Jioni
nayo akamrudisha nyumbani wakizungumzia mambo mengine kabisa. Hakutaka kurudia
kabisa mazungumzo ya mambo ya ndoa ila kumfurahia Joshua kama Joshua na yale
anayompa. Heshima aliyoirejesha kwake na upendo wa dhati. Naya akajionya
kutoanzisha kitu chochote kitakachowopotezea amani. Akajiambia japokuwa
anatamani sana ndoa, lakini atasubiri. Akapoa kabisa na kuendelea kumfurahia
Joshua.
Walipofika
nyumbani kwao akatoa habari njema kwa baba Naya. “Nimezungumza na GM mwenyewe.
Amesema kesho mida ya saa nne unaweza kufika kwenye ofisi zao pale Ubungo,
mkazungumza. Nikijana mdogo tu, mtulivu sana, lakini kama nilivyokwambia,
amefanikiwa sana. Ukiweza kumuweka sawa huyo, ujue ndio umeshafanikisha
kila kitu. Muungwana sana na anaakili za upendeleo. Naomba fungua moyo
kwa ushauri pia.” “Nakushukuru sana Joshua. Najua kukutanishwa na watu kama hao
ni muujiza.” Wakacheka na kuendeleza mazungumzo. Usiku huo Joshua
hakuzungumzia chochote juu ya Bale na hakuna aliyemuuliza wakijua anakumbuka
juu ya maswala yake ya ajira.
Ijumaa.
Asubuhi
kama kawaida alikwenda kumchukua Naya. Ila safari hii akamsubiria nje ya gari.
“Jana nilijipunja. Sikukupata vizuri.” Naya akacheka na kumkumbatia kwa haraka
kwani alishajua anachokiongelea, akampokea vizuri. Ilikuwa bado tu ni giza.
Peke yao nje ya nyumba ya kina Naya. Yaakanza mabusu kwa wawili hao tena bila
haraka, Naya akiwa amejituliza hapo kama ametunikiwa ulimwengu wote! “Nakupenda
Joshua.” Akamsikia akinong’ona huku akipitisha vidole taratibu upande aliokuwa
amemshikilia wakati Joshua akimbusu na kumshikilia sehemu za shingoni
akimchezea na nywele. Akamvuta mbele kidogo na kumwangalia. “Na mimi nakupenda
Naya. Nakupenda sana mpenzi wangu. Umeondoa upweke kwenye maisha yangu.” “Hata
mimi Joshua. Umerejesha amani na utulivu ndani yangu. Umenipa heshima ya hali
ya juu. Nakushuru kwa kunivumilia tokea tunaanzana. Najua haikuwa rahisi.
Lakini niliihitaji mtu kama wewe wakunivumilia mpaka nirudie hali ya
kawaida kama binadamu wengine.” Joshua akacheka na kurudi kumkumbatia kidogo na
kumfungulia mlango, Naya akaingia garini na Joshua naye akarudi kwenye kiti
chake, safari ya kuelekea kazini ikaanza.
Jioni
akamrudisha na kumkuta baba Naya amejawa furaha haswa. “Naona mambo yamekwenda
vizuri. Geb amekusifia sana.” Baba Naya akacheka. “Na yeye mwenyewe amekusifia
sana. Nilibahatika na kumuona mkewe, Nanaa. Ni binti mzuri sana. Wanatamani sana
kumuona Naya. Lakini nikawaambia hafanani na mimi hata kidogo. Naya anafanana
na mama yake.” Naya akashangaa. “Wanaharaka hao! Nanaa ndio msumbufu zaidi.”
“Na yeye ndiye aliyekuwa akitaka hata picha ya Naya.” “Nilijua tu ni yeye.”
Joshua akaongeza na kucheka kwa pamoja.
“Na mimi
nimewakatalia wote na mama yao, nimewaambia watakuja kumuona Naya mwenyewe,
kabla ya picha. Naya akacheka akifikiria. “Ila ni kweli ni watu wazuri sana na
bado ni vijana wadogo tu. Halafu ni kweli wamefanikiwa kupita kiasi. Geb
mwenyewe alinitembeza kwenye hilo jengo zima, akanionyesha mifano ya vitu
wanavyofanya, hakika anayo akili yakuzaliwa.” Akasifia baba Naya.
“Amenishauri
nisianze na kitu kimoja, kitanichelewesha na ninaweza kukwama. Ameshauri pia
kufikiria mkaa. Amesema ni biashara ya mama yake, ila anajua inamlipa sana.
Amesema niweke hata banda dogo tu nje, nichukue majunia machache niuze, pamoja
na mafuta. Amesema uzuri wa mkaa, hauhitaji uwekezaji mkubwa, ni banda tu
lililofunikwa vizuri na vifaa vya kupimia kwa kuanzia, ila baadaye kuanza kuuza
kwa junia. Pamoja na mafuta halisi. Ameshauri upande wa mazao nisianze mchele
tu, nifanye pamoja na maharage, na hivyo vyote anasema anaingiza hapa mjini
kutoka mashambani, na anapitisha hapahapa kwetu, au tuseme pale Kibaha. Kwa
hiyo amesema nikiwa tayari, nimwambie ili awaambie madereva wake waanze
kushusha. Lakini Joshua!” “Ndiyo mzee.” Baba Naya akacheka kwa kuguna huku akifikiria.
“Yule
kijana anajua anachokifanya! Anaujua mchele kwenye junia kwa mahesabu
mpaka shilingi ya mwisho! Akikupigia mahesabu ya gunia moja, kuanzia kwa kipimo
kidogo mpaka kikubwa, pesa utakayoingiza, gharama utakayowekeza mpaka muda wako
wa kusimama wewe mwenyewe na kumuuzia mteja!” “Baba!” Naya akashangaa. “Hakika
huwezi kuchezea hata shilingi moja. Kwanza aliniuliza swali lililonifanya
nijisikie vibaya.” “Swali gani baba?” Naya akataka kujua.
Baba naya
akajicheka. “Aliniuliza ninapanga kuingiza faida kiasi gani kwa mwezi wa
kwanza. Hilo ni swali la kwanza kabisa. Akasema akijua hilo, atajua jinsi
yakunishauri ninze na nini. Hakika nilijisikia vibaya kwa kuwa sikuwahi
kulifikiria hilo. Amenichangamsha na kunifanya nijue ni wapi nimekuwa
nikikosea. Akaniambia yeye baba yake alimfundisha ni lazima kila mwaka
unapoanza, awe anajua anataka kufunga na kiasi gani cha pesa. Anasema imemfanya
kutobweteka. Haoni shida hata kuuza pipi, ili kupata shilingi ya kuhakikisha
hiyo pesa inatimia kwa huo mwaka.” “Baba!” “Joshua anaposema amefanikiwa, amini
wamefanikiwa. Mkewe mzuri sana. Watulivu, ni kweli utajisikia
vizuri kuwa nao karibu. Wale ni watu wakuwaweka karibu.” “Afadhali kama mzee
wangu kama umekubaliana na mimi juu ya hilo. Mimi nilihakikisha naomba urafiki.
Huwezi kuharibikiwa ukiwaweka wale karibu.”
“Mimi
mwenyewe amenichangamsha sana yule kijana. Sana. Tatizo tu ni mtaji. Ila
amenipa mawazo mazuri sana. Mkaa wenyewe tu, hiyo biashara anayosema anafanya
mama yake, amenipigia mahesabu, mpaka nikatamani nianze kesho!” “Safi sana.”
Naya akanyamaza. Akapoa kabisa. Akajua wamerudi palepale kwenye tatizo la pesa.
“Ila nakushukuru Joshua. Nimechangamka akili. Nilianza kuona nimezeeka. Lakini
nimegundua jinsi hawa watu walivyofanikiwa, ufikiriaji wao ni tofauti
kabisa na wengine. Jinsi yule kijana anavyozungumza, utaelewa ni kwa nini
amefanikiwa vile.” “Na uzuri wake, ile juhudu ameweka mpaka kwenye ndoa
yake.” “Hilo nimeliona.” “Kweli baba?” “Kabisa. Kama alivyosema Joshua,
utafikiri ndio anataka kumchumbia yule binti. Kumbe ni mke wa watoto
watatu!” Wakacheka.
“Na
mwenyewe huyo Nanaa msafi sana. Amependeza sana. Halafu mcheshi,
anaheshima. Kwa kweli ni vijana walionivutia.” “Nimepatwa hamu
yakuwafahamu.” Joshua akamcheka Naya. “Bwana siku ile unaniambia juu yao nilikuwa
na mawazo ndio maana. Ila sikuwapuuza.” “Basi ndio baba amewajua kabla yako.”
“Na mimi nitawafahamu tu.” Joshua akatulia kidogo.
“Naomba
kuwaalika nyumbani kwangu ramsi siku ya kesho.” Wote wakamwangalia kasoro baba
Naya, yeye alitabasamu tu. “Mimi nataka kuja.” Akadakia Zanoyi. “Kesho saa
ngapi?” Naya akauliza. “Kuanzia saa 11 jioni sio mbaya. Na kina Magesa
watakuwepo, pamoja na wageni wachache. Nimewaalika kwa chakula cha jioni.” Naya
akatulia kidogo kama anayefikiria. “Vipi?” “Acha nitazungumza na baba kwanza,
kisha nikujibu Joshua. Ila tunashukuru kwa mwaliko.” “Karibu. Ni chakula cha
jioni, na kutakuwa na marafiki zangu, ningependa na nyinyi kama watu wangu wa
muhimu, wawafahamu au mfahamiane. Zaidi hao kina Magesa.” “Tena Nanaa, mkewe
Geb ameniambia atakuwepo kesho na ndipo atanikutanisha na wajukuu.” “Wana watoto
wazuri! Naona niache kuwasifia mpaka mkajionee wenyewe.” Wakacheka.
“Kweli.
Naona mtaona nimewazidishia sifa. Lakini hakika pale Mungu amempendelea Geb.
Mimi mwenyewe nimemwambia Geb, akaniambia hata yeye anajua, ndio maana hazembei
kwa chochote zaidi kwa familia yake. Anasema siri ya alipo sasa hivi ni utulivu
wa fikra, anaopata kwenye ndoa yake. Huwa ananiambia kabisa, nyumbani
kukitulia, huna utakalofanya, ukashindwa kufanikiwa. Na anasema
hamaanishi kufanikiwa kipesa tu, anamaanisha mafanikio ya mpaka nafsi.
Kwamba na mtu wa ndani atastawi na kupata utulivu wa ndani. Na ni kweli. Geb
ametulia kwenye ndoa yake. Hana papara, hata ukimkuta nyumbani, ametulia.
Mama yao mcheshi mno na mkarimu. Naona niishie hapo.” Wakacheka sana. “Joshua
na kina Magesa!” “Acha uje ukutane nao, ndio utanielewa. Ila naomba msikose
kesho.” “Nitakujibu Joshua.” “Sawa.” Usiku huo nao Joshua akaondoka bila
kuzungumzia chochote juu ya Bale wala kugusia maswala ya ndoa.
Jumamosi.
Asubuhi
hiyo nayo Naya alipoingia garini akakutana na Joshua mwimbaji haswa. “Ni mapema
sana kuwa na furaha ya kiasi hicho Joshua bwana! Leo umeota ndoto gani?” Joshua
akacheka sana. “Usicheze na Mungu wangu.” “Amefanya nini tena?” Naya akauliza
huku wakielekea kazini. Hapakuwa hata na mazingira ya busu kwani Joshua alijawa
furaha na kuimba kwingi. “Mimi naona mpaka uje ushuhudie mwenyewe. Nikikwambia
unaweza ukaona nazidisha sifa.” Naya akacheka. “Hajuagi kunipunja.” “Joshua na
Mungu wake!” “Ndio Baba yangu. Ananitengenezeaga njia, pasipo na njia. Halafu
anapenda kupigana na watesi wangu. Hataki mwanae nitokwe jasho. Kila
anayenisogelea, huwa namsemelea tu, halafu kimya, Baba yangu anawashughulikia
kwa namna yake, na utukufu unabakia kwake, mimi nasonga mbele.” Naya
akamwangalia na kucheka tu.
Joshua
akarudia kuimba. Siku hiyo aliimba njia nzima. Naya akamuona amechangamka
kweli. “Nisaidie basi Naya!” “Ni asubuhi sana Joshua jamani! Mimi ni mwimbaji,
lakini si wa kabla ya jogoo kuwika.” Joshua alicheka mpaka machozi. “Naya!”
“Kweli bwana Joshua. Wewe unachangamkaje asubuhi hivi! Kwanza leo jumamosi,
mwenzio nguvu ya week nzima zinaniishia siku za jumamosi.” “Basi wewe kaa
uburudike.” Naya akatulia kimya akimsikiliza akiimba mpaka walipofika kazini.
“Mbona
sasa hujauliza kama tunakuja kwako jioni au la! Au hututaki tena wageni sisi?”
Joshua akacheka. “Najua mtakuja tu.” “Hee! Kwa nini?” “Baba Naya sasa hivi
anazungumza lugha moja na Geb. Na nimemwambia Geb atakuwepo, lazima amepata
sababu ya kuwepo. Zayoni amesema anataka kuja.” “Na mimi?” “Wewe najua lazima
uje kwa kuwa wageni wangu ndio wako. Lazima uwepo kukaribisha wageni. Bale naye
najua nyinyi mkiwepo, na yeye atakuwepo. Sina wasiwasi.” “Joshua wewe ujue
umeelewa vibaya! Baba amekataa.” Joshua akashituka mpaka Naya akamuona, akaanza
kumcheka. “Nilitaka utulie kidogo, sio uwe umechangamka zaidi yangu!” Joshua
akanza kucheka. “Furaha hii huwezi kushindana nayo Naya. Hata kwa kunitisha.”
Wakashuka garini.
“Lakini
ulitishika kidogo.” “Hapana. Baba Naya na mimi tunaelewana!” “Nyie
Joshua anavyojiamini!” “Nimepewa kibali na Mungu Naya. Acha wivu.” Joshua
akaendelea kuimba. “Leo Fina na Jema watakoma.” Joshua akacheka sana, huku
akimsindikiza ofisini kwake. Akamuwashia taa. Alipomuona amekaa, akatoka
akiimba. “Wala sio vizuri! Bado ni mapema sana.” Akamsikia Joshua akicheka huku
akiondoka. Naya akabaki akicheka.
~~~~~~~~~~~~~~~
Naya
akaanza kusikia minong’ono ya kulalamika kwa wengine kutoalikwa nyumbani kwa
Kumu siku hiyo jioni. Akabaki ameinama akisikiliza. Walikuwa wakimlalamikia
Jamal kuwa Jema hajawapa na wao mualiko. Walisimama karibu sana na sehemu ya
kuingilia hapo. “Jema ametubania tu!” “Mimi ameniambia amepewa nafasi za watu
watano tu. Sasa kila mtu analalamika, angemchangua nani na kumuacha nani?
Mngemuelewa Jema.” “Jamal anaongea hivyo kwa kuwa yeye kapata mwaliko. Sasa
kulikuwa na ulazima gani kukaribisha watu wa vitengo vingine wakati sisi watu
wake Kumu tupo?” Naya akashangaa sana jinsi wanavyolalamikia kualikwa nyumbani
kwa Kumu!
“Wewe
umezoeana na Naya. Muombe basi amuombe Kumu nafasi hata 3 tu nyingine! Jema
amesema yeye...” Jamal akasikika akicheka huku akikataa. “Mnataka nigombane na
Kumu! Yaani Kumu aje ajue nazungumza na mwanamke wake mambo kama hayo zaidi ya
kazi! Naheshimiana sana na Kumu. Tafadhali msiniharibie. Anayetaka, amfuate Naya
mwenyewe.” Jamal akaondoka. “Twende tumfuate Naya sisi wenyewe, Chege.” “Wee!
Mimi mwenyewe sitaki matatizo na Kumu. Kama Jema kaamua kutuacha, basi.” Naya
akakunja uso asielewe. Akageuka kuangalia ni kina nani, akakuta ofisi nzima
wanamtizima yeye. Naya akakunja uso kama anao washangaa. Alipoona kimya
akageuka na kuendelea na kazi zake.
~~~~~~~~~~~~~~~
“Mzima
Naya?” Naya akageuka akamkuta Jema amemsimamia kwenye meza yake. “Mimi mzima.
Kwanza asante kwa pafyumu. Joshua ameniambia wewe ndio ulinunua.” “Umeipenda?”
“Nzuri.” Jema akacheka. “Mbona kama sio sana?” “Sio mbaya. Niambie.” “Kwanza
niambie juu ya pafyumu.” Naya akacheka. “Ila nimekushukuru kwanza.” “Wewe
niambie usijali, ili siku nyingine nisikosee.” Jema akaweka msisitizo. “Ila
usimwambie Kumu. Mimi huwa situmii pafyumu zenye citrus. Napenda aina za
woody.” Jema akatoa macho nakumfanya Naya aanze kucheka. “We Naya! Ndio
nini?” Naya akazidi kucheka.
“Mimi
naona hilo zoezi la pafyumu tuje tulifanye wote. Na mimi nijifunze. Maana mimi
nachukua kutokana na bei na nikivutiwa na harufu.” “Basi tutakuja kulifanya
hilo zoezi siku moja. Mimi ni mpenzi sana wa harufu nzuri. Na ninazijua pafyumu
kwa harufu.” “Ndio maana hujaitumia?” Naya akacheka.
“Basi
nipe mimi Naya.” “Siwezi kukupa kwa kuwa imetoka kwa Joshua.” Jema
akacheka sana. “Naya!” “Kweli. Hata yeye usimwambie. Nimefurahia sana kuona
amenifikiria na kuniletea.” “Ila siku nyingine nitaenda kununua mimi mwenyewe,
aina ya woody.” Wakamsikia Joshua akijibu. Naya alishituka mpaka akasimama,
hawakujua kama alikuwa akisikiliza. “Jumatatu tutakuletea pafyumu yako Jema.
Haya, naomba tupishe.” Jema akacheka sana. “Tusiigawe bwana!” “Sasa utaiweka
mpaka lini? Mpe tu Jema, tutatafuta nyingine, na wala sijaumia.” “Kweli
Joshua?” “Kweli. Kwanza nimefurahi kujua aina ya pafyumu unazopenda. Sikuwa
nikijua ndio maana nikamtuma Jema wakati akijinunulia vitu vyake, nikamuomba
akununulie pafyumu nzuri. Basi. Hata sikumwambia aina gani.” Naya akacheka kwa
aibu akamwangalia Jema.
“Sasa sio
tumeagana kule, halafu uje huku umgande tena Naya. Natoka naye, kwa hiyo
changamka Jema. Malizana naye utupishe.” “Kwani kuna kitu ulitaka kuniambia?”
Naya akamuuliza Jema. “Tena nilitaka kusahau!” Jema akawa kama amekumbuka.
“Huwa unapenda keki aina gani?” Naya akakunja uso na kumwangalia Joshua. “Mbona
unaniangalia mimi badala ya kujibu?” Joshua akamuuliza akicheka. Naya
akababaika kidogo akifikiria kisha akajibu. “Yeyote ile.” “Kweli Naya?” Joshua
akaingilia kwa swali. “Kweli, kwenye keki si mchaguzi. Unataka kuniletea keki,
Jema?” “Kwa kuniletea ile pafyumu jumatatu, nakuletea keki.” Naya
akacheka, Jema akaondoka.
“Upo
tayari? Nilikwambia leo tunawahi kutoka.” “Sijamaliza jambo moja, Joshua. Wewe
tangulia.” Joshua akaweka mikono mfukoni na kusimama vizuri akimshangaa kabisa.
Naya akacheka. “Basi kaa hapo nisubirie nimalize, nisiharibu kwa Jamal.”
“Naya!” “Sikawii. Kuna kazi imechelewa kuingia, nimeona niifanye tu mwenyewe.
Kaa basi nimalizie mara moja.” “Ni nini?” “Njoo uone.” “Hapana bwana! Kwa nini
umechukua kazi mpya wakati nilikwambia tunawahi kutoka!?” “Hivyo
unavyolalamika, ndio tunazidi kuchelewa.” “Nikupe dakika ngapi?” “13 tu.”
Joshua akaangalia saa. “Naomba isizidi Naya. Na usiongeze kazi nyingine.
Wagawie wenzio wafanye. Leo nakutaka mapema.” “Hapo dakika imeshaisha
tena.” Joshua akatoka bila kuaga, Naya akamcheka. “Nashukuru kwa laptop
kiongozi. Nimepewa mpyaa!” Akamsikia Jamal akipaza sauti “Ianze kufanya kazi.”
Joshua akasikika akiwa anapotelea koridoni. “Utaona matunda yake.” Joshua
hakusikika akijibu tena.
~~~~~~~~~~~~~~~
Walitoka
hapo saa sita kamili mchana. “Leo jikaze uje kula nyumbani. Wataandaa chakula
kizuri sana.” “Sasa wewe husikii njaa?” Naya akauliza kwa kujali. “Nipo sawa.
Kwanza mwenzio mchana si mlaji sana. Mara nyingi nakuwa na kazi.” “Sasa
tutafikaje nyumbani kwako? Mimi sijawahi kufika huko Goba.” “Nitakuja
kuwachukua mimi mwenyewe. Saa kumi na nusu nitaomba tuwe tunaondoka nyumbani
ili wageni watukute tumeshafika Goba, sisi tukiwasubiria. Tuwakaribishe.”
“Wageni wenzetu wanaanza kufika saa ngapi?” Joshua akacheka. “Wakifika wao saa
1 usiku, watakuta wewe umeshakuwa mwenyeji, unawakaribisha tu.” Naya
akacheka. “Sawa. Utatukuta wote tayari.” Joshua akaanza kuimba tena. Naya
akabaki akicheka.
“Umefanya
kazi kweli wewe leo?” “Sana. Nimekuwa na masaa 4 ya mchakamchaka, nikikomboa
wakati. Nashukuru kila kitu kilienda kama alivyopanga Jema.” “Jema anaonekana
anaijua kazi yake, eeh?” “Na anaipenda sana. Ndicho anachonifurahisha. Si
mlalamishi hata kidogo, ila mtu wa kutafuta suluhu. Hata kama atashindwa, ujue
amejaribu. Halafu mwepesi wa mambo. Ukimwambia unahitaji kumuona au kuzungumza
na mtu fulani, hata awe nani, atahangaika mpaka aniunganishe na huyo mtu, tena
bila kuchelewa.” “Anaonekana. Hata tembea yake ni kama anakimbia kwa haraka.”
Wakacheka, Joshua akaanza kuimba tena. Naya akabaki kimya akimsikiliza na
kucheka mpaka wakafika nyumbani kwa kina Naya, Kiluvya.
Hawakumkuta
mtu. “Hawa watakuwa hawajarudi. Baba aliniambia walikwenda kukata nywele.”
“Acha na mimi nikasafishe kichwa changu.” “Ila nikwambie ukweli Joshua.”
“Niambie tu.” “Wewe ni msafi mpaka unavutia.” “Kufanyaje?” Naya akacheka sana.
“Joshua!” Joshua akaanza kucheka. “Asante Naya. Nimefurahi kusikia hivyo haswa
kutoka kwako. Inaniongezea ujasiri.” “Kwani ulikuwa hujui?” “Hata wakisema watu
1000, lakini sio wewe, kwangu haileti maana kama wewe ukisema.” “Jamani
Joshua wangu! Basi ujue wewe ni mzuri na unavutia.” “Naona na
sifa imeongezeka.” Naya akacheka. “Asante mpenzi wangu.” Akamsogelea na kumbusu
shavuni.
“Upendeze
sana leo. Mwenzio nitapendeza.” “Sitakuangusha Joshua.” “Ni kwa ajili yako
mwenyewe. Sitaki uje ujisikie vibaya. Mimi sitajali hata nikikuona hivyohivyo.”
“Basi nitajiwakilisha vizuri. Usijali.” Joshua akambusu tena shavuni na kutoka
kwa haraka.
Kwa Mara ya kwanza Naya Nyumbani kwa Joshua, akiwa na Familia Yake.
Saa 10:20
jioni hiyo Joshua akawa ameshawasili nyumbani kwa kina Naya. Akakuta wote wapo
tayari, ila Naya tu alikuwa chumbani, ndugu zake walikuwa wakisubiria sebuleni.
“Umependeza sana Joshua!” Naya akamsikia baba yake akimsifia. “Asante mzee
wangu. Hata nyinyi mmependeza. Mnaweza kutangulia tu kwenye gari. Nimeacha
wazi.” Wakatoka na kuwaacha ndani. Joshua akimsubiria Naya. “Namalizia Joshua.”
“Sawa.” Joshua akawa mtulivu tu akisubiria. Naya hakuchukua muda mrefu akatoka
na kumfanya Joshua abakie mdomo wazi.
“Naya!”
“Nimejiwakilisha vizuri?” Naya akawa akigeuka akicheka. “Nikwambie siri ya hii
nguo?” “Tukiwa tunaondoka.” “Basi acha nifunge mlango.” “Umependeza sana, mpaka
natamani ungesema unaniwakilisha na mimi!” Naya alicheka sana. “Unaumbile zuri
na imekukaa vizuri kwa heshima na kufanya uvutie vizuri SANA.” “Asante.
Niliipenda sana hii nguo lakini nikawa sina pesa. Alikuwa akiuza Madamu Vane,
yule mama nilikusimulia habari zake, niliyekuwa nikimfanyia kazi tokea nipo
sekondari. Nikamuomba asiiuze, anitunzie ila awe ananikata kidogokigogo mpaka
nikamaliza. Na aliniuzia kwa bei kubwa sana. Sikuwahi kupata sehemu ya kuivaa,
ndio leo naivaa rasmi kwa mara ya kwanza. Nilikuwa nikiivaa tu chumbani nikiwa
nina mawazo. Najizungusha kwenye kioo mpaka niridhike ndipo naivua na
kuirudishia kwenye mfuko wake.” Joshua akacheka huku akimsaidia kufunga mlango.
“Hiyo
nguo kweli ina uwezo wakukutoa mawazo.” “Na wewe umependeza sana.” “Wewe
ukisema, ndio najisikia vizuri.” Naya akacheka akimwangalia na kumtafakari
Joshua vile anavyomuonyesha anamjali na kumuhitaji. “Sasa mbona
haonyeshi kutaka kunioa?” Naya akawaza wakati wakielekea kwenye gari.
“Hivyo
ulivyopendeza, naomba heshima ya kukufungulia mlango wa gari.” Walikuta wote
wamesimama nje ya gari hawajaingia ndani ya gari wakiwasubiria. Naya akacheka
na kumpisha. “Lakini baba ndio atakaa mbele. Mimi nitakaa nyuma.” Naya
akamnong’oneza Joshua, akaelewa. “Sawa.” “Akamfungulia mlango wa nyuma ya
dereva. Akapanda, Joshua akamfungia mlango, ndipo wengine nao wakapanda garini,
wakimpisha baba yao kiti cha mbele. Safari ya Goba ikaanza. “Mjiandae kwa
safari ndefu kidogo. Pana umbali!” “Nilihisi tu, ndio maana huwa nakushukuru
kuja mpaka huku asubuhi na jioni, Joshua. Kweli nakushukuru.” “Usijali kabisa
mzee wangu. Huwa tunapata muda mzuri sana njiani.” Naya akacheka na kunyamaza.
Joshua akaendelea kukanyaga mafuta.
“Vipi
Bale?” Bale alikuwa kimya sana. Joshua akavunja ukimya. “Nipo tu.” “Safi sana
na Zayoni?” “Mimi naendelea vizuri. Gari yako safi!” Wote wakacheka. “Asante
Zayoni. Lakini unaonekana unapenda vitu vizuri!” “Sana. Nikiwa na hela nitakuwa
nanunua vitu vizuri halafu nakuwa msafi. Hata nguo zangu huwa zinakuwa safi,
muulize Naya. Sirudii nguo mara mbili. Nikivaa mara moja, basi. Hata kama
hainuki jasho, nafua.” Zayoni akajisifia nakufanya wacheke. “Halafu mimi sio
mvivu wakufua.” “Safi sana. Unaonekana pia kama ni msafi.” “Na wewe umeniona
kama na mimi ni msafi!?” Akamuuliza Joshua, wote wakacheka. “Usafi
huwa haujifichi. Unaonekana kabisa kama ni msafi.” “Asante. Basi Naya huwa
ananinunulia mashati meupe kama mama. Mama naye alikuwa akininunulia nguo
nyeupe kwa sababu anasema mimi huwa sijichafui. Nabakia msafi.” Wakaendelea
kucheka.
“Kwa hiyo
wewe kila kitu chako nikisafi?” Zayoni akamuuliza tena Joshua. Joshua akacheka.
“Ninafanya juhudi za makusudi kila kitu changu kiwe kisafi. Na nimtunzaji pia
kama wewe. Huwa namwambia Naya, huwa nakuwa na vitu vichache, na huwa navitunza
vizuri. Huwa nahakikisha kila kitu changu kinajua kama ni changu na ninakitunza
vizuri, hata kama ni soksi tu.” “Basi na mimi nataka kuwa hivyohivyo.” Zayoni
akaongeza. Alionekana mkimya lakini akitaka kuzungumza, huzungumza haswa.
“Basi na
Zayoni yupo hivyohivyo. Msafi na mtunzaji sana. Pale nyumbani ndio mfano wetu.”
“Asante Naya. Na Bale pia huwa ananisifia, si ndiyo Bale?” “Kabisa. Wewe
mtunzaji. Ndio maana huwa naona shida kukaa hata kitandani kwako, naona bora
kitandani kwa Naya kuliko kwako.” Wote wakacheka. “Zayoni anatandika mashuka
meupe kitandani kwake!” Naya akaongeza. “Na akitandika utafikiri amepiga pasi
hicho kitanda kwa jinsi kinavyo nyooka!” Bale akamsifia tena. Baba yao akabaki
kimya tu.
Nyumbani kwa Joshua.
Kwanza
wakavutiwa na huo ukuta. Gari zima likatulia. “Baada ya safari ndefu hatimaye
tumefika. Karibuni.” Hakuna aliyeitika. Wakashangaa, geti linajifungua
taratibu. Wanakaribishwa na madhari nzuri sana ndani. Kila mtu macho yakamtoka.
“Haaaa!” Akasikika Zayoni ambaye huwa hawezi kuficha hisia zake. “Karibuni
sana.” Naya alipoa kutoka moyoni. Akavuta gari mpaka sehemu yakuegeshea magari.
Kulikuwa na gari nyingine. Haikutofautiana sana na hiyo anayoendesha, ila
yenyewe ilikuwa nyeusi. Ilionekana bado mpya.
“Na hiyo
pia ni gari yako!?” Akauliza Zayoni. Joshua akacheka. “Ndiyo Zayoni. Lakini ni
ya muda mrefu, huwa siitumii.” Akashuka na kuwakaribisha tena. Akamfungulia
Naya mlango. Akashuka akiwa amepoa haswa. “Vipi Naya?” “Hukuniambia kama
unaishi kwenye hoteli ya kifahari hivi!” Joshua akacheka sana mpaka akainama.
“Naya!” “Kweli tena. Sasa hapa hata ukija kuoa, huyo mkeo anaanzia wapi
kupaita hapa na yeye ni kwake!?” Hilo lilimshitua sana Joshua maana Naya
hakuonekana kutania.
Alionekana
kuishiwa nguvu kabisa. “Kweli Joshua. Huyo mwanake anakuwa anaanzaje kupaita
hapa nyumbani!?” Naya akasikika waziwazi kuwa amekata tamaa. Ndugu zake wote
walimsikia, japo alizungumza kwa sauti yachini. Joshua akawa kama na yeye
amekosa chakusema. Akapoa kabisa. Kisha akawa kama amegutuka. Akawegeukia
wengine ambao walikuwa wakisiliza lakini macho yakiendelea kupata fahari yake.
“Karibuni jamani. Karibuni ndani.” “Asante Joshua! Kwakweli umejijenga vizuri
sana. Hongera sana!” “Nashukuru mzee wangu.” Akamgeukia Naya ambaye alikuwa
amepoa, ameegemea gari kama aliyekwisha kata tamaa kabisa kama anayejishauri
hata kuingia ndani. “Ndio maana anashindwa kuoa! Unaingizaje mwanamke
tu kwenye maisha kama haya!” Naya akaendelea kuwaza na kumsahau Kumu
anayenunuliwa na makampuni makubwa kwa mamilioni ya pesa. Alifikiri zile nyumba
za Malon ndio amemaliza, anakuja kukutana na mjengo wa hatari wa Joshua,
aliyekuwa ametulia tu, tena mnyenyekevu!
“Naomba
tuingie ndani, Naya.” Akashituliwa na Joshua aliyemshika mkono kabisa. Naya
akatoa tabasamu, lakini Joshua aliliona halikuwa halisi. “Twende.” Akamvuta
kidogo huku akiwa kama anambembeleza. Joshua alijua Naya amepaniki. Mazingira
ya nyumbani kwao yalikuwa ya kawaida sana. Vyumba vidogo haswa. Mtu akiwa
chumba chochote humo ndani, unasikia yote yanayoendelea sebuleni. Sebule
yenyewe hawawezi kukaa watu wengi kwa wakati mmoja jinsi ilivyojibana halafu
ikawekwa na meza ya chakula hapohapo karibu! Vyumba vitatu tu, tena sakafu ya
kawaida sana, madirisha ya nondo, wavu, na mbao, wamemaliza. Jiko, walipikia
nje na kuingiza chakula ndani.
Haya,
akakutana na Malon ambaye kwake aliona ni kiwango cha juu sana, akaona kuna
mwanya hata wakuja kujijenga naye zaidi. Kwamba wakapambana na kujijenga zaidi
na yeye Naya akihitajika. Lakini kwa Joshua ni kama alikuta amekamilika
kabisa! Kwenye upande wa kazi, yupo kiwango cha juu kabisa. Hakuna pa
kupanda zaidi, amefika mwisho. Kwa Mungu wake, ametulia. Hana papara,
Naya hana chakuongeza hapo kumjenga. Joshua anamfahamu Mungu, na anaitambua
nafasi yake kama yeye ni mwanadamu, na Mungu ni wakutogusa utukufu wake.
Haya, upande wa maisha, amekutana na huo mjengo wa nguvu, ambao kwa nje tu
macho hayakuwa yametosheka. Gari ya maana, na nyingine ya kifahari ipo tu nje
na bado kwa wadhifa wake, anatakiwa awe anaendeshwa kila mahali. Akaishiwa nguvu
kabisa. Akatangulia akiwa amemshika Naya mkono.
“Naomba
usinikatie tamaa.” Hayo maneneo ya Joshua yakaingia mpaka moyoni kwa Naya kama
aliyekuwa akisoma moyo wake. “Siwezi Joshua.” Naya akajibu lakini Joshua
hakusadiki. Akamtizama wakiwa wanatembea.
Mlango tu
wakuingilia ndani ulikuwa wa kushangaza. Waliingia ndani wote kwa pamoja
wakajikuta wanasema “Waw!” Wakasimama kwa pamoja, nakuduaa, macho juu
wakiangalia huo muundo wa wazi, uliopanda hapo katikati kwa ustadi wa namna
yake, ukajivuta kwa namna ya kuvutia mpaka kufikia dari ya kioo juu kabisa
gorofani. Hiyo dari huko juu ilikuwa ya muundo wake na kona zenye ncha
maridadi, nzuri sana. Likashuka rembo kubwa sana. Kutoka juu mpaka katikati
hapo sebuleni lenye mataa mazuri sana. Ngazi ilizungushiwa kioo kizuri chenye
maua mazuri mno ya dhahabu kuzunguka hivyo mpaka kufikia vyumba vya juu. Vyumba
vya juu vilizungushiwa uzio wa thamani sana nao ni kioo kama kilichotoka chini
kabisa kwenye ngazi ya kwanza mpaka juu ila kulikuwa na vyuma vya urembo pia.
Naya akavuta pumzi kwa nguvu na kurudisha macho kwa Joshua. Akakuta Joshua
ametulia akimwangalia yeye. “Chooni ni wapi?” “Twende nikupeleke.” Akamshika
mkano. “Karibuni mkae tu kwenye makochi, tutarudi sasa hivi.” Joshua akaaga.
Yeye na Naya wakaondoka.
Akamvuta
Naya kwenye kona. “Naomba niambie wasiwasi wako Naya. Tafadhali.” “Hamna
wasiwasi. Ila nilitaka kutumia choo.” “Sio kweli Naya. Ulitumia choo kabla
hatujatoka nyumbani.” Naya akavuta pumzi kwa nguvu. “Uliniruhusu nikutambulishe
kwa watu. Nimeita watu leo, nikijua tutakuwa upande mmoja. Naomba usinigeuke
sababu ya hili jengo, tafadhali Naya.” Naya akacheka taratibu akiangaza macho.
“Naya?” “Mimi nipo na wewe.” “Mimi nitasimamia hapohapo. Naomba toa hiyo hali
iliyokuingia gafla, changamka, nisaidie kuweka mambo sawa, ili wageni
watakapofika tuweze kuwapokea vizuri. Nanaa ameniahidi watawahi kidogo ili
kunisaidia yeye na mama yake, ni mara yangu ya kwanza kualiaka watu hapa. Sina
uzoefu na chochote ndio maana nilitaka na wewe uwahi. Unafikiri unaweza
kunisaidia?” “Unataka nifanye nini?” “Hayo ndio maneno. Cha kwanza twende
tukaangalie sehemu waliyotayarisha kwa ajili ya chakula. Kisha unishauri.”
Wakawaona wanapita upande wa pili.
Joshua
akafungua mlango mkubwa sana ulikuwa juu kidogo pakawa kama holi. Napo hapo
akampoteza tena Naya. “Naomba punguza hiyo hali Naya, tuandae mazingira mazuri
kwa wageni.” Naya akacheka. “Joshua!” “Usifikiri nimejenga jumba lote hili kama
kufuru! Au kwa kuwa sina pakupeleka pesa! Nina maana yangu Naya. Kumbuka
historia ya maisha yangu. Nimekuwa mtoto wa mtaani nikiteseka. Mama yangu
amefia nyumbani kwao wakimnyanyasa. Kweli unataka mke wangu na watoto waje
waishi au wapite kule ambako mimi nimepitishwa nakuona ni hatarishi! Nimefanya
hivi kwa ajili ya familia yangu. Nawazia familia yangu na ukoo wangu kwa jumla
kwa kuwa najua Mungu atanibariki tu uzao. Sasa natamani hata vijukuu na vitukuu
wapate kwao. Wajue hapa ni kwao maana mimi sina ndugu, ndio mimi tu
niliyesimama hapa. Yaani mimi ndio nitakuwa muanzilishi wa ukoo wangu. Ndio
maana hata eneo huko nyuma pia ni kubwa sana. Nimenunua heka nyingi sana, kwa
makusudi kabisa, sio kufuru.” Joshua akajikuta akijitetea.
“Nimekuelewa
Joshua. Na hongera. Sema nimepatwa tu na mshituko. Sikuwahi kuingia kwenye
mazingira ya namna hii tokea nazaliwa! Wewe unajua mazingira yetu. Na nimewahi
kuingia kwenye majumba mazuri, lakini sio kama hivi!” “Najua ni ya kipekee. Na
haipo hivi kwa bahati mbaya. Nimekwambia niliijenga nikiwa naangalia mbali
sana. Na ninataka hii nyumba ibebe historia kubwa ambayo Mungu akijalia,
isimuliwe kwa kizazi hadi kizazi ndio maana unaona hata kuna huu ukumbi.
Nitakwambia zaidi baadaye. Sasa hivi nisaidie kuandaa.” “Sawa.”
Wakaingia
ndani. “Nasikia harufu ya vyakula!” “Wanakaribia kumaliza kupika. Nanaa
amenitumia dereva na hivi vyombo.” Akamuonyesha vilikuwa kwenye maboksi. Naya
akavutiwa na hivyo vyombo. “Sijawahi kualika mtu hapa. Yaani hata vyombo sikuwa
navyo. Nanaa alitaka tukodishe, lakini sikutaka wageni wangu waje nyumbani
kwangu, watumie vyombo visivyo vyangu. Ndio akaniambia ataninunulia,
wataniletea.” “Vinaonekana ni vizuri sana na ni vya hali ya juu.” “Vyote hivyo
wamenipa zawadi, kasoro glasi na vijiko ndio nilimwambia nitamsaidia.”
“Mnaonekana mnaelewana sana na Nanaa.” “Sana. Utampenda tu akija.
Amesema hatachelewa. Ila kwa kuwa wewe umekuwa wa kwanza hapa, naomba ndio
umkaribishe. Tafadhali Naya. Isiwe yeye ndio anakukaribisha hapa.” “Sasa sijui
yeye alikuwa na mpango gani na haya yote!” Naya akasita.
“Chakwanza
ujue yeye hapafahamu kabisa hapa. Mimi nilimtuma tu vyombo, akamtuma dereva.
Naomba wewe shika usukani.” Naya akaangalia ule ukumbi. Alishakuwa na uzoefu wa
kuhudumia kumbi. Meza zilikuwa nzuri, zinavutia. “Chakwanza, kwa aina hizi za
meza zako, naona ni kosa kuzifunika. Huo muundo hapo juu naomba uonekane.”
“Hayo ndio maneno.” “Naomba nimuombe Bale na Zayoni wanisaidie. Tuoshe hizo
sahani tuzipande pamoja na napkins.” “Ngoja nimwite Josee akuletee napkins.
Alininunulia za rangi nyekundu pamoja na cream, akasema atatusaidia kukunja.”
“Si atakuwa busy na mapishi?” “Ana watu wanne wanao msaidia. Usijali.” Naya na
ndugu zake wakaanza kazi hapo ukumbini. Alitoa kabisa kiatu cha juu akafunga
nywele alizokuwa ameziachia, akazifunga juu pamoja. Akaendelea na kazi kama
mwenyeji haswa.
Magesa.
“Twende
tukawapokee kina Magesa. Wamekuja.” Joshua akamfuata pale ukumbini.
“Unapaonaje?” “Sikutegemea! Nimekwambia lakini Naya. Umepapendezesha sana. Na
sitaki mtu aguse tena. Patabakia hivyohivyo.” Naya akacheka. “Nimefurahi kama
umependa. Twende.” Walimkuta baba Naya amekaa hapo sebuleni kimya kama hayupo,
na glasi ya juisi pembeni. “Baba Naya.” Naya akamwita. “Pole nimekuacha peke
yako baba yangu, namalizia.” “Hutaki nikusaidie?” “Namalizia. Acha
nikawakaribishe kina Magesa.” Naya akamfuata Joshua nje.
Naya
alikutana na viumbe ambavyo vilimfanya atoe macho. “Hawa watoto wamewatoa
wapi!?” Nanaa alikuwa akimtoa mtoto mmoja upande huu na mwingine Geb akitoa
mtoto mwingine. “Salimia bwana Liv, ni nini?” Alikuwa mama G. Joshua akacheka.
“Nisalimie basi Liv.” “Huyo ndio anti Naya?” Akauliza Liv akicheka. Wote
wakacheka. “Huyo ndiye Naya. Njoo msalimie basi.” Joshua akamnyooshea mkono.
Akamshika Joshua na kumchungulia Naya. “Mimi naitwa Liv, binti Magesa.
Shikamoo.” Naya alicheka sana. “Jamani binti Magesa! Marahaba. Nimefurahi
kukufahamu, nimesikia habari zako nzuri tupu!” Akacheka tu na kujificha kwa
Joshua. “Mimi hujanisalimia Liv.” “Nimekusalimia kwenye simu anko. Unataka
tena?” Liv akamuuliza Joshua akicheka. “Mimi sikumbuki.” “Na mimi anko. Na mimi!”
Alikuwa Magesa.
“Tulia
bwana Magesa! Hujapitwa na chochote.” Mama yake akamtuliza. “Na mimi anko.”
Naya akawa hajaelewa. “Shikamoo.” Akamsalimia mama G, akaona wanaangaliana na
Nanaa, nakuanza kucheka. Geb akatingisha kichwa akicheka. “Wewe mama ungeitikia
salamu ya Naya kwanza.” Geb akamwambia mama yake wakati wakicheka na Nanaa
kishabiki. “Naya Kumu!” Akadakia Nanaa akiendelea kucheka. “Kwani niliongopa?”
Akauliza Joshua. “Hakika hujaongopa Joshua mwanangu.” Mama G akaitika akicheka
na kumsogelea Naya. “Sifa zako mama, zimejaa huko kwetu, mpaka dada yake Jimmy
ameomba tukupige picha tumpelekee, tumbo linamuuma, ameshindwa kuja.” Naya
akacheka kwa aibu na kumtizama Joshua kama asiyeelewa.
“Joshua
ameniambia juu yenu. Naamini huyu ni...” “Sasa hapo subiri Naya. Ukitaka kuwe
na amani, mwache baba mzazi mwenyewe atoe utambulisho. Hapo mtapatana.” Naya
akacheka lakini akawa hajaelewa. “Haya, Magesa. Anti Naya anasubiri.” Nanaa
akamwambia mwanae. Akacheka kwa furaha. “Mimi hapa naitwa Magesa Magesa. Mimi
ndio kaka mkubwa, Magesa mwenyewe.” Naya akacheka. “Hajamaliza.” Nanaa
akamtahadharisha Naya. “Kumbe bado! Ehe?” “Huyu anaitwa Oliva Magesa. Dada
mkubwa. Lakini bibi naye anaitwa Oliva Magesa. Kwa hiyo huyu dada mkubwa yeye
anaitwa Liv Magesa, binti Magesa, kwa kuwa tuna Liv wawili.” Magesa
alikuwa amechangamka, alionekana bado mdogo lakini anaelewa anachozungumza.
“Umeelewa
anti? Usije kuchanganya.” “Nimeelewa Magesa. Na huyu?” “Huyu ni mdogo wetu.
Anaitwa Jimmy Magesa. Tunampenda Jimmy. Si ndio mama eeh?” “Ndiyo.” Akamvuta na
kumbusu. “Taratibu bwana Magesa, usimuumize!” Nanaa akamtahadharisha. “Nambusu
tu.” Akarudia tena. “Hajamaliza utambulisho. Naomba mvumilie tu.” Nanaa
akamnong’oneza Naya. “Nakupenda Jimmy. Umesikia?” Jimmy akatingisha kichwa
kukubali. “Jimmy yeye hapendi kuongea kama Liv. Ila anasikia na kuelewa kila
kitu. Na huwa anacheza na mimi. Huwa anaongea na mimi. Si ndio Jimmy, eeh?”
Jimmy akatingisha kichwa kukubali. “Nakupenda Jimmy.” Akarudia tena wote
wakiwatizama. Naya aliwapenda hao watoto akabaki akiwaangalia.
“Haya,
huyu bibi yetu. Ananipenda sana mimi.” “Na mimi pia ananipenda.” Liv akadakia.
“Ila mimi zaidi na Jimmy pia.” Mama G alikuwa akicheka huku akitingisha kichwa.
“Mimi nawapenda wote.” “Ila mimi zaidi bibi.” “Wote zaidi. Haya maliza basi huo
utambulisho mimi nikakae bwana Magesa! Nimechoka kusimama juani.” Bibi yake
akalalamika. “Haya bibi. Halafu huyu hapa ni mami yetu. Anaitwa Nanaa. Hata dad
anampenda.” Hapo walicheka wote. “Hajamaliza.” “Huyu ni dad wetu. Ila yeye sio
Magesa Magesa kama mimi. Kwa hiyo usimuite Magesa. Wewe muite Geb. Mimi ndio
Magesa.” Geb akatingisha kichwa akimwangalia. Wakacheka. “Halafu huyu ni anko
wetu, anaitwa Joshua.” Walicheka tena. “Huyo anamjua bwana. Umesahau?”
“Ninakumbuka. Ila nataka kuingia ndani.” “Sasa taratibu Magesa. Na usishike
kitu mpaka tuje.” “Nisimame tu?” “Simama tu.” “Sawa mami.” Akaongoza njia.
Wakabaki
wakicheka. “Mna watoto wazuri!” “Lakini muongeaji ni huyo tu. Hawa wengine ndio
kama unavyowaona. Wapo kama mimi. Wamechukua upole wangu.” Nanaa akajisifia
nakufanya wote wacheke. “Sasa wewe Geb unachocheka ni nini? Kwani uongo?” “Mimi
nashauri ungemuacha tu Naya mwenyewe afananishe.” “Mimi namsaidia Naya.
Atuelewe mapema. Kuna kundi la wapole na watundu. Sasa Magesa yule ni kama baba
yake. Na hapo anakusubiria ndani akakueleze mambo yake ya utafiti. Sisi
wapole.” Akijionyeshea yeye na kina Liv. “Mpaka hapo Naya kashapata jibu.” Mama
G akaongeza. “Sasa mbona kama mimi sikuelewi mama!?” “Mbona mimi nipo upande
wako Nanaa! Upande wa wapole.” Akajibu mama G nakufanya wazidi kucheka.
“Mwaya
tumefurahi kukuona Naya. Tulikuwa tukisubiri hii siku kwa hamu kweli! Huyo
Joshua alikuwa mpaka anaombewa kwa kushikwa mikono na mama!” Naya akacheka. “Na
kweli subira imevuta heri mwanangu Joshua.” “Nilikwambia mama!” Wakaendelea
kucheka wakionekana kumfahamu Joshua vizuri na kama wanajua wanachozungumzia
zaidi, Naya akabaki akicheka tu akiwasikiliza. “Naya mama, karibu kwenye
familia.” “Asante sana. Na mimi nimefurahi kuwaona. Nyinyi ni watu wa kwanza
kuwasikia kutoka kwa Joshua. Alitaka kunileta jumamosi iliyopita, ila alikuwa
safarini.” “Alituambia.” Akajibu Nanaa.
“Karibuni
ndani.” “Asante.” Naya akasaidia kubeba mabegi ya watoto. “Umeona nilivyo na
vifurushi! Kama msafiri kumbe watoto watatu tu!” Naya akacheka. “Dada yao
mgonjwa. Alitaka sana kuja.” Akadakia mama G huku wakielekea ndani. Geb na
Joshua walitangulia mbele yao kidogo tu. “Nashukuru kwa vyombo. Vizuri sana.”
Joshua akamsikia Naya akishukuru, hilo likamfurahisha. “Afadhali kama
umevipenda. Ni mama huyo. Mama anapenda sana vyombo. Tulienda naye, akanisaidia
kuchagua vyombo vyote tulivyoleta.” “Nimeshaosha na kupanga. Twendeni
mkaangalie mnishauri.” “Sawa.” Nanaa akakubali bila shida.
“Joshua!”
Nanaa akamwita wakiwa wanatembea. Wakageuka pamoja na mumewe, Geb. “Bwana
mjengo huu wa hatari! Au unasemaje Geb?” “Ndio nilikuwa nikimpa sifa zake.
Sijawahi ona hii ramani! Anasema amebuni mwenyewe.” “Asante Nanaa.” “Hongera
Joshua mwanangu. Ndio maana huwa nakusifia, Nanaa anasema nazidisha. Haya ndio
maendeleo. Kitu kama hiki kinadumu kizazi hadi kizazi.” “Ametoka kuniambia
hivyohivyo.” Naya akaongezea kwa mama G. “Asanteni sana. Nimefurahi mmekuja
jamani. Karibuni ndani.” Wakaingia ndani.
“Shikamoo
baba Naya.” “Marahaba Nanaa. Hujambo mama?” “Sijambo. Nimekuletea wajukuu wote.
Umemuona huyo kaka mkubwa?” “Nimeshasalimiana na Magesa Magesa. Ameniambia baba
yake nimuite tu Geb, ila kama ninataka kumuita kwa jina la Magesa, basi lazima
niweke Geb ili kuwatofautisha.” Wote wakacheka. “Amesema dada mkubwa anaitwa
Liv, na kaka mdogo ambaye wote mnampenda, anaitwa Jimmy. Ila Jimmy yeye
haongei. Mpole kama Liv, lakini Jimmy amezidisha upole. Halafu bibi yao pia
anaitwa Oliva, kama Liv. Ila wote ni kina Magesa.” Wakazidi kucheka. “Kama ni
hivyo basi amemaliza, hakuna aliyeachwa. Mwanangu huyo anaakili kama zangu.”
Nanaa akajisifia tena nakufanya wazidi kucheka. “Ila huo utundu na uzungumzaji
kachukua kwa baba yake. Akili mimi.” Wote wakacheka tena. “Karibuni sana. Naona
mimi na Magesa tumeshakuwa wenyeji.” Baba Naya akaongeza.
“Anko!
Unajua hizi ngazi watu wanapanda hapa pakubwa, katikati. Lakini wanaogopa
kupanda huku pembeni ili wasianguke. Lakini ujue...” “Hapana Magesa. Nenda
kakae.” Baba yake akamkatiza kwa haraka na kumfanya atulie. “Kwani alikuwa
anataka kusema nini?” “Wewe humuwezi Magesa. Acha baba yake amtulize. Macho
yake yanavutwa na vitu vizuri tupu, pamoja na vya hatari. Hapo alikuwa
anakupanga kwa mahesabu, ili atakapokwambia anataka kupanda pale nje ya ngazi,
muwe ukurasa mmoja.” “Haiwezekani!?” Naya akacheka.
“Anaakili
huyo! Muone hivyohivyo. Akitaka jambo lake, hata kama ni la hatari, utajikuta
unamkubalia bila kujijua. Ni mpaka baba yake akimsikia ndio anamuelewa kwa
haraka. Akijua jambo ni la hatari, haruhusiwi kufanya, anaanzia mbali. Anakupa
madhara yake, kisha faida zake na jinsi ya kuepuka madhara yake, akimaliza
hapo, unajikuta wewe mwenyewe ndio unamsaidia kulitenda hilo jambo.” Wakacheka
sana wakati Nanaa akiwasimulia.
“Sasa
baba yake huwa anamuwezea. Kama hapo si umemuona ametulia na amerudi kukaa,
anafikiria jinsi yakumpanga tena baba yake. Apige lugha gani mpaka amruhusu
kupanda pale. Au yeye mwenyewe Geb ahusike katika huo mpango,
amsaidie kupanda pale.” “Kwani hapo hajaridhika?” “Hata kidogo. Kwamba ndio
jambo limeisha hapo? Hata!” Bibi yake akadakia.
Nanaa
akaendelea. “Lakini hapo ashajua nani mwenye kupinga yeye kupanda pale. Baba
yake. Ndio anampigia mahesabu jinsi ya kumrudia tena. Hakubali kushindwa. Sasa
wakati yeye anampigia mahesabu baba yake, sisi twende tukafanye kazi.” Naya na
Nanaa wakaondoka wakicheka, wakamuacha mama G akisalimiana na baba Naya vizuri.
“Na mimi nataka kusaidia mami.” Wakamsikia Liv, wote wakageuka. “Njoo kipenzi
changu. Ila Magesa wewe kaa na mtoto. Mcheze naye.” “Mimi nampenda Jimmy. Si
ndio Jimmy?” “Wewe kaka mzuri Magesa. Cheza na Jimmy.” Akakubali bila shida.
Wakaondoka.
~~~~~~~~~~~~~~~~~
Naya
akampenda sana Nanaa, ikawa rahisi kumzoea. Mwepesi, mchapa kazi halafu
mchangamfu. Akavutiwa na uzuri wake pia. Wakaandaa kwa pamoja mpaka wakamaliza,
na mama G alikwenda kuwasaidia huku akitaniana na Nanaa. Walionekana
kumchangamkia Naya, mpaka Naya akajikuta amewazoea na kuingia kwenye tani zao.
Muda wakukaribia kuwasili wageni ulipofika, Nanaa akamshauri Naya
akajitengeneze kidogo ili wageni wamkute ametulia na nadhifu. Naya akacheka na
kumfuata Joshua. “Nataka ni freshup kidogo.” Mrembo huyo mtoto wa mjini anajua
lazima mwanamke kuwa na vipodozi kwenye pochi. Joshua akapanda naye mpaka
chumbani kwake.
“Hakika
Joashua umejijenga!” “Nashukuru kama umepapenda.” “Mhh! Huku tu chumbani kwako
ni kama ile nyumba yetu nzima! Mpaka sebule!” “Niliamua Naya. Nilikusudia.”
“Hongera. Mpaka naona shida kuweka vitu vyangu chini! Naona ni kama
nakuchafulia!” “Naomba kuwa na amani kabisa, usiwe na wasiwasi wowote!” Akampa
kitaulo kidogo na kumuonyesha upande wa bafu, Naya akaenda kujisafisha, na
kujitengeneza hukohuko. Akatoka amependeza kama alivyokuwa amekuja hapo.
“Nakushukuru kwa kila kitu Naya wangu. Umefanya ile sehemu ivutie zaidi,
umeweza kupokea wageni vizuri. Nakushukuru mpenzi.” “Karibu na asante
kuniamini, imenipa ujasiri.” “Karibu. Sasa twende tukapokee wageni wengine.
Najua leo utachoka, nivumilie.” “Usijali. Nikazi nilikuwa nikifanya usiku
kuchwa. Nimezoea.” Joshua akacheka, akamshika mkono wakatoka.
Naya
akashangazwa na aina ya wageni walio kuwa wamealikwa hapo. Lakini akajirudi. Ni
Joshua! Lazima awe na wageni wa namna hii. Viongozi wakubwa watupu wa kazini
kwao walikuwepo hapo. Akashangaa kumuona na Chege pamoja na rafiki yake, waliokuwa
wakimlalamikia Jamal kuwa hawajaalikwa, nao walifika hapo. Akajua walihangika
mpaka wakaalikwa. Walijawa furaha na kuwaona wakipiga picha kila wakati. Joshua
alikuwa amemshika Naya mkono wakati wakikaribisha watu mpaka akaridhika wageni
wake wote wamefika pale.
Mambo Ya Mungu.
Aliporidhika
kuwa wageni wake wote wanavinywaji wakiwa nje ya ukumbi wakifanya cocktail tu,
Joshua akaomba watu wote watulie, wasikilize kabla hawajaelekea kwenye chakula.
Alikuwa amesimama na Naya, akasogea sehemu ya juu kidogo ili aonekane na wageni
wake wote. “Naomba niongee kidogo juu ya historia ya maisha yangu.
Najua wengi hawaifahamu.” Akaanza Joshua. “Naahidi sitawachosha na historia
ndefu maana harufu ya chakula imeenea, kuashiria chakula kipo
tayari.” Wakacheka kidogo.
“Nilizaliwa
kama watoto wengine wanaoitwa ni wa bahati mbaya. Baba alikuwa mume wa mtu.
Mwenye familia yake nzuri tu, na mama yangu kama mwanamke duni tu, muhudumu tu
wa nyumba ya kulala wageni huko mkoni, na ndipo alipo kutana na baba yangu na
mimba yangu kutungwa. Kufupisha habari, mama alipofariki nikawa mtoto wa
kukataliwa na kila mtu. Na kwa baba nako nilipoenda nikaonekana kama mtoto
muingiliaji tu kwenye familia yake. Ndipo nikaishia kuwa mtoto wa mtaani
kabisa. Nikilala mtaani kabisa kwa kuwa hata ndugu walinikataa.” Palizuka
ukimya mkubwa sana wakisikiliza.
“Nilifanikiwa
kwenda chuoni, nikapata msichana, naye alipogundua historia yangu na hali ya
umasikini niliyokuwa nayo, aliniacha na kwenda kuanzisha mahusiano na mwanaume
mwingine. Nikarudi kuwa peke yangu tena. Nilihangaika sana mpaka Mungu
aliponihurumia na kunirudisha kulala ndani ya nyumba na si mtaani tena ambako
alinitetea kwenye hatari nyingi sana za kufa nikiwa nikikimbiwa na watu hata
wale ambao huwa hupokea kila mtu, mimi walinifukuza. Nilipofanikiwa, nilijiapia
kitu kimoja.” Joshua akatulia kidogo.
“Nilijiambia,
sitarudia kosa alilofanya baba yangu. Kwamwe sitakuja kulala na mwanamke ambaye
Mungu hajanipa hata kama tamaa za mwili zimenizidia kwa namna gani, nilijiambia
nitasubiri tu mpaka Mungu atakaponipa mwanamke wangu. Nilianza kuwa mpweke, na
kadiri siku zilivyozidi kwenda ndivyo upweke uliponizidia na kuzidi kumsihi
Mungu anipe huyo mwanamke. Hakika nilisubiri na kuwa mwaminifu sana ili Mungu
anipunguzie siku za upweke na mimi niwe na wangu lakini ikawa ni kama Mungu
anakawia. Wengi hupenda kulikotengenezwa tayari, kwa hiyo sio kwamba nilikosa
mwanamke, lakini kila aliyenijia kipindi hiki nikiwa ninapo pakuishi, rohoni
nilishuhudiwa kabisa si wangu. Walikuja wa kila namna wa sura, maumbile, lakini
sikuwahi kupata amani ya umiliki.” Joshua akaendelea.
“Siku
moja nikiwa nimemuachia Mungu kabisa, kwa kuwa nilishaumwa na nyoka, nikawa
mwoga wa wanadamu sana. Namjua mwanadamu anapokuwa kwenye nyumba ya ibada na
anapotoka nje ya nyumba ya ibada jinsi anavyoweza kuwa mkatili kuliko simba
mwenye njaa kali. Na huwa haijalishi jinsia. Awe wa kike au wakiume, Mungu
amempa mwanadamu nguvu na uwezo wa ajabu sana. Akiamua anaweza akawa kitu cha
ajabu sana. Maisha yakanifundisha kuwa mwangalifu na makini sana kwa kiumbe
mwanadamu. Sina haraka naye.”
“Nikiwa
nimetoka ofisini kwangu nipo ofisi ya mwajiri, nikiwa na mambo mengine kabisa.”
Joshua akacheka kidogo, Naya akainama. “Mnaweza msielewe, lakini ni kama kitu
kikaniambia kunyanyua uso. Moja kwa moja nikamuona msichana amekaa nje ya ile
ofisi, ameinama. Mapigo ya moyo yakakabadilika, isivyo kawaida macho yakataka
kuangalia kilichobadilisha mapigo ya moyo.” Nanaa akaanza kucheka nakufanya
wageni wengine waanze kucheka. “Mimi mwenyewe nikashangaa! Sikuwahi kupata hiyo
hali! Ikabidi nikae sawa niangalie. Mbaya zaidi alikuwa ameinama, hata
haniangalii. Nikajiambia labda ni wa pembeni yake aliyekuwa akizungumza na
mwingine wa nyuma yake, nikajaribu kukaza macho, lakini nikarudi kwa yuleyule
aliyekuwa ameinama. Nikajiuliza huyu Mungu anataka nini kwangu!” Watu
wakacheka.
“Naomba
muelewe aina ya wanawake wanaonizunguka, na ninao kutana nao. Leo moyo unashituka
kwa msichana aliyekata nywele kama mtoto wa kiume! Hana hata urembo japo
hereni! Nikamuuliza Mungu ni nini hicho kinanifanya nimwangalie au kuna kitu
kingine! Nikataka kumfuata na kuzungumza naye japo kumfahamu jina kama njia
yakuelewa zaidi ni nini kimenitokea, na hapo sikuwa hata na mpango na mwanamke
na nilikuwa busy na kazi pamoja na shule, napambana kumaliza shahada yangu ya
tatu. Lakini Roho wa Mungu ndani yangu akanionya kabisa nisimfuate, tena hapo
nikazidi kushangazwa. Nikaona nitii nisimfuate, ila nikamuuliza Jamal. Ndio
maana na Jamal yupo hapa leo, kama atakumbuka.”
“Nilimuuliza
katika lile kundi la wasichana pale nje ni kina nani, maana nilikuwa na Jamal
karibu yangu. Akaniambia ndio aliowaita ili kuwafanyia usahili kwa ajili ya
idara yake. Kwa kuwa na mimi nilikuwa kwenye hali ya sintofahamu, sikujua
niulize nini tena. Nikamaliza kilichokuwa kimenileta pale kwenye ofisi za
mwajiri, nikamuacha Jamal na usahili. Lakini niliondoka pale nikiwa na maswali
juu ya kile nilichojisikia wakati ule. Kabla sijaondoka nikamsihi Mungu asaidie
hata anyanyue kichwa, aangalie upande niliokuwepo, angalau basi niione sura
yake. Nikasubiri mpaka nikakosa sababu ya kusubiri, Naya alikuwa amejiinamia
muda wote. Nikakata tamaa. Wakati nataka kuondoka tu, akanyanyua uso na
kutizama upande uleule. Lakini wao hawakuwa wakituona kule ndani. Sitaongeza
neno ili kuongeza nguvu ya hiki ninachotaka kuwaambia, lakini aliniangalia,
moyo ulipata kama kitu kimepiga.” Nanaa na mama G wakacheka sana. Na
wengine wakacheka. Joshua akacheka na kuendelea. Naya alibaki ameinama akicheka
taratibu.
“Kama
nilivyowaambia, Mungu alinionya kabisa nisimfuate. Niliondoka pale na maswali,
zaidi kwa Mungu. Hivi huyu Mungu anataka nini juu yangu na kile alichokipitisha
nilipomuona Naya! Mimi sikuamka siku hiyo hata na wazo la mwanamke! Ananiletea
Naya, halafu hataki nimfuate hata kumuuliza jina! Nikaacha. Baada ya siku mbili
nikamsikia Jamal akilalamika kuwa katika lile kundi hakupata watu anaowataka
isipokuwa watatu ndio angalau wananafuu. Akaja kuita watu wengine kuwafanyia
usahili, hakupata mtu. Akabaki akilalamika, mwishoe akaamua aite wale watatu wa
mwanzoni. Hapo sikuwa nikijua kama na Naya alipitishwa na Jamal. Tena Jamal
aliwaita kama kuwajaribisha tu kazi, ili kuona.”
“Naya na
wenzake wakaanza kazi mimi nikiwa na mambo mengi mno. Watu ambao wapo kwenye
kitengo changu, lakini sikuwahi kukutana nao. Jema msaidizi wangu, anayeratibu
ratiba yangu, alishaweka miahadi ya kukutana nao ili mimi kama kiongozi wa
kitengo niwakaribishe rasmi, lakini ikashindikana. Kila muda alioweka Jema
kukutana nao, ikawa ikitokea kitu kingine kinachonihitaji zaidi. Naya na wenzie
wakaanza kazi. Lakini Jamal akawa amempenda sana Naya. Alipenda sana utendaji
kazi wake, akawa haachi kumsifia lakini pia sikuwa nikijua kama anamzungumzia
yeye. Naya akaanza kujulikana kwa uadilifu pale kazini. Mtu wakuja kazini mapema
sana, na akiwepo kazini hana mambo mengi ila kazi. Jamal akaanza kumuamini kwa
majukumu ya pale idarani kwao, mimi nikiwa hata sijakutana nao bado na Naya ni
mgeni tu. Sekretari wangu akaniambia kwa kumtania Jamal kuwa safari hii Jamal
kapata jembe, anamfanyia kazi vizuri, naona amepunguza kelele.” “Fina!” Jamal
akahamaki na kufanya wote wacheke.
“Isivyo
ya kawaida, Jamal akaanza kupigania Naya aajiriwe akimtaka yeye hata kabla ya
muda wa majaribio haujaisha. Siku moja nikamkuta Jamal akibishana na mwajiri akimtaka
Naya aajiriwe, akataka utetezi wangu, mimi nikamwambia amalizane na mwajiri
yeye mwenyewe, kwanza nina mambo mengi. Jamal alikasirika, lakini sikuwa hata
nikiwajua hao wafanyakazi na sikutaka tuajiri mtu ambaye tungekuja kumfukuza
kazi siku chache baadaye. Nilitaka Jamal akae nao hao wafanyakazi wapya kwa
miezi 6 mpaka ajiridhishe, ndipo kutangazwe ajira, lakini Jamal akawa
aking’ang’ania ajira kwa mmoja. Nikaona ni jambo ambalo nimuachie nalo yeye
mwenyewe.”
“Kufupisha
habari, Jema aliniambia nina dakika 10 tu siku hiyo naweza kukutana na Jamal
pamoja na watu wa idara yake na ndipo itakuwa wakati mwafaka wakukutana na
wafanyakazi wageni. Hapo sikujua kama yule aliyeni...” “Badilisha mapigo
ya moyo.” Akamalizia Nanaa nakufanya wacheke. “Nanaa!” Geb akatingisha kichwa.
“Ewaaa! Sawasawa Nanaa. Sikujua kama na yeye yupo, na ndiye Naya anayepiganiwa
na Jamal. Niliingia chumba cha mkutano, kwa mara ya kwanza nikasahau ni nini
nilitakiwa kuzungumza nao baada ya kumuona Naya.” Watu wakacheka sana.
“Mimi
huwa sisahau kitu ninachotaka kuzungumza mbele za watu na huwa siandiki. Ila
siku ile nilishituka na nikashindwa kujielewa. Na Naya naye akawa kama
amenipuuza. Aliniangalia tu nilipoingia na kuwasalimia, akarudisha macho yake
chini ambapo baadaye nilijitahidi kuchungulia na kujua anaangalia nini,
nikagundua anaangalia simu yake. Sasa nikaumia kidogo. Nikasema amenidharau.
Sifa za Naya nilizozisikia kwa Jamal akiwaambia watu kuwa hana muda na simu.
Mimi naongea siku hiyo ndio macho kwenye simu! Kidogo ikanisumbua.
Lakini nikajua kuwa katika lile kundi la warembo wote siku ile, Jamal
alimwajiri. Kutokana na sifa zake nilizokuwa nikizisikia, nikajiambia labda
Mungu alitaka kuniongezea mfanyakazi bora pale kwenye kitengo chetu, lakini
zile hazikuwa hisia za mfanyakazi mwenzangu. Nikaona niwe na subira.”
“Siku
zilizidi kwenda Roho wa Mungu akinionya kabisa nisimfuate Naya. Ipo siku
nikamsihi tu angalau nipate nafasi yakumfahamu nione ni nini cha tofauti
alichonacho Naya na Mungu kuona kitanifaa mimi! Lakini sikupata ruhusa kutoka
kwa Mungu mpaka siku moja nikapata wasaa. Mungu alinipa kibali wakati ambao
hata mimi sikumuelewa Mungu. Ndio nilikuwa naanza mitihani, Naya na wenzake
walitumwa kikazi na Jamal Mbeya, ndio na mimi nikapata kibali hata
chakuzungumza naye! Nikamwambia Mungu hiyo sio sawa. Naya anakuwepo
palepale ofisini, ananizuia hata nisimsogelee, leo yupo nje ya jiji,
ninamtihani jumatatu, eti ijumaa ndipo niende nikamuone! Nikanung’unika
kidogo lakini ikanilazimu. Nilishasubiri sana, ikabidi kukusanya shule yangu
yote na kumfuata Naya mkoni Mbeya nikiongozana na Jamal akijua naenda naye
kikazi tu, kumbe nilikwenda nikiwa na agenda ya pili pia.” “Naya!” Akamalizia
Nanaa watu wakaanza kucheka.
“Siku
nilitaka kumsikia Naya, napo ilibidi kumuomba Mungu. Asubuhi hiyo walikuwa
wakifanya matangazo yao sokoni, Mbeya, Naya alikuwa busy mpaka nikaelewa ni kwa
nini Jamal anampenda. Hakukaa hata mara moja, alikuwa na kazi wakati wote
nikashindwa hata kumsogelea. Niliporudi tu hotelini, wote walikimbilia kula na
kunywa, yeye akakimbilia chumbani nikaambiwa amelala. Nikajua ni sababu ya
kuchoka. Nilimsubiria Naya, mpaka karibu giza linaingia. Nimekaa sehemu ya kula
nikimuwinda pengine atashuka chini sehemu ya mgahawa ale ndipo angalau niisikie
sauti yake, maana siku ya kikao alijitambulisha tu jina lake bila maneno mengi
akakaa. Wenzake walikuwa wakinywa mpaka wakaanza kulewa, Naya yupo chumbani.”
“Nikaanza
kumuuliza Mungu kama anaelewa kipindi nilichonacho. Kwamba nipo kwenye mitihani
na kazi inayonisubiria kwa asilimia zote, halafu akaniambia ndio wakati wa
kumfuata Naya, Naya mwenyewe hayupo! Nikamuuliza Mungu ule ulikuwa usumbufu au
kulikuwa na jambo!” Watu wakacheka. “Wakati nimekaa peke yangu na vitabu vyangu
hapo mgahawani na laptop yangu, nikamuona Naya anakuja pale mgahawani.
Nilikaribia kutupa laptop kwa furaha. Halafu alikuwa peke yake.” Watu wakazidi
kucheka.
“Kazi
ikawa ni jinsi gani ya kuzungumza naye maana mimi ni kiongozi wake mkubwa sana
Naya. Nikamuacha akae, ndipo nilipomfuata. Akataka kunikimbia kwa hofu. Alikuwa
akitetemeka, nikajua hatutaweza kuzungumza. Nikaanza kumsihi Mungu amfanye
atulie, angalau arudi kukaa.” “Kwani alishasimama?!” Nanaa akauliza kwa sauti.
“Zamani sana. Aliponiona tu nimemsogelea, akasimama kama akimbie wakati
nilimuona ameshaagiza chakula, pale alikuwa amekaa akisubiria lakini gafla
akataka kuondoka!” Naya akacheka mpaka akajifunika uso.
“Nikaanza
kuzungumza naye kwa maswali ili kumfanya afikirie, atulie. Akaanza kunijibu kwa
kifupi huku akitaka kuondoka, nikaendelea kumuuliza mpaka nikamuona ametulia.
Hazikuchukua dakika 10 mbeleni wakati tukizungumza naye, kuelewa kwa nini ni
Naya kwangu na sio msichana mwingine. Moyoni nikasema Aaahaaaa!
Nikamuuliza Roho wa Mungu, sasa kwa nini hukuniambia tu tokea zamani,
ukanisumbua vyote hivyo?” Watu wakacheka.
“Nilikaa
nikimsikiliza Naya akijibu swali fulani hivi, yaani akawa ni kama ameandika
insha nzima, na kunielewesha hata kwa machungu niliyokuwa nikipitia na maswali
niliyokuwa nayo juu ya hata kukimbiwa na mwanamke wa zamani. Naya alizungumza
kwa kawaida tu, lakini Mungu aliyapa yale maneno nguvu ya ajabu nikabaki
nikimtizama nakuelewa kuwa Naya ni wangu. Sasa kabla sijanogewa zaidi maana
Naya alishatulia, nikanogewa na mazungumzo mazuri, tukaingiliwa na mtu
aliyekuwa akimfahamu Naya na yeye alikuwa amemfuata hapo hotelini kama mimi tu.
Ila mwenzangu alikuwa na nafasi kubwa ya ushindi kuliko mimi. Nikataka kukata
tamaa, lakini Mungu akanionya kabisa kupaniki ila kutulia. Jamani Mungu yupo
na humpa amtakae.”
“Mwenzangu
alionekana anayo amri kubwa kwa Naya kuliko mimi, ikabidi mimi niondoke pale
nilipokaa, nimpishe yeye akae. Niliondoka pale kama niliyenyang’anywa tonge
mdomoni. Ila nikawa nimepata jibu ni kwa nini ni Naya na si msichana
mwingine. Nilirudi chumbani kwangu nikimuamini tu Mungu na ahadi zake kwangu,
lakini kama binadamu nikiwa sijui chakufanya. Usiku Jamal aliingia chumbani
kwangu akaongea tu kwa kifupi, kuwa wote wameamua kubaki pale kumalizia weekend
hawatarudi Dar siku inayofuata. Moja kwa moja nikajua na Naya naye ameamua
kubaki na yule mgeni wake. Jamal aliondoka na kuniacha nakodolea macho vitabu
wala sioni maandishi, kwa maumivu.”
“Nikaanza
kumuhoji Mungu pengine hakunituma pale Mbeya, nilijipeleka tu mimi mwenyewe,
lakini najijua, sina tatizo lakumsikia Mungu. Alinipitisha kwenye mazingira
ambayo, hapakuwa na jinsi isipokuwa kujifunza na kuelewa sauti yake. Hata
akinong’ona, kama anazungumza na mimi, huwa namjua Mungu wangu. Niliimaliza ile
siku kwa kusononeka, lakini sikuwa na jinsi isipokuwa kutii na kutulia pale
chumbani.”
“Asubuhi
nikiwa najiandaa, Jamal akagonga na kuniambia dereva ameshampigia simu kuwa
amefika, tujiandae safari ya kurudi Dar ianze. Nikamkubalia, ila nikamuona ni
kama kuna kitu anasita kusema. Nikamuuliza ni nini Jamal!? Akasema anaomba
aondoke na mtu mmoja hapo, tumpe lifti mpaka Dar. Akasema ni binti aliyetulia,
hataki hata kumuacha pale wasije kumshawishi ujinga. Nikamuuliza ni nani huyo?
Ndipo akasema Naya.” Nanaa akaanza kupiga makofi. “Nanaa wewe mtoto acha
ushabiki!” Mama G akaongea nakufanya watu wacheke.
“Mimi
mwenyewe sikuamini. Nikamuuliza Jamal, anauhakika kama ni Naya na amekubali?
Akasema amekubali. Nikaanza kucheka moyoni. Kwamba nitakuwa na Naya safarini!
Nikafurahia sana. Alipotoka tu Jamal, nikapiga magoti nikamwambia Mungu wangu,
asante.” “Jamani Joshua!” “Nanaa wewe!” Mama G akamshangaa. “Wewe huoni kama ni
Mungu huyo!?” Nanaa akamuuliza mama G. “Kweli ni Mungu Nanaa. Ni Mungu. Naya
alipoona kwenye hiyo gari na mimi nitakuwepo akaingiwa hofu tena na kutaka
kubadili mawazo, hapo nikajikaza na kumuomba Jamal nizingumze naye mimi
mwenyewe. Nikamwambia asiwe na wasiwasi, atakuwa salama na hatadaiwa
baadaye. Akaonekana kuelewa akatulia. Tukapanda tu kwenye gari, akampigia simu
baba yake. Kilichonivutia na kuelewa ni kwa nini Naya, ni pale baba yake alipomwambia
Naya afunge macho hapohapo amuombee. Akamuombea binti yake, mpaka akamaliza,
nikamsikia Naya akisema ‘Amina’. Nikajiambia kwa hiyo ni
muombaji, na baba yake pia anamuombea! Nikasema na mimi nitaponea hapohapo.”
Watu wakacheka.
“Ndipo kuanzia
hapo nikaanza kumng’ang’ania Naya, asielewe ni kwa nini, asijue mwenzie
nilipewa na Mungu. Nilimwambia Naya, huwa namfahamu yeye, au natambua uwepo
wake popote alipo kwa mapigo yangu ya moyo.” Watu wakacheka na kupiga makofi.
“Sitanii. Alipo Naya, bila kuiona sura yake, moyo wangu unajua yupo.
Nilimwambia awe amenenepa, au amekonda. Ananywele ndefu au fupi. Nitamjua tu.
Ni nitamtambua hata wawe wamechoma hiyo ngozi yake nzuri akawa kitu kingine
tofauti na huo muonekano wake, akiwepo mahali Naya wangu, nitajua
kutoka...” “Moyoni!” Akashabikia Nanaa, Geb akaina ana kutingisha kichwa. Watu
wakacheka tena.
“Nipo na
Naya, naelewa ni kwa nini yeye. Ninayo hii nyumba, lakini sasa hivi nalala
nikimsikia Naya akiwa anakoroma masikioni kwangu akiwa upande wa pili.” “Jamani
Joshua! Si ulisema nilikoroma mara moja tu!” “Yaah! Ulikoroma mara moja tu,
ulikuwa umechoka.” Watu wakacheka. “Naya hakoromi jamani.” “Ushasema nakoroma!”
Naya akalalamika akicheka. “Mara moja tu. Yaani nakuwa humu ndani, naendelea na
mambo yangu, nikiwa na Naya masikioni. Ameleta maana nyingine kabisa kwenye
maisha yangu. Mungu amenipa faraja ya ajabu. Huwa analala, nakuniacha
nikimsikiliza huku nikiendelea na shughuli zangu mpaka nikiwa tayari kulala,
ndipo nakata simu na mimi nalala.” “Waw!” Watu wakashangaa.
“Hakika
sikutegemea faraja aliyoongeza Naya kwenye maisha yangu. Ni zawadi kutoka kwa
Mungu. Nina utulivu wa tofauti nikijua Mungu amenipa Naya.” Joshua akamsogelea
na kumshika mikono yote miwili, Naya akimshangaa. Kisha akapiga goti mbele
yake. Wengi ndio wakaelewa, lakini Naya yeye alibaki na mshangao mkubwa sana
usoni. “Hili litabakia kuwa jengo tu Naya, mpaka wewe upafanye hapa nyumbani.”
Joshua akaanza taratibu akimtizama Naya. Naya akamuachia mkono mmoja na
kujifuta machozi kwa haraka akiwa ameshaelewa anachotaka kufanya. Joshua akatoa
pete mfukoni. “Nakupenda Naya. Na wakati wote nimekuwa nikikwambia
nakuhitaji wewe kama Naya. Naomba tuone, na mimi nipate familia. Nipate
ndugu wa kwanza na sehemu nitakapopaita nyumbani.” Naya hakuamini. Ni
Joshua huyu aliyemuuliza anataka wafunge ndoa lini, akashindwa kumjibu.
“Mimi
nilijua hutaki ndoa Joshua!” Naya akamwambia akilia asiamini. “Nilikuwa
naandaa hii siku maalumu ndio maana nilishindwa kukujibu siku ile kwenye gari. Nakupenda
Naya, nimeandaa hii siku maalumu kwa ajili yako.” Naya hakuwa akiamini.
Akamwangalia baba yake akakuta akimwangalia, akarudi tena kumwangalia Joshua.
“Naya?” Joshua akamwita taratibu akiwa amepiga magoti. “Subiri
kwanza Joshua. Usiondoke.” Watu wakawa hawajaelewa. Kila mtu
akashangaa sana. Naya akamuacha Joshua amepiga magoti akaenda mpaka alipokuwa
amesimama baba yake na ndugu zake.
Akalia
hapo mbele yake ameficha uso watu wote kimya kisha akamsogelea baba yake karibu
zaidi, mpaka upande wa bega la kushoto alikokuwa amesimama. “Mimi
nampenda Joshua, baba.” Naya akasikika akinong’ona. “Haaa! Ndio
kina Liv wote hawa!” Akasikika Nanaa akihamaki kwa sauti ya mshangao na
kumuangalia mumewe, Geb. Joshua alibaki amepiga magoti akisubiria akacheka
akijua alishapata kibali kwa baba Naya, kwani alishamuomba kumuoa Naya,
na siku hiyo alishajua kuwa Naya anachumbiwa. Baba huyo alishaomba pamoja na
Joshua, akimkabidhi kwa Mungu na kumuombea baraka zote. Ila hakumwambia hata
Naya mwenyewe. Joshua anawakaribisha nyumbani kwake, Naya anasema atazungumza
na baba yake, Joshua alishazungumza na baba Naya, wakakubaliana.
“Joshua
ananipenda kwa dhati na ananijali.” Akarudia Naya akilia.
“Mimi nawaombea baraka za Mungu Naya. Mungu yupo na nyinyi.” Naya alifurahi
sana, akamuinamia baba yake na kuendelea kulia asiamini. Alikuwa amependeza
sana. “Bibi harusi wangu ataondoa urembo wote!” Nanaa akamsogelea Naya. “Bado
Joshua amepiga magoti.” Akamnong’oneza Naya huku akimsugua mgongoni taratibu
kwa upendo. Watu wakacheka kidogo na Naya naye akacheka na kumwangalia Joshua.
Akarudi pale alipokuwa amepiga magoti, Naya akaushika mkono ule usio na pete,
akaunyanyua na kuubusu kiganjani kabisa. “Na mimi nakupenda
Joshua.” Mama G akapiga vigelegele na Nanaa akampokea na wengine
wakaendelea kupiga makofi wakati Joshua akimvisha pete Naya mpaka akamaliza.
Wakaanza
kupewa pongezi Naya akiwa ameshikwa vizuri na Joshua. Furaha aliyokuwa nayo
Joshua, haikuweza kufichika. Yeye alionekana amefurahi zaidi hata ya Naya
mwenyewe. Mabusu shavuni kwa Naya hayakuisha. Hapo mbele ya watu hakuvuka
mipaka kabisa, akiweka heshima kwa baba yake Naya, kwa kuyajua na kuyazingatia
mahusiano ya Naya na baba yake. Akaishia mabusu ya shavuni tu. “Nimefuhi sana,
natamani leo ndio ingekuwa ndio harusi yetu.” Joshua akamnong’oneza Naya
sikioni. Naya akamwangalia akicheka. “Inamaana leo usingeondoka hapa, tukabaki
wote tukisheherekea. “Mungu atatupa uzima Joshua. Hiyo siku na sisi tutaiona.”
“Amina Naya.” Hilo likamfurahisha sana Joshua, na kumuhakikishia ndoa.
Mahari Yakushangaza Ya Naya.
Walibakia
na kina Magesa tu hapo pamoja na kaka yake Nanaa, James ambaye ndiye aliyemlea
Nanaa. Na yeye alihudhuria kwenye hiyo tafrija na baba yake mzazi Nanaa
waliyekutana naye ukubwani naye akaonekana kufahamiana vizuri tu na Joshua,
alikuwepo hapo kwenye tafrija pia. Na mwenyewe alibakia nyuma baada ya wageni
wote kuondoka. Wote watatu, Gebu, Joshua na baba yake mzazi Nanaa walikuwa
wanachama wa hiyo club wanakokwenda kuendesha boti huko. Ndio Naya akajua huwa
wakati mwingine wanakutanaga huko na kuendesha boti wakishindana kisha kuvua
samaki pamoja. Walitaniana kwa hili na lile ndipo Geb akaomba kuzugumza na baba
Naya.
“Naona
leo mambo yamekwenda vizuri, tunamshukuru Mungu.” Watu wote wakatulia
kusikiliza. Watoto wao walishalala. Joshua na Naya wakawalaza chumba cha chini
ambacho kipo hapo karibu nao. Mama yao alijiandaa mpaka na nguo zao za kulalia
kama aliyejua watakuwepo hapo kwa muda mrefu. “Joshua anataka kuoa kwa haraka,
na kamati hapa naona imekamilika. Tunaomba tu utaratibu wa mahari, tuje
kulipa.” Naya akashangaa kwamba kulikuwa na mipango ya harusi tayari! Watu wote
wakatulia. Pakazuka ukimya kama kumpa baba Naya nafasi ya kuzungumza.
“Anachozungumzia
Gebu ni ile orodha ya vitu vinavyohitajika kuletwa kama sehemu ya mahari ya
Naya.” Naya akabaki ametulia pembeni ya Joshua. “Mahari ya Naya haitakuwa
mali.” Watu wote kimya wakitaka kujua na kumsikia baba huyo mkimya haswa.
Akaendelea. “Kama kamati imekamilika na ni nyinyi tu mliopanga kuja kuilipa
hiyo mahari, tunaweza kumalizana hapahapa. Lakini kama kuna aliyepungua,
tunaweza kupanga hiyo siku.” “Nafikiri kwa sehemu unaijua historia ya Joshua.
Sisi ndio familia, kwamba tumeshakamilika.” Akajibu Geb. “Basi hii ndio mahari
ya Naya.” Baba Naya akajiweka sawa kwa kujivuta kabisa mbele ya kiti ili
kuhakikisha wote wanamuona vizuri na kumuelewa.
~~~~~~~~~~~~~~~~~
Usipitwe na MAHARI ya Naya. Baba Naya anataka nini kwenye mahari ya
binti yake? Kina Magesa ndani ya nyumba. Usikose muendelezo.
ILI KUJUA KISA KIZIMA JUU YA KINA MAGESA, FUATILIA SIMULIZI YAKE
YA kuvutia na KUSISIMUA YA “Ni wangu!”
0 Comments:
Post a Comment