli alitoka amependeza haswa. Baba yake hivyohivyo. Alivaa mpaka saa
aliyonunuliwa na Naya. Nguo nzuri za maana tupu, Naya mwenyewe alifurahi.
Waliingia kanisani, ukweli watu waliwashangaa. Kama sio wao! Zayoni na mwenyewe
alikwenda kunyolewa nywele siku iliyopita, akawa amependeza. Ila Bale alikuwa
amenyongea sana. Walikwenda sehemu ya kula baada ya ibada, wakakaa wanne hao na
kuagiza kila mmoja anachotaka. Hapakuwa na mazungumzo mengi sababu ya Bale kuwa
kimya sana, walikula na kuamua kurudi nyumbani ndipo njiani Naya akampigia simu
Joshua kumshukuru kwa siku nzuri na kumwambia dereva anaweza kwenda kufuata
gari.
Wakiwa
wamekaa tu hapo sebuleni, Bale akaingia chumbani kwake akatoka na vitu vyote
alivyoazima vya baba yake. “Naona sitavihitaji tena. Malon alishaondoka kwenda
Mbeya, na simpati kwa simu.” “Weka tu hapo kitandani kwangu.” Baba yake akajibu
hivyo tu kwa ufupi, ila kwa kuumia. Naya naye aliumia sana. “Inamaana
ameondoka bila kumuaga!” Akaumia sana Naya, na kurudi chumbani kwake.
Akajisikia machozi kumtoka, asijue baba yao ndio analia zaidi ndani ya nafsi
yake akiwahurumia wanae jinsi wanavyohangaika.
~~~~~~~~~~~~~~~~
Zikapita
siku mbili Bale akiwa ametulia tu hapo ndani kama aliyekosa dira. Akawa
ameishiwa morali kabisa. Naya akatoka kazini siku hiyo ya jumanne akamfuata
jikoni. “Bale, ungependa nizungumze na Joshua kama anaweza kukusaidia kupata
kazi hata pale kazini kwetu?” “Kwa cheti gani Naya!? Nimeishiwa nguvu kwa kuwa
niliweka tumaini kubwa sana kwa Malon! Ingekuwa ni rahisi kufanya kazi kwake na
kutengeneza pesa kwa haraka bila maswala yakuingiza elimu. Hata kama ningesema
nitumie matokeo ya nyuma, wewe unajua mimi sio kipanga, Naya. Sina matokeo ya nyuma
yakutisha. Napatiwa kazi wapi, na nani na kwa sifa gani?” “Acha Joshua arudi
tuone. Anasikilizwa sana pale kazini. Wamiliki wa ile kampuni wote
wanamuheshimu sana. Na hata kama sio pale, basi anaweza kutusaidia kwengine.
Unakumbuka kule tulipokwenda kuendesha boti?” Naya akamuuliza taratibu tu.
“Nakumbuka.”
“Ni club ya watu wenye pesa zao na wasomi watupu wenye vyeo
vinavyolingana na yeye. Hawezi kukosa mtu wa kukuunganisha naye.” “Naogopa hata
kuweka matumani Naya! Malon amenigeuka vibaya sana. Sasa hivi naona simu
zinaingia ila hataki kupokea!” “Mungu atatusaidia Bale. Tupambane bila kukata
tamaa. Ipo siku na sisi naamini tutafanikiwa tu.” Bale akanyamaza, Naya akajua
bado anauchungu na Malon.
Mapenzi!
Siku ya
jumatano karibu na siku ya kazi kuisha, akiwa amejiinamia mezani kwake kama
kawaida, akahisi ukimya wa ghafla kwamba hakuna hata stori zilizokuwa
zikiendelea wakati wenzake walikuwa wakizungumza na kucheka bila yeye kuchangia
chochote. Naya akashangaa ule ukimya, akageuka. Alishituka sana kumkuta Joshua
amesimama kwenye sehemu yakuingilia hapo ameegemea. “Joshua!” Naya akashangaa
sana, hakutegemea.
Balada
amfuate, akajikuta anainama na kulia. Watu wote wakashangaa. Joshua akamsogelea
na kwenda kuinama pale alipokuwa ameinamia meza akilia. “Mimi nilitegemea
unikimbilie, unikumbatie!” Naya akaendelea kulia taratibu. “Nimekuletea maua.”
Naya akajifuta machozi na kumgeukia. “Mwenzio nilikuwa nahamu
na wewe mpaka nikaanza kujisikia kuumwa! Kwa nini hukuniambia kama unarudi
leo!?” Naya akalalmika kwa sauti ya chini.
Joshua
akambusu shavuni. “Hujanipigia simu.” Joshua akaanza
kucheka. “Sijakusindikiza mpaka kazini wewe?” “Sasa
baada ya hapo ukawa kimya!” Joshua akamcheka. “Nina
hamu na wewe Joshua! Nilitaka kukuringishia nilivyopendeza, ona sasa
umeharibu suprise yangu!” Joshua akazidi
kucheka. “Lakini yangu imefanikiwa.” “Wala hujafanikiwa!” Joshua
akazidi kucheka. “Mwenzio nimekumiss Joshua!” “Na mimi sana. Twende
basi.” Naya akaanza kucheka kama anayejua ni wapi anapoitiwa. “Muone!” “Nimefurahi
kukuona Joshua! Sikutegemea! Nilijua hutarudi leo!” Bado
walikuwa wameinama. “Kweli umeniletea maua?” “Haya hapa mkononi.”
Naya akakaa akijifuta machozi.
Yalikuwa
mengi na ni aina ya roses tupu. Inanukia vizuri kama rose halisi. Naya akabaki
akiyanusa, Joshua akimwangalia. “Nilikuwa na hamu na wewe Joshua!” Naya
akarudia tena. “Na mimi Naya. Unafikiri kwa nini nipo hapa leo?” Naya
akapandisha mabega akiashiria hajui. “Kwa ajili yako! Vikao vingine nimehamishia
kwa simu. Nilitaka tuje tuwe wote.” Naya akambusu hapohapo tena mdomoni. Joshua
akacheka. “Asante kwa maua.” “Twende.” Wakatoka. “Nilikuwa na hamu na wewe
Joshua! Nilikuwa natamani kukwambia ufanye haraka urudi tuwe wote, lakini
sikutaka kukufanya ushindwe kutulia na kazi. Nimefurahi umerudi.” Wakawasikia
wakizungumza huku wakiondoka.
Wakaelekea
ofisini kwa Joshua. “Sitaki simu Fina!” “Sawa bosi. Kwanza hakuna anayejua kama
umerudi.” “Na ibakie hivyohivyo nitakuwa kazini kesho. Leo sipo kikazi.” Naya
akacheka huku wakiingia ofisini kwake. Alichokifanya Joshua ni kufunga mlango
na kumvuta Naya karibu yake, yakaanza mabusu ya kina. Naya akajitoa kidogo.
“Nilikuwa na hamu na wewe Joshua! Umeshanizoesha kuwa na mimi asubuhi na
jioni.” “Usizoee. Gari yako inakuja.” “Tutafanyaje? Naona kama nimeshazoea kuwa
na wewe! Au nivibaya?” Joshua akacheka taratibu akimwangalia na kumpapasa
shingoni. “Sio vibaya.” “Nakupenda Joshua. Wewe ni wakuaminika.” “Na mimi
nakupenda sana Naya. Nafurahi, nakuona umebadilika. Sasa hivi hata ukisema
unanipenda, naisikia moyoni mwangu.” “Kweli?” “Umebadilika Naya. Nakushukuru
kunifungulia Moyo.” Naya akajilaza kifuani. “Nimefurahi umerudi Joshua wangu.”
Joshua akamkumbatia vizuri wakatulia.
“Bado
natamani kukukiss Naya.” Naya akacheka taratibu kwa deko. “Nilimiss hiyo
midomo!” “Na mimi.” Akanyanyua uso akakuta Joshua akimwangalia. Akajisogeza
midomo yake karibu, Joshua akampokea, yakaendelea mabusu ya muda mrefu bila
kuchoka, Naya akitoa mihemo mizuri kwa Joshua ambaye hakuwa ameshika mwanamke
kwa miaka mingi sana, Naya mzoefu wa penzi. “Natamani unikumbatie hivi tu.”
Joshua akacheka taratibu.” “Nimekuletea zawadi nzuri.” “Zaidi ya hivi!” Joshua
akacheka. “Umependeza sana Naya! Umezidi kuwa mrembo!” “Nimependa ulivyokuwa
ukizichezea nywele huku ukinikiss.” Joshua akacheka taratibu akimwangalia pale
alipojilaza kifuani kwake.
“Kweli
huna kazi zakufanya kwa leo?” “Nimekufuata wewe hapa. Isingekuwa wewe
nisingekuwa hapa. Kwanza nisingerudi leo.” “Nimefurahi umekuja hapa kwa ajili
yangu. Nilikuwa ninahamu na wewe Joshua! Nimefurahi sana. Na asante kwa zawadi
japo sijajua ni nini. Na mimi nilikununulia zawadi.” Joshua akatoa tabasamu.
“Ni nini?” “Mashati yanayofanana na magauni niliyojinunulia. Jumapili
nilipendeza! Acha nikuonyeshe picha.” Akatoa simu na kuanza kumuonyesha. “Kweli
ulipendeza! Aina hii ya Naya sikuwahi kukutana nayo! Ndio unapendeza hivi!”
Naya akafurahi. “Umependa?” “Sana.” “Sasa hujaniona nikiwa kwenye gari yako!
Mpaka Ino akashindwa kunisalimia.” Joshua akacheka sana. “Nilipendeza sana.
Mimi mwenyewe nilijiona.”
“Upo na
kazi nyingi sana?” “Nishamaliza kazi za Jamal. Pale ulinikuta nilikuwa
nikifanya vitu vyangu binafsi. Unataka kunipa kazi bosi wangu?” “Sasa hivi ni
mpenzi wako, kazi ninayotaka kukupa ni kutulia hapa mikononi mwangu,
nikukumbatie tu. Hamu haijaisha.” Naya akarudisha simu mfukoni haraka,
akajisogeza karibu yake. “Mimi mwenyewe nataka kazi ya kukumbatiwa ila na
kubusiwa.” Joshua akacheka sana. “Naya!” “Midomo yako mitamu Joshua! Unajua
kunishika vizuri na kunibusu. Unanichezea nywele vizuri mpaka nimefurahia kuwa
na nywele ndefu! Sikujua kama nilikuwa nikijipunja hivi!” Joshua akamshika tena
vizuri na kuanza kumbusu tena na tena mpaka yeye mwenyewe hali ikawa mbaya.
Akamuachia
na kwenda kuhema pembeni akiwa ameinamia meza yake. Naya akaenda kumlalia
mgongoni. “Nakupenda Joshua.” Joshua akamgeukia pale alipokuwa amemlalia na
yeye akimchungulia. Akavuta pumzi kwa nguvu. “Inabidi tuondoke hapa ndani.
Twende nikakuonyeshe zawadi zako.” Naya akambusu pale alipokuwa amemuegamia.
“Nisindikize nikachukue pochi yangu.” Naya akajiweka vizuri nywele zilizokuwa
zikichezewa na Joshua. Akazifunga kama zilivyokuwa kabla Joshua hajazivuruga.
“Nimefurahia
sana maua. Yale mengine bado nilikuwa nayo.” “Hujayakausha?” “Bado.
Nimebadilisha tena maji. Ila itabidi ninunue vessal nyingine ya kuwa naweka
yakiwa bado fresh, ile uliyoninunulia ni ya kutunzia yakikauka.” Joshua
akacheka kidogo, wakatoka hapo. “Kesho Fina.” “Mimi sijaletewa zawadi?”
Akauliza akicheka. “Anayo Jema.” Akajibu Joshua akiondoka, Naya akamsikia Fina
akishangilia. Wakaelekea ofisini kwa Naya, akamsubiria akifunga laptop yake.
“Kiongozi
nimeambiwa umerudi?” Akaingia Jamal akikimbia. “Bado.” Joshua
akajibu kwa haraka nakumfanya Jamal acheke. “Maana hamkawii! Mimi nipo hapa kwa
ajili ya Naya tu. Kazini kesho.” “Jambo dogo tu. Najua ukiweka neno wewe, IT
watachangamka.” “Bado unasumbuana nao tu!?” “Huoni nimekimbia niliposikia upo mjengoni?
Nisaidie kaka. Wale hawatafanya mpaka uwaambie.” “Unaniharibia mipango yangu
Jamal!” “Kwani utaongea sana? Wala huna haja yakutoka hapo ulipo simama,
nakusogezea simu hapohapo.” “Halafu Fina nilimwambia mimi leo sipo! Kwa nini
ametangaza kama nipo?” “Anaijua shida yangu, Kiongozi. Nikunihurumia tu. Sema
neno moja tu, wanipe haki yangu.” Joshua akamwangalia Naya.
“Nivumilie
Naya wangu.” “Usijali.” Naya akavuta kiti na kukaa. Jamal akamvutia simu ya
mezani. “Mwambie Fina ampigie Ayush, kisha aniunganishe naye.” “Hapo umemaliza.
Maana ukiongea na Ayush mwenyewe, itakuwa umeua mzizi wa fitina.” “Muda Jamal!”
Joshua akasisitiza. Jamal akampigia Fina. “Naomba muunganishe Kiongozi
hapa na Ayush.” “Dakika moja.” Fina akajibu. “Ni wewe
mwenyewe au!? Maana nimeambiwa upo safarini.” “Ni mimi. Unanikwamisha Ayush.” Jamal
akalifurahia hilo. Akabaki akisikiliza. “Ni nini tena!?” “Issue ya
Jamal ipo kwenu zaidi ya week sasa, mnategemea afanyeje kazi na wewe unajua
namtegemea sana?” “Hilo sikujua Kumu. Acha nifuatilie.” “Naomba likamilike
tafadhali.” “Bila shaka.” Ayush akajibu na sauti yake ya kihindi. Joshua akakata simu.
“Si
umeona Mkuu. Maneno machache tu, mimi kesho napewa haki yangu.” Joshua
akamtizama na kumgeukia Naya. “Twende.” Jamal akacheka. “Nakushukuru lakini.”
“Umeniharibia mipango yangu.” “Mbona Naya mwenyewe hana shida Kiongozi! Naya
anajua tatizo langu.” Joshua hakumjibu, akamshika Naya mkono nakutoka.
Naya Na Joshua Tena.
“Unataka
twende wapi?” Joshua akacheka. “Unataka unitoe?” “Popote unapotaka. Mimi
nitalipa. Nimefurahi umerudi kwa ajili yangu Joshua. Nilikuwa na hamu na wewe!”
Hilo Naya alilirudia bila kuchoka. “Na mimi Naya. Sasa hivi naanza kuchukia
kuishi mbali na wewe.” Naya akacheka kidogo na kuinama. Joshua akatoa gari.
“Unafikiria nini sasa?” “Sijui.” “Acha bwana Naya.” Naya akacheka kidogo akiwa
anafikiria. “Nini?” “Nafikiria maisha yakuja kuishi na wewe.” “Unafikirije?”
Joshua akamuuliza. “Naogopa hata kufikiria.” Joshua akakunja uso. “Kwa nini
tena?” Naya akacheka kidogo. “Naona kama wakati mwingine sikustahili Joshua!
Halafu naogopa usije ukanizoea ukaanza kunipuuza.” Kidogo Joshua akaridhika alidhani
Naya hamtaki.
“Cha
kwanza ujue mimi ni wako Naya. Hilo nina uhakika nalo, sina wasiwasi nalo.
Pili, sijitahidi kukufanyia chochote na mimi sio mwigizaji. Hakuna kitu
nakufanyia cha maigizo ili tu kukuvuta kwangu. Hapana. Nafanya kwa kuwa nakupenda.
Namuomba Mungu anisaidie nisipelee ila kunipa hekima ya kuishi na wewe kwa kila
hatua ya maisha yetu. Ukiwa mchumba, mke na mama. Ila kwenye kuwa mke, hapo
nitaomba tusubirie kwanza watoto. Nataka nibaki peke yangu kwanza kwa muda
kabla watoto hawajaja na kukuchukua mwili na akili.” Naya alicheka mpaka
akajifunika uso.
“Joshua!”
“Nakuwa mkweli na nimewahi mapema. Acha nikufaidi mimi kwanza, ndipo lije swala
la watoto.” “Kwa muda gani?” “Kama unayo haraka ya watoto, basi nipe mimi miaka
hata miwili tu. Iwe mimi tu. Akili na mwili wako vyote vije kuwa vyangu tu.
Baada ya hapo, hata ukitaka kuzaa mchana na usiku, sina neno.” Naya alicheka
sana asiamini mipango ya Joshua. Alimwangalia na kurudia kucheka. “Mimi
nimekuwa mkweli. Nimeeleza haja yangu.” “Acha Joshua.” “Kweli Naya.” “Sasa
unataka tuanze tu kwenye ndoa, na uzazi wa mpango?” “Hata kabla ya harusi.
Naomba tutafute mtaalamu wa kutushauri. Tufanye yote. Ili tukiingia kwenye
ndoa, tusiwe na wasiwasi.” “Lini?” Naya akauliza taratibu, Joshua akacheka na
kunyamaza. Naya akashangaa ila hakutaka kulazimisha, akaona anyamaze kwa kuwa
alijua amemsikia.
Wakatulia
kimya Naya akiwa amejiinamia. Ghafla akajisikia kukosa raha. Akahisi Joshua
hataki kuja kumuoa kwa haraka. Akajua yatatokea yaleyale yakuja kuachwa kama kwa
Malon, mahusiano yasiyo na mwisho. Akabaki ameinama, ameshikilia maua yake.
“Unataka tupitie vessal sasa hivi?” “Abee!” Ikawa kama amemtoa kwenye mawazo.
“Kifaa chakuwekea hayo maua?” Naya akabaki kama hajaelewa. “Mbona mawazo
yamehama tena?” “Samahani, sikuwa nimekusikia tokea mwanzo. Kifaa cha nini
tena!?” Naya akawa kama amechanganyikiwa kabisa.
“Ni sawa
tukienda sasa hivi kununua kifaa chakuwekea maua yakiwa mabichi?” “Hapana.”
Joshua akawa hajamuelewa. “Hapana tusinunue!?” “Ndiyo.” “Naya! Sikuelewi mpenzi
wangu. Tukanunue sasa hivi au tusinunue?” “Sio lazima kununua sasa hivi. Naweza
hata kununua wakati mwingine.” “Leo utayaweka kwenye nini?” “Jagi. Tunalo
jagi.” “Kama hutajali, basi naomba tupitie sasa hivi.” “Sawa.” Naya akajibu na
kutulia kabisa.
Joshua
akaendesha mpaka sehemu ya kupata kifaa, wakanunua. “Nimependa. Asante. Ila
nilitaka kulipia. Sikutaka kukuongezea tena gharama.” “Usijali. Upo sawa?”
“Nipo sawa kabisa.” Naya akajibu na tabasamu la wasiwasi usoni, Joshua
akamuona. “Ila naomba ule kabla hatujaachana, Joshua. Kama hutakubali chakula
cha kununua, basi niahidi utakwenda kusubiria chakula cha nyumbani. Angalau
ulale nikijua umeshiba.” Ilimgusa sana Joshua. “Sawa. Naomba nikasubirie
chanyumbani ili nipate muda na kina Zayoni pia.” Naya akacheka kuonekana
ameridhia. “Si ni sawa?” “Ningependa hilo, japo nahisi wanakuogopa kidogo.”
“Nimeliona hilo.” Wakaanza safari yakurudi kwa kina Naya.
“Kwani
tofauti yangu na Malon kwao ni nini?” Naya akacheka akifikiria kidogo. “Kwanza
ujue Malon ni mtoto wa mtaani, aliyefanikiwa. Anamjua binadamu kwa kuishi
naye.” “Mbona ni kama mimi tu.” “Wewe ulikwenda shule, na ukakusudia kubadili
maisha kwa uzuri. Upo kujenga jamii. Malon hakurudi shule, yupo kuthibitishia
jamii shule si kila kitu, na alijitahidi kuifikia jamii kwa kuiharibu.
Hiyo ndio tofauti yenu. Alihakikisha anatenga muda wakutosha mtaani, kumfikia
mwanamke na mwanaume kuonyesha shule si kila kitu ndio maana wanawake zenu bado
wanaweza kulala na yeye muda na wakati wowote anaotaka yeye.
Akawaonyesha haohao wanaume kuwa, shule zao si kila kitu kwa kuwa bado
haziwasaidii kukidhi mahitaji yao ya muhimu. Aligawa pesa kwa kadiri ya uwezo
wake, japo pia amejaliwa utoaji. Anao muda wakutosha kumfikia mtu yeyote yule
amtakaye. Mama yangu alimuonyesha hamtaki sababu hakusoma. Na yeye
akamuonyesha yeye ni bora kuliko wanaume wote wosomi waliokuwa
wakinitaka. Ndipo akajaa pale nyumbani. Yeye mwenyewe na pesa yake.” “Hapo
nimekuelewa.” Joshua akacheka.
“Huwezi
kushindana na Malo kwa kuwa yeye alitaka ushindani na kudhihirishia watu
hajaharibikiwa. Alichokiacha kwa ndungu zangu sasa hivi, ni majonzi kama
waliompoteza ndugu wa maana, wakati ni Malon! Mimi namjua. Atakuja kurudi tu.”
“Haiwezekani Naya!” Naya akacheka. “Mimi namjua Malon. Na ninashukuru kunitia
moyo kuwa karibu na Bale. Amemuumiza sana Bale. Nilikwambia amemuacha kama
amepigwa na butwaa?” “Bado tu!?” “Utamuhurumia Bale. Na ninahisi ameingiwa hofu
kwa baba, maana alitusema vibaya sana mimi na baba. Na ubaya wa baba si
mzungumzaji kujua la moyoni. Heri ingekuwa mama. Angemsema, yakaisha. Ila baba
amenyamaza kimya wala hajamuuliza ni kwa nini hajaondoka. Hajamuuliza chochote
kile mpaka natamani kumuomba baba angalau azungumze naye, ili atulie. Hali wala
hazungumzi. Unaweza ukamkuta amekaa pale mezani, ameangalia sehemu moja bila
hata kusogea.” “Lakini subiri kwanza Naya.” Joshua akawa kama hajaelewa.
“Huyu
Malon unasema anaweza kurudi tena!?” “Tena na sababu inayosikika vizuri
mno. Itakayoeleweka na ukamuunga mkono. Sijui aliumbwa vipi Malon! Lakini
ndivyo alivyo. Na akirudi ndio anakuwa vile kama unavyomuona. Mwingi mno.
Anajaa kila mahali na kwa kila mtu mpaka mjisikie vizuri. Anarudi na mipango
mizito kama vile ulivyomuona kwa Bale. Ikifika sasa karibu. Akaona itamfanya
ajifunge kwako. Ikawa ni jambo la muda mrefu. Sio la muda mfupi. Ukamuwekea
mipango ya kudumu kama vile Bale mpaka sijui kufanya biashara naye ikawa kubwa,
sijui huwa anaingiwa hofu, sijui ni roho chafu inakuwa inamuingi! Anakimbia.
Kwa sababu nzuri tu.” Joshua akachoka kabisa.
“Wewe
kweli mvumilivu Naya. Mimi mtu mwenye sababu siwezi. Nachoka haraka sana.”
“Wanakujua pale kazini.” “Basi nafikiri ni kote. Hata huko nilikotoka.
Ninapoacha jambo lifanyike, ukakubali utalifanya kwa muda tuliokubaliana, huwa
nataka matokeo. Hata yawe mabovu, yawepo tu. Si maneno matupu! Hapana. Hata
wale makaburu wameshanijua. Na huwa nahakikisha wanaelewa tulichokubaliana.
Sitaki kupotezewa muda.” “Joshua! Mpaka huko kwa wazungu?” “Kwani uzembe ni rangi
ya mwili?” Akamuuliza.
“Hauchagui
unazungumza lugha gani au una rangi gani ya mwili. Yuko jamaa alisemaga huu
usemi, nikauelewa sana. Alisema hivi, unaweza ukawa mweupe, yaani mzungu,
lakini ndani yako ukawa mweusi kabisa akimaanisha kujawa giza lakupita kiasi. Uzembe
ni roho inayofanya kazi ndani ya mwanadamu bila kuchagua. Zipo sababu
100 zakutowajibika, lakini huwepo moja au mbili za kuwajibika. Ndipo
ujue ni wapi mizani hulemea.” Joshua akaongea.
“Sipendi
kufanya kazi na mwanadamu awaye yeyote yule, mwenye kupenda kutoa sababu ya kwa
nini ameshindwa bila hata kujaribu! Hapana. Na huwa sijali rangi yako ya
mwili, nitakwambia kabisa. Unanipotezea muda wangu. Kwa hiyo hata kule
wakiniita, huwa wanajiandaa. Sitaki nifike kule, waanze kunikwamisha kwa sababu
zozote zile! Hapana. Ni bora tokea tunapanga mimi na wewe, uniambie kabisa.
Muda tuliokubaliana, hautakutosha. Unataka tuongeze, hapo sawa.
Ila ukishasema ndiyo, napenda ubakie hapohapo. Na ikishindikana wakati wa kazi,
nijulishe kabla ya ule muda, maana huwa najua kuna mambo huwa yanatokea. Lakini
sio sababu kama zile za Jamal! Hata yeye anajua namuhesabia tu. Nikimbadilikia,
hataamini.” “Joshua!” Naya akashangaa sana.
“Naya!
Nimeaminiwa na kampuni kama ile, unafikiri tungekuwa hapa leo kama ningeruhusu
mambo kama hayo!?” “Lakini kweli.” “Siwezi. Juzi Njama alimtuma
mwanasheria wake aje amuombee msamaha pale kwenye kampuni.” “Joshua!” “Kabisa.
Amegonga mwamba. Wameona hana kesi ila yeye ndio alishitakiwa kwa kufanya fujo
na kutukana. Wapi watamuajiri tena?” Naya kimya. “Hakuna.” Joshua akajibu
mwenyewe. “Tabia mbaya zinaenea kwa haraka Naya, kuliko njema. Sasa hivi Njama
anafahamika kwenye hayo makampuni kwa matusi aliyotukana ofisi ya Mwajiri na
mpango wake wakutaka kufilisi kampuni ili ajinufaishe. Waliponiuliza
kama naweza kumsamehe na kumrudisha, kwa haraka sana niliwaambia nafasi yake nimeifuta,
siajiri mtu kwenye kitengo changu, nataka kupunguza. Hayo niliyajibu
kupitia Jema, nilipokuwa safarini. Jema anasema ameambiwa na Fina, wote pale
wamejawa hofu ndio maana umemuona Jamal ameniwahi na kuuza kesi.” “Joshua!
Kumbe!” Joshua akacheka akitingisha kichwa.
“Jamal
mjanja sana. Alijua kama ni kupunguza watu pale, ningeanza na yeye. Jema
ameniambia amekuwa akitumiwa ripoti ambazo hata hajaomba.” Naya akaanza
kucheka. “Sasa ripoti za nini?” “Basi tu, kuonyesha kila mmoja yupo kazini.”
“Kwa hiyo ni kweli umefuta nafasi ya Njama?” “Kabisa. Hata ofisi yake sasa hivi
haina kitu chochote kile. Nilimwagiza Fina, isafishwe kabisa, iachwe tupu
wakati nikifikiria nini chakufanya.” “Sasa nani anafanya majukumu yake?”
“Nafanya mwenyewe.” “Hulemewi?” “Ndiyo na hapana. Sijapata mtu kama Njama.
Nikikimbilia kuweka mtu, nitalemewa zaidi. Nitakuja kuijaza, lakini sio sasa
hivi. Nataka kupata mtu sahihi kama Njama. Njama alikuwa mtu wa kazi. Mwepesi
na muelewa. Mapungufu yake yalikuwa yakawaida tu kama mtu mwingine yeyote yule,
lakini alikuwa akinirahisishia sana kazi. Ile fujo ya juzi ya watu
kutomaliza ripoti kwa wakati, isingetokea kama Njama angekuwepo. Njama
alikuwa akiwaweza, na mkali kwao bila kujali umri ila kazi tu.” Naya akataka
kuuliza sasa ni kwa nini hamsamehi Njama na kumrudisha kazini, lakini akaona
anyamaze tu.
Wakawa
wamefika nyumbani, Naya alishampigia simu baba yake akimuomba Zayoni
awafungulie geti. Wakakuta lipo wazi. Joshua akavuta gari mpaka ndani.
“Nisubiri wakati nakuandalia chakula.” “Na wewe?” “Mwenzio siku hizi nakula
chakula cha nyumbani kwake Joshua Kumu. Naletewa mpaka kazini!” Joshua alicheka
sana. “Naya!” “Nakula chakula anachopika shefu mwenzio! Usiniletee
mchezo.” “Kweli wewe sio mwenzangu. Sasa usiku?” “Usiku nakula vitu vyepesi.
Asubuhi kifungua kinywa cha baba Naya, basi.” “Hutaki kunenepa?” “Ulijuaje?”
Wakashuka garini wakicheka.
“Karibu
ndani.” Naya akamkaribisha akiwa amebadilika. Ile hali ya ukimya na
kuchanganyikiwa aliyoipata kwenye gari baada ya Joshua kutojibu swala la
ndoa, ikamuisha kabisa. Akatulia. “Njoo kwanza Naya.” Naya akarudi upande wa
Joshua. “Kuna zawadi hii ya Zayoni. Yakumpongeza kwa kufaulu vizuri. Mwambie
inatoka kwetu wote.” “Jamani Joshua! Ni nini?” “Angalia. Ulisema anapenda
kupiga picha. Nimemnunulia kamera.” Naya akafungua na kushika mdomo kwa
mshangao. “Itafaa?” “Sana. Kikamera tulichomnunulia na Malon, kiliharibika
mapema sana. Nahisi haikuwa na ubora mzuri. Asante Joshua.” Naya akambusu
shavuni. “Karibu. Na wewe zawadi zako zipo kwenye hiyo mifuko mingine.” “Nakushukuru
sana Joshua. Asante.” Wakasaidiana kutoa mizigo garini, ndipo wakaingia ndani.
~~~~~~~~~~~~~~~~
Walimkuta
Bale amekaa mezani kama kawaida yake, ila peke yake. Zayoni sebuleni na baba
yake, lakini kimya wote macho kwenye luninga. Naya akapitiliza chumbani kwake,
akamuacha Joshua nyuma. “Umerudi Joshua?” “Ndiyo Zayoni. Nimerudi. Naya
ameniambia matokeo yametoka, umefaulu vizuri sana.” “Ndiyo. Ila sitaki kwenda
shule za bweni. Nataka kusoma hapahapa kama Bale. Baba amesema ataenda kunifanyia
mpango, wasinipeleke mbali.” “Hongera sana.” “Joshua amekununulia zawadi ya
kufaulu.” Naya akaongea akiwa chumbani. “Ni kutoka kwangu na Naya, sio mimi
peke yangu.” Wakamsikia Naya akicheka.
Akamsalimia
baba Naya. “Marahaba Joshua. Naona umepokelewa na maneno mengi ya Zayoni.”
Wakacheka. Zayoni akamfuata dada yake. “Niingie Naya?” “Subiri kwanza.
Usiingie. Kama ni zawadi nakuletea hukohuko.” Zayoni akasimama mlangoni
akisubiria. “Vipi Bale? Upo mzima?” “Nipo.” Bale akasimama kwenda kumpa mkono.
“Karibu.” “Asante.” Joshua akatafuta sehemu akakaa. “Vipi lakini? Mapumziko
yanakwendaje?” Joshua akamuuliza Bale pale alipokuwa amesimama. “Hivyohivyo
nipo tu. Nilikuwa na mpango wa kwenda kufanya biashara na Malon, sijui nini
kimetokea, naona hata simu zangu hapokei tena.” Bale akajikuta anaongea hapo
mbele ya baba yake akimwambia Joshua.
“Nimekuwa
kama nimepoteza dira! Sijui niseme nimechanganyikiwa au vipi? Nimekwama.”
Akajieleza Bale akisikika kupoa haswa. “Hutakiwi kukata tamaa. Huo ni mlango
mmoja tu uliojifunga kati ya mingi inayokusubiria.” “Nahisi hata nimepoteza
lengo.” “Haitakiwi iwe hivyo Bale! Lengo lazima libakie ila njia ndio imefunga.
Na sio mwisho. Tafuta njia nyingine kufikia hilo lengo. Hakuna kitu rahisi
Bale. Usikate tamaa ila fikiria zaidi.” “Daah! Ndio nafikiria lakini nahisi
nipo kwenye mshituko bado.” “Inaeleweka kabisa, ila usikae hapo kwa muda mrefu
kwa kuwa unajichelewesha kufikia milango mingine.” Joshua akapata
ujasiri wa kuzungumza naye.
“Nilikusikia
ukiwa unazungumza na Naya, ulikuwa na malengo mazuri sana. lazima uhakikishe
unapambana kufanikisha. Nina uhakika biashara ya mazao ni wengi tu wanafanya.
Swala ni wanafanyaje?” “Ile ya Malon ilionekana rahisi kweli! Na ingefanikiwa
kwa haraka.” “Sasa haipo tena.” Akadakia baba yake. “Utakaa ukiwaza hapo juu ya
Malon mpaka lini?” Baba yake akamuuliza kwa ukali kidogo.
“Nahisi
niliweka tumaini kubwa sana kwake. Naomba unisamehe baba.” Pakazuka
ukimya wa ghafla. “Niliongea maneno yasiyo mazuri kwa kuwa nilimwamini sana Malon.
Lakini nimejifikiria, nimeona nilikukosea baba yangu, naomba unisamehe.” Bale
akaanza kutokwa na machozi. Akamgeukia tena baba yake akiomba msamaha. Naya
akatoka akiwa amebadili nguo, amevaa tu kigauni cha nyumbani. Lakini akapendeza
na nywele akavuta juu kabisa, akazibana zikawa zikining’inia na mawimbi mazuri.
Akavaa na hereni nyingine sio kama alizovaa akiwa kazini, akaenda kupiga magoti
pembeni ya baba yake. Akamvuta mkono na kuuegamia. Lakini baba yake alijua
anamuombea msamaha Bale.
“Ni
nini?” Baba yake akamuuliza. “Mimi nakupenda baba Naya.” Baba yake akabaki
akimwangalia Naya pale alipojiegemeza. “Nimekosa baba, naomba
unisamehe. Lakini nia ilikuwa nzuri baba yangu.” “Umeniudhi sana Bale.
Nimechukia kutaka kumrudisha Naya kule ulikokuwa ukimuona akiteseka! Yote hayo
sababu ya maendeleo! Hapana Bale. Isiwahi kurudia tena. Usiwahi kuuza
binti yangu sababu ya pesa. Iwe nikiwa hai au nimekufa, shida
isikopotezee utu. Nilikwambia kabla, lakini hukunisikiliza, ukaja kunigombeza
hapa mbele ya binti yangu, nikiwa nimeshakwisha kukuonya!” “Nisamehe
baba.” Bale akapiga na yeye magoti. Joshua kimya akabaki amenyamaza
kama Zayoni.
“Nimekukosea
baba yangu. Na zaidi nilikosa adabu kwako. Nisamehe. Lakini nimejifunza.
Naogopa naona kama nimejilaani! Kuanzia sasahivi nitakuwa nikikushirikisha kama
Naya, ili uwe unanishauri, nisipotee tena. Nimekosa baba.” Naya
akamuegemea baba yake zaidi. Akamwangalia. Akamuona na yeye Naya anaanza kulia.
“Nimekusamehe. Na wewe acha kulia, nenda kaandae chakula, mwenzio ale kabla
hajaondoka.” Naya akaanza kucheka taratibu akisimama. “Asante
baba. Hakika nimejifunza.” Bale na yeye akasimama. “Labda Naya
angenipa kabisa zawadi yangu, baba.” Zayoni akaongea kwa kujihami kama
asiyetaka kuharibu. “Zayoni naye!” “Si mara moja tu Naya?” Naya akaenda
kumchukulia. Pakatulia kwa muda.
“Labda
niulize kama naruhusiwa.” “Karibu Joshua.” Baba Naya akamwitika kwa kiungwana.
“Wazo la biashara ya mazao, linatoka kwa nani?” Pakazuka ukimya kidogo, na
Joshua naye akatulia kuwapa nafasi. “Labda niseme ni kwangu.” Akajibu baba
Naya. “Kuna kipindi nilikwenda kufanya kazi kwa Malon, nikaona ni biashara
nzuri. Niliporudi hapa, nikawaeleza vile alivyofanikiwa Malon kwenye hilo eneo.
Nafikiri ndipo hapo Bale napo akapata hilo wazo. Ila jinsi ya kufanya na sisi
ndio imekuwa changamoto. Lilianza swala la eneo. Eneo hilo ni kama
linakamilika, sasa pakupata bidhaa ndio ikawa changamoto.” “Kwa hiyo kama
nimeelewa sawasawa mzee wangu, bado ni kitu ambacho unafikiri ungependa
kifanyike?” Joshua akauliza tena. Naya akisikiliza akiwa jikoni. Alikuta Bale
alishapika, akaanza kuandaa meza huku akipasha moto.
“Sio
biashara mbaya. Ikifanywa kwa njia sahihi. Ukweli inalipa. Na uzuri biashara ya
mazao si ya msimu. Watu wanahitaji kula kila siku.” Joshua akacheka. “Ndivyo
anavyozungumza jamaa mmoja. Nilimwambia Naya nitakwenda kumtambulisha kwake na
familia yake. Nikija wa kama huu umri wangu tu. Lakini baba, yule kijana amefanikiwa.
Mimi nikikwambia mtu amefanikiwa, simaanishi mafanikio yakuweza kubadili mboga
nyumbani.” Baba Naya akacheka na kugeuka vizuri ili kusikiliza.
Kisha
akauliza. “Na ni biashara ya mazao tu?” “Mazao na sasa anakusanya na mafuta.
Aliajiriwa na BOT, lakini akaacha kazi. Anafanya hiyo biashara akisaidiana na
mkewe. Baba Naya?” Joshua akaita kwa kuhamasika. Mpaka wote wakacheka. “Ndiyo!”
Baba Naya akaitika. “Wamefanikiwa! Wamefanikiwa mno. Mimi namtania kwa
jina la GM, lakini anajulikana kama Geb Magesa, wengi wanamuita Magesa tu. Na
mkewe anaitwa Nanaa. Mtulivu sana huyo jamaa. Sana. Ile mkimya wakupitiliza,
ila anaakili na yenyewe niyakupitiliza. Akiongea lugha ya biashara,
utaelewa ni kwa nini amefanikiwa.”
“Anafamilia
nzuri mno. Nilimfahamu kupitia shemeji yake, lakini nilihakikisha ananisogeza karibu
yake kwa vile alivyo mtu wa familia. Anaishi na mkewe kama ndio anataka kuomba
kuoa! Jicho lake lipo kwa mkewe muda wote, wakati wote. Popote walipo jicho
lake litamfuata mkewe. Na Nanaa mkewe, anajua kama mumewe anampenda. Ni
binti mdogo tu, lakini ametulia kwa mumewe. Anaonekana ana upendo, na huwa
ananitania na kuniambia, hana mazoea kwa mpenzi wake. Na nafikiri
ndio siri ya mafanikio ya ndoa yao. Ni mama wa watoto watatu, lakini mtulivu
haswa. Anampenda mumewe na familia yake kupita maneno nitakayo kwambia ukaelewa.
Ameweza kujichanganya katikati ya ndugu wa Geb, utavutiwa tu. Wanaishi
na mama yake Geb. Ukiwa nao, unaweza sema mama G ni mama yake Nanaa!
Wanaelewana sana. Hakika utapenda familia yao.” Joshua akasifia.
“Sasa
huyo ndiye anayezungumza kama wewe baba. Biashara ya chakula si ya
msimu.” “Ni kweli. Wao wanafanyaje?” “Anayo malori yake, na maofisi pamoja na
maghala huko mikoni na hapa mjini pia. Wanamkusanyia mazao, na kuleta huku
mjini. Anasema alianza hapa Dar, lakini sasa hivi hapa pamekuwa ni eneo la
kuyakusanya, anafungasha kwa muundo wake yeye, na kusambaza. Mimi mwenyewe
mchele wangu, aina yote ya mafuta yakupikia nanunu kwao.” “Au ndio hawa mifuko
yao imeandikwa Magesa LtD?” “Haohao.” “Bale anapenda kweli mchele wao, japo
gharama!” “Basi hata ubora wake upo juu.” Wakabaki wakizungumza baba Naya na
Joshua, wakipokezana maneno.
Kwa
kumsikia tu baba Naya hapo, ungejua amemfungulia moyo Joshua. “Sasa acha
nitazungumza naye kesho. Maana kama nilivyokwambia, yeye ni mtu wa familia
sana. Mida kama hii ngumu kumpata, anakwambia anacheza magari na watoto wake.”
Baba naya akacheka. “Kesho nitazungumza naye, nione jinsi anavyoweza kukusaidia
mzee wangu.” “Nitashukuru sana Joshua.” “Karibu.” Bale akabakia kimya pembeni
ya kiti cha Joshua.
Joshua
akamgeukia. “Sasa Bale?” “Mimi nimekwama. Vyeti bado havijatoka, naona na
biashara imegoma!” “Kuna mambo mawili. Unaweza kuamua kufanya na baba hiyo
biashara ya mazao, japo ningemshauri baba aongeze na mafuta.” “Mtaji Joshua!” “Upo
na mtu mkubwa sana humu ndani mzee wangu! Mfanyakazi wa Coca! Huwezi kukosa
pesa.” Naya akacheka sana. “Usiniangushe bwana Naya!” “Sawa bosi wangu. Tumeni
maombi.” Bale akaanza kucheka. “Basi hapo pumu imepata mkohozi.” “Wewe kama
unashida, tuma maombi nikufikirie.” “Sawa Naya.” Bale akakubali.
“Joshua,
umesema mambo mawili, lapili ni nini?” “Lapili kufanya kazi. Wakati mwingine
unaweza kupata kazi kwa kufahamiana tu, si lazima vyeti. Vyeti ni utaratibu
tu.” “Sasa nani ananifahamu mimi, Joshua?” “Kwanza jua unataka kufanya nini.
Hilo ndilo la msingi. Mimi nilijua sitafanya biashara, ila kuajiriwa.
Nikahakikisha nakua kwenye soko la ajira. Kutafuta uzoefu, ndio maana nilikuwa
nikisoma nikiwa kazini. Uzoefu ndio umenifikisha hapa kuliko hata
elimu. Sijui kama unanielewa.” “Nahisi.” “Ubora ndio utakufikisha mbali. Ni
rahisi mimi kukuamini nikakupa kitengo nikijua nikisafiri kitengo kitabaki
salama kwa mtu anayejua kitu gani chakufanya, kuliko mwenye vyeti halafu hajui
chakufanya. Sijui kama unanielewa?” “Hapo nimekuelewa.” Bale akakubali.
“Pale
kwenye kitengo chetu, kuna mzee nimempa idara ya mambo ya Products.
Anaongoza wasomi, hata Naya anamfahamu, lakini yeye hana hata shahada, ila
elimu ya chuo ya miaka miwili tu na uzoefu kazini. Sijui kama unanielewa?” “Naelewa.”
“Vijana wote wanaokuwa chini yake, sijampata kama yule mzee. Kwanza anayo
nidhamu kuliko wengi tu pale. Ukimpa kazi, ataifanya bila kulalamika. Mzee wa
muda mrefu, halafu mwadilifu mno. Sasa wewe jiulize ni nini unataka? Kama ni
upande kama huu wangu, jiingize kwenye kazi, huku ukisoma. Ni shida. Lakini
unapata mambo mawili kwa wakati mmoja. Uzoefu wa kazi na shule. Au jikite
kwenye biashara kama huyu jamaa yangu. Halafu anza mapema, ili kama haya
yaliyokupata hapa, iwe sehemu yako. Hushituki, ila kutafuta suluhu kwa haraka
na kuendelea. Unapata uzoefu.” “Hapo nimeelewa.” “Lakini.” Joshua akageuka
vizuri.
“Chochote
utakachochagua, hata Naya nimemwambia. Lazima uhakikishe unakimudu, tena kwa kiwango
cha juu ndipo utafanikiwa. Kama ni kazini, hakikisha unachagua jambo moja, na
kusimama nalo vizuri. Sijui mnazungumza nini na Naya, lakini baada ya mwaka
mmoja tu, Naya atakuwa mbali sana. Mimi huwa nachukua kazi zake na
kuwaringishia jamaa wengine wa kampuni nyingine ambao wanavyeo kama mimi,
lakini tayari wanamtaka Naya. Ana moyo wa kufundishika, na nimchapa kazi. Na
Mungu akampendelea akili ya ubunifu. Sikwambii kwa kujivuna tu, lakini Naya
wangu ni bora sana kuliko hata baadhi ya viongozi wake.” Bale akacheka na kuinama,
vile Joshua alivyoongea. Tena kwa kujivuna na kupunguza sauti.
“Maua
yale ya kwanza ilibidi tu kumpa kwa kazi nzuri aliyofanya. Japokuwa ni mgeni,
sasa hivi anaongoza kitengo chao kilichokuwa kikilalamikiwa na kiongozi wao, na
ameongezewa access, na Naya amekimudu bila kelele. Sijui kama amekwambia baba!”
“Ameniambia.” “Basi huyo ndio Naya wangu. Sasa mtu kama huyo, ukimpa mwaka
mmoja tu kazini, na akaendelea hivyo, kwa nini usimpe idara nzima?” “Ni kweli.”
Bale akaafiki. “Juhudi, kujituma, na ujue unataka nini. Boresha kitu kimoja au
viwili, kisha vijue haswa.” Bale akavuta kiti karibu.
“Lakini
naona kwa sasa kuna uhitaji wa pesa zaidi.” “Hapana Bale. Wenye pesa tunalilia
mlichonacho nyinyi hapa. Familia kwanza. Sijui kama unanielewa?” Bale
akainama. “Familia kama hii, haipatikaniki kwa pesa. Weka mipango sahihi,
utafanikiwa tu. Unaweza ukadhania unachelewa, lakini Bale, upo katika familia sahihi,
na wakati sahihi. Tambua unacho kitu cha thamani sana. Kishikilie
kwa kila namna, Mungu ataweka mkono wake.” “Nashukuru kumkumbusha hilo. Bale
anahisi amechelewa sana.” Baba yake akaongeza.
“Hata
kidogo Bale. Wewe bado kijana mdogo. Unayo maadili mazuri sana. Mungu
amekutengenezea njia sahihi ambayo wengi hatukubahatika. Mimi ningetamani
nipite ulipopita wewe Bale. Kukuzwa kwenye familia kama hivi wewe, nisome
nikijua ninapo nyumbani. Sikubahatika Bale. Ndio namtaka Naya, kwa umri
huu, aje anitengenezee nyumbani! Hudhani kama wewe unayo bahati!?”
Ilimgusa Naya, mpaka akasimama huko alipo, akajishika kifuani. Bale akainama.
“Upo katika njia sahihi sana, usikubali mtu mwingine akakupotosha. Kwanza
umesoma. Mimi shahada ya kwanza nimepata kwa shida mno. Kwanza sikupata shahada
kama yako. Nimeungaunga kweli! Tulia ndani ya familia. Fikiria ni nini
unataka. Swala la biashara tayari ni la mzee. Ukitaka kujiunga naye, sawa.
Ukitaka ajira pia fikiria unataka kitengo gani, kisha tuanzie hapo. Lakini
ukiwa umetulia na unajiamini.” “Nashukuru Joshua. Asante sana.” “Na mimi asante
kwa kamera.” Zayoni akaingilia kwa haraka akicheka.
“Muone
naye huyu!” “Nilikuwa nikisubiria na mimi nimshukuru ili nianze kutumia kamera
yangu. Amenijia na kila kitu! Asante sana.” “Umshukuru na Naya. Naya anakusifia
sana Zayoni. Anasema wewe mtoto mzuri, unapenda shule na mtunzaji pia.” Zayoni
akacheka. “Hata baba ananiambia hivyohivyo. Mimi nimefanana na baba, sio kama
Bale na Naya. Wao wamefanana na mama yetu.” Wote wakacheka. “Nimefurahi sana.”
“Karibu Zayoni.” Zayoni akamfuata Naya jikoni.
“Nikwambie
ukweli Joshua?” Joshua akamgeukia Bale. “Karibu.” “Mimi sina moyo wa biashara kama
hivyo Zayoni na Naya. Nafikiri wao wamepata kwa baba. Mimi nilitaka kufanya ili
tu kumfurahisha baba, na kusaidia mambo ya hapa ndani. Naomba nisaidie kama
naweza kupata kazi. Mimi ni mzuri sana kwenye mambo ya uongozi. Tokea
nipo shule ya msingi mpaka chuo, nimekuwa nikiwa kiongozi tu. Nimesomea mambo
ya utawala. Na pale chuoni pia nilikuwa kiongozi kwenye sehemu nyingi tu na
kuhusika kwenye vikao vingi hata na wakubwa wa nchi waliokuwa wakija pale
kuzungumza na wanachuo. Matatizo yalipokuwa yakitokea pale chuoni na mimi
nilikuwa miongoni mwa kamati za viongozi waliokuwa wakitafuta suluhu mpaka
kwenye uongozi wa chuo. Kwa hiyo nikipata kwenye ofisi za HR, nahisi nitakua
vizuri bila shida.” “Safi sana. Yaani mpaka hapo tu, jinsi ulivyojieleza, kama
ni usahili, umepata kazi.” “Kweli?” Bale akauliza akicheka. “Kabisa. Umeongea
kwa lugha nyepesi tena ufasaha na kuonyesha pia uwezo wakufanya kazi ukiwa
kwenye mazingira magumu.” “Joshua unajua kumjenga mtu!” “Lakini si kweli mzee
wangu!? Umemsikia mwenyewe.” Joshua akauliza wakicheka.
“Mi kweli
Bale amekuwa kiongozi maisha yake yote.” Baba yake akasifia. “Basi ndicho kitu
alichopewa na Mungu ili kukifanyia kazi. Kama nilivyomwambia Naya, na wewe
hivyohivyo. Jipe muda kazini, na usichezee nafasi yeyote utakayopewa.”
“Hakikisha ukiitwa sehemu kwa chochote, unaacha historia ya kuja kuitwa tena.”
Akaingilia Naya. “Fanyia mazoezi kila kitu unachotaka kukisema mbele za watu.
Namaanisha ofisini.” Joshua akacheka sana. “Umemsikia Naya wangu. Ameiva
kabisa.” “Kweli ameiva.” Wakacheka. “Na Naya hakudanganyi. Juma lililopita
ametoka kusoma ripoti ya kitengo chao, tena kwa kushitukizwa mbele ya idara
nzima!” “Aliweza?” Bale akauliza.
“Usicheze
na Naya.” Wote wakacheka. “Nakwambia mimi mwenyewe alinishangaza, nikabaki
nikijivuna tu. Kila kitu kilisimama, nikaenda kununua maua.” Wakazidi kucheka.
“Ilikuwa ripoti nzuri sana, tena aliiandaa yeye mwenyewe, kiongozi wake hakuwa
tayari.” “Ila nilitayarisha ripoti kubwa sana!” Naya akalalamika. “Ule ulikuwa
mwanzo tu. Tena sio kwamba ilikuwa mbaya. Hapana. Ila ilikuwa ikifaa kwa
kitengo chote, si kwa idara moja. Huoni hata idara nyingine walikuomba wakatoe
kopi? Ulifanya vizuri sana. Sasa ndio utaalamu huo, hamishia kwa Bale,
wakati tukimtafutia sehemu yakuanza kazi.” “Asante Joshua.” Naya akashukuru,
Joshua akacheka.
“Kweli na
mimi nakushukuru, Joshua. Nilikuwa nimechanganyikiwa kupita kiasi. Nilikuwa
naangalia lakini sioni kitu. Ikawa giza tupu.” “Ndio changamoto za maisha Bale.
Unabadili tu gia, bila kusimama.” Wakacheka.
“Karibuni
mezani. Kikao kihamie hapa. Chakula tayari.” Naya akawakaribisha. “Naona
umefanya haraka?” “Bale alishapika. Nimepasha tu moto.” “Ooh! Nashukuru.” “Ila
unampishi mzuri!” Akasifia baba Naya. “Aisee kweli! Ile chapati aliileta Naya
jumamosi! Kama kabechi jinsi ilivyo chambuka!” “Ni mpishi mzuri sana. Kila siku
Naya anakazi yakusifia chakula chake!” “Nimemwambia baba jinsi ninavyokula
vizuri siku hizi huko kazini.” Yakaendelea mazungumzo hapo, mpaka Joshua
alipoaga na kuondoka. Akaiacha hiyo familia na kicheko sio majonzi aliyowaachia
Malon.
~~~~~~~~~~~~~~~~
0 Comments:
Post a Comment